Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. Harrison George Mwakyembe (34 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naanza kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuniamini kuwa mmoja wa wasaidizi wake. Vilevile natumia fursa hii kuwapongeza sana wapigakura wa Kyela kwa uamuzi wao wa busara wa kubaki njia kuu, kwa sababu madhara ya michepuko yanaonekana wazi, viti vitupu hapa! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wamarekani wanasema hotuba ya Mmarekani mwenzao mmoja mweusi, Martin Luther King Junior aliyoitoa mwaka 1963, ndiyo hotuba bora kupita zote katika historia ya Taifa hilo ya miaka 229. Hiyo hotuba ilimgusa kila Mmarekani anayeipenda nchi yake. Na mimi naweza kudiriki kusema, ukiachia hotuba za Mwasisi wa Taifa hili, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, hotuba aliyoitoa Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alipokuwa anazindua Bunge hili tarehe 20 Novemba, nayo ni hotuba bora kupita zote iliyogusa mioyo ya Watanzania wote wenye nia njema na nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba yenyewe ukiiangalia ni fupi tu, ina aya 160. Nimejaribu kufanya utundu tu hapa kuangalia, maana imerekodiwa kama Hansard. Rais wetu alipigiwa makofi na vigelegele mara 137 yaani ni zaidi ya 86! Nilipokuwa najaribu ku-check history, Martin Luther King Junior, alipigiwa vigelegele mara ngapi; ilikuwa kama asilimia 75. Kwa hiyo, imevunja rekodi! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba hii imewaweka mahali pabaya sana wenzetu wa upinzani waliozoea kupinga kila kitu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la hotuba hii, ukijaribu kuipinga, wananchi huko nje wanakuona wa hovyo. Ndiyo maana wakaona watafute kisingizio cha hoja tu ya TBC, Waingereza wanasema ni red hearing, unatafuta hiyo ili usiwepo kwenye mjadala, maana ukiwepo, utasifia tu hii hotuba! Ndiyo shida hiyo! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawahakikishia Watanzania, hatujavunja sheria yoyote, Madaraka, Mamlaka ya Bunge, Kanuni za Bunge, hatujavunja. Mmoja alisema tumevunja Katiba ya Ibara ya 18. Sasa mimi ni Mwanasheria, Mwanakatiba. Ibara ya 18(d) inasema nini? “Kila mtu anayo haki kupewa taarifa.” Sawa, tunakubali. Inasema, “wakati wote.” Siyo wakati tu UKAWA wanapoongea ndipo kuna haki ya kupewa taarifa, no. Ni wakati wote! Ndiyo maana Waziri wetu wa Habari hapa ameipeleka kwenye prime time, usiku, Watanzania wengi waone. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri sisi Bunge tuna wajibu kuomba radhi Watanzania kwa fedha yao walipa kodi tunavyoichezea hapa. Tunatakiwa tufanye kazi, siyo mchezo mchezo huu! Hii radhi ya mdomo sasa hivi kwa kweli imepitwa na wakati! Naomba nisome Ibara ya 23; sisi ndio watunga sheria ni lazima tuonyeshe mfano.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ibara ya 23 (1) inasema, “Kila mtu bila kuwepo ubaguzi wa aina yoyote, anayo haki ya kupata ujira unaolingana na kazi yake.” Kama umekuja tu hapa kufanya fujo, hujapata pesa kihalali unayolipwa posho. Inabidi kiti chako sasa kiamue, watu ambao wamekuja hapa kufanya mzaha, wasivunje Katiba ya nchi. Huku ni kuvunja Katiba ya nchi, nakuomba sana! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kusema tu kwamba kuna watu wameongelea kuhusu vitu viwili hapa ambavyo vingine nitaviongelea wakati wa Mpango. Kuna suala la Mahakama Maalum ya Mafisadi. Naomba niwahakikishie Watanzania, Kiongozi wa Serikali wa awamu ya tano akitoa tamko, akitoa agizo, hilo lazima litekelezwe. Kwa hiyo, hivi sasa tumefikia hatua nzuri, tutawatangazia Watanzania kuhusu suala hilo ambalo amelitamka Mheshimiwa Rais na sisi tunalitekeleza. Hilo lazima waelewe. (Makofi)
Mheshimwia Naibu Spika, la pili, kuna wengine wamegusia kuhusu suala la Katiba Mpya, sasa sijui niseme nini zaidi ya kuwakumbusha Watanzania kwamba kwanza Watanzania wakumbuke, Rais wetu hajakaa mwaka mzima kama Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, huu ni mwezi wa pili tu na siku 23, hawezi kuyafanya yote katika kipindi cha miezi miwili na siku 23. Maana wengine wanamwangalia hata Waziri Mkuu hapa, inakuwa kama amekaa miezi tisa. Jamani ni miezi miwili tu na siku 23. Tuwaombee kwa Mungu, tuwasaidie kuweza kutimiza malengo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais alisema kwenye hotuba hii, “nimeachiwa kiporo, nitakitekeleza.” Hivi jamani leo hii tuanze kusema, kwanini asianze hiyo? Sasa ukianza hayo…
(Hapa kengele ililiia kuashiria kwisha kwa
muda wa Mzungumzaji)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Aah, kakengele nako haka! Basi tutakuja huko baadaye tutamalizia mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nashukuru kwa michango yote na ningeomba tu usikivu kwamba sijaja hapa kujibizana na mtu. Mimi sifanani kabisa na yule jamaa aliyekuwa anaoga, kichaa akaja akachukua nguo zake akaanza kumfukuza, kwa hiyo, mimi nabakia kwenye maji. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee namshukuru sana Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mheshimiwa George Masaju kwa kuungana na mimi katika kujibu baadhi ya hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge. Vilevile na kwa namna ya pekee kabisa niishukuru sana Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kwa maoni na ushauri wao kwa kweli uliokwenda shule. Maoni yote ya Waheshimiwa Wabunge na ya Kamati ya Kudumu ya Bunge tumeyachukua kama Wizara na tunaahidi kuyafanyia kazi na kuyatolea majibu kwa maandishi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa wengi wameongea na wengi wametuletea kwa maandishi hivyo nashindwa kupata idadi maana zinakuja karatasi mpaka sasa lakini kama nilivyosema majibu tutaleta kwa maandishi na muda nilionao ni mfupi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna baadhi ya hoja zimeletwa hapa chache nitazijibu kwa haraka haraka. Hoja ya kwanza ya Kamati ni kuhusu deni la mkataba wa ubia wa jengo la RITA. Naomba kusema kwamba mazungumzo tayari yanaendelea kati ya taasisi zinazohusika na ubia huu wa jengo la RITA. Lengo kuu ni kuhakikisha kwamba tunaishauri Serikali kulitwaa deni hilo na kupunguza ongezeko la deni linaloendelea katika mradi huu wa ujenzi huu wa jengo la RITA.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kifuate sheria za NACTE na walimu wawe na sifa za shahada na uzamifu za kufundishia vyuo vikuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto tukumbuke wote kilianzishwa mwaka 1988 kwa ajili ya kutoa mafunzo endelevu kwa Majaji, Mahakimu na watumishi wa Mahakama. Kwa kweli chuo hiki kimefuata miundo kabisa ya vyuo vingine vilivyopo Kenya, Afrika Kusini na Canada vinavyotoa ujuzi wa kuboresha utendaji wa Mahakama.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba tunaweza kufika huko lakini kwa sasa tumejikita na lengo la awali la kutoa mafunzo endelevu kwa Majaji na Mahakimu na watumishi wa Mahakama lakini baadaye kama hali kwa kweli ita-demand tuanze kutoa mpaka degrees tutafanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja ya kufanya mapitio ya kisheria kuhusu adhabu ya kifo ili tuifute hapa Tanzania. Naomba tu niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge kwamba utafiti uliofanyika mwaka 2009 na Tume ya Kurekebisha Sheria ulionyesha kuwa Watanzania wengi bado wanataka adhabu ya kifo iendelee. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wanasema hivi kutokana na vitendo vya kikatili na vya kutisha kama vile kuwakata viungo wenzao hasa kwa mfano ndugu zetu wenye ualibino, kuua vikongwe, kuua watoto wachanga na huko nyuma kulikuwepo na mchezo wa kuchunana ngozi. Kutokana na hayo, Watanzania wengi wanaamini kwamba kuendelea na adhabu hii ni tishio zuri, it is a deterrent ambayo hatuwezi kuachana nayo haraka haraka hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja kwamba Mahakama ihakikishe ufanisi na ufasaha katika umaliziaji wa mashauri kwa kuzingatia kuwa justice delayed, is justice denied na kwamba justice hurried is justice buried. Nakubaliana kabisa na Kamati kwamba katika kuharakisha sana kumaliza hizi kesi tunaweza kujikuta kweli tunakanyaga baadhi ya haki za watu. Naomba tu Waheshimiwa Wabunge tukubaliane kwamba tulikuwa na mzigo mkubwa sana wa kesi (backlog). Mimi naipongeza sana timu ya uongozi wa Mahakama ya sasa kwa kuhakikisha kwamba tunaondokana na huu mzigo wa kesi na baada ya mwaka mmoja au miwili tutarudi sasa kukazania kuhusu substance na quality ya judgements hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, niende haraka kuzungumzia kuhusu mchakato wa Mahakama ya Kadhi. Mheshimiwa Ahmed Juma Ngwali anasema mchakato wa kuanzisha Mahakama ya Kadhi umeishia wapi?
Mimi niombe tu kusisitiza kwa Mheshimiwa Ngwali kwamba kimsingi Mahakama ya Kadhi ipo na inafanya kazi. Serikali ilichotaka kukifanya katika Bunge la Kumi kwa wale tuliokuwepo hapa ni kuyapa nguvu ya kisheria maamuzi yanayotokana na Mahakama hiyo kupitia sheria ya Bunge. Mliokuwepo mnakumbuka kwamba katika Bunge la Kumi Serikali ilipowasilisha Muswada huo wa Mabadiliko ya Sheria ulikabiliwa na upinzani mkubwa siyo tu ndani hata nje ya Bunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, madai mengi yalikuwa kwamba hatukulifanyia hili suala kazi ya kutosha kuwahoji Watanzania wengi inavyostahili. Vilevile nje ya Bunge kulikuwa na mhemko mkubwa wa mawazo kiasi cha wananchi wawili kumfungulia Mwanasheria Mkuu wa Serikali kesi mbili. Alikuwepo, wote mnamkumbuka, Marehemu Mchungaji Christopher Mtikila alimfungulia kesi Mwanasheria Mkuu Mkuu wa Serikali kuhusu hili hili suala, kesi namba 7 ya mwaka 2015. Vilevile alikuwepo Shehe Rajabu Katimba na wenzake nao wakamfungulia kesi Mwanasheria Mkuu wa Serikali, tukalazimika kuliondoa suala hili Bungeni kwa lengo la kulifanyia kazi zaidi na suala hilo tayari tumelipokea rasmi kutoka Serikali ya Awamu ya Nne na sasa tunalifanyia kazi. Si suala jepesi maana lengo ni kupata muafaka wa Watanzania tuweze kuishi vizuri katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Ngwali vilevile naomba nichukue fursa hii kumshukuru sana kwa kunikumbusha kuhusu The Waqf Commission na vilevile Dkt. Suleiman naye alituongezea elimu yake kuhusu suala hili na sheria yenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa taarifa ni kwamba sheria hiyo haipo ila vipengele vyake vimekuwa incorporated kwenye Probate and Administration of Estate Act, Sura ya 352 na ukiangalia kifungu cha 142 kinaongelea kuhusu hiyo Waqf Commission. Namuomba Mheshimiwa Ngwali aniamini, nitalifuatilia. Nimekushukuru to bring it to my attention. Tuna sehemu ya kujifunza, wenzetu Zanzibar Sheria yao ya Waqf and Trust Commission inaweza kutoa mafunzo mazuri kwetu lakini kama nilivyosema nimelichukua hilo, nakushukuru sana kwa kunikumbusha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Profesa Anna Tibaijuka amelalamika sana kuhusu Mahakama Wilaya ya Muleba hasa za Mwanzo, zinajisahau kama ni Mahakama. Anasema Mahakimu wamekuwa kama machifu wadogo wadogo kule. Vilevile Mheshimiwa Dkt. Dalaly Peter Kafumu amelalamikia Mahakama za Mwanzo Wilayani Igunga kufikia mpaka kuwabambikizia wananchi kesi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme mawili, unapofikia mahali ambapo hujaridhika na uamuzi wa mahakama hizo za chini na ili tusiingilie uhuru wa mahakama, tafadhali Waheshimiwa Wabunge tuwatie moyo wale ambao wamesikitishwa wakate rufani. Siyo hivyo tu, nawaomba Waheshimiwa Wabunge tusiwe sehemu ya watu wanaolalamika, tuwe sehemu ya watu ambao wanasaidia kui-operationalise, kuitekeleza Sheria ya mwaka 2011 ambayo inaunda District Ethics Committees za watumishi wa mahakama. Kila Wilaya inatakiwa iwe na Kamati ya Wilaya ya Maadili ya Watumishi wa Mahakama. Sasa Wabunge tuhakikishe tunapofika Wilayani kwetu tumuulize Mkuu wa Wilaya kama tayari ameunda Kamati hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati hii itatusaidia sana kwa sababu Wajumbe wake ni Mkuu wa Wilaya ambaye anakuwa Mwenyekiti lakini wapo walioonesha kwamba ni tatizo kubwa hilo kwa Wakuu wa Wilaya kuwemo humo. Tulilijadili vizuri hapa, litakwenda vizuri kama Waheshimiwa Wabunge mtasaidia katika kuhamasisha hizi Kamati ziundwe haraka na tuweze kurejesha nidhamu hasa kwenye Mahakama zetu za chini. Mbali na Mkuu wa Wilaya tunaye DAS pale ndiye anakuwa Katibu. Mkuu wa Wilaya anateua Wajumbe wawili mmoja kiongozi wa dini anayeheshimika anaweza kuwa muislamu au mkristo na mtu wa pili atakuwa ni mzee mwenye heshima katika jamii ambaye kila mtu ukisema ameteuliwa wanasema sawa kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Jaji Mfawidhi katika eneo husika atateua wajumbe wawili ambao ni Wanasheria, wanaweza kuwa Mahakimu na Hakimu wa Wilaya vilevile anakuwa ni sehemu ya hiyo Kamati. Kwa hiyo, madudududu kama hayo yapelekwe moja kwa moja kwenye hiyo Kamati. Hiyo Kamati haina mamlaka ya mwisho itapeleka mapendekezo yake kwenye Judicial Service Commission ambacho ni chombo cha kikatiba. Ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge tukifanya vizuri hapa, tunaweze tukaleta mabadiliko makubwa sana badala ya sisi kuwa tunalalamika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa George Lubeleje ameongelea uhitaji wa miundombinu ya Mahakama katika Wilaya ya Mpwapwa. Mheshimiwa Omary ameongelea Wilaya ya Kilindi, nafikiri wengi wameongelea suala hili.
Waheshimiwa Wabunge, katika hotuba yangu nimeeleza kuwa tuna tatizo kubwa la miundombinu ya mahakama. Kama nilivyosema, the ideal situation tulitakiwa tuwe na mahakama zinazofanana angalau na kata tulizonazo maana tunaamini kuwa proper access to justice nchini kwetu inahitaji mahakama moja katika kila kata. Tuna kata 3,957 lakini tuna Mahakama za Mwanzo 976 tu!
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi naupongeza sana uongozi wa Mahakama chini ya Jaji Mkuu Othman Chande na Mtendaji Mkuu Katanga kwa kazi nzuri ambayo wameifanya katika kipindi kifupi sana kwa kuanza kampeni ya ujenzi wa Mahakama za Mwanzo za Wilaya na kwa kweli hata Mahakama Kuu, hata jengo la Mahakama ya Rufani hatuna. Kwa hiyo, tulikuwa tumelala kidogo kipindi kirefu sasa hivi ndiyo tumeamka na hawa watu wanahitaji kutiwa moyo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameliezea vizuri sana suala alilokuwa analalamikia mdogo wangu Mheshimiwa Tundu Lissu hapa kuhusu instrument ya mpangilio wa kazi za Mawaziri. Kaeleza vizuri kwamba mbona instrument ilishatoka? Tt the same time, it is not such a big deal mpaka Mheshimiwa Tundu Lissu unasahau kwamba sisi ni kaka zako, tumekusomesha sisi mpaka unaongea maneno mazito kutuita wajinga lakini sasa walimu wako wakiwa wajinga wewe unafikiri utakuwa nani? You could even be worse than that. Kwa sababu sisi kwenye Wizara bahati mbaya ni kaka zako. Niko na Profesa Mchome pale, ni mwalimu wako. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Rais anapoteua Mawaziri anatumia Katiba, Ibara ya 55. Akishamteua Waziri kuna condition moja tu inakuwa imebaki ili Waziri aweze kufanya kazi siyo lazima iwepo instrument! Ibara ya 56 inasema; ―Waziri au Naibu Waziri hatashika madaraka yake ila mpaka awe ameapa kwanza mbele ya Rais Kiapo cha Uaminifu na pia kiapo kingine chochote kinachohusika na utendaji wa kazi yake kinachowekwa kwa mujibu wa sheria inayotungwa na Bunge.‖
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna instrument hapa ili uwe Waziri! Rais anaweza akaacha hata akakaa miaka mitatu bila instrument lakini Serikali ikaenda. Maana tumefika mahali pa kuona kuwa hata Waziri Mkuu alikuwa anafanya kazi bila uhalalai, hapana! Tusome vizuri Katiba Ibara ya 52 imempa kazi ya kufanya Waziri Mkuu. Inasema; ―Waziri Mkuu atakuwa na madaraka juu ya udhibiti, usimamiaji, utekelezaji wa siku hata siku wa kazi na shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano.‖
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kusema tu kwamba tusilitie chumvi sana hoja hii, tukafika mahali kusema kwamba tulikuwa tumepotea, hapana! Hii ni Serikali ya Awamu ya Tano, Rais anafanya mabadiliko makubwa katika mfumo wa Serikali ilibidi tumpe muda kuweza ku-come-up na hiyo instrument ambayo tayari alishaitoa. Watanzania bahati nzuri mimi nafurahi kwamba wame-appreciate kazi anayoifanya ni kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Kakunda yeye anadai ameachia Ofisi ya Mbunge Sikonge ili iwe ya Mahakama. Dah! Sasa hapa ni kazi kwa sababu siyo kila ofisi inaweza ikatosha kuwa Mahakama na Ofisi ya Mahakimu. Mimi nashukuru tu kwamba umetupa hiyo ofisi, kwa heshima na taadhima tutafika kuiangalia. Nitaongea na Mtendaji Mkuu wa Mahakama aangalie kama miundombinu ya kuweza kufanya hiyo kazi ipo. Cha msingi ni kwamba Sikonge tumeiweka kwenye orodha ya Wilaya ambazo tutazijengea Mahakama, uwe na subira tu, usiende haraka sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Sheria ya Manunuzi, Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali nakushukuru sana umelijibu, umelimaliza suala hili. Haikuwa kazi rahisi Waheshimiwa Wabunge kuipitia sheria hii. Wengi wanaisema tu hawajawahi kuiona wala kuosoma. Mimi ningesema nipitishe mtihani hapa, sitaki kusema! Maana hii sheria ina vifungu 108, ina majedwali makubwa matatu na ina Kanuni zake 380 na majedwali ya Kanuni 19.
Watanzania hatupendi kusoma tunakimbilia tu magazeti ya Tanzania Daima na kadhalika, lakini hii document iko hivyo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, muda wangu ni mfupi sana, Mheshimiwa Koshuma naye ameongelea kuhusu Sheria ya Ndoa. Tulishasema hili suala Serikali imelipa kipaumbele sana. Katika Mkutano huu huu nilishasema, hata hivi juzi nilisema tutaleta mapendekezo ya kubadilisha Sheria ya Elimu ili mtoto yeyote ambaye yuko shule ya msingi na sekondari ni marufuku kuoa au kuolewa na ni marufuku kupata mimba! Sasa hiyo marufuku tutaisimamia namna ya kuifanya, tutaileta hapa ninyi wenyewe ndiyo wazazi mtaona hiyo marufuku ya kupata mimba tutaifanyafanyaje. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa anasema kwamba eti Serikali inashindwa kesi nyingi sana! Unachosema una uhakika nacho? Unajua hili Bunge linahitaji facts. Mimi sasa nafikiri nitakuja hapa niwaeleze jinsi ambavyo vijana wetu wanavyofanya kazi nzuri na ya ajabu sana katika mazingira magumu sana. Tuna Ofisi ya Mwendesha Mashtaka, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wanafanya kazi kubwa sana under extremely difficult conditions lakini wanashinda kesi dhidi ya matajiri, watu wenye kesi kubwa na Mawakili wanaolipwa sana, vijana wetu hata nyumba za kukaa hawana. Kwa hiyo, tusiwakatishe tamaa vijana wetu, kazi wanayoifanya ni kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie tu haraka haraka mambo mawili, matatu. La kwanza, Mheshimiwa Tundu Lissu alikuwa anauliza hivi Jaji Mkuu atastaafu lini? Mimi namwomba mdogo wangu awe anasomasoma hii Katiba kwani Ibara ya 120 ina majibu, sikutegemea wewe uulize swali hilo.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Ana umri gani? Jibu lipo hapa kwenye Ibara ya 120(2) ambayo inasema kwamba; ―Jaji yeyote wa Rufani aweza kustaafu Ujaji wa Rufani wakati wowote baada ya kutimiza umri wa miaka sitini, isipokuwa kama Rais ataagiza kwamba asistaafu, na iwapo Rais ataagiza hivyo basi, huyo Jaji wa Rufani atakayehusika na maagizo hayo ya Rais hatakuwa na haki ya kustaafu mpaka upite kwanza muda wowote utakaotajwa na Rais kwa ajili hiyo.‖ (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Ibara ya 120(3) inaendelea kusema kwamba; ―Iwapo Rais ataona kuwa kwa ajili ya manufaa ya umma inafaa Jaji wa Rufani aliyetimiza umri wa miaka sitini na tano aendelee kufanya kazi, na Jaji huyo wa Rufani anakubali kwa maandishi kuendelea kufanya kazi, basi Rais aweza kuagiza kwamba...
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, unaweza ukafika miaka sabini na zaidi, yote iko ndani ya Katiba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo mengi mazito yameongelewa hapa. Mheshimiwa Maige anasema Jimboni kwake kuna majengo mazuri ya mahakama lakini hakuna Hakimu. Hili nalisikia na Ndugu yangu Katanga akisikia hivyo atashtuka sana kwamba kuna majengo mazuri Jimboni kwa Maige lakini hakuna Hakimu, tutalifuatilia hili kwa karibu sana tena sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mbunge wa Ulanga, Bwana Mdogo Mheshimiwa Goodluck Mlinga anasema kwake hakuna miundombinu ya Mahakama. Umenishtua sana, sisi hatupendi kusikia kitu kama hicho kwamba Wilaya ipo lakini hakuna kabisa miundombinu. Nitakaa na ndugu zangu upande wa Mahakama tuweze kutembelea Jimbo lako na mimi nakuhakikishia kuwa kama hali ni mbaya kiasi hicho hatuwezi kuliacha Jimbo lako la Ulanga kwenye mpango wa miaka mitano wa ujenzi wa Mahakama za Wilaya na Mahakama za Mwanzo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli nimeelewa masuala aliyoyalalamikia Mheshimiwa Augustine Holle ya sheria za kazi na hali ya migodini. Wakati wataalam wa Tume ya Kurekebisha Sheria bado wako hapa, hata kesho tunaweza tukapata muda kukusikiliza ulete yote unayofikiria ni muhimu tuyaangalie.
Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mengi hapa yameongelewa, pengine niongelee la mwisho la Mheshimiwa Tindu Lissu kuhusu kuanzishwa Mahakama ya Mafisadi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa na Mahakama ya Wahujumu Uchumi, ni kweli. Tulivyoanza, pengine huwezi kukumbuka ulikuwa bado mdogo pengine shule ya msingi, tulipoanza na hiyo Mahakama it was a non-starter kwa sababu it was a tribunal nje ya mfumo rasmi wa Mahakama. Kwa hiyo, hiyo tribunal sisi tukiwa university tuliipinga sana na ilibidi sasa ibadilishwe tena ikawa appeal zinakwenda kwa Rais. Sasa hiyo ndiyo ikawa mbaya zaidi na ikashindikana, ndipo marekebisho yakaja kwamba High Court yenyewe inaweza ikasikiliza hizo economic crimes cases. Kwa taarifa tu ni kwamba kuanzia mwaka 2011 mpaka leo mimi sijaona kesi pale, wewe mwenyewe ni Wakili hujaona Mahakama Kuu ikisikiliza kesi za namna hiyo kama Mahakama ya Uhujumu Uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, lengo kubwa hapa ni kurekebisha hitilafu tulizokuwanazo katika msururu wa sheria zetu hizi tuje na kitu kizuri zaidi, tutakileta mbele yenu hapa si muda mrefu. Atakayeileta hapa ni yule yule Mwanasheria wetu Mkuu mahiri George Masaju ambaye mimi nimekaa naye muda mrefu na mimi nawaambia hii ndiyo kamusi ya weledi upande wa sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja ya Rais kuonekana ni dikteta! Mimi imenishangaza sana! Maneno yanayoongelewa hayafai, eti Mawaziri wanaogopa, Rais hashauriwi! Jamani!
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu dakika mbili hizi nimalizie, unajua hii mimi inanikumbusha kuhusu mchezo wa mpira. Ukienda kuangalia watu wanaangalia screen inacheza timu nzito kama Barcelona na Manchester, utaona sasa pale wanaoangalia wanajua zaidi mpira kuliko wanaocheza! Unamsikia mtu anasema aah Messi angedokoa tu pale kidogo kwa kisigino, wewe! Ukimwangalia mtu mwenyewe pengine ana miguu yote ya kushoto utadokoa vipi mpira pale? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna hilo tatizo hapa! Tunajua zaidi kupita watu ambao wako jikoni! Sisi tuna uzoefu wa kuendesha Serikali. Unapomwona Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ametoa directive, hiyo directive imetolewa na presidency! Sisi kama Mawaziri, we are part of that presidency. Haiwezekani leo Rais amesema twende kushoto unafikiri ameamua mwenyewe? Ana cabinet yake ni sisi tuko sehemu yake. Kwa hiyo, siyo uwoga ndiyo utaratibu wa kuendesha Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Ndugu zangu mnajua mambo yalikuwa hayaendi vizuri sana, Rais amejitahidi kwa kweli kurekebisha mambo mengi sana. Amejitoa sana kiongozi wetu, kafanya mambo mengi ambayo hayajapata kutokea na dunia nzima inamuimba leo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano kuondoa pesa za sherehe akanunulia vitanda Muhimbili ni udikteta? Kuondoa fedha za sherehe akajenga barabara ni udikteta? Ndugu zangu itakuwa tunayoongea hapa ni tofauti kabisa na thinking ya public huko nje. Hicho kitu kinampa Mheshimiwa Rais comfort kubwa ndani ya moyo kwa sababu wananchi wanachokisema kinamtia moyo sana. Sisi wenyewe hapa tulikuwa tunalalamika ooh, uongozi huu legelege, dhaifu, limekuja tingatinga, malalamiko tena eee, nini tena? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikia kengele ikilia, kwa mara nyingine tena mimi nakushukuru wewe binafsi kwa kutuongoza vyema katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria. Nawashukuru pia Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia katika mjadala huu…
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunaongea halafu kuna vichaa humu ndani wanaongeaongea...
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunaongea halafu kuna vichaa humu ndani wanaongeaongea...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Halima Mdee, tafadhali.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mimi nashindwa kuelewa sijui wanakula yale majani yale, sielewi?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi napenda tu kurudia kuahidi kwamba maoni na ushauri ambao Waheshimiwa Wabunge mmeutoa tuta-compile na tutawaletea majibu yake yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru sana kwa kuruhusu niletewe maji hapa juu ya meza kwa sababu nakohoa sana. Nisingesema haya, najua ningepigwa Mwongozo sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuunga mkono hoja na vilevile kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kuwasilisha hotuba yao kwa ufasaha mkubwa. Niongelee kwa kifupi sana kilio cha maslahi ya wasanii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kuingilia maudhui ya mashauri ambayo yako mahakamani sasa hivi, mimi naona mabadiliko makubwa sana na ya kutia moyo katika mentality ya vijana wetu sasa hivi. Vijana wetu sasa hivi wanathubutu, wanakwenda mahakamani, wanaachana na tabia iliyoanza kujengeka hapa ya kutunga ngonjera za kulalamika tu, ni kulalamika na kutegemea kila kitu wafanyiwe na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetunga Sheria ya Hatimiliki mwaka 1999. Nashukuru Mungu kwamba mimi nilihusika kama mtaalam, nilihusika kuiunda COSOTA vilevile; na nilikuwa Mjumbe wa kwanza wa COSOTA; na vilevile nilihusika kuanzisha kozi ya Intellectual Property Law, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na yote hii ni kutetea wasanii wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi hicho tulikuwa tunabezwa, kwamba aah, alinacha hiyo. Wengine waliotubeza walikuwa wasanii, lakini walikuwa hawaelewi. Vilevile tuliungwa mkono na nguli wa muziki kama akina Hamza Kalala, akina King Kiki (Kikumbi Mwanza) na leo jioni tuko naye na kitambaa cheupe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachosema tu ni kwamba nafurahi vijana wanapokwenda mahakamani to battle for their rights. Sheria hatutungi ziwekwe kabatini, zinatungwa ziweze kutumika na vijana na hii inatufurahisha. Hata mwanasayansi nguli, Newton aliwahi kusema; “an object at rest will always remain at rest unless acted upon.” Kwa hiyo, vijana tayari tumewawekea mazingira, tuna sheria. Ile sheria ni nzuri tu, piganieni haki zenu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimkumbushe pia Mheshimiwa Ahmed Ngwali, ameongelea kidogo kuhusu sheria moja kwenye michezo, kwamba Waziri unafanya nini? Hapana! Mheshimiwa Ngwali, basi wewe hujaelewa unafanya nini hapa. Siyo kazi ya Waziri wa Katiba na Sheria kuzunguka nchi nzima kusema sheria hii inawafaa au la! Ni stakeholders. Ni ninyi wenyewe mnaotumia sheria hiyo kusema sheria hii sasa imepitwa na muda; kama ulivyofanya sasa hivi, na wewe ni Mbunge, ilete Bungeni. Sio Waziri wa Sheria aende Ibadakuli, aende sijui Mtwara aulize hii sheria inawafaa au laa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu nigusie haraka haraka sana kwa sababu muda wenyewe ni mdogo, mambo mawili matatu ambayo yameongelewa na Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni. Ukisoma hotuba yake ukurasa wa pili, wa tatu na wa nne Mheshimiwa Mbilinyi anaonesha kuamini kabisa kuwa uhuru wa kutafuta, kupata na kusambaza habari ni absolute, ni uhuru unaotakiwa usiwe na mipaka kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mipaka yoyote ikionekana kwenye tasnia hii, basi huo ni udikteta. Hapana Mheshimiwa, hapana kabisa. Katika dunia hii, hakuna uhuru wala haki isiyo na mipaka. Sijawahi kuona. Hakuna nchi iliyofungulia milango kila kitu. Kama nchi hiyo ipo, nakuhakikishia Mheshimiwa Waziri Kivuli, mimi nitachangisha fedha tukuhamishie huko. Hakuna! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba usome tu Ibara moja maarufu inaitwa Artcle 19. Waandishi wa Habari wote wanaifahamu. Kwasababu, Article 19 ambayo iko kwenye Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa, ndiyo inayoweka msingi wa haki hiyo Kikatiba duniani kote. Ilipitishwa na Umoja wa Mataifa. Article 19 loh, sasa sijui utaniruhusu Mheshimiwa nisome…
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Nimemwomba Mwenyekiti, siyo ninyi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Article 19 inasema: “Everyone shall have the right to freedom of expression. This right shall include freedom to seek, receive and impart information and the ideas of all kinds” bila kuingiliwa. Unahakikishiwa kupata habari, usiingiliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini article hiyo hiyo inakuja kwenye clause (3); “The exercise of the rights provided for in paragraph two above, carries with it special duties and responsibilities,” yaani wajibu na majukumu maalum. Hupewi tu haki na kuachiwa nenda kaogelee. Hilo tulikubali dunia nzima. It may therefore be subject to certain restrictions, yaani masharti maalum. But these shall only be such as are provided by law; na sisi kama tulivyofanya Tanzania, tume-provide by law for respect of the rights or reputation of others;” kwa heshima ya watu wengine na haki za watu wengine. Vilevile inasema kwa kulinda usalama wa Taifa lako mwenyewe. Kwa hiyo, hakuna uhuru usio na mipaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona wengi hapa wanatoa mifano ya nchi nyingi zenye uhuru usio na mipaka, wa ajabu sana. Marekani ndiyo inasemekana kwamba ina uhuru usio na mipaka, hapana. Marekani pia ina-enjoy privileges chini ya Article 19, lakini vilevile Marekani ni nchi ambayo ime-retain Sheria mbovu kweli kweli za kubana vyombo vya habari kwa miaka zaidi ya 239. Sheria zenyewe ni kwanza Press Law/Press Code yao ni Cap. 115 kitu kama hicho. Vile vile wana Sheria ya Alien and Sedition Act iliyotungwa mwaka 1789. Wewe andika kitu ambacho kina-threaten stability ya Marekani, halafu uje usimulie kuhusu uhuru huo wa Marekani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka tu niseme kwamba Mheshimiwa Waziri Kivuli kwa kweli ameichora kwenye hotuba yake hii nchi yetu kama ni ya kidikiteta hivi; mimi nauliza tu Mheshimiwa Waziri Kivuli, hii nchi ingekuwa ya kidikiteta, ungeweza kweli ukafyatuka jinsi unavyofyatuka hapa? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Waziri Kivuli amenukuu tafiti nyingi sana, lakini mimi nafahamu kwa watu wengi ambao wako katika hii tasnia kuna reliable data. Kwa mfano, Press Freedom Index ambayo inachangiwa na taasisi nyingi za Kimataifa. Ile press index, mimi nimeangalia mwaka 2014, 2015 na 2016, inatoka kila mwaka, imetaja nchi 20 duniani ambazo zina hali mbaya ya vyombo vya habari na utoaji haki kwa wanahabari, Tanzania haimo. Imetoa orodha ya nchi kumi ambazo hali ni mbaya kupita kiasi, Tanzania haimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo madai ya kwamba kuna ukiukwaji wa Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninayo hapa, hii ni kutokana na uamuzi wa Bunge kuwa na studio yake na kurusha matangazo pale. Mimi naomba kwa haraka tu nisome Ibara ya 18. Inasema: “Kila mtu:-
(b) anayo haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila ya kujali mipaka ya nchi.” Imeiga kabisa ile Article 19!
“(d) anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu ya jamii.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapewa haki ya kutafuta, kupokea, kusambaza habari hapa, kusambaza taarifa, lakini Katiba hii haisemi hizo habari lazima ziwe live. Sijaiona hapa! (Makofi/Kicheko)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA:Mheshimiwa Mwenyekiti, naongea kama mwanasheria, naomba… (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba…
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiendelea na tabia hii, hili siyo Bunge tena! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiendelea hivi hili siyo Bunge tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma Ibara ya 18; there is no canon of constitutional interpretation itakuletea neno live hapa. Ninachosema, tusichanganye vitu viwili hapa, matakwa ya Kikatiba na matakwa ya kisiasa, ambayo yote ni muhimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu anakuja anasimama hapa anasema wananchi wanataka live. Wewe unawafikiria wananchi wapi? Wanaocheza pool ama wakulima ambao ni asilimia 80 ya Watanzania ambao asubuhi wanakuwa mashambani? Unaposema wananchi wanataka wakuone saa 4.00… (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaniongezea muda mrefu tu, kwa sababu huu upuuzi, siwezi…
(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila mpangilio)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakimaliza kuongea, naomba uniambie niendelee.
MWENYEKITI: Naomba uendelee Mheshimiwa. Mheshimiwa naomba uendelee, jamani tufanye ndani ya muda…
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Meshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Dakika tano, nafikiri umeziona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unaposema wananchi wanataka live, wananchi ambao leo ndiyo Taifa la leo na kesho ni wanafunzi wako vyuo vikuu, sekondari, wako darasani saa hizo!
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii the most popular program katika televisheni ni taarifa za habari. Taarifa za habari zote duniani ni mixture ya live na recorded programs. Nafikiri Bunge letu nalo limeiga huko huko, ni mixture ya live na recorded programs. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namheshimu sana Mheshimiwa Devotha, alisema Mheshimiwa Waziri wa Habari alisema gharama ya live ni shilingi bilioni nne; hakusema kweli, kwani gharama ni shilingi bilioni mbili tu! Nikasema ehee ehee ehee, jamani! Serikali ya Awamu ya Tano, hata senti tano, it matters to us. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, shilingi bilioni mbili hizo, zitajenga matundu mangapi ya choo? Zitajenga shule ngapi? Zitajenga barabara ngapi? Leo kwa sababu ya mahitaji ya kisiasa uonekane live. Tena mimi namshukuru Mungu, nasema kwa aibu inayotokea hapa, mizozo mizozo isiyo ya msingi, ingekuwa live hapa, wengi wasingerudi hapa. (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Nkamia. Anasema jamani sisi ni Wabunge, let us think outside the box. Ametuletea mifano ya BBC, ametuongelea kuhusu masuala ya tv license yanayoifanya BBC iendelee, siyo hii TBC yetu ambayo inalia njaa na bajeti yake wenyewe mnalalamikia hapa. Hiyo ndiyo kazi yetu sisi kama Wabunge, siyo kudai tu kama watoto wadogo, nataka uji, nataka uji, uji umeutolea hela?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Tunaambiwa, live imezuiwa kwa sababu CCM wanaogopa madudu, jamani… (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, let us be fair to ourselves. Mimi nadhani hata kukatisha hizi live programs tumewapendelea sana Upinzani.
(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila mpangilio)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ingekuwa kila siku wananchi wanayasikia mambo ambayo Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Dkt. Pombe Magufuli inayofanya mambo makubwa nchi hii, upinzani hawana nafasi kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kelele hizi za yeehee, yeehee, yote ni kukosa hoja. Kwa hiyo, ni kupiga kelele tu kama watoto wadogo.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Nape Nnauye na mwenzako, mmetoa bajeti nzuri, tutawalinda na tutaipitisha! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipa fursa niweze kuchangia. Naomba nianze kwa kuunga mkono hoja na vilevile kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na uongozi wa Wizara kwa hotuba nzuri ya bajeti ya Wizara yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo mawili, matatu niongee kwa haraka haraka. Nianze na mchango wa Mheshimiwa Naghenjwa Livingstone Kaboyoka ambao ni mchango mzuri. Sisi kama Serikali tunaheshimu sana constructive criticism. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ameongelea kuhusu Wabunge wa EALA kwamba hawana ofisi. Nataka kusisitiza tu kwamba tofauti na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki sisi ndiyo wenyeji, sisi ndiyo tume-provide headquarters ya EAC. Kwa hiyo, kiti chetu sisi kiko Arusha, ndiyo sehemu kuu ya East African Community na pale Wabunge wote wana ofisi zao. Tulitaka Wabunge wa EALA wawe na ofisi Dodoma sijui wakifanya nini, wawe na ofisi Dar es Salaam wakifanya nini? La msingi tukubaliane kwamba tuimarishe ofisi zao za Arusha waweze kukaa pale kwa ajili ya kufanya research zao na kutuwakilisha vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, niongelee kuhusu mchango wa Mheshimiwa Hamidu Hassan Bobali kuwa Kenya na wenzetu wana Wizara mahsusi kwa ajili ya Afrika Mashariki. Nafikiri hapa tuongozwe na Treaty. Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ukiangalia Ibara ya 8(3)(a) inasema kwamba:-
“Each partner state shall designate a Ministry for East African affairs”.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ita-designate ina maana ita-appoint (itateua). Haisemi kwamba itakuwa na a Ministry exclusive for East African affairs. Hata ukiangalia Article 13(a), inahusu chombo cha juu cha maamuzi cha community, The Council of Ministers, kinasema:-
“The Council shall consist of the Minister responsible for East African Community affairs. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni Wizara ambayo imekuwa designated, ni Wizara imekuwa entrusted kubeba masuala ya East Africa. Hata Serikali ya Kenya walivyoanza chini ya Mheshimiwa Rais Kenyatta walikuwa na Wizara ya Biashara, Utalii na Jumuiya ya Afrika Mashariki na mimi wakati huo nilikuwa East Africa na juzi tu wamebadilisha sasa ni Wizara ya Kazi na Jumuiya ya Afrika Mashariki. Unaangalia mwenyewe strategic interests za nchi yako ufanyeje! Hata unaweza kuamua kuwa na Wizara ya Ulinzi na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa sababu hili ni suala tu ku-entrust Wizara yeyote iweze kui-house hiyo community. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine ambalo napenda niliongelee kidogo, ni hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani ukurasa wa sita na wa saba. Kama nilivyosema sisi tunaheshimu sana constructive criticism, hatuna tatizo kwa uhuru walionao, wameongea haya, lakini lazima tuweke record sawasawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, anasema kwamba amefanya uchunguzi ambao unaonesha kuwa chini ya Serikali ya CCM Ubalozi unatolewa kama zawadi kwa Makada walioisaidia kwenye kampeni, kwa Makada wa CCM wasiojua kitu kuhusu diplomasia ya uchumi ndiyo wanaokabidhiwa dhamana ya kuhakikisha Tanzania ifanikiwe kimataifa, wengi wao wangeweza kuwa Mabalozi wazuri sana wa nyumba kumi kumi lakini siyo kuwa Mabalozi wa nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliona kwamba hili tuliweke vizuri tu, naomba nisisitize kwamba tangu uhuru, viongozi wetu wamejitahidi sana kuwa waangalifu kuteua wanaotuwakilisha nje ya nchi. Ushahidi upo kwamba Mabalozi wetu wanapokuwa nje huko, Jumuiya ya Kimataifa inawaona, inawapa majukumu makubwa zaidi na siyo juzi tu, tumeanza toka kipindi cha Mwalimu Nyerere. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wengine wadogo hapa ngoja niwakumbushe. Tulikuwa na Kada wa CCM, Mzee Daudi Mwakawago alikuwa Katibu Mtendaji wa CCM, akapewa Ubalozi. Cha msingi hapa jamani ni kitabu, jamaa alikuwa amepiga kitabu vizuri hadi Kofi Annan akamuona pamoja na Ubalozi wake akamteua kuwa Mwakilishi wa Kofi Annan Sierra Leone na Mkuu wa UN Mission kule. Yote haya yanaonesha kuwa kitabu ndiyo kitu cha kwanza kinachotuongoza sisi kuteua Mabalozi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yupo Balozi James Kateka kama mmewahi kumsikia, ni judge wa International Tribunal for the Law of the Sea huko Humburg. Yeye ndiyo Mtanzania wa kwanza kuingia International Law Commission amekaa kule 10 years. Huwezi ukasema ana-qualification za nyumba kumi kumi.
Balozi Dkt. Asha Rose Migiro, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Nitolee mfano wa Balozi mmoja ambaye hafai.
Mimi naomba Wapinzani muwe wavumilivu! Ninyi mkisema sisi tunakaa kimya, mbona utamaduni huo hamna? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Balozi Profesa Costa Ricky Mahalu, mimi naenda kufanya Uzanifu Ujerumani nimemkuta anawafundisha Wajerumani pale international law. Hawa ndiyo Mabalozi wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Balozi Kagasheki alikuwa hapa hapa, nimemkuta mimi Geneva akiwa Deputy Secretary General wa World Intellectual Property Organization. Tunajua kuteua watu! Balozi Dkt. Agustine Mahiga jamani huyo ana-record iliyotukuka, ameshakuwa Rais wa Baraza la Umoja wa Mataifa. Bila shule huwezi kuwa Rais UN utajiminyaminya tu midomo tu hovyo! Ameshakuwa mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Somalia na amefanya kazi iliyotukuka kule. Hawa ndiyo Mabalozi wetu wanaoteuliwa na Serikali ya CCM. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Balozi Getrude Mongela, Spika wa Bunge la Afrika; Balozi Juma Mwapachu, Katibu Mkuu EAC; Balozi Ally Mchumo, Mkurugenzi Mtendaji Mfuko wa Pamoja wa Mazao Brussels na wengine wengi wenye sifa nyingi. Wengine wana sifa zilizotukuka, mchukulie Balozi Ally Hassan Mwinyi nimuelezee nini? Balozi Salim Ahmed Salim nimuelezee nini? Balozi Benjamin Mkapa, naona niishie tu hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema taarifa ya Kambi ya Upinzani imejitahidi kwa kurasa nyingi kutuchora kama Serikali isiyo serious, non serious government! Wakisikia wanachama wa East Africa kwamba tunaitwa Serikali isiyo serious watashangaa kweli kweli kwa sababu sisi tumekuwa critical na ndiyo sababu Rais aliyepita Mheshimiwa Kikwete amekuwa Mwenyekiti kwa mwaka mzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Uenyekiti tunaenda kwa rotation basis lakini haikuwa accident alipoingia Rais mpya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli viongozi wa East Africa wakasema mzee tunaomba uendelee wewe mwenyewe kuwa Mwenyekiti, it is unprecedented! Ni kwa sababu we have a critical role katika Jumuiya ya Afrika ya Mashariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kifupi sisi tumefanya mambo mengi East Africa. Niwakumbushe machache tu, sisi ndiyo tumesimamia mchakato mzima wa admission ya South Sudan tukiwa Wenyekiti wa Jumuiya na mimi wakati huo nikiwa Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki. Siku hiyo tumekesha mpaka saa tisa kuweza kutengeneza proposal kwenda Summit kwa ajili ya admission ya South Sudan. East Africa inatambua mchango wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Mungu kampa macho makini Mheshimiwa Rais kwa kugundua nyota ya Tanzania na kumfanya Waziri wa hii Wizara Mheshimiwa Dkt. Mahiga, he is a jewel, lazima tujivunie hapa. Sisi Watanzania tumesimamia mchakato wa kuishawishi Serikali ya Marekani kurefusha ule mpango wa AGOA wa kuuza bidhaa kwenye soko la Marekani bila kulipia ushuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niliongoza ile delegation ya Mawaziri wa East Africa tumekwenda Marekani ku-negotiate na Serikali ya Marekani na interests za Tanzania zilikuwa mbele sana. Lengo letu kubwa lilikuwa ni kwamba tuki-extend AGOA Watanzania tu-play a much more meaningful role katika biashara hiyo. Ndiyo maana tukaishia ku-sign the Cooperation Agreement on Trade Facilitation, Sanitary and Phytosanitary Measures and Technical Barriers to Trade.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkataba utatusaidia zaidi Tanzania kuliko nchi nyingine, tuliweza kuwa-convice wenzetu kwa sababu sisi Tanzania kinachotuangusha sana ni packaging, umaliziaji wa bidhaa zetu hivyo hatuwezi ku-penetrate kwenye masoko makubwa. Wenzetu Kenya sasa hivi wamechukua mpaka biashara zetu kwa sababu wao hata vitunguu wanajua namna ya kuvikata, kuvihifadhi na kukidhi zile sanitary measures na kuweza kupeleka kwenye masoko ya nje. Chini ya mkataba huu, Wamarekani wamekubali ku-extend hiyo technical service kwetu hapa na sasa hivi tumeongea na Mheshimiwa Waziri wa Biashara amelivalia njuga suala hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudie kusema naunga mkono hoja na namtakia Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kazi njema katika kuijenga nchi yetu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuishukuruKamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa ushauri na mapendekezo yake yanayolenga kuimarisha utendaji wa Wizara yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, aidha, namshukuru Waziri Kivuli na Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Joseph Osmond Mbilinyi na Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia katika hotuba yangu kwa kauli na maandishi. Natambua kuwa Waziri Kivuli tuliyenaye safari hii ni mdau mkubwa wa sekta ya sanaa nchini hususani tasnia ya muziki, hivyo, maendeleo ya sekta hii yanamgusa moja kwa moja kiasi ambacho hata jina la Wizara yangu ameligeuza kwenye hotuba yake yote, badala ya kuita Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo anaiita Wizara ya Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, nafikiri anajifikiria mwenyewe. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema kuwa Wizara yangu inaupokea ushauri wote uliotolewa hapa na itauzingatia katika utekelezaji wa bajeti yake ya mwaka 2017/ 2018. Hotuba yangu imechangiwa na jumla ya Waheshimiwa Wabunge 67 ambapo waliochangia kwa maandishi ni 30 na kwa kauli ni 37.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri sana aliyofanya Naibu Waziri, Mheshimiwa Anastazia Wambura ya kuzitolea ufafanuzi baadhi ya hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge bado naamini kuwa muda nilionao ni mfupi sana sitaweza kuzitolea ufafanuzi hoja zote. Hivyo, naahidi kuzitolea ufafanuzi kwa maandishi na nitahakikisha kila Mheshimiwa Mbunge anapata nakala yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na baadhi ya hoja za Kambi Rasmi ya Upinzani. Kwanza Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani ukurasa wa tatu na wa nne wa hotuba yake anaeleza kuwa katika suaa la ulinzi wa uhuru wa habari, Tanzania tumepoteza sifa kabisa katika medani za Kimataifa na hivyo tuko kwenye orodha ya nchi zinazokandamiza uhuru wa habari duniani. Ushahidi wake ni utafii uliofanywa na Reporters Without Borders ambao amedai Mheshimiwa Waziri Kivuli kuwa umeiweka Tanzania nafasi ya 122 kati ya nchi 198 duniani zilizofanyiwa utafiti kuhusu uhuru wa habari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeisoma taarifa hiyo ya utafiti kwa makini (Press Freedom Index) inayoandaliwa kila mwaka, lakini mimi nimepata picha tofauti kidogo kwamba Tanzania tuko nafasi ya 83 badala ya 122 kati ya nchi 180 zilizofanyiwa utafiti huo. Kama ilivyo kila mwaka, Tanzania inaongoza katika Jumuiya ya Afrika Mashariki katika nafasi hiyo ya 83 maana Kenya inatufuatia nafasi ya 95 pamoja na kwamba waandishi wengi wa habari wanaotuma taarifa kuhusu ukandamizwaji Tanzania wengi wako Nairobi, lakini wao ni 95, Uganda wako 112, Sudan ya Kusini wenzetu wako 145 wamejitahidi sana nchi mpya ile imepata uhuru hivi karibuni, Rwanda 159, Burundi 160, nchi nyingi tunazoziheshimu nazo tumeziacha kwa mbali, Brazil ni 103, Nigeria ya 122, India 136, Malaysia 144, Urusi 148, Singapore
151, Uturuki 155 na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisemi kushika nafasi ya 83 basi tumefanikiwa sana, hapana hata kama tumezipita nchi 107 duniani. Ninachosema na naomba Waheshimiwa Wabunge mnielewe, laiti hawa Reporters Without Borders wangekuwa wanafanya utafiti wao kisayansi nina uhakika Tanzania tungekuwa tumeshika nafasi bora zaidi, nasema hivyo kwa sababu kuu tatu.

Kwanza, utafiti wanaoufanya hauangalii quality of journalism (ubora, weledi katika uandishi wa habari) ni kama wanaendekeza matumizi ya watu ambao hawajasomea uandishi wa habari (makanjanja) ambao hawajui maadili ya taaluma. Matokeo yake tunapata uandishi ambao hauna accuracy na nasema hili kwa masikitiko sana maana mimi ndiyo mwenzao katika Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nilikwenda kwenye sherehe za uhuru wa vyombo vya habari Mwanza. Amini usiamini nimetoa hotuba tena kwa pole pole, kwa kuzingatia hali ya magazeti yetu sasa hivi, magazeti yote sasa hivi yanashindwa kuuza hata asilimia 50 ya kile wanachozalisha ni kutokana na vyombo vya elektroniki kusoma magazeti hayo kwa undani mno, sasa kuna haja gani ya kununua magazeti? Kwa hiyo, nikaeleza jamani hebu tufuate kama nchi zingine zilivyo, tusome vichwa vya habari. Baada ya dakika 30 tu kutoka hapo taarifa ya chombo cha habari cha siku nyingi inasema Mwakyembe kapiga marufuku usomaji wa magazeti. Sasa niko mimi pale, tunaongelea uhuru wa vyombo vya habari na uhuru ndiyo huo inaccuracies.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, wiki iliyopita ilikuwa siku ya Ijumaa, gazeti kubwa kabisa hapa ukurasa wa 30, sitalitaja wataona kama nawaonea lakini mliosoma mmeona. Ipo taarifa inasema, mke wa Malkia wa Uingereza astaafu. Hivi Malkia wa Uingereza ana mke? Unajua inaweza kutuletea matatizo makubwa hata ya kidiplomasia, gazeti linaandika hivi? Unajua katika uandishi wa habari tunahitaji sana sana uangalifu, mnafanya kazi muhimu ambayo watu wote wanategemea na Watanzania na dunia inawaamini, sasa mkifanya vikosa vidogo vidogo kama hivyo heshima itakuwa wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe angalia tu leo hii tuna msiba mkubwa katika Taifa letu, tena niwape pole sana Watanzania wote na wazazi waliopoteza watoto na ndugu zetu wote ambao leo wapo huko wakiomboleza, lakini mwandishi yeyote ambaye amesomea taaluma ya habari hawezi akatoa mbele mapicha tu ya watoto wamezagaa pale wameumia, wamelazwa, majani yamefunikwa unakuwa insensitive.

Mheshimiwa Spika, katika uandishi wa habari tunasema you have to minimize harm. Huo ndiyo uandishi wa Tanzania, ukiwaita kesho kuwahoji oooh uhuru wa habari unaingiliwa, wewe kasome brother ndiyo hicho tu utaelewa. Sasa hivi tuna mitandao ya jamii ambayo kila mtu tu ni mwandishi, jana alikuwa anauza sijui mikate kesho na yeye ni mwandishi, ni matatizo makubwa. Kwa hiyo, tuna kazi ya kudhibiti sekta hiyo lakini wenzetu hawa Reporters Without Borders hawaangalii haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, utafiti huu haurutubishwi na ushahidi wa kimazingira (circumstantial evidence) kwamba inakuwaje kwa mfano nchi ina ukandamizaji mkubwa wa uhuru wa vyombo vya habari kama Tanzania inavyosemekana bado ni moja ya nchi bora katika Bara la Afrika ambayo inavutia uanzishwaji mkubwa wa vyombo vya habari, ni moja ya nchi inayoongoza katika Bara la Afrika hata duniani tupo katika orodha. Leo hii Tanzania ina majarida 428, ina redio 148, vituo vya television 32, watumiaji wa mitandao wako takribani milioni 20 na line za simu milioni 41, ni nchi gani yenye ukandamizaji unaweza ukakuta rutuba ya namna hiyo ya vyombo vya habari? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, freedom index inaangalia vigezo vitatu vikuu; cha kwanza wanaangalia uhuru wa vyombo vya habari; pili, wanaangalia ulinzi na usalama wa waandishi wa habari, lakini kwa kuangalia kwanza sheria zilizopo nchini na kuongea na wadau mbalimbali. Kigezo cha tatu wanakiita level of pluralism hata kwa kiswahili kutafsiri vizuri, ni uhuru pengine wa ujumla katika jamii (diversity). Katika hicho kigezo Watanzania muelewe mtapoteza point kila siku. Mimi nitatoa mfano kwa sababu tunawaudhi wakubwa, Watanzania shida yetu ambayo mimi nasema lazima tujivunie ni kwamba hatuwezi kukubali kuyumbishwa tukaua utu, uhuru na utamaduni wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano, mwaka jana Tanzania iliitwa Geneva mbele ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kutetea rekodi yake ya Haki za Binadamu, tulikuwa tunakabiliwa na masuala 227. Naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mwamasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria, Profesa Mchome na wataalam wote wa sheria walioko pale kwa sababu ilibidi kukaa chini kuangalia je, tukubali kuyumbishwa ama tusimamie misimamo ya nchi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kifupi tulikubali kutekeleza masuala 131 ambayo yamo kwenye programu ya utekelezaji wa nchi yetu, ni mengi tu kwa mfano, kuondoa tozo kwa ajili ya vyeti vya watoto, kushughulikia kwa mfano suala la Sheria ya Ndoa ambalo na sisi wenyewe it is a problem, sisi tuko tu kwenye mchakato lakini masuala mawili tulikubali kidogo tukasema tuyaangalie lakini masuala 94 tuliyakataa katakata ili kulinda utu, uhuru na utamaduni wetu. Nitawatolea mifano ya baadhi ya mashinikizo kama ifuatavyo:-

(i) Kuhalalisha utoaji mimba, tukasema msitushinikize sasa hivi. (Makofi)

(ii) Kufuta ndoa za wake wengi, tukasema hapo mnaingilia utamaduni wetu, mnaingilia imani zetu, hatukubali. Hata kama mnaondoa sijui hiyo misaada iondoke. (Makofi)

(iii) Tukubali ndoa za jinsia moja, tukasema hilo over our dead bodies pengine tufe wote kizazi hiki waingie hao ambao watakubali upuuzi wa aina hiyo, tumekataa Tanzania lakini ukikataa wakubwa wapo. Lobbying ya masuala hayo ni kubwa katika dunia. (Makofi)

(iv) Tukubali haki za mashoga na tuutambue ushoga kama ni haki ya binadamu, tukasema hapana. (Makofi)

(v) Tuliondoe suala la ushoga kwenye Sheria zetu za Adhabu, tukakataa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuwambia Watanzania, the gay and lesbian lobby in the world is very strong, wana pesa hao. Ukiwafanyia fujo wanakuyumbisha kila sehemu. Mimi nilijua tutapunguziwa marks ndiyo wanaotoa pesa kwenye mashirika mengi yanayotufanyia assessment. Kwa hiyo, Watanzania tuwe macho, mara nyingine hizi statistics lazima tuziangalie kwa macho mwili kama Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikimbile suala lingine muhimu ambalo Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani amenukuu ukurasa wa tano wa hotuba yake akisema Ibara ya 19(2) ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa na kuonyesha jinsi ibara hiyo inavyotoa haki ya kujieleza, ya kutafuta, kupata na kusambaza taarifa kwamba haina vikwazo vyovyote na kwamba maudhui yake yamerudiwa katika Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mimi nimekubaliana naye kabisa Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu ile Ibara ya 18. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja hii aliisisitiza zaidi Mheshimiwa Tundu Lissu kwa kusema Ibara ya 18 haina clawback clause yaani kipengele kinachobana au kudhibiti haki hiyo. Picha hii ya kwamba vipengele hivi vinabeba haki na uhuru usio na mipaka inatokana na mdogo wangu Mbilinyi, Waziri Kivuli kusoma Ibara moja tu yaani Ibara ya 19(2) ya huo mkataba hakwenda Ibara ndogo ya (3). Angeenda Ibara ndogo ya (3) angekuta kuna masharti ya kutekelezwa, masharti hayo yanasema, kwanza, haki hii utaitekeleza lakini kwa kuheshimu haki na heshima ya watu wengine na pili kwa kulinda usalama wa Taifa, afya na maadili. Kwa hiyo, hakuna haki isiyo na mipaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, vilevile katika kutafsiri Katiba, najua Mheshimiwa Tundu Lissu amefanya makusudi tu, anaelewa, huwezi ukatafsiri Katiba kwa kipengele kimoja kimoja. Kila kipengele cha Katiba ni sehemu ya tungo moja ambapo vipengele vyote lazima uviweke juu ya meza, uvisome kwa pamoja kuelewa maana ya kila kipengele. Any constitutional provision is but a component in an ensemble of interacting provisions which must be quote or brought into play as part of a larger composition. Hii ni principle wanasheria wote wa constitutional law wanajua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 18 lazima isomwe na Ibara ya 30 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayosema, katika kufurahia haki na uhuru wako hakikisha huathiri haki na uhuru wa wengine, huathiri maslahi ya umma na huathiri usalama wa Taifa lako. Kwa hiyo, hiyo ndiyo mipaka nilitaka tu kusisitiza hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge wote hapa kwamba mwaka 2004, nchi za Kiafrika ziliamua kuunda Mahakama ya Haki za Binadamu ya Afrika. Nchi zilikuwa 30 na mojawapo ilikuwa Tanzania. Tungekuwa nchi ya ukandamizaji wa haki za binadamu tusingeweza kukubali kuanzisha mahakama hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini siyo hivyo tu, kuna kipengele kinachosema, nchi lazima ikubali ili raia wake wanapokuwa wamekwazwa wataleta mashauri yao kwenye mahakama hii. Ni nchi saba tu toka mwaka 2004 zimesaini kuweza kushtakiwa na watu wake Tanzania nayo imo. Sasa jamani nchi ambayo inajiona kwamba iko notorious katika ku-abuse human rights inaweza kweli ikakubali kuingia kwenye kifungu hicho?(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukiangalia yote haya unaweza hata kushangaa kwamba hii ndiyo Serikali ya kuteka waandishi wa habari? Nafikiri tunabangaiza tu hoja mpaka jana nimeshangaa tu kusikia hata eti Katibu Mkuu wa CCM ametekwa? Yaani imekuwa sasa utani nchi hii ukiitwa na polisi umetekwa, mtu amefumaniwa huko ametekwa, tunafanya mzaha kwenye kitu muhimu sana katika jamii yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema kwamba Edward Snowden ambaye amekimbia nchi yake 2013 kujificha Urusi hakimbizwi na Serikali ya Tanzania, anakimbia Marekani kwa kuvuka mipaka, unavuka mipaka. Siyo hivyo tu, tuna Julian Assange ambaye toka mwaka 2012 nafikiri anakaa kwenye kachumba kamoja tu kwenye Ubalozi wa Equador, anakimbia wakubwa, kote kuna mipaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nilipokuwa Mwanza tumekaa kidogo na kijana wangu mmoja mwandishi nikamwambia nakupa swali. Je, ni nchi gani ambayo watu 230 pamoja na waandishi sita walikamatwa kwa kufanya maandamano wakati wa kuapishwa kwa Rais wa nchi yao? Akasema Tanzania.Nikamuuliza lini? Akafikiri sana. Baadaye nikamwambia hapana, huyo Rais ameapishwa mwaka huu, akashindwa. Nikamwambia ilikuwa ni Marekani. Alisema haiwezekani.

Mheshimiwa Spika, ndiyo tatizo tulilonalo Waafrika tunaamini kwamba chochote cha nje ni bora cha kwetu siyo bora. Watu 230 walikamatwa na wakiwa waandishi wa habari sita na wakafunguliwa mashtaka. Hayo tunafikiri yanafanyika Tanzania tu, yanafanyika nchi za Kiafrika lakini sisi kwa kweli tuko katika nchi inayojitahidi sana katika kuheshimu haki za binadamu za wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii vilevile imebaini kuwa Kanuni za Urushaji wa Matangazo ya Dijitali na Kanuni za Leseni zitazuia uwepo wa channel za umma yaani public broadcaster katika vifurushi vya matangazo ya Direct To Home (DTH). Jambo hili hili limeongelewa na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge ambao kwa kweli kwenye majibu yangu ya maandishi nitawataja wote.

Mheshimiwa Spika, naona kama tumewahi kidogo lakini naomba niseme kwamba kanuni mpya ambazo zinapendekezwa hapa hazitaawaathiri watumiaji wa channel za umma kwa kuwa wataendelea kuwa na haki ya kupata matangazo ya televisheni za umma hata baada ya vifurushi vya kawaida vya kulipia kumalizika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi kilichopita Waheshimiwa Wabunge kilikuwa cha mpito, kwa hiyo, kilikuwa na matatizo mbalimbali ambayo lazima tuyavumilie. La msingi hapa ni kuwa hizo zinazoitwa kanuni ni mapendekezo ya kanuni ambayo wamepelekewa wadau wayaangalie halafu wayarudishe Serikalini, halafu kinaendeshwa kikao cha pamoja cha kujadiliana. Nafikiri tumewahi mno, tumeleta wasiwasi mapema sana kabla ya kufika tunakotakiwa kufika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwepo na suala la upungufu kwenye Sheria ya Haki Miliki. Wizara yangu imeona umuhimu wa kufanya marekebisho ya sheria, sio tu ya Haki Miliki lakini sheria zote katika sekta hizi kwa mfano sheria inayogusa tasnia ya filamu na sanaa ikiwemo Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza Namba 4 ya mwaka 1976 na Sheria ya Baraza la Sanaa la Taifa Namba 23 ya mwaka 1984. Tayari Wizara imeshaanza kuchukua hatua kwa kuanza uandaaji wa marekebisho ya sera ili kukidhi matakwa ya sasa. Kwa upande wa Sheria ya Haki Miliki tunashirikiana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji tuweze kuifanyia marekebisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwepo na suala la Serikali iwezeshe timu za Taifa ili ziweze kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali, hayo ni mawazo ya Kamati. Sisi tunaikubali hiyo changamoto na tayari tunafanya hivyo. Serikali imeendelea kutenga bajeti kila mwaka hata kama sio toshelezi. Mfano mdogo tu ni kwamba mwaka 2016/2017 tuliweza kugharamia wanamichezo wote saba walioshiriki katika Olympic nchini Brazil.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka kesho mwezi Aprili tuna mashindano ya Jumuiya ya Madola yatafanyika Australia. Tayari Serikali ipo kwenye mazungumzo ya mwisho na nchi za Ethiopia kwa ajili ya kupeleka wakimbiaji wetu (wanariadha wetu); Cuba kwa ajili ya kupeleka timu yetu ya ngumi na vilevile China kwa ajili ya wachezaji wetu wa mpira wa meza. Hizo zote ni juhudi za Serikali na mwaka 2019 nilishalisema hili kwamba sisi ni wenyeji wa mashindano ya AFCOM kwa vijana wa chini ya miaka 17. Tayari timu yetu ya vijana wa miaka 13 – 14 ipo kambini. Ikifika mwaka 2019 watakuwa tayari wana miaka 16 - 17. Kwa hiyo, Serikali inafanya juhudi na tumelizingatia hilo vilevile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna suala la Kambi ya Upinzani na Mheshimiwa vilevile Mheshimiwa Devotha Minja alilisema hili kwamba kuyumba kwa uchumi kunakotokana na sera za Serikali za Awamu ya Tano, kumeiathiri sekta binafsi ya habari na vyombo vya habari sasa hivi vinapunguza wafanyakazi.

Mheshimiwa Spika, naomba niseme tu mnielewe, si kweli hatua za kimageuzi zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano kwamba zimeleta matokeo hasi. Mageuzi haya yameleta matokeo mengi chanya ikiwemo kuongezeka mapato ya Serikali na kutekeleza miradi mingi tena mikubwa ya maendeleo ambayo wote tunaijua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, madai kwamba ni sera za Serikali ya Awamu ya Tano zinafanya vyombo vya habari kuanza kupunguza wafanyakazi, kwa kweli kama nilivyosema si kweli. Naomba niulize kama wote mnafuatilia vizuri mitandao na vyombo vya habari, mwezi Julai, 2015 Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) lilitangaza kupunguza wafanyakazi 1000, Serikali ya Awamu ya Tano ya Tanzania haikuhusika.

Mheshimiwa Spika, Machi 2017, Shirika la Habari la ESPN lilipunguza wafanyakazi 100, mtandao wa Twitter ulipunguza asilimia tisa ya wafanyakazi wake wote, tena ilikuwa ni Oktoba, 2016. Kati ya mwaka 2010 hadi 2016 CNN yenyewe imeshapunguza zaidi ya wafanyakazi 100 wakiwemo wahariri na wachambuzi waandamizi. Yote haya ni matokeo tu ya uchumi wa dunia hayahusiani kabisa na Serikali ya Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la Bunge live ambalo tumelijibu, tumelijibu, tumelijibu imefika mahali naomba sasa nilielekeze kwa Bunge, after all nina taarifa kwamba tayari TCRA imewakabidhi Bunge leseni sasa hivi wana uwezo wa kufanya chochote wanachotaka. Kwa hiyo, naomba hili nilielekeze huko badala ya mimi kujibu baadaye mtasema ulisema, ulisema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi Rasmi ya Upinzani inasema Serikali iache kuangalia mtandao wa kijamii kwa jicho hasi bali ionekane kama sehemu ya ajira ili kukuza kipato. Hivyo ndivyo tunavyofanya, tumejenga mazingira mazuri ya mitandao na Watanzania ambao wapo kwenye mitandao kwa sasa ni mamilioni. Tunachosema hapa ni matumizi mabaya ya mitandao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanasiasa maarufu wa Marekani nafikiri Hillary Clinton alisema mwezi Desemba, 2016 kuwa matumizi mabaya ya mitandao ni ugonjwa hatari unaoweza kuteketeza dunia. Alisema hivyo kwa sababu mwezi Desemba 2016 kulikuwepo taarifa kwenye mitandao kwamba Serikali ya Israel inasema itaipiga Pakistan ikipeleka askari Syria. Pakistan wakajibu jaribu na sisi tutakushughulikia, kuja kugundua ni maneno wala hayajatoka Israel. Kwa hiyo, kwa kweli mitandao ya jamii kama hatujaidhibiti inaweza kutuingiza katika matatizo makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengi mtakumbuka kisa cha kijana wa kiingereza aitwaye Liam Stacey aliyetumia vibaya uhuru wake wa habari na mnajua kwamba hivi karibuni tu amemaliza kifungo chake baada ya Mahakama ya Mjini Swansea kumkuta na hatia ya kumkashifu mchezaji wa zamani wa Bolton Wanderers mwenye asili ya Afrika Fabrice Muamba aliyekuwa ameanguka uwanjani baada ya kupata shambulizi la ghafla la ugonjwa wa moyo. Kwa hiyo, sio sisi tu ambao kwa kweli tunahangaika namna ya kudhibiti hata wenzetu wanafunga lakini tunaambiwa sisi tu Tanzania ambao tumewapeleka watu mahakamani, lazima tufanye hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi Rasmi ya Upinzani na Mheshimiwa Profesa Jay (Mheshimiwa Joseph Haule) na Waheshimiwa Wabunge wengi wamesema Serikali inawapuuza wadau wa masuala ya sanaa hasa baada ya kuwatumia kwenye chaguzi mbalimbali. Serikali haijawahi kuwapuuza wasanii nchini na kama nilivyosema kwenye hotuba yangu kwa kweli tumechukua hatua mbalimbali ya kuwajengea weledi, kwa kuwatambulisha na kuwakutanisha na wadau wa maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe wito tu kwa baadhi ya vyama vya siasa ambavyo kwa kweli wanasiasa wao wanawachochea hawa vijana kuimba nyimbo za kisiasa, hii ni entertainment industry. Mimi naomba vijana wangu wanisikilize, nimewaambia wanipe mfano wa mwanamuziki yeyote duniani aliyefanikiwa kwa kutukana viongozi, nimewaambia hivyo.

Mheshimiwa Spika, mimi nimeenda Nigeria, wasikilize P-Square, Tiwa Savage, Davido, Don Jazzy, ni vijana ambao wengine wamenunua mpaka ndege, very successful lakini nimewaambia hebu niambie umewahi kusikia wanasema ooh Mr. President your wrong. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewaambia wewe imba nyimbo ambazo zitakuletea mafanikio mwenyewe. Kama unataka siasa nenda kagombee Udiwani huko au kagombee nafasi yoyote huko, hii nientertainment industry siyo political industry na wengi wamenilewa. Angalia Afrika Mashariki akina Chameleon kuna wimbo wowote Chameleon anaongelea Serikali ya Uganda? Nani successful musician hapa anafanya hivyo, namfahamu mmoja tu, alijitia mwanasiasa Fela Ramsome Kuti lakini aliishia pabaya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tuna vijana wanang’ara hapa kina Diamond, Ally Kiba, sikiliza nyimbo zao hakuna hata moja wanaongea mambo ya kipuuzi sijui anajifanya mwanasiasa, utakuwa mwanasiasa wewe? Mimi naomba kazaneni kuboresha vipaji vyenu, let me tell you vijana wangu the sky is the limit. Mimi nimewahakikishia nitawasaidia kwa kila hali muweze kufika anga ya juu kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja hapa ambayo imeongelewa na Mheshimiwa Sakaya, Kambi ya Upinzani, Mheshimiwa Shekilindi, Mheshimiwa Sixtus Mapunda kwamba Serikali iwekeze katika michezo kwani haiwezi kutegemea mafanikio bila kuwekeza fedha. Nafikiri hili suala nimeshaliongelea, kwa kweli uwekezaji ni suala ambalo tunaliona ni muhimu sana tena sana na tunalifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kitu kimoja tu, nilikuwa naongelea kuhusu vijana wangu wa muziki tunapenda mno kulalamika. Nichukue fursa hii kuwapongeza vijana wawili wasanii, Ndugu Hamis Mwinjuma (Mwana FA) na mwenzake Ndugu Ambwene Yessaya (AY) ambao badala ya kulalamika wameibeba Kampuni kubwa ya Tigo kuipeleka mahakamani kwa sababu imekuwa ikitumia miziki yao kama ringtones kwa muda mrefu na Mahakama ya Ilala ikaiamuru Kampuni ya Tigo kuwalipa wale vijana zaidi ya shilingi bilioni 2.185, wame-appeal iko High Court. Mimi nasema vijana wa Tanzania tukiwa namna hiyo (pro-active) siyo kukaa tu kutunga ngonjera za kulalamika, tutafika mbali sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetunga sheria kandamizi za uhuru wa habari mfano Cyber Crime Act, Sheria za Huduma za Habari hivyo zibadilishwe. Mheshimiwa Tundu Lissu, Mheshimiwa Joseph Mbilinyi, Mheshimiwa Devotha Minja, Mheshimiwa Godbless Lema, Mheshimiwa John Mnyika na wengine ambao nitakuwa nimeruka majina yao wameliongelea suala hili. Tofauti na mtizamo wa watu wachache sheria hizi zinalinda uhuru wa wanahabari na wananchi na kwa sasa zimethibitishwa hata na Mahakama Kuu kuwa ni sheria nzuri na hazikiuki Katiba ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza katika uamuzi wake nimeona niupitie huu wa Machi 9, 2017 kuhusu Shauri la Madai Na. 2 la mwaka 2017, Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania na Hali Halisi Publishers Ltd. dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mheshimiwa Jaji De-Melo alitupilia mbali shauri la kupinga Sheria za Huduma za Habari kwa kuwa walalamikaji hawakuwa na hoja za msingi na taratibu za kisheria kupinga sheria hiyo.

Mheshimiwa Spika, vilevile Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam katika Shauri la Kikatiba Na. 6 la mwaka 2016 kati ya Jamii Media Company Ltd. dhidi ya Attornery General na IGP, kwa kweli uamuzi uliotolewa na Majaji Kitusi, Koroso na Khalfani ulikuwa ni mzuri. Uamuzi huo ulisema licha ya kasoro ndogo ya utoaji wa dhamana walifikia hitimisho kuwa Sheria ya Makosa ya Mitandaoni ya mwaka 2015 haikiuki misingi ya Katiba wala haki za watu kujieleza. Hukumu hii imezima rasmi hisia na mawazo ya kuwa sheria hizi ni mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikia kengele imegonga sipendi sana uniambie mara ya pili. Mambo mliyoyasema ni mengi, naomba nizungumzie lugha ya kiswahili. Tumempongeza Mheshimiwa Rais kwa kutumia lugha ya kiswahili mara kwa mara na naomba viongozi wote tuige na tuongee kiswahili sanifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kwa upande wetu Baraza la Kiswahili la Kitaifa nalo linafanya juhudi kubwa, limetoa kamusi nyingi na sasa wametoa Kamusi standard, hii hapa, ningetamani kila Mheshimiwa Mbunge apate. Ni kamusi ya kisasa, ni kubwa na imekubalika na nchi nyingi za Kenya, Uganda na nchi zingine. Naomba Mwenyekiti ufikishe ombi langu kwa Mheshimiwa Spika ukimkata Mheshimiwa Mbunge hela kidogo tu shilingi 25,000 kila mmoja atakuwa kwenye pigeon hole ana kamusi hii, naomba sana iwe hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna suala moja ambalo ameliongelea mdogo wangu Kubenea, mwandishi wa habari wa siku nyingi, analalamika kwamba nimewakatisha tamaa wanahabari kwa kusema asilimia 90 hawana weledi. Sio mimi, ndiyo shida hiyo, sasa huyu anayeongea ni mwandishi wa habari wa siku nyingi lakini amekaa na hiki kitabu siku tatu hata kuelewa hajaelewa, ananishangaza sana Mheshimiwa Kubenea.

Mheshimiwa Spika, naomba nisome, wala siongelei magazeti hapa, yeye anasema nimewasema watu wa magazeti. Nimesema kwamba Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania inaendelea kusimamia ubora wa huduma za utangazaji (broadcasting quality of service) na ndiyo waliofanya utafiti kwa vituo vyote vya redio na television, yeye anamfikiria Mwanahalisi hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania wanasema katika ukaguzi uliofanywa asilimia 90 ya wafanyakazi wamebainika hawana sifa stahiki katika taaluma ya uandishi wa habari na utangazaji katika vituo vya redio na television. Vilevile nimkumbushe Mheshimiwa Kubenea hiyo inakuja pia kwa waandishi wa habari, tumewapa miaka mitano nendeni shule ndugu zangu, dunia imebadilika sasa hivi. Haiwezekani umetoka darasa la saba tu unakuwa mwandishi wa habari eti nawe unatafsiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku moja niliona clip moja kijana mmoja anatafsiri alikuwa anaongea na Mmarekani mmoja mtalii, yule mtalii anasema waambie Watanzania nchi yao ni nzuri, yeye anasema ninyi Watanzania mnapenda kuomba chakula tafuteni ninyi wenyewe chakula. Kwa hiyo, mimi naomba tuwe na weledi katika tasnia hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie tu kwa kusema hoja zenu zote sisi tutazifanyia kazi na kuzigawa kwa kila Mbunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.
Azimio la Bunge la kuridhia Mkataba (Intergovernmental Agreement – IGA) baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamuhuri ya Uganda kuhusu Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (East Africa Crude Oil Pipeline – EACOP) kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA): Mheshimiwa naibu Spika, nianze kwa kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kuonesha kupitia michango yao mbalimbali hapa, kwa kweli mshikamano na Serikali katika suala hili kimsingi simuoni hata mmoja ambaye anaona kwamba huu mradi hauna tija kwetu. Wote wanaunga mkono, na ni maeneo machache tu ambayo Waheshimiwa Wabunge wanataka kufanyike fine tuning (marekebisho ya uboreshaji) na kuipa Serikali tahadhari hapa na pale, hayo tunayapokea. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge waliochangia hoja hii ni saba, sita kwa kuongea na mmoja kwa maandishi; na hoja kubwa ambayo nimeiona katika michango yote hapa, pengine nianze na Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini; ni kuwa mkataba huu ukiuangalia kwa umakini unakinzana na Sheria yetu ya mamlaka ya nchi kuhusiana na umiliki wa rasilimali na maliasili na unaiona hoja hiyo hiyo ikitolewa na Kambi Rasmi ya Upinzani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba niiongelee kwa kifupi hoja hiyo. Naomba nianze kusisitiza kwamba Sheria yetu hii ya Maliasili na Rasilimali tuliyoipitisha, ya sovereignty inahusu maliasili zetu. Katika mkataba huu na mradi huu, tunachokiongelea hapa ni mafuta ya Uganda. Sisi ni wasafirishaji, sisi tuna lori lakini mikungu ya ndizi iliyoko ndani tunayoitoa Kyela kuileta Dar es Salaam si yetu ndiyo maana naona maudhui ya sasa hayaoani na yale ya Sheria ya permanent sovereignty.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukumbuke kwa mfano juzi hapa tumepitisha Sheria hapa ya Azimio la Bonde la Mto Songwe lililetwa tena hilo suala. Sasa hizi ni shared resources, sasa wakati tunakuta nchi mbili zenye sovereignty zimekaa pamoja, lakini sisi sheria yetu ndiyo ikachukua pre-dorminants na ikawa na over-riding effect kupita sheria zao wenyewe pia wenzetu upande wa pili hilo katika sheria za kimataifa sijawahi kuliona. Mnakaa chini mnajadiliana na mkataba huu ni zao la makubaliano kati ya nchi mbili zenye sovereignty. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunafaidika na kodi, kwa ajira pamoja biashara kadhaa zitakazojitokeza. Mimi pengine niungane na Profesa Tibaijuka hapa amesisitiza pia. Hebu tuone tofauti kati ya mkataba, tuna mikataba ya madini na Serikali, ni tofauti na mikataba kati ya Serikali na Serikali ambazo ni international treaties ipo tofauti kubwa naomba tusiichanganye. Mimi nakushukuru sana Profesa Tibaijuka kwahuo mchango wako.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tumepokea hoja nzuri tu kutoka kwa Kambi Rasmi ya Upinzani lakini kuhusu kifungu cha pili kiko katika ukurasa wa tatu wa hotuba ya Kambi ya Upinzani; kwamba kifungu hiki kinazuia taarifa na kwamba inafanana kabisa na mikataba inayoingiwa kisirisiri na mpaka hata Bunge hili linanyimwa hizo taarifa. Nilitaka tu kusema kuwa kifungu hiki hakizuii utoaji wa taarifa, bali kinaweka utaratibu bora tu wa kutoa taarifa hiyo kwa kuitaarifu nchi iliyotoa taarifa nayo iweze kutoa taarifa yake, ni heshima tu. Ni sawa na kusema leo hii sisi Wabunge tuna haki ya kuwa na mikataba, lakini huendi tu wewe mwenyewe moja kwa moja kwenda kuchukua, unapitia kwa Spika. Sasa huo utaratibu wa kupitia kwa Spika ikaonekana ni kizuizi hilo itakuwa ni tatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kusema tu kwamba, haya tu ni makubaliano kati ya nchi na nchi, ni utaratibu tu kama ule ambao tumejiwekea hapa hata wa mikataba, hebu pata ridhaa basi ya nchi mwenzako. Mwenzano amekupa taarifa sasa wewe unaisambaza tu maan taarifa inahitajika na Bunge. Mimi nina uhakika kwa ushirikiano tulionao, Uganda si nchi ya kigeni, si nchi iliyo nje ya bara hili, ni majirani zetu, wote tuko chini ya East African Community mimi nina uhakika mambo yatakuwa mazuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile si kweli kuwa tumetoa uhuru mkubwa mno kwa Uganda kiasi cha kwamba tumewapa hata umilikiwa wa Chongoleani ya Tanga, habana. Tulichofanya sisi ni kuipa Uganda haki ambazo zinasimamiwa na sheria za kimataifa. Uganda ni land locked state na land locked state zote duniani zina haki zao sawa hasa ukisoma Sheria yetu hii UN Convention on the Law of the Sea, wana haki ya kupewa treatment ya kupitisha mizigo yao, kuwapa haki sawa, wasijisikie kwamba wanapoteza kwa kufanya hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo wameongea wote wanaoguswa na bomba, nimefurahi sana. Mheshimiwa Mussa Mbarouk anasema tuwe waangalifu na fidia ya ardhi kwa wananchi wetu. Mimi nafikiri hili ni wazo zuri, tumelipokea na tunaomba sasa Serikali haina mikono mingi, sisi wawakilishi wa wananchi bomba litapita kwenye maeneo yetu, sisi tuwe mstari wa mbele kutetea haki za wananchi wetu hasa upande wa ardhi. Serikali itaweza kuchukua hatua tukisikia wawakilishi wa wananchi mko mstari wa mbele na kusema hapana, hapa kunaonekana kuna hitilafu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna hoja ya kuwapa priority aliyotoa Mheshimiwa Mbarouk, kwamba tutoe priority ya ajira kwa wale wanaopitiwa na mradi, hiyo ni sahihi kabisa, hili ni suala la utekelezaji. Hata hivyo naomba nisisitize kwamba mradi huu tumesema unatekelezwa na private sector ambayo inahitaji efficiency, inahitaji kukimbilia fursa. Huwezi tu umekaa chini ya mwembe sasa wewe kwa sababu unapita kwako basi ubembelezwe ili ukafanye kazi pale. Tuchangamkie fursa na Waheshimiwa Wabunge tuwe mstari wa mbele kuchangamkia fursa kwa niaba ya wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Profesa Tibaijuka kwa kweli nakushukuru sana kwa michango yako. Mimi nafikiri…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri subiri kidogo. Waheshimiwa Wabunge kwa mujibu wa Kanuni ya 28(2) nataka kuongeza muda wa nusu saa ili tumalizie hoja hii ya Mheshimiwa Waziri hapa. Kwa hivyo nitawahoji maana fasili hii inaitaka niwahoji.

(Hoja Ilitolewa Iamuliwe) (Hoja Iliamuliwa na Kuafikiwa)

NAIBU SPIKA: Sawa, ili kumbukumbu zikae sawa sawa, Wabunge wamehojiwa kuongeza nusu saa na wamekubali. Mheshimiwa Waziri.

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa ongezeko hili la muda ingawa sijawatendea haki wale wa mwanzo nilikuwa nakimbia kwa sababu najua muda ulikuwa umekwisha. Hata hivyo, naomba tu nimshukuru sana Mheshimiwa Profesa Tibaijuka, ameongelea suala la ulinzi. Kwa kweli suala la ulinzi ni kitu muhimu sana kwetu wote Watanzania. Bomba hili ambalo linalopita nchini kwetu lina faida, lina tija kwa Taifa na kama alivyosema, ni wajibu wetu mkubwa Watanzania wote kuhakikisha usalama wa hili bomba.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Nkamia naye vilevile kama ilivyo kwa Mbarouk, kama ilivyo kwa Profesa Tibaijuka, wote wamepitiwa na hili bomba na Mheshimiwa Nkamia amesisitiza kuhusu ulipwaji wa fidia stahili na kwa muda muafaka. Mimi nafikiri hili ni suala la muhimu, tunalipokea kama Serikali, ni masuala haya ya utekelezaji ambayo lazima angalizo tulichukue. Lakini vilevile kuna kitu kimoja ambacho ningependa nikiongelee kidogo, ameongelea kuhusu suala la kiwango cha pesa tutakachopata kila siku, amesema ni kikubwa sana. Najua tunafaidika, lakini tusije tuka-exaggerate kiasi cha kupata tukafika mahali ambapo sasa kesho asubuhi tukadaiwa kila mtu anunuliwe bajaj.

Mheshimiwa Naibu Spika, kiwango cha pesa tutakachopata, tukisoma vizuri maelezo niliyoyatoa ni kwamba kila pipa lita-generate dola 12.2; sawa, kwa siku kutakuwa na mapipa 216,000 lakini pesa hiyo si kwamba yote inakuja Tanzania, kisome vizuri kile kifungu, tukisoma vizuri kile kifungu ni pesa inatosha kwa sababu hapa tunaongelea economies of scale, hatimaye tunapata pesa ya kutosha; lakini si kwa kiasi ambacho kilioneshwa na Mheshimiwa Nkamia kwamba hiyo yote sasa inakuja kwetu hapana! Itakwenda in proportion na hisa zetu. Naomba tuisome vizuri hiyo provision, itakwenda in proportion na hisa. Pamoja na angalizo hilo bado pesa ni nzuri, tunafaidika at the end of the day.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Vedastus Manyinyi ambaye kwa kweli ni kama amerudia tu hoja za wenzako zote. Hata hivyo nisisitize kitu kimoja; kwamba mradi huu haujadondoka kwetu kama zawadi au kama embe dodo tu umekaa chini ya mti likadondoka, tumeupigania kama Taifa. Ndiyo maana tumemshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa aliyofanya ya kidiplomasia kuweza kushawishi nchi jirani kwamba njia bora kupitisha bomba hilo ni Tanzania na faida ni kubwa sana, na ndiyo maana hata ukiisoma hotuba ya upinzani hilo imekubali kabisa kwamba kwa kweli huu mradi una tija kubwa kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe wito tu kwa Watanzania kwamba lazima maeneo ambayo mradi unapita na vilevile Mkoa wa Tanga wenyewe ambapo ndiyo hatma ya hilo bomba kuishia naomba jamani tuzichangamkie fursa tele ambazo zinajitokeza. Nilipokuwa Tanga kwenye mkutano wa biashara tulikuwa na Mheshimiwa Mbarouk, nilitoa taarifa kwamba tayari kuna watu (agents) wapo Tanga na Dar es Salaam wakishawishi makampuni yatakayokuwa based Tanga pale kwamba aah! Sehemu nzuri kukaa ni jirani tu hapa, kuna mahoteli mazuri mnakuja kwa gari asubuhi au kwa helikopta. Sasa hiyo Watanzania tumeshajifunza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna sehemu tulikuwa tunachoronga kule Songosongo, watu walikuwa wanakuja na ndege asubuhi kulala. Ni fursa sasa kujenga mahoteli ya kutosha, fursa sasa kujenga miundombinu ya maisha ya kila siku kwa sababu watakaokuwepo Tanga wana watoto watahitaji kwenda shule, wana familia zitahitaji hospitali, wana familia zitahitaji hospitali, maduka ya dawa mazuri na huduma mbalimbali. Ndiyo maana nasema, la msingi kabisa hapa si Serikali tena, ni sisi Watanzania kuchangamkia fursa zilizopo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naomba nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuniamini kumsaidia kuongoza Wizara hii ya Habari, Utamaduni na Michezo na vilevile kwa kumteua Mbunge kijana, mchapakazi na mwanamichezo hodari Mheshimiwa Juliana Daniel Shonza kunisaidia kuongoza hii Wizara.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii na ninampongeza sana Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango na Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji kwa kazi nzuri wanayoifanya ya weledi mkubwa na katika Wizara hii nyeti katika maendeleo ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze kwenye baadhi tu ya michango iliyogusia Wizara yangu ambayo inahitaji ufafanuzi wa kina kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na madai ya Mbunge wa Mbeya Mjini, Mheshimiwa Joseph Mbilinyi, kwamba Mkurugenzi wa Idara ya Habari ambaye vilevile ni Msemaji wa Serikali alitumia kifungu cha 54(1) cha Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari kulifungia Gazeti la Tanzania Daima, kitu ambacho anasema kwamba siyo sahihi, alichotakiwa kufanya si kulifungia gazeti, lakini kuwawajibisha waandishi waliohusika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, madai haya ya Mheshimiwa Mbilinyi yanagusia utekelezaji mzima wa sheria hii mpya, hivyo nafikiri kuna umuhimu sana wa kutoa uchambuzi wa kina kidogo kuhusu sheria hii na hapa tulipofika ili tusiendelee kuwachanganya wanaotusikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbushane kidogo tu kuwa Sheria hii ya Huduma za Vyombo vya Habari tuliipitisha wenyewe hapa Bungeni tarehe 5 Novemba, 2016 na tarehe 16 Novemba, 2016 Mheshimiwa Rais akaridhia hii sheria na tarehe 31 Desemba sheria hii ikaanza kutumika rasmi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kurahisisha na kuwezesha utekelezaji wa sheria hii uende vizuri zaidi ikabidi tutengeneze Kanuni na kanuni zenyewe pia zikawa tayari na tarehe 3 Februari, 2017 zikaanza kutumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nielezee hili wanisikilize vizuri hata wadau katika masuala ya habari vizuri kwa makini kwamba chini ya sheria hii na kanuni zake kuna vyombo vikuu vinne vya kusimamia uendeshaji na maendeleo ya vyombo vya habari hapa nchini ambavyo vinatakiwa viundwe. Kwanza ni Independent Media Council of Tanzania ambalo ni Baraza Huru la Habari ambalo linaundwa na wanahabari wenyewe, lakini ni wanahabari ambao ni accredited walishapata ithibati. Chombo cha pili kilichotakiwa kuundwa hapa ni Bodi ya Ithibati yenyewe (Accreditation Board). Kwa sababu tulishakubaliana kwamba Uandishi wa Habari sio kitu cha kubahatisha tena ni taaluma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama zilivyo taaluma zingine lazima kiwepo chombo kinachofuatilia training ya uandishi, weledi wao na nani atambuliwe kuwa mwandishi wa habari ndiyo maana tuna chombo hicho kinaitwa chombo cha ithibati (Accreditation Board). Tatu ni Kamati ya Kimahakama ya malalamiko ambayo kazi yake kubwa ni kusikiliza malalamiko ya wananchi kama kuna upotofu wa maadili, kama mtu ameonewa na hicho chombo kitakuwa na mamlaka kama ya Mahakama, ndiyo maana ukiona hujaridhika unakwenda Mahakama Kuu kudai kwamba haki yako kwa kweli imefinywa, pengine hukusikilizwa vizuri ama kuna uvunjifu wa hizi kanuni tunaita principles of natural justice. Kwa hiyo, hicho chombo ni Quasi Judicial Board, ni almost kama Mahakama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, chombo cha nne ni Mfuko wa Habari ambao kazi yake kubwa ni kuandaa waandishi wa habari vizuri zaidi waweze kupata weledi katika kazi na vilevile kufanya utafiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nasema hayo yote kwamba dhamira ya sheria hii ilikuwa nzuri sana, kuwa vyombo hivi vinne vikifanya kazi vizuri kwa kushirikiana, sio tu vyenyewe vilevile na Serikali na kwa kuzingatia maadili na sheria za nchi, basi tasnia ya habari ingeweza kujiendesha wenyewe kwa kweli bila mtu yeyote kuvisogelea Vyombo vya Habari, hilo ndilo lilikuwa lengo la sheria.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kuna swali limekuwa linaulizwa mpaka kwenye Kamati kwamba, vyombo hivyo ulivyovitaja mbona havijaanza kufanya kazi mpaka leo? Ndiyo ni kwa sababu kubwa mbili, sababu kwanza tumeanzisha usajili mpya wa majarida na magazeti yote, tatizo moja ni kwamba hatujapata ushirikiano mzuri kutoka kwa wadau wenyewe, tumeahirisha zaidi ya mara tatu deadline ya usajili. Mwisho tumekuja kusajili tarehe 31 Oktoba ambazo ni wiki mbili tulizopita na ni robo tu ya majarida na magazeti yaliyoandikishwa. Tumefungua milango wanaweza kuendelea kujiandikisha. Kwa hiyo, hatuwezi kupata idadi ndogo ya wadau hao tukaanzisha vyombo hivi muhimu kesho utaambiwa Serikali imelazimisha hivyo vitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili tukumbuke kwamba kuna uwepo wa kipindi cha mpito (transition period) katika hii sheria, yote ilitokana na hoja za Wabunge hapa. Wabunge wanasema hatuwezi kuwawajibisha waandishi wa habari kwa sababu kazi ya uandishi wa habari ni kazi nzito ya kutafsiri mtu amesema nini, anakaa kwenye chumba cha habari, unahitaji elimu at least basic education ambayo tukubaliane hapa. Ndiyo maana wote tukasema tunaiga na nchi zingine kama Uganda ambapo lazima uwe na degree mbili, tukasema lakini hapa angalau uwe na Diploma au Shahada ya Chuo Kikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge mkasema tuwape miaka mitano tusiwe unfair kawa hawa watu tukatoa miaka mitano, wenzetu wajipange vizuri waingie ili waweze kuwa accredited kama waandishi wa habari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake ni kwamba utekelezaji mzima wa uanzishwaji wa vyombo hivi vinne unachelewa mpaka pale wadau wenyewe haitokuwa Serikali, wadau wenyewe walisema pale to speed up, tuko tayari hata tukaanzisha kesho Media Council na wale waandishi wenye shahada na wenye diploma wanatosha hao waliopo, tukifanya hivyo kama Serikali itakuwa na mgogoro mkubwa. Kwa hiyo, tunasubiri wadau wenyewe watuambie muda umefika tuitekeleze hiyo sheria sasa tuepukane na transitional period, hiyo hatuwezi kuamua kama Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana namjibu Mheshimiwa Mbilinyi kwamba Mkurugenzi wa Habari hajawahi hata siku moja kulifungia gazeti lolote kwa chini ya sheria hii mpya na wala hajawahi kutumia hicho kifungu cha 54. Kifungu cha 54 kinatoa ufafanuzi tu wa kosa la kuchapisha habari za uongo na kuitia jamii katika hofu. Madaraka anayoyazungumzia Mheshimiwa Mbilinyi ni madaraka ya Waziri nilitaka nilieleze hili. Pamoja na sheria hii kuunda vyombo vinne ambavyo vitaweza kabisa kuleta pengine nidhamu kama kweli Watanzania tutaamua kutumia vyombo hivi kuheshimu kanuni na maadili ya nchi, kuna kitu kinaitwa residual powers of the government, hizo residual powers hatujanyanganywa na hii sheria ningeshangaa sana tungenyanywa na hii sheria. Duniani kote Serikali lazima iwe na residual powers kuhakikisha kwamba inalinda haki za watu wake na pili inalinda usalama wa nchi hizo lazima tuwe nazo, hata kama kuna vyombo vingine
vinafanya hiyo kazi. Sasa hayo madaraka yamo katika sheria mpya katika kifungu cha 59 ndiyo ambayo Waziri anatumia. Ukiona trend ya gazeti toka siku ya kwanza unaionya, siku ya pili unaionya, siku ya tatu unamwambia bwana eeh, unaleta uchochezi mara ya sita unaonya unasema aah, pengine ukapumzike miezi mitatu utafakari vizuri, ndiyo hicho tunachofanya ili kulinda mstakabali wa nchi yetu hii.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo hatuyafanyi Tanzania tu iko dunia nzima na tunafanya kwa kuzingatia matakwa ya Mkataba wa Kimataifa tulioingia Watanzania International Covenant on Civil Political Rights ya mwaka 1966, sisi ni signatories dunia yote ni signatories na kila nchi imechukua hayo maudhui yako kwenye Ibara ya 19 ya huu mkataba na sisi tumechukua tumeingiza kwenye Katiba yetu Ibara ya 18 na Ibara ya 30 kwamba hata kama una haki, hata kama una uhuru, uhuru huo lazima uwe na mipaka kwa ajili ya maslahi ya nchi. Mipaka lazima iwepo na hata hii sheria imeingizwa katika kifungu cha 59 kwamba pamoja na kuwaachia mjiendeshe yanapokuja maslahi ya Taifa, inapokuja kulinda usalama wa nchi, lazima Serikali iwe na sauti hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kitu kimoja Mheshimiwa Saada Mkuya naye aliongelea kuhusu ujenzi wa mazingira wezeshi ya michezo kuitangaza nchi kimataifa. Nampongeza sana Mheshimiwa Saada Mkuya kwa kuja na hilo wazo, ni wazo zuri sana. Sasa hivi tunamalizia utengenezaji wa rasimu ya Sera ya Michezo ya Taifa mpya, imefika mbali sana, nina uhakika ndani ya miezi sita tutakuwa sera mpya ya michezo hapa Tanzania. Hata kabla hiyo sera haijakamilika tumeshaanza kutekeleza, kuhakikisha kwamba tunatumia michezo kuitangaza nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu mapema tumeweza kuleta timu ambayo iko kwenye Premier League ya Uingereza iitwayo Everton, kuja kucheza kwenye uwanja wetu wa kisasa hapa kitendo hicho tu peke yake kimeweza kuinyanyua Tanzania katika macho ya ulimwengu na ndiyo maana tukaweza kupata hata ufadhili wa kutengeneza kiwanja chetu upya na nitakabidhiwa nafikiri tarehe 24 na mwenzangu Naibu Waziri kikiwa na nyasi ambazo zitakaa kwa zaidi ya miaka kumi bila kutusumbua tena ama kupata ugojwa wa moyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo asubuhi nimeingia kutoka Arusha baada ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kuniruhusu kwenda kufunga michezo ya golf. Naomba nimshukuru tena Mheshimiwa Dkt. Mpango na mwenzake Mheshimiwa Dkt. Ashatu kwa kutoa pesa kuelekeza kwenye mahitaji ya barabara, hii barabara kwenda Arusha imekamilika. Hii shortcut kwenda Arusha nimetoka Arusha saa 11 asubuhi nimewahi kipindi asubuhi, hayo ndiyo maendeleo Mheshimiwa Mpango hongera sana, Mheshimiwa Kijaji hongera sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikwenda Arusha kufunga mashindano ya golf ambayo yamevutia wacheza golf wa kimataifa wa mataifa 250. Nampongeza sana mwekezaji wa Arusha ambaye amejenga kiwanja cha golf ni Mholanzi Mtanzania wamejenga kiwanja cha golf cha kisasa kupita vyote katika Afrika ya Mashariki na Kati. Wamekuja wageni wengi na ndiyo maana tumekubaliana na Mheshimiwa Waziri wa Utalii hapa tufanye kazi kwa karibu sana kwa sababu michezo sasa hivi na utalii vinaenda pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wote duniani michezo ya golf inachezwa na matajiri, kwa hiyo, ukivisogeza karibu na mbuga za wanyama unapata watu wazito kweli. Nimepishana tu juzi na mcheza sinema mashughuli wa Marekani Harrison Ford amekaa hapo akicheza golf wiki nzima, siyo yeye tu wengi wanakuja. Ndiyo maana naomba nitoe wito kwa viongozi wenzangu hasa huku kwenye Wilaya kama kulikuwa na kiwanja cha golf zamani naomba msivigeuza kuwa magulio, maana kulikuwa na imani kwamba hii michezo ya golf siyo yetu, hapana!

Mheshimiwa Mwenyekiti, kijana aliyeshinda golf tournament ya kimataifa ya Arusha jana ni kijana wa Kitanzania kwa jina la Victor Joseph na ni mwanafunzi, mtoto wa kawaida tu. Unajua hawa vijana ambao hawajawahi kucheza golf Mungu amewapa kipaji cha ajabu, anapiga tu mara moja anaingia moja kwa moja kwenye shimo utafikiri Tiger Woods! Tiger Woods wapo wengi, naomba ndugu zangu tutenge maeneo kwa ajili ya kujenga viwanja vya kisasa vitatusaidia. Ukinipa tu eneo nitatafuta Wawekezaji kama ambavyo tumefanya upande wa Arusha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema naunga mkono hoja hii kwa nguvu kweli. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kuwashukuru Wabunge wote waliochangia katika Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ya mwaka 2018/2019 kwa kauli na maandishi. Naishukuru Kamati yangu ya Kudumu ya Bunge ya Huduma ya Maendeleo ya Jamii kwa maoni na ushauri walioutoa kupitia hotuba ya Kamati hiyo ambayo imewasilishwa mapema leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba michango yote iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge ni muhimu sana kwa maendeleo ya sekta ya habari, utamaduni, sanaa na michezo. Pia namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mheshimiwa Juliana Shonza kwa kuyatolea maelezo baadhi ya maswali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba yangu imechangiwa na jumla ya Waheshimiwa 41, ambapo waliochangia kwa maandishi ni Waheshimiwa 23 na kwa kauli ni Waheshimiwa 18. Wabunge hawa 41 wamezalisha hoja na maswali 214, hivyo basi majibu na ufafanuzi tutakaotoa utajikita kwenye baadhi tu ya hoja za Kamati na baadhi tu ya hoja za Waheshimiwa Wabunge na nitaeleza kwa kifupi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya Kamati ya kwanza ambayo nimeona ni muhimu kuijibu ni kwamba, lini Serikali itakamilisha uundaji wa Bodi ya Ithibati na Baraza Huru la Habari. Ningependa nieleze tu kwamba pamoja na kwamba mwaka huu wa fedha tumeshaomba fedha kwa ajili ya uanzishwaji wa Bodi ya Ithibati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, bado mchakato huu unavihusu sana vyombo vya habari vyenyewe, kwa sababu Serikali ikikimbia sana ikaanzisha Bodi ya Ithibati, ikaanzisha Baraza Huru la vyombo vya Habari, kesho tutaambiwa hilo ni baraza lenu nyie wenyewe, sisi haituhusu. Naviomba vyombo vya habari vijitokeze na vyombo vyao mbalimbali ili tuweze kukamilisha zoezi hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo kubwa la hii sheria ni kutaka vyombo vya habari vijiendeshe vyenyewe, viwe self governing, tunataka tuwe na self governing media industry na itaunda Baraza Huru la Habari. Kutakuwa na Bodi ya Ithibati na Kamati ya Malalamiko na Mfuko wa Habari kwa ajili ya Maendeleo ya hii Tasnia. Inaitambua tasnia hii sheria mpya, kuwa ni taaluma na wana taaluma hawa wawe na sifa stahili kuanzia Diploma na kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa lilipokuja hapa Bungeni, ndipo utata ukajitokeza kwamba sasa hawa waliosoma hawapo, lakini tunajua wapo wengi, ndipo kikatolewa kipindi cha miaka mitano kuruhusu Waheshimiwa ndugu zetu Waandishi wa Habari waweze kusoma, lakini nina uhakika hata tukianza kesho Waandishi wenye Diploma, wenye Degree wako wengi sana. Nawaomba Waheshimiwa Waandishi wa Habari wenyewe wawe mstari wa mbele. Tukiunda sisi, zitaanza hizo ngonjera za kwamba hiyo ni Kamati ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine lilikuwa Kanuni za Sheria za Habari hazijatungwa mpaka leo. Hii ni hoja ya Kamati, lakini kwa heshima kubwa kabisa naomba kusema kwamba Wizara ilishakamilisha Kanuni za Sheria ya Habari na kanuni hizo zilichapishwa kwenye Gazeti la Serikali mwaka jana mwezi Februari tarehe tatu na zilishaanza kutumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ilikuwa ni Serikali iweke mkakati wa kuwa na Kanzidata Wataalam wote wa Kiswahili nchini ili watumike kama Wakalimani katika maeneo mbalimbali hasa mikutano ya Kimataifa. Kwenye hotuba yetu iko wazi na huu ni ubunifu mkubwa wa Wizara ambao tayari tumeshaanza kuutekeleza. Tunachotaka tu ni kutoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge ambao tunaelewa, baadhi yenu hapa ni mabingwa wa lugha ya Kiswahili kwa kusomea, naomba na ninyi mjitokeze kujisajili katika tovuti hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwepo na suala la wizi wa kazi. Suala hili tumelifanyia kazi sana na nimelieleza kwenye hotuba yangu kwamba tumefanya kaguzi mara kwa mara katika sehemu mbalimbali korofi na tumeweza kukamata kazi nyingi za sanaa ambazo zinaingia kinyemela kuweza kuumiza vijana wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Mkoa wa Dar es Salaam tuna kesi tunayoisema sana ambayo tulifanikiwa kesi ya jinai namba 414 ya mwaka 2011 ambapo Mahakama ya Wilaya ya Ilala ilitoa hukumu ya kutaka kazi ambazo zilikuwa zimeingia kinyemela, zinauzwa kinyemela kuwaumiza wasanii, ziweze kuharibiwa chini ya usimamizi wa Mahakama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli tulilipongeza sana Jeshi la Polisi kwa kazi kubwa iliyofanyika na Mahakama kufanya uamuzi huo haraka. Kwa hiyo, tunafanya hiyo juhudi kubwa kuhakikisha kwamba wasanii hawaendelei kunyonywa. Sasa hivi tunaipitia Sheria ya Haki Miliki na nina uhakika italeta sura nzuri tu baada ya muda siyo mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwepo na suala la mapato ya Uwanja wa Taifa na Uwanja wa Uhuru kwamba yasichanganywe. Kamati kwa kweli tunashukuru sana kwa hoja hii, lakini ningependa tu nisisitize pengine tupate maelekezo mengine ya wazi kabisa ya Kamati pesa yote inakusanywa kwa njia ya kielektroniki. Mapato yote ya hivi viwanja na kwa sababu fedha yote hii inakwenda Mfuko Mkuu, wahusika kule wanaona kabisa hii ni Uwanja wa Taifa, hii ni Uwanja wa Uhuru kwa sababu hakuna anayeshika hela taslimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninachoomba tu ni kwamba kama Wizara kwa kweli tuna kifungu kimoja tu cha kukusanya mapato hayo kwa jina la Uwanja wa Taifa na code yake tena ni 140259, lakini kama ni muhimu sana tupate code ya pili itawezekana, lakini kwa kweli tunakusanya hiyo pesa lakini imetoka wapi, inaeleweka kabisa kwa mtu anayepokea kwenye Mfuko Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala kwamba uchunguzi ufanywe kuhusu fedha za Mchina, yaani kuna Wachina wanapewa fedha zinazokatwa katika kila mchezo na Bunge lako Tukufu lipewe taarifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii hoja imesisitizwa sana na Kamati yangu. Ningependa nilieleze ili pengine nieleweke vizuri pole pole, kwamba katika mgawanyo wa fedha unaofanyika kwa asilimia, hakuna kipengele cha fedha ya Mchina au Wachina, sijawahi kuona mimi tangu niingie kama kiongozi wa Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ila ninaambiwa huko nyuma kulikuwepo na utaratibu wa kuwalipa Wachina. Kuna technical team ipo pale uwanja wa Taifa ilikuwa inalipwa kwa kazi iliyokuwa inafanyika, ni huko nyuma, lakini sasa hivi sijaona wala Afisa Masuuli wangu Katibu Mkuu hajawahi hata siku moja akaidhinisha hela iende kwa Mchina au Wachina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishuhudie tu kitu kimoja, kwamba tukishapata mapato mgawanyo ni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tunatoa asilimia 18 ya VAT na asilimia tano ya Selcom ambao ndio waliokuwa service providers. Ikishatolewa hii kinachobaki ndio asilimia 100. Sasa mgawanyo unakuwa kama ifuatavyo:- asilimia 15 ni ya uwanja ambayo pia hatukai nayo tunaipeleka Mfuko Mkuu, asilimia tano ni ya TFF, asilimia 40 ni ya timu mwenyeji, asilimia 20 ni ya timu ngeni, asilimia tisa ni bodi ya ligi, asilimia saba gharama za mchezo na hizo gharama za mchezo na hiyo pesa inakwenda TFF huko huko, asilimia moja inaenda BMT na asilimia tatu DRFA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, pengine nitumie nafasi hii vile vile kumwelezea Mheshimiwa Kadutu, alisema sana kwamba BMT inapata hela nyingi hapo. Hapana si asilimia 15 ni asilimia moja tu na kwamba hiyo moja pengine tuipe TFF lakini TFF hapa wana asilimia tano kuna asilimia saba gharama za mchezo; ndio hao TFF, kuna asilimia tisa bodi ya ligi; hao hao ndio TFF, BMT asilimia moja. Kwa hiyo, nafikiri nimejieleza, limeeleweka kuhusu hayo malipo ya Mchina; hayapo tena na kama yalikuwepo hapo nyuma ilikuwa ni utaratibu wa kuwalipa wale technical team ya kichina iliyopo pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lilikuwepo lingine la uwepo wa udhibiti wa mapato yatokanayo na uuzaji wa tiketi kwa njia ya kielektroniki. Nashukuru sana, hili wazo zuri, Kamati yangu kwa kweli ni makini sana. Wizara kwa kutambua umuhimu wa kudhibiti mapato imeshakamilisha mchakato ulio wazi wa kumpata mtoa huduma ya kukusanya mapato kwa mfumo wa kielektroniki katika uwanja wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo huo tutauunganisha na mfumo wa Serikali wa ukusanyaji mapato (Government Payment Gateway System) ili kuimarisha udhibiti wa mapato. Hili tunaahidi na nadhani tutakapokutana na Kamati tena wataona hicho kimefanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwepo kwa maandalizi mazuri ya Timu ya Taifa ili ziweze kushiriki kikamilifu kwenye mashindano na kurudi na ushindi. Waheshimiwa Wabunge wengi sana nitashindwa wengine kuwataja, wengi kwa maandishi na kwa kuongea hapa, wamelalamikia sana hilo na kwamba Serikali ipo ipo tu, hatufanyi chochote kuhusu hizi timu zinaenda tu; hiyo si picha ya kweli. Mheshimiwa Chumi, Mheshimiwa Mwamoto, Mheshimiwa Ngeleja, Mheshimiwa Sima na Waheshimiwa Wabunge wengi wameongelea hilo na wametoa na mfano vilevile kuhusu timu yetu ilipokwenda Australia kwenye Jumuiya ya Madola.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge kwamba ukichukulia michezo iliyokwisha juzi ya riadha, ndondi na michezo mingine Australia, wawakilishi wetu waliandaliwa vizuri, hivyo naomba niwasisitizie hilo na tumeiandaa sisi Serikali. Tulipewa nafasi 34 lakini tukaamua sisi wenyewe kwa ajili ya kujali viwango waende 22 tu. Kushindwa kupata medali ni kawaida ya mchezo, asiyekubali kushindwa si mshindani. Tulishindwa na timu ambazo zilijiandaa vizuri kutupita sisi, lakini tulijiandaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano wa timu ya table tennis. Ilikuwa na wachezaji wanne; watoto wa kike wawili na watoto wa kiume wawili, wazuri sana. Wamefanya mazoezi hapa nyumbani, tukawapeleka China ambako kuna mabingwa wazuri sana wa table tennis, wamekaa China kufanya mazoezi kwa siku 80. Jamani kama Serikali tufanye nini zaidi ya hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumewapeleka wameenda wamerudi, wameenda huko Australia; na watoto hawa wamecheza vizuri wameenda round ya kwanza, ya pili, round ya tatu ndiyo wameondolewa. Tusiwalaumu, tusiwakatishe tamaa kwa kauli zinazotoka kwenye hili Bunge kwamba tulipeleka vilaza kule. Hapana ni vijana waliokuwa wameandaliwa vizuri kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na mwanariadha mmoja wa mbio, Ally Gullam nafikiri kutoka Zanzibar, ambaye mbali na mazoezi hapa nchini ilibidi tumpeleke Brunei kwenda kufanya mazoezi ya ziada chini ya mwanariadha maarufu nchini hapa Suleiman Nyambui. Suleiman Nyambui sasa hivi ni kocha wa Taifa wa riadha wa hilo taifa la Brunei. Kafanya mazoezi huko, kijana wetu amejitahidi ameshindwa. Nina uhakika tutaendelea kufanya hivyo huyu bwana mdogo hatimaye atashinda, practice makes perfect. Tutaendelea kufanya mazoezi, atashinda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanariadha wetu wa mbio za marathon, bwana Said Makula nafikiri wote mlimuangalia. Mimi nilikuwa naangalia sana pale amekuwa wa tatu mpaka kilometa 41 marathon, tumepata sasa na sisi bronze, akaanguka. Amemaliza kilometa 41, kabakiza tu kilometa 42.2 akaanguka bahati mbaya. Akakimbizwa hospitali kuangalia oxygen ilikuwa imepungua kichwani.

Hakuanguka peke yake, walianguka wengi wa Ireland na kadhalika kutokana na attitude ya sehemu hiyo. Kwa hiyo, ni kijana alijitahidi, tulikuwa tuwe namba tatu pale lakini sijui shetani gani aliingia pale, basi kijana wetu akaanguka akakimbizwa hospitali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwingine Kassim Mbwana aliyekuwa tegemeo letu kubwa sana kwenye boxing na alisema anaahidi kwamba akifika atatuletea gold. Amefika kule bahati mbaya sana wenzake wote waliokwenda kule Kenya, Uganda na South Africa wakapewa wapiganaji wa ajabu ajabu huko; yeye peke yake mchezo wa kwanza akapewa apambane na bingwa wa Commonwealth ambaye alipata dhahabu mchezo uliopita na huyo kijana ana silver ya Olympic, ni bingwa kutoka India.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wakasema ni maafa wengine wakaanza kusema jitoe wewe cheza cheza kidogo tu ukimbie lakini yule kijana amecheza mpaka round ya mwisho, ametolewa kwa point za Majaji. Yule mshindi amepata Majaji watatu wa kwetu amepata Majaji wawili. Anastahili pongezi za hili Bunge badala ya kuwakatisha tamaa hawa vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kwa sababu wamelalamika sana Waheshimiwa Wabunge, naomba niseme zaidi hapo. Hata soka la Tanzania linapanda, soka linapanda. Mimi naona kabisa kuna maendeleo makubwa. Msisahau Serengeti Boys mwaka jana ilituinua kwenye viti hapa Watanzania, ilifuta mkosi wa nchi hii, miaka 37 hatuendi hata semifinals za AFCON. Hawa vijana wameenda fainali za AFCON mwaka jana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu angalia dozi wanayotoa kwa timu, sita bila, Serengeti hao; sasa hivi ni mafanikio tu. Kwa kweli tuwape nguvu hawa vijana; kwa sababu tumegundua kwamba kufanikiwa katika michezo ni mazoezi na kuwekeza. Hakuna tena kwenda sijui wapi mkachezeshwe usiku na hirizi, hamna. Ni mazoezi tu na ndio maana tunafanikiwa vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikimbie tu kueleza vile vile kwamba pengine Wizara mwaka huu itaongeza zaidi kampeni ya kuelezea mafanikio yetu. Kwa mfano mwaka jana tulifanya vizuri sana, katika riadha. Ukimwacha mwanariadha wetu huyu Simbu ambaye alipata medali ya shaba London Marathon mwaka jana, lakini tulikuwa na kijana ambaye nimeona ni-note hapa niwaeleze Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana kuna kijana anaitwa Cecilia Panga, ambaye Beijing International Marathon alipata gold medal. Ni binti, sawa yupo jeshini lakini ndiye aliyetuletea Tanzania hiyo gold medal. Kuna binti mwingine Madgalena Shauri alikuwa wa tano Hamburg Marathon ambayo ilihusisha wakimbiaji 25,000. Ukiwa wa tano hapo lazima ushikwe mkono kusema kijana umefanya vizuri. Tulikuwa na mwingine Emmanuel Giliki Gesamuda alipata gold medal Shanghai International Marathon.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ushindi wote huu tunapata lakini huwa tunakaa kimya, safari hii sikai kimya itabidi tu tupige sound sana hapa tunapopata mafanikio yoyote. Hii ni kwa sababu tukikaa kimya tutaonekana kwamba hakuna kinachofanyika, mengi yanafanyika na yote ni juhudi ya Serikali si kama, kuna Mheshimiwa Mbunge mmoja anasema kwamba hiyo ni juhudi binafsi, hapana. Juhudi binafsi gani, Serikali ndio ina-create hiyo enabling environment tunafanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna hoja ya kufufua vyuo vya michezo nchini ili viweze kuendelea kutoa mafunzo kwa Walimu wa michezo. Vyuo vya Ualimu vya shahada na stahada ya elimu ya michezo na sanaa vipo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Ninaomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, tunaongea vizuri sana na Wizara ya Elimu na Mheshimiwa Waziri kuhusu kuvirejesha angalau tuanze polepole baadhi ya vyuo sasa viendelee na ile mitaala ya nyuma ya michezo na sanaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Elimu kwa kuwa very proactive na tayari tumeshakaa mara ya kwanza, wanaendelea wataalam wetu kuliangalia hili suala kwa undani. Wizara ya Habari sisi tuna chuo pekee cha Maendeleo ya Michezo, Malya kinachotoa stashahada ya michezo katika nyanja za uongozi na utawala katika michezo, elimu ya ufundishaji michezo na elimu kwa michezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tu Mheshimiwa Waziri wa Elimu aliposikia ametajwa kuhusu chuo hiki ambacho wala hakisimamii, lakini tayari amesema kuna umuhimu sana watendaji wetu wakae chini waangalie hiki chuo kama Wizara ya Elimu nayo ifanye nini. Kwa hiyo, yote haya ni maendeleo makubwa na nina uhakika tutafika mbali sana katika ushirikiano huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja nyingine, iliyotolewa na Mheshimiwa Silafu Maufi kwamba kwa nini bajeti ya Wizara imeshuka sana na vilevile Kamati yangu ya Bunge nayo imeongelea hivyo hivyo. Naomba niseme hapana. Nafikiri pengine ilikuwa ni makosa tu ya kuandika kwa sababu Kamati hii ya Kudumu ya Bunge imenisaidia sana, imeisaidia sana Wizara kupata bajeti kubwa zaidi. Bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 ni shilingi bilioni 33.35 ikilinganishwa na ya mwaka jana iliyokuwa shilingi bilioni 28.21, ni ongezeko kubwa, ongezeko la asilimia kumi na nane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lilikuwepo suala pia ambalo ameuliza Mheshimiwa Maufi kwamba sababu za bajeti ya mishahara ya Wizara kupungua. Nimewaelezea kwa kirefu kwenye hotuba yangu ukurasa wa 14 kwamba sababu ni kuhama kwa Idara ya Maendeleo ya Vijana kwenda Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado watu wengi wanadhani Idara ya Vijana ipo Wizara ya Habari, hapana imeenda Ofisi ya Waziri Mkuu. Kutokana na kuhama kwa ile idara ambayo ilikuwa kubwa ndiyo maana kumetokea kitu kama hicho. Vile vile kuna mambo mengine pia ya vyeti feki na wengi wametoka kwa hiyo lazima mishahara itaonesha upungufu huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chaneli ya Bunge ionekane mubashara kwenye chaneli zote. Hii hoja ni ya Mheshimiwa Devotha Minja na imeungwa mkono na Waheshimiwa Wabunge wengi tu, lakini kwa ajili ya muda nashindwa kupanga majina sasa hivi hapa. Ningeomba tu nisisitize kwamba wahusika wa hii Chaneli ya Bunge ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na nina uhakika anayehusika zaidi hapa ni Spika si mimi, kwa sababu ndio anayesimamia hiyo chaneli, ni ya kwake, ni ya Bunge la Jamhuri ya Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Mbunge akihoji kukosoa Serikali baadhi ya taarifa zinahaririwa na kutoonekana kwenye chaneli hiyo wakati zinaonekana kwenye hansard. Lah! Hii ni tuhuma nzito sana Mheshimiwa Devotha Minja, hili haliko kwangu, vile vile bado linaelekezwa kwa Mheshimiwa Spika ninyi ndio mwenye hansard na hiyo Chaneli ya Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini magazeti yanasajiliwa upya kila mwaka. Nataka niseme tu kwa kifupi sana kwamba chini ya Sheria mpya ya Magazeti, Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya mwaka 2016, kwa kweli magazeti husajiliwa mara moja tu na kupewa leseni ya uchapishaji kila mwaka. Pengine alikuwa ana maana hiyo kwamba leseni ya uchapishaji kwa nini iwe kila mwaka. Sheria hii ilipitishwa na Bunge hili Tukufu kwa lengo la kuimarisha sekta ya habari na kuondoa ubabaishaji uliokuwepo. Kuna watu walikuwa wanakaa tu na vichwa vya majina ya magazeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilibidi Mkurugenzi wa Maelezo mwaka jana afute vichwa vya magazeti 200, vimekaa tu ooh “Mwakyembe Leo” sijui ‘Devotha Kesho” yaani jina tu la gazeti liko pale wakati halina kazi. Ndiyo maana tunasema kwamba kuonyesha upo live na uko serious, si kwamba inatokea opportunity imetokea sasa nafasi uanze kuandika mambo yako kumshambulia mtu ndio unaanzisha hilo gazeti, unaanza kulifanyia kazi. Ndio maana tukasema hapana kama upo serious basi hata kama ada ni ndogo lakini kila mwaka ulipe, lakini leseni unabaki nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamba kwa nini vyombo vya habari vinavyokosoa Serikali vinafungiwa, Serikali ingalie upya suala la kufungia magazeti. Ukweli kwa heshima na taadhima, hili suala limeulizwa vilevile na Mheshimiwa Lucy Owenya na Mheshimiwa Aida Joseph Khenani. Sheria ya Huduma za Habari imeeleza wazi makosa yanayostahili kupewa adhabu iwapo vyombo vya habari vitakiuka sheria hiyo. Vyombo vya habari vinavyofungiwa vimekiuka sheria na ni pale ambapo suala la usalama wa nchi limeguswa. Hata Dkt. Ally Yusuph anasema Serikali isifungie magazeti na redio, Waziri avilee vyombo vya habari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemwelewa. Nataka nimweleze kwamba tunawalea vizuri waandishi wa habari kwa sababu hatujawahi hata siku moja kuchukua hatua bila kukaa na vyombo vya habari mara tano, sita, saba; ndugu zetu angalieni hiki sio sahihi. Kulikuwepo na aina fulani ya fikra katika nchi yetu kwamba uhuru unaweza ukawa usiwe na mipaka. Sasa hao tunaona sasa wamezidi kiasi lazima sasa tuwafundishe kwa kuwafungia kwa muda na wengi wanaporudi wanaenda vizuri tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ni kulea vile vile tunapeleka waandishi wa habari nje ya nchi kwenda kusoma. Kwa mfano mwaka jana tumepeleka vijana 10 China waandishi wa habari, wawili kutoka Serikali na wanane kutoka private media, kwenye hilo hatufanyi kabisa upendeleo. Mwaka huu tumeshapata nafasi za masomo China na Sweden na nawahakikishia tutakuwa na waandishi wa habari wa vyombo binafsi wengi zaidi kupita wa Serikali kwa sababu wote wanatimiza lengo kubwa la kikatiba la kuhabarisha umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Devotha Minja vile vile na Mheshimiwa Lucy Owenya wanasema kwa nini Serikali haitoi tamko pale waandishi wanapotekwa na wengine kupotea. Lah! Sasa Mheshimiwa Minja ananipa mtihani mgumu sana na ametoa mfano kwa mfano mwandishi wa Guardian.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe ushauri kwa mfano huu alioutoa wa mwandishi wa Guardian; hebu naomba yeye mwenyewe aulizie vizuri alikuwa wapi maana nisingependa mimi kuwa sasa chanzo cha kuharibia majina watu hapa. Yeye mwenyewe aulizie alikuwa wapi, atapata majibu tu huko Guardian maana yupo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana tumefika kipindi ambacho kuna watu wengine wanajiteka wenyewe. Sasa mimi Waziri mzima nikakurupuka kutoa statement wakati suala lenyewe ni la jinai linahusu polisi, nafikiri polisi wakishapeleleza basi na sisi tunaweza tukatoa kauli. Tunaheshimu na kuthamini sana waandishi wetu, mchango wao ni mkubwa katika maendeleo ya Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa George Lubeleje, anasema Serikali ina mpango gani wa kuboresha maslahi ya wafanyakazi wa TBC na Maafisa Habari wa Idara ya Habari Maelezo. Mheshimiwa Lubeleje, kaka yangu namheshimu sana, namshukuru sana kwa mapenzi makubwa aliyonayo kwa waandishi wa habari wa TBC na wengine wa Idara ya Habari Maelezo. Nadhani tuwe wakweli; watumishi wa Idara ya Habari Maelezo, watumishi wa TBC, hawa ni waajiriwa wa Serikali ambao maslahi yao huboreshwa sambamba na watumishi wengine wa Serikali. Mimi sioni kama wana matatizo makubwa hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwe mkweli na nilishashutumiwa sana katika Bunge hili kwa kusema ukweli, kwamba watu ambao ni wa kuwaonea huruma ni waandishi wa habari ambao wako kwenye vyombo binafsi. Kuna waandishi wanapata, si kima cha chini, ni chini ya kima cha chini cha mshahara, ni mishahara ya kitumwa wanayopewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hili, mwandishi wa habari abishe aende nyumbani kwake mke wake atamkuta amekasirika kwa sababu nyumbani hajaacha kitu. Hakuna mkataba wa kazi, vijana wangu wanachezewa sana, hawawekewi bima, hakuna kuwekewa pesa kwenye Mifuko ya Jamii; ndiyo maana sheria hii mpya, nawaomba waandishi wa habari jitokezeni mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachoogopa sisi tukiunda Media Council hapa watasema ni ya kwetu Serikali; waunde Media Council yao tutawasaidia. Chini ya sheria hii wana uhakika wa kuwa na ajira inayowalinda wao wenyewe. Waandishi wa habari wengi hawaelewi wanapiga kelele ya wamiliki, ndiyo shida hiyo tuliyonayo. Nashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Lijualikali anasema kuna ubaguzi mkubwa katika kutoa adhabu katika baadhi ya magazeti, magazeti mengine yanafungiwa. Kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari, kama nilivyosema, kuna namna mbili za utoaji wa adhabu; kama kosa linaathiri usalama wa Taifa kwa kuihusisha Serikali au viongozi wa kitaifa ambao hawawezi kujitetea, Waziri anaweza kutumia kifungu cha 59 cha sheria dhidi ya gazeti husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ni mtu binafsi, akidhalilishwa na gazeti hiyo ni kesi ya kudhalilishwa, ni kesi ya defamation, anaweza kulalamika Idara ya Habari Maelezo ili hatua za kimaadili zichukuliwe, lakini vile vile anaweza kabisa kwenda mahakamani kupitia kifungu cha 41 cha sheria kudai fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa si Maelezo wala Wizara ambayo imepokea malalamiko rasmi ya viongozi au mtu yeyote kunyanyaswa na gazeti tusichukue hatua. Tulipata kesi moja ya gazeti moja linasemwa sana hapa, tuliwaita Wahariri, tumewaandikia onyo la mwisho lakini haikuwa onyo kwamba wametishia kitu chochote, walimchafua mwenzao kwamba utapelekwa mahakamani na hii ni kinyume cha maadili; huo wajibu tunaufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, usikivu wa TBC Nkasi Kusini, kandokando ya Ziwa Nyasa; namwomba Mheshimiwa Desderius John Mipata kuwa ndugu yangu akae mkao wa usikivu mzuri tu kwa sababu katika bajeti tuliyoweka sasa hivi tunaweka transmitter mpya Mbeya, transmitter mpya Dodoma, lakini vilevile namhakikishia kwamba katika bajeti hii inayokuja eneo lake pia lipo kati ya maeneo ambayo tumeyapa kipaumbele, ikiwemo Zanzibar na Simiyu vilevile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, usikivu wa Redio Zanzibar, Mheshimiwa Machano Othman; kama nilivyosema katika bajeti ya mwaka huu ambayo naomba aipitishe leo Mheshimiwa Machano Othman, tuna Zanzibar, Songwe, Simiyu, Njombe, Katavi kuweza kuyafikia na nina uhakika tutayafikia. Tumeshapata uzoefu wa maeneo tuliyopitia sasa hivi; Rombo, Kibondo, Nyasa, Longido na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kusajiliwa na kulipwa tozo kwa blogu; Mheshimiwa Devota amelalamikia kuhusu suala la kulipa tozo kwa blogu mbalimbali kwamba tunaonea; lakini si yeye tu, Waheshimiwa Wabunge wengi wamelalamikia sana hizi kanuni mpya tulizozitoa. Nataka nitoe taarifa tu kwamba wakati humu sisi tunaongea, taarifa nimeipata dakika kumi zilizopita kwamba usajili wa watoa huduma za maudhui mtandaoni, maombi tuliyopokea mpaka sasa ni 86 na tumesha-approve moja ambayo vigezo vyote vimekamilika. Wengine wanaendelea kusaidiwa, kuelekezwa ili warekebishe karatasi zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tumechukua hatua hiyo? Waheshimiwa Wabunge naomba kwa sababu ninyi ndio wawakilishi wa wananchi, vyombo hivi sasa duniani vinabeba nafasi sawa na vyombo rasmi vya habari katika kuhabarisha. Nina uhakika ndani ya mwaka mmoja, miwili,
mitatu ijayo, vitakuwa vyombo vikubwa zaidi vya kuhabarisha kuliko hata vyombo rasmi tulivyonavyo kama TV, magazeti na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wetu Tanzania vyombo hivi; blogu, majukwaa mitandaoni, redio na TV mtandaoni vimeanza pole pole kuwa vyombo muhimu na vikubwa vya kuhabarisha na kuhabarishana na kutaarifu na kutaarifiana. Leo hii itisha press conference Mheshimiwa Mbunge, vyombo vitakavyokuwa mbele yako pale, vyombo rasmi vitakuwa vinne, lakini utashangaa microphones mara nne ya pale au mara tatu, mara mbili ni vyombo hivi vya kimtandao. Vimeanza kuwa ni vikubwa, vimeanza kuwa ni muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo ni kwamba tofauti na wenzao wale wachache, hawana utambulisho rasmi kuwa ni wanahabari, hilo la kwanza. Hawana miiko wala masharti rasmi ya kazi, wao ilimradi kimetoka, wapo pale wanachukua habari. Hawabanwi na maadili yoyote katika kazi wanayofanya; hawalipi kodi pamoja na kwamba wanashindana na vyombo rasmi vinavyolipa kodi kugombea matangazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani, tuwe fair, let us be fair. Tunachokifanya sisi sio peke yetu, tumefanya utafiti nchi nyingi zimefanya hivyo na lazima tuwahi, tusije tukajikuta tumetengeneza dude kubwa likatushinda mbele ya safari. Watu wengi siku hizi ndugu zangu, si Tanzania tu, wanaweza akakaa siku moja, mbili, tatu, hata wiki nzima hajasoma gazeti wala hajaangalia TV, yeye yuko bize na twitter, anaangalia tu kuna nini kwenye instagram, kuna nini kwenye mitandao, inamtosha, imemhabarisha, sasa hivi ndiyo imeendelea hiyo trend sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi vyombo vina changamoto kubwa vile vile, vimekuwa sasa mainstream katika kuhabarisha umma, lazima viwe na maadili, viwe na miiko. Sababu, tatizo kubwa la vyombo vya mitandaoni ni fake news, kama wanavyosema Wamarekani, ni taarifa za
upotoshaji, za uongo, kwa sababu hao watu wamechukua, ni kikundi tu cha kuongea, unaongea unachotaka, lakini kuna watu wanachukulia kwa nguvu sana kwamba ni ukweli. Kuna nchi zimekaribia kwenda vitani kwa ajili ya taarifa fake, taarifa za uongo katika vyombo hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu, na kwa mujibu wa taarifa ya mwaka 2017 ya Freedom House, wote mnaijua hiyo; ni chombo cha wanaharakati wa kidemokrasia, wanasema asilimia 75 ya nchi duniani zote zimechukua hatua kudhibiti maudhui katika mitandao; lazima zidhibiti. Wao wanasema wanalinda watoto, sisi ndio hatuna watoto? Nasi tuna watoto. Kwa hiyo na sisi tumesukumwa na sababu hizo hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu nyingine upande wa Tanzania ni hitaji la wanahabari mitandaoni kutaka nao watambuliwe kama wanahabari. Imetokea wakati amekuja Rais wa FIFA hapa, Infantino, anataka waandishi wa habari 20 tu wenye press cards, hawa hawana. Wakasema, Waziri tunataka na sisi tutambuliwe, tukasema lakini ninyi sijui ni watu gani, sijui na ninyi ni waandishi, nao wanataka watambuliwe kama ni formal media institutions. Sasa tulichokifanya ni hicho, ni kuwaweka nao kuwa wanatambuliwa kama wanahabari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ukisoma taarifa ya Reporters Without Borders, nao ni wanaharakati wa demokrasia hawa, wanataja nchi nyingi ambazo zimeweka masharti katika kutumia mitandao. Nchi nyingi ambazo ni kongwe kidemokrasia zimo humo; Marekani, Australia, Uingereza, Canada, India na kadhalika, ambao hoja yao kuu ni kuwalinda watoto. Sasa sisi hatuna watoto jamani, sisi ndio hatuna watoto?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata sisi Tanzania tuna wajibu wa kuweka mazingira ya matumizi salama ya mitandao ama sivyo, kama nilivyosema kwenye kitabu changu, ukurasa wa 64, teknolojia badala ya kuitumia, itatutumia na ni madhara makubwa sana mbele ya safari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu vyombo hivi vinafanya kazi ya Kikatiba ndiyo maana kwa kweli tumesema tuchukue hatua. hivyo basi, kanuni zetu zinatambua kazi yao, hawa wenzetu wa blogu na kadhalika na zinawaingiza kwenye mfumo ule ule wa maadili wa vyombo vingine vya habari na kama kuna tatizo tuongee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kwenye mitandao ni kwamba tunawatoza dola 925 kwa mwaka, hapana, kiingilio ni shilingi laki moja. Sema muda sina, lakini naweza kuonesha tunavyowatoza wale wenye vyombo vyenyewe vilivyokaa, wao tunawatoza shilingi laki moja, lakini vyombo rasmi tunavitoza, kama TV kweli iko pale, ni dola 5,000, hawa laki moja, wengine dola 5,000. Sasa tufike tu-argue lakini tukiwa na facts tayari. Baadaye nikiulizwa nitatoa, ninazo hizo figures tayari lakini nikizitoa sasa hivi nitatumia muda mrefu mno na nafikiri sasa hivi nitapigiwa kengele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naambiwa fungiafungia kwa wasanii, msanii mzuri, anafanya kazi nzuri, akikosea mnamfungia. Mimi nashindwa kuelewa, hivi tungefungia wasanii 20, nafikiri hii nchi ingepasuka. Sisi ni walezi, kama wenzetu ni walezi ninyi ndani ya nyumba, mtoto anakosea unamuimbia nyimbo kumsifu, sisi wengine ni walezi ambao mtoto akikosea lazima ajue kwamba kuna adhabu. Kwa sababu wengine wataendelea kufanya hivyo na hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ameeleza vizuri Mheshimiwa Naibu Waziri hapa; tuna utaratibu mzuri sana kisheria, usitoe wimbo wowote bila kwanza kupata opinion, ushauri wa BASATA, BASATA ni walezi; hakuna anayefanya. Nchi hii imezoea, utii wa sheria bila shuruti ni kitu cha ajabu, siku hizi imekuwa yaani lazima mtu afanye anavyotaka. Sasa tukiingia kwenye sheria maneno yanaweza kuwa mengi sana. Hakuna mtu tuliyemfungia tukasema wewe sasa sio msanii tena, tunataka vijana waelewe wana wajibu kwa hii jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Mheshimiwa Amina Mollel ameeleza hapa, jana amenionesha picha ya ajabu sana inazunguka kwenye mitandao. Wako kwenye steji jamaa anatoza pesa nyingi, laki mbili watu kuingia mle ndani lakini mule wanaitwa watu wasimame wavue nguo, mengine siwezi kusema, hii ni TV, lakini hayo mambo hatuwezi kukubali nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuja hapa na kitu very controversial tunakifanyia utafiti ndani ya Wizara yangu. Wenye pesa Ulaya wengi ni mashoga, wameanzisha foundations, yametawanywa kila nchi Afrika. Sasa hivi Tanzania tumekuwa earmarked kama kitovu kizuri cha kuwa ndiyo centre ya huduma za mashoga katika Bara la Afrika, hatuwezi kukubali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upuuzi huu upitie kwenye mitandao, usipitie kwenye mitandao sisi tutadhibiti; wakubwa wakasirike, wasikasirike, hili ni Taifa letu lina maadili yake na utamaduni wake. Mwalimu alisema; sitasahau hilo; Taifa lisilo na utamaduni wake ni taifa mfu na sisi sio taifa mfu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la visimbuzi, imetoka kwa Mheshimiwa Chumi, kwamba ni kwa nini havioneshi hizi TV stations zetu tano, sita, saba ambazo ni Free to Air. Hili suala liko Mahakamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa harakaharaka, naona kengele ya kwanza imelia. Mheshimiwa Shekilindi amesema Serikali iwasimamie wasanii wasidhulumiwe. Kwa kweli dhuluma ilikuwepo kubwa sana kwa kutumia middlemen, watu wenye pesa wamewachezea sana wasanii wetu Tanzania. Hili limeanza kubadilika, tumeanza kuwa-empower wasanii wetu kwa kutumia TEHAMA, wasitumie middlemen.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba msome kitabu change nimeeleza vizuri njia tulizotumia, lakini wachukulie vijana wazuri kama akina marehemu Kanumba, amefariki Kanumba kila mtu anajua ni milionea, hapana, waliotajirika ni wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii mwanasanaa mzuri mzee Majuto anaumwa, anaomba pesa mimi nachanga kutoka mfukoni. Leo hii nusu ya mabango ya biashara ni ya Majuto, matangazo ya biashara kwenye TV ni Majuto. Naomba sasa nitumie nafasi hii kusema nimeunda Kamati ya Wanasheria, tunaanza na kesi ya mzee Majuto. Mashirika yote, kampuni zote zilizoingia mkataba na Majuto tutapitia hiyo mikataba kama ameonewa lazima ilipwe familia yake; tumeshachoka. Tukishamaliza Majuto tutarudi kwa Kanumba, na msanii yeyote ambaye anaona aliingia mkataba wa kipumbavu aje atuone. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inaudhi lakini ndiyo hivyo. Leo mzee yuko hospitali anakosa shilingi laki tano, mimi Waziri nitume, pesa yenyewe ndiyo hiyo mnaelewa maisha yalivyo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja tu nitakalolaumiwa na wananchi, kwamba Mheshimiwa Amina Mollel amesema kuna Mtanzania aliyetoroka kambi. Ni kweli kabisa, tumepata aibu, kati ya vijana wetu waliokwenda Australia kwenye mashindano ya Commonwealth mmoja amejongo huko, amepotea huko, hakurudi na jina lake kweli kama alivyosema Mheshimiwa Amina Mollel, ni Fatihiya Hassan Pazi wa Ukonga, Dar es Salaam, ambaye alikuwa mmoja wa wachezaji wetu wa table tennis, mzuri sana katika table tennis.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulimpeleka China kama nilivyosema siku themanini kuimarisha kazi yake na walifanya kazi nzuri sana, baada ya kumaliza mchezo tarehe 11, Aprili, tarehe 12 hakuonekana. Kiongozi wetu, Dkt. Singo ambaye alikuwa nao alijua kabisa huyu hajapata ajali maana alikuwa ametoatoa nguo zake zote safi akaacha tu traksuti mle ndani, na vile vile jana yake alikuwa amenunua pia na sim card ya kule, kwa hiyo ilikuwa ni maandalizi tu ya kupotea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini alivyokwenda polisi kuripoti akakutana na wenzetu wa Kenya wakisema nao wawili wamepotea; Uganda nao wawili wamepotea. Aliyekuja ameinamisha shingo kabisa alikuwa ni mtu kutoka Cameroon, wanane walikuwa wameondoka kwenye kambi yake. Tumesharipoti hili suala mambo ya nje na uhamiaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Nazipongeza Kamati zote tatu kwa taarifa ambazo zimewasilishwa mapema leo asubuhi na naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Spika, pili, nina kila sababu kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uthubutu, upeo mpana alionao na ujasiri anaouonyesha hasa pale ambapo anaziona fursa za kusukuma mbele Taifa hili. Nasema hivyo kwa sababu mwaka jana tulitembelewa na Rais wa FIFA na alipofika Mheshimiwa Rais aliacha ujumbe mfupi sana na huo ujumbe aliuwasilisha Waziri Mkuu wetu Mheshimiwa Kassim Majaliwa kwamba Rais anachotaka ni viwanja kumi vizuri.

Mheshimiwa Spika, nafikiri Rais wa FIFA hajazoea vitu kama hivyo, kwa kweli aliupokea huo ujumbe kutoka nchi ambayo imedhamiria kazi. Alichoahidi tu ni kwamba atashirikiana na nchi yetu na kuisaidia kuifungulia TFF haraka ile kesi iliyokuwa imefungwa na ana uhakika kwamba tutapata viwanja hivyo na tutawasiliana naye. Naomba tu nitoe taarifa kwamba sasa hivi tumefunguliwa na FIFA, msaada wa FIFA umeanza kuja. Kwa kweli ile rai ya Mheshimiwa Rais tutaanza kuitekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kifupi napenda kusema kwamba tumekaa na wenzetu wa TFF na sehemu ya fedha fedha ambayo tumepata tutaitumia kuboresha viwanja kumi nchini kwa kuanzia kama ambavyo Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alivyotaka. Kwa sababu Aprili, Rais wa FIFA Gianni Infantino atakuwa hapa si ajabu akaulizia kuhusu hilo, ndiyo maana kwa kweli tumeona hilo lazima tulitekeleze. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mbali na viwanja hivyo kumi, tutakarabati upya kabisa Uwanja wa Karume, kujenga hostel mpya, ofisi na majukwaa ya uwanja huo. Mimi naahidi hatutarejea tulikotoka maana kulikuwa na udokozi mkubwa kweli TFF. Miaka kadhaa iliyopita nchi tano, sita kila nchi tulipewa dola 400,000, sisi tukaishia kujenga vile vibanda pale Ilala, lakini Rwanda na Sudan wana maghorofa, huwezi kuamini tulipewa pamoja. Vilevile tutajenga Hosteli ya TFF Tanga, madarasa na ukumbi mkubwa pamoja na kiwanja, kwa hiyo tunaendelea vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika fedha iliyoanza kuingia ilikuwa shilingi milioni kadhaa mara moja nimeona TFF wakitenga pesa kwenda ZFA, zaidi ya shilingi milioni 100. Tutaendelea na ushirikiano namna hiyo.

Mheshimiwa Spika, kuna hoja aliyoitoa leo asubuhi Mheshimiwa Khatib Haji kuhusu uhusiano kati ya TFF na ZFA. Kwa kifupi sana TFF na ZFA ni mashirikisho dada, nikitumia muktadha wa Kiingereza kama sister federations. Moja inasimamia soka upande wa Tanzania Bara na nyingine Tanzania Zanzibar. Mashirika haya mawili ni wanachama wa CECAFA wanaojitegemea, CECAFA ina nchi 11 lakini tukienda CAF vilevile tunajitegemea lakini ujumbe wa Zanzibar siyo kamili sana kwa sababu ni mwanachama ambaye ni associate, ni mshiriki. Ndiyo Zanzibar anapata kila kitu lakini hawezi kupiga kura. Tunapokwenda FIFA (Shirikisho la Mpira Duniani), hapa ndipo ambapo Zanzibar hawana nafasi kabisa inabidi kwa kweli wasimamiwe na wenzao wa TFF.

Mheshimiwa Spika, nachotaka kusisitiza hapa ni kwamba tutambue kwamba TFF na ZFA si idara za Serikali, hizi ni taasisi huru zenye vyombo vyake vya maamuzi, Wizara sisi tunao tu ule ushawishi wa kisera. Nataka niendelee kuamini kuwa ZFA itaendelea kupokea misaada mbalimbali kutoka FIFA kupitia TFF. Pale penye utata, vyombo hivi viwili viendelee kujadiliana na ukiwa mkubwa zaidi basi wasisite kutuona sisi. Kwanza nisisitize tu kwamba wenzetu ZFA wasinyamaze wakiona kuna tatizo na pengine kutafuta mpaka Wabunge waje waliongee suala hilo ndani ya Bunge hili.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Haji nikusisitizie tu kwamba tunaongelea Uwanja wa Gombani kama tulivyosema leo asubuhi tumeutolea mfano, ni kama vile ambavyo tunatoa mfano hapa wa viwanja viwili tu pamoja na ukubwa wa nchi hii; ni Uwanja wa Kaitaba na Uwanja wa Nyamagana. Ni kwa sababu tulikotoka kwa kweli matumizi ya pesa hayakuwa mazuri sana; pengine tungepata viwanja kumi kumi kama tungekuwa waangalifu lakini sasa tumefungua ukurasa mpya kama nilivyosema.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la Mheshimiwa Nkamia na Mheshimiwa Kabati kuhusu Ligi ya Wanawake na ligi za Daraja la Kwanza na nyingine, pale ambapo ligi hizi hazina ufadhili (sponsorship) kwa kweli kuandaa home and away matches ni kuwatesa sana vijana wetu. Nawahakikishia kwamba tutakaa chini tuliangalie upya na nawaonea huruma Waheshimiwa Wabunge wengi sana wanabeba mizigo hiyo ya kusafirisha timu na kuzilaza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mwamoto ameongelea kuhusu mashindano ya AFCON. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mwamoto kwamba limekaa vizuri kama ambavyo Mheshimiwa Waziri Mkuu amelielezea vizuri leo asubuhi. Tuna Local Organizing Committee ambayo naiongoza mimi lakini ina wajumbe wengi kutoka taasisi mbalimbali za Serikali na tuna viongozi mbalimbali kama wajumbe akiwemo Waziri wa Maliasili na Utali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji na viongozi wengine mbalimbali na kwa kweli tumejipanga ili mwezi Aprili kisiharibike kitu. Tarehe 12 naongea na Wahariri wa vyombo vya habari kuhusu ugeni mkubwa tutakaoupata na tutaanzisha hiyo kampeni nchi nzima. Vilevile tarehe 14 tunakutana tena kuweza kujadiliana kwa kirefu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mara nyingi umeshakuwa mgeni rasmi kwenye mechi, Uwanja wa Taifa uko katika ukarabati mkubwa sana. Vilevile Uwanja wa Uhuru uko kwenye ukarabati mkubwa ambapo tunang’oa kabisa zile nyasi na nyasi zake za bandia ziko melini na tutaziweka baada ya muda si mrefu pale uwanjani. Uwanja mwingine wa Chamanzi ambao utatumika ukarabati wake unamaliziwa, kwa hiyo umekaa vizuri sana.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Joseph Mbilinyi ameshangaa CCM kumiliki Channel Ten na Magic FM, sijui kama yupo…

MBUNGE FULANI: Hawezi kuwepo.

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, atapata ujumbe tu kwamba asisahau kuwa CCM ina vyombo vya habari vyenye umri sawa na uhuru wa nchi hii. Vyombo vingine kimkakati ni kawaida duniani kushikiliwa na wapenzi wa chama na si kitu cha ajabu sana. Kwa mfano, gazeti la Tanzania Daima linamilikiwa na mpenzi wa CHADEMA, si la CHADEMA ni la mpenzi wa CHADEMA lakini siku litakapohamia CHADEMA utashangaa kweli? Huwezi kushangaa! Sasa unashanga kwa nini anashangaa mpenzi wa CCM aliyekuwa na chombo kwenda CCM, asishangae ndivyo mambo yanavyokwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Kabati ameongelea soka la kike. Naomba nimhakikishie kwamba soka la kike linakwenda vizuri, mimi mwenyewe nimefarijika sana. Naomba niwakumbushe tu wenzetu hapa kwamba tuna Twiga Stars, tunasahau tunashikilia tu timu za wanaume, Twiga Stars ni ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamechukua kombe la CECAFA mara mbili mfululizo; mwaka 2016 na 2018. Hawa akina mama ni mashujaa kweli kweli na kwa kweli soka la kike tunalikazania sana. Kuna wenzao wengine Kilimanjaro Queens nayo imekuja juu; mmesikia hivi karibuni ikichukua ubingwa wa Afrika Mashariki kwa mara ya kwanza. Sifa ya timu hii ni kutokuwa na huruma inapocheza, inabamiza watu magoli mengi sana. Kwa mfano, mchezo wa kwanza na Burundi watu wengi walishangaa, ilikuwa ni taarifa Afrika nzima, baada ya kuipiga Burundi magoli nane kwa moja. Akina mama hawa hawana huruma kabisa, mchezo wa marudiano ikiwa tano bila. Ni timu nzuri sana na naomba nimtaje mfungaji bora ambaye ni Mwanahamisi ambaye peke yake alifunga magoli saba. Tumezoea kuwataja wanaume tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie tu kwa kuwaomba Waheshimiwa Wabunge ushiriki wao katika maandalizi ya AFCON ambayo yatafanyika Aprili na yatahusisha nchi nane bora katika Bara la Afrika. Tuiombee Serengeti Boys, timu ambayo kwa kweli imebeba matumaini ya Watanzania. Ikishinda mechi mbili tu Tanzania kwa mara ya kwanza tangu uhuru tutashiriki katika Kombe la Dunia kupitia timu ya Serengeti.

Mheshimiwa Spika, sipendi uniambie nikae chini, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa. Nianze nami kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango na Naibu wake kwa kazi nzuri sana. Kwenye hotuba ya Waziri na makabrasha naona hapa, wameongelea kuhusu maboresho yanayofanyika Bandari ya Itungi, lakini kwa kifupi sana, nataka nieleze tu, kuyapanua kwa sababu nilikuwa huko hivi majuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli yanayotokea Bandari ya Itungi, ni mapinduzi makubwa, katika historia ya miundombinu nchini. Kwa sababu kwa mara ya kwanza toka Uhuru, Tanzania inajiondoa kwenye utegemezi kwa nchi ndogo ya Malawi katika kukarabati vyombo vyake vya majini. Sasa hivi kutokana na chelezo ambayo imefungwa pale, Tanzania tunaweza sasa katika Ziwa Nyasa kujenga vyombo vyetu sisi wenyewe, kuviunda vipya na kukarabati vyombo vipya. Sasa hivi zinajengwa bajezi mbili pamoja kuanzia mwezi wa sita tunajenga meli yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 200 za mizigo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni initiative ya TPA na baada ya pale wanahamia Lake Tanganyika na Lake Victoria. Kwa hiyo, wananchi wanaona hayo na tuendelee tu na juhudi hizo. Nimefurahi vilevile kusikia, kwenye hotuba ya Waziri kuhusu ujenzi wa hivi vituo, Kituo cha Utoaji Huduma Pamoja, hivi vinavyoitwa One Stop Border Posts, tumejenga nyingi kwa Rwanda, Burundi, tunayo Uganda, kwa mpaka wetu na Kenya tunazo tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunajenga Zambia, sasa ipo ya Malawi na Tanzania. Kwa kweli, ni taarifa nzuri sana kwa wafanyabiashara wa Malawi na Tanzania na vile vile fursa ya kufanya biashara kubwa kwa wananchi wa Wilaya Kyela na Kasumulu upande wa Malawi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dogo tu kuhusu masuala ya Katiba. Wiki hii tumekuwa tukijenga msingi wa kutekeleza masharti ya Ibara ya 63(3)(c) ya Katiba ambayo inasema; “Bunge hili, litajadili na kuidhinisha Mpango wa muda mrefu au muda mfupi wa Taifa.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, wengi walidhani Serikali inakuja na Mpango, ilionekana hapa katika majadiliano ya mwanzo pale. Inakuja na Mpango, hapana hapana, hili ni zoezi shirikishi la Kikatiba, linataka sisi tuchangie. Nataka nisisitize tu hapa kwamba, dhana ya zoezi hili kuwa shirikishi, linatokana na masharti ya Ibara ya 8 ya Katiba hii, inayosema kwamba; “Wananchi wa Tanzania ndiyo msingi wa mamlaka yote. Pili, lengo kuu la Serikali ni ustawi wa wananchi. Tatu, Serikali inawajibika kwa wananchi. Nne, wananchi washirikishwe au watashiriki katika shughuli za Serikali.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongeze maneno yangu, kupitia wawakilishi wao ambao ni Wabunge. Sasa Ibara ya 63(3)(c) inatutaka sisi wawakilishi wa wananchi, sasa tuchangie tuweze ku-reflect haya, kwamba Serikali katika mipango yake, inajali ustawi wa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikimbie tu neno moja dogo la haraka haraka lingine, maana muda wenyewe ndiyo huo. Kumekuwa pia na kejeli katika kuiangalia hii kaulimbiu ya hapa kazi tu, inaonekana kama ni kauli ngeni, kauli ya kipropaganda tu, lakini nataka kusisitiza hapa kwamba hii ni kaulimbiu ya Kikatiba, tena Katiba yenu wenyewe hii hapa, niliyoishika hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 25(1) inasema: “Kazi pekee ndio huzaa utajiri wa mali katika jamii, ndiyo chimbuko la ustawi wa wananchi na kipimo cha utu na kila mtu anao wajibu wa kushiriki kwa kujituma na kwa uaminifu katika kazi halali na ya uzalishaji mali.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Ibara ya 9(e), Katiba inasema; “Serikali itahakikisha kwamba kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi, anafanya kazi na kazi maana yake ni shughuli yoyote ya halali, inayompatia mtu riziki yake.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiendelea tena ibara ya 22 inatupa confidence, inasema…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DKT. HARRISON G. MWAKYEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kuwapongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kwanza kwa kuwasilisha hotuba ya Bajeti ya Wizara yao kwa ufasaha mkubwa na pili kwa kusimamia utekelezaji wa shughuli za Wizara kwa ujasiri mkubwa. Hivyo bila kigugumizi chochote, naunga mkono hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua fursa hii vilevile kuipongeza Wizara hii kwa kuitikia kilio changu cha muda mrefu cha kuanzisha Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Kyela. Kilio changu kiliitikiwa mwezi Julai, 2014 kwa kuanzisha Baraza hilo lakini kwa kutumia Mwenyekiti na Maafisa wengine wa Baraza ambao huazimwa kutoka Mbeya zaidi ya kilometa 100 kutoka Kyela.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu huo sasa umegeuka kero kubwa kwa wananchi kukosa huduma ya uhakika ya Baraza kutokana na Mwenyekiti na Maafisa wake kushindwa kufika Kyela pale inapobidi na kuwaacha wananchi wengi wakisubiri, wakienda na kurudi bila mafanikio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba Mheshimiwa Waziri na Naibu wake wanipatie uongozi/uendeshaji wa Baraza wa kudumu badala ya kusubiri maafisa wa kuazima kutoka Mbeya ambao hawafiki Kyela kwa sababu wanazozijua wenyewe. Nina uhakika, timu hii imara ya uongozi wa Wizara itasikia ombi langu na kulifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara nyingine tena naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kushukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa hotuba nzuri iliyosheheni maoni na ushauri ambao Wizara yangu inaahidi kuuchukua na kuufanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, aidha, nitumie nafasi hii vilevile kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia katika hotuba yangu ya bajeti ya mwaka 2019/20 kwa kauli na kwa maandishi. Michango mingi iliyotolewa kwa kweli inalenga kuimarisha na kuendeleza Sekta ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na ni sekta ambazo zinasimamiwa na Wizara yangu, hivyo, niseme tu kwamba michango yote tumeipokea na tutaizingatia katika utekelezaji wa majukumu kwani wajibu wetu sote ni kuwahudumia Watanzania waliotupa dhamana na wenye matarajio mbalimbali kwetu.

Mheshimiwa Spika, kutokana na muda, nitajibu machache. Kwa kifupi bajeti yangu imechangiwa na Waheshimiwa Wabunge 46 ambapo waliochangia kwa maandishi ni 28 na kwa kauli ni 18. Niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliotambua jitihada zinazofanywa na Wizara katika kuendeleza sekta inazozisimamia kwa kutoa pongezi mbalimbali. Kwa niaba ya Wizara nazipokea pongezi hizo na ushauri uliotolewa kwa kuboresha zaidi utekelezaji wa majukumu yetu.

Mheshimiwa Spika, namshukuru vilevile Naibu Waziri kwa kutolea ufafanuzi hoja kadhaa, tena nyingi, kwa haraka. Nami nitatolea ufafanuzi hoja zingine chache kadri muda utakavyoruhusu.

Mheshimiwa Spika, nianze na mchango adhimu wa Mheshimiwa Dkt. Jasmine Tisekwa ambaye aliongelea masuala mengi muhimu kuhusu uzalendo na umuhimu wake katika maendeleo na ulinzi wa taifa. Ameongelea masuala ya Tunu za Taifa na umuhimu wake kwa maana ya utambulisho wa taifa ukiwemo Mwenge wa Uhuru, yote aliyoyasema namhakikishia Mheshimiwa Dkt. Tisekwa tumeyazingatia kwa maana ya kuyafanyia kazi ya ziada. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, moja tu la Mwenge nilitolee mkazo zaidi kwamba kila taifa duniani lina tunu zake ambazo zinalitambulisha na kulipa msingi wa uwepo wake na mwelekeo wa taifa hilo kisiasa, kijamii na kiuchumi. Waliotangulia kujitawala, chukulia wenzetu kama Wamarekani ambao wana Katiba ya mwaka 1787, wana stars and stripes (nyota na mistari) ambayo ni bendera yao na inaakisi historia na dira yao. Nyota zile 50 ni yale Majimbo yaliyoungana kuunda Marekani na ile mistari 13 ni yale makoloni yaliyomgomea Muingereza kuweza kuendelea kutawala. Pia wana tai kwenye nembo zao na tunu zao na yote hii inaashiria malengo pamoja na dhamira ya taifa hilo.

Mheshimiwa Spika, wenzetu Wahindi wana Tiranga, bendera yao yenye rangi tatu, ambayo inaashiria ujasiri, amani na imani. Vilevile katikati wana gurudumu ambalo linaelezea ndoto aliyokuwa nayo Mahatma Gandhi ya India kuwa na viwanda vya nguo kuweza kujitosheleza.

Mheshimiwa Spika, sisi tuna bendera yetu yenye rangi nne zinazoakisi amani na umoja na rasilimali tele ambazo Mungu ametubariki na ambazo sisi tuna wajibu wa kuzilinda kwa faida yetu na vizazi vinavyokuja. Pia tuna Mwenge wa Uhuru na Kiswahili. Kwa hiyo, utambulisho wetu umeainishwa kwenye sera, nina uhakika Waheshimiwa Wabunge wote wameiona Sera yetu ya Utamaduni lakini utekelezaji kisheria wa maudhui ya sera yetu haujawa wa kasi kutokana na Wizara zinazosimamia utamaduni kubadilika mara kwa mara, nafikiri tumekuwa na Wizara kumi zikisimamia utamaduni katika historia yetu.

Mheshimiwa Spika, nitoe tu mfano mdogo kwamba Sera yetu inasema lazima tuwe na taratibu maalum ambazo zitalinda hadhi ya utambulisho wetu. Nitoe mifano michache tu, kwanza, misingi ya Katiba ya Taifa ifundishwe kwa wanafunzi wote katika ngazi za elimu ya msingi na sekondari. Pili, Wimbo wa Taifa ufundishwe kwa wanafunzi wote kuanzia shule za awali na inasema Wimbo wa Taifa utaimbwa kila siku kabla wanafunzi hawajaingia darasani katika shule za awali, msingi na sekondari. Watu wote watasimama kuimba Wimbo wa Taifa kabla ya kuanza maonesho na michezo yote yenye hadhi ya kitaifa na kimataifa. Tatu, itakuwa marufuku kupandisha Bendera ya Taifa iliyopasuka au iliyopauka. Nne, Mwenge wa Uhuru utaendelea kukimbizwa nchini na Serikali itahakikisha kwamba wananchi wote wanauthamini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi naona ipo sababu pamoja na kwamba Wizara zinabadilikabadilika kwa hiyo utekelezaji wa maudhui wa mambo mengi imekuwa siyo rahisi sana, ipo sababu kwa kweli kwa Wizara kutafsiri maudhui ya sera kisheria ili tusiyumbe tena. Namshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Jasmine kwa mchango wake.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa William Ngeleja ameongelea maendeleo ya soka nchini na wengine wengi wamegusia suala hili. Ni kweli kabisa tumepiga hatua kubwa pamoja na Timu yetu ya Vijana kukwama kusonga mbele katika Fainali za AFCON Jijini Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, tumejifunza mengi, nimepata bahati ya kukutana na akina El Hadji Diouf, Tim Etoo na wengine ambao wapo Dar es Salaam kufuatilia vipaji vya Tanzania, wanasema Tanzania tayari ni kivutio cha mataifa na wataalam mbalimbali kuja kuangalia vipaji vilivyopo hapa. Siyo kwa kubahatisha ni kwa sababu sasa hivi, pengine Watanzania hatuoni tu lakini kwa kweli anayeongoza kwa ufungaji magoli Ulaya ni kijana kutoka Bara la Afrika na kijana kutoka Tanzania, kwa hiyo, tuna vivutio vingi sana. Tatizo letu ni kwamba tuko juu changamoto yetu ni kubakia hapo juu na kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante Mheshimiwa Ngeleja kwa wazo la kuwa na sports academies kikanda ili kuvuna vipaji vikubwa tulivyo navyo pembe zote za nchi. Wazo ni zuri lakini haliwezi kufanywa na Serikali peke yake, tunahitaji kwa kweli ushirikiano wa karibu na sekta binafsi. Changamoto tuliyonayo ni kwamba tunapovumbua vipaji vizuri sana kupitia UMITASHUMTA na UMISETA na vipaji vingine mitaani, tunakosa mahali pa kuvilea kwa mpangilio.

Mheshimiwa Spika, wakati tunahimiza sekta binafsi kushiriki katika ujenzi kwa kweli wa hizo academies kwenye kanda zetu, Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI na Wizara ya Elimu kwa kweli tunataka tuanze mara moja kujadiliana na sports academies zilizopo na zipo nyingi, kama tano, sita, tuangalie tunaweza kushirikiana kiasi gani kuweza kuchukua vijana wenye vipaji. Tuna Azam, Alliance ya Mwanza, Trust St. Patrick Schools Arusha, Lord Baden-Powell ambayo ipo Bagamoyo na Fountain Gate Academy Dodoma. Nafikiri tukikaa chini tunaweza tukaanza mahali fulani tukasogea. Nakuhakikishia tutafanya hivyo ndani ya muda siyo mrefu kutoka sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nije upande wa habari lakini naomba nianze na utangulizi mfupi ili tuelewane. Habari yoyote inayoandikwa na kuchapishwa yenye athari ya kuharibu sifa ya mtu katika jamii ni kashfa. Ni haki kwa mtu aliyekashifiwa kwenda Mahakamani kudai fidia kwa maumivu aliyosababishiwa chini ya kifungu cha 41 cha Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016. Mara zote tunawahimiza walalamikiwa kutumia kifungu cha 40 kuomba radhi (offer of amends) na ukiomba radhi kwa anayejisikia kuathirika, hakuna haja hata kwenda Mahakamani.

Mheshimiwa Spika, mara zote tunawasisitizia pia na ningependa pia hili lieleweke hapa kwamba tuepuke kujichukulia sheria mikononi kwa kumnanga aliyekukashifu kupitia njia mbalimbali za mawasiliano, sasa unaondoa uzito wa kesi yako mwenyewe. Wanasheria tunayo kanuni ya haki (equitable principle) ambayo inasema he who seeks equity should come with clean hands. Anayehitaka haki, basi njoo na mikono misafi. Ukisema umetupiwa madongo, kweli umejaa madongo kwenye shati na wewe umeshika madongo kumtupia mwingine, hoja yako haiwezi kuwa safi sana wakati na wewe una madongo mikononi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mkurugenzi wa Idara ya Habari ndiye mwenye mamlaka chini ya sheria ya kutoa Leseni ya Magazeti kuchapishwa na kuuzwa kwa kuzingatia masharti kadhaa. Hii siyo Tanzania tu, ipo duniani kote. Ana mamlaka chini ya sheria hiyo ya kifungu cha 9 ku-suspend, yaani kusimamisha leseni hiyo pala anapoona masharti ya leseni yanakiukwa. Tatizo la walio wengi, wakishasimamishiwa leseni, hawaendi Mahakamani, bali wanakimbilia kwenye Balozi. Hiki ni kitu cha ajabu nimekiona hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Devotha Minja alinioji, napata wapi mamlaka ya kufungia gazeti kwa muda; kama nilivyofanya huko nyuma? Nitamjibu, lakini nami namwomba kupita kwako atafakari ni kifungu kipi cha sheria kinasema usipokubaliana na Mkurugenzi wa Maelezo, basi kimbilia kwenye Balozi? Sijakiona hicho kifungu. Sijui, nadhani ni aina fulani ya ulimbukeni.

Mheshimiwa Spika, maana sheria inasema, kata rufaa kwa Waziri. Hakuna anayekata rufaa kwa Waziri na wanasema hata Waziri akishatoa uamuzi wake, bado una haki ya kwenda Mahakamani kumshungulikia huyo Waziri pamoja na Mkurugenzi. Hatutumii hiyo nafasi, tunakimbilia Ubalozi; na Balozi zinakuja kila mara kwetu nasi tunawajibu, mmesoma hiyo sheria?

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kumjibu Mheshimiwa Devotha kuwa Waziri ana mamlaka chini ya kifungu 59 kinachosema, Waziri ana mamlaka ya kuzuia uchapishaji wa maudhui yenye athari kwa usalama wa nchi au amani katika jamii. Waziri anafikia hatua hiyo siyo tu haraka haraka, hapana. Ni baada ya mtu kuonywa au gazeti kuonywa mara nyingi sana; mara nane, tisa, kumi. Nyie hamwezi kuona hivyo, kwa sababu hamfanyi kazi kwenye hayo magazeti. Sisi tunafahamu, hatuchukui hatua hizi bila kumwonya mtu mara kadhaa. Hii ni kwa mujibu wa mkataba wa Kimataifa wa haki za kisiasa na kiraia ya mwaka 1966. Wengi hawapendi kuisikia hiyo, lakini ndiyo hiyo International Covenant on Civil of Political Right duniani kote tumeridhia na hata wakubwa wanaitumia hiyo hiyo. Wewe mchukulie kama Bwana Hasanja ambaye huu ni mwaka wa saba hayupo huru akikwepa kupelekwa Marekani kujibu mashitaka ya kuhatarisha usalama wa Marekani. Ila kwa sababu ni Marekani, aah, ila Tanzania ikitumia hiyo sheria, haki za binadamu kwa sababu pengine NGO’s nyingi zinafadhiliwa kutoka huko, hatuoni hiyo ya huyo anayetoa hela.

Mheshimiwa Spika, siyo kweli, kinyume na alivyosema Mheshimiwa Devotha kuwa tunafungia magazeti kila siku. Sasa kila siku kweli! Pengine hiyo ni lugha tu, siyo kweli. Tulifungia magazeti manne mwaka juzi, 2017 ili Waandishi na wamiliki na wadau waelewe kuna sheria mpya ambayo walikuwa hawaitaki. Hawaitaki tu, hata kuisoma hawajaisoma.

Mheshimiwa Spika, leo hii nikisema nimwulize mtu gani ameisoma Sheria ya Huduma za Habari, naomba Mungu awe shahidi yangu nina uhakika, hata wanaolalamika hapa hawajaisoma hiyo sheria. Ndiyo tatizo letu kubwa tulionalo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka 2018 sijafungia gazeti lolote; ni juzi tu Citizen waliadhibiwa na Mkurugenzi kwa siku saba kwa kushindwa kufuata masharti ya leseni baada ya kuonywa na kuonywa. Baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wanadai kuwa Tanzanite halichukuliwi hatua, siyo kweli kwa sababu nyie hamko ofisini kwetu, uliza uweze kupata taarifa. Kwanza mnataka hatua zipi tuchukue? Kulifungia?

Ndugu zangu, malalamiko mengi zaidi ya Tanzanite, kama ilivyo kwa gazeti la Tanzania Daima na mengine, ni kashifa. Unakashiwa wewe, heshima yako imeshushwa; unaitaka dola ifanye nini kwa heshima yako kudhalilishwa? Nenda Mahakamani. Ukija kwetu, sisi kazi yetu kubwa ni kumwita chini ya kifungu cha 40 kumwambia omba radhi, huyu akikupeleka Mahakamani utalipa fidia kubwa. Wengi wanaomba radhi, wengine wanakwenda Mahakamani.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu muda wenyewe ndiyo unakimbia hivi, Mheshimiwa Aida Joseph Khenani amedai usalama wa wanahabari nchini ni mdogo sana, kuna vitisho, yaani ni hatarishi. Bahati mbaya ametoka, napenda nimwombe Mheshimiwa Mbunge kupitia kwako atembelee tovuti www.forb.com. Forb ni chombo maarufu cha takwimu duniani aangalie taarifa yao ya mwisho wa Desemba mwaka 2019 inayohusu deadliest countries for journalist in 2018, nchi hatari kweli kweli kwa Waandishi wa Habari duniani. Inataja India, Mexico, Marekani yenyewe, Brazil na Israel. Tanzania hatumo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawaomba Waheshimiwa Wabunge tupunguze Kauli kali sana hizi bila kufanya hata utafiti, pengine kwa sababu hatujui yanayotendeka sehemu nyingine.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Joseph Osmund Mbilinyi na Anatropia Theonest wameongelea uamuzi wa Mahakama ya Afrika Mashariki kukosoa baadhi ya vipengele kwenye Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 na kutaka viondolewe baadhi ya vifungu. Hii ni mara ya tatu sheria hii inapelekwa Mahakamani. Mara ya kwanza tulikwenda Mwanza haikufanikiwa, mara ya pili Mahakama Kuu Dar es Salaam haikufanikiwa. Sasa imepelekwa Mahakama ya Afrika ya Mashariki.

Mheshimiwa Spika, nataka kusisitiza hii ni haki ya Watanzania wanapoona hawajaridhishwa na maamuzi, pengine wana wasiwasi na maamuzi ya vyombo vya ndani, nenda, ndiyo fursa. Ndiyo maana nchi yetu inajivuna kwamba tumewapa wananchi wetu uhuru mpana. Nenda; Mahakama ya Afrika Mashariki wamekwenda. Wengine wanachukulia kama Serikali hapa imeshtuliwa kweli kwa kupelekwa Mahakamani. Hapana, sisi ni Waasisi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Spika, Mkataba wa Afrika Mashariki sehemu kubwa kwa Tanzania tumechangia na kuanzishwa hii Mahakama, nenda kwenye records, sisi ndiyo tumepiga kelele lazima tuwe na Mahakama ya Afrika Mashariki kwa sababu tunataka wananchi wetu wakiona hawawezi kupata haki, waende sehemu nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka tu nisisitize kwamba uamuzi huo tumeona una upungufu na tarehe 11 mwezi huu Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ilipeleka notes ya kusudio la kukata rufaa ngazi ya juu ya East Africa Court Justice. Sisi tunataka tu tuelewane kwenye vipengele mbalimbali, lakini kwa sababu liko Mahakamani sitalijadili sana. Tuna hoja nzito, nina uhakika tutashinda.

Mheshimiwa Spika, siwakatishi tamaa Watanzania wetu ambao mmepewa na nchi yenu uhuru mpana zaidi. Bado wana nafasi ya kwenda Mahakama ya Haki za Binadamu ya Afrika, ipo Arusha. Hiyo Mahakama iliazishwa mwaka 1998, nchi 30 zilikubali tukaanzishwa.

Mheshimiwa Spika, naomba ni sisitize, kuielewa nchi yetu ilivyo, ni nchi tano tu kwa muda mrefu zimekubali wananchi wake waweze kuishitaki Serikali kwenye hiyo Mahakama. Tanzania tumo, sasa hivi tuko tisa. Jamani, mnyonge, mnyongeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Khatibu Haji na Mheshimiwa Devotha Minja walioji kwa nini Mkurugenzi wa Maelezo alivitaka Vyombo vya Habari vilivyoandika habari za ACT vijieleze?

Mheshimiwa Spika, naomba nisisitize kuwa hali haikuwa hivyo. Tarehe 4 Aprili, Kiongozi wa ACT Wazalendo, Mheshimiwa Zitto aliitisha Mkutano na vyombo vya habari kutoa maoni yake kuhusu Ripoti ya CAG. Hili siyo kosa. Naomba nisisitize Watanzania; Mtanzania ana haki. Ripoti ya CAG iko pale, zungumza unavyotaka u-base kwenye hiyo ripoti, hatuna shida. Mheshimiwa Zitto alitumia haki yake ya kikatiba kuweza kujadili Ripoti ya CAG. Aidha, kisheria hakuna kosa lolote kwa chombo cha habari kunukuu kile kilichomo kwenye taarifa hiyo. Sasa nashangaa ilionekana kwamba tumezuia, haiwezekani kunukuu chochote, hapana, siyo hivyo. Tena naomba nisisitize kwamba tatizo lililojitokeza pale ambapo magazeti yalipoiacha Taarifa ya CAG na kujielekeza kwenye maoni binafsi ya Mheshimiwa Zitto.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Zitto alianzisha ya kwake, sasa tukawa na CAG wawili. Sasa kwa maadili ya Uandishi wa Habari, kwa sababu hiki ni kitu kipya, siyo based kwenye ripoti ya CAG, inabaidi umhoji na yule mwingine ambaye anatuhumiwa humo kwamba amepoteza shilingi bilioni 800, ni pesa hii kwamba haionekani, hiyo ni yake wala hata CAG hakusema. Ndiyo maana Mkurugenzi wa Habari akasema, jamani eeh, hebu elezeeni, mbona mnakiuka maadili? Hiki kitu kipya wala hakipo kwenye taarifa ya CAG. Kule kuuliza tu imekuwa nongwa; na hakuna hata mmoja aliyesimamishwa kwamba unasimamishwa kwa sababu ulimnukuu Zitto wa ACT.

Mheshimiwa Spika, naomba tu kusema kwamba Mkurugenzi wa Idara ya Habari alifanya hivyo kwa mujibu wa Kifungu cha 27 cha Sheria ya Huduma ya Habari, hakukosea popote. Mheshimiwa Joseph Kasheku ameongelea hali ya wana tasnia wa filamu; wapo wengi sana hapa; kuwa wana hali ngumu mno na hivyo wanasababisha kujihusisha na kula michango ya misiba; pili, kuendesha madanguro.

Mheshimiwa Spika, napenda kumwelezea Mheshimiwa Musukuma kupitia kwako kuwa vitendo hivyo havikubaliki kisheria. Ni kosa la jinai kuendesha madanguro. Ukisoma penal code cap 16, ni kosa. Namwomba tu Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani asilichukulie hili kwa nguvu. Nadhani Mheshimiwa alikuwa anatia tu chumvi kidogo ili asikike zaidi hapa.

Mheshimiwa Spika, naelewa vijana wetu wa filamu wanafanya vizuri kuliko kipindi chochote katika historia ya nchi hii. (Makofi)

Ndugu zangu, kwa mara ya kwanza naweza pia kusema katika historia ya tasnia ya filamu, Wizara imeingilia kati mikataba ya wanatasnia wa filamu. Kwa mfano, Kampuni ya Jerusalem ya JB na Kampuni ya kijana wetu Kigosi RJ zililipwa jumla ya shilingi milioni 32 kwa intervention ya Wizara. Bodi ilikuwa pale kwa niaba ya Wizara, ikafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siyo hiyo tu, tuna mifano mingi ambapo Kampuni, huyu Hussein Kim, amelipwa shilingi milioni
18 na Kampuni ya Proin Promotions na Puppy Zee. Ninachotaka kusema tu ni kwamba hebu rudi kwenye kitabu changu cha hotuba, tumefanya mengi sana kuweza kuisaidia tasnia ya filamu na sanaa nzima. Najivuna kwamba katika kipindi changu nimeweza hata katika kutetea vijana wetu, wasanii wawili, wanamuziki wameweza sasa hivi kuwa mamilionea kwa sababu wamelipwa zaidi ya shilingi bilioni mbili kwa haki ambayo ilikuwa inapotea. Bila Wizara kusimama kidete wasingepata hiyo pesa.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mwakajoka, amezungumzia uhuru wa habari. Ahsante kwa ufafanuzi ulioutoa Mheshimiwa Spika. Unajua uhuru anaoulilia Mheshimiwa Mwakajoka mdogo wangu pale. Sijui ndiyo ule uhuru wa mtu anaamka tu asubuhi anaamua kumfungisha ndoa Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe na Mheshimiwa Halima Mdee! Maana ndiyo uhuru mnaoutaka huo, bila kujali kwamba unafanya hivyo wakati sisi watu wengine tuna familia, tuna watoto. Ina-impact kubwa sana, lakini ndiyo uhuru tunaoutaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mtu amekaa tu; na uzuri wake nimewaomba wataalamu wa TCRA waangalie ni nani. Sitaki kumtaja jina hapa, ni mtu mzima ana familia yake, kakaa nyumbani anaanzisha rumors za kipuuzi kama hizo. Sasa hizo turuhusu, itakuwa nchi gani hii? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mwakajoka amemwongelea Ansbert Ngurumo. Nafikiri hao wengine aache tu wajitetee wenyewe kwa sababu nikisema niletee hapa ushahidi kwamba Ngurumo amewahi kutuhumiwa na Serikali hata siku moja; ndiyo utagundua kwamba watu wengine wanaenda Ulaya ni mshiko tu. Kwa kweli hajatuhumiwa na mtu yeyote yule.

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa sababu nimepigiwa kengele, niongelee kidogo tu kuhusu hoja aliyoelezea Mheshimiwa Juma Nkamia kwamba vijana wetu wa Serengeti kwa kweli hawakuandaliwa vizuri, pengine ndiyo maana hawakufanya vizuri sana, hapana. Mpira ni mpira. Tuliwaandaa vizuri sana.

Mheshimiwa Spika, niulize swali, hawa vijana wamechukua makombe competitive kama CECAFA na COSAFA kwa kubahatisha? Hapana, ni kwa sababu ya mazoezi mazuri waliyokuwa nayo, lakini mpira ni mpira, lazima mtu mmoja ashindwe na mwingine ashinde.

Mheshimiwa Spika, vilevile vijana wetu walikuwa na pressure kubwa mno ya kubeba matumaini ya Watanzania. Umri wa miaka 16 ni mdogo sana. Vilevile nawalaumu watu wanaoitwa ma-agents. Wamekuja ma-agents kutoka nchi mbalimbali, wote akina Diouf hao, kundi la Etoh, kuja kwa watoto wadogo wale unawaambia tunakuhitaji kwenye timu yetu, tutakulipa shilingi milioni 100 kwa mwezi, kanachanganyikiwa. Kanacheza pale kanaangalia ile hela; wazazi wengine wanapata taarifa kwamba mtoto wako bwana ameahidiwa shilingi milioni 100 mpaka 200 kwa mwezi. Wanawaambia, mwanangu usicheze, utavunjika mguu. Hii hela ndiyo itatutoa.

Mheshimiwa Spika, sasa nafikiri imetufundisha. Nimeiagiza BMT itengeneze Kanuni kwa ajili ya kuendesha shughuli za u-agency hapa nchini kuhusu vijana wetu. Nimalizie na Mheshimiwa Aida Khenani, kwamba Serikali inasema nini kuhusu Azory? (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli niwaombe Waheshimiwa Wabunge, tunaongelea kesi ambayo ni dhaifu sana, tena sana. Mwandishi huyu amepotea. Eneo ambalo mamia ya Watanzania wengine wamepotea hawaulizwi wao, huyo mmoja ndiyo dhahabu. Halafu inaulizwa Serikali ambayo yenyewe imeshughulikiwa kwa kiasi kikubwa kweli kweli.

Mheshimiwa Spika, Maafisa wetu wa Serikali wamekufa wengi kule. Leo tunaulizwa mmoja, it is extremely unfair. Najua mnawalisha Wazungu na wafadhili wengi, matango pori hayo, acha wayapate, lakini ninachosema hatujakosa chochote, acha tushushwe hayo madaraja, sisi bwana uhuru wetu kwanza tunauthamini, hayo madaraja baadaye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa neno moja tu kuhusu hoja ya Mheshimiwa Rashid Shangazi. Kwanza namshukuru kwa kunukuu Ibara ya 18 na 30 kwa pamoja, kueleza kwamba uhuru duniani kote lazima uwe mipaka. Walikuwa kuniona wale Waandishi wa (International Press Institute - IPI). Huyo Mhindi ndio alikuja akaniambia kwamba tumekuja Tanzania kwa sababu tuna taarifa ya kwamba kuna Waandishi wa Habari 30 wako kizuizini. Nikamwambia naomba usitoke ofisini kwangu unithibitishie hao 30 ni akina nani? Baadaye akaishia kusema nimeona kwenye mtandao wa jamii.

Mheshimiwa Spika, naomba niishie hapo. Naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa na mimi fursa nianze kwa kuunga mkono hoja na vilevile kuwapongeza sana viongozi wa Kamati yangu na Wajumbe kwa kazi kubwa wanayofanya ya kutushauri Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli tumeanza vizuri mwaka huu na kama alivyosema Mheshimiwa Mtulia nyota wetu wa soka ambaye vilevile nahodha wa timu ya Taifa akatufungulia milango, akawafungulia milango vijana wetu Watanzania kuingia kwenye ligi ya heshima duniani, kubwa ya EPL ila tu niombe Watanzania najua mmehamasika sana tujiebushe na kauli zisizo na staha kwenye mitandao ya michezo inayotumiwa na wengi, badala ya kumsaidia Samatta hatumsaidi bali tunamjengea uwasama kijana wetu na wenzake huko ughaibuni nawaomba sana hasa katika kutumia mitandao na bahati mbaya sana wanaowatafsiria wenzetu huko Aston Villa siyo Watanzania, ni wenzetu ambao hawatutakii nia njema ni Kiswahili watapotosha tu, kwa hiyo, hebu tujihadhari sana na mihemuko iliyopitiliza.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwaeleza tu Watanzania na Waheshimiwa Wabunge sasa hivi tuna wachezaji 22 wanaocheza nje nchi ambao tukiwahitaji wakati wowote wapo tayari kuisaidia timu ya Taifa bila kumsahau kinda wetu Kelvin John ambaye sasa hivi yupo kwenye football academy ya Uingereza na timu nyingi kwa kweli zinamtolea macho sasa hivi. Leo tumempokea hapa Bungeni Salim Mtango wa Tanga kwa kubeba mkanda wa UBO wa dunia na mwenzake vilevile Mchanje Yohana wa Tanga huko huko naye amebeba mkanda wa UBO nawapa pongezi sana tena sana. Sasa hivi Tanzania tuna jumla ya mikanda 12 ya Kimataifa. Kwa hiyo, tunafanya vizuri sana kwa ndondi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rashid Shangazi namshukuru Mbunge wa Mlalo amelalamikia usikivu hafifu wa TBC maeneo kadhaa ya nchi yetu. Nitumie nafasi hii kuelezea tu kwamba mara baada ya Uhuru Baba wa Taifa alihakikisha nchi hii inajenga minara minane ya masafa ya kati dhidi ya (medium wave) na hiyo minara kwa kweli, ni kama iliweza kujitosheleza nchi nzima ilikuwepo Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Kigoma, Dodoma vilevile Mbeya, Songea na Nachingwea, lakini teknolojia ya mawasiliano inakwenda kwa kasi sana, mitambo ya medium wave ilianza kupoteza/kuondoka kabisa katika teknolojia ikaingia mipya kabisa ambayo kwa kweli kusikia inafurahia lakini ina matatizo pia kwa upande hasa sehemu ambayo kuna vizuizi kama milima, tukaingia huu teknolojia ya frequency modulation (fm) na mitambo ile kwa sababu imekosa watengenezaji waliacha kabisa ikakosa kwakweli vipuli kwahiyo nchi ikaingia kwenye mtikisiko mkubwa sana wa jinsi gani tutatoka huko ndiyo tukaanza kutumia kuweka sehemu mbalimbali za nchi mitambo ya fm.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeweza kwa mfano katika muda mfupi uliopita Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia usikivu wa TBC ulikuwa asilimia 54 tu sasa tunaelekea kwenye asilimia sabini na kitu, tumekwenda Wilaya za mpakani Rombo, Longido, Tarime, Kibondo na Nyasa, lakini huwezi tu ukaweka ukaacha inabidi urudie tena kuangalia kwa sababu mawimbi haya yana tabia ya kuhama kutokana na topography.

Kwa hiyo, tumepita hivi karibuni tumeenda Tanga kuangalia mitambo yetu tukakuta kweli bado tuna matatizo baadhi ya sehemu kutokana na mitambo yetu kukosa nguvu, sasa iliyoko sehemu ya Mnyuzi sehemu kama Mkinga na Kilindi inabidi turudie na ninawahakikishia Wabunge kutoka Mkoa wa Tanga kwamba eneo hilo tumeliona Mkinga na Kilindi kuna matatizo. Vile vile tulikwenda Lushoto tumeona kuna mitambo pale lakini hata tukiikarabati na tutaikarabati ndani ya miezi mitatu ijayo bado Bumbuli na Mlalo wanatatizo ambalo wanahitaji kwa kweli kulifanyia kazi na tunawahakikishia ndani ya mwaka huu tutatatua tatizo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekwenda kilimo cha Mabungo ambacho kipo Moshi vilevile mtambo wetu vimeshika sana nguvu yake inahitaji ukarabati, vipuri vyote vimeshafika, lakini hata tukisha karabati bado Rombo itaendelea kupata matatizo kutokana na milima milima sehemu ile, Rombo inahitaji kwa kweli tuifanyie kazi zaidi pamoja na kwamba Rombo hapo hapo tuna mitambo mipya inabidi tuongeze mitambo mingine ni kama ambavyo tutakavyofanya Longido ambako tuna mitambo tayari Namanga, tuna mipambo Longido DC lakini mitambo Longido DC lakini bado lazima tuongeze mitambo mingine kutokana na topography ta eneo hilo, tumeenda Manyara, tumeenda Singida hali iko hivyo hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu mwaka huu wa fedha tunaweka mitambo Unguja na Pemba kwa bajeti mliopitisha hapa, tunaweka mitambo Simiyu na vilevile tunaboresha usikivu Songwe na Ludewa kwa Mheshimiwa Ngalawa. Vilevile, kwa ushirikiano kwa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote tutaweka mitambo Kilwa, tutaweka Itigi, Ruangwa, Kilombero na bila kusahau Kyela.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Amina Mollel kwa kuona juhudi za Wizara katika kuboresha matangazo ya TBC.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati ya Maendeleo ya Huduma za Jamii imelalamikia ubovu wa miundombinu ya michezo; napenda kusisitiza kwamba ndugu zangu kwa kweli ni jukumu letu sote si jukumu la Serikali peke yake Wizara, Taasisi, Mashirika ya Umma, sekta binafsi na hata sisi Waheshimiwa Wabunge unaweza ukajenga hata kiwanja cha volleyball kwa kutumia pesa ya Mfuko wa Jimbo au kiwanja cha netball.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli ni wajibu wetu wote tusisubiri tu Serikali peke yake na wito huu tumeshautoa na umepokewa kweli na mikoa mingi, tunashukuru sana Mkoa wa Arusha ambao umetoa agizo, umeazimia kwamba kila Halmashauri itajenga viwanja vya michezo na wao Jiji la Arusha wameamua wameanza nimeenda kuangalia kiwanja cha Ngarenaro, ni kiwanja changamani kuna netball, kuna basketball, kuna mchezo wa soka pale kiwanja kizuri kimemalizika kwa asilimia 80 wanajenga kwa jumla ya shilingi milioni 360. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeenda sehemu inaitwa Sinoni, kuna Mtanzania pale anaishi Marekani amekumbuka nyumbani, amejenga kiwanja kizuri sana kina taa mpaka za usiku kwa ajili ya watoto kwa shilingi milioni 126; hawa vijana wa kutolewa mfano kuliko vijana wenzetu wengi wanaokaa nje muda mwingi wako kwenye mitandao ya kijamii. Unafuatiwa Mkoa wa Dar es Salaam, nilishasema naipongeza Simba Sports Club wanajenga viwanja viwili, kimoja cha nyasi na kingine kiwanja cha nyasi bandia huko Bunju. Vilevile Manispaa ya Kinondoni inajenga uwanja wa kisasa Mwenge kwa shilingi bilioni 2.7 na ukamilika mwaka huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa sijawatendea haki Manispaa ya Songea Mjini kwa Mheshimiwa Dkt. Ndumbaro, wametenga eneo la ekari 50 katikati ya Kata ya Lirambo na Peramiho kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja cha kisasa cha gofu. Sasa hapa tutaona ndugu zetu wa Songea hiyo gofu watakapoanza kujifunza, lakini kwa kweli nina uhakika kutokana na uzuri wa eneo lenyewe na hakika nchi nyingi zitakimbia kuja kufanya mchezo kule wa gofu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii vilevile kuwatahadharisha wana Tanga wanaonisikiliza saa hizi wanaovamia eneo la TFF la Mianjani ambako kutajengwa training center yenye viwanja na vilevile hosteli. Naomba niwasisitizie kwamba hawatalipwa fidia, kuna mtu anawadanganya danganya sehemu za ardhi/ofisi zetu hizi kwamba hebu jengeni mtalipwa fidia, fidia haitalipwa, nataka niwahakikishie hilo na ujenzi utaanza muda si mrefu kutoka sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Kubenea amelalamikia anauita ushabiki wa TBC, nilitaka nisisitize tu kwamba Mheshimiwa Kubenea kupitia kwako kwamba TBC ni chombo la Serikali, hilo haliwezi kubadilika na TBC inachokifanya siyo tofauti na vyombo vingine vya Serikali duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, TBC iko pale kuelezea kwa kinagaubaga utekelekezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo za Serikali ambavyo hivi vitu haviwezi kupata nafasi kwenye vyombo vya habari binafsi ambavyo vinaangalia zaidi faidi at the end of the day. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pengine wengine hawana habari, BBC mnayoiona kila siku msije mkafikiri iko pale kwa msaada hapana. BBC leo iko pale kwa umri wa miaka 98 haijawahi kuzimwa hata siku moja, iko pale kwa maslahi ya Serikali ya Uingereza, sio inatusaidia na sisi tupate taarifa iko pale kwa maslahi. VOA huu mwaka wa 78 haijawahi kuzimika inatangazwa kwa lugha 47, BBC lugha 40, wafanyakazi zaidi ya 3500 kila chombo kwa ajili ya nini. Kama ingekuwa kuwatangazia Waingereza wenyewe si ingekuwa kiingereza peke yake hivi ni vitu vya kimkakati kila nchi inafanya, msiishambulie TBC bila sababu, kuna Serikali inafannya vitu, lazima vitangazwe. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, sijui nimesikia kengele? Ooooh!

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa Mwaka 2016
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuhitimisha hoja iliyoko mbele yetu kwa kujibu rai, mawazo na mapendekezo mbalimbali ya Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya Waheshimiwa Wabunge 39 wamechangia Muswada huu kwa kuongea na Waheshimiwa Wabunge watano kwa njia ya maandishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ufafanuzi mzuri wa Waheshimiwa Wabunge mbalimbali pamoja na Mheshimiwa Waziri Nape, Mheshimiwa Naibu Waziri Possi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, naomba niongelee hoja chache tu za ujumla zilizochukua sehemu kubwa ya hotuba za baadhi za Waheshimiwa Wabunge, jana na hata leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kwa kifupi tu Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Mheshimiwa Abdallah Mtolea, Mbunge wa Temeke ambaye kwa bahati mbaya aliamua kutengeneza Muswada wake wa Habari na kuujadili, badala ya kujadili Muswada wa Taarifa ambao nimeuwasilisha hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Msemaji wa Upinzani ameongelea kwenye hotuba yake kila kinachomkera, NGO’s, magazeti kufungiwa, watuhumiwa kubambikiziwa kesi na polisi na kadhalika vitu ambavyo kwa kweli viko nje kabisa ya maudhui na muktadha wa muswada ulioko mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma kwa karibu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 18(b) na (d), inasema, naomba turudie, wenzangu wamejaribu sana kuelezea hii. Ibara ya 18(b) inasema: “Kila mtu ana haki ya kutafuta;” yaani to seek (to look for), kupokea (to receive) na kutoa (to disseminate), kusambaza habari bila ya kujali mipaka ya nchi. Sasa hii inaongelea habari without frontiers; unakwenda popote. Unaweza kutuma kwenda Marekani. Hii inahusu habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 18(d) inazungumza: “Kila mtu anayo haki ya kupewa taarifa.” Sasa badala ya habari, imekuja taarifa, wakati wote. Tena hili “wakati wote,” neno hili nakumbuka jana Mheshimiwa Mwalimu Bilago alifurahia sana akasema ehee ni kila wakati. Nikawa naogopa, nasema eeh Mwalimu siyo maana ya kila wakati, hata ukilala unapewa tu taarifa; usingizini unapewa taarifa. Utawehuka, sio hivyo! Ukiisoma kwa context, ukitumia; sisi tunaita contexualist approach, haina maana ya kila wakati, ina maana ya pale unapohitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, inasema kila mtu anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili liko wazi, lakini ni huku kujichanganya kwa hii dhana kwamba tunaongelea habari badala ya taarifa ndiko kulifanya huu muswada kwa mara ya kwanza kwenye Bunge la Kumi kuondolewa na tukaagizwa kuufanyia kazi zaidi na kwa kweli tumeufanyia kazi zaidi kama ambavyo Bunge lilivyoagiza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria - Mheshimiwa Mchengerwa, ameelezea hapa katika hotuba yake ukurasa wa tatu kuwa Kamati yake iliita makundi mbalimbali ya wadau. Yalikuwa makundi 10 ukisoma, lakini matano kati ya hayo yalikuwa makundi ya wanahabari na ameyataja, sitaki kupoteza muda, ameyataja ukurasa wa tatu. Makundi matano, watu wazito katika tasnia ya habari. Alifanya hivyo kwa makusudi mazuri sana, ni kwa sababu wanahabari ndio walikuwa kwa kweli ni chanzo kikubwa cha huu muswada kuondolewa Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimsikia Mheshimiwa Anatropia Theonest hapa akisema uandishi wa habari wa nini kwenye Muswada wa Taarifa? Hapana! Ilikuwa lazima tuwaite Mheshimiwa kwa sababu nzuri tu ya kwamba walikuwa wao ndio sababu kubwa ya huu muswada kuondolewa Bungeni kwa sababu walidhani muswada huu ni wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa rafiki zangu hapa siwaoni, Mheshimiwa Lema, Mheshimiwa Msigwa…
Aha! Vilevile na Mheshimiwa Silinde, jana walitumia muda mwingi wakidai kuielewa zaidi tasnia ya uandishi wa habari kuliko waandishi wa habari wenyewe waliokuwepo. Waliokuwepo tumekaa nao kwenye Kamati kwa muda mrefu sana. Huu Muswada umechukua miaka kumi kufika hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi kama mwandishi, kwa background yangu naweza kusema kwamba sheria hii inawaongezea waandishi wa habari wigo zaidi. Kwa nini? Ni kwa sababu sheria hii inamhusu mtu wa kawaida, Mtanzania yeyote na mwandishi wa habari ni sehemu ya Watanzania. Anaweza akapata taarifa kama mwananchi na hiyo taarifa akiipata yeye anaigeuza kuwa habari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa pili chini ya Sheria ya Habari, yeye ana Press Card chini ya Sheria ya Uandishi wa Habari ambayo itaheshimu kipengele cha Katiba kinachosema ana haki ya kutafuta, ana haki ya kupokea, ana haki ya ku-disseminate, ana madaraka makubwa zaidi kuliko sisi hapa tunamfikiria mtu wa kawaida kwamba hili Taifa limegeuka la waandishi wa habari watupu, hapana.
Kwa hiyo, wenzangu Waheshimiwa Wabunge jana wameongelea sana kuhusu waandishi wa habari, wakafikia hata hatua wakasema siku moja eti CCM isijisahau, inaweza kuwa Upinzani na CHADEMA ikawa Chama Tawala. Aah, wapi na wapi bwana (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbushane tu kwamba Kiongozi wenu mwenyewe mnamjua, amekiri kuwa nyie bado ni kikundi cha wanaharakati, bado kukua kuwa chama cha siasa. Na mimi sijawahi kuona duniani hapa kikundi chochote cha wanaharakati kikaunda Serikali. Mtasubiri sana kama fisi yule wa hadithi ambaye alisubiri mkono wa binadamu udondoke, mpaka mtoke kwenye uanaharakati. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Silinde anadai Mheshimiwa Rais kashauriwa vibaya kuhusu muswada huu. Mheshimiwa Silinde alikuwepo Bunge la Kumi. He is not honest! Muswada huu anajua una umri wa miaka kumi na alikuwepo ulipoondolewa hapa Bungeni. Sasa huyu Rais Magufuli anatokea wapi katika muswada huu na akashauriwa vibaya? Muswada huu tumeupokea ndiyo maana tumeusoma mara ya pili na ya tatu tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Lema na Mheshimiwa Msigwa wamenituhumu mimi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kushindwa kumshauri Mheshimiwa Rais vizuri, yaani tumshauri wanavyotaka wao. Hivi ndugu zangu, tena yupo hapa ndugu yangu Mheshimiwa Mbowe, anapowaambia wote tutoke ndani ya Bunge hili na wote mnatoka kama kumbikumbi, mnatoa ushauri gani ninyi? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza; namuuliza Mheshimiwa Lema na Mheshimiwa Mchungaji Msigwa! Kuweni wavumilivu…
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nivumiliwe tu kwa sababu ninayo right of reply kwa yale yaliyosemwa hapa na yameingia kwenye Hansard.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imeongelewa hapa kwamba tunamshauri Mheshimiwa Rais vibaya. Na mimi nauliza, Mheshimwa Silinde na Mheshimiwa Msigwa mlivyokuwa mnasema hapo jana, wakati ndugu yangu Mheshimiwa Slaa anaenguliwa, anaingizwa mtu ambaye wala hamkumchagua kushika bendera, mlikuwa wapi kumshauri? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sikujua, mkuki kwa nguruwe, kumbe kwa binadamu mchungu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuja huko, naweka tu basis ya argument kwamba leo Mheshimiwa Lema na Mheshimiwa Msigwa mmetumia muda mrefu mki-question integrity ya Attorney General na mimi, na mimi nawajibu hapa kwamba ninyi hamna moral authority ya kuweza ku-question integrity yetu sisi kwa sababu ninyi hamna integrity! (Makofi/Kicheko/Vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa linamkumbuka Mheshimiwa Lema na Mheshimiwa Msigwa, mmezunguka mkimtangaza Mheshimiwa Lowassa kuwa fisadi, leo mnalamba nyayo zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niruhusiwe kujibu hoja zote zilizosemwa jana hapa na nina muda wa kutosha.
Naomba nisisitize, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hajavunja sheria yoyote, hajavunja Katiba, alichofanya ni kuheshimu kiapo chake cha kuhifadhi, kuilinda na kutetea Katiba na sheria za nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameeleza vizuri sana hapa, wajibu…
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimezoea, hii ndiyo style ya wanaharakati, kwa hiyo hamna wasiwasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosema tu ni kwamba alichofanya Mheshimiwa Rais ni kuzuia siasa za shari za uanaharakati zisilisambaratishe Taifa letu. Ndiyo alichokifanya na ni wajibu wake Kikatiba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais najua leo ali-perceive danger, hence the moratorium. Nilitegemea busara kwa chama chochote kwenda mahakamani kama alivyosema Attorney General. Kama huendi mahakamani basi jipange, hebu dai majadiliano na Serikali. Mpaka leo sijaona, nimemuuliza Attorney General, hata ofisini kwangu hatujapata hata siku moja hata indication ya kwamba wenzenu tunataka tujadiliane hili suala. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais kama unadhani alisema kitu ambacho siyo sahihi, lakini jibu lake siyo wewe ku-call for civil disobedience nchi nzima bila ukomo, hilo halikubaliki! If you believe the President was wrong still, two wrongs do not constitute a right! Na sisi wanasheria tunasema, he who seeks equity, should come with clean hands. I don’t see clean hands across this floor. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tulivyosema mimi na Attorney General hatujawahi kupokea mawazo yoyote kutoka kwa Upinzani. Tubadilike, tuwe chama; milango yetu iko wazi. Tusiupe uanaharakati nafasi katika shughuli zetu za kuendesha nchi. Mengine nayaacha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya haya mafupi ya utangulizi, sasa naomba nisisitize tu kuwa muswada ambao uko mbele yetu leo, unalenga kupanua wigo wa upatikanaji wa taarifa, siyo tu kwa wananchi, lakini hata kwa wale tunaodhani wamelengwa kuminywa (waandishi wa habari) na hii inalenga kama nilivyosema mwanzoni na wenzangu wengi wamesema, kwa kweli kutekeleza matakwa ya Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, muswada huu naomba sana Waheshimiwa Wabunge tuusome vizuri. Haukusudiii kudhibiti vyombo vya habari, not at all! Haukumdhibiti mtu yeyote mwingine lakini kupanua tu wigo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba vile vile uamuzi wa Serikali kuleta Muswada huu, pia umechagizwa na Malengo Endelevu (Sustainable Development Goals). Yaliyowekwa na nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa ambao na sisi ni wanachama, tarehe 25 Septemba, 2015 lengo namba SDG16.10 linasema, “every country to ensure public access to information.” Lengo hili kimsingi linakusudia kupanua wigo wa upatikanaji wa taarifa kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo haya ya jumla, naomba sasa nijibu hoja moja moja, nyingine zimeshajibiwa na wenzangu, kwa hiyo, nitazigusia tu juu juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu adhabu inayopendekezwa kutolewa kupitia kifungu cha 6(6) cha hii sheria inayopendekezwa kwa wale watakaotoa taarifa zilizozuiliwa, tumetafakari kwa kirefu hoja zilizotolewa na Kamati na Waheshimiwa Wabunge wawili Mheshimiwa Zedi na Mheshimiwa Mhagama na hivyo tunapendekeza kwenye schedule of amendment ya kifungu cha 6(6) kwa madhumuni ya kutenganisha adhabu kati ya kosa la kutoa taarifa zilizozuiliwa zinazohusu Usalama wa Taifa na kutoa taarifa zilizozuiliwa zisizohusu Usalama wa Taifa.
Hivyo basi, Jedwali la Marekebisho linapendekeza adhabu ya kifungo kisichopungua miaka mitatu na kisichozidi miaka mitano kwa kutoa taarifa ambazo zilizuiliwa na ambazo hazihusu masuala ya usalama wa Taifa. Marekebisho hayo pia yanapendekeza kuwa endapo mtu atatiwa hatiani kwa kosa la kutoa taarifa zilizozuiliwa zinazohuzu masuala ya Usalama wa Taifa adhabu yake itolewe kwa mujibu wa Sheria ya Usalama wa Taifa. Hayo ndiyo marekebisho tumeyafanya kutokana na maoni yenu hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuzuia baadhi ya taarifa zisitolewe kwa umma, napenda kumjibu Mheshimiwa Mollel, Mheshimiwa Waitara, Mheshimiwa Selasini na Mheshimiwa Riziki nafikiri waliongelea hili. Huu ni utaratibu wa kawaida duniani, sijawahi kuona nchi yoyote yenye open door policy kwenye masuala yake ya kiusalama. Aidha, haki na uhuru wowote duniani una mipaka na hata sisi tumeweka mipaka na mipaka yote ya namna hiyo inaruhusiwa Kikatiba, ndiyo maana kama alivyosema Mheshimiwa Waziri Possi, Bwana Julian Assange anajibanza kwenye Ubalozi wa Ecuador, London tangu mwaka 2012 mpaka leo hajatoka, tena akiwa amekera nchi kubwa duniani Marekani, Uingereza na Sweden.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi zote duniani ambazo zina sheria ya upatikanaji wa taarifa zimeweka mipaka ya aina hiyo ya taarifa ambazo zinazoweza kutolewa kwa umma na zisizoweza kutolewa kwa umma. Aidha, hata taasisi za Kimataifa ambazo zimekuwa zikiandaa sheria za mifano kwa nchi zetu ambazo zilikuwa bado hazina hiyo Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa zinaweka vifungu vinavyozuia baadhi ya taarifa kutolewa kwa umma. Mathalani Sheria ya Mfano wa Upatikanaji wa Taarifa ya Umoja wa Mataifa (Model Law on Access to Information for Africa) inaweka masharti yanayozuia baadhi ya taarifa kutotolewa kwa umma. Kwa faida ya Bunge lako Tukufu sheria hiyo ya mfano imeandaliwa na Kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu ambayo ina dhamana ya kusimamia haki za binadamu katika Bara letu la Afrika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwepo kwa kifungu cha 6 kinachoweka masharti ya kuzuia baadhi ya taarifa kutolewa kwa umma kumefanywa kwa nia njema na kwa maslahi ya Taifa, raia wote na ustawi wa jamii nzima ya Kitanzania. Hivyo, niliombe Bunge lako Tukufu kuridhia masharti ya kifungu hicho kama ilivyopendekezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge, nakumbuka Mheshimiwa Mollel na Mheshimiwa Kangi Lugola waliochangia muswada huu wameonesha wasiwasi wa kutokuwepo kwa tafsiri ya neno national security na kwa maneno hayo yanaweza kutumika kufifisha haki ya upatikanaji wa taarifa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwatoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge kuwa taarifa zinazohusu national security zimefafanuliwa kwa kina katika Ibara ya 6(3), sijui wengine hapa hawakusoma muswada huu ndiyo maana walikuwa wanalalamika. Taarifa za national security zimeelezwa kuwa ni taarifa zinazohusu, pengine ninukuu kwa haraka haraka tu, section ya 6 inasema, zinazohusu mikakati ya kijeshi, mafundisho, uwezo, nafasi au usambazaji; taarifa ya Serikali ya kigeni inayohusisha Usalama wa Taifa na kazi za kijasusi, vyanzo, uwezo, utaratibu au usiri.
Kwa hiyo, vimeainishwa humu pamoja na kwamba wengine wetu tuliona kwamba kwa kweli kuna mapengo makubwa katika muswada huu. Masuala haya kwa ujumla wake ni nyeti kwa usalama wa nchi na mahusiano yake na mataifa mengine na hivyo hayatakiwi kutolewa kwa umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, umeoneshwa wasiwasi na Mheshimiwa Ruth Mollel kuhusu taarifa zinazohusu faragha ya mtu, amelijibu vizuri sana Naibu Waziri Mheshimiwa Dkt. Possi. Nisisitize tu kwamba msingi wa kuzuia taarifa za faragha unatokana na Katiba, Ibara ya 16(1) inayoeleza kuwa kila mtu anastahili kuheshimiwa na kupata hifadhi kwa nafsi yake, maisha yake binafsi na familia yake. Hivyo basi, tunapendekeza pia katika muswada huu kuzuia ukiukaji wa haki ya faragha isipokuwa kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Katiba na Sheria ilipendekeza kufanyia marekebisho kifungu cha 7 kwa minajili ya kumtaka mkuu wa taasisi anayeshindwa kumteua Afisa Taarifa kuwa Afisa Taarifa mwenyewe kwa madhumuni ya sheria inayopendekezwa. Kimsingi Wizara yangu haina pingamizi na pendekezo hilo na tayari Jedwali la Marekebisho linapendekeza hilo ambalo Waheshimiwa Wabunge walitaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu muda wa siku thelathini wa kushughulikia maombi ya taarifa kuonekana mrefu sana, ni rai ya Wizara yangu kuwa muda huo ni muafaka tukizingatia wingi wa taarifa zitakazokuwa zikiombwa na ukubwa wa nchi yetu. Hata hivyo, kupitia Jedwali la Marekebisho tunapendekeza muda wa kushughulikia maombi hayo iwe mapema iwezekanavyo na si zaidi ya siku thelathini tangu kupokelewa kwa maombi husika kutoka kokote kule nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kanuni ambazo tumeanza kuandaa zinaainisha aina ya taarifa na muda wa kutolewa siku moja, mbili, tatu na kadhalika lakini muda hautazidi siku thelathini, hiyo ndio maana yetu. Kwa mantiki hiyo basi zipo taarifa ambazo kwa mujibu wa kanuni zitakazotengenezwa zitatolewa ndani ya muda mfupi kama siku moja na hivyo kuondoa uwezekano wa kuwepo kwa ucheleweshaji usio wa lazima. Kwa mfano, kama nilivyosema katika hotuba yangu ya mwanzo mtu yuko kijijini anaomba BOQ ya barabara inayojengwa kijijini kwake, sisi katika kanuni zetu tutapendekeza apewe ndani ya siku moja maana BOQ iko pale pale Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati vilevile ilipendekeza kuwa Waziri asiwe na mamlaka ya mwisho ya kushughulikia rufaa zitakazotokana na maamuzi ya wamiliki wa taarifa kutotoa taarifa kwa mujibu wa sheria inayopendekezwa. Niseme tu katika nchi yetu inayoheshimu utawala wa sheria, kwa mujibu wa Ibara ya 107A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina kauli ya mwisho katika masuala yote ya utoaji haki. Aidha, Mahakama Kuu ina mamlaka ya asili tunaita inherent jurisdiction ya kufanya intervention au kufanya mapitio ya uamuzi wowote uliofanywa na chombo chochote cha utendaji na pale Waziri anapokuwa anasikiliza pengine appeal hawi mahakama ni quasi- judicial body.
Vilevile bado tunadhani mahakama hata bila kutaja maana sheria nyingi zinaeleza hivyo zinapomtaja Waziri zinamtaja kiongozi wa upande wa utendaji lakini madaraka ya Waziri ni ya utendaji tu, lakini hayawezi kuifunga mahakama. Kwa hiyo, bado mahakama itakuwa na mamlaka ya mwisho ya kuamua hatma ya maombi ya taarifa yatakayokataliwa na mmiliki wa taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tumeboresha kifungu cha 19 kwa kuongeza kifungu kidogo cha (4) kinachosema pale ambapo mmiliki wa taarifa anayelalamikiwa yupo ndani au yuko chini ya Wizara ambayo itakuwa Wizara yangu basi Waziri katika suala hilo hatakuwa na mamlaka ya rufaa na mlalamikaji atakuwa huru kwenda Mahakama Kuu. Tumefanya maboresho hayo na lengo la kwenda Mahakama Kuu ni kupitia maamuzi hayo. Hayo yamo kwenye schedule of amendment.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema wakati wa kuwasilisha Muswada huu mbele ya Bunge lako Tukufu taarifa ni nyenzo muhimu ya kufikia malengo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii katika jamii yoyote. Mwanafalsafa wa kale wa China aliwahi kusema, the journey of a thousand miles begins with one step yaani safari ndefu huanza na hatua moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nasema kwamba sasa ndiyo tunapiga hatua yetu ya kwanza ya kutekeleza masharti ya Ibara ya 18(d) ya Katiba kuhusu haki ya kupata taarifa. Kwa msingi huo, niliombe Bunge lako Tukufu liliridhie sheria imhusu raia wa Jamhuri ya Muungano pekee kwa kuanzia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi Rasmi ya Upinzani, Mheshimiwa Anatropia Theonest, Mheshimiwa Mwalongo, Mheshimiwa Amina Mollel na Mheshimiwa Devotha Minja waliongelea hili, lakini mimi naomba waelewe kwamba huu ni mwanzo, tunahitaji kujifunza na kujidhatiti kabla ya kufungua milango yote na madirisha kwa watu wasio raia kunufaika na masharti ya sheria hii. Tukifungua milango na madirisha yote wakati huu wa mwanzo kuna hatari sana ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge ya kuingiza vitu tusivyovitarajia na hatimaye kuhatarisha usalama wa Taifa letu. Kupanga ni kuchagua na kila jambo lina wakati wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati vilevile ilipendekeza kuwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ipewe mamlaka ya kusimamia utekelezaji wa sheria inayopendekezwa. Wengine wamependekeza kuwa kiundwe chombo mahsusi kitakachosimamia utekelezaji wa sheria inayopendekezwa. Ni maoni ya Wizara yangu kuwa kwa mujibu wa principles zinazotoa mwongozo wa muundo wa mamlaka wa vyombo aina ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora tuliyonayo hapa Tanzania si muafaka kwa Tume kupewa wajibu huo kwani kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria inayoanzisha Tume, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ni chombo cha ushauri kwa Serikali na hivyo hakiwezi tena kufanya shughuli za uratibu ambazo kwa kweli zinatakiwa kufanywa na Serikali yenyewe. Bado wananchi wana haki ya kupeleka malalamiko yao kwenye Tume wakiona haki yao ya kupata taarifa inakanyagwa kinyume na sheria. Tume ni ombudsman yenye wigo mpana wa kufanya intervention wakati wowote.
Aidha, kwa sasa Serikali bado haioni haja ya kuwa na chombo mahsusi kabisa kushughulikia masuala ya upatikanaji wa taarifa, itakuwa gharama bure kwa Taifa. Hivyo basi, tunapendekeza jukumu la usimamizi wa sheria inayopendekezwa kwa kuanzia liachwe mikononi mwa Wizara husika yenye dhamana ya masuala ya haki itakayowajibika kusimamia, kufuatilia na kufanya tathmini ya utekelezaji wa sheria inayopendekezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mengine nitaruka kutokana na muda, hatua gani zitachukuliwa kwa mmiliki wa taarifa atakayetoa taarifa potofu, hii ni Kambi Rasmi ya Upinzani na Mheshimiwa David Silinde na Mheshimiwa Waitara. Naomba niseme tu kwamba Ibara ya 21 ya muswada inapendekeza adhabu ya faini isiyozidi shilingi milioni tano au kifungo kisichozidi miezi kumi na miwili kwa mtu yeyote atakayetiwa hatiani kwa kubadili, kufuta maandishi yasisomeke, kuzuia, kuharibu au kuficha kumbukumbu zozote zinazoshikiliwa na mmiliki wa taarifa kwa dhamira ya kuzuia upatikanaji wa taarifa.
Mheshimiwa Kangi Lugola alisema Serikali iweke wajibu kwa taasisi za umma zinazomiliki taarifa ili zitoe taarifa kila baada ya kipindi fulani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nimrejeshe Mheshimiwa Kangi Lugola Ibara ya 9 ya muswada huu ambayo inajieleza vizuri sana. Hata wenzangu waligusia katika maelezo, Ibara ya 9 inasema; “Kila mmiliki wa taarifa, si zaidi ya miezi thelathini na sita baada ya kuanza kutumika kwa sheria hii, atatoa kwenye gazeti, tovuti au gazeti linalopatikana kwa wingi likiwa na, maelezo juu ya aina, kazi na majukumu ikijumuisha majukumu yoyote ya kisheria ya maafisa au kamati za ushauri; maelezo ya jumla ya aina za taarifa zinazopatikana kwa mmiliki wa taarifa huyo; maelezo ya vijarida vyote na aina nyingine za nyaraka na kadhalika. Kwa hiyo, nilitaka kueleza tu hapa kwamba tumeweka kifungu kwenye sheria hii kuwataka wamiliki wote wa taarifa kutoa hizo taarifa, ukiingia kwenye Wizara, kwenye ofisi yoyote ya mmiliki wa taarifa ukute hizo taarifa, it should be a standard practice.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Hussein Bashe alitaka Serikali iweke utaratibu wa kurekebisha mfumo wa utoaji adhabu katika sheria zilizopo na zilizopitishwa na Bunge. Ni wazo zuri na Wizara yangu imelipokea na tutalifanyia kazi. N kweli kabisa kwamba tunahitaji policy ya kutu-guide kuhusu masuala ya adhabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwalongo alisema taarifa zitolewe kulingana na shughuli za uzalishaji za eneo husika na nafikiri nimelieleza hilo kwamba Ibara ya 9 itatusaidia sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa muswada unaopendekezwa kila mmiliki wa taarifa popote alipo ndani ya mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anawajibika kutoa taarifa alizonazo kulingana na shughuli zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Mheshimiwa David Silinde, nimeshalieleza hilo la kwamba Serikali imebadili maudhui ya muswada, hapana hatujabadili maudhui. Yeye alikuwepo katika Bunge la Kumi anaelewa kilichotokea, huu ni Muswada wa Taarifa siyo wa Habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile taarifa zinazozuiliwa na maslahi ya kibiashara ziondolewe katika muswada kwa kuwa zinaweza kusababisha mikataba inayoingiwa na Serikali kuwa siri.
Waheshimiwa Wabunge, pengine mmesahau kwamba nyie mna madaraka ya kuitisha mkataba wowote mkauangalia lakini taarifa inazuia endapo kutolewa kwake kunaweza tu kuathiri maslahi ya kibiashara yakiwemo pia ya mmiliki wa taarifa ikiwemo Serikali. Ni vyema kipengele hiki Waheshimiwa Wabunge kikaendelea kuwepo ndani ya muswada huu na hii ndiyo practice ya dunia nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, kutoa taarifa ya nchi nyingine ambayo itasaidia usalama wa nchi ni kosa, aliuliza Mheshimiwa Hussein Bashe. Mimi ninachotaka kusema kwa ujumla ni kwamba ukiwa na taarifa za nchi nyingine zenye athari kwa usalama wa nchi yetu si vyema kutangaza, share with the government, unakuwa pale na wewe kama a whistleblower itasaidia zaidi kuliko kwenda peke yako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwita Waitara, Mheshimiwa Joseph Selasini, Mheshimiwa Anatropia Theonest, Mheshimiwa Pauline Gekul waliuliza kwa nini sheria hii inapendekezwa itumike Tanzania Bara tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri imeelezwa sana na Waheshimiwa Wabunge wengi, kwanza niseme kwamba hii si sheria ya kwanza ya aina hiyo. Tumetunga sheria nyingi sana ambazo application yake ni Bara na wala haziendi mpaka Zanzibar na wenzetu Zanzibar wakishaona umuhimu wa hiyo sheria nao wanai-domesticate kupitia Baraza lao la Wawakilishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili msingi wa Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa tumesema ni Ibara ya 18 ya Katiba yetu na vilevile kwa Katiba ya Zanzibar nao wana Ibara ya 18 inaeleza hayo hayo na mimi nimepata mwelekeo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar nayo itakuwa na sheria hiyo hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Pauline Gekul alikuwa anasisitiza sana jana kwamba hii ni Sheria ya Katiba hapana hii siyo Sheria ya Katiba ni sheria ya kawaida. Sheria zote nchini msingi wake ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie na vitu vingine vichache. Mheshimiwa Hussein Bashe, Mheshimiwa Magdalena Sakaya, sheria imlinde third party au mchapishaji wa taarifa ambaye ataitoa in good faith kama inavyomlinda mtoa taarifa in good faith.
Naomba tu niwahakikishie kwamba kwa maudhui ya ibara hii ni kumlinda mtu aliye chini ya mmiliki wa taarifa dhidi ya hatua za kisheria, kiutawala au kiajira, pale anapotoa taarifa zinazofichua maovu ya mmiliki wa taarifa kwa nia njema akiamini kuwa taarifa hizo ni za kweli. Msingi wa ibara hii ni kuendana na masharti ya Sheria ya Kuwalinda Watoa Taarifa za Uhalifu wa Mashahidi (The Whistleblower and Witness Protection Act) ambayo tumeipitisha sisi wenyewe kwenye Bunge hili na imeanza kufanya kazi. Hivyo basi, mtu anayechapisha taarifa ya aina hiyo kwa nia njema akiamini kuwa ni kweli anaweza pia kuchukuliwa kuwa ni mtoa taarifa ya uhalifu anayestahili kulindwa kwa mujibu wa sheria hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Mheshimiwa Mwita Waitara alisema simu itumike kama mojawapo ya njia za kutoa taarifa. Ni wazo zuri, kanuni tunaziandaa sasa hivi, zitaainisha njia mbalimbali za kutoa taarifa na hatutasahau huo mchango wa Mheshimiwa Waitara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, neno habari litafsiriwe, Mheshimiwa Omar King. Muswada huu unahusu taarifa na si habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kupigiwa hiyo kengele ya kwanza, kwa kumalizia nisisitize kuwa muswada huu umeletwa kwa nia njema ya kupanua wigo wa upatikanaji wa taarifa ambazo ni chachu kwa maendeleo ya Taifa letu. Niliombe Bunge lako Tukufu kuupitisha muswada huu ili wananchi waanze kunufaika na taarifa mbalimbali muhimu kwa mustakabali wa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.
Muswada wa Sheria ya Huduma ya Msaada wa Kisheria wa Mwaka 2016
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuwapongeza sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia katika hoja hii mbele yetu. Hoja imechangiwa na jumla ya Waheshimiwa Wabunge 13, Wabunge wanane kwa kuongea na wengine Wabunge watano kwa maandishi, wote nawashukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaanza kuiangalia hii michango iliyokuja hapa, naomba tu kusisitiza kwamba wananchi wetu wengi hawajui kusoma na kuandika na sheria zetu zote zimeandikwa. Lakini pili, sheria zetu nyingi ziko katika lugha ya kiingereza, Watanzania wengi lugha hiyo ni ngeni kwao, hawaijui. Tatu, tuna mila na desturi zilizopitwa na muda ambazo wala hazitambuliwi na sheria za nchi za sasa, lakini kutokana tu na sintofahamu iliyopo maeneo mengi nchini kwetu mila hizo na desturi zilizopitwa na wakati bado zinatumika na kuumiza watu wengi sana hasa katika masuala ya ndoa, mirathi, umiliki wa mali kama vile ardhi, talaka, masuala ya adoption ya watoto na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, sheria zetu sehemu kubwa hazikubali utetezi kwamba hukujua sheria. Tunasema ignorance of the law is not a defence. Mpaka pale sheria kwa maneno yake itake wewe uwe na hiyo taarifa, iwe inataka hiyo knowledge uwe nayo. Kwa yote haya au katika hali hii tunahitaji sana huduma hii ya msaada wa kisheria ambayo imeshuka mpaka kwa wananchi wetu wa kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na mchango wa Kamati ya Katiba na Sheria, lakini nitagusia na mingine michache badae, ambayo inajibu maoni mengi yaliyojitokeza hapa, siwezi kuyarudia-rudia tena. Kamati ya Katiba na Sheria wamekuja na hoja ya kwamba katika kifungu chetu cha tafsiri neno “advocate” liendane na tafsiri iliyomo katika kifungu cha 4 cha Sheria ya Tafsiri (Interpretation of Laws Act).
Mheshimiwa Naibu Spika, mapendekezo haya tulijadiliana na Kamati na kimsingi tumeyakubali, lakini sisi tumeona ni vema zaidi tutumie sheria iliyo karibu zaidi na muswada huu ambayo ni Sheria ya Mawakili (The Advocates Act, Cap. 341). Kwa hiyo, ni mapendekezo yetu kuwa tafsiri ya neno hilo kama ilivyo kwenye sheria mama badala ya Sheria ya Tafsiri itumike na itasomeka kama ifuatavyo; “Advocate has the meaning ascribed to it under the Advocates Act.”
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, Kamati imesema maneno Legal Advice na Legal Assistance yatenganishwe katika kifungu kile cha tafsiri. Maoni haya pia tulijadiliana na Kamati. Tumekubaliana kuyaondoa na kuacha maneno Legal Aid Services ambayo tayari tafsiri yake imeshatolewa katika muswada huu na inajumuisha maneno legal advice na „legal assistance‟ kama sehemu ya legal aid services. Na ninaishukuru sana Tanganyika Law Society ndio waliotoa hiyo tafsiri. Sasa itasomeka, Legal Aid Services include the provision of legal education and/or information legal advice assistance or legal representantion to indigent persons.”
Mheshimiwa Naibu Spika, neno “Lawyer” katika hichohicho kifungu cha tafsiri, lipewe tafsiri ili kutofautisha hawa wenzetu waliosomea sheria na paralegals yaani wasaidizi wa sheria. Tumeona neno sahihi la kuwatengenisha wenye Shahada ya Sheria na Wasaidizi wa Sheria, neno lenyewe ni Mwanasheria (Lawyer). Hivyo, tunapendekeza tafsiri ya neno Lawyer isomeke kama ifuatavyo, “Lawyer means any person who is a holder of a Bachelor Degree in laws or its equivalent and provides legal services under the legal aid provider in accordance with this act.”
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile neno “Paralegal” Kamati ilitaka litafsiriwe. Mapendekezo yameafikiwa hivyo, tunatafsiri neno “Paralegal” kama ifuatavyo; Paralegal means a person who is accredited and certified to provide legal aid services in accordance with provisions of this act.
Mheshimiwa Naibu Spika, tano, tumeshauriwa tuondoe, sasa tuko katika kifungu cha 6(2), tuondoe neno “director” badala yake tuweke neno “person.”
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeafiki maoni ya Kamati na neno director limeondolewa na badala yake tumetumia neno person. Inaleta maana nzuri zaidi na sisi tumekubali.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati inataka kifungu cha 7 kiboreshwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, maoni haya yameafikiwa, hata hivyo tumeongeza maneno ukienda kwenye kifungu cha 7, “In consultation with a legal aid providers educational and training accreditation bodies” ili kupanua wigo wa consultation.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Kamati ilitaka wigo wa kusajili watu wenye taaluma ya sheria uongezwe, upanuliwe zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili kwa kweli tumekubaliananao tumeliboresha kama ifuatavyo, tunataka two advocates, one advocate and one lawyer, one advocate two paralegals, one lawyer, two paralegals or three paralegals. Tumeona tuchukue scenarios mbalimbali ili hii huduma iweze kutolewa kwa urahisi popote pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika kifungu cha 13 Kamati inapendekeza kwamba notice ya kukataliwa kusajiliwa kwa mwombaji itolewe ndani ya siku saba baada ya maombi kufanyika, lakini baada ya majadiliano tulikubaliana na Kamati kwamba, notice ya kukataliwa itolewe baada ya siku 14 ambazo kwa kweli ni utaratibu wa kawaida katika Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu cha 14, sheria iweke wazi haki ya rufaa ya mwombaji kama hajaridhishwa na uamuzi wa Waziri. Hili limeguswa na Waheshimiwa Wabunge wengi kwa maandishi na hata kwa kuongea.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili ni la rufaa dhidi ya uamuzi wa Waziri. Hata hivyo, kimsingi misingi ya haki ya asili (principles of natural justice) inampa fursa mtu kufungua shauri mahakamani hata bila kuelekeza, hivyo uamuzi wa Waziri hauwezi ukawa final and conclusive, hauwezi kuwa wa mwisho kama inavyofafanuliwa kwenye Sheria ya Law Reform (Fatal Accidents and Miscellaneous Provisions) Act; na tayari limekuwa likitendeka, umekwishakuwa utamaduni nchini hapa, hakuna uamuzi wa Waziri ambao hauwezi kupelekwa mahakamani, na ndio utaratibu tunaoutumia katika sheria zetu. Sasa tukitaka kuwa very prescriptive pia sheria yetu haitaonekana very tide.
Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu cha 16 kuna ushauri kwamba mtoa huduma apewe muda wa kutosha kushughulikia tatizo na kutoa taarifa kwa Msajili kuhusu hatua alizochukua kabla ya Msajili kufuta leseni.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekubaliana na maoni ya Kamati, hivyo kimeongezwa kifungu kidogo cha (4) kitakachosomeka kama ifuatavyo; “Notwithstanding the provisions of sub-section three the registrar shall not cancel a certificate of registration of the legal aid provider if it had notified the registrar in respect of paragraph (d), (e), (g) and has taken necessary internal measures to rectify the situation.”
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna suala ambalo limebeba interest ya Waheshimiwa wengi ambalo pia, Kamati iligusia. Shughuli za siasa zifafanuliwe katika kifungu cha 16(1)(f) na vilevile ukienda kifungu cha 43 na Waheshimiwa Wabunge wengi mmeliongelea hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mapendekezo yaliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge tumeyaelewa, tumeyaafiki hivyo tunapendekeza kuwa kifungu hicho kifutwe na kuandikwa upya na kisomeke kama ifuatavyo ili kuondoa hizi hisia za kisiasa; “A legal aid provider has discriminated aided person yaani hicho ni kifungu kidogo cha (f), a legal aid provider has discriminated aided person in terms of gender, religion, race, tribe or political affiliation.” Nafikiri mmelielewa hilo kwamba tumeipanua zaidi ili mtoa huduma huyo kwa kweli asioneshe upendeleo wa aina yoyote katika mazingira yoyote haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu cha 19; sheria iwatambue wasaidizi wa kisheria iwatambue wasaidizi wa kisheria wenye elimu ya sekondari na wale ambao wamekuwa wakifanya kazi hizo kwa zaidi ya miaka miwili.
Mheshimiwa Naibu Spika, mapendekezo haya yameafikiwa na kifungu hicho kimefanyiwa marekebisho hivyo tunakubaliana na mapendekezo hayo. Kifungu hicho kisomeke kama ifuatavyo, nitaomba kukisoma:-
“19(1) A paralegal shall be required to possess any of the following:-
(a) Any Bachelor Degree say for a Bachelor Degree in Laws or its equivalent from an accredited institution.”
Mheshimiwa Naibu Spika, hapana hili nafikiri sasa nimejibu yote mawili. Kuna hii moja ya siasa nimeshaieleza, kuna hii nyingine ambayo naisisitiza nisije nikawa nimeichanganya, ya kwamba tutambue hata wale wa shule za sekondari limeongelewa mwishoni hapa na Mheshimiwa Zedi. Kwa hiyo, nilikuwa naomba Waheshimiwa twende wote pamoja kwenye haya masahihisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, 19 tumeibadilisha sasa isomeke badala ya ile iliyopo huko. 19(1) A paralegal shall be required to possess any of the following:-
(a) Any bachelor degree save for a bachelor degree in laws or is equivalent from an accredited institution;
(b)Any diploma or certificate from an accredited institution; or
(c) Any certificate of secondary education.
(2) In addition to the requirement under sub-section one, a paralegal shall undergo necessary training as maybe prescribed in the regulations.
(3) Notwithstanding the generality of the provisions of sub-sections 1 and 2 any person who has been a paralegal for at least two years and has undergone training and the current arrangement prior to the coming into force of this Act, shall qualify as a paralegal for the purpose of this section.”
Mheshimiwa Naibu Spika, wamelalamika watu wengi, lakini nafikiri tumeona sasa tuirekebishe kwa njia hiyo na; 19(4) subject to sub-section three the registrar shall have power to recognize and accredit paralegals trained under a registered legal aid provider.
(i) Who meets the basic requirements set out in the provisions of section 19(1) and;
(ii) In accordance with the proved curriculum.”
Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu cha 20(c) na (f) vifutwe, havina mantiki, Kamati ilipendekeza hiyo. Tumeliangalia hilo kwa pamoja na sisi tumekubali vipengele hivyo (c) na (f) vimefutwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati na Kambi ya Upinzani nao wameleta mawazo yao kwamba urasimu wa kutuma maombi ya kupatiwa msaada wa kisheria uondolewe. Kwa kweli mapendekezo haya sisi hatukuyapinga kwa sababu lengo sisi tupate sheria ambayo kila Mtanzania ataiona ni rafiki. Kifungu hicho pamoja na maelezo yake ya pembeni vimefutwa na kuandikwa upya na kusomeka kama ifuatavyo, ni kifungu cha 21-
21(1) “An indigent person who intends to receive legal aid may approach any legal aid provider and apply for legal aid services.
(2) upon receipt of an applicationmade under subsection 1 the legal aid provider shall proceed processing the case.”
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri tusaidie, hayo marekebisho unayotusomea yapo kwenye Jedwali la Marekebisho au hapana?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Ndiyo yote yapo.
NAIBU SPIKA: Kwenye Jedwali?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Yah, yapo kwenye Jedwali. Wasiwasi wangu tu ni kwamba nikiyaacha pengine yatajirudia tena wakati tukiingia kwenye Kamati, nilitaka niwe as detailed as possible. Kifungu cha 20 (c); tumeshaongea hiyo, na ninafikiri tumemaliza hiki kifungu cha 21.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na hoja ya kwamba tusiishie tu kwenye Mahakama, kuna umuhimu kwa wigo wa kupatiwa msaada wa kisheria katika Mabaraza ya Ardhi, Kodi na taasisi nyingine na huko tuwe na msaada wa kisheria. Mapendekezo ya kuongeza wigo wa mamlaka zitakazoelekeza mtu kupatiwa msaada wa kisheria yameafikiwa; mapendekezo hayo yatasomeka kama ifuatavyo:-
“The presiding judge, a magistrate or chairman of the land, labour and tax tribunal and any other tribunal as the Minister may, by order published in the Gazette determine or adjudicatory body, shall cause such person to obtain legal aid.”
Na pia mapendekezo yameafikiwa ya kifungu hicho kisomeke kama ifuatavyo pia; “Where the legal aid provider withdraws or is discharged by the client the legal aid provider shall immediately notify all parties to the proceedings and record of the facts.”
Mheshimiwa Naibu Spika, Kambi ya Upinzani vilevile imeenda kifungu cha 29 hicho kilikuwa cha 21 kwamba mtoa huduma awe na haki ya kupokea sehemu ya tuzo ya Mahakama ili kufidia gharama. Mmemsikia hapa akiongelea Mheshimiwa Ally Saleh, Mheshimiwa Tundu Lissu. Maoni haya yameafikiwa, hata hivyo kanuni zitaweka utaratibu wa namna mtoa huduma ya msaada wa kisheria atakavyorejeshewa gharama alizotumia. Kifungu hicho kimefanyiwa marekebisho na kitasomeka kama ifuatavyo na nitaelezea kidogo:-
“Where cost are awarded in any proceedings such cost shall be placed in the funds of the board provided that legal aid provider may have right to deduct from the awards the cost incurred in respect of the proceedings in the manner prescribed in the regulations.”
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, tunapenda ifahamike kuwa msaada wa kisheria ni huduma inayotolewa kwa watu wasio na uwezo kwa maana ya kuwasaidia na si kwa maana ya kufanya biashara kwa lengo la kupata faida. Na hilo naomba nilisisitize kwa sababu hata alipokuwa anaongea Wakili Tundu Lissu hapa kwa kweli hakuongea kama Mbunge aliongea kama Wakili kabisa akiona kama Mawakili wanakuwa short changed, hapana. Hili ni suala la kujitolea na kila mtu ana wajibu wa kujitolea na hili ndio eneo pekee ambalo Mawakili vilevile lazima waoneshe social responsibility. Kama makampuni yanafanya hivyo under corporate social responsibility na sisi Mawakili katika eneo hilo.
Mhesimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo Kanuni za Sheria ya Mawakili zinatoa motisha na kuwatambua Mawakili wanaotoa huduma ya msaada wa kisheria kwa kuwapa CLE points (Continuing Legal Education) ambazo mtu anazipata za mafunzo endelevu ya sheria kwa kutoa huduma ya msaada wa sheria. Na point hizi zina umuhimu wake, pamoja na mambo mengine humsaidia Wakili katika kuhuisha leseni yake ya kufanya shughuli zake za Uwakili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu cha 36 kwamba Jeshi la Polisi na Magereza waweke mazingira ya kuwapatia msaada wa kisheria watu walio vizuizini, limeongelewa hapa. Mapendekezo haya kimsingi tumeyaafiki na kifungu hiki kitasomeka kama ifuatavyo:-
36(1) The Police Force or Prison Services shall designate a mechanism for facilitating the provision of legal aid services by legal aid providers to accused or convict in custody in the manner to be prescribed in the regulations.
Minister responsible for Home Affairs.
Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu cha 43 tumeombwa tuangalie namna ya kukiboresha hicho kifungu kama tulivyofanya kwenye kifungu cha 16 kuhusu masuala ya siasa. Kifungu cha 43(1) kinafutwa na kuandikwa upya ili kilingane na kile kingine kama ifuatavyo:-
“Subject to the provisions of this Act no legal aid provider, advocate, lawyer or paralegal shall provide legal aid on the basis of discriminating aided person on his gender, religion, race, tribe of political affiliation.”Tumeona hiyo inaweza kuondoa kidogo friction hapa ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati na Kambi ya Upinzani wameendelea kwenye kifungu cha 42 kwamba taratibu za mpito; taasisi zote ambazo zinatoa huduma za msaada zichukuliwe kuwa tayari zimesajiliwa na kupewa cheti kwa mujibu wa sheria hii. Ndugu zangu tumelijadili hili, tumeona mantiki yake, maoni yameafikiwa na kifungu hiki kimeboreshwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, halafu kwenye jedwali kuhusu muundo wa bodi; kuna bodi mbili hapa inasemwa lazima ziongezwe. Maoni haya pia yameafikiwa na muundo wa bodi umerekebishwa kwa kuzingatia maoni ya Kamati yetu. Maoni yao ilikuwa ni kwamba kuwepo na mjumbe mmoja kutoka Chama cha Mawakili yaani Tanganyika Law Society na mjumbe mmoja kutoka Jukwaa la Haki Jinai; mtaona katika marekebisho tuliyoyafanya ambayo mmeyapata.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Adadi Rajab pamoja na Kambi ya Upinzani, Serikali imekwepa kuanzisha taasisi mahususi ya kusimamia masuala ya utoaji wa msaada wa kisheria nchini kama ilivyo kwa Kenya. Sasa kama kila kitu tuwe kama Kenya na wao watakuwa kama Tanzania lini? Sasa haya ni ya kwetu yanatuhusu sisi, utaratibu wa utoaji wa msaada wa kisheria hauna viwango ambavyo ni lazima vifanane au vilingane kati ya nchi moja na nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nchini msaada wa kisheria umekuwa ukitolewa kwa muda mrefu sana na kwa ufanisi mkubwa. Kilichokuwa kinakosekana kwakweli ilikuwa ni uratibu na utaratibu wa kuiona hili eneo likienda vizuri bila mikwaruzano hasa sasa hivi ambapo inapanuka kwa kasi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kwa kuangalia uwezo wa nchi yetu kila jambo linaanza kwa utaratibu na kwa hatua. Kwa kuanzia Serikali imeanzisha utaratibu tuliokuja nao na tunauona huu utaratibu ni muafaka, basi endapo mazingira yataruhusu na ninyi ndio Waheshimiwa Wabunge tulete hapa mapendekezo, tupanue wigo kama ilivyo kwenye nchi zingine kama kweli wenzetu ambao wameanza juzi tu kama nao wataendelea vizuri na kuwa watu wa kuigwa. Na inawezekana kabisa nchi nyingi nazo zikaiga kwetu baadaye kutokana na ufanisi wake kadri tunavyo endelea kutekeleza hili suala.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Victor Mwambalaswa yeye amefika mbali kidogo kwamba atatumia Mfuko wa Jimbo kununulia vijana watakaokuwa wanatoa msaada wa kisheria pale pikipiki. Nampongeza sana kwa mawazo hayo, hata mimi mwenyewe nitawanunulia vijana wangu watakaofanya legal aid pikipiki ili waweze kumfikia kila mtu mwenye matatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu cha 21 hadi 36 havioneshi ni makosa gani ya kutolea msaada wa kisheria. Hayo ni maoni yaliyotolewa na Balozi Mheshimiwa Adadi Rajab. Muswada huu ukiusoma umetoa masharti kuhusiana na masuala ya kutolea msaada wa kisheria. Nina maana hapa ukiangalia kifungu cha 27 kinatoa ufafanuzi wa namna ya utoaji wa msaada wa kisheria katika mashauri ya madai na kifungu cha 33 kinatoa ufafanuzi kuhusu mashauri ya makosa ya jinai.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu nina muda kidogo sasa nimalizie tu kusema Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Mheshimiwa Tundu Lissu kwakweli ametusaidia sana kwenye Kamati na mimi nilikuwepo hapo, lakini aliyokuja kuyasema leo kwa kweli sikubaliani nayo sana maana ametupa historia ndefu sana ya haki na msaada wa kisheria Marekani na kunukuu matamko mbalimbali ya Majaji wa Supreme Court ya Marekani.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili niliseme kidogo tu kwamba kwakweli kwa kipindi sasa hili Bunge naona kama kipimo halisi cha usomi hapa ni watu kuzama kwenye google na kuibuka na nukuu chungu mbovu za kizungu na wazungu lakini bila kuzingatia context, muktadha, bila kuzingatia mazingira na hata historicity ya hizo nukuu zenyewe. Nasema hivyo kwa sababu kipindi chote ambacho Mheshimiwa Tundu Lissu, mdogo wangu namuheshimu sana amekitolea mfano ni toka mwaka 1893 mpaka miaka ya 1960 ambacho ni kipindi cha ubaguzi wa rangi uliokubuhu Marekani. Na ukiongelea legal aid kipindi hicho haikuwa legal aid kwa mtu mweusi; ni mzungu na hauwezi kuwa mfano mzuri kwetu sisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunalichukulia hili suala kiwepesi sana, ni rahisi kupotosha vijana. Marekani katiba yao ni ya mwaka 1787 lakini Wamarekani imewachukua miaka 178 mtu mweusi kupata haki ya kupiga kura, tuanze kusema hayo ukweli. Sasa utapata best practice pale? Sisi ndio tunatakiwa tuigwe mfano na Marekani, tumepata uhuru mwaka 1961; 1961 hiyo hiyo mwarabu, mhindi na yeyote aliekuwepo hapa Tanganyika alipiga kura na wengi wazungu na wahindi wakawa kwenye Baraza la Mawaziri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mtu mweusi amepiga kura marekani mwaka 1965 ndiyo maana nasema hiyo legal aid ilikuwa wapi? Halafu mimi kilichonisikitisha ni kule kunukuu sana Supreme Court ya Marekani, hiki ni chombo ambacho kimechangia sana kukandamiza haki ya watu weusi Marekani, na mimi nataka nimuombe mdogo wangu Tundu Lissu kama anaenda kutoa lecture Marekani asiseme haya mambo unaweza ukatupiwa mawe hivi hivi. Haiwezekani watu zaidi ya miaka 200 mnanyanyaswa halafu leo mtu unakuja una sugarcoat hiyo historia, sio vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namuomba akasome pengine naona bwana mdogo wangu yupo hapa mbele hebu aandike hii kesi ya Dred Scott dhidi ya Sandford ya mwaka 1857 ambayo ni uamuzi wa Supreme Court ukisema kamwe mtu mweusi zao la mtumwa akawa raia wa Marekani, hiyo ni supreme court na hiyo usifikiri kwamba extremity hiyo ilikuwepo miaka ya 1800 ni mpaka 1965 supreme court ikiwa very negative kwa weusi. Sasa mimi kwenye haki hizi msaada wa kisheria tukiwa-quote sana watu hawa tunatoa picha tofauti sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi ningeomba tu Waheshimiwa Wabunge, tukiwanukuu sana wazee wetu kwa mfano, akina Mwinamila, Nyungu ya Mawe, Mkwawa, akina Nyerere, wameongea mengi mazito sana jamani yanayohusu haki na ndiyo waliyokuwa wanapigani – akina Kinjekitilie, lakini hawa akina sijui Winterbottom na kadhalika na quotations ndefu huku wanawakandamiza watu wetu, hiyo mifano haifai kwa hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa kusema, kuna neno moja amesema, nchi zinazojali usawa mbele ya sheria kwenye hotuba yake na haki ya kusikilizwa…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwakyembe, tafadhali naomba umalizie.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, namalizia tu kwamba kuna hoja nzuri ambayo aliisema Mheshimiwa Tundu Lissu nilitaka niizungumzie kidogo tu kwamba alisema nchi zinazojali usawa mbele ya sheria na haki ya kusikilizwa zimetunga sheria zinazolazimisha mamlaka za nchi kutoa msaada wa kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sisi hatuhitaji kulazimishwa, sisi tumekuja kwa hiari kwa sababu haya ndiyo maendeleo taratibu ya nchi yetu, tumefika mahali ambapo sasa tunahitaji sheria hii ikamguse kila mtu kijijini ambaye anahitaji hilo. Nimalizie tu kwa kuwashukuru wote kwa michango yenu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tena kutoa hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DKT. HARRISON G. MWAKYEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na wasaidizi wake kwa hotuba nzuri ya bajeti ya Wizara. Naunga mkono hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Serikali ya Marekani kuuongezea muda Mpango wa AGOA kwa miaka 10, mpango ambao unazipa fursa nchi za Kiafrika kuuza bidhaa zake kwenye Soko la Marekani bila kutozwa ushuru, Tanzania bado haijatumia fursa hii vizuri. Soko la AGOA katika Jumuiya ya Afrika Mashariki limetawaliwa na nchi ya Kenya ambapo mwaka 2013 nchi hiyo imeuza zaidi ya asilimia 96 ya bidhaa zote toka Afrika Mashariki, ikifuatiwa na Tanzania 3%, Uganda 0.4%, Rwanda 0.2% na Burundi asilimia 0%. Bidhaa zitokazo Kenya kwenda Soko la Marekani kwa asilimia kubwa ni mazao ya kilimo cha maua, chai, kahawa, pamba na mazao yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mazao makubwa yaliyofanywa na Kenya yamechangiwa na nchi hiyo kuwa na mkakati mahsusi wa Kitaifa wa AGOA unaoainisha maeneo ya vipaumbele. Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo hazina mkakati mahsusi wa Kitaifa wa AGOA, hivyo kushindwa kuitumia fursa hiyo adimu na adhimu kikamilifu. Mwaka 2015 kulikuwa na jitihada za Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa kushirikiana na sekta binafsi kuandaa mkakati ya Kitaifa wa AGOA. Ni muhimu tujue tumefika wapi na hatua hiyo muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya udhaifu tulionao Tanzania ni ufungashaji mbovu wa bidhaa zetu na usalama kiafya wa mazao tunayotaka kuuza nje, udhaifu ambao umetufanya tuwaachie Wakenya kununua vitunguu, hiliki, tangawizi, viazi, pilipili, mchele mzuri nakadhalika, kutoka mashambani mwetu kwa bei ndogo na wao kumalizia kwa ufungashaji bora na kuzingatia masharti ya afya ya usindikaji, hatua ambazo zinaongeza thamani ya bidhaa na kuwaingizia fedha nyingi za kigeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2015 tarehe 26 Februari, 2015 Tanzania tuliongoza nchi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwenye kikao muhimu cha kujadili masuala haya ya kibiashara na Serikali ya Marekani jijini Washington DC. Pamoja na mambo mengine, mkutano huo uliwezesha nchi zetu kusaini makubaliano na Serikali ya Marekani ya urahisishaji wa biashara (Cooperation Agreement on Trade Facilitations, Sanitary and Phytosanitary measure and technical Barriers to trade). Makubaliano haya yametufungulia njia Watanzania kurekebisha upungufu wetu, kuomba msaada wa kiufundi pale tutakapokuwa tayari kusonga mbele. Moja ya hatua muhimu za kujiandaa ni kuja na huo mkakati wa Kitaifa wa AGOA niliouelezea awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina imani kubwa na Mheshimiwa Waziri na timu yake ya wachapakazi ambayo imeonyesha utayari wa kuchakarika ili nchi yetu sasa ijenge uchumi wa viwanda. Hivyo nina imani kuwa mkakati huo wa Kitaifa wa AGOA utakuwa tayari na kuanza kufanyiwa kazi. Wilaya ya Kyela inasubiri kwa hamu fursa ya kuuza kwenye Soko la Marekani bidhaa zake kuu mbili; mchele wenye ladha nzuri ya pekee na unaonukia na kokoa “organic” ambayo haitumii mbolea zozote za kemikali na ambayo imepata sifa kubwa Ujerumani na Uholanzi. Tatizo letu kubwa ni afya ya mimea na bidhaa zetu kuendana na viwango vya Kimataifa na ufungashaji wa bidhaa zetu ambao bado una ukakasi. Hatua tuliyofikia na wamarekani ni nzuri, tuitumie bila kuchelewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara nyingine tena naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na mimi kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika hoja zilizoko mbele yetu hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, wiki hii kutakuwa na matukio mawili muhimu ya sehemu ya mahusiano ya kimataifa tuna mechi mbili za mpira kati ya Timu za Tanzania na timu kutoka Seychelles na kutoka Djibouti. Sasa Mheshimiwa sijui kuna kitu nafikiri kiliongelewa hapa maana kwenye simu yangu nakuta kila mtu ananiuliza kwamba kuna tatizo na tumefanya upendeleo kwa timu ya kimataifa kufanya mazoezi kwenye uwanja wa Taifa, lakini timu ya hapa Tanzania haijapewa nafasi kufanya.

Ningeomba nitumie fursa hii kwa sababu ni mambo ya foreign affairs haya niweze kuitolea ufafanuzi kwa kifupi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, wote mnajua tu kwamba tumefanaya ukarabati mkubwa wa kiwanja chetu uwanja wetu wa Taifa mwaka huu majuzi tu, tumekamilisha baada kiwanja hicho kutuhudumia kwa zaidi ya miaka 10 na ukarabati tulioufanya vilevile nyasi tulizoweka pale zinategemea zitatuhudumia kwa zaidi ya miaka 10 na ili ziweze kufika miaka 10 kuna masharti yake, haturuhusiwi hicho kiwanja kukitumikisha kikabeba michezo zaidi ya mitatu kwa wiki moja, ukifanya hivyo unaingiza uswahili na hata ikiharibika mapema huwezi hata kwenda kudai mtu aliye ku-gurantee kwamba kitaa miaka 10.

Kwa hiyo, wiki hii tuna mechi mbili muhimu; kesho wanaingia Young Africans wanashindana na timu kutoka Seychelles na kesho kutwa wanaingia Simba na timu kutoka Djibouti. (Makofi)

Kanuni za kimataifa zinataka timu ngeni hiyo ya kimataifa lazima ifanye mazoezi kwenye hicho kiwanja kitakachofanyiwa mechi na vilevile FIFA inatambua kwamba hiki kiwanja ni cha timu ya hapa nchini kwa hiyo uwanja wa Taifa ni uwanja wa Yanga, uwanja wa Simba unategemewa ujue uwanja wako sasa wale wengine hawajajua ndio maana wanaopewa priority kuweza kufanya mazoezi pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, tayari tuna mechi mbili na kwa sababu tunaruhusu hawa wageni kufanya mazoezi pale ambao ni lazima kwa hiyo tutakuwa tumekiuka tayari tuna michezo minne ndani ya wiki moja. Na usisahau wiki hii hii Azam na Simba wamecheza uwanja huo huo, kwa hiyo mara tano, uswahili umeanza kuingia katika uwanja wetu wa Taifa.

Mimi nashukuru kwa haya maneno niliyoyapata nadhani kuna vijana wangu pale wanahitaji kwa kweli wadhibitiwe, utaruhusuje mechi tano katika uwanja huo ambao utarudia mara tatu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilitaka kufafanua tu kwamba ni haki ya wageni kupewa nafasi na sisi tuweze kutumia viwanja vyetu na naniombe nitoe rai na wito kwa wapenda mpira hapa, timu ya Yanga ina umri wa miaka 83 timu ya Simba ina umri wa miaka 82 timu zetu sasa zifike muda nazo zijenge viwanja vyake.
Azimio la Bunge Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Udhibiti wa Matumizi ya Dawa na Mbinu za Kuongeza Nguvu Michezoni
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nami nikushukuru kwa kunipa fursa niweze kuchangia kwenye hoja iliyoko mbele yetu. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kutuletea hoja hii sasa pamoja na kwamba, kama walivyosema wachangiaji wengine wanaona imechelewa kidogo. Naomba niseme mapema kabisa kwamba naunga mkono hoja hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee kidogo hotuba fupi ya Kambi Rasmi ya Upinzani iliyowasilishwa hapa na huyu msanii kutoka Mbeya, hotuba ambayo ilikuwa ya mzaha tu, tusiendeleze mambo kama haya katika Bunge hili Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama wewe haupo Bungeni unaitwaje kuja kuwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani? You should be here to stand up to be counted. Sasa tukianza kupiga kura tutamtuma Askari kwenda kuhesabu kura zao kule nje au tuwaite kuja kupiga kura kwa kitu ambacho hawajashiriki?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba tu kwamba tufuate Kanuni zetu bila wasiwasi wowote. Kwanza umewahi kusikia wapi mtu ambaye hakumaliza shule leo anadiriki eti kutilia shaka uelewa wa Daktari wa Falsafa mwenye Shahada na Stashahada sita? Haya yanatokea tu kwenye nchi ambazo zina underdeveloped economies. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Pilato aliwahi kusema wenye busara husema wanapokuwa na kitu cha kusema. Wapumbavu husema ilimradi waseme chochote. Sasa kwa msingi huo naomba sasa niseme kwa kuwa nina kitu cha kusema kuhusu hoja hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa miaka mingi nafikiri sasa ni miaka 11 nchi yetu haikuweza kuridhia Mkataba huu. Je, ni hasara au faida gani tumepata? Naona ni hasara tu kwa kutokuridhia, ninaziona ni hasara. Hasara kubwa kupita zote ni image, sura ya Tanzania machoni mwa Jumuiya ya Kimataifa, kuwa ya kutiliwa mashaka mashaka tu. Sasa leo ambapo biashara ya madawa ya kulevya duniani imeshamiri sana. Ndiyo sababu kwa kutokusaini vitu kama hivi, kutoridhia Watanzania tukisafiri nje ni watu wa kutiliwa mashaka kweli kweli! Tunapekuliwa bila huruma. Unamwona mwenzako kutoka nchi nyingine anapita tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tusisahau mwaka 2013, hivi majuzi, binti yetu mmoja amekwenda kwenye michezo Brazil, namkumbuka kwa jina moja tu la Sara. Alikutwa na dalili kwa mbali tu kwamba kulikuwa na dalili za nguvu kuongezeka, lakini anatoka Tanzania ambayo haijaridhia mikataba kama hii, kafungiwa miaka miwili. Kwa hiyo, kutoridhia kumetuathiri kwa kiasi. Tutoke huko sasa tuingie katika kuridhia, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuridhiwa kwa mkataba huu hakutuongezei tu heshima katika Jumuiya ya Kimataifa, lakini inatupa fursa ya kushiriki katika uendeshaji wa michezo duniani. Kwa sababu, sasa hivi hata tukitakiwa kupimwa Watanzania inabidi matokeo yetu tupeleke Kenya. Lakini hapa watatuletea vifaa. Kutakuwa na faida ya vijana ya wetu, wataalam wetu nao kupata mafunzo, kuendesha vifaa hivyo na vile vile ku-interact na wenzao Kimataifa kuweza kupata ujuzi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tukiwa humu ndani nasi ni sehemu ya Jumuiya ya Kimataifa ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya kwa upande wa michezo. Tunaweza kuwa na fursa kuwaeleza wenzetu tofauti kati ya bangi na mlenda, tofauti kati ya bangi na matembele. Maana ni kama yule binti wetu aliyekamatwa huko Brazil, siyo ajabu alikuwa amekula ugali hapa wa muhogo pamoja na matembele yakaonekana kama yameongeza nguvu, lakini wenzetu kama Kenya wanatumia mirungi na ni zao la biashara, lakini sijaona kama wanatingishwa sana, ingawa kwa kweli sasa hivi ndiyo wameanza kutingishwa kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kutoridhiwa kwa mkataba huu bado tuna changamoto kubwa kama ambayo nimeisema hasa kudhibiti madawa tunayoyalima hapa ndani, bangi. Nafikiri kuna umuhimu Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wakae na Wizara ya Katiba na Sheria vilevile Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi tuangalie ni jinsi gani tunaweza kuboresha udhibiti wa dawa kama bangi zinazolimwa nchini na kutumiwa na vijana wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tuna tatizo hapa, mmea kama mirungi, kwa wenzetu wa Kenya ambao ni sehemu ya Afrika ya Mashariki lile ni zao biashara na juzi wote tumeona Serikali imeongeza ten million US Dollars kuwasaidia wakulima kuhamasisha zao hilo. Sasa na mipaka yetu kama Afrika Mashariki ni very porous, mirungi inaingia kwa wingi sana hapa. Sasa inabidi tukae chini, tuiangalie hiyo hali tunaidhibiti vipi mirungi ambayo inatokea Kenya ambako wenzetu ni zao la biashara, lakini sisi hapa tumeharamisha kwa muda mrefu sana na tusirudi nyuma katika hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu nimegongewa kengele ya kwanza, naomba tu niseme kwamba Azimio hili limekuja katika muda mzuri sasa na naliunga mkono kwa asilimia mia moja. Ahsante sana.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nasimama mbele ya Bunge lako Tukufu kwa sauti ya huruma sana na kwa unyenyekevu mkubwa, ninategemea pia ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge mtanisikiliza vilevile kwa unyenyekevu huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nazipongeza Kamati zote mbili kwa kazi nzuri. Nitachangia vitu vichache tu. Mheshimiwa Kabwe Zuberi Ruyagwa amesema kitu kizito sana leo hapa kwamba kunajengeka utamaduni mpya hapa nyumbani wa kwamba ukituhumiwa tu, wewe ujue tayari umehukumiwa. Hiyo wamesema; once accused, you are condemned guilty. Ni kitu kizito amekisema ambacho sikubaliani naye, lakini kwa hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Susan Lyimo naye hakuwa mbali, asubuhi leo ameongelea hayo hayo akisema kuwa katika vita hii dhidi ya dawa za kulevya kuna Wakuu wa Mikoa wanataja tu majina ya watu, lakini kwa kweli alikuwa anamzungumzia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Vilevile Mheshimiwa Lucy Owenya naye anaona kwa kweli kuitwa tu polisi ni kama kuhukumiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kulithibitishia Bunge lako Tukufu kuwa katika operation hii dhidi ya dawa za kulevya, hakuna mtu aliyekurupuka na katika hili Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye ndio alianzisha hii operation, hajaenda nje kabisa ya sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ninukuu kifungu cha 10 cha Drug Control and Enforcement Act kinachoipa Serikali wajibu wa kuja na mikakati na hatua mbalimbali kupambana na tatizo hili la dawa za kulevya. Alichokifanya Mheshimiwa Paul Makonda - Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ni kutekeleza tu sheria hii, naye ni sehemu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi/Kicheko/)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo kidogo hapa Bungeni, sijui tunawaonaje Wakuu wa Mikoa, pengine tunawaona hawana wajibu huo kisheria. Naomba tu jamani, sisi ndio tunaotunga sheria, tukumbushane. Ukienda kifungu cha 5 cha Regional Administration Act, kinatamka kwamba Mkuu wa Mkoa ndiye mwakilishi wa mhimili wa utendaji katika eneo lake (The Regional Commissioner shall be the principal representative of the government within the area of his jurisdiction).
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kulikuwepo neno moja aliliongelea Mheshimiwa Kabwe hapa, akatoa na mfano wa Kigoma kule kwamba kuna kachura kapo juu, pale chini unajua kuna mtu; hili hakuna la kuficha! Mkuu wa Mkoa anateuliwa na Rais wa nchi na hawezi kufanya vitu ambavyo havina baraka ya Rais wa nchi. Ukienda kifungu cha 6 cha Regional Administration Act, it is clear, inasema; “The President may delegate any of his functions and duties under written law to any Regional Commissioner.”
(Hapa kulikuwa na muingiliano wa sauti)
tunaanza mambo ya kitoto haya ya kuzimiana microphone, nimepewa…
(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila mpangilio)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naeleza tu kwamba Mkuu wa Mkoa ana hayo mamlaka, lakini vile vile ukienda kifungu cha 7 kinamruhusu Mkuu wa Mkoa kuagiza mtu kutiwa ndani. Kasome tu, Regional Administration Act, kimepitishwa na Bunge hili hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kulikuwepo na hoja Mheshimiwa Halima Mdee; naomba nimhakikishie Mwanasheria Mdee kwamba sim-quote out of context, lakini aliongelea hapa kwamba vita dhidi ya dawa za kulevya inataka tuwe na pesa kwanza. Ametoa hata mfano wa Marekani, wametumia matrilioni ya pesa katika pesa hii. Angetaka leo na sisi tutumie matrilioni ya shilingi katika hii vita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu, Wamarekani wameshindwa kwa sababu walitanguliza pesa, siyo dhamira, ndiyo maana hii vita imeshindikana mpaka leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi hatujatanguliza pesa, tumetanguliza dhamira. Shida ya Bunge letu hili, tumejaa mgawanyiko kushindana shindana. Leo tungekuja na pesa, mngesema dhamira iko wapi? Tumekuja na dhamira; eeh, pesa iko wapi? Tuacheni tufanye tunavyoweza na tutafika tutakapofika. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuitwa na polisi sio kuhukumiwa. Unajua kuna tatizo hapa la public perception na legal reasoning, wanasheria mko wengi hapa, sio kwamba ukiitwa na polisi basi umefungwa, hapana, umeitwa pale kuisaidia Serikali kujua kiini cha tatizo na kuweza kujua tatizo lenyewe upana wake ukoje ili tuweze kumfikisha mtu anayehusika mahakamani.
Naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa ujasiri, kwa uthubutu wa kujitoa muhanga kuonesha mfano kwamba tunaweza tukapambana na hili tatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kelele za leo ni kelele za mwanzo tu, tusubiri kesho, keshokutwa kama hii operation itaishia hapo mnapofikiria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nimalizie kitu kidogo kwa sababu imekuwa ni kelele kama ya shule ya msingi, naomba tu nimalizie kitu cha mwisho nisiendelee tena.
Mheshimiwa Hussein Bashe ameongea kitu kizuri sana hapa, kwamba tuna matatizo hapa mengine ya ushoga ambayo alianzisha Mheshimiwa Makonda tukamuachia mwenyewe, nataka kumthibitishia Mheshimiwa Mbunge kwamba hatukumuachia na Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla ameligusia vizuri.
Naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba suala lile tulilibeba na tumeendelea nalo kwa sababu tatizo hilo ni kubwa hatutaki kukurupuka nalo, ni kubwa na tutaliambia Taifa ndani ya mwezi huu tumechukua hatua gani. Kwa sababu tumekuja kubaini, kuna NGOs hapa nchini zinatumwa na nchi ambazo zinaamini kwamba mahusiano ya jinsia moja ni haki za binadamu na hizo nchi zinazoamini hivyo zinafadhili baadhi ya vyama vya siasa hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana tunachukua muda tuje na ushahidi wa kutosha ili tuchukue hatua. Wanasema aisifuye mvua imemnyea, unapiga kelele nini kama huusiki!
heshimiwa Mwenyekiti, jamani, nimalizie tu kwa kusema naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Umeniomba niongee kwa muda mfupi sana nitajitahidi kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo machache ambayo yamejitokeza yanahitaji niyatolee majibu. Nianze na la kwanza ambalo ni suala la uelewa tu ambalo Mheshimiwa Nkamia alionesha mshangao hapa kuniona mimi niko pamoja na huyu msanii kwa jina la Roma Mkatoliki
anayedaiwa kutekwa pamoja na wenzake watatu siku chache zilizopita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati na mimi namsikiliza Mheshimiwa Nkamia Dar es Salaam nilikuwa na kundi kubwa la waandishi wa habari nao walikuwa wanamshangaa kwa nini anashangaa kwa sababu amekuwa kiongozi kwenye Wizara hii anaelewa kabisa Idara ya Habari Maelezo ni Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, kwa hiyo, ni ofisi yangu ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni tumehamia Dodoma na Makao Makuu ya Wizara yako hapa LAPF, nikiwa Dar es Salaam ofisi yangu iko Maelezo. Sasa mtu akinikuta Maelezo nimemfuata yeye au yeye amenifuata? Ni vitu ambavyo nataka vieleweke. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kijana huyo alipokuwa amepotea mimi ndiye nilikuwa napigiwa simu na ndugu zake na waandishi wa habari, hakupigiwa Mheshimiwa Nkamia au mtu mwingine, napigiwa mimi. Mimi ndiye mlezi wa hii sekta. Mimi nilikuwa nahangaika na polisi huyu kijana kaenda wapi maana ni vitu ambavyo katika Taifa hili hatujavizoea.
Sasa huyu kijana anakuja kuniona ofisini kwangu, kimekuwa kioja tena! Nimekuwa na mkutano naye for one hour ofisini kwangu lakini yule kijana ana picha tofauti kabisa kuliko ramli ambazo zinapigwa huko nje na humu ndani ya Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, amekuja ananiambia aliyeniteka Mheshimiwa naomba tu upelelezi ufanyike in detail kuwa na bastola haina maana mtu lazima atoke Serikalini maana bastola kila mtu anazo. Alichoomba tu alisema tafadhali naomba upelelezi wa kina ufanyike. Kwa hiyo, niliona lazima nimsindikize, ni suala ambalo ni topic nchini, I am the Minister responsible ili kuhakikisha kwamba Watanzania wanaacha kupiga ramli tunapata ushahidi wa kutosha, ndiyo upelelezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu niseme kwamba sasa hivi Sera ya Wizara ni constructive engagement na vijana hawa wasanii. Ndiyo maana hata wiki iliyopita alikuja huyu kijana mwingine anaitwa Ney wa Mitego, akaja ofisini kwangu, sasa mlitaka sijui nimkimbie nikae naye kwenye mgahawa, namkaribisha ofisini kwangu ndio hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wiki ijayo nakaa na Diamond, ni kijana ambaye nimeona wana mfumo mzuri sana wa haki miliki wanauendesha pale katika mfumo wao, it can be used hata katika nchi nzima kwa wasanii wengine. Sasa ukinizuia nisikutane nao, ukutane nao wewe ili ufanye
nao nini? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, umenipa muda mfupi sana. Kuna suala limejitokeza la lugha za alama, ni Mheshimiwa Ikupa na Mheshimiwa Mollel wameliongelea hili. Ni kweli kabisa, TV zetu bado hazijaanza kutoa huo msaada. Kwa kweli siyo kitu kizuri sana kwa sababu hata Mheshimiwa Waziri Mkuu amelikazania suala hilo. Tuna TV kama tisa hivi nchini hapa ukiachia zile za cable na zote hazijaanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hapa ni gharama tu kwamba ukianza kutumia ukalimani lazima kwa siku uwe na wakalimani sio chini ya wanne lakini tumeshaanza majadiliano. Naomba kukuhakikishia kwamba angalau kwa taarifa za habari tu na sitaki nishinikize TV binafsi kabla
sijaanza kuhakikisha kwamba TBC inaonesha mfano yenyewe katika suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine Mheshimiwa Kapufi ameongea suala la muhimu sana hapa kwamba hebu tuachane na mipango ya zimamoto katika michezo tuwe na mipango endelevu. Nakubaliana kabisa na Mheshimiwa Kapufi. Kwa muda mrefu sana nchi hii, kwa miongo zaidi ya
mitatu tumekuwa tunalegalega kwenye michezo. Kwa kweli Mzee wetu, baba yetu Ali Hassan Mwinyi hakukosea kusema tulikuwa kama kichwa cha mwendawazimu, kila mtu alikuwa anakuja kujifunzia kunyoa hapa, lakini yote ni kwa sababu tulikuwa hatuamini katika maandalizi ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tumebadilika, naomba niliseme hili na ndiyo maana sasa hivi tunaweza kujivunia hata katimu kama Serengeti kwamba possibility ni kubwa kakarudi na kombe la dunia hapa nyumbani kwa sababu ya malezi. Vijana wale wamelelewa toka wakiwa na umri wa miaka 12, 13, 14, 15 sasa hivi ni under seventeen na hao ndiyo under nineteen watakaotuchezea baada ya miaka kadhaa lakini timu nyingine imeandaliwa sasa hivi kuziba nafasi yao. Tumejifunza hilo kwamba tunahitaji kwa kweli kuandaa hizi talents. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wanatumia academies lakini sisi kwa uchumi wetu kutokana na sera zetu kwamba tunahitaji kila kijana apate opportunity, sisi tumeamua, tena naishukuru sana TAMISEMI, upo hapa Mheshimiwa Waziri kwamba tutumie peoples academies
ambazo ni shule zetu za msingi na sekondari hizi hizi. Ndiyo maana mwaka huu Mheshimiwa Waziri Mkuu amesisitiza lazima tuwe na michezo ya UMISETA na UMITASHUMTA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nimekwenda kupokea kifimbo cha Malkia kuelezea tu kwamba kuna michezo next year ya commonwealth ambayo tulikuwa tunafanya vibaya. Can you believe toka Filbert Bayi avunje rekodi ya dunia miaka 43 bado tuko tu chini sisi. This time tutakuja na medali Watanzania kwa sababu tumeanza maandalizi sasa tena ya nguvu kweli kweli kwa ajili ya michezo hiyo inayokuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uliniomba nikuachie dakika chache, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii na nianze kwa kuunga mkono hoja na vilevile kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI na mwenzake wa Utumishi na Utawala Bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yamesemwa mengi hapa ambayo yanahitaji ufafanuzi ili tusiupotoshe umma. La kwanza ni kauli tuliyoanza kuisikia jana hapa, imesemwa kwa nguvu hapa, ooh, Mawaziri wa Tanzania ni waoga, hawana ujasiri. Nimekuwa najiuliza, ujasiri wa aina gani? Wa kumkaidi Waziri Mkuu? Kumkaidi Rais? Ujasiri upi wa kukataa pengine three-line whip? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ni hivyo, umeona wapi dunia ya leo ambapo Mawaziri hawaongozwi na kanuni ya kuwajibika kwa pamoja Bungeni katika Parliamentary system? Hii ndiyo inaitwa collective responsibility, siyo kwamba tumeiokota tu, iko katika Katiba, twende Ibara ya 53.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 53(2) inasema: “Mawaziri, chini ya uongozi wa Waziri Mkuu watawajibika kwa pamoja Bungeni.” Sasa tnapowajibika kwa pamoja Bungeni, aah, hawa sio majasiri.

Nyie mkija kuunda Serikali, maana ni mwaka 2090 huko, bahati nzuri mimi sitakuwepo. Mtakuwa watu gani ambao mna Serikali moja kila mtu anaongea la kwake? Siyo hivyo tu, Waziri Mkuu mwenyewe ambaye sisi tunafanya kazi chini yake, Katiba inasema 53(1), Waziri Mkuu atawajibika kwa Rais kuhusu utekelezaji wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ndiyo chain ya accountability katika Serikali. Kwa hiyo, tusiwapotoshe wananchi, waoga, tunaogopa kitu gani? Mmeona mtu yeyote anatetemeka hapa? Hatuogopi chochote hapa. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nashangaa sana, tunapenda kuongelea wenzetu wakati sisi wenyewe tuna...; mimi nimeona, Mheshimiwa Kiongozi wa Upinzani Bungeni alipoingia hapa, watu mpaka mikanda inalegea, wanatetemeka hapa, kimya! Sisi leo kumheshimu Waziri Mkuu wetu ambapo tuna wajibu, lazima tutamheshimu. Lazima! It is our obligation, ni kitu cha ajabu! Tuache mizaha hapa, wananchi wanatuzikiliza, wanatuona we are not serious. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, suala la Richmond, hili suala limeibuliwa jana na Mbunge wa Arumeru Mashariki Mheshimiwa Nassari kwamba Kamati Teule iliyochunguza suala hilo haikumtendea haki Mheshimiwa Edward Lowassa kwa sababu haikumhoji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naelewa, ni kazi ngumu sana leo hii kutaka kumsafisha Mheshimiwa Edward Lowassa kutokana na kesi ya Richmond ambayo ilishakwisha. Ndiyo maana sioni ajabu ili kusema aliyosema, ilibidi Mheshimiwa Nassari anywe pombe kwanza. Ninayasema haya Kiongozi wa Upinzani Bungeni ajue kwamba tuna tatizo hilo. Na mimi ninawapongeza sana vijana wetu wa Usalama waliokamata hiyo chupa hapo. Maana angeruhusiwa na hiyo chupa, huenda hata angetapikia rangi zetu za Taifa humu ndani, ingekuwa ni scandal kubwa kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeelezea mara nyingi sana katika Bunge hili, hata Bunge la tisa lililoshughulikia suala la Richmond kuwa Kamati Teule iliyoundwa na Bunge hili kazi yake ilikuwa kuchunguza, siyo kutoa maamuzi. Unapochunguza requirement ya audi alteram partem rule, hiyo requirement haipo pale wakati wa uchunguzi; ipo wakati wa maamuzi. Ndiyo maana sisi tulikuja hapa tukaleta kesi hapa tukiwa na mashahidi zaidi ya arobaini wakisubiri nje.
Aliyetakiwa kuhojiwa hapa, akajiuzulu. Unamlaumu Mwakyembe kwa hilo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba msipotoshe umma. Ooh, hakuhojiwa. Ahojiwe vipi? Unajua ni aibu! Ni sawa na mtu anaenda mahakamani, anasema unajua polisi hawakunipa haki ya kuhojiwa. Polisi? Upo Mahakamani ndipo pakuhojiwa hapo. Pakuhojiwa ilikuwa hapa! Kwa hiyo ndugu zangu, naomba tusipotoshe watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tulipata nyaraka za Serikali 104; na tukahoji watu 75, tuliwauliza maswali 2,717. Ipo kwenye Hansard! Hatukuona sababu yoyote ya kumwita Mheshimiwa Lowassa. Hatukuona! Tulikuwa na kila kitu, tulikuwa na ushahidi wote. Naomba kama kuna mtu yeyote hapa bado anakereketwa na kesi ya Richmond, aache maneno maneno hapa, alete hiyo kesi iibuliwe kama hatutawanyoa nywele kwa vipande vya chupa, ilete hapa! Acha maneno ya kienyeji hapa! Tumeshachoka! We are tired of this! Jamani eeh, ileteni hiyo kesi hapa, mnaruhusiwa na kanuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwamba, mimi naahidi, siku ambayo kuna moja atakuwa jasiri hapa kusema nalileta suala la Richmond lirudiwe tena, mimi nitamwomba Mheshimiwa Rais anipumzishe Uwaziri niweze kuishughulikia hii kesi sasa kikamilifu iishe moja kwa moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja nyingine aliyoileta hapa kuwa kwenye Ph.D Thesis yangu nilikiri kuhusu Serikali tatu, lakini sasa hivi nasema Serikali mbili.
Anyway, la kwanza ni kwamba kwanza alilewa ndiyo maana alikuwa anasema tu hayo, maana ameambiwa, hajasoma hata hiyo Ph.D Thesis, lakini la pili ni kwamba watu wanaelewa watu wenye integrity, watu wasio na integrity tunawajua hapa ambao wanakesha miaka mitano kumtukana mtu kumwita fisadi, leo wanamkumbatia, wanalamba na nyayo zake, ndio vigeugeu namba moja hao! Halafu leo mnajidai kuja kumsafisha! Huwezi ukasafisha madoa ya lami eti kwa kutumia kamba ya katani au maji, haiwezekani! Lileteni hili suala hapa tulimalize.
Naomba niseme tu kwamba katika ile thesis yangu, naongelea kuhusu mfumo wa two governments, three jurisdictions; na mfumo huo katika hiyo thesis tunasema it is not sui generis; siyo pekee, inatumika katika mataifa mbalimbali yanayotaka ku-partner yakiwa na tofauti kubwa sana ya ukubwa wa eneo, yakiwa na tofauti kubwa sana ya idadi ya watu, yakiwa na tofauti kubwa sana ya rasilimali watu na vilevile maliasili, ndiyo unatumika huo utaratibu. Sasa soma yote, kurukaruka tu, hutaelewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nasema tu kwamba it is a federal variant, ndiyo hoja kubwa katika hiyo thesis. Kwa hiyo, naomba tu bwana mdogo akipata muda asome kama atapata muda, mimi sijui, mtoto wa Mchungaji yule lakini ndiyo hivyo, ameingia hapa na kachupa ka pombe. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie suala la mwisho. Naomba nirudie tena, wengine hapa katika kupambana na udhalimu, kupambana na matendo mbalimbali, sisi wengine hapa tumeumia sana, unapoleta masuala hapa kimzaha mzaha; tutakujibu to the maximum. Mimi I am ready for anything. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba akina Mheshimiwa Kubenea na magazeti yao, leteni kesi ya Richmond hapa, nawaomba, chonde chonde, ileteni hapa! Jamani, naomba kwa Mungu, mkiileta hapa, nitafurahi! Kwa sababu ninachosema hapa na ushahidi nilionao hapa ni kwamba sisi tulimkuta huyu jamaa in flagrante delicto, ndivyo wanasema wanasheria, we have everything na mpaka leo hatujafa, tutakuwa hapa kuthibitisha hilo suala.

Kwa sababu mmekuwa na makubaliano ya kumsafisha, hamtaweza kumsafisha. Leteni kesihapa!
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa. Awali ya yote naunga mkono hoja na napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wa Fedha kwa bajeti nzuri na vilevile kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuirejeshea nchi yetu sifa na heshima yake ya zamani, sifa na heshima ya kuthubutu, sifa na heshima ya kupigania haki, usawa, na uhuru bila kigugumizi, bila uoga na bila hata kujali aliyeko upande wa pili, je, ana fedha nyingi, ni mkubwa sana au yukoje. Na msimamo huo dunia nzima ilitambua kwamba hiyo ndio Tanzania. Mwalimu alianza kuonesha sifa hii ya Tanzania mara tu baada ya uhuru baada ya kuiweka nchi yetu kama ngome kuu ya upiganiaji uhuru katika Bara la Afrika na dunia yote ilijua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikukumbushe kitu kimoja kwamba katika hali ya kawaida huwa ni tajiri tu ndiye anayeweza kumuwekea vikwazo mtu maskini, lakini kipindi cha Mwalimu nchi masikini ya Tanzania ilikuwa inawawekea vikwazo hata nchi kubwa. Na ukiwekewa vikwazo na Tanzania una hali mbaya, chukulia mfano Uingereza walipoanza kuchezacheza na haki ya uhuru wa watu wa Zimbabwe, tarehe 16 Disemba, 1965 Tanzania tukavunja uhusiano wa kidiplomasia na Uingereza na dunia ikaona, just a question of principle! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulipoungana na Zanzibar mwaka 1964 Ujerumani wakaanza kutumia ile wanaita the Hallstein Doctrine ambayo ilikuwa inasema kama wewe ni rafiki wa Ujerumani Magharibi basi vunja urafiki na Ujerumani Mashariki; Mwalimu akasema I see, hebu acheni kutuchezea hapa, ondokeni Wajerumani wote. Hiyo, ndiyo Tanzania, Tanzania ya kuthubutu, Tanzania yenye principles. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulifundishwa na Mwalimu kwamba Nchi hii ili iweze kuendelea hatuhitaji big brother, hatuhitaji pesa, hiyo ni akili ya kitumwa, pesa ni matokeo. Tunachohitaji ni vitu vinne tu; watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora, huo ndio ulikuwa msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini mjadala wa makinikia au mashapo kwa mujibu wa Kamusi tuliyoizindua tu hapa jana; mjadala huu ambao umeendelea kwa wiki kama mbili hivi, hauakisi Tanzania ya Nyerere. Wakati wananchi wanaunga mkono na kushangilia uthubutu wa Rais, Mheshimiwa John Pombe Magufuli kutetea rasilimali za nchi na wao wanaelewa mikataba tuliyoingia, mchanga unachukuliwa yanaachwa mashimo hapa, hakuna hata makubaliano kwamba basi mkishachenjua kule turudishieni mchanga tuzibe haya mashimo au mtatengenezaje?

Mheshimiwa Spika, tuna makampuni hapa kama Williamson Diamond, miaka 77 haipati faida lakini ikiwa Botswana inapata faida, wananchi wanalielewa hilo, lakini sisi wasomi sasa tunasema hapana, jamani tuwe waangalifu, tuwe waangalifu sana! Oooh, wazungu hawa, tuwe waangalifu nao; mimi nashangaa.

Mheshimiwa Spika, sasa ili tuendelee tunahitaji vitu vinne watu, ardhi, siasa na uongozi bora, sasa hivi imebadilika imekuwa ili tuendelee tunahitaji fedha na wazungu, maana tunawaogopa wazungu kupita kiasi, imenitisha.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Spika, leo hii tuna vita ya kiuchumi, kijana msomi, mwanasheria, unasimama hapa unatutishia nyau! Ooh! Tuna MIGA na Wanyakyusa kuna watu wanaitwa kina Minga, wananiuliza hivi huyu Minga ametokea wapi? Tuna MIGA! What is MIGA? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mbunge wa Mwibara hapa, alituletea mkataba hapa, kasoma tu kifungu kimoja, Ibara ya 12, lakini namwambia asome na ya 11, hatuwezi kushindwa kesi chini ya sheria hii ndogo ya MIGA, ni mkataba wa kawaida tu kama mikataba mingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, taarifa ya Profesa Osoro, ya Mruma ni takataka! Huo ni umamluki wa hali ya juu. Tuko kwenye vita! Tuko kwenye vita hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sio tu MIGA, lakini sisi tuna mikataba ya kimataifa inayosimamia good faith katika mikataba. Tuna UN Convention on Contrast for International of Sale of Goods, tuna UCC ambayo ni Unfair Commercial Code ambayo tunaitumia, yote inasisitiza good faith katika mikataba. Good faith inatokea wapi, mikataba hii ya madini ambapo mtu anasema nachukua mchanga wako kwenda kuchenjua, tuna-calculate percentage kule, kumbe ameshauza siku nyingi. There is no good faith! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, MIGA Convention yenyewe inasema nini; MIGA inasema ukitaka kutumia MIGA faida yake hapa lazima uheshimu sheria za nchi. Sheria za nchi zinasema nini? Zinasema kwamba ukitaka kuingia mkataba lazima kuwepo na union of minds, wanasheria wanajua, tunaita concensus ad idem, haiwezekani ikawepo concensus wakati wewe unamwambia mwenzako naenda kuchenjua halafu nakokotoa, kumbe huwa kabla ya kuchimba umeshauza hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndio maana nasema hatuwezi hata kidogo kushindwa hiyo kesi. Tuliweza kushinda mtihani wa Devolution Agreements wakati wa uhuru, tutashindwa MIGA? Tutashindwa MIGA? Tukishindwa kesi hii basi tumezungukwa na Mayuda Iskariote wa kutisha, lakini nashukuru wako wachache sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Devolution Agreements zilikuwa ni nini, niseme kwa kifupi. Tulipokuwa tunapata uhuru Barani Afrika Waingereza walikuwa wanakuja na mikataba inayosema, mimi nakubali mikataba yote aliyoingia Uingereza inayonibana inibane mimi kama nchi huru. Ni Mwalimu Nyerere peke yake aliyepeleka note ya kukataa hiyo Umoja wa Mataifa akisema mimi nilikuwa sijazaliwa kama taifa huru, mikataba hiyo mliingia kwa hiyari yenu hamkuni-consult, mlinitawala bila kibali changu, sitaki kuingia kwenye hiyo biashara; na tangu toka hapo ndipo ikazaliwa dhana katika Sheria ya Kimataifa inaitwa The Nyerere Doctrine of State Succession ambayo watu wengi wameifanyia mpaka Degree za Uzamivu, hii nchi ina historia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, msimamo wa Mwalimu uliokoa mengi sana nchi hii. Tulikuwa na Belbase Agreement alioingia Mwingereza na Ubelgiji. Mwingereza aliitoa Bandari ya Kigoma na Bandari ya Dar es Salaam kuwapa Wabelgiji waimiliki, tukakwepa kutokana na Mwalimu msimamo wake wa kwamba hatukubali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilishaunga mkono hoja.
Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Kamisheni ya Pamoja ya Bonde la Mto Songwe kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Malawi
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa nami nichangie kwa kifupi tu kuhusu moja ya mazimio yaliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mshituko mkubwa nilioupata kwa taarifa uliyotupa hapa kuhusu Mbunge mwenzetu, naungana nawe kabisa kumwombea mwenzetu apate ahueni haraka na vilevile namwomba Mwenyezi Mungu atupe ustahimilivu mkubwa katika kipindi hiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, nalazimika kusimama kama nilivyosema, kuchangia kuhusu Azimio la Kuanzisha Kamisheni ya Pamoja ya Bonde la Mto Songwe kati ya Tanzania na Malawi. Kuanzishwa kwa Kamisheni hii ambako kuna miradi chini yake kadhaa ya maendeleo kwa wananchi, ni sawa kabisa na kutumia jiwe moja na kuua ndege watatu kwa pamoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa Azimio hili litawanufaisha watu zaidi ya laki tatu; ni idadi kubwa sana hii ambayo iko katika hilo bonde hasa kupitia miradi yao hiyo ya umwagiliaji, miradi hiyo ya maji safi na vilevile miradi ya umeme, kama ambavyo wenzangu wameeleza nisingependa kurudia.

Pili, tutakuwa tumetatua tatizo sugu la muda mrefu la Mto Songwe kupindapinda kubadilisha njia yake kila wakati na kusababisha watu waliokuwa Tanzania kuwa wa Malawi mara nyingine na Wamalawi kuwa Watanzania. TRA najua watashangilia sana kusikia hili, maana wanaowadai kodi, mara nyingine wanashindwa kwenda kuwadai maana tayari wako Malawi kutokana na maamuzi ya huo mto.

Mheshimiwa Naibu Spika, mara nyingine wengine hapa tunategemea kura kwa Watanzania wetu. Kuna kipindi nimewahi kukuta ngome yangu kubwa yote imehamia Malawi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa haya ndiyo mambo ambayo watu wote kwa kweli katika Bonde hili watashangilia sana kwamba Azimio hili linaenda kutatua tatizo lililokuwa sugu kati ya Tanzania na Malawi kuhusu mpaka huo ambapo tuliwahi kufikia hata mahali hata eti kufikiria kujenga nguzo katikati ya huo mto. Kutokana na haya mabwawa matatu, hakutakuwa na mafuriko ya kutushangaza tena eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, Azimio hili linatupa fursa maalum, fursa muhimu ya maelewano zaidi kati ya Tanzania na Malawi. Sasa hivi tumeanza ushirikiano, nami nina uhakika huu utakuwa ndiyo msingi wa maelewano zaidi na zaidi kati ya nchi zetu hizi mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuhakikishie tu kitu kimoja kwamba nilikuwa namwangalia rafiki yangu ananiangalia hapa, kwamba mimi eneo langu pale Kyela halijawahi kuhamia Malawi. Sasa tusije tukaanza kueleweka vibaya hapa, halijawahi. Muda wote mimi niko mbali kidogo na huo mto, lakini naongelea tu kwa meneo yote ambayo yanahusika Wilaya ya Kyela.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kuipongeza sana Serikali kwa Azimio hili, kwa uamuzi huu kupitia Wizara yetu ya Maji na Umwagiliaji, kwa sababu watakaofaidika sana katika mradi huu; ni pamoja na Wilaya yangu, Jimbo langu la Uchaguzi la Kyela, hasa Kata zetu za Ngana, Katumbasongwe, Ikimba, Njisi, Ikolo, Ngonga, Bujonde, wote hapa katikati tutafaidika sana na Azimio hili tunalolipitisha leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nisipoteze muda wako mwingi, naomba tu kusema, naunga mkono Azimio hili. Ahsante sana.
Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Uamuzi wake wa Kuendeleza Mji wa Dodoma na Kuupa Hadhi ya Jiji
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kupanga kwa kweli ni kuchagua na uteuzi wa Makao Makuu ya Nchi unaendana na matakwa ya wenye nchi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme tu kwamba naunga mkono Azimio hili na niwakumbushe tu ndugu zangu historia fupi kwa kifupi tu kwamba mwaka 1891 Mjerumani alipoitwaa nchi yetu kuitawala wakati huo ikiitwa Deutsch- Ostafrika ikiwepo na Rwanda na Burundi, akateua Kijiji cha Bagamoyo kuwa Makao Makuu ya Deutsch-Ostafrika. Wakati huo Bagamoyo ilikuwa na nyumba moja tu ya bati, lakini uteuzi huo ulikuwa na maana ya kuweka changamoto kwamba sasa inajengwa Bagamoyo kuwa sasa ndiyo capital na Jiji la Deutsch-Ostafrika. Baadae ikahamia Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana naomba tu nipongeze uamuzi tu wa kuhamia Dodoma na uamuzi wa kutangaza Dodoma kuwa Jiji, kwamba hii inakamilisha uhuru wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uteuzi wa Dar es Salaam na Dodoma ulikwenda na vigezo vya mkoloni kwamba alihitaji sehemu ambayo atanyonya chochote kilichoko Tanganyika na kukipeleka kwao. Sasa tunajiangalia ndani, tunahitaji Mji Mkuu ambao uko katikati ya Tanzania, ambao utatuhudumia wote kwa pamoja. Ndiyo maana tunaunga mkono uamuzi huu wa kijasiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimweleze tu kidogo ndugu yangu Mheshimiwa Kubenea anasema kwamba usafiri kuja Dodoma ni mgumu sana. Ni kawaida miji yote ambayo imekuwa mikuu baadae, leo usafiri kwenda Lagos ni rahisi kuliko kwenda Abuja. Safiri kidogo Mheshimiwa Kubenea, usikae tu kwenda Bagamoyo. Vilevile nenda Uganda, usafiri kuingia Entebe ni rahisi kuliko kwenda Kampala. Ni vitu vya kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla muda haujaniishia, nimalizie tu kusema tu, ndugu zangu hebu tumwache Mheshimiwa Rais atekeleze majukumu yake kwa kufuata Katiba hii. Hebu niwasomee tu Ibara ndogo ya 37 ndiyo niishie hapa, inasema; “Mbali na kuzingatia masharti yaliyomo katika Katiba hii na Sheria za Jamhuri ya Muungano katika utendaji wa kazi na shughuli zake, Rais atakuwa huru na hatalazimika kufuata ushauri atakaopewa na mtu yeyote.”
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa. Awali ya yote naunga mkono hoja na napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wa Fedha kwa bajeti nzuri na vilevile kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuirejeshea nchi yetu sifa na heshima yake ya zamani, sifa na heshima ya kuthubutu, sifa na heshima ya kupigania haki, usawa, na uhuru bila kigugumizi, bila uoga na bila hata kujali aliyeko upande wa pili, je, ana fedha nyingi, ni mkubwa sana au yukoje. Na msimamo huo dunia nzima ilitambua kwamba hiyo ndio Tanzania. Mwalimu alianza kuonesha sifa hii ya Tanzania mara tu baada ya uhuru baada ya kuiweka nchi yetu kama ngome kuu ya upiganiaji uhuru katika Bara la Afrika na dunia yote ilijua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikukumbushe kitu kimoja kwamba katika hali ya kawaida huwa ni tajiri tu ndiye anayeweza kumuwekea vikwazo mtu maskini, lakini kipindi cha Mwalimu nchi masikini ya Tanzania ilikuwa inawawekea vikwazo hata nchi kubwa. Na ukiwekewa vikwazo na Tanzania una hali mbaya, chukulia mfano Uingereza walipoanza kuchezacheza na haki ya uhuru wa watu wa Zimbabwe, tarehe 16 Disemba, 1965 Tanzania tukavunja uhusiano wa kidiplomasia na Uingereza na dunia ikaona, just a question of principle! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulipoungana na Zanzibar mwaka 1964 Ujerumani wakaanza kutumia ile wanaita the Hallstein Doctrine ambayo ilikuwa inasema kama wewe ni rafiki wa Ujerumani Magharibi basi vunja urafiki na Ujerumani Mashariki; Mwalimu akasema I see, hebu acheni kutuchezea hapa, ondokeni Wajerumani wote. Hiyo, ndiyo Tanzania, Tanzania ya kuthubutu, Tanzania yenye principles. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulifundishwa na Mwalimu kwamba Nchi hii ili iweze kuendelea hatuhitaji big brother, hatuhitaji pesa, hiyo ni akili ya kitumwa, pesa ni matokeo. Tunachohitaji ni vitu vinne tu; watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora, huo ndio ulikuwa msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini mjadala wa makinikia au mashapo kwa mujibu wa Kamusi tuliyoizindua tu hapa jana; mjadala huu ambao umeendelea kwa wiki kama mbili hivi, hauakisi Tanzania ya Nyerere. Wakati wananchi wanaunga mkono na kushangilia uthubutu wa Rais, Mheshimiwa John Pombe Magufuli kutetea rasilimali za nchi na wao wanaelewa mikataba tuliyoingia, mchanga unachukuliwa yanaachwa mashimo hapa, hakuna hata makubaliano kwamba basi mkishachenjua kule turudishieni mchanga tuzibe haya mashimo au mtatengenezaje?

Mheshimiwa Spika, tuna makampuni hapa kama Williamson Diamond, miaka 77 haipati faida lakini ikiwa Botswana inapata faida, wananchi wanalielewa hilo, lakini sisi wasomi sasa tunasema hapana, jamani tuwe waangalifu, tuwe waangalifu sana! Oooh, wazungu hawa, tuwe waangalifu nao; mimi nashangaa.

Mheshimiwa Spika, sasa ili tuendelee tunahitaji vitu vinne watu, ardhi, siasa na uongozi bora, sasa hivi imebadilika imekuwa ili tuendelee tunahitaji fedha na wazungu, maana tunawaogopa wazungu kupita kiasi, imenitisha.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Spika, leo hii tuna vita ya kiuchumi, kijana msomi, mwanasheria, unasimama hapa unatutishia nyau! Ooh! Tuna MIGA na Wanyakyusa kuna watu wanaitwa kina Minga, wananiuliza hivi huyu Minga ametokea wapi? Tuna MIGA! What is MIGA? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mbunge wa Mwibara hapa, alituletea mkataba hapa, kasoma tu kifungu kimoja, Ibara ya 12, lakini namwambia asome na ya 11, hatuwezi kushindwa kesi chini ya sheria hii ndogo ya MIGA, ni mkataba wa kawaida tu kama mikataba mingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, taarifa ya Profesa Osoro, ya Mruma ni takataka! Huo ni umamluki wa hali ya juu. Tuko kwenye vita! Tuko kwenye vita hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sio tu MIGA, lakini sisi tuna mikataba ya kimataifa inayosimamia good faith katika mikataba. Tuna UN Convention on Contrast for International of Sale of Goods, tuna UCC ambayo ni Unfair Commercial Code ambayo tunaitumia, yote inasisitiza good faith katika mikataba. Good faith inatokea wapi, mikataba hii ya madini ambapo mtu anasema nachukua mchanga wako kwenda kuchenjua, tuna-calculate percentage kule, kumbe ameshauza siku nyingi. There is no good faith! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, MIGA Convention yenyewe inasema nini; MIGA inasema ukitaka kutumia MIGA faida yake hapa lazima uheshimu sheria za nchi. Sheria za nchi zinasema nini? Zinasema kwamba ukitaka kuingia mkataba lazima kuwepo na union of minds, wanasheria wanajua, tunaita concensus ad idem, haiwezekani ikawepo concensus wakati wewe unamwambia mwenzako naenda kuchenjua halafu nakokotoa, kumbe huwa kabla ya kuchimba umeshauza hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndio maana nasema hatuwezi hata kidogo kushindwa hiyo kesi. Tuliweza kushinda mtihani wa Devolution Agreements wakati wa uhuru, tutashindwa MIGA? Tutashindwa MIGA? Tukishindwa kesi hii basi tumezungukwa na Mayuda Iskariote wa kutisha, lakini nashukuru wako wachache sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Devolution Agreements zilikuwa ni nini, niseme kwa kifupi. Tulipokuwa tunapata uhuru Barani Afrika Waingereza walikuwa wanakuja na mikataba inayosema, mimi nakubali mikataba yote aliyoingia Uingereza inayonibana inibane mimi kama nchi huru. Ni Mwalimu Nyerere peke yake aliyepeleka note ya kukataa hiyo Umoja wa Mataifa akisema mimi nilikuwa sijazaliwa kama taifa huru, mikataba hiyo mliingia kwa hiyari yenu hamkuni-consult, mlinitawala bila kibali changu, sitaki kuingia kwenye hiyo biashara; na tangu toka hapo ndipo ikazaliwa dhana katika Sheria ya Kimataifa inaitwa The Nyerere Doctrine of State Succession ambayo watu wengi wameifanyia mpaka Degree za Uzamivu, hii nchi ina historia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, msimamo wa Mwalimu uliokoa mengi sana nchi hii. Tulikuwa na Belbase Agreement alioingia Mwingereza na Ubelgiji. Mwingereza aliitoa Bandari ya Kigoma na Bandari ya Dar es Salaam kuwapa Wabelgiji waimiliki, tukakwepa kutokana na Mwalimu msimamo wake wa kwamba hatukubali. (Makofi)

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nilishaunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nianze kwa kumpongeza sana Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Mheshimiwa Peter Serukamba na Makamu wake Mheshimiwa Mussa Zungu na Wajumbe wote kwa kweli kwa taarifa nzuri iliyokwenda shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie machache tu kwa ufafanuzi. Suala la kwanza Kamati inasema sheria ya Baraza la Michezo na BMT ina upungufu mwingi kwa kweli unaokwamisha utendaji wa baraza. Nakubaliana kabisa na Kamati kwa kweli sheria ni ya siku nyingi sana ya mwaka 1967 miaka 51 iliyopita, najua ilishafanyiwa marekebisho mwaka 71 lakini bado ni miaka 47 iliyopita na tumeshaanza hiyo kazi nzuri ya kuifanyia marekebisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na timu yake ya wataalam kwa kukaa na wataalam wangu wa Wizara kuifanyia first drafting hii ya hii sheria na mtaiona baada ya muda si mrefu mbele yenu hapa Waheshimiwa wa Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la uboreshaji wa TBC limeongelewa na Kamati na vilevile Mheshimiwa Amina Moleli naye ameingolea na amezungumzia kuhusu vifaa kwamba vimechoka yeye anaongelea studio mle ndani sawa. Hata hivyo, nataka tu kusema kwamba Serikali inalijua hilo na tumeanza kulifanyia kazi vizuri kabisa sisi hatujaanza kwa mwonekano wa ndani kwa sababu unaweza ukawa na makochi mazuri, lakini kwa kweli huko chumbani kuna matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sisi tumeanza na mitambo kuboresha usikivu na vile mwonekano wa TBC. Leo hii najua wote nyie mtakuwa mashahidi wangu kwamba mwonekano wa TBC wa picha umeongezeka tena kitaalam wanasema umeongezeka toka asilimia 52 hadi asilimia 88 na yote ni kwa ajili ya ukarabati wa mitambo ambayo inasaidia urushaji wa matangazo. Hata radio za TBC FM na TBC Taifa nazo usikivu wake umeongezeka toka asilimia 60 mpaka asilimia 90 na hiyo yote ni kwa ajili ya ukarabati tunaoufanya wa mitambo yake.

Ukifika pale Mikocheni kuna dude kubwa pale tunaita Satellite uplink ilikuwa wakati huo miaka miwili iliyopita ilikuwa na njia moja tu ambayo tulikuwa tunashindwa kuikarabati, lakini leo zote njia mbili zinafanya kazi na ndiyo maana mwonekano wa TBC umekuwa mzuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo hoja ya kwamba BASATA iko mbali na wasanii, kwa kweli hapana, si kweli. Nitatoa mifano michache, BASATA huwa inatoa ushauri consultancy kwa wasanii wetu na nitoe mfano mdogo tu wa mwaka jana kuanzia mwezi Julai hadi mwezi Desemba, wasanii 995 wamefika BASATA kupewa ushauri kuhusu kazi yao ya sanaa. Sasa kama hauna mawasiliano mazuri watu 995 katika miezi minne mitano wakafika isingetokea kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu tukumbuke kwamba pia vijana wetu wengi siku hizi wanaalikwa nje ya nchi kwa ajili ya muziki na ni BASATA inayohangaika kuwapeleka Balozini kuwatambulisha wapate VISA. Kwa kweli mnyonge mnyongeeni, haki yake tumpe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uboreshaji wa tasnia ya filamu, nakubaliana kabisa na maoni ya Kamati lakini nataka kwamba kama tasinia kwenye sanaa imepiga hatua kubwa sana katika kipindi kifupi ni tasnia ya filamu ambapo leo hii, nadhani sisi ni wa pili kwa Nigeria hata kwa uzalishaji wa filamu kwa mwaka tunazalisha kwa wastani filamu 1,400 kwa mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sawa kuna suala la ubora wa filamu zetu kweli zipo zingine hazifurahishi kabisa, lakini katika hizo 1,400 bora zimejitokeza na ndiyo maana leo hii Tanzania tunajivunia tuzo za kimataifa zaidi ya 44 za waigizaji wetu waandaaji wa filamu na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile ndiyo maana leo hii hata wawekezaji wamejitokeza sasa kwa ajili ya filamu industry. Leo tunawapongeza sana AZAM TV kwa kuanzisha a dedicated Channel kwa ajili ya sinema zetu za Kiswahili inaitwa Sinema Zetu za Kiswahili. Si hao tu wenzetu multichoice na wameanzisha a dedicated Channel kwa ajili ya sinema za Kiswalihi na sasa hivi tuna TV mpya imeanzishwa Jasson TV ni kwa ajili ya sinema za Kiswahili. Yote haya ni mafanikio yalikuwa hayapo haya ndio yameanza kujitokeza na hii ni ushahidi mkubwa kwamba tasnia ya filamu nchini inaendelea kwa kasi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoka na muda naomba nigusie mambo mawili matatu ambayo Mheshimiwa Devotha Minja ameongelea kuhusu vyombo vya habari. Ameongelea kuhusu maelezo wamemwandikia Tanzania daima barua kwa nini uchaguzi wa Kinondoni wanaandika upande mmoja. Anasema kama wana haki kwa nini hawajawaandikia Uhuru, nimecheka nimemwambia Mheshimiwa Minja ulitaka nao Uhuru wakuletee hiyo barua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua huo ni ushahidi tosha kwamba hata waliokuletea barua hawana weledi, there are not professionals huwezi ukaandikiwa barua na Taasisi ya Serikali na Idara. Badala ya kuwasiliana nao wewe unapeleka kwa Mbunge ni kukosa weledi tu, Uhuru hawawezi kufanya hivyo au gazeti la maana kama Mtanzania na mengine wakakuletea wewe Mbunge hapa barua ambayo ulitakiwa wewe uwajibu, sijui hawajui kujibu wamekuomba wewe uwajibie. (Makofi)

Mheshimwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Minja anasema Waziri nina mamlaka gani chini ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 kuweza kuadhibu…

T A A R I F A . . .

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, inanishangaza, namheshimu sana Mheshimiwa Komu, lakini nashangaa leo anaongea utafikiri yeye haelewi, etiquette ya uandishi wa habari kutoka Serikali na kwako basi uwajibie, endelea kuwajibia tu, hongera na utafanikiwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala la Waziri kufungia magazeti sio mimi tu, lakini sheria ya mwaka 2016 iko wazi kabisa, akisoma kifungu cha 59 naomba ukaisome, sijui kama umeisoma, kasome vizuri itaelewa. Ni kweli kabisa pengine nitumie dakika chache zilizobaki kwamba tulipotunga hii sheria lengo letu kubwa ni kuanzisha vyombo vya habari ambavyo ni self regulatory ,vinaweza vikajiendesha wenyewe, vikajidhibiti vyenyewe na vitajidhibiti kupitia vyombo vikuu vinne. Hili nimelisema mara nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyombo hivi ni:-

(i) Baraza Huru la Wanahabari, Independent Media Council;

(ii) Bodi ya Ithibati;

(iii) Kamati ya malalamiko ambayo tena chini ya sheria hiyo ina madaraka kabisa kama ya Mahakama is a Quasi judicial Body; na

(iv) Mfuko wa sanaa vyombo hivi havijaweza kuundwa kwa sababu ya kipengele ambacho nyie wenyewe Waheshimiwa Wabunge akiwemo la Mheshimiwa Minja kulalamika kwamba hatuwezi kumwadhibu Mwandishi wa Habari moja moja kwa sababu hata weledi bado hawana. Kwa hiyo tuwape kipindi cha miaka mitanowaweze sasa ku- meet requiments za hii sheria za kuwa na Diploma au Degree kuweza kuwa Mwandishi wa Habari kuweza kutambuliwa kwamba hii ni taaluma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuko katika kipindi hicho cha mpito hatuwezi kufanya chochote. Ningetegemea Mheshimiwa Minja kama una uchungu kabisa wa hii tasinia, hebu njoo tuweze kuondoa hicho kipengele cha transition ili tuweze kuunda hivi vyombo, nitakuelewa vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019; na Mapendekezo ya Serikali Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA
MICHEZO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Nianze kwa kuunga mkono hoja na vile vile kumpongeza Waziri wa Fedha na Naibu wake kwa kazi nzuri na yenye viwango. Katika dakika tano pengine nigusie suala moja tu, muda ukibaki nitaongelea suala la pili na pengine la tatu.

Mheshimiwa Spika, jana lilijitokeza suala la ukabila hapa, ambalo haliwezi likabaki kwenye Hansard bila ya ufafanuzi. Kwa bahati mbaya sana liliibuliwa na Mbunge ambaye namheshimu sana na ambaye mimi mwenyewe najivunia kwa kumwita mdogo wangu Mheshimiwa James Mbatia.

Mheshimiwa Spika, pamoja na Wabunge wenzangu hapa, pamoja na maudhi yote ambayo tunaweza kuyapata, maana sisi wote ni binaadam, tuna upungufu mwingi sana; sisi viongozi tusikubali kwa njia yoyote ile kuwa abiria kwenye basi la ukabila na basi la udini. Tukifanya hivyo, tutafuta kabisa mafanikio makubwa ambayo Taifa hili limepata kupita Taifa lolote lile katika Bara la Afrika hasa katika kujenga umoja wa kitaifa na sisi kujisikia ni Watanzania na si ni wakabila.

Mheshimiwa Spika, ndugu yetu Mheshimiwa Selasini ni Mheshimiwa mmoja Mbunge na ambaye vile vile namheshimiwa sana; jana aliweza kutoa sababu kwa nini imekuwa hivyo, akagusia magazeti mawili, kwamba kuna magazeti mawili hapa, Tanzanite na Jamvi kwamba ndiyo sababu hasa nafikiri kwamba kuna ubaguzi wa Wachaga.

Mheshimiwa Spika, lakini haya magazeti yanaweza kushtakiwa tu na Sheria ya Huduma ya Habari kifungu cha 41, mtu akileta upuuzi upuuzi mpeleke Mahakamani. Sisi kama Wizara ya Habari tutakuwa mashahidi wenu tutafungiaje, kesho tutafungia mtasema tunaminya uhuru wa habari.

Mheshimiwa Spika, Wizara hatuwezi kufungia kitu ambacho hakiko direct katika kuvunja usalama wa nchi hii. Kama umetukanwa wewe nenda Mahakamani, kifungu cha 41 kinakuruhusu, lakini ukileta hapa kwa sababu umesema wewe ukaleta Wachaga wote wanabaguliwa ni maneno ambayo kwa kweli yanaturudisha nyuma sana Watanzania.

Mheshimiwa Spika, naomba niseme neno moja, hivi leo Mchaga ni nani katika Taifa leo la Watanzania? Yupi hapa anaweza akashika jiwe akamtupia, akatupa jiwe kwenye kabila lingine asimguse mkwewe au mjomba wake kule? Hili Taifa limebadilika sana; mimi niko kwenye hali ngumu hapa, mimi natoka Mbeya huko lakini siwezi kutupa jiwe kwa Mchaga, watoto wangu wenyewe ni Wachaga wana damu hiyo na ndiyo Tanzania nzima iko hivi.

Mheshimiwa Spika, mwaka 1961pengine tukumbushane kwa vijana wadogo wadogo hapa; tulipopata Uhuru, ulikuwa ni uhuru wa makabila haya zaidi ya 120 ambayo hawakuwahi kukaa na kukubaliana kwamba sisi ni Taifa. Kwa hiyo kazi kubwa aliyokuwa nayo Baba wa Taifa ni kuunda a Nation State; ataiundaje?

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana Baba wa Taifa ilibidi afanye kazi kubwa ambayo viongozi wengine wote Afrika walidharau na ndiyo maana kwao bado ukabila ni mkubwa. Sisi hatuna ukabila hapa, yeyote yule anayepanda basi la ukabila hana safari ndefu huyo, atapotea, ndiyo maana kitu cha kwanza Mwalimu ikabidi tusitishe mamlaka ya Machifu katika Serikali, ilikuwa nzuri tu, ili tuunde national state.

Mheshimiwa Spika, pili lugha ya Kiswahili kuwa ndiyo lugha yetu ya Taifa; lakini tatu education system yetu. Unakumbuka na viongozi wengine hapa, unamaliza darasa la saba wewe unatoka Kyela sekondari utakwenda Bukoba, wa Bukoba atakwenda Nachingwea, wa Nachingwea ataenda Tanga, wa Tanga ataenda Kigoma.

Mheshimiwa Spika, tumejichanganya na tuna tafiti za kisosholojia hapa, watu wote waliopitia mfumo huo, asilimia zaidi ya 85 hawajaoa maeneo yao, wameoa maneo mengine; na ndilo Taifa alilokuwa anataka kuliunda Mwalimu Nyerere.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba sana, nimeanza ndani ya Bunge hili tumeanza kupanda mabasi ya ukabila, mabasi ya udini. Kuna sentensi za udini na za ukabila, tuache kabisa sisi ni viongozi, hawa watoto, bahati mbaya nimepewa dakika tano, lakini ujumbe wangu ulikuwa ni kwamba jana nilishtushwa, nikasema haya yasiongelewe hapa, tusiongee kabisa, tumefika mbali, tumefanikiwa sana kama Watanzania.

Mheshimiwa Spika, nakuhakikishia hili ni Taifa jipya, hapawezi kabisa kuwa na mtu akisema watu fulani tunabaguliwa, haiwezekani utambagua nani? Maana wote ni wale wale. Ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati Hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa nami nichangie kwenye hoja iliyotolewa leo asubuhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimelisikia suala la Star Times likiongelewa hapa nikaona ni muhimu sana nilitolee ufafanuzi angalau kwa kifupi kwa sababu tutakuja na ufafanuzi wa kina katika Bunge hili na kwa kutumia njia nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Star Media ambayo ni kampuni ya ubia kati ya Star Times ya China na Shirika letu la Utangazaji la TBC ni suala ambalo liliibuliwa ndani ya Serikali na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano mwenyewe, baada ya kuhoji kwa nini ubia uliodumu zaidi ya miaka saba usioneshe faida?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kauli ya Mheshimiwa Rais, Bodi ya Wakurugenzi ya TBC ikamwomba CAG afanye special audit, lakini nami vile vile kwa nafasi yangu ya Uwaziri nikaunda Kamati Maalum ambayo iliongozwa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi wa Maelezo, Dkt. Abbass pamoja na Mtendaji kutoka Star Times nao wafanye uchunguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliogopa kwamba pengine uchunguzi wa CAG ungechukua muda mrefu sana. Taarifa zote mbili zimetoka na tumeweza kubaini madudu mengi sana katika ubia huo. Madudu yale yenye mwelekeo wa kijinai, tumeyawasilisha kwenye vyombo husika vya Serikali vya masuala hayo. Yale ya kiutendaji tumeyafanyia marekebisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kulitaarifu Bunge hili, kwa mara ya kwanza hata sisi wenyewe tumeanza kuona vitu vimeanza kuonekana positive. Mwaka huu Star Media imeweza kuchangia shilingi milioni 500 Hazina kwa mara ya kwanza. Siyo hivyo tu, mimi nina barua hapa sasa, Star Media imekubali kwa ule upungufu uliojitokeza uliosababishwa na baadhi ya watendaji wake, kulipa TBC shilingi bilioni tatu kuanzia mwezi wa tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mambo yanaenda vizuri na tumeyafanyia kazi na taarifa ndefu itatolewa katika Bunge hili na kwa kutumia njia nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa na mimi kuweza kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa mimi naunga mkono hoja na nataka nitamke mapema kabisa kwamba kama kuna taasisi hapa nchini yenye rekodi ndefu iliyotukuka ya nidhamu, maadili, weledi na utendaji wa hali ya juu basi taasisi hiyo ni Jeshi letu la Wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, dalili za Jeshi kuwa mfano bora wa kuigwa nchini ilijitokeza mapema tu baada ya uhuru, wakati wa uhuru ambapo Baba wa Taifa alimkabidhi Luteni Alexander Ngwebe Nyirenda, bendera na mwenge wa uhuru akauweke juu ya Mlima Kilimanjaro, kitendo ambacho Baba wa Taifa alikielezea kishairi shairi kwamba mwenge huo utamulika ndani nan je ya mipaka yetu ili ulete matumaini pale ambapo hakuna matumaini, ulete upendo mahali penye chuki na heshima mahali palipo na dharau na kwa hakika mwenge ulitusaidia kuona mapema kabisa baada ya uhuru kwamba kuna dhuluma ndani ya Bara la Afrika na ndiyo maana Tanzania tukawa ngome kuu ya mapambano ya harakati za kupigania uhuru katika Bara la Afrika na ndiyo maana mwaka 1963 nchi yetu ikapewa heshima kuwa ndiyo Makao Makuu ya Kamati ya ukombozi wa Bara la Afrika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile mwaka 2011 nchi yetu ikapewa heshima kubwa kuwa ndiyo Kituo Kikuu cha Kumbukumbu ya Historia ya Harakati za Ukombozi wa Bara la Afrika na ukiongelea harakati za ukombozi kwa kweli tunapata hiyo heshima kutokana na Jeshi letu la Wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Nduli Iddi Amin alipojaribu kuleta jeuri hiyo jeuri ilizimwa na majeshi yetu, tunawapongeza sana. Na kwenye vurugu popote pale duniani vijana wetu wakienda wanaacha alama ya heshima na ndiyo maana leo hii ukienda Kinshasa, Lubumbashi unatembea kifua mbele kama Mtanzania kutokana na kazi kubwa ambayo akina Jenerali Mwakibolwa waliifanya hao wote ndiyo JWTZ. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie tu kwa kusema nalipongeza sana Jeshi letu hasa kwa upande wa michezo. Hawajaanza jana hawa. Akina Filbert Bayi wakiwa jeshini ndiyo Mtanzania wa kwanza kutuletea sifa hapa mwaka 1974 baada ya kuvunja rekodi ya dunia ya mita 1,300 Christchurch – New Zealand, hiyo JWTZ. Sio huyo tu, tunae mweznake Juma Ikangaa mwanajeshi mwenzake ambaye alikuw abingwa wa mbio za New York za marathon mwaka 1988, JWTZ hiyo, sio huyo tu, tuna Samson Ramadhan, mshindi wa marathon Melbourne – Australia mwaka 2006 ni JWTZ.

Mheshimiwa Mwenyekiti, orodha ni ndefu sana, nisimsahau kijana wetu Simbu, mshindi wa medali ya dhahabu Mumbai Marathon na vilevile medali ya shaba London Marathon…

MWENYEKITI: Ikangaa.

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO:Mheshimiwa Mwenyekiti, Ikangaa nimemtaja ndiye mshindi wa marathon ya New York, kuna wengi. Tuna akina Cecilia Panga bingwa wa Beijing International Marathon, Emmanuel Gisamoda, Shanghai International Marathon. Kwa kweli jeshi letu limetupa heshima kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naona muda wangu umekwisha, naomba tu niseme naunga mkono hoja na kwakweli Jeshi letu linastahili heshima kutoka kwa kila Mtanzania. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kunipa fursa. Naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Manaibu wake kwa kazi nzuri wanayoifanya katika sekta hii. Nami naunga mkono hoja moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako naomba nitumie nafasi hii vilevile kutoa pole kwa Watanzania wote wakiwemo wananchi wa Kyela, kwa matatizo makubwa waliyoyapata hasa baada ya mvua hizi kubwa kunyesha, kupata mafuriko, wamepoteza mazao, wamepoteza watu, wamepoteza maisha na vilevile miundombinu kuharibika. Leo hii ninavyoongea wasaidizi wangu wako Jimboni Kyela wakigawa chakula kwa walioathirika sana. Kwa hiyo, hata Waheshimiwa Wabunge ambao wanaweza wakapata huruma kidogo basi tunapokea michango tutaifikisha hapo kwa waathirika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pengine niongelee kitu kifupi sana maana dakika tano siyo nyingi, kuhusu suala la ushirika ambalo aliongelea Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani, kwamba ushirika ni tabu tu kwa wakulima, lakini pengine kwa mazao mengine, lakini naomba niongelee zao la kokoa kwamba, ushirika ndiyo mkombozi kwa wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu sana sisi Kyela tunazalisha sehemu kubwa ya kokoa nchini. Kokoa haijawahi kupanda bei zaidi ya Sh.3,000 kwa kilo, hiyo ni bei kubwa sana, lakini kuanzia Novemba, tulipoanzisha huu mfumo, tumeweza, kupitia hii minada, kupata bei nzuri ya kuanzia Sh.4,500, haijashuka imeendelea kuwa Sh.5,000, ikaenda Sh.5,600, tunaelekea kwenye Sh.6,000 sasa hivi kwa kilo. Vilevile mfumo huu umetufanya tuweze kuelewa pia unyonyaji mkubwa unaoendelea, hasa kutokana na wenzetu hawa wa katikati hawa, kwingine wanaitwa kangomba, sisi tunaita njemke.

Mheshimiwa Spika, kule kwetu kilo moja, lakini wala siyo kilo, ni kitini kimoja kinaitwa sado, ni Sh.800 analipwa mkulima, lakini hicho hicho kitini kimoja kinaitwa sado, kina kilo tatu ndani yake. Kwa hiyo, mkulima analipwa Sh.800, yeye akienda kwenye soko, anapata zaidi ya shilingi elfu 16, ni unyonyaji mkubwa sana! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nafurahi kwamba Serikali imeshatunga Sheria ile ya Microfinace Act ya 2018 ambayo inatupa msingi sasa wa sisi kuweza ku-regulate hii, hatuwafukuzi hawa watu, lakini kuwa-regulate sasa, kwa sababu chini yah ii sheria tunaweza kabisa tukatunga kanuni ambayo inaendana na zao kwa zao. Kwa mfano, mimi mwenyewe, nitakuwa wa kwanza katika kukimbilia kwa hii fursa kwamba tuwe na kanuni kwa zao la kokoa kwa kuwaelewesha ili hao wenzetu njemke wasipate faida kupitiliza, angalau nusu ibakie kwa mkulima na yeye nusu ifidie gharama zake za kwenda huko na kule. Kwa kweli ni kazi ambayo inawezekana kabisa ikafanyika na ikaleta tija katika soko.

Mheshimiwa Spika, la mwisho, ni suala ambalo tuliliongelea juzi, aliliongelea Mheshimiwa Mwambe hapa la Ministerial responsibility. Alisema lazima Waziri anapofanya kosa sisi tuliseme hapa, ni kweli kabisa hakuna tatizo kabisa kuhusu Ministerial responsibility. Nilichokuwa nalalamikia mimi ni kwamba kuna suala ambalo, haliihusu hiyo Wizara yenyewe, lakini linahusu Mawaziri watatu, wanne, si sahihi ukam-single out Waziri mmoja huyo huyo kwa kumrushia mawe. Sasa inakuwa kama una kitu fulani kwake, ndiyo maana nikasema, chini ya Ibara ya 53, sisi ndani ya Bunge, chini ya Waziri Mkuu, tunawajibika kwa Bunge kwa pamoja, (collectively), kwa hiyo, ndiyo hicho nilitaka kufafanua tu waelewe kwamba sasa kama kuna Mawaziri wawili, watatu wanahusika, mmoja tu ukiendelea kumtupia mawe siyo sahihi hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili ni suala letu, hata mimi mwenyewe ukinilaumu, mimi mwenyewe nitaitetea Serikali hapa kwa sababu ni suala la kiserikali na hakuna ambaye amelikimbia na bado ulivyomsikia Waziri wa Viwanda na Biashara, ameeleza vizuri sana, hoja nyingi sana hapa zinaweza kuyeyuka kama mshumaa.

Mheshimiwa Spika, nimalizie tu kwa kusema, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza mtoa hoja, Mheshimiwa Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi, kwa kuwasilisha Mpango na Makadirio ya Bajeti ya Wizara yake kwa umahiri mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaongelea masuala mawili mafupi tu ndani ya muda huu mdogo nilionao ambayo yamegusiwa na Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Mheshimiwa Salome Makamba.

Mheshimiwa Naibu Spika, pengine nianze kwa upande huo vilevile kwa kumpongeza Mheshimiwa Makamba kwa kukiri mbele yetu kwamba nyuma ya mwanamke yeyote mwenye mafanikio yupo mwanaume. Hii ni dhahiri kabisa kwamba ana familia yenye furaha katika nchi hii. Mimi naomba nimkumbushe tu kwamba pale ambapo kuna familia yenye furaha basi nyuma yake kuna Serikali inayojali na Serikali hiyo ni ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani ametoa picha ukurasa ule wa saba wa nchi yetu kuwa yenye ukandamizaji mkubwa na amenukuu tafiti mbalimbali alizozisoma yeye. Mimi naomba tu nimkumbushe vilevile tafiti ambazo zimefanywa na vyombo vyenye heshima kubwa sana duniani.

Mheshimiwa Naibu Spika, Taasisi inayoheshimika duniani upande wa Travel Advisory, Atlas and Boots, inatoa orodha ya usalama wa nchi duniani kila mwaka inaitwa Global Peace Index. Inasema kwa mwaka 2018 nchi 100 zilikuwa na hali mbaya sana ya usalama.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitangaze hapa na niko tayari kuweka juu ya Meza hapo, kwamba Tanzania haipo kati ya nchi 100 hatari duniani. Nilizoziona humu ni Syria, Afghanistan, Russia, Pakistan, Uturuki, Israeli, Colombia, na USA ni ya 43, sisi kwenye 100 hatumo. USA yenyewe ambayo wengi wanadhani ni paradiso ya usalama ni ya 43. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi zilizobaki salama zingine ziko kama 80; Ufaransa (103), Vietnam (104), Uingereza (107), Qatar (108), Tanzania (113) yaani tuko juu ya hata hao. Ndiyo shida ya kunukuu hivi vitu, basi nukuu vyote ili kupata picha comprehensive. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma worldpopulationreview.com inatoa orodha ya nchi 55 za kidikteta duniani, tena 55 imefikia mwisho, Tanzania siyo mojawapo. Kwa hiyo, ukitaka kuleta data hapa uwe comprehensive, jaribu kusoma nyingi uweze kupata picha kamili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, amedai vilevile kuwa kuna ukosefu wa uhuru wa vyombo vya habari Tanzania. Anasema hii ndiyo dosari kubwa kwelikweli hapa nchini. Mimi nataka tu niwahoji wenzangu ambao wanakuja na hiyo hoja mara kwa mara, wanaposimama hapa Bungeni hebu wanitolee mfano wa nchi moja tu yenye uhuru wa vyombo vya habari usio na mipaka, nitafurahi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pengine wanafikiri ni hao wakubwa, sasa kama ni wakubwa, hivi kama wakubwa hawana mipaka ni kitu gani kinawafanya mpaka leo huu mwaka wa saba wanahangaika na Assange? Ni kitu gani kinawafanya mpaka leo wanahangaika na Snowden? Yote ni kwamba wamekiuka ule uhuru wa habari uliopo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwasisitizie Watanzania na Waheshimiwa Wabunge kupitia kwako kwamba nchi zote zenye heshima duniani zimesaini Mkataba wa Civil and Political Rights, ile convention ya mwaka 1966. Convention hiyo inatoa uhuru kwa vyombo vya habari lakini kwa sharti la kwamba usiingilie uhuru na haki ya mtu mwingine na usihatarishe usalama wa nchi yako. Sasa kama unahatarisha usalama wa nchi yako wewe utakaa kwenye nchi gani? Kwa hiyo, ndiyo maana nchi zote zinasema sisi tunafuata uhuru wa vyombo vya habari lakini tunazingatia hiyo International Convention ya Civil and Political Rights. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusema tu kwamba Tanzania tunapewa marks kubwa kwa sababu ya utayari wetu na vilevile kuwa champions wa kuanzisha vyombo vya ulinzi wa haki za binadamu. Nimefurahi sana leo Chief Whip hapa ameelezea kuhusu Mahakama zote za Afrika na za kimataifa ziko Arusha kwa sababu ya track record ya human rights ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi ndiyo tulikuwa waanzilishi wa hoja tuwe na East African Court of Justice hapa na Mahakama ya Afrika. Siyo hivyo tu, Mahakama ya Afrika tukawa moja ya nchi tano tu tuliokubali wananchi wetu watupeleke kwenye hiyo Mahakama kama kuna ukiukwaji wa haki za binadamu, tano, kati ya nchi zote za Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
The Written Laws (Miscellaneous Amendment) Bill, 2016
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ili nami niweze kuchangia. Kwanza kabisa naomba nimpongeze Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuwasilisha hoja hii kwa ufasaha mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nimefarijika sana kwani sioni hoja za ukinzani kwa yote yale ambayo Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameyasema. Ningeomba pengine nigusie suala moja tu, maana nikiongelea mawili mwishowe Mwanasheria Mkuu wa Serikali atashindwa hata kusema baadaye.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili moja limeongelewa na Kamati, limekuja kugusiwa na Mheshimiwa Bashe na kidogo amekuja kuligusia Mheshimiwa Shangazi. Ni suala la mabadiliko tunayopendekeza; ambapo Jaji Mkuu anapewa madaraka specific, expressly kwamba tuna mamlaka ya kuanzisha Division za Mahakama.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati inasema kwamba, ukurasa huu wa 11 ndipo paliponishtua kidogo, tunapoongelea kuhusu mawasiliano baada ya Jaji Mkuu kuamua at least kuwe na consultation na Rais wa Nchi, Kamati inasema haioni mantiki ya Mheshimiwa Rais kuingilia Mamlaka ya Jaji Mkuu!
Mheshimiwa Naibu Spika, sidhani huko ni kuingilia mamlaka. Pamoja na kwamba Kamati ukurasa wa 13 inaweka nukuu nzito sana ya Baron de Montesquieu, mwanafalsafa aliyezaliwa mwaka 1689, zaidi ya miaka 327 iliyopita. Sasa Kamati inataka tuone hiyo falsafa yake kwamba mpaka leo isitingishike hata kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kusema tu kwamba hiyo ni sawa. Huyo mwanafalsafa alisisitiza sana kuhusu mgawanyo wa madaraka, lakini huu mgawanyo wa madaraka siyo total separation! Yaani hamkutani mahali popote, hapana! Hii dhana baadaye imekuja kuzua dhana mpya ambayo ni ya ushirikishwaji zaidi, dhana ya checks and balances.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunachotaka hapa ni kwamba, Jaji Mkuu anapoamua wakati wowote kuanzisha Division, ni mamlaka yake afanye hivyo, lakini kum-consult, kuwasiliana na kiongozi mwenzake wa mhimili ambaye ndiye anatafuta pesa ni muhimu, sasa inakuwa tatizo, kwamba anaingilia madaraka. Sasa huwezi ukaanzisha Division bila financial implications kuna pesa zinahitajika.
Mheshimiwa Naibu Spika,Sasa hivi huwezi ukamteua Jaji tu, ukaweka deski ukasema anza kazi! Hapana, kuna viyoyozi, kuna majengo mapya na yote yanaingilia Mfuko wa Hazina, mipango yote ya nchi. Kwa hiyo, ni suala tu la kuwasiliana, kwamba mwenzangu nataka kuanzisha hiki na Mheshimiwa Rais naye a-take into account kwamba katika next financial year tuna mzigo huo! Ndiyo hicho tu na ningeomba Waheshimiwa Wabunge mlielewe hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimshukuru Mheshimiwa Shangazi vilevile ametukumbusha Ibara ya 33 ya Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania. Ibara hii kwa kweli inaelezea utatu au nguvu tatu ambazo Mheshimiwa Rais anazo. Inasema Rais wa Nchi ndiye Mkuu wa Nchi. Hayo ni madaraka tofauti kabisa. Pia Rais wa Nchi ndiye Kiongozi wa Serikali na tatu Rais wa Nchi ndiye Amiri Jeshi Mkuu; Commander in Chief of the Armed Forces.
Mheshimiwa Naibu Spika, sSasa tukichanganya haya tukaona mamlaka moja inakuwa ngumu. Sasa consultation inapofanyika, inafanyika na Mkuu wa Nchi ambaye anasimamia income yote ya nchi, tutafanye mwaka kesho tupate pesa zaidi, ni suala la consultation tu, lisilete mgongano.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba niwapongeze Waheshimiwa Wabunge wote kwa kuelewa Muswada huu uliowasilishwa hapa. Sioni ajabu kwa nini hakuna mjadala mkubwa sana, kwa sababu, nadhani toka niingie Bunge hili sijawahi kuona majadiliano ya kina na ya muda mrefu kati ya Kamati, Wizara na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, kama yalivyofanyika katika Muswada huu ulioko mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mtu asije akapata hisia kwamba hawa hawaongei pengine sijui… hapana! Tumekaa zaidi ya wiki mbili na naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mwenyekiti na Wajumbe wenzake wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, kwanza kwa uvumilivu wao, wamekuwa wanakuja vikaoni mpaka Jumapili kutaka kuelewa kila kipengele cha mabadiliko haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari za Mwaka 2016
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na vile vile Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii. Naomba niseme mapema kabisa naunga mkono hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiwa Nairobi si kawaida kumwona mtu ananunua au ameshikilia magazeti mawili, matatu, manne ya kusoma atakuwa pengine na Daily Nation, The Standard, au Taifa leo. Ukiangalia sana unabaini kwamba magazeti hayo yanajitosheleza, yanatoa kiu yake yote kwa gazeti moja moja, si lundo la magazeti. Ukienda Uganda, nenda Kampala utakuta mtu anasoma The Monitor, au The Daily Mirror.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nakaa Ujerumani na wenzangu watatu, mwenzangu alikuwa anasoma Dzus Deutsche Zeitung, mimi nilikuwa nasoma Frankfurter Allgemeine Zeitung, ni magazeti ya kijerumani, lakini uwezi kwenda upande wa pili, kwa sababu yanajitosheleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania si kawaida kumkuta mtu ananunua gazeti moja, lazima ununue sita ili upate angalau picha ya kilichotokea ni nini katika nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba zipo sababu. Sababu ya kwanza magazeti yetu yako kibiashara sana, kurasa 16 kurasa 20, mwisho 40 ndiyo magazeti makubwa kabisa mawili siyataji. Sasa mtu anasoma bado ana kiu ya kujua, matangazo kwenyewe ni nusu ya gazeti zima. Lakini pili naweza kusema yapo mashaka ya wasomaji kupata accurate information kutoka kwenye magazeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme, niliwahi kusema kwenye Bunge hili nilishambuliwa zaidi ya miezi sita lakini imezidi kuniimarisha na niko tayari kwa hili lakini nataka kusema kwamba tuna crisis ya weledi wa uandishi wa habari katika nchi hii na ni lazima tukubali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii crisis tumeilea sisi wenyewe mpaka kufikia hapa, sasa muda umefika tunamalizane na hii crisis na huu Muswada unatupa hiyo solution. Naomba niseme, ukweli tuna waandishi wazuri wenye weledi (world class) wachache katika nchi, lakini wengi hawana ueledi completely, sisi wote ni viongozi hapa. Unahutubia mkutano, umemaliza unatoka unafuatwa na waandishi hivi ulitaka kusema nini, tunaomba utuelezee vizuri. Huko ni kukosa ueledi katika journalism.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sijawahi kuona kitu kama hicho, hakitokei dunia nyingine, ni Tanzania tu. Unaongea kwenye mkutano bado unafuatwa ulitaka kusema nini pale, lakini umeongea Kiingereza pale, naomba Kiswahili, ina maana hatuko tayari kufanya kazi ya uandishi, tumewaweka watu ambao hawafai katika hii tasnia, hii tasnia inaharibika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naona aibu sana, anakuja mgeni kutoka nje, mwandishi wa habari anatoa not book yake, your name please! Write here! Katika proper journalism hiyo ni aibu haijapata kutokea duniani, leo hali ni mbaya. Mheshimiwa Nape Nnauye nikushukuru sana mwenzako kwa kutuletea huu Muswada. Mwandishi wa habari anakuja unamwona kabisa midomo imepauka, huyu kijana hana mshahara, hana bima, anategemea source impe nauli kurudi ofisini. Hatutakuwa serious katika journalism tukifanya hivi. Jamani tuache kupakana mafuta ya uongo, hali mbaya na hii hali mbaya tui-sort out. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi wa Chuo cha Uandishi wa Habari, tena Mwenyekiti wa mwisho, nikahamishiwa niende Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Nilipokuwa pale wananchi kwa mamia wanakuja kuniomba nafasi vijana kusoma au niwatafutie kazi. Anakuja mzazi, Mwenyekiti, mtoto amefeli darasa la saba, naomba angalau umtafutie nafasi ya uandishi wa habari, mtoto wangu amefeli form four basi angalau kazi ya uandishi wa habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani uandishi wa habari wanakwenda watu ambao wameshindwa katika maeneo mengine yote, ndiyo Iilikuwa mentality ya hiyo, tutoke huko, uandishi wa habari is a profession. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba tusilewe na hizi propaganda za hawa intellectual wa ki-liberally hasa wengi kutoka Marekani kwamba waandishi wa habari is not professional at all. Hapana, fani yoyote ambayo inakulazimu ujikite kusomea maadili yake, miiko, kanuni zake is a profession.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo haiwezekani ukasema kwamba kila Mtanzania, unajua pengine niseme tu kidogo kwamba kila mtu ni huru katika nchi hii kuvaa joho lolote hata joho jeupe, lakini si kila mtu anayevaa joho jeupe ni Daktari, anaweza kuwa mfanyakazi wa bucha, lakini kumtofautisha huyo na daktari, madaktari wana-undergo specialize training na wakishafuzu wana maadili, miiko na taratibu zao na ndiyo maana lazima kuwe na accreditation, mimi ni Daktari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wanasheria kila mtu ana uhuru kusoma sheria lakini si kila mtu aliyesoma sheria ni Mwanasheria, na si kila Mwanasheria ni Wakili na ukishakuwa Wakili lazima tu ku-identify, tuku-distinguish na wengine, kuna accreditation.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mtu anaweza kuwa mwandishi wa habari, haiwezekani ila kila mtu ana haki kikatiba kutafuta habari, kupokea na kutoa kwa mtu mwingine, hiyo sawa, unampa mke wako, mjomba, lakini pale ambapo unakusanya habari ili utawanye kwa wengine, at a fee, regulation inabadilika. Is not just a question of passion ya kukusanya habari ni expertise, unaenda kwenye chuo cha habari unakuwa trained, I have an advance diploma in journalism here, naelewa ni kazi unasoma, sasa siyo tu kwamba unakaa tu pale, ni uandishi. Sasa ukishafika hapa rules of the game zinabadilika lazima uwe accredited wewe ni mwandishi wa habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetembea duniani kote sijawahi kuona waandishi wa habari ambao si accredited, ni wapi? Wamarekani wasitudanganye sana jamani, unajua ndiyo walikuwa wanaendesha hii liberalism, nimekaa nao sana kwenye USIS, nikiendesha semina zao huko. Wanapenda sana kusema hivyo, lakini wale watu siyo wa kuwaamini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Marekani imepata Katiba 1787, Mmarekani huyo huyo miaka 68 baadaye 1865, akabadilisha katiba ikifuta utumwa Marekani. Miaka mitatu baadaye ikim-declare kila mtu aliyezaliwa Marekani n Mmarekani ana haki sawa mbele ya sheria. Imewachukua miaka 100 mtu mweusi kupiga kura, miaka 100 mtu mweusi kutambuliwa kama ni binadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo sisi tumepata uhuru mwaka 1961, we are more advanced, tujiamini Watanzania, mwaka 1961 tumepiga kura, kila mtu anapiga kura, Serikali yetu ya kwanza kuna wazungu ndani akina Dkt. Leader Starling, Bryson, tuna wahindi akina Mzee Jamal, a mult cultural Nation, kwa hiyo sisi tuna experience zaidi kupita hawa tunaowanukuu nukuu as if kwamba wao ndiyo wanatuzidi kwa kila kitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Marekani leo hii kati ya majimbo 50, majimbo 28 yana sheria kali kweli kuhusu uandishi wa habari. Ukifanya upuuzi deformation ni up to five thousand dollar, lakini kifungo ni up to five years kwenda jela. Lakini wakija huku, aaa! Liberal press na sisi tunaimba liberal press, hakuna cha liberal press hapa, hakuna uhuru usio na mipaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie tu kwa kusema, kuna suala hili la accreditation alilokuwa anaongelea hapa mdogo wangu Tundu Lissu, ni kweli, amejenga hoja kisomi lakini ana-miss point moja kubwa. Sisi kwenye Serikali tuliamini kabisa katika regulation ya media profession na ndiyo maana mwaka 1995 tukaanzisha Media Council of Tanzania ambayo…
Mheshimiwa Mwenyekiti, basi naomba kuunga mkono.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) wa Mwaka 2019
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sanakwa kunipa fursa ya kuchangia. Nianze kwa kumpongeza sana Profesa Kilangi kwa kuwasilisha Muswada huu kwa ufasaha mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nami niunge mkono hoja na nianze kwa kusisitiza; usajili wa Asasi za Kiraia ambazo zinashughulikia masuala ya kijamii, usajili wake chini ya Sheria ya Makampuni, sheria ambayo inajishughulisha na vyombo ambavyo vinafanya masuala ya kiuchumi, masuala ambayo mtu anategemea kupata faida baadaye, kwa kweli ni mkanganyiko unaokaribisha vurugu katika usimamizi na udhibiti. Sababu ziko nyingi kwa nini Asasi za Kiraia zinakwenda kujisajili kwenye Sheria ya Makampuni, sababu kubwa ni kwamba ni Asasi ambazo zinajitambua kwamba hazina sifa kuweza kusajiliwa chini ya Sheria ya Vyama ambayo iko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani au chini ya Sheria ya NGO, ambayo iko chini ya Wizara ya Afya.

Sasa kwa kufanya hivyo wao wamepata kichochoro sasa kwenda kujisajili chini ya Sheria ya Makampuni na kugeuka kuwa popo mwenye sifa maalum, maana ni ndege na vilevile mnyama, tena mnyama ambaye yeye mwenzetu kazi yake anaifanya usiku.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kampuni hizi zinaitwa Companies Limited by guaranteena kampuni hizi ni kampuni ambazo mimi naziona kwamba zinakwepa udhibiti wa BRELA na udhibiti wa mamlaka zinazosimamia NGOs, ni kutokana na upopo wa Asasi hizi. Naamini kabisa kwamba tukiziondoa hizo Asasi huko na kuzipeleka sehemu yake tunaleta kwa kweli utaratibu mzuri sana na pengine wenzetu hapa niwataarifu tu Waheshimiwa Wabunge kwamba chini ya Sheria ya Makampuni Cap 212, tuna companies limited by guarantee ndiyo hizo ambazo wale wanaoanzisha kampuni inabidi wakubaliane mwanzoni kwamba tukipata matatizo tutachangia kiasi fulani cha pesa katika asset za kampuni.

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo kampuni zingine mbili kuna private companies limited by shares na public companies limited by shares. Hizi wale wanaoanzisha wanakuwa na hisa zao ambazo zinapanda kutokana na profit za kampuni na pale ambapo kampuni inapata shida inaelekeza sheria msiwafuate majumbani kwao ni hisa zile walizoweka ndizo ambazo zitasaidia kuongezea kwenye assets za kampuni kulipia liability. Kwa hiyo hizi ni kampuni tofauti kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda Australia ambao tunafanana nao sana katika mfumo wetu wa sheria nao ni common law system, wenzetu wale companies hizo hizo companylimited byguaranteezimewekewa kabisa vyombo vya usimamizi. Sasa hatuhitaji sisi Tanzania tuunde vyombo vya usimamizi kwa ajili ya companies limited byguarantee baada ya kufanya kuleta hii vurugu ambayo tunaiona sasa hivi. Tunavielekeza tu kwamba nyie ambao mko huku mmejiingiza kwenye Sheria ya Makampuni, hamtengenezi faida,mnahudumia jamii, nendeni huko mkakae na wenzenu ambao wapo katika kuhudumia masuala ya jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni uholela huu ambao umetusababishia Asasi nyingi kuingia hapa nchini, kukwepa kwepa tu udhibiti, leo hii ndiyo vinara wa kuhamasisha ushoga hapa nchini, tutalileta hilo suala hapa Bungeni, ni tatizo kubwa sana linatupata kutokana na hizi Asasi ambazo zimetoka nje, maana wenzetu kule nje sasa hivi ushoga ni haki ya binadamu, ambayo ni kinyume kabisa cha utamaduni wa Mtanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikimbilie haraka haraka kwaMsemaji Mkuu Kambi ya Upinzani, Mheshimiwa Salome Makamba na Mheshimiwa Ally Saleh, wamelalamikia suala la rawfootage katika mabadiliko ya Sheria ya Filamu nakala ghafi na sinema iliyokamilika kuachwa nchini. Nataka kusisitiza tu kwamba nakala ghafi si ya kuitumia sisi kwenye luninga zetu. Nakala ghafi niya kuiwezesha Serikali kupitia Bodi ya Filamu Tanzania kuwa na ushahidi wa matumizi ya hiyo rasilimali waliyoitoa hapa na kama wamefanya kama tulivyokubaliana, hiyo itakuja kutusaidia baadaye, lakini si kwa matumizi yetu sisi hapa kuanza kuonyesha. Ni kwa makubaliano na haya makubaliano tutayaelezea vizuri katika kanuni si katika sharia.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ni la profit return, wameilalamikia vilevile nafikiri kwa nia njema tu kwamba tutafukuza wawekezaji, hapana hatutafanya hivyo. Tulilala kwa muda mrefu, tumechangia watu wengine kutajirika kwa rasilimali zetu, sisi huku hatupati hata chochote. Sasa tunachotaka sisi angalau ukitoka ukapata faida uturudishie kitu kidogo. Nitaeleza, sihitaji kutoa mifano mingi hapa, katika kufikia uamuzi huu tumewasiliana na Shirikisho la Dunia la Haki Miliki (World IntellectualProperty Organization). Wametuambia Watanzania as long as nyie wenzetu mmetunga Sheria ya Ulinzi waRasilimali za Nchi, ile ya mwaka 2017, kaeni chini mtengeneze profit sharing agreement na makampuni yote yanayokuja hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kabisa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Oohoo, naunga mkono hoja.