Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Philipo Augustino Mulugo (15 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi ya kuchangia Wizara hii ya Maliasili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ya msingi ni moja tu katika Wizara hii. Najaribu kukumbuka kwamba katika Maziwa madogo madogo katika Afrika, Ziwa Rukwa ndiyo Ziwa pakee kwa nchi ya Tanzania ambalo limetengwa kwa ajili ya kufuga mamba. Mamba ni wengi kweli na hata sasa hivi ninavyoongea samaki hakuna Ziwa Rukwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wangu wa vijiji vya Some, Manda, Udinde, Rukwa, Maleza, Mbangala wanategemea samaki, lakini wanapoenda kuvua samaki hakuna samaki na wamedumaa. Nilikuwa nawasiliana na Mheshimiwa Mwigulu alipokuwa kwenye Wizara yake hapa nikamwambia jamani hebu tengeni fedha kwa ajili ya kufanya utafiti wa kuona kwa nini samaki hakuna Ziwa Rukwa. Katika hali ya kawaida samaki hawapo kwa sababu ya mamba ni wengi sana. Serikali inavuna mamba kidogo kwa mwaka vibali vya mamba 60 kwa mwaka wakati mamba wanazaliana sana kwa kila mwaka. Mheshimiwa Waziri, hebu jaribu kuliangalia hilo jamani wenzenu tunakufa kwa mamba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani mimi kule Jimboni kwangu, Jimbo la Songwe malaria au magonjwa mengine haya hatuyajui sana, lakini mamba ndiyo kilio kikubwa kwa wananchi wa Jimbo la Songwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kwa Mheshimiwa Malocha kule Jimbo la Kwela ni vilio vya mamba, vijiji ambavyo vimezunguka Ziwa Rukwa hata kwenye Jimbo la Mheshimiwa Silinde vilio ni mamba. Sasa wenzenu tunakufa kwa mamba Serikali inakuja hapa inasema eti huwa inawafidia watu wanaoliwa na mamba! Hebu niambieni mlishawahli kumfidia nani ambaye ameliwa na mamba?
Naomba kesho Mheshimiwa Waziri uniambie ulishawahi kumfidia mwananchi gani katika Ziwa Rukwa ambaye ameliwa na mamba ama labda mamba amemkamata hata mkono, sijawahi kuona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayesema hapa ndiyo muhanga wa mamba namba moja, baba yangu Mzee Augustino amekamatwa na mamba ni marehemu na mimi ndiyo nimemrithi, sijawahi kuona kwamba kuna pole ya Serikali, sasa siyo kuja kudanganya hapa kwamba huwa mnawafidia watu. Kesho nitashika shilingi uniambie fedha za baba yangu zipo wapi, hakuna! Huyo ni baba yangu, lakini mdogo wangu amekamatwa na mamba hakuna fidia, mama yangu aliyenizaa mimi amekamatwa na mamba hakuna fidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni muhanga namba moja ndiyo maana nasema nachangia kwa uchungu au labda nitoe machozi hapa. Mimi ni yatima kwa sababu ya mamba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia tena mimi ni yatima kwa sababu ya mamba! Mamba ni adui yangu namba moja. Sasa kama mamba ni adui kwa sababu yupo kwenye maji siwezi kumkamata, adui yangu mwingine ni Mheshimiwa Maghembe, Waziri wa Maliasili na Utalii kwa sababu ya mamba.
Naomba kesho uniambie fedha za baba yangu na mama yangu kwa ajili ya kunifidia mimi, kunipa pole ya mamba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo nimefanya research toka mwaka 1990 mpaka leo wananchi wangu 128 wameuliwa na mamba. Wengine wananchi hawaendi kuvua samaki wanakwenda kuoga, wanakwenda kufua nguo na kadhalika wanajeruhiwa miguu, mikono, ni mamba. Nenda hospitali ya Mwambani pale Mkwajuni majeruhi ni kwa ajili ya mamba, sasa Serikali ipo wapi? Jamani tuoneeni huruma. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi lete watu wafanye utafiti, samaki wapo wapi Ziwa Rukwa mbona mmelitelekeza Ziwa Rukwa, hakuna namna nyingine yoyote ukisikia bajeti hapa zinakwenda Lake Tanganyika, zinakwenda Lake Victoria, zinakwenda Lake Nyasa, utafiti wa bahari, jamani Ziwa Rukwa kwetu ndiyo uchumi wetu ukiacha kilimo! Hebu njooni muangalie wenzenu tunakufa jamani, kama nilivyosema mimi nimeathirika sana naomba niache tu, naweza nikaanza kulia hapa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Wizara hii ya Nishati. Nianze na mgogoro uliyopo kule Songwe, Mheshimiwa Waziri naomba anisikilize vizuri. Ni kweli Waziri ni mgeni katika Wizara hii lakini Maafisa wa Serikali wako pale na hasa TPDC. TPDC wametugonganisha kule Songwe, wametoa eneo moja linaitwa South Tanzania kule Kijiji cha Maleza, Jimbo la Songwe, kwamba wanakwenda kutafiti mafuta na gesi. Pale ukifika hata Mheshimiwa Kalemani wakati ule alishafika, wakaona ule uwanja na wakaanza kuona viashiria vya gesi na mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo watu wa kutafiti helium nao wakaenda, wakakuta kuna dalili hizo. Kwa hiyo wakawa wamepata certificate ya kwenda kufanya utafiti kwa ajili ya helium Wizara ya Madini, lakini vilevile TPDC wakatoa tena certificate ya wale wa heritage Tanzania wakafanye utafiti wa mafuta na gesi kwenye kitalu hichocho, kinaitwa South Tanzania. Sasa tunajiuliza Serikali ni moja hiyohiyo kwa nini mambo hayo yanatokea na hivi ninavyosema wananchi pale wanasubiri walishafidiwa mashamba, mahindi, kila kitu. Sasa naomba Mheshimiwa Waziri alichukue hili akaongee na watu wa TPDC waweze kuona jambo hili linakwendaje kwa sababu tunazo rasilimali tayari kule Ziwa Rukwa na mafuta yapo, kumbe gesi ipo, helium ipo, lakini ni just utafiti tu, mambo yamegongana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu Miradi ya REA kwenye Jimbo la Songwe. Miradi ya REA Jimbo la Songwe nashukuru Mungu kwa asilimia 30 bado kidogo vijiji vyote kuweza kutimia angalau asilimia 70 tayari, lakini hivi Vijiji vya Ngwara, Itiziro, Itindi, Maleza, Namkukwe, Manda, Isanzu, Muheza, Mpona, Ilea, Iyovyo na Kijiji cha Somi, vijiji 13 bado umeme, lakini tayari Mkandarasi ameshapatikana, ameshamwaga na nguzo, amechimba mashimo halafu akakimbia akaondoka, toka mwaka jana mwezi Septemba, mpaka hivi ninavyoongea Mkandarasi haonekani. Juzi nilikuwa Jimboni, nimetembelea Vijiji hivyo Mkandarasi haonekani kabisa, sasa sijajua Mkandarasi amepotelea wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna vijana ambao walikuwa wamechimba mashimo, wanadai fedha mpaka sasa hivi, wanamkimbilia Mbunge, Mbunge Serikali imetudhulumu, unajua wale kule hawajui masuala ya ukandarasi, hawajui masuala ya tender, sijui private company, no, wao wanachoangalia kwamba tunachimba shimo ili umeme uje, ni Serikali ndiyo imeleta umeme, ndivyo ilivyo. Kwa hiyo Mbunge akienda kufanya ziara pale, kwenye mkutano wa hadhara nimekutana na maswali sana Mheshimiwa Waziri, kwamba hawajalipwa fedha walizofanya kazi kwa ajili ya yale mashimo. Kwa hiyo naomba Mkandarasi aliyeshika tender kwenye Mkoa wa Songwe atafutwe haraka popote alipo akamalizie kazi kule ili umeme uweze kufika maeneo yale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo nilikuwa na hayo tu kwenye Wizara hii, otherwise fine Waziri anafanya vizuri, hongera sana. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Spika, ahsante na mimi kwa kunipa fursa hii ya kuchangia Wizara hii ya Maliasili. Nina vipengele vitatu, pongezi, malalamiko na hatimaye ushauri kwa Serikali.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa heshima kubwa kabla sijaanza kuchangia naomba niamini kwamba mimi ni Mkristo, ni-quote kifungu cha Biblia, Kitabu cha Mwanzo, mstari wa 24 hadi wa 30 kinasema hivi na naomba Maliasili mnisikilize; “Mungu akasema, nchi na ijae kiumbe hai kwa jinsi zake, mnyama wa kufugwa, nacho kitaambacho na wanyama wa mwituni kwa jinsi zake, ikawa hivyo. Mungu akamfanya mnyama wa mwitu kwa jinsi zake na mnyama wa kufugwa kwa jinsi zake na kila kitu kitaambaacho juu ya nchi kwa jinsi yake, Mungu akaona kuwa ni vyema. Mungu akasema, na tumfanye mtu kwa mfano wake, kwa sura yake, wakatawale samaki...,” naomba mnielewe, huyo mtu aliyeumbwa huyo, akatawale samaki wa baharini, ndege wa angani na wanyama wote wa nchi yote pia na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi, huyo mwanadamu akavitawale. (Makofi)

“Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimuumba mwanamume na mwanamke. Mungu akawabariki wote, akawaambia zaeni mkaongezeke, mkaijaze nchi na kuitiisha, mkawatawale samaki wa baharini, mkawatawale ndege wa angani na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi mkakitawale.” (Makofi)

“Mungu akasema tazama nimewapa kila mche utoao mbegu anampa binadamu, ulio juu ya uso wa nchi yote pia na kila mti ambao matunda yake yana mbegu vitakuwa ndivyo chakula chenu. Mungu akasema na chakula cha kila mnyama wa nchi na kila ndege wa angani na cha kila kitu kitambaacho juu yake chenye uhai, majani ya miche yote ndiyo chakula chenu ikawa hivyo. Mungu akaona kila kitu ni chema alichokifanya, ikawa asubuhi, ikawa usiku, siku ya sita.” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeyasema haya nikiwa na maana kwamba yawezekana miaka hii ambayo nimekaa Bungeni huu mwaka wa kumi na mbili sijawahi kuona kabisa Wizara ya Maliasili na Utalii ikileta sheria za kubadilisha kwa haya mambo tunayoyasema, kwa sababu kila siku ni manung’uniko ya Wabunge. Wenyeviti wa Vijiji wanalalamika, watu wanauliwa na mamba na tembo na simba, lakini no reaction na fidia yenyewe ni ndogo sana, hakuna hata sheria yakuja kubadilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia kwenye fidia hapa, nilikuwa naandika hapa, mtu aliyejeruhiwa na tembo analipwa shilingi 200,000 majeruhi wa kawaida, lakini aliyejeruhiwa jeraha la kudumu yaani maana yake amekatwa mkono, amekatwa mguu yaani hajafa analipwa shilingi 500,000 maskini ya Mungu; toka mwaka 1980 sheria haijabadilika. Mtu aliyekufa anapewa shilingi milioni moja basi na inawezekana wengine hata wazazi walishafariki hata hii milioni moja hatujawahi kuiona.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Maghembe amesema hajawahi kunipa, Mheshimiwa Kigangwalla amesema hajawahi kunipa, huyu Bwana Ndumbaro hajawahi kunipa, Mheshimiwa Pindi Chana naye miezi mingapi sijui kama atanipa. Lakini ninachotaka kusema ni nini? Wizara ya Maliasili tufumue sheria zote. Wizara ya Maliasili tutawaonea bure hata wale maafisa kwa sababu ni sheria zimekuwa za hovyo hovyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, miaka ya 1980 wakati sheria zinaundwa hizi za maliasili, vijiji sasa hivi vimepanuka. Ukienda pale Mkwajuni makao makuu ya Wilaya ya Songwe kilikuwa ni kijiji na vitongoji viwili, leo ndiyo makao makuu ya Wilaya na ndiyo mji mkubwa wa Mkwajuni. Ukitembea mita 500 wanakwambia hii ni TFS, ukitembea upande mwingine mita 200 huwezi kukusanya kuni, huwezi kuvuna mkaa yaani ni shida tupu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Diwani wa Kata ya Mkwajuni, mdogo wangu Shaibati anafanya kazi nzuri pale, haki ya Mungu tena bila yeye sijui mimi ingekuwaje, kwa sababu anaunganisha watu, wanakwenda wanaomba hata TFS angalau wakatiwe kaeneo kadogo wanatafuta kuni, lakini imeshindikana. Nao TFS wanakuja na sheria.

Sasa jamani ndio maana nimesoma hata neno la Mungu hapo; Mungu amemuumba binadamu akaitawale dunia, akaitawale na nchi na vitu vyote vilivyoumbwa tuvitawale sisi. Leo hii eneo la mapori tengefu Tanzania nzima yako maeneo 26. (Makofi)

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Mulugo kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Charles Kimei.

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Spika, nani huyo tena?

T A A R I F A

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, kataarifa kadogo tu kwa ajili ya kizuri unachozungumza Mheshimiwa Mbunge. Hata Nusu Maili iliyokuwa imewekwa kwenye hifadhi ya Mlima Kilimanjaro na mkoloni toka mwaka 1923 hawa wameiua. (Makofi)

SPIKA: Haya; Mheshimiwa Mulugo, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, lakini Wabunge hebu mniache niongee vitu vya maana, leo nalihutubia Taifa hapa. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nitoe hii elimu, nimesema eneo la mapori tengefu Tanzania idadi ni maeneo 26 yanatawaliwa na TAWA; Mapori ya Akiba Tanzania yako 27 yako chini ya TAWA; Mapori ya Hifadhi ya TANAPA ni maeneo 22; Mapori ya Hifadhi ya Misitu (TFS) yako 419. Nchi yetu ni eneo kubwa sana square kilometer 946,000. Lakini square meter 307,800 zote ni maeneo ya hifadhi, asilimia 32.5 ni maeneo ya hifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa Mungu amesema nendeni mkazae, mkaongezeke, tunaongezeka kila siku. Mwaka 1970 anaosema Mheshimiwa pale mwaka 1980, mwaka 1990, 2000, 2010, 2020 vizazi na vizazi vimeongezeka. Ninaposema Mkwajuni ilikuwa ni kijiji leo ni Wilaya, sasa wananchi waende wapi? yaani kule kwetu sisi maeneo yote ya Kapalala, maeneo ya Udinde, maeneo ya Gua, maeneo ya Kanga, maeneo ya Ngwala ni shida tupu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maana ukienda kwa wachimbaji wadogo kila wakitaka kuziona dhahabu, wameziona nina dhahabu zile pale, TFS anakuja, anasema ondokeni, wanawafukuza, wanawapiga, ni shida tupu. Hii nchi jamani ni ya kwetu sisi, Mungu alituumba tuitawale. Hata neno la Mungu linasema, zaeni mkaongezeke, tutawale. Mama wa watu anakwenda kukusanya kuni, anafukuzwa, anakwenda kukusanya mkaa anafukuzwa. Sasa wakinamama ambao hawana umeme maskini ya Mungu, hata gesi hamna kwenye vitongoji. Mheshimiwa Waziri wa Umeme juzi ananiambia kwamba vitongoji tutaanza kupeleka umeme, lakini unaweza kushangaa ikachukua hata miaka 10, ni maneno tu tunayopewa kama sera. Lakini leo wananchi wanaishije jamani? Hali ni ngumu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niwaambie Wabunge, toka tumeanza kuchangia hii Wizara, mimi ni mwanakamati pale, nani ameipongeza Wizara ya Maliasili hapa? Tunapongeza Royal Tour tu, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kutuletea Royal Tour. Hakuna mtu yeyote anayeweza kusema kwamba labda hongereni, TAWA mmefanya hivi, TANAPA mmefanya hivi, TFS mmefanya hivi. Bila Royal Tour hapa hii Wizara haiwezi hata kupongezwa, ni hatari, ni malalamiko tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kila siku Wabunge wanalalamika, sasa kwa nini Serikali isichukue hatua? Ni kweli wale wanatumia sheria, sasa sheria ni sisi Wabunge tuzibadilishe, hali ni mbaya sana huko, maeneo ni yetu sisi wenyewe. Ukienda kuvuna mbao hupati kibali. Juzi Mkuu wa Mkoa kule kwetu ameenda kule Kapalala, ameenda kule Buha, maana yake sasa hivi wananchi wa Kapalala hawawezi kulima. Mheshimiwa Bashe ametupa mpaka na zile mbegu za korosho, hawawezi kulima kwa sababu hakuna maeneo ya kulima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pale Mkwajuni Mji umetapakaa, umeenea, huku wanaweka sekondari za kata, huku sijui wanajenga majengo ya Serikali, wanaingia kwenye hifadhi, jamani hii hali tuibadilishe. Ukienda kwenye tembo huko ndiyo nisiseme, Kata ya Buha, Kata ya Kapalala, tembo wanaua watu, tembo wanakanyaga watu, mazao ya wananchi, hapa nina list ya majina karibuni 84 ningeweza kuyasoma, nitakuandikia, nitakuletea. Watu 84 mazao hakuna na mwaka huu kuna njaa sana. Tembo ni nani? Tembo ni nani mpaka atuzidi sisi wakati Mungu ametupa kibali cha kuwatawala hawa wanyama? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mungu ametupa kibali cha kutawala wanyama. Tutawale na wanyama na kwenye maji kule. Ndugu zangu…

SPIKA: Sasa Mheshimiwa Mulugo umesema unalihutubia Taifa, lakini tuongozane vizuri hapa. Umetaja hapo watu 84, umeanza kwa kusema watu wanauawa, watu wanakanyagwa na tembo, mazao. Sijajua hao 84 wako kundi gani? Maana unasema na wewe una majina hapo.

Waheshimiwa Wabunge, lazima ukisema jambo humu ndani tuwe na uhakika nalo. Kwa hiyo, tutarejea kule kwa Mheshimiwa Waitara. Hebu tuweke vizuri kwenye hao watu 84 hapo.

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Spika, ukiona mtu kama Mulugo anasema haya Bungeni nina ushahidi. Hii taarifa nimetoa kwenye Halmashauri ya Wilaya yangu ya Songwe kwamba kuna watu hapa wamekufa kwa mamba ni wengi. Nimekusanya taarifa za miaka mitano iliyopita. Nimekusanya taarifa za miaka mitano za watu walioharibiwa na tembo mazao yao. Kwa hiyo, kama ni hivyo nitakupa, wako watu 84 wameathirika na mamba pamoja na tembo. Kwa hiyo, ni kitu ambacho nina uhakika. (Makofi)

SPIKA: Sawa. Ngoja, ngoja twende vizuri, twende vizuri.

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana.

SPIKA: Kwa sababu unao huo ushahidi na unasema Halmashauri yako ndiyo iliyoleta hizo taarifa.

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Spika, yes. Ndio, ndio.

SPIKA: Na wewe hizo taarifa Jumanne nitaomba nizipate.

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Spika, nitakuletea, ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine ni masuala ya mipaka, hizi GN za hawa watu wa hifadhi, Maliasili. Kijiji cha Ngwala na Kijiji cha Buha hali ni mbaya, wakati Mheshimiwa Waziri anachangia hapa, Mheshimiwa Waziri wa Ardhi namheshimu sana, alisimama akasema Tume ilikuja. Nasema kwa ushahidi nilionao, Tume ya Mawaziri haijawahi kufika Songwe kwenye vijiji vyangu vya migogoro. Mimi ndiyo Mbunge kule na kila nikifika wanasema hawajawahi kuona, hawajawahi kufika Ngwala, hawajawahi kufika Kapalala, hawajawahi kufika Udinde, hawajawahi kufika Mkwajuni, hawajawahi kufika Patamela, hawajawahi kufika Saza, hawajawahi kufika Ngwala. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapana tusidangaye hapa, kama walienda maeneo mengine lakini siyo maeneo yetu wengine, ni migogoro mitupu. Jamani alisema Mheshimiwa Silaa siku ile pale, tunakwenda kwenye uchaguzi 2025, tupeni raha na sisi huko tukaseme vizuri kwa wananchi. Naomba taarifa ambazo Wabunge tunatoa ndani ya Bunge humu tunakuwa tumezikusanya kwenye vijiji, kwenye kata, kutoka kwa Madiwani, zinakuwa ni taarifa rasmi. Naomba Serikali itusikilize. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda maeneo kama ya Guha pale, sasa watu walime nini sasa?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Sekunde 30, muda wako umeisha. Sekunde 30 malizia.

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Spika, Wizara ya Kilimo inasema tulime, lakini Wizara ya Maliasili tuvune mbao, tuvune na mkaa, maeneo hakuna.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba, ombi langu la mwisho tufumue Wizara ya Maliasili yote, tubadilishe sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru sana kwa kunipa nafasi jioni hii kuchangia na kuweza kushauri mambo mbalimbali kuhusu Wizara ya ELimu. Na-declare interest kwamba mimi ni Mwalimu by profession lakini vile vile ni mmiliki wa shule binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutalaumu sana, tutaongea sana mambo ya Wizara ya Elimu lakini kidogo kuna mambo ya mkanganyiko wa sheria, sera, kanuni na nyaraka mbalimbali. Mambo yanaweza yasiende tukamlaumu Mheshimiwa Profesa Ndalichako, mambo yanaweza yasiende tukamlaumu Mheshimiwa Simbachawene, mambo yanaweza yasiende kumbe yako Wizara ya Utumishi kwa dada yangu pale; na mambo mengine mengi, lakini mengine yako Wizara ya Fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano mdogo tu, anayelipa mishahara ya Walimu, ni Wizara ya Fedha; anayepandisha Walimu madaraja katika nafasi mbalimbali ni Utumishi; anayesimamia elimu mashuleni ni TAMISEMI, ndiye anayeangalia kama madawati yapo, kama Walimu wamefika tayari wanafundisha, nyumba za walimu na kujenga madarasa; na usimamizi wote wa elimu kule Shule za Msingi na Sekodari. Ni TAMISEMI wala siyo Wizara ya Elimu. Anayetengeneza Sera ya Elimu ni Wizara ya Elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naona wenzangu hapa wanachangia na kila kitu wanapiga madongo kwa Wizara ya Elimu. Well and good kwa sababu yote ni Serikali kwa ujumla. Nataka vile vile Serikali mjue hilo kwamba lipo jambo moja na lingine linaweza likasababisha huku kukawa kuzuri ama kukawa kubaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa baada ya kushauri hilo, naomba niingie kwenye hoja zangu. Kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, Profesa Ndalichako kwa kuteuliwa kuwa Waziri katika Wizara hii. Namfahamu vizuri sana, tumefanya naye kazi vizuri sana. Ni mama mwenye msimamo, lakini mimi huwa namwita ni mama wa quality of education. Namfahamu toka akiwa pale Baraza la Mitihani la Taifa. Huwa hapendi mchezo na hataki mambo holela holela! Nadhani mtakuwa mmeona anavyoendelea hata kutumbua baadhi ya majipu fulani fulani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima mama huyu tumshauri; na kwa hii miezi sita aliyokaa Wizarani yapo baadhi ya mambo yanaonekana, lakini akikaa miaka mitano, tunaweza tukaanza kuona impact ya baadhi ya mambo mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshauri Mheshimiwa Waziri. Suala la kuanzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Elimu Nchini ni suala muhimu sana. Nami kwa sababu ni mzoefu wa mambo haya, Waheshimiwa Wabunge naomba nitoe hili jambo mlione jinsi lilivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Katibu Mkuu wa Wizara ya ELimu, kama nilivyosema, anatunga sera, lakini Katibu Mkuu wa Wizara ya TAMISEMI ndiye mwenye Shule za Sekondari na Msingi kama Serikali. Vile vile kuna shule za private upande mwingine, hawa watu wa TAMONGSCO na TAPIE, kwa wamiliki wa shule. Sasa inakuwaje tena pale pale kwenye Wizara ya Elimu kwa Mheshimiwa Profesa Ndalichako pana watu wanaitwa Wakaguzi wa shule ambao watakapokwenda kukagua shule, wakakuta kwenye Shule ya Msingi matundu ya vyoo ni machache, ama Walimu darasani hawapo, ama shule haina madawati, ama kuna mlundikano wa wanafunzi, wanaandika ripoti, wanampelekea mwajiri. Unategemea mwajiri atafanya nini? Naomba niseme, mwajiri atafanya nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tukipata kitu ambacho kinajitegemea, kama ilivyo EWURA, au kama zilivyo bodi nyingine na mambo mengine ambapo labda tumeanzisha Wakala wa Serikali ama mamlaka ambazo ni independent zinajitegemea, ni autonomous, agency, ili ikague shule zote kwa usawa. Ikienda kwenye private wasema bwana shule yako haina ubora, haina fence, haina vyoo, haina Walimu wenye vyeti vizuri, haina madirisha fulani, haina vitabu na kadhalika, iandike kwamba shule hii imepata asilimia 70. Ikienda na kwenye shule za Umma iandike vile vile, shule hii haina vyoo, ifanye hivi; imwandikie TAMISEMI arekebishe na itoe siku 60 shule irekebishwe; mambo yatakwenda vizuri sana, kuliko tunavyofanya sasa. Kwa sababu sasa hivi anayeandika ripoti anampelekea mwajiri wake ambaye akiandika vibaya anaweza hata akamfukuza kazi. (Makofi)
Kwa hiyo, ni suala ambalo kidogo naomba mlifikirie, mimi nina udhoefu nalo. Naomba tuanzishe mamlaka huru ya udhibiti wa shule. Leo tunasema ada elekezi; tukipata hicho kitu kitaangalia kila kitu kwenye shule zetu. Mfano mdogo, unaposajili shule ya private, sekondari ama primary kuna vigezo vingi sana pale Idara ya Udhibiti ambapo zamani ilikuwa Idara ya ukaguzi. Unakuta mwenye shule anajenga kila kitu, anakamilisha madarasa nane, anaweka miundombinu ya shule, walimu vizuri halafu ndipo Serikali inasajili shule maana ina vigezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nenda kwenye shule za Umma, shule inaanzishwa hata kama ina madarasa mawili. Tukimpata huyo ambaye atakuwa ana-regulate, shule ya Umma haiwezi kunzishwa kwenye madarasa matatu; Haiwezi kuanzishwa haina madawati; haiwezi kuanzishwa hawana vyoo; haiwezi kuanzishwa watoto wakakaa 80 darasani. Kwa sababu yule mtu atakuwa ni independent, atatoa ripoti ambayo haina upendeleo. Naomba niishauri Serikali na Mheshimiwa Waziri naomba a-take care jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naomba sana nimshauri dada yangu Mheshimiwa Profesa Ndalichako, Wizara hii umepewa utakaa miaka mitano hapo, lakini naomba ufanye mambo mengine tutakayoweza kukukumbuka. Katika nchi hii hatuna Chuo cha Ualimu kinachofundisha Walimu kwenda kufundisha English Medium. Nani aseme ni chuo gani kipo hapa nchini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Serikali imekataza shule za binafsi kuchukua Walimu kutoka nchi ya Rwanda, Uganda, Kenya ama mataifa mengine, tunataka tujiweke sisi kama ni kisiwa, tumepandisha kodi mbalimbali ili shule hizi zibanwe, zianze kuchukua Walimu wa ndani ambao hawana hiyo taaluma. Tunaua elimu sisi wenyewe, kwa nini? Kwa nini tuue elimu sisi wenyewe wakati tunajua hatuna Chuo cha namna hiyo? Vyuo vyetu vya elimu vinafundisha certificate ya kwenda kufundisha masomo yanayofundishika kwa Kiswahili japo content ni ile ile na syllabus ni ile ile, wanatafsiri tu mtihani.
Leo ukienda wanapotunga mtihani wa Darasa la Nne kwenye English Medium wanachukua maswali kwa Kiswahili halafu wanatafsiri. Kuna ada tunalipa shule za binafsi kwa sababu unasema eti katafsiri mtihani wa Darasa la Nne. Jamani! Tafadhali, Mheshimiwa Waziri naomba uliangalie hili kwa makini sana. Mimi ni Mwalimu, naliona, ni hatari kubwa! Kwa nini tuweke wigo kwa shule za binafsi zisiajiri Walimu kutoka nchi za nje? Tujue Tanzania hii siyo kisiwa, kuna Mabalozi wapo hapa, kuna wafanyakazi mbalimbali kutoka nchi za nje wapo hapa, wawapeleke wapi watoto wakasome shule? Naomba hili nalo lifanyiwe kazi vizuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba lingine niishauri Serikali; yapo mambo jamani kwa kweli niseme kama ni kero hivi; ama yupo mtu mmoja Wizarani pale akilala akiamka anasema ngoja leo niandike hivi. Hivi unawezaje ukaandika kwamba shule za private hakuna kukaririsha wanafunzi? Mzazi anaamua kumpeleka mtoto kwenye shule ya private; kwanza naomba nitoe elimu hii. Serikali inachukua wanafunzi waliofaulu, the best students, wanawachagua kuwapeleka Shule za Serikali mwezi Januari. Baada ya hapo, wanaokuwa wamebaki, maana yake ni slow learners; hujawachagua wewe kuwapeleka kwenye shule zako za Serikali. Shule za private zinaokoa jahazi, zinawachukua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwatambue kwamba wale ni slow learners. Slow learner huyo unamwingiza darasani, wengine ndiyo kama hivyo, hawajui hata kusoma na kuandika; unamwingiza darasani, ni lazima umfundishe pole pole. Inafika mwisho wa mwaka ili afanye mtihani wa Form Two, hajui chochote, mzazi anakwambia mimi hapa nalipa ada shilingi milioni mbili kwa mwaka, mtoto wangu bado ana umri mdogo, nataka arudie shule. Serikali inasema aah, aendelee. Jamani! Ulishawahi kuona wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwe huru, waachieni wazazi wa nchi hii wawe huru. Unaandika barua kwa Afisa Elimu wa Mkoa, wanasema Serikali imesema hakuna kukaririsha. Si ulimwacha mwenyewe huyu motto, ni slow learner, sasa amekwenda kwa watu wengine wamfundishe. Kama wanamfundisha na mtu analipa, anafundishika pole pole huyo! Mwache asome. Ruhusuni shule za binafsi zianze kukaririsha. Hata shule za Serikali vile vile zikaririshe kama zamani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo watu wengine tulisoma, tusingekariri tusingekuwa hapa! Tulirudia shule tukasoma, ndiyo maana kuna private schools, ndiyo maana kule kwenye mitihani ya Form Two kuna kitu kinaitwa Qualifying Test, wanasoma hata Elimu ya Watu Wazima. Nini maana ya kuweka kwamba elimu ni free? Jamani!
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya, lingine, naomba niishauri Serikali. Tunataka kuua Elimu ya Ualimu nchini. Tumevichukua Vyuo vya Ualimu kuvipeleka NACTE. Mungu wangu! Hebu naomba nifafanue.
Mheshimiwa Mwenyekiti, NACTE maana yake ni National Council of Technical Education, yaani Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi. Sasa unamchukua Mwalimu anayesoma education in general unampeleka akasomee huko. Hakuna utaalam wa kuwalea walimu kule! Turudishe Walimu kwenye Wizara ya Elimu kama ilivyokuwa zamani.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga hoja mkono.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kupewa nafasi hii ya kuchangia Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Kwanza, napenda niwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Songwe, kwa kunirudisha tena kuwa Mbunge wa awamu hii ya pili. Nataka niwahakikishie kwamba, nitawasaidia sana namna ya kufuatilia huduma zao za afya, elimu, umeme, maji na mambo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari jambo ambalo nilikuwa nimeahidi kwenye uchaguzi wa mwaka 2010 kwamba, nitahakikisha napigania kupata Mkoa mpya na Wilaya mpya ya Songwe sasa nimepata, sasa ni hapa kazi tu. Nitahakikisha mambo yanakwenda vizuri. Napenda vilevile nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa wanayoifanya katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kipindi kifupi takribani kama miezi sita nchi imebadilika, hali ya hewa imebadilika kabisa Tanzania, tunaanza kuiona Tanzania yenye asali japo ndugu zetu hawa Wapinzani wao kama ambavyo wanaitwa Wapinzani hawana zuri, hawana dogo, wao kila kitu ni kupinga. Kwa hiyo, nawashauri Wapinzani mbadilike, hii nchi ambayo tulikuwa tunaitegemea ndiyo hii ya Tanzania nakumbuka kwenye Bunge la Kumi ninyi ndio mlikuwa watu wa kwanza kusema Serikali ni dhaifu, sasa leo Serikali siyo dhaifu, Serikali hii sasa ni imara, naomba mwendelee na ninyi kupongeza jitihada. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nirudi katika hoja za wananchi wa Mkoa mpya wa Songwe na Jimbo la Songwe na Wilaya mpya ya Songwe. Tumepata Mkoa mpya, Mheshimiwa Waziri Simbachawene anajua hilo, lakini Mkoa huu mpya Mheshimiwa Simbachawene juzi ama jana wakati naangalia taarifa za habari kwamba, Mheshimiwa Rais ameteua ma-RAS katika kila Mkoa lakini Mkoa wetu wa Songwe tayari Mkuu wa Mkoa amesha-report ameshafika mama yetu Chiku Galawa, lakini sijaona pale kwenye list ya ma-RAS kwamba tumepata RAS naomba hilo Mheshimiwa Waziri ali-note asiweze kusahau.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iweze kututeulia Katibu Tawala wa Mkoa haraka ili maendeleo vilevile katika Mkoa huu yaweze kwenda haraka sana. Vilevile bado na Wakuu wa Wilaya, Wilaya yetu hiyo mpya bado haina Mkuu wa Wilaya, nadhani hilo liko chini ya vetting na mnaendelea na taratibu hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimesema daima mikoa mipya na wilaya mpya zina changamoto zake. Naomba Serikali pale mtakapokuwa mnaweka vipaumbele katika bajeti ya maendeleo, basi msisahau kuweka hizi halmashauri na Wilaya mpya pamoja na mikoa mipya kuweka kipaumbele, kwa sababu ukiangalia kama Halmashauri yangu mpya ya Songwe pale Makao Makuu ya Halmashauri maji ni tatizo na miundombinu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna nyumba ya Mkuu wa Wilaya, hakuna nyumba ya Katibu Tawala, hakuna nyumba ya Maofisa wa Serikali, hakuna nyumba yoyote ya Kiserikali ambayo sasa wale viongozi wakija watakuja kuhamia pale maana yake Mkuu wa Wilaya atakaa hotelini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliomba special fund milioni kama 403 tuletewe mapema ili tuanze maandalizi, lakini mpaka sasa hatujapata hizo fedha. Hizo fedha zingekuja kukarabati jengo ambalo liko pale Mkwajuni ili Mkurugenzi akija aweze kupata ofisi, Mkuu wa Wilaya aweze kupata nyumba pamoja na Mkuu wa Mkoa pale Vwawa aweze kupata nyumba. Fedha hizo Mheshimiwa Waziri hatujapata mpaka sasa. Kwa hiyo, naomba jambo hilo lichukuliwe katika uzito wa namna yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba vilevile nipongeze Kamati ya Mgao wa Mali pamoja na Watumishi katika Wilaya ya Chunya. Nampongeza sana kwanza Mkurugenzi dada Sophia Kumbuli alishirikiana sana na ile Kamati. Mimi mwenyewe nadhani last week hamkuniona hapa nilienda kuweka kambi pale Chunya kuhakikisha tunagawa mali vizuri, kugawa magari vizuri, kugawa watumishi vizuri wenye career mbalimbali ili kuona kwamba, Mkurugenzi anaweka mambo vizuri. Kwa kweli, yule mama amenisaidia sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yetu ile tumefunga mjadala, Baraza la Madiwani limepitisha na jana DCC imekaa, imepitisha kwamba, tumegawa vizuri, kwa hiyo hakuna malumbano wala hakuna mambo mengine yoyote. Kwa hiyo naomba niseme kwamba, limeenda vizuri, sasa ni kazi ya RCC ikae ipitishe na Mheshimiwa Waziri atapata hiyo document waweze kutupatia GN namba haraka sana kwenye Halmashauri mpya ya Songwe. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri, vilevile ningemwomba afanye ziara kwenye Halmashauri yangu hii mpya, aje pale Mkwajuni aliniambia hata wakati ule kwamba, atakuja Songwe. Naomba basi atembelee mkoa mpya pale Vwawa lakini vilevile afike na pale Mkwajuni jimboni kwangu aone jinsi hali ilivyo kwenye Halmashauri mpya ya Songwe, ataona ukubwa na umbali kutoka Kata moja mpaka Kata nyingine unakuta ni kilometa 30. Tumeomba kwenye Bodi ya Barabara kwamba, Kata zingine kutoka Kapalala mpaka Ngwala tungeomba zile barabara ziingie kwenye barabara ya Mkoa kuliko kuweka kwenye Halmashauri ambazo fedha zikija, zinakuwa ni kidogo, haziwezi kukidhi mahitaji ya matengenezo. Hiyo ndiyo changamoto yangu iliyopo huko kwenye Mkoa mpya na Wilaya mpya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie jambo lingine kwenye upande wa Watumishi wa Halmashauri hasa ma-VEO na ma-WEO. Mimi wakati nafanya ziara kwenye jimbo langu kushukuru mwezi Februari nimekutana na changamoto, ukifika vijijini unakuta hakuna VEO, kwenye Kata hakuna WEO, lakini wanasema tuna barua ya Mkurugenzi amemteua Mwalimu Mkuu wa Shule ndiye anakaimu WEO ama anakaimu VEO.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye hotuba yake amesema kwamba, sasa hivi mapato ya Halmashauri ama mapato ya ndani yatakusanywa na hawa viongozi ma-VEO na ma-WEO kwenye Serikali za Mitaa. Sasa je, tuanze kumtoa mwalimu darasani akakusanye mapato? Naomba suala la ajira la ma-VEO na ma-WEO lifanyiwe haraka ili wale Wakurugenzi wapate vibali tuweze kuajiri haraka angalau vijiji vyetu viwe na viongozi hao ili wakusanye mapato kwa upande wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba vilevile nichangie upande wa elimu. Mimi ni mwalimu by professional lakini elimu bure dhana hii nimeichukulia vizuri sana na wananchi wameshaanza kuielewa, lakini ningeweza tu kuishauri Serikali kwenye baadhi ya vipengele. Mheshimiwa Waziri, elimu bure inawafanya hata wazazi wasichangie hata madawati, elimu bure inamfanya mzazi asiweze hata kumnunulia mtoto wake sare, elimu bure inawafanya hata wazazi wasichangie hata michango ya UMISETA, elimu bure inawafanya wazazi waache hata kuchangia mitihani mock.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetoka Mbeya juzi tu hapa nilikuwa namuuliza Mwalimu mmoja wa shule ya private kwamba, hivi mock Mkoa wa Mbeya ama mock Wilaya ya Mbeya Mjini ama Vijijini ama Chunya, mnafanya lini? Wakasema mpaka leo hatujapata mwongozo wa mitihani hii ya mashindano ya mock kwenye Wilaya na Mkoa kwa sababu Serikali haina fedha. Zamani walikuwa wanachangia wao wenyewe wanafunzi kutoka kwenye mifuko ya wazazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Serikali kama kweli tumeshaanza kuibeba dhana ya elimu bure, basi fedha zile zijumuishwe pamoja na michango ya mock itafikia mahali shule za Serikali wataacha kufanya real practical kwa sababu hakuna hela. Sasa kama na shule zikianza kutokufanya real practical maana yake ndiyo tunaua sayansi kwenye shule za Serikali. Naomba Mheshimiwa Waziri hili walichukulie kiumakini sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mwalimu najaribu kushauri kwamba, tukikosa mock kwenye shule za Serikali ila tukawa na mock kwenye shule za private huwezi kufundisha bila ya kuwa na zile academic competitions ili angalau wanafunzi waweze kufanya vizuri. Kunakuwa na mashindano ya kitaaluma kwenye shule, sasa tumeyaua hayo halafu baadaye tunasema elimu bure, matokeo ya mitihani yakitoka unakuta shule zinakuwa labda hazijashika namba vizuri, halafu tunaanza kuongea tofauti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana kwenye suala la elimu, mock iweze kufanyika. Mheshimiwa Waziri wa Elimu yuko pale, Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI na Naibu wake hebu jaribuni ili mliangalie, mimi nawashauri; pigeni simu kwa ma-REO wa nchi nzima mseme mock ipo mwaka huu, maana inaonekana mock haipo kwa sababu fedha hakuna. Fedha zile ambazo tunapeleka kwenye Shule za Msingi kama capitation grants hazitoshi kwa ajili ya matumizi ya shule, kununulia chaki, Mwalimu kufanya mikutano na mambo mengine. Kwa hiyo, hawana fedha za mock, hawana fedha za kufanya real practical, naomba hili mliangalie, mimi nawashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, nisingependa dakika ziniishie, naomba ushauri wangu uzingatiwe. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. PHILIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana angalau kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hoja hii iliyoko mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na mfumo mzima wa miradi ya REA. Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini alifika Jimboni kwangu, wakati anakuja kusuluhisha mgogoro wa Saza nashukuru sana angalau sasa hivi mgogoro umemalizika, japo yapo mambo madogo madogo ambayo nadhani mimi na wewe tunaendelea kuya-solve pole pole, kwa sababu migogoro ya wachimbaji wadogo wadogo, haiwezi kwisha leo wala kesho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu mfumo wa REA, kwenye Jimbo langu la Songwe, kwanza Awamu ya Kwanza sikupata kijiji hata kimoja. Awamu ya Pili nimekuja kupata vijiji vinne; na sijajua hii Awamu ya Tatu, nitapata vijiji vingapi. Naweza kusema ni kama kuna upendeleo fulani hivi, kwa sababu wakati ule wana-sort kwenye Awamu ya Kwanza, walipokuwa wakiandika tu neno Chunya, basi REA vijiji vingi vilienda upande mmoja kwa Mheshimiwa Mwambalaswa, Mbunge wa Jimbo la Lupa. Jimbo la Songwe sikupata kijiji hata kimoja. Baadaye nikawa nimeenda pale Mkoani Mbeya nikaambiwa basi angalau utapata baadhi ya vijiji kwenye Awamu ya Pili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Awamu ya Pili mwaka 2012 Mheshimiwa Simbachawene alipokuwa Naibu Waziri wa Wizara hii, alitembelea Jimbo langu tukaja tukaandika vijiji kama 15, lakini mpaka hivi ninavyosema ni vijiji vinne ndiyo angalau kuna nguzo na waya lakini hata matransfoma bado na vijiji havijaanza kuwaka. Kwa hiyo, Jimboni kwangu niseme katika huu mradi, hata kijiji kimoja umeme haujaanza kuwaka; toka Awamu ya Kwanza, Awamu ya Pili, leo tunakwenda kwenye Awamu ya Tatu. Jamani ninaposema kwamba kuna upendeleo katika baadhi ya maeneo, huo ni upendeleo wa waziwazi Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba hata kama kesho utakapokuwa unatoa majibu, hebu turidhisheni sisi ambao Awamu ya Kwanza tulikosa na Awamu ya Pili bado vijiji ni vichache. Basi kwenye Awamu ya Tatu mtujazie vijiji vingi tuweze kulingana na wenzetu ambao mliwapa Awamu ya Kwanza na Awamu ya Pili; kwa kweli inasumbua sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata yule Mkandarasi ambaye amekaa kule Mbeya, SINOTEC yule Mchina, sijui kama ameshindwa kazi, lakini Mheshimiwa Muhongo kwa namna ninavyokufahamu, Waziri uko makini na unachukua hatua pale pale unapoona mtu anakosa, njoo Mbeya utembelee maeneo yale ya Chunya, utakuta kabisa yule mkandarasi labda ameshindwa kazi. Si afukuzwe tu wapewe watu wengine?
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji 12 ni vijiji vinne tu na sijajua maeneo ya kwa mama Mbene kule Ileje kama nako kuna kazi zinafanyika. Wapeni wazawa basi hizi kazi kuliko kuwapa Wachina hizo tender. Wapeni wazawa, mbona wanaweza wakafanya kazi vizuri? Hali ni mbaya sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba vilevile niongelee upande wa madini. Nadhani kwa Mkoa wa Mbeya Jimbo langu ndiyo lenye migodi mingi kuliko sehemu nyingine, ama tuseme Mkoa mpya wa Songwe, nina migodi karibu 12. Naomba niongelee kitu fulani kinaitwa 0.03 ambayo inaenda kwenye Halmashauri, tunaita service levy.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hii inapokuwa calculated, watu wa Halmashauri wanakuwa hawapo, kwa sababu pale panakuwa pana TMAA, panakuwa na watu wa TRA, lakini vile vile panakuwa na mmiliki mwenyewe wa mgodi, kama kule kwangu niseme labda moja kwa moja Shanta. Mtu wa Halmashauri anayewakilisha kwamba sasa yule ndiye mzawa, mwenye mgodi mwenyewe anakuwa hayupo pale ambapo unakuta ndege inakuja, inachukua dhahabu, TRA yupo, TMAA yupo, lakini mtu wa Halmashauri anakuwa hayupo.
Mheshimiwa Waziri nilikuwa naomba turekebishe sheria hiyo, kwa sababu tunaibiwa. Mnatupa asilimia 0.03 lakini hatujui ni ya nini kutoka kwenye nini, kwenye mapato gani? Nadhani hata wenzangu wenye migodi kama mkiliangalia hilo, ni kama vile tunaibiwa. Labda Mheshimiwa Waziri uje utufafanulie vizuri juu ya hilo jambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba niishauri Serikali, mtueleweshe vizuri, Ile service levy mnayotupa kwenye Halmashauri, ile ela imetoka kwenye mapato ya nini? Sasa kwa nini ndege inapokuja pale Saza, inachukua madini, TRA yupo, anawakilisha Serikali Kuu, TMAA yupo, naye anawakilisha Serikali Kuu, lakini mtu wa Halmashauri anakuwa hayupo, kama yupo labda yupo Afisa Madini ambaye naye sio mkazi wa maeneo yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka sisi wakazi, maana yake Baraza la Madiwani liteue labda Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango na Fedha wa Halmashauri, awe anakuwepo pale ambapo ndege inakuja inachukua dhahabu na yeye yupo, tuweze kujua kwamba basi kama ni bilioni kadhaa, ndiyo una-calculate sifuri nukta sifuri tatu ndiyo imechukuliwa hapa, ndio inakuja kwenye Halmashauri, ningependa sheria hiyo kidogo tuweze kuirekebisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu sikuwa hata nimesomwa kwamba nitaweza kuchangia leo, nimesomwa tu huku nimetoka kusalimia huko, nilikuwa natembea kidogo nimetoka nje, lakini nilikuwa nimejiandaa angalau mambo mawili haya niweze kuchangia Wizara hii. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, angalau nami nimepata nafasi ya kuchangia Wizara ya Elimu na naomba niseme kwamba mimi ni mdau, ni Mwalimu, kwa hiyo, angalau naelewa mambo mengi ya hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha sana; kabla sijaanza kuchangia hoja zangu za msingi, lakini angalau nilalamike kuhusu suala moja la Halmashauri yangu ya Songwe. Nilikuwa napitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri hapa kwenye kitabu hiki, naona Halmashauri yangu ya Wilaya ya Songwe haijapata vitabu kabisa katika huu mgao wa vitabu. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri alichukue hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mawaziri wengi wanachanganya ama niseme sijui ni Makatibu Makuu; wanapoandika Mkoa wa Songwe, wanapoanza kuorodhesha zile Wilaya hawaiweki tena Songwe kwamba kuna Wilaya ya Songwe. Naomba watambue, kuna Mkoa wa Songwe halafu kuna Wilaya ya Songwe, Mbozi, Ileje na Halmashauri ya Tunduma na Momba. Kwa hiyo, kuna Halmashauri tano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimesoma humu nakuta vitabu vyote vimeenda Ileje, vimeenda Momba, vimeenda Tunduma, vimeenda na kule Momba. Sasa huku kwangu sipati. Kwa hiyo, mwaka huu sijapata vitabu, sasa sijui nimwendee nani. Kwa hiyo, nitakwenda pale Wizarani wanipe vitabu nisafirishe mimi mwenyewe nipeleke, maana naona hii sasa ni hatari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo sasa nichangie hoja zangu zile za msingi. Nianze na kuunga mkono hotuba ya Kamati ya Huduma za Jamii iliyosomwa na Mheshimiwa Bashe pale kwenye kuishauri Wizara kuhusu mambo fulani na changamoto za Wizara ya Elimu. Tukianza na utaratibu wa viwango vya ufaulu katika shule binafsi. Mimi ni mdau, naomba ku- declare interest hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ikifika mwezi wa Kwanza shule za private tunakuwa na joining instruction, wanaandika; ili uingie katika shule yangu, unatakiwa ufaulu asilimia labda 41 ama 50 kama zilivyo Seminari. Shule za Serikali utaratibu huo hamna, ukishafaulu arasa la saba, unaendelea mpaka ukaukute Mtihani wa Taifa wa Form Two na mpaka umalize Form Four. Form Two yenyewe ni alama 30 ambayo mimi kama Mwalimu nasema bado ni alama ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inafika mwezi wa 12, mtoto yule hajafikisha hata wastani wa alama 33 mpaka 35. Wanaambiwa; sasa bwana inabidi urudie darasa. Anayekuja kulalamika mtoto kurudia darasa ni mzazi mwenyewe aliyelipia ada, lakini ukienda kwa Afisa Elimu wa Wilaya na Afisa Elimu wa Mkoa wanasema Serikali imekataa wanafunzi kukariri, wasirudie, lazima waendelee. Sasa unajiuliza, hela ni zangu, mtoto ni wangu, elimu ni yangu, atakuja kuajiriwa, mimi mwenyewe ndiyo atakuja kunilinda, sasa iweje tena unanikatalia mimi mtoto kurudia shule? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016 nilizungumza kwa uchungu mkubwa hapa. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anamaliza hoja, hebu alitamke hili. Walilizungumza mwaka 2016 lakini hawakulitolea waraka. Tunaomba shule za private ziwe huru kukaririsha, hakuna shida pale mbona! Tatizo ni nini? Yeye alishasema kwamba huyu mtoto ni slow learner akamwacha; nilizungumza na mwaka 2016 hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wale watoto ambao ni slow learners, kama hawajifikisha kiwango fulani cha marks wasiendelee, warudie mwaka ili wasome vizuri na wazazi ndio wanaotaka wenyewe. Sasa wanawakingia nini? Hilo naomba niliongee kwa uchungu mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni conflict of interest. Sasa hivi wanaoendesha shule Tanzania ni wadau wanne; Wizara ya Elimu ina shule za mazoezi, za msingi na sekondari zile za mazoezi kwenye Vyuo vya Walimu kwa hiyo nao wanamiliki shule, Wizara ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TAMISEMI wanamiliki shule chini ya Mkurugenzi na ni shule nyingi sana, nadhani ndiyo ziko huko kwenye Halmashauri, Sekondari na Primary. TAMONGSCO wanamiliki shule pamoja na TAPIA wamiliki wa shule binafsi, wana umoja wao, wanamiliki shule. Sasa wadau hawa wanne wanaomiliki shule, tunataka tuwe na Regulatory Body ambayo itakaa pale juu kuzisimamia hizi shule kwa sababu kuna conflict of interest.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkaguzi huyu ni mtu wa Serikali, ametoka kwa Mkurugenzi pale pale ama ametoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu; anakwenda kukagua shule ya umma, anaona kuna matundu mawili ya vyoo, anaandika ripoti pale inakwenda kwa Mkurugenzi halafu inakaa tu pale na mambo hayaendi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye shule za private, akikagua akakuta kuna matundu mawili, yaani shule inafungwa siku hiyo hiyo. Ni hapo hapo, hakuna mjadala. Kwa nini wanawanyanyasa hivyo? Kwa nini vile vile na sisi tusiwe na chombo kitakachokuwa kinasimamia hizi shule? Wakaguzi wale wametoka Serikalini, wanaandika ripoti inaenda kwa Katibu Mkuu. Ndivyo hivyo hivyo tupate mtu fulani kama zilivyo mamlaka nyingine, tuwe na mamlaka itakayosimamia hizi shule zote, hao wanaomiliki shule kwa pamoja kuliko hali hii ya kuonewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi kuna mmiliki mmoja wa shule alilalamika akasema Mheshimiwa Mulugo wanataka kunifungia shule. Nikauliza kuna nini? Akasema, wanafunzi walikuwa 48 darasani, maana sheria inasema angalau wanafunzi 40 mpaka 45. Wanafunzi 48 shule moja ya Kigoma, Mkaguzi ameenda pale kama mbogo, anataka kumfungia shule kwamba kuna wanafunzi 48. Nikamwambia hivi, nyuma geuka! Nenda shule ya Serikali, kuna wanafunzi 120 darasani, fungeni nayo hiyo! Jamani vitu hivi viwe realistic! Wanakuwa mpaka 150 na wenyewe wafunge! Tena angalau mambo ya madawati tumeyamaliza, maana walikuwa hata wanakaa chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukienda kwenye shule za private na mmetupa miongozi ninyi wenyewe, tunafuata kila kitu, lakini jamani katika neno la ukaguzi angalau hata asilimia 10 inaweza ikapotea. Watu ni kama wana hasira fulani hivi! Naomba Mheshimiwa Waziri, hebu wasimamie jambo hili, kuna kero nyingi sana kenye shule huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Simbachawene wiki mbili zilizopita, wamiliki wa shule walikuwa Dodoma hapa walikuwa na mkutano wao wa kujadili mambo, tukamualika akawa mgeni rasmi wa kuja kufunga kile kikao. Tukamworodheshea kero zote na kodi zote ambazo tunalipa kule kwenye shule ambapo kero nyingine ni wazazi wenyewe ndiyo wanalipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kibao kinaelekeza labda Mwambao Secondary School kiko pale njia panda. Halmashauri na Mkurugenzi wanakuja wanasema lazima kilipiwe kodi, kwenye shule. Ni huduma ile! Tunalipia kupata vibao ambapo bado unaposajili shule Wizara ndiyo inakwambia kwamba lazima uwe na kibao, tunalipia kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Simbachawene, amekaa na wale wadau, ametulia akaona kwamba kweli hii ni kero. Amesema, kuanzia leo nafuta zile kodi za Halmashauri kwa ajili ya vibao. Tulimpigia makofi na kelele za shangwe na hivi tunasubiri waraka tuweze kufuta ile kodi. Kuna kodi nyingi! Kuna OSHA, property tax; jamani kuna vitu vingine ni vya ajabu kweli kule kwenye shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri, kwa sababu yeye ndiye mdhamimi wa elimu, atusaidie. Naomba tafadhali siku nyingine wawe wanakaa na wadau wa elimu kwenye Halmashauri kule na kwenye Wilaya, waweke watu wa Serikali, watu wa TAMONGSCO na TAPIA wawe wanajadili mambo ya elimu kwa pamoja. Sio maadui, wote ni watoto wetu wa Tanzania kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni ada za mitihani. Mtihani wa Taifa uko Darasa la Nne, Darasa la Saba, Form Four, Form Two na Form Six. Serikali ya Mheshimiwa Kikwete iliamua toka miaka minne iliyopita kwamba hii iwe ni ruzuku kwa wanafunzi wote kwamba wasilipie mtihani wa Taifa. Baraza la Mitihani litoe mitihani bure, lakini ilipokuja huku kwenye utekelezaji wakabagua kwamba hapana shule za private waendelee kulipia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wasifikiri wanakomoa shule za private pale, wala siyo hela ya mmiliki, ni hela ya mzazi mwenyewe ndiye anayechangia. Ukienda kwenye joining instruction tumeandika mzazi alipie ada ya mtihani na Waheshimiwa Wabunge asilimia 90 hapa mna watoto wenu wanasoma kule. Hiyo hela mnailipia ninyi wenyewe. Naomba ile ada ya mtihani wa Form Two na Form Four ifutwe kama zilivyofutwa kwenye shule za Serikali. Mzazi abakie kulipa ada tu, ahenyeke kwenye ada lakini siyo kwenye masuala mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbona Wizara ya Afya chanjo wanatoa bure! Mbona hawabagui inapokuja kwenye chanjo za Shule za Serikali za Msingi na Sekondari! Kwa sababu ni afya ya pamoja; hata elimu wale watoto ni wa pamoja. Wale watoto wakisoma katika shule za private hawaendi kufanya kazi Uganda, hawaendi Kenya wapo Tanzania hapa hapa, ni huduma ya kawaida hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo inaniuma sana. Nashukuru hata kwenye Kamati ukurasa wa maoni Mheshimiwa Bashe, kwa sababu tu muda umekwisha, lakini wameliandika hili wanapendekeza ada ya mtihani ifutwe Form Two na Form Four na Darasa la Nne, kwenye shule za private, iwe kama ruzuku, (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nije lingine ambalo naweza nikatoa machozi kuhusu vitabu. Mungu wangu! Mheshimiwa Susan Lyimo alionesha vitabu hapa lakini nami tayari nilikuwa nimeshafanya search kama Mwalimu. Ninavyo vitabu hapa, Geography for Secondary Schools, Form Three, English for Secondary; Form Four, ni hatari; na hii ni maajabu ya dunia. Ni aibu!

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua kuna mambo mengine lazima tuseme. Serikali ni ya kwangu, nchi ni ya kwangu, watoto ni wa kwangu, Chama ni cha kwangu tunaposema mbili ongeza mbili, mtu mwingine akasema ni sita wakati jibu ni nne, hatuwezi kumfumbia macho.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, kwanza ni-declare interest, mimi ni mwalimu na mdau wa shule binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuipongeza Serikali kwa maamuzi ya kutoa elimu bure nchini, na sisi tunaona na kama walimu tunaona kabisa namna ambavyo hali ni nzuri sana kwenye shule za msingi vijijini huko, wilayani, mkoani, mambo ni mazuri sana. Na hii inasababisha hata kuongezeka kwa uandikishaji na namna ambavyo Form One wanakuwa wengi, Form Five, kwa kweli hali ni znuri sasa tumebaki tu kwenye ule ubora wa elimu (quality education) ndilo tatizo ambalo kidogo naomba Serikali niweze kuingia kuwashauri katika upande huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, dada yangu na rafiki yangu, Mheshimiwa Prof. Ndalichako, kwa kweli ni mtu ambaye ukienda kwenye dawati lake ukimueleza jambo anashaurika, pamoja na Naibu Waziri, na inatusaidia sana kupunguza baadhi ya kero. Ukienda ukimwambia Mheshimiwa kuna hiki na hiki kwa kweli anafuatilia na mambo yanakwenda vizuri, na ndiyo maana mmeona hata kelele zimepungua sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zamani siku kama ya leo wamiliki wa shule binafsi wangekuwa Dodoma hapa zaidi ya mia wanalalamikia mambo yanayoendelea kutokea huko, lakini baada ya kuingia Waziri huyu na Naibu wake wameweka dawati maalum pale Wizarani, pamoja na Katibu Akwilapo, wameweka baadhi ya viongozi, kamishna wanakaa pamoja wanajadili mambo ya kero zinazoendelea kutokea kwenye shule binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema mwaka jana kwamba elimu ni ya wote, Serikali ina shule, Wizara ya Elimu ina shule, shule za mazoezi za sekondari na za primary, lakini TAMISEMI ina shule nyingi sana kwenye halmashauri huko na wadau; TAPIE, TAMONGSCO nao wana shule. Kwa hiyo, kwa pamoja nikawa nimeshauri kwamba tupate chombo fulani hapa juu kitakachokuwa kinamulika hizi shule zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nadhani nilitoa hilo wazo mwaka juzi, mwaka jana nikarudia, na mwaka huu naendelea kushauri. Tupate chombo kitakachokuwa kinaangalia mifumo ya elimu nchini, kwamba shule za TAMISEMI zikaguliwe na chombo hicho, shule za Serikali zikaguliwe na chombo hicho na shule za binafsi zikaguliwe na chombo hicho kuliko kuacha Serikali yenyewe inajikagua yenyewe inafanya kila kitu yenyewe halafu inakwenda na kuwakagua wenzao, wakiharibu ndiyo wanawafungia, hii sio sawa kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba kuendelea kumshauri Waziri, pamoja na hizi changamoto ambazo zipo za kitaaluma, za ubora wa elimu nchini, hebu tupeni nafasi na sisi tuwe tunawashauri mambo yatakwenda vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali kwa kuimarisha Idara ya Udhibiti Ubora wa Elimu Nchini. Kwa kweli Idara ya Ukaguzi – sasa hivi wanaita Udhibiti. Sasa hivi kwa kweli nimeona kwenye bajeti ya Waziri mtajenga ofisi, mtaongeza na magari, nimefarijika sana kwa sababu hii idara naifahamu vizuri sana, bila ukaguzi shuleni huko hakuna kitakachokuwa kinaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamesema wenzetu hapa, hata Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, kuhusu walimu wa Sayansi. Ni kweli kabisa huko shuleni, kwa sababu wanaotakiwa wakaone walimu wa Sayansi hawapo, vipindi vinafundishwa, lesson plans zinaandaliwa, ni wakaguzi ambao ndio wadhibiti ubora, naomba muwawezeshe wafike katika shule, wafike vijijini muwape wagari wakakague shule halafu walete ripoti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ndicho nilichokuwa nasema, kwamba hiyo ripoti kwa sababu wewe ni Serikali unajikagua mwenyewe ripoti unapeleka wapi? Tupate chombo ambacho hicho sasa ndiyo mtakuwa mnapeleka hizo ripoti ili hiyo ripoti inakuja inawasema jamani hapa ni pabaya, hapa ni pazuri, ndiyo hasa hoja yangu ya kusema kwamba tutafute chombo ambacho kitakuwa kinaangalia hizi shule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti VETA; miaka minne iliyopita tulikuwa tuna mpango wa kujenga VETA kila wilaya, na wakati ule ikiwa Wilaya ya Chunya tulichagua mahali fulani tujenge VETA, panaitwa Mkwajuni ambapo sasa hivi ndiyo Jimbo la Songwe. Sasa hii hoja sijui imekimbilia wapi, naona wanatangaza vyuo vya VETA 16 hapa lakini ile Mkwajuni haipo, Wilaya ya Songwe sasa sijui imetupiliwa mbali, sijajua. Kwa hiyo, ninaomba tayari tulishatafuta uwanja, hatimiliki tayari ipo ekari 100, mtuletee VETA pale Songwe, wilaya mpya kwa sababu kitika vigezo ilikuwa inakubalika, kwamba kuna migodi, kuna Ziwa Rukwa, kuna kilimo, kuna misitu ambavyo ndiyo vitu hasa vinavyosababisha tuweze kupata VETA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Shangazi kidogo amejaribu kutafuna zile points ambazo nilikuwa nimeziandaa, lakini ntazirudia tu katika ubora wa kiualimu kwa sababu yeye sio mwalimu, mimi ngoja nizirudie upya. Kuhusu TET, Taasisi ya Elimu Tanzania, wanaochapisha vitabu; kwa kweli naweza nikasema, nitumie neno kwamba majanga bado ni makubwa, Mheshimiwa Waziri naomba tupia jicho pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu nitoe mfano mdogo tu; mwaka juzi Bunge tuliamua, na Mheshimiwa Waziri alitamka, vitabu vyote ambavyo vilikuwa vimeletwa shuleni vimesambaa vilikuwa vibovu vikatolewa, aidha kama mmechoma, hamkutuambia mmepeleka wapi, mlivitoa, na sisi shule za private na sisi tukavitoa tukawa tumekula hasara kwa sababu sisi tulinunua, shule za Serikali waligawiwa bure ila sisi tulinunua kwa fedha zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nikawa nimemwambia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wakati ule alikuwa bwana nani yule, nikataka kuandika barua, wenzangu walisema kwamba tuandike barua tuiambie Serikali na sisi watugawie bure kwa sababu makosa waliyafanya wao na sisi tulinunua kwao. Kwa hiyo, naomba hoja hii niilete tena mwaka huu, na leo nitashika shilingi kwenye kipengele cha Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba vitabu vyote ambavyo shule za private tulinunua vikaonekana ni vibovu tukavitoa, shule za Serikali zimeshagawiwa tayari bure na sisi tupewe bure kwa sababu tuligharamia aidha, mturudishie fedha zetu kwa sababu tulinunua kwenu ninyi wenyewe na mkaviharibu ninyi wenyewe, kwa hiyo naomba baadaye nitashika shilingi, leo nina shilingi kama tatu hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyosema Darasa la Kwanza hadi la Tatu hakuna vitabu vya lugha ya kiingereza kwenye shule za English Medium, amesema Mheshimiwa Shangazi hapa. Na Waheshimiwa Wabunge mjue watoto wenu wengi, asilimia 80 ya Wabunge mnasomesha watoto huko, hata Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na wengine pale Wizarani, mnasomesha watoto huko; hatuna vitabu. Wanachofanya walimu wa shule za private ni kuchukua kitabu kilichaondikwa Kiswahili Histori wanakwenda kufanya translation. Sasa mwalimu wa History hajui kiingereza ila anajua History, anajua content ya Somo la History kwa kiingereza lakini hajui Lugha ya kiingereza kwa hiyo tunawapotosha watoto kule shuleni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba hii Taasisi ya Elimu kama imeshindwa kazi warudishe kama mfumo wa zamani kuwapa ma-publishers private ili mambo yaweze kwenda vizuri. Naongea kama mwalimu na kama nina shule ambaye naona kule tunahangaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jamaa mmoja yuko pale Iringa ni muuzaji wa vitabu vizuri sana, nimemsahau jina lake. Anasema tuna miaka miwili tunatafuta vitabu havipo, na Serikali ilitoa mwongozo na waraka tuwe na text mode moja tu, yaani tuwe na kitabu kimoja nchi nzima tukitumie kama text book. Sasa umetu-limit tusinunue kwa publishers wengine, tunununue TIE, TIE huna sasa tufanyeje? Kwa hiyo, ninaomba Mheshimiwa Waziri, fanya ziara pale TIE uhakikishe vitabu vinatolewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka juzi Serikali ilifuta baadhi ya tozo kwenye shule za private, ilifuta tozo ya kodi ya zimamoto (fire) na ikafuata na SDL na kodi ya mabango, lakini bado watumishi wa Serikali wa halmashauri wanakuja kwenye shule kuwasumbua wamiliki na wengine mpaka wanawaweka na ndani, na Mheshimiwa Waziri ntakupa ushahidi, wanasumbuliwa sana. Hebu tupeni basi tamko leo, tupeni waraka – hili na lenyewe ntashika shilingi – mtupe waraka unaosema mwaka 2017 Waziri wa Fedha alifuta tozo hizi na hizi kwenye shule za private. Kwa nini halmashauri kule wanasumbua, ndiyo maana nimesema kuna disorganization kati ya halmashauri, wizara na wamiliki, tukae pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ungeweka dawati la dialogue au wewe mwenyewe na Katibu Mkuu. Kama tulivyokaa siku moja Serena pale; mimi, wewe, Mheshimiwa Rweikiza, Mheshimiwa Esther na wadau mbalimbali, tukakaa tukaongea mambo yakaenda vizuri. Tuwe tunakaa angalau mara mbili kwa mwaka mambo yatakwenda vizuri sana. Kwa hiyo, ninashauri Mheshimiwa Waziri tufanye hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kingine naomba niishauri Serikali, mpaka hivi ninavyoongea – na hii ntashika shilingi baadaye…

WABUNGE FULANI: Ziko kumi.

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: …kabisa, ntashika shilingi. (Makofi)

MWENYEKITI: Unashika shilingi eeh!

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna chuo chochote cha Serikali kinachotoa mafunzo ya walimu au kuna mtaala wa shule binafsi kwa English Medium. Labda nirudie tena; Waheshimiwa Wabunge naomba mnielewe, nimetoka kwenye field najua; hakuna chuo chochote chenye mtaala wa English Medium hapa Tanzania na Serikali haijajenga chuo hata kimoja, ila vipo vyuo vinafundisha mtaala huo kwa Lugha ya Kiswahili lakini hakuna kwa English Medium, ndiyo tukiwachukua walimu Kenya tunakuja tunakumbana na matatizo makubwa sana ya namna ya immigration hapa Tanzania.

Naomba Serikali, katika hivyo vyuo Mheshimiwa Prof. Ndalichako unavyovikarabati tenga kimoja TET watengeneze mtaala wa kufundishia masomo ya English Medium kwenye shule za private, mtakuwa mmetuokoa. Nasema hayo kwa sababu najua shule zinahangaika namna ya kutafsiri… tunatasiri na mitihani. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Unga mkono hoja basi. (Makofi)

Mheshimiwa, unga mkono hoja.

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja lakini nitashika shilingi kesho. (Makofi/ Kicheko)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. PHILIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa wasaa huu niweze kuchangia bajeti Kuu ya Serikali. Kwanza kabisa pamoja na ushauri wa mambo mengi nitakao shauri hapa niunge kabisa mkono bajeti hii ni nzuri na Mheshimiwa Waziri wa Fedha hongera sana. Lakini tumpe hongera sana mama yetu Samia Suluhu kwa sababu ndiyo Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hongereni sana kwa kuja na bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini masikitiko yangu kidogo tu kabla sijaanza kuchangia Waheshimiwa Wabunge tunaposema tunachangia bajeti ya Serikali bajeti kuu nilitegemea Mawaziri wote wawepo humu ndani. Hapa nawaona Mawaziri watano na kwa sababu nawaona Mawaziri watano, nitachangia kwenye hoja zangu kutokana na Mawaziri ninaowaona kwa sababu lazima wanisikie na wasikie ushauri wangu huwezi kuwa unachangia sehemu ambayo Waziri hayupo halafu inakuwaje. Bajeti Kuu ya Serikali siyo kwa ajili ya Mheshimiwa Dkt. Mwigulu peke yake Bajeti Kuu ya Serikali ni bajeti kuu yote pamoja na Mawaziri wote. Kwa hiyo nilikuwa nataka kwanza kutoa hiyo scenario tunaomba Mawaziri wawepo Bungeni…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mulugo subiri kidogo nitoe ufafanuzi Waheshimiwa Wabunge nimeshasema mara kadhaa humu ndani leo nitazungumza kwa kifupi Serikali iko Bungeni.

Kwa hiyo, msiwe na wasiwasi Mheshimiwa Mlugo kama huwaoni hapa ni kama vile ambavyo viti vingine vya Wabunge vipo huko nje vikizungumza na hawa Waheshimiwa Mawaziri kwa hiyo lazima wawasikilize Wabunge lazima kazi zote zifanyike kwa pamoja. Na wakati huo huo hii bajeti tunayojaribu kuijadili hapa Wabunge mmeshatoa mawazo mengi ambayo mengine yanatakiwa kuanza utekelezaji mara moja hayo yote lazima Serikali ikayafanyie kazi.

Mheshimiwa NaibU Spika, kwa hiyo, usiwe na wasiwasi Mheshimiwa Mulugo changia hata zile Wizara ambazo unaona Waziri hayupo hapa kwa sababu Serikali ipo ndiyo maana wewe unazungumza na mimi ujumbe kwangu wataupata usiwe na wasiwasi wowote Mheshimiwa Mulugo.

MHE. PHILIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, unilindie dakika zangu, nianze na Wizara ya Madini Mheshimiwa nchi hii ingekuwa na fedha nyingi sana nchi hii kwa jinsi unavyoiona hata Mheshimiwa marehemu Mhe. Dkt. Magufuli alikuwa akisema Mungu amlaze mahali pema peponi. Lakini ni kutokana na watumishi wetu wa Serikali wanakuwa ni legelege katika kufanya mambo mengine ambayo unaona kabisa fedha zile pale unaziona.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitatoa mfano mmoja kwenye jimbo langu kule kwangu kuna sehemu kunaitwa Ngwala toka mwaka 2010 kuna kampuni inaitwa Heritage Tanzania imefanya utafiti wa madini, madini adimu duniani yanaitwa rare earth madini hayo kama yangeazwa kuchimbwa Serikali ingeweza kukusanya kodi nyingi sana zaidi ya bilioni 25 Serikali ingepewa kodi mwaka mmoja. Zaidi ya bilioni 83 zinakwenda kwenye gharama za uendeshaji, zaidi ya bilioni 7 mrahaba wa Serikali na mambo mengine ajira peke yake karibuni watu 1300 kule kwangu wangepata ajira na nchi nzima kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini toka mwaka 2010 wanazungushwa kupata leseni special mining nilikuwa nakuomba Mheshimiwa Biteko nakuomba kwa unyenyekevu mkubwa wapatieni leseni hawa Ngwala Peak Resource waweze kuchimba madini hayo ni madini ambayo hayapo Tanzania hii, hayapo Afrika hii yapo kule Songwe na Mheshimiwa Waziri unajua nilikuwa nakuomba ikiwezekana mwezi wa saba usiishe uwape leseni wale watu wanataka kukata tamaa wanataka kuondoka nchini kama walivyoondoka watu wengine ambao walikuwa pale Mbangala wameondoka mafuta yamepatikana pale ukingoni mwa Ziwa Rukwa wamefanya utafiti Serikali imekuja imesema hapana.

Mheshimiwa Naibu Spika, mlikuwa mnafanya utafiti wa gesi mmepata mafuta mmepata na gesi lakini kabla hamjapata mafuta wamekutana na madini ya helium. Baada ya hapo TPDC wamekuja wamesema hapana tufanye pamoja wameshindwa wamekasirika wameondoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, inauma sana. upande mwingine ambao ningeweza kuishauri Serikali naomba nirudi kwenye Wizara…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mulugo kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Dotto Biteko Waziri wa Madini.

T A A R I F A

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa tu taarifa ndogo kwa Mheshimiwa Mulugo najua anachangia kwa hisia kubwa na angetamani uwekezaji ule utokee naomba kutoa taarifa kwenye Bunge lako Tukufu kwamba Kampuni ya PLG itapatiwa leseni ya uchimbaji mkubwa kwa mujibu wa sheria na tuko kwenye taratibu za mwisho za kuwapatia leseni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili kuhusiana na utafiti wa mafuta pamoja na gesi ya helium naomba kumpa taarifa vilevile kwamba kampuni ya helium one tayari imeshapewa leseni ya kufanya utafiti kwenye eneo hilo na taratibu zinaendelea.

NAIBU SPIKA: Ahsante sana; Mheshimiwa Mulugo unapokea taarifa hiyo?

MHE. PHILIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimepata furaha ya ajabu sana hawa ndiyo Mawaziri wanaotakiwa katika nchi hii nimefarijika sana na huo ndiyo unapelekea kwamba kweli mimi naongea ubunge. Ubunge lazima uongee halafu Waziri a take reaction ndiyo maana nilikuwa nimekwambia mara ya kwanza kwamba kuna Mawaziri ukiongea wanakuwa hawapo nilishawahi kuongea mwaka juzi kuhusu…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mulugo ngoja ngoja tuelewane vizuri Waheshimiwa Wabunge nimesema hivi Serikali iko Bungeni na Waziri hapa angeweza kunyamaza wala siyo kazi yake yeye kutoa taarifa angeweza kuja kuchangia na yeye kama Mbunge mwingine na ndiyo maana Wabunge wengine ambao pengine Waziri hajasimama kujibu kwenye hoja yako haimaanishi wewe hujachangia sawasawa ama hajakusikia.

Nadhani tuelewane vizuri hilo Mheshimiwa Mulugo wewe ulikuwa Serikalini unajua zaidi mambo haya kuliko watu wengine ambao hawajawahi kuwa Serikalini. Mheshimiwa Mulugo malizia mchango wako.

MHE. PHILIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naomba dakika zangu zilindwe nimalizie mchango wangu kwa amani. Nije upande wa elimu, ni mwalimu na declare interest kwamba nilikuwa Serikalini kweli kwa kutumikia Wizara ya Elimu kama Naibu Waziri, lakini vilevile nina shule binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lipo jambo lazima tulichangie lakini na dada yangu Mheshimiwa Prof. Ndalichako pale unanifahamu wewe ni rafiki yangu tunaongea mengi na ninakushauri mengi naomba ushauri huu uupokee vizuri. Wakati Mheshimiwa Rweikiza akichangia jambo moja hapa ulisimama ukatoa na mwongozo lakini binafsi sijakuelewa Mheshimiwa Waziri naomba nikushauri kama mwalimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaposema darasa la mitihani darasa la nne, darasa la saba, form two, form four, form six kwa mwaka husika hakuna popote duniani ambapo madarasa hayo yanaweza yakawa hayana mkakati wa kufaulu mitihani hakuna na wote hapa Wabunge tumetoka kusoma wote tumetoka form four huko tumetoka form six tulikuwa darasa la saba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa darasa la saba mwaka sijui tisini na ngapi huko lakini Mheshimiwa Waziri nilikuwa nasomea koroboi mpaka nikafaulu mitihani ni mkakati wa kusoma usiku zinaitwa prepo hata mchana sasa watu wameanzisha June program shule zimeanzisha June program na mfano mzuri ni kwa Mheshimiwa Mtaka Mkuu wa Mkoa wa Simiyu na mpaka Mheshimiwa Rais alikuwa anamsifia namna alivyoanzisha academic June program wakati wa likizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii Mheshimiwa Waziri unasema kwamba hapana watoto warudi nyumbani, darasa la saba mtoto yule akirudi nyumbani saa hizi na mtihani wa Taifa ni mwezi wa tisa watafeli mitihani ndiyo maana Watoto wanafeli lakini sababu ni viongozi nyie mnakataza zile program. Angalia shule binafsi wanavyofanya Watoto wanasoma usiku, wanasoma March program, wanasoma June program, wanasoma September program. Madarasa ya mitihani lazima yawekewe program check it walimu kwenye shule za Serikali tunakosa walimu wa mathematics, tunakosa walimu wa physics tunakosa walimu wa chemistry wakati shule zimefunga, tunasema darasa la sita walimu kwa sababu watoto wameenda nyumbani wale walimu wanaofundisha darasa la sita masomo ya sayansi waweze kuwasaidia kaka zao pale walimu wanajitolea wazazi wameamua kwa pamoja wamelipa fedha ya chakula wamelipa fedha ya malazi, wamelipa fedha za stationary wameamua wenyewe watoto wao wabaki shuleni waweze kujisomea kwa ajili ya mitihani…

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa!

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mulugo, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Cosato David Chumi.

T A A R I F A

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa taarifa Mheshimiwa Mulugo kwamba mimi pale Mafinga shule ya Changarawe haijawahi kuwa na mwalimu wa physics. Kwa hiyo, Juni hii tunachukua walimu kutoka Mafinga Seminary ili waje pale watusaidia kuwa-brush wale Watoto naomba kumpa taarifa. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mulugo unapokea taarifa hiyo?

MHE. PHILIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea kwa miguu miwili na mikono miwili, naongea jambo ambalo mimi naishi huko niko kwenye field mimi ni mwalimu nafundisha economics Form V na VI wakati wa mitihani lazima tuwawekee wanafunzi program, na wewe ulikuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pale ndivyo ilivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri leo naomba nikatae kabisa program zako eti watoto darasa la saba leo warudishwe nyumbani wakienda kule watakuwa wanatumwa sokoni, watakuwa wanacheza cheza acheni wakae shuleni wasome ni jambo zuri naomba sometime Serikali muwe mnasikia mawazo ya wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine la mwisho kipo kitu lazima tukifanye kwenye elimu kinaitwa PPP, naomba nitoe takwimu ambayo ukiyapata hayo unaweza ukaona nini naongea mwaka kesho Serikali itashindwa kuwapeleka watoto form one kwenye shule za Serikali kwa sababu gani. Mpango wa elimu bure ulianza miaka sita iliyopita watoto waliopo leo darasa la sita wako takribani 1,800,000 wanakwenda wapi? Serikali ina uwezo wa kuchukua kwenye darasa yao na madawati Watoto 750,000 tu kwa hiyo ni asilimia kama 100 kwa mwaka kesho lazima Serikali ijenge shule zaidi ya hizi zilizopo shule za Serikali sijui kama tutaweza.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Rais ametoa shule moja moja kila Jimbo lakini bado tuko moja ya mia moja. Serikali naomba ije na mpango wa PPP shule za private zina madarasa, zina madawati zina walimu lakini zinakosa wanafunzi. Nchi ni yetu wote watoto ni wetu wote twendeni tukakae pamoja watu wa shule za binafsi tukae na Serikali tuone namna gani watoto hawa wengine waanze kwenda kwenye shule za private wakajaze madarasa huko halafu Serikali ianze kuwalipa mishahara kule mbona ni kitu kile kile kama ambavyo mlifanya kwenye afya ni jambo jema mno naiomba sana Serikali isikilizage ushauri huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nasema naunga mkono hoja lakini naomba mawazo yangu yachukuliwe na Waziri wa Elimu ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. PHILIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa niweze kuchangia Wizara hii ya Elimu lakini before that nitoe kwamba ni mdau wa elimu na ni mwalimu na ninamiliki shule. Kwa hiyo, nitakayoongea hapa nayaishi kwa kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya hapo ni lazima tuelewe kabisa kwamba Awamu hii ya Sita toka tumepata uhuru ukienda huko vijijini, kama Mbunge na-declare kabisa kwamba tumepeleka fedha nyingi sana kwa ajili ya shule zetu za msingi na sekondari. Hata kwenye kata yangu nilikozaliwa Udinde Kata ya Udinde, nimepewa milioni 600 na Serikali na wananchi wamejenga shule na wamenipa heshima inaitwa Mulugo Sali. Sasa hii ni heshima kubwa nitakufa lakini jina litabaki. Kwa hiyo, lazima nimshukuru Mheshimiwa Rais, kwa kazi kubwa anayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri, Pfofesa Mkenda na Naibu Wake Kaka Kapinga, wanavyoshirikiana vizuri siku hizi na shule binafsi. Tumekaa baadhi ya vikao mara mbili mara tatu tofauti kabisa na miaka ya nyuma ilikuwa mkiandika barua Wizara ya Elimu mkae na shule binafsi wanaogopa kabisa kukaa. Sijajua walikuwa wanaogopa nini? Nadhani Mheshimiwa Profesa Mkenda, umekuwa na GB kubwa sana na unatusikiliza kwa unyenyekevu mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekaa na wewe na wadau wa nchi nzima wametoka mikoani kuja pale Morena, umetusikiliza matatizo yetu yote na mengine unaendelea kuyatatua. Lakini nikuambie ukweli sio siri wanaokuangusha ni watu wako wa chini. Ulikuja wewe ukaja na Katibu Mkuu baada ya hapo kuanzia Kamishina na ngazi nyingine za huku chini yale tuliyoongea no implementation. Yaani hamyatejkelezi yale sasa sijui wanaokuangusha ni akina nani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ile kauli ya kusema kwamba hao ni wanasiasa tu kwa kweli hii kauli nchini hapa huwa ninakwaza sana. Hata juzi imejitokeza pale Kariakoo, yaani wizarani wanamuona waziri kama ni mwanasiasa, kama vile akisema jambo watu wa chini huku hawawezi kutekeleza. Jamani hili jambo ni baya sana kitaifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi Mheshimiwa Waziri Mkuu amekemea hata mambo ya TRA pale Kariakoo. Nimeshakuwa Naibu Waziri najua pale wizarani Maafisa wa kawaida wengi wanamwambia tu waziri si mwanasiasa huyo. Jamani hili jmbo tulikomeshe kwa sababu waziri ana mamlaka makubwa kwenye wizara yake. Naomba hili jambo yaani ni jambo baya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tulifanyie utafiti tuone kwamba ni kweli viongozi wengine huku chini wanadharau mamlaka ya waziri. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, nikupongeze na endelea kuwa na moyo huo huo. Vilevile, lazima nikushauri mambo mawili matatu ili twende vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nipongeze mfumo huu wa Sera mpya na Mtaala mpya wa elimu, kama mwalimu naona umekaa vizuri. Nimepitia sana nimesoma, vipo vitu vidogo vidogo ambavyo tutaendelea kushauri na uzuri mimi na wewe ni rafiki yangu siku hizi tunaongea. Zamani ulikuwa hupokei simu zangu lakini siku hizi unapokea simu zangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafurahi Profesa Mkenda hata ukimuita hivi njoo mnaongea nae, canteen unaongea nae ni mtu mzuri sana. Sasa lazima tukushauri ili wizara yako ikae vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza, katika mtaala huu mpya wa elimu na sera msisahau mambo ya kiutawala. Mmekwenda kwenye practical, kwenye madarasa, sekondari, elimu ya awali na msingi lakini mmesahau kwenye utawala huku ambako ndiko mnakosimamia elimu. Huku na kwenyewe kumeoza kabisa. Mwingiliano wa TAMISEMI na Wizara ya Elimu yaani huku ndiko kumeoza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Profesa jitahidi una shule za msingi karibu 16000 nchini. Tungekuona unafanya ziara unatembelea shule za msingi uone maisha ya kule chini wanavyokuwa wamekaa wale watoto lakini uone majukumu yanavyoingiliwa na TAMISEMI. Yaani Wizara ya Elimu wewe huonekani kabisa, kule wanaonekana Maafisa wa TAMISEMI tu yaani Wizara ya Elimu imepokonywa kabisa mamlaka yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona kuna utofauti mkubwa sana. Sheria Namba 25 ya Mwaka 1978 inasema “Mtaaluma Mkuu katika nchii hii ni Kamishina wa Elimu” ambae unae wewe pale ofisini kwako na una maafisa wako pale. Sasa wachukueni Maafisa wa TAMISEMI basi muwarudishe Wizara ya Elimu. Kwa sababu huu ugatuaji umetuletea shida mno na hasa kwenye utitiri wa mitihani. Yaani kule chini Mheshimiwa Waziri, kuna mitihani ya kata mara mbili kwa wiki, mitihani ya wilaya mara moja kwa mwezi, mitihani ya mkoa mara tatu kwa miezi minne. Sasa kwa mfano sisi shule binafsi kwa nini mnatuingilia? Tuacheni na mitihani yetu. Sisi mitihani yetu inaweza kuwa bora kuliko mitihani yenu mnayoifanya pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TAMISEMI wasimamie shule zao kwa sababu TAMISEMI ina shule zao na sisi shule za private mnatupotezea muda kutuletea mitihani ambayo tunakuja kufanya kwenye Mock. Mbona kwenye Mock tunatii na tunachangia na kwenye NECTA wanatuletea mitihani lakini jamani mpaka mitihani ya kata kweli? Yaani Afisa Mtendaji wa kata anawaambia shule za private siku fulani kuna mtihani halafu tunabaki kutoa hela tu na hizo hela wazazi hawaoni kwa sababu tunatoa shule. Mngekuwa mnatuambia mapema tuweke kwenye joining instruction.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunachangia shule za kata shilingi 100,000 kila wiki. Jamani maisha gani haya? Mitihani ya wilaya kila mwezi yaani wanabaki tu wanafaidi kwenye computer, photocopy kuna posho wanapata ndio maana wanang’ang’ania ile mitihani. Fanyeni mitihani yenu kule chini kama shule za TAMISEMI. Ndio maana nakwambia Mheshimiwa Waziri kwenye utawala hapa msiache. Tunapokwenda kufanya mabadiliko kwenye elimu naomba twendeni na jambo la kupata chombo huru cha kusimamia elimu kwenye nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huku kwingine kote Mheshimiwa Waziri utaweza lakini usipofanya jambo hilo mkachukue basi hawa wadhibiti ubora wa elimu Tanzania hawa basi wabadilisheni hao kiwe ni chombo huru kiwe na mamlaka kama ilivyo TCU kwenye vyuo vikuu, kama ilivyo NACTE kwenye vyuo vya kati. Sasa shule ya awali, shule ya msingi na sekondari hawana msimamizi yaani hawana Baba na Mama kabisa. Tena sisi private ndo tumbaki kama yatima hivi. Yaani unafikiri jambo sijui niende Wizara ya TAMISEMI, sijui niende kwa Mheshimiwa Profesa Mkenda lakini husikilizwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalia mambo ya tozo hapa nani wa kutusikiliza? Hamna. Waziri wa Elimu, huwezi kuzitoa tozo, najua Sheria huwezi kuzitoa tozo. Waziri wa TAMISEMI, ndiye anayetoza tozo kule chini kwa sababu mlilazimishwa mkatupa leseni za biashara. Kwa hiyo, nyie mmezi-term hizi shule kama biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii na-quote kwa sababu Afisa wako wa Baraza la Mitihani siku ametoa ranking anasema “hapa tunafanyia watu biashara” Mungu wangu. Watoto wetu ni watanzania hawa hawa wanapokuwa wamefanya vizuri kwenye private ni watoto wa ndani hawa hawa, wanakwenda kuajiriwa Serikalini huko huko watapata uelewa mkubwa na GB kubwa kwa kufanya kazi za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa naomba Waheshimiwa Wabunge, tumsaidie Mheshimiwa Waziri afanye mabadiliko haya lakini baadhi ya mabadiliko Mheshimiwa Waziri hawezi. Sheria Namba 25 ya Mwaka 1978 inaniambia kama private nakwenda kusajili shule yangu kwa kamishina ananipa kibali, ananipa cheti lakini sikuambiwa kama ni biashara. Bila hivyo, shule hizi zisingeanzishwa ndio maana unaoana siku hzi hata uwekezaji wa shule umedolola kabisa. Nani anatamani kujenga shule saa hizi? Tuliojenga tumejenga kama ni kula hasara tumekula hasara. Mheshimiwa Waziri, tuwe creative, jambo ni kubwa mno nendeni huku chini mkaone mambo yanavyokuwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado niendelee kuisisitiza jambo lingine kuhusu ranking, Mheshimiwa Waziri, ranking duniani kote, uliongea vizuri sana lakini kwa sababu Mheshimiwa Waziri anapoongea huwezi kumpinga wala huwezi kusema mwongozo kwa sababu tu unatoa taarifa. Jamani Profesa ulitusomesha vizuri pale lakini uliongelea upande wako mmoja. ungetukaribisha na sisi wadau wa elimu kama zinavyofanya wizara nyingine, kwamba kabla hamjaamua mambo mnakaa na wadau wanaokuwa kwenye sekta hiyo mnakaa pamoja mnasema jamani tuondoe ranking au msiondoe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo shuleni watoto hawasomi kabisa wanacheza madarasani. Hakuna ushindani kwenye taaluma. Tunakwenda kuleta watoto mbumbumbu baada ya miaka 10 mtakuja kuniambia. Mimi nadhani sasa shule za private ndio zinakuwa maabara za kuangalia mfano kwamba hawa kumbe ndio wanakwenda hivi. Kwa sababu kama alivyosema Mheshimiwa Waitara, kwenye private kuna kila kitu, Tunagharamia kila kitu kiwepo ili nyie watu wa Wizara za Serikali muige kule tupate Watoto ambao ni wazuri lakini sasa hivi ninyi mnashindana na sisi. Ngoja tutoe hiki ili hawa wa–suffocate, ngoja tutoe hiki ili hizi shule zife. Tutakufa sawa hakuna shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Serikali ikiamua tutakufa lakini baada ya hapo tutapata vijana ambao ni mbumbumbu kwa miaka ijayo. Mheshimiwa Waziri na wote humu mnajua ndio maana nilishasema siku moja, asimame mtu hapa aseme mimi mtoto wangu anasoma shule za Serikali. Sio kwamba na-challenge shule za Serikali lakini nataka nikupe changamoto ili uweze kuboresha shule zako. Ndio maana hata Serikali mmeweka baadhi ya shule kuwa ndio shule za mfano zipo, twendeni huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe sana lakini lingine ni kuhusu nyaraka za Serikali, ni utitiri, mwenzangu jana Mheshimiwa Rweikiza ameongea hapa. Nimesoma hapa yaraka 110 za Serikali yaani kama vile Sheria haifanyi kazi. Yaani kila bada ya miezi sita mpaka ukute waraka shuleni. Siku moja nilikwambia pale Mheshimiwa Waziri, mbona Wizara yako haitulii? Angalia wizara nyingine zilivyotulia hatuna malalamiko ni machache machache lakini Wizara ya Elimu kila siku mnataka kukwaza watu. Yaani hauwezi kutulia, huwezi kumfundisha mtoto kuanzia darasa la kwanza mpka form four angalau anakwenda katika mwelekeo wa elimu hii. Katikati pale anavurugwa, mara ondokeni boarding kuna wakati nashangaa sana siijui nani aliyewashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo ni darasa, kuna waraka unaosema kwamba daradsa la nne ni lazima wamalizie pale plae na mmetoa na namba ya kumalizia shule pale pale halafu mmetoa nan amba ya kumalizia shule shule palepale halafu mwezi wa saba mnasema waondoke, itakuwaje sasa? Nina shule Mbeya mtu anakuja kutoka Tunduma amekuja pale St. Marcus shuleni kwangu halafu sasa mwezi wa saba arudi Tunduma. Kule Tunduma aliko kule Chapwa hakuna English medium atakwenda wapi? Atahamia wapi? Lakini ulishampa namba ya NECTA afanyie mtihani pale pale kwenye kile kituo. Sometimes mnafanya vitu ambavyo hamshirikishi Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi kwa kupewa nafasi dakika tano hizi za kuchangia Wizara Kuu ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina hoja ndogo sana leo, Mheshimiwa Dkt. Mpango naomba unielewe, nakuwa nazungumza kila siku kwenye hotuba zangu namna ambavyo Wizara yako, hususan pale Hazina, sijui kuna mfumo gani mnaoweka, jinsi mnavyopendelea kutuma fedha kwenye Halmashauri. Baadhi ya Halmashauri hatupati fedha, hata kama ni hizo hela ambazo mnakuwa mmekusanya ndogo baadhi ya Halmashauri hatupati fedha, tunalalamika kila siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nasema kila siku hapa, nina Wilaya mpya lakini sina maji, sina barabara ya lami, sina vijiji vyenye umeme kama vijiji vingine, sina kiwanda hata kimoja, hata Chuo cha VETA hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2013 niliambiwa nitafute eneo, tukatafuta eneo ekari 100 pale Mkwajuni na hatimiliki ipo, lakini mpaka leo hakuna mikakati yoyote ya kuniletea VETA pale Wilaya ya Songwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kila siku nasema, nina Wilaya mpya sina Hospitali ya Wilaya, sasa nataka kuona bajeti ya mwaka huu kama mnaniletea hivi vitu, kwa sababu sehemu nyingine wanavyo. Sasa mnapogawa fedha pale Hazina kwa nini hakuna Kamati Maalum ambayo angalau ingekuwa inatenga kwamba okay, hiki kinakwenda Same, Same wana hiki na hiki, labda hiki kinakwenda Halmashauri ya Tunduru, Tunduru hawana hiki basi hiki kiende kwenye Halmashauri fulani, yaani kuwe na relation fulani ya kuona kwamba Halmashauri nyingine wana hiki basi na hawa wapewe hiki, tungekuwa tunakwenda hivyo nchi hii ingeendelea hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kuna watu wanapewa ambulance hapa, wengine hata haijulikani tunapewa lini. Yaani unakuta kila siku wewe ni mtu wa mwisho tu. Jamani mnataka tuseme nini humu ndani, sisi wengine sio Wabunge? Naomba, nimelia Barabara ya kutoka Mbalizi kwenda Mkwajuni kilometa 90 tupate lami, hakuna, lakini ukija kwa Waziri wa Barabara hapa unakuta barabara inakwenda maeneo fulani. Wanazo barabara, lakini wana hospitali, wana majengo ya Wilaya, sisi wengine mtatupa lini vitu vyetu? Jamani, wote ni Watanzania tugawane keki hiyo, nalalamika kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Wizara hii hupati chochote, ukienda huku hupati chochote. Juzi nimelia habari za umeme hapa; nashukuru sana Mheshimiwa Dkt. Kalemani hapa amenitafutia watu wa REA nimekaa nao tumepanga vitu. Yaani mpaka useme ndio upate, usipolalamika hupati, kwa nini? Mnataka tuje tuanze kulia machozi humu ndani ya Bunge? Jamani, tunataka na sisi tupate keki ya Taifa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka juzi hapa, sijui ni mwaka gani, kuna Mbunge mmoja hapa alisema Serikali inapendelea, tena alisema wazi, nadhani alikuwa ni Mheshimiwa Zitto, na mimi nataka kusema Serikali inapendelea, kwa nini wengine hatupati wengine mnapata? Mikoa ya Rukwa, Katavi, Songwe na Kigoma, hatuna chochote, fedha zote zinakwenda mikoa mingine, kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Dkt. Mpango, weka pale Hazina tume ndogo itakayokuwa inaangalia kwamba hiki kama kimekwenda mahali fulani basi trip nyingine wapate na wengine hivi, tugawane jamani, wote ni Wabunge humu ndani na wote ni wananchi, kila siku tunalia mambo hayo hayo, eeh, jamani. Tafadhali, ninaomba kwenye bajeti hii mnipe Hospitali ya Wilaya pale Songwe, ni mbali sana kutoka pale Songwe tunakwenda kuhudumiwa na Mkoa wa Mbeya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalia kila kitu, mimi nikisimama hapa kila siku ni malalamiko tu, hakuna siku ya kuja kusema jamani na mimi angalau nimepata hiki. Nataka na mimi niwe ni Mbunge ambaye nikisimama niseme Serikali nashukuru mmenipa hiki, sasa kila siku mimi ni kulalamika tu, hamnionei huruma? Kila siku tunalalamika tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafadhali naomba sana, Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, nataka kwenye bajeti hii mnipe maji. Mwaka kesho kwenye bajeti ya Serikali hapa mtanitambua kama hamjanipa hivi vitu. Tupatieni basi, ni hilo tu kwa leo. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/2018
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ili kuweza kuchangia katika Wizara hii ya Nishati na Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa hatua zote alizozichukua kuhusu masuala ya mchanga. Nakubaliana naye kabisa kwa asilimia 100 na tunasubiria hiyo Kamati nyingine ambayo inashughulika na masuala ya kiuchumi na sheria tuje tuone na yenyewe itasema nini, halafu baada ya hapo twende mbele. Hata hivyo, kwa hatua mpaka hivi sasa tunavyosema nakubali kwa asilimia 100 kwamba Mheshimiwa Rais ni mzalendo sana katika nchi hii na anavaa kabisa uzalendo katika nchi hii kwa ajili ya kulitumikia Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nirudi kwenye masuala ya Jimbo langu la Songwe. Daima nikiwa nachangia hapa huwa nasema miaka yote, kwamba; sasa sijui nitumie neno Serikali kwa ujumla ama niseme tu Wizara hii; Wizara ya Nishati na Madini Jimbo la Songwe naona kama vile inapendelea. Mheshimiwa Mwijage utakumbuka ulipokuwa Naibu Waziri wa Wizara hii alifika jimboni kwangu, Kata ya Kanga na aliniahidi kunipa umeme na hivi nimwambie Kata ya Kanga umeme unawake kwa initiatives zako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Jimbo la Songwe lina kata 18 na hivi ninavyosema kata sita angalau zina umeme na kata 12 hazina umeme. Hata hivyo, Waheshimiwa Mawaziri hawa wanasahau kwamba tulikuwa Mkoa wa Mbeya zamani, sasa tuko Mkoa wa Songwe. Kule kwa Mheshimiwa Mwambalaswa vijiji vingi vina umeme, kule Mbozi vijiji vingi vina umeme, kule Momba kwa Mheshimiwa Silinde vijiji vingi vina umeme, kasoro Jimbo la Songwe, kuna nini? Mheshimiwa Dkt. Kalemani, nimekwenda mara nyingi sana ofisini kwake, nimekwenda kwenye dawati lake kumlalamikia, kwa nini Jimbo la Songwe hawatuletei umeme? Tumekosa nini mbele za Mungu?

Mheshimiwa Naibu Spika, wiki iliyopita nilichangia hapa kwenye Wizara ya Elimu, nikasema kwamba wenzetu kule, sisi wilaya mpya hatuna chochote, hatuna majengo ya wilaya, hatuna nyumba za watumishi, hatuna barabara ya lami, hatuna VETA, hatuna maji makao makuu ya wilaya, yaani kila kitu hatuna, hata umeme vijijini hatuna, yaani hata umeme tu tukose? Kwa kweli kesho nitakuwa mkali sana kwenye kushika shilingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sijawahi kuwa mkali kwenye hilo, lakini kesho, Mheshimiwa Mwijage, nitashika shilingi yake, kwa sababu yeye ameshawahi kufika kwenye jimbo langu, anawafahamu wananchi wangu na tulimpa na ng’ombe na mbuzi siku ile Mheshimiwa Mwijage, tukamweka akawa Mtemi kwa sababu alifanya jambo zuri sana na alichangia na maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo Kata za Gua, Udinde, Kapalala, Mbangala, Manda, Namkukwe na Mpona na vijiji zaidi ya 30, hatuna umeme. Nimekwenda pale REA Makao Makuu kulalamika lakini mpaka leo umeme hakuna, kuna nini Songwe na ni mkoa mpya na ni wilaya mpya? Jamani naomba na sisi watufikirie tuweze kula keki ya Taifa na sisi, wanatunyanyasa mno, hatuna chochote, nalalamika kila siku hapa. Mwenzenu sina barabara, nimesema hapa, sina chochote, basi hata umeme wa REA. Naomba, Mheshimiwa Dkt. Kalemani, nimemlalamikia sana kila siku nikija anasema atanipa mkandarasi, siwaoni hao wakandarasi wa Songwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mtu wamemweka kule Mbeya anayesimamia masuala ya nishati ya umeme Mkoa wa Songwe, hapatikani na Mheshimiwa Naibu Waziri, nimemlalamikia huyo mtu kwa nini wasimuwajibishe. Hataki kushirikiana na Wabunge wa Songwe masuala ya umeme na anamfahamu na nilimpa na namba zake za simu, please, naombeni umeme. Safari hii na mimi sasa nitakuwa mkali, nimekuwa mpole mno, nitakuwa mkali sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Shanta Gold Mining ambao kule kwetu wanajiita New Luika Gold Mining; kwa kweli watu wa madini hawa; ndiyo maana nimempongeza na Mheshimiwa Rais; watu hawa ni waongo sana. Mwaka wa jana amekuja Mheshimiwa Profesa Muhongo kwenye jimbo langu, tumekwenda kwenye Kijiji cha Saza, tumekubaliana na Mheshimiwa Dkt. Kalemani anajua, watu wa Kijiji cha Saza wamelalamika, kuna eneo la wachimbaji wadogo wadogo lakini watu wa Shanta wameliingilia eneo lile mpaka kwenye nyumba za wananchi, makaburi, miembe, miti, kila kitu kimekwenda Shanta, kwa nini.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kumlalamikia Mheshimiwa Profesa Muhongo, wamekuja na Mheshimiwa Kandoro aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya mwaka jana wamefika pale, tumekaa vikao siku sita, tumehukumu kesi na watu wa Shanta wakashindwa mbele ya wanakijiji, mbele ya mkutano wa hadhara na TBC walionesha na mimi nilikuwepo pale. Hata hivyo, Mheshimiwa Waziri alitoa ruling pale pale, kwamba eneo hili tuwape wananchi, lakini mpaka leo sina barua inayowaonesha wananchi kwamba wamepata lile eneo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Kalemani na yeye nakumbuka nilimwambia, naomba kesho aniambie, baada ya Waziri kutamka kwamba lile eneo ni la wananchi na wamuulize Mheshimiwa Profesa Muhongo popote huko alipo aseme baada ya pale nini kilichoendelea, nakwenda ofisini kila siku anasema subiri. Hawa watu wa Shanta wana nini? Wametoa nini huko?

Mheshimiwa Naibu Spika, haya, juzi nilikuwa Jimboni, nimeuliza swali jana hapa kwa Mheshimiwa Waziri wa Maji, nasema hivi; hawa watu wa Shanta hawa tena wamefunga tayari mto. Mto unatoka Rwika unakwenda Mbangala mpaka Maleza wamefunga kwa ajili ya wananchi wasipate maji, kwa nini wanatuonea hivi jamani? Vijana wa Mbangala mpaka wakataka kufanya fujo lakini Polisi wakawaweka ndani, tunawaonea wananchi bure. Hawa watu wa madini ni waongo sana na mimi ndio maana sielewani nao kwa sababu ya hiyo toka mwaka jana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu nilipomwambia Mheshimiwa Profesa Muhongo amekuja pale sasa na hilo eneo tumewanyang’anya, basi leo ni chuki ya Mbunge na wananchi hatuelewani kule Songwe. Naomba tafadhali sana, maji yafunguliwe la sivyo mimi nitakwenda jimboni kuwachukua watu wa Saza na kuwachukua watu wa Mbangala tukashirikiane tuchukue majembe na shoka tukatoboe lile bwawa ili na mimi mje mnipige, mnifunge, haiwezekani kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mikataba wameweka na kijiji lakini ni mikataba feki; na wamesema wao wenyewe kwamba; mikataba tumeweka, hamuwezi kutufanya chochote kwa sababu sisi Serikali inatulinda. Tafadhali sana Mheshimiwa Mwijage, Mheshimiwa Dkt. Kalemani, nawaomba suala hili walitamkie kesho watu wa Ashanti watoboe lile bwawa na wananchi wangu waweze kupata maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo wala siwezi kuchangia mambo mengi sana, naomba tupate...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzunguzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutumia fursa hii kukushukuru kunipa nafasi hii ili kuweza kuchangia Wizara hii kubwa namna tunavyoendesha nchi yetu kwa sababu hapa ndiyo penyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, utakumbuka mwaka jana kama siyo mwaka juzi, nilichangia hapa mifumo ya Serikali tunavyoendesha hasa katika ugawaji wa rasilimali. Nililalamika sana hapa Mheshimiwa Mpango ulinisikia lakini napenda kushukuru kwamba baada ya malalamiko yale, naweza sasa leo nikajidai hapa nikasema sasa Songwe tuna hospitali na kila kitu ambacho nilikilalamikia pale ikiwemo miradi ya maji. Kwa haya yote, nikupongeze sana kwa namna ulivyonisikia na namna ulivyotekeleza mambo kwenye Mkoa wetu wa Songwe na Jimboni kwetu. Naishukuru sana Serikali ya Awamu hii ya Tano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa mambo yote yanayoendelea kutekelezwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Vilevile nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kikao alichokifanya cha wafanyabiashara two weeks ago pale Dar es Salaam. Kwa kweli kikao kile kimetupa dira na kimeleta mwelekeo mzuri wa wafanyabiashara Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Wabunge tumekuwa tukilalamika sana humu ndani na Waheshimiwa Wabunge mtaniambia, mengi ambayo tumekuwa tukiongea sasa ndiyo yaleyale ambayo aliongea na wafanyabiashara lakini Mawaziri wetu ni kama vile mna-ignore Wabunge. Tukiongea sisi hata wale watumishi wenu wanasema aah wameongea tu wanasiasa, ni siasa tu, lakini tumeongea sana humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka hata Mheshimiwa Musukuma alivyoongea pale aliongea yaleyale ambayo kila siku anaongea humu ndani na sisi tunaongea hayohayo. Hata hivyo, kwa sababu kilikuwa ni kikao special ameitisha Mheshimiwa Rais yakachukuliwa kama vile ndiyo mambo ambayo ni makubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli naomba Waheshimiwa Mawaziri, Mheshimiwa Dkt. Mpango na sisi Wabunge tukiongea mambo hapa undeni Tume ya kufuatilia yale ambayo tunakuwa tumeyaongea, mtapata faida nyingi. Tusingefikia pale kama mngekuwa mnachukua michango ya Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kusema kwamba Mkoa wa Songwe kule Jimboni kwangu, hivi ninavyoongea kuna kampuni moja inaitwa Heritage Rukwa Tanzania Ltd wale Wazungu wameenda kwao kwa sababu hawajaelewana na TPDC. Hawajaelewana nao kwa sababu hawa watu wa kampuni ya Heritage walikuja kufanya utafiti wa kuchimba mafuta.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kampuni hii ndiyo iliyofanya utafiti wa kupata mafuta kule Uganda ambapo sasa hivi pipeline inaendelea kutengenezwa kufika Tanzania. Ni kampuni kubwa ambapo tungeweza kunufaika nayo sana. Wamefika Jimboni kwangu Kijiji cha Maleza, wameanza kufanya utafiti wao, wamechimba na wameyakuta mafuta. Baada ya pale wamerudi Serikalini kufanya negotiations katika sheria zetu ambazo zimebadilika mwaka juzi kuhusiana na masuala ya mafuta na madini. Mpaka hivi ninavyozungumza Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wale watu wameondoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali ifuatilie ule mgogoro ni nini hasa? Maana yake mpaka sasa hivi wameshatumia million 3.6 USD; wameshajenga madaraja na wameshafanya kila kitu. Ukiongea nao unaweza ukatoa na machozi lakini kuna watu wapo pale Shirika la Petroli sijui wamefanya nini na wale Wazungu. Naomba Serikali hebu lichukueni hili kama ni serious issue. Mheshimiwa Rais akija Songwe nitamwambia na nitamfikisha sehemu ile. Sasa kabla Mheshimiwa Rais hajafika Songwe, naomba Serikali na nyie mkae na watu wa Heritage Tanzania wapo pale Dar es Salaam muone tatizo ni nini. Hii inatupotezea umaarufu mkubwa sana wa kujipatia fedha kwa ajili ya masuala ya mafuta. Wenzetu Uganda walikubali na wamefanya na sasa hivi mafuta yamepatikana kule Uganda.

Mheshimiwa Naibu Spika, yule RAS ambaye Mheshimiwa Rais ametupa Songwe ni very creative yule kijana anaitwa David Kafulila. David Kafulila ameshawishi Mkoa wetu kupitia RCC tumeanzisha kampuni inaitwa Songwe Business Company Ltd. Wakurugenzi wa Halmashauri ndiyo wadau na ndiyo board directors kwenye kampuni ile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kampuni hii tayari TAMISEMI walishaturuhusu na imeshaanza kufanya kazi. Naomba kila Halmashauri au kila mkoa kama wangeweza kupitisha kwenye RCC zao tuwe na kampuni kama hizo ambazo zinamilikiwa na RAS pale mkoani, inafanya biashara kuliko kutekeleza kule Halmashauri ambako kuna bureaucracy nyingi sana. Ni jambo zuri na mtakuja kuona faida yake. Sisi baada ya miaka mitano tunaweza tusiwe tunaomba hela Serikali Kuu, RAS wetu Kafulila anafanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hiki kitu ni kikubwa sana, siku moja Waheshimiwa Wabunge nitawaletea ile Memorandum of Understanding ya RCC ya Songwe, ni jambo kubwa sana Mheshimiwa Mama Mbene anaweza akani- support hapa. Kwa hiyo, naomba hata Halmashauri zingine ziweze kufanya hivyo, hii kampuni inamilikiwa na Halmashauri zote tano za Mkoa wa Songwe na Ma-DED ndiyo board members wa kuendesha miradi ya kibiashara kwenye Halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda nilichangie ni kuhusu suala la EPICA, kuna kitu kinaitwa EPICA kwenye mfumo wa fedha. Nataka niseme kabisa kwa machozi makubwa, hii EPICA, of course sisi siyo wataalam wa kujua EPICA ni nini lakini angalau mimi najua. EPICA hii inasumbua sana baada ya kupitisha bajeti hii, tarehe 30 Juni, 2019 kesho kutwa baada ya bajeti kupitishwa hapa, fedha zote za kwenye Halmashauri zinafungwa. Kuanzia tarehe 1 Julai, 2019 mpaka ije ifike tarehe 30 Julai, 2019 kule kwenye Halmashauri kunakuwa hakuna mfumo kabisa wa namna ya ku-access fedha za Serikali mpaka tarehe 1 Agosti au mpaka Septemba.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka mwaka jana mpaka Halmashauri wananiuliza Mbunge tuna mfanyabiashara gani mkubwa hapa tunaweza kumkopa fedha tuweze kukamilisha labda mahitaji ya Halmashauri. Naomba tutafute mfumo mwingine ambao unaweza ukasaidia ili baada ya bajeti kupita, angalau tarehe 15 au hata baada ya wiki mbili Serikali ifungue mifumo yake ya fedha. Nini maana ya kujenga mkongo wa Serikali kwa Halmashauri? Kwa hiyo, mifumo ya kompyuta ifunguke mara moja ndani ya wiki mbili Halmashauri ziweze ku-access fedha ili tuweze kutumia. Najua Waheshimiwa Wabunge wenye Majimbo mtakuwa mnahangaika sana na mifumo ya fedha kuanzia Julai na Agosti kwenye Halmashauri zetu, kwa kweli mimi kule kwangu inasumbua sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, mimi mchango wangu leo ilikuwa ni hayo, hasa mfumo wa EPICA na Heritage Company, watu wa TPDC waweze kukaa na Serikali na wale Wazungu ili mambo yaweze kwenda.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. PHILIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nimwombe sana Mwenyezi Mungu niweze kuzungumza katika hali ya kawaida nisi-panic kwa sababu Wizara hii ilitaka kusababisha mimi nipoteze uhai kwa sababu ya suala la stakabadhi ghalani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naongea hapa kwa niaba ya wananchi wa Songwe, Wilaya ya Songwe ambayo takribani miezi miwili sasa tulipata kidogo mgogoro juu ya suala la stakabadhi ghalani. Cha kwanza, nataka nielezee Wizara ya Kilimo sijui kama wanafanya utafiti. Suala la stakabadhi ghalani Wizara ya Kilimo au Serikali kwa ujumla wanasema ni suala la mpango wa kumkomboa mkulima, si sawa kila suala hili ni zao la kumchanganya mkulima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mkulima hana amani kabisa na suala la stakabadhi ghalani. Ni kweli jambo hili lipo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na naomba ikiwezekana kama tunaweza hata tukalirekebisha tulitoe kabisa kwa sababu kule vijijini haliji katika mfumo wa kubembelezana, ni jambo la lazima kwa Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haiwezekani! Mkulima huyu wakati anaandaa shamba Serikali haipo wala haimwoni, mkulima huyu anapopalilia Serikali haipo wala haimwoni, anakopa fedha kwa wachuuzi wa zao la ufuta au alizeti Serikali haipo, halafu baadaye mwezi Machi au Aprili, ufuta umeshang’aa sasa umekomaa, Serikali ndiyo inakuja inasema, sasa ufuta wote huu tunaomba msiuze kwa huko mlikokuwa mmekopa hela ila mpeleke stakabadhi ghalani. Haiwezekani katika hali ya kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilihama Bungeni hapa sikuwepo takribani mwezi mzima, nilikuwa Jimboni nashughulikia wakulima wangu hapa. Ni kero kubwa, nimshukuru sana Mheshimiwa Bashe nilimpigia simu, Mheshimiwa Waziri nilimpigia simu alipokea baadaye akasema atanipigia na hakunipokea, nina jambo naye, lakini namshukuru sana Mheshimiwa Bashe kwa sababu alipokea simu na kesho yake aliwatumia Mrajisi na Mr. Bangu, Mkurugenzi wa Stakabadhi Ghalani, akaja mpaka Songwe Jimboni. Nimewaona wale pale wamekaa, waseme wenyewe waliona nini kule jimboni. Haiwezekani mambo kama haya Serikali tunaangalia tu! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba Wabunge wenzangu kesho waniunge mkono, kesho nitavaa suti nyeusi hapa kwenye kushika shilingi, kwamba stakabadhi ghalani tunaizika kesho, haiwezekani! Kesho ni msiba wa stakabadhi ghalani nchini Tanzania. Haiwezekani kabisa, nakataa. Jambo hili ukiwaona wale wakulima wanahangaika nalo.

Mheshimiwa Spika, kule Songwe kuna maghala matatu…

MHE. KIZITO J. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

T A A R I F A

MHE. KIZITO J. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Mulugo kwamba stakabadhi ghalani inatamkwa kwa jina Tanzania, lakini practice ya stakabadhi ghalani Tanzania ni collection center ya mazao, inalenga kukusanya mapato ya Serikali, na siyo kuwasaidia wakulima wadogo. (Makofi)

SPIKA: Sisi Mkoa wa Dodoma, maeneo yaliyokuwa yanalima ufuta mwaka huu wameacha kabisa kulima ufuta. Wameacha kwa sababu ya kutotaka kugombana na Serikali kuhusu stakabadhi ghalani, maana ukishapata huo ufuta unaweza ukafungwa bure na zao la kwako mwenyewe. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mulugo, endelea.

MHE. PHILIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa kwa mikono miwili na miguu miwili. Kama nilivyosema, mkulima huyu tunasema eti tunamtetea mkulima huyu. Wilaya ya Songwe ni kubwa kuliko hata Mkoa wa Songwe wenyewe ukilinganisha Wilaya ya Mbozi, Momba na Ileje, lakini tulikuwa tumewekewa center tatu za ukusanyaji wa ufuta, Mkwajuni, Chang’ombe na Kanda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kutoka Mkwajuni mpaka uende nilikozaliwa mimi Kijiji cha mwisho kabisa karibu na Ziwa Rukwa kule ni kilometa 168. Mkulima huyu anyanyue debe mbili za ufuta alete Mkwajuni aje auze, nilikataa na nilimwambia Mkuu wa Wilaya utaniweka ndani bure. Haiwezekani katika mazingira ya kawaida, lakini Serikali inaendelea kulazimisha, Mrajisi yuko pale nimemuona aseme mwenyewe aliona nini Songwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mkuu wa Wilaya ya Songwe Ilikuwa ukiwa na ufuta akikukamata anakuweka ndani, mpaka ninavyosema hivi, pikipiki ziko ndani, alikuwa ameshikilia magari yote ya wakulima, haiwezekani tu katika mazingira ya kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini hata hivyo, wale watumishi wa Serikali wa Wilaya ya Songwe hasa Afisa Kilimo, alikuwa akienda vijijini anasema elimu imetolewa. Mimi ndiyo mfadhili mkubwa wa vikoba kwenye jimbo langu, wanakwenda kwa mwenyekiti wa vikoba wanasema, naomba uandike barua hapa nakupa shilingi 100,000/=, saini hapa, sema hiki Kikoba, ni Chama cha Ushirika cha Msingi, ni uongo mtupu. Haiwezekani katika mazingira ya kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kesho, Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Bashe, tuseme kesho, stakabadhi ghalani ndio basi haiwezekani, ni jambo baya mno kwa mkulima, tuweke kama tulivyoweka kwenye ada elekezi. Serikali ilisema ije na ada elekezi kwenye shule binafsi, tukasimama kidete tukasema hivi, kila mtu ana fedha zake ampeleke mtoto anakotaka mtoto kusoma shule. Aende Kenya akasome shule, aende Marekani akasome shule, tumuache mkulima kwenye ufuta akauze anakotaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nenda sasa hivi Wilaya ya Songwe wakulima wa ufuta wanauza Mbalizi, wanauza Mkwajuni, wanauza Tunduma, wanauza Mbozi they are free, tuwaache wawe free kwa sababu, ndiko wanakofaidika huko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mkulima katika maisha ya mwaka mzima anakopa fedha za kwenda kujitibu masikini ya Mungu, anakopa fedha kumpeleka mtoto shule mwezi wa kwanza, anakopa fedha kwa ajili ya kuendeshea mifumo ya chumvi, sabuni. Leo hii amechukua fedha pale kwa jirani yake ambapo amemuambia atamlipa ufuta wameandikishana, butter trade wameandikishana, leo Serikali inakuja kusema kwamba, ufuta wote mpeleke pale mkauze kwa stakabadhi ghalani, tunakupa risiti, tutakupa fedha baada ya masaa 48. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii Mbunge nalipa wakulima wangu wa pamba toka mwaka 1995 niko form six, watu walikuwa wanauza pamba hawajalipwa mpaka leo na risiti ninazo, nitakuletea Mheshimiwa Bashe risiti za wakulima wa Songwe wanaodai fedha za pamba, ilikuwa ni mambo ya stakabadhi ghalani. Nazungumza kwa uchungu mkubwa sana naomba ninyamaze. Siungi hoja mkono. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia wasaa nami niweze kuchambua hoja, lakini mimi nijikite kwenye mambo makubwa mawili hasa sekta ya elimu, nami ni mdau wa elimu hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wabunge mnisikilize. Lipo jambo linaendelea kwenye mashule yetu nchi nzima ambalo jipya mno halijawahi kutokea toka tumepata uhuru. Jambo hilo linaitwa utekelezaji wa Kalenda mpya katika mtaala uliopo hapa nchini. Jambo hilo limetolewa mwezi wa Kwanza na Ofisi ya TAMISEMI, kitu ambacho hakijawahi kutokea TAMISEMI akatoa miongozi ya implementation za curriculum. Anayetakiwa kutoa masuala yote ya kitaaluma nchini ni Mtaaluma Mkuu kwa suala la elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kisheria, Mtaaluma Mkuu Tanzania hii ni mmoja tu na yuko Wizara ya Elimu. Sasa TAMISEMI leo wamevaa utaaluma wa kutoa maagizo kwenye shule zetu zote, tena wanaingilia mpaka kwenye shule za private. Jambo hili ni gumu na limeshindwa kutekelezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TAMISEMI wametoa mwongozo, ninao hapa nitakuletea kwa sababu upo kwenye simu, lakini kesho naweza nikauchapa vizuri nikakuletea. Nchi nzima, mashule yote binafsi na mashule ya TAMISEMI wameagizwa wafuate Kalenda ya Utekelezaji iliyotolewa na maafisa wa secondary ya primary pale TAMISEMI kwamba kuanzia mwaka huu shule zote nchini zifuate kalenda hiyo kwa vipindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama shule hii haina somo la mwalimu wa physics, basi wanaachwa wanakwenda kwenye somo lingine, ndiyo wanakuwa hawawezi kutekeleza ile kalenda. Shule ambayo imeshapata mwalimu wa physics na wanafundishwa, basi wasiende mbele mpaka wasubiriane kwa huyu mwalimu ambaye hakuwepo. Sijawahi kuona jambo kama hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali imeharibika mashuleni. Ukiwauliza wanasema maagizo yametoka juu. Yametoka juu kwa nani? Ukiwauliza Wizara ya Elimu wanasema yametoka TAMISEMI, ukiwauliza TAMISEMI wanasema Wizara ya Elimu haiwezi kutuingilia mambo kama haya. Jamani tunakwenda wapi katika nchi hii? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Mheshimiwa Profesa hapa amezungumza jambo kubwa sana, hebu tutafute regulator wa elimu ni nani hapa nchini? Kwa sababu kama nilivyosema mwaka juzi, TAMISEMI wana shule zao, wanatakiwa wawe na mikakati yao namna ya kuendesha vipindi mashuleni na kufaulisha. Shule za Seminari zina utaratibu wao na shule za private zina utaratibu wao. Haya mambo yanatokea wapi? Leo hii wanasoma katika ile Kalenda yao, maana yake hakutakuwa na revision za topics. Maana wameacha wiki moja kabla ya mtihani wa mwisho kwa mwanafunzi wa Darasa la Saba ama wa Form Four ama wa Form Two ama Form Six maana yake nchi nzima hakutakuwa na revision katika masomo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kama ni somo gumu la hesabu, hakutakuwa na topic ya kufanyia revision kwa sababu Kalenda ile inamtaka mwanafunzi asome hiki na kile, hata kama shule inakuwa kwenye mfumo wa michepuo; kwa mfano, shule niliyosoma mimi O’level, Mbeya Sekondari, ina 15. Masomo kama ya cookery yako pale, masomo ya dini yako pale na masomo mengine na vile vile masomo ya sayansi na ya biashara. Pia kuna shule za Kata kule Kapalala ina masomo nane mpaka tisa, unakuja kuwawekea ratiba moja katika mwaka mzima kwamba wataenda Pamoja; haliwezekani jambo kama hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali isitishe jambo hili, ni baya. Siyo kwa shule za private tu, hata kwa shule za Serikali jambo hili ni baya, haliwezekani. Wanatuvurugia elimu nchini. Kila mtu akiamka, anakuja anasema hili. Umekuta mtu anasema kwenye TV; mara, kuanzia leo hakuna likizo za wanafunzi. Yaani mtu anaamka tu anakuja kuongea jambo kama hili. Elimu ni shirikishi. Watushirikishe wadau, tuwe tunaongea masuala ya elimu. Hakuna mtu ambaye amezaa mtoto wake peke yake hapa. Wote wamezaa watoto hapa, twendeni kwa pamoja. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyikiti, naunga mkono hoja. (Makofi)