Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Oran Manase Njeza (37 total)

Halmashauri ya Mbeya ina vijiji vingi ambavyo havijapata umeme katika Mpango wa REA na pia utekelezaji wa REA II uko nyuma sana:-
(a) Je, ni vijiji vingapi vya Halmashauri ya Mbeya vimo kwenye REA II na mradi utakamilika lini?
(b) Je, Kwa nini mradi wa REA II haujalenga kupeleka umeme kwenye huduma za kijamii kama vile Shule, Zahanati, Nyumba za ibada na vyuo?
(c) Je, ni lini sasa vijiji vilivyobaki vitapewa umeme wa REA?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vya Halmashauri ya Mbeya vilivyomo kwenye REA Awamu ya Pili ni 27, vikiwemo vijiji vya Chang’ombe, Hatwelo, Haporoto, Idimi, Kasele, pamoja kijiji cha Wambishe.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi unaotekelezwa katika Awamu ya Pili , unafanywa na Mkandarasi SINOTEC ambao umefikia asilimia 54.33 na mradi huu unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2016/2017.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, katika miradi yote inayotekelezwa na Serikali kupitia Mfuko wa REA Vijijini, kipaumbele kimewekwa kwenye huduma za kijamii kama vile shule, zahanati, vituo vya afya, nyumba za ibada na mashine za kusukuma maji. Katika Mpango wa Awamu ya Pili ya umeme vijijini maeneo ya huduma za jamii ambayo yatafikishwa huduma ya umeme katika Halmashauri ya Mbeya Vijijini ni pamoja na shule za msingi 23, shule za sekondari tano, zahanati 10, kituo cha afya kimoja, pamoja na nyumba za ibada 42.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vingine vya Mbeya Vijijini ambavyo havikupata umeme kwenye Mpango wa REA kabambe Awamu ya Pili, vimewekwa kwenye Awamu ya Tatu unayotarajiwa kutekelezwa mara baada ya bajeti hii ya mwaka 2016 kupitishwa na Waheshimiwa Wabunge. Jumla ya vijiji 111 katika kata 30 za Mbeya Vijijini vimejumuishwa katika REA Awamu ya Tatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya kupeleka umeme kwenye maeneo yanayojumuisha ujenzi wa shule za umeme pamoja na zahanati, inafanyika kwa ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 480; ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 530, ufungaji wa transfoma 137 za ukubwa mbalimbali pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 7,465. Gharama ya kazi hii inakadiriwa kufikia shilingi bilioni 51.52
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-
Katika Halmashauri ya Mbeya kuna mradi wa uchimbaji wa madini unaotarajiwa kuanza kwenye eneo la Mlima Songwe, lakini pia kuna mradi mwingine mkubwa wa joto ardhi kwenye Kata za Swaya, Ijombe na Bonde la Songwe.
(a)Je, kwa nini Serikali Kuu haihusishi Halmashauri ya Mbeya katika mradi hiyo ili elimu iweze kutolewa kwa wananchi?
(b)Je, wananchi wa Jimbo la Mbeya Vijijini watanufaika vipi na miradi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa kifungu Namba 95(1)(b) cha Sheria Sheria ya Madini Namba14 ya 2010, kabla ya kuanza utafutaji na uchimbaji wa madini, mmiliki wa leseni husika hutakiwa kupata kibali cha kumruhusu kuingia na kushughulika na utafutaji na uchimbaji wa madini kutoka kwenye Halmashauri za zilaya pamoja na mkoa. Kampuni za Cradle Resources Ltd/RECB Co. Ltd. ilipewa leseni tatu za uchimbaji wakati wa madini ya niobium. Leseni hizo ni ML 237, 238 na 239 zilitolewa mwaka 2006 zenye jumla ya ukubwa wa eneo la kilometa za mraba 22.06. Kwa sasa kampuni hiyo inakamilisha maandalizi kabla ya kuanza kwa ujenzi wa mgodi huo ifikapo mwaka 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa utafiti wa madini hayo ya niobium kampuni ya Cradle Resources Ltd/RECB Co. Ltd. inayomiliki leseni ilijitambulisha kwa uongozi wa mkoa wa Mbeya ikiwa ni pamoja na Gereza la Songwe ambapo mradi huo upo. Aidha, kampuni hiyo hivi sasa iko kwenye mazungumzo ya Gereza la Songwe pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani kuona namna ya kulihamisha Gereza hilo kabla ya kuanza uchimbaji kwenye eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa niobium utakuwa na faida kubwa kwa uchumi wa viwanda ikizingatiwa kwamba Serikali inajikita katika kufufua na kukuza viwanda nchini. Miongoni mwa matumizi ya madini haya ni kutumika kama alloy kwenye chuma kwa kuboresha uimara wake. Vilevile madini hayo hutumika katika kutengeneza mabomba mathalani mabomba ya kusafirisha gesi asilia. Matumizi mengine ya madini haya ni matengenezo ya sumaku pamoja na utengenezaji wa injini za ndege na rocket.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kampuni ya Tanzania Geothermal Development Company Limited (TGDC) ni kampuni tanzu ya Shirika la Umeme nchini (TANESCO) ambayo imepewa dhamana ya kusimammia miradi ya kufua umeme wa joto ardhi katika Ziwa Ngozi lililopo kati ya Mbeya Vijijini. Mradi huu pia utazalisha umeme wa megawati 20 kwa kuanzia na baadaye utaweza kuzalisha megawati 100. Shughuli za utafiti wa mradi huu zilianza mwaka 2015 na zinatarajiwa kukamilika mwaka 2018 kwa kuzalisha umeme wa megawati 20. Mwezi Agosti 2015, kampuni ya TGDC iliendesha mafunzo kwa viongozi wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya, watendaji wa Kata na vijiji wa Mbeya yaliyolenga kuwajengea uelewa wananchi hao. Aidha, mafunzo kama hayo yalitolewa kwa njia ya mihadara kwa wananchi wa Vijiji vya Ijombe, Mwakibete, Nanyara na Swaya vinavyozunguka maeneo yanayofanyiwa utafiti wa joto ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na joto ardhi kutumika kuzalisha umeme manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi wanaozunguka eneo la mradi ni pamoja na kutumia maji ya moto majumbani lakini pia katika vitalu vya kilimo. Kadhalika itatumika katika kufugia samaki, kukausha mazao, kujenga mabwawa ya kuogelea na kwa matumizi mengine ya viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla miradi ya uwekezaji hunufaisha wananchi wa eneo husika katika ukuaji wa shughuli za kiuchumi na ajira. Miradi hii miwili itakapotekelezwa wananchi wa Halmashauri ya Mbeya Vijijini, Rungwe, Mbeya pamoja na Watanzania wote watanufaika kwa kupata ajira, ushuru pamoja na tozo mbalimbali pamoja na huduma za jamii.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-
Mji Mdogo wa Mbalizi uliomo kwenye Halmashauri ya Mbeya ni kati ya miji inayokua kwa kasi sana lakini inakosa miundombinu muhimu na uhaba na maji pia.
(a) Je, ni lini Mji huo utapewa hadhi ya kuwa Halmashauri ya Mji?
(b) Je, ni lini Serikali itatatua tatizo kubwa la maji kwenye Mji huo?
(c)Je, ni lini Serikali itajenga vituo vya afya kwenye kata zilizo ndani ya Mji wa Mbalizi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, uanzishaji wa Halmashauri za Miji nchini unazingatia Sheria ya Serikali za Mitaa Sura 288 (Mamlaka za Miji) ambayo imeainisha taratibu na vigezo vinavyopaswa kuzingatiwa. Hivyo, nashauri pendekezo hili lijadiliwe kwanza katika vikao vya Kamati za Maendelo ya Kata, Baraza la Madiwani na Kamati ya Ushauri ya Mkoa. Endapo vikao hivyo vitaridhia, Ofisi ya Rais - TAMISEMI haitasita kuyafanyia kazi mapendekezo hayo ya wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mji Mdogo wa Mbalizi unapata maji kutoka chanzo cha Ilunga chenye uwezo wa kuzalisha mita za ujazo 3,024 za maji kwa siku pamoja na visima kumi vya maji ambavyo vina uwezo wa kuzalisha mita za ujazo 6,300 kwa siku. Mji wa Mbalizi umeingizwa katika Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Maji awamu ya pili ambapo Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa kushirikiana na Halmashauri inakusudia kuunganisha Mji huo na Mamlaka ya Maji Mkoa wa Mbeya ili kupata maji yatakayotosheleza mahitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Mji wa Mbalizi wanapata huduma za afya kupitia Hospitali Teule ya Mbalizi pamoja na Hospitali ya Jeshi la Wananchi ambako Halmashauri imeendelea kutoa mchango wa dawa na watumishi. Hivyo, katika mwaka wa fedha 2016/2017, kipaumbele kimewekwa katika kukamilisha ujenzi wa zahanati nane ndani ya Halmashauri zilizoanza kujengwa kwa nguvu za wananchi.
MHE. ORAN M. NJEZA Aliuliza:-
Ili kuboresha elimu Serikali inashirikiana na Mashirika mbalimbali ikiwemo UNICEF ambao wanatoa misaada kwa sekta ya elimu:-
(a) Je, kwa mwaka 2014/2015 msaada wa UNICEF kwa Halmashauri ya Mbeya ulilenga mahitaji gani ya kuboresha elimu?
(b) Je, ni kiasi gani na asilimia ngapi ya msaada huo ulitumika katika miradi ya maendeleo ya elimu?
(c) Je, ni kiasi gani na asilimia ngapi ya msaada huo ulitumika katika matumizi ya kawaida?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/2015 Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) lilitoa msaada kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya uliolenga katika uendeshaji wa shughuli za elimu ya msingi, hususan kutoa mafunzo kwa walimu, wanafunzi, wazazi na walezi, kamati ya bodi za shule, wenyeviti wa vitongoji na vijiji, kuhusu malezi na haki za msingi za watoto kwa kupata elimu bora. Kwa kuzingatia makubaliano hayo yaliyopo kati ya UNICEF na Serikali fedha hizo ni kwa ajili ya kujengea uwezo (capacity building) na hazitumiki kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule.
(b) Mheshimiwa Spika, hadi Juni, 2015 Halmashauri ilipokea shilingi milioni 308.6 sawa na asilimia 64.8 ya shilingi milioni 475.9 zilizopangwa kutolewa na UNICEF kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
(c) Mheshimiwa Spika, fedha zote zilizopokelewa sawa na asilimia 100 zilitumika kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-
Uhitaji wa zao la pareto duniani ni mkubwa sana kiasi kwamba inahitajika kwa takribani tani 18,000 hadi 20,000 katika Soko la Dunia na Tanzania tuna uwezo wa kuzalisha hadi tani 8,000 tukiwa na mazingira rafiki.
(a) Je, ni kwa misingi gani pareto imepangiwa mnunuzi mmoja tu wa kigeni huku ikiwafungia milango wanunuzi wadogo wa Kitanzania?
(b) Je, Serikali inachukua hatua gani kusimamia bei
ya zao hilo ambayo imeporomoka kutoka shilingi 2,400 katika kipindi cha wanunuzi wengi hadi shilingi 1,500 chini ya mnunuzi mmoja?
(c) Je, Serikali ina mkakati gani wa muda mrefu na muda mfupi wa kuwawezesha wanunuzi wadogo wa Kitanzania kuingia kwenye ushindani na wanunuzi wageni?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, lenye sehemu (a),(b) na (c) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Sheria na Kanuni za Pareto zinamtaka kila mnunuzi kuongeza thamani ya pareto kwa kuzidua sumu ya pareto kupata sumu ghafi. Pia mnunuzi anatakiwa kuwa na maabara ya kupima kiwango cha sumu kwenye maua na kuwalipa wakulima kulingana na kiwango hicho cha sumu. Kwa sasa mnunuzi aliyetekeleza masharti hayo ni Kampuni ya Pareto Tanzania. Serikali inasisitiza mnunuzi yeyote kutimiza vigezo vilivyopo katika sheria na kanuni ili kulinda ubora na soko.
Mheshimiwa Spika, bei ya zao la pareto hupangwa katika Mkutano Mkuu wa Wadau ambao ni wa Kisheria na hufanyika kabla ya mwezi Julai kila mwaka kabla ya kuanza msimu mpya. Mkutano huo, huhudhuriwa na wanunuzi na wawakilishi wa wakulima na viongozi wa Halmashauri zinazolima pareto nchini.
Mheshimiwa Spika, Serikali inasisitiza wakulima kuzingatia kanuni za kilimo bora. Kwa mfano, pamoja na bei ya juu kuwa shilingi 2,200 msimu wa 2012/2013 na shilingi 2,700 msimu wa 2014/2015 ubora wa pareto ulikuwa chini ya asilimia moja. Baada ya baadhi ya wakulima kutekeleza kanuni za kilimo bora cha pareto katika msimu wa 2015/2016, ubora ulifikia asilimia 1.8 na bei ya juu kuwa shilingi 2,700.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, mkakati wa muda mrefu ni kuendelea kuhamasisha wazawa kujiunga pamoja na kukopa ili wawekeze katika viwanda vya kuongeza thamani ya zao la pareto kufikia kiwango cha crude extract na hatimaye kuingia kwenye ushidani na wanunuzi wa kigeni.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-
Ili kuboresha kilimo na ujasiriamali inahitajika elimu kwa wakulima pamoja na kuwa na vyanzo vya mitaji.
(a) Je, ni lini Serikali itaanzisha Mfuko wa Kuzunguka (Revolving Fund) kwa kila kijiji kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wakulima na wajasiriamali?
(b) Je, Benki ya wakulima ina mtaji kiasi gani na imetoa mikopo katika mikoa gani?
(c) Je, ni lini Benki ya Wakulima itaanza kutoa mikopo kwa wakulima wadogo wa Mbeya Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini, lenye sehemu (a), (b), na (c) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto ya upatikanaji wa mikopo vijijini hali inayochangia kukosekana kwa mitaji katika kuendeleza shughuli za kilimo na ujasiriamali. Hata hivyo, kwa kuwa suala la kuanzisha Mfuko wa Kuzunguka (Revolving Fund) kwa kila kijiji kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wakulima na ujasiriamali linahitaji fedha nyingi na usimamizi wa karibu kuhakikisha fursa ya upatikanaji wa fedha hizo haitumiwi na watu wachache kwa manufaa yao, Serikali imefanya uchambuzi wa kina ili kuona namna bora ya kusimamia mifuko ya aina hiyo na ambayo itawanufaisha wakulima na wajasiriamali na kuandaa mapendekezo ya mfuko stahiki kwa ajili ya kuridhiwa na Serikali. Juhudi hizo zipo katika ngazi ya maamuzi Serikalini. Aidha, kwa sasa Serikali inawashauri na kuwahamasisha wakulima na wajasiriamali kuunda vikundi au kujiunga na vyama vya kuweka na kukopa yaani SACCOS ili waweze kukopesheka.
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Juni, 2017 Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania imefikisha mtaji wa shilingi bilioni 65.6 ambayo umepanda kutoa shilingi bilioni 65.3 kama ulivyokuwa katika robo ya kwanza ya mwaka 2017. Kutokana na udhamini wa Serikali, benki imepata mkopo wa bei nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) kiasi cha shilingi bilioni 209.5 fedha ambazo zinatolewa kwa awamu, ambapo awamu ya kwanza ya shilingi bilioni 104.6 imeshapatikana. Aidha, hadi kufikia Juni, 2017 TADB imetoa mikopo ya jumla ya shilingi bilioni 7.46 katika Mikoa ya Tanga, Morogoro na Iringa ambapo jumla ya wakulima 2,252 wamenufaika na mikopo hiyo moja kwa moja.
Mheshimiwa Spika, TADB inalenga kufungua Ofisi za Kanda nchi nzima ili kurahisisha na kupunguza gharama za upatikanaji wa mikopo. Benki itaanzisha Ofisi ya Kanda Mkoani Mbeya. Hata hivyo, kama ilivyofanyika maeneo mengine, kabla ya ufunguzi wa ofisi hiyo, wakulima wa Mbeya walio katika vikundi watanufaika na mikopo ya TADB kuanzia msimu ujao wa kilimo.
MHE. ORAN M. NJENZA aliuliza:-
Kuna mgogoro wa muda mrefu wa ardhi kati ya TANAPA na Wananchi wa Kata za Ilungu, Igoma, Uleuje na wananchi walikuwa tayari kuachia ardhi yao ili upanuzi wa Hifadhi ya TANAPA lakini Serikali imeshindwa kuwalipa wananchi hao fidia:-
(a) Je, ni lini Serikali itafanya tathmini mpya ya fidia kwa wananchi wa Ilungu, Igoma na Uleuje?
(b) Kama Serikali imeshindwa kulipa fidia; je, ni lini itarudisha eneo hilo kwa wananchi wa Kata hizo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Oran Manase Njenza, Bunge wa Mbeya Vijijini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Taifa Kitulo ilianzishwa mwaka 2005 ili kuhifadhi vyanzo vya maji kwa ajili ya Bonde la Ziwa Nyasa, Bonde la Usangu na Mto Ruaha Mkuu ili kuhifadhi baioanuai ya aina za mimea adimu zikiwemo Chitanda. Hifadhi ya Taifa Kitulo imejumuisha maeneo yaliyokuwa yakimilikiwa na taasisi za Serikali. Maeneo hayo yanajumuisha Msitu wa Livingstone, Msitu wa Numbe na eneo lililokuwa shamba la mifugo (Diary Farming Company-DAFCO).
Mheshimiwa Mwenyekiti, tathmini iliyofanywa na Mkoa wa Mbeya kufuatia malalamiko ya wananchi wa Kijiji cha Kikondo, Kata ya Ilungu ilibaini kuwa kuna baadhi ya wananchi ambao taarifa ziinaonesha kuwa hawakulipwa fidia mwaka 1965 wakati shamba la DAFCO lilikuwa linaanzishwa. Serikali inakusudia kufanya uthamini kwa wananchi mwezi Februari mwaka 2018 ambao hawakulipwa fidia mwaka 1965. Aidha, Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Mbeya itahakikisha kuwa fidia inalipwa katika mwaka wa fedha 2017/2018.
MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA (K.n.y MHE. ORAN NJEZA) aliuliza:-
Wananchi wa Jimbo la Mbeya Vijijini wanaipongeza Serikali kwa kuanzisha Wilaya ya Kipolisi Mbalizi.
• Je, ni lini Ofisi ya Wilaya ya Kipolisi ya Mbalizi itajengwa zikiwemo nyumba za kuishi askari?
• Je, Wilaya ya Kipolisi ya Mbalizi ina magari mangapi na Serikali ina mpango gani wa kuboresha miundombinu ya vituo vya polisi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua ukosefu wa Kituo cha Polisi chenye hadhi ya Wilaya na ukosefu wa nyumba za kuishi askari Wilaya ya Kipolisi Mbalizi. Ni lengo la Serikali kukamilisha ujenzi wa vituo vya polisi kwenye wilaya 65 zilizosalia na ujenzi wa nyumba za makazi. Ujenzi huu utatekelezwa kwa awamu kutegemeana na upatikanaji wa fedha zitakazotengwa katika bajeti kila mwaka na kutumia rasilimali zilizopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kipolisi ya Mbalizi ina magari mawili, moja liko Mbalizi na lingine lipo kituo kidogo cha Inyara. Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya Vituo vya Polisi katika Halmashauri ya Mbeya na kwingineko kadri ya upatikanaji wa fedha utakavyoongezeka.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-
Barabara Kuu ya kwenda nchi jirani ya Zambia imepita katikati ya makazi ya watu na sehemu za biashara hasa katika Mji Mdogo wa Mbalizi na barabara hiyo inatumiwa na magari ya mizigo ambayo mara nyingi huwa ni chanzo cha ajali.
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara mpya ili kuhakikisha ajali zinapungua?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Tanzam highway inayoelekea nchi jirani ya Zambia ni barabara inayopita katika maeneo yenye makazi ya watu. Aidha, kutokana na tabia ya watu kupenda kufanya biashara ndogondogo kandokando ya barabara, kumekuwepo na msongamano mkubwa wa watu katika sehemu zinazopitiwa na barabara hii. Hali hii imejitokeza hasa katika maeneo ya Mbeya Mjini, Mbalizi, Uyole, Mlowo, Vwawa, Tunduma, Igawa, Chimala na Igurusi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ipo kwenye mpango wa kuikarabati barabara kuu ya Tanzam kuanzia Igawa hadi Tunduma ambapo katika mradi huo maeneo yenye matukio mengi ya ajali, ikiwemo eneo la mteremko wa Mbalizi, yataboreshwa ili kupunguza ajali. Mradi huu utajumuisha ujenzi wa barabara ya mchepuo kuanzia Uyole hadi Songwe na kazi hii ipo kwenye hatua ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-
Katika Mji Mdogo wa Mbalizi kuna ardhi ya ukubwa wa zaidi ya ekari 5,000 iliyotengwa kwa ajili ya Tanganyika Packers ambayo haijaendelezwa kwa zaidi ya miaka 30 iliyopita.
(a) Je, ni lini Serikali itawarudishia wananchi wa Mji Mdogo wa Mbalizi eneo hilo kwa lengo la kuliendeleza kwa kubadili matumizi kutokana na kukua kwa kasi kubwa kwa Mji wa Mbalizi?
(b) Pamoja na kubadili matumizi ya ardhi hiyo, je, Serikali ina mpango gani kwa wananchi wanaotumia ardhi hiyo hasa ikizingatiwa kuwa wengi wao hawakupewa fidia yoyote?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, shamba namba 760 lenye hekta 102.4 na shamba namba 761 lenye hekta 1985.4 yaliyoko katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ambayo kwa pamoja yana ukubwa wa hekta 2,087.8 sawa na ekari 5,219.5 ni mali ya Serikali. Mwaka 1974 Serikali ilijenga Kiwanda cha Kusindika Nyama cha Tanganyika Packers kwenye shamba namba 760 na shamba namba 761 lilikuwa maalum kwa ajili ya kupumzisha mifugo na kuilisha vizuri kabla ya kuchinjwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya uzalishaji kiwandani kusimama kutokana na changamoto kadhaa za kiuendeshaji na kiuchumi, baadhi ya wananchi walivamia maeneo ya mashamba hayo na tarehe 4/3/2016, Halmashauri ya Wilaya iliomba kwa Msajili wa Hazina kubadilisha matumizi ya eneo hilo kuwa makazi na huduma nyingine. Ombi hilo lilikataliwa kwa kuwa nia ya Serikali kuliendeleza eneo hilo kama eneo la viwanda haijawahi kubadilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ndiyo maana ili kuona kuwa haki inatendeka Serikali ilifungua kesi Namba 1 ya mwaka 2015 Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya dhidi ya wavamizi ambayo ilihukumiwa tarehe 20/2/2018 kwa Serikali kupewa haki ya kuendeleza eneo lake. Taratibu za kisheria za kuwaondoa wavamizi ili eneo hilo litumike kama ilivyokusudiwa zitakamilishwa hivi karibuni. Serikali haijawahi na haina mpango wa kubadili matumizi ya eneo hilo, kwani kufanya hivyo kwa maeneo kama hayo ni kukwamisha juhudi za kujenga Tanzania ya viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo wananchi waliokuwa wanastahili fidia kwa mujibu wa sheria wote walilipwa.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-
Wananchi wa Jimbo la Mbeya Vijijini wanaipongeza Serikali kwa kuanzisha Wilaya ya Kipolisi Mbalizi.
• Je, ni lini Ofisi ya Wilaya ya Kipolisi ya Mbalizi pamoja na nyumba za askari zitajengwa?
• Je, Wilaya ya Kipolisi ya Mbalizi ina magari mangapi na Serikali ina mpango gani wa kuboresha miundombinu ya vituo vya polisi katika Halmashauri ya Wilaya Mbeya?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oran Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini kama ifuatavyo:-
i. Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kipolisi ya Mbalizi ni miongoni mwa Wilaya Mpya za Kipolisi zilizoanzishwa hivi karibuni. Jeshi la Polisi kwa kutambua ukosefu wa Ofisi ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya pamoja na nyumba za makazi ya askari linashirikiana na wananchi na wadau mbalimbali kujenga jengo la Ofisi ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya ambalo linajumuisha Kituo cha Polisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa jengo hili umefikia hatua ya umaliziaji na changamoto iliyobaki ni ujenzi wa nyumba za kuishi askari.
ii. Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kipolisi ya Mbalizi ina magari matatu ambapo gari moja ni chakavu linahitaji matengenezo ili liweze kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya vituo vya Polisi katika Halmashauri ya Mbeya pamoja na kwingineko nchini kwa awamu kwa kutegemea rasilimali zilizopo na upatikanaji wa fedha.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-

Wilaya ya Mbeya, Mkoa wa Mbeya na Wilaya za Ileje na Songwe Mkoa wa Songwe zinaunganishwa kwa barabara za vumbi kuanzia Mbalizi kuelekea Ilembo, Iwinji hadi Ileje na Mbalizi kuelekea Mshewe.

(a) Je, ni lini Serikali itaunganisha barabara hizo kwa lami?

(b) Je, ni lini Serikali italipa fidia wananchi waliopisha upanuzi wa barabara za Mbalizi, Mshewe, Mjele hadi Mkwajuni Songwe?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara alizotaja Mheshimiwa Mbunge ni barabara za Mbalizi - Shigamba - Isongole zenye urefu wa kilometa 96.8 na barabara ya Mbalizi – Chang’ombe – Mkwajuni – Patamela – Makongolosi yenye urefu wa kilometa 117. Barabara hizo ni za Mkoa na zinahudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mbeya na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Songwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Serikali kwa sasa ni kuunganisha Makao Makuu ya Mikoa na nchi jirani kwa barabara za kiwango cha lami, ambapo tayari Makao Makuu ya Mkoa wa Mbeya na Mkoa wa Songwe yameunganishwa kwa barabara ya lami ya Mbeya hadi Tunduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kwa kuzingatia umuhimu wa barabara hizo, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imefanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili kuijenga kwa kiwango cha lami kwa barabara ya Mbalizi – Chang’ombe – Mkwajuni – Patamela – Makongolosi kilometa 117, sehemu ya Mbalizi hadi Galula kilometa 56. Aidha, Serikali imekuwa ikizifanyia matengenezo mbalimbali ya barabara hizi za Mbalizi – Shigamba – Isongole kilometa 96.8 na barabara ya Mbalizi – Chang’ombe – Mkwajuni – Patamela – Makongolosi kilometa 117 kila mwaka ili ziweze kupitika na majira yote ya mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu wananchi watakaopisha ujenzi wa barabara ya Mbalizi – Mshewe – Mjele – Galula. Serikali itawalipa fidia kutokana na sheria na taratibu kabla ya kuanza ujenzi.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-

Je, ni lini uzalishaji wa madini ya Niobium utaanza katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajibu swali, niungane na Watanzania wote kuwatakia kheri Waislam wote katika Mfungo wa Ramadhani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda sasa kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Uchimbaji wa Madini ya Niobium unaomilikiwa na Kampuni ya Panda Hill Mines Limited, kampuni hii ina ubia na kampuni ya Cradle Resources Limited asilimia 50 na Tremont Investment asilimia
50. Kampuni hiyo inamiliki leseni tatu za Uchimbaji wa Kati wa Madini Na.237, 237 na 239 za mwaka 2006 zilizotolewa tarehe 16 Novemba, 2006 zikiwa na jumla ya kilomita za eneo la mraba 22.1. Mradi utausisha uchimbaji wa madini ya Niobium ambayo yataongezewa thamani kwa kuchanganywa na madini ya chuma na kuwa Ferro-Niobium, zao ambalo litauzwa kwa wanunuzi mbalimbali walioko Ulaya, Asia na Amerika ya Kaskazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwekezaji ameshafanya upembuzi yakinifu (feasibility study) uliokamilka mwaka 2016 na kujiridhisha uwepo wa mashapo ya kutosha utakaowezesha uhai wa mgodi huo ambao utadumu kwa takribani miaka 30. Hata hivyo, kufuatia mabadiliko ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2017, mwekezaji alilazimika kupitia upya na kurekebisha taarifa za upembuzi yakinifu ili kuzingatia viwango vipya vya mrabaha, kodi na hisa za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, mwekezaji amewasilisha andiko la mradi la kuomba ufafanuzi wa vipengele mbalimbali kwa sheria na kutoa mapendekezo yake juu ya utekelezaji wa mradi huo, pamoja na suala la fidia ya ardhi kwa Gereza la Mbeya ambalo linatakiwa kuhamishwa ili kupisha mradi huo. Baada ya kupokea andiko hilo, hatua mbalimbali zimechukuliwa ikiwemo majadiliano na mwekezaji ambapo Wizara inatarajia kutoa mapendekezo yatakayowezesha kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-

Halmashauri ya Mbeya ina upungufu mkubwa wa maji karibu kwenye Vijiji zaidi ya 153 na hasa katika Kata ya Mjele. Je, Serikali ina mpango gani wakupeleka maji kwenye Vijiji hivyo na hasa Vijiji vya Mjele, Chang‟ombe na Ipwizi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njenza, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua tatizo la maji lililopo katika Halmashauri ya Mbeya Vijijini, katika mwaka wa fedha wa 2019/2020, Serikali imepanga kutekeleza miradi tisa ya maji ambayo ni Idimi - Haporoto, Iwindi, Mshewe, Ipwizi, Mjele - Chang‟ombe, Galijembe, Nsenga - Wimba, Iyawaya na Isangala group . Kiasi cha shilingi bilioni 6.4 kimetengwa katika bajeti ya 2019/20 kwa ajili ya kazi hiyo. Hadi kufikia mwezi Disemba 2019, jumla ya miradi 2 ya Idimi - Haporoto na Iwindi imekamilika na kiasi cha fedha shilingi bilioni 1.5 kimetumika katika ujenzi wa miundombinu ya maji.

Mheshimiwa Spika, baada ya Serikali kukamilisha miradi yote iliyopo kwenye bajeti ya 2019/2020, jumla ya vijiji 21 vitapata huduma ya maji vikiwemo vijiji vya Mjele, Chang‟ombe na Ipwizi ambapo jumla ya wakazi wapatao 44,364 watanufaika.
MHE. ORAN M. NJEZA Aliuliza:-

Ili kuboresha kilimo na ujasiriamali inahitajika elimu kwa wakulima ikiwa ni pamoja na kuwa na vyanzo vya uhakika vya mtaji.

(a) Je, Benki ya Kilimo ina mtaji kiasi gani?

(b) Je, Benki ya Kilimo ina mkakati gani wa kuwafikia wakulima wadogo wa Wilaya ya Mbeya?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO Alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ilipatiwa mtaji wa shilingi bilioni 60 mwezi Novemba, 2014. Aidha, tangu ilipoanza rasmi shughuli zake mwaka 2015, Benki ya Maendeleo ya Kilimo imefanikiwa kujiendesha na kukuza mtaji wake hadi kufikia shilingi bilioni 67.5 zilizorekodiwa mwishoni mwa robo ya kwanza ya mwaka 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha kuwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo inakuwa na fedha za kutosha kwa ajili ya kutoa mikopo na hivyo kufikia malengo ya kuanzishwa kwake, Serikali imeipatia benki hii kiasi cha shilingi bilioni 103 kupitia mkopo wa gharama nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika. Aidha, kwa sasa benki inaendelea na mchakato wa kukamilisha masharti ya kupatiwa awamu ya pili ya mkopo wa shilingi bilioni 103 kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania imefikisha huduma zake Mkoani Mbeya na kuongeza kasi ya utoaji wa mikopo kutoka shilingi milioni 799.9 mwezi Desemba, 2017 hadi shilingi bilioni 2.54 kwa taarifa ya mwisho wa mwezi Aprili, 2019. Mikopo hiyo imetolewa kwa miradi saba ya kilimo na kuwanufaisha wakulima 509 wa Wilaya za Mbozi, Momba na Mbarali.

Napenda pia kulifahamisha Bunge lako tukufu kwamba Benki ya Maendeleo ya Kilimo imefanikiwa kufungua ofisi ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Mkoani Mbeya. Malengo ya ufunguzi wa ofisi hiyo ni kuhakikisha kwamba benki inasogeza huduma zake karibu zaidi na wateja wake ambao ni wakulima wote wa Nyanda za Juu Kusini ikiwa ni pamoja na wakulima wadogo wa Wilaya ya Mbeya Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutumia nafasi hii kuwahimiza wadau wote wa kilimo nchini ikiwa ni pamoja na wakulima wa Wilaya ya Mbeya Vijijini, kuwasiliana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo ili waweze kupata maelekezo sahihi ya uandaaji wa miradi itakayokidhi vigezo vya kupatiwa mikopo na benki yao na pia kupatiwa maelezo ya fursa nyinginezo zinazopatikana katika benki yao.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-

Katika kukabiliana na ushindani na Bandari za nchi jirani, Mamkala za Usimamizi wa Bandari Tanzania ina mpango wa kuanzisha bandari kavu katika eneo la kimkakati la Inyala lililopo Wilaya ya Mbeya:-

(a) Je, ni lini tathmini ya fidia kwa wananchi itakamilika?

(b) Je, ni lini ujenzi wa Bandari Kavu ya Inyala utaanza;

(c) Je, kuna mkakati wa ujenzi wa reli kuunganisha Bandari Kavu ya Inyala na Bandari ya Itungi (Kyela)?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-

(a) Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) ina mpango wa kujenga Bandari Kavu katika eneo la kimkakati la Inyara, Mbeya ili kuhudumia wateja wa Zambia, Malawi, DRC na wafanyabiashara wa Tanzania kutoka Nyanda za Juu Kusini ili kukabiliana na ushindani na bandari za nchi jirani. Katika bajeti ya mwaka 2019/2020 TPA imepanga kufanya upembuzi yakinifu katika eneo lenye ukubwa wa ekari 100 ili kubaini mahitaji halisi na eneo linalofaa kwa ajili ya kujenga Bandari Kavu. Baada ya kukamilisha zoezi hilo, uthamini utafanyika na baada ya kukamilika taratibu za kulipa fidia kwa wananchi watakaopisha mradi huo zitaanza.

(b) Ili Bandari Kavu itakayojengwa ilete tija, mpango wa Serikali kupitia TAZARA ni kufanya upembuzi yakinifu kwa lengo la kutandika reli kuelekea kwenye eneo itakapojengwa Bandari Kavu ya Inyala. Mpango huu unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2020/21.

(c) Mkakati uliopo ni kuunganisha Bandari Kavu ya Inyala na Itungi iliyoko Kyela kwa reli ya TAZARA ili kuweza kuhudumia nchi jirani za DRC, Zimbabwe, Malawi na Zambia.

Hata hivyo, mkakati huu utaanza kutekelezwa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kipande cha reli ya TAZARA.
MHE. ORAN M. NJEZA Aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuongeza uzalishaji wa zao la pareto ambalo mahitaji yake duniani ni makubwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mahitaji ya maua makavu ya pareto duniani ni wastani wa tani 11,000 na yanatarajiwa kuongezeka kwa asilimia mbili hadi kufikia tani 14,000 kwa mwaka ifikapo 2025. Ongezeko hilo linatokana na kuongezeka kwa matumizi ya viuatilifu na bidhaa za tiba kwa kuwa, pyrethrin ni halisi kwa maana ni organic.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi zinazoongoza kwa uzalishaji wa pareto duniani ni Australia, Tanzania, Rwanda na Papua Guinea ambapo Tanzania inazalisha wastani wa tani 2,400. Bei ya pareto inategemea kiwango cha sumu kinachopatikana kwenye pareto na kwa sasa mkulima anapata malipo ya awali ya Sh.2,500 kwa kilo na hadi mwisho wa kukamilika kwa mzunguko wa mauzo inafikia hadi Sh.4,000 kwa kilo kutegemea kiwango cha sumu inayopatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na kuendelea kuongezeka kwa mahitaji ya pareto duniani malengo ya awali ni kuongeza uzalishaji wake kutoka wastani wa tani 2,400 kwa mwaka hadi kufikia tani 3,200 ifikapo mwaka 2025. Aidha, kufikia malengo hayo Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali ikiwemo kuanzisha mashamba ya pamoja, kwa maana ya block farming, kwenye halmashauri zinazozalisha pareto ikiwemo Halmsahauri za Mbulu na Mufindi ambazo zimeonesha utayari wa kutenga maeneo ya mashamba ya pamoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, mikakati mingine tumeanzisha mfumo wa uendelezaji wa zao wa kanda (zone) unaowashirikisha wawekezaji na wadau wote kwa mnyororo wa thamani. Ili kudhibiti ulanguzi wa pareto tumeelekeza halmashauri zote zinazolima pareto kuanzisha na kuimarisha vituo rasmi vya ununuzi wa pareto badala ya kuuza pareto majumbani na kwenye maeneo ya maficho. Vilevile katika kuhakikisha mkulima anapata bei nzuri kulingana na ubora wa pareto, Serikali imeanzisha utaratibu wa kuweka mtaalam wa maabara wa Serikali kutoka TARI Uyole kwa ajili ya kuhakiki viwango vya sumu kiwandani badala ya kutegemea viwango vinavyotumiwa na wanunuzi.
MHE. ORAN M. NJEZA Aliuliza:-

Je, ni lini uzalishaji wa madini ya niobium utaanza katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya?
NAIBU WAZIRI WA MADINI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mradi wa uchimbaji wa madini ya niobium katika Wilaya ya Mbeya unahusisha leseni tatu za uchimbaji wa kati na eneo hili lina jumla ya kilometa za mraba 22.1. Mradi huu unatarajiwa kuwa na uhai wa miaka 30 na unamilikiwa na Kampuni ya Panda Hill Tanzania, ambayo ni kwa ubia wa 50:50 na kampuni za Cradle Resources Limited na Tremont Investments. Mradi huu utahusisha uchimbaji wa madini ya niobium ambayo yataongezwa thamani nchini kwa kuchanganywa na madini ya chuma ili kuwa na mchanganyiko wa madini ya FerroNiobium, zao hili ndilo lenye soko katika nchi za Ulaya, Asia na Amerika ya Kaskazini.

Mheshimiwa Spika, Mwekezaji aliwasilisha Wizarani maombi ya misamaha ya kodi katika uwekezaji wake. Mwekezaji alielekezwa na Wizara kufuata matakwa ya Sheria ya Madini ambayo ndiyo inayotumiwa na wawekezaji wengine wote katika Sekta ya Madini.

Mheshimiwa Spika, nitoe rai kwa mwekezaji kukamilisha taratibu za kumwezesha kuanza utekelezaji wa mradi ikiwepo pia kupata ridhaa ya maandishi kutoka kwa wamiliki wa maeneo katika leseni zake kama ilivyo Sheria ya Madini. Ahsante.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha miundombinu ya Chuo Kikuu cha Afya Mbeya pamoja na Ndaki ya Afya na Sayansi Shirikishi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam – Mbeya?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Ndaki ya Afya ya Sayansi Shirikishi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ilihamia Mbeya mwezi Desemba, 2017 ili kupata hospitali kubwa ya kufundishia. Ndaki ilipewa nafasi katika majengo ya Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, baadhi ya majengo yaliendelea kutumika kama yalivyokuwa na baadhi yalihitaji ukarabati.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kupitia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, imefanya upanuzi na ukarabati mkubwa wa bwalo la chakula na ukarabati wa madarasa na maabara. Pia Chuo kilinunua na kufunga jenereta la dharura kwenye maabara. Kutokana na ufinyu wa nafasi ndani ya Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, kama mkakati wa muda mfupi, majengo matatu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yaliyopo eneo la Uzunguni yamekarabatiwa na kuwekewa samani ili yaweze kutumika. Pia Serikali imefunga vifaa vya TEHAMA katika majengo mbalimbali ya Chuo na kuweka mtandao wa internet kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.

Mheshimiwa Spika, mkakati wa Serikali wa muda mrefu ni kupata ardhi Jijini Mbeya ili kuanza ujenzi wa majengo ya Ndaki ya Afya na Sayansi Shirikishi. Mkakati huo utatoa fursa ya kuongeza miundombinu ya kisasa ya kufundishia na kujifunzia na kuongeza udahili wa wanafunzi wa shahada mbalimbali za Afya na Sayansi Shirikishi. Maombi ya ardhi yameshawasilishwa na ufuatiliaji unaendelea. Ahsante.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi wa barabara ya Mbalizi – Shigamba kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Mbalizi – Shigamba yenye urefu wa kilometa 52.2 ni barabara ya mkoa inayounganisha Mkoa wa Mbeya na Songwe kupitia Wilaya ya Mbeya Vijijini na Wilaya ya Ileje. Barabara hii ni ya changarawe na udongo ambayo hupita sehemu zenye miinuko na miteremko mikali, hivyo kupitika kwa shida wakati wa mvua kutokana na utelezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa katika Kampeni za Uchaguzi wa mwaka 2020, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, alipokuwa akiongea na wananchi wa Mji Mdogo wa Mbalizi aliahidi kuijenga Barabara ya Mbalizi – Shigamba kwa kiwango cha lami. Hata hivyo, utekelezaji wa ahadi za Viongozi, ikiwemo ahadi ya ujenzi wa Barabara ya Mbalizi – Shigamba hufanyika kwa awamu kulingana na upatikanji wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali inatafuta fedha ili kuanza kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hiyo ili ijengwe kwa kiwango cha lami. Wakati Serikali inatafuta fedha za kuanza taratibu za ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali kwa kiwango cha changarawe ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka. Ahsante.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza: -

(a) Je, ni Vijiji vingapi vya Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya vimepata umeme wa REA II, Densification na REA III?

(b) Je, ni lini vijiji vilivyobaki vitapatiwa umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Mbeya Vijijini ina jumla ya vijiji 140. vijiji 101 vina umeme ambao umepatikana kupitia miradi mbalimbali kama ifuatavyo;

REA II Vijiji 21; ujazilizi (Densification) vijiji 24; na mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa kwanza vijiji 45. Vijiji 11 vimepatiwa umeme kupitia miradi inayotekelezwa na Shirika la Umeme nchini (TANESCO).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya kupeleka umeme katika vijiji 39 vilivyobaki ilianza mwezi Mei, 2021 na kazi hiyo, itakamilika ifikapo Disemba, 2022. Gharama ya mradi ni shilingi bilioni 8.05.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kugharamia matengenezo ya Reli ya TAZARA ambayo miundombinu yake imechakaa na ni muhimu sana kwa uchumi wa Tanzania na hata nchi jirani za SADC?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mamlaka ya Reli Tanzania na Zambia (TAZARA) ilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya TAZARA Na. 23 ya mwaka 1975 iliyorekebishwa kwa Sheria ya TAZARA Na. 4 ya mwaka 1995. Reli hiyo inamilikiwa kwa uwiano wa hisa hamsini kwa hamsini baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Zambia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Tanzania inatambua umuhimu wa kugharamia matengenezo ya reli ya TAZARA na ndiyo maana inaendelea na jitihada za kukamilisha marekebisho ya Sheria Na. 4 ya mwaka 1995 ambayo kukamilika kwake kutaondoa changamoto zinazoathiri uwekezaji katika reli hiyo kwani uwekezaji unaofanyika sasa hauongezi thamani ya hisa za nchi inayowekeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuwepo kwa changamoto hiyo, Serikali ya Tanzania imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa TAZARA inaendelea kutoa huduma wakati jitihada za marekebisho ya sheria zikiendelea. Kwa mfano, katika bajeti ya mwaka 2017/2018 Serikali ya Tanzania iliipatia TAZARA jumla ya shilingi bilioni Kumi kwa ajili ya ununuzi wa vipuri vya kutengenezea vichwa saba vya treni na vifaa vya kuongeza uwezo mgodi wa mawe na kiwanda cha kutengenezea mataruma ya zege vilivyopo Kongolo Mkoani Mbeya.

Mheshimiwa Naibu Spika, vipuri na mashine hizo vimeshanunuliwa na matengenezo ya injini yamekamilika mwaka 2020 na hivi sasa zinafanya kazi. Mashine kwa ajili ya Kongolo zinafanya kazi pia. Aidha, Serikali ya Tanzania inaendelea kulipa mishahara ya wafanyakazi wa TAZARA upande wa Tanzania ambapo katika Bajeti ya mwaka 2021//2022 zimetengwa jumla ya shilingi bilioni 14.98.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni matumaini ya Serikali kuwa mchakato wa kurekebisha Sheria ya TAZARA utaisha hivi karibuni baada ya Serikali ya Zambia kukamilisha zoezi linaloendelea la uteuzi wa viongozi katika ngazi mbalimbali na kuwa tayari kwa kikao cha pande zote mbili kwa ngazi ya Makatibu Wakuu na hatimaye Mawaziri ili kuridhia mapendekezo ya marekebisho ya Sheria tunayoyasubiri. Ahsante.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itamaliza mgogoro wa muda mrefu wa ardhi kati ya TFS/TANAPA na wananchi wa Kata za Inyala, Itewe na Ilungu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Hifadhi ya Taifa Kitulo haina mgogoro na vijiji vya Kata za Inyala, Itewe na Ilungu. Changamoto iliyopo ni kuongezeka kwa mahitaji ya ardhi kwa wananchi wa maeneo hayo kwa ajili ya kufanya shughuli za kiuchumi. Maeneo hayo yalikuwa yanatumiwa kinyume cha sheria kwani kwa eneo ambalo ni Hifadhi ya Taifa Kitulo lilikuwa ni shamba la Serikali la mifugo ambamo ndani yake kulikuwa na (ng’ombe na kondoo wa sufu) lililojulikana kama Kitulo Dairy Farm.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na kuongezeka kwa uhitaji wa ardhi zaidi, wananchi wamekuwa wakidai maeneo waliyo kuwa nayo wanatumia kabla ya Hifadhi ya Taifa Kitulo kuanzishwa mwaka 2005 yarudishwe kwao ili kukidhi mahitaji zaidi ya ardhi kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji. Kutokana na hali hiyo, Serikali kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa uhifadhi na hifadhi za mazingira kwa ujumla ili kutatua changamoto hiyo.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutumia mfuko uliopo BoT wa trilioni moja kutoa dhamana kwa waagizaji mbolea kwa njia ya hedging/options?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia Agosti, 2021 BoT ilianzisha mkopo maalum wa shilingi trilioni 1.0 kwa benki na taasisi za kifedha ili kuziwezesha kutoa mikopo kwenye sekta ya kilimo ikiwemo mifugo, uvuvi na misitu. Kupitia mkopo huu, mkopaji anaruhusiwa kutumia kwa kununua au kuagiza mbolea na pembejeo za kilimo kwa utaratibu atakaoona unafaa ikiwemo hedging or options. Ahsante.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza: -

Je ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Ndaki ya Sayansi ya Afya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika Mamlaka ya Mji wa Mbalizi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali na Mheshimiwa Oran Manase Njeza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimeanza hatua za awali kwa kuwasilisha kwa Msajili wa Hazina maombi ya kupewa ardhi yenye ukubwa wa hekari 2000 kwenye eneo lililokuwa shamba la Tanganyika Packers kwa ajili ya ujenzi. Kwa sasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinaendelea kufuatilia maombi haya kwa Msajili wa Hazina.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Ndaki ya Sayansi ya Afya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam - Mbalizi utaanza mara moja pale upatikanaji wa ardhi utakapokamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kupunguza bei za mbolea zinazopanda kwa kasi kwenye Soko la Dunia ili kumpunguzia mkulima mzigo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika msimu wa 2021/2022 bei ya mbolea imeendelea kupanda katika Soko la Dunia kutokana na athari za UVIKO-19 na Vita ya Urusi na Ukraine zilizosababisha kupungua kwa uzalishaji na ongezeko la gharama za malighafi zinazotumika kutengeneza mbolea.

Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hiyo, Serikali imeanza kuchukuliwa hatua za haraka, muda wa kati na muda mrefu katika kukabiliana na changamoto ya kupanda kwa bei. Hatua za haraka ni pamoja na kudhibiti upandaji holela wa bei usiozingatia gharama halisi za uingizaji mbolea nchini kwa kutangaza bei elekezi zinazopaswa kuzingatiwa na wafanyabiashara katika maeneo ya uzalishaji.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekutana na uongozi wa kiwanda cha mbolea cha Minjingu kwa lengo la kuzipatia ufumbuzi changamoto za kiwanda ili kuhakikisha kinaongeza uzalishaji wa mbolea kutoka wastani wa tani 30,000 hadi kufikia tani 100,000 kwa mwaka. Aidha, Serikali inaendelea kuhamasisha wawekezaji wapya wa viwanda vya mbolea ambapo kampuni ya Intracom Fertilizers Limited kutoka Burundi imejitokeza na inajenga kiwanda katika Mkoa wa Dodoma chenye uwezo wa kuzalisha tani 600,000 kwa mwaka.

Mheshimiwa Spika, hatua hizo zinazochukuliwa na Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi zitasaidia kupunguza bei ya mbolea.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kukabiliana na kupanda kwa bei za pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza Mbunge wa Mbeya Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imepanga mikakati ya muda mfupi, kati na ya muda mrefu katika kukabiliana na kupanda kwa bei za mbolea hapa nchini. Mikakati hiyo ni pamoja na kutekeleza Mpango wa Utoaji Ruzuku ya Mbolea kwa wakulima msimu wa 2022/2023, kuhimiza matumizi ya mbolea mbadala wa DAP na UREA kama vile NPK, NPS, NPS- zinc, Minjingu, mbolea za asili na chokaa, kupunguza gharama za meli kukaa bandarini ambazo pengine mwisho wake hujumuishwa kwenye mjengeko wa bei ya mbolea, kuhimiza wafanyabiashara wa mbolea kutumia njia ya reli ya TAZARA na Reli ya Kati kusafirisha mbolea kwa wingi kwenda mikoani na kuhamasisha uwekezaji katika kuzalisha mbolea ndani ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kupitia mpango wa ruzuku ya mbolea, Serikali imeweka bei elekezi ili kuwawezesha wakulima kununua mbolea za DAP, Urea na NPK kwa Shilingi 70,000 kwa mfuko wa kilo 50, Shilingi 60,000 kwa mfuko wa kilo 50 wa mbolea ya CAN na Shilingi 50,000 kwa mfuko wa kilo 50 wa mbolea ya SA. Aidha, Serikali inaendelea kushirikiana na Sekta Binafsi vikiwemo viwanda vya Minjingu Mines and Fertilizer Limited na Itracom Fertilizers Limited kuhakikisha uzalishaji na upatikanaji wa mbolea hapa nchini kwa gharama nafuu unaimarika na kupunguza utegemezi wa kuagiza mbolea kutoka nje ya nchi.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza: -

Je, ni lini Serikalii itajenga barabara ya mchepuko ya Mlima Nyoka (Uyole) hadi Uwanja wa Ndege wa Songwe ili kuondoa msongamano na ajali?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ipo kwenye maandalizi ya kujenga barabara ya Igawa – Songwe – Tunduma yenye urefu wa kilomita 218 pamoja na barabara ya mchepuo ya Mlima wa Nyoka pale Uyole hadi Uwanja wa Ndege wa Songwe (Uyole – Songwe Bypass) yenye urefu wa kilomita 48.9 kwa utaratibu wa EPC+F. Hadi sasa Mkandarasi amekwishapatikana na mkataba wa ujenzi utakuwa umesainiwa kabla ya mwisho wa mwezi Juni, 2023, ahsante.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-

Je, lini barabara ya Irambo - Nsonyanga ambayo inaunganisha barabara ya Isyonje – Makete hadi Njombe na TANZAM itapandishwa hadhi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 09 Januari, 2023, kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Njombe kilifanyika ambapo moja ya barabara zilizopendekezwa kupandishwa hadhi ni Barabara ya Irambo – Nsonyanga yenye urefu wa kilometa 22.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Kitaifa ya Kupanga Barabara Katika Hadhi Stahiki (NRCC) ilifika Mkoani Mbeya tarehe 24 Februari, 2023 na kutembelea barabara zilizoombwa kupandishwa hadhi ikiwemo barabara ya Irambo – Nsonyanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo ya Kamati yamewasilishwa kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi na yanachambuliwa na uchambuzi ukikamilika taarifa itatolewa. Endapo barabara hiyo itakidhi vigezo vya kupandishwa hadhi, itakuwa barabara ya Mkoa na itahudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza: -

Je, lini ujenzi wa KV 400 kutoka Iringa, Mbeya, Tunduma hadi Sumbawanga utaanza pamoja na kulipa wananchi waliopitiwa na laini hiyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa KV 400 yenye urefu wa kilometa 620 kutoka Iringa hadi Sumbawanga kupitia Mbeya na Tunduma unatarajiwa kuanza mwezi Juni, 2023 na kukamilika mwezi Septemba, 2025. Mradi huu unalenga kuunganisha Gridi ya Taifa na Nchi za Kusini mwa Afrika (Southern African Power Pool) na utagharimu jumla ya shilingi 1,380,000,000,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tayari imetoa shilingi bilioni 16.43 kwa ajili ya malipo ya fidia kwa wananchi 6,500 wanaopisha mradi na kazi ya ulipaji fidia imekamilika kwa awamu ya kwanza ambapo wananchi 4,750 wamepokea shilingi bilioni 13.67 na maandalizi ya awamu ya pili yanaendelea na malipo yanatarajiwa kufanyika ifikapo Julai, 2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaipandisha hadhi barabara ya Mjele – Ikuwa hadi Mlima Njiwa kuwa ya Mkoa?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Mbeya kupitia kikao chake cha tarehe 9 Januari, 2023 kilitoa mapendekezo ya kuipandisha hadhi Barabara ya Mjele – Ikuwa hadi Mlima Njiwa kuwa ya Mkoa. Baada ya mapendekezo hayo kuwasilishwa kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, tarehe 24 Februari, 2023, Kamati ya Kitaifa ya Kupanga Barabara Katika Hadhi Stahiki (NRCC) ilitembelea barabara zilizoombwa kupandishwa hadhi Mkoani Mbeya ikiwemo Barabara ya Mjele – Ikuwa hadi Mlima Njiwa.

Mheshimiwa Spika, Mapendekezo ya Kamati yamewasilishwa kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi na yanachambuliwa na uchambuzi ukikamilika taarifa itatolewa. Endapo barabara hiyo itakidhi vigezo vya kupandishwa hadhi, itakuwa barabara ya mkoa na itahudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-

Je, ni lini wananchi wa Wilaya ya Mbeya waliopisha mradi wa njia kuu ya kusafirisha umeme mkubwa wa Kilovolti 400 watalipwa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TANESCO inaendelea na maandalizi ya ujenzi wa mradi wa njia ya kusafirisha umeme mkubwa wenye msongo wa kilovoti 400 kutoka Iringa kupitia Mbeya, Tunduma hadi Sumbawanga yenye urefu wa kilomita 616. Mradi huu pia unahusisha ujenzi wa Vituo vya Kupoza Umeme vya Iringa, Kisada, Mbeya, Tunduma na Sumbawanga pamoja na ujenzi wa kilomita nne za njia ya umeme msongo wa kilovoti 400 kwenda kwenye mpaka wa Tanzania na Zambia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uthamini unafanywa na TANESCO kwa kushirikiana na Wathamini wateule wa Wilaya za Iringa, Mufindi, Mafinga, Mbarali, Mbeya, Jiji la Mbeya, Mbozi, Tunduma, Momba na Sumbawanga ambapo katika maeneo hayo mradi unapita. Hadi kufikia Mwezi Aprili, 2022, majedwali ya fidia ya Halmashauri za Iringa, Mufindi, Mafinga, Momba na Mbarali tayari yameshaidhinishwa na Mthamini Mkuu wa Serikali na kukabidhiwa TANESCO kwa ajili ya kuanza maandalizi ya malipo. Majedwali ya Wilaya za Mbeya, Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Mbozi, Tunduma na Sumbawanga yapo katika hatua za mwisho za ukamilishwaji. Fidia hizi zinatarajia kuanza kulipwa mwaka wa fedha 2022/2023.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-

Je, kuna Mkakati gani wa Kujenga Viwanda Maalum na Maghala ya ubaridi kwenye eneo la Tanganyika Packers Mbalizi?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mipango na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo la Tanganyika Packers Mbalizi Shamba Na. 761 la kulishia mifugo la Nsalala lenye ukubwa ekari 4,900, Serikali imeshafanya maamuzi ya kulikabidhi eneo hilo kwa Mamlaka ya Maeneo Maalum kwa Mauzo Nje (EPZA) kwa ajili ya uwekezaji. Baada ya makabidhiano, eneo hilo litatumika kwa ajili ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na ujenzi wa viwanda mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imechukua maoni ya Mheshimiwa Mbunge ya ujenzi wa viwanda maalum na maghala ya ubaridi katika eneo hilo na itayafanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza: -

Je, Serikali imejipangaje kuongeza tija kwenye sekta ya kilimo na kuimarisha soko la bidhaa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali kwenye sekta ya kilimo kwa nia ya kuongeza tija kwenye uzalishaji kupitia uwekezaji katika miundombinu ya umwagiliaji, pembejeo, utafiti, huduma za ugani, matumizi ya sayansi na teknolojia na kurasimisha sekta ya kilimo mazao. Serikali kupitia Soko la Bidhaa inaendelea kutoa elimu kwa wakulima na wadau kuzalisha kwa tija na kuuza katika soko rasmi (Soko la Bidhaa Tanzania) ambalo linawakutanisha na wanunuzi wakubwa wa nje na wa ndani na kuwapatia bei zenye ushindani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Serikali inaendelea kuhamasisha kilimo cha kibiashara kinachozingatia mahitaji ya soko, kushiriki makongamano na maonesho ya kibiashara na uwekezaji kwa lengo la kutangaza bidhaa na maeneo ya uwekezaji katika sekta ya kilimo, kushirikiana na sekta binafsi katika ujenzi wa miundombinu ya masoko, kuimarisha mifumo ya kielektroniki ikiwa ni pamoja na kuanzisha kituo rasmi cha Intelijensia ya Masoko ya Mazao ya Kilimo (Agricultural Market Intelligence and Data Centre), ambayo itawezesha upatikanaji wa taarifa za masoko kwa wakati, kutoa mafunzo kuhusu kilimo biashara kwa Maafisa Ugani na wakulima na kuendelea kufungua masoko mapya katika nchi mbalimbali kwa kufanya tafiti za mahitaji kwa nchi husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali kupitia soko la bidhaa inaendelea kutoa elimu kwa wakulima na wadau kuzalisha kwa tija na kuuza katika soko rasmi ambalo linawakutanisha wanunuzi wakubwa wa nje na wa ndani na kuwapatia bei zenye ushindani. (Makofi)
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-

Je, kuna fursa na changamoto gani kwa Tanzania kushiriki kwenye biashara ya carbon.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna fursa kubwa ambayo Tanzania inanufaika katika biashara ya kaboni. Fursa ya kwanza ni uhifadhi wa baioanuai na pili, ongezeko la pato la Taifa. Hivi karibuni halmashauri mbalimbali zimepokea fedha zilizotokana na biashara ya carbon kutoka katika kampuni mbalimbali ambazo zinatumika kujenga miundombinu ya kusaidia jamii katika halmashauri mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na fursa zilizopo bado kumekuwa na changamoto kadhaa katika biashara ya kaboni. Kwanza ni uelewa mdogo wa jamii katika utekelezaji wa biashara ya kabon na pili ni uwazi wa biashara ya kaboni katika soko la dunia. Pamoja na changamoto hizo, Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wadau wote ili kuhamasisha uwekezaji wa miradi ya biashara ya kaboni katika sekta mbalimbali pamoja na biashara ya kaboni kwa wadau mbalimbali ili kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu biashara hii, ahsante.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-

Je, lini Serikali itamaliza mgogoro wa muda mrefu wa ardhi kati ya TANAPA Kitulo/TFS na wananchi wa Kata za Ilungu, Igoma na Inyala?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Mbeya Vijijini na uongozi wa kata zilizopakana na Hifadhi ya Taifa ya Kitulo imefanya mikutano 15 kati ya tarehe 17 Mei, 2023 na tarehe 9 Novemba, 2023. Mikutano hiyo ililenga kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa uhifadhi, dhana ya ujirani mwema na kuwashirikisha wananchi katika juhudi za pamoja za kutambua mipaka ya hifadhi kwa faida za hifadhi, jamii na Taifa kwa ujumla. Kufuatia mikutano hiyo, mgogoro huu umemalizika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuendeleza mahusiano mema na jamii zinazozunguka hifadhi, Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia TANAPA kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Mbeya imepanga kuweka vigingi kwenye mpaka wa hifadhi kwa umbali wa kilometa 82 katika mwaka wa fedha 2024/2025 ili kurahisisha utambuzi wa mipaka ya hifadhi na vijiji.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itarekebisha mipaka ya Vijiji, Kata ya Utengule na Usongwe ikiwemo Kijiji cha Mbalizi ambacho hakiungani kabisa na Vijiji vingine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, uanzishaji wa maeneo ya utawala katika Mamlaka za Serikali za Mitaa hufanyika kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Sura 287 na (Mamlaka za Miji) Sura 288 pamoja na Mwongozo wa Uanzishwaji wa Maeneo ya Utawala wa mwaka 2014.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia Sheria hizi na mwongozo uliopo, utaratibu wa uanzishaji au mabadiliko ya mipaka ya vijiji inapaswa kuanza kujadiliwa kwenye Mkutano Mkuu wa Kijiji, Kamati ya Maendeleo ya Kata, Baraza la Madiwani, Kamati ya Ushauri ya Wilaya na Kamati ya Ushauri ya Mkoa ambayo huwasilisha mapendekezo hayo Ofisi ya Rais - TAMISEMI kupitia Katibu Tawala Mkoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vema Halmashauri na Mkoa kufuata taratibu hizi na ombi hili liwasilishwe Ofisi ya Rais - TAMISEMI kupitia Katibu Tawala Mkoa kwa hatua zaidi.