Supplementary Questions from Hon. David Ernest Silinde (38 total)
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, asante sana. Tatizo la maji Tanzania ni kubwa na ndiyo maana kwenye Bunge letu kila Mbunge akiulizwa atakueleza hilo. Sera ya Maji ya Taifa inataka mwananchi wa kawaida apate maji umbali wa mita 400 toka makazi anayoishi. Sasa Mheshimiwa Waziri, na Naibu Waziri atueleze ni lini Sera hiyo ya Taifa itaanza kutekelezwa kikamilifu ili Watanzania waondokane na hii kero ya maji?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Silinde kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli Sera ya Maji ya mwaka 2002 tunasema kwamba umbali wa mtu kupata maji kwenye kichoteo ni mita 400. Kazi hii tulishaianza kuitekeleza kuanzia mwaka 2007 katika awamu ya kwanza ya programu ya maji ambayo imeishia Disemba, 2015.
Mheshimiwa Spika, matokeo ya awamu ya kwanza ni mazuri ijapokuwa hatukufikia lengo ambalo tulitaka kufika, sasa ile miradi ambayo tayari imeshanza kwenye programu tunaiingiza kwenye programu ya pili ambayo inaanza Januari mwaka huu. Ili kukamilisha miradi ile iliyokwisha kuanza ili tuweze kufikia azma hiyo ambayo kila mwananchi atapata maji kutoka umbali wa mita 400.
Mheshimiwa Spika, nikuhakikishie wakati wa kampeni Dkt. John Pombe Magufuli aliahidi adhima hiyo maeneo mengi na Serikali ya awamu ya tano itahakikisha kwamba suala la maji ni ajenda ya kwanza, na kuhakikisha kila mwananchi atapata maji, ijapokuwa tunasema asilimia 95 Mijini na asilimia 86 Vijijini, azma ya sasa ni kwamba tunataka tupate maji kwa asilimia 100 katika miaka mitano ijayo.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini niseme Serikali inaonekana haiko serious katika hizi Halmashauri mpya ambazo tumekuwa tukizianzisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2014/2015 Halmashauri ya Wilaya ya Momba tuliomba shilingi bilioni mbili fedha maalum, maombi maalum, kwa ajili ya kuanzisha ujenzi wa Makao Mkuu yaani kwa maana ya kujenga boma na nyumba za watumishi ili watumishi watoke katika Halmashauri mama ya Mbozi kwenda Momba eneo la Chitete wakaanze kazi maalum. Mwaka 2014/2015 ukiangalia hapa hapa Serikali haijatenga kitu chochote, ni kwa nini Serikali inakuwa haiko serious inapoanzisha Wilaya mpya kwa ajili ya maandalizi ya watu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali (b), Halmashauri ya Momba ipo katika Mkoa mpya wa Songwe ambao na wenyewe umeanzishwa hauna Mkuu wa Mkoa, hauna ofisi, hauna chochote. Ni kwa nini Serikali imekuwa ikianzisha jambo la msingi lakini utekelezaji imekuwa ikishindwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka kupata majibu lini Mkoa Mpya wa Songwe utapelekewa Mkuu wa Mkoa na ofisi itakuwepo pamoja na Halmashauri ya Mombo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Silinde anasema kwamba Serikali haina nia ya dhati. Kikubwa zaidi naomba kwanza Bunge lako hili, tukiri kwamba miongoni mwa mambo ambayo Watanzania wametendewa haki na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni pale ambapo maombi yamepelekwa ya Mikoa, Halmashauri na Wilaya mpya na Serikali ikaamua kutekeleza hili ili mradi suala la kuleta huduma kwa wananchi, naomba tukiri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo ukija kuangalia katika ujenzi wa Ofisi za Wilaya peke yake, takribani Serikali ilitenga ujenzi wake kupitia TBA zaidi ya bilioni 12.9. Katika mchakato huo zaidi ya bilioni 5.6 zimepelekwa na mchakato mwingine unaendelea. Naomba tukiri kwamba rasilimali fedha ndiyo lilikuwa tatizo, lakini Serikali inajitahidi kuhakikisha kwamba, Halmashauri na Wilaya zilizojengwa na Mikoa iweze kufanikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala zima hususan la Mkoa wa Songwe, Serikali imejipanga itajitahidi kwa kadri iwezekanavyo na ukija kuangalia hivi sasa, tuna Mikoa hii mipya iliyoanzishwa na lengo kubwa ni kukusanya mapato. Mwisho wa siku ni kwamba ofisi hizi na hasa masuala ya kiutawala, ngazi za utawala ziweze kukamilika ilimradi wananchi waweze kupata huduma, lakini Serikali imejidhatiti katika hilo kwa ajili ya kuleta huduma kwa wananchi.
MHE. GEORGE B. SIMBACHAWENE - WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (TAMISEMI): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa. Pengine bila kurudia yale aliyoyasema, nimesimama ili tu niongezee jibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Silinde anasema Mkoa wa Songwe umeanzishwa, mchakato wa Mkoa wa Songwe kuanzishwa haujakamilika kwa sababu hadi sasa hatuja-gazette. Kwa hivyo, huwezi ukaanza kumhudumia mtoto kabla hajazaliwa, unamnunulia nguo za kwenda shule.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutakachofanya kwa sasa baada ya muda tutatoa tamko rasmi la Serikali na tamko la Serikali huwa lipo kwa mujibu wa sheria. Kwa hiyo, tukishaipa GN, tutatamka kwamba Rais ameuanzisha huo Mkoa. Naomba uvumilie, lakini napongeza pia, najua una hamu kweli kuanza kuingia katika Mkoa wa Songwe, lakini taarifa hiyo uliyoitoa ni kwamba bado hatujauanzisha rasmi Mkoa wa Songwe, subiri tutatamka wakati wowote Serikali itakapokuwa tayari imemaliza mchakato wake. (Makofi)
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri kwamba kuna changamoto katika ujenzi wa nyumba za Polisi pamoja na vituo. Sasa swali langu ni je, kwenye Polisi kuna kitengo cha Usalama Barabarani yaani Trafiki, ambacho kimekuwa kikikusanya fedha nyingi, almost kwenye bajeti huwa tunatenga ni zaidi ya bilioni 10 kwa mwaka.
Je, ni kwa nini sasa Serikalli isiamue kuruhusu Polisi kutumia fedha zinazotokana na Polisi wa barabarani kwa ajili ya kuondoa kero ya ujenzi wa nyumba za polisi, pamoja na Vituo vya Polisi katika Wilaya zote nchini?
Swali la pili, katika majibu ya Mheshimiwa Waziri, amesema Serikali inatajarijiwa kukopa kutoka Benki ya Exim China; je, haijatueleza ni kiwango gani mnatarajia kukopa na namna ambavyo mtalipa, kwa sababu suala la Polisi siyo miradi ya maendeleo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI YA WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna fedha ambazo zinakusanywa kupitia faini ambazo zinakusanywa na Trafiki, lakini fedha hizi hazirudi Polisi, zinakwenda Hazina. Kwa hiyo, wazo lake Mheshimiwa Mbunge, nadhani siyo wazo baya labda tunaweza tukalitafakari pamoja kwa baadaye tuone jinsi gani ya kufanya.
Hata hivyo, Polisi ina mikakati mizuri tu ya kuweza kujenga nyumba za ziada kwa ajili ya kutatua changamoto hizo. Nimezungumza mradi wa ujenzi wa nyumba 4,138 hii ikiwa ni awamu ya kwanza, lakini kuna mradi ambao utaweza kuhakikisha kwamba tunahitaji nyumba 3,500 kwa mwaka, kwa maana nyumba 35,000 hadi kufikia mwaka 2025. Hiyo ni mikakati ya muda mirefu.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili, ambapo ameuliza huu mkopo wa Exim Bank ya China, mkopo huu unakadiriwa kufikia shilingi bilioni 500 ambao ni mkopo kutoka Serikali ya Exim Bank ya China ambao vilevile utalipwa na Serikali kulingana na kusainiwa kwa memorundum of understanding. Kwa hiyo, niseme tu kwamba taratibu zitakapokamilika, mkopo huu utakapokuwa tayari ujenzi utaanza mara moja na changamoto ya nyumba inaweza kupungua kwa sehemu kubwa sana.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, ningependa kuuliza maswali mado mawili.
Moja ya kero inayowakuta wafugaji wanapokuwa minadani, inatokea mahali mtu amekwenda kuuza bahati mbaya akiwa pale mnadani hajauza mfugo wake, na anapotoka pale anadaiwa ushuru wakati hajapata hiyo fedha. Sasa nilitaka nifahamu kauli ya Serikali juu ya wale wote ambao wanashindwa kuuza mazao ama mifugo yao katika maeneo hayo?
Swali la pili, je, ni kiwango gani ambacho mtu anapaswa kulipa, kwa sababu kuna watu wanatoka mashambani labda ana mahindi wanakwenda nyumbani kwao kuyatunza. Sasa wakikutana na kizuizi, mtu ana gunia mbili, gunia tatu anaambiwa lazima alipe ushuru hata kwenye yale mahindi ya kutumia.
Je, ipi ni kauli ya Serikali juu ya hili jambo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI (TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika mazoea ya kawaida watu wengine wanapeleka mazao yao sokoni, lakini kwa bahati mbaya wakifika pale wanakosa kuyauza. Ina maana na concept ya ushuru wa mazao, maana inataka mtu akishauza, yule mnunuzi sasa maana yake anatakiwa alipia ule ushuru. Lakini kama hajauza ukimwambia kwamba yule mkulima sasa aweze kutoa ushuru maana yake unambana mkulima. Na kauli ya Mheshimiwa Rais alipokuwa katika kampeni alizungumza wazi kwanza lengo lake ni kutoa huu usumbufu wa ushuru mdogo mdogo ambao unamkabili mwananchi wa kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa zaidi nawahimiza Watendaji wetu hasa katika Halmashauri, jinsi gani wabainishe kwamba katika maeneo yao kuna watu hawa wa kawaida ambao wanaenda kuuza. Kuna mfanya biashara mkubwa ambaye anakuja kuchukuwa mazao pale site, akishachukua lazima alipie ushuru. Lakini yule mtu anayefanya kazi ya kuchuuza kwa ajili ya maisha yake tu hili ni jambo ambalo ni suala zima kuwaelekeza watendaji wetu katika Halmashauri zetu watafanya vipi kuondoa kero hii kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ni kwa kiwango gani, nadhani suala la pili sikulipata vizuri lakini kikubwa zaidi ni nini. Ni kwamba mifugo yote inayopelekwa pale eneo la mnada, ndiyo maana nimesema sijalipata vizuri swali la pili, tuangalie kwamba kwa sababu sheria ndiyo inaelekeza kati asilimia tatu mpaka asilimia tano, sasa mtu anapoenda kuuza mfano ana ng’ombe wake mmoja, ng’ombe wake wawili, ndiyo nimesema hapa utaratibu mkubwa unaotakiwa ni katika Halmashauri husika. Kwa sababu tunajua Halmashauri nyingine zinategemea asilimia karibuni 70 ya mapato yake katika ushuru wa mazao.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jinsi gani kama Baraza la Madiwani pamoja na Watendaji wao watafanya kuangalia mazingira ya kijiografia katika eneo husika ili kuwasaidia wananchi hali kadhalika kuongeza uchumi katika Halmashauri zao.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mchakato mzima wa uzalishaji umeme katika Mto Malagarasi umetumia vilevile fedha za Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC I). Ninataka nifahamu kwamba watu wa MCC wamekuwa wakipeleka fedha zao nyingi kwenye mradi wa umeme, na sasa hivi wamejitoa.
Je, sasa Serikali itupe commitment ya miradi yote ya umeme ambayo fedha zake zilikuwa za MCC, sasa Serikali itatumia vyanzo gani kuhakikisha kwamba miradi iliyopangwa inakamilika kwa wakati.
NAIBU WAZIRI NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba MCC wamejitoa kwenye mradi wa Awamu ya Pili, lakini kazi ya MCC iliyofanyika awamu ya kwanza ilifanyika vizuri, na pesa zote zilitumika. Sasa Serikali inafanyaje.
Mheshimiwa Spika, katika awamu ya mradi huu wa 2016/2017, nichukue mfano kwa Mto Malagarasi shilingi bilioni moja ilikuwa ni fedha za ndani, lakini dola za Marekani bilioni moja pamoja na zingine dola za Marekani bilioni tatu zitafadhiliwa na World Bank pamoja na Benki ya Dunia ya Maendeleo.
Mheshimiwa Spika, pamoja na MCC kujitoa halijaharibika jambo. Ahsante sana.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu yaliyotolewa. Naomba tuweke rekodi vizuri. Hakuna ujenzi wa miundombinu uliokamilika katika Mkoa wa Kigoma hilo la kwanza, Pili, Kampuni ya Kigoma Sugar haifanyi utafiti wa miwa wala BTC hawafanyi utafiti wa chai.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa ruhusa yako naomba swali langu kipengele (a) litafutiwe majibu muafaka kwa sababu hayo siyo majibu yake. Kwa sababu shamba la chai limeachwa limekuwa poro kwa muda mrefu na hakuna utafiti kama huo. Swali la kipengele cha (b) limejibiwa sawasawa. Swali (c)….
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Nsanzugwanko kuna nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kwa hiyo umechagua kusahihisha jibu au utauliza swali la nyongeza? Kwa sababu kama una malalamiko kuhusu jibu umeshayaleta na Kiti kimepokea kitatoa uamuzi. Kama ni hayo tu tumalize au kama unauliza swali la nyongeza uliza swali, suala la kulalamikia jibu tumeshalipata.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nina swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, shamba la Bugaga ambalo Mheshimiwa Waziri anajibu kwamba halikuendelezwa kwa sababu ya ufinyu wa fedha ni kwamba shamba hili hata mwaka huu wa fedha halina fedha. Kwa hiyo ni vizuri tu Wizara waturudishie shamba letu kama wameshindwa kuliendeleza shamba hili la Bugaga tunaomba waturudishie shamba letu ili tulitumie kadri tutakapoona inafaa, kwa sababu inaonekana Serikali haina nia hata kidogo ya kufufu shamba hili la Mbegu.
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri ya swali la Mheshimiwa Nsanzugwanko. Tunaposemea Serikali tunapanga kulifufua shamba hilo hatumaanishi tu kwamba tunategemea bajeti ya Serikali, hata mashamba mengine ambayo tunasemea tunategemea kuyafufua, tumeweka arrangement za tofauti. Kwa mfano, tulisema kwenye shamba la Kitulo tunawategemea ndugu zetu wa Banki ya Kilimo, wiki mbili zijazo wataenda kutembelea shamba hilo waweze kuangalia miundombinu iliyopo na mahitaji ili waweze kuwakopesha nuclear farm pale waweze kuliendeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata kwenye lile shamba la Bugaga, tunategemea kutumia sekta binafsi kama ambavyo tumetumia kwenye lile shamba ambalo liko kule Mbozi na tunategemea pia kutumia ule utaratibu tuliosema kwa wale vijana ambao watakuwa tayari kushiriki kwenye shughuli hizi za kilimo waweze kushiriki kwa arrangement hizo tofauti za kuitumia sekta binafsi na baadae kuuza mbegu zile kwenye taasisi yetu ya mbegu ya Taifa ili iweze kuuza kwa wakulima.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Nsanzugwanko, uridhie tu kwamba tumeshaanza utaratibu wa kuweza kulifufua na kulifanyia kazi na hiyo itaenda sambamba na utaratibu wa kuwarejesha vijana kwenye shughuli za kilimo, sawa na kuwafanikisha vijana kuyafikia masoko kama swali lile lililoulizwa na Mheshimiwa Esther Mmasi ambalo linatupatia masoko mengine ambayo vijana wanaweza wakafikia wakafanya kazi hiyo. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge baada ya Bunge kuwa limeisha, natarajia kuzungukia kwenye shamba hilo na yeye atakuwepo na tutakuwa pia na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu ikiwa ni mikakati ya kwenda kwenye utekelezaji wa jambo hili ambalo tunalisema.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, ukiliangalia jibu unaona kweli fupi na linaridhisha.
Mheshimiwa Spika, nina maswali madogo mawili ya nyongeza, ni nini kinachochelewesha Wizara kuchukua hatua ya kujibu barabara zote ikiwemo hii ya Kakozi - Kapele mpaka Ilonga, kupata majibu mapema iwezekanavyo tofauti na jibu ambavyo limewekwa hapa?
Jambo la pili, barabara hii tulikuwa tunaiombea kupandishwa hadhi karibu mara tatu kukamilisha vigezo, mwaka 2011, mwaka 2013 na mwaka 2015 kupitia Road Board ya zamani tulipokuwepo ya Mkoa wa Mbeya. Wizara mlitushauri tuombe special funds kwa ajili ya kuikarabati barabara hii, tumeomba fedha na mpaka sasa hazijaja.
Kwa nini mnatushauri tuchukue maamuzi ambayo hamuwezi kutekeleza? Ahsante.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, ni kweli inachukua muda mrefu, baadhi ya kati, kupandisha hizi barabara kwa sababu kuna mchakato lazima na tujiridhishe whether barabara hiyo imekidhi viwango au sivyo. Vinginevyo kila maombi tunayoletewa kama tutazipandisha itakuwa hatufanyi sahihi. Kuna utaratibu ambao umewekwa na vigezo ambavyo vimewekwa kuhakikisha kwamba barabara hiyo inakidhi vigezo hivyo ndiyo ipandishwe.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa barabara ya Mheshimiwa Silinde, ni kweli barabara hii inakidhi. Kwanza barabara hii inaunganisha mpaka baina ya Tanzania na Zambia; pili inaunganisha Mkoa wa Rukwa ambao kwa upande wa Mkoa wa Rukwa barabara hii ni ya Mkoa lakini kwa upande wa Mkoa wa Songwe ni ya Wilaya (District Road). Kwa vile tutaipandisha na baada ya kuipandisha, fedha hizo tutatoa ili kuikarabati barabara hii.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Pamoja na uhaba wa Maafisa wa Ardhi na uhaba wa fedha, lakini zoezi la kupima ardhi nchini limekuwa likisuasua na mahitaji ya wananchi kujenga yamekuwa yakiongezeka, kwa hiyo ukiangalia katika hali ya kawaida wananchi wengi wamekuwa wakijenga katika maeneo ambayo hayajapimwa, sasa nataka kauli ya Serikali, ipi ni kauli ya Serikali juu ya wananchi wote wanaojenga katika maeneo ambayo hayajapimwa na Serikali bado inasuasua kwenye kupima maeneo hayo ya ardhi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kasi ya wananchi kujenga ni kubwa kuliko speed ya Serikali katika kupima maeneo, na ni maeneo mengi ambayo kwa sasa yamekaliwa katika mpangilio usio sahihi na ndiyo maana Wizara imeliona hili na tukaja na programu ile ya miaka mitano ya kuhakikisha kwamba wale ambao wamekuwa na speed kali kuliko Serikali tunajaribu kurasimisha maeneo yao ili wakae katika utaratibu mzuri waweze kutambuliwa na Serikali iweze pia kupata kodi zake kupitia katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, lakini katika kuona hili pia tunalifanyia kazi, Serikali imesajili makampuni, ina makampuni karibu 55 ambayo yanafanya kazi ya upimaji katika maeneo, na upimaji wao wanaofanya wanafanya kulingana na mipango iliyoko katika maeneo hayo kwa maana ya ile mipango miji kwenye yale maeneo, masterplan zao ambazo wameziweka pale.
Kwa hiyo kikubwa tunachosema, kasi ya wananchi ni kubwa, Serikali ina speed ndogo na eneo lililopimwa ni dogo, kwa hiyo tunaomba Halmashauri zilizotayari ziyatumie haya makampuni ambayo tumeyabainisha katika suala zima la upimaji, na nilisema pia wakati najibu swali hili tarehe tisa, nikasema orodha tayari tunayo, Halmashauri yoyote iliyo tayari tuwasiliane ili tuwape ile orodha waweze kufanya mawasiliano.
Mheshimiwa Spika, lengo letu ni kuhakikisha Miji imekaa vizuri na imepangika na tunawaomba wananchi, tunawasihi wasianze kuvamia maeneo ovyo sasa hivi kwa sababu kadri tunavyozidi kuweka mikakati ndivyo jinsi ambavyo wao watakuwa katika hatua nzuri ya kuweza kupangiwa maeneo yao, kwa hiyo wasikimbie sana kwa sababu tayari kama Wizara tunaamua kufanya kazi hii kwa weledi mkubwa.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Suala la idadi ya wanafunzi ambao wametokana na bajeti linaendana na sifa za wanafunzi wanaotakiwa kujiunga na vyuo vikuu. Ningependa kuuliza swali dogo tu, kwamba, sasa hivi Serikali imetoa kauli mbili tofauti, mwezi Julai iliweka vigezo vya wanafunzi kujiunga na Chuo Kikuu vya GPA ya 3.5 kwa watu wa diploma, si zaidi ya hapo. Hata hivyo, juzi wametoa tena tamko lingine la GPA ya 3.0 kwa watu wa ordinary diploma. Je, Serikali itueleze hapa, ni kwa nini inawasumbua wanafunzi katika kipindi hiki ambacho wanafunzi wengi walikuwa wameshakata tamaa na hawaku-apply katika Vyuo Vikuu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, kama ambavyo siku Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania analihutubia Bunge; alisisitiza kwamba Awamu hii ya Tano, jukumu lake kubwa litakuwa ni kuongeza ubora. Vile vile lazima ikumbukwe kwamba, Serikali kwa kushirikiana na wananchi imefanya kazi kubwa ya kuwezesha wanafunzi wengi kusoma na kiasi kwamba tunao wengi wenye sifa za ufaulu wa juu. Hiyo imejidhihirisha wazi hata katika udahili wa mwaka huu wa Vyuo Vikuu, waombaji ni wengi na waliofaulu ni wengi sana kiasi cha kupandisha zile points ili tuweze kuendana na haki katika kuwachukua.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika suala hilo katika maeneo hayo pia kuna ushindani mkubwa, lakini Wizara kila wakati inaangalia kama hao watu wenye sifa hizo itaonekana kwamba hawapatikani hapo ndipo tunaweza tukafikiria zaidi namna ya kusema tushuke chini, lakini kama wanapatikana basi hamna haja ya kumchukua mtu ambaye ana ufaulu wa chini ukamuacha mtu ambaye ana ufaulu wa kiwango cha juu.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kabla ya kuanza kwa Mradi wa REA III, kuna baadhi ya maeneo Miradi ya REA I na REA II bado haijakamilika ikiwemo katika baadhi ya maeneo ya Jimbo la Momba. Sasa tunataka assurance ya kukamilisha miradi kwanza ya REA I na REA II kabla ya hiyo REA III, lini itakamilika miradi hii, REA I na REA II? Ahsante Sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Silinde kwanza nakupongeza, Miradi ya Awamu ya Pili ya REA imeshakamilika na mahali ambapo Mradi wa REA ikitokea kwamba haukukamilika ni vijiji ambavyo sasa vitaanza kutekelezwa katika Miradi ya REA Awamu ya Tatu.
Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Silinde kama kuna kijiji specific ambacho hakijakamilika kupitia mradi wa pili, naomba tukae na tuanze kutekeleza hata kabla ya kuingia Mradi wa REA Awamu ya Tatu. Na vijiji vyote ambavyo havikukamilika kupitia miradi ya REA Awamu ya Pili, ambavyo havijakamilika, vitaanza kukamilika kwanza ndio tunaingia kwenye REA Awamu ya Tatu. Kwa hiyo, vijiji vyote Mheshimiwa Silinde katika Jimbo lako la Momba vitapatiwa umeme wa uhakika kupitia Mradi wa REA Awamu ya Tatu.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, changamoto katika sekta ya afya ukiacha vifaa tiba, sasa hivi pameibuka changamoto kubwa mpya, ambao wananchi wanakuwa wakilipa bima zao za afya, wanakwenda katika hospitali, wanaandikiwa tu dawa lakini wanashindwa kupatiwa pale. Kwa hiyo, nilitaka nijue ipi ni kauli ya Serikali kwa wananchi ambao wamelipia bima zao lakini hawapati matibabu katika hospitali husika?
shimiwa Spika, ningependa kujibu swali la Mheshimiwa Silinde kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mwananchi yeyote ambaye ana kadi ya Bima ya Afya anatakiwa kupata huduma zote za afya bure ikiwemo vipimo. Nikiri kwamba katika baadhi ya vituo vya afya vya umma, hasa nadhani unazungumzia CHF tuna changamoto ya upatikanaji wa dawa zote katika vituo vyetu, ndiyo maana Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya una maduka ya dawa ambapo kama umeiokosa ile dawa katika hospitali husika unatakiwa kwenda katika duka la dawa ambalo limetambuliwa na NHIF.
Mheshimiwa Spika, kwa CHF kidogo hapo niseme kuna changamoto. Kwenye mikoa ambapo tumeenda kwenye Bima ya Afya iliyoboreshwa wao wanaweza wakapata dawa katika maduka ya dawa, kwa hiyo tunaifanyia kazi changamoto hii.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante sana. Tatizo la viongozi kukosa semina elekezi juu ya masuala ya uongozi yamekuwa yakionekana kuanzia ngazi za juu, kwa mfano mdogo tu hapa katika swali lililopita unakuta Mawaziri wamejibu, Naibu Waziri naye anajibu kwa hiyo, protocol inakuwa inaonekana pale haijafuatwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, suala langu ninalotaka kujua ni kwamba taratibu kama hizi, viongozi ambao wanakosa semina za mafunzo elekezi na contradiction inaonekana ndani ya Bunge lako Tukufu…
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilitaka nijue makosa kama haya yataendelea mpaka lini kwa viongozi ambao hawana semina kama Mawaziri? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na semina elekezi au mafunzo elekezi kabla watu hawajaingia katika madaraka nimeshaeleza awali.
Lakini pili, kwa mwaka huu wa fedha peke yake Taasisi ya Uongozi imetoa mafunzo kwa viongozi 544, lakini pia tumekuwa tukitoa mafunzo kwa Mawaziri, tumekuwa tukitoa mafunzo kwa Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na nafasi nyinginezo na tutaendelea kufanya hivyo kila wakati itakapobidi.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kutokana na ukubwa wa tatizo la maji, Bunge lako liliidhinisha Sheria hapa ya kuweka zuio la fedha ambazo Mheshimiwa Naibu Waziri hapa amekiri kwamba fedha zipo, lakini maji hakuna. Sasa swali ambalo nataka watupatie majibu, tumewapa fedha, lakini kwenye miji na vijijini kwetu kule maji hakuna. Nini kinachowafanya wanakwamisha miradi ya maji mpaka sasa hivi inashindwa kukamilika? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, ni kweli tulipitisha Sheria ya Mfuko wa Maji; na fedha hizi huwa zinatolewa kila mwezi; lakini ili fedha hizi zitumike tulipeleka mwongozo kwenye Halmashauri zetu za Wilaya. Pamoja na mwongozo, tumefanya semina nchi nzima na Wakurugenzi pamoja na Wahandisi wa Maji kwamba fedha hizi zitatolewa kwa mfumo wa certificate. Kwa sababu tulishakubaliana katika bajeti ya mwaka huu kwamba kwanza tukamilishe miradi inayoendelea.
Mheshimiwa Spika, nimetembelea baadhi ya Halmashauri, unakuta fedha wanazo zilizo-carry forward kutoka mwaka uliopita, lakini hawajafanya jambo lolote, wanasubiri wapelekewe fedha. Mwongozo tumewapa na tumewaelekeza. Kwa hiyo, kuna baadhi ya Halmashauri ziko na ile hali ya ufanyaji kazi wa kimazoea, hawataki kwenda na kasi ya Awamu ya Tano tunavyotaka matokeo.
Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge, awe karibu sana na Halmashauri yake kuweza kuona kwa nini hiyo miradi haiendelei? Kwa sababu, wakileta certificate, hakuna certificates ambazo zimebaki, tumeshapeleka fedha. Sasa hivi tuna certificates chache sana. Kila mwezi zikija, tunapeleka fedha. Kwa hiyo, nashauri tukae tuweze kuona kwa Halmashauri yako hasa ni nini kinachoendelea?
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Hili swali la ujenzi wa daraja ninaliuliza leo ni mwaka wa saba mfululizo nikiwa ndani ya Bunge hili Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada ambazo nimeanza kuziona ambazo zinaweza kuzaa matunda hivi karibuni, ni kwamba wametangaza tender tarehe 11.01.2017; sasa ninachotaka kujua ni kwamba, ili tupunguze maneno maneno mengi, je, Serikali itakamilisha lini utaratibu wa tenda ili ujenzi huo uanze? Wananchi wangu kule wameshachoka story hizi wanataka waone daraja likiwa limejengwa kwahiyo hicho ndiyo kitu cha kwanza, commitment ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la pili; ni kwamba palipokuwa na ahadi ya ujenzi wa daraja ilikuwa inaambatana na muendelezo wa ujenzi wa barabara ambayo Mheshimiwa Haonga alikuwa ameuliza katika swali la nyongeza kutokea pale Kamsamba mpaka Mlowo kilometa 166.
Sasa ninachohitaji kujua ni kwamba wakati wa awamu ya nne Waziri Mkuu alipokuwa analijibu hili swali alisema umeingizwa katika mradi wa MCC 3 lakini bahati mbaya wale watu wa Marekani wa MCC 3 walishajitoa katika kuhudumia miradi ya ndani ya nchi yetu. Sasa, je, Serikali ile miradi ambayo iliondolewa na MCC katika Serikali hii ya Awamu ya Tano itatekelezwa vipi ili kuhakikisha kwamba daraja linakamilika na liendane na ujenzi wa lami? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi Mheshimiwa Mbunge na ninaamini ni kwa niaba ya wananchi wake, wanahoji udogo udogo au utaratibu unaotumika, kwamba kasi yake kama ya konokono. Mimi nikuhakikishie, hii ni Serikali ya Awamu ya Tano, Serikali hii iko tofauti, Serikali hii imewaahidi wananchi sehemu mbalimbali na umeshaanza kuona sehemu mbalimbali magoli yanaanza kufungwa. Ninakuhakikishia na goli lako litafungwa, daraja na hizo barabara ninazoongelea kabla ya miaka hii mitano haijakwisha. Tuache utaratibu huu wa kitaalam ukamilike na nina uhakika kwa kuwa wameshaanza haitachukua muda kuikamilisha hii kazi ya usanifu na mimi mara baada ya hapo, kwa kuwa fedha tayari tunazo nitahakikisha nalisimamia hili eneo likamilike na hasa kwa sababu mwenzako, jirani yako; na mimi nawasifu sana ninyi Wabunge wawili, wewe na Mheshimiwa Ignas Aloyce Malocha. Ninawasifu sana kwa ushirikiano mnaotumia katika kuhakikisha Daraja la Momba linajengwa.Ni daraja linalohudumia watu, halina Silinde wala halina Ignas Malocha. Mheshimiwa Ignas Malocha anakuja ofisini, Silinde anauliza hapa, wote wanawalenga wananchi wa Momba pamoja na watu wa Kwela.
Mimi niwahakikishie, kazi hii tutaifanya kwa umakini na kama ambavyo tumekuwa tukiwaahidi tutaikamilisha kwa wakati muafaka kabla hiki kipindi chetu hakijaisha.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, natambua jitihada ambazo zimefanyika kwenye hii barabara ikiwemo ujenzi wa daraja la Momba.
Mheshimiwa Spika, nataka tu niulize swali dogo, barabara hii imekuwa katika ahadi, Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete mwaka 2009 alipokwenda kwenye Halmashauri ya Momba aliweka ahadi ya kujenga hii barabara. Mheshimiwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipokwenda kule vilevile alitoa ahadi ya kuhakikisha hii barabara inakamilika kwa sababu hili bonde linaunganisha Mikoa mitatu na ni muhimu kwa mazao yetu.
Mheshimiwa Spika, Rais wa Awamu ya Tano Mheshimiwa John Pombe Magufuli alisema katika Serikali yake hataki kusikia mambo ya michakato, ahadi, tunatafuta fedha, alisema mwenyewe. Watu wa Mikoa wa Songwe, Rukwa pamoja na Katavi tumekuwa tukilia kila mwaka ni kwa nini sasa mwaka huu msiweke commitment katika barabara zote mkatenga tu fedha kuelekeza katika Mkoa huu wa Rukwa, hususan hii barabara kutoka Mlowo mpaka Kamsamba na Kilyamatundu kwa kiwango cha lami ili tuache
kuwasumbua tena katika kipindi cha miaka mitano. Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, nikuhakikishie barabara ya Mbande – Kongwa tunaijenga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kumhakikishia
Mheshimiwa Silinde kwamba daraja la Kamsamba nadhani maswali yake yote ya nyuma yalikuwa yanaelekea hapo. Umeona kwamba sasa hii siyo ahadi tena tunatekeleza, siyo michakato, tunatekeleza. Kabla hujatekeleza taratibu za usanifu, upembuzi lazima zifanyike vinginevyo huwezi ukatekeleza. Kwa hiyo, hatua ya kwanza ya kufanya usanifu wa kina na upembuzi yakinifu tunaianza kwa kutafuta fedha na mara tutakapopata fedha, kazi hii tutaanza. Suala siyo
michakato hapa tutatekeleza kama tulivyoahidi.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Kwa kuwa tatizo la maji limekuwa ni kero ya nchi nzima, ni kwa nini sasa Serikali, hususan kupitia kwenye bajeti ya Bunge hili, isikubali kutengeneza Wakala wa Maji Vijijini ambaye atasaidia kupeleka maji vijijini kote kama ambavyo tumefanya katika REA ambapo kwenye suala la umeme wameweza kufanikiwa vizuri. Kwa nini wasifanye hivyo ili maji yafike hata kule Momba, Chitete, pamoja na vijiji vingine? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge lako Tukufu katika bajeti iliyopita liliagiza Wizara ya Maji ianze taratibu za kuunda Wakala wa Maji nchini, tayari tumeshaanza kazi hiyo na wakati wowote itawasilishwa hapa kwa ajili ya kupewa mjadala na kupitishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo suala hilo tayari
linafanyiwa kazi.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwenye majibu ya Mheshiwa Waziri amesema, endapo mtumishi hajaridhika na hatua za kinidhamu alizochukuliwa, akate rufaa. Sasa endapo mtumishi huyo ametumbuliwa na Mheshimiwa Rais na hajaridhika na hayo matokeo, wapi achukue hatua za kuja kukata rufaa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza Mheshimiwa Silinde ameuliza swali zuri sana; na kama atakuwa amefuatilia hata katika hotuba yangu ya bajeti ya Ofisi ya Rais (Utumishi), ziko kesi mbalimbali ambazo hata Ofisi ya Rais (Utumishi) pia tunashitakiwa. Wako ambao wanafungua kupinga maamuzi ya Mheshimiwa Rais, wako ambao wanafungua kesi kupinga maamuzi ya Katibu Mkuu Kiongozi, lakini pia
katika Tume yetu ya Utumishi wa Umma ambayo ni mamlaka yenye Mamlaka ya Urekebu wamepokea kesi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, katika mwaka huu wa fedha tu peke yake, zaidi ya watumishi wa umma 76 wameweza kukata rufaa katika Tume ya Utumishi wa Umma na endapo hawataridhika, bado tunacho Kitengo cha Rufaa chini ya Mheshimiwa Rais pia (Public Service Appeals) wanaweza pia wakakata rufaa nyingine. Kwa hiyo, namhakikishia tu Mheshimiwa Mbunge kwamba taratibu zipo na zinafuatwa na ziko wazi kabisa na wako ambao hata wanajikuta walikata rufaa dhidi ya Mheshimiwa Rais na wakaja kushinda endapo kama kuna taratibu inaonekana hazikufuatwa.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Utumishi kwa majibu mazuri sana. Nilitaka kuongezea, kuna moja ambalo limewataja Wakuu wa Mikoa
na Wakuu wa Wilaya kuchukua hatua za kuwasimamisha au kuwafukuza kazi watumishi wa umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma kifungu cha (5) cha Sheria ya Tawala za Mikoa, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya ndio wawakilishi wa Serikali Kuu kwenye maeneo yao. Ukisoma pia kifungu cha 87 cha Sheria ya Mamlaka za Serikali za Mitaa, kinawataja hawa na kwa ajili ya usahihi wa nukuu, napenda nisome kwa sababu wakati mwingine tunauliza swali lile lile kila siku. Bahati mbaya imeandikwa kwa Kiingereza, inasema hivi; “In relation to the exercise of the powers and performance of the functions of the Local Government Authorities confered by this Act, the role of the Regional Commissioner and the District Commissioner shall be to investigate the legality when questioned of the actions and decisions of the Local Government Authorities within their areas of jurisdiction and to inform the Minister to take such other appropriate action as may be required.”
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukisoma kifungu hiki unaona kabisa kwamba wao kuchukua hatua zozote zile, ziwe za kiutumishi ni sahihi, isipokuwa utaratibu aliouzungumza Mheshimiwa Waziri wa Utumishi ndiyo unaotakiwa.
Kwa mfano, Mkuu wa Mkoa anaposema wewe hufai, umefanya makosa haya, akasema publicly, siyo ndiyo kafanya tendo hilo la kumsimamisha au kumuadhibu yule mtumishi, anachofanya pale, baada ya tamko lile, sasa Mamlaka ya Nidhamu ya mtumishi husika ndiyo inachukua hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, katika level ya Halmashauri, sasa Mkurugenzi atamwandikia barua kama ni ya kumsimamisha au kumtaka atoe maelezo fulani kulingana na maagizo ya Mkuu wa Wilaya, au Mkuu wa Mkoa atafanya hivyo. Kwa ngazi ya Mkoa, RAS ndio Mamlaka ya Utumishi, naye anaweza kuagizwa na kufanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, siyo kutamka tu kwa Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya, ndiyo tayari basi yule amemchukulia hatua za kinidhamu.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kuuliza maswali madogo ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoka Masasi mpaka Nachingwea ni kama kilometa 42 na kutoka Masasi mpaka Ndanda ni kama kilometa 40; na kwenye bajeti iliyokuwa imeitengwa ambayo imeombwa mwaka 2017/2018 kama shilingi bilioni tatu, ni fedha ndogo ambayo haiwezi kukidhi kumaliza barabara hiyo. Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kukamilisha barabara hiyo kwa kiwango cha lami kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge alikuwa ameomba, kwa sababu fedha iliyotengwa ni ndogo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali dogo la pili la nyongeza ni kwamba, matatizo ya Jimbo la Ndanda yanafanana kabisa na Jimbo la Momba kule; sasa naomba niulize kwamba barabara ya kutoka Kakozi kwenda Kapele mpaka Namchinka kilometa 50.1 imepandishwa hadhi na Wizara yako, lakini mpaka sasa haijawahi kuhudumiwa na hiyo barabara ni mbovu. Ni kwa nini barabara hizi mnazipandisha hadhi na hamzihudumii kwa wakati? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu udogo wa fedha, kitu ninachojaribu kumweleza ni kwamba katika ule mpangilio wa kutekeleza ahadi sasa tumefikia kuanza utekelezaji wa ahadi ya barabara hii na tumeanzia na hizi fedha ndogo kutokana na bajeti tuliyopata mwaka unaokuja wa 2017/2018. Nimhakikishie, katika miaka yote inayofuata, barabara hii itakuwa inaendelea kupewa fedha za kutosha ili hatimaye katika kipindi chetu tulichoahidi, barabara hii itakuwa imekamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu barabara ya Kakozi – Kapele na kuendelea ambayo imechukuliwa na TANROAD, nimhakikishie tu kwamba tutahakikisha TANROAD inapanga fedha za kutosha kwa ajili ya utekelezaji wa barabara hii kama ilivyokusudiwa kwa kupandishwa hadhi.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa tatizo la maji nchini ni kubwa na Tanzania ni moja ya nchi ambayo tuna sifa ya kuwa na Maziwa makubwa pamoja na mito mingi; yaani ni nchi ya Maziwa Makuu tofauti na zile nchi za kwenye jangwa kule kama Libya ambao wana maji zaidi ya asilimia 80. Sasa ni kwa nini Serikali isione aibu ya kushindwa kutatua hili tatizo kwa muda mrefu ilhali tuna maji mengi? Sasa hivi ukiangalia moja ya sifa ya nchi yetu ambayo tumekuwa tukijitamba na Serikali mmekuwa mkijisifu kwamba mmekuwa mkikusanya mapato mengi. Ni kwa nini sasa…
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejitahidi, kila mwaka inatenga fedha na inazipeleka kwenye Halmashauri. Ni kazi ya Halmashauri kuhakikisha inatumia hiyo hela kuwapatia wananchi maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeandaa kitabu kinachoonesha bajeti iliyotengwa katika Halmashauri na kiasi cha fedha ambacho Halmashauri imetumia. Halmashauri nyingi zimeshindwa kutumia fedha zilizotengwa kwenye bajeti. Sasa lawama hii iende kwa nani wakati sisi wenyewe ni Madiwani kwenye hizo Halmashauri?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba nchi yetu ina maji ya kutosha kilichobaki ni kuweka fedha na kusambaza na Serikali inaendelea kuweka fedha. Imeweka fedha mwaka uliopita na mwaka huu fedha tayari ipo kwa ajili ya Halmashauri kuhakikisha kwamba mnatumia zile fedha kuwapa wananchi maji na Wizara ya Maji na Umwagiliaji imeshatoa maelekezo ya jinsi ya kufanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niwaambie Waheshimiwa Wabunge Halmashauri yangu tayari imeshatengeneza mpango kazi leo tarehe 3 Julai, hebu jiulize wewe kwenye Halmashauri yako kwenye bajeti mpya je, mpango kazi umeshaanza kufanya? Ndugu zangu naomba sana bajeti ipo tusimamie Halmashauri waweze kutekeleza miradi ya maji hakuna haja ya kulaumiana.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri kukubali kwamba watafanya mazungumzo na mmiliki ambaye ni Chama cha Mapinduzi, shule hii ni muda mrefu sana imefungwa, karibu miaka kumi hamna mwanafunzi anayesoma pale. Ni kwa nini msione sasa ni wakati muafaka wa kuirudisha kwa wananchi ili tuweze kuitumia?
Mheshimiwa Spika, ombi letu la pili, tunaomba shule hii tuitumie kwa ajili ya kidato cha tano kwa sababu Halmashauri ya Wilaya Momba haina shule ya kidato cha tano? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema shule hii inamilikiwa na Chama cha Mapinduzi kupitia Jumuiya yake ya Wazazi. Kwanza naishukuru Jumuiya ya Wazazi kwa sababu imefanya intervention kubwa kwa nchi hii kujenga shule mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kweli naomba niweke katika kumbukumbu kwamba Jumuiya ya Wazazi kupitia Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, alitusaidia sana kupatikana kwa Shule ya Umumwani, ambayo Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo alikuja kutukabidhi pale na juzi nimeenda kule Kagera watoto wanasoma pale. Kwa hiyo, tunaishukuru sana jumuiya hiyo kwa kazi kubwa sana inayofanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama Serikali, hatuwezi kuirudisha tu hivi hivi, isipokuwa kuna utaratibu wa negotiation, pale Jumuiya ya Wazazi itakapoona inafaa, kwa sababu jukumu lake kubwa ni kuwasomesha watoto wa Tanzania kwa mbinu muafaka, basi inawezekana tukaongea na Mwenyekiti pale ambaye nadhani ni Mjumbe wa Kamati Kuu, aangalie nini cha kufanya, aidha kuiboresha mwenyewe ili ichukue watoto ama kuangalia utaratibu kama alivyotusaidia kule Umumwani kwa lengo la kuwasaidia Watanzania. Hili siyo jambo baya sana.
Mheshimiwa Spika, katika suala zima la kuifanya shule hii iwe ya Kidato cha Tano na cha Sita, nadhani hili ni wazo zuri na Jumuiya ya Wazazi pale watakapoona, aidha wenyewe kuifanya na kuiboresha miundombinu yake iwe ya kidato cha tano na cha sita kwa Tanzania, ama kuirudisha Serikalini. Mwenyekiti wa jumuiya hiyo yuko humu, atatuelekeza nini tufanye kwa muktadha wa kusaidia wanafunzi na watoto wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Pamoja na majibu yanayoridhisha ya Mheshimiwa Naibu Waziri, mimi nilikuwa tu nataka niweke msisitizo kwenye hili jambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba, Mheshimiwa Rais amekuwa akirudia na wewe leo hapo umejaribu kuweka msisitizo, lakini bado kuna shida kule chini kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kukataa hili agizo kwa maana circular bado haijafika.
Sasa nataka nijue tu kabisa kwamba, je, circular hiyo inahusu ile mizigo ya wakulima ama wananchi wa kawaida wenye chini ya tani moja, kama Rais alivyoagiza kwamba ukisafirisha mzigo kutoka eneo moja kwenda lingine, chini ya tani moja hutakiwi kulipa ushuru; kwa hiyo, nilitaka nijue kama circular na yenyewe inazungumzia hivyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetangulia katika jibu langu la msingi kwamba tozo hizi ziliondolewa ndani ya Bunge lako Tukufu na ndani ya Bunge hili tulisema ni tozo zipi ambazo zinafutwa kwa sababu ni kodi kero. Hakuna by-law yoyote kwenye halmashauri ambayo inazidi Sheria ambayo inatungwa na Bunge lako Tukufu. Kwa hiyo, nazidi kuomba na nawasihi wakurugenzi wote hawana option nyingine zaidi ya kutekeleza Sheria ambayo imepitishwa na Bunge lako Tukufu.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya kuridhisha ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali madogo mawili. Swali la kwanza, miradi ya umeme ya REA III imezinduliwa karibu nchi nzima katika kila Mkoa, lakini utekelezaji wake mpaka sasa hivi haupo, isipokuwa ipo katika mipango kama hivi ambavyo inaonesha. Nini ambacho kinasababisha au kimesababisha kucheleweshwa kwa miradi ya REA III kuanza kukamilika tofauti na iliyopo katika maandishi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili ni kwamba pamoja na majibu yake, Miradi ya REA tuliiwekea zuwio la fedha, yaani tuli-ring fence fedha zake ambazo zilitakiwa zisiguswe, lakini mpaka sasa hivi miradi hii haitekelezeki kwa sababu hizi fedha hazieleweki mahali ziliko.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu nataka niulize je, hizi fedha ambazo tumezi-ring fence kwa ajili ya utekelezaji wa hii miradi, kwa nini hazitumiki kutekeleza mradi ikizingatiwa kuna fedha ambazo tunakata katika mafuta shilingi 50 kwenye kila lita ya mafuta? Kwa nini zinashindwa kutumika kwa ajili ya kumalizia hii miradi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli miradi hii ya umeme vijijini ilizinduliwa mwezi wa Sita mwaka 2017. Naomba nimhabarishe Mheshimiwa Mbunge kwamba wakandarasi wote ambao waliteuliwa takribani 27 tulikutana nao tarehe 13 Januari, 2018 hapa Dodoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa miradi una kazi mbalimbali. Kwanza, walikuwa wana-survey na mnakumbuka Waheshimiwa Wabunge wengi mlileta mapendekezo, maombi ya vijiji mbalimbali, kwa hiyo, lazima survey ifanyike.
Pili, baada ya survey lazima kuwe na michoro, lakini nimthibitishie kwa Mkoa wake wa Songwe na Wilaya yake ya Momba, mkandarasi wake ameshaagiza vifaa na kesho tarehe 31 Januari na tarehe 01 TANESCO wanaenda Mkoa wa Arusha kuangalia zile transfoma. Kwa hiyo, ni wazi kwamba miradi hii inatekelezeka, lakini zipo hatua mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, niongezee kwa kusema pia, vipo vijiji ambavyo vimeshawashwa umeme REA hii ya III. Kwa hiyo, inategemea Mkandarasi na huo muda. Kwa mfano, Geita kuna vijiji vimewaka; Mwanza Halmashauri ya Bumbuli pia umeme umewaka REA hii ya III. Kwa hiyo, miradi inaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili alikuwa anasema kwamba, vipi kuhusu pesa zake za miradi hii ya umeme vijijini? Ni kweli nalishukuru Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Bunge hili iliwekwa tozo maalum kwenye mafuta na mfuko huo kweli umelindwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niishukuru Wizara ya Fedha kwamba pesa zimekusanywa, zimewasilishwa na mpaka sasa tumeshapata shilingi bilioni 170.
Kwa hiyo, pesa kwenye miradi hii siyo tatizo. Tatizo ambalo lipo, changamoto tuliyokuwa tunaiona ni hawa wakandarasi kujipanga kwa mujibu wa wakati na ratiba wanavyozipanga. Ndiyo maana baada ya kuona hilo tatizo, tumekutana nao hapa Dodoma na tumewapa maelekezo kwamba mwisho tarehe 28 Februari, wakandarasi wote waanze kazi. Siyo kazi ya survey, kazi ya kuweka nguzo na miundombinu mingine ili miradi itekelezeke.
Mheshimiwa naibu Spika, nilithibitishie Bunge lako, miradi hii muda wake, hii awamu ya kwanza hii ni kipindi hiki mpaka Aprili, 2019.
Kwa hiyo, niwatoe hofu. Kwa kuwa pia tumeweka usimamizi mzuri, kila mkoa tumemtaka engineer mmoja asimamie, kila Wilaya kuwe na engineer mmoja kwa ajili ya miradi ya REA tu. Kwa hiyo, ninaamini, hata kasoro ambazo zilijitokeza kwa miradi ya REA awamu nyingine, kwa Awamu hii ya III itaenda vizuri na itakamilika kwa wakati. (Makofi)
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri kujaribu kueleza sheria mbalimbali za kudhibiti fedha za umma, lakini kuna changamoto moja kubwa. Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali ndio mtu pekee ambaye amekuwa akisimamia na kudhibiti hili suala la umma na kutuonesha wapi kwenye mapungufu na matumizi sahihi. Lakini Serikali imekuwa haipeleki fedha za kutosha kwa CAG ili aweze kudhibiti hizi fedha.
Je, Serikali haioni kwamba yenyewe ndio yenye jukumu la kuzorotesha Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kushindwa kufanya kazi yake ili tuweze kujua hayo mapungufu, kwa kushindwa kupeleka hizo fedha?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu swali la pili la Mheshimiwa Hasunga kwamba Bunge hili hata wiki haijapita tangu tumepitisha Bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango, ndani yake ikiwepo bajeti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na sote tumeona commitment ya Serikali yetu katika kuiongezea ofisi hii bajeti ya kutosha. Katika taasisi zote za Serikali ni taasisi hii tu ambayo imepata bajeti yake kwa mwaka huu kwa zaidi ya asilimia mia moja. Hii ni commitment ya kutosha kabisa na tunahakikisha kwamba itaendelea kuimarishwa kama nilivyosema. (Makofi)
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri hapa amesema wataongeza kipato kwa Madiwani ikiwa mapato ya Serikali yataongezeka; lakini kwa mwaka sasa Serikali imekuwa ikitangaza kuongezeka kwa mapato, yaani makusanyo yamekuwa makubwa, ninachokitaka badala tu ya kuwalipa posho kwa nini sasa Madiwani wasilipwe mishahara kama tunavyolipwa sisi Wabunge ili wafanye kazi hiyo kwa moyo. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Menyekiti, Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo la kulipwa mshahara na posho; kwa sababu kuna nafasi mbalimbali zimetengwa kwa utaratibu wake; kwa utaratibu Madiwani wanalipwa posho sawasawa na Wenyeviti wa Vijiji, kwamba kuna posho ile ya asilimia 10 kwa Wenyeviti wa Vijiji, lakini kuna posho maalum ya Madiwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wazo la mshahara, hili tuseme ni wazo tu ambalo Wabunge wanatoa kuona jinsi gani jambo hili linaboreshwa. Hata hivyo, mara nyingi Serikali inafanya tathmini katika maeneo mengi zaidi na hasa kuangalia wage bill ya Serikali itakuwaje baadaye endapo Madiwani wataingizwa katika eneo hilo kwa wakati mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hiyo nasema kwamba ni mawazo au chemchem ambayo inasaidia kuboresha ili unapofika wakati tuangalie jinsi ya kufanya; lakini kwa sasa hivi utaratibu tunaokwenda nao ni utaratibu wa posho kwa mujibu sheria.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa, swali lilivyoulizwa na majibu ni kwamba Chuo hicho ambacho kinataka kuanzishwa kipo katika Jimbo la Momba ambalo mimi naongoza. Sasa nataka tu nimuulize pamoja na ahadi hii ambayo imetolewa na tunaamini kwamba kitaanza hivi karibuni na nina uhakika ni mwaka huu wa fedha. Je, endapo hicho anachokizungumza kisipotekelezwa ni hatua gani tumchukulie yeye kama Waziri kuwadanganya wananchi wa Momba? (Makofi/Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi ninavyojibu lengo langu sio kusherehesha, ni lengo la kueleza Serikali ni mikakati gani inachukua. Kwa hiyo huu ni mkakati ambao hatujalazimishwa bali tunaona ni wajibu wetu kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma inayostahili. Ndiyo maana tunataka kuanza na mafunzo hayo ya kawaida wakati mikakati mingine inaendelea. (Makofi)
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante sana, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri kuwa ya jumla kwa sababu swali nililouliza nilitaka nijue kama Momba kitapatikana kiwanda, kitajengwa au hakitajengwa. Kwa hiyo, jibu ni kwamba wananchi wa Momba huko mnakonisikia hamna kiwanda kitakachojengwa na Serikali ya Awamu ya Tano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu ya Mheshimiwa Waziri yanaainisha kwamba jukumu la ujenzi wa viwanda ni la sekta binafsi, lakini kauli za Serikali na viongozi wa Serikali mitaani huko, kila siku statement ambazo wamekuwa wakizitoa ni kwamba Serikali inajenga viwanda. Ni kwa nini sasa Serikali isibadilishe kauli yake ikawaambia wananchi jukumu la kujenga viwanda sio la Serikali, Serikali kazi yake ni kuwezesha mazingira wezeshi kama ambavyo mmekuwa mkitamka hapa. Ninayasema haya kwa sababu tumekuwa tukisia hapa…
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio nataka niulize kabisa kwamba kwa nini sasa wasibadilishe hiyo kaulimbiu kwa sababu mind set ya wananchi ni kwamba Serikali inajenga viwanda wakati ukweli ni kwamba Serikali haijengi viwanda?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali imejinasibu hapa kwamba inaweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi pamoja na wafanya biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ninachotaka nijue jitihada za Serikali juu ya hawa watu wa sekta binafsi kwa sababu moja kumekuwa na malalamiko, mazingira wezeshi kwa mfano huko Momba barabara mbovu, maji hayapatikana, umeme unayumbayumba, mitaji hakuna, riba zimekuwa zinapitiliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka nijue jitihada za Serikali kukabiliana na changamoto hizi ili hii sera ya viwanda iweze kuwa inatekelezeka.
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo linalofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano si la kuamka na kufanya. Tunafuata Dira ya 2025, tunafuata Mpango wa Pili wa Miaka Mitano na tunafuata maelekezo ya Mheshimiwa Rais. Imeandikwa katika Mpango wa Pili wa Miaka Mitano kwamba Serikali jukumu lake ni kuweka mazingira wezeshi na kazi ya sekta binafsi ni kujenga viwanda. Sasa sisi Tanzania sisi Serikali ya Awamu ya Tano tunajenga viwanda sisi sekta binafsi sisi ni Serikali tunakwenda pamoja huwezi kutenganisha sekta binafsi na Serikali. Huyo anatengeneza mazingira wezeshi huyu anajenga. Huyu anachota maji, huyu anasonga ugali wote mnapika chakula. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Silinde rafiki yangu usisahau umeme wa Momba kama si Serikali, kama sio mimi nikiwa Naibu wa Nishati usingefika. Tumefyeka msitu, sasa ushukuru kwa kidogo ulichopata nije nikupatie kingine.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Majibu ya Serikali ni majibu ya siku zote ambayo yameshindwa kutatua tatizo la ajira nchini. Unaweza kuonesha tu mifano midogo kwa mfano, sera ya uchumi na viwanda kwenye bajeti tu peke yake Serikali imeshindwa kupeleka fedha ambayo ingeweza kuwezesha hivyo viwanda kuanzishwa na wananchi kupata ajira, kipengele cha tano utaona kabisa kwamba inasema kwamba Serikali moja ya mkakati wake ni kuwapa mikopo nafuu kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, lakini kwenye bajeti tuliyoipitisha hapa unakuta Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ni bilioni moja wakati vijana ambao wako mtaani ni wengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, ni kwa nini Serikali isikubali ama ikashauriana na taasisi za kifedha ili wanafunzi wa Vyuo Vikuu watumie vyeti vyao walivyomalizia elimu ya juu, kama sehemu ya kukopea ili kuwasaidia waweze kujiajiri?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni kwa nini sasa Serikali kupitia Wizara ya Ardhi wasigawe ardhi katika yale maeneo muhimu kabisa bure kwa wanafunzi wote wanaomaliza Vyuo Vikuu ili waweze kujiajiri kwa kufanya hizo kazi na baada ya hapo warejeshe hiyo mikopo yao, kwa nini wasitumie hii mikakati ya muda mfupi ambayo inaweza kuwawezesha hawa watu kupata hiyo ajira au kujiajiri? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza ni kweli katika taasisi za kifedha moja ya masharti ya mtu yeyote kuweza kupata mkopo ni uwasilishaji wa dhamana (collateral) ili aweze kufikia uwezo huo wa kupata mkopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Silinde kwamba asilimia kubwa ya wahitimu wa vyuo vikuu na vyuo vya elimu ya juu bado hawajawa na uwezo wa kuwa na hizo collateral ndiyo maana Serikali na kupitia Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi tumeona njia pekee na bora ya kuweza kusaidia kundi hili la vijana kwa kuanzia, kwanza ni kuwahamasisha kukaa katika vikundi, pili ni kuwawezesha kupitia mifuko mbalimbali ya uwezeshaji ambao chini ya Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi tuna mifuko takribani 19 ya uwezeshaji inayotoa mikopo na inayotoa ruzuku ambayo ina ukwasi wa kiasi cha shilingi trilioni 1.3 kwa maana ya liquidity.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa wahitimu wote wa Vyuo Vikuu na Vyuo vya Elimu ya Juu bado wanayo fursa kutumia mifuko yetu hii ambayo ina riba nafuu sana, ambayo pia inaweza ikawasaidia wakabadilisha maisha yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya mfano ukienda pale Sokoine University tuna vijana wana kampuni yao wanaitwa SUGECO ambao walihitimu pale wamekaa pamoja ninavyozungumza hivi sasa SUGECO wanafanya miradi mikubwa ya kilimo hapa nchini na wameanza kuwasaidia mpaka na vijana wenzao kwa sababu walipitia utaratibu huu, Serikali ikawawezesha na sasa hivi wamefika mbali sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusiana na masuala ya ardhi, Novemba mwaka 2014, Mheshimiwa Waziri Mkuu aliwaita Wakuu wa Mikoa wote hapa Dodoma likatengenezwa Azimio la Wakuu wa Mikoa wote kwenda kutenga maeneo maalum kwa ajili ya shughuli za vijana, juzi Waziri Mkuu amesisitiza hilo jambo na mpaka ninavyozungumza hivi sasa zimeshatengwa takribani hekari 200,000 nchi nzima kwa ajili ya shughuli za vijana ambao maeneo haya tumeyapa jina mahsusi kabisa kwamba ni Youth Special Economic Zones (Ukanda Maalum Uchumi kwa ajili ya vijana).
Mheshimiwa Naibu Spika, rai yangu ni kwamba niendelee kuwaomba Wakuu wa Mikoa na viongozi wote katika Tawala za Mikoa kwa agizo la Waziri Mkuu watekeleze kwa kutenga maeneo ili vijana wengi zaidi wapate nafasi ya kwenda kufanya shughuli za ufugaji, kilimo na biashara. (Makofi)
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana na uzuri umeona idadi ya Wabunge waliosimama hii ni kuashiria kwamba maji ni tatizo.
Mheshimiwa Spika, mimi tu niulize swali dogo ambalo litaambatana na ushauri. Moja ya sababu inayopelekea kuwepo kwa tatizo kubwa la maji ni kwa sababu Serikali haijakita maji kama moja ya kipaumbele chake. Ni kwa nini sasa Serikali isikubali maji kuwa moja ya vile vipaumbele vitatu vikubwa vya Taifa, kwamba tutenge bajeti walau asilimia 20 kwa kuhakikisha tunatatua tatizo la maji nchi nzima? Kwa nini msikubaliane na jambo hilo ili tuondoe tatizo hili nchi nzima? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la Mheshimiwa Silinde, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilishaweka kipaumbele kuhusiana na utekelezaji wa miradi ya maji safi na salama. Ilianza mwaka 2006/2007 ambapo tulianza programu ya utekelezaji wa miradi ya maji nchini na ndiyo tulipoweka mikakati ya kujenga miradi 1,810 na hadi leo tumeshatekeleza miradi 1,468.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika mkakati huo tume-ring fence, tumeweka fedha Sh.50 zinatolewa katika kila lita ya mafuta. Huo ni mkakati maalumu kuonyesha kwamba sasa Serikali imeshaona suala la maji ni la kipaumbele na ndiyo maana kutoka kwenye huo mfuko kila mwaka tunatengewa shilingi bilioni 158.5. Ninyi Waheshimiwa Wabunge mmeendelea kusema kwamba fedha hiyo iongezwe ili iweze kutumika kwenye miradi. Kwa hiyo, Serikali tayari ilishaweka kipaumbele cha maji na tutahakikisha wananchi wanapata maji safi na salama.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Unavyoona Wabunge wamesimama ujue ndiyo hali ya maji nchini tatizo jinsi lilivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri wakati anajibu amekiri kabisa kwamba tatizo la maji lipo Wilaya ya Momba na sio tu Momba peke yake lipo nchi nzima. Sasa kauli mbiu ya ahadi ya kumtua mama ndoo kichwani imekuwa ngumu kweli kweli kutekelezeka kama ilivyo ahadi ya kupeleka milioni 50 kwa kila kijiji. (Makofi)
Je, Serikali inaweza ikatueleza kwa nini imekuwa rahisi kununua ndege ama Bombadier kuliko kupeleka maji safi na salama kwa wananchi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya mijini maji tunayotumia ku-flash kwenye vyoo ni bora kuliko maji ambayo wanatumia wananchi wa vijijini kwa sababu maji yale wananywea ng’ombe na wananchi wa kawaida wanakunywa huko huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa nini sasa Serikali isiwe na huruma kwa wananchi wa vijijini nchi nzima ili muweze kutatua hili tatizo la maji na sisi tuondokane na hii kero ambayo wananchi wamekuwa wanauliza kila siku wanahitaji maji safi na salama? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza napenda nimjibu Mheshimiwa Mbunge kuwa Mungu anaposema kwamba yapaswa kushukuru kwa kila jambo, Serikali inafanya jitihada kubwa sana katika kuhakikisha inatatua matatizo ya maji. Tunaona miradi mikubwa ambayo inatekelezwa, tunatoa maji kutoka Ziwa Victoria kupeleka Tabora pamoja na miji ya Igunga, tunaona Mheshimiwa Rais anavyozindua miradi kila kukicha Nansio na maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge sisi kama Wizara ya Maji jukumu letu ni kuhakikisha tunwapatia wananchi maji kwa maana ya maji safi, salama na yenye kuwatosheleza na nimefanya ziara katika Mkoa wa Songwe kwa kuona changamoto hiyo, tumetenga kiasi cha shilingi bilioni tisa na katika Jimbo lako tumetenga bilioni 1.77 katika kuhakikisha tunatatua tatizo hilo la maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Mbunge kazi ya Mbunge ni kusimamia. Naomba asimamie fedha hizo katika kuhakikisha wananchi wako wanapata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, lengo la Wizara yetu sio kuwapa wananchi maji masafi. Niwaombe sana wataalam wetu kwa maana ya wahandisi wa maji, wabuni miradi ambayo itakuwa na tija kwa wananchi wetu katika kuhakikisha wanapata maji yaliyo safi na bora ili kuhakikisha wanapata huduma hii muhimu.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nami nina swali dogo la nyongeza. Tatizo lililopo katika Jimbo la Igalula lipo vilevile katika Jimbo la Momba hususan katika barabara ya kutoka Kakozi-Kapele - Ilonga ambako ni Jimbo la Mheshimiwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Kandege, Jimbo la Kalambo.
Mheshimiwa Spika, wakati tunasubiri ahadi ya TANROADS ya kutengeneza barabara hiyo na yeye sasa hivi ndiye Waziri, haoni sasa ni wakati muafaka kutengeneza barabara hiyo ambayo inaunganisha mikoa miwili ya Songwe pamoja na Mkoa wa Rukwa, lakini vilevile Jimbo la Momba na Jimbo lake la Kalambo? (Makofi). Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nataka nimwombe Mheshimiwa Silinde tu avumilie kwa sababu sijatembelea Mkoa wa Songwe, lakini utaratibu wa Serikali kisera ni kwamba umuhimu wa kwanza ni kuhakikisha tunaunganisha mikoa. Kwa hiyo, asiwe na wasiwasi na katika bajeti yetu tuna provision na nikienda kule tutazungumza kwa upana zaidi ili aone namna ambavyo tumejipanga kuijenga barabara hii Mheshimiwa. Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Tatizo la maji katika shule za sekondari pamoja na shule za misingi lipo Tanzania nzima na nimemsikia Mheshimiwa Naibu Waziri hapa wakati anajibu anasema tatizo hilo litatatuliwa katika shule zote za sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka nifahamu jambo hilo litatekelezwa lini kwa kuwa tumeshapitisha bajeti na hakuna fedha yoyote iliyopitishwa kwa ajili ya kupeleka maji katika shule za sekondari. Upi ni mpango ambao utasaidia kupeleka maji shule za sekondari na shule za msingi Tanzania nzima ikiwemo Momba? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa David Silinde, Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kitandula, nimetoa ufafanuzi kwamba tunakamilisha mchakato wa mwisho wa kupata hizi fedha ambao ni mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia, dola milioni 350 si hela ndogo, ni hela ndefu. Kwa hiyo, mchakato huu unaweza ukakamilika vizuri kabisa 2018/2019 na fedha hizo zikaanza kutumika 2019/2020 kwa ajili ya kuhakikisha kwamba shule zetu zote zinaondolewa matatizo kabisa ya kukosa huduma ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika bajeti ambayo tumeipitisha Bungeni hapa ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji na fedha nyingine chache tulizipitisha katika kasma yetu ya TAMISEMI ambazo zote sasa tutazipeleka Wizara ya Maji ili ziweze kusimamiwa vizuri zaidi, zipo bajeti ambazo si kubwa sana kwa ajili ya kuhakikisha tumepeleka huduma za maji katika baadhi ya shule. Ahsante sana.
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Napenda kuongezea kidogo majibu mazuri ambayo yametolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba kupitia Mradi wa SWASH kuna kiasi cha shilingi bilioni 16 ambazo zimetengwa kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya maji shuleni. Kwa hiyo, mimi hiyo naona si hela kidogo, tayari Serikali imeonesha commitment, shilingi bilioni 16 zipo kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya maji shuleni kwa mwaka wa Fedha 2018/2019. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kifupi sana. Kwa kuwa Serikali kupitia Hazina ilitenga shilingi bilioni 299.9 katika bajeti yake ya mwaka huu wa fedha na mpaka sasa wametoa shilingi bilioni 1.67 sawa sawa na 0.6; na maji bila fedha ni sawa sawa na hakuna kitu. Kwa hiyo swali langu ni dogo; ipi ni commitment ya Serikali kwamba watatoa hizo fedha kabla ya mwaka huu wa fedha kwisha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua sisi kama Serikali kwamba maji ni uhai na utekelezaji wa miradi ya maji inategemeana na fedha, lakini Serikali imekuwa na vyanzo mbalimbali katika kuhakikisha tunatatua matatizo ya maji.
Moja, tuna Mfuko wa Maji, Bunge lako Tukufu limeidhinisha kiasi cha shilingi bilioni 158. Nataka nimhakikishie kwamba mpaka sasa zaidi ya shilingi bilioni 80, tumeshazipata katika kuhakikisha tunatatua tatizo la maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, hii ni Serikali ya Awamu ya Tano, tunaahidi, tunatekeleza katika kuhakikisha tunamtua mwanamama ndoo kichwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia fursa hii. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, bado nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Benki Kuu ya mwezi Februari, 2019 kwa maana ya Monthly Economic Review, inaonyesha kwamba kasi ya ukuaji ya ujazo wa fedha imeshuka kutoka asilimia 7.5 mwaka 2018 mpaka asilimia 3.3 mwaka 2019.
Je, Serikali haioni kuwa utekelezaji wa Sera ya Fedha umeleta matokeo tofauti kwa ukuaji wa ujazo wa fedha kuanguka zaidi kuliko mwaka 2018?
Swali la pili; kasi ya ukuaji ya mzunguko wa fedha nchini ni moja ya kiashiria muhimu sana cha kasi ya ukuaji wa uchumi; na ushahidi unaonyesha kwa miaka 20 kwamba unapokuwa na kasi ya ukuaji wa uchumi ya 7% maana yake kasi ya mzunguko wa fedha unakuwa katika double digit kati ya asilimia 12 mpaka 15. Kwa kutumia kiashiria cha mzunguko wa fedha na mfumuko wa bei, kwa nini Serikali isiache kutoa taarifa za uongo humu ndani ya Bunge na kwa Umma kwamba uchumi unakua kwa 7% ilhali hali halisi ni chini ya 4%.
Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nianze na swali lake la pili kwa sababu ameisingizia Serikali, ni kwamba Serikali siku zote inasema ukweli na haijawahi kudanganya Bunge, wala kudanganya sehemu yoyote. Nayasema haya kwa sababu zifuatazo:-
Mheshimiwa Spika, katika Mkutano wa Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC) uliomalizika wiki mbili zilizopita, Tanzania imepongezwa kwa ukuaji wa uchumi mzuri kwa mfululizo wa miaka mitano. Kwa hiyo, siyo kwamba Serikali inayasema haya ndani ya Bunge peke yake, hapana. Serikali inayasema haya ndani ya Bunge, nje ya Bunge na Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF) kwa taarifa yake limeipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ukuaji mzuri wa uchumi kwa kuweka nyenzo nzuri zinazohakikisha ukuaji wa uchumi wetu kuwa imara.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge tusiwadanganye Watanzania, uchumi wa Tanzania uko imara. Kwa Afrika Mashariki sisi ni wa kwanza na kwa Afrika sisi hilo ni jambo la kawaida. Nendeni kwenye google, m-google halafu mtajua nini tunachokisema. Uchumi wetu uko imara.
Mheshimiwa Spika, uchumi wetu uko imara na tuna uhakika kama ambavyo prediction zetu zilionyesha. Kwa mwaka 2018 tutakua kwa asilimia 7.2 kama prediction zetu zilivyoonyesha.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la kwanza, ni sahihi kabisa alichokisema kwamba ujazi wa fedha ukilinganisha mwaka 2018 na mwaka 2019 taarifa iliyotelewa na Benki Kuu, ujazi wa fedha umepungua. Hiyo haimaanishi kwamba uchumi haufanyi vizuri. Unaposoma ile taarifa, soma na sababu, kwa nini ujazi wa fedha umepungua?
Mheshimiwa Spika, ujazi wa fedha umepungua kwa sababu Watanzania sasa hata hapa ndani tukijaribu kuchukua simu ya kila mmoja wetu, ndani ya kila simu ya mmoja wetu kuna fedha za kutosha ndani ya simu yake na anafanya transaction electronically kwa siku zaidi ya jinsi ambavyo anafanya cash transaction kwa fedha taslimu halisi.
Kwa hiyo, kunapokuwa na ongezeko la transaction electronically, fedha halisi sokoni zinapungua, lakini fedha zilizopo kwenye mzunguko zipo za kutosha. Kama nilivyosema, sera yetu ya fedha inahakikisha mzunguko wetu wa fedha unalingana na shughuli za kiuchumi ambazo zinaendelea ndani ya Taifa letu.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwa niaba ya wananchi wa Momba na wananchi wa Kwela kwa ndugu yangu Malocha tunashukuru sana kwa ujenzi wa daraja bora kabisa ambalo nafikiri wananchi tutakavyo kwenda kulizindua wataona kazi ambayo tumeifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, daraja hili ni muunganisho wa hiyo Mikoa mitatu ya Katavi, Rukwa na Songwe lakini barabara inayozungumzwa inatokea kwenye Jimbo la Malocha inapitia Jimbo langu halafu inakwenda mpaka katika halmashauri ya Wilaya ya Mbozi. Ni barabara ndefu zaidi ya kilomita mia mbili na kitu, na barabara hii inajumuiya ya watu wasiopungua zaidi ya 150000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachoomba ni commitment ya Serikali ni lini itakwenda kuanza ujenzi ili wananchi hawa sasa wapate barabara ya lami kama ambavyo ahadi ya Mheshimiwa Rais Kikwete na ahadi ya Mheshimiwa Rais Dkt. Magufu itekelezwe kabla ya kumaliza mwaka huu wa uchaguzi. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli eneo lile lina watu wengi lakini kwa kweli ni eneo la kimkakati kwa sababu kuna uzalishaji mzuri sana wa mazao mbalimbali ambayo yanasaidia kwenye uchumi wa nchi. Kama nilivyozungumza hapa awali tunaleta bajeti yetu hivi karibuni, tunaliomba sana Bunge lako Tukutu litupitishie bajeti yetu halafu tuanze ujenzi baada ya kupata fedha mara moja.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu ya Serikali kuonyesha baadhi ya miradi ambayo inayofanyika katika Jimbo la Momba lakini bado tatizo la maji ni kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Maji inataka kwamba mwananchi achote maji umbali wa mita 400 na Jimbo la Momba lina zaidi ya vitongoji 400 na kiukweli mpaka sasa hivi tukienda katika level ya vitongoji peke yake vyenye maji haviwezi kufika hata 30. Kwa hiyo, nilichokuwa nataka kabla ya kwenda kwenye Uchaguzi Mkuu Serikali watupe hapa jibu la uhakika ni lini wananchi wa Momba maji yatatoka? Kwa sababu wananchi wanachohitaji pale ni maji pekee. Hilo ni swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, sisi kama Bunge hapa tuliitaka Serikali iongeze tozo kwenye mafuta kwa lengo moja tu la kupata fedha kwa ajili ya kupeleka kwenye miradi ya maji. Je, ni kwa nini ile tozo ambayo Bunge tuliipendekeza mpaka sasa Serikali haijaitekeleza? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, maji ni uhai na sisi kama viongozi wa Wizara ya Maji tunafanya jitihada kubwa sana za usiku na mchana katika kuhakikisha tunatatua tatizo hili la maji. Tumebainisha Mikoa 17 na Halmashauri 86 ambazo zimekuwa na changamoto kubwa sana ya maji ikiwemo Jimbo la Momba. Zaidi ya Sh.5,641,000,000 tumezipeleka kwenye Mkoa wa Songwe na katika Jimbo lake zaidi ya shilingi bilioni 1.3 zipo kwa ajili ya kutekeleza miradi mikubwa mitano katika kuhakikisha tunatatua tatizo la maji. Azma ya Mheshimiwa Rais ni kumtua mwanamama ndoo kichwani, nataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tutajipanga kuhakikisha miradi hii kwa wakati ili wananchi wake waweze kupata huduma ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Serikali kutoa fedha nyingi sana, moja ya changamoto kubwa sana ya Wizara ya Maji ilikuwa katika suala zima la usimamizi wa miradi ya maji na uendeshaji. Miradi ilikuwa ikitekelezwa kwa gharama kubwa sana zaidi ya mfano wake. Mfano, ukienda katika Jimbo la Nkasi kulikuwa na mradi ambao unatekelezwa estimation yake ni shilingi bilioni 6 lakini Mheshimiwa Makame Mbarawa na timu ya Wizara imepitia na kugundua mradi ule unatakiwa kutelezwa kwa shilingi bilioni 3.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tumeona kwamba pamoja na utekelezaji wa miradi lakini kwenye estimation za utekelezaji wa miradi zimekuwa kubwa sana. Sisi kama Wizara ya Maji tumepanga miradi yote kutekelezwa kwa Force Account kwa maana ya kutumia wataalam wetu wa ndani. Kwa hiyo, zile fedha ambazo tutakazopatiwa na Serikali zitatuwezesha kutekeleza miradi kwa wakati na tuta-save gharama kubwa sana. Kwa hiyo, nina imani fedha hizi zitaweza kutusaidia kutekeleza miradi mingi kwa kutumia wataalam wetu wa ndani na kuzuia ubadhirifu unaofanywa na wataalam wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, moja ya kero kubwa ya wachimbaji wadogo ilikuwa ni ile sheria ambayo tulipitisha hapa Bungeni, ya kodi ya zuio ya asilimia tano kwa bei ya kuuzia madini kwa wachimbaji wadogo, lakini Bunge lako tukufu mwaka huu mwezi wa pili tulibadilisha hiyo sheria na kuondoa hilo zuio.
Sasa nataka kujua utekelezaji baada ya kuondoa hiyo sheria umefikia wapi kwa sababu ile sheria ilikuwa inapelekea madini mengi kutoroshwa nje ya nchi? Ahsante sana.
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Silinde la nyongeza. Ni kweli kama alivyosema tumekuwa tukipata malalamiko ya baadhi ya watu, hasa maeneo ya Arusha na mikoa mingine kwamba, pamoja na kwamba withholding tax na VAT zimefutwa kwa mujibu wa sheria, wako watu wanaendelea kuzitoza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomab kutoa wito na kutoa maelekezo rasmi kwa watu wote wanaohusika kwenye utozaji wa kodi na tozo mbalimbali kwenye sekta ya madini. Kodi ambazo zimefutwa na Bunge hili hakuna mtu mwingine yeyote wa aina yoyote anaruhusiwa kutoza hizo kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na ninasema hili na iwe marufuku kwa mtu yeyote na tutakapopata taarifa tena, kwa mtu ambaye anaendelea kutoza hizo kodi, hatua kali zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria. (Makofi)
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii, na mimi niulize swali dogo la nyongeza kwenye swali hili la msingi mwaka wa fedha 2017/ 2018 Serikali ilitenga shilingi bilioni 251 kwa ajili ya kumalizia majengo ya zahanati, maboma pamoja na maboma ya shule za msingi, lakini fedha hizo katika mwaka huu hawakutoa kitu na mwaka wa fedha uliofuatia 2018/2019 ambao tupo Serikali ilitoa shilingi bilioni 69 kwa ajili ya shughuli kwa maana shilingi bilioni 39 kwenye majengo ya zahanati na shilingi bilioni 28 kwenye majengo ya shule za msingi.
Sasa nataka kujua commitment ya Serikali ya shilingi bilioni 184 zilizobaki za fedha za ndani kwenda kumalizia maboma hayo ya zahanati katika nchi zetu ikiwemo Jimbo la Momba? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kama tunavyofahamu kwamba ukiangalia katika kipindi cha karibuni Serikali imefanya investment kubwa sana katika maeneo hayo na hasa katika upande ule wa Maboma kuna takribani shilingi bilioni 38 kwanza zilitoka kwa ajili ya sekta ya afya awamu ya kwanza, lakini juzi juzi mwezi wa tatu hapa zilitoka karibuni shilingi bilioni 29.9 kwa ajili ya sekta ya elimu.
Mheshimiwa Spika, lakini, naomba nikuhakikishie kwamba mwezi wa nne hapa katikati tumetenga tena karibuni shilingi bilioni 35.6 kwa ajili ya kuhakikisha kwamba suala la sekta ya elimu kuhakikisha maboma mbalimbali yanatekelezeka.
Mheshimiwa Spika, Kwa hiyo naomba nikutoe hofu Mheshimiwa Silinde kwamba Serikali ni nia yake kubwa kwamba kuhakikisha maeneo yote yenye changamoto yanaweza kufanyiwa kazi kwa lengo kubwa Watanzania wapate huduma vizuri. (Makofi)
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya ngongeza.
(a) Ni kwa nini sasa fedha za Wahisani zinachelewa kufika kwa wakati na nyingi zinakuja wakati tunamaliza mwaka wa fedha?
(b) Naomba sasa Serikali itoe orodha ya nchi wahisani ikionesha mwenendo wa walichochangia katika kipindi cha miaka mitatu ya fedha iliyopita?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Washirika wa Maendeleo hutoa fedha kulingana na makubaliano ya kimkataba yaliyopo kati ya Serikali na washirika hao. Kwa kutambua hilo, baadhi ya Washirika wa Maendeleo hutoa fedha mwishoni mwa mwaka wa fedha wa Serikali kutokana na kupishana kwa kalenda kati ya mwaka wa fedha wa Serikali na kalenda za mwaka wa fedha wa Washirika wa Maendeleo, jambo ambalo Serikali hulizingatia katika mipango yake.
Hivyo basi, siyo kweli kwamba fedha za wahisani zinachelewa kufika kwa wakati. Fedha hizo hutolewa kwa mujibu wa mikataba hiyo ambayo inaainisha muda ambao Washirika wa Maendeleo wanatakiwa kutoa fedha hizo ili kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo iliyopangwa kutekelezwa na Serikali.
(b) Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita (2016/2017 – 2018/2019), Serikali imekuwa ikipokea fedha za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kutoka kwa nchi wahisani kwa kiwango cha kuridhisha kutoka kwa nchi wahisani pamoja na Washirika wa Maendeleo wakiwemo Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, Umoja wa Ulaya, Japan, Korea, India, Finland, Ufaransa, Ujeruman, Global Fund, IFAD, Norway, Umoja wa Mataifa (UN) pamoja na Sweden.
Aidha, orodha ya nchi wahisani pamoja na Washirika wa Maendeleo ikionesha mwenendo na kiasi walichochangia kwa kipindi hicho tutaiwasilisha kwa Mheshimiwa Mbunge baada ya kufanya uchambuzi wa kina kama alivyoomba.