MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Napenda vilevile nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hatua ambazo Serikali imechukua kuhakikisha kuwa wakulima wetu wanapata pembejeo za ruzuku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, napenda niulize swali dogo tu la nyongeza. Pamoja na hizo pembejeo za ruzuku, Ilani ya Chama chetu cha Mapinduzi tuliahadi kupunguza bei za pembejeo kwa msimu huu. Je, Serikali imechukua hatua gani au mkakati gani kuhakikisha kuwa kwa msimu huu pembejeo zote zinakuwa na nafuu kwa wakulima wetu? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli azma yetu Serikali ni kuhakikisha kwamba mkulima anapata pembejeo kwa gharama nafuu, lakini pia kwa wakati ili aweze kulima mazao mengi zaidi ili pia tuondokane na shida ya chakula nchini, lakini pia aweze kuuza mazao hayo pale ambako wanahitaji kuuza kwa ajili ya kuongeza uwezo wa kifedha ndani ya familia yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo tumesema kwamba Serikali inatoa pembejeo kwa asilimia 25 ya mahitaji ya pembejeo na asilimia zilizobaki mkulima mwenyewe huwa anaweza kuendelea kuongeza ili kuweza kupata pembejeo; hii ni gharama nafuu, lakini tutaendelea kuangalia unafuu zaidi ili kumwezesha mkulima kupata pembejeo kwa gharama nafuu aweze kulima kilimo chenye tija kwa gharama nafuu vile vile.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nichukue jambo lako na tuendelee kuingia kwenye Serikali tuone utaratibu wa kuweza kupunguza gharama hizi ili wakulima wetu waweze kulipa fedha kidogo zaidi kuliko ilivyokuwa awali.