Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Eng. Hamad Yussuf Masauni (393 total)

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri kwamba kuna changamoto katika ujenzi wa nyumba za Polisi pamoja na vituo. Sasa swali langu ni je, kwenye Polisi kuna kitengo cha Usalama Barabarani yaani Trafiki, ambacho kimekuwa kikikusanya fedha nyingi, almost kwenye bajeti huwa tunatenga ni zaidi ya bilioni 10 kwa mwaka.
Je, ni kwa nini sasa Serikalli isiamue kuruhusu Polisi kutumia fedha zinazotokana na Polisi wa barabarani kwa ajili ya kuondoa kero ya ujenzi wa nyumba za polisi, pamoja na Vituo vya Polisi katika Wilaya zote nchini?
Swali la pili, katika majibu ya Mheshimiwa Waziri, amesema Serikali inatajarijiwa kukopa kutoka Benki ya Exim China; je, haijatueleza ni kiwango gani mnatarajia kukopa na namna ambavyo mtalipa, kwa sababu suala la Polisi siyo miradi ya maendeleo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI YA WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna fedha ambazo zinakusanywa kupitia faini ambazo zinakusanywa na Trafiki, lakini fedha hizi hazirudi Polisi, zinakwenda Hazina. Kwa hiyo, wazo lake Mheshimiwa Mbunge, nadhani siyo wazo baya labda tunaweza tukalitafakari pamoja kwa baadaye tuone jinsi gani ya kufanya.
Hata hivyo, Polisi ina mikakati mizuri tu ya kuweza kujenga nyumba za ziada kwa ajili ya kutatua changamoto hizo. Nimezungumza mradi wa ujenzi wa nyumba 4,138 hii ikiwa ni awamu ya kwanza, lakini kuna mradi ambao utaweza kuhakikisha kwamba tunahitaji nyumba 3,500 kwa mwaka, kwa maana nyumba 35,000 hadi kufikia mwaka 2025. Hiyo ni mikakati ya muda mirefu.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili, ambapo ameuliza huu mkopo wa Exim Bank ya China, mkopo huu unakadiriwa kufikia shilingi bilioni 500 ambao ni mkopo kutoka Serikali ya Exim Bank ya China ambao vilevile utalipwa na Serikali kulingana na kusainiwa kwa memorundum of understanding. Kwa hiyo, niseme tu kwamba taratibu zitakapokamilika, mkopo huu utakapokuwa tayari ujenzi utaanza mara moja na changamoto ya nyumba inaweza kupungua kwa sehemu kubwa sana.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mwaka 2012 katika Bunge hili niliuliza swali kama hili linalohusiana na Askari wa Jimbo la Konde kuendelea kukaa kwenye magofu yaliyoachwa na Mkoloni. Nataka Mheshimiwa Waziri, unijibu kati ya Mpango huo unaokuja, Jimbo la Konde kujengewa Askari nyumba hizo umo au haumo, kama haumo ni kwa nini?Mpango huo unaokuja, Jimbo la Konde kujengewa Askari nyumba hizo umo au haumo, kama haumo ni kwa nini?
NAIBU WAZIRI YA WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, programu hizi za ujenzi wa nyumba za Askari zinapofanyika zinaangalia maeneo yote ya pande za Muungano. Kwa mfano, mtakumbuka kwamba tulikuwa tuna mradi ambao haujakamilika hata hivyo wa ujenzi wa nyumba kupitia NSSF, kulikuwa kuna nyumba zilizojengwa pia Zanzibar ikiwemo Pemba. Katika mradi huo ambao utatarajiwa kujenga nyumba 4,136 kati ya nyumba hizo nyumba 150 zitajengwa Pemba.
Kwa hiyo, nataka nimtoe wasiwasi tu Mheshimiwa Khatib, kwamba labda baadaye tuonane tuone Konde ni ngapi lakini kati ya nyumba hizo nyumba 150 zitajengwa Pemba. Hata hivyo, huu mradi nimeuzungumza wa muda mrefu wa nyumba 3,500 kila mwaka kufikia 2025, pia utazingatia mahitaji ya sehemu zote. Huu mradi wa nyumba 4,136 utaanza mikoa 17 kwanza baadaye tutamalizia mikoa mingine.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na takwimu nzuri za Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu matukio ya uporaji kwa watu wanaotoka kuchukua fedha tasilimu benki, ni miongoni mwa matukio mengi yanayotokea hivi sasa na kwa kuwa kuna imani na minong‟ono miongoni mwa wananchi kwamba watumishi na wafanyakazi wa benki kwa namna fulani wanahusika na kuwezesha uhalifu huu. Serikali inatoa kauli gani kuhusu imani hiyo na minong‟ono ya Watanzania?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa baadhi ya matukio ya uporaji wa pesa, watu wanavyotoka kuchukua pesa tasilimu benki yanahusisha matumizi ya pikipiki na kwa kuwa pikipiki zinatoa ajira halali kwa vijana wa bodaboda, lakini wachache wanatumia kuichafua na kuumiza Watanzania. Serikali inasema nini kuhusu kushindwa kwake kuwadhibiti hao wachache ambao wanatumia vibaya vyombo vya usafiri ambavyo vinatoa ajira na masilahi mengine kwa Watanzania katika kudhibiti hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na wizi wa benki ni kweli kumetokea na wimbi la kuiba benki katika kipindi cha karibuni, lakini wananchi wamechukua hatua madhubuti ikiwa ni pamoja na kufanya kazi karibu kabisa na benki hizo ili kuona kwamba kama kuna miongoni mwa wafanyakazi ambao sio waaminifu waweze kuchukuliwa hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile siyo tu miongoni mwa wafanyakazi ambao siyo waaminifu, lakini pia wale ambao wana kawaida ya kuchukua fedha nyingi, ni vizuri kabisa wakafanya utaratibu wa kuweza kuwasiliana na polisi ili waweze kuwapa ulinzi. Wakati mwingine taarifa hizi zinatoka miongoni mwa sehemu au makampuni ambayo yanajihusisha ya biashara mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kutoa wito kwa makampuni yote au wafanyabiashara wote ambao wanaweza kusafirisha fedha nyingi kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine, walitaarifu Jeshi la Polisi na Jeshi la Polisi litatoa ulinzi ili kudhibiti hali kama hiyo, wakati huo huo Jeshi la Polisi likiwa linafanya kazi ya ziada kuhakikisha kwamba, linawatia mikononi na kuweza kuwapeleka katika vyombo vya sheria wale wote ambao wanahusika kwa njia moja ua nyingine na limeshaanza kufanya kazi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusiana na suala la pikipiki. Polisi haijashindwa kuwadhibiti hawa watu wachache ambao wanatumia vibaya fursa hii ya vijana ambao wana pikipiki, siyo tu bodaboda hata pikipiki za kawaida zimekuwa zikitumika katika uhalifu mbalimbali. Ndio maana sasa hivi kuna mazoezi mbalimbali yanaendelea nchini ikiwemo kuhakikisha kwamba wanazikagua pikipiki hizi ili kuweza kubaini uhalali wake, lakini pia uhalali wa wale ambao wanaendesha pikipiki hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nawaomba Waheshimiwa Wabunge tushirikiane kipindi hiki ambapo Polisi inaendesha zoezi la kuweza kuhakiki pikipiki hizi ili kuweza kuhakikisha kwamba, sheria zinafuatwa na waendesha pikipiki hizi iwe kwa utaratibu wa wafanya biashara kwa maana ya boda boda au utaratibu wa kutumia pikipiki kwa matumizi ya kawaida.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, matukio ya wananchi kujichukulia sheria mikononi yanasababishwa na mambo mawili. Jambo la kwanza, ni baadhi ya Askari Polisi kupewa taarifa za matukio na kutokwenda kwenye maeneo ya matukio kwa wakati unaotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya pili ni wahalifu kupelekwa vituoni na baada ya muda mfupi kuonekana wakirandarada mitaani bila kuchukuliwa hatua stahiki na Jeshi la Polisi. Sasa je, Serikali inawaambia nini Watanzania hasa kutokana na uzembe huu ambao unafanywa na baadhi ya Askari Polisi unaosababisha wananchi kukata tamaa na kujichukulia hatua mikononi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nianze kwanza tu kueleza jambo tu kwa kifupi sana kabla sijajibu hili swali. Ni kwamba Jeshi letu la Polisi ni jeshi ambalo linajitahidi kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na weledi wa hali ya juu.
Hata hivyo, Jeshi letu la Polisi linakumbana na changamoto mbalimbali, kwanza idadi ya polisi ambao tunao hawatoshelezi, kwani sasa hivi Polisi mmoja anahudumia kati ya watu 300 mpaka 350, idadi ambayo ni kubwa ukilinganisha na kiwango cha Kimataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata hivyo tumeona malalamiko mengi ya Waheshimiwa Wabunge kuhusiana na matatizo mbalimbali yakiwemo makazi, usafiri na kadhalika kutokana na hali ya uchumi wa nchi yetu kwa ujumla wake. Kwa hiyo, mbali ya changamoto hizi nyingi ambazo Jeshi letu la Polisi linakabiliana nazo lakini linajitahidi kadri ya uwezo wake kuweza kufanya kazi zake kwa kuzingatia maadili, weledi pamoja na sheria za nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, hiyo haiondoshi ukweli kwamba wakati mwingine inatokeza baadhi, kama ilivyo mtu mwingine wa sehemu nyingine yoyote, kwamba baadhi ya polisi wanaweza kuwa na upungufu wa hapa na pale. Kadri hali hiyo inavyojitokeza, hatua madhubuti za kisheria zimekuwa zikichukuliwa. Wapo baadhi ya polisi wamekuwa wakichukuliwa hatua za kisheria kupitia Mahakama za Jeshi la Polisi yenyewe, lakini na wale ambao wameweza kutenda makosa ya jinai vilevile sheria imekuwa ikifuata mkondo wake.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pia namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri aliyonipatia, lakini naomba kuuliza swali langu la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali imejipanga vyema kwa ujenzi wa barabara hizo. Je, Serikali ina mpango gani wa kupanua zaidi barabara hizo ili ajali zisitokee?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, upanuzi wa barabara unakwenda sambamba na bajeti. Nadhani Serikali ina mipango mizuri na imefanya kazi kubwa ya kuimarisha mitandao ya barabara nchini na sasa hivi nimesikia kuna mradi wa upanuzi wa barabara ambayo inatokea Dar es Salaam kupitia Chalinze na mbele zaidi. Kwa hiyo, ni mipango ambayo inaendelea kufanyika hatua kwa hatua kadri uwezo wa Serikali utakavyoruhusu.
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na ninashukuru majibu ya Serikali. Naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
(a) Kwa kuwa Serikali imekiri kwamba kuna upungufu wa vitendea kazi, kwa maana ya magari na mafuta; je, ikiongeza kununua magari, italipatia Jeshi la Polisi Wilaya ya Magu hasa Kituo cha Kabila gari lingine?
(b) Kwa kuwa Jeshi la Polisi ni walinzi wa mali na raia lakini maisha yao ni magumu sana, hata wanapostaafu, wanaendelea kuwa na maisha magumu.
Je, Serikali kwa sababu askari katika Wilaya ya Magu wako 135 na nyumba wanazoishi askari kumi ziko tano tu; Serikali ina mpango gani wa kujenga nyumba Wilaya ya Magu? Nipatiwe majibu ni nyumba ngapi zitakazojengwa. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Magu kuongezewa gari moja, ni kwamba sasa hivi, Kituo cha Magu kina gari tatu tayari, lakini nadhani zitakapokuwa tayari hizi gari nyingine ambazo nimesema kwamba kuna gari jumla 777 zinatarajiwa kukamilika, ukiacha zile ambazo zimeshatolewa, hilo jambo tutalichukua na tutalifanyia kazi. Ni jambo ambalo linawezekana, tutalizingatia.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni kuhusiana na nyumba. Kwanza nirekebishe tu, Magu kuna askari 147 siyio 135 kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema. Kwa hiyo, suala la nyumba kama ambavyo nimezungumza kwamba kuna mpango wa kujenga nyumba 4,136 na katika Mikoa ambayo nyumba hizo zitajengwa, Mwanza ni mojawapo. Labda baadaye tuangalie katika orodha ya nyumba zitakazojengwa Mwanza kama Magu ipo. Kama haipo vilevile ni jambo ambalo tunaweza kuliangalia kwa pamoja baadaye.
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kunipa nafasi hii ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa tunafahamu majengo haya yanazidi kuwa magofu na baadaye gharama, fedha za Serikali zinapotea kwa wingi kwa sababu haya baadaye yanabomoka tu, vilevile watu wanafugia ng‟ombe. Je, Mheshimiwa Waziri, ni lini Wizara itampatia Mkandarasi huyu amalize kituo hiki? Je, Wizara itachukua jitihada gani kuhakikisha kituo hiki kinamalizwa mapema? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kituo hiki ambacho kimeanza kujengwa mwaka 2011 kimechukua muda mrefu kukamilika. Hata hivyo, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Mkokotoni, Mheshimiwa Juma Hija ambaye naye amekuwa akifuatilia kwa karibu ujenzi wa kituo hiki. Nilichomwambia ambacho naendelea kukizungumza hapa mbele ya Bunge lako Tukufu ni kwamba, ni kweli tumempatia tayari Mkandarasi karibu shilingi milioni 50 ili kuweza kukamilisha hiki kituo, lakini bado kuna deni ambalo anahitajika alipwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefikiria kwamba, katika bajeti ya mwaka 2016/2017, tuweze kushughulikia madeni ya Wakandarasi mbalimbali ambao wamekuwa wakifanya kazi za vituo katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu ikiwemo Mkandarasi ambaye anajenga Kituo hiki cha Mkokotoni.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu yenye takwimu na hakikisho la usalama, lakini hivi sasa vitendo vya wale wanaoitwa mazombi na masoksi vinaendelea vikifanywa fawaisha kila siku na hata juzi watu kadhaa walipigwa katika Mtaa wa Kilimani na wengine wakapigwa katika Mtaa wa Msumbiji. Pia watu hawa wamekuwa wakiranda na silaha za moto, misumeno wa kukatia miti, wamekuwa wakivamia vituo vya redio, wamekuwa wakipiga watu mitaani. Swali langu la kwanza, je, kitu gani kinazuia kukamata uhalifu huu unaofanywa fawaisha kila siku na ambao unakuza culture of impunity katika nchi yetu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Serikali haioni vijana hao wanaoitwa mazombi wanaotumia magari ya KMKM ya KVZ, volunteer, magari ya Serikali waziwazi na namba zake zinaonekana kila kitu. Je, Serikali haioni kwamba kuruhusu hali hiyo kuendelea kunaitia doa Serikali katika suala zima la haki za binadamu na utawala bora? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Naibu Spika, siku zote Jeshi la Polisi ama vyombo vya dola vimekuwa vikifanya kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi. Haya ambayo anazungumza Mheshimiwa Ally Saleh, nadhani amezungumza maneno mazombi, sijui ana maana gani, lakini ninachotaka kusema ni kwamba kama kuna uvunjifu wa sheria katika nchi yetu, basi taarifa hizi ziwasilishwe polisi na polisi itachukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri aliyonijibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni kesi ngapi zilizolipotiwa kwa kipindi hiki cha mwaka wa uchaguzi?
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ni kwa nini kesi zinacheleweshwa wale walemavu hawapi haki zao kwa haraka?
Na je, ni mikoa mingapi inayoongoza kwa mauaji ya maalbino? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuhusu Mikoa ambayo inaongoza ni Mkoa wa Mwanza, Mkoa wa Shinyanga na Kigoma.
Swali lake la pili anauliza kwamba ni kesi ngapi, takwimu halisi zilizotokea baada ya kumalizika uchaguzi naomba nimpatie baadaye lakini ninachoweza kusema ni kwamba toka mauaji haya yameanza mwaka 2006 mpaka mwaka jana takribani watu wanakadiriwa kwenye 40 mpaka 43 wameweza kufariki, lakini watuhumiwa karibu 133 na kati ya hao watuhumiwa ambao wamehukumiwa kwa adhabu ya kifo ni 19 tayari ambao wameonekana wana hatia. Kwa hiyo, hizi takwimu za baada ya uchaguzi mpaka saa hivi, hizi naomba nikupatie baadaye. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa matatizo yaliyoulizwa na Mheshimiwa Mgeni kwenye swali namba 106 yanafanana kabisa na matatizo yaliyoko Jimbo la Geita Vijijini. Takribani wanawake wazee wanne kwa mwezi wanauwawa kwa kukatwa mapanga kwa imani ya kishirikina na Jeshi la Polisi halijawahi kufanikiwa kuwakamata wakataji mapanga hao kwa kuwa jiografia ya kutoka Geita kwenda eneo husika ni mbali.
Je, Serikali inajipangaje kupeleka gari maalum na kuunda Kanda Maalum kwa ajili ya kuokoa akina mama wanaokatwa mapanga kwenye Jimbo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Polisi linajitahidi sana kuweza kukabiliana na mauaji haya, lakini kama ambavyo nimezungumza wakati nikijibu maswali wiki iliyopita kuhusiana na changamoto ambazo zinakabili Jeshi la Polisi. Naomba nichukue fursa hii kuweka sawa kidogo takwimu wakati nilikuwa najibu swali la Mheshimiwa Selasini juzi, nilieleza kwamba moja katika changamoto inakabili Jeshi letu la Polisi ni kwamba idadi ya polisi tulionao ni kidogo na kiukweli kihalisia takwimu zinaonyesha kwamba ukiangalia takwimu za kidunia polisi mmoja anatakiwa ahudumie kati ya watu 400 mpaka 450 takriban na siyo 300 mpaka 350. Sisi hapa nchi yetu polisi mmoja kwa upande wa Tanzania Bara anahudumia watu kwenye 1000 mpaka 1200. Kwa hiyo utaona ni tofauti kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa changamoto hizi na changamoto nyingine ambazo tumekuwa tukikabiliana nazo hatua kwa hatua kama hii ya usafiri, nataka nimhakikishie tu Mheshimiwa Musukuma kwamba tumekuwa na changamoto ya usafiri kwa muda mrefu lakini tumepata magari takribani magari 387 ambayo yameweza kugawiwa katika maeneo mbalimbali. Tutaangalia eneo hilo kama halijafika gari tuone ni jinsi gani na uzito wa hali yenyewe ilivyo tushauriane tuone ni nini tutakachofanya ili tuweze kukabiliana na tatizo hilo. Lakini mengine ni changamoto ambazo tunaenda nazo kadri ya uwezo wa bajeti unavyoruhusu.
MHE. HAFIDH ALI TAHIR: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jawabu zake, lakini swali langu lilikuwa na msisitizo ukizingatia kuwa Zanzibar inajiandaa na marudio ya Uchaguzi Mkuu, ndiyo sababu swali langu kubwa lilikwenda huko. Kurudiwa kwa Uchaguzi Zanzibar siyo jambo geni, mwaka 1961 Uchaguzi ulifutwa na ukarudiwa mwaka1963. (Makofi)
Sasa kwa tokeo hili Mheshimiwa Waziri swali langu la kwanza, huoni kwamba kuna haja ya kuweka umaksudi wa kupatia usafiri Wilaya nilizozitaja wakati huu tukielekea katika uchaguzi ili yale mazombi yanayozungumzwa yapunguke kufanya kazi?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili, namwomba Waziri aniambie kwamba kwenye Bajeti ijayo ameahidi kwamba atatupatia magari Wilaya alizozitaja, Mheshimiwa Naibu Waziri naomba ukubali hii ni ahadi na nikungoje kwenye bajeti? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie kwamba nilizungumza vilevile kuhusiana na hili suala la magari ambalo kwa bahati mbaya kuna baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wamelipotosha kwa makusudi ama hawajalielewa. Lakini naomba nichukue fursa hii kwa kueleza tu kwa ufupi ni kwamba Jeshi la Polisi na ninyi Wabunge ni mashahidi mara nyingi mmekuwa mkihoji, vituo vyangu havina magari, Jimbo langu kwenye kituo fulani hakuna magari, na ndiyo kwa kuzingatia hilo Serikali kupitia Jeshi la Polisi, likaandaa mkakati kabambe wa kupunguza hiyo hali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulimaliza kwa wakati mmoja, siyo rahisi kwa sababu katika nchi tuna zaidi ya vituo 4,500, kwa hiyo, kupata gari 4,500 kwa mpigo ili kila kituo kiweze kupata gari ni jambo ambalo ni gumu. Kwa hiyo kulikuwa kuna mpango wa kwanza wa kuweza kupata gari 777 kupitia mkopo wa Exim Bank ya India, ambapo kati ya hizo tuliweza kupata gari 104, lakini pia Serikali iliweza kutoa gari takribani 203 kwa hiyo kufanya jumla ya idadi ya gari ambazo zilipatikana kuwa ni 387. Kati ya gari hizo, gari 37 zilipelekwa Zanzibar na nimhakikishie Mheshimiwa Hafidh Ali Tahir kwamba gari hizi bado hazijagawiwa katika Wilaya, nina hakika kwamba wakati mgao utakapokuwa umefanyika, basi Wilaya hizo ambazo zimezungumzwa vituo vya Wilaya yake ya Magharibi A na Magharibi B vitapata gari.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali lake la pili, alizungumzia kuhusiana na hali ya usalama kwa ujumla. Mimi nataka nimhakikishie tu kwamba pamoja niichukue fursa hii, kuwaeleza Wananchi wa Zanzibar kwamba Jeshi la Polisi ama Serikali itahakikisha inalinda usalama wa raia kama ambavyo majukumu yake ya msingi yanavyotaka. Kwa hiyo, wasiwe na wasiwasi wajitokeze kwa wingi kushiriki uchaguzi utakaporudiwa na hakuna wasiwasi wowote kila mtu ambaye atakuwa na haki ya kupiga kura, apige kura kwa usalama na amani. (Makofi)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, ninaomba niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa shida ya ulinzi iliyopo Dimani inafanana sana na Jimbo la Ukonga, nina Kata 13, sina kituo kikubwa cha Polisi, na ni eneo la pembezoni ikiwepo Msitu wa Kazimzumbwi, lakini hata kituo cha Sitakishari ambacho kinahudumia Jimbo la Segerea na Ukonga hakuna gari, sasa nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri, atatujengea Kituo cha Polisi Ukonga au apeleke gari Segerea Sitakishari ili ihudumie wakati mipango mingine inaendelea?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwasilishe, ahsanteni.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani ule umuhimu wa magari ambayo nimekuwa nikiuzungumza umeongezeka uzito wake, sasa niweke tu wazi kwamba katika yale magari ambayo tumeyapata, magari mengi ni kwa ajili ya doria, operation na matumizi ya kawaida ya polisi. Hayo magari yanayoitwa ya washawasha sidhani hata 24 sujui kama yanafika.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Waitara nadhani utakubaliana na mimi na Wabunge wengine kwamba, Jeshi la polisi linahitaji magari zaidi, ikiwemo katika Kituo chako ulichozungumza, mimi naomba hili nilichukue tuone tutalifanyia kazi vipi.
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, wabheja sana. Kwa kuwa Jimbo la Kishapu halikupata mgao wa magari mapya ya polisi katika awamu hii na Jimbo hili lenye watu sharp na askari wanaofanya kazi zao kwa u-sharp, lina magari mawili mabovu yenye umri wa zaidi ya miaka mitano.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, nilipata ahadi kuwa mwezi wa pili tutapata magari mapya ya polisi, uko tayari kunihakikishia Jimbo sharp litapata magari mapya ili Wananchi waweze kupata huduma hasa za kiusalama wanapohitaji kuliko hivi sasa polisi wangu wa Kishapu wanavyohangaika? Wabheja
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Nchambi kwamba Serikali hii ya Awamu ya Tano ya hapa kazi tu huwa haina desturi za kutoa ahadi ambazo hazitekelezeki. Kwa hiyo, kama ni ahadi ambayo imetolewa, basi nitaifuatilia hiyo ahadi yenyewe halafu tuone hatua zilizofikiwa zimefikiwaje na kama imekwama imekwama vipi, halafu tutaonana mimi na yeye tuone ni jinsi gani ya kufanya.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 20 Oktoba, 2015 aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne alipokea magari ya washawasha 399 kati ya magari 777. Kati ya magari hayo ni magari 50 tu yalitumika. Nime-google bei ya gari moja ni sawa kabisa na kipimo cha MRI na Scanner kwa maana ya kwamba gari moja ni kama dola 400 na hiyo mashine bei yake ni hiyohiyo.
MWENYEKITI: Dola 400?
MHE. SUSAN A.J. LYIMO: Dola 400,000. Je, ni kwa nini sasa Serikali haioni kwamba huo ni upotevu mkubwa wa fedha na kutokuwajali wananchi na kwamba fedha hizo zingetosha kununua Scanner na MRI kwa nchi nzima kwenye Hospitali zote za Rufaa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI (K.n.y. NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSI, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, si kweli kwamba magari ya washawasha yamenunuliwa na hayana tija. Magari ya washawasha yamenunuliwa ikiwa ni miongoni mwa ile programu ya kununua magari 777 kwa ajili ya matumizi ya Askari. Kwa hiyo, magari haya yamesaidia sana na bado mengine yatafika kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kipolisi. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, ninaomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa sasa uhalifu umeongezeka katika bonde la Yayeda Chini, hasa ubakaji na mengineyo mengi; gari lililosemwa hapo kwanza ni bovu au chakavu katika eneo hilo la polisi au kituo cha polisi, Hydom. Lakini hiyo haitoshi hapo, mvua ikinyesha kidogo bonde la Yayeda Chini halipitiki kutoka Haidom kwa gari lolote.
Je, Serikali haioni kwamba bado wananchi wa Yayeda Chini wana haki ya kulindwa wao na mali zao?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa kuwa wananchi wa Yayeda Chini wanahitaji kulindwa: Je, tukiwahamasisha, Serikali iko tayari ku- chip in ili kujenga kituo hicho pamoja na wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi, ni kwamba hatua zilizochukuliwa kwa kiasi fulani zimesaidia sana kupunguza tatizo la uhalifu, hasa wizi wa mifugo katika Bonde la Yayeda Chini. Nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba jitihada hizo zinahitaji kuongezwa ili kuondosha kabisa masuala ya uhalifu, hasa wizi wa mifugo katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, hii inadhihirisha kutokana na ukweli kwamba kwa mfano kwa takwimu za mwaka 2014/2015 katika Wilaya ya Mbulu ambayo imeonesha kwamba kuna matukio karibu 21 ya wizi wa mifugo, eneo la Yayeda Chini lilikuwa na takwimu ya matukio matano ambayo ni makubwa zaidi ukilinganisha na maeneo mengine katika Wilaya hiyo. Hata hivyo, kwa mfano, katika Mkoa mzima wa Manyara, Wilaya ya Mbulu ndiyo iko chini ukilinganisha na Wilaya nyingine kama Kiteto ambayo inaongoza kwa matukio 71, ikifuatiwa na Babati yenye matukio 41 pamoja na Simanjiro 27 na Hanang 26. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kutokana na hayo basi, naomba nichukue fursa hii kumwomba Mheshimiwa Mbunge akubaliane nami kwamba baada ya Bunge hili tukae pamoja ili kujiridhisha kwamba kama kuna haja ya kuchukua hatua zaidi. Hatua zaidi zitategemea mambo makubwa matatu; kwanza, siyo tu kwamba kutokana na wingi wa matukio ya uhalifu, lakini inategemea vilevile na idadi ya watu, inategemea hali ya kijiografia ya sehemu husika pamoja na upatikanaji wa fedha. Kwa hiyo, tutakapokuwa tunafanya ziara pamoja na Mheshimiwa Mbunge, tutajua jinsi ya kufanya kulingana na upatikanaji wa fedha kadri utakavyoruhusu.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili kwamba wananchi wa Jimbo lake na yeye mwenyewe wakishirikiana Serikali itachukua hatua gani? Mimi nataka nimpongeze sana kwa hatua zake hizo nzuri kwamba tunaamini kabisa kwamba Serikali ina ufinyu wa bajeti na hivi sasa vituo karibu kumi ambavyo viko katika hatua za ujenzi vimekwama kutokana na upungufu wa fedha. Sasa ikiwa Mheshimiwa Mbunge atashirikiana na wananchi wake katika kuwahamasisha ili kuisaidia nguvu Serikali, basi tutamuunga mkono.

Mheshimiwa Spika, nataka niahidi tu kwamba Serikali itakuwa pamoja kushirikiana naye pamoja na wananchi wake kuhakikisha kwamba inasaidia kuimarisha ulinzi katika eneo hilo.
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza, je, Serikali iko tayari kuwahakikishia wananchi hawa ni lini wale ambao hawajaamua kubaki au kuondoka na kurudi Burundi? Kwa sababu siyo kweli kwamba watu wote wameshapata uraia; wako ambao hawajapata na hawajasema wanataka nini. Je, Serikali iko tayari kutoa tamko nini kifanyike?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna takribani wakimbizi 8,800 ambao hawajapatiwa uraia kati ya wale 162,000 na zaidi ya wale ambao walipatiwa uraia, lakini kulikuwa na sababu kadhaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa sababu hizo ni kwamba wengine ni watoto wa wakimbizi ambao walizaliwa baada ya wazee wao kupata uraia, lakini wakati ambapo Waziri wa Mambo ya Ndani alikuwa hajaidhinisha bado uraia. Wapo wengine ambao hawakupewa uraia; walinyimwa kwa sababu mbalimbali ikiwemo hali zao za uhalifu na mambo mengine ambayo hayakuweza kukidhi vigezo na sifa za kupata uraia nchini kwetu.
Mheshimiwa Spika, sasa ninachoweza kumwambia Mheshimiwa Mbunge ni kwamba kwa wale ambao hawakupata uraia na wamekidhi vigezo na wameomba uraia, maombi yao yanashughulikiwa na yatakapokuwa yamekamilika watapewa uraia kwa wale ambao watakuwa wamekidhi vigezo.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, vitendo hivi vya kuwaua wazee wetu ama tunavyoita vikongwe lakini hao mimi kwa lugha hii ya vikongwe hata siipendi, wazee wetu! Wazee ni dhamana yetu sisi vijana ama wananchi wote, lakini kuna watu katika mikoa mingine wanawaua wazee wetu, wengine wakiwa hai wanawafukia. Hiyo tunaoneshwa kabisa katika vyombo mbalimbali vya habari. Wengine wanawaua watu kwa kuwafukia kwa sababu wazee wetu wana macho mekundu na watu hawajui kwamba kuwa na macho mekundu ni kupikia kuni kwa wingi, sasa...
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Na mavi ya ng‟ombe, wengine wanasema kinyesi cha ng‟ombe, wanapikia kinyesi cha ng‟ombe wengine macho yanakuwa mekundu.
Je tutawasaidiaje wazee hawa kuwaondoshea kuwa na macho mekundu kwa kuwapelekea gesi kwa wingi kule vijijini ili waweze kuwa na macho mazuri, wasipate kuuliwa kwa itikadi za kishirikina? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri amejibu hapa kama kunatolewa elimu.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Faida hilo ni swali la nyongeza au la pili?
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: La pili la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri amesema kwamba hapa Serikali inatoa elimu, hata sisi Wabunge tunapaswa kutoa elimu katika maeneo yetu, lakini sasa athari hii ya kuwaua wazee wetu itakwenda vizazi na vizazi vijavyo huko mbele. Watoto wetu wanajifunza nini kuhusiana na jambo hili hapo mbele?
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inawachukulia hatua gani kuwaondosha hawa watu wanaowaua wazee wetu? Inawachukulia hatua gani kali kukomesha hasa katika mikoa hiyo ya Mwanza, Shinyanga, Tabora na kwingineko, wazee wetu wanauliwa sana? Naomba jibu maridhawa.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna mikakati mbalimbali ambayo tayari imeshaanza kuchukuliwa na Serikali kuhakikisha kwamba matumizi ya kuni ama hayo mavi ya ng‟ombe kwa ajili ya kupikia yanapungua, ikiwemo kuanzisha kwa nishati mbadala, matumizi ya majiko bunifu na kadhalika, lakini pia harakati za Serikali kusambaza umeme vijijini zinasaidia sana kuhakikisha wananchi wanatumia nishati iliyokuwa bora zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lake la pili anazungumzia kwamba hatua gani ambazo Serikali imechukua ili kudhibiti matukio kama haya. Nataka tu nimhakikishie kwamba takwimu ambazo tunazo kuanzia mwezi Julai, 2015 mpaka Machi, 2016 tayari kuna watuhumiwa 135 ambao wameshakamatwa na kesi kama 222 ambazo zinaendelea mahakamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Jeshi la Polisi ama Serikali kupitia Jeshi la Polisi, linafanya kazi kubwa sana kuhakikisha kwamba linawadhibiti wale wananchi wote ambao wamekuwa wakijichukulia sheria mkononi.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Imekuwa ni kawaida kwa Serikali kuleta majibu mara zote juu ya masuala yanayohusu vituo vya polisi, juu ya usafiri na uchakavu wa vituo hivi wakitoa majibu ya kufanana kwamba hali ya uchumi itakapotengemaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukishuhudia matumizi makubwa na ya nguvu yanayotumika kwa kununua mabomu, virungu, kila wapinzani wanapojaribu kufurukuta kwenye nchi hii. Mnatoa wapi bajeti ya kuwezesha mambo haya yakiwemo yale ya Operation Harass Wapemba kama mlivyofanya karibuni; mlitoa wapi fedha zile; mnaposhindwa kutekeleza mahitaji muhimu ya vituo vya polisi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli ni kwamba hali ya usalama ya nchi yetu na jinsi ambavyo imekuwa tulivu, ni jawabu tosha kwamba maamuzi ya Serikali katika kuhakikisha kwamba inatawanya rasilimali zake kulinda ulinzi na usalama wa nchi yetu ni sahihi. Yote hayo yanafanyika kwa wakati mmoja. Ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kwamba wananchi wa nchi hii wanakuwa salama wakati wa uchaguzi, baada ya uchaguzi na kabla ya uchaguzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunajaribu kuhudumia vituo vya oolisi, nyumba za askari na kadhalika, lakini wakati huo huo inapofika nyakati za uchaguzi tuna wajibu wa kuhakikisha kwamba usalama wa nchi yetu unaendeleaa kuimarika.
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, itakumbukwa kwamba miaka ya 1990 tulipokea wakimbizi kutoka Burundi na wakawekwa kwenye kambi ya wakimbizi ya Nduta. Baada ya hali ya amani kurejea, ile kambi ilifungwa, Serikali ikawapatia wananchi kuanzisha kijiji cha mfano cha Nduta.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wakimbizi hali ya amani iliyokuwa siyo nzuri tena Burundi, wakimbizi tena walirejea na Serikali ikawaomba wale wananchi waondoke kwa ahadi kwamba itawalipa fidia. Sasa ni lini wananchi hao watalipwa fidia yao? Swali la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ujio wa wakimbizi mara nyingi pamoja na mambo mengine huwa ina athari za kimazingira na kimiundombinu hasa barabara na maji. Kuna ombi ambalo Kiwilaya tulitoa na Serikali ya Mkoa ikatuunga mkono kuhusu miundombinu ya maji kwa kuwa ujio wao umesababisha kuongezeka kwa watu wanaotumia miundombinu ile ile ya maji na barabara…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa naomba uulize swali tafadhali.
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mheshimiwa Naibu Waziri anajua, juzi juzi alikuwa Kibondo na akajua kwamba tumepeleka ombo UNHCR kwa ajili ya kupata maji.
Je, Serikali imefanya msukumo gani hadi sasa hivi ili tuweze kupatiwa maji?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli nilifanya ziara hivi karibuni huko kwenye kambi za wakimbizi na katika ziara hiyo pia tulikutana na maandamano ya wananchi ambao walikuwa wana madai ambayo Mheshimiwa Mbunge ameeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hatua ambayo tumechukua ni kuweza kuzungumza na UNHCR ili waangalie uwezekano wa kuwalipa; siyo fidia lakini ni kama kifuta machozi. Kwa sababu kwa mujibu wa taratibu, wale wananchi waliruhusiwa kulima pale, lakini eneo lile ni miliki ya Serikali na limetengwa maalum kwa ajili ya kuhifadhi wakimbizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Engineer Nditiye kwamba mazungumzo ambayo tumefanya na UNHCR yameonekana kuzaa matunda na tunatarajia kwamba wananchi hawa wanaweza wakapatiwa kifuta jasho.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala lake la huduma za jamii, moja katika mikakati mikubwa ya Serikali ambayo hata Mheshimiwa Waziri Mkuu alipofanya Ziara katika maeneo hayo, alitoa msisitizo muhimu wa maeneo ambayo wananchi wanaoishi maeneo yanayozunguka kambi za wakimbizi kuweza kufaidika na huduma mbalimbali za kijamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la Nduta, kwa mfano sasa hivi UNHCR wamekubali kutoa nusu ya mahitaji ya madawati yanayohitajika katika maeneo hayo, lakini pia tumefanya nao mazungumzo kuhakikisha kwamba katika maeneo ya huduma za maji na afya wanaweza kutoa michango yao ili wananchi waweze kufaidika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nadhani kabisa kwamba baada ya mazungumzo hayo tunaweza kuona mafanikio kuhusiana na miradi ya maji katika maeneo hayo.
MHE. MARYAM S. MSABAHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naona Mheshimiwa Naibu Waziri sijui alikuwa kalala, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Kambi hii niliyoitaja hasa hii Mesi ya Ulinzi na Usalama ipo katika mazingira ambayo siyo rafiki sana na jamii iliyowazunguka, upande kuna Skuli ya SOS na upande kuna Msikiti, pia kunakuwa na vitendo ambavyo vinaendelea pale ambavyo siyo rafiki na jamii inayowazunguka. Je, ni lini Serikali itahakikisha inatenga fedha za kutosha ili kukarabati Kambi hii na hasa hii Mesi ya Jeshi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa vikosi vingi vya Ulinzi na Usalama vinaishi uraiani na vinakuwa siyo rafiki sana na wananchi hasa wananchi ambao siyo waadilifu na nchi yao. Je, ni lini Serikali itahakikisha vikosi vyote vya Ulinzi na Usalama vinajengewa makazi bora na yenye sifa kama vikosi vya Ulinzi na Usalama?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI (K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Maryam Msabaha kwamba maoni yake tutayazingatia katika bajeti ya mwaka wa fedha ujao tutaangalia uwezekano wa kutilia maanani mapendekezo yake, hasa ukizingatia kwamba amezungumza changamoto ambazo ni za msingi kabisa .
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na nyumba, tayari kuna program ya ujenzi wa nyumba na hilo liko tayari katika mipango ya Serikali, nadhani muda siyo mrefu suala la nyumba litaanza kupunguzwa kadri ya uwezo wa nchi kifedha utakapokuwa unaruhusu.
MHE. HALIMA ALI MOHAMMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza:
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa yupo Mkandarasi ambaye amejenga makao Makuu ya Polisi Kusini Pemba pamoja na nyumba ya RPC kwa asilimia 100, vile vile amejenga Kituo cha Polisi cha Mkokotoni kwa asilimia 70, je, ni lini Serikali itamlipa Mkandarasi huyo?
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Wakandarasi wako kibiashara zaidi na kwa kuwa muda aliojenga Mkandarasi huyu ni mrefu, je, sasa Serikali iko tayari kumlipa kwa thamani ya shilingi iliyoko sokoni sasa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyozungumza katika jibu langu la msingi ni kwamba, kila mwaka tunatenga bajeti kwa ajili ya maendeleo na katika fedha hizo, ndipo tunatumia sehemu ya fedha hizo kwa ajili ya kuwalipa Wakandarasi na Mkandarasi ambaye amejenga kituo cha Tumbatu na kituo hicho ambacho umekizungumza kilichopo Kusini Pemba ni miongoni mwa Wakandarasi mbalimbali ambao wanatudai, tutakuwa tukiwalipa. Mwaka huu katika Wakandarasi ambao tumepanga kuwalipa kiasi kitakachoweza kulipwa ni huyo ambaye amemzungumza Mheshimiwa Mbunge.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri napenda kumuuliza swali moja la nyongeza:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza katika majibu yake ya msingi anasema kwamba, Serikali imepata kiwanja! Sijui maana yake ni nini kwa sababu hicho kiwanja ni chetu watu wa Jimbo, siyo Serikali! Pamoja na hayo mpaka sasa hivi hatuoni dalili za uharaka wa ujenzi wa suala hili. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anatuambia ni lini angalau wataanza kuweka msingi katika suala hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tuna dhamira ya dhati ya kujenga hiki kituo, lakini kama ambavyo nimezungumza mwanzo kwamba, tuna changamoto nyingi sana za mahitaji ya vituo mbalimbali. Kwa hiyo, ningechukua fursa hii kutoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge, akiwemo Mheshimiwa Mbunge wa Tumbatu, kuangalia uwezekano wa kuharakisha jitihada hizi kwa kuanza kushirikisha wananchi na hata ikibidi kutumia Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo ili baadaye Serikali iweze kuongeza nguvu zake.
MHE. MASOUD ABDALLA SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza. Pamoja na maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba, kuna mkakati wa kupeleka Polisi
NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT)
18
kwenye Kisiwa cha Tumbatu siku hadi siku kukabiliana na matatizo ya usalama, lakini Mheshimiwa Naibu Waziri bado hujatueleza ni mkakati gani wa ziada wa kuweza kuwabaini na kuwakamata wale ambao walifanya uhalifu wa kuchoma moto nyumba za watu kule Tumbatu, ambapo hadi sasa watu wengine wamekosa makazi. Je, kuna mkakati gani wa Waziri na Serikali kuhakikisha kwamba, matatizo yale hasa yanaepukwa na hayatokei tena na yanakoma na wahusika wanakamatwa? Naomba maelezo!
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, siku zote Jeshi la Polisi limekuwa likichukua hatua kadri ya matukio ya uhalifu yanapotokea ikiwemo tukio la uhalifu ambalo limetokea Tumbatu. Kuna mambo mawili makubwa ambayo tumefanya tayari, la kwanza, ni kuhakikisha kwamba, tunachukua hatua kwa wale ambao tumewakamata, watuhumiwa kwa ufupi kwa kuwapeleka katika vyombo vya sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ya pili, ni kudhibiti hali ile isijitokeze tena, ndiyo maana katika jibu langu la msingi nilizungumza kwamba kumeongezeka doria na sasa hivi nadhani kwa kipindi kirefu kidogo, matukio yale ya uhalifu ya kuchomeana moto nyumba yamepungua ama yamesita Tumbatu.
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza:-
Kwa kuwa, Naibu Waziri amekiri kwamba wameshaanza kujenga uzio katika kituo cha Ziwani pale Zanzibar, tunashukuru sana Serikali. Naomba kumuuliza sasa, Zanzibar ina vituo vingi sana ikiwemo na vituo vya Pemba, je, ni lini Seriali itajenga uzio katika vituo vya kule Pemba?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amejibu kwamba itajenga uzio katika maeneo mbalimbali ya Tanzania, ninavyoelewa kwamba bila ya bajeti uzio hizo hazitoweza kujengwa na hatujaona katika bajeti yake kukiwemo ni makisio hayo. Je, Serikali itakubaliana na mimi kwamba katika mwaka ujao wa 2017/18 iweze kuweka bajeti ya kuwajengea uzio katika vituo mbalimbali na makambi ya Polisi. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza kwamba ni lini vituo vitajengewa uzio. Kama ambavyo nimekuwa nikizungumza kila siku kwamba ujenzi wa uzio, ukarabati wa vituo na kadhalika inategemeana na uwezo wa kifedha. Hata hivyo, kwa kuwa malengo ya kujenga vituo ambavyo kwa mujibu wa PGO namba 287 inaonesha kwamba maeneo ambayo vituo vinavyohitaji kujengewa uzio ni vituo class (a) na (b), lakini kwa mujibu wa PGO namba 314 vilevile inaonesha dhamira ya ujenzi wa uzio ni kuhakikisha usalama unaimaridhwa katika maeneo husika.
Hata hivyo kwa kukidhi ile PGO 314 ni kwamba unaimarisha ulinzi katika maeneo hayo katika kipindi hiki ambako bado bajeti haijaweza kukidhi kujenga vituo vyote. Kwa hiyo, kimsingi ni kwamba tunaweza kutekeleza hili jambo la kuimarisha usalama katika vituo vyetu kwa kuimarisha ulinzi. Kwa kuanzia wakati huo huo tunatafuta fedha za kuweza kujenga uzio.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ni kwamba anajaribu kupendekeza bajeti ya mwaka ujao wa fedha tuweze kuwa na bajeti ya kutosha kwa ajili ya kujenga uzio. Mimi naamini kabisa chini ya utaratibu ambao Serikali hii ya Awamu ya Tano tunakwenda nao ya kuhakikisha kwamba tunaongeza kukusanya mapato katika nchi hii, basi imani yangu ni kwamba kadri ya miaka inavyokwenda mbele tunaweza kupata bajeti ya kutosha na Wizara ya Mambo ya Ndani kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo ujenzi wa uzio katika vituo vyetu vya Polisi.
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Kwanza napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri na Wizara hii ya Mambo ya Ndani kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuimarisha ulinzi na usalama katika nchi yetu.
Mheshimiwa Waziri atakubaliana na mimi kwamba katika majengo hayo ambayo yamejengwa 360 kwa misimu hiyo iliyopita ni jengo moja ninalolikumbuka mimi ambalo lipo pale Mkoa wa Mjini - Ziwani Polisi kwenye Jimbo langu. Pia Serikali imejenga jengo lingine kwa upande wa Zanzibar kule Pemba, haya majengo ukitazama ki-percentage ni madogo zaidi. Lakini mimi sina uhakika na taarifa hizi za 360; sasa namuuliza Mheshimiwa Waziri katika 360 ni majengo mangapi yalijengwa kule Zanzibar na katika haya 4,130 mangapi yanatarajia yatajengwa kule Zanzibar? Hilo swali la kwanza.
Mheshimiwa Spika, swali la pili Seriklai iliji-commit katika mwaka 2011, Juni kwamba kwa kupitia bajeti wa mwaka ule ingelifanya ukarabati majengo ya Ziwani Polisi, lakini pia wangelijenga na uzio na mpaka hivi sasa ninavyozungumza kwamba askari wanajitegemea wenyewe kufanya ukarabati katika nyumba ambazo wanaishi.
Je, Waziri atanihakikishia ni lini Serikali itakuja kufanya ukarabati wa majengo yale ya Ziwani Polisi pamoja na kujenga uzio? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge wa Jang‟ombe kwa ushirikiano wake mzuri sana ambao anatupa kwani ameshiriki katika ujenzi wa Kituo cha Afya pale Ziwani pamoja na uchimbaji wa kisima cha maji. Tunampongeza sana na tunamuahidi ushirikiano zaidi.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na maswali yake mawili, ni kwamba mradi wa nyumba 4,136 ambazo tunatarajia tujenge ni nyumba 200 ambazo zinatarajiwa kujengwa Unguja na nyumba 150 zinatarajia kujengwa Pemba, kwa hiyo ukifanya jumla ya idadi ya nyumba zote 350. Pia ameuliza kuhusiana na zile nyumba ambazo zilijengwa kupitia mradi wa NSSF. Ni kwamba nyumba zilizojengwa ni kweli maghorofa yale yalikuwa ni mawili kwa maana ya Unguja na Pemba lakini yana uwezo wa kukaa familia 12 kila moja kwa hiyo kufanya jumla ya familia 24.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la ukarabati wa nyumba za Ziwani ni kweli nyumba zile ni chakavu lakini kama ambavyo tunazungumza siku zote kwamba, nyumba hizi za Polisi nyingi ni chakavu. Ndiyo maana tuna mchakato wa kuweza kurekebisha nyumba hizi pamoja na kujenga mpya. Kwa hiyo, niseme tu kwamba tunafahamu gharama za ujenzi wa nyumba hizo, ukarabati huo ambao unakadiriwa kufika takribani shilingi milioni 400; kwa hiyo tutajitahidi kwamba pale fedha itakapopatikana tuweze kuanza hiyo kazi haraka itakapowezekana.
Mheshimiwa Spika, tunafahamu umuhimu wa nyumba za Ziwani, ikiwa ni Makao Makuu ya Jeshi la Polisi na chimbuko la historia hata Mapinduzi ya Zanzibar yalianzia pale.
MHE. RAISA ABDALLAH MUSSA: Mheshimiwa Spika, asante kwa kuniona kwa sababu ni mgeni ndiyo maana jina langu hukunitaja naitwa Raisa Abdallah Mussa, Viti Maalum kutoka Zanzibar CUF. Napenda nimuulize Mheshimiwa Waziri swali moja la nyongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Waziri katika vituo vidogo vya polisi vilivyoko Zanzibar, kuna baadhi ya vituo vimehamwa na nikutajie kwamba kituo cha Kidongo Chekundu Mentally Hospital, pale ni kituo muhimu sana kwa maeneo yale ya Kidongo Chekundu na Sogea, sasa hivi kile kituo kimehamwa na pamekuwa hasa kama gofu mpaka pamefanywa vijana wamekaa maskani yao pale pembeni yake.
Mheshimiwa Naibu Waziri, nataka uniambie una mpango gani na kukihuisha kituo kile cha Polisi cha Kidongo Chekundu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna baadhi ya vituo vya polisi ambavyo kidogo havifanyi kazi ikiwemo kituo hicho ambacho nilizungumza Mheshimiwa Mbunge, lakini pia kuna kituo cha Vuga na Shaurimoyo.
Mheshimiwa Spika, lakini kuna sababu mbalimbali ambazo zinasababisha vituo hivi kwa muda visiweze kufanyakazi. Vingine ni kwamba mahitaji ya vituo katika maeneo hayo yanakosekana umuhimu kulingana na changamoto za uhalifu na ukaribu wa vituo vingine vikubwa vya polisi vilivyopo maeneo hayo. Hata hivyo, kutokana vilevile na uhaba wa idadi ya askari waliopo tunashindwa kufungua vituo vyote katika maeneo yote ya Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, sasa niseme tu kwamba, kituo cha Kidongo Chekundu ni moja kati ya vituo hivyo, hata hivyo nimuhakikishie Mbunge pamoja na wananchi wanaosikiliza kwamba Serikali haijakitupa kituo hicho, pale ambapo mahitaji yatakapoonekana ya muhimu tutakifanyia ukarabati na kuweza kukitumia kwa haraka sana.
MHE. HAFIDH ALI TAHIR: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana pamoja ya kuwa sauti ilikuwa ndogo lakini nashukuru sana majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, amezungumzia suala la wakati wa kampeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa kampeni ya uchaguzi na baada ya uchaguzi kule Zanzibar nyumba ya Kamishna wa Polisi ilichomwa moto, lakini mikarafuu mingi kule kisiwani Pemba ilikatwa, mazao machanga nayo yaliharibiwa.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri pamoja na mambo yote yaliyotokea haya hivi sasa umechukua hatua gani ya kukomesha vitendo kama hivi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa sababu hivi sasa kuna mambo mengi yanatokea na kwa kuitikia wito wa Rais Magufuli ambaye amesema sasa hivi uchaguzi umekwisha tunataka maendeleo.
Je, utawachukulia hatua gani wale ambao watatekeleza ukorofi katika siasa badala ya kuleta maendeleo ndani ya Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Hafidh Ali Tahir anataka kujua kwamba ni hatua gani zimechukuliwa dhidi ya watu ambao wamevunja sheria baada ya uchaguzi, akataja matukio mawili specifically, moja linahusu kurushwa bomu kwenye nyumba ya Kamishna na mambo ambayo yamekuwa yakijitokeza siku za karibuni ya ukataji mashamba ya mikarafuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimjulishe tu Mheshimiwa Hafidh Ali Tahir kwamba mpaka sasa hivi Polisi imeshafanya kazi ya kuwakamata watuhumiwa, mimi binafsi juzi nilifanya ziara na nilikuatana na Viongozi wa Polisi Zanzibar pamoja na Makamanda wa Polisi wa Mikoa ya Kusini na Kaskazini Pemba. Dhamira ya ziara ile ni kuweza baada ya kupata taarifa mbalimbali ambazo tumekuwa tukizipata kila siku juu ya hatua ambazo tunachukua, lakini kujionea wenyewe jinsi hatua hizo zilivyofikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoweza kusema ni kwamba mpaka sasa hivi kuna watuhumiwa kadhaa wameshakamatwa na katika watuhumiwa waliokamatwa ni matukio mawili ambayo yamefikishwa Mahakamani, matukio mengine bado kesi zao zipo kwa DPP. Nilijaribu kutoa wito kwa DPP kuweza kufanya kazi kwa karibu kabisa na Polisi ili kuharakisha kesi hizo ili watu hao waweze kuchukuliwa hatua kali za kisheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili ambapo alitaka kujua kwamba baada ya kauli ambayo ameizungumza Mheshimiwa Rais, nataka nisisitize kwamba Jeshi la Polisi ndiyo chombo pekee chenye dhamana ya kuweza kutathmini hali ya usalama katika nchi yetu. Kama ambavyo imefanya kupitia Kamishna wake wa operation walitoa agizo kwamba kulingana na hali ya usalama nchini wamezuia mikutano ya kisiasa. Nataka nitoe wito tu kwamba wananchi ama vyama vya siasa vitii agizo hilo la Polisi, kama kuna yeyote ambaye hatii agizo hilo basi sheria ichukue mkono wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumewahi kuzungumza mara nyingi hapa kwamba hakuna mtu ambaye yuko juu ya sheria, kwa hiyo basi tunataka na mamlaka husika, kwa maana ya kwamba viongozi wa Jeshi la Polisi wa ngazi za chini wahakikishe kwamba wanatekeleza maelekezo ya ngazi za juu. Kwa hiyo, watu ambao wanahusika kutoka vyama vya siasa watii sheria hiyo, lakini watu ambao wanapaswa kuisimamia sheria hiyo waisimamie ipasavyo katika maeneo yote ya nchi yetu ikiwemo Pemba, Zanzibar na maeneo ya Tanzania Bara mpaka pale mamlaka husika ama Jeshi la Polisi watakapoamua vinginevyo kwa mujibu wa taarifa zao za ki-intelijensia na taratibu zao za kazi na utaalam ambao wanao.
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba watachukuliwa hatua kali za kisheria wale wote walioshiriki vitendo hivi, lakini pia kuna wengine ambao tayari sasa hivi wameshakamatwa, yaani watuhumiwa wameshakamatwa, je, Serikali itakubaliana nami kwamba baada ya kugundulika watu hawa waliofanya vitendo hivi kwa raia wa Zanzibar, Serikali iko tayari pamoja na hatua kali zitakazochukuliwa za kisheria, iko tayari kuwataka walipe fidia kwa wale wote waliowafanyiwa vitendo hivi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na uamuzi wa hatua gani za kuchukua baada ya kubainika na makosa ni maamuzi ya Mahakama. Kwa hiyo, pale ambapo Mahakama itaamua kulingana na sheria za nchi yetu basi nadhani ndivyo ambavyo inapaswa kutekelezwa. Siyo jukumu la Jeshi la Polisi kuamua hukumu gani ambayo watuhumiwa hawa wachukuliwe.
MHE. MUNIRA MUSTAFA KHATIBU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa wanaoathirika zaidi ni wanachama wa CCM kwa kule Pemba; Je, Serikali haioni umuhimu wa chama hiki cha CUF kukifutia usajili na kuweza kupata amani ndani ya Tanzania yetu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kwa upande wa Pemba matukio haya, wakati wa uchaguzi wa marudio na baada ya uchaguzi kumalizika, Pemba kulikuwa na amani, ambapo mpaka sasa hivi amani ipo. Matukio haya ya kihalifu ya kukatakata mikarafuu na kufanya mambo mengine ya hovyo zaidi yalijitokeza baada ya viongozi wa CUF, kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge alivyosema, kufanya ziara kule Pemba. Ndiyo maana nikasisitiza kwa Jeshi la Polisi kuhakikisha kwamba wanachukua sheria kali kwa Kiongozi yeyote wa chama chochote kiwe cha CUF au chama kingine ambacho kinahatarisha ama kinachochea amani ya nchi yetu.
Kuhusiana na suala la kukifutia usajili chama hiki nadhani hayo ni mamlaka ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuona kama kuna haja hiyo kulingana na taratibu na sheria za nchi yetu zilivyo. Si jukumu la Serikali ama Jeshi la Polisi kuamua.
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALOSS NYIMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa, toka tumalize Uchaguzi Mkuu Zanzibar imekuwa na baadhi ya watu wakitoa kauli za vitisho, hususan wakati huu wa sikukuu wanatoa kauli za vitisho kupitia mitandao ya kijamii;
Je, Serikali inawaambia nini wananchi wa Zanzibar, hususan vijana na watoto ambao wanatarajia kusherehekea sikukuu ya Eid al-Fitr.(
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inachoweza kuwaeleza wananchi wa Zanzibar na Watanzania kwa ujumla ni kwamba wasiwe na wasiwasi wowote, nchi yetu iko salama na itaendelea kuwa salama. Ninyi ni mashahidi kwa kazi nzuri ambayo imekuwa ikifanywa na Jeshi la Polisi. Kwa matukio ya hivi karibuni jana na juzi mmejionea. Pia kwa upande wa Zanzibar juu ya hawa watu ambao wanajaribu kutaka kutuletea mrafaruku katika nchi yetu, tumewadhibiti. Nataka nitoe tu wito kwa wananchi kuacha kukubali kuchochewa na baadhi ya wanasiasa, wahakikishe kwamba wanaendelea kufuata sheria za nchi yetu, yeyote ambaye atakiuka sheria hiyo kama ambavyo tumekuwa tukizungumza kila siku, kwamba ikiwa ni mwanachama wa chama cha siasa, ikiwa ni kiongozi basi hatua kali za kisheria zitachukuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nisisitize tu kwamba wananchi wasiwe na wasiwasi, waendelee kusherehekea siku ya Eid-al-Fitr bila wasiwasi wowote. Serikali yao ipo itaendelea kuwalinda wao pamoja na mali zao.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza; namshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri yaliyonyooka, ningependa sana kujua swali langu la kwanza kwamba, pamoja na fedha zilizotengwa, ni kiasi gani cha fedha hasa kilichotengwa kwa sababu hiyo ingetusaidia kuwa uhakika na hii bajeti kwamba fedha hizi zilizotengwa zitakwenda kukamilisha majengo haya, ili kuwafanya Askari hawa waliosubiri takribani miaka minne sasa walau hizi familia ishirini zipate makazi bora na salama ya kukaa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa sababu tunafahamu Nyamagana ndiyo kitovu cha Mkoa wa Mwanza, nyumba hizi zinazotarajiwa kukamilika zinaweza kukidhi mahitaji ya familia zisizozidi ishirini na tano. Ukweli ni kwamba Askari ni wengi na umuhimu wa kambi hii ni mkubwa sana kwenye Mkoa wa Mwanza. Sasa ningependa tu kujua mpango wa Serikali, kuongeza nyumba zingine kwa muda na wakati ili Askari hawa wanaoishi kwenye kambi hiyo ya Mabatini na familia zao ambao sasa ina mwingiliano mkubwa na wananchi wa kawaida waweze kupata makazi mengine bora zaidi ili waweze kuwa kwenye mazingira salama nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mabula kwa jitihada zake za kushughulikia changamoto za Jimbo lake. Tulikuwa pamoja kwenye ziara wakati nilipokwenda kutembelea Nyamagana na alitupa ushirikiano mkubwa sana. Kuhusiana na kiwango ambacho kimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba hizo ni takribani shilingi milioni 565 kwa kuwa nyumba zenyewe zimefika katika hatua ya mwisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili alitaka kujua kwamba kwa kuwa hizo ni familia chache ambazo zitakidhi kukaa katika nyumba hizo, kuna mpango gani mwingine nilitaka nimjulishe tu kwamba, tuna mpango wa kujenga nyumba takribani 300 kupitia ile programu ambayo iko katika hatua nzuri za utekelezaji wa ujenzi wa nyumba 4,136 nchi nzima.
MHE. KANGI A. LUGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona.
Kwa kuwa, Jimbo la Mwibara ambalo kwa muda mrefu kulingana na jiografia yake matukio kwenye visiwa ya ujambazi tulishaomba kuwa na Wilaya ya kipolisi. Je, Serikali mpaka sasa ina mpango gani wa kujenga kituo cha Polisi na kutupa hadhi ya Wilaya ya kipolisi. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, upo mpango wa kujenga vituo vya Polisi nchi nzima, ambapo kimsingi tuna upungufu mkubwa wa vituo vya Polisi vinavyokadiriwa kuwa zaidi ya 4,500 nchi nzima ikiwemo eneo ambalo Mbunge amelizungumza. Kwa hiyo, nichukue fursa hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tunatambua changamoto ya upungufu wa vituo vya Polisi ikiwemo katika Jimbo lake na tupo katika harakati za kuhakikisha kwamba tunapunguza tatizo hilo katika Jimbo hilo na maeneo mengine ya nchi nzima.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi naomba niulize swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa, humu ndani maswali yote huwa yanaelekeza nyumba za Polisi. Je, Waziri anasema nini kuhusu nyumba za Askari Magereza hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli pia tuna tatizo la upungufu wa nyumba katika Jeshi la Magereza. Kama ambavyo ipo katika Jeshi la Polisi, pia iko programu ya ujenzi wa nyumba ambazo zinakwenda sambamba na hizi za Polisi, kwenye Polisi tuna nyumba 4,136 na Magereza tuna nyumba takribani 9,500 kama nitakuwa sijakosewa sawasawa takwimu zake. Kwa hiyo, tunatambua hiyo changamoto na zipo katika hatua nzuri tu za utekelezaji naamini kabisa katika kipindi cha miaka mitano hii, tutaanza kuona miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba hizi pindi mipango ya upatikanaji wa fedha na taratibu za kifedha kupitia Hazina itakapokamilika basi nyumba za Polisi na Magereza kwa pamoja zitakwenda sambamba.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii.
Kwa kuwa, tatizo la Nyamagana la nyumba za makazi ya Polisi linafanana sana na tatizo la makazi kwa Polisi wa Kisiwa cha Mafia. Je, Mheshimiwa Naibu waziri anaweza kulitolea maelezo gani tatizo la makazi kwa Polisi wa Kisiwa cha Mafia? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli lipo tatizo la makazi ya Polisi pia katika Jimbo la Mafia. Nataka tu nimpe taarifa Mheshimiwa Dau kwamba katika ujenzi wa hizi nyumba ambazo tunataka kujenga, kwa upande wa Pwani tunatarajia kujenga nyumba 150. Mpaka sasa hivi, bado mchanganuo wa ujenzi kwa kila Wilaya ama kila Jimbo haujakamilika. Kwa kuwa, Mheshimiwa Mbunge amelizungumza hilo tatizo la Mafia basi tutalichukua tuone katika ujenzi wa hizo nyumba 150 kwa upande wa Pwani tuone uwezekano wa kuweza kuhakikisha kwamba naamini kabisa Mafia itakuwa imo katika mpango huu, lakini siwezi kuzungumza ni nyumba ngapi kwa upande wa Mafia, hilo tunaweza tukafanya kazi kwa kushirikiana mimi na yeye baadaye.
MHE. KANGI. A. LUGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona.
Kwa mujibu wa Ibara ya 14 ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kila raia wa nchi hii anayo haki ya kuishi na katika Ibara hiyo haikuainisha haki ya kuishi kwa kutumia vigezo vya itikadi za vyama, wala kigezo cha ukabila, wala kigezo cha udini, wala kigezo cha umri.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatoa kauli gani kwa Watanzania na hata Wabunge ambao wamekuwa na tabia ya kuhusisha kila vifo vinavyotokea na masuala ya itikadi za kisiasa ili liwe fundisho kwa wananchi wenye tabia hiyo kwa sababu maswali kama hayo yanaleta uchochezi na yanaweza yakasababisha maafa na hata uhasama wa kudumu kati ya koo ambazo yule mwananchi amekufa? Ahsante.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri na niseme kitu hiki na Watanzania wasikie na wapokee.
Moja, Mtanzania hawi na madaraja kutokana na chama chake, dini yake ama kabila lake. Hakuna nusu Mtanzania kwa sababu ya chama alichonacho na hakuna Mtanzania daraja la pili kutokana na chama alichonacho. Watanzania wote ni Watanzania daraja la juu na wana haki sawa za kuishi na viongozi wanaowagawa Watanzania na kuwatengenezea chuki hata wakadhuriana kwa misingi ya kisiasa wanapaswa kupuuzwa na ndio maana sisi tukiona kiongozi anayefanya vitu vya aina hiyo tunachukua hatua.
Kwa hiyo, wao kwa watanzania maeneo popote pale walipo wasije wakagawanywa kwenye misingi hiyo na niliwahi kuisema eneo moja na ninarudia tena wasije wakaenda kwenye kuuana kwa misingi ya vyama ile hali sisi ambao tunakuwa viongozi huku na wakati mwingine tunawasukuma kufanya hivyo tukija huku wakishatuchagua tunagongesha glass za juice marazote tunapoonana hapa ili hali wao kule wameshasababisha yatima, wajane na kusababisha matatizo katika familia. Kwa maana hiyo nitoe rai kwa Watanzania na nitoe rai kwa kila mmoja wetu kuhakikisha kwamba tunalinda Utanzania wetu na undugu wetu ambao tumeachiwa na hawa waasisi wetu na ili Taifa letu liweze kupata heshma inayolinda utu.
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nilikuwa naomba kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Kwa kuwa Jeshi la Polisi pamoja na kazi nyingine kazi yake kubwa ni kulinda mali na raia, nilitaka kufahamu kuna ukweli gani kuhusiana na raia kupigwa na polisi huko Pemba? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Niabu Spika, sio kweli kwamba polisi wamekuwa wakipiga raia huko Pemba na ninaomba nichukue fursa hii mbele ya Bunge lako Tukufu kutoa mfano halisi ambao ulijitokeza siku za hivi karibuni kule Pemba kwa kitendo cha maigizo na usaniii kilichofanywa na watu kutoka chama cha upinzani cha kisiasa kwa makusudi kabisa ili kupotosha jamii na dunia kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati polisi imefanya kazi yake ya kuwakamata wahalifu ambao wanafanya vitendo vya uhalifu Pemba kuna mhalifu mmoja alijifanya kwamba amekufa na amepigwa na baada ya kuhojiwa na polisi alikimbia na kukamatwa, mtu ambaye amekufa anawezaje kukimbia.
Kwa hiyo, huo ni ushahidi wa usanii ambao unafanywa kwa kulipaka matope jeshi la polisi. Naomba dunia na Watanzania watambue kwamba polisi hata siku moja hawezi kufanya kazi kinyume na sheria, maadili yake na weledi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kauli hiyo sio kweli kinachofanyika ni kwamba kuna raia ambao wamefanya vurugu za makusudi na polisi inachukua jitihada za kuwakamata na kupeleleza na baadae kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimalizie tukwa kuendelea kutoa wito kwamba tuendelee kuhakikisha kwamba tunalinda amani ya nchi yetu lakini vilevile tusitumie kauli ama vitendo vilivyokuwa sio vya kweli kulipaka matope Jeshi la Polisi na kuipaka matope nchi yetu mbele ya Watanzania na mbele ya Jumuiya za Kimataifa.
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri isipokuwa kwa mujibu wa Tume mbalimbali za Haki za Binadamu na hasa ile ya Umoja wa Mataifa ratio ya polisi na wananchi wanasema inapaswa kuwa 1:450 lakini katika nchi yetu ni 1:1300. Mheshimiwa Waziri amesema kwamba wameamua kusitisha kwa muda ajira kutokana na mambo hayo mengine ambayo wanayafanya, naomba niulize haoni kwamba kufanya hivyo ni kuendelea kukuza lile tatizo la uwiano? Pia katika hiyo ratio ambayo nimeitaja, wanawake ni wachache kweli na ndiyo maana hata humu ndani ya Bunge ikitokea kitu chochote askari wa kiume wanakuja kuwakabili wanawake kwa sababu ya upungufu. Hilo ni swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, zipo taarifa kwamba katika jeshi letu wako watu wanaajiriwa na inachukua muda sana kwenda kwenye mafunzo ya msingi ya uaskari wakati jambo hili la uaskari linahitaji maadili ambayo ni maalum kwa sababu ni jambo nyeti. Siku zote kisingizio kimekuwa ni bajeti, sasa nataka kujua hali ikoje sasa hivi kama wameshakuwa na uwezo wa kumudu hali hiyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nirekebishe kidogo, uwiano wa askari kimataifa ni askari 1:400 na kwa upande wa Tanzania Bara ni askari 1:1200, kwa hiyo kidogo kuna utofauti na maelezo ambayo ametoa Mheshimiwa Mbunge. Niseme tu usitishaji huu hauathiri kwa sababu ni usitishaji wa muda mfupi sana, kuna mambo tu kidogo ambayo yanawekwa sawa, nadhani muda si mrefu tutaendelea na utaratibu wetu kama kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusiana na swali lake la pili kwamba kuna upungufu wa wanawake katika Jeshi la Polisi, ni kweli na tunapoelekea kwenye fifty-fifty basi nitoe wito tu kwa wanawake kuhamasika zaidi ili kujiunga na vyombo vya ulinzi na usalama.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nasikitika sana kwa majibu ya kukatisha tamaa yaliyotolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri. Wilaya ya Liwale ina umri wa miaka 41 leo, Serikali ya Chama cha Mapinduzi inasema haina mpango wowote wa kujenga Kituo cha Polisi pale, anaposema kwamba ni zaidi ya Wilaya 65, sidhani kama hizi Wilaya nyingine ambazo anazi-include yeye zina umri wa miaka 40. Wilaya ya Liwale ina jumla ya kilometa 66,000 na hizi tarafa anazozisema zipo umbali wa kilometa zaidi ya 60 kutoka Liwale Mjini… (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Kuchauka, swali sasa!
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, najenga hoja. Wilaya ya Liwale mpaka leo, nimetembelea kile kituo, mafaili yale wanafunika na maturubai, lile jengo walilopanga la mtu binafsi linavuja. Sasa ninachoomba, nipewe time frame, ni lini Kituo cha Polisi Liwale kitajengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile katika Tarafa ya Kibutuka, ndiyo tarafa inayoongoza kwa ufuta na wafanyabiashara wakubwa wako pale na Kata ya Lilombe sasa hivi kuna machimbo na wafanyabiashara wengi wako pale, ni lini Kata hizi zitajengewa vituo vya Polisi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba nichukue concern ya Mheshimiwa Mbunge Kuchauka kuhusiana na unyeti na umuhimu wa kujenga kituo pale Liwale, lakini kama nilivyomwambia kwamba vituo hivi pamoja na vingine ambavyo tumepanga kuvijenga, tutavijenga kadri ya fedha zitakavyoruhusu.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kwa kuwa Mheshimiwa Mbunge amezungumzia kwa uchungu kuhusiana na matatizo makubwa yaliyopo katika Wilaya yake, basi niseme tu kwamba pale ambapo tutapata fedha tutatoa kipaumbele kwenye kituo cha Liwale.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili, anauliza kwamba, katika Tarafa ya Kibutuka, ninachoweza kusema ni kwamba kama nilivyojibu katika jibu la msingi, kwamba tumejaribu kupeleka Askari katika Tarafa ile ili waweze kusaidia ulinzi kwa wakati huu, wakati tunajiandaa na ujenzi wa kituo pale ambapo fedha zitapatikana.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na kutokuwepo kwa gari ya zimamoto Tunduma, kumeleta madhara makubwa sana kwa wakazi wa Tunduma. Kwa mfano, siku za hivi karibuni kumetokea suala la moto ambalo liliteketeza karibu maduka 500. Hali hii kwa kweli imesababisha wafanyabiashara wengi na wajasiriamali, hali yao kuwa mbaya sana, mitaji yao imepotea. Je, kwa kuwa Serikali leo hii kipaumbele chake ni kununua magari ya washawasha badala ya kununua magari ya zimamoto, iko tayari sasa kuwafidia wale wananchi ambao maduka yao yaliungua kwa sababu ya uzembe wa Serikali? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi kuna tatizo pia kubwa ambalo maaskari wetu pale hawana nyumba na nyingine ambazo nyingi zimejengwa kipindi cha Ukoloni na nyumba nyingi zina nyufa na kituo chenyewe cha Polisi kipo kwenye hali mbaya sana. Je, Serikali itaanza lini ujenzi wa nyumba za maaskari wetu pale Mbozi na Kituo cha Polisi ambacho kwa kweli kimejengwa tangu kipindi cha ukoloni?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Magari ya washawasha nimelizungumzwa hapa mara mbili, tatu kwamba tunatarajia kuyatumia magari haya vile vile kwa ajili ya kuzimia moto. Tupo katika huo mpango, mazungumzo yameshaanza kati ya Jeshi la Zimamoto na Jeshi la Magereza. Haya magari machache ambayo nimezungumza juzi, yatasaidia. Kwa hiyo, hoja yako Mheshimiwa Frank Mwakajoka imekuja wakati muafaka kwamba hukupaswa kulaumu badala yake upongeze tu kwamba una tatizo la upungufu wa magari ya kuzimia moto, usilaumu kuhusu magari ya washawasha, upongeze kwamba haya washawasha yatakusaidia vilevile. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusiana na nyumba za askari nalo hili tumelizungumza katika Bajeti yetu vizuri tu kwamba tuna mpango wa kujenga nyumba 4,316 katika mikoa kwa awamu ya kwanza takribani 16. Kwa hiyo, umesema kwamba eneo lako la Tunduma pia unahitaji. Labda nilichukue hili nione jinsi gani katika mgawanyo ule tunaweza kuzingatia ombi lako pia. Siwezi kukuahidi sasa hivi, lakini nalichukua ombi hili tulifanyie kazi.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kituo cha Polisi Lushoto ndiyo cha kwanza na ndiyo kituo kikongwe Tanzania na sasa hivi kinajengwa upya na kinaishia kwenye mtambaa wa panya na kwenye Bajeti sijaona fungu lolote lililotengwa kwa ajili hiyo.
Je, Serikali ina mpango gani wa kumalizia kituo kile?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tuna matatizo ya uchakavu na upungufu wa Vituo vya Polisi katika maeneo mbalimbali nchini. Kwa hiyo, Kituo cha Lushoto ni kimojawapo katika maeneo ambayo yana changamoto hizo. Niseme tu kwamba kama ambayo nimekuwa nikijibu mara kadhaa hapa, tunafahamu changamoto hizo na tutajitahidi kuzipunguza kwa kadri ambavyo tunaweza kupata fedha za kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kabisa, kwa kasi hii ambayo Serikali yetu ya Awamu ya Tano imeanza nayo ya ukusanyaji na udhibiti wa matumizi, basi katika muda wa miaka michache ijayo tunaweza tukapata bajeti ya kutosha kuweza kurekebisha matatizo haya ya Vituo vya Polisi pamoja na makazi ya Polisi.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Ahsante Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri aliyoyatoa, nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa ajali zinazotokea huacha athari nyingi mfano vifo, ulemavu, uharibifu wa mali na hata ya mayatima, je, kwa nini Serikali sasa isianzishe Mfuko wa Ajali yaani Accident Fund kwa ajili ya wahanga wanaofikwa na matatizo hayo? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili kwa nini wale abiria wanaopanda ndani ya gari ambao umetuambia kwamba mnawashusha na kuwarejeshea fedha zao. Ningeona kwa nini na wao wasingetozwa faini ikawa kama ni sehemu ya wengine kuogopa kupanda magari ambayo watu wamezidi? Wakiona wanatozwa faini najua na wale watakuwa kama kigezo kwamba nikiingia kwenye gari hii na mimi nitatozwa faini wakati gari imejaa? Naomba Mheshimiwa unijibu.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ametoa ushauri kwamba tuanzishe mfuko kwa ajili ya wahanga wa ajali hizi lakini pia ametoa ushauri kwamba abiria ambao wamezidi kwenye mabasi nao washitakiwe kwa maana ya kulipishwa faini. Naomba tu nishauri kwamba mapendekezo yake haya mawili niyachukue kwa ajili ya kuyafanyia kazi.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru kwa majibu ambayo tumeyapata kwa swali hili, kidogo yana mchanganuo ambao unafaa tofauti na mara ya mwanzo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba niulize maswali yangu mawili ya nyongeza. Dhiki katika Jeshi la Magereza ni uzembe kwa sababu kwa maoni yangu Jeshi hili ni Jeshi tajiri, Jeshi hili lilikuwa na Gereza la Kilimo Songwe ambalo lilikuwa linafanya kazi vizuri sana, Gereza la Karanga lilikuwa na kiwanda kizuri sana cha viatu, Gereza la Ukonga lilikuwa na kiwanda kizuri sana cha nguo; lakini tender zinatolewa kununua nguo za Magereza na za Polisi, tender zinatolewa kununua viatu vya Polisi na Magereza. Kwa nini, Serikali isiboreshe viwanda vya Jeshi hili, ili Jeshi likafanye biashara na likaweza kutatua matatizo yake pamoja na matatizo ya nyumba na hata kuisaidia Serikali, badala yake inatoa kazi ambazo Jeshi hili linaweza likazifanya kwa watu wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, nashukuru kwa mchanganuo uliotolewa. Naomba kumuuliza Waziri, kwa kuwa Askari Magereza katika Jimbo langu pale Rombo wanaishi katika nyumba zinazoitia aibu Serikali kwa kweli, wanaishi kwenye mabanzi. Je, Waziri yupo tayari kuandamana na mimi akakague nyumba hizo na kwa sababu hiyo, hizi zilizotengwa 390 angalau chache zianze kujengwa Rombo kwa ajili ya kunusuru makazi ya wale Askari pale Rombo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Magereza limepanga kuongeza uzalishaji wa mapato ya kilimo, ushonaji na ufugaji. Kwa hiyo, msingi wa swali lake kwamba Jeshi la Magereza limezembea siyo sahihi, kuna mipango kabambe tu ya kuhakikisha kwamba Jeshi la Magereza linajitegemea kwa chakula, lakini pia linaendeleza ujuzi na rasilimaliwatu ilizokuwa nazo katika kuhakikisha kwamba linachangia juhudi za Serikali za kuweza kuifanya sekta ya viwanda kuchukua sehemu kubwa katika uchumi wa nchi yetu katika miaka inayokuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kupitia utaratibu huo Jeshi la Magereza limeandaa andiko ambalo linaainisha miradi minane. Uzalishaji wenye matokeo makubwa ya haraka (quick win projects) na limeshawasilishwa Serikalini ili kuweza kupata fedha. Miradi hiyo ambayo ni ya kokoto Msalato; unenepeshaji wa ng‟ombe wa nyama Mbigili na Ubena; uzalishaji wa mafuta ya alizeti Ushora, Kongwa na Msalato; ushonaji wa viatu Ukonga na Karanga Moshi ambako ni kwa Mheshimiwa Selasini. Halafu kuna mradi wa samani ambao uko Arusha; kilimo cha umwagiliaji Idete Morogoro na kuimarisha kikosi cha ujenzi ili kiweze kumudu na kufanya kazi kubwa za ukandarasi.
Pia Jeshi hilo limeandika mpangokazi wa kujitosheleza kwa chakula ambalo pia limeshawasilishwa Serikalini ili kupata fedha za uendeshaji. Kwa hiyo, Jeshi linatekekeza sera ya uwezeshaji kwa kuingia ubia pia na taasisi mbalimbali binafsi kupitia utaratibu wa PPP ili kupata mitaji ya kuongeza uzalishaji. Mpaka sasa Jeshi limeshaingia ubia na kampuni ya Tabin ya Uturuki kwa ajili ya kutekeleza kilimo cha mpunga Gereza la Kigongoni. Pia limeainisha maeneo yenye madini na kupata leseni ya uchimbaji karibu 181, hatua za kutangaza maeneo hayo kwa ajili ya uwekezaji zinafanywa. Hilo nadhani lilikuwa ni swali lake la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, ametaka kujua kuhusiana na Kilimanjaro. Kilimanjaro tuna aina mbili, mbali ya ile miradi ambayo nimeizungumza, kuhusiana na huo ujenzi wa nyumba 3,500, lakini pia kuna utaratibu ambao Jeshi la Magereza linaenda nao, kwa kutumia rasilimali zilizopo katika maeneo husika. Kwa Mkoa wa Kilimanjaro tayari nyumba karibu 38 zimejengwa kupitia mradi huo. Kinachofanyika ni kwamba tunatumia rasilimali za nguvukazi zilizopo jeshini pamoja na ujuzi tulionao kuweza kujenga nyumba hizi kufikia katika level ya kuezeka halafu baadaye kupitia fedha za bajeti tunafanya finishing. Kwa hiyo, kupitia utaratibu huo kwa Mkoa wa Kilimanjaro tumeshajenga nyumba 38.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niko tayari kuambatana na Mbunge wakati wowote kwa ajili ya kwenda kuhakikisha kwamba tunatembelea miradi hii na mipango mingine ambayo atakuwa nayo Mheshimiwa Mbunge na tutashirikiana kwa pamoja. Tunapenda Wabunge wa aina yake ambao wako tayari katika kuchangia maendeleo ya nchi yetu.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa idadi ya karibu vifo 12,000 vilivyosababishwa na ajali za barabarani kwa miaka hiyo mitatu vinaweza kulinganishwa na mauaji ya kimbari, mauaji ya halaiki, na majeruhi 44,444 ni sawa na kiwanda cha kutengeneza Watanzania kupata ulemavu wa viungo mbalimbali. Je, Serikali inatueleza nini kuhusu kuja na suluhisho lenye mashiko na kutatua tatizo hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa ajali za barabarani hasa za mabasi ya abiria zinashiriki sana kwenye kutengeneza vifo na majeruhi, tena kwa kiwango kikubwa kwa mara moja, Je, Serikali ina mkakati gani pia kudhibiti ajali za barabarani zinazohusisha mabasi ya abiria?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa na mipango na mikakati mbalimbali ya muda mrefu na muda mfupi. Miongoni mwa mikakati hiyo ni kama ifuatavyo:-
Kwanza, tunajaribu kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo mbalimbali vya habari. Pia Jeshi la Polisi kupitia Askari wa Usalama Barabarani wamekuwa wakifanya doria za mara kwa mara na ukaguzi ili kuweza kuwabaini na kuwakamata wale ambao wanavunja sheria. Pia kumekuwa na utaratibu wa kutumia zile kamera za tochi ambazo zinabaini wale ambao wanakiuka taratibu za usalama barabarani ikiwemo kuongeza kiwango cha speed zaidi ya kilichowekwa kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa pia tukiangalia mchakato wa kuangalia utaratibu wa utoaji leseni vile vile ili kudhihirisha kwamba kwa kushirikiana na mamlaka nyingine watu wote ambao wanaendesha vyombo vya moto barabarani basi wawe ni ambao wana leseni zilizopo kisheria na isiwe kuzipata kinyemela. Pia kuna utaratibu wa kuchukua hatua stahiki kwa wanaovunja sheria siyo tu wale ambao wanaendesha vyombo hivi, hata wasimamizi wa sheria hizi mara moja inapotokea kutaka kulitia madoa Jeshi la Polisi basi hatua zimekuwa zikichukuliwa dhidi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na mifumo ambayo tumejaribu kuanza nayo sasa hivi, mifumo ya matumizi ya point ambayo bado haijaanza ipo katika utaratibu mzuri, nadhani muda siyo mrefu sana tutaweza kutumia ili kuwafanya sasa watu wawe na hofu zaidi ya kuvunja sheria hizo za barabarani. Pia kuna utaratibu wa tozo za papo kwa papo na hii imesaidia sana kiasi fulani kudhibiti ajali hizo. Tuna utaratibu wa kutumia TEHAMA kwa ajili ya kudhibiti ajali za barabarani. Pia tuna mipango, maana alitaka mipango ya sasa hivi na baadaye, tunayo mipango ya matumizi ya kamera ambayo nayo vile vile ipo katika michakato na ukaguzi wa lazima kwa magari yote. Kwa hiyo, hizo ni baadhi ya hatua ambazo Serikali imekuwa ikichukua katika Jeshi la Polisi kupitia kitengo cha Polisi cha Usalama Barabarani kudhibiti hali ya ajali nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kiasi fulani imepungua, na ndiyo maana ukiangalia kwenye takwimu nilizozisoma kwenye swali la msingi utakuta ajali za barabarani zimekuwa zikipungua mwaka hadi mwaka.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na sababu ambazo Mheshimiwa Waziri amezizungumza, naamini kabisa baadhi ya ajali, tena ajali nyingi sana zinatokea kwa sababu ya kutokuwa na alama barabarani pamoja na matuta makubwa sana. Tulishasema hapa Bungeni matuta yawe na standards. Ni lini Serikali itafanya matuta nchi nzima yawe ya standard ili kuepusha ajali ambazo siyo za lazima?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kudhibiti ajali barabarani ni suala ambalo ni mtambuka linahusisha taasisi mbalimbali. Kwa mfano, suala ambalo Mheshimiwa Suzan Lyimo amelizungumza ni la msingi, ambalo kwa upande wa Serikali linahusisha Wizara ya Ujenzi na ndiyo maana tukawa na mkakati kabambe wa kushirikisha wadau wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, muda muafaka utakapofika tunaweza tukauanika mpango huu, tupo katika hatua nzuri ambapo tuna ushirikiano mzuri na SUMATRA, Wizara ya Ujenzi kupitia TANROADS, TBS na shule za udereva pamoja na Polisi, tunakaa pamoja ili tuweze kuwa na utatuzi wa kudumu wa matatizo ya ajali kwa kuunganisha nguvu kwa pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimtoe tu wasiwasi kwamba mambo hayo tunayafanyia kazi na wakati muafaka utakapofika basi tutauweka hadharani.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo tu la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhahiri kwamba wingi wa wafungwa magerezani unakwenda sambamba na wingi wa mahabusu waliopo magerezani. Na mara nyingi ni kwamba baadhi ya mahabusu wanakamatwa kwa kupakaziwa makosa na askari wa Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, napenda kuiuliza Serikali, ni hatu zipi ambazo Serikali inazichukua za dhahiri, kukomesha kitendo hiki ambacho kinawatesa wananchi lakini kinaitia Serikali hasara kwa kuwashikilia watu ambao hawana hatia?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nilikuwa nataka nijaribu kuweka kauli yake sawa ambayo ameizungumza kuhusiana na shutuma dhidi ya Jeshi la Polisi. Amezungumza kana kama kwamba Jeshi la Polisi lote kazi yake ni kubambikia watu kesi, ninachoweza kusema ni kwamba kuna matukio machache ya baadhi ya polisi ambao wamekuwa wakilichafua Jeshi la Polisi, lakini ni wachache mno, ambao Jeshi la Polisi limekuwa likiwachukulia hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, na wote ni mashahidi, juzi wakati wa bajeti kuna hoja ilizungumzwa kuhusiana na yule kijana ambaye alibambikiwa kesi pale gerezani. Ninachotaka kulithibitishia Bunge lako Tukufu mpaka sasa hivi ni kwamba askari waliohusika na jambo lile watatu wameshafukuzwa kazi na bado wanaendelea kuchukuliwa hatua za kijinai.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo si kweli kwamba Jeshi la Polisi limekuwa likizembea kwa kuwachukulia hatua askari wachache sana ambao wamekuwa wakifanya matendo haya ambayo yanakinzana kabisa na taratibu za sheria za nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kimsingi ni kwamba hayo ambayo ameyazungumza Mheshimiwa Selasini kuhusiana na tuhuma dhidi ya Jeshi la Polisi niliona niyaweke sawa kwa statement hiyo.
MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Spika, ni kawaida kwa Wizara hii ya Mambo ya Ndani kila siku kuja na jawabu lilelile. Swali langu la mwanzo ni kukosekana kwa boti ya doria katika Kisiwa cha Pemba na mazingira ya jiografia yalivyo ya Kisiwa cha Pemba ni hatari kwa mazingira yela yalivyo; je, Mheshimiwa Waziri haoni kwamba kuwakosesha wanamaji hawa wa boti ya doria ni kuhatarisha mazingira ya amani kwa nchi yetu hii ya Tanzania?
Swali la pili, kimsingi Wizara ya Mambo ya Ndani imekuwa ikitenga bajeti ya lita kadhaa za mafuta yasiyopungua 1200 kila mwezi je, Mheshimiwa Waziri anaweza kutueleza mafuta haya yanatumikaje ukizingatia kwamba ndani ya Kisiwa cha Pemba hakuna boti ya doria kwa Kikosi cha Wanamaji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimejibu katika swali la msingi kwamba wakati jitihada za kupeleka boti Pemba pale uwezo utakapopatikana linaendelea kwa sasa hivi tunafanya kazi kwa mashirikiano mazuri na vikosi vingine mbalimbali kama vile vikosi vya SMZ ambavyo wana boti za doria zinazokidhi mahitaji kwa kipindi hiki kutoa huduma maeneo ya Pemba ikiwemo Jimbo la Wingwi.
Mheshimiwa Spika, lakini kuhusiana na mafuta kimsingi ni kwamba fedha kwa ajili ya matumizi ya mafuta ya Jeshi la polisi kiujumla hazitoshi kwa hiyo, ningedhani kwamba Mheshimiwa Mbunge badala ya kuhoji matumizi angehoji uwezekano wa kuongeza kwa sababu hata zilizopo hazikidhi mahitaji ya huduma katika matumizi ya Jeshi la Polisi.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, nina maswali tu madogo mawili ya nyongeza.
Pamoja na askari wa Iringa kuishi kwenye mazingira magumu sana, lakini zaidi ya nusu ya askari wanaishi nje ya makambi yao yaani uraiani. Pia katika Mkoa huo wa Iringa, Wilaya ya Kilolo Serikali haijaweza hata kujenga jengo lolote la ofisi wala makazi ya askari na katika majibu yake Serikali imesema kwamba itakuwa inajenga kadri itakavyokuwa inapata fedha.
Je, Serikali ipo tayari sasa kutoa kipaumbele kwa Mkoa wetu wa Iringa ili askari wetu waweze kuishi kwenye mazingira bora yajengwe mapema sana? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa askari wa Mkoa wa Iringa wanadai posho na stahiki zao kiasi kikubwa sana cha pesa na Serikali imesema kwamba bado wanafanya uhakiki. Je, ni lini sasa uhakiki utakamilika ili askari wetu wa Mkoa wa Iringa waweze kupata stahiki zao na posho kwa sababu familia zoa zimekuwa zikiishi kwa shida sana na hasa watoto na wake za askari? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, wakati tunakamilisha mchakato wa ujenzi wa nyumba za askari ule ambao nimekuwa nikiuzungumza hapa Bungeni kila siku ambao pia utahusisha na Mkoa wa Iringa tunajipanga kutumia rasilimali za ndani pamoja na rasilimali zilizopo katika maeneo husika pamoja na rasilimali watu ili kupunguza tatizo au changamoto za makazi kwa askari wetu na vituo vya polisi.
Mheshimiwa Spika, nataka nichukue fursa hii kwanza kabisa na kwa dhati nimpongeze Mheshimiwa Ritta Kabati kwa jitihada zake kubwa sana ikiwemo ujenzi wa Kituo cha Polisi Iringa, ambapo sasa hivi nguvu zake anazielekeza maeneo ya Kilolo, lakini kwa kutambua kwamba Mheshimiwa Mbunge amefanya kazi kubwa sana pale Iringa ya ujenzi wa kituo nataka nimhakikishie kwamba tutakuwa pamoja na yeye tutashirikiana naye ili tuweze kuona kwa haraka sana tutatumia mpango huu wa matumizi ya rasilimali katika eneo husika ili kupunguza changamoto ya makazi pamoja na vituo vya polisi.
Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge baada ya kikao hiki cha Bunge tukae kwa pamoja tushauriane tuone iko vipi kwa haraka sana mpango huu ambao tumeubuni hivi karibuni tunaanza kutekekeleza kwa Kilolo.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusiana na lini ukaguzi utamalizika. Naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutafanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba tunakamilisha ukaguzi haraka iwezekanavyo ili malipo haya yaweze kulipwa.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu na nimpongeze sana niongezee tu kwa kumpa assurance Mheshimiwa Mbunge ambaye jambo hili amekuwa akilifuatilia kwa umakini sana la maisha ya polisi na vitendea kazi vyao kwamba tarehe 9 Septemba, 2016 wale wenzetu ambao tulikuwa tunaongea nao kuhusu mkataba wa ujenzi wa nyumba za askari kiongozi wao mkubwa atakuja na atakutana na IGP pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara na baada ya hapo tutabakiza mawasiliano ya ndani ya Serikali kwa ajili ya kwenda kwenye utekelezaji wa jambo hilo.
Mheshimiwa Spika, la pili Wizara tumeamua kwenda na jambo hili sambamba kwamba jitihada zitakazofanyika za kibajeti tuzioanishe na jitihada za rasilimali tulizonazo ndani ya taasisi zetu hizi na nimeelekeza mikoa yote wafanye tathmini ya kila mkoa tuna wafungwa wangapi wanaoweza kufanya kazi za kufyatua tofali na wafanye tathmini ya vitendea kazi vinavyoweza kutumika kufyatulia tofali hizo na aina ya tofali ambazo zinatakiwa, lakini pia na kutumia bajeti kidogo zilizopo kwa ajili ya vitendea kazi vingine ambavyo vitatakiwa kama cement ama nondo kwa ajili ya kuanza miradi hiyo katika maeneo ambayo kazi hiyo si kubwa sana kwa ajili ya kupunguza tatizo hili sambamba na jitihada za kibajeti ambazo tunazifanya.
Kwa hiyo, Serikali inatambua ukubwa wa tatizo hili na inaweka uzito unaostahili na Mheshimiwa Rais tayari alishatuelekeza wasaidizi wake na sisi tunatembea kwenye nyayo zake kuhakikisha tunamaliza tatizo hilo la manung‟uniko ya askari.
Mheshimiwa Spika, hivyo hivyo kwenye upande wa madai yao nimeelekeza kila ambaye anatunza kumbukumbu za askari waweze kuhakikisha kwamba wanaorodhesha vizuri kuwarahisishia wale wanaokagua, wanaofanya ukaguzi ili madai hayo ya askari yasikae muda mrefu sawasawa na maeneo mengine ambayo yana uficho ama yana tatizo la kuweza kufanya ukaguzi kwa sababu askari anapokuwa kazini huku anadai inampunguzia morali ya kazi na inampunguzia uwezo wake wa kufanya kazi.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niulize maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa Mkoa wa Kigoma unapakana na nchi za Burundi na DRC, na kwa kuwa eneo kubwa la mpaka halina ulinzi, hali inayopelekea wahalifu kupita na kupitisha silaha nzito kuingia Tanzania, wahalifu hao kwa kushirikiana na raia wasiokuwa waaminifu hufanya ujambazi na unyang‟anyi.
Je, Serikali iko tayari kufanya utafiti wa kukagua mpaka upya na kubaini maeneo yasiyokuwa na ulinzi ili kuweza kuweka ulinzi maeneo yasiokuwa na ulinzi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; kwa kuwa mara nyingi vituo vya polisi hukabiliwa na ukosefu wa mafuta, hivyo kuwafanya polisi kushindwa kufanya kazi yao kikamilifu. Je, Serikali iko tayari kuongeza bajeti ya vituo vya polisi, hasa Mkoa wa Kigoma ili polisi waweze kukabiliana na majambazi hao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la Mheshimiwa Genzabuke limekuja wakati muafaka kwa sababu jana tulikuwa tuna kikao kizito ambacho kilikuwa kinahusisha Wakuu wa vyombo vyote vya usalama vilivyopo nchini, vilivyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Moja katika ajenda ya msingi ambayo tulizungumza ilikuwa ni hiyo.
Ninachotaka kumuelezea tu kwa sasa hivi ni kwamba tumetoa jukumu hilo kwa Idara ya Uhamiaji ambayo kazi hii wameshaianza kufanya huo utafiti ambao anauzungumza wa kubaini vipenyo vyote ambavyo vinakisiwa viko vipenyo takribani 248 nchi nzima. Kuazia Mkoa wa Kagera, nchi nzima kwa maana ya mikoa yote ambayo imepakana na nchi jirani. Kwa hiyo, tumeshaanza hiyo kazi na pale itakapokamilika wataliwasilisha hilo andiko Serikalini.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia haina maana kwamba hivi tunavyozungumza kuna tatizo kiasi kikubwa hivyo, kwa sababu kuna kazi kubwa ambayo inafanywa na vyombo hivi vya usalama, ikiwemo kuendesha doria na misako katika maeneo hayo ambayo ni maeneo tete. Lakini kutoa elimu vilevile kwa wananchi pamoja na Wenyeviti wa Mitaa na Vitongoji wa maeneo ambayo yanapakana na mipaka hiyo pamoja na kuimarisha vitendea kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili ambalo amezungumzia changamoto ya mafuta; ninataka tu nimueleze kwamba moja katika majukumu ya msingi ya Wizara yetu hii ambayo tumefanya kwa mafanikio makubwa ni kuhakikisha kwamba kuwepo kwa wakimbizi katika maeneo hayo ambayo yapo katika Mikoa inayopakana na mikoa hii ambayo ina machafuko ikiwemo Kigoma, kusilete athari kwa wananchi na badala yake kuwe kuna manufaa. Katika kufanya hivyo tumeweza kuzungumza na mashirika haya ambayo yanahudumia wakimbizi kuweza kuchangia, siyo tu kwa maendeleo ya jamii ya wananchi ambao wanaishi pale, lakini hata kwa vyombo vya usalama wakati wa kutekeleza majukumu yao. Moja katika mafanikio hayo ni kwamba hivi tunavyozungumza UNHCR wametoa magari sita, pikipiki mbili kwa kambi tatu za Nyarugusu, Mtendeli na Nduta, na gari moja aina ya Land Cruiser kwa Ofisi ya RPC. Pia shirika hilo huwa linatoa mafuta kwa kuwalipa posho ya shilingi 15,500 kwa siku, kwa askari ambao wanalinda kambi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na jitihada za Serikali ambazo zinafanyika kuweza kuimarisha bajeti ya polisi ya mafuta kadri hali ya uchumi itakavyoimarika. Kwa hiyo, kuna kazi ambayo inafanyika tu na imekuwa na mafanikio kwa kiasi kikubwa, hata hivyo tunazitambua changamoto ambazo Mheshimiwa Genzabuke amezungumza na hii mikakati niliyoizungumza ni moja kati ya njia ambazo tunakabiliana nazo.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa fursa hii uliyonipatia.
Kwa kuwa tatizo la ujambazi linaloipata Mikoa ya Kagera na Kigoma lipo pia tatizo la namna hiyo katika Jimbo letu na Wilaya yetu ya Mkuranga ambapo hapa karibuni tulipata tatizo la uvamizi wa majambazi katika Benki yetu ya NMB, Bupu na pale Mbagala Rangitatu na mengineyo.
Je, Serikali sasa iko tayari kuhakikisha kwamba Wilaya yetu ya Mkuranga inapata nyongeza ya vifaa kazi lakini pia na Kituo cha Polisi chenye hadhi ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba kwa kuwa hili ni ombi, basi tunalichukua, halafu mimi na yeye tutakaa, tunajuana ma-comrade, tuweze kuona uwezekano wa kulitimza hilo.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba kwa kuwa hili ni ombi, basi tunalichukua, halafu mimi na yeye tutakaa, tunajuana ma-comrade, tuweze kuona uwezekano wa kulitimza hilo.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kuuliza swali la nyongeza.
Kumekuwepo na wimbi kubwa sana la ujambazi ambalo linafanywa na hawa vijana wanaojulikana kama panya road ambao wamekuwa wakileta utata sana katika miji mikubwa na sasa hivi mpaka Iringa wameshatokea, Serikali ina mpango gani ama mkakati gani wa kuondoa ujambazi, hawa panya road kwa sababu ni vijana ambao nasikia wanafahamika kwenye mitaa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la panya road, ni kweli kulikuwa na kundi la vijana ambalo lilikuwa linafanya uhalifu. Lakini nataka nimhakikishie Mheshimiwa Kabati kwamba Jeshi la Polisi limefanya kazi nzuri kudhibiti kundi la vijana hawa na nadhani Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi kwamba kwa kipindi fulani sasa matukio hayo hayajitokezi na vijana hao wamedhibitiwa.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Kwa kuzingatia kwamba Mkoa wa Songwe ni mpya na ni mkoa ambao uko mpakani, lakini kiongozi ambaye anahusika na mambo ya ulinzi na usalama wa Mkoa wetu wa Songwe ambaye ni RPC anaishi kwenye nyumba ambayo ni sawa na gofu. Nilitaka kupata kauli ya Serikali kwamba ni lini RPC wa Songwe atapatiwa nyumba nzuri?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua changamoto ambayo inakabili makazi ya RPC kule Songwe hasa ukitilia maanani kwamba mkoa huu ni mpya, kwa hiyo utakumbana na changamoto mbalimbali na unahitaji muda mpaka kuweza kukaa sawa. Kwa kulitambua hilo basi, nikiamini kabisa kwamba tuna programu kabambe ya ujenzi wa nyumba za makazi kwa askari ambazo tumekuwa tukizizungumza hapa kila siku, tutaangalia huo uwezekano kufikia utaratibu huo ama utaratibu mwingine wowote ili tuweze kurekebisha hilo jambo, tunalifahamu na tutalifanyia kazi.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nilitaka kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Wananchi kwenye vijiji vya Majimbo yetu wanapojichukulia sheria mkononi, kunavyopigwa mwano, pengine kumetokea kibaka, polisi wanakuja kukamata viongozi wa vijiji na kuwa-suspect na ile kesi, lakini kwenye mgodi ni tofauti, zinapookotwa maiti zenye risasi za moto na matukio mengine mabaya, hakuna suspect yeyote anayekamatwa kutoka kwenye Mgodi wa GGM na zinachukuliwa maiti zinakwenda kutelekezwa hospitali ndugu wanakwenda kutambua na kuchukua bila kuchukuliwa hatua yoyote.
Je, Waziri yuko tayari kufuatana na mimi baada ya Bunge hili kwenda katika Kijiji cha Nyakabale ambacho kina wahanga zaidi ya 100 waliopigwa risasi za moto na kuumishwa mbwa wa mgodi, kwenda kuwaona na kuja kutoa majibu sahihi kwenye Bunge lijalo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tatizo ndiyo hilo, kwa nini Mgodi wa GGM usiweke uzio kama ilivyo migodi mingine hapa nchini kama Acacia, Nyamongo na Kahama Mine?
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimejibu swali langu la msingi ambapo nilitolea mfano wa hatua ambayo Serikali ilichukua kwa askari ambaye aliwapiga risasi wananchi, kwa hiyo nadhani siyo kweli kwamba hakuna hatua hazijachukuliwa, hatua zinachukuliwa na huo ni mfano mmoja tu. Inawezekana pengine kuna baadhi ya matukio hayajachukuliwa hatua labda kwa kukosekana kupatikana taarifa kwa mamlaka husika. Sasa wazo lake hili alilolitoa la kuambatana mimi na yeye nadhani ni wazo la msingi ili aweze kunionesha maeneo ambayo yalipaswa kuchukuliwa hatua lakini hatua hazikuchukuliwa tuweze kuchukua hatua. Kwa hiyo ombi lake hilo tumelipokea kwa mikono miwili ni wajibu wetu kuweza kushirikiana na Waheshimiwa Wabunge kuwatumikia wananachi, hasa wanyonge, ambao wamekuwa wakionewa, kwa hiyo kwa kuwa yeye ana ushahidi basi tutafuatana pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kwamba Mgodi ya GGM haujawekwa uzio, hili siwezi nikalijibu sasa hivi kwa sababu sijafika kwenye mgodi huu. Lakini kwa kuwa tuna ziara hiyo mimi na yeye nadhani wakati huo utakuwa ni muafaka wakuweza kutembelea kuangalia mazingira pale tukashauriana kwa pamoja sasa na vyombo vinavyohusika na usalama kuimarisha usalama katika mgodi huo ili wananchi wasiweze kupata athari zaidi.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona. Kwa kuwa katika Wilaya yetu ya Lushoto tuna pakana na nchi jirani ya Kenya na Kituo cha Polisi cha Mnazi kina upungufu mkubwa wa vitendea kazi zikiwemo pamoja na silaha.
Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusu suala hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, hili jambo niseme tu kwamba tutalichukua tuangalie upungufu huo ambao anauzungumzia Mheshimiwa Mbunge kwa kushirikiana na yeye tuone hatua muafaka ya kuchukua ikiwemo kuongeza vitendea kazi kadri ya mazingira na hali halisi na ushauri wa kitaalamu utakapokuwa unaruhusu. Maana yake wakati mwingine uwekaji wa vitendea kazi hivi unazingatia vigezo vingi ikiwemo silaha, kwa hiyo, kuna haja ya kukaa na wataalam kwa maana ya Jeshi la Polisi kushauriana ni sababu gani ambazo zimesababisha eneo hilo liwe na upungufu halafu tuchukue hatua stahiki kwa wakati muafaka.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa suala la ulinzi na usalama ni tatizo na sasa hivi ukichukulia kumetokea mauaji ya mara kwa mara nchi hii, na watu wamelalamika kwamba hawasikilizwi wanapokwenda kwenye vituo vya polisi na mahakama na kwa hivyo kujichukulia sheria mkononi. Serikali haioni sasa inabidi ifanyie kazi suala hili ili kupunguza haya mauaji ambayo yamekuwa ni kero na shida katika nchi hii?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza jambo ambalo ni la muhimu sana wananchi wakalifahamu mauaji ni kweli yanatokea, lakini siyo sahihi kwamba hali ya mauaji haya imekuwa kubwa na inaongezeka zaidi ya ilivyokuwa. Ninasema hivyo kwa uthibitisho wa kitakwimu ambapo takwimu za haraka ukiangalia kwa mfano katika kipindi cha Januari mpaka Aprili, 2016 jumla ya matukio yaliripotiwa yalikuwa ni 1,030 na idadi ya watu waliouawa ni 1,060 ukilinganisha na watu 1,173 katika kipindi kama hicho ambayo ilikuwa kwa matukio 1,153 kwa mwaka uliopita.
Kwa hiyo, inaonekana kuna upungufu wa matukio kama 123 ambayo ni sawa na asilimia 10.7. Hata hivyo punguzo hilo halimaanishi kwamba hatuyachukulii uzito matukio ambayo yanatokea hasa katika kipindi hiki cha karibuni tumeona kulikuwa na matukio yameshamiri kidogo ya mauaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nieleze Bunge lako Tukufu pamoja na kujibu swali la Mheshimiwa Mwamoto kwamba nataka niwatoe wasiwasi wananchi na Wabunge, kimsingi matukio haya ya mauaji yanasababishwa na vyanzo tofauti, kwa mfano kwa haraka haraka nizungumze najua muda ni mfupi lakini asilimia 33 ya matukio ya mauaji ambayo yamejitokeza kipindi cha karibuni ni yanatokana na wizi, 11.6 yanayotokana na ugomvi wa kifamilia, imani za kishirikina asilimia 10.3, wivu wa mapenzi asilimia 7.6, risasi asilimia 6.5, ugomvi wa ardhi asilimia 6.2 na nyinginezo asilimia 24 nukta kadhaa.
Kwa hiyo, utaona kwamba matukio haya ingelikuwa yanatokana na tukio moja tu tungesema kwamba kuna mtandao hatari labda wa jambo fulani. Hata hivyo Serikali lazima ichukulie kwa uzito kupotea kwa maisha ya raia mmoja iwe kwa chanzo chochote kile. Na ndiyo maana sasa Jeshi la Polisi likafanya kwa mafahikio makubwa kwa haraka sana kuweza kuwakamata watuhumiwa mpaka sasa hivi matukio hayo yaliyotokezea aliyoyazungumza Mheshimiwa Mwamoto kwa karibuni watuhumiwa 72, mpaka sasa hivi ambao wanatupa dalili nzuri ya kuwashughulikia na wengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuendelee na hiyo kazi na naamini kabisa kazi hiyo ya Jeshi la Polisi itaifanya kwa mafanikio na Waheshimiwa Wabunge na wananchi msiwe na wasiwasi watu wote ambao wamejihusisha katika matukio haya ya mauaji iwe kwa sababu yoyote. Iwe kwa wivu wa mapenzi, iwe kwa ujambazi, iwe kwa ugomvi wa ardhi, iwe kwa kifamilia watatafutwa popote walipo na watachukuliwa hatua za kisheria.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwamba sehemu kubwa ya askari ambao wanalinda maeneo ya kuzunguka Mgodi wa GGM wanalinda mawe ambayo hayana thamani ambayo hata mgodi hawayahitaji, matokeo yake ndiyo wanakamata watu kila siku. Je, ni lini Serikali itaondoa askari hao kwenda kulinda usalama wa raia sehemu nyingine?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, tutalichukua swali lake tuone umuhimu huo kama bado upo, kama utakuwa haupo kama Mbunge anavyoshauri basi tutaondoa kama upo wataendelea kubakia.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kuna raia wa kigeni ambao wamekuwa wakitumia udhaifu wa mfumo wa hati za kusafiria na kuwawezesha kusafiri kinyume cha utaratibu na kuwawezesha kutenda makosa kwa kigezo cha Utanzania. Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba wanapatikana lakini hatujajua wala hatujawahi kusikia ni hatua gani ambazo zimekuwa zikichukuliwa. Je, Serikali imewachukulia hatua gani maofisa hawa wanaojihusisha na utoaji wa hati hizo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na Maafisa Uhamiaji ambao wanajihusisha na ukiukwaji wa taratibu wamekuwa wakichukuliwa hatua mbalimbali. Miongoni mwa hatua hizo ni kuwafukuza kazi pamoja na kuwashtaki. Hata hivyo, naomba nichukue fursa hii kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba tupo katika hatua za mwisho za ukamilishwaji wa uanzishwaji wa Mahakama ya Kijeshi katika Idara ya Uhamiaji kama ilivyo katika majeshi mengine ikiwemo Polisi ili kuweza kuwa na utaratibu wa uchukuaji wa hatua hizo kwa haraka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naamini kabisa pale mchakato huo utakapokuwa umekamilika, basi tutaweza kufanya kazi hiyo kwa ufanisi zaidi. Kwa wale ambao tumekuwa tukiona mazingira tu yanaashiria utendaji mbovu au ukiukwaji wa sheria ikiwemo rushwa bila ya kupata ushahidi tumekuwa tukichukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwahamisha katika vituo vyao vya kazi.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa kwa siku hizi za karibuni Watanzania wameshuhudia mauaji ya kutisha katika Mikoa ya Mwanza na Tanga. Je, Serikali ina mkakati gani wa dhati wa kuzuia mauaji haya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili lina majibu mapana sana kwa sababu linagusa vyombo kadhaa vilivyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani na hususan Jeshi la Polisi. Kwa sababu swali la msingi linahusu Idara ya Uhamiaji, naomba nilijibu kwa mtazamo wa Idara ya Uhamiaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Idara ya Uhamiaji suala la udhibiti wa uhalifu nchini inajikita zaidi katika kuhakikisha tunadhibiti uingiaji wa wahamiaji haramu nchini ambao mara nyingi wamekuwa wakihusishwa na kuongeza wimbi la uhalifu katika nchi yetu kwa kuingiza silaha pamoja na kujihusisha na vitendo mbalimbali vya uhalifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kufanya hivyo, tumeandaa mkakati kabambe ambao utahakikisha kwamba unadhibiti vipenyo vyote vilivyopo mipakani. Mpaka sasa hivi tumefanya uhakiki katika baadhi ya mikoa na kubaini zaidi ya vipenyo 280 na bado tunaendelea katika baadhi ya mikoa ambayo hatujakamilisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatafuta fedha ili tuweze kufanya hiyo kazi ya kudhibiti mipaka yetu ili tuweze kuzuia hawa wahamiaji haramu wasiweze kuingia katika nchi yetu. Hata hivyo, tumekuwa tukifanya kazi kubwa sana ya kuhakikisha kwamba tunawakamata wahamiaji haramu na kuwachukulia hatua zinazostahiki kwa kufanya misako katika maeneo mbalimbali nchini. Tumefanya kazi hiyo kwa mafanikio makubwa sana na wahamiaji haramu wengi tayari wameshakamatwa na wameshachukuliwa hatua za kisheria kwa kipindi kifupi tangu Serikali ya Awamu ya Tano ilivyoingia madarakani.
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri na majibu yanaleta matumaini kwa hawa askari wetu, lakini nilikuwa na maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, katika mpango huu wa Serikali wa kujenga nyumba za askari wetu, Wilaya yetu ya Uyui itaangaliwa kwa macho mawili? Kwa sababu Halmashauri yetu ya Tabora kwa maana ya Uyui imetumia zaidi ya shilingi milioni 300 kujenga kituo kile cha polisi, kwa sasa kama nilivyosema kwenye swali la msingi askari wetu hawana makazi ya kukaa wanakaa kwenye nyumba za mabati.
Lakini la pili, Serikali ina wajibu wa kuwapatia makazi bora askari wetu, ukiangalia nchi nzima askari wetu wanakaa katika nyumba za kupanga mitaani kwa sababu hakuna makazi ya askari wetu.
Je, Serikali inawalipa posho ya makazi askari hawa au ina mpango gani wa kuwalipa posho za makazi askari hawa kwa sababu wanakaa nyumba za kupanga uswahilini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza ni swali ambalo limekuwa likiulizwa takribani kila siku katika Bunge hili na kila Mbunge amekuwa akiuliza kwamba nyumba zitajengwa katika eneo lake, vituo vitajengwa katika eneo lake. Nimekuwa nikijibu na vitajengwa lini, likiwemo suala la Mheshimiwa Mbunge la Uyui. Na nimekuwa nikijibu swali hili mara nyingi kwa mfumo ambao umezoeleka hapa, lakini naomba leo nije na jibu lingine kidogo ambalo litakuwa ni mbadala ambayo yale najibu. Si kwa majibu ya majibu ambayo nilikuwa nimejibu mwanzo yatakuwa hayamo, majibu ambayo nilikuwa nimeyajibu mwanzo yataendelea kubakia vilevile kwamba tunaendelea kujenga kadri ya hali ya uwezo wa bajeti utakaporuhusu ukiachilia mbali programu ambazo tayari ziko mezani.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jibu ambalo nataka niongezee sasa hivi ni kwamba nilikuwa naomba nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge kwamba katika fedha za Mfuko wa Jimbo ambazo tunapata basi tuweke kipaumbele kuhakikisha kwamba tunaimarisha makazi ya askari kwa yale maeneo ambayo bado ujenzi wake haujakuwa katika ratiba za hivi karibuni pamoja na vituo vya polisi. Kwa hiyo, pamoja na nyongeza hiyo na hili lingine lilikuwa kama ni ushauri nilitaka nitoe Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kimsingi ni kwamba ujenzi wa nyumba 4,136 unahusisha mikoa 17, lakini wamechukua mikoa miwili ya Zanzibar. Kimsingi Mikoa ya Zanzibar ni mitano kwa hiyo inakuwa takribani 20. Sasa labda Mheshimiwa Ntimizi, mimi na yeye tukae baadaye tuone kama katika Wilaya yake ya Uyui, katika Awamu ya Kwanza unaingia ama kama haimo katika awamu ya kwanza basi tuweze kushirikiana mimi na yeye kuhakikisha tunaingiza katika Awamu ya Pili ya ujenzi wa nyumba hizo 4,136.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali lake la pili alikuwa ameuliza ni kwamba je, kuna utaratibu wa kuwalipa askari posho wale ambao hawakai katika nyumba za Serikali, ni kweli upo utaratibu huo, na kuna posho ya pango, ni asilimia 15 ya mshahara.
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru, kwa kuwa tatizo la Mazingira magumu kwa Jeshi la Polisi linafanana kabisa na Jimbo la Igalula, je, ni lini Naibu Waziri atafika katika Jimbo la Pangani kuhakikisha kwamba tunaenda kuangalia manyanyaso askari wanayopata katika Jimbo langu la Pangani hususan katika suala zima la makazi, pamoja na kituo kibovu cha Jeshi la Polisi?
Kwa hiyo, nilikuwa nataka commitment ya Naibu Waziri yupo tayari kushirikiana na mimi kwenda Pangani kuhakikisha kwamba akaone hali halisi ya Manyanyaso wanayoyapata Jeshi la Polisi wa Pangani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Spika, niko tayari, kwa hiyo, baada ya kikao hiki tupange ratiba.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu matatizo ya Jimbo la Igalula ni sawa na matatizo ya Jimbo la Nyamagana, nigeomba pia kutumia nafasi hii kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri.
Katika Jimbo la Nyamagana ziko nyumba za polisi ambazo zimejengwa toka mwaka 2010 tarehe 24 Mei zilitarajiwa kukamilika baada ya wiki 36. Lakini kwa masikitiko makubwa mpaka hivi ninavyozungumza leo nyumba zile hazijakamilika. Wangeweza kukaa askari zaidi ya 24 na familia zao na Jeshi la Polisi likaonesha motivation kubwa kwa askari hawa kuishi kwenye mazingira bora na salama ili waweze kufanya kazi zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni lini Mheshimiwa Waziri ananithibitishia nyumba hizi zitajengwa na kukamilika kama ambavyo mkataba wa mkandarasi unavyosema miaka minne baadaye?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli mradi wa nyumba ambazo zingeweza kuwa na makazi ya takribani familia 24 pale Mwanza, ulikuwa umesuasua kidogo. Lakini katika bajeti yetu ya mwaka huu katika bajeti ya mendeleo tumetenga fedha kwa ajili ya kukamilisha mradi huo pamoja na miradi mingine ambayo imekuwa ikisua sua ikiwemo mradi ule wa nyumba ambayo familia 12 Kagera, kuna Musoma -Mara, Ludewa - Njombe, na Makao Makuu ya upelelezi ya Makosa ya Jinai pale Dar es Salaam.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru, niulize swali la nyongeza linalolingana na Wilaya ya Uyui. Katika mji wa Makambako kipolisi ni Wilaya ya Kipolisi, pamoja na maelezo ambayo Serikali imetoa mazuri. Je, Serikali ina mpango gani hasa hususani kituo cha Makambako ambacho ndicho kiko barabarani yaani kiko njia panda ya kwenda Mbeya, Songea na askari hawa hawana nyumba kabisa hata moja ya kuishi?
Je, Serikali ina mpango gani wa kuzijenga nyumba katika kituo cha Polisi cha Makambako na wakati eneo la kujenga nyumba lipo? Nakushukuru
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu swali ambalo liliulizwa la nyongeza la Mheshimiwa Ntimizi, ni kwamba tuna ujenzi wa nyumba za askari kwa awamu mbili. Kwa hiyo, hoja yake kwamba eneo la Makambako limo katika utaratibu huo ama halimo?
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani cha kufanya anipatie muda nipitie kwenye orodha ya zile Wilaya maana kujua Wilaya zote kwa Mikoa ni rahisi sana, lakini kujua Wilaya zote na maeneo yote nchi nzima exactly ni wapi nyumba hizi zitajengwa hasa ukiangalia kwamba inawezekana baadhi ya Wilaya mgao haujafanyika. Inahitaji nipitie kwa hiyo baada kupitia nitamjulisha, ikiwa haimo katika awamu ya kwanza basi tutazingatia katika awamu ya pili.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na namshukuru Waziri kwa masuala yake mazuri aliyonipatia, lakini napenda kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni hatua gani zinachukuliwa kwa wale askari ambao watabainika kuchukua rushwa kwa madereva ambao wametenda makosa?
Na je, madereva wanaojaza abiria kwenye magari kuliko level seat, hawa wanachukuliwa hatua gani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ambazo askari wanachukuliwa wanapobainika wanajihusisha na vitendo vya rushwa ni kufukuzwa kazi mara moja. Lakini pamoja na kufukuzwa kazi, pia kushitakiwa.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona. Kwa kuwa usalama barabarani ni pamoja na kusimamia kuhakikisha kwamba ajali hazitokei mara kwa mara.
Je, Korogwe kutoka Chalinze hadi Same ni kilometa kama 370 na kitu, je, Serikali kwa maana ya Wizara ya Mambo ya Ndani, askari wa Korogwe Mjini wao ni mara nyingi ndiyo ambao huwa wanashughulikia ajali kutoka kwenye maeneo hayo niliyoyasema hizo kilometa zote hizo. Watakuwa tayari kuwapatia gari askari wa barabarani ili waweze kufanya patrol ili waweze kupunguza ajali zinazotokea barabarani?

MHE. MARY P. CHATANDA: Korongwe Mjini.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mary Chatanda, Mbunge wa Korogwe Vijijini?

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, tupo tayari kupeleka gari la nyongeza hapo cha msingi ni kuyapima mazingira hayo, kwa hiyo, nawalekeza Jeshi la Polisi kulipitia ombi la Mheshimiwa Chatanda na kuangalia uwezekano wa kuongeza gari moja pale litakapokuwa limepatikana.
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Naibu Spika, asante, kwa kuwa usalama barabara ni sio tu kuangalia magari bali pia na kuhakikisha wale wanaoangalia usalama wa barabarani wanakuwa katika mazingira mazuri.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwajengea askari hawa wa barabarani vibanda ili wajihifadhi wakati wa mvua badala ya kuwa wanakaa chini ya miti na sio hivyo tu na watawasaidiaje hasa kina mama wale askari wanapohitaji kujisitiri?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa concern yake aliyokuwa nayo kwa askari wetu hawa wa usalama barabarani ambao wanafanya kazi zao katika mazingira magumu ambayo ameelezea. Lakini Jeshi la Polisi lina changamoto nyingi na changamoto za vituo vya kudumu na changamoto ya vituo vya dharura.
Kwa hiyo, niseme tu kwamba kadri ya hali ya uwezo wa fedha ya Jeshi la Polisi utakavyokuwa unaruhusu tutaendelea kutafuta changamoto hizi moja baada ya moja kulingana na kipaumbale.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hata hivyo kuna hatua ambazo za dharura kwa mfano tuna utaratibu wa mobile police post ambazo tumekuwa tukizitumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo kupitia mradi wa BRN ambao tumechukua case study ya Mkoa wa Kinondoni mtaona kwamba tumeyazingatia hayo mapendekezo ya Mheshimiwa Mbunge na kama nilivyosema uwezo utakaporuhusu ile case study ya kinondoni tutaitawanya au kuisambaza maeneo mengine ya nchi.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri swali moja ya nyongeza.
Kwa kuwa baadhi ya askari ambao wanaotumia mashine za kielektroniki njiani mle huwa zinawashinda kuzitumia na utaona wanahangaika nazo.
Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kuniambia elimu waliyoipata kwa askari wale ilichukua muda gani hata baadhi yao hadi leo hawajaweze kuzitumia vizuri?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ametaka kujua muda ambao elimu askari wale wamechukua basi nitafanya utafiti wa kujua muda huo halafu nitampa majibu hayo baadaye.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri kuhusu masuala ya ajali barabarani. Sasa nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, Tarafa ya Kitunda ambayo iko umbali wa kilometa 180 kutoka Makao Makuu ya Wilaya ya Sikonge ina Kituo cha Polisi kidogo ambacho kina polisi wanne ambao hawatoshi kuhudumia wakazi zaidi ya 80,000 kwenye Tarafa hiyo. Maana kuna majengo chakavu, polisi wenyewe ni wachache na hawana gari hata moja; lini Serikali itawasaidia polisi hao ili wafanye kazi yao vizuri? Hilo la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, mwezi Machi, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyahwa alichinjwa kama kuku na hadi leo wauaji wale hawajakamatwa. Ni lini Serikali itafanya kazi yake kikamilifu ili wauaji hao wakamatwe na kuondoa hofu Kijiji cha Nyahwa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Kakunda kwamba concern yake ambayo amei-raise hapa tutaifanyia kazi ya kwa maana ya kwamba tutaongeza idadi ya askari katika kituo hicho. Kwa hiyo, nachukua fursa hii kuwaelekeza Jeshi la Polisi wale askari ambao wako depot, tunaotarajia kuwa-deploy karibuni, basi tuangalie uwezekano wa kuwapeleka Sikonge kuongeza ile idadi ya askari waliopungua pale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia pale ambapo magari ambayo tunatarajia yataingia wakati wowote, nayo tuone uwezekano wa kufanya hivyo kwa kuzingatia changamoto eneo hilo baada ya kulifanyia utafiti wa kina pamoja na mahitaji ya nchi nzima.
MHE. MBONI M. MHITA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri kwamba Jimbo la Handeni Vijijini ambalo kwa upande mmoja ni barabara kubwa ya Mkata kupitia Korogwe kuja mpaka Misima; ila askari wa Jimbo la Handeni ama Wilaya nzima ya Handeni hawana usafiri wa ku-patrol, jambo ambalo naamini kama wangeweza kuwa na usafiri huo kwa namna moja ama nyingine wangeweza kupunguza idadi ya ajali ambazo zinatokea. Lakini pia, swali langu la pili…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mboni, swali la nyongeza huwa ni moja.
MHE. MBONI M. MHITA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali hili nalo vilevile tumelichukua. Tutaangalia vilevile utaratibu na hali halisi ilivyo na changamoto ya eneo la Handeni na changamoto za maeneo mengine na idadi ya magari ambayo tutayaingiza kwa awamu inayokuja. Pia tutalipa uzito kwa kutilia maanani changamoto ambazo ametueleza Mheshimiwa Mbunge.
MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. La kwanza, katika mgodi wa JPM ambao uko katika Kata ya Mpanda Hoteli ilikuwa ni sehemu ambayo imewekwa mizinga ile ya kijeshi; lakini hapo hapo katika mgodi huo wa JPM kwa sababu wengi ni wawekezaji wageni, lakini wananchi wa mahali pale wanapata shida sana. Naomba Serikali iweze kutoa tamko kwa sababu wananchi hao wananyanyaswa.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, mimi natoka Mbeya, lakini pale Mbeya sehemu ya Mbalizi kuna Jeshi la Wananchi ambao wako pale na liko jirani sana na wananchi hususan Kata ya Iwindi na Utengule, Usongwe. Sasa nina wasiwasi kwamba lisije likatokea jambo ambalo lilitokea Mbagala. Serikali inatoa tamko gani kwa wananchi hawa ambao wanaweza wakapata madhara kama ya Mbagala? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI (K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mary Mwanjelwa anazungumzia unyanyasaji aliouita unyanyasaji ambao unafanywa na Jeshi la Wananchi kwenye mgodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe hili jambo tulifanyie utafiti na tulichunguze uhalisia wake. Baada ya hapo ndiyo tutakapoweza kutoa tamko la Serikali. Sehemu ya pili, swali lake la pili kuhusiana na Mbeya ni kweli, baada ya kutokea matatizo yale ambayo yalitokea Mbagala, Serikali ilichukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kwamba inadhibiti matatizo kama yale yasijitokeze. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nichukue nafasi hii kuwahakikishia tu Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla kwamba hatutarajii matatizo kama haya yajitokeze kwa sababu Serikali imechukua hatua madhubuti. Hata hivyo, hatutalidharau jambo hili ambalo amelizungumza Mheshimiwa Mbunge nalo pia tutalichukua, tulifuatilie kwa kina tuone kama kuna kasoro tuweze kuzifanyia kazi na kuzirekebisha.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na majibu ya Naibu Waziri. Wilaya ya Busega, Itilima na Kituo cha Polisi cha Mwandoya kilichopo Jimbo la Kisesa katika Wilaya ya Meatu, Askari wa Jeshi la Polisi wanaishi katika mazingira magumu. Nikisema mazingira magumu namaanisha hata zile nyumba za wananchi ni za shida sana kupatikana kwa ajili ya kupanga. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri katika mikoa aliyopanga kutembelea yuko tayari kutembelea Mkoa wa Simiyu ili aweze kujionea namna Askari wa Jeshi la Polisi wanavyoishi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; Wilaya ya Meatu ilianzishwa mwaka 1986 na majengo hayo yalijengwa mwaka 1999, yapata sasa ni miaka 17. Majengo hayo yameanza kuchakaa na kuoza, lakini kwa mujibu wa majibu ya Naibu Waziri, nimeona hata kwenye ule mgawo wa nyumba 4,136 majengo hayo hayamo. Je, Serikali sasa haioni haja ya kukamilisha majengo hayo na kuweza kuyanusuru?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza, kwamba niko tayari kutembelea Wilaya ya Busega? Jibu, niko tayari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kwamba, katika mradi wa nyumba 4,136, Wilaya ya Busega na Itilima haimo. Ukweli ni kwamba, katika Mkoa Mpya wa Simiyu katika mradi wa nyumba 4,136 tunatarajia kujenga nyumba 150. Sasa nadhani sasa hivi kwa concern ambayo ameonesha Mheshimiwa Mbunge, tujaribu kuangalia sasa katika mgawo wa nyumba 150, tuhakikishe kwamba, zinakwenda katika Wilaya ya Busega na Itilima ili kukabiliana na changamoto kubwa ya makazi ambayo Mheshimiwa Mbunge amelizungumza na sisi tunalifahamu.
MHE. DOTO M. BITEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Kwa kuwa, matatizo yaliyoko Itilima yako vilevile Bukombe na Kituo cha Polisi cha Uyovu ambacho kinahudumia Wilaya za Bukombe, Biharamulo na Chato kiko kwenye hatari ya kuanguka wakati wowote kwa sababu jengo lile limechakaa. Je, Waziri anatuambia nini wananchi wa Bukombe juu ya Kituo hicho ambacho kina hali mbaya sana?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua kwamba, tuna changamoto kubwa sana ya vituo nchi nzima. Tuna vituo vibovu vingi tu na tuna sehemu nyingi ambazo hata vituo hamna. Takribani tunahitaji ujenzi wa vituo vipya kama 4,119 hivi kwa hesabu za haraka haraka, kwa hiyo tuna changamoto kubwa na tunafahamu kwamba kwa kutekeleza ujenzi wa vituo vyote na kukarabati vituo vyote nchi nzima kwa wakati mmoja si jambo jepesi, tutakuwa tukifanya hivyo hatua kwa hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nimezungumza katika maswali mbalimbali niliyokuwa nikijibu, kwamba tuna mpango wa kuweza kurekebisha vituo hivyo awamu kwa awamu. Kwa hiyo, niseme tu Mheshimiwa Mbunge ni kwamba kwa kuwa amesimama hapa na ame-raise hii hoja ya kituo chake, basi tutajitahidi kadri ambapo uwezo utaruhusu ili tuweze kukikarabati kituo hiki.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Vituo vya Kirando na Kabwe ni majengo ambayo Wizara ya Mambo ya Ndani ilinunua kwa wananchi wa kawaida. Ni majengo yaliyojengwa kwa tofali mbichi na hata leo akienda kuyaona hayana milango, saruji na yanabomoka na baadhi ya nyumba za uani wanazolala polisi hazina milango kabisa. Je, katika hizo nyumba 4,136 vituo vya Kirando ni miongoni mwa vituo vitakavyokarabatiwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kufanya ziara katika Wilaya ya Nkasi kuvitembelea Vituo vya Polisi Kirando na Kabwe na vituo vya Uhamiaji vya Mwambao wa Ziwa Tanganyika ambavyo viko katika hali mbaya sana, havistahili Polisi kuishi wala kufanyia kazi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa nyumba 4,136 hausiani na ukarabati wa vituo vya Kabwe na Kirando. Hata hivyo, kama nilivyozungumza katika jibu langu la msingi ni kwamba tuna program vilevile ya ujenzi wa vituo vya polisi nchi nzima. Ingawa kutokana na udharura wa vituo vya Kabwe na Kirando kwa kuwa ujenzi wa vituo na uimarishaji wa usalama katika nchi yetu unakwenda sambamba na maendeleo ya nchi hii, basi ikiwa Mheshimiwa Mbunge ataona inafaa si vibaya katika Mfuko wa Jimbo akaangalia uwezekano wa kukarabati vituo hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusiana na ziara, tutaangalia uwezekano huo. Kama ambavyo nimekuwa nikizungumza kila siku, wajibu wetu ni kuweza kufanya ziara nchi nzima katika maeneo yote kuangalia changamoto zinazokabili vyombo hivi ambavyo viko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani na Nkasi ni moja ya sehemu hizo.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo. Kwa kuwa matatizo ya Wilaya ya Nkasi yanafanana na matatizo ya Mkoa wa Tabora na kwa kuwa nyumba za Polisi na Magereza za Mkoa wa Tabora ni mbovu sana ikiwa ni pamoja na miundombinu ya vyoo. Pamoja na kipaumbele katika Mkoa wa Tabora yuko tayari twende naye kwa gharama zangu akaone hali halisi ya vyoo?
NAIBU WAZIRI WA MAMABO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nipo tayari lakini siyo kwa gharama zake. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati nzuri nilikuwa na ratiba ya kutembelea Tabora pamoja na Rukwa katika kipindi hiki kwenye ile ziara yetu pamoja na Waheshimiwa Wabunge wanaotokea huko kwenye kambi za makazi ya waliokuwa wakimbizi. Basi tutaunganisha ziara hiyo weekend moja kabla hatujaondoka Dodoma, tuwasiliane baadaye kwa ajili hiyo.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri, majibu yenye matumani makubwa katika Mkoa wetu wa Lindi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niipongeze Serikali kwa kuanzisha Mfuko huu wa UCSAF. Kwa utekelezaji wake katika Mkoa wetu wa Lindi ni kata 25 na vijiji 99 ambavyo tunavitarajia vianze kupata mawasiliano. Ningependa kujua ni kwa namna gani Serikali watapeleka msukumo kwa watoa huduma hii ya mawasiliano ili vijiji hivi 99 na kata 25 za Mkoa wa Lindi ziweze kupata mawasiliano?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa juhudi zake za kufuatilia suala hili. Alikuja ofisini na alikutana na Waziri wangu na kwa kweli pamoja na Wabunge wengine wa Mkoa wa Lindi wanalifuatilia sana suala hili ikiwa ni pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuthibitisha kwamba tutayafuatilia haya makampuni yanayotoa huduma. Kwa wale ambao hawana huduma za kutosha tutahakikisha UCSAF inaingilia ili yapatikane mawasiliano kama ambavyo tumekusudia kutoa mawasiliano kwa vijiji vyote vya Tanzania.

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema kwamba tutazifuatilia hizi kampuni kuhakikisha kwamba zinatimiza wajibu wake wa kupeleka mawasiliano katika vijiji husika vya Mkoa wa Lindi vyote 99 katika kata 25 pamoja na vijiji vyote Tanzania nzima.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuiuliza Serikali maswali mawili tu ya nyongeza. Katika mpango wa Serikali wa kujenga nyumba 4,136, nataka tu kujua: je, Wilaya yangu ya Songwe ambayo ni wilaya mpya, itajengewa nyumba ngapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika mgao huo, ni pamoja na Askari Magereza pamoja na hawa Askari Polisi wa kawaida? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika majibu ya msingi ni kwamba Mkoa mpya wa Songwe ni moja katika mikoa ambayo itafaidika na awamu ya kwanza ya ujenzi wa nyumba 4,136.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na kwamba Wilaya yake ya Songwe itahusika ama la, labda nichukue ili tuweze kulifanyia kazi, lakini ninachojua ni kwamba mkoa mzima utafaidika, kwa maana hiyo mgawanyo huu utafanyika kwa wilaya zote za mkoa mzima. Sasa kuhusiana na kiwango cha nyumba ngapi zitakwenda Wilaya ipi na ipi, takwimu hizo siwezi kumpatia kwa sasa hivi, lakini nitakapokuwa nimefanya utafiti, tutaweza kumjulisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kwamba je, katika suala hilo la ujenzi wa nyumba hizo Magereza wanahusikaje? Magereza wana mpango wao vile vile wa ujenzi wa nyumba ambao wao nyumba zao ni nyingi zaidi; zaidi ya nyumba 9,500 kama sikosei kwa ajili ya Magereza ambapo ni nyumba nyingi zaidi ya hizi za Polisi kwa nchi nzima.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nampongeza Naibu Waziri kwa majibu sahihi aliyoyatoa na pia nampongeza sana Mheshimiwa Mulugo kwa sababu amekuja mara nyingi sana ofisini kufuatilia jambo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mulugo, pamoja na mikoa yote mipya kwamba tutatoa kipaumbele kwa mikoa hiyo kwa sababu, licha ya makazi ya askari kutokuwepo, hata nyumba tu za kawaida za kupanga katika mikoa ile mipya na wilaya mpya ni kazi sana kwa Askari hao kupata tofauti na maeneo mengine. Kwa hiyo, tutalizingatia hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja la faraja la kwanza, wakati tunaendelea kujadiliana, tutalifanyia kazi kwa umakini zaidi suala la pango allowance ambayo maaskari wetu wamekuwa wakipewa, kwanza kuwaondolea usumbufu.
Pili, kutengeneza utaratibu ambao utaendana na kiwango ambacho kina-reflect bei zaidi ya soko tofauti na sasa ambapo askari anapata asilimia 15 akiwa ngazi ya chini lakini hata akipanda, kiwango kile kinaendelea kuwa kilekile licha ya mshahara wake kupanda.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Zanzibar kumekuwa na matukio ambayo yanaendeshwa na vikosi vya Janjaweed; na kama Kikosi cha Polisi mna taarifa hiyo, ni kwa nini kikosi hiki kimekuwa kikifanya matukio ya kuumiza wananchi na kuwasababishia ulemavu wa kuendelea na hata kutokujitafutia riziki kwa mahitaji yao ya kila siku?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Serikali kipindi cha uchaguzi kunakuwa na matukio mengi sana ya kupiga wananchi ambao hawana silaha na mnapambana nao na kuwaachia ulemavu wa kudumu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba majibu ya Serikali.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Maryam Msabaha anataka kujua kwamba kuna Kikundi cha Janjaweed ambacho kinapiga watu. Niseme tu kwamba kikundi cha Janjaweed mimi sikielewi. Ninachoweza kusema ni kwamba, kama Mheshimiwa Mbunge ana taarifa za kikundi chochote ambacho kinavunja sheria za nchi, basi ana wajibu wa kuhakikisha kwamba anashirikiana na nchi kufikisha taarifa hizo kwa Polisi ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na Polisi kupiga watu wakati wa uchaguzi, Polisi imefanya kazi kubwa sana kuhakikisha kwamba uchaguzi wetu unakwenda vizuri na sote ni mashahidi kwamba uchaguzi wa mwanzo na uchaguzi wa marudio Zanzibar ulikwenda kwa salama na amani na wananchi walitumia haki yao kidemokrasia vizuri kuchagua wale ambao wameamua wenyewe kuwachagua. Kwa hiyo, siyo sahihi kusema kwamba uchaguzi ulikwenda vibaya na Polisi wameshiriki katika kufanya uvunjifu wa sheria katika uchaguzi huo.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Spika, naomba niulize maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Wilaya ya Kigamboni ina askari takribani 100, magari yanayofanya kazi matatu na nyumba chache sana za askari. Je, Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ina mkakati gani wa kuongeza askari katika Wilaya mpya ya Kigamboni ili kukidhi mahitaji, hususan tukizingatia kwamba, Wilaya mpya ya Kigamboni ina changamoto kubwa sana ya uvuvi haramu, uhamiaji haramu pamoja na ongezeko la uhalifu?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, nilitaka kujua; katika majibu ya Mheshimiwa Waziri amejibu kwamba ujenzi wa kituo kipya cha Wilaya utajengwa katika Kata ya Kibada mara fedha zitakapopatikana. Je, Wizara inaweza ika-make commitment kwamba itaingiza ujenzi wa kituo kipya cha Polisi cha Wilaya katika bajeti hii inayokuja ya mwaka wa fedha 2017/2018?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kuhusiana na pendekezo la Mheshimiwa Mbunge kuhusu haja ya kuongeza idadi ya Askari Kigamboni, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali kupitia Jeshi la Polisi imeliona hilo na tunategemea pengine katika askari ambao wanaweza wakaajiriwa katika mwaka ujao wa fedha tuweze kuangalia uwezekano wa kuongeza idadi ya askari katika maeneo yote ambayo kuna upungufu wa askari ikiwemo Kigamboni.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ametaka kujua kwamba katika bajeti ya mwaka huu wa fedha kwamba fedha hizo za ujenzi wa Kituo cha Kigamboni zitaingizwa. Naomba kwanza nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mpaka sasa hivi hatua ambazo zimefikiwa ni hatua za kuridhisha kwani mbali na kupatikana eneo la ujenzi wa kituo, lakini tayari hatua za awali ikiwemo utayarishaji wa ramani kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho umeshafanyika.
Mheshimiwa Spika, ninaomba nichukue fursa hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba wazo lake tutazingatia ingawa inawezekana ikawa kwa bajeti ya mwaka huu ikawa tumechelewa, lakini tutaangalia utaratibu mwingine wa kuweza kuangalia jinsi gani ya kupiga hatua zaidi na pale ambapo tutaweza kuingiza katika bajeti ya mwaka mwingine wa fedha, tutaziingiza kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho.
MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema mnyonge mnyongeni haki yake mpeni, napenda niipongeze Serikali kwa kukubali kwamba kuna tatizo la utesaji na torture kwa sababu siku hizi kumekuwa na utaratibu na utamaduni wa kukataa na kukanusha kila kitu. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kukubali kwamba kuna tatizo la utesaji na torture. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali langu limejibiwa kwa wepesi na ujumla sana. Kwenye swali langu la msingi nili-cite kwa mfano, kinachoendelea kuhusu Mwalimu Msigwa na wenzake ambao walimfanyia torture au shambulio la kudhuru mwanafunzi wa Mbeya Sekondari ambapo mpaka leo hii wazazi wana hofu na watoto wao katika shule ile kiasi kwamba wanamsukuma Mbunge kutaka kujua ni nini hatma ya wale walimu kwa sababu maneno yamekuwa mengi. Mara wanasema amri kutoka juu imesema kwamba waachiwe na kadhalika...
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejiuliza sana na juzi nimeuliza kwenye Kamati lakini Waziri wa Elimu anasema hana habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nimeuliza kwenye Kamati wanasema chuo kimeunda tume, chuo kinafanya uchunguzi wa jinai toka lini wakati suala hili liko wazi kwenye video ilienda viral wale walimu walitesa watoto tunawatetea walimu lakini wanapovunja sheria ni lazima hatua zichukuliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka kujua ni nani aliyetoa amri kwamba wale walimu waachiwe wasichukuliwe hatua za kisheria kwa kosa la jinai walilofanya? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika Watanzania wanaowatesa wenzao ni pamoja na Polisi. Watanzania hawa Polisi, kwa mfano wakati wa Operesheni UKUTA ambayo tuliisitisha kwa maslahi ya Taifa, walikamata watu, waka-torture mfano Mtanzania Nyagali maarufu kama Mdude wa Mbozi ambaye mpaka leo hii amevunjwa miguu na hayuko sawasawa. Sasa Taifa hili limekuwa Taifa la disappearance watu wanapotea...
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nijue kwa nini isiundwe Tume ya Kimahakama kama ile aliyounda Mheshimiwa Kikwete ya kuchunguza Operesheni TOKOMEZA ili kuchunguza maovu haya yanayofanywa na Watanzania ambao wana uniform za kipolisi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la walimu ambao wamewanyanyasa wanafunzi kwenye shule ya Mbeya Day niseme ni mtambuka kwa hiyo hatua mbalimbali zinachukuliwa na mamlaka husika. Kwa upande wa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Mashtaka DPP kuna hatua ambazo zinaendelea kuchukuliwa na pale ambapo ushahidi na uchunguzi utakapokamilika watafikishwa katika vyombo vya sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ni kuhusu kuundwa Tume ya UKUTA, kwanza tulishazungumza mapema kwamba mkusanyiko wowote ambao si halali hautaruhusiwa na hivyo Jeshi la Polisi litasimamia kuhakikisha kwamba linalinda usalama wa nchi hii kwa kuzuia mikusanyiko yoyote ambayo siyo halali. Kwa hiyo, kama ikiwa Jeshi la Polisi limetekeleza majukumu yake kuzuia mkusanyiko ambao si halali limefanya hivyo katika kutekeleza majukumu ya kawaida na tunawasihi wananchi pale wanapoelekezwa kutii sheria za nchi, basi watii sheria za nchi.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami naomba niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa kumekuwa na tabia ya wananchi au vyombo vya ulinzi na usalama na wengine ambao wanakwenda kwenye mafunzo ambayo siyo halali kutesa raia wasiokuwa na hatia na kuwasababishia maumivu makali na hatimaye kupelekwa rumande bila kupatiwa huduma za kiafya. Je, Serikali hamuoni kama mnavunja haki za binadamu na utawala bora?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la Mheshimiwa Maryam Msabaha liko too general, nadhani si sahihi kusema Polisi kazi yao ni kutesa raia. Polisi wamekuwa wakifanya kazi ya kulinda raia na kazi hii imefanyika kwa mafanikio makubwa sana na ndiyo maana mpaka leo nchi yetu iko salama. Ningemwomba Mheshimiwa Maryam Msabaha kama ana tukio specific ambalo linamhusisha Polisi kwa kufanya tendo lolote ambalo limekwenda kinyume na sheria basi aliwasilishe ili hatua zichukuliwe.
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli sijaridhika kabisa na majibu ya Naibu Waziri, Jeshi la Zimamoto linafanya kazi katika mazingira magumu sana. Mfano, Mkoa wangu wa Njombe hawana ofisi, wanatumia majengo ya Idara ya Maji, hawana magari; na tukiangalia Mkoa wa Njombe kijiografia umekaa vibaya sana na matukio ya moto ni mengi.
Nilikuwa nataka kujua time frame, ni lini Serikali itatoa vifaa au vitendea kazi kwa Jeshi la Zimamoto?
Swali langu la pili, kwa kuwa huduma ya Zimamoto iko zaidi mijini, lakini matatizo ya moto yako mengi sana vijijini. Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha hata watu wa vijijini wanapata huduma hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba ambavyo nimejibu kwenye swali la msingi kwamba tuna matatizo ya ofisi pamoja na vitendea kazi nchi nzima kwa Jeshi la Zimamoto; na ukiangalia katika Wilaya zote takribani za nchi nzima kwa upande wa Tanzania Bara ni Wilaya 20 ambapo kuna Ofisi za Zimamoto mpaka sasa hivi pamoja na magari.
Hata hivyo, Serikali imefanya jitihada kubwa sana kuhakikisha kwamba tunatanua wigo ili huduma hizo ziweze kufika mpaka vijijini na ndiyo maana tuna mpango sasa hivi wa kuhakikisha kwamba tunapeleka huduma za Zimamoto katika Wilaya zote nchini hatua kwa hatua kwa kuanza kupeleka Maofisa ili waweze kutoa elimu na baadaye kadri vifaa vitakavyopatikana tutapeleka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na magari pamoja na vitendea kazi, katika bajeti ya mwaka huu tumetenga takriban shilingi bilioni 1.5 kununua magari mawili, tutaangalia ni maeneo gani ya kipaumbele tuweze kupeleka.
Naomba nichukue fursa hii kumwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutashauriana na Makao Makuu Idara ya Zimamoto tuone uharaka wa kufanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tuna mpango mwingine, tunafanya mazungumzo sasa hivi na Austria pamoja na Belgium, Kampuni ya SOMAT ya Belgium ili kuweza kupata mkopo wa Euro bilioni tano pamoja na Euro milioni 1.9 ambazo zitasaidia kuweza kununua vifaa viweze kupunguza makali ya upungufu wa vifaa katika maeneo mbalimbali nchini mwetu.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Jeshi la Polisi lina uhaba wa vitendea kazi vya kisasa kuweza kudhibiti matukio ya uhalifu; je, Serikali ina mpango gani kutoa vifaa vya kisasa zaidi kwa askari wetu waliopo katika maeneo ya mipakani?
Swali langu la pili; ili askari aweze kufanya kazi zake na kudhibiti matukio ya uhalifu kwa ufanisi ni muhimu akawa na mazingira rafiki kuanzia nyumbani.
Je, ni lini Serikali itatekeleza kwa vitendo ahadi ya kujenga makazi ya hadhi ya askari wa Jeshi la Polisi katika Wilaya zote za Mkoa wa Kagera?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa na concern ya hali ya usalama katika mpaka wa Kagera, lakini naomba tu nimthibitishie kwamba, si Jeshi la Polisi ama Serikali kupitia Jeshi la Polisi kwa kutambua umuhimu na unyeti wa maeneo ya nchi yetu yaliyoko mipakani ikiwemo Kagera huwa kwa kawaida inatoa kipaumbele katika ugawaji wa vifaa katika maeneo hayo hususan vitendea kazi ikiwemo silaha, magari na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mzuri ni kwamba, kwa Mkoa wa Kagera pekee tunahakikisha kwamba tunawapatia Askari wetu walioko mipakani silaha za kutosha lakini silaha nzito ili kuweza kukabiliana na wimbi la wahamiaji haramu ambao mara nyingi wamekuwa wakisababisha ukosefu wa amani katika mikoa yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia hakuna hata Kituo kimoja cha Polisi katika mipaka ya nchi yetu ambacho hakina gari mpaka sasa hivi tunavyozungumza. Kwa hiyo, ni kuonesha kwamba tunatoa nguvu kubwa sana na kipaumbele katika maeneo ambayo yapo mpakani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili ni kweli kuna matatizo ya makazi, sio tu Kagera lakini katika mikoa mbalimbali nchi nzima na ndiyo maana tumekuwa tukizungumza hapa kuna mipango ya Serikali ya ujenzi nyumba 4,136 ambayo mpaka sasa hivi tunasubiri approval kutoka Hazina ili mradi ule uanze kutekelezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Kagera, kuna ujenzi wa nyumba 12 ambazo tunaendelea nazo hatua kwa hatua kadri ya pesa zitakazopatikana tumalize katika eneo la Buyekera ambalo litasaidia kupunguza makali ya matatizo ya makazi kwa askari wetu.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo ni majibu ya Serikali. Lakini kwa kuzingatia kwamba Ngara ni miongoni mwa Wilaya za Mkoa wa Kagera, Wilaya inayopakana na nchi mbili, Rwanda na Burundi imekuwa ni waathirika wakubwa sana wa hali ya usalama katika eneo hilo. Sasa swali langu, je, ni lini sasa Serikali itaanzisha Kanda Maalum ya kipolisi kwa Wilaya hii ya Ngara ambayo kwa muda mrefu wamekuwa ni waathirika wa hali ya usalama? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tumekuwa tukiangalia maeneo ambayo yamekuwa na changamoto kubwa sana za kiusalama nchini mwetu na maamuzi ya kuongeza Wilaya katika maeneo hayo yanatokana na wingi wa matukio ya uhalifu. Ngara ni moja kati ya sehemu ambayo kuna matukio ya uhalifu kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema, hasa kutokana na kupakana na nchi jirani. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge atuachie hili tunalifanyia kazi na baadaye pale ambapo hatua itakapofikiwa, tutamjulisha.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwanza kabisa namshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya kuridhisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Kituo cha Polisi cha Maswa ni cha muda, kiko kwenye hifadhi ya barabara ambapo kinaweza kikabomolewa wakati wowote ili kupisha ujenzi wa barabara; je, ni lini Serikali itajenga kituo cha kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa vile tatizo lililoko Wilaya ya Maswa liko sawa kabisa na tatizo lililoko Wilaya ya Itilima, hakuna kituo cha Polisi cha Wilaya; je, ni lini Serikali itajenga kituo cha Polisi cha Wilaya ya Itilima?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Esther alitaka kujua ni lini Serikali itajenga kituo cha Polisi Itilima pamoja na Kituo cha Kudumu Maswa. Naomba nimjulishe Mheshimiwa Esther kwamba kama nilivyojibu katika swali langu la msingi ni kwamba tunatambua upungufu wa vituo 65 nchi nzima katika Wilaya 65 ikiwemo Maswa na Itilima. Kwa hiyo, pale ambapo tutafanikiwa kupata fedha za ujenzi huu tutatoa kipaumbele katika maeneo hayo kama ilivyo maeneo mengine ya Wilaya zilizobakia 65 ambazo hazina vituo vya Polisi mpaka sasa hivi.
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa Serikali inatenga fedha kwa ajili ya kuwahudumia mahabusu na kwa kuwa fedha hizo huwa hazitoshi kuwahudumia mahabusu wao. Je, Serikali ina mpango gani kwa mwaka wa fedha 2017/2018 ili kuhakikisha kwamba Askari Polisi hawatoi tena fedha mifukoni kuwahudumia mahabusu wanaowekwa ndani kenye vituo vyao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Serikali imesema ina mpango wa kujenga nyumba 4,136 kwa awamu. Je, kati ya nyumba hizo ni nyumba ngapi zitajengwa katika Wilaya ya Masasi?
swali la msingi nilionesha takwimu ambazo zinaonesha kuongezeka kwa fedha zilizotengwa kwa ajili ya mahabusu ambapo nilisema kwamba mwaka 2015/2016 tulitenga zaidi ya shilingi bilioni 1.5 na mwaka unaofuata kwa maana ya mwaka huu tulionao tumetenga zaidi ya shilingi bilioni 1.7. Hii inaonesha kwamba kadri tunavyokwenda mbele bajeti kwa ajili ya kuhudumia mahabusu inaongezeka. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba lengo la Serikali ni kuhakikisha tunaongeza bajeti kila mwaka ili kuweza kutoa huduma za mahabusu vizuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusiana na nyumba ngapi zitajengwa Masasi, migao katika ngazi ya Wilaya bado haijafanyika, lakini nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakapofanya mgao kwa ajili ya Mkoa wa Mtwara vilevile tutazingatia na Jimbo au Wilaya yake ya Masasi.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa. Niongezee tu sehemu ndogo ile ya upande wa vyakula kwa mahabusu na niunganishe pamoja na wafungwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwepo na tatizo la kibajeti lakini pamoja na tatizo hilo pia kuna tatizo la matumizi ya fursa tulizonazo za uzalishaji katika taasisi zetu za Wizara ya Mambo ya Ndani. Mpango wa muda mrefu tunaopanga ikiwa ni ziada ya majibu aliyoyatoa ya kibajeti ni namna ya kutumia fursa tulizonazo hasa hasa katika magereza yetu. Magereza yetu yana mashamba makubwa, juzi nilienda Kigoma, mkoa ambao mazao yanakubali kuliko mikoa yote kwa msimu kama huu ambao una ukame lakini kwenye shamba lile lenye ekari karibuni 10,000 walilima kama ekari 50 hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika magereza yote tukilima vizuri, tutalisha magereza, tutalisha mahabusu na tunaweza tukalisha mpaka na shule za sekondari. Kwa hiyo, mpango tulionao ni kwenda kujitegemea katika uzalishaji ili tuweze kulisha wafungwa na mahabusu. Tunamwomba ndugu yetu Mheshimiwa Dkt. Tizeba na Mheshimiwa Mwijage watusaidie tu matrekta ili tuweze kwenda kulima kisasa hata NFRA tutawauzia mazao kwa ajili ya kuisaidia Serikali.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mazingira magumu ya ukosefu wa vitendea kazi kama magari, mafuta na makazi ya askari yanayowakabili askari wa Masasi yanaakisi hali halisi ilivyo Wilayani Mpanda. Je, ni lini Serikali itafikiria kujenga makazi ya Askari Polisi Wilayani Mpanda? Katika hili nafarijika Waziri alikuwa huko na alijionea hali ilivyo ya askari wetu Wilayani Mpanda.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni sahihi anachozungumza Mheshimiwa Kapufi hasa ukitilia maanani Mkoa wa Katavi kama ilivyo mikoa mingine mipya, ina changamoto siyo tu za makazi hata ofisi za vyombo vya usalama. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba katika mgao ambao tumezungumza maeneo ambayo ni mapya kimkoa na kiwilaya yatapewa kipaumbele ikiwemo Jimbo la Mpanda Mjini.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza ifahamike kwamba Wilaya nyingi zilizopo Mkoani Ruvuma zipo mpakani, kwa mfano Wilaya ya Nyasa inapakana na Malawi, Wilaya ya Tunduru inapakana na Msumbiji. Kuwa na makazi bora ya polisi katika maeneo haya kutahamasisha polisi wetu kuishi katika makazi salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Mheshimiwa Waziri ameeleza kuna nyumba 9,500 zinategemewa kujengwa nchi nzima. Napenda kujua kati ya nyumba hizo ni ngapi zitajengwa Mkoani Ruvuma?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, pale Wilayani Tunduru kulikuwa na jengo ambalo lilikuwa linatumiwa na Askari Polisi wanapokuja kuhamia, jengo lile liliungua moto. Jengo lile lilikuwa linasaidia sana na hasa kwa askari wa kike kupata makazi pale wanapokuja kuhamia. Naomba kujua Serikali imejipangaje katika kuhakikisha jengo lile linajengwa tena ili liwasaidie askari wale?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na nyumba ngapi zinatarajiwa kujengwa Mkoa wa Ruvuma ni 320.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusiana na jengo hilo ambalo amelizungumza tunachukua concern yake tuone ni hatua gani tutachukua ili kuweza kulifanyia ukarabati ikiwezekana katika bajeti zinazofuata.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Wilaya ya Kilolo imeanza toka mwaka 2002 takribani sasa ni miaka 15, lakini kwa muda mrefu OCD amekuwa akikaa tarafa nyingine na makao makuu yako Tarafa nyingine na inabidi kuwasafirisha mahabusu kwani wako kule anakokaa OCD zaidi ya kilomita 100 kuwapeleka katika tarafa nyingine ya Kilolo. Kama Serikali yenyewe bado haijajiweka vizuri, kwa nini isitumie National Housing au NSSF kujenga nyumba pale Kilolo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo tumekuwa tukieleza kila siku na leo vilevile, mipango ya ujenzi wa nyumba upo njiani. Kwa hiyo, hakuna haja ya kufikiria kwamba labda suala la OCD wa Kilolo kutokuwa na nyumba halijatiliwa maanani. Namwomba Mheshimiwa Mbunge avute subira, pale ambapo mipangilio yetu itakapokamilika na mikataba itakapokuwa imesainiwa, basi ujenzi huo utaanza na tatizo ambalo linamkumba OCD wetu huyo wa Kilolo na Ma-OCD wengine popote nchini litakuwa limepata ufumbuzi.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na nina swali moja la nyongeza. Kwa vile hali ya kiusalama sasa Zanzibar ni shwari na naomba niendelee kuipongeza Serikali kwa hilo, je, Serikali ina mpango gani wa kuzidi kuimarisha hali hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tunashukuru Mheshimiwa Khadija Nassir kwa kuona jitihada na mafanikio makubwa ya hali ya kuimarisha usalama sio tu kwa Zanzibar lakini Tanzania nzima na tunaomba Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla waendelee kutoa ushirikiano wao kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili hali hiyo iweze kudumu. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wetu kama ambavyo nimejibu kwenye swali la msingi tutaendelea kuhakikisha kwamba hali hii inadumu kwa kuhakikisha kwamba tunaimarisha vitendea kazi na uwezo kwa maana ya uwezo wa kiutendaji wa vyombo hivi vya ulinzi tukitarajia kabisa ushirikiano kati ya wananchi na vyombo hivyo utaongezeka ili kuweza kupata taarifa za kiintelejensia kabla ya kuanza kufanya kazi za kuweza kuwakamata wahalifu ambao wamekuwa wakisumbua Taifa letu kwa kiwango fulani katika nchi yetu.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa vitendo hivi vya uhalifu vipo nchi nzima na kule Jimboni Mlalo mwezi wa nane/tisa vikundi vya ugaidi vimeua watu wawili na kuchoma mabweni ya Chuo Kikuu cha SEKOMU. Je, ni lini Serikali itaimarisha ulinzi katika maeneo ya Jimbo la Lushoto ikiwa ni pamoja na kujenga seliya kuwekea silaha katika Kituo cha Mlalo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuna kazi kubwa imefanyika ya kuweza kupambana na ujambazi katika maeneo mbalimbali ikiwemo Mkoa wa Tanga. Kimsingi nchi yetu haina ugaidi, tunasema tunavimelea vya ugaidi. Kwa hiyo, kilichofanyika Tanga na ninyi ni mashahidi katika maeneo ya Amboni na kwingineko ni kazi kubwa sana ambayo imefanyika kwa mafanikio makubwa na hakika kwamba mafanikio yale ndiyo ambayo yamesababisha mpaka sasa hivi Mkoa wa Tanga kwa ujumla wake ikiwemo Lushoto kuendelea kuwa katika hali ya usalama. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kuwa suala la uhalifu ni suala ambalo linaendelea kuwepo, tutaendelea kuhakikisha kwamba tunaimarisha kazi hiyo ifanyike zaidi na zaidi ili kutokomeza kabisa uhalifu katika maeneo ambayo yamesalia katika nchi yetu.
MHE. SALMA M. MWASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Kumekuwa na utaratibu wa vituo vya polisi vidogo (police post) hasa kwa Mkoa wa Dar es Salaam kufungwa saa kumi na mbili hii inasababisha matukio mengi ya uhalifu hasa yanatokea usiku. Je, Serikali haioni inahatarisha usalama wa wananchi hasa Mkoa wa Dar es Salaam wenye wakazi zaidi ya milioni tano?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa PGO kuna vituo vya polisi vya aina tatu; kuna Class A, Class B na Class C. Kwa hiyo, vituo vya Class C kwa kawaida havifunguliwi zaidi ya saa 12. Sasa sina hakika Mheshimiwa Mbunge kituo ambacho anakizungumzia ni kituo kiko katika class gani labda pengine baada ya hapo tuone kama kitakuwa kipo katika nje ya class ambayo inapaswa kifungwe zaidi ya hapo na kinafungwa basi tutachukua hatua tuone nini kinafanyika tufanye uchunguzi tujue tatizo ni nini. Lakini nadhani kulijibu moja kwa moja swali lako kwasababu hajaainisha kituo chenyewe ni kituo gani kwa wakati huu itakuwa ni vigumu.
MHE. KHATIBU SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuijaalia nchi yetu kuwa miongoni mwa nchi ambayo haiko katika matishio ya kigaidi. Lakini cha kusikitisha sana katika mahabusu walioko magerezani miongoni mwao ni washitakiwa wa makosa ya kigaidi. Hivi nchi isiyo na tishio la kigaidi inawezaje kuwa na mrundikano wa mahabusu wanaotokana na makosa ya kigaidi? La kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Waziri wa Vikosi vya SMZ-Zanzibar na Makamu wa Rais wa Zanzibar wamewahi kunukuliwa wakisema kwamba wamewaleta Masheikh wa Uamsho kutoka Zanzibar ili wanyee kwenye ndoo katika magereza Tanzania Bara. Hapa katika jibu imeambiwa siku 60 inatosha kutoa ushahidi na kama ushahidi haukupatikana watuhumiwa waachiwe huru. Masheikh wa Uamsho wana miaka minne sasa wako katika magereza na ushahidi umeshindwa kupatikana. (Makofi)
Nataka kujua, familia za watuhumiwa wale wanataka kujua, dunia inataka kujua, Wazanzibari wanataka kujua watuhumiwa wale wanawekwa kwa amri ya viongozi wa SMZ au wanawekwa kwa sababu wana kesi ya kujibu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu katika jibu langu la msingi kwenye jibu (b). Muda wa kisheria wa kuondoa shauri mahakamani kama upelelezi haujakamilika ni siku 60. Maswali yake mawili yote hayapingani na majibu yangu ya msingi kama ambavyo walitaka kueleweshwa Wabunge pamoja na wananchi ambao wanatusikiliza hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kimsingi ni kwamba kesi za hawa watuhumiwa zote ziko mahakamani na kwa mujibu wa sheria zetu hatupaswi kuzungumza mashauri ambayo yapo mahakamani.


WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba swali alilouliza ni swali mtambuka ambalo liko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na vilevile Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kusisitiza yafuatayo na siyo lazima upende jibu lake lakini ndiyo ukweli wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nisahihishe kauli hatarishi sana kwa kwamba Tanzania haina tishio la ugaidi. Tumeshakabiliwa na matatizo ya kigaidi, umeshalipuliwa ubalozi wa nchi kubwa sana hapa nchini na baadhi ya Watanzania wamehusika, lakini leo hii tukiona kuna usalama nchi hii tuelewe kwamba vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinafanya kazi ndiyo maana huoni hayo matukio mara kwa mara. Naomba nichukue fursa hii kuvipongeza vikosi vyetu vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri ambayo vinafanya kuzima wimbi la ugaidi nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pengine ningemuomba Mheshimiwa Haji ajijibu mwenyewe lakini naomba mimi nijibu kama Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, suala la mtuhumiwa yeyote aliyeko mahakamni ni muda gani kesi yake ataruhusiwa kuendelea kukaa mahakamani kama upelelezi haujaisha? Naibu Waziri ameeleza ni siku 60. Lakini pale ambapo upelelezi haujakamilika Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa analeta maombi mahakamani na inaweza kuongezwa hizo siku lakini siyo hivyo tu, baada ya hapo suala linakuwa chini ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DPP) ambaye kulingana na uzito wa suala lenyewe anaweza akaomba mahakama kuongeza muda na muda utaongezwa. Suala la ugaidi siyo suala dogo, ni suala ambalo upelelezi wake rahisi kwa sababu ni suala la kimtandao. Kutambua huo mtandao wa ugaidi siyo kitu rahisi tu. Usalama wa nchi hii…(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata Mheshimiwa Mbunge leo aliyeuliza swali amekuja salama hapa kwa sababu kuna vyombo vya ulinzi vinamsimamia usalama wake.
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu ya kunakili kila swali anapoulizwa majibu yake ndiyo haya haya kwa hiyo ana-copy na ku-paste. Sasa kwa taarifa yako Waziri wa Mambo ya Ndani tarehe 5 Februari, 2017 alifanya ziara katika Jimbo la Mlimba na kuona hali halisi tete ilivyokuwa kule vituo vya polisi vimebandikwa pale TAZARA kwa hiyo hali ni mbaya zaidi ya kiusalama na akatoa ahadi kwenye mkutano wa hadhara baada ya kuona hali ni tete kwamba mwaka huu sisi tutafute kiwanja na kiwanja kimeshatafutwa karibuni ekari 80 kwa matumizi ya umma na sasa tulete ili iingie kwenye bajeti, nakushangaa unajibu swali huwasiliani na Waziri wako.
Sasa je, kwa ahadi aliyotoa Waziri wako tarehe 05 Februari, 2017 Serikali sasa iko tayari kuingiza kwenye mpango wa bajeti ya mwaka 2017/2018 ili Wananchi wa Mlimba wapate kituo cha polisi?
Kwa kuwa ndani ya Jimbo la Mlimba inafanana kabisa na Jimbo ya Kilombero, katika Makao Makuu ya Wilaya Ifakara, kituo cha polisi cha Wilaya kiko kwenye kituo cha maliasili na wakati wa mvua maji yanajaa askari wanaogelea kama bata. Ni lini sasa Serikali itapeleka pesa katika Mpango wa Bajeti wa mwaka 2017/2018 kuhakikisha wanajenga kituo cha Wilaya ya Polisi Ifakara maeneo ya Kibaoni ambapo kiwanja kimeshapatikana?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka nimhakikishie Mheshimiwa Susan kwamba hakuna kupingana wala kugongana kokote kati ya mimi na Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alichokifanya ndiyo tunakifanya ndiyo msimamo wetu. Alifanya ziara Mlimba na hivi juzi tu nimerudi kufanya ziara katika mikoa minne na nataka nikupe mfano ambao nimeuona katika Mkoa wa Mbeya kwenye Jimbo la Mbeya Vijijini ambapo Mbunge wake Mheshimiwa Oran amehamasisha wananchi kuweza kutafuta kiwanja, kuchangia fedha za awali za ujenzi na tukaahidi kama ambavyo Mheshimiwa Waziri alivyokuahidi wewe kwamba tutaangalia kama ambavyo jibu langu la msingi nimejibu pale ambapo fedha zitapatikana tuweze kuingiza katika bajeti kwa ajili ya kumalizia nguvu hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi niseme tu kwamba Mheshimiwa Waziri alikuja na aliunga mkono jitihada hizo na naendelea kutoa wito tu kwa Waheshimiwa Wabunge wengine wote, wale ambao wataonakuna haja ya kufanya hivyo, kuongeza jitihada za Serikali kama ulivyotambua tuna upungufu mkubwa sana wa vituo katika nchi nzima. Wilaya, Tarafa na Kata tuna upungufu wa vituo 65 katika wilaya 65 nchi nzima. Kwa hiyo tatizo ni kubwa katika maeneo mengi nchini.
Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Susan usivunjike moyo, wewe endelea hivyo hivyo kuhamasisha wananchi, wachangishe na Mheshimiwa Waziri ahadi yake iko pale pale kwamba fedha zitakapopatikana tutachangia nguvu hizo.
MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa wananchi wa tarafa ya Chipanga Wilaya ya Bahi, kwa takribani miaka 15 iliyopita waliamua kuchanga wao wenyewe na kujenga kituo cha polisi na wakakikamilisha kwa thamani ya wakati huo shilingi milioni 40.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimehangaika sana, nimempeleka Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani wakati huo alikuwa Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha akakiona kituo akashangaa kwa nini hakifunguliwi, nikampeleka Mheshimiwa Naibu Waziri Silima wakati huo akakiona kituo akaona kwanini hakifunguliwi, lakini pia nimemuandikia sasa barua Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Mheshimiwa Naibu Waziri lakini mpaka leo kituo kile hakijafunguliwa.
Sasa nilikuwa nataka kujua hapa leo ama Serikali inatoa kauli ya kufungua kituo cha polisi kile mara moja au itoe kauli ya kutokifungua sisi na wananchi wa tarafa ya Chipanga tukifanyie kazi nyingine? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Badwel pamoja na wananchi wake kwa jitihada hizo lakini nimhakikishie kwamba hili jambo aliwahi kulizungumza mimi sikuwa na hakika na taarifa kwamba mpaka leo bado kituo hicho hakijafunguliwa. Lakini Mheshimiwa Badwel nataka nikuahidi kwamba tukitoka hapa tukae, tufuatilie tuone lini tutafungua kituo hiki ili wananchi waendelee kupata moyo na wsivunjike moyo wa maeneo mengine na Jimbo lako kwa ujumla wake.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jengo la Polisi la kituo cha Kingeja ni bovu, chakavu, linavuja na jengo hili Serikali walinyang’anya kutoka kwa hao wanaitwa Wakoloni. Kwa bahati mbaya sana wamenyang’anya kutoka kwa hawa wanaitwa wakoloni wakawa wameshindwa kueliendeleza na linahatarisha maisha ya polisi na Naibu Waziri amefika kituo cha Polisi cha Kingeja huku akiwa na ahadi lukuki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka utuambie leo Mheshimiwa Waziri, una mikakati gani ya ziada kuhakikisha kwamba kituo cha polisi cha Kingeja ambacho mlinyang’anya kwa wakoloni, jengo lile sasa hivi linapatiwa ukarabati wa hali ya juu ili polisi wale wasipate madhara yoyote? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, anachokizungumza Mheshimiwa Masoud ni sahihi, binafsi nilifanya ziara katika Jimbo hilo la Mtambile na nilikitembelea hiki kituo, kwa kweli hiki kituo kiko katika hali mbaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nataka nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba hatujakaa kimya wala hatujadharau. Tunatambua changamoto kubwa ya ubovu wa kile kituo kama ambavyo vituo vingine vingi katika nchi yetu na kama ambavyo nimezungumza mwanzo kwamba pale ambapo tutapata fedha za ujenzi na ukarabati wa vituo hivyo tutafanya hivyo haraka sana.
MHE. SABREENA H.SUNGURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini bado kuna mambo ya msingi ambayo yanapelekea ajali za barabarani kuendelea kutokea ambayo hayajakuwa mentioned katika majibu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hususani njia inayoelekea Kigoma, kuanzia Itigi kwenda Tabora mpaka Kigoma, tumekuwa na railway cross nyingi sana katika eneo hilo, lakini nyingi katika hizo hazijawekewa alama kiasi kwamba msafiri anapokuwa anaendesha ama madereva wanapokuwa wanaendesha wanashindwa kutambua. Ni kwa mita chache sana alama hizo zipo na maeneo mengine alama hizo hakuna kabisa, kitu ambacho kinaweza kikapelekea sasa magari yetu na treni zije zisababishe ajali kubwa hapo baadaye. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba wana-fix vibao vinavyoonesha railway cross barabarani katika njia hiyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa kumekuwa na shida kubwa sana hasa ya wafugaji, hususani wafugaji wa ng’ombe, hufuga maeneo ambayo ni pembezoni mwa barabara na wakati mwingine ng’ombe wale hupelekea ajili zisizokuwa za msingi na kwa kuwa kumekuwa na tendence ya traffic hasa katibu miji mikubwa kama Mwanza, Dar es Salaam, Dodoma na kadhalika, hususani Dar es Salaam ambapo taa za barabarani zinafanya kazi, hapo hapo na traffic wanafanya kazi, kitu ambacho kinapelekea ku-confuse madereva barabarani na kuweza kusababisha ajali.
Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya mambo haya mawili?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tumekuwa tukikabiliana na changamoto za kukosekana katika baadhi ya maeneo alama za barabarani zinazotakiwa kuelekeza madereva kuona maeneo ambayo ni hatarishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kulitambua hilo ndiyo maana katika jibu langu la msingi nilieleza kati ya mikakati 14 moja katika eneo tulilokuwa tulifanyia kazi ni eneo hilo na kwamba tumejaribu kwa kiasi kikubwa sana kuweza kuwasiliana na kufanya kazi kwa karibu na mamlaka husika ili kuweza kudhibiti na kuweka hizo alama ambazo anasema kuwa zimekosekama. Bahati nzuri Makamu Mwenyekiti wa Baraza letu la Usalama Barabani ni Mheshimiwa Naibu Waziri wa Uchukuzi, kwa hiyo tumelifanya hili kwa ufanisi mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo kubwa ambalo linasababisha alama hizi kupotea. Mara nyingi ni kutokana na tabia mbaya za baadhi ya wananchi ambao wamekuwa waking’oa kwa makusudi alama za barabarani na kuvitumia vyuma hivi kama vyumba chakavu. Naomba nitoe wito kwa wananchi kuacha tabia hiyo na kwamba mamlaka husika ziko macho kwa wale wote ambao watakiuka sheria za nchi, kwa kung’oa vibao vya alama hizi tutawachukulia hatua za kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili lilikuwa linahusiana na askari wa barabarani pamoja na taa za barabarani. Mara nyingi askari wa barabarani wanakaa wakati ambao kuna msongamano wa magari barabarani, hasa wakati wa asubuhi wakati watu wanakwenda kazini na wakati wa jioni wanapokuwa watoka kazini. Hii ni kwa sababu taa za barabarani zilipowekwa haziwezi kukidhi mahitaji ya nyakati husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo kuna wakati ambao kuna msafara mwingi unatokea katika upande mmoja, kwa hiyo kutegemea taa za barabarani peke yake kunaweza kusababisha msongamano mkubwa. Kwa maana hiyo hao traffic police wanakaa pale kwa lengo la kudhibiti na kuzuia msongamano huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaendelea kuhakikisha kwamba askari hao wanaendelea kutumika kusaidia kupunguza msongamano wa magari hasa katika nyakati hizo za watu ambao wanakwenda kazini na kurudi kazini asubuhi na jioni.
MHE. RICHARD P.MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nina swali dogo kuhusiana na makazi ya Katumba, yaliyokuwa makazi ya wakimbizi. Makazi haya ya Katumba yana barabara takribani nne ambazo zinaingia kwenye eneo hilo. Tuna barabara kuu ya kijiji cha Msaginya ambako kuna geti ambalo limekuwa ni usumbufu mkubwa kwa wananchi wa Katumba hususani kuanzia saa 12.00 jioni kutokana na sheria za wakimbizi. Sasa kwa kuwa wananchi wa eneo hilo takribani asilimia 90 wameshapewa uraia na wengine hawaishi ndani ya eneo hilo.
Je, Serikali haioni sasa ni muda muafaka kwa lile geti la Msaginya kuendolewa au muda kuongezwa hata ikawa saa 24?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake tumelichukua na tutalitafakari tuone jinsi gani tutalifanyia kazi.
MHE. OTHMAN OMAR HAJI:Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza madogo tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya tarehe 20 Machi, 2016 ambapo vyombo vya dola vilikamilisha kusimamia zoezi la uchaguzi wa Zanzibar, ambao uliiweka madarakani Serikali
haramu inaongozwa na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein jambo ambalo wakati huo palitokea tuhuma dhidi ya wafuasi wa CUF kwamba wanapita wakiharibu mali za wafuasi wa CCM, shutuma ambazo ziliwapelekea wafuasi wa CUF kukamatwa, kupigwa, kuwekwa mahabusu……
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na matokeo hayo ambayo yalitokea katika Kisiwa cha Pemba, katika Kisiwa cha Unguja maeneo ya Tumbatu kulitokea nyumba za wafuasi……
Mheshimiwa Naibu Spika, najenga hoja.
Nyumba za wafuasi wa CUF kuchomwa moto na wafuasi wa CCM, kwa kuthibitisha majibu ya Mheshimiwa Waziri Je, kwa nini wafuasi hawa walioshutumia na CUF katika Kisiwa cha Tumbatu, kwa nini mpaka leo hawajakamatwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, inapotokea Wapinzani wanataka kufanya mikutano, Jeshi la Polisi wanasema wana taarifa za kiintelijensia kwamba hakuna usalama. CCM wanapofanya mikutano yao, Jeshi la Polisi linakusanyika pote ili kulinda mikutano hiyo. Je, kwa nini Jeshi la Polisi linailinda mikutano ya CCM lakini pale ambapo Upinzani wanafanya mikutano hawataki kuilinda?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nataka nimthibitishie pamoja na Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein ni halali ambayo imechaguliwa na wananchi kupitia Uchaguzi Mkuu halali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kauli kama hizi katika Bunge lako Tukufu ambazo zinapotosha umma siyo tu kupotosha na kudhalilisha Serikali halali na maamuzi sahihi ya wananchi ziendelee kupingwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili anauliza swali kwamba baada ya uchaguzi kuna wafuasi wa CUF ambao walishutumiwa kwa tuhuma mbalimbali ambao walikamatwa na akatolea mfano wa Kisiwa cha Tumbatu kuna wafuasi ambao hawakuchukuliwa hatua nadhani alikusudia wa vyama vingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya Uchaguzi Mkuu baadhi ya Vyama vya Upinzani ikiwemo chama chake, viongozi walijitokeza kuhamasisha wananchi kufanya mambo ambayo yanakiuka sheria za nchi yetu. Kuna matukio mbalimbali ambayo yamejitokeza ikiwemo kuchomwa moto kwa nyumba, kuchomwa mashamba, kurusha mabomu ikiwemo nyumba ya Kamishna Mkuu wa Polisi wa Zanzibar ambayo kwa uchunguzi uliofanyika mpaka sasa hivi tunavyozungumza watu ambao wamekamatwa kuhusika na urushaji bomu katika nyumba ya Kamishna ni Viongozi Waandamizi wa Chama cha CUF. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Polisi imeshakamilisha uchunguzi wake na suala lipo kwa DPP na linahitajika kupelekwa Mahakamani ili hatua za kisheria zichukuliwe. Kwa hiyo, nataka kusema kwamba, watu hawa ambao wamefanya matukio ya ukiukwaji wa sheria wapo wengi, mpaka sasa hivi zaidi ya watu 24 wameshapelekwa katika vyombo vya sheria na wengine wapo katika hatua mbalimbali za uchunguzi. Kwa hiyo, siyo sahihi kwamba Jeshi la Polisi linafumbia macho uvunjifu wa sheria. Iwe Tumbaktu, Pemba, Unguja ama sehemu yoyote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yeyote ambaye anakiuka sheria za nchi atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ni kuhusiana na hoja ya kwamba mikutano ya CCM inaruhusiwa na Polisi lakini mikutano ya CUF hairuhusiwi. Naomba nikuthibitishie pamoja na Wabunge na wananchi wote kwa ujumla, kwamba hakuna ubaguzi kama nilivyojibu katika swali langu la msingi katika kuhakikisha kwamba Jeshi la Polisi linafanya kazi yake kwa mujibu wa sheria, halibagui chama cha siasa. Tunapozungumza sasa hivi mikutano ya hadhara imezuiliwa kwa vyama vyote ikiwemo Chama cha Mapinduzi. Hakuna sehemu yoyote ambayo Chama cha Mapinduzi kinaruhusu mikutano ya hadhara zaidi ya Waheshimiwa Wabunge waliochaguliwa katika Majimbo yao. Mikutano ya ndani inaruhusiwa kwa vyama vyote na haijawahi kuzuiliwa kwa chama chochote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Mbunge kama ana uthibitisho wa mikutano halali ya chama chake ambayo imezuiliwa basi atuletee taarifa ili tufuatilie tuweze kuchukua hatua stahiki.
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mara nyingi Jeshi la Polisi linapohitajika kuwahi kwenye matukio ya kuwalinda raia na mali zao wanapata shida sana ya kuwahi kwenye matukio hayo kutokana na matatizo waliyonayo kwenye magari yao, magari mengi yanakosa matairi, mafuta na ni mabovu, tatizo hilo ni karibia nchi nzima lakini nazungumzia katika Mkoa wangu wa Manyara. Je, Serikali ina mpango gani mahsusi kabisa wa kuhakikisha kwamba magari ya Jeshi la Polisi yanakuwa na vifaa hivyo muhimu ili kuhakikisha kwamba ulinzi wa raia na mali zao unakuwa wa uhakika?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiri kwamba tuna changamoto ya upungufu wa vitendea kazi kwa ujumla katika Jeshi letu la Polisi na hii inatokana na ufinyu wa bajeti tulionao. Tutajitahidi katika bajeti ya mwaka huu kuongeza fedha kwa ajili ya matumizi kwa Jeshi la Polisi ili tuweze kukidhi mahitaji hayo, siyo tu kwa Mkoa wa Manyara pia kwa nchi nzima kwa ujumla wake.
MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi hii. Juzi hapa tumetoka kwenye Uchaguzi Mdogo Ifakara tarehe 23 ambapo kwanza Mwandishi wa Mwananchi Juma Mtanda alitekwa na wanachama na wafuasi wa CCM, wakampora iPad, simu na Kamera, akaenda Polisi akalalamika. Matokeo yake Polisi wakawatafuta watu wa CCM na wakamrudishia. Maana yake ni kwamba Polisi wanawajua wanaofanya uhalifu huu, mpaka leo hakuna ambacho kimefanyika, hakuna kesi wala chochote, hiyo ni moja. (Makofi)
Pili, kwenye uchaguzi ule kuna Askari WP Huruma alipigwa na jiwe na tofali akapasuka, ameshonwa nyuzi tano na amepigwa na wanachama wa CCM, lakini Polisi wanamuachia anatembea, anafanya chochote taarifa ipo. Namwomba Mheshimiwa Waziri anaiambie kama CCM wanaruhusiwa kufanya vurugu mpaka kujeruhi Askari wetu halafu wakaachiwa huru?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Lijualikali anazungumzia tuhuma za wanachama wa CCM kuwajeruhi Askari Polisi, pia kupora Waandishi wa Habari. Kwanza kabisa nashindwa kulijibu swali hili moja kwa moja kwa sababu unapozungumzia tuhuma kwamba hawa ni wafuasi wa chama fulani inahitaji uthibitisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoweza kusema…

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa
Naibu Spika, ninachoweza kusema ni kwamba uhalifu wa aina yoyote utakaofanywa na mtu yoyote wa chama chochote, dhidi ya raia yoyote ikiwemo Waandishi wa Habari na Jeshi la Polisi ndiyo kabisa. Jeshi la Polisi liko hapa kwa ajili ya kulinda usalama wetu, hatutakubali kamwe mtu yeyote acheze na Jeshi la Polisi na siyo tu Jeshi la Polisi hata Waandishi wa Habari wamekuwa wakifanya kazi vizuri sana ya kuelimisha jamii na kutoa taarifa nzuri kwa umma. Hatuwezi kukubali Waandishi wa Habari au Jeshi la Polisi kufanyiwa matukio yoyote ya kihalifu na raia mwingine yeyote, tutachukua hatua kali za kisheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Mbunge kama ana ushahidi wa hilo jambo alete, lakini siwezi nikasema hapa kwamba chama fulani kimefanya jambo fulani bila uthibitisho.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali fupi la nyongeza. Kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji ningeomba Mheshimiwa Naibu Waziri aniambie sawa na jibu lake la msingi ya kwamba kazi mojawapo ya Polisi ni ulinzi wa raia na mali zao. Je, Serikali inawahakikishiaje wananchi wa Wilaya hii ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji juu ya usalama wao na wa mali zao kipindi hiki cha operesheni ya kutafuta wahalifu ili waweze kufanya kazi zao kwa uhuru bila ya kubigudhiwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Mkuranga, Kibiti na Rufiji kama ambavyo kila mmoja anafahamu kwamba limekuwa na changamoto ya matukio mbalimbali ya uvunjifu wa amani ambapo mpaka sasa hivi kuna raia wengi wamepoteza maisha, pia mnakumbuka hivi karibuni Askari wetu takribani nane walipoteza maisha kwa mpigo. Mimi binafsi nilifanya ziara katika maeneo hayo ambayo nimeyazungumza na kufanya mkutano wa hadhara na wananchi. Katika mambo ambayo tumeyazungumza alifanya ziara Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi; kuna mambo makubwa matatu ambayo tumeyasisitiza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, tumeendelea kuwasisitiza wananchi kulisaidia Jeshi la Polisi kutoa taarifa juu ya matukio ya uhalifu na wahalifu ambao wanawashuku katika maeneo yao ili kazi ya Jeshi la Polisi iweze kuwa rahisi. Pili, tumeendelea kuwahakikishia wananchi wa Mkoa huo kwamba Serikali itafanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba kwamba amani na usalama wa wananchi wa maeneo hayo linakuwa ni jambo la kipaumbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kufanya hivyo ni lazima Jeshi la Polisi liwe karibu na wananchi vilevile, wananchi wawe karibu na Jeshi la Polisi na Jeshi la Polisi liwe karibu na wananchi, kwa maana ya kujenga mahusiano mazuri kati ya pande hizi mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kukiomba kwa Mheshimiwa Mbunge akiwa Mwakilishi wa wananchi wa Jimbo la Mkuranga pamoja na Wabunge wengine wa maeneo yale, kuhakikisha kwamba wanaendelea kuwaelimisha wananchi waendelee kuwa karibu na Jeshi la Polisi, kuwasaidia kupata taarifa mbalimbali za uhalifu wakati huu ambapo Jeshi la Polisi na Serikali kwa ujumla inafanya jitihada kuhakikisha kwamba maisha ya wananchi wa maeneo hayo yanalindwa pamoja na mali zao, pamoja na maisha, usalama wa Askari wenyewe ambao wanalinda usalama huo wa raia.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nasikitika kwamba Wizara ya Mambo ya Ndani leo hii inaita kwamba ni Wilaya ya Tarime/Rorya haijui kwamba ni Mkoa wa Kipolisi wa Tarime/Rorya.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya masikitiko yangu, nipende kumwambia Naibu Waziri kwamba tayari tuna miuondombinu kwa maana ya mtandao wa TRA pale, tayari wananchi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wamejenga hilo jengo na tuna rasilimali watu. Sasa nataka kujua ni lini sasa baada ya kutambua kwamba Tarime/Rorya ni Mkoa wa Kipolisi na hivyo ni Makao Makuu ya Mkoa wa Kipolisi, ni lini mtakuja kufunga huo mtambo ili kupunguza adha ya wananchi kwenda kwenye Mkoa wa Polisi wa Mara kutafuta huduma? (Makofi)
Swali la pili ni kuhusiana na kujenga ofisi ya Mkoa wa Polisi Tarime/Rorya ambao Mheshimiwa Waziri amesema ni mkoa mpya. Mkoa wa Polisi Tarime/Rorya ni wa siku nyingi ukilinganisha na Katavi, Simiyu na Geita. Kwa mikakati yenu ya ndani ningependa kujua ni lini mtakuja kujenga jengo zuri lenye hadhi ya Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya ili kuondokana na kukaa kwenye magodauni ambayo wanakaa sasa hivi na kushusha hadhi ya Kipolisi Mkoa wa Tarime/Rorya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka nirudie majibu yangu ya msingi ambayo nimejibu kwamba, changamoto kubwa ambayo inakabili kutokukamilisha ujenzi wa vituo vya Polisi na miundombinu mingine ikiwemo hii miundombinu ya utoaji wa leseni ni ufinyu wa kibajeti. Azma ya Serikali ni kuhakikisha kwamba mikoa na wilaya zote nchini zinapata huduma hizo muhimu. Changamoto nyingine kubwa ambayo nimeizungumza ni katika mikoa ile mipya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nichukue fursa hii kumhamasisha Mheshimiwa Mbunge, nimefanya ziara katika maeneo mbalimbali ikiwemo hii mikoa mipya na nimeona jitihada mbalimbali ambazo viongozi wa maeneo hayo wamekuwa wakifanya ili kuhamasisha wananchi, pamoja na sisi tupo tayari kuweza kuwasaidia nguvu kazi kupitia Jeshi la Magereza kuanza mchakato wa ujenzi wa vituo vya kisasa kwa mikoa mipya hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati hayo yakiendelea tutaendelea kuhakikisha kwamba tunajitahidi itakavyowezekana kadri ya bajeti itakavyoruhusu kwa upande wetu kujenga vituo hivyo vya Polisi, wakati huo huo kuzungumza na mamlaka ya TRA kuhakikisha kwamba huduma za utoaji leseni zinapatikana katika mikoa na wilaya zote nchini Tanzania, ikiwemo sehemu ambayo Mheshimiwa Mbunge anatoka.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona. Kuna changamoto kubwa sana ya vijana wa Lushoto hasa wa bodaboda kupata leseni; Je, ni lini Serikali itaipandisha hadhi Wilaya ya Kipolisi Lushoto ili vijana wa Lushoto waweze kupata leseni bila kutumia gharama kubwa za kwenda hadi mkoani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, ili Wilaya iweze kupandishwa hadhi, iwe Kanda Maalum ama Mkoa wa Kipolisi kuna utaratibu ambao unatakiwa ufuatwe kabla ya kutoa maamuzi. Naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Lushoto siyo katika maeneo ambayo mpaka sasa tumeweza kupata maombi rasmi ya mchakato wa kuongeza hadhi ya Kipolisi, ikiwa kuna vigezo vinakidhi basi Mheshimiwa Mbunge kwa kushirikiana na Viongozi wa Jeshi la Polisi katika eneo lake waanze mchakato huo ili tuweze kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa taratibu zilizopo.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa, kumekuwa na vijana wengi sana wa bodaboda nchini maeneo mbalimbali wamejiajiri kwa kubeba abiria, lakini bodaboda hao wengi hawana leseni. Je, Serikali ipo tayari kuwasaidia bodaboda kuwapatia leseni, kwa kuwa wengi walikuwa wanajihusisha na matukio ambayo siyo mazuri sasa wameamua kujiajiri. Sasa Serikali ipo tayari kuwapatia leseni bodaboda ili kuwasaidia?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa kuendesha bodaboda au chombo chochote cha usafiri bila leseni ni uvunjifu wa sheria. Hatutakuwa tayari kuendelea kulea uvunjifu wa sheria. Hatuwezi kuwapa leseni watu kwa kisingizio kwamba walikuwa wanaendesha bila leseni kuhalalisha uvunjifu wa sheria.
Tunachokisisitiza hapa ni kwamba Mheshimiwa Mbunge uendelee kuhamasisha wananchi wote kufuata sheria ikiwemo hao vijana ambao wanaendesha bodaboda bila leseni. Wafuate utaratibu wa kupata leseni kwa kufanya test ili waweze kupata leseni kisheria, siyo kupata leseni kwa sababu wamekiuka sheria. Sisi tutawachukulia hatua za kisheria wale wote ambao tutawabaini kwamba wanaendesha gari na pikipiki kinyume na sheria. Tunaomba ili sheria isiweze kuwakumba basi wafuate sheria kwanza.
MHE. HALIMA ALI MOHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu ambayo hayaridhishi aliyotoa Mheshimiwa Naibu Waziri naomba sasa ni muulize maswali mawili ya nyongeza:
Kwa kuwa, wanawake wanaposafiri na kupitia bandarini kwenda Zanzibar au kutoka Zanzibar kuja Dar es Salaam wanavuliwa nikabu kuanzia katika geti la bandari, na kwa kuwa wanawake hawa wanapata manyanyaso na lugha za kejeli.
Je, ni muulize Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari sasa kupokea ushahidi?
Swali la pili, wapo wanaume wanaovaa mavazi na wakajipamba kujifananisha na wanawake, je, Serikali ina mpango gani wa kuwachukulia hatua wanaume hawa?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimezungumza katika jibu langu la msingi kwamba kama kuna matukio yoyote ambayo yameonekana kukiuka sheria za nchi ikiwemo hilo ambalo amelizungumza, kama ushahidi upo aulete tutaufanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ingawa nikiri kwamba kuna baadhi ya maeneo kwa mfano, tulifanya ziara katika bandari ya Zanzibar tuliona utaratibu ambao unatumika katika kuwakagua abiria siyo mzuri na bahati nzuri tulikuwa na Naibu Waziri wa Miundombinu wa Zanzibar, hilo tumelizungumza na Serikali italifanyia kazi karibuni utaratibu ule utabadilika.Hata hivyo binafsi sikushuhudia wala kutokea malalamiko yoyote juu ya yale ambayo ameyazungumza Mheshimiwa Mbunge, lakini kama yapo na ushahidi upo basi tutafanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la pili kwamba kuna wanaume wanavaa mavazi ya kike na wanawake wanavaa mavazi ya kiume. Tafsiri ya mavazi ya kiume na ya kike nayo ni tafsiri pana maana suruali ni vazi la kiume sijui tuliite la kike, mwanamke anavaa na mwanaume anavaa. Kwa hiyo, sidhani kama kuna tafsiri sahihi ya kusema hili ni vazi la kiume na ipi ni ya kike ili Serikali iingilie katika uhuru wa wananchi kuamua jinsi gani wanataka kuvaa ni uhuru wao Kikatiba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naona swali lake hili linahitaji kwenda ndani kidogo, limekosa ufafanuzi kwa hiyo linakosa majibu ya wazi ya moja kwa moja. (Kicheko)
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Kwa kuwa Serikali imetambua urefu mkubwa uliopo kutoka Ofisi ya Uhamiaji ilipo mpaka Wenje, Makande na Kazamoyo; na kwa kuwa wananchi hawa wa maeneo haya hawana uwezo mkubwa wa kuweza kufuata huduma hii ya uhamiaji zaidi ya kilometa 90 ziliko ofisi; na kwa kuwa Serikali inakosa mapato kutokana na tozo zinazotolewa kwenye hati hizi ya kusafiria; je, kwa nini Serikali haioni umuhimu kwa sasa wa kuweza kutoa huduma hii kwa njia ya mobile ili wananchi hawa waweze kupata huduma hii kwa haraka?
Swali la pili, katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru
Ofisi ya Uhamiaji ina gari ambalo kwa muda mrefu ni bovu halina huduma yoyote katika maeno yote yaliyopo. Je, Serikali ni lini itatoa gari kwa ajili ya kurahisisha huduma hii ili wananchi wale wahudumiwe kwa urahisi zaidi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kukosa mapato Serikali si hoja ya kukosekana kituo karibu na mpaka. Kwa sababu kwa mujibu wa Sheria ya Uhamiji namba 54 pamoja na Kanuni zake mwaka 2015, inaeleza kabisa kwamba ili mtu aweze kuvuka kutoka nchi yetu na kwenda nchi nyingine anahitaji kuwa na nyaraka za aina tatu.
Nyaraka hizo aidha ni passport ama hati ya dharula ya kusafiria ama kibali maalum. Kwa hiyo, kwa mwananchi yoyote anahitaji kuvuka lazima apitie katika njia hizo whether ofisi ipo katika mpaka, ofisi ipo katika Wilaya ama ofisi iko katika Mkoa, kwa hiyo hiyo naona ni hoja ambayo siyo sahihi, ninaomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kuwasisitiza wananchi wake juu ya umuhimu wa kuweza kutii sheria za nchi yetu ili kuepusha uvukaji wa mipaka kiholela na kuikosesha Serikali mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusiana na gari, hili naomba Mheshimiwa Mbunge atuachie tulichukue, kwa sasa hivi hatuna gari za kutosha kwa Uhamiaji, pale ambapo gari zitapatikana tutaangalia na changamoto zingine za maeneo mengine na vipaumbele vilivyopo ili tuzingatie na kuchukua hatua stahiki.
MHE. HAJI KHATIB KAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumejengeka dhana ya askari wa KMKM kule Zanzibar kujiona wao peke yao ndio wenye haki ya kufanya doria baharini, jambo ambalo hupelekea askari hawa ambao ni askari Marine ambao wamepata mafunzo maalum kujiona wametelekezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri atakubaliana na mimi kwamba sasa ni wakati muafaka wa askari wa Police Marine - Pemba kupata boti ili aweze kufanya doria ya haraka ambayo itaweza kuokoa usalama kwa Pemba lakini kwa Watanzania kwa jumla? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wananchi wa Jimbo langu la Micheweni, raia wema na raia wenye kupenda amani idumu nchi hii wamewahi kushika boti za Kisomali zaidi ya mara mbili; na boti hizi zinapofanyiwa upekuzi zimegundulika na maganda ya risasi.
Je, kwa kuwa askari wa Marine Pemba wanasema kila mwezi hutolewa mafuta lita 500 kwa ajili ya doria baharini, utakubaliana na mimi sasa kwamba ni vema Police Marine - Pemba kuwa na boti ya doria ili kuweza kuimarisha ulinzi wa baharini, lakini pia kuweza kunusuru usalama wa nchi hii na raia?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge juu ya umuhimu wa Police Marine - Pemba Micheweni kuwa na boti yake. Ndiyo maana katika jibu langu la msingi nilizungumza kwamba azma ya Serikali ni kuhakikisha kwamba Wilaya zote ambazo zinapaswa kuwa na boti, polisi wanapatiwa kadri hali ya kibajeti itakavyoruhusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hiyo ndiyo azma ya Serikali na pale ambapo bajeti itakapokuwa inaruhusu, tutafanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na askari wa KMKM, Jeshi la Polisi kutokana na kutokuwa na vifaa vya kutosha ikiwemo uchache wa boti zilizomo katika maeneo mballimbali nchini, hufanya kazi kwa ushirikiano na vyombo vingine vya usalama nchini ikiwemo Kikosi cha KMKM.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme Mheshimiwa Mbunge ana bahati kwamba katika Wilaya yake ajue kwamba Jeshi la Polisi limekosa boti kwa wakati huu, lakini zipo boti za KMKM ambazo zinasaidiana na Jeshi la Polisi kufanya kazi kwa pamoja kusimamia ulinzi katika upande wa bahari.
MHE. DKT. SULEIMAN ALLY YUSSUF: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ajali za baharini zimekuwa nyingi sana siku hizi na kadhalika majanga ya baharini (disasters) naiuliza Serikali: Je, imejipangaje kwa kujenga vituo karibu na bahari na pia kutumia sayansi ya kileo, yaani kutumia kama drowns ili kuweza kubaini haraka sehemu zilizofikwa na mabalaa na kuweza kutoa huduma ya mwanzo haraka sana? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimthibitishie pia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua umuhimu wa kuimarisha usalama katika maeneo ya bahari hasa pale ajali zinapotokea. Ndiyo maana kwa kulitambua hilo, Serikali imeamua kuunda kikosi kazi cha coast guard ambapo Jeshi la Polisi ni taasisi mojawapo ambayo imo katika kikasi hicho. Kwa pamoja na mambo mengine, kikosi hicho kinaangalia masuala yote yanayohusu uokoaji pale majanga yanapotokea ikiwemo upatikanaji wa vifaa vya kisasa kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amezungumza.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa Wilaya ya Mafia imezungukwa na bahari na hakuna Police Marine na kuna matishio ya Maharamia wa Kisomali. Je, ni lini sasa Serikali itafikiria uwezekano wa kuleta doria ya Police Marine katika Kisiwa cha Mafia? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Mafia ni kati ya maeneo ambayo tumeyawekea kipaumbele katika kuimarisha usalama katika maeneo ya bahari. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunalitambua hilo; na pale ambapo hali ya bajeti itakaporuhusu, tutalifanyia kazi.(Makofi)
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali moja dogo la nyongeza. Gereza la Kondoa linahudumia Wilaya ya Chemba na Wilaya ya Kondoa. Gereza hili limejengwa mwaka 1919, lina hali mbaya sana.
Je, Serikali haioni ipo haja sasa pengine hata Waziri aende tu aone pale kama kweli hawa wafungwa bado ni binadamu, lakini wanaishi kwenye mazingira mabaya sana. Askari wana hali mbaya sana, hata Mkuu wa Gereza anatembea na boda boda. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari hata kwenda tu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na mwaliko wa Mheshimiwa Juma Nkamia na mara kwa mara amekuwa mstari wa mbele kuunga mkono jitihada na mahitaji yanayotakiwa katika Wizara ya Mambo ya Ndani ikiwepo nyumba za Polisi, nyumba za Askari Magereza, Zimamoto pamoja na Uhamiaji. Kwa hiyo, sina tatizo na kwenda Wilayani kwake pamoja na Wilaya jirani ya kondoa ili kuweza kujiridhisha na mazingira hayo ili kuweza kuweka utekelezaji mzuri zaidi wa ujenzi wa gereza ili wafungwa pamoja na askari waweze kufanya kazi katika mazingira ya usalama zaidi. Nitafanya hivyo baada ya bajeti yetu kuwa imepita.
MHE. RAISA ABDALLAH MUSSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kawaida wafungwa wanawake au kisheria wanatakiwa walindwe au wasimamiwe na askari magereza wanawake na tunaamini kwamba magereza wale ambao wamefungwa kule wako katika mikono salama. Inakuwaje akina mama wale wanapata ujauzito wakiwa katika magereza? (Makofi)
Swali la pili ni kwamba, je, Waziri haoni kwamba iko haja ya akina mama hawa kupewa vifungo vya nje ili kutoa haki kwa watoto wale wasiwemo ndani ya magereza kama walivyo mama zao? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa mujibu wa utaratibu na ndivyo hali ilivyo kwamba wafungwa wanawake wanasimamiwa na askari magereza wa kike. Sasa hoja kwamba wafungwa wale wanapata mimba wakiwa gerezani hiyo inahitaji uthibitisho, kwa sababu katika hali ya kawaida huwezi kujua mimba ile ameipata vipi. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kimsingi mazingira hayaruhusu hali hiyo kutokea katika Magereza. Kwa hiyo, ni dhahiri kabisa kwamba inawezekana pengine waliingia pale hali ya kuwa walikuwa na mimba changa. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusiana na vifungo vya nje kwa akina mama hawa. Tunao utaratibu ambao haubagui jinsia ya kuweza kuwapatia vifungo vya nje kwa mujibu wa taratibu. Tuna utaratibu wa huduma za jamii, tuna utaratibu vilevile wa msamaha na wanawake wanafaidika katika taratibu zote mbili. Kwa hiyo, utaratibu huo upo lakini inategemea na makosa. Kwa wanawake ambao makosa yao hayakidhi vigezo vya kuweza kupata fursa hiyo wataendelea kutumikia vifungo vyao kwa mujibu wa sheria za nchi yetu. (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naona Waheshimiwa Wabunge wamesimama wengi sana.
Waheshimiwa Wabunge, nimezunguka takriban Magereza ya Mikoa yote na katika zunguka ile hakuna eneo hata moja ambako nimefika nikaelezewa kwamba mama ama mwanamke aliyekuwa amefungwa kifungo cha muda mrefu amegundulika amepata mtoto akiwa katika kifungo cha muda mrefu. Ni kweli unaweza ukakuta wale waliokuwa wana vifungo vya muda mfupi wakajifungua wakiwa gerezani, lakini kujifungua wakiwa gerezani haina maana kwamba mimba kaipatia gerezani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge niwaambie tu vyombo vyetu hivi ni vyombo vinavyofanya kazi kwa sheria kali sana. Haingewezekana mwanamke apatie mimba ndani halafu ijifiche isijulikane kwamba kapatia mimba pale. Kwa hiyo, hatua zingeshachukuliwa na wale watu ni wachukuaji wa hatua kweli kweli. (Makofi)
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Pamoja na majibu ya Waziri na swali la msingi kumekuwa na msongamano mkubwa katika magereza ya wanawake, pia inaonekana kuna matatizo makubwa sana ya kisaikolojia kwa wale watoto wanaokulia pale gerezani kwa sababu mazingira siyo rafiki. Je, ni lini sasa Serikali itatenga kituo maalum kwa ajili ya wale wanawake wanaofungwa wakiwa na mimba na wakiwa na watoto wachanga? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na mazingira ya magereza ya wanawake, Serikali imekuwa ikijitahidi kuboresha mazingira ya magereza yetu kila mwaka kadri hali ya uwezo wa bajeti inavyoruhusu ikiwemo maeneo ambayo magereza ya wanawake yapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo Mheshimiwa Waziri amezungumza, tumekuwa tuna utaratibu wa kufanya ziara kwenye magereza haya. Naomba nikiri hapa kama kuna maeneo ambayo yana mazingira mazuri ni magereza ya wanawake kuliko wanaume.
Kwa hiyo, nichukue fursa hii kuwapongeza sana akina mama inaonekana siyo tu katika hali ya maisha ya kawaida lakini hata hali ya gerezani maeneo yao yanakuwa ni maeneo ambayo yanakuwa safi na mazuri zaidi kimazingira pia Serikali inafanya jitihada kwa kutoa kipaumbele maalum katika maeneo ambayo magereza ya akina mama wenye watoto yapo.
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninashukuru sana kwa majibu ya Serikali.
Kwa kuwa tuna kituo cha polisi chenye hadhi ya Wilaya, hiki ni kituo kipya na bado kina changamoto, tunao askari wachache 38 tu, lakini askari hawa wanafanya kazi nzuri kwa kushirikiana na wananchi, Madiwani na Halmashauri.
Pia kwa kuwa hakuna vifaa/vitendea kazi yakiwemo magari, kwa sasa Halmashauri ya Ushetu tumewapa Polisi jengo pamoja na gari. Tunahitaji kuwa na vituo vidogo kandokando kwa sababu Jimbo la Ushetu ni kubwa, linapakana na majimbo nane na tumedhamiria kutokomeza kabisa mauaji ya wazee na walemavu.
Je, ni lini Serikali itatupatia vifaa ikiwemo magari pamoja na askari ili angalau tufikishe askari 100. Hii itasaidia sana pia kupunguza makosa katika majimbo nane ambayo napakana nayo. Ni lini sasa Serikali itatusaidia?
Swali la pili, kwa kuwa tunazo jitihada za kujenga vituo vidogo kando kando katika maeneo ya Kata ya Chambo, Kata ya Ulowa, Kata ya Ubagwe na kata Idahina na kwa kuanzia katika Kata ya Idahina tuna jengo ambalo tumetumia nguvu za wananchi, Mbunge pamoja na wachimbaji wadogo, na litaweza kuwa accommodate ofisi pamoja na askari wapatao watano.
Je, Serikali iko tayari sasa kutusaidia kukamilisha jengo hili ili tuweze kupata askari tuweze kuimarisha masuala ya usalama katika eneo hili ambalo linakuwa kwa kasi?Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa jitihada zake kubwa alizonazo za kuhakikisha kwamba hali ya usalama katika Jimbo lake inaimarika, amekuwa akifuatilia kwa karibu sana maendeleo ya vyombo vyetu vya usalama katika Jimbo lake naomba nimpongeze sana kwa niaba ya wananchi wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la kuongeza idadi ya askari na vitendea kazi vingine ikiwemo magari, naomba nilichukue hilo nikitambua kwamba katika bajeti ya mwaka huu wa fedha tuna matarajio ya kuongeza na kuajiri vijana wapya japokuwa ni kweli tuna uchache wa askari siyo tu katika Jimbo lake, ni katika maeneo mengi nchi nzima. Kwa hiyo, tutazingatia kulingana na mahitaji ya nchi nzima ili tuone jinsi gani tunaweza kufanya kusaidia jitihada za askari wetu pale katika Jimbo lake pamoja na usafiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na jengo lake ambalo amezungumzia vilevile kama nilivyokuwa nikijibu mara nyingi hapa, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba majengo ya hivi vituo vyetu vya vyombo vya usalama vyote ni malengo ya Serikali kuhakikisha kwamba vinaimarika, tuna upungufu huo vilevile katika maeneo mengi nchini. Nichukue fursa hii kumhakikishia kwamba jitihada zinafanyika hata nje ya bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tumekuwa na utaratibu wa kutumia taasisi yetu ya Jeshi la Magereza kuweza kuanza ujenzi kwa kutumia rasilimali za maeneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kutoa wito kwa Mheshimiwa Mbunge kulitumia Jeshi la Magereza katika eneo lake kwa ajili ya kuanza harakati za ujenzi wa kituo hicho na baadaye pale itakapofikia katika hatua nzuri tunaweza kulikamilisha kwani katika mwaka huu wa fedha tumetenga bajeti fedha za kutosha kuhakikisha kwamba tunamaliza maboma yote ambayo yamejengwea kwa nguvu za wananchi pamoja na nguvu na vyombo vyetu vya usalama kwa kutumia rasilimali za maeneo yale.(Makofi)
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nina maswali mawili ya nyongeza.
(a) Kwa kuwa baadhi ya vyombo vya habari vilizungumzia kwamba baadhi ya watuhumiwa ambao walihusika na dawa za kulevya wanapokuwa gerezani wanaishi maisha ya kifahari, je, tuhuma hizi zina ukweli?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwa na sober house zake wenyewe ili iwe ni sehemu ya ufuatiliaji wa vita ya dawa za kulevya kutokana na hivi sasa kuwa kazi inakuwa kama ya zimamoto, haiwi endelevu? Je, wanajipanga vipi ili kuifanya kazi hii iwe endelevu isiwe ya msimu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na ukweli wa tuhuma ambazo zinasambazwa, kimsingi siyo kweli. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge na Watanzania kwa ujumla kwamba Jeshi la Magereza linafanya kazi zake za kusimamia na kuwahifadhi wafungwa na kuwarekebisha tabia kwa umahiri, weledi na umakini wa hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, siyo rahisi. Nasi katika kufuatilia kwetu ambapo tumekuwa tukifanya ziara hizi Magerezani mara kwa mara, tumeshuhudia jinsi ambavyo Askari Magereza ama Jeshi la Magereza linavyofanya kazi yake vizuri na kwa weledi wa hali ya juu. Kwa hiyo, tuhuma hizo kimsingi siyo za kweli na ninaomba Watanzania wazipuuze.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na urekebishwaji wa tabia za watumiaji wa dawa za kulevya, naomba kumjibu Mheshimiwa Fakharia kwa kumjulisha kwamba Serikali kupitia Jeshi la Polisi ina utaratibu huo kwa kutumia vikundi mbalimbali vya michezo na miradi ya kuzuia uhalifu kama vile Familia yangu Haina Mhalifu, Klabu za Usalama Kwetu Kwanza na kadhalika na programu nyingine nyingi ambazo tunafanya kuhakikisha kwamba tunasaidia kurekebisha tabia za watumiaji wa dawa za kulevya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wakati huo huo kupitia sober house ambapo wadau mbalimbali wamekuwa wakizianzisha, tumekuwa tukishirikiana nazo kwa kuweza kuwapatia misaada mbalimbali kuhakikisha kwamba vijana wetu ambao wameathirika na dawa za kulevya wanaweza kutengamaa.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa, lakini nimevutiwa na swali la Mheshimiwa Fakharia, nimshukuru sana kwa kulileta.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaelezee Watanzania kwamba kuhusu mambo ya Sober house ni kweli, kuna baadhi ya sober house kwa sababu ya kutokuwa na standard zinazotakiwa zimekuwa zikileta matatizo. Kwa maana hiyo, tumekubaliana na Wizara ya Afya na Wizara ya TAMISEMI, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwamba tutashirikiana sisi zote ili kwenye Halmashauri zetu tukae na Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya tuweze kutengeneza standard za sober houses zikiwemo zile ambazo zitakuwa kwenye Halmashauri ili watu wetu wanaokwenda kule wasije wakapata matatizo makubwa zaidi. (Makofi)
MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali moja la nyongeza.
Katika majibu yake ya msingi anasema kwamba Serikali inakamilisha mipango ya kupata fedha ya kujenga kituo hiki. Je, anaweza kutuambia kwa kiasi gani mipango hii imefikia? Under what percentage imefikia? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO NA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimejibu katika swali langu la msingi ni kwamba wakati Serikali inajipanga kuweza kuanza mchakato wa ujenzi wa Kituo cha Polisi Tumbatu, tayari kuna jitihada mbalimbali ambazo zimeshachukuliwa kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yale. Ukiachia mbali jitihada ambazo nimezijibu katika swali la msingi za kuhakikisha kwamba tunaendeleza kupeleka askari wa doria mara kwa mara, lakini pia sasa hivi karibu na eneo la Tumbatu kwenye eneo la Mkokotoni kuna ujenzi wa Kituo cha Polisi Mkokotoni ambapo kiko katika hatua za mwisho kukamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka huu tumetenga fedha takribani shilingi milioni 200 kwa ajili ya kulimpa mkandarasi ili aweze kuendelea na kukamilisha kituo hicho ambacho kipo katika hatua ya mwisho. Tunaamini kabisa kwamba Kituo cha Mkokotoni kikimalizika, kitasaidia sana kuweza kusogeza karibu na Tumbatu huduma za polisi wakati ambapo jitiahada za ujenzi wa Kituo cha Tumbatu zikiwa zinaendelea.
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo ya nyongeza. Namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na pia nimshukuru kwa kutupa Kituo cha Wilaya cha Polisi katika Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Sheria Na.23 ya mwaka 2002 inatoa fursa kwa msajili kwa ajili ya kusimamia hawa waganga wa tiba asili na tiba mbadala lakini kwa kuwa kamatakamata hii imesababishwa na wale waganga wasio waadilifu na hawajasajiliwa ambao kimsingi wamesababisha kuwa na mgongano na kusababisha mauaji ya vikongwe. Kwa mfano, katika Halmashauri ya Ushetu kuna watu 25 wameuawa katika kipindi cha mwaka 2012 na 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa kuwa, kamatakamata hii inaleta usumbufu kwa waganga wanaofanya shughuli hii kihalali, je, Serikali imejipangaje kuliimarisha Baraza hili la Tiba Asili au Tiba Mbadala ili lishirikiane na vyombo vingine kama polisi na kuwaondoa kabisa waganga wanaowachonganisha wananchi na kuwalinda vikongwe hawa dhidi ya mauaji? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni lini Serikali itafungua vituo vya usajili mikoani ili kurahisisha usajili na kudhibiti waganga hawa na kuweza kushughulikia kabisa wasiokuwa na sifa na kuboresha huduma hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli utaratibu wa kusajili waganga wa kienyeji ambao kimsingi wanasajiliwa na Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, baada ya mganga kuthibitishwa na Baraza hilo ndipo anapatiwa usajili, kwa hiyo, ni utaratibu mzuri tu. Kupitia utaratibu huu na mabaraza haya, nishauri waganga wote ambao wanajishughulisha na tiba asili kujisajili kisheria ili waweze kutambulika kihalali. Nina hakika watakapofanya hivyo hata kazi ya Jeshi la Polisi kuwabaini waganga wachochezi wanaopiga ramla chonganishi itakuwa ni nyepesi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na hoja ya kupeleka vituo hivi vya usajili mikoani, nadhani ni wazo zuri na kama Serikali tutalichukua na tutalifanyia kazi.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika jibu alilotoa Waziri kuhusu usalama uliosababisha kufungwa kwa Ofisi ya Uhamiaji Muhange miaka ya 1990 si la kweli. Miaka zaidi ya 20 Muhange ni salama na hakuna ofisi pale, wananchi wako pale, ofisi nyingine zote za Serikali zipo, inakuwaje Ofisi ya Uhamiaji ndiyo ishindikane kuwepo Muhange kwa sababu za kiusalama?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Burundi ni miongoni mwa Nchi za Afrika Mashariki kama zilivyo Kenya, Rwanda na kadhalika. Mipaka inayopakana na nchi hizi wananchi wake wananufaika kwa kubadilishana biashara kama mipaka ya Tunduma, Sirari, Namanga na kadhalika, pale kwetu, Jimbo la Buyungu wapo Warundi wanaokuja asubuhi kulima mashamba na kurudi nyumbani au sokoni na kurudi jioni, lakini Warundi hao wamekuwa wakikamatwa, mbona wale wa Sirari, Namanga na kadhalika hawakamatwi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, nilipojibu swali langu la msingi nilieleza sababu zilizosababisha kituo kile kufungwa ni hali ya usalama Burundi, sio Tanzania. Kwa hiyo, hoja yake kwamba Muhange ni salama sio hoja ambayo nimeijibu katika swali la msingi, ni kwa sababu ya hali ya machafuko Burundi ilivyoanza, ndiyo sababu ambayo nilijibu katika swali la msingi.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili, ni kweli wananchi waliopo mipakani katika nchi yetu na nchi jirani, zikiwemo Burundi, Uganda, Rwanda na kadhalika, tumekuwa na mahusiano ya muda mrefu na ndiyo maana kuna utaratibu ambao upo kwa mujibu wa sheria zetu. Kuna utaratibu ambao upo kwa mujibu wa Sheria ya Uhamiaji wa jinsi gani raia wa kigeni wanapaswa kuingia nchini na nini wafanye na ni aina gani ya viza wawe nayo. Na tunaendelea kusisitiza kwamba sheria hizi ambazo zimetungwa kwa maslahi ya Taifa letu wananchi wa nchi jirani waendelee kuzitii.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kumekuwa kuna utaratibu wa utoaji wa vibali maalum kwa wananchi ambao wanaishi mipakani kwa masafa yasioyozidi kilometa kumi ambavyo vinaitwa vibali vya ujirani mwema. Vibali hivi vinatolewa bila ya malipo ili kuweza kuhamasisha na kusaidia wananchi ambao wamekuwa wakiishi mipakani kuendelea kutekeleza shughuli zao wanapokuwa wanavuka mipaka kwa shughuli za kawaida.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Mheshimiwa Naibu Waziri, kumekuwepo na ongezeko kubwa la jamii ya Warundi katika Kambi ya Ulyankulu kule Tabora, hali ambayo inatishia usalama wa raia na mali zao, lakini zaidi wazawa maeneo ya Ulyankulu. Je, unafahamu ongezeko hili na una mikakati gani ya ziada kuweza kukabiliana na tatizo hili ili ongezeko hili lisiendelee tena?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na jitihada mbalimbali ambazo zinafanyika kuweza kuhakikisha kwamba tunapunguza idadi ya wakimbizi katika makambi yetu, na ni shahidi hivi karibuni mmeona kuna zoezi la kurudisha wakimbizi ambao wanarudi Burundi kwa hiari yao ambalo linaendelea. Hii yote ni kwa sababu ya kazi kubwa ambayo Serikali yetu pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki imefanya katika kuhakikisha kwamba amani inarudi Burundi na wananchi wanaendelea kufanya shughuli zao za kawaida.
Mheshimiwa Spika, kwahiyo, kitu ambacho nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ni kwamba kambi zetu zote za wakimbizi hivi tunavyozungumza, kuna pungufu la wakimbizi ambao wanaingia, lakini pia harakati za kurudisha wakimbizi Burundi zinaendelea kwa kasi kubwa sana. Niendelee kumtoa wasiwasi, lakini vilevile niendelee kuwaomba kuwa nasihi wananchi ambao wanaishi mipakani kuendelea kutoa ushirikiano wao kwa baadhi ya wale wakimbizi ambao bado wanahisi kwamba sio wakati muafaka wa kurejea Burundi kwa sasa hivi, kuendelea kuwa- host kama ambavyo tumekuwa tukifanya miaka yote mpaka pale ambapo wataamua kuondoka wote kwa pamoja.
MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kuna magari 13 yanatoa huduma za doria katika maeneo hayo. Nataka nimfahamishe tu Mheshimiwa Naibu Waziri, mimi naishi karibu na kituo hiki, hata kilomita moja haitimii. Yameshatokea matukio kadhaa na Askari wanawajibika kuondoka kituoni kwenda kwenye matukio yale wanashindwa kufanya hivyo na wakati mwingine tumekuwa tukitoa msaada wa magari yetu binafsi kuwasaidia. Je, kati ya magari haya 13, kwa nini sasa gari moja lisipelekwe Kituo cha Polisi Mfenesini.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa ufahamu wangu mkataba wowote wa kuagiza vifaa vyovyote vile vya kijeshi ama vya kiraia unakuwa na makubaliano na supplier vitu vile vitawasili lini. Magari haya tunaambiwa yanakuja kwa awamu na swali lilikuwa yatawasili lini hata kama kwa awamu, je, magari yatawasili lini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimejibu katika majibu ya msingi, kwamba tutapeleka gari katika kituo cha Wilaya cha Mfenesini kwa kutambua kwamba magari haya 13 ya Mkoa na gari ambalo anatumia OCD hayakidhi haja. Nimhakikishie tu kwamba hivi sasa tuna mpango wa kupata magari 50, bahati mbaya hatuna hakika kama yapo magari ya kutosha yenye sifa za kukidhi kuwa magari ya kituo, kwa sababu mengi ya magari ambayo tunatarajia yaje sasa hivi ambayo tayari yameshafika tupo katika mkakati wa kuyatoa mengi ni malori.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ikionekana kwamba magari hayo yanakidhi vigezo vya kuweza kuhudumia Kituo cha Mfenesini, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kituo chake cha Mfenesini ni moja katika maeneo ambayo yatapata gari hizo.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona. Tatizo lililopo Mfenesini linafanana kwa ukaribu kabisa na tatizo ambalo lipo katika Mkoa wa Songe na ukizingatia kwamba Mkoa wa Songwe ni mpya na umekuwa na changamoto kubwa sana za kiuhalifu. Changamoto kubwa iliyopo ni suala la usafiri kwa Jeshi la Polisi hususan katika Wilaya mpya ya Songwe. Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka magari katika Mkoa wa Songwe hususan katika Wilaya mpya ya Songwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua Mikoa na Wilaya mpya nyingi zina changamoto sio tu za magari pamoja hata na vitendea kazi, ofisi na nyumba. Kwa hiyo, ni kipaumbele cha Wizara yetu kuona kwamba tunapopata vifaa na uwezo wa kuweza kuimarisha vitendea kazi katika maeneo hayo, tunaangalia mikoa hii ambayo ni mipya ukiwemo Mkoa wa Songwe.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kituo cha Polisi Himo kinatoa huduma kwa watu zaidi ya laki tano na kipo mpakani na Serikali ilishaahidi hapa Bungeni tangu mwaka 2013 kwamba itapeleka magari mawili (2) mapya kwa ajili ya kutoa huduma kwenye kituo hicho kutokana na umuhimu wake. Hali sasa ni tete sana, kituo kinatumia pikipiki wako kwenye hali mbaya sana. Je, sasa Serikali ni lini kwa dharura itapeleka magari haya mawili waliyoahidi kwa zaidi ya miaka minne (4) katika Kituo cha Polisi cha Himo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbatia kwamba kama ni ahadi ambayo imetolewa na Serikali ya kupeleka gari katika kituo cha Himo, basi nitaifuatilia nitakapotoka tu hapa, kujua ni kitu gani kinachokwamisha ahadi hiyo isitekelezwe mpaka leo ili tuone jinsi gani tunaweza tukaitekeleza pale tutakapopata uwezo wa magari ya kutosha tuangalie haraka iwezekanavyo tunaweza vipi kutimiza ahadi hiyo ya Serikali ya muda mrefu.
MHE. MAGANLAL MEISURIA BHAGWANJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana umenipa nafasi, Mungu akuweke.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme jambo moja katika Jimbo langu la Chwaka, hakuna gari katika Jimbo la Chwaka pamoja na Jozani kwa sababu pana bahari na hoteli zipo nyingi sana. Kwa hiyo, wanaweza kuja majambazi, inaweza kuwa ni mambo ya siasa, hivyo ni muhimu sana gari ipatikane haraka kwa watu wangu wa Jimbo la Chwaka pamoja na Jozani, kwa hisani yako. (Makofi/Kicheko
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, tumelipokea ombi la Mheshimiwa Mbunge na tutalifanyia kazi. (Makofi)
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kumuuliza Naibu Waziri maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania imekuwa kisiwa cha amani, lakini kuna genge la wahuni ambalo hatujui wanapata wapi silaha za kijeshi na kushambulia raia wasiokuwa na hatia.
Je, Serikali haioni sasa imefika wakati muafaka kufanya doria katika sehemu zote za mipaka na barabarani na hata katika vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha genge hili halina nguvu kwa sababu linachafua taswira ya Tanzania katika medali za kitaifa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa bado silaha hizi zinaendelea kuuzwa sehemu za starehe kama vile minadani na sehemu mbalimbali na kuhatarisha amani ya ambao wanafika katika kupata huduma katika sehemu hizo.
Je, Serikali ina mikakati gani ya ziada kuhakikisha suala hili kuuza silaha holela linakomeshwa na wale wanaokamatwa wachukuliwe sheria kali ili suala hili likome mara moja? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni bahati mbaya sana Mheshimiwa Mbunge hajalitaja jina la kundi ambalo amelizungumza, lakini kimsingi nataka nimueleze tu kwa ufupi kwamba hali ya matumizi ya silaha kufanya uhalifu nchini imepungua, ndiyo maana hata ukiangalia takwimu tokea Juni, 2016 mpaka Agosti, 2017, hakuna matukio makubwa ya mauaji ya kutumia silaha za jadi nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, utaona ni kazi kubwa ambayo Serikali imefanya kupitia Jeshi la Polisi kuweza kudhibiti wahalifu na magenge mbalimbali ambayo yamekuwa yakitumia silaha hizo za jadi kwa ajili ya kufanya uhalifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwamba mafaniko hayo yamepatikana kwa sababu gani? Kuna mikakati mingi ambayo imefanyika ili kuweza kufikia malengo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tumeendelea kutoa elimu kwa Umma kuhusiana na makundi ambayo yamekuwa yakijitokeza, kwa mfano, maeneo ya Kanda ya Ziwa kuna watu walikuwa wanaitwa wakata mapanga, ukija huku Mbeya na kadhalika, wapo watu ambao walikuwa wanafanya mauaji kwa vikongwe kwa imani za kishirikina. Kwa hiyo, Jeshi la Polisi kwa kupitia utaratibu wake wa ulinzi shirikishi tumekuwa tukifanya jitihada kubwa sana za kutoa elimu kwa jamii ili kufahamu madhara ya matumizi ya silaha za jadi, hasa matumizi ya kujichukulia sheria mkononi kwa jamii, hilo moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, tumekuwa tukiendelea kufanya doria na ukaguzi barabarani kuweza kusimamisha magari na watu ambao wakipita na silaha hizo za jadi na kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria. Hii doria imekuwa ikiendelea na ndiyo maana mpaka sasa hivi tumeweza kufanikiwa kwa mujibu wa takwimu ambazo nimezieleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tumeendelea kuhakikisha kwamba huduma zetu za Jeshi la Polisi zinashuka katika ngazi ya Tarafa na Kata. Tuna Ofisi za Ukaguzi katika ngazi ya Tarafa na Kata ili kusogeza huduma ya Polisi karibu na wananchi kuweza kukabiliana na matukio mbalimbali ya uhalifu ya aina kama hii ambayo Mheshimiwa Mbunge amezungumza. Kwa hiyo, nikiri tu kwamba kwa jumla kazi kubwa imefanyika na mafanikio yake mpaka sasa hivi ndiyo haya ambayo nimeyaeleza, ni makubwa ya kuridhisha kwa kiasi fulani.
MHE. MHANDISI ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba tu kwanza nimpe taarifa tu kwamba maji yalitoka ndani ya miezi sita tu kama na siku nane halafu mpaka sasa hivi toka 2010 lile gereza halina maji ya uhakika na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakati huu mradi unatengenezwa kipindi kile tulikuwa hatuna wakimbizi sasa hivi ninapoongea 2015 tumepokea wakimbizi 120,000 na kati ya hao kuna wahalifu mbalimbali ambao nao wanatumia gereza hilo hilo ambalo kipindi hicho kulikuwa na upungufu wa lita 39,000. Tunapozungumzia kwamba maji ni uhai na kwa kuwa na idadi ya wafungwa sasa imeongezeka, Serikali ina mpango gani wa dharura hata wa kuwashirikisha UNHCR ambao ndiyo wana dhamana ya wakimbizi katika kutatua tatizo hilo? Hilo ni swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa sheria inawapa kinga wafungwa wa kisiasa na wafungwa wengi ambao wanatoka kwa wakimbizi siyo wa kisiasa, ni wafungwa wa makosa ya kawaida na kwa kuwa sasa wameanza kurudishwa makwao, Serikali haioni umuhimu sasa wa kuwarudisha wale wafungwa ambao wako kwenye gereza ili kupunguza idadi ya wafungwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, kuhusu ushauri wake wa kulichukulia kwa uzito unaostahili tatizo hilo ambalo yeye kwa kuwa ni Mbunge amekuwa karibu na gereza na ameona shida hiyo inaathiri vilevile wananchi la kuhusisha UNHCR ni wazo zuri na tutalichukua. Tumekuwa tukishirikiana na UNHCR kwa miradi mbalimbali ya maendeleo hasa katika maeneo ambayo wilaya/majimbo/vijiji vilivyopo karibu na maeneo ya wakimbizi ikiwemo maji.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hatuoni kwa nini tusichukue na hili jambo tukaliingiza katika mpango huu hasa ukitilia maanani ni juzi tu Mheshimiwa Makamu wa Rais amezindua mpango kabambe ambao utaweza kuwanufaisha zaidi wananchi wanaohusika katika maeneo ambayo wakimbizi wanaishi. Kwa hiyo, ni wazo zuri ambalo tumelichukua kwa uzito unaostahili.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na hoja yake ya wafungwa ambao wamefungwa kwenye magereza, tuna utaratibu wa kubadilishana wafungwa katika nchi mbalimbali ambao upo kabisa kisheria na kupitia utaratibu huo hilo jambo linafanyika. Kwa hiyo, siyo jambo geni limekuwa likifanyika miaka yote tu.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Spika, kwenye majibu ya msingi ya Mheshimiwa Waziri, migogoro ni moja ya sababu inayokwamisha jambo hilo, lakini migogoro hiyo haijazuia wananchi wetu kufanya biashara. Ni kwa nini Serikali isirahisishe movement ya wananchi wetu hasa hasa vijana wa Kitanzania kuchangamkoa fursa ya soko kubwa la Congo ikizingatiwa Congo ni land locked country? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, hivi tunavyozungumza tuna utaratibu mzuri tu ambao unatumika na uko kwa mujibu wa sheria, wa wananchi ambao wanahitaji kufanya biashara, kwa Watanzania ambao wanahitaji kwenda Congo na wale wa Congo ambao wanahitaji kuja Tanzania. Utaratibu uliopo sasa hivi ni utaratibu wa kutumia viza ambazo zinaitwa business visa kwa nchi ya DRC. Lakini hoja ya msingi hapa ilikuwa ni jinsi ambavyo tunaweza kufanya ili kuwa na utaratibu ambao utakuwa ni mzuri zaidi. Ninachoweza kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge ni kwamba utaratibu wa viza uliopo sasa hivi si kikwazo kwa biashara kwa mtu yeyote ambaye anahitaji kufanya biashara katika nchi hizi mbili.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo kwa kutambua umuhimu wa kurahisisha zaidi tunatarajia kwamba amani itakapokuwa imetengemaa katika DRC mazungumzo yetu yatakamilika haraka ili tuweze kuwa na utaratibu mzuri zaidi.
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Pamoja na majibu ya Serikali, imesema kwamba hawana ushahidi na Serikali ina mkono mrefu, je, ni kwa nini Mheshimiwa Waziri katika Wizara yake wasiweke mkakati wa operation maalum ili kuweze kuwakamata wahalifu hawa ambao wamekuwa wakizorotesha uchumi wa wavuvi? Hilo ni swali la kwanza.
Swali la pili, kwa kuwa wavuvi wengi Kanda Ziwa wakiwemo wavuvi wa Mkoa wa Mwanza na mikoa ya jirani kama vile Kagera ikiwepo Kata ya Kerebe ambayo iko Bukoba, Ukerewe pamoja na Kalebezo na Kayenze wamekuwa wakiteseka sana na uporaji wa mali zao, hizi bodi pamoja na samaki, suala ambalo limekuwa likizorotesha sana uchumi wa wavuvi, je, ni lini sasa Serikali itatimiza ahadi yake ambayo imekuwa ikiahidi kwa takribani miaka kumi sasa ya ununua boti ambazo zinaweza zikafanya doria ili kuwakamata hawa wahalifu ambao wanawapora wavuvi mali zao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na mkakati, mkakati upo na kuna mahitaji ya task force ambayo inahusisha wadau mbalimbali na majukumu yake makubwa ni kukabiliana na uhalifu katika maeneo ya majini. Kama ambavyo nimejibu katika swali la msingi kwamba mikakati hiyo ikiwemo katika eneo ambalo anazungumzia Mheshimiwa Mbunge ya Ziwa Victoria, tulipeleka hiyo timu na tukaweza kubaini upungufu kadhaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wenyewe ambao umeelekezwa ni kwamba kuna umuhimu wa kuweza kupata boti zaidi zenye uwezo mkubwa zaidi kwa ajili ya kukabiliana na uhalifu huo. Ndiyo maana nikamweleza katika jibu la msingi kwamba Serikali inafanya jitihada kuweza kupata boti hizo za kisasa ili kuweza kudhibiti hali hiyo. Kuhusiana na kwamba wahalifu hawa wanatoka ndani au nje; ndiyo maana nimemwambia kwamba tunashirikiana na nchi jirani ili kuweza kuwabaini na kuwachukulia hatua za kisheria kupitia Wizara yetu ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa jibu lake zuri. Vilevile lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Masauni kwa ziara aliyoifanya ndani ya Jimbo langu na kupunguza uhalifu, nimpe hongera sana. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Je, ni lini nyumba hizi zitaanza kujengwa kwa upande wa Unguja?
Swali la pili, kuna vituo vya polisi ambavyo hali yake ni mbaya sana kwa sasa hasa ukiangalia kama kituo cha Ng’ambu pamoja na Mfenesini na vipo vingi ambavyo hali yake ni mbaya sana, je, Serikali ina mkakati gani wa kuvifanyia marekebisho vituo hivyo angalau vilingane na hadhi ya Jeshi la Polisi kwa sasa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru sana kwa pongezi zake. Ni kweli Jimboni kwake kuna eneo ambalo lilikuwa ni hatarishi sana kwa usalama wa wananchi na tulifanya ziara pamoja na yeye na tukaweza kuchukua hatua. Napongeza sana Jeshi la Polisi kwa kuweza kudhibiti ile hali. Sasa hivi nimeambiwa kwamba hali ni shwari na wananchi wanafanya shughuli zao vizuri. Kuhusiana na hizi nyumba kwamba ni lini zitajengwa, ni pale ambapo taratibu za kifedha zitakapokamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lingine anazungumzia kuhusu vituo vya polisi kwamba vina hali mbaya. Ni kweli tuna matatizo ya vituo vya polisi, siyo tu vina hali mbaya, lakini ni pungufu. Tuna upungufu wa takribani vituo 65 hasa katika Wilaya za Kipolisi nchini. Kwa hiyo, hili vilevile linakwenda sambamba na hali ya kibajeti. Pale ambapo hali ya kibajeti itaruhusu tutajenga vituo vipya katika maeneo ambayo hakuna, lakini vilevile kukarabati vile ambavyo viko katika hali mbaya.
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, Gereza la Karanga lina tatizo kubwa sana la vyombo vya usafiri kwa maana ya magari. Naomba majibu ya Serikali kwamba ina mpango gani wa kununua gari ili kusaidia wafungwa wanaokata rufaa pamoja na askari ili kulinda usalama wa wafungwa kwa sababu gari lililopo ni chakavu sana na hata matairi halina?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Gereza la Karanga limekuwa na tatizo la madeni makubwa kwa matibabu ya wafungwa wanaotibiwa nje ya zahanati ya gereza hilo. Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba madeni yanayodaiwa gereza yanalipwa ili wafungwa waendelee kupata huduma ya matibabu? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tuna matatizo ya upungufu wa magari katika Jeshi la Magereza maeneo mbalimbali nchini ikiwemo kwenye Gereza la Karanga kiasi tumefikia hatua ya kuweza kufikiria uwezekano kuwapatia magari matano miongoni mwa magari 50 ambayo tunatarajia kuyapokea hivi karibuni kupitia Jeshi la Polisi. Tutalichukua hili suala la Gereza la Karanga tuone kama katika maeneo yaliyo na changamoto kubwa Karanga ni mojawapo ili tuweze kuangalia uwezekano wa kuwapatia gari yatakapokuwa yamewasili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la zahanati, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tunajitahidi kulipia madeni ya magereza ikiwemo zahanati kadri fedha zitakavyokuwa zinaingia. Pia nataka nimkumbushe Mheshimiwa Mbunge kwamba tuna uwekezaji mkubwa katika Gereza la Karanga wa kiwanda chini ya uwekezaji wa Shirika la PPF na moja katika mpango ambao tunataka kutekeleza ni ujenzi wa zahanati kubwa na ya kisasa katika gereza hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti,unaamini kwamba tutakapomaliza ujenzi huo, changamoto hii ya gharama ya matibabu kwa maeneo hayo itasaidia kupatiwa ufumbuzi. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge aendelee kuvuta subira wakati matatizo haya tunayatatua kwa hatua za muda mfupi na muda mrefu.
MHE. JAKU HASHIM JAKU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri na Waziri wake kwa majibu yao ya umakini kabisa. Naomba kuuliza maswali madogo tu ya nyongeza yenye fungu (a) na (b):-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu yako Mheshimiwa Naibu Waziri, swali la msingi umesema Waziri amesema katika mwaka wa fedha 2017/2018 Jeshi la Polisi limetenga jumla ya shilingi bilioni 2.2 kwa ajili ya kupunguza madeni ya wakandarasi waliotekeleza miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa ujenzi wa huu wa Kituo cha Mkokotoni. Umetenga shilingi milioni 200 na kutenga maana yake ni kitu tayari umekiweka pembeni na huyu mtu ni mgonjwa, hili suala nimelisemea karibu mara nne katika chombo hiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini nije naye mguu kwa mguu ili asije akapata usumbufu apate haki yake hii, ili akamalize kituo hiki na yeye mwenyewe apate matibabu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwa vile deni hili lina muda mrefu kwa nini, Serikali au Wizara haitoi priority ikammalizia deni hili, ili kumaliza ujenzi huu wa vituo vyetu vilivyokuwa huko Unguja na Pemba? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa hii kwa niaba ya Serikali kumpa pole sana huyu mkandarasi kutokana na maradhi ambayo ameyapata na tunamuombea Mwenyezi Mungu amjalie aweze kupona haraka. Nimuombe sana Mheshimiwa Mbunge hana haja ya kumhangaisha mkandarasi kuja naye hapa mguu kwa mguu, asiwe na wasiwasi wowote fedha hizi shilingi milioni 200 zimetengwa kwa ajili yake katika bajeti ya mwaka huu na kwa hiyo basi, fedha hizo zitakapokuwa zimeingia tu atalipwa bila hata kumsumbua mkandarasi kwa kuja naye hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kwamba lisiwe kipaumbele. Ni kipaumbele na ndiyo maana tukatenga hizo fedha kwa ajili ya kumlipa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge tunaomba vile vile awe na subira wakati tukisubiri fedha hizi wakati zitakapokuwa zimeingia na tutamlipa mara moja.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Naomba Naibu Waziri aliombe Bunge lako Tukufu radhi kwa kulidanganya. Amesema Tarafa ya Gonja ina Kituo cha Polisi cha Daraja B, naomba afanye home work, tarafa hii mimi ndiyo natoka na hakuna hata Kituo cha Daraja C, sasa hicho cha Daraja B amekitoa wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, hata huko anakosema kipo Kituo cha Daraja C, iko nyumba haijawahi kuwekwa polisi hata siku moja. Naomba sana Mheshimiwa Naibu Waziri aeleze Bunge lako Tukufu kwa nini anatoa taarifa za uongo ambapo hata wananchi katika Jimbo langu watashangaa kwamba hicho kituo Daraja B, kiko wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, Waziri atakumbuka kwamba nimeshawaandikia Wizara yao barua mara mbili kuomba kituo hiki kilichopo Maore, Tarafa ya Ndungu ambacho kimejengwa mwaka 1959, kimechakaa ceiling board zimedondoka, vigae vilivyowekwa hata kabla ya Uhuru vimebomoka hata OCS hana mahali pa kukaa kufanyia kazi, aseme lini Serikali itaweza kukarabati kituo hiki?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili amesema Polisi wanafanya doria kwenye Jimbo hili, atajua kwamba Polisi wa Kituo cha Maore chenye Daraja B kama anavyosema kipo Tarafa ya Ndungu hawana hata matairi kwenye magari yao, usafiri wao ni wa shida, sasa hiyo doria wanaifanyaje? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nilichokieleza katika majibu yangu ya msingi, nilieleza kwamba kulingana na maeneo ambayo walileta maombi ya ujenzi wa vituo katika Tarafa ya Gonja kwamba kuna Kituo cha Daraja B sio C. Katika Tarafa ya Mamba nilichokisema ni kwamba wananchi wametoa eneo, kwa hiyo tupo katika mchakato wa ujenzi wa kituo hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kituo cha Maore ni kweli Mheshimiwa Mbunge aliwahi kuwasilisha barua yake kwa Mheshimiwa Waziri kuhusiana na ukarabati wa kituo hiki na barua yake tunaifanyia kazi na pale uwezo utaruhusu basi tutafanya marekebisho ya kituo hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusiana na ubovu wa magari kwa ajili ya doria, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba natarajia muda siyo mrefu kufanya ziara katika Jimbo lake nitamwomba na yeye kama atakuwa na nafasi tuambatane ili tukaone changamoto hizo. Tatizo la usafiri katika nchi yetu ni kubwa sana, kwa hiyo itategemea uzito tutakavyoona katika eneo hilo kulinganisha na maeneo mengine katika nchi nzima tuone uwezekano wa kusaidia usafiri ili waweze kufanya kazi zao vizuri hasa maeneo ya milimani ambapo hakuna mawasiliano mazuri ya usafiri.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza sina budi kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kulitamka vizuri jina langu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza ambapo maswali ya msingi amenijibu vizuri na yameeleweka lakini kuna kifungu cha mwisho hapa ambacho kimenifanya niweze kupata maswali ya nyongeza. Amekiri kwamba watoto 184 walipotea na 176 wamepatikana na nane hawajapatikana lakini bado wanaendelea kutafutwa. Sasa napenda kumuuliza hivi Mheshimiwa Waziri kwa hao waliopatikana na hao waliokutwa nao, Serikali imechukua hatua gani ya kuwawajibisha kisheria? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wale watoto baada ya kupatikana ambapo alikuwa hayuko kwenye mazingira ya wazazi lazima afya itakuwa ni mgogoro. Je, Serikali au vyombo vimechukua hatua gani baada ya watoto hao kupatikana kupelekwa kwenye vyombo vya utibabu ili kuangaliwa hali yao na wazee kuweza kujiridhisha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika majibu yangu ya msingi kwamba, kupotea kwa watoto hawa 184 kulitokana na sababu mbalimbali ambapo miongoni mwa sababu hizo ilikuwa ni mazingira magumu ambayo wanaishi baadhi watoto, imani na kishirikina, visasi, kukosekana uangalifu wazazi/walezi na sababu nyingine ni kupotea kwa bahati mbaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa sababu hizi ni tofauti na hatua ambazo zinachukuliwa zinategemea na sababu husika. Kwa zile sababu ambazo zimesababishwa na njia ya uhalifu basi hatua mbalimbali zimeshachukuliwa kwa mujibu wa sheria kwa watu ambao wamehusika na upotevu huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utakumbukuka juzi tu kulikuwa na tukio la kijana mmoja ambaye amejihusisha na utekaji wa watoto na kuomba fedha, kijana yule alikamatwa na kwa bahati mbaya alipata majeraha na akafariki. Nikuhakikishie kwamba Serikali kupitia Jeshi la Polisi iko makini sana kuhakikisha kwamba inalinda watoto wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni kuhusu hatua ambazo watoto hawa wanachukuliwa. Kama ambavyo nimesema kwamba kwa kuwa sababu ni tofauti kwa wale watoto ambao wamepatikana na madhara mbalimbali basi nao vilevile hufikishwa katika mamlaka husika kwa ajili ya kuweza kupata huduma mbalimbali ili kuwaweka katika hali nzuri ya kimaisha na kiafya.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Naibu Spika, asante kwa kuwa haya maswali tumekuwa mara kwa mara tunauliza na hakuna utekelezaji. Je, naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri nusu mwaka wa fedha unakwishwa. Ni majengo mangapi yamekarabatiwa kwa upande wa Zanzibar na ni vituo vingapi vya kambi vya Kambi za Jeshi kwa upande wa Zanzibar vimekarabatiwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwa kuwa hivi vituo vya afya tunavyoviulizia ambavyo vipo kwenye makambi ya Jeshi havihudumii tu majeshi na familia zao, zinahudumia pia na jamii zilizowazunguka na hasa hichi kituo nilichokiulizia kiko sehemu ambapo ajali zinatokea mara kwa mara.
Je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha vituo vyote vya majeshi vinapata dawa kwa wakati muafaka na sitahiki zinazofaa kwa wakati muafaka? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI (K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA): Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nilivyojibu katika majibu ya msingi kwamba kwa bajeti ya mwaka 2018/2019 Serikali imeazimia kuvifanyia ukarabati vituo vyote ikiwemo vya Zanzibar na kikiwemo hiki cha kwenye Brigedi ya Nyuki, Migombani. Kwa hiyo, mwaka wa fedha 2018/2019 bado haujaisha kadri ambavyo fedha kama ambavyo nimesema zitapatikana basi vituo hivi pamoja na hiki cha Migombani vitafanyiwa ukarabati. Sambamba na kuvipatia huduma nyingine muhimu kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa kwa hatua za awali.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ikumbukwe kwamba vituo hivi kwa kawaida vinatumika kwa ajili ya kutoa huduma za awali kabla ya kuweza kuwapeleka wagonjwa wenye matibabu makubwa katika Hospitali za Kikanda kwa upande wa Zanzibar ikiwemo Hospitali ya Jeshi ya Bububu.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize maswali madogo ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, pamoja na jitihada zote zinazofanywa na Serikali kutatua tatizo la makazi ya askari. Je, kwa kipindi hiki cha 2017/2018 Mkoa wa Tabora umetengewa kiasi gani?
Swali la pili, kwa kuwa hivi karibuni kumekuwa na wimbi kubwa la wakimbizi kutoka Congo na kwa kuwa hivi karibuni pia wamesema kwamba baadhi ya wakimbizi wale wametawanyika katika Mkoa wa Kigoma inawezekana wakaja na Mkoa wa Tabora. Je, Serikali inatoa kauli gani kwa sasa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mwanne Mchemba kwa swali lake zuri la pili la nyongeza kutokana na changamoto ya mfumuko wa Wakimbizi ambao wanaingia nchini kutoka DRC hasa kutoka katika maeneo ya Kivu kutokana na changamoto ya hali ya usalama nchini DRC. Kabla sijatoa ufafanuzi wa swali lake hilo la pili nimjibu kwamba kwa bajeti ambayo nimeizungumza ya maendeleo ambayo nilisema ni takribani bilioni 12.3 ya mchanganuo mbalimbali ikiwemo shilingi bilioni 7.2 ya Magereza ni fedha ambazo zimetengwa kwa maendeleo nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Jeshi la Magereza hakuna utaratibu wa sub vote kwenye Jeshi hilo ingawa Jeshi la Polisi ipo lakini kwa ujumla kwa mwaka huu wa fedha hakuna fedha ambayo imetengwa kwa ajili ya mradi wa maendeleo kwa Tabora specifically, lakini kwa sababu tunatambua kwamba kuna maeneo mengi nchini ambayo kuna majengo mengi ya Polisi ambayo yapo katika hatua za mwisho kukamilika, kwa mfano, kule Mtambaswala
- Mtwara, Njombe, Mabatini Mwanza, Musoma na kadhalika, kwa hiyo fedha hii ya maendeleo mwaka huu tunataka tuilekeze katika majengo ambayo tayari yapo katika hatua za mwisho kukamilika kabla hatujaanza miradi mipya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii sasa kuweza kuzungumzia hoja yake ya pili muhimu ya wimbi la wakimbizi kutoka DRC. Mpaka hivi naomba nitoe taarifa rasmi kwamba Wakimbizi ambao wametoka DRC kuingia nchini tokea Januari wanakadiriwa kufika zaidi ya 2,500 na katika hao takribani wakimbizi 1,960 tayari wameshakuwa wamehifadhiwa katika Kambi ya Wakimbizi Nyarugusu na wengine 300 na zaidi wapo kwenye vituo vya kupokelea Wakimbizi. Changamoto ambayo amezungumza ya kwamba kuna baadhi ya wakimbizi ambao wamekuwa wana desturi aidha ya kutoroka kwenye makambi kutoka DRC na kuingia mitaani ama kupita njia za panya kuingia nchini kwetu kwa kisingizio cha machafuko DRC.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nitoe kauli ifuatayo, jambo la kwanza nataka nitoe angalizo ama onyo kali kwa wakimbizi kama hao kuacha desturi hiyo. Tumeshatoa maelekezo katika vyombo vyetu vya usalama nchini kuhakikisha jambo la kwanza kwa Idara ya Uhamiaji kuendelea kufanya msako kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, ikiwemo Jeshi la Polisi hasa katika Mkoa wa Kigoma ambao una changamoto kubwa sana ya wakimbizi, hii inadhihira na takwimu ambavyo zipo kwa mwaka jana.
Mheshimiwa Naibu Spika, takribani asilimia 30 ya wahamiaji haramu waliokuja Tanzania wametokea katika Mkoa wa Kigoma. Kwa hiyo, tumewekeza nguvu nyingi sana katika Mkoa wa Kigoma kuhakikisha kwamba inadhibiti wimbi la wahamiaji haramu kuingia. Vilevile tumetoa maelekezo kwa Idara ya Wakimbizi ambayo ipo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuhakikisha kwamba inafanya uhakiki na kuimarisha ulinzi katika makambi yetu hasa Kambi ya Nyarugusu ambayo ndiyo kambi ambayo inapokea wakimbizi kutoka DRC ili kuhakikisha kwamba wale wote ambao watakiuka sheria na utaratibu wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria ya wakimbizi kwa kushtakiwa ili baadaye sheria ichukue mkondo wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo ndiyo kauli ya Serikali kuhusiana na swali lake la pili.
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri Mheshimiwa Masauni, nina maswali mawili ya nyongeza.
Je, ni lini Serikali au Wizara yake itaanza kufanya ukarabati wa nyumba hizo?
Swali la pili, nafahamu Wizara ina mpango mzuri wa kulinda raia na mali zake, kuna kituo cha Shaurimoyo, kuna kituo kidogo cha Mwembeladu lakini vituo hivi vimefungwa kwa muda mrefu sasa.
Je, ni lini Wizara yake itavifungua vituo hivi na kuendelea na kazi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, anauliza ni lini ukarabati huo utaanza. Kama ambavyo nimejibu katika jibu la msingi kwamba pale tu ambapo tutaweza kupata fedha tuaanza huo ukarabati. Kwa hiyo, siwezi kusema exactly ni siku gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia swali lake la pili alikuwa alitaka kujua kwa ni nini kituo cha Shaurimoyo pamoja na kituo cha Mwembeladu havitumiki. Kituo cha Shaurimoyo hakitumiki kwa sababu kwanza, takwimu zinaonyesha kwamba eneo hilo la Shaurimoyo halina uhalifu.
Lakini pili kuna vituo vingi sana ambavyo vipo karibu na kituo cha Shaurimoyo ikiwemo kituo cha Ng‟ambo, kituo cha Mwembemakumbi na Makadara ambapo imezidi maili moja kutokea kituo kilichopo kituo cha Shaurimoyo. Kwa hiyo, kwa kutilia maanani kwamba hali ya kituo hicho siyo nzuri kituo kimechakaa sana tumeamua kituo hicho kwa sasa hivi kitumike kwa ajili ya matumizi ya Polisi Jamii na wananchi wanaendelea kutumia vituo vilivyo karibu na kituo cha Shaurimoyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusiana na kituo cha Mwembeladu ambapo kipo mpakani mwa Jimbo langu vilevile, kituo hiki kilijengwa kwa ajili ya matumizi ya traffic, lakini kutokana na mkakati wa kipolisi wa matumizi ya shughuli za ki-traffic Wilaya, uratibu huo unafanyika katika kituo cha Malindi ambacho nacho hakipo mbali sana na eneo hilo. Pia miundombinu ya kituo cha Mwembeladu haikidhi haja ya kufanya shughuli za traffic kwani hata ukikamata magari siyo zaidi ya gari moja linaweza kukaa katika eneo hilo. Kwa hiyo, kwa kutilia maanani hoja hizo kwa sasa hivi tunaangalia uwezekano wa kubadilisha matumizi ya eneo ili tuweze kupata maeneo mengine ya kuweze kuimarisha shughuli za traffic badala ya kutumia kituo cha Mwembeladu.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza.
Kwa kuwa tatizo la makazi ya polisi yamekuwa makubwa sana haswa katika Mkoa wangu wa Arusha, polisi wamekuwa wakiishi katika nyumba mbovu na chafu na wengine kuishi uraiani. Kwa kuwa tuna ekari 30 tulizopewa na Magereza kwa ajili ya makazi haya ya polisi. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kutumia zile ekari 30 tulizopewa na Magereza kwa ajili ya kujenga makazi haya ya polisi Mkoa wa Arusha?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mpango wa kujenga nyumba katika maeneo mbalimbali. Nilizungumza jana kwamba tuna mpango wa kujenga nyumba 4136 kwa awamu ya kwanza katika mikoa 17 ikiwemo Arusha. Lakini wazo lake la kutumia eneo la Magereza basi tutalichukua tuone tunalifanyia kazi kwa kiasi gani.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, na mimi naomba kumuuliza Naibu Waziri swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa baadhi ya vituo vingi Zanzibar ni vibovu na majengo ni chakavu na askari hawana vitendea kazi wanapokamata wahalifu kama wino wa kuchapisha barua na mahitaji mengine muhimu na hata wahalifu wale hawapati hata mkate kwa sababu siyo wahalifu wote wana jamaa wa kwenda kuwaangalia kwenye vituo vya polisi wanapokuwa mahabusu.
Je, ni lini Serikali itahakikisha vituo vyote vinapatiwa huduma stahiki za kuendesha kazi zao kwa wakati muafaka.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pale ambapo Serikali itapata uwezo wa kifedha.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, Mwenyekiti wangu wa zamani wa vijana.
Mheshimiwa Spika, kama ilivyo kwenye majibu yake, anasema moja ya mikakati ni kuhakikisha wanafanya doria imara; ni jambo zuri kabisa. Sasa huwezi kufanya doria imara kama huna magari mazuri.
Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ya Bunda kuna magari mawili na mabovu na ndiyo ambayo yanatakiwa yafanye doria kwenye Jimbo la Kangi na Jimbo la Boni. Sasa uhalifu unazidi kuongezeka.
Mheshimiwa Spika, maswali yangu, katika kuhakikisha
hiyo doria imara kama Mheshimiwa Waziri amejibu, je, Serikali iko tayari sasa kutupatia gari jipya ili kupunguza vitendo vya uhalifu kwa kufanya hiyo doria imara? (Makofi)
Swali la pili, ili kuweza kukabiliana na hizi changamoto, moja ya vituo ambavyo vipo hohehahe ni Kituo cha Polisi cha Bunda. Sasa wameanza mradi wa ujenzi wa jengo la upelelezi kupitia michango ya polisi, ya wadau, nami Mbunge wa Jimbo kupitia Mfuko wa Jimbo nimewachangia. Serikali mpo tayari kuungana na jitihada zetu kukamilisha jengo hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la magari, naomba nichukue nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tumepokea changamoto yake ya magari. Wakati ambapo magari yatapatikana tutatoa kipaumbele kwa Jimbo lake ili tumpatie gari la ziada ili aweze kuongeza nguvu ya yale magari machache yaliyopo sasa hivi.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni suala la ujenzi
wa kituo cha upelelezi. Kwanza nachukua fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuamua kutoa fedha za Mfuko wake wa Jimbo kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha polisi. Natambua kwamba Mfuko wa Jimbo una fedha kidogo na Majimbo yetu yanachangamoto nyingi. Kwa hiyo, kitendo cha Mheshimiwa Mbunge kuamua kwamba sehemu ya fedha hizo ziende kwenye ujenzi wa vituo vya polisi ambavyo vina changamoto kubwa ni jambo la kupongezwa na kuungwa mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Ester kwamba jitihada zake pamoja na za wananchi zimezaa matunda, kituo hicho kimekamilika, tunatarajia wakati wowote mwaka huu tutakizindua. (Makofi)
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa matukio ya Bunda yanazidi kuwa mengi kidogo, ni lini sasa Waziri au Naibu Waziri atatembelea Bunda ili kuona hali halisi ya mambo hayo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimuahidi kwamba tutashauriana na Mheshimiwa Waziri ili kati yangu ama yeye tuweze kwenda Bunda haraka iwezekanavyo. Tutakaa pamoja tushaurine ratiba hiyo ya kutembelea Bunda muda siyo mrefu sana. (Makofi)
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Matatizo ya usalama katika eneo la Bunda yanafanana sana na Jimbo langu la Mji wa Tunduma.
Mwaka 2016 katika swali langu la msingi, niliuliza kuhusiana na ujenzi wa kituo chenye hadhi ya Wilaya, lakini pia niliuliza kuhusiana na nyumba zenye gharama nafuu kwa ajili ya polisi wetu kwenye Mji wa Tunduma. Majibu yake ni kwamba walisema katika Bajeti ya mwaka 2016/2017 nyumba hizi zingeweza kujengwa pamoja na Kituo cha Polisi chenye hadhi ya Wilaya. Je, Serikali inasema nini kuhusiana na changamoto hizi katika mji wetu wa Tunduma? (Makofi)
NAIBU WAZIRI MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nakiri kabisa kwamba Jimbo la Tunduma lipo mpakani na lina changamoto nyingi sana za kiusalama. Kwa hiyo, mahitaji ya kuwa na kituo cha polisi cha kisasa pamoja na nyumba za askari ni mambo ya kipaumbele.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ahadi hiyo iliyotolewa na Serikali iko pale pale na hatua ambazo zitafikiwa tutamjulisha kwa kadri ambavyo upatikanaji wa fedha utakavyokuwa unaruhusu.
MHE. USSI SALUM PONDEZA AMJAD: Mheshimiwa Spika, napenda kuuliza swali moja la nyongeza. Je, ni lini watapata fedha na ukarabati wa kituo hicho kwa sababu, eneo hili ni maarufu na lina matatizo sana ya huduma za kipolisi?
Kwa hiyo, kutoa nafasi kwa saa 12 tu haitoshelezi kwa sababu, kuna maeneo mengi ya uhalifu na historia inaonesha na ripoti zipo, lakini muda unakuwa ni mchache ambapo wananchi wakihitaji huduma za kipolisi wanashindwa kuzipata mpaka wazifuate sehemu za mbali na uhalifu unakuwa umeshatendeka. Je, Mheshimiwa Waziri haoni umuhimu kukipa kipaumbele kituo hiki kwa bajeti hii?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ussi Pondeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kituo cha Maruhubi kinafungwa saa 12.00 jioni siyo kwa sababu ya ukosefu wa fedha, lakini kwa mujibu wa taratibu kulingana na Police General Order (PGO) Namba 287(9) inaeleza utaratibu wa vituo vya polisi vilivyo; kuna class A, B na C. Kwa hiyo, Kituo cha Maruhubi ni Class C ambacho kwa kawaida kinapaswa kifunguliwe saa 12.00 na kifungwe saa 12.00 jioni.
MHE. MASOUD ABDALLA SALIM: Mheshimiwa Spika, na mimi nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri katika jibu la muuliza swali la msingi (b) alieleza kwamba yuko tayari kukarabati kituo cha polisi husika ambacho kimetajwa, lakini kituo cha polisi cha Kengeja ni kibovu, chakavu, kinavuja na kuta zake zimeanza kudondoka na ni athari sana kwa polisi na kituo hicho mmerithi kutoka kwa wakoloni.
Je, hamuoni kwamba ni aibu na fedheha kwamba hamuwezi kukikarabati na inawezekana kikapelekea askari hawa kupoteza maisha? Hamuwezi kukarabati hata lile ambalo mmerithi kwa wakoloni!?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nakiri kabisa kwamba kituo cha Kengeja hali yake siyo nzuri, hata mimi niliwahi kufanya ziara pale, lakini siyo Kengeja tu, ni maeneo mengi ndani ya nchi yetu vituo vya polisi haviko vizuri sana. Kwa mfano, Mkoani ni zaidi! Nadhani Kituo cha Mkoani kina hali mbaya zaidi kuliko Kengeja.
Mheshimiwa Spika, kama alivyozungumza mwanzo Mheshimiwa Mbunge, ni kwamba tuna mkakati wa kuvifanyia ukarabati vituo hivi na utaratibu huo utakuwa unaenda hatua kwa hatua kulingana na hali ya fedha itakavyoruhusu. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Masoud uvute subira.
MHE. SOPHIA M. SIMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii, na ninamshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri lakini kidogo yananitatanisha.
Mheshimiwa Spika, anazungumzia ujenzi wa magereza 11 katika kipindi cha miaka 20. Speed hii si nzuri, na pia hayo magereza pamoja na kwamba amesema hayajamalizika lakini wanayatumia, nadhani hapo pana hitilafu kubwa.
Ningependa niulize katika hayo magereza yanayojengwa ni lini anafikiri wanaweza wakaboresha ile mahabusu ya watoto iliyopo Upanga Dar es Salaam; ni mahabusu ya miaka mingi na ni ndogo na haifanani kuwa mahabusu ya watoto? Na sidhani kama zipo mahabusu nyingi kama hizo, Waziri wa Ardhi ana viwanja vingi Dar es Salaam ni vyema akaihamisha pale, ni lini watafikiria kuiondoa ile mahabusu pale?
Mheshimiwa Spika, la pili, kumejitokeza msongamano mkubwa sana kwenye mahabusu na magereza, hasa mahabusu pale wanapokamata watu wengi kwa wakati mmoja. Ningependa kujua hivi kule polisi au magereza wana utaratibu gani wanapokamata watu wengi kwa pamoja, wa kuweza kupunguza wengine kwenda maeneo mengine kwasababu pale ndipo kuna gross breach ya human rights, watu wanapumuliana, wale watuhumiwa wanashindwa hata kukaa na wanalala wakiwa wamesimama.
Mheshimiwa Spika, ningependa kujua kuna utaratibu gani kupunguza hilo tatizo kwa sababu ni la muda tu wanakamatwa kwa muda? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kasi ya kuongeza idadi ya magereza ama kuboresha magereza yaliyopo, naomba tu nichukue fursa hii kumjulisha Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inajitahidi sana kuhakikisha kwamba magereza yetu yanaendelea kuongezeka ukubwa kwa kupanua na kujenga mabweni mapya. Na mfano mzuri wa hilo ni bajeti ya mwaka huu ambayo tumeipitisha hivi karibuni; ambapo tumetenga takribani shilingi bilioni tatu kwa ajili ya kazi hiyo ambayo itahusisha ukarabati mabweni karibu 15 katika maeneo mbalimbali nchini.
Mheshimiwa Spika, baadhi ya maeneo hayo ni kama vile Nzega, Babati, Ushora, Tarime na kadhalika. Lakini pia itahusisha kukamilisha kwa mabweni kama saba ambayo yameshaanza kujengwa ambayo yapo maeneo mbalimbali, likiwemo hilo la Chato, Mpwapwa, Biharamulo, Mkuza, Urambo na kadhalika; pamoja na kuimalisha maeneo ya huduma katika magereza yetu ambapo itahusisha ujenzi wa jiko katika Gereza la Segerea pamoja na mazingira mengine ya magereza yetu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kazi hiyo inafanyika hatua kwa hatua kadri hali ya uchumi utakavyoruhusu na tutaendelea kufanya hivyo katika bajeti ya kila mwaka.
Mheshimiwa Spika, lakini kuhusiana na lile Gereza la Watoto la Upanga ambalo Mheshimiwa Sophia Simba ameliulizia; ni kwamba kimsingi lile lipo chini ya Wizara ya Afya kwenye Idara ya Ustawi wa Jamii. Kwa hiyo, sisi tunachokifanya ni kwamba hatuna magereza ya watoto ukiachia Gereza la Vijana la Wami ambalo lipo Morogoro; linalochukua vijana wa miaka 16 mpaka 21, kimsingi watoto wanopatikana kwenye hatia katika magereza hupelekwa katika Idara ya Ustawi wa Jamii kwa ajili ya kuhudumiwa kama watoto na si wafungwa. Kwa hiyo, kimsingi jibu la swali lake lilikuwa hivyo.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili linahusu kupunguza msongamano magerezani. Kuna njia mbalimbali zimefanyika, ukiachia hizi ambazo tumezungumza za kuona jinsi gani tunapanua mabweni na kujenga magereza mapya pia kuna hatua mbalimbali ambazo zimesaidia kufanikisha kupungua kwa idadi ya wafungwa kutoka 38,000 mpaka sasa hivi takribani 34,000 tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingia madarakani.
Mheshimiwa Spika, hali hiyo ilitokana na hatua mbalimbali ikiwemo kuhakikisha kwamba tunatumia njia za parole, huduma za jamii, probation na njia nyingine ili kuona sasa wafungwa ambao wana kesi ndogo ndogo ama wana hatia ndogo za miaka michache kukaa magerezani basi watumie vifungo vya nje badala ya kurundikana magerezani na kusababisha msongamano usio ulazima. (Makofi)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, niseme kwanza nimefurahi kukuona hapo.
Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani kwa majibu mazuri. Ni kweli kwamba mahabusu za watoto ziko chini ya wizara yangu, lakini nataka kumthibitishia mama Sophia Simba kwamba katika mwaka huu wa fedha tumetenga zaidi ya bilioni mbili kwa ajili ya kuboresha kwanza makazi ya wazee lakini pia tutaboresha hizo nyumba za kuwarekebisha tabia watoto. Tunajaribu ku-avoid neno mahabusu kwa sababu tunataka kuwarekebisha tabia, ndilo neno ambalo tunapenda kulitumia.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mama yangu Sophia hatukuwa na mpango wa kulihamisha lakini sasa kabla hatujaboresha naomba nichukue hoja yako tuone kama je, tuboreshe au tulihamishe tulipeleke sehemu nyingine. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, napenda kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa magereza mengi nchini ni kweli miundombinu ni michakavu sana; na kwa kuwa asilimia zaidi ya 75 mahabusu waliopo magereza ni wale ambao wana kesi za kudhaminika lakini wananyimwa dhamana. Swali langu linakuja kwamba Gereza la Tarime linachukua mahabusu na wafungwa kutoka Wilaya ya Rorya na unakuta ina msongamano mkubwa kutoka 209 mpaka 560 mpaka 600.
Mheshimiwa Spika, ningependa kujua sasa Serikali ni lini itajenga gereza Rorya, kwa sababu ile ni Wilaya inajitegemea, ili kupunguza msongamano wa mahabusu na wafungwa Tarime ambayo inaweza ikapelekea magonjwa mbalimbali na ukizingatia miundombinu ni mibovu sana? Lakini pia kwa haki za kibinadamu wanatoka kule Rorya kufuatilia kesi Tarime, kuja kuona mahabusu Tarime, kuja kuona wafungwa Tarime. Ni lini sasa mtajenga Gereza la Rorya kupunguza msongamano katika Gereza la Tarime? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ni kweli tunakiri kwamba kuna msongamano wa wafungwa katika Gereza la Rorya na kuna umuhimu mkubwa wa kujenga Gereza pale. Lakini changamoto ya upungufu wa magereza katika Wilaya zetu mbalimbali nchini halipo Rorya tu; kwenye maeneo mengi ya Wilaya nchini bado magereza yamekuwa ni upungufu.
Kwa hiyo tutajaribu kuhakikisha kwamba tunapunguza msongamano huo kwa kujenga magereza katika Wilaya ambazo zina upungufu katika nchi nzima, na utekelezaji wa mpango huo utategemea upatikanaji wa rasilimali fedha, kwani mpaka sasa hivi kati ya Wilaya 92 ni Wilaya 43 nchini ndio ambazo zina magereza.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kimsingi tunalifahamu hili tatizo, niombe tu Mheshimiwa Mbunge awe na subira pale ambapo hali itakapo ruhusu tutashughulikia pamoja na hizo Wilaya nyingine 43 ambazo nimezizungumza zenye mapungufu hayo. (Makofi)
MHE. FAKHARIA SHOMARI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona.
Kwa kuwa kituo cha polisi Ziwani Zanzibar kuna baadhi ya majengo yamechakaa na yanahitaji ukarabati. Je, Mheshimiwa Waziri anawajulisha nini askari hao polisi wa Ziwani kuhusu ukarabati wa majengo yao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Makao Makuu ya Polisi Ziwani kuna changamoto ya miundombinu ikiwemo uchakavu wa majengo. Serikali tunalitambua hilo na tupo katika mbalimbali za kuhakikisha kwamba tunafanya marekebisho hayo kadri ya hali ya upatikanaji fedha itakaporuhusu.
MHE. OMARY A BADWELI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa wananchi wa Tarafa ya Chipanga wameitikia wito wa kujenga kituo cha polisi miaka 13 iliyopita, kituo kikubwa kizuri na cha kisasa na wakati huo kilighalimu 40,000,000. Hata hivyo tangu nikiwa diwani mpaka nimekuwa Mbunge kipindi cha miaka 13 nimehangaika na Wizara ya Mambo ya Ndani wafungue wapokee na wafungue kituo kile cha polisi hawajafanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya kumpeleka Mheshimiwa Shamsa Vuai Nahodha akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani akaagiza kifunguliwe hakikufunguliwa; nikampeleka Mheshimiwa Silima akaagiza kifunguliwe na akawahaidi wananchi wa pale ndani ya miezi sita kwamba kituo kile kitakuwa kimefunguliwa mpaka leo hakijafunguliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali langu, je, Serikali inajua kwamba miezi sita waliohaidi wananchi wa Kata ya Chipanga na Tarafa ya Chipanga kwamba imekwisha na hawajapokea kituo hicho cha polisi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kama leo sikupata majibu ya uhakika ya kwamba wanakipokea na kuja kukifungua kituo kile cha polisi nawaambia Jumamosi ijayo nakwenda kuwakabidhi wananchi kituo chao cha polisi ili wafanyie shughuli zingine ikiwemo kukaa watumishi kama nyumba ambao na wenyewe wana matatizo makubwa. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani hii si mara ya kwanza Mheshimiwa Badwel kuuliza swali hili Bungeni na binafsi nilipata fursa ya kuzungumza naye kuhusianana mchakato wa ufunguzi wa kituo hiki na nilikuwa nimemwambia kabisa niko tayari kwenda kufungua wakati wowote. Lakini Mheshimiwa Badwel tulikubaliana kwamba tuchukue hatua kwanza kuhakikisha kwamba RPC wa Mkoa wa Dodoma anakwenda kulikagua ili kuona maandalizi yote kabla ya ufunguzi yamekamilika. Makubaliano hayo baina yangu mimi na Mheshimiwa Mbunge. Kwa hiyo nashangaa sana leo Mheshimiwa Badwel hazungumzii zile hatua ambazo tumepiga mimi na yeye binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kitu ambacho kilikwamisha ufunguzi ni changamoto ambayo imetokana na wananchi wenyewe pamoja na Mheshimiwa Mbunge wa eneo lile. Tulichokubaliana na Mheshimiwa Badwel ni kwamba kutokana na hali ya kituo ilivyo inahitaji kiweze kuwekwa sawa vizuri. Nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge na wananchi wake kwa kazi kubwa waliyoifanya kwa muda mrefu. Hiyo hiyo hatuwezi kuwa wezi wa fadhila tusipompongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa hali ya bajeti ilivyo mwaka huu wa fedha tumepanga takribani shilingi milioni 150 ambazo tutatoa kipaumbele katika kukamilisha vituo ambavyo vimefikia katika hatua kama ambavyo kituo hiki ambacho kiko katika Jimbo la Mheshimiwa Badwel kilipofikia.
Lakini kipindi hiki ambapo bado fedha hazijapatikana, ikiwa kuna uwezekano wa kuendelea kukamilisha yale marekebisho madogo madogo ili kiweze kufikia viwango vya kuweza kufunguliwa rasmi waweze kufanya hivyo, vinginevyo tusubiri bajeti itakapokuwa imekamilika ili tuweze kukikamilisha na kuweza kukizindua. Wakati wowote hayo yatakapofanyika nitakuwa tayari kwenda kukizindua ili wananchi waweze kukitumia.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru ingawa kwa kweli majibu ya Waziri, Naibu Waziri yanakatisha tamaa maana tumekuwa tukisikia siku zote kadri fedha zitakavyopatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ulinzi wa raia na mali zao ni muhimu sana katika nchi yetu. Kwenye Jimbo la Tarime Mjini katika Kata zote nane tuna kituo cha poilisi kwenye Kata ya Bomani tu, na Kata zingine ambazo za pembezoni wananchi wamejitolea kujenga vituo vya polisi. Tunataka kujua mkakati thabiti wa Serikali katika ku-support zile juhudi za wananchi hasa Kata ya Nyandoto, Kenyamanyoli, Nkende na Kitale ambazo ni mbali na mji, na kuna gari moja tu ambayo inafanya patrol.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nini mkakati wa Serikali maanake mnakusanya mapato mengi, muweze kuelekeza kwenye kumalizia vituo vya poilisi ili tuweze kuimarisha ulinzi wa raia na mali zao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nieleze tu kwa ufupi, ni kwamba changamoto ya vituo vya polisi haipo tu katika vituo vya polisi vya ngazi ya kata na tarafa, tuna Mikoa ya kipolisi takribani 34 nchi nzima. Kati ya hiyo majengo ambayo ya makamanda wa mikoa yaliyopo nchini ni 19. Kwa hiyo takribani mikoa 15 haina Ofisi ya Makamanda wa Mikoa. Mikoa miwili Manyara na Mara ndiyo ambapo ujenzi wa Ofisi mpya za makanda unaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mtaona changamoto hii ni pana sana, na ndiyo maana wakati wote tumeendelea kuwashawishi wadau werevu ikiwemo ninyi Waheshimiwa Wabunge ambao wengi wenu mmekuwa mkijitolewa na sisi tumekuwa tukichukua jitihada mbalimbali kuhamasisha wananchi kujitolea kuchangia ujenzi wa vituo hivyo vya polisi ili kabiliana na changamoto hii; wakati ambapo Serikali kila mwaka imekuwa ikitenga bajeti kwa ajili ya ujenzi pamoja na ukarabati wa vituo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hii haiwezi kumalizika kwa wakati mmoja. Naamini wewe Mheshimiwa Mbunge ni Mbunge wa Jimbo na una fedha za Mfuko wa Jimbo. Unaweza ukatumia hizo vilevile kusaidia jitihada hizi za Serikali katika kuhakikisha kwamba ina punguza changamoto ya upungufu wa vituo vya polisi nchi nzima kuanzia ngazi ya Wilaya, Kata na Tarafa. Serikali kama ambavyo tunasema pale fedha zitakapopatikana tutapunguza tatizo hili hatua kwa hatua, hatuwezi tukamaliza kwa wakati mmoja.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo yaliyoko Songwe yanafanana kabiasa na matatizo yaliyoko kwenye Jimbo la Geita Vijijini. Jimbo la Geita Vijijini lina wakazi kama 650,000, na tuna vituo viwili vikubwa ambavyo wasimamizi wao ni askari wenye nyota mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumelalamika muda mrefu sana kwa ngazi ya Mkoa wetu naona sasa tutafute msada huku kwa Waziri. Jimbo zima na vituo hivi vikubwa havina askari wa kike, kwa hiyo askari wa kiume wanawapekua wanawake.
Sasa pengine kwa kuwa sisi ni vijijini hakuna haki za binadamu, nilikuwa namuomba Mheshimiwa Waziri, ni lini utatuletea askari wa kike kwenye vituo vile vikubwa ili wake zetu wakapekuliwe na askari wa kike na si askari wa kiume? (Makofi).
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yake ni ya msingi tutaifanyia kazi.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ningependa kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tukisubiri sungura mdogo huyu wa Serikali kugawanywa nchi nzima sisi watu wa Rombo tumeamua kujiongeza, na tumejenga Kituo cha Polisi Useri kimeshaanza kufanya kazi, Kituo cha Ngoyoni kiko kwenye rooffing, kituo cha Kirongo Samanga pamoja na nyumba ya polisi karibu inafika kwenye linta na kituo cha Mahida kiko kwenye msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ningependa jibu la hakika ili wananchi wa Rombo waamasike kuchangia zaidi ujenzi wa hivi vituo. Ni lini mtakuja kufanya hiyo tathimini ili kuwatia moyo wananchi wakamilishe hivi vituo kwa sababu kazi ya kuchangia vituo vya polisi ni ngumu kuliko hata kuchangia zahanati na shule?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa sababu ya urefu wa mpaka wa Rombo na Kenya na njia za panya kuwa nyingi, Jeshi la Polisi Rombo lina magari ya zamani sana na chakavu.
Je, Serikali iko tayari kuweka katika bajeti ijayo gari kwa ajili ya kusaidia shughuli za polisi katika Wilaya ya Rombo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue furusa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge, na hii ndiyo aina ya Wabunge wakutolewa mfano. Kazi waliyoifanya ni kubwa ya kushirikiana na kuhamasisha wananchi wake kujenga vituo vitatu hivi kituo cha Ngoyoni, Mahida na Kirongo si kazi ndogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwahakikishie mbele ya Bunge hili Tukufu kwamba jitihada za aina kama hii za Mbunge Selasini na Wabunge wengine wengi tu wamo katika Bunge hili wanafahamu wamefanya kazi nzuri kama hii. Serikali itaziunga mkono na mimi nimuhakikishie kwamba nitahakikisha tathimini hii imekamilika haraka na natarajia kufanya ziara hiyo karibuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikwenda kushuhudia hii kazi mimi mwenyewe na ndiyo maana nazungumza kwa kujiamini sana. Nilikwenda nilifanya ziara Rombo na nikaona kazi hii inafanyika vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa hiyo basi namuhakikishia kwamba nitakuja tena Rombo karibuni ili tushirikiane kwa pamoja. Kuna mambo mawili ambayo tutafanya; la kwanza tutatoa kipaumbele katika bajeti ambayo inakuja ili kuhakikisha vituo hivi vinakamilika; lakini la pili nitashirikiana na Mheshimiwa Mbunge ili kuendelea kuhamasisha wadau zaidi ili tumalize vituo hivi ili viweze kutumika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, kulingana na kazi nzuri ambayo Mheshimiwa Mbunge anaifanya nina uhakika kabisa tutaangalia uzito wa changamoto ya gari katika Mkoa wa Rombo ili tuone katika gari ambazo tunatarajia kuzipokea wakati wowote tuweze kupeleka huko zisaidie kupunguza changamoto za askari.
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi naomba niulize swali la nyongeza.
Wilaya ya Itilima iliyoko Mkoani Simiyu ni miongoni mwa Wilaya zilizoanzishwa mwaka wa fedha 2012/2013, lakini ninavyozungumza hivi Wilaya hiyo haina Kituo cha Polisi. Ni lini mkakati wa Serikali kuhakikisha Wilaya hiyo mpya inapata Kituo cha Polisi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua Wilaya ya Itilima ina changamoto hiyo, lakini kama ambavyo tunatambua maeneo mengine vilevile na tuna mikakati ya kukabiliana na tatizo hilo, kama nilivyozungumza katika majibu yangu ya msingi na hili nalo tunalichukua, tunalijua na tutalifanyia kazi. Pale ambapo hali itakaporuhusu kituo kitajengwa katika Wilaya hiyo.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kilindi ina takribani miaka 20 toka imeanzishwa lakini hali ya kusikitisha ni kwamba kituo kinachotumika ni kama post wakati ikiwa ni Wilaya ya Handeni zamani. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri au Waziri yuko tayari kutembelea Jimbo la Kilindi ili kujionea hali halisi ya jinsi ambavyo hata OCD anakaa guest house mpaka leo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumjibu Mheshimiwa Shekilindi, Mbunge wa Kilindi kuwa....
Samahani Mheshimiwa Kigua, Mbunge wa Kilindi kuwa tutakuja Kilindi.
MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo hayaridhishi pia nina maswali mawili ya nyongeza.
Katika jibu la msingi Mheshimiwa Waziri amesema kwamba busara na utu wa mwanadamu huwa unazingatiwa, lakini naomba niseme kwamba siyo kweli kwamba busara na utu wa mwanadamu unazingatiwa.
Mimi binafsi nimefanyiwa tendo hili na nilipodai kwamba kwa nini hamkuja na askari wa kike wakalazimisha kutumia nguvu. Sasa naomba niulize Jeshi la Polisi, je, tabia hii mbaya itamalizika lini?
Swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuniletea orodha ya malalamiko ya matendo haya yaliyotendeka? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la kwanza kwamba inawezekana kuna tukio ambalo Mheshimiwa Mbunge anathibitisha lilimtokea binafsi la kufanyika upekuzi bila kuhusisha askari wa kike, naomba hili tulichukue ili tuelewe ni sababu gani iliyosababisha hilo litokee, halafu tuone sasa mimi na yeye Mheshimiwa Mbunge labda baadae tukae tuweze kulijua suala hili lilikuwaje ili tuone hatua gani ya kuchukua. Orodha tutampatia lakini siwezi kumpatia hapa kama Mheshimiwa Naibu Spika alivyosema.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, lakini kabla ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kumpongeza aliyekuwa Kaimu Waziri Mkuu Mheshimiwa Mwakyembe kwa kazi nzuri aliyoifanya Kukaimu Kiti cha Waziri Mkuu.
Baada ya hapo nichukue fursa hii swali la msingi linahusu mwanamke na mwanaume, je, kuna sheria gani iliyopitishwa na Bunge kama mtu kafanya kosa mume akakamatwa mke kuna utaratibu gani au kuna sheria iliyopitishwa? Vilevile ninavyojua mimi utaratibu…
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Jaku anataka kujua kama kosa la mwanamke anakamatwa mwanamume. Kosa aliyefanya ndiye atakayekamatwa, kwa hiyo, haiwezekani Mheshimiwa Jaku kosa akafanya mtu mwingine ukakamatwa wewe.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na majibu ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri amejibu, anasema ni askari 105 ambao wamechukuliwa hatua za kinidhamu. Katika matukio ambayo yametokea ambayo hayana shaka, ni matukio ya wazi, ni matukio ambayo yametokea kwa Mheshimiwa Nape Nnauye ya kutolea bastola hadharani lakini pia Mdude Nyangali ambaye amepigwa mpaka sasa hawezi kutembea vizuri, Husna Amri ni kiongozi wetu wa CHADEMA ambaye amefanyiwa hicho kitendo mpaka sasa hivi tuko hospitali. Je, katika hao askari ambao wamechukuliwa hatua za kinidhamu ni miongoni mwa hao 105?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa kuna askari ambao umekiri kwamba wamechukuliwa hatua za kinidhamu na hawa watu wanaoteswa wengine hawawezi tena kuendelea na shughuli zozote, wanapata fidia gani kulingana na madhara ambayo wamekuwa wameyapata? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa naibu Spika, swali lake ameuliza kwa kutoa mifano michache ya baadhi ya watu ambao walipata majeraha mbalimbali, lakini naomba nichukue fursa hii kutoa ufafanuzi kidogo wa majibu ya swali hili, nadhani itasaidia kuweza kutoa uelewa mpana wa utaratibu wa jinsi ambavyo polisi wanafanya shughuli zao wanapokabiliana na changamoto ya uvunjifu wa sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimezungumza katika jibu langu la msingi kwamba ukamataji nchini unasimamiwa chini ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kifungu namba 11 ambacho kinaeleza kwamba polisi anapaswa atumie njia ya kumshika muhusika (physical contact) pale tu ikiwa yule mtuhumiwa amegoma. Katika hali ya kawaida ni kwamba polisi wanapohitaji kumkamata mtuhumiwa inamueleza na watuhumiwa ambao wanafuata sheria bila shuruti huwa polisi hawana haja ya kuwashika au kuwakamata kwa kutumia mikono yao. Hii inadhihirishwa na hata Waheshimiwa Wabunge huwa ni mashahidi mara nyingi, wakiwemo viongozi ambao wamekuwa wakituhumiwa kwa mambo mbalimbali wanapelekewa taarifa kwa njia ya simu au hata kwa barua waweze kujisalimisha wenyewe polisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, njia ya pili ni ambayo sheria hii inaainisha ni kwamba endapo mtu huyo atakuwa amebisha, basi polisi wataweza kutumia njia yoyote ambayo ni stahiki kuweza kumkamata mtuhumiwa, kwa kiingereza wanasema; “may use all means necessary to effect the arrest.”
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hivi ndivyo ilivyoandikwa katika Sheria yenyewe ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai. Hata hivyo, hata hii nayo imefafanuliwa katika PGO namba 274 ambayo inaeleza utaratibu wenyewe hata wa kukamata ukoje na unazingatia mambo mengi. Kwa mfano, unaweza ukaangalia aina ya tishio kwamba je, madhumuni ya mtu huyu ni yapi na mazingira ambayo yanahusisha mtuhumiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo mengine mengi ambayo yanaangaliwa miongoni mwayo wanaangalia vilevile, kwa mfano; wanaangalia resistance ilivyo. Wakati mwingine inawezekana mtu akawa amesimama tu au ameshikilia kitu au wakati mwingine ameshikilia silaha, kwa hiyo vile vile maamuzi ya kumkamata yanategemea aina ya mtuhumiwa mwenyewe mazingira yake aliyopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia inetegemea aina ya silaha ambazo polisi anazo, inategemea vilevile utafiti ambao polisi wanafanya kabla, mbinu gani watumie. Wanaweza wakahitaji kupata taarifa za kiintelijensia kabla ya kumkamata muhusika. Niliona nitoe ufafanuzi huo ili nieleweke vizuri. Hata matumizi ya nguvu kwa wale ambao ni majambazi au wanaotumia silaha nao kuna utaratibu wake kwa mujibu wa PGO namba 7 na 8.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kujibu specifically suala la watu ambao wanawataja itategemea na mambo yote ambayo nimeeleza, kwamba je, mazingira ambayo mtuhumiwa alikuwepo yalikuwa ni yapi? Sasa kusema sasa hivi kwamba mtu fulani alikuwa amechukuliwa hatua gani kwa maelezo ya hapo moja kwa moja, nadhani cha msingi ni kwamba tunashughulika na kesi kwa kesi kulingana na aina ya mtuhumiwa jinsi ambavyo ametenda lile kosa. (Makofi)
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Kwa kuwa Serikali inakiri kuwepo na tatizo kubwa la upungufu wa nyumba za makazi ya askari polisi na vyombo vingine ambavyo viko ndani ya Jeshi la Mambo ya Ndani. Serikali haioni sasa mipango na mikakati iliyonayo bado haiwezi kuwa ni kigezo cha kukamilisha tatizo hili kubwa tulilonalo nchini?
Swali langu la pili, pamoja na matatizo haya ziko nyumba ambazo zimeshaanza kujengwa takribani miaka mitano leo, zikiwemo nyumba za Mabatini Barracks katika Jimbo la Nyamagana na maeneo mengine kama Musoma na Mikoa mingine yenye matatizo kama haya.
Je, ni lini Serikali itahakikisha nyumba hizi ambazo zikikamilika kwa wakati kwanza tunaokoa upotevu wa fedha nyingi, lakini inasaidia watu wetu wanaohangaika kutafuta makazi kukaa kwenye makazi yaliyo bora na kuwafanya wafanye kazi yao kwa uaminifu na uhakika zaidi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianzia na mradi wa nyumba ambazo zipo katika Jimbo lake nikiri kwamba nyumba zile zimefika katika hatua za mwisho kukamilika. Mimi na yeye tuliwahi kufanya ziara kutembelea, tuliona kwamba kuna umuhimu wa nyumba zile kukamilika kwa haraka ili kuweza kutatua tatizo la makazi katika eneo la Nyamagana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo Nyamagana tu, tuna nyumba maeneo mbalimbali nchini ambazo zipo katika hatua za kukamilika, ikiwemo Musoma Mjini, Kagera, Mtambaswala huku Mtwara, Ludewa na kadhalika. Kwa hiyo, kwa kutambua kwamba kuna haja ya kumaliza nyumba hizi ambazo zimefika katika hatua nzuri katika bajeti ya mwaka huu ya maendeleo ambayo tumetenga takribani zaidi ya shilingi bilioni 5.2 malengo ni kukamilisha miradi hii ambayo imefikia katika hatua nzuri na za mwisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba tunatarajia katika kipindi cha mwaka huu wa fedha tutamaliza project ile ya Nyamagana (Mabatini) pamoja na nyingine ambazo nimezitaja. Kwa hiyo, ni miongoni mwa mikakati ya Serikali ya kutatua matatizo ya nyumba za askari nchini.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kituo cha Polisi cha Himo ambacho kinatoa huduma kwa wakazi takribani 400,000 na kiko mpakani, Serikali iliahidi hapa kwamba itafanya ukarabati wa miundombinu ya kituo hicho hasa Ofisi. Sasa ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya tangu mwaka jana na hali ya kituo inazidi kuwa hoi bin taabani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, jibu la suala hili, halitofautiani sana na jibu langu nililojibu mwanzo, kwamba kituo hiki cha Himo ni moja kati ya vituo ambavyo vina changamoto na hasa ukitia maanani kipo karibu na mpakani kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amezungumza. Kitu ambacho kimekwamisha kama ambavyo nimezungumza mwanzo ni suala la bajeti. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge avute subira tuna mpango wa kujenga vituo na kukarabati vituo vingi nchini kama nilivyozungumza katika jibu langu la msingi kwamba tuna upungufu wa vituo katika Wilaya 25 na vituo vingi vipo katika hali mbaya nchini, lakini tutafanya kazi ya kuvirekebisha na kujenga hatua kwa hatua.
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa Gereza la Bukoba Mjini linakuwa na msongamano mkubwa sana wa wafungwa na tuna Magereza ambazo zimechakaa sana kwa mfano kama Kitengule, Rwamlumba ni lini Serikali itapanua hiyo Rwamlumba ili kuweza kuwapunguza wafungwa walioko Bukoba Mjini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukitenga pesa za bajeti kuongeza mabweni mwaka hadi mwaka na hii ni kwa sababu ya kutambua changamoto za msongamano wa Magereza yetu nchini. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hilo tumelipokea, tutajitahidi katika mwaka wa fedha ujao tuweze kuweka Gereza Bukoba Mjini miongoni mwa Magereza ya vipaumbele vya kuongeza mabweni ili kupunguza idadi ya msongamano katika Magereza yetu nchini.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante, majibu ya Wizara yanaonekana ni mepesi sana kwa sababu nchi nyingi anazozitaja ni nchi za kiafrika na lengo mahususi ya hili swali tulikuwa tunataka tujue nchi zote ulimwenguni lakini natambua kwamba nchi zilizopo chini ya Umoja wa…

Nchi zilizopo chini ya Umoja wa Madola (Commonwealth) tuna utaratibu huu wa visa on entry or visa on arrival. Je, kwa nini wananchi wa India wanapokuja Tanzania wanakuja kwa visa on arrival, lakini sisi tunapokwenda nchi kama India lazima uombe visa hasa ikichukuliwa kwamba Watanzania wengi wanakwenda India kwa ajili ya kupata huduma za matibabu?
Swali la pili, zipo nchi za Afrika Magharibi ambazo wanaingia kwa visa ya referred visa ikiwemo Cote d’voire, Senegal na Mali. Je, kwa nini sasa isiwe ni wakati muafaka wa kuiunganisha Nigeria katika nchi hizi kwasababu inaonekana kwamba mara nyingi wanapoingia huku kwetu wanahatarisha usalama wa nchi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli nchi za Jumuiya ya Madola zina utaratibu wa wananchi wake kutembeleana bila visa. Lakini kama nilivyojibu katika swali langu la msingi kwamba ushirikiano na matengamano hayo ikiwemo la Jumuiya ya Madola, utaratibu wake unaweza kubadilika kulingana na mahusiano pamoja na hali za kiusalama. Kwa hiyo, sio jambo la kushangaza kuona India na Nigeria juu ya kwamba zote mbili ni wanachama wa Jumuiya ya Madola lakini utaratibu wa visa on arrival ukawa hautumiki.
MHE. RAISA ABDALLAH MUSSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kawaida wafungwa wanawake au kisheria wanatakiwa walindwe au wasimamiwe na askari magereza wanawake na tunaamini kwamba magereza wale ambao wamefungwa kule wako katika mikono salama. Inakuwaje akina mama wale wanapata ujauzito wakiwa katika magereza? (Makofi)
Swali la pili ni kwamba, je, Waziri haoni kwamba iko haja ya akina mama hawa kupewa vifungo vya nje ili kutoa haki kwa watoto wale wasiwemo ndani ya magereza kama walivyo mama zao? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa mujibu wa utaratibu na ndivyo hali ilivyo kwamba wafungwa wanawake wanasimamiwa na askari magereza wa kike. Sasa hoja kwamba wafungwa wale wanapata mimba wakiwa gerezani hiyo inahitaji uthibitisho, kwa sababu katika hali ya kawaida huwezi kujua mimba ile ameipata vipi. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kimsingi mazingira hayaruhusu hali hiyo kutokea katika Magereza. Kwa hiyo, ni dhahiri kabisa kwamba inawezekana pengine waliingia pale hali ya kuwa walikuwa na mimba changa. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusiana na vifungo vya nje kwa akina mama hawa. Tunao utaratibu ambao haubagui jinsia ya kuweza kuwapatia vifungo vya nje kwa mujibu wa taratibu. Tuna utaratibu wa huduma za jamii, tuna utaratibu vilevile wa msamaha na wanawake wanafaidika katika taratibu zote mbili. Kwa hiyo, utaratibu huo upo lakini inategemea na makosa. Kwa wanawake ambao makosa yao hayakidhi vigezo vya kuweza kupata fursa hiyo wataendelea kutumikia vifungo vyao kwa mujibu wa sheria za nchi yetu. (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naona Waheshimiwa Wabunge wamesimama wengi sana.
Waheshimiwa Wabunge, nimezunguka takriban Magereza ya Mikoa yote na katika zunguka ile hakuna eneo hata moja ambako nimefika nikaelezewa kwamba mama ama mwanamke aliyekuwa amefungwa kifungo cha muda mrefu amegundulika amepata mtoto akiwa katika kifungo cha muda mrefu. Ni kweli unaweza ukakuta wale waliokuwa wana vifungo vya muda mfupi wakajifungua wakiwa gerezani, lakini kujifungua wakiwa gerezani haina maana kwamba mimba kaipatia gerezani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge niwaambie tu vyombo vyetu hivi ni vyombo vinavyofanya kazi kwa sheria kali sana. Haingewezekana mwanamke apatie mimba ndani halafu ijifiche isijulikane kwamba kapatia mimba pale. Kwa hiyo, hatua zingeshachukuliwa na wale watu ni wachukuaji wa hatua kweli kweli. (Makofi)
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Pamoja na majibu ya Waziri na swali la msingi kumekuwa na msongamano mkubwa katika magereza ya wanawake, pia inaonekana kuna matatizo makubwa sana ya kisaikolojia kwa wale watoto wanaokulia pale gerezani kwa sababu mazingira siyo rafiki. Je, ni lini sasa Serikali itatenga kituo maalum kwa ajili ya wale wanawake wanaofungwa wakiwa na mimba na wakiwa na watoto wachanga? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na mazingira ya magereza ya wanawake, Serikali imekuwa ikijitahidi kuboresha mazingira ya magereza yetu kila mwaka kadri hali ya uwezo wa bajeti inavyoruhusu ikiwemo maeneo ambayo magereza ya wanawake yapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo Mheshimiwa Waziri amezungumza, tumekuwa tuna utaratibu wa kufanya ziara kwenye magereza haya. Naomba nikiri hapa kama kuna maeneo ambayo yana mazingira mazuri ni magereza ya wanawake kuliko wanaume.
Kwa hiyo, nichukue fursa hii kuwapongeza sana akina mama inaonekana siyo tu katika hali ya maisha ya kawaida lakini hata hali ya gerezani maeneo yao yanakuwa ni maeneo ambayo yanakuwa safi na mazuri zaidi kimazingira pia Serikali inafanya jitihada kwa kutoa kipaumbele maalum katika maeneo ambayo magereza ya akina mama wenye watoto yapo.
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninashukuru sana kwa majibu ya Serikali.
Kwa kuwa tuna kituo cha polisi chenye hadhi ya Wilaya, hiki ni kituo kipya na bado kina changamoto, tunao askari wachache 38 tu, lakini askari hawa wanafanya kazi nzuri kwa kushirikiana na wananchi, Madiwani na Halmashauri.
Pia kwa kuwa hakuna vifaa/vitendea kazi yakiwemo magari, kwa sasa Halmashauri ya Ushetu tumewapa Polisi jengo pamoja na gari. Tunahitaji kuwa na vituo vidogo kandokando kwa sababu Jimbo la Ushetu ni kubwa, linapakana na majimbo nane na tumedhamiria kutokomeza kabisa mauaji ya wazee na walemavu.
Je, ni lini Serikali itatupatia vifaa ikiwemo magari pamoja na askari ili angalau tufikishe askari 100. Hii itasaidia sana pia kupunguza makosa katika majimbo nane ambayo napakana nayo. Ni lini sasa Serikali itatusaidia?
Swali la pili, kwa kuwa tunazo jitihada za kujenga vituo vidogo kando kando katika maeneo ya Kata ya Chambo, Kata ya Ulowa, Kata ya Ubagwe na kata Idahina na kwa kuanzia katika Kata ya Idahina tuna jengo ambalo tumetumia nguvu za wananchi, Mbunge pamoja na wachimbaji wadogo, na litaweza kuwa accommodate ofisi pamoja na askari wapatao watano.
Je, Serikali iko tayari sasa kutusaidia kukamilisha jengo hili ili tuweze kupata askari tuweze kuimarisha masuala ya usalama katika eneo hili ambalo linakuwa kwa kasi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa jitihada zake kubwa alizonazo za kuhakikisha kwamba hali ya usalama katika Jimbo lake inaimarika, amekuwa akifuatilia kwa karibu sana maendeleo ya vyombo vyetu vya usalama katika Jimbo lake naomba nimpongeze sana kwa niaba ya wananchi wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la kuongeza idadi ya askari na vitendea kazi vingine ikiwemo magari, naomba nilichukue hilo nikitambua kwamba katika bajeti ya mwaka huu wa fedha tuna matarajio ya kuongeza na kuajiri vijana wapya japokuwa ni kweli tuna uchache wa askari siyo tu katika Jimbo lake, ni katika maeneo mengi nchi nzima. Kwa hiyo, tutazingatia kulingana na mahitaji ya nchi nzima ili tuone jinsi gani tunaweza kufanya kusaidia jitihada za askari wetu pale katika Jimbo lake pamoja na usafiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na jengo lake ambalo amezungumzia vilevile kama nilivyokuwa nikijibu mara nyingi hapa, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba majengo ya hivi vituo vyetu vya vyombo vya usalama vyote ni malengo ya Serikali kuhakikisha kwamba vinaimarika, tuna upungufu huo vilevile katika maeneo mengi nchini. Nichukue fursa hii kumhakikishia kwamba jitihada zinafanyika hata nje ya bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tumekuwa na utaratibu wa kutumia taasisi yetu ya Jeshi la Magereza kuweza kuanza ujenzi kwa kutumia rasilimali za maeneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kutoa wito kwa Mheshimiwa Mbunge kulitumia Jeshi la Magereza katika eneo lake kwa ajili ya kuanza harakati za ujenzi wa kituo hicho na baadaye pale itakapofikia katika hatua nzuri tunaweza kulikamilisha kwani katika mwaka huu wa fedha tumetenga bajeti fedha za kutosha kuhakikisha kwamba tunamaliza maboma yote ambayo yamejengwea kwa nguvu za wananchi pamoja na nguvu na vyombo vyetu vya usalama kwa kutumia rasilimali za maeneo yale.(Makofi)
MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, lakini kidogo hayaniridhishi, kwa sababu yeye mwenyewe Naibu Waziri amekwenda kujionea kituo hicho cha Bububu, alikitembelea.
Je, kituo kile kwa sababu hakina computer, hakina photocopy machine na mpaka hivi sasa hivi wanaenda kutoa photocopy nje ya kituo. Ni lini Serikali itachukua hatua ya kukipatia computer na photocopy machine?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa sababu huko nyuma niliulizwa suala la gari ya polisi, kwa sababu kituo changu kipo barabarani na kina uhalifu mwingi katika Jimbo langu la Bububu.
Je, ni lini Serikali itatupatia gari hilo la Polisi ili kupunguzia wananchi usumbufu? Kwa sababu sasa hivi wakiomba gari binafsi wanachukua ili kwenda kusaidia kufanya doria?
Naiomba Serikali ijitahidi ili kituo changu kipate gari ya doria ili kupunguza usumbufu kwa wananchi. Ahsante.
NAIBU WAZIRI MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mwantakaje kwa jitihada zake za kuhakikisha kwamba mazingira ya askari wetu hasa katika Kituo cha Polisi Bububu katika Jimbo lake yanakuwa mazuri.
Mheshimiwa Spika, ni kweli tulifanya ziara ya pamoja kwenye kituo hiki na kuna mambo mengi tuliyarekebisha, lakini nimhakikishie, kama tumeweza kurekebisha mambo makubwa ambayo mwenyewe anafahamu, sidhani kama hili la photocopy na computer litatushinda. Nimwombe tu avute subira, tutalifanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, upande wa suala la pili kuhusiana na gari, kwa sasa bado hatuna magari, lakini tunatarajia kupata magari. Kwa hiyo, tutaangalia ukubwa wa changamoto zilizopo nchi nzima, kwa sababu upungufu haupo Bububu peke yake, yako maeneo mbalimbali nchini. Kwa hiyo, kadri ya idadi ya magari itakapopatikana, tutaangalia uwezekano vilevile wa kukipatia Kituo cha Polisi cha Bububu. (Makofi)
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali aliloulizia Mheshimiwa aliyezungumza sasa hivi, halina tofauti kabisa na Gereza la Keko ambalo miundombinu yake ni mibaya na pia kuna msongamano mkubwa sana wa wafungwa na wengi wao zaidi ya nusu ni mahabusu na hivyo hivyo kwenye Gereza la Segerea.
Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba justice inakuwa dispense, mapema watu watoke na magereza yawe na wafungwa ambao ndio wangestahili kukaa pale na hiyo miundombinu iliyokuwepo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, tunakiri juu ya tatizo la msongamano, kwani ukiangalia takribani Magereza yote kwa ujumla nchini ukiachia mbali la Keko na mengine, mpaka leo tunavyozungumza, tuna takriban wafungwa wanaokadiriwa kufika mpaka 40,000 na wakati capacity ya Magereza yetu haizidi 30,000. Kwa hiyo, utakuta tuna idadi ya wafungwa kama 10,000 hivi ambao wamezidi kiwango magerezani.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua hilo, ndiyo maana Serikali inachukua jitihada mbalimbali kupunguza msongamano huu ikiwemo kupitia zile sheria nne tulizozipitisha hapa Bungeni za kuwapatia kifungo cha nje wafungwa kwa utaratibu wa parole, lakini pia utaratibu wa community services za EML, lakini pia kwa kupitia msamaha wa Rais. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa jitihada zake alizochukua za kupunguza idadi ya wafungwa mwaka 2017.
Mheshimiwa Spika, pia moja ya jitihada ambazo Serikali inachukua, ni kuhakikisha kwamba tunatenga bajeti ya kutosha kadri ya hali ya fedha inavyoruhusu kupanua Magereza yetu yaweze kuwa na ukubwa zaidi na kuongeza magereza mengine nchini.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hizo ndizo jitihada ambazo tunachukua na tunaamini kabisa kadri tunavyokwenda hivi, sasa hivi uchumi wetu wa nchi, unakwenda vizuri, naamini miaka ya mbele tatizo la msongamano litapungua kama siyo kuisha kabisa.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona na kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, mwuliza swali alikuwa anauliza kuhusu ukarabati wa kituo, lakini kwa kuwa Wilaya ya Kilolo ni ya siku nyingi sana na haijawahi kujengewa Makao Makuu ya OCD yalipo Makao Makuu ya Wilaya toka imeanzishwa, na kufanya OCD kukaa mbali na DC. (Makofi)
Je, ni lini sasa Serikali itaona umuhimu wa kujenga Makao Makuu ya Polisi yalipo Makao Makuu ya Wilaya ya Kilolo?
NAIBU WAZIRI MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, ni sahihi kabisa, Kilolo hatuna Kituo cha Polisi cha Wilaya na hii ni moja ya vituo 65 vya wilaya nchini ambavyo hatunavyo na ambavyo vipo katika mpango wa Serikali wa kuvijenga. Kwa hiyo, Kilolo ni kimojawapo.
Mheshimiwa Spika, wakati jitihada hizi za Serikali za kuweza kuona jinsi gani tunafanya kujenga vituo 65 zinaendelea, basi nataka nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutafanya ziara katika Mkoa wa Iringa hivi karibuni ili tushirikiane tuangalie namna gani nyingine ambayo tunaweza tukafanya ili kuweza kuunga mkono jitihada za Serikali za kujenga kwa kushirikisha wadau mbalimbali.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri amejibu kipengele kimoja tu cha swali na kipengele kinachofuata hajakisoma. Kwa kuwa nimepewa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza nafikiri atakisoma atakaporudi kwenye jukwaa.
Mheshimiwa Spika, Gereza la Njombe lina msongamano mkubwa sana na katika msongamano huu wako akina mama wenye watoto wadogo mle ndani ya Gereza.
Je, Serikali sasa iko tayari kuwapa chakula maalum watoto wale ili kutokuwaathiri makuzi yao na kuwafanya wakue wakiwa na afya bora? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, katika Gereza la Njombe, yuko Mahabusu anaitwa Erick Mgoba. Mahabusu huyu amepelewa Hospitali ya Rufaa kwa kushirikiana na Gereza la Njombe ili apatiwe matibabu. Alivyofika Hospitali ya Rufaa Mbeya akatakiwa kulipa shilingi 300,000 ili atibiwe na akarudishwa Njombe bila kutibiwa na afya yake ni mbaya.
Je, Serikali iko tayari kumtibu mahabusu huyu ili kuokoa maisha yake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, kwanza nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mbali ya upungufu wa fedha ambazo tunatumia kwa kumlisha chakula mfungwa, ambayo nimezungumza katika jibu langu la msingi kwamba ni shilingi 1,342; lakini tunahakikisha kwamba chakula ambacho anakula mfungwa ni chakula chenye kiwango cha kutosha. Tunapima hivyo kulingana na calories ambayo nadhani ni 2,200 na kitu kwa kila mfungwa; 2,200 kwa mfungwa mwanaume na 2,500 kwa wafungwa wanawake.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, suala la watoto na wafungwa wa kike na wa kiume kwa ujumla, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba wanapata chakula chenye ubora na chenye kiwango cha kuridhisha, juu ya upungufu wa fedha, lakini kiwango tunahakikisha kwamba kinakuwa kwa maana ya lishe, inakuwa ni lishe ambayo iko sawa kabisa kitabibu.
Mheshimiwa Spika, la pili, kuhusiana na matibabu ya mfungwa ambaye amemzungumza amesema kama tuko tayari, naomba baada ya Bunge hili mimi na yeye tukutane tuone jinsi gani tunalishughulikia hili jambo. Ni lazima tuhakikishe kwamba mfungwa huyu anapata matibabu. (Makofi)
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ufanisi na utendaji wa Mahakama unategemea ushahidi katika utendaji wake, lakini imekuwa ni jambo la kawaida ukiwa katika Mahakama zetu mara baada ya kusomwa Shauri Namba, Waendesha Mashtaka kusimama na kuiambia Mahakama tunaomba Mheshimiwa Hakimu au Jaji uahirishe shitaka hili kwa sababu upelelezi haujakamilika, hivyo ni vitu vya kawaida sana.
Je, Serikali kwa kushindwa kupeleka ushahidi haraka katika Mahakama kwa kesi zinazoendelea ndiyo chimbuko la kusababisha mlundikano wa mahabusu katika Magereza yetu na jambo hilo ndilo linalosababisha wananchi wengi kukosa imani na Mahakama na kuona hazitendi haki, je, hamuoni kwamba kuchelewesha kupeleka ushahidi katika Mahakama mnasababisha lawama kwa Mahakama ambazo kimsingi siyo za kwao? (Makofi)
Swali la pili, katika nchi yetu lilitokea tukio kubwa na baya la ugaidi ambalo lilisababisha maisha ya watu wetu kupotea katika Ubalozi wa Marekani pale Dar es Salaam. Kuna watuhumiwa ambao walichukuliwa hapa kwenye nchi yetu na wakapelekwa Marekani kwa ajili ya mashtaka hayo na upelelezi wa makosa hayo, lakini haikuchukua zaidi ya miaka miwili watuhumiwa wale walionekana hawakuwa na makosa na wakaachiwa huru Marekani na Tanzania.
Je, ni kwa nini mpaka leo watuhumiwa wa ugaidi, Mashekhe wa Uamsho kutoka Zanzibar ambao hawakuua hata kuku katika mashtaka yao, mpaka leo mmeendelea kuwashikilia ilihali mmeshindwa kupeleka ushahidi. Mpaka lini Serikali mtaendelea kuwashikilia wazee wa watu wale na mmeshindwa kuthibitisha makosa yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la upelelezi ni jambo la msingi ili kuhakikisha kwamba haki inatendeka. Lazima Jeshi la Polisi lifanye uchunguzi wa kina na kujiridhisha juu ya makosa ambayo yamefanywa na mtuhumiwa ili hatimae mtuhumiwa yule aweze kutendewa haki. Kwa hiyo, ninaomba Mheshimiwa Mbunge aelewe kwamba siyo dhamira ya Serikali wala Jeshi la Polisi kuchelewesha upelelezi, lakini kuna aina ya makosa ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi ya ziada ambayo yanahusisha taasisi nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano kunahitaji kufanyika utafiti kutoka katika vyombo na mamlaka nyingine, masuala ya mawasiliano kwa mfano TCRA, kuna masuala yanayohusu uhamiaji, masuala ya taasisi nyingine mbalimbali za ndani na nje ya nchi. Kwa hiyo, ili kuweza kuhakikisha kwamba mtuhumiwa yule anatendewa haki lazima Jeshi la Polisi lipate muda wa kutosha. Hakuna Serikali ama chombo chochote cha Serikali kinachohitaji kumkomoa mwananchi wake, hilo la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili kuhusiana na suala la watuhumiwa wa Uamsho. Tuhuma ambazo zinawakabili watu hawa ni nzito, kwa hiyo basi ni lazima uchunguzi wa kina vilevile ufanyike ambao utahitaji muda. Kwa hiyo, naomba jambo hili kwa kuwa liko Mahakamani siyo busara kwa mujibu wa sheria za nchi na Katiba ya nchi hii kulijadili katika Bunge hili Tukufu, tuacha mamlaka husika na mhimili wa dola ufanye kazi yake.
MHE. JUMA S NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
• Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri anasema Jeshi la Polisi likishirikiana na wadau Wilayani Chemba wamekaribia kuanza ujenzi ningeomba anihakikishie ni wadau gani hawa ambayo yeye ana taarifa kwamba tayari wanaanza kushirikiana kujenga kituo cha polisi?
• Binafsi nimechangia kwa kiwango kikubwa sana katika ujenzi wa kituo kipya cha Polisi kule Kwa Mtoro na Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani Komredi Mwigulu alinihaidi hapa ndani ya Bunge kwamba kutokana na mazingira ya Kwa Mtoro hadi Makao Makuu ya Wilaya ya Chemba ambao ni karibu kilometa zaidi ya 120 Serikali ingeweza kuwapatia askari wale gari la kuweza kuwasaidia kwa sababu wanapita kwenye Hifadhi ya Swagaswaga na kuna wanyama wakali. Je, hilo gali litapatikana lini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimejibu katika swali langu la msingi nilieleza kwamba Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ikishirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo wananchi wameanza mchakato wa ujenzi wa kituo hiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusiana na swali lake la pili kwanza nimpongeze kwa juhudi zake za kuchangia maendeleo ya Jeshi la Polisi katika Wilaya yake, lakini kuhusiana na hali ya Mheshimiwa Waziri nataka nimhakikishie kwamba ahadi ya Mheshimiwa Waziri kama alitoa iko palepale tatizo linalokwamisha ni kwamba bado magari hayo hayajapatikana, naamini kabisa wakati ambapo tumepata magari ya kutosha basi ahadi hiyo itatekelezwa.
MHE. ANDREW J. CHENGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Gereza la Matongo ni miongoni mwa Magereza yaliyoanzishwa na Serikali katikati ya miaka 1970 kwa lengo hilo hilo ambalo Waziri amesema katika jibu lake, lakini zaidi ya miaka 40 ukifika pale Matongo hakuna cha maana kinachoendelea. Mheshimiwa Naibu Waziri katika majibu yake anasema Gereza hili limo kwenye mpango wa kuboresha kilimo, ni lini mpango huu mahsusi kwa Gereza la Matongo utaanza kutekelezwa na Serikali? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri katika majibu yake ametambua mazao yanayolimwa katika eneo hilo likiwepo eneo lenyewe la Matongo. Je, yuko tayari na ikiwezekana kushirikiana na Mbunge wa eneo hilo kutafuta mwekezaji ili kuanzisha kiwanda ili kuongeza thamani ya mazao yatakayolimwa na Magereza lakini pia kusaidia soko kwa wananchi ambao wanazunguka eneo hilo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza nimeshamjibu katika majibu yangu ya msingi, naomba tu nichukue fursa hii kufafanua. Nimesema kwamba tuna mkakati wa kuhakikisha kwamba Jeshi la Magereza linajitosheleza kwa chakula. Kwa sasa hivi Jeshi la Magereza linajitosheleza kwa chakula kwa asilimia 30, malengo yetu ni kuhakikisha kwamba tunafikia asilimia 70.
Mheshimiwa Spika, mkakati huu utatekelezwa baada ya kuhakikisha kwamba tumepata fedha za kutosha kuwekeza. Katika bajeti ya maendeleo ya mwaka huu tunatarajia kupata takribani shilingi bilioni 3 ambazo zitatumika katika moja ya mikakati ya kuimarisha kilimo pamoja na kujitosheleza katika Magereza yetu. Pia tuna mpango vilevile kupitia jitihada za Mheshimiwa Waziri Mkuu kupata matrekta 50 kwa kuanzia ambayo tutayapeleka katika Magereza ikiwemo Gereza hili la Matongo ili kuweza kusaidia kuimarisha kilimo katika maeneo hayo. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge aendelee kuvuta subira lakini ni jambo ambalo tayari liko katika hatua nzuri za utekelezaji.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili kwamba kama Serikali iko tayari kushirikiana na mwekezaji kuwekeza. Ndiyo mikakati ya Serikali ya Awamu ya Tano kuhakikisha kwamba nchi yetu inafikia uchumi wa kati kupitia viwanda. Kwa hiyo, nina uhakika kabisa Mheshimiwa Mbunge akiweza kuwasiliana na mamlaka husika kwa maana ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji atapata mwongozo na msaada mzuri wa kuweza kusaidia jitihada za Serikali za kuimarisha viwanda katika nchi yetu. Sisi kama Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi pale ambapo tunaweza kutoa mchango wetu kwa namna yoyote ile tutakuwa tayari kushirikiana naye.
MHE. TWAHIR AWESU MOHAMMED: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba nimuulize maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, imekuwa ni kawaida sasa katika nchi yetu watu kutekwa, kupigwa, kuumizwa na hata kuuliwa. Kumekuwa na dhana kwamba Jeshi la Polisi linafahamu fika tendo hili, lakini wamelinyamazia. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anataka kuwaambia nini Watanzania ili isije ikafika hatua wakajichukulia sheria mikononi mwao? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kumekuwa na katazo la kufanya mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa. Siku ya tarehe 8 Aprili, 2018, CCM mikoa miwili ya Pemba waliandamana chini ya ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi wakiwa wamebeba mabango wakiimba nyimbo za kuhatarisha amani, za uchochezi. Mheshimiwa Naibu Waziri nataka aniambie, hili katazo linahusu Vyama vya Siasa vya Upinzani pekee au ni kwa vyama vyote vya siasa? (Makofi).. Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza sikubaliani na maoni ya Mheshimiwa Mbunge maana maoni yoyote yanahitaji yathibitishwe, yahalalishwe, yalinganishwe. Kwa takwimu ambazo ninazo zinaonesha hali ya uhalifu nchini inaendelea kupungua. Sasa anaponiambia kwamba sasa hivi kuna ongezeko la mambo ya uhalifu, akataja mengi tu, ninachoweza kusema ni kwamba tuna Jeshi la Polisi kwa sababu ya hulka ya baadhi ya binadamu kufanya au kufikiria kufanya uhalifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika nchi zote majeshi ya polisi au vyombo vya dola vipo kuzuia hizo hali, kwa hiyo hatuwezi kusema kwamba kuna Taifa duniani ambalo litakuwa halina element yoyote ya uhalifu. Ninachoweza kumhakikishia ni kwamba Jeshi la Polisi linafanya kazi yake nzuri na ndiyo maana hali ya uhalifu imepungua nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusiana na wananchi, kwamba wachukue sheria mkononi, naomba tu nimsisitize Mheshimiwa Mbunge kwa wananchi wake na wananchi wengine ambao wananisikiliza hapa kwamba tunaendelea kusisitiza kwamba wausijaribu kuchukua sheria mkononi. Mamlaka za dola zipo kwa ajili yao na pale ambapo wanaona kwamba kuna tatizo lolote la uhalifu basi wawasilishe malalamiko yao katika vyombo husika na sheria itachukua mkondo wake. Kitendo cha kuchukua mkononi hakihalalishi aliyechukua sheria mkononi asichukuliwe hatua na yeye za kisheria pindi atakapokuwa amevunja sheria, hata kama atakuwa ametendewa kosa.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ametoa mfano wa tarehe fulani ambayo CCM waliandamana, bahati mbaya sina taarifa hizo, lakini ninachoweza kusema ni kwamba suala la kuandamana, suala la kufanya mikutano na kadhalika linapotokezea ni lazima Jeshi la Polisi litoe ulinzi ili shughuli ile kama ni maandamano au mkutano, kama umeruhusiwa lakini kwa mujibu wa sheria na taratibu zimefuatwa, lazima Jeshi la Polisi liwepo kutoa ulinzi wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo sisi tunachoweza kusema ni kwamba kipindi hiki ambapo Serikali yetu ya Awamu ya Tano ina shughuli nyingi za mafanikio makubwa kiuchumi na ninyi mnaona, ni mashahidi, kwamba Taifa letu linaendelea kupiga hatua kwa kasi kabisa na uchumi wetu unainuka na kero nyingi zimetatuliwa, Jeshi la Polisi lina jukumu la kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama. Hatuwezi kuendekeza kutoa ulinzi kwa maandamano, mikutano, hatuna askari wa kutosha kuweza kufanya shughuli hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana tunasema kwamba kwa taasisi yoyote au chombo chochote ambacho kitahitaji kufanya maandamano na mikutano isiyokuwa na tija, Jeshi la Polisi halina muda huo, lina muda wa kulinda maisha ya wananchi na usalama wao katika kipindi hiki ambapo Serikali yetu inapiga hatua kubwa ya maendeleo. Kwa hiyo, hii si kwa chama chochote, si kwa mtu yeyote haibagui mtu, ni sheria msumeno inakata pande zote mbili. (Makofi)
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri tuliyoyazoea, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, takriban tangu kuungua kwa kitu hiki ni miaka tisa na kipindi hicho chote askari wanafanya kazi katika mazingira magumu sana kiasi wanahatarisha afya zao. Kwa kuwa Serikali imeshindwa kukamilisha kituo hiki katia muda mwafaka, je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kukifunga kituo hiki mpaka ujenzi wake ukamilike kwa usalama wa skari wetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imetenga shilingi bilioni 2.2 kwa ajili ya kupunguza madeni ya wakandarasi. Kituo cha Mkokotoni kimetengewa shilingi milioni 200 kwa ajili ya mkandarasi aliyejenga kituo kile, nataka kujua, je, mkandarasi huyo ameshalipwa pesa zake? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi hatuna mpango wa kukifunga hiki kituo kwa sababu mipangilio ya kukiendeleza, kukikamilisha iko mbioni na ndiyo maana naomba nichukue fursa hii kumjulisha Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tumeshafanya uhakiki na kuwasilisha Hazina ili mkandarasi aweze kulipwa na ujenzi uweze kukamilika. Kitakapo kamilika kituo hiki kitatumika. (Makofi)
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza naomba nimpongeze Mkuu wa Wilaya ya Mlele, tayari ameshaanza kufanya hamasa kwa ajili ya Kituo cha Polisi Wilaya ya Mlele, lakini kwa kuwa jengo hili la polisi ambalo wanalitumia sasa hivi ni jengo ambalo walijenga wananchi wakati ikiwa Kata ya Inyonga kwa ajili ya usalama wao, sasa hivi imekuwa Wilaya na matukio yamekuwa mengi zaidi kupita nyuma na uhitaji wa usalama unahitajika zaidi kwa sababu sasa hivi ni Wilaya siyo Kata na wananchi wale walivyojenga hili jengo ambalo walilikabidhi Polisi, walijenga Kituo kidogo na chumba cha mahabusu kidogo…
Mheshimiwa Naibu Spika, kama wananchi walijenga, Serikali inatakiwa ifanye maboresho. Je ni lini Serikali itafanya maboresho ili sasa kile kituo kionekane kama kituo cha Wilaya?
Swali langu la pili, kutokana na chumba kidogo cha mahabusu, kwa sababu sasa hivi mahabusu wale wanachukuliwa wanapelekwa Mpanda Mjini, halafu wanarudishwa Inyonga, gharama kila siku gari limekwenda Mpanda linarudi Inyonga, Serikali haioni ni vyema zile gharama ambazo zitumika kila siku kupeleka gari Mpanda Mjini na kurudisha Inyonga zikatumika kujenga Kituo cha Polisi katika Wilaya ya Mlele?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge na wananchi wake wa eneo hilo na Mbunge wa Jimbo husika kwa jinsi ambavyo wameweza kufanikiwa kuanza ujenzi wa kituo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimekuwa nikijibu mara kadhaa hapa, siyo kwamba Serikali haina mpango wa kujenga vituo vya polisi hususan katika ngazi za Wilaya, mpango huo upo. Nilizungumza jana kwamba tuna mpango wa kujenga vituo takribani 95 nchi nzima, lakini kwa sasa hivi bado hali ya kibajeti haijakaa sawa. Pale ambapo hali ya kibajeti itakapokaa vizuri, eneo hili ni moja katika vipaumbele vyetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kabisa tutakapojenga kituo katika eneo hilo, litatatua vilevile changamoto ya udogo ya chumba cha mahabusu. (Kicheko)
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; Wilaya ya Itilima Makao Makuu yake yako Kata ya Lagangabiliri na Kituo cha Polisi kipo Kata ya Luguru. Je, Serikali ina mpango gani kuhamishia Kituo cha Polisi katika Makao Makuu ya Wilaya ya Itilima? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa kituo kinachotumika kwa sasa kilitolewa kwa hisani ya Ndugu Paulo Ng’hwani kwa muda mrefu na kituo hicho kwa maana ya hilo jengo limeharibika, je, mna mkakati gani sasa wa kupeleka fedha angalau kukarabati jengo hilo ambalo lilitolewa kwa hisani ya Ndugu Paulo Ng’hwani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kwanza kutoa pongezi zangu za dhati kwa Mbunge wa Itilima, Mheshimiwa Njalu ambaye wakati wa ziara yangu nilipofanya kule niliona jitihada zake kubwa sana ambazo amekuwa akizitoa katika kufanikisha kutatua changamoto kwenye eneo la Polisi kwa ujumla wake. Moja kati ya jitihada hizo ni kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Kituo cha Polisi ambacho sasa hivi kinaendelea na ujenzi wake. Vile vile Mheshimiwa Mbunge aliniahidi kwamba kazi hiyo ataendelea nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge Dotto naye namshukuru vilevile kwa kuona changamnoto hizo. Naomba tu aendelee kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo na Serikali kwa pamoja tutashirikiana kufanikisha ujenzi ukamilike kwa haraka ili kituo hiki kiweze kutumika. Ukarabati wa kituo kingine utategemea na hali ya upatikanaji wa fedha.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri nimeyasikia na naomba anisikilize kwa makini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba eneo hilo la Tarafa ya Kipatimu lina zaidi ya wakazi 60,000, hatuna kituo cha Polisi, jitihada hizo zimefanywa na wananchi, nikiwemo na Mbunge, nimetoa mifuko 100 ya saruji ku-support na wananchi tayari wamefyatua matofali, tunayo matofali, lakini shida kubwa tunayopata ni ushirikiano kutoka kwa ofisi yake ya Mkoa ambayo mpaka sasa tumehitaji kupata ramani imekuwa shida, tumehitaji kupata mchanganuo imekuwa shida. Je, sasa Mheshimiwa Waziri yuko tayari kunipatia ramani na mchanganuo wa ujenzi ule ili ujenzi uweze kuendelea kwa sababu wananchi wana ari kubwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza kwa mchango wake katika kufanikisha ujenzi wa kituo hicho.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na ramani na ushirikiano mwingine nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge kwamba atapata. Naomba tu baada ya maswali tukutane ili niweze kumpa utaratibu huo namna gani ambavyo anaweza akapata ushirikiano huo, naamini kabisa inawezekana tu tatizo ni mawasiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kawaida Vyombo vyetu vya Dola, kwa maana ya Jeshi la Polisi, vimekuwa vikipenda sana kufanya kazi karibu na wadau mbalimbali ikiwemo Wabunge na wamekuwa wakitoa ushirikiano wa haraka. Kwa hiyo, nadhani kama kulikuwa na changamoto ya mawasiliano, basi baada ya maswali nitakuwa tayari kumsaidia kufanikisha hilo kwa haraka. (Makofi)
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na Kituo cha Kipatimo ambacho amesema Mbunge mwenzangu wa Kilwa Kaskazini, Mbunge wa Kilwa Kusini kuna kituo cha Polisi ambacho kimejengwa na wananchi lakini bado kumalizika kule Kijiji cha Nanjilinji. Je, Mheshimiwa Waziri, unaweza kutusaidia ili kituo hicho kimalizike?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Kituo cha Nanjilinji ni miongoni mwa vituo vingi ambavyo vimejengwa kwa nguvu za wananchi ambavyo vinahitaji kukamilika. Hiyo ni dhamira ya Serikali, kuhakikisha kwamba vituo vyote hivyo nchi nzima ambavyo vimejengwa kwa nguvu za wananchi vinakamilika, siyo tu kwa sababu ya faida na manufaa ya matumizi ya vituo hivyo, lakini pia kwa kuweza kutokuwavunja moyo wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Kituo cha Nanjilinji, pale ambapo hali ya kifedha itakaa vizuri, tutakimaliza pamoja na vituo vingine, lakini Mheshimiwa Mbunge vilevile anaweza akatumia fursa hiyo kusaidia kuweza kufanikisha ujenzi huo kwa kuhamasisha wananchi wake ama wadau kuendeleza jitihada hizi za Serikali na Serikali pale ambapo uwezo utakuwa tayari basi tutavimaliza.(Makofi)
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Ujenzi wa Kituo cha Polisi Keza, Wilaya ya Ngara, kilichojengwa kwa nguvu za wananchi, kitakamilika lini maana kina zaidi ya miaka saba kimeezekwa bado finishing. Je, ni lini Serikali itamalizia ujenzi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Kituo cha Keza nacho ni miongoni mwa vituo ambavyo havijakamilika. Bahati njema ni kwamba mwaka huu wa fedha katika Mkoa wa Kagera tumetenga takribani bilioni 1.56 kwa ajili ya kumaliza miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo haijakamilika, ikiwemo nyumba pamoja na vituo vya Polisi. Hiyo inaonesha azma ya Serikali ya kuweza kukabiliana na changamoto ya kumaliza vituo hivi ambavyo havijakamilika pamoja na nyumba za Askari nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba dhamira ya Serikali ipo na pale ambapo hali ya kifedha itakaa vizuri basi tutakamilisha kituo hicho pamoja na vituo vingine ambavyo kama alivyosema mwanzo kwamba viko sehemu mbalimbali katika nchi yetu. (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo Mheshimiwa Oliver Semuguruka amesema, ni kweli tuna vituo vingi ambavyo vimeshafikia hatua hiyo, niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge kwa sababu wamechangia kwa kiwango kikubwa sana. Kwa sababu ni wengi tu siwezi kuwataja wote, lakini natambua Mheshimiwa Maige, Mheshimiwa Ritta Kabati, Mheshimiwa Oran Njeza na wengine wengi ambao mmechangia ujenzi wa vituo hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kituo kilichoulizwa, Mheshimiwa Ulega hapa ndiye aliyekianzisha, niwaombe Waheshimiwa Wabunge kwa sababu wameongelea sana masuala haya ya vituo ambavyo vimeshafikia hatua ya kukamilishwa pamoja na nyumba za vijana wetu ambazo zimejengwa kwa nguvu za wananchi, kwa sababu bado tuko hapa na bajeti tumeshapitisha, niwaombe Waheshimiwa Wabunge wanipenyezee maeneo ambayo yana vituo hivyo ili tunavyomaliza Bunge twende tukae ngazi ya Wizara tuweze kuweka vipaumbele ili tusiharibu nguvu kazi za wananchi ambazo zimeshafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Joseph Selasini ameliongelea sana jambo hili, leteni hivyo vituo ili tutakapokwenda kukaa kwenye ofisi tuweze kuona kile tulichonacho na kuweza kumalizia vile ambavyo vimeshafikia hatua za kumaliziwa. (Makofi)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba niwashukuru sana Jeshi la Polisi la Zimamoto. Juzi walipata ajali ya moto katika Kata ya Zingiziwa na ukaunguza maduka zaidi ya 15 lakini kwa mara ya kwanza Zimamoto waliwahi mapema wakasaidia kuzima moto ule pamoja na kwamba mdhara yalikuwa makubwa lakini walisaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki kituo kimejengwa kwa nguvu za wananchi pamoja na wadau mbalimbali na Naibu Waziri anafahamu kwamba hii sehemu ndiyo mpakani mwa Mkuranga, unaenda Mkuranga, Kisarawe, mapori ya Dondwe na kama alivyosema vingine vyote ni Police Post. Kwa hiyo, naomba hii hoja ya kutafuta gari, kabla ya kuleta hili swali hapa Bungeni nimewasiliana na mapolisi, wanapata shida na eneo ni kubwa, Ukonga sasa ina watu zaidi ya 900,000. Kwa hiyo, kwa kweli tunahitaji gari kwani hilo gari lililopo linafanya kazi ya OCS na ikitokea dharura wanakuwa stranded wanakimbiza watu na pikipiki jambo ambalo ni hatari. Eneo hili Benki ya CRDB imefungwa kwa sababu ya kiusalama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningeomba hii hoja ya kutafuta gari ipewe uzito, gari liende pale liwe stagnant kwamba kuna gari ambalo viongozi wanalitumia na gari la doria kwa maana ya ku-control Ukonga yote. Kwa hiyo, ningeomba hilo lizingatiwe. Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza…
Haya la pili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Kata ya Kivule tunalo eneo tayari la kituo cha polisi, kama ambavyo Chanika wamejenga wananchi tumechangia, ningeomba commitment ya Waziri au Jeshi la Polisi, ni lini tutaenda kufanya harambee eneo lile kwa sababu tayari wananchi wameweka msingi eneo hili. Bunge lililopita Waziri aliahidi hajaja, kwa hiyo, leo naomba kauli yake.
Lini twende Kivule, tuchangishe fedha tujenge kituo kingine ili tupunguze uhalifu katika eneo lile? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya ya Mheshimiwa Waitara, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimepokea pongezi zake kwa niaba ya Jeshi la Zimamoto kuhusiana na kazi nzuri ambayo inaendelea kufanywa. Hii inathibitisha juu ya kuimarika kwa huduma za vyombo hivi vilivyo chini ya Wizara ya Mambo ya Nchi ikiwemo Jeshi la Zimamoto katika kutekeleza majukumu yake na kuwapatia huduma wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la kwanza, kama ambavyo nimejibu katika swali langu la msingi kwamba tutaangalia uwezekano huo. Kama unavyofahamu kwamba tuna changamoto za magari maeneo mengi nchini, kwa hiyo, tutaangalia vile vigezo na kulingana na idadi ya magari ambayo tutapokea ndipo tutaamua eneo hili linapaswa lipelekewe gari sasa hivi ama baadaye. Hata hivyo, tunatambua umuhimu wa kupeleka gari katika eneo hilo na maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ni kuhusu lini tutafanya harambee. Kwanza nimpongeze Mbunge kwa jinsi ambavyo ameweza kuhamasisha kuhusiana na hili suala la harambee, mimi nimwambie tuko tayari hata sasa hivi. Kwa hiyo, baada tu ya Bunge hili Tukufu tukae tuweze kupanga ratiba ya kuweza kufanya hiyo kazi. Tunathamini sana jitihada za Wabunge na wadau mbalimbali katika kusaidia kukabiliana na changamoto za vituo vya polisi nchini na hili jambo tutaliunga mkono.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi. Kwa kuwa tatizo kwenye swali la msingi la 323 la usafiri wa patrol kwa vituo vya polisi lipo karibu nchi nzima. Je, Serikali sasa inajipangaje kwenda kutatua tatizo hili la usafiri wa patrol katika vituo vya polisi hasa katika Jimbo langu la Kavuu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Kikwembe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama ambavyo nimesema mwanzo kwamba tuna mpango wa kuweza kuona jinsi gani tutapunguza changamoto ya vitendea kazi ikiwemo magari katika kutoa huduma za Jeshi la Polisi. Nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba ndiyo maana sasa hivi tupo katika jitihada za kuweza kukamilisha na kurekebisha mapungufu ambayo yalijitokeza ili tuweze kusambaza magari hayo ambayo yanategemewa kusaidia kupunguza changamoto hiyo ikiwemo katika Jimbo lake, kulingana na vigezo ambavyo nimevieleza katika swali langu la msingi.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mkoa wa Arusha jiografia yake ni pana sana na mkoa huu upo mpakani, hivyo unahitaji uangalizi mkubwa kiusalama, lakini magari mengi ya polisi ni mabovu. Je, ni lini Serikali inafikiria kutuletea magari ya polisi mapya ndani ya Mkoa wa Arusha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Catherine Magige, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Arusha, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya magari iliyopo katika Mkoa wa Arusha nayo tunaitambua. Katika mkakati wetu siyo tu kupeleka magari mapya lakini tunajitahidi kuangalia uwezekano wa kuyafanyia matengenezo yale magari ambayo yanaweza yakarekebishika. Kazi hiyo imewezwa kufanywa katika baadhi ya mikoa na Arusha tutaangalia uwezekano wa kuweza kukarabati magari hayo lakini wakati huohuo magari yatakapokuwa yamepatikana tutaweza kuyasambaza katika mikoa yote nchini ikiwemo Mkoa wa Arusha.
MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza bado sijaridhika na majibu aliyotoa kwa sababu hayo ni majibu ya kila siku. Baada ya hapo, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa miundombinu ya Kituo cha Konde ni mibaya sana hasa wakati wa mvua mpaka askari avue viatu ndiyo aweze kuingia kwenye kituo kutokana na maji yanayopita mbele ya kituo. Je, hili nalo linahitaji fedha za bajeti?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, Kituo hicho cha Konde pamoja na nyumba za askari ni mbovu kabisa hazikaliki. Waziri amenijibu kuwa anasubiri fedha ni mwaka gani huo, mwaka huu au miaka kumi ijayo? Nataka kupata jibu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba arejee swali la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza halijasikika vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu kwa pamoja maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mgeni Kadika, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo hicho cha Konde ni kweli kinahitaji marekebisho na sisi tuna mpango wa kurekebisha pale ambapo tutakapopata fedha na azma hii ipo palepale. Hata hivyo, Mheshimiwa Mbunge pia ana nafasi kwa yale mambo ambayo yanaonekana kwamba ni ya dharura, ni mambo madogo madogo ambayo Mbunge hayamshindi kama mabati, anaweza akachangia jitihada hizo kurekebisha mambo hayo lakini sisi kwa upande wetu kama Serikali tuna mambo mengi tunafanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala lake la pili kuhusiana na changamoto za nyumba za askari, nadhani Mkoa wa Kaskazini Pemba ni miongoni mwa mikoa ambayo inafaidika na ujenzi wa nyumba za askari takribani nyumba 12 na Mheshimiwa Rais ametoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba nyingine 400 vilevile Mkoa wa Kaskazini Pemba tutajenga. Kwa hiyo, hiyo ni katika jitihada ambazo Serikali tunafanya na vilevile tunapokea msaada kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge au wadau wowote katika kusaidia jitihada za Serikali kupunguza changamoto hii kubwa ya vituo vya polisi pamoja na makazi ya askari hapa nchini.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Itakumbukwa kwamba kuna vituo vya polisi ambavyo walijenga wakoloni, mkarithi lakini mmeshindwa kuviendeleza. Hivi karibuni kuna vifaa ambavyo mmepeleka Kisiwani Pemba viko Wilaya ya Mkoani.
Swali, je, vifaa hivyo ndiyo vinaenda kujenga Kituo cha Kengeja ambapo ni muda wa miaka 16 unaahidi lakini hutekelezi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Masoud, Mbunge wa Mtambile, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, vifaa ambavyo tumepeleka si kwa ajili ya kujenga Kituo cha Polisi cha Kengeja bali ni kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za Askari Polisi katika Mkoa wa Kusini na Kaskazini Pemba.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunitendea haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri atakubaliana na mimi kwamba Jimbo la Konde na Mji wa Konde ndiyo uliokuwa Makao Makuu ya Wilaya kabla ya mabadiliko yaliyofanyika na kupelekwa katika Jimbo la Micheweni lakini haikuondoa uhalisia kwamba Mji wa Konde ndiyo Mji Mkuu katika Wilaya ya Micheweni hilo analielewa. Pamoja na hilo, bado Mahakama ya Wilaya ya Micheweni…
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado ipo katika Jimbo la Konde na miundombinu hii miaka yote, Mheshimiwa Waziri jibu lake ni hili kwamba Serikali mpaka ipate pesa ndiyo ifanyie marekebisho. Serikali hii hii...
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini hasa Waziri atachukua juhudi za kufanya marekebisho katika Kituo cha Polisi cha Konde ili askari wetu wapate uhakika wa maisha yao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Khatib, Mbunge wa Konde, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, jibu linakuwa linafanafana lakini na mabadiliko yanaonekana, maana mwaka jana tulizungumza kwamba tukipata fedha na utaona kwamba mwaka huu tumepata fedha za kurekebisha baadhi ya changamoto hizi za Askari wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusiana na eneo hilo kama ambavyo nimemjibu Mheshimiwa Kadika kwamba dhamira ya Serikali ipo palepale na hatua ambazo tunapiga za kupunguza changamoto hizi nchi nzima, hatua kwa hatua na awamu kwa awamu tunazipokea jitihada za Wabunge ikiwemo hata Mheshimiwa Mbunge kama ataamua Mfuko wake Jimbo atoe kidogo fedha kwa ajili ya kukarabati hicho kituo tutamkaribisha sana.
MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Wananchi wa Kondoa Mjini walikusanya nguvu sana wakajenga Kituo cha Polisi kidogo pale Mjini Stand. Kituo hiki sasa kina zaidi ya mwaka kimefungwa kutokana na upungufu na ukosefu wa askari. Je, ni lini sasa Serikali itatuletea askari kituo kile kifunguliwe na kifanye kazi iliyokusudiwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Edwin Sannda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ni kweli sababu hasa ni askari peke yake tunatarajia kuajiri askari 1,500 hivi karibuni, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutupatia kibali cha kuajiri askari hao, tunaamini kwamba itasaidia kupunguza changamoto ya askari. Nimwombe Mheshimiwa Mbunge, mimi na yeye tupange utaratibu hata weekend moja twende hapo tukaangalie ili kama changamoto tu ni hiyo na kwa sababu tunahamasisha wananchi washiriki ujenzi wa vituo haikubaliki hata siku moja kuona kituo kimekamilika halafu hakitumiki. Mimi nataka nimuahidi kwamba kama itakuwa ni changamoto tu ya askari mimi na yeye tutashirikiana kulikamilisha hilo na tutakizindua kituo hicho ili kiweze kufanya kazi.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo yametoa mwangaza kwa Watanzania, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wahamiaji haramu wanapoingia nchini bila kutambuliwa kisheria baadhi yao huzaa watoto hapa nchini. Je, hawa watoto wanakuwa raia wa nchi gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa wale Watanzania ambao wanawakaribisha wahamiaji haramu hapa nchi na wanajua kisheria siyo utaratibu, je, Serikali inachukua hatua gani kwa raia hao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Fakharia Shomar, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa suala la watoto wa wahamiaji haramu na wenyewe pia itakuwa ukaazi wao nchini ni kinyume na sheria za nchi yetu. Kama ambavyo tunafahamu kwa mujibu wa Sheria ya Uhamiaji mtu anaweza kuwa raia wa nchi ikiwa angalau mmoja wa wazazi wake wakati anazaliwa alikuwa raia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusiana na suala la raia ambao wamekuwa wakihifadhi wahamiaji haramu, kwanza tunataka kutoa wito kwa wananchi wenye tabia hizo kuacha mara moja kwani kufanya hivyo ni kinyumbe na sheria za nchi lakini vilevile adhabu yake ni kali sana. Moja katika jitihada ambazo tunazifanya kukomesha au kutokomeza kabisa hii biashara ya uhamiaji haramu ni kushughulika na mitandao ya wale ambao wanajihusisha na biashara hii ikiwemo wanaosafirisha, wanao-organize pamoja na wanaohifadhi. Kwa hiyo, wote hawa tukiwakamata tutawachukulia hatua za kali kabisa kwa mujibu wa sheria za nchi yetu.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Tatizo la wahamiaji haramu ni kubwa sana katika magereza nyingi za nchi hii na wengine wako under age. Tatizo kubwa ni pale ambapo hawa wahamiaji haramu kwa mfano Waethiopia wanakuwa wamemaliza vifungo vyao mfano mzuri ni Gereza la Lwanda, Mbeya Waethiopia 41 wamemaliza vifungo vyao zaidi ya miezi mitano, Serikali haina pesa za ku-process kuwarudisha nyumbani kwao wanaendelea kula chakula chetu. Ni lini Serikali itafanya mchakato wa makusudi wa kuwarudisha? Shahidi mzuri ni Mheshimiwa Sugu ambaye alikuwa katika gereza hilo.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mchungaji Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafanya jitihada nyingi sana kuhakikisha kwamba wahamiaji hawa wanarudi majumbani kwao baada ya kukamilisha kifungo chao. Si tu kwa kutumia rasilimali zetu chache tulizokuwa nazo, lakini pia kwa kutumia ushirikiano na uhusiano tuliyokuwanayo na Taasisi ya Uhamiaji ya Dunia (IOM).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mchungaji Msigwa atambue kwamba jitihada hizo tuendelee nazo kwa kasi. Hatupendelei wafungwa hawa waendelee kuishi magerezani kwani kufanya hivyo ni kuitia hasara Serikali. Sisi tutaendelea jitihada hizo kadri uwezo unavyoruhusu. Nadhani matukio kama haya ni machache sana nchini wengi tumekuwa tukiwarudisha.
MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza. Pamoja na majibu ya Waziri naomba niulize kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; kwa kuwa watumishi wa Jeshi la Zimamoto wanafanya kazi katika mazingira magumu na mazingira hatarishi, lakini hawana vifaa vya kufanyia kazi. Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha watumishi hawa anapata vitendea kazi nchi nzima?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Mkoa wa Njombe hadi sasa Jeshi la Zimamoto hawana Ofisi, je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha inajenga Ofisi pale Njombe? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Spika, ni kweli tuna changamoto ya vifaa ama vitende kazi kwenye Jeshi la Zimamoto na tunafanya jitihada mbalimbali kukabiliana na changamoto hiyo. Moja katika jitihada ambazo tunafanya ni kutenga fedha kwenye bajeti yetu kila mwaka ili kuweza kununua vifaa zaidi ikiwemo magari na vitendea kazi vingine mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, vile vile tunajaribu kuimarisha mahusiano kati ya Jeshi la Zimamoto kupitia halmashauri pamoja na majiji mengine. Wakati huo huo tumekuwa tukibuni mikakati mbalimbali ikiwemo mikakati ya kuweza kuchukua program za mikopo ambazo sasa hivi tuna mchakato ambao unaendelea. Nisingependelea kuzungumza sasa hivi kwa sababu haujafikia katika hatua ya mwisho, lakini ni moja katika jitihada ambazo tunafanya kuhakikisha kwamba Jeshi la Zimamoto linapata vifaa.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la Njombe, ni changamoto ya Ofisi katika mikoa hii mipya. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunalifahamu hilo na tunalichukulia kwa uzito na pale ambapo hali ya kifedha itaruhusu tutakabiliana na changamoto ya Ofisi katika Mkoa wa Njombe na mikoa mingine hususani mikoa mipya.
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Spika, ahsante, nashukuru kwa kunipa nafasi. Tumekuwa na tatizo la kuungua kwa majengo mbalimbali ya Serikali ikiwemo vyuo na shule za sekondari hata katika Halmashauri ya Wilaya ya Monduli. Je, nini mkakati wa kuhakikisha kwamba angalau kila halmashauri inapata gari moja la Zimamoto?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Spika, swali lake linafanana sana na swali ambalo limeulizwa kwenye swali la msingi ambalo nimeshalijibu. Kwa hivyo jibu lake linakuwa vile vile, kwamba, mikakati ni ile ile ambayo nimeizungumza kuhakikisha kwamba tuna dhamira hiyo hiyo ya kuona kwamba magari yanafika katika maeneo takribani yote. Ndiyo maana tumeanza jitihada sasa hivi za kutanua wigo wa kuweza kupeleka huduma ya Zimamoto katika Wilaya nyingi zaidi.
Mheshimiwa Spika, kila mwaka tumefanya jitihada hizo kwa kufungua Ofisi, kupeleka Maaskari wetu kuanza kutoa huduma za kutoa elimu ili pale ambapo magari yatakapokuwa yamepatikana na vifaa vingine tuweze kuvifikisha huko viweze kusaidia jitihada hizi ambazo tumeanza nazo kwa mafanikio makubwa.
MHE. BHAGWANJI MAGANLAL MEISURIA: Mheshimiwa Spika, nampongeza Naibu Waziri amesema maneno mazuri naunga mkono. Hata hivyo, nataka nimwambie wananchi wa Jimbo langu la Chwaka wana matatizo vilevile. Wabakaji wengi na watu mbalimbali wanakuja kufanya uhaini katika Jimbo langu huko Chwaka na Jozani. Mimi mwenyewe nimeshachangia computer moja Jozani lakini nimeomba gari mbili angalau hata moja ipatikane kwa sababu hali ni ngumu na ni lazima tupate gari moja kwa heshima na taadhima.
Mheshimiwa Spika, ni hayo tu, naomba Serikali na Waziri wanipatie gari gari moja ya Polisi ili liweze kusaidia wananchi wa Jimbo langu. Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bhagwanji, Mbunge wa Chwaka, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimejibu swali la msingi kwamba mchakato utakapokamilika wa upatikanaji wa magari kwa kuzingatia vigezo ambavyo nilivyovieleza tutaangalia kuona kama Chwaka inakidhi vigezo hivyo na idadi ya magari yaliyopo ili tupeleke. Nimuombe Mheshimiwa Mbunge avute subira mpaka magari hayo yatakapokuwa yamepatikana.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa Mkoa wa Singida unakua kwa kasi na majanga ya moto yamekuwa yakitokea mara kwa mara, yakihusisha makazi na pia vile vile kwenye barabara kuu. Je, Serikali ina mpango gani wa kuupatia Mkoa wa Singida gari la kisasa la zimamoto ili kuokoa maisha na mali za wananchi wake?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa gari la zimamoto lililopo ni bovu na halikidhi mahitaji; na ili kutoka Singida Mjini hadi kufika Wilayani Iramba, Manyoni, Mkalama na Ikungi kuna umbali mrefu. Je, Serikali ina mpango gani wa kuzipa kipaumbele Wilaya hizi kwa kuzipatia magari ya kisasa ya zimamoto? Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ni mpango gani wa Serikali wa kupeleka magari Singida pamoja na wilaya nyingine ambazo inazunguka; ni kama ambavyo nimejibu kwenye swali la msingi, kwamba, kwanza tutahakikisha tunafanya ukarabati wa lile gari bovu haraka iwezekanavyo pale tu fedha itakapopatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, katika bajeti yetu mwaka huu tumepanga kununua gari tano, kwa hiyo tutaangalia Singida kama ni mmoja wa Mkoa wa vipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kama ambavyo nimesema, ule mchakato wa kurekebisha sheria utakapokuwa tayari nadhani itasaidia sasa Halmashauri za Wilaya zilizopo katika Mkoa wa Singida kuweza kuchangia katika kununua magari haya yaweze kusaidia katika wilaya za nchi nzima.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Swali namba 19 lililoulizwa linafanana kabisa na changamoto iliyopo Jimbo la Ngara. Hivi juzi tulishuhudia gari zikiungua border ya Rusumo na ikapelekea kifo cha dereva, hakukuwa na gari la zimamoto. Je, ni lini Serikali itatuletea gari la zimamoto Wilaya ya Ngara?
NAIBU WAZIRI MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Oliver kutokana na kuumwa kwake na maendeleo ya vyombo ama taasisi zetu zilizopo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mkoa wa Kagera ikiwemo Jeshi la Zimamoto. Kuhusiana na Wilaya ya Ngara, ukiachilia mbali mikakati ambayo nimeizungumzia nikijibu swali la msingi la Mheshimiwa Aisharose Matembe ambalo linagusa Wilaya zote nchini, mikakati ni ile ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tuna pia tuna mipango mingine mbalimbali ambayo tunaendelea nayo, ambayo tunaamini kabisa ikikaa sawa basi changamoto hii ya upungufu wa magari ya zimamoto itapungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mpango wa kuweza kupata mkopo kupitia nchi za Belgium na Australia ambayo itatuwezesha kupata vitendea kazi ikiwa ni pamoja na magari mapya kabisa. Michakato ya kupata mikopo hiyo nayo inakwenda vizuri na iko katika hatua nzuri pale ambapo itakapokuwa imekamilika naamini kabisa tukichanganya na mikakati niliyozungumza katika swali la msingi basi matatizo ya magari ya zimamoto na vitendea kazi nchini ikiwemo Ngara yatakuwa yamepungua kwa kiasi kikubwa. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa, Mwenyekiti, pamoja na kwamba…
Mheshimiwa Oliver Semuguruka ameuliza swali hilo lakini nataka kusema kwamba Ngara ni sehemu ambayo ni special zone, ni mpakani. Tuna vituo viwili vya forodha vya pamoja, one stop border post kwenye mpaka wa Burundi na Tanzania na mpaka wa Rwanda na Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ajali iliyotokea ya moto ya tarehe 19 mwezi wa jana ni ajali kubwa, gari sita zikaungua, dereva akafa, kwa hiyo tunaiomba Serikali iweze kuchukua nafasi na iweze kuchukua hatua ili tuweze kupata gari kwenye vituo hivi ambavyo sasa kumekuweko na msongamano mkubwa. Tayari Kamati ya Ulinzi na Usalama ilikwisha andika barua tangu tarehe 18 Mei, kwa hiyo tunaomba ichukue hatua ya dharura kwa ajili ya maeneo haya (Makofi). Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya Mheshimiwa Mbunge ni ya msingi na tunaichukulia kwa uzito unaostahili. Tunatambua changamoto na location ya ile wilaya yake, Wilaya ya Ngara ama jimbo lake lilivyo, kuna umuhimu wa kuwepo kwa gari la polisi pale kwa sababu Mkoa wa Kagera tuna gari nadhani hazizidi nne ambazo zinasaidia kutoa huduma ikiwemo maeneo ya Ngara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua umuhimu wa hilo jambo na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutalichukulia uzito unaostahili.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa, Serikali imekiri kutokuwa na nyumba ya mahabusu au kutokuwa na mahabusu ya wanawake katika Wilaya ya Igunga na kuwasababishia ndugu kutokuwasalimia na kutokujua afya zao kwa hao mahabusu ambao ni wanawake na kuwanyima haki zote.
Je, Serikali iko tayari kujenga mahabusu maalum ya wanawake kama dharura ili kuwaondolea adhabu wanayoipata wanawake na usumbufu wa kutoka Igunga kwenda Nzega mara kwa mara? Naiomba Serikali iangalie kwa jicho la huruma.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, nilizungumza wakati najibu swali la msingi kwamba ujenzi wa gereza hili ambao ulianza mwaka 2003 haujakamilika na nilisema kwamba utakapokuwa umekamilika basi changamoto ya mahabusu kwa wanawake itakuwa imepatiwa ufumbuzi. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge astahamili wakati ambapo tunajiandaa kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga gereza hili ili tuweze kupata ufumbuzi.
Mheshimiwa Spika, kuna jitihada ambazo tumeweza kuchukua katika baadhi ya maeneo mengine nchini ambapo tumeweza kutumia rasilimali za maeneo husika pamoja na wafungwa na nguvu na ushirikiano wa wananchi pamoja na Wabunge wa maeneo husika kuhamasisha katika ujenzi wa mabweni. Naomba nichukue fursa hii kumuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba nitafanya ziara rasmi katika gereza hili ili tushirikiane pamona na Mbunge wa Jimbo hilo kuona jinsi gani tunaweza tukafanya kutafuta njia za hatua za dharura kuweza kukabiliana na changamoto hii wakati tukisubiri fedha za bajeti za ujenzi wa gereza hili.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, namshukuru Naibu Waziri amejibu vizuri lakini waendesha bodaboda hawa wengi hawana ujuzi wa Sheria na Kanuni za Barabarani. Je, kuna mkakati gani wa kuwapatia elimu hii ili kusudi waweze kuepukana na usumbufu na faini wanazozipata?
Swali la pili, kwa kuwa usafiri wa bodaboda unatoa usafiri kwa watu wengi lakini waendesha bodaboda hawa hawana leseni na hawana ujuzi wa kuendesha pikipiki hizi, kiasi kwamba wanasababaisha ajali nyingi na vifo.
Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti tatizo hili? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la elimu kuna jitihada mbalimbali ambazo zinafanyika katika kutoa elimu kwa waendesha bodaboda. Miongoni mwa jitihada hizo ni kwanza Jeshi la Polisi limekuwa likitumia utaratibu wa kuwafuata kwenye vijiwe vyao hawa ambao wanaendesha bodaboda na kuwapa elimu, pia kupitia vipindi mbalimbali ambavyo vinaandaliwa kwenye television, kwenye radio na kupitia kwenye wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani ambavyo vinatumika kwa ajili ya kutoa elimu, kwa hiyo jitihada za kutoa elimu zinafanyika kwa kiwango kikubwa sana.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili kwamba vijana ambao wanaendesha bodaboda bila leseni. Kwanza nichukua fursa hii kuendelea kusisitiza kwamba kuendesha bodaboda ama chombo chochote cha usafiri bila leseni ni kuvunja sheria na hivyo basi Jeshi la Polisi litaendelea kuwachukulia hatua wale wote ambao wanakiuka sheria za nchi katika eneo la usalama barabarani ikiwemo kuendesha bodaboda bila leseni. Kwa hiyo, nitoe wito kwa vijana wetu ambao hawana leseni kufuata taratibu za Kisheria ili waweze kujipatia leseni.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nashukuru majibu ya Serikali. Ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, tunacho Kituo cha Mlyama ambacho kimejengwa kwa muda mrefu sasa hakijamalizika na Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani analijua hilo na pale Wilayani tuna kituo ambacho kinatumiwa kwenye nyumba ambayo siyo nzuri na haitoshi; na kwa majibu haya kwamba wametenga eneo; swali linauliza kwamba ni lini wanaanza kujenga? Hayo maeneo tunashukuru wanayo, lakini swali, wanaanza kujenga lini?
Mheshimiwa Spika, la pili; tuna matukio makubwa sana ya ujambazi yanayotokea hasa baada ya Wakimbizi kurudishwa kwenda Burundi na Jimbo langu linavamiwa kila siku iendayo kwa Mungu na juzi mwanajeshi mmoja ameuawa baada ya kuwa wameenda ku-intervene mashambulio hayo na vitendea kazi ni hafifu.
Je, ni lini sasa vitendea kazi vya magari na pikipiki vitaongezwa kwenye Wilaya ile? Yeye mwenyewe anayo taarifa kwamba ujambazi ni kila siku. Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na lini kituo hiki kitajengwa; nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa kutambua changamoto ya location ya Jimbo lake, pale ambapo tutapata fedha ni katika vituo ambavyo tutavipa kipaumbele.
Mheshimiwa Spika, sambamba na kujibu swali lake la pili ambalo litahusisha vilevile pamoja na upelekaji wa vitendea kazi ili tuweze kukabiliana na changamoto ambayo ameizungumza ambayo tunaitambua na tumeshaanza kushughulika nayo.
MHE. NURU A. BAFADHILI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Katika Kata za Jiji la Tanga miaka ya 1990, kata zilihamasishwa kujenga vituo mbalimbali vya Polisi ambavyo vilisaidia kupunguza uhalifu, matokeo yake sasa hivi vituo vile vimetelekezwa, vimekuwa ni nyumba za vibaka.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuvifufua vituo hivyo ili kuweza kuweza kuzuia uhalifu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, mara zote tumekuwa tukihamaisha Waheshimiwa Wabunge na wananchi kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na upungufu wa Vituo vya Polisi nchini. Kwa hiyo, ni jambo la ajabu sana kama Serikali tutakubali kuona kwamba jitihada hizi za wananchi wanavunjwa moyo.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba siyo dhamira ya Serikali kuvitelekeza vituo hivyo ambavyo vina umuhimu mkubwa.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu Mheshimiwa Mbunge hakutaja kituo gani ambacho kimetelekezwa, kwa hiyo, ni vigumu kumpa sababu ya kituo hicho ambacho amekusudia kwamba hakitumiki mpaka sasa hivi kwa sababu gani? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, baada ya Bunge hili nitakuwa tayari kukutana naye ili aweze kunipa taarifa za kina tufuatilie na kuchukua hatua za haraka. (Makofi)
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Alhaji Masauni.
Mheshimiwa Spika, wapo askari wanaowaweka ndani watuhumiwa zaidi ya saa 24 wakati hawana makosa ya kuwekwa ndani zaidi ya saa 24. Serikali inawachukulia hatua gani askari hawa wakibainika wanakiuka Sheria za Jeshi la Polisi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Watanzania wengi hawana elimu ya Sheria ya Jeshi la Polisi. Serikali ina mkakati gani wa kutoa elimu ili Watanzania wakafahamu haki yao ya kimsingi ili waweze kujua taratibu za kuwekwa ndani zaidi ya saa 24 na sheria ambazo haziwahusu kuwekwa ndani zaidi ya saa 24? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, nataka nimjibu Mheshimiwa Mattar kwamba sheria niliyoizungumza inahusisha watu wenye makosa ya aina ambayo nimeyataja.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama kutakuwa kuna Askari Polisi ambaye amemweka mtu ndani na hakufanya makosa ambayo nimeyataja, naye Mheshimiwa Mattar anamfahamu, basi ni wajibu wake kuweza kuwasilisha taarifa hiyo ili tuweze kuchukua hatua kama ambavyo tumefanya kwa askari wengine wenye makosa mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, katika kipindi cha miezi sita ya mwaka huu, takriban askari 15 ambao walifanya makosa ya kukiuka maadili ya utendaji wao wa kazi ambao tumeweza kupokea taarifa zao na kati ya hao mpaka sasa hivi tayari askari wawili wameshachukuliwa hatua. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mattar kama ana taarifa hizo aziwasilishe katika mamlaka husika ili hatua ziweze kuchukuliwa.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, suala la elimu linaendelea kutolewa na ni wajibu wa kila mtu akiwemo yeye Mheshimiwa Mbunge kuweza kutusaidia kutoa elimu kwa wananchi wake, ingawa kutokufahamu sheria hakuhalalishi juu ya uvunjifu wa sheria.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi kwamba tutaendelea kujitahidi kadri itakavyowezekana watusaidie Waheshimiwa Wabunge akiwemo Mheshimiwa Mattar kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na ufahamu wa sheria mbalimbali katika nchi yetu. (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba niongezee majibu ya nyongeza kwenye majibu mazuri ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ameyasema.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kulikuwa na malalamiko kwa wananchi kwa kuwekwa ndani na baadhi ya askari ambao sio waaminifu, siyo waadilifu kwenye makosa ambayo hayastahili, lakini pia wamekuwa wakiwaweka ndani baadhi ya wananchi kwenye makosa ambayo pia hayahitajiki hata kuwekwa ndani, hata nusu dakika au sekunde.
Mheshimiwa Spika, tayari nimeshatoa maelekezo kwamba Makamanda wote wa Polisi wa Mikoa na Wakuu wa Polisi wa Wilaya, kituo chochote ambacho kitaonekana na malalamiko ya kukiuka utaratibu huu wa kuweka wananchi ndani, viongozi hao watawajibika. Hivi karibuni nitaanza ziara kwenye mikoa yote ya Tanzania pale ambapo nitakuta vituo, askari bado wanalalamikiwa, askari hao hawatakuwa na nafasi ya kuendelea kulichafua Jeshi zuri la Polisi ya nchi yetu.(Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri amejibu kwamba ikigundulika askari wanaowaweka kituoni wananchi kwa muda watachukuliwa hatua. Wakati nachangia bajeti iliyopita ya Wizara ya Mambo ya Ndani nilieleza bayana kabisa kwamba kuna baadhi ya mahabusu kituo cha Kawe waliwekwa ndani kwa zaidi ya miezi mitatu na nikasema kabisa na nikamtaja na askari aliyehusika mpaka leo hajachukuliwa hatua.
Je, ni kwa nini Mawaziri wanatumika kwenye Bunge Tukufu kuwadanganya watanzania bila kuchukua hatua?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na hii hoja ya mahabusu Kituo cha Kawe, tulishawahi kutoa maelekezo, uchunguzi ufanyike ili hatua ziweze kuchukuliwa, lakini kama Mheshimiwa Mbunge atataka kulithibitishia Bunge hili tukufu mpaka kama hatua hazijachukuliwa, basi nimuahidi kwamba nitakapotoka hapa nitafuatilia nijue ni kwa nini hatua kama hazijachukuliwa ama pengine wanastahili kuendelea kukaa ndani kwa mujibu wa sheria.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Spika, ninafikiri kwamba ni vema Mawaziri wetu wanapokuja kutoa majibu hapa wajue Watanzania wanawaangalia na Watanzania wanasikitika sana pale wanapokuwa wanatoa taarifa ambazo siyo za kweli. Kwa mfano, juzi amekamatwa Mwenyekiti wa Kijiji anaitwa Tanzania Omutima, Kijiji cha Kewanja kwa tuhuma tu, amekaa siku nne hajafikishwa Mahakamani na wala hajapelekwa polisi. Pia amekamatwa kijana anaitwa Mudude Nyagali, amewekwa ndani zaidi ya siku 30.
Mheshimiwa Spika, ninachoomba Waziri atoe tamko kwamba ni marufuku kuanzia sasa watu wa abide na sheria, kukamata mtu na kukaa naye zaidi ya yale masaa ambayo sheria inaruhusu kama mtu amefanya hivyo afikishwe kwenye utaratibu, ashitakiwe kwa kukiuka sheria ambayo tunayo mpaka sasa.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, kwanza napingana kabisa na kauli yake kwamba Mawaziri hapa tunatoa majibu ambayo siyo sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, majibu ambayo tunayotoa hapa ni majibu ambayo tumeyafanyia utafiti wa kina na tunajiamini kwamba tunachokizungumza hapa ni kitu ambacho ni sahihi kwa kiwango kikubwa sana.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anataka tutoe tamko, matamko tumekuwa tukitoa kila siku na siyo lazima atoe matamko kwa sababu sheria zinajulikana, tunachokifanya ni kusimamia sheria ambazo tumezitunga humu Bungeni na Mheshimiwa Heche anazifahamu. Kwa hiyo, iko wazi kwamba yeyote ambaye hafuati sheria na hakuna ambaye yuko juu ya sheria, ikiwemo Wasimamizi wa Sheria ambao ni Vyombo ya dola.
Mheshimiwa Spika, tunasema kila siku kwamba kama kuna Askari yeyote ambaye anatumia nafasi yake vibaya kinyume na maadili yake ya kazi, tutamchukulia hatua na tumekuwa tukifanya hivyo, tukiwachukulia na tutaendelea kufanya hivyo. (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri juu ya swali ambalo limeulizwa na Mheshimiwa Heche.
Mheshimiwa Spika, pengine nitoe fursa ya kuelimisha kidogo hii dhana ya saa 24 kukaa mahabusu. Kwenye Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, unapomkamata kwa mara ya kwanza mtuhumiwa na kumuweka mahabusu, kwa maana ya matakwa ya saa 24. Saa 24 yale yanaendana na upelelezi wa awali. Kuna mazingira ambapo uliyemweka ndani hata kabla ya saa 24 hayajafika mtamtoa ndani katika upelelezi ama kuna mahala anaenda kuonesha silaha, ama kuna mahala anaenda kuonesha ushahidi fulani kutokana na maelezo yake. Mnapotoa atakaporudi mahabusu huyo mtuhumiwa anaanza kuhesabiwa masaa yake upya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa bahati mbaya wananchi wanahesabu tangu alipokamatwa, lakini kisheria tunahesabu tofauti. Kwa hiyo, nimuelimishe Mheshimiwa Heche, huyo anayemsema Mwenyekiti wa Kijiji ambaye aliyekamatwa pale Nata, kulikuwa na masuala ya vielelezo vya documents kwa sababu fedha za kijiji zaidi ya shilingi milioni 300, vilevile ilikuwa inahusisha na Kampuni ya Uwekezaji wa Grument. Kwa hiyo, aliyekuwa amekamatwa tulitoa maelekezo. Mheshimiwa Heche dhana hii muifahamu vizuri ya masaa 24.
Mheshimiwa Spika, nilikuwa naona wananchi waelewe dhana ya saa 24 inaanza wakati gani na inaisha wakati gani. Siyo nia ya Serikali kuwatesa wananchi wake, na ndiyo maana majibu niliyoyatoa mwanzo nilisema wale askari ambao watakiuka sheria hiyo ya kuwaweka ndani tunachukua hatua, hakuna yeyote ambaye tunamfumbia macho. Kwa hiyo, Mheshimiwa Heche uwe na amani huyo mtu unayemsema tumeshatoa maelekezo na tunajua concern yako. Ahsante sana.(Makofi)
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na hasa hili la kukubali ombi la kutuletea angalau gari moja kwa ajili ya kusaidia shughuli za polisi. Pamoja na hayo nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwa kutambua kwamba Jeshi la Polisi lina idadi ndogo sana ya askari, wananchi wa Msalala pamoja na kanda nzima ya ziwa walishaanzisha utaratibu wa ulinzi wa jadi (Sungusungu) ambao ni askari wa kujitolea na husaidia sana shughuli za polisi kukabili matukio pale ambapo polisi wanakuwa hawajafika. Kwa bahati mbaya sana Wizara ya Mambo ya Ndani na Jeshi la Polisi limekuwa likitoa ushirikiano mdogo sana kwa watu hawa ambao wanafanya kazi kwa kujitolea na mara nyingi wamekuwa wakiwa-harass pale tukio linapotokea badala ya kuwatafuta wahalifu wanakwenda kukamata wale viongozi wa Sungusungu na kuwalazimisha au kuwataka kwamba wasaidie kutaja au kutoa taarifa ambazo zingeweza kusaidia Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua Serikali au Wizara inachukua au ina mkakati gani wa kushirikiana na Jeshi la Sungusungu ili kusaidia jitihada ambazo tayari zipo kwa sababu pia askari wenyewe wa polisi si wengi kama ambavyo jibu limejitokeza? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kumekuwepo na matukio mengi ya askari polisi kubambikizia wananchi kesi mbalimbali jambo ambalo limekuwa likiwavunja moyo sana wananchi kutoa ushirikiano kwa polisi, jambo hili limekuwa likijitokeza kwenye vituo mbalimbali hasa vilivyoko Kata ya Isaka , Kata ya Bulige na hata Kata ya Bulyanhulu. Je, ni lini Mheshimiwa Naibu Waziri atakuja kukutana na wananchi wa maeneo hayo ili kuweza kusikia kero hii na kuweza kukemea askari hao wenye tabia mbaya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la kwanza nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba siku zote tumekuwa tukihamasisha na tunaona umuhimu wa ushiriki wa wananchi katika kushirikiana na vyombo vya dola kukabiliana na uhalifu nchini na ndiyo maana kupitia Kamisheni yetu ya Polisi Jamii ambayo tunayo, tumekuwa tukiandaa utaratibu mzuri, ili utaratibu huo ambao umekuwa ukitumika wa kushirikisha wananchi, ikiwemo Polisi Jamii, ikiwemo Sungusungu, uweze kufuata misingi ya kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kupitia Kamisheni yetu hii ya Polisi Jamii tumekuwa tukitoa miongozo mbalimbali, ili wananchi waweze kutekeleza majukumu yao bila kukinzana na sheria za nchi yetu. Kama kutakuwa kuna mambo yametokea ambayo yanaweza kuwa yamesababishwa aidha na kutokana na uelewa mdogo wa ufahamu wa sheria wa jinsi ya hawa ambao wanaisaidia Polisi kutekeleza hizi shughuli za Polisi Jamii ama itakuwa mengine yametokea labda kwa makosa mengine, labda Mheshimiwa Mbunge labda atuwasilishie tuweze kuyashughulikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali lake la pili kuhusiana na ubambikaji kesi, binafsi nilifanya ziara katika Mkoa wa Shinyanga na moja katika mambo ambayo niliyakemea baada ya kutembelea baadhi ya vituo na magereza katika maeneo ya Mikoa ile ya Kanda ya Ziwa na kupata malalamiko ya baadhi ya wananchi ambao walikuwa wamesema wamebambikiwa kesi, moja ni jambo hili ambalo tulilichukulia kwa uzito unaostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, ombi lake la kutaka nifanye ziara katika jimbo lak mahususi, kwa ajili ya kufanya kazi hii ambayo tumeshaifanya katika maeneo mengine ya Mkoa wa Shinyanga na mikoa mingine nchini ambayo imesaidia sana kupunguza malalamiko haya kwa wananchi tutaifanya baada ya Bunge hili kumalizika tutaandaa hiyo ziara ya kwenda jimboni kwake kwa ajili ya kushughulikia jambo hili mahususi.
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Swali langu la nyongeza. Sasa hivi Kibiti imekuwa Kibiti salama, je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha maslahi ya Polisi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuhakikisha kwamba, inaboresha maslahi na mazingira ya utendaji kazi wa vyombo vyetu vya Polisi hatua kwa hatua na kadiri ya uchumi wa nchi utakavyokuwa unaimarika.
MHE. ZAYNAB M. VULLU: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante sana. Kwa kuwa, biashara mara nyingi ni muuzaji na mnunuaji; na kwa kuwa, biashara ya ukahaba mara nyingi inaita machangudoa; na kwa kuwa, katika bahari kuna changudoa, kuna changuchole, kuna changufatundu. Je, Serikali haioni kuna haja sasa ya hawa machangu wengine wakakamatwa na wakapewa elimu ya kutosha, waachane na vitendo vya ukahaba kwa sababu, wao kama hawakwenda sokoni, hii biashara haitakuwepo. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuhakikisha wasichana wote wanawawezesha kwa mikopo na elimu ya ujasiriamali, pamoja na juhudi alizozisema Mheshimiwa Naibu Waziri? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, pamoja na juhudi za Serikali, Taasisi Zisizo za Kiserikali, na baadhi ya raia kumekuwa na mkusanyiko mkubwa wa biashara hii maeneo mbalimbali, ikiwemo eneo maarufu kwa Uwanja wa Fisi, Mburahati, Dar-es-Salaam na biashara hii inafanyika katikati ya maeneo wanayoishi wananchi. Je, Serikali haioni sasa kuna haja ya kwenda katika maeneo hayo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuvunja hayo maeneo, kujenga miundombinu ambayo itawawezesha wasichana waliojiingiza katika biashara hizo kwa kutokutarajia kutokana na hali ngumu ya maisha na pia wataepukana na maradhi ya UKIMWI; Serikali ikiweza kujenga hiyo miundombinu na kuwapa mikopo hawa wasichana haioni kwamba, tutakuwa tumekwamua Taifa ambalo tunalitegemea? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza swali lake na concern yake Mheshimiwa Mbunge kuhusiana na janga hili. Naungana mkono na yeye kabisa kuhusiana na umuhimu wa kushughulika sio tu na wauzaji, lakini wanunuzi, lakini si tu na wanunuzi, mpaka na mazingira ambayo wale wanayaweka. Maana kuna wengine sio wanaouza, kwa mfano wenye madanguro, ni watu ambao sio wauzaji na sio wanunuzi, lakini wanahamasisha hivi vitendo. Kwa hiyo, yote hayo na wote ambao wanashiriki kwa namna moja ama nyingine katika hii biashara kuna haja ya kuhakikisha kwamba, tunachukua hatua na ndivyo ambavyo Serikali inafanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kumekuwa na changamoto mbalimbali ambazo nadhani Bunge hili ni wakati muafaka wa kuzitafakari. Moja ni changamoto ya sheria; labda nitoe mfano wa sheria ambazo pengine zinakwaza mapambano dhidi ya vita ya makahaba. Ukiangalia kwenye Kanuni ya Adhabu Namba 176(a), Sura ya 16, adhabu ambayo inatakiwa itolewe kwa watu ambao wanafanya biashara ya madanguro wanasema ni fine isiyozidi 500/= ama iwapo ni kosa la mara ya pili na kuendelea atatozwa fine isiyozidi 1,000/=.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mtaona kwamba, adhabu kama hii inaweza kuwa inahamasisha utendaji wa huu uhalifu. Kwa hiyo, kuna haja ya Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kuangalia na kutafakari juu ya sheria hizi ambazo zimepitwa na wakati ili hatimaye kazi kubwa ambayo inafanywa ya kuwakamata hawa makahaba kila siku, pamoja na wahamasishi wanaoshiriki na wanunuzi iweze kuwa na tija kwani mara nyingi wanapokamatwa wanarudia tena makosa kwa sababu, ya wepesi wa sheria zilizopo. Kwa hiyo, kimsingi hilo ni jibu la swali lake la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusiana na elimu; nimhakikishie kwamba, tunaendelea kutoa elimu, lakini vilevile na mamlaka nyingine kama ambavyo nimezungumza katika swali la msingi kwamba, kwa sababu, suala hili ni mtambuka tumekuwa tunashirikiana kama Serikali na mamlaka nyingine na taasisi mbalimbali, ili kuweza kutoa elimu kwa jamii juu ya madhara haya, ikiwemo kuwashirikisha vilevile viongozi wa dini ambapo nilizungumza kwamba, viongozi wa dini ni sehemu muhimu sana katika kutoa elimu ya maadili juu ya wananchi.
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Naibu Waziri, swali langu msingi wake ni kwamba, wananchi ambao wameumizwa, wametekwa, wamepotea, sio suala la kuimarisha Vituo vya Polisi kwenye ulinzi shirikishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu je, Serikali ina mpango gani wa kushikika wa kulinda raia hawa ambao wamekuwa wakijitolea kutetea nchi yao kwa maslahi ya Watanzania wote?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni lini Serikali itakamilisha uchunguzi na kuleta ripoti Bungeni ya matukio ya kihalifu yanayofanana na ugaidi ambayo wamefanyiwa watu mbalimbali, akiwemo Mheshimiwa Tundu Lissu, Mwandishi wa Habari wa Gazeti la Mwananchi, Abisalom Kibanda na Dokta Stephen Ulimboka na wengineo? (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nataka nichukue fursa hii kumpinga na kumkosoa vikali kabisa Mheshimiwa Saed Kubenea, kutokana na utangulizi wa swali lake ambalo ameuliza; na kimsingi Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Jeshi la Polisi, imekuwa ikihakikisha inalinda usalama wa raia wote na mali zao. Hakuna matabaka katika kusimamia ulinzi wa raia na mali zao, hiyo ndio kazi ya Jeshi la Polisi ya kila siku kwa hiyo, kusema kwamba kuna watu wanakosoa Serikali, sijui kuna watu wana nini, hizo ni kauli potofu na si sahihi na nadhani kwa mamlaka yako ungeelekeza hata zifutwe katika Hansard. Kwa sababu, ni upotoshwaji mkubwa kwa jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika hilo suala la kulinda usalama wa raia na mali zao jitihada kubwa zimekuwa zikifanyika. Imani yangu ni kuwa kwa kadri ambavyo tunakwenda mbele tumekuwa tukifanya hivyo kwa kutumia mbinu mbalimbali za kitaalam, kukusanya taarifa za kiintelijensia, kufanya doria, kuangalia maeneo tete, kuangalia takwimu, kumbukumbu za uhalifu nchini na ndio maana mpaka leo nchi yetu imeendelea kuwa salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoelekea katika Serikali ya Uchumi wa Viwanda, Serikali ya Uchumi wa Kati, tunaamini kabisa kutakuwa kuna mabadiliko makubwa sana ya kiteknolojia katika utekelezaji wa majukumu yake kwenye vyombo vyetu vya dola. Kwa hiyo, tutakapoimarisha na kuwekeza katika maeneo ya teknolojia tunaamini kabisa kazi hii itafanywa katika mazingira mepesi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu uchunguzi. Kazi ya uchunguzi imekuwa ikiendelea kufanyika, ingawa kazi ya uchunguzi kama alivyozungumzia yeye katika eneo mahususi la ugaidi, lina changamoto nyingi kwa sababu, tuhuma za ugaidi zinahusisha taarifa nyingine ambazo zinatoka katika mamlaka za nchi nyingine, lakini na taasisi nyingine nje ya Jeshi la Polisi. Kwa hiyo, katika kufanya uchunguzi ambao unahitaji taarifa kupata katika nchi nyingine, kupata katika mamlaka nyingine, si jambo ambalo linaweza likawa limefanyika kwa wakati mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, mpaka sasa kutokana na matukio mengi yaliyojitokeza kuna hatua kubwa imeshafikiwa katika uchunguzi wa kesi mbalimbali, ziko ambazo zimeshafika mwisho, ziko ambazo zinaendelea kuchunguzwa. Pale ambapo uchunguzi utakamilika hatua zitachukuliwa kwa wahusika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe wito kwa watu wote ambao wanahusika kutoa ushirikiano kwa mamlaka katika kutekeleza majukumu yake. Mfano huu ambao ameuzungumzia wa kesi ya Mheshimiwa Tundu Lissu, tumekuwa mara nyingi tukitaka ushirikiano kutoka katika chama hiki ambacho Mheshimiwa Kubenea anatoka, ili tuweze kupata watu ambao wanaweza kutusaidia kutupa taarifa, ikiwemo dereva yule ambaye alikuwa na Mheshimiwa Tundu Lissu, lakini wenyewe wamekuwa wakifanya jitihada za kufifisha kupatikana kwa dereva huyo. Kwa hiyo, ushirikiano kwa wananchi ikiwemo na wewe mwenyewe Mheshimiwa Mbunge na chama chake ni muhimu katika kukabiliana na kuharakisha uchunguzi wa kesi yetu. (Makofi)
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tabia hii ya polisi kutumia vibaya madaraka na kubambika kesi imekithiri sana katika nchi yetu. Mimi mwenyewe ni muathirika wa kubambikiwa kesi. Mfano mzuri ni RCO (Afisa Upelelezi) wa Mkoa wa Iringa ambaye amekuwa akibambikiza kesi na kuwalazimisha hasa wanachama wa CHADEMA wahame chama cha CHADEMA waingie Chama cha Mapinduzi ili wasifunguliwe mashtaka.
Je, Serikali itakuwa tayari kufanya uchunguzi kwa RCO huyu ambaye anatumitumia madaraka yake vibaya mfano mzuri ni mimi mwenyewe nimebambikiziwa kesi nimekuwa muathirika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Msigwa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, madai hayo Mheshimiwa Msigwa amekuwa akiyatoa mara kwa mara Bungeni na binafsi nimeshamuomba mara kadhaa kama ana vithibitisho wa tukio lolote la aina hii alilete lakini mpaka leo hajaleta.
Kwa hiyo, narudia tena maelezo ambayo Mheshimiwa Msigwa nimekuwa nikikupa mara nyingi wakati mwingine nje hata ya Bunge kwamba kama una uthibitisho wa jambo kama hilo lilete tulifanyie kazi.
Kwa taarifa zilizopo mpaka sasa hivi hakuna askari polisi ambaye amemzungumza ambaye amefanya matukio kama hayo kinyume na utaratibu wa sheria.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na namshukuru Naibu Waziri kwa majibu lakini naomba nipeleke pongezi kwa wananchi wa Kijiji cha Luganza na Ntumagu kwa sababu ni nguvu zao za wananchi za ujenzi wa kituo hicho ambazo ndio zimesababisha utulivu, nina maswali mawili.
Ni lini Serikali Wizara itajenga nyumba za askari kwasababu hivi tunavyozungumza askari wanne na familia zao wanaishi ndani ya kituo, kwa hiyo, kuna muingiliano wa minong’ono na mazungumzo baina ya familia za askari na mahabusu hasa nyakati za usiku? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili ni lini Serikali itatoa usafiri walau pikipiki kwasababu eneo hili kijiografia limekaa kwa namna ambayo askari wale wanahitaji usaidizi zaidi wa namna ya kufika kwenye maeneo wanayohudumia? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la nyumba kama ambavyo nimekuwa nikijibu katika siku za karibuni kwamba kuna jitihada mbalimbali ambazo zimefanyika ambazo zinahusisha pia Mkoa wa Kagera kwa ujumla pamoja na Wilaya ya Biharamulo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Mkoa wa Kagera tunakumbuka kwamba kuna nyumba ambazo zimefikia takribani asilimia 75 kukamilika pale Buekera ambazo katika bajeti ya mwaka huu tunatarajia kuzikamilisha, lakini sambamba na hilo katika fedha ambazo Mheshimiwa Rais ametupatia hivi karibuni za ujenzi wa nyumba 400 basi maeneo hayo yatahusika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la gari ni kweli kuana changamoto ya usafiri lakini tumefanya jitihada kupeleka magari nadhani kama ni manne sasa hivi kwa mkoa wa Kagera kwa ujumla na kipaumbele chetu kimeelekea zaidi katika maeneo ambayo yako mpakani ili kudhibiti uhalifu hasa kwa wahamiaji haramu ambao wamekuwa wakiingia na kufanya uhalifu katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nichukue changamoto hii katika eneo lake ambapo tuna magari katika kituo hiki ambacho nimekitaja cha Nyakanazi tuna gari mbili zinasaidia kufanya doria katika maeneo ya kituo hiko, hata hivyo tunakubaliana na ombi la Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna haja ya kuongeza pale ambapo magari yatapatikana tutaongeza vilevile kulingana na changamoto ya hali ya mahitaji mengine nchi nzima.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Swali langu lilikuwa very specific kwa Gereza la Mng’aro, lakini naona Waziri ananijibu na magereza mengine nchini. Sasa gereza hili limejengwa kwa miti pamoja na udongo na linahatarisha hata usalama wa wafungwa ambao wako pale. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kuhakikisha kwamba, badala ya kusubiri changamoto za nchi nzima, kuwa na mpango wa muda mfupi wa kukarabati gereza hili?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa, gereza hili ni la kilimo na liko katika Skimu ya Kilimo ya Mng’aro ambayo ni kilimo cha mpunga na lilikuwa na uwezo wa kulisha magereza yote ya Mkoa wa Tanga. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka kulipa zana bora za kilimo ili liweze kuzalisha zaidi na kuweza kulisha magereza yote ya Mkoa wa Tanga?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge, mara nyingi amekuwa akifuatilia sana maendeleo ya vyombo hivi vya usalama vilivyopo chini ya Wizara yetu ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Leo hili swali lake lake linaonesha msingi wa dhamira yake hiyo ya dhati.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusiana na swali lake la kwanza ambalo ametaka kujua kuhusu mpango mahususi wa ukarabati wa Gereza la Mng’aro; naomba nijibu swali hili pamoja na swali la pili kwa sababu yanaingiliana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Shangazi na Waheshimiwa Wabunge wengine, kwamba tumekuwa tukifanya jitihada mbalimbali ambazo zinasaidia kuboresha magereza yetu ambayo yako katika hali mbaya, ukiachilia mbali jitihada za Serikali kupitia bajeti kuu ambayo hata mwaka huu wa fedha tumetenga fedha hizo. Mifano iko mingi tu ambayo mimi binafsi nimefanya ziara maeneo kadhaa na tumeweza kushirikiana katika kuhakikisha kwamba tunafanya ukarabati kwa kutumia rasilimali katika maeneo husika. Naomba nichukue fursa hii kwa kutumia mfano huohuo ambao nimeweza kuona kwamba, umefanya kazi katika maeneo mengine ili tuupeleke Mlalo.
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri hivi karibuni nilipofanya ziara katika Mkoa wa Lindi, watu wa Magereza wa Mkoa wa Lindi waliniambia kwamba, wangekuwa wamepata mashine za kufyatulia matofali ingerahisisha huu mchakato ambao tunauzungumza hapa. Nichukue fursa hii kumpa pongezi sana Kaimu Mkurugenzi wa National Housing Corporation ambaye baada ya kutoka Lindi nilimwandikia barua kumwomba mashine hizo na ametupatia mashine 10 kwa kuanzia ambazo nitazipeleka Lindi, lakini nitatumia mamlaka niliyokuwanayo kuchukua mashine moja ile kuipeleka kwa Mheshimiwa Shangazi, Mlalo, tukafanye kazi ile ya kuweza kuanza kufanya kazi ya ukarabati wa gereza letu lile kwa kutumia rasilimali za pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hiyo itasaidia vile vile kuhamasisha ujenzi wa mabweni ya ziada, kwa sababu suala la kilimo, kama swali lake la pili ambalo amelizungumza, linategemea vile vile nguvukazi ya wafungwa; ambapo kwa kiwango cha wafungwa waliopo Mng’aro sasa hivi na aina ya ukubwa wa shamba lile la karibu ekari nadhani zaidi ya 300 wafungwa wale hawatatosheleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tutafanya jitihada za kuongeza mabweni, ili tupate wafungwa zaidi na wakati huohuo nimuahidi pia Mheshimiwa Shangazi kwamba tuna mpango vile vile wa kupata matrekta sita mapya ambayo tutayagawa katika magereza ambayo ni ya kilimo makubwa. Vile vile kule kuna matrekta ambayo ni chakavu, kwa hiyo tutachukua trekta moja chakavu tutalitengeneza vizuri tuweze kulipeleka Mng’aro. Tukifanya hayo tutakuwa tumetatua matatizo yote mawili kwa pamoja, tutakuwa tumeimarisha miundombinu wakati huohuo suala la kilimo cha mpunga katika eneo lile litakuwa limepatiwa ufumbuzi.
MHE.MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Gereza la Kitai lililopo Wilayani Mbinga ni moja ya magereza kongwe nchini. Gereza hili linakabiliwa na ukachavu wa miundombinu yake ikiwemo uchakavu wa lango kuu la kuingilia gerezani, bwalo la kulia chakula la wafungwa, lakini pia uzio wa kuzunguka gereza hilo umechakaa na unahatarisha usalama wa Maafisa Magereza wanaolinda wafungwa hao. Je, ni lini Serikali itakwenda kukarabati miundombinu katika gereza hilo la Kitai?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, jibu la swali hili halitatofautiana sana na jibu ambalo nimejibu katika swali la msingi la Mheshimiwa Shangazi. Kitakachokuwa tofauti ni kwa sababu lilikuwa ni swali la msingi. Inawezekana pengine bahati ile ambayo Mheshimiwa Shangazi ameipata isiende sambamba na gereza la Kitai kwa maana ya kupata ile mashine, lakini ni kutokana na uchache wa hizo mashine zenyewe na changamoto tulizokuwa nazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo nichukue fursa hii kumwomba Mheshimiwa Mbunge kwamba tushirikiane kutumia dhana ile ile ambayo nimeizungumza katika jibu langu la msingi; kwamba tunaweza haya matatizo madogo madogo ya kukarabati magereza yetu tukayafanya kwa kutumia rasilimali za maeneo husika bila kutengemea bajeti ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, Bajeti ya Serikali imetengwa lakini changamoto ni nyingi. Hivyo, kwa mambo madogo madogo kama haya tunaweza tukakaa tukashirikiana na Mheshimiwa Mbunge tukakae, baadaye tuandae utaratibu ikiwezekana hata mimi niende kwenye ziara kwenye jimbo lake ili nikapeleke uzoefu ambao nimeupata katika maeneo mengine uliosaidia kufanya marekebisho na ukarabati wa magereza ya maeneo mbalimbali nchini.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Suala la uchakavu na wingi wa mahabusu na wafungwa kwenye magereza, yaani kwa maana kwamba magereza kuzidiwa. Kwa mfano Gereza la Tarime lilijengwa mwaka 1947 kwa ajili ya kuchukua wafungwa 140 tu. Hivi tunavyoozungumza kuna watu mpaka 700. Je, Serikali ya CCM haioni kwamba kubeba watu wengi ndani ya magereza ni kukiuka haki za binadamu na kuwaumiza watu ndani ya magereza haya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, wingi wa watu magerezani si ukiukwaji wa haki za binadamu kwa sababu wako magerezani kwa mujibu wa sheria. Kitu ambacho nadhani ningemshauri Mheshimiwa Mbunge ni kwamba aendelee kuwa balozi mzuri wa wananchi wa Tarime kuhakikisha kwamba wanafuata sheria na wasifanye uhalifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itajitahidi kupunguza msongamano pale ambapo inawezekana na tunafanya hivyo. Nachukua fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amekuwa akifanya kazi nzuri ya kuona kwamba atumie mamlaka yake ya Kikatiba aliyokuwa nayo kusamehe wafungwa wale ambao amekidhi vigezo.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa gereza la Uyui Mkoa wa Tabora ni kongwe linafanana na gereza la Mng’aro. Kawaida ya gereza lile lilitakiwa kuchukua wafungwa 1,360 lakini mpaka ninavyosema hivi sasa lina wafungwa 1,860. Je, Serikali ina mpango gani wa kupanua gereza au kuwapunguza wafungwa waende sehemu nyingine?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la msongamano wa wafungwa ni suala pana na niseme bora nizungumze kwanza kwa ujumla wake kabla sijaenda specifically kwenye gereza la Uyui kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameuliza, maana yake naona masuala yote yanaingiliana katika hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, imsingi suala hili nimekuwa nikilijbu mara kadhaa katika kipindi cha nyuma kwamba tunaweza tukatatua tatizo la msongamano wa wafungwa kama ambavyo Serikali tunavyofanya kwa kufanya mambo yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, moja, tunapanga bajeti ya kuongeza mabweni yetu na kazi hiyo inaendelea kadri ya hali ya uwezo wa kibajeti utaporuhusu. Katika kipindi cha miaka mitano tumefanya hivyo katika magereza, nadhani takribani mawili kama sikosei.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo tunatumia sheri zetu zile tatu ama nne, Sheria ile ya Parole, Sheria ile ya Community Services pamoja na kutumia vile vile mamlaka ya kikatiba ya Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo haya ni mambo ambayo tunayafanya kimsingi kupunguza msongamano wa wafungwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine kubwa zaidi ni kuhakikisha kwamba tunafanya kila linalowezekana kupitia vyombo vingine vya dola kusimamia sheria. Ndiyo maana jeshi letu la polisi sasa hivi linafanya kazi kubwa ya kutoa elimu kwa wananchi ili kuepukana kufanya makosa ambayo yanaweza kuepukika ili kuweza kupunguza msongamano katika magereza yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, specifically kuhusiana na kwenye gereza la Uyui, nimwombe Mheshimiwa Mbunge kwamba kama ambavyo nimezungumza kwenye majibu yangu mengine haya mawili utaratibu ndio huo huo tu, aidha bajeti ya Serikali au utaratibu wa kuweza kutumia rasilimali za eneo husika kuweza kufanya marekebisho madogo madogo.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Swali langu, je, ni lini Serikali itaamisha gereza la Songwe ili kupisha mradi wa mgodi wa niobium ambao una thamani ya zaidi ya dola bilioni 6.8 ambayo ni sawa na shilingi bilioni 15. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lake linauliza ni lini, nadhani sitaweza kujibu kwa lini sasa hivi hapa kabla ya kuweza kulifanyia utafiti. Ningeomba anipatie muda nilifanyie utafiti jambo lake hili nijue hasa undani wa hili tatizo lake lilivyo ili niweze baadaye kukaa nizungumze naye pembeni kuweza kumfahamisha kama ni lini litahamishwa au kama kuna mipango mingine ambayo ipo ya kuweza kukabiliana na tatizo ambazo amelizungumza.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa zaidi ya wafungwa katika Gereza la Kasulu ni wakimbizi hali inayochangia gereza hilo kubeba mzigo mkubwa. Je, Serikali iko tayari kukaa na Shirika la UNHCR ili iweze kuchangia pesa katika Gereza la Kasulu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; kwa kuwa miongoni mwa huduma nyingine za wafungwa ni pamoja na usafiri; na kwa kuwa gereza la Kasulu ninakabiliwa na ukosefu mkubwa wa gari la kubebea mizigo, lori la kusombea vitu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuni za kupikia chakula; je, ni lini Serikali itapeleka pesa kwa ajili ya kununua gari kwa ajili ya gereza la Kasulu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba UNHCR wamekuwa wakishirikiana na Serikali katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za wakimbizi, lakini hata na wananchi ambao wanazunguka maeneo husika. Kwa hiyo hili jambo tunalolifanya si jambo ambalo linalotakiwa lianze sasa hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la gari tuna changamoto kubwa sana ya uhaba wa magari katika Jeshi la Magereza, kwa hiyo kwa sasa hivi siwezi kutoa ahadi yoyote kwa sababu gari hizo hazipo; lakini zikapopatikana nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunachukua changamoto yake kama moja ya vipaumbele.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, sijaridhika sana, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na athari kubwa sana zilizoletwa na ujio wa wakimbizi Mkoani Kigoma, ongezeko la watu, miundombinu isiyotosheleza, ni lini hasa mpango kabambe utaletwa? Naomba commitment ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, ujio wa wakimbizi ndani ya Mkoa wa Kigoma, Makambi ya Wakimbizi ya Kibondo, Kasulu na Kakonko yamesababisha uharibifu mkubwa wa mazingira; je, Serikali inalijua hilo? Ni mikakati gani ya Serikali katika kusaidia Mkoa wa Kigoma kutokana na athari hizo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza naona halijawa wazi zaidi, lakini kwa nilivyolielewa, ameuliza kuna mpango gani kabambe? Nadhani alikusudia mipango ambayo Serikali inafanya kwa kushirikiana na Jumuiya za Kimataifa katika kuhakikisha kwamba shughuli na huduma za maendeleo katika jamii, wananchi ambao wanazunguka makambi yale wanafaidika. Kama hivyo ndiyo, basi nataka nimhakikishie Mheshimwa Mbunge kwamba kuna miradi mingi ambayo imeshatekelezwa kwa kushirikiana na Serikali na mashirika haya ya kimataifa chini ya UNHCR katika kuboresha huduma za jamii katika maeneo husika, kama ambavyo nimezungumza katika sekta ya afya, masoko, maji, elimu na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusiana na mazingira, ni kweli nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba ujio wa wakimbizi katika Mkoa wa Kigoma kwenye makambi yetu umeleta athari kwenye eneo la mazingira. Kwa kutambua hilo, ndiyo maana Serikali imechukua jitihada mbalimbali ili kuhakikisha kwamba inakabiliana na changamoto hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja katika mambo ambayo tumefanya, kwanza ni matumizi ya majiko ambayo wanaita majiko ya ubunifu, ambayo sasa hivi badala ya kutumia kuni kukata miti ovyo, aina ya upikaji na uandaaji wa chakula kwa wakimbizi umebadilika kwa kutumia teknolojia ambazo zinapunguza athari kwa mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika ukataji miti ambapo fito zilikuwa zikitumika kwa ajili ya ujenzi wa nyumba, umepungua kwa kiasi kikubwa. Sasa hivi nyumba ambazo zinajengwa ni za kudumu kwa kutumia matofali, pamoja na kutoa elimu kwa wakimbizi na jamii husika juu ya umuhimu wa kuweza kudhibiti mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hayo ni miongoni mwa mambo ambayo Serikali imekuwa ikifanya kuhakikisha kwamba athari ya mazingira inapatiwa ufumbuzi katika maeneo hayo ambayo yana makambi ya wakimbizi.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa Wizara inayo dira na inayo dira na mpango mkakati ambapo inatambua matatizo yaliyopo na hayo matatizo yanaiwekea katika mipango yake mikakati. Je, kwa mujibu wa mpango mkakati wake hizo nyumba za Askari wa Masasi zitajengwa lini?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa mujibu wa mpango wa mkakati huohuo na dira yake haya magari mawili au zaidi kwa Wilaya ya Masasi yatatolewa lini badala ya kuacha tu bila kuwekewa muda?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, kwamba kulingana na mipango tuliyokuwa nayo kuhusiana na ujenzi wa nyumba za Polisi Masasi pamoja na kupeleka gari, kama ambavyo nimejibu katika swali langu la msingi kwamba mipango hii inategemea na upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Spika, katika eneo hili la nyumba bahati njema ni kwamba tayari tumeshapata fedha za kuanzia ambayo tunatarajiwa kujenga nyumba 400. Kwa hiyo, katika Mkoa wa Lindi pia nyumba hizo zitajengwa, naomba baada ya Bunge hili niangalie ili niweze kumpa takwimu halisi za wilaya ya Masasi kuhusiana na nyumba hizo zipoje.
Mheshimiwa Spika, katika eneo la gari nimezungumza kwamba, kulingana na hali ya uhalifu, hasa kubwa zaidi jiografia ya Masasi ilivyo inastahili kupata gari. Nikaeleza kwamba, pale ambapo magari yatapatikana basi katika maeneo ya vipaumbele vilevile Wilaya ya Masasi ni mojawapo. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge avute subira magari yakipatikana tutapeleka na bajeti ikikaa vizuri nyumba tutajenga. (Makofi)
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Waziri, kama Waziri mwenye dhamana, nyumba za Magereza zilizoko pale Isanga hazifai, hazifai, hazifai kabisa kukaliwa na binadamu.
Mheshimiwa Spika, hata wewe kwa sababu ni mtu wa Dodoma, ukienda pale ukiona zile nyumba utasema hizi nyumba wanakaa binadamu? Naomba kupata tamko la Serikali, lini nyumba hizo zitajengwa upya kwa ajili ya Askari wetu hawa wa magereza katika Gereza Kuu la Isanga?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, ni kweli hata katika Jeshi la Magereza tuna changamoto ya uhaba wa nyumba na uchakavu wa nyumba za Askari Magereza. Ndiyo maana tunatumia njia mbalimbali ukiachilia mbali utaratibu wa kawaida wa kibajeti, tumekuwa tukitumia rasilimali katika maeneo husika kuzikarabati nyumba hizo, hasa ukitilia maanani kwamba,
Jeshi la Magereza lina kitengo madhubuti kabisa kinachojishughulisha na ujenzi pamoja na nguvu kazi ya wafungwa.
Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukifanya hivyo maeneo mbalimbali katika nchi, lakini fursa kubwa ambayo inaangukia katika Gereza la Isanga lililopo Dodoma ni juu ya hatua ya Serikali kuhamisha Makao Makuu yake rasmi kuja Dodoma. Jambo hilo limesababisha sasa hivi kuwa na fursa pana ya kutanua wigo wa mazingira ya ufanyaji kazi pamoja na makazi ya Askari wa vyombo vyetu vyote. Ndiyo maana mtaona sasa hivi kwamba, katika eneo la Magereza, Uhamiaji na Jeshi la Polisi kuna maendeleo makubwa ya kuboresha makazi ya Askari Dodoma ili kwenda sambamba na kasi ya ongezeko la ukuaji wa Mji wa Dodoma kutokana na maamuzi thabiti ya Serikali ya kuhamishia Makao Makuu Dodoma.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kituo cha Himo kiko mpakani na kinahudumia zaidi ya watu 500,000 na ukiangalia hali ya uhalifu, hasa mambo ya biashara za magendo mpakani ni kubwa. Serikali imekuwa ikiahidi kupatia kituo hiki gari, gari lililopo ni la zaidi ya miaka 10 na tulipewa na CRDB na gari hili limekuwa ni kazi ya Mbunge kulikarabati kila mwaka. Serikali imeshawahi kutoa ahadi zaidi ya mara tatu kuhakikisha wanapeleka gari Kituo cha Himo ili haki ya ulinzi na usalama wa Taifa ni kazi namba moja ya Serikali. Serikali watamke hapa ni lini wanapeleka gari hilo waliloahidi hapa immediately kabla Bunge hili halijamalizika kituo cha Himo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Mbatia amekuwa akiguswa sana na hili suala, nadhani si mara yake ya kwanza kuuliza hapa, mara ya mwisho nilimjibu na narudia jibu ambalo nimempa mara ya mwisho.
Mheshimiwa Spika, tunatambua changamoto za vituo vya Polisi vilivyopo mipakani, kikiwemo kituo cha Himo kama ambavyo amezungumza. Changamoto ambayo tunaipata sasa hivi ni kwamba, bado hatujapata magari mapya. Kwa hiyo, nikazungumza kwamba, tutaangalia sasa magari yatakapokuja yamekuja magari mangapi na wapi panahitaji zaidi.
Mheshimiwa Spika, natambua kituo ambacho amezungumza ni moja kati ya maeneo ambayo yanahitaji zaidi, itategemea wapi panahitaji zaidi sana na idadi ya magari yaliyopo. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge avute subira naamini kabisa kama siyo leo, kesho kama siyo kesho keshokutwa, lakini Serikali inatambua sana umuhimu wa maeneo haya, hasa mipakani kuwa na usafiri imara zaidi ili kudhibiti uingiaji na utokaji wa watu na bidhaa haramu katika nchi yetu.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Halmashauri ya Wilaya ya Liwale ina umri wa miaka 43 sasa, licha ya kukosa nyumba za Askari walioko kule hata kituo cha Polisi hatuna, umri wa miaka 43. Ni lini Serikali itatujengea Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Liwale, kuondokana na adha ya kupanga kwenye nyumba ambayo wamepanga, nyumba yenyewe nayo ni mbovu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, ni sahihi. Liwale pia, inahitaji kuwa na kituo, niliwahi kuongea na Mheshimiwa Mbunge tukakubaliana kwamba, mara litakapomalizika Bunge twende pamoja mimi na yeye Jimboni kwake tuweze kushirikiana tuone jinsi gani tunaweza tukafanya ili kuharakisha huu mchakato wa ujenzi wa kituo hiki ikiwezekana kwa kuanzia kuwashirikisha wananchi na wadau mbalimbali wakati tukisubiri jitihada za Serikali za kukamilisha ujenzi wa kituo hiki zitakapokuwa zimekamilika. Kwa hiyo, ahadi yangu na Mheshimiwa Mbunge kama tulivyozungumza iko pale pale. (Makofi)
MHE. MUSSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Pia nashukuru majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri kama alivyosema na kutupongeza wananchi, Mkurugenzi na mimi kwa nia nzuri ambayo tumeionesha ya kushirikiana na Jeshi la Polisi katika uhakikisha kero za ujambazi na usalama wa wananchi wetu zinatekelezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo hiki kimekamilika takribani miaka mitatu sasa na hayo marekebisho ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri ameyasema kama Mbunge nilikwishatoa fedha kwa maana mifuko ya simenti na nondo kurekebisha ile Amari ili kituo hiki kiweze kuanza kazi, takribani mwaka mmoja uliopita. Je, ananihakikishia vipi Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba kituo hichi sasa kitaenda kufunguliwa haraka kutokana na mahitaji yake?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini (b) Wilaya yetu ya Uyui ni Wilaya kubwa katika Mkoa wa Tabora ina majimbo mawili ya Igalula, Tabora Kaskazini lakini katika majibu yake amesema tuna magari matatu ambayo kwa kweli hayakidhi haja ya mahitaji ya Wilaya yetu. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kutuletea magari pamoja na mgao mkubwa wa mafuta ili kuweza kutoa huduma zilizo bora katika Wilaya yetu? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa hii kuendelea kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa jitihadi zake ambazo amekuwa akizifanya katika kuhakikisha kwamba kituo hiki kinakamilika haraka. Ni sahihi kabisa Mheshimiwa Mbunge kama ambavyo nimesema awali kwamba, amechangia katika kukamilika ujenzi wa Kituo cha Loya, ni jambo jema. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi kwamba, si dhamira ya Serikali kuona jitihada zake na wananchi ambao wametumia nguvu zao kujenga kituo hiki ziende bure bure kwa kuchelewesha kukitumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu katika swali la msingi ni kwamba, tatizo lililopo ni kwamba tunahitaji kukamilisha Lockup pamoja na amari ili ziwe katika hali nzuri kabla ya matumizi. Jambo hilo tunatarajia kulikamilisha katika muda mfupi sana ujao. Nitahakikisha kwamba nitakapotoka hapa nitafuatilia ili katika kipindi cha mwezi mmoja tuweze kukamilisha vitu hivyo viwili na kituo hiki kianze kutumika mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na magari, ni sahihi kwamba katika Wilaya ambazo zina changamoto za magari mojawapo ni Wilaya ya Uyui katika Mkoa wa Tabora. Ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba maeneo yote ikiwemo Wilaya ya Uyui hasa kulingana na ukubwa wa kijiografia wa Wilaya ile yanapata magari ya kutosha zaidi ya yale magari matatu ambayo nimeyazungumza katika jibu langu la msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho tunaweza kusema kwamba sasa hivi kinatukwaza au kinatukwamisha kutekeleza hilo ni kwamba bado mgao huo haujafanyika kutokana na changamoto mbalimbali ambazo zinakabili programu zima ya uletaji wa magari yaliyodhamiriwa kuletwa katika Serikali. Changamoto hizo zitakapopata ufumbuzi na magari hayo yatakapokuwa tayari kugawiwa, basi nina uhakika basi Mkoa wa Tabora ikiwemo Wilaya ya Uyui na Wilaya nyingine kama Nzega haina gari hata moja zitapewa kipaumbele.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Mkoa wa Arusha ni Mkoa ambao una shughuli nyingi sana haswa za kipolisi, zikiwemo na ku-escort viongozi mbalimbali, lakini inasikitisha sana Mkoa wa Arusha RPC wetu hana gari la polisi kutokana na gari lake lilipata ajali muda mrefu. Je, Serikali haioni ni muhimu kulichukulia jambo hili kama la dharura na kumpelekea RPC wetu wa Mkoa wa Arusha gari?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna umuhimu mkubwa RPC kuwa na gari. Nataka tu nimthibitishie kwamba kama gari la RPC limepata ajali basi tutaangalia uwezekano wa kulifanyia ukarabati gari hilo, likishindikana basi RPC wa Tabora tutampatia gari nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Samahani ni RPC wa Arusha.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Ukizunguka Tanzania nzima kwenye vituo vya polisi vyote utakuta magari mengi sana mabovu ambayo ni ya polisi wenyewe kwa maana ya kwamba ni ya Serikali hayajatengenezwa na hayafai tena kutengenezwa yanavyoonekana mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo ukija Jimbo la Ndanda, Kituo cha Polisi cha Ndanda ambacho kinahudumia jimbo zima na tuna kituo kimoja tu cha polisi hivi karibuni tuliletewa gari ambalo nalo linaonekana ni bovu kwa sababu toka limefika halijawahi kutumika. Sasa nataka Waziri atuambie ni lini mahususi kabisa wataamua kutengeneza gari la Kituo cha Polisi cha Ndanda kwa ajili ya kuweza kutoa huduma maeneo ya Jimbo la Ndanda ambayo yanasaidia pia na Jimbo la Ruangwa.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nizungumze kwa ujumla kwamba, tunakiri juu ya uwepo wa baadhi ya magari chakavu katika maeneo mbalimbali nchini. Hata hivyo, nataka nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wengine wote waliopo humu ndani na wananchi kwa ujumla kwamba tuna jitihada mbalimbali zinafanyika. Nyingine zinafanyika katika mikoa lakini nyingine zinafanyika katika ngazi ya Kitaifa kuhakikisha kwamba magari haya yanakuwa katika hali nzuri. Magari mengi tu ambayo yapo katika maeneo mbalimbali nchini tumeanza kuyafufua yanatumika, yale ambayo yanawezekana kufufulika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala la gari hii ya Ndanda specifically kwanza nataka nilichukue hili suala kwa sababu ni jambo ambalo haliingii akilini kwamba gari inapelekwa katika kituo na wakati huo gari haijaanza kutumika inakuwa mbovu. Kwa hiyo, nijue kwanza gari hii ilitoka wapi na kwa nini iwe haitumiki? Halafu tuangalie sasa baada ya hapo nini kifanyike ili kuweza kurekebisha.
MHE. BONIPHANCE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Vituo vya polisi vya Nyamuswa, Mgeta vimejengwa miaka ya 60, majengo yake sasa hivi ni hatarishi na wananchi wako tayari kusaidiana na Serikali kujenga vituo vile kwa kutoa nguvu kazi ya tofali, maji, kokoto na mawe. Je, Serikali iko tayari kushirikiana na wananchi kujenga vituo hivyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Getere kwa jitihada zake za kuhamasisha wananchi kuweza kupata vifaa ambavyo amevizungumza kwa ajili ya ujenzi wa vituo. Nataka nimhakikishie kwamba, Serikali itahakikisha kwamba tunaunga mkono jitihada hizo ili kuweza kufanikisha malengo ambayo wameyakusudia.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Hali ya vituo vya Polisi vya Kata pale Temeke ni mbaya sana, mapaa yameoza kabisa na Polisi muda mwingi wanafanya kazi chini ya miti badala ya kukaa kwenye ofisi kwa sababu hazikaliki. Hata hivyo, hata zile ofisi chache ambazo tumezijenga kwa nguvu za wananchi kama pale Makangalawe na Buza ambazo tumeshindwa kumalizia vyumba vya mahabusu na vya kutunzia silaha Serikali nayo imeshindwa kuvimalizia ili viweze kufanya kazi masaa 24. Sasa labda kwa sababu Mawaziri hawafahamu hali halisi iliyopo huko kwenye vituo hivyo ndio maana kila siku wamekuwa wakisema wanasubiri bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, kwa kadri watakavyoweza kujipanga ni lini watakuwa tayari kuja kufanya ziara Temeke ili wakajionee hali halisi ya vituo hivi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza si sahihi kwamba hatufahamu au hatujafika. Binafsi nimeshafanya ziara katika Jimbo lake na Wilaya yake na nimeshiriki katika ujenzi wa kituo pale nimesahau jina la kile kituo, lakini ni maeneo ya Mbagala. Hali kadhalika nikashiriki katika uzinduzi wa kituo kingine cha Polisi nikizindua maeneo ya kule Wilaya hiyo ya Temeke lakini Jimbo la Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni kwamba hali ya vituo vya Polisi vya Temeke tunaifahamu vizuri, kwa sababu physically nimekwenda na nimeshuhudia na tumeshiriki na wananchi kuweza kufanya kazi ya kuvijenga na kuvikarabati vituo vingine ambavyo ni vichakavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho ningemwomba Mheshimiwa Mbunge atusaidie ni kwamba, naye aendelee kuunga jitihada zetu hizi mkono kwa sababu si rahisi kuweza kukabiliana na changamoto hizi za vituo kwa wakati mmoja. Ndio maana tunafanya kazi hizi kwa awamu na kuhamasisha wadau kama sio wananchi na Mheshimiwa Mbunge kama ambavyo niliwapongeza Waheshimiwa Wabunge waliopita hapa, Mheshimiwa Getere, Mheshimiwa Ntimizi katika suala hili hili la msingi ambalo nimejibu, basi na Mheshimiwa Mtolea naye tunakukaribisha aweze kuhamasisha wananchi hata kama akiamua fedha yake ya Mfuko wa Jimbo aingize katika kukarabati vituo hivi, tutamshukuru sana.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nitaomba kuuliza maswali ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Ngara kimejengwa tangu enzi za ukoloni na majengo yake yamechakaa pamoja na nyumba za watumishi kwa maana nyumba za askari wetu. Sasa ni lini Serikali itaweza kukarabati kituo hiki cha polisi na nyumba za askari wetu?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, wananchi wa Jimbo la Ngara wameathirika kwa kiasi kikubwa sana na operesheni zinazoendelea hususani za Uhamiaji. Maeneo mengi Dar es Salaam, Kahama, Arusha, Ngara kwenyewe wananchi hawa wanapokamatwa kwa kuhisiwa na kueleza kwamba wanatokea Ngara moja kwa moja wanachukuliwa kwamba ni wahamiaji haramu. Wamekuwa wakipigwa na kuumizwa na baadaye baada ya kujiridhisha inaonekana kwamba ni Watanzania halisi. (Makofi)
Sasa je, Serikali iko tayari pale inapobainika kwamba wananchi hawa wamehisiwa, wakadhalilishwa, wakapigwa wako tayari kulipa fidia kwa hawa wananchi wanaokuwa wamedhalilishwa na kupigwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza alitaka kujua kuhusiana na uwezekano wa kukarabati Kituo cha Polisi Ngara pamoja na nyumba za polisi. Kama ambavyo nimejibu kwenye jibu langu la msingi kwamba dhamira hiyo kwa Serikali ipo na pale tu ambapo hali ya kifedha itaruhusu tutakarabati kituo hicho cha Ngara na nyumba za polisi pamoja na maeneo mengine nchini ambako kuna changamoto kubwa za uchakavu wa vituo na nyumba za polisi.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na wananchi ambao wamepigwa na kuonekana kwamba wamedhaniwa kwamba si Watanzania. Kwanza si utaratibu wa Jeshi la Polisi kupiga raia ama hata wageni. Kuna utaratibu wa kisheria ambao ikiwa mgeni ama raia amevunja sheria unatakiwa uchukuliwe kwa mujibu wa sheria. Nadhani suala hili labda Mheshimiwa Mbunge baada ya Bunge hili tukae tuone jinsi gani tunaweza kulichunguza ili tujue hatua za kuchukuliwa baada ya hapo kama kutakuwa kuna ukiukwaji wa sheria, sheria iweze kufuata mkondo wake.
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Matatizo yaliyopo Ngara ni sawa kabisa tena yanapita ya Jimbo la Mlimba. Jimbo lenye kata 16 halina kituo cha polisi wala gari la polisi na kupelekea Mahabusu kukaa muda mrefu sana ili kuwapeleka katika Mahakama au Magereza yaliyoko kilometa 265. Je, ni lini sasa Serikali itaboresha miundombinu ya Jeshi la Polisi ndani ya Jimbo la Mlimba angalau uwapatie gari basi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, ni sahihi katika Jimbo la Mlimba kuna upungufu ama ukosefu wa Kituo cha Polisi, lakini kama sehemu ya mkakati wa Serikali wa kujenga vituo 65 vya polisi nchi nzima tunaamini Mlimba ni moja ya katika maeneo hayo. Kwa hiyo, tu nimuombe Mheshimiwa Mbunge avute subira pale ambapo mpango huo utakapokuwa umekamilika kituo cha polisi kitapatikana Mlimba.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Swali la kwanza la Mheshimiwa Gashaza lilikuwa ni Ngara kuanzishiwa Kanda Maalum ya Kipolisi na Wilaya ya Ngara, Kakonko, Kibondo, Kasulu na Kigoma ni maeneo ambayo yanapakana na nchi nne yaani Burundi, Rwanda, Congo na Zambia kwa upande wa majini Kusini. Ni kwanini Serikali isione umuhimu wa kuanzisha kanda maalum kwa sababu zone ile ndiyo zone inayopitisha silaha ambazo hatimaye zinakuja kutushambulia katikati ya nchi yetu. Ni kwa nini Serikali isione umuhimu wa wilaya hizo tano kuanzishiwa Kanda Maalum ya Kipolisi ili kudhibiti uingizaji wa silaha katika nchi yetu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimejibu katika swali langu la msingi kwamba kuna jitihada kadhaa ambazo tumezichukua za kuimarisha hali ya usalama katika maeneo ya Mkoa wa Kigoma kwa ujumla wake ikiwemo hasa maeneo ya Wilaya ya Ngara. Kutokana na jitihada hizo imepelekea kwamba eneo hilo kwa sasa hivi kukosa vigezo vya kuweza kuanzisha ama umuhimu wa kuanzisha Kanda Maalum. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge aridhike kwamba kwa sasa hivi akubaliane na sisi kwamba eneo la Ngara bado halijakidhi vigezo hivyo kutokana na kuimarika kwa hali ya usalama katika maeneo hayo.
MHE. BHAGWANJI MAGANLAL MEISURIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru Waziri amejibu vizuri. Katika Mkoa nimepata gari lakini mimi nagombania Jimboni kwangu Chwaka na Jozani nipate gari kwa sababu pana vibaka, ubakaji na wananchi wameongezeka. Kama sijapata hilo gari itakuwa matatizo katika Jimbo langu.

Swali la pili, kama sijapata hilo gari hii Baniani peke yake Bungeni sitaweza kurudi kwa mara ya pili. Kwa hiyo, naomba nipatiwe hiyo gari ili niweze kurudi na wananchi wangu wapate huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo machache Mheshimiwa Waziri, naomba nipate gari katika Jimbo la Chwaka. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka nimpongeze Mheshimiwa Bhagwanji kwa jinsi ambavyo amekuwa mstari wa mbele kabisa kupigania maslahi ya askari wetu kwenye Jimbo lake. Mimi ni shahidi mara kadhaa hapa nimekuwa nikijibu maswali yake na nikiona jitihada zake na hata wananchi wake, nina hakika wanaona jitihada hizo. Kwa hiyo, kwa jitihada hizo sioni kama wananchi wake watakuwa na mashaka naye na kuacha kumrudisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na ombi lake, kama ambavyo nimejibu swali la msingi kwamba kwa sasa hivi tumepata magari machache ambayo tumeyagawa katika level ya Mikoa na gari mbili za Mkoa Kusini Unguja zimeenda kwenye Ofisi za Wilaya zote mbili. Hata hivyo, kwa kuwa gari nyingine zinakuja na kuzingatia vipaumbele ambavyo nimevieleza basi tunalichukua ombi lake na kulifanyia kazi kwa uzito unaostahili.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali na napongeza juhudi kubwa za Serikali kwa kujenga Kituo kipya huko Chukwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Chukwani ni nyuma kidogo, Mazizini ni barabarani na ni centre na karibu na Shehia nyingi kama vile Shakani, Kombeni, Maungani na kadhalika. Sasa kile Kituo cha Wilaya kwa nini hiki cha Mazizini mnataka kukiua?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, kwa nini msifanye taratibu kama hivyo mnavyoshirikiana na wadau kufanya kampeni ya kuboresha vyoo na vyumba vya mahabusu kwa nchi zima mkianzia na hapo Mazizini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, hatutarajii kukiua Kituo cha Mazizini, kitu ambacho tunafanya ni kuhamisha kuwa Kituo cha Wilaya, kuhamishia Chukwani. Kwa hiyo Kituo cha Mazizini kitaendelea kutumika tu, tutafanya jitahada ya kukikarabati na kwa kuwa kiko barabarani kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema, tunaamini kwamba kinahitajika kuendelea kutoa kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, kuhusu ukarabati wa vituo vyetu kwa ujumla wake ikiwemo mahabusu, ni jambo ambalo tunakwenda nalo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wake kuhusu kuwatumia wadau ndiyo tumekuwa tukiufanya kazi, wako wadau ambao wamekuwa wakishirikiana nasi kwa dhamira ya kurekebisha mazingira ya Vituo vyetu vya Polisi ikiwemo mahabusu.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na maelezo ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, msingi wa hoja ni Serikali ianze mchakato wa kimkataba wa makubaliano, ndiyo msingi wa hoja. Kama kubadilishana wafungwa kunaongozwa na mkataba, ni lini Serikali yetu itaanza mchakato huo kati ya nchi ya DRC na Burundi ambazo zina wafungwa wengi Kasulu na Kigoma?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri anataka kuniambia wale wafungwa wa Kongo na Burundi waliopo Kibondo, Kasulu na Kigoma kwa ujumla wanatoka Taifa gani kama siyo wakimbizi toka nchi hizo nilizozisema?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Daniel Nsanzungwanko, Mbunge wa Kasulu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ni ushauri ambao tumeuchukuwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni kweli wale ni wakimbizi lakini kwa maana ya tafsiri ya kisheria wamefanya makosa wamekuwa ni wafungwa. Kwa hiyo, kimsingi kwa tafsiri ya kisheria wale ni wafungwa.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuuliza swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa kumekuwa na operesheni ambayo inafanywa na Jeshi la Polisi ya kusaka watu ambao wanasema hawana kazi mtaani. Cha ajabu hawa watu wanakamatwa kipindi kile cha jioni tayari wamesharudi makazini wakiwa wamepumzika barazani huko Dar es Salaam na maeneo mengine ya Tanzania hali ambayo inapelekea kujaza mahabusu zetu katika maeneo mengi ya nchi hii. Serikali inatoa tamko gani kuhusu operesheni hii inayofanywa na Jeshi la Polisi ambayo inapelekea kujaza mahabusu bila sababu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maftaha, Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina taarifa ya maelezo ambayo ametoa Mheshimiwa Mbunge kwamba Polisi wanachukuwa mtu yeyote. Nachojua katika utaratibu wa kawaida wa Jeshi la Polisi ni kufanya doria na pale wanapoona watu wanaojihusisha na uhalifu ama wana viashiria vya uhalifu kuwachukuwa na kufanya uchunguzi wao ili hatua zaidi zichukuliwe. Taarifa za ziada kwamba kuna watu ambao anadhani yeye hawakupaswa kuchukuliwa na Jeshi la Polisi kutokana na shughuli hiyo, labda angetupatia taarifa mahsusi ili tuweze kuzifanyia kazi.
MHE. KABWE Z.R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukienda Segerea utakuta idadi ya mahabusu ni wengi zaidi kuliko watu ambao wameshahukumiwa na hii inatokana na sheria kandamizi ambazo zinanyima watu dhamana kama zilivyonyima dhamana Wabunge wetu wawili; Mheshimiwa Mbowe na Mheshimiwa Matiko na Sheria ya Anti Money Laundering ambayo makosa yanawekwa tu ili kuweza kuwaweka ndani watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haioni kwamba imefikia wakati kwa watu ambao umri wao ni kuanzia miaka 75 na kuendelea kama ilivyokuwa kwa Mheshimiwa William Shelukindo ambaye aliwekwa kwenye Gereza la Maweni kwa kukosa dhamana tu, kuweka utaratibu watu hawa wawe wanafungwa kifungo cha nyumbani kwao badala ya kuwajaza magerezani bila sababu kutokana na umri wao kama ambavyo nchi nchi nyingine wanafanya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Zitto amezungumza vitu viwili kwa pamoja suala la mahabusu na wafungwa. Suala la wafungwa siku zote nimekuwa nikieleza mikakati ya Serikali ya jinsi ya kupunguza msongamano kwenye magereza kupitia njia mbalimbali. Tumeona Mheshimiwa Rais akitoa msamaha kwa wafungwa, tuna sheria za parole, sheria za huduma za jamii na nyinginezo. Pia tunafanya jitihada ya kujenga magereza ili kupunguza ule msongamano. Kwa hiyo, kimsingi kwa wafungwa huo ndiyo mkakati wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la mahabusu ni suala la kisheria zaidi, kumchukua mahabusu na kumpa kifungo cha nje anakuwa bado hajahukumiwa. Kwa hiyo, cha msingi ni kufuata sheria za dhamana ili aweze kupata dhamana wakati huo huo sisi tukifanya jitihada za kuboresha mahabusu zetu ili kuepusha msongamano na madhara yanayoweza kujitokeza.
MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza na nieleze masikitiko yangu kwamba swali langu nilileta mwaka 2016 lakini kwa bahati mbaya limekuja 2019. Nishukuru kwa maendeleo ambayo yamefanywa ya kusambaza hizo mashine za kielektroniki nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kusambazwa mashine hizo sasa hivi Jeshi la Polisi limekuwa sehemu ya chanzo kikuu cha mapato ya Serikali na wanapangiwa viwango vya fedha za kukusanya. Kwa hiyo, uwepo wa mashine hizi pamoja na kwamba tulidhani ingekuwa ni suluhisho lakini imekuwa chanzo cha kuwabambika makosa watumia barabara ili kuzalisha mapatao. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwanusuru watumia barabara kwa makosa haya ya kubambikizwa na kulazimishwa kulipa faini ili tu kufikia viwango za fedha walizokubaliana vitendo vinavyofanywa na askari wa usalama barabarani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, hivi karibuni Mheshimiwa Kangi Lugola, Waziri mwenye dhamana ya Mambo ya Ndani alitoa maelekezo kwamba gari linapokamatwa hata kama litakuwa na makosa zaidi ya moja basi liandikiwe kosa moja lakini hadi tunavyozungumza, magari mengi yanaandikiwa faini zaidi ya kosa moja na kutozwa faini na penalties kinyume na maelekezo ya Mheshimiwa Waziri. Je, Serikali inaweza kurejea tena agizo lake kupitia Bunge letu Tukufu ili liwe maelekezo rasmi ya Serikali kwa watekeleza sharia? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Magereli, Mbunge wa Viti Maalum, kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na hoja ya kubambikiwa kesi ambayo ametuhumu Askari wa Usalama wa Barabarani, nimwambie tu kwamba yanapotokea matukio kama haya kwa baadhi ya askari wetu tunachukua hatua na hata hili agizo la Mheshimiwa Waziri lilikuwa linalenga kuziba mianya ya aina kama hiyo. Kwa hiyo, nimhakikishie Mbunge kwamba Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nchi ndiye mwenye dhamana ya mwisho ya Wizara hii na maagizo yake ni lazima yatekelezwe. Maagizo haya yanatekelezwa ikiwa kuna upungufu katika utekelezaji wake, kama labda kuna watu ambao hawatekelezi, hiyo taarifa hatujaipata rasmi lakini kimsingi Mheshimiwa Waziri ametoa agizo na linapaswa kutekelezwa kwa maslahi ya wananchi wa nchi yetu ambao wanatumia barabara.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Serikali imetoa majibu kitaalam sana na Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri mwenyewe kwamba uwepo wa gereza mahalI unapunguza gharama za usafiri, unaharakisha uendeshaji wa kesi, vilevile unapunguza msongamano magerezani ambao ni kubwa sana kwa sasa. Pamoja na majibu hayo mazuri, nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Chunya ni Wilaya kongwe sana hapa nchini. Katika Wilaya tatu kongwe Chuya imo, mwaka huu inatimiza karibu miaka 80. Je, rasilimali fedha itakapopatikana Mheshimiwa Waziri ananihakikishia kwamba ataipa Chunya kipaumbele kujenga gereza Wilayani?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, katika kipindi cha mpito kabla ya kujengwa kwa gereza hilo, je, Serikali ipo tayari kujenga walau chumba, siyo gereza, chumba cha mahabusu ili kuweza kupunguza gharama hizi ambazo Serikali imezisema?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mhehimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Victor Mwambalaswa, Mbunge wa Rukwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba pale bajeti itakapokaa vizuri Chunya itakuwa eneo la kipaumbele. Kwanza, nichukue fursa hii kumpongeza yeye binafsi kwa kushirikiana na wananchi wa eneo hilo kuanza mchakato ambao unaendelea wa ujenzi wa bweni moja na jengo la kuishi Askari ambao umefikia 90%.

Mheshimiwa Spika, ni matarajio yetu kwamba litakapokamilika kwa 100% tutaanza kupeleka wafungwa na kuanzisha kambi ambapo wafungwa hao tutawatumia kwa ajili ya kufyetua matofali ikiwa ni maandalizi ya ujenzi wa gereza. Wakati tunasubiri bajeti ikae vizuri Serikali tutaunga mkono nguvu hizo kwa kuhamasisha wafungwa na kutumia rasilimali zilizopo Chunya ili tuweze kutatua tatizo hili angalau kwa kuanzia gereza la mahabusu ili kupunguza msongamano.
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Katika majibu yake Mheshimiwa Naibu Waziri amesema ujenzi wa magereza katika maeneo mbalimbali vilevile utasaidia kupunguza msongamano wa mahabusu. Pia amesema kuwa ujenzi huo kwa sasa unakwamishwa na uhaba wa rasilimali.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ujenzi huu hauwezi kuendelea kwa haraka kwa sasa; na kwa kuwa kuna msongamo mkubwa wa mahabusu katika magereza mbalimbali kutokana na kubambikiziwa kesi ama mashtaka yasiyokuwa na dhamana na hukumu ambazo kimsingi zinajaza tu magereza yetu, je, Serikali ipo tayari sasa kutekeleza operesheni maalum ya kupunguza mahabusu katika magereza mbalimbali nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mhehimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa John Mnyika, Mbunge wa Ubungo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nirekebishe kauli yake si kwamba msongamano wa mahabusu chanzo chake kikubwa ni ubambikiziwaji wa kesi. Tunajua tuna changamoto ya ubambikiziwaji wa kesi na pale ambapo tunabaini na tumekuwa tukifanya kazi hiyo ya kuhakikisha wale ambao wanahusika na upambikaji kesi wanachukuliwa hatua za kisheria.

Mheshimiwa Spika, lakini msongamano wa mahabusu unatokana na changamoto za uhaba wa magereza. Magereza yetu yamejengwa muda mrefu na idadi ya watu inaongezeka na changamoto ya uhalifu inasababisha msongamano huu pia kuongezeka. Hata hivyo, Serikali tumefanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha kwamba tunapunguza msongamano huu.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake kuhusu operesheni, hivi tunavyozungumza tuna utaratibu wa kamati za kuharakisha kesi ambazo zinahusisha wadau mbalimbali ambapo wanahakikisha wale ambao wanatakiwa dhamana kwa haraka wanasikilizwa. Vilevile, tumekuwa tukitumia sheria zetu mbalimbali, kwa mfano, Sheria ya Bodi ya Parole, Sheria ya Huduma za Jamii, Sheria ya EML na msamaha Mheshimiwa Rais ambao amekuwa akitoa kila mwaka, yote haya yanasaidia kupunguza msongamano wakati Serikali ikiendelea na jitihada zake za kujenga mabweni na kuongeza na kupanua idadi ya magereza yetu ili yaweze kuchukua idadi kubwa zaidi ya wafungwa.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2014 Serikali ilitenga eneo la hekari zaidi ya 30 katika Kata ya Ushokora kwa ajili ya kujenga Gereza la Wilaya lakini kwa miaka sita (6) sasa wananchi wa Pozamoyo pale Ushokora hawajawahi kuambiwa chochote na waliondolewa kwenye makazi na mashamba yao wameenda kujibanza kwenye maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, Serikali ina mpango gani sasa angalau kufidia wananchi wale iliyowahamisha pale ambao wamepanga maeneo mbalimbali waweze kwenda kutafuta makazi sahihi na wakati huo huo Serikali iweze kujenga hilo gereza maana ni muda mrefu sasa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mhehimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Magdalena Sakaya, Mbunge wa Kaliuwa na Naibu Katibu Mkuu mpya wa Chama cha CUF, kama ifuatavyo:- (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama nimeelewa vizuri swali lake anazungumzia wananchi ambao wametakiwa kuhamishwa kwa ajili ya ujenzi wa gereza na ambao pengine anadhani wanahitaji kulipwa fidia. Kama hivyo ndivyo kwa sababu swali lake hili ni mahsusi naomba nilipokee na tuweze kulifanyia kazi na nitampatia mrejesho.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kama ilivyo kwa Wilaya ya Chunya, Wilaya ya Kyela haina mahabusu ya wanawake hivyo kupelekea kupelekwa Wilaya ya Rungwe. Je, ni lini Serikali itajenga mahabusu ndogo ya wanawake kwa Wilaya ya Kyela?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimezungumza kwamba changamoto inayosababisha tusiwe na ujenzi wa magereza yetu ambao siyo wa kasi kubwa sana ni kutokana na ufinyu wa bajeti. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Gereza la Wanawake Kyela ni miongoni mwa maeneo ambayo tunayaangalia kwa jicho la kipaumbele sana. Kwa hiyo, pale ambapo bajeti itakaa vizuri Gereza la Wanawake Kyela litakuwa ni jambo la kipaumbele.
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS NYIMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii ya kuuliza maswali mawili. Ningependa kufahamu njia gani zinazotumika katika kutoa elimu hiyo hususan vijijini?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili kwa kuwa Mkuu wa Mkoa amekuwa mdau mkubwa wa kuwapigania watoto wanaoachwa na wazazi wao wa kiume, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuja na sheria za kuwabana wanaoacha watoto hususan wakiwemo na raia wa kigeni.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza kwa pamoja ya Mheshimiwa Tauhida kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa tunayo sheria ambayo inaharamisha matukio ambayo yanahusisha mtu yeyote kutelekeza mtoto ama kutotoa matunzo na sheria hiyo si nyingine ni Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 kifungu cha 166, kwa hiyo sheria tunayo tayari. Niwaombe akinamama wote ambao wameathirika na jambo hili kwa kuwa ni la jinai, waende kwenye vituo vya polisi vilivyo karibu wafungue kesi hizi ili Serikali tutumie sheria nyingine zozote tulizonazo za kuwarejesha nchini wajibu mashtaka.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo zoezi alilolifanya Mheshimiwa Makonda Mkuu wa Mkoa ambalo Mheshimiwa Mbunge ame-refer ni zoezi ambalo lilionyesha dhahiri kwamba sio wageni tu wanaotelekeza watoto isipokuwa hata Watanzania wanatelekeza watoto na tulishuhudia wengine humu ndani sura za watoto zikiwa zinawafanana.

Mheshimiwa Spika, nitoe wito kwa akinamama wa Tanzania, nawaomba mtumie kilicho ndani ya nchi, kilicho chenu kuliko kuanza kukimbilia kutumia raia wa kigeni ilhali hata humu ndani, rudini humu ndani kumenoga.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, nakubaliana kabisa na maelezo ya Mheshimiwa Waziri kuwa pale Polisi anapokuta kuna umuhimu wa kusimamisha gari ambalo limevunja sheria ni muhimu wafanye hivyo.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwa tumekuwa na hivi vituo maalum vya ukaguzi, sasa hivi kumekuwa na changamoto kubwa hasa kwenye mabasi ya daladala. Kumekuwa na unnecessary stop na kusababisha ucheleweshaji wa wananchi kwenda kufanya shughuli zao. Nitakupa mfano, unakuta daladala imesimamishwa na Traffic yuko pembeni ana-argue na Konda kwa nini hana proper uniforms? Haya ilibidi yafanywe kabla huyu abiria hajaingia kwenye gari.

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, nilitaka kujua sasa kama Serikali na Jeshi la Polisi tumejipanga vipi kuhakikisha sasa tunakuwa na hii mandatory car inspection tofauti na utoaji wa stika wa sasa ukizingatia hizi stika zimekuwa zinatolewa kwenye magari yasiyo na viwango na kusababisha ajali kubwa za barabarani. Nakushuru sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mazuri sana na ya msingi. Baada ya pongezi hizo sasa nitoe majibu ya maswali yake mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mbali ya sheria ambayo nimeinukuu inayotoa mamlaka kwa Askari kusimamisha gari popote anapoitilia hitilafu, ambapo madhumuni ya sheria ile kimsingi inatokana na baadhi ya madereva wetu nchini ambao wamekuwa wakikiuka Sheria za Barabarani mara kwa mara, kwa mfano, utakuta mtu anaendesha gari kwa speed. Kwa hiyo, Askari akiona utaratibu wa uendeshaji kama huo, lazima achukue hatua.

Mheshimiwa Spika, kwanza nitoe wito kwa wananchi hasa madereva kutii Sheria za Barabarani ili kuepusha usumbufu. Pili, nataka nichukue fursa hii pia kutoa wito kwa Askari wetu wa usalama barabarani nchi nzima ambao kama wapo kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge najua atakuwa ame-experience hiyo, kama wapo ambao wanafanya utaratibu wa kusimamisha magari kiholela kwa kujifichia chini ya mwamvuli wa sheria hii bila kuwa na makosa yoyote, basi waache mara moja.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la kuwa na utaratibu wa ukaguzi wa lazima, nataka nimwelezee Mheshimiwa Mbunge kwamba kama Serikali tumeshalitafakari kwa kina suala hilo na tunatambua kuwa na utaratibu wa ukaguzi wa lazima ni jambo ambalo ni muhimu na haliepukiki katika karne hii tuliyokuwa nayo, siyo tu kwamba litasaidia kutoa fursa kwa magari yetu kukaguliwa vizuri zaidi na hivyo kuwa na magari salama barabarani, lakini itasaidia kuiongezea mapato Serikali na hususani Jeshi la Polisi katika kukabiliana na changamoto mbalimbali ambazo tunazikabili. Kwa hiyo, kwa kutambua hilo tumekuja na mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza tunatamani kwamba katika mabadiliko ya sheria ambayo itakuja, utaratibu huo utakuwa unasimamiwa na baraza jipya la usalama barabarani ambalo tunatarajia lije na muundo mwingine. Kwa hiyo, ni Baraza Tendaji, lakini hata kama matamanio yetu hayo bado hayajafikiwa au yatakuwa yamechelewa kufikiwa, tumeshatoa maelekezo kwa Shirika la Jeshi la Polisi (Police Cooperation Soul) kuanza mchakato wa kuanzisha utaratibu huo wa ukaguzi lazima.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nichukue fursa hii vilevile kuwaelekeza Jeshi la Polisi kupitia Shirika hilo la Maendeleo kuharakisha huo mchakato ili uweze kuanza mapema ikiwezekana hata kabla ya Awamu hii ya Kwanza ya utawala wa Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli haijamaliza muda wake.

Mheshimiwa Spika, nashukuru.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa vituo hivi vya ukaguzi wa magari barabarani siyo tu muhimu kwa wananchi vilevile ni muhimu sana kwa Askari wetu. Tunatambua kazi kubwa wanayofanya Askari wa Barabarani, lakini Askari hawa mara nyingi wanapopata ajali kulipwa haki zao inachukua muda mrefu. Kwa mfano tu, katika Mkoa wangu wa Arusha kuna Askari wengi waliopata ajali wakiwa kazini, lakini mpaka sasa hivi hawajalipwa stahiki zao.

Je, ni lini Serikali italipa maaskari ambao wamepata ajali kazini haki yao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza lazima nikiri kwamba kulikuwa na changamoto za baadhi ya malipo ya stahiki mbalimbali za Askari wetu nchi nzima ikiwemo hii ambayo Mheshimiwa Mbunge ameizungumza, lakini lazima nichukue fursa hii kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano, lazima tujipongeze kwa pale ambapo tutafanya vizuri.

Mheshimiwa Spika, sehemu kubwa ya malimbikizo haya yameanza kulipwa na tunaamini kwamba kama kutakuwa kuna maeneo ambayo bado hayajakamilika, kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amezungumza, hii fidia ya Askari ambao wanapata ajali barabarani, basi tutakamilisha pale michakato mingine ikiwemo uhakiki pamoja na bajeti itakapokaa sawa.

Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Mbunge, kama ana maombi mahususi ya Askari ambayo anafahamu, basi aweze kutupatia ili tufuatilie tujue ni tatizo gani lililosababisha mpaka leo wawe hawajapatiwa stahiki zao?
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nami kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza. Pamoja na mabadiliko ya Muswada wa Sheria ya Usalama Barabarani ambayo inatarajiwa kuletwa hapa Bungeni, kuna malalamiko kwa madereva mbalimbali kwamba kosa lolote linapotokea, basi hakuna onyo, hakuna karipio. Karipio kubwa ni shilingi 30,000/= kwa haraka sana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, inaonekana kwamba Polisi kwa wakati huu wanakusanya zaidi fedha kwa njia ya mapato zaidi kuliko kutoa karipio au kutoa onyo. PGO inaelekeza nini pale ambapo dereva amefanya kosa dogo la kwanza juu ya tatizo hili?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza ni imani yetu na imani ya Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote waliomo humu ndani kwamba mtu yeyote ambaye amechukua chombo cha usafiri na kuingia barabarani, maana yake kwanza amepata mafunzo ya kutosha na ana leseni.

Mheshimiwa Spika, hiyo ni moja, lakini la pili nina hakika Mheshimiwa Masoud anatambua kwamba tumekuwa tukifanya kazi kubwa sana ya kutoa elimu kuhusiana na usalama barabarani kwa kutumia njia mbalimbali ili kuwakumbusha wale madereva ambao wamekuwa wakighafirika katika kufuata Sheria za Usalama Barabara.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kwa kuzingatia hayo mawili ni imani yetu kwamba mtu yoyote ambaye yuko barabarani anaendesha gari, anatambua wajibu wake na hivyo basi, sidhani kama ni jukumu la Jeshi la Polisi kuanza sasa kutoa elimu barabarani wakati mtu anahatarisha uhai wa raia wengine. Kwa hiyo, niendelee kusisitiza kwamba, ni vizuri kila mmoja ambaye anaendesha gari barabarani ajue kwamba kuna sheria na afuate sheria hizo.

Mheshimiwa Spika, jukumu la Jeshi la Polisi ni kuhakikisha kwamba wale ambao hawafuati sheria basi wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria ikiwemo kutozwa faini. Hata hivyo, kuna baadhi ya changamoto ambazo tumekuwa tukizizungumza kila siku zinahitaji busara katika kuzikabili na niendelee kutoa wito kwa Askari Polisi kuzingatia busara wakati mwingine pale ambapo kuna matatizo ambayo yanaweza kuepukwa. Kwa mfano, kama ambavyo hata Mheshimiwa Waziri amekuwa akizungumza mara zote, unakamatwa mtu kwa kosa moja linazalisha makosa mengi, mtu anashtakiwa kwa makosa zaidi ya matano au sita. Kwa hiyo, mambo kama haya na mambo mengine ambayo yamekuwa kero kwa wananchi, hayo tumekuwa tukitoa maelekezo kwa Jeshi la Polisi litumie busara katika kuyakabili. Hata hivyo, tunataka kusisitiza umuhimu wa kutii sheria bila shuruti ili kuepusha ajali na kuokoa maisha ya Watanzania ambao wamekuwa wakipoteza maisha yao na kupoteza vyombo vyao kila siku.
MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwenye barabara kuu ya Dar es Salaam - Morogoro tumeona sasa hivi wamefunga cameras. Sasa kwa nini camera zile zisifungwe nchi nzima ili sasa baada ya kufungwa zile camera Askari wanaokaa barabarani warudi vituoni, waende wakashughulike na masuala mengine ya wahalifu, kwa sababu msingi wao wa kukaa barabarani mkubwa ni speed. Sasa kwa kuwa zinafungwa camera ambazo zitakuwa zinachukua picha, zinatuma report kwenye database, wherever halafu zile report zinafuatiliwa hata baada ya wiki mbili, mwezi mmoja mtu anapelekea tiketi kwa mujibu wa details za gari lake. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMB0 YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Mbilinyi, Mbunge wa Mbeya Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, huu ndiyo mwelekeo wa Serikali yetu. Ni imani yetu kwamba, mambo yatakapokuwa yamekaa vizuri kibajeti tutafunga camera katika Miji mikuu yote na maeneo mengine nchi nzima. Kwa hiyo ni suala tu la kuvuta subira na kazi hiyo itafanyika hatua kwa hatua kadri ya hali ya fedha itakapokuwa inaruhusu.
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Swali la kwanza, kuna askari ambao wanawaweka ndani wananchi wetu bila ya kuwa na makosa ya kuwekwa ndani. Vilevile, wengine wanawaweka ndani zaidi ya saa 24 wakiwa hawana makosa ya kuwekwa ndani saa 24. Je, Wizara yako inatoa kauli gani juu ya Maaskari hawa kuhakikisha wanaepuka kuwaweka ndani wananchi wetu zaidi ya saa 24?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Watanzania wengi hawana elimu ya sheria hii ya Jeshi la Polisi. Je, Serikali ina mikakati gani ya kutoa elimu kwa wananchi wetu ili waweze kujua haki zao za msingi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mattar, Mbunge wa Shaurimoyo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu langu la msingi nilieleza kwamba ukiachilia mbali Kifungu 148(5) ambacho kimeainisha makosa ambayo hayana dhamana, lakini kuna Kifungu cha 65 pamoja na 66 vya sheria hiyo hiyo ambayo vinaeleza ni kwa jinsi gani hayo makosa ambayo yana dhamana itatolewa kwa utaratibu upi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Kifungu cha 65 kinaeleza umuhimu wa kufahamu historia na familia ya mhusika lakini kifungu cha 66 kinaeleza kwamba mtuhumiwa huyu ambaye anaomba dhamana anatakiwa aweze kuandika kwa mkono wake kwamba atarudi siku ya kesi yake itakapokuwa imeitwa. Kwa hiyo, pamoja na mambo mengine, dhamira kubwa ni kuona jinsi gani mtu huyu anapoachiwa kwenda nje hawezi kuwa hatari kwa usalama wake mwenyewe ama kwa jamii ambayo inamzunguka. Kwa hiyo, inawezekana labda wananchi wanashindwa kufahamu kwamba Polisi wanapomweka mtu zaidi ya saa 24 wakati makosa yana dhamana kwamba kuna mambo ambayo masharti yake hayajatimizwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitutoe wito kwa wananchi kuweza kutumia fursa ya Jeshi letu la Polisi pamoja na Serikali kwa ujumla tunapoweza kuzungumza mara kwa mara kuwaelimisha ili wafahamu sheria za nchi yetu na wafahamu haki zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ni jukumu la Wabunge kuweza kuwaelimisha wananchi wetu ikiwemo Mheshimiwa Mattar kupitia mikutano yake mbalimbali katika jimbo lake…

MWENYEKITI: Ahsante.

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: …atumie fursa hiyo kuweza kuwawezesha wananchi kufahamu sheria za nchi hii ili waweze kuepuka madhara…

MWENYEKITI: Haya, ahsante sana Mheshimiwa Waziri. Mheshimiwa Selasini.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Waziri wa Mambo ya Ndani alitoa maelekezo mazuri sana kwa trafiki juu ya matumizi ya tochi za barabarani, kutopiga kamera gari kwa nyuma na kurusha picha kwa wenzao mbele ya safari. Lakini mtindo huu unaendelea na juzi siku ya Ijumaa Kuu walimkamata Diwani wangu wakampeleka polisi pale Himo…

MWENYEKITI: Swali, swali Mheshimiwa.

MHE. JOSEPH R. SELASINI: …na kum-harass sana. Sasa je, Waziri uko tayari kufafanua hayo maelekezo ili yaweze kutumika vizuri wananchi waache kusumbuliwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hii hoja ya maelekezo ya Mheshimiwa Waziri ambaye ndiyo mwenye dhamana ya mwisho katika Wizara yetu na vyombo ambavyo anavisimamia inapaswa itekelezwe na tulitolea ufafanuzi vizuri katika kongamano ambalo tulifanya juzi la usalama barabarani, watu walileta hoja mbalimbali kuhusiana na umuhimu wa kutokuitekeleza hoja ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tulikuwa tuna vigezo na hoja za msingi za kusimamia maamuzi ya Mheshimiwa Waziri. Kwa hiyo, nisisitize kwamba askari wote nchi nzima waendelee kutii na kufuata maelekezo ambayo tunayatoa kama Wizara. Na sisi tutaendelea kutoa ufafanuzi pale ambapo tutapata fursa.
MHE. MACHANO OTHMAN SAID: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake, lakini pamoja na majibu hayo, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Kwa kuwa Wizara mbili zinahusika sana na makusanyo ya Viza katika nchi za nje kupitia Balozi zetu. Je, Wizara ya Mambo ya Ndani inakuwa inafanya nini katika kuhakikisha fedha hizo na zinawekwa katika vitabu vya Wizara gani?

Pili, katika mwaka wa fedha 2018/2019 wa bajeti, Viza kwa upande wa Zanzibar zimekusanywa kiasi gani kwa sababu tuna watalii zaidi ya 500,000 kwa mwaka. Je, ni kiasi gani cha fedha ambacho kimekusanywa kwa kupitia Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kuhusu hoja ya kwamba kuna Wizara mbili zinashughulikia nataka nimthibitishie tu kwamba baada ya Mheshimiwa Rais kuzindua utaratibu wa kuwa na mfumo wa e-visa ambayo inahusisha, tunapuzungumzia immigration inahusisha e-visa e-passport n.k. na sasa hivi nitoe taarifa hii hapo Bungeni kwamba mfumo huu umeshafungwa katika Balozi zetu nchi za nje. Kwa hiyo, sasa ile changamoto ambayo ilikuwepo mwanzo, haipo. Sasa hivi fedha yote tena inaingia katika mfumo na hivyo basi hiyo hoja ambayo Mheshimiwa ameuliza imeshapatiwa ufumbuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na takwimu naomba nimhakikishie Mheshimiwa Machano kwamba nitampatia hizo takwimu baadaye.
MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, naomba nimuulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, ni ukweli usiopingika kwamba yapo matukio ambayo yalitikisa sana ya aina hii Tanzania. Matukio haya ni pamoja na kitendo cha jaribio la mauaji ya Mheshimiwa Tundu Lissu, kutekwa kwa Mohamed Dewji, kutekwa, kupigwa na hatimaye kuuawa kwa Mheshimiwa Ali Juma Suleiman pale Unguja, matukio ya Kilwa na matukio ya kutekwa vijana saba pale Mkoa wa Kaskazini Pemba, Jimbo la Mtambwe. Je, Serikali inatuambia kwamba pamoja na matukio haya makubwa na mazito na ya kutisha, ndiyo ni mtu mmoja tu hadi sasa ambaye amekamatwa na kuchukuliwa hatua?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, naomba kutaka kufahamu, je, Serikali ipo tayari sasa kuunda Tume ili kuchunguza matukio haya ili kuyabainisha na kuwabainisha wanaohusika na matukio haya ili kuchukuliwa hatua za kisheria?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Juma Kombo Hamad, Mbunge wa Wingwi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ametaja matukio mbalimbali ambayo yametokea kwa wakati tofauti. Nataka tu nimthibitishie kwamba matukio haya kila moja Jeshi la Polisi liliyachukulia kwa uzito unaostahili na yapo katika hatua mbalimbali za upelelezi, yako ambayo upelelezi wake umeshakamilika na yameshawasilishwa kwa DPP, mengine yamepiga hatua hata zaidi ya hapo. Kwa hiyo, kuyazungumzia kwa pamoja matukio ambayo ni tofauti na yana mazingira tofauti inakuwa ni changamoto. Hata hivyo, nimthibitishie kwamba, kwa sababu suala la upepelezi mchakato, ni imani yetu kwamba matukio haya yataweza kufikia katika hatua nzuri na hatimaye haki itaweza kupatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusiana na hoja yake ya kuundwa Tume, sijui sijaelewa anazungumzia Tume ya aina gani lakini nataka nimthibitishie tu kwamba Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi pale ambapo imekuwa ikipokea malalamiko mbalimbali ambayo yanapelekwa katika vyombo vyetu vya usalama ikiwemo Jeshi la Polisi, tumekuwa na utaratibu wa kuunda Tume. Kuna Tume mbalimbali tumekuwa tukiunda na zimekuwa zikifanya kazi vizuri, kwa hiyo, si jambo geni.
MHE. MACHANO OTHMAN SAID: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa matatizo makubwa ya Askari Polisi wakati wa uchaguzi ni uchache wao, je, Wizara iko tayari kushirikiana na vikosi vya SMZ kuongeza idadi ya Askari wakati wa uchaguzi huo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa imedhihirika kwamba kufanya uchaguzi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ule wa Zanzibar kwa siku moja unaleta matatizo zaidi. Je, Serikali iko tayari kutenganisha chaguzi hizi na kufanywa siku mbili tofauti?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Machano Othman Said, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anauliza kama tuko tayari na ndivyo ambavyo inatokea kwamba vyombo hivi vinafanya kazi kwa ushirikiano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la mabadiliko ya uchaguzi, nadhani hili suala linazungumzika na ni hoja ya msingi. Kwa hiyo, tunaichukua tuone kipi kinaweza kufanyika kwa kutilia maanani maoni yake.
MHE. SAADA MKUYA SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mheshimiwa Waziri ameelezea jinsi gani vikosi vyetu vitashiriki katika kuhakikisha kwamba amani inakuwepo wakati wa uchaguzi. Changamoto inayoonekana ni kwamba kunakuwa na uchache wa muda wa kutoa elimu ya uchaguzi (voters education). Je, ni kwa kiasi gani wamejitayarisha kushirikiana na Tume ya Uchaguzi kuona kwamba hiyo voters education inatolewa kipindi kirefu zaidi kabla ya uchaguzi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Saada Mkuya Salum, Mbunge Welezo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie kwamba wakati wowote tutakuwa tayari kushirikiana na Tume za Uchaguzi pale ambapo watapanga ratiba zao vizuri. Naamini kabisa Tume hizi zimekuwa zikijifunza kulingana na changamoto zilizopita. Kwa hiyo, kama kulikuwa na mapungufu ya muda watarekebisha utaratibu huo na sisi tutakuwa tayari kushirikiana nao pale ambapo watapanga ratiba hizo.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana kabisa na hoja ya Mheshimiwa Bagwanji kwamba wakati wa uchaguzi kunakuwa na fujo nyingi Zanzibar. Ni kweli vilevile kwamba wakati huo kunakuwa kama uwanja wa vita Zanzibar; vifaru, magari ya deraya na vitendo vya kiharamia vingi vinafanywa na vikosi vya SMZ. Je, ni lini Serikali ya Muungano itaacha kutaka interest za matokeo ya Zanzibar kwa kuingilia kwa njia mbalimbali na badala yake waaachie mfumo wa demokrasia ufanye kazi na mshindi apewe ushindi wake?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Ally Saleh, Mbunge Malindi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza si sahihi kwamba Serikali imekuwa ikiingilia chaguzi. Hata hivyo, kuhusiana na hoja yake ya ulinzi kuimarika nyakati za uchaguzi Zanzibar hii inatokana na vitendo vya kiharamia ambavyo vimekuwa vikifanywa mara nyingi na hasa na vyama na upinzani. Tumeshuhudia katika uchaguzi mbalimbali hususani Chama Kikuu cha Upinzani Zanzibar wamekuwa wanaongoza katika ukiukwaji wa taratibu za sheria za uchaguzi.

WABUNGE FULANI: Aaaaa.

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza hivyo kwa uthibitisho nikiwa nasimamia Jeshi la Polisi, nakijua nachokizungumza kwamba nathibisha kwamba Chama Kikuu cha Upinzani Zanzibar kimekuwa kikikiuka taratibu za uchaguzi na kufanya vitendo ambavyo ni kinyume na sheria. Kwa hiyo, Jeshi la Polisi ama vyombo vya dola vitakuwa imara zaidi kudhibiti uvunjifu wa sheria ambao unafanywa na vyama hivyo katika chaguzi mbalimbali.
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kupata fursa ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa gari alizozitaja Toyota Land Cruiser na Grand Tiger ni gari mbovu sana ambazo hazifai kufanya kazi katika kipindi hiki ambacho Polisi wana majukumu makubwa. Pia gari la Leyland ambalo amelitaja siyo la kazi ngumu kwa sababu kwanza halina hata four-wheel drive. Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kufanya jambo hili ni la dharura kwa askari wetu wa Jeshi la Polisi waishio Masasi ili waweze kupata gari haraka iwekekanavyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa hali ya nyumba za Askari Polisi waishio Masasi ni mbaya sana maana zimejengwa tangu enzi ya mkoloni. Je, Naibu Waziri yuko tayari kuongozana nami hadi Masasi baada ya Bunge hili ili akashuhudie hizo anazoziita nyumba 15 zilizopo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge wa Masasi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na hoja ya umuhimu wa kupeleka magari mengine katika Jimbo la Masasi ni muhimu na nilieleza hivyo kwenye jibu langu la msingi tunaamini kwamba kuna haja ya kupeleka magari Masasi. Kwa hiyo, tunakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba magari yaliyopo hayatoshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli magari yale mawili ni ya zamani ingawa yakitengenezwa yatasaidia. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kuwa tunatambua umuhimu wa Wilaya ya Masasi kuwa na magari ya ziada, kwa sasa hivi hatuna magari mapya lakini pale ambapo yatapatikana katika maeneo ambayo tutayaangalia kwa jicho la karibu moja ni Wilaya ya Masasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la pili nimthibitishie kwamba niko tayari kwenda pamoja naye katika Jimbo la Masasi kwa mara nyingine tena. Niliwahi kufika Masasi na nayafahamu mazingira ya Masasi lakini kwa kuwa Mheshimiwa Mbunge anahisi kuna haja ya kuambatana naye kwa mara nyingine tena basi tutafanya hivyo ili kwa pamoja mimi na yeye tuweze kuona jinsi gani tunaweza tukakabiliana na changamoto mbalimbali zinazohusu vyombo vyetu vya usalama vilivyopo pale hususan Jeshi la Polisi.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru umenipa nafasi ili niulize swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niishukuru sana Wizara ya Mambo ya Ndani kutupatia fedha kujenga nyumba sita za askari pale Babati Mjini, kwenye Mtaa wa Bagala Ziwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jengo la RPC katika Mkoa wetu wa Manyara liko Mtaa wa Komoto. Tangu mwaka 2006 liko kwenye lenta, miaka 13 sasa Wizara hamjatuletea fedha. Mmeweza kutuletea shilingi milioni 150 kazi inaendelea, ni lini sasa mtatuletea fedha kwa ajili ya kukamilisha jengo la RPC pale Babati Mjini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Pauline Gekul, Mbunge wa Babati Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni sahihi kabisa kwamba jengo hilo linahitaji kukamilika. Tunayo majengo kadhaa nchi nzima ambayo yanahitaji kukamilishwa, siyo tu kwa Jeshi la Polisi, kwa upande wa Jimbo lake la Babati, nadhani atakubaliana nami hata jengo la Uhamiaji nalo linahitaji kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, si dhamira ya Serikali kuona majengo haya yanafikia robo ama nusu kukamilika. Dhamira ya Serikali ni kuona majengo haya ambayo yametumia fedha nyingi na yana umuhimu mkubwa kwa ajili ya vyombo vyetu yakamilike haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ambayo inatukabili ni fedha kwamba bajeti haitoshi kukamilisha majengo yote kwa wakati mmoja. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge avute subira, pale ambapo hali ya kibajeti itakaa vizuri tutakamilisha majengo yote mawili ikiwemo la Polisi na Uhamiaji katika Jimbo lake pamoja na majengo mengine ambayo yanasubiri kukamilishwa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka huu tumetenga fedha kiasi ambazo zitaendelea kutatua changamoto hiyo. Kadri miaka inavyokwenda na hasa tukitilia maanani uchumi wa nchi yetu unakwenda vizuri sasa kutokana na kazi kubwa ya Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, naamini kabisa miaka ya mbele tutakuwa na fedha za kutosha kuweza kukamilisha majengo yote ambayo hayajakamilika.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Mtwara kimejengwa enzi ya Mkoloni na hivi sasa ukiingia mle ndani kinakaribia kubomoka, kinauliza kabisa niue nikuache, niue nikuache? Kila mwaka tunazungumza ndani ya Bunge na Serikali inasema imetenga bajeti. Kwa nini mpaka leo Serikali haileti fedha kwa ajili ya kukarabati kituo hiki ambacho hivi sasa kinatarajia kubomoka?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maftaha Nachuma, Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu yatakuwa ni yale yale tu kwamba vituo vinavyohitaji kukarabatiwa ni vingi ikiwemo hiki cha Mtwara Mjini. Hata hivyo, kwa sababu kituo hiki nakifahamu na gharama zake za ukarabati si kubwa sana pengine mimi na Mheshimiwa Mbunge wakati tukisubiri hali ya bajeti ikae vizuri tushauriane ikiwezekana hata kwenda pamoja jinsi ya kutafuta njia zingine mbalimbali za kusaidia kukiweka vizuri kituo hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanya hivyo katika maeneo mbalimbali nchini kwa kutumia rasilimali nyingine nje ya kibajeti. Nina hakika kwa gharama ndogo za ujenzi zinazohitajika katika kituo hicho tunaweza tukafanikiwa tukashirikiana. Naamini Mheshimiwa Maftaha ni mchakapazi kwa hiyo, hata nikimshawishi na yeye kupitia fedha za Mfuko wa Jimbo achomoe kidogo halafu tushirikiane kutafuta wadau basi tutaweza kukitendea haki kituo hiki.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Swali lwa kwanza, kama ambavyo Serikali inakiri umuhimu wa kituo hiki lakini ni muda mrefu sasa majibu yamekuwa ni haya haya kwamba bajeti itakaporuhusu, bajeti itakaporuhusu. Juzi tumepitisha bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani na ujenzi wa kituo hiki haupo kwenye bajeti hiyo. Sasa nataka kujua Mheshimiwa Naibu Waziri anavyotuambia tusubiri bajeti itakaporuhusu ni bajeti ipi anayoizungumzia?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wananchi wamekuwa wakijitahidi kujenga vituo vya polisi lakini vingi havifanyi kazi kwa saa 24 yaani havipewi hadhi ya kufanya kazi saa 24. Kwa mfano, Kituo cha Polisi cha Buza ambacho wananchi wamekijenga kwa kiwango cha hali ya juu lakini mpaka leo ni miaka mitano bado kinafanya kazi kwa saa 12 tu. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari sasa kutoa amri kituo hicho kianze kufanya kazi kwa saa 24?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mtolea, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nikijibu swali lake la kwanza kwamba bajeti ya mwaka huu haikuhusisha ujenzi wa Kituo cha Polisi Mbagala. Hata hivyo, si Kituo cha Polisi Mbagala tu, vituo vya polisi vingi havikuhusishwa sababu ni kama nilivyozungumza mwanzo kwamba hatuwezi tukategemea bajeti ya mwaka mmoja itatue changamoto ya vituo vyote au maeneo yote. Kwa hiyo, kazi hii itaenda kwa awamu na kituo hiki kama hakijaweza kupata fursa katika bajeti hii basi kinaweza kupata fursa katika bajeti zinazokuja. Cha muhimu atambue Serikali inathamini na inatambua juu ya umuhimu wa ujenzi wa kituo hiki hasa ukitilia maanani changamoto za usalama katika Mkoa wa Kipolisi Temeke na Wilaya ya Mbagala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la pili, kwanza niwapongeze yeye pamoja na wananchi wa Mkoa wa Kipolisi Temeke kwa ujumla wao kwa jitihada zao kubwa ambazo wanachukua katika kusaidiana na Serikali kupunguza changamoto ya vituo vya polisi. Nami ni shahidi kwani nimeshiriki katika programu mbalimbali ikiwemo programu ya uchangishaji fedha wa kituo cha Chamanzi, ambapo sasa kipo katika hatua nzuri ya ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo, nimhakikishie kwamba tutakapomaliza kujenga vituo hivi madhumuni yake ni vitumike kama ilivyokusudiwa. Hoja ya kutumika saa 24 inategemea na aina ya kituo. Kwa mujibu wa PGO kuna Class A, B na C. Kuna vituo ambavyo vinapaswa vitumike kulingana na category ya class ya kituo hicho kwa muda wa saa 24 na viko ambavyo havipaswi kutumika kwa muda wa saa 24.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo ambacho amekizungumza ni Class C, kwa hiyo, hakiwezi kutumika kwa saa 24. Si kwa sababu labda hatuna askari wa kupeleka ama tumekitelekeza au hatuoni umuhimu huo lakini ni kwa sababu ya aina ya kituo na utaratibu ambao tumejiwekea kwa mujibu wa PGO.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Jimbo la Mbagala limekuwa na ongezeko kubwa la watu hali ambayo inachangia sana kuwa na ongezeko kubwa la uhalifu lakini mazingira ya Kituo cha Polisi Mbagala Kizuiani ni mabaya sana pamoja na makazi ya polisi. Pamoja na hayo, Serikali imeeleza wazi kwamba utaratibu wa kujenga kituo hiki kwa sasa haupo. Je, Serikali ina mkakati gani basi wa kuwaboreshea angalau makazi ya askari wale jamani, hali mbaya, nyumba zile haziendani na eneo lile? Mbagala sasa imekua, mabasi ya mwendokasi yanakuja, zile nyumba za Polisi pale zinatisha. Je, Serikali mna mkakati gani wa kufanya angalau maboresho ya eneo lile?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mariam Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Dar es Salaam, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya uchakavu wa nyumba za askari katika eneo la Mbagala Kizuiani tunaifahamu. Nichukue fursa hii kumpongeza kwa mara nyingine tena Mheshimiwa Rais kwa kuliona hilo na kutupatia fedha ambazo tunatarajia kujenga takriban nyumba 400 nchi nzima. Katika maeneo ambayo nyumba hizo zitajengwa ni Kanda Maalum ya Dar es Salaam ikiwemo Mkoa wa Kipolisi wa Temeke. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge na nimpongeze kwa concern na huruma aliyokuwa nayo kwa askari wetu, Serikali inalitambua na tunaendelea kulitatua hatua kwa hatua.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza, askari wa usalama barabarani wamekuwa na matukio ya kujificha vichochoroni, wanajificha vichakani sasa magari yanakuwa yanakwenda kwa speed na wanasimamisha gari kwa ghafla na huku nyuma kuna msururu wa magari. Hili Morogoro imeshawahi kutokea na Tukuyu imeshawahi kutokea kutokana na Askari wa Usalama Barabarani.

Je, Serikali ina mikakati gani kuwapitia askari wote ambao wanakaa kwenye vituo vya Usalama Barabarani kuhakiki hii tabia ya kujifichaficha vichochoroni kwani hakuna mbinu mbadala ya kusimamisha magari mpaka mtu utoke vuup na kusimaisha gari?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa matrafiki wa barabarani uweledi wao wakufanya kazi baadhi yao ni changamoto hasa kwa barabarani. Je, Serikali ina mikakati gani kuwapeleke matrafiki wote kuwapa mafunzo ya mbinu mbadala na zile tochi kuzitumia kwa sababu zile tochi wananchi wamekuwa wakizilalamikia sana, wanaweza kusema unapigwa tochi wanasema inakwenda speed, lakini ile speed haifanani na ile tochi? Naomba majibu ya Serikali.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili kwa pamoja ya Mheshimiwa Maryam Msabaha kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu swali langu la msingi kwamba tumefanikiwa kupunguza ajali kwa asilimia 43 na hususan ambazo zinasababishwa na magari ya abiria, mafanikio hayo pamoja na mambo mengine yalisababishwa kutokana na mbinu na uweledi wa askari wetu katika kubaini mbinu na njama ambazo zinatumika na madereva wasiokuwa waaminifu kuweza kukiuka sharia. Kwa hiyo hili suala ambalo amelizungumza kwa askari kukaa barabarani kuweza kujificha na mengine yote, malengo yalikuwa ni ya nia njema, lakini kama kutakuwa na upungufu katika utekelezaji wa hayo kwa baadhi ya askari basi tunachukua kama ni changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo nimwombe Mheshimiwa Mbunge afahamu kwamba dhamira ya Jeshi letu la Polisi kupitia Vikosi vya Usalama Barabarani si kuburuza wananchi, lakini kusaidia wananchi kuokoa maisha yao hususan kwa wale madereva ambao hawafuati sheria.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Kumekuwa na tatizo kubwa wananchi kubambikizwa kesi hasa kwenye hizi kamera, mtu unapigwa kamera ukienda kuhoji wanasema kwamba imekosewa namba ya gari kwa hiyo wananchi wengi wamekuwa wanabambikiziwa makosa ambayo si ya kwao. Je, Serikali inasemaje kuhusiana na kamera ambazo zimekuwa zinawabambikia wananchi makosa ambayo siyo ya kwao.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ritta Kabati kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi haya ya teknolojia tumeanzia na kamera, tuna mfumo VTS na tuna mambo mengine mengi ambayo tunaelekea nayo huko, yote haya yana dhamira ya kupunguza hizo dhana dhidi ya askari wetu kuhusiana na kubambikia watu makosa.

Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba matumizi ya tochi yamekuwa yakitusaidia sana. Hata hivyo, ikiwa kuna changamoto upungufu wa kimaadili wa baadhi ya askari wetu na hilo hatuwezi kulikataa kwa sababu askari nao ni binadamu huwezi kuwa na askari wote hawa wakose wawili watatu ambao watakuwa na upungufu wa kimaadili, tumekuwa tukiendelea kuchukua hatua pale ambapo tunapata taarifa na uthibitisho juu ya kubambikia wananchi makosa ambao hawahusiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumsisitiza Mheshimiwa Mbunge kwamba tusaidiane kwa pamoja kufichua wale askari wachache ambao watakuwa wanatuhumiwa ama wanajihusisha na tabia kama hizo zilizokuwa kinyume na maadili ya utendaji kazi wa Jeshi la Polisi.
MHE. JOHH J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Katika kujibu swali la msingi, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema Serikali iliandaa mkakati maalum wa kudhibiti ajali barabarani na kwamba umetekelezwa kwa kiwango cha ajali kupungua kwa asilimia 43. Sasa Je, Serikali ipo tayari kuleta huo mkakati iliouandaa Bungeni pamoja na taarifa ya utekelezaji Bungeni ili tuweze kupima kama Wabunge ni ukweli ajali zimepungua kwa asilimia 43?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa John Mnyika Mbunge wa Ubungo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeeleze kwanza kwa ufupi kabisa kuhusiana na mkakati huu. Mkakati huu upo kwa awamu, tulianza mkakati wa miezi sita ambao ulikuwa na lengo la kupunguza ajali kwa asilimia kumi, tukafanikiwa kupunguza ajali kwa asilimia kumi na moja. Tukaja mkakati wa awamu ya pili ambao ulikuwa miezi sita, tuka-target asilimia kumi, tukapunguza ajali kwa asilimia 45 nadhani. Tukaona kwamba tuna haja ya kuongeza sasa malengo tukaweka mkakati wa asilimia 25 kupunguza ajali wa miezi sita vilevile, ambao tulifanikiwa kupunguza ajali kwa asilimia 25. Hivi tunazungumza tupo katika mkakati wa awamu ya nne ambao tumelenga kupunguza ajali kwa asilimia 25. Kwa hiyo asilimia 43 tuliyozungumza ni kwa jumla wake kwa maana ya mwaka mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niliona nimpe kwanza utangulizi huo aelewe kwamba si mkakati mmoja, ni mkakati ambao tumekuwa tukijipima awamu kwa awamu kupitia Baraza la Usalama Barabarani na mkakati huu upo wazi na Mheshimiwa Mbunge atakapohitaji wakati wowote sisi tutakuwa tayari kumpatia. Tumekuwa tukifanya hivyo kwa sababu malengo ya mikakati hii tunapomaliza tunakuwa tunashirikisha wadau mbalimbali ikiwemo Wabunge, hata yeye mwenyewe Mheshimiwa tulimwalika juzi katika Kongamano letu la Usalama Barabarani ambapo tulizungumzia mkakati huu Dar es Salaam na Wabunge wengine wa Mkoa wa Dar es Salaam wote, lakini bahati mbaya hatukumwona Mheshimiwa Mnyika japokuwa barua niliisaini mimi mwenyewe kwa mkono wangu ili kuonyesha kwamba hili jambo ni jambo shirikishi na tunatambua umuhimu wa kuwashirikisha na tutaendelea kuwashirikisha Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo nimeridhika nayo na napenda nitoe pongezi kwa Mkuu wa Gereza la Segerea kwa kutekeleza hayo yote ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri ameyasema kupeleka watoto kwenye Nursery na kuwarudisha gerezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa matatizo yanayowapata watoto magerezani yanatokana na makosa ya mama zao; na kwa kuwa zipo adhabu nyingi wanazoweza kupewa mahabusu au wafungwa wenye makosa yasiyo ya kijinai; kwa nini Serikali isitoe adhabu ya kifungo cha nje kwa akina mama wenye watoto wadogo ili waweze kuwalea watoto wao vizuri uraiani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa tatizo kubwa la akina mama waliopo katika gereza la Segerea na magereza mengine yote ni kutokana na kesi zao kutokupelekwa mahakamani kwa wakati, jambo ambalo linawafanya akina mama wale wakae muda mrefu mahabusu bila ya kutambua hatima yao: Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa wanapeleka kesi mahakamani kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI (K.n.y WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO): Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya, naomba kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mariam Kisangi kwa kujali akina mama na watoto hawa. Nachukua fursa hii kumhakikishia Mheshimiwa Mariam Kisangi kwamba huu uchungu ambao aliokuwa nao yeye ni sawa sawa na uchungu ambao Serikali tunao. Ndiyo maana katika kushughulika na kesi hizi za hao akina mama wenye watoto, huwa Serikali inatoa kipaumbele maalum, hata mahakama hufanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo basi, nimhakikishie kwamba hata inapokuja katika ule utaratibu ambao tunautumia kwa ajili ya kutoa kifungo cha nje na mipango mingine mbalimbali ya kupunguza mahabusu na kusamehe wafungwa, akina mama wenye watoto huwa wanapewa kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili; vilevile katika suala la kuhakikisha kwamba tunaharakisha upelelezi na kesi hizi zinamalizika, tuna utaratibu wa kuharakisha kesi ziweze kwenda kwa haraka. Tunaweza kutumia njia mbalimbali kufanya hivyo, tunafanya ziara kwenye magereza kwa kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria, lakini tunapobaini kwamba kuna kesi ambazo hazihitaji kukaa muda mrefu bila kuchunguzwa, hasa hizi zinazohusu akina mama na watoto tunakuwa tunazipa kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimalizie kwa kumhakikishia Mheshimiwa Mariam Kisangi kwamba Serikali inaliangalia sana kwa karibu suala hili na haipendelei kuona watoto wadogo wakikaa magerezani kwa muda mrefu.
MHE. MOHAMMED JUMA KHATIB: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu hayo nina maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai pamoja na Kanuni za Utendaji wa Jeshi Polisi bado jambo hili linaendelea na ni sugu sana.

Je, Serikali haioni kwamba iko haja ya kubadili mfumo wa utendaji kazi wa Polisi likaingizwa suala la haki za binadamu ili kuwa-conscientious Polisi katika utendaji wao wa kazi wakazizingatia hizo haki za binadamu?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili, kwa kuwa Katiba yetu inakataza uteswaji na pia kwa kuwa kuna Mkataba wa Kimataifa wa Convention Against Torture, je, Serikali haioni kwamba iko haja ya kuridhia Mkataba huu ili hawa watu wanaoteswa wakapata fursa ya kwenda kushtaki katika Mahakama za Kimataifa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mohamed Khatib, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na pendekezo lake la kuubadili mfumo, tunadhani tatizo siyo mfumo, mfumo wa Jeshi letu la Polisi uko vizuri kwani Askari Polisi kabla hajaajiriwa tuna utaratibu mzuri wa kutoa mafunzo. Moja katika mambo ambayo tunayazingatia kuwaelimisha kuhusiana na sheria na kanuni pamoja na kutenda kazi zao kwa uadilifu kwa kufuata sheria na kanuni hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini inapotokea changamoto ambazo zinahusu ukiukwaji wa sheria, ni matatizo ya baadhi ya Askari mmoja mmoja. Kama nilivyojibu katika swali lake la msingi kwamba tunapogundua kwamba kuna Askari ambaye anafanya vitendo hivyo vya kunyanyasa raia huwa tunachukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwashtaki na kuwafukuza kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi kwa maelezo hayo naona nimejibu maswali yake yote mawili kwa pamoja.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kumekuwa na malalamiko kutoka kwa watuhumiwa wanaoteswa wakiwa mikononi mwa Polisi kwa lengo la kulazimishwa kusema ukweli, hasa ule ambao Polisi wanautaka wakati mtuhumiwa ana haki ya kutoa hoja yake au kuzungumza ukweli akiwa na Wakili au Mahakamani.

Je, Serikali haioni ni muda muafaka wa kufuatilia mateso haya ambayo watuhumiwa wanapewa na Askari ili kuondoa malalamiko haya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aida Khenani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Ushahidi ya mwaka 1967, kifungu cha 31, inaeleza kuhusu namna ambavyo Polisi wanaweza kutumia nguvu kiasi katika kumhoji mtuhumiwa ili waweze kupata ushahidi. Pia sheria hiyohiyo inaeleza kwamba ushahidi ambao utapatikana si lazima Mahakama uuzingatie, Mahakama itazingatia ukweli wa jambo husika. Tafsiri yake ni nini? Tafsiri yake ni kwamba inapelekea kuwa-discourage Polisi kutumia nguvu katika kupata ushahidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimezungumza katika jibu la msingi la swali kwamba tunapogundua kwamba kuna raia ambaye amefanyiwa vitendo ambavyo si kwa kibinadamu na Polisi basi sisi huwa tunachukua hatua. Tunaomba tutoe wito na rai kwa wananchi wote pale itakapotokea wananchi kupata madhara kama hayo basi wachukue hatua stahiki za kutoa taarifa ili tuweze kuchukua hatua. Hatuwezi kuliruhusu au kukubali wananchi wetu wanyanyaswe na baadhi ya skari wetu ambao pengine hawafuati maadili ya kazi zao.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo taarifa kuwa vituo vikubwa vinapima ulevi lakini kuna baadhi ya madereva wa magari makubwa wenye kuendesha masafa marefu wanavyopata muda wa kupumzika vituo vya njiani wanakesha wakinywa pombe na kusababisha ajali.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwadhibiti madereva hawa ili kupunguza ajali za barabarani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Dodoma, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ambazo tunachukua katika kudhibiti madereva walevi, likiwemo kusimamisha magari hasa haya ambayo amezungumza yanayobeba abiria na mizigo na kuwapima vilevi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukifanya kazi hiyo maeneo mbalimbali nchini na kwa kiwango kikubwa tumefanikiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa aina ya madereva ambao wanaendesha magari hali wakiwa wamelewa. Pale ambapo tunawabaini basi hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi yao.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, la kwanza, kwa kuwa madeni haya ni ya muda mrefu na imetokea mara nyingi Serikali imekuwa ikilipa madeni yaliyokuja baadaye wanaacha yale ya nyuma. Sijui ni vigezo gani vinatumika kuacha madeni yale ya muda mrefu na kulipa yale ambayo yamekuja baadaye?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; wazabuni wengi wanaodai magereza kwa maana wale wanaofanya zabuni ya chakula wengi sasa wana hatari ya kuuziwa nyumba zao hasa wale ambao wamekopa katika taasisi mbalimbali za fedha. Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha hawa wazabuni mbalimbali inawakomboa wasiweze kuuziwa nyumba zao na taasisi za kifedha?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, madeni ambayo yanalipwa ni miongoni mwa madeni ambayo tumeshalipa kama ambavyo nimeeleza katika jibu la msingi pia yako madeni ya zamani na nilieleza kwamba madeni mengine ambayo hayajalipwa ni kutokana na kwamba mengine yameshahakikiwa na hivyo basi pale fedha ambapo zitapatikana yatalipwa. Naamini kabisa yatakapokuwa yamekamilika madeni hayo kulipwa kama ambavyo nia ya Serikali ilivyo basi yale matatizo ambayo yanakabiliwa na hawa wazabuni yataweza kupatiwa ufumbuzi. Ni dhamira ya Serikali kuhakikisha madeni haya yanalipwa ili kuepusha usumbufu wowote kwa wazabuni wetu.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, ni dhahiri kwamba Serikali imekuwa haitoi kipaumbele kwenye huduma muhimu za binadamu badala yake wamekuwa wakiwekeza zaidi kwenye vitu.

Mheshimiwa Spika, magereza ni moja ya sehemu ambazo inatakiwa wapewe vipaumbele na wapewe huduma stahiki kama inavyoelekeza. Wazabuni wengi wanadai na wameacha kutoa huduma za vyakula na mambo mengine.

Mheshimiwa Spika, cha kusikitisha zaidi nilitaka nijue, Serikali ni lini itatoa nguo kwa wafungwa ambao mnasema kabisa wakishafungwa wavae yale mavazi. Niliona hiyo nikiwa Segerea, lakini juzi nilivyotembelea Gereza la Tarime pamoja na matatizo mengi ambayo yametokana na kutokulipa madeni ya wazabuni na kuweza kutoa vifaa hivi unakuta mpaka Askari Magereza anachukua nguo zake anavisha mfungwa kama anavyotoka nje.

Ni lini sasa Serikali itaondoa hii fedheha ihakikishe kwamba wafungwa ambao wanastahili kuvaa nguo waweze kupewa zile nguo ambazo wataweza kujihifadhi? Na wajue kabisa kwamba waliopo Serikalini leo magereza ni yao kesho. (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimsahihishe siyo sahihi kwamba Serikali haitoi kipaumbele kwenye huduma mbalimbali ikiwemo za wafungwa. Nimhakikishie kwamba wafungwa hawa tumekuwa tukiwapatia uniform na siyo wote kama ambavyo umetaka ieleweke kwamba hawana uniform, lakini changamoto hii itaendelea kupungua hatua kwa hatua. Hata hivyo, sehemu kubwa ya wafungwa tayari wameshaanza kupatiwa nguo kwenye magereza.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante.

Mheshimiwa Spika, naomba niwakumbushe kuwa tarehe 24 Januari, 2020 Serikali imesaini makubaliano ya kuchukua asilimia 16 kutoka Barrick Gold Tanzania, kwa hiyo sasa hivi Serikali ina 16%, maana yake watu wengi hawajaisikia hiyo, kwa hiyo inabidi tuongeze sauti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Gereza la Ulanga mwaka wa tano sasa hivi mahabusu wanapelekwa mahakamani kwa kutumia bodaboda. Hii ni hatari sana kwa mahabusu kutoroka. Naomba kuuliza swali la nyongeza, je, ni lini Serikali itapeleka gari la mahabusu Gereza la Ulanga? (Makofi/ Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mlinga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mlinga kwa jinsi ambavyo anaweza kujenga hoja zake kwa msisitizo, sisemi kwamba anatia chumvi, lakini anajenga hoja kwa msisitizo na anatukumbusha mambo muhimu kama ambavyo ametukumbusha hili suala la mafanikio kwenye sekta ya madini.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mlinga kwamba najua anapozungumza bodaboda alitaka tu kuongeza uzito wa hoja yake, lakini tunatambua juu ya changamoto ya usafiri katika baadhi ya magereza yetu nchini na nimhakikishie pale ambapo gari mpya zitakapopatikana, tutampelekea katika gereza hilo la Jimboni kwa Mheshimiwa Mlinga ili kukabiliana na changamoto hiyo ya usafiri.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, swali hili naliuliza kwa mara ya pili, niliuliza kwa mara kwanza kwama 2016 na Serikali kweli ni sikivu ilifanya ukarabati mdogo mwaka 2016/2017. Hata hivyo, ukarabati huo haukumaliza tatizo kwa sababu bado maji taka yanachirizika kutoka gerezani kwenda kwenye makazi ya watu na ni hatari zaidi kwa kipindi hiki cha mvua ambayo maeneo hayo mengi yamefurika na maji ya mvua. Kwa hiyo kuna hatari kubwa ya kutokeza magonjwa ya mlipuko.

Je, Serikali ipo tayari sasa kama hatuwezi kujenga mashimo ya kutosha basi tuzibe zile njia zisitiririshe maji kwenda kwenye makazi ya wananchi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, gereza hili ni gereza VIP ni gereza ambalo limejengwa kwa upekee sana ukifananisha na magereza mengine, ndio maana huhifadhiwa watu maarufu au wenye kesi kubwa kubwa, je, Serikali haioni kuna haja sasa ya kulitazama gereza hili kwa jicho lingine ili watenge fedha za kutosha kwa ajili ya kufanya ukarabati wa gereza lote kwa pamoja?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mtolea, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze wakati ule alivyoleta hoja yake ya changamoto ya gereza hili na yeye ameona uungwana wa kuipongeza Serikali kwa kutilia maanani yale aliyoeleza hapa Bungeni na tukayafanyia kazi. Nimhakikishie kwamba kama ambavyo tumefanya kipindi kile na haya ambayo ameyazungumza sasa hivi na yenyewe tatayachukua ili tuweze kuyafanyia kazi.
MHE. ALFREDINA A. KAHIGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi kwa mara nyingine tena. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri kama yanatekelezwa lakini nina maswali yangu mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikibainika mwanamke aliyefungwa gerezani akachukua mimba, je, ni hatua gani za kisheria atakazochukuliwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; iwapo mwanamke huyo aliyefungwa amehukumiwa kufungwa miaka 10 na zaidi, je, yule mtoto ambaye amejifungulia humo gerezani atakaa nae mpaka kifungo chake kiishe? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ameuliza ikibainika atachukua mimba lakini moja kwa moja nilivyomuelewa ni kwamba anakusudia atachukulia mimba nje ya gereza kwa sababu hakuna uwezekano wa kuchukua mimba akiwa gerezani. Na kama akiwa amechukua mimba akiwa nje ya gereza utaratibu ndio kama ambavyo nimeuzungumza katika jibu langu la msingi kwamba atajifungua, atakapokuwa amejifungua atapewa utaratibu maalum kwa mujibu wa sheria ambayo nimeinukuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala ni kwamba je, akishakujifungua ambalo ni swali lake la pili. Akishajifungua na amefungwa muda mrefu, nini hatma ya yule mtoto? Jibu ni kwamba mtoto yule atakapofikia umri wa kumaliza kunyonya, maafisa Ustawi wa Jamii wanakwenda katika magereza kwa ajili ya kuzungumza na yule mama ili mtoto yule aweze kupata fursa ya kupata malezi nje ya gereza aidha kwa jamaa zake ama kwa watu au taasisi zozote ambazo zimekuwa zikihudumia watoto ikiwa hana jamaa. Huo ndio utaratibu wa kawaida ambao tupo nao kwa sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi ambacho wapo magerezani watoto wale wanahudumiwa vizuri kwa kadri ambavyo sheria inazungumza ikiwemo hata kuweza kuwapatia huduma ya elimu za awali katika shule zilizopo karibu na magereza.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa hali ya maumbile ya mwanadamu, hasa mwanamke yanapelekea kujifungua au kupata watoto: Je, Serikali inachukua hatua gani kudhibiti utungwaji mimba ndani ya Magereza ili kupunguza shida ambazo watoto hao watapata katika kulelewa katika mazingira ambayo siyo rafiki kama Magereza; kwa kuwa bado inasemekana kwamba kuna mchanganyiko wa wanawake na wanaume na wanapata access ya kukutana? Sasa Mheshimiwa Waziri atuambie atadhibiti vipi utungwaji mimba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilieleza wakati najibu swali la msingi kuhusiana na uwezekano wa mwanamke kupata mimba ndani ya Magereza. Nimezungumza hivyo kwa sababu zifuatazo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba Magereza yametenganishwa, hakuna mchanganyiko kati ya Magereza upande wa wanawake na wanaume; hata Askari ambao wanahudumia wafungwa na mahabusu wa kike basi wanakuwa ni Askari wa kike. Kwa hiyo, mara nyingi tunapozungumzia upataji mimba wa Magereza inakuwa ni kwa wafungwa ama mahabusu ambao wameingia tayari Magerezani ikiwa mimba zimeshaanza kutungwa.
MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Moja, kwa kuwa wananchi wengi sana wa Tanzania ambao wamekuwa wakipelekwa mahabusu, whether wana kesi za kujibu ama hawana, ama ni kesi zinazopata udhamini, wamekuwa wakiingia mahabusu bure, lakini kutoka ni hela; napenda kuuliza: Je, Serikali imewahi kufanya utafiti kwamba suala hili linatokea na ni hatua gani wanachukua? Kwa sababu siyo suala la kisheria kwamba mtu akiingia mahabusu kutoka lazima atoe hela ndiyo atolewe. Ni suala la practice, sisi tuliopo mitaani tunajua kwamba mtu anapelekwa mahabusu lakini siku ya kutoka wengi wao wanakuwa wanachajiwa. Je, Serikali inachukua hatua gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa kuwa kumekuwa kuna wimbi kubwa la kesi, hususan za uhujumu uchumi na utakatishaji fedha kwa vijana hasa vijana hawa kama akina Tito, Kabendera na wengine wengi ambao hatuwajui, wamekuwa wakikaa mahabusu kwa muda mrefu na kesi zao zikiendelea huko; inawezekana siku ya siku wakaja kukutwa na hatia ama wasikutwe na hatia; lakini kwa kuwa tulipitisha sheria hapa Bungeni ya pre-bargaining ambayo inamtaka mshtakiwa ama wakili wake ama mwendesha mashtaka kuomba mahakamani waweze kupata ili kupunguza ukubwa wa adhabu, kupunguza muda wa adhabu lakini kuondoa baadhi ya kesi; pia Mheshimiwa Rais kupitia maombi maalum ya barua alikuwa akiwahi kutoa msamaha; sasa Bunge halioni ni wakati muafaka sasa tuje tufanye mabadiliko ya Sheria ya Uhujumu Uchumi ili kuweka flexibility kwa Majaji na Mahakimu ambao wamekuwa wakiendesha kesi hizi na wenyewe waweze kuangalia ukubwa wa kosa na kuweza kutoa dhamana? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa sababu Bunge tumetunga sheria, tumewafunga mikono kwamba hawawezi kutoa dhamana kwa makosa ya uhujumu uchumi. Hata hivyo, mtu anaweza akahujumu uchumi ama kufanya utakatishaji fedha kwa 20,000/=, mwingine shilingi bilioni moja, wote wananyimwa dhamana kitu ambacho kinasababisha mlundikano wa kesi.

Je, Bunge sasa halioni ni wakati muafaka wa kuleta mabadiliko ya sheria hii ili vijana ambao hawana hatia na wanateseka huko Magerezani waweze kupunguza idadi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anazungumzia kwamba kuna kauli ambayo inatapakaa katika jamii kwamba unaingia mahabusu bure na unatoka kwa pesa. Siwezi nikapingana na kauli hii kwa sababu mbali ya kazi kubwa na nzuri ambayo Askari wetu wamekuwa wakiifanya ya kusimamia usalama wa nchi hii na ndiyo maana nchi yetu iko salama, lakini tunakiri kwamba wako baadhi ya Askari ambao wamekuwa wakikiuka maadili na ndio hao ambao pengine wanatuhumiwa na mambo kama ambayo amezungumza Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba pale ambapo tunabaini Askari yeyote anayekiuka maadili yake kwa kufanya utaratibu kama ambao ameueleza wa kuwatoza mahabusu fedha ama kuwabambikia ama kuwaonea, tumekuwa tukichukua hatua. Wapo Askari kadhaa ambao wamechukuliwa hatua mbalimbali kila mwaka ingawa ni wachache mno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la mabadiliko ya sheria, nadhani ni mamlaka ya Bunge hili kutunga sheria na kubadilisha pale ambapo inaona inafaa. Naye ni Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kanuni anazifahamu. Kama kuna utaratibu ambao Mheshimiwa Mbunge anadhani kuna haja ya kuleta hoja binafsi ama utaratibu mwingine ambao ataona unafaa, basi ni juu ya Mbunge yeyote kutumia haki yake ya Kikatiba na kikanuni.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; hivi sasa Manispaa ya Mtwara Mikindani kumekuwa na baadhi ya Viongozi wa vyama vya siasa wa wilaya na mkoa ambao wameweza kuratibu vikundi mbalimbali kwa ajili ya kufanya uhalifu kwenye uchaguzi unaotarajia kufanyika mwaka huu 2020. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, je Serikali Mheshimiwa Waziri yuko tayari hivi sasa kuja Mtwara kuweza kuchukua ushahidi ambao nitampatia kwa mikono yangu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili Manispaa ya Mtwara Mikindani kuna baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wanachukua na kuwatumia baadhi ya askari polisi kwenda kuwafanyia hujuma Wapinzani usiku saa nane, saa tisa na kuwagongea majumbani kwao na kuwakamata bila sababu yoyote ya msingi na kwenda kuwaweka ndani eti kwa sababu tu wanafanya kazi ya kunadi Chama cha Wananchi - CUF na vyama vingine vya Upinzani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali iko tayari hivi sasa kuwachukulia hatua Askari wa aina hiyo wanaotumika kwa ajil ya Chama Tawala? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maftaha Nachuma kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza ameuliza kama nipo tayari kwenda kuchukua ushahidil; nimuhakikishie kwamba niko tayari kufanya hivyo kama ushahidi huo ni kweli anao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ametoa tuhuma nzito kwa Jeshi letu la Polisi kwamba linashirikiana na vyama sijui chama gani. Mimi nimuhakikishie Mheshimiwa Maftaha na Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla kwamba tunavyotambua na ilivyo kabisa, si tunavyotambua, na uhalisia ulivyo, Jeshi letu la Polisi kwa kiwango kikubwa wanajitahidi kufanya kazi zake kwa kufuata weledi, sheria na maadili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwa kuwa yeye Mheshimiwa Maftaha ambaye mimi ninamheshimu sana kama ni miongoni mwa viongozi wasio wengi sana makini wa upinzani anaweza kusema ana ushahidi wa jambo kama hilo wa tuhuma hizo nzito; imani yangu ni kwamba nitakapokuwa nimeambatana naye kama alivyoomba katika swali lake la msingi basi atatupatia ushahidi huo ili tuweze kuchukua hatua. (Makofi)
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amesema Serikali imeteua maafisa watano; na tunajua kwa miaka mitano ya uongozi wa awamu hii maafisa wengi wamerejeshwa Tanzania na hivyo Balozi nyingi hazina maafisa kwa sababu ya hofu labda ambazo wanazijua ndani ya chama chenu. Sasa maafisa watano tu katika Balozi nyingi ambazo ziko kwenye nchi mbalimbali hamuoni kwamba mnawapatia Watanzania wanaoishi nje ya nchi matatizo ya kupata huduma ambayo ni ya kimsingi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; tarehe 31 mwezi wa kwanza mwaka huu Serikali ilisitisha matumizi ya passport za zamani; na tunajua Watanzania wanaoishi nje ya nchi wanahitaji passport ambayo ndiyo inawapa uwezo wa kuishi huko wanakoishi na kufanya shughuli zao. Ni lini Serikali itahakikisha Watanzania wanaoishi huko wanapata huduma hii kwa haraka ili wasionekane kama wamekuwa-condemned kurudishwa huku kwa sababu hawana passport?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Heche kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimuhakikishie kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi haina hofu, ni suala la utaratibu tu. Kwamba kama ambavyo nimeeleza kwenye jibu la msingi, kwamba kwa kutambua upungufu huo wa Maafisa Uhamiaji ndiyo maana maafisa watano wako mbioni kupelekwa wakati wowote. Hata hivyo nataka nimhakikishie kwamba kutokuwa na Maafisa wa Uhamiaji katika kila Balozi hakumaanishi kwamba wananchi au wageni wanaotaka kupewa huduma hizo wanashindwa kupata; kwa sababu kwanza hivi sasa hivi tuna Mfumo wa Uhamiaji Mtandao ambao nitauelezea kwa kifupi ili pamoja na mambo mengine utakuwa umeweza ku-cover lile swali lake la pili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfumo wa Uhamiaji Mtandao ambao unahusisha uhamiaji kwa maana ya e-passport, e-visa, e-permit pamoja na e-gate umerahisisha sana kutoa huduma kwa wananchi kwani sasa haihitaji mwananchi kwenda moja kwa moja kwenye Ofisi zetu na badala yake anaweza kwenda kwenye mtandao tu na kujaza fomu zake na kuweza kupata huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo maafisa ambao wapo katika Balozi zetu wameshapata training juu ya matumizi haya ya uhamiaji mtandao, na pale ambapo wananchi ama wageni wanapohitaji huduma hizo kwa maeneo ambayo hakuna Maafisa Uhamiaji basi Maafisa wa Mambo ya Nje waliopo katika Balozi zetu huwa wanatoa msaada kwa wale ambao wanahitaji huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia maelezo hayo kwa ufupi ni dhahiri kwamba uchache huo wa maafisa ambao ameuzungumzia Mheshimiwa Heche hauna madhara yoyote mpaka sasa hivi kwa huduma mbalimbali za raia na wageni ambao wanataka kuzipata katika Balozi zetu duniani.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, katika tafiti nilizozifanya kuna makundi manne, kuna kundi la hawa watoto wanaofanya kazi majumbani, akina mama ambao wanajiuza na wanafunzi. Swali linakuja hivi, kuna akina baba ambao wana akili zao timamu na wengine ni watu wa Serikali wamekuwa wakiyalaghai makundi haya niliyoyataja na kuwapa ujauzito na wakati wanawafuata labda wanataka huduma za kijamii wanawatosa na wengine kuwatishia na bunduki. Naomba kujua ni nini kauli ya Serikali kwa wale wanaobainika kuhusika na matukio haya? Watu hawa wanapopelekwa kwenye Vituo vya Polisi au Serikali za Mitaa wachukuliwe hatua za kinidhamu na sheria kali ili iwe fundisho kwa wengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa majiji makubwa Mwanza, Arusha, Dodoma, Dar es Salaam na Mbeya, yamekuwa na ongezeko la wanawake ambao wanafanya biashara za kujiuza (biashara za ngono). Je, Serikali ina mikakati gani hasa katika Jiji la Dodoma ambalo ni Makao Makuu ya Serikali kudhibiti hali hii ili kupunguza ongezeko la kutupa watoto majalalani? Naomba kauli ya Serikali. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maryam Salum Msabaha, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, hakuna kitu chochote ambacho kinaweza kuhalalisha juu ya hatua yoyote ambayo atachukua mama kumtupa mtoto wake. Pili, wale ambao wanahusika kuwapa ujauzito mabinti hawa wadogo ambapo wengine ni wanafunzi na wale ambao amewataja, imeelezwa wazi katika sheria kama ambavyo nimejibu katika swali langu la msingi kwamba kuna Sheria ya Mtoto lakini pia Kanuni ya Adhabu ambazo zinaelezea wajibu wa mtu ambaye ameamua kuzaa mtoto kwa hiari yake ama amejitolea kuwa mlezi wa mtoto yule na jinsi ambavyo sheria inazungumza kwa wale ambao watashindwa kutekeleza wajibu huo. Kwa hiyo, sheria iko wazi na adhabu inaeleza kwamba kwa mtu ambaye atashindwa kuhudumia mtoto wake kutimiza wajibu huo anaweza kufungwa kifungo kisichopungua miaka mitano. Kwa hiyo, sheria iko wazi katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na hoja yake ya pili kuhusu madada wanaojiuza, sina hakika kama utafiti wake aliouzungumza una usahihi kiasi gani kuhusu mahusiano ya akina mama ambao wanatupa watoto na wale madada wanaojiuza. Hata hivyo, niseme tu kwamba Jeshi la Polisi limekuwa likifanya jitihada mbalimbali kukabiliana na aina ya watu ambao wanafanya biashara haramu ikiwemo biashara za ngono.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe wito kwa wananchi wote kwa ujumla ikiwemo na akina baba kujiepusha kuwa wateja wa biashara hizo. Kwa hiyo, hapa ni shilingi inaangaliwa pande zote mbili, kwa hawa akina dada ambao wanafanya biashara hizi lakini mpaka wanunuzi wa biashara hizi. Kwa hiyo, wote wawili wanafanya makosa na pale ambapo watabainika basi sheria itachukua mkondo wake.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza naomba nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake kwa niaba ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza ambalo nilikuwa naomba kujua, kwa sababu kituo hiki cha kanda ambacho kiko 41KJ kinahudumia wananchi wanaotoka maeneo ya Kilimani Hewa, Nampemba, Mtepeche, Mkotokuyana pamoja na Mandai; pamoja na mkakati ambao Serikali imeusema, hebu aniambie ni mkakati gani ambao Wizara wanaweza wakaufanya kwa haraka ili kuhakikisha wataalam wanapatikana katika kituo hiki ili wananchi waendelee kupata huduma pamoja ukarabati ambao tayari umeshafanyika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili ambalo nilikuwa naomba kujua, ni suala hili la ukarabati wa kituo cha karakana ambacho kiko pale kikosi cha mizinga. Vijana wengi wa Nachingwea sasa hivi wanakosa sehemu ambako wanaweza kwenda kuendelea na masomo yao. Karakana hii kwa sasa inachukua idadi ndogo sana ya wanafunzi au wanachuo. Nini mkakati wa Wizara ili kuhakikisha jitihada hizi za kuihamisha hii karakara kuipeleka VETA unafanyika au kutoa fedha kwa ajili ya kununua vifaa na kuongeza wataalam ambao watakwenda kutoa huduma kwa vijana wa Wilaya ya Nachingwea?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza kwa dhati kabisa Mheshimiwa Masala kwa jitihada zake mbalimbali ambazo anachukua katika kuwasaidia wananchi wa Jimboni kwake Nachingwea. Amekuwa akifanya hivyo hata kwa taasisi na vyombo vilivyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, katika kujibu swali lake, kwanza kwenye eneo la wataalam kama ambavyo nimejibu katika swali langu la msingi, ni kwamba tayari hivi tunavyozungumza kuna madaktari takribani 300 ambao wanaendelea na mafunzo katika chuo chetu cha Monduli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yangu kwamba madaktari wale watakapokuwa wamekamilisha mafunzo yao, basi miongoni mwao tutawapeleka katika hospitali ile iliyopo katika kikosi cha 41KJ, eneo la Nachingwea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la mkakati wa kuboresha Chuo cha VETA; ni kweli Chuko cha VETA hiki kinasaidia sana na kitaendelea kusaidia zaidi wananchi hususan kwa maeneo ya Nachingwea na maeneo mengine nchini kitakapokuwa kimeimarishwa. Ndiyo maana dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba inakiimarisha chuo hiki ikiwa kimo katika mpango kazi wa Jeshi la Wananchi Tanzania. Miongoni mwa mambo ambayo tunatarajia kufanya ni kuhakikisha kwamba chuo hiki kinaunganishwa na VETA.

Mhehsimiwa Mwenyekiti, hivi sasa tunavyozungumza, ni kwamba tunatoa huduma ile kwa kuazima Walimu kutoka VETA kuja kufundisha, lakini pale ambapo mikakati hii itakapokamilika, tutakuwa tuna Walimu wa kutosha ambao watakuwa pale pale chuoni muda wote. Mbali ya hiyo, tutakuwa tunaweza kuongeza vifaa pamoja na kuimarisha majengo ya chuo hicho ili kiweze kutoa huduma kwa wananchi wengi zaidi wakiwemo wananchi wa Mheshimiwa wa Jimbo la Nachingwea kwa Mheshimiwa Hassan Masala.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Serikali imekuwa ikichukua vijana wengi kuwapeleka kwenye mafunzo ya JKT na baada ya mafunzo hayo, vijana wachache sana ambao wanapata ajira na vijana wengi wanakuwa wako mitaani. Kwa nini Serikali isije na mikakati ya hao vijana ambao wanamaliza mafunzo ya JKT kuwatafutia ajira mbalimbali kama vile kwenye migodi na maeneo mengine ili kuweza kupunguza vijana hao kuzurura mitaani na baadaye kuandaa bomu ambalo ni hatari? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza malengo ya kuwapeleka vijana JKT, haina maana kwamba vijana wote watakaopelekwa JKT wataajiriwa na vikosi vyetu vya ulinzi na usalama, ni kwa sababu idadi ya nafasi za ajira zilizopo katika vyombo vyetu hivi ni chache kulinganisha na idadi ya vijana ambao wanaingia JKT. Hata hivyo, kwa kuwa mafunzo haya ya JKT yanaimarisha uzalendo na kujenga ujuzi mbalimbali, kwa hiyo, ni imani ya Serikali kwamba maandalizi ya vijana ambao wanakwenda JKT yatawasaidia kuweza kutumia fursa nyingine zilizopo nchini za kuweza kupata ajira ikiwemo katika taasisi binafsi, taasisi za Serikali, pamoja na kujiajiri wenyewe.
MHE. SAADA MKUYA SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Pamoja na kazi nzuri ambazo zinafanywa na vikosi vyetu hivi vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania, kuna maeneo ambako kuna Kambi za Majeshi na kumekuwa kuna uwekezaji ambao unaendelea, hususan kumbi za disco, pamoja na mambo mengine ambayo yanafanana na hayo ambayo mara nyingine zinaleta athari za kiutamaduni na maadili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inasemaje kuhusiana na kambi hizo ambazo zinakuwa zinapigwa disko katika maeneo ya wananchi na hivyo kuathiri utamaduni pamoja na maadili ya maeneo yanayohusika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi ya kumbi za starehe katika nchi yetu yapo kwa mujibu wa taratibu tulizojiwekea na siyo katika makambi ya Jeshi tu, ni maeneo mbalimbali. Hata kumbi ambazo zipo katika maeneo ya Kambi za Jeshi kwa ajili ya starehe zinatakiwa zifuate utaratibu ule ule ambao tumejiwekea wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sidhani kama ni sahihi kuonyesha kidole katika maeneo ya kambi ya Jeshi peke yake, imani yangu ni kwamba ukizingatia maadili na misingi ya Jeshi letu la Wananchi wa Tanzania, nadhani itakuwa ni sehemu ya mwisho kuonyeshwa kidole katika ukiukwaji wa sheria hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kama ana kesi mahususi ambayo anadhani inahitaji kufuatiliwa, namwomba Mheshimiwa Saada Mkuya atupatie taarifa ya eneo la kambi ambalo anazungumza ili tufuatilie na kuona hatua za kuchukua.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza napenda kumpongeza Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri; lakini kama ilivyoelezwa kwenye swali la msingi kwamba kumekuwa na malalamiko mengi katika Vituo vyetu vya Polisi pale wananchi wetu wanapokwenda kuhudumiwa katika maeneo yale:

Sasa je, ni mkakati gani wa Serikali katika kuhakikisha siku zijazo kunafungwa CCTV Camera katika hayo maeneo ili kuleta ushahidi katika yale matukio wanayofanyiwa wananchi pale? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninafahamu kwamba Serikali ina dhamira ya dhati katika kuhakikisha Jeshi la Polisi linafanya vizuri, lakini kama litafanya vizuri bila kutunza kumbukumbu haitasaidia. Ni lini sasa mkakati wa Serikali katika kuhakikisha matukio yote yanakuwa katika kumbukumbu ili linapohitajika jambo lolote kwa mtuhumiwa yeyote linapatikana kwa urahisi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Sikudhani Chikambo kwa maswali yake mazuri. Nimhakikishie kwamba kama ambavyo nimejibu katika jibu la msingi, ni kwamba dhamira hiyo Serikali kupitia Jeshi la Polisi ya kufanya maboresho katika mfumo mzima wa TEHAMA ikiwemo maeneo mawili ambayo ameyazungumza ya mifumo ya CCTV na kumbukumbu kwa kutumia teknolojia ya kisasa, dhamira hiyo ipo na pale ambapo bajeti itaruhusu, basi sisi tutakamilisha huo mpango.
MHE. WILLIAM D. NKURUA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Awali ya yote nitoe shukrani zangu kwa Serikali kwa sababu Wilaya yetu ya Nanyumbu pia tulikuwa na matatizo ya usafiri kwa Jeshi la Polisi lakini siku za hivi karibuni Serikali imetupatia na sasa polisi wana uwezo wa kufanya kazi kiurahisi. Hata hivyo, pamoja na shukrani hizo, nataka niongeze swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekiri kwamba Nanyumbu ni miongoni mwa wilaya mpya na hatuna jengo lenye hadhi ya kuwa na hadhi ya Kituo Kikuu cha Polisi cha Wilaya. Sasa kwa kuwa Serikali inajua hilo.

Je, nitarajie sasa kwenye bajeti ijayo kuona haya maandalizi ambayo Serikali imesema ipo katika maandalizi ya ujenzi wa kituo hicho; je, kwenye bajeti hii ijayo nitarajie kuona hiyo bajeti inasomwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa William Dua, Mbunge wa Nanyumbu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie kwamba kama ambavyo alivyokuja kulizungumzia suala la mapungufu ya usafiri na tukalifanyia kazi, basi na suala la kuhakikisha kwamba tunafanya kila linalowezekana ili kuimarisha kituo cha polisi katika Wilaya ya Nanyumbu nacho vilevile tutachukulia kwa uzito kama ambavyo tumechukulia uzito wa suala la changamoto ya gari katika wilaya yake.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza swali la nyongeza. Kwanza naipongeza Serikali kwa jitihada kubwa walizozifanya katika Jimbo la Makambako, lakini vilevile eneo la Polisi la Makambako lilipimwa na kufanyiwa uthamini kwa ajili ya kulipa fidia wananchi ambao walikuwepo ndani ya eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, nataka kujua, lini Serikali itawalipa wananchi hawa pesa zao kama fidia?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Wilaya ya Wanging’ombe tuna changamoto ya Kituo cha Polisi; nichukue nafasi hii kulipongeza Kanisa Katoliki kwa kuona umuhimu wa usalama wa raia na kujitolea baadhi ya majengo kutumika kama Kituo cha Polisi ndani ya Wilaya yetu ya Wanging’ombe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe imeshatoa kiwanja, nilitaka kujua: Je, lini Serikali itajenga Kituo hiki cha Polisi ndani ya Wilaya yetu ya Wanging’ombe?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kuhusiana na fidia ya wananchi, nataka nimjulishe Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeamua kuwaachia hilo eneo wananchi, kwa hiyo, suala la fidia halipo tena.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la Kituo cha Polisi, niwapongeze Kanisa kwa kuanzisha hizo jitihada pamoja na wananchi wa eneo hilo; na niwahakikishie kwamba pale ambapo hali itaruhusu tutaongezea nguvu jitihada hizo ili Kituo hicho kiweze kukamilika. Tunatambua umuhimu wa Kituo hicho.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo yanaonesha kabisa Serikali ina nia nzuri ya kusaidia wananchi wake. Kwa niaba ya wanawake wa Mkoa wa Kaskazini Unguja nilikuwa nina maswali mawili ya kuongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nilitaka kujua: Je, huduma ya uokoaji na kuzima moto kuna gharama zozote ambazo mhudumiwa anatakiwa alipe?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili: Je, kama gharama hizo zipo, ni utaratibu gani unatakiwa ufanywe ili aliyepatiwa huduma aweze kulipa bila kuwa na taharuki? Maana kipindi kile anakuwa amechanganyikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwa dhati kabisa nimpongeze sana Mheshimiwa Malembeka kwa kazi nzuri ambayo anayoifanya katika Mkoa wake wa Kaskazini. Kwa kweli anawatendea haki wapiga kura wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nikijibu maswali yake pamoja, kwanza huduma za kuzima moto ni za bure, hakuna gharama. Hata hivyo, kwa mujibu wa sheria ya Jeshi la Uokoaji na Zimamoto ya mwaka 2007 Sura ya 427, inaeleza kwamba Jeshi la Zima Moto na Uokoaji lina Mamlaka ya kuweza kutoa leseni kwa makampuni binafsi kutoa huduma hizo ikiwemo huduma ya kuzima moto pamoja na vifaa.

Mheshimia Naibu Spika, kwa hiyo, makampuni haya ndiyo ambayo yanaingia mikataba na Taasisi binafsi na ndiyo yanakubaliana malipo, lakini kwa maana ya huduma hizi za zimamoto ni bure.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na utaratibu ambao unatumika, unapiga namba 114 na kikosi chetu kinafika pale haraka iwezekanavyo kutoa huduma hizo bila malipo yoyote. (Makofi)
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina swali moja la nyongeza. Kwa kushirikiana na Mwekezaji anayejenga hii Coating Yard pale Sojo Igusule, Kijiji cha Sojo Igusule tumefaidika kwamba sasa tutapata maji kwa msaada wa huyu mwekezaji na pia tutapata umeme kwa haraka kuliko ulivyokuwa kwenye mpango, lakini pia kituo cha afya cha pale, kitakuwa upgraded kuwa kituo cha afya cha kisasa. Sasa swali langu ni kwamba, je, Serikali haioni kwamba kuna haja ya kufanya mazungumzo na huyu mwekezaji anayejenga hiyo coating yard pale, kwa sababu atawekeza zaidi ya bilioni 600 na hivyo na yeye pia atahitaji masuala ya usalama? Je, Serikali iko tayari kufanya naye mazungumzo ili na yeye achangie ujenzi wa hicho kituo cha polisi kama ambavyo amechangia kuleta maji, umeme na kupandisha hadhi kituo cha afya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Selemani Zedi, Mbunge wa Bukene, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kutumia fursa zilizopo ndani ya jimbo lake kwa ajili ya kuweza kueneza huduma mbalimbali za kijami katika jimbo lake. Kuhusiana na wazo ambalo amelitoa, pia ni wazo zuri, lakini nataka nimjulishe kwamba, wazo hilo siyo geni, kwa mfano katika Mradi wa Stiegler’s Gorge ambao unaendelea kule Rufiji, tumefanikiwa kupata kituo, tupo katika mchakato wa ujenzi wa kituo cha polisi, ambapo unatokana na mradi huo. Kwa hiyo, tutatumia mawazo yake pamoja na mbinu ambazo tumetumia kule Stiegler’s Gorge kwa ajili ya kufanya mazungumzo na wawekezaji hao waliopo katika jimbo lake wa mradi huo wa bomba la gesi ili tuone uwezekano wa wao kushiriki kusaidia ujenzi huo wa kituo cha polisi.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi. Matukio ya ajali ya za moto, malori ya matenki ya mafuta yanaendelea kughalimu maisha ya Watanzania kwa kushabisha vifo na vilema vya kudumu. Tukio la Agosti 10, 2019 katika eneo la Msamvu eneo la Morogoro watu zaidi ya 100 walipoteza maisha, lakini umbali wa Ofisi za Zimamoto pale Morogoro haifiki kilometa moja kuelekea pale msamvu lilipotokea tukio.

Je, Serikali haioni kwamba kuna haja ya kuwalipa fidia wapendwa waliopoteza maisha yao pale, kwa sababu fire ilifika pale kuzima moto wakati watu wameshateketea na kuwa majivu na kuni? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Waziri Mkuu wakati wa mazishi yale pale Msamvu aliagiza kuunda Tume ya Kuchunguza Ajali ya Msamvu.

Je, ni kwa nini mpaka sasa Ofisi ya Waziri Mkuu haijatoa tamko lolote juu ya tume iliyouzwa kuchunguza ajali ya tukio la Msamvu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabla sijajibu swali lake, naomba nisisitize majibu ya msingi ambayo niliyazungumza kuhusiana na mkakati wa Serikali ya kuimalisha Jeshi letu la Zimamoto na Uokoaji katika kulipatia vifaa mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, mbali na jitihada ambazo nimezungumza za kutenga bajeti ambapo kwa mwaka huu peke yake tumeshapokea karibu shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ununuzi wa magari ya moto na vifaa vya uokoaji, lakini pia kuna mipango mbalimbali ikiwemo mkopo ambao nimezungumza, wa takribani Euro milioni 408 ambayo tunatarajia pamoja na mambo mengine kujenga vituo katika kila wilaya, kununua vifaa mbalimbali vya uokoaji ikiwemo magari, helkopta, boti na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, ni imani yangu kwamba tukapokuwa tumekamilisha mikakati hii na ikawa ipo vizuri, basi changamoto zote zinahusiana na majanga ya moto ikiwemo kama hili ambalo limetokea Morogoro, yatakuwa sasa tunayakabili kwa ufanisi zaidi.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na hoja yake specific kuhusu ripoti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kamati ya Mheshimiwa Waziri Mkuu imepewa kazi. Kwa kuwa hii ilikuwa ni Kamati ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, nadhani siyo mamlaka yangu kuitolea kauli.

Mheshimiwa Spika, nina hakika kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu kupitia Ofisi yake, kuna utaratibu ambao umewekwa wa kuweza kuitolea taarifa pale ambapo mwenyewe ataona inafaa. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge avute subira ambapo Serikali inaendelea kulifanyia kazi suala hili. Ni imani yangu kwamba Kamati ile imeendelea kufanya kazi yake vizuri.

Mheshimiwa Spika, lengo na dhamira ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ni kuhakikisha kwamba taarifa ya ripoti ile inatupatia mapendekezo ambayo yanasababisha hatua zichukuliwe, lakini pamoja na kuepukana na matatizo kama haya yasitokeze siku zijazo.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona niweze kuulizwa swali dogo la nyongeza. Wilaya ya Ngara hatuna gari la Zimamoto na yameshatokea majanga mara nyingi na ya kusababisha vifo; na ni barabara inayopitisha magari makubwa yanayobeba mafuta yakielekea nchi za jirani Rwanda, Burundi na Kongo:-

Je, ni lini Serikali itatuletea gari la Zimamoto Wilaya na Ngara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza niendelee kumpongeza Mheshimiwa Oliver kwa jinsi ambavyo amekuwa akipambana kuhakisiha kwamba changamoto mbalimbali zinazohusu vyombo vya usalama katika Mkoa wa Kagera zinapatiwa ufumbuzi.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na hoja yake ya kupeleka gari la zimamoto katika Wilaya ya Ngara, nimhakikishie kwamba pale ambapo mikakati ambayo nimeizungumza kwenye jibu la msingi itakapokuwa imekaa tayari, basi moja katika maeneo ambayo tunayazingatia ni Wilaya ya Ngara.
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, ajali za moto zimekuwa ni kubwa sana katika taifa; katika taasisi za Serikali na hata katika mabweni ya shule. Sasa nauliza, najua ni lazima kuwepo na fire extinguishers katika maeneo yote.

Mheshimiwa Spika, ni kwa nini sasa sheria isije Bungeni ikarekebishwa, au kanuni ikarekebishwa kusudi iwe ni lazima kuwa na smoke detectors katika mabweni ya shule na katika taasisi za Serikali ili ule moshi uweze kung’amuliwa mapema na kuzia madhara makubwa yanayosababishwa na moto?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ruth Molel, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hoja ya Mheshimiwa Mbunge ni ushauri basi tunaipokea na tuitafakari na kuona ni jinsi gani tunaweza tukaifanyiakazi.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Spika, nashukuru.

Kwa kuwa majanga yanayosababishwa na binadamu ni zaidi ya asilimia 96 ya majanga yote. Serikali haioni umuhimu wa kuhakikisha kunakuwa na somo rasmi kwenye mfumo rasmi wa elimu wa namna ya kujilinda, kujinga na kujiokoa na majanga hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mabtia, Mbunge wa Vunjo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nao vilevile ni ushauri; nadhani mamlaka husika zimeusikia, lakini kama Serikali tumeuchukua na tutafakari kuona kama kuna haja ya kufanya hivyo kwa wakati huu.
MHE. ASHA ABDULLA JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri yaliyosheheni vigezo.

Mheshimiwa Spika, askari wa Jeshi letu la Polisi wanafanyakazi nzuri sana ikiwepo usalama barabarani, usalama wa raia na mali zao na kutuelimisha kutii sheria bila shuruti.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wako baadhi ya askari ambao hawakupandishwa cheo mpaka wamefikia kustaafu, na kwa kuwa kutokupandishwa huko si kosa lao, ni kosa la mfumo; je, Serikali ina mpango gani wa kuwafidia ili wasiwe wamepoteza haki zao na hasa kwa vile sasa hivi wako wastaafu wanahitaji sana fedha hizo?

Mheshimiwa Spika, swali langu lingine; Je, Serikali haioni umuhimu wa kuandaa mfumo na utaratibu uliowazi kabisa unaoonyesha namna gani na vigezo gani vya kuweka nafasi ya kwenda course ili uweze kupandishwa cheo na utaratibu huo uwe wazi na haki kabisa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Asha Abdalla Juma, Mbunge wa Viti Maalum kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mfumo ambao tunao sasa hivi wa upandishwaji askari vyeo uko vizuri; na nimeeleza katika jibu la msingi vigezo ambavyo vinatumika. Hata hivyo kulingana na wingi wa askari tuliokuwanao na uchache na ufinyu wa nafasi hizo inasabbaisha wakati mwingine askari wengine kutumia muda mrefu zaidi katika kupata vyeo.

Hata hivyo tumekuwa tukifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha kwamba wale askari ambao wanatimiza vigezo wanapata fursa ya kupandishwa vyeo; kwa hiyo nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Asha Abdalla Juma kuhusiana na hilo.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusiana na hoja yake, kama nitakuwa nimemuelewa vizuri, ya kuwafidia, nadhani hilo halipo katika utaratibu. Kimsingi tu ni kwamba tutaendelea kuhakikisha tu kwamba askari ambao wenye sifa wanapandishwa vyeo. Katika kipindi cha mwaka huu mmoja, hivi karibuni tulipandisha vyeo askari kwa upande wa Jeshi la Polisi pekee kwa haraka haraka nadhani ni zaidi ya askari 9000 ukiachilia mbali majeshi mengine yaliyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Utaona kwamba tunafanya jitihada kama Serikali kuona askari hawa ambao wanafanyakazi vizuri wanapata fursa ya kupandishwa vyeo kadri ya hali na uwezo wa Serikali unavyoruhusu.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na majibu ya Serikali kwanza tunashukuru kwamba, wameweza kutupatia gari la canter kwa ajili ya kubeba mahabusu katika Wilaya ya Uvinza, lakini tunaomba sasa ni lini Serikali itampatia OCD wa Wilaya ya Uvinza gari la kufanyia patrol kwa sababu kwa kipindi kirefu sana hakuna gari la kwa ajili ya kufanya patrol?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Katika Wilaya ya Lushoto ambayo ndio wilaya kongwe ya kipolisi nchini jengo la utawala ambalo anatumia OCD limesimama kwa muda mrefu sasa na jengo hili linajengwa kwa msaada wa fedha za DFID. Je, ni lini jengo hili la Polisi Wilaya ya Lushoto litakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na gari la OCD, kama ambavyo nimejibu katika swali la msingi Uvinza, lipo gari aina ya Land Cruiser ambayo anatumia OCD kwa sasahivi. Ingawa tukipata gari jingine tutaongeza tunatambua umuhimu wa mahitaji ya gari hasa katika Wilaya ya Uvinza na Mkoa wa Kigoma kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na hoja ya kituo cha Polisi ambacho ujenzi wake umesita kule Lushoto; kimsingi nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kituo hiki ambacho kilikuwa kinajengwa chini ya ule mradi pesa za ufadhili kutoka mradi wa STAKA pamoja na Serikali, ilisita kwa muda, hata hivyo tumeshafanya tathmini na kugundua kwamba, zinahitajika fedha kwa ajili ya kukamilisha kituo hiki na ninadhani takribani kama shilingi milioni 300 si pesa nyingi. Fedha hizi tunatarajia kuzipata kupitia kwenye mfuko wa Tuzo na Tozo, hivyo tutakapokamilisha kupata fedha hizo tutamaliza kituo hiki kiweze kutumika.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona, pamoja na majibu mazuri ya kwenye swali la msingi la Naibu Waziri, Wilaya ya Korogwe ina Halmashauri mbili ambapo Polisi wanakaa kwenye jengo la mkoloni ambalo Mkuu wa Wilaya yumo, Mahakama imo na hiyo Polisi ipo hapo.

Je, katika mipango ambayo wanakusudia sasa kuanza baadaye atakuwa tayari kuipa kipaumbele Korogwe ili wawe na jengo la ofisi kwa sababu kiwanja wanacho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu kwenye swali la msingi kwamba, tuna upungufu wa vituo vya Polisi katika baadhi ya wilaya nchini na hivyo basi nimhakikishie kwamba, katika mipango ya Serikali ya kujenga vituo hivyo na Korogwe ni moja katika maeneo ambayo tunayatambua hayana kituo na hivyo ni moja katika maeneo ambayo tuna mpangonayo wa kujenga vituo pale ambapo mipango hiyo itakapokamilika, hususan katika eneo la upatikanaji wa fedha.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante kwa kunipa nafasi. Swali hili nauliza kwa mara ya tatu leo, kwa kuwa Milima ya Kitonga, Ruaha Mbuyuni mpaka Mikumi Iyovi, Malolo, kituo wanachotegemea cha Polisi ni kimoja cha Ruaha Mbuyuni, lakini hawana gari la Polisi na hivi juzi nimetoa pikipiki mbili kwenye kile kituo. Sasa je, Serikali haini ni wakati muafaka wa kuniunga mkono kwa sababu, accident inapotokea wanapata shida kubwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze kwa kuchangia pikipiki kwa askari wetu, lakini na mimi namjibu tena kwa mara nyingine kwamba, pale ambapo magari yatafika tutaangalia uwezekano wa kuweza kupeleka pale kwa sababu, sasahivi tunavyozungumza hatuna magari ambayo yamepatikana kwa hiyo, avute subira Mheshimiwa Mbunge.
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, kwa kuwa mwaka 2015 mimi mwenyewe niliifadhili Wizara ya Mambo ya Ndani gari la Polisi kutoka Japan, jipya, na nikalipeleka kwenye kituo cha Polisi kilichoko Maore kwa ajili ya Jimbo la Same Mashariki, lakini Serikali mpaka leo mnashindwa kutoa hata pesa kidogo kwa ajili ya kupeleka service gari lile. Waziri unaniambia nini sasa hivi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunathamini sana jitihada za Mheshimiwa Anna Kilango Malecela za kuweza kutusaidia gari kwa matumizi ya Jimbo la Same. Namhakikishia Mheshimiwa kwamba hatushindwi kufanya service hiyo gari; na kama kuna tatizo la service, basi tumelipokea na tutahakikisha kwamba gari hiyo inafanyiwa service ili iweze kutumika. (Makofi)
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Wilaya ya Ikungi ni Wilaya iliyoanzishwa mwaka 2013; na hivi tunavyoongea, ofisi au OCD anakaa kwenye majengo ambayo yalikuwa ni maghala ya mkoloni. Kwa sababu ulishaanzwa ujenzi wa kujenga jengo la OCD kwa maana ya wilaya, ni lini sasa Serikali itamaliza, kwa sababu limesimama muda mrefu, miaka mitatu iliyopita?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mimi na Mheshimiwa Mtaturu tulishazungumza pembeni kwamba niende Jimboni kwake, nimhakikishie kwamba moja katika mambo ambayo tutafanya ni kwenda kukitembelea kituo hiki kwa pamoja halafu tushauriane juu ya utaratibu muafaka wa kukimaliza kituo hiki kwa haraka.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa vile Serikali ikishawekeza pesa nyingi kujenga Kituo cha Polisi cha Mkalama; na kwa vile Naibu Waziri alishafika na akakiona kituo hicho sasa kinaanza kuharibika, ni lini kituo hicho kitakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kituo hiki nakifahamu na tuliambatana na Mheshimiwa Kiula kukitembelea. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kama ambavyo tulizungumza wakati wa ile ziara, nami nimeshawasilisha hiyo taarifa na hivi sasa Serikali ipo katika harakati za kutafuta fedha ili kituo hiki kiweze kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Kiula avute subira wakati Serikali inaendelea na jitihada hizo za kupata fedha za kumaliza Kituo hiki cha Polisi.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Halmashauri ya Geita DC ina population zaidi ya watu 1,300,000 na tunaye OCD mmoja peke yake ambaye anafanya kazi kwenye Halmashauri hiyo ya watu 1,300,000 plus Geita Mjini yenye watu zaidi ya 600,000.

Je, Waziri ananiambiaje kuhusiana na kutafuta Kanda Maalum Nzela ili kumsaidia OCD wa Geita, kumpunguzia ukubwa wa eneo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, maamuzi ya kutengeneza kanda maalum yanategemea sababu mbalimbali au vigezo mbalimbali ikiwemo ukubwa wa kijiografia, hali ya uhalifu katika eneo husika na kadhalika. Kwa hiyo, sitaki nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaweza kufanya hilo jambo kama ambavyo amependekeza kwa sasa hivi, kwa sababu sina hakika kwamba eneo hilo imekidhi vigezo ambavyo vinahitajika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tunalipokea na tuone, kama imekidhi vigezo na kama hali itaruhusu, basi tutalitafakari na kulitolea maamuzi sahihi kwa wakati muafaka.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niulize swali la nyongeza. Wilaya ya Liwale ni Wilaya kongwe yenye umri zaidi ya miaka 44 sasa; pamoja na kwamba Halmashauri wametenga eneo kubwa kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi, lakini hadi leo Wilaya ya Liwale haina Kituo cha Polisi. Nini kauli ya Serikali namna ya kuwapatia wananchi wa Liwale ujenzi wa Kituo cha Polisi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Mheshimiwa Kuchauka hiki kimekuwa ni kilio chake cha muda mrefu sasa, lakini nimhakikishie kwamba kilio chake siyo cha peke yake, hata sisi Serikali tuna kilio hicho hicho kuhakikisha kwamba Wilaya ya Liwale kulingana na umuhimu wake inapata Kituo cha Polisi. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba pale ambapo tutaweza kufanikiwa kupata fedha, basi tutajenga hicho Kituo.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwanza naipongeza Serikali kwa kazi kubwa inayofanya ya kuhakikisha kwamba usalama wa barabarani unasimamia mazingira yote. Kwa kuwa usalama barabarani wanafanya kazi kubwa na kwa kuwa waendesha bodaboda kwa sasa pamoja na kupunguza ajali, wapo wanaovunja sheria na baada ya kuvunja sheria wao pia wanakuwa vyanzo vya watu kupata ulemavu: Je, Serikali inatoa adhabu gani kali kwa hao ambao wanavunja sheria?

Mheshimiwa Spika, swali la pili: Je, ni lini sasa Serikali itahakikisha inasajili bodaboda zote hapa nchini ili kupunguza uhalifu na kupunguza ajali pale inapotokea wale wenye bodaboda wanapokimbia?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, aina ya adhabu zipo kwa mujibu wa Sheria ya Usalama Barabarani lakini inategemea pia aina ya kosa la mhusika. Hata hivyo nikiri kwamba inawezekana adhabu hizo sasa hivi zikawa zimepitwa na wakati, ndiyo maana tupo katika hatua za mwisho za mchakato wa marekebisho makubwa ya Sheria za Usalama Barabarani. Ni imani yetu kwamba sheria hiyo itakapokamilika, inaweza ikasaidia sasa kuweka adhabu ambazo zitawabana zaidi wavunjifu wa sheria za usalama barabarani hususan waendesha bodaboda.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la usajili, nimhakikishie kwamba tupo katika hatua za kuanza mchakato huo tukiamini kwamba utaratibu huo utasaidia sana katika kupunguza malalamiko ya baadhi ya waendesha bodaboda ya uonevu wanaofanyiwa dhidi ya baadhi ya Askari wetu, lakini pia itasaidia sana kuweza kuwadhibiti na kuwakamata pale ambapo wanafanya makosa hayo kwa urahisi na uvunjifu wa Sheria za Usalama Barabarani kwa wanaotumia bodaboda.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Katika maelezo ya Mheshimiwa Waziri, yaani majibu yake, anasema kwamba ajali zimepungua lakini vifo vimeongezeka.

Mheshimiwa Spika, kwa idadi ya vifo ambavyo wamevitaja kuanzia mwaka 2017, 2018, 2019 hadi Juni inaelekea kwamba jumla ya vifo vilivyotokea ni 1,270. Hawa ni Watanzania, idadi ni kubwa. Mheshimiwa Naibu Waziri tuambie hasa mkakati wa ziada wa mwarobaini ili kukomesha vifo hivi visiendelee tena. Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, niliposoma takwimu tokea mwaka 2016 mpaka 2019 kwa ujumla ajali, vifo na majeruhi vyote vinaonekana kushuka, lakini takwimu ambazo nilisema kwamba vifo vinaongezeka ni za kipindi cha Januari mpaka Juni 2019. Kwa hiyo, ni kipengele kimoja na cha kipindi kimoja ambacho tumeona kwamba upande wa vifo umeongezeka, lakini kwa ujumla ajali zimepungua.

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimeeleza, haya ni mafanikio ya usimamizi wa Sheria ya Usalama Barabarani ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupunguza ajali za barabarani ambao tumeuandaa kupitia Baraza la Usalama la Taifa kwa maana mkakati huu umegusa katika maeneo mengi. Moja, ndiyo hili eneo ambalo nimezungumza katika jibu langu la msingi kwamba ni kuhakikisha kwamba Askari wetu wanasimamia Sheria ya Usalama Barabarani kwa nguvu zote na kwa mujibu wa sheria.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Spika, ahsante. Sina budi kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jawabu alilonipa ambalo ni zuri na linaridhisha na kaamua kusema ukweli wake hali halisi ya Kambi hiyo, lakini ni nana maswali mawili ya nyongeza:-

Kwa kuwa, uzio ambao ninaupigia kelele kila siku, sasa hivi wanataka waukarabati kufanya wa matofali na sasa bado upo wa waya, lakini hata hivyo wamejitahidi upande wa School ya Jang’ombe tayari wameufanyia ukarabati, ningeomba na upande wa Matarumbeta, upande wa kwa Alinatu, upande wa Kwahani kwa sababu hizo njia za panya zimekaa sehemu mbaya na watu bado wanazitumia kama vichaka au njia za kupitia wangelifanya kila mbinu na sehemu hizo wakafanyia ukarabati kabla hata kufanya ukarabati huo utakaozungushwa kwa matofali.

Swali la pili, kwa kuwa tayari amekubali kwamba nyumba za kambi hizo zote zimechakaa na kweli zimechakaa, maana zimejengwa kabla ya Mapinduzi ya 1964 na kwa kuwa nyumba hizo hasa zili wanazokaa Askari wa wa kawaida siyo Maofisa ambao ni kama mabanda nyumba hizo zimechakaa na haziridhishi kukaa binadamu ningeomba angalau wangeanza kuzifanyia ukarabati hizo ili Askari wetu wakaishi maisha bora.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote kwanza naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Fakharia kwa jitihada zake kubwa anazochukua katika kukabiliana na changamoto mbalimbali katika Majimbo ya Mkoa mzima wa Mjini. Mimi ni shahidi ni Mbunge ambaye anashirikiana nami vizuri katika Jimbo langu ambalo lipo katika Mkoa wake katika kukabiliana na changamoto hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo za dhati kwa Mheshimiwa Fakharia naomba sasa nijibu maswali yake kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa amekiri ameridhishwa na jitihada ambazo tumeshaanza kuchukuwa katika kukarabati uzio kwa upande uliopo karibu na school ya Jang’ombe nimhakikishie kwamba jitihada hizo ambazo zimeanza ndizo ambazo tutaendelea nazo katika kukamilisha uzio wote lakini pamoja na kukarabati nyumba za Askari Polisi pale ambapo fedha zitakapokuwa zimepatikana kama ambavyo nimejibu katika jibu langu la msingi.(Makofi)
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kumekuwa na msongamano mkubwa sana kwenye magereza mbalimbali hapa nchini na hasa ukiangalia kwa mfano kama Gereza letu la Ilembo pale Vwawa wafungwa wanaotakiwa kukaa pale pamoja na mahabusu ni 120; lakini mpaka sasa hivi kuna mahabusu pamoja na wafungwa zaidi ya 400 na hili limekuwa ni tatizo katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Je, Serikali ina mpango gani wa kupanua haya magereza kutokana na mrundikano huo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kumekuwa na matatizo makubwa sana katika magereza haya, hakuna zahanati katika magereza yetu na kumekuw ana tatizo kubwa sana la wafungwa kutolewa kwenye haya magereza na kupelekwa kwenda kutibiwa katika hospitali mbalimbali hapa nchini wakati huo magereza hawana magari.

Serikali ina mpango gani wa kujenga zahanti katika magereza yetu yote hapa nchini ili wafungwa na mahabusu katika maeneo haya wawe wanatibiwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna utaratibu wa kujenga magereza mapya, kuongeza mabweni na kupanua kadri ya hali ya fedha inavyoruhusu. Kwa mfano, katika kipindi cha karibuni tumekamilisha ujenzi wa Gereza la Ruangwa, Gereza la Chato lakini pia na kufanya uongezaji wa mabweni katika magareza kadhaa nchini, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba pale ambapo hali itaruhusu na Gereza la Vwawa vilevile nalo tutafanya upanuzi wa gereza hilo ingawa upanuzi wa magereza siyo njia pekee ya kupunguza msongamano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtakumbuka hivi karibuni, nichukue fursa hii kwanza kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kutokana na dhamira yake ya dhati ya kuwatumikia wananchi wa nchi hii hususani wanyonge na hasa pale katika jitihada zake za kuona kwamba wanyonge wa nchi hii hawaonewi, alivyofanya ziara katika Gereza la Butimba hivi karibuni alitoa maelekezo nchi nzima ambayo yameshaanzakufanyiwakazi na yamesaidia sana kupunguza idadi ya mahabusu ambayo kimsingi msongamano huu kwa kiwango kikubwa unasababisha na mahabusu ambao ni wengi wakati mwingine wanapita hata idadi ya wafungwa.

Kwa hiyo, baada ya maelekezo yale na hatua ambazo mbalimbali zimechukuliwa sasa idadi ya mahabusu imeendelea kupungua nchini na hivyo kupunguza msongamano.

Lakini kwenye eneo hili la pili la zahanati, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tuna utaratibu katika magereza yetu yote kuwa na madakrati pamoja na zahanati. Kwa hiyo, ninachoweza kusema ni kwamba katika maeneo ambayo tunaona labda kuna upungufu wa nguvukazi ya madaktari pamoja na madawa tufanye jitihada za kuongeza ili tuweze kukabiliana na changamoto ya wafungwa wetu na mahabusu ambao wanahitaji matibabu katika magereza. Kwa hiyo, hii kama katika Gereza la Vwawa ni changamoto nitalichukua na nifuatilie ni la ukubwa kiasi gani na tuweze kuchukua hatua stahiki.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nina maswali mawili: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kupongeza Serikali kwa jitihada kubwa za maboresho kwenye magereza na pia tumeona juhudi za Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli pale alipo tembelea Gereza na Butimba na maelekezo aliyotoa na hatua zinazochukuliwa na Serikali nzima katika kupunguza kadhia ya magereza. Kama tunavyofahamu kwamba gerezani siyo kuzuri. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweka takwimu, data ya wakosaji makosa na adhabu wanazozipata wakiwa magerezani na kuziweka wazi takwimu hizi ili kuona kwamba udhibiti upo na kwamba haya makosa yanaendelea yamedhibitiwa au yanapungua?

Swali la pili, Je, Serikali haioni kwamba sasa ni wakati muafaka wa kufikiria kuweka wigo wa kutoa adhabu za kutumikia ndani ya jamii kwa wale ambao wanamakosa ambayo si ya kuleta dhara kwenye jamii zaidi, kuliko kuwarundika kwenye magereza kwa kuwa kufanya hivyo itaweza kupunguza mzigo mkubwa wa mkusanyiko magerezani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yake ya kwanza ilikuwa ni ushauri ambao tunaupokea kuhusiana na takwimu kuziweka wazi. Lakini swali la pili ambalo aliuliza kimsingi jambo hilo tunalo tuna utaratibu ambao unaitwa kwa lugha ya kiingereza extramurally labor ambao utaratibu huu kwa kawaida unatumika kutoa adhabu kwa maana ya adhabu za vifungo vya nje kwa baadhi ya watuhumiwa kulingana na masharti na vigezo vilivyowekwa. Kwa hiyo, utaratibu huo tunao na tunaendelea nao. (Makofi)
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza:
Mheshimiwa Naibu Waziri Gereza la Babati linadaiwa na BAWASA shilingi milioni 182 bili za maji hawajawahi kulipa, maana yake wafungwa wanavyokuwa wengi na matumizi ya maji yanakuwa mengi, muda mrefu watu wa BAWASA wamedai sana hiyo bili milioni 182.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nifahamu ni lini Serikali italipa deni hili la Gereza la Babati kwa BAWASA? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima nikiri kwamba taarifa za hilo deni ndiyo nazipokea hapa, kwa hiyo ninachoweza kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya kujibu maswali tutafuatilia tuweze kujua ni kwa nini deni hilo halijalipwa na ili tuweza kuangalia utaratibu wa kuweza kulipa pale ambapo tutakuwa tumepata kasma ya ulipaji wa madeni kama tunavyofanya katika magereza mengine nchini.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali kwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri kwamba Magereza mengi nchini zina mlundikano mkubwa wa wafungwa lakini wapo wafungwa ambao wamefungwa kwa ajili ya kesi ndogo ndogo kwa mfano wizi wa kuku, kugombana na waume zao na kadhalika na wamefungwa kwa sababu ya kukosa hela ya faini. Je, kwa kuwa faini hizo ni ndogo, Serikali haioni sasa kuna haja ya wafungwa hao kuwatoa na kufanya shughuli za kijamii nje ya jamii ili waweze kufidia fedha hizo ambazo Serikali inapoteza?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie pia kwamba utaratibu huo upo tuna idara maalum chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambayo inashughulika na wanasema huduma za jamii moja kati ya jukumu lake ni kuhakikisha kwamba inazingatia aina ya wafungwa wenye sifa kama ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitaja ili kuweza kuwapatia kazi zingine za kufanya nje, pamoja na utaratibu mwingine ambao nimeuzungumza wakati najibu swali la msingi la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo utaratibu huo tunao.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo tu kwamba wanadhurika vijana mahabusu kwa kuona tabia za wale wafungwa wabakaji, wezi na madawa ya kulevya lakini tumeshuhudia akina mama wanakuja wajawazito wanajifungulia gerezani, kuna akina mama wanakamatwa wakiwa na watoto wanakuwa nao gerezani wanachangamana na hao watu ambao wanatabia za tofauti tofauti na tunajua kabisa kwamba mtoto mchanga kuanzia zero age mpaka five years anakuwa ndiyo muda ambao anajifunza na kuweza kuweka vitu akilini, mtoto yule anakua kwenye makuzi ya gerezani anafuata zile tabia ambazo hazina maadili kabisa.

Je, Serikali ni kwa nini sasa isitafuta mbadala kama inashindwa kuwapa dhamana hawa mahabusu wenye watoto ni kwanini isitenge sehemu kabisa ya wamama wajawazito na wamama wanaonyonyesha waweze kukaa na wale watoto mpaka watakapofikia umri wa kuweza kuwatoa gerezani, kuliko kuchangamana wanaona wale akina mama saa nyingine wako uchi, wako hivi ni tabia mbaya na haiwatendei haki hawa watoto. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto hawa wanaruhusiwa kuchukuliwa na familia zao, kwa hiyo, watu wengi ambao wanafungwa, wakinamama ambao wana watoto wanapofikia umri baada ya kuacha kunyonyesha, mara nyingi huchukuliwa na jamaa zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa wale ambao watakuwa wanaendelea kubakia magerezani aidha kwa sababu ya kukosa jamaa wa kuwaangalia nje, kuna utaratibu mzuri ambao unaandaliwa na mimi binafsi nimetembelea magereza mengi sana na ninapotembelea kwenye magereza hayo hutembelea katika maeneo ya wanawake na katika mambo ambayo tunaangalia moja ni hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahakikisha kwamba watoto wale wanapata elimu, wanaandaliwa mazingira mazuri na wanasoma katika shule za nje ya gereza. Kwa hiyo, kimsingi jambo hili tunaliangalia kwa uzito wa aina yake ili kuhakikisha kwamba watoto wale hawapati madhara ya kisaikolojia wakati wanapokuwa gerezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, niendelee kutoa wito kwa wakinamama kujiepusha na kufanya vitendo vya kiharifu ili kuepusha kuwaingiza katika matatizo watoto hawa hasa wanapokuwa katika umri mdogo.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kupata nafasi hii, nashukuru sana Mheshimiwa Waziri wa majibu yako mazuri lakini nitakuwa na suala moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa muingiliano umekuwa mkubwa na watu wamekuwa wengi, kwanini hiki kituo kisitafutiwe sehemu nyingine, kikajengwa huko, kikawa na nafasi kubwa kikaelekea kama kituo kweli cha polisi kuliko pale kilivyokaa, hakijapendeza wala haifai. Huku kituo, huku soko, nafikiri Serikali ifikirie kukihamisha kikapate nafasi kubwa zaidi na majengo ya kisasa yaliyokuwa bora zaidi. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kuhusiana na hoja ya kuhamisha kituo hiki kwa sababu ya ufinyu wa nafasi kiusahihi ni kwamba eneo la kituo lile ni kubwa mno, labda Mheshimiwa Mbunge tukipata nafasi tukatembelee ili nimuoneshe. Ni juzi tu hapa kuna eneo ambalo liliwahi hata kupewa mwekezaji na kutokana na maelekezo ya Mheshimiwa Rais ya kwamba maeneo ya vyombo vya usalama yabakie kwa matumizi ya vyombo hivi tulitoa maelekezo na kuhakikisha kwamba tumemhamisha yule mwekezaji.

Mheshimiwa Spika, lakini utakumbuka pia hata eneo ambalo liko pembeni ya kituo cha polisi ambacho kimetumika kama soko kama alivyozungumza kwenye swali la msingi ni eneo pia la polisi ukiachia mbali eneo la nyuma ambalo ni kubwa. Kwa hiyo, kimsingi kuhamisha kituo hiki kwa sababu ya ufinyu wa eneo nadhani haitakuwa sahihi kwa sababu kuna eneo la kutosha. Cha msingi ni kuendelea kutoa wito kwa wananchi kutumia nafasi yao yoyote ya kuvamia maeneo ya polisi kuacha maeneo ya polisi yaendelee kutumika kwa ajili ya shughuli za kiusalama.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Mheshimiwa Naibu Waziri kwanza nikushukuru kwa kutupatia zile 150,000,000 ambazo zimetusaidia kujenga majengo ya polisi katika eneo la Bagara Ziwani na nyumba zinakamilika.

Mheshimiwa Spika, sasa eneo hilo halijawahi kufidiwa, wananchi hawajawahi kufidiwa tangu 2004, polisi wanajenga majengo yao, wananchi hawajalipwa fidia tangu 2004. Nini kauli ya Serikali juu ya wananchi hawa ambao wametoa eneo kwa polisi lakini hawajapatiwa fidia mpaka leo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa tunachukua pongezi kama Serikali kutokana na kazi ambayo inaendelea nchi nzima maeneo mbalimbali ya ujenzi wa nyumba za askari polisi.

Mheshimiwa Spika, la pili nimpongeze yeye binafsi kwa kufuatilia kwa karibu hii kadhia ya wananchi wake kutolipwa fidia. Hata hivyo, naomba nimhakikishie kwamba jambo hilo nimelichukua na tutalifanyia kazi na baadaye tutarudi kwake kuweza kumpatia majibu ya hatua ambazo zimefikiwa na changamoto gani kama zipo na nini mikakati ya Serikali katika kukabiliana na changamoto hizo ili hatimaye wananchi hawa waweze kupata fidia stahiki.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize maswali ya nyongeza na nishukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa umbali yalipo mahabusu, Ofisi ya OCD, karibu kilometa 70 mpaka yalipo Makao Makuu ya Kilolo, hivi Serikali inatumia gharama kubwa sana kusafirisha mahabusu, kumsafirisha OCD na askari kwenda yalipo Makao Makuu. Je, Serikali huwa inaangalia tathmini ya gharama inazozitumia kwa kuchelewesha kujenga hizi Ofisi za Wilaya.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa nyumba za polisi zilizopo wilaya ya Mufindi, zilizopo FFU Kihesa na Central line polisi Iringa Mjini ni nyumba ambazo kwakweli ni chakavu mno, vyo haviingiliki, askari wetu wamekuwa wakiishi familia 5 chumba kimoja na kuna adha nyingi sana ambazo wanazipata hata watoto na kinamama ambao wanaishi katika zile nyumba.

Mheshimiwa Spika, nimuombe Mheshimiwa Waziri anipe siku, tarehe na mwezi ambao tutakwenda kukagua nyumba zote za Mkoa wa Iringa na kubwa ambazo wamekuwa wakizipata askari wetu walioko katika Mkoa Iringa, ili mwenyewe ajionee na aone jinsi gani ambavyo pamoja na ufinyu wa bajeti yeye mwenyewe ataona kwamba iko haja sasa haya majengo ya Askari au nyumba za askari ziweze kukarabatiwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza kwa dhati ya moyo wangu Mheshimiwa Ritta Kabati, kwa jinsi ambavyo amekuwa akitetea sana Jeshi letu la Polisi katika Mkoa wa Iringi, lakini siyo kwamba amekuwa akitetea kwa maneno, ni miongoni mwa Wabunge ambao wameshiriki kikamilifu katika kuhakikisha kwamba wanapunguza changamoto za Askari wetu kwa yeye mwenyewe kujitolea kujenga kituo cha polisi kilichopo eneo la Semsema.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, baada ya pongezi hizi, Mheshimiwa Rita Kabati na jitihada kubwa ambazo tunaziona anazozifanya katika kupigania polisi, nimhakikishie kwamba tutaambatana mimi na yeye kwa ruhusu ya Mheshimwa Spika, ili twende tukashirikiane kwa pamoja kubabiliana na changamoto ambazo amezizungumza. Hata hivyo, nataka nimhakikishie kwamba tayari Serikali imeshaanza jitihada. Kwa mfano hivi tunavyozungumza kuna ujenzi wa nyumba sita unaendelea kwenye Makao Makuu ya FFU pale Iringa ni kuonesha kuguswa na upungufu na uchakavu wa nyumba za Askari katika Mkoa wa Iringa.

Mheshimiwa Spika, lakini pia tayari kuna eneo ambalo tumelibaini kwa ajili ya ujenzi wa kituo kwa baadaye kwenye wilaya yake, tukitambua kwamba kuna umuhimu wa Makao Makuu ya Polisi ya Wilaya kuwa katika Makao Makuu ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nadhani nimeshamjibu maswali yake mawili ya nyongeza kwa pamoja.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa hii nafasi. Kwa kuwa swali limekuwa likijirudia kila mara na majibu ambayo yanatofautiana, sasa niombe, tu kwa kuwa umbali huo ni mrefu na gari hakuna, Serikali itakuwa tayari sasa kutoa gari na kuongeza mafuta kwa ajili ya kwenda Kilolo na kurudi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, tutakuwa tayari kupeleka gari Kilolo pale ambapo fedha zitakapopatikana.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kama inavyofahamika, kituo cha Polisi katika Wilaya ya Lushoto ni cha tangia Mkoloni, lakini
nashukuru Serikali imetutengea fedha tumejenga kituo cha Polisi lakini kituo kile mpaka sasa hivi takribani miaka mitano sasa kiko kwenye mtambao wa panya. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kumalizia kituo kile?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shekilindi, Mbunge wa Lushoto kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa lugha ambayo ameitumia kidogo imenipa utata kuielewa…

SPIKA: Iko kwenye leta.

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Ameseama mtambaa wa panya…

SPIKA: Iko kwenye lenta, pale, wanaita mtambaa wa panya.

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, sawa sawa. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge, kama ambavyo amependekeza, tutakweda mimi na yeye kuangalia nini cha kufanya ili sasa tuvuke hapo mtandaa panya kuelekea kwenye kukimaliza kitu hicho.
MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, katika majibu yake ya msingi Mheshimiwa Naibu Waziri aliesema kwamba kwa upande wa wilaya mpya, Serikali inatafuta fedha ili iongeze bajeti kwa ajiliya ujenzi. Sasa Wilaya yetu ya Ubungo ni Wilaya mpya na Serikali kupitia Serikali, nguvu za wananchi na Mfuko wa Jimbo, tumejega kituo cha polisi cha wilaya pale Gogoni.

Mheshimiwa Spika, sasa kituo kile cha polisi ni kituo kikubwa, lakini huduma zinakuwa finyu kwa sababu Askari wanatoka maeneo ya mbalimbali sana. Sasa je, Serikali iko tayari, katika kutafuta fedha za ujenzi, itafute vilevile fedha za kujenga nyumba za Askari katika Jimbo la Kibamba karibu na Kituo cha Polisi cha Gogoni?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza naye nimpongeze kwa jitihada zake kama alivyozungumza, kwamba kupitia Mfuko wake wa Jimbo na nguvu za wananchi wameweza kujenga hicho kituo. Nikijibu swali lake ni kwamba, tutakuwa tayari, pale ambapo fedha zikipatikana basi tutashirikiana naye katika kumaliza ujenzi wa nyumba iki kituo hicho kiweze kutumika masaa yote.
MHE. MACHANO OTHMAN SAID: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jibu lake lakini pamoja na majibu hayo nataka kumuuliza swali lifuatalo, kwa kuwa mwaka wa fedha 2018/ 2019 umebakisha kama mwezi mmoja kumalizika, na kwa kuwa ajira hizi bado hazijafanyika, na kwa kuwa upungufu huu wa wafanyakazi unasababisha wafanyakazi zaidi ya wale wa malindo kuingia kazini usiku na asubuhi kurejea tena kazini, Je, Mheshimiwa Waziri anatuhakikishia vipi kwamba ajira hizi 505 zitafanyika kwa wakati.

(b) lakini, Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Mjini Magharibi inafanya shughuli zake, wananchi wengi wa Zanzibar badala ya kwenda kwenye Mkoa wanakwenda Makao Makuu, Ofisi Kuu kwa sababu kule Mkoa hakuna nyenzo za kufanyia shughuli zao hasa passport. Ni hatua gani Serikali itachukua ili kupunguza mzigo Ofisi Kuu na wananchi kwenda katika Mkoa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na ajira, kama ambavyo nimezungumza kwamba tunatarajia kuajiri na hivyo, basi pale ambapo kibali kitakuwa kimepatikana kutoka Utumishi vijana hao wataajiriwa, lakini swali lake la pili kuhusiana na kuboresha mazingira ya Ofisi ya Mjini Magharibi, ili kupunguza msongamano Makao Makuu nataka nimuhakikishie kwamba katika mwaka wa fedha tumetenga takribani shilingi milioni mia tatu kwa ajili ya kukamilisha matengenezo ili tuweze sasa kutumia vizuri zaidi, mara kazi hizo zitakapokamilika kwa mwaka huu, basi ni dhahiri kwamba sasa mazingira ya kazi katika Ofisi ya Mjini Magharibi yataboreka na msongamano utapungua.
MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya juhudi kadhaa ambazo zimefanywa lakini bado unyanyasaji wa watu Maafisa Uhamiaji kwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma, na hasa Manispaa ya Kigoma Ujiji kwenye masuala ya Uraia bado ni mkubwa, sasa Serikali haioni kwamba inge-priortise watu kupewa vitambulisho vya Uraia kwa haraka, ili kuweza kuhakikisha kwamba tunaondoa hili tatizo la watu kila wakati kukisiwa kwamba sio raia? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimuhakikishie Mheshimiwa Zitto, kwamba, malalamiko ambayo yeye pamoja na Waheshimiwa Wabunge wa Kigoma ambayo walikuwa wanayatoa kipindi cha nyuma kuhusiana na unyanyasaji wa wananchi tuliyafanyia kazi na kipindi ambacho tulikwenda kwenye ziara nikiwa nimeambatana na Mheshimiwa Waziri Mkuu na yeye alikuwepo nadhani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulilithibisha hilo kwamba sasa hali siyo kama ilivyokuwa, hata hivyo nimpongeze kwa rai yake na nimuhakikishie kwamba rai ambayo amezungumza ndio rai ya Serikali na ndiyo maana katika Bajeti yetu iliyopita tulieleza kwa mapana kuhusu malengo ya Serikali ya kuhakikisha kwamba tunafikia yale malengo tuliyoyapanga ili wananchi waweze kupata Vitambulisho hivi na hatimaye iweze kurahisisha mambo mbalimbali ikiwemo hayo ambayo yamezungumzwa, lakini na mambo mengine mengi ambayo yanatokana na faida za kuwa na kitambulisho hiki cha uraia.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na nashukuru kwa majibu japo hayajajitosheleza Kilimo cha Umwagiliaji ndiyo njia pekee ya kuhakikisha kwamba tunapata chakula cha uhakika, au mavuno kwa uhakika, lakini ukiangalia katika Magereza yote tuliyonayo nasema kwamba ni Gereza la Idete pekee ndiyo wenye Kilimo hicho cha Umwagiliaji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hata Bajeti ya mwaka huu, ya maendeleo bado Wizara hii imeendelea kutenga shilingi Bilioni tatu kwa ajili ya Kilimo, jambo ambalo bado litaendelea na utegemezi. Je, Wizara haioni sasa kuna kila sababu ya kuhakikisha kwamba wanaendeleza Kilimo cha Umwagiliaji ili Magereza wetu na Mahabusu waweze kupata chakula? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa takwimu zinaonyesha kwamba mahabusu ni wengi kuliko wafungwa na kwa maana hiyo ndiyo sababu chakula hakitoshi, Je, Serikali haioni sasa kuna kila sababu ya kuhakikisha kwamba mahabusu hasa wale wenye kesi za madai, kwa mfano kesi ya kuiba kuku nakadhalika nakadhalika, hawakai ndani ya Magereza kwa muda mrefu na kupewa shughuli nyingine ili wale wafungwa ambao ndiyo wanapaswa kufanya kazi, kwa sababu tunajua kwamba mahabusu hawaruhusiwi kufanya kazi yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Serikali isihakikishe kwamba wale mahabusu ambao ndiyo wengi kuliko wafungwa wanaondoka kwenye Magereza na kupata kazi nyingine za nje, ili sasa Magereza wetu au wafungwa waweze kufanya kazi na waweze kujitosheleza?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimuhakikishie kwamba mawazo yake aliyoyatoa ni mawazo ya Serikali, na ndiyo maana katika Bajeti yetu ya mwaka huu tumeongeza kwa kutenga fedha hizo kwa ajili ya specifically kwenye eneo la Umwagiliaji, kwa Magereza kwa Kitengule na Isopilo, kwa hiyo siyo Idete peke yake, kuna Magereza mengine. Hata juzi juzi tu nilikwenda kwenye Gereza la Songwe na niliwasisitiza juu ya umuhimu wa kufikia malengo na tukakubaliana malengo hayo yatafikiwa kwa kuhakikisha kwamba wanatumia utaratibu wa umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hii hoja ya Umwagiliaji ni hoja ambayo ni ya msingi kama ulivyozungumza na sisi kama Serikali kupitia Jeshi la Magereza tumeiona na tunaifanyia kazi. Kuhusu suala la pili, kuhusu mahabusu ni kweli hatufurahishwi na msongamano wa mahabusu katika magereza yetu. Kama ambavyo nimejibu kwa kina wakati nikichangia bajeti hapa kwamba Serikali inafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha kwamba tunapunguza idadi ya mahabusu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini moja katika jambo ambalo ni la msingi ambalo nadhani hili wananchi watusaidie pamoja na wewe Mheshimiwa Mbunge ni kuhakikisha kwamba tunajitahidi kadri inavyowezekana kupunguza kufanya makosa. Tutakapopunguza kufanya makosa basi nadhani hata idadi ya mahabusu na wafungwa itapungua wakati ambapo Serikali inaendelea na jitihada nyingine mbalimbali ikiwemo kuharakisha ksi hizi ziweze kusikilizwa haraka. (Makofi)
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa muda mrefu baadhi ya vituo vya mahabusu, mahabusu wamekuwa wakitumia ndoo kama sehemu ya kujihifadhia wanavyokuwa mle ndani kwenye hivyo vituo. Je, kutumia hivyo vindoo ni sehemu ya adhabu? Kwa sababu imekuwa si tu inadhalilisha watu bali ni kukiuka haki za binadamu.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie kwamba kwa kiwango kikubwa matumizi ya ndoo yanapungua na nina takwimu baadaYe nimpatie zinazoonesha kwmaba tumefanya jitihada za kutosha kupunguza matumizi ya ndoo kwa maana ya kuongeza ujenzi vya vyombo katika magereza yetu na kwa hakika kwa kasi hii ambayo tunaenda nayo basi miaka si mingi sana tutaondokana kabisa na tatizo hili la matumizi ya ndoo katika magereza.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri swali dogo la nyongeza. Jeshi la Magereza ni kati ya taasisi ambazo zilipewa kazi maalum ya kuzalisha mbegu na hasa mbegu za nafaka. Ni kwa nini hadi sasa Jeshi la Magereza pamoja na JKT hawafanyi kazi hiyo na tatizo la mbegu ni kubwa na Wizara ya Kilimo wamekiri kwamba jambo hili limekuwa ni zito sana kwao. Ni kwa nini Jeshi la Magereza halifanyi kazi hiyo kikamilifu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango mkakati wetu wa kujitosheleza na kilimo ambao nimezungumza kwamba tumeuandaa na tunauboresha kwa mwaka huu umegusia maeneo mengi. Nimesema kwamba katika mkakati huo kuna malengo ya kuhakikisha kwamba tuna magereza 10 ya kimkakati ya kilimo ambayo yatakuwa yanazalisha chakula cha kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika kutimiza azma hiyo tunabidi tuliwezeshe Jeshi letu la Magereza kifedha ili liweze kutimiza malengo haya na ndiyo maana tunavyozungumza tayari tuna mazungumzo na Benki ya TIB, na TID kwa ajili ya kuweza kupata fedha kwa ajili ya shughuli hizo. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba katika mkakati huo, umeangalia maeneo mengi sio tu katika maeneo ya uzalishaji lakini unapozungumzia uzalishaji pamoja na zana za vitendea kazi, upatikanaji wa matrekta na ongezeko la idadi ya wafungwa katika magereza hayo ya kimkakati lakini pia na maeneo maalum ya kuweza kuhakikisha kwamba tunazalisha mbegu kwa ajili ya uzalishaji. Na hilo tutalianza katika gereza Kitwanga kule Kigoma kwenye Mkoa ambao Mheshimiwa Nsanzugwanko anatoka ili kuweza kwenda sambamba na ile dhana ya Serikali ya kuhakikisha kwamba zao la mchikichi linachukua nafasi yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba wazo lake ni zuri lakini ni sehemu ya mipango ambayo tunayo na mipango hii ambayo tunadhani kwamba ni muhimu sana na imetiliwa mkazo sana na Serikali hii kwa pamoja tukishirikiana tutafanikiwa.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Gereza la Kwa Mngumi lililopo Korogwe linafanya shughuli za kilimo pamoja na mabwawa ya samaki na kwa bahati nzuri Naibu Waziri umeshafika pale tukushukuru kwa kuwasaidia mashine zile za kufyatulia tofali. Je, sasa mtakuwa na mpango wa kuweza kuwasaidia kuwawezesha ili waweze kupanua yale mabwawa pamoja na kilimo kama ambavyo mnaelekeza kwamba magerea waweze kujitegemea katika uzalishaji?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwenye gereza Kwamgumi lazima nikiri na naomba Mheshimiwa Mbunge hili alifikishe kama kuna uongozi ambao binafsi ulinivutia ni uongozi wa gereza la Kwamgumi wamefanya kazi kubwa sana. Ni gereza ambalo wenyewe kwa bidii zao wameweza kukamilisha miradi ya ujenzi wa nyumba nyingi kwa muda mfupi na kukamilisha zote, sio tu kufikia kile kiwango cha lenter lakini kukamilisha nyumba zote. Ndiyo maana ahadi ambayo tulitoa ya kuwapatia zile mashine za matofali tulitimiza kwa haraka na pia tukawaahidi kwamba tutawapatia mashine hizi powertiller kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, nina uhakika kwamba najua jitihada zako za kufuatilia, uendelee kunisumbuasumbua, ahadi yetu iko pale pale na nadhani tutakapoweza kufanikisha kupata powertiller tutazipeleka kwa sababu tunaamini uongozi wa gereza hili unaweza na hii iwe mfano wa magereza mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata katika ule mradi wa samaki, nimeshazungumza na kumuelekeza CDP kuhakikisha kwamba anapeleka fedha haraka ili mradi ule wa samaki wa ufugaji uweze kuendelea. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nakubaliana na wewe kuhusiana na gereza hili, kazi nzuri ambayo inafanya na nikupongeze na wewe kwa kufuatilia na kuwa karibu na Jeshi letu la Magereza kufanikisha malengo hayo. (Makofi)
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Spika, kwanza nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina swali moja tu la nyongeza. Kwa kuwa Mheshimiwa Kuchauka ameuliza maswali ambayo yanahusiana na utendaji kazi wa Jeshi la Polisi, na kwa kuwa yamo masuala ya ukiukwaji wa haki za binadamu. Je, Mheshimiwa Waziri uko tayari sasa ukutane na Mheshimiwa Kuchauka ili aweze kukupa maelezo kama yapo specific uweze kuyafanyia kazi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze kwa swali lake zuri ameuliza suala kitaalam sana na nimuahidi kwamba huo ndiyo utaratibu mzuri kwa pale ambapo wawakilishi wa wananchi kama Wabunge wanapoona kuna tatizo Specifically limejitokeza kwa wananchi wao Serikali tupo kwa sababu hiyo. Kwa hiyo, wakati wowote Mheshimiwa Kuchauka atakapokuwa amerejea tutakuwa tayari kukaa naye tuweze kujua kama anakusudia kuna tatizo mahsusi ambalo analifahamu na uthibitisho wa tatizo hilo ili tuweze kusaidiana kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.
MHE. SAADA MKUYA SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naishukuru Serikali, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri kabisa hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, inaonekana kwamba utaratibu huu wa utoaji wa elimu hauko effective na ndiyo maana haya matukio yameendelea kwa kiasi hicho ambacho Mheshimiwa Waziri amekitaja.

Je, Serikali haioni kama kuna umuhimu wa kubadilisha utaratibu wa utoaji wa elimu kwa wananchi ili wasiendelee kuchukua sheria katika mikono yao?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, inawezekana kabisa yanatokea haya mauaji kwa sababu wananchi wenyewe wanakuwa wanakosa imani na jeshi la polisi na kwamba pengine wale watuhumiwa wakipelekwa katika vituo vyetu vya polisi, kesho yake wanawaona wako mitaani. Kwa hivyo, Serikali ina mkakati gani wa kuliondoa hili miongoni mwa jamii ili kuona kwamba haki inatendeka kwa kila ambaye amefanya kosa na wale ambao hawajafanya makosa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Sasa nijibu maswali yake mawili ya nyongeza kama ifuatavyo; kuhusiana na utaratibu ambao tunatumia nadhani siyo utaratibu mbaya, hata hivyo tunachukua mapendekezo yake kama ni changamoto ili tuangalie jinsi gani tunaweza tukfikia zaidi wananchi waweze kupata taarifa. Hata hivyo nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba wananchi kwa kiasi kikubwa wana imani na jeshi lao la polisi na kutokana na amani na utulivu na upungufu wa takwimu za uhalifu nchini ambao unaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nikiri kwamba kwa wale wananchi ambao wanakosa imani na baadhi ya askari polisi wachache ambao pengine wamekuwa wakitekeleza majukumu yao kinyume na maadili, niwahakikishie wananchi kwamba wakati wote tunavyobaini askari wa aina hiyo tumekuwa tukichukua hatua stahiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo bahati njema ni kwamba askari hao ni wachache, walio wengi wanafanya kazi zao vizuri kwa uadilifu na ndiyo maana nchi yetu inaendelea kuwa salama mpaka sasa hivi.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri na yenye tija ndani yake na pia nakiri kwamba katika kituo cha Dunga ni kweli tayari hili jengo liko katika kukamilisha mwisho wake kuwa zuri sana na lifanye kazi. Niseme maswali yangu mawili ya nyongeza, kwa kuwa jengo la Makunduchi la muda mrefu na mwaka 2015 waliamua polisi kuweka foundation pale ili wapate kituo chao cha uhakika, je sasa swali langu liko hapa; Serikali itamaliza ujenzi huu lini? Swali langu la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwamba eneo la Makunduchi ni eneo la utalii. Kila mwaka kule Makunduchi kunakuwa kunafanywa Mwaka Kogwa, na ukizingatia hata mwaka jana Mheshimiwa Waziri wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikuwa yeye ndiyo mgeni rasmi alikwenda kule. Swali langu lipo hapa, Serikali ina mpango gani wa kuweka ulinzi katika eneo lile hasa sambamba na ujenzi wa vituo vya polisi? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na swali lake la kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika maeneo ambayo tunayaangalia kwa karibu pale ambapo bajeti itakapokaa vizuri tuweze kumaliza ni hilo jengo ambalo amelizungumza la kituo cha polisi Makunduchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kuimarisha ulinzi hasa ukizingatia eneo la Makunduchi ni sekta ya utalii, nimhakikishie kwamba sasa hivi tunavyozungumza tuna mkakati kabambe wa kuimarisha usalama katika maeneo hususan Ukanda wa Pwani wa Zanzibar maeneo ambayo yamekuwa yanatumika kiutalii ili tuweze kuongeza imani ya watalii na wawekezaji katika ukanda huo. Kwa hiyo, tutakapokamilisha mkakati huo, sehemu ya Makunduchi ni moja katika maeneo ambayo yatafaidika.
MHE. HAJI KHATIB KAI: Mheshimiwa Spika, ahsante pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ninayo masuala mawili ya nyongeza. Mkoa wa Kaskazini Pemba una Wilaya mbili za Kipolisi kwa maana ya Wilaya ya Wete na Wilaya ya Micheweni. Ma-OCD hawa walikaimu au wamekaimu zaidi ya miaka mitatu katika nafasi za OCD mwaka 2016 hadi mwaka 2019 na kwa OCD ya Wilaya ya Wete alikaimu nafasi hiyo hadi pale muda wake wa kustaafu ulipomfikia bila kupata maslahi yoyote ya cheo cha OCD. Mheshimiwa Naibu Waziri je, ni utaratibu gani wa Serikali kupitia Wizara yako inaweza ikafidia ma-OCD kama hawao kaimu bila kupata maslahi ya kazi hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili kwa kuwa kukaimu nafasi ya OCD kuna changamoto za kiutendaji na si tu changamoto za kiutendaji hata changamotoza kimazingira. Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kuwa Serikali imekuwa ikitoa kiasi kidogo sana cha mafuta kwa mwezi shilingi 1,000,000 jambo ambalo linamfanya OCD anayekaimu kutumia fedha zake za mfukoni kama Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani na unajua umuhimu wa mafuta kwa Polisi, umesimamiaje Serikali kuhakikisha kwamba inaongeza mafuta ili kuondoa tatizo la mafuta kwa Jeshi la Polisi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimefarijika kuona Mheshimiwa Kai leo amekuwa mtetezi wa Askari wetu na hii inadhihirisha kwamba kumbe Askari wetu wanafanya kazi vizuri sana kule Pemba, wanashirikiana vizuri sana na Mheshimiwa Kai pamoja na Waheshimiwa Wabunge wengine ambao kwa Pemba tunajua asilimia kubwa Wabunge wanatoka Chama gani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo nataka nimjibu kama ifuatavyo. Kwanza hakuna fidia katika kukaimu niseme tu labda nishee pamoja na yeye masikitiko yake kuhusu kukaimu kwa muda mrefu bila kupandishwa cheo. Maana kama amekaimu miaka mitatu maana anaiweza hiyo nafasi lakini nimthibitishie kwamba ili mtu aweze kupanda cheo kuna taratibu ambazo nimezieleza katika jibu la msingi. Na moja katika mambo ambayo yanapelekea vilevile kupandishwa cheo kwa Askari ni kutokana na kuwepo kwa hizo nafasi, sasa inawezekana kwa bahati mbaya katika kipindi hiki ambacho wanakaimu hakukuwepo na fursa za kuweza kupandishwa cheo kwa Askari wahusika. Na kama unavyojua kwamba mahitaji ya Askari ambao wanahitaji kupandishwa cheo ni wengi na wengi vilevile wana sifa, kwa hiyo nafasi ni chache lakini wenye sifa ni wengi na ndio maana tunapandisha kwa awamu.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na bajeti ya mafuta nimuhakikishie kwamba tutajitahidi kadri ya miaka inavyokwenda kulingana na hali ya ukuaji wa uchumi wetu kuongeza bajeti katika Jeshi la Polisi ikiwemo bajeti ya mafuta. Tunatambua kwamba bajeti ya mafuta katika maeneo mengi bado haikidhi lakini tutaendelea kuizidisha katika maeneo yote ikiwemo katika Wilaya ya Micheweni na Wilaya ya Wete ili hatimaye tuweze kuhakikisha kwamba Askari wetu wanafanya kazi zao vizuri na kwa ufanisi.
MHE. RUKIA KASSIM AHMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini bado nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa wakimbizi kutoka Somalia pamoja na wakimbizi kutoka Ethiopia, hawawezi kuingia nchini mpaka wapitie nchi ya Kenya. Je, Serikali haioni kwamba ipo haja kwa kushirikiana na nchi ya Kenya kuwazuia wakimbizi hawa wasiingie katika nchi yetu?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa ukiacha wakimbizi walioko katika magereza, kuna wakimbizi ambao wako katika kambi za wakimbizi. Kwa mfano, Kadutu - Kigoma, Ulyankulu - Tabora pamoja na kambi nyingine. Wakimbizi hawa wana tabia ya kuzaana sana na kwa kweli idadi yake inaongezeka ukizingatia miaka 10 iliyopita sasa hivi wako mara mbili zaidi.

Je, Serikali, kwa kuwa nchi zao tayari zina amani, wana mkakati gani wa kuwarejesha wakimbizi hawa ili wasiendelee kuzaana hapa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na rai yake ya kwanza, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba rai yake ambayo ameitoa tumeshaanza kuifanyia kazi. Hivi karibuni tulikuwa tuna kikao kilichoshirikisha ngazi ya Mawaziri wa Tanzania, Kenya na Ethiopia, ili kujadiliana namna ya pamoja ya kudhibiti wimbi la wahamiaji hawa hususan wanaotokea Ethiopia ambao wanaingia kwa wingi kupitia Kenya na jambo hilo limeleta mafanikio makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusu suala la wakimbizi kurudi makwao, kama ambavyo nimejibu swali langu la msingi kwamba kwa takwimu za mpaka Aprili, 2019 tuna zaidi ya wakimbizi 99,000 ambao wameamua kurudi kwa hiari. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba nalo hili ni jambo ambalo tumeshaanza kulifanyia kazi na tunaendelea nalo. Kwa sababu ni kweli kama alivyozungumza Mbunge kwamba hali ya amani katika nchi hizi imetulia, hakuna sababu ya wakimbizi hawa kuendelea kubaki katika nchi yetu kwa kipindi hiki.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa Wilaya ya Tanganyika ni jiografia yake ni ngumu sana na Makao Makuu ya Wilaya yako Majalila, lakini OCD anakaa Mishamo na ukizingatia jiografia ile ni pana sana, watu wa Karema wanashindwa kwenda Mishamo.

Je, Serikali itaweka mikakati gani kuhakikisha basi kile kituo cha polisi hata kama bado fedha hazijapatikanika, lakini kituo kiwekwe center ili watu wote katika Wilaya ile waweze kujua kituo chao cha polisi kiko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kutokana na jiografia mbaya ya Wilaya ya Tanganyika, je, ni lini Serikali itatuletea magari ya polisi kwa ajili ya patrol kwa sababu kuna misitu mingi, mikubwa sana katika wilaya ile, sasa majambazi wako wengi na uhalifu unafanyika mara kwa mara. Serikali itatuletea lini magari kwa ajili ya patrol ya Wilaya yetu ya Tanganyika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani hoja ya Mheshimiwa Lupembe ni ya msingi, na kwa kuzingatia msingi wa hoja yake, sasa tutalifuatilia kwa karibu tuone lile eneo ambalo Halmashauri imekusudia kulitenga kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi, liwe Majalila kama ambavyo amependekeza ambapo ni Makao Makuu ya Wilaya. Sambamba na ule ujenzi wa nyumba nne ambazo mchakato wake unaendelea wa ujenzi katika eneo hilo la Wilaya ya Tanganyika, liende sambamba pamoja na rai ambayo Mheshimiwa Mbunge ametoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusianana na magari nayo, kwa sasa hatuna magari mapya ambayo yameingia, lakini kwa kutambua umuhimu wa jiografia ya Tanganyika kama alivyoeleza Mheshimiwa Mbunge, basi suala lake tumelichukua na pale ambapo magari yatapatikana basi tutazingatia.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwanza nisikitike sana kwa majibu ambayo yametolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, uthaminishaji wa maeneo yale umefanyika zaidi ya miakakaribia miaka minne, na kwa mujibu wa sheria inabidi warudi tena kufanya uthaminishaji upya.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama wameshindwa huu wa kwanza kulipa, watawezaje kufanya uthaminishaji wa awamu ya pili? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, je, mko tayari kuwatangazia wananchi wa Rwenkorongo pale Kyerwa kuwa mmeshindwa kuwalipa ili waweze kuendeleza maeneo yao? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa sababu inaonesha moja kwa moja mmeshindwa kuwalipa wananchi, mko tayari kuongea na Halmashauri ili iwatafutie maeneo mengine ambayo hayatahitaji fidia? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haijashindwa kulipa fidia wananchi na Serikali ina nia ya kulipa fidia wananchi. Kama ambavyo nimezungumza katika majibu yangu ya msingi, ni kwamba fidia hizi, maeneo haya ni mengi ambayo yanahitaji kulipwa fidia na suala hili haliwezi likafanyika kwa wakati mmoja.

Kwa hiyo, ninalirudia jibu langu la msingi ambalo nimejibu kwamba fidia za eneo hili ambalo lilichukuliwa kwa ajili ya magereza na maeneo mengine, najua kuna Waheshimiwa Wabunge ambao maeneo yao mengine vilevile yanahitaji kulipwa fidia, zitalipwa kwa awamu kadri hali ya kifedha na kibajeti itakavyoruhusu.
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vitambulisho hivi vya Taifa ni muhimu kwa maendeleo na vinatambuliwa, hata mtu akiwa nje ya nchi vitambulisho hivi vinatabuliwa. Sasa kwa sababu vitambulisho hivi ni muhimu lakini ukitazama zoezi linaloendelea linasuasua na hususan kwa wananchi wa kawaida, maana watu ambao wamevipata ni watu kama sisi Wabunge na watumishi wa Serikali, wananchi wa kawaida kwa kweli hawajavipata.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali langu, Mheshimiwa Waziri amesema Serikali inaendelea kukamilisha usajili wa watu wenye sifa kwa kuchukua alama za vidole, picha na saini za kielektroniki. Kwa kuwa katika Wilaya ya Kakonko takribani kata tano kati ya 13 wamekwishakamilisha zoezi hili, kwa nini sasa vitambulisho hivi hawavipati? Swali la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ninapenda kujua sasa, mara ya mwisho Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani alisema Watanzania takribani milioni 16 wamekwishapata vitambulisho, je, hivi sasa ni wananchi wangapi wa Tanzania wakiwemo wale wa vijijini, wote kwa ujumla wamekwishapata vitambulisho hivi muhimu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Chiza, ni miongoni mwa Wabunge ambao wamekuwa wakiuliza maswali yao kwa umakini wa hali ya juu. Lakini kuhusiana na hoja zake mbili kwa pamoja, nataka nimjibu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Nabu Spika, moja, nina mashaka juu ya takwimu ambazo amezitoa akimkariri Mheshimiwa Waziri kwa sababu uhalisia uliopo ni kwamba mpaka sasa hivi tumeshatoa vitambulisho takribani milioni tano huku vitambulisho takribani milioni 13 vikiwa vipo katika hatua za mwisho kutolewa, wakati malengo yetu mpaka itakapofika mwezi Desemba ni kama milioni 24.2. Kwa hiyo utaona kwamba tupo vizuri kwa sababu milioni 18 ni kama vile tayari process yake imekamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nikijibu swali lake la mwanzo sasa kwamba inawezekana miongoni mwa watu ambao wananchi wake wa Kakonko ambao hawakupata vitambulisho ni hawa ambao vitambulisho vyao ni hivi milioni 13 ambavyo vinafanyiwa kazi. Kwa hiyo nimuombe Mheshimiwa Mbunge avute subira, muda si mrefu vitambulisho hivi vitatolewa na wananchi wake wengi nina uhakika watakuwa wamepata vitambulisho hivyo kama watakuwa wamekamilisha, kama nilivyosema, processes zote za kuweza kujisajili.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza naipongeza Serikali kwa majibu mazuri waliyoyatoa, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, kwa kuwa utafiti na maeneo mengi yanaonyesha kwamba bodaboda wengu katika nchi na hasa kwa Mkoa wa Mara wanafanya kazi ile bila kupata mafunzo rasmi ya kazi yao. Sasa ni lini Serikali itatoa mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu kwa vijana wote wanaoendesha bodabora katika Mkoa wa Mara?

Swali la pili, kwa jimbo langu la Bunda na hasa Wilaya ya Bunda kumekuwepo na usumbufu mkubwa wa bodaboda wakati wa siku za minada, hasa Mnada wa Mgeta, Bitalaguru na mnada wa Bulamba. Sasa je, Waziri uko tayari kuja Bunda na hasa Jimbo la Bunda kukutana na viongozi wa bodaboda na watalaam wako wa traffic katika jimbo la Bunda ilikuona namna gani ya kutatua kero hiyo hasa siku za mnada inakuwa kama inafanya operation?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeza sana Mheshimiwa Mwita Getere, nakumbuka niliwahi kufanya ziara katika jimbo lake tulishirikiana kwa karibu sana kuhakikisha kwamba changamoto ambazo zinawakabili wananchi wake zinazohusu vyombo vyetu vinavyohusu Mambo ya Ndani ya Nchi tunavikabili.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie kwamba hata katika hili suala ambalo amelizungumza la usumbufu wa wananchi wake kwenye minada na amenitaka niende basi namhakikishia kwamba nitafanya hivyo kama ambavyo nilifanya wakati ule.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusiana na mafunzo kwa Mkoa wa Mara tumekuwa na utaratibu mzuri kupitia Jeshi la Usalama barabarani kwa kutoa mafunzo watumiaji wa vyombo vya usafiri barabarani. Hata hivyo nichukue nafasi hii kumhakikishi kwamba kwa kuwa nitakwenda katika jimbo lake basi tunaweza kushauriana kuwa mpango mahususi wa jimbo lake kuhusiana na utararibu wa kutoa elimu ili kuepusha usumbufu kwa wananchi wake au hususani vijana wanaendesha bodaboda waweze kutii sheria na kuepusha usumbufu na hatimaye kupunguza ajali zinaendelea kupoteza maisha ya wananchi.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, katika Wilaya ya Mbozi kumekuwa na usumbufu mkubwa sana kwa vijana wa bodaboda ambao wameamua kujiajiri ili kuweza kujikimu katika maisha na wamekuwa wakinyanganywa pikipiki hasa katika Mji Mdogo wa Mlowo pamoja na Mji wa Vwawa na maeneo mengine wamekuwa wakisumbuliwa sana na pikipiki zao zimekuwa zikichukuliwa kupelekwa Vituo vya Polisi.

Je, Serikali haioni kwamba huko ni kuwanyanyasa vijana ambao wameamua kujiajiri kupitia kazi hii ya bodaboda inayo wapatia kipato wao na wengine wameamua kuachana na maisha yao ya awali ambao hayakuwa mazuri wameamua kujiajiri. Sasa ni lini Serikali itakataza askari wasiwanyanyase vijana hao ambao wanafanya kazi hii ya bodaboda katika Wilaya Mbozi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, hatukubali kuona wala haturuhusu kuona askari wakinyanyasa wananchi. Si jukumu la askari kunyanyasa wananchi, lakini kuhusiana na suala ambalo amelizungumza kuhusiana na jimbo la Mbozi kuhusu vijana hawa ambao anadai kwamba wananyanyaswa na waendesha bodaboda nisema yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza hili tulishalitolea maelekezo hapa Bungeni kwamba kuna aina ya makosa ambayo pikipiki zikikamatwa zinakuwa katika Vituo vya Polisi kuanzia sasa na tumeshatoa waraka huo katika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi ili wautekeleze. Sasa sina hakika kama hawa anaowazungumzia Mheshimiwa Haonga wapo katika yale makosa ambayo tumeyaruhusu waweze kukamatwa ama katika makosa ambayo tulishakata yasikamatwe.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninachoweza kumhakikishia ni kwamba tutafuatilia kujua kama yatakuwa makosa ambayo tulishaelekeza yasikamatwe vijana hao basi tutachukua hatua kwa kushindwa kutekeleza maelekezo ya Wizara. Lakini kama itakuwa ni makosa ambayo yanaruhusika na tumeruhusu waweze kukamatwa basi tutamuelimisha Mheshimiwa Haonga ili aweze kuelimisha wananchi wake wafahamu na waepuke kufanya makosa kama hayo.
MHE. BHAGWANJI MAGANLAL MEISURIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nataka nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri, hao watu wa bodaboda wana tabia moja mbaya sana, na mimi wameshafanyiwa wageni wangu, wanapora simu, halafu wanakimbia na hapa juzi katika eneo la Area D ninapokaa mimi, mama mmoja alikuwa na simu wamekuja watu wa bodaboda wamepora, sasa hatua gani Mheshimiwa Rais anawapenda wanyonge watu wa bodaboda lakini tabia hii ni mbaya sana kwa kupora.

Mheshimiwa Spika, kesho watakuwa na bastora watakwenda majumbani au madukani, kwa hiyo, mimi naomba Mheshimiwa Naibu Waziri atuambie ni sheria gani hawa watu wa bodaboda wanafanya tabia hiyo mbaya kwa kupora simu pamoja na begi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, si sahihi nadhani kuwajumuisha waendesha bodaboda na matukio ya wizi, waendesha bodaboda ni raia ambao wanafanya kazi zao, wanapaswa kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria ya kujipatia riziki ambazo zimeruhusiwa kisheria ni shughuli za kihalali.

Mheshimiwa Spika, sasa kama kuna watu ambao wanatumia pikipiki ama hiyo pikipiki ya kawaida ama iwe bodaboda kwa ajili ya uporaji hao ni wahalifu kama wahalifu wengine na kwa hiyo basi kama ambavyo ilivyo kawaida na desturi ya Jeshi letu la Polisi kuweza kukabiliana na wahalifu imekuwa ikifanya hivyo kushughulika na watu ambao wakitumia pikipiki ama bodaboda kwa ajili ya kupora wananchi na tutaendelea kufanya hivyo kuwashughulikia bila huruma wale wote ambao wanatumia pikipiki ama bodaboda kwa ajili ya kufanya uporaji.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kutokana na uhaba wa ajira na ukosefu wa mitaji, vijana wengi wanaomaliza shule sasa hivi wameiona kazi ya bodaboda kama ni kazi ambayo inawaingizia kipato. Jimboni kwangu ukienda Mamsera pale, Mengwe, Mkuu, Useri na Tarakea vijana waliomaliza chuo kikuu na form six wamejiingiza katika biashara hii na inawaletea kipato kizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambasamba na hilo, kuna vijana wengine ambao tabia zao siyo njema sana, nao wamejiingiza kufanya sasa vijana wote wa bodaboda waonekane kwamba ni vijana ambao hawafai na baadhi ya polisi wanalalamikiwa kufanya hii kazi ya bodaboda ionekane ngumu zaidi kwa kuchukua rushwa na kuwabambikia makosa.

Je, Jeshi la Polisi au Wizara hamuoni sasa kutokana na ukubwa wa kazi hii ya bodaboda kuweka polisi maalum, trafiki maalum kabisa katika kila Kituo ambaye kazi yake itakuwa ni ku-deal tu na bodaboda ili kuweza kupunguza haya matatizo yao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, Nakubaliana kabisa na Mheshimiwa Selasini kwamba biashara ya bodaboda ni biashara ambayo ni kama biashara nyingine na ndiyo maana mara nyingi sana tumekuwa tukiwaelimisha watumiaji hasa viongozi wa vijiwe hivi vya bodaboda kwamba watusaidie kuwaelimisha wenzao ambao wanafanya kazi hii kwa pamoja ama ambao wanawaongoza ili biashara ya bodaboda isivunjiwe heshima ikaonekana kwamba ni kazi ya kihuni.

Mheshimiwa Spika, na kwa kufanya hivyo nadhani itasaidia sana kuondoa taswira mbaya iliyopo kwa baadhi ya wananchi mbele ya waendesha bodaboda ama biashara za bodaboda. Sasa kuhusiana na hoja yake kwamba tuweke askari maalum, sisi tuna Kitengo cha Usalama Barabarani ambacho kinashughulika na masuala yote yanayohusu usalama barabarani yakiwemo ya waendesha bodaboda na kazi hiyo imekuwa ikifanyika kwa ufanisi mkubwa. Kwa hiyo sioni kama kuna haja ya kusema tubague labda bodaboda iwe mbali, magari ya daladala yawe mbali, mabasi yawe mbali, nahisi kwamba utaratibu uliopo unakidhi mahitaji na tutaendelea kuboresha pale ambapo tutaona kuna mapungufu katika kusimamia Sheria za Usalama Barabarani kwa bodaboda na vyombo vingine.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii.

Mheshimiwa Spika, bodaboda ni kitu chema na bodaboda imerahisisha usafiri, bodaboda imesaidia sana kuleta ajira kwa vijana wa Taifa letu la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio hayo, lakini kuna changamoto zinazoweza kujitokeza pale inapotokea bodaboda imesababisha ajali barabarani, baadhi yao kwa muda mfupi wanajaa eneo la tukio na hatimaye kuweza kuchukua hatua za papo kwa papo na matokeo yake wanaweza kusababisha vifo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, je, Serikali inachukua hatua gani juu ya kutoa elimu kwa waendesha bodaboda kwamba wasichukue hatua za mkononi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salma Kikwete, swali zuri na muhimu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli matukio kama haya yamekuwa yakitokea, na ni matukio ambayo yanasikitisha sana na hayakubaliki katika jamii iliyostaarabika kama jamii ya Watanzania na kwa hiyo, naendelea kutoa wito hapa, kwanza nichukue fursa hii nikitumia jukwaa hili la Bunge kama ni moja katika njia ya elimu kwa waendesha bodaboda wote nchini kuepuka kuchukua sheria mkononi na wale wote ambao wamekuwa wakifanya hivyo hatma yao haijawa njema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo sidhani kama kuna mwendesha bodaboda ambaye anataka hatma ya maisha yake iishie gerezani au iishie kwa kuhukumiwa hukumu ya kunyongwa kwa kusababisha mauaji yasiyokuwa na lazima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niendee kusisitiza kwamba utaratibu wetu wa utoaji wa elimu kwa bodaboda utiliwe maanani na mkazo zaidi katika eneo la kuhakikisha kwamba waendesha bodaboda hawatumii, hawachukui sheria mkononi inapotokea matatizo ya usalama barabarani na kuacha vyombo na sheria za nchi zifuate mkondo wake. (Makofi)
MHE. KEMILEMBE J. LWOTA: Mheshimiwa Spika, ahsante nakushukuru kwa kuweza kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, suala la ajali za bodaboda siyo kwa Mkoa wa Mara tu, ni Tanzania nzima kwa ujumla wake. Bodaboda hawa wengi wao wanakata third part insurance ambayo kimsingi inatakiwa iwasaidie pale wanapopata matatizo lakini kiuhalisia insurance hii haiwasaidii chochote bodaboda hawa wanapopata matatizo.

Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kukaa na hawa watu wa insurance ili baadhi ya fedha inayotozwa/ wanayolipa hawa watu wa bodaboda iweze kwenda kwenye Halmashauri zetu ili waweze kupata msaada kwenye hospitali ambapo hospitali hizi ndiyo zinawapokea na kuwatibu watu hawa? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, wazo lake linafikirika na kwa hiyo basi tunalichukua, tulitafakari.
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru tena kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Mtera lina kata 22, na lina vijiji zaidi ya 60 na kitu, Mheshimiwa Naibu Waziri kwenye jibu lake la msingi anasema wana mpango wa kujenga vituo kila kata, haelezi mpango huo unaanza lini? Lakini Jimbo la Mtera lina Tarafa tatu.

Swali langu la kwanza dogo la nyongeza linasema, kama kwenye Tarafa tu hawajajenga Kituo hata kimoja, je hiyo kwenye kata itawezekana? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, barabara kubwa ya Iringa - Dodoma inayopita kwenye Jimbo la Mtera, Kibakwe, Isimani Waheshimiwa Wabunge wengi na Mawaziri wanapita njia ile lakini haina Kituo cha Polisi hata kimoja chenye gari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, matokeo yake ajali zote kubwa zinazotokea njia ile, polisi inawachukua muda mrefu sana kufika, kwa mfano wiki mbili zilizopita ilitokea ajali mbaya sana mama mmoja mzazi alipoteza maisha, nesi alipoteza maisha, pamoja na wasindikizaji, polisi walikuwa wanakuja wengine na lori, fuso iliwachukua muda sana kwenda kumaliza tatizo pale.

Je, Serikali ni basi itakipatia Kituo cha Mvumi Misheni gari, walau liweze kusaidia kufanya mzunguko katika barabara hiyo kubwa? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza linahusu ujenzi wa Kituo cha Polisi kutokana na majibu yangu ya msingi kwamba nilimwambia tuna mpango wa kujenga vituo vya polisi nchi nzima katika kila kata.

Mheshimiwa Spika, nataka nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba ujenzi huu au mpango huu wa ujenzi wa vituo ni mchakato ambao mchakato unahusisha pia upatikanaji wa rasilimali fedha.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo dhamira tunayo, sababu tunayo na uwezo pia tunao, lakini uwezo huo utaenda sambasamba na kadri ambavyo hali ya kibajeti itaruhusu kwa awamu, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ujenzi wa Kituo cha Polisi katika Kata ya Mvumi Misheni utapewa kipaumbele pale ambapo bajeti itakaa vizuri na mpango wetu utaanza utekelezaji wake mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Lusinde kwa sababu inaonekana ni Mbunge ambaye hapendi kujipa ujiko mwenyewe, lakini kiukweli hili jambo tulilizungumza mimi na yeye pamoja na Mheshimiwa Chumi ambao Majimbo yao yanapakana katika eneo hilo na wenyewe wao walikuja na wazo zuri sana la upatikanaji wa magari mawili katika eneo hilo na mchakato huo umeshaanza, naamini kabisa mimi nikishirikiana na wao tutafanikisha kupata hayo magari mawili kwa utaratibu ambao tumeuzungumza mimi, yeye pamoja na Mheshimiwa Chumi na wananchi wasikie waone jitihada za Mheshimiwa Lusinde katika hili na manufaa yake watayaona muda siyo mrefu kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu. (Makofi)
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza Mheshimiwa Naibu Waziri je, yupo tayari kuwaeleza Watanzania ni namna gani wanatakiwa kuzitumia alama za barabarani ikiwemo pamoja na zebra cross kwa sababu sasa hivi hata kama hakuna mtu lakini kuna askari wanasimama maeneo hayo na kuwavizia watu ili wakipita wawakamate sehemu inayofuata? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kumekuwa na tabia mbaya sana ya askari wetu wa usalama barabarani kwa vijana wetu wa bodaboda na hii nadhani ni Tanzania nzima, wanapotaka kuwakamata huwa wanakimbiza na kuwachapa viboko migongani na wengine kuwavuta na wale vijana wanadondoka chini wanaumia. Ni nini tamko la Serikali kuhusu suala hili kwa sababu nia ni kuzuia ajali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na elimu juu ya matumizi ya alama barabarani nadhani alama za barabarani ziko nyingi, kwa hiyo, kuanza kuzungumzia elimu hapa itachukua muda mrefu, lakini yeye ametoa mfano wa hii zebra cross ni kwamba utaratibu wake unatakiwa unapofika kwenye zebra cross unaangalia kulia, unaangalia kushoto, unaangalia kulia tena halafu unakata kwa mwendo wa kawaida si kwa kukimbia wala mwendo wa taratibu na huo ndio utaratibu na gari ambapo inapopita inapokuja inatakiwa itakapoona mtu amegusa kwenye ile zebra cross isimame na kumsubiri na sio kuongeza speed ili yule mtu asivuke.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kuhusiana na swali lake la pili kwamba askari wanachapa viboko, askari wa Jeshi la Polisi hawachapi viboko, mimi hiyo sijawahi kuona pahala au kusikia kwamba kuna askari wa Jeshi la Polisi amechapa viboko badoboda. Kwa hiyo naomba nisizungumze hatua kwa sababu hakuna hilo tukio ambalo tumelipokea kuhusiana na tuhuma za askari polisi kuchapa viboko waendesha bodaboda. (Makofi)
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na kwa dhati kabisa nitambue kazi nzuri na kubwa inayofanywa na Jeshi la Polisi nchini, lakini majibu haya haya hayaakisi hali halisi iliyopo kwenye maeneo yetu kule. Magari mengi ya Polisi yanapoharibika hutegemea zaidi hisani ya wadau mbalimbali hasa Wabunge kuweza kuyatengeneza. Jambo hili linaathiri sana utendaji wa Jeshi letu la Polisi.

Nini sasa mkakati wa Serikali kuhakikisha utaratibu huu unatekelezwa na magari ya Polisi yanatengenezwa katika mazingira mazuri kama utaratibu ulivyoelekezwa na Mheshimiwa Naibu Waziri?

Swali la pili; kama ilivyo kwa tatizo la magari vituo vyetu vya Polisi vinakabiliwa na upungufu mkubwa sana wa vitendea kazi vya kila siku kama mafuta ya magari, karatasi, wino na kadhalika. Jambo hili linaathiri sana utendaji wa kila siku wa Jeshi letu la Polisi lakini hata kuchelewesha haki za wananchi wa kawaida kule kwenye vituo vyetu vya Polisi.

Nini sasa Mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba inawezesha Jeshi letu kupata vifaa vya utendaji kazi vya kila siku kama hivi ili waweze kutimiza wajibu wao wa kila siku?

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto kubwa ambayo inagusa maeneo yote mawili aliyozungumza ni ufinyu wa bajeti. Uwezo wa Jeshi letu la Polisi kutengeneza magari kwa maana ya kiutalam tunao lakini wakati mwingine magari haya wanapohitaji kutengeneza yanahitaji ununuzi wa vipuli na matengenezo makubwa ambayo yanahitaji fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kuwapongeza wadau wote mbalilmbali ikiwemo Waheshimiwa Wabunge ambao wameona changamoto hii na wameona umuhimu wa kusaidiana na Serikali kukabiliana na changamoto ya ubovu wa magari yetu katika Jeshi la Polisi. Ninawatia moyo waendelee hivyo nasi Serikali pamoja na Jeshi la Polisi mbali ya kuwa na Serikali inaendelea kuongeza bajeti la Jeshi la Polisi kadri ya hali inavyoruhusu lakini tumekuwa tukibuni mbinu mbalimbali za kuweza kuyarekebisha magari haya yaweze kuwa bora zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna magari katika Mikoa mbalimbali ambayo tumefanya matengenezo kwa njia hii za ushirikishaji wa wadau. Hii inakwenda sambamba na hoja yake ya pili ambayo inahusu vitendea kazi kwa ajili ya Jeshi la Polisi nami nikuhakikishie kwamba kama ambavyo sote tunatambua jinsi ambavyo uchumi wetu unavyoendelea kukua vizuri hivyo Serikali kuongeza uwezo wa kuhudumia taasisi zake ni imani yangu kwamba changamoto hizi zitaendelea kupungua mwaka hadi mwaka. (Makofi)
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza. Namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, pamoja na majibu yake nina maswali mawili madogo ya nyongeza:

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ambayo tumeayaombea vituo vya Polisi yapo mbali sana na vituo ambavyo Mheshimiwa Waziri amevisema ambavyo pia ni chakavu sana. Maeneo hayo ofisi ya OCD pia ina magari matatu tu ambayo inahudumia Halmashauri ya Singida DC pamoja na Manispaa. Je, Wizara ipo tayari sasa wakati tukisubiri ujenzi wa hivyo vituo kuongeza vitendeakazi magari pamoja na mafuta ili Askari wetu waweze kufanya kazi vizuri?(Makofi)

Swali la pili; Jeshi letu la Polisi hasa Singida lina watumishi wachache mno ambao wanatakiwa kutoa huduma katika Halmashauri zetu mbili. Je, Wizara ipo tayari sasa kuongeza idadi ya watumishi hasa Askari katika Ofisi ya OCD Singida ili waweze kutoa hudama bora kwa wananchi?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kweli Jimbo la Singida Kaskazini linahudumiwa na OCD wa Singida Mjini na ni dhahili kabisa kwa maana hiyo naweza hoja ya Mheshimiwa Mbunge inahitaji kufuatiliwa na kufanyiwa kazi. Kwa sababu Majimbo mawili eneo lake la kijiografia ni kubwa kwa hiyo nimhakishie Mheshimiwa Mbunge tunalichukua kwa uzito ingawa hatuwezi kumuahidi sasa hivi kwamba tutampatia gari kwa sababu gari hizo hazipo lakini pale ambao zitapatikana tutazingatia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hili la kuongeza fedha kwa ajili ya huduma zingine ikiwemo mafuta, hili narudia kama ambavyo nimejibu swali ambalo limepita kwamba kadri ambavyo hali ya kibajeti itaruhusu basi bajeti ya Polisi ikiwemo huduma ya mafuta itaongezwa katika maeneo yote ni changamoto nchi nzima, ninaamini kabisa hilo Serikali tunalitambua na tumekuwa tukilifanyia kazi kwa kadri hali inavyoruhusu na ninaamini kabisa hali itakuwa nzuri zaidi siku zinavyokwenda mbele kutokana na hali ya uchumi wetu inavyokuwa vizuri.
MHE. DKT. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali ni la muda mrefu na majibu pia ni ya zamani, lakini hali ya mauaji ya vijana wa bodaboda katika Wilaya Masasi bado inaendelea mpaka sasa. Hata wiki tatu zilizopita tumezika vijana wawili.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba swali la kwanza liwe Mheshimiwa Waziri atoe kauli sasa kwa kuwa Wasaidizi wake kule wameshindwa kudhibiti mauaji haya kauli yake ni ipi ili kuhakikisha kwamba vijana hawa hawapotezi maisha?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Mheshimiwa Waziri naomba atueleze ni watuhumiwa wangapi mpaka sasa wamekwishafikishwa Mahakamani kwa makosa haya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kauli ya Serikali kulingana na hoja ambayo ameizungumza ni kwamba tutaendelea kuhakikisha kwamba tunadhibiti mauaji nchi nzima, hata mimi na yeye Mheshimiwa Mbunge kwa sababu anaonekana kutokuridhika na takwimu ambazo mimi naamini ni sahihi za mauaji ya watu wanne kwa mwaka 2018/2019, nitakuwa tayari tupange tuende katika Wilaya yake tuweze kuthibitisha hilo, nilifika katika Wilaya ya Masasi lakini tutakwenda tena kwa ajili ya suala hili kwa sababu suala linalogusa uhai wa Watanzania ni suala ambalo linahitajika kuchukuliwa kwa uzito unaostahiki. Kwa hiyo, ili kuweza kujua kama ana taarifa ambazo hazijafika katika Jeshi la Polisi tutazichukua na kuzifanyia kazi kwa pamoja na Jeshi la Polisi katika eneo husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuhusiana na swali lake la kutaka kujua idadi ya watu ambao wamechukiliwa hatua, kwa wale watu wanne ambao nimewazungumza tayari watu wawili wameshakamatwa na wapo katika hatua mbalimbali za kisheria. (Makofi)
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri, lakini chanzo cha kituo kile kuchomwa ni mgogoro wa ugomvi wa usalama barabarani kati ya Askari pamoja na bodaboda, hii ndiyo imekuwa tabia ya Askari wasiokuwa wa usalama barabarani kuwakamata bodaboda na kuwapiga bila kuwaeleza makosa yao.

Je, nini kauli ya Serikali kuhusiana na tabia hiyo ya Askari wasiokuwa wa usalama barabarani kuwakamata bodaboda na kuwapiga bila kuwaeleza makosa yao?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Jimbo la Tunduru Kusini limepakana na Msumbiji likiwa na Tarafa tatu. Tarafa ya Namasakata tangu imeundwa haijawahi kuwa na Kituo cha Polisi. Je, Serikali haioni haja sasa ya kupeleka Kituo cha Polisi Misechela na Namasakate yenyewe kwa kituo cha polisi ili kuwahudumia wananchi wa Jimbo la Tunduru Kusini na Tarafa ya Namasakata kwa ujumla.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza hatuwezi kuhalalisha jambo lolote na vitendo vya uchomaji vituo vya Polisi, kwa hiyo hata kama kulikuwa kuna matatizo kati ya bodaboda iwe na Askari wa Usalama barabarani ama awe Askari yeyote basi haihalalishi uchomaji wa kituo cha polisi, hilo moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na hoja yake kwamba kuna watu ambao siyo Askari wa Usalama Barabarani wanawapiga bodaboda. Niliwahi kujibu swali hili siku chache zilizopita na nilieleza kwamba hatujapata taarifa ya kuona Askari Polisi wakipiga bodaboda na kama kuna taarifa hizo basi ni vema tukapatiwa ili tuzifanyie kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Mbunge amekiri kwamba wanaofanya hivyo siyo Askari wa Usalama Barabarani, kwa sababu tunaamini askari wa usalama barabarani wamepata mafunzo na weledi wa kutosha katika kutekeleza majukumu yao, Askari wa aina nyingine yoyote ama watu wa aina nyingine yoyote ambao wanafanya vitendo kama hivyo kama wapo kauli ya Serikali ni kwamba ni kinyume na utaratibu hivyo watumie weledi katika kuhakikisha kwamba wanawakamata wanaovunja sheria ikiwemo hawa waendesha bodaboda.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusu maeneo hayo mawili aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge ambapo anataka kujua ni lini tutajenga kituo cha polisi. Jibu ni kwamba katika maeneo yote nchini tutajenga kuanzia kwenye wilaya hata ngazi ya kata ikiwemo maeneo ambayo ameyataja Mheshimiwa Mbunge pale ambapo hali ya kifedha itaruhusu.
MHE. USSI SALUM PONDEZA AMJADI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini nina swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, amesema kuna upungufu wa maaskari lakini katika Jimbo langu la Chumbuni tuna matatizo sana ya kupatiwa kituo cha polisi. Kuna kituo kidogo cha Polisi ambacho kinahudumia majimbo zaidi ya manne ya Shaurimoyo, Mwera, Mto Pepo na Chumbuni yenyewe ambao watu wanaoishi pale ni zaidi ya 67,000.

Mheshimiwa Spika, nimekuwa nikiuliza zaidi ya mara saba au nane humu ndani ya Bunge na nimepata ahadi mara nyingi kutoka kwa Mheshimiwa Waziri au Wizara kuwa watafanyia matengenezo au watakiboresha kituo kile kidogo. Je, yupo tayari kuniahidi au kuiahidi hadhara hii kuwa watakijenga kituo kile kwa kushirikiana na Mbunge?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza kwa dhamira yake ya dhati ya kushiriki katika ukarabati wa kituo hicho. Nimhakikishie kwamba tupo tayari kushirikiana naye kuhakikisha kwamba kituo hiki kinafanyiwa matengenezo ili kiweze kutumika vizuri zaidi.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Polisi Yaeda Chini kimejengwa na wananchi mpaka kufikia mwisho, kilichobaki ni nyumba za askari. Je, Serikali ipo tayari kuleta fedha za kujenga nyumba za askari ili kituo hicho kifunguliwe?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Flatei, Mbunge wa Mbulu Vijiji, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Flatei kwa jitihada zake kubwa sana. Niliwahi kwenda huko tukashirikiana naye katika kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto hii na ameichukua kwa haraka sana na kuifanyia kazi, amejenga kituo kizuri tu.

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Flatei kwamba Serikali inazithamini sana jitihada zake na za wananchi wa jimbo hilo na hivyo basi katika mkakati wetu wa nyumba za askari nchi zima, tutakapokuwa tumefanikiwa kupata uwezo basi tutashirikina naye vilevile kutatua tatizo hilo la makazi ya askari ili kituo hicho kiwezi kufanya kazi vizuri zaidi. Ahsante.
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini, sambasamba na majibu yake ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, tunatambua kwamba bodaboda baadhi yao ni kweli huwa wanafanya makosa barabarani na wanapofanya makosa barabarani wanatozwa faini ya Sh.30,000, lakini hata magari pia wanapofanya makosa barabarani ambako ni matairi manne pia hutozwa faini ya Sh.30,000. Sasa kwa kuwa tozo hizi zinatokana na Kanuni na Mheshimiwa Waziri anayo mamlaka ya kubadilisha Kanuni wakati wowote, swali langu, kwa nini sasa Waziri asibadilishe Kanuni ili bodaboda yenye matairi mawili pamoja bajaji yenye matairi matatu waweze kupunguziwa tozo hii ya Sh.30,000 na hatimaye ishuke chini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, tunafahamu kwamba SUMATRA huwa wanatoza tozo ya Sh.22,000 kwa bodaboda, lakini Sh.25,000 kwa hiace na Sh.120,000 kwa mabasi. Ada hii imekuwa ni kubwa sana kwa watu wa bodaboda ukigawanya 25,000 kwa hiace abiria wako 15, ukigawanya hiyo unaipata kila abiria mmoja wa hiace analipa 1,666 lakini kwa bodaboda wanalipa 22,000, ukiigawanya kwa dereva na abiria inakuwa analipa 11,000 sasa swali langu, ni kama hili la kwanza, kwa nini sasa hizi Kanuni zisibadilike ili SUMATRA waweze kuwatoza angalau 10,000 kwa mwaka badala ya 22,000? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili muhimu ya nyongeza ya Mheshimiwa Hasna Mwilima, Mbunge wa Kigoma Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nataka nichukue nafasi hii kulitaarifu Bunge lako Tukufu na umma kwa ujumla kwamba tupo katika hatua za mwisho katika Marekebisho ya Sheria ya Usalama Barabarani na tunatarajia mchakato huo utakapokuwa umekamilika sheria hiyo italetwa hapa Bungeni ili Waheshimiwa Wabunge tuweze kuijadili na hatimaye kuipitisha na sheria hiyo itakapokuwa imekamilika itapelekea vilevile kutoa fursa kwa Mheshimiwa Waziri kufanya mabadiliko ya Kanuni kulingana na Sheria itakavyokuwa imepitishwa na Bunge. Katika mambo ambayo tumeona kwamba ni muhimu kuyabadilisha katika Sheria ya Usalama Barabarani, moja, tumeona kwamba Sheria iliyopo sasa hivi inachangia ama inakwaza mapambano dhidi ya kupunguza ajali za barabarani nchini na moja katika jambo ambalo tuliona kwamba tutalipendekeza katika sheria hiyo ni juu yenu Waheshimiwa Wabunge kuona kama linafaa au halifai ni kuziangalia hizi tozo ambazo zinatozwa kwa hawa watu ambao wanafanya makosa ya usalama barabarani.

Mheshimiwa Spika, kama wataona kwamba tozo zilizopo sasa hivi ni ndogo na hivyo zinapaswa kuongezwa na kufanya hivyo pengine itasaidia kuwafanya waendesha vyombo hivi waogope, basi ni juu ya Waheshimiwa Wabunge na huo ndiyo mtazamo ambao nauona ni sahihi. Kwa mtazamo wangu mimi, nahisi kwamba baadhi ya waendesha vyombo vya moto wamekuwa wakifanya makosa kwa sababu wanaona wanaweza wakalipa hizi faini kwa kuwa ni kidogo na wanaweza wakalipa mara moja na wakaendelea na shughuli zao. kwa hiyo hili niseme kwamba kwa kuwa litakuja hapa Bungeni, tulipatie muda.

Mheshimiwa Spika, hili linakwenda sambasamba vilevile na swali lake la pili ambalo lilikuwa linazungumzia vilevile masuala ya tozo, ingawa hili la pili linahusiana na masuala ya SUMATRA ambayo kwa kuwa Serikali ni moja, basi nina hakika tutakaa pamoja na Wizara ya Uchukuzi ili kuona kwamba mambo haya mawili tutakwenda nayo vipi kwa pamoja.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Serikali ya kuridhisha kwa kiasi, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, pamekuwa na watumishi wengi ambao wamekaa muda mrefu, zaidi ya miaka kumi hadi ishirini wakiwa wanalilia suala la muundo huu ambapo umetoka Waraka Na.3 wa Mwaka 2015 bila kutekelezwa kwa wakati. Serikali ina mpango gani wa kupandisha vyeo vyao kwa mserereko ili kuzingatia muda waliotumia kazini?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, suala la hadhi ya Kitengo cha Uhasibu, ni kweli Serikali inajibu juu ya vigezo ambavyo vinafanyiwa tathmini mara kwa mara na Ofisi ya Rais, Utumishi. Natambua vigezo vyenyewe vinazingatia job analysis na job design. Kwa msingi huo, ni ukweli kada hii imeacha kutumia local standards kwa muda mrefu sana na sasa wanatumia international standards katika kutengeneza mizania mbalimbali ya taasisi. Vilevile hata ripoti za CAG tunaziona jinsi gani zinavyotoka tayari kila mmoja anahamaki juu ya kuiona hadhi ya taasisi inabebwa na sehemu au kitengo hiki. Tunao mfano, juzi tu taarifa ya CAG baada ya kuitoa tayari viongozi wa Serikali wametoa maelekezo magumu kwa section hii, yaani Wakuu wa Idara au Vitengo hivi.

Mheshimiwa Spika, lakini mwisho hadhi hii inategemea kazi kubwa wanayoifanya. Tayari uchumi na mipango wana hadhi ya Kurugenzi…

SPIKA: Mimi nilifikiri swali huwa linakuwa ni swali.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, ni swali, natengeneza hoja ya kuuliza swali la mwisho hili.

SPIKA: Hapana, unahutubia Mheshimiwa.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, basi kwa misingi hiyo miwili sasa Serikali haioni ni muda mwafaka wakifanya analysis yao wa kukipa hadhi Kitengo hiki cha Uhasibu na Idara ya Ukaguzi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mtemvu, Mbunge wa Kibamba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza; kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mtemvu kwa kuwatetea watumishi hawa, lakini nimjulishe kwamba ni dhamira ya Serkali na Serikali imekuwa ikifanya hivyo kila mwaka kuhakikisha kwamba inapandisha vyeo na hadhi za wafanyakazi na watumishi wake ambao wanafanya kazi vizuri. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba hao Wakaguzi wa Hesabu, Wahasibu pamoja na Wasaidizi wao watapandishwa vyeo pale ambapo hali ya bajeti itaruhusu lakini kwa kuzingatia vigezo ambavyo vimewekwa.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusiana na vigezo hivyo, kama ambavyo nimejibu katika swali lake la msingi ni kwamba utaratibu huu ambao umewekwa upo kwa mujibu wa Sheria ile ya Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi ambayo ndiyo imesababisha kutayarishwa Waraka huu Na.3. Kwa kuzingatia sheria hiyo na Waraka ule, ndiyo utaratibu huohuo ambao utaendelea kama ambavyo nimejibu katika swali la msingi.
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa jawabu hili zuri naipongeza sana Serikali kwa kuwa na utaratibu mzuri wa kuwajali wananchi wake dhidi ya vitendo hivi vya uhalifu vinavyotokeza katika mabenki ambavyo hufanywa na watumishi ambao sio waaminifu. Nimepata tamaa sasa na mimi. Swali la kwanza; je, ni lini Serikali itawalipa wateja 103 wa Tawi la NBC la Zanzibar Forodhani ambao fedha zao kiasi cha milioni 400 ziliibwa na watumishi wa benki hii ya NBC Forodhani kule Zanzibar pamoja na kuichukulia hatua au adhabu hiyo benki ya NBC kwa kutowalipa wateja hao?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; ili kuhakikisha kwamba hawa wazee wanalipwa fedha zao hizi za kiinua mgongo ambao wengine tayari wameshafariki; je, Serikali iko tayari kufuatilia kwa haraka pamoja na mimi kuhakikisha kwamba haya waliyosema yanatokea?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ali Hassan King kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimejibu katika swali la msingi nilieleza kwamba, kwanza nieleze kwa mujibu wa Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya Mwaka 2006 inaeleza kwamba moja ya majukumu ya Benki Kuu ni kusimamia ufanisi na usalama wa wateja, kusimamia na benki nyingine ili kuhakikisha usalama na ufanisi wa amana za wateja katika benki. Hiyo ndiyo dhamana yake kubwa. Kwa hiyo ikiwa tukio hili ambalo limejitokeza katika Benki ya National Bank of Commerce (NBC) ya uhalifu ambao umetokezea sasa haijaelezewa na muuliza swali kwamba uhalifu huu umesababishwa na nani. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge muuliza swali kwamba nitakapotoka hapa nitafuatilia suala hili tujue kwamba je, wizi huu ulivyofanyika, uchunguzi umeshafanyika kama ambavyo nimejibu katika swali la msingi? Kama uchunguzi huu umefanyika ni nani ambaye amesababisha uhalifu huu? Kama suala hili limesababishwa na wafanyakazi watumishi wa benki, basi hatua zitachukuliwa. Kama suala hili limesababishwa na mifumo ya Benki, basi Benki Kuu ya Tanzania itachukua dhamana ya kuhakikisha kwamba fedha zile zinarudishwa na benki ile na zitachukuliwa hatua benki husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niseme kwa sababu suala lake sio suala ambalo ni mahsusi, nahitaji kufahamu kwa undani hasa kujua hasa wizi huu uliojitokeza chanzo chake ni nini na kama uchunguzi umefanyika, umefikia katika hatua gani ili tuweze kutoa maelekezo ya jinsi gani hatua zitachukuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kwamba tutakuwa tayari kufuatilia, ndiyo maana nikaeleza kwamba kwa sababu jambo hili ni jambo ambalo yeye Mheshimiwa Mbunge analifahamu zaidi tutakuwa tayari mimi na yeye tushirikiane tufuatilie ili tufahamu kabisa kwamba jambo hili limefika katika hatua gani na tuweze kuchukua hatua pale ambapo tumefikia.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa huduma za fedha za Kibenki na huduma za fedha za mtandao zote ziko chini ya Sheria ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania, naomba kuuliza; je, Serikali ina mpango gani kukomesha na kudhibiti wizi wa mitandao ambao imekuwa ni kero kubwa kwa wananchi wetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zaytun Swai, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli wizi wa mtandao ni moja kati ya njia ambazo zinatumika kuweza kufanya uhalifu wa kibenki na pale ambapo inabainika wizi huo wa kimtandao umefanywa na watumishi wa benki husika, basi watumishi hao huchukuliwa hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyozungumza awali kwamba Benki Kuu ya Tanzania (BOT) inasimamia benki zingine kuhakikisha kwamba kwanza inaajiri wataalam au wafanyakazi ambao wanakuwa ni wenye weledi na wenye maadili ili kuhakikisha kwamba inasimamia sera na rasilimali watu kwenye benki. Benki Kuu yenyewe ya Tanzania inafanya tathmini kila mwaka kuhakikisha kwamba Menejimenti ya benki zote nchini inasimamiwa na Mameneja au Wakurugenzi ambao watakuwa na uadilifu.

Tatu, kumekuwa kuna utaratibu wa kuwa na registry ya kuhakikisha kwamba kuna orodha ya watumishi wote ambao wanakuwa sio waaminifu na pale ambapo wanakuwa sio waaminifu orodha ile inatawanywa katika benki zote ili watumishi wale wasiweze kupata fursa ya ajira katika benki nyingine kupunguza uhalifu wa aina kama hiyo ambao unakuwa unasababishwa na baadhi ya wafanyakazi au mameneja wa benki husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania inafanya jitihada kubwa sana kuona benki zetu nchini zinadhibiti uhalifu wa kimtandao usijitokeze hasa pale ambapo uhalifu huo unasababishwa na benki.

Mheshimiwa Naibu Spika, uhalifu wa mtandao mwingine ambao uko nje ya benki kama ambavyo unatokezea katika taasisi mbalimbali na wenyewe Serikali inashirikiana na vyombo vya dola ikiwemo Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi pale ambapo yanajitokeza matatizo kama hayo na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nimesikia majibu ya Serikali lakini ukweli bado wafanyabiashara wana kilio hapa nchini, hawana raha na Serikali yao kulingana na madeni hayo maana hawakuwa na elimu ya hizi mashine za EFD. Hivyo sasa, naomba Mheshimiwa Waziri utoe kauli ili nchi nzima wajue kwamba walishasamehewa hayo madeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili je, ni lini sasa Serikali itafuta madeni ya mgodi wa Bulyanhulu ili waweze kutimiza makubaliano yao katika mkataba wao wa ujenzi wa barabara itokayo Kahama ya lami kwenda Bulyanhulu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango ya Mheshimiwa Nicodemus Maganga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza suala la kauli ya Serikali kuhusu kusamehe madeni haliwezi kutolewa kwa utaratibu huu. Msamaha wa madeni unatokana na uko kwa mujibu wa sheria, hata yale maamuzi ambayo yalisababisha kusamehe madeni ya kipindi kile yalitokana na utaratibu wa kisheria ambao ulipitishwa na Bunge hili. Kwa hiyo, hatuwezi kusimama hapa tukatoa tu tamko la kusema tunamsamehe nani madeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili vilevile kuhusiana na kusamehe madeni na kwenyewe kuna repercussions zake. Kwa mfano, best practice wataalam wanasema kwamba utaratibu ule wa kusamehe madeni hauwezi kufanywa kila wakati kwa sababu unaathiri wigo mpana wa ukusanyaji kodi chini.

Kwa hiyo, lengo kubwa lilikuwa ni kuhakikisha kwamba kwanza tunawasaidia wale ambao walikuwa na madeni ya muda mrefu, lakini la pili ilikuwa ni kuhakikisha kwamba tunakusanya kwa kipindi kile ambacho maamuzi yale yalitoka kwa haraka.

Kwa hiyo, ili msamaha mwingine utoke, lazima tukae chini na kuweza kufanya tathmini na utafiti wa kina kupima athari na faida za kufanya hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili kuhusiana na hoja ya Bulyanhulu napokea maelekezo yako nadhani ni suala mahsusi kwa hiyo basi tutalifanyia kazi na kumpatia majibu Mheshimiwa Mbunge baada ya kupata hizo takwimu. (Makofi)
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Spika, ahsante; humu mna jibu hakuna jawabu, kwa sababu nilichoomba kwamba ni lini Serikali itafungua Ofisi ya Hazina Ndogo lakini jibu lililokuwemo humu wamesema watafanya mashirikiano na Wizara ya Fedha ya Zanzibar kitu ambacho hakiwezekani kwamba taarifa za Serikali ya Jamhuri ya Muungano zikawepo katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Hawa wazee taarifa zao zipo Wizara ya Fedha ya Muungano, wanapokuwa na matatizo wanakwenda Dar es Salaam na wanachukua muda mwingi hadi wengine wanasamehe mafao yao. (Makofi)

Sasa nataka jawabu Serikali ina mpango gani wa kuwa na ofisi kama ilivyokuwa ofisi nyingine? Mpango wa kuwa na ofisi, hilo lingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, je, hawa wazee wanaokuja mpaka wakakata tamaa wakarudi wakasamehe mafao yao Serikali itachukua hatua gani?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ali Omar Hassan King, Mbunge wa Jang’ombe kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza hatujapokea malalamiko ambayo yanaonesha kuna usumbufu wa malipo ya wastaafu kupitia utaratibu ambao tunao sasa hivi wa kushirikiana kati ya Wizara za Fedha za pande mbili za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge kama ana malalamiko mahususi ambayo pengine hayajatufikia sisi, basi ayawasilishe tutayashughulikia haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na lini tutajenga ofisi, masuala ya ujenzi wa ofisi ni masuala ambayo yanahitaji bajeti na uwezo wa kifedha na maandalizi. Kwa hiyo, kutoa kauli hasa ni lini kwa sasa hivi inaweza ikawa sio rahisi sana hata hivyo Mheshimiwa Mbunge nimhakikishie kwamba kwa sababu ofisi hizi ndogo zilizopo mikoani kwa upande wa Tanzania Bara ambazo zimejengwa huwa zinafanya kazi kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya Umma na Kanuni zake ambayo pamoja na mambo mengine, zinahudumia Ofisi za Makatibu Tawala wa Mikoa pamoja na Idara za Serikali ya Muungano ambazo kwa upande wa Zanzibar Ofisi za Tawala za Miko ana hizi Idara za Serikali shughuli zake zinafanywa na Wizara ya Fedha ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Kwa hiyo, shughuli zile hazijakwama kwa upande wa Zanzibar kwa sababu zinasimamiwa na Wizara ya Fedha ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambayo sio masuala ya Muungano.

Mheshimiwa Spika, zipo taasisi ambazo tayari zimeshajengwa majengo huko kama BOT na TRA zina Ofisi Zanzibar, kwa hiyo, masuala mengine ya ujenzi wa miundombinu ni masuala ambayo hayaendi kwa wakati mmoja, yanakwenda hatua kwa hatua.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba concern yake Serikali tunaitambua na pale ambapo hali itaruhusu basi tutakamilisha utaratibu huu ambao amependekeza.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini bado nina maswali ya nyongeza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, je, Serikali inaweza kutoa ruzuku ambayo zamani ilikuwa ikitoa kwa wakulima kwa mazao mbalimbali sasa iende kwenye Benki ya Kilimo halafu benki isimamie na kutoa mikopo hiyo kwa riba ndogo sana? Kilimo hakiwezi kukopeshwa zaidi ya asilimia 10.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, hivi karibuni Benki Kuu imetangaza fedha za kusisimua uchumi trilioni moja.

Je, haiwezekani Benki Kuu ikapeleka sehemu ya fedha hiyo kwenye Benki ya Kilimo ili yenyewe isimamie kwa kuwakopesha wakulima kwa riba ndogo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Almas Maige kwa pamoja, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na ruzuku ya shilingi trilioni 1 ambayo urejeshaji wake utakuwa ni wa riba asilimia 3 ni mkakati maalumu ikiwa ni moja kati ya hatua tano ambazo BoT imeziweka kwa ajili ya mabenki yote nchini. Kwa hiyo, TADB ni moja kati ya mabenki ambayo yanapaswa kutumia fursa hiyo. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba TADB ni miongoni mwa mabenki kadhaa ambayo tayari yameshapeleka maombi hayo kwa ajili ya kupatiwa fedha hizo kwa ajili ya kutekeleza malengo na mikakati yake ikiwemo dhima kubwa ya kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba riba zinapungua kwa kiwango kisichozidi asilimia 10.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, kuna jitihada mbalimbali ambazo kama Serikali inachukua za kuhakikisha kwamba tunaiongezea uwezo TADB pamoja na benki nyingine zilizo chini ya mamlaka ya Serikali ili ziweze kupata mitaji ya kutosha pamoja na zenyewe kuwa na utaratibu wa kubuni njia za kujiwezesha kuongeza ukwasi ili waweze kutoa mikopo zaidi na kusaidia sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi pamoja na sekta nyingine mbalimbali nchini.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Benki hii ya Kilimo ipo Dar es Salaam lakini wakulima walio wengi wapo katika mikoa mbalimbali kwa maana ya Nyanda za Juu Kusini, Mikoa ya Kaskazini na kwingineko. Je, ni lini sasa huduma hizo zitapanuka ili wakulima wote waweze kupata huduma hiyo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecilia Paresso, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Cecilia Paresso amezungumza hoja ya msingi, nimhakikishie kwamba kwa kipindi hiki ambacho TADB haijawa na matawi katika maeneo yote nchini imekuwa ikifanya kazi zake kwa utaratibu mzuri wa kuwasaidia wakulima kwa kuweka utaratibu maalumu wa kuratibu kupitia Idara Maalumu ambayo inajihusisha na masuala ya wakulima wadogo wadogo katika benki hiyo. Hata hivyo, kwa kuwa wazo hili ni jambo jema, nimhakikishie kwamba tumelipokea na tutalifanyia kazi. Pale ambapo hali itaruhusu tutaweza kusambaza huduma ya TADB katika maeneo mbalimbali nchini.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza; ni lini sasa Serikali itatoa huo mwongozo mpya ili tuweze kusaidia zile halmashauri ambazo zina uhitaji mkubwa wa kuwekeza kwenye miradi ya kimkakati?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; katika Jimbo la Manyoni Mashariki hatuna stendi ya mabasi. Sasa nini commitment ya Serikali kuhakikisha kwamba kwa kupitia huu mfumo itakuwa tayari kusaidia Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni kujenga stendi ya mabasi ili itumike kama kitega uchumi kwa halmashauri?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na mwongozo mpya ilitokana na mapendeezo ambayo Mheshimiwa Mbunge amewasilisha. Kwa hiyo pale ambapo utakuwa umekamilika kwa kuzingatia haya mapendekezo ambayo ametupatia tutampatia. Hata hivyo, kwa huu mwongozo ambao tunaendelea nao na tunadhani mpaka sasa hivi haujaleta changamoto kubwa, ninao hapa na nitampatia baadaye.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili; niwapongeze kwanza yeye Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wake wa jimboni kwake kwa jitihada ambazo wameanzisha, lakini nimhakikishie kwamba kama ambavyo tumekuwa tukifanya siku zote kuhakikisha tunasaidia ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri zetu mbalimbali ikiwemo miradi ya stendi za mabasi, basi na jimbo lake na lenyewe tumelichukua tutaangalia tuingize katika mpango wetu wa utekelezaji pale tutakapofanya upembuzi wa kina kubaini kwamba ni utaratibu gani muafaka wa kuweza kuendelea na mradi huo na bajeti itakapokuwa imeruhusu.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kuniona. Kwa kuwa suala la kujenga uwezo wa halmashauri na hasa katika miradi hii ya kimkakati linakwenda sambamba na suala la kuinua hali za wananchi kiuchumi ili waweze kushiriki vizuri katika miradi hii, nini hatua ya Serikali mpaka sasa katika kilio kikubwa cha wananchi cha kupunguza riba za mabenki?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka hapa wakati wa mjadala wa bajeti, Mheshimiwa Kilumbe alikuwa miongoni mwa Waheshimiwa Wabunge ambao walilizungumzia sana tatizo hili la ukubwa wa riba katika mabenki yetu ya biashara. Muda mfupi Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo kwa Serikali kuangalia jinsi gani ambavyo tutapunguza riba hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi, kama ambavyo nilikuwa nimeeleza jana wakati najibu swali, naomba nirudie kuwahakikishia kwamba yale maeneo matano ambayo Benki Kuu ya Tanzania iliyaainisha kuwa kama ni njia ya kuweza kufikia malengo hayo tayari yameshaanza kufanyiwa kazi. Kwa hiyo, nimthibitishie Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda kwamba, wakati wowote kuanzia sasa mabenki kadhaa tayari yameshaanza kupeleka maombi yao kwenye Benki ya Tanzania kwa ajili ya kutumia fursa hizo zilizotolewa zenye dhamira ya kufikia malengo haya ya kuhakikisha kwamba riba inakuwa nafuu kwa kiwango kisichozidi asilimia kumi.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa moja kati ya vigezo vilivyopo katika mwongozo ni halmashauri iwe na hati safi kwa miaka mitatu mfululizo; na kwa kuwa kigezo hiki ni kandamizi kwa wananchi kwa sababu wanaosababisha hati kuwa chafu au safi siyo wananchi bali ni watumishi wa halmashauri.

Je, Serikali haioni kwamba hata kama kuna marekebisho yanafanywa kigezo hiki kiondolewe mara moja ili halmashauri zote zipate haki ya kuomba miradi hii ya kimkakati? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Justin Nyamoga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inapoandaa miradi hii ya kimkakati moja katika dhamira zake kubwa ni kuhakikisha kwamba miradi hii inakuwa na tija kwa ujumla wake. Ndiyo maana miongoni mwa vigezo, ukiachilia mbali hicho ambacho Mheshimiwa Mbunge amekizungumza, ni kuangalia mtiririko mzima wa fedha katika mradi ili kuona kwamba mradi ule utaweza kujiendesha kwa faida na baadaye uweze kuwa na tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hati chafu inapokuja inatoa kiashiria hasi juu ya ufanisi wa mradi husika. Hata hivyo kwa kuwa jambo hili ni la kitaalam, naomba nilichukue halafu tukaiwasilishe hoja yake kwa wataalam, tuone jinsi gani inaweza ikafanyika bila kuathiri lengo halisi la kuona tija inapatikana katika mradi ule, lakini wakati huohuo isiathiri dhamira njema ya wananchi kwa makosa ambayo hayawahusu.
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyogeza.

Kwa kuwa vigezo vipya vya kufungua maduka vimekuwa vigumu kwa wafanyabiashara wengi, ikiwa ni pamoja na uoga wa kupoteza fedha kama ilivyotokea mwanzo, Serikali ina mpango gani wa kuweka masharti ambayo ni rafiki ili wafanyabiashara wengi zaidi wafungue biashara hizo kwa sababu maeneo ya mpakani/mikoa hii ya mpakani kumeshaanza kuwepo kwa black market ambapo wale wanaobadilisha fedha wanabadilisha kwa bei ya chini sana? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; maduka yale yaliyofungwa fedha taslimu zilichukuliwa na baadhi ya wafanyabiashara zilichukuliwa mali zao nyingi ikiwepo hati za viwanja na nyumba, hati za magari kwa maana ya kadi za magari na hawajarejeshewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni nini hatma ya watu hawa ambao wamefungwa mikono na mali zao zimeshikiliwa na Serikali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Tarimo Mbunge wa Moshi Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge amesema kwamba vigezo vilivyowekwa ni vigumu, lakini bahati mbaya hakuainisha vigezo hivyo ni vipi vigumu; kwasababu imani yangu ni kwamba pengine angetusaidia kutuambia ni kipi kigumu tungeweza kukifanyia kazi. Hata hivyo kwa ujumla vigezo vilivyowekwa mpaka sasa hivi tunadhani tumeviwekwa kwa kuzingatia maslahi ya nchi pamoja na maslahi ya Serikali. Ingawa bado kuna mwanya wa kuweza kuviangalia kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema, lakini kwa uelewa wangu vigezo hivyo kwa kweli si vingi sana. Labda kigezo kimoja ambacho kimekuwa kikilalamikiwa sana ni kigezo cha kiwango cha mtaji kutoka shilingi milioni 300 kuja bilioni moja.

Mheshimiwa Spika, mantiki ya kuweka kigezo hiki ilikuwa ni nia njema tu ya Serikali kuhakikisha kwamba hawa wafanyabiashara wa maduka haya ya kubadilisha fedha wanatumia fedha zao wenyewe kuendesha biashara. Kwasababu wakati ambapo umefanyika utafiti kupitia forensic audit iliyofanywa iligundulika kwamba wengi wafayabiashara wa biashara hizi za kigeni walikuwa wanazungusha fedha isiyokuwa yao, kwa hiyo, hiyo ndio ikawa mantiki ya kuweka kiwango hicho na hivyo nadhani ndiyo malalamiko mengi makubwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Mbuge labda pengine angetusaidia kwa wakati wake kuweza kuainisha vigezo. Kama kuna vigezo ambavyo tunaona kwamba vinahitaji kuangaliwa basi tutaviangalia.

Mheshimiwa Spika, lakini swali lake lingine ambalo ameuliza anazungumzia kuhusiana na hatma ya vifaa vilivyochukuliwa. Ni kwamba baada ya hatua ambazo zimechukuliwa kujitokeza wafanyabiashara hawa waliitwa ili kufanya majadiliano na mamlaka husika; na baada ya majadilliano kumalizika walitakiwa wale ambao walipaswa kulipa walipe, wale ambao walitakiwa kwenda kuchukua vifaa vyao waende wakavichukue.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nitoe wito, kama kuna wafanyabiashara ambao bado hawajachukua vifaa vyao na wanastahili kwenda kuvichukua vifaa vyao waende wakachukue vifaa vyao, na hakuna sababu yoyote ambayo Serikali inaweza kukaa na mali ya mtu bila sababu ya msingi. Kwa hiyo niendelee kuwasisistiza kwamba kauli rasmi ya Serikali ni kwamba kama ambavyo majadiliano yalifanyika wakaelezwa wale ambao wanastahili kwenda kuchukua au wanahitaji kuvichukua basi waende wakavichukue. Kama kuna mapungufu yoyote basi tuletewe hizo taarifa ili tuweze kuzifanyika kazi.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, nilitaka kujua kama Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Benki Kuu waliamua kufunga maduka ya fedha za kigeni kwa sababu yalikuwa hayafuati taratibu, na sasa zipo financial institution nyingi mjini humu ambazo zinakopesha kwa riba ya juu na kuumiza walimu na watumishi wengine wa umma. Hivi Serikali inapata kigugumizi gani kuzifunga hizi ambazo zinatesa wananchi na badala yake inakwenda kufunga maduka ya fedha za kigeni ambayo yalikuwa hayalalamikiwi na wananchi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda, Mbunge wa Kigoma Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kilichofanyika ilikuwa ni kuzifuta leseni kwa wale ambao walibainika kuwa wamekiuka taratibu; na hii ipo kwa mujibu wa sheria pamoja na regulation ambazo tumetunga za mabadiliko ya fedha za kigeni, wanaita Foreign Exchange Act, kwa hiyo hii ilichofanyika imefanyika kwa mujibu wa sheria.

Sasa kuhusiana na kwamba kwanini kuna taasisi nyingine ambazo zinaumiza wananchi wa riba kubwa, jana nilimpongeza sana Mheshimiwa Kilumbe hapa, kwasababu nilisema kwamba kama kuna Wabunge ambazo walishiriki katika mjadala wa Bunge la Bajeti lililopita, kuzungumza kwa uchungu na hisia kazi juu ya baadhi ya taasisi ambazo zimekuwa zikinyanyasa wananchi kwa kuwakopesha kwa riba kubwa bila msingi yeye alikuwa ni mmojawapo. Nikasema kwamba kwa kusikia kilio hicho hicho kwa Waheshimiwa Wabunge Mheshimiwa hakuchelewa kwa kutoa maelezo ili jambo hilo lifanyiwe kazi.

Mheshimiwa Spika, na nimewahakikishia juzi na jana wakati najibu maswali kwamba kwanza niwapongeze BOT kwa kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais, sasa hivi mchakato huu umeshaanza. Kwa hiyo ni matarajio yangu sasa kile kilio cha Waheshimiwa Wabunge akiwepo Mheshimiwa Kilumbe cha kupunguza riba sasa kimepatiwa dawa. Kwa hiyo hoja hizo mbili zote zinachukuliwa hatua kwa utaratibu wake kulingana na sheria na taratibu za nchi yetu.
MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imetangaza nia yake ya kuendelea kurejesha imani ya wafanyabiashara na kujenga mahusiano mazuri kati ya Serikali na wafanyabiashara. Na kwa kuwa sasa hivi Serikali inaendelea kujadiliana na watu hawa wa maduka ya kubadilisha fedha.

Je, Serikali itakuwa tayari kuweka bayana kiasi cha fedha kilichokusanya wakati wa operation hiyo, na kiasi cha fedha ambazo zitakuwa zimerudishwa kwa wale wasio na hatia na sababu zitakazopelekea wale ambao fedha zao zitachukuliwa na kwamba zitakuwa zimechukuliwa kwa misingi ipi? Naliweka hili na naomba swali langu lijibiwe. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ole-Sendeka, Mbunge wa Simanjiro kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni sahihi kabisa, Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria sana kuhakikisha kwamba imani ya wafanyabiashara inaimarika Zaidi. Na kama ambavyo Mheshimiwa Rais mwenyewe amekuwa akisema kwamba Serikali yake itahakikisha kwamba itafanya kila linalowezekana kuhakikisha inaibua vyanzo vya mapato. Jtihada mbalimbali mmeshaziona ambazo Mheshimiwa Rais mwenyewe binafsi amezifanya katika kuhakikisha kwamba anahamasisha uwekezaji nchini ili tuweze kupata wawekezaji wengi wakubwa waweze kutupatia kodi katika nchi hii; na amesema mara kadhaa kwamba hataki kuona kodi ya dhuluma.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Wizara ya Fedha na Mipango tutakuwa watu wa mwisho sana kuona kwamba kama kuna mwananchi yeyote anadhumumiwa kupitia utaratibu wa kodi na tukalifumbia macho jambo hilo.

Kwa hiyo, niwahakikishie tu kwamba katika hoja hii hawa ambao wanahusiana na maduka ya fedha za kigeni tumefuatilia kwa kina na tumebaini kulingana na taarifa ambazo tunazo na vielelezo kadhaa ambavyo tunavyo, kwamba walihusishwa wenyewe mara kadhaa katika mchakato mzima wa mgogoro uliojitokeza. Imani yetu ni kwamba kama nilivyozungumza, kwamba wengi wao wamekubaliana na hali halisi baada ya kupewa ushahidi juu ya matukio mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, lakini kama kuna wale mnadhani bado, basi bado nafasi hiyo ipo kwa sababu Serikali hii imetoa mwanya na nafasi kwa yeyote ambaye anadhani bado hajatendewa haki kuweza kufuata taratibu za kudai haki yake ili aweze kuipata.
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Spika, kwa sababu kumekuwa na malalamiko mengi sana kwa wafanyabiashara wa bureau, kwamba assessment ambazo zimefanyika hazikufanya na competent authority kwa sababu zilifanya na task force badala ya kufanywa na TRA kama wahusika.

Je, Wizara ya Fedha haioni sasa kwamba wakati umefika kwa TRA kwenda kupitia upya zile assessment ili yale makadirio yaani makadirio ambayo yapo kwa mujibu wa sheria?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mrisho Gambo Mbunge wa Arusha Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ninatambua Mheshimiwa Mrisho Gambo ni miongoni mwa watu ambao wananchi wa jimboni kwake wameathirika na jambo hili; na ikiwa kama Mbunge anawajibu anapopelekewa malalamiko na wananchi hapa ndipo sehemu yake pa kuyasemea.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo nimhakikishie Mheshimiwa Gambo kwamba assessment hii imefanywa na TRA kupitia Kitengo kile cha Investigation, kwa hiyo ni assessment ambayo imefanywa kwa mujibu wa taratibu na sheria na mamlaka sahihi kabisa ambayo inapaswa kufanya assessment.

Mheshimiwa Spika, lakini kama nilivyosema mwanzo, kwamba tuna utaratibu ambao iwapo mtu hajaridhika na assessment yote kuna utaratibu wa kufuata ili kuweza kuhakikisha kwamba anakata rufaa katika ngazi mbalimbali na kuangalia kama kuna uwezekano wa kuweza kui-review assessment yake ukafanyika hivyo.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu kwamba jambo hili lilisimamiwa na TRA wenyewe katika eneo la investigation.
MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Spika, sote tunafahamu dhamira ya Rais wetu aliyoionesha kwenye eneo la michezo, na tarehe 15 Juni, 2021 alipokuwa anazungumza na vijana wa nchi hii pale Mwanza alizungumzia eneo hili la msamaha wa kodi. Na katika maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri amesema wataanza kufanya practice kwenye upande wa majijii na halmashauri za manispaa, na wakifanya vizuri watahamia kwenye Wilaya.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; ina maana wanamaanisha kwa mfano kama Dodoma Mjini wakipewa hayo majaribio waki under perform basi ina maana Kongwa hawatapewa kwenye phase two.

Mheshimiwa Spika, hii nadhani si sawa. Ni vyema kama wanakwenda kufanya majaribio wafanye kote kwenye halmashauri za manispaa, majiji na kule kwingine.

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Ili kurahisisha utekelezaji wa jambo hili Je, Mheshimiwa Naibu Waziri na Serikali kwa ujumla haioni sasa umefika wakati wa kuanzisha wakala wa vifaa vya michezo nchini ili kurahisisha upatikanaji wa vifaa vya michezo kirahisi kuanzia kwenye shule zetu hata kwa Wabunge wenyewe ambao kimsingi kila mwaka wamekuwa wakiagiza vifaa vya michezo kwa wananchi wao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwakiposa Mbunge wa Mufindi Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, dhamira ya Serikali kuanza na majiji na halmashauri hayakuwa na maana ya kuangalia mapungufu ambayo yanaweza kusababisha maeneo mengine yasipate sipokuwa yalikuwa yana lengo la kuangalia mapungufu ili yatakapopelekwa maeneo mengine mapungufu yale yasijitokeze. Kwa mfano katika matumizi ya nyasi hizi bandia yamekuwa yakitumika katika shughuli mbalimbali wakati mwingine unaweza ukaenda hata kwenye bar ukakuta hizi nyasi bandia zipo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nikuhakikishie kwamba Serikali inadhibiti matumizi mabaya ya fursa hii njema iliyowekwa na kwa dhamira njema ya Serikali ni vyema tungeanza hatua kwa kwa hatua. Kwa hiyo elimu ambayo tumeipata katika utekelezaji katika awamu ya halmashauri na majiji itatusaidia tunapopanua wigo katika maeneo mengine mengi zaidi kuweza kufahamu ni mapungufu yapi na tukayoweza kuyadhibiti kirahisi ili kuepuka madhara na hasara kwa Serikali; hiyo ndiyo iliyokuwa dhamira. Malengo ni kuhakikisha kwamba tunasambaza huduma hizi katika maeneo yote nchini hatua kwa hatua na awamu kwa awamu.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na wazo lake la pili, ni jambo jema sana na Mheshimiwa Mwakiposa amekuwa kwakweli ni mpambanaji sana wa suala hili. Mara nyingi amekuwa akija akituulizia kuhusiana na utekelezaji, na kwamba angependa kuona mabadiliko na maboresho makubwa katika eneo hili. Kwa hiyo kuhusiana na hoja hii ya pili nadhani ni hoja ya msingi. Mheshimiwa Waziri wa Michezo na Mheshimiwa Naibu wake hapa wapo, wamesikia na ninahakika watalitafakari na kama wataona kuna tija basi watalitekeleza. Hili lipo katika Wizara ya Michezo na Serikali hapa ipo, tumelisikia.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa michezo ni afya na kwa sasa dunia nzima ikiwemo Tanzania tunakabiliwa na hili janga la corona na hivyo tunawahamasisha wananchi wetu waweze kufanya mazoezi ikiwepo kushiriki michezo na vifaa vya michezo ni ghali sana. Na kwa kuwa michezo ni ajira kama Taifa tunahitaji kuwekeza kwenye michezo kuanzia kwenye makuzi ya awali ya watoto wetu ili baadaye waje kuwa na vipaji mbalimbali kwenye soka, riadha, basket na mengine; lakini zaidi michezo ni moja ya sekta ambayo inatangaza nchi yetu na kutangaza utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, je, Serikali haioni kwamba ni vyema sasa iweze kufanya exemption kwa vifaa vyote vya michezo ili viweze kuwa na bei nafuu na watanzania wengi waweze kununua na kujiendeleza kimichezo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Matiko Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, suala la exemption si jambo ambalo linaweza likatolewa kauli Bungeni, linahitaji mambo mengi ikiwemo uchambuzi wa kina wa kitaalam juu ya faida na hasara zake. Sisemi kwamba vifaa vya michezo havina faida lakini ni jambo ambalo siwezi ukalizungumza hapa. Niseme tu kwamba tumelichukua tuone jinsi gani litakavyokuwa linakidhi mahitaji na vigezo kwa wakati husika basi tutalifanyia kazi.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi, lakini nishukuru pia na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Naomba niulize maswali mawili ya nyogeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, ucheleweshaji wa umuhimu wa eneo la mpaka wa Kirongwe si tu ina umuhimu kwa Wilaya na Halmashauri ya Rorya lakini pia ina umuhimu pia kwa Serikali kwa ujumla wake kwa sababu ya sensitivity ya eneo lenyewe lilivyo kati ya mpaka wa Tanzania na Kenya. Lakini mpaka sasa hakuna kifaa chochote vile vifaa tofauti naweza nikasema na counter book na kalamu kwa upande wa Tanzania na Kamba peke yake. Je Serikali haioni kuna umuhimu sasa kipindi ambacho tunakwenda kwenye bajeti ya utekelezaji wa mwaka huu kuweka vifaa vya kisasa ili kuimarisha mpaka ule lakini kudhibiti mapato yanayopotea kwenye eneo lile?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili kwa kuwa ucheleweshaji wa eneo hili linaathiri pia mapato ya halmashauri ndani ya Jimbo letu la Rorya. Je Serikali haioni kuna umuhimu, pamoja na maboresho yanayokwenda ya nyumba za watumishi, kuweka soko kubwa la kimataifa ambalo litakuwa ni sehemu ya fursa kati ya wananchi wa Wilaya yangu ya Rorya pamoja na wananchi wa upande wa pili wa Kenya?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jafari Chege Mbunge wa Rorya kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hoja zake zote mbili ni za msingi sana. Hoja ya kuhakikisha kwamba tunatafuta vifaa vya kutosha ili kuwezesha huduma katika mpaka wa Kirongwe pamoja na ujenzi wa soko ni hija za msingi. Nimwombe Mheshimiwa Mbunge atupe muda Serikali wakati tunakamilisha, kama nilivyoeleza kwenye jibu la msingi, hatua za ujenzi wa nyumba kwa bajeti ya mwaka huu basi na hili la vifaa tulichukue na hili la soko lenyewe Serikali imelipokea itaangalia pale hali itakaporuhusu ili liweze kufanyiwa kazi.
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, mwezi wa nane mwaka huu nikiwa na Kamati ya Bajeti tulipata nafasi ya kutembelea border post ya Namanga. Lakini katika jambo ambalo lilitushangaza ni kwamba border post ile haikuwa na Cargo scanner; na katika kuuliza tukaambiwa kuna border post nyingine vilevile hazina cargo scanner, jambo ambalo linahatarisha mapato ya Serikali vilevile kuchelewesha upitishaji wa mizigo.

Mheshimiwa Spika, ningeomba Serikali itueleze ni nini msimamo wa Serikali katika kuhakikisha border post zote kubwa zinapata cargo scanners ili kuweza kuondokana na matatizo yaliyopo? Ahsante, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Abbas Tarimba Mbunge wa Kinondoni kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba nimjulishe Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali iko katika mpango wa miaka mitano kuanzia mwaka 2020/2021 mpaka mwaka 2024/2025, ambapo mpango huu unalenga pamoja na mambo mengine kuimarisha ama kuboresha utendaji kazi wa vituo vyetu vyote tisa vya one stop border kote nchini; ikiwemo kuweza kuipatia vifaa, watumishi, kuwajengea uwezo watumishi, kuweza kuviimarisha kwa njia mbalimbali. Kwa hiyo mpango huu utakapokuwa umekamilika hii changamoto za scanner na changamoto za vitendea kazi vingine pamoja na mifumo ya TEHAMA kwa ujumla wake, maabara nakadhalika na nyingine ambazo nimezitaja zitakuwa zimepatiwa ufumbuzi.

Mheshimiwa Spika, nimwombe avute subra wakati kipindi cha utekelezaji wa mkakati huu utakapokamilika ni imani yangu kwamba tatizo la scanner Namanga na maeneo mengine litakuwa imepatiwa ufumbuzi.
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naishukuru sana Serikali kwa majibu mazuri yanayotia moyo hasa pale ambapo wananchi wamejitolea kufanya kazi kubwa na Serikali inapounga mkono. Pamoja na majibu hayo, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza; kwa kuwa kituo hiki kinahudumia siyo tu Kata ya Galapo, lakini Tarafa nzima ya Babati ikiwemo Kata ya Kashmamire, pamoja na vijiji vya Jirani vya Wilaya za Kondoa na Kiteto: Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kituo hiki kupatiwa gari? Hilo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili: Je, Waziri yupo tayari sasa kuelekeza kwamba kituo hiki kifanye kazi masaa 24 kuliko ilivyo sasa hivi ambapo kinafungwa saa 12.00 jioni? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali ya nyongeza mawili ya Mheshimiwa Daniel Sillo, Mbunge wa Babati Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaona umuhimu wa kituo hiki kuwa na gari hivyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba pale ambapo tutaweza kupata gari za kutosha, tutazingatia maombi yake ya kupeleka gari katika kituo hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la pili, kwamba hatuoni sasa kuna umuhimu wa kituo hicho kufanya kazi masaa 24; hili nimelichukua. Tutaangalia hali halisi ya kituo kilivyo kama kinaruhusu kuweza kutoa huduma kwa masaa 24, basi tutafanya hivyo. (Makofi)
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niulize swali dogo la nyongeza. Wilaya ya Liwale ni miongoni mwa wilaya kongwe lakini haina Kituo cha Polisi mpaka leo sambamba na nyumba za watumishi. Nami kutoka kwenye Mfuko wa Jimbo kutokana na shida hiyo, nimetoa shilingi milioni 10 kusaidia ujenzi wa Kituo cha Polisi. Nini kauli ya Serikali kuwasaidia wananchi wale wapate Kituo cha Polisi? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kuchauka, Mbunge wa Liwale, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kutoa shilingi milioni 10 kwa kupitia kwenye Mfuko wa Jimbo kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa kituo. Nimhakikishie kwamba Serikali tutaelekeza Jeshi la Polisi kupitia utaratibu wa Mfuko wa Tuzo na Tozo kama ambavyo nimejibu katika swali msingi la Mheshimiwa Daniel Sillo ili uangalie uwezekano wa kutumia fedha hizo kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Mbunge katika kuhakikisha kwamba ujenzi wa kituo hiki unaendelea. (Makofi)
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Tatizo la uwepo wa vituo vya polisi kwenye wilaya mbalimbali limekuwa ni changamoto. Tarafa ya kwa Mtoro na Farqwa, Wilayani Chemba tuna kituo kimoja ambacho kipo kwa Mtoro. Kituo kile kimejengwa kwa nguvu za wananchi, ni kwa miaka zaidi ya 10 sasa baadhi ya majengo yamebomoka kutokana na Serikali kutokuunga juhudi za wananchi nguvu zao wanazojitolea. Pia kituo hicho hakina gari kwa ajili ya kuwasaidia polisi kwenda kuhakikisha wanawahudumia wananchi. Je, ni lini Serikali itawapatia fedha kituo cha polisi kwa Mtoro, kwa ajili ya kukarabati na kukamilisha majengo yaliyopo kwa sasa na kuwapatia gari kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu. Lilitakiwa liwe swali moja kwa hiyo nitachagua moja katika haya mawili kwa mwongozo wako.

MWENYEKITI: Ndiyo.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na aidha ni suala la gari ama jengo. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kunti, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu ya swali hili yanafanana na majibu ya maswali mawili ambayo nimeshayajibu. Kwa hiyo, naomba nirudie majibu yale yale ya maswali mawili ambayo nimeyajibu. Kuhusiana na kwanza pongezi kwa wananchi ambao wameshiriki katika kuunga mkono jitihada za Serikali, kuhakikisha vituo vyetu vya polisi vinajengwa ama vilivyokuwa katika hali mbaya vinakuwa katika hali nzuri, pamoja na kuhakikisha kwamba tunaweza kuwasaidia, askari wetu kuweza kuwa na usafiri kwa ajili ya kuwahudumia wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme kwamba kwa kuwa kituo hiki kinahitaji ukarabati, kwanza nitafanya jitihada, aidha, mimi au Mheshimiwa Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwenda kukitembelea, tuone kituo hiki kiko katika hali gani. Tutakapokuwa tumefika hapo na kuona mazingira tutafikiria, sasa ni njia gani ambayo ni muafaka zaidi ya kuweza kukifanyia aidha ukarabati kituo hiki. Pamoja na suala la usafiri kama ambavyo nimejibu katika maswali mengine ya msingi kwa sasa hivi, gari hatuna lakini tutakapokuwa tumepata gari, basi vilevile tutazingatia na kituo hiki. (Makofi)
MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, nina maswali mawili ya nyongeza; swali la kwanza; ni mifumo ipi ya kisheria ambayo mpaka sasa haijatengenezwa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, mchakato huo utachukua muda gani ili wafungwa wetu waweze kupata haki ya msingi na tumpunguzie haki balozi wa afya ya akili?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali yote ya nyongeza ya Mheshimiwa Bahati Ndigo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba ieleweke kwamba suala la tendo la ndoa si haki ya msingi, ni haki lakini si haki ya msingi. Haki ya msingi ambayo tunatoa kwa wafungwa, chakula malazi, mavazi kwa hiyo, kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi kwamba kuna mambo ya kuzingatia ambayo yanapaswa kuzingia kwanza kabla ya kuruhusu haki hiyo ambayo Mheshimiwa Mbunge anapigania.

Mheshimiwa Spika, hata ukiangalia katika nchi zilizoendelea basi utaratibu huo haupo kama hivyo, kuna utaratibu ambao wale wafungwa wanapelekwa kwenda kutembelea familia, siyo inafanyika katika magereza, lakini ukitaka ifanyike magereza unahitaji kwanza uangalie miundombinu, mila zetu na desturi. Kwa sababu wakati mwingine inakuwa siyo jambo jema kwa mila zetu na desturi, kwamba kila mtu anajua sasa hawa wanakwenda kufanya tendo la ndoa. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, naomba kwa maelezo hayo naomba Mheshimiwa Bahati aridhikena majibu yangu ya msingi.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, ni kwa nini Serikali isiweke utaratibu wa kuwawezesha mahabusu au wafungwa kupata fursa ya kuzungumza na familia zao angalau mara moja kila baada ya miezi mitatu, kuliko hivi sasa unaongelea kwenye nondo, unakuta hakuna usikivu wowote ule?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Matiko, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, suala la namna ya kuboresha utaratibu wa kuzungumza aidha wenza wao na familia zao ni jambo ambalo linazungumzika. Kimsingi tukubaliane kwamba sasa hivi utaratibu huo upo, labda Mheshimiwa Esther yeye haridhiki na ile frequency ama muda. Sasa hilo linategemea na mambo mengi, mazingira, kwa sababu masuala ya magereza yanazingatia usalama, kwamba watu walioko ndani na watu wanaokuja, ni lazima mazingira ya magereza iendelee kulindwa kiusalama ili wanaokuja wasihatarishe usalama wa magereza na wafungwa walioko ndani. Ndiyo maana utaratibu huo umewekwa kwa sasa hivi, lakini pale ambapo miundombinu itaruhusu na pengine utaratibu wa kuweza kuwaona mara kwa mara si jambo baya, lakini nadhani ni jambo linalotakiwa kuangaliwa na kutafakariwa kulingana na usalama wa magereza yetu.
MHE. EMMANUEL MWAKASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Magereza zetu zimekuwa na tatizo ambalo linatokana na hili swali la msingi kwamba kwa kuwa hawa watu wanakosa faragha, wengine wanafanya vitendo wenyewe kwa wenyewe mle magerezani. Je, Serikali ili kupunguza hivyo vitendo vya watu kugeuzana wenyewe kwa wenyewe magerezani, inachukua hatua gani kupunguza vitendo hivyo ambavyo vinasababisha kuwa kinyume hata na mila na desturi zetu?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Emmanuel Mwakasaka, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuna njia nyingi ambazo Serikali inachukua, la kwanza ni kuhakikisha tunaimarisha ulinzi katika magereza na kuimarisha ulinzi kuna njia nyingi vilevile, tuna mifumo ya ki-intelligence kupata taarifa kabla matukio hayajajitokeza. Pia kuna utaratibu ambao kuna askari waliopo katika magereza kuangalia mienendo na mazingira ya wafungwa katika magereza na tabia zao vilevile.

Mheshimiwa Spika, kubwa zaidi ni kwamba kupitia Serikali ya Awamu ya Sita, kuna mikakati kabambe ya kufanya maboresho makubwa katika vyombo vyetu vya usalama. Moja ni kuhakikisha tunaimarisha na kuboresha miundombinu ya magereza ili kutenganisha kati ya wafungwa kwa mfano, kutenganisha wafungwa wenye umri fulani mpaka umri fulani, wenye historia ama rekodi ya uharifu zaidi kuliko wengine na mambo mengine, ili kutoa nafasi kwa kuweza kupeleka nguvu zaidi ya uangalizi katika maeneo ambayo yanastahili kulingana na uzito na changamoto ya mfungwa husika.
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa kumejitokeza suala la uhalifu ambao unafahamika kwa jina la panya road, je, Serikali ina mikakati ipi ya kuweza kuwaelimisha wananchi ili kuendelea kujikinga na suala hili la panya road?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa kuwa uhalifu huu unafanyika Zaidi kwa silaha za jadi pamoja na silaha nzito. Serikali ina mkakati gani juu ya udhibiti wa silaha hizi?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Tauhida, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na utaratibu wa elimu kwa jamii kuhusu kukabiliana na uhalifu wa aina mbalimbali ikiwemo uhalifu ambao ameuzungumza Mheshimiwa Mbunge. Kwanza hivi karibuni tumeweka utaratibu wa kupeleka askari katika kila kata, kuna askari ambao walihitimu mafunzo ya kuupandishwa vyeo na hawa tumewatawanya katika kata zote nchi nzima kwa ajili ya kwenda kusaidia utaratibu na mifumo ya ulinzi shirikishi katika maeneo husika pamoja na utoaji elimu kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, kama hilo halitoshi hivi karibuni tumepata maelekezo kutoka kwa Amiri Jeshi Mkuu kwamba tuhakikishe tunakamilisha ununuzi wa magari ambayo yatakwenda moja katika wilaya na utaratibu wa kupeleka mafuta uende moja kwa moja wilayani kusaidia kuimarisha vitendea kazi kwa askari wetu walio karibu na wilaya na kata zetu kwa lengo la kuandaa mipango thabiti ya elimu kwa umma kuhusiana na ulinzi shirikishi pamoja na jitihada nzima za kushirikisha wananchi katika kusaidia vyombo vyetu vya usalama hususan Jeshi la Polisi katika kudhibiti uhalifu, si katika elimu tu hata kujipanga katika kudhibiti matukio ya kiuhalifu yasijitokeze.

Mheshimiwa Spika, nimjulishe Mheshimiwa Mbunge kwamba, baadaye Jeshi la Polisi watafanya mazungumzo na vyombo vya habari, watazungumza kutoa na kuainisha mkakati kabambe wa kupambana na waharifu ikiwemo Mkoa wa Dar es Salaam, hatua zilizofikia, mafanikio, changamoto, sababu na mipango ya kudhibiti jambo hilo lisiendelee kutokea zaidi. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge pamoja na Waheshimiwa Wabunge wengine, wananchi wanaweza kupata ufafanuzi zaidi wa kina juu ya jambo hili hapo baadaye.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Kumekuwepo na ongezeko kubwa la uhalifu na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwenye mabasi yanayobeba wanafunzi wa shule za msingi na sekondari. Je, Serikali haioni ni wakati sahihi sasa kutoa maagizo kwamba mabasi haya yaendeshwe na madereva wanawake na makondakta wawe wanawake ili tunusuru ukatili wa kijinsia unaoendelea?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Saashisha Mafuwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, inawezekana ikawa ushauri wake ni moja kati ya mambo yanayoweza kusaidia, kwa hiyo tunauchukua. Hata hivyo, ziko na hatua zingine ambazo Serikali inazifanyia kazi, kwa pamoja tutajumuisha na ushauri wake ili tuweze kufanyia kazi ili matatizo kama haya yasijitokeze tena.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, asante sana kwa kuniona.

Swali langu ni kwamba je, Serikali ina mpango gani wa kujenga vituo vya polisi katika Tarafa za Kipatimu, Njinjo na Mandawa Wilayani Kilwa ili kudhibiti vitendo vya uhalifu katika Wilaya ya Kilwa?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Francis Ndulane, Mbunge wa Kilwa Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nikiri juu ya changamoto ya upungufu wa vituo vya polisi katika kata za jimbo ambalo Mheshimiwa Mbunge ameeleza, lakini nizungumze kwa ujumla wake kwamba tuna upungufu wa vituo vya polisi tuna mpango wa kuongeza vituo vya polisi kwa miaka kumi zaidi ya mia tatu na hamsini na kitu ambavyo tunahitaji zaidi shilingi bilioni mia moja sitini na kitu.

Nataka nimwakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mikakati ya kufanikisha mkakati huu wa ujenzi na Wabunge wengine ambao wana shida ya vituo vya polisi katika maeneo yao kwa miaka kumi, mwelekeo wa kuutekeleza mkakati huo katika kipindi kifupi sana upo katika hatua nzuri. Kwa hiyo, wakae mkao wa kula, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wengine kwamba tuna mkakati kabambe na upo katika hatua nzuri ya kuukamilisha kabla ya muda uliopangwa ambao utatusaidia sana kupunguza changamoto za vituo vya polisi katika nchi hii.
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Spika, nashukuru pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, kwenye Kata nilizotaja za Oldonyosambu, Ololosokwan, Solosambu pamoja na Soitsambu ni kwamba kuna wananchi wengi ambao fomu zao zimezuiliwa kwenye Ofisi ya Uhamiaji.

Je, ni lini Serikali itamaliza uhakiki kwa haraka ili wananchi wapate Vitambulisho vya Taifa pamoja na vyeti vya kuzaliwa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili kuna wananchi wengi Wilaya ya Ngorongoro hasa Kata ya Orgosorok Loliondo; wengi wao wazazi wao walizaliwa Tanganyika wamefanya kazi walikuwa watumishi na wengine wamestaafu lakini bado wanasumbuliwa hata kupata vitambulisho vya Taifa pamoja na vitambulisho vya kuzaliwa.

Je, Waziri yuko tayari kuongozana nami kwa ajili ya kutatua matatizo ya wananchi hao?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Emmanuel Shangai, Mbunge wa Ngorongoro kwa pamoja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nikianza na ombi lake la kutaka tuambatane pamoja kwenye jimbo lake kutatua changamoto hizi mbili; nimhakikishie Mheshimiwa Lekisho Shangai tutafanya hivyo. Naamini tutakapokuwa tumekwenda kwenye hiyo ziara jimboni kwake tutaweza kujua na kupata undani wa changamoto alizozungumza ili tuweze hatua stahiki ili wananchi hawa wanaostahiki haki yao ya msingi ya kupata vitambulisho waweze kupata; ikiwemo wale ambao amezungumza mara ya kwanza ambao fomu zao Mheshimiwa Mbunge anasema kwamba zimezuiwa uhamiaji. Vile vile hata wale ambao amesema ni raia lakini bado wameshindwa kutambuliwa

Mheshimiwa Spikam, changamoto zote hizi mbili tutazishughulikia mimi na yeye kwa pamoja.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kuwa vitambulisho vya Taifa, kwa mfano NIDA, ni kazi kubwa kuvipata au ni janga kubwa kwa wananchi kuweza kuvipata.

Je! Mheshimiwa Waziri ataliambia Taifa au atawaambia wananchi watu ili kuweza kuvipata kwa wepesi waweze kupita njia gani ikiwa ni haki yao? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Fakharia kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna changamoto kidogo ya upatikanaji wa vitambulisho na changamoto hii inatokana na ukweli kwamba, tulikuwa na changamoto ya kimikataba kati ya mkandarasi ambaye alikuwa anapaswa kutoa huduma hiyo. Changamoto nyingine ilitokana na upungufu wa kadi ghafi ambazo ndizo zinatumika kuzalisha vitambulisho.

Mheshimiwa Spika, ikiwemo na changamoto ya tatu vilevile ambayo ni changamoto ya upatikanaji wa kadi ghafi zenyewe katika soko la dunia zilizosababishwa na athari za UVIKO-19. Kwa hiyo changamoto hizo ndizo zilizosababisha tukajikuta kwamba hatuna kadi za kutosha za kuzalisha vitambulisho hivi.

Mheshimiwa Spika lakini nataka nimkikishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba Serikali imefanya jitihada kuhakikisha changamoto zote hizi tatu zinatatuliwa. Nimani yangu kwamba changamoto za upatikanaji vitambulisho zitapungua hatua kwa hatua. Hata hivyo, nitoe wito kwa wananchi ama Waheshimiwa Wabunge kuwajulisha wananchi katika maeneo ambayo wanayasimamia na kuyaongoza, kwamba upatikanaji wa namba ya utambulisho bila kuwa na kadi unawezesha vilevile kuwafanya waweze kupata huduma mbalimbali za kijamii. Hivyo, kwa wale ambao bado wanasuburi kupata kadi zao waendelee kutumia namba za utambulisho wakati Serikali inaendelea na jitihada za kuhakikisha kwamba watanzania wote waliosajiliwa na kutambuliwa wanapata vitambulisho vya Taifa.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ndani ya Jimbo la Momba wapo baadhi ya wananchi wengi kadhaa ambao wamekosa kunufaika na Mfuko wa TASAF na zoezi la kuandikishwa kwenye mbolea kwa sababu wamekosa vitambulisha vya Taifa.

Je, ni lini Serikali itachukuwa jambo hili kwa haraka na kwa dharula ili wananchi hawa waweze kupata haki yao ya msingi kwenye mahitaji hayo? Ahsante.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Condester Sichalwe Mbunge wa Momba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na wananchi kukosa huduma mbalimbali, nilieleza katika swali la nyongeza la Mheshimiwa Fakharia kwamba namba za utambulisho zinaweza kutumika katika kupata huduma mbalimbali. Lakini kama kuna changamoto katika maeneo mahususi ambayo ameyagusia Mheshimiwa Mbunge, kwa mfano eneo hili la TASAF na sensa kama nilivyosikia sawa sawa.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, na mbolea.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, na mbolea! Basi nilichukuwe pamoja na kukaa na Mawaziri wa sekta husika hili tuweze kulifanyia kazi kama Serikali. Lakini suluhisho la kudumu ni kuhakikisha kwamba watanzania wote wanapata vitambulisho vyao, na ndicho kipaumbele cha Serikali na tunachukuwa jitihada ili kuhakikisha hili linatekelezeka. Na kwa bahati njema katika bajeti hii ya mwaka huu wa fedha tumetenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 42.5 kwa ajili ya ununuzi wa kadi ghafi milioni nane laki tano.

Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa kadi ghafi hizo utasaidia sana kuepukana na changamoto mbalimbali ikiwemo changamoto ambazo Mheshimiwa Mbunge amezungumza.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tulipokuwa tunafanya elimu ya sensa katika Mkoa wetu wa Iringa kuna baadhi ya vijiji wana vijiji kabisa hawajui kabisa kama wanapataje namba za utambulisho, na kuna baadhi wana namba za utambulisho muda mrefu sana hawajapatiwa NIDA.

Je, ni lini sasa waliopata namba watapata na wale ambao hawajasajiliwa watapata angalau elimu wajue wanasajiliwaje?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nikubaliane na Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna haja ya kuongeza jitihada za kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na huduma hii ya vitambulisho na katika kufanya hivyo kuna njia kadhaa. Njia moja ni kuhakikisha kwamba huduma hizi zinasogea karibu na wananchi. Katika kufanya jitihada hizo, Serikali imefanya kazi kubwa sana kuhakikisha inaimarisha Ofisi za NIDA katika ngazi za chini kwa maana ya Wilayani ili Maafisa hawa wa NIDA waweze kuwa karibu na wananchi na waweze kutoa huduma ikiwemo hii huduma ya Elimu kwa Umma.

Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza hilo, katika bajeti ya mwaka huu tunatarajia kuongeza ujenzi wa vituo zaidi 31 katika wilaya 31 nchini. Lengo ni kuhakikisha kwamba Wilaya zote katika nchi hii zinapata huduma ya NIDA ili kuwa karibu na wananchi waweze kupata huduma mbalimbali ikiwemo elimu itakayowezesha kuwasaidia kujua haki zao za msingi katika kupata kadi na vitambulisho vya NIDA kwa ujumla wake.
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Kwenye taasisi nyingi za Serikali na zisizo za Serikali kuna mkanganyiko mkubwa kwamba wananchi wengi wenye namba za NIDA hawapati huduma. Naomba kauli ya Serikali leo kuhusiana na wananchi wenye Namba za NIDA ambao hawana vitambulisho na wanakosa huduma hasa kwenye mikopo. Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Njau, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kauli ya Serikali ni kwamba huduma za Serikali popote zilipo zinatakiwa zitolewe kwa kutambua uhalali wa namba za vitambulisho. Kwa sababu hatuwezi kumhukumu mwananchi kutokupata huduma kwa kosa ambalo siyo lake. Kama amechukua hatua zote za kisheria kuweza kujisajili, amepatiwa namba ya kitambulisho na kadi hatujampa kwa kosa ambalo siyo lake, lazima huduma yake ya msingi apate.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kauli ya Serikali ni kwamba taasisi zote zinazohusika za Serikali, kama kuna changamoto basi tutakaa tuzungumze ndani tuone, inawezekana pengine kuna baadhi ya Taasisi kulingana na masuala ya kisheria au masuala ya kimiundombinu zinashindwa kutekeleza hayo. Tutalichukua kama Serikali kwa pamoja tuzungumze tuone tunalitatua vipi maeneo ambayo bado kuna tatizo katika kukibali ama kuzipokea namba hizo za utambulisho wa wananchi. (Makofi)
MHE. MOHAMED ABDULRAHMAN MWINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa wananchi ambao wamejisajili mwaka 2018, 2019 na 2020 na baadhi yao mpaka leo hawajapata vitambulisho hivyo: Nini kauli ya Serikali? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Mohamed Abdulrahman Mwinyi, Mbunge wa Chambani, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza wakati najibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro, kuhusu changamoto hii ya upatikanaji wa vitambulisho nilizungumza kwa ujumla wake na majibu yale yale yanaweza kusaidia kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Mwinyi kuhusu changamoto hii ya upatikanaji wa vitambulisho kwa nchi nzima ambayo inakumba majimbo yote likiwemo jimbo la Chambani.

Mheshimiwa Spika, nilieleza hatua gani Serikali imechukua ili kukabiliana na jitihada hizo. Hivyo basi, namwomba Mheshimiwa Mbunge aridhie na majibu yale yale ambayo nimeyajibu ambayo yaliainisha hatua ambazo Serikali inachukua kukabiliana na changamoto ya upungufu wa upatikanaji wa kadi kwa wananchi wa nchi nzima wakiwemo wananchi wake wa Jimbo la Chambani.
MHE. MAULID SALEH ALI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Kwa kuwa kumekuwa na wakandarasi wengi kutoka nje ambao wanatekeleza miradi yao nchini bila kutekeleza miradi hiyo kwa wakati; je, Serikali haioni haja sasa ya kuweza kudhibiti passport za Wakandarasi hao mpaka watakapomaliza miradi hiyo kwa wakati? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa maulid Saleh, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tatizo la Wakandarasi kutokutekeleza miradi ni la kimikataba na pia linahusisha mamlaka nje zaidi ya Uhamiaji. Kwa hiyo, hatua za kudhibiti zinaweza kuwa nyingi kulingana na mkataba husika. Hata hivyo, kama nilivyoeleza katika jibu langu katika swali la msingi, kwamba pale ambapo Jeshi la Uhamiaji linahitajika kutumia sheria hii ambayo nimeiorodhesha hapa ambayo inaipa mamlaka kufanya hivyo kwa ajili ya maslahi mapana ya Taifa, kwa misingi ya sheria hii ambayo nimeizungumza, ikihitajika kufanyiwa hivyo; na imeshafanya hivyo mara kadhaa, lakini haiwezi ikatoka ikasema kila mradi ambao haujakamilika, basi twende tukakamate passport bila kufuata utaratibu.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwanza nimshukuru Waziri kwa majibu mazuri ambayo ameyatoa, nina swali moja tu la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mkoa wa Kilimanjaro ni mojawapo ya Mikoa ambayo ina uhitaji wa magari ya polisi hasa magari ya doria; je, Serikali ina mpango gani Mkoa wa Kilimanjaro kupata magari katika awamu hii ya kwanza ya magari 78 ambayo yanaingia nchini mwezi Aprili? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zuena Athumani Bushiri kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kutokana na jitihada zake anazochukua za kuhangaikia Mkoa wake wa Kilimanjaro basi tumepokea mapendekezo yake na tutahakikisha kwamba magari haya yakija tutaangalia uwezekano vilevile tuweze kupeleka Mkoa wa Kilimanjaro. (Makofi)
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia kwamba Mkoa wa Songwe ni mpya na upo mpakani na kwenye jibu la Mheshimiwa Waziri amesema kwamba magari yatapelekwa kwenye maeneo ambayo yanauhitaji mkubwa, Mkoa wa Songwe una uhitaji mkubwa wa magari ya Polisi.

Mheshimiwa Spika, naomba kufahamu nini ahadi ya Serikali katika kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto ya magari katika Mkoa wa Songwe? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juliana Shonza, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Songwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimejibu katika swali la msingi kwamba magari yale yatakapokuja tutayapeleka katika Mikoa ambayo ina uhitaji zaidi na Mheshimiwa Mbunge amethibitisha kwamba Mkoa wa Songwe ni moja kati ya Mikoa ambayo ina mahitaji basi tutalizingatia hilo.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa hii nafasi.

Mheshimiwa Spika, swali langu ni kwamba hali ni mbaya katika Wilaya ya Mbozi hivi ninavyoongea Mkuu wa Polisi wa Wilaya hana gari hata la kutembelea. Kwa hiyo, katika hayo magari 78 Mheshimiwa Waziri naomba unihakikishie gari moja liende katika Wilaya ya Mbozi ili kumuokoa yule Mkuu wa Polisi wa Wilaya. Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nitakuwa sijakosea nadhani Wilaya yake ndiyo ile ya Mheshimiwa Silinde, kama hivi ndivyo hivi karibuni tulipeleka gari huko ambalo halikuwa jipya, kwa hiyo litasaidia nadhani tatizo litakuwa limepata ufumbuzi kama itakuwa siyo Wilaya hiyo ni Wilaya nyingine basi tutalizingatia vilevile. (Kicheko)
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa na mimi nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Liwale ilikuwa na gari moja tu ambalo kwenye Uchaguzi uliopita gari lile lilichomwa moto mpaka sasa hivi Wilaya nzima ile haina gari hata moja. Ni nini mpango wa Serikali kutupatia miongoni mwa hayo magari 78?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza nikushukuru kwa kuliweka vizuri.

Mheshimiwa Spika, naomba nijibu sasa swali la Mheshimiwa Kuchauka Mbunge wa Liwale kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimejibu kwenye swali la msingi kwamba magari haya yatakapokuja tutayapeleka katika maeneo ambayo yana mahitaji zaidi, kwa kweli maeneo ambayo yana mahitaji zaidi ni mengi kwa hiyo siyo rahisi kuweza kukamilisha kwa wakati mmoja kwa mwezi huu.

Kwa hiyo, niombe nikubaliane na Mheshimiwa Spika kwamba hoja za Waheshimiwa Wabunge tunajua ni za msingi, lakini magari yatakuja kwa awamu basi tutazingatia wapi kuna mahitaji zaidi.

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimejibu katika maswali yaliyopita ikiwemo na Mheshimiwa Mbunge Kuchauka kama itaangukia katika maeneo ambayo yana mahitaji zaidi na zaidi utapata mapema lakini nikuhakikishe kwamba tunafahamu na tunafanyia kazi. (Makofi)
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana swali langu dogo tu la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na magari mengi ambayo mmeyatuma yatakuja kwa awamu. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kutenga fedha za kutengeneza magari yaliyopo ambayo ni mengi tunayaona yapo katika vituo vingi vya Polisi ni mabovu. Sasa ni wakati mzuri labda muweze kutenga fedha ili tuweze kutengeneza haya yaliyopo tukisubiri hayo mageni, nashukuru. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kilave Mbunge wa Temeke kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hoja yake ni ya msingi lakini nimhakikishie kwamba tumekuwa tukifanya hivyo na hata ndani ya Jeshi la Polisi tuna kitengo maalum kwa ajili ya matengenezo ya magari ya Polisi yale ambayo yanaweza kutengenezeka tunafanya hivyo na tutaendelea kufanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo tunafikiria kuja na mpango mwingine ambao utasaidia sana kuweza kutatua changamoto ya ubovu wa magari, nadhani wakati tutakapokuja kuwasilisha bajeti yetu hapa tutakuwa na nafasi pana zaidi ya kuweza kufafanua, lakini nimpongeze kwa wazo lake ni zuri na tunaendelea kulifanyia kazi na tutazidi kuliboresha zaidi.
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Mheshimiwa Waziri ni kwamba hali ya gari la Sengerema anajua mpaka Mheshimiwa Simbachawene aliniahidi mwaka jana tutapata gari jipya. Sasa haya magari yanayokuja mwezi huu unanihakikishia gari moja linakwenda Sengerema kwa sababu hali iliyopo ni mbaya. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa
Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tabasam Mbunge wa Sengerema kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama mwongozo wako ulivyoutoa na kama ambavyo nimejibu nyuma kwamba tutapeleka magari haya kulingana na uhitaji zaidi, kwa hiyo tutaangalia kama Jimbo la Sengerema limeangukia katika eneo hilo atapata kama itabidi asubiri basi atapata siku za mbele pale ambapo yatapatikana magari ya ziada.
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Tunduru ni Wilaya ambayo ipo mpakani na jiografia yake ni mbaya lakini pia kituo cha polisi kuna gari moja tu na tuna kilomita za mraba 18,778.

Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kunihakikishia kwamba katika magari hayo 78 nasi tutapata gari moja? (Makofi/Kicheko)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba nirejee tena majibu yangu kama ambavyo nimejibu mwanzo kwamba tunatambua kwamba Jimbo la Tunduru lina uhitaji wa gari basi na lenyewe vilevile tumepokea.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza, nina maswali mawili: -

Kwanza, kwa kuwa katika Tarafa mbili zilizobaki ambazo Serikali bado haijawekeza ujenzi wa vituo vya Polisi, kumekuwa na changamoto kubwa ya mapigano kati ya wafugaji na wakulima lakini wakati huo huo Tarafa hizo zipo umbali mrefu sana kutoka kule ambapo vituo vya Polisi vipo hivi sasa: -

Je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu katika Tarafa za namna hii zenye changamoto kubwa ya wakulima na wafugaji kuweza kuwekeza kama ilivyowekeza katika sekta nyingine ujenzi wa Vituo vya Afya kwa kuanzia na bajeti ya mwaka huu? (Makofi)

Pili, ningeomba Mheshimiwa Waziri anifahamishe ni lini atakuwa na nafasi ya kuweza kutembelea katika Wilaya ya Kilwa ili tuweze kushirikiana na Wizara yake katika kutatua changamoto ambazo zinakabili upatikanaji wa vituo vya Polisi. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza kwa pamoja ya Mheshimiwa Francis Ndulane, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza alitaka kujua mpango wa Serikali wa kujenga vituo vya Polisi kama vile ambavyo tunafanya katika vituo vya Afya na shule, nataka nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba wazo lake tumeshaanza kulifanyia kazi, tulikuwa na mazungumzo kati ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi pamoja na Wizara ya TAMISEMI.

Nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Innocent Bashungwa kwa kulipokea wazo hili na hivi sasa tunavyozungumza wataalam wetu, Makatibu Wakuu wa Wizara hizi mbili na wataalam wetu wanakaa kuangalia uwezekano huo kupitia kwenye Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hili ni jambo ambalo tunalichakata na kama litakuwa limekwenda vizuri tunaweza tukaliwasilisha hapa Bungeni kulingana na mapendekezo ambayo wataalam watatupatia.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la mimi kutembelea, hilo halina mjadala. Nimhakikishie Mheshimiwa Francis Ndulane kwamba tutapanga ratiba ili tuweze kwenda katika Jimbo lake kuhamasisha wananchi, kama vile nilivyojibu kwenye swali la msingi kwamba kama wananchi wataweza kufanya utaratibu wa kupata eneo na hata wakianza wa kwa nguvu zao, kama ambavyo kuna maeneo Waheshimiwa Wabunge wamefanya, naye pia alifanya hivyo katika baadhi ya vituo vyake, hata juzi hapa Waziri wa Ardhi, Mheshimiwa Dkt. Angeline Mabula katika Jimbo lake pale, alifanya jitihada za kuhamasisha wananchi kujenga Kituo cha Polisi Ilemela. Kwa hiyo, jitihada kama hizi tutaziunga mkono.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Ndulane ninajua jitihada zake katika kupigania wananchi wake na hivyo basi nimhakikishie tutashirikiana kutafuta njia mbadala ya haraka wakati tukisubiri mipango ya muda wa kati na muda mrefu wa Serikali kutatua changamoto hii kwa kudumu.
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Spika, ahsante kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, maeneo mengi Mkoa wa Lindi yana changamoto ya usalama hasa katika migogoro ya wakulima na wafugaji hata wakati wa msimu wa korosho na ufuta usalama wa wananchi unakuwa mgumu. Maeneo mengi yapo mbali na Makao Makuu ya Wilaya, mfano Kilimarondo ipo kilometa 120, Nambiranje Wilaya ya Ruangwa napo ni mbali, pia Nangaru Wilaya ya Lindi.

Je, Serikali itajenga lini Vituo vya Polisi maeneo hayo ili kuwahakikisha usalama wa wananchi. Ahsante? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuhusiana na changamoto hiyo ama uhitaji huo wa vituo vya Polisi katika Mkoa wa Lindi, lakini kuna kazi ambayo tayari tumeshaanza kuifanya. Kwa mfano, katika bajeti hii ambayo tunaendelea nayo kuna maeneo ambayo Serikali inaendelea na ujenzi wa vituo vya Polisi na hata bajeti inayokuja tumezingatia hilo.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo hatuwezi kutatua changamoto hii kwa wakati mmoja kwa maeneo yote, lakini nitakapokuja kwenye ziara kuitembelea Kilwa Kaskazini nitamuomba Mheshimiwa Mbunge nae tuwe pamoja ili tuangalie namna gani tunaweza kuharakisha utatuzi wa changamoto hii. (Makofi)
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naamini Serikali inafanya kazi kubwa katika sekta zote, ninaamini na kujua kwamba ulinzi na usalama ni jambo muhimu sana katika ustawi wa wananchi na raia wake.

Mheshimiwa Spika, Jimbo langu la Mchinga lina Kata 11 na Tarafa nne, Tarafa mbili tu ndiyo zenye Vituo vya Polisi. Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba Tarafa hizi Mbili zilizobaki zinapata Vituo vya Polisi? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Salma Kikwete Mbunge wa Mchinga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nijibu kwa ujumla wake kwamba mahitaji ya vituo vya Polisi kwa kweli ni makubwa labda nitoe mfano mmoja tu. Vituo Daraja ‘B’ vilivyopo ni 93 wakati mahitaji ni 563 utaona tofauti ilivyokuwa pana sana, kwa hiyo changamoto hii ipo maeneo mengi ikiwemo kwenye Jimbo la Mheshimiwa Salma Kikwete Mchinga.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie kwamba kama Serikali tunatambua changamoto hiyo na tupo katika hatua ambazo nyingine nilizieleza katika majibu yangu ya awali na hivyo basi tupewe muda ili tuweze kutatua changamoto hii kwa mapana yake kwa ujumla katika maeneo yote ambayo yana changamoto ikiwemo Jimbo la Mchinga. (Makofi)
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Chemba ujenzi wake umesimama kwa miaka minne sasa, naomba kumuuliza Waziri ni lini sasa watatoa fedha za kumalizia? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika utaratibu wa kumaliza vituo vya Polisi tumekuwa tukitumia njia mbalimbali ikiwemo kutumia Mfuko wetu wa Tuzo na Tozo ambao upo chini ya Jeshi la Polisi, ambao katika mwaka huu wa fedha tumeshaufanyia ujenzi na ukarabati wa vituo kadhaa katika maeneo mbalimbali nchini. Hivyo basi nichukua hoja hii ya kituo cha Chemba tuona kama tunaweza kumaliza kupitia Mfuko wa Tuzo na Tozo katika kipindi cha mwaka huu wa fedha unaokuja.

Mheshimiwa Spika, tuangalie kimefikia kiwango gani na mahitaji ni kiasi gani na uwezo wa fedha zilizopo ni kiasi gani na vipaumbele vilivyopo ni vipi.(Makofi)
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Katavi na Wilaya zake kumekuwa na wimbi la mauaji ya mara kwa mara hii ni kwa sababu hakuna vituo vingi vya polisi.

Je, ni lini mtatujengea kituo cha Polisi katika Kata ya Kasekese Wilaya ya Tanganyika?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Selemani Kakoso kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ninaomba nilichukue hili tulifanyie kazi ili tuone hatua ya kuchukua.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwanza nitumie fursa hii kutoa pole kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Ukerewe, kwa msiba wa askari uliopatikana jana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada hayo, nina maswali mawili ya nyongeza, la kwanza; kwa kuwa tathimini tayari imeshafanyika, lakini miundombinu iliyoko pale hasa mifumo ya maji safi na maji taka pamoja na mapaa ya kituo chenyewe na nyumba za watumishi ni mbovu sana, sasa Serikali haioni sababu kuchukua jambo hili kama la dharura na ikalifanyia kazi kwa haraka kadri inavyowezekana ili kujenga mazingira mazuri ya utendaji kwa watumishi wetu pale?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri haoni sababu, namwomba ikiwezekana twende naye pale ili aangalie mazingira kwa uhalisia tuweze kujadiliana tuone namna njema ya kuboresha mazingira ya utendaji kwa watumishi wetu wa Ukerewe? Nashukuru sana. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Ukerewe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza alikuwa anaomba tuchukue jambo hili kama dharura; basi kwa sababu Mheshimiwa Mbunge anakifahamu vizuri kituo hiki naomba nikubaliane naye kwamba tunalichukulia hili jambo kama la dharura. Kwa hiyo nitatoa maelekezo kufuatilia, kuona jinsi gani ambavyo tunaweza tukafanya ili yale mambo ya dharura tuweze kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kuhusu suala la mimi kwenda kwenye Jimbo lake, hilo halina tatizo, tutapanga ratiba baada ya Bunge hili kumalizika ili tuweze kwenda kutembelea jimbo lake kuona wenyewe jinsi ambavyo tunaweza kusaidiana kutatua changamoto za kidharura ambazo Mheshimiwa Mbunge amezieleza.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kumekuwa na ukosefu wa amani katika baadhi ya maeneo hasa katika Kata ya Ngaya na kata ya Buriye na kupelekea wananchi sasa kuweza ku-share na Mbunge wao ambaye ni mimi kujenga Kituo cha Polisi na sasa kimefikia kwenye hatua ya lenta. Sasa swali langu ni lini Mheshimiwa Waziri atafika kuja kuweka jiwe la msingi sambamba na kutenga fedha kuja kumalizia Kituo hicho cha Polisi? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Iddi, Mbunge wa Msalala, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge na wananchi wake kujitolea kujenga kituo hiki na kama ambavyo nilivyokuwa nimejibu jana kwa zile jitihada ambazo zimeanzishwa na wananchi, tumeshajitahidi kuziendeleza. Tuna mfuko wetu wa tozo na tozo, japokuwa hauwezi kukidhi maeneo yote, lakini tutajitahidi kuangalia tutakachoweza kufanya ili tuongeze jitihada hizo ambazo Mheshimiwa Mbunge na wananchi wake wamezifikia. Nitakuwa tayari kwenda kuweka jiwe la msingi wakati wowote ambapo Mheshimiwa Mbunge mimi na yeye tutashauriana yaani muda muafaka wa kuweza kufanya kazi hiyo.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona, kwa miaka 20 sasa Wilaya ya Kilolo haina Makao Makuu ya Polisi na wala kwenye Wilaya penyewe hakuna Kituo cha Polisi.

Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi za viongozi mbalimbali kujenga Makao Makuu ya Polisi katika Wilaya ya Kilolo kwenye Mji wa Kilolo?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri kwamba Mheshimiwa kwenye Jimbo lake la Kilolo kama ambavyo Wilaya kadhaa zimekuwa zina ukosefu wa Vituo vya Polisi vya Wilaya na hii ni moja kati ya mambo ambayo jana niliyazungumza na mikakati ya Kiserikali ya kiujumla ya kukabiliana na tatizo hili, hivyo nimwombe Mheshimiwa Mbunge avute Subira, lakini suala hili tumelichukua kwa uzito wake.
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza msitu wa Rubya umetoa milioni 50 kwa ajili ya kujenga Kituo cha Polisi, pale Rubya.

Je, Serikali ipo tayari kuwaongezea fedha ili kituo hicho kiweze kukamilika pamoja na nyumba za maaskari?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli fedha hizo zimetolewa, lakini mpaka sasa taarifa nilizokuwa nazo ni kwamba kazi hizi zinaendelea vizuri na hakujaonekana dalili za kushindwa kukamilika wala wafadhili hawajaonesha dalili ya kushindwa kuendelea kukamilisha kituo hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba tuwape muda wakamilishe tuone watafikia wapi, kama kutatokea changamoto baadaye, basi tutaangalia namna gani ya kuweza kulikabili.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kituo cha Polisi cha Wilaya Bunda ni chakavu sana na Mheshimiwa Waziri anakijua, amefika pale na kinahudumia Majimbo matatu Mwibara, Bunda Mjini na Bunda. Je, ni lini Mheshimiwa Wizara atakikarabati kituo hicho ili kiendane na hadhi ya Wilaya?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Kituo cha Bunda kiko chakavu na binafsi nakumbuka niliwahi kutembelea kituo hiki na hata Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo hili naye vilevile alinikumbushia juu ya ukubwa wa changamoto hii. Hivyo basi, nimhakikishie Mheshimiwa Ester Bulaya kwamba tunafahamu na pale ambapo hali ya kibajeti itakapokaa vizuri, basi tutakifanyia kazi kituo hiki.
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kata ya Kilungule, Jimbo la Mbagala wananchi wamejenga Kituo cha Polisi kwa nguvu zao, lakini sasa ni mwaka wa tatu Serikali haijafanya juhudi ya kufungua kituo hicho. Je, ni lini Wizara italeta watumishi ili kituo hicho kifanye kazi?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janejelly, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kituo hiki vilevile nakifahamu nakumbuka wakati ambapo tunaanza jitihada za kujenga hiki tulishiriki kufanya harambee. Niwapongeze sana wananchi walioshiriki lakini niwahakikishie kwamba juhudi hizo za wananchi hazitapotea bure kwa vituo vyote ambavyo wananchi wametoa nguvu zao, basi Serikali tutaangalia kadri itakavyowezekana, hali itakaporuhusu tuweze kuvikamilisha.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Napenda kuuliza kwamba,je, Serikali ina mpango gani wa kujenga kituo cha Polisi Nanyamba kwa sababu sasa hivi Nanyamba ni Makao Makuu ya Halmashauri ya Mji wa Nanyamba na kuna changamoto za kiulinzi kule mpakani? Nakushukuru.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chikota, Mbunge wa Nanyamba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mpango wa kujenga vituo vikubwa zaidi, kukarabati, kujenga vipya katika maeneo ambayo hakuna, lakini mambo haya hatuwezi kuyakamilisha kwa wakati mmoja na ndio maana hata ukiangalia bajeti inayokuja mwaka huu tunatarajia kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Makao Makuu ya Polisi Mtwara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mnaona jitihada ya Serikali tunaenda hatua kwa hatua. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kuwa hata Makao Makuu ya Mtwara tunataka kujenga, ina maana hata changamoto za Wilaya nazo tutazifanyia kazi hatua kwa hatua. Kwa hiyo nimwombe mvute Subira.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa idadi kubwa ya waathirika wa ukatili ni wanawake na watoto.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuzuia idadi kubwa ya takwimu tunazoletewa hapa ili kupunguza ukatili huo? (Makofi)

Swali la pili, pamoja na kuwa Serikali imetoa taarifa kuwa wanaume 3,077 ndiyo waliofanyiwa ukatili wa kulawitiwa, sina shaka idadi kubwa itakuwa ni watoto wa kiume.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwalinda watoto wa kiume ili kusudi wasifanyiwe ukatili? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la takwimu linaweza kuonekana kwamba ni nyingi kwa sababu ya jitihada ambazo Serikali imechukua kupitia Jeshi la Polisi la kuanzisha Dawati la Kijinsia, ambapo hapo zamani watu wengi ilikuwa wanapata shida au wanaona aibu kuripoti matukio kama haya kwenye counter ya polisi. Kupitia uendeshwaji wa dawati hili watu wengi zaidi wamekuwa wakijitokeza na kutoa taarifa na hivyo basi kufanya sasa yale matukio ambayo hayatolewi taarifa zamani sasa yanaweza kutambulika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la mikakati ya kuwalinda. Suala la kuwalinda watoto wetu si jukumu la Serikali peke yake, hili ni suala la kila mmoja wetu tukianzia wazazi. Kwa hiyo, niseme wakati Serikali inafanya kila jitihada kuhakikisha kwamba inaweka mazingira mazuri ya ulinzi ikiwemo kuhakikisha kwamba inachukua hatua kali kwa wale wote ambao wanahusika na vitendo vya kuzalilisha Watoto wetu naomba sana wazazi na wenyewe wachukue majukumu yao ipasavyo, kwa maana ya kuangalia kuhakikisha wanafuatilia nyendo za watoto wao na kuhakikisha kwamba wanawalinda na kuwasimamia. (Makofi)
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru.

Kwa kuwa vitendo vya ukatili vimezidi kuongezeka kila siku tunasikia matukio mbalimbali, na kwa kuwa adhabu mbalimbali zinatolewa lakini vitendo vinazidi kuongezeka.

Je, Serikali sasa haioni ni wakati muafaka wa ku-review hizi adhabu ili ziwe kali zaidi watu wasiendelee kufanya hivi vitendo vya ukatili? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tunza Malapo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ametoa wazo zuri nadhani ni jambo la kulichukua na kulitafakari na kulifanyia kazi. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kumekuwa na mauaji na vipigo vingi sana kisa wivu wa kimapenzi. Serikali inachukua jukumu gani la kuhakikisha wale wanaofanya vitendo hivyo wanachukuliwa hatua kali na za haraka ili mambo hayo yasiendelee kutokea katika jamii ya kitanzania. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sophia Mwakagenda kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli yametokea matukio ya mauaji yenye vyanzo mbalimbali ikiwemo chanzo ambacho amekizungumza Mheshimiwa Mbunge. Mheshimiwa Mbunge anasema kwamba adhabu hizo hazijasaidia. Lakini labda nieleze kwa ufupi kwamba, ukiangalia katika kipindi cha mwezi Januari mpaka Februari tulishuhudia matukio mengi sana ya mauaji ya vyanzo mbalimbali kwenye jamii, ikiwemo vyanzo hivyo vya wivu wa mapenzi, ushirikina, ulevi uliokithiri, kugombania mali, urithi na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumechukua hatua ya kuunda Tume, Tume imefanya kazi yake vizuri imetuletea mapendekezo mengi, lakini katika mambo makubwa na ya msingi ambayo nimetaka nilizungumze hapa kwamba mbali ya kuchukua hatua jambo kubwa la msingi ni kuhakikisha kwamba tunadhibiti matukio kama haya yasijitokezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia taarifa ambayo tumepewa na Tume kuna hatua mbalimbali ambazo tumezichukua za kuhakikisha tunadhibiti. Moja katika hatua muhimu sana ambayo tumechukua ni kuhakikisha kwamba tunaimarisha mifumo katika ngazi za Kata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Jeshi la Polisi mtakumbuka hivi karibuni walihitimu askari zaidi ya zaidi ya 4,200 na zaidi, hao wote tumewapeleka kwenye kata kuhakikisha kwamba kwenye kata tuna askari wa kutosha ambao wana weledi wa kusimamia masuala ya usalama katika ngazi husika na kushirikiana na Kamati za Ulinzi za Kata pamoja na wadau mbalimbali ikiwemo wananchi kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, mbali ya kuchukua hatua lakini jitihada kubwa vilevile tunazielekeza katika kudhibiti matukio kama haya yasiweze kujitokeza.
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Niishukuru Serikali kwa majibu mazuri na kwa operesheni inayoendelea maana Dar es Salaam ilikuwa kila ukikaa unasikia koro koro nyuma ya gari yako, kitu ambacho ni kinyume cha sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Kifungu cha 54 cha Sheria, Sura ya 168 ya Usalama Barabarani; je, Waziri ameshatoa vibali vingapi mpaka sasa vya utumiaji wa ving’ora ukiondoa magari yaliyoorodheshwa?

Swali la pili; je, Serikali ina mpango gani wa kufanya marekebisho ya sheria hii ambayo ni ya muda mrefu ili kuweza kutoa adhabu stahiki kwa watu wanaovunja sheria hii, vilevile kuweza kuona namna ya kuongeza viongozi wenye kustahili heshima hii na kuweza kuwaondolea taharuki wananchi. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jerry Silaa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa tokea nimepewa dhamana hii sijawahi kutoa kibali hata kimoja.

Pili, kuhusu mabadiliko ya sheria tunao mchakato ambao unaendelea wa mabadiliko ya sheria ya usalama barabarani, kwa hiyo kwa kuwa mchakato huu hatma yake ni hapa Bungeni, basi Mheshimiwa Mbunge naomba hoja zake aziandae vizuri ili kuweza kuhakikisha mchakato huu utakapofika Bungeni aweze kusaidia kutoa hoja za kuongeza yale ambayo anahisi yanafaa katika marekebisho hayo ya sheria itakapokuja. (Makofi)
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; kwa kuwa eneo la kutoka Sikonge kwenda Inyonga lenye kilometa 161 halina mawasiliano. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kunakuwepo na usalama kwenye eneo hilo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Mheshimiwa Waziri katika majibu yake amesema kwamba wamiliki wa mabasi wanaweza kuomba kuondoka, kuanza safari zao pale Dar es Salaam muda wa saa tisa usiku au saa kumi. Je, Mheshimiwa Waziri uko tayari kutoa tamko hapa Bungeni kwamba mabasi hayo yanaweza kuanza safari muda wa saa tisa au saa kumi?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Taska Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na mkakati ambao tunao katika kuhakikisha eneo hilo linakuwa salama. Kwanza nikupongeze wewe binafsi kwa kuweza kutupatia changamoto ya kufikiria kuanza usafirishaji wa mabasi ya abiria usiku.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari kutekeleza maagizo Mheshimiwa Spika na maombi ya Waheshimiwa Wabunge tumeshaanza kulifanyia kazi suala hilo.

Mheshimiwa Spika, tumekaa na Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi ambao ndiyo wadau wakubwa kuangalia jinsi ya kuweza kufanya na tumeamua kulipa majukumu Baraza la Usalama Barabarani la Taifa ambalo limesheheni wajumbe ama wadau kutoka taasisi muhimu ikiwemo Jeshi la Polisi, LATRA, TANROADS na kadhalika ili wataalam hawa waweze kutushauri namna bora ambayo itaweza kusaidia kuruhusu magari haya kuweza kutembea usiku ikiwemo hili eneo ambalo umeliruhusu.

Mheshimiwa Spika, miongoni mwa mambo ambayo tunategemea kutoka kwa wataalamu hawa ni jinsi ya kuweza kudhibiti changamoto zilizopelekea maamuzi ya Serikali mwaka 1990 kuzuia ambayo ilikuwa ni mambo mawili makubwa.

Mheshimiwa Spika, moja; ilikuwa ni kutokana na changamoto ya ujambazi na utekaji kipindi hicho; pili; ilikuwa ni ajali ambazo zilikuwa zikitokea usiku na kuharibu maisha ya Watanzania wengi.

Mheshimiwa Spika, hivyo basi; tunataka kuhakikisha kwamba wakati ambapo tunalitafakari jambo hili tutakaporuhusu tuweze kuhakikisha kwamba mabasi haya yanaruhusiwa kusafiri lakini wananchi wetu wanaendelea kubakia salama. Hivyo Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie kwamba jitihada hizi za kuhakikisha kwamba eneo hilo na maeneo mengine nchi nzima yanakuwa salama kuruhusu usafiri wa usiku yanaendelea.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni kuhusu tamko; kama ambavyo nimezungumza kwamba tunaomba nitoe tamko kwamba wale ambao wanaona kuna haja ya kuanza safari zao mapema basi walete maombi na tamko ni kwamba tutaridhia maombi hayo kwa wale ambao watakuwa na haja ya kuanza safari hizo wakati tunaendelea na jitihada hizo za kutafutia ufumbuzi wa kudumu suala hili.

SPIKA: Mheshimiwa Waziri maombi anakuwa analeta nani, mmiliki wa chombo cha usafiri au unaleta mkoa husika au nani analeta hayo maombi?

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, maombi yawasilishwe na wenye vyombo vya usafiri ama wamiliki wa mabasi hayo ambayo yanahitaji kusafiri kwa nyakati hizo.
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Mabasi ya abiria yanayosafiri kutoka Mkoa wa Dar es Salaam kwenda Mkoa wa Kagera na Nchi jirani ya Uganda kupita Wilaya ya Misenyi hulazimika abiria kulala katika Mji wa Kahama na wananchi kupata adha kubwa usiku kucha.

Mheshimiwa Spika, katika Pori la Biharamulo kuna vituo vya polisi vingi kila baada ya kilometa chache ambayo ni pongezi kubwa kwa Serikali.

Je, ni lini sasa mabasi yanayotoka katika Mkoa wa Dar es Salaam kwenda Mkoa wa Kagera na Nchi ya Uganda kuruhusiwa kusafiri mpaka kufika bila wananchi kulala njiani na kupata adha kubwa?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kyombo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali lake linafanana na swali ambalo la msingi ambalo Mheshimiwa Taska Mbogo ameuliza. Hivyo niombe majibu ambayo nimeyajibu kwenye swali la msingi yaendelee kubakia hivyo hivyo.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi. Sheria zilizopo sasa Tanzania mabasi na malori yanatembea mchana na malori ndiyo yanayotembea usiku lakini duniani kote mabasi yanatembea muda wote, malori yanatembea mchana mwisho saa 12:00. Je, ni lini na sisi Tanzania tutakwenda na utaratibu ambao uko duniani ili twende na wenzetu katika maendeleo?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa
Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Yahaya Massare kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, lengo ni kuhakikisha kwamba shughuli za uchumi zinaendelea kufanyika nyakati zote. Tunaamini kabisa kwamba mabasi na malori na magari yote yakiweza kutembea masaa 24 yatachangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, hivyo siyo suala la kusema yupi ni bora kuliko mwingine lakini changamoto ambayo nimeizungumza ni kwamba lazima tutakapofanya hivyo tuzingatie usalama wa wananchi wa nchi yetu na tumegundua kwamba mabasi na malori ndiyo ambayo ni visababishi vikubwa vya ajali. Nitatoa mfano wa ajali zilizotokea hivi karibuni ajali ambayo imetokea pale Tanga hivi karibuni ambayo iliua takribani Watanzania 20 ilikuwa ni kati ya lori na basi tena nyakati za usiku. Ajali iliyotokezea hapa Kongwa halikadhalika.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba concern ya Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wengine kuona kwamba huduma hizi zinaweza kuimarishwa na kutoa nafasi kwa wananchi wetu kuweza kutoa mchango wao katika uchumi wa nchi yetu kwa ufanisi zaidi tumezipokea na tutazifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza mikakati hiyo imeshaanza na tuvute subira pale ambapo wataalam wetu watatushauri utaratibu bora zaidi wa kufanya basi tuweze kuruhusu mabasi hayo yaweze kutembea muda wote.
MHE. MWATUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kujibu maswali yangu yenye kina na ambayo mimi mwenyewe nimeyaelewa. Napenda kumuuliza swali langu hivi, je, ni lini sasa hizo milioni 15 ambazo zimekisiwa kwenda kununuliwa mapikipiki pamoja na hayo magari katika wilaya nyingine pamoja na Mikoa, lini sasa Serikali itapeleka pesa hizo ili zifanyike kununulia magari hayo? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwatum Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama Ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, shilingi bilioni 15 sehemu ya fedha hiyo tayari imekwisha tolewa na gari hizo tayari zimekwishaagizwa. Tunatarajia mwezi Agosti, 2023 tuweze kupokea magari hayo utaratibu wa Serikali ambao tunanunua magari hayo kupitia GPSA. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba sehemu ya fedha hizo tayari zimeshatolewa na sehemu ya magari hayo yamekwishaagizwa na mara yatakapowasili basi tutaanza utaratibu wa kuyagawa katika wilaya kama ambavyo tumepanga.
MHE. AGNESTA. LAMBERT KAIZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Kwa kuwa sheria zetu siyo amri ya Mungu na kwa kuwa ndani ya Bunge hili tumekwisha rekebisha sheria mbalimbali. Je, Serikali inapata kigugumizi gani kuleta Muswada wa Marekebisho ya Sheria hii ya Uraia Pacha? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kwa kuwa Katiba yetu ya nchi inakataza ubaguzi wa aina yoyote ile. Je, Serikali haioni kuwa kama raia wake ambao wamepata urai nchi nyingine kwamba huu nao ni ubaguzi kwao? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili kwa pamoja ya nyongeza ya Mheshimiwa Agnesta Lambert, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli sheria siyo msahafu na sheria hizi zinatungwa kwa maslahi ya watu, lakini pia zinatungwa kwa matakwa ya watu. Bado Serikali haijajiridhisha kwamba uraia pacha ni takwa la wananchi walio wengi na ndiyo maana hata ukiangalia katika mchakato wa Katiba uliyokwama ambao ulihusisha maoni ya wananchi mbalimbali Serikali ilipendekeza hadhi maalum na siyo uraia pacha. Kwa sababu halikuwa takwa la wananchi waliyo wengi lakini ikitokezea haja hiyo Serikali italiangalia.

Mheshimiwa Spika, sheria hii na hili haina maana kwamba Serikali ina ubaguzi na ndiyo maana tupo katika hatua za mwisho mwisho kuanzisha utaratibu wa kuwa na hadhi maalum kwa ndugu zetu hawa ambao wananchi nje ambao utaweza kuwapa fursa mbalimbali, wataweza kupata fursa nyingi ambazo wenyewe wamependekeza kulingana na maoni waliyotoa. Kuna fursa kama kumi ambazo utaratibu huu utakapokamilika zitaweza kutolewa kwa ndugu zetu hawa Watanzania waliochukua uraia wa nchi nyingine.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa diplomasia ya kiuchumi inafanya watanzania wengi kwenda nchi mbalimbali duniani kutafuta mazingira ya kiuchumi na ili wasibaguliwe kule na wanataka kufaidika na huduma hiyo…

SPIKA: Mheshimiwa swali lako.

MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Je, Serikali haioni sasa ni muda muafaka wa kufanya marekebisho ya sheria hizo ili Watanzania hao waweze kufaidika na uchumi wa dunia? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu katika majibu yangu ya swali la msingi la Mheshimiwa Agnesta, kwamba Serikali imeona juu ya umuhimu wa waliokuwa watanzania hawa waliochukua uraia wa nchi nyingine kuweza kufaidika na fursa mbalimbali hapa nchini. Lakini siyo tu kwa wao kufaidika, hata kutoa michango yao katika uchumi wa nchi yetu na maendeleo ya nchi hii.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana nimeeleza kwamba katika kuliona hilo tupo katika hatua za kuweza kuruhusu utaratibu wa hadhi maalum kwa raia hawa ambao wataweza kufaidika na mambo mbalimbali na wataweza kuchangia vilevile katika maendeleo ya nchi yetu. Miongoni mwa fursa hizo ni fursa tatu tu ambazo zitahitaji baadae marekebisho ya sheria na wakati huo utakapofika tutazileta, lakini fursa zingine zote hazihitaji mabadiliko ya kisheria na zitaweza kuruhusika kwa pale ambapo utaratibu huu utakapokuwa umekamilika.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Serikali lakini ni ukweli usiopingika kwamba maslahi ya watumishi wa idara hii ya Jeshi la Polisi bado yanahitaji maboresho.

Je, Serikali ina mpango gani mahususi wa kuboresha maslahi ya Askari Polisi ili sasa watakapokuwa wanastaafu waweze kupata mafao ambayo yana endana na hali halisi ya maisha?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Rashidi Shangazi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa kuangalia maslahi ya askari wa vyombo vya usalama Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameamua kuunda Tume ya Haki Jinai ambayo pamoja na mambo mengine inakwenda kuangalia vilevile eneo hili la maslahi ya askari. Kwa hiyo nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hilo Mheshimiwa Rais ni katika mambo ambayo anayapa uzito mkubwa sana, na tusubiri pale ripoti ya Tume itakapomaliza ili tione sasa utekelezaji wake utakuwa vipi.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kati ya mwezi wa nne mpaka mwezi wa tano kuna mauaji yamefanyika katika Mji wa Sirali wameua mtu pale Kubiterere Mwema wameua mtu katika Kata ya Pemba, wamepiga risasi pale Kiru kwenye kata yangu, na juzi walimuua daktari katika Kituo cha Afya cha Kilende Nyamungo. Kuna kata nane watu wanapigwa risasi hadharani, na hali hiyo haijafuatiliwa. Ningeomba nijue kauli ya Serikali wanachukua hatua gani za dharura ili kurejesha amani katika Jimbo la Tarime na hasa Mji wa Sirali ambao ni mji wa mpakani na biashara kwa kweli imekuwa hali siyo nzuri sana.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Waitara, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza jambo la kwanza na la muhimu ambalo ningependa Watanzania ambao wanatusikiliza hapa walifahamu ni kwamba hali ya usalama katika nchi yetu ni imara. Matukio ambayo yoyote yanayotokezea katika nchi yetu ya uhalifu wa aina yoyote unaofanywa na mtu yoyote hakuna hata tukio moja ambalo linatokea na polisi ama vyombo vya usalama visifanikiwe kulidhibiti.

Kwa hiyo, mauaji ya aina yoyote ambayo yamekuwa yakitokezea nchini aidha hatua zimeshachukuliwa ama zinaendelea kuchukuliwa. Wako ambao waliohusika wameshapelekwa katika vyombo vya sheria wako ambao uchunguzi unaendelea kufanyika. Na hata suala la jimbo lake, kwa sababu ametoa takwimu, sasa sina hakika kwa aina yake ya kusema ni nani na kwa hiyo siwezi nikamjibu hapa kumwambia tukio hili liko katika hatua gani. Nimhakikishie tu kwamba hakuna sehemu yoyote katika nchi hii ikiwemo katika jimbo la Mheshimiwa Waitara ambapo kutatokea uhalifu wa aina yoyote na vyombo vyetu vya usalama vikiwemo jeshi la polisi vishindwe kuchukua hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe Mheshimiwa Mbunge, kama ana jambo mahsusi katika jimbo lako ambalo unahisi mpaka sasa hivi hajaridhishwa na hatua iliyochukuliwa naomba, kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maswali unipatie taarifa hizo ili tuweze kuzifanyia kazi.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali kwamba kuna fedha imetengwa. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, uboreshaji wa vituo hivi ulihitaji vile vile uongezaji wa idadi wa askari. Nini kauli ya Serikali juu ya uongezaji wa askari kwenye vituo hivi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Uboreshaji wa vituo hivi vile vile ulihitaji kujenga nyumba za askari kwenye maeneo ya vituo hivi. Nini kauli ya Serikali kwenye ujenzi wa nyumba hizo? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bryceson Magessa, Mbunge wa Busanda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la upungufu wa askari, hivi karibuni tunaendelea na mchakato wa kuajiri askari wapya. Wako askari ambao wanakamilisha mafunzo yao hivi karibuni na wengine tumetangaza hivi karibuni askari wapya. Kwa hiyo, miongoni mwa askari hao watakapomaliza mafunzo yao tutawapeleka ili kukabiliana na upungufu wa askari kwenye maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, halikadhalika tunatambua pia changamoto ya makazi ya askari katika maeneo hayo. Namwomba Mheshimiwa Mbunge awe na subira tukikamilisha ukarabati katika bajeti ijayo tutaangalia vile vile uwezekano wa kutatua changamoto au kupunguza changamoto ya makazi ya askari katika eneo hilo.