Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Janet Zebedayo Mbene (19 total)

MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasikitika sana kuwa masuala mengi yanayohusiana na mambo ya wanawake yanatafutiwa kila sababu yasifanyike yakakamilika. Tunataka kupata majibu ni lini sasa hizi sheria zitapitiwa na zilete majibu yanayotakiwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, wanawake ni zaidi ya asilimia 51 ya nchi hii lakini mambo yao yanapigwa danadana kila siku. Tunataka hili jambo likamilishwe sasa, lilikuwa lisingoje Katiba kwa sababu ni la miaka mingi kabla hata ya Katiba. Ahsante sana.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilikuwa na dhamira njema kutumia mtindo wa white paper badala tu ya kupokea mapendekezo kutoka Wizara ya Katiba na Sheria ili wananchi wengi iwezekanavyo waweze kushiriki kwenye zoezi hili. Kama nilivyoeleza kwenye majibu yangu ya awali ni kwamba kipindi hicho ambacho tulitakiwa sisi tutumie utaratibu wa white paper ndiyo kipindi ambacho kulikuja pia mchakato wa Katiba Mpya ambao ulitutaka sasa tuwafikie wananchi wengi na ni gharama ambayo tusingeweza kuibeba kwa pamoja, huku tunafanya usahili kuhusu masuala ya Katiba Mpya na huku tunaendelea na masuala ya white paper kuhusu huo mchakato wa kubadilisha sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Janet Mbene, Serikali imefanya makubwa mno kuleta mabadiliko ya hali ya wanawake Tanzania. Mwaka 1999, naomba nimkumbushe Mheshimiwa Mbunge, Serikali ilifanya maamuzi makubwa kwa sheria zake mbili za ardhi, Sheria Na.4 na 5 kuhakikisha kwamba mwanamke hadhaliliki tena katika kumiliki na kutumia ardhi. Sasa hivi mwanamke ana haki sawa kabisa na mwanaume.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile katika Mkutano huu tunaleta Muswada wa Sheria utakaohakikisha watoto wetu wote wanaosoma shule za msingi na sekondari wasiweze kukatisha masomo yao kutokana na masuala haya ya ndoa za mapema. Muswada huo utakuwa ni miscellaneous amendment, ambao utaleta mabadiliko kwenye Sheria ya Elimu ambapo watoto wote wa shule za msingi na sekondari hawataruhusiwa kuolewa, hawataruhusiwa kuoa ili wafaidi fursa iliyojitokeza chini ya Serikali ya Awamu ya Tano ya elimu bure kwa wote na wote ni mashahidi hapa jinsi ambavyo wananchi na watoto wengi wameitikia fursa hii ya elimu bure na tunataka na watoto wa kike nao wafaidike as much as possible. Ahsante sana.
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake, lakini vile vile Ileje ina changamoto kubwa sana ya shule ya sekondari ya bweni ya wasichana. In fact hakuna shule ya bweni ya wasichana peke yake, hii inaleta changamoto kubwa kwa watoto kusafiri kwenda Wilaya nyingine au Mikoa mingine na ni gharama kubwa kwa wazazi na inaleta usumbufu. Watoto wengine wameshindwa hata kumaliza masomo yao. Je, Serikali iko tayari kutusaidia kujenga shule ya bweni ya wasichana kwa kuchangia nguvu na wananchi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Ileje vile vile ni katika wilaya ambazo hazina vyuo vya ufundi vya aina yoyote. Tumejitahidi sana, tumepata mfadhili ametujengea VETA, hivi sasa karibu imalizike. Je, Serikali iko tayari kuchukua ile VETA kuiendesha, kuiwekea vifaa na kuwalipa Walimu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kukosekana kwa shule ya wasichana; tukiri wazi, ni katika miongoni mwa changamoto kubwa sana inayoikabili nchi yetu na kusababisha tatizo la ujauzito kwa vijana wetu ambao kwa njia moja au nyingine wanaposafiri kutoka majumbani mwao kwenda shuleni, katikati huwa wanakumbana na changamoto kubwa sana za ushawishi. Hili nimpongeze Mbunge huyu kwa kuona kwamba kuna kila sababu ya kuhakikisha kwamba wasichana wanatengenezewa eneo maalum kwa ajili ya elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikiri wazi kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa sababu watu wa Ileje wameshaanza hili na sisi kwa njia moja au nyingine, tutashirikiana nao kwa pamoja ili kuhakikisha kwamba tunapata wasichana wengi ambao kesho na keshokutwa watakuwa viongozi wa nchi yetu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge tutashirikiana na Jimbo lako na Wilaya yako katika eneo hilo ili kuhakikisha kwamba wasichana wanathaminiwa na kupata elimu bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niwapongeze ninyi kwa kufanya harakati kubwa na kupata wadau mbalimbali walioshiriki mpaka kujenga hiki chuo cha VETA. Ofisi ya Rais kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu tutaangalia jinsi gani tutafanya ili kuangalia jinsi gani chuo hicho kiweze kutumika kwa upana wake ili kuwafanya Watanzania hasa watoto wa Ileje na maeneo jirani waweze kupata elimu hiyo. Naomba tulichukue hilo kwa ajili ya kulifanyia kazi ofisini kwetu na Wizara ya Elimu.

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, TAMISEMI, nataka kumthibitishia Mheshimiwa Mbene na Waheshimiwa Wabunge wote na Watanzania, Serikali ya Awamu ya Tano itawachukulia hatua za kisheria wanaume wote wanaowapa ujauzito watoto wa shule. Hatutakuwa na msalie Mtume, wanawake wamejaa mitaani ambao siyo wanafunzi, kwa hiyo hatutacheka na mwanaume yeyote ambae anawapa ujauzito watoto wa shule.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaagiza Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya, Kata na Mikoa kuwafuatilia wanaume wote hao na kuhakikisha wanafikishwa Mahakamani haraka iwezekanavyo.

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri aliyoyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba niongeze jibu la swali linalohusiana na VETA kwa Mheshimiwa Janet Mbene kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba wananchi hao wana majengo mazuri ambayo yalijengwa kwa kushirikiana na wafadhili wa JICA lakini hata kwa kuwatumia VETA walishakwenda wakakagua na wakaona yanakidhi viwango, isipokuwa sasa baada ya kutuandikia na kuona kwamba tuweze kukichukua, tulichowafahamisha kupitia Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya, Ndugu Rosemary Staki Senyamule wanachotakiwa ni kwanza eneo hilo lipimwe na kwa kuwa kile chuo kilikuwa kinamilikiwa na NGO, tunawaomba wakabidhi rasmi kwa Halmashauri. Halmashauri kupitia vikao vyake vya kisheria viridhie na kupitia kwenye RCC ili sasa hati hiyo ikishakuwa tayari ambayo pia ni pamoja na kuongeza kidogo eneo la chuo hicho, tutakuwa tayari kukichukua na kukifanya kiwe chuo cha Wilaya ya Ileje. Tunampongeza sana Mheshimiwa Janet Mbene kwa jitihada anazozifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Hizo huduma zinazosemekana kuwa zinatolewa kwa out growers, Je kuna mkakati maalum au inategemea na huruma ya huyo mwekezaji mkubwa?
Swali la pili linahusiana na soko; Kwa kuwa sasa hivi huu utaratibu wa minada ya Kahawa unaathiri kwa kiasi kikubwa mapato yanayopatikana kwa wakulima wadogo. Je, Serikali iko tayari kuruhusu wakulima wa kahawa na wao wenyewe kujitafutia masoko katika maeneo ambayo ni nish kwa ajili yao ili na wao waweze kupata mapato makubwa zaidi kwa ajili ya kahawa yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, Je, hii minada ni lazima iwe Kilimanjaro tu, hatuwezi kuwa na minada katika maeneo makubwa ambayo Kahawa inalimwa? Ahsante sana
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, moja, kuhusu huduma zinazotolewa na Wakulima wadogo kwenye out grower schemes hamna mkakati wowote maalum ambao umewekwa, isipokuwa uhamasishaji umekuwa ukifanywa ili mashamba hayo yaweze kutoa huduma mbalimbali ikiwepo kama nilivyosema kuwasaidia kupata teknolojia nzuri zaidi, kuwasaidia katika ukoboaji, kimsingi mashamba yale yanaangalia ni nini wanahitaji kwa ajili ya kuongeza tija katika uzalishaji wao na katika kupata masoko.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inachofanya ni kujaribu kuhamasisha na kuwashauri waweze kutoa huduma mbalimbali ambazo zitawasaidia wakulima wale wanaozunguka kuweza kupata tija katika uzalishaji
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu masoko; Serikali kimsingi haikatazi wakulima kujitafutia masoko ilimradi wafuate taratibu ambazo zimewekwa ili kusiwepo na uholela pia vilevile ili wakulima wetu waweze kulindwa na mifumo ya kinyonyaji, kwa sababu ukiachia tu iende kiholela, wakulima wetu wanaweza wakaumia. Kwa hiyo kimsingi, masoko yanaweza kutafutwa na tayari kuna wakulima ambao wanauza Kahawa moja kwa moja nje lakini ilimradi taasisi zinazohusika na udhibiti zifanye kazi ili wakulima wasiweze kuonewa.
Pia, aliuliza kuhusu Je ni lazima soko la kahawa likafanyike tu Kilimanjaro. Kimsingi kuna aina tatu ya uuzaji wa kahawa. Kwa kutumia soko la Moshi, wakulima wanaweza wakauza moja kwa moja nje pia kuna utaratibu wa kutumia manunuzi ya wakati lakini kimsingi Serikali iko tayari kufikiria namna bora ya kuendesha soko la kahawa ikiwa ni pamoja na kuruhusu uanzishwaji wa masoko mengine kwa maeneo ambayo yana uzalishaji mkubwa.
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na kwa kuitikia wito wetu wa kusaidia kupokea hiki chuo kiwe cha Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo letu kubwa Ileje na maeneo mengi ya pembezoni ni upimaji wa ardhi kwa ajili ya kuweka taasisi muhimu kama hizi za vyuo na masuala mengine. Naomba Serikali kwa ujumla itusaidie kwa sababu kupima viwanja muhimu kama hivi kwanza ni gharama lakini vilevile hatuna wataalam katika maeneo yetu wa kutupimia kwa haraka ambayo tungeitegemea. Je, Serikali ipo tayari kupitia Wizara nyingine yoyote ambayo inahusika na mambo haya kusaidia Wilaya ya Ileje tuweze kupima viwanja vyote muhimu tulivyoviainisha kwa ajili ya taasisi kwa mfano viwanda, elimu kama hivyo, vyuo vya unesi na vyuo vingine mbalimbali vya ualimu ili tuweze kupata maendeleo haraka zaidi? La sivyo tukiendelea kungojea tu mpaka sisi wenyewe tuwe na uwezo wa kupima tutachelewa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lingine, kwa kuwa sasa hivi tumeshaanzisha mkakati wa kuwa na chuo cha ufundi, tungeomba sasa tunapoendelea na mipango basi hiki chuo kiwe na mitaala ambayo itatusaidia kuzalisha vijana watakaokuja kufanya kazi katika viwanda kwa sababu sasa hivi tunalenga kwenda kwenye uchumi wa viwanda. Ahsante
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA MAFUNZO YA UFUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ni kweli kama ambavyo amezungumza Mheshimiwa Mbunge Janet Zebedayo Mbene kwamba kuna tatizo kubwa katika baadhi ya halmashauri kushindwa kumudu kupima viwanja hususani vile vinavyohitajika katika maendeleo ya vyuo na taasisi mbalimbali za kiuchumi. Suala hilo linatokana na hali halisi ya uchumi katika halmashauri hizo. Sisi pia kwa upande wetu Wizara kwa kupitia VETA imekuwa ikicheleweshwa sana katika upatikanaji wa viwanja kutokana na halmashauri husika kushindwa kuleta hati za viwanja au maeneo ambayo yameshapimwa kwa ajili ya shughuli hizo. Hilo suala tumeliona na nadhani linahitaji pia kuangaliwa kwa mapana zaidi.
Katika hili nachukua nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Waziri wa Fedha alivyozungumzia kuangalia mapato katika halmashauri kwa upana zaidi na kuweza pia kuangalia namna ya hizi halmashauri nyingine ambazo zipo katika hali ngumu ya kiuchumi nazo ziweze kupata mitaji hasa katika upimaji kadiri itakavyowezekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia katika suala la kuangalia mitaala inayoendana na shughuli za viwanda, ni kweli kwamba kabla Chuo cha VETA hakijajengwa mahali popote, kitu kinachofanyika ni kuangalia mitaala na kozi ambazo zitaweza kutolewa katika maeneo hayo tukiwa na lengo la kuwanufaisha hata wananchi wengi wa maeneo hayo kutegemeana na shughuli mbalimbali zinazofanyika katika maeneo hayo. Kwa hali hiyo ni kwamba kabla hiki chuo hatujaweza kukichukua na kuanza kukiendesha, suala hilo la kuangalia mitaala litakuwa ni mojawapo ya shughuli zitakazozingatiwa. Nachoomba Mheshimiwa Mbene jitahidi kadiri inavyowezekana kumalizia angalau hasa zile taratibu za awali za makabidhiano rasmi kupitia vikao vya kisheria wakati masuala mengine yakiendelea.
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona.Ningependa kupata jibu, kwakuwa masuala ya madini hasa yale ambayo si ya kawaida yapo hata katika Mkoa wa Songwe; tuna migodi ya marumaru hususan Mbozi, Ileje, Chunya, yote haya bado hayajaendelezwa kwa kiasi ambacho yangeweza kuleta tija, je, Wizara ya Nishati na Madini itafanya lini utafiti wa kuja kutuletea na sisi uchimbaji wa migodi hii kwa sababu ina faida sana. Badala ya kuagiza tiles nje tungeweza kutumia za kwetu na ubora wake ni mzuri kuliko ule wa nje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile, je, mgodi wa Kiwira ambao uko Ileje na haujawahi kuifaidia Ileje utazinduliwa lini? Ahsante sana
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa katika Mkoa wa Mbeya pamoja na maeneo ya Songwe na Ileje kuna madini ya aina nyingi sana mbali na dhahabu. Na madini mengi yaliyoko katika maeneo yale ni madini ya viwandani. Kama nilivyosema kwenye swali langu la msingi, madini ya niobium yanapatikana kwenye Mkoa wa Mbeya na hasa kwenye maeneo ya Songwe karibu na Gereza la Songwe. Madini haya ya niobium ni adimu sana, na ni madini ya kwanza kupatikana kwa Tanzania na Afrika Mashariki. Kama nilivyosema madini haya yatatumika sana kwa shughuli za viwandani na hasa baadaye kwa kutengeneza computer, engine za ndege pamoja na rocket,, kwa hiyo ni madini ambayo yanapatikana sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti niongeze tu, kwamba sasa madini mengine yaliyoko pale utafiti unafanyika. Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) linaendelea na kufanya utafiti ili kubaini madini mengine ambayo yanapatikana kwenye maeneo ya Songwe, Mbeya Vijijini pamoja na Ileje ili na yenyewe yaweze kuchimbwa kwa faida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije sasa kwenye mgodi wa Kiwira. Kama mnavyojua Mgodi wa Kiwira unatarajiwa kabisa kwa kuanza kuzalisha umeme, lakini kwa shughuli za uchimbaji wa Mgodi wa Kiwira sasa hivi kinachofanyika ni kukamilisha detail design na taratibu za kumpata mkandarasi. Na kwa utaratibu ambao kwenye bajeti yetu tutakayoisoma Alhamisi wiki hii tutawaeleza, taratibu za kuanza ujenzi huu zitaanza mwaka 2018 na mgodi huu utachukua takribani miaka 20 na kuendelea.
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, kwa kuwa kumekuwa na matamshi yanayotofautiana kutoka Serikalini kuhusiana na maendeleo ya mgodi huu, tungependa sasa kupata tamko rasmi ambalo wananchi watalielewa kuhusiana na uendelezwaji wa mgodi huu. Mwaka jana mwishoni tuliambiwa kuwa tayari mwekezaji ameshapatikana na karibu ataanza kazi. Tukaja kuambiwa mwekezaji yule ameonekana hafai na anatafutwa mwingine. Sasa tunaambiwa wako kwenye hatua za mwisho za kumtambulisha mwekezaji. Napenda kupata tamko rasmi kuwa ni lini huyo mwekezaji atapatikana na wananchi wategemee kuanza kufaidika na mgodi huo lini?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa mgodi huu umetolewa leseni kwa miaka 25 na kwa muda mrefu sana huu mgodi umekaa bure. Je, huo muda wa leseni utaongezwa pindi atakapopatikana huyo mwekezaji au la sivyo mategemeo ni yapi mwekezaji huyo akija?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la kwamba mgodi umechukua muda mrefu bila kuanza kazi zake, ni kweli kabisa. Labda nitoe historia kidogo ni kwamba Mgodi huu wa Kiwira ulikuwa uanze tangu mwaka juzi lakini mkandarasi aliyepatikana kwa ajili ya ujenzi huo baada ya kufanya upekuzi rasmi (due diligence) hakuonekana kuwa na uwezo wa kifedha. Kutokana na msimamo wa Serikali, tuliona tusitishe badala ya kuingia hasara kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya pesa kupatikana sasa na kama mlivyoona tumepitisha shilingi bilioni mbili kwenye bajeti yetu na tunawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, tutaanza shughuli za awali ambazo zitahusisha pia ujenzi wa awamu ya kwanza pamoja na kuwalipa pia wakandarasi waliohusika katika feasibility study. Ujenzi kamili unatarajiwa kuanza Desemba 2017 au 2018 na utachukua miaka mingi kama inavyoonekana. Kwa hiyo, ujenzi wa mradi huu utaanza baada ya kumpata mkandarasi na matarajio makubwa mwaka 2018 utaanza kujengwa rasmi.

NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naona kwenye jibu langu nilijumlisha kwa harakaharaka. Labda nimweleze, ni kweli mgodi huu unachukua miaka 25 na miaka 25 ulikuwa ni uhai wa Mgodi wa Kiwira sawa na migodi mingine mikubwa hapa nchini. Sasa imechukua takribani miaka 11 wakati shughuli za upembuzi zinakamilika bila kuanza uzalishaji. Kwa utaratibu wa Sheria ya Madini Na. 14 ya 2010, kifungu cha 111, kama mwekezaji atagundua kwamba anahitaji kuongezewa muda anaweza pia kuongezewa uhai wa muda wa miaka 25 mingine mpaka atakapokamilisha shughuli za uchimbaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, uhai wa leseni, kama akiona reserve inatosha kuchimbwa na reserve iliyopo pale Kiwira ni tani milioni 30, kwa hiyo ni kweli kwamba tani milioni 30 inawezekana isichimbwe kwa ndani ya miaka 14 akahitaji muda mwingine mrefu. Akihitaji muda mwingine mrefu anaweza akaongezewa miaka mingine 25.
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kutupa moyo na kutuhakikishia kuwa tayari mikakati ya kutuwekea kituo cha forodha iko njiani. Hata hivyo, nataka vilevile nimtake
Mheshimiwa Waziri na Serikali kuharakisha mipango hiyo kwa sababu hivyo vituo vya jirani anavyovizungumza bila shaka anazungumzia Kasumulo iliyopo Kyela, anazungumzia Tunduma ambavyo vyote viko mbali sana na Ileje na Ileje
kama inavyofahamika hakuna barabara hata moja
inayopitika vizuri, kwa hiyo kutuambia sisi twende tukatumie vituo vile ni kama kutudhihaki. Pamoja na hayo, tayari ardhi imeshaanza kupimwa na inamaliziwa, tayari maeneo yameshaainishwa, tayari wahusika wameshakuja kukagua maeneo, namwomba sasa Mheshimiwa Waziri anihakikishie
kuwa sasa hatua itakayofuata ni ujenzi.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na Malawi; Malawi
tayari wana kituo, wanatungojea sisi. Miundombinu yetu sisi ndiyo inachelewesha kile kituo cha Malawi kushirikiana na cha kwetu. Kwa hiyo, naomba sana hilo lifahamike na
atuhakikishie hapa ni lini sasa hatua hizo zitafanyika? Ahsante sana.
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumthibitishia Mheshimiwa Mbunge Janet Zebedayo Mbene, Mbunge wa Ileje kwamba maoni yake yatazingatiwa.
MHE. JANET Z. MBENE: Mhehimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Mazingira anayozungumzia Mheshimiwa Chagula hayana tofauti na mazingira mengi ya Wilaya zetu na mikoa yetu ya pembezoni.
Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Ileje ilibahatika kupata fedha kwa ajili ya kujenga Hospitali ya Wilaya ambayo imejengwa na sasa hivi imesimama karibu miaka miwili. Nataka kuomba kuuliza, je, Wizara ya TAMISEMI iko tayari kuimalizia hospitali hiyo kwa sababu ni hospitali kubwa na kwamba kama ingetumika vizuri ingesaidia kiasi kikubwa sana. Sasa hivi wagonjwa wetu wa-referral wanakwenda Malawi. Kwa sababu Mbeya ni mbali zaidi, wanakwenda Malawi kutibiwa sasa hii si sahihi. Mheshimiwa Waziri atuambie, je, itawezekana kututengea fedha bilioni 1.3 kwa ajili ya kumalizia hosptali ile?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba tulichukulie jambo hilo kwa uzito wake na nakumbuka Mheshimiwa Mbunge hata wakati tunajadili mambo mbalimbali hasa katika jimbo lake la Ileje na hata kituo chake cha kimoja cha afya alikuwa akizungumzia suala zima la changamoto ya afya katika Halmashauri ya Ileje. Naomba nikuhakikishie kwamba tutahakikisha tunakamilisha hizo Hospitali za Wilaya ili kupunguza changamoto hizi.
Mheshimiwa Spika, jambo hili liko maeneo mbalimbali, liko Mvomero, Kilolo na maeneo mengine hospitali zime-stack. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge siweze kuthibitisha kwamba by kesho tutatoa fedha, tunachokifanya Serikali kwa sababu tulikuwa na mchakato mpana wa kuhakikisha tunakabati vituo vya afya vipatavyo 100 na zoezi hili la kukarabati vituo vya afya 100 katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania litaanza ndani ya mwezi huu au mwezi ujao.
Mheshimiwa Spika, vilevile tutapeleka maelekezo makubwa kwenye Hospitali za Wilaya ambazo hazijakamilika, na tukimaliza hili tutakuwa tumehakikisha kwamba jukumu la Serikali yetu katika kuwahudumia wananchi litakuwa limefika mahali pazuri.
Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge naomba nikuhakikishie kwamba kwanza katika zile fedha za LGDG ambazo mwanzo zilikuwa sasa hivi tutaelekeza na kuweka nguvu vya kutosha ili fedha zote zipatikane. Vilevile tutazisimamia vizuri ili tuhakikishe kwamba tunamaliza suala hili la miundombinu ili wananchi wetu waweze kupata afya bora.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itashikirikiana nawe katika jimbo lako kuhakikisha sekta ya afya inakwenda vizuri.
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba niulize swali moja la nyongeza. Mkoa wa Songwe hususan Wilaya ya Ileje iko katika ukanda River Songwe Basin na kulikuwa kuna mpango katika mojawapo ya vitu vya kufanya katika mradi ule wa kuwa na mabwawa kwa ajili ya kufugia samaki na mpaka sasa hivi watu walizuiwa kutumia eneo hilo la Bupigu kwa sababu hiyo.
Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kutueleza ni lini sasa mpango huo utafanyika ili vijana wetu wapate ajira na vipato? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama anavyosema kwamba mpango uliokuwepo wa kuanzisha mabwawa ya samaki katika eneo la Buhengwe umesimamishwa kutokana na haja ya kuangalia athari zinazoweza kutokea za mazingira. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie kwamba pindi tathmini hiyo itakapokamilika, jibu sahihi au mwelekeo utafahamika.
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa jibu la Mheshimiwa Waziri lakini halijanipa faraja hata kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ileje ina fursa nyingi, kuwa mazao mengine sasa hivi hayajajitosheleza, ni kwasababu hakuna masoko, lakini fursa zipo. Sasa hivi hayo maeneo tuliyotenga, nilimuita Meneja wa SIDO Mbeya, alikuwa hajawahi kufika Ileje hata siku moja. Amekuja pale akatuambia tengeni eneo, hakutupa viwango, tutenge eneo kiasi gani? Hakutupa maelekezo yoyote. Miaka miwili imepita, wala hajarudi tena kuangalia kitu gani kinaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuna fursa kubwa sana ya viwanda vidogo vya usindikaji wa nafaka. Tunalima mahindi mengi, karanga nyingi na ulezi mwingi. Hivyo ni vitu ambavyo tunaweza kuanzia kwa sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnaposema sisi tutayarishe miundombinu yote wezeshi, kwa uwezo gani wa Halmashauri zetu masikini watu wa pembezoni kama sisi? Nini maana ya ile Sera ya Kuendeleza Viwanda ya 1996 mpaka 2020 inayosema mtapeleka viwanda nchi nzima na mtakwenda mpaka maeneo ya pembezoni? Sisi ndio watu wenyewe wa pembezoni, mnakuja lini kutusaidia kuweka viwanda? Msituachie huo mzigo wa kutengeneza miundombinu, hatuna uwezo huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, lini Mawaziri watakuja Ileje? Naomba Mheshimiwa Waziri wa Afya, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo waje Ileje. Mkija mkajionea wenyewe hali halisi ndiyo mtajua majibu ya kutupa humu ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naelewa na ninaweza kusikia uchungu alionao Mheshimiwa Mbunge kuhusu Wilaya yake na hasa kuhusu maeneo ya pembezoni. Nianze na lile swali ambalo ni rahisi. Nimeshapata mwaliko kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Katavi na Rukwa. Tarehe 6 Agosti, nitakwenda kutembelea mikoa hiyo tukiwa pamoja na shughuli za Nane Nane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Sera ya Viwanda (Sustainable Industrial Development Strategy) ya mwaka 1991 – 2020 katika jibu langu nimeeleza, tumegundua mwendo usio sawa katika viwanda vinavyoenea Wilayani. Kutokana na hiyo na kwenye jibu langu nimeeleza na kwenye bajeti yangu nimeeleza, ndiyo maana tunatengeneza mwongozo. Huo mwongozo utaweza kuwasukuma Watendaji wetu wafuate kama mwongozo unavyosema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge, nikuhakikishie nitafanya kazi na wewe na kuhusu suala la tangawizi tuanze shughuli hapa. Nenda kamfuate Mheshimiwa Mama Kilango akueleze alifanyaje kufufua Kiwanda cha Tangawizi na amepata wapi zile pesa shilingi bilioni 1.7 za kuendesha kiwanda cha Same? Akuelekeze, tuanzie hapo. (Makofi)
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na naipongeza Serikali kwa kuja na huu mpango mkakati wa kuhakikisha kuwa Bonde la Mto Songwe linaendelea kuwa endelevu kwa ajili ya matumizi ya wananchi wanaozunguka mto huo. Lakini nataka niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji iliyowasilishwa hapa Bungeni kwa ajili ya mwaka 2016/2017 tulielezwa kuwa kuna mambo ambayo tayari yameshafanyika kuhusiana na juhudi za kuendeleza rasilimali za bonde hili, lakini vilevile katika masuala mazima ya kutengeneza mpango wa biashara kwa ajili ya kuendeleza bonde hili. Nataka kujua na ilisemekana kuwa vingekuwa vimekamilika kwa mwaka 2015. Je, jambo hili lilifanyika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunavyozungumzia mkakati mzima wa uendelezwaji wa Bonde la Mto Songwe, wananchi wa kawaida katika maeneo ambayo yanahusika na yanaguswa na bonde hili hawana taarifa zozote wala elimu ya aina yoyote wala hawajui ni nini kinachoendelea.
Je, hii ofisi ndogo ya muda iliyoundwa imeanza kufanya kazi gani ili wananchi wetu waanze kupata uelewa ili hata mkakati huu utakapoanza kufanya kazi wawe tayari kuupokea? Ahsante sana.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nishukuru Bunge lako Tukufu, katika Bunge lililopita tulipitisha hii Kamisheni ya Songwe ambayo imeanza kazi na kwamba ofisi ipo Kyela pale na wananchi wanaitambua. Lakini tayari tumeshaomba fedha kwa ajili ya kujenga mabwawa matatu kupitia hilo Bonde la Mto Songwe ili kuweza ku-control mafuriko. Mabwawa hayo yatatumika pia kuzalisha umeme, lakini pia na kilimo cha umwagiliaji zaidi ya hekta 6,200.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa mchakato mzima wa uandaaji wa huo mradi, wananchi wote wa Mkoa wa Mbeya walishirikishwa kupitia Halmashauri zilizopo ndani ya Mkoa wa Mbeya; kwa hiyo, wananchi wapo aware.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tuendelee kushirikiana kama kuna hitaji la kuendelea kuwafahamisha basi tuendelee kuwafahamisha, lakini mradi unakuja na kwamba tayari kupitia taasisi yetu ya SADC mradi huu umeshaingizwa kwa ajili ya kuombewa fedha na utekelezaji uweze kuanza. (Makofi)
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Naomba nami niulize swali la nyongeza kuhusiana na masuala ya matumizi ya Maafisa Maendeleo ya Jamii na nipendekeze kwa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kuna upungufu mkubwa wa Maafisa Maendeleo ya Jamii, vilevile kuna kundi zima la vijana wengi wanaomaliza shule kuanzia Darasa la Saba, Kidato cha Pili, Kidato cha Nne mpaka Kidato cha Sita. Je, kuna uwezekano wa kuwatumia hawa kuwapa mafunzo ili watumike katika Vijiji vyao kama Maafisa Maendeleo ya Jamii hata kama ni Para Community Development Officers wa kufanya uraghibishi wa aina mbalimbali ili waweze kusaidia katika nguvu ya maendeleo ya jamii yaliyopo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Janeth Mbene ametoa ushauri kwa Serikali kwamba kwa sababu sasa hivi tunaelekea Tanzania ya viwanda na tuna changamoto kubwa sana ya vijana ambao hawana ajira; mawazo yake tunayapokea, tutaenda kuyafanyia kazi na kuangalia jinsi gani ya kuweza kuwashirikisha vijana katika kuleta maendeleo. (Makofi)
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kweli nasikitika hili jibu ni la juu juu mno. Hii Wizara imeshafanya mambo mengi tunayoyajua, ningetegemea hapa ingekuwa ndio wakati Serikali ingetueleza ambayo wameshafanya na yale ambayo bado. Hata hivyo, tumeletewa taarifa ambayo mwananchi wa kawaida anayesikiliza sasa hivi wala haelewi kama Serikali imefanya chochote katika masuala ya viwanda katika maeneo maalum wakati nafahamu kuwa yameshafanyika mengi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, basi baada ya kusema hivyo nina maswali mawili ya nyongeza. Sasa katika hayo maeneo ambayo yametengwa ambayo nayafahamu kuna industrial parks, stand alones na kuna maeneo mengine ambayo ni ya Wilayani; ni mangapi ambayo mpaka sasa hivi yameshawekewa hiyo miundombinu saidizi na miundombinu wezeshi na kiasi gani ambacho tayari kinazalishwa na mapato kiasi gani nchi inapata na ajira kiasi gani kimeshazalishwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuzingatia kuwa katika changamoto ambazo zinakwamisha na ambazo zimekuwa zikikwamisha kuendelezwa maeneo haya nyingi ziko katika uwezo wetu kuzitekeleza. Hiyo miundombinu inayozungumzwa ni kitu ambacho kiko kwenye uwezo wetu tukiamua. Haya masuala ya utata kati ya special economic zones na economic processing zones yanaweza kutatuliwa. Sasa ni kwa nini basi hatujakamilisha japo tuwe tuna maeneo mawili kila mwaka yanayofanyiwa kazi? Maana yameshatengwa na wananchi wamezuiwa kuyaendeleza lakini sisi hatujayafanyia chochote zaidi ya miaka 10 sasa. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nashukuru pia kwa majibu na maelezo ya Mheshimiwa Mbene. Kimsingi majibu yaliyoletwa ni majibu sahihi isipokuwa kwa maswali yake ya nyongeza naomba nimjibu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza; katika suala la uendelezaji wa maeneo hayo, ninavyofahamu ni kwamba katika uendelezaji wa miundombinu kuna miundombinu ambayo ni direct inayotokana na uwekezaji wa moja kwa moja katika eneo la economic processing zone au (SEZ); lakini pia kuna maeneo wezeshi yanayofanywa na sekta nyingine kama nishati pamoja na maji na miundombinu mingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa misingi hiyo, kwa mfano, ukisikiliza katika michango ya jana kuna uwezeshaji mkubwa uliofanyika na Serikali kwa ajili ya bomba la gesi ambalo mpaka sasa limezunguzwa kwamba itatumika takribani asilimia sita; lakini bomba hilo itakuwa tayari kuwekeza viwanda 190 vinavyotarajiwa katika Bagamoyo Economic Zone na maeneo mengine. Kwa hiyo, ni tayari Serikali imeshawekeza fedha nyingi katika miundombinu ya aina hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukirudi pia Benjamini Mkapa pale kuna miundombinu ambayo imewekezwa na Serikali lakini pia na wadau binafsi jumla yake ni takribani bilioni thelathini na saba na ina uwezo kuajiri watu moja kwa moja 5,000 ambao wanazalisha ajira zisizo rasmi zaidi ya 12,500. Hiyo yote ni uwekezaji ambao umefanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kwa upande wa Kigoma economic processing zone, pale tumepata mwekezaji binafsi ambaye yeye amewekeza umeme wa sola wa takribani mega watt 5 ambao uko tayari inangojewa tu kuunganishwa kwa upande wa TANESCO. Kwa hiyo kimsingi Serikali imekuwa ikiwekeza na inaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande maeneo ambayo yalitengwa katika mikoa Serikali imelipa fidia maeneo mbalimbali ikiwemo Kurasini ambayo tumelipa takribani shilingi bilioni mia moja na tatu na maeneo mengine kama Songea na Mara na mengine. Kimsingi tunachozungumza sasa hivi ni kwamba badala ya kuchukua fedha yoyote ya Serikali kuifungia katika kuilipia maeneo na wakati mwingine hao wawekezaji wanakuwa hawajajitokeza. Kwa hiyo tunachofanya sasa ni kuwashirikisha wawekezaji wenyewe ili yule anayehitaji eneo maalum basi aweze kusaidia katika kulipa fidia na kulitumia kwa malengo ambayo yanakuwa yamekusudiwa kwa win win stuation kwa upande wa Tanzania na huyo mwekezaji wetu.
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Na mimi naomba kuuliza swali la nyongeza kuwa hili suala la kutenga asilimia 10 wa ajili ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu linaonekana kama halijakaa kisheria sana na ndiyo maana wakati mwingine wanatumia hiyo loopholes za kuepuka kutenga hilo fungu.
Je, Serikali ina mkakati wowote wa kuhakikisha kuwa sheria au kanuni zinarekebishwa ili kuhakikisha kuwa hili jambo linakuwa kisheria zaidi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. GEORGE J. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nilijulishe Bunge lako Tukufu kwamba tumeshapokea maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu pendekezo la kupitia upya sheria ambayo ndiyo tunaiangalia ambayo ilikuwa ndio misingi wa kuanzishwa hii mifuko ili tuweze kuona kwamba tunaweza kurekebisha sehemu gani ili kuweze kuzibana zaidi Halmashauri kuhusu kutenga asilimia 10.
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali moja la nyongeza kuhusiana na VETA ya Ileje. VETA ya Ileje mimi ndiyo nilienda kuomba fedha kwa wafadhili zikapelekwa pale na VETA imejengwa kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo, hayo masharti kuwa lazima tuwe na hati ndiyo yametukwamisha mpaka sasa hivi. Kupima na kupata hati pia ni suala la Serikali vilevile. Sasa kwa nini hicho Chuo kisianze wakati suala la upimaji linaendelea? Kwa sababu ni miaka miwili sasa Chuo kimesimama na kile Chuo kingekuwa tayari kinasaidia vijana wetu wengi sana wakati suala la hati likiendelea maana nalo ni sehemu ya Serikali vilevile.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sioni kama kuna ugumu kama watu wameamua, kwa sababu kimsingi utoaji wa hati au hatua za kuweza kuchukua eneo na kupeleka eneo lingine linaanzia huko kwenye Halmashauri. Hata hivyo, toka kipindi hicho tulichoongea mpaka leo sijaona kama kuna jitihada yoyote iliyofanyika, kwa sababu maeneo mengine wameshafanya hivyo na wakafanikiwa na wao hawajafanya chochote kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani tukikubaliana si lazima ipatikane hati kabisa, lakini basi hata yale makubaliano ya kwamba Chuo hiki sasa wanakikabidhi kwa VETA basi itakuwa ni jambo jema lakini hatuwezi kwenda tu kuvamia mali ambayo sio mali ya VETA. (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nishukuru kwa swali na kwa niaba ya Waziri wa Elimu naomba nijibu swali la nyongeza kama ambavyo limeulizwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokupatikana kwa hati inaweza kuwa ni kigezo kweli cha wafadhili kushindwa kuwasaidia. Hata hivyo, ningeomba pengine baadaye tuonane na Mheshimiwa Mbene tujue wamekwama wapi, kwa sababu kama ni suala la taasisi ambayo ni ya Kiserikali na imepitia katika process zote sasa kuna mahali watakuwa wamekwama wao wenyewe katika kufuatilia hati ama kwenye malipo au kitu kingine. Kwa hiyo, nitawasiliana nae ili nijue wamekwama wapi na tuone tunawasaidiaje ili waweze kupata huo ufadhili.
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na pia nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwa kuwa suala la madaraja yanayounganisha Wilaya kwa Wilaya au hata Kata kwa Kata ni ya muhimu sana; Ileje tulijiongeza kuhusiana na suala hilo kuwa fedha inayohitajika ni kubwa, lakini mahitaji yaliyopo ni madogo. Kwa hiyo tumeomba kwa ombi maalum kuomba fedha ya kimkakati kwa ajili ya daraja linalopita mto Mwalwisi ambalo ndiyo linalotumika na mgodi wa makaa ya mawe Kiwira na Kabulo. Kwa hiyo nilitaka kujua hatima yake ni nini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipata fursa ya kutembelea Ileje, na nimefika Jimboni kwake naomba nimpongeze sana jinsi ambavyo wananchi wa Ileje; hakika Ileje ambayo ilikuwa inatazamwa miaka hiyo siyo Ileje ya sasa hivi, Ileje inafunguka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba katika maeneo ambayo yana uwekezaji wa kimkakati ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba yanatatuliwa changamoto ili tunapoongelea kwenda kufuata makaa ya mawe kule isiwe ni adha. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika mipango ya Serikali ya kuhakikisha kwamba makaa yale tunaanza kuyatumia lazima tufike daraja likiwa limekamilika. (Makofi)

MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza, kwa kuwa mradi huu ni mradi ambao unatambulika kuwa ni mradi wa kimkakati na kwa kiasi mpaka 2013 ulikuwa unatengewa fedha ya maendeleo lakini kuanzia mwaka wa fedha 2014/2015 hadi sasa hivi hakuna fedha yoyote ambayo imekuwa ikitengewa mradi huu ilhali sasa hivi mradi huu umeanza kufanya kazi na tayari mbia amepatikana na wiki hii ameshaweka saini pamoja na STAMICO ya kuanza kuchimba makaa ya mawe katika Mgodi wa Kabulo.
Je, Serikali imeuondoa mradi huu katika miradi ya kimkakati? Na kama ni hivyo, je, hiyo fedha ya kuendeleza hasa ukarabati wa Mgodi wa Kiwira wenyewe inayohitajika sasa hivi kwa sababu tayari mbia ameshapatikana itapatikana?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa mradi huu ambao umekuwa kwa muda mrefu ukinufaisha Wilaya nyingine ya jirani sasa hivi umeanza kutambulika rasmi kuwa ni mradi wa Ileje na kwa urahisi wa kuufikia mradi huu kuna daraja katika Mto Mwalisi ambalo liliharibika kwa muda mrefu la kilometa karibu saba na barabara yake, imesababisha mradi huu sasa kuwa unatumia njia ndefu ya kupitia Kyela ambayo ni karibu kilometa 36 na kuleta gharama kubwa na kuongeza gharama kubwa kwa mradi huu.
Je, Serikali iko tayari sasa kuhakikisha kuwa hii barabara pamoja na Daraja la Mwalisi ambalo ndilo linalounganisha Wilaya ya Ileje na Mradi wa Kiwira na Kabulo inatengenezwa haraka sana ili mwekezaji huyu sasa hivi aanze kufanya kazi bila matatizo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya. Ni mama ambaye yuko makini, anafuatilia sana majukumu yake ya kuwawakilisha wananchi wa Ileje kama Mbunge. Ni kweli mama huyu amejitosheleza sana katika jimbo hilo, Mungu ambariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ni kwamba je, Mradi huu wa Kiwira tumeuondoa katika miradi ya kimkakati? Jibu jepesi kabisa na la haraka ni kwamba bado mradi huu tunautambua kwamba ni mradi wa kimkakati ikiwa ni pamoja na miradi mingine mikubwa ambayo kwa kweli tunafahamu kama Serikali kwamba miradi ya kimkakati ni ile miradi mikubwa ambayo inawezesha miradi mingine au sekta nyingine kufanya kazi. Na kwa sababu sasa hivi tunataka nchi yetu iende katika kuwa nchi ya viwanda, makaa ya mawe ni kitu muhimu sana katika uendelezaji wa viwanda vyetu na hasa viwanda vya simenti. Kwa hiyo, mradi huu bado ni mradi wa kimkakati tunautambua kama miradi mingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni lini sasa Serikali tutaiwezesha kujenga barabara hii ya Kiwira – Kabulo. Sisi kwa kushirikiana na TARURA, Wizara ya Madini tumekwishawaandikia TARURA barua ya kuhakikisha kwamba kilometa zile saba zinajengwa katika mradi huu ili kupunguza kilometa 36 ambapo mwekezaji huyu anatumia kwa maana ya kupeleka kusafirisha makaa ya mawe, inaingiza gharama kubwa kwa sababu tunatambua kuwa makaa ya mawe ni bulky mineral, ni mzigo mkubwa. Kwa hiyo unapoweka katika hali ya kusafirisha mwendo mrefu gharama inakuwa ni kubwa na mtumiaji wa mwisho analipa gharama kubwa kiasi kwamba inamfanya huyu mwekezaji apate shida katika kuendeleza mradi wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali tumelitambua hilo na imetengwa shilingi bilioni 2.5 ya kujenga kilometa saba na vilevile imetengwa bilioni 1.5 ya kujenga daraja ambalo liko pale.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi, sisi tunaendelea kulisimamia na sisi kama Wizara ya Madini tunahakikisha kwamba tuko pamoja na Serikali kuwawezesha wawekezaji wote katika sekta ya madini wafanye kazi kwa faida na wasifanye kazi kwa hasara. Ahsante sana.
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri, lakini ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza itambulike kuwa huu mradi umeanza kubuniwa muda mrefu sana na ninashukuru kuwa hii awamu ya tatu sasa ndiyo inaafikiwa. Lakini ninapenda kujua, huko nyuma ilionekana kabisa kama tayari kuna uwezekano mkubwa wa kupata mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika. Je, hatua hizo zimefikia wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali inaweza ikatupa timeline au ratiba maalum itakayoonesha kabisa hatua zinazoendelea kwenye mradi huu ili tuanze kupata manufaa yake? Huu ni mradi ambao kwetu sisi Mkoa wa Songwe ni wa kimkakati kwa sababu utatuzalishia umeme, utatuwezesha kulima kwa kumwagilia na vilevile utaboresha miundombinu mbalimbali. Kwa hiyo, naomba sasa kujua kama kuna timeline ambayo imeshatengenezwa na Serikali ya kujua ni lini sasa hasa tutaanza kuona matokeo ya utekelezaji? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze kabisa, ni kweli amekuwa anakuja ofisini kufuatilia utekelezaji wa mradi huu na malengo yake alipenda uanzie kutekelezwa Songwe Juu, eneo ambalo ni la jimbo lake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ni kuhusu mkopo, kwa sasa hivi Serikali hizi mbili mkopo huu utakopwa na Serikali mbili, Serikali ya Malawi na Serikali ya Tanzania.
Kwa hiyo, naomba tu Mheshimiwa Mbene uziachie Serikali, tunaifanyia kazi kwa haraka sana ili kuhakikisha tunapata huu mkopo, tuweze kutekeleza huu mradi. Na kama mwenyewe ulivyosema kwamba una manufaa makubwa, kuna kilimo cha umwagiliaji, kuna kuzalisha umeme lakini pamoja na kupata huduma ya maji ya kunywa safi na salama na pia tutazuia mafuriko ya Mto Songwe ambao umekuwa unabadilisha mpaka kila mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu muda (time frame), ni lini; Mheshimiwa Mbene nikwambie tu kwamba tukishapata fedha programu imeshaandaliwa, lakini sasa ile programu itakuwa effective kwamba inaaza tarehe ngapi, baada ya kupata fedha ndiyo tutaweza kukupa majibu ambayo yana uhakika.
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sekta ya utalii ni sekta ambayo ina fursa nyingi sana na kubwa za kulisaidia Taifa kimapato. Suala la Mikumi kama ambavyo limejibiwa sasa hivi, tunapoteza fursa kubwa sana. Mikumi ilikuwa ni kivutio katika vivutio vya mwanzo kabisa vya utalii nchi hii. Ilikuwa inatoa fursa kubwa sana kwa utalii wa ndani hasa kwa vijana, wanafunzi na taasisi mbalimbali wanaotaka kwenda kuangalia mambo ya utalii. Jinsi ilivyo sasa hivi imekwama kwa muda mrefu na hii sawa na sehemu nyingine nyingi tu.
Je, Serikali sasa hivi iko tayari kuja na mkakati mahususi unaohakikisha kuwa sehemu zote za kitalii zinaendelezwa kwa kutumia sekta binafsi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba Mikumi ilikuwa ni moja ya hifadhi ambayo ilikuwa inatoa mchango mkubwa sana katika pato la Taifa, lakini kumekuwa na changamoto ya hivi karibuni kwamba mchango ule kidogo umeshuka sana kutokana na mambo mbalimbali. Ndiyo maana kwa kutambua hilo, Serikali tumekuja na mradi mkubwa wa kuboresha utalii Kusini. Katika mradi huo, moja ya maeneo ambayo yamepewa uzito ni pamoja na hifadhi ya Mikumi, kwa sababu ule mradi wa kukuza utalii wa Kusini, tunahudumia Selous upande wa Kaskazini, Udzungwa, Mikumi na Ruaha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika huo mradi tunaboresha miundombinu yote, tutatangaza ipasavyo kuhakikisha kwamba tunawavutia watalii mbalimbali wa ndani na nje ya nchi ili waweze kuingiza mapato na Serikali iweze kupata mapato ya kutosha na kuweza kuendeleza nchi yetu.