Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Atupele Fredy Mwakibete (38 total)

MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini pia niseme tu kwamba barabara hii katika maeneo mengi, kama ulivyokiri kwenye jibu lako la msingi kuna baadhi ya maeneo inateleza, kuna utelezi mkali. Je, Serikali ina mipango gani kuhakikisha kwamba kwa kipindi hiki cha mvua ambapo haipitiki inaweza kujengwa kwa haraka iwezekanavyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa tuna maeneo mengi sana katika nchi hii yenye matatizo ya mawasiliano ya barabara. Tumetoa maelekezo mahsusi kwa kila Meneja wa TANROADS Mkoa kuhakikisha kwamba muda wote wanapata taarifa wapi kuna matatizo na wayashughulikie haraka. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, maelekezo hayo yamekwenda Mkoa Mbeya na pengine nichukue nafasi hii kama walikuwa hawana taarifa sasa wamepata taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mbunge, wakalishughulikie hilo eneo kwa kadri ya maelekezo ya jumla ambayo Mameneja wote wameelekezwa.
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu ya Serikali ambayo wananchi wa Busekelo hawajaridhika nayo, kwa sababu wananchi hawa wako pale tangu miaka ya 1950 na mipaka imefanyika mwaka 2006/20007, ni mwaka wa tisa sasa bado wananyanyaswa sana na watu wa TANAPA.
Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusiana na watumishi wa TANAPA ambao wanawanyanyasa wananchi na wanashindwa hata kuendeleza maeneo yao ya kilimo, shule pamoja na makanisa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, atakuwa tayari tuongozane twende akajionee kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa Bonde la Mwakaleli ili ukajithibitishe hiyo mipaka?
NAIBU WAZIRI WA MALIASISILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, askari wanaosimamia utekelezaji wa sheria upande wa misitu na wanyamapori, wanaosimamia hifadhi walio wengi wanajitahidi kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria. Hata hivyo, kwa wale wachache ambao wanafanya hayo yaliyotajwa na Mheshimiwa Mbunge ya unyanyasaji na tabia nyingine zozote ambazo si nzuri, zinazoipaka matope Serikali wanafanya makosa na tunaomba pale ambapo inajitokeza, wanaohusika watolewe taarifa katika vyombo vinavyohusika watachukuliwa hatua zinazohusika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kwenda, niko tayari kati ya Mkutano huu na Mkutano ujao, hebu tukutane baadaye tuweze kupanga vizuri ratiba, tunaweza kwenda wote kuangalia na kupata ufumbuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni kwamba, Serikali imejipanga sasa na kwa sababu matatizo haya ni ya muda mrefu, sasa tumejipanga vyema zaidi na katika kipindi cha muda mfupi ujao mtashuhudia tunavyoweza kurudia kuweka mipaka kwa namna kabisa ya maelewano ya wale tunaopakana nao ili baada ya kuwa tumeshaweka mipaka hiyo, tunatarajia wananchi wataheshimu mipaka hiyo na wataacha kuvuka mipaka hiyo kwenda kwenye maeneo ya hifadhi.
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, asante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, lakini kwa mujibu wa swali nilivyouliza pamoja na majibu ambayo yametolewa ni dhahiri kwamba kwa vijiji ama Kata ambazo amezisema mimi mwenyewe ni shahidi kwamba kuna hela ambazo hazijafika hadi sasa hivi na katika jibu lake la msingi amesema zimefika. Kwa mfano Kata ya Mpata, nimepeleka mabomba zaidi ya milioni 10 lakini Serikali mpaka sasa hivi haijatoa chochote. Mheshimiwa Waziri unaweza ukathibitishia wananchi wa Mpata kwamba hizo fedha zimefika kule? Hilo ni swali la kwanza.
Swali la pili, kuna baadhi ya Kata ya Ntaba, kijiji cha Ilamba wananchi pamoja na wakazi wa eneo la pale wananyang’anyana maji, wananchi na mamba, na zaidi ya wananchi kumi na moja wameshauawa na mamba ama kuliwa na mamba kwa sababu ya kutafuta maji, je, Serikali inatoa tamko gani kwa ajili ya wananchi hawa na ikizingatiwa kwamba kuna mradi ambao umeshafanyiwa upembezi yakinifu tangu mwaka 2008 hadi leo hii kwa thamani ya shilingi milioni 100, haikufanya kitu chochote.
NAIBU WAZIRI (TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Naibu Spika, asante.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwa taarifa aliyosema kwamba fedha hazijafika ni kwamba ngoja nita-cross check vizuri katika Ofisi yangu nijue ni nini kilichotokea lakini kikubwa ni nini? Ni kwamba kuna changamoto ya upelekaji wa fedha, siyo mradi huo tu isipokuwa maeneo mengi sana, fedha zimeenda kwa kusuasua na hivi karibuni ndiyo maana Waziri wa Maji juzi juzi alikuwa anazungumza kwamba kutokana na kusuasua kwa kupeleka fedha katika miradi ya maji na miradi hii mingi sasa mingine ilikuwa imesimama, sasa Serikali iliamua kwamba ile outstanding payment ambazo zilikuwa zinakaribia karibuni bilioni 28, kwamba fedha hizi sasa zipelekwe katika maeneo mbalimbali ilimradi wale Wakandarasi walio-demise mitambo waweze kuendelea.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge naomba nikuambia kwamba nitazifuatilia kwa karibu ilimradi kwamba huu mradi lengo letu liweze kufanikiwa na wananchi waweze kupata huduma ya maji.
Lakini sehemu ya (b) ni kwamba kuna changamoto ya wananchi wanakamatwa na Mamba. Kwanza nitoe masikitiko yangu sana katika eneo hilo, kwa sababu kama watu wanaliwa na mamba ina maana kwamba ni changamoto kubwa, tunapoteza jamii ya Watanzania.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge naomba nikiri kwamba nimesikia hili na nakumbuka tulifanya discussion juzi juzi kwamba katika ziara yangu nitakapokuwa nimeenda katika Mkoa wa Mbeya nimesema kipambele katika Jimbo lako la Busokelo litakuwa ni sehemu mojawapo ambayo nitaenda kutembelea ilimradi mambo haya yote kwa ujumla wake tuweze kuyatazama vizuri tukiwa site na kuweze kupanga mipango mizuri, mwisho wa siku wananchi wa Jimbo hili waweze kupata huduma ya maji, kila mtu aweze kujiona ana faraja na nchi yake.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Mkoa wa Mbeya umebarikiwa sana kuwa na madini pamoja na vyanzo mbalimbali vya umeme. Nataka nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa mfano, kuna vyanzo vya umeme vya jotoardhi kule Busokelo lakini pamoja na Lake Ngozi, kuna makaa ya mawe, kuna maporomoko ya maji na vitu vingine katika sehemu nyingine mbalimbali. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, ni lini vyanzo hivi vitaanza kufanya kazi ili wananchi wa Mbeya na Tanzania kwa ujumla ipate umeme wa kutosha?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa, kati ya mikoa hapa nchini iliyojaliwa kwa kuwa na rasilimali za madini pamoja na maporomoko ya maji ni pamoja na Mkoa wa Mbeya na hasa Mbeya Vijijini. Nikubaliane naye, kwa sasa Wizara yetu inafanya utafiti na inakamilisha utafiti wa jotoardhi (geothermal) ambapo sasa tumegundua madini hayo yatakuwa na megawati 20 kwa kuanzia lakini baadaye tutakwenda hadi megawati 100, hiyo ni kwa jotoardhi. Bado tunafanya upembuzi yakinifu katika makaa ya mawe pamoja na maporomoko ya maji katika mito hiyo na hasa katika Mto Ngozi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hatua tunazochukua ni kukamilisha utafiti huo yakinifu na kadri itakavyowezekana tukipata fedha, shughuli ya kutekeleza miradi hiyo itaanza. Mradi wa geothermal unaanza kutekelezwa mwezi Julai, 2017.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali moja. Kwa kuwa tatizo la Barabara ya Kalambo linakwenda sambamba na tatizo la barabara iliyopo Jimbo la Busokelo Wilayani Rungwe inayotoka pale Tukuyu Mjini kuanzia Katumba – Suma – Mpombo – Isange – Ruangwa – Mbwambo hadi Tukuyu Mjini; na barabara hii imekuwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi zaidi ya miaka 10: Je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami Kilometa 73 zilizobaki?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, utakumbuka tulikaa pamoja kati yako wewe, Mheshimiwa Mbunge pamoja na Waziri wangu kuhusu barabara hii. Nilikiri wakati ule na ninarudia kukiri hapa kwamba hatujaitendea haki, kwamba ni ahadi ya muda mrefu sana, lakini tumepanga kujenga Kilometa moja tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuahidi na Mheshimiwa Mwakibete nilimwahidi kwamba mwaka ujao wa fedha mazingira hayo hayatajirudia. Naomba nirudie ahadi hii sasa hapa, maana yake pale hatukuwa hadharani, leo tuko hadharani.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa Sera ya Afya inasema, kila Kijiji kijenge Zahanati na kila Kata ijenge Kituo cha Afya; nakumbuka mwaka 2007 tulikuwa na program ya kujenga sekondari kwa kila Kata na kulikuwa na uhaba mkubwa sana wa watumishi; tulikuwa tunasema ni Vodacom ama Voda faster kwa sababu tu walikuwa wanamaliza Form Six na kwenda kufanya kazi. Je, Serikali imejipangaje ukizingatia hii ni afya kwa ajili ya watumishi watakaoajiriwa kwa vituo ama vijiji 12,000 na kitu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Halmashauri ya Busokelo ni changa sana; tuna Hospitali moja tu, nayo hiyo Hospitali ni CDH kwa maana ya kwamba ni Council Designated Hospital; na tuna Kituo kimoja tu cha Afya. Je, Serikali ipo tayari sasa kushirikiana na wananchi nguvu kazi tunazozifanya ili iweze ku-upgrade Kituo cha Kambasegela, Kituo cha Afya Isange pamoja na Kanyerere?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli sera ya afya ni kwamba kila Kijiji kiwe na Zahanati na kila Kata iwe na Kituo cha Afya. Suala la watumishi ni kweli kuna changamoto, lakini tulivyokuwa katika bajeti yetu ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI), hali kadhalika wiki iliyopita tulikuwa na bajeti ya Wizara ya Afya; na Waziri wa Afya alisema wazi kuhusu mkakati wa kuajiri watumishi takriban 10,000 kwa kipindi hiki ili mradi kwenda kuziba zile gap.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili liko katika utaratibu na naamini kwamba, wale watumishi watakapoajiriwa, nimwambie Mheshimiwa Atupele kwamba, tutalipa kipaumbele Jimbo lake ili mradi ile changamoto ambayo inalikabili sasa hivi ya upungufu wa watumishi tuweze kupunguza ile kasi yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, tunahimiza hata vyuo vyetu vile vile kuongeza idadi ya watumishi, ili mwisho wa siku ile needs assessment tukiweza kuifanya, watu waweze kupatikana, basi katika soko, wawepo watu wa kutosha kuwapeleka katika hivi Vituo vya Afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kushirikiana na watu wa Jimboni kwa Mheshimiwa Mbunge, kwanza namsifu sana, kwani ni miongoni wa Wabunge aliyenipa proposal mkononi, kwamba mimi nina proposal yangu ya Sekta ya Afya katika Jimbo langu. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hilo, naomba nikiri wazi kwamba Ofisi ya Rais, (TAMISEMI) itashirikiana naye, kuhakikisha kwamba changamoto zilizoko katika Jimbo hili, tuone tutazifanyaje kwa pamoja. Najua Jimbo hili hata Profesa alikuwa huko zamani. Kwa hiyo, tutashirikiana kwa pamoja kuona jinsi gani tutafanya ili mradi watu wa Jimboni kwake waweze kupata huduma ya afya hususan katika suala zima la kuongeza miundombinu.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwanza nimpongeze kwa jinsi ambavyo amekuwa akifuatilia suala la afya kwa Jimbo langu la Busokelo, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, je, ni lini hasa hospitali hii itaanza kujengwa ikizingatia kuwa wananchi wa Jimbo la Busokelo pamoja na Mbunge wao tupo tayari kushirikiana na Serikali kujenga hospitali hii?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, pamoja na kwamba hizi shilingi bilioni mbili ambazo zimetamkwa kwenye jibu la msingi yalikuwa ni maombi maalum, je, Mheshimiwa Naibu Waziri unaweza ukawathibitishia wananchi wa Jimbo la Busokelo kwamba hizi fedha sasa na maombi yao yamekubaliwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, juu ya lini hospitali hii itajengwa, nimesema hapa.
Kwanza mimi naomba niwapongeze hawa Wabunge wote unaowaona humu. Wabunge unaowaona humu jana wamefanya tukio kubwa sana la kupitisha Bajeti ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Bajeti ile sasa inatupa uwezo wa kwenda kutekeleza matatizo ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikwambie sisi Mawaziri tutakuwa serious kuhakikisha kuwa hawa Wabunge kutokana na kelele na juhudi kubwa wanayoifanya tunawahudimia kwa nguvu zetu zote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimueleze Mheshimiwa Mwakibete kwamba kwa sababu pesa imetengwa; na nilikuambia kwamba bajeti ya Serikali hapa imeshapitishwa, na kwamba inafanyiwa kazi; kama swali lako linavyosema fedha hii imetengwa kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya yako. Jukumu letu kubwa sisi sasa ni kuweza kusimamia ili wananchi wako wapate huduma na hatimaye wa- appreciate kwamba wamepata Mbunge kijana wa kuwatumikia. Kwa hiyo ondoa hofu katika hilo.
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa niweze kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la Shule ya Sekondari Ndembela linaendana sana na tatizo la Shule Sekondari ya Kandete Wilayani Rungwe ambapo sasa tumeanza kujenga ili iwe ya wasichana pekee. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza akawadhibitishia wananchi wa Busokelo kwamba Serikali itashiriki kikamilifu ili ianze mapema mwakani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge amesema kwamba kama ikiwezekana Serikali ianzishe mchakato wa kuifanya Shule ya Sekondari ya Kandete ili kuwa sekondari ya bweni. Nimerudia hapa mara kadhaa kwamba tumekuwa na changamoto kubwa ya vijana wetu wasichana kupata mimba na nikasema tumetoa kipaumbele sana katika ujenzi wa shule za bweni. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Halmshauri yake ikianza na sisi Ofisi ya Rais – TAMISEMI lazima tutaweka nguvu ya kutosha kwa sababu ajenda kubwa ni jinsi gani tutamsaidia msichana aweze kupata elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama Mheshimiwa Mbunge watakuwa wameanza juhudi hizo basi, naomba nimuambie kwamba na sisi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, kwa vile watakuwa wameweka katika bajeti yao tutahakikisha bajeti hizo zinapitishwa ili sekondari hiyo ambayo inatarajiwa kubadilishwa kuwa sekondari ya wasichana iweze kuwa sekondari ya wasichana vijana waweze kumaliza vizuri, waweze kupata elimu na hapo baadaye tuwe na viongozi wengi wasichana kutoka maeneo hayo.
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa, tatizo la Karagwe linaendana sana na tatizo la maji lililopo Jimboni Busokelo, Wilaya ya Rungwe. Je, Serikali ina mpango gani hasa katika Kata za Ntaba, Itete, Isange pamoja na Kandete kuwapelekea maji ukizingatia Kata ya Ntaba kuna bwawa la asili ambapo wananchi 12 wameuawa kwa sababu ya kutafuta maji?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge pamoja na Wabunge wengine ambao wangeweza kusimama kuuliza Kata zao, Vijiji vyao ambavyo vipo tofauti na swali la msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba, anayeamua ni kijiji kipi tuanze nacho ni ninyi wenyewe kwenye Halmashauri yenu. Kwa hiyo, katika Bajeti ya mwaka huu, wamesema ni Kata ipi tunaanza halafu tutaendelea na Kata nyingine. Tulisema kwenye mradi huu wa Vijiji 10, kwanza tunakamilisha miradi ambayo tayari ilishakuwa imeanza au ina mikataba haijaanza, tukamilishe ile halafu tutaingia kwenye mikataba mipya. Sasa katika kuingia vijiji vipi, mnachagua ninyi kule kule, Waziri hawezi kuwachagulia.
Kwa hiyo, naomba sana ndugu zangu tushirikiane na Halmashauri zetu kuweka vipaumbele vijiji vile ambavyo vina shida kubwa ya maji ndivyo tuanze navyo. Vile vyenye shida au miradi ilishakuwepo labda imechoka iwe ni phase ya pili. Kwa hiyo, naomba sana tushirikiane ili tuchague Vijiji vile ambavyo vina shida zaidi ya maji, tuanze navyo katika Bajeti ya Mwaka 2016/2017.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kwa masikitiko makubwa sana na nisononeke moyoni mwangu kwamba Mheshimiwa Waziri majibu aliyoleta hapa sio niliyouliza kwenye swali langu la msingi. Nimeuliza, barabara itajengwa lini ya Mkoa wa Mbeya na Njombe yeye amenitajia barabara za Katumba – Lusanje – Kandete. Nilikuwa namaanisha barabara inayotoka Mwakaleli kwenda mpaka Makete halafu iunganishwe na Njombe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini zaidi swali la pili nimeuliza Jimbo la Busokelo litaunganishwa na Jimbo la Rungwe. Lakini Waziri anasema Serikali haifikirii kufungua barabara kuunganisha maeneo hayo kutokana na milima mikali, hivyo barabara ziendelee kutumika zilizopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisikitike kwa sababu wananchi wa Jimbo la Busokelo katika Vijiji nilivyovitamka Suma pamoja na Kilimansanga ni zaidi 5,000. Akisema kwamba waendelee kutumia barabara hizo hizo wakati tayari hakuna muunganisho wa hizo barabara nashindwa kuelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hili swali ningeomba liweze kujibiwa kwa mara nyingine tena kwa sababu majibu aliyojibu hapa sio, hayaniridhishi.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimsihi Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya kumaliza Bunge hili mimi nitakuwa na ziara eneo hilo. Kwa sababu katika jibu la msingi barabara anayoongelea ya Mkoa wa Mbeya kuunganisha na Njombe tumesema inapitia Mwakaleli, Kata ya Kandete na Luteba; na tumesema inapitia Katumba - Lusanje - Kandete - Ikubo hadi Luteba. Maadam anasema narudia yale yale, sasa kama nilichokisema anasema sio sahihi, naomba tukakutane site ili tuweze kupata uhakika wa kile ambacho yeye anakiamini wakati sisi hiyo ndio tunavyofahamu.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na
majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naipongeza Serikali kwa jinsi
ambavyo wameushughulikia mradi huu wa masoko na miradi mingine iliyo ndani
ya Wilaya ya Rungwe. Nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza; kwa kuwa,
mradi huu wa maji umechukua muda mrefu na Mkandarasi aliyekuwa amepewa kazi hiyo Osaka, baada ya kutangazwa tenda ya mara ya pili anaondolewa.
Tungependa kufahamu ni sababu gani zimesababisha Mkandarasi huyu wa
mara ya kwanza ashindwane na Halmashauri?
Swali la pili; kwa kuwa, miradi hii ya maji ni ya thamani kubwa, zaidi ya
bilioni tano tungependa tumwombe Mheshimiwa Naibu Waziri aweze
kuitembelea hii miradi pamoja na ya Mwakaleli One pamoja na Kapondelo
ikiwemo na hii ya Masoko. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika,
ameuliza sababu zilizofanya Mkandarasi asimamishwe kuendelea na kazi,
sababu ziko kimkataba. Kwa hiyo, sababu za kimkataba hatuwezi kuzijadili sisi
Waheshimiwa Wabunge, lakini la kuelewa tu ni kwamba, alishindwa ku-perform
vile ilivyokuwa imetakiwa kimkataba ndiyo maana Halmashauri kwa kutumia
vifungu vya mkataba ikamsimamisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimpongeze Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Rungwe. Kwa mara ya kwanza ameleta bajeti ya miaka mitano na nimefurahi
sana. Ameweka mpango wa miaka mitano na bajeti inayotakiwa akaweka na
kifungu cha matengenezo ya miradi atakayokuwa ameitekeleza ili kuhakikisha
kwamba miradi tunayojenga basi inakuwa ni ya kudumu na mabomba
yanaendelea kutoa maji mwaka mzima.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Serikali kwamba Halmashauri ya Busokelo haijakidhi vigezo vya kuwa Wilaya, nina maswali mawili kwa Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo vigezo anavyosema haijakidhi sijui ni vipi kwa sababu vigezo ambavyo vinazingatiwa, hasa ni idadi ya watu pamoja na jiografia ya eneo husika, kwetu kwa sababu hii tathmini ilishafanyika tangu miaka 2013 na sasa hivi ni 2017. Hauoni kwamba kuna
umuhimu sasa wa kuanzisha hiyo Halmashauri ya Busokelo iwe inaitwa Wilaya ya Busokelo badala ya sasa ilivyo? Swali la pili, kwa kuwa Mkuu wa Wilaya pamoja na DAS wanafanya kazi nzuri katika Wilaya ya Rungwe, kwa bahati mbaya kwa sababu ya jiografia ya Rungwe ilivyo kuna zaidi ya kata 40 na huyu Mkuu wa Wilaya hawezi kusimamia ama kufuatilia zote kwa wakati mmoja kufuatana na jiografia ilivyo.
Je, hauoni pia ni miongoni mwa sababu ambayo
inaweza ikasababisha ianzishwe Wilaya ya Busokelo na hivyo iweze kuanzishwa haraka iwezekanavyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwa sababu specification inataka angalau eneo hilo liwe na eneo lisilopungua kilometa za mraba 5,000 nwakati pale kiuhalisia ziko kilometa za mraba 969. Kwa hiyo, hii ilikuwa ni kigezo kimojawapo ambacho kimesababisha isiweze ku-qualify. Kipindi kile idadi ya watu kwa muongozo inatakiwa watu wasiopungua 250,000 lakini katika kipindi kile tathmini ilivyofanyika kulikuwa na watu takribani 96,348.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninafahamu muda mrefu sasa hivi umeshapita kutoka kipindi kile mpaka sasa hivi hii tathmini ukiiangalia huenda population imeongezeka, lakini vilevile hata ukiangalia suala zima la tarafa, vigezo lazima angalao kuwe na tarafa tatu pale ukiangalia ni tarafa moja. Ninafahamu kwamba mlikuwa na juhudi ya kuitenga ile Tarafa moja mpate tarafa nyingine tatu, hii nilidhani kwa sababu Mbunge mnafahamu kama ulivyosema mna kata zipatazo 40, mnaweza mkakaa kwa pamoja sasa na RCC
yenu kuangalia mnaweza kuishauri vizuri nini cha kufanya. Baadae ikionekana vigezo hivi sasa vimekaa vizuri basi Serikali itaona nini cha kufanya na jinsi gani ya kupata eneo hili kuwa eneo la kiutawala la Kiwilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala kwamba Mkuu wa Wilaya ya Busokelo anahudumia eneo kubwa sana, kwa hiyo kuna haja ya kuona hili jambo sasa ikiwezekana Wilaya ile sasa Busokelo iwe Wilaya kamili. Kama nilivyosema pale awali ni kwamba hivi sasa ninyi angalieni jinsi ya kufanya. Nafahamu kwamba ni kweli Mkuu wa Wilaya ya Rungwe anafanya kazi kubwa sana, nilikuwa nae pale site siku ile tulipopata lile tatizo, kweli ni miongoni mwa Wakuu wa Wilaya ambao wanajituma sana katika kazi yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile wote kama Viongozi Wakubwa na Mheshimiwa Naibu Spika uko hapa, nadhani mtaliangalia kwa uzito wenu kwa jinsi gani mtafanya, kama Busokelo, kama Rungwe kwa wakati mmoja ni jinsi gani hata mtafanya mipaka yenu na kila kitu. Lengo kubwa ni kupeleka huduma kwa wananchi na Serikali mkiona kwamba mmekidhi vigezo hivyo, haitasita kufanya maamuzi sahihi.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa niweze kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, wewe ni miongoni mwa
watu ambao ni washabiki na wapenzi wa ngoma za asili, pamoja na kwamba wewe ni mpenzi wa ngoma za asili, hata huku Dodoma kuna ngoma za asili zinaitwa Chigogo.
Je, Serikali imejipangaje kuwezesha wale wote ambao wanaanzisha ngoma za asili katika mashindano hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Swali lake liko nje ya michezo, lakini liko ndani ya Wizara yetu ni ngoma za asili.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuhamasisha wananchi wote waendelee kuenzi ngoma za asili, hata vyombo vya habari tunavihamasisha ili viweze kupiga ngoma za asili katika vipindi vyake kwa zile asilimia 60 za local content ambazo zimepewa. Ahsante.

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kujibu vizuri hilo swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kukupongeza wewe binafsi kwa ubunifu, ujasiri na uthubutu kuanzisha mashindano ya ngoma zetu za utamaduni katika Ukanda wa Kusini.
Mheshimiwa Naibu Spika, lilivyoanza hili Waheshimiwa Wabunge ilikuwa kwa Wilaya mbili tu, Wilaya ya Rungwe na Kyela sasa imepanuliwa zaidi kuhusisha Mkoa mzima na Mikoa ya jirani. Ninatoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge wote katika maeneo yenu tusisubiri Serikali ianzishe hayo, hebu tufuate mfano alioutoa Naibu Spika, wote tuanzishe hayo mashindano. Sisi kama Serikali tutasaidia kuboresha hizo ngoma zetu za utamaduni. (Makofi)
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina swali moja tu la nyongeza. Taifa lolote duniani ili lisonge mbele linahitaji watu waliosoma kada mbalimbali, iwe ni sanaa, sayansi au biashara.
Je, Serikali ina mpango gani wa ku-balance wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi, pamoja na wanafunzi wanaosoma sanaa ili isitokee kama sasa tuna ziada ya wanafunzi wa sanaa zaidi ya 7,463 na inapelekea kutokuwa na ajira. Serikali ina mpango gani kwa miaka ya hivi karibuni na baadaye? (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Serikali, imekuwa ikiendelea kuweka mazingira mazuri na kuhamasisha wanafunzi kusoma masomo ya sayansi. Katika mwaka 2015 mpaka 2016 Serikali ilijikita zaidi katika kuhamasisha Shule za Sekondari kujenga maabara. Katika mwaka 2016/2017 tunasambaza vifaa vya maabara. Hizo zote ni jitihada za kuongeza wanafunzi wa masomo ya sayansi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba wanafunzi wanayo hiari ya kuchagua masomo. Kwa hiyo, kama Serikali tunatoa mazingira mazuri. Nangependa kuwaomba Waheshimiwa Wabunge tushirikiane kuwahamasisha wanafunzi pia kuona kwamba masomo ya sayansi na teknolojia nayo ni muhimu ili waweze kuyachukua kwa wingi zaidi. (Makofi)
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa furda hii niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri Dkt. Mary Mwanjelwa Dada yangu niipongeze Serikali katika majibu haya.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa katika jibu lake la msingi amekiri kwamba Serikali ina vituo ama vyuo 14 kwa ajili ya kilimo hapa nchini, lakini chuo/kituo hiki kilianza kujengwa tangu 2009 na kilikabidhiwa kwa halmashauri na halmashauri imeshindwa kukiendeleza. Je, hauoni kuna umuhimu sasa kupitia Wizara yako muweze kuchukua jukumu hili ili chuo hiki kiweze kukamilika maana ni zaidi ya miaka nane hadi sasa?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, pamoja na kwamba kuna vyuo hivyo 14, tumekuwa tukitoa wataalam na watafiti mbalimbali na wanakuwa wanazalisha kwa tija; lakini changamoto kubwa iliyopo ni kwamba anapokwenda kufanya kazi ama kwenye field changamoto kubwa ni kwamba masoko ya mazao wanayozalisha yanakuwa hayapo. Wizara imejipangaje, ni mechanism gani itatumika kutafutia masoko kwa bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini hasa hasa katika kilimo ukizingatia kwamba mahindi sasa hivi yameshuka bei, viazi mviringo vimeshuka bei, choroko zimeshuka bei na mazao mbalimbali? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, katika swali lake la (a) amezungumzia kwamba kituo hiki kimechukua miaka nane; na mimi ni kweli ninakiri kwamba kituo hiki kimechukua miaka nane. Hata hivyo kwenye majibu yangu ya msingi nilishaeleza kwamba kituo hiki kilikabidhiwa kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe.
Mheshimiwa Spika, sisi kama Wizara; na kwa sababu masomo yanayofundishwa pale yanahusiana na kilimo; ningependa niwasiliane na Mheshimiwa Mbunge ili tuweze kuangalia ni taratibu gani ambazo zinatakiwa kufuatwa, na ikiwezekana kwenye bajeti ya msimu wa fedha ujao basi tuweze kukiingiza. Vilevile niko radhi kwenda kutembelea kituo hiki ili niweze kujithibitishia kitu amcaho kiko mahali pale.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la (b) Mheshimiwa Mbunge amzungumzia kwamba kuna wataalam wengi ambao wanasoma katika vyo vyetu hivi vya mafunzo. Ni kweli na mimi naomba niendelee kusisitiza na kwamba sisi kama Wizara tunasisitiza sana kuwa na uzalishaji wa tija. Kwa hiyo nini kifanyike sasa? Ni kwamba tunaendelea kuwahamasisha wakulima wote kujiunga katika vikundi vya SACCOS kwa sabbau wataendelea kupata mikopo ambayo itakuwa na riba nafuu na vile vile waweze kujiajiri wenyewe binafsi. Ahsante
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mbunge wa Rungwe Mheshimiwa Saul Henry Amon, Mji wa Tukuyu ni miongoni mwa miji mikongwe katika nchi hii hata utaitwa Tokyo. Lakini mradi wa Masoko aliousema Mheshimiwa Naibu Waziri una changamoto nyingi na hadi umepelekea Mkandarasi wa mara ya kwanza walipelekeana Mahakamani pamoja na Halmashauri na hata sasa amepatikana Mkandarasi mwingine, lakini Mkandarasi huyu wa pili bado naye hajalipwa fedha zake na wanakoelekea inawezekana ikawa kama Mkandarasi wa kwanza. Je, Serikali inatoa kauli gani ili akinamama ambao wanatoka mabondeni na maeneo mengine mbalimbali tuwatue ndoo kichwani ili huyu Mkandarasi aweze kulipwa fedha zake.
Swali la pili, Mji wa Tukuyu una milima, mabonde pamoja na mlima Rungwe, tuna maji ya kutosha. Hatuna sababu yoyote Serikali kutopeleka maji kule kwa sababu hata maji ya gravity tu yanatosha kwa ajili ya wananchi waweze kupata maji. Serikali inatoa kauli gani ili wananchi wa eneo hilo waweze kupata maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nirejee, siku ya Jumatatu nilikuwa Rungwe, miongoni mwa mambo ambayo tulijadili na Mwenyekiti wa Halmashauri, DC na Kaimu Mkurugenzi ni suala zima la mradi huu wa maji mkubwa ambao katika njia moja au nyingine ukiweza kukamilika utasaidia watu wa Mji wa Tukuyu kupata maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wanaotumia pale Tukuyu ni mradi ambao ulibuniwa miaka ya nyuma, wakati huo population ilikuwa ndogo sana, lakini sasa hivi idadi imekuwa kubwa sana, ndiyo maana katika kurudi kwangu hapa tulichokubaliana ni kwamba nitawasiliana na wenzetu wa Wizara ya Maji ili kuangalia tutafanya jinsi gani kwa sababu changamoto kubwa ya mradi wa Masoko ni suala zima la fedha. Hata Mheshimiwa Atupele aliposema kwamba Mkandarasi wa kwanza alikoma na wa pili hivi sasa, ni kweli!
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi hata kazi pale site imesimama changamoto kubwa sana ni fedha, ndiyo maana siku zote tunasikilizana humu katika Bunge letu, katika kipindi cha sasa Serikali inaona miradi mingi ya maji ambayo mwanzo ilikuwa imesimama, sasa inatekelezeka kwa sababu kwamba nguvu kubwa ya Serikali imewekwa katika ukusanyaji wa mapato. Imani yangu kubwa baada ya hii nitampa reference nilichokipata kule juzi, Waziri wa Maji, tutaangalia kwa pamoja jinsi gani tutafanya mpango mkakati mpana kuhakikisha watu wa Tukuyu ule mradi unakamilika, ili kutoa ile kadhia kwa akinamama katika Mji wa Tukuyu.
Mheshimiwa Naibu Spika, agenda ya pili ni kweli. Tukuyu nilipopita juzi nimeona maeneo mengi sana kuna maji ya chemichemi, lakini katika mipango ya Serikali hapa na Wizara ya Maji ilizungumza katika Bajeti yake kwamba tutajielekeza katika vile vyanzo rafiki vilivyopo kuhakikisha kwamba vyanzo vilivyopo vinatumika vizuri. Imani yangu kwa sababu Mji wa Tukuyu ni takribani miezi miwili tu wanakosa mvua, tutatumia vyanzo hivi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutashauriana na Serikali yetu kwa ujumla, TAMISEMI na Wizara ya Maji, lengo kubwa ni kwamba Mji na Wilaya kongwe ile ya Rungwe uweze kunufaika na suala zima la maji na vilevile katika Jimbo la Busokelo ambako ndugu yangu Mheshimiwa Fredy Atupele anapatikana kule.
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa niulize swali moja la nyongeza. Ugonjwa wa UKIMWI siyo tishio kwa maana ya kuua, tishio kubwa ni magonjwa nyemelezi. Kwa bahati mbaya Serikali imekuwa ikinunua dawa hasa hasa kwa ajili ya kufumbaza Virusi vya UKIMWI aina ya TLA (Tenofovir, Lamivudine na Efavirenz). Je, ni lini Serikali itaanza kununua dawa kwa ajili ya magonjwa nyemelezi (Opportunistic Infections -OI drugs) hasa hasa Azithromycin, Fluconazole na Co- trimoxazole?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inanunua dawa za Opportunistic Infections lakini siyo kwa kiwango ambacho tunanunua dawa hizi za UKIMWI za moja kwa moja kama hizo anazosema Mheshimiwa Mbunge za Tenofovir, Lamivudine, Zidovudine, Efavirenz na nyinginezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na upungufu tulionao sasa hivi tunaboresha kwa ujumla wake mfumo wa kutoa dawa nchini. Kwa hivyo, kadri mfumo wa dawa utakavyoboreka, dawa za kutibu magonjwa nyemelezi pia na zenyewe zitaongezeka kuwepo katika vituo vyetu. Kwa hivyo, ni lini, ni kadri tunavyoendelea kuboresha ndivyo ambavyo tutaendelea kuwa na dawa hizi kwenye vituo vyetu.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante, wananchi wa Busekelo kwa kushirikiana na mimi nikiwa Mbunge wao tumeamua kulima barabara inayounganisha Mkoa wa Njombe na Mkoa Mbeya kwa kutumia zana za jembe la mkono.
Je, ni lini Serikali itatupa support ili tuweze kukamilisha barabara hii ambayo ni muhimu sana kwa wananchi wa Busekelo na Makete na ukizingatia kwamba…
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru sana kwa jinsi anavyopigania wananchi wa jimbo la Busokelo katika kuhakikisha kwamba wanapata huduma nzuri za barabara. Ni kweli nakiri kwamba nilimwona juzi kwenye vyombo vya habari akihamasisha na kufanya kazi sambamba na wananchi kuhakikisha kwamba barabara inapitika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli barabara hii imo kwenye Ilani, Serikali inalitambua na tumeona jitihada za Mbunge na kwenye bajeti yetu ya mwaka huu imesomeka kwenye hatua za upembuzi yakinifu na details design. Kwa hiyo, tutalishughulia.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kabla sijauliza maswali yangu mawili ya nyongeza nataka niweke kumbukumbu sahihi kwamba mimi ni Mbunge wa Busokelo ambayo iko ndani ya Wilaya ya Rungwe.
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba kuna sera, kuna miongozo kuna vitengo mbalimbali vya kufuatilia forensic wizi wa mitandaoni, lakini bado wizi unaendelea; Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kuwatumia wataalam wetu wa ndani kushirikiana na nchi ambazo zimefanikiwa kutatua tatizo hili la wizi wa mtandaoni ikiwemo Israel ama India?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, sekta ya mawasiliano inachangia asilimia 13 ya pato la Taifa. Kwa msingi huo sekta hii ni muhimu sana, lakini Serikali bado haijaanzisha Bodi ya TEHAMA. Nchi ambazo zimefanikiwa katika TEHAMA kwa mfano Finland wamefanikiwa kugundua Nokia ukienda Korea Kusini kuna Samsung, ukienda Marekani akina Job Steve - Apple na Mataifa mengine mbalimbali. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuanzisha hii Bodi ya TEHAMA ili professionals ambao wamesoma hii TEHAMA waweze kutambulikana na kuongeza Pato la Taifa zaidi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Spika, ahsante. Ni kweli kwamba wizi au uhalifu wa kimatandao bado unaendelea na kwa msingi huo Serikali tumejipanga kwamba tutawashirikisha wataalam wetu wa ndani.
Mheshimiwa Spika, naomba pia nitambue kwamba Mheshimiwa Mwakibete ni mtaalam sana wa mambo ya ICT na TEHAMA ambaye amefanya kazi maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi na hasa nchi za Ulaya ili kutengeneza software au programs ambazo zinaweza kupunguza au kumaliza kabisa tatizo hili.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwa-support wataalam wetu kwenda kujifunza nje ya nchi kwa nchi ambazo zimefanikiwa tatua tatizo hili, nchi kama Israel, India na Marekani. Tutambue tu kwamba uhalifu wa mtandao ni kitu ambacho kipo dunia nzima na jinsia ambavyo siku zinakwenda watu wanagundua njia mpya na Serikali tunawa-support wananchi na wataalam mbalimbali kuhakikisha kwamba wanatafuta programs za kuzuia uhalifu huo.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ni kweli kwamba kumekuwa na utitiri wa watu wengi sana wanaojifanya kwamba ni wataalam wa TEHAMA na kwa sasa kuna umuhimu kama Serikali wa kuunda bodi ya kusimamia wataalam wa TEHAMA.
Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo kupitia Kamisheni ya TEHAMA ambayo ilitangwazwa na Mheshimiwa Rais mwaka 2015 tunaamini ndani yake tutaunda Bodi ambayo itawatambua wataalam wa TEHAMA kwa elimu zao, lakini tutahakikisha vilevile wanafanya mitihani ili kuwa competitive katika masuala mazima ya TEHAMA kama ilivyo Bodi ya Uhasibu NBAA au Bodi ya Wahandisi ya ERB.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa niweze kuuliza swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa Mkoa wa Mbeya una vivutio vya asili kama ulivyo Mkoa wa Iringa na vivutio hivyo vya asili ni kama Mlima Rungwe, Mlima Kejo, Ziwa Nyasa na maeneo mengine kama Maziwa ya Masoko, Kingururu, Iramba pamoja na Daraja la Mungu.
Je, Serikali ina mpango gani kuvitangaza vivutio hivi ili wananchi wanaoishi maeneo hayo waone umuhimu wa uwepo wa vivutio hivyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kweli kabisa Mkoa wa Mbeya una vivutio vingi sana kama ulivyo Mkoa wa Iringa na kama ilivyo mikoa mingi. Hivi sasa kama nilivyosema, tunayo mikakati kabambe ya kuhakikisha kwamba vivutio vyote nchi nzima vinatangazwa. Nimesema tutaanzisha studio ya kutangaza na tutaanzisha channel ya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika mikakati hii, maeneo yote yenye vivutio vya utalii Mkoa wa Mbeya nayo yataingizwa katika huo mpango kabambe wa kutangaza ili kusudi watalii mbalimbali waweze kujua Tanzania na Mkoa wa Mbeya kuna nini? Nina uhakika Mheshimiwa Mbunge atafaidika sana hasa baada ya kuanza kutangaza maeneo haya. (Makofi)
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ili niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Mkoa wa Mbeya ni mkoa wa pili kwa wananchi wake kuwa na pato la Taifa ukitanguliwa na Mkoa wa Dar es Salaam, lakini miundombinu yake si rafiki kwa wananchi wake. Je, ni lini Serikali itatengeneza barabara iliyoahidi kutoka mchepuo wa Uyole kwenda Mbalizi pamoja na barabara kutoka Katumba, Ruangwa, Masoko mpaka Mbambo na Tukuyu yenye kilometa 83? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu barabara hii amekuwa akiizungumza kweli. Tumezungumza naye hapa ndani ya Bunge, tumezungumza naye nje ya Bunge na hata wakati akitoa mchango wake wakati wa Wizara hii tulivyowasilisha bajeti aliizungumza barabara hii, hata akasema kama hatutengenezi basi yuko tayari kutupeleka shambani tukashirikiane naye kulima, nami nilikuwa tayari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, niwapongeze pia wananchi wa Busokelo kwamba wamepata mwakilishi mzuri kwa sababu anashughulikia sana mipango na mambo mbalimbali kuhakikisha wananchi wake wananufaika na rasilimali za nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu barabara hii ya Katumba – Suma – Ruangwa – Mbambo kuja Tukuyu ni kati ya barabara ambazo pia tumezitengea fedha. Natambua kwamba mwaka 2017/2018 pia tulitenga fedha na mwaka huu tumetenga fedha. Niseme tu kwamba ukiangalia kwenye kitabu cha bajeti huu mradi namba 4150, tumetenga bilioni 17 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hii. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mwakibete na kwamba barabara hii tunakwenda kuijenga, muda sio mrefu harakati za ujenzi zitakuwa zimeanza, fedha zipo na nalishukuru Bunge kwa kutenga fedha hizi kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa nami niweze kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme unaotokana na joto ardhi ama geothermal ni endelevu na sustainable ama renewable na Serikali ingeweza kutumia vyanzo vyote tungepata zaidi ya Megawati 5,000. Je, ni lini Serikali itaweza kukamilisha mradi wake ambao ilikuwa inaendelea kuufanya wa kuchoronga visima katika Ziwa Ngosi lililopo Wilayani Rungwe pamoja na Mto Mbaka uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa swali zuri. Kusema ukweli kati ya maeneo ambayo tunayafanyia upembuzi yakinifu kwa ajili ya kujua mashapo ya geothermal, yako zaidi ya 50. Tunachofanya sasa hivi, tunapitia marejeo ya takwimu sahihi katika Ziwa Ngosi ambao liko Mbozi, maeneo ya Katavi pamoja na Rukwa. Tathmini za awali zinaonesha kwamba mashapo yaliyopo ya geothermal yanaweza kutupa jumla ya Megawati 5,000 kwa wakati mmoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa tunakwenda hatua kwa hatua, tunataka kuanza Megawati 20 hadi Megawati 100. Kwa hiyo, ni matarajio yetu kwamba ndani ya miaka hii miwili tutakuwa tumeshapata mashapo sahihi ili tuanze sasa na Megawati 100 kwa ajili ya geothermal.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali kuhusiana na swali hili, hasa hasa ujenzi wa Kiwanda cha Maziwa kule Isange, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, wananchi wa Jimbo la Busokelo hasa Kata za Lupata, Kandete, Luteba, Mpombo, Isange, Lwanga, Kabula pamoja na Itete, wanafuga sana ng’ombe wa maziwa wapatao zaidi ya 35,000 na wanazalisha lita zaidi ya milioni 54 kwa mwaka lakini mbegu walizonazo bado ni ng’ombe wale wa zamani. Je, Serikali itawasaidiaje kupata ng’ombe wapya ambapo inaweza kufanyika kitu kinaitwa uhimilishaji kwa ajili ya uzalishaji zaidi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wananchi hawa pamoja na ufugaji wao wanajitahidi sana kukusanya maziwa na kupeleka sehemu ambapo kuna matenki kwa njia ya baiskeli pamoja na pikipiki. Je, Serikali itawasaidiaje kutafuta ama kupata gari la kisasa lenye tenki ili liwasaidie kwa ajili ya kukusanya kwa wakulima na wafugaji ambao wanafuga ng’ombe hawa wa maziwa mpaka sehemu ya viwanda?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwakibete, Mbunge wa Busokelo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajibu swali hili, naomba kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mwakibete kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya ya kuhakikisha kwamba wapiga kura wake wa pale Busokelo Rungwe wanafanya kazi ya uzalishaji na kujenga nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ameniuliza juu ya programu tuliyonayo kama Serikali ya kuhakikisha kwamba tunasaidia katika kuondoa kosaafu zile za kizamani na kuboresha kosaafu zetu mpya. Wizara yetu katika mpango mkakati wa mwaka 2018/2019, tumejipanga kuhakikisha tunazalisha ndama wa kosaafu hizi za kisasa wasiopungua milioni moja kwa kutumia njia ya uhimilishaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndama hawa milioni moja watakaozalishwa watatawanywa katika halmashauri zetu kwa ajili ya kuendeleza kosaafu mpya hizi zenye tija na thamani zaidi kwa uzalishaji wa maziwa na nyama. Moja katika halmashauri zitakazonufaika na mpango huu ni pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, ni namna gani tunaweza tukawasaidia wazalishaji wa maziwa kule Busokelo. Naomba nichukue fursa hii kuwapongeza sana wadau binafsi wanaoshirikiana vyema na Serikali na nampongeza pia Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri hiyo anayoifanya kuwashirikisha wadau hawa binafsi. Wadau wetu wa ASAS DAIRIES wanafanya kazi nzuri sana ya kuwaunganisha wazalishaji wa maziwa katika eneo hili la Busokelo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kwamba wamepeleka vyombo vya usafiri kama pikipiki kwa ajili ya kukusanyia maziwa. Nafahamu pia ya kwamba wadau hawa wanayo malalamiko madogo madogo, sisi kama Wizara kwa kupitia Bodi yetu ya Maziwa tunafahamu malalamiko yao, tayari tunayafanyia kazi katika kuleta utengamanisho ili wazalishaji wetu waendelee kunufaika. Tunawashawishi sasa ASAS DIARIES badala ya kutumia pikipiki zile, waingize magari yenye cold storage waende kukusanyia maziwa ya wananchi wale ili wananchi waweze kupata faida zaidi ya uzalishaji wao wa maziwa haya.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa niweze kuuliza swali moja la nyongeza.
Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kuweza kupata nafasi ya kuja katika Jimbo langu la Busokelo, lakini nina swali moja tu kwamba ulivyokuja wana Busokelo tulikuomba kwamba vijiji vyote ambavyo vipo kwenye scope ya REA III na kwa bahati mbaya sana hivi vijiji baadhi yao vina nyumba za nyasi lakini hii leo ninavyouliza swali kwako Mheshimiwa Waziri ni kwamba vile vijiji vimerukwa. Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya Vijiji 8 ambavyo vimerukwa kwenye scope ambayo ipo sasa kwa REA III? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Atupele, tulifanya ziara pamoja katika Jimbo lake na kwa kweli katika Jimbo la Busokelo vijiji takribani 50 vipo katika REA hii ya Awamu ya Tatu na mkandarasi Stag International tulimwelekeza afanye tathmini katika maeneo yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hyo, naomba nimthibitishie vile vijiji nane ambavyo vipo kati ya vijiji 50 ambavyo vitapatiwa umeme katika REA awamu hii mzunguko wa kwanza tunamwelekeza mkandarasi vyote avifanyie tathmini na kwa kuwa Serikali imeelekeza nyumba yoyote iwe ya tembe au kawaida zote zinapatiwa umeme na tumeshuhudia mara kadhaa tukizindua umeme na nyumba hizi ambazo zimewekewa umeme. Kwa hiyo, nataka niseme hakuna nyumba mbayo itabaguliwa na mkandarasi atavifikia vile vijiji vinane, asante sana. (Makofi)
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, napenda kuweka kumbukumbu sahihi kwamba mimi ni Mbunge wa Jimbo la Busokelo na si Rungwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Halmashauri ya Busokelo ina utajiri mkubwa sana wa madini aina ya marble pamoja na carbondioxide gas. Serikali imekiri hapa kwamba madini ya marble yanapatikana katika Kijiji cha Kipangamansi, Kata ya Lufilyo. Je, ni lini Serikali itakuja kufanya tafiti katika milima ya safu za Livingstone kwani inasadikika pia kuwa kuna madini aina ya dhahabu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Waziri tumekuwa tukiongea mara nyingi kwamba atutembelee Halmashauri ya Jimbo la Busokelo ili apate kushuhudia wananchi wangu wanaojishughulisha na hizo shughuli za marble. Ni lini Waziri atakuja kuwatembelea wananchi wa Jimbo langu na kuona shughuli hizo za madini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwakibete, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajibu namuomba radhi kidogo Mheshimiwa Mbunge kwa kukosea kutaja jina lake. Nieleze tu kwamba Mheshimiwa Mwakibete ni miongoni mwa Wabunge ambao kwa kweli katika kufuatilia masuala ya madini kwenye Jimbo lake amekuwa mstari wa mbele. Kama alivyoeleza hapa, mara nyingi amekuwa akitualika Wizara twende kwenye Jimbo lake na mara ya mwisho tulizungumza tukakubaliana tutakwenda. Nataka nimuhakikishie kwamba tutakwenda mara baada ya kukamilisha Bunge la Bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni lini tutafanya utafiti kwenye Milima ya Livingstone, naomba nimjulishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Taasisi yetu ya GST inaendelea kufanya tafiti mbalimbali kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini ili kubaini maeneo yenye madini ikiwemo eneo la Busokelo na Lufilyo kama alivyoomba.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na nimpongeze pia Waziri mwenye dhamana kwa namna ambavyo waliweza kutembelea Jimbo langu la Busokelo na kufanya mikutano mingi na wananchi wale.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa mradi huu umechukua muda mrefu, ni zaidi ya miaka 21 sasa tangu upembuzi yakinifu ufanyike, je, Serikali haioni umuhimu wa kuharakisha mradi huu ili ifikapo 2022 uweze kukamilika badala ya mwaka ambao Mheshimiwa Waziri ameusema?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa umeme wa jotoardhi ni umeme endelevu kwa maana ya renewable na tumeona katika nchi yetu na tafiti zimeonyesha tunaweza kupata megawatts zaidi ya 5,000 kwa vyanzo vyote ambavyo vimeainishwa kwa nchi nzima ya Tanzania. Je, Serikali ina mpango gani wa kuviendeleza vyanzo hivyo ili Tanzania ifikapo 2025 iwe ni nchi ya uchumi wa kati?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake ya awali ambayo ametoa ufafanuzi mzuri sana katika mradi wa kuzalisha umeme wa jotoardhi. Sambamba na shukrani kwa Naibu Waziri wangu, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge Mwakibete kwa anavyofuatilia masuala ya rasilimali ya jotoardhi katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, katika maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwakibete, la kwanza amesema imechukua muda mrefu kufanya utafiti kwa takribani miaka 21. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge lakini niwape taarifa Watanzania kwamba katika hatua za utekelezaji wa upembuzi yakinifu, mradi ambao umeenda kwa kasi katika miradi ya jotoardhi ni pamoja na mradi huu wa Ngozi ambao utatuzalishia MW 20.

Mheshimiwa Spika, kwa kawaida miradi ya jotoardhi, upembuzi yakinifu huchukua takribani miaka 25 - 40. Kwa hatua hii, ndiyo maana tunasema tumekwenda kwa kasi na tuna matumaini ya kukamilisha mapema mwaka uliotajwa wa 2023 tutapata MW 30.

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili, nchi yetu ina rasilimali nyingi sana na madini ya jotoardhi (geothermal) kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge. Rasilimali tuliyonayo inaweza kutuzalishia megawatt zaidi ya 5,000, ingawa kwa sasa tathmini zinavyoonyesha tunaweza tukaanza kuzalisha MW 200 kwa kuanzia ifikapo miaka mitano ijayo. Tutaanza na MW 30 ambayo itatoka kwenye eneo la Ngozi kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Spika, lakini nieleze tu kidogo, niwapongeze sana wananchi wa Mbozi na wananchi wengine wa maeneo yanayozunguka mradi huu kwa sababu wametupa ushirikiano mkubwa wa kufanya tathmini. Hivi sasa tunaendelea na kufanya tathmini ya maeneo mengine mengi nchini ikiwemo eneo la Majimoto kule Katavi ambayo nayo itatuzalishia megawatt za uhakika. Kwenye mradi wetu tutapata MW 5,000 miaka kumi au ishirini ijayo lakini itakuwa ni umeme wa uhakika ambao uta-stabilize sana upatikanaji wa umeme hapa nchini. Ahsanteni sana.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwanza nisikitike kwa niaba ya wananchi wa Busokelo kwa sababu barabara hii aliitembelea aliyekuwa Naibu Waziri wa Ujenzi kipindi hicho, Mheshimiwa Eng. Ngonyani tangu tarehe 21 Novemba, 2016 na aliahidi kwamba ingetengenezwa kwa kiwango cha changarawe kilometa 7.5. Hili swali nimeliuliza Bungeni zaidi ya mara tatu na kila jibu linalokuja linakuwa tofauti na jibu lililotangulia. Wananchi wa Busokelo wanataka kujua ni lini Serikali itaunga mkono juhudi za wananchi wa Jimbo la Busekelo, Kata ya Luteba ambao wameanza kutengeneza barabara hii kwa kilometa 4 wao wenyewe kwa jembe la mkono pamoja na Mbunge wao?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa barabara hii imeanzishwa na nguvu za wananchi na kwa maana hiyo Serikali haitambui kama iko TARURA, TANROADS ama kwenye vijiji. Ni lini sasa Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari kuunganisha nguvu za pamoja za TANROADS na TARURA ili tujue ni nani atakayehusika na barabara hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Fredy Atupele Mwakibete, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza, uniruhusu nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu tumezungumza sana juu ya barabara hii na mimi kipande hiki cha barabara nilikitembelea eneo hili kweli lina changamoto kubwa. Barabara hii kimsingi inasimamiwa na wenzetu upande wa TARURA na sisi kwa maelekezo ya aliyekuwa Naibu Waziri wakati ule ni kwamba TANROADS twende tusaidie kutambua mahitaji na namna nzuri ya kuiboresha barabara hii, kazi ilifanyika na mawasiliano yalikuwa yanaendelea ya kupata fedha. Nitumie nafasi hii kuwaelekeza wenzetu wa Mfuko wa Barabara wafanye haraka kwa maana ya kuitoboa barabara hii ili ianze kutumiwa na wananchi na mimi nitaifuatilia ili kuhakikisha tunaitoboa barabara hii.

Mheshimiwa Spika, lakini tunasanifu barabara hii ambayo nimeitaja kutoka Isyonje – Kikondo - Makete na hiki kipande cha kilometa 7.5 kinatoka eneo la Busokelo kinaunga kwenye barabara hii ambayo itasanifiwa. Labda nielekeze pia wakati wa usanifu tuiangalie barabara hii kwa sababu kwenye milima hii ni hatari sana, kama itawezekana tuifanye kuwa spur ya barabara hii ambayo tutakuwa tukiisanifu. Kwa hiyo, wakati wa usanifu wa kilometa 7.5 tuiweke ili siku za usoni barabara hii iwe bora na iendelee kuwasaidia wananchi wa maeneo haya.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nipongeze Serikali kwa juhudi pekee ya kuinua bei ya zao la chai kutoka 241 kwa kilo ya majani mabichi chai mpaka kufikia 315, na nimpongeze kipekee Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mheshimiwa Rais kwa kutembelea Jimbo hili la Busokelo na concern yetu ya zao la chai tuliwaambia na kuunda Tume kwa ajili ya kushughulikia tatizo hili.

Mheshimiwa Spika, Bonde la Mwakaleli tuna Kiwanda cha Chai ambacho kimekuwa kikizalisha chai lakini kwa msimu, kuanzia mwezi wa Disemba mpaka Juni kila mwaka na hivyo miezi Sita mingine huwa hakifanyi kazi; Je, Serikali ina mpango gani mkakati wa kukifanya kiwanda hiki cha chai cha Bonde la Mwakaleli kiweze kufanya kazi mwaka mzima badala ya sasa tunaki- underutilize. (Makofi)

Swali la pili, hivi sasa katika Jimbo langu la Busokelo tunalima viazi mviringo na ni wakati wa msimu wa mavuno lakini bei yake ipo chini sana, kiasi kwamba hata wanunuzi wa viazi hivi wanawaibia zaidi wakulima wana-collude kwa kushirikiana na yale makampuni yanayotengeneza mifuko kwa kufanya kitu kinachoitwa lumbesa. Kwa mfano, mfuko mmoja ambao una debe tano wao wanafanya debe sita na nusu na wananchi hawa wanakuwa wamekopa wamenunua pembejeo, wamelima kwa shida, lakini bei zao ziko chini na kiasi hiki kinafanya mkulima akate tamaa kabisa kuendelea kulima zao hili la viazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, je, Serikali inatoa tamko gani wewe ukiwa Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara kuja site ili uone namna mateso ya wananchi wangu wa Bonde la Mwakaleli, Busokelo pamoja na Wilaya nzima ya Rungwe hadi Uyole - Mbeya kwamba wanahitaji masoko ya uhakika katika zao hili la viazi. (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwakibete Mbunge wa Busekelo kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mwakibete kwa pongezi kwa Serikali kuongezeka kwa bei ya chai kutoka shilingi 241mpaka shilingi 315 lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Mwakibete kwa kweli anawapambania wananchi wa Busekelo tunakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza la Mheshimiwa Fredy Mwakibete Mbunge wa Busekelo ni kuhusu Kiwanda cha Chai kuzalisha miezi Sita peke yake na yeye angetamani pamoja na wananchi wa Busekelo kuona kiwanda hiki kinazalisha kwa mwaka.

Mheshimiwa Spika, kama alivyoomba nitatenga muda niweze kwenda nae Jimboni Busekelo tutembelee Kiwanda hiko tuangalie changamoto zilizopo na kuona ni nini Serikali inahitaji kufanya na upande wa Mwekezaji wanahitaji kufanya nini ili kuhakikisha kiwanda hiki kinazalisha kwa mwaka mzima.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Mwakibete angependa kuujua nini mkakati wa Serikali kuhakikisha wananchi wake wa Busekelo tunawapatia soko la uhakika la viazi mviringo.

Mheshimiwa Spika, katika ziara ambayo nitaifanya tutahakikisha tunatoka na mkakati wa kuwapatia masoko ya uhakika wa viazi mviringo tunaujadili na pale inapowezekana tutawaunganisha wakulima hawa kwenye masoko ya viazi mviringo. Suala la lumbesa, halitasubiri ziara Mheshimiwa Mbunge baada ya maswali tutakaa pamoja tuangalie namna ya kushughulikia jambo hili, haliwezi kusubiri ziara, tutafuta namna ya kuliratibu vizuri ili wananchi wako wasiendelee kupunjwa kupitia mfumo wa lumbesa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru. (Makofi)
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Pamoja na juhudi nzuri za Serikali zilizofanywa pamoja na Kampuni hii ya Tanzania Oxygen Limited kuweza kuzuia baadhi ya wanyama watambaao pamoja na binadamu kwenda kwenye eneo hili la kisima ambacho mara nyingi miaka ya nyuma Wananchi na wanyama wengine walikufa kutokana na kuvuta gesi hii ya carbondioxide. Swali la kwanza; je, ni lini Serikali itaendelea kutoa elimu kwa wananchi ambao wanazunguka kisima hiki na kwa kuwa nguvu za asili za volcano bado zipo na volcano nii ni hai ili kuzuia madhara yatokanayo na kuvuta gesi hii ya carbondioxide?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa Serikali imeonesha nia njema kwa ajili ya kujenga viwanda hapa nchini lakini kumekuwa kuna changamoto kubwa kuingiza gesi hii ya carbondioxide ndani ya Nchi yetu ya Tanzania tukitambua kwamba carbondioxide gas inatumika katika mazingira ama kwenye vitu vingi ikiwemo vyakula pamoja na vinywaji ili visiharibike. Ni kwa kiwango gani Serikali itavutia zaidi wawekezaji kwenye maeneo mengine ambayo gesi hii ya carbondioxide bado haijaanza kuchimbwa.
WAZIRI NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri katika majibu ya msingi ya suala la Mheshimiwa Mwakibete, lakini vilevile nimpongeze sana Mheshimiwa Mwakibete kwa kufuatilia masuala haya ya matumizi ya carbondioxide.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwanza ni lini Serikali itaendelea kutoa elimu; Kampuni ya Tanzania Oxygen kwanza imetenga takribani dola milioni tano kila mwaka kawa ajili ya kutoa elimu katika maeneo yao ya leseni. Kwa hiyo shughuli za kutoa elimu zinaendelea, lakini sambamba na hilo Serikali kwa kushirikiana na Tanzania oxygen zimeweka timu mahususi kwa ajili ya mpangokazi wa kutoa elimu kila mwezi katika maeneo hayo. Kwa hiyo shughuli za utoaji wa elimu ni endelevu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala la pili la kulinda soko la ndani; ni kweli, kwanza kuna nchi ambazo zinzalisha carbondioxide kama Tanzania, mathalani; DRC, Kenya na Nchi ya Msumbiji. Kwa Tanzania tunachofanya kwa sasa tumeunda timu mahususi kwa ajili ya kufanya tathmini ili kuangalia mahitaji ya ndani na uwezo tulionao ndani ya miezi mitatu, tukishajiridhisha kwamba uwezo wa ndani wa carbondioxide unatosha kuzalisha vinywaji kama soda pamoja na vinywaji vya bia, tutazuia kabisa carbondioxide kutoka nje badala yake tutumie viwanda vya ndani.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa niulize swali moja la nyongeza. Matatizo ya Korogwe Mjini yanafanana sana na matatizo ya Wilaya ya Rungwe hususan Busokelo kwa kukatika katika umeme. Kwa siku umeme unaweza kukatika zaidi ya mara 10 na tatizo kubwa lililokuwepo ni kwamba, nguzo za umeme chini yake kuna miti.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru Wizara pamoja na Waziri kwa maana ya kuleta timu maalum kwenda ku-clear ama kukata hiyo miti, lakini bado tatizo kubwa limeendelea kuwepo. Ni mikakati gani Serikali iko nayo kuhakikisha kwamba wananchi wa Jimbo la Busokelo wanapata umeme masaa 24 kwa siku kuliko hivi ilivyo kwa sasa? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri katika swali la msingi, lakini hata la nyongeza kwa Mheshimiwa Chatanda; na niendelee kumpongeza Mheshimiwa Mwakibete kwa swali linalofafana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Shirika letu la umeme nchini na kwa niaba ya Serikali, napenda tu nisema mambo mawili kwamba ukarabati unaoendelea. Jambo la kwanza tumetenga kila Mkoa wa ki-TANESCO kwa nchi nzima takriban shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya kufanya ukarabati mkubwa.

Kwa hiyo, wananchi katika maeneo yote ya mikoa yetu ambayo kuna kero ya kukatika kwa umeme, kwanza haukatiki kwa sababu ya hali ya umeme, isipokuwa tunakata kufanya matengenezo. Kwa hiyo, naomba nitoe taarifa hiyo kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, tumetoa muda mahususi wa miezi sita kukamilisha ukarabati wote kwa nchi nzima. Kwa hiyo, ni matumaini yetu Mheshimiwa Mwakibete katika eneo lake ambalo lilikuwa na kero kubwa sana ndani ya miezi sita ukarabati utakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, tumeleta transforma kubwa, tunabadilisha transformer kutoka ndogo kwenda kubwa, kwa sababu shughuli za uchumi za wananchi zinaongezeka. Kwa hiyo, tunaomba radhi kwa wananchi wote ambako ukarabati unaendelea. Tunaomba mtuvumilie tukamilishe kazi hiyo. Ahsante sana.
MHE. FRED A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa fursa niweze kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Wilaya ya Rungwe ni miongoni mwa wilaya ambazo zina maji mengi ya kutosha na vyanzo vingi lakini wananchi wetu hawana maji ya kutosha. Je, ni lini Serikali itakamilisha miradi ambayo imeanzisha ya maji hususan miradi ya Mwakaleli I pamoja na miradi ya masoko na Kandete pamoja na Kata za Rwangwa. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, kiukweli amekuwa mfuatiliaji hata wewe Naibu Spika, masuala ya masoko na maeneo mengine umekuwa mfuatiliaji na kutuulizwa maswali mara kwa mara.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Wizara Mheshimiwa Waziri alinituma, nimekwenda lakini pia Waziri mwenyewe amekwenda na tukawa na kikao cha pamoja na Mheshimiwa Mbunge na sasa hivi kuna kazi ambayo inaendelea kule Masoko. Nataka tumhakikishie sisi kama viongozi tutakuwa wafuatiliaji katika kuhakikisha miradi ile inakamilika kwa wakati na wananchi wake waweze kupata huduma hii muhimu ya maji. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa niulize swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto zilizopo Same Magharibi zinafanana sana na changamoto zilizopo Jimbo la Busokelo. Kata ya Ntaba tuna Daraja ambalo linaitwa Mto Ngubwisya, liliondolewa na maji tangu tarehe 30 Aprili, 2019 na daraja hili linaunganisha Kata za Kisegese, Itete, Kambasegera pamoja na Luangwa.

Je, ni lini Serikali inakwenda kujenga daraja hili ili wananchi wangu wa Busokelo waunganishwe kama ilivyokuwa zamani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Fredy Makibete, Mbunge wa Busokelo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba daraja hilo muhimu ambalo linaunganisha kata na vijiji mbalimbali katika Jimbo la Busokelo lilivunjwa na maji mwaka 2019. Serikali inatambua sana umuhimu wa kwenda kulifanyia tathmini na usanifu daraja hilo ili liweze kutengewa fedha kadri ya upatikanaji wa fedha na kuweza kujengwa ili liweze kurejesha huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kushirikiana na Halmashauri ya Busokelo na Mheshimiwa Mbunge ili kuweza kuona namna gani usanifu unafanyika na fedha zinatafutwa na kujenga daraja hilo kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Serikali nataka kufahamu ni hatua gani za kinidhamu zinazoweza kuchukuliwa na Serikali kwa wataalam wetu wanaosababisha variation ya miradi kuwa na gharama kubwa, kwa mfano, daraja hili la Mbaka ambalo limechukua muda mrefu sana. Kuna kitu tunaita geotechnical investigation hakikufanyika na ndiyo maana imechukua muda mrefu zaidi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa daraja hili litakapokamilika kutakuwa kuna madaraja mawili, kutakuwa kuna daraja hili ambalo linajengwa pamoja na lililokuwepo la chuma.

Je, Serikali ipo tayari kulichukua hili daraja la chuma kupeleka katika mto huo huo Mbaka lakini kwa kuweza kuunganisha kati ya Majimbo ya Busokelo, Kyela pamoja na Rungwe katika Kijiji cha Nsanga? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Atupele Mwakibete, Mbunge wa Busokelo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tayari ni utaratibu wa Serikali pale ambapo mfanyakazi yeyote amefanya kinyume na utaratibu anachukuliwa hatua na kwa sababu umakini huo ndiyo maana ilionekana kwamba daraja hili lilikosewa design na ikafanyiwa redesign na tayari ujenzi unaendelea kwa hiyo ni utaratibu wa kawaida pale panapotokea tatizo hatua zinachukuliwa.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, anauliza endapo daraja la chuma lililokuwepo litakwenda kwenye daraja lingine alilolisema ni utaratibu wa Serikali kwamba madaraja haya ya chuma ni madaraja ambayo yanatumika kwa ajili hasa ya dharura. Kwa hiyo utaratibu utawekwa kama itaonekana ni muhimu liende hapo litakwenda lakini vinginevyo tunayatunza maeneo ambayo ni ya kimkakati ili kunapotokea tatizo la dharura basi hayo madaraja yatakwenda hapo. Ahsante.
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwepo na malalamiko mengi ya wanafunzi wenye sifa za kupata mikopo ya elimu ya juu lakini hawapati hiyo mikopo; na mimi ni shuhuda kwa kuwaleta wanafunzi wa jimbo langu, kwenda Bodi ya Mikopo lakini hawakuweza kufanikiwa kupata Bodi ya Mikopo, zaidi ya wanafunzi 20.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali je, serikali ni lini itahakikisha kwamba wanafunzi wenye sifa hakika wanapata mikopo badala sasa takwimu zinaonesha wanapata lakini uhalisia hawapati mikopo hiyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa wale waliofanikiwa kupata mikopo, kwa maana ya ukimaliza umeweka kanuni ama utaratibu kwamba mwanafunzi akimaliza chuo kikuu mara tu baada ya kumaliza aanze kurudisha huo mkopo na baada ya miezi 24, kwa maana ya miaka miwili, asipoanza kurudisha huo mkopo mmeweka kanuni kwamba atatozwa riba ya asilimia 10.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali, kwa wanafunzi ambao hawajapata ajira na sasa ajira ni changamoto, pengine miaka mitano, mingine kumi, wengine 20 na wengine hawapati kabisa; Serikali imejipangaje kuhakikisha kwamba wanawawezesha kwanza hao wanafunzi kuwa-link na mashirika na taasisi ili fedha zilizokopwa na wanafunzi hawa zisipotee? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwakibete kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza kwenye swali langu la msingi,, kwamba Serikali imekuwa ikitoa mikopo hii kwa walengwa na wale ambao wamefikia sifa hizo. Kwa hiyo nichukue hoja ya Mheshimiwa Mbunge; lakini Serikali inaendelea kuboresha bajeti yake ya mwaka hadi mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, mikopo yetu imepanda kutoka bilioni 427 kwa 2017/2018 mpaka shilingi bilioni 464 2020/2021; na mwaka ujao wa fedha tunatarajia kutoa mikopo hii kwa jumla ya shilingi bilioni 500. Kwa hiyo tunaamini katika kuongeza wigo huu wa bajeti tunaweza tukawafikia walengwa wengi na changamoto hii ya vijana wetu kukosa mikopo inaweza ikatatulika. Hata hivyo tunarudi palepale, kwamba vigezo vya uhitaji ansifa zeke lazima viziingatiwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hili eneo la pili la hizi asilimia; na hili naomba tulibebe kwasababu yamekuwa ni malalamiko ya wanufaika wengi na ni malalamiko ya muda mrefu, tuweze kwenda kuliangalia na kufanya review halafu tutaleta hoja hapa katika Bunge lako Tukufu kwamba namna gani tunaweza kwenda kuzishughulikia hizi tozo ambazo zimekuwa ni kero.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la hawa vijana sasa la kuwa-link kwenye taasisi na maeneo mengine ya ajira ni kwamba, jukumu la Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ni kutoa taaluma kwa vijana, sio jukumu lake kutafuta ajira kwa vijana. Sasa hili tunaomba tulibebe kama serikali tuweze kuangalia vijana wetu wanapomaliza namna gani tunaweza kuwa-link na maeneo mengine ya kuweza kupata ajira ili fedha hizi ziweze kurudishwa kwa haraka ili na wanufaika waweze kuwa wengi zaidi. Ahsante.
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa changamoto za stendi katika Jimbo la Arusha Mjini, zinafana sana na changamoto za kukosekana stendi katika Jimbo la Busokelo. Je, ni lini Serikali itajenga stendi za Miji ya Ruangwa, Ruangwa Mjini pamoja na Kandete?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Atupele Mwakibete, Mbunge wa Busokelo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali inatambua uhitaji wa masoko ya kisasa katika Kata hizo ambazo Mheshimiwa Atupele Mwakibete amezitaja, lakini pia katika maeneo mengine kote Nchini. Naomba nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge kwamba dhamira hiyo ya Serikali bado ipo na mipango ya kutafuta fedha kwa ajili ya kuwezesha ujenzi wa masoko hayo ya kisasa inaendelea. Mara fedha hizo zitakapopatikana tutahakikisha tunatoa vipaumbele katika maeneo hayo ambayo tayari yamekwishatambuliwa ili tuweze kuwekeza miradi hiyo ya kimkakati na kuwezesha huduma kuendelea. Kwa hiyo, naomba nimhakikishe Mheshimiwa Mwakibete kwamba maeneo hayo pia tutayapa kipaumbele mara fedha zikipatikana ili ujenzi wa masoko hayo uweze kuanza.
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kabla sijauliza maswali mawili ya nyongeza naomba kwanza nikushukuru sana pamoja na Serikali kwa changamoto ambazo tulizipata Jimbo la Busokelo kwa mafuriko ambayo yalisababisha nyumba zaidi ya 30 pamoja na mtu mmoja kufariki, lakini wewe pamoja na timu yako mlikuja kutoa msaada. Ahsanteni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza, pamoja na majibu ya Serikali, huu Mradi wa Mto Rumakali upo katika halmashauri mbili kati ya Halmashauri ya Busokelo pamoja na Mkoa wa Njombe, lakini mradi huu katika utekelezaji wake inaonyesha kwamba licha ya kwamba megawati hizo zitazalishwa tunahitaji kujua wananchi wa Busokelo, je, ni kwa kiwango gani kupitia Corporate Social Responsibility ya mradi huu watanufaika wananchi wa Busokelo pamoja na Kata hii ya Lufilyo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa mradi huu utaanza kuzalishwa hivi karibuni na tunafahamu kwamba Halmashauri ya Busokelo ni halmashauri changa, je, ni kwa kiwango gani Serikali imejipanga kuboresha miundombinu kufikia sehemu ya uzalishaji wa mradi huu kupitia Halmashauri ya Busokelo hususani madaraja ya Mto Lufilyo pamoja na madaraja ya Mto Malisi? Ahsante.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Atupele, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapotekeleza miradi mikubwa ya namna hii kipande cha Corporate Social Responsibility kwa maana ya manufaa ya mradi kwa umma ni kipande ambacho kinaongozwa na sheria tuliyokuwa nayo kwetu Tanzania na tunakiweka kwenye mkataba kwa ajili ya kukubaliana kwamba katika mapato na kazi utakayoifanya kiasi hiki basi kirudi kurudisha huduma katika jamii husika. Tunakwenda afya, tunakwenda kwenye maji, tunakwenda kwenye elimu na kwenye miundombinu kama hiyo ya barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mzuri ni katika mradi wetu wa Mwalimu Nyerere, katika mradi wetu ule tunazo trilioni sita, lakini asilimia nne zimeenda kwenye CSR kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakapokuwa tumeingia mkataba na mkandarasi wa kujenga mradi ule, lazima tuwe na kifungu cha Corporate Social Responsibility ambacho kitawanufaisha wananchi wa Busokelo, lakini pia na Makete ambapo ndiyo bwawa linapoanzia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali la pili, umuhimu wa kufikia ile miundombinu itakayotengenezwa ndiyo itakayofanya miundombinu ya barabara iwepo, kwa sababu mradi kama mradi kwa maana ya ujenzi wa bwawa, lakini pia ujenzi wa ile power house, sehemu ambayo umeme utazalishwa, lazima tuwe tuna barabara nzuri zinazopitika kwa sababu tunayo mizigo mikubwa ambayo tunatakiwa kuisafirisha kuifikisha katika maeneo yale. Kwa hiyo tutajenga barabara hizo ikiwa ni faida kwa kuhudumia mradi, lakini pia na kuhudumia wananchi wa maeneo hayo kwa ajili ya kufikika katika maeneo yote.
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Serikali nina maswali mawili ya nyogeza.

Mheshimiwa Spika, kutokana na kwamba mipaka ya Hifadhi hii ya Kitulo ilikosewa kwa sababu walikuwa wanatumia vijana ambao walikuwa wakibeba zile zege au beacon na kwa kuwa zilikuwa ni nzito sana walikuwa wanatua mahala ambapo siyo mipaka. Maana wanapotua ndiyo hapo hapo wanafanya mpaka na kusababisha baadhi ya taasisi kama shule mbili pamoja na jamii/familia/kaya kuwa ndani ya hifadhi. Je Serikali iko tayari sasa kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi kwenda kurekebisha mipaka hii ili iwe na uhalisia ama original yake ilivyokuwa inatakiwa iwe? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Hifadhi ya Kitulo inajulikana kama bustani ya Mungu kwa sababu ina maua ambayo yanachua na ni hifadhi pekee kwa Afrika ambayo ina maua mazuri sana na kwa bahati mbaya sana haijatangazwa ipasavyo. Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba Hifadhi hii ya Kitulo inatangazwa ili ijulikane kama zilivyo hifadhi nyingine? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Atupele Mwakibete, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusu mipaka kwamba ilikosewa, nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaongozana na yeye pamoja na watalaam wa Wizara ya Maliasili na Utalii lakini pia nitaomba wataalam wanaotoka katika Wizara ya Ardhi ili twende kuangalia. Pale ambapo itathibitika kwamba mipaka hii ilikosewa basi tutaweza kuirekebisha.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala hili linalohusiana na utalii, nimhakikishie tu Mbunge kwamba bajeti ya mwaka 2021/2022 imezingatia maeneo muhimu likiwemo eneo hili la Hifadhi ya Kitulo kuitangaza kwa nguvu zote na ukizingatia kwamba hifadhi hii ni ya kipekee hapa nchini. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba hifadhi hii itatangazwa kwa nguvu zote ili watalii waweze kufika katika hifadhi hiyo.

NAIBU WAZIRI WA ARDHI: Mheshimiwa Spika, kwanza nishukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii. Kutokana na changamoto zinazojitokeza katika tafsiri hasa ya mipaka kwenye maeneo ya wananchi pamoja na hifadhi, Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii tutaweka utaratibu ambao tunakwenda kupitia mpaka mmoja baada ya mwingine ikiwemo hata ile ya Kazimzumbwe ambayo imekuwa na shida nyingi. Kwa hiyo, tutaifanya kazi hiyo tukishirikisha na wananchi wa maeneo husika ili tuweze kupata tafsiri sahihi tujue ni kweli mipaka imehama au namna gani kwa sababu kumekuwa na kelele nyingi kuhusiana na maeneo ya hifadhi na wananchi. (Makofi)
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa niulize swali moja la nyongeza.

Barabara ya kutoka Katumba - Suma – Mwakareli - Luwanga - Mbambo mpaka Tukuyu yenye urefu wa Kilometa 82, imeanza kujengwa kipande cha kutoka Luhangwa – Mbambo – Tukuyu.

Je, ni lini kipande cha kutoka Luhangwa - Mwakareli - Suma - Katumba kitajengwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwakibete kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ni mwendelezo wa ujenzi ambao unaendelea, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika bajeti hii kuna fedha ambayo imetengwa ambapo barabara hii ya Katumba hadi Luhangwa itaendelea kujengwa, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Busokelo pamoja na wananchi wa Busokelo kwamba barabara hii itaendelea kujengwa kadri fedha itakapokuwa inapatikana na tayari imeshaanza kwa hiyo Serikali itaendelea kuijenga barabara hii. Ahsante.