Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Philipo Augustino Mulugo (10 total)

MHE. PHILLIPO A. MULUGO aliuliza:-
Kata za Wilaya ya Songwe zipo mbalimbali kwa zaidi ya kilometa 40 kutoka kata moja hadi nyingine. Iliyokuwa RCC ya Mkoa wa Mbeya ilisharidhia kupandisha hadhi barabaraya Kapalala hadi Gua na Kininga hadi Ngwala ziingie kwenye barabara za Mkoa lakini mpaka sasa hakuna utekelezaji.
Je, ni lini sasa Serikali itapandisha hadhi barabara hizo?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Phillipo Augustino Mulugo, Mbunge wa Songwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa kupandisha hadhi barabaa unafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Barabara Namba 13 ya mwaka 2007 na kanuni zake za mwaka 2009. Aidha, maombi ya kupandisha hadhi barabara ya Kapalala hadi Gua na Kininga hadi Ngwala kuwa za Mkoa yanaendelea kufanyiwa kazi na Wizara yangu sambamba na maombi kutoka Mikoa mingine. Mara baada ya kukamilika kwa zoezi hilo taarifa itatolewa na Serikali kupitia kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Songwe.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga nyumba za Askari Polisi katika Wilaya mpya ya Songwe, hasa ikizingatiwa kuwa Maaskari wengi wameripoti ndani ya Wilaya hii mpya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Phillipo Augustino Mulugo, Mbunge wa Songwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua tatizo la makazi ya Askari Polisi katika Wilaya mpya ya Songwe na maeneo mengine nchini hususan kwenye mikoa mipya. Nia ya Serikali ni kutatua tatizo la upungufu wa makazi ya Askari Polisi kwa kujenga nyumba kwa awamu kupitia mpango wa ujenzi wa nyumba 4,136 nchi nzima. Mkoa wa Songwe ambao Wilaya ya Songwe inapatikana, ni sehemu ya mpango huo ambao utaanza kutekelezwa baada ya utaratibu wa mikopo kukamilika.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO Aliuliza:-
Katika miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia baadhi ya sheria zetu hapa nchini kutoendana na mabadiliko na kasi ya maendeleo ya Taifa na kuonekana kuwa zimepitwa na wakati.
Je, ni lini Serikali italeta hoja ya kufanya marekebisho ya kuboresha baadhi ya sheria zilzopitwa na wakati?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Phillipo Augustino Mulugo, Mbunge wa Songwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia kupitia Wizara mbalimbali imekuwa ikiwasilisha Miswada ya Sheria mbalimbali Bungeni kwa lengo la kuhakikisha Taifa linakuwa na Sheria zinazochochea ukuaji wa uchumi, uboreshaji wa huduma na ustawi wa jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali pia kupitia Bunge lako Tukufu imekuwa ikifanya marekebisho ya Sheria Mbalimbali ili ziendane na wakati kupitia Miswada ya Sheriaya Marekebisho Mbalimbali (Written Law Miscellaneous Amendments).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya kuboresha sheria ni endelevu katika kuhakikisha sheria zetu zinaendana na mabadiliko yanayotokea katika jamii na kwa hiyo, Serikali itaendelea na utaratibu uliopo wa kuhakikisha kuwa sheria za nchi zinaendana na wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria za nchi hubadilika kulingana na mabadiliko ya kijamii, kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni, kisayansi na kiteknolojia. Mabadiliko yanapojitokeza, yanaweza kuathiri sheria zilizopo na hivyo kuonekana kuwa zimepitwa na wakati au kuwa na upungufu hivyo kutokidhi matakwa ya wakati. Hali hii hulazimu kufanyika kwa marekebisho ya sheria husika ili kuendana na wakati kulingana na mabadiliko yaliyotokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia ukweli huo, mwaka 1980 Serikali iliunda Tume ya Kurekebisha Sheria kama chombo maalum chenye dhamana ya kuzifanyia mapitio Sheria zilizopo ili kukidhi malengo na makusudio ya kutungwa kwake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, takribani miaka 37 sasa tangu kuundwa kwa Tume ya Kurekebisha Sheria, imekuwa ikifanya tafiti mbalimbali za sheria na kupendekeza maboresho pale inapoonekana kuna umuhimu wa kufanya hivyo. Maboresho hayo yanaweza kupelekea kufutwa, kutungwa upya au kufanyiwa marekebisho sheria iliyopo ili kuendana na wakati uliopo.
MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA (K.n.y. PHILIPO A. MULUGO) aliuliza:-
Mji wa Mkwajuni ndio Makao Makuu ya Wilaya mpya ya Songwe. Katika mji huu hakuna maji na idadi ya wananchi na wakazi wanaongezeka kwa kasi:-
Je, ni lini Serikali itajenga miradi katika mji huu pamoja na sehemu nyingine zisizo na maji katika Jimbo la Songwe?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Philipo Augustino Mulugo, Mbunge wa Songwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua tatizo la upungufu wa maji katika Mji wa Mkwajuni lililosababishwa na ongezeko la watu mara baada ya kutangazwa kwa Mji wa Mkwajuni kuwa Makao Makuu ya Wilaya ya Songwe.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuweza kutatua changamoto za upatikanaji wa maji safi na salama katika Jimbo la Songwe. Katika kuboresha huduma ya maji katika Halmashauri ya Songwe, Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 694.7 kwenye Bajeti ya Mwaka 2017/2018 ili kuhakikisha hali ya upatikanaji wa maji inaendelea kuimarika.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia imetenga kiasi cha shilingi milioni 100 katika Bajeti ya Mwaka 2017/2018 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na uandaaji wa vitabu vya zabuni katika Mji wa Mkwajuni ambao ni Makao Makuu ya Wilaya ya Songwe. Kukamilika kwa kazi hiyo kutatoa gharama halisi ya utekelezaji wa mradi mkubwa katika Mji wa Mkwajuni.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO aliuliza:-
Ziwa Rukwa lina wanyama wengi aina ya mamba waliofugwa humo ambao husababisha vifo kwa wananchi waishio pembezoni mwa ziwa hilo, wakiwemo wananchi wa Songwe na Serikali imekuwa ikitoa vibali vichache kuvuna mamba hao:-
(a) Je, kwa nini Serikali isiongeze idadi ya kuvuna mamba hao ili kuwapunguza?
(b) Kwa kuwa vifo vingi vya wakazi wa maeneo hayo vinatokana na kuliwa na mamba na Serikali haitoi mkono wa pole kwa wananchi walioathirika na vifo hivyo; je, Serikali haioni haja ya kuwafikiria wafiwa hao?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimwa Philipo Augustino Mulugo, Mbunge wa Songwe, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Spika, uwindaji wa mamba katika mbalimbali nchini hufanyika kwa kuzingatia takwimu kuhusu idadi ya mamba kwa mujibu wa sensa zinazofanywa katika maeneo husika. Lengo la uwindaji wa mamba ni pamoja na kupunguza madhara yanayosababishwa na wanyama hao kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kupitia taasisi ya utafiti wa wanyama pori Tanzania TAWIRI, imepanga kufanya sensa ya mamba na viboko kwa nchi nzima kwa mwaka wa fedha 2017/2018. Sensa hii inalenga kubaini idadi ya wanyama hao ili kuwezesha upangaji wa mgao utakaovumwa. Maeneo yatakayohusika katika sensa hii, ni maeneo ya maziwa na mito yote ikiwemo Ziwa Rukwa ambako kwa sasa inaonekana kuwa na tatizo la mamba.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu hufanya malipo ya kifuta machozi na jasho kwa wahanga baada ya kupata taarifa zenye takwimu ya matukio ya wananchi kuuawa au kujeruhiwa na mamba kutoka kwenye maeneo husika. Malipo hayo hufanyika kwa mujibu wa Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 na kanuni za kifuta jasho na machozi za mwaka 2011. Aidha, malipo hayo hayawahusu watu waliopoteza maisha au kujeruhiwa wakati wakifanya shughuli ambazo haziruhusiwi kisheria kwa mujibu wa kifungu cha 71(3) cha Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeandaa mikakati ya muda mfupi na muda mrefu ya kukabiliana na wanyama pori wakali wakiwemo mamba katika Ziwa Rukwa…..
Mheshimiwa Spika, napenda kutoa rai kwa Waheshimiwa Wabunge na Mamlaka za Wilaya husika ili ziwasilishe nyaraka zinazothibitisha wananchi kuathirika na wanyamapori wakali ili Serikali iweze kuchua hatua sitahiki.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO aliuliza:-
Wananchi wa Jimbo la Songwe kwa michango yao wenyewe wamejenga jengo kubwa kwa ajili ya Kituo cha Polisi katika Kata ya Mpona tangu mwaka 2014 ili kupambana na majambazi wanaovamia wananchi hasa wakati wa mavuno ya zao la ufuta.
Je, ni lini Serikali itasaidia kuamlizia jengo hilo na kupeleka askari polisi ili kituo hicho kianze kutoa huduma?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Phillipo Augustino Mulugo kwa uhakika, Mbunge wa Songwe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Songwe ni kati ya mikoa mipya iliyoanzishwa hivi karibuni ambayo ina changamoto nyingi ya vituo vya polisi, ofisi pamoja na nyumba za askari kama ilivyo katika maeneo mengine ya nchini. Aidha, katika mkoa mpya wa Songwe hakuna Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa na Wakuu wa Polisi wa Wilaya mbili mpya za Momba na Songwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa jitihada alizofanya yeye na kushirikiana na wananchi wa Kata ya Mpona za kujenga Kituo cha Polisi katika eneo hilo. Aidha, kwa sasa kipaumbele ni ujenzi wa Ofisi ya Kamanda wa Mkoa pamoja na Wilaya mpya. Hata hivyo Serikali inafanya jitihada ili kukamilisha kituo hicho kulingana na upatikanaji rasilimali.
MHE. ORAN M. NJEZA (K.n.y. MHE. PHILIPO A. MULUGO) aliuliza:-
Wilaya ya Songwe ina jumla ya vijiji 43 lakini mpaka sasa hakuna kijiji hata kimoja chenye umeme kwa mpango wa umeme wa REA toka awamu ya kwanza na ya pili:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inatoa upendeleo maalum kwa vijiji vya wilaya hii mpya katika awamu ya tatu ya REA?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Philipo Augustino Mulugo, Mbunge wa Songwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Jimbo la Songwe lina jumla ya vijiji 43 ambapo kati ya vijiji hivyo, sita vilipatiwa umeme kupitia mradi wa REA awamu ya kwanza na Vijiji 14 vya Ilasilo, Galula, Kanga, Mbala, Iseche, Majengo, Tete, Ifenkenya, Nahalyongo, Chang’ombe, Ifuko, Maamba, Songambele, Totowe na Mbuyuni vilipatiwa umeme kupitia mradi wa REA Awamu ya Pili.
Mheshimiwa Spika, Vijiji vya Itiziro, Undinde, Mbangala, CHUDECO, Kambarage, Ilasilo, Kaloleni, Ndanga na Mwagala ni miongoni mwa vijiji 14 vinavyotarajiwa kunufaika na utekelezaji wa mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa kwanza. Utekelezaji wa mradi huu ulianza mwezi Julai, 2017 ambapo Mkandarasi M/S STEG International Services alipewa kazi za mradi katika Mkoa wa Songwe. Kazi zinazofanyika kwa sasa ni pamoja na kuleta vifaa katika maeneo ya mradi. Mradi huu unatarajiwa kukamilika mwezi Julai, 2019.
Mheshimiwa Spika, wigo wa mradi katika Jimbo la Songwe unajumuisha ujenzi wa kilometa 46.64 za njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 na kilometa 52.09 za njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4, ufungaji wa transforma 14 na kuunganisha wateja wa awali 3,980. Gharama za mradi ni shilingi bilioni 13.05.
Mheshimiwa Spika, vijiji vilivyobaki vitapatiwa umeme kupitia mradi wa REA Awamu ya Tatu mzunguko wa pili unaotarajiwa kuanza kutekelezwa mwezi Julai, 2019 na kukamilika mwezi Juni, 2021. Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. PHILIPO A. MULUGO aliuliza:-
Je, Serikali haioni haja ya kuipandisha hadhi Hospitali Teule ambayo inamilikiwa na Kanisa Katoliki Dayosisi ya Mbeya iwe Hospitali Teule ya Wilaya ili wananchi wa Songwe waweze kupata huduma stahili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Philipo Augustino Mulugo, Mbunge wa Songwe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo tarehe 2 Januari, 2018, Halmashauri ya Wilaya ya Songwe ilisaini mkataba na Kanisa Katoliki, Jimbo la Mbeya uliopandisha hadhi ya Hospitali ya Mwambani kuwa Hospitali Teule ya Wilaya ya Songwe. Kufuatia mkataba huo, Serikali imeongezea fedha za ununuzi wa dawa na vifaa tiba kwa hospitali hiyo kutoka shilingi milioni 27.5 kwa mwaka 2017/2018 hadi shilingi milioni 105 kwa mwaka 2018/2019. Mkataba huo utaendelea hadi Serikali itakapokamilisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Songwe, ambayo katika mwaka wa fedha 2018/2019 imetengewa shilingi milioni 1.5.
MHE. PHILIPO A. MULUGO aliuliza:-
(a) Je, ni nini mpango wa Serikali kuhusu Ziwa Rukwa hasa kwa kuzingatia kudumaa na kukosekana zao la samaki katika Ziwa hilo?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuliendeleza bonde la Ziwa Rukwa hasa katika kilimo cha umwagiliaji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Philipo Augustino Mulugo, Mbunge wa Songwe, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa shughuli za uvuvi katika Ziwa Rukwa hudumaa na kukosekana kwa zao la samaki. Hali hii ilkuwa ikisababishwa na changamoto mbalimbali kubwa ikiwa ni uvuvi haramu ambapo wavuvi hutumia dhana haramu za uvuvi ambazo ni makokoro na nyavu zisozoruhusiwa kuvua. Pia uchafuzi wa mazingira unaotokana na kuongezeka kwa shughuli za binadamu kama vile uchimbaji wa madini na shughuli za kilimo karibu na Ziwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na Halmashauri zinazozunguka Bonde la Ziwa Rukwa imeweka utaratibu unaozingatia sheria ambapo shughuli za uvuvi kwa baadhi ya maeneo hufungwa ili kuwapa nafasi samaki kukua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Bonde la Ziwa Rukwa linafaa kwa shughuli za kilimo cha umwagiliaji kutokana na kuwa na mito mingi yenye kutiririsha maji mwaka mzima na maeneo yanayofaa kwa kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na uwepo wa fursa hizo katika bonde hilo Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeendelea kuboresha kilimo cha umwagiliaji kupitia Skimu za Ifumbo, Mshewe na Utengule, Bara, Ipunga, Iyura na Mbulumlowo, Naming’ongo, Sakalilo na Ng’ongo, Kilida, Mwamkulu, Kakese, Uruila na Usense.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji itaendelea kuboresha skimu zote za umwagiliaji zilizopo kwenye Bonde la Ziwa Rukwa na hivi sasa Serikali imeliweka Bonde la Ziwa Rukwa kwenye mpango ulioboreshwa na kuendeleza kilimo cha umwagiliaji Kitaifa.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO aliuliza:-

Makao Makuu ya Mkoa mpya wa Songwe yapo Mbozi na hakuna barabara ya kuunganisha Wilaya mpya ya Songwe kufika mkoani hadi upitie Mbeya:-

Je, Serikali haioni haja ya kutengeneza barabara ya mkato toka Songwe kupitia Kata ya Magamba kwenda Mbozi Makao Makuu ya Mkoa ili kuwarahisishia usafiri wananchi wa Wilaya ya Songwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Phillipo Augustino Mulugo, Mbunge wa Songwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ilikwishaona haja ya kutengeneza barabara ya mkato kutoka Wilaya ya Songwe kwenda Wilaya ya Mbozi kupitia Kata ya Magamba. Barabara iliyopendekezwa inaitwa Galula – Itindi – Magamba yenye urefu wa kilometa 32.

Mheshimiwa Spika, barabara hii imeshaanza kutengenezwa kupitia TARURA ambayo katika Mwaka wa Fedha 2018/2019 imetengwa shilingi milioni 65 kwa ajili ya kujenga daraja lenye urefu wa mita tisa katika Kijiji cha Itindi na mpaka sasa Mkandarasi anaendelea na kazi. Vilevile katika mwaka wa fedha 2019/2020, barabara hii imeombewa kiasi cha shilingi milioni 63 kwa ajili ya kufanya matengenezo sehemu korofi kwa urefu wa kilometa saba.

Mheshimiwa Spika, TARURA Wilaya ya Songwe inaendelea kufanya usanifu wa kina ili kujua mahitaji na gharama halisi za kufanyia matengenezo makubwa. Mara kazi hiyo itakapokamilika Serikali itatafuta fedha kuhakikisha inajenga barabara hiyo na kufanya ipitike majira yote ya mwaka.