Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Frank George Mwakajoka (6 total)

MHE. DAVID E. SILINDE (K.n.y MHE. FRANK G. MWAKAJOKA) aliuliza:-
(a) Je, Serikali ina Mpango gani wa kugenga Kituo cha Polisi chenye hadhi ya Wilaya hapa Tunduma ili kuendana na ongezeko la watu na wageni wanaoingia nchini?
(b) Je, Serikali haioni vema ujenzi wa kituo hicho uende sambamba na ujenzi wa nyumba zenye gharama nafuu kwa Polisi wetu ambao wana shida kubwa ya makazi?
SPIKA: Sasa Mheshimiwa Silinde wewe Tunduma si ulishaondoka, majibu ya swali hilo Mheshimiwa Naibu, Waziri Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Hamad Yussuf Masauni. (Kicheko)
NAIBU WAZIRI YA WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Frank George Mwakajoka, Mbunge wa Tunduma, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa Kituo cha Polisi Tunduma ni kidogo na hakina nyumba za kutosha. Wilaya ya Momba inahitaji nyumba 150 ili kukidhi mahitaji ya makazi ya Askari. Kama ilivyo kwa maeneo mengi hapa nchini, changamoto kubwa ya ujenzi wa vituo vya Polisi na nyumba za askari ni uhaba wa fedha. Aidha, kwa Kituo cha Polisi Tunduma changamoto nyingine ni eneo la kufanya upanuzi wa kituo kilichopo sasa kwani kituo hicho kipo mpakani kando mwa barabara ya Sumbawanga.
Mheshimiwa Spika, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha Jeshi la Polisi linaboreshewa makazi na kuwa na ofisi ili kuwezesha utoaji huduma kwa wananchi kuwa mzuri. Jeshi la Polisi chini ya utaratibu wa mikopo nafuu kutoka taasisi za kifedha za ndani na nje ya nchi lina mpango wa kujenga nyumba na ofisi za Polisi maeneo mbalimbali nchini. Kwa hivi sasa Serikali inakamilisha taratibu za kupata mkopo toka Bank ya Exim ya China ili kujenga nyumba 4,136 za makazi ya Askari katika Mikoa 17 hapa nchini.
MHE. PASCAL Y. HAONGA (K.n.y. MHE. FRANK G. MWAKAJOKA) aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itapeleka huduma ya Zimamoto katika Mpaka wa Tunduma ili kuokoa mali za wafanyabiashara wanaosubiri kuvuka pindi ajali ya moto inapotokea?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Frank George Mwakajoka, Mbunge wa Tunduma, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma lina kituo katika eneo la Mtaa wa Kilimanjaro, Wilaya ya Momba katika Mkoa wa Songwe kinachohudumia Wilaya zote ukiwemo mpaka wa Tunduma. Kwa sasa kituo hiki kina gari moja lililopo matengenezoni Mjini Mbeya. Hata hivyo, Askari wanaendelea kutoa Elimu ya Kinga na Tahadhari ya Majanga ya Moto na Utumiaji wa Vifaa kwa Huduma za Kwanza, sambamba na ukaguzi wa majengo na kutoa ushauri kwa wakandarasi na makampuni ya ujenzi kuhusu ujenzi bora wa miundombinu yenye usalama kwa umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni azma ya Serikali kupeleka huduma ya zimamoto katika maeneo yote nchini ikiwemo Tunduma. Hata hivyo azma hii nzuri inategemea sana upatikanaji wa rasilimali fedha. Serikali itaendelea kusogeza huduma za zimamoto na uokoaji katika maeneo mbalimbali nchini karibu na wananchi kadri hali ya upatikanaji fedha itakavyoruhusu.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatumia wataalam wake katika kupanga Miji na kuondokana na ujenzi holela unaoendelea nchi nzima?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Frank George Mwakajoka, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu imeshaanza kushughulikia jambo hili kwa kuhakikisha kuwa katika kila Kanda tulizoanzisha tunapeleka wataalam wa kutosha wa fani zote. Hii yote ni kuhakikisha kuwa usimamizi wa uendelezaji miji nchini unakuwa katika viwango vinavyokubalika. Aidha, pamoja na jitihada hizo bado tuna changamoto kubwa ya uhaba wa maeneo yaliyopangwa na kupimwa nchini ambayo pia ni chimbuko la ujenzi holela katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na changamoto hii, Wizara yangu imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na:-
(i) Kuandaa program ya miaka mitatu ya kuandaa mipango kabambe ya Miji, Manispaa na Halmashauri za Miji yote Tanzania. Utayarishaji wa mipango kambambe ya Miji ya Mwanza, Musoma, Singida, Kibaha, Tabora, Iringa na Mtwara upo katika hatua za kutangazwa katika gazeti la Serikali ndani ya siku 90 ili watu waweze kutoa maoni yao.
Katika Jiji la Dar es Salaam zoezi hili bado halijakamilika lakini pia katika Jiji la Arusha zoezi hili halijakamilika kwa sababu zile Halmashauri hazikuelewana kwa hiyo, inabidi wakae waridhie. Aidha, katika mwaka wa fedha 2015, Wizara yangu pia ilitoa wataalam wa Mipango Miji kusaidia utayarishaji wa mipango kabambe katika Miji ya Iringa, Mtwara na Shinyanga. (Makofi)
(ii) Vilevile, Wizara imeendelea kuhakikisha kuwa kila kipande cha ardhi kinapimwa nchi nzima na Serikali imeshaanza kufanya upimaji katika Wilaya ya Kilombero, Ulanga na Malinyi kupitia mpango wa Land Tenure Support Progamme.
(iii) Kuruhusu makampuni binafsi ya Mipango Miji kushiriki katika kutayarisha mipango kabambe na mipango ya kina katika miji yote nchini.
(iv) Wizara pia ilitoa wataalam katika zoezi la urasimishaji makazi katika Manispaa ya Kinondoni katika Kata za Kimara na Saranga na katika Halmashauri ya Wilaya ya Makete katika Kata ya Tandala. Katika mwaka huu wa fedha Wizara yangu inatarajia kupeleka wataalam katika Halmashauri za Manispaa ya Sumbawanga, Lindi, Kigoma Ujiji, Singida, Musoma na Tabora kwa ajili ya kuwezesha zoezi kama hilo.
(v) Vilevile kuzijengea uwezo Halmashauri nyingine ili ziweze kurasimisha maeneo yao kwa kutumia wataalam wake. Hii ni utekelezaji wa program ya miaka mitano ya urasimishaji wa maeneo ambayo hayajapangwa, ambapo Wizara yangu imeandaa mwongozo wa namna ya kufanya urasimishaji, mwongozo utakapokamilika utasambazwa katika Halmashauri zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe rai kwa Halmashauri zote kuandaa mipango kabambe ya maeneo ambayo yamefikia hadhi ya kuanzishwa kuwa miji ili upimaji ufanyike mapema kwa lengo la kuepusha ujenzi holela. Aidha, kwa maeneo ambayo yamejengwa kiholela Wizara yangu kwa kushirikiana na Halmashauri na wananchi wa maeneo husika tutaendelea kuboresha kwa kuyarasimisha kwa kadri ya mahitaji. (Makofi)
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA aliuliza:-
Mji wa Tunduma una vijana wengi wanaohitimu kidato cha nne lakini wanakosa nafasi za kuendelea na masomo ya juu:-
Je, Serikali inasema nini kuhusu kujenga Chuo cha Ufundi VETA ili vijana wengi waweze kupata ujuzi na kujiajiri na kuongeza kipato chao?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Frank George Mwakajoka, Mbunge wa Tunduma, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haitaweza kujenga Chuo cha VETA katika Halmashauri ya Tunduma kwa sasa kwa sababu ya ukosefu wa fedha. Wakati juhudi mbalimbali zinaendelea za kutafuta vyanzo vya ufadhili wa kujenga Vyuo vya Ufundi Stadi kupitia VETA, wananchi wa Mji wa Tunduma waendelee kutumia vyuo vilivyopo katika mikoa jirani hususan Mkoa wa Mbeya wenye Chuo cha VETA cha Mkoa na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs) vya Nzovwe kilichopo katika Manispaa ya Mbeya na Katumba katika Wilaya ya Rungwe. Aidha, wananchi wanashauriwa kuendelea kutumia vyuo vingine vilivyosajiliwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) katika mikoa mbalimbali nchini ili kupata mafunzo ya ufundi stadi.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA aliuliza:-
Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusiana na ada ya Zimamoto ambayo wanatozwa wafanyabiashara katika Halmashauri ya Mji wa Tunduru huku kukiwa hakuna Jeshi la Zimamoto na Uokoaji eneo hilo?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Frank Mwakajoka, Mbunge wa Tunduma kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ada zinazotozwa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ni kwa mujibu wa Sheria Na. 14 ya 2007 ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Kanuni za Ukaguzi za mwaka 2008 na Marekebisho yake ya mwaka 2012 na 2014. Sheria na Kanuni hizi zinamtaka mmiliki wa chombo cha usafiri pamoja na usafirishaji, mmiliki wa jengo refu au fupi, chombo cha usafiri na usafirishaji, mfanyabiashara au ofisi kulipia tozo ya ukaguzi. Tozo hizo zimepangwa kutokana na ukubwa wa jengo na hatari ya moto kwenye eneo husika.
Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ya Momba Mkoani Songwe, Halmashauri ya Tunduma ina kituo cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ambacho kipo katika Mtaa wa Kilimanjaro na kina askari kumi na gari moja la kuzimia moto. Kwa sasa gari hilo lipo Jijini Mbeya kwa ajili ya matengenezo. Wizara kupitia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji inafanya jitihada za haraka ili gari hilo litengamae na kurejea kituoni.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, askari wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji wanaendelea na majukumu yao mengine ya kutoa elimu ya kinga na tahadhari za moto na ukaguzi wa majengo ili kuzuia ajali za moto na majanga mengine. (Makofi)
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA aliuliza:-
Je, ni kwa nini Serikali haiwapatii wananchi wa Mji wa Tunduma ruzuku ya asilimia 0.3 kama ilivyo kwa wananchi wanaoishi katika maeneo yenye kuchimbwa madini?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Frank George Mwakajoka, Mbunge wa Tunduma, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa ya mwaka 1982 yaani Local Government Finance Act, Cap. 290, kifungu cha 6(1)(u), Halmashauri ulipo mgodi hutoza asilimia 0.3 ya mapato yote kabla ya kuondoa gharama za uzalishaji wa madini kama ushuru wa huduma yaani service levy. Aidha, kabla ya kuanza kutoza ushuru huo, Halmashauri husika inatakiwa kutunga Sheria Ndogo ya Halmashauri yaani District Council By-Laws ambazo zinaidhinishwa na Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa yaani TAMISEMI kwa mujibu wa kifungu cha 153(1) cha Mamlaka ya Serikali Mitaa yaani Local Government District Authority Act, Cap. 287.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, eneo la Halmashauri ya Tunduma hakuna leseni ya uchimbaji iliyotolewa. Hivyo, tunaendelea kuhimiza wawekezaji wa ndani na nje ili wawekeze katika utafiti na hatimaye kuanza kuchimba madini katika maeneo mbalimbali yenye madini nchini na Tunduma ikiwa mojawapo. Ahsante.