Answers to Primary Questions by Hon. Atupele Fredy Mwakibete (61 total)
MHE. CAPT. ABBAS ALI MWINYI aliuliza: -
Je, Serikali imewekeza kiasi gani cha fedha katika ununuzi wa ndege 11 za ATCL na ni lini uwekezaji huo utarudisha fedha zilizowekezwa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu, nikiwa kwenye nafasi hii ya Naibu Waziri kwenye Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, kwenye Sekta ya Uchukuzi, napenda nimshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kupitia mtumishi wake Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuniona na kuniteua kwamba nimsaidie kwenye Sekta hii ya Uchukuzi. Naahidi kwamba nitafanya kadri ya uwezo wa Mwenyezi Mungu lakini pia kwa nguvu, weledi na uadilifu mkubwa. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizi, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi, napenda nijibu swali la Mheshimiwa Abbas Ali Mwinyi, Mbunge wa Fuoni, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wakala wa Ndege za Serikali kwa maana Tanzania Government Flight Agency-TGFA imewekeza kiasi cha Shilingi trilioni 1.44 katika ununuzi wa ndege 11 ambapo, kati hizo, ndege mbili ni za safari za masafa marefu aina ya Boeing 787-8 Dreamliner, Ndege nne ni za safari za masafa ya kati aina ya Airbus A220- 300 na ndege Tano za safari za masafa mafupi aina ya De Havilland Dash 8 Q400.
Mheshimiwa Spika, biashara ya usafiri wa anga faida yake haitokani na uendeshaji wa ndege zinazotumiwa na Kampuni katika kutoa huduma zake tu, bali hutokana pia na mchango wake katika ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi kama utalii, viwanda, madini, kilimo, mifugo, uvuvi, biashara, kuitangaza nchi kimataifa na kuwezesha usafirishaji wa abiria na mizigo ndani na nje ya nchi. Aidha, ATCL imeleta ushindani mkubwa na kuzuia upandaji wa nauli katika usafiri wa anga.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuchangia kwenye ukuaji wa Sekta nyingine, ATCL imeendelea kujiendesha kibiashara na kupunguza utegemezi kwa Serikali kwa kuanzisha vitengo vya kibiashara ambavyo vinasimamia huduma za matengenezo ya ndege, huduma za chakula cha abiria wa ndani ya ndege na huduma za abiria na mizigo kwa maana grounds handling services. Uwepo wa vitengo vinavyotoa huduma hizo umewezesha ATCL kupunguza gharama za uendeshaji. Mashirika mengine ya ndege yanayotumia utaratibu huu ni pamoja na Shirika la Ndege la Ethiopia. Ahsante. (Makofi)
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaboresha Bandari Kavu ya Isaka?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Santiel Eric Kirumba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania kwa maana ya TPA, imenunua na kupeleka vifaa vya kuhudumia mizigo ambavyo ni forklift moja na reach stacker moja ambavyo vinatumiwa na Shirika la Reli Tanzania kwa maana TRC kuendesha Bandari Kavu ya Isaka, Shinyanga kwa sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la kununua na kupeleka vifaa hivyo katika Bandari Kavu ya Isaka ni kuongeza ufanisi wa utoaji huduma za usafirishaji mizigo kati ya Dar es Salaam, mikoa ya Jirani na Shinyanga na Nchi jirani za Rwanda, Congo na Burundi. Bandari Kavu ya Isaka imekuwa ikitumika japo kwa kiwango kidogo kutokana na changamoto ya mabehewa ya kubeba makasha na injini inayoikabili. TRC mwaka jana Disemba, 2021, imepokea mabehewa 44 na injini tatu za treni kwa ajili ya kuhudumia mizigo kati ya Bandari ya Dar es Salaam na Bandari Kavu ya Isaka. Aidha, Serikali kupitia TPA na TRC inaendelea kufanya ushawishi kwa wateja wa bandari na wasafirishaji wakiwemo wale wa kutoka Nchi jirani za Rwanda, Congo na Burundi kutumia zaidi Bandari Kavu ya Isaka. Ahsante. (Makofi)
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK aliuliza: -
Je, Serikali inakusanyaje ushuru kwenye Boti zinazoondoka saa moja kamili asubuhi katika Bandari ya Dar es Salaam ilhali watumishi hufika kazini kuanzia saa moja na nusu na zaidi?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Amour Khamis Mbarouk, Mbunge wa Tumbe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), pamoja na wadau wote muhimu ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), hutoa huduma za kibandari kwa saa 24 kwa siku saba za juma katika Jiji la Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, Kanuni za Utumishi kwa Wafanyakazi wa Bandari za mwaka 2019 zimetoa Mwongozo wa Muda wa Kuwa Kazini, ambapo wafanyakazi wote wa Bandari wanaopangiwa maeneo ya kutoa huduma kwa meli ama boti za mizigo hupaswa kuingia kazini kwa zamu (shifts) tatu kama ifuatavyo; saa 1:00 asubuhi hadi saa 9:00 alasiri; shift ya kwanza; saa 9:00 alasiri hadi saa 5:00 Usiku; shift ya pili na saa 5:00 Usiku hadi saa 1:00 asubuhi shift ya tatu.
Mheshimiwa Spika, aidha, watumishi wa TPA wanaopangiwa zamu katika eneo la boti zinazosafiri kati ya Dar es Salaam na Zanzibar wanapaswa kuwepo kwenye eneo la kazi na kuhakikisha kuwa huduma zote muhimu za kibandari zinatolewa ikiwemo ukusanyaji wa mapato ya Bandari. Nitumie fursa hii kuitaka TPA kusimamia kwa karibu utaratibu uliowekwa. Ahsante. (Makofi)
MHE. MIRAJI J. MTATURU aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itarudisha huduma ya treni Manyoni – Singida?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Miraji Jumanne Mtaturu, Mbunge wa Singida Mashariki, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TRC katika bajeti ya mwaka 2022/2023 imetenga fedha kwa ajili ya kufanya tathmini na maadalizi ya awali ya kufufua njia ya Manyoni – Singida yenye urefu wa kilometa 115 ambayo ilifungwa takribani miaka 30 iliyopita. Lengo la kufufua njia hii ni kuboresha usafirishaji wa mizigo na abiria pamoja na kukuza uchumi wa maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) inaendelea na mchakato wa ununuzi wa wakandarasi watakaofanya tathmini ya mahitaji na maandalizi ya awali ya kutekeleza mradi huo. Ahsante.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka usafiri wa majini Ziwa Tanganyika?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. FREDY A. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali katika bajeti ya mwaka huu wa 2022/2023 imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa meli mbili mpya, chelezo na ukarabati wa meli za Mv Liemba na MT. Sangara ili kuboresha hali ya usafirishaji katika Ziwa Tanganyika. Kati ya meli zitakazojengwa, moja ni ya kubeba abiria 600 na tani 400 za mizigo na ya pili ni ya kubeba mabehewa na malori yenye uzito wa tani 3,000.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali kupitia Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) inaendelea na mchakato wa ununuzi wa Wakandarasi wa kutekeleza miradi hiyo.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE aliuliza: -
Je, Serikali haioni haja ya kuufanya Uwanja wa KIA kutumika kuinua kilimo na kuruhusu ndege za mizigo kutua bila kulipa Landing Fees?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saasisha Elinikiyo Mafuwe, Mbunge wa Hai, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa sasa hakuna ndege mahsusi za mizigo zenye ratiba maalum zinazotua KIA. Mizigo yote inayopitia KIA hubebwa na ndege za abiria kwenye sehemu ya mizigo. Aidha, kwa sasa idadi ya ndege kubwa za abiria imeongezeka na hivyo kuongeza uwezo wa kubeba mizigo.
Mheshimiwa Spika, Serikali inafanya juhudi mbalimbali kuimarisha biashara ya usafirishaji wa mizigo kwa njia ya anga ikiwemo kununua ndege maalum ya mizigo (Boeing 767 – 300F) ambayo inatarajiwa kuingia nchini kufikia Juni, 2023, kwa lengo la kuhakikisha kwamba biashara hiyo inaimarika. Aidha, ili kuvutia biashara ya mizigo, Serikali ipo tayari kufanya mapitio ya landing fee kwa ndege za mizigo kama ilivyopendekezwa na Mheshimiwa Mbunge. Ahsante.
MHE. MOSHI S. KAKOSO K.n.y. MHE. KABULA E. SHITOBELO aliuliza: -
Je, ni lini serikali itakamilisha ujenzi wa bandari zilizopo Mkoa wa Mwanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kabula Enock Shitobela, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) imekuwa ikiboresha miundombinu ya Bandari za Mwanza Kaskazini na Kusini kwa kutumia bajeti zinazopangwa kila mwaka. Katika mwaka wa fedha 2020/2021, TPA imekamilisha uboreshaji wa jengo la abiria, awamu ya kwanza na matenki manne ya kuhifadhia mafuta katika Bandari ya Mwanza Kaskazini.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka fedha 2022/2023 Serikali kupitia TPA imepanga kufanya utanuzi wa eneo la maegesho ya meli (berth extension), kuongeza kina cha maji (dredging) barabara ya kuingia Bandarini na kuboresha miundombinu saidizi katika bandari ya Mwanza Kaskazini. Kwa upande wa Bandari ya Mwanza Kusini, TPA imepanga kuongeza eneo la maegesho ya meli (berth extension), barabara ya kuingia Bandarini na uboreshaji wa Miundombinu saidizi. Aidha, uboreshaji huo utaenda sambamba na ununuzi wa mitambo ya kuhudumia mizigo bandarini. Ahsante.
MHE. SYLVIA F. SIGULA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Bandari Kavu katika Mkoa wa Kigoma?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sylvia Francis Sigula, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa Bandari Kavu umepewa kipaumbele katika Mpango Kabambe wa Mamlaka ya Bandari Tanzania ulioanza 2009 na utaisha 2028. Mpango huo umeziainisha Bandari Kavu za King’ori iliyoko mkoani Arusha, Ihumwa (Dodoma), Inyala (Mbeya), Shinyanga (Isaka), Fela (Mwanza), Katosho (Kigoma), Kwala (Pwani) na Songea kuwa bandari za kipaumbele kutokana na matarajio ya kuongezeka kwa shehena katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali kupitia TPA imetenga fedha kwa ajili kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa bandari hizo ikiwemo ya Katosho ilioko mkoani Kigoma. Kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu inatarajiwa kukamilika mwezi Aprili, 2023. Kukamilika kwa kazi hiyo kutapelekea manunuzi ya Mkandarasi wa ujenzi wa bandari hiyo ambayo ni muhimu kwa kuhudumia shehena za nchi jirani za ukanda wa Ziwa Tanganyika. Ahsante.
MHE. HASSAN HAJI KASSIM aliuliza: -
Je, kuna mkakati gani wa kuitanua sehemu ya kusafirishia abiria wanaokwenda Zanzibar katika Bandari ya Dar es Salaam?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Haji Kassim, Mbunge wa Mwanakwerekwe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali kupitia TPA imetenga kiasi cha Sh.1,500,000,000 kwa ajili ya maboresho ya sehemu ya abiria katika Bandari ya Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, hatua iliyofikiwa sasa ni manunuzi ya Mkandarasi kwa ajili ya maboresho ya eneo la kusafirisha abiria kwenda Zanzibar. Maboresho yatahusisha ukarabati wa miundombinu ya gati la kuhudumia abiria ikiwa ni pamoja na ujenzi wa jengo jipya la abiria ili kuongeza uwezo wa kuhudumia abiria, kuweka mkanda wa mizigo (conveyor belt), ukarabati wa kingo za gati, maboresho ya sehemu ya abiria mashuhuri (VIP), sakafu na vyoo. Aidha, Mkandarasi anatarajiwa kupatikana na kuanza kazi mwezi wa Desemba, 2022.
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza: -
Je, ni lini utekelezaji wa Mkataba wa kibiashara kati ya Serikali na Kampuni ya Dubai World utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mwezi Februari 2022 Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), ilisaini Hati ya Makubaliano (MoU) na Kampuni ya Dubai Port World (DP-World) ya Umoja wa Falme za Kiarabu, kuhusu uwekezaji katika maeneo ya bandari nchini. Aidha, tarehe 25 Oktoba, 2022 Serikali ilisaini makubaliano na Serikali ya Dubai (Inter-Governmental Agreement - IGA).
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mkataba wa kibiashara unakwenda katika hatua mbalimbali. Hatua ya kwanza ni mkataba kati ya nchi na nchi (Intergovernmental Agreement - IGA) ambao tayari umesainiwa. Mkataba huo unaweka msingi wa Serikali za pande mbili kuanza majadiliano kuhusu maeneo ya uwekezaji. Baada ya kusainiwa kwa mkataba huo, majadiliano yataendelea kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi ili kuhakikisha kwamba uwekezaji huo unakuwa na tija kwa nchi. Matarajio ya Serikali ni kuwa majadiliano hayo yatafikia tamati mwishoni mwa mwezi Desemba, 2022.
MHE. AMINA ALI MZEE K.n.y. MHE. TOUFIQ SALIM TURKY aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kuiwezesha TASAC iweze kuhudumia meli nyingi?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Toufiq Salim Turky, Mbunge wa Mpendae, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika kuiwezesha TASAC kuhudumia meli nyingi, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuongeza watumishi wa ukaguzi wa meli kutoka watumishi 23 hadi watumishi 34. Watumishi walioongezwa wamepelekwa mikoa yote yenye kuungana na bahari na maziwa. Aidha, katika kuboresha uwezo wa wakaguzi, TASAC imepata mkaguzi wa michoro na ujengaji wa meli (naval architect) na imepeleka mkaguzi mmoja kwenda kusomea uchoraji na ujengaji wa meli nchini Uingereza.
Mheshimiwa Spika, TASAC pia imeingia makubaliano na Chuo cha International Maritime Safety, Security and Environment Academy kilichopo Nchini Italia ili kupatiwa mafunzo ya ukaguzi kwa meli za ndani na meli za nje (Flag State Inspection and Port State Inspection). Ahsante.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA K.n.y. MHE. KABULA E. SHITOBELO aliuliza: -
Je, ni sheria gani inayotumika kwenye tozo za bandari nchini?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kabula Enock Shitobela, Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, tozo za bandari zinatozwa kwa mujibu wa Sheria ya Bandari Namba 17 ya mwaka 2004. Kwa mujibu wa sheria hiyo, kitabu cha viwango vya tozo (tariff book) huidhinishwa na mdhibiti ambaye ni Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC).
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Bandari Namba 17 ya mwaka 2004 imeeleza vyanzo vya mapato vya TPA ambavyo vinajumuisha tozo za bandari (kifungu Na. 67). Aidha, sheria hiyo inaelekeza TPA kuandaa tariff book inayoainisha viwango vya tozo za bandari kwa kila huduma, ahsante.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA aliuliza: -
Je, nini mpango wa Serikali wa kuboresha usafiri wa reli ya Kigoma-Dar es Salaam ambao unafanya safari mara mbili kwa wiki?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kilumbe Shaban Ng’enda, Mbunge wa Kigoma Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Shirika la Reli Tanzania (TRC) linafanya safari mbili kwa wiki kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma na hii ni kutokana na uhaba wa mabehewa ya abiria. Ili kuondokana na changamoto ya upungufu wa mabehewa, Shirika lilianza taratibu za kukarabati mabehewa 37 ambapo mwezi Juni, 2021 ulisainiwa mkataba wa ununuzi wa vipuri kwa ajili ya ukarabati wa mabehewa hayo. Vipuri hivyo vinatarajiwa kuingia nchini mwishoni mwa mwezi Aprili, kwa maana ya mwaka 2022 na mara vitakapowasili kazi ya ukarabati itaanza. Kazi hiyo ya ukarabati inatarajiwa kufanyika kwa muda wa miezi nane hadi Desemba, 2022 kupitia mafundi wetu wa ndani.
Aidha, Shirika limesaini Mkataba wa ununuzi wa mabehewa mapya ya abiria 22. Mabehewa hayo yanatarajiwa kuingia nchini mwezi Septemba, 2022.
Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua fursa hii kumwomba Mheshimiwa Kilumbe Shaban Ng’enda pamoja na wananchi wa Kigoma kuwa na subira wakati Serikali inaendelea na zoezi la ukarabati na ununuzi wa mabehewa ya abiria. Baada ya utekelezaji wa kazi hizo, idadi ya safari za treni kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma zitaongezeka kutoka safari mbili hadi nne kwa wiki.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani wa kukarabati reli ya TAZARA?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deodatus Philip Mwanyika, Mbunge wa Njombe Mjini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kuboresha miundombinu ya reli ya TAZARA. Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 13.1 kwa ajili ya ununuzi wa mataruma ya mbao kwa ajili ya kufanyia ukarabati madaraja 172 yaliyopo upande wa Tanzania, ununuzi wa mtambo wa kisasa wa kushindilia kokoto kwenye reli, na ununuzi wa mtambo wa kuvunjia kokoto (secondary crusher) kwa ajili ya kuongeza kokoto za aina mbalimbali zinazotumika katika kufanyia matengenezo ya njia ya reli kati ya Dar es Salaam – Tunduma na Msolwa - Kidatu. Aidha, fedha hizo pia zitatumika kukarabati mabehewa 21 ya treni za abiria za Udzungwa na treni za abiria za mjini (commuter) za Jijini Dar es salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa mikakati ya muda wa kati na mrefu, Serikali za Tanzania na Zambia zimeandaa mpango wa biashara wa miaka mitano ambao unatarajiwa kupitishwa na Baraza la Mawaziri wa TAZARA mwishoni mwa Novemba, 2022. Aidha, Serikali za Tanzania, Zambia na China zimeunda timu ya pamoja kwa ajili ya kuandaa mkakati wa pamoja kwa kuishirikisha Serikali ya Watu wa China katika kugharamia maboresho ya TAZARA. Ahsante.
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK aliuliza: -
Je, ni kwa nini mizigo ya wasafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar kwa kutumia meli kubwa inapekuliwa na mbwa badala ya scanner?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Amour Khamis Mbarouk, Mbunge wa Tumbe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mizigo yote ya wasafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar kupitia Bandari ya Dar es Salaam inakaguliwa kwa mdaki (scanner). Katika kuimarisha usalama wa bandari, wasafiri pamoja na mizigo inayosafishwa kwenda Zanzibar, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) iko kwenye hatua za manunuzi ya mdaki (scanner) mwingine mpya kwa ajili ya eneo la meli zifanyazo safari kati ya Dar es Salaam na Zanzibar ili kupunguza muda unaotumika kukagua mizigo na hivyo kufanya eneo hilo kuwa na Midaki miwili. Mdaki mpya unaonunuliwa unatarajiwa kuwasili nchini mwishoni mwa mwezi Aprili, 2023.
Mheshimiwa Spika, matumizi ya mbwa katika Bandari ya Dar es Salaam hufanyika kwa ukaguzi maalum wa mizigo baada ya mizigo hiyo kukaguliwa kwa kutumia mdaki na kuonekana si salama kuruhusiwa kupita, ahsante.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza: -
Je, ni lini wastaafu wa ATCL watalipwa mafao yao?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Angelina Malembeka Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kabla ya kuanza kwa juhudi za ufufuaji wa ATCL Septemba 2016, ATCL ilikuwa ikikabiliwa na changamoto za uendeshaji kwa kukosa mtaji, kuwa na ndege mbovu, kushindwa kulipa madeni ya wazabuni na kutowasilisha michango ya wafanyakazi katika mifuko ya hifadhi ya jamii. Aidha, baada ya mwaka 2016, ATCL imekuwa ikiwasilisha michango ya wafanyakazi kwenye mifuko ya jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia uhakiki uliofanyika, ATCL ina madeni ya jumla Shilingi 4,864,673,387.85 yanayotokana na kutowasilisha michango ya wanyakazi kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii. Fedha za kulipa madeni hayo zimetengwa katika bajeti ya mwaka 2022/2023. Hivyo, madeni hayo ya michango ya wafanyakazi kwenye mifuko ya jamii yatalipwa katika mwaka huu wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali italeta sheria ya wamiliki wa vyombo vya usafiri kuwa na miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dokta Ritta Kabati, Mbunge wa viti maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2019, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Sheria ya kuanzishwa kwa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) na kuweka kifungu katika Sheria hiyo kinachozingatia uwepo wa miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kifungu cha 6(e) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini Sura ya 413, kimeeleza kuwa moja ya Majukumu ya LATRA ni kuhakikisha uwepo wa huduma ya usafiri wa umma unaoweza kutumiwa na watu wote wakiwemo watu wenye vipato vya chini, waishio vijijini, na watu wenye mahitaji maalum ambayo inajumuisha watu wenye ulemavu. Aidha, Kifungu cha 5(c) (i) na (ii) kimeeleza kuwa moja ya Kazi za LATRA ni kuweka viwango vya bidhaa na huduma pamoja na vigezo na masharti ya utoaji wa huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, itakumbukwa kuwa kupitia marekebisho ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2022, Kifungu cha 5(1) na (2) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini Sura ya 415 kilirekebishwa kwa kuiondolea LATRA jukumu la kuweka viwango vya bidhaa na huduma zinazodhibitiwa. Jukumu hilo kwa sasa linatekelezwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ambalo ndilo lenye dhamana ya kuweka viwango vya bidhaa na huduma mbalimbali nchini. LATRA imebaki na jukumu la kusimamia utekelezaji wa viwango na kuweka masharti na vigezo vya bidhaa na huduma zinazodhibitiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naielekeza LATRA ishirikiane na TBS katika kuweka na kusimamia utekelezaji wa viwango vya vyombo vya usafiri wa umma ili viwe na miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu. Ahsante.
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Kyatema – Kanazi – Ibwela – Katoro – Kyaka kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Kyatema – Kanazi – Ibwela – Katoro – Kyaka yenye urefu wa kilometa 60.6 umekamilika mwezi Oktoba, 2022. Kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi, ahsante.
MHE. SUBIRA K. MGALU aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatenga fedha za ujenzi wa kiwango cha lami kwa barabara ya Mziha – Kibindu – Mbwewe?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Subira Khamis Mgalu, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kabla ya kuanza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, kunahitajika kufanyika upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa barabara ya Mziha – Kibindu – Mbwewe yenye urefu wa kilometa 68.63. Baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na gharama za ujenzi kujulikana Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi huu, ahsante.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga gati ya kuegesha boti na vyombo vya usafiri Bagamoyo ili kuvutia watalii kutembelea Mbuga ya Saadan?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Bagamoyo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuendeleza miundombinu ya kisasa ya kuegesha vyombo vya usafiri katika pwani ya Wilaya ya Bagamoyo ili kuvutia watalii kutumia miundombinu hiyo kwenda kutembelea vivutio vya utalii katika mbuga ya Saadan pamoja na Visiwa vya jirani.
Mheshimiwa Spika, katika kutimiza azma hii, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchi kwa maana ya TPA iko katika hatua za mwisho za kuhuisha mpango kabambe wa kuendeleza miundombinu ya bandari nchini ambao utaainisha mahitaji sahihi ya miundombinu ya gati zinazotakiwa kujengwa kwa ajili ya kuegesha boti na vyombo mbalimbali vya usafiri katika Bandari ya Bagamoyo. Maandalizi ya Mpango Kabambe yanatarajiwa kukamilika Juni, 2022 na kufuatiwa na usanifu wa kina ili kupata taarifa za msingi ikiwa ni pamoja na gharama za utekelezaji wa mradi huo. Kazi hii itafanyika katika Mwaka wa Fedha 2022/2023. Ahsante.
MHE. VENANT D. PROTAS K.n.y. MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha mifumo ya upatikanaji wa tiketi kwa wasafiri wa reli ya kati?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) imekamilisha na imeanza matumizi ya mifumo ya kielektroniki kwa maeneo yote yenye huduma ya internet ikiwemo Tabora kwa ajili ya kuboresha huduma na kurahisisha upatikanaji wa tiketi mtandao kwa wananchi. Mfumo wa ukatishaji tiketi kwa maana ya e-ticketing ulizinduliwa mwezi Aprili, 2020, kwa lengo la kupunguza matumizi, kuongeza mapato na ufanisi wa Shirika pamoja na kuondoa mianya ya upotevu.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, Serikali inaendelea na jitihada za kuongeza vitendea kazi kwa maana ya injini na mabehewa kwa lengo la kuboresha huduma kwa kuhudumia wananchi wengi zaidi. Tayari pia imesaini mkataba wa ununuzi wa mabehewa 22 ya abiria na vipuri kwa ajili ya ukarabati wa mabehewa 37 ya abiria. Aidha, kuongezeka kwa vitendea kazi hivi kutaongeza idadi ya safari za treni za abiria na hivyo kupunguza changamoto ya upatikanaji wa tiketi kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza: -
Je, mpango wa ujenzi wa reli ya Kusini kutoka Mtwara hadi Ruvuma na matawi yake ya Liganga na Mchuchuma umefikia wapi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) imekamilisha kazi ya upembuzi na usanifu wa awali kwa ajili ya ujenzi wa njia ya reli ya Mtwara-Mbambabay na matawi yake ya Liganga na Mchuchuma kilomita 1,000. Upembuzi uliofanyika ulipendekeza kuwa utekelezaji wa mradi huo ushirikishe sekta binafsi. Kwa sasa Serikali inaendelea na taratibu za kumwajiri Mshauri Elekezi (Transaction Advisor) kwa ajili ya kuandaa Andiko, makabrasha ya zabuni ili kumpata mwekezaji kwa utaratibu wa ubia baina ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP).
Mheshimiwa Spika, aidha Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika -SADC imeahidi kutoa kiasi cha Dola za Marekani 6,000,000 kwa lengo la kumgharamia Mshauri Elekezi. Utaratibu wa kupata fedha hizi unaendelea na kazi hii inatarajiwa kufanyika Mwaka wa Fedha 2022/2023, ahsante.
MHE. ALI JUMA MOHAMED aliuliza: -
Je, Shirika la Ndege nchini (ATCL) limeshaanza kulipa madeni ya Makampuni yaliyokuwa yanatoa huduma?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. FREDY A. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante na kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ali Juma Mohamed Mbunge wa Shaurimoyo kama Ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kulipa madeni ya makapuni yanayotoa ama yaliyokwisha kutoka huduma kwa ATCL baada ya kuyafanyia uhakiki. Mwaka 2016 kabla ya Serikali kuanza mpango wa kuifufua ATCL Kampuni ilikuwa inadaiwa kiasi cha shilingi bilioni 141.77 na watoa huduma mbalimbali wa ndani na nje. Hadi kufikia mwezi Aprili, 2022 Serikali imelipa madeni jumla ya shilingi bilioni 127.07.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuiwezesha ATCL kulipa madeni yaliyobaki kulingana na uwezo wa kibajeti. Ahsante.
MHE. STELLA S. FIYAO aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Bandari kavu katika Mji wa Tunduma?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. FREDY A. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stella Simon Fiyao, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imekamilisha zoezi la kufanya upembuzi yakinifu wa kuendeleza bandari kavu zote nchini ikiwemo ya Bandari Kavu ya Tunduma.
Mheshimiwa Spika, Kiuchumi na kibiashara, Bandari Kavu ya Tunduma ni muhimu sana kwa sababu ndilo langu kuu la kupitisha bidhaa za nchi za Zambia, DRC na nchi nyingine kusini mwa Afrika.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Bandari hiyo ina mvuto zaidi wa kibishara, mpango wa Serikali ni kushirikisha sekta binafsi ikiwa pamoja na halmashauri kwenye maeneo husika. TPA inaendelea na vikao vya wadau ili kushawishi uwekezaji huo.
MHE. KUNTI Y. MAJALA aliuliza: -
Je, lini Serikali itamaliza kulipa fidia Wananchi wa Makole waliopisha upanuzi wa Uwanja wa Ndege na Mkonze waliopisha ujenzi wa SGR?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kunti Yusuph Majalla, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya ndege Tanzania (TAA) imekamilisha malipo ya fidia kwa wananchi kutoka kaya 14 za Mtaa wa Chaduru B, Kata ya Makole, Dodoma Mjini, zilizopisha upanuzi wa Kiwanja cha Ndege Dodoma. Fidia hiyo, iligharimu kiasi cha shilingi 1,900,000,000, ilihusu upanuzi wa kiwanja kwa mita 150 zilizohitajika. Serikali haitahitaji kupanua zaidi Kiwanja cha Ndege cha Dodoma kwa kuwa imeanza kujenga Kiwanja cha Ndege cha Msalato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) imekamilisha tathmini ya fedia kwa wananchi wote wa Mkonze ambao maeneo yao yatatwaliwa kwa ajili ya ujenzi wa SGR. Zoezi la ulipaji wa fidia lilianza kufanyika kuanzia tarehe 4 Aprili, mwaka huu 2023. Naomba wananchi ambao bado hawajalipwa wawe na subira wakati zoezi la malipo likiendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, naomba kuwafahamisha Waheshimiwa Wabunge kuwa, ujenzi wa reli ya SGR unafanyika kwa utaratibu wa Sanifu na Jenga (Design and Build), hivyo utwaaji wa maeneo ya nyongeza utaendelea kufanyika kwa kadiri ya mahitaji, kwa mujibu wa sheria, na taratibu za nchi, ahsante.
MHE. MRISHO M. GAMBO aliuliza:-
Je, lini Wananchi wa Kata ya Moshono katika barabara ya mzunguko ya Kona ya Kiserian watalipwa fidia?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, Mbunge wa Arusha Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi walioathirika na kupisha ujenzi wa barabara ya mzunguko (Arusha bypass) kwa mujibu wa Sheria ya Barabara Na. 13 ya mwaka 2007.
MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itapeleka Meli ndogo ya abiria Muleba pamoja na kutumia meli ya MV Victoria kujaribu masoko ya nchi za Uganda na Kenya?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa ujenzi na uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Charles John Mwijage, Mbunge wa Muleba Kaskazini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua hitaji kubwa la usafiri wa wananchi Wilayani Muleba hususani waishio katika Visiwa. Kwa kutambua hitaji hilo, Serikali kupitia Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) imetenga meli moja iitwayo MV Clarias kutoa huduma katika Visiwa vya Godziba Wilayani Muleba na Visiwa vya Gana Wilayani Ukerewe. Meli hiyo iliyokuwa imeanza kutoa huduma katika visiwa hivyo tarehe 3 Machi, 2023 ilisimama tarehe 22 Machi, 2023 baada ya kupata hitilafu za kiufundi. Huduma hizo zitaendelea kuanza tena mwanzoni mwa mwezi Mei, 2023 baada ya matengenezo kukamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu huduma za safari za kwenda Uganda na Kenya, MSCL inatarajia kuanza safari hizo kwa kutumia meli ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu mara baada ya ujenzi wake kukamilika. Meli ya MV Victoria haitaweza kutumika kwani ndiyo meli pekee inayotegemewa katika utoaji wa huduma za usafiri kati ya Mwanza na Bukoba kupitia Kemondo na ni msaada mkubwa kwa wakazi wa ukanda huo. Ahsante. (Makofi)
MHE. GODWIN E. KUNAMBI aliuliza: -
Je, lini vituo vidogo vya treni vya Njage na Itongowa katika reli ya TAZARA vitarejeshwa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Godwin Emmanuel Kunambi, Mbunge wa Mlimba kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, TAZARA ilipokea barua za maombi ya kufunguliwa kwa vituo vidogo vya Njage na Itongowa katika vipindi tofauti tangu mwaka 2022. Tathmini iliyofanywa ilibainisha yafuatayo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo kidogo cha Itongowa. Kituo hiki kinachoombwa kuanzishwa kipo kati ya Stesheni kubwa za Chita na Mngeta. Katikati ya Stesheni mbili hizo za Chita na Mngeta kipo kituo kidogo cha siku nyingi cha Ikule. Kituo hiki cha Ikule kipo kilometa sita kutoka aidha Chita ama Mngeta. Kituo cha Itongowa kinachoombwa kuanzishwa kitakuwa kilometa sita kutoka Mngeta stesheni au kilometa saba kutoka Ikule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo kidogo cha Njage. Kituo hiki kinachoombwa cha Njage kipo kati ya Stesheni kubwa za Mngeta na Mbingu ambazo treni za abiria zinasimama. Umbali kati ya stesheni hizo ni kilometa 18 yaani Mngeta na Mbingu. Kitongoji cha Njage kipo katikati Mngeta na Mbingu yaani kilometa tisa kutoka kila upande, Mngeta au Mbingu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo Wizara imeelekeza sasa TAZARA ifanye tathmini ya haraka kwa kina kuona uwezekano wa kuanzisha vituo hivi vilivyoombwa na Mheshimiwa Mbunge ili wananchi wasitembee umbali mrefu.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga uwanja wa Ndege Lindi kwa kiwango cha lami pamoja na kukarabati Uwanja wa Ndege Nachingwea?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ,napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Ahmad Pathan, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha kazi ya kufanya marejeo ya usanifu wa kina kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Lindi kwa kiwango cha lami. Marejeo ya usanifu wa kina yalifanyika ili kuzingatia mahitaji ya sasa ya kiwanja, ikiwemo kuwezesha utekelezaji wa Mradi wa Gesi katika maeneo hayo. Kwa sasa, Serikali inakamilisha maandalizi ya makabrasha ya zabuni hiyo ili iweze kutangazwa.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Kiwanja cha Ndege cha Nachingwea, Serikali imekuwa ikifanya matengenezo ya miundombinu ya kiwanja hicho ili kiendelee kutumika ambapo mwaka 2020 ilikamilisha ukarabati mkubwa wa barabara ya kuruka na kutua ndege kwa kiwango cha changarawe.
Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa Kiwanja cha Ndege Nachingwea, Serikali inaendelea na utwaaji wa eneo la ziada ili kujenga kiwanja hicho kwa kiwango cha lami. Aidha, mnamo mwezi Machi, 2023 wataalam wa Wizara walifanya uhakiki wa daftari la fidia na kuwasilishwa kwa Mthamini Mkuu wa Serikali kwa idhini, ahsante.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza: -
Je, lini mpaka wa Kasesya/Zombe utafanya kazi kwa ufanisi ili kupunguza msongamano wa malori katika mpaka wa Tunduma?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua uwepo wa mpaka wa Tunduma/Nakonde na mpaka wa Kasesya/Zombe ambayo inatumika kupitisha mizigo inayokwenda au kutoka Zambia. Aidha, wasafirishaji wana hiari ya kuchagua mpaka upi wautumie katika kusafirisha mizigo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka wa Tunduma/Nakonde umekuwa ukitumiwa zaidi na wasafirishaji wanaosafirisha mizigo kutoka Dar es Salaam kwenda Zambia na DRC kwa kuwa ndiyo mpaka wenye umbali mfupi ukilinganishwa na mpaka wa Kasesya/Zombe. Kwa mfano, kutoka Dar es Salaam hadi Tunduma ni kilomita 922, kutoka Dar es Salaam kwenda Kasesya kupitia Tunduma na Laela ni kilometa 1,172; kutoka Dar es Salaam kwenda Kasesya kupitia Tunduma na Sumbawanga ni Kilometa 1,249; na kutoka Dar es Salaam kwenda Kasesya kupitia Dodoma,Tabora na Mpanda ni Kilometa 1,530. Ahsante.
MHE. JUMA USONGE HAMAD aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani kupitia TBA kuwajengea nyumba watumishi wa Serikali ya Muungano kwa upande wa Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Usonge Hamad, Mbunge wa Chaani kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umeanzishwa chini ya Sheria ya Wakala, Sura 245 ikisomwa pamoja na Agizo la Uanzishwaji wa Wakala GN. Na. 24 la tarehe 14 Februari, 2003. Moja ya jukumu la msingi la TBA ni kujenga na kukarabati nyumba na majengo ya Serikali kwa ajili ya makazi kwa watumishi wa umma Tanzania Bara.
Mheshimiwa Spika, Jukumu la ujenzi wa nyumba kwa watumishi wa Umma kwa upande wa Zanzibar liko chini ya Wakala wa Majengo Zanzibar (ZBA). Hata hivyo, TBA na ZBA wanashirikiana na kushauriana kwenye mambo mbalimbali ya kitaalam na kujengeana uwezo, ahsante.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza: -
Je, lini Serikali itajenga meli katika Bandari ya Mtwara itakayorahisisha mawasiliano na nchi ya Comoro?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa mawasiliano baina yake na mataifa jirani, hasa Nchi ya Comoro. Serikali kupitia Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), imetenga fedha kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu (feasibility study) katika Bahari ya Hindi kwa lengo la kujiridhisha na kiwango cha mahitaji ya usafiri huo kwa wananchi wa mwambao wa Pwani ya Bahari ya Hindi na nchi jirani ikiwa ni pamoja na Visiwa vya Comoro. Upembuzi huo utasaidia Serikali kuamua aina ya meli itakayojengwa kulingana na hitaji la wananchi na soko kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hatua hiyo ya kufanya upembuzi yakinifu, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari imefanikiwa kuishawishi Kampuni ya Meli ya CMA CGM kutumia Bandari ya Mtwara kama kitovu (hub) cha mizigo inayokwenda Visiwa vya Comoro. Hivyo, mizigo inayotoka Nchi za Ulaya na Asia kwenda Comoro na ile inayotoka Tanzania kwenda Comoro (transshipment) imeanza kuhudumiwa katika Bandari ya Mtwara.
Mheshimiwa Spika, meli ya Kampuni ya CMA CGM ilianza safari za kupitia Bandari ya Mtwara tarehe 20 Aprili, 2023 na itaendelea kutoa huduma hiyo kila baada ya wiki moja. Aidha, meli ya kwanza kutoka Mtwara kwenda Comoro iliondoka tarehe 02 Mei, 2023 na itaendelea kutoa huduma hiyo kila baada ya wiki mbili, ahsante.
MHE. LUHAGA J. MPINA aliuliza: -
Je, kwa nini ilitumika njia ya single source kumpata Mkandarasi wa SGR Lot No. 6 Tabora – Kigoma na kusababisha hasara ya trilioni mbili?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina, Mbunge wa Kisesa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Manunuzi ya Umma imeainisha njia mbalimbali za manunuzi ya mkandarasi zinazoweza kutumiwa na Serikali ikiwa ni pamoja na njia ya single source. Aidha, Manunuzi ya Mkandarasi kwa kipande cha Tabora - Kigoma yalifuata Sheria za Manunuzi ya Umma Na. 7 ya Mwaka 2011 na Kanuni zake Na. 161 (1) (a) mpaka (c) (Single source Procurement for works) ya Kanuni za Manunuzi ya Umma ya Mwaka 2013 na Marekebisho yake ya mwaka 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kuwa hakuna hasara yoyote iliyosababishwa na ununuzi wa mkandarasi wa ujenzi wa njia ya reli ya Tabora – Kigoma, bali ununuzi wa mkandarasi ulifuata taratibu zote za manunuzi ikiwemo majadiliano kwa lengo la kuhakikisha gharama sahihi za mradi zinapatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, makadirio ya gharama za kihandisi (Engineering Estimates) yalikuwa dola za Marekani bilioni 3.066 sawa na shilingi trilioni 7.2 ikilinganishwa na gharama halisi za bei ya Mkandarasi (base price) baada ya majadiliano ambayo ni dola za Marekani bilioni 2.216 sawa na shilingi trilioni 5.2. Hii ni baada ya majadiliano yaliyookoa dola za Marekani milioni 273,913,703.25 sawa na shilingi bilioni 632.74 kutoka kwenye zabuni ya awali ya dola za Marekani 2,490,124,575.00 sawa na shilingi trilioni 5.8.
Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe kuwa utaratibu wa manunuzi kwa njia ya Single source ndiyo uliotumika kumpata Mkandarasi YAPI MERKEZI wa Ujenzi wa kipande cha tatu kutoka Makutupora kwenda Tabora, na Kipande cha nne, yaani Tabora - Isaka, ambapo gharama zake ni dola za Marekani bilioni 2.213 sawa na Shilingi za Kitanzania trilioni 5.19, ahsante.
MHE. MARIAM M. NYOKA aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kujenga Barabara ya Mletele - Msamala – Mkuzo hadi Namanditi kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu Swali la Mheshimiwa Mariam Madalu Nyoka, Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Ujenzi wa Barabara ya Mletele – Msamala – Mkuzo hadi Namanditi (Songea Bypass) yenye urefu wa kilometa 14 umejumuishwa katika mradi wa ujenzi wa Barabara ya Makambako hadi Songea yenye urefu wa kilometa 280. Sehemu ya kutoka Songea – Rutikira (km 97) ambao unagharamiwa kwa fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia chini ya mradi wa Tanzania Transport Integration Project (TanTIP). Maandalizi kwa ajili ya kutangaza zabuni za kumpata mkandarasi wa ujenzi yanaendelea, ahsante.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kuzuia mmomonyoko wa barabara ya Dodoma – Iringa katika Mlima wa Nyang’oro?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa ujenzi na uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ritta Enespher Kabati, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka 2022/2023, Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi milioni 250 kwa ajili ya kazi ya kufanya uchunguzi wa miamba na udongo unaomomonyoka katika eneo la Nyang’oro katika Barabara ya Dodoma kwenda Iringa ili kujua tabia za miamba na udongo huo na kuja na mapendekezo ya kitaalam ya jinsi ya kuzuia kumomonyoka huo. Tathmini za zabuni ya kumpata mshauri (consultant) wa kufanya kazi hiyo iko hatua za mwisho na Mkataba utakuwa umesainiwa kabla ya mwisho wa mwezi Juni, 2023. Baada ya taarifa ya kitaalam kutolewa, Serikali itatenga fedha za kutekeleza mapendekezo ya kuzuia mmomonyoko huo, ahsante.
MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga barabara ya Kibaoni – Majimoto hadi Inyonga kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Martha Festo Mariki, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Kibaoni – Majimoto hadi Inyonga yenye kilometa 162. Hadi sasa jumla ya kilometa 9.3 zimejengwa kwa kiwango cha lami sehemu ya Inyonga kilometa 4.2 na Majimoto kilometa 2.6 na Usevya kilometa 2.5 ambapo ni Makao Makuu ya Halmashauri ya Mpimbwe. Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuendelea na ujenzi kwa sehemu iliyobaki, ahsante.
MHE. IDDI K. IDDI aliuliza: -
Je, lini Serikali itajenga vivuko ili kuweza kupita magari, pikipiki na baiskeli katika Reli ya Bandari Isaka - Msalala?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, Mbunge wa Msalala, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mpango wa kuimarisha usalama katika maeneo yote ya makutano ya reli na barabara kuu kwa kujenga madaraja au kuweka mageti ya kisasa yanayojifungua na kujifunga yenyewe ili kuzuia watumiaji wa barabara kupita pale treni inapopita kwenye makutano.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kuweka mageti hayo katika makutano yote ya reli na barabara yaliyopo kwenye barabara kuu yakiwemo makutano ya Isaka. Kwa sasa Serikali imeweka walinzi eneo hilo kwa saa 24 ili kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara hiyo, ahsante.
MHE. ZAYTUN S. SWAI K.n.y. MHE. DANIEL A. TLEMAI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya ujenzi wa Barabara ya Matala – Mwanhuzi – Lalago kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Tlemai Awack, Mbunge wa Karatu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya barabara ya Matala – Mwanhuzi – Lalago yenye kilometa 148.4 ya kutoka Lalago – Mwanhuzi – Sibiti – Nyahaha imo kwenye mradi wa ujenzi wa Barabara ya Maswa – Lalago - Sibiti River – Haydom – Mbulu – Karatu yenye urefu wa kilometa 339 ambao utatekelezwa kwa utaratibu wa Engineering, Procurement and Construction plus Financing (EPC+F) ambao hadi sasa mkandarasi amepatikana na mkataba wa ujenzi utakuwa umesainiwa kabla ya mwishoni mwa mwezi Juni, 2023. Kwa sehemu ya Nyahaha kwenda Matala (kilometa 25) Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. TUNZA I. MALAPO K.n.y. MHE. SHAMSIA A. MTAMBA aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kujenga kwa kiwango cha lami barabara inayotoka Mtwara Mjini kuelekea Msimbati?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shamsia Azizi Mtamba, Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara inayotoka Mtwara Mjini mpaka Msimbati ni barabara ya Mangamba – Madimba hadi Msimbati yenye urefu wa kilometa 35.63 inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS). Kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hii imekamilika. Kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami.
MHE. MASACHE N. KASAKA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatoa fedha za ujenzi wa barabara inayounganisha Mikoa ya Mbeya, Tabora na Singida inayoanzia Makongolosi hadi Rungwa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Masache Njelu Kasaka, Mbunge wa Lupa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inajenga kwa kiwango cha lami barabara ya Mbeya – Chunya – Makongolosi – Rungwa – Mkiwa yenye kilometa 503.36 kwa awamu. Sehemu ya Mbeya – Chunya – Makongolosi yenye kilometa 111 ujenzi umekamilika. Ujenzi wa sehemu ya Noranga - Itigi (Mlongoji) kilometa 25 umefikia asilimia 12 na taratibu za kumpata Mkandarasi wa ujenzi sehemu ya Noranga – Doroto kilometa 6 na Itigi – Mkiwa kilometa 25.6 zimekamilika na Mkataba umesainiwa. Kwa sehemu iliyobaki ya Makongolosi – Rungwa - Noranga kilometa 356 na Mbalizi – Makongolosi kilometa 50 Serikali inaendelea kutafuata fedha kwa ajili ya ujenzi.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA aliuliza: -
Je, kwa nini Serikali haijazikarabati Meli za MV Liemba, MV Mwongozo na MV Sangara ambazo zimesimama kufanyakazi?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kilumbe Shabani Ng’enda, Mbunge wa Kigoma Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kukarabati meli za MV. Liemba, MV Mwongozo na MV Sangara ili kuboresha huduma za usafiri kwa njia ya maji katika Ziwa Tanganyika. Ili kufikia azima hiyo, Serikali kupitia Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) inaendelea na ukarabati wa Meli ya MV Sangara ambapo kwa sasa kazi hiyo imefikia asilimia 90.7 na inatarajiwa kukamilika Septemba, 2023.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia MSCL ilikamilisha taratibu za zabuni kwa ajili ya kumpata mkandarasi wa ukarabati wa meli ya MV Liemba tarehe 5 Machi, 2023 na kwa sasa MSCL inaendelea kufanya majadiliano na mkandarasi kabla ya kusaini mkataba. Mkataba wa ukarabati wa meli hiyo unatarajiwa kusainiwa Juni, 2023.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kuhusu Meli ya MV Mwongozo ambayo ilisimamishwa kutokana na changamoto ya msawazo (stability), MSCL inakamilisha taratibu za kumwajiri Mhandisi Mshauri kwa ajili kufanya tathmini ya kina na kuishauri Serikali ipasavyo. Mhandisi Mshauri anatarajiwa kuanza kazi hii mwezi Juni na kukamilisha mwezi Novemba, 2023. Ahsante.
MHE. TUNZA I. MALAPO aliuliza: -
Je, Utekelezaji wa mradi wa Mtwara Corridor umefikia hatua gani?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tunza Issa Malapo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Ushoroba wa Mtwara (Mtwara Corridor) unajumuisha miradi ya Sekta mbalimbali ikiwa pamoja na Madini, Uchukuzi na Kilimo. Kwa upande wa Sekta ya Uchukuzi, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imetekeleza miradi ya ujenzi wa gati kubwa na la kisasa katika Bandari ya Mtwara lenye urefu wa mita 300. Ujenzi wa Bandari ya Ndubi ambao ulikamilika tangu Desemba, 2021 na Ujenzi wa bandari mpya ya Mbamba Bay ambao upo katika hatua za manunuzi ya Mkandarasi.
Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali kupitia Shirika la Reli (TRC) imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali kwa ajili ya ujenzi wa reli ya Standard Gauge ya Mtwara - Mbamba Bay na matawi yake kuelekea Liganga na Mchuchuma. Mradi huu unatarajiwa kutekelezwa kwa utaratibu wa ubia kati ya sekta ya Umma na sekta binafsi.
Mheshimiwa Spika, pamoja na taarifa hizo za miradi, naomba kulifahamisha Bunge lako kuwa, gati jipya lililojengwa katika Bandari ya Mtwara limeanza kuhudumia meli za makasha pamoja na shehena ya Kichele na takriban kila baada ya wiki moja kuanzia tarehe 20/04/2023 limekuwa likihudumia mizigo ya makasha ya yanayokwenda visiwa vya Comoro.
Mheshimiwa Spika, vikao vya wadau wa Ushoroba wa Mtwara vimeanza kuratibiwa chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ili kuweka mikakati ya kuendelea kuutangaza zaidi ushoroba huo na kuwavutia wananchi waishio ukanda huo pamoja na nchi jirani kutumia Bandari ya Mtwara na kuufanya ushoroba huo kutumika ipasavyo, ahsante.
MHE. FRANCIS K. NDULANE aliuliza: -
Je, lini Serikali itaanza kujenga kwa kiwango cha lami Barabara ya Nangurukuru - Liwale?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Kumba Ndulane, Mbunge wa Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), inaendelea na kazi ya Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Nangurukuru hadi Liwale yenye urefu wa kilometa 230. Kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ipo katika hatua za mwisho. Katika mwaka wa fedha wa 2023/24, Serikali itaanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami kwa awamu ya kwanza, kuanzia Liwale.
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza: -
Je, lini Bandari ya Karema itafunguliwa na kuanza kufanya kazi kwa kuwa ujenzi umekamilika kwa asilimia 87?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania imeshakamilisha ujenzi wa Bandari ya Karema na huduma katika bandari hiyo zimeanza kutolewa rasmi kuanzia tarehe 1 Septemba, 2022 baada ya kufanyiwa uzinduzi na Mkuu wa Wilaya ya Ziwa Tanganyika. Bandari hiyo inahudumia abiria na shehena mbalimbali za ndani ya nchi na zile zinazosafirishwa kati ya Tanzania na nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kudhibiti vyombo vya baharini vinavyozidisha mizigo na abiria?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantum Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vyombo vikubwa ikiwa ni vyombo vyenye urefu zaidi ya mita ishirini na nne. Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania TASAC linajukumu kisheria kufanya ukaguzi wa michoro ya meli kabla ya hatua ya ujenzi kuhakikisha mstari wa ujazo (load line) umewekwa kwenye kina sahihi cha meli, kisha Msajili wa meli anathibitisha michoro hiyo na kutoa ruhusa ya ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, TASAC kufanya ukaguzi kipindi cha ujenzi wa meli. TASAC hufanya Ukaguzi kuhakikisha Meli inapakia mizigo bila kupitiliza mstari wa ujazo uliothibitishwa na Msajili, na endapo itabainika kuwa meli imezidisha ujazo wa abiria, mizigo au vyote kwa pamoja itakuwa imetenda kosa kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, meli hiyo itapaswa kuzuiliwa bandarini na Mamlaka ya Bandari Tanzania itajulishwa ili kusitisha kutoa kibali kwa meli hiyo hapo bandarini. Kwa hatua zaidi, TASAC humtoza mmiliki au nahodha wa meli faini na kisha kusimamia upunguzwaji wa abiria, mizigo na vyote kwa pamoja kisha kuruhusu meli hiyo pindi Mkaguzi atakapojiridhisha kuwa Meli ipo salama kwa kuanza safari.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa vyombo vidogo vyenye urefu chini ya mita ishirini na nne, TASAC inajukumu kisheria kufanya ukaguzi wa vyombo vidogo na kutoa leseni ya uendeshaji inavyotaka ujazo wa abiria au mizigo unaostahili kuzingatiwa katika uendeshaji wa chombo.
Mheshimiwa Naibu Spika, endapo itabainika kuwa chombo kimezidisha ujazo wa abiria au mizigo, nahodha atakuwa ametenda kosa kisheria na chombo hicho kitazuiliwa bandarini au mwaloni ili kulipa faini na TASAC kusimamia upunguzwaji wa abiria au mizigo kabla ya kuruhusu chombo kuendelea na safari, ahsante.
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza: -
Je, kwa nini ujenzi wa barabara ya Tarime – Nyamwaga – Serengeti umeanzia katikati badala ya kuanzia Mjini?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Elibariki Immanuel Kingu, Mbunge wa Singida Magharibi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkandaasi kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Singida kuanzia Sabasaba – Sepuka – Ndago – Kizaga yenye urefu wa kilometa 77.6 amepatikana na mkataba wa ujenzi unatarajiwa kuwa umesainiwa kabla ya mwisho wa mwezi Juni, 2023, ahsante.
MHE. ELIBARIKI I. KINGU aliuliza: -
Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Singida – Sepuka - Ndago hadi Kizaga kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Elibariki Immanuel Kingu, Mbunge wa Singida Magharibi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkandaasi kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Singida kuanzia Sabasaba – Sepuka – Ndago – Kizaga yenye urefu wa kilometa 77.6 amepatikana na mkataba wa ujenzi unatarajiwa kuwa umesainiwa kabla ya mwisho wa mwezi Juni, 2023, ahsante.
MHE. DKT. THEA M. NTARA aliuliza: -
Je, Serikali imefikia wapi katika mpango wake wa kurudisha Reli ya Mtwara – Mbamba Bay na eneo la Mchuchuma?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Thea Medard Ntara, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali kwa ajili wa ujenzi wa reli ya Standard Gauge ya Mtwara – Mbamba Bay na matawi yake ya kuelekea Liganga na Mchuchuma. Aidha, taarifa hiyo ya upembuzi yakinifu na usanifu ilipendekeza kuwa mradi huu utekelezwe kwa utaratibu wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (Public Private Partnership – PPP).
Mheshimiwa Spika, ni matarajio yetu kuwa marekebisho ya Sheria ya PPP yatakayofanyika hivi karibuni yatasaidia kuwapata wawekezaji kwa ajili ya kujenga reli hii muhimu. Naomba kuchukua fursa hii kumuomba Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Mtwara na Ruvuma kuwa na subira wakati Serikali inashughulikia kwani suala hili litapewa kipaumbele na Serikali katika mwaka 2023/2024 ili kukamilisha taratibu za kumpata mjenzi, ahsante.
MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza:-
Je, mpango wa ujenzi wa Reli ya Kusini umefikia wapi?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali kwa ajili ya ujenzi wa Reli ya Standard Gauge ya Mtwara - Mbamba Bay na matawi yake ya kuelekea Liganga na Mchuchuma. Aidha, taarifa hiyo ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali, ilionyesha kuwa mradi huu unaweza pia kutekelezwa kwa uratibu wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (Public Private Partnership - PPP).
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua iliyofikiwa kwa sasa ni kumwajiri Mshauri wa Kifedha (Transaction Adviser) ili aweze kufanya mapitio ya Upembuzi uliokamilika mwaka 2016 kwa lengo la kuandaa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa mwekezaji kwa utaratibu wa ubia (PPP – Public Private Partnership), ahsante.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA aliuliza:-
Je, Serikali inatoa tamko gani kwa mabasi yasiyoingia stendi na ambayo hushusha abiria nje ya stendi?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nicholaus George Ngassa, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mabasi yote ya masafa marefu hupangiwa ratiba na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ambazo huonyesha stendi za kupakia na kushusha abiria pamoja na muda wa kusimama kwenye stendi hizo. Aidha, mabasi ya masafa marefu yamepangiwa kusimama katika stendi moja tu kwa kila Mkoa isipokuwa pale ambapo basi hilo lina abiria anayeshuka katika stendi ya Wilaya. Utaratibu huo umepangwa ili kuondoa usumbufu na ucheleweshaji wa abiria wa masafa marefu kwa kuwalazimisha kuingia kwenye stendi hata kama hawana abiria wa kupanda au kushuka.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Ngassa anatoka Igunga, naomba kumtaarifu kuwa, Stendi ya Igunga haimo kwenye stendi ambazo mabasi ya masafa marefu hulazimika kuingia ama kusimama isipokuwa kama yana abiria wa kupanda au kushuka kwenye stendi hiyo. Hata hivyo, stendi hiyo hutumika kwa magari yote yanayotoa huduma ndani ya Mkoa wa Tabora na Mikoa jirani.
Mheshimiwa Spika, kwa madereva wanaokaidi kuingia stendi na kushushia abiria nje ya stendi hususan barabarani, madereva hao wanakiuka maelekezo ya Kifungu cha 50(1) cha Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168 kinachomzuia mtu yeyote kuegesha au kusimamisha gari barabarani bila kujali watumiaji wengine wa barabara, hivyo, huvunja Sheria. Ahsante.
MHE. GEOFFREY I. MWAMBE aliuliza:-
Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa kilometa 1,000 za reli ya Standard Gauge kati ya Mtwara - Mbamba Bay na Songea – Ludewa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Geoffrey Idelphonce Mwambe, Mbunge wa Masasi Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali kwa ajili wa ujenzi wa kilometa 1,000 za reli ya Standard Gauge ya Mtwara hadi Mbamba Bay na matawi yake ya kuelekea Liganga na Mchuchuma. Aidha, taarifa hiyo ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali, ilionesha kuwa mradi huu unaweza pia kutekelezwa kwa utaratibu wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (Public Private Partnership - PPP).
Mheshimiwa Spika, hatua iliyofikiwa kwa sasa ni kumuajiri Mshauri wa Kifedha (Transaction Adviser) ili aweze kufanya mapitio ya upembuzi uliokamilika mwaka 2016 kwa lengo la kuandaa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa mwekezaji kwa utaratibu wa ubia (PPP), ahsante.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kukabiliana na ajali za majini?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) imeanza kutekeleza Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Kikanda cha Uratibu wa Shughuli za Utafutaji na Uokoaji Majini (Regional Maritime Rescue Coordination Center – MRCC) kupitia mradi unaoendelea katika Ziwa Victoria na vituo vidogo vinne vya uratibu wa shughuli za utafutaji na uokoaji majini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi huu unatekelezwa kwa fedha za ndani pamoja na mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ambapo katika mwaka 2023/2024 umetengewa Shilingi bilioni 1.74. Aidha, kupitia mradi huo zitanunuliwa boti tatu kwa ajili ya shughuli ya utafutaji na uokoaji ambazo kwa sasa zipo katika hatua za manunuzi, ahsante.
MHE. ALLY M. KASSINGE aliuliza:-
Je, ni lini wananchi 144 wa Kilwa Masoko ambao maeneo yao yalichukuliwa kwa lengo la upanuzi wa Kiwanja cha Ndege watalipwa fidia?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Mohamed Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi waliopisha upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kilwa Masoko, Serikali imehuisha uthamini wa mali za wananchi ndani ya kipindi cha robo ya kwanza ya Mwaka wa Fedha 2022/2023, ambapo idadi ya wananchi iliongezeka kutoka 144 waliofanyiwa uthamini mwaka 2013 hadi kufikia wananchi 438.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali ipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya uwekaji wazi Daftari la Fidia (Valuation Report Disclosure) kwa wananchi husika kabla ya kuwasilishwa kwa Mthamini Mkuu wa Serikali kwa idhini, ahsante.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE aliuliza: -
Je, ni lini Mamlaka ya Viwanja vya Ndege itaruhusiwa kukusanya na kutumia passenger service charge kuboresha viwanja vya ndege ?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Mwanaisha Ng’anzi Ulenge, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) imewekewa utaratibu wa kukusanya moja kwa moja ada za kutua na maegesho ya ndege; ada ya usalama (security fee); tozo za ukodishaji wa ofisi, karakana, majengo ya kuhifadhia mizigo, migahawa na maduka; tozo za maegesho ya magari, na tozo za mabango. Aidha, Sheria ya Huduma za Viwanja vya Ndege (The Airport Service Charge Act) Sura ya 365 inaipa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) jukumu la kukusanya tozo kwa abiria wanaosafiri kupitia viwanja vya ndege (passenger service charge) na kuwasilisha Hazina.
Mheshimiwa Spika, fedha zinazokusanywa na TRA kutoka kwa abiria na kuwasilishwa Hazina zinatumika kuendeleza miundombinu ya viwanja vya ndege nchini pamoja na kulipa mishahara ya watumishi, matumizi ya uendeshaji wa TAA na kufanya matengenezo ya viwanja. Aidha, Serikali hutoa fedha kila mwaka kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya viwanja vya ndege, ahsante.
MHE. KILUMBE S. NG'ENDA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kukiendeleza Chuo cha Hali ya Hewa kilichopo Kigoma ili kiwe Chuo Kikuu kishiriki cha Dar es Salaam na kiweze kutoa taaluma nyingine?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kilumbe Shabani Ng'enda, Mbunge wa Kigoma Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imeendelea na jitihada za kukiendeleza Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa kuwa Chuo Kikuu kishiriki cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Tayari andiko kwa maana ya dhana concept note kuhusiana na ushirikiano huo limeandaliwa na Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa (NMTC) na kuwasilishwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ahsante
MHE. KILUMBE S. NG'ENDA aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kukiendeleza Chuo cha Hali ya Hewa kilichopo Kigoma ili kiwe Chuo Kikuu kishiriki cha Dar es Salaam na kiweze kutoa taaluma nyingine?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kilumbe Shabani Ng'enda, Mbunge wa Kigoma Mjini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imeendelea na jitihada za kukiendeleza Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa kuwa Chuo Kikuu kishiriki cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Tayari andiko kwa maana ya dhana concept note kuhusiana na ushirikiano huo limeandaliwa na Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa (NMTC) na kuwasilishwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ahsante.
MHE. HASSAN S. MTENGA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga Daraja la Mto Ruvuma ili kufungua Shughuli za Kibiashara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. FREDY A. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Selemani Mtenga, Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali za Tanzania na Msumbiji zilijenga Daraja la Umoja (Mtambaswala) ili kufungua shughuli za kibiashara. Kwa sasa Serikali ya Tanzania inategemea kuanza kufanya mazungumzo na Serikali ya Msumbiji, ili kuanza taratibu za ujenzi wa Daraja la Kilambo, Mto Ruvuma.
Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. BONNAH L. KAMOLI aliuliza: -
Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya wananchi wa Kipunguni waliozuiwa kuendeleza maeneo yao kupisha upanuzi wa uwanja wa ndege?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bonnah Kamoli, Mbunge wa Segerea, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali ipo katika hatua za mwisho za kufanya uthamini mpya kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi wote wa Kipunguni waliopisha ununuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA). Zoezi la uthamini linatarajiwa kukamilika mwezi Septemba, 2022. Ahsante.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI K.n.y. MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itawaajiri vibarua wapatao 20 ambao wamefanya kazi Shirika la Reli Mkoa wa Katavi kwa miaka mitano?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. FREDY A. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Festo Mariki, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Katavi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua mchango uliofanywa na vijana wa Kitanzania ambao wamekuwa wakishiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ya reli ikiwemo ukarabati wa njia ya reli katika Mkoa wa Katavi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania inaendelea kuwatumia vijana hao katika miradi mbalimbali ya ujenzi na ukarabati wa njia ya reli na imekuwa ikiwahimiza vijana hao kujiendeleza ili kuwa na sifa ya kuajiriwa katika utumishi wa umma kwa kuzingatia Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma. Kupitia utaratibu huo vibarua wawili wamejiendeleza na kuajiriwa na wengine wanaendelea kuhamasishwa.
MHE. KABULA E. SHITOBELA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itapunguza tozo zinazotozwa na TPA kwani imekuwa ikitoza tozo kubwa kwenye mizigo kuliko Makampuni binafsi?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE FREDY MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kabula Enock Shitobela, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuhakikisha Bandari zote za Tanzania zinatoa huduma bora na kwa gharama nafuu ili kuendana na hali halisi ya ushindani katika bandari za ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika. Katika kufikia azma hiyo, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ipo katika hatua za mwisho za kufanya mapitio ya gharama za huduma za bandari. Hivi sasa, uchambuzi wa maoni yaliyowasilishwa na wadau mbalimbali yanafanyiwa kazi na zoezi hili linatarajiwa kukamilika Julai, 2022.
MHE. FATMA H. TOUFIQ K.n.y. MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa treni ya mwendokasi kutoka Kaliua-Mpanda hadi Karema?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TRC imekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa awali wa ujenzi wa njia ya reli ya Kaliua – Mpanda – Karema kwa kiwango cha Standard Gauge. Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuanza maandalizi ya ujenzi wa reli hii.