Answers to Primary Questions by Hon. Dr. Harrison George Mwakyembe (22 total)
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM aliuliza:-
Moja ya majukumu ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa mujibu wa Ibara ya 130(c) ya Katiba ya nchi ni kufanya uchunguzi juu ya mambo yanayohusu uvunjaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora:-
Je, ni kwa kiasi gani Tume imefanikiwa kutekeleza jukumu hilo kwa kipindi cha mwaka 2010 - 2016?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdallah Salim, Mbunge wa Mtambile, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora katika majukumu yake kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2010 - 2016 ilipokea na kuyachunguza jumla ya malalamiko 13,709. Kati ya malalamiko hayo, malalamiko 6,169 yalihitimishwa na malalamiko 7,540 yanaendelea kuchunguzwa. Mchanganuo wa malalamiko ni kama ifuatavyo:-
(i) Migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wawekezaji, wakulima na wafugaji, wananchi wa maeneo ya hifadhi;
(ii) Matumizi mabaya ya madaraka kwa watendaji;
(iii) Ukatili dhidi ya wanawake na watoto;
(iv) Ucheleweshwaji wa haki kwa mahabusu na wafungwa; na
(v) Matumizi ya nguvu kwa vyombo vya dola.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na taarifa hiyo, katika kipindi cha mwaka 2010 - 2016 Tume ilifanya tafiti kuhusu haki za watoto, ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi, kutoa elimu kwa umma kuhusu haki za binadamu na misingi ya utawala bora, kutembelea magereza na kufanya uchunguzi wa matukio ya uvunjwaji wa haki za binadamu.
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza:-
Baadhi ya sheria ikiwemo Sheria ya Mirathi ya Kimila, Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 pamoja na Sheria ya Hali za Watu zimekuwa na mapungufu makubwa na hivyo kuhitaji kutazamwa upya ili kufanyiwa marekebisho:-
Je, Serikali ina nia gani ya dhati ya kuwasadia wanawake na watoto wa kike kwa kuzifanyia marekebisho sheria hizo kandamizi na za kibaguzi hasa ikizingatiwa kuwa nchi yetu imeridhia mikataba mbalimbali ya Kimataifa na ya kikanda juu ya masuala ya kuondoa ukatili na unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina nia ya dhati kabisa ya kizifanyia marekebisho Sheria ya Ndoa na zile zinazosimamia mirathi na urithi. Katika kutekeleza nia hiyo, mwaka 2008 Wizara iliandaa Waraka wa Baraza la Mawaziri wenye mapendekezo ya kufanya marekebisho katika Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 na mapendekezo ya kutunga Sheria mpya ya Mirathi na Urithi. Baraza la Mawaziri ililiagiza Wizara ya Katiba na Sheria kuandaa Waraka Maalumu wa Serikali (White Paper) kwa ajili ya kukusanya maoni ya wananchi wengi iwezekanavyo kuhusu sheria hizo mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia agizo hilo, Wizara iliandaa Waraka wa Baraza la Mawaziri wa utekelezaji wa maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusu kukusanya maoni ya wananchi juu ya marekebisho ya Sheria ya Ndoa na kutungwa kwa Sheria mpya ya Mirathi na Urithi. Waraka huo ulifikishwa katika Baraza la Mawaziri mwezi Machi, 2010. Pamoja na kubainisha hoja ambazo wananchi wangetakiwa kuzitolea maoni, Waraka huo pia uliainisha utaratibu wa kukusanya maoni ya wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi Disemba, 2010 kabla ya Waraka huo haujajadiliwa na Baraza la Mawaziri, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa wakati huo, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliridhia kuanza kwa mchakato wa Mabadiliko ya Katiba na aliahidi kuunda Tume itakayokuwa na majukumu ya kukusanya maoni ya wananchi juu ya Mabadiliko ya Katiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutekeleza azma ya Rais, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 ambayo ilisainiwa na Rais tarehe 29 Novemba, 2011. Sheria hii ndiyo iliyounda Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na kuundwa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba mchakato wa kuandaa Waraka Maalumu wa Serikali (White Paper) kwa ajili ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 na mapendekezo ya kutungwa Sheria mpya ya Mirathi na Urithi ulisitishwa kwa muda. Serikali ilikuwa na matarajio kuwa wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba inakusanya maoni ya wananchi kuhusu mabadiliko ya Katiba huenda wananchi vilevile wangetoa maoni yanayohusu Sheria ya Ndoa na Sheria ya Mirathi na Urithi.
Baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kukamilisha kazi yake imebainika kwamba maoni ya wananchi hayakujielekeza kwenye maudhui ya Sheria ya Ndoa na Sheria ya Mirathi na Urithi kama ilivyotarajiwa. Hivyo basi, Wizara ya Katiba na Sheria imeamua kuendeleza juhudi zake za awali kwa kukamilisha taratibu kuhusu kupata maoni ya wananchi juu ya marekebisho ya Sheria ya Ndoa na kutungwa kwa Sheria mpya ya Mirathi na Urithi.
MHE. RASHID A. SHANGAZI (K.n.y. MHE. ASHA ABDULLAH JUMA) aliuliza:-
Majengo mengi ya Mahakama za Mwanzo yamechakaa sana:-
(a)Je, Serikali ina mpango gani wa kuyafanyia ukarabati au kuyajenga upya?
(b)Je, Serikali haioni kama Mahakama ya Mnazi Mmoja - Dar es Salaam imeelemewa na kesi nyingi hivyo iangalie namna ya kupunguza kesi?
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inao mpango wa ujenzi na ukarabati wa Mahakama wa miaka mitano 2015 - 2020 na hivi sasa inaufanyia marekebisho ili kukidhi mahitaji sahihi ya wakati husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka 2015/2016, Serikali lilitoa fedha ya kiasi cha shilingi bilioni 12.3 za miradi ya maendeleo sawa na asilimia 100% ya fedha zilizopangwa. Fedha hizo zitatumika katika ujenzi na ukarabati wa Mahakama za Wilaya 12 ambazo ni Mahakama za Bariadi, Kilindi, Kasulu, Kondoa, Bukombe, Makete, Sikonge, Nkasi, Bunda, Chato, Nyasa na Namtumbo. Aidha, fedha hizo zitatumika katika ujenzi wa Mahakama mpya za mwanzo 10 za Longido (Manyara), Terati (Simanjiro-Manyara), Machame (Hai), Makongolosi (Chunya-Mbeya), Unyankulu (Urambo-Tabora), Sangabuye (Ilemela-Mwanza), Mtowisa (Sumbawanga), Njombe Mjini, Gairo (Morogoro) na Mangaka (Mtwara).
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali kwa mwaka wa fedha 2015/2016, itakamilisha ukarabati wa Mahakama Kuu Shinyanga, Mtwara, Tanga na Mbeya. Maandalizi ya utangazaji wa zabuni za ujenzi wa Mahakama Kuu Kigoma na Mahakama Kuu Mara yanaendelea.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali ina mpango wa kujenga Mahakama mpya ya Kinyerezi na Ilala. Hivyo, ni matarajio yangu kuwa kukamilika kwa miradi hii kutawezesha kupunguza mlundikano wa mashauri katika Mahakama ya Mnazi Mmoja.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA aliuliza:-
(a) Je, ni utaratibu upi uliotumika na Serikali kuzuia malipo ya 80% kwa mwezi kwa Majaji Wastaafu ambayo ni haki yao ya msingi na malipo ya mafao yao yanayotambulika kwa mujibu wa Sheria ya Majaji?
(b) Je, ni utaratibu upi unaotumika sasa kuzuia malipo hayo kwa baadhi ya Majaji?
WAZIRI WA SHERIA NA KATIBA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Katiba ya Jamhuri ya Muungano 1977, Ibara 142(1) na (5) imeelezea kuwa malipo ya mishahara na mafao ya Jaji wa Mahakama ya Rufani na Jaji wa Mahakama Kuu yanalipwa kupitia Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali. Aidha, Sheria ya Mafao na Maslahi ya Majaji ya mwaka 2007 na Sheria ya Mafao na Hitimisho la Kazi kwa Watumishi wa Umma Na.2 ya mwaka 1999 nazo zimefafanua kuwa malipo ya mishahara na mafao ya Jaji wa Mahakama ya Rufani na wa Mahakama Kuu yatalipwa na Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Fedha na Mipango hutekeleza wajibu wa kulipa 80% ya pensheni kwa Jaji aliyestaafu baada ya kupata na kuzifanyia uhakiki nyaraka zote muhimu kutoka Mahakama na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ambayo Jaji husika alichangia. Kwa Jaji Mstaafu ambaye ana stahili ya kulipwa pensheni ya kila mwezi na PSPF au Mfuko wowote aliouchangia, stahili yake ya 80% hulipwa kwa kuongeza kiwango cha fedha inayopaswa kufikia 80% ya mshahara wa Jaji aliyeko madarakani.
Mheshimiwa Naibu Spika, endapo Jaji Mstaafu hastahili kulipwa pensheni ya kila mwezi kutokana na kutotimiza sharti la kuchangia muda wa chini katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ambao ni kipindi cha miaka 15, asilimia 80 ya pensheni yake ya kila mwezi hulipwa na Hazina kwa asilimia 100. Malipo haya ya asilimia 80 huhuishwa kila wakati na Hazina kulingana na viwango vya mishahara ya Majaji waliopo madarakani.
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA aliuliza:-
Matukio ya kubakwa na ulawiti kwa watoto nchini yamekuwa yakijirudia mara kwa mara na watuhumiwa walio wengi huachiwa au humalizana na wazazi wa waathirika kifamilia:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa kesi hizo hazimalizwi kifamilia?
(b) Je, ni mkakati gani umewekwa ili kuhakikisha kuwa watuhumiwa hao wanapopatikana na hatia wapewe adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine wenye nia mbaya?
(c) Je, watoto waliopatwa na matukio hayo wamewekewa mazingira gani ili kuwaondoshea msongo wa mawazo na kuendelea na elimu bila kubughudhiwa na wenzao.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Agelina Adam Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b), na (c), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli matukio ya kubakwa na kulawitiwa, watoto yamekuwa yakitokea na kuripotiwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini. Pia ni kweli kuwa baadhi ya kesi za aina hiyo zimekuwa zikimalizwa kifamilia kwa maridhiano kati ya mtuhumiwa na wazazi wa mtoto muathirika. Hivyo kuwapa shida sana Wapelelezi wa kesi hizo kupata ushahidi.
(a) Tatizo la kuficha ushahidi na kuzimaliza kesi hizo kifamillia haliwezi kumalizwa na Vyombo vya Dola vinavyofanya uchunguzi peke yake bila ushirikiano na wananchi wanaoishi na watuhumiwa. Hivyo, Serikali imekuwa ikitoa elimu kwa umma kwa kuficha ushahidi na kuyamaliza matukio hayo ati kifamilia siyo kosa la jinai peke yake, bali vile vile, utaratibu huo unachochea vitendo hivyo kuendelea katika jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, ili kuweka mazingira rafiki kwa waathirika na wananchi wenye taarifa au ushahidi wa aina hiyo, Serikali imeanzisha madawati ya jinsia katika vituo mbalimbali vya Polisi yanayopokea taarifa kutoka kwa wananchi na kuliwezesha Jeshi la Polisi kuendesha upelelezi kwa ufanisi. Pindi tukio la kubaka au kulawiti linaporipotiwa upelelezi hufanyika na mtuhumiwa hufunguliwa mashtaka mara moja. Kwa utaratibu huu Serikali inahakikisha kuwa matukio haya hayamalizwi nje ya utaratibu wa haki jinai.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Bunge lako Tukufu tumetunga sheria zenye adhabu kali kwa watuhumiwa wa makosa hayo, wanapopatikana na hatia. Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, imeweka adhabu ya kifungo cha maisha kwa mtu yeyote anayekutwa na hatia ya kumbaka msichana, hicho ni Kifungu cha 136(1) au miaka 14 kwa anayekutwa na hatia ya kujaribu kumbaka msichana, Kifungu cha 136(2). Pia sheria imeweka adhabu ya kifungo cha miaka 14, kwa kosa la kulawiti Kifungu cha 154.
Mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kuwa, sheria hizi zinasimamiwa ipasavyo na kuendelea kuimarisha upelelezi na uendeshaji wa mashauri ya ubakaji na ulawiti ili kuiwezesha Mahakama kutoa adhabu stahiki pindi mtuhumiwa anapopatika na hatia.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, waathirika wa vitendo hivi viovu, hupata msongo wa mawazo na kujisikia vibaya mbele ya wenzao, hali ambayo ina athari mbaya kwenye masomo yao na makuzi ya watoto hao. Serikali imeanza utekelezaji wa mwongozo wa mwaka 2015 wa kuzuia ukatili dhidi ya watoto, mwongozo ambao unataka Walimu Washauri, wateuliwe kila shule ya Msingi na Sekondari na kupatiwa mafunzo ya ushauri nasaha.
Kwa mujibu wa Ibara ya 45(1)(a) na (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano Rais anayo mamlaka ya kutoa msamaha kwa wafungwa waliopo magerezani.
Je, Rais anayo mamlaka kisheria ya kutoa msamaha kwa watuhumiwa wa uhalifu wa aina yoyote ambao mashauri yao yapo katika vyombo vya dola kwenye hatua za uchunguzi/upelelezi au mahakamani?
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khatib Said Haji, Mbunge wa Konde kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Ibara ya 45(1)(a) mpaka (d) inampa Rais mamlaka ya kwanza kutoa msamaha kwa mtu yeyote aliyepatikana na hatia mbele ya mahakama, pili kumuachilia kabisa au kwa muda maalum mtu yeyote aliyehukumiwa au kuadhibiwa kwa ajili ya kosa lolote, tatu, kubadilisha adhabu yoyote aliyopewa mtu yeyote kwa kosa lolote iwe adhabu tahafifu na nne kufuta adhabu yoyote au sehemu ya adhabu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia masharti hayo ya Katiba msamaha wa Rais unatolewa kwa mtu aliyetiwa hatiani na kupewa adhabu na mahakama. Watuhumiwa wa uhalifu ambao mashauri yao yako katika hatua ya upelelezi au uendeshaji mahakamani hawaguswi na masharti ya ibara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu hiyo basi, Rais hawezi kisheria kutoa msamaha kwa watuhumiwa wa uhalifu wa aina yoyote ambao mashauri yao yapo katika vyombo vya dola kwenye hatua za uchungu, upelelezi au mahakamani. Hatma ya watuhumiwa hao inakuwa bado ipo katika mamlaka husika za uchunguzi, mashitaka na mahakama.
MHE. ISSA A. MANGUNGU aliuliza:-
Jimbo la Mbagala lina wakazi zaidi ya 800,000 kutokana na sensa ya watu na makazi lakini ina Mahakama ya Mwanzo Kizuiani tu.
(a) Je, kwa nini Serikali imeshindwa kujenga mahakama katika Jimbo la Mbagala kwa kuzingatia idadi kubwa ya wakazi?
(b) Kwa kuwa kuna mahitaji makubwa ya huduma za mahakama Jimbo la Mbagala katika Kata za Chamazi, Mbande, Kijichi, Kibungwa, Kibondemaji na Tuangoma; je, Serikali ipo tayari kujenga mahakama katika kata hizo hata kwa mpango wa dharura?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, namshukuru Mungu kukuona na afya njema.
Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ali Mangungu, Mbunge wa Mbagala, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kifungu cha 4 cha Sheria ya Mahakimu Namba 2 ya mwaka 1984, Mahakama ya Wilaya huanzishwa kwa kuzingatia kuwepo kwa Mamlaka ya Wilaya ya Kiserikali. Uanzishwaji wa Makahama ya Wilaya hutegemeana na hali ya upatikanaji wa rasilimali watu, rasilimali fedha na miundombinu mingine kama majengo, viwanja na kadhalika.
Mheshimiwa Spika, aidha, uanzishwaji wa Mahakama za Mwanzo (Primary Courts) huhitaji walau kila kata za Wilaya husika iwe na Mahakama ya Mwanzo moja ingawa hakuna kizuizi kwa mamlaka kuanzisha Mahakama za Mwanzo zaidi ya moja kwenye kata moja kutegemeana na mahitaji ya eneo husika na vipaumbele vya mahakama na wananchi.
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Dar es Salaam kwa sasa una Wilaya tano kiutawala (Ilala, Temeke, Kinondoni, Kigamboni na Ubungo) na kata zaidi ya 102 zenye idadi ya wakazi zaidi ya 5,000,000 wanaohitaji huduma hii muhimu, ni dhahiri kwa takwimu tajwa hapo juu Mkoa wetu wa Dar es Salaam unahitaji Mahakama za kisasa za Wilaya tano na Mahakama za Mwanzo 102 angalau kukidhi kila kata ukilinganisha na mahakama 12 zilizopo sasa hivi.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua mahitaji hayo, tayari Wizara kwa kushirikiana na mahakama tumepeleka maombi maalum kwa uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Wilaya na Halmashauri zake waweze kutupatia viwanja vya umma (public plots) vyenye kutosheleza mahitaji ya Mahakama za Mwanzo na Wilaya kwenye maeneo ya makazi ya mjini na yenye shughuli nyingi kama Jimbo la Mbagala. Tunashukuru uongozi wa baadhi ya Wilaya kwa kuanza kutupatia viwanja ambavyo tumeanza kufanya maandalizi ya ujenzi wa mahakama hizo.
(b) Mheshimiwa Spika, tunamuhimiza Mheshimiwa Mbunge na uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Wilaya zake kutoa viwanja vyenye nyaraka rasmi ili tuweke kwenye mpango wa dharura wa ujenzi wa Mahakama za Mwanzo kwenye maeneo yenye kuhitaji kama vile Chamazi, Mbande, Kijichi, Kiburugwa na Kibondemaji.
MHE. RITTA E. KABATI (K.n.y MHE. UPENDO F. PENEZA) aliuliza:-
Kufuatia vifo vyenye utata vya kisiasa na vinavyohusisha vyombo vya dola, aliyekuwa Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda alitoa ahadi katika Bunge la Kumi ya Serikali kuunda Mahakama ya Coroner (Coroner‟s Court) kwa ajili ya kuchunguza vifo mbalimbali vyenye utata:-
Je, Serikali iko katika hatua gani kutekeleza ahadi hiyo?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Upendo Furaha Peneza, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na msingi wa swali hili kuwa na utata, napenda ieleweke wazi kuwa uchunguzi wa vifo vinavyotokea katika mazingira yenye utata ambayo sababu zake hazijulikani, hufanywa kwa uchunguzi maalum (inquest) na mchunguzi maalum anaitwa coroner kwenye Mahakama Maalum ya Uchunguzi (Coroner‟s Court). Utaratibu huu tumekuwa tukiutumia hata kabla uhuru chini ya Sheria ya Uchunguzi Maalum (Inquests Ordinance) Sura ya 24. Sheria hii ilifutwa na kutungwa upya kuwa Inquests Act No. 17 ya 1980 ili kuendana na mazingira mapya ya haki jinai nchini baada ya uhuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, sheria hii mpya iliridhiwa na Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hayati Mwalimu Julius Nyerere tarehe 21 Mei, 1980, chini ya kifungu cha 5(1) Waziri wa masuala ya Sheria wa wakati huo alitangaza sifa za uteuzi za kuwa Coroner na chini ya kifungu cha 5(2) na (3), Jaji Kiongozi kwa kushauriana na Jaji Mkuu, aliwateua Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya na za Hakimu Mkazi kuwa Coroners au Makorona.
Aidha, kwa tangazo la Serikali Na. 252 la tarehe 16 Julai, 2004, Mahakama za Wilaya na za Hakimu Mkazi ziliteuliwa kuwa Mahakama za Coroner pale zinapoketi kwa uchunguzi wa vifo vyenye utata.
MHE. OTHMAN OMAR HAJI aliuliza:-
Kwa kuzingatia usalama na utulivu wa nchi yetu, viongozi wa Serikali wamekuwa wakitoa kauli zenye msisitizo kwa wananchi kuepuka kuhubiri siasa katika nyumba za ibada na kuchanganya dini na siasa katika mikutano.
Je, ni kifungu gani cha Katiba au Sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambacho kinafafanua juu ya kauli hizo?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Othman Omar Haji, Mbunge wa Gando, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inaeleza katika utangulizi wake kuwa Tanzania inaongozwa na Serikali yenye kufuata misingi ya demokrasia, ujamaa na isiyokuwa na dini.
Aidha, Ibara ya 3(1) ya Katiba hiyo hiyo inaeleza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa isiyokuwa na dini na yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa. Ibara ya 19(1), (2) na (3) inaeleza kuwa kila mtu anastahili kuwa na uhuru wa mawazo, imani na uchaguzi katika mambo ya dini pamoja na uhuru wa mtu kubadilisha dini au imani yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, ibara ya 3(2) inaeleza kuwa mambo yote yanayohusu uandikishaji na uendeshaji wa vyama vya siasa nchini yatasimamiwa kwa mujibu wa masharti ya Katiba na sheria iliyotungwa na Bunge kwa ajili hiyo. Hivyo basi, sheria ya vyama vya siasa Sura ya 258 inaeleza bayana katika kifungu cha 9(2) kuwa chama cha siasa, hakitastahili kusajiliwa endapo katiba yake au sera zake zina mwelekeo wa kuendeleza maslahi ya imani ya kidini au kundi la kidini.
MHE. FATMA HASSAN TOUFIQ aliuliza:-
Sheria ya Kutambua Haki ya Msaada wa Kisheria (Legal Aid) ambayo pia inawatambua wasaidizi wa kisheria (paralegals) mchakato wake umeanza tangu mwaka 2010 kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo taasisi zisizo za Kiserikali, lakini sheria hii imekuwa ni ya muda mrefu na sasa ni zaidi ya miaka sita bado haijatajwa wala kuletwa Bungeni.
Je, Serikali ina mkakati gani wa haraka wa kuhakikisha sheria hii inatungwa?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha hatua zote za awali za kuwasilisha Muswada wa Sheria ya Huduma ya Msaada wa Kisheria katika Bunge lako Tukufu. Muswada huo unalenga kuweka utaratibu wa kisheria wa kuratibu huduma ya msaada wa kisheria nchini na kuwatambua Wasaidizi wa Kisheria waliokidhi vigezo mahususi vya ujuzi katika utoaji huduma hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa Serikali baada ya kutungwa kwa sheria hii ni kuhakikisha huduma ya msaada wa kisheria inapatikana nchi nzima hususani kwa wananchi walio vijijini na ambao hawana uwezo wa kumudu gharama za Mawakili ambao wengi wao wanaishi na kufanya shughuli za mijini tu.
MHE. AMINA N. MAKILAGI aliuliza:-
Sheria ya Ndoa imekuwa kandamizi kwa wanawake na watoto:-
Je, ni lini sheria hii italetwa Bungeni ili ifanyiwe marekebisho?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Amina Nassoro Makilagi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 ni matokeo ya mjadala mpana na shirikishi kupitia Waraka wa Serikali namba moja wa mwaka 1969. Lengo la mjadala huo lilikuwa kupata muafaka kuhusu maudhui ya sheria hiyo ambayo yaligusa imani, mila na desturi za Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya miaka zaidi ya 20 kupita tangu sheria hiyo ya ndoa itungwe, Serikali kupitia Tume ya Kurekebisha Sheria iliifanyia mapitio ya sheria hiyo na kubaini maeneo kadhaa yenye udhaifu na hivyo kuhitaji kufanyiwa marekebisho. Kutokana na maoni hayo ya Tume, Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria iliandaa mwaka 2008 Waraka wa Baraza la Mawaziri uliokuwa na mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971.
Kwa kuzingatia chimbuko la sheria hiyo, Baraza liliiagiza Wizara kuandaa Waraka Maalum wa Serikali (White Paper) ili kupata mjadala mpana na shirikishi kama ilivyokuwa awali. Mapema mwaka 2010 Wizara ilikamilisha maandalizi ya waraka huo ambao pamoja na kubainisha hoja ambazo wananchi wangetakiwa kuzitolea maoni uliainisha utaratibu wa kukusanya maoni ya wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi Desemba, 2010 kabla waraka huo haujajadiliwa na kuridhiwa na Baraza la Mawaziri mchakato wa mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukaanza na kulilazimu Baraza kusitisha kwa muda mchakato wa marekebisho ya ndoa. Serikali ilikuwa na matarajio kuwa wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba inakusanya maoni ya wananchi kuhusu mabadiliko ya Katiba, wananchi wangetoa maoni kuhusu Sheria ya Ndoa, Mirathi na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kukamilisha kazi yake, ilibainika kwamba wananchi wengi hawakujielekeza kwenye maudhui ya Sheria ya Ndoa, hivyo Wizara ya Katiba na Sheria ikaamua kuendeleza juhudi za awali kwa kukamilisha taratibu za kupata maoni ya wananchi kwa utaratibu wa White Paper, zoezi hili litakamilika ndani ya muda si mrefu.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA aliuliza:-
Katika bajeti ya 2013/2014, Serikali iliahidi kujenga Mahakama ya Wilaya ya Chunya.
Je, ni lini ahadi hiyo itatekelezwa?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Victor Kilasile Mwambalaswa, Mbunge wa Lupa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Mahakama ya Tanzania ni kusogeza huduma za utoaji haki karibu na wananchi kwa kujenga miundombinu na kuhakikisha kwamba haki inapatikana kwa wote na kwa wakati. Katika kusogeza huduma, Serikali imedhamiria kujenga Mahakama Kuu kila Mkoa, Mahakama ya Wilaya kila Wilaya nchini na Mahakama za Mwanzo kila Kata.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika mwaka wa 2014/2015 tuliahidi kujenga Mahakama za Wilaya na za Mwanzo katika sehemu mbalimbali nchini ikiwemo Wilaya ya Chunya. Hata hivyo ahadi hiyo haikuweza kutekelezwa kikamilifu kutokana na upatikanaji hafifu wa fedha za maendeleo. Mahakama katika mwaka 2014/2015 ilipata asilimia nane tu ya fedha za maendeleo zilizotengwa, hivyo haikuweza kutekeleza miradi yote iliyopangwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Chunya umezingatiwa katika mpango wetu wa ujenzi kwa mwaka 2016/2017.
MHE. ALLAN J. KIULA aliuliza:-
(a) Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama ya Wilaya na kuteua Mahakimu wa Wilaya?
(b) Je, kwa nini Serikali isiridhie Mahakama ya Mwanzo iliyopo ifanywe kuwa Mahakama ya Wilaya?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Allan Joseph Kiula, Mbunge wa Iramba Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila wilaya ya kiutawa nchini inatakiwa kuwa na Mahakama ya Wilaya. Kutokana na utaratibu huu Serikali imekuwa ikijitahidi kwa kushirikiana na mahakama kuhakikisha kuwa wilaya zinazoanzishwa zinakuwa pia na huduma ya mahakama. Vigezo vinavyotumika kuanzisha mahakama katika eneo lolote ni pamoja na:-
(i) Hati ya kisheria ya kuwepo kwa Wilaya, Mkoa au Kata;
(ii) Umbali wa upatikanaji wa huduma za mahakama;
(iii) Idadi ya wakazi wa eneo hilo;
(iv) Uwepo wa huduma nyingine za Kiserikali kama Polisi na Magereza;
(v)Upatikanaji wa rasilimali fedha, watu na miundombinu mingine kama viwanja na majengo; na
(vi) Aina ya shughuli za kiuchumi na kijamii za eneo hilo zinazovuta aina fulani ya mashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto ya kukidhi baadhi ya vigezo nilivyoainisha hususan miundombinu, bado kuna Wilaya ambazo zinapata huduma ya mahakama kupitia Wilaya nyingine. Kwa sasa jumla ya Wilaya 21 nchini zinapata huduma ya mahakama kupitia Wilaya nyingine ikiwemo Wilaya ya Mkalama inayohudumiwa na Wilaya ya Iramba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali imepanga kujenga jengo la Mahakama ya Wilaya ya Mkalama kwa mwaka wa fedha 2017/2018. Aidha, Mahakama imeomba kupatiwa kiwanja katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, bado mipango ya upatikanaji wa kiwanja hicho haijakamilika. Tunaiomba Halmashauri kupitia kwa Mheshimiwa Mbunge waweze kutupatia kiwanja hicho mapema ili kutuwezesha kujenga mwaka ujao wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila ngazi ya mahakama ina mipaka yake kwa mujibu wa sheria na kanuni na hivyo kila moja inahitajika. Hivyo, hatuwezi kubadilisha Mahakama ya Mwanzo kutumika kama ya Wilaya. Aidha, kutokana na udogo wa jengo la Mahakama ya Mwanzo iliyopo sio rahisi kwa jengo hilo kutumika kwa Mahakama ya Wilaya na ya Mwanzo. Nimuombe Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Mkalama kuwa wastahimilivu wakati tunasubiri kujenga mahakama yao ya Wilaya.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO (K.n.y. MHE. LAMECK O. AIRO) aliuliza:-
Wilaya ya Rorya ilianzishwa mwaka 2007, ina ukubwa wa kilometa za mraba 9,345 na idadi ya watu wapatao 400,000, lakini inakabiliwa na tatizo la uhaba wa watumishi katika Mahakama ya Mwanzo ya Kineri, Ryagoro, Obilinju na Shirati. Hadi sasa Wilaya ya Rorya inatumia Mahakama ya Wilaya ya Tarime inayosababisha kesi kuchelewa kusikilizwa kwa wakati.
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Mahakama ya Wilaya kwenye Jimbo la Rorya?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lameck Okambo Airo, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, natambua kuna upungufu wa watumishi katika Mahakama za Mwanzo zilizotajwa kwenye swali hili ambapo kuna upungufu wa watumishi takribani tisa wakiwemo Mahakimu na Wasaidizi katika Mahakama hizo. Katika mwaka huu wa fedha 2016/2017, Mahakama imejipanga kupeleka watumishi hao katika mahakama hizo hususan Mahakama ya Mwanzo ya Nyaburongo ambayo inahitaji Hakimu. Mahakama ya Mwanzo ya Kinesi ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja kwa sasa haitumiki kutokana na uchakavu wa miundombinu yake ambayo itafanyiwa kazi katika mipango ya ukarabati ya baadae.
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Rorya umewekwa katika mpango mkubwa wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya mahakama kwa mwaka wa fedha 2017/2018. Aidha, katika mwaka wa fedha huu, Mahakama imepanga kujenga Mahakama ya Wilaya Bunda na Mahakama Kuu - Mara.
MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:-
Tatizo la kesi za ubakaji na ulawiti kwa watoto wadogo limekuwa likiongezeka siku hadi siku katika Mkoa wa Iringa.
(a) Je, nini mkakati wa Serikali kunusuru hawa watoto wasiendelee kufanyiwa matendo haya ya kikatili?
(b) Je, ni utaratibu gani unatumika kushughulikia watuhumiwa wa kesi hizi?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, ili kudhibiti vitendo hivi haramu dhidi ya watoto tumetunga sheria zenye adhabu kali kwa watuhumiwa wanaopatikana na hatia ya makosa ya ubakaji na ulawiti. Kifungu cha 136(1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, kimeweka adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa mtu yeyote anayekutwa na hatia ya kubaka na kifungu cha 132(2) kinatoa adhabu ya kifungo cha miaka 14 jela kwa yeyote anayekutwa na hatia ya kujaribu kubaka. Aidha, kifungu cha 154 kimeweka adhabu ya kifungo cha miaka 14 jela kwa kosa la kulawiti. Lengo la kutoa adhabu hizo kali lilikuwa kutoa fundisho na onyo kwa yeyote mwenye dhamira ya kutenda makosa hayo ya jinai.
Mheshimiwa Spika, matukio mengi ya aina hiyo Mkoani Iringa yanahusisha ndugu au jamaa wa familia moja au sehemu moja. Ushahidi wa msingi hufichwa unapohitajika na wahusika wa pande zote mbili huyamaliza masuala husika kwa maelewano kifamilia na hivyo kuchochea matendo hayo ya jinai kushamiri.
Napenda kuchukua fursa hii kutoa wito kwa wananchi kuvisaidia vyombo vya dola wakati wa upelelezi na uendeshwaji wa mashauri haya mahakamani ili kukomesha kabisa matukio hayo. Ninamwomba Mheshimiwa Mbunge na wenzako Mkoani Iringa kuwa mstari wa mbele katika kampeni hii ya kuomba ushirikiano na wananchi.
Mhesimiwa Spika, aidha, ili kuweka mazingira rafiki kwa waathirika na wananchi wenye taarifa au ushahidi wa aina hiyo, Serikali imeanzisha madawati ya jinsia katika vituo mbalimbali vya polisi yanayopokea taarifa mbalimbali kutoka kwa wananchi na kuliwezesha Jeshi la Polisi kuendesha upelelezi kwa ufanisi. Pindi, tukio la kubaka au kulawiti linaporipotiwa upelelezi hufanyika na mtuhumiwa hufunguliwa mashitaka mara moja.
(b) Mheshimiwa Spika, utaratibu unaotumika kushughulikia watuhumiwa wa kesi za kubaka na kulawiti umefafanuliwa katika Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20, Sheria ya Ushahidi, Sura ya 6 na Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16. Sheria hizi zimeainisha namna ya kushughulikia makosa hayo kuanzia wakati wa kupokea taarifa ya kutokea kitendo cha ubakaji na ulawiti mpaka hatua ya kutoa adhabu kwa wahusika wa vitendo hivyo.
Mheshimiwa Spika, pamoja na taratibu za kisheria zilizoainishwa katika sheria hizo, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa kesi za kubaka na kulawiti zinamalizika mapema na kuwa sheria zinasimamiwa ipasavyo.
Aidha, Serikali inaendelea kuimarisha upelelezi na uendeshaji wa mashtaka kwa lengo la kujenga kesi na kuwa na ushahidi usiotia shaka ili kuiwezesha Mahakama kufikia maamuzi ya kuwatia hatiani watuhumiwa wa vitendo hivyo.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO aliuliza
(a) Je, kuna wachezaji wangapi wa nje wanaoruhusiwa kucheza kwenye Ligi Kuu Tanzania?
(b) Je, tulianza na wachezaji wangapi miaka ya nyuma na sasa wako wangapi?
(c) Je, ni zipi sababu za kuongeza au kupunguza wachezaji na ni nini manufaa yake?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Venance Methusalah Mwamoto, Mbunge wa Kilolo, lenye vipengele (a), (b) na (c), kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa taratibu za usajili za TTF wachezaji wa nje wanaoruhusiwa kucheza kwenye Ligi Kuu Tanzania ni saba kwa kila klabu. Tulianza na wachezaji watano kati ya mwaka 2010 hadi 2015 na baadaye kuanzia msimu wa 2015/2016 idadi imeongezeka na kufikia wachezaji saba.
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu ya kuongeza wachezaji wa nje kwenye Ligi Kuu hii ya Tanzania ni maombi ya wadau wenyewe wa mpira wa miguu, vikiwemo vilabu vya mpira wa miguu na mazingira mazuri ya mpira wa kulipwa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, uwepo wa wachezaji wa nje kwenye ligi kuu ya Tanzania umeongeza ushindani miongoni mwa wachezaji wetu kiweledi na kinidhamu na kuwa chachu ya vilabu kupanua wigo wao wa mapato kwa ajili ya usajili. Aidha, kuchanganya wachezaji wazawa na wageni ni fursa kwa wachezaji wetu kujifunza kutoka kwa wenzao na kunatangaza ligi yetu nje ya nchi ambako wachezaji wa kigeni wanatoka na maendeleo yao yanafuatiliwa kwa karibu na timu zao za Taifa.
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itapitia upya Sera ya Michezo nchini?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako naomba kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo, nitoe pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wa Watanzania wenzetu 11 waliopoteza maisha na wengine 15 waliojeruhiwa katika ajali nyingine mbaya ya Mlima Igawilo, Mkoani Mbeya, Mungu aziweke roho zao pema peponi.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kufa ni wajibu na maisha lazima yaendelee, niruhusu vilevile nielezee kidogo yaliyotokea Uingereza usiku wa kuamkia jana kwa Mtanzania mwenzetu Hassan Mwakinyo wa Tanga kwa ushindi mnono alioupata huko Birmingham, Uingereza, baada ya kumchakaza mwanamasumbwi nyota wa Uingereza Sam Eggington katika raundi ya pili tu kati ya raundi 10. (Makofi)
Kabla ya pambano hili kufanyika bondia wa Uingereza alikuwa bondia namba nane kwa ubora duniani kati ya Mabondia 1,852 wakati Hassan Mwakinya alikuwa ni Bondia wa 174 na sasa hivi kutokana na matokeo haya Hassan ni wa 16 duniani, ni bondia bora wa kwanza Barani Afrika na bondia wa kwanza Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya haya, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Sera ya Maendeleo ya Michezo inayotumika sasa hivi ni ya mwaka 1995, ni dhahiri kuwa katika miaka 23 ya sera tuliyonayo sasa tasnia ya michezo imepitia mabadiliko mengi yanayoleta hitaji la mabadiliko kisera kama vile michezo kuwa chanzo kikubwa cha ajira ya uhakika duniani, kuibuka kwa michezo ya kulipwa, ongezeko la mahitaji ya shule na vyuo mahsusi vya michezo mbalimbali kwa lengo la kulea vipaji toka udogoni kwa wavulana na wasichana, ongezeko la hitaji la viwanja vizuri na vya kutosha ngazi za shule za msingi, sekondari, vyuo, sehemu za kazi na makazi kwa lengo la kuibua viipaji na kupunguza gharama za matibabu kwa magonjwa yanayotokana na mwili kukosa mazoezi, ongezeko kubwa la mahitaji ya vifaa mbalimbali vya michezo na umuhimu wa kujenga uwezo wa ndani kuzalisha vifaa hivyo.
Mheshimiwa Spika, ni kutokana na hali hii halisi Wizara ilianzisha mwaka jana zoezi la kuipitia upya Sera ya Maendeleo ya Michezo ya mwaka 1995, zoezi ambalo limehusisha ukusanyaji wa maoni kutoka kwa wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi. Uandaaji wa rasimu kamili ya Sera mpya ya Maendeleo ya Michezo umefikia hatua za mwisho na ni matarajio ya Wizara kukamilisha zoezi hili ndani ya muda mfupi ujao.
Mheshimiwa Spika, kupatikana kwa sera mpya kutaleta tija na kutuwezesha kuleta mabadiliko chanya katika tasnia ya michezo nchini ikiwa ni pamoja na kutuwezesha kubadili sheria iliyoanzisha Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ili iweze kuleta ufanisi katika uendeshaji wa michezo nchini, ikiwa ni pamoja na kuainisha vyanzo rasmi na endelevu vya mapato katika maendeleo ya michezo nchini.
MHE. TUNZA I. MALAPO (K.n.y MHE. DEVOTHA M.
MINJA) aliuliza:-
Viwanja vingi vya michezo vinavyomilikiwa na Chama cha Mapinduzi vimechakaa kutokana na kutoendelezwa kwa muda mrefu. Mfano, Kiwanja cha SabaSaba Mkoani Morogoro.
Je, Serikali haioni kuna haja ya kubinafsisha viwanja hivyo ili viendelee kutumika katika michezo?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Devotha Mathew Minja, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Sera ya Maendeleo ya Michezo ya mwaka 1995 inaelekeza kuwa utunzaji wa viwanja utafanywa na taasisi zinazomiki viwanja hivyo. Kwa hiyo, viwanja vinavyomilikiwa na Chama cha Mapinduzi mfano kiwanja cha SabaSaba katika Manispaa ya Morogoro ni sawa na viwanja vingine vya michezo vya taasisi binafsi, mashirika ya umma, vilabu na vyama vya michezo. Hivyo, suala la utunzaji na ukarabati vinabakia kuwa jukumu la mmiliki.
Mheshimiwa Spika, viwanja vyote bila kujali mmiliki wake vinatakiwa kutunzwa vizuri ili vitumike kulingana na makusudio yake. Pale ambapo uwezo haupo inashauriwa kutafuta wabia na wafadhili ili wananchi waendelee kunufaika na rasilimali hiyo.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO (K.n.y. MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO) aliuliza:-
Serikali imekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha maendeleo ya michezo mbalimbali lakini sheria inayosimamia michezo ya mwaka 1967 ina upungufu makubwa sana.
(a) Je, kwa nini Serikali haijatunga sheria mpya ya michezo ambayo itakwenda sambamba na mahitaji ya jamii kwa sasa?
(b) Je, kwa nini Serikali haina bajeti kwa ajili ya Timu za Taifa zinazobeba bendera kwa ajili ya kuitangaza nchi Kimataifa?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba kwa ridhaa yako kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ndumbaro nitoe pongezi kwa Mabingwa wa Ligi ya Tanzania Bara Simba, kwa kufanikiwa kutinga fainali ya michuano ya Sport Pesa Super Cup nchini Kenya. Simba wamethibitisha kuwa hawakupata ubingwa wa Tanzania Bara kwa kubahatisha, bali kwa soka la viwango na sasa wanaingia fainali kupambana na mabingwa wa Kenya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Damas Daniel Ndumbaro, Mbunge wa Songea Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iko katika hatua za mwisho kabisa kukamilisha maboresho ya sera ya michezo ya mwaka 1995 na sera mpya tutakayoipitisha ndani ya mwaka huu, itakuwa msingi wa sheria mpya ya michezo nchini.
b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatenga bajeti kila mwaka kwa ajili ya michezo nchini ambayo inaendana na ukubwa wa mashindano yanayotukabili. Kwa mfano, mwakani Tanzania ni mwenyeji wa mashindano ya AFCON ya mpira wa miguu kwa vijana chini ya umri wa miaka 17. Hivyo, mbali na vyanzo vingine vya fedha, Bunge hili tukutu limeidhinisha shilingi bilioni moja itumike kuboresha miundombinu ya Kiwanja cha Taifa na Kiwanja cha Uhuru na shilingi 293,619,000 kwa maandalizi mengine yanayohusiana na AFCON.
MHE. ALLY SALEH ALLY aliuliza:-
Mchezo wa chess au sataranji unakuza akili, uwezo wa kufikiri na kufanya maamuzi na ni mzuri sana kwa vijana ambao wanakulia na kuingia hasa katika masomo ya sayansi na ufundi.
(a) Je, mchezo huo umejikita kiasi gani hapa nchini hadi sasa?
(b) Je, kunaweza kuwa na mipango ya kufanya juu ya mchezo huo kuwa wa lazima na sehemu ya mtaala kwa kuiga hasa nchi za Ulaya ya Mashariki?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Saleh Ally, Mbunge wa Malindi, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Ally Saleh Ally kama ilivyo kwa michezo mingine, mchezo wa chess au saratanji unakuza akili, hilo tunakubali, uwezo wa kufikiri na kufanya maamuzi. Hata hivyo, mchezo huu bado haujaenea sana hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa michezo ikiwemo mchezo wa chess inaimarika nchini. Wizara, kupitia Baraza la Michezo la Taifa na Chuo cha Maendeleo ya Michezo - Malya kwa kushirikiana na wadau wa mchezo huu itaangalia uwezekano wa kutoa mafunzo kwa lengo la kuueneza mchezo huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali itaendelea kuhamasisha wananchi katika maeneo mbalimbali kushiriki katika mchezo huu kama inavyofanya katika michezo mingine ili kuueneza mchezo huu kwa manufaa ya jamii kwa ujumla, kwani tayari umeshasajiliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kwa sasa Serikali haina mpango wa kuufanya mchezo huu kuwa wa lazima kufundishwa kwenye shule kwa kuuingiza kwenye mitaala yetu. Pia suala la kuingiza mchezo kuwa sehemu ya mtaala linahusisha wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Wizara mbalimbali na hasa baada ya kujiridhisha kwa kufanya tafiti za kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema hapo awali, Waheshimiwa Wabunge na wadau wote wa Sekta ya Michezo waendelee kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha kuwa michezo, ikiwemo mchezo wa chess inasonga mbele. (Makofi)
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-
Je, ni vigezo vipi ambavyo Serikali imeviweka juu ya kampuni zinazowekeza kwenye michezo nchini kuruhusiwa Ligi husika kubeba majina ya kampuni hizo kama vile Vodacom Premier League badala ya Tanzania Premier League?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kuongezeka kwa gharama za mfumo wa uendeshaji wa Mpira wa Miguu Duniani, Shirikishao la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limelazimika kutafuta wadhamini au wafadhili wa kusaidia kuendesha shughuli za mpira wa miguu nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kati ya makubaliano yanayofikiwa kati ya Shirikisho na Wadhamini ni mdhamini kujitangaza kupitia mchezo wenyewe. Kwa mfano, ligi kuu ya Uingereza wakati ikifadhiliwa na Benki ya Backlays, ligi ilijulikana kwa jina la Backlays English Premier League. Hapa Afrika Mashariki kuna mashindano ya Kagame Cup ambayo mfadhili wake ni Rais wa Rwanda, Mheshimiwa Paul Kagame na yanajulikana kama CECAFA Kagame Cup.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo suala la ligi kuu ya Tanzania kutumia jina la Mdhamini wa ligi hiyo, Kampuni ya Vodacom, linatokana na makubaliano ya kimkataba baina ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania na mdhamini wa ligi hiyo ambayo ni kampuni ya Vodacom.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mkataba huo, miongoni mwa masuala waliyokubaliana ni pamoja na mdhamini kuwa na haki ya kutumia jina lake (Naming Right) katika uendeshaji wa ligi hiyo.
MHE. ZUBEDA H. SAKURU aliuliza:-
Kumekuwa na vyama vingi vinavyotambuliwa kama vyama vya wasanii na wanamichezo nchini.
(a) Je, kuna jumla ya vyama vingapi halali vya wasanii na wanamichezo ambavyo vinatambuliwa kwa mujibu wa sheria?
(b) Serikali imechukua hatua gani dhidi ya vyama visivyo na usajili vya Sanaa na Michezo?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zubeda Hassan Sakuru Viti Maalum lenye sehemu A na B kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia mwezi Disemba mwaka 2019 vipo vyama 69 ambavyo vinatambuliwa kwa mujibu wa Sheria ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Na. 23 ya mwaka 1984, ikisomwa pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2019. Kwa upande wa michezo vipo jumla ya vyama 11 kwa ngazi ya kata vyama 28 vya Wilaya, Vyama 193 vya Kimkoa na Vyama 74 vya Kitaifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya BASATA namba 23 ya mwaka 1984; ikisomwa pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2019 na BMT ni kosa la jinai kwa mtu yeyote kujihusisha na shughuli za Sanaa na Michezo pasipo na usajili na vibali halali vya Serikali. Vyama vya Michezo visivyosajiliwa haviruhusiwi kushiriki kwenye michezo yoyote rasmi inayofanyika kwenye ngazi za Wilaya, Mkoa au Taifa.