Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Oran Manase Njeza (123 total)

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa pongezi kwa Rais Dkt. John Magufuli pamoja na timu yake ya Mawaziri kwa kuleta matumaini ya Watanzania:-
Utumbuaji Majipu; Kuondoa wafanyakazi hewa; Kuondoa wafanyakazi wazembe; Kuondokana na uchumi tegemezi; Kuondokana na mikopo; na Kuweka mazingira ya kuongeza FDI.
Mheshimiwa Naibu Spika, Hotuba ya Mpango wa Pili wa Maendeleo. Natoa pongezi kwa Rais Dkt. John Magufuli kwa:-
Utumbuaji majipu; Kuondokana na uchumi tegemezi, FDI vs Misaada; Uchumi wa viwanda; Kuboresha elimu; na Kuboresha kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika huduma za Fedha:-
Mitaji ya benki za TIB na TADB 212 bilioni na 60 bilioni; Jinsi ya kunufaisha wakulima na wajasiriamali wadogo; Riba haziko rafiki na wakopeshe wadogo (Wajasiriamali na Wakulima); Matumizi ya Mobile Money – M Pesa; Payment system inahama kutoka ma-bank kwenda kwenye mitandao ya simu; usimamizi/ulinzi/protection; na TR na usimamizi wa mashirika.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kilimo (3.4%):-
Napongeza Mpango wa Serikali wa kutoa milioni 50 kwa kila Kijiji/Mtaa; Elimu ya kilimo na ujasiriamali; Mapinduzi katika kilimo; Kuongeza thamani ya mazao ya kilimo; Msisitizo wa viwanda vidogovidogo vijijini; na Msisitizo uwe kuongeza na kuboresha uzalishaji wa kilimo; US$ against TZS – itakuwa imara tukiongeza uzalishaji na kupunguza imports.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Barabara/Reli/Miundombinu Vijijini:-
Barabara za Vijijini ziboreshwe kusaidia usafirishaji wa mazao; Kuboresha Reli ya TAZARA; Barabara za kupunguza msongamano; Barabara ya Tanzania – Zambia kupita katikati ya miji yetu mikubwa kama Jiji la Mbeya, hatari ya ajali/msongamano; Barabara za kuunganisha mikoa; Isyonje (Mbeya) Kikondo – Kitulo - Makete – Njomb; na Mbalizi – Galula, Mbalizi – Ilembo – Ileje.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu maji:-
Changamoto za maji vijijini; Maji/afya ya wananchi na gharama ya tiba; na Miradi ya maji Kata ya Mjele, Mji Mdogo wa Mbalizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika elimu, mitaala ya elimu iendane na mipango yetu; ujasiriamali wa kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Nishati na Madini:-
Vyanzo vya umeme; jua, maji, upepo na gesi; Madini ya Songwe; na Umiliki wa wananchi
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na timu yake mahiri ya Mawaziri kwa kazi nzuri wanayofanya na hasa ya kutumbua majipu na kuinua uchumi wa nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuondoa umaskini kupitia TASAF; pamoja na mafanikio makubwa yatokanayo na mpango wa kunusuru kaya maskini, TASAF, kuna changamoto nyingi ambazo zinatakiwa kushughulikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa rai kwa Serikali kuhakikisha changamoto mbalimbali zinazotokana na utekelezaji zinatatuliwa ili kuhakikisha fedha hizi zinakidhi malengo. Serikali ihakikishe TASAF imetimiza malengo ya kuondoa umaskini. Napendekeza mpango huu wa TASAF uboreshwe hasa usimamizi wa kutambua kaya maskini. Pia napendekeza hasa katika maeneo ya vijijini fedha ya TASAF itumike kuboresha huduma za kijamii ili hiyo pesa kidogo ifanye kazi pana zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Utawala Bora; pamoja na muundo mzuri wa Serikali na taasisi zake, kuna changamoto ya nafasi nyingi za Uongozi kuwa na Makaimu kwa muda mrefu. Pia kuna Mashirika mengi ya Umma yanaendeshwa bila Bodi za Wakurugenzi kwa kipindi kirefu. Hii inapelekea Idara na Mashirika hayo kutoendeshwa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa rai kwa Serikali kuboresha uteuzi wa Bodi za Wakurugenzi, kuzingatia taaluma na uwezo badala ya uwakilishi wa Idara za Serikali. Msajili wa Hazina (TR) ahusike kikamilifu katika zoezi la kuteua Wakurugenzi wa Bodi. Pia Serikali izingatie uwezo na taaluma katika kuteua Wakuu wa Idara wakiwemo Wakurugenzi wa Halmashauri na Viongozi wengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa rai kwa Serikali kutowavumilia Viongozi na Watumishi wenye tuhuma za ubadhirifu na uadilifu wa mashaka, badala ya kuwahamisha au kubadilisha kituo waondolewe kwenye Utumishi wa Serikali na Taasisi zake.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Waziri na Naibu wake pamoja na timu nzima ya Wizara kwa kazi nzuri na hotuba nzuri ya bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dunia ya leo ni kama kijiji, hivyo suala la elimu ni muhimu sana kuliko wakati wote uliopita. Tulizoea kulinganisha ubora wa bidhaa (product competitions) kwa brand „nation brand‟ Elimu bora ni muhimu sana kwa nchi yetu kuwa na nation competitive advantage.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza mindombinu na mitaala ya elimu iboreshwe kulingana na dunia ya leo. Napendekeza elimu kwa vitendo ianze toka shule za msingi elimu ya vitendo ijikite kwenye kilimo ufundi, ujasiriamali na TEHAMA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi za Mashariki ya Mbali, (tiger countries) zimefanikiwa sana kwenye uchumi wao kutokana na elimu bora ikiwa na nafasi kubwa katika orodha ya sababu za hayo mafanikio yao. Pamoja na muundo wa elimu ya nchi yetu napendekeza Wizara iweke mikakati ya kuboresha miundombinu na maslahi ya Walimu. Tunapoenda kwenye uchumi wa kati elimu ni muhimu sana hasa elimu inayowatayarisha vijana kujitegemea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia hotuba ya Wizara ya Viwanda na Biashara ambayo ni Wizara muhimu sana hasa kwa Serikali ya Awamu ya Tano kwa sababu ni Serikali ya viwanda na kwa ajili ya kukuza uchumi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Waziri, Naibu Waziri na timu yake yote ya wataalam pamoja na watu wote wanaomsaidia, wanafanya kazi vizuri sana. Ni kweli pamoja na kwamba watu wanasema labda Mheshimiwa Mwijage anaongea kwa utani lakini kwa jinsi navyomwangalia nafikiri yupo serious ndiyo sababu hata Mheshimiwa Rais amemwamini kwa kipindi chote hicho amebaki kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa ambacho nataka nichangie kwenye Wizara hii, naona tumejikita mno kwenye viwanda, hatujaangalia biashara. Leo hii ukiniuliza hata mimi, masoko yako kwa nani? Yako kwa Wizara ya Viwanda au yako Kilimo au Mifugo au yako kwa nani, sijui. Wakulima wanahangaika na sehemu ya kuuza mazao yao. Ni nani mwenye jukumu hilo, hatuelewi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kwenye kilimo, tumehangaika kuhusu mahindi hapa, aliyesulubiwa ni Waziri wa Kilimo. Nimezungumza kwa muda mrefu kuhusu pareto hapa. Nilikuwa naongelea kupitia kwa Waziri wa Kilimo lakini leo hii nilipoangalia hotuba hii, nikakuta kuna chombo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara kinaitwa TANTRADE, kazi yake ni kutafuta masoko ya viwandani na mazao. Jiulize humu ndani kama kweli hawa watu hizo kazi wanazifanya zaidi ya Maonyesho ya Sabasaba. Inabidi tusifumbiane macho, tunapata shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwangu nalima pareto. Nimeongelea kuhusu pareto mpaka Wizara imeamua iifute pareto kwenye mazao manne ya kimkakati Tanzania wakati pareto tunayolima Tanzania tunaongoza Afrika na ni ya pili duniani. Sasa uangalie ni kwa kiasi gani wakati mwingine tunafanya vitu vya ajabu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pareto tunayozalisha leo hii haizidi tani 1,000 ndiyo tumejitahidi sana, lakini potential ni karibu tani zaidi ya 10,000, ndiyo inatakiwa duniani. Kwa nini hatufiki huko? Kwa sababu mnunuzi ni mmoja. Ni nani alitakiwa atutafutie wanunuzi? Ni huyu mtu anaitwa TANTRADE au Wizara ya Viwanda ba Biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachomwomba Mheshimiwa Waziri aje na mkakati ni namna gani atusaidie Tanzania kwa sababu potential tuliyonayo Tanzania ni kuwa wazalishaji wakubwa wa pareto duniani. Leo hii pareto tunaiuza mkulima anapata kwa bei kati ya Sh.2,300 mpaka Sh.2,700 lakini ukipeleka sokoni moja kwa moja, wale wanaonunua wanapata kati ya Sh.8,000 mpaka Sh.10,000 na hiyo ni kwa vile ni biashara wanaotuchezea. Anayenunua na anayezalisha Tanzania ndiyo huyo huyo anayenunua Marekani. Anapeleka Marekani kama crude, anakwenda kuichakata kule na sisi Tanzania hatuonyeshwi kama ndiyo tumeizalisha hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kiwanda kilianzishwa Inyala kikajaribu kupeleka pareto nje, wale waliponunua na kuingia mkataba, wakatishiwa kwamba kwa sababu mnanunua pareto kwa huyu mzalishaji mwingine kutoka Tanzania, nasi ndiyo tumekamata zao la pareto duniani, basi hatutawaletea tena pareto, kwa hiyo, wale watu wakaogopa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona kuna chombo chini ya Wizara hapa kinaitwa FCC kama sikosei na kazi zake, sijui kama haya wanayaona ya kwamba zao ambalo tunaongoza Afrika, hata FCC sijui kama wanajua ni kiasi gani wakulima wananyonywa? Mnunuzi ni mmoja, ame-dominate soko la pareto ndiyo giant duniani. Tukiendelea namna hii tutakuwa tunamsaidia vipi mkulima wa Tanzania? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho nilitaka nichangie kidogo ni kuhusu kufufua viwanda. Watu wameongelea kuhusu kufufua viwanda na Mheshimiwa Waziri ametamka kuwa ana nia ya kufufua Kiwanda cha Nyama kwa kutafuta mnunuzi wa Kiwanda cha Nyama cha Tanganyika Packers kule Mbeya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nimfahamishe Mheshimiwa Waziri, tuna kiwanda ambacho kimejengwa na Halmashauri. Ni kiwanda cha thamani ya shilingi bilioni 2, kimejengwa kwa asilimia 90. Vifaa ya UNIDO vimeshawekwa mle ndani na sasa hivi Halmashauri inaomba pesa kidogo tu kama shilingi milioni 900 ili waweze kumalizia. Kiwanda hiki ni cha kisasa na ni kizuri kuliko hicho ambacho wanataka kufufua sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanganyika Packers ilijengwa kabla ya mwaka 1970, yale mashamba sasa hivi yamezungukwa na jiji, yako mjini. Kuna ekari pale karibu 5,000 ziko mjini na mjini huruhusiwi kufuga wala kulima zaidi ya ekari tatu. Sasa unakuta Mheshimiwa Waziri naye anasimama anasema tunatafuta mwekezaji kwa ajili ya Tanganyika Packers. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba muwe mna- coordinate. Halmashauri imeomba lile eneo wapewe na wao wametoa ekari 7,000 kwenye sehemu ambayo ndiyo kuna ng’ombe wengi iwe kama holding ground, lakini tubakize kiwanda, kutoka pale ni kilomita 30. Wizara ya Ardhi walishauja, Naibu Waziri wa Ardhi alikuja, Katibu Mkuu wa Ardhi alikuja, wote waka-recommend nami mwenyewe nimeongea na Treasury Registrar akaona hilo ni wazo zuri ili lile eneo sasa ambalo lilikuwa ni la Tanganyika Packers libadilishane na hili eneo, Halmashauri iliendeleze hili eneo kwa ajili ya kuupanga mji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hilo ni karibu kabisa na Songwe International Airport. Sasa badala ya kutenga maeneo kwa ajili ya EPZ unataka wewe ukachungie ng’ombe, nafikiri hivyo ni vitu ambavyo katika dunia ya leo havikubaliki. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hilo kwa makusudi kwa vile hiki kiwanda ni kwa ajili ya soko la ndani na nje. Kiwanja cha ndege sasa hivi kimetengenezwa ili kiwezeshe ndege kubwa kutua Mbeya ziende moja kwa moja Ulaya, tuweze kupeleka nyama kutoka Mbeya kwenda Ulaya na tupeleke maparachichi na kadhalika. Kwa hiyo, hatukatai Kiwanda cha Nyama ila tunachosema ni mfumo gani tuuchukue ambao unaendana na leo? Ile spirit ya 1970 huwezi ukaitumia hiyo hiyo mpaka leo ukawa unaimba humo Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho napenda kuchangia kidogo ni hii taasisi mpya ya inaitwa Tanzania Commodity Exchange Market, ni nzuri mno na inaweza kuwa mkombozi. Sasa ndiyo hivyo ambavyo nachanganyikiwa kwamba, je, itakuwa chini ya nani; Wizara ya Viwanda, Wizara ya Fedha au labda Wizara ya Kilimo? (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hilo kwa makusudi. Kilimo sasa hivi walikuwa wanahangaika jinsi ya kuuza kahawa. Unajaribu kuangalia, je, kuuza kahawa ni Wizara ya Kilimo, au ni Wizara ya Viwanda au ni TANTRADE? Sasa Wizara ya Kilimo badala ya kuboresha kilimo wanaanza kuhangaika na kutafuta masoko. Nafikiri tutapoteza mwelekeo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hivi vitu tuvifanye kwa makini. Imarisha Tanzania Commodity Exchange, tuige Ethiopia, Nairobi wana soko la kuuza kahawa. Tanzania tunauza kahawa kwa kilo 50 dola 150 wakati Nairobi ni kati ya dola 350 mpaka 400 na Ethiopia ni zaidi hapo. Sasa angalia ni kiasi gani uchumi wa nchi hii tunavyoupoteza kwa kutokuwa na mipango mizuri? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba hili wenzetu nao wakajipange vizuri. Zao la kahawa liingie moja kwa moja kwenye Tanzania Commodity Market Exchange. Kwa sababu gani TCB wao ni regulator, huwezi ukamfanya regulator vilevile akawa ni muuzaji. Sisi wengine ni wakulima wa kahawa, unaona kabisa kuna watu pale wanajifanya wana mnada lakini wanaangalia kahawa ya leo ya Tanzania tununue kwa shilingi ngapi? Tumenyonywa kiasi cha kutosha, naomba tubadilike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa Wakala wa Vipimo. Amezungumza Mheshimiwa Lwenge akafikiria labda viazi vya kutoka Mporoto ambako ndiyo Jimboni kwangu labda kuna nafuu, sisi ndiyo kuna usumbufu mkubwa, hatulali. Magari yanakuwa yamebeba viazi, wakulima maskini amekodi gari tani saba siyo ya mtu mmoja, hana hela, akiuza Dar es Salaam ndiyo apate nauli ya kumrudishia mwenye gari lakini…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee ninaomba kuungana na Watanzania wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kutimiza mwaka mmoja wa kuongoza nchi yetu akiwa Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tumeshuhudia mafanikio makubwa katika kuimarisha miundombinu hususan barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari, huduma za kiuchumi na kijamii kama vile ujenzi wa madarasa, hospitali, zahanati na vituo vya afya, huduma za maji, utawala bora pamoja na kuhamasisha uwekezaji na utalii. Pia naomba nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Philip Isidor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri iliyotukuka ya kumsaidia Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mawaziri na Naibu Mawaziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka. Tathmini zinathibitisha mafanikio mazuri ya utekelezaji na usimamizi wa Mpango wa Kwanza na wa Pili kupelekea Taifa letu la Tanzania kufanya vizuri mno kuinua uchumi katika kipindi hiki kigumu. Kutokana na taarifa za Benki ya Dunia, ni Tanzania pekee ambayo uchumi wake umekua kwa asilimia 4.9, wakati nchi karibu zote za Afrika Mashariki zimekua na ukuaji hasi (negative GDP growth).

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi na Naibu Spika kwa kuchaguliwa kwa kura zote asilimia 100. Pia napenda kupongeza uongozi wote wa Bunge kwa uongozi mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza Mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Taifa letu katika ya ushindani wa kimataifa (National Competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2021 mpaka Februari, 2022 Serikali imeendelea kutekeleza miradi ya kimkakati kwa mafanikio mkubwa sana na utekelezaji huu unaonekana mpaka kwenye ngazi ya Halmashauri zetu. Mafanikio makubwa yamejikita kwenye uboreshaji wa miundombinu ya barabara, reli, bandari, mtandao wa mawasiliano na uboreshaji wa usafiri wa anga. Napongeza Serikali kwa hatua nzuri za utekelezaji wa mradi wa kihistoria wa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR na ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (megawati 2,115). Miradi hii miwili ya SGR na umeme, ni nguzo imara ya kiushindani katika uchumi wetu na nchi za Maziwa Makuu na hata za Kusini mwa Afrika na Kati.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio hayo, uchumi wa dunia umekumbwa kwa kiasi kikubwa na athari za UVIKO-19 na hivi sasa kuathirika zaidi na vita ya Urusi na Ukraine. Kwa mujibu wa Taarifa ya Shirika la Fedha la Kimataifa ya Januari, 2022 kasi ya ukuaji wa uchumi wa dunia inatarajiwa kupungua hadi kufikia asilimia 4.4 mwaka 2022 ikilinganishwa na asilimia 5.9 mwaka 2021. Hali hiyo inatarajiwa kusababisha kuvurugika zaidi kwa mnyororo wa uzalishaji na usambazaji wa bidhaa na huduma na athari hizo zinaikumba hata Tanzania. Hivi karibuni kumekuwepo na taarifa za uhaba na upandaji wa bei kwenye bidhaa za petroli, ujenzi, vyakula, nishati na hata pembejeo za kilimo.

Mheshimiwa Spika, kutokana na athari za UVIKO-19 na vita ya Urusi na Ukraine, Serikali inatakiwa kuchukua hatua za kibajeti kukabiliana hasa na mfumuko wa bei na kuporomoka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani na sarafu kuu zingine. Kwa kuzingatia kuyumba kwa uchumi wa dunia, dajeti hii ijielekeze kuchukua hatua za kuimarisha pato la Taifa kupitia sekta za kilimo, madini, utalii na uchukuzi. Hatua hizi ziende sambamba na kuimarisha mazingiara ya uwekezaji hasa kwenye sekta ya kilimo na madini. Kutokana na mfumuko wa bei kwenye bidhaa za petroli na mtikisiko wa thamani ya shilingi, kutapelekea mahitaji zaidi ya fedha za kigeni na hivyo msukumo uwepo kwenye kuongeza uzalishaji wa madini na mazao ya kilimo. Hatua hizi ni muhimu kuimarisha uhimilivu wa deni la Taifa hasa kwenye kigezo za ulipaji wa deni la nje kwa kulingamisha na uuzaji wa bidhaa nje (mapato ya fedha za kigeni).

Mheshimiwa Spika, pamoja na msukumo kwenye kilimo, madini na utalii, Serikali inatakiwa kuwekeza hasa kwenye miundombinu ya usafirishaji ikiwemo barabara, reli, bandari na usafiri wa anga hasa kwa mizigo. Katika Halmashauri zetu tumekuwa tunakabiliwa na changamoto hasa kwenye miundombinu ya barabara. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, barabara zinazohudumiwa na TARURA kwa asilimia zaidi ya 80 zipo kwenye hali mbaya sana kutoka na mafuriko. Maeneo mengi ya vijijini barabara hazipitiki kutokana na madaraja kusombwa na mafuriko. Naomba Serikali ichukue hatua za haraka kunusuru hali hii ili wananchi waweze angalau kusafirisha mazao yao.

Mheshimiwa Spika, naomba Serikali iweke msukumo zaidi kwenye kuboresha miundombinu ya barabara kurahisisha usafirishaji wa mazao ya kilimo. Kutokana na fursa za uzalishaji mkubwa kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, napendekeza muendelezo wa uboreshaji wa barabara za TANZAM kipande cha Igawa - Tunduma; barabara ya bypass ya Uyole - Songwe; barabara ya Mbalizi – Shigamba – Isongole kutokana na uzalishaji wa mazao ya kilimo; barabara ya Mbalizi – Galula – Makongorosi kutokana na uzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo na madini; na pia barabara ya Isyonje – Kikondo – Makete ambayo ni muhimu sana katika kusafirisha mazao ya kilimo ikiwemo maua, parachichi na viazi kwa soko la nje. Uboreshaji wa barabara hizi pamoja na uwanja wa ndege wa Songwe ni muhimu sana kwa usafirishaji wa mazao yetu kwa soko la ndani na nje, na kwa kiasi kikubwa utaongeza mapato ya fedha za kigeni.

Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto za vita ya Urusi na Ukraine, bado kuna fursa kubwa kwa Tanzania hasa kwenye uzalishaji wa ziada wa mazao mbalimbali na hasa nafaka kuziba pengo la nafaka kutoka Urusi na Ukraine kwenda nchi kadhaa za Afrika na mabara mengine. Serikali iimarishe upatikanaji wa pembejeo bora kwa bei nafuu na kuimarisha upatikanaji wa masoko ya uhakika. Kutokana na jitihada walizofanya Wizara ya Kilimo kuwapatia vitendea kazi Maafisa Ugani, ichochee kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya kilimo kutoka uzalishaji wa sasa ambao upo chini sana ikiwemo uzalishaji wa kilo 1,000 za mahindi kwa eka mpaka kilo 4,000 kwa eka ya mahindi.

Mheshimiwa Spika, kwa lengo la kuvutia wawekezaji na kuongeza pato la fedha za kigeni, napendekeza Serikali kuchukua hatua kuharakisha uwekezaji kwenye mradi wa madini ya Niobium ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kiwanda cha Ferroniobium (FeNb) ambacho kitakuwa cha kwanza Afrika na cha nne duniani. Kutokana na mahitaji makubwa ya ujenzi wa reli, madaraja yakiwemo reli ya SGR, kuna mahitaji makubwa ya vifaa vya chuma ambavyo ni imara, lakini vyepesi na vyenye ubora wa kimataifa. Kwa kutumia sheria zetu za uwekezaji, Serikali itumie fursa za kipindi hiki ili kuvutia wawekezaji kwenye madini ya viwandani ili yaongezwe thamani hapa kwetu na pia kuvutia malighafi ya madini toka nchi zingine ili yachakatwe hapo kwetu. Tanzania imebahatika kuwepo kwa madini ya Niobium ambayo inapatikana milima ya Panda Hill Wilaya ya Mbeya, na mahitaji ya Ferroniobium (FeNb end product) ni makubwa duniani na hapa kwetu pia. Kwa kutumia rasilimali zetu za madini, Serikali inaweza kutengeneza fursa nyingi na kupitia Mradi wa Niobium na Kiwanda cha Ferroniobium, ajira 2,000 zitakazozalishwa wakati wa ujenzi na pia kutakuwepo ajira za kudumu zaidi ya 600 na indirect jobs 7,000.

Mheshimiwa Spika, mradi utazalisha mapato kila mwaka shilingi bilioni 500 (dola za Kimarekani milioni 220) ambapo mapato kwa Serikali kila mwaka shilingi bilioni 50 (dola za Kimarekani milioni 22) uhai wa mgodi ni zaidi ya miaka 30. Hiki kitakuwa kiwanda cha kisasa cha kwanza Afrika (Modern Manufacturing Plant and Smelter). Pamoja na kuingiza teknolojia hii adimu na ujuzi (skills transfer) pia itakuwa itachangia huduma za kijamii (Corporate Social Investment in Community) na chanzo cha fedha ya kigeni.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa fursa na mimi ya kuchangia kwenye hii Hotuba ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti,nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na timu yake kwa hotuba yake nzuri ambayo imeonesha ni kiasi gani kulikuwa na mafanikio makubwa ya utendaji wa Serikali hasa ukizingatia hiki kipindi tunachopitia. Tanzania si Kisiwa; sisi wenyewe tumeshuhudia kiasi gani ambavyo mtikisiko wa dunia umeathirika kutokana na UVIKO-19 pamoja na vita vya Urusi na Ukraine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mataifa makubwa yametikisika kikubwa. Wenzetu huko ukiangalia mfumuko wa bei ni zaidi ya tarakimu mbili na kuna wengine wanakaribia tarakimu tatu. Sasa, ukiangalia hotuba ya Waziri Mkuu inaonesha sisi tuko chini ya asilimia tano ambayo ni asilimia 4.7 kwa mwaka huu. Vilevile tunategemea hata hali itakuwa nzuri kwenye bajeti ijayo. Sasa utaona ni maajabu kiasi gani kwa nchi kama Tanzania tunafanya vizuri ukilinganisha na mataifa makubwa. Leo hii kuna benki kubwa za dunia ambazo tulikuwa tunaziamini, nazo zimetikisika. Kwa hiyo hili si jambo dogo, ni jambo la kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa aliyoifanya katika kuhakikisha kuwa Tanzania tunakuwa katika hali hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiangalia hata ukuaji katika repoti ya Waziri Mkuu inaonesha kuwa ukuaji wa uchumi kwa Tanzania bado ni mzuri ukilinganisha na wenzetu. Ukiangalia ukusanyaji wa mapato bado ni mzuri ukilinganisha na wenzetu. Kwa nini tunajilinganisha na wenzetu? Ni kwa vile mpango wetu ni wa ushindani kiuchumi, ambao unahitaji kuonesha kiasi gani Tanzania tufanye vizuri ukilinganisha na mataifa mengine. Nchi jirani hapa tumeona mtikisiko wa uchumi, ukuaji wa uchumi umekuwa hasi. Vilevile leo hii hata ukusanyaji wa mapato wenzetu majirani wameshindwa kukusanya kiasi ambacho umepelekea hata kushindwa kulipa mishahara ya wafanyakazi wao. Sisi tunajivunia kwa Mheshimiwa Rais wetu pamoja na timu yake nzima ambavyo wameendelea kufanya vizuri na hali inakuwa na matumaini mazuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti,namshukuru Mheshimiwa Rais vile vile kwa jimbo langu na Wilaya yangu ya Mbeya, ametutendea mengi mno. Kwenye maji kwa kweli hata nikiuliza swali hapa litakuwa ni swali la kupongeza kwa sababu miradi mingi ya maji imeenda vizuri na inaendelea kutekelezwa. Hivi juzi Serikali imesaini mkataba wa mradi mkubwa wa maji ambao ni kwa Wilaya nzima ya Mbeya, likiwemo jimbo langu, pamoja na Mkoa wa Songwe, Mradi wa Kiwila.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye barabara vilevile kilikuwa ni kilio kikubwa. Mheshimiwa Rais naye ameidhinisha ujenzi wa barabara ya njia nne kuanzia Nsalaga ambayo iko jimbo la Mbeya Mjini mpaka Songwe ambayo iko Jimbo la Mbeya Vijijini. Hii ni hatua kubwa kwa sababu pamoja na changamoto zote, lakini Watanzania wengi wamepoteza maisha kwa ajili ya ufinyu na barabara ilivyokuwa mbovu, hii barabara yetu ya TANZAM.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kumalizia ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Songwe, kwa kweli Mbeya ni ya kimkakati. Uwanja wa Ndege wa Songwe ambao ni mahsusi utakuwa wa kimataifa kwa ajili ya kusomba mizigo kupeleka nchi za kigeni. Mheshimiwa Rais amefanya jambo hili katika wakati mwafaka ambao tunategemea kuwa sasa Tanzania, badala ya mazao yetu kuoneshwa yanatoka nchi jirani, sasa hivi kwakweli tutakuwa hatuna sababu tena kuona maparachichi au kahawa zinatoka nchi jirani badala ya kwamba zinatokea Tanzania.

Mheshimiwa Spika, katika hili naomba Serikali, iangalie ni namna gani sasa ule uwanja uzungukwe na eneo maalumu la viwanda (industrial park) au EPZ, kama alivyozungumza mwenzangu. Pale tunahitaji tuwe na cold rooms za kutosha. Ule uwanja si kwa ajili ya Mbeya peke yake, ni kwa ajili ya Nyanda za Juu Kusini. Wenzetu wanalalamika kuhusu maparachichi yanaharibika; lakini huwezi kupeleka maparachichi, lazima yaandaliwe. Pia tunazalisha mazao mengi, matunda mengi na mboga mboga. Sasa tujiandae wakati huu ambao tumenunua ndege ya mizigo iweze kufanya kazi ya kusafirisha mizigo ambayo itakwenda kiushindani kwenye masoko ya nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Rais vilevile kwa miradi ya umeme. Tumeenda vizuri na sasa hivi tunamalizia vijiji 40 vya mwisho ambapo nategemea kabla ya mwaka huu vijiji vyote vitakuwa vimeguswa ili tuendelee na utekelezaji kwenye vitongoji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote hayo ili tuweze kustahimili na kukaa katika utulivu kwenye nchi yetu tunahitaji haya mambo yaweze kuendelea kama ilivyo sasa na yaboreshwe. Naomba Serikali iendelee kujenga barabara. Barabara ya TANZAM ni muhimu sana. Kipande cha kuanzia Igawa mpaka Tunduma kiko kwenye hali mbaya sana. Naomba Serikali ichukue hatua za haraka kwa sababu hii barabara inatuweka katika ushindani na Bandari yetu ya Dar Es Salaam ili iweze kushindana na bandari za nje. Kwa hiyo hili suala siyo la barabara ni suala la kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hiyo barabara napendekeza vilevile barabara ya Mbalizi-Shigamba, Mheshimiwa Waziri Mkuu uliahidi wewe mwenyewe hii barabara na ukasema hutaki tena usikie nauliza swali wala niongelee kuhusu hii barabara. Nakuomba mwaka huu kwenye bajeti hii, hii barabara iweze kujengwa kwa kiwango cha lami. Pia Barabara ya Isyonje-Ikondo nayo ni barabara muhimu kwa ajili ya kulisha uwanja wa Songwe. Vilevile barabara ya Mbalizi-Gadula naomba nayo ikamilishwe haraka kwenye bajeti ya mwaka huu. Pia by pass ambayo inaanzia Uyole mpaka Songwe nayo ni muhimu ikakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yote haya tunahitaji Serikali iboreshe reli ya TAZARA. Reli ya TAZARA ni muhimu; na mimi naweza kusema uboreshaji wake ni quick wins, haiitaji mambo makubwa. Nina imani Serikali ikitenga angalau bilioni 300 ile reli inaweza kuboreshwa. Kwa sababu ukiboresha reli ya TAZARA unakuwa umeweka mizigo asilimia zaidi ya 70 ambayo inapita Bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya soko la nje itapitia kwenye Reli ya TAZARA na bandari yetu itakuwa competitive.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bandari yetu sasa hivi iko kwenye ushindani mkubwa na inawezekana tukashindwa kushindana kwa vile kuna Lobito ambazo ziko Angola. Wale wenzetu wametengeneza mpaka barabara za kuja kwenye masoko yetu. Vilevile kuna bandari za Afrika…

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa, inatoka wapi taarifa.

T A A R I F A

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe taarifa kuhusu hoja inayozungumzwa sasa. Shirika la Reli la TAZARA ni shirika ambalo lilianzishwa kwa ubia wa Tanzania na Zambia sasa katika mgawanyo wa hisa ilikuwa ni kwamba Tanzania ina hisa 50 na Zambia asilimia 50. Sasa kuna changamoto ya kisheria, kwamba hakuna yeyote anayeweza kuongeza mtaji au akaboresha hiyo Reli akaongeza gharama kwa sababu bado atabaki na asilimia ile ile asilimia 50. Kwa hiyo namuunga mkono mzungumzaji ahsante sana.

MWENYEKITI: Mheshimiwa unapokea taarifa hiyo?

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa mwenyekiti, naipokea hiyo taarifa, hayo ni mojawapo ya maboresha ambayo yanatakiwa yafanyike kwenye reli ya TAZARA. Ni kweli inahitaji maboresho kwenye mkataba na nina imani kwa vile Mheshimiwa Rais pamoja na Rais wa Zambia walikutana hivi karibuni na katika ajenda yao ilikuwa ni namna gani wanaweza kuboresha reli ya TAZARA kwa hiyo nina imani kwamba kwenye kipande cha Tanzania sisi tuchukue hatua zaidi ili twende mbele zaidi kwa sababu hili ni suala la ushindani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwenye suala la umeme ninaomba Serikali ikamilishe haraka Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, lakini kwenye suala la kilimo ninaomba Serikali iangalie ni namna gani tukitumie kilimo kuleta fedha nyingi za kigeni, hasa kwa kuongeza uzalishaji tija ili bidhaa zetu ziweze kufika kwenye masoko ya kigeni. Leo bidhaa zetu nyingi zikiwemo kahawa na maparachichi zinauzwa kwa label za mataifa mengine. Huo ni upotevu wa fedha za kigeni. Na tunahitaji pesa za kigeni kwa sababu sasa hivi tuna matatizo ya urali wa biashara. Urali wa biashara sisi hatuko vizuri sana, bidhaa tunazoagiza nje ni kubwa kuliko bidhaa tunazopeleka nje. Hii maana yake nini…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umemalizika.

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti,nashukuru sana naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee ninaomba kuungana na Watanzania wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kutimiza miaka miwili wa kuongoza nchi yetu akiwa Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tumeshuhudia mafanikio makubwa katika kuimarisha miundombinu hususan barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari, huduma za kiuchumi na kijamii kama vile ujenzi wa madarasa, hospitali, zahanati na vituo vya afya, huduma za maji, utawala bora, pamoja na kuhamasisha uwekezaji na utalii. Na pia naomba nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Philip Isidor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri iliyotukuka ya kumsaidia Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mawaziri, na Naibu Mawaziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka. Tathmini zinathibitisha mafanikio yao mazuri ya utekelezaji na usimamizi wa Mpango wa Kwanza na wa Pili kupelekea Taifa letu la Tanzania kufanya vizuri mno kuinua uchumi katika kipindi hiki kigumu. Ukuaji wa uchumi wa Tanzania kwa mwaka 2022 umepungua hadi kufikia wastani wa asilimia 4.7 kutoka ukuaji wa asilimia 4.9 mwaka 2021 na kuongezeka hadi kufikia asilimia 5.3 mwaka 2023.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi na Naibu Spika na pia uongozi wote wa Bunge kwa uongozi mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri iliojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Taifa letu katika ya ushindani wa Kimataifa (National Competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2022 mpaka Machi, 2023 Serikali imeendelea kutekeleza miradi ya kimkakati kwa mafanikio mkubwa sana na utekelezaji huu unaonekana mpaka kwenye ngazi ya Halmashauri zetu. Mafanikio makubwa yamejikita kwenye uboreshaji wa miundombinu ya barabara, reli, bandari, mtandao wa mawasiliano na uboreshaji wa usafiri wa anga. Naipongeza Serikali kwa hatua nzuri za utekelezaji wa mradi wa kihistoria wa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR na ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (megawati 2,115). Miradi hii miwili ya SGR na umeme ni nguzo imara ya kiushindani katika uchumi wetu na nchi za Maziwa Makuu na hata za Kusini mwa Afrika na Kati.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio hayo, uchumi wa dunia umekumbwa kwa kiasi kikubwa na athari za UVIKO- 19 na hivi sasa kuathirika zaidi na vita ya Urusi na Ukraine. Hivi karibuni kumekuwepo na taarifa katika nchi jirani za changamoto za ukwasi, uhaba na upandaji wa bei kwenye bidhaa za petroli, ujenzi, vyakula, nishati na hata pembejeo za kilimo.

Mheshimiwa Spika, kutokana na athari za UVIKO-19 na vita ya Urusi na Ukraine, Serikali inatakiwa kuendelea kuchukua hatua za kibajeti kukabiliana hasa na mfumuko wa bei na kuporomoka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani na sarafu kuu zingine. Kwa kuzingatia kuyumba kwa uchumi wa dunia, bajeti hii ijielekeze kuchukua hatua za kuchochea uzalishaji wa ndani ili kupunguza balance of payment – BOP, kuimarisha Pato la Taifa kupitia sekta za kilimo, madini, utalii na uchukuzi. Hatua hizi ziende sambamba na kuimarisha mazingira ya uwekezaji hasa kwenye sekta ya kilimo na madini.

Mheshimiwa Spika, pia Serikali iendelee kusimamia sera ya fedha na bajeti ikiwemo kuimarisha mifumo na kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za Serikali. Kutokana na mfumuko wa bei kwenye bidhaa za petroli na mtikisiko wa thamani ya shilingi, kutapelekea mahitaji zaidi ya fedha za kigeni na hivyo msukumo uwepo kwenye kuongeza uzalishaji wa madini na mazao ya kilimo. Hatua hizi ni muhimu kuhakikisha utulivu wa thamani ya shilingi na pia kuimarisha uhimilivu wa deni la Taifa hasa kwenye kigezo cha ulipaji wa deni la nje kwa kulinganisha na uuzaji wa bidhaa nje (mapato ya fedha za kigeni).

Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto za vita ya Urusi na Ukraine, bado kuna fursa kubwa kwa Tanzania hasa kwenye uzalishaji wa ziada wa nafaka kuziba pengo la nafaka kutoka Urusi na Ukraine kwenda nchi kadhaa za Afrika na mabara mengine. Serikali iimarishe upatikanaji wa pembejeo bora kwa bei nafuu na kuimarisha upatikanaji wa masoko ya uhakika. Kutokana na ruzuku kwenye mbolea na jitihada walizofanya Wizara ya Kilimo kuwapatia vitendea kazi Maafisa Ugani, ichochee kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya kilimo kutoka uzalishaji wa sasa wa kilo 1,000 za mahindi kwa eka mpaka kilo 4,000 kwa eka ya mahindi.

Mheshimiwa Spika, pamoja na msukumo kwenye kilimo, madini na utalii, Serikali inatakiwa kuwekeza hasa kwenye miundombinu ya usafirishaji ikiwemo barabara, reli, bandari na usafiri wa anga hasa kwa mizigo. Katika Halmashauri zetu tumekuwa tunakabiliwa na changamoto hasa kwenye miundombinu ya barabara. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, barabara zinazohudumiwa na TARURA kwa asilimia zaidi ya 80 zipo kwenye hali mbaya sana kwa kukosa matengenezo ya mara kwa mara. Maeneo mengi ya vijijini barabara hazipitiki kutokana na ufinyu wa bajeti ukilinganisha na mtandao wa barabara zinazohudumiwa na TARURA. Naomba Serikali ichukue hatua za haraka kunusuru hali hii ili wananchi waweze angalau kusafirisha mazao yao.

Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuidhisha ujenzi wa barabara ya njia nne kuanzia Nsalaga (Uyole) mpaka Uwanja wa Ndege wa Songwe. Kipande hiki cha barabara ambacho ni sehemu ya barabara kuu ya TANZAM, ni muhimu sana kwa kuinua uchumi wa Tanzania na hata kupunguza ajali za mara kwa mara zinazotokea katika mteremko wa Mlima Iwambi kuelekea Mji wa Mbalizi.

Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa usafirishaji wa mazao yetu kwa soko la ndani na nje ikiwemo fursa za biashara ukanda wa SADC na uzalishaji mkubwa kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, napendekeza muendelezo wa uboreshaji wa barabara za TANZAM kipande cha Igawa - Tunduma; barabara ya bypass ya Uyole - Songwe; barabara ya Mbalizi – Shigamba – Isongole kutokana na uzalishaji wa mazao ya kilimo; barabara ya Mbalizi – Galula – Makongolosi kutokana na uzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo na madini; na pia barabara ya Isyonje – Kikondo – Makete.

Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya kazi kubwa kuhakikisha ujenzi wa SGR unaendelea kwa kasi ile ile na pia napongeza jitihada za kuendelea kutafuta vyanzo vya fedha vya masharti nafuu kugharamia ujenzi huo. Pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa, Serikali imefanya maboresho makubwa ya miundombinu na huduma katika bandari zetu hususan bandari ya Dar es Salaam ili kukabiliana na ushindani mkubwa wa bandari zingine za ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika. Bandari ya Dar es Salaam inakumbana na ushindani mkubwa toka bandari za Mombasa (Kenya), Beira (Msumbiji), Nacala (Msumbiji), Durban (Afrika Kusini), Lobito (Angola) na Walvis Bay (Namibia). Maboresho ya bandari zetu iendane na kuondoa changamoto zingine ambazo zinasababisha gharama kubwa za usafirishaji kwa bandari zetu na kusababisha kupoteza biashara ya usafirishaji kwa bandari shindani. Ufanisi wa bandari unategemea pia maboresho ya barabara, reli ya kati (TRL), Reli ya TAZARA, utendaji wenye tija wa wadau wote wa bandari na hata watumishi ili kupunguza gharama za usafirishaji kwa wateja wa bandari zetu.

Mheshimiwa Spika, kwa taarifa zilizopo, karibu asilimia 72 ya mzigo wote wa nchi za nje unasafirishwa kwa kupitia Dar es Salaam Corridor ambapo DR Congo ni asilimia 36, Zambia asilimia 31 na Malawi asilimia tano. Pamoja na fursa za kijografia ya bandari zetu, mzigo unaopita sasa kwenye bandari ya Dar es Salaam ni asilimia 50 tu ya biashara yote ambayo kwa sasa inashikiliwa na bandari shindani. Kwa ajili ya kunusuru biashara hii inayopotea kwa bandari shindani, Serikali ichukue hatua za haraka kuboresha huduma za TAZARA ikiwa ni pamoja ya maboresho ya miundombinu ya reli, ununuzi wa vichwa vya reli, mabehewa na vitendea kazi vingine.

Mheshimiwa Spika, napendekeza Serikali kwa haraka ishughulikie maboresho ya mkataba wa TAZARA na kisha kutafuta fedha ya masharti nafuu angalau kiasi cha shilingi bilioni 300. Katika kipindi hiki cha ushindani mkubwa na hata mfumuko wa bei wa mafuta ya petroli, mbolea na bidhaa mbalimbali, usafirishaji wa reli ni mojawapo ya suluhisho kubwa kupunguzo mzigo wa bei kubwa kwa wateja wa bandari zetu na hata wananchi.

Mheshimiwa Spika, pamoja na maboresha ya reli ya TAZARA, napendekeza kuendelea na ujenzi wa bandari kavu Mbeya ambayo ina fursa kubwa katika kipindi hiki katika kuwezesha kupunguza gharama za kusafirisha kwa wateja wa bandari na hata kupunguza bei za mafuta ya petroli, pembejeo na mazao ya kilimo. Bandari kavu ya Mbeya ni njia panda kwa wateja wa nchi za Malawi, Zambia, DRC Lubumbashi na hata kwa Zimbabwe na Msumbiji.

Mheshimiwa Spika, reli ya TAZARA ambayo ni tegemeo kusafirisha mizigo kwa mikoa ya Pwani, Morogoro, mikoa yote ya Nyanda za Juu Kusini na pia mizigo ya nchi za nje ikiwemo, Zambia, Malawi, na DRC Congo, miundombinu inaendelea kuchakaa kutokana na kukosa matengenezo ya mara kwa mara. Serikali ichukue hatua za haraka kuinusuru reli ya TAZARA hata ikibidi kurekebisha mikataba ya umiliki na uongozi ili mradi iendeshwe kwa tija. Kuna kuchukua hatua za makusudi kwa kutumia zaidi TAZARA kusafirisha mizigo ambayo imeelemea hata uwezo wa barabara zetu. Usafirishaji wa mizigo kwa kutumia TAZARA ilenge kupunguza gharama za mafuta ya petroli, pembejeo kwa wakulima na wakati huo kupunguza gharama za kusafirisha mazao ya wakulima.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuboresha TAZARA, napendekeza kukamilisha taratibu za ujenzi wa bandari kavu ya Mbeya ambapo Mamlaka ya Bandari kwa kipindi kirefu wamewahakikishia wananchi kulipa fidia ya eneo lao wanalolichukua.

Mheshimiwa Spika, kwa lengo la kuvutia wawekezaji na kuongeza pato la fedha za kigeni, napendekeza Serikali kuchukua hatua kuharakisha uwekezaji kwenye mradi wa madini ya Niobium ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Kiwanda cha Ferroniobium (FeNb) ambacho kitakuwa cha kwanza Afrika na cha nne duniani. Kutokana na mahitaji makubwa ya ujenzi wa reli, madaraja na reli ya SGR, kuna mahitaji makubwa ya vifaa vya chuma ambavyo ni imara, lakini vyepesi na vyenye ubora wa kimataifa. Kwa kutumia sheria zetu za uwekezaji, Serikali itumie fursa za kipindi hiki ili kuvutia wawekezaji kwenye madini ya viwandani ili yaongezwe thamani hapa kwetu na pia kuvutia malighafi ya madini toka nchi zingine ili yachakatwe hapo kwetu.

Mheshimiwa Spika, Tanzania imebahatika kuwepo kwa madini ya Niobium ambayo yanapatikana milima ya Panda Hill, Songwe Wilaya ya Mbeya na mahitaji ya Ferroniobium (FeNb end product) ni makubwa duniani na hapa kwetu pia. Kwa kutumia rasilimali zetu za madini, Serikali inaweza kutengeneza fursa nyingi na kupitia Mradi wa Niobium na Kiwanda cha Ferroniobium, ajira 2,000 zitakazozalishwa wakati wa ujenzi na pia kutakuwepo ajira za kudumu zaidi ya 600 na indirect jobs 7,000. Mradi utazalisha mapato kila mwaka shilingi bilioni 500 (US$ 220 million) ambapo mapato kwa Serikali kila mwaka shilingi bilioni 50 (US$ 22 million), uhai wa mgodi ni zaidi ya miaka 30. Hiki kitakuwa kiwanda cha kisasa cha kwanza Afrika (Modern Manufacturing Plant and Smelter). Pamoja na kuingiza teknolojia hii adimu na ujuzi (skills transfer) pia itakuwa itachangia huduma za kijamii (Corporate Social Investment in Community) na chanzo cha fedha ya kigeni.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mawaziri na viongozi wote wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha uendelezaji wa miradi ya kimkakati na pia utayari wetu wa ushindani wa kimataifa (national competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miezi kumi ya bajeti inayoishia Juni, 2023 Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imetekeleza miradi mingi ya miundombinu ya barabara, reli, bandari na uimarishaji wa safari za anga ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa viwanja vya ndege. Naipongeza Serikali kwa hatua nzuri za utekelezaji wa mradi wa kihistoria wa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR pamoja na uboreshaji wa bandari utaimarisha kwa kiasi kikubwa uchumi wa nchi yetu. SGR na bandari ni nguzo imara ya kiushindani katika biashara ya usafirishaji wa ndani na nchi za Maziwa Makuu na hata za Kusini mwa Afrika na Kati. Bandari za Tanzania ni lango la usafirishaji kwa Zambia, Malawi, DR Congo, Uganda, Burundi, Rwanda, Sudan ya Kusini na hata Zimbabwe na Msumbiji.

Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya kazi kubwa kuhakikisha ujenzi wa SGR unaendelea kwa kasi ile ile na pia napongeza jitihada za kuendelea kutafuta vyanzo vya fedha vya masharti nafuu kugharamia ujenzi huo. Pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa, Serikali imefanya maboresho makubwa ya miundombinu na huduma katika bandari zetu hususana bandari ya Dar es Salaam ili kukabiliana na ushindani mkubwa wa bandari zingine za ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika. Bandari ya Dar es Salaam inakumbana na ushindani mkubwa toka bandari za Mombasa (Kenya), Beira (Msumbiji), Nacala (Msumbiji), Durban (Afrika Kusini), Lobito (Angola) na Walvis Bay (Namibia). Maboresho ya bandari zetu iendane na kuondoa changamoto zingine ambazo zinasababisha gharama kubwa za usafirishaji kwa bandari zetu na kusababisha kupoteza biashara ya usafirishaji kwa bandari shindani. Ufanisi wa bandari unategemea pia maboresho ya barabara, Reli ya Kati (TRL), Reli ya TAZARA, utendaji wenye tija wa wadau wote wa bandari na hata watumishi ili kupunguza gharama za usafirishaji kwa wateja wa bandari zetu.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa karibu asilimia 70 ya mzigo wote wa nchi za nje unasafirishwa kwa kupitia Dar es Salaam Corridor ambapo DR Congo ni asilimia 38, Zambia asilimia 26, na Malawi asilimia 6. Pamoja na fursa za kijografia ya bandari zetu, mzigo unaopita sasa kwenye bandari ya Dar es Salaam, ni chini ya asilimia 50 ya biashara yote ambayo kwa sasa sehemu kubwa inashikiliwa na bandari shindani.

Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa za kiushindani zinatokana na ufanisi usiokidhi ushindani na gharama kubwa za bandari na watoa huduma wa Bandari ya Dar es Salaam. Pia kuna changamoto za kiutendaji kwa mashirika ya reli ya TAZARA na hata reli ya kati (TRL) inayopelekea gharama kubwa ambazo siyo za kiutendaji, kwa ajili ya kunusuru biashara hii inayopotea kwa bandari shindani, Serikali ichukue hatua za haraka kuboresha huduma za TAZARA ikiwa ni pamoja ya maboresho ya miundombinu ya reli, ununuzi wa vichwa vya treni, mabehewa na vitendea kazi vingine.

Mheshimiwa Spika, napendekeza Serikali kwa haraka ishughulikie maboresho ya Mkataba wa TAZARA na kisha kufuta fedha ya masharti nafuu angalau kiasi cha shilingi bilioni 200. Katika kipindi hiki cha ushindani mkubwa na hata mfumuko wa bei wa mafuta ya petroli, mbolea na bidhaa mbalimbali, usafirishaji wa reli ni mojawapo ya suluhisho kubwa kupunguza mzigo wa bei kubwa kwa wateja wa bandari zetu na hata wananchi.

Mheshimiwa Spika, pamoja na maboresha ya reli ya TAZARA, napendekeza kuendelea na ujenzi wa Bandari Kavu Mbeya ambayo ina fursa kubwa katika kipindi hiki katika kuwezesha kupunguza gharama za kusafirisha kwa wateja wa bandari na hata kupunguza bei za mafuta ya petroli, pembejeo na mazao ya kilimo. Bandari Kavu ya Mbeya ni njia panda kwa wateja wa nchi za Malawi, Zambia, DRC Lubumbashi na hata kwa Zimbabwe na Msumbiji. Serikali ichukue hatua za haraka kuinusuru reli ya TAZARA hata ikibidi kurekebisha mikataba ya umiliki na uongozi ili mradi iendeshwe kwa tija. Kuna kuchukua hatua za makusudi kwa kutumia zaidi TAZARA kusafirisha mizigo ambayo imeelemea hata uwezo wa barabara zetu.

Mheshimiwa Spika, usafirishaji wa mizigo kwa kutumia TAZARA ilenge kupunguza gharama za mafuta ya petroli, pembejeo kwa wakulima na wakati huo kupunguza gharama za kusafirisha mazao ya wakulima. Pamoja na kuboresha TAZARA, napendekeza kukamilisha taratibu za ujenzi wa Bandari Kavu ya Mbeya ambapo Mamlaka ya Bandari kwa kipindi kirefu wamewahakishia wananchi kulipa fidia ya eneo lao wanalolichukua.

Mheshimiwa Spika, napendekeza Bandari ya Dar es Salaam kuingia makubaliano na TAZARA na TRL ili iweze kumiliki mabehewa yake kwa lengo la kuongeza ufanisi na kupunguza gharama ambazo sio za kiushindani. Pamoja na hatua hiyo, kuna fursa kubwa ya kutafuta mwekezaji mwenye uzoefu mkubwa ikiwemo mtandao wa bandari kwa lengo la kuboresha utendaji hasa kwenye upande wa makontena. Serikali ifanye jitihada ya kupata mwekezaji ikiwemo kwa mfumo wa PPP kwa lengo la kuongeza biashara ikiwemo kurudisha biashara iliyopotea kwa bandari shindani.

Mheshimiwa Spika, kwa siku za hivi karibuni kuna mahitaji makubwa ya kusafirisha makaa ya mawe kwenda soko la nje na pia uingizwaji wa Sulphur kutoka nje lakini imepelekea kuthibitisha upungufu mkubwa wa gari kubwa hasa aina ya tiper. Upungufu huu unapelekea kuzorota kwa ufanisi wa huduma ya bandari.

Mheshimiwa Spika, napendekeza Serikali iendelee na mkakati wa kutafuta mwekezaji wa Bandari ya Mbegani – Bagamoyo ambayo ina lango lenye kina cha asili cha mita 18 na haina kikomo cha upana wa meli ambazo zinaweza kuingia na kutoka bandarini hapo. Kutokuwepo kwa ukomo katika lango, bandari hiyo inaweza kuhudumia meli ambazo zinahudumiwa kwenye bandari kubwa duniani zenye urefu wa mita 400 na uwezo wa kubeba makasha hadi TEUs 22,000. Aidha, uwezo huu ni mkubwa katika eneo la Afrika Mashariki na Kati kwani kwa sasa hakuna bandari yenye uwezo kama huo. Hivyo, uendelezaji wa Bandari ya Mbegani, Bagamoyo utasaidia kupunguza msongamano wa shehena katika Bandari ya Dar es Salaam na kupelekea bandari zote kuwa shindani.

Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto za mfumuko wa bei za mafuta na pembejeo, kuna fursa kubwa na hasa mahitaji makubwa ya mazao ya kilimo kwa soko la ndani na nje. Uzalishaji kwa tija unategemea kwa kiasi kikubwa ubora wa miundombinu ya barabara, reli na hata anga. Serikali iweke msukumo zaidi kwenye kuboresha miundombinu ya barabara ili kurahisisha usafirishaji wa pembejeo na mazao ya kilimo. Kutokana na fursa za uzalishaji mkubwa kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, napendekeza mwendelezo wa uboreshaji wa barabara za TANZAM kipande cha Igawa - Tunduma; barabara ya bypass ya Uyole - Songwe; barabara ya bypass ya Iwambi - Mbalizi; barabara ya Mbalizi – Shigamba – Isongole kutokana na uzalishaji wa mazao ya kilimo; barabara ya Mbalizi – Galula – Makongorosi kutokana na uzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo na madini; na pia barabara ya Isyonje – Kikondo – Makete ambayo ni muhimu sana katika kusafirisha mazao ya kilimo ikiwemo maua, parachichi na viazi kwa soko la nje.

Mheshimiwa Spika, uboreshaji wa barabara hizi pamoja na uwanja wa ndege wa Songwe ni muhimu sana kwa usafirishaji wa mazao yetu kwa soko la ndani na nje, na kwa kiasi kikubwa utaongeza mapato ya fedha za kigeni. Maboresho ya uwanja wa ndege wa Songwe uende sambamba na ujenzi wa maghala mahususi wa maua, mbogamboga, parachichi, nyama, viwanda vya kuengeza thamani za mazao na madini, na EPZ/Industrial Park.

Mheshimiwa Spika, kutokana na ajali za mara kwa mara za Mlima Iwambi, Mbalizi na msongamano wa magari yakiwemo malori ya mizigo na mafuta ya petroli, tunashukuru kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchukua hatua za haraka kuanza ujenzi wa barabara ya njia nne kwa barabara ya TANZAM kipande cha Uyole mpaka Uwanja wa Ndege wa Songwe. Katika vipindi mbalimbali, viongozi wa Kitaifa waliagiza upanuzi wa kipande hiki cha TANZAM pamoja na ujenzi wa bypass ya Uyole – Songwe kilometa 40 na bypass ya Mbalizi – Iwambi kilometa 6.5. Ujenzi wa barabara hizi utanusuru wananchi kuendelea kupoteza maisha kwa ajali za mara kwa mara katika eneo hilo. Hatari zaidi ni kwa magari makubwa yanayosafirisha mafuta kupita barabara yenye msongamano mkubwa katikati ya Jiji la Mbeya. Msongamano wa magari makubwa katika barabara ya TANZAM ni sehemu ya changamoto zinazopelekea bandari zetu kupoteza biashara kwa bandari shindani.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mawaziri na viongozi wote wa Wizara ya Fedha na Mipango, kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza Waziri wa Fedha na Mipango, kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha ubunifu wa ukusanyaji mapato na usimamizi mzuri wa matumizi ya Serikali ikiwa ni pamoja na uendelezaji wa miradi ya kimkakati na pia utayari wetu wa ushindani wa kimataifa (national competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha miezi kumi, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imesimamia kwa ufanisi ukusanyaji mapato na utekelezaji wa miradi mingi ya miundombinu ya barabara, reli, bandari na kaadhalika. Napongeza Serikali kwa mwendelezo mzuri wa utekelezaji wa mradi wa kihistoria wa umeme Mto Rufiji, Mradi wa kihistoria wa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR pamoja na uboreshaji wa bandari utaimarisha kwa kiasi kikubwa uchumi wa nchi yetu. Umeme, reli na bandari ni nguzo imara ya kiushindani katika uchumi wa Tanzania na nchi za Maziwa Makuu na hata za Kusini mwa Afrika na Kati.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi hiki wakati dunia inapambana na athari za vita vya Urusi na Ukraine na pia janga la corona virus (covid-19), tumejifunza umuhimu wa kuwepo kwa mikakati mbadala kutokana na nchi nyingi tunazoshirikiana kibiashara na kiuchumi kukumbwa na mtikisiko wa kiuchumi. Biashara zilizoathirika kwa kiasi kikubwa ni za usafirishaji hasa wa anga uliathirika sana na napongeza mkakati wa shirika la ndege kwa utendaji wenye tija na hata kununua ndege mpya ya mizigo na kujipanga kuanza kutumia ndege zake kusafirisha mizigo. Mkakati huu ambao umetumiwa na hata mashirika makubwa ya ndege duniani, utawezesha usafirishaji wa mazao yetu ya kilimo kufikia masoko kirahisi na hapo hapo uhakika wa mapato kwa shirika la ndege hasa kipindi hiki kukiwa na uhutaji mkubwa wa usafirishaji mizigo kwa ndege.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Msajili wa Hazina anapaswa kuendelea kuimarisha mitaji kwa mashirika ambayo yatachochea ukuaji wa uchumi ikiwemo Benki za TADB, TCB, TIB na ATCL ili iweze kusimama kibiashara ikiwa ni nguzo muhimu hata kwa sekta zingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, napongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali kwa kurudisha Tume ya Mipango na hata maboresho ya Ofisi ya Msajili wa Hazina. Tume ya Mipango ni nguzo muhimu katika kuimarisha uchumi wa nchi yetu hasa katika kipindi hiki tunapotekeleza miradi mingi ya kimkakati. Upangaji na utekelezaji wa miradi unahitaji kuwa na chombo madhubuti kinachoweza simamia miradi kitaifa badala ya kusimamiwa kisekta. Msajili wa Hazina anapaswa kupewa nguvu zaidi ili asimamie mashirika ya umma ili yaendeshwe kibiashara na kwa tija ya kiushindani kwa hapa nchini na hata nje ya nchi. Kuongezeka kwa tija kwenye mashirika ya kibiashara itapunguza kwa kiasi kikubwa utegemezi wa mapato ya kikodi na hata mikopo kwa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, napendekeza kuhakikisha ujenzi wa SGR unaendelea hata kwa kutafuta vyanzo mbadala vya fedha kugharamia ujenzi huo, kwa vile kutakuwa na fursa kubwa za usafirishaji. Pamoja na ujenzi wa SGR, napendekeza kuendelea na kuboresha reli ya TAZARA na uboreshaji wa bandari zetu ikiwemo ujenzi wa bandari kavu ikiwemo ya Inyala, Mbeya ambayo ina fursa kubwa katika kipindi hiki ili kupunguza gharama za kusafirisha pembejeo na mazao. Serikali ichukue hatua za haraka kuinusuru reli ya TAZARA hata ikibidi kurekebisha mikataba ya umiliki na uongozi ili mradi iendeshwe kwa tija. Kuna umuhimu mkubwa kuchukua hatua za makusudi kwa kutumia zaidi TAZARA kusafirisha mizigo ambayo imeelemea hata uwezo wa barabara zetu. Usafirishaji wa mizigo kwa kutumia TAZARA ilenge kupunguza gharama za usafirishaji mizigo kwa wateja wa bandari kutoka Zambia, DRC, Malawi na hata kwa kupunguza gharama za usafirishaji wa pembejeo kwa wakulima na wakati huo kupunguza gharama za kusafirisha mazao ya wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, napendekeza Serikali iwekeze angalau shilingi bilioni 200 kwa mwaka kwa kipindi cha miaka mitatu kwa ajili ya kuboresha mindombinu ya reli na karakana. Uwekezaji huu utawezesha TAZARA kujiendesha kwa faida na hata kuipunguzia Serikali mzigo wa kulipa zaidi ya shilingi bilioni 15 kwa mwaka ikiwa ni mishahara ya wafanyakazi wa TAZARA. Uwekezaji huu unahitajika haraka wakati Serikali za Tanzania na Zambia zinaendelea na jitihada za kurekebisha mikataba ikiwemo wa uendeshaji wa TAZARA. Pamoja na kuboresha TAZARA, napendekeza kukamilisha taratibu za ujenzi wa Bandari Kavu ya Inyala, Mbeya ambapo Mamlaka ya Bandari kwa kipindi kirefu wamewahakishia wananchi kulipa fidia ya eneo lao wanalolichukua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna fursa nyingi za muda mfupi za kuongeza mapato kupitia hatua za kiutawala ikiwemo ya kuondokana na matumizi na malipo ambayo hayana tija kwa Serikali na hata walipakodi. Kutokana na mahitaji makubwa ya uwekezaji kwenye miradi ya kimkakati, uchumi wetu utaendelea kuwa na mahitaji makubwa ya mikopo ya pesa za kigeni na wakati huo huo kulipa mikopo iliyoiva. Serikali iweke mkakati wa kuhakikisha mapato ya fedha za kigeni yanaongezeka kupitia mazao ya kilimo, madini na utalii. Kuongezeka kwa mapato ya fedha za kigeni yatasaidia kuimarisha uhimilivu wa deni la Taifa na pia kuendeleza utulivu wa shilingi yetu dhidi ya sarafu kuu za kigeni na hata kuhakikisha utulivu wa mfumuko wa bei.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ihakikishe kipaumbele cha kuwekeza kwenye kilimo ikiwemo pembejeo na umwagiliaji kwa lengo la kuongeza tija na pia kuongeza mapato ya fedha za kigeni na kulinda mfumuko wa bei. Serikali inashauriwa kuchukua hatua zaidi za kuimarisha sekta za kilimo, utalii, na madini ili kukabiliana na athari za kiuchumi wa kidunia. Kutokana na athari za kiuchumi uliokumba dunia nzima ikiwemo changamoto za upatikanaji wa fedha za kigeni, hatua za kuimarisha sekta hizo hapo juu, inaweza kuwa fursa kwa Serikali kuvutia uwekezaji zaidi kwenye madini hasa dhahabu, viwanda vya mbolea kutokana uwepo wa malighafi za madini ya calcium carbonate, lime na phosphate. Dhahabu ina historia ya bei kutoyumba kwenye soko la dunia kwa vile mabenki yanatumia dhahabu kwenye kuwekeza na kutokana pia na kuyumba kwa thamani ya shillingi na hata dola ya Marekani, Serikali inaweza kutumia dhahabu kama mbadala wa kuwekeza amana zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mabadiliko ya kiuchumi kidunia, Benki Kuu nyingi duniani zimeanza kuwekeza zaidi kwenye dhahabu na hii ni ishara nzuri kwa bei ya dhahabu kuendelea kuimarika kwenye soko la dunia ambapo kwa mwezi Aprili, 2023 bei zaidi ya asilimia 11 ukilinganisha na bei za Desemba, 2022. Serikali ijielekeze kununua dhahabu kwa shilingi toka kwa wachimbaji wadogo na kisha kuzitafutia soko la kigeni la moja kwa moja na hatua hii itapunguza na kuzuia uvujaji wa mapato ya fedha za kigeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Mradi wa Liganga na Mchuchuma, napendekeza Serikali kuchukua hatua kuharakisha uwekezaji kwenye mradi wa madini ya Niobium ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kiwanda cha Ferroniobium (FeNb) ambacho kitakuwa cha kwanza Afrika na cha nne duniani. Kutokana na mahitaji makubwa ya ujenzi wa reli, madaraja na reli ya SGR, kuna mahitaji makubwa ya vifaa vya chuma ambavyo ni imara, lakini vyepesi na vyenye ubora wa kimataifa. Kwa kutumia sheria zetu za uwekezaji, Serikali itumie fursa za kipindi hiki ili kuvutia wawekezaji kwenye madini ya viwandani ili yaongezwe thamani hapa kwetu na pia kuvutia malighafi ya madini toka nchi zingine ili yachakatwe hapa kwetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania imebahatika kuwepo kwa madini ya Niobium ambayo inapatikana Milima ya Pandahill Wilaya ya Mbeya na mahitaji ya Ferroniobium (FeNb end product) yanaendelea kuwa makubwa duniani na hapa kwetu pia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inahitaji kujiwekekea mikakati ya haraka (quick wins) ili kuhakikisha inaimarisha uchumi ikiwemo kuboresha urari wa biashara kukabiliana na athari za Covid-19 na sasa vita vya Urusi na Ukraine. Kwa kutumia rasilimali zetu za madini, Serikali inaweza kutengeneza fursa nyingi na kupitia Mradi wa Niobium na Kiwanda cha Ferroniobium, ajira 2,000 zitakazozalishwa wakati wa ujenzi na pia kutakuwepo na ajira za kudumu zaidi ya 600 na indirect jobs 7,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu utazalisha mapato kila mwaka shilingi bilioni 500 (US$ 220 million) ambapo mapato kwa Serikali kila mwaka ni shilingi bilioni 50 (US$ 22 million) uhai wa mgodi ni zaidi ya miaka 30. Hiki kitakuwa kiwanda cha kisasa cha kwanza Afrika (modern manufacturing plant and smelter).

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuingiza teknolojia hii adimu na ujuzi (skills transfer) pia itakuwa itachangia huduma za kijamii (Corporate Social Investment in Community) na chanzo cha fedha ya kigeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na upotevu mkubwa wa fedha za Serikali ikiwemo miradi ya Serikali Kuu na Halmashauri, napendekeza Serikali kuimarisha Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani ili kuongeza ufanisi na uhuru wa Wakaguzi wa Ndani. Serikali ihakikishe Mkaguzi wa Ndani wakati wote anakuwa huru kutoka kwa Afisa Masuuli.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wakaguzi wa Ndani wa Halmashauri wasimamiwe na Mkaguzi Mkuu wa Mkoa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Serikali iimarishe uhuru wa Mkaguzi Mkuu wa Ndani (Internal Auditor General) na napongeza Serikali kupandisha hadhi ya Ofisi kuwa na Fungu la Bajeti linalojitegemea.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Nami napenda kumpongeza Waziri wa Kilimo na Naibu wake na timu nzima ya Wizara ya Kilimo kwa kazi kubwa wanayoifanya na kukabiliana na changamoto zilizopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli kama walivyosema wenzangu, hii Bajeti ya Kilimo haijakaa vizuri. Asilimia 0.9 ya bajeti nzima ya Serikali kuipeleka kwenye kilimo, nafikiri hatuitendei haki Sekta hii ya Kilimo. Niliangalia vizuri sana Bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ambayo ilikuwa na mabadiliko makubwa sana. Aliibadilisha kutoka asilimia 15 ya maendeleo mpaka asilimia 70 ya maendeleo. Sasa tulitegemea mabadiliko kama hayo yangekuwepo vilevile kwenye sekta hii muhimu ya kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la uzalishaji na tija ya kilimo linasababishwa sana na ufinyu wa bajeti ya kilimo. Ukiangalia, kama sisi tunaotoka kwenye maeneo ambayo ni ya kilimo, kwenye Wilaya ya Mbeya tunalima karibu mazao yote ya biashara na mazao ya chakula. Kabla ya mwaka 2010, Wilaya ya Mbeya ilikuwa ni mojawapo ya wazalishaji wakubwa sana wa pareto Tanzania na Afrika, lakini kwa leo hii zao hilo limeporomoka sana. Sababu kubwa ya kuporomoka kwa zao hilo ambalo lina soko zuri sana duniani ni ufuatiliaji na ubora na usimamizi mbovu.
Mheshimiwa Naibu Spika, soko halina uhakika kabisa! Watu waliopewa majukumu ya kulisimamia Soko la Pareto leo hii wameweza kuweka mnunuzi mmoja wa pareto na huyo mnunuzi ambaye ni mwekezaji ndio ana Kiwanda cha Pareto. Unategemea mkulima atafaidika namna gani kwa monopoly ya namna hii?
Mheshimiwa Naibu Spika, pareto ilipokuwa na wanunuzi wengi, wakulima walipata sh. 2,400/= kwa kilo. Leo hii wakulima wanapata sh. 1,500/=. Bei ya huko kwa wenzetu nchi nyingine ni sh. 4,000/= kwa kilo. Sasa unategemea maajabu gani kuitoa nchi hii katika huu umaskini wakati umaskini unazalishwa na sisi wenyewe? Angalia hiyo tofauti ya sh. 1,500/= na sh. 4,000/=. Ukiweza kuibadilisha tu hiyo, ni kwamba uchumi wetu utakuwa umebadilika kwa zaidi ya asilimia 200.
Mheshimiwa Naibu Spika, nami namwomba Waziri na nashukuru alikuwa amelifanyia kazi suala hili, lakini inavyoelekea kuna matatizo kwenye Bodi ya Pareto. Uliagiza kuwa wakutanishwe wanunuzi wadogo na yule mwekezaji (PST) pamoja na wakulima, lakini mpaka leo, licha ya kwamba Waziri Mkuu vilevile alisimamia suala hilo, hawajakutana na hawataki kuwakutanisha hawa watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama tuna bodi tunazozisimamia, hazipokei maagizo kutoka juu, tunategemea nini? Nafikiri Mheshimiwa Waziri inabidi uangalie ni namna gani utalishughulikia hili suala. Hali hii inakatisha tamaa wakulima, nami mwenyewe kama ni mkulima, nasikitika kuona wakulima wa Mbeya wanapata sh. 1,500/= na soko huko nje wanapata sh. 4,000/=, kisa ni utendaji mbovu wa Bodi ya Pareto. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia huu uzalishaji wetu, tulikuwa tunaongoza duniani; nchi zetu hizi tatu za Afrika Mashariki ikiwemo Kenya, Rwanda na Tanzania. Tulikuwa tunazalisha zaidi ya asilimia 70 ya pareto inayozalishwa duniani. Leo hii baada ya haya matatizo, kisiwa kidogo cha Tasmania huko Australia ndiyo kinazalisha zaidi ya asilimia 70 ya pareto na wenzetu kule wanapata zaidi ya sh. 4,000/= kwa kilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri tuanze kuangalia ni namna gani tunasimamia sera zetu na strategic objectives tulizonazo ili tukishazitatua hizo, nafikiri badala ya kuongeza maeneo ya kilimo, tuangalie ni namna gani haya maeneo yetu tuliyonayo sasa hivi yatatoa mazao yetu ya kilimo kwa tija zaidi na kabla ya kuongeza maeneo ya kilimo.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kule kwangu, Wilaya ya Mbeya…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Njeza muda wako tayari!
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Waziri, kwa hotuba nzuri ambayo inalenga Tanzania kuwa nchi ya viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umuhimu wa sekta ya viwanda na biashara kwa maendeleo ya kiuchumi ya nchi na watu wake unahitaji mtazamo tofauti. Nchi za Tiger (Tiger nations) zimeendelea kiuchumi ukilinganisha na Tanzania kwa sababu ya viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kiasi kikubwa sekta hii inaleta ufunguo wa sekta nyingine hasa kilimo. Serikali iweke mkazo kwenye viwanda vidogo vidogo vya kuongeza thamani za mazao ya kilimo. Kutokana na kazi nzuri ya REA, napendekeza kuangalia uwekezaji mdogo mdogo wa viwanda vijijini ili kuongeza thamani ya mazao yetu na pia kuongeza ajira kwa vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa la mitaji linaweza kutatuliwa na benki mpya ya kilimo (TADB). Napendekeza milioni 50 kwa kila kijiji, zipelekwe TADB, kwa kusimamia hizo pesa ambazo ni mfuko wa kuzunguka (Revolving Fund) kwa kila kijiji. Hii itawezesha TADB kutoa huduma moja kwa moja kwa wakulima ikiwa ni pamoja na kuiongezea mtaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kufanikisha ufanisi wa viwanda na biashara ndogo ndogo, ni muhimu kutoa elimu za muda mfupi kwa vijana na hasa wa vijijini, ili ujasiriamali uwe na tija na mafanikio makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na umuhimu wa kufufua viwanda vyetu, zoezi hilo liendeshwe kwa uangalifu mkubwa kutokana na kubadilika kwa teknolojia na ushindani mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Halmashauri ya Mbeya, imetenga eneo mahsusi katika kijiji cha Mjele kwa ajili ya Kiwanda cha Nyama na bidhaa zingine zitokanazo na mifugo. Hilo eneo ni mbadala wa eneo lililokuwa la Tanganyika Packers ambalo kwa sasa limezungukwa na makazi ya watu (Mji mdogo wa Mbalizi).
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isidor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mawaziri na viongozi wote wa Wizara ya Fedha na Mipango, kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Waziri wa Fedha na Mipango, kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha ubunifu wa ukusanyaji mapato na usimamizi mzuri wa matumizi ya Serikali ikiwa ni pamoja na uendelezaji wa miradi ya kimkakati na pia utayari wetu wa Ushindani wa Kimataifa (National Competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.” Pia mapendekezo haya yanazingatia dhima ya bajeti 2023/2024 ambayo ni kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi, kuhimili na kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi, na kuimarisha sekta za uzalishaji ili kuboresha hali ya maisha.

Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto za uchumi katika nchi nyingi duniani yakiwemo mataifa makubwa, Tanzania imefanya vizuri katika kusimamia ukuaji wa pato la Taifa lilikua kwa asilimia 4.7 ukilinganisha na wastani wa asilimia 3.9 kwa nchi za Afrika zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara; mfumuko wa bei umeendelea kubaki katika wigo wa tarakimu moja ambapo kwa mwaka 2022 ulikuwa asilimia 4.3 ukilinganisha na wastani wa asilimia 11 kwa nchi za Afrika Mashariki; na thamani ya shilingi ta Tanzania dhidi ya dola imeendelea kuwa tulivu ambapo kwa mwaka 2022 ilibadilishwa kwa wastani wa shilingi 2,314.50 kutoka shilingi 2,309.2 kwa mwaka 2021.

Mheshimiwa Spika, pia pamoja na upungufu wa fedha za kigeni, bado akiba ya fedha za kigeni ilikuwa USD milioni 5,177.2 sawa na uwezo wa uagizaji wa bidhaa na huduma kwa miezi 4.7 kutoka akiba ya USD milioni 6,386 ya mwezi Desemba, 2021 sawa na miezi 6.6 ya uagizaji. Upungufu wa fedha za kigeni kwa kiasi kikubwa umesababishwa na mfumuko wa bei katika soko la dunia, ulipaji wa madeni ya nje, pamoja na kugharamia miradi ya kimkakati. Hali hii imepelekea kuongezeka kwa nakisi ya urari wa malipo kufika USD milioni 4,414.2 kwa mwezi Julai, 2022 kutoka USD 2,516.1 kwa Julai, 2021.

Mheshimiwa Spika, kutokana na uhaba wa fedha za kigeni, napendekeza Serikali iendelee kwa kasi na jitihada za kununua na kutunza dhahabu kama sehemu ya fedha za kigeni. Ununuzi ulenge pia kununua dhahabu toka kwa wachimbaji wadogo hata kwa bei ya ushawishi ili kuzuia utoroshaji unaosababisha kupunguza mapato ya fedha za kigeni. Kutokana na mabadiliko ya kiuchumi kidunia, Benki Kuu nyingi duniani zimeanza kuwekeza zaidi kwenye dhahabu na hii ni ishara nzuri kwa bei ya dhahabu kuendelea kuimarika kwenye soko la dunia ambapo kwa mwezi Aprili, 2023 bei imepanda kwa zaidi ya asilimia 11 ukilinganisha na bei za Desemba, 2022.

Mheshimiwa Spika, Serikali imechukua hatua nzuri za kurudisha Mfuko wa Dhamana kwa Wakopaji Wanaozalisha Bidhaa kwa Soko la Nje (Export Credit Guarantee Scheme) ambayo itachochea kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa nje. Pamoja na uanzishwaji wa mfuko huu, Serikali isimamie uzalishaji wa tija na pia kusaidia kupata masoko ya nje ili bidhaa zetu zipate bei ya kiushindani.

Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kulipa fidia ya wananchi wanaopisha Mradi wa Liganga na Mchuchuma. Baada ya fidia, napendekeza Serikali kuchukua hatua za kuharakisha uwekezaji kwenye mradi wa chuma (Liganga Iron Ore) ikiwa ni pamoja na makaa ya mawe (The Mchuchuma Coal Mining and Power Projects). Mradi wa Liganga na Mchuchuma unatarajia uwekezaji wa zaidi ya US$ bilioni tatu na kuzalisha ajira zaidi ya 30,000.

Mheshimiwa Spika, pamoja na Mradi wa Liganga na Mchuchuma, napendekeza Serikali kuchukua hatua kuharakisha uwekezaji kwenye mradi wa madini ya Niobium ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Kiwanda cha Ferroniobium (FeNb) ambacho kitakuwa cha kwanza Afrika na cha nne duniani. Kutokana na mahitaji makubwa ya ujenzi wa reli, madaraja na reli ya SGR, kuna mahitaji makubwa ya vifaa vya chuma ambavyo ni imara, lakini vyepesi na vyenye ubora wa kimataifa.

Mheshimiwa Spika, kwa kutumia sheria zetu za uwekezaji, Serikali itumie fursa za kipindi hiki ili kuvutia wawekezaji kwenye madini ya viwandani ili yaongezwe thamani hapa kwetu na pia kuvutia malighafi ya madini toka nchi zingine ili yachakatwe hapa kwetu. Tanzania imebahatika kuwepo kwa madini ya Niobium ambayo yanapatikana Panda Hill Wilaya ya Mbeya, na mahitaji ya Ferroniobium (FeNb end product) yanaendelea kuwa makubwa duniani na hapa kwetu pia.

Mheshimiwa Spika, Serikali inahitaji kujiwekekea mikakati ya haraka (quick wins) ili kuhakikisha inaimarisha uchumi ikiwemo kupunguza urari wa malipo ambao umefika USD milioni 4,414.2 kwa Julai, 2022 kutoka USD 2,516.1 kwa Julai, 2021. Kwa kutumia rasilimali zetu za madini yakiwemo ya chuma, makaa ya mawe, na Niobium, kuna fursa ya kuvutia uwekezaji wa nje (FDI) ambao ni zaidi ya USD bilioni tatu katika kipindi cha miaka miwili mpaka mitatu. Pamoja na fursa ya ajira ya zaidi ya 30,000 kwa Liganga na Mchuchuma kuna fursa ya kuvutia uwekezaji (FDI) wa zaidi ya USD bilioni tatu, wakati huo huo Niobium ina fursa ya uwekezaji wa zaidi ya USD milioni 200 na kuzalisha ajira 2,000 zitakazozalishwa wakati wa ujenzi na pia kutakuwepo ajira za kudumu zaidi ya 600 na indirect jobs 7,000.

Mheshimiwa Spika, mradi utazalisha mapato kila mwaka shilingi bilioni 500 (US$ 220 million) ambapo mapato kwa Serikali kila mwaka shilingi bilioni 50 (US$ 22 million) uhai wa mgodi ni zaidi ya miaka 30. Hiki kitakuwa kiwanda cha kisasa cha kwanza Afrika (Modern Manufacturing Plant and Smelter).

Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki wakati dunia inapambana na changamoto za kiuchumi, napongeza hatua za Serikali kwa kuwasilisha Muswada wa Mapendekezo ya Marekebisho ya Sheria ya PPP, Sura 103 na ambayo yamepitishwa na Bunge tarehe 13 Juni, 2023. Serikali imeonesha utayari wa kujenga reli ya Kusini ya Mtwara – Mbambabay na reli ya Kaskazini (Tanga-Arusha-Mara) kwa njia ya ubia baina ya Serikali na sekta binafsi (PPP).

Napendekeza pia kuharakisha ujenzi wa barabara ya Kibaha – Morogoro (kilometa 205) na baadae Morogoro hadi Dodoma ili iweze kutekelezwa kwa utaratibu wa PPP, na iende sambamba na ujenzi kwa kiwango cha lami kwa barabara ya mzunguko wa nje katika Jiji la Dodoma (kilometa 112.3).

Mheshimiwa Spika, pamoja na PPP napongeza Serikali kwa kuanza utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa kiwango cha lami kwa barabara saba zenye jumla ya urefu wa kilometa 2,035 zenye gharama ya takribani shilingi trilioni 3.7 kujengwa kwa kutumia mfumo wa Engineering, Procurement, Construction and Financing (EPC+F). Katika barabara hizo saba ni pamoja na barabara ya TANZAM kipande cha Igawa – Songwe – Tunduma (kilometa 218) pamoja na barabara ya mchepuo ya Uyole – Songwe (kilometa 48.9).

Mheshimiwa Spika, kutokana na fursa za uzalishaji mkubwa kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, napendekeza muendelezo wa uboreshaji wa barabara za Mbalizi – Shigamba – Isongole kutokana na uzalishaji wa mazao ya kilimo; barabara ya Mbalizi – Galula – Makongolosi kutokana na uzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo na madini; na pia barabara ya Isyonje – Kikondo – Makete ambayo ni muhimu sana katika kusafirisha mazao ya kilimo ikiwemo maua, parachichi na viazi kwa soko la nje.

Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya kazi kubwa kuhakikisha ujenzi wa SGR unaendelea kwa kasi ile ile na pia napongeza jitihada za kuendelea kutafuta vyanzo vya fedha vya masharti nafuu kugharamia ujenzi huo. Pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa, Serikali imefanya maboresho makubwa ya miundombinu na huduma katika bandari zetu hususana Bandari ya Dar es Salaam ili kukabiliana na ushindani mkubwa wa bandari zingine za ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Mheshimiwa Spika, Bandari ya Dar es Salaam inakumbana na ushindani mkubwa toka Bandari za Mombasa (Kenya), Beira (Msumbiji), Nacala (Msumbiji), Durban (Afrika Kusini), Lobito (Angola) na Walvis Bay (Namibia). Maboresho ya bandari zetu yaendane na kuondoa changamoto zingine ambazo zinasababisha gharama kubwa za usafirishaji kwa bandari zetu na kusababisha kupoteza biashara ya usafirishaji kwa bandari shindani.

Mheshimiwa Spika, ufanisi wa bandari unategemea pia maboresho ya barabara, Reli ya Kati (TRL), Reli ya TAZARA, utendaji wenye tija wa wadau wote wa bandari na hata watumishi ili kupunguza gharama za usafirishaji kwa wateja wa bandari zetu. Kwa sasa karibu asilimia 70 ya mzigo wote wa nchi za nje unasafirishwa kwa kupitia Dar es Salaam Corridor ambapo DR Congo ni asilimia 38, Zambia asilimia 26 na Malawi asilimia sita. Pamoja na fursa za kijiografia ya bandari zetu, mzigo unaopita sasa kwenye Bandari ya Dar es Salaam, ni chini ya asilimia 50 ya biashara yote ambayo kwa sasa sehemu kubwa inashikiliwa na bandari shindani.

Mheshimiwa Spika, napongeza Serikali kwa maboresho ya uwanja wa ndege wa Songwe, na kutokana na maboresho hayo napendekeza kujengwe maghala (cold rooms) kwa ajili ya kuhifadhi mboga mboga, matunda, nyama na samaki kwa soko la nje. Uwanja wa ndege wa Songwe upo kimkakati kwa kuhudumia wafanyabiashara wa hapa nchini na pia nchi jirani za Zambia, DRC na Malawi.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa ATCL iboreshe muundo wake wa utumishi kulingana na biashara iliyopo ya usafiri wa anga ili kupunguza mzigo wa gharama na kuongeza ufanisi. Pia ATCL ianzishe njia za safari za ndani na za nje zenye fursa ya kuongeza biashara kama vile safari za moja kwa moja za Mbeya – Dodoma, Mbeya – Lilongwe, Mbeya Lubumbashi na Mbeya – Lusaka.

Mheshimiwa Spika, napendekeza Serikali iangalie upya mapendekezo ya kuboresha muundo wa mfuko wa asilimia 10 kwa ajili ya mikopo kwa vijana, wakina mama na makundi maalum. Napendekeza mfuko huu uboreshwe na uwe sehemu ya mpango wa kuwawezesha kiuchumi makundi lengwa kwa misingi ya huduma za kifedha shirikishi (financial inclusion). Msukumo uwe kwenye elimu ya ujasiriamali na kuwasimamia kwa karibu wakopaji ili kuongeza tija na pia kuboresha uchumi wa wakopaji na Tanzania kwa ujumla.

Napendekeza pia kujumuisha huu mfuko uwe kitaifa na uendeshaji uwe katika misingi ya taasisi za kifedha, lakini kwa masharti nafuu ikiwemo bila riba na Serikali iunganishe mifuko yote ya makundi maalum na yaunde taasisi moja imara chini ya Wizara ya Fedha na Mipango.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee naomba kuungana na Watanzania wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutimiza miaka mitatu kwa kuongoza nchi yetu akiwa Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tumeshuhudia mafanikio makubwa katika kuimarisha miundombinu hususan barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari, huduma za kiuchumi na kijamii kama vile ujenzi wa madarasa, hospitali, zahanati na vituo vya afya, huduma za maji, utawala bora, pamoja na kuhamasisha uwekezaji na utalii. Pia, naomba nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri iliyotukuka ya kumsaidia Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi na Spika na pia uongozi wote wa Bunge kwa uongozi mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Taifa letu katika ya Ushindani wa Kimataifa (National Competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni: “Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.”

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi chake akiwa Waziri Mkuu, tathmini zinathibitisha mafanikio makubwa ya utekelezaji na usimazi wa Mpango wa Kwanza na wa Pili na kupelekea Taifa letu la Tanzania kufanya vizuri mno kuinua uchumi katika kipindi hiki kigumu. Katika kipindi cha Januari hadi Septemba, 2023 ukuaji wa uchumi wa Taifa ulikuwa asilimia 5.3 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 5.2 katika kipindi kama hicho mwaka 2022. Kutokana na mwendelezo huo mzuri wa kiuchumi, kampuni ya Moody’s imechapisha matokeo Machi, 2024 ambapo Tanzania imepanda kutoka daraja la chini la B2 (with Positive Outlook) na kwenda ngazi ya juu ya B1 (with Stable Outlook). Matokeo hayo ni ya juu kabisa katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki na hivyo hatuna budi kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa uongozi wake mahiri uliowezesha Taifa kupata mafanikio hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kukua hadhi kimataifa, bado kuna kigugumizi kwa baadhi ya taasisi za kifedha nchini kuelekeza mikopo kwenye sekta muhimu za kiuchumi ikiwemo kilimo. Serikali kupitia Benki Kuu (BoT), ilitenga shilingi trilioni moja kuwezesha benki kutumia dirisha hili kukopesha sekta ya kilimo kwa riba isiozidi 10%. Kwa muda mrefu sasa hilo dirisha halijaonesha mafanikio ya kuchochea benki kupunguza riba kwenye mikopo ya kilimo na hata taasisi za Serikali zinazonunua mazao ya kilimo bado zinahangaikia kupata hiyo fursa na badala yake kulazimika kukopa kwa riba za juu. Kilimo kama ilivyo kwa madini na utalii, zinaliingizia Taifa asilimia kubwa ya fedha za kigeni, Serikali iweke mkakati wa kuvutia uwekezaji ikiwemo mikopo ya benki ili kuongeza tija na ushindani katika masoko ya kimataifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha Julai, 2023 mpaka Machi, 2024 Serikali imeendelea kutekeleza miradi ya kimkakati kwa mafanikio mkubwa sana na utekelezaji huu unaonekana mpaka kwenye ngazi ya halmashauri zetu. Mafanikio makubwa yamejikita kwenye uboreshaji wa miundombinu ya barabara, reli, bandari, mtandao wa mawasiliano na uboreshaji wa usafiri wa anga. Napongeza Serikali kwa hatua nzuri za utekelezaji wa mradi wa kihistoria wa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR na ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (megawati 2,115). Miradi hii miwili ya SGR na umeme ni nguzo imara ya kiushindani katika uchumi wetu na Nchi za Maziwa Makuu na hata za Kusini mwa Afrika na Kati.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatakiwa kuendelea kuchukua hatua za kibajeti kukabiliana hasa na mfumuko wa bei na kuporomoka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani na sarafu kuu zingine. Kwa kuzingatia kuyumba kwa uchumi wa dunia, bajeti hii ijielekeze kuchukua hatua za kuchochea uzalishaji wa ndani ili kupunguza nakisi ya urari wa biashara (Balance of Payment – BOP), kuimarisha pato la Taifa kupitia sekta za kilimo, madini, utalii na uchukuzi. Hatua hizi ziende sambamba na kuimarisha mazingira ya uwekezaji hasa kwenye sekta ya kilimo na madini. Pia, Serikali iendelee kusimamia sera ya fedha na bajeti ikiwemo kuimarisha mifumo na kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na utekelezaji wa miradi ya kimkakati, kunapelekea mahitaji makubwa ya fedha za kigeni na hivyo msukumo uwepo kwenye kuongeza uzalishaji wa madini na mazao ya kilimo. Hatua hizi ni muhimu kuhakikisha utulivu wa thamani ya shilingi na pia kuimarisha uhimilivu wa deni la Taifa hasa kwenye kigezo za ulipaji wa deni la nje kwa kulinganisha na uuzaji wa bidhaa nje (mapato ya fedha za kigeni).
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na changamoto za tabianchi, bado kuna fursa kubwa kwa Tanzania kwenye uzalishaji wa ziada wa nafaka ukilinganisha na nchi za ukanda huu. Serikali iimarishe upatikanaji wa pembejeo bora kwa bei nafuu na kuimarisha upatikanaji wa masoko ya uhakika kupitia NFRA na Soko la Bidhaa (TMX). Kutokana na ruzuku kwenye mbolea na jitihada walizofanya Wizara ya Kilimo kuwapatia vitendea kazi Maafisa Ugani, ichochee kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya kilimo kutoka uzalishaji wa sasa wa kilo 1,000 za mahindi kwa eka mpaka kilo 4,000 kwa eka ya mahindi. Tanzania ina fursa kubwa ya biashara ya hewa ukaa (carbon credit) ikiwa ni pamoja na kuwa chanzo cha uhakika wa fedha za kigeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na msukumo kwenye kilimo, madini na utalii, Serikali inatakiwa kuwekeza hasa kwenye miundombinu ya usafirishaji ikiwemo barabara, reli, bandari na usafiri wa anga hasa kwa mizigo. Kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha zimesababisha uharibifu mkubwa kwenye miundombinu ya barabara na hata reli. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, barabara zinazohudumiwa na TARURA kwa asilimia zaidi ya 80 zipo kwenye hali mbaya sana kutokana na mvua kubwa na pia kwa kukosa matengenezo ya mara kwa mara. Maeneo mengi ya vijijini barabara hazipitiki kutokana na ufinyu wa bajeti ukilinganisha na mtandao wa barabara zinazohudumiwa na TARURA. Naomba Serikali ichukue hatua za haraka kunusuru hali hii ili wananchi waweze angalau kusafirisha mazao yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuidhisha ujenzi wa barabara ya njia nne kuanzia Nsalaga (Uyole) mpaka Ifisi jirani na Uwanja wa Ndege wa Songwe. Kipande hiki cha barabara ambacho ni sehemu ya barabara kuu ya TANZAM, ni muhimu sana kwa kuinua uchumi wa Tanzania na hata kupunguza ajali za mara kwa mara zinazotokea katika mteremko wa Mlima Iwambi kuelekea Mji wa Mbalizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na umuhimu wa usafirishaji wa mazao yetu kwa soko la ndani na nje ikiwemo fursa za biashara ukanda wa SADC na uzalishaji mkubwa kwa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, napendekeza mwendelezo wa uboreshaji wa Barabara za TANZAM kipande cha Igawa - Tunduma; Barabara ya bypass ya Uyole - Songwe; Barabara ya Mbalizi – Shigamba – Isongole kutokana na uzalishaji wa mazao ya kilimo; Barabara ya Mbalizi – Galula – Makongosi kutokana na uzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo na madini; na pia Barabara ya Isyonje – Kikondo – Makete.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanya kazi kubwa kuhakikisha ujenzi wa SGR unaendelea kwa kasi ile ile na pia napongeza jitihada za kuendelea kutafuta vyanzo vya fedha vya masharti nafuu kugharamia ujenzi huo. Pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa, Serikali imefanya maboresho makubwa ya miundombinu na huduma katika bandari zetu hususani Bandari ya Dar es Salaam ili kukabiliana na ushindani mkubwa wa bandari zingine za ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika. Bandari ya Dar es Salaam inakumbana na ushindani mkubwa toka Bandari za Mombasa (Kenya), Beira (Msumbiji), Nacala (Msumbiji), Durban (Afrika Kusini), Lobito (Angola) na Walvis Bay (Namibia).

Mheshimiwa Naibu Spika, maboresho ya bandari zetu iendane na kuondoa changamoto zingine ambazo zinasababisha gharama kubwa za usafirishaji kwa bandari zetu na kusababisha kupoteza biashara ya usafirishaji kwa bandari shindani. Ufanisi wa bandari unategemea pia maboresho ya barabara, Reli ya Kati (TRL), Reli ya TAZARA, utendaji wenye tija wa wadau wote wa bandari na hata watumishi ili kupunguza gharama za usafirishaji kwa wateja wa bandari zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa taarifa zilizopo zaidi ya 70% ya mzigo wote wa nchi za nje unasafirishwa kwa kupitia Dar es Salaam Corridor inayohudumia Nchi za DR Congo, Zambia na Malawi. Pamoja na fursa za kijografia ya bandari zetu, mzigo unaopita sasa kwenye Bandari ya Dar es Salaam, ni 50% tu ya biashara yote ambayo kwa sasa inashikiliwa na bandari shindani. Kwa ajili ya kunusuru biashara hii inayopotea kwa bandari shindani, Serikali ichukue hatua za haraka kuboresha huduma za TAZARA ikiwa ni pamoja ya maboresho ya miundombinu ya reli, ununuzi wa vichwa vya reli, mabehewa na vitendea kazi vingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, napendekeza Serikali kwa haraka ishughulikie maboresho ya Mkataba wa TAZARA na kisha kutafuta mbia mwenye uwezo wa kifedha na uendeshaji. Katika kipindi hiki cha ushindani mkubwa usafirishaji wa reli ni mojawapo ya suluhisho kubwa kupunguza mzigo wa bei kubwa kwa wateja wa bandari zetu na hata wananchi. Pamoja na maboresho ya reli ya TAZARA, napendekeza kuendelea na ujenzi wa bandari kavu Mbeya ambayo ina fursa kubwa katika kipindi hiki katika kuwezesha kupunguza gharama za usafirishaji kwa wateja wa bandari na hata kupunguza bei za mafuta ya petroli, pembejeo na mazao ya kilimo. Bandari kavu ya Mbeya ni njia panda kwa wateja wa Nchi za Malawi, Zambia, DRC Lubumbashi na hata kwa Zimbabwe na Msumbiji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa lengo la kuvutia wawekezaji na kuongeza pato la fedha za kigeni, napendekeza Serikali kuchukua hatua kuharakisha uwekezaji kwenye mradi wa madini ya kimkakati kidunia, ikiwemo na gesi ya Helium na madini ya Niobium. Serikali iweke msukumo kuanza kwa uzalishaji wa gesi ya Helium na uzalishaji wa madini ya Niobium ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Kiwanda cha Ferroniobium (FeNb) ambacho kitakuwa cha kwanza Afrika na cha nne duniani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mahitaji makubwa ya ujenzi wa reli, madaraja na reli ya SGR, kuna mahitaji makubwa ya vifaa vya chuma ambavyo ni imara, lakini vyepesi na vyenye ubora wa kimataifa. Kwa kutumia Sheria zetu za Uwekezaji, Serikali itumie fursa za kipindi hiki ili kuvutia wawekezaji kwenye madini ya viwandani ili yaongezwe thamani hapa kwetu na pia kuvutia malighafi ya madini toka nchi zingine ili yachakatwe hapa kwetu. Tanzania imebahatika kuwa na madini ya Niobium ambayo inapatikana milima ya Panda Hill, Songwe Wilaya ya Mbeya na mahitaji ya Ferroniobium (FeNb end product) ni makubwa duniani na hapa kwetu pia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutumia rasilimali zetu za madini, Serikali inaweza kutengeneza fursa nyingi na kupitia Mradi wa Niobium na Kiwanda cha Ferroniobium, ajira 2,000 zitakazozalishwa wakati wa ujenzi na pia kutakuwepo ajira za kudumu zaidi ya 600 na indirect jobs 7,000. Mradi utazalisha mapato kila mwaka shilingi bilioni 500 (USD 220 million) ambapo mapato kwa Serikali kila mwaka shilingi bilioni 50 (USD 22 million), uhai wa mgodi ni zaidi ya miaka 30. Hiki kitakuwa kiwanda cha kisasa cha kwanza Afrika (modern manufacturing plant and smelter). Pamoja na kuingiza teknolojia hii adimu na ujuzi (skills transfer) pia itakuwa inachangia huduma za kijamii (Corporate Social Investment in Community) na chanzo cha fedha ya kigeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mawaziri na viongozi wote wa Wizara ya Uchukuzi, kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi na Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Waziri wa Uchukuzi kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha uendelezaji wa miradi ya kimkakati na pia utayari wetu wa ushindani wa kimataifa (national competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 ambayo ni “Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.”

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miezi kumi ya bajeti inayoishia Juni, 2024 Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi imetekeleza miradi mingi ya miundombinu ya reli, bandari na uimarishaji wa safari za anga ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa viwanja vya ndege. Napongeza Serikali kwa hatua nzuri za utekelezaji wa mradi wa kihistoria wa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR pamoja na uboreshaji wa bandari utaimarisha kwa kiasi kikubwa uchumi wa nchi yetu. Reli ya SGR, TAZARA na Bandari ni nguzo imara ya kiuchumi na kiushindani katika biashara ya usafirishaji wa ndani na nchi za maziwa makuu na hata za Kusini mwa Afrika na Kati. Bandari za Tanzania ni lango la usafirishaji kwa Zambia, Malawi, DR Congo, Uganda, Burundi, Rwanda, Sudan ya Kusini na hata Zimbabwe na Msumbiji.

Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya kazi kubwa kuhakikisha ujenzi wa SGR unaendelea kwa ufanisi mkubwa ambapo kipande cha Dar es Salaam – Morogoro na Morogoro – Makutopora umekamilika kwa asilimia karibu zote na huduma ya treni imepangwa kuanza hivi karibuni. Pia napongeza jitihada za Serikali za kuendelea kutafuta vyanzo vya fedha vya masharti nafuu kugharamia ujenzi wa vipande vilivyobaki. Pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa, Serikali imefanya maboresho makubwa ya miundombinu na huduma katika bandari zetu hususan Bandari ya Dar es Salaam ili kukabiliana na ushindani mkubwa wa bandari zingine za ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Mheshimiwa Spika, Bandari ya Dar es Salaam inakumbana na ushindani mkubwa toka bandari za Mombasa (Kenya), Beira (Msumbiji), Nacala (Msumbiji), Durban (Africa Kusini), Lobito (Angola) na Walvis Bay (Namibia). Maboresho ya bandari zetu iendane na kuondoa changamoto zingine ambazo zinasabisha gharama kubwa za usafirishaji kwa bandari zetu na kusababisha kupoteza biashara ya usafirishaji kwa bandari shindani. Ufanisi wa bandari unategemea pia maboresho ya barabara, Reli ya Kati (TRL), Reli ya TAZARA, utendaji wenye tija wa wadau wote wa bandari na hata watumishi ili kupunguza gharama za usafirishaji kwa wateja wa bandari zetu.

Mheshimiwa Spika, kutokana na maboresho ya miundombinu hususan Bandari ya Dar es Salaam, kwa mwaka 2022/2023 mchango wa mapato yanayokusanywa na TRA kutokana na huduma za kibandari kwenda Mfuko wa Serikali umeendelea kuongezeka hadi kufikia shilingi trilioni 9.354 ambayo ni asilimia 41.37 ya mapato yote yanayokusanywa na TRA.

Mheshimiwa Spika, katika ushuhuda wa mchango huu mkubwa, Serikali inashauriwa kuongeza uwekezaji zaidi katika kuboresha miundombinu ya bandari zetu ikiwemo mifumo ya TEHAMA. Mamlaka ya Bandari (TPA) inapaswa kuhimili ushindani, kwa kutoa huduma za uhakika, zenye ubora wa hali ya juu kuliko washindani wake. Katika kipindi hiki cha mahitaji makubwa ya kuboresha miundombinu ya bandari zetu, napendekeza mapato ya wharfage yakusanywe na TPA badala ya TRA. Katika utaratibu wa sasa, TPA itashindwa kujiendesha kibiashara kwa kusoma fursa ya kutumia karibu shilingi bilioni 700 za mapato ya wharfage ambayo ni zaidi ya asilimia 50 ya mapato ya shughuli za bandari. Utaratibu huu hautakuwa mgeni kwa vile duniani kote, mapato ya wharfage yanakusanywa na bandari kama chanzo cha kuboresha miundombinu ili kuboresha huduma za kibandari.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa karibu asilimia 70 ya mzigo wote wa nchi za nje unasafirishwa kwa kupitia Dar es Salaam Corridor ambapo DR Congo ni asilimia 36, Zambia asilimia 31 na Malawi asilimia tano. Pamoja na fursa za kijiografia ya bandari zetu, mzigo unaopita sasa kwenye Bandari ya Dar es Salaam ni chini ya fursa ya asilimia 50 ya biashara yote ambayo kwa sasa sehemu kubwa inashikiliwa na bandari shindani.

Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa za kiushindani zinatokana na ufanisi usiokidhi ushindani na gharama kubwa za bandari na watoa huduma wa Bandari ya Dar es Salaam. Pia kuna changamoto za kiutendaji kwa mashirika ya reli ya TAZARA na hata reli ya kati (TRL) inayopelekea gharama kubwa ambazo siyo za kiutendaji. Kwa ajili ya kunusuru biashara hii inayopotea kwa bandari shindani, Serikali ichukue hatua za haraka kuboresha huduma za TAZARA ikiwa ni pamoja ya maboresho ya miundombinu ya reli, ununuzi wa vichwa vya reli, mabehewa, na vitendea kazi vingine.

Mheshimiwa Spika, napendekeza Serikali kwa haraka ishughulikie maboresho ya Mkataba wa TAZARA ili kuwezesha kutafuta mkandarasi mwenye uwezo wa uendeshaji na menejimenti. Katika kipindi hiki cha ushindani mkubwa na hata mfumuko wa bei wa mafuta ya petroli, mbolea na bidhaa mbalimbali, usafirishaji wa reli ni mojawapo ya suluhisho kubwa kupunguza mzigo wa bei kubwa kwa wateja wa bandari zetu na hata wananchi.

Mheshimiwa Spika, pamoja na maboresha ya reli ya TAZARA, napendekeza kuendelea na ujenzi wa bandari kavu Mbeya ambayo ina fursa kubwa katika kipindi hiki katika kuwezesha kupunguza gharama za kusafirisha kwa wateja wa bandari na hata kupunguza bei za mafuta ya petroli, pembejeo na mazao ya kilimo. Bandari kavu ya Mbeya ni njia panda kwa wateja wa nchi za Malawi, Zambia, DRC Lubumbashi na hata kwa Zimbabwe na Msumbiji. Serikali ichukue hatua za haraka kuinusuru reli ya TAZARA hata ikibidi kurekebisha mikataba ya umiliki na uongozi ili mradi iendeshwe kwa tija. Kuna kuchukua hatua za makusudi kwa kutumia zaidi TAZARA kusafirisha mizigo ambayo imeelemea hata uwezo wa barabara zetu. Usafirishaji wa mizigo kwa kutumia TAZARA ilenge kupunguza gharama za mafuta ya petroli, pembejeo kwa wakulima na wakati huo kupunguza gharama za kusafirisha mazao ya wakulima.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuboresha TAZARA, napendekeza kukamilisha taratibu za ujenzi wa bandari kavu ya Mbeya, ambapo Serikali ya Mkoa imetenga maeneo makubwa mkabala na uwanja wa ndege wa Songwe na pia kuna njia ya reli ya TAZARA na barabara ya TANZAM. Eneo hili ni la kimkakati zaidi kutokana na kuwa ni njia panda ya nchi zote za Kusini mwa Afrika ikiwemo DRC. Pia eneo la kiusalama zaidi kutokana na kuwepo vikosi vyetu vya majeshi, pia Mamlaka ya Bandari kwa kipindi kirefu wamewahakishia wananchi wa Inyala, Mbeya kulipa fidia ya eneo lao wanalolichukua.

Mheshimiwa Spika, napendekeza Bandari ya Dar es Salaam kuingia makubaliano na TAZARA na TRL ili iweze kumiliki mabehewa yake kwa lengo la kuongeza ufanisi na kupunguza gharama ambazo sio za kiushindani. Pamoja na hatua hiyo, kuna fursa kubwa ya kutafuta mwekezaji mwenye uzoefu mkubwa katika uendeshaji wa reli kwa lengo la kuboresha utendaji hasa kwenye upande wa makontena. Serikali ifanye jitihada ya kupata mwekezaji ikiwemo kwa mfumo wa PPP kwa lengo la kuongeza biashara ikiwemo kurudisha biashara iliopotea kwa bandari shindani.

Mheshimiwa Spika, napendekeza Serikali iendelee na mkakati wa kutafuta mwekezaji wa Bandari ya Mbegani – Bagamoyo ambayo ina lango lenye kina asili cha mita 18 na haina kikomo cha upana wa meli ambazo zinaweza kuingia na kutoka bandarini hapo. Kutokuwepo kwa ukomo katika lango, bandari hiyo inaweza kuhudumia meli ambazo zinahudumiwa kwenye bandari kubwa duniani zenye urefu wa mita 400 na uwezo wa kubeba makasha hadi TEUs 22,000. Aidha, uwezo huu ni mkubwa katika eneo la Afrika Mashariki na Kati kwani kwa sasa hakuna bandari yenye uwezo kama huo. Hivyo, uendelezaji wa Bandari ya Mbegani, Bagamoyo utasaidia kupunguza msongamano wa shehena katika Bandari ya Dar es Salaam na kupelekea bandari zote kuwa shindani.

Mheshimiwa Spika, napongeza Serikali kwa uwekezaji kwenye viwanja vya ndege na pia kufufua shirika letu la ndege la ATCL. Kutokana na uzalishaji mkubwa wa mazao na madini, napendekeza Serikali iongeze ndege za mizigo na kuboresha viwanja vyetu kwa kujenga maghala yanayokidhi viwango vya kimataifa. Pia ATCL ianzishe safari za Mbeya - Dodoma na pia Mbeya na nchi za SADC ikiwemo DRC, Lubumbashi, Zambia na Malawi.

Mheshimiwa Spika, nashauri Serikali ikamilishe kulipa fidia za wananchi waliopisha ujenzi wa viwanja vya ndege kikiwemo kiwanja cha ndege cha Songwe, Mbeya.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza Waziri na Naibu Waziri kwa hotuba nzuri na kazi kubwa wanayoifanya. Sekta ya Kilimo inatoa mchango mkubwa kwa sekta nyingine hasa viwanda, fedha, usafirishaji na biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na umuhimu wa kilimo, hakijapewa kipaumbele inavyostahili. Uzalishaji kwa eneo ni mdogo na tija ni ndogo; miundombinu ya barabara vijijini ni mibovu, mfumo wa masoko ni duni na uwezo wa kupata fedha toka vyombo vya fedha ni mdogo; vile vile Sekta ya Kilimo hupewa chini sana asilimia 0.9 badala ya asilimia 10 kama ilivyo kwenye Azimio la Maputo na changamoto za upatikanaji wa pembejeo bora.
Mheshimiwa Spika, uzalishaji wa pareto unaporomoka sana na hata kwa huo uzalishaji mdogo, bei kwa wakulima ni ndogo sana ukilinganisha na msimu wa mwaka 2013/2014. Sababu kubwa za kuporomoka uzalishaji na bei:-
(1) Mnunuzi ambaye ndiye mwekezaji ni mmoja na wanunuzi wadogo wazalendo wamefungiwa kununua kwa kuwekewa masharti magumu sana;
2) Ukosefu wa wataalam kusimamia zao hili hupelekea ubora wa pareto yetu koporomoka sana;
(3) Kutokana na monopoly ya mnunuzi, bei imeporomoka kutoka sh. 2,400/= kwa kilo mwaka 2014 mpaka sh. 1,400/= kwa kilo mwaka 2015;
(4) Mwaka 2010 Tanzania na nchi nyingine za Afrika Mashariki zilikuwa zinazalisha asilimia zaidi ya 70 ya mahitaji ya dunia. Leo hii Kisiwa kidogo cha Tasmania (Australia) ndiyo kinaongoza kwa kuzalisha asilimia zaidi ya 65 wakati bei ya pareto kwa mkulima Tanzania ni sh. 1,500/= kwa kilo. Wakulima wa nchi nyingine ni zaidi ya sh. 4,000/= kwa kilo. Naomba Waziri uagize Bodi ya Pareto iwakutanishe wanunuzi wadogo, wawakilishi wa wakulima na bodi ili kupanga utaratibu mzuri wa ununuzi wa pareto; na
(5) Pia Serikali iweke mazingira ya kujenga Kiwanda cha Pareto Mbeya.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto kubwa ya zao la kahawa ni uzalishaji duni na usimamizi mbovu wa Soko la Kahawa. Ni lini Commodity Exchange Market itaanza kufanya kazi?
Mheshimiwa Naibu Spika, bei ya kahawa (Arabica) kwa wenzetu Kenya wenye Nairobi Coffee Exchange ni zaidi ya sh. 8,000/= kwa kilo wakati kwenye soko la TCB Moshi ni chini ya sh. 4,000/= kwa kilo. Kwa nini mkulima wa Tanzania anaibiwa kiasi hicho? Wanunuzi ni wale wale!
Mheshimiwa Naibu Spika, Benki ya TADB ina umuhimu mkubwa sana kwenye Sekta hii muhimu. Mtaji wa shilingi milioni 60 ni mdogo sana. Serikali kama ilivyoahidi, iongeze mtaji wa Benki hii ili iweze kukidhi mahitaji makubwa ya wakulima na wajasiriamali wa kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, napongeza sana mpango wa Serikali wa shilingi milioni 50 kwa kijiji. Kiasi hiki cha pesa zikisimamiwa vizuri zinaweza kubadilisha kwa kiasi kikubwa tija na uzalishaji wa kilimo. Napendekeza hizi shilingi milioni 50 zilizotengwa kwa kila kijiji zisimamiwe kwa ukaribu na TADB.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mafunzo ya wakulima na Maafisa Ugani:-
Serikali iongeze idadi ya Maafisa Ugani vijijini;
Vijana wapewe elimu ya ujasiriamali wa kilimo; na
Vyuo vyetu na hasa Vyuo vya Utafiti vitumike kupima udongo ili tuweze kutumia pembejeo sahihi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza Waziri, Naibu Waziri na timu nzima ya Wizara ya Nishati na Madini kwa kazi nzuri hasa ya usambazaji wa umeme Vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, napendekeza Serikali izingatie mipango ya umeme Vijijini (REA) ili itekeleze mipango mizuri ya kusambaza umeme ambao ni muhimu kwa uchumi wa viwanda. Naomba Serikali izingatie utekelezaji wa miradi ya Halmashauri ya Mbeya ambayo wananchi waliahidiwa na kusisitiza kuwa bajeti ya kusambaza umeme katika Vijiji vya Halmashauri ya Mbeya umetengewa shilingi bilioni 52.
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Wizara na Serikali kwa michakato ya miradi mikubwa ya madini ikiwemo niobium ya milima ya Panda Hill.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ukurasa wa 62 hotuba inaonesha haya madini ya niobium yanapatikana Wilaya ya Songwe. Naomba isahihishwe kuwa haya madini ya niobium yanapatikana katika milima ya Panda Hill (Songwe) Wilaya ya Mbeya na siyo Wilaya ya Songwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na madini ya niobium, milima ya Panda Hill yamegunduliwa madini ya calcium ambayo yanatumika kutengeneza mbolea ya NPK. Naomba Serikali iweke mkakati wa haraka kufufua mradi huu na kuwanufaisha wananchi wa Wilaya ya Mbeya, kuongeza uchumi na pia uzalishaji wa mbolea za NPK hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kupongeza shirika la TANESCO kwa kazi nzuri licha ya changamoto mbalimbali. Napendekeza, Serikali ichukue hatua za makusudi kupunguza mzigo mkubwa wa madeni ya TANESCO hasa yale ya fedha za kigeni. Kuna uwezekano mkubwa wa restructuring ya hii mikopo iwe ya shilingi badala ya forex. Pia hatua za makusudi zichukuliwe, kuondokana na kununua umeme kwa fedha za kigeni, kutoka kwa wazabuni wa TANESCO - ikiwemo Songas.
Mheshimiwa Naibu Spika, napendekeza Serikali iweke kipaumbele cha umeme wa joto ardhi ambao gharama iko chini na upatikanaji wake ni wa uhakika na hauna madhara kwa mazingira. Serikali ihakikishe mradi wa joto ardhi wa ziwa ngozi uanze na kukamilika haraka.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ichukue hatua za kuimarisha rasilimali watu katika shirika la TANESCO ili iendane na usambazaji wa REA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya nadra kuniweza na mimi kuchangia katika hotuba ya Waziri wa Serikali za Mitaa, TAMISEMI, pamoja na Utawala Bora, pia ningependa kumpongeza Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mahali popote kwenye mabadiliko kibinadamu, lazima washtuke, ndiyo sababu namuomba Rais kazi anayoifanya ni nzuri sana na ukiona watu wanaanza kushtuka, penye changes yoyote kibinadamu lazima watu washtuke na kazi anayoifanya Mheshimiwa Rais ni nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais na Baraza lake la Mawaziri, kazi mnazozifanya Mawaziri ni nzuri sana, mmeleta mabadiliko kwenye nchi hii na wananchi wana imani kubwa sana na ninyi.
Katika ukurasa wa tatu Waziri wa TAMISEMI amejaribu kuainisha kazi za TAMISEMI ikiwemo usimamizi wa Halmashauri, vilevile, na kusimamia maendeleo vijijini. Kwa kweli Wizara mnafanya vizuri sana na tumeona Waziri pamoja na Naibu Waziri, jinsi mnavyofuatilia maendeleo na Naibu Waziri umetembelea Jimbo langu umekagua miradi na kweli nakushukuru sana na ninakuomba urudi tena na tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu la Mbunge ni kushauri, pale unapoona kidogo kunahitaji ushauri ili Serikali iweze kufanya kazi zake vizuri. Katika suala la maji, kwenye Jimbo langu la Mbeya Vijijini toka mwaka 2010 miaka zaidi ya mitano sasa hivi, tulikuwa tumepewa miradi karibu ya bilioni nne, zimelipwa bilioni 2.5; katika miradi yote hiyo hakuna hata mradi mmoja unaotoa maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI pamoja na Naibu wako, jaribuni kuliangalia hili kwa sababu katika kazi zenu za kusimamia hizi Halmashauri pamoja na Utawala Bora, kuangalia Serikali imepeleka bilioni nne, Mbeya Vijijini wananchi wake miaka zaidi ya tano hawapati maji. Jana wenzangu wamekwenda kutembelea hiyo miradi wamekuta pesa zimelipwa shilingi bilioni 2.5 lakini makandarasi hawapo site. Kwa hiyo, nakuomba sana ndugu yangu Waziri ujaribu kuifuatilia hiyo miradi ya vijiji vya Swaya, Horongo, Izumbwe, Iwindi, Mbawi na Mshewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Waziri, katika Halmashauri yetu ya Mbeya tuna tatizo kubwa sana la maji, pamoja na kuwa tuna vyanzo vingi vya maji, ikiwemo vyanzo vile ambavyo vinapeleka maji katika Jiji letu la Mbeya, lakini hivyo vyanzo havinufaishi Halmashauri yetu. Kuna tatizo kwenye kata ya Mjele, hakuna maji kabisa na nikiangalia katika makabrasha haya sioni kama zimetengwa pesa zozote katika maeneo yote ya kata na vijiji vile ambavyo havina maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nilitaka kuchangia, ni suala la usimamizi wa maendeleo ya Miji, ambayo iko kwenye ukurasa wa 16 wa hotuba ya Waziri. Upimaji wa ardhi ni mpango mzuri sana kwa sababu ardhi ndiyo utajiri wa Watanzania kwa ujumla, lakini kwa kiasi kikubwa ardhi hasa vijijini ilikuwa haijapimwa, wananchi hawajatumia ule utajiri wa ardhi kwa ajili ya maendeleo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba sana mipango miji ipate msisitizo na msukumo wa juu na kuhakikisha kuwa Miji midogo ambayo inajitokeza vijijini na inakuwa kwa haraka; iweze kupimwa. Maeneo yaweze kuainishwa ya mifugo, viwanda, vilevile viwanda vidogovidogo kwa ajili ya vijana wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kama Mji Mdogo wa Mbalizi hatuna hata sehemu ya kujenga maeneo ya ofisi za Serikali, hospitali, vituo vya polisi, vilevile kutokana na ongezeko la watu, kuna uhaba mkubwa wa maeneo ya ujenzi wa makazi, kwa sababu kadri ya Jiji la Mbeya linavyokua na watu wanaongezeka, ongezeko hilo linapumulia kwenye Halmashauri ya Mbeya. Kwa hiyo, nakuomba sana Serikali izingatie kupima haya maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri imeleta ombi Serikalini kwa eneo ambalo lilikuwa linamilikiwa na Tanganyika Packers ili hilo eneo ambalo liko ndani ya Mji sasa hivi ipewe Halmashauri na wananchi wapate fidia kwa wale ambao walikuwa hawajapata fidia zaidi ya miaka 40 na Tanganyika Packers, waweze kufidiwa na hili eneo ikishapewa Halmashauri liweze kupimwa viwanja na wale wananchi waweze kupata fidia, badala yake Halmashauri imetenga eneo kwa ajili ya mifugo na kwa ajili kujenga kiwanda cha nyama, kwenye kata yetu ya Mjele ambayo ina mifugo mingi na ardhi nzuri kwa ajili ya shughuli za ufugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nilitaka kuchangia, ni suala la barabara za vijijini. Kama alivyosema kwenye hotuba yake ukurasa wa 20 miundombinu ni muhimu sana kwa maendeleo ya kilimo. Tunazalisha sana mazao kwenye Halmashauri yetu ya Mbeya ikiwemo viazi, mbao, kahawa, pareto na mazao mengine, lakini barabara za vijijini haziko katika hali nzuri. Kwa hiyo, naomba hilo lifikiriwe katika bajeti yako kwa namna gani wakati tunaangalia kukuza uzalishaji wa kilimo tuangalie na kuboresha miundombinu ya barabara zetu za vijijini zina hali mbaya sana, zikiwemo zile barabara ambazo zinaunganisha vijiji kwa vijiji kwenye kata zetu kama za Isuto, Ilungu na kadhalika pia zile barabara ambazo zinaunganisha Mkoa wetu wa Mbeya na Mkoa wa Njombe, kama barabara ya Isyonje kwenda Kikondo, kwenda mpaka Kitulo, Makete na Njombe. Vilevile tuna barabara ya Mbalizi, Mjele kwenda mpaka Mkwajuni ambayo inaunganisha na Mkoa mpya wa Songwe, hizi barabara haziko katika hali nzuri ungejaribu kuangalia namna gani ziweze kuboreshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nilitaka kulichangia kwa siku ya leo ni suala zima la elimu. Suala la elimu nashukuru sana kwa mpango wa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari; limehamasisha na watu wamepata mwitikio mzuri, lakini kunachangamoto ndogo ndogo ambazo inabidi tuziangalie na kuzitatua. Changamoto hizo ni pamoja na upungufu wa waalimu kwenye shule zetu za vijijini, zote za sekondari pamoja na za msingi. Kwa shule za sekondari upungufu mkubwa uko kwenye walimu wa sayansi. Kwa hiyo, naomba uangalie hilo, tunapohamasisha elimu tuweze kuhakikisha kuwa elimu inakuwa bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nilitaka nichangie ni suala la afya. Wananchi wa Halmashauri ya Mbeya kama ilivyo kwa Halmashauri zingine wamejitokeza sana kujenga zahanati kwa kila kijiji na vituo vya afya kwenye kata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo majengo ambayo mengine yamejengwa kwa muda mrefu sana…
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umeisha naomba ukae.
MHE. ORAN M. NJENZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga hoja kwa asilimia mia moja. Naomba mchango wangu wa maandishi uingizwe kwenye Hansard.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa huo muda wa dakika tano, nafikiri itanitosha kwa vile ya kwangu ni machache sana.
Napenda kuanzia kwa kumpongeza kwanza Waziri na Naibu wake na timu nzima ya Wizara hii kwa hotuba yao nzuri. Pia napenda kusisitiza katika mipango yao wangejaribu kuangalia mawasiliano ni muhimu sana katika uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ameongelea kuhusu mobile money banking kwenye hotuba yake ya kwamba Tanzania inaongoza duniani kwa kuwa na mzunguko wa karibu shilingi trilioni 4.5 za mobile money. Tujaribu kuangalia, je, hizo pesa zote ambazo ziko kwenye mzunguko wa shilingi trilioni 4.5 kwa mwezi zina umuhimu gani kwa Taifa letu hasa kwenye uchumi wetu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini cha kuangalia zaidi ni namna gani zinasimamiwa? Ninaangalia haya makampuni mengi ambayo yanaendesha hii biashara hata mahesabu yao yanaonesha kuwa yanapata hasara. Sasa hii pesa ambayo ni 20% ya pesa zote za amana za nchi hii zinasimamiwa na makampuni ambayo yanapata hasara na hizi ni pesa za wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, namuomba Waziri pamoja na mwenzake Waziri wa Fedha waangalie mifumo ya benki sasa hivi imebadilika kutoka kule kwenye traditional banking kuja kwenye hizi benki za kileo ambazo zaidi zinatumia teknolojia. Tujiangalie ni kwa nini sisi Tanzania tuongeze hapa, are we in control, sidhani! Inaweza kuwa ni bomu hili, kwa hiyo tujiangalie sana kwa hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo napenda kuchangia ni uwanja wetu wa Songwe, miaka 14 uwanja haujakamilika na Mbeya ni geographical strategic kwa nchi yetu. Nchi zote zinazotuzunguka ni nchi kubwa za SADC na abiria wengi wanatoka huko, hivyo tukimalizia huo uwanja utatusaidia kukuza uchumi wa nchi. Kule tuna mazao mengi ikiwemo maua na mbogamboga na wenzetu wote wa Nyanda za Juu Kusini wanategemea sana huu uwanja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine ni TAZARA, watu wengi hapa hawajaongelea umuhimu wa TAZARA, kwa nini tujenge vitu vipya badala ya kuimarisha vitu tulivyonavyo? Investment ya TAZARA ni kubwa sana. Unaongelea bandari bila ya kuongelea TAZARA utakuwa unapoteza muda wako. TAZARA ndiyo tunaitegemea lakini haina menejimenti imara, muundo wake ni mbovu na wa kizamani tuuangalie. Naomba sana pamoja na kuboresha TAZARA angalia vilevile kujenga Bandari Kavu Mbeya kwenye kijiji cha Inyara itasaidia nchi zote zinazotuzunguka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine la mwisho ni suala la barabara zinazounganisha mikoa. Tuna barabara yetu ya Isyonje – Kikondo -Makete na Njombe, ni ahadi ya Rais, aliahidi akiwa Igoma na akaahidi tena akiwa Kikondo kuwa hii barabara itakamilika kwenye bajeti ya mwaka huu sasa mmeiweka wapi? Haya ndiyo maeneo yenye uchumi mkubwa wa nchi hii. Kwa nini hatu-invest kwenye vitu ambavyo vitazalisha na kuleta uchumi mkubwa kwenye nchi hii? Tunahangaika na vitu vingine ambavyo unaweza kusema labda ni vitu vya anasa hata kama ni muhimu lakini ni anasa zaidi lakini vitu ambavyo ni kwa ajili ya kujenga uchumi wa nchi hii hatuviangalii. Naomba hiyo barabara iwemo kwenye bajeti ya mwaka huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie hapo, naunga mkono hoja, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri na timu nzima ya Wizara kwa hotuba nzuri ya bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dunia ya leo uhusiano wa Mataifa ni sehemu ya kukuza uchumi na pia ni kipimo cha Nation Brand. Tanzania ina sifa kubwa na heshima kwa nchi nyingi duniani kutokana na utamaduni, amani, demokrasia na hata historia ya kuwa mstari wa mbele katika ukombozi wa Afrika. Economic diplomacy inaenda pamoja na branding ya nchi yetu kwa kuhakikisha tunaimarisha Nation Brand ya Tanzania. Hii ni pamoja na kuhakikisha Balozi zetu zinaendelea kuitangaza Tanzania na kuangalia ni jinsi gani nchi yetu inakuwa na competitive advantage na nchi jirani na Bara zima la Afrika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza Wizara iendelee kuangalia namna ya kuimarisha diaspora katika kuchangia uchumi wa Tanzania. Nchi zinazoendelea zilizo nyingi zinategemea sana fedha ya kigeni kutokana na diaspora. Tunapoangalia ushiriki wa diaspora katika uchumi wetu, napendekeza Wizara iweke utaratibu wa vijana wetu kupanua ajira ya nchi za nje. Kutokana na changamoto za ajira ni bora pia kuangalia soko la ajira la nchi za nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na maneno ya mpaka wa Ziwa Nyasa kati ya Tanzania na Malawi. Napendekeza Mheshimiwa Waziri aliambie Bunge huu mgogoro wa mpaka kama upo umefikia wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu sasa nchi jirani imetumia fursa tulizonazo hapa nchini kuzitangaza kuwa zipo kwao. Napendekeza Wizara ichukue hatua mahsusi kukomesha tabia hii. Pia ni wakati muafaka kwa Wizara kuangalia fursa za kibiashara hasa kwa nchi mpya kama Sudan ya Kusini.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kupata nafasi hii ili niweze kuchangia hii Wizara muhimu ya Ardhi. Napenda kwanza kuanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa kazi nzuri waliyoifanya na pia, kwa kuangalia hata orodha ya migogoro ambayo ametupa, inaonesha ni namna gani amejikita kuhakikisha kuwa, matatizo yote ya ardhi atayatatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hii orodha ambayo ametupa leo, katika Wilaya ya Mbeya kuna mgogoro wa muda mrefu sana kati ya Kijiji cha Kikondo na Hifadhi ya TANAPA. Waziri alitoa maelekezo kuwa wakae, ili waweze kuitatua na Serikali ya Wilaya walikaa pamoja na hifadhi kwa ajili ya kulitatua hilo tatizo, lakini tatizo linaelekea ni kwa hawa TANAPA, wamekataa kuwalipa wananchi! Wanapiga danadana! Namwomba Mheshimiwa Waziri, ajaribu kuongea na Waziri mwenzake wa Maliasili ili walitatue hili tatizo! Wananchi wako tayari kuwaachia TANAPA eneo hilo kwa ajili ya hifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wenyewe sasa hivi wanasema kabla ya bajeti hii kwisha waambiwe watapata fidia au hawatapata fidia ili waweze kuendelea na shughuli zao za kilimo! Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri aje na hilo na kama haiwezekani kupata fidia, ile ardhi ni mali kwetu tunahitaji kwa ajili ya kuendeleza kilimo. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri aliangalie hilo kwa umuhimu mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine ni kwenye mgogoro wa Wilaya ya Mbozi na Wilaya ya Mbeya kwenye Kitongoji cha Mtakuja kilichopo Kijiji cha Mjele. Hili ni tatizo la muda mrefu, naomba sana Mheshimiwa Waziri, hujaorodhesha kwenye hii orodha yako na kuna matatizo ambayo ni makubwa! Vilevile kuna hifadhi ambayo haieleweki kama ni hifadhi! Kwa vile wananchi walivamiwa pale, ng’ombe wao wakachukuliwa, nyumba zao zikachomwa moto na mpaka leo hatuelewi nini kinachoendelea!
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili tatizo waliolishughulikia ni Wilaya nyingine, Serikali ya Wilaya ya Mbozi badala ya Wilaya ya Mbeya! Hilo ni tatizo kubwa. Kitongoji kizima wananchi walishachomewa nyumba! Ng’ombe wao hawajarudishiwa mpaka leo! Naomba Wizara iangalie, hilo ni tatizo kubwa linavuruga sana Wizara, inaonekana kama nayo ni sehemu ya migogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la Mipango Miji. Kama Mheshimiwa Waziri alivyoelezea kwenye Kitabu chake cha Hotuba, ameelezea vizuri sana ni mipango gani ambayo wanayo kuhakikisha kuwa wanaendeleza mipango miji na vijijini. Kuna suala la miji midogo, naomba liangaliwe sana liwekwe msisitizo kwa vile hii ndiyo Wizara Mama ya kuangalia hayo masuala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna upungufu sasa hivi wa ardhi, Mji Mdogo wa Mbalizi umepanuka kiasi kikubwa mno kutoka wananchi chini ya 10,000 sasa hivi ni zaidi ya 100,000. Sehemu hata ya kujenga shule, huduma mbalimbali hakuna! Vituo vya Huduma za afya hatuna, lakini kuna eneo kubwa karibu hekta 2,000 ambayo ilikuwa ni eneo la Tanganyika Packers. Naomba hilo nalo Mheshimiwa Waziri alitatue haraka. Uzuri wake katika Sheria alizotupa leo nimeangalia katika Sheria ya mwaka 2007, hili shamba halitakiwi likae mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Halmashauri ya Mbeya wametenga eneo lingine mahususi kwa ajili ya kunenepeshea ng’ombe. Tunaomba hili eneo ipewe Halmashauri ya Mbeya ili waliendeleze na waweze kuwalipa wale wananchi ambao walikuwa hawajalipwa malipo yao ya fidia. Hili liwe la haraka, hili ni eneo muhimu kwa vile ndiyo linapakana na kiwanja chetu cha Songwe. Kwa usalama nafikiri ni eneo ambalo linahitaji liboreshwe, ili na mazingira vilevile ya kiwanja cha Songwe ambacho ni International Airport kiwe kimezungukwa na eneo ambalo linaleta sura nzuri ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la TAZARA; kama alivyosema mwenzangu ambaye hakumalizia, tuna tatizo la Sheria zetu ambazo wananchi hawaelimishwi. Mheshimiwa Waziri, TAZARA ilikuwa na hifadhi ya mita 30 kila upande, sasa hivi zimeongezwa 20 kila upande! Wananchi hawakuelimishwa! Wananchi hawajapewa fidia! TAZARA yenyewe iko hoi! Badala ya kufanya shughuli za usafirishaji wanafanya shughuli za kuonesha kwamba, wanawatishia wananchi kubomoa nyumba zao!
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kabla haya masuala ya kubomoa nyumba kutekelezwa wananchi kwanza waweze kupata fidia zao. Elimu kwanza itolewe, hii kusema ignorance of law is not defence! Kwa sisi wananchi wetu zaidi ya 80% wanaishi vijijini, unategemea hizi Sheria wataziona wapi? Hizi Sheria zimefichwa na sijui zimefichwa wapi? Siku ya kubomolewa ndiyo unaambiwa kuna Sheria ya mita 30. Naomba hilo liangaliwe na hatua zichukuliwe; kwanza ya kuwashughulikia watu wa TAZARA na hawa wananchi wapate fidia zao. Hayo maeneo ni ya Mji Mdogo wa Mbalizi na Kata ya Inyala, naomba hilo lishughulikiwe haraka iwezekanavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la mortgage finance. Hizi mortgage finance kwa sisi watu wa vijijini zitatufikia namna gani? Sisi asilimia 80 ya Watanzania tutapata vipi hii mikopo? Au nchi hii ni kwa ajili ya watu wachache wanaoishi mijini? Hatuoni hata siku moja tukaelimishwa kuwa kuna mikopo! Naomba Mheshimiwa Waziri aliangalie hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kuwapongeza National Housing Corporation, wanafanya kazi nzuri, ina management nzuri, ni mfano wa Watanzania ambao wanaweza ku-transform Shirika la Umma likafanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Nami niendeleze pale wenzangu walipokuwa wanakupongeza na pia kukupa moyo na kukuhakikishia hiyo kazi yako kila mmoja ameridhika kuwa ni nzuri, unafanya kazi vizuri, uendelee na moyo huo huo na uendelee na uzi huo huo na wengi tuna imani ya kwamba hiyo kazi kwako ni Mwenyezi Mungu amekupatia. Bunge hili ndilo lililokuweka wewe hapo siyo mtu mwingine na unafanya kazi vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hilo, napenda nimpongeze Waziri, Naibu Waziri na timu yake. Naye niendeleze kumtia moyo kwa kusema mtoza kodi hasifiwi hata siku moja. Kwa hiyo, awe na moyo huo kuangalia kwamba chochote atakachokifanya hata mimi mwenyewe unaponitoza kodi sitakufurahia. Mheshimiwa Waziri anafanya kazi vizuri, Wizara yake inafanya kazi vizuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuanza labda ningenukuu hitimisho la hotuba ya Waziri kidogo tu, ukurasa wa 93 anasema:-
“Mheshimiwa Spika, wananchi wetu wengi wamechoka na adha ya umaskini: Watanzania wanataka kipato cha kuweza kukidhi mahitaji yao ya msingi. Wananchi wanataka huduma bora zaidi hususan upatikanaji wa maji, elimu, afya, umeme na makazi”.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri hili ni hitimisho zito sana na kwamba Waziri imani yake ni hiyo, anatambua kuwa Watanzania tupo katika dimbwi la umaskini. Asilimia 75 ya Watanzania tunaishi vijijini, ni wakulima lakini ajaribu kuangalia na hilo hitimisho lake ametuangalia vipi sisi wananchi wa vijijini na hasa wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika ukurasa wa 95 amesema kuwa:-
“Misaada pia inaweza kuchochea rushwa na kuzorotesha jitihada za ndani hususan za ukusanyaji wa mapato”.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia amemnukuu mwanazuoni anaitwa Sebastian Edward ambaye naye alikiri kwamba Tanzania hii misaada nayo imesababisha kuharibu uchumi wetu na haikutusaidia, nami nakubaliana naye.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kulisoma hilo na mimi nikaenda kwenye kitabu kingine ambacho ameandika mwana dada Mzambia Mchumi Mbobezi, Dkt. Dambisa Moyo katika kitabu cha Dead Aid naye ameelezea hivyo hivyo kwa uchungu kabisa. Huyu ni mtaalam wa Benki ya Dunia na amepingwa na watu wengi ambao wamekuwa wakileta misaada huku. Alichosema nchi zetu hazihitaji misaada ya handout wanatufanya tuwe maskini zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, akaendelea kusema, sasa kuondokana na hilo, sisi Waafrika tunachotakiwa ni kwamba, tuweke mazingira mazuri ya kuvutia ili hawa watu waweze kutuletea mitaji ambayo itaongeza ajira kwa watu wetu. Nami nakubaliana na hilo na ndiyo sababu Serikali yetu ya Mheshimiwa John Pombe Magufuli amesema anataka Tanzania iwe ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, ukiangalia katika bajeti hii nafikiri Waziri kwa kiasi kikubwa hakupata muda wa kuiangalia vizuri, inawezekana wataalam wetu wanapotosha Mawaziri wetu. Huwezi ukazungumza maneno mazito namna hiyo halafu ukiangalia bajeti ya kilimo haieleweki. Utakuwa vipi mchungu na umaskini wakati mkulima bajeti yake ya pembejeo hujaonyesha kuwa umemwekea kiasi gani kwa ajili ya kupunguza bei ya mbolea. Watanzania tunafanya kazi kwa bidii sana, wakulima tunazalisha lakini masoko yetu hayaeleweki. Hii bajeti haioneshi ni namna gani sisi mazao yetu yatakuwa shindani na wenzetu wa Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sisi tunaolima kahawa, chai, pareto, viazi, tumbaku, bei zetu ni ndogo mno. Bei ya Kahawa ya Tanzania (Arabica) ni karibu nusu ya bei ya kahawa ile ile ya Kenya, ni kwa nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kumtoa umaskini huyu Mtanzania tuangalie tu kuboresha haya masoko.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri ameonesha kuna mkakati wa kuanzisha commodity exchange ambalo ni wazo zuri sana, lakini sijaona huo mkakati ameuelezea wapi. Faida za commodity exchange ni kubwa mno, wakulima tunalima hatuna mahali pa kuweka mazao yetu yanaharibika. Walanguzi ndiyo wanasubiri wakati wa mavuno waweze kuwanyonya wakulima. Kahawa yetu inanunuliwa na wale wanunuzi wa kutoka Ulaya ambao wananunua na Kenya lakini kwa nini kahawa yetu tulipwe nusu ya bei ya Kenya, Ethiopia au Rwanda? Naomba hilo Waziri aliangalie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumsaidia mkulima, naomba pia aangalie uanzishwaji wa Benki ya Kilimo, huu mtaji hautoshi. Nami naendelea kumshauri, najua labda hilo atakuwa halipendi, ile shilingi milioni 50 ingeenda kwenye Benki ya Kilimo. Uzoefu unaonesha hizi pesa zikienda moja kwa moja zinaenda huko kuharibu hata uchumi wa nchi yetu. Naomba tuziwezeshe SACCOS zetu, tuiwezeshe Benki ya Wakulima ili ziweze kutoa huduma kwa wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni huduma za kibenki. Huduma za kibenki ni muhimu sana kwa uchumi wetu, lakini unapoanza kuweka tozo (VAT) kwenye huduma za kibenki ina maana unazifanya zile huduma ziwe ghali zaidi na unawakatisha tamaa Watanzania kutumia huduma hizi, naomba hilo aliangalie. Waziri kwenye hotuba yake ameongelea kuwa tofauti iliyoko kati ya riba ya deposit na riba ya lending ni kubwa, sasa ukiongeza hii VAT ina maana nayo itaongeza zaidi gharama za kibenki.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania sasa hivi tunahitaji financial inclusion na huwezi ukaanza kuweka tozo wakati huo huo una-encourage financial inclusion. Huwezi ukaanza kuweka tozo kwenye capital market, capital gains tax unataka u-introduce ya nini, limetoka wapi hili wazo? Sasa hivi Watanzania tunataka tuwekeze kwenye soko la hisa unaanza kuwakatisha tamaa watu wasiwekeze huko. Utakusanya vipi kwanza hiyo tozo kwani transaction cost zinaweza kuwa kubwa kuliko hata hiyo unayotaka kukusanya. Kwa hiyo, naomba Waziri hilo aliangalie kwa upana wake na huko ndiyo mahali ambako Watanzania tunataka kwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie…
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii kuchangia kwenye hoja ya Wizara muhimu, Wizara ya fedha. Nianze kwanza kwa kuipongeza Wizara, Waziri pamoja na timu yake kwa kufanya kazi zao vizuri sana na kwa hotuba nzuri na pia kwa kutupa muelekeo ni kwa namna gani wamejipanga kuhakikisha kuwa yale malengo ambayo walikuwa wametupa mwanzoni yatatimia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo nilitaka na mimi nijaribu kushauri mambo machache. La kwanza ni suala zima la ukusanyaji wa mapato. Naona kwa muda mrefu sana tumetegemea mapato yetu kupitia TRA. Sidhani kama tukiendelea namna hiyo itakuwa sustainable ili tuweze kufikia hayo malengo na kukiangalia ni namna gani kipindi chote kilichopita tulikuwa tunazungumzia kuhusu miradi mbalimbali na Wabunge wengi tumezungumzia kuhusu namna ya kutumia pesa, hatukupata muda namna gani hizo pesa tutakazotumia zitatoka wapi na zitakusanywa wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kiasi kikubwa naona nchi yetu ina uwezo mkubwa wa kujitegemea na bila hata kutegemea misaada kutoka nje. Tukiweza kujipanga vizuri, tukaangalia zile fursa tulizonazo ambazo ni nje ya zile za kodi ambazo tulikuwa tumezizoea nafikiri malengo yetu yanaweza kutimia kwa haraka sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, angalia ofisi ya TR, tunashukuru kwanza imeimarishwa sasa hivi kuna timu nzuri. Nafikiri tukiendelea kuimarisha hii timu, kuna nafasi ya kukusanya pesa nyingi kutoka kwenye mashirika yetu. Tuangalie ni kiasi gani ambacho Serikali imewekeza mitaji kwenye hayo mashirika. Je, haya mashirika yamepewa malengo ya kurudisha kiasi gani Serikalini? Mabilioni na mabilioni yapo huko lakini ukisoma kwenye report ya Waziri anaangalia ni namna gani ya kuyasaidia haya mashirika yalipe madeni, nafikiri hilo Waziri jaribu kuangalia, dunia ya leo ni dunia ambayo inaangalia zaidi tuende Kibiashara zaidi. Tuongeze capacity kwenye mashirika yetu, tuwe na management zinazoeleweka, tuangalie mifano ya mashirika yanayofanya vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, angalia Shirika kama NMB, benki kama NMB ilivyokuwa? Ilikuwa imefilisika lakini leo inafanya kazi vizuri sana. Sababu yake kubwa ni nini? Ni kwa sababu Serikali ilihakikisha kuwa inaweka management nzuri na leo hii ukilinganisha NMB na NBC ninaimani NMB inafanya vizuri zaidi. Angalia Shirika la Nyumba lilivyokuwa hoi lakini baada ya kuweka management nzuri, Shirika la Nyumba sasa hivi linafanya vizuri sana. Kwa hiyo, na haya mashirika mengine naomba mpe uwezo mkubwa sana TR aweze kuangalia hata vilevile management zitakazokuwepo pale na bodi zitakazokuwepo pale, hilo lizingatiwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nilichokuwa namuomba Waziri aangalie ni Benki ya Wakulima. Naona kwenye repoti ya Kamati wametoa mawazo mazuri sana ya milioni 59 zile ambazo zililengwa kwenda kwa ajili ya Mfuko wa Vijiji zipelekwe kwenye Benki ya Wakulima na mimi hilo naungana nao. Hizi zitasaidia sana ili zilete chachu huko vijijini, wakulima waweze kupata mikopo kirahisi lakini pia na zile pesa ziweze kusimamiwa kitaalamu. Lakini vilevile milioni 59 ni kidogo mno, naomba ziongezwe zifikie hiyo bilioni 196 ambayo ni asilimia 20 ya bilioni 980.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo ningependa zaidi Wizara iliangalie; ushiriki wa mabenki kwenye uchumi wa nchi yetu. Riba za mabenki ni kubwa sana ukilinganisha tofauti ya riba anayolipwa anayeweka pesa (depositor) na anayekopa ni kubwa kupita kiasi na tumeona kwa muda mrefu haya mabenki yanatengeneza pesa nyingi sana, lakini ni namna gani hizi pesa wanazozitengeneza ambazo zimetokana wakati mwingine na amana za walalahoi zimeweza kurudisha kwa wale watu ambao ni depositors. Nafikiri hili nilijaribu kuliangalia, hizi riba za asilimia 20, asilimia 18 ni kubwa mno. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine; unapoangalia amana nafikiri Mheshimiwa Waziri aangalie pesa zinazozunguka kwenye miamala ya M-pesa or mobile money, ni kubwa mno. Hizi tumeziangalia vipi ya kwamba nazo zinawezakusaidia kwenye uchumi wa nchi hii? Zinasimamiwa vipi? Nafikiri hilo tuendelee kuliangalia vizuri. Ukiangalia katika hotuba ya Wizara hapa, hajaiona hiyo kama ni sehemu mojawapo ya amana tulizonazo nchi hii ambazo zinaweza kusaidia katika uchumi wa nchi yetu. Amana inayozunguka kwa mwezi mmoja ni zaidi ya trilioni 4.5, hizo ni nyingi mno. Chukulia kidogo tu, ya kwamba unaweza kuchukuklia hata 0.5 zirudi kwenye uchumi wetu, utapata bilioni zaidi ya 270. Naomba na hilo liangaliwe kwa karibu, tuweke mfumo vilevile wa kuzilinda.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ningependekeza tuangalie vilevile ni namna gani tuweke usimamizi wa hizi pesa ambazo Wizara zinakwenda kwenye miradi yetu. Nafikiri hapa kuna tatizo kubwa kwa sababu kama Wizara itapeleka pesa kwenye Halmashauri au kwenye miradi asilimia yote ile ikaliwa hiyo mojawapo ni kwamba yale mapato tunakuwa tumeyapoteza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunakuwa hatuna sababu ya kuzungumzia kutafuta mapato wakati tunashindwa kusimamia vizuri matumizi ya hayo mapato. Ukichukulia mfano, kwenye Halmashauri ya kwangu kuna bilioni zaidi ya two point five zimepelekwa kwa ajili ya miradi ya maji lakini mpaka leo unashindwa kuuliza ni nani ambaye anasimamia zile pesa. Maji hayatoki, miradi huioni! Makandarasi huwaoni!
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hizo ni pesa za wananchi, ni pesa za kodi, nani anazisimamia? Zimetoka Wizara ya Fedha labda zimekwenda Wizara ya Maji na zimekwenda Halmashauri, msimamizi ni nani hapo katikati? Na hili nafikiri ni tatizo kubwa, nafikiri tuweke coordination kati ya hizi Wizara zinazohusika ili tuweze kusimamia hii miradi yetu vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Sika, baada ya kusema hayo ningependa kwa kumalizia kuipongeza hii Wizara na pia suala zima la commodity exchange ingawa nimeongelea kwa kiasi kidogo sana lakini nafikiri hiki ni chombo muhimu sana hasa kwa wakulima. Tuiangalie kianzishwe haraka ili kiweze na wakulima wakafaidika na mazao hayo ambayo kwa sasa hivi tunapovuna, mahindi bei inakuwa kidogo sana lakini baada ya muda mfupi bei zinapanda. Kwa hiyo, kama kukiwa na chombo kama hiki kinaweza kusaidia ili wakulima waweze kufaidika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii ya kuchangia mapendekezo ya Mpango na Mwongozo wa Bajeti.
Kwanza nianze kumpongeza Waziri na timu yake kwa mapendekezo mazuri sana ambayo yanaelekeza ni namna gani kwa mwaka unaokuja tutatekeleza maendeleo ya nchi yetu. Pia nampongeza kwa jinsi alivyojaribu kuangalia review kwa kipindi kilichopita na kutulinganisha na sisi na nchi zetu ambazo zinatuzunguka tuna-perform namna gani? Nafikiri huo ni muendelezo mzuri kwa sababu katika nchi yoyote katika dunia ya leo ya ushindani, nchi kama ya kwetu lazima tuangalie ni namna gani tunashindana na majirani zetu, ni namna gani tunashindana vilevile na mashirika mengine ambayo yanatuzunguka. Kwa hiyo, hilo nakupongeza sana Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo nina mapendekezo machache la mapato, unapoongelea matumizi ni lazima kuwe na mapato ya uhakika. Nchi yetu imejaaliwa neema kubwa mno, naona mapendekezo kwa kiasi kikubwa yanajilenga mno kwenye mapato ya ndani (tax revenue). Nilikuwa naomba sana Waziri jaribu kuangalia ni namna gani tukuze mapato ya non revenue hasa kutokana na investment tulizoziweka kwenye mashirika yetu. Hali ilivyo sasa haya mashirika yanahitaji msukumo ili yaweze kuzalisha mapato ya kutosha na yaongeze Pato la Taifa ili tuwe na hela nyingi, tuwe na vyanzo vingi ambavyo vina uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mojawapo ambalo linatakiwa lisimamiwe ni lile la kuangalia kwamba mashirika yetu yanatekeleza yale majukumu yake ya msingi na yasifanye vitu ambavyo haviko katika msingi wa shughuli ambazo tulikuwa tunazitegemea. Kwa mifano, mashirika yetu ya pension funds mengi yalienda kujiingiza kwenye kuwekeza kwenye majengo. Shirika letu la National Health (NHIF) nalo kwa kiasi kikubwa badala ya kuangalia kuboresha afya nalo likajiingiza kwenye real estate.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unapoangalia ni namna gani tunaweza ku-finance zahanati, vituo vya afya nafikiri tungeitumia NHIF tusingepata shida sana hapa, tungetimiza lengo letu la kujenga zahanati kwa kila kijiji, vituo vya afya kwa kutumia hela ya NHIF. Kwa sababu Halmashauri zinauwezo wa kulipa hilo deni kutokana na mapato ya hizo zahanati na vituo vya afya. Kwa hiyo, naomba jaribu kuliangalia hilo tutoke kule tulikozoea tuende kwenye njia mpya ambazo zinaweza ku-finance bajeti yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine wenzangu wameliongelea sana suala la kilimo. Viwanda na kilimo vinaenda pamoja, unapoongelea viwanda tuongelee ni namna gani tutaboresha kilimo chetu. Kwa mfano, kwa Jimbo langu la Mbeya Vijijini mkituwezesha kulima pareto na kahawa ili tuweze kushindana na Kenya, Rwanda, Ethiopia tuna uwezo wa kuleta pato kubwa sana kwa nchi hii tena la forex.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa hotuba nzuri aliyowasilisha Bungeni kwa Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018. Napenda pia kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia napenda kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri sana ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2015 - 2020.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ni muhimu sana kwa uhai wa Muungano wetu na wamefanya kazi kubwa sana ya kuondoa kero za Muungano. Kwa kiasi kikubwa Muungano wetu umetuletea sifa nyingi kutoka kila pande za dunia; changamoto kubwa tuliyonayo ni uharibifu wa mazingira na tabianchi. Katika maeneo mengi kuna uharibifu mkubwa sana wa mazingira unaotokana na shughuli za kibinadamu. Uharibifu huo unasababisha changamoto za tabianchi ikiwemo upungufu wa mvua na majanga mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira napendekeza Wizara iimarishe elimu ya utunzaji mazingira na pia kuimarisha ofisi na wataalam katika maeneo ya kimkakati, kama vile Mikoa ya Mbeya na Iringa ambayo ni vyanzo vikuu vya mito ikiwemo Mto Ruaha. Pamoja na elimu, wananchi wa maeneo ya kimkakati ya mazingira wanahitaji motisha ili watunze mazingira yao. Motisha kama vile kupewa kipaumbele cha nishati, miundombinu, elimu na hata kupatiwa miche bure itasaidia kwa kiasi kikubwa utunzaji wa mazingira. Maeneo haya yanahitaji upendeleo wa makusudi ili kukuza uchumi wa wananchi katika maeneo haya na kwa kiasi kikubwa kupunguza uharibifu wa mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na utunzaji wa mazingira Wizara ya Kilimo ishirikishwe ili kuhimiza kilimo cha kuhifadhi ardhi ambapo mkulima ahitaji kulima kwa jembe wala kuchoma moto. Elimu ya kilimo cha hifadhi ardhi kiendane na pembejeo bora zikiwemo mbegu bora ili wakulima waone tija ya hiki kilimo cha kuhifadhi ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uharibifu wa vyanzo vya mito umesababisha mito mingi kukauka na pia michanga na udongo kujaza maziwa yetu ikiwemo Ziwa Rukwa ambalo limo hatarini kutoweka. Serikali za Mitaa zihimizwe kutafuta maeneo mbadala ya uchimbaji mchanga ili kunusuru vyanzo vyetu vya mito.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kama walivyosema watangulizi wangu, nianze kwanza kwa kuzipongeza hizi Kamati mbili za PAC na LAAC kwa kazi nzuri walizofanya na ripoti zao ni nzuri sana na pia recommendation zao nazo ni nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, labda nianzie pale alipoishia msemaji wa mwisho. Ukiangalia masuala yote haya inaonekana udhibiti wa haya mashirika yetu na hata taasisi zetu kuna mahali pana legalega. Ukijaribu kuangalia kwa mfano mdogo tu kwa ripoti kama ya NSSF achilia mbali hiyo ya Mradi wa Dege lakini wamekopesha mikopo kwa SACCOS mabilioni mengi na wao sio benki, hawana utaalam wa taasisi za kibenki. Kawaida ya SACCOS unategemea kwamba hawa wanafanya savings and credit unakuta SACCOS ndiyo zinaanza kukopa, ni kitu cha hatari sana katika uchumi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tungetegemea SACCOS zikusanye savings huko na zikopeshe wale members wao. Sasa unakuta shirika kama NSSF ambapo siyo kazi yake inakwenda kukopesha SACCOS na hizo SACCOS kama ripoti inavyosema zingine ni hewa, zaidi ya shilingi bilioni 70 imetolewa kama ilivyoelezwa kwenye ripoti humu. Hizo pesa zote ni za umma na zimekwenda sehemu ambayo siyo. Kama ripoti ya PAC ilivyosema ufanyike uchunguzi kuangalia namna hiyo mikopo ilivyotolewa na ilikwenda kwa nani na kwa jinsi gani. Sidhani kama wana kitengo maalum kwa ajili ya kukopesha na sidhani kama wana software ya kibenki ambayo inaweza kufanya tracking ya mikopo hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni la usimamizi wa mashirika yetu. Kuna mifano imetolewa ya EWURA na SUMATRA kuwa yale makusanyo yao yote wameyatumia katika matumizi ya mishahara na matumizi ya kawaida. Ukiangalia EWURA wametumia zaidi ya 71% na SUMATRA wametumia 82% ya pesa walizokusanya. Sasa unajaribu kuangalia hawa SUMATRA na EWURA ni vyanzo vya mapato ya Serikali, badala ya kutumia hizo pesa kutunisha Mfuko wa Hazina wenyewe wamezitumia kwa matumizi ya kama kujilipa mishahara, posho na matumizi mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naungana na PAC kushauri kwamba Ofisi ya Msajili wa Hazina iweze kuimarishwa ili iweze kuyasimamia mashirika haya kwa ukaribu zaidi. La sivyo tutaendelea kutegemea tax revenue na tukaacha hili eneo ambalo Serikali yetu kama ikilisimamia vizuri litaondoa kabisa kutegemea kodi ambazo zinaongezeka kila siku. Tukisimamia hizi investments, haya mashirika tuna uwezo hata wa kupunguza kodi kwa wafanyabiashara wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wenzangu waliongelea kuhusu Internal Auditor (Mkaguzi wa Ndani). Nafikiri huu mfumo uliopo sasa hivi kwa Wakaguzi wa Ndani kwenye Halmashauri zetu kuwa chini ya Wakurugenzi siyo sahihi. Internal Auditor kama alivyo External Auditor wanatakiwa wawe na uhuru wa aina fulani kwa watu wanaowakagua. Sitegemei Internal Auditor anayeripoti kwa Mkurugenzi amkague Mkurugenzi atatoa ripoti nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kikawaida hata code of ethics za Internal Auditors zinasema Internal Auditor awe independent anatakiwa aripoti kwa mtu ambaye ni tofauti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile nilivyokuwa naangalia governance za hizi Halmashauri zetu nafikiri kuna vitengo ambavyo vinahitaji kuimarishwa kama Audit Committee na Risk Committee. Ukiangalia composition za hivi vitengo nafikiri haziko sawasawa. Kama tungekuwa na Internal Audit Committee na Risk Committee ambazo zinajitegemea tungeweza vilevile tukaagiza hawa Internal Auditor waripoti kwenye hizi committee ambazo ziko nje ya utawala wa DED. Mimi naona kwa vile kuna Director of Internal Audit ambaye yuko chini ya Wizara ya Fedha labda angejaribu kuwa karibu zaidi kuwaangalia na kuwasimamia hawa Internal Auditors ili waweze kulinda maslahi ya pesa zetu na kusiwe na ufujaji mkubwa wa hizi pesa zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kumpongeza Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kazi nzuri ya kuendeleza michezo na sanaa. Pia napenda kuwapongeza kwa hotuba nzuri ya bajeti ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi uliotukuka na hasa kuhakikisha maendeleo mazuri ya Sekta ya Habari, kuendeleza utamaduni, mila na desturi za Mtanzania, kuimarisha tija na kulinda kazi za sanaa na pia kuendeleza michezo katika Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, napenda kuwapongeza Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri za kusimamia shughuli za Serikali na kuhakikisha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015 - 2020.

Mheshimiwa Spika, Tanzania kama ilivyo kwa nchi zingine ina jukumu kubwa la utambulisho wa Taifa, kupitia Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo. Nchi yetu imesheheni vipaji mbalimbali na kinachohitajika ni kuibua hivi vipaji na kuviendeleza.

Mheshimiwa Spika, vipaji vingi vya michezo vipo vijijini na juhudi za makusudi zinahitajika kuibua vipaji vya michezo na sanaa huko vijijini ili viendelezwe. Michezo na sanaa ni ajira nzuri sana kwa dunia ya leo na pia ni utambulisho mzuri wa Taifa letu (National brand) na michezo pamoja na sanaa vinaleta heshima kubwa kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Mbeya Vijijini na hata Mkoa mzima wa Mbeya kuna vipaji vingi katika michezo hasa mpira wa miguu na riadha. Serikali ichukue hatua za makusudi za kimkakati wa kuibua hivi vipaji ikiwa ni pamoja na kuhimiza michezo mashuleni na kujenga viwanja vya michezo vijijini.

Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa kipekee wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) ambalo ni tegemeo la Watanzania walio wengi vijijini kupata habari mbalimbali kwa muda mrefu TBC haisikiki katika maeneo mengi vijijini na wananchi wanakosa fursa ya kupata habari. Pamoja na kutengewa bajeti ya shilingi bilioni moja katika Mwaka wa Fedha 2016/2017, lakini ripoti ya Kamati inaonesha bado utekelezaji na pia kiasi hiki ni kidogo ukilinganisha na mahitaji halisi ya uwekaji wa vyombo vya aina yake. Naungana na maoni ya Kamati ya kushauri Serikali kuwekeza vya kutosha katika Shirika la Utangazaji (TBC).

Mheshimiwa Spika, kutokana na tatizo la wizi wa kazi za Wasanii wakiwemo waimbaji wa Injili, nashauri Serikali iweke mkakati wa kulinda kazi za wasanii ili waongeze kipato kwa kazi zao na pia mapato ya Serikali yataongezeka.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza Waziri wa Fedha na Mipango kwa kuandaa mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa pamoja na mwongozo wa kutayarisha mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada nzuri zinazochukuliwa na Serikali katika kuongeza pato la Taifa kwa kiasi kikubwa tegemeo kubwa ni mapato ya ndani (tax revenue) kuliko kuangalia vyanzo vingine vya mapato (non tax revenue)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vema Serikali ikajielekeza katika vyanzo vingine vya mapato (non tax revenue). Serikali ijiimarishe katika usimamizi wa taasisi zake zilizo chini ya Msajili wa Hazina ili zijiendeshe kibiashara na kurudisha mapato Serikalini kupitia gawio (dividend) na hata mapato mengine nje ya gawio. Serikali ichukue hatua za kurekebisha Mashirika yanayolegalega na hata kuyafunga yale ambayo hayana tija. Katika kufufua Mashirika na viwanda ambavyo havifanyi kazi, Serikali ichukue tahadhari kubwa hasa pale inapopelekea ubinafsishaji kwa wageni.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na lengo zuri la kufufua viwanda ambavyo kwa muda mrefu havifanyi kazi, lengo liwe kuanzisha kitu kipya katika mazingira ya sasa. Kwa mfano, Kiwanda cha Tanganyika Packers cha Mbeya, kwa sasa yaliyolengwa kuwa mashamba ya malisho (holding ground) kwa sasa yapo katikati ya mji na sheria za mipango miji zina ukomo wa shughuli za kilimo kwa mijini. Hivyo ni bora kuangalia kupata eneo mbadala jipya nje kidogo ya mji.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuipongeza Serikali kwa kujikita katika kuimarisha uchumi kupitia sekta ya viwanda. Pamoja na mkakati wa kuimarisha uchumi kupitia viwanda, Serikali iweke mkakati wa kuimarisha kilimo cha mazao yote. Nchi yetu kwa asilimia zaidi ya 70 wananchi wake wanategemea kilimo hivyo viwanda vilenge kutumia malighafi inayozalishwa Tanzania ili ukuaji wa uchumi uwaguse Watanzania walio wengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania imejaaliwa kuwa na ardhi kubwa na nzuri ambayo inaweza kuzalisha mazao mbalimbali yenye soko zuri la ndani na nje. Zao kama pareto limeachwa yatima licha ya mahitaji makubwa katika soko la dunia. Kuna haja ya kuongeza uzalishaji wa pareto na pia kuwepo na viwanda vya pareto maeneo yanayolima pareto. Kwa sasa soko la pareto hapa Tanzania linayumba kutokana na kukosa ushindani katika manunuzi toka kwa mkulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iangalie utekelezaji wa miradi iliyomo katika mipango iliyopita. Pamoja na mahitaji ya miradi mipya, mikakati iwepo ya kutekeleza miradi ya nyuma kama vile miradi ya maji, zahanati na vituo vya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mashirika kama NHIF yajikite katika malengo yake ya msingi na yakisimamiwa vizuri wanaweza kuwekeza katika ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na uwekezaji huo una uhakika wa kuilipa NHIF kutokana na mapato ya hizo zahanati na vituo vya afya. Kwa sasa NHIF wamejiingiza katika kuwekeza kwenye real estate badala ya kuboresha afya za Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, napongeza Serikali kwa kutenga shilingi milioni 50 kwa kila kijiji na mtaa. Ili kutimiza lengo hilo, napendekeza Serikali itenge angalau shilingi bilioni 300 kila mwaka kuanzia 2017/2018 ili kukamilisha upelekaji wa fedha hizo kwenye maeneo yote kabla ya 2020.
Mheshimiwa Naibu Spika, dhamira ya milioni 50 kwa kila kijiji inahitaji kuandaa utaratibu mzuri kushirikisha SACCOSS na pia napendekeza kuitumia Benki ya kilimo TADB. Kwa kuitumia TADB Serikali itatimiza malengo ya kuinua uchumi, wakulima pia kuiwezesha TADB kupata mtaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na ujenzi wa reli ya kati kwa standard gauge, Serikali iweke mkakati wa kuboresha utendaji wa TAZARA ikiwemo kujenga matawi ya reli kuunganisha Liganga na Mchuchuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iweke mkakati wa kuboresha miundombinu ya Baraza la vijijini kuwezesha usafirishaji wa mazao na kurahisisha masoko ya mazao.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwapongeza Kamati ya Nishati na Madini kwa taarifa nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na utekelezaji mzuri wa miradi ya REA, naungana na Kamati kupendekeza kuwepo kwa usimamizi mzuri wa hii miradi ili iwe endelevu kitaalam. Usambazaji kwa maeneo ya vijijini, waya zinawekwa umbali mrefu na pia miundombinu ya nguzo za kawaida ni changamoto kutokana na mazingira ya vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kazi nzuri inayofanywa na REA, napendekeza Serikali iwe na mkakati wa kuimarisha wataalam wa TANESCO ili waendane na ongezeko na kasi ya usambazaji wa umeme kwa mpango wa REA. Kutokana na ongezeko la usambazaji wa umeme kumesababisha kuzorota kwa huduma za dharura (emergency) hasa katika maeneo ya vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii adimu ya kuchangia hizi Kamati mbili muhimu; Kamati ya Ardhi na Kamati ya Kilimo. Kamati zote mbili zimewasilisha ripoti nzuri sana na maoni yao ni mazuri sana na naiomba sana Serikali ichukue haya maoni na mapendekezo kwa uzito kulingana na umuhimu wa ardhi ya nchi yetu pamoja na kilimo kwa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na suala la mipango miji. Sheria ya Ardhi ya Mipangomiji na Vijiji ni nzuri sana, lakini ukiangalia mipangilio yetu ya miji toka 2007 ilipotoka hiyo sheria kwa kweli inasikitisha sana. Napendekeza; kwa uzito wake wa mipangomiji sasa hivi hakuna miundombinu kwenye miji yetu, hakuna barabara, hakuna sehemu ya kupitisha mabomba; hilo lingezingatiwa na kuhakikisha namna ya kuzishirikisha taasisi binafsi na National Housing wakafanya kazi kwa pamoja kuhakikisha kuwa tunakuwa na mipangomiji mizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri nilionao ni kwenye Mji Mdogo wa Mbalizi. Pale Mji mdogo wa Mbalizi kulikuwa na watu 2,000 miaka 10 iliyopita lakini sasa hivi kuna watu wanaokaribia 150,000; lakini ukienda pale ni squatters tu hakuna mitaa. Kwa watu hao 150,000 hata miundombinu ya maji ni ile iliyokuwepo kwa ajili ya watu 2,000. Sasa hii inatuonesha ni namna gani tuko nyuma katika kupanga miji yetu. Wananchi wetu wanataka hizi huduma na sisi tunaiomba Serikali iangalie jinsi ya kuwasaidia wananchi. Sasa hivi vijiji vingi vinageuga kuwa miji, badala ya watu kujenga kiholela Serikali iwe ya kwanza kuhakikisha kuwa inapanga hayo maeneo na yanapimwa kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Mbalizi kuna ekari zaidi ya 6,000 za iliyokuwa Tanganyika Peckers miaka zaidi ya 50 iliyopita, kile kiwanda hakikuanza kufanya kazi, hizo ekari 6,000 zote hazijafanyiwa chochote na halmashauri na wananchi wote wa Mbeya DC waliamua kuwa waombe hili eneo ili liweze kupimwa liwe makazi ya watu, wautengeneze mji bora ambao utaonesha kioo cha Mbeya kwa sababu hilo eneo ndilo eneo ambalo liko karibu na uwanja wa ndege, ndilo eneo ambalo unatoka katika nchi jirani za Zambia mpaka Afrika Kusini unapoingia Mbeya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wananchi wameomba hilo eneo ili wapewe kuwe na mpangomji na Sheria Namba Nane kama sijakosea inasema uwekezaji wa mashamba kwa mijini usizidi eka tatu. Kwa hiyo hiyo eka 6,000 kwa kuwekwa mjini kwa ajili ya malisho ya ng’ombe nafikiri tutakuwa tunachekesha. Uzuri wake halmashauri imetenga eneo mbadala kwa sababu nao wanahitaji hiki kiwanda cha nyama na vilevile wanahitaji maboresho kuhakikisha kuwa tunafuga mifugo bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, walichokifanya halmashauri, wamejenga wao machinjio ya kisasa kwa ajili ya soko la ndani na soko la nje. Kwa hiyo, eneo mbadala limepatikana na Serikali itakapopata mwekezaji eneo tunalo tayari. Sisi tunachoomba, hili eneo ambalo liko mjini iachiwe Halmashauri ya Mji wa Mbalizi ili tutengeneze makazi ya kisasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi shule zetu za msingi na sekondari zina idadi ya wanafunzi kubwa mno na hatuwezi kupanua shule, wanafunzi wakifaulu darasa la saba wanakwenda sekondari za mbali ambazo wanatembea zaidi ya kilometa 10, sidhani katika hali ya sasa hivi kama hayo yanakubalika. Kwa hiyo, tunaomba sana huu ushauri Serikali iuchukue.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tumeona kwamba ardhi yetu pamoja na kuwa tajiri wanaofaidi ni wageni. Nilipotembelea National Housing na kamati yangu pale Tanganyika Peckers, Kawe, tuliambiwa kuwa ile ardhi mwekezaji alinunua kwa bilioni sita kwa ajili ya kiwanda, hakujenga, hakuendeleza. National Housing walipokwenda pale kutaka wapate lile eneo mwekezaji akakataa, alipotaka kununua kakataa, akakubali kwamba waingie joint venture, kwa bilioni sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti,Investment iliyoko pale sasa hivi ni mabilioni kama sio trilioni. Sasa jaribu kufikiria mtu mgeni unampa utajiri wa namna hii kwa mali yetu, hajafanya chochote. Sasa hilo lisijirudie katika maeneo mengine ya iliyokuwa Tanganyika Peckers.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kilimo; mimi ni mkulima. Ili umsaidie mkulima unahitaji uwekezaji kwanza, unahitaji umpe mtaji, unahitaji utaalam, unahitaji masoko. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wamelichangia hili kwa umakini mkubwa sana, lakini angalia, mtaji utapata wapi? Benki ya wakulima leo hii haina mtaji, bilioni 60 ilizokuwa nazo imewekeza karibu bilioni tatu tu, sasa wakulima nani atawasaidia?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kwenye wataalam wataalam wenyewe hatuwaoni wakija kwenye mashamba yetu. Mimi nikiwa kama mkulima sanasana wageni wangu wanaonitembelea kutoka Serikalini ni OSHA na…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, Naibu Waziri na Timu nzima ya Wizara kwa ripoti nzuri na pia bajeti nzuri ya mwaka 2017/2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Mheshimiwa Samia Hassan Suluhu Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa Mbunge, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuiongoza vema nchi yetu katika utekelezaji wa Ilani ya CCM 2015/2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano ni muhimu sana katika uchumi wa nchi yetu na katika kipindi cha bajeti ya 2016/2017. Serikali imefanya vizuri sana kama ifuatavyo:-

(1) Ujenzi wa reli ya standard gauge umeanza;
(2) Serikali imeendelea kulipa madeni ya wafanyakazi wa TAZARA ambapo shilingi billioni 16.8 zimelipwa kati ya shilingi billioni 22.9 zilizokuwa zinadaiwa;
(3) Serikali iliingia mkataba wa ununuzi wa ndege sita, ndege mbili aina ya Bombardier dash 8-Q400 ziliwasili nchini Septemba, 2016;
(4) Ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa mawasiliano;
(5) Ujenzi wa barabara za juu kwenye makutano ya TAZARA unaendelea vizuri; na
(6) Ujenzi wa barabara na madaraja mbalimbali unaoendelea nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dunia ya leo ya ushindani mkubwa wa kibiashara umepelekea biashara ya Kimataifa kuwa ya masaa 24 na siku saba za wiki na ili kuwe na tija na ufanisi katika uchumi wetu tunahitaji uboreshaji wa miundombinu ya barabara, reli, bandari pia mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto za usafirishaji na miundombinu ya bandari yamepelekea kwa kiasi kikubwa gharama kubwa za ndani (domestic supply chain costs) kwa bidhaa zetu na hata pembejeo za kilimo ukilinganisha na nchi zingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama kubwa ya mbolea kwa mkulima wa Tanzania imebebwa na gharama za bandari, usafiri wa barabara na hata ucheleweshwaji wa kutoa mzigo bandarini. Mnyororo wa gharama za mbolea kwa mkulima wa Tanzania, hivi sasa asilimia 47 ni gharama za ndani port charges, transportation, taxes and mark up, wakati asilimia 53 ni gharama ya kununulia nje ya nchi CIF kwa kulinganisha na nchi ya Ufilipino gharama ya ndani ni asilimia 16 tu na CIF ni asilimia 84. Pia nchi ya Myanmar gharama za ndani za mbolea ni 23% tu wakati gharama za kununulia CIF ni asilimia 77, hivyo mzigo mkubwa wa bidhaa za Tanzania unatokana na uchukuzi, tozo mbalimbali za bandari na matumizi ya barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali iboresha TAZARA pia ili mbolea isafirishwe kwa reli badala ya barabara ambayo ni gharama kubwa sana. Pia napendekeza Serikali iendelee kuboresha bandari ili meli kubwa ziweze kuingia kwa urahisi, vilevile shehena za mizigo ya mbolea zipewe kipaumbele cha kupakuliwa bandarini. Pia kuwepo na kituo kimoja cha huduma kwa wateja one stop centre.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuboresha bandari ya Dar es Salaam na TAZARA napendekeza kujenga bandari kavu katika eneo la kimkakati la Inyala, Mbeya ili wateja wa Zambia, Malawi, DRC Congo na hata wafanyabiashara Watanzania kutoka Nyanda za Juu Kusini wasilazimike kuchukua mizigo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu ndiyo chachu na tija bora hasa katika sekta ya kilimo ambayo ndiyo mhimili wa uchumi wetu wa Tanzania. Barabara za vijijini ni muhimu sana kwa kusafirisha mazao ya kilimo na pia kupunguza gharama za usafiri wa pembejeo na urahisi wa kupeleka mazao sokoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuboresha usafirishaji wa mazao ya kilimo na pia kuunganisha mikoa kwa barabara za lami (trunk roads) napendekeza Serikali kuboresha barabara zinazounganisha Mkoa wa Mbeya na mikoa mingine kama vile babaraba ya Isyonje-Kikondo Makete - Njombe, barabara ya Mbalizi-Shigamba-Ileje inaunganisha Mbeya na Ileje - Songwe, barabara ya Mbalizi-Makongorosi inaunganisha Mbeya na Songwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuboresha usafirishaji wa mazao na pembejeo, napendekeza kupandishwa hadhi barabara za kimkakati zikiwemo Kawetere-Mwabowo- Ikukwa, Mbalizi-Iwindi-Jojo, Inyala-Simambwe na Imezu – Garijimbe (mchepuo/bypass)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Serikali inajenga barabara ni muhimu pia kuzingatia vigezo vya kiuchumi pamoja na ahadi za Marais waliostaafu na Rais aliye madarakani, pamoja na barabara zilizotajwa hapo juu. Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne na Rais wa sasa waliahidi ujenzi wa barabara ya mchepuo by pass ya kilomita 40, kuanzia Mlima Nyoka Inyala-Ijombe-Swaya-Igale-Iwindi- Songwe. Pamoja na kupunguza msongamano pia ni barabara inayounganisha machimbo mapya ya umeme wa jotoardhi na mgodi mpya wa Pandahill.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto za kiwanja cha ndege cha Songwe ni pamoja na kukosekana kwa uzio wa uwanja na kutokuwa na navigational aids, ikiwemo taa katika njia za kutua na kurukia ndege. Eneo la uwanja wa Songwe lina ukungu hususani wakati wa asubuhi na hivyo kuwa vigumu kwa marubani wa ndege kuona kiwanja vizuri. Kukosekana kwa taa kumepelekea na kusababisha usumbufu mkubwa kwa abiria na hata mashirika ya ndege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na ukanda wa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kuwepo kwa mazao mengi ya kilimo, hasa matunda, mbogamboga na hata maua, kuna fursa za ndege za mizigo kuchukua hayo mazao na kupeleka moja kwa moja soko la nje. Kutokana na ukosefu wa taa navigation aids na uzio mashirika ya ndege za mizigo yameshindwa kuanza usafirishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali kuhakikisha kabla ya mwaka wa fedha 2016/2017 kwisha, fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya taa, navigation aids na uzio wa kiwanja cha Songwe, zinatolewa ili kukamilisha kazi hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyokuwa uchukuzi, na ujenzi, mawasiliano ni muhimu sana kwa wakulima vijijini. Serikali inapoangalia kuanzisha soko la mazao Tanzania, commodities exchange market ni muhimu sana kwa sasa kuhakikisha maeneo ya vijijini yanakuwa na minara ya mawasiliano. Napendekeza Serikali iharakishe ujenzi wa minara ya mawasiliano hasa kwa vijiji ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, vikiwemo Vijiji vya Itala, Mkuyuni, Ulenje, Wambishe, Ihango, Mashese, Nyalwela, Mwela, Shango, Ngole, Ikukwa, Ipusizi, Izyira, Shizuvi, Shisyete, Isonso na Igalukwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeoe ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa hotuba nzuri ya Bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2017/ 2018. Pia napenda kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri na wataalam wote wa Wizara hiyo kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuhakikisha kwamba kila Mtanzania anapata huduma hiyo stahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mwongozo wake imara kwa nchi yetu hasa katika kuimarisha huduma za afya na ustawi wa jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pia napenda kumpongeza Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wao mzuri na kusimamia Ilani ya Uchaguzi ya CCM na hasa katika masuala ya afya na ustawi wa jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wote tunatambua umuhimu mkubwa na wa mwanzo kabisa wa afya ya wananchi wetu. Afya ni suala la msingi katika ustawi na hata uchumi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na umuhimu wa afya kwa kila Mtanzania inabidi Serikali kuangalia namna mbadala za kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora ya afya. Katika ukurasa wa 65 na 66 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya ameeleza kuwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) una wanachama 792,987 hadi kufikia Machi 2017; vilevile idadi ya wanufaika ni 3,880,088 hadi kufika Machi 2017. Kwa upande wa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ulikuwa na kaya 1,595,651 na wanufaika wa CHF walikuwa 9,573,906

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufikia Machi 2017, Mifuko ya Bima ya Afya ya NHIF ilikuwa na wanachama (kaya) 2,388,638 zenye wanachama 13,453,994 tu. Hii ni sawa na asilimia 38 ya Watanzania wengi hasa wa vijijini wanaoendelea kukosa huduma ya afya kwa ukosefu wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya uzinduzi wa bodi mpya mwaka 2016 ya Wakurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Waziri wa Afya alisema mkakati wa Serikali ni kufikisha huduma ya bima ya afya zaidi ya asilimia 50 kwa Watanzania wote ifikapo mwaka 2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza muswada huo wa bima ya afya uwasilishwe mapema iwezekanavyo ili Watanzania wengi zaidi wajiunge na bima ya afya na mazingira ya muswada yepelekee ulazima wa kila kaya kuwa na bima ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tutafikia kaya 15,000,000 kwa malipo ya shilingi 30,000 kwa mwaka kwa kila kaya, mfuko utakusanya shilingi bilioni 450 kwa mwaka. Makusanyo hayo kwa mwaka yatawezesha mfuko kutoa huduma bora zaidi kwa Watanzania wengi na wanaweza
hata kukopesha Halmashauri kujenga zahanati na vituo vya afya nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuongezeka kwa vituo vya afya na zahanati kutachochea ongezeko kubwa la wanachama na pia mapato makubwa kwa mfuko. Kwa mkakati huu wa kuboresha bima ya afya si tu itaboresha huduma za afya, lakini itapunguza kwa kiasi kikubwa bajeti ya Wizara ya Afya na hata TAMISEMI kutegemea mfuko wa Hazina unaotokana na kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua fursa hii kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, kwa kazi nzuri ya kuliongoza Taifa katika kulinda amani na utulivu ikiwemo kulinda mipaka yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Waziri na Wataalam wote wa Wizara katika kudumisha amani na usalama kwa kushirikiana na nchi nyingi duniani. Napenda kusisitiza umuhimu wa mafunzo ya jeshi kujikita katika mafunzo ya maadili na uzalendo. Mafunzo haya ni muhimu sana katika ustawi wa nchi yetu pia jeshi letu kuendelea kuwa na heshima hapa kwetu na nje ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua mchango na umuhimu wa askari wetu katika masuala ya ulinzi na usalama na hasa katika mchango wa ukombozi wa Bara la Afrika. Nashauri askari wastaafu waongezewe maslahi yao kulingana na hali ya sasa. Pia kuna Askari waliopata ulemavu wakiwa katika majukumu yao, napendekeza wapewe maslahi mazuri kutokana na kujitoa kwao kulinda nchi yetu na pia ukombozi wa Afrika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza makambi yetu muhimu ikiwemo Kambi ya Mbalizi, kuyaweka katika mkakati wa kuyatafutia maeneo nje ya Miji. Kambi za Jeshi kwa nje ya Miji na makazi ya watu ni muhimu sana kiusalama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza Serikali kuboresha huduma za hospitali za Jeshi kwa vile ni muhimu sana kwa huduma za askari na pia raia, hospitali za Jeshi letu zina sifa nzuri ya huduma kwa wananchi na kwa kuboresha zitapata ngazi nzuri na heshima za kimataifa. Napendekeza kuwepo mafunzo endelevu katika Jeshi letu ikiwemo mafunzo ya teknolojia za kisasa na kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa fursa hii ya kuchangia hii Wizara muhimu ya Kilimo. Kwanza nianze kwa kumpongeza Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Wizara nzima kwa bajeti nzuri. Pia napongeza na uchambuzi wa Kamati, kwa kweli wamekuwa makini sana Kamati, wamekuja na report nzuri sana ambayo imetusaidia hata katika huu mchango nitakaoutoa mimi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze kwa kipekee kabisa Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa juhudi ambazo wanazifanya kuondoa zile changamoto zilizopo kwenye mazao yetu na hasa zao la pareto kule Mbeya, naona sasa hivi kuna kiwanda kimeanzishwa pale Inyala ambacho kimeongeza ushindani lakini nina imani kuwa zile changamoto ndogo ndogo ambazo zimebaki wanaendelea kuzishughulikia ili tuondokane na zao la pareto kutoka leo chini ya tani 3,000 twende mpaka tani 8,000 ambazo ndiyo potentials, tunaweza kuzalisha Tanzania. Vile vile waendelee kuboresha bei ya pareto kutoka hii iliyopo sasa hivi ya Sh.2,500/= ifike angalau Sh.4,000/= kwa kilo, ambayo nafikiri itamsaidia hata wale wauzaji wa nje wanaweza nao kupata faida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nampongeza Waziri kwa report yake hii ambayo ameonyesha ni namna gani inalenga kuwasaidia wakulima kupata pambejeo kwa bei nafuu. Ni kweli kabisa pembejeo au mazao ya kilimo hata mashirika ya nje yanaangalia kwa karibu sana ni namna gani wamsaidie mkulima. Wenzetu ambao ni wanunuzi wakubwa kule nje na wazalishaji wakubwa wanaangalia ni namna gani mkulima wasimnyonye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo nampongeza Waziri kwa vile umelisema mwenyewe katika ukurasa wa 51, ambapo ameelezea kuwa mwenendo wa bei za mbolea katika soko la dunia zipo kwenye viwanda vichache na zinauzwa kwa bei ya chini katika muda muafaka, hilo ni zuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na hii bulk procurement ya fertilizer. Hata hivyo, inabidi tuangalie, je, ni peke yake Wizara ya Kilimo atafanikisha mkulima apate hii faida? Bila kuungana na wenzako hii haitafanikiwa kwa sababu (value chain) ya mbolea ni ndefu mno na hapa kwetu bei ya mbolea haitokani peke yake na bei ya kununulia (CIF), inatokana na gharama kubwa za usambazaji kuanzia Bandarini. Bei ya kununulia ni asilimia 53 tu lakini bei ya ukiritimba wa usambazaji kutoka Bandarini, tunatumia magari, barabara zetu mbovu inachangia hiyo asilimia nyingine 47. Sasa ukija kuchanganya na kwa vile mbolea tunanunua nje, kama hatutaweza kudhibiti mfumuko wa exchange rate ina maana vile vile hatutawasaidia wakulima wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sisi ambacho kinaweza kutusaidia ambacho naiomba Seriakli ijaribu kutusaidia, ni namna gani tupunguze gharama hii ya asilimia 47 ambayo ni mzigo mkubwa sana kwa mkulima. Kwa sababu ukilinganisha na wenzetu wa Ufilipino, ni asilimia chini ya 10, ukienda kanchi kadogo kama Myanmar ni asilimia chini ya 20, sasa sisi kwanini mkulima achangie asilimia 47 ya bei ya CIF? Inamuumiza sana mkulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshauri Mheshimiwa Waziri na timu yake wakae chini na Wizara ya Miundombinu, mahali kama Mbeya huhitaji kusafirisha mbolea kwa magari, ni gharama kubwa. Tani moja inakwenda zaidi ya 100,000 na ikifika pale inabidi iende kijijini. Kwa nini hiyo mbolea ikija kwa bulk itoke kwenye meli iingie kwenye mabehewa ya TAZARA, tuwe na bandari kavu Mbeya ili tuweze kusambaza Ukanda mzima wa Nyanda za Juu na packing ifanyikie pale Mbeya na si Dar es Salaam?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo itasaidia vile vile na mazao mengine ambayo kahawa sasa hatutakuwa na sababu ya kuipeleka bandarini, tutaisafirisha kwenye Ulaya kutoka kwenye Bandari kavu pale Mbeya. Hii itapunguza gharama na mzigo mkubwa kwa mkulima. Kwa hiyo namwomba sana ndugu yangu, anafanya jitihada kubwa, zimeshaonekana na leo hii watu wanasifia hizo tozo ambazo zimepunguzwa, kama kwenye kahawa, ni lini zitaanza na nina imani kuwa zinaanza mara moja, wakulima wamefurahia na kweli hiyo itatupunguzia mzigo mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kilimo chetu tunakuwa maskini wakati mwingine kwa sababu wataalam hawatusaidii vizuri. Ukilima vizuri hekta moja ya mahindi unaweza kutumia mifuko kama mitano ya mbolea na huhitaji hata kulima kilimo cha hifadhi ardhi. Unachohitaji ni kuweka mbolea muafaka ambayo inalingana na udongo, na siyo lazima iwe Urea ama DAP. Hilo nalo Waziri ajaribu kuliangalia kwa vile sasa tumebadilika, hatulimi tena kwa kupandia na DAP, hatulimi tena kwa kukuzia na Urea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo cha sasa hivi tunachotumia, nikitumia mbolea labda ya NPK 17-17-17 or NPK 15-15-15, nina uwezo kwa hekta moja kupata kilo 13,000 ambazo zinaweza kuniletea milioni 12 kwa hekta. Kwa mkulima wa kawaida ambaye amelima, ametumia mifuko mitatu mingine anauwezo wa kupata kilo 6,000 na akapata milioni tano. Vile vile mkulima atakayelima kwa hizi mbolea ambazo nazisema, atapata kilo 1,800 ambayo ni hela kidogo sana, inamwendeleza kuwa masikini. Kwa hiyo hapa suala siyo mbolea tu na mbolea ni tofauti na petrol. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbolea ni product kutokana na udongo. Tunahitaji hii lime inayozalisha hapa Dodoma iletwe Mbeya iboreshe ili wakulima waweze kupata kilo 13,000 kwa hekta. Ni zao zuri sana, limejaribiwa na uzuri wake hata kile Chuo cha Kilimo Uyole, waliwapeleka wakulima kwa mkulima mmoja Iringa, tumekuta yule halimi yeye ardhi ile; anapanda kisasa, anatumia mbolea kisasa na tumeangalia kwa macho yetu kulinganisha na mashamba ya jirani yake na hiyo ni Wizara iliyotupeleka pale. Sasa kwa nini tusielekee hiyo kwa ajili ya kumsadia mkulima? Hiyo ndio itakayotusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii bila kumsaidia mkulima umaskini utaendelea kututesa na kilimo tukifanye cha kijasiriamali mno, cha mahesabu. Tusiseme tu ya kwamba tutaleta DAP na UREA, tuseme ya kwamba kwenye eka moja utazalisha nini? Utaondoka vipi kwenye umaskini huu tulionao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina imani tukilifuatilia hilo kwa sisi tunaotoka kwenye majimbo ya kilimo, tunalima viazi; ukilima kisasa unakuwa tajiri, ukilima mahindi unakuwa tajiri, ukilima kahawa unakuwa tajiri na haya mazao yetu yana bei nzuri huko duniani kuliko kwingine. Ni competitive kwa sababu ukiangalia kahawa ya kwetu ni changamoto tu zinafanya bei inakuwa ndogo kuliko Kenya au Ethiopia. Ukiangalia mahindi ni changamoto tu zinafanya bei inakuwa ni ndogo kuliko ya Zambia. Tunaomba Serikali iwe na mkakati na iangalie ni namna gani itaondoa hilo ili tuweze kumsaidia mkulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu mwingine nitachangia kwa maandishi. Naunga mkono hoja na ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kuniheshimu, na mimi nakuheshimu sana na huwa sikosi nafasi ukikaa hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuwapa pole wale wenzetu wote waliofiwa kwa ajali ya gari kule Arusha, na mimi kwenye jimbo langu tulikuwa kati ya watu ambao tuliathirika kwa kufiwa na mtoto wetu kwenye kijiji cha Irambo. Kwa hiyo, poleni sana Watanzania wote na tunategemea haya mambo hayatajirudia tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuwapongeza hawa Waheshimiwa Mawaziri na Wizara nzima, ni watu ambao kwa kweli Wabunge watakubaliana na mimi, ukiongea nao hatakukatalia kitu, wana moyo wa kusaidia sana, hata ukienda Wizarani watakupokea vizuri sana. Hata hivyo, labda kitu kimoja tu, ukiwa na moyo inabidi vilevile uwe na maini. Nafikiri hapa leo tunazungumzia ni namna gani hawa tuwasaidie kwa moyo wao ule vilevile wamepewe na maini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya maji ni muhimu sana kwa Tanzania, lakini mimi nakubaliana na wenzangu wote kwamba hii bajeti iongezeke. Tozo ya kuongeza ya shilingi 50 ni muhimu na tusipinge hapa, kuna wengine wanafikiri ukiongeza hiyo labda itaongeza inflation, hapana. Mafuta tunanunua kwa dola, 2015 dola ilikuwa 2150, leo ni 2200, hata tukiongeza hiyo shilingi 50 haina impact yoyote kwenye inflation; na ukiongeza hiyo shilingi 50; na kwa ripoti ya EWURA tuliingiza mafuta kwa ajili ya matumizi ya Tanzania kama shilingi bilioni 3.4, ina maana tunaweza kuongeza kwenye bajeti zaidi ya shilingi 170,000,000,000, ni hela nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ninachoomba mimi hapa, kwa sababu kuongeza mapato ni suala lingine, je, haya mapato unakwenda kuongezea kwenye kikapu gani? Unaweza kwenda kuongeza kwenye kikapu ambacho kimetoboka, na hilo ndilo tatizo tulilonalo. Kwa sababu Sekta ya Maji kwa experience niliyonayo kwenye jimbo langu haina control kabisa, hela zote zinazopelekwa hazifanyi kazi ile inayotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu mwaka 2010 Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ilipewa zaidi ya shilingi bilioni
6.2 lakini leo hii ninapozungumza katika miaka yote hiyo hakuna mradi hata mmoja ambao unafanya kazi kwa hizo pesa zilizokwenda. Sasa tunaweza kuzungumzia hapa kuongeza pesa, unaongeza maji kwenye kikapu ambacho kimetoboka, unafanya kazi ya bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi ninachoomba hapa yawepo mambo mawili, iongezwe pesa kwenye bajeti kusaidia maji lakini vilevile kuwe na udhibiti wa pesa za maji. Udhibiti huo utasaidiwa kwa kuunda kile chombo cha Wakala wa Maji Vijijini na hiyo utekelezaji wake uje mara moja. Nalisema hilo kwa uchungu mkubwa kwa sababu Wabunge hapa ni mashahidi, niliuliza swali kuhusu matatizo, changamoto ya maji Mbalizi nikajibiwa kuwa hakuna matatizo ya maji Mbalizi na maji yapo ya ziada na wananchi mpaka leo wanashangaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo miradi ambayo sisi tulipewa, yote, ukiangalia orodha ya Wizara inaoneshwa hiyo miradi imekamilika. Sasa unauliza, huyu ni nani anayemdanganya Mheshimiwa Waziri? Ukionesha miradi imekamilika wananchi nao kule wanajua kuwa miradi imekamilika…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, ahsante.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Waziri, Naibu Waziri na timu nzima ya wataalam wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa hotuba nzuri ya bajeti.

Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada za Serikali kuwekeza katika maliasili zetu bado kuna changamoto nyingi za migogoro ya mipaka kati ya hifadhi za wananchi.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Wilaya ya Mbeya wamekuwa wadau wakubwa wa hifadhi zetu ikiwemo Hifadhi ya Kitulo na Hifadhi ya Misitu ya Kata ya Inyala. Kuna mgogoro wa muda mrefu kati ya TANAPA (Hifadhi ya Kitulo) na wananchi wa Kata za Ilungu, Igoma na Ulenje. Pamoja na juhudi za Serikali za kutatua mgogoro huu, pia Mheshimiwa John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliahidi kumaliza mgogoro huu kwa kuwafidia wananchi zaidi ya 600 waliopisha maeneo yao kwa ajili hifadhi.

Mheshimiwa Spika, inaelekea TANAPA kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Mbeya badala ya kumaliza mgogoro wameanza kuchochea chuki na wananchi pasipo kushirikisha uongozi wa chini ikiwemo vijiji na Halmashauri. Wameanza kuchukua hatua za kutaka kuhamisha wananchi wa Kijiji cha Kikondo na kukipeleka kwenye Hifadhi ya Msitu wa Kijiji cha Ilungu ambacho ni chanzo kikubwa cha maji na kimekuwepo kisheria kabla ya uhuru. Bila kushirikisha Serikali Kijiji cna Baraza la Madiwani TANAPA wameenda kupima hekta 800 kwa ajili ya kuhamisha wananchi wa Kijiji cha Kikondo ambacho kipo kisheria.

Mheshimiwa Spika, wananchi wanajiuliza ni kwa nini kuhamishia wananchi kwenye hifadhi ambayo ni chanzo muhimu cha maji? Hata hivyo, wadai ni zaidi ya 600 ambao walihakikiwa tangu awali, miaka zaidi ya mitano iliyopita na si 20 wanaokusudiwa kupata fidia.

Mheshimiwa Spika, hatua zinazoshawishiwa na TANAPA zinachochea migogoro isiyokuwa ya lazima, ukichukulia hawa wananchi ndio wanaotegemewa na Serikali katika kulinda hifadhi hizi. Hifadhi ya kituo na misitu ya Kata ya Ilungu ni muhimu sana kwa ajili ya vyanzo vya maji ikiwemo Mto Ruaha. Pamoja na mgogoro wa hifadhi ya Kitulo, wananchi wa vijiji vya Kata ya Inyala wameporwa maeneo yao na TFS. Naomba Serikali kuchukua hatua za kutatua mgogoro huu ambao eneo lililochukuliwa kinyemela ni dogo sana ukilinganisha na athari za mgogoro.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Kijiji cha Mjele, Kitongoji cha Mtakuja, wanapata usumbufu mkubwa kutoka TFS na mara kwa mara wamekuwa wanapata usumbufu wa kuchomewa nyumba zao na kuharibu mazao yao kwa mazingira ya uonevu. Serikali irekebishe hii mipaka ambayo wananchi wapo hapo kabla ya mwaka 1940.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza Waziri, Naibu Waziri na timu nzima ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa kuboresha miundombinu na upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na umuhimu wa maji, changamoto kubwa ya utekelezaji wa bajeti ya maji ni ufinyu wa mapato uliopelekea Wizara kupokea asilimia 19. 8 tu ya fedha zote za bajeti ya maendeleo zilizoidhinishwa na Bunge kufikia Machi 2017 kwa mwaka 2016/2017. Changamoto nyingine ambayo ni sugu ni fedha za miradi ya maji kutumika vibaya kutokana na kutokuwepo na usimamizi wa kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, miradi karibu yote ya kuanzia mwaka 2013/ 2014 ya shilingi bilioni 6.2 ambayo pesa imelipwa zaidi ya nusu miradi hiyo mpaka sasa haifanyi kazi. Kati ya miradi hiyo, ripoti ya CAG inaonesha kuwa malipo yalifanyika bila ukaguzi na kwa kazi ambazo hazikufanyika. Mradi wa Swaya/Lupeta zimelipwa shilingi milioni 120 kati ya shilingi milioni 520 na kazi iliyofanyika haizidi shilingi milioni 50. Pia mradi wa Mbawi na Jojo wa shilingi milioni 804, zimelipwa karibu asilimia 100 lakini mradi haufanyi kazi. Pia mradi wa Horongo/Itimu/Mwampalala zimelipwa shilingi bilioni 1.2 (100%) na uko chini ya kiwango na malipo yalifanyika bila kuzingatia utaratibu wa malipo ya Serikali ikiwemo kutofanyika kwa ukaguzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kukosekana kwa usimamizi wa miradi ya maji, fedha za miradi ya maji zinatumika vibaya na wananchi wanaendelea kukosa huduma ya maji salama. Pamoja na miradi hiyo kutofanya kazi, ripoti za Wizara ya Maji zinapotoshwa kuonyesha kuwa miradi iliyotajwa hapo juu na mingine ambayo wala haijaanza imekamilika wakati wananchi walengwa katika vijiji hivyo hawana maji. Ripoti hizo za kupotosha zimepelekea kwa makusudi hata majibu ya swali la maji katika Mji Mdogo wa Mbalizi kujibiwa kwa kupotosha kuonyesha hakuna uhaba wa maji na pia kuonyesha vyanzo vya maji ambavyo havipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi kupitia Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya wameniagiza kumwomba Waziri wa Maji atembelee hiyo miradi aliyodanganywa na pia Bunge lielezwe hao wahusika wa upotevu wa fedha za miradi iliyotajwa ni hatua gani zimechukuliwa kwani hadi leo hii miradi iliyotajwa hapo juu haifanyi kazi. Kutokana na changamoto za usimamizi usioridhisha, naunga mkono mapendekezo ya kuanzishwa kwa Wakala wa Maji Vijijini (Rural Water Agency). Kuanzishwa kwa Wakala huyu kutaongeza tija ya bajeti ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, naungana na mapendekezo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ya kuongeza tozo ya mafuta kwa kila lita ya dizeli na petroli kutoka Sh.50/= ya sasa kufikia Sh.100/=. Ripoti ya EWURA ya mwaka 2015 inaonyesha lita 3,380,097,164 ziliingizwa nchini na kwa tozo ya Sh.100/= kwa lita, mfuko ungekusanya shilingi bilioni 338. Hili ongezeko la tozo ni muhimu kutekelezwa haraka iwezekanavyo ili kunusuru hali ya maji vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ina vyanzo vingi vya maji ya mserereko. Pamoja na kuwepo vyanzo vingi, zaidi ya asilimia 60 ya wananchi hawana maji salama. Kuna Vijiji vichache kama vya Ngole, Iwala, Idugumbi na Chombe, wananchi wamejihamasisha na kuanzisha miradi ya kujitolea. Vijiji vya Mjete ni eneo la ukame na hakuna maji kabisa. Pia kuna vijiji zaidi ya 100 pamoja na kuwepo vyanzo vizuri vya maji ya mserereko lakini hawana maji salama. Wizara iangalie namna ya kupeleka miradi ya maji katika vijiji hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwani katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita imefanikiwa kuleta mageuzi ya kiuchumi na kijamii katika nchi yetu hususan Jimbo la Mbeya Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kushauri Serikali kupitia Wizara mpya ya Uwekezaji kuendelea kuhamasisha na kuvutia wawekezaji kutoka nje na ndani. Nchi yetu imejaliwa rasilimali mbalimbali yakiwemo madini. Katika Wilaya ya Mbeya kuna madini ya niobium ambayo ni adimu sana na mahitaji yake ni makubwa kwa viwanda vya vyuma, mabomba ya mafuta, injini za ndege na hata vifaa vya kielektroniki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza TIC, EPZ na Wizara ya Madini waweke mkakati wa kuvutia wawekezaji katika viwanda vya vyuma na niobium ambayo yanaweza kusaidia kupunguza gharama na hasa pesa za kigeni kwa kuagiza vyuma toka nje ya nchi. Kutokana na miradi mingi ya ujenzi wa madaraja, bomba la mafuta, SGR na vivuko, kiwanda cha niobium kitakuwa msaada mkubwa kupunguza gharama na pia kuwezesha nchi yetu kuuza madini yetu ambayo yameongezwa thamani na kwenda moja kwa moja kwa walaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na azma yetu ya Tanzania ya viwanda, kuna mahitaji makubwa ya mafundi mchundo (technicians) na mafundi wasaidizi (artisans). Kwa vile Taasisi ya Maadilisho iliyopo Irambo, Mbeya DC ina miundombinu ambayo ni under-utilized, napendekeza Serikali (Wizara ya Afya) iruhusu shule hii ibadilishwe matumizi na kuwa chuo cha ufundi kwa Kanda nzima ya Mikoa ya Kusini Magharibi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Mbeya ina changamoto kubwa za barabara na viongozi wa kitaifa walitoa ahadi za ujenzi wa barabara zifuatazo kwa kiwango cha lami, napendekeza ahadi hizo zitekelezwe. Barabara hizo ni Mbalizi – Shigamba – Isongole; barabara ya Mbalizi – Makongolosi na barabara ya Isyonje - Kikondo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iimarishe usimamizi wa soko la zao la pareto. Pia nashauri liwe mojawapo ya mazao ya kimkakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada za kupeleka maji vijijini katika Jimbo la Mbeya bado upatikanaji wa maji ni changamoto kubwa hasa Kata ya Mjele na Mji Mdogo wa Mbalizi. Naomba Serikali itimize ahadi za kutatua kero hii kubwa ya maji katika Jimbo la Mbeya Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Kamisheni ya Pamoja ya Bonde la Mto Songwe kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Malawi pamoja na Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Amani na Usalama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Nami kwanza niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumwombea mwenzetu uponyaji wa haraka kwa haya yaliyompata.

Mheshimiwa Naibu Spika, Azimio hili la leo ni muhimu sana kwa nchi yetu, hata kwa nchi zinazotuzunguka. Labda ningeanzia pale kwenye Azimio, nafikiri kunahitaji masahihisho kidogo ya jina la Wilaya. Kuna Wilaya pale imetajwa, Mbeya Vijijini. Hatuna Wilaya ya Mbeya Vijijini, ila tuna Wilaya ya Mbeya. Kwa hiyo, labda kwa ajili ya kumbukumbu sahihi za Bunge, ingebadilishwa na kusahihishwa kuwa Wilaya ya Mbeya.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hivyo, niende zaidi kwenye maoni. Niungane kwanza na maoni ya Kamati, walivyosisitiza kuwa katika mkataba huu labda ndiyo wakati muafaka wa Serikali kuangalia ni namna gani huu mkataba vile vile unaweza kutusaidia katika kutatua tatizo la mgogoro wa mpaka ulioko katika Ziwa Nyasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri hiki kinaweza kuwa ni chanzo kizuri sana na Ziwa Nyasa linatokana na Mto songwe na Mto Songwe kwa kiasi kikubwa unatoka kwetu, kwa hiyo, nafikiri hiyo inaweza kuwa ni chanzo kizuri ni namna gani tukaondoa hili tatizo la mgogoro wa Ziwa Nyasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili katika maoni ya Kamati, vile vile waligusia elimu kwa wananchi. Nafikiri hili ni jambo muhimu sana kuangalia ni namna gani wananchi wakashirikishwa kikamilifu na kuwapa elimu ya namna ya kuhifadhi haya mabonde yetu na hivi vyanzo vya mito.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia tunapozungumzia bonde la Mto Songwe, kuna Mto Songwe ambao unakwenda Ziwa Nyasa na kwa kweli kilichonifurahisha hapa ni namna gani yatajengwa yale mabwawa matatu na faida za yale mabwawa matatu ambayo yatazalisha umeme takriban Megawatt 182.2. Pamoja na hilo, hayo maji yatatumika kwa ajili ya umwagiliaji na vile vile kwa ajili ya matumizi ya majumbani.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia yale maeneo ya kwetu hasa katika Wilaya yangu, pamoja na kuwa na mito mingi ambayo ndiyo vyanzo vya mito hii inayokwenda Songwe na ile Songwe inayokwenda Rukwa, vile vile ndiyo chanzo cha Mto Ruaha, lakini yale maji kwa kiasi kukubwa wananchi hawayafaidi. Kwa hiyo, kwa mtazamo huu uliopo kwenye mkataba huu nina imani ya kwamba Serikali itaangalia ni namna gani wananchi nao wafaidike na haya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapoliangalia bonde la Mto Songwe ambao unaelekeza maji yake kwenye Ziwa Nyasa, napendekeza kuwa Serikali vile vile iangalie bonde la Rukwa ambalo nalo lina Mto Songwe ambao unapeleka maji Ziwa Rukwa. Hili ni bonde muhimu sana na kwa kiasi kikubwa Ziwa Rukwa karibu linaanza kupotea kwa ajili ya udongo na mmomonyoko ambao unasongwa na mto Songwe kupelekwa Ziwa Rukwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa katika huu mtazamo ambao tunauona hapa leo, nafikiri itakuwa ni jambo jema sana, tuanze sasa hivi kuangalia kuchukua hatua za haraka, ili haya yanayofanyika kwenye Bonde la Mto Songwe unaopeleka maji Ziwa Nyasa, vile vile iende na kwenye Mto Songwe unaopeleka maji Ziwa Rukwa. Tufanye hivyo hivyo, kwa vyanzo vingine vya mito vilivyoko kwenye milima ya Uporoto na Kitulo ambao maji yake ndiyo chanzo cha Mto Kiwira ambao unapeleka maji vile vile Ziwa Nyasa na vile vile ndiyo chanzo cha Mto Ruaha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hivi vyanzo vyote ni muhimu sana. Kwa hiyo, elimu itakuwa muhimu sana kwa wananchi, lakini tufanye mikakati ya makusudi, ni namna gani tuwasaidie hawa wananchi ili waone manufaa vile vile, nao wahusike katika kuhifadhi hivi vyanzo vya hii mito.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuipongeza Wizara ya Katiba na Sheria na hasa Mahakama kwa kusimamia sheria na haki za Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kushauri Serikali, kama ilivyopendekezwa na Kamati ya Bajeti, kuhakikisha fedha zilizotengwa kwa maendeleo zipelekwe ili kukamilisha miradi ya maendeleo. Maeneo mengi yakiwemo miji na miji midogo haina Mahakama au miundombinu imechakaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji Mdogo wa Mbalizi hauna jengo la Mahakama badala yake shughuli za Mahakama zinafanyika kwenye jengo lililopo katika soko kwenye msongamano mkubwa. Napendekeza na kusisitiza Wizara iharakishe ujenzi wa Mahakama ya Mbalizi kwa usalama wa watumishi wa Mahakama na hata watuhumiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia bajeti ya Serikali. Kama walivyosema wenzangu bajeti ya mwaka huu kwa kweli ni bajeti ya kimapinduzi, (transformation) imeelekeza nguvu zote kuwasaidia wanyonge wakiwemo wakulima ambao ni wengi katika Tanzania yetu hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika bajeti hii kodi za mitaji zimesamehewa (Capital goods budget), kodi imeondolewa ya kuondoa kodi ya thamani ya usafirishaji (ancillary transport services), kodi ya maeneo ya ufugaji nayo imeondolewa na kuwapa unafuu sana wakulima wetu huko vijijini.

Mheshimiwa Spika, vilevile kufutwa kwa road licence kwa kweli hii kodi ilikuwa ni kero, ilikuwa haitusaidii kabisa. Nina imani kuwa hii kodi mapato yake ukilinganisha na gharama zilizokuwa zinatumika zilikuwa haziendani sawa sawa. Nashukuru baada ya kuisoma vizuri bajeti hii kuwa ongezeko la Sh.40/= linaongezwa kwenye pato, hii sio mbadala wa road license.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimeilewa vizuri sana kwa sababu hata ile notion ya kwamba hii inakwenda kuwaumiza wakulima kwa sababu wanalipia road license. Road license imefutwa kama inasomeka vizuri kwenye bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la ujenzi wa reli kwa standard gauge, hayo ni mapinduzi makubwa sana ya kiuchumi. Vilevile mpango wa kujenga reli kutoka Tanga mpaka Musoma, hayo ni mapinduzi makubwa sana katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bomba la mafuta toka Uganda kwenda Tanga kwa kweli hayo ni mapinduzi makubwa sana. Pamoja na hayo tusisahau vilevile kwamba hizi investments

tulizokuwa nazo kama TAZARA, bomba la mafuta kwenda Zambia nazo ziboreshwe kuhakikisha zinafufuliwa na zinafanya kazi inavyotakiwa.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, nalisema hilo kwa makusudi kwa sababu punguzo la mbolea litawapa nafuu sana wakulima, lakini tusipoboresha usafirishaji hilo punguzo wakulima hawataliona, kwa sababu kodi nyingi zimeondolewa katika mbolea. Hata hivyo, ukiangalia value chain ya mbolea kutoka huko tunakoagiza nje asilimia 53 ni CIF ambayo ni gharama ya kununua mpaka bandarini lakini asilimia 47 ni ya kumplekekea mkulima, bila kuipunguza hiyo kwa kweli wakulima wetu hawataona huo unafuu. Kwa hiyo naiomba sana Serikali ijaribu kuelekeza ni namna gani tuondoe urasimu pale bandarini, ni namna gani tuboreshe TAZARA, reli ya kati ili mbolea zote zisafirishwe kwa reli na hiyo italeta ushindani mzuri kwa mazao yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi yetu ni ya kilimo kwa asilimia kubwa sana, Mbeya tunalima pareto. Pareto ni zao ambalo linatumika kutengeneza sumu, madawa kwa ajili ya kuulia wadudu, inatokana na maua, halihitaji mbolea. Hili zao kwa sasa hivi lina soko kubwa mno, tunazalisha tani 2000 lakini mahitaji sasa hivi ni karibu tani 10,000. Kwa kuangalia hili zao linaweza kutuletea foreign exchange kama tutapeleka nguvu huko, nguvu tunayoihitaji ni kidogo hatuhitaji kuongeza bajeti, tunachotakiwa kuongeza hapo ni usimamizi wa kumsaidia mkulima kwenye masuala ya masoko.

Mheshimiwa Spika, leo hii wakulima wanalima pareto lakini soko limekuwa dominated na mtu mmoja, wengine wanapokuja wananyimwa nafasi ya kwenda kununua. Mwaka huu Bodi ya Pareto hata ule mkutano wa wadau wameahirisha, hatujui mkutano utakuwa lini kwa sababu ule ndio tulikuwa tunaangalia changamoto nyingi za hili zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zao letu lingine la kahawa halifanyi vizuri ukilinganisha bei za Tanzania na bei za majirani zetu Kenya. Wote tunalima kahawa aina ya Arabica, Kenya

inalimwa huku kwa wenzetu Kilimanjaro na Mbeya lakini kwa Nairobi coffee exchange bei ya sasa hivi ni dola 300 kwa kilo 50, kwa sisi ni chini ya dola 150. Sasa hii yote hii inatokana na nini, kwa nini kahawa ile ile na wanunuzi ni wale wale, kahawa ya kwetu Tanzania bei iwe chini? Inanikumbusha kwamba matatizo tuliyonayo kwenye madini ni yale yale matatizo waliyonayo wakulima wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali iangalie ni namna gani tutawasaidia wakulima ili tuwe na masoko ya uhakika ya kipindi chote ikiwemo masoko ya kahawa, pareto, viazi, ndizi, ndizi zetu kule Mbeya zinabebwa na magari kupelekwa nchi jirani for export na hata siku moja hutaona kwenye kumbukumbu zetu kuwa tuna export ndizi. Sasa yote haya tukiboresha masoko yetu nafikiri nchi yetu itapata forex nyingi kutokana na kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa tozo za mazao ya kilimo. Nashukuru sana kwa kweli kuna unafuu wa wakulima lakini je, hili punguzo la tozo tutazisaidia vipi Halmashauri kwa vile zilikuwa zimejumuishwa kwenye bajeti za Halmashauri. Kwa Halmashauri ya Mbeya mapato tunategemea zaidi kwenye kilimo na tunapata karibu nusu bilioni na hii nusu bilioni yote kama nilivyokuwa naiangalia leo kwenye bajeti ni kwamba hiyo imeenda na hiyo ni karibu asilimia 50 ya bajeti ya mapato ya ndani ya Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, tusipoyakusanya hayo mapato Halmashauri itawajibika na kuadhibiwa. Sasa labda ningeomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujumuisha hayo mapato ambayo yameondolewa kwenye Halmashauri yatafidiwa vipi ili Halmashauri zetu ziendelee kufanya kazi kama kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kilimo bila miundombinu mizuri kwa kweli hatuwezi kufanikiwa, naomba sana kuboresha miundombinu vijijini ikiwemo umaliziaji wa ujenzi wa kiwanja cha Songwe, ambacho mpaka leo hakina taa za kuongozea ndege na hakuna wigo kwa usalama wa uwanja...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, ahsante na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, Naibu Waziri Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji, Katibu Mkuu na Naibu Makatibu Wakuu pamoja na Wataalam wa Wizara kwa kazi nzuri ikiwa ni pamoja na kuandaa hii bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi ya kusimamia mapato, jukumu la Wizara ya Fedha ni kusimamia udhibiti wa matumizi ya fedha za umma. Matumizi mazuri ya fedha, yanaweza kutekelezeka kama kutakuwepo na utendaji wenye tija kwa kada ya ukaguzi wa ndani pamoja na Kamati za Ukaguzi katika Halmashauri zetu. Imezoeleka kuona Idara ya Ukaguzi wa Ndani kutofanya kazi zake kwa uhuru, kwa muundo tulionao sasa ambapo Mkaguzi wa Ndani anasimamiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri. Pia hata Wakuu wa Idara ya Uhasibu imekuwa kawaida kutekeleza kazi zao kinyume na misingi na kanuni za fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya kushangaza imejitokeza katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kwa Mhasibu mwenye sifa na mwaminifu kuondolewa kwenye nafasi yake kwa kuwa alikataa maagizo ya Mkurugenzi kufanya malipo kinyume na kanuni. Huyu Mhasibu mwenye cheti cha juu cha uhasibu (CPA) amehamishiwa kufanya kazi za ukarani kwenye Sekondari ya Kijijini. Pia Idara ya Ukaguzi wa Ndani akiwemo Mkuu wa Idara wapo katika wakati mgumu kwa vile waliandika ripoti iliyoibua ubadhirifu kwenye miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na ripoti hiyo Baraza la Madiwani lilichukua hatua za kinidhamu kwa wahusika, lakini kwa sasa linapingwa na viongozi kiasi cha kuwagawa Madiwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza Wizara ya Fedha, kuimarisha Idara ya Ukaguzi wa Ndani ikiwemo idara hii kuwa huru (Independent). Pia Wizara ifanye ukaguzi wa miradi ya maendeleo ambayo kwa kiasi kikubwa kuna upotevu mkubwa wa fedha. Kuwepo na mkakati wa kudhibiti matumizi ya fedha za umma badala ya kusubiri ripoti za Mkaguzi (CAG) ambayo ni postmortem.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Msajili wa Hazina ina umuhimu wa kipekee wa kusimamia Mashirika ya Umma. Mashirika ya Umma ni muhimu na chanzo kikubwa cha mapato yasiyo ya kodi. Lengo kuu la Ofisi ya Msajili wa Hazina ilielekezwa kuboresha utendaji wa Mashirika ili yatoe mchango mkubwa kwenye kuinua uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Msajili wa Hazina ifanye tathmini ya mashirika ambayo hayana tija na kuyatengenezea mkakati wa kuyafufua au kubadilisha malengo kupelekea yawe na tija. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kuna mashamba makubwa yaliyokuwa ya Tanganyika Packers katika Mji Mdogo wa Mbalizi kutokana na Sheria za Mipango Miji mashamba hayo yanakosa sifa za kuwepo Mjini. Kutokana na hali hiyo, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya imetafuta ardhi kubwa ya zaidi ya ekari 7,000 kuwa mbadala wa haya yaliyokuwa mashamba ya kunenepesha ng’ombe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kukumbusha Wizara, kukubaliana na ombi la Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ili uwekezaji wa iliyokuwa Tanganyika Packers uhamishiwe kwenye eneo mbadala ambalo ni muafaka kwa mazingira ya sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma za kibenki hazijafika vijijini kama ilivyo mijini. Mabenki karibu yote yanasita kuhudumia wakulima wadogo na wananchi wa vijijini. Huduma za kibenki ni muhimu sana kwa kilimo cha tija ambacho ndiyo mhimili wa uchumi wa Tanzania. Kutokana na changamoto za mtaji wa Benki ya Wakulima (TADB) napendekeza Serikali ielekeze revolving fund ya shilingi milioni 50 kwa kila kiijiji kusimamiwa na TADB. Kwa kuipa TADB jukumu la kusimamia huu mfuko wa milioni 50 kwa kila kijiji utawezesha usimamizi mzuri wa huu mfuko na wakati huo kuiwezesha TADB kutekeleza majukumu yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Waziri na Naibu Waziri, pamoja na Wataalam kwa hotuba na pia kwa kazi nzuri ya kusimamia Wizara hii muhimu. Pamoja na mikakati mizuri ya Wizara iliyoonyeshwa kwenye bajeti hii, kuna changamoto nyingi ambazo nashauri Wizara ichukue hatua za kutatua. Napendekeza, Wizara kujenga mabwawa ya maji kwa wafugaji wa Kata ya Mjelena Mshewe, katika Wilaya ya Mbeya ili kukabiliana na ukame.

Mheshimiwa Spika, napendekeza hatua zichukuliwe za kulinda hali ya mazingira ya Ziwa Rukwa ambalo kwa kiasi kikubwa linazidiwa na mchanga unaotokana na mmomomyoko wa mito inayoingiza maji katika Ziwa Rukwa. Pia hatua za makusudi zichukuliwe za kuhamasisha vijana kuanzisha miradi ya ufugaji samaki katika Ziwa Rukwa.

Mheshimiwa Spika, napendekeza Wizara iangalie uwezekano wa kuanzisha shamba ka kisasa la mifugo ya ng’ombe wa nyama na pia ujenzi wa kiwanda cha nyama katika eneo jipya lililotengwa na halmashauri kwa kunenepesha mifugo na kiwanda cha nyama. Halmashauri imetenga zaidi ya eka 6,000 katika Kata ya Mjeta ili kubadilishana na eneo la iliyokuwa Tanganyika Packers ambayo kwa sasa limezungukwa na Mji Mdogo wa Mbalizi. Eneo hili jipya litawezesha Wilaya ya Mbeya kuzalisha ng’ombe wa kiwango kizuri sana na kuweza kukidhi ushindani wa soko la Kimataifa.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nijikite kidogo tu kwenye sehemu ndogo ya mapato pamoja na udhibiti wa matumizi ya pesa za umma. Kama alivyosema mwenyewe Waziri kwenye ripoti yake ukurasa wa 25 ya kwamba jukumu lake kubwa ni pamoja na kusimamia mapato na matumizi ya Serikali, jukumu hili ni muhimu sana kwa sababu ukisimamia vizuri matumizi na kukawa na cost saving, nayo inakuwa ni sehemu ya mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika uzoefu wangu kwenye Halmashauri zetu, nimeona upotevu mkubwa sana wa pesa kwenye matumizi ambayo sio yaliyolengwa. Waziri amezungumzia kuhusu kuimarisha ukaguzi wa ndani, ukaguzi wa ndani ni kitengo muhimu sana kwenye Halmashauri, lakini ukiangalia nafikiri Wizara ina wataalam wengi wa mambo ya uhasibu, itakuwaje Mkaguzi wa Ndani amkague Mkurugenzi halafu yeye aripoti kwa Mkurugenzi, unategemea hiyo ripoti ya Mkaguzi wa Ndani itakuwa na maana yoyote? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hilo kwa experience tulizonazo huku kwenye Halmashauri zetu. Pesa nyingi zinazokwenda kwenye Halmashauri ambazo ni sehemu kubwa sana ya mapato zinapotea. Kwenye Halmashauri yangu tuna Mkaguzi mzuri sana, ameleta ripoti nzuri sana na bahati nzuri Madiwani wakazifanyia kazi, baada ya kuzifanyia kazi yule Mkaguzi wa Ndani akaonekana kuwa hakutenda jema kwa sababu aliweza kuwaambia Madiwani uovu ambao umekuwa ukifanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi katika suala la usimamizi, hata yule aliyekuwa Mhasibu wa ile Halmashauri naye alipata matatizo, baada ya kuandika ripoti kuwa tuna matatizo ya matumizi ya pesa alihamishwa kupelekwa kijijini kutoka Halmashauri. Fikiria Serikali imemsomesha mtu kwa kiwango cha CPA, ndiye Mhasibu wa Halmashauri, kwa vile tu ameandika ripoti ambayo inaeleza maovu kwenye Halmashauri anahamishwa ili waendelee kuficha yale maovu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba hiyo Wizara yako kwa vile inasimamia matumizi bora ya hizi rasilimali, iweke hili kama chanzo kimoja wapo cha mapato ya Serikali kwa sababu tukikusanya pesa tena kwa shida kabisa zikaenda kutumika sehemu ambazo hazikulengwa, hayo mapato yote ambayo tunakusanya yanakuwa ni kazi bure. Naomba sana tuimarishe ukaguzi wa ndani. Vilevile, umezungumzia kuhusu Kamati za Ukaguzi kwenye Halmashauri zetu, hizi Kamati za Ukaguzi hatuzioni, ambazo nazo ni chombo muhimu sana cha kusimamia mapato na matumizi ya Halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la vyombo vya fedha kusaidia katika kilimo, hasa hii Benki ya Maendeleo ya Kilimo. Wabunge wengi hapa wamechangia kuhusu mtaji mdogo wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo, kuna mchangiaji hapa kaongelea kuhusu shilingi milioni 50 kwa kila kijiji. Sasa nilichokuwa najaribu kuangalia, labda na kuishauri Wizara, kwa nini kama kuna hiki chombo ambacho ni kwa ajili ya kuwasaidia wakulima kikapewa nafasi ya hizi pesa ambazo ni shilingi milioni 50 kwa ajili ya kila kijiji wakapewa, sio lazima iwe mtaji, ila wao wakawa ni wakala wa Serikali kwa sababu hizi pesa nazo ambazo zitakwenda huko ni kwa ajili ya kukopesha wakulima na wajasiriamali wadogo wadogo, kwa hiyo zinahitaji usimamizi mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya Kilimo ni mahala pazuri na itapata nafasi hata ya kuweza kujitanua kwenda mahali mbalimbali hapa Tanzania. Ningeomba hizi milioni hamsini hizo hata shilingi bilioni 60 ambazo sasa hivi zimezungumziwa kuwa zitatolewa mwaka huu pamoja na zile shilingi bilioni 52 ingepewa Benki ya Kilimo ili iweze kuanza kufanyia kazi zake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni masoko kwa ajili ya wakulima. Kuna chombo ambacho kilikuwa kinazungumzwa kuwa kingeanzishwa (commodity exchange), sijaiona katika hii report labda kwa ajili yakuangalia haraka kama imezungumziwa, lakini kwa wakulima hiki ni chombo muhimu sana. Wakulima wetu wanalima sana na wakati wa mavuno bei zinakuwa chini, tungekuwa na chombo kama hiki kingetusaidia sana kuhakikisha kuwa bei za mazao yetu zinakuwa stable.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni Msajili wa Hazina. Naomba sana tena sana Wizara ijaribu kuimarisha hiki kitengo cha Msajili wa Hazina vilevile wapewe bajeti ya kutosha. Kwa sababu kwa mchango wao mwaka huu wa shilingi bilioni 500 mpaka mwezi Machi, nina imani kuwa ingekuwa mara mbili au mara tatu zaidi kama wangepata nafasi ya kusimamia haya Mashirika yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ajili ya muda kumalizia ni suala la deposits zilizochukuliwa na Serikali kutoka kwenye mabenki kupelekwa Benki Kuu. Jana jioni nilikuwa namsikiliza Mkurugenzi wa Benki ya Mkombozi akielezea kuwa Benki zimepata matatizo baada ya Serikali kuondoa zile deposits kutoka kwenye Benki za Biashara na kuzipeleka Benki Kuu.

Sasa lile lilinishtua kidogo kuwa inawezakana labda hayakuwa maksudi ya Serikali, lakini kwa kuondoa zile deposits zilipunguza ukwasi (liquidity) kwenye haya Mabenki. Labda nalo ningeiomba Serikali ijaribu kuangalia kwasababu nia na madhumuni ni namna gani tunaweza kuzisaidia hizi Benki ziweze kuwakopesha wakulima, ziweze kwenda vijijini, kuwe na a real financial inclusion. Kwa hiyo, naomba sana tena sana tuangalie kurudi nyuma wakati mwingine siyo vibaya kama tutafanya marekebisho ambayo yatasaidia kwa ajili ya uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nashukuru sana. Naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.

Kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Wizara nzima ya Fedha kwa mwongozo mzuri wa mpango wa mwaka 2018/2019 na kweli unatuonesha mwelekeo mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba nijikite zaidi kwenye vipaumbele vile vinne vya mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipaumbele cha kwanza kinaelezea kuhusu viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda na mimi naona hiki ni kipaumbele kizuri sana; lakini ningependa zaidi kuona kwamba hiki kipaumbele kinajikita zaidi kwenye kilimo kwa sababu viwanda vyetu, uchumi wetu wa Tanzania kwa kiasi kikubwa utategemea kilimo ambacho kinaajiri zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja na mpango wake kwa mwaka huo pamoja na bajeti, uangalie ni namna gani utajikita kuinua kilimo Tanzania kwa sababu hiki kilimo ndio kitatupelekea kupata malighafi kwa ajili ya viwanda vyetu. Nalizungumzia hilo la kilimo kwa sababu kubwa ambayo imejitokeza hivi karibuni. Wakulima kwa kiasi kikubwa wamezalisha sana mazao, hasa nafaka. Hata hivyo leo hii ukiangalia bei ya nafaka hasa mahindi na mbaazi ziko chini sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali ijaribu kuangalia ni namna gani iwasaidie wakulima yale mazao wanayoyazalisha bei iweze kuwa inaeleweka, kuwe na price stabilization. Vilevile kuwe na masoko ya uhakika. Tusipokuwa na masoko ya uhakika, bei ya mazao yetu isipoeleweka kwa kweli nchi yetu itakuwa katika hali ambayo sio nzuri na uchumi wetu utakuwa katika hali mbaya kwa sababu bei zetu za mazao ukilinganisha na wenzetu sisi zipo chini sana. Kwa hiyo, ningeomba hapa Serikali iangalie jinsi gani ambavyo tutaanzisha masoko ya mazao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nimesikiliza kwenye taarifa ya habari walikuwa wanazungumzia kuhusu commodity exchange market. Ikianza mapema hiyo nafikiri inaweza kutusaidia sana kuhakikisha kuwa mazao yetu yanakuwa na bei inayoeleweka na vile vile kunakuwa na masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kilimo kinahitaji zaidi pembejeo, napenda niishukuru Serikali kwa mpango wake wa kuagiza mbolea kwa jumla (bulky procurement); hii imesaidia sana kiasi ambacho mbolea leo za DAP bei imeteremka karibu nusu. Kwa kule kwetu DAP inanunuliwa kwa shilingi 51,000 kwa mfuko wa kilo 50 na Urea inanunuliwa kwa shilingi 41,000 kwa mfuko, hayo ni mafanikio makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hizi mbolea kushuka bei namna hiyo bado ninaona kuna njia ambazo zinaweza kusaidia mbolea ikashuka zaidi; kama tukiboresha zaidi miundombinu ya barabara na miundombinu ya reli. Kwa sehemu ambazo tuko ukanda wa reli ya TAZARA, kama TAZARA ikiboreshwa, bei ya mbolea inaweza kushuka zaidi. Kwa hiyo, ninaomba katika hiki kipaumbele cha kufunganisha uchumi na maendeleo tuangalie zaidi ni namna gani wananchi wanaweza kufaidi bei ya pembejeo zikawa chini zaidi kwa kuboresha huduma za miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri vilevile Serikali iliangalie suala la afya, hasa miundombinu ya afya. Wananchi wamejenga zahanati nyingi, wamejenga vituo vya afya na bado vipo kwenye mtambaapanya wakitegemea kuwa Serikali itakuja kumalizia. Katika huu mpango unaokuja katika hii bajeti inayokuja ninapendekeza kipaumbele kiwe kumalizia hizi zahanati na vituo vya afya ambavyo kwa kiasi kikubwa wananchi wameshajenga na wengine bado wanaendelea kujenga. Kwa hiyo, upendeleo uwe kwa wananchi wale ambao wameshafikia hatua nzuri, tuweze kuwatia nguvu ili waweze kuendelea kuchangia katika ujenzi wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la maji. Maji kwa wananchi wetu hasa vijijini na mijini ni muhimu sana, kwa hiyo, tunapoangalia maendeleo tuangalie ni namna gani hii miundombinu ya maji hasa kwa vijijini itaweza kuboreshwa. Kwa kiasi kikubwa Serikali imewekeza sana kwenye miundombinu, imetoa hela nyingi sana kwa ajili ya miundombinu ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hii miundombinu sehemu nyingi likiwemo Jimbo langu la Mbeya Vijijini bado haifanyi kazi. Ukiangalia kwa kule Mbeya Vijijini tulipata miradi ya vijiji kumi na miradi ile asilimia 80 ya pesa ilishakwenda, lakini mpaka leo ni mradi mmoja tu ndiyo umekabidhiwa. Sasa katika hii bajeti, iangalie ni namna gani hii miradi iweze kukamilika ili tuweze kuanzisha miradi mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika miradi ya maji ninapendekeza kwa kule Mbeya tungeanza na vyanzo vingine mbadala. Kuna chanzo cha Mto Kiwira, naomba kipaumbele kiwepo cha chanzo cha Mto Kiwira kwa ajili ya kupeleka maji Wilaya yetu ya Mbeya hasa Jimbo la Mbeya Vijijini, nafikiri itatukomboa kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo linaweza kutusaidia katika mpango mzima wa maji nafikiri ni kuunganisha hizi mamlaka; mamlaka za maji mijini na mamlaka za miji midogo (clustering). Kwa hiyo, napendekeza katika mpango wa bajeti unaokuja tuhakikishe kuwa Mamlaka ya Maji Jiji la Mbeya inaunganishwa na Mamlaka ya Maji Mbalizi, lakini vilevile na miji midogo mingine ya Mbeya Vijijini iweze kuunganishwa ili kupata maji ya uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ni kipaumbele ni suala la ujenzi wa mazingira wezeshi, nafikiri hili ni muhimu sana kwa sababu unapojenga uchumi kusipokuwa na mazingira wezeshi kutakuwa na changamoto nyingi sana ili kufikia malengo yetu. Pendekezo langu hapa ni kwamba tungeangalia ni namna gani wakati tunaendelea na ujenzi wa reli ya standard gauge na ile miradi mingine ya kimkakati vile vile tuboreshe na reli yetu ya TAZARA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuboresha reli ya TAZARA tunaomba vilevile tujenge bandari kavu ambayo itasaidia kwa mizigo inayoenda nchi za nje; Zambia, Malawi, Kongo, na nchi nyingine zinazotuzunguka ambazo tuna ushindani nazo kwa bandari za Beira Msumbiji, Afrika Kusini na Angola.

Tukiboresha hii TAZARA na tukajenga bandari kavu na pia tukajenga reli ambayo itatuunganisha sisi na wenzetu wa Malawi kuanzia pale Mbeya na hii reli vilevile itatusaidia kuboresha huduma za meli mbili ambazo zimeshaundwa na zimeshaanza kufanya kazi kwenye Ziwa letu la Nyasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ujenzi wa mazingira…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Nashukuru sana, naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, pamoja na timu nzima ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuleta mapendekezo mazuri ya Mpango na pia Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa mwaka 2018/2019. Naomba nipendekeze kuwa katika kipaumbele cha viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi na viwanda msukumo wa kuboresha kilimo, hasa katika suala la bei na uhakika wa masoko ya mazao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuboresha kilimo tutaweza kuwa na malighafi ya kutosha kwa viwanda vyetu. Pamoja na msukumo wa kuanzisha kanda maalum za kiuchumi na kuimarisha SIDO, napendekeza katika mpango kuwepo na viwanda vidogo huko vijijini ili kuongeza thamani ya mazao, uwepo msukumo wa viwanda vya kuchakata pareto kutokana na mahitaji makubwa ya duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipaumbele cha kufungamanisha uchumi na maendeleo ya watu, kipaumbele hiki ni muhimu sana hasa ukizingatia kuwa kukua kwa uchumi wetu kuendane na hali za wananchi hasa vijijini. Katika mpango wa mwaka 2018/2019 napendekeza Serikali iweke katika bajeti ya maendeleo umaliziaji wa miradi iliyokwama kwa muda mrefu. Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya wananchi wamejitoa sana katika ujenzi wa zahanati na vituo vya afya na pia ujenzi wa madarasa pamoja na ujenzi wa kituo cha polisi cha wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya upatikanaji wa maji hairidhishi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya. Kati ya miradi tisa iliyoanzishwa mwaka 2013, ni mradi mmoja tu uliokabidhiwa wakati zaidi ya shilingi bilioni 4.2 kati ya shilingi bilioni 5.5 ambayo ni 84% zimelipwa, lakini wananchi hawapati maji, Serikali ihakikishe miradi hii inakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo huo napendekeza mradi wa maji wa chanzo cha Mto Kiwira kwa matumizi ya Wilaya ya Mbeya. Pia kuwepo na kuunganisha Mamlaka ya Maji ya Jiji la Mbeya na Mamlaka ya Maji ya Mji Mdogo wa Mbalizi. Pia kuwepo kwa bajeti ya ujenzi wa mabwawa kwa wafugaji wa Kata ya Mjele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipaumbele cha ujenzi wa mazingira wezeshi, napendekeza msukumo uwepo wa kuboresha miundombinu ya barabara vijijini. Pamoja na uchumi mzuri wa Wilaya Mbeya, hali ya barabara ni changamoto kubwa. Napendekeza msukumo uelekezwe kuboresha barabara za kuunganisha mikoa, ikiwemo barabara ya Mbalizi – Makongorosi, barabara ya Mbalizi – Shigamba, barabara ya Isyonje – Kikondo – Makete – Njombe, barabara ya Mjele – Mlima Njiwa, barabara ya Kawetere – Ikukwa, barabara ya Mbalizi – Songwe – Jojo, barabara ya Ilembo – Mwala, barabara ya Ilembo Isonso na pia, by pass ya Mlima Nyoka (Uyole) – Songwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza reli ya TAZARA iboreshwe na iende sambamba na uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Bandari Kavu Inyala, Mbeya. Pamoja na uboreshaji wa reli ya TAZARA, pia iwekwe kwenye bajeti ujenzi wa Reli ya Uyole, Mbeya kwenda Malawi, ili kukabiliana na ushindani wa biashara ya Bandari yetu ya Dar es Salaam na bandari nyingine kama Beira, Msumbiji na zile za Afrika Kusini na hata Angola.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipaumbele cha kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa Mpango, napenda msukumo uwekwe kuboresha ufuatiliaji na utoaji taarifa za utekelezaji, ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa mfumo utakaotoa taarifa sahihi. Taarifa nyingi za miradi zimekuwa hazina uhalisia na zinapotosha, taarifa za miradi ya maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya zimekuwa zinapotoshwa. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na wataalamu wote wa Wizara ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kazi nzuri inayoendelea, Jimbo la Mbeya Vijijini ambalo kwa kiasi kikubwa vijiji vyake vinalizunguka Jiji la Mbeya bado kuna kata tatu na Vijiji hakuna umeme.

Mheshimiwa Spika, naomba Wizara iharakishe kuwa inapeleka umeme kwenye Vijiji vya Kata ya Maendeleo, Itawa na Kata ya Shizuri, ikiwa na vijiji vingine 42 ambavyo bado havijafikiwa na umeme. Kutokana na uchumi mzuri wa maeneo hayo kutakuwa na manufaa mapana kwa taifa letu na hata kuongeza kipato kwa Shirika la TANESCO.

Mheshimiwa Spika, Kutokana na faida za umeme unaotokana na jotoardhi, napendekeza pia Serikali iweke msukumo mkubwa wa upatikanaji wa umeme wa chanzo hiki cha jotoardhi ambao unategemea kuongeza MW 200.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa hii nafasi ya kipekee nami niweze kuchangia hizi Kamati mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuzipongeza Kamati zote mbili zimeleta ripoti zao nzuri na mapendekezo mazuri sana ambayo nina imani kama yakifanyiwa kazi na Serikali tunaweza kwenda kwenye hatua nyingine ambayo ni nzuri zaidi kimkakati kwenye mambo ya kilimo na ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyoeleza taarifa ya Kamati ya Kilimo nafikiri na jinsi walivyoongelea wenzangu, tuna changamoto kubwa sana kwenye sekta hii ya kilimo hasa ukizingatia kuwa kilimo ndiyo sehemu kubwa inayoajiri Watanzania zaidi ya asilimia 75, lakini kwa kiasi kikubwa hatuoni mikakati madhubuti kabisa inayochukuliwa ukilinganisha na umuhimu wa sekta hii ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mdogo kule kwangu katika Halmashari ya Mbeya tunalima pareto na zao hili lina umuhimu wa kipekee sana duniani. Halmashauri yetu tunaongoza kwa kilimo cha pareto Tanzania. Bahari nzuri kwa pareto ile inayolimwa kule vilevile inaongoza kwa
uzalishaji kwa Bara zima la Afrika. Pareto inayolimwa kwenye Halmashauri ya Mbeya na sisi ni namba mbili katika uzalishaji wa pareto duniani, lakini huwezi kuona mahali popote katika makaratasi ambapo limeupa umuhimu wa kipekee hili zao la pareto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshukuru Waziri pamoja na Naibu Waziri wamechukua hatua ambazo kidogo zinaanza kuonesha mwanga wa kwamba labda hili zao nalo linaweza kuwaletea manufaa Watanzania. Kwa kipekee kabisa Naibu Waziri alitembelea Jimbo langu, akakutana na wakulima, akaona wakulima wanavyopata tabu ya soko la pareto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa la pareto hii ni monopoly. Tuna mnunuzi mmoja tu anayenunua zao hili na kwa bahati mbaya mnunuzi huyu katika mnyororo wa zao la pareto yeye ana-control kutoka kwa mkulima, uzalishaji na mpaka soko la dunia kwa vile kwenye soko la dunia nako amelikamata yeye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shida tunayoipata ni kwamba yeye sasa ndiyo atampangia mkulima bei na kwa bahati mbaya hana huruma na mkulima na Tanzania. Kwa bei ya mkulima ni Sh.2,300 kwa kilo lakini kwa bei ya pareto hiyo hiyo ni Sh.8,000 kwa kilo anayouzia yeye sasa angalia hiyo spread, angalia ni kiasi gani katika dunia ya leo mkulima ananyonywa kiasi hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, pendekezo la langu, Kamati iongeze katika taarifa yake mapendekezo kuwa Serikali iweke mkakati wa kipekee kuangalia ni namna gani zao hili la pareto litakuwa na manufaa kwa wananchi. Vilevile huu uzalishaji wa pareto badala ya hii kampuni kupeleka crude extract na powder ya pareto waweze kutengeneza finished product ambazo zinaweza kuuzwa na zikapata jina ya kwamba hii pareto inatoka Tanzania. Tumenyonywa kwa kiasi kikubwa nafikiri hii itaweza kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunazungumzia Tanzania ya viwanda, nafikiri Serikali iweke mkakati namna gani tuwe na viwanda vidogo vidogo kwa ajili ya kuchakata hayo mazao ikiwemo pareto. Kiwanda cha Pareto kinahitaji mtaji wa dola laki moja na nusu tu ambazo ni karibu milioni 300. Nafikiri hizi kwa kiasi kikubwa kama kweli tuna nia nzuri ya kukiendeleza kilimo, tunaweza tukaanzia kwenye pareto tukawa na viwanda vingi na tukawasaidia wakulima waweze kupata faida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiachilia mbali pareto, kwa kiasi kikubwa mwaka huu tumepata matatizo sana kwenye mazao na hasa zao la mahindi. Serikali ilikuwa imepiga marufuku kupeleka mahindi nje ya nchi. Matokeo yake leo hii mahindi kwenye soko letu la Mbeya yameteremka bei kutoka Sh.12,000 mpaka Sh.5,000 kwa debe, leo hii linauzwa kwa Sh.3,800.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa fikiria mkulima amepata hasara ya namna gani na hata hii Sh.3,800 huwezi kupata mnunuzi. Masoko ya huko nje tuliyozuia wenzetu wame-take advantage wamepeleka mahindi kutoka Zambia, Malawi na South Africa yamejaa kwenye yale masoko tuliyokuwa tunapaleka sisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri tujaribu kujitathmini na kuangalia kama hizi taarifa tunazozipata kwa wataalam wetu zinatusaidia katika ku-make decision. Nafikiri tunawaumiza wakulima na tukiumiza wakulima kwa kiasi kikubwa tunawaumiza Watanzania walio wengi ambao wanategemea kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kutoa pendekezo langu na kuiunga mkono taarifa ya Kamati ya Maji kuwa Serikali iweke mkazo tuanzishe Wakala wa Maji Vijijini kwa sababu kwenye Halmashauri zetu tuna tatizo kubwa, hatuna wataalam wa maji, tuna mainjinia na kadhalika lakini uwezo wao wa kusimamia miradi hii mkubwa ya maji ni mdogo sana. Ni afadhali tuweke chombo cha wataalam kusaidia kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Mbeya tuna maji mengi sana lakini toka 2013 hakuna mradi hata mmoja wa maji uliokamilika licha ya bajeti kubwa ya Serikali tuliyoletewa. Nina imani kuwa Wakala wa Maji atutasaidia kama tulivyoona kwenye REA na barabara. Kwa hiyo, naungana na Kamati wahakikishe kuwa hiki chombo kinaanzishwa...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa hii nafasi na mimi naomba nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya hasa kwenye miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtizamo tu wa kawaida ujenzi wa reli ya kati watu wanaweza kufikiri ni kitu kidogo sana kwa Standard Gauge au ujenzi wa viwanja vya ndege na ununuzi wa ndege. Hiki ni kitu kikubwa kwa heshima ya nchi yetu na kwa kweli inatu-position mahali pazuri sana na branding yake kwa nchi yetu nafikiri inatuweka mahali pazuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshukuru Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayoifanya pamoja na timu yake. Amefanya kazi nzuri sana na anaendelea kufanya kazi nzuri sana na amefanya ziara Mbeya. Alipofanya ziara Mbeya pamoja na mambo mengine alitembelea kuna meli tatu zimejengwa pale kwenye Ziwa Nyasa. Aliona ni namna gani Watanzania wana uwezo mkubwa, meli mbili zimekamilika na zimeshaanza kazi na zimejengwa na Watanzania. Kwa kweli, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu ulichokifanya siku ile ni kitu kikubwa sana na kimeleta hata impact kwa majirani zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba niwapongeze Mawaziri wote, wamejitahidi wamefanya ziara kwenye majimbo yetu na ziara zake matokeo yake ni mazuri sana. Wote walipokuja kwenye Jimbo langu wameacha matokeo mazuri sana. Sasa naomba nianzie kwenye
miundombinu ambayo ndiyo Serikali yetu imejikita kwa kiasi kikubwa sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa reli ya kati wa Standard Gauge ni kitu kimekuja kwa wakati muafaka, pia na uboreshaji wa bandari umekuja kwa wakati muafaka. Kwa sababu hivi vyote vinaifanya Tanzania iwe ni njia kuu kwa ajili ya kibiashara kwenda kwenye masoko ya kidunia. Napendekeza pamoja na ujenzi wa reli na uboreshaji wa reli ya kati, ningeomba vilevile Serikali ije na mkakati ni namna gani itaifufua TAZARA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hilo kwa maksudi kabisa nilikuwa naangalia wenzetu majirani wanafanya nini leo hii. Nilikuwa naiangalia Msumbiji inafanya nini. Msumbiji ilikuwa katika dimbwi la vita. Usalama ulikuwa mdogo sana. Kwa hiyo, nchi jirani hazikutegemea sana zile bandari zake. Leo hii Msumbiji wanaboresha reli na bandari inaitwa Nakala. Hiyo Nakala ambayo itakuwa ni kati ya bandari kubwa katika ukanda wetu huu wa Indian Ocean itapitia katikati ya Malawi na vilevile inaenda kwenye Jimbo linaitwa Tete ambalo jimbo la Tete ni ndani ya Msumbiji hiyo na ni jirani sana na Zambia na ni jirani sana na Zimbabwe.

Sasa sisi kwa biashara yetu ya bandari ambayo kwa kiasi kikubwa nina imani zaidi ya asilimia 75 kwa ajili ya soko la nje inategemea sana sana border post yetu ya Tunduma, kwa ajili ya Zambia, Malawi, Congo na kwa kiasi kidogo Zimbabwe. Sasa hawa wenzetu hili soko tayari wameshaliangalia na wameshaanza ujenzi kuna project pale ya dola bilioni tano ambayo katika hizo bilioni 300 zinatoka ADB (African Development Bank), sasa ikikamilika hiyo je, sisi biashara yetu ya bandari kwa ajili ya nchi hizi za Zimbabwe, Zambia, Malawi na Congo itaathirika namna gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naiomba Serikali iweke mkakati wa kuiboresha TAZARA. Kuna umuhimu sana wa kuiboresha TAZARA, kama bandari ina asilimia 75 inazitegemea hizi nchi ambazo leo hii nchi zote hizi zinaangaliwa na wenzetu wa Afrika Kusini, Angola na sasa
hivi Msumbiji tutakuwa tumejiweka wapi kwenye soko la usafirishaji. Kwa hiyo, naomba Wizara itakapokuja Wizara husika, ijaribu kuangalia ni namna gani itaboresha TAZARA lakini vilevile ni namna gani tujenge bandari kavu Mbeya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo bandari kavu kwa sababu kuna kilomita pale 120 za kwenda ziwa Nyasa, nazo tuangalie kwa ajili ya ushindani ili reli ile itoke Mbeya kwenda ziwa Nyasa kwa ajili ya ushindani ambao wameuonyesha hawa wenzetu wa Msumbiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye viwanja vya ndege, kuna Wabunge wengi wameongelea uwekezaji na ujenzi wa uwanja wa ndege wa Songwe. Ni kweli ni miaka mingi bajeti zimekuwa zikitengwa lakini mpaka leo uwanja hauna taa za kuongozea ndege, uwanja hauna uzio.

Mheshimiwa Mwenekiti, leo hii bidhaa kama maua, bidhaa kama viazi, bidhaa mbalimbali za matunda zinatoka Mbeya kupelekwa kiwanja cha ndege cha Dar es Salaam kwa sababu hatuna taa kwenye uwanja wa ndege wa Songwe. Naiomba Serikali itoe hizo hela haraka kwa sababu kwa kiasi kikubwa kwanza ukiangalia hata abiria wengi wanatoka nchi zetu hizi za jirani. Tunapata pesa nyingi za kigeni, lakini vilevile tuna-potential ya ku-export vitu vingi kwa kutumia..., ndege kubwa zinahitaji kutua moja kwa moja kwenye uwanja ule, huwezi ukatumia ndege kubwa ukasema itue kwanza Dar es Salaam ndiyo ije Mbeya. Wenyewe wanataka wakichukua mzigo aende moja kwa moja New York au aende moja kwa moja Russia.

Kwa hiyo, tunaomba ule ukamilishaji wa ule ujenzi na kwa vile ilishatoka kwenye bajeti sioni kama kuna tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni la uzio, ni muhimu sana kujenga uzio kwa ajili ya usalama. Tumeona kiwanja cha ndege cha Mwanza juzi hapa binadamu amehatarisha abiria na ndege na hilo linaweza kuja kutokea kwenye kiwanja cha Songwe kwa vile pembezoni mle watu
wanafuga ng’ombe, ng’ombe wana tabia ya kufukuzana. Sasa fikiria ng’ombe wanafukuzana halafu ndege ndiyo inatua, sijui hiyo hatari nani ataibeba.

Naomba sana Wizara itakapokuja hapa iseme ni namna gani katika hivi viwanja ambavyo ni potential. Potential kwanza ni vya mpakani, lakini vilevile ni soko kubwa pia ni viwanja vikubwa tuvimalizie ili biashara na tuweze kupata bei nzuri, tuweze kupata pesa nyingi za kigeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni suala la kilimo. Suala la kilimo kila mmoja kaongea kabisa uchumi wetu kwa kiasi kikubwa unategemea kilimo na kweli haipingiki. Lakini nilikuwa najaribu kusoma makala mbalimbali ambazo zinaonyesha ni namna gani kuna hatari ya upungufu mkubwa wa chakula mwaka 2030 mpaka 2050. Tanzania tumejiandaa vipi kwa hilo. Wenzetu ukisoma wamejiandaa sana, wana- invest sana ili waweze kukabiliana na hii hali na hiyo sisi tunaiweza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoongelea kuhusu maji ni namna gani maji yatusaidie kwenye umwagiliaji, ni namna gani maji ya mvua tuweze kuyavuna, bila hivyo mwaka 2030 target ya wenzetu kwa kweli itatumaliza na Tanzania kwenye ongezeko la watu inaonekana speed yetu ni kubwa, tunaongezeka kwa haraka, lakini uzalishaji wa chakula ni mdogo sana. Kwa hiyo, naiomba Wizara ije na mkakati ni namna gani imejipanga kuhakikisha kuwa mazao ya chakula hayaitwi tu mazao ya chakula, nayo yawe katika orodha ya mazao ya biashara. Hii ya kusema kuna kahawa, cocoa, korosho ndio mazao ya bishara nafikiri ni mfumo wa kizamani, kwa sababu ni mazao ambayo tulikuwa tunategemea fedha za kigeni. Lakini kibiashara leo viazi, mahindi, maharage kwa kiasi kikubwa nafaka ndiyo wakulima wanategemea kwa kiasi kikubwa kama mazao ya biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo nafikiri tusije tukafanya makosa ya kuzuia haya mazao tena kuuzwa nchi za nje. Leo hii Kenya mahindi kwa kiasi kikubwa wananunua kutoka Uganda. Sasa ukiangalia Uganda wanazalisha mahindi? Mahindi yanayozalishwa Uganda ni tani kama milioni mbili na laki nane tu, lakini Tanzania tunazalisha karibu tani milioni sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa mafanikio makubwa ya kiuchumi na kijamii katika kipindi kifupi cha takriban miaka miwili na nusu. Napenda pia, kumpongeza Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Mbunge, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia, napenda kumpongeza Waziri na Manaibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu na wataalam wote kwa kazi nzuri yenye mafanikio makubwa kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ni miongoni mwa nchi tatu barani Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa kasi. Pamoja na jitihada za kukuza uchumi napendekeza kuimarisha mikakati ya kuboresha miundombinu ya bandari zetu, reli pamoja na barabara wakati tunaendelea kwa kasi na ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha SGR na kuboresha bandari ya Dar es Salaam, Serikali iweke mkakati wa kulinda biashara ya bandari zetu kwa kuboresha reli ya TAZARA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miradi mikubwa inayoendelea ya kuboresha bandari na reli za nchi jirani kama mradi wa The New Port of Nacal Development Corridor Project ya Msumbiji. Mradi huu unalenga kuifanya Msumbiji kuwa lango kuu la kibiashara za kimataifa kwa nchi za Malawi na hata Zambia, Zimbabwe na DR Congo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, reli ya TAZARA ina umuhimu wa kipekee katika kuinua uchumi, kilimo, madini, utalii, ikiwa ni pamoja na kulinda biashara ya Bandari ya Dar es Salaam, ili kuwa lango la kibiashara za kimataifa kwa nchi jirani. TAZARA ilijengwa kuwa na uwezo wa kuhimili treni ya spidi ya kilomita 110 kwa saa, ikiwa na uwezo mkubwa wa kusafirisha mizigo ya kilimo, mbolea, madini kwa nchi za Tanzania, Zambia, Malawi na hata DRC na Zimbabwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuboresha pia, ijengwe bandari kavu ya Mbeya. Aidha, imebainika kuwa, Reli ya TAZARA inaendeshwa kwa hasara na kusababisha inatumia kodi ya wananchi badala ya kujiendesha yenyewe na kwa faida. Nashauri Serikali za Tanzania na Zambia kuweka mtaji mpya, pia kuimarisha uongozi wa TAZARA, ikiwa ni pamoja na kutekeleza ushauri wa kitaalam wa mfumo bora wa kuendesha reli hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri ya utekelezaji wa miradi ikiwemo miradi ya maji. Pamoja na ujenzi wa miradi ya maji bado kuna mahitaji makubwa ya maji na huku kukiwa na tishio la tabianchi. Nashauri Serikali iweke mkakati wa kuvuna maji ya mvua kwa matumizi ya kilimo na matumizi ya kibinadamu. Uvunaji wa maji ya mvua umefanyika kwa mafanikio makubwa kwa nchi za Kusini mwa Afrika ambazo zinafanana kijiografia na Tanzania. Nchi hizi zimefanikiwa hata kuuza maji ya mabwawa hayo kwa nchi jirani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuipongeza Serikali kwa kuboresha sekta ya afya ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya na hospitali za wilaya. Pamoja na ujenzi wa miundombinu napendekeza Serikali iweke mkakati wa kuhamasisha Watanzania wote kuwa na bima ya afya, NHIF au CHF. Kuwepo kwa bima ya afya kwa Watanzania kwa wingi wetu kutawezesha sekta ya afya kujitegemea na kuwepo kwa huduma bora za afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kupata nafasi ya kuchangia hotuba ya bajeti ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa, Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu pamoja na watendaji wote kwa kazi nzuri yenye mafanikio kwenye sekta zote.

Mheshimiwa Spika, awamu hii imeweka historia ya nchi hii kwa ujenzi wa reli ya kisasa SGR, ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa Mwalimu Nyerere, ununuzi wa ndege na kufufua shirika la ndege, uboreshaji wa huduma ya afya ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya na hospitali za Wilaya, ujenzi wa maboma ya shule za msingi na sekondari na msingi, mafanikio ya usambazaji umeme vijijini na pia miradi mikubwa ya maji.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hotuba nzuri ya bajeti, napendekeza Serikali iendelee kuimarisha Kamati ya kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa virusi vya corona (covid-19) ikiwa ni pamoja na kuwezesha kuwepo kwa coronavirus contingency plan kwa sekta zote. Hii itasaidia kuimarisha utambuzi wa changamoto za kiafya na za kiuchumi lakini kutambua pia fursa zilizopo na ambazo zinaweza kupunguza athari za kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, napendekeza kuchukua hatua za kuchochea ubunifu katika kukabiliana na changamoto zinazotukabili ikiwemo hata watalaam wetu kushiriki uvumbuzi wa chanjo ya covid-19'.

Mheshimiwa Spika, napendekeza Serikali iangalie fursa kwenye sekta ya kilimo na madini na kuongeza uwekezaji na hata kuvutia wawekezaji kwenye uzalishaji wa mazao ya chakula.

Mheshimiwa Spika, napendekeza mpango wa haraka kuvutia wawekezaji katika madini ya chuma, bati na Niobium. Pia Serikali iongeze mtaji wa Benki ya Kilimo (TADB) na Benki ya Rasilimali (TIB).

Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki tunaposhuhudia mtikisiko wa uchumi kidunia, napendekeza Serikali kuangalia jinsi ya kusaidia mabenki na hata uwekezaji kwenye kilimo kuwezesha kuwepo kwa stimulus package. Kuna fursa kwenye uzalishaji wa mazao ya chakula na hata mazao ya mifugo. Katika kipindi hiki Serikali iendelee kusisitiza kuimarisha matumizi ya teknolojia kwenye masoko ya mazao (TMX) na mfumo wa stakabadhi ghalani.

Mheshimiwa Spika naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa hii nafasi adimu. Nianze kwa kuipongeza Wizara inafanya vizuri sana hasa kwa kuboresha bandari nafikiri kwa kiasi kikubwa hii itapunguza gharama ya malighafi zinazokuja kutoka nje zikiwemo mbolea, lakini vilevile itapunguza gharama za bidhaa zetu ambazo tunasafirisha kwenda nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuboresha hii bandari yetu lakini inakabiliwa na ushindani mkubwa sana hasa na bandari za jirani. Ninapendekeza Serikali iangalie namna gani iboreshe TAZARA, TAZARA kwa kiasi kikubwa ni standard gauge; speed ya treni pale ni kilometa 110 kwa saa. Tukiboresha hii ambayo maboresho yake sidhani kama yanahitaji hela nyingi, labda Serikali ijaribu kutuambia ni kiasi gani itaboresha Menejimenti ya TAZARA na vilevile namna gani itaondoa ukiritimba ili TAZARA iendeshwe kibiashara, kwa sasa hivi TAZARA haiendeshwi kibiashara na nina wasiwasi mpaka leo wafanyakazi wa TAZARA wanalipwa na hela kutoka Serikalini, wanalipwa na walipakodi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiboresha TAZARA tutakuwa tumejiweka katika position nzuri sana ya kiushindani lakini vilevile tukijenga bandari kavu Mbeya ili mizigo ambayo ni zaidi ya asilimia 70 inayokwenda nchi za nje inapitia barabara hiyo, iondokane na kuharibu barabara zetu. Tukishajenga bandari kavu pale, mbolea zote kwa ajili ya nyanda za juu kusini na mizigo yote ya kutoka Congo, Malawi na Zambia yote isipitie barabara hizo, itue pale ili ipunguze gharama na vilevile itaongeza ushindani. Vilevile ningependekeza tujenge reli ya kuanzia Mbeya kwenda Ziwa Nyasa ili tuwe na ushindani mzuri na Bandari za Msumbiji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kwenye barabara nilikuwa ninaomba sana Serikali iangalie namna ya kuboresha barabara zetu ambazo zilikuwa ni ahadi za Mheshimiwa Rais, barabara ya Mbalizi – Makongolosi, Mbalizi
– Shigamba – Isongole na barabara ya Isyonje – Kikondo – Makete mpaka Njombe vilevile barabara ya bypass ili iweze kuondoa msongamano wa magari pale Mbeya Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kwenye Kiwanja cha Ndege cha Songwe; hiki kiwanja kimetengewa hela nyingi lakini mpaka leo hatuna taa pale za kuongozea ndege na hakuna uzio. Naiomba sana Serikali iangalie ni namna gani itaboresha Uwanja wa Ndege wa Songwe kwa kuwekea taa za kuongozea ndege vilevile na uzio. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tuna bidhaa nyingi ambazo zinahitajika kwenda nchi za nje kutoka nchi jirani, lakini vilevile kutoka Mbeya yakiwemo maparachichi na matunda mengine lakini yanasafirishwa mpaka Dar es Salaam na haya yana masoko nje. Ukienda kwenye supermarket za Uingereza leo hii utapata bidhaa kutoka Mbeya, lakini zinakwenda kwa gharama kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la fidia, suala la fidia waliopisha ujenzi Uwanja wa Ndege wa Mbeya mpaka leo halijashughulikiwa. Wananchi wale wanalalamika miaka mingi na Mheshimiwa Waziri tumeongea naye mara nyingi na imo kwenye ripoti ya Kamati ya Kudumu ya Miundombinu ambayo nao walipendekeza hawa wananchi walipwe. Ni shilingi milioni 800 tu lakini usumbufu uliopo ni mkubwa na ninashangaa kwa nini wananchi wale mpaka leo wanadhulumiwa pesa zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wananchi ambao katika ripoti yao walipewa fidia ya shilingi 2000 au shilingi 5000 kwa maheka na maheka. Sasa hili wizara ingeangalia hawa TAA wahakikishe wanawalipa wale wananchi hizo shilingi milioni 800 ambazo wanadai. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala la TARURA, TARURA zinaendana na TANROADS, lakini mgao wa pesa zinazoenda TARURA ni ndogo mno. Kwenye Jimbo langu tuna kilometa zaidi ya 1,000 mtandao wa barabara lakini bajeti yake ni kama shilingi milioni 1.6. TARURA wakiongezewa pesa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha muda wa Mzungumzaji)

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, asante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Waziri, Naibu Waziri na viongozi wote kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka wa Wizara ya Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi kinachoishia mwezi Aprili, 2022 Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani imesimamia kwa uadilifu na ufanisi mkubwa masuala yote ya usalama wa raia hasa kurudisha uwabikaji kazini iliopelekea kupungua kwa uhalifu. Pia kwa kusimamia vizuri, rushwa na upendeleo umepungua kwa kiasi kikubwa kupelekea wananchi kushiriki kikamilifu shughuli za ujenzi wa Taifa.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio hayo makubwa ya ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Mbalizi kwa kushirikisha wananchi, askari bado wanaendelea kufanya kazi katika mazingira magumu kutokana na kutokuwepo kwa nyumba za askari hasa katika eneo jirani na Kituo cha Polisi. Ni vigumu sana kwa Wilaya yenye askari zaidi ya 150 na inatoa huduma kwa wakazi karibu 500,000. Kunapotokea dharura, viongozi na hata askari inakuwa vigumu kujikusanya kwa muda muafaka. Pia wananchi wameonesha nia ya kushiriki kujenga vituo vingine katika miji midogo ya Ilembo, Isuto na Igoma. Kuna uhitaji mkubwa wa kuwepo vituo vya polisi katika maeneo haya kutokana na shughuli za kichumi na pia umbali toka makao makuu ya Wilaya.

Mheshimiwa Spika, napendekeza Serikali ianze mchakato na itenge bajeti ya angalau shilingi milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vipya vya Ilembo, Isuto na Igoma. Kwa vile wananchi wameonesha nia ya kushiriki ujenzi wa vituo vitatu vipya vya polisi, bajeti hii inayoombwa ya shilingi milioni 300 itachochea kumaliza ujenzi wa maeneo muhimu ya vituo hivi na kuwezesha motisha na ufanisi kwa askari. Pia napendekeza kuongeza magari kwa ajili ya usafiri hasa ukizingatia jiografia ya Wilaya ya Kipolisi ya Mbalizi.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii na mimi nianze kwa kumpongeza kwanza Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanayoifanya pamoja na timu yake ya wataalam ikiongozwa na Katibu Mkuu, wamefanya kazi nzuri sana. Ukiangalia katika hii ripoti utaona ni kiasi gani wamefanya mageuzi katika hii Wizara. Mwaka uliopita utendaji ulikuwa ni asilimia 25 lakini kwa mwaka huu tulionao wa 2017/2018 Wizara hii imetekeleza kwa asilimia zaidi ya 56. Hiyo ni mara mbili ya ule utekelezaji wa mwaka jana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ninapenda kumpongeza Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa ziara walizozifanya kwenye Jimbo langu, zimeleta mageuzi makubwa. Naibu Waziri alikuja, alishuhudia mwenyewe miradi ya mabilioni ya pesa ambayo ripoti zake zinaonesha kuwa imetekelezwa na amekwenda site kwenye tenki akaambiwa hilo tenki lina maji, akapanda kwenye tenki kuangalia badala ya maji akakutana na mazalia ya popo. Kwa hiyo, inasaidia sana hizi ziara za Mawaziri wanapokwenda wenyewe site na kujionea ni nini kinachofanyika huko. Utekelezaji kwenye miradi mingi hasa ya vijijini ni kwa kiasi kidogo sana. Ni hela nyingi sana nchi hii zimeliwa, nakubaliana na wenzangu ambao wamependekeza kuundwe Tume ichunguze miradi ya maji ili tujue ni kiasi gani cha pesa zilizoliwa kwa vile tutaongeza tozo tutamlalamikia Waziri wa Fedha lakini kusipokuwa na usimamizi, hali huko vijijini ni mbaya sana, pesa zimeliwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni shahidi wa kilichotokea kwa Mheshimiwa Waziri kuchukua miradi ya Mbeya Vijijini, tulikuwa na asilimia mbili tu kwa mwaka uliopita lakini alipokuja Waziri akachukua miradi yote ya Mbeya Vijijini, leo tuko na asilimia zaidi ya 60 za utekelezaji. Miradi mingi inatekelezwa vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kuna mradi wa Iwindi, Izumbe, Mwashiwawala uko katika utekelezaji mzuri sana. Mradi wa Mbalizi tulikuwa tunalalamikia Mbalizi hakuna maji, lakini Waziri amechukua initiative zake za kuunganisha Mamlaka ya Maji Mbalizi na Mamlaka ya Maji Jiji. Miradi yote ya vijiji kumi ambayo ilikuwa imekwama kwa miaka zaidi ya saba leo hii iko kwenye utekelezaji mzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata wewe mwenyewe ni shahidi, ninaomba kukushukuru kwa juhudi zako na jitihada zako umeweza kutusaidia mradi wa Irota ambao leo hii tuna imani tutaletewa zaidi ya shilingi milioni 250 kwa ajili ya kile kijiji ambacho kilikuwa hakina maji kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naisoma vizuri sana hii ripoti, tunaomba maji lakini ukiangalia ukurasa wa tano, hayo maji tunayoyaombea pesa hayapo! Mwaka 1962 uwezo wa maji tuliokuwa nao ilikuwa ni mita za ujazo 7,800, mwaka jana zimepungua mpaka mita za ujazo 1,800 kwa mtu kwa mwaka. Mwaka 2025 inaonesha tutakuwa na mita za ujazo 1,500; maana yake nchi hii itakuwa imeingia kwenye nchi ambazo hazina maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tutaongea sana hapa, tunataka bajeti za maji, maji yako wapi? Naliomba Bunge lako liunganishe nguvu za Wizara hizi mbili, Wizara ya Mazingira na Wizara ya Maji zifanye kazi kwa karibu. Wenzetu wameshachukua kwa makusudi kabisa kuvuna maji. Kuvuna maji ya mvua yamewasaidia vilevile hayo maji yanayozalishwa imekuwa ni zao ambalo linaloziletea hizo nchi pesa za kigeni kwa vile maji ukiangalia nchi zinayoizunguka Afrika Kusini wanayakusanya maji ya mvua na yale maji yanapelekwa Afrika Kusini na inazipatia pesa za kigeni hizo nchi, pesa nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikitoa mfano wa kule Jimboni kwangu, tuna mvua nyingi sana lakini mito mingi sasa hivi inakauka, mto Nzovwe unakauka, Mto Songwe unakauka na ukiangalia kuna mimomonyoko ya udongo, mvua zikishanyesha udongo wote unakwenda Ziwa Rukwa, na ziwa karibu linakauka. Nafikiri Wizara iangalie bajeti kubwa, ningeomba kwanza uanzie kwenye Jimbo langu kwenye Kata ya Mjele, jenga mabwawa ya kutosha ili tuweze kuvuna maji ya kutosha tuongeze huu ujazo wa maji badala ya kufanya projections za maji kukauka, tufanye projections za maji kuongezeka, hiyo trend ibadilike. Tusiongelee mita za ujazo 1,500, tuongelee ni namna gani turudishe mita za ujazo 7,800 na zaidi. Hilo ni jambo muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika bajeti ya Waziri wengi sana wamejadili kuhusu kuanzisha Mamlaka ya Maji Vijijini. Kama nilivyosema, Halmashauri yangu iwe ni pilot, imefanya kazi vizuri mno. Nakuomba Waziri, hili suala litakapoanza tumia modal uliyotumia Mbeya Vijijini iende kila Halmashauri, italeta mageuzi mno na hatutahitaji pesa nyingi kwa ajili ya maji. Tutahitaji bajeti ndogo, pesa ndogo sana kwa ajili ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naungana na wenzangu kuhusu kuongeza tozo kutoka shilingi 50 kwenda 100. Ni jambo muhimu, litatuletea neema sana, ukiangalia bajeti ya mwaka huu kwa kiasi kikubwa imetegemea tozo ya mafuta ya dizeli pamoja na petroli, bila hivyo tusingefikia hiyo asilimia 56. Kwa hiyo, tunaomba tuangalize zaidi namna ya kujitegemea badala ya kuangalia ni namna gani tutegemee misaada kutoka nje ambayo kutokana na hali ilivyo sasa siyo ajabu hatutaipata hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ningeomba Wizara ya Fedha ingeangalia. Kwa ile mitambo ya kuchimba mabwawa ya maji na ile mitambo na vifaa vyote vya maji vingeondolewa kodi ili viwezeshe kupunguza gharama za uchimbaji wa maji na miradi ya maji. (Makofi)

Baada ya kusema hayo, naomba na mimi niunge mkono hoja. Nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Engineer Isack A. Kamwelwe (Mbunge), Waziri wa Maji na Umwagiliaji na Mheshimiwa Jumaa Aweso (Mbunge), Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo, Katibu Mkuu pamoja na wataalam wote wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa kazi nzuri waliofanya katika kipindi cha mwaka 2017/2018. Mpaka Machi, 2018 utekelezaji wa Wizara ni zaidi ya asilimia 56 ambayo ni zaidi ya mara mbili ukilinganisha na asilimia 25 ya mwaka 2016/2017.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee naomba kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa ziara wanazozifanya nchi nzima, zimeleta tija kubwa katika utekelezaji wa miradi. Katika ziara ya Naibu Waziri Mheshimiwa Aweso, alibaini mapungufu makubwa ya mradi ya maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya. Mheshimiwa Aweso alipokagua mradi wa maji wa vijiji vya Horongo, Itimu na Mwampalala alijionea udanganyifu mkubwa wa mradi kutekelezwa chini ya kiwango na hata pale alipoambiwa mradi unatoa maji aligundua hata matenki hayakuwa na maji. Pia Mheshimiwa Kamwelwe alishuhudia utekelezaji wa asilimia mbili tu ya bajeti ya mwaka 2016/2017 huku taarifa zikipotosha kuwa miradi imekamilika na kulikuwepo madai ya wakandarasi wakati siyo kweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya ziara ya Waziri wa Maji aliagiza miradi yote iliyokuwa imekwama kwa zaidi ya miaka saba isimamiwe na Wizara ya Maji kupitia kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Mbeya, uamuzi huo umeleta matunda na miradi ifuatayo iko katika hatua nzuri sana za utekelezaji, mradi wa kijiji cha Ganjembe umekamilika asilimia
90. Mradi wa vijiji vya Swaya na Lupeta umekamilika kwa zaidi ya asilimia 80. Mradi wa Mbawi na Jojo umekamilika kwa asilimia zaidi ya 90.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa vijiji vya Idimi na Haporoto umekamilika kwa zaidi ya asilimia 60. Mradi wa vijiji vya Mshewe, Muvwa, Njelenje, Mapogoro na Njele bado upo kwenye hatua za mwanzo. Mradi wa kijiji cha Ilota upo kwenye hatua za mwanzo na napenda kuwashukuru Tulia Trust kuahidi kuchangia shilingi milioni 250. Mamlaka ya Maji ya Mji Mdogo wa Mbalizi imekubalika kuunganishwa na Mamlaka ya Maji Mbeya ili kuboresha huduma ya maji kwa Mji wa Mbalizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa maji wa Izumbwe, Iwindi na Mwashiwawala umekamilika kwa zaidi ya asilimia 50. Mradi wa skimu ya umwagiliaji kwa kijiji cha Mashewe umekamilka kwa zaidi ya asilimia 90.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hatua nzuri ya miradi hapo juu bado kuna mahitaji makubwa ya maji kwa maeneo mengi ya Wilaya ya Mbeya hasa kwenye miji midogo ya Ilembo, Inyala, Isuto, Santilya, Iwigi, Ikhoho, Mjele. Kunahitajika maji kwenye vituo vya afya, zahanati na mashule karibu yote hayana maji. Nashukuru kuwepo kwa mradi wa maji kutoka Mto Kiwira na Truu ni mkombozi pia kwa Mbeya Vijijini na hata Mji Mdogo wa Mbalizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na upungufu mkubwa wa maji kwenye mito kutokana na mabadiliko ya tabianchi na changamoto zingine napendekeza kujenga mabwawa makubwa kwenye maeneo ya vyanzo vya mito ambayo iwe pamoja na mabwawa makubwa kwenye vijiji vyenye uhaba wa mvua kama vile Mjele, Mshewe na Songwe. Rasilimali ya maji inaendelea kupungua kwa kasi kutokana na ongezeko la watu, uharibifu wa mazingira na pia mabadilko ya tabianchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wastani wa maji umepungua kutoka mita za ujazo 7,862 kwa mtu katika mwaka 1962 na kupungua hadi wastani wa mita za ujazo 1,800 kwa mtu kwa mwaka 2017. Inaelekea mwaka 2025 upungufu utafika mita za ujazo 1,500 kwa mtu ambayo ni chini ya wastani wa mita za ujazo 1,700 kwa mtu. Kwa mwaka 2025 tutakuwa tumeingia kwenye kundi hatarishi (water stressed countries). Kutokana na hali hiyo napendekeza Wizara ichukue hatua kubwa za kukabiliana na changamoto hizi ikishirikiana na Wizara ya Mazingira. Jitihada za kukabiliana na changamoto za upungufu wa maji zionakane kwenye bajeti ikiwemo kuongeza bajeti ya mabwawa na utunzaji wa vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mahitaji makubwa ya bajeti ya maji na pia changamoto za upatikanaji wa fedha za nje napendekeza kuongeza tozo za mafuta kwa kila lita ya petroli na dizeli kutoka shilingi 50 hadi shilingi 100. Imedhihirika kwa mwaka 2017/2018 Mfuko wa Maji ulikusanya shilingi bilioni 158 na Wizara imetumia ipasavyo na imeleta mafanikio makubwa katika utekelezaji wa kwenye miradi ya maji vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na changamoto za utekelezaji wa miradi ya maji katika Halmashauri zetu napendekeza uanzishwaji wa Wakala wa Maji Vijijini. Wakala wa Maji Vijijini atawezesha kupunguza uhaba wa wataalam wa maji na pia ataongeza uwajibikaji katika utekelezaji kwa wakala wa maji vijijini kutawezesha utekelezaji wa miradi ya maji kwa ubora na ufanisi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Kutokana na muda mfupi nitaenda moja kwa moja kwenye suala la mbolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, rejea ukurasa wa 41 wa kitabu hiki cha bajeti ya Wizara. Utafiti wa udongo unaonesha kuwa mbolea inayofaa karibu kwa kanda nyingi zinazolima mahindi na nafaka nyingine ni Nitrogen Phospharus Sulphur (NPS) na NPS Zinki. Huo ndiyo utafiti aliotuletea kwenye bajeti yake Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kwenye ukurasa wa 26 Mheshimiwa Waziri anatuambia kuwa mbolea ambayo inaagizwa kwa pamoja (Bulk Procurement System) ni mbolea ya DAP na Urea. Sasa kitaalam maana yake nini? Tunasisitiza tufanye utafiti, wakulima walime kwa tija, sasa wewe unang’anga’ania DAP na Urea kwa sababu tumeizoea. DAP ni kwa ajili ya mizizi na Urea inatengenezwa kutokana na zao la petroli, asilimia 70 ukiiweka inayeyuka, inapotea. Sasa mnatulepeka wapi? Kwa kweli hivi ndiyo vitu nafikiri Waziri alipotoka kidogo tu labda akija kesho ajaribu kutuambia kwa nini hafuati utafiti unavyosema? (Makofi)

Mheshmiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kulisemea ni kahawa. Uzalishaji wa kahawa unapungua mwaka hadi mwaka. Tulikuwa na tani 61,000 mwaka 2015/2016 zikapungua kuja tani 48,000, zikapungua mwaka jana kuja tani 36,000 na sasa hivi kuna projections kidogo na tulitegemea kwamba zitafika tani 100,000. Tatizo nalo liko wapi hapa? Tatizo lipo kwenye usimamizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la kahawa linasimamiwa na TCB. Nikiangalia muundo wa TCB mpaka leo nashindwa kuuelewa. Kwa sababu TCB alitakiwa kuwa regulator lakini vilevile ndiye anayehusika na masoko. Mnada wa kahawa unasimamiwa na TCB, kwa kiasi kikubwa wakulima wananyonywa sana. Leo hii mnada wa kahawa ya Tanzania arabica ni dola 3 kwa kilo, kwa Kenya jirani zetu kahawa hiyo hiyo ya arabica ni kati ya dola 7 -10, angalia tofauti hiyo. Ukienda Ethiopia bei inakuwa ni nzuri zaidi, ni kwa nini? Kwa sababu huwezi ukamuweka regulator mtu mmoja huyo anasimamia uuzaji wa kahawa na pale bei hazipangwi kwenye mnada, watu wanakubaliana nje ya mnada. Wakienda pale ni kuthibitisha tu kwamba hii kahawa tunatainunua kwa dola, anayenyonywa ni nani? Anayenyonywa ni mkulima na ndiyo sababu wakulima hataki kuendelea tena na kulima kahawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kununua mbolea, achilia mazao mengine, kwa sasa hivi ukilima mahindi huwezi kununua ambolea. Kwa hiyo, tukisema kuwa tunaongeza mazao, tunaongeza uzalishaji, tunaongeza productivity, sasa hivi huu mfumo tulio nao ukilinganisha masoko na uzalishaji haviendi pamoja. Leo mfuko wa mbolea kwa ajili ya kahawa ni zaidi ya Sh.70,000 unahitaji mifuko mitatu, ukiuza kwa dola 3,000 huwezi tena kulihudumia hilo shamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kuna chombo kipya cha bidhaa za mazao (Tanzania Commodity Exchange Market), hiyo ndiyo tuifuate. Inafanya vizuri Nairobi na Ethiopia, itaweka bei wazi. Vilevile hata ukwasi (liquitidy) kwa ajili ya wakulima itakuwa nzuri. TCB tunalipa baada ya wiki mbili lakini nina imani kwa Sheria ya Tanzania Commodity Exchange Market ni siku moja, wanaita T+1, siku ya pili unalipwa hela yako. Sasa hizi siku 14 zile hela zikikaa TCB ni nani anayefaidi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo wakulima wananyonywa sana ni kwamba kahawa tunauza kwa forex na halmashauri zetu ile service levy nayo anakatwa mkulima kwa forex lakini exchange rate inayotumiwa na TCB wanaamua wenyewe, ni pesa nyingi sana inayopotea. Naomba Wizara au Serikali kwa ujumla ielekeze kwamba haya mazao yote, iwe nafaka, korosho, kahawa ziende kwenye soko la bidhaa, ndivyo duniani kote biashara za namna hiyo ndiko zinakokwenda huko. Huku tulikozoea huku, ushirika ndiyo nakubaliana wakusanye wapeleke sokoni, lakini sokoni kule ziuzwe kisasa na chombo hicho tunacho, tukitumie.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mawaziri na viongozi wote wa Wizara ya Afya, kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Waziri wa Afya, kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Serikali katika utekelezaji wa sera ya afya ikienda sambamba na ustawi wa jamii na maendelo endelevu, na hii ni mojawapo ya nguzo kuu katika utayari wetu wa ushindani wa Kimataifa (national competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni “Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu”.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Awamu ya Sita, Serikali kupitia Wizara ya Afya, imetekeleza miradi mingi ya miundombinu ya afya. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya na kwa kushirikiana na TAMISEMI, imeendelea kutekeleza kwa ufanisi mkubwa miradi ya Hospitali ya Wilaya na vituo vitano vya afya vya kata za Ikukwa, Ilembo, Santilya, Ilungu na Swaya. Vituo vyote vitano vinaendelea kutoa huduma kwa ufanisi mkubwa hasa huduma ya watoto na wakina mama. Hospitali ya Wilaya pamoja na vituo vya afya vimekamilika na maandalizi ya vifaa tiba yapo katika hatua za mwisho ili vianze kutoa huduma kwa ukamilifu.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki tunapopambana na janga la corona virus (Covid-19), tumejifunza umuhimu wa utayari wa huduma ya afya hasa kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali na hivyo Serikali iongeze msukumo wa kupeleka vifaa tiba na kumalizia vituo vya afya na zahanati zilizojengwa kwa nguvu za wananchi. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, wananchi wa kata za Igoma na Isuto wamejenga vituo vya afya na kuna maendeleo mazuri ya kukamilisha, na pia Mji Mdogo wa Mbalizi wenye wakazi zaidi ya 150,000 hawana kituo cha afya, hivyo napendekeza Serikali kutoa kipaumbele katika bajeti hii kwa vituo vya afya hivi ili vianze kutoa huduma. Pamoja na vituo vya afya vya Ilungu, Igoma, Isuto na Mbalizi, napendekeza kukamilisha zahanati zote ambazo zimejengwa kwa nguvu za wananchi.

Mheshimiwa Spika, kutokana na maboresho ya miundombinu ya hospitali na vituo vya afya, Serikali ihakikishe bajeti ya mwaka huu inajielekeza zaidi ajira ya madaktari na watumishi wa afya kwa ujumla. Pamoja na maboresho hayo ya miundombinu, vifaa tiba na ajira kwa watumishi, napendekeza Serikali ikamilishe mpango kabambe wa Bima ya Afya kwa Wote na hasa kwa wazee na wenye mahitaji maalum.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, na mimi naomba niungane na wenzangu kwa kuipongeza Wizara ya Fedha, inafanya kazi vizuri hasa kwenye mambo ya forex stabilization pamoja na inflation, wamefanya vizuri sana.

Mheshimiwa Spika, vilevile naiomba Serikali irudishe haraka Tume ya Mipango inayoonekana. Inawezekana tuna shughuli za mipango lakini tungeiona Tume ya Mipango ambayo ni huru. Wakati kama huu wa leo ambapo tuna miradi mikubwa mingi ya muda mrefu, inahitaji vyombo mbalimbali kwa ajili ya kusimamia hiyo miradi. Nina imani kuwa Tume ya Mipango ingesaidia sana kuingalia; je, mradi wetu wa standard gauge utakwendaje? Hela kwa ajili ya standard gauge itatoka wapi? Kwa vile hii ni investment ya muda mrefu, itahitaji vilevile na financing ya muda mrefu na vilevile miradi kama ile ya Stiglers Gorge. Kwa hiyo, ni muhimu sana Serikali ikaliangalia hili, ikalirudisha na hii Tume ya Mipango iwe huru. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili ni suala zima la namna gani tunaweza kuongeza mapato ya Serikali hasa yale ambayo yasiyokuwa ya kodi. Nina imani kuwa Msajili wa Hazina (Treasury Registrar) ni muhimu sana kutuletea mapato yasiyokuwa ya kodi. Hii italeta unafuu kwa walipa kodi. Tutaonekana Tanzania tunapunguza hata viwango vya kodi. Kodi zimekuwa nyingi mno ambazo hazihitajiki. Investment za TR ni shilingi trilioni 47. Asilimia kumi tu ni shilingi trilioni 4.7, ni hela nyingi kama Serikali tukiitumia vizuri hii ofisi. Ukiangalia bajeti yao ilikuwa kuileta Serikalini shilingi bilioni 500 tu, ni hela kidogo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Waziri wa Fedha na hasa TR ayape malengo haya mashirika. Tumeona mashirika kama NMB ilikuwa imefilisika, lakini leo kwa ajili ya utendaji mzuri wa management inailetea Serikali dividend kubwa, CRDB inafanya vizuri, nina imani nayo tumepata dividend kutoka CRDB. Kwa hiyo, hilo ni muhimu sana.

Mheshimiwa Spika, lingine ni ulipaji wa madeni. walimu hawajalipwa stahiki zao. Jimboni kwangu kuna walimu karibu 1,000 wanadai toka mwaka 2017 shilingi milioni 482. Tunashindwa nini kuwalipa walimu? Wako frustrated, muda mwingi wanakuja kufuatilia hela zao Dodoma. Sasa unaangalia, hela anayofuatilia Dodoma ni kidogo sana.

Mheshimiwa Spika, je, nauli tu ya kwenda na kurudi watajikuta ya kwamba hata hiyo shilingi milioni 482, nayo imepotelea kwenye nauli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho, ushauri wangu kwa shilingi milioni 50, hizi ni mfuko wa kuzunguka. Mfuko wa kuzunguka maana yake siyo matumizi. Tumeona jana Mheshimiwa Rais amefanya uamuzi mzuri sana wa kushauri tuimarishe Benki ya Wakulima. Ni kwa nini tusiitumie Benki ya Wakulima ikapewa hizi pesa? Siyo lazima iwe mtaji, wawekewe tu hizo shilingi milioni 50 kwa vijiji vyetu, hasa kwa kuanzia ili wao wasimamie, kwa sababu tuna imani Benki ndiyo wataalam wa kukopesha na wataalam wa kutumi vizuri mifuko kama hii.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ushauri wangu kwa Wizara ya Fedha na kwa kweli ipo kwenye Ilani, tukishindwa hili, hata kuitengea Benki ya Wakulima ikawasaidie wakulima huko vijijini, shilingi milioni 50 kwa kila kijiji ili vijana wafanye ufugaji...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mawaziri na viongozi wote wa Wizara ya Katiba na Sheria, kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Spika, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Waziri wa Katiba na Sheria, kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha kuwa mhimili wa Mahakama ni chombo kikuu cha kusimamia utolewaji wa haki nchini. Chombo hiki ni muhimu sana katika ustawi wa jamii na maendelo endelevu, na hii ni mojawapo ya nguzo kuu katika utayari wetu wa Ushindani wa Kimataifa (National Competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha Ofisi ya Mahakama imefanikiwa kuboresha mifumo ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) ikiwemo mfumo wa usimamazi wa mashauri na kupelekea kuongeza tija katika utatuzi wa mashauri ikiwemo yaliyodumu kwa kipindi kirefu. Ofisi ya Mahakama imeendelea kutekeleza mpango wa ujenzi na ukarabati wa majengo ya mahakama katika ngazi mbalimbali nchini ikiwemo jengo la Makao Makuu Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa majukumu yake, Ofisi ya Mahakama inaendelea kukabiliwa na upungufu wa watumishi wa kada mbalimbali na pia uchakavu wa majengo ya Mahakama za ngazi zote. Kama ilivyoshauriwa kwenye taarifa ya Kamati ya Bajeti, kuna haja kwa Ofisi ya Mahakama kuongeza watumishi katika mahakama zote nchini ili kuongeza tija na ufanisi. Pia napendekeza Serikali kuhakikisha inatenga fedha za maendeleo za kutosha ili kuendeleza ujenzi na ukarabati Mahakama za Mwanzo, Mahakama za Wilaya, Mahakama kuu pamoja na nyumba za Majaji ili kuboresha na kusogeza huduma hii muhimu kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Mbeya bado ina changamoto za uhaba wa Mahakama za Mwanzo na inapelekea wananchi kusafiri umbali mrefu kupata huduma ya Mahakama ya Mwanzo. Mji Mdogo wa Mbalizi wenye idadi ya watu zaidi ya 100,000, ina Mahakama ya Mwanzo ambayo ni ndogo sana na chakavu ambayo ni hatarishi kwa usalama na afya ya watumishi na hata wananchi kwa ujumla. Napendekeza Serikali ijenge Mahakama ya Mwanzo katika eneo la Utengule Usongwe ambalo limetolewa na wananchi. Pia naomba kuwepo na kipaumbele cha ujenzi wa Mahakama za Mwanzo angalau mbili kwa kila Tarafa za Usongwe, Isangati na Tembela.

Mheshimiwa, Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa hii nafasi ya kuchangia katika hii Wizara yetu muhimu ya Fedha. Nianze kwa kuipongeza Wizara, Waziri mwenyewe, Naibu Waziri, lakini pamoja na Wataalam wote, wanafanya kazi vizuri sana. Pia napenda niipongeze Serikali kwa ujumla kwa niaba ya wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ambalo ndiyo Jimbo la Mbeya Vijijini, kwa kweli utekelezaji wa bajeti iliyopita ilikuwa nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye afya pamoja na kutengewa bilioni moja na nusu kwa ajili hospitali ya Wilaya lakini tuna vituo vya afya vitatu vinavyoendelea na tuko kwenye hatua ya umaliziaji sasa hili. Kuna Kituo cha Afya cha Ilembo, Santilia pamoja na Ikukwa. Tuko vizuri na tunaendelea vizuri tunategemea nafikiri kama kwa kazi hii Serikali itaendelea kutupa pesa zaidi kwa ajili ya kumalizia zaidi ya vituo 50 vya zahanati zetu ambazo ziko katika hatua nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye barabara nako Serikali kwa kweli imefanya vizuri kwenye Halmashauri yangu. Kuna barabara nyingi ambazo zimejengwa pamoja na jiografia yetu ambayo ina changamoto nyingi, lakini tunaishukuru Serikali kwa sababu mpaka sasa hivi kuna utekelezaji wa barabara za lami za kilomita 27 ambazo zimetoka kwenye barabara tulikuwa na barabara zenye kilomita mbili tu, sasa kuongezewa mpaka 27 kwa kweli inabidi tuishukuru Serikali. Pamoja na hiyo tuna kilomita kama 47 ambazo ni za barabara ya mchepuko. Tunaiomba sasa Serikali ikamilishe hizo barabara kwa haraka mno kwa sababu zinapita maeneo muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye umeme Serikali imefanya vizuri kwenye Halmashauri yangu, kwenye elimu nayo tunashukuru sana tumepewa pesa kwa ajili ya miundombinu ya shule za msingi na shule za sekondari naishukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye maji napenda nimshukuru kwa kipekee Waziri wa Maji amefanya kazi kubwa sana. Tulikuwa na changamoto za utekelezaji lakini mpaka sasa hivi kuna miradi mingi ya maji ambayo inaendelea. Kwenye Mji Mdogo wa Mbalizi sasa hivi tumeunganishwa na Jiji, kwa hiyo tuna uhakika wa kupata maji namwomba Waziri ahakikishe kuwa asije akatuangusha. Sasa hivi tunaenda kiangazi tuhakikishe maji yanamwagika Mbalizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kwenye mradi wa Mbawi Jojo, mradi wa Haporoto Itimu, Haporoto Idimi, Izumbwe Iwindi, Horongo Itimu Mwampalala, Shongo, Igale, Swaya na Rupeta pamoja na Mshewe Muvwa, Njelenje Mapogoro na Mjele. Hii ni miradi muhimu namwomba sana Mheshimiwa Waziri aikamilishe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija kwenye bajeti ya mwaka huu, wenzangu wameongelea sana kipaumbele ukiangalia namba moja ni kilimo. Ukiangalia Serikali imetenga kiasi gani kwenye kilimo huwezi kuziona. Nilikuwa najaribu kuangalia bajeti ya Kenya kwa sababu katika vitu vingine hivi lazima tujilinganishe linganishe. Wenzetu wa Kenya wamefanya nini? Wana vipaumbele vinne katika kipaumbele kimojawapo ni hifadhi ya chakula hawajaita kilimo. Wametenga nini kwenye hifadhi ya chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia dash board ya bajeti ya Kenya. Kwenye kilimo hifadhi ya chakula (food reserve) wametenga bilioni 32; kwenye nafaka wametenga bilioni 43; kwenye nafaka tena wametenga bilioni 20; kwenye umwagiliaji wametenga bilioni 192; na kwenye subsidy ya mbolea wametenga bilioni 97. Kwa jumla kwenye kilimo wametenga bilioni 409. Sasa hizo ukiangalia kwenye bajeti ya Waziri huwezi kuziona mara moja zimefichwa wapi. Tungeomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja ili wananchi wajue ni namna gani wakulima tunawajali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo kinaenda pamoja na miundombinu. Tuna tatizo sana la usafirishaji wa mbolea.

Leo hii kupeleka mbolea Mbeya kwa tani ni Sh.90,000 mpaka Sh.120,000. TAZARA quotation yao ni laki moja na ishirini kwa tani, lakini barabara ni elfu tisini kwa tani. Sasa unajaribu kuangalia kwa nini kuna tatizo hili. Ukija kwenye Reli ya Kati mpaka Tabora ni elfu sabini lakini kwa barabara ni zaidi ya laki moja na ishirini. Ningeomba sana Serikali ingechukua jukumu ni namna gani tuiboreshe TAZARA ili tuweze kuwakomboa wakulima. Tukipunguza bei ya mbolea tutakuwa tunamsaidia mkulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nafikiri limeongelewa kwa kiasi kikubwa na wenzangu waliotangulia ni suala la hii akaunti ya Treasury Single Account. Ningependa kupendekeza kwa Serikali ingeangalia kwa uangalifu sana, hizi hatua inazozichukua wakati mwingine zinaweza kutupeleka mahali pabaya. Kwa sababu ukichukua pesa zote za Halmashauri benki ambazo zimefungua matawi zitabakiwa na nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, iangalie NMB, CRDB, na NBC, pesa nyingi ambazo wanazo kwenye Halmashauri zetu kule, kwenye Wilaya zetu ni pesa za Serikali. Ukizikusanya zote hizi unazipeleka Benki Kuu na Benki Kuu ni kwa ajili shughuli za benki siyo retail banking. Shughuli za Benki Kuu ni Benki kwa Serikali na Benki wa Mabenki, hata wenzetu waliochukua hatua za kufungua hii Treasury Single Account hawakwenda kwenye Halmashauri, kwa sababu imegundulika kuwa katika hizo nchi kulikuwa na abuse kubwa sana, kulikuwa na ubadhirifu mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nia na madhumuni ya hii Tresuary Single Account ni kwa ajili ya ukwasi liquidity, cash management siyo kwa ajili ya financial control, kwa sababu huwezi ukahamisha responsibility za Maafisa Masuuli kuzipeleka kwa Waziri wa Fedha. Hii Wizara watashindwa kui-manage. Waziri ali-make reference nyingi tu, ningependa vilevile aende kumsoma mtu mmoja anaitwa … (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia. Kwanza nianze kwa pongezi za dhati kabisa, napenda kumpongeza kwa dhati kabisa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa kazi kubwa aliyoifanya hasa kwenye jimbo langu. Ameleta mageuzi makubwa sana kwenye sekta karibu zote, kwenye miundombinu, maji na pia sasa hivi hata kwenye kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kumpongeza Mheshimiwa Jafo, Waziri wa TAMISEMI na Mheshimiwa Kakunda na Mheshimiwa Kandege Naibu Mawaziri, wamefanya kazi kubwa sana na kweli kazi imeonekana. Wananchi wa Jimbo la Mbeya Vijijini wamenituma nizilete pongezi zenu hizo pamoja na wataalam wenu katika Wizara zenu ikiwemo na Wizara ya Utumishi wamefanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazitoa hizo pongezi kwa sababu moja tu. Jimbo la Mbeya Vijijini tunategemea sana kilimo lakini tulikuwa hatuna barabara kabisa huko vijijini, mazao tulikuwa tunashindwa kuleta mjini. Leo hii tuna kilomita za mtandao kama 1,007, tulikuwa hatuna barabara kabisa za kuaminika. Tulikuwa na kilomita moja tu ya barabara ya lami ukiachilia mbali zile barabara za TANROAD kwa barabara yetu ya TANZAM ya kutoka Dar es Salaam kwenda Zambia. Hivi navyozungumza kutokana na jitihada alizofanya Mheshimiwa Jafo na timu yake pamoja na matunda mazuri ya ziara yake, leo hii kuna maandalizi ya kilomita 37 ambazo zitajengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hizo kilomita 37 lakini leo hii kuna design ya kilomita 126 ambazo nazo tunategemea zitajengwa kwa kiwango cha juu. Kwa vile pesa zipo wakimaliza design tu hizi barabara zitatangazwa na wananchi wameshaliona hilo kwa sababu wameshaziona survey zinazofanyika, kwa kweli kazi ni nzuri na timu ya TARURA tuliyonayo ya Country Manager wa Mbeya Vijijini ni kijana mzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamwomba Mheshimiwa Jafo huyu kijana anachohitaji pale ni motisha, hana gari. Utatembelea vipi mtandao wa kilomita zaidi ya 1,000 wakati huna usafiri? Vilevile ukiangalia hii kazi iliyoko mbele yake kilomita 163 ata-supervise namna gani akiwa hana usafiri?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na barabara hizo, tunaomba vilevile wenzetu wa TANROAD kuna barabara ya mchepuko ambayo inaingiliana na hizi barabara waweze kuimalizia. Kwa hiyo, itategemea ni kiasi gani watafanya haraka kuijenga ile barabara ya kuanzia Mlima Nyoka kuja mpaka Songwe ili ziende pamoja kwa vile kiuchumi hizi barabara ni muhimu sana na ndiyo zitatuongezea mileage sana kwa ajili ya ushindani na nchi jirani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hizi barabara naomba waangalie ni namna gani wataipandisha hadhi barabara ya kuanzia Mbalizi kwenda Shigamba mpaka Isongole. Hii barabara Mheshimiwa Mbena asubuhi alipiga magoti, ni barabara muhimu sana kiuchumi kwa vile hizi barabara ndiyo zinakuja kutuunganisha sisi Tanzania na majirani zetu wa Zambia. Kwa hiyo, tumeomba hizi kilomita 96 za hii barabara, wenzetu wa TANROAD wafanye mchakato wazipe bajeti za upendeleo kabisa ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hizi barabara, Mbeya sisi pale tuko kimkakati, biashara ya bandari inategemea zaidi nchi za Zambia, Congo, Malawi na kwa kiasi fulani Zimbabwe. Bila kuboresha TAZARA na bila kuwa na bandari kavu pale Mbeya biashara yetu ya bandari hasa kwa nchi za nje kwa kweli itapata mtikisiko sana. Nilizungumzia juzi ni namna gani wenzetu Msumbiji wamejiandaa kuchukua soko hilo, wameshaanza ujenzi tayari wa reli na wanaboresha bandari yao ya Nakao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipofanya haraka na wenzetu wa Wizara ya Miundombinu wasipochukua uamuzi wa haraka kwa sababu eneo limeshatolewa, wananchi wameshatangaziwa bila kujenga bandari kavu pale soko lote kwa ajili ya hizo nchi litachukuliwa na wenzetu wa Msumbiji. Pamoja na hilo, naiomba Serikali iangalie namna gani itajenga reli ya kuanzia Mbeya mpaka Ziwa Nyasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri ni suala zima la maji. Nililalamika sana hapa kuhusu miradi ya maji lakini leo hii kwa ajili ya ubunifu wake tulikuwa tunadanganywa kuwa hela hazitoki lakini amekuja kutuambia Waziri wa Maji kuwa pesa zipo na leo natoa ushuhuda…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Waziri, Naibu Waziri na viongozi wote kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka wa Wizara ya Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Spika, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi kinachoishia Aprili, 2023 Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani imesimamia kwa uadilifu na ufanisi mkubwa masuala yote ya usalama wa raia hasa kurudisha uwajibikaji kazini iliyopelekea kupungua kwa uhalifu. Pia kwa kusimamia vizuri rushwa na upendeleo umepungua kwa kiasi kikubwa kupelekea wananchi kushiriki kikamilifu shughuli za ujenzi wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio hayo makubwa ya ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Mbalizi kwa kushirikisha wananchi, askari bado wanaendelea kufanya kazi katika mazingira magumu kutokana na kutokuwepo kwa nyumba za askari hasa katika eneo jirani na Kituo cha Polisi. Ni vigumu sana kwa Wilaya yenye askari zaidi ya 150 na inatoa huduma kwa wakazi karibu 500,000. Kunapotokea dharula, viongozi na hata askari inakuwa vigumu kujikusanya kwa muda muafaka. Pia wananchi wameanza ujenzi wa Kituo cha Polisi Daraja C, pia wananchi katika Tarafa zingine wameonesha nia ya kushiriki kujenga vituo vingine katika Miji Midogo ya Ilembo, Isuto na Ikukwa. Kuna uhitaji mkubwa wa kuwepo vituo vya polisi katika maeneo haya kutokana na shughuli za kichumi na pia umbali kutoka makao makuu ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza Serikali ianze mchakato na itenge bajeti ya angalau shilingi milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vipya vya Igoma, Ilembo, Isuto na Ikukwa. Kwa vile wananchi katika baadhi ya kata wameanza ujenzi na wamehamasika kushiriki ujenzi wa vituo vinne vipya vya polisi, bajeti hii inayoombwa ya shilingi milioni 300 kwa kila kituo itachochea kumaliza ujenzi wa maeneo muhimu ya vituo hivi na kuwezesha motisha na ufanisi kwa askari. Pia napendekeza kuongeza magari kwa ajili ya usafiri hasa ukizingatia jiografia ya Wilaya ya Kipolisi ya Mbalizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi nzuri sana ikiwa ni pamoja na miongozo ambayo imetoa dira katika kuboresha utendaji Serikalini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kumpongeza Mheshimiwa Seleman Jafo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, na Mheshimiwa Joseph Kakunda na Mheshimiwa Josephat Kandege, Naibu Mawaziri, TAMISEMI pamoja na Watendaji wote wa TAMISEMI kwa kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ziara za Waziri alipotembelea Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya alishuhudia changamoto za mtandao wa barabara ambazo kwa kiasi kikubwa hazipitiki kipindi chote. Pia alishuhudia daraja la Mto Idiwili katika Kata ya Isuto ambalo lilijengwa chini ya kiwango kupelekea kuvunjika mpaka leo hakuna mawasiliano ya hiyo barabara ambayo ni muhimu sana kwa uchumi wa Tarafa ya Isangati na Wilaya nzima ya Mbeya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri kupitia TAMISEMI warekebishe hilo daraja la Idiwili, pia barabara nyingi ziko katika hali mbaya sana ikiwemo barabara ya Mjele – Ikukwa, Ilembo – Mwala na Daraja la Izyira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na ufinyu wa bajeti ya TARURA, napendekeza uongezwe mgao kutoka mfuko wa barabara kutoka asilimia 30 na kuwa asilimia 50.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara ikamilishe ahadi ya Rais ya kumalizia ujenzi wa stendi ya Mbalizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu miradi ya maji haikukamilika kutokana na usimamizi usioridhisha ikiwemo ubadhirifu. Napenda kupongeza ziara za Mheshimiwa Kakunda, Naibu Waziri wa TAMISEMI na pia Mheshimiwa Waziri wa Maji na Naibu Waziri wa Maji, ziara zao zimeleta tija kubwa na sasa miradi ya maji imeanza kutekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza Wizara ikamilishe kuunganisha Mamlaka ya Maji Jiji la Mbeya na Mamlaka ya Maji Mji Mdogo wa Mbalizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza pia Wizara iweke mkakati wa kupeleka maji katika vituo vya afya, zahanati na shule zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru Serikali na kwa kipekee Wizara ya TAMISEMI kwa ujenzi wa Vituo vya Afya vya Ikukwa, Sautilya na Ilembo. Pia napenda kushukuru kwa kutenga bajeti ya shilingi bilioni 1.5, kwa ajili ya hospitali ya Wilaya ya Mbeya DC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuomba Serikali kuunga mkono ujenzi wa zahanati zaidi ya 40 na Vituo vya Afya vya Kata ya Ilungu na Isuto ambavyo wananchi wamejenga kwa nguvu zao na vipo katika hatua mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza Wizara iweke mkakati wa ujenzi wa mabweni katika shule za kata. Kipekee kuna ujenzi kwa nguvu ya wananchi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Galijembe na Sasyaka (Masoko), ambazo kwa sasa napendekeza Wizara iunge mkono nguvu ya wananchi kumalizia shule hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza Wizara iweke mkakati wa haraka, wa mpango miji kwa Mji wa Mbalizi na Miji Mdogo inayokuwa kwa haraka kama vile, Inyala, Ilembo, Isuto, Igoma na Songwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza Serikali iridhie/ maombi ya Halmashauri ya Mbeya DC ya kubadili matumizi ya shamba ya iliyokuwa Tanganyika Packers ili litumike katika kupanga Mji Mdogo wa Mbalizi, ikiwemo maeneo ya ujenzi wa viwanda, hospitali, mashule na makazi ya wananchi na halmashauri imetenga eneo mbadala katika Kijiji cha Mjele kubadilishana na eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, inajenga machinjio ya kisasa kwa soko la ndani na nje ya nchi na vifaa vimetolewa na UNIDO. Kwa sasa kunahitajika bajeti ya Serikali kumaliza ujenzi wa kiwanda hiki cha nyama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Mbeya Vijijini lina ukubwa wa kilomita za mraba 2,432, tarafa tatu na vijiji 152, lakini Tarafa ya Tembela haiungani na tarafa zingine na utokana na idadi kubwa ya wananchi, Serikali ya Mkoa (RCC) waliomba kugawanywa kwa jimbo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza Serikali iridhie kugawa Jimbo la Mbeya Vijijini na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mawaziri na viongozi wote wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Spika, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Serikali katika utekelezaji wa ustawi wa jamii na maendelo endelevu, na hii ni mojawapo ya nguzo kuu katika utayari wetu wa Ushindani wa Kimataifa (National Competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ya kuimarisha mahusiano ya kimataifa, na pia kwa mafanikio makubwa ya Royal Tour ambayo imeanza kuleta matunda makubwa ya kiuchumi kwa nchi yetu hususani sekta ya kitalii na uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza Serikali kuimarisha diplomasia ya uchumi kwa lengo la kuongeza uwekezaji toka nje (FDIs), masoko ya uhakika kwa mazao ya kilimo, madini na utalii, pamoja na kuongeza mapato kwa Taifa letu, itaisaidia kuongeza fedha za kigeni na kuimarisha uchumi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kutoa mchango wangu katika Wizara hii muhimu, Wizara ya Madini. Ni kweli hii Wizara ndiyo inayosimamia rasilimali zetu muhimu sana ambazo Mwenyezi Mungu ametupatia sisi kama Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuwapongeza Waziri mwenyewe na Naibu wake wawili wanafanya kazi nzuri sana. Pia nimpongeze Katibu Mkuu na uongozi mzima wa Wizara. Hawa watu nimeshuhudia mwenyewe wanafanya kazi long hours. Walinipa appointment na mkutano na wao saa 2.00, nikauliza saa 2.00 ya asubuhi wakasema hapana ni saa 2.00 usiku. Kweli tumefanya mkutano saa 2.00 usiku mpaka midnight. Nilipotoka nikawauliza walinzi hivi hawa ndiyo style yao ya kufanya kazi wakasema ndiyo na tunategemea watatoka saa mbili baadaye. Kwa kweli hiyo ni ishara nzuri, hii Wizara ni mpya, ina mambo mengi mageni, inahitaji watu wenye moyo wa aina hii, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia hata kwenye matokeo ya Wizara, tulitegemea wangekusanya kama shilingi bilioni 194 lakini kwa miezi tisa wamekusanya shilingi bilioni 225, hilo ni ongezeko kubwa sana. Kwa miezi tisa kama ni shilingi bilioni 225, nina imani kwa mwaka mzima kama makusanyo yanaendelea evenly kwa miezi itakuwa ni shilingi bilioni 300. Hili ni ongezeko kubwa ambalo ni karibu asilimia 54, kwa kweli huu ni utendaji mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na Kamati uchambuzi wao ni mzuri sana, umesema matokeo mazuri haya yametokana kwanza na udhibiti wa utoroshaji wa madini, pia ongezeko la mrabaha na kuna 1% ya makusanyo ambayo hiyo ni kodi mpya. Nafikiri imetuletea matokeo mazuri na mimi nafikiri tukijikita katika haya machache tu, kwa vile haya ndiyo yatakuwa makusanyo yenye uhakika kwa muda mrefu yatatuletea sustainable growth kwa muda mrefu kuliko yale one off ambayo labda tunategemea tutapata makusanyo kiasi hiki hayatatusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nikubaliane na maoni ya Kamati. Kwa muda mrefu tumeona utendaji wa STAMICO si mzuri. Mimi ningeomba sana Serikali katika hizi Wizara ingeangalia majukumu yao ya kimsingi, yale ambayo ni operational wayaache. STAMICO sasa hivi inapata hasara kubwa sana, madeni ya shilingi bilioni 60 na sijaangalia balance sheet yao huko inaonesha ina shimo la kiasi gani. Sasa ukiwa na hali ya namna hiyo huna haja ya kuyalea mashirika ya aina hii. Zile shilingi bilioni 8.6 ambazo wametengewa na Wizara nafikiri Wizara ingeangalia kupeleka mahali pazuri zaidi ambapo kutaisaidia Wizara kuongeza mapato na maduhuli ya shirika hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama walivyo-recommend Kamati, nafikiri hiyo migodi ambayo ilikuwa inaendeshwa na STAMICO wapewe Watanzania wazawa, wachimbaji wadogo wadogo na wachimbaji wa kati. Nina imani kuwa Serikali itapata mapato makubwa kupitia kwa hawa kuliko tukitegemea kuendelea na STAMICO. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba kuikumbusha Wizara tu, nafikiri ilikuwa ni overlook. Kuna mgodi wa Niobium kule Mbeya unaitwa Panda Hill Niobium Project. Mgodi huu thamani yake ni dola kama bilioni 6.8, project nzima na tunategemea Serikali kama ukianza utaleta kodi kama ya dola bilioni 1.4 ambazo nafikiri ni pesa nyingi mno.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nimelisema hilo? Ni kwa sababu huu mgodi si wa leo ni wa siku nyingi, uligunduliwa mwaka 1953. Hii kampuni mpya imepewa license ya mgodi huu mwaka 2013 na wameshawekeza zaidi ya dola milioni 28 sasa hivi walikuwa wanajipanga kuanza. Huu mgodi ni muhimu kwa Tanzania lakini ni mgodi pekee Afrika wa Niobium, migodi ya aina hii iko mitatu duniani; migodi miwili iko Brazil na mgodi mmoja Canada. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika biashara ya madini hatuko peke yetu inategemea speed ya kuingia sokoni. Nina imani huu mgodi ukianza haraka utailetea Serikali pesa nyingi sana. Dola bilioni 1.2 si ndogo, ni nyingi, zikiongezwa kwenye mfuko wa Serikali, nafikiri itaipunguzia mzigo hata Wizara ya Fedha tunapolia maji kuna hela huku zimebaki. Kwa hiyo, naiomba Wizara iharakishe process, kwanza ukiangalia Wizara ni mpya hii inaweza kuwa project kubwa ya kwanza ya madini kwa mwaka huu ukiachilia mbali za miaka mingi za dhahabu, almasi na tanzanite.

Mheshimiwa Naibu Spika, orodha ya madini ambayo nimeikuta pale nje kwenye maonesho ni kubwa mno, ni namna gani twende haraka sokoni. Madini vilevile yanaendana na teknolojia. Tusubiria dhahabu na tanzanite lakini teknolojia iki-change unaweza kukuta yakabaki kama mawe tu tunayoangalia huko nje milimani. Kwa hiyo, naiomba sana Wizara ijitahidi kufanya haraka ili hizi rasilimali zetu tuzitumie vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mawaziri na viongozi wote wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Serikali katika kuendeleza ulinzi na usalama wa Taifa letu, na hii ni mojawapo ya nguzo kuu katika utayari wetu wa ushindani wa kimataifa (national competitiveness).

Mheshimiwa Spika, ulinzi na usalama ni mojawapo ya nguzo kuu katika kuongeza imani kwa wawekezaji hasa wa kutoka nje (FDI). Bajeti hii inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni “kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu.”

Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio makubwa ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, bado kuna wapiganaji wetu ambao ni wastaafu na wengine walishiriki kwenye vita kwa kulinda mipaka yetu hususani vita ya Kagera, wanalalamikia stahiki zao kutolipwa kikamilifu. Kwa kuzingatia kuwa wamefanya kazi kwa uzalendo mkubwa na iwe motisha kwa askari wetu wote kwenye majeshi yetu yote, napendekeza Serikali iangalie jinsi ya kutatua changamoto hii na kuangalia upya stahiki zao ikiwemo kuboresha mafao ya pensheni zao.

Mheshimiwa Spika, napendekeza Wizara ya Ulinzi kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu kuangalia jinsi ya elimu ya ulinzi na usalama kuunganishwa kwenye mitaala ya elimu. Pia Serikali iendelee kuboresha mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa ikiwemo mafunzo ya uzalendo na ujasiriamali. Kutokana na mafaniko makubwa huku nyuma ya mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria, Serikali irudishe utaratibu wa mafunzo hayo kwa miezi kumi na mbili na mafunzo haya yawe maandalizi ya kuwajenga vijana kwenye uzalendo na ulinzi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii adimu ili na mimi niweze kuchangia na kutoa maoni kwenye Mpango wetu wa Maendeleo kwa mwaka kesho 2019/2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Waziri na timu yake yote. Kwa kweli huu mpango ni mzuri sana, umeangalia vipaumbele vyote muhimu na umetengenezwa kitaalam sana kiasi ambacho hata ukiangalia na maoni ya Kamati nayo yamefanya kazi nzuri sana, yameuchambua vizuri na maoni yake yote naomba niyachukue na mimi labda niongezee pale tu ambapo hayakugusa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika huu mpango wetu ukiangalia vilevile unaangalia tulikotokea, tumefanya nini katika miundombinu, katika kilimo, uvuvi, elimu na kadhalika. Na ukiangalia mwenendo trend inaonesha tumefanya vizuri katika sehemu nyingi, zinaridhisha. Na kwa kujikumbusha tu kwamba bajeti haina maana ya kwamba umepewa license ya kutumia, hapana, ni matarajio, ni mategemeo. Kwa hiyo, kwa kiasi pale ambapo tumefanya vizuri mimi nilikuwa namuomba Waziri aangalie ni namna gani tuweze kuboresha huko nyuma wakati tunaangalia na mipango ya vipaumbele vya sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukifanya vizuri sana katika uboreshaji wa bandari, ununuzi wa ndege na ujenzi wa reli. Tumefanya vizuri katika hayo maeneo, lakini mimi naomba tu nipendekeze, kwa sababu kwa Bandari yetu ya Dar es Salaam tu sasa hivi ina ushindani mkubwa sana kutoka kwa majirani zetu, ukanda wa kusini, nchi kama Angola, Namibia na Msumbiji. Hizo nchi zimelilenga soko letu na zimelilenga soko la Bandari ya Dar es Salaam. Sasa je, sisi tumejipanga vipi kupambana na hilo? Kwa sababu huwezi kuzuia watu wasikuingilie kwenye soko lako, wewe ndio unatakiwa ujipange namna ya kujiimarisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa maboresho niliyokuwa napendekeza mimi kwa sababu hili soko bado tunalihitaji sana pamoja na utengenezaji na ujenzi wa standard gauge lakini soko la nchi za DRC, Zambia na Malawi ni soko muhimu sana kwa Bandari yetu ya Dar es Salaam na kwa uchumi wa nchi yetu. Sasa wenzetu wamefanya nini, wamejenga reli ya kutoka Lobito Port, Angola kuja kwenye nchi za DRC na wanazipeleka mpaka kwenye machimbo, reli ambazo ni za kisasa ni standard gauge ambazo zinaweza kuchukua mzigo mkubwa sana na hizo reli vilevile zinalenga kuziunganisha Bandari za Msumbuji lakini na kwa kiasi fulani wanalenga vilevile na kuiunganisha na Bandari yetu ya Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa angalia nia yao nini hawa; wamepunguza gharama zao kwa kiasi kikubwa, gharama zimekuwa ndogo kiasi wafanyabiashara wote sasa hivi wanaangalia ni namna gani watumie Bandari ya Lobito ambayo ni kilometa 1,300 tu kutoka DRC ukilinganisha na sisi zinakaribia karibu kilometa 2,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo ya kwangu kwenye mpango wa mwaka kesho, Serikali ilikuwa inafikiria kujenga bandari kavu Mbeya na hiyo bandari kavu ni muhimu kwa vile imekaa mahali kwa kimkakati ambapo inaliangalia soko la Malawi, soko la Zambia na soko la Kongo, lakini kwa miaka miwili sasa hivi Mamlaka ya Bandari haijaruhusiwa kuwalipa fidia wananchi waliotoa maeneo yao kwa ajili ya kujenga bandari kavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wenzetu malengo yao ni kujenga bandari kavu nyingi kwenye nchi za Namibia – kuna sehemu inaitwa Walvis Bay, Namibia, lakini vilevile na Angola nako wanajenga bandari kavu, ukija Msumbiji nao wamejiimarisha, nao wamejenga reli kutoka kwenye bandari ambayo ni kubwa namba mbili kwa Msumbiji inaitwa Nacala, wamejenga hiyo bandari mpaka nchi ya Malawi na sasa hivi wanalenga kuingia Zambia na wakiishaingia Zambia wanalenga vilevile iende mpaka DRC, sasa ukiangalia sisi tutabaki na nini tusipokwenda kishindani zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba katika huu mpango nimeona kwamba kuna jitihada za kuboresha TAZARA ambazo ni jitihada nzuri, zitasaidia, lakini mkazo uwe hapo; hatutatumia pesa nyingi sana lakini ukiweza kwenda pamoja ku-improve ile mipango ambayo wameshaitekeleza inasaidia vilevile hata kutekeleza mipango inayokuja ya mwakani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la umeme tumefanya vizuri sana, REA inakwenda vizuri na pesa nyingi ambazo kwa kiasi kikubwa ni za ndani zimefanya kazi nzuri sana. Sasa je, katika mpango wetu tutaboresha vipi hii mipango ya umeme vijijini iwe endelevu? Sasa huioni moja kwa moja kama iko kwenye hii mipango kwa sababu bila hivyo kama hakutakuwa na mipango ya kuifanya hii mipango yetu utekelezaji wetu unakuwa endelevu tutakuwa tunapoteza hela bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naangalia kwa hizi pesa nyingi tulizotumia, je, zimeigia katika Mfuko wa TANESCO kama capital? Na kama imeingia capital mbona inaonekana ni hela nyingi sana, je, zinaisadia vipi TANESCO kupata faida?

Sasa wakati Waziri anaangalia namna ya kuboresha mapato ya ndani aangalie ni namna gani wakati hizi pesa nyingi tunaweza kwa wakati mwingine tunasahau kwamba pesa zote ambazo tumezitumia kwenye ujenzi wa umeme vijijini (REA) zimehamishiwa TANESCO kama kuziongezea mtaji, je, ule mtaji unatuzalishia kiasi gani? Je, tunaiona hiyo? Ukiangalia vijiji vingi sana sasa hivi vimeongeza wateja kwa TANESCO, je, tuione wapi hiyo faida ya investments ambazo tumeziweka kwenye umeme? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kwenye maji vilevile pesa nyingi sana tumezitenga kwa ajili ya miradi ya maji lakini ukirudi nyuma kuangalia ufanisi wa miradi ya maji huwezi kuiona kwa sababu nayo hatukujiwekea mipango endelevu ya hii miradi ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa hii fursa nami nichangie katika bajeti muhimu Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa kasi kubwa anayoifanya kuhakikisha kuwa Serikali yetu inaendeshwa na kuleta ufanisi katika maeneo yote ili uwepo ufanisi katika kuwaletea wananchi maendeleo ya kiuchumi na pia ya kijamii. Napenda pia kuwapongeza Mawaziri wote na watendaji wote wa Wizara hii na bila kusahau kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuleta transformation (mageuzi) makubwa kwa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ajili ya muda labda napenda niorodheshe machache tu aliyofanya nikianzia kwenye Jimbo langu. Kwenye suala la umeme tulikuwa na vijiji 10 tu mwaka 2015 lakini leo tuna asilimia karibu 80 ya vijiji vinavyokaribia 200. Angalia ni mafanikio ya aina gani ambayo yamepatikana katika kipindi hiki kifupi. Pia tunategemea hizi kata mbili zilizobaki nazo zitakamilishwa ndani ya miaka hii miwili. Tunashukuru sana kwa utendaji wa Wizara na Mheshimiwa Rais kwa maagizo yake yeye mwenyewe ambayo yametufanya Mbeya Vijiji tukafanya vizuri kwenye nishati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la afya. Katika Wilaya yetu ya Mbeya tulikuwa hatuna Hospitali ya Wilaya na katika Miji mikubwa kama Mbalizi tulikuwa hatuna hata kituo cha afya lakini katika kipindi hiki cha miaka mitatu tumeweza kufanikiwa kujenga vituo vya kisasa vitatu katika Kata za Ilembo, Ikukwa na Santilia. Kwa kuongezea, tumepata na pesa kwa ajili ya kujenga Hospitali ya Wilaya. Tunaishukuru sana Serikali, kwa kweli hayo ni mageuzi makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo tuishukuru vilevile Serikali kwa kuweza kuifikiria Mbeya Vijijini kutuletea Chuo Kikuu cha Afya. Chuo hiki kitakuwa sehemu ya Chuo Kikuu cha Muhimbili ambacho nategemea katika mikakati kitaanza kufanya kazi hivi karibuni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la elimu nalo tumefanya vizuri sana, imeirudisha Mbeya katika zile nafasi zake muhimu. Kwa mwaka huu Mbeya iko kwenye nafasi 10 bora na kitaaluma maeneo yote tumefanya vizuri mno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye jimbo langu tumeweza kuongeza shule tatu za sekondari na shule moja ya high school. Katika hizo shule tatu, tuna shule ya wasichana ya bweni ambayo imejengwa na wananchi lakini tumepata msaada kidogo wa Serikali. Kwa hiyo, tunaishukuru sana Serikali kwa hilo na tunategemea waendelee tena kuipa msukumo elimu kwa vile ndiyo msingi wa maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye miundombinu Serikali imetufanyia mengi mazuri ikiwemo barabara lakini bado tuna changamoto kubwa kwenye barabara zetu za Mbeya Vijijini. Kama alivyosema mwenzangu aliyotangulia tuna tatizo la TARURA. TARURA wanafanya kazi vizuri lakini bajeti yao ni ndogo. Bajeti ya matengenezo ya dharura hakuna, sasa kwa maeneo ya mvua nyingi kama Mbeya Vijijini wanatengeneza barabara leo, madaraja yote unakuta yameondolewa na mafuriko, hawana namna ya kutusaidia. Tunaiomba Serikali iangalie namna gani itaboresha bajeti ya TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la maji, Wizara ya Maji pamoja na Serikali kwa ujumla wamefanya kazi kubwa kwa Halmashauri yetu ya Wilaya ya Mbeya. Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri wamekuja wao na wameweza kusukuma na tumekamilisha miradi ya vijiji karibu zaidi ya 10. Tumekamilisha miradi ya Mbawi, Jojo, Haporoto na Idimi na sasa hivi tunakamilisha vijiji kwenye Kata za Igale na Izumbwe lakini bado tunahitaji maboresho kwenye Mji Mdogo wa Mbalizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la kilimo ambacho ndiyo msingi wa kila kitu, kwa kweli pamoja na juhudi za wananchi lakini bado tuna changamoto kubwa za masoko. Naiomba Serikali ijaribu kuangalia ni namna gani itaboreshe masoko ya mazao yetu. Kwenye kahawa, pareto na hata mahindi hatufanyi vizuri. Pamoja na matumizi ya mbolea napo hatuko vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iangalie namna gani tutumie malighafi tulizonazo hapa nchi kwa ajili ya kuanzisha viwanda vya pembejeo. Chokaa inazalishwa sana hapa nchini lakini ni muhimu sana kama sehemu ya pembejeo. Chokaa inasaidia kutibu ardhi kwa vile ina calcium na magnesium ambayo inasaidia ardhi yetu iliyochoka ili mbolea iweze kutumika vizuri. Ukiweza kufanya application ya chokaa udongo utakuwa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la kahawa, juzi tulikuwa na Mkutano wa Wadau wa Kahawa na niishukuru sana Bodi ya Kahawa iliandaa mkutano mzuri sana, tukaangalia changamoto nyingi sana. Kitu ambacho nimekipenda ni mkakati wa kuboresha soko la kahawa ambalo napenda msisitizo uwe kwenye direct export, wananchi waweze kuuza kahawa yao moja kwa moja nje ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile na uanzishwaji wa hiki chombo kipya kinaitwa Tanzania Commodity Exchange Market (TMX) inaweza kutusaidia kutuokoa katika janga kubwa ambapo kahawa yetu ni nzuri lakini bei yake ni ndogo ukilinganisha na wenzetu wa jirani. Kwa mfano tu, kahawa ya Kenya arabica wenzetu katika kipindi hiki wanauza mpaka dola 200 kwa kilo 50 sisi ni chini ya dola 100 pamoja na kahawa yetu kuwa nzuri kuliko yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuna pareto, nashangaa ni kwa nini haijaingizwa katika mazao muhimu ya kimkakati. Tanzania sisi tunaongoza Afrika kwa kulima pareto na ni wa pili duniani. Sasa zao kama hili la kimkakati ni kwa nini limesahauliwa na fursa bado zipo za kuweza kuzalisha pareto nyingi, mahitaji ni zaidi ya tani 20,000 na uzalishaji duniani ni chini ya tani 10,000. Tanzania pamoja na kuwa wa pili na wa kwanza Afrika tunazalisha tani 1,000 tu. Katika zao hili nalo naomba suala la masoko liweze kutiliwa maanani ili wananchi waweze kupata faida ya uzalishaji wa pareto.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Njeza, muda wetu hauko rafiki.

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa hii nafasi ili nami niweze kuchangia bajeti ya Wizara hizi muhimu, bajeti ya TAMISEMI na bajeti ya Utumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kuwapongeza Mawaziri wote wawili pamoja na team zote mbili, kwa kweli wanafanya kazi nzuri sana. Wanafanya kazi nzuri na kwa ushahidi kabisa, kwenye Jimbo langu TAMISEMI wamefanya kazi nzuri sana katika eneo la TARURA, eneo la Afya na eneo la Elimu. Kwa kweli nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda vilevile kumpongeza Mheshimiwa Rais naye kwa kazi nzuri iliyotukuka. Amefanya mageuzi makubwa ya nchi hii, amefanya makubwa mno. Ushahidi ni mkubwa pamoja na miradi ya kimkakati kwenye Jimbo langu, ni mambo mengi ambayo ameyafanya na haijawahi kutokea toka enzi za ukoloni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa suala la TARURA. TARURA chombo chenyewe ni kizuri sana, lakini kuna tatizo kubwa kwamba TARURA haina pesa kabisa. Kwenye Jimbo langu nina mtandao wa barabara usiopungua 1,000. Bajeti tumepewa shilingi bilioni 1.5 ambazo ni kilometa 35 kama sikosei. Kuna madaraja chungu nzima, hayapungui 200. Utamaliza miaka mingapi kukamilisha hiyo kazi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri tungeenda kiuchumi zaidi, tuangalie ni namna gani haya maeneo ambayo ni muhimu yapewe kipaumbele. Unapozungumzia Mbeya Vijijini, unazungumzia kilimo cha nchi hii. Mazao yanatoka kwenye mashamba, lakini hatuna barabara kabisa. Mazao hayawezi kutoka shambani kuja sokoni na vile vile hatuwezi kupeleka pembejeo kwa wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyozungumza hivi leo, barabara ya kuanzia Songwe Viwandani kwenda Jojo haipitiki kwa vile daraja lilikuwa limeshabomoka. Daraja hilo moja linahitaji zaidi ya shilingi milioni 250. Leo ni mwaka wa tatu wananchi wanasumbuka daraja halijajengwa. Pamoja na maombi maalum, inavyoelekea, tatizo katika bajeti, tuangalie ni namna gani TARURA waongezewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara nyingine ya kuanzia Kawetere kwenda Ikukwa, barabara ya Irambo kuja Ihango mpaka Nsonyanga, barabara za Mbonile mpaka Nyarwerwa. Tuna barabara nyingi mno ambazo ni muhimu na za kiuchumi lakini hazimo kabisa hata kwenye mpango wa bajeti. Kama nilivyosema, kwa bajeti ya shilingi bilioni 1.5 utafanya nini kwenye mtandao kilometa 1,000?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali ijaribu kuangalia ni namna gani itatunusuru kwenye barabara? Bila barabara hakuna kilimo, bila barabara hakuna elimu, bila barabara hakuna hata shughuli za afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kuchangia kidogo katika Wizara hizi mbili ni suala la afya. Napenda kwanza kumpongeza Mheshimiwa Rais na Waziri Mheshimiwa Jafo, wamefanya kazi kubwa mno. Halmashauri ya Mbeya tulikuwa hatuna Hospitali ya Wilaya, tulikuwa hatuna vituo vya afya vya kutosha, lakini wametupatia vituo vya afya vitatu; Kituo cha Afya cha Ikukwa, Kituo cha Afya cha Ilembo na Kituo cha Afya cha Santiria. Vituo hivi vimebadilisha kabisa muundo na huduma za afya katika Halmashauri yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tunahitaji mahitaji makubwa zaidi. Wananchi wamejenga zahanati, maboma hayapungui 70 ambayo yanahitaji msukumo na bajeti ya Serikali. Pia kuna vituo vya afya vilivyojengwa kwa nguvu za wananchi; kuna Kituo cha Afya cha Ifupa, wananchi wameshajenga, wametumia karibu shilingi milioni 200. Kwa hiyo, tunaomba tu kama shilingi milioni 200 tuweze kumalizia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Kituo cha Afya cha Isuto, nacho kimefikia hatua nzuri, tuna Kituo cha Afya cha Ihoho, Kituo cha Afya cha Maendeleo na Kata ya Tembela. Hivi viko katika hatua nzuri. Kama ikiwezekana, tunaiomba tena TAMISEMI waangalie ni namna gani kwa upendeleo kabisa hivi vituo vipate bajeti ya ku tosha ili tuweze kuvikamilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la elimu, napo napenda kupongeza tu kwa vile tumefanya vizuri, Serikali kwa kweli imefanya jitihada na wananchi wenyewe nao wamefanya jitihada kiasi cha Halmashauri yangu ya Mbeya kiufaulu tumefanya vizuri sana. Shule zimefanya vizuri na wananchi wameweza kufungua shule tatu ikiwemo moja ya high school na shule moja ya wasichana ambayo ni ya bweni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mahitaji ni mengi. Sasa ukiangalia tuna wanafunzi karibu 70,000, walimu tulionao ni 1,035, angalia gap hiyo. Pamoja na jitihada za wazazi, bado tunahitaji walimu ili waweze kuinua uchumi wa vijana wetu. Kuna shule ambayo ina mwalimu mmoja, inaitwa Ilindi. Hii shule ina wanafunzi karibu 300, mwalimu mmoja. Kimaajabu ile shule imefaulisha watoto na ikapata nafasi nzuri. Kwa mshangao wa kila mtu akauliza, itakuwaje shule ya mwalimu mmoja, madarasa saba ikafaulisha kuliko shule zenye walimu wengi? Tukagundua kumbe hata wazazi nao wanashiriki kwenda darasani kufundisha watoto wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hali kama hii nafikiri siyo nzuri sana. Ili tuweze kushindana na wenzetu, inabidi elimu yetu nayo iwe nzuri, tufanye vizuri katika elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda nichangie kidogo, ni suala la uendelezaji wa miji na mipango miji. Kwa sisi ambao tunazunguka majiji, majiji sasa hivi yamejaa na watu wengi ujenzi unakuja kwenye vijiji vyetu ambavyo havijapimwa. Kwa hiyo, tunaongeza squatters zile ambazo tulizikuta. Sasa hivi squatters zinahamia kwenye Halmashauri ambazo zinaizunguka Jiji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Wizara ijaribu kuangalia iwe na mkakati wa kuhakikisha kuwa vijiji vyote ambavyo vinazunguka majiji, vipimwe, viwe katika mpangilio mzuri na yale maeneo ambayo yapo mijini kama maeneo ya Tanganyika Parkers, haya yagawiwe kwa wananchi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Njeza.

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kupata hii nafasi ya kucahngia hii Wizara muhimu ya miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Eng. Kamwelwe, Manaibu Waziri, Engineer Nditiye na Naibu wake, CPA Kwandikwa kwa kazi nzuri walioyoifanya pamoja na Makatibu wao Wakuu. Kwa kweli wanafanya kazi nzuri, hata ukiangalia hii bajeti waliyopewa nafikiri wanastahili, nasi wachukue maoni yetu waweze kuboresha zaidi sekta hii ambayo ni mtambuka ambayo kwa kiasi kikubwa itatusaidia hata kuboresha kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru vilevile kwa ziara aliyoifanya Mheshimiwa Rais katika Mkoa wetu wa Mbeya na mengi aliyoyazungumzia ni pamoja na miundombinu ya barabara. Napenda kumkumbusha Mheshimiwa Waziri kuwa katika ahadi aliyoifanya siku ile, siku ya mwisho ilikuwa ni ujenzi wa barabara ya Mbalizi - Shigamba mpaka Isongole. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii barabara ni muhimu sana kwa vile inapitia kwenye maeneo ambayo ni ya kilimo cha mazao yanayotuletea pesa za kigeni; kahawa, pareto, viazi na pia kwenye mazao ya mbao. Vile vile hii barabara inatuunganisha na wenzetu wa Malawi na vilevile inapita kwenye bonde la Mto Songwe ambao ni ubia wa Serikali yetu ya Tanzania na Serikali ya Malawi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri aangalie kwani wananchi wanasubiri sana hii ahadi yake ikiwa ni pamoja na barabara ya Isyonje - Kikondo na barabara ya Mbalizi - Chang’ombe kwenda Makongorosi. Hizi ni barabara muhimu sana. Kwa hiyo, nilipenda niliweke hili mwanzoni ili wasije wakajisahau kwa vile hizi ni ahadi za Marais waliotangulia na Rais wetu kasisitiza kwamba hii barabara ijengwe kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda vilevile nichangie reli yetu ya TAZARA. Tunapoangalia ujenzi wa kuimarisha miundombinu ya reli ya nchi hii, naomba Wizara isije ikasahau miundombinu ya TAZARA. Reli ya TAZARA uwezo wake ni wa kubeba mizigo isiyopungua metric tonnes milioni tano, lakini mpaka leo hii nilikuwa naangalia report ya Mheshimiwa Waziri hapa, kwa mwaka 2018 na mwaka 2017 ni wastani wa metric tonnes 150,000 tu. Sasa hii ni chini ya asilimia tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia uwezo wa TAZARA; na hii reli ni ya kimkakati, bila hii reli, mizigo mingi ambayo inakwenda kwenye nchi za Zambia, DRC, Malawi na kwa kiasi fulani nchi ya Zimbabwe, hatutakuwa katika ushindani mzuri. Sasa hivi ushindani mkubwa wa Bandari yetu ya Dar es Salaam ni Bandari za Msumbiji, Bandari za Angola na Bandari za South Africa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naangalia Bandari moja tu ya Msumbiji inaitwa Nakal ambayo wakilinganisha na gharama yake na Bandari yetu ya Dar es Salaam wao wako chini kwa asilimia 40. Sasa bila kuiboresha TAZARA na tukategemea hii mizigo iendelee kupitia kwenye barabara, sisi tutaondoka kwenye hiyo biashata na tutajikuta badala ya ku-create value ya bandari yetu lakini kwa kupitia TAZARA, tutakuwa tunafanya value evaporation. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Hongera sana.

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba vilevile kwa sababu hii reli ni ya ubia kati ya Zambia na Tanzania, inaelekea wenzetu wa Zambia hawana tena umuhimu na hii reli. Nguvu wamezipeleka kwenye hizo nchi nyingine nilizozitaja na wanaona kuna manufaa zaidi ya kutumia hizo bandari nyingine kuliko hii reli yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri Wizara na Serikali iangalie ni namna gani kuangalia upya huo mkataba tulionao kwa sababu hadi leo tunashindwa hata kuchukua pesa ambazo Serikali ya China iko tayari kutukopesha. Kwenye Itifaki Na. 16 nimeona kwenye report hapa bado tunaendelea, tunaangalia namna ya kuharakisha lakini miaka inaenda, hata kukopa tu hizi pesa nayo bado imekuwa kwenye mkakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nimeona kwenye report ya Kamati, deni la wafanyakazi ni shilingi bilioni 434, hizo ni pesa nyingi sana. Siamini kama kweli hili deni kubwa namna hii kama ni la wafanyakazi tu na zimehakikiwa na hazijalipwa. Je, hii TAZARA itakuwa hai au imefilisika? Kwa sababu kama deni halijalipwa shilingi bilioni 434 ni la wafanyakazi, limehakikiwa toka 2016, leo 2019 hazijalipwa na ninaamini kwamba wafanyakazi wengi wa TAZARA wako katika umri wa kustaafu. Je, mkakati gani ambao unachukuliwa kuhakikisha kuwa tunaajiri wafanyakazi wapya wa reli hii? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na reli hii, ili ifanye kazi vizuri tunahitaji tuwe na Bandari Kavu pale Mbeya na vilevile tuwe na reli ya kutoka Mbeya -Inyala kwenda Kyela ili iwe kiungo cha Nchi ya Malawi, Msumbiji pamoja Zimbabwe na tuweze kutumia vizuri zile meli zetu tatu ambazo ziko kwenye Ziwa Nyasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni muhimu sana. Hata ukiangalia katika maandiko ya nchi majirani na maandiko ya Kimataifa, zinaonyesha ni kiasi gani tutapoteza biashara ya TAZARA kwa nchi majirani kwa sababu reli ya TAZARA ilikuwa muhimu wakati ule wa ukombozi. Leo nchi zile zimeshakombolewa, nazo ndiyo zinafanya mikakati ya kuhakikisha kuwa watatunyang’anya biashara zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na TAZARA, lakini vilevile napenda kuongelea kwa kifupi sana barabara zetu nyingine za Mkoa wa Mbeya ikiwemo barabara ya bypass na upanuzi wa barabara ya kutoka Tunduma kuja mpaka Igawa. Hizi barabara ni muhimu sana kwa ajili ya uchumi wetu. Gharama kubwa za kilimo zinachukuliwa na gharama za usafirishaji ikiwemo usafirishaji wa mbolea na usafirishaji wa mazao yetu.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Muda umekwisha Mheshimiwa. Kengele ya pili imeshagonga.

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. ORAN M. NJEZA: Nashukuru sana Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kunipa nafasi na mimi ya kuchangia hii Wizara muhimu ya Kilimo. Ningependa kuanza kwa kutoa pole kwa wananchi waliopoteza maisha na majeruhi kutokana na ajali ya gari iliyotokea jana pale Mji Mdogo wa Mbalizi Wilaya ya Mbeya. Kwa kweli eneo lile limekuwa ni hatarishi sana, nafikiri Wizara ya Miundombinu pamoja na Mambo ya Ndani pamoja na juhudi wanazozifanya wangejaribu kuangalia namna ya kupunguza ajali katika eneo lile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuisema hiyo nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Hasunga, Naibu wake Mheshimiwa Mgumba, na Naibu wa pili Mheshimiwa Bashungwa; kwa kweli wanafanya kazi nzuri sana, ni timu nzuri timu ya wataalamu. Ukiangalia na hii hotuba yao ya bajeti kwa kweli imesheheni utaalamu mwingi unaoonesha matarajio mengi, na imekaa kimkakati mno. Kwahiyo inaonesha kabisa ya kwamba wataalamu watatu walikaa vizuri na wakaitengeneza hii hotuba yao vizuri. Mimi ningependa kuongezea kidogo tu katika hicho ambacho nao wametuletea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi nimezungumzia zao la pareto hapa na watu inawezekana wanashangaa hii pareto ni nini. Pareto Tanzania inaongoza Afrika, na sisi ni wa pili duniani. Kwa miaka mingi tulikuwa tunazalisha takriban tani zaidi ya elfu nane lakini leo hii tunazalisha chini ya tani 2000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilo moja ya pareto huko sokoni duniani ni dola kati ya 150 mpaka dola 300, kwa kilo moja; sasa angalia umuhimu wa hili zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tuna fursa za kuweza kuzalisha zaidi pareto. Sasa ningemuomba Mheshimiwa Waziri aliangalie kwa jicho la kipekee, ni namna gani atusaidie; kwa kuanzia usimamizi wa hili zao sio mzuri tuna Bodi ya pareto na siwezi kuwalaumu sana wataalamu inawezekana katika ule muundo sio mzuri sana. Kwasababu Mheshimiwa Waziri hapa amesema anajaribu kuangalia namna ya kuboresha ile sheria ya kilimo. Ile Bodi ya pareto kwa kweli haijatusaidia.

Mimi kama Mbunge wa Bunge la Mbeya Vijijini tunalima zaidi ya asilimia 85 ya pareto yote inayozalishwa Tanzania, lakini inavyoelekea katika wadau wa pareto Mbeya Vijijini haimo. Sasa ukianzia hapo tu utaona ya kwamba hili ni tatizo, ya kwamba hata wadau wenyewe hawajulikani. Bei ya pareto iliyooneshwa kwenye kitabu cha Waziri kwa kilo ni 3,700, wakulima wanalipwa shilingi 2,300. Sasa unajaribu kuangalia, hizi takwimu zinatoka wapi? Utakwenda kuwaambia nini wakulima? ya kwamba pareto yenu mnayolima mnalipwa shilingi 3,700 wastani ilhali zaidi zaidi wanalipa 2,300.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimesema kuwa kilo moja ya extract ambayo inatokana na kuichuja ile pareto, kilo moja inakwenda mpaka dola 300; na hata Kenya wenzetu wananunua kwetu kwa dola 70, India kwa dola 90 mpaka 100 na Korea vivyo hivyo. Sasa huyu mkulima unayemlipa 2300 inatoka wapi? Sasa je, kama nchi tunapoteza kiasi gani? Nilikuwa najaribu kuangalia hata ile Kampuni inayonunua pareto, nimegundua katika hisa mle kuna asilimia 15 ambazo ni za wakulima. Hizo asilimia 15 mpaka leo hatujui ni nani anayezifaidi. Asilimia 15 ya hisa ni nyingi. Kwa makusudi kabisa Serikali baada ya kubinafsisha hiki kiwanda ikasema wakulima nao wawe sehemu ya maamuzi ya hiki kiwanda, lakini mpaka leo hizo asilimia 15 hazieleweki nafikiri Waziri labda akiwa pamoja na TR waje watuambie hizo asilimia 15 ziko wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa vile vile niongelee na kwenye kahawa. Fursa tulizonazo kwenye kahawa bado ni kubwa, bei ya kahawa hapa kwetu ni ndogo. Leo hii sisi tunauza dola mbili kwa kilo, Kenya ni zaidi ya dola tatu, lakini ukiangalia kwenye soko la ICO kule paundi moja ni kama senti 144 ambazo ni dola 1.44 sasa hii tofauti yote inatoka wapi? Hii kahawa yetu ya arabika tunayolima Tanzania ni nzuri sana kwasababu ndiyo inayotumika kwenye blending kwenye kahawa nyingine kwa vile sisi tunachuma kwa mkono hizi kahawa, kwa hiyo ina heshima ya kipekee. Sasa hiyo hela tofauti hiyo inayopotea inaenda wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tukienda zaidi kwenye masoko, hata ya mahindi. Nimemsikia msemaji hapa mama Anna Lupembe amezungumzia hoja ya muhimu sana kuhusu soko la mahindi la Kongo. Ni kweli tuna soko zuri Kongo, kuna rafiki zangu na ndugu zangu ambao wame-access hilo soko, lakini wamekuwa wakipitishia hiyo mizigo Zambia. Zambia sasa hivi wameweka masharti, lakini sisi tunapakana na Kongo. Sasa kwanini tusitumie njia ya Kongo na barabara za lami hizo zipo?

Sasa haya ndiyo mambo ambayo Wizara ikikaa mkakati kama walivyokuwa Mawaziri, tutumie brain zenu kuweza kuwaokoa wakulima tuachane na kufanyakazi kwa mazoea. Kama kuna timu zinawakwamisha huko angalia hizo timu zinazowakwamisha namna gani mzifumue sio wakati wake huu wa kuanza kulea watu ambao hawatusaidia katika kazi zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo napenda tu niunge mkono hoja nashukuru sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa fursa hii ya kuchangia Mpango wetu wa Maendeleo pamoja na mwongozo wa bajeti kwa mwaka 2020/21.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Waziri, Naibu Waziri na timu nzima ya Wizara ya Fedha kwa kazi nzuri wanayoifanya. Ukisoma utekelezaji katika ripoti hii, utaona katika maeneo mengi, kwa kweli wamefanya vizuri sana kuliko vile tulivyotarajia na pia hata kwa kutulingalisha na nchi jirani. Kwenye Pato la Taifa, urari wa biashara na kwenye fedha zetu za kigeni tunafanya vizuri. Vilevile ukiangalia hali ya chakula, ndiyo sasa hivi inaonyesha maeneo mengi kuna tatizo lakini kuna maeneo mengi ambayo yana chakula cha ziada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niendeleze tu kumpongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake lakini pia yote haya yanatokana na kazi nzuri anayoifanya Mheshimiwa Rais wetu mpendwa, tunamshukuru sana kwa kazi nzuri anayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia haya mapendekezo ya mpango utaona kwa kiasi kikubwa yamelenga kukua kwa uchumi katika Sekta ambazo hazitoi ajira kwa Watanzaia walio wengi ambao ni wakulima. Ripoti inaonesha kuwa sekta ya kilimo inaajiri zaidi ya 65% ya Watanzania, lakini inachangia 28% tu na ukuaji wake ni wastani wa 6%. Sasa ukiangalia katika hali ya namna hiyo ina maana Watanzania walio wengi hawashiriki katika kuchangia kukua kwa uchumi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pendekezo langu kwa Mheshimiwa Waziri aangalie ni kwa jinsi gani uwekezaji kwenye sekta ya kilimo uongezeke. Uwekezaji kwenye sekta ya kilimo ningependekeza nchi yetu ya Tanzania imejaliwa ardhi nzuri sana maeneo mengi lakini kuna upungufu wa mvua na mvua zikija zinanyesha nyingi kunakuwa na mafuriko. Ningependekeza huu mpango pamoja na bajeti uangalie kuongeza sekta ya umwagiliaji na ujenzi wa mabwawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hilo kwa makusudi kwa sababu nchi nyingi zinazotuzunguka, majirani zetu wanategemea zaidi kilimo cha umwagiliaji na sisi Tanzania ndio tuna maji mengi hapa kwetu Afrika hata duniani sisi tulijaliwa, Mwenyezi Mungu ametupa akiba kubwa sana ya maji lakini hayo maji tumekuwa hatuyatumii. Namwomba Mheshimiwa Waziri pamoja na Serikali waangalie namna gani washiriki katika kukuza na kuboresha sekta ya umwagiliaji pamoja na ujenzi wa mabwawa ambayo yatasaidia kwa ajili ya binadamu na pia kwa ajili ya mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizalisha vilevile utahitaji ni namna gani upate masoko ya hayo mazao. Masoko ya mazao yetu kwa kweli hayako katika hali nzuri. Ukitulinganisha sisi na nchi jirani uchukulie zao kama la kahawa, zao la kahawa sisi tuna soko letu ambalo tunatumia minada inayoendeshwa na Bodi ya Kahawa, lakini hii kahawa kwa mfano kahawa ya arabika ambayo na nchi ya Kenya, Ethiopia na Rwanda wanailima, bei ya kahawa kwa hapa kwetu ni shilingi dola 100 kwa mfuko wa kilo 50 lakini wenzetu Kenya ni zaidi ya kilo Dola 250, wenzetu Ethiopia ni zaidi ya hapo. Sasa angalia kwa nini Tanzania sisi tupate bei ndogo, tukipata bei ndogo ina maana vilevile inaathiri ukuaji wa uchumi wetu kwenye sekta ya kilimo na hizi ndio pesa tunazozihitaji kwa ajili ya kuboresha urari na vilevile pesa tunazozihitaji kwa ajili ya kuboresha mapato ya nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia pendekezo langu ni namna gani tuimarishe maghala ya kisasa, mazao yetu mengi tunayoyazalisha yanaharibika, kunakuwa na uharibifu mkubwa wa wadudu. Ningependekeza uwekezaji vilevile uende kwenye maghala ya kisasa na biashara ya masoko sasa hivi inaendana pamoja na maghala ya kisasa. Ukiwa na warehouse receipt system ambayo inafanya kazi ndio soko la bidhaa linaweza kufanya kazi, kukiwa na soko la bidhaa bila warehouse receipt system hilo soko la bidhaa haliwezi kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwa mazao yetu sasa hivi tukitaka tufanye vizuri katika mazao yote ya nafaka na mazao ambayo tulizoea kuita ni mazao ya biashara inabidi tuimarishe soko la bidhaa TMX ili lifanye kazi yake vizuri na ili lifanye kazi vizuri hili linahitaji kuwe na maghala, kuwe na warehouses ambazo zitatusaidia. Kwa sasa hivi bila hivyo hili soko letu haliwezi kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye kilimo kunahitaji miundombinu ambayo ni mizuri. Miundombinu yetu huko vijijini haiko vizuri, barabara haziko vizuri, ziko katika hali mbaya sana na hawa wanaozihudumia hizo barabara bajeti wanayopewa ni kidogo sana. Sasa napendekeza, ili tuboreshe kilimo, ili tuboreshe barabara miundombinu ya vijijini, hawa TARURA wangeongezewa bajeti katika mwaka unaokuja ili waweze kuboresha miundombinu ya barabara za vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika miundombinu ukiangalia reli, naishukuru kwanza Serikali kwa ujenzi wa SGR, SGR katika awamu hizi mbili inaonesha itafika Makutupora, lakini kuwe na mpango mahususi ambao unaonesha ni lini hiyo reli itafika katika matawi yake ya Mwanza na tawi la Kigoma. Bila hivyo kazi itakuwa kubwa sana ya mizigo yetu ambayo sasa hivi inasafirishwa kwa barabara na kuna uharibifu mkubwa sana wa barabara zetu, bila kumalizia SGR mpaka Mwanza, mpaka Kigoma bado tutakuwa hatujafikisha lengo la matumizi mazuri ya hii reli ya kisasa ya SGR na hii itasaidia vilevile utendaji mzuri wa Bandari yetu ya Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii reli nayo inahitaji iwe na matawi; kuwe na tawi la kuunganisha na TAZARA kwa upande wa Tunduma kuwa na reli ya kutoka Tunduma mpaka Ziwa Tanganyika lakini vilevile katika mpango imeonesha kuwe na reli ya kuanzia ra mpaka Mbambabay. Hii reli itakuwa na manufaa zaidi vilevile, kukiwa na kipande kingine cha reli kitakachotoka Mbeya ambacho kinaunganishwa na TAZARA kinakuja mpaka Itungi Port au Kiwila Port kwenye Ziwa Nyasa. Hapa utakuwa umekamilisha network yote ya reli zetu zitakuwa zimeunganishwa vizuri na kwa sababu ukiangalia tunapojenga SGR huku na reli ya TAZARA vilevile ni iko kwenye standard ya SGR, kwa hiyo utakuwa umeiunganisha Tanzania vizuri kwa kuwa na reli za kisasa na itatusaidia hata katika kuimarisha biashara ya sisi na nchi za jirani yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna matumizi bora ya ardhi; matumizi bora ya ardhi ni muhimu sana katika kuendeleza kilimo, lakini vilevile ni muhimu sana katika ufugaji, lakini ni muhimu vilevile katika makazi. Ardhi yetu, maeneo mengi ya mijini hayajapimwa, kwa hiyo miji iko holela, sasa na kwa vijiji vinavyoizunguka hii miji, vingi sasa kutokana na miji imejaa watu wanahamia huku vijijini na wanahamia kwa ujenzi holela, kwa hiyo huu mpango ungeonesha ni namna gani kuwe na mpangilio mzuri wa ujenzi wa miji.

Kwa hiyo, mipango miji nayo iongezewe pesa kwa makusudi kwa sababu bila kupangilia ardhi kwa kweli matumizi yetu ya ardhi ambayo haiongezeki yatakuwa sio mazuri. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Oran Njeza.
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa fursa hii ya kuchangia mapendekezo ya huu Mpango. Kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha pamoja na timu yake. Kwa kweli, wamekuja na mpango ambao ni wa kibunifu sana hasa kwa dunia ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia dhima nzima ya huu mpango ambao ni ushindani kwa kweli, unabeba kitu kikubwa zaidi ambacho duniani kote sasa hivi ushindani sio wa bidhaa peke yake, lakini mataifa yanashindana kuangalia resources zao walizonazo ni namna gani wazitumie vizuri na sisi kwa Tanzania Mwenyezi Mungu ametujalia resources nyingi sana ambazo kwa kweli ni za kishindani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza kwa uchache tu kwa ajili ya muda, ukianza uzalishaji wa madini yetu. Kwanza nashukuru Serikali kwa kutunga Sheria ya Madini, lakini yale madini tutayatumia namna gani ili yatuletee kipato na kuongeza pesa za kigeni? Nina imani Waziri wa Fedha anahitaji FDIs nyingi. FDIs atazipata kutokana na mazao yetu ya madini. Kwetu Mbeya, Wilaya ya Mbeya ambayo na Mheshimiwa Mwenyekiti na wewe ndio unakotokea wilaya hiyo, sisi hatujaanza kuzalisha, lakini tuna madini yanaitwa niobium. Inawezekana likawa ni jina geni sana kwa Wabunge, lakini madini ya niobium ni madini adimu sana na huo mgodi ambao unaanzishwa utakuwa wa kwanza Afrika na wa nne duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninachoiomba Serikali ni namna gani kufuatia mpango huu iweke hii mipango kwenye mpango wa muda mfupi, lakini iiweke vilevile kwenye mpango wa miaka mitano kwa sababu, haya madini yanategemewa yanaweza kuvunwa kwa miaka zaidi ya 30 mpaka 50. Sasa hayo madini yanatumika kwenye nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo madini kwa kiasi kikubwa yanatumika kwenye kuimarisha vyuma, kwa hiyo, yataendana pamoja na madini ambayo tunayazalisha ya chuma cha Liganga. Hawa wawekezaji wanataka waanzishe hiki kiwanda cha kwanza Afrika, kwa hiyo, watachimba na kuchenjua, ili bidhaa hii ambayo inaitwa niobium ambayo ni ya kwanza kwa Afrika iweze kuzalishwa hapa kwetu na rasilimali kutoka mataifa mengine yaje hapa kwetu yalete hiyo rasilimali na sisi tuwe wazalishaji wakubwa. Haya ndio madini yanayotakiwa kwa leo ili tuweze kujenga madaraja ya baharini, madaraja ya ziwani, reli SGR na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile ukiangalia wataleta nini; hawa wanaleta FDI ya karibu zaidi ya bilioni 250 ambazo kila mwaka zitazalisha zaidi ya dola milioni 220, ukiangalia hiyo ni asilimia kubwa sana. Sasa ningeomba katika mikakati ya namna hii Wizara ziwe zinashirikiana isiwe kitu cha Wizara moja. Hizi ni opportunities, hizi ni fursa na haya madini kadri miaka inavyokwenda na teknolojia inavyobadilika si ajabu yakawa mawe ya kawaida tunayoyaona kama tunavyoyaona haya ya hapa mwanzo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna suala zima la kilimo cha pareto. Nalo ni zao ambalo inawezekana watu wengi wakashangaa, lakini pareto tunayolima Tanzania kwenye Wilaya ya Mbeya ni ya kwanza Afrika na ya pili duniani. Inatumika kutengeneza dawa za kuua wadudu, lakini zaidi zaidi inatumika sasa hivi kwenye kutengeneza dawa za kuhifadhi nafaka na hii ni organic. Sasa viwanda vya namna hii inatakiwa viwekwe kwenye kipaumbele, ndio tunavyovihitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara ya Kilimo iangalie kwa kipekee namna gani tuweze kuvutia viwanda vitakavyozalisha dawa zinazotokana na pareto. Kwa vile hatuna mshindani, wenzetu jirani zetu wanakuja kuchukua kwetu raw materials kutoka Tanzania, wanatengeneza hiyo raw materials, wanasafirisha kwenda nje. Sasa hivi Uganda na Kenya pamoja na Rwanda ndio wamekuwa wateja wazuri sana kwa wakulima wangu kule Mbeya kwenye mazao haya ambayo sisi yanakuwa ni semi processed.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Wizara iangalie namna gani tuchukue majukumu ambayo yataisaidia nchi yetu kupunguza pengo la pesa za kigeni. Pesa za kigeni zikipungua hatari yake ni nini? Hata ile kuingia kwenye uchumi wa chini wa kati ni rahisi tukaporomoka mara moja. Sasa hivi tuna dola 1,080 ambayo iko chini kabisa. Exchange rate kama sio tulivu ina maana tunaweza kuporomoka tukarudi tulikotoka. Sasa tuki-take advantage hii kwa fursa tulizonazo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa, kengele imegonga.

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii na mimi ya kuchangia Mpango wetu wa Tatu wa Taifa.

Mheshimiwa Spika, naomba kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali. Kama ulivyosema mwenyewe, huu mpango unatupa fursa ya tathmini lakini vile vile inakuangalia tunaenda vipi mbele ya safari yetu.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia tathmini ya tulikotoka tumefanya vizuri kiuchumi, kutoka uchumi wa chini kwenda uchumi wa chini kati nafikiri ni hatua nzuri sana. Lakini ukiangalia vile vile kwenye miundombinu tumefanya vizuri na maeneo mengi tumefanya vizuri sana. Kwa hiyo napenda sana kumshukuru na kumpongeza Mheshimwa Rais, Serikali yake nzima, Mheshimiwa Waziri wa Mipango kwa kutuletea hii taarifa nzuri sana ambayo kwakweli ukiangalia inatupa matumaini makubwa sisi kama Taifa, na ukiangalia dhima nzima ya huu mpango ni kujenga uchumi shindani, lakini vile vile inaenda pamoja na viwanda na maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Spika, kwakweli uzito wa hiyo dhima ni mkubwa mno. Lakini nilikuwa najaribu kuangalia, sisi kama Taifa pamoja na hii dhima, je, tunasimama wapi?

Mheshimiwa Spika, hii dhima nguzo kubwa ziko kwenye uimara wa uchumi; uchumi wetu je, ni imara au si imara? Kama tathmini tuliyoifanya tumetoka uchumi wa chini sasa hivi tupo kwenye uchumi wa kati ina maana uchumi wetu ni imara. Vile vile nguzo yake ingine ni miundombinu, je, tuna misingi mizuri ya miundombinu? Ndiyo, tumeanza vizuri tumejijenga vizuri katika miundombinu na tunakwenda vizuri, nakadharika, nakadhalika.

Mheshimiwa Spika, ukianza na hii hatua ya kwanza tu ya uchumi. Nina imani ya kwamba kuna maboresho machache sana ambayo tunaweza kuyafanya katika nchi yetu. Tunategemea sana kilimo, kilimo ndiyo nguzo ndicho kinachoajiri asilimia kubwa ya Watanzania. Watu wengi tunafikiri masoko hayapo, masoko yapo, na masoko ya Tanzania ya mazao yetu naweza kusema kwa kiasi fulani ni ya upendeleo.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia zao la kahawa, hasa arabica, kwenye Soko la Dunia la New York bei yetu ya kahawa inaongezewa senti thelathini mpaka hamsini kutegemea na bei shindani ya New York hiyo ina maana kuwa wakulima wetu wangepata bei nzuri sana ya Kahawa kutokana na upendeleo tulionao kwenye Soko la Dunia.hata hivyo hali siyo hivyo, kuna matatizo tuliyonayo ambayo usimamizi wa masoko haya ambayo yapo inaelekea kuna mahali hatufanyi vizuri.

Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia huu mpango wa tatu tungeangalia hizi fursa zilizopo, tufanye namna gani haya masoko yaliyopo yaende vizuri. Kama tumeongezewa bei ya arabica kwa senti thelathini mpaka arobaini kwa kila lb, lb 2.2 ndio sawa na kilo moja, kama tumeongezewa hizo kwanini hatufanyi vizuri?

Mheshmiwa Spika, kwenye mahindi Mwenyezi Mungu ametupa ardhi nzuri, lakini nayo uzalishaji wetu si wa ushindani kwasababu uzalishaji wa Tanzania kwa mahindi ukilinganisha na majirani zetu kwakweli hatufanyi vizuri.

Mheshimiwa Spika, soko la nje la majirani zetu, ukiangalia nchi zinazotuzunguka, hasa Zambia wanaweza kuuza kwa faida mahindi yao kwa kilo kwa shilingi 300, lakini kwa sisi tunaozalisha Tanzania ukiuza kwa shilingi 500 kwa kilo ni hasara; ni kwanini? Kwasababu bei ya mbolea kwa hapa kwetu si Rafiki, na hiyo inasababisha kwa kiasi kikubwa na utendaji ambao sio mzuri katika miundombinu.

Mheshimiwa Spika, usafirishaji unachukua kiasi kikubwa sana cha bei ya pembejeo. Kwa hiyo tukiweze kuboresha miundombinu, tukaboresha vile vile na wenzetu wa Barandari ambao walikuwa wanaendelea na maboresho nafikiri kwa kiasi kwa kiasi kikubwa tunaweza kuwa na ushindani. Huwezi wenzetu wa Zambia wakauza Mahindi yao kwa faida kwa shilingi 300 na sisi tukauza bila faida kwa shilingi 500, hiyo haileti ile dhama nzima ya Uchumi wa ushindani. Ina maana sisi hatutakuwa washindani kwa hiyo hata ukitafuta soko, soko ambalo utauza kwa bei ambayo ni ya hasara hilo soko litakuwa baya. Kwa hiyo tuanze kwanza na kuboresha kilimo cha tija.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la Miundombinu, mwenzangu amezungumzia kuhusu TAZARA. sasa ni kwanini ukiangalia TAZARA kwenye mpango haizungumziwi kama mradi ambao ni quick win? Reli ya TARAZA ipo pale na ni Standard Gauge lakini bidhaa nyingi zinazokwenda nje ya nchi asilimia zaidi ya 70 zinatumia barabara yetu ya TANZAM na hawatumii TAZARA. Mimi mwenyewe nimejaribu kuulizia usafirishaji kwa kupitia TAZARA ni takriban mara mbili ya usafirishaji kwa gari. Sasa unashangaa, tungetegemea reli iwe rahisi kuliko barabara; hasa ni kwa nini usafirishaji kwa reli hapa kwetu umekuwa ni tatizo na bei ya juu? Ina maana hapa tunatatizo kubwa.

Mheshimiwa Spika, tunaomba, ninaomba sana tuangalie tunapoboresha SGR tuangalie ni namna gani tunaweze kuiunganisha SGR na mtandao wa Reli za kwetu za Afrika Mashariki pamoja na nchi za SADC, ikowemo kuunganisha TAZARA pamoja na SGR. Kama alivyosema mtangulizi wangu, kuna kumuhimu wa kuunganisha Reli ya TAZARA na Port ya Kasanga kutokea Tunduma, lakini vile vile kuanzia Mbeya kwenda Ziwa Nyasa, ili uwe na muunganiko mzuri sasa na wa Reli ya Mtwara mpaka Mbamba Bay, na hapo sasa kutakuwa na mzunguko mzuri wa reli yetu.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la uzalishaji wa viwanda na fursa za pesa za kigeni. Tuna Madini mengi hapa nchini wawekezaji wapo, lakini ukiritimba tulionao wakati mwingine unasababisha wawekezaji wanakosa imani na kuwekeza hapa kwetu. Nimezungumzia mara nyingi kuhusu madini ya Niobium. Madini ya niobium ni madini ambayo ni adimu. Kiwanda ambacho kinategemewa kuwekeze hapa nchini kwetu kitakuwa ni cha nne duniani, na hiki kiwanda kitatumia rasilimali zetu na madini yaliyoko Tanzania na kitatuletea mapato kwa kila mwaka zaidi ya Dola 200 na Serikali itapata Dola zaidi ya milioni 20 kwa kila mwaka.

Mheshimiwa Spika, Ukiangalia direct investment ni zaidi ya Dola milioni 200 vile vile. Sasa, ni ka nini tusichukue fursa kama hizo kama hao watu wapo tayari nao kwenda pamoja na sheria tulizonazo nchini kwetu?

Mheshimiwa Spika, nafikiri tukiweza kuyaboresha haya na yakawepo kwenye mpango wetu, tukawa na mazingira ambayo ni rafiki tukapunguza gharama, hayo tutakwenda vizuri sana. Lakini kwenye miundombinu, hata ukiangalia TARURA sasa hivi barabara ziko hoi. Kwenye Wilaya ya Mbeya Jimbo la Mbeya Vijijini barabara zetu takriban kilometa 1000 zote zina hali mbaya. Lakini unaangalia, wakati mwingine ni utendaji wa watendaji wetu. Kwenye Bajeti ya mwaka huu tu bado miezi miwili ametumia asilimia 20, wananchi hawaweze kusafirisha mazao yao.

Mheshimiwa Spika, sasa tusipoboresha hata kilichopo nina imani kuwa hatuweze kufanya vizuri. Hivyo ninaiomba Serikali kupitia TARURA iboreshe Miundombinu ya barabara zetu, lakini barabara zetu ambazo zina fursa za kwenda mipakani kama kutuunganisha sisi na Zambia, sisi na Malawi nazo zipewe kipaumbele.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ningeomba Barabara kama hii ya Mbalizi kwenda Shigamba ambayo inakwenda mpaka Isongole karibu na mpaka na Malawi iwe kwenye kipaumbele cha mpango wetu.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana niendelee tena kumpongeza Mheshimiwa Waziri, na ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kupata fursa hii ya kuchangia bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwa kuanzia kabisa naomba kwa kipekee nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu mama Samia Hassan Suluhu kwa kushika nafasi ya Urais. Ameanza vizuri na wote tumeona. Pia napenda kumpongeza Mheshimiwa Mpango naye kwa kuteuliwa na kushika nafasi ya Makamu wa Rais. Naye kwa kweli tumeona ameanza vizuri sana na kweli timu imekamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile napenda nimpongeze Waziri Mkuu. Kwa kweli Waziri Mkuu amefanya kazi kubwa sana. Ofisi yake inafanya kazi ya coordination ya Wizara zote, kwa hiyo mafanikio ambayo tumeyapata katika Serikali yetu ya Awamu ya Tano na yanayoendelea mpaka sasa hivi yote ni juhudi ya ofisi yake ambayo imeweza kuzi- coordinate Wizara zote na Serikali kwa ujumla. Wote ni mashuhuda wa mikakati ambayo tunayo mpaka sasa hivi ambayo ni endelevu. Pamoja na mafanikio yaliyoko kwenye miradi ya mkakati, lakini hata huko chini kwenye Halmashauri zetu tumeona mafanikio makubwa mno. Kwenye maji, kwenye umeme hata kwenye miundombinu tumeona mafanikio makubwa mno.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye jimbo langu tumeona mafanikio makubwa ya ujenzi wa hospitali, vituo vya afya vitatu ambavyo ni vya kihistoria na sasa hivi tunakamilisha tu ili viweze kuanza kufanya kazi vizuri. Kwenye miundombinu vile vile kwa mara ya kwanza kwenye historia tumeona barabara za kiwango cha lami zikianza kujengwa vijijini kwa ajili ya kwenda maeneo mahsusi ya wakulima wetu ili kuweza kufanya miundombinu ya vijijini iwe rahisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye umeme nako tumefanya vizuri sana. Kwenye Halmashauri yangu tulikuwa na vijiji vingi sana, vijiji karibu 200 lakini sasa hivi ndiyo Serikali inamalizia vijiji 40 vya mwisho ili tuweze kufikia asilimia mia moja ya vijiji vyote kuwa na umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mafanikio hayo hapawezi kukosa changamoto, lakini changamoto zetu tulizonazo naona suluhisho lipo na tunategemea sana Serikali ya mama yetu Samia Suluhu Hassan. Ataweza kuzikabili hizo changamoto, sio kubwa kiasi hicho, ni ndogo na ukiangalia mpango wetu ambao tumeupitisha sasa hivi ni mpango ambao ni mzuri, unaangalia Taifa letu la Tanzania ni namna gani litakuwa shindani kwenye ukanda wetu lakini vile vile na kidunia. Kwa hiyo, kikubwa hapo ni kuangalia miundombinu ambayo itatufanya sisi tuwe washindani, tuweze kufanya vizuri ukitulinganisha na wenzetu huko duniani.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ambazo tunaziona hasa kwa sisi tunaotoka majimbo ya vijijini ni miundombinu ya barabara. Barabara za vijijini ambazo zinahudumiwa na TARURA kwa kweli kwa asilimia kubwa zina hali mbaya sana. Tukiongelea kilimo bila ya kuwa na miundombinu mizuri ya barabara hatuwezi kufanikiwa kwa sababu gharama ya pembejeo itakuwa kubwa, tutashindwa kushindana. Lakini mazao yetu yatashindwa kwenda sokoni. Kwenye halmashauri yangu nina kilometa zaidi ya 1,000 ambazo zinahudumiwa na TARURA, lakini leo hii zaidi ya asilimia 90 hazipitiki. Wakulima wanashindwa kupeleka mazao yao sokoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, sio hilo tu, vile vile hata halmashauri haiwezi kukusanya kwa sababu halmashauri yetu ambayo inakusanya karibu bilioni tatu kwa mwaka kutokana na mazao ya kilimo kwa miezi yote ambayo mvua zinanyesha wameshindwa kukusanya ambao ni karibu nusu mwaka. Sasa hii inaweza kutupeleka mahali pabaya sana. Tunakuja na bajeti zetu, ambazo ni nzuri kiasi hicho, lakini tunashindwa kutekeleza yale malengo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kulikuwa na ahadi ya Mheshimiwa Rais, hata Mheshimiwa Rais Samia naye aliahidi pale kwetu Mbeya. Kuna barabara yetu, kipande cha barabara ambacho kinasababisha sana ajali, Mlima Iwambi pale Mbalizi na wewe ni shuhuda, hatuna barabara nyingine zaidi ya hiyo, ukiachilia mbali msongamano wa pale Mbeya Mjini lakini ile barabara imeua wananchi wetu wengi. Mwaka 2018, Mheshimiwa Hayati Dkt. Magufuli aliahidi ijengwe haraka kwa kiwango cha lami. Nina Imani hata Viongozi Wakuu wengine waliwajibika kwa ajili ya hilo. Alikuja mama, wakati huo akiwa Makamu wa Rais naye akaahidi ijengwe haraka. Mpaka leo hakuna chochote kinachofanyika, sasa ukiangalia ile barabara ndiyo inabeba mzigo wote ambao ni karibu asilimia 75 ya mizigo yote inayotoka bandarini kwa ajili ya majirani zetu na hiyo barabara inapita katikati ya Jiji. Kunapita na ma-tanker ya mafuta pale ambayo ni hatari kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Waziri wa Ujenzi atuambie ni nini kinakwamisha hilo kwa sababu tuliambiwa mwanzoni kwamba hata wadau wetu wa maendeleo walikuwa tayari kuijenga hiyo barabara ya Mlima Nyoka sehemu za Uyole kwenda Songwe, lakini mpaka leo hakuna kinachoendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara zingine pia ambazo ni za kimkakati; barabara ya Isyonje – Kikondo kwenda mpaka Makete ambayo tunategemea iweze kubeba mazao mengi sana, matunda matunda pamoja na sasa hivi kuna utalii kwa jirani zetu wale wa Makete. Hiyo barabara nayo pamoja na kuwekwa kwenye bajeti hatuoni kinachoendelea. Kuna barabara nyingine ambayo nayo ni ya kimkakati; barabara ya Mbalizi – Galula – Makongolosi ambayo inatokea mpaka kwa majirani zetu wa Mikoa ya Tabora na Singida. Hiyo barabara imekuwepo kwenye bajeti kwa miaka mingi, lakini mpaka leo na hivi juzi juzi ilikuwa haipitiki. Kuna barabara yetu nyingine ambayo ni ya kimkakati; barabara ya Mbalizi – Shigamba ambayo nayo inaenda mpaka Isongole karibu na mpaka wetu na Malawi, hii ni barabara ya kimkakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba hizi barabara zote zipewe kipaumbele ikiwemo na barabara zetu za vijijini, zina hali mbaya sana na ikiwezekana Waheshimiwa Wabunge tuangalie ni namna gani tuiwezeshe TARURA itusaidie ili wakulima wetu waweze kusafirisha mazao yao kutoka vijijini tuweze kupunguza gharama za mazao yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Madini
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa hii fursa ya kuchangia Wizara ya Madini ambayo ni Wizara muhimu sana kwenye Uchumi wa Tanzania. Nianze kwanza kwa kumpongeza Waziri na timu yake, kwa kweli wamefanya kazi nzuri sana na kazi imeonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia hata kwenye taarifa yake, pato letu mchango wa madini ulianzia 4%, 2014, lakini kwa sasa hivi unaelekea kwenye 6% na nina imani kabisa kuwa katika hiyo appetite yao ya kufikia asilimia 10 itawezekana kabisa. Kwa hiyo, namshukuru sana tena sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi yako nzuri na Wizara kwa jinsi mnavyofanya kazi vizuri, coordination imekuwa ni nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, madini kwa kiasi kikubwa duniani kote yanaweza kutumika kama rasilimali kwenye viwanda. Nasi Tanzania tumebahatika kupata madini mengi ambayo yanaweza kutumika viwandani. Kipindi hiki wakati uchumi wa dunia unayumba yumba sisi Tanzania tuna fursa ambazo zipo kupitia madini kama ilivyokuwa kwenye kilimo ambayo tunaweza kutumia madini yetu kupata hizo fursa za kuanzisha viwanda vingi kama hivi vilivyoanzishwa vya dhahabu ambavyo vimeanza kufanya kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilikuwa napendekeza na nimekuwa nikipendekeza mara nyingi, tuna madini ambayo ni adimu sana duniani na ni adimu sana Afrika. Tuna mgodi wa madini Panda Hill Songwe Wilaya ya Mbeya. Huu mgodi utazalisha Niobium na huu mgodi kuna fursa ya kuanzisha kiwanda ambacho kitakuwa ni cha kipekee cha kwanza Afrika nzima; na cha nne duniani. Kuna uwekezaji wa kutoka nje wa dola zisizo pungua milioni 200, vile vile kitazalisha kwa mwaka Dola zisizopungua milioni 200 na Serikali itapata mapato yasiyopungua Dola milioni 50 kwa mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ukiangalia kwa haraka haraka inawezekana hizi projections zikaonekana kama ni za ajabu, lakini hiyo ndiyo hali halisi. Kwa sababu kazi zote zimefanyika za namna gani waweze kuendesha huo mgodi na hicho kiwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri na Serikali, hivi viwanda vya aina hii tungevipa kipaumbele hasa katika kipindi hiki ambacho tunahitaji sana pesa za kigeni hasa katika hiki kipindi ambacho tunahitaji ajira. Kwa sababu hiki kiwanda wakati wa ujenzi kitazalisha ajira zisizopungua 2,000, lakini mbele ya safari kitakuwa na ajira za kudumu siyo chini ya 600. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli wakati mwingine tunakuwa tunalala na fursa tulizonazo na hili ndiyo tatizo ambalo tunakuwa nalo. Kwa sababu kama hiki kiwanda kikiwepo cha kwanza Afrika ina maana madini ya namna hiyo yanayozalishwa nchi nyingine duniani, siyo Afrika peke yake yataletwa Tanzania kama rasilimali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya madini ya Niobium, hiyo product watakayozalisha inaitwa ferroniobium, ambayo ndiyo sasa hivi inatumika kutengeneza vyuma ambavyo vitasaidia kwenye ujenzi wa reli na madaraja kwa vile ndiyo vyuma vya kisasa ambavyo ni vyepesi na vinatumika hata kwenye madaraja ya kwenye maji na hata baharini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba labda kwa kipekee Wizara ya Madini pamoja na Wizara ya Uwekezaji na Viwanda wangejaribu kuliangalia kwa pamoja na nina imani Mheshimiwa Waziri yupo vizuri sana katika kusimamia sheria na mikakati yake ya kulinda rasilimali za Taifa Letu. Nina imani kwa kuzingatia hayo, tukiangalia vile vile katika win win situation tutaona namna gani nchi yetu inaongeza mapato kupitia haya madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli Mheshimiwa Waziri yeye mwenyewe ni shuhuda, alishafika kwenye huo mgodi, aliutembelea na wawekezaji wamekuja mara nyingi kuonana nao. Nafikiri katika hatua tuliyofikia leo, anaweza kuangalia ni namna gani nchi yetu inaweza kuongeza pato la Taifa na vile vile fedha za kigeni ili tuweze kuimarisha uchumi wetu na ili tufikie lengo letu la pato la Taifa ambalo linachangiwa na madini kufikia asilimia kumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mawaziri na viongozi wote wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Serikali katika utekelezaji wa ustawi wa jamii na maendelo endelevu, na hii ni mojawapo ya nguzo kuu katika utayari wetu wa ushindani wa kimataifa (national competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ya kuimarisha mahusiano ya kimataifa, na pia kwa mafanikio makubwa ya Royal Tour ambayo imeanza kuleta matunda makubwa kwa nchi yetu hususani sekta ya kitalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, napendekeza Serikali kuimarisha diplomasi ya uchumi kwa lengo la kuongeza masoko ya uhakika kwa mazao ya kilimo, madini na utalii. Pamoja na kuongeza mapato kwa Taifa letu, itaisaidia kuongeza fedha za kigeni na kuimarisha uchumi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa nami ya kuchangia hii Wizara ya Fedha ambayo kwa kweli ni muhimu sana katika uchumi wetu na imekuwa ikifanya vizuri sana katika kipindi chote na hata sasa imeendelea kufanya vizuri sana. Nami niendelee kumpongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake, kwa kweli wanafanya vizuri sana tena sana. Ukiangalia hata kwa kutulinganisha na nchi za majirani, nchi yetu imekuwa ikifanya vizuri sana na wenzangu wamezungumzia kipindi hiki ambacho tuna changamoto za kiuchukumi kutokana na janga la Corona, lakini nchi yetu ya Tanzania imekuwa ikifanya vizuri sana tena sana. (Makofi)

Mhehimiwa Spika, napenda kumpongeza vilevile Mheshimiwa Rais, naye kwa kulisimamia hilo na kuendeleza pale alipoishia Rais wetu wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. Magufuli. Tunashukuru sana, tena sana. Namshukuru sana Mwenyekiti, hata kwa jinsi tulivyoendelea na makusanyo. Haya makusanyo yanatakiwa yalindwe. Mimi nitazungumzia yale makusanyo ambayo mara nyingi hayazungumzwi hapa ndani. Makusanyo ambayo ni chanzo kizuri, ni kusanyo linaitwa Cost Serving. Namna ya kupunguza gharama; namna ya kupunguza ufujaji wa fedha; nafikiri Mheshimiwa Waziri ukiangalia hilo, chanzo kipya cha mapato kinaweza kutusaidia sana kutusogeza na kutufikisha mahali pazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kutoa labda mfano mmoja tu wa hivi karibuni. Katika ukusanyaji wa Ushuru wa Forodha kulikuwa na mfumo ambao unaotumika mpaka sasa hivi unaitwa ETS. Ni mfumo mzuri sana, lakini gharama yake ya kuuendesha kwa kweli ni gharama kubwa kiasi ambacho gharama inazidi hata yale makusanyo yenyewe. Kwa hiyo, naomba, kwa haya mafunzo tuliyoyapata kutumia mfumo wa ETS na wenzangu wamezungumzia kuhusu uhaba wa wafanyakazi upande wa TRA; tuimarishe hasa Idara ya TEHAMA ili kazi kama hizi za mifumo kama hii ambayo kwa kweli ni generic, ipo mingi, Serikali isiingie hasara ya kuingia kulipa mkandarasi. Zaidi ya shilingi bilioni 34 zimekuwa zikilipwa kwa mkandarasi na hizi hazingii kwenye Mfuko wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haujaleta manufaa yoyote kwa sababu imeonekana kuwa yale makusanyo yaliyokuwepo kabla ya huu mfumo, hasa katika makusanyo kutokana na vinywaji vya bia, hayakuongezeka. Kwa hiyo, ina maana huu mfumo haujatusaidia. Ulisaidia kidogo kwenye vinywaji vikali spirits ambavyo vimeongezeka spirits kama kwa asilimia 40.

T A A R I F A

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Oran pokea taarifa.

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru, ahsante.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, kuongezea mchango wa Mheshimiwa Oran Njeza, Mfumo wa ETS anaozungumza, hizo shilingi bilioni 34 zinahusu kampuni mbili tu; Kampuni ya Serengeti Breweries na ile kampuni nyingine ya bia. Ni kampuni mbili tu za bia. Tukizungumzia Kampuni ya Sigara wao wenyewe wamemlipa Mkandarasi shilingi bilioni 13. Kwa hiyo, tukifanya majumuisho ya makampuni mbalimbali ambayo yanatumia hii huduma ya ETS kwa kupitia Mkandarasi aliyekuwepo, unakuta kampuni binafsi inapata, Serikali haipati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilikuwa nampa taarifa tu kuchagiza, kuonesha kwa namna gani tunapigwa kwa vitu vidogo vidogo vya teknolojia ambayo kama nchi tunaweza tukawekeza. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Oran, unapokea taarifa hiyo?

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, mheshimiwa exceptionally naomba niipokee taarifa yake, ni nzuri; na huu ndiyo mwelekeo wenyewe.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hiyo, ukichukua hiyo shilingi bilioni 34 ambayo imeongeza pressure ya haya makampuni kuongeza bei, ina maana wakiongeza bei, wateja watakimbia na Serikali itapunguza mapato. Vile vile Serikali inapoteza shilingi bilioni 10 kutokana na hizo, kwa sababu hizo zimepunguza faida kutoka kwenye haya makampuni.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tatizo ni kwamba hasara tunayoipata ni kubwa. Kwa hiyo, naomba tunge-localize; acha hii ETS ifanyike na kampuni za ndani au Serikali yenyewe ichukue hili jukumu. Ukichukulia hizi fedha zote, hizo shilingi bilioni 34 zinakwenda nje, ina maana vile vile inaipa pressure foreign exchange reserve ya kwetu. Kwa hiyo, nilikuwa nasema hizi ni hatua ambazo Wizara ya Fedha inaweza kuzichukua kwa ajili ya kuongeza mapato yetu na vilevile kuimarisha uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine, namwomba TR, Msajili wa Hazina kupitia kwa Waziri wa Fedha aangalie kuimarisha yale mashirika ambayo yanaweza kutuletea fedha nyingi kuongeza mapato yetu kwenye Serikali. Nilikuwa naangalia utendaji wa TAZARA. TAZARA kwa kipindi kirefu, kwa miaka 26 Serikali imekuwa ikilipa mishahara ya wafanyazi wa TAZARA, karibu shilingi bilioni 14 kwa mwaka; na hiyo ni asilimia 80 tu, lakini hakuna uwekezaji wowote ambao umepelekwa TAZARA. Hii inatufanya sisi ambao hii Dar es Salaam Corridor, ambayo ndiyo kubwa hapa Tanzania kwa njia ya Dar es Salaam kuelekea nchi za SADC; siyo Tanzania tu, ni kubwa nafikiri kwa Afrika, tunakuwa tunakosa ushindani kwa sababu tunashindwa hata kuwekeza kidogo kwenye TAZARA.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, naomba Serikali iangalie, iwekeze angalau shilingi bilioni 50 kwa mwaka, kwa miaka matatu ili tuokoe TAZARA ili iweze kufanya vizuri zaidi ili iweze kupata fedha za kujenga reli zetu nyingine, ukichukulia kwamba Reli ya TAZARA yenyewe haipo kwenye Mfuko wa Reli.

Mheshimiwa Spika, ni kitu cha ajabu ya kwamba tuna reli muhimu ya TAZARA, Reli ya Uhuru lakini hatuitazami kwa karibu kiasi hicho. Naomba Mwenyekiti shilingi bilioni 50 ziende kwa miaka mitatu ili tuweze kuiokoa TAZARA.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuchangia hii bajeti muhimu. Nianzie pale walipoishia wenzangu kumpongeza hasa hasa, Mheshimiwa Rais wetu mpendwa kwa jinsi alivyokuwa mbunifu na bajeti yake hii ambayo ni ya kwanza katika utawala wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli hii bajeti imetushangaza wengi katika ubunifu ambao wameuonyesha, lakini pia najua pamoja na yeye na timu yake, timu ya Makamu wa Rais Dkt. Mpango, Mheshimiwa Waziri Mkuu, mpendwa wetu, naye kuna mchango katika bajeti hii, lakini kuna Wizara ya Fedha pamoja na wataalam wote wa Wizara ya Fedha pamoja na Serikali nzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, wewe pia kwenye bajeti hii mchango wako ni mkubwa mno. Nilikuwa najaribu kufanya analysis ya bajeti hii, zaidi ya asilimia 70 ya michango ya Wabunge, nimeangalia kwenye Hansard katika miaka 15 iliyopita, ile michango mizuri yote ya Wabunge imechukuliwa na Serikali safari hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hicho kinaonyesha namna gani sisi kama Wabunge ni muhimu katika utayarishaji wa bajeti. Kwa hiyo lile jukumu letu la msingi la utayarishaji wa bajeti, nafikiri kwa safari hii limefanyika vizuri sana. Kwa hiyo pongezi kwa Bunge lako vile vile pamoja na Wabunge wote kwa bajeti hii nzuri. Nashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napongeza hivyo, nikiangalia bajeti hii imezingatia tija kwenye kilimo, imezingatia ushindani kwenye masoko yetu. Vile vile, ukiangalia ni kiasi gani ambapo karibu majimbo yote yameweza kunufaika kwa milioni mia tano ambazo amezitoa Mheshimiwa Rais kwa ajili ya kuziboresha barabara zetu za vijijini, lakini tumeshangazwa vile vile na nyongeza ya milioni 600 kwa ajili ya shule zetu za sekondari katika kata ambazo hazina shule.

Mheshimiwa Naibu Spika, napongeza zaidi hasa kwenye bajeti hii ambayo imeonyesha vile vile kuwa kutakuwa na barabara yetu ya TANZAM, kipande kile cha Igawa mpaka Tunduma ambayo imezingatia vile vile kuwa na njia nne katika kipande cha Uyole mpaka uwanja wetu wa ndege wa Songwe, nafikiri hiyo ni hatua muhimu sana. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa ku-consider hiyo lakini nashukuru kwa ujenzi vile vile wa barabara ya Isyonje kwenda mpaka Kikondo Makete.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru vile vile kwa Barabara ya Mbalizi kwenda Makongorosi. Pia nashukuru kwa kuwemo kwenye bajeti Barabara ya Mbalizi Shigamba ambayo hii ina matawi yake ya kwenda Isongole mpakani na Malawi. Kwa kweli nashukuru sana. Vile vile nashukuru kwa miradi ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilipoiangalia hii bajeti imelenga kwenye kilimo, lakini imelenga zaidi kwenye maandishi. Ukiangalia bajeti hii, hakuna mahali utaona kuna uwekezaji kwenye kilimo, hakuna. Kama kuna uwekezaji ni kidogo mno, wala hata huwezi kuuona, lakini nimeshangazwa badala ya uwekezaji, nimeona bajeti inaonyesha ongezeko la kodi kwa wakulima, ongezeko la kodi ya asilimia mbili kwa kilimo chetu ambacho hakina tija. Kwa kweli Mheshimiwa Waziri aende akaliangalie hilo, pamoja kwenye hotuba yake ya Kiswahili ameonyesha kwamba hiyo kodi haitamgusa mkulima mdogo. Hii kodi haijabagua, kwenye sheria ambayo imeandikwa Kiingereza hii kodi ni kwa mkulima yeyote, hata mtu anayekwenda kuuza kuku, anaenda kuuza mayai kwenye hoteli itabidi akatwe hiyo kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ukiangalia dhima ya kwetu ni kumjenga mkulima, kuwawezesha wananchi wetu ambao ni wengi. Sasa ukianzisha hii kodi ina maana hao wakulima kwa kiasi kikubwa unawaongezea mzigo, kwa vile mfanyabiashara yeye atataka faida, lakini mzigo wa hii kodi utaenda kwa mkulima. Mkulima wa Tanzania leo hii ukimlinganisha na mkulima wa nchi jirani yetu hata kwa kiasi tu cha mahindi, mkulima wa mahindi anazalisha mahindi kwa gharama ya zaidi ya 300,000, lakini mapato yake ya mahindi ni 100,000 na tena hayo mahindi akiyauza NFRA. Sasa huyo mkulima unamtoza kodi kutokana na nini na hii kodi ni ya mapato, mtu apate faida, huyu mkulima hana faida, kwa nini umtoze hii kodi?

Mheshimiwa Naibu Spika, huu uchumi wetu tunaoongelea uchumi shindani, inabidi tujilinganishe na wenzetu. Kwenye kahawa, uzalishaji wa Tanzania kwa mti mmoja ni gram 350 lakini mzalishaji wa jirani yetu Kenya kwa kahawa ya arabika ni karibu gram 400, mzalishaji wa Brazil ni gram zaidi ya 1,200. Sasa wote tunaingia sokoni, tufanye nini ili tumsaidie mkulima wetu aweze kuingia kwenye ushindani kwa vile bei haichagui kwamba hii ni kahawa ya Tanzania, Kenya au Brazil.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nategemea Mheshimiwa Waziri atakapokwenda kuiangalia hiyo bajeti tumsaidie vipi mkulima. Ili uzalishe vizuri unahitaji mbolea. Kwa hiyo tupeleke fedha isiyopungua bilioni 40 kuwasaidia wakulima kwenye ruzuku ya pembejeo, lakini pia tupeleke pesa kwa ajili ya utafiti ili wakulima wetu waweze kuzalisha kwa tija. Kwa hiyo, bado kuna haja ya kuongeza bajeti ya kilimo kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumzia suala la utafiti, nitatoa mfano mdogo tu. Tuna kilimo cha pareto ambayo inatumika kwa ajili ya kuhifadhi mazao. Pale kwenye halmashauri ya kwangu, wakulima wameshaanza kutumia maua ya pareto kwa ajili ya kuhifadhi mazao na imeonyesha kuwa inatumika vizuri zaidi, ina hifadhi kuliko viatilifu vingine. Kwa hiyo ningeomba fedha zipelekwe kwenye Taasisi yetu ya Utafiti ili pareto iingie sasa hivi kwenye uzalishaji wa viatilifu kwa ajili ya kuhifadhi mazao yetu na kupunguza post harvest loses.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naangalia leo kwenye taarifa ya habari kuhusu ushindani na majirani zetu, ushindani na nchi Jirani, wameanzisha sasa hivi sheria ya kuzuia malori ya Tanzania kuingia na kusafirisha mizigo kwenye nchi zao. Sasa tusipojitahidi katika hilo tutajikuta Tanzania tumekuwa kisiwa, bandari yetu itatumika vipi kama hawa wasafirishaji watazuiwa na ukichukulia kwamba hata uboreshaji wa reli yetu nao vile vile una changamoto ambazo zinatokana na majirani hao hao. Namwomba Mheshimiwa Waziri aangalie ni namna gani tuboreshe ushindani katika suala la usafirishaji, likiwemo la kuboresha bandari; la kuboresha reli yetu ya TAZARA, lakini vilevile tuangalie kupeleka meli kwenye Ziwa letu la Tanganyika ili zisafirishe mizigo kwenda Zaire.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli pendekezo langu kubwa ambalo naliona katika bajeti hii, iende ikae chini iangalie ni namna gani ya kumsaidia mkulima. Leo hii mkulima hasaidiwi kwa aina yoyote na hiyo kodi ya asilimia mbili, naomba iondolewe ilikuwepo kwa NFRA, inawezekana labda ni kwa ajili ya kuisaidia NFRA. Naiomba hata kule NFRA na kuondoke ili mkulima aweze kupata bei nzuri na hiyo sio kwa ajili ya mahindi tu, lakini hii asilimia mbili ni kwa mazao yote, kwa hiyo utakuwa ni mzigo mkubwa kwa wakulima wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja nashukuru sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii nami nichangie maboresho ya Mpango wetu. Kwanza nianze kabisa kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais na Serikali. Katika hii ripoti, imeonesha kabisa kuwa utekelezaji wa bajeti zilizopita ulikuwa ni mzuri sana. Pia ni hivi juzi tu Mheshimiwa Rais ametupelekea zaidi ya shilingi trilioni 1.3 kwenye Halmashauri zetu. Hizo zimeleta mabadiliko makubwa sana kwa nchi yetu na hayo mabadiliko nafikiri yatakuwa endelevu kwa jinsi ninavyoyaona mambo yanakwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa hotuba yake ya juzi, alipokuwa kwenye mkutano. Ile hotuba imeniwezesha hata mimi kujaribu kuuangalia huu Mpango vizuri zaidi, na nikagundua kuwa huu Mpango wetu umeacha kipengele ambacho ni muhimu sana. Kilimo hakijawekwa kama ni kipaombele katika huu Mpango. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapoongelea suala la tabia ya nchi, kilimo kinabeba kwa kiasi kikubwa hayo madhara ya tabia nchi. Dhima ya Mpango wetu tulionao ni kujenga uchumi shindani. Uchumi shindani unashindana na nani? Sasa ukiangalia huu Mpango wetu haujatuonesha kuwa huo ushindani wetu sisi tunashindana na nani? Nina imani ya kwamba sisi kama nchi, kama Tanzania, unapojenga uchumi shindani, unajilinganisha na wengine ambao tupo kwenye ukanda mmoja, kama East Africa, SADC au Afrika kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hilo kwa sababu, nchi za wenzetu, kilimo wamekipa kipaombele sana. Uzalishaji kwenye kilimo ukiangalia nchi kama wenzetu Zambia, uzalishaji wa mahindi ni magunia 30 mpaka 40 kwa eka, ukilinganisha na sisi ni magunia ambayo hayazidi 10. Sasa unaona ni kiasi gani sisi hatujajijengea kilimo kikawa ushindani kwenye ukanda wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naangalia mapato yanayotokana na zao la kahawa kwa wenzetu Waganda. Kwa mwaka 2020, wenzetu foreign exchange ya kahawa wamepata dola karibu milioni 515 ambayo ni karibu shilingi trilion 1.2; wakati sisi tulichopata hakizidi shilingi milioni 135, ambayo ni asilimia 30 au theluthi tu ya ile ya wenzetu wa Uganda. Sasa ukiangalia ungetegemea wapi tupate mapato mengi ya kigeni yanayotokana na kilimo cha kahawa? Kwa imani yangu, nafikiri sisi tungepata nyingi zaidi inawezekana hata mara mbili ya hizo. Ni kwa nini wenzetu wamepata fedha nyingi hizo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huhitaji hata elimu kubwa. Wanachokifanya wezetu, kwanza wamejenga ile chain ya uzalishaji. Kwenye production wamehakikisha kuwa wakulima wanapewa ruzuku (subsidy) kwenye mbolea na wakulima wanapewa malengo. Sasa hapa kwetu hiyo haipo. Naangalia hata kwa nchi ya Rwanda, nayo wameweka hivyo hivyo; kwenye kilimo kuna ruzuku kwenye mbolea, na wanzetu ruzuku yao ni zaidi ya nusu; asilimia mpaka 60, lakini sisi ruzuku hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitengeneza hesabu kwenye kilimo cha Watanzania, hakuna mkulima hata mmoja anayeweza kwenda na jembe shambani, kwa sababu hutakuwa na nguvu hiyo, hata kwa bei hizo zilizokuwepo. Mkulima wa kwetu, uwekezaji kwenye eka moja ya mbolea, atakachopata hata akawauzia NFRA, ni nusu tu ya ile gharama ya uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilikuwa naomba tunapoiangalia nchi kama Tanzania ambapo tegemeo kubwa ni kilimo, seriously kwenye mipango yetu tuangalie kilimo tutakisaidia namna gani ili tufanye kilimo cha kisasa, na huku ndiyo kutakuwa na mabilionea ambao Mheshimiwa Shangazi alikuwa anawaulizia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na wenzangu, kwa mwaka huu hivi sasa Serikali iagangalie namna gani itawapatia wakulima ruzuku ya mbolea na isisubiri Mpango. Leo hii kilimo kimeanza, lakini hakuna maandalizi yoyote ya kilimo. Pamoja na hali ya hewa kuwa mbaya, lakini wakulima wanaogopa kuandaa mashamba kwa sababu ya bei ya mbolea ambayo hakuna mtu atakayeweza kuimudu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ombi langu, kwa hesabu ya haraka haraka, nilikuwa naona Serikali ikitenga (sijui itazipata wapi, nina imani itazipata), kama shilingi bilioni 200 mpaka 250 zinaweza kusaidia zikaiokoa nchi yetu ili janga la njaa litakalotokana na ukame mwakani tuweze kuzalisha kwa tija. Kwa hiyo, naomba pamoja na mwendelezo wa hii ruzuku, lakini tungeanzia sasa hivi na uharaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Spika kwa lile agizo aliloipa Serikali. Nafikiri lile ni agizo muhimu, naiomba Serikali iangalie kwa haraka sana ni namna gani iweze kuwasaidia wakulima. Hilo tamko lisichelewe, kwa sababu kwa ukanda kama ule ninaotoka mimi, sasa hivi watu ndio wanatafuta mbolea ya kupandia, na kwa bahati mbaya hata mbolea za kukuzia leo wanaoagiza mbolea nina imani ni pungufu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipojaribu kuuliza wakasema, wazalishaji wote sasa hivi hawawezi kuzalisha kwa sababu order zilizopo kwenye wazalishaji nje ya nchi, labda mwezi March au April next year, 2022. Sasa hiyo inaweza kutusababishia sisi, kama tulikuwa hatujajiandaa kwa hilo, hata hiyo mbolea ambayo tunaitegemea isiwepo. Hata hizi mbolea za kupandia nazo hazipo. Sasa hii yote inatokana na sababu kwamba katika mipango yetu kilimo hakijawekwa katika kipaumbele. Kwa hiyo, naomba Serikali katika huu Mpango, iweke kipaumbele cha kilimo ikiwezekana namba moja, ili tuweze kusaidia jamii yetu ya Watanzania ambao ni zaidi ya asilimia 60 wanaotegemea kilimo. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata na mimi fursa ya kuchangia katika mapendekezo ya mpango wetu huu. Nianze kwa kuwapa pole wananchi wa Mbeya kwa ajali mbaya ya gari ambayo imetokea kwenye Mlima Iwambi mteremko wa kwenda Mbalizi, ambayo imesababisha vifo ikiwemo familia ya Katibu wa BAKWATA wa Mkoa, lakini hayo ni matokeo ya utekelezaji wa shughuli ambao unachelewa. Hilo eneo ilikuwa barabara ipanuliwe lakini mpaka leo haijapanuliwa. Kwa hiyo, tunapojadili hii mipango tuangilie vilevile athari zinazotokea kutokana na kucheleweshwa kwa utekelezaji wa hii mipango. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niwape pole wananchi wa Kagera na Watanzania kwa ujumla kwa ajali ya Precision Air ambayo imetokea na kupoteza Watanzania wenzetu. Pia ninapenda kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa utekelezaji wa Ilani. Ilani ya Chama cha Mapinduzi imetekelezwa vizuri, maeneo mengi ukiangalia hata miradi ya kimkakati kwa kweli imeibadilisha nchi yetu kwa kiasi kibwa. Naweza kusema hata brand ya Tanzania kwa kweli imebadilika kwa kiasi kikubwa. Hata wageni wanapokuja tumeshuhudia wageni wanatoka nchi mbalimbali hata Wabunge kutoka Mataifa mengine wamekuwa wakisifia wanavyoiona Tanzania inavyobadilika kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo ukiangalia huu mpango wetu kwa kweli mapendekezo ni mazuri lakini yamekaa kinadharia mno. Ukiangalia uhalisia haupo kwa sababu haielezi ya kwamba tutajipima vipi? Dhima ya mpango ni kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu, hiyo dhima ibebeba vyote hivyo lakini ukianza kuangalia huu mpango huoni sisi ya kwamba je tumeji position vipi kwenye ushindani kwenye Ukanda huu wa East Africa, kwenye ukanda wa SADC na kidunia, na hiyo ndiyo inatakiwa mpango ukae namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kama walivyosema wenzangu kuna upungufu mkubwa wa governance structure ya Wizara ya Fedha, ni bora ikarudishwa Tume ya Mipango ili iwe nje ya Wizara ya Fedha iweze ku coordinate Wizara zote, ili mipango ya Wizara zote iweze kupitia sehemu moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia leo sidhani kama kuna coordination ya aina hiyo, inawezekana kama ipo lakini haionekani na bila kuwa na hiyo na bila kurudisha ile BRN (Big Results Now), kwa kweli tutakuwa tunapanga mipango hapa na hakuna anayeifuatilia na hatujui ni nini kinachotokea. Tutampa wakati mgumu sana Mheshimiwa Rais kujua Serikali yake ina perform vipi, hata Chama cha Mapinduzi kurudi kwa wananchi nachi itakuwa ni kazi kubwa mno. Nayasema haya, tumekuwa tukizungumzia monitoring and evaluation kwa muda mrefu iko wapi? Bila kuangalia nini tulichokipanga na tunafanya nini inatuletea changamoto kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia tunazungumzia Deni la Taifa, tunasema Deni la taifa ni himilivu, kwa kiasi kikubwa utazungumza ndiyo kwa kuwaambia watu kwamba Deni la Taifa ni himilivu, kwa sababu hata modes naye kasema ni positive kwa hiyo ametu-evaluate vizuri. Lakini ukiangalia kwenye ripoti hii ya leo ule ukomo wa deni ukilinganisha na mauzo ya nje tumefikia kwenye mstari wa njano tunaenda kwenye mstari mwekundu. Maana yake nini? Maana yake ni nini? Ni kwamba tunakopa lakini uwezo wa kulipa hii mikopo ya kigeni inawezekana ikatushinda, sasa hili siyo jambo zuri kwa nchi yetu! Tulitaka tuone katika huu mpango measures gani umechukua ili ku- address hilo pesa za kigeni zipatikane nyingi ili nchi iweze kuendelea. Hizo fursa zipo lakini kwa sababu hatuna Tume ya Mipango hizo fursa huwezi kuziona. Kwa vile, mtu wa Madini fursa zipo anafanya yeye mwenyewe, mtu wa maliasili anafanya yeye mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hata kwenye kilimo bajeti imeenda nzuri sana lakini je, Wizara ya Kilimo ndiyo itaenda kulima? Hapana ni binafsi! Ile bajeti kubwa ungeiweka benki, watu wakaenda kuchukua mikopo wakajenga mabwawa badala ya Serikali kuanza kufanyakazi ambazo zinatakiwa zifanywe na sekta binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia yote hayo, Mheshimiwa Rais katoa Trilioni Moja zikakopeshe wakulima; Je, zimekwenda? hazijaenda Trilioni Moja! Kama kungekuwa na ubunifu, Je, kuna watu wabunifu hakuna! Ilitakiwa kuwe na watu wabunifu ya kwamba hii Trilioni Moja tuitumie namna gani na siyo ametoa fedha taslimu Hapana! Yeye inakuwa ni window ili watu waweze ku- access zile pesa ziende kwenye sekta ya kilimo tuweze kuzalisha na kilimo kitaibadilisha Tanzania kwa kiasi kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu kwenye kilimo ni kwamba tungeondoa masoko kwenye Kilimo. Masoko ikiwezekana yakajitegemee tusichanganye uzalishaji na masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii bei ya kahawa haiendi vizuri kwa sababu gani, kahawa Tanzania siyo kwamba tunashindana na Brazil Hapana! Bali kahawa ya kwetu tunashindana kwa ajili ya ubora wa kahawa ya Tanzania. Lakini ni nani amekwenda kuuza huo ubora? Hakuna! Kwa hiyo, mtu anaenda sokoni hajui atauza kwa kiasi gani. Wakulima walijaribu wasiende sokoni lakini bei ya kahawa inaendelea kuporomoka, hiyo maana yake nini? inapunguza uwezo wa Taifa kwenye pesa za Kigeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba sana Bunge lako liielekeze Serikali iweze kutatua matatizo haya kwa haraka na haya matatizo yanaweza kutatuliwa kukiwa na checks and balances kwenye Wizara zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naangalia suala la mikopo kwa watu binafsi. Makusanyo ya ndani kwa Halmashauri ni Bilioni 860, asilimia 10 ni Bilioni 86, hizo asilimia 10 ni kwa ajili ya kuwakopesha vijana na wakina mama, siyo pesa ndogo! Mtaji wa Benki ni Bilioni 15. Hizi pesa zingepelekwa kwa wataalam tukaangalia tukawasaidia wakina mama pamoja na vijana Tanzania inaweza kubadilika ndani ya miaka Mitatu na wewe ukashangaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bilioni 86 ni leo, mwaka kesho tena zipo zingine zitaenda kwenye hiyo Mfuko. Changanya na hiyo Mifuko mingine ambayo iko kwenye Wizara zingine, kwa kuwa Mkopo siyo kumpa mtu hela! Mkopo ni kumsaidia mtu aweze kuzalisha, mkopo ni kumsaidia mtu aondoke kwenye umaskini awe tajiri. Sasa hatuwezi kuwasaidia vijana wetu, wamekuwa wakichukua hizi fedha za mikopo lakini unakuta siku ya marejesho wanakimbia na sisi tunaotoka mipakani wengine wanakimbilia mpaka nchi jirani. Kwa hiyo, ningeomba hili lichukuliwe kwa uzito wake na tusianze mambo mapya wakati mambo mazuri yapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, innovation haina maana uanze na kitu kipya. TAZARA inafanya nini! Trillions of money zimelala ardhini! TAZAMA pipeline, Tanzania ina asilimia 33 imelala inafanya nini! Magari yanaua watu wetu barabarani badala yake mafuta yangesukumwa yakaenda Nyanda za Juu Kusini, kukawa na Dry Port pale Mbeya wakachukua mafuta kutoka hapo! Lakini unaweza kuyasafirisha hayo mafuta yakaenda mpaka Malawi na Zambia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwa na mtazamo wa namna hiyo ndiyo sababu ni bora tukawa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Njeza muda wako umekwisha, ahsante.

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na mimi kupewa fursa hii ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimwia Rais kwa matokeo mazuri sana ya utekelezaji ambayo imepelekea ni nchi pekee katika Afrika Mashariki ambayo ilikuwa na ukuaji ambao ni chanya. Tulikuwa na ukuaji ambao nchi nyingine zote ukuaji wake ulikuwa na negative GDP. Kwa hiyo ningependa sana kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa hilo lakini pia na Serikali nzima akiwemo Makamu wa Rais na Waziri Mkuu. Kazi iliyofanyika ni kubwa mno ni nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo yote mazuri lakini sasa hivi tunashuhudia dunia nzima inaingia kwenye changamoto kubwa za uchumi, na huo mdororo wa uchumi umeshaanza kuonekana hapa kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipokuwa najaribu kuangalia wenzetu hili suala wamelionaje na wamelichukuliaje na sisi Tanzania kama sehemu ya dunia je, tujiweke wapi?

Kwa kweli kwa kiasi kikubwa ukiangalia mashirika makubwa ya fedha ikiwemo IMF pamoja na J. P. Morgan wameonesha ya kwamba pamoja na hizo changamoto lakini kwa nchi kama Tanzania hii ni fursa. Kwa hiyo badala ya kuangalia zile changamoto zilizopo zinazotokana na hii hali sisi sasa tungejipanga kuangalia fursa ambazo zipo kutokana kwanza na athari za UVIKO na pia na athari zinazotokana na vita ya Urusi pamoja na Ukraine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanzia hatua za haraka, nina imani Serikali kupitia Ibara 140 ya katiba yetu na Sheria ya Bajeti Ibara ya 35 mpaka 39 ilichukua hatua hizo ambazo zimeitaka Serikali kuwa na mfuko wa dharura (contingence fund). Kwa hiyo katika hali ya namna hii ninategemea kwamba Serikali itatumia mfuko huo kuchukua hatua za haraka ili tuweze kunusuru hali ya mfumuko wa bei. Lakini siyo mfumuko wa bei tu, vile vile kutakuwa na mfumuko wa mahitaji ya pesa za kigeni ambayo yanaweza kutuweka katika hali ngumu zaidi. Sasa tufanye nini ili tuweze kuondokana na hilo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe mwenyewe unajua, kuwa mikopo yetu mingi tunalipa kwa pesa za kigeni. Kama kutakuwa na mfumuko na mahitaji makubwa ya pesa za kigeni, nchi yetu ifanye nini? Nina imani ya kwamba hatuwezi kuahirisha kulipa madeni lakini tutahitaji pesa za kigeni nyingi. Uchumi wetu unategemea kilimo. Nawashukuru sana Wabunge wameongea kwa kiasi kikubwa umuhimu wa kilimo kwa Tanzania. Lakini nchi yetu ina madini, nchi yetu ina utalii, nchi yetu ina bandari. Hivyo vitu vitatu vikipelekewa msukumo na Serikali ikajikita katika hivyo vitu vitatu vinne nina imani tutavuka salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kilimo unachohitaji ni kuwa na kilimo chenye tija, huhitaji zaidi ya hapo. Kilimo chenye tija. Kwa mfano leo kilimo chetu heka moja ya mahindi tunazalisha tani moja wakati kawaida kabisa heka moja ya mahindi inatakiwa izalishe tani nne. Kwa hiyo tukianzia na hiyo tuu, ina maana tutakuwa tumejipeleka mahali pazuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini namshukuru sana Mheshimiwa Rais kupitia Wizara ya Kilimo anavyofanya mageuzi (transformation) kwenye kilimo, nafikiri katika hiyo na motisha walizopata wakulima nina imani ya kwamba kupitia kilimo hili tutaliweza. Kwa hiyo tunahitaji pesa za kigeni kupitia hata nafaka. Nimesema hii ni fursa kwa sababu Ukraine na Russia ndio walikuwa tunaingiza kwa kiasi kikubwa ngano. Lakini nchi za jirani walikuwa wanaingiza mpaka mahindi wanaagiza kutoka Russia. Sasa mahindi yetu yatapata soko kubwa na bei zimeshaanza kuwa nzuri. Kwa hiyo tukijikita kwenye kilimo cha mahindi nina imani kuwa tutaenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye madini tuna fursa kubwa lakini kuna wawekezaji ambao wanahitaji kuwekeza kwenye madini bado wanazungushwa, hawapewi kipaumbele. Mfano mmoja wapo kwa muda mrefu nimesimama hapa Bungeni; tuna madini yanaitwa Niobium. Kuna wawekezaji toka miaka ya 2015 mpaka leo wanashindwa kupata leseni. Mpaka financial institution wameamua waachane na huu mradi. Wawekezaji nao wanataka kuachana na huu mradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi ombi langu, kwa ajili ya hii hali miradi mingine kama hiyo tuichukue kwa dharura. Tukikosa pesa za kigeni inawezekana tukakosa hata chakula. Hii mbolea tunayoisema tunahitaji pesa za kigeni. Pesa za kigeni tutazipata wapi? Pesa za kigeni hatuwezi kuzipata kwenye kuondoa tuu ruzuku. Pesa za kigeni zitapatikana kwenye uzalishaji wetu kwenye kilimo, madini na utalii. Kwa hiyo ningeomba kwa kiasi kikubwa Serikali ichukue hatua za makusudi. Hii hali tuliyonayo sasa hivi ya uchumi wa dunia ni hali ambayo inaweza kutupeleka mahali pabaya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vile vile tunahitaji kuboresha miundombinu. Kwa sababu miundombinu nayo inaweza kutuletea inflation. Sasa kwa kiasi kikubwa...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Oran Njeza kwa mchango wako.

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mawaziri na viongozi wote wa TAMISEMI, kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kutumia fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Taifa letu katika kuboresha maisha ya wananchi na pia utayari wetu wa ushindani wa Kimataifa (national competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha miezi tisa ya mwaka huu wa bajeti, Serikali kupitia TAMISEMI imesimamia kwa uadilifu na ufanisi mkubwa mwendelezo wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya vituo vya afya na miundombinu ya shule za msingi na sekondari na pia ukarabati wa barabara za vijijini. Jimbo la Mbeya Vijijini limenufaika kwa ujenzi wa vyumba 204 vya madarasa kwa shule za msingi na sekondari. Kupitia miradi ya UVIKO-19 Halmashauri imepata zaidi ya shilingi bilioni 4.8 na pia ujenzi unaendelea kwa shule ya sekondari mpya ya Mjele. Ujenzi wa miundombinu ya afya na elimu umeweka historia ya kipekee katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya. Wananchi wana imani kubwa ya huduma nzuri zitakazotolewa ikiwemo kuwepo wa watalaam bingwa, vifaa tiba vyote muhimu na madawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio hayo makubwa, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya bado ina changamoto za kumalizia miundombinu ya zahanati na vituo vya afya vilivyojengwa kwa nguvu za wananchi ikiwemo vituo vya afya kwa Kata ya Ilungu, Kata ya Isuto, Kata ya Bonde la Songwe, na zahanati kwa kila kijiji. Wananchi wamejitahidi kujenga maboma ya zahanati na vituo vya afya na wanategemea Serikali itawaunga mkono kumaliza kazi zilizobakia bila kuchelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara za lami katika maeneo ya kilimo cha kahawa na mbogamboga. Kazi zinazoendelea ni barabara ya Inyala – Simambwe ya kilometa zaidi ya 16 inayopita Kata za Inyala, Itewe, Maendeleo na Tembela. Pia kuna ujenzi kilometa 10 za barabara ya Lupeta – Wimba - Izumbwe, inayopita Kata za Swaya na Igale. Pamoja na kuwepo fedha ya wafadhili, ujenzi wa barabara hizi unasuasua sana. Serikali ichukue hatua za haraka kunusuru miradi hii muhimu kwa maendeleo ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio hayo makubwa, katika Halmashauri zetu tumekuwa tunakabiliwa na changamoto hasa kwenye miundombinu ya barabara. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, barabara zinazohudumiwa na TARURA kwa asilimia zaidi ya 90 zipo kwenye hali mbaya sana kutokana na mafuriko. Maeneo mengi ya vijijini barabara hazipitiki kutokana na madaraja kusombwa na mafuriko. Naiomba Serikali ichukue hatua za haraka kunusuru hali hii ili wananchi waweze angalau kusafirisha mazao yao. Hali ya mtandao wa barabara wa zaidi ya kilometa 1,000 ni mbaya na hazipitiki kirahisi hasa kipindi cha mvua. Barabara ambazo zipo kwenye hali mbaya sana ni pamoja na Ifiga (Ijombe) – Iwalanje; Shamwengo - Us/Muungano - Simambwe; Irambo – Nsonyanga; Nsenga – Swaya - Nzove; Ilembo – Mbawi; Madugu – Ilindi – Isuto; Ilembo – Mbagala; Ilembo – Mwala; Iwowo-Igalukwa -Mlowo; Horongo – Igale; Songwe Viwandani – Jojo; Kawetere – Ikukwa; Mbalizi – Ilota; Nyalwela – Ngole; Nyalwela, Mbonile – Itala na Igawilo - Hatwelo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bajeti ndogo ambayo ni kilometa chini ya 100 kwa mwaka, ni vigumu kutatua changamoto za barabara hizi, kwa kiasi kikubwa zinabeba uchumi wa kilimo na madini kwa Mbeya na Tanzania kwa ujumla. Napendekeza Serikali iweke msukumo zaidi kwenye kuboresha miundombinu ya barabara kurahisisha usafirishaji wa mazao ya kilimo, itasaidia kuimarisha uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza kuwepo na msukumo wa kuhakikisha Halmashauri zinasimamia kikamilifu elimu ya kujitegemea kwenye ngazi zote za msingi na sekondari. Kwa shule za vijijini kushirikisha Maafisa Ugavi wa Kilimo na Uvuvi kuanzisha mashamba darasa kwa kila shule za vijijini. Kwa shule za mijini kuna fursa pia kuweka msukumo wa elimu ya kujitegemea kulingana na mazingira ya shule ikiwemo elimu ya ufundi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na umuhimu wa mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, napendekeza Serikali iboreshe mfumo wa mikopo hii kuendana na madhumuni ya mikopo ya kuimarisha kundi hili kiuchumi. Uendeshaji wa mikopo hii uwe na misingi ya huduma za kifedha jumuishi (financial inclusion) ikiwemo elimu ya matumizi ya mikopo na usimamizi wa kitalaam wa mikopo. Kwa ukubwa wa mfuko huu kitaifa kuna umuhimu wa kuunda taasisi ya kifedha kuusimamia kwa tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Halmashauri ya Mbeya kuna Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mbalizi ambao una wakazi zaidi ya 100,000 na shughuli nyingi za kiuchumi ikiwemo viwanda, madini na hata Uwanja wa Ndege wa Songwe. Pia katika Kata ya Utengule Usongwe kuna Kijiji cha Mbalizi ambacho mipaka yake haiungani na vijiji vingine vya kata hiyo. Napendekeza Serikali irekebishe mipaka ya Mbalizi na ipandishe hadhi kutoka Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mbalizi kuwa Halmashauri ya Mji wa Mbalizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo ya kugawa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ni kilio cha muda mrefu, na Hayati Dkt. Magufuli mwaka 2020 aliagiza zoezi la kugawa lifanyike haraka na aliagiza kubadilisha jina la Jimbo la Mbeya Vijijini haraka iwezekanavyo. Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ina sifa zote za kugawa ikiwemo uwezo kiuchumi ni mkubwa sana, idadi kubwa ya wakazi na pia changamoto za kijiografia. Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya inapakana na Halmashauri zote za Mikoa ya Mbeya na Songwe kasoro Kyela na Tunduma na pia inapakana na hata Mkoa wa Njombe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mawaziri na viongozi wote wa wa Ofisi ya Rais – Utumishi, kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka wa Ofisi ya Rais – Utumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Utumishi, kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Taifa letu katika kuboresha maisha ya wananchi na pia utayari wetu wa ushindani wa Kimataifa (National Competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mapitio ya kipindi cha bajeti 2021/2022, Serikali kupitia Wizara ya Utumishi na Utawala Bora imesimamia kwa uadilifu na ufanisi mkubwa masuala yote ya utumishi na hasa kurudisha uwabikaji kazini iliopelekea ufanisi mkubwa hasa kwenye utekelezaji wa miradi. Jimbo la Mbeya Vijijini limenufaika kupitia miradi ya TASAF ambapo imebadilisha maisha ya wananchi katika vijiji husika. Pia kwa kusimamia vizuri, rushwa na upendeleo umepungua kwa kiasi kikubwa kupelekea ufanisi mkubwa sehemu za kazi na hata miradi kukamilika kwa ufanisi mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio hayo makubwa, napendekeza kuendeleza mafunzo ili kuboresha weledi wa watumishi ikiwemo upanuzi wa Chuo cha Watumishi Mbeya na eneo muafaka kwa ujenzi wa chuo kipya na cha kisasa ni Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ambapo kuna maeneo mazuri ikiwemo yaliyokuwa mashamba ya Tanganyika Packers, Mbalizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na upungufu mkubwa wa watumishi katika sekta mbalimbali, napendekeza Serikali iendelee kutoa ajira zaidi hasa kwenye maeneo ya kuchochea uchumi na pia sekta ya afya, elimu na kilimo. Kutokana na idadi kubwa ya wahitimu kukosa ajira na wametapakaa kila kona ya Tanzania hasa vijijini, napendekeza Serikali kuhakikisha ajira zinatolewa kwa usawa wa maeneo yote ya Tanzania kulingana na sifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na majukumu na unyeti wa mashirika ya kadhaa ya umma ikiwemo ushindani wa kupata watalaam wazuri, mashirika haya yaruhusiwe moja kwa moja kutoa ajira ili yaendane na mahitaji yao na Tume ya Ajira wawe na jukumu la ushauri/udhibiti. Taasisi kama CAG kisheria anatakiwa awe huru ikiwemo uhuru wa kuajiri na hata taasisi kama mabenki, TANESCO, Bandari, TRA ni muhimu wakapewa uhuru wa kuajiri kulingana sifa ila kupata watalaam wazuri kiushindani na pia kulingana na bajeti za mashirika husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na maboresho ya mfumo wa TASAF, napendekeza pia kuboresha zaidi mfumo huo ikiwemo msukumo wa miradi ilenge maeneo yatakayochochea uzalishaji wa mali ili zisaidie jamii kwa upana mkubwa. Pamoja na maeneo ya uzalishaji, msukumo ujumuishe kuimarisha masoko ya bidhaa zitakazozalishwa katika maeneo ya mradi. Miradi ilenge kuboresha elimu na hata kusomesha watoto wanaotoka kwenye kaya maskini ya maeneo husika. Serikali iboreshe taratibu za kupata maeneo ya miradi ya TASAF ili kupunguza malalamiko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mawaziri na viongozi wote wa Wizara ya Maliasili na Utalii, kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Waziri wa Maliasili na Utalii, kwa hotuba nzuri iliojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Serikali katika utekelezaji wa ustawi wa jamii na maendelo endelevu, na hii ni mojawapo ya nguzo kuu katika utayari wetu wa ushindani wa kimataifa (national competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 ambayo ni Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.

Mheshimiwa Spika, pamoja na programu ya kutunza maliasili zetu, Serikali iweke usimamizi wa msitu hasa ya asili ambayo inaendelea kupotea kwa matumizi ya nishati. Katika kupangilia matumizi mazuri ya ardhi, ihusishe Wizara zote zinazosimamia Maliasili, Ardhi, Kilimo, Wizara za Maji na pia Wizara inayosimamia Mazingira. Kwa vile binadamu tunaongezeka ni muhimu kuhakikisha ulinzi kwa kuhifadhi mazingira yetu na kuwepo msukumo zaidi kwenye kuboresha mazingiara.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hatua zinazochukuliwa na Serikali kurejesha mahusiano mazuri kati ya TANAPA (Hifadhi ya Kitulo) na wananchi wa Kata za Ilungu, Igoma, Ulenje na Inyala, bado suluhu haijapatikana. Kuna mgogoro wa miaka mingi wa mpaka kati ya TFS na wananchi wa Kijiji cha Mwashoma. Pia kuna mgogoro wa TANAPA (Hifadhi ya Kitulo) na wananchi wa Kijiji cha Kikondo ambao eneo lao lilichukuliwa na TANAPA bila kulipa fidia. Pamoja na changamoto hiyo ya GN za Hifadhi ya Kitulo, pia kuna utata wa mpaka wa Wilaya ya Mbeya na Wilaya ya Makete na inahitajika Wizara ya Ardhi kupitia upya mipaka na kurekebisha. Kutokana na mgogoro huu kuchukua muda mrefu na kusabisha uvunjifu wa amani, kuna ahadi ya mwaka 2015 alitoa Mheshimiwa Hayati Magufuli na kumwelekeza Waziri wa Ardhi na pia Waziri wa Maliasili na Utalii wa wakati huo kupitia upya mipaka, ili wananchi wa Kata za Ilungu na Inyala, hususani Kijiji cha Kikondo na Mwashoma waachiwe maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Madini
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Phillip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mawaziri na viongozi wote wa Wizara ya Madini, kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza Mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Waziri wa Madini, kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Taifa letu katika kuboresha maisha ya wananchi na pia utayari wetu wa ushindani wa Kimataifa (National Competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio ya sekta ya madini, Serikali inashauriwa kuchukua hatua za kuimarisha zaidi sekta hii muhimu ili kukabiliana na athari za kiuchumi kutokana Covid-19 na sasa vita vya Urusi na Ukraine. Kutokana na athari ya kiuchumi uliokumba dunia nzima, hii inaweza kuwa fursa kwa Serikali kuvutia uwekezaji zaidi kwenye madini hasa dhahabu, madini ya chuma na madini ya calcium carbonate, limestone na phosphate. Dhahabu ina historia ya bei kutoyumba kwenye soko la dunia kwa vile mabenki yanatumia dhahabu kwenye kuwekeza na kutokana pia na kuyumba kwa thamani ya shilingi na hata dola ya Marekani, Serikali inaweza kutumia dhahabu kama mbadala wa kuwekeza amana zake.

Mheshimiwa Spika, vita vya Urusi na Ukraine vimesabisha upungufu mkubwa wa uzalishaji wa mbolea na hii ni fursa kwa Serikali kuwekeza kwenye viwanda vya mbolea kwa kutumia malighafi zinazopatikana hapa nchini kama vile phosphates, calcium carbonate, limestone na natural gas. Katika kipindi cha mtikisiko wa uchumi, bei ya madini ya chuma na hata makaa ya mawe haiyumbi na Serikali inaweza kupata mapato mengi katika kipindi hiki.

Mheshimiwa Spika, napendekeza Serikali kuchukua hatua za makusudi na kuharakisha uwekezaji kwenye mradi wa chuma (Liganga Iron Ore) ikiwa ni pamoja na makaa ya mawe (the Mchuchuma coal mining and power projects). Mradi wa Liganga na Mchuchuma ulitarajia uwekezaji wa dola za Kimarekani bilioni tatu na kuzalisha ajira zaidi ya 30,000 na hii inaweza kuwa fursa nzuri katika hiki kipindi cha balaa la athari za Covid-19 na vita vya Urusi na Ukraine.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mradi wa Liganga na Mchuchuma, napendekeza Serikali kuchukua hatua kuharakisha uwekezaji kwenye mradi wa madini ya NIOBIUM ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Kiwanda cha Ferroniobium (FeNb) ambacho kitakuwa cha kwanza Afrika na cha nne duniani. Kutokana na mahitaji makubwa ya ujenzi wa reli, madaraja na reli ya SGR, kuna mahitaji makubwa ya vifaa vya chuma ambavyo ni imara, lakini vyepesi na vyenye ubora wa Kimataifa. Kwa kutumia sheria zetu za uwekezaji, Serikali itumie fursa za kipindi hiki ili kuvutia wawekezaji kwenye madini ya viwandani ili yaongezwe thamani hapa kwetu na pia kuvutia malighafi ya madini toka nchi zingine ili yachakatwe hapa kwetu.

Mheshimiwa Spika, Tanzania imebahatika kuwepo kwa madini ya NIOBIUM ambayo inapatikana milima ya Pandahill Wilaya ya Mbeya na mahitaji ya Ferroniobium (FeNb end product) ni makubwa duniani na hapa kwetu pia.

Mheshimiwa Spika, Serikali inahitaji kujiwekekea mikakati ya haraka (quick wins) ili kuhakikisha inakabiliana na athari za kiuchumi kutokana Covid-19 na sasa vita vya Urusi na Ukraine. Kwa kutumia rasilimali zetu za madini, Serikali inaweza kutengeneza fursa nyingi na kupitia Mradi wa Niobium na Kiwanda cha Ferroniobium, ajira 2,000 zitakazozalishwa wakati wa ujenzi na pia kutakuwepo ajira za kudumu zaidi ya 600 na indirect jobs 7,000. Mradi utazalisha mapato kila mwaka shilingi bilioni 500 (US$ 220 million) ambapo mapato kwa Serikali kila mwaka shilingi bilioni 50 (US$ 22 million) na uhai wa mgodi ni zaidi ya miaka 30. Hiki kitakuwa kiwanda cha kisasa cha kwanza Afrika (Modern Manufacturing Plant and Smelter). Pamoja na kuingiza teknolojia hii adimu na ujuzi (skills transfer) pia itachangia huduma za kijamii (corporate social investment in community) na chanzo cha fedha ya kigeni. Naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari za Mwaka 2016
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, pamoja na timu nzima ya Wizara yake kwa kuleta Muswada wa Sheria ya Huduma za
Habari wa Mwaka 2016 (The Media Services Bill, 2016). Taaluma ya habari ni mojawapo ya taaluma muhimu sana katika jamii yetu kwa kuuhabarisha umma mambo mbalimbali yakiwemo ya kisiasa, kiafya, kielimu na masuala ya uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taaluma ya habari ni tegemeo kubwa la jamii yetu na hivyo inahitaji a high degree of trust; na kwa kwa hali hiyo taaluma hiyo inahitaji kuaminiwa na jamii na pia kuwa na maadili ya hali ya juu. Napongeza Muswada huu kwa vile unalinda uhuru wa vyombo vya habari kuhakikisha habari zina ukweli na usahihi na pia Muswada huu unalinda utu na heshima ya kila mtu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono Muswada huu kwa vile unalenga kuhakikisha nchi yetu inaendeleza kupinga ubaguzi wa aina yoyote ile. Pia Muswada huu uhakikishe kwa namna yoyote ile unazuia vitendo vya rushwa kwa wanahabari na vyombo vya habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taaluma ya habari ihakikishe inalinda umoja na amani ya nchi yetu. Kwa vile Tanzania ni sehemu ya dunia, hivyo Muswada huu uhakikishe kuwa unazingatia sheria na maadili mema yaliyo katika Miswada ya nchi nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Waziri, Naibu Waziri na viongozi wote kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti,napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti,katika kipindi kinachoishia Aprili, 2022 Serikali kupitia Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imesimamia kwa uadilifu na ufanisi mkubwa masuala yote ya viwanda na pia kuna mwelekeo mzuri wa kuboresha mazingira ya biashara (blueprint). Pia kwa kusimamia vizuri diplomasia ya uchumi, imejenga imani kubwa kwa wawekezaji ambao wameonesha nia ya kuwekeza kwenye maeneo muhimu ya uchumi wetu. Katika kipindi cha mwaka mmoja na miezi minne, Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara, imetekeleza miradi mingi ya viwanda na pia kuboresha mazingira ya biashara (blueprint) kwa kuondoa tozo, ada na kodi ambazo zimekuwa kikwazo katika shughuli za uchumi. Kupitia blueprint, Serikali inatambua umuhimu wa kuweka mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji ili kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini wa kipato. Pamoja na jitihada za Serikali, bado kuna mahitaji makubwa ya viwanda vya kuongeza thamani ya madini, kuongeza thamani ya mazao yetu vijijini na pia kuna changamoto za uhakika wa masoko ya mazao ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza Serikali iendelee na msukumo wa kujenga viwanda vya mazao ili tuweza kuongeza thamani hapa nchini na pia kuzalisha ajira. Kutokana na neema ya kijiografia, nchi yetu inazalisha mazao ya aina mbalimbali ikiwemo zao la pareto na Tanzania inaongoza Afrika, pia ni wa pili duniani kwa uzalishaji wa pareto. Uwekezaji zaidi kwenye Kiwanda cha Viuadudu cha Kibaha kuna fursa kubwa ya kuzalisha mbolea na hata viuatilifu kutokana na pareto inayolimwa hapa nchini. Serikali ichukue hatua za kutafuta wawekezaji wa viwanda vya viuatilifu ambavyo mahitaji yake ni makubwa hapa nchini na hata soko la nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti,pia nchi yetu ina neema ya madini ambayo ni malighafi ya kutengeza aina mbalimbali za mbolea. Madini aina ya calcium (chokaa ya kilimo) na phosphate inapatikana kwa wingi hapa nchini na malighafi muhimu kutengeneza mbolea aina ya CAN na DAP na hata NPK. Kuwepo kwa gesi asilimia ni fursa nyingine kwa viwanda vya mbolea aina ya Urea ambayo mahitaji yake ni makubwa sana Tanzania na duniani kote.

Mheshimiwa Mwenyekiti,pamoja na madini hayo kuna madini adimu duniani kama vile NIOBIUM ya Pandahill Mbeya ambayo kuna fursa ya kujenga kiwanda cha kuchakata hayo madini ili kutengeza FERRONIOBIUM ambayo mahitajika yake ni makubwa hapa nchini na pia nje ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mradi wa Liganga na Mchuchuma, napendekeza Serikali kuchukua hatua kuharakisha uwekezaji kwenye mradi wa madini ya NIOBIUM ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kiwanda cha Ferroniobium (FeNb) ambacho kitakuwa cha kwanza Afrika na cha nne duniani. Kutokana na mahitaji makubwa ya ujenzi wa reli, madaraja na reli ya SGR, kuna mahitaji makubwa ya vifaa vya chuma ambavyo ni imara, lakini vyepesi na vyenye ubora wa kimataifa.

Kwa kutumia sheria zetu za uwekezaji, Serikali itumie fursa za kipindi hiki ili kuvutia wawekezaji kwenye madini ya viwandani ili yaongezwe thamani hapa kwetu na pia kuvutia malighafi ya madini toka nchi zingine ili yachakatwe hapa kwetu. Tanzania imebahatika kuwepo kwa madini ya NIOBIUM ambayo inapatikana milima ya Pandahill, Wilaya ya Mbeya na mahitaji ya Ferroniobium (FeNb end product) ni makubwa duniani na hapa kwetu pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti,Serikali inahitaji kujiwekekea mikakati ya haraka (quick wins) ili kuhakikisha inakabiliana na athari za kiuchumi kutokana Covid-19 na sasa vita vya Urusi na Ukraine. Kwa kutumia rasilimali zetu za madini, Serikali inaweza kutengeneza fursa nyingi na kupitia Mradi wa Niobium na Kiwanda cha Ferroniobium, ajira 2,000 zitakazozalishwa wakati wa ujenzi na pia kutakwepo ajira za kudumu zaidi ya 600 na indirect jobs 7,000. Mradi utazalisha mapato kila mwaka shilingi bilioni 500 (US$ 220 million) ambapo mapato kwa Serikali kila mwaka shilingi bilioni 50 (US$ 22 million) uhai wa mgodi ni zaidi ya miaka 30. Hiki kitakuwa kiwanda cha kisasa cha kwanza Afrika (Modern Manufacturing Plant and Smelter).

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuingiza teknolojia hii adimu na ujuzi (skills transfer) pia itakuwa itachangia huduma za kijamii (Corporate Social Investment in Community) na chanzo cha fedha ya kigeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana fursa za kijografia, napendekeza msukumo zaidi kwenye EPZ na industrial parks hasa kwenye bandari zetu na maeneo yanayozunguka viwanja vya ndege kikiwemo Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Songwe kilichopo Wilaya ya Mbeya. Napendekeza Serikali ichukue hatua za haraka kubadilisha matumizi ya eneo ya iliokuwa Tanganyika Packers litumike kwa EPZ na industrial parks hasa kwa mahitaji ya viwanda mbalimbali ikiwemo vya mazao ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napongeza mkakati wa Serikali kwa kuanzisha soko la bidhaa (The Tanzania Mercantile Exchange - TMX). Wizara ya Viwanda na Biashara iwe mstari wa mbele kuimarisha hili soko la bidhaa ambapo wauzaji na wanunuzi wanakutana na kubadilishana bidhaa na fedha katika mtindo wenye mpangilio na utaratibu maalum. Kuanzishwa kwa soko la bidhaa kutamwezesha mkulima kuweza kuuza mazao yake katika utaratibu unaoeleweka bila kulanguliwa. Pia soko la bidhaa linatupa mwanga na mwanzo mzuri wa kuboresha soko la madini kuwa sehemu ya TMX.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan - Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango - Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa - Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Waziri, Naibu Waziri na viongozi wote wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miezi kumi ya mwaka wa 2021/2022, Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imesimamia kwa uadilifu na ufanisi mkubwa masuala yote ya elimu hasa kuboresha ufaulu na hata miundombinu ya madarasa na mabweni. Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya imekuwa inapitia kipindi kigumu cha changamoto za kuporomoka kutoka kuongoza kimkoa katika ufaulu wa elimu ya sekondari. Pia ufaulu kwa shule za msingi unapitia katika changamoto kubwa hasa kutokana na mazingira ya shule za vijijini ikiwemo upungufu wa walimu. Pamoja kuwa ni jukumu jumuishi kwa wazazi, bado kunahitaji uharaka wa kupitia sera ya elimu kuweza kuboresha taaluma kwa shule za vijijini ambazo kwa kiasi kikubwa hazifanyi vizuri ukilinganisha na shule za mijini.

Mheshimiwa Spika, walimu bado wanaendelea kufanya kazi katika mazingira magumu kwa kukosa majengo ya nyumba za kuishi. Napendekeza Serikali kuendelea kushirikiana na wananchi katika ujenzi wa nyumba za walimu iende sambamba na ujenzi wa maboma na pia madawati kwa wanafunzi wote. Ni muhimu kuhakikisha motisha kwa walimu ili kuboresha taaluma iwe ya kiushindani kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki, SADC na hata Afrika. Napendekeza pia Serikali itoe kipaumbele kwa kulipa madai ya malimbikizo kwa walimu ili kupunguza muda wa kufuatilia malipo yao na badala yake waelekeze muda zaidi kwenye kufundisha.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki tunapopambana na magonjwa yasiyo ya kuambukizwa yakiwemo magonjwa ya kansa, shinikizo la damu, figo, moyo na kadhalika, narudia tena kuishauri Serikali kuweka kipaumbele cha kuboresha elimu ya afya, ikiwemo upanuzi wa ujenzi wa ndaki ya sayansi ya afya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam - Mbeya College of Health and Allied Sciences (UDSM-MCHAS). Serikali itoe kipaumble cha kutenga eneo la kutosha kwa chuo hiki kutoka kwa eneo la iliyokuwa Tanganyika Packers Ltd., Mbalizi Mbeya.

Mheshimiwa Spika, katika kuwezesha uwekezaji na uendelezwaji wa viwanda endelevu, Tanzania inahitaji kuzalisha watalaam wengi na hasa ujasiriamali na taalum ya ufundi ngazi za kati na chini ambapo mahitaji ni makubwa. Pamoja na kujiwekea malengo ya kuongeza viwanda, naishauri Serikali ilitazame upya suala la uwepo wa nguvu kazi (vijana kupata mafunzo ya ufundi na ujasiriamali) ya kutosha na itakayowezesha kufikia malengo yaliyokusudiwa. Kutokana na mabadiliko mbalimbali hasa ya kisayansi na kiteknolojia na hata kiuchumi, yanayoendelea duniani, kuna haja ya sera na mitaala ya elimu kuwa ya kisasa zaidi ili kuendana na mabadiliko hayo.

Mheshimiwa Spika, kwa miaka kadhaa iliyopita Tanzania imeshuhudia mafundi mchundo wengi wakiongeza (upgrade) ngazi za utaalamu wao kwa kusomea kozi za uhandisi wakati idadi ya mafundi mchundo wanaofuzu masomo ya ufundi mchundo ikipungua huku mafundi wa kawaida (artisans) wanaoongeza utaalamu wao ikiwa haiongezeki. Hali hii imepelekea kupungua kwa kasi idadi ya mafundi mchundo pamoja na mafundi wa kawaida na hivyo kuathiri utendaji wa viwanda (na sekta nyingine) kwa kuwa hawa ndio wanaotenda kazi kwa mikono. Ukizingatia kuongezeka kwa uwekezaji katika viwanda, hali hii inabidi irekebishwe haraka kwa kuongeza idadi ya mafundi husika ili kukidhi mahitaji ya uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa uwiano wahandisi/ mafundi mchundo/mafundi wa kawaida ni wa chini sana na hautaweza kuisiadia Tanzania kufikia malengo tarajiwa. Hata ukilinganisha wataalamu wa juu wa stadi mbalimbali za taifa na wenye stadi za kati na za chini uwiano wake sio mzuri ukilenga uwezo wa kusimamia viwanda vya kisasa kiasi cha kuhitaji marekebisho ya uwiano kama mpango wa Taifa wa kuendeleza stadi unavyotegemea (National Skills Development Strategy).

Mheshimiwa Spika, napendekeza Serikali iongeze msukumo kwenye mafunzo ya mafundi mchundo na mafundi wa kawaida na pia elimu yetu ilenge mafunzo ya ujasiriamali. Hii pia ishirikishe elimu ya kujitegemea toka elimu ya awali na hata kutumia watalaam wetu wa kilimo, mifugo na uvuvi kuanzisha mashamba darasa mashuleni.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mawaziri na Viongozi wote wa Wizara ya Maji, kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Waziri wa Maji kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Serikali katika utekelezaji wa ustawi wa jamii na maendelo endelevu, na hii ni mojawapo ya nguzo kuu katika utayari wetu wa ushindani wa Kimataifa (national competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miezi kumi ya bajeti ya mwaka 2021/2022, Serikali kupitia Wizara ya Maji imetekeleza miradi mingi ya maji. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya inatekeleza kwa ufanisi mkubwa miradi ya vijiji vya Ruanda, Ilembo, Inyala, Igoma, Iwalanje, Galijembe, Tembela, Pashungu, Shigamba, Santilya, Inyala Ilembo, Mshewe, Muvwa, Njelenje, Mapogoro, Mjele, Chang’ombe, Iwizi, Ikukwa, Simboya, Itimba, Utengule, Ihombe, Idugumbi, Iwala, Ilota, Ikhoho na pia mradi mkubwa katika Mji Mdogo wa Mbalizi. Miradi yote hiyo imetekelezwa kwa ufanisi mkubwa, ingawa kunahitajika uboreshaji wa miundombinu ya mabomba hasa katika mradi wa Mbalizi kuna upotevu mkubwa wa maji kutokana na uchakavu wa mabomba yaliyokuwepo awali.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio hayo makubwa, katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya bado kuna changamoto kubwa ya maji salama kwa wananchi. Pamoja na kuwepo kwa vyanzo vingi vya mseleleko (gravity), asilimia kubwa ya vijiji havina maji salama. Nashukuru kwa kuwepo bajeti ya mradi mkubwa wa Mto Kiwira ambao utakuwa mkombozi wa maeneo mengi ya Mkoa wa Mbeya na hata Songwe. Napendekeza Serikali iendelee kutekeleza miradi ya maji kwa mpango wa force account ambao umeonesha mafanikio ya kupunguza gharama za miradi na pia utekelezaji ni wa haraka na kwa ufanisi mkubwa.

Mheshimiwa Spika, napendekeza Serikali iweke msukumo mkubwa wa kuharakisha utekelezaji wa miradi iliyomo kwenye mradi wa Bonde la Mto Songwe (Songwe River Basin Development Programme - SRBDP), wenye ofisi zake Kyela, Tanzania. Mradi huu unaotekelezwa kwa pamoja na Serikali za Tanzania na Malawi ni muhimu sana kwa sasa kutokana hasa na ujenzi wa mabwawa ambayo pamoja na manufaa mengine, yatasaidia kupunguza mafuriko ya Bonde la Kyela. Mabwawa haya yamelenga kuzalisha umeme, kilimo cha umwagiliaji, shughuli za uvuvi na hata utalii ambao unahitajika sana katika Wilaya ya Mbeya na ukanda wote wa Nyanda za Juu Kusini.

Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto za tabianchi, kumekuwepo na uharibifu mkubwa wa mazingira na ongezeko la upungufu wa vyanzo vya maji. Uharibifu unaotokana na shughuli za kibinadamu umepelekea misitu mingi kuharibiwa na uchomaji moto, ukataji mkaa na hata kilimo kwenye vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Spika, napendekeza Serikali iongeze msukumo wa Wizara za Maji, Kilimo, Maliasili na Mazingira kufanya kazi kama timu moja ili kukabiliana na janga hili kubwa ikiwemo ujenzi wa mabwawa makubwa katika maeneo yanayokumbwa na mafuriko. Kama ilivyo kwa athari za mafuriko ya Kyela, hata Ziwa Rukwa linaathirika sana na kujaa mchanga na udongo unaosombwa na mito kutokana na mmomonyoko wa udongo.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (no. 6) Bill, 2021
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kwanza nianze kwa kukushukuru wewe mwenyewe. Wewe hii hoja uliiona kwa macho mwenyewe, baada ya kuiona, yote haya yametokea. Nami nianze kwa kukushukuru wewe. Kwa hiyo, ilianzie hapa Bungeni, kuna Mbunge akauliza hilo swali na kweli hii imewaumiza sana wananchi.

Mheshimiwa Spika, hii 2%, siyo tu ilikuwa inawaumiza wakulima, lakini hizi ni kodi ambazo zinasababisha mazao yetu yatoroshwe kupelekwa nchi jirani. Kuna ushahidi mkubwa kuwa hata kahawa, pareto na mahindi kwa kiasi kikubwa wananchi wamekuwa wanatorosha kwa ajili ya kodi zetu wakati mwingine ambazo zinaonekana ni mzigo sana kwa wananchi. Naishukuru sana Serikali kwa hii hatua, namshukuru vile vile Mheshimiwa Rais kwa hatua aliyochukua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haya marekebisho kwenye Tax Administration Act (Na. 7), hii ni muhimu sana tena sana kwa sababu, itatuwezesha na sisi kama nchi Tanzania Pamoja na hii ya sasa hivi ambayo imerekebishwa, kutambua kuwa maeneo ambayo tunaweza kuwa na double tax agreements yanaweza kuwa na manufaa makubwa sana kwa nchi yetu na isiishie hapa tu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilikuwa naiomba Serikali iangalie namna gani iboreshe eneo hili ili ikiwezekana tuangalie double tax agreements ambazo sasa hivi zinaonekana kwa muda mrefu hatujaingia nazo, nazo ziwe sehemu ya hili eneo ambalo ni section seven ya hii tax administration.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, tena sana. Kwa haya, nami naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mawaziri na viongozi wote waTAMISEMI, kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Taifa letu katika kuboresha maisha ya wananchi na pia utayari wetu wa ushindani wa kimataifa (national competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni “Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.”

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miezi tisa ya mwaka huu wa bajeti, Serikali kupitia TAMISEMI imesimamia kwa uadilifu na ufanisi mkubwa mwendelezo wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya vituo vya afya na miundombinu ya shule za msingi na sekondari na pia ukarabati wa barabara za vijijini. Jimbo la Mbeya Vijijini limenufaika kwa ujenzi wa shule mbili mpya za msingi na pia ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa shule za msingi na sekondari. Ujenzi wa miundombinu ya afya na elimu umeendelea kuweka historia ya kipekee katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya. Wananchi wana imani kubwa ya huduma nzuri zitakazotolewa ikiwemo kuwepo wa watalaam bingwa, vifaa tiba vyote muhimu na dawa.

Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa ikiwemo utaratibu mpya wa mikopo kwa vijana, wakina mama na watu wenye ulemavu kupitia kwenye taasisi za fedha. Huu ni mfumo mzuri sio tu kulinda huo mfuko, lakini itakuwa ni sehemu ya kuboresha sera ya huduma ya fedha jumuishi (financial inclusion).

Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio hayo makubwa, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya bado ina changamoto za kumalizia miundombinu ya zahanati na vituo vya afya vilivyojengwa kwa nguvu za wananchi ikiwemo vituo vya afya kwa Kata ya Ilungu, Kata ya Isuto, Kata ya Bonde la Songwe na zahanati kwa kila kijiji. Wananchi wamejitahidi kujenga maboma ya zahanati na vituo vya afya na wanategemea Serikali itawaunga mkono kumaliza kazi zilizobakia bila kuchelewa.

Mheshimiwa, Spika, Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara za lami katika maeneo ya kilimo cha kahawa na mbogamboga. Kazi zinazoendelea ni barabara ya Inyala – Simambwe ya kilometa zaidi ya 16 inayopita Kata za Inyala, Itewe, Maendeleo na Tembela. Pia kuna ujenzi kilometa 10 za barabara ya Lupeta – Wimba - Izumbwe, inayopita Kata za Swaya na Igale. Pamoja na kuwepo fedha ya wafadhili, ujenzi wa barabara hizi unasuasua sana. Serikali ichukue hatua za haraka kunusuru miradi hii muhimu kwa maendeleo ya Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio hayo makubwa, katika Halmashauri zetu tumekuwa tunakabiliwa na changamoto hasa kwenye miundombinu ya barabara. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, barabara zinazohudumiwa na TARURA kwa asilimia zaidi ya 90 zipo kwenye hali mbaya sana kutokana na mafuriko. Maeneo mengi ya vijijini barabara hazipitiki kutokana na madaraja kusombwa na mafuriko. Naiomba Serikali ichukue hatua za haraka kunusuru hali hii ili wananchi waweze angalau kusafirisha mazao yao. Hali ya mtandao wa barabara wa zaidi ya kilometa 1,000 ni mbaya na hazipitiki kirahisi hasa kipindi cha mvua. Barabara ambazo zipo kwenye hali mbaya sana ni pamoja na; Haporoto – Ileya – Ishinda; Shamwengo - Us/Muungano; Irambo – Nsonyanga; Nsenga - Swaya-Nzovwe;

Mjele - Ikukwa; Ilembo – Isonso; Madugu – Ilindi – Isuto; Ilembo – Mbagala; Ilembo – Mwala; Iwowo - Igalukwa -Mlowo; Horongo – Igale; Songwe Viwandani – Jojo; Kawetere – Ikukwa; Mbalizi – Ilota; Nyalwela – Ngole; Nyalwela - Mbonile – Itala; Ilembo – Mbawi; na Igawilo - Hatwelo. Kwa bajeti ndogo ambayo ni kilometa chini ya 100 kwa mwaka, ni vigumu kutatua changamoto za barabara hizi kwa kiasi kikubwa zinabeba uchumi wa kilimo na madini kwa Mbeya na Tanzania kwa ujumla. Napendekeza Serikali iweke msukumo zaidi kwenye kuboresha miundombinu ya barabara kurahisisha usafirishaji wa mazao ya kilimo, itasaidia kuimarisha uchumi.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2022 Kamati ya TAMISEMI walifanya ziara Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya na Mheshimiwa Bashungwa aliyekuwa Waziri wa TAMISEMI, aliahidi Kamati ya TAMISEMI na kuagiza TARURA wajenge kwa dharura barabara kuu tatu ambazo zimejifunga kwa kipindi kirefu. Kwa masikitiko makubwa mpaka leo hakuna kilichofanyika kwa barabara hizo tatu za Haporoto – Ileya – Ishinda; Mjele - Ikukwa; na Madugu – Iyunga Mapinduzi – Isuto.

Mheshimiwa Spika, katika mazingira haya, wananchi wanakosa imani na viongozi wao na kupelekea hata uchumi kuporomoka ukichukulia haya ni maeneo muhimu kwa kilimo na uzalishaji wa madini. Kutokana na kupoteza fedha za kigeni kwenye madini na mazao ya kibiashara, naomba Wizara itoe fedha kwa udharura ili barabara hizo zitengenezwe.

Mheshimiwa Spika, napendekeza kuwepo na msukumo wa kuhakisha Halmashauri zinasimamia kikamilifu elimu ya kujitegemea kwenye ngazi zote za msingi na sekondari. Kwa shule za vijijini kushirikisha Maafisa Ugani wa Kilimo na Uvuvi kuanzisha mashamba darasa kwa kila shule za vijijini. Kwa shule za mijini kuna fursa pia kuweka msukumo wa elimu ya kujitegemea kulingana na mazingira ya shule ikiwemo elimu ya ufundi.

Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, napendekeza Serikali iboreshe mfumo wa mikopo hii kuendana na madhumuni ya mikopo ya kuimarisha kundi hili kiuchumi. Kama ilivyopendekezwa kwenye hotuba ya Waziri, uendeshaji wa mikopo hii uwe na misingi ya huduma za kifedha jumuishi (financial inclusion) ikiwemo elimu ya matumizi ya mikopo na usimamizi wa kitalaam wa mikopo. Kwa ukubwa wa mfuko huu kitaifa kuna umuhimu wa kuunda taasisi ya kifedha kuusimamia kwa tija.

Mheshimiwa Spika, katika Halmashauri ya Mbeya kuna Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mbalizi ambao una wakazi zaidi ya 100,000 na shughuli nyingi za kiuchumi ikiwemo viwanda, madini na hata Uwanja wa Ndege wa Songwe. Pia katika Kata ya Utengule Usongwe kuna Kijiji cha Mbalizi ambacho mipaka yake haiungani na vijiji vingine vya kata hiyo. Napendekeza Serikali irekebishe mipaka ya Mbalizi na ipandishe hadhi kutoka Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mbalizi kuwa Halmashauri ya Mji wa Mbalizi.

Mheshimiwa Spika, mapendekezo ya kugawa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ni kilio cha muda mrefu, na Hayati Dkt. Magufuli mwaka 2020 aliagiza zoezi la kugawa lifanyike haraka na aliagiza kubadilisha jina la Jimbo la Mbeya Vijijini haraka iwezekanavyo. Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ina sifa zote za kugawa ikiwemo uwezo kiuchumi ni mkubwa sana, idadi kubwa ya wakazi, na pia changamoto za kijografia. Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya inapakana na Halmashauri zote za Mikoa ya Mbeya na Songwe kasoro Kyela na Tunduma na pia inapakana na hata Mkoa wa Njombe. Vikao vyote vya kisheria toka ngazi za chini mpaka ngazi ya Kamati za Ushauri vya Wilaya na Mkoa katika wakati tofauti vimepitisha mapendekezo hayo.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mawaziri na viongozi wote wa Ofisi ya Rais – Utumishi, kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka wa Ofisi ya Rais – Utumishi.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Utumishi, kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Taifa letu katika kuboresha maisha ya wananchi na pia utayari wetu wa ushindani wa kimataifa (national competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.”

Mheshimiwa Spika, katika mapitio ya kipindi cha bajeti 2022/2023, Serikali kupitia Wizara ya Utumishi na Utawala Bora imesimamia kwa uadilifu na ufanisi mkubwa masuala yote ya utumishi na hasa kurudisha uwabikaji kazini iliopelekea ufanisi mkubwa hasa kwenye utekelezaji wa miradi. Jimbo la Mbeya Vijijini limenufaika kupitia miradi ya TASAF ambapo imebadilisha maisha ya wananchi katika vijiji husika. Pia kwa kusimamia vizuri, rushwa na upendeleo umepungua kwa kiasi kikubwa kupelekea ufanisi mkubwa sehemu za kazi na hata miradi kukamilika kwa ufanisi mkubwa.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio hayo makubwa, napendekeza kuendeleza mafunzo ili kuboresha weledi wa watumishi ikiwemo upanuzi wa Chuo cha Watumishi Mbeya na eneo muafaka kwa ujenzi wa chuo kipya na cha kisasa, ni Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ambapo kuna maeneo mazuri ikiwemo yaliyokuwa mashamba ya Tanganyika Packers, Mbalizi. Kuna mahitaji makubwa ya elimu/mafunzo ya uongozi kwa viongozi wa ngazi mbalimbali, napendekeza Serikali irudishe utaratibu wa mafunzo maalum ya viongozi kwa kushirikiana na Vyuo Vikuu ikiwemo Mzumbe, UDSM, IFM na hata nje ya nchi. Mafunzo yanahitajika ni kama vile Executive Development Pragrammes kwa viongozi kulingana na ngazi zao. Mafunzo nje ya nchi ni muhimu kwa kuleta ujuzi kutoka nje hasa nchi zilizoendelea na hata zile zinazoendelea na zinafanya vizuri.

Mheshimiwa Spika, kutokana na upungufu mkubwa wa watumishi katika sekta mbalimbali, napendekeza Serikali iendelee kutoa ajira zaidi hasa kwenye maeneo ya kuchochea uchumi na pia sekta ya afya, elimu na kilimo. Kutokana na idadi kubwa ya wahitimu kukosa ajira, na wametapakaa kila kona ya Tanzania hasa vijijini, napendekeza Serikali kuhakikisha ajira zinatolewa kwa usawa wa maeneo yote ya Tanzania kulingana na sifa. Serikali iangalie kuboresha sera za kikodi ili zichochee kuongeza ajira pamoja na kukuza uchumi.

Mheshimiwa Spika, kutokana na majukumu na unyeti wa mashirika ya kadhaa ya umma ikiwemo ushindani wa kupata watalaam wazuri, mashirika haya yaruhusiwe moja kwa moja kutoa ajira ili yaendane na mahitaji yao na Tume ya Ajira wawe na jukumu la ushauri/udhibiti. Taasisi kama CAG kisheria anatakiwa awe huru ikiwemo uhuru wa kuajiri, na hata taasisi kama mabenki, TANESCO, Bandari, TRA ni muhimu wakapewa uhuru wa kuajiri kulingana sifa ila kupata watalaam wazuri kiushindani na pia kulingana na bajeti za mashirika husika.

Mheshimiwa, Spika, pamoja na maboresho ya mfumo wa TASAF, napendekeza pia kuboresha zaidi mfumo huo ikiwemo msukumo wa miradi ilenge maeneo yatakayochochea uzalishaji wa mali ili zisaidie jamii kwa upana mkubwa. Pamoja na maeneo ya uzalishaji, msukumo ujumuishe kuimarisha masoko ya bidhaa zitakazozalishwa katika maeneo ya mradi. Miradi ilenge kuboresha elimu na hata kusomesha watoto wanaotoka kwenye kaya maskini ya maeneo husika. Serikali iboreshe taratibu za kupata maeneo ya miradi ya TASAF ili kupunguza malalamiko.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii nami nichangie Wizara hii muhimu, hasa kwa uchumi wetu. Nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais pamoja na Waziri wa Madini kwa kazi nzuri waliyoifanya kuisimamia hii sekta ya madini ambayo imeonesha mwelekeo mzuri. Ukiangalia hata kwenye pato la Taifa sekta ya madini imekuwa ikichangia kwa wastani mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Tanzania siyo kisiwa, ni sehemu ya dunia na tunaona mabadiliko makubwa ya kiuchumi duniani. Nasi rasilimali zetu tulizonazo inabidi tuzitumie vizuri na rasilimali mojawapo ambayo inaweza kuibadilisha Tanzania kwa haraka ni hii sekta ya madini. Speed tuliyonayo pamoja na hayo mafanikio, inabidi iongezwe kidogo kwa sababu, ukiangalia mtangulizi wangu hapa amezungumzia kuhusu mradi wa Mchuchuma au Liganga na Mchuchuma. Angalia muda mrefu ulivyopita, lakini kuna miradi mingi ambayo inaendana pamoja na hiyo, kwa sababu, hizi rasilimali tusipozitumia leo baadaye zinaweza kugeuka zisiwe na thamani tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Wizara iangalie namna gani kwa kushirikiana na Wizara nyingine Serikalini kuvutia wawekezaji ili kuhakikisha hizi rasilimali zinabadilishwa na zinatafsiri kuongeza uchumi wa nchi yetu. Kwa hiyo, napendekeza Serikali ichukue hatua za haraka kuhakikisha kuwa miradi kama Liganga na Mchuchuma inaenda kwa speed ya haraka ili tupate pesa za kigeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi mingine ambayo enaendana sawa na Liganga na Mchuchuma, kuna mradi wa Niobium hapa. Nafikiri Mheshimiwa Waziri nisingesema hili neno angenishangaa. Nitaendelea kulisemea hilo kwa sababu inaelekea wenzetu bado hawaoni zile fursa tulizonazo kama Tanzania. Kuleta kiwanda cha uchenjuaji Niobium cha kwanza Afrika, cha nne duniani na mahitaji ya ferroniobium ni makubwa mno duniani. Kwa kweli ni jambo ambalo linabidi lichukuliwe kwa haraka ili Tanzania ibadilike hapa tulipo. Tumekuwa tukifanya vizuri kwenye uchumi wa nchi yetu, lakini hatujafanya vizuri sana kama tungeweza kutumia rasilimali hizi tulizonazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ferroniobium ninayoizungumzia ambayo inapatikana Mbeya, yale madini ndiyo yangetumiwa kwenye ujenzi wa madaraja yetu, ujenzi wa reli yetu tunayoijenga sasa hivi, na vilevile haya madini yanahitajika zaidi huko nje. Ukiwa na hiki kiwanda ina maana hata nchi Jirani, haya madini yao yatakuja kutengenezwa au kuongezwa thamani hapa nchini kwetu. Kwa hiyo, naona kabisa ya tunaitaka Tanzania ya viwanda. Kwa hiyo, ukiwa na kiwanda cha namna hii, ndiyo unafikia yale malengo ambayo yamo kwenye millennium goals. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, baada ya kulisema hilo, kwa ajili ya muda, mwenzangu amezungumzia kuhusu umuhimu wa dhahabu kuwa sehemu ya fedha za kigeni ambayo itatunzwa na Benki Kuu. Dunia imebadilika sana. Mataifa makubwa leo hii yanaachana na kutumia zile fedha za kigeni tulizozizoea kama Dola, Sterling Pounds au Euro kama sehemu ya kuwekeza, yamekuwa sasa hivi yananunua dhahabu na kuwekeza kwenye hizo benki na kuwa sehemu ya pesa zao za kigeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili umuhimu wake mkubwa kwa sababu, dhahabu thamani yake mara nyingi inaongezeka kwa haraka zaidi wakati Dola inapungua. Kwa hiyo, ukiangalia huo mtazamo kwa muda mrefu, nilikuwa naangalia takwimu za mwaka 2022 Desemba, ukilinganisha na leo, miezi minne tu, bei ya dhahabu imepanda kwa asilimia 11 ambayo hiyo ni asilimia kubwa sana. Ina maana nchi yetu ingeweza kuwekeza kwenye dhahabu, hiyo thamani kubwa tungeweza kuipata badala ya kuendelea kuwekeza pesa zetu kwenye pesa za wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwekeza pesa za kigeni kwenye benki za wenzetu inawezekana hata wengi hawajui, ni sawa na kuwakopesha. Kwa hiyo, zile thamani ya pesa tulizonazo sisi kule, ina maana tumewakopesa, lakini ukiwa na dhahabu ambayo umeinunua Tanzania hapa hapa na tunazalisha Tanzania hapa hapa, utakuwa umetumia shilingi yetu kununua hiyo dhahabu na ukaibadilisha ikawa pesa ya kigeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunapozungumzia urari wa biashara ambao sasa hivi tuliona kwa kiasi kikubwa ulikuwa hauendi vizuri sana, kwa hiyo, kwa kununua dhahabu, Benki Kuu ikianza huo mpango itawezesha nchi yetu kuwa na urari wa biashara ambao ni mzuri. Labda ni kuchukua tu tahadhari ya kwamba huko nyuma hawakufanya vizuri, kwa hiyo, sasa hivi kinachohitajika, wajifunze kutokana na upungufu uliokuwepo, ili tuweze kurekebisha taratibu zetu tuhakikishe kuwa kile tutakachonunua kitatuletea faida badala ya kutuletea hasara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzuri wake, sasa hivi kuna mashirika makubwa sana ambayo yanalisimamia hilo. Kwa hiyo, hutanunua dhahabu kama dhahabu, utanunua dhahabu ambayo itaongezwa thamani kufikia mpaka asilimia 99.95 mpaka 99.99 ambayo inasimamiwa na mashirika makubwa kama lile la London Bullion Market Association. Ninashauri kuwa Benki Kuu waanzishe haraka hiyo ili tuepukane na kuweka fedha zetu kwenye Dola ambayo mpaka leo hatuoni kama itaendelea kutuletea faida hasa kulingana na mitikisiko ya kiuchumi na hii mivutano iliyoko hapa duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo tungelitumia vizuri kwa Wizara ya Madini; tumeona bei za mbolea zikipanda kwa haraka mno. Hizi mbolea zinatengenezwa kwa madini ambayo yanapatikana Tanzania. Calcium tunayo, phosphate tunayo, lime tunayo, natural gas tunayo, hatuna sababu ya kuendelea kutegemea mbolea za kutoka nje. Kwa hiyo, tujipange vizuri tuangalie ni namna gani nchi yetu ianze kutumia hizi rasilimali zetu tuweze kupeleka mbolea nje badala ya sisi kuwa waagizaji wa mbolea kutoka nje. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mawaziri na viongozi wote wa Wizara ya Madini, kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Waziri wa Madini, kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Taifa letu katika kuboresha maisha ya wananchi na pia utayari wetu wa Ushindani wa Kimataifa (National Competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 ambayo ni Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mafaninikio ya sekta ya madini, Serikali inashauriwa kuchukua hatua za kuimarisha zaidi sekta hii muhimu ili kukabiliana na athari za kiuchumi kutokana COVID-19 na sasa vita vya Urusi na Ukraine. Kutokana na athari ya kiuchumi iliyoikumba dunia nzima, hii inaweza kuwa fursa kwa Serikali kuvutia uwekezaji zaidi kwenye madini hasa dhahabu, madini ya chuma na madini ya calcium carbonate, lime na phosphate. Dhahabu ina historia ya bei kutoyumba kwenye soko la dunia kwa vile mabenki yanatumia dhahabu kwenye kuwekeza na kutokana pia na kuyumba kwa thamani ya shillingi na hata dola ya Marekani, Serikali inaweza kutumia dhahabu kama mbadala wa kuwekeza amana zake.

Mheshimiwa Spika, kutokana na mabadiliko ya kiuchumi kidunia, Benki Kuu nyingi duniani zimeanza kuwekeza zaidi kwenye dhahabu na hii ni ishara nzuri kwa bei ya dhahabu kuendelea kuimarika kwenye soko la dunia ambapo kwa mwezi Aprili, 2023 bei imepanda kwa zaidi ya asilimia 11 ukilinganisha na bei za Desemba, 2022.

Mheshimiwa Spika, vita vya Urusi na Ukraine vimesabisha upungufu mkubwa wa uzalishaji wa mbolea, na hii ni fursa kwa Serikali kuwekeza kwenye viwanda vya mbolea kwa kutumia malighafi zinazopatikana hapa nchini kama vile phosphates, calcium carbonate, limestone na natural gas. Katika kipindi cha mtikisiko wa uchumi, bei ya madini ya chuma na hata makaa ya mawe haiyumbi na Serikali inaweza kupata mapato mengi katika kipindi hiki.

Mheshimiwa Spika, napendekeza Serikali kuchukua hatua za makusudi na kuharakisha uwekezaji kwenye mradi wa chuma (Liganga Iron Ore) ikiwa ni pamoja na makaa ya mawe (The Mchuchuma Coal Mining and Power Projects). Mradi wa Liganga na Mchuchuma ulitarajia uwekezaji wa US$ 3 billion na kuzalisha ajira zaidi ya 30,000 na hii inaweza kuwa fursa nzuri katika hiki kipindi cha balaa la athari za COVID-19 na vita vya Urusi na Ukraine.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mradi wa Liganga na Mchuchuma, napendekeza Serikali kuchukua hatua kuharakisha uwekezaji kwenye mradi wa madini ya Niobium ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Kiwanda cha Ferroniobium (FeNb) ambacho kitakuwa cha kwanza Afrika na cha nne duniani. Kutokana na mahitaji makubwa ya ujenzi wa reli, madaraja na reli ya SGR, kuna mahitaji makubwa ya vifaa vya chuma ambavyo ni imara, lakini vyepesi na vyenye ubora wa kimataifa. Kwa kutumia sheria zetu za uwekezaji, Serikali itumie fursa za kipindi hiki ili kuvutia wawekezaji kwenye madini ya viwandani ili yaongezwe thamani hapa kwetu na pia kuvutia malighafi ya madini toka nchi zingine ili yachakatwe hapa kwetu. Tanzania imebahatika kuwepo kwa madini ya Niobium ambayo inapatikana Milima ya Pandahill Wilaya ya Mbeya, na mahitaji ya Ferroniobium (FeNb end product) yanaendelea kuwa makubwa duniani na hapa kwetu pia.

Mheshimiwa Spika, Serikali inahitaji kujiwekekea mikakati ya haraka (quick wins) ili kuhakikisha inaimarisha uchumi ikiwemo kuboresha urari wa biashara kukabiliana na athari za COVID-19 na sasa vita vya Urusi na Ukraine. Kwa kutumia rasilimali zetu za madini, Serikali inaweza kutengeneza fursa nyingi na kupitia Mradi wa Niobium na Kiwanda cha Ferroniobium, ajira 2,000 zitakazozalishwa wakati wa ujenzi na pia kutakwepo ajira za kudumu zaidi ya 600 na indirect jobs 7,000. Mradi utazalisha mapato kila mwaka shilingi bilioni 500 (US$ 220 million) ambapo mapato kwa Serikali kila mwaka shilingi bilioni 50 (US$ 22 million) uhai wa mgodi ni zaidi ya miaka 30. Hiki kitakuwa kiwanda cha kisasa cha kwanza Afrika (Modern Manufacturing Plant and Smelter). Pamoja na kuingiza teknolojia hii adimu na ujuzi (skills transfer) pia itakuwa itachangia huduma za kijamii (Corporate Social Investment in Community) na chanza cha fedha ya kigeni.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mawaziri na viongozi wote wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Waziri wa Mifugo na Uvuvi, kwa hotuba nzuri iliojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Serikali katika utekelezaji wa ustawi wa jamii na maendeleo endelevu, na hii ni mojawapo ya nguzo kuu katika utayari wetu wa ushindani wa kimataifa (national competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 ambayo ni kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Spika, kulingana na takwimu za mifugo na uvuvi ya mwaka wa kilimo 2022/2023 inaonesha kuwa idadi ya ng’ombe ilikuwa milioni 36.6 kutoka milioni 35.3 waliokuwepo 2021/2022. Kati ya hao, wakulima wadogo walikuwa na ng’ombe milioni 36.4 na mashamba makubwa yalikuwa na ng’ombe milioni 0.2. Aidha, wakulima wadogo walikuwa na mbuzi milioni 26.3 na mashamba makubwa mbuzi milioni 0.34.

Kwa upande wa kondoo, wakulima wadogo walikuwa na kondoo milioni 8.9 na mashamba makubwa kondoo milioni 0.24. Vilevile nguruwe waliofugwa na wakulima wadogo walikuwa milioni 3.7 na mashamba makubwa yalikuwa na nguruwe 5,123 na kulikuwa na jumla ya kuku milioni 98 ambapo wakulima wadogo walikuwa na kuku milioni 85.5 na mashamba makubwa yalikuwa na kuku milioni 12.5.

Mheshimiwa Spika, pamoja na idadi hiyo kubwa ya mifugo, mchango wa sekta ya mifugo na uvuvi wa asilimia saba bado ipo chini sana na tija ikiboreshwa kuna fursa kubwa ya sekta hii kuchangia sehemu kubwa ya pato la Taifa.

Mheshimiwa Spika, mifugo na uvuvi ni utajiri mkubwa, lakini pamoja na ukuaji wa asilimia tano, na Tanzania kuwa nafasi ya tatu kwa nchi za Bara la Afrika, na kuchangia asilimia saba katika uchumi wa Taifa, sekta hii ya mifugo na uvuvi inazalishwa kwa tija ndogo sana. Katika hali hii, sekta ya mifugo haijamsaidia mfugaji na mvuvi kwa kiasi kikubwa kunajinasua kwenye umaskini na kimeendelea kutoa mchango mdogo kwenye pato la Taifa.

Mheshimiwa Spika, Serikali ichukue hatua zaidi ili kuboresha sekta ya mifugo na uvuvi ikiwemo ujenzi wa mabwawa, kuwezesha mashamba ya kuzalisha lishe/chakula cha mifugo, kuwezesha sekta binafsi kuzalisha mitamba ya kisasa na vifaranga wa samaki. Napendekeza Serikali ianzishe vitalu vya mifugo katika Kata za Mjele na Mshewe, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, ikiwemo kuchimba mabwawa na visima.

Pia napendekeza kuwezesha kuanzisha mashamba makubwa ya kuzalisha lishe ya mifugo ikiwemo ya umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, nashauri Serikali imalizie kujenga Kiwanda cha Nyama cha Utengule (Mji wa Mbalizi) ambacho kwa muda mrefu ujenzi umesimama pamoja na kuwepo vifaa vyote muhimu vilivyotolewa na wafadhili. Kutokana na kuwepo uwanja wa Kimataifa wa Songwe ambao ni wa kimkakati kusafirisha mazao ya kilimo na mifugo kwa masoko ya nje, napendekeza umaliziaji wa kiwanda hiki cha nyama na pia uwezeshaji wa vitalu vya kunenepesha mifugo katika Kata za Mjele na Mshewe.

Mheshimiwa Spika, Serikali iongeze Maafisa Ugani; waliopo kwenye Halmashauri ya Mbeya ni wachache na wale waliopo hawaonekani kutoa huduma za ugani kwa wananchi. Wizara iweke msukumo wa kuhamasisha, kuanzisha na kutoa elimu kuhusu kilimo cha malisho ili kuwezesha malisho kutosheleza mifugo mwaka mzima na pia kwa soko la nje ili isaidie mapato ya fedha za kigeni.

Pia Serikali iongeze kasi ya uzalishaji wa mitamba kutokana na idadi ndogo ya ng’ombe wazazi kwenye mashamba ya Serikali na matumizi madogo ya teknolojia ya uhimilishaji kwa kutumia mbegu bora za mifugo. Kuwepo na mkakati wa kuongeza mazao ya uvuvi ikiwemo deep sea fishing ili kuwezesha samaki wapatikane kwa tija na kuwezesha ushindani kwa soko la nje. Vijana wenye nia thabiti na wanaopenda kujishughulisha na ujasiriamali wa ufugaji samaki kwenye mabwawa watambuliwe na uwekwe utaratibu maalum wa uwezeshaji kupitia Halmashauri zao kupata mitaji na utaalam wa kufuga samaki kwenye vizimba na mabwawa na hivyo kuweza kujiajiri wenyewe na kujipatia kipato. Serikali ishughulikie changamoto ya chakula cha samaki na uhaba wa

vifaranga hapa nchini. Vijengwe vitotoleshi vingi katika vituo vya ukuzaji viumbe maji.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Waziri, Naibu Waziri na viongozi wote kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi kinachoishia Aprili, 2023 Serikali kupitia Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imesimamia kwa uadilifu na ufanisi mkubwa masuala yote ya viwanda na pia kuna mwelekeo mzuri wa kuboresha mazingira ya biashara (blueprint). Pia kwa kusimamia vizuri diplomasia ya uchumi, imejenga imani kubwa kwa wawekezaji ambao wameonesha nia ya kuwekeza kwenye maeneo muhimu ya uchumi wetu. Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara, imeendelea kutekeleza miradi mingi ya viwanda na pia kuboresha mazingira ya biashara (blueprint) kwa kuondoa tozo, ada na kodi ambazo zimekuwa kikwazo katika shughuli za uchumi.

Mheshimiwa Spika, kupitia blueprint Serikali inatambua umuhimu wa kuweka mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji ili kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini wa kipato. Pamoja na jitihada za Serikali, bado kuna mahitaji makubwa ya viwanda vya kuongeza thamani ya madini, kuongeza thamani ya mazao yetu vijijini na pia kuna changamoto za uhakika wa masoko ya mazao ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, napendekeza Serikali iendelee na msukumo wa kujenga viwanda vya mazao ili tuweza kuongeza thamani hapa nchini na pia kuzalisha ajira. Kutokana na neema ya kijografia, nchi yetu inazalisha mazao ya aina mbalimbali ikiwemo zao la pareto na Tanzania inaongoza Afrika, pia ni wa pili duniani kwa uzalishaji wa pareto. Uwekezaji zaidi kwenye Kiwanda cha Viuadudu cha Kibaha kuna fursa kubwa ya kuzalisha mbolea na hata viuatilifu kutokana na pareto inayolimwa hapa nchini. Serikali ichukue hatua za kutafuta wawekezaji wa viwanda vya viuatilifu ambavyo mahitaji yake ni makubwa hapa nchini na hata soko la nje.

Mheshimiwa Spika, pia nchi yetu ina neema ya madini ambayo ni malighafi ya kutengeneza aina mbalimbali za mbolea. Madini aina ya calcium (chokaa ya kilimo) na phosphate inapatikana kwa wingi hapa nchini na malighafi muhimu kutengeneza mbolea aina ya CAN na DAP na hata NPK. Kuwepo kwa gesi asilimia ni fursa nyingine kwa viwanda vya mbolea aina ya urea ambayo mahitaji yake ni makubwa sana Tanzania na duniani kote. Pamoja na madini hayo kuna madini adimu duniani kama vile Niobium ya Panda Hill Mbeya ambayo kuna fursa ya kujenga kiwanda cha kuchakata hayo madini ili kutengeza Ferroniobium ambayo mahitajika yake ni makubwa hapa nchini na pia nje ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, pamoja na Mradi wa Liganga na Mchuchuma, napendekeza Serikali kuchukua hatua kuharakisha uwekezaji kwenye mradi wa madini ya Niobium ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Kiwanda cha Ferroniobium (FeNb) ambacho kitakuwa cha kwanza Afrika na cha nne duniani. Kutokana na mahitaji makubwa ya ujenzi wa reli, madaraja na reli ya SGR, kuna mahitaji makubwa ya vifaa vya chuma ambavyo ni imara, lakini vyepesi na vyenye ubora wa kimataifa.

Mheshimiwa Spika, kwa kutumia sheria zetu za uwekezaji, Serikali itumie fursa za kipindi hiki ili kuvutia wawekezaji kwenye madini ya viwandani ili yaongezwe thamani hapa kwetu na pia kuvutia malighafi ya madini toka nchi zingine ili yachakatwe hapa kwetu. Tanzania imebahatika kuwepo kwa madini ya Niobium ambayo inapatikana milima ya Panda Hill, Wilaya ya Mbeya na mahitaji ya Ferroniobium (FeNb end product) ni makubwa duniani na hapa kwetu pia.

Mheshimiwa Spika, Serikali inahitaji kujiwekekea mikakati ya haraka (quick wins) ili kuhakikisha inakabiliana na athari za kiuchumi kutokana Covid-19 na sasa vita vya Urusi na Ukraine. Kwa kutumia rasilimali zetu za madini, Serikali inaweza kutengeneza fursa nyingi na kupitia Mradi wa Niobium na Kiwanda cha Ferroniobium, ajira 2,000 zitakazozalishwa wakati wa ujenzi na pia kutakuwepo na ajira za kudumu zaidi ya 600 na indirect jobs 7,000. Mradi utazalisha mapato kila mwaka shilingi bilioni 500 (US$ 220 million) ambapo mapato kwa serikali kila mwaka shilingi bilioni 50 (US$ 22 million) uhai wa mgodi ni zaidi ya miaka 30. Hiki kitakuwa kiwanda cha kisasa cha kwanza Afrika (Modern Manufacturing Plant and Smelter). Pamoja na kuingiza teknolojia hii adimu na ujuzi (skills transfer) pia itachangia huduma za kijamii (Corporate Social Investment in Community) na chanzo cha fedha ya kigeni.

Mheshimiwa Spika, kutokana fursa za kijografia, napendekeza msukumo zaidi kwenye EPZ na industrial parks hasa kwenye bandari zetu na maeneo yanayozunguka viwanja vya ndege kikiwemo Kiwanja cha Kimataifa cha Songwe kilichopo Wilaya ya Mbeya.

Mheshimiwa Spika, napendekeza Serikali ichukue hatua za haraka kubadilisha matumizi ya eneo ya iliyokuwa Tanganyika Packers litumike kwa EPZ na industrial parks hasa kwa mahitaji ya viwanda mbalimbali ikiwemo vya mazao ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, pia napongeza mkakati wa Serikali kwa kuanzisha Soko la Bidhaa “The Tanzania Mercantile Exchange (TMX).” Wizara ya Viwanda na Biashara iwe mstari wa mbele kuimarisha hili soko la bidhaa ambapo wauzaji na wanunuzi wanakutana na kubadilishana bidhaa na fedha katika mtindo wenye mpangilio na utaratibu maalum. Kuanzishwa kwa soko la bidhaa kutamwezesha mkulima kuweza kuuza mazao yake katika utaratibu unaoeleweka bila kulanguliwa. Pia soko la bidhaa linatupa mwanga na mwanzo mzuri wa kuboresha soko la madini kuwa sehemu ya TMX.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mawaziri na viongozi wote wa Wizara ya Kilimo, kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Waziri wa Kilimo kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Serikali katika utekelezaji wa ustawi wa jamii na maendeleo endelevu, na hii ni mojawapo ya nguzo kuu katika utayari wetu wa ushindani wa kimataifa (national competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Spika, kulingana na taarifa ya Wizara ya Kilimo, Tanzania ina hekta milioni 44 zinazofaa kwa kilimo cha mazao, kwa wastani hekta milioni 10.8 tu sawa na asilimia 24 ndizo zinazolimwa kila mwaka. Sekta hii kwa mwaka 2021/2022 imechangia asilimia 26.1 kwenye Pato la Taifa, imetoa ajira kwa wananchi kwa wastani wa asilimia 65 na imechangia asilimia 65 ya upatikanaji wa malighafi za viwanda. Sekta ya kilimo ni mhimili wa uchumi wa nchi na inachangia pato la mkulima mmoja mmoja, kaya na Taifa kwa ujumla. Sekta ya kilimo na hususani sekta ndogo ya mazao imechangia asilimia 15.4 katika Pato la Taifa na zaidi ya asilimia 100 ya upatikanaji wa chakula kinachozalishwa nchini na kupelekea utulivu wa mfumuko wa bei kwa takriban asilimia 59.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kujitosheleza kwa chakula na kuchangia katika uchumi wa Taifa, takribani mazao yote yanazalishwa kwa tija ndogo katika eneo husika. Uzalishaji wa mahindi wa chini ya tani mbili kwa hekta moja ni asilimia 29 tu ya uzalishaji unaotegemewa wa tani sita kwa hekta moja. Uzalishaji huu wa chini kwa mazao yote kwa kiasi kikubwa unatokana na ukosefu wa ushauri wa watalaam wa kilimo ikiwemo matumizi yasiyo sahihi ya mbolea na pembejeo zingine. Katika hali hii, kilimo hakijamsaidia mkulima kwa kiasi kikubwa kunajinasua kwenye umaskini na kimeendelea kutoa mchango mdogo kwenye pato la Taifa.

Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa mbolea nchini hadi Februari, 2023 ulikuwa tani 748,890 ambayo ilikuwa juu ya mahitaji ya tani 667,730. Pamoja na bei za mbolea kwenye soko la dunia kuwa juu, tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutoa ruzuku ya karibu asilimia 50 na kupelekea tani 300,179 kununuliwa kwa bei ya ruzuku. Hatua hii muhimu ni mafanikio makubwa katika safari ya kuleta tija kwenye kilimo nchini na napendekeza kuendelea na ruzuku ya pembejeo pamoja na kuanzisha Price Stabilization Fund kwa pembejeo hasa mbolea ili kuongeza tija kwenye uzalishaji wa mazao ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, nashauri Serikali iendelee kuimarisha usalama wa chakula nchini kwa kununua na kuhifadhi nafaka kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula. Kutokana na vita ya Urusi na Ukraine kunaashiria kuendelea kuwa na upungufu mkubwa wa nafaka na kwa kuzingatia gharama kubwa za uzalishaji wa karibu asilimia 100, Serikali ichukue hatua za makusudi kusaidia wakulima wapate bei nzuri ya NFRA badala ya kuuza kwa walanguzi na kutorosha chakula nje ya nchi. Kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu, kufikia mwaka 2030 biashara ya mazao ya chakula inakadiriwa kufikia dola za Kimarekani trilioni moja. Serikali ichukue hatua za makusudi kuboresha uzalishaji wa mazao ya chakula kutosheleza soko la ndani na nje. Uzalishaji wenye tija kwenye kilimo utaongeza upatikanaji wa fedha za kigeni na kupunguza pengo la urari wa biashara.

Mheshimiwa Spika, Serikali iangalie fursa za Kiwanda cha Viuadudu cha Kibaha kuanza uzalishaji wa viuatilifu inayotokana na pareto ambayo inazalishwa hapa nchini na imekuwa inauzwa nchi za nje kama semi-finished product kwa bei ndogo ya kutupa. Viuatilifu kutokana na pareto ni suluhisho la soko la pareto na pia suluhisho kwa upotevu wa mazao kushambuliwa na wadudu (post-harvest losses).

Mheshimiwa Spika, Serikali ianze mchakato wa kuanzishwa viwanda vya mbolea kwa kutumia madini (calcium carbonate, agricultural lime, phosphates, natural gas etc.) yanayopatikana kwa wingi hapa Tanzania, kuanza uzalishaji wa mbolea hapa nchini. Kutokana na athari za vita ya Urusi na Ukraine zinazoendelea, iwe fursa kwetu kwa kuanza kutumia rasilimali zinazopatikani nchini.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha bajeti ya 2022/2023 Serikali ilitenga shilingi 834,382,834,000 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo sehemu kubwa ilielekezwa kwenye miundombinu ya umwagiliaji. Utekelezaji wa miradi hadi kufikia Februari, 2023 hasa utekelezaji kwa fedha za nje uko chini sana. Sehemu kubwa ya miradi inategemea kuchukua miezi 24 na kuna matumaini ya utekelezaji kwenda kama ulivyotarajiwa. Matumaini pekee ni hatua zilizooneshwa kwenye bajeti ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji na Serikali iweke mikakati madhubuti kuhakikisha ufanisi wa utekelezaji wa bajeti hii ya umwagiliaji. Serikali iangalie utelezaji wa miradi ya mabwawa kuunganisha uratibu kwa mahitaji ya jumla kama vile mahitaji ya Wizara ya Mifugo na hata Wizara ya Maji, kunaweza kuwa na tija kuwa na chombo kimoja chenye nguvu zaidi.

Mheshimiwa Spika, pia mikakati hii iweke nyongeza za ujenzi wa mabwawa hasa maeneo yenye mafuriko makubwa ikiwa ni pamoja na kuzuia mafuriko. Pia napendekeza Serikali iweke msukumo mkubwa wa kuharakisha utekelezaji wa miradi iliomo kwenye mradi wa Bonde la Mto Songwe (Songwe River Basin Development Programme - SRBDP), wenye ofisi zake Kyela, Tanzania. Mradi huu unaotekelezwa kwa pamoja na Serikali za Tanzania na Malawi, ni muhimu sana kwa sasa kutokana hasa na ujenzi wa mabwawa ambayo pamoja na manufaa mengine, yatasaidia kupunguza mafuriko ya Bonde la Kyela. Mabwawa haya yamelenga kuzalisha umeme, kilimo cha umwagiliaji, shughuli za uvuvi na hata utalii ambao unahitajika sana katika Wilaya ya Mbeya na ukanda wote wa Nyanda za Juu Kusini.

Mheshimiwa Spika, Serikali ichukue hatua za haraka kuleta Bungeni mapendekezo ya Sheria ya Kilimo ambayo pamoja na mambo mengine itawezesha usimamizi wa matumizi bora ya ardhi ya kilimo ambayo inaendelea kupotea kwa matumizi ya makazi. Pia kutokana na changamoto za tabianchi, kumekuwepo na uharibifu mkubwa wa mazingira, na ongezeko la upungufu wa vyanzo vya maji. Uharibifu unaotokana na shughuli za kibinadamu umepelekea misitu mingi kuharibiwa na uchomaji moto, ukataji mkaa, na hata kilimo kwenye vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Spika, napendekeza Serikali iongeze msukumo kwa Wizara za Maji, Kilimo, Maliasili na Mazingira kufanya kazi kama timu moja ili kukabiliana na janga hili kubwa ikiwemo ujenzi wa mabwawa makubwa katika maeneo yanayokumbwa na mafuriko. Kama ilivyo kwa athari za mafuriko ya Kyela, hata Ziwa Rukwa linaathirika sana na kujaa mchanga na udongo unaosombwa na mito kutokana na mmomonyoko wa udongo.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mawaziri na viongozi wote wa Wizara ya Maji, kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Waziri wa Maji, kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Serikali katika utekelezaji wa ustawi wa jamii na maendelo endelevu, na hii ni mojawapo ya nguzo kuu katika utayari wetu wa ushindani wa kimataifa (national competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miezi kumi ya bajeti ya 2022/2023, Serikali kupitia Wizara ya Maji imetekeleza miradi mingi ya maji. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya inatekeleza kwa ufanisi mkubwa miradi ya vijiji vya Simambwe, Usoha Njiapanda, tembela, Iyawaya, Izyira, Ruanda, Ilembo, Inyala, Igoma, Iwalanje, Galijembe, Tembela, Pashungu, Shigamba, Santilya, Inyala Ilembo, Mshewe, Muvwa, Njelenje, Mapogoro, Mjele, Chang’ombe, Ipwizi, Ikukwa, Simboya, Itimba, Utengule, Ihombe, Idugumbi, Iwala, Ilota, Ikhoho na pia mradi mkubwa katika Mji wa Mbalizi. Miradi yote hiyo imetekelezwa kwa ufanisi mkubwa, ingawa kunahitajika uboreshaji wa miundombinu ya mabomba hasa katika mradi wa Mbalizi kuna upotevu mkubwa wa maji kutokana na uchakavu wa mabomba yaliyokuwepo awali.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio hayo makubwa, katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya bado kuna changamoto kubwa ya maji salama kwa wananchi katika maeneo mengi ya vijijini. Pamoja na kuwepo kwa vyanzo vingi vya mseleleko (gravity), asilimia kubwa ya vijiji havina maji salama. Nashukuru kwa kuwepo bajeti ya mradi mkubwa wa Mto Kiwira ambao utakuwa mkombozi wa maeneo mengi ya Mkoa wa Mbeya na hata Mkoa wa Songwe. Napendekeza Serikali iendelee kutekeleza miradi ya maji ikiwa ni pamoja na kuweka mkakati wa kuhakikisha upatikanaji wa maji unakuwa endelevu na mafanikio ya kupunguza gharama za miradi na pia utekezaji uwe wa haki na haraka na kwa ufanisi mkubwa.

Mheshimiwa Spika, napendekeza Serikali iweke msukumo mkubwa wa kuharakisha utekelezaji wa miradi iliyomo kwenye Mradi wa Bonde la Mto Songwe (Songwe River Basin Development Programme - SRBDP), wenye ofisi zake Kyela, Tanzania. Mradi huu unaotekelezwa kwa pamoja na Serikali za Tanzania na Malawi, ni muhimu sana kwa sasa kutokana hasa na ujenzi wa mabwawa ambayo pamoja na manufaa mengine, yatasaidia kupunguza mafuriko ya Bonde la Kyela. Mabwawa haya yamelenga kuzalisha umeme, kilimo cha umwagiliaji, shughuli za uvuvi na hata utalii ambao unahitajika sana katika Wilaya ya Mbeya na ukanda wote wa Nyanda za Juu Kusini.

Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto za tabianchi, kumekuwepo na uharibifu mkubwa wa mazingira na ongezeko la upungufu wa vyanzo vya maji. Uharibifu unaotokana na shughuli za kibinadamu umepelekea misitu mingi kuharibiwa na uchomaji moto, ukataji misitu kwa matumizi ya mkaa, na hata kilimo kwenye vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Spika, napendekeza Serikali iongeze msukumo wa Wizara za Maji, Kilimo, Maliasili, na Mazingira kufanya kazi kama timu moja ili kukabiliana na janga hili kubwa ikiwemo ujenzi wa mabwawa makubwa katika maeneo yanayokumbwa na mafuriko. Kama ilivyo kwa athari za mafuriko ya Kyela, hata Ziwa Rukwa linaathirika sana na kujaa mchanga na udongo unaosombwa na mito kutokana na mmomonyoko wa udongo.

Mheshimiwa Spika, kutokana na mahitaji ya maji kwenye kilimo, mifugo na hata mahitaji ya mabwawa kwa ajili ya kuzuia mafuriko ikiwemo kwenye miundombinu yetu ya reli na barabara, kuna haja na kuwepo kwa taasisi moja kuratibu na kusimamia mipango ya matumizi ya maji. Nchi yetu ina neema kubwa ya maji na hii ni fursa ya kipekee kutumia haya maji kama mojawapo ya nguzo kuu kukuza uchumi wetu.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mawaziri na viongozi wote wa Wizara ya Afya kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Waziri wa Afya kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Serikali katika utekelezaji wa sera ya afya ikienda sambamba na ustawi wa jamii na maendeleo endelevu na hii ni mojawapo ya nguzo kuu katika utayari wetu wa ushindani wa kimataifa (national competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Awamu ya Sita, Serikali kupitia Wizara ya Afya, imetekeleza miradi mingi ya miundombinu ya afya. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya na kwa kushirikiana na TAMISEMI imeendelea kutekeleza kwa ufanisi mkubwa miradi ya Hospitali ya Wilaya na vituo vitano vya afya vya Kata za Ikukwa, Ilembo, Santilya, Ilungu na Swaya. Vituo vyote vitano vinaendelea kutoa huduma kwa ufanisi mkubwa hasa huduma ya watoto na wakina mama. Hospitali ya Wilaya pamoja na vituo vya afya vimekamilika na maandalizi ya vifaa tiba yapo katika hatua za mwisho ili vianze kutoa huduma kwa ukamilifu.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki tunapopambana na majanga magonjwa ya mlipuko ikiwemo la corona virus (covid-19), tumejifunza umuhimu wa utayari wa huduma ya afya hasa kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali na hivyo Serikali iongeze msukumo wa kupeleka vifaa tiba na kumalizia vituo vya afya na zahanati zilizojengwa kwa nguvu za wananchi. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, wananchi wa Kata za Igoma, Isuto wamejenga vituo vya afya na kuna maendeleo mazuri ya kukamilisha na pia Mji Mdogo wa Mbalizi wenye wakazi zaidi ya 150,000 ujenzi wa kituo cha afya haujakamilika.

Mheshimiwa Spika, hivyo napendekeza Serikali kutoa kipaumbele katika bajeti hii kwa vituo vya afya hivi ili vianze kutoa huduma. Pamoja na vituo vya afya vya Ilungu, Igoma, Isuto na Mbalizi, napendekeza kukamilisha zahanati zote ambazo zimejengwa kwa nguvu za wananchi.

Mheshimiwa Spika, kutokana na maboresho ya miundombinu ya hospitali na vituo vya afya, Serikali ihakikishe bajeti ya mwaka huu inaendelea kujielekeza zaidi kwenye ajira ya madaktari na watumishi wa afya kwa ujumla. Pamoja na maboresho hayo ya miundombinu, vifaa tiba na ajira kwa watumishi, napendekeza Serikali ikamilishe mpango kabambe na Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote na hasa kwa wazee na wenye mahitaji maalum.

Mheshimiwa Spika, napendekeza Serikali iangalie jinsi ya kuboresha Bohari ya Madawa (MSD) ikiwa ni pamoja na Serikali kuhakikisha inaongeza mtaji wa MSD na kuboresha muundo wa shirika ili uendane na jukumu kubwa kutoa huduma kwa tija na ufanisi. Katika kipindi hiki ambapo Serikali inaangalia kuanzisha Bima ya Afya kwa Wote, kipaumbele kielekezwe kwenye maboresho ya upatikanaji wa madawa pamoja na madawa na kuwezesha huduma ya hospitali zetu kutoa huduma bora zaidi kwa ukanda huu wa Afrika.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Waziri, Naibu Waziri na viongozi wote wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miezi kumi ya mwaka wa 2022/2023, Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imesimamia kwa uadilifu na ufanisi mkubwa masuala yote ya elimu hasa kuboresha ufaulu na hata miundombinu ya madarasa na mabweni. Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya imeendelea kupitia kipindi kigumu cha changamoto za kuporomoka kutoka kuongoza kimkoa katika ufaulu wa elimu ya sekondari. Pia ufaulu kwa shule za msingi unapitia katika changamoto kubwa hasa kutokana na mazingira ya shule za vijijini ikiwemo upungufu wa walimu. Pamoja kuwa ni jukumu jumuishi kwa wazazi, bado kunahitaji uharaka wa kupitia sera ya elimu kuweza kuboresha taaluma kwa shule za vijijini ambazo kwa kiasi kikubwa hazifanyi vizuri ukilinganisha na shule za mijini.

Mheshimiwa Spika, walimu bado wanaendelea kufanya kazi katika mazingira magumu kwa kukosa majengo ya nyumba za kuishi. Napendekeza Serikali kuendelea kushirikiana na wananchi katika ujenzi wa nyumba za walimu iende sambamba na ujenzi wa maboma na pia madawati kwa wanafunzi wote. Ni muhimu kuhakikisha motisha kwa walimu ili kuboresha taaluma iwe ya kiushindani kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki, SADC na hata Afrika. Napendekeza pia Serikali itoe kipaumbele kwa kulipa madai ya malimbikizo kwa walimu, ili kupunguza muda wa kufuatilia malipo yao na badala yake waelekeze muda zaidi kwenye kufundisha.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki tunapopambana na magonjwa yasiyo ya kuambukizwa yakiwemo magojwa ya kansa, shinikizo la damu, figo, moyo na kadhalika, narudia tena kuishauri Serikali kuweka kipaumbele cha kuboresha elimu ya afya, ikiwemo upanuzi wa ujenzi wa ndaki ya sayansi ya afya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam - Mbeya College of Health and Allied Sciences (UDSM-MCHAS). Serikali itoe kipaumble cha kutenga eneo la kutosha kwa chuo hiki kutoka kwa eneo la iliokuwa Tanganyika Packers Ltd., Mbalizi Mbeya.

Mheshimiwa Spika, katika kuwezesha uwekezaji na uendelezwaji wa viwanda endelevu, Tanzania inahitaji kuzalisha wataalam wengi na hasa ujasiriamali na taalum ya ufundi ngazi za kati na chini ambapo mahitaji ni makubwa. Pamoja na kujiwekea malengo ya kuongeza viwanda, nashauri Serikali ilitazame upya suala la uwepo wa nguvu kazi (vijana kupata mafunzo ya ufundi na ujasiriamali) ya kutosha na itakayowezesha kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, kutokana na mabadiliko mbalimbali hasa ya kisayansi na kiteknolojia na hata kiuchumi, yanayoendelea duniani, napongeza hatua ya Serikali kwa kuchukua hatua za kuboresha mitaala ya elimu kuwa ya kisasa zaidi ili kuendana na mabadiliko hayo.

Mheshimiwa Spika, kwa miaka kadhaa iliyopita Tanzania imeshuhudia mafundi mchundo wengi wakiongeza (upgrade) ngazi za utaalamu wao kwa kusomea kozi za uhandisi wakati idadi ya mafundi mchundo wanaofuzu masomo ya ufundi mchundo ikipungua huku mafundi wa kawaida (artisans) wanaoongeza utaalamu wao ikiwa haiongezeki. Hali hii imepelekea kupungua kwa kasi idadi ya mafundi mchundo pamoja na mafundi wa kawaida na hivyo kuathiri utendaji wa viwanda (na sekta nyingine) kwa kuwa hawa ndio wanaotenda kazi kwa mikono. Ukizingatia kuongezeka kwa uwekezaji katika viwanda, hali hii inabidi irekebishwe haraka kwa kuongeza idadi ya mafundi husika ili kukidhi mahitaji ya uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa uwiano wahandisi/mafundi mchundo/mafundi wa kawaida ni wa chini sana na hautaweza kuisiadia Tanzania kufikia malengo tarajiwa. Hata ukilinganisha wataalamu wa juu wa stadi mbalimbali za Taifa na wenye stadi za kati na za chini uwiano wake sio mzuri ukilenga uwezo wa kusimamia viwanda vya kisasa kiasi cha kuhitaji marekebisho ya uwiano kama mpango wa Taifa wa kuendeleza stadi unavyotegemea (National Skills Development Strategy).

Mheshimiwa Spika, napendekeza Serikali iongeze msukumo kwenye mafunzo ya mafundi mchundo na mafundi wa kawaida na pia elimu yetu ilenge mafunzo ya ujasiriamali. Hii pia ishirikishe elimu ya kujitegemea toka elimu ya awali na hata kutumia watalaam wetu wa kilimo, mifugo na uvuvi kuanzisha mashamba darasa mashuleni.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na mimi kwa kunipa fursa hii ya kuchangia Wizara hii muhimu ambayo inafanya kazi nzuri. Kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, kwa kweli kwa kazi nzuri anayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri nakupongeza ulipokuja Mbeya uliweza kutusainia mkataba wa barabara muhimu ya njia nne kuanzia Uyole mpaka Songwe licha ya wewe unasema kutoka Uyole mpaka Ifisi. Mheshimiwa Waziri hiyo ni hatua nzuri sana. Kwa sababu uchumi wa Tanzania kwa kiasi kikubwa unategemea zaidi barabara hizi za TANZAM. Vilevile jana umeongelea kuhusu kujenga barabara hiyo ya TANZAM, kipande cha Igawa mpaka Tunduma kwa EPC + Finance. Hiyo ni hatua muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuomba sana Mheshimiwa Waziri, alipokuwa anasaini mkataba pale Mbeya aliwaahidi wananchi wa Mbeya Vijijini kuwa bajeti hii atahakikisha kuwa barabara ya Mbalizi – Shigamba inakuwemo kwenye bajeti hii ili ijengwe kwa kiwango cha lami. Mheshimiwa Waziri ninakuamini sana na ninaimani kabisa kuwa ile ahadi yako kwa wananchi sio wa Mbeya tu, lakini Tanzania nzima ni ahadi muhimu utaitekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Waziri kuna bartabara ambazo ni kiunganishi kikubwa kwa nchi zetu zinazotuzunguka Malawi pamoja na Zambia, lakini na kulisha uwanja wa ndege. Kuna barabara Isyonje – Kikondo – Makete ni barabara muhimu sana. Mheshimiwa Waziri hebu chukulia hiyo umuhimu wa kipekee na kuipa kipaumbele ili iweze kujengwa haraka. Kwa sababu uchumi wa mikoa yetu Mbeya, Njombe, Ruvuma na Iringa inategemea zaidi usafirishaji wa mizigo ili iweze kubebwa na kupelekwa nje na Tanzania iweze kupata pesa za kigeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini barabara nyingine ambayo ni muhimu ni barabara ya Mbalizi – Chang’ombe – Mkwajuni kwenda mpaka Makongorosi. Kwa umuhimu wake namuona Mheshimiwa Mulugo amekuja kukaa hapa karibu ili nisije nikasahau kuizungumzia. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri hii barabara ni ahadi ya muda mrefu sana, lakini imekuwa haipewi umuhimu. Nakuomba sana katika bajeti hii, barabara hii ipewe kipaumbele cha pekee iweze kujengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wamezungumzia umuhimu wa nchi yetu kijiografia. Kiushindani Tanzania Mwenyezi Mungu ametupa neema ya sisi kiushindani akatupa jiografia nzuri, tuna bandari, tuna maziwa, lakini bado hatujazitumia vizuri hizi kwa upendeleo ambao Mwenyezi Mungu ametupa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bandari yetu ya Dar es Salaam ufanisi wake ukilinganisha na bandari nyingine inawezekana sisi ni wa pili kutoka mwisho na wa mwisho nafikiri ni Mogadishu – Somalia. Sasa hatuwezi kuanza kujilinganisha namna hiyo. Tuchukue hatua za haraka ili tuboreshe ufanisi wa bandari yetu. Pia sio kuboresha bandari tu lakini tuboreshe na reli zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali na Mheshimiwa Rais kwa pesa nyingi alizozipeleka kwenye SGR, lakini tunakuomba Mheshimiwa Waziri, kwa umuhimu huo huo hebu iboreshe Reli ya TAZARA. Reli ya TAZARA ni muhimu sana kwa ushindani wa Bandari yetu ya Dar es Salaam, lakini vilevile Bandari ya Katanga kwa ajili ya soko la DRC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tunapoteza biashara zetu kwa kiasi kikubwa kwa nchi jirani kwa bandari jirani kutokana na ufanisi tulio nao kwenye bandari yetu ya Dar es Salaam. Mfano mdogo tu, kwa kupitisha mizigo yetu Zambia, Tanzania inapoteza karibu shilingi bilioni 60 kwa kipande hicho tu cha Tunduma mpaka Zambia ili mzigo ufike Congo, hii sio pesa ndogo. Pesa hii ukiijumlisha kwa miaka mitano inatosha kabisa kuboresha Bandari ya Katanga na hata kujenga barabara kwenda Lubumbashi. Hiyo itaongeza ufanisi na vilevile itanongeza ushindani.

Kwa hiyo, nakuomba sana Mheshimiwa Waziri, toa umuhimu kwenye Bandari yetu ya Dar es Salaam ipate wawekezaji wazuri na biashara sio ifanye Serikali, biashara tuwaachie watu binafsi. Mfano ni TAZARA watu binafsi wafanya vizuri na TAZARA imepata pesa nyingi kwa sababu ya wale watu mliokodisha wafanye biashara ndogo ya TAZARA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna changamoto nyingine ambazo ziko bandarini kutokana na ufinyu wa bandari yetu. Mimi binafsi naona Bandari ya Bagamoyo itatuweka Tanzania mahali pazuri zaidi na tusifikirie kujenga wenyewe, tufikirie uwekezaji wa wenzetu kwa PPP. Ninaimani bandari ya Bagamoyo ambayo ina kina cha asili cha mita 18 ina uwezo wa meli kubwa kuja Tanzania zenye ukubwa wa mpaka mita 400. Hiyo itatufanya sisi tuweze kufanya biashara vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile nilikuwa naangalia Shirika letu la Ndege la Tanzania; wenzangu wameongelea ni namna gani tuliweke katika position ambayo inaweza kufanya vizuri zaidi. Mimi ningejikita zaidi kuhakikisha kwamba tuna nunua ndege za mizigo, lakini tunajenga viwanja vya ndege vingi zaidi na hivyo vilivyopo tuviboreshe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nakuomba Serikali inunue ndege za ziada za mizigo ili mizigo yetu iweze kufanya vizuri kwenye soko la dunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mawaziri na viongozi wote wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Serikali katika utekelezaji wa ustawi wa jamii na maendeleo endelevu na hii ni mojawapo ya nguzo kuu katika utayari wetu wa ushindani wa kimataifa (national competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni “Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru Serikali kwa kuanzisha mikopo inayotolewa kwa ajili ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha (KKK) ardhi. Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ni mnufaika wa programu hii na imekopeshwa shilingi 1,857,586,634. Mji Mdogo wa Mbalizi kumepimwa viwanja 35,000 kwa gharama ya shilingi 1,273,038,500 na Kijiji cha Mwashoma, Kitongoji cha Inolo vimepimwa viwanja 565 kwa gharama ya shilingi 584,548,134 na umefanyika kwa ufanisi mkubwa sana. Kutokana mahitaji makubwa na faida itayopatikana kwenye mauzo ya viwanja hivi, ipangiwe matumizi yanayolenga kuendeleza ardhi ikiwemo kuweka miundombinu kwenye maeneo yanayopimwa. Kutokana na mafanikio katika utekelezaji huu wa mwanzo, napendekeza Serikali iweke kipaumbele cha kuendeleza programu katika maeneo mengine hususani yanayolizunguka Jiji la Mbeya kutokana na mahitaji makubwa ya makazi yaliyopimwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza Serikali iendeleze programu hii katika vijiji vya Swaya; Lupeta; Nsenga; Ifiga; Nsongwi Mantanji; Nsongwi Juu; Izumbwe; Iwindi; Igoma; Ilembo; Idimi na Haporoto. Upimaji kwenye vijiji ambavyo ni vinakuwa haraka kuwa Miji (growing towns) utawezesha kupunguza na hata kuondoa kabisa makazi holela na pia kuongeza wigo wa walipa kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na programu ya makazi, Serikali iweke usimamizi wa matumizi bora ya ardhi ya kilimo ambayo inaendelea kupotea kwa matumizi ya makazi. Katika kupangilia matumizi mazuri ya ardhi, ihusishe Wizara za Kilimo, Wizara za Maji na Wizara inayosimamia mazingira. Kwa vile binadamu tunaongezeka ni muhimu kuhakikisha ulinzi kwa kuhifadhi ardhi inayofaa kwa kilimo na pia kutenga ardhi kwa ajili ya wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali kurejesha mahusiano mazuri kati ya TANAPA (Hifadhi ya Kitulo) na wananchi wa Kata za Ilungu, Igoma, Ulenje na Inyala suluhu haijapatikana. Serikali ichukue hatua pia za kumaliza mgogoro wa miaka mingi wa mpaka kati ya TFS na wananchi wa Kijiji cha Mwashoma. Wananchi wa Wilaya ya Mbeya wamekuwa walinzi wazuri wa hifadhi zetu na ni jukumu la Serikali kuhakisha uendelevu huu na kuondoa migogoro ambayo haina maslahi kwa Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mawaziri na viongozi wote wa Wizara ya Nishati, kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Waziri wa Nishati kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Serikali katika utekelezaji wa ustawi wa jamii na maendelo endelevu, na hii ni mojawapo ya nguzo kuu katika utayari wetu wa Ushindani wa Kimataifa (National Competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025 /2026 ambayo ni “Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.”

Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali kupitia Wizara ya Nishati kwa kuendelea kutekeleza kwa ufanisi mkubwa miradi ya umeme ikiwemo Miradi ya Kusambaza Umeme Vijijini (REA) na ujenzi mkubwa wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) litakalozalisha umeme wa megawati 2,115. Miradi hii ya Kusambaza Umeme Vijijini umeiweka Tanzania katika nafasi ya juu Afrika na umeweza kuchochea kasi ya ukuaji wa viwanda na uchumi.

Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto za vita ya Ukraine na Urusi na kupelekea kupanda kwa bei ya mafuta ya petroli, napongeza Serikali kushirikisha Wizara ya Nishati, Wizara ya Fedha, EWURA na wadau wengine kuweka mkakati wa kuanzisha Mfuko wa Kudhibiti Mabadiliko ya Bei za Mafuta (Fuel Price Stabilization Fund) ili kukabiliana na kupanda kwa bei za mafuta. Pia Serikali ichukue hatua stahiki za kuanzisha Hifadhi ya Taifa ya Kimkakati ya Mafuta (Strategic Petroleum Reserve-SPR) ili kukabiliana na dharura na kuimarisha usalama na uhakika wa mafuta kwa Taifa.

Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto za upatikanaji wa dola za Kimarekani (USD) kwa kipindi kirefu sasa, makampuni yanayoagiza mafuta yanapata changamoto za kulipia mafuta kwa wakati na kulazimika kulipa faini kwa Shirika la PBPA. Kutokana na ukame wa USD kwenye soko la fedha za kigeni, makampuni yamelazimika kukopa kwenye mabenki kwa namna tofauti (post import loans, swaps, forward contracts etc). Kutokana na changamoto za upatikanaji wa dola, makampuni yameshindwa kuagiza mafuta ya kutosha na hali hii ni hatarishi kwa uchumi wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, pamoja na makampuni kulazimika kununua USD kwa gharama kubwa zaidi ya bei elekezi ya Benki Kuu, makampuni yameshindwa kulipia na kupelekea kushindwa kupokea mafuta.

Mheshimiwa Spika, nashauri Serikali kuchukua hatua za haraka kuchochea upatikanaji wa USD hasa kutoka vyanzo vya madini na kilimo na ikiwezekana kuanzisha utaratibu wa biashara ya Serikali kwa Serikali na nchi rafiki zinazozalisha mafuta kwa makubaliano kulipa baada ya makusanyo ya mauzo ya madini na kilimo. Serikali inaweza kuratibu mfumo mzuri wa kununua dhahabu yote toka kwa wachimbaji wadogo kwa shilingi na kulipa bei nzuri zaidi kuliko hata ya soko na ikifanya hivyo kwa mazao ambayo yamekuwa yanatoroshwa kinyemela nje ya nchi. Dhahabu na mazao yaliyonunuliwa kwa shilingi yapate soko zuri kwa wanunuzi kwa dola za Kimarekani kusaidia uagizwaji wa mafuta. Kwa taarifa za makampuni yanayoagiza mafuta yanahitaji zaidi ya USD bilioni moja ili kulipia mzigo uliofika nchini ila haujapokelewa na kila mwezi inatakiwa kutenga USD milioni 250 kwa ajili ya kuagiza mafuta ya ndani ya nchi.

Mheshimiwa Spika, mfumo wa kununua mafuta kwa pamoja (BPS) umeonesha mafanikio makubwa na napendekeza uendelee ikiwa ni pamoja na kuvutia kutumika kwa mahitaji ya mafuta kwa nchi jirani. Mfumo huu uboreshwe hasa katika kuweka vinasaba kwa kutumia mashine (automation) na pia kuwepo na ulinganifu wa taarifa ya kila siku kati ya kiasi cha vinasaba vilivyotumika na kiasi cha mafuta yaliyopakiliwa. Na pia magari ya kubeba vinasaba yafungwe kamera kwa ajili ya udhibiti mafuta yanayoenda nchi za nje pasipo kutorudi kinyemela kutumika nchini.

Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto za kupakua mafuta bandarini, napendekeza kupanua na kuboresha miundombinu ya kupakulia na kupokelea mafuta ikiwemo kupakua mafuta kwa saa 24. Napendekeza pia kujenga miundombinu ya kuhifadhi mafuta kwa matumizi ya ndani na pia kwa nchi jirani, na usafirishaji uwe wenye tija kubwa ikiwemo kusafirisha kwa treni. Pia Serikali iangalie uwezekano wa kujenga bomba la mafuta kwenye MKUZA wa TAZAMA na kujenga miundombinu ya kuhifadhi mafuta kwenye bandari kavu eneo la Inyala, Mbeya kwa matumizi ya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na nchi jirani za DRC, Zambia, Malawi na hata Zimbabwe.

Mheshimiwa Spika, pamoja na REA kutekeleza miradi ya kupeleka umeme kwenye makao makuu ya karibu vijiji vyote vya jimbo la Mbeya Vijijini, bado kuna uhitaji mkubwa wa umeme kufika kwenye vitongoji vyote. Napendekeza kuendelea kwa kasi utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mradi wa REA III (REA III, Round II) na kufikisha umeme katika vijiji vyote vilivyobakia na pia kuendelea na utekelezaji wa Mradi wa Ujazilizi (Densification). Napendekeza utekelezaji utoe kipaumbele kwa Kata za Itawa na Shizuvi na pia kwenye vitongoji vinavyolizunguka Jiji la Mbeya, ikiwemo Mina na Lusungo Kata ya Iwindi, Kijiji cha Shongo, Kijiji cha Wambishe, kwenye shule zote ikiwemo Shule ya Sekondari Iwiji.

Mheshimiwa Spika, katika vijiji vilivyopatiwa umeme kwa kiasi kikubwa imechochea ukuaji wa viwanda hasa vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo. Nashauri TANESCO iongeze speed ya kuunganisha umeme na pia kushughulikia maombi ya wateja wengi wanaosubiria umeme ikichukuliwa hii ni fursa pia kwa TANESCO kuongeza mapato ya shirika.

Mheshimiwa Spika, pamoja na vyanzo vya sasa, napendekeza Serikali itekeleze miradi ya vyanzo vingine kama vile vyanzo vya Jotoardhi, Umeme wa Jua, Upepo na Mkaa wa Mawe ili nchi yetu iendane na mahitaji makubwa ya umeme kwa hapa Tanzania na hata kuuza kwa nchi zingine za Afrika. Ni muda mrefu sasa, TANESCO kupitia Kampuni Tanzu ya Uendelezaji wa Jotoardhi nchini (TGDC) inaendelea na tafiti katika maeneo mbalimbali nchini kama vile eneo la Ziwa Ngozi lililoko Mkoani Mbeya ambapo ndipo yalipo makutano ya Bonde la Ufa la upande wa Mashariki na lile la Magharibi.

Napendekeza Serikali iharakishe utekelezaji wa miradi huu wa Jotoardhi na ule wa Mkaa wa Mawe wa Mchuchuma na Kiwira ili tuweza kuzalisha umeme zaidi kwa mahitaji ya ndani na nchi za nje.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mawaziri na viongozi wote wa Wizara ya Maliasili na Utalii, kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Waziri wa Maliasili na Utalii, kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Serikali katika utekelezaji wa ustawi wa jamii na maendelo endelevu, na hii ni mojawapo ya nguzo kuu katika utayari wetu wa Ushindani wa Kimataifa (National Competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.”

Mheshimiwa Spika, pamoja na programu ya kutunza maliasili zetu, Serikali iweke usimamizi wa msitu hasa ya asili, ambayo inaendelea kupotea kwa matumizi ya nishati. Katika kupangilia matumizi mazuri ya ardhi, ihusishe Wizara zote zinazosimamia Maliasili, Ardhi, Kilimo, Wizara za Maji na pia Wizara inayosimamia Mazingira. Kwa vile binadamu tunaongezeka ni muhimu kuhakikisha ulinzi kwa kuhifadhi mazingira yetu na kuwepo msukumo zaidi kwenye kuboresha mazingiara.

Mheshimiwa Spika, napongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali kurejesha mahusiano mazuri kati ya TANAPA (Hifadhi ya Kitulo) na wananchi wa Kata za Ilungu, Igoma, Ulenje na Inyala. Kuna mgogoro wa miaka mingi wa mpaka kati ya TFS na wananchi wa Kijiji cha Mwashoma, Kata ya Inyala. Kutokana na mgogoro huu kuchukua muda mrefu na kusababisha hata uvunjifu wa amani, kuna ahadi ya mwaka 2015 alitoa Mheshimiwa Hayati Magufuli na kumwelekeza Waziri wa Ardhi na pia Waziri wa Maliasili na Utalii wa wakati huo kupitia upya mipaka ili wananchi wa kata za Inyala, hususani Kijiji cha Mwashoma waachiwe maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, maeneo yenye mgogoro ni mashamba ya wananchi na wamekuwa walinzi wazuri wa misitu na vyanzo vya maji, ni imani yangu wakiachiwa hayo maeneo yanayogombewa na TFS, kuna maslahi mapana kwa Taifa.

Mheshimiwa Spika, napongeza juhudi za Serikali kuweka umuhimu wa kipekee na kupewa kipaumbele kwa sekta ya utalii ili iendelee kuchangia pato la Taifa, uhifadhi wa mazingira, na ustawi wa jamii kupitia fursa za matumizi endelevu ya rasilimali za utalii. Mheshimiwa Rais amekuwa mstari wa mbele kutangaza utalii kwa kutumia mikakati mbalimbali ikiwemo Programu ya Tanzania - The Royal Tour ambapo kwa mwaka 2022, idadi ya watalii imeongezeka kwa asilimia 58 kufikia watalii 1,454,920. Kwa mwaka 2022 mapato yatokanayo na watalii yameongezeka kwa asilimia 93 hadi kufikia dola za Marekani milioni 2,527.72.

Mheshimiwa Spika, mchango huu wa sekta ya utalii bado ni mdogo sana kulinganisha na nchi shindani na hata kulingana na maoteo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi na Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo. Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 na Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III 2021/2022-2025/2026) umeelekeza kufikia idadi ya watalii wapatao milioni tano na kukusanya mapato ya kiasi cha dola za Kimarekani bilioni sita kufikia mwaka 2025/2026.

Mheshimiwa Spika, mchango wa sekta ya utalii unakabiliwa na changamoto ya ushindani mkubwa katika soko la utalii wa kimataifa hasa kutokana na miundombinu na hata mazingira ambayo siyo rafiki kwa wawekezaji ikiwemo utitiri wa tozo. Biashara ya utalii ni sawa na biashara zingine za nje zinazotegemewa katika mapato ya fedha za kigeni, lakini inakabiliwa na utitiri wa tozo katika mnyororo mzima na kupelekea kuwa mzigo mkubwa kupambana na ushindani wa kimataifa.

Mheshimiwa Spika, watalii kama ilivyo kwa biashara zingine wanaangalia sana ubora wa huduma pamoja na gharama katika mnyororo mzima wa utalii. Pamoja na nchi yetu kubarikiwa utajiri wa vivutio vya aina mbalimbali, inatakiwa kuwepo na mkakati madhubuti wa kuhakikisha uendelezaji wa vivutio ili kuongeza wigo wa shughuli za utalii na hata kuondoa tozo ambazo ni mzigo kibiashara. Serikali iangalie kuondoa kodi zote ambazo hazotozwi na nchi shindani na pia mnyororo wa biashara ya utalii ichukuliwe kama biashara ya nje (export).

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mawaziri na viongozi wote wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Spika, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Serikali katika utekelezaji wa ustawi wa jamii na maendelo endelevu, na hii ni mojawapo ya nguzo kuu katika utayari wetu wa ushindani wa kimataifa (nation competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwapongeza wanamichezo wote kwa kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa. Kwa namna ya pekee napenda kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa hamasa na msukumo alioweka katika michezo yote na hasa mafanikio makubwa ya timu ya Yanga katika mashindano ya Kombe la Shirikisho (CAF Confederation Cup). Napenda pia kuwapongeza Klabu ya Yanga kwa kushinda ugenini Algeria katika raundi ya pili ya fainali na kufanya jumla ya magoli mawili kwa mawili kushika nafasi ya pili kikanuni ya Kombe la Shirikisho (CAF Confederation Cup). Kutokana na hamasa ya Mhe. Rais, Klabu ya Yanga imeandika historia na kuipa nchi yetu heshima kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inastahili pongezi kwa mkakati wake katika kuimarisha, kuziwezesha na kufanikisha ushiriki wa timu za Taifa na vilabu katika michezo na michuano mbalimbali ya kimataifa na kikanda. Kama sehemu ya mkakati huo Wizara iweke msukumo zaidi wa kuhamasisha kujenga, kukarabati na kuboresha miundombinu ya viwanja vya michezo hususani vya mpira wa miguu. Viwanja vingi vya mikoani vipo katika hali mbaya na kwa kiasi kikubwa ni sehemu ya changamoto katika maendeleo ya michezo nchini. Michezo na sanaa ni muhimu sana katika kujenga sura na sifa ya Taifa letu (nation brand). Hivyo ni muhimu kwa Serikali kuhakikisha inaweka umuhimu mkubwa wa ushiriki wa timu zetu za Taifa na kuwepo kwa mkakati wa kitaifa wa kuhakikisha timu zetu za Taifa na vilabu zinafanya vizuri kwenye mashindano ya kikanda na kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati huu katika michezo na sanaa ni nguzo muhimu katika kutekeleza Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026. Serikali itenge bajeti ya kutosha kuhakisha tija katika ushiriki wetu katika mashindano ya kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na kuboresha miundombinu ya viwanja, Wizara ijikite katika kuibua vipaji mbalimbali vya michezo na sanaa kwa kuimarisha ushirikiano na Wizara nyingine hususani Elimu na TAMISEMI. Pamoja na kutokuwepo kwa miundombinu rafiki, mikoa mingi imekuwa inatoa wachezaji wenye vipaji vikubwa katika mpira wa miguu, riadha na hata sanaa mbalimbali. Imefika muda sasa wa kuwepo kwa mkakati wa kuibua na kuendeleza vipaji hivyo ambavyo vimekuwa vinaonekana kikanda zaidi kama vile riadha kwa Mikoa ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kusini na Mikoa ya Kati. Pia kwa upande wa mpira wa miguu kumekuwepo na mikoa kadhaa ya vipaji vikubwa na huko ndio Serikali iweke msukumo zaidi wa kuibua na kuendeleza hivyo vipaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kwa wasanii, kuna Mikoa imekuwa inatoa idadi kubwa ya vipaji kwenye uigizaji, uimbaji ikiwemo nyimbo za injili ambazo zinapata umaarufu sana duniani. Kutokana na vipaji vingi vya michezo hususani mpira wa miguu na riadha, napendekeza Shule ya Sekondari Santilya ya Wilaya ya Mbeya iongezwe kwenye orodha ya shule teule za michezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na umuhimu wa Kiswahili kuwa Lugha rasmi Kimataifa, napendekeza uwekezaji zaidi katika kuitangaza na pia kuwezesha Ulimwengu kujua kuwa mizizi na ustawi wa Kiswahili ni Tanzania pekee na wengine wanaigiza kwetu. Serikali iendelee kuchukuwa hatua zaidi ya kukistawisha Kiswahili katika Mataifa mengine Barani Afrika na kwingineko kwa kushirikisha vyuo vikuu hapa nchini na vyuo vikuu mbalimbali duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa fursa hii ya kuchangia bajeti ya Serikali. Nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi alivyosimamia vizuri uchumi wa Tanzania katika hiki kipindi kigumu ambacho dunia na nchi zote sasa hivi zinapambana na hali mbaya ya kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli nchi yetu ukilinganisha yale malengo ambayo tulijiwekea wenyewe lakini ni malengo ya millennium (MDGs) tumefanya vizuri sana. Hongera sana Mheshimiwa Rais, lakini hongera sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa sababu wewe ndiyo uko mstari wa mbele kuhakikisha ya kwamba haya yanayotokea yanatokea kwa manufaa ya Watanzania kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia ukuaji wa pato la Taifa nchi yetu ilikua kwa 4.7% ukilinganisha na nchi za Jangwa la Sahara 3.9%. Kwa hiyo, Tanzania imefanya vizuri kuliko nchi zingine ambazo zilikuwa na wastani wa 3.9%. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile exchange rate ya kwetu kwa muda mrefu imekuwa himilivu ukilinganisha na wenzetu na kwa nini inabidi Mheshimiwa Waziri wa Fedha aiangalie sana hii exchange rate isije ikatuyumbisha kwa sababu ukiliangalia nakisi yetu ya bajeti nyingi ni fedha za kigeni. Kwa hiyo, tukiyumba kwenye fedha ya kubadilishia ya shilingi yetu ina maana uchumi wetu utayumba na hii hata inflation tunayoisema sasa hivi ya 3.4% hatutaimudu tena.

Kwa hiyo, tunakushukuru sana kwa hatua tuliyofikia mpaka leo ya kwamba tumeendelea kufanya vizuri, lakini hata ukija kwenye fedha za kigeni bado nchi yetu imefanya vizuri zaidi pamoja na kuongezeka kwa nakisi ya malipo, bado nchi yetu inaonesha kuwa tunaweza kuagiza bidhaa nje kwa miezi zaidi ya minne ukilinganisha na miezi sita ambayo ilikuwepo mwaka jana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ili tuweze kujirekebisha katika hali hii nilikuwa napendekeza Serikali iangalie vigezo ambavyo vinatufanya sisi tuwe washindani ukilinganisha na nchi zingine.

Mheshimiwa Spika, Sekta ya Madini ndiyo inayotuletea fedha za kigeni. Nashukuru Mheshimiwa Waziri amesema kuwa Benki Kuu itaanza kununua dhahabu kama sehemu ya kuwekeza fedha za kigeni na hii ni hatua muhimu, kwa sababu Benki Kuu itanunua dhahabu kwa kutumia shilingi, lakini dhahabu itakayonunuliwa ni sawa na fedha za kigeni. Ombi langu ni kwamba Serikali iangalie jinsi ya kuwalipa hawa hasa wachimbaji wadogo bei ambayo ni nzuri ukilinganisha na wanunuzi wengine. Kwa hiyo, kila wakati Serikali iwe flexible kuwa itakachowalipa hawa wachimbaji wadogo wadogo bei yao iwe nzuri zaidi ili tuweze kukusanya dhahabu ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa ubunifu wake kwa sababu katika hii dunia ya ushindani bila ubunifu unaweza kwenda na maji. Juzi mimi nilikuwa shuhuda wa Serikali ilikuwa inasaini mikataba ya ujenzi wa barabara kwa njia ya EPC+F (Engineering, Procurement na Construction + Finance); huu ni ubunifu mkubwa mno. Sijawahi kuona ujenzi wa barabara kilometa zaidi ya 2,000 na mkataba wa shilingi trilioni 3.7 ambayo ni mbadala wa tulivyozoea ku-finance ujenzi wa miundombinu ya barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nikiri kabisa inawezekana tulichelewa kufanya mifumo ya aina hii ya utekelezaji wa miradi yetu na nina imani kwa sababu mikataba imeshasainiwa, imani ya kwangu ni kwamba hizi kilometa zaidi ya 2,000 zitakamilika ndani ya muda mfupi. Serikali hapo haitaingiza tena mfukoni kwake kwa ajili ya kulipa ujenzi wa hizo barabara mpaka mradi utakapokamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watu wengi wanaweza kuwa wanajiuliza itakuwaje wakishamaliza? Kinachotakiwa hapa ni jinsi ya kufanya management ya ukwasi wa Serikali yetu. Kwa hiyo, planning ni muhimu kuhakikisha kuwa itakapoiva hii mikataba tuweze kuwalipa ili tuendelee hata katika miradi mingine. Ninashukuru vilevile katika hizi barabara, imo barabara ya TANZAM kuanzia Igawa mpaka Tunduma ambayo itakuwa ya njia nne na hii siyo barabara kwa ajili ya Tanzania peke yake, ni barabara pamoja na majirani zetu wa nchi za SADC ikiwemo DRC Congo, Zambia, Malawi, Zimbabwe lakini mpaka Afrika Kusini na hii ndiyo inabeba uchumi wa Tanzania kwa Dar es Salaam Corridor. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hii EPC+ Finance, lakini Serikali imeonesha kuwa sasa hivi miradi mingi tutakwenda kwa mfumo wa PPP. Kwa muda mrefu Mradi wa PPP ilitakiwa uanze lakini ilichelewa kutokana na sheria yetu ilikuwa siyo rafiki kwa wawekezaji. Bunge lako mwezi huu limeshapitisha marekebisho ya hiyo sheria na kutokana na hayo marekebisho, itaanza na ujenzi wa barabara ya Kibaha – Chalinze – Morogoro ambayo itakuwa ni express highway lakini baadae itakuja Morogoro mpaka Dodoma na itakuja na ring road au barabara ya mzunguko hapa Dodoma na nina imani vilevile itaenda kwenye ujenzi wa reli ya Kusini Mtwara – Mbamba Bay, lakini na barabara ya Kaskazini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huu mfumo wa PPP ndiyo mifumo inayotakiwa sasa hivi katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu kwa sababu risk yote ya miradi unaihamishia kwa sekta binafsi ikiwemo na EPC ni kwamba risk zote unakuwa umezihamishia kwa watu binafsi, kwa hiyo, Serikali kinachotakiwa ni kuisimamia na kuhakikisha kuwa kile tulichokubaliana kinaenda sawia, lakini vilevile na ubora. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni imani yangu kutokana na maboresho ya bandari ambayo yanafanyika sasa hivi, nina imani kuwa fedha za kigeni zitakuja za kutosha kwa ajili ya kuhimili madeni haya yote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini ninachoomba Serikali pamoja na hayo maboresho kutakuwa na ongezeko la mizigo, tuhakikishe tunakamilisha SGR kwa muda mfupi, lakini tukamilishe vilevile reli ya TAZARA ni muhimu kwa ajili ya biashara ya bandari yetu kwa sababu hiyo mizigo asilimia 70 yote haitakuwa bora yaanze kupita tena kwenye expressway, tupitishe kwenye reli ambayo itatufanya gharama za usafirishaji za kwetu ziwe za chini ukilinganisha na nchi zingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na kupambana na hali hii ya uchumi, naiomba Serikali iangalie zaidi na iweke kipaumbele cha kwanza kuhakikisha inaboresha biashara ya madini. Madini ndiyo yanayotuletea fedha zetu za kigeni kwa sasa hivi. Nimeona juzi nampongeza tena Mheshimiwa Rais ameidhinisha kulipa fidia ya wananchi wa Liganga walipwe zaidi ya shilingi bilioni 15 kwa ajili ya kufufua ule mradi mkubwa. Ule mradi utailetea Tanzania FDI zaidi ya shilingi bilioni tatu ambayo ni fedha nyingi sana. Ajira zaidi ya 30,000 lakini utakapochimba chuma na haya makaa ya mawe naomba haya yachakatwe hapa hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo naiomba Wizara ya Madini Serikali iharakishe vilevile machimbo ya madini ya niobium kule Mbeya kwa sababu yale ndiyo utakuwa mgodi wa kwanza Afrika na mgodi wa tatu duniani na madini ya niobium ni kwa ajili ya kutengeneza kifaa kinaitwa...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Sekunde 30 malizia Mheshimiwa.

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, madini ya niobium ni kwa ajili ya kutengeneza chuma kinaitwa ferroniobium ambacho kinahitajika sana kwenye ujenzi wa madaraja pamoja na reli zetu, lakini vilevile naiomba Serikali tunaporekebisha hiyo miundombinu vilevile na barabara ambazo zinalisha hizi barabara kuu kama barabara ya Mbalizi – Shigamba nayo ipewe kipaumbele, barabara ya Isyonje – Kikondwe ipewe kipaumbele, barabara ya Mbalizi – Chang’ombe – Makongorosi ipewe kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa hii fursa ya kuchangia hii Wizara muhimu. Nami napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu na Wizara hii kwa kutuletea bajeti nzuri sana ya kilimo. Hii bajeti ya kilimo kwa kuiangalia kwa juu juu, itatuletea mapinduzi makubwa ya uchumi wetu hapa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nami napenda kuishukuru Kamati ya Kilimo, imetoa maangalizo mazuri sana ambayo naomba Mheshimiwa Waziri, ayafuatilie kwa ukaribu, la sivyo bajeti hii asipoangalia hayo maangalizo ya Kamati, inaweza isitekelezeke kama anavyotarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala ambalo Kamati imeelekeza, ni kwa jinsi ya wataalam waliopo kilimo inaona kama hawajitoshelezi, lakini naona kama wataalam wanajitosheleza. Unapokuwa na transformational budget kama hii, inabidi lazima ubadilishe na culture ya watu utakaowakuta. Kwa vile kwa muda mrefu walikuwa hawajawahi kuona fedha nyingi kiasi hiki, sasa unapowapelekea fedha nyingi kiasi hiki, watashindwa hata namna ya kuzitumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi fedha ukiziangalia zinatokana na mkopo wa IMF ambao wana discipline kubwa katika matumizi ya fedha zao. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, nina imani na taaluma yake kwa kiasi kikubwa, hebu aangalie kwa namna gani haya matumizi ya fedha za IMF ambazo ni za uhakika zitatuletea fedha nyingi zaidi? Naamini Sekretarieti yake, Katibu Mkuu wake, ni mtu mwenye uwezo mkubwa sana; hebu mtumie vizuri, nina imani kuwa Wizara hii itabadilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mbolea siyo ruzuku tu, mbolea ni namna ya uagizaji wa mbolea. Mwelekeo wa bei za mbolea sasa hivi haueleweki. Shilingi bilioni 150 zinaweza kusaidia, lakini hizi zitawapa matumaini wananchi. Mimi naona bado tunahitaji kuufumua muundo mzima wa mbolea. Mbolea haiagizwi kama kama tunavyokwenda sokoni, mbolea inatumia taasisi ambazo ninaimani Waziri anazifahamu kuna mambo yanaitwa futures, hygiene na kadhalika na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi ndiyo ambazo zinaweza kutusaidia kununua mbolea kwa wakati muafaka, wakati bei ni sahihi kwa nchi yetu. Kwa kuwatumia wafanyabiashara watanunua kwa bei kubwa watatuuzia kwa bei kubwa. Kwa hiyo, nchi ichukue jukumu la kuagiza mbolea yenyewe, aidha kwa kuwadhamini hao wafanyabiashara, tununue katika kipindi ambacho Brazil na zile nchi ambazo zinatumia mbolea kwa kiasi kikubwa haziagizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, jukumu la kuagiza mbolea lisiwe kwa walanguzi wafanyabiashara. Hawa ni traders, hawawezi kukusaidia. Hebu chukua jukumu wewe mwenyewe, weka miongozo, lakini hiyo iendane pamoja vile vile Shukuma kuwepo na Sheria ya Kilimo. Transformation kama hizi huwezi ukazitekeleza bila ya kuwa na sheria sahihi ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hiyo, napenda kwenye kuongeza thamani za mazao; zao la pareto. Pareto inaweza kutusaidia kwenye viuadudu. Kwa kutumia kiwanda chetu cha Kibaha, pareto inaweza kusaidia kuzalisha viuatilifu. Sasa ni kwa nini tusiwe na mpango kabambe wa taasisi zetu za utafiti ifanyike haraka ili tuweze kukisaidia kile kiwanda kiweze kuzalisha viuatilifu pamoja na mbolea? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo jambo ni muhimu sana, litatusaidia, kwa vile pareto inayolimwa Tanzania, wengi hawajui, tunaongoza Afrika, ni wa pili duniani. Hii inaweza kutusaidia kutuletea fedha nyingi za kigeni na kuwasaidia wananchi ambao kwa sasa hivi wanalanguliwa sana kwa bei ndogo ya pareto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti na Bunge hili, kwa hiyo, naomba kwa sababu Bunge hili tuliamini na tunaamini kuwa ni Bunge ambalo litajikita kwenye kilimo, kwa hiyo, tunaomba huo mwongozo ambao ulikuwa umeutoa tuendelee nao tuhakikishe kuwa kilimo ndiyo kinabebwa na Bunge lako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mawaziri na viongozi wote wa Wizara ya Kilimo, kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Waziri wa Kilimo kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Serikali katika utekelezaji wa ustawi wa jamii na maendeleo endelevu na hii ni mojawapo ya nguzo kuu katika utayari wetu wa ushindani wa kimataifa (national competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Spika, kulingana na taarifa ya Wizara ya Kilimo, Tanzania ina hekta milioni 44 zinazofaa kwa kilimo cha mazao, kwa wastani hekta milioni 10.8 tu sawa na asilimia 24 ndizo zinazolimwa kila mwaka. Sekta hii kwa mwaka 2020 imechangia asilimia 26.9 kwenye Pato la Taifa, imetoa ajira kwa wananchi kwa wastani wa asilimia 61.1 na imechangia asilimia 65 ya upatikanaji wa malighafi za viwanda. Sekta ya kilimo ni mhimili wa uchumi wa nchi na inachangia pato la mkulima mmoja mmoja, kaya na Taifa kwa ujumla. Sekta ya kilimo na hususani sekta ndogo ya mazao imechangia asilimia 15.4 katika Pato la Taifa na zaidi ya asilimia 100 ya upatikanaji wa chakula kinachozalishwa nchini na kupelekea kupunguza mfumuko wa bei kwa takribani asilimia 59.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kujitosheleza kwa chakula na kuchangia katika uchumi wa Taifa, takribani mazao yote yanazalishwa kwa tija ndogo katika eneo husika. Uzalishaji wa mahindi wa tani 1.76 kwa hekta moja ni asilimia 29 tu ya uzalishaji unaotegemewa wa tani sita kwa hekta moja. Uzalishaji huu wa chini kwa mazao yote unatokana na ukosefu wa ushauri wa watalaam wa kilimo ikiwemo matumizi yasiyo sahihi ya mbolea na pembejeo zingine. Katika hali hii, kilimo hakijamsaidia mkulima kwa kiasi kikubwa kunajinasua kwenye umaskini na kimeendelea kutoa mchango mdogo kwenye Pato la Taifa.

Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa mbolea nchini hadi Februari, 2022 ulikuwa tani 436,452 sawa na asilimia 63 ya mahitaji ya tani 698,260, lakini kutokana na bei kubwa ya mbolea mauzo yalikuwa tani 173,957 tu sawa na asilimia 25. Wakulima wengi walishindwa kumudu kununua mbolea kutokana na mfumuko wa bei wa asilimia 100 na ikichangiwa na hali isiyoridhisha ya mvua inaweza kupelekea upungufu wa uzalishaji hasa mazao ya nafaka. Napendekeza Serikali ichukue hatua za kurudisha ruzuku ya pembejeo pamoja na kuanzisha Price Stabilization Fund kwa pembejeo hasa mbolea ili kuongeza tija kwenye uzalishaji wa mazao ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, nashauri Serikali iendelee kuimarisha usalama wa chakula nchini kwa kununua na kuhifadhi nafaka kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula. Kutokana na vita ya Urusi na Ukraine kunaashiria upungufu mkubwa wa nafaka na kwa kuzingatia gharama kubwa za uzalishaji wa karibu asilimia 100, Serikali ichukue hatua za makusudi kusaidia wakulima wapate bei nzuri ya NFRA badala ya kuuza kwa walanguzi na kutorosha chakula nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, Serikali iangalie fursa za kiwanda cha Viuadudu cha Kibaha kuanza uzalishaji wa viatilifu inayotokana na pareto ambayo inazalishwa hapa nchini na imekuwa inauzwa nchi za nje kama semi-finished product kwa bei ndogo ya kutupa. Viatilifu kutokana na pareto ni suluhisho la soko la pareto na pia suluhisho kwa upotevu wa mazao kushambuliwa na wadudu (post-harvest losses). Pia Serikali ianze mchakato wa kutumia madini (calcium carbonate, agricultural lime, phosphates, natural gas etc.) yanayopatikana kwa wingi hapa Tanzania, kuanza uzalishalishaji wa mbolea hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha bajeti ya mwaka 2021/2022, Serikali ilitenga shilingi 164,748,000,000 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ambapo shilingi 82,180,000,000 ni fedha za ndani na shilingi 82,568,000,000 ni fedha za nje. Utekelezaji wa miradi hadi kufikia Februari, 2022 hasa utekelezaji kwa fedha za nje uko chini sana. Kutokana na hali hii sekta ya kilimo imeendelea kudorora katika kuchangia Pato la Taifa. Matumaini pekee ni hatua zilizooneshwa kwenye bajeti ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji na Serikali iweke mikakati madhubuti kuhakikisha ufanisi wa utekelezaji wa bajeti hii ya umwagiliaji. Pia mikakati hii iweke nyongeza za ujenzi wa mabwawa hasa maeneo yenye mafuriko makubwa ikiwa ni pamoja na kuzuia mafuriko.

Mheshimiwa Spika, pia napendekeza Serikali iweke msukumo mkubwa wa kuharakisha utekelezaji wa miradi iliyomo kwenye mradi wa Bonde la Mto Songwe (Songwe River Basin Development Programme - SRBDP), wenye ofisi zake Kyela, Tanzania. Mradi huu unaotekelezwa kwa pamoja na Serikali za Tanzania na Malawi, ni muhimu sana kwa sasa kutokana hasa na ujenzi wa mabwawa ambayo pamoja na manufaa mengine yatasaidia kupunguza mafuriko ya Bonde la Kyela. Mabwawa haya yamelenga kuzalisha umeme, kilimo cha umwagiliaji, shughuli za uvuvi na hata utalii ambao unahitajika sana katika Wilaya ya Mbeya na ukanda wote wa Nyanda za Juu Kusini.

Mheshimiwa Spika, Serikali ichukue hatua za haraka kuleta Bungeni mapendekezo ya Sheria ya Kilimo ambayo pamoja na mambo mengine itawezesha usimamizi wa matumizi bora ya ardhi ya kilimo ambayo inaendelea kupotea kwa matumizi ya makazi. Pia kutokana na changamoto za tabia nchi, kumekuwepo na uharibifu mkubwa wa mazingira na ongezeko la upungufu wa vyanzo vya maji. Uharibifu unaotokana na shughuli za kibinadamu umepelekea misitu mingi kuharibiwa na uchomaji moto, ukataji mkaa na hata kilimo kwenye vyanzo vya maji.

Napendekeza Serikali iongeze msukumo kwa Wizara za Maji, Kilimo, Maliasili na Mazingira kufanya kazi kama timu moja ili kukabiliana na janga hili kubwa ikiwemo ujenzi wa mabwawa makubwa katika maeneo yanayokumbwa na mafuriko. Kama ilivyo kwa athari za mafuriko ya Kyela, hata Ziwa Rukwa linaathirika sana na kujaa mchango na udongo unaosombwa na mito kutokana na mmonyoko wa udongo.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mawaziri na viongozi wote wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia, ya Habari kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Spika, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa hotuba nzuri iliojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Serikali katika utekelezaji wa ustawi wa jamii na maendeleo endelevu na hii ni mojawapo ya nguzo kuu katika utayari wetu wa ushindani wa Kimataifa (national competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni “Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu”.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na taarifa ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inaonesha kuna mafanikio makubwa kwenye sekta za habari, mawasiliano ikiwemo mikakati ya kupunguza gharama za mawasiliano kwa wananchi. Utendaji kazi ulilenga pia kuboresha miundo ya TEHAMA kuwezesha mwelekeo mzuri wa kulea ubunifu ili Tanzania iendane na kasi ya dijitali ya kiuchumi (digital economy).

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza msukumo mkubwa kwenye kuendeleza maboresho ya mtandao wenye kasi zaidi na kuhakikisha matumizi mazuri ya Data Center ili kuwezesha ubunifu wa miundombinu ya TEHAMA hasa Serikalini iweze kusomana. Kutokana na kuwepo mifumo tofauti kwenye taasisi za Serikali ni muhimu sana kuunganisha mifumo yote iweze kusoma ili kuleta ufanisi unaoendana na dunia ya leo. Mwelekeo wa dunia ya leo ni kufanya shughuli zote za ki-TEHAMA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kuboresha muundo wa Wizara na Taasisi zake ili kuwepo na idara mahususi itayoongozwa na Afisa TEHAMA Mkuu (CIO) ngazi ya Kamishna. Kuwepo kwa muunganiko wa mifumo yote (Core Government System), ni muhimu kuboresha e-government na itawezesha ufanisi na kupunguza gharama kwa kiasi kikubwa sana. Kuwepo kwa Mkongo wa Taifa na Data Center ni fursa kwa kuwezesha kutengeneza mfumo wa kuratibu na kuendeleza ubunifu katika TEHAMA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, teknolojia imewezesha huduma ya kifedha juimishi (financial inclusion) na hii fursa pia kwa Serikali kuratibu miamala ili iwe sehemu ya mfumo rasmi wa malipo kwa usimamizi wa Benki Kuu na TCRA. Napendekeza maboresho kwenye tozo za miamala itakayoongeza mapato ya Serikali lakini ikizingatia kupunguza mzigo kwa wateja. Serikali kwa kushirikisha wadau, itumie uzoefu wa sasa kuboresha huduma za miamala kwa kuoanisha ufanisi kwa huduma ya kifedha juimishi na tozo mbalimbali na mchango wa huduma hii kwenye kukuza uchumi wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio makubwa ya utekelezaji wa Wizara ikiwemo zoezi la postikodi, kuna maeneo mengi ambayo bado hayajapata huduma za minara ya mawasiliano na hata kwenye maeneo kadhaa yenye minara katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya hayapati huduma ya mawasiliano. Vijiji vingi ikiwemo katika Kata za Ulenje, Iyunga Mapinduzi, Mshewe, Mjele, Ilembo na Ihango havina minara na vingine kuna minara ambayo kwa muda mrefu haina mawasiliano. Kwa kuzingatia lengo la kupeleka TEHAMA kwa kila shule, Serikali iharakishe kujenga minara maeneo yote kwenye vijiji na vitongoji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa hii nafasi ya kuchangia. Nami napenda kwa kuanzia kwanza kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa uwekezaji aliouweka kwenye Wizara hii ikiwemo miundombinu ya barabara, miundombinu ya bandari na miundombinu ya anga. Kwa kweli kazi inayofanyika ni kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nampongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake ya Manaibu Waziri, kazi yako ni nzuri sana na kwa kweli umedhihirisha kuwa kazi unayoifanya kwa kweli itatuletea mapinduzi makubwa katika uchumi wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nayasema hayo kutokana na maboresho yanayofanyika kwenye miundombinu ya bandari. Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye miundombinu ya bandari. Mapinduzi ya Bandari zetu za Dar es Salaam, Tanga pamoja na Mtwara yanaweka nchi yetu katika ushindani mzuri katika ukanda huu wa Afrika Mashariki pamoja na Afrika ya Kati.

Mheshimiwa Naibu Spika, bandari zetu zikifanya vizuri, tutakuwa na nafasi kubwa ya kuhakikisha kuwa tunashindana na bandari zinazotuzunguka; Bandari ya Beira Mozambique, Durban, Weisberg pamoja na bandari nyingine zote; Robito ambazo zimekuwa zikinyang’anya soko letu la bandari ya Dar es Salaam na mzigo wa Bandari ya Dar es Salaam umekuwa ukiporomoka hasa kwa nchi ya Zambia, DRC Congo na hata Malawi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia uwezo wa bandari yetu kuhudumia nchi hizo tatu, nina imani ni zaidi ya tani milioni sita, lakini leo hii nilipokuwa naangalia taarifa, ni Shilingi milioni tatu tu ambazo zinahudumiwa na bandari yetu kupitia Dar es Salaam Corridor. Kwa hiyo, ukiangalia nchi kama ya DRC Congo ambayo ni 36% na nchi ya Zambia 31% na Malawi 5% ya mzigo unaopitia bandari yetu ya Dar es Salaam umepungua kwa kiasi kikubwa mno. Ukiangalia sababu ambazo zimetolewa kwenye hizi ripoti tulizonazo ni zile ambazo zipo ndani ya uwezo wa Serikali kujirekebisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, mojawapo ni uwezo wa utendaji wa reli zetu; Reli ya TAZARA na pamoja na Reli ya Kati. Mzigo mwingi ambao nimeusema hapo unapita kwenye barabara zetu. Kwa hiyo, mzigo huu umekuwa unasababisha hata kuharibu barabara zetu na kwa kiasi kikubwa unaufanya usafirishaji kwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam kuwa wa ghali mno ukilinganisha na bandari nyingine. Mfanyabiashara anachoangalia, ni wapi atapata usafirishaji kwa bei nafuu?

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukiongelea hapa bei ya mafuta, bei ya mbolea na bei ya mazao kuwa ni kubwa, lakini hizo bei zinasababishwa vilevile na gharama zilizopo kwenye usafirishaji. Leo hii bei ya mbolea kufika bandarini Dar es Salaam ni kama shilingi 140,000 lakini ikija kufika pembezoni mwa Tanzania itakuwa zaidi ya shilingi 170,000. Kwa hiyo, kukiwa na efficiency kwenye bandari yetu na Serikali ikachukua hatua za makusudi kuhakikisha mizigo yote hii inapita kwenye reli, hakutakuwa na haja hata ya kupunguza mapato ya Serikali. Kwa hiyo, tukiongeza ufanisi na tija tunaweza kuwapunguzia Watanzania wetu mzigo mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ombi langu na ushauri kwa Mheshimiwa Waziri, aangalie, naye ajiulize ni kwanini hawekezi pamoja na matatizo yote ya Mkataba wa TAZARA? Ni kwa nini hatujawekeza kwenye kuboresha Reli ya TAZARA? Kama asilimia 72 ya mzigo wote unaoenda nje ya Tanzania unapitia kwa barabara ambazo kwa mzigo ambao ungechukuliwa na TAZARA sasa huwezi kuwa na sababu yoyote ile ya kuangalia ni kwanini Wizara haitaki kuwekeza kwenye TAZARA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, TAZARA ina historia ndefu, TAZARA haikuanzishwa tu na Mwalimu Nyerere pamoja na Kaunda, ilianza toka enzi; na mawazo yalikuwa ni ya Ma-settler, wakulima, walitaka kurahisisha usafirishaji wa pembejeo na usafirishaji wa mazao. Hata hivyo, ilitusaidia sisi baadaye wazo lilipokuja kwamba tuichukue TAZARA kama sehemu ya kutusaidia katika ukombozi, ndiyo sababu ikaitwa Reli ya Uhuru, lakini sasa hivi hii ni reli ya ukombozi na mapinduzi ya kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Rais ametoa kama Shilingi bilioni 13 mwaka huu 2022 kwa ajili ya maboresho madogo ya TAZARA. Nilivyoiangalia haraka, hii ni asilimia tatu tu ya mahitaji ya TAZARA. Naomba haya marekebisho ya mkataba yafanyike haraka ili tuweze kuwekeza kiasi cha kutosha. Nakuhakikishia kuwa uwezo wa Serikali wa Shilingi bilioni 200 mpaka Shilingi bilioni 400 ambazo zitaibadilisha hii TAZARA ika-transform na hii mizigo yote ambayo inachukuliwa na nchi shindani na bandari shindani ikaweza kuchukuliwa kupitia bandari yetu ya Dar es Salaam, hatutalalamika kuhusu fedha za kigeni, hatutalalamika vilevile kamba kodi kubwa. Kwa hiyo, tutakuwa tumepunguza mzigo mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nalisema hilo ili na wenzetu wanapoangalia waone namna ya kuweka michakato, ni namna gani tuboreshe upatikanaji wa mbolea na kusafirisha mizigo nje. Isiwe kila mmoja anaangalia kwake, Hapana. Hii ichukuliwe kwa pamoja, na nina imani katika hii crisis ya mafuta sasa hivi, tukiweza kuboresha TAZARA tukajenga bandari kavu upande wa reli ya kati na reli ya TAZARA, badala ya mafuta kuzagaa zagaa Dar es Salaam, kubakia kwenye Bandari ya Dar es Salaam kwa muda mrefu na ikaongoeza bei ya mafuta, hayo mafuta yangeenda moja kwa moja kwenye bandari kavu na wateja wa kutoka Congo, Zambia, Malawi na kadhalika wachukulie huko mipakani hayo mafuta badala ya kuyafuata Dar es Salaam ambapo mzigo unakuwa mara mbili. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Oran, ni kengele ya pili.

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba niunge mkono hoja, lakini naomba sana reli ya TAZARA iweze kuboreshwa.
Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mawaziri na viongozi wote wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.
Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha uendelezaji wa miradi ya kimkakati na pia utayari wetu wa ushindani wa kimataifa (national competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miezi kumi ya bajeti inayoishia Juni, 2022 Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imetekeleza miradi mingi ya miundombinu ya barabara, reli, bandari, na uimarishaji wa safari za anga ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa viwanja vya ndege. Utekezaji huu ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020-2025.

Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM na Serikali nzima kwa hatua nzuri za utekelezaji wa mradi wa kihistoria wa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR pamoja na uboreshaji wa bandari utaimarisha kwa kiasi kikubwa uchumi wa nchi yetu. SGR na Bandari ni nguzo imara ya kiushindani katika biashara ya usafirishaji wa ndani na nchi za maziwa makuu na hata za Kusini mwa Afrika na Kati. Bandari za Tanzania ni lango la usafirishaji kwa Zambia, Malawi, DR Congo, Uganda, Burundi, Rwanda, Sudan ya Kusini na hata Zimbabwe na Msumbiji.

Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya kazi kubwa kuhakikisha ujenzi wa SGR unaendelea kwa kasi ile ile na pia napongeza jitihada za kuendelea kutafuta vyanzo vya fedha vya masharti nafuu kugharamia ujenzi huo. Pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa, Serikali imefanya maboresho makubwa ya miundombinu na huduma katika bandari zetu hususan bandari ya Dar es Salaam ili kukabiliana na ushindani mkubwa wa bandari zingine za ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika. Bandari ya Dar es Salaam inakumbana na ushindani mkubwa toka Bandari za Mombasa (Kenya), Beira (Msumbiji), Nacala (Msumbiji), Durban (Afrika Kusini), Lobito (Angola) na Walvis Bay (Namibia). Maboresho ya bandari zetu iendane na kuondoa changamoto zingine ambazo zinasabisha gharama kubwa za usafirishaji kwa bandari zetu na kusababisha kupoteza biashara ya usafirishaji kwa bandari shindani. Ufanisi wa bandari unategemea pia maboresho ya barabara, Reli ya Kati (TRL), Reli ya TAZARA, utendaji wenye tija wa wadau wote wa bandari na hata watumishi ili kupunguza gharama za usafirishaji kwa wateja wa bandari zetu.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa karibu asilimia 72 ya mzigo wote wa nchi za nje unaosafirishwa kwa kupitia Dar es Salaam Corridor ambapo DR Congo ni asilimia 36, Zambia asilimia 31, na Malawi asilimia tano. Pamoja na fursa za kijiografia ya bandari zetu, mzigo unaopita sasa kwenye Bandari ya Dar es Salaam, ni asilimia 50 tu ya biashara yote ambayo kwa sasa inashikiliwa na bandari shindani. Kwa ajili ya kunusuru biashara hii inayopotea na kuchukuliwa na bandari shindani, Serikali ichukue hatua za haraka kuboresha huduma za TAZARA ikiwa ni pamoja ya maboresho ya miundombinu ya reli, ununuzi wa vichwa vya treni, mabehewa, na vitendea kazi vingine.

Mheshimiwa Spika, napendekeza Serikali kwa haraka ishughulikie maboresho ya mkataba wa TAZARA na kisha kutafuta fedha za masharti nafuu angalau kiasi cha shilingi bilioni 200. Katika kipindi hiki cha ushindani mkubwa na hata mfumuko wa bei wa mafuta ya petroli, mbolea na bidhaa mbalimbali, usafirishaji wa reli ni mojawapo ya suluhisho kubwa la kupunguza mzigo wa bei kubwa kwa wateja wa bandari zetu na hata wananchi. Kutokana na TAZARA kuhudumia mzigo wa tani chini ya 200,000 (asilimia sita tu) kati ya tani milioni tatu ni kiasi kidogo sana na kupelekea mzigo kuelemea barabara zetu.

Mheshimiwa Spika, pamoja na maboresha ya reli ya TAZARA napendekeza kuendelea na ujenzi wa bandari kavu ya Mbeya ambayo ina fursa kubwa katika kipindi hiki katika kuwezesha kupunguza gharama za kusafirisha kwa wateja wa bandari na hata kupunguza bei za mafuta ya petroli, pembejeo na mazao ya kilimo. Bandari kavu ya Mbeya ni njia panda kwa wateja wa nchi za Malawi, Zambia, DRC Lubumbashi na hata kwa Zimbabwe na Msumbiji. Serikali ichukue hatua za haraka kuinusuru reli ya TAZARA hata ikibidi kurekebisha mikataba ya umiliki na uongozi ili mradi iendeshwe kwa tija. Serikali ichukue hatua za makusudi kwa kutumia zaidi TAZARA kusafirisha mizigo ambayo imeelemea hata uwezo wa barabara zetu. Usafirishaji wa mizigo kwa kutumia TAZARA ilenge kupunguza gharama za mafuta ya petroli, pembejeo kwa wakulima na wakati huo kupunguza gharama za kusafirisha mazao ya wakulima.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuboresha TAZARA, napendekeza kukamilisha taratibu za ujenzi wa bandari kavu ya Mbeya ambapo Mamlaka ya Bandari kwa kipindi kirefu wamewahakikishia wananchi kulipa fidia ya eneo lao wanalolichukua.

Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto za mfumuko wa bei za mafuta na pembejeo, kuna fursa kubwa na hasa mahitaji makubwa ya mazao ya kilimo kwa soko la ndani na nje. Uzalishaji kwa tija unategemea kwa kiasi kikubwa ubora wa miundombinu ya barabara, reli na hata anga. Serikali iweke msukumo zaidi kwenye kuboresha miundombinu ya barabara kurahisisha usafirishaji wa pembejeo na mazao ya kilimo. Kutokana na fursa za uzalishaji mkubwa kwa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, napendekeza muendelezo wa uboreshaji wa barabara za TANZAM kipande cha Igawa - Tunduma; barabara ya bypass ya Uyole - Songwe; barabara ya Mbalizi – Shigamba – Isongole kutokana na uzalishaji wa mazao ya kilimo; barabara ya Mbalizi – Galula – Makongosi kutokana na uzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo na madini; na pia barabara ya Isyonje – Kikondo – Makete ambayo ni muhimu sana katika kusafirisha mazao ya kilimo ikiwemo maua, parachichi na viazi kwa soko la nje.

Mheshimiwa Spika, uboreshaji wa barabara hizi pamoja na uwanja wa ndege wa Songwe ni muhimu sana kwa usafirishaji wa mazao yetu kwa soko la ndani na nje, na kwa kiasi kikubwa utaongeza mapato ya fedha za kigeni. Maboresho ya uwanja wa ndege wa Songwe uende sambamba na ujenzi wa maghala mahususi wa maua, mbogamboga, parachichi, nyama, viwanda vya kuongeza thamani za mazao na madini, na EPZ/ Industrial Park.

Mheshimiwa Spika, kutokana na ajali za mara kwa mara za Mlima Iwambi Mbalizi na msongamano wa magari yakiwemo malori ya mizigo na mafuta ya petroli, naomba Serikali kuchukua hatua za haraka kujenga barabara ya mchepuo ya Uyole - Songwe kilometa 40 na pia upanuzi wa barabara ya TANZAM kipande cha Uyole mpaka Ifisi/Uwanja wa Ndege wa Songwe.

Mheshimiwa Spika, katika vipindi mbalimbali, viongozi wa Kitaifa waliagiza upanuzi wa kipande hiki cha TANZAM pamoja na ujenzi wa bypass ya Mbalizi – Iwambi kilometa 6.5. Pamoja na kwamba mikakati hiyo ilikuwa ya muda mfupi, mpaka leo hii huo mkakati haujatekelezwa na wananchi wanaendelea kupoteza maisha kwa ajali za mara kwa mara katika eneo hilo. Hatari zaidi ni kwa magari makubwa yanayosafirisha mafuta kupita barabara yenye msongamano mkubwa katikati ya Jiji la Mbeya na Mji wa Mbalizi. Msongamano wa magari makubwa katika barabara ya TANZAM ni sehemu ya changamoto zinazopelekea bandari zetu kupoteza biashara kwa bandari shindani.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mawaziri na viongozi wote wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza Waziri wa Mifugo na Uvuvi kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Serikali katika utekelezaji wa ustawi wa jamii na maendeleo endelevu, na hii ni mojawapo ya nguzo kuu katika utayari wetu wa ushindani wa kimataifa (national competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulingana na Sensa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya mwaka wa kilimo 2019/2020 inaonesha kuwa idadi ya ng’ombe ilikuwa milioni 35.3; kati ya hao, wakulima wadogo walikuwa na ng’ombe milioni 35.1 na mashamba makubwa yalikuwa na ng’ombe 142,968. Aidha, wakulima wadogo walikuwa na mbuzi milioni 25.5 na mashamba makubwa mbuzi 33,847. Kwa upande wa kondoo wakulima wadogo walikuwa na kondoo milioni 8.8 na mashamba makubwa kondoo 24,075.

Vilevile nguruwe waliofugwa na wakulima wadogo walikuwa milioni 3.2 na mashamba makubwa yalikuwa na nguruwe milioni 3.4 na kulikuwa na jumla ya kuku milioni 92.8 ambapo wakulima wadogo walikuwa na kuku milioni 80.1 na mashamba makubwa yalikuwa na kuku milioni 12.7. Pamoja na idadi hiyo kubwa ya mifugo, mchango wa sekta ya mifugo na uvuvi wa asilimia saba bado ipo chini sana na tija ikiboreshwa kuna fursa kubwa ya sekta hii kuchangia sehemu kubwa ya pato la Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Tanzania kuwa nafasi ya tatu kwa nchi za Bara la Afrika na kuchangia katika uchumi wa Taifa, sekta hii ya mifugo na uvuvi inazalishwa kwa tija ndogo. Katika hali hii, sekta ya mifugo haijamsaidia mfugaji na mvuvi kwa kiasi kikubwa kunajinasua kwenye umaskini na kimeendelea kutoa mchango mdogo kwenye pato la Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ichukue hatua zaidi ili kuboresha sekta ya mifugo na uvuvi ikiwemo ujenzi wa mabwawa, kuwezesha mashamba ya kuzalisha lishe/chakula cha mifugo, kuwezesha sekta binafsi kuzalisha mitamba ya kisasa na vifaranga wa samaki. Napendekeza Serikali ianzishe vitalu vya mifugo katika Kata ya Mjele na Mshewe, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, ikiwemo kuchimba mabwawa na visima. Pia napendekeza kuwezesha kuanzisha mashamba makubwa ya kuzalisha lishe ya mifugo ikiwemo ya umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali imalizie kujenga kiwanda cha nyama cha Utengule (Mji Mdogo wa Mbalizi) ambacho kwa muda mrefu ujenzi umesimama pamoja na kuwepo vifaa vyote muhimu vilivyotolewa na wafadhili. Kutokana na kuwepo uwanja wa Kimataifa wa Songwe ambao ni wa kimkakati kusafirisha mazao ya kilimo na mifugo kwa masoko ya nje, napendekeza umaliziaji wa kiwanda hiki cha nyama na pia uwezeshaji wa vitalu vya kunenepesha mifugo katika Kata za Mjele na Mshewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iongeze Maafisa Ugani, waliopo kwenye Halmashauri ya Mbeya ni wachache na wale waliopo hawaonekani kutoa huduma za ugani kwa wananchi. Wizara iweke msukumo wa kuhamasisha, kuanzisha na kutoa elimu kuhusu kilimo cha malisho ili kuwezesha malisho kutosheleza mifugo mwaka mzima. Pia Serikali iongeze kasi ya uzalishaji wa mitamba kutokana na idadi ndogo ya ng’ombe wazazi kwenye mashamba ya Serikali na matumizi madogo ya teknolojia ya uhimilishaji kwa kutumia mbegu bora za mifugo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuwepo na mkakati wa kuongeza mazao ya uvuvi ili kuwezesha samaki wapatikane kwa tija kuwezesha ushindania kwa soko la nje. Vijana wenye nia thabiti na wanaopenda kujishughulisha na ujasiriamali wa ufugaji samaki kwenye mabwawa watambuliwe na uwekwe utaratibu maalum wa uwezeshaji kupitia Halmashauri zao kupata mitaji na utaalam wa kufuga samaki kwenye vizimba na mabwawa na hivyo kuweza kujiajiri wenyewe na kujipatia kipato.

Aidha, Serikali ishughulikie changamoto ya chakula cha samaki na uhaba wa vifaranga hapa nchini. Vijengwe vitotoleshi vingi katika vituo vya ukuzaji viumbe maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mawaziri na viongozi wote wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Serikali katika utekelezaji wa ustawi wa jamii na maendelo endelevu na hii ni mojawapo ya nguzo kuu katika utayari wetu wa ushindani wa kimataifa (national competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali kwa kuanzisha mikopo inayotolewa kwa ajili ya kupanga, kupima na kumiikisha (KKK) ardhi. Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ni mnufaika wa programu hii na imekopeshwa shilingi 1,857,586,634. Mji Mdogo wa Mbalizi kumepimwa viwanja 35,000 kwa gharama ya shilingi 1,273,038,500 na Kijiji cha Mwashoma Kitongoji cha Inolo vimepimwa viwanja 565 kwa gharama ya shilingi 584,548,134 na umefanyika kwa ufanisi mkubwa sana. Kutokana mahitaji makubwa na faida itayopatikana kwenye mauzo ya viwanja hivi, ipangiwe matumizi yanayolenga kuendeleza ardhi ikiwemo kuweka miundombinu kwenye maeneo yanayopimwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mafanikio katika utekelezaji huu wa mwanzo, napendekeza Serikali iweke kipaumbele cha kuendeleza programu katika maeneo mengine hususani yanayolizunguka Jiji la Mbeya kutokana na mahitaji makubwa ya makazi yaliopimwa. Napendekeza Serikali iendeleze programu hii katika vijiji vya Swaya, Lupeta, Nsenga, Ifiga, Nsongwi Mantanji, Nsongwi Juu, Izumbwe, Iwindi, Igoma, Ilembo, Idimi na Haporoto. Upimaji kwenye vijiji unaharakisha kuwa miji (growing towns) utawezesha kupunguza na hata kuondoa kabisa makazi holela na pia kuongeza wigo wa walipa kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na programu ya makazi, Serikali iweke usimamizi wa matumizi bora ya ardhi ya kilimo ambayo inaendelea kupotea kwa matumizi ya makazi. Katika kupangilia matumizi mazuri ya ardhi, ihusishe Wizara za Kilimo, Wizara za Maji na Wizara inayosimamia mazingira. Kwa vile binadamu tunaongezeka ni muhimu kuhakikisha ulinzi kwa kuhifadhi ardhi inayofaa kwa kilimo na pia kutenga ardhi kwa ajili ya wafugaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hatua zinazochukuliwa na Serikali kurejesha mahusiano mazuri kati ya TANAPA (Hifadhi ya Kitulo) na wananchi wa Kata za Ilungu, Igoma, Ulenje na Inyala, bado suluhu haijapatikana. Kuna mgogoro wa miaka mingi wa mpaka kati ya TFS na wananchi wa Kijiji cha Mwashoma. Pia kuna mgogoro wa TANAPA (Hifadhi ya Kitulo) na wananchi wa Kijiji cha Kikondo ambao eneo lao lilichukuliwa na TANAPA bila kulipa fidia. Pamoja na changamoto hiyo ya GN za Hifadhi ya Kitulo, pia kuna utata wa mpaka wa Wilaya ya Mbeya na Wilaya ya Makete na inahitajika Wizara ya Ardhi kupitia upya mipaka na kurekebisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mgogoro huu kuchukua muda mrefu na kusabisha uvunjifu wa amani, kuna ahadi ya mwaka 2015 alitoa Mheshimiwa Hayati Magufuli na kumwelekeza Waziri wa Ardhi wa wakati huo kupitia upya mipaka, ili wananchi wa Kijiji cha Kikondo waachiwe eneo leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan - Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango - Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa - Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mawaziri na viongozi wote wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Serikali katika utekelezaji wa sera ya maendeleo ya jamii ikienda sambamba na ustawi wa jamii na maendeleo endelevu, na hii ni mojawapo ya nguzo kuu katika utayari wetu wa ushindani wa kimataifa (national competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 ambayo ni kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Spika, Shule ya Maadilisho ilianzishwa mwaka 1972 baada ya Serikali kubadili matumizi ya miundombinu iliyokuwepo kutoka Kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na kuwa shule ya kulelea/kuadili vijana watukutu wanaolazimika kutengwa na jamii kufuatia vijana husika kufanya makosa mbalimbali katika jamii. Kwa sasa shule bado ina vijana wachache chini ya 30 ambao wanalelewa/kuangaliwa/kuadiliwa wakiwa chini ya uangalizi wa wafanyakazi 16. Majengo mbalimbali pamoja na yale ya shule ya msingi yaliyopo hapo hayatumiki kikamilifu. Kwa upande wa shule ya msingi, idadi ya wanafunzi ni 102 ukilinganisha na uwezo wa shule hiyo wa zaidi ya wananafunzi 350. Pamoja na miundombinu mbalimbali zipo ekari zaidi ya 448 ambazo zinaweza kutumika kwa ajili ya shughuli za mafunzo ya kilimo na pia kukipatia chuo mahitaji yake ya msingi ya chakula na shughuli nyingine za maendeleo. Kutokana na mabadiliko ya kijamii kuna umuhimu mkubwa wa kuboresha matumizi ya hii shule kuwa Chuo cha Maendeleo ya Jamii na ufundi na pia eneo la Kituo cha Afya.
Mheshimiwa Spika, naomba Serikali kuboresha matumizi ya Shule ya Maadilisho iliyopo Irambo, Kata ya Ulenje, Wilaya ya Mbeya kuwa eneo maalum ili kuanzisha mafunzo ya maendeleo ya jamii, ufundi na hivyo kuiwezesha nchi kutumia nguvu kazi na rasilimali ya vijana kikamilifu na kwa ajili ya maendeleo ya jamii na uchumi wa nchi yetu kwa ujumla. Pamoja na kuwepo kwa shule hii ya sasa, eneo hili liwe kwa ajili ya Shule na Chuo cha Ufundi na Maendeleo ya Jamii pamoja na jamii yote ya Kata ya Ulenje na Tanzania yote.

Mheshimiwa Spika, ombi hili limejikita katika ukweli kwamba kwa kutoa elimu ya maendeleo ya jamii na ufundi kwa vijana, Tanzania itakuwa inaongeza ajira na pia ueledi kwa vijana katika kujenga nchi hasa kutokana na ukweli kwamba nguvu kazi kubwa iko katika vijana.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mawaziri na viongozi wote wa Wizara ya Nishati, kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Spika, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Waziri wa Nishati kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Serikali katika utekelezaji wa ustawi wa jamii na maendelo endelevu, na hii ni mojawapo ya nguzo kuu katika utayari wetu wa ushindani wa kimataifa (national competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/26 ambayo ni kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kupitia Wizara ya Nishati kwa kuendelea kutekeleza kwa ufanisi mkubwa miradi ya umeme ikiwemo miradi ya kusambaza umeme vijijini (REA) na ujenzi mkubwa wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) litakalozalisha umeme wa megawati 2,115. Miradi hii ya kusambaza umeme vijijini imeiweka Tanzania katika nafasi ya juu Afrika na imeweza kuchochea kasi ya ukuaji wa viwanda na uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto za vita ya Ukraine na Urusi na kupelekea kupanda kwa bei ya mafuta ya petroli, napongeza Serikali kushirikisha Wizara ya Nishati, Wizara ya Fedha, EWURA na wadau wengine kuweka mkakati wa kuanzisha Mfuko wa Kudhibiti Mabadiliko ya Bei za Mafuta (Fuel Price Stabilization Fund) ili kukabiliana na kupanda kwa bei za mafuta. Pia Serikali inachukua hatua stahiki za kuanzisha Hifadhi ya Taifa ya Kimkakati ya Mafuta (Strategic Petroleum Reserve-SPR) ili kukabiliana na dharura na kuimarisha usalama na uhakika wa mafuta kwa Taifa. Mkakati huu uende sambamba na uanzishaji wa bandari kavu Mbeya na ujenzi wa matenki makubwa kuhifadhi mafuta kwa nchi jirani za Zambia, DR Congo, Malawi na pia kwa matumizi ya Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na REA kuendelea kutekeleza miradi ya kupeleka umeme kwenye makao makuu katika vijiji vyote vya Jimbo la Mbeya Vijijini bado kuna uhitaji mkubwa wa umeme kufika kwenye vitongoji vyote. Napendekeza kuendelea kwa kasi utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mradi wa REA III (REA III, Round II) na kufikisha umeme katika vijiji vyote vilivyobakia na pia kuendelea na utekelezaji wa Mradi wa Ujazilizi (Densification). Napendekeza utekelezaji utoe kipaumbele kwa kata za Itawa na Shizuvi ambavyo hakuna kijiji kilichowashiwa umeme, na pia kwenye vitongoji vinavyolizunguka Jiji la Mbeya ikiwemo Mina na Lusungo Kata ya Iwindi, Kijiji cha Shongo, Kijiji cha Wambishe kwenye shule zote ikiwemo Shule ya Sekondari Iwiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vijiji vilivyopatiwa umeme kwa kiasi kikubwa imechochea ukuaji wa viwanda hasusani viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo. Nashauri TANESCO iongeze speed ya kuunganisha umeme na pia kushughulikia maombi ya wateja wengi wanaosubiri umeme ikichukuliwa hii ni fursa pia kwa TANESCO kuongeza mapato ya shirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na vyanzo vya sasa, napendekeza Serikali itekeleze miradi ya vyanzo vingine kama vile vyanzo vya Jotoardhi, Umeme wa Jua, Upepo na Makaa ya Mawe ili nchi yetu iendane na mahitaji makubwa ya umeme kwa hapa Tanzania na hata nchi zingine za Afrika. Ni muda mrefu sasa, TANESCO kupitia Kampuni tanzu ya Uendelezaji wa Jotoardhi nchini (TGDC) inaanze uzalishaji katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo eneo la Ziwa Ngozi, Kata za Ijombe na Bonde la Songwe Mkoani Mbeya ambapo ndipo yalipo makutano ya Bonde la Ufa la upande wa Mashariki na lile la Magharibi.

Napendekeza Serikali iharakishe utekelezaji wa miradi hii ya Jotoardhi na ule wa Makaa ya Mawe wa Mchuchuma na Kiwira ili tuweza kuzalisha umeme zaidi kwa mahitaji ya ndani na nchi za nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mawaziri na viongozi wote wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, kwa hotuba nzuri iliojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Serikali katika utekelezaji wa ustawi wa jamii na maendeleo endelevu na hii ni mojawapo ya nguzo kuu katika utayari wetu wa ushindani wa kimataifa (nation competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Spika, Serikali inastahili pongezi kwa kuwezesha timu ya Taifa ya Wanawake ya umri chini ya miaka 17 kufuzu kushiriki fainali za Kombe la Dunia. Pia naipongeza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mkakati katika kuimarisha, kuziwezesha na kufanikisha ushiriki wa Timu za Taifa na vilabu katika michezo na michuano mbalimbali ya kimataifa na kikanda. Kama sehemu ya mkakati huo Wizara iweke msukumo zaidi wa kuhamasisha kujenga, kukarabati na kuboresha miundombinu ya viwanja vya michezo hususani vya mpira wa miguu. Viwanja vingi vya mikoani vipo katika hali mbaya na kwa kiasi kikubwa ni sehemu ya changamoto katika maendeleo ya michezo nchini. Michezo na sanaa ni muhimu sana katika kujenga sura na sifa ya Taifa letu (nation brand). Hivyo ni muhimu kwa Serikali kuhakikisha inaweka umuhimu mkubwa wa ushiriki wa timu zetu za Taifa na kuwepo kwa mkakati wa kitaifa wa kuhakikisha timu zetu za Taifa na vilabu zinafanya vizuri kwenye mashindano ya kikanda na kimataifa.

Mheshimiwa Spika, mkakati huu katika michezo na sanaa ni nguzo muhimu katika kutekeleza Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026. Serikali itenge bajeti ya kutosha kuhakisha tija katika ushiriki wetu katika mashindano ya kimataifa.

Mheshimiwa Spika, sambamba na kuboresha miundombinu ya viwanja, Wizara ijikite katika kuibua vipaji mbalimbali vya michezo na sanaa kwa kuimarisha ushirikiano na Wizara nyingine hususani Elimu na TAMISEMI. Pamoja na kutokuwepo kwa miundombinu rafiki, mikoa mingi imekuwa inatoa wachezaji wenye vipaji vikubwa katika mpira wa miguu, riadha na hata sanaa mbalimbali. Imefika muda sasa wa kuwepo kwa mkakati wa kuibua na kuendeleza vipaji hivyo ambavyo vimekuwa vinaonekana kikanda zaidi kama vile riadha kwa Mikoa ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kusini na Mikoa ya Kati. Pia kwa upande wa mpira wa miguu kumekuwepo na mikoa kadhaa ya vipaji vikubwa na huko ndio Serikali iweke msukumo zaidi wa kuibua na kuendeleza hivyo vipaji. Hata kwa wasanii, kuna mikoa imekuwa inatoa idadi kubwa ya vipaji kwenye uigizaji, uimbaji ikiwemo nyimbo za injili ambazo zinapata umaarufu sana duniani. Kutokana na vipaji vingi vya michezo hususani mpira wa miguu na riadha, napendekeza Shule ya Sekondari Santilya ya Wilaya ya Mbeya iongezwe kwenye orodha ya shule teule za michezo.

Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa Kiswahili kuwa lugha rasmi kimataifa, napendekeza uwekezaji zaidi katika kuitangaza na pia kuwezesha ulimwengu kujua kuwa mizizi na ustawi wa Kiswahili ni Tanzania pekee na wengine wanaigiza kwetu. Serikali iendelee kuchukua hatua zaidi ya kukistawisha Kiswahili katika mataifa mengine Barani Afrika na kwingineko kwa kushirikisha vyuo vikuu hapa nchini na vyuo vikuu mbalimbali duniani.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan - Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango - Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa - Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mawaziri na viongozi wote wa Wizara ya Fedha na Mipango, kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Waziri wa Fedha na Mipango, kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha ubunifu wa ukusanyaji mapato na usimamizi mzuri wa matumizi ya Serikali ikiwa ni pamoja na uendelezaji wa miradi ya kimkakati na pia utayari wetu wa ushindani wa kimataifa (national competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miezi kumi ya bajeti ya mwaka huu, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imesimamia kwa ufanisi ukusanyaji mapato na utekelezaji wa miradi mingi ya miundombinu ya barabara, reli, bandari na kadhalika. Napongeza Serikali kwa mwendelezo mzuri wa utekelezaji wa mradi wa kihistoria wa umeme Mto Rufiji. Mradi wa kihistoria wa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR pamoja na uboreshaji wa bandari utaimarisha kwa kiasi kikubwa uchumi wa nchi yetu. Umeme, reli na bandari ni nguzo imara ya kiushindani katika uchumi wa Tanzania na nchi za Maziwa Makuu na hata za Kusini mwa Afrika na Kati.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki wakati dunia inapambana na janga la corona virus (covid-19), tumejifunza umuhimu wa kuwepo kwa mikakati mbadala kutokana na nchi nyingi tunazoshirikiana kibiashara na kiuchumi kukumbwa na mtikisiko wa kiuchumi. Biashara ya usafirishaji hasa wa anga imeathirika sana na napongeza mkakati wa shirika la ndege kuanza kutumia ndege zake kusafirisha mizigo. Mkakati huu ambao umetumiwa na hata mashirika makubwa ya ndege utawezesha usafirishaji wa mazao yetu ya kilimo kufikia masoko kirahisi na hapo hapo uhakika wa mapato kwa shirika la ndege hasa kipindi hiki kukiwa na upungufu wa abiria. Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Msajili wa Hazina anapaswa kuendelea kuimarisha mitaji kwa mashirika ambayo yatachochea ukuaji wa uchumi ikiwemo Benki za TADB, TIB na ATCL ili iweze kusimama kibiashara ikiwa ni nguzo muhimu hata kwa sekta zingine.

Mheshimiwa Spika, napendekeza kuhakikisha ujenzi wa SGR unaendelea hata kwa kutafuta vyanzo mbadala vya fedha kugharamia ujenzi huo, kwa vile kutakuwa na fursa kubwa za usafirishaji. Pamoja na ujenzi wa SGR, napendekeza kuendelea na kuboresha reli ya TAZARA na uboreshaji wa bandari zetu ikiwemo ujenzi wa bandari kavu ikiwemo ya Inyala, Mbeya ambayo ina fursa kubwa katika kipindi hiki ili kupunguza gharama za kusafirisha pembejeo na mazao. Serikali ichukue hatua za haraka kuinusuru reli ya TAZARA hata ikibidi kurekebisha mikataba ya umiliki na uongozi ili mradi iendeshwe kwa tija.

Mheshimiwa Spika, kuna kuchukua hatua za makusudi kwa kutumia zaidi TAZARA kusafirisha mizigo ambayo imeelemea hata uwezo wa barabara zetu. Usafirishaji wa mizigo kwa kutumia TAZARA ilenge kupunguza gharama za pembejeo kwa wakulima na wakati huo kupunguza gharama za kusafirisha mazao ya wakulima.

Napendekeza Serikali iwekeze angalau shilingi bilioni 100 kwa mwaka kwa kipindi cha miaka mitatu kwa ajili ya kuboresha mindombinu ya reli na karakana. Uwekezaji huu utawezesha TAZARA kujiendesha kwa faida na kuipunguzia Serikali mzigo wa kulipa zaidi ya shilingi bilioni 15 kwa mwaka ikiwa ni mishahara ya wafanyakazi wa TAZARA. Uwekezaji huu unahitaji haraka wakati Serikali za Tanzania na Zambia zinaendelea na jitihada za kurekebisha mikataba ikiwemo wa uendeshaji wa TAZARA. Pamoja na kuboresha TAZARA, napendekeza kukamilisha taratibu za ujenzi wa bandari kavu ya Inyala, Mbeya ambapo Mamlaka ya Bandari kwa kipindi kirefu wamewahakishia wananchi kulipa fidia ya eneo lao wanalolichukua.

Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto za mapato kutokana na janga la Covid-19, kuna fursa nyingi za muda mfupi za kuongeza mapato kupitia hatua za kiutawala kiwemo ya kuondokana na matumizi na malipo ambayo hayana tija kwa Serikali na hata walipakodi. Kutokana na mahitaji makubwa ya uwekezaji kwenye miradi ya kimkakati, uchumi wetu utaendelea kuwa na mahitaji makubwa ya mikopo ya pesa za kigeni na wakati huo huo kulipa mikopo iliyoiva.

Pia Serikali iweke mkakati wa kuhakikisha mapato ya fedha za kigeni yanaongezeka kupitia mazao ya kilimo, madini na utalii. Kuongezeka kwa mapato ya fedha za kigeni yatasaidia kuimarisha Deni la Taifa kuwa himilivu na pia kuendeleza utulivu wa shilingi yetu dhidi ya sarafu kuu za kigeni na hata kuhakikisha utulivu wa mfumuko wa bei. Serikali ihakikishe kipaumbele cha kuwekeza kwenye kilimo ikiwemo pembejeo na umwagiliaji kwa lengo la kuongeza tija na pia kuongeza mapato ya fedha za kigeni na kulinda mfumuko wa bei.

Mheshimiwa Spika, kutokana na upotevu mkubwa wa fedha za Serikali ikiwemo miradi ya Serikali Kuu na Halmashauri, napendekeza Serikali kuimarisha Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani ili kuongeza ufanisi na uhuru wa Wakaguzi wa Ndani. Serikali ihakikishe Mkaguzi wa Ndani wakati wote anakuwa huru kutoka kwa Afisa Masuuli. Wakaguzi wa Ndani wa Halmashauri wasimamiwe na Mkaguzi Mkuu wa Mkoa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Serikali iimarishe uhuru wa Mkaguzi Mkuu wa Ndani (Internal Auditor General) na hata kupandisha hadhi ya Ofisi kuwa na Fungu la Bajeti linalojitegemea.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana nami kupata fursa hii ya kuchangia na kutoa maoni yangu kwenye bajeti hii ya Serikali. Nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Tanzania na Serikali nzima kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ilani yetu imetekelezwa vizuri mno na kwa asilimia nzuri mno, na nina imani katika kipindi hiki kinachoishia mpaka Juni kwa kweli tutakuwa tumefanya yale ambayo hayakutegemewa kutokana na changamoto za kidunia zilizokuwepo. Wengi hatukutegemea kuwa bajeti hii itatekelezwa kwa kiwango hiki hasa kutokana na vita ambayo imetukumba dunia sasa hivi, pia na ugonjwa wa UVIKO. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana vilevile kwa Serikali na Mheshimiwa Rais kwa kuja na hii bajeti. Hii bajeti ni ya kimapinduzi, hii bajeti tunaweza kusema ni ya kimapinduzi au kwa lugha nyingine wanasema transformation budget, imetuonesha mwelekeo mzuri mno na ukiangalia dhima ya mpango wetu ni kujenga uchumi shindani na viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ina maana kubwa mno kwa vile uchumi shindani hatushindanishi mazao yetu au mashirika yetu hapa, lakini tunashindana globally, tunashindana dunia nzima. Kwa hiyo, uchumi wetu tunapouangalia kibajeti, tuangalie sisi je, ni sehemu gani ya dunia ambayo tumeimega na nchi yetu inahakikisha kuwa inakuwa na ushindani ambao ni mzuri? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hii bajeti, kwa kweli kwa kiasi kikubwa imekidhi. Ukuaji wa GDP imeonesha kuwa katika kipindi cha COVID nchi yetu ilifanya vizuri, lakini hata hiki kipindi tunachokwenda, ukuaji wa asilimia 5.3 ni wajuu kuliko nchi zote za Kusini mwa Jangwa la Afrika. Hiyo rekodi ni kubwa sana ukilinganisha na wastani wa 4% tu ambapo nchi nyingine zote ni 4%, sisi tuna asilimia 5.3. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia vile vile, tunaendelea kuhakikisha uchumi wetu unaendelea kuwa imara. Mfumuko wa bei ambao ni kati ya 3% mpaka 5% na sasa hivi ni chini ya 4%, hiyo ni rekodi nzuri sana. Kwa sababu katika hiki kipindi ambacho mfumuko wa bei duniani ni mkubwa, hata nchi zilizoendelea zimeshindwa kuhimili kuweza ku-contain hiyo inflation yao, lakini unashangaa Serikali yetu chini ya Mheshimiwa Rais, ni maajabu gani wanayoyafanya? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia utulivu wa Shilingi, nilikuwa najaribu kuangalia kwa mazoea tulizoea kuona exchange rate ya dola ilikuwa inalingana na bei ya petrol kwenye kituo cha mafuta, lakini leo hii mafuta ni zaidi ya 3,000, lakini exchange rate ni Shilingi 2,300/=. Ina maana Benki Kuu na Serikali kwa jumla wanafanya vizuri mno. Kwa hiyo, hata ile imported inflation nayo bado haijatuathiri kwa kiasi kikubwa. Kwa hiyo, nakushukuru sana Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, Mheshimiwa Waziri umefanya kazi nzuri sana na timu yako, na nimefurahi zaidi nilipoona bajeti yako imeweka kipaumbele cha kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo kinaajiri asilimia 65 ya Watanzania, lakini kilimo kinachangia asilimia 25 tu ya uchumi. Kwa kweli huo uwiano siyo mzuri, haiwezekani Watanzania zaidi ya asilimia 65 wachangie tu asilimia 25 ya uchumi. Hiyo siyo dalili nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napendekeza Serikali iangalie, pamoja na bajeti ya kilimo kuongezeka kutoka Shilingi bilioni 294 mpaka karibu Shilingi bilioni 954, ongezeko hilo ni kubwa mno; ni mara tatu. Kwa hiyo, tunategemea mchango wa kilimo uende mara tatu; na ukienda mara tatu nchi hii itakuwa imefika mahali pazuri mno. Mchango wa kilimo ulikuwa mdogo kwa sababu ya ufanisi, lakini tunashukuru kwa mpango aliokuja nao Waziri wa Kilimo, unatuonyesha kuwa unaweza kututoa hapa tulipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hili kwa sababu, bila kuhakikisha kuwa kilimo kinatutoa hapa tulipo, nchi yetu itakuwa ni maajabu tukipata hayo maendeleo tunayoyafikiria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za kigeni tunazitegemea kutokana na mazao ya kilimo, madini na utalii, lakini zaidi zaidi tunategemea kwenye kilimo. Kwa hiyo, tunaomba nguvu kubwa iende kwenye kilimo. Tunashukuru kwa ruzuku ya mbolea, lakini hii ruzuku ya mbolea iliyooneshwa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa 80, kile kiasi alichokitaja mwanzoni na hata alichokitaja Waziri wa Kilimo hakijaonekana. Amezungumzia tu ya kwamba katika kilimo kutakuwa na ruzuku ya pembejeo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunakuomba ruzuku ya pembejeo ya mbolea ilenge kupunguza bei ya mbolea zote wanazotumia wakulima kwa mazao ya biashara na vilevile mazao ya chakula. Hiyo itatupeleka mahali pazuri zaidi, kwa sababu sasa hivi commodity prices zinakwenda vizuri sana. na kwasababu commodity prices zinakwenda vizuri, tukizalisha tunahitaji masoko, na masoko yanahitajika ya kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba commodity exchange market iimarishwe. Hii itasaidia uhakikika wa masoko ya mazao yetu, lakini unapoimarisha hii, uimarishe pia warehouse receipt finance. Ni muhimu kwa vile zinaenda pamoja. Pamoja na hiyo, tunaomba usajili wa ma-warehouse yote na sheria ibadilike ili kulinda hizi warehouses na hii biashara yote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba sana, kuna huu mfumo mpya wa ujenzi wa barabara wa EPC and finance. Huu mfumo inabidi uwe coordinated vizuri kwa sababu inawezekana Wizara ya Ujenzi ikaenda na huu mfumo ikategemea labda ni free lunch, yaani ni kitu ambacho tutapewa bure, Hapana. Huu ni mkopo. Kwa hiyo, tuangalie hii mikopo tutailipa namna gani? Kwa hiyo, zile securities, zile mortgages ambazo tutazifanya, tuwe waangalifu kwa kuangalia nchi za wenzetu walifanya nini mpaka wakaangukia kubaya kwa ajili ya hii mikopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imetajwa barabara ya Tanzam kipande cha Igawa - Mbeya mpaka Tunduma. Hiki kipande ni muhimu sana kwa ajili ya biashara ya bandari. Naomba sana, inawezekana huu mfumo haujawa tayari, lakini katika hii barabara kuna kipande cha Uyole - Songwe bypass wananchi hawajalipwa fidia mpaka leo. Hebu walipeni fidia wale wananchi tunaposubiri hii mipango. Naomba ujenzi wa hii barabara upewe kipaumbele, na barabara zote za Isionje - Kikondo - Makete nayo ipewe kipaumbele kwani ilishaanza, na ni muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Mbalizi - Makongorosi ipewe kipaumbele; na barabara ya Mbalizi - Shigamba ipewe kipaumbele. Vilevile kumalizia ujenzi wa uwanja wa ndege wa Songwe uliopo Mbeya upewe kipaumbele. Hii itaenda pamoja kuhakikisha kuwa mazao yetu yanafika kwenye masoko ya kidunia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Nashukuru sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na mimi kwa kupata fiursa hii ya kuchangia Mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa mafanikio makubwa ambayo tumeyapata sisi Tanzania. Ukiangalia huu Mpango ni sehemu ya Mpango wetu wa Taifa wa miaka mitano. Vile vile, huu ni Mpango wa nne. Dhima ya Mpango wetu ilikuwa ni kujenga uchumi shindani, viwanda na maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, nimeuangalia huu Mpango wetu, kwa kweli nawashukuru sana hawa Waheshimiwa Mawazii wawili na hizi Wizara mbili pamoja na Tume ya Mipango; wamefanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipouangalia huu Mpango, ukiuangalia umesheheni taarifa nyingi ambazo zinaonesha ni kiasi gani Tanzania tuko vizuri kiushindani Afrika lakini hata nje ya mipaka yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye utulivu wa shilingi yetu kwa kweli tuko vizuri sana. Nilikuwa nalinganisha utulivu wa shilingi kuanzia mwaka 2015 mpaka mwaka 2023. Nimekuja kupata taarifa kwamba shilingi ya kwetu ukilinganisha na Naira ya Nigeria, shilingi ya kwetu imepanda thamani kwa zaidi ya asilimia 350. Ukiilinganisha na Kenya, shilingi ya kwetu imepanda thamani kwa zaidi ya asilimia 122. Vile vile, yote hayo ukiangalia na Afrika Kusini, shilingi ya kwetu bado imepanda thamani. Hii maana yake ni kwamba utulivu wa uchumi wetu ni kutokana na hawa wenzetu na Mheshimiwa Rais ambao kwa kweli kazi yao ilikuwa ni nzuri mno. Kwa hiyo, utulivu tunaouona na hizi taarifa tunazoziona zinadhirisha kwamba, pamoja na changamoto tulizonazo duniani Tanzania tuko vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuendelee kuwa vizuri ni nini cha kuangalia? Mimi kwenye mpango huu nilijikita kwenye vihatarishi. Tusipojipanga ku-manage hivi vihatarishi (risk management), haya mafanikio yote tunayoyaona na hii mipango yetu hatuwezi kwenda. Katika Mpango wameweka vihatarishi ambavyo nilipoangalia kwenye Ripoti ya Kamati ya Bajeti, wameweza kuvijumuisha katika sehemu tatu. Kwanza ni strategic risk au risk za kimkakati, ya pili ni operational risk au risk za kiutekelezaji. Sasa nilipoangalia hizi mbili zote na ukiangalia mpango, huwezi kuona kiasi gani tutaweza kuzi-manage hizi risk; kwa sababu dunia ya leo imebadilika sana. Management ya leo ni tofauti na huko tulikotoka. Management ya leo ukiangalia majadiliano ya wiki iliyopita kwa zile Kamati tatu, ukiangalia matatizo makubwa inawezekana hatukuweza ku-manage hizo risk zetu ambazo zilikuwepo. Kwa hiyo, katika mipango hii kama hatutajipanga vizuri, inawezekana haya mafanikio yote tuliyoyapata tusiweze kwenda nayo vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu; kwa sababu kwenye vihatarishi vya kimkakati (strategic risk) hapa ndiyo unaangalia sasa kwenye ile dhima ya ushindani Tanzania tutashindana vipi na wenzetu? Kwa sababu kwenye uchumi wa leo wa dunia, hizi nchi zimebaki kama vijiji, kwa hiyo Tanzania hatuwezi kuwa kama kisiwa. Kwa hiyo, sasa ni namna gani tunapopanga mipango yetu, kama huu mpango kwa hatua alizochukua Mheshimiwa Rais za kuhakikisha kuwa tunaboresha ufanyaji kazi wa Bandari zetu ambalo ni jambo jema sana, ambalo linaweza kuwa sehemu ya kutukomboa sisi kwenye changamoto zote hizi tulizonazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimeizungumzia hiyo, naangalia ya kwamba, je, tumeboresha pale, mizigo itafika vipi kwa wateja wetu hasa wa nchi za nje? Hapo inabidi mkakati uwe ni kuhakikisha kuwa reli yetu ya SGR kipande cha Dar es salaam mpaka Makutupola, kikamilishwe haraka na kianze kufanya kazi. Hiyo itawezesha kupunguza msongamano hasa wa mizigo na hasa hata msongamano wa magari. Kwa hiyo, presha tuliyonayo ya magari sasa hivi itapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine. Ili tuhakikishe kuwa sehemu yetu ya biashara ya bandari inafanya vizuri ukilinganisha na wezetu, inabidi Serikali ichukue hatua ngumu ya kuiboresha TAZARA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kandege, amezungumza asubuhi, nimemsikiliza kwa makini sana. Mizigo yetu ya nje inapitia ukanda au mkondo huu wa Reli ya TAZARA au Barabara ya TANZAM. Kwa hiyo, tusipoiboresha TAZARA inawezekana ushindani wetu usiwe mzuri kwa sababu wenzetu tayari wamekwishaanzisha Lobito Corridor ambayo ni kwa ajili ya kushindana na bandari ya Dar es salaam. Vile vile, kuna Naccala Corridor.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ingawaje watu wanachukua kwa wepesi lakini mkakati uliopo ni kuua biashara yetu. Sasa, ningeiomba Serikali ifanye mkakati wa kuichukulia hii kama kihatarishi cha biashara yetu na kupoteza biashara za nje. hivyo iboreshe TAZARA. Pia, mimi ningependelea zaidi siyo kuboresha tu, hizi reli zetu mbili ziendeshwe na watu binafsi. Na uzuri wake katika mpango, Mawaziri wameonesha ni namna gani washirikishe sekta binafsi katika biashara za reli, bandari, na viwanja vya ndege; na huo ndiyo uwe mwendelezo. Kwa sababu Serikali isijiingize kufanya biashara sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na tatizo la Sheria ya TAZARA. Kwa hiyo Serikali ichukue hatua katika kuhakikisha kuwa lile tatizo linatatuliwa mara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo limeoneshwa kwenye Mpango (Vipaumbele) ni madini. Resources hizi tulizonazo hazitakuwa na maana tukichelewa kuzitumia. Uzuri wake Serikali imeonesha kwa kiasi kikubwa kuwa itaweka nguvu kubwa kwenye madini hasa haya madini ya kimkakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mgano mdogo sana. Kwa Mbeya, Songwe tuna madini hayo ya kimkakati ambayo Serikali imechelewa mno kuamua ni namna gani tuyapeleke sokoni na ni namna gani tuingie sokoni. Kwa Mbeya tuna madini yanaitwa Niobium. Nimeongea mara nyingi sana inawezekana hata jina lilibadilika nikaitwa bwana Mheshimiwa M-niobium.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo madini ingechukuliwa 2016 mzigo wa vyuma kwa ajili ya Reli yetu ya SGR ambao tunalalamika sasa hivi na majengo yetu, isingekuwepo. Kwa sababu wale wawekezaji wako tayari kujenga kiwanda cha kwanza Afrika na cha nne duniani ambacho kitaleta ajira nyingi lakini na FDI nyingi ambazo ndiyo Serikali yetu inahitaji leo kutokana na changamoto za forex. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiendelea kuchelewa tunajichelewesha wenyewe. Hayo Madini yatagunduliwa sehemu zingine na hao watu wanatafuta sehemu zingine ambazo wanaweza kufanya biashara zao vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la barabara na reli ni muhimu sana na twende kwenye barabara ambazo zina-impact kubwa kwenye uchumi. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa ujenzi wa kuboresha barabara ya TANZAM na barabara ya Dar es Salaam – Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya TANZAM inahitajika siyo leo ilikuwa inahitajika juzi. Kwa hiyo naiomba Serikali ifanye haraka kukamilisha hiyo mipango iliyopo ili faida yetu ya hawa watu ambao wanaendesha Bandari iweze kuleta matunda ikiwemo vilevile na ujenzi wa Bandari Kavu ambazo zitaleta pressure zitaongeza ushindani kwa hawa wenzetu ambao wanataka kupoka soko letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mawaziri na viongozi wote wa Wizara ya Kilimo, kwa uongozi wao na utendaji uliotukuka.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika na uongozi wote wa Bunge kwa uongozi wenu mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Waziri wa Kilimo kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Serikali katika utekelezaji wa ustawi wa jamii na maendelo endelevu. Hii ni mojawapo ya nguzo kuu katika utayari wetu wa Ushindani wa Kimataifa (National Competitiveness). Bajeti hii inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni “Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.”

Mheshimiwa Spika, kulingana na taarifa ya Wizara ya Kilimo, Tanzania ina hekta milioni 44 zinazofaa kwa kilimo cha mazao, kwa wastani hekta milioni 10.8 tu sawa na 24% ndizo zinazolimwa kila mwaka. Sekta hii kwa mwaka 2022 imechangia asilimia 26.1 kwenye pato la Taifa, imetoa ajira kwa wananchi kwa wastani wa 65% na imechangia 65% ya upatikanaji wa malighafi za viwanda. Sekta ya Kilimo ni mhimili wa uchumi wa nchi na inachangia pato la mkulima mmoja mmoja, kaya na Taifa kwa ujumla. Sekta ya Kilimo na hususani sekta ndogo ya mazao imechangia 15% katika pato la Taifa na zaidi ya 100% ya upatikanaji wa chakula kinachozalishwa nchini na kupelekea utulivu wa mfumuko wa bei kwa takriban 59%.

Mheshimiwa Spika, kutokana na ongezeko kubwa la mauzo ya mazao nje ya nchi kufikia dola za Marekani bilioni 2.3, nashauri Serikali ichukue hatua za kuhamasisha taasisi za fedha kuongeza utoaji mikopo kwenye Sekta ya Kilimo ili kuoanisha na mchango wa kilimo kwenye pato la Taifa, nashauri Serikali kuboresha mifumo ya TEHAMA ili isomane kati ya Taasisi za Kilimo, Wizara ya Kilimo, Benki Kuu, Wizara ya Fedha, TRA na hata Bandarini. Kwa kuboresha mfumo mzuri wa TEHAMA unaosomana, Serikali itaweza kupata taarifa sahihi za uzalishaji, mauzo nje ya nchi, mapato ya fedha za kigeni na hata kuongeza mapato ya kodi. Kwa sasa mchango wa kilimo wa chini ya asilimia moja kwenye makusanyo ya kodi, ni mdogo sana kulingana na kilimo kuajiri zaidi ya 65% ya Watanzania. Pamoja na kushamiri kwa biashara ya mazao nje ya nchi, bado mapato ya fedha za kigeni kutokana na biashara hizo, hayajawa bayana kupunguza urari wa biashara.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kujitosheleza kwa chakula na kuchangia katika uchumi wa Taifa, takribani mazao yote yanazalishwa kwa tija ndogo katika eneo husika. Uzalishaji wa mahindi wa chini ya tani mbili kwa hekta moja ni asilimia 29 tu ya uzalishaji unaotegemewa wa tani sita kwa hekta moja. Uzalishaji huu wa chini kwa mazao yote kwa kiasi kikubwa unatokana na ukosefu wa ushauri wa watalaam wa kilimo ikiwemo matumizi yasiyo sahihi ya mbolea na pembejeo zingine. Katika hali hii, kilimo hakijamsaidia mkulima kwa kiasi kikubwa kujinasua kwenye umaskini na kimeendelea kutoa mchango mdogo kwenye pato la Taifa.

Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa mbolea nchini hadi Aprili, 2024 ulikuwa tani 1,052,218.4 ambayo ilikuwa juu ikilinganishwa na tani 819,442 mwaka 2022/2023. Pamoja na bei za mbolea kwenye soko la dunia kuanza kupungua, bado zilikuwa ni za juu na tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kutoa ruzuku. Hatua hii muhimu ni mafanikio makubwa katika safari ya kuleta tija kwenye kilimo nchini na napendekeza kuendelea na ruzuku ya pembejeo pamoja na kuanzisha Price Stabilization Fund kwa pembejeo hasa mbolea ili kuongeza tija kwenye uzalishaji wa mazao ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, nashauri Serikali iendelee kuimarisha usalama wa chakula nchini kwa kununua na kuhifadhi nafaka kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula. Kutokana na ukame maeneo mengi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na pia kuendelea kwa vita ya Urusi na Ukraine kunaashiria kuendelea kuwa na upungufu mkubwa wa nafaka katika maeneo yanayotuzunguka. Kwa kuzingatia gharama kubwa za uzalishaji, Serikali ichukue hatua za makusudi kusaidia wakulima wapate bei nzuri ya NFRA badala ya kuuza kwa walanguzi na kutorosha chakula nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu, kufikia mwaka 2030 biashara ya mazao ya chakula inakadiriwa kufikia dola za Marekani trilioni moja. Serikali ichukue hatua za makusudi kuboresha uzalishaji wa mazao ya chakula kutosheleza soko la ndani na nje. Uzalishaji wenye tija kwenye kilimo utaongeza upatikanaji wa fedha za kigeni na kupunguza pengo la urari wa biashara.

Mheshimiwa Spika, Serikali iangalie fursa za Kiwanda cha Viuadudu cha Kibaha kuanza uzalishaji wa viatilifu inayotokana na pareto ambayo inazalishwa hapa nchini na imekuwa inauzwa nchi za nje kama semi-finished product kwa bei ndogo ya kutupa. Viatilifu kutokana na pareto ni suluhisho la soko la pareto na pia suluhisho kwa upotevu wa mazao kushambuliwa na wadudu (post-harvest losses).

Mheshimiwa Spika, Serikali ianze mchakato wa kuanzishwa viwanda vya mbolea kwa kutumia madini (calcium carbonate, agricultural lime, phosphates, natural gas etc) yanayopatikana kwa wingi hapa Tanzania ili kuanza uzalishaji wa mbolea hapa nchini. Kutokana na athari za vita ya Urusi na Ukraine zinazoendelea, iwe fursa kwetu kwa kuanza kutumia rasilimali zinazopatikani nchini.

Mheshimiwa Spika, Serikali iendelee kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo hasa kwenye miundombinu ya umwagiliaji. Matumaini pekee ni hatua zilizooneshwa kwenye bajeti ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji na Serikali iweke mikakati madhubuti kuhakikisha ufanisi wa utekelezaji wa bajeti hii ya umwagiliaji. Serikali iangalie utelezaji wa miradi ya mabwawa kuunganisha uratibu kwa mahitaji ya jumla kama vile mahitaji ya Wizara ya Mifugo na hata Wizara ya Maji, kunaweza kuwa na tija kuwa na chombo kimoja chenye nguvu zaidi.
Mheshimiwa Spika, pia mikakati hii iweke nyongeza za ujenzi wa mabwawa hasa maeneo yenye mafuriko makubwa ikiwa ni pamoja na kuzuia mafuriko, lakini pia napendekeza Serikali iweke msukumo mkubwa wa kuharakisha utekelezaji wa miradi iliyomo kwenye Mradi wa Bonde la Mto Songwe (Songwe River Basin Development Programme - SRBDP), wenye ofisi zake Kyela, Tanzania. Mradi huu unaotekelezwa kwa pamoja na Serikali za Tanzania na Malawi, ni muhimu sana kwa sasa kutokana hasa na ujenzi wa mabwawa ambayo pamoja na manufaa mengine, yatasaidia kupunguza mafuriko ya Bonde la Kyela. Mabwawa haya yamelenga kuzalisha umeme, kilimo cha umwagiliaji, shughuli za uvuvi na hata utalii ambao unahitajika sana katika Wilaya ya Mbeya na ukanda wote wa Nyanda za Juu Kusini.

Mheshimiwa Spika, Serikali ichukue hatua za haraka kuleta Bungeni mapendekezo ya Sheria ya Kilimo ambayo pamoja na mambo mengine itawezesha usimamizi wa matumizi bora ya ardhi ya kilimo ambayo inaendelea kupotea kwa matumizi ya makazi. Pia kutokana na changamoto za tabia nchi, kumekuwepo na uharibifu mkubwa wa mazingira na ongezeko la upungufu wa vyanzo vya maji. Uharibifu unaotokana na shughuli za kibinadamu umepelekea misitu mingi kuharibiwa na uchomaji moto, ukataji mkaa na hata kilimo kwenye vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Spika, napendekeza Serikali iongeze msukumo kwa Wizara za Maji, Kilimo, Maliasili na Mazingira kufanya kazi kama timu moja ili kukabiliana na janga hili kubwa ikiwemo ujenzi wa mabwawa makubwa katika maeneo yanayokumbwa na mafuriko. Kama ilivyo kwa athari za mafuriko ya Kyela, hata Ziwa Rukwa linaathirika sana na kujaa mchanga na udongo unaosombwa na mito kutokana na mmomonyoko wa udongo.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa Mwaka 2018
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi ya kuchangia Muswada huu muhimu sana katika nchi yetu, kwa kweli haya marekebisho yamekuja katika muda muafaka, kama alivyosema aliyenitangulia, ukiziangalia hizi ni amendments, marekebisho tu ya sheria, lakini nakumbuka wakati tunachakata haya marekebisho tulipata shida sana kwa sababu kulikuwa na sheria ya mwaka 2010, ikaja 2014 na sheria nyingine mbalimbali. Sasa kuzioanisha zile ilikuwa ni ngumu sana. Ushauri wangu kwa kuanzia katika utungaji wa sheria ili iwe nzuri ni bora kukawa na consolidation ya hizi amendments zote zikawa kwenye sheria moja. Nafikiri hiki ni ni kitu muhimu sana ambacho kinaweza kuwasaidia mawakili lakini hata taasisi za elimu vilevile ili waweze kufanya reference ya sheria ambayo ni sahihi. Nafikiri hiyo ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho ni kizuri sana katika hii sheria ni namna gani sasa hivi, tunakwenda kuimarisha hii taasisi yetu pamoja na uimarishaji wa kisheria lakini kikubwa zaidi namna gani inamtambua Waziri wa Fedha kuwa yeye ndiyo atalibeba hili jukumu na hilo ndiyo muhimu sana kwa sasa hivi kwa sababu PPP haina maana ya kubinafsisha, PPP ownership iko kwa Serikali, hai-transfer ubinafsishaji. Sasa naona katika mazungumzo hapa nakubaliana na Makamu Mwenyekiti kwamba inawezekana labda ikahitaji elimu pana zaidi kwa ajili ya umuhimu wa Miswada na miundo ya uwekezaji kama hii ili tuweze kutofautisha ni mradi gani utakaokwenda TIC, ni mradi gani ambao utakwenda kwenye PPP Center. Nafikiri hicho ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna umuhimu mkubwa kwa kuwepo chini ya Wizara ya Fedha, kwa sababu kubwa ya suala la kibajeti. Ukiangalia inawezekana kiharaka haraka tukafikiria kwamba Serikali itakuwa imejiondoa katika kugharamia hizi PPP. Mimi naiona hapana, kwa sababu ukiangalia kwenye stakeholder analysis, kuna sponsors ambao wana-contribute only asilimia 30 kama equity, asilimia 70 inaweza kutokana na consortium ya lenders na hao lenders wanaweza kutoka nje. Sasa je, hii mikopo kama itakuja Tanzania tutaichukua vipi? Serikali itakuwa na mzigo au itakuwa na exposure?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba ukiangalia kwa kiasi kikubwa PPP wanasema private partner ndiye anachukua risk kubwa, je, Serikali haina risk? Sasa ukiangalia katika nchi zetu kama hizi maskini kwa sababu tunahitaji PPP kwa ajili labda ya ku-finance miundombinu au services mbalimbali ambazo ni muhimu haziwezi ku- attract investor binafsi.

Sasa ni namna gani Serikali pale ambapo hii project itakuwa haina faida, hatuwezi kuiacha kwa vile bado tunahitaji hizi FDI’s, bado tunahitaji hizi pesa kutoka nje, bado tunahitaji kupunguza mzigo mkubwa wa Serikali wa kukopa. Sasa ni jinsi gani Wizara ya Fedha iweze kuibeba hizi projects ambazo hazina faida kwa yule mwekezaji. Nafikiri kwa kiasi kikubwa inawezekana nimeangalia kwa haraka ni jinsi gani na sisi kama nchi tukachukua mifano ya wenzetu ambayo kwa kiasi kikubwa wanaangalia viability gap funding ambayo inakuwa ni capital investment ya Serikali toka pale mwanzo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ni jambo muhimu sana na nafikiri Wizara ya Fedha iliangalie kwa karibu sana hilo kwamba ni namna gani hizi exposure za capital, kwa hiyo Serikali ijiandae ya kwamba katika bajeti yake lazima kutakuwa na element ya ku-support hizi PPP achilia mbali ile facilitation fund.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwa sababu risk kubwa iko kwa huyu private partner, huyu tutam- compensate namna gani na hiyo risk yake kubwa. Kwa hiyo ni vitu vya kuangalia ni kwamba ile project itakapoanza ni namna gani Serikali itahakikisha kuwa malipo yanafanyika kwa muda muafaka ili tuweze kui-support ile project. Bado nasisitiza ya kwamba umuhimu mkubwa kwenye hizi project kwa vile zina-promote innovation ambazo ni nzuri sana hasa kwa vijana wetu wanaomaliza vyuo vikuu sasa hivi, ni muhimu sana tukazichukulia kwa haraka ili ziweze kuleta ajira kubwa ziende mpaka huko vijijini, mpaka kwenye Halmashauri ili tuwe na miradi mingi ambayo inaendeshwa na vijana wetu.

Kwa hiyo, training ya PPP ni muhimu kwa sababu hata wengine pamoja na uzoefu tulionao hizi PPP bado hatuzielewi vizuri. Kwa hiyo, kwa vijana wanaomaliza Vyuo Vikuu wapate elimu ya kutosha ya namna ya kutafuta ajira za wao wenyewe hasa kwa kupitia hizi PPP. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naunga mkono hoja.
Sheria ya Fedha ya Mwaka 2019
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa hii nafasi ya kuchangia kwenye hii hoja muhimu kwa ajili ya kodi zetu. Kwanza ningeanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na timu nzima ya Wizara ya Fedha. Kwa kweli wamefanya kazi kubwa sana, lakini pia nipeleke na pongezi kwa Kamati yangu ya Bajeti nafikiri nao wamefanya kazi kubwa ambayo inawezesha hata huu Muswada ukawa mzuri kiasi hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiri kabisa kulikuwa na hoja nyingi za wadau na hoja nyingi za Kamati ya Bajeti, lakini Waziri ameweza ku-accommodate hoja zote hizo kwa kiasi kikubwa, labda ni mambo machache tu ambayo yanahitaji maboresho kidogo. Kwa hiyo, ningependa tu niende kwenye mapendekezo ya hayo masuala machache ambayo labda Mheshimiwa Waziri angeangalia ni namna gani anaweza kuyaboresha kwenye huu Muswada. Jambo mojawapo ni suala la wafugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania katika Afrika ni mojawapo wa wafugaji wakubwa, tunazalisha ngozi nyingi, lakini hii ngozi inatozo mbili kubwa. Kuna 10% ambayo inatozwa kwenye export ya ngozi ambayo imetayarishwa kiwango cha wet blue, lakini kuna tozo ya asilimia 80 ambayo inatozwa kwa ngozi ghafi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hizi tozo, zilikuwa ni kwa ajili ya kulinda viwanda vyetu. Sasa kwa hali ilivyo sasa hivi, nafikiri wengi watakubaliana na mimi kwamba tannery zilizokuwepo ambazo tulikuwa tunataka tuzilinde zipate malighafi sasa hivi hazifanyi vizuri. Kwa hiyo, anayeumia hapa ni mkulima, anazalisha ngozi lakini ngozi haina soko. Mimi katika jimbo langu tunazalisha ngozi sana na sisi ni wafugaji, kwa kiasi kikubwa ile ngozi haina soko! Utapeleka wapi kwa vile mnunuzi mfanyabiashara yeye ile kodi siyo ya kwake, kodi inaangukia kwa mfugaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja kwamba kutakuwa na mahitaji ya wenzetu wa nchi za Afrika Magharibi, ambao hii ngozi wanaitumia kama chakula. Sasa hawa walikuwa wananunua ngozi kutoka kwenye nchi ambazo zinazalisha sana ngozi za Ethiopia pamoja na Sudan na hawa walisitishab kupeleka ngozi huku, kwa sababu katika hali ya kawaida ngozi tunategemea tuivae kama viatu au bidhaa mbalimbali na ziweze kulete utajiri mkubwa kwa nchi yetu. Kwa hiyo, napendekeza ya kwamba, ile hoja ya export levy ya 10% wangejaribu kuangalia ni namna gani ili tuwe competitive na wenzetu, iondolewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kodi vilevile hii ya asilimia 80, excise duty inamuumiza mfugaji, iondolewe. Wakulima wetu kwa kweli hawapati manufaa yoyote ya ngozi, kiasi kinachopelekea kwamba hata ngozi yenyewe sasa hivi haina ubora kwa sababu inakuwa haina thamani tena. Kwa hiyo, naiomba Serikali iangalie hilo suala kwamba, anayeumia hapa ni mfugaji na siyo mfanyabiashara. Kwa hiyo, hii ingeondolewa kabisa na ingewezekana wangepunguza hata nusu ingeweza kuwasaidia wafugaji wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuna mahitaji mengi sana ya maji, sasa hivi kutokana na karibu vijiji vingi vimepelekewa umeme vijijini, kwa hiyo, kutakuwa na urahisi wa kuchimba visima ambavyo vitatumia umeme. Naungana na wenzangu ambao wanapendekeza tuondoe kodi kwenye vifaa vya kuchimbia visima, zikiwemo pumps. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni suala muhimu, ni suala ambalo linaendana na sera yetu, ni suala ambalo litaisaidia sana Wizara kuweza kupeleka maji vijijini. Kwa sababu kukiwa na umeme, ukachimba visima, majirani zetu, nchi zetu majirani hawana mito, wanategemea visima hata kwenye umwagiliaji. Kwa hiyo, tukichimba mabwawa na tukichimba visima, tunaweza kupeleka maji kwenye vijiji vingi kama ilivyokuwa kwenye umeme wa REA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna suala la kodi kwenye mikopo ya kutoka nje, Serikali imeweka pendekezo kwenye huu Muswada kwamba iondolewe kodi kwenye riba ya mikopo inayopatikana kutoka nje. Hilo ni suala zuri, litaipunguzia Serikali mzigo wa kuanza kutoza kodi kwenye fedha zao wenyewe ambazo wamezikopa kutoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependekeza iende zaidi, tuna mahitaji mengi hapa ya FDI, fedha kutoka nje kutokana na mikopo. Ili mabenki yaweze kukopoa huko nje, nayo yanalipa riba na hii riba inakwenda kwa wakopaji, kwa hiyo, ningependekeza, hii nafuu ambayo imewekwa kwenye mikopo ambayo Serikali inapokea moja kwa moja, iende vilevile na kwenye mabenki yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, umuhimu wake hapa, ni kwa sababu, fedha tuliyonayo hapa nchini, nyingi ni ya muda mfupi, lakini ili uweze ku-finance miradi unahitaji fedha ya muda mrefu na fedha za muda mrefu unaweza kuzipata kwenye masoko ya nje. Kwa hiyo, naomba Serikali iangalie ni namna gani iendani na hilo wazo langu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine, ambalo ni muhimu sana ni hiki kitengo kipya, cha Tax Ombudsman, hii ni hatua nzuri sana, ila ninachoomba, ili ionekane hiki kitengo kiko huru, kisiwe chini ya TRA na wala kisiwe chini ya Wizara, kiwe nje ya hizi ofisi, kitaonekana kiko huru zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho nataka tu nisisitize kwamba hatua nyingi hizi ambazo Serikali inachukua, ziangalie ni namna gani vievile tuna improve administration, mengi hapa yameongelewa, tumelalamika sana, lakini unakuja kugundua kuwa, nafuu zilikuwepo, lakini administrations za kodi hazikuwa nzuri. Nilikuwa najaribu kuangalia hapa, East African Community Gazette, kumbe kulikuwa na suala ambalo kulikuwa na nafuu sana, kodi ziliondolewa, kwenye haya mataulo, mwaka 2017, lakini hili nafikiri wengi hatukulijua, mpaka leo tunafikiria kwamba hii kodi bado ipo. Kwa hiyo, ningependekeza kwamba tu- improve kwenye administration ili hizi kodi ziende moja kwa moja kuleta nafuu kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2020 (Toleo la Kiingereza)
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia Muswada wa Sheria ya Fedha ambao ni muhimu sana kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti hii ambayo imepitishwa jana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukikumbuka ni kwamba baada ya kupitishwa bajeti, uhalali wa makusanyo ya aina yoyote ya kodi inabidi uzingatie Ibara ya 138 ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo zoezi la leo ni zoezi muhimu sana kwa Bunge lako na inabidi tuzingatie sana na kuangalia ni kiasi gani haya yaliyomo kwenye huu muswada yana maudhui yaleyale kama ilivyokuwa imeandikwa kwenye bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake. Lakini najua hayo yote ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais, alivyofanya ukusanyaji wa kodi kuwa rahisi sana kwa kipindi hiki na mwaka huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri na timu yako, kwa kweli bajeti, hata huu muswada wenyewe umeandikwa vizuri sana. ndiyo sababu hata wewe yale mapendekezo ya Kamati ya Bajeti umeyachukua. Lakini ukiangalia hata Kamati ya Bajeti nayo kwenye taarifa yake imekubali karibu mapendekezo yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hii taarifa ya Kamati ya Bajeti pamoja na kukubali ina maelekezo ambayo Wabunge wjaribu kuyaangalia. Inatoa tahadhari kubwa. Tahadhari kubwa iko kwenye uandishi wa huu muswada. Hauko vizuri katika maeneo kadhaa ambayo Kamati ya Bajeti imeyaelezea vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende tu kumkumbusha Mheshimiwa Waziri ya kwamba arejee Ibara ya 138 ya Katiba yetu ili iendane na huu muswada ambao ameupendekeza leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini cha kufurahisha zaidi ni kwamba huu muswada unajaribu kuboresha mazingira ya uwezeshaji, ya ufanyaji kazi hapa kwetu ya blueprint pamoja na kuongeza wigo wa ukusanyaji kodi, lakini vilevile kulinda viwanda vyetu. Lakini ili hilo litimizwe inabidi uandishi uwe mahususi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye Sura ya 147 ya huu muswada ambayo inazungumzia kuhusu uongezeko la kwenye vinywaji, hasa vinywaji vikali. Silisemei hilo kwa sababu labda nataka niwatetee watu wanaokunywa vinywaji vikali, lakini ni kuwatetea labda wakulima wa zabibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia ongezeko hili, pamoja na kupunguza kuwa asilimia 30, lakini ongezeko la asilimia 20 bado ni kubwa mno, linaweza kuleta athari kwa wakulima wetu ambao malighafi zao ndiyo zinatumika kwenye uzalishaji wa hizi pombe kali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninamuomba Mheshimiwa Waziri ajaribu kuangalia, kama ilivyo kwenye maudhui kuwa ongezeko lisiwe nje sana ya inflation rate. Inflation rate ya sasa hivi iko kati ya asilimia 3 mpaka 4, sasa kukiwa na ongezeko mpaka asilimia 20, hiyo ni kubwa sana. kwa hiyo ajaribu kuangalia kwa sababu hizi biashara zetu nazo tunaangalia na wenzetu, mataifa yanayotuzunguka, wanafanya nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda vilevile kuboresha hii Sura ya 134 ambayo ni Sheria ya Mikopo na Misaada. Ni muhimu kwa kweli ukiangalia kwa mazingira ya sasa hivi, ya kwamba inawezekana labda hii imelenga hasa kuwasaidia hii kampuni yetu ambayo ipo kwenye ujenzi wa bomba la mafuta kati yetu na Uganda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na guarantee au hizi dhamana ambazo Serikali itazitoa, kiuhalisia inakuwa ni contingent liability au wanasema off-balance sheet. Lakini kwa wale watu ambao wanaangalia deni letu la Serikali, hizi zitaongezwa kwenye deni la Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hilo kwa uzoefu. Ya kwamba wewe unaposema hii ni off-balance sheet, wenzako wanapokwenda kule wanafanya adjustment ya balance sheet yako na wanaileta kwenye on-balance sheet, hizo dhamana zote. Kwa hiyo, kuweka na misingi ambayo tunasema deni letu liwe himilivu hii inaweza kuongeza deni letu lisiwe himilivu tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sura ya 332 ambayo ni kodi ya zuio. Hii kodi ya zuio, hasa kwenye mazao ya kilimo, asilimia mbili, inaonekana nzuri lakini ni mbaya sana kwa wakulima. Sheria inasema hii asilimia mbili ya zuio haitawagusa wakulima wadogo – ndiyo sababu nimetoa tahadhari ya uandishi wa hizi sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haitamgusa vipi mkulima mdogo hii asilimia mbili? Kwa sababu yule anayekusanya anakusanya kwa niaba ya mkulima. Kwa hiyo, italeta presha kubwa sana kwenye bei yetu ya mazao, siyo nafaka tu, lakini mazao hata kama kahawa, pareto n.k.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba Mheshimiwa Waziri aende aliangalie vizuri hilo. Sasa hivi kilimo kinahitaji transformation. Kilimo siyo mahali kwa kwenda kurundika kodi. Tumepunguza kodi kwenye kilimo, siyo vizuri ukaongeza kodi kwenye kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimeridhika sana kwai le three percent waliyoondoa kwenye kampuni za FEMATA ambao ni wachimbaji wadogowadogo wa madini. Kwa kweli hiyo ni hatua nzuri. Ile ingetuletea athari sana, kungekuwa na utoroshaji mkubwa sana wa madini yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sura ya 418 ya CAG, vilevile hatua nzuri iliyochukuliwa na Serikali ya kwamba CAG akague mashirika tu yale ambayo ina asilimia zaidi ya 50 ya uwekezaji, hiyo ni hatua nzuri. Lakini nimkumbushe tu Mheshimiwa Waziri, kinachotakiwa hapa ni kuimarisha misingi ya internal controls za mashirika yetu, siyo ukaguzi. Ukaguzi postmortem, tutampa lawama bure CAG, CAG kazi yake siyo kwenda kuimarisha mashirika. CAG ni kutupa taarifa sisi, kuangalia kama haya mashirika yetu mahesabu yake yametengenezwa namna gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Waziri aimarishe Msajili wa Hazina (Treasury Registrar), huyo ndiye atasaidia kuyawezesha mashirika yetu yasimamiwe vizuri, siyo CAG. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hata kwenye ile sura nyingine ambayo inasema mapato yote ya Mamlaka ya Bandari, TCRA, yaende Serikali Kuu. Nia ni nzuri, lakini kinachotakiwa pale ni kuhakikisha kuwa haya mashirika yanakuwa na uongozi mzuri, bodi nzuri, management nzuri, hata ukihamisha hizo pesa inawezekana ukaleta matatizo hata hayo makusanyo tunayokusanya sasa hivi yakawa madogo kwa vile watajiona hawa watu ya kwamba wao inawezekana hawaaminiki. Sasa hiyo inaweza kutupeleka mahali ambapo siyo pazuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru sana Kamati ya Bajeti kwa pendekezo la kwamba kunapokuwa na punguzo la bei ya mafuta duniani, lile punguzo badala ya kupunguza bei za rejareja, ile tofauti ikienda kwenye Mfuko wa Barabara. Kwa kweli itaongezea mfuko wetu pesa nyingi ambazo zitanufaisha Watanzania kwa kiasi kikubwa. Lakini kwa kiasi kikubwa inawezekana hizi pesa walikuwa wanafaidi wachache tu wenye makampuni hayo ya mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, kwa kweli niendelee tu kumshukuru Mheshimiwa Waziri kwa sababu hii sheria ni nzuri sana. Tunaomba aangalie kwenye uandishi, unakumbuka…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante na muda wako umekwisha.

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)