Answers to supplementary Questions by Hon. Dr. Harrison George Mwakyembe (58 total)
MHE. HAJI KHATIB KAI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Baada ya kupata maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali imeshauri wananchi kuzitambua na kuzitumia fursa za soko la Afrika Mashariki na kwa kuwa Serikali na Wizara husika, ina wajibu wa kutoa elimu kwa wananchi wa Tanzania kuhusiana na soko la Pamoja la Afrika Mashariki. Ni kwa nini na ni lini Serikali au Wizara husika itatoa elimu kwa wananchi wa Kaskazini Pemba hasa Jimbo langu la Micheweni ili waepukane na tabu ambazo wamekuwa wakizipata kila mara?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema, endapo matatizo yatatokea au vikwazo vitatokea wananchi wawasiliane na Wizara yake au Balozi zetu. Binafsi wananchi hawa au Watanzania hawa wapatao 130 wanaotoka Jimbo langu na Majimbo mengine, waliposhikwa nchini Kenya waliwasiliana na mimi na mimi nikawasiliana na Balozi zetu zote mbili Nairobi na Mombasa kwa ajili ya msaada, msaada ambao ulishindikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilifuata utaratibu wa kwenda Ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nje kwa msaada zaidi na nilikutana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara na tulikubaliana kilichofanyika si sahihi. Kwa bahati mbaya, naomba kumwuliza swali Mheshimiwa Waziri, hadi sasa sijapata mrejesho wowote, je, atakubaliana nami kwamba Watanzania hawa ambao hawakupata msaada si ni wazi kwamba, kutokana na itikadi yao ya kisiasa ndilo jambo ambalo lilipelekea kushindwa kupatikana msaada wowote? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya swali la msingi. Ningependa nimjibu Mheshimiwa Kai, Mbunge wa Micheweni maswali yake mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, pengine kwa upande wa Tanzania nimekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Afrika Mashariki kwa mwaka mzima. Hili suala analolieleza hapa ndiyo nalisikia kwa mara ya kwanza. Kwa hiyo, ningeomba tu Mheshimiwa Mbunge hilo analolisema ni kitu kizito sana, itabidi tukae chini na Wizara husika tuweze kuelewa kilitokea kitu gani hata kama alikwenda Ubalozi wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kifupi, naomba kutoa wito kwa wananchi wa Tanzania wanaofanya biashara katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, ukipata matatizo kama Naibu Waziri alivyosema kwenye jibu la swali la msingi, hakikisha unakwenda Ubalozi, ukishindwa nenda Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, ukishindwa nenda TCCIA (Tanzania Chamber of Commerce and Industrial and Agriculture), ukishindwa nenda Tanzania Exporters Association (TEA).
Kwa hiyo, taasisi zote hizi zitakusikiliza lakini hakikisha Wizara inapata taarifa kwa sababu tuna miundombinu tayari ya kulalamika.Wenzetu wanajua sana kulalamika, Watanzania tunalalamika chini kwa chini.
La pili, lini tutatoa elimu kwenye Jimbo lake? Elimu tunatoa kuanzia hii Wizara ilipoanzishwa, tunatoa kupitia vipindi vya redio, television, pamphlets, kupitia mikutano, hatuwezi kufanya specifically kwa Jimbo moja, lakini naomba niwahakikishie Watanzania kwamba biashara Afrika Mashariki sasa hivi imeongezeka kwa kasi na Watanzania tunachangia kwa kiasi kikubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe wito tu kwa wafanyabiashara wa Kitanzania, tutumie hii fursa ya kupeleka bidhaa katika nchi za Afrika Mashariki kwenye bei nzuri, hulipi chochote kwa bidhaa zote ambazo zina uasilia wa Afrika Mashariki, unachotakiwa tu ni kupata hiyo certificate ya origin pale unapofika mpakani hasa kama bidhaa yako haizidi dola 2,000 na kwa wafanyabiashara wakubwa wao wanapata kutoka TCCIA.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri ametuelekeza Watanzania wachangamkie fursa zinazojitokeza katika Soko la Pamoja la Afrika Mashariki na Jimbo la Vunjo ni sehemu ya kuchangamkia fursa hizo especially eneo la Taveta. Sasa lini Serikali itaharakisha ujengaji wa soko la Kimataifa la Lokolova pale Himo ili fursa hizo ziweze kutumika kwa Watanzania?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa soko la analolieleza Mheshimiwa Mbatia ni moja tu ya miradi mingi ambayo Serikali imefanya kuongeza fursa ya Watanzania kushiriki katika biashara ya Afrika Mashariki. Yeye mwenyewe atakuwa ni shahidi kwamba Serikali sasa hivi ina miradi ambayo nusu yake imekamilika ya kujenga vituo vya pamoja kwenye mipaka vinane, tunaita one stop boarder post na tumejenga vituo vizuri sana ambavyo vimeharakisha biashara katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile analolisema Mheshimiwa Mbatia ni suala ambalo tunafikiri ni muhimu kwa Wizara sasa hivi ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa maeneo yote ya mipakani, kwa kweli tuharakishe kumalizia miradi yote ambayo tumeianza na ambayo tunaifikiria ya masoko ya pamoja kwa sababu wenzetu upande wa pili wamechangamkia kweli fursa hiyo. Nadhani huo ni wajibu wa Serikali kuliangalia hilo kwa makini kwa kila mpaka siyo tu kwenye Jimbo la Vunjo.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, nina maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, uvunjwaji huu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora inaathiri sana usalama wa raia na mali zao. Katika majibu ya Mheshimiwa Waziri amekiri na amesema kwamba mambo yaliyochunguzwa ni matumizi mabaya ya madaraka ya watendaji na matumizi ya nguvu ya vyombo vya dola.
Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri kile kinachoitwa Uchaguzi wa Marejeo kule Zanzibar na kubadilika kuwa Uchafuzi wa Makusudio, ni kwa kiasi gani Serikali ilifanya uchunguzi ikagundua udhalilishaji huu wa watu kupigwa bila hatia na kule Tumbatu nyumba zao kuchomwa moto? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika majibu ya Mheshimiwa Waziri amesema kwamba wametembelea magereza na kufanya uchunguzi wa kina. Naomba Mheshimiwa Waziri aniambie katika kutembelea magereza, wamefanya uchunguzi kiasi gani, wakafuatilia kiasi gani na wakagundua jambo gani pale ambapo Mashehe waliotoka Zanzibar waliopelekwa Tanzania Bara, waliofanyiwa vitendo vibaya, viovu, vichafu, vya kikatili na vya kishenzi walipolawitiwa. Tarehe 28 mimi nilikwenda kwenye Gereza la Segerea na wakasema kwamba hali yao ni mbaya na kinyesi chao hakizuiwi wanavuja mavi. (Makofi)
Je, tuambie Serikali hii, katika misingi ya uvunjaji wa haki za binadamu…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Masoud hilo ni swali la tatu sasa.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Hilo ni la pili.
NAIBU SPIKA: La pili umeshauliza…
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Sijauliza swali la pili.
NAIBU SPIKA: Kwa namna gani, kwa namna gani mara tatu, sasa hayo ni maswali mengi already. Kama unafuta hilo la pili basi uliza sasa hili lile la katikati ulifute. (Makofi)
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Mheshimiwa Waziri wakati unajibu umesema kwamba mlikwenda kwenye magereza na kufanya uchunguzi, ni kiasi gani mmegundua malalamiko yaliyoko kwenye magereza na hasa pale ambapo kuna malalamiko ya muda mrefu ya Mashehe waliotoka Zanzibar ambapo walilawitiwa, vitendo vichafu, viovu…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Masoud, tafadhali uliza swali, umeanza na je, malizia. Uliza swali tafadhali, hayo maelezo tumeshayasikia.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Waziri, ni kwa kiasi gani malalamiko haya ya vitendo hivi viovu, vichafu, vibaya, vya kishenzi na vya kinyama walivyofanyiwa Mashehe wetu mtavifuatilia kwa kina?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kazi yake kubwa ni kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi. Mheshimiwa Mbunge anaposema kumetokea udhalilishaji wa haki za binadamu za kupindukia, napenda kujua kama hayo masuala malalamiko yalipelekwa kwenye Tume kwa sababu nachozungumzia hapa ni Tume ya Haki za Binadamu na jinsi ninavyojibu ni malalamiko ambayo yametolewa na wananchi. Kama nilivyosema kati ya mwaka 2010 mpaka mwezi huu ninapoongea Tume imepokea na kushughulikia zaidi ya 13,709. Sasa kama hiyo ni mojawapo taarifa ya Tume nitaletewa na nitakuja kuiweka hapa Mezani kama Katiba inavyonitaka chini ya Ibara ya 131(3).
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa Serikali haijaanza kupokea maoni, je, imepangaje kushirikisha wanawake wengi zaidi katika kutoa maoni yao?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Wizara itaanza lini maandalizi ya kuchukua maoni hayo? Ahsante!
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara pamoja na Tume ya Kurekebisha Sheria imepanga kulifanya zoezi hili kama tulivyoelekezwa mwanzoni kwa kina na kwa kuwafikia wananchi wengi kadri iwezekanavyo na ndiyo sababu ya Baraza la Mawaziri kusema tusileta mabadiliko hapa bila kutumia utaratibu wa white paper ambao una lengo la kuwafikia wananchi wengi iwezekanavyo.
Kwa hiyo, tutahakikisha wanawake wengi iwezekanavyo tunawafikia na natoa wito kwa wananchi wote na wanawake wote Tanzania pale watakaposikia mchakato umeanza naomba wajitokeza kutoa maoni kuhusu sheria hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kuhusu maandalizi yanaanza lini, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Fatma Toufiq kwamba maandalizi yalishaanza na sasa hivi tunapitia nyaraka zote za mwanzo ziendane na hali halisi ya leo.
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasikitika sana kuwa masuala mengi yanayohusiana na mambo ya wanawake yanatafutiwa kila sababu yasifanyike yakakamilika. Tunataka kupata majibu ni lini sasa hizi sheria zitapitiwa na zilete majibu yanayotakiwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, wanawake ni zaidi ya asilimia 51 ya nchi hii lakini mambo yao yanapigwa danadana kila siku. Tunataka hili jambo likamilishwe sasa, lilikuwa lisingoje Katiba kwa sababu ni la miaka mingi kabla hata ya Katiba. Ahsante sana.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilikuwa na dhamira njema kutumia mtindo wa white paper badala tu ya kupokea mapendekezo kutoka Wizara ya Katiba na Sheria ili wananchi wengi iwezekanavyo waweze kushiriki kwenye zoezi hili. Kama nilivyoeleza kwenye majibu yangu ya awali ni kwamba kipindi hicho ambacho tulitakiwa sisi tutumie utaratibu wa white paper ndiyo kipindi ambacho kulikuja pia mchakato wa Katiba Mpya ambao ulitutaka sasa tuwafikie wananchi wengi na ni gharama ambayo tusingeweza kuibeba kwa pamoja, huku tunafanya usahili kuhusu masuala ya Katiba Mpya na huku tunaendelea na masuala ya white paper kuhusu huo mchakato wa kubadilisha sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Janet Mbene, Serikali imefanya makubwa mno kuleta mabadiliko ya hali ya wanawake Tanzania. Mwaka 1999, naomba nimkumbushe Mheshimiwa Mbunge, Serikali ilifanya maamuzi makubwa kwa sheria zake mbili za ardhi, Sheria Na.4 na 5 kuhakikisha kwamba mwanamke hadhaliliki tena katika kumiliki na kutumia ardhi. Sasa hivi mwanamke ana haki sawa kabisa na mwanaume.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile katika Mkutano huu tunaleta Muswada wa Sheria utakaohakikisha watoto wetu wote wanaosoma shule za msingi na sekondari wasiweze kukatisha masomo yao kutokana na masuala haya ya ndoa za mapema. Muswada huo utakuwa ni miscellaneous amendment, ambao utaleta mabadiliko kwenye Sheria ya Elimu ambapo watoto wote wa shule za msingi na sekondari hawataruhusiwa kuolewa, hawataruhusiwa kuoa ili wafaidi fursa iliyojitokeza chini ya Serikali ya Awamu ya Tano ya elimu bure kwa wote na wote ni mashahidi hapa jinsi ambavyo wananchi na watoto wengi wameitikia fursa hii ya elimu bure na tunataka na watoto wa kike nao wafaidike as much as possible. Ahsante sana.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amesema kwamba wametenga pesa kwa ajili ya uanzishaji wa Mahakama nyingi za Wilaya na kama alivyozitaja, lakini napenda kumuuliza, ni lini sasa Wilaya ya Temeke ambayo inatumia majengo ya Halmashauri ya Manispaa ya Temeke itakuwa na majengo yake?
Mheshimiwa Naibu Spika, je, kwa Wilaya mpya ya Kigamboni ambayo imeanzishwa ni lini itapatiwa Mahakama?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
WAZIRI WA SHERIA NA KATIBA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango wa miaka mitano wa ujenzi na ukarabati wa Mahakama zetu, Mahakama ya Tanzania ina mpango mzuri kabisa wa kujenga Mahakama ya Wilaya Temeke. Vile vile Mahakama Kigamboni Mheshimiwa Shangazi tayari imeshajengwa, tupo katika kumalizia tu na ni Mahakama ya kisasa ambayo ningeomba tu utakapomaliza Bunge hili ukaiangalie ndiyo mfano wa Mahakama ambazo tutakuwa tunajenga Tanzania kwa Mahakama zote za mwanzo.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba Wilaya ya Rufiji ni Wilaya kongwe. Ni miongoni mwa Wilaya za awali, ina miaka zaidi ya 55 toka izaliwe lakini kutokana na mgawanyo wa Wilaya, Wilaya hii imebaki kuwa ni Wilaya pekee ambayo haina Mahakama ya Wilaya. Wananchi wangu wanalazimika kusafiri umbali wa zaidi ya kilometa 100 kufuata huduma za Mahakama ya Wilaya. Je, ni lini Serikali itakuwa na mpango wa kujenga Mahakama ya Wilaya kuwasaidia wananchi wangu wa Jimbo la Rufiji?
Mheshimiwa Naibu Spika, tofauti ya mshahara kati ya Hakimu na Jaji ni kubwa sana na kazi wanazofanya Mahakimu takribani ni kubwa kuliko wanazofanya Majaji. Nataka nifahamu Serikali inajipanga vipi kuboresha maslahi ya Mahakimu katika suala zima la mishahara, msaada wa nyumba (house allowance) pamoja na non-practicing allowance kwa Mahakimu nchi nzima?
WAZIRI WA SHERIA NA KATIBA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuchomekea maslahi ya Jimbo lake la Rufiji katika swali hili. Naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara inaelewa hali maalum ambayo Jimbo lake inayo hasa baada ya kumegwamegwa, tumepata hapo Kibiti na Mafia na tunaelewa kabisa kwamba miundombinu ya Mahakama katika Jimbo lake ni mbaya. Naomba nimhakikishie katika mpango wa Mahakama wa miaka mitano, suala la miundombinu ya Mahakama ya Rufiji tutalitilia maanani sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusu tofauti ya mishahara ya Mahakimu na Majaji, naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba tunaangalia pia mishahara ya maafisa ya Mahakama walioko chini. La msingi tu ni kwamba ili kukidhi matakwa ya Kimataifa na pia matakwa yetu ya kikatiba, ni lazima tufikie vigezo vya kuwalipa Majaji vizuri wasiwe na vishawishi vya kuweza kuchukua rushwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri katika hili kwa upande wa Majaji Tanzania tumefanikiwa sana. Kazi yetu kubwa ni kuangalia Mahakama za chini siyo tu Mahakama za Hakimu Mkazi, Mahakama ya Wilaya lakini mpaka Mahakama za Mwanzo kwani kwa upande wa Mahakama za juu tumejitahidi. Nafikiri sisi ni moja ya nchi chache duniani ambazo kwa kweli tumefikia viwango stahili katika kujali maslahi ya Mahakama zetu za juu.
MHE. DKT. CHARLES J. TIZEBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sengerema hali haiko tofauti sana na Rufiji. Mahakama za Mwanzo tisa zilifungwa kwa sababu mbalimbali zaidi ya mwaka mmoja na nusu sasa. Je, upo utaratibu sasa katika Wizara yako unaoweza kuziwezesha Mahakama hizi kufunguliwa ili haki iweze kupatikana kirahisi kwa wananchi?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nina bahati kwamba, mwezi uliopita nilitembelea Jimbo la Sengerema na Buchosa. Kwa kweli hali ya miundombinu ya Mahakama hata mimi mwenyewe nimeona inahitaji kusaidiwa kwa jicho la pekee. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika Mpango wa Mahakama wa miaka mitano ambao ni mkubwa kupita mipango yote toka uhuru, hatuwezi kusahau kabisa miundombinu mibovu katika Jimbo la Buchosa na Sengerema hasa upande wa Mahakama za Mwanzo na Mahakama za Wilaya. Pia tutazingatia kwamba Wilaya ya Sengerema ina visiwa zaidi ya 28 kitu ambacho nilikiona ni kigumu sana kukiacha hivi hivi bila kuingilia kati kwa mpango maalum wa kuwasaidia.
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Kwa kuwa, adhabu mojawapo aliyoitaja ni kifungo cha maisha kwa wale ambao watapatikana hatia na huko gerezani tayari wameshakuwa na tabia kama hiyo, haoni kwamba kwa kuwaweka gerezani maisha wataendelea kufanya shughuli hiyo, kwa nini adhabu isiongezwe na waweze kuhasiwa ili wasirudie tena kitendo hicho?
Swali la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba vitendo vya ubakaji vinajirudia mara kwa mara; Je, anaweza kunipa taarifa kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita ni kesi ngapi zimepelekwa Mahakamani na ngapi zimetolewa hukumu. Ahsante.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge yeye anaona adhabu ya gereza haitoshi, hata kwenda jela maisha haitoshi ila anataka vile vile wahasiwe. Siwezi kuwa na jibu hapa kwa sababu hili ndilo Bunge linalotunga sheria za nchi, ningeomba tu Mheshimiwa Mbunge aje na hilo wazo liletwe mbele ya Bunge hapa, ni ninyi mtakaopitisha kwamba wanaume wahasiwe wanaokutwa na hilo tatizo au la, lakini siyo Serikali kuja na shauri hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, anataka kujua statistics, kujua ukubwa wa tatizo hili. Naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tatizo la kubaka na kulawiti nchi hii sasa hivi limefikia mahali pabaya kwa sababu, ukichukua takwimu za miaka mitatu au miaka minne iliyopita, tuna matukio kumi na tisa kila siku ya Mungu ya kubaka na kulawiti. Hayo matukio 19 ya kila siku ya Mungu ni yale ambayo yanaripotiwa, sasa siyo ajabu yakawa mara tatu ya hapo yale ambayo yanapita bila kuripotiwa na kupelekwa Mahakamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hili ni tatizo kubwa, Waheshimiwa Wabunge lazima tushirikiane. Kati ya mwezi Januari mpaka mwezi Machi mwaka huu tu nimepata taarifa hapa kwamba tuna mashauri 2,031, miezi mitatu tu! Mpaka sasa naipongeza Mahakama kwamba pamoja na uchache wao wameweza kuzikamilisha kesi 111, watuhumiwa 96 wamefungwa. watuhumiwa 18 wameachiwa huru kwa kukosa ushahidi, lakini bado kesi 1,920 kwa miezi mitatu bado hazijakamilika. Hiyo ndiyo changamoto tuliyonayo ambayo naona Waheshimiwa Wabunge wote ni kazi yetu kuweza kuitatua.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nikueleze tu kuridhika kwangu na majibu ya Kaimu Waziri Mkuu, majibu yamekwenda shule na yana viwango. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na majibu hayo, kwamba Rais hana mamlaka ya Kikatiba kusamehe watuhumiwa ambao mashauri yao yako katika hatu za kiuchunguzi; katika uongozi wa Awamu ya Nne tulimshuhudia Rais Jakaya Kikwete akitoa msamaha kwa watuhumiwa wa EPA na kutaka walipe na hakuruhusu wapelekwe mahakamani. Je, kutokana na kitendo hicho Rais Kikwete alivunja Katiba ya nchi kwa kutumia madaraka yake vibaya?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa mujibu wa majibu yako ni dhahiri kwamba watuhumiwa wa EPA bado wanastahiki kupelekwa mahakamani kwa sababu msamaha walioupata haukuwa wa Kikatiba, je, Serikali inatoa kauli gani juu ya kuwafikisha watuhumiwa wale wa wizi wa EPA mahakamani ili kukabiliana na tuhuma zao? Ahsante sana.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, swali linaloulizwa hapa, lililoletwa mbele ya WIzara yangu ni je, Rais ana mamlaka ya kutoa msamaha kwa mtu yeyote aliyetuhumiwa? Na jibu langu ni la Kikatiba, na ninalolisema ndivyo Katiba inavyosema, na mimi si mwanasheria tu lakini vilevile ni mwalimu wa sheria. Ninasema, chini ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 45 Mheshimiwa Rais madaraka yake yako katika kumsamehe mtu ambaye tayari amehukumiwa na amepewa adhabu, inaitwa constitutional…(Makofi)
Kwa hiyo, naomba basi nikueleweshe...
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba makofi yapungue kidogo ili nieleweshe vizuri. Huu msamaha hana Rais wa Jamhuri ya Muungano tu, hata Rais wa Zanzibar chini ya Ibara ya 59 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ambapo Rais pale ambapo kuna makosa anaweza akasamehe. Sasa umenitolea mifano miwili, mitatu ambayo Rais aliyepita unasema aliwasamehe watuhumiwa. Mimi kwa taarifa nilizonazo Mheshimiwa Rais hakutumia kifungu cha 45 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MHE. ISSA A. MANGUNGU: Mheshimiwa Spika, nashukuru, na ninashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri wa Katiba, lakini ningependa kumuuliza maswali mawili.
Swali la kwanza; viwanja katika eneo la Kijichi, Tuangoma na Chamazi vipo na nitampelekea orodha hiyo baada ya kikao hiki, je, yupo tayari sasa kuanza mpango huo wa ujenzi haraka iwezekanavyo ili wananchi waweze kupata huduma hiyo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Mahakama ya Kizuiani ambayo iko moja inahudumia zaidi ya watu 800,000, haina choo, haijafanyiwa ukarabati kwa muda mrefu, ipo karibu na soko, uendeshaji wa kesi pale unakuwa ni mgumu, haki inachelewa kupatikana; je, Serikali ina mpango gani wa kufanya marekebisho na matengenezo ya dharura katika mahakama ile?
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, kwa upungufu wa mahakama 102 kwa Mkoa wa Dar es Salaam, Serikali yenyewe haioni kwamba inachelewesha haki na kusababisha vitendo viovu kama rushwa na mambo mengine?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, kwanza, anasema viwanja vipo, hiyo ni taarifa nzuri sana kwangu, namuomba sasa atuwasilishie rasmi hivyo viwanja ambavyo tayari vina nyaraka zake.
Mheshimiaw Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mangungu kwamba tuna pesa ya kujengea mahakama sasa, mkikumbuka mapema mwaka huu Mheshimiwa Rais aliagiza pesa yote ya maendeleo ya mahakama itolewe, kwa tuna shilingi bilioni 12.3 tayari, lakini vilevile Waheshimiwa Wabunge mmetuidhinishia shilingi bilioni 22 katika mwaka huu wa fedha, tuna jumla ya shilingi bilioni 34.3 na hizo pesa tunajenga Mahakama za Mwanzo 50, anayewahi kwa hoja za msingi tutampa hiyo mahakama, sasa nakuomba Mheshimiwa Mangungu badala ya kuongea jenga hiyo hoja kimaandishi.
Mheshimiwa Spika, tunajenga vilevile Mahakama za Wilaya 20 na tunajenga Mahakama Kuu mpya mbili katika mikoa ya Mara na Kigoma na vilevile Mahakama za Hakimu Mkazi tunajenga saba, tano katika mikoa hii mipya na mahakama nyingine mbili katika mikoa ya Ruvuma na Lindi.
Mheshimiwa Spika, la pili; Mheshimiwa Mangungu anasema mahakama yake haina choo, hilo ungelisema hata bila hapa mbele ya Bunge ningeweza tu kukusaidia naomba tuonane baadaye, ni vitu vidogo sana kuviongelea hapa. Ahsante sana.
MHE. OTHMAN OMAR HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, iwapo itatokea kiongozi wa Umma atazungumzia masuala ya kisiasa ndani ya nyumba ya ibada; je, ni kifungu gani cha katiba au sheria kinachoweza kumtia hatiani kiongozi huyu? (Makofi)
Swali la pili, iwapo katika matamshi yake aliyoyazungumza katika nyumba hiyo inakwaza jamii moja katika Jamhuri yetu ya Muungano wa Tanzania.
Je, ni adhabu gani amestahiki Kiongozi kama huyu? (Makofi/Kicheko)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilishaeleza katika jibu langu la swali la msingi kwamba mtu yeyote ambaye atafanya kinyume na ambacho Katiba inaelekeza na vilevile sheria, atakuwa amefanya makosa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nisisitize tu hapa kwamba, Katiba ya nchi ndiyo inayozaa sheria. Kwa hiyo, siyo siyo tu mtu, hata chama cha siasa ambacho kinaendekeza masuala ya kidini nacho kinakuwa kimekosea, lakini siyo suala la mtu mmoja kuamua kuwa umekosea, kuna utaratibu wa kuweza kulifikisha hilo suala mbele ya Msajili wa Vyama vya Siasa na hatua za kisheria kuweza kuchukuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo hivyo kwa viongozi wa Kiserikali, anaingia kwenye Kanisa au Msikitini, siyo Serikali iweze yenyewe kuwa kila sehemu, lakini ijengwe hoja na wananchi ambao wamefika pale na huko ndiko kulinda utawala wa sheria katika nchi yetu. (Makofi)
MHE. FATMA HASSAN TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa Serikali imeshakamilisha hatua za kuwasilisha muswada huu, je, ni lini muswada huu utawasilishwa Bungeni?
Swali la pili, je, Serikali ina mpango wowote wa kuandaa mtaala wa Wasaidizi wa Kisheria ili wote waweze kupata mafunzo kulingana na mtaala huo? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Fatma Toufiq kwa maswali yanayogusa wananchi wa kawaida na hili suala kwa kweli hata sisi kama Wizara tunaona ni muhimu na ndiyo maana tumelifuatilia kwa karibu na Serikali imeridhia tuweze kuja na muswada huo ambao utajadiliwa na Bunge.
Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge baada ya taratibu kukamilika, muswada huu hautakuja moja kwa moja Bungeni hapa lakini utapitia katika Kamati, pia tutakuwa na mjadala wa muda mrefu kabla ya kuja na text ambayo Waheshimiwa Wabunge mtakuja kuijadili.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba maandalizi ya kutosha tumeyafanya, kwa mfano, sasa hivi tuna mitaala kabisa iliyowekwa kwa ajili ya kuwafundisha hawa Wasaidizi wa Sheria. Ni kazi kubwa imefanywa na Chama cha Wanasheria Tanganyika na ninaomba nimhakikishie tu kwamba tumejiandaa vizuri sana kubeba hili jukumu.
Tunasema hivyo kwa sababu Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaongelea kuhusu usawa mbele ya sheria. Tunaamini Muswada huu unatupeleka Watanzania karibu zaidi katika kukidhi mahitaji ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ili uwepo usawa wa kutosha kabisa mbele ya sheria.
MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri na kuipongeza Serikali kwa kuleta Muswada na Bunge lililopita Wabunge tukatunga sheria kali sana ambayo itawabana wale wote waliokuwa na tabia ya kuwaoa watoto. Ningependa kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni hivi karibuni Mahakama Kuu ya Tanzania iliiagiza Serikali iifanyie marekebisho Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971, kama kweli dhamira ni nzuri kama ambavyo Mheshimiwa Waziri ameeleza, ningependa kujua, ni kwa nini Serikali iliamua kukata rufaa badala ya kutekeleza maamuzi ya Mahakama? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa sheria nyingi sana ambazo zinawakandamiza wanawake na watoto, bado zipo katika nchi yetu ya Tanzania, zikiwepo hata sheria za kimila na nyingine na nyingine. Ningependa kujua sasa, Serikali ina mkakati gani na hasa Wizara ya Katiba na Sheria, kuhakikisha inaleta sheria zote kandamizi zinazowabana wanawake na watoto ili sheria hizi tuweze kuzifanyia marekebisho? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Amina Makilagi kwa kupigania haki za akinamama bila kuchoka, matunda ya juhudi zenu, wewe mwenyewe Mheshimiwa pamoja na wanawake wenzako yanaonekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kuhusu kesi iliyokuwepo Mahakamani na kwa nini Mwanasheria Mkuu wa Serikali imebidi akate rufani, nimeeleza katika jibu langu la msingi kwamba Serikali inaona tatizo katika Sheria ya Ndoa, si kwamba haioni tatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilichotupeleka Mahakama ya Rufani ni vitu viwili. Kwanza, Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, tayari iko katika mchakato chini ya Wizara yangu na utaratibu tunaoutumia tulidhani itakuwa vyema kwa mshikamano wa Taifa letu tukaendeleza majadiliano kama tulivyofanya wakati wa kuitunga hii sheria ya mwaka 1971. Sisi tunataka tu kupata busara za Mahakama ya Rufani kuhusu suala hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, haki ya kukata rufani si tu ya wananchi, lakini vilevile hata Serikali pale ambapo inaona kuna kitu ambacho kinahitaji kupewa msimamo madhubuti zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii anaweza akatokea Jaji mwingine wa Mahakama Kuu akatoa uamuzi tofauti kwa sababu wote wako katika maamuzi. Sasa tunachotafuta na anachotafuta Attorney General ni kupata sasa maamuzi kwenye Mahakama yetu ya juu katika nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, ni kweli kabisa bado kuna baadhi ya sheria zinamkandamiza mwanamke lakini naomba nimhakikishie Mheshimiwa Amina Makilagi na wanawake wenzake kwamba tumepiga hatua kubwa mno toka uhuru katika kuhakikisha kwamba mwanamke anapata haki sawa kama ambavyo Katiba yetu inavyosema chini ya Ibara ya 13.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukumbuke, tumefanya mabadiliko ya sheria nyingi, tukumbuke Sheria ya Ardhi namba Nne (4) na namba Tano (5) imeondoa kabisa ubaguzi uliokuwepo kwa mwanamke. Sasa hivi mwanamke ana haki sawa chini ya sheria hizo. Leo si kawaida tena kwa mume akatoka tu asubuhi akauza nyumba, akauza kiwanja bila kupata ridhaa ya mama na mama akienda Mahakamani hiyo sale ama mauzo hayo hayana maana kabisa. Leo hii akinamama talaka haitokei akaondoka hivi hivi lazima kugawana matrimonial property, hizo zote kwa kweli ni faida ambazo tumezipata katika mabadiliko mbalimbali ya sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii nenda Jela; wafungwa wengi wanaotumikia vifungo virefu katika nchi hii ni wale ambao wana makosa ya kunyanyasa akinamama. Namshukuru Mheshimiwa Makilagi ameelezea kuhusu sheria tuliyobadilisha juzi tu hapa Sheria ya Elimu ambapo leo hii mtoto wa kike aliye sekondari, aliye shule ya msingi, akipata mimba ole wako wewe uliyefanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, yote hii ni kulinda na baada ya muda si mrefu tutaleta Muswada hapa wa Huduma ya Msaada wa Sheria ambayo nakuhakikishia utakuwa mkombozi mkubwa hasa kwa akinamama walioko vijijini ambao katika mfumo tulionao usiojali mtu kutokujua sheria; kwamba ignorance of the law is not defence, akinamama wengi watafaidika sana. (Makofi)
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Katika imani ya dini ya Kiislam, suala la ndoa na mirathi ni jambo ambalo halina mjadala wala mbadala. Je, mabadiliko yote ya sheria yanatuhakikishiaje kwamba hayataingilia uhuru na imani katika dini ya Kiislam? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimjibu kwa kifupi sana Mheshimiwa Mbunge kwamba hii ndiyo sababu. Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali anakwenda Mahakama ya Rufani akidai si moja kwa moja, lakini kama nilivyowaeleza hapa kwamba mchakato tuliouanza Serikali wa majadiliano sisi Watanzania, maridhiano utumike badala ya sisi kuja na Muswada, wanaosema ndiyo, ndiyo tukapitisha sheria hapa, nadhani nimeeleweka na Mheshimiwa Mbunge.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na pia nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini pamoja na majibu hayo nina maswali madogo mawili ya nyongeza:-
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amenihakikishia kwamba Serikali imetenga fedha sasa kwa ajili ya kujenga Mahakama ya Wilaya katika Wilaya ya Chunya, je, ni lini Mheshimiwa Waziri atakuja Chunya ili nimwonyeshe viwanja vilivyo ambavyo Halmashauri imetenga kwa ajili ya kazi hiyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, Jimbo langu lina tarafa mbili, Tarafa ya Kiwanja na Tarafa ya Kipembawe. Tarafa ya Kiwanja ina Mahakama za Mwanzo mbili, moja iko Chunya, nyingine iko Makongorosi. Tarafa ya Kipembawe haina Mahakama ya Mwanzo hata moja. Sasa je, Serikali inasemaje kuhusu kuleta Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Wilaya ya Chunya ili Halmashauri iweze kumtengea eneo la kuweka Mahakama hiyo katika Tarafa ya Kipembawe?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimefarijika sana kumsikia Mheshimiwa Mbunge akisema viwanja tayari wanavyo na hivi majuzi tu nimetoka kujibu swali la Mbunge wa Temeke nadhani, nikielezea tu kwamba ni vizuri Wabunge sasa hivi mkahamasisha Halmashauri zenu kutuainishia viwanja ambavyo tayari vina hati iweze kuwa rahisi kwa Mahakama kuweza ku-identify maeneo hayo na kuweza kujenga maana pesa angalau sasa hivi tunayo ya kuweza kuanza ujenzi wa Mahakama za Mwanzo, Wilaya na hata Mahakama Kuu. Na tunashukuru kwamba kiwanja anacho Mheshimiwa Mwambalaswa, nitamfikishia ujumbe huu Mtendaji Mkuu wa Mahakama. Ningefurahi kama rai yake aliyoitoa hapa itafuatiwa na barua ili itiwe na kumbukumbu kabisa kwenye mafaili yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kuhusu Kipembawe kwamba hakuna Mahakama ya Mwanzo, ningemwomba, hiki ndiyo kipindi ambacho Mahakama inaangalia priorities tuanzie wapi katika kujenga jumla ya Mahakama 50 za mwanzo. Tafadhali tunaomba alete andiko la hayo mahitaji yawekwe pia kwenye file tuweze kuliangalia pamoja na mambo mengine.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika nakushukuru kwa kunipa nafasi, nina swali moja la nyongeza. Tatizo la ukosefu wa Mahakama katika Wilaya ya Chunya ni sawasawa na tatizo llililopo katika Mahakama ya Herujuu. Jengo lililokuwepo la tangu enzi za ukoloni limebomoka kabisa hivyo huduma ya Mahakama wanakaa chini ya miti. Je, ni lini Serikali itatoa pesa kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama ya Herujuu?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikiri mbele yenu kwamba hali ya miundombinu ya Mahakama nchini si nzuri. Nikielekeza macho tu, upande wa Mahakama za Mwanzo tunahitaji ili tuwe na access to justice sawasawa tuwe na Mahakama za Mwanzo katika kila Kata. Tuna kata zaidi ya 3,900 nchini lakini Mahakama tulizojenga mpaka sasa hazizidi 900, kwa hiyo pengo ni kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Josephine Genzabuke, kuhusu mahitaji halisi katika eneo lake, tunaomba atuandikie hiki ndiyo kipindi ambacho tunaangalia mahitaji kufuatana na demand iliyopo katika maeneo yote tuliyonayo. Kwa hiyo tunasubiri ndani ya siku mbili, tatu atatufikishia hayo mahitaji ya jimbo lake.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kutuahidi kwamba mwaka wa fedha 2017/2018 tutaanza kujengewa mahakama, lakini cha pili nimhakikishie kwamba kiwanja atapata, kiwanja kipo. Sasa naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu wananchi wa Mkalama wanapata adha kubwa na wanakwenda kilometa zaidi ya 100 kupata huduma hiyo Kiomboi, katika kipindi hiki cha mpito haoni umuhimu wa kuanzisha mahakama ya Wilaya ya mpito kwa maana kwamba hiyo mahakama ya Wilaya iliyopo inaweza kuhamishiwa katika mahakama iliyopo Gumanga au Iyambi, takribani kilometa 15, ambazo kilometa 15 ni ndani ya kilometa zinazokubalika ili wananchi waanze kupata huduma hiyo wakati wakisubiri hilo jengo jipya na la kisasa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Waziri atakuwa tayari kutembelea Wilaya ya Mkalama katika kipindi hiki cha Bunge, maana tukitawanyika hapa tunakuwa hatuonani tena, ili aweze kujionea uhitaji wa Mahakama ya Wilaya na aone viwanja vilivyopo kwa wingi na huduma nyingine za Mahakama za Mwanzo?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nianze na suala la kutembelea MkaLama, Mheshimiwa Kiula nakuhakikishia mkipata kiwanja, kama unavyosema mmepata, lakini chenye nyaraka zote, hata kesho mimi nakuja na nitajitahidi nije na viongozi wa Mahakama kuwathibitishia wananchi kuwa tumedhamiria kuwamalizia tatizo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, naelewa pressure aliyonayo Mheshimiwa Kiula kuwapunguzia adha wananchi wa Wilaya mpya ya Mkalama. Namuomba Mheshimiwa avute subira, hiyo mikakati ya mpito haitakuwa na tija sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili yasijitokeze maswali mengine ya nyongeza, nimeona Wabunge wengi wamesimama, naomba niwatulize Waheshimiwa Wabunge wote kuwa katika mwaka huu wa fedha Mfuko wa Mahakama umetengewa jumla ya shilingi bilioni 46.76 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo, lakini katika fedha hiyo ujenzi wa mahakama ni shilingi bilioni 36; kwa hiyo ukiunganisha na pesa tuliyokuwa nayo mwaka 2015/2016 ya shilingi bilioni 12.3 tuna shilingi bilioni 48.3 kwa ujenzi wa mahakama. Fedha hizi zitatumika kujenga mahakama 40 nchini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya ujenzi kwa mwaka 2015/2016 na 2016/2017 kwa fedha hii niliyoitamka itakuwa kama ifuatavyo ili Waheshimiwa Wabunge msisumbuke kusimama tena. Tunajenga Mahakama Kuu mpya nne katika Mikoa ya Mara, Kigoma, Dar es Salaam na Arusha.
Tunajenga Mahakama za Mikoa sita za Hakimu Mkazi, katika Mikoa ya Simiyu, Geita, Katavi, Njombe, Songwe na Lindi. Makakama za Wilaya tunajenga 14 ambazo ni Bunda, Kilindi, Bukombe, Chato, Makete, Ruangwa, Kondoa, Kasulu, Nkasi, Sikonge, Chamwino, Namtumbo, Nyasa na Hanang. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama za Mwanzo vilevile tunajenga mpya 16, tena katika kipindi kifupi. Tunajenga Mwanga, Makuyuni (Arusha), Ludewa Mjini, Longido, Lukuledi (Mtwara), Gairo (Morogoro), Nangaka (Nanyumbu), Makongorosi sasa hivi iko Mbeya, Ulyankulu (Tabora), Sangabuye (Nyamagana), Telati (Simanjiro), Mtowisa (Sumbawanga), Uyole (Mbeya), Kibaya (Kiteto), Mgandu (Wanging‟ombe) na Chanika (Dar es Salaam). (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie tu kwamba katika ujenzi wa mahakama hizi, Mahakama kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Ardhi na Baraza la Taifa la Ujenzi watatumia ujenzi wa gharama nafuu, lakini majengo yatakuwa bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetumia teknolojia hii mpya kujenga Mahakama ya Wilaya ya Kibaha ambayo wengi mmeiona tena kwa gharama ndogo ya asilimia 40 chini ya bei ya kawaida ya hizi conventional methods tena kwa kipindi kifupi cha miezi mitatu tu na kwa kiwango kikubwa cha ubora wa jengo.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hali ya Wilaya ya Tarime kule Rorya inafahamika, kesi ni nyingi na zinachukua muda mrefu kuamuliwa na hivyo, kuwatia hasira watu wa Rorya, kama ambavyo tunajua.
Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuongeza watumishi wengi zaidi ili kesi ziende haraka? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa matatizo yaliyoko Rorya yanafanana kabisa na yaliyoko Kilolo na kwa kuwa Kilolo ni Wilaya ambayo imeanzishwa toka mwaka 2000, lakini haina Mahakama yoyote.
Je, Serikali sasa haioni ni wakati muafaka wa kuanzisha Mahakama ya Wilaya kwa kuwa kesi nyingi za Wilaya ya Kilolo mnajua hasira zao huwa zinaishia wapi ili waanzishe haraka?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, nakubaliana kabisa na Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna umuhimu wa kuongeza watumishi katika mahakama zetu mbalimbali ili kesi ziweze kwenda haraka. Pia niweze tu kutoa tahadhali vilevile kwamba hata kama kuna watumishi wapo wa kutosha, bado kesi ambazo zinachukuwa muda mrefu ni kesi za jinai ambazo zinahitaji kwa kweli uangalifu wa kutosha hasa upande wa upelelezi na vilevile katika kuchambua ushahidi ambao unajitokeza.
Mheshimiwa Spika, naomba tu kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa upande wa mahakama tutajitahidi kuongeza watumishi kama nilivyosema kwa upende wa Wilaya hiyo ya Rorya na tutajitahidi vilevile kuharakisha usikilizaji wa kesi nchini. Nimpe tu taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba mahakama imejipanga kwamba, baada ya mwezi Disemba mwaka huu, kuanzia mwaka kesho Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu zitahakikisha hazina kesi za zamani zilizozidi umri wa miezi 24 yaani miaka miwili. Vilevile Mahakama za Wilaya na Mahakama ya Hakimu Mkazi hazitazidi mwaka mmoja na Mahakama za Mwanzo hazitakuwa na kesi za zamani za miezi sita.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kwamba Kilolo haina Mahakama ya Wilaya, namuomba sana Mheshimiwa Mbunge, hizo Wilaya tunazihitaji, lakini ujenge na hoja tuletee kwa maandishi, vilevile tuhakikishie una eneo lenye nyaraka stahili tuweze kuingiza katika mpango wa ujenzi wa mwaka ujao wa fedha.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri aliahidi kuja kufanya ziara katika Mkoa wa Mara na hususan Wilaya ya Rorya, lakini kwa sababu zisizoweza kuzuilika alikomea Musoma.
Je, yuko tayari sasa baada ya Bunge hili kuambana na Mbunge wa Rorya ili kwenda kuona usumbufu wa wale wananchi wa Rorya?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, sijawahi kwa kweli kuahidi kwenda Wilaya ya Rorya, lakini ahadi yangu ipo palepale ya kuzuru Mkoa wa Mara mzima. Kutokana na tatizo hili kwamba Rorya kweli ina special conditions za kutembelea, naomba tu Mheshimiwa Mbunge ajenge hoja mimi nina muda wa kutosha wa kuweza kufika huko na tukakagua maeneo mbalimbali. Lakini ziara ya Mkoa wa Mara ipo palepale tutafuatana na Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, kwa sababu lengo letu kubwa ni kukagua vilevile Magereza Mkoani Mara.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Spika, kiukweli nasikitika kwa majibu ya Waziri wa Katiba na Sheria kuhusiana na umuhimu wa kuwa na Mahakama ya Wilaya katika Wilaya ya Rorya. Tangu Bunge la Kumi nakumbuka nikiwa Mbunge wa Viti Maalum nimekuwa nikiongelea suala zima la kupatikana kwa Mahakama ya Wilaya ya Rorya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kukiwa hakuna Mahakama Wilaya ya Rorya, Mahakama ya Wilaya ya Tarime inakuwa na kesi nyingi na ndiyo maana mwisho wa siku tunakuwa na mrundikano wa kesi ambazo hazifanyiwi uamuzi kwa muda muafaka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa sababu Rorya tayari wana ardhi na kwa sababu tumekuwa tukiongea umuhimu kuwa na Mahakama ya Wilaya ya Rorya tangu Bunge la Kumi, ni vegezo vipi ambavyo vilitumika kwa bajeti ya mwaka 2016/2017 wasipeleke Mahakama ya Wilaya Rorya wakaamua kupeleka sehemu nyingine Tanzania ikizingatiwa jiografia ya Wilaya Rorya ni kubwa, watu wanatoka mbali sana kuja Wilaya ya Tarime. Naomba kujua ni vigezo vipi vimetumika kwa Serikali isiweze kujenga Mahakama ya Wilaya ya Rorya mwaka huu wa fedha hadi waseme ni mwaka ujao wa fedha?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, nimetamka mbele ya Bunge lako Tukufu kwamba tuna tatizo kubwa la miundombinu ya mahakama, kuanzia Mahakama ya Mwanzo hadi Mahakama Kuu katika nchi yetu. Nimelieleza wazi hili na tatizo hili haliko Rorya tu!
Mheshimiwa Spika, nilimeshaeleza wakati ninajibu maswali ya Waheshimiwa Wabunge watatu katika Mikutano iliyopita kwamba ninalishukuru Bunge lako Tukufu limetupitishia shilingi bilioni 46.76 kwenye Mfuko wa Mahakama na hizo shilingi bilioni 46.76, tutatumia shilingi bilioni 36 kujengea mahakama hii haijapata kutokea. Vilevile, tuna fedha ambayo mapema mwaka huu, mnakumbuka Mheshimiwa Rais aliagiza wapewe zote mahakama shilingi bilioni 12.3 jumla ni bilioni 48.3.
Mheshimiwa Spika, tumesema tunaanza kwa ujenzi wa mahakama 40 katika mwaka huu wa fedha, ninaomba utuamini kwa sababu mahakama sasa hivi imeshaanza ujenzi wa kisasa wa mahakama tena nafuu, lakini ujenzi uliyo bora kwa miezi mitatu anapata mahakama ya kisasa kama tulivyofanya mahakama ya Wilaya ya Kibaha.
Namuomba Mheshimiwa Mbunge avumilie tu, tumeipanga Rorya katika mwaka wa fedha 2017/2018, wavumilie kama Wilaya zingine zinavyovumilia kwa sasa.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri.
Mheshimiwa Spika, kwa kweli katika Mkoa wetu wa Iringa tatizo hili limekuwa kubwa sana. Kwa mwaka 2016 tu zimeripotiwa karibu kesi 221 na kesi zilizopo Mahakamani zilizofikishwa ni 37 tu. Kwa kuwa kumekuwa na ukiritimba mkubwa sana wa kushughulikia hizi kesi, sasa kutokana na ukubwa wa tatizo hilo ni kwa nini Serikali isianzishe Mahakama Maalum ya kushughulikia kesi hizi yaani Sexual Offence Court kama wenzetu South Africa?
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa suala hili ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu kama ilivyo Mahakama ya Mafisadi, Mahakama ya Ardhi. Kama jambo hili ni gumu ni kwa nini kesi hizi zisipewe kipaumbele kama kesi za watu wenye ualbino? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa, hili tatizo kwa kweli limekuwa likiwaathiri sana watoto wanaobakwa, wazazi, hata sisi viongozi. Na kesi hizi zimekuwa zikichukua muda mrefu sana na kuathiri ushahidi mzima na mbaya zaidi hawa wenzetu wabakaji wamekuwa wakitumia wanasheria wanapopelekwa mahakamani, lakini hawa wenzetu ambao wamekuwa wakipata hizi kesi wamekuwa hawana uwezo, wengi hawana uwezo wa kuwatumia wanasheria.
Ni kwa nini, Serikali isiweke utaratibu wa kuwapatia msaada wa kisheria waathirika wa tatizo hili, badala ya kutegemea NGO ambazo nyingi haziko huko vijijini?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nikiri kabisa kwamba kuna tatizo kubwa siyo tu Iringa, lakini na sehemu zingine za Tanzania. Jana na juzi nilikuwa Mkoani Iringa kujiridhisha mimi mwenyewe kuhusu hali hiyo, nimefika mpaka magerezani.
Mheshimiwa Spika, kwa kweli kwa takwimu Kitaifa kwa miaka miwili mitatu iliyopita ni kwamba, kila siku ya Mungu kuna matukio 19 ya kubaka na kulawiti hapa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, tatizo kubwa la matendo haya kwa upande wa Iringa ni kwamba yanatokea katika familia na ndugu, lakini familia hizo tunapopeleka kesi mahakamani ama tunapochunguza wanalindana, hawatoi ushirikiano kwa vyombo vyetu vya upelelezi ndiyo maana kesi nyingi zinachelewa. Hata tukianzisha mahakama hiyo ya Sexual Offences Court or whatever, bado hiyo mahakama itakwama kwa sababu wananchi hawajapata uelewa kwamba, wanavyolindana ndivyo wanazidi kuchochea hayo makosa.
Mheshimiwa Spika, namuomba Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote kutoka Mkoa wa Iringa akiwemo Mheshimiwa Msigwa na wengine, naomba tuendeshe kampeni kwa pamoja kuwaomba wananchi wetu, wapiga kura wetu, waachane na mchezo huu wa kulindana katika makosa haya. Otherwise Iringa baada ya muda si mrefu tutakuwa na idadi kubwa ya vijana waliokwishaharibika.
Mheshimiwa Spika, suala la kutoa msaada kwa waathirika hilo liko wazi na leo hii akisoma Mheshimiwa Mbunge Order Paper, nawasilisha hapa Muswada wa Msaada wa Kisheria. Sheria hiyo, nawahakikishia wananchi utawasaidia sana Watanzania, siyo tu waathirika wa vitendo hivi, lakini vilevile wajane, wanawake wanaonyanyaswa wakati wa mirathi, katika ndoa, katika talaka na kadhalika ili tuweze kukidhi matakwa ya Ibara ya 13 ya Katiba ya usawa kwa kila mtu mbele ya sheria. Ahsante.
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti tarehe 12 Januari, 2017 nilifika kwenye Gereza la Babati nikakuta watuhumiwa wa kesi ya mauaji na dawa za kulevya wamekaa zaidi ya miaka minne na sheria haijaweka time frame, hizo siku 60 ni kwa makosa ya kawaida. Mheshimiwa Waziri tuambie ni lini mtafanya marekebsho ya sheria ili hata kwa makosa haya ya mauaji na dawa za kulevya watu wasikae magerezani au mahabusu kwa muda mrefu kama ilivyo sasa?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kuna baadhi ya makosa na hata makosa mengine yanawafanya Watanzania wengi walioko magerezani kukaa huko kwa muda mrefu. Lakini swali hili lilikuwa linauliza tunachukua hatua zipi? Naomba kumuelezea Mheshimiwa Mbunge hatua ambazo Serikali imezichukua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, sasa hivi tunaangalia njia za kuboresha mifumo yetu ya adhabu mbadala ambayo mnafikiri wote Waheshimiwa Wabunge mnajua mmepitisha sheria nyie wenyewe hapa ya Parole, kuna suala la community service na vilevile kuna kitu kinaitwa extra mural penal employment, lakini vilevile ipo haja na hili ni suala pia linawahusu Waheshimiwa Wabunge tukiwaletea bajeti hapa kuongeza vikao vya Mahakama Kuu ambayo Mahakama Kuu ndiyo pekee inakaa kufanya sessions kwa ajili ya murder cases na wafungwa wengi kwa kweli, mahabusu wengi tunawakuta magerezani wa murder cases kwa kweli vikao vya mahakama ni vichache, inabidi tuongeze hiyo frequency.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile tatu, kuna tatizo sasa siyo tu kwa wale wanao-face murder cases hata kwa watuhumiwa wengine kwamba kuna tatizo la ucheleweshaji wa hukumu za mahakama na mwenendo wa mashitaka ambao unawafanya watuhumiwa waweze kwenda mahakamani au wafungwa au mahabusu kwenda mahakamani kudai haki zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe wito sasa hivi kwa mahakama ku-adhere, kuheshimu au kufuata, kutekeleza waraka namba moja wa mwaka jana wa Jaji Mkuu unaotaka mashauri yote na mwenendo wake unapokwisha ichukue siku 21 tu kila kitu kiweze kupatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala la mrundikano wa kesi mahakamani na watu kukaa ndani tumelifanyia kazi kubwa mno na tukiangalia record ya nchi hii miaka mitatu iliyopita tulikuwa na mrundikano wa kesi zaidi ya asilimia 60 za zamani, lakini leo mrundikano wa kesi umebakia ni asilimia 5.8 hivi na ambao ni kesi hizo za jinai kama alizoziongelea Mheshimiwa Gekul.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ni muda mrefu sasa wananchi wa Wilaya ya Lushoto hawapati mawasiliano hasa ya redio ya Taifa na hili swali nimekuwa nikiliuliza mara kwa mara.
Je, ni lini Serikali itajenga mitambo hiyo ili wananchi wa Wilaya ya Lushoto waweze kupata taarifa kama ilivyokuwa kwa wananchi wengine waishio mjini?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu kumuomba Mheshimiwa Mbunge awe na subira swali linalokuja linaongelea masuala ya usikivu wa redio katika nchi ya Tanzania.
MHE. GRACE S. KIWELU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Timu yetu ya Serengeti imeendelea kufanya vizuri huko ilipo, ningependa kujua Serikali imetenga kiasi gani, kwa ajili ya kuisaidia timu yetu hii ili iweze kufanya vizuri na kurudi na kombe hapa nchini? (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwanza kwa kumpongeza sana Naibu Waziri kwa kujibu maswali vizuri sana. Ninataka tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba timu hii ya Serengeti haijaibuka tu, tumeanza nayo miaka mitatu iliyopita, kwa kushindanisha vijana wa chini ya umri wa miaka kumi na tano, tukapata timu bora, tumeilea hiyo timu na kuhakikisha kwamba inashiriki kwenye mashindano ya kimataifa kabla ya hizi mechi 22 ambayo haijapata kutokea toka historia ya nchi hii, yote hii huu ni uwezeshaji na uwekezaji wa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka nisisitize kwamba figure kamili yaani ni kiasi gani tumetumia kama Serikali tutaiandaa tumpe Mheshimiwa Mbunge, lakini Serikali imejitoa kwa hali na mali kuhakikisha kwamba timu hii inatuletea ushindi katika mashindano haya. (Makofi)
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake, naomba kuuliza maswali tu madogo ya nyongeza.
Swali la kwanza, kwa kuwa jibu katika swali langu la msingi linakiri kuwa kumbukumbu na hukumu katika Mahakama za Wilaya hadi Mahakama ya Rufani ni kwa Kiingereza. Je, Serikali haioni kuwa kumbukumbu na hukumu katika lugha ya kigeni yaani Kiingereza ni kikwazo kikubwa kwa mwananchi anayetaka kukata rufaa kwa kupata haki yake?
Swali la pili, kwa kuwa kauli mbiu ya Serikali ni haki sawa kwa wote na kwa wakati, lakini tumekuwa tukishuhudia Mahakama zikijitahidi kumaliza kesi zake, lakini hukumu zinakuwa zinapatikana kwa kuchelewa sana, hali inayopelekea wengine kutokukata rufaa kwa wakati na walioko gerezani kuendelea kuteseka gerezani.
Je, Serikali inatoa kauli gani? (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba kukubaliana na Mheshimiwa Ritta Kabati kwamba ana hoja ya msingi, lakini nikumbushe tu Waheshimiwa Wabunge wote kwamba tuliamua mwaka 1964 kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya Taifa, vilevile Kiingereza kuwa lugha ambayo tunaitumia katika shughuli za Serikali. Ni kama Mheshimiwa Baba wa Taifa alivyosema kwamba Kiingereza ndiyo Kiswahili cha dunia.
Kutoka 1964 mpaka sasa tumeweza kufanya maandalizi ya kutosha kuhakikisha kwamba tunakiingiza Kiswahili katika mfumo wa Mahakama bila kupotosha utoaji haki.
Mheshimiwa Spika, kwanza ni suala la utumiaji wa Kiswahili kwa kumbukumbu, kwa hukumu, kwa uendeshaji katika Mahakama za Mwanzo ambao umefanikiwa sana. Hatujaona kabisa miscarriage of justice pale.
Mheshimiwa Spika, pili Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) ambayo mwanzoni ilikuwa inaitwa TUKI (Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili) chini ya Profesa Mlacha, iliweza kushirikisha Baraza la Kiswahili la Tanzania pamoja na Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wa Sheria, nilikuwepo mimi pamoja na Marehemu Profesa Joan Mwaikyusa, Mungu aiweke roho yake pema, peponi, tukaweza kutoa Kamusi ya kwanza ya Kiswahili ya Kisheria, yote haya ni maandalizi.
Mheshimiwa Spika, tatu, kila Muswada wa Sheria leo hii ukiletwa hapa Bungeni na sheria zenyewe, lazima ije kwa Kiingereza na Kiswahili na hilo wewe mwenyewe umekuwa ukisisitiza sana.
Mwisho BAKITA imeshakusanya sasa hivi Istilahi zaidi ya 200 za kisheria ambazo zinasubiri tu kusanifishwa (standardize). Kwa msingi huo, Mahakama yetu ambayo ni chombo huru katika Katiba yetu ni Muhimili unaojitegemea, una msingi sawa wa kutosha tuweze kupanua wigo wa matumizi ya Kiswahili katika kumbukumbu na hata kutoa hukumu hata kwenda Mahakama za Wilaya na Mahakama za Hakimu Mkazi kwa kuanzia.
Mheshimiwa Spika, nimwambie tu Mheshimiwa Kabati kwamba tunachoepusha hapa ni kukurupuka tu kuingia na kutumia Kiswahili ilikuwa tu ni kuepusha utata katika nyaraka zetu, ambiguities na kuwa equivocal, kuwa na utata katika utafsiri nyaraka za Kimahakama, ndiyo maana tumekwenda polepole sana.
Mheshimiwa Spika, suala la pili, nakubaliana naye kwa kweli haki iliyocheleweshwa ni haki iliyonyimwa, lakini ni kweli vilevile kuwa haki iliyowahishwa sana mara nyingi hukosa umakini. Kesi nyingi zinachelewa hasa za jinai kumalizika si kwa sababu ya Mahakama lakini kutokana na mchakato mzima wa utoaji haki. Kwa mfano, suala la upelelezi huchukua muda mrefu sana, na inachukua muda mrefu si kwa sababu vyombo vyetu vya dola havifanyi kazi, lakini kuna tatizo la kutopata ushirikiano mzuri kwa mashahidi mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, Iringa anakotoka Mheshimiwa Kabati, tuna kesi nyingi sana, sana za makosa ya kujamiiana na yanatokea ndani ya familia, kupata ushahidi mle ndani ni kazi kubwa kweli na ndiyo maana tunatoa wito kwa wananchi wote kushirikiana na vyombo vya dola pale inapotokea kosa, kusaidia katika ushahidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la kwamba, uthibitisho wa makosa mengine unahitaji Mkemia Mkuu achunguze na atoe jibu, inachukua muda mrefu, Mkemia Mkuu anaweza kuwa na mafaili 3000 ya uchunguzi na yote yanahitaji kwenda Mahakamani, kwa hiyo kazi ni kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na la mwisho ni uhitaji wa kisheria kwamba kila kosa lazima lithibitishwe beyond reasonable doubt yaani pasipo na wasiwasi wowote. Sasa hiyo hatuwezi kulikwepa ili kuweza kulinda haki za kila mtu.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwenye Kijiji cha Mnara, Kata ya Mnara, Tarafa ya Rondo Jimboni Mtama kwa kupindi cha miaka mitatu sasa imepita tumekamilisha jengo zuri la kisasa la Mahakama, lakini kwa kipindi chote hicho Serikali imekuwa kwa namna moja ama nyingine pengine inapiga chenga kufungua na kuruhusu jengo hili litumike.
Mheshimiwa Spika, Mbunge aliyepita alisaidia ujenzi, ameomba Serikali tulifungue, lakini mpaka leo Serikali haijafungua. Sasa ni lini Mheshimiwa Waziri Serikali itaruhusu jengo hili litumike ili haki itendeke kwa watu wangu hawa kupata huduma karibu na maeneo yao.
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana yeye pamoja na wananchi wa Jimbo lake kwa kupata jengo la Mahakama zuri, lakini mimi mwenyewe nasikitika kwamba mpaka sasa halijaweza kuzinduliwa.
Naomba nitoe ahadi kwamba tutakapotoka tu hapa, tena nataka niwe mbele yake, nitampigia Mtendaji Mkuu wa Mahakama, tuhakikishe kweli hili jengo linaanza kutumika. Kwa sababu huko ndiko kusogeza huduma za Mahakama kwa wananchi. (Makofi)
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niulize maswali madogo tu mawili ya nyongeza.
Kwanza nikushukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yako, ningependa kujua tofauti kati ya hizi Mahakama za kawaida na Mahakama za Coroner?
Swali la pili, kwa kuwa hata katika Mkoa wetu wa Iringa, vipo vifo ambavyo huwa vinatokea vyenye utata; je, ni vifo vingapi ambavyo vilipelekea kuundwa hii Mahakama ya Coroner?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ipo tofauti kati ya Mahakama ya Coroner na Mahakama za kawaida za Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya.
Kwanza kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, Mahakama ya Coroner kazi yake kubwa ni kupata chanzo cha kifo ambacho kimetokea na kina utata, kujua chanzo chake ni nini. Kwa hiyo, hiyo ndiyo kazi kubwa Mahakama ya Uchunguzi inafanywa ikiongozwa na Coroner na ndipo hapo unakuta atatumia madaktari, ma-pathologist, forensic experts, criminologist waweze kumsaidia kujua chanzo cha hicho kifo ni nini.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa upande wa Mahakama za Hakimu Mkazi, Mahakama ya Wilaya, wao wanakwenda mbele zaidi, wakishapata tukio kwamba limetokea wao sasa wanaangalia vilevile dhamira ya yule aliyetenda hilo kosa.
Mheshimiwa Naibu Spika, wewe mwenyewe ni Mwanasheria na kwa Waheshimiwa Wabunge ambao ni Wanasheria pia wataelewa lakini naomba nieleze tu kwamba Mahakama za Hakimu Mkazi, wao wanaongozwa na Kanuni ya Sheria inayosema tendo pekee halitoshi kuweza kumhukumu mtu, lazima liendane na dhamira ovu ya yule aliyetenda, yaani the act alone haitoshi it must be accompanied by blameworthy state of mind na kwa kilatini mnakumbuka mliosoma sheria „actus non facit reum nisi mens sit rea; kitendo pekee hakitoshi. Kwa hiyo, Mahakama ya Hakimu Mkazi kazi yake ni kuangalia kitendo kiendane vievile na dhamira ovu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kuhusu swali la pili la matukio yaliyotokea na kwa nini iliundwa hiyo Mahakama. Mheshimiwa naomba tu nikiri kwamba naliona tatizo la elimu kwa umma hapa, kwamba haijatosha na ndiyo maana pengine huduma hii ya Coroner naona Watanzania wengi hawajaielewa sana. Hili naliona ni tatizo ambalo Wizara yangu sasa nafikiri tutalikazania sana katika kipindi hiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba mashauri yanayopelekwa kwa Coroner au kwenye Mahakama hizi yapo, nakumbuka shauri moja ambalo mimi mwenyewe nilihusika ni Shauri Na. 152 la mwaka 2003, lilitokea Mbeya ambapo Mahakama ya Hakimu Mkazi ilikaa chini ya Coroner ya kuweza kupata ufumbuzi wa kitu kilichotokea katika Kituo cha Polisi na matokeo yake yalikuwa mazuri. Ndiyo maana nimesema kwa kweli ni wajibu wa Wizara hii sasa kuuelewesha umma vizuri zaidi kuhusu huduma hii ambayo ipo na hata muuliza swali wa kwanza alidhani kwamba hii mahakama haipo ni huduma ambayo tunafikiria kuianzisha.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu TBC 1 na TBC Redio ni visemeo vya Taifa, ndiyo spika ya Serikali. Je, kwa sababu matatizo ni mengi, usikivu karibu nchi nzima hawasikii vizuri, Je, Mheshimiwa Waziri hivi unatambua kwamba TBC1 na Redio TBC 1, televisheni ni kisemeo cha Taifa. Kwa nini sasa Serikali isiwekeze ili kuondoa kutokusikia vizuri katika maeneo mbalimbali?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Seneta Ndassa kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa TBC katika nchi hii na ndiyo maana umeona uwekezaji ukiongezeka kila mwaka. Sasa hivi tupo katika kuboresha usikivu katika Wilaya tano kwa pesa tuliyoongezewa tuna uwezo kuongeza usikivu katika Wilaya zingine 15. Kwa hiyo, tunapoongeza hizo Wilaya 15 tunaenda kuangalia sehemu ipi ambayo ina hali mbaya zaidi tutaendelea kuboresha hii bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa na matatizo ya kifedha, sasa hivi tumeanza kuangalia pia mifumo yetu ya ndani ambayo imekuwa ikitunyima kupata kipato zaidi. Tuna mikataba ambayo mmekuwa mkiipigia kelele hapa kama StarTimes, tumeanza kuchunguza, ninakuhakikishia kwamba katika zoezi tunalolifanya sasa hivi kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais tutafika mahali pazuri. Kwa taarifa tu kwa Bunge hili lako Tukufu Mheshimiwa Rais wa StarTimes Group kutoka China imebidi naye afunge safari kama mwenzetu wa makinikia kuja kutuona kwa ajili ya suala hilo.
MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na matatizo ya usikivu pia TBC kuna matatizo ya weledi kwa watangazaji. Mfano, kuna watangazaji wa TBC walitangaza uongo kwamba Donald Trump alimpongeza President Magufuli, upambe uliopitiliza mpaka tajiri anashtuka. Sasa wale watu walisimamishwa lakini hivi karibuni nimeanza kuwaona kwenye tv. Walipewa adhabu gani ili wasirudie tena upambe? (Kicheko)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tulichukua hatua za kinidhamu kwa kosa ambalo ni la kiufundi tu ambalo mtu yeyote duniani hapa anaweza kulifanya. Yametokea matatizo kama hayo hayo Kenya yalifanyika na watangazaji wamerudi, tulichokifanya ni kuchukua tu hatua ya muda mfupi. Wazungu wanasema it’s a deterrent kwamba uwe muangalifu zaidi. Ni kitu kinafanyika kila siku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii nikikuletea, tuchukulie tu mfano wa magazeti yote yanayochapishwa kila siku, ninakuhakikishia asilimia 60 utakuta kuna matatizo/makosa ndani, ni kitu cha ubinadamu. Ahsante. (Makofi)
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda naomba usikilize vizuri kwa sababu ni kiwanda hicho. Kwa kuwa ligi bora duniani ni Uingereza na ndiyo ligi yenye wachezaji wengi wa kigeni kuliko ligi nyingine lakini timu ya Taifa ya Uingereza ni moja ya timu mbovu ambazo zinashindwa kufanya vizuri kwa kuwa ina wageni wengi. Ligi bora katika Afrika Mashariki ni Tanzania, lakini kwa kuwa inawachezaji wengi wa kigeni timu ya Taifa imeendelea kuwa kichwa cha mwendawazimu. Kwa kuwa mwaka 2000 wakati tukiwa hatuna wachezaji wengi wa kigeni timu yetu ilifikia rank ya kimataifa ya 65 na leo tumeongeza idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni tumefikia kwenye rank ya 139. Je, Serikali sasa haioni kwamba kuendelea kuruhusu wachezaji wengi wa kigeni ni kuua timu yetu ya Taifa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Kanuni za TTF ziko wazi ili timu ishiriki Ligi Kuu lazima iwe na kiwanja, ikate bima kwa ajili ya wachezaji wake na iwe na timu ya under 20 vyote hivyo vinakiukwa. Je, Serikali inasemaje kuhusiana na suala hili?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza siwezi kupingana naye kwamba ongezeko kubwa la wachezaji wa nje linaweza kuwa na athari kubwa kwa maendeleo ya soka ndani ya nchi. Katika jibu langu kwa swali la msingi nimesema kati ya mwaka 2010 mpaka 2015 tulikuwa tunaruhusu wachezaji watano wa nje na baadaye ndipo tumeruhusu wachezaji saba. Ukiangalia wenzetu Kenya wao walianza na saba na sasa hivi wanaruhusu watano.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini uzoefu tulioupata katika msimu huu ni kwamba tulikuwa na timu 16 kwenye Ligi Kuu na timu zote kikanuni zinaruhusiwa kusajili wachezaji 30 na kati ya hao saba wanaweza kuwa wanatoka nje. Wadau wanasema kwa kweli hii saba ni ukomo tu na mara nyingi ukomo huo hatuufikii.
Vilevile kwa nchi ambayo tayari imekubali professional football huo wigo wa saba siyo mbaya hata kidogo. Ni kweli timu zote hizo 16 zingesajili wachezaji saba kwa mfano tungekuwa na wachezaji wa kulipwa nchini 112 lakini mwaka huu ni wachezaji 35 tu ambao ni asilimia saba ya wachezaji wote. Kwa sababu timu 16 mara wachezaji 30 kama 480 kwa hiyo ni asilimia saba tu ndiyo ambao waliweza kuajiriwa kutoka nje. Kwa hiyo, ni ukomo tu na usitutie wasiwasi hata kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, timu zilizofanya vizuri sana katika ligi hii Mheshimiwa Mwamoto unaelewa zilikuwa hazina wachezaji kutoka nje. Chukulia timu ya Kagera Sugar ambayo ilikuwa ya tatu ilikuwa haina mchezaji kutoka nje, chukulia Mtibwa ilikuwa namba tano ilikuwa haina mchezaji yeyote kutoka nje. Vilevile mimi mwenyewe nimehusika katika utoaji zawadi kwa ajili ya wachezaji waliokuwepo kwenye Vodacom Premier League, wachezaji waliofunga magoli kwa kiwango cha juu na kupata zawadi walikuwa ni wawili mmoja kutoka Ruvu Shooting Stars (Abdulrahman) na mwingine kutoka Yanga (Msuva) wote ni Watanzania, hakuna mchezaji wa nje. Kwa hiyo, nimshawishi Mheshimiwa Mwamoto akubali tu kuwa na wigo wa wachezaji saba ila tu tusiongeze wakawa wachezaji kumi na kuendelea huko, lakini hii idadi inatosha kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, umeongelea kuhusu timu zinazoshiriki kwenye ligi yetu kuu kwamba zingine nadhani hazina vigezo kwa mfano kuwa na vijana wa under 20 na zingine hazina viwanja. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mwamoto kwamba timu zote zinazoshiriki Ligi Kuu sharti lao lazima ziwe na timu za vijana chini ya umri wa miaka 18 siyo under 20 actually. Kwa sababu hawa wanaosajiliwa 30 ni umri wa miaka 18 na kuendelea lakini lazima uwe na timu ya vijana ya miaka 18 ambapo tunaruhusu vijana watano kushiriki kwenye Ligi Kuu. Vilevile naomba tu baadaye aniambie ni timu gani ambayo haina kiwanja inachezea barabarani kufanya mazoezi.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru. Kwa kuwa Tanzania ina wachezaji wachache sana wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi na kwa kuwa vijana wetu wa Serengeti Boys Under 17 walionesha kiwango kikubwa sana. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwekeza kwa vijana hawa ili tuwe na wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba timu yetu ya Taifa ya Serengeti imefanya vizuri sana katika historia ya nchi yetu na naomba nimhakikishie Mheshimiwa Sima kwamba juhudi za Serikali sasa hivi ziko katika maeneo mawili. Moja ni kuhakikisha timu hii tunaendelea kuilea kwa sababu hawa ndiyo wawakilishi wetu katika michuano yetu ya olympiki mwaka 2020, kwa hiyo hatuwezi kuwaacha tunaendelea kuwalea kwa karibu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba nimhakikishie kwamba tuko kwenye mazungumzo na wadau mbalimbali, tumepata watu wengi nje ambao sasa hivi tunashirikiana kwa karibu kama Sport Pesa na timu ya Everton FC ambayo iko Premier League ya Uingereza ambao tuna mahusiano mazuri, tumeanza kuongelea kuhusu uwezekano wa kuweza kuchukua baadhi ya vijana wetu. Hayo ni mazungumzo bado hatujapata guarantee nisije nikasikia kesho magazeti yakesema sasa wanakwenda huko, tuko kwenye mazungumzo na tutaendelea kufanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nikuhakikishie Mheshimiwa Sima katika kipindi changu cha uongozi wa Wizara hii sitaruhusu kijana yeyote kwenye timu ya Serengeti achukuliwe na timu ambayo ina historia ya uchovu uchovu kiweledi hata kipesa na mimi mwenyewe nitasimamia katika kuangalia mikataba yao. Niwahakikishie tunawaangalia vijana wetu na wataendelea kutusaidia katika kuinua jina letu kwenye ulimwengu wa soka. (Makofi)
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu TBC 1 na TBC Redio ni visemeo vya Taifa, ndiyo spika ya Serikali. Je, kwa sababu matatizo ni mengi, usikivu karibu nchi nzima hawasikii vizuri, Je, Mheshimiwa Waziri hivi unatambua kwamba TBC1 na Redio TBC 1, televisheni ni kisemeo cha Taifa. Kwa nini sasa Serikali isiwekeze ili kuondoa kutokusikia vizuri katika maeneo mbalimbali?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Seneta Ndassa kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa TBC katika nchi hii na ndiyo maana umeona uwekezaji ukiongezeka kila mwaka. Sasa hivi tupo katika kuboresha usikivu katika Wilaya tano kwa pesa tuliyoongezewa tuna uwezo kuongeza usikivu katika Wilaya zingine 15. Kwa hiyo, tunapoongeza hizo Wilaya 15 tunaenda kuangalia sehemu ipi ambayo ina hali mbaya zaidi tutaendelea kuboresha hii bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa na matatizo ya kifedha, sasa hivi tumeanza kuangalia pia mifumo yetu ya ndani ambayo imekuwa ikitunyima kupata kipato zaidi. Tuna mikataba ambayo mmekuwa mkiipigia kelele hapa kama StarTimes, tumeanza kuchunguza, ninakuhakikishia kwamba katika zoezi tunalolifanya sasa hivi kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais tutafika mahali pazuri. Kwa taarifa tu kwa Bunge hili lako Tukufu Mheshimiwa Rais wa StarTimes Group kutoka China imebidi naye afunge safari kama mwenzetu wa makinikia kuja kutuona kwa ajili ya suala hilo.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kuna Kamati ya Maudhui, siku za karibuni tumekuwa tukishuhudia wasanii wetu wengi wakifungiwa nyimbo zao, wasanii ambao wamehangaika kutafuta pesa za kurekodi kwa shida na ukizingatia kuna uhaba wa ajira.
Je, Mheshimiwa Waziri anaweza akatuambia Kamati hiyo ya Maudhui imeshindwa kazi, kwa sababu wamekuwa wanaachia mpaka nyimbo zinatoka ndiyo wanakuja kuwafungia wasanii wetu? (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kila Taifa lina utamaduni wake na lazima liulinde kwa udi na uvumba. Tunachokifanya sio kwamba tuna vita na wasanii wetu, hapana! Lengo letu ni kulinda maadili ambayo katika kipindi hiki cha utandawazi na maendeleo ya kasi ya kiteknolojia na habari, kuna mmomonyoko mkubwa sana wa maadili katika nchi yetu ni lazima tuchukue hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunachokifanya hapa siyo kitu cha pekee duniani, kila mtu anafanya hivyo na hawa wasanii wetu tumeshawasamehe wasirudie tena. Nitoe mfano mmoja mdogo…
Mheshimiwa Naibu Spika, mwanamuziki Rick Ross ambaye amepiga muziki pamoja na kijana wetu nyota wa muziki Diamond hapa, wimbo wao huu wa wakawaka, huyo mwanamuziki miezi michache iliyopita amepata matatizo Marekani kwa kuimba wimbo unaoitwa U.O.E.N.O ambao maudhui yake yanaleta picha ya kwamba anaunga mkono ubakaji. Marekani nzima akina mama walikuja juu, wimbo ukaondolewa kwenye televisions zote, lakini na yule kijana akaomba radhi kwa wanawake wote kwamba amewaudhi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania tumekuwa kokoro, tupokee kila kitu, kwa sababu hatuna utamaduni. Baba wa Taifa alisema mwaka 1962, Taifa lisilo na utamaduni wake ni Taifa mfu nasi hatuwezi kukubali kuwa Taifa mfu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yanayotokea Tanzania yanatokea duniani kote. Nitoe tu maelezo kidogo, maana Viongozi wetu hapa wanalalamika ni kwa sababu dunia pana hawajaielewa. Davido mwanamuziki maarufu duniani ambaye amepiga na kijana wetu Diamond hapa kafungiwa nyimbo zake mbili na Nigerian Broadcasting Corporation mwaka huu. Siyo huyo tu, Wizkid kafungiwa nyimbo zake, Nine Eyes kafungiwa nyimbo zake, sijasikia Wabunge wa Nigeria wakilalamikia sheria zao wenyewe, sisi ni Wabunge kazi yetu kubwa ni kuhakikisha jamii inaheshimu, inalinda sheria za nchi na tutaendelea... (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano wa mwisho, Koffi Olomide amepiga wimbo unaitwa Ekotite, huu wimbo ni marufuku kupigwa Congo (DRC)…
Mheshimiwa Naibu Spika, ninawaomba Waheshimiwa Wabunge mnaosafiri kwenda Congo, unaambiwa tukupigie wimbo gani ukisema Ekotite watakushangaa! Huo wimbo ni matusi wameufungia. Sisi hapa Wabunge tunakuwa wa kwanza kuruhusu nchi yetu iwe kokoro.
Mheshimiwa Naibu Spika, BBC ambayo iko Uingereza ambako ndugu zangu wanadhani ndiko mwanzo wa ustaarabu, wamefungia nyimbo 237 katika historia yao, hapa tunalalamika nyimbo mbili kufungiwa. Tutaendelea kufungia kulinda utamaduni wa nchi yetu. Ahsante. (Makofi)
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana ushoga usagaji na kutukuna matusi mithili ya bomu la nyuklia siyo maadili yetu na desturi ya Mtanzania, lakini vitendo hivyo vimekithiri kartika mitandao yetu ya kijamii. Kwa mfano, wapo mashoga maarufu wanajitangaza katika mitandao yetu ya kijamii na siyo utamaduni wa Kitanzania; kwa mfano kuna mtu mmoja maarufu anaitwa James Delicious.
Mheshimiwa Spika, kuna vikundi vya matusi kabisa katika mitandao ya kijamii. Mfano kuna team Wema, team Zari, team Diamond, team Shilole, hawa wamekuwa wakitukana matusi katika mitandao ya kijamii.
Je, nini kauli ya Serikali kutokana na hili kwa sababu linachangia kwa kiwango kikubwa sana kuharibu maadili na utamaduni wa Kitanzania? (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Tulitunga Sheria ya EPOCA mwaka 2010 lakini tulikosa Kanuni za kuweza kubana hasa maudhui upande wa mitandao. Tumeshatunga hizo Kanuni na sasa hivi hizo Kanuni zimeanza kufanya kazi. Naomba nitoe taarifa kwa Waheshimiwa Wabunge kwamba kuna baadhi ya wasanii wetu ambao walianza kufanya uhuni uhuni ndani ya mitandao, jana tumeweza kumkamata mwanamuziki nyota Tanzania, Diamond tumemfikisha polisi na anahojiwa kutokana na picha alizozirusha. Vilevile imebidi hata Binti Nandy naye apelekwe polisi kuhojiwa. Tunaangalia namna ya kuwapeleka mahakamani.
Mheshimiwa Spika, naomba nitoe wito kwa vijana wote nchini, mitandao siyo kokoro la kupeleka uchafu wote ambao umezuiwa na sheria zingine. Hii nchi ina utamaduni wake. Tunahitaji kulinda kizazi cha leo, kesho na kesho kutwa cha Taifa hili. Ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru.
Mheshimiwa Spika, tunapozungumza mmomonyoko wa maadili kwa vijana mara nyingi tunazungumza habari ya vijana wasanii, wanaocheza filamu, wanamuziki na kadhalika. Lakini mmomonyoko pia mkubwa sana upo kwa vijana wa mitaani na hawa mara nying ni kwa sababu ya kukata tamaa.
Sasa naomba niiulize Serikali, pamoja na mifuko mbalimbali ya kuwaendeleza vijana, ni mkakati gani ambao Serikali inao ili kuwasaidia kisaikolojia na namna vilevile ya kuweza kuona matumaini katika maisha yao vijana waache kuingia kwenye tabia ambazo kwa kweli zinasababisha mmomonyoko mkubwa sana wa maadili? (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii na ninakushukuru kwa kujibu sehemu ya hilo swali kwamba huu ni wajibu wa jamii nzima. (Makofi). Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imekuja kwa nguvu sana na kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu ili Watanzania wathamini kazi. Kazi ndiyo ufunguo wa kila kitu ningeomba Watanzania wote tushirikiane kuhakikisha kwamba kila mtu Tanzania anafanya kazi, mambo ya njia za mpito kuweza kuishi hayana nafasi tena ndiyo yanayozua matatizo.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili wazazi tuna nafasi kubwa sana kuweza kubadilisha hii hali kwa upande wa watoto wetu tukiweka mbele suala la kazi kama tulivyokuwa tunafanya wakati wa uhuru ambapo tulikuwa tunasema uhuru ni kazi na leo ni hapa kazi tu. Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kwanza niungane na Mheshimiwa Dkt. Harrison Mwakyembe kwa kukubaliana naye kwamba suala la kubadilisha utaratibu wa mfumo wa maisha kwa vijana pamoja na kwamba ni suala la jamii kwa ujumla, lakini napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba pia kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu tumeandaa programu mbalimbali ambazo tunashirikiana na Halmashauri za Wilaya kuhakikisha Halmashauri zetu Idara za Vijana zinajipanga kutoa elimu ya kubadilisha mawazo na mtazamo kwa vijana ili kuwasaidia kujenga mtazamo mpya wa kujiajiri na kuondoka katika tabia za kupoteza muda kwenye vijiwe na kuingia kwenye shughuli ndogondogo za kuweza kujiajiri.
Mheshimiwa Spika, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge tusaidiane kwa pamoja na Halmashauri zetu, hasa wale vijana ambao wamekuwa wakipoteza muda mwingi kwenye vijiwe. Wageuze vijiwe vyao kuwa ni shughuli za kiuchumi badala ya kutumia vijiwe kuwa ni maeneo ya kupoteza muda. Mifuko ya kuwawezesha hao vijana kupitia Idara ya Vijana kwenye Halmashauri zetu ipo na Serikali tumeshajiandaa na Wabunge ambao wapo tayari tutafanya nao kazi hiyo kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi hii.
Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, lakini hapo utaona amesema kwamba muda mfupi ujao watakuwa wamekamilisha ukusanyaji wa maoni ya wadau.
Swali langu la kwanza, je, wadau ambao ni Waheshimiwa Wabunge na ambao ni wawakilishi wa wananchi mpaka sasa naona bado hatujashirikishwa, haoni kwamba kuliacha kundi kubwa kama hili kunaweza kukaweka matobo tena kwenye sera ambayo inarekebishwa?
Swali la pili, je, ni kwa kiasi Serikali itachukua wajibu hasa kuhakikisha kwamba michezo ya kubahatisha inakuwa sehemu katika sera hii mpya ili kutanua mfuko wa michezo na kuweza kutoa udhamini wa kutosha katika michezo ili hata hawa wanamichezo wasiwe wanajiandaa wenyewe na wakati wakileta sifa za Taifa tunazipokea kama nchi? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba rasimu ya sera imejadiliwa na wadau mbalimbali, lakini hatujaleta Bungeni na siyo kawaida. Kutokana na umuhimu wa Bunge hili na vilevile mchango ambao kwa kweli mara nyingi unakuwa umefanyiwa kazi na Waheshimiwa Wabunge tutaangalia uwezekano wa kabla ya kufikia mwisho tuweze kupata mawazo ya Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Spika, pili kuhusu michezo ya kubahatisha ni kweli kabisa katika sera tuliyonayo sasa hivi ya mwaka 1995, michezo ya kubahatisha siyo sehemu ya michezo na tumechukua hatua ya kuingia katika mabadiliko ya sheria mbalimbali ambayo yatawasilishwa leo Bungeni hapa tunafanya mabadiliko ya sheria hiyo ili michezo ya kubahatisha nayo iwe sehemu ya michezo na iweze kuchangia katika maendeleo ya michezo nchini.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, pamoja na sifa nyingi Mheshimiwa Waziri alizozimimina kwa bondia Hassani Mwakinyo, kama ulivyosema ni kwamba hajulikani, hata nchi ilikuwa haijui kama anapigana mpaka jana usiku baada ya kutoka matokeo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia katika Kombe la Dunia mchezaji mwingine kutoka Tanga alijitokeza akichezea timu ya Denmark tukabaki tunauma vidole tu, hatukujua kwamba mchezaji yule yupo na anaweza kuisaidia Tanzania.
Mheshimiwa Spika, je, Mheshimiwa Waziri haoni sasa kuna haja ya kuwa na kanzi data endelevu ili kufuatilia vipaji vya watoto wetu wanaozaliwa nje, kuwashawishi kuja kuchezea Tanzania katika timu mbalimbali? kanzi data endelevu? (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, naomba tu nimtaarifu Mheshimiwa Ally Saleh kwamba mwanamasumbwi Mwakinyo katika tasnia ya michezo tulikuwa tunamfahamu kabla ya ushindi wake mkubwa, alikuwa Bingwa wa WBA Bara la Afrika sasa huyu mtu Bingwa wa Afrika, usipomjua sasa na wewe lakini tulikuwa tunamtambua.
Mheshimiwa Spika, lingine nimeeleza kwamba katika Wanamasumbwi 1,854 wa Welterweight katika dunia alikuwa wa 174, hapo pia siyo padogo ni pakubwa. Kwa hiyo, tumpongeze tu huyu kijana na tunachukua hatua kweli sasa hivi kuhakikisha kwamba vijana wetu wengi wanaofanya vizuri katika michezo duniani tunawatambua na tunaendeleza vipaji vyao.
Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie tu Mheshimiwa Ally Saleh kwamba hatua hizo tumeshachukua na utaona baada ya muda siyo mrefu kwamba tunawakusanya wote kuweza kuchangia maendeleo ya michezo hapa nchini.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Chama cha Mapinduzi kimeshindwa kuendeleza viwanja vingi vya michezo, ikiwemo kiwanja cha Nangwanda Sijaona katika Manispaaa ya Mtwara Mikindani.
Je, Serikali haioni sasa ni wakati mwafaka wa kurudisha viwanja hivyo Halmashauri kama ilivyofanya kwenye mashamba yasiyoendelezwa ya watu binafsi? (Makofi)
Swali langu la pili, kwa kuwa michezo ni afya, michezo ni ajira, na michezo ni furaha. Kwa kuwa chama cha Mapinduzi kimeshindwa kuviendeleza viwanja hivi na kuwafanya wanamichezo wetu wacheze katika mazingira duni...
Mheshimiwa Spika, naomba unisikilize. Michezo ni afya, ni furaha na ni ajira. Kwa kuwa, Chama cha Mapinduzi kimeshindwa kuviendeleza viwanja hivi hatuoni kwamba Chama cha Mapinduzi kina nia ya kudunisha wanamichezo wetu kwa sababu wanapata ajali mbalimbali wanapokuwa wanachezea katika viwanja hivyo? Nakushukuru. (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nikuhakikishie kupitia Bunge lako tukufu kwamba, siyo kweli kwamba CCM imeshindwa kwa sababu asilimia 99 ya michezo yote nchini inaendeshwa kwenye viwanja hivyo, sasa kushindwa huko kukoje? Sasa hivi tunaanza Ligi Kuu ya Tanzania na sehemu kubwa ya michezo hiyo itachezwa kwenye viwanja hivyo hivyo.
Mheshimiwa Spika, nakubaliana na wewe kwamba vingi haviko kwenye hali nzuri sana na Wizara ilikuwa imeiachia Shirikisho la Soka nchini kufanya majadiliano na wenye viwanja, sasa tumeona maendeleo siyo ya kasi ya kutosha, Wizara imeamua yenyewe sasa siyo tu kwa kushirikisha Shirikisho la Soka nchini, mashirikisho yote ya michezo nchini, kukaa pamoja na wamiliki tuweze kukubaliana namna ya kuboresha hivi viwanja na kuweza kupata misaada ambayo kwa kawaida itakwenda kwa urahisi zaidi kwa taasisi ambazo zina ubia na Serikali. Tunataka watuachie ubia wawe na ubia na Serikali ili tuweze kurabati viwanja, kama ambavo FIFA ilivyoweza kukarabati Kiwanja cha Kaitaba na Kiwanja cha Nyamagana.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Swali langu kwa Mheshimiwa Waziri pamoja na majibu yake ya swali la msingi, tukumbuke kwamba viwanja hivi vilitengwa wakati mfumo wa chama kimoja na maeneo mengi yalitengwa na wakoloni, kwa maana ya kwamba wananchi wote wafaidike na maeneo hayo. Chama cha Mapinduzi kime-take advantage na kwa kweli kimekuwa hakiendelezi hivyo viwanja.
Mheshimiwa Spika, hamuoni kwamba mnapingana na sera yenu ya kutenda haki na usawa katika nchi kwa kuendelea kupora na kunyang’anya hivo viwanja, kuwadhulumu Watanzania wote ambao walishiriki kutengeneza na kuviandaa viwanja hivyo?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, viwanja hivi havikuporwa kwa mtu yeyote, hii dhana ya kuporwa inaondoka kabisa kwenye swali la msingi alilouliza Mheshimiwa Devotha Minja.
Mheshimiwa Spika, naomba tu kukuhakikishia tu kwamba kama kuna hoja ya msingi kwamba kuna kuporwa, maana kuporwa is a criminal act, basi naomba hili suala lifikishwe Mahakamani ili liweze kuamuliwa inavyostahili. (Makofi)
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa utatuzi wa migogoro katika sekta ya michezo bado ni changamoto kubwa sana; je, Serikali haioni sasa kuna haja ya kuanzisha chombo ambacho kitakuwa chini ya BMT ili kuweza kusaidia kutatua migogoro badala ya kuacha watu wanaenda mpaka FIFA kwenda kufuata haki zao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inasisitiza suala la uimarishaji na ujenzi wa viwanda na michezo ni moja ya kiwanda kikubwa; je, Serikali sasa itakuwa tayari kuandaa kongamano la Waheshimiwa Wabunge wanamichezo na wadau ili kujitathmini tulikotoka, tulipo na tunakokwenda?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO:
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado mpaka sasa sijaona kama utaratibu tuliouweka chini ya Baraza la Michezo Tanzania na chini ya Mashirikisho yanayohusika ya michezo kwamba umeshindikana kiasi cha kuunda chombo kingine kipya. Sisi kama Wizara tuko tayari kupokea maoni kutoka kwa wanamichezo kama Mheshimiwa Mwamoto, tuweze kuelewa umuhimu wa kuunda chombo kipya sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kuhusu kuandaa kongamano, namwomba Mheshimiwa Mwamoto, yeye mwenyewe anaweza kuanzisha hilo, na sisi tutamuunga mkono kwa sababu suala la kongamano ni kujadiliana tuweze kusonga mbele katika michezo.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ligi yetu ya Tanzania imekuwa ikitumia gharama kubwa sana hata kwenye usajili wa zaidi ya shilingi bilioni moja kwenye timu kadhaa, lakini wanaenda kupokea shilingi milioni 86 na wamecheza kwa mwaka mzima.
Je, Serikali ina mkakati gani kuifanya ligi hii ya Tanzania kuwa ina ushindani? (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, sijui kama nimemwelewa vizuri Mheshimiwa Sima kuhusu usajili na ushindani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nimweleze Mheshimiwa Sima kwamba sisi kama Wizara bado hatujaona tatizo la usajili na ushindani katika ligi, lakini kama ni matumizi ya pesa, kwa kweli soka la leo ni la pesa. Usipokuwa na pesa, huwezi kabisa ukaendesha mchezo wowote wa mpira. Ndiyo maana unaweza kuona maendeleo mazuri ya timu kama Singida United, nao naomba niwapongeze kwa kazi nzuri ambayo wameifanya Kenya na tuwaombee kama ambavyo tunawaombea Simba waweze kufanya vizuri wawe washindi wa tatu katika mashindano ya Kenya.
MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Michezo ni pamoja na viwanja. Naipongeza sana Serikali kwamba tuna uwanja mzuri sana, Uwanja wa Taifa, lakini uwanja ule kwenye eneo la VIP na juzi wananchi wote na Mheshimiwa Rais walikwenda pale kushuhudia mechi ya Simba na mechi ya Kagera. Eneo lile halina kibanda au kinga ya jua au mvua wakati hali ya hewa inabadilika.
Je, Serikali ina mpango gani sasa kuhakikisha kuwa eneo lile sasa linawekewa kibanda maalum kuzuia mvua kwa watazamaji wa kawaida na viongozi wa Kitaifa watakapokwenda kutazama mpira?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba kuna upungufu katika Uwanja wetu wa Taifa na ndiyo maana tulipokuja mbele ya Bunge lako tukufu kuomba tutengewe pesa kwa ajili ya ukarabati wa Uwanja wa Taifa, hiyo ni moja ya upungufu ambao utatatuliwa kwa pesa ambayo tumeiomba na ambayo inakidhi viwango vya CAF na FIFA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata walipokuja juzi, tulipowaeleza kwamba matarajio yetu ni kutumia hiyo shilingi bilioni moja kwa ajili ya marekebisho ya aina hiyo katika Uwanja wa Taifa, walitukubalia. Kwa hiyo, mabadiliko kama hayo tuyategemee katika Uwanja wa Taifa katika muda sio mrefu kutoka sasa.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Wizara na Baraza la Michezo zimekuwa zikiweka nguvu katika kuushughulikia mchezo mmoja tu wa mpira wa miguu na kusahau michezo mingine na ndiyo maana hata wakati uwanja mkubwa wa Taifa unajengwa, tuliambiwa kwamba inajengwa sports centre, lakini imejengwa football ground. Kwa maana hiyo, wenye michezo mingine wanashindwa kutumia miundombinu hiyo. (Makofi)
Je, Serikali itakuwa tayari sasa kutenga ukumbi mmoja kati ya kumbi zilizokuwa kwenye Uwanja wa Taifa kuwa Boxing Academy ili wacheza ngumi na wenyewe waweze kupata sehemu ya kufanya michezo?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna jumla ya michezo 38 iliyosajiliwa hapa nchini na tuna michezo mipya kabisa tisa ambayo mingine nikiitaja hapa wengine hatuwezi kuielewa. Kwa hiyo, kutokana na hiyo, sisi Kiwizara tunapanga mipango yetu kwa mahitaji na jinsi ambavyo michezo yenyewe inavyoendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo kwamba kuna mchezo mwingine tunaupendelea, hapana, ni kutokana na wadau wenyewe.
Kwa mfano, leo hii hatuwezi tukasema tuweke katika mipango yetu namna ya kuendelea na mchezo wa freese B ambao ni mchezo wa kisahani umeingia nchi, kuna mchezo wa kabadi, kuna mchezo wa kengele (goal ball), kuna mchezo wa roll ball, kuna mchezo wa wood ball; sasa hiyo michezo tunawategemea wadau mwiendeleze ifikie kiwango ambacho tunasema tunaweza kuwa na ushindani katika nchi hii na tukaweza kuifanyia utaratibu kamili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo la Mheshimiwa Mtolea ni zuri kwamba tuna maeneo makubwa sana Uwanja wa Taifa, lakini pale penye mahitaji, wadau wenyewe waeleze na sisi tunaweza kutoa maeneo hayo kuweza kuyaendeleza kwa michezo mingine.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mchezo wa chess unachezwa na karibu watu milioni 800 duniani kote, lakini pia katika hali ya ushindani wa hali ya juu unachezwa na karibu watu milioni 20. Pia kuna chess olympia yaani olympic ya chess peke yake. Kwa jibu hili la Serikali, sioni nia yao kama wanataka mchezo huu ukue ufikie katika huo ukubwa (magnitude) ambayo nimeielezea kwa sababu wanasema kwamba ukuzwe na wadau.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali iko tayari; kwa sababu mchezo huu hauna gharama kubwa katika kuuwekeza, ipo tayari kuwashawishi Cooperate Tanzania iuchukue mchezo huu, iukuze na uweze kuchezwa katika upana mkubwa angalau tuwakute wenzetu Kenya, Uganda na Zambia majirani zetu ambao wapo mbele?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba mchezo huu unakuza akili na ufikiri, lakini mchezo huu maumbile yake unafundisha namna ya kujihami na namna ya mbinu za kijeshi. Je, Serikali iko tayari kutumia nafasi yake kuona kwamba mchezo huu unachezwa katika hali ya kukuza vyombo vya ulinzi? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba tu nisisitize kama nilivyosema kwenye swali langu la msingi kwamba kwa kweli hakuna mchezo wowote hapa nchini uliokuzwa na Serikali bila wadau, haitawezekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Ally Saleh ajitahidi kwa nafasi yake ya Ubunge kuhimiza wadau mbalimbali waweze kuubeba huu mchezo kama michezo mingine inavyofanyika na Serikali tupo tayari kutengeneza miundombinu sahihi na mazingira ya kuweza kuhakikisha kwamba mchezo huu unakua kwa kasi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mchezo wa chess ni kweli kabisa nakubaliana naye kwamba ni mchezo ambao unahitaji akili, kama vilevile ambavyo mchezo wetu wa utamaduni wa bao unavyohitaji akili katika kuucheza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi nimefurahi sana wadau wa bao wameamua sasa huu mchezo uende Kitaifa. Nampongeza sana mwanabao mashughuli hapa nchini Mandei Likwepa na wenzake waendelee na sisi tutawasaidia kuweza kuuhamasisha huu mchezo ambao ndiyo chess ya Kiafrika. Nina uhakika tukiuongezea vilevile manjonjo mbalimbali unaweza kuwa pengine bora kupita hata huo wa chess kwa sababu hatujaufanyika kazi vya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimalizie tu kwa kusema kwamba tunakubali mchezo wa chess ni muhimu, ni mkubwa na unahitaji akili hata kwa majeshi ungefaa sana, lakini hata kwa wanafunzi wetu kutoka shule ya msingi mpaka Vyuo Vikuu unafaa sana, lakini naomba wadau wawe mstari wa mbele badala ya kuisubiri Serikali ndiyo itangulie mbele katika mchezo huu.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Swali la kwanza, kwa kuwa Serikali imekiri kabisa kwenye ligi ya Uingereza ilijulikana kama Backlays English Premier League na siyo Backlays Premier League, pia hata Kagame Cup haikujulikana kama Kagame Cup inajulikana kama CECAFA Kagame Cup. Serikali haioni haja sasa kwamba umefika wakati wa kuitangaza Tanzania kwenye michezo na league yetu ikaitwa Tanzania Vodacom Premier League? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Kampuni ya Azam wameanzisha mashindano makubwa sana yanaitwa Azam Sports Federation Cup, nichukue fursa hii kuwapongeza sana, je, Serikali haioni haja sasa ya kushawishi na makampuni mengine yaweze kuanzisha mashindano ili ku-promote soko la Tanzania? (Makofi
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwalimu Mussa Sima kwa kifupi sana, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza pendekezo la kuweka jina la Tanzania kabla ya jina la mdhamini lina mashiko, tutalifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la kampuni nyingine kuiga mfano wa Azam, nami naunga mkono suala hilo. Natoa wito kwa makampuni mengine yajaribu kuiga mfano wa Azam ili tuweze kukusa soka katika nchi yetu.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa soka la wanawake limekuwa likifanya vizuri sana hapa nchini na kimataifa, lakini soka hili halina wadhamini wa kulidhamini. Je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kuhamasisha wadau mbalimbali ili waweze kulidhamini soka hili la wanawake nchini? (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Toufiq, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, soka la wanawake pamoja na kwamba limechelewa sana kupewa uzito stahili katika nchi yetu, tayari lina wadhamini. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Toufiq kwamba kila mwaka tunazidi kuongeza juhudi za kuwapata wadhamini. Moja ya nyenzo kuu ya kuwapata wadhamini wengi zaidi ni kuhakikisha kwamba tunaomba au tunaingia mikataba na kampuni mbalimbali za utangazaji ili soka hiyo iweze kuonyeshwa live katika luninga zetu na hata kutangazwa katika redio mbalimbali.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kweli udhamini katika soka la wanawake hauridhishi na league ya mpira wa miguu ya wanawake inaendeshwa katika mazingira magumu sana. Ni kwa nini isiwe ni lazima kila udhamini unaopatikana kwa league ya wanaume uende sambamba na udhamini pacha wa league ya wanawake? (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mtolea, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba udhamini kwa timu za wanawake siyo mkubwa kama ulivyokuwa kwenye timu za wanaume, lakini lazima tuangalie historia kwamba league kuu nchi hii miaka 50 iliyopita ilianza kwa wanaume tu na tulianza na timu chache tu kama sita, lakini sasa hivi tuna timu 16 na mwaka ujao tutakuwa na timu 20. Kwa hiyo, imeongezeka ukubwa na udhamini wake lazima tuupiganie nao uwe mkubwa vilevile. Sasa hivi ndiyo tumeanza na ligi ya wanawake, tumepata udhamini mdogo, lakini tunaendelea na juhudi kuongeza ukubwa wa udhamini wa timu za wanawake kulingana na ukubwa wa league yenyewe.
MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Swali kama hili ambalo Mheshimiwa Ngombale leo ameuliza, nililiuliza mimi 2016 na majibu yalikuwa haya haya. Sasa Mheshimiwa Naibu Waziri Mkoa wa Lindi usikivu wa TBC ni tatizo sana, naomba commitment ya Mheshimiwa Naibu Waziri kama alivyotoa wakati anajibu kwa Mheshimiwa Ngombale; kwamba katika mwaka huu wa fedha huo mnara aliosema utajengwa ili Watanzania wanaomsikia wajue kwamba Serikali imeji-commit ndani ya Bunge.
WAZIRI WA HABARI UTAMADUNI SANAA NA MICHEZO:
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa ambayo ameyatoa kwa maswali aliyoulizwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kumjibu Mheshimiwa Bobali kwamba, kwanza si sahihi kusema kwamba eti majibu tuliyotoa sasa ndio majibu tuliyotoa kipindi kilichopita miaka miwili iliyopita wakati kuna miradi tayari tumeitekeleza mwaka huu na mwaka jana. Ni kichekesho, sasa sisi tumekuwa waganga wa kienyeji kwamba tumetekeleza hayo mambo mwaka huu..
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge awe na imani na Serikali yetu, kwamba tumehakikisha kwamba katika mwaka 2018/2019 mradi wa kujenga mtambo wa FM kurusha matangazo eneo la Nangurukuru utatekelezwa.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri kuhusu viwanja, pamoja na kwamba hata viwanja vitakavyofanyika michezo ya AFCON naomba niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa jana tumehakikishiwa kwamba timu yetu itakayoshiriki michezo ya AFCON itashinda nataka kujua tu wamefanya maandalizi gani, watuambie maandalizi yaliyofanyika ili tuwe na uhakika kwamba timu yetu sasa tunaenda kubakiza kombe hapa Tanzania?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyonyeza la Mheshimiwa Mwamoto kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kujibu maswali vizuri sana, lakini vilevile naomba nirejee kauli ya Waziri Mkuu ya jana, kwamba tumejipanga vizuri. Timu yetu ya Taifa ya Vijana Chini ya Umri wa Miaka 17 (Serengeti Boys) iko kambini kwa wiki tatu sasa na kazi yetu kubwa sasa hivi ni kuipambanisha na timu mbalimbali za wakubwa wao hasa wa chini ya umri wa miaka 20, kuweza kuwaimarisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana kulikuwa na mechi kubwa sana na timu nzuri katika Afrika Mashariki Azam FC under 20 na matokeo yake ni kwamba Serengeti Boys imewachapa kaka zao magoli matano kwa bila. Tukumbuke vilevile kwamba Azam FC ina baadhi ya wachezaji wa Ligi Kuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kesho timu ya Serengeti inakwenda Arusha angalau kuji-acclimatize (kujizoesha) na hali ya Arusha na kuweza kupambana na timu mbalimbali kabla ya kwenda Uturuki kwa mwaliko wa UEFA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Watanzania tujivunie ubora wa timu yetu, kwamba imeweza kutambuliwa kama moja ya timu bora katika Afrika kuitwa kwenye mashindano ambayo yanaunganisha timu nne za Afrika na timu nne za Ulaya. Tunakwenda kule na mechi yetu ya kwanza itakuwa tarehe 4 mwezi wa tatu dhidi ya Guinea; na baadaye tutacheza na Australia na kumalizia na timu yka Uturuki. Sasa hivi naongea na wenzetu wa TBC tuweze kupata live coverage kutoka huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mashindano hayo yataisha tarehe 11 Machi na timu hiyo haitarudi Tanzania, tunaitafutia pesa lazima iende Spain ikafanye mazoezi na mashindano kidogo na wenzao na baadaye iende Cameroon ikashindane na baadhi ya timu kule ndipo itarejea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie, wiki ya kwanza mwezi wa Aprili tumekaribishwa na Rwanda kujipima nguvu na timu nne bora za Afrika ambazo ni Cameroon, Rwanda na Uganda. Baada ya hapo inarejea nchini kwa mechi ya ufunguzi dhidi ya Nigeria ambayo nina uhakika tutaishangaza Afrika katika matokeo yake. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Tatizo la ubakaji watoto linaoneka ni kubwa sana Mkoani Mara. Kamati ya Katiba na Sheria juzi ilikwenda Mara na tukapata taarifa za kutisha kutoka kwa Mkuu wa Mkoa Mheshimiwa Malima. Kuna Mwalimu kwa mfano amewafanya wake zake watoto 10 wa darasa la kwanza.
MBUNGE FULANI: Darasa la kwanza?
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, nitarudia, amewafanya wake zake watoto 10 wa darasa la kwanza.
MBUNGE FULANI: Aaaah.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, kuna taarifa nyingi za kutisha juu za ubakaji kwa rika zote, kwa watu wazima na kwa watoto. Je, Serikali ama kupitia Wizara ya Afya au Bunge haioni haja sasa ya kuunda Tume au ya kutafuta utaratibu wa kwenda kulitazama tatizo hili ambalo ni kubwa inafika watu wanauliwa? Risasi zinatumika halafu watu wanakimbia upande wa pili wa Kenya inakuwa vigumu kulishughulikia. Mkuu wa Mkoa Adam Malima alikuwa na pain kubwa alipokuwa akituelezea juu ya suala hili. Naomba Serikali ifikirie jambo hili, ahsante.
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, pamoja na shinikizo kubwa kutoka nchi za Magharibi, shinikizo la ndoa za jinsia moja, shinikizo la kuuona ushoga kama haki za binadamu, bado nchi 38 kati ya nchi 54 za Afrika zinapinga masuala hayo na Tanzania ni mojawapo. Si hivyo tu, sisi tume-criminalize yaani vitendo hivyo ni makosa ya jinai na watu wanafungwa. Kwa hiyo, bado sisi ni moja ya nchi ambazo tumekaa vizuri katika kulinda jamii yetu.
Mheshimiwa Spika, tatizo kubwa ni kwamba jamii inaficha haya matatizo. Kwa mfano, matatizo ya watoto kulawitiwa au kubakwa kwa sehemu kubwa yanafanywa na ndugu katika jamii. Tukianza upelelezi familia zinawalinda hawa watu hawatoi ushahidi, ni tatizo kubwa sana.
Mheshimiwa Spika, katika sheria kama hakuna ushahidi huwezi ukamfunga mtu na kosa hili ni kubwa, adhabu ni kali sana.
Mheshimiwa Spika, naomba nitoe wito kwa Tanzania tatizo ni kubwa sasa, tunaomba ushirikiano kwa vyombo vya dola ili tuweze kuwapata hawa wahalifu wanaojaribu kuchafua generation ya kesho, kesho kutwa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipa nafasi ya swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TCRA imeruhusu TBC kama TV ya Taifa kuonekana kwenye ving’amuzi vyote, lakini TCRA inaisimamia vipi TBC kuweza kuonyesha habari kwa uhakika na bila upendeleo kwa vyama vyote na wananchi wote? Ahsante.
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru sana
Mheshimiwa Naibu Waziri Mhandisi kwa majibu mazuri sana aliyotoa kwa maswali aiyoulizwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa swali la nyongeza napenda niseme tu kwamba TBC kama vituo vyote vya kitaifa duniani vina hadhi ya must carry ambayo kila kisimbusi lazima kibebe, kwa hiyo, siyo kitu cha Tanzania tu, kipo duniani kote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, hili ni suala la maudhui; suala la maudhui upande wa TBC ni wazi, kama una maudhui yako tafadhali peleka TBC. Hakuna upendeleo wowote unaofanyika, wewe kama unaamini ni upendeleo ni shauri yako, lakini leta maudhui yako yaoneshwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi naomba nikusisitizie, kama kuna mtu hapa ana wasiwasi maana wengi wanaongea hawajawahi hata kupeleka maudhui, nileteeni mimi kama hayo maudhui hayataoneshwa. Ahsante sana.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa njema ni vyema zikawa na sauti, leo asubuhi kuanzia saa 12.00 TBC haikuwa na sauti kabisa na hakuna namba yoyote iliyokuwa inaonesha pale tupige kwa dharura wale ambao tuna ving’amuzi vya Azam TV.
Je, Mheshimiwa Waziri anatuambia nini na wakati walipokuja kurudi kutupatia sauti saa 1:10 asubuhi hawaku- apologize?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa hata mimi mwenyewe nimeona hiyo hitilafu ikitokea leo, lakini siyo leo tu imekuwa ikitokea mara kwa mara kwa sababu TBC, television yenu ya Taifa sasa hivi ipo katika programu ya mageuzi makubwa sana kiteknolojia ndiyo maana muonekano wa TBC sasa hivi ni bora kupita miaka iliyopita nyuma na naomba ndani ya mwezi mmoja mtaona hata background, nyuma ukiangalia TBC haitatofautiana sana na CNN. Kwa hiyo, kaa mkao wa kuangalia Television ya Taifa.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Ni kweli siyo Mwanamichezo, lakini nawakilisha wanamichezo. Watanzania wote leo tunamshangilia na kumfurahia Samatta kwa kusajiliwa na hiyo timu ya Uingereza. (Kicheko)
SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, wanataka kujua tu ni timu gani hiyo. Inaitwaje hiyo? (Kicheko)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, Aston Villa. (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, amesajiliwa kwa sababu ya jitihada zake mwenyewe, sasa inatuambia Watanzania kwamba tunaweza kuwa na Samatta wengi kwa kadri inayowezekana kama Serikali ikiwezekeza vya kutosha kwenye michezo. Sasa kwa nini Serikali isianzishe Sports Arena kwenye Majiji Makuu kama ambavyo wanafanya Nchi ya Rwanda ili kuwatoa Samatta wengi?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kujibu maswali vizuri sana ya michezo. Naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Paresso kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, sasa hivi kutokana na juhudi za Serikali pamoja na wananchi wenyewe, tuna wachezaji 22 wanacheza nje ya nchi yetu, wanacheza Kimataifa siyo Samatta peke yake na hii inatokana na uelewa tulioupata Watanzania kwamba vipaji hivi havipatikani ukubwani unaanzia huku chini ndiyo maana Serikali inaingia gharama kila mwaka kuendesha mashindano ya UMITASHUMTA na UMISETA kwa shule za Msingi na shule za Sekondari.
Mheshimiwa Spika, nimalizie tu kwa kusema, sasa hivi wito wetu wa kushiriki kila mtu kujenga viwanja, miundombinu siyo tu Kinondoni imeitikia hata vilabu binafsi kama Simba Sports Club wamejenga viwanja viwili Dar es salaam vya nyasi bandia pamoja na nyasi za kawaida, viwanja vizuri nimeenda kuvitembelea. Siyo hivyo tu, Mkoa wa Arusha unaongozwa unastahili pongezi, Halmashauri ya Jiji la Arusha sasa hivi imejenga Ngarenaro kiwanja changamani kizuri ambacho kina Netball, Basketball pia Soccer lakini vilevile katika Kata nafikiri ya Sinoni kuna Mtanzania ambaye anaishi Marekani anajenga kiwanja kizuri sana kimefikia asilimia 90. Nitoe wito kwa vijana wetu pia wanaoishi Ulaya, nje ya nchi waige huo mfano, wasishinde tu kwenye mitandao ya kijamii. Ahsante sana.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Chakula pia ni moja ya utamaduni. Je, Serikali inasema nini juu ya vyakula vinayotoka nje ya nchi ambavyo ni kinyume na utamaduni wetu wa chakula cha asili ambacho tulikuwa tunakitumia? Nataka kujua tunatoa tamko gani kuzuia vyakula ambavyo siyo vya utamaduni wetu na vinaathiri afya za Watanzania?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwakagenda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya maswali yaliyotangulia. Napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba swali alilouliza ni mtambuka linalohusu biashara ya nje na sekta mbalimbali ambapo Wizara yangu haiwezi kulitolea tamko hapa kwamba kuanzia sasa vyakula ambavyo siyo vya utamaduni visiingie nchini. Hili ni suala pana ambalo hata Bunge lako Tukufu lina mamlaka ya kuweza kulijadili kwa upana zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Katika majibu ya msingi ya Mheshimiwa Naibu Waziri alituambia kwamba yuko katika mkakati na mchakato wa kuendeleza Kiswahili nje ya nchi lakini inaonekana kwamba Kiswahili kinachofundishwa nje ya nchi siyo standard Swahili, siyo lugha sanifu ndani ya Tanzania ni Kiswahili cha nchi jirani. Je, wana mkakati gani wa ziada kuhakikisha Kiswahili chetu cha Tanzania ambacho ni Kiswahili sanifu (standard Swahili) ndicho ambacho kinatumika nje ya nchi na siyo Kiswahili cha nchi ya jirani?
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Masoud, Kiswahili si ni lugha, sijaelewa unamaanisha lafudhi au lugha, hebu uliza swali lako vizuri.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, standard Swahili (Kiswahili sanifu) ndicho ambacho kinaongelewa au kinaandikwa hapa Tanzania lakini katika nchi nyingine, unapokwenda huko duniani katika nchi za Ulaya Kiswahili ambacho kinafundishwa ni cha nchi jirani siyo cha Tanzania.
MBUNGE FULANI: Kweli.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo ni kweli na ndiyo uhalisia. Mheshimiwa Naibu Waziri atuambie …
NAIBU SPIKA: Sawa, umeeleweka Mheshimiwa.
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa ya kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba katika matumizi ya lugha yoyote duniani kuna kitu kinaitwa standardization, kila mtu lazima atumie lugha ambayo ni sanifu. Ndiyo maana Jumuiya ya Afrika Mashariki imeunda Kamisheni ya Kiswahili ambayo Makao Makuu yake yako Zanzibar na moja ya kazi yake kubwa ni kufanya lugha ya Kiswahili iwe na urari wa aina moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili, tuna kazi pia kubwa ya kufanya kati ya sisi upande wa Tanzania Bara na upande wa Zanzibar kuoanisha baadhi ya misemo na maneno ili tusiwe na lugha mbili. Kwa mfano, jana nimeona Kamusi kutoka Zanzibar inaitwa ‘Kamusi Sanifu la Kiswahili’ wakati sisi huku Bara Kamusi haiwezi kuwa ‘likamusi’ ni ‘Kamusi ya Kiswahili’. Sasa sisi wenyewe tuna matatizo ndiyo maana inabidi tukae, Baraza la Kiswahili la Zanzibar na Baraza la Kiswahili la Tanzania wakae pamoja kwanza tuwe na lugha ya aina moja ili tuweze kuwashawishi wenzetu wa Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza, maeneo yote ya mipakani mwa nchi, Mkoa wa Rukwa, Katavi, Kigoma ni Mikoa ambayo haina usikivu wa TBC redio a wananchi wengi wanasikia redio jirani mfano ukienda Kasanga wanasikiliza redio Zambia, ukija Kirando wanasikiliza redio ya kutoka nchi ya DRC na Kigoma wanasikiliza redio za nchi jirani ya Burundi.
Ni lini Serikali itapeleka mawasiliano ya karibu ya redio ili kuwafanya wananchi wasikie taarifa za kutoka kwenye Taifa lao?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri kwa maswali yaliyotangulia, napenda kulijibu swali la Mheshimiwa Kakoso kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu swali hili limejitokeza mara nyingi sana hapa Bungeni naomba tu nisisitize kwamba nchi yetu imekuwa ikitegemea vituo vinane vya kurushia matangazo miaka yote hii vituo vya masafa ya kati mid-wave ambavyo vilikuwa Dar es Salam, Arusha, Mwanza, Kigoma, Dodoma, Songea, Nachingwea na Mbeya. Vituo vyote hivi vya midwave vimechakaa na vingi kwa kweli vimeharibika kabisa haviwezekaniki kutengenezwa kwa sababu vinatumia teknolojia ya kizamani. Ndiyo maana ni karibu miaka kumi ilioyopita tumeanzisha mradi wa kuweza kuboresha usikivu wa redio yetu hii ya Taifa kwa kutumia mitambo ya FM.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Bunge hili linaanza tulianza na vituo vitano vya mpakani, tulianza na Longido, Rombo, Tarime, Kibondo na Nyasa, hali ni nzuri; tukafatia Lushoto na baadhi ya maeneo ya Mtwara. Sasa hivi katika bajeti ya mwaka huu tunahangaika na Pemba, Unguja, Simiyu, Songwe na Njombe. Vilevile tumeingia mkataba na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ambapo tutashambulia maeneo ya Kilwa, Kilombero, Kyela, Itigi na Rungwa na kufanya ongezeko la Wilaya 33 katika kipindi hiki kuweza kusikika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea, tumefika Wilayani kwa Mheshimiwa Kakoso, tayari tumepeleka wataalamu wanaangalia ni maeneo yapi upande wa Ziwa Tanganyika tuweze kuyapelekea mitambo ya FM.
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali moja dogo tu la nyongeza. Shirika la Utangazaji (TBC) ni Shirika la Taifa na linaendeshwa kwa kodi za wananchi wote wakiwepo Wana- CHADEMA, CCM na hata wale ambao hawana chama; lakini ukifungua TBC kila mara utakuta ni shughuli za chama tawala tu ndiyo zinaonyeshwa. Hata kama kwa mfano CHADEMA wamefanya Press Release fulani au chama kingine cha Upinzani huwezi kuona wakiirusha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nauliza, kama hili ni Shirika letu la Taifa nasi tunalipia kodi zetu kuliendesha: ni lini sasa TBC itakuwa inarusha vipindi vyake kwa usawa bila upendeleo? (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, TBC haiendeshi kwa upendeleo wowote kwa vyama, ili mradi kwanza ukubali kama kuna vipindi vya kulipia, kama wewe ni mkono wa birika, hatuwezi tukarusha vipindi wakati unatakiwa kulipia. Kwa hiyo, kuna gharama yake pale.
Pili, tukiletewa vipindi tunatangaza. Watuambie lini wametuletea vipindi tumeshindwa kutangaza? Haya malalamiko ya jumla jumla hayatatusaidia hata kidogo. (Kicheko)