Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Frank George Mwakajoka (25 total)

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kujua barabara ya Tunduma - Mpemba yenye kilometa 12 itajengwa lini na Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi kwa sababu barabara ile inasababisha msongamano mkubwa sana wa magari kwenye Mji wa Tunduma na wananchi kushindwa kutimiza majukumu yao. Kwa hiyo, nataka Waziri atueleze ni lini barabara hii itaanza kujengwa kwenye Mji wetu wa Tunduma haraka iwezekanavyo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii inahitaji takwimu, ninamwomba Mheshimiwa Mbunge, avute subira tuwasiliane na wataalam ili tuweze kumpa jibu lililo na uhakika.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa sababu matatizo ya maji katika jimbo langu yanafanana sana na Jimbo la Kigoma Kaskazini, ninapenda nimuulize Mheshimiwa Waziri swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Serikali hii itakamilisha Mradi wa maji katika Mji wa Tunduma kwa sababu imekuwa inaahidi mara nyingi kwamba itatengeneza maji na hata wakati Mheshimiwa Rais anaomba kura kwa wananchi pia alisema kwamba ataweza kuwaletea maji haraka iwezekanavyo ndani ya mwaka mmoja mradi utaanza kutekelezwa. Leo hii kuna kampuni ambayo tayari imekubali kujenga…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwakajoka, swali si umeshauliza? Nadhani swali umeshauliza, kwamba huo mradi utakamilika lini?
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nataka nikumbushe kidogo kwa sababu kuna kampuni leo imekuja hapa na mradi ule umeshapitishwa na Wizara lakini tunashangaa Wizara ya Fedha hawataki kukubali mradi ule uanze kujengwa haraka. Kwa sababu mradi ule ulitakiwa uanze kujengwa mwanzoni mwa mwaka huu lakini mpaka sasa hivi hakuna kinachoendelea. Tunataka kupata majibu.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuwapatia wananchi wote maji safi na salama kwa kiwango cha asilimia 85 ifikapo mwaka 2020. Kwa hiyo, naomba nikuhakikishie, hayo unayoyazungumza ni historia, Serikali inakwenda kutekeleza Mradi wa Maji Tunduma ambao nina uhakika na tuwashauri wananchi wa Tunduma waiamini Serikali ya Awamu ya Tano. Ahsante.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Barabara hii ahadi yake ilikuwa ni kujengwa kwenye bajeti ya mwaka 2009/2010 na daraja lile ilikuwa ni 2009/2010, lakini mpaka leo daraja lile halijajengwa. Je, majibu ya msingi ya Mheshimiwa Waziri yataleta matumaini kwa wananchi wa Jimbo la Momba hasa eneo la bondeni kwamba itaanza kujengwa mapema mwaka 2016/2017?
Swali la pili, Momba ni Wilaya mpya ambayo inaunganisha Mji wa Tunduma na kutoka Tunduma kuelekea Makao Makuu ya Momba, eneo la Chitete ni Kilometa 120. Je, Serikali inasema nini kuhusiana na kutujengea daraja katika Mto Ikana katika Kijiji cha Chitete, Kata ya Msangano ili wananchi wa Tunduma waweze kufika kule wakiwa wanatumia barabara ile ambayo itakuwa na kilomita 68?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema na kama nilivyoelekezwa na Waziri wangu wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, ahadi yake kwa Mheshimiwa Ignas Aloyce Malocha, Mbunge wa Kwela, ambaye ndiye amekuwa akifuatilia ujenzi wa daraja hili pamoja na barabara kwa upande ule wa Mkoa wa Rukwa, utatekelezwa kama ulivyoahidiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali dogo la pili linalohusu Mto Ikana, namwomba Mheshimiwa Mbunge alilete swali hili rasmi Wizarani ili Watalaam walipitie kabla mimi Naibu Waziri sijatoa commitment ili commitment yangu izingatie ushauri wa Watalaam.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nami napenda kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Tunduma ni lango kuu la nchi za Kusini na Kati mwa Afrika na kwa sababu Mheshimiwa Waziri amenihakikishia kwamba mradi mkubwa wa maji utajengwa kwenye Mji wa Tunduma lakini kuna mradi ambao ulijengwa mwaka 1973, mradi wa maji wa kutega kwenye Kijiji cha Ukwire ambapo ulikuwa unahudumia Kata za Mpemba, Katete na Chapwa na sasa hivi mradi ule hautoi maji ya kutosha. Ni lini Serikali itakwenda kukamilisha mradi ule wa Mpemba ambao unalisha kata tatu katika Mji wa Tunduma?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Mji wa Tunduma tayari study imeshafanyika kwa ajili ya kuweka mradi mkubwa wa maji. Tuna mfadhili ambaye ameshajitokeza, tunaongea naye, Serikali bado inafanya mazungumzo na yeye kwa sababu alikuwa amekuja na masharti ambayo yanaweza yasiwe na manufaa kwa upande wa wananchi wa Tunduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba moja, tunaweza tukapitia mradi huo mkubwa unaokuja, lakini pili ni kwamba mpango wa Serikali ya Awamu ya Tano inahakikisha kwamba inakarabati miradi yote iliyokuwa imejengwa hapo awali ili kuondoa upungufu ukiwemo mabomba ya maji ambayo yamechakaa, mitambo ambayo imechakaa na vilevile kuongeza huduma kwa sababu kila kunapokucha watu wanaongezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika programu hiyo tutahakikisha kwamba, hayo maeneo Mheshimiwa Mbunge ambayo anayataja nayo tumeyapitia ili kurudisha upatikanaji wa maji ambao umepungua kwa sasa na hasa kwa kuzingatia kwamba Mji wa Tunduma unapanuka sana. Nafikiri upunguaji huo wa upatikanaji wa maji ni kutokana na kwamba watu wameongezeka katika Mji wa Tunduma.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wetu wanavyokwenda katika nchi ya Zambia hasa katika Jimbo la Copperbelt wamekuwa wanakamatwa wakiwa stand na wanapelekwa gerezani bila kupelekwa Mahakamani. Je, Serikali inasema nini kuhusiana na jambo hili kwa sababu kuna vijana wengi sana ambao wako magereza na hawajapelekwa Mahakamani mpaka sasa hivi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili nalipokea na Wizara yangu pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani tutalifanyia kazi, ahsante.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii ili niweze kuuliza swali la nyongeza kwa niaba ya wananchi wangu wa Mji wa Tunduma. Swali la kwanza; Mji wa Tunduma ni mji uliopo mpakani mwa Tanzania na Zambia na ni lango kuu la nchi za Kusini na Kati mwa Afrika. Kwa tafsiri hiyo ni kwamba wageni wote kabla hawajingia katika nchi ya Tanzania ni lazima wapitie Tunduma kutoka katika nchi hizo.
Je, Serikali ina mpango gani wa makusudi na wa haraka wa kupima ardhi katika Mji wa Tunduma ili kuondoa ujenzi holela unaoendelea kwa hivi sasa? (Makofi)
Swali la pili; nini mwongozo wa Wizara ya Ardhi ikishirikiana na TAMISEMI kupitia Halmashauri zetu kwenye Idara ya Ardhi ili kutoa fursa kwa Halmashauri kukopa fedha katika taasisi za fedha, lakini pia kukubali makampuni binafsi ambayo yanaweza yakapima ardhi mfano UTT katika maeneo yetu ili kuhakikisha kwamba tunapunguza ujenzi holela katika maeneo yetu ya Mji wa Tunduma na maeneo yote nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza, nikubaliane naye kwamba ni kweli Tunduma ni lango kuu na lipo mpakani na uingiaji wa watu pale ni mkubwa sana kwa hiyo panahitaji kuwa na mipango iliyo thabiti. Ameuliza tuna mpango gani wa kupima ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, jukumu la kupima ardhi siyo la Wizara peke yake, Halmashauri zenyewe zinatakiwa kuwa na mipango yake ambayo inakuwa imeandaliwa. Wizara inakwenda kutoa msaada hasa wa wapimaji labda na vifaa kupitia Kanda pale ambapo Halmashauri imeshindwa yenyewe kutekeleza jukumu hilo. Kama mna mpango huo tayari Tunduma, Wizara yangu itakuwa tayari kushirikiana nanyi kuhakikisha kwamba maeneo yale yanapimwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ametaka kujua nini mwongozo wa Wizara katika suala zima la upimaji kwa kutumia mashirika au makampuni binafsi ukatolea mfano wa UTT. Naomba niseme tu kwamba, Wizara tayari imeshabainisha makampuni 55 na orodha kamili tunayo na Wabunge kama mtahitaji tutawatolea copy tuwape ili muweze kushirikiana nayo kwa sababu baadhi ya makampuni mengine siyo wakweli katika kufanya kazi, lakini tunayo ambayo tumeainisha yapo makampuni 55 ambayo tumeruhusu yanaweza kufanya kazi na Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa ni ninyi wenyewe Waheshimiwa kuzungumza na yale makampuni na kuweza kukubaliana namna bora ya kuweza kufanya upimaji. Kwa sababu wakati mwingine yale makampuni yanaweza yakapima kwa kutumia rasilimali zao, lakini kuna namna ambavyo Halmashauri inakubaliana nao wawalipe kiasi gani katika kazi wanayofanya au wanaweza wakawasiliana na wananchi moja kwa moja wenye mashamba makubwa, lakini kupitia Halmashauri kujua mpango wenu ukoje katika maeneo yale, wanakubaliana namna ya kulipana katika zoezi hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, milango iko wazi, mashirika na makampuni mbalimbali yapo, yanaweza yakafanya kazi hiyo ni kiasi cha Waheshimiwa kufanya mawasiliano nayo. Orodha ipo kwa yeyote atakayehitaji tutatoa copy ili aweze kujua ni kampuni gani anaweza akafanya nayo kazi. (Makofi)
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Tatizo la ardhi kwenye Wilaya ya Mbozi linafanana sana na tatizo lililopo kwenye Mji wetu wa Tunduma. Katika Mji wa Tunduma katika Kata ya Mpemba kuna ardhi karibu ekari 500 ambazo zinamilikiwa na Shirika la Nyumba la Taifa na mpaka sasa hivi eneo lile halijaendelezwa zaidi ya miaka minane. Je, Serikali inasema nini ili kuikabidhi halmashauri, ambayo haina hata eneo la kujenga makao makuu ili iweze kutumia ardhi ile?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na swali hili ambalo limekuwa kila Mheshimiwa Mbunge akiliulizia, naomba tu nitoe wito kwa Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na Maafisa wetu Wateule wa Ardhi popote nchini, katika maeneo na katika malalamiko ya namna hii, Sheria ya Ardhi Namba 4 ya Mwaka 1999 imewapa nguvu. Kwa hiyo, walianzishe jambo hili watuletee na sisi kama Serikali hatutawaangusha.
MHE. FRANK MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio mimi, naitwa Frank George Mwakajoka. Nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kwa kipindi hiki cha miaka miwili kumekuwa na tatizo kubwa sana la malalamiko ya wafanyabiashara katika nchi hii na wafanyabiashara wengi sana wamekuwa wakifunga biashara zao, wafanyabiashara wa maduka pamoja wafanyabiashara wa hoteli, lakini pia wawekezaji wa kutoka nje, wamekuwa wakifunga shughuli zao na kuondoka. Je, Serikali ina mpango gani wa kushughulikia malalamiko ya wafanyabiashara kuhakikisha kwamba wafanyabiashara wanaendelea kuwekeza katika nchi yetu?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme tu kwamba katika biashara yoyote ile kuna kupanda na kushuka. Kwa hiyo pamoja na kuwa tumeona kwamba baadhi ya biashara zimefungwa lakini ni ukweli pia kwamba baadhi ya biashara nyingine zimechipuka, hilo ni la kwanza. Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili mkakati wa Serikali ni kuendelea kuzungumza na wafanyabishara ili kuelewa changamoto ambazo zinawakabili, na zile ambazo zinahusu Serikali tutazitatua.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya wananchi wa Mji wa Tunduma, napenda kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu wananchi wa Mji wa Tunduma wamekubali ushauri wa viongozi wao na kuondoa nyumba katika maeneo mbalimbali na kuhakisha kwamba barabara 42 zimepatikana kwenye Mji wa Tunduma, Serikali ina mpango gani wa kuwaunga mkono ili kuhakikisha kwamba barabara zile zinakuwa kwa kiwango cha lami kwenye Mji wa Tunduma, ukizingatia mji unaendelea kukua?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukulie kwamba taarifa hii ni ombi na kule wakati tunapita kwenye kampeni tulitoa ahadi zinazofanana na hayo ambayo ameyasema. Nimhakikishie tu kwamba ombi hili tutalipeleka katika timu ya wataalam ambayo ndiyo huwa inaandaa vipaumbele kulingana na ahadi za viongozi wakuu, ahadi za Wabunge, na kadhalika, waweze kuliangalia ili tuweze kulitekeleza kama ambavyo tuliahidi wakati wa uchaguzi.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Matatizo ya usalama katika eneo la Bunda yanafanana sana na Jimbo langu la Mji wa Tunduma.
Mwaka 2016 katika swali langu la msingi, niliuliza kuhusiana na ujenzi wa kituo chenye hadhi ya Wilaya, lakini pia niliuliza kuhusiana na nyumba zenye gharama nafuu kwa ajili ya polisi wetu kwenye Mji wa Tunduma. Majibu yake ni kwamba walisema katika Bajeti ya mwaka 2016/2017 nyumba hizi zingeweza kujengwa pamoja na Kituo cha Polisi chenye hadhi ya Wilaya. Je, Serikali inasema nini kuhusiana na changamoto hizi katika mji wetu wa Tunduma? (Makofi)
NAIBU WAZIRI MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nakiri kabisa kwamba Jimbo la Tunduma lipo mpakani na lina changamoto nyingi sana za kiusalama. Kwa hiyo, mahitaji ya kuwa na kituo cha polisi cha kisasa pamoja na nyumba za askari ni mambo ya kipaumbele.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ahadi hiyo iliyotolewa na Serikali iko pale pale na hatua ambazo zitafikiwa tutamjulisha kwa kadri ambavyo upatikanaji wa fedha utakavyokuwa unaruhusu.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kumekuwa na mkanganyiko mkubwa sana katika Halmashauri mbalimbali nchini baada ya kauli ya Mheshimiwa Rais katika sherehe za Mei Mosi juzi kule Kilimanjaro alivyosema kwamba Halmashauri yoyote au Baraza lolote la Madiwani litakalojitokeza na kutaka kumuondoa Mkurugenzi kazini au kumfukuza, Baraza hilo litavunjwa mara moja na yeye ndiye mwenye mamlaka ya kumteua Mkurugenzi kwa hiyo atahakikisha anaifuta Halmashauri hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa mujibu wa Sheria
za Serikali za Mitaa, Waheshimiwa Madiwani ndiyo wasimamizi wa shughuli na miradi ya maendeleo na mapato na matumizi ya fedha za Halmashauri.
Je, Mkurugenzi akiwa ametumia fedha vibaya na akatumia madaraka yake vibaya, ni utaratibu gani ambao Waheshimiwa Madiwani watautumia kama siyo kumuondoa Mkurugenzi wakati Rais tayari ameshawaonya na amewaambia kwamba ataivunja Halmashauri hiyo? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza si kweli kwamba kauli ya Mheshimiwa Rais imeleta mkanganyiko. Kauli ya Mheshimiwa Rais imemaanisha pale ambapo mkakati unafanywa na Waheshimiwa Madiwani kumuondoa Mkurugenzi kwa maslahi binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uzoefu wa mwaka wangu mmoja na miezi kadhaa yote mawili yanatokea, wakati mwingine kunakuwa na mkakati wa upande wa watumishi kumuondoa Mwenyekiti na wakati mwingine kuna mkakati kwa upande wa Madiwani kumuondoa Mkurugenzi kwa sababu tu maslahi yamegongana. Kwa hiyo, Mheshimiwa Rais anapolizungumzia hili hazungumzii kwa scenario unayoisema ya kwamba kumetokea ubadhirifu na wala Mheshimiwa Rais halindi wabadhirifu, anazungumzia pale ambapo kuna utaratibu unapangwa wa Madiwani kumuondoa Mkurugenzi anayesimamia watu wasifanye wizi, ndicho anachokizungumzia.
Kwa hiyo, huo mfano mwingine baki nao lakini wa
Rais ni huu aliokuwa anausema kwamba pale kunapokuwa kuna mkakati wa kumuondoa Mkurugenzi ambaye anasimamia fedha za Halmashauri hapo yuko tayari kuivunja Halmashauri na mimi mwenyewe nasema wala haitafika hata kwake mimi mwenyewe nitavunja hiyo Halmashauri.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Sera ya nchi na ya Serikali ni kuhakikisha kwamba kila kijiji na kila kitongoji kuna kuwa na zahanati, na katika mji wa Tunduma katika mtaa wa Makambini eneo la Sogea wananchi wameamua kujenga zahanati katika eneo ambalo lilikuwa limetengwa na Serikali, lakini kutokana na mgogoro uliokuwepo na ambao alikuja kuumaliza Naibu Waziri wa Ardhi, alitoa maelezo kwamba eneo hilo lisianze kujengwa mpaka atakavyotoa ruhusa ya wananchi kuendelea kujenga Zahanati pale. Je, ni lini atatoa ruhusa ili wananchi wa mji wa Tunduma eneo la Makambini waweze kuendelea na ujenzi wa zahanati kama ambavyo sera za nchi zinasema?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli nadhani Mheshimiwa Waziri wa Afya alivyopita pale wananchi waliandamana katika suala zima katika kituo kile cha afya nadhani tutafanya utaratibu kupitia ofisi yetu ya TAMISEMI nini kifanyike, lakini kutokana na changamoto ya Tunduma kwa sababu ukipita pale siku niliyopita pale population ni kubwa sana na ndio maana tunaamua kwenda kukiimarisha kituo cha Chipaka na lengo kubwa ni kwamba angalau ile kituo cha afya cha Chipaka kiweze kuwa accommodate wagonjwa wengi na tunakwenda kufanya kazi hizyo muda si mrefu ndani ya mwezi mmoja ujao kwa ajili ya wananchi wa Tanzania lengo letu ni kuboresha maeneo yale.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kutokana na majibu ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kauli mbiu ya Serikali sasa ni viwanda, lakini viwanda havitakuwepo katika nchi hii kama hatutoweza kuzalisha mafundi mchundo wengi ili waweze kutekeleza majukumu mbalimbali ndani ya viwanda hivyo. Je, Serikali haioni kwamba inapoteza muda wa kutamka kwamba itakuwa ni Serikali ya viwanda wakati haitaki kuzalisha mafundi mchundo wengi ili waweze kutekeleza wajibu wao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika hali halisi
ya majibu ya Mheshimiwa Waziri jana wakati anajibu hoja mbalimbali za Waheshimiwa Wabunge alisema kwamba Serikali imejipanga kujenga Vyuo vya VETA nchi nzima na maeneo mbalimbali katika Taifa hili. Leo katika majibu yake anatuambia kwamba Serikali haina mpango wa kujenga Chuo cha VETA katika Mji wa Tunduma. Je, jana alikuwa akiwadanganya Wabunge katika majibu yake ya msingi aliyokuwa akiyatoa ndani ya Bunge hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi Serikali inatambua juu ya umuhimu huo wa kuendelea kuzalisha mafundi sanifu na mafundi mchundo pamoja na wahandisi, lakini njia za kuzalisha mafundi hao haziko tu kupitia VETA, zipo pia kupitia vyuo binafsi lakini pia kupitia mafunzo ya muda mfupi ambayo wanafundishwa na kuweza hata kujitegemea katika viwanda vidogo vidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huo upo, kwa mfano mwaka huu, kuna mafunzo ya vijana wapatao 23,000 ambayo yanaendeshwa na VETA ambayo ipo chini ya Wizara yetu lakini pia kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Ajira, Vijana na watu Wenye Ulemavu kuhakikisha kwamba vijana wengi wanapata fursa hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kuhusiana na majibu yangu kwamba jana nimesema tutajenga vyuo nchi nzima. Kwanza naomba nipende kuliomba Bunge lako Tukufu, naona kuanzia jana hiyo kama ulivyosema na pengine siku zote Waheshimiwa Wabunge pengine huwa hawanisikilizi vizuri ninapotoa majibu yangu kiasi kwamba wameanza kuniwekea maneno ambayo sijazungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosema ni hivi Serikali ina dhamira ya kujenga Vyuo vya VETA katika kila Wilaya lakini vilevile kuhakikisha kwamba inaimarisha Vyuo vya Wananchi kila mahali vilipo ambapo vipo 55. Hata hivyo, kwa sasa kutokana na hali halisi ya kibajeti tumesema tutaimarisha kwanza vyuo vilivyopo na vile ambavyo vilishakuwa vimeanza mchakato wa kuanza kuvijenga. Kwa hiyo, sio kwamba tutajenga tu kila mahali bila utaratibu au bila fedha, naomba nieleweke hivyo tafadhali. (Makofi)
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Serikali imekuwa ikidaiwa fedha nyingi sana na mifuko ya hifadhi, mfano, PSPF ilikuwa inaidai Serikali zaidi ya shilingi 2,671,000,000,000 pia LAPF ilikuwa inaidai Serikali zaidi ya shilingi bilioni 47 kwa ajili ya asilimia 15 ya makato kwa ajili ya wafanyakazi. Je, Serikali imelipa kiasi gani na hali ikoje kwa wastaafu hawa mpaka sasa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa Serikali ilikuwa ikidaiwa kama hiyo asilimia 15, shilingi trilioni 1.4 mpaka sasa tumeshalipa trilioni 1.1, bado shilingi bilioni tatu, ambayo mwezi huu Mei, tunakamilisha kulipa hiyo iliyobaki. (Makofi)
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini zipo taarifa ambazo si rasmi sana kwamba zabuni ile ya kumpata mkandarasi wa kujenga daraja la Mto Momba zilisitishwa hivi karibuni na kuleta wasiwasi mkubwa sana kwa wananchi wa mikoa ya Songwe, Katavi na Rukwa kwamba daraja lao inawezekana lisijengwe. Leo Waziri anawathibitishia nini wananchi wa mikoa hiyo kwamba daraja hilo litaanza kujengwa lini?(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Wilaya ya Momba ina kanda mbili, kuna ukanda wa juu na kuna ukanda wa chini na katika Ukanda wa Chini kuna Kata za Msangano, Chitete, Chilulumo, Mkulwe, Kamsamba pamoja na Ivuna. Ukanda wa Juu kuna Kata za Kapele, Miunga Nzoka, Ikana pamoja na Ndalambo na Halmashauri ya Mji wa Tunduma. Barabara za kuingia katika Makao Makuu ya Wilaya mpya hazipitiki kabisa. Ni lini Serikali itahakikisha kwamba inatenga fedha za kujenga barabara ya kutoka Ikana mpaka Chitete na Tunduma kuelekea Chitete?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mwaka huu wa fedha wa 2016/2017 tumetenga shilingi milioni 2,935 na taratibu za kumpata mkandarasi zinazofanywa na TANROADS ziko katika hatua za mwisho. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba taratibu hizo mara zitakapokamilika, mkandarasi akipatikana atalipwa fedha hizo kama advance payment. Mwaka unaofuata ambao ujenzi utaendelea zimetengwa tena shilingi bilioni tatu kwa ajili ya kuendeleza ujenzi huo, naomba nimhakikishie hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu maeneo ya barabara aliyoyataja, hayo majina kwangu ni mageni kidogo lakini kama ana maana ya ile barabara inayounganisha hii mikoa mitatu ambapo sehemu kubwa inapita eneo la Mkoa wako wa Songwe, nadhani anafahamu na mara nyingi tumekuwa tukijibu hapa kwamba mara tutakapomaliza kujenga hili daraja la Momba tutaingia sasa kwenye suala la ujenzi wa barabara. Kama ana maana ya barabara nyingine, naomba nimkaribishe ofisini tukutane na wataalam tupate ratiba ya nini hasa kitafanyika katika mwaka huu wa fedha na mwaka ujao wa fedha na hatimaye tupate majibu ya suala lake na tuweze kuwaridhisha wananchi anaowawakilisha.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kumekuwa na tafsiri ambayo siyo sahihi sana kwa vijana ambao wananunua Kwacha kwenye mpaka wa Tunduma na Zambia ambapo fedha hizo, Wazambia wanapokuwa wamekuja kununua bidhaa kwenye Mji wa Tunduma wanakuja na Kwacha na baadaye vijana wananunua zile Kwacha na Serikali imekuwa ikisema kwamba vijana wale hawalipi kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kununua zile Kwacha, wanakwenda Lusaka kununua dola na baada ya kununua zile dola wanakuja ku-change kwenye benki zetu za Tanzania. Hawa wafanyabiashara wa Kwacha wanakuwa tayari wamelipa kodi.
Je, Serikali haioni kwamba nao pia ni walipa kodi katika Taifa hili na badala yake wanaendelea kuwasumbua? Wataacha lini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, katika mipaka ambayo kuna black market ya kutisha ndani ya Taifa letu ni mpaka alioutaja wa Tunduma na ndiyo maana wiki iliyopita Mheshimiwa Waziri wa Fedha alikuwa mpakani kule na sasa tumeimarisha na tutahakikisha Mheshimiwa Mwakajoka tunakusanya kodi yote. Hawawezi kutoa Kwacha huku wakaenda kuibadilisha na wakarudi nchini bila kukusanya kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeapa kulinda na kuweza kukusanya kodi yetu, tutaikusanya kodi hii kwa kila mtu anayefanya biashara hii. (Makofi)
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali. Dhamira ya Serikali ya kuanzisha Benki ya Kilimo ilikuwa ni kuwainua wakulima nchini. Wakati Serikali inafikiria kuanzisha Benki ya Kilimo ilikubali kutoa mtaji wa shilingi bilioni 800, lakini fedha iliyotolewa ni shilingi bilioni 60 tu na benki hii imeshindwa kabisa kuwahudumia wakulima wa nchi hii.
Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wakulima wanapata mikopo na wanalima kilimo chenye tija? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwakajoka, nafikiri limekaa sawa kwa sababu linaendena hasa na jitihada ya Serikali kujaribu kuwekeza na kuwasaidia wavuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa anavyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba huko nyuma kulikuwa na jitihada kujaribu kuhakikisha kwamba Benki ya Maendeleo ya Kilimo inapata shilingi bilioni 800. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa benki hiyo imeweza kupata shilingi bilioni 246 tayari zimeshaingia benki na yote itaelekezwa katika kilimo ikiwa ni pamoja na kilimo cha mazao, uvuvi na ufugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge labda tukitoka hapa leo anione nimfahamishe taratibu za kuweza kupata hizo fedha kwa ajili ya wavuvi wake. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba hizo fedha zimepatikana.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Tunduma ni mji unaokuwa sana na una msongamano mkubwa sana wa watoto; na mwaka wa jana Waheshimiwa Madiwani kwa kushirikiana na wananchi waliweza kuanzisha shule mpya nane ambazo zingine zina madarasa matatu, zingine zina madarasa nane lakini shule hizi mpaka sasa hivi hazijaanza kutumika kwa sababu DC amewasimamisha Madiwani. Kwa, hiyo kuna baadhi ya shughuli ambazo zilitakiwa zifanyike kama vioo na mambo mengine hayajafanyika kwa sababu wananchi pia walikuwa wanategemea Madiwani. Je, ni lini Serikali itatia mkazo kuhakikisha kwamba Madiwani wanarudi kazini ili shule hizi zianze kutumika haraka iwezekanavyo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Halmashauri ilijitahidi ikajenga shule nane na hizi shule hazijaanza kutumika, ni kweli; lakini ni matokeo ya migogoro ambayo haina sababu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana wenzetu wa Halmasahuri ya Mji wa Tunduma walipokaa kwenye kikao cha rasmi walikataa ushirikiano wa aina yoyote na Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya. Sasa hilo likawa ni chanzo cha matatizo ambayo yamesababisha Waheshimiwa Madiwani wasiweze kutimiza majukumu yao. Suala lao tunalishughulikia kitaifa na namwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutalitatua hivi karibuni, ili kusudi waweze kuendelea kutekeleza majukumu yao kama kawaida. (Makofi)
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, toka tumeanzisha Wakala wa Barabara (TARURA) katika Mkoa wa Songwe na Wilaya ya Momba hakuna barabara yoyote ambayo inajengwa sasa hivi kwenye bajeti ya mwaka 2017/2018, je, kazi hii ya TARURA itaanza kutekelezwa lini na hasa barabara ya kutoka Kakozi - Ndalambo kuelekea Kapele? Barabara ni mbaya sana na sasa haipitiki. Ahsante sana.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli na kama tunavyofahamu, ni kwamba tarehe 7 Julai, 2017 ndiyo Wakala huu umeanza kufanya kazi rasmi katika mwaka huu wa fedha tunaoendelea nao. Huu ni Wakala mpya na lengo lake ni kuhakikisha kwamba zile kazi zilizokuwa zinafanywa na Halmashauri zetu, sasa zitafanywa na Wakala huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri mwezi uliopita nilikuwa na kikao na Watendaji wote wa TARURA wa Nyanda za Juu Kusini pale Mjini Mbeya na kuwapa maelekezo mbalimbali, lakini zoezi hilo lilikuwa limekamilisha semina na maelekezo mbalimbali kwa wataalam wote wa TARURA nchi nzima. Baada ya kufanya zone zote nne, tulianza Bagamoyo tukaenda Tanga, tukaenda Mwanza na tukamalizia kule Mbeya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba wakala huu sasa uko katika mchakato wa stage mbalimbali. Ndiyo maana wale wanafahamu mikoa mbalimbali hivi sasa. Sasa kandarasi zinaanza kutoa mikataba kwa wakandarasi wa aina mbalimbali na mingine kutokana na zile bajeti zake zilizopita ziko kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nikuhakikishie kwamba mchakato huu unaenda na maeneo yote ya Tunduma na mikoa yote hivi sasa itashughulikiwa kwa kadri kandarasi hizo zilizotangazwa. Naomba niwahakikishie kwamba katika hili hatutakuwa na masihara katika usimamizi hasa wa ukandarasi utakaofanyika kule site, lengo letu ni kwamba Halmashauri zipate barabara bora kwa lengo kubwa la kuwasaidia wananchi wetu.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Mji wa Tunduma uko mpakani mwa Zambia na Tanzania na ni Mji ambao unahudumia Mataifa zaidi ya Nane yanaotumia Mpaka wa Tunduma, lakini kumekuwa na tatizo kubwa sana la umeme kukatika mara kwa mara na kusababisha usalama wa wageni pamoja na Wakazi wa Mji wa Tunduma kuwa hatarini. Je, ni lini Serikali itaweka umeme wa uhakika, kama ambavyo wenzetu wa Zambia pale ng’ambo walivyoweka umeme wa uhakika? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii na napenda nimshukuru Mheshimiwa Frank kwa swali lake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme Wilaya ya Tunduma ipo katika Mkoa wa Songwe, Mkoa ambao awali ulikuwa Mkoa mmoja wa Mbeya, kwa hiyo line zote zinazopeleka umeme katika Mkoa mpya wa Songwe zinatokana na Mkoa wa Mbeya. Kwa hiyo ni wazi njia ndefu ya kupeleka umeme katika Mkoa wa Songwe inasababisha kukatikakatika kwa umeme katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa Serikali kwa sasa pia ni kujenga Sub Station kubwa Tunduma ili kuwezesha upatikanaji wa umeme vizuri. Kwa sasa pia kuna mpango wa kujenga line ya kV 400 ambayo inaanzia maeneo ya Tunduma mpaka Mbeya inaenda mpaka Sumbawanga kwa ajili ya kurahisisha usafirishaji wa umeme katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge Serikali ya Awamu ya Tano inatambua hilo tatizo, lakini mipango hii ipo na itatekelezeka na baada ya muda umeme utakuwa ume-stabilize katika Mkoa Mpya wa Songwe. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo langu la Tunduma na Wilaya yetu ya Momba kulikuwa na majengo ambayo yalikuwa yanatumika na Kampuni ya CC iliyokuwa inajenga barabara ya kutoka Tunduma kwenda Sumbawanga. Majengo hayo yaliteuliwa kwamba yangeweza kutumika kama Hospitali ya Wilaya, lakini sasa hivi inaonesha kuna mabadiliko. Waziri anawaambia nini wananchi wa Mji wa Tunduma kuhusiana na majengo yale kwa sababu aliwahakikishia kwamba itakuwa Hospitali ya Wilaya?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza nitaenda kufanya follow up kujua kwamba ni Waziri gani alitoa commitment hiyo.
Jambo la pili, nafahamu wazi kwamba kuna maeneo mengi sana majengo yaliyokuwa yakitumika na wenzetu wa Wizara ya Ujenzi, hasa yale makampuni, majengo yale mengi sana yameombwa kwa ajili ya ama vituo vya afya au maendelezo ya Hospitali za Wilaya. Ninafahamu wazi kwamba Tunduma kuna changamoto kubwa kwa sababu idadi ya watu pale ni kubwa na ndiyo maana tunaanza ule ujenzi wa kituo cha afya, japokuwa umekuwa ukisuasua lakini tutasimamia kwa karibu ili uweze kukamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo hilo ndugu yangu Mheshimiwa Mwakajoka naomba niseme kwamba tunalichukua kwenda kulifanyia tathmini kuona nini kimekwamisha, kwa sababu hatimaye tunataka wananchi wa Tunduma wapate huduma vyema kabisa. Kwa hiyo tutalifanyia kazi Serikali kwa ujumla wake wote.
MHE. FRANK. G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mji wa Tunduma una shida kubwa sana ya maji na mwaka jana katika bajeti ya mwaka 2016/2017 ilikuwa imetengwa fedha Euro milioni 100 ambayo ilitaka kutekelezwa na Kampuni ya Aspac International kutoka Ubelgiji, lakini katika bajeti hii fedha hiyo haijatengwa na mradi huo hauonekani kabisa. Nataka nijue mradi wa kupunguza tatizo la maji katika Mji wa Tunduma utatekelezwa siku gani na kwa nini umeondolewa hauonekani katika bajeti ya mwaka 2017/2018?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba Serikali imepanga kukopa fedha kutoka Ubelgiji. Mazungumzo yanaendelea kati ya Hazina na Serikali ya Ubelgiji kupitia Benki hiyo ambayo imeonesha nia ya kutuazima hiyo fedha. Kwa hiyo mazungumzo yakishakamilika, basi huo mradi utaendelea, anashangaa kwa nini haujaonekana katika mwaka ujao wa fedha ni kwa sababu mazungumzo hayajakamilika Mheshimiwa Mbunge. Hata hivyo, nimhakikishie sasa hivi nazunguka kwenye Miji yetu ya mipakani nchi nzima. Namwahidi kwamba ninapokwenda nyumbani nitapita Tunduma lazima tufanye hatua za dharura kama nilivyofanya Namanga na maeneo mengine ili wananchi wapate maji safi na salama pale Tunduma.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kabla sijauliza swali la nyongeza ningependa nitumie fursa hii kuishukuru sana Serikali ya Zambia kwa kazi kubwa ambayo wamekuwa wakiifanya ya kuhakikisha kwamba wanatuazima gari yao ya Zimamoto kwa ajili ya kuzima moto kwenye mji wa Tunduma, ninasema mwasalifya sana mwe wantu wa Kuzambia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza; najua kabisa kwamba Tunduma iko mpakani mwa Zambia na Tanzania na shehena kubwa sana ya mizigo inayoshuka kwenye bandari ya Dar es Salaam inapita Tunduma na Tunduma hatuna gari ya Zimamoto. Je, Serikali haioni kwamba inahatarisha maisha ya wana Tunduma lakini pia na mizigo inayopita kwenye mpaka wa Tunduma?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, wananchi wa Tunduma wanaendelea kutoa ada za zimamoto wakati huduma ya zimamoto kwenye Mji wa Tunduma haipo, hatuoni kama huu ni uzulumaji wa wazi kabisa wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa wananchi wa Tunduma kuendelea kutozwa fedha hizi bila kupata huduma ambayo ni muhimu katika maisha yao? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Spika, kwanza alivyotoa shukurani hizi nikapata mashaka sana, maana mipakani kule kuna mwingiliano sana wa uraia na nilipoona sifa nyingi sana zinaenda Zambia nikataka kujua sana babu zake wake wako wapi. (Makofi/Vicheko)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Spika, lakini yote kwa yote ni kheri. Niseme tu kwamba yale aliyoyasema Mheshimiwa Mwakajoka kwa utaratibu wetu, tungekuwa hatuna gari kabisa katika eneo husika ingekuwa ni hatari sana, lakini vitu hivi vya moto huwa vinaharibika, na kama nilivyosema kimeenda matengenezo na baada ya hapo kitarudi.
Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu kuwatoza hii ni kwa mujibu wa sheria na sheria za kodi za nchi yetu, si kila kodi inakwenda specific huduma kwa mtu aliyechangia kodi hiyo, na tukifanya hivyo tutakuwa tumekosea kwa sababu kuna maeneo mengine makusanyo ni kidogo.
Kwa hiyo, mimi nitoe rai kwa wananchi wetu waendelee kutoa kodi hizo na hivi tunavyoongea kwenye bajeti iliyopita tumepitisha bajeti ya magari mengine, tunategemea kupata magari mengine kwa ajili ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na huduma hiyo itasambaa katika maeneo mengi zaidi kama ambavyo tumepanga katika malengo yetu. (Makofi)
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Katika Bunge lililopita niliuliza swali kuhusiana na hospitali ya wilaya ambayo tulikuwa tumeambiwa kwamba itajengwa katika Kata ya Chipaka kwenye Kijiji cha Chipaka. Sasa hivi inaonesha kwamba kuna mabadiliko ambayo yanataka kufanyika hospitali ile ikajengwe maeneo mengine ambayo hayana majengo kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo tulilokuwa tumeliteua ni eneo ambalo lilikuwa na majengo ambayo yalikuwa yanatumika kwa ajili ya mradi wa kujenga barabara kutoka Tunduma kwenda Sumbawanga, kuna majengo zaidi ya 20, leo hii wanataka kupeleka maeneo ambayo hayana majengo kabisa. Mheshimiwa Waziri aliniambia hapa atahakikisha kwamba analifuatilia jambo hili na hospitali inajengwa eneo ambalo walikuwa wametuambia kwamba ni lazima itajengwa pale. Je, amefuatilia na anatoa majibu gani kwa wananchi wa Tunduma ili wawe na uhakika wa hospitali katika eneo la Chipaka na Kata ya Chipaka? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la nyongeza la Mheshimiwa Marwa nimeeleza kwamba ramani kwa ajili ya hospitali za wilaya ambazo zimekuwa designed na Ofisi ya Rais, TAMISEMI zinajitosheleza. Katika pesa ambazo tunakwenda kuanzia tunakwenda kuanza na jumla ya shilingi bilioni 1.5 kwa ramani ambayo ni sahihi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa asingependa tukaenda kwenye majengo ambayo hayakidhi ramani ambazo tunazo, ni vizuri tukapeana nafasi na naamini na yeye mwenyewe akiona ramani pendekezwa ataafiki kwamba ni vizuri majengo yale yakatafutiwa kazi nyingine, lakini sisi tungependa tujenge hospitali ya wilaya yenye hadhi ya kulingana na Mheshimiwa Mbunge ambaye anatoka Tunduma.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa kigezo cha kutoa asilimia 0.3 kwenye Halmashauri ambazo kuna kazi za uchimbaji unaofanywa na migodi inatokana na athari ambazo wananchi wa maeneo hayo wanapata. Katika Mji wa Tunduma kuna forodha ambayo inahudumia nchi karibu nane Kusini na Kati mwa Afrika na kumekuwa na madhara mengi sana kwenye mpaka wa Tunduma ambayo yanafanana kabisa na maeneo wanayochimba migodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, kuna magonjwa ya UKIMWI lakini kuna miongamano mkubwa sana wa magari na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi wangu ambao wanashindwa kutekeleza majukumu yao ya kimaendeleo vizuri.
Je, Serikali haioni kwamba sasa ni muda muafaka kuona na sisi kama Halmashauri ya Tunduma tunaweza kupata asilimia 0.3 ya ruzuku kama ambavyo wanapata katika maeneo ambayo wanachimba migodi? Ahsante.
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na nipende kujibu swali la Mheshimiwa Mwakajoka, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kama ambavyo kifungu cha 6(1)(u) cha Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa kinavyoeleza, fedha hii ya ushuru wa huduma si kwa ajili ya madhara ni kwa ajili ya wao kupata stahiki ya huduma mbalimbali na mapato yaliyotokana na shughuli za uchimbaji. Kama ambavyo tumeeleza, kwa upande wa Tunduma bado hakuna leseni ya uchimbaji madini ambayo ilitolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa ufuatiliaji tumekuwa makini kufuatilia kutaka kujua kwa nini Mheshimiwa Mbunge amekuwa akitaka kuulizia suala hili. Tumefuatilia katika eneo la Mkombozi na Chapwa ambapo katika eneo la Chapwa kulikuwa na shughuli za uchimbaji wa madini ya ujenzi ya kifusi, lakini yalikuwa yakichimbwa kwa ajili ya upanuzi wa barabara. Kwa sasa tunachokifanya tumeanza kurasimisha ili leseni ziweze kutolewa kwa wale ambao waliokuwa wakichimba kwa kificho basi waweze kuingia katika shughuli hizo za uchimbaji kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu na waweze kugaiwa leseni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge asubiri tu, leseni zitakaporasimishwa kwa wachimbaji wale katika eneo la Chapwa pamoja eneo la Mkombozi basi wataweza kupata ushuru huu wa huduma au service levy.