Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA) (59 total)

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa. Tatizo la ajira katika nchi yetu, na hasa kwa wahitimu wa Vyuo Vikuu limekuwa ni kubwa sana, kama kwa mwaka mmoja inaonyesha idadi hiyo bado hawana ajira.


Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kuliambia Bunge hili ni lini hasa watakuja na mkakati wa kuanza kutoa labda mikopo midogo midogo ambayo itakuwa ni mitaji kwa hawa vijana ambao wanamaliza Vyuo vya Elimu ya Juu ambao hawana kazi kwa muda mrefu?, hilo swali la kwanza.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa sasa inaonekana kwamba Serikali bado haina orodha kamili ya wahitimu wa Vyuo Vikuu ambao hawana kazi.


Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kukubaliana na mimi kwamba umefika wakati sasa kuanza kuwa na data bank ya kujua wahitimu wote wa Vyuo vya Elimu ya Juu ili kuweza kujua ni ujuzi wa aina gani na weledi wa namna gani ambao upo katika nchi hii, na kuweza kuwashauri waajiri mbalimbali na sehemu mbalimbali? Nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WALEMAVU - (MHE. ANTONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Spika, katika hoja ya kwanza ya mikopo midogo midogo Serikali inatambua ya kwamba asilimia kubwa ya wahitimu hawa ambao wengi wangependa pia kufanya shughuli za kujiajiri wanakabiliwa na tatizo kubwa la upatikanaji wa mikopo.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeandaa programu ambayo itasaidia katika upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi waliohitimu elimu ya vyuo vikuu ambapo ziko fedha, ambazo zitatolewa kwa ajili ya wahitimu hao kupitia vikundi vyao na kampuni mbalimbali ambazo zitaundwa.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, ipo Kampuni ya Wahitimu kutoka SUA ambayo inaitwa SUGECO, wenyewe walipatiwa fedha za mikopo na wanaendelea na shughuli za uzalishaji mali. Kwa hiyo, mipango hiyo ipo na itaendelea kuwepo.

Pili, katika suala la orodha kamili ya wahitimu, Serikali imekuwa ikifanya tafiti kila mwaka kuweza kubaini ni asilimia ngapi ya vijana ambao hawana kazi waliohitimu Elimu ya Vyuo Vikuu na Elimu ya Juu. Ilianza kuanzia mwaka 2006 kutumia utafiti wa labour force survey ambayo ilifanyika mwaka 2006/2014. Utafiti huo unahitaji fedha, kila mara fedha inapopatikana utafiti huu umekuwa ukifanyika na huwa unafanyika kila baada ya miaka mitano.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kufanya utafiti kupata taarifa kamili ya vijana hao ambao wamehitimu elimu ya juu na hawana ajira ili tuone hatua stahiki za kuchukua.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwa kuwa, ulipaji wa kodi ili kuiwezesha Serikali kuweza kutoa huduma nzuri kwa wananchi ni wajibu wa kila raia wa nchi hii na kwa kuwa kumekuwa na matatizo mengi katika mfumo wa ulipaji wa kodi katika Serikali Kuu na Halmashauri, kodi usumbufu mkubwa kwa walipa kodi. Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha mfumo wa ulipaji kodi ili uwe wazi zaidi na kuwawezesha wananchi kuweza kulipa kodi zile zinazotakiwa kulipwa?
Mheshimiwa Spika, pili, kwa kuwa wananchi wengi hawajui umuhimu wa kulipa kodi, je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwa wananchi na hasa walipa kodi ili waweze kuzijua aina zote za kodi na kuweza kulipa kama inavyotakiwa.ambazo zimekuwa zikileta
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ameuliza mpango gani wa kurekebisha mfumo wa ulipaji kodi. Sasa hivi kama mlivyoona na kwa kaulimbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano ya „SASA KAZI TU‟ tumeimarisha mfumo wa ulipaji kodi kuanzia katika ngazi ya Taifa mpaka Halmashauri zetu na mmeona jinsi ambavyo sasa tunaweza kukusanya kodi kwa kiasi kikubwa.
Pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaendelea kuimarisha na Mamlaka yetu ya Mapato Tanzania imejipanga vizuri kuhakikisha kwamba hilo linafanyika katika ngazi ambayo wanafanyia kazi wao na pia mpaka Halmashauri zetu kule wanakokusanya uimarishaji wa ukusanyaji kodi utakuwa wazi kabisa na kila mmoja ndani ya Halmashauri mwenye jukumu hilo anayafanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuhusu kutoa elimu, mpaka sasa hivi tayari tuna kitengo cha utoaji elimu ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania na elimu hii huwa inatolewa moja kwa moja kupitia televisheni zetu mbalimbali tuna vipindi ndani ya wiki na pia utoaji huu wa elimu ya kodi pia hufanywa kwa semina mbalimbali na warsha zinazofanywa na watoa elimu wetu kutoka Mamlaka ya Kodi Tanzania.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri naomba niulize maswali mawili ya nyongeza:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa imeonekana taasisi nyingi hazifuati mfumo huu wakati Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2008 iliweka ni lazima kwa kila mtumishi kujaza hizo fomu na kutekeleza mfumo huu. Je, ni hatua gani ambazo Serikali imekusudia kuchukua kwa taasisi na watumishi ambao hawafuati huu mfumo ambao ni wa lazima kwa mujibu wa sheria?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa kutangaza hadharani taasisi ambazo zimefanya vizuri katika kutekeleza mfumo huu kungesaidia sana kuwapa motisha wafanyakazi wanaofanya kazi katika taasisi hizo. Je, Mheshimiwa Waziri atakubaliana nami kwamba umefika wakati sasa taasisi zinazofanya vizuri na zile ambazo zinafanya vibaya zitangazwe moja kwa moja hadharani?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA (MHE. ANGELLAH J. KAIRUKI): Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza, kuhusiana na hatua gani ambazo Serikali inakusudia kuchukua kwa watumishi ambao hawazingatii mfumo huu, nipende tu kumwambia kwamba, kuanzia mwaka 2012, Katibu Mkuu Utumishi alitoa Waraka na ilielekeza kwamba kuanzia kipindi hicho hakuna mtumishi wa umma atakayepandishwa cheo endapo hajaweza kujaza fomu ya OPRAS. Vile vile tunakusudia kuweka tozo maalum kama adhabu kwa ajili ya watumishi ambao hawatazingatia sharti hili.
Mheshimiwa Spika, katika swali la pili alitaka kufahamu endapo Serikali iko tayari kutangaza hadharani taasisi zinazofanya vizuri. Nipende tu kusema kwamba, tunafikiria pia kuweka tuzo, lakini tunapokea ushauri na tutaangalia ni kwa namna gani suala hili linaweza kutekelezwa kwa kutangaza hadharani.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Pamoja na majibu haya ambayo ameyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mazingira ya kimondo chenyewe yako kwenye hali mbaya sana, na ukiangalia miundombinu na barabara zinazoenda kule ziko kwenye hali mbaya sana, hivi sasa hivi kimondo kile hata uzio wa kukizunguka kimondo kile ku-protect haupo. Sasa je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha mazingira ya kimondo kile ili kiwe ni kivutio kizuri sana kwa utalii pamoja na kuinua pato la Mkoa mpya wa Songwe na Jimbo langu la Vwawa?
Mheshimiwa MWenyekiti, swali la pili; kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi ilishaandika barua ya kuomba Wizara hii ikikabidhi kimondo kwenye Halmashauri ili waweze kukiendeleza na kuweka vivutio mbalimbali ikiwa ni pamoja na migahawa, hoteli na vitu mbali mbali vitakavyowavutia watalii wa ndani na nje, Serikali ni lini sasa itakubali kukikabidhi kimondo hicho katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi?
NAIBU WAZIRI, MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza kutoka kwa Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga Mbunge wa Vwawa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza linahusu changamoto ya miundombinu kutokuwa bora au kutokuwa rafiki kwa shughuli za utalii kwenye eneo hili ambako kimondo chetu kipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua wazi kwamba ili kuweza kuboresha utalii miongoni mwa maeneo ambayo yanatakiwa kutiliwa mkazo, na kwakweli yanatiliwa mkazo na Serikali, ni pamoja na kuboresha miundombinu kwenye maeneo yenye vivutio kama hili la kwenye kimondo cha pale Mbozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango ya Serikali ambayo ametaka kuifahamu Mheshimiwa Mbunge ni kuboresha miundombinu hiyo kwa kutumia bajeti zake lakini pia kwa kushirikisha wadau. Kwa hiyo wakati Serikali inaendelea na utaratibu wa kutumia fedha zake za bajeti kuboresha miundombinu bado mheshimiwa Mbunge kwa kuungana na Serikali aweze kutafuta namna ambayo anaweza kushirikiana na Serikali kuweza kuwafikiwa wadau mbalimbali kwenye eno la Mbozi ikiwa wanaweza kufanya jitihada kuungana na Serikali katika kuboresha miundombinu kama alivyoitaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na kimondo kukabidhiwa kwa Halmashauri, suala hili haina tofauti kubwa sana kiuendeshaji, Serikali ni ile ile, Halmashauri bado ni Serikali na Serikali kuu bado ni Serikali. Mawazo mema na mazuri yanaweza kupokelewa kulingana na ubora wake na wakati. Kwa hiyo nimshauri mheshimiwa Mbunge ashirikiane na Halmashauri na washauri waweze kutuandikia Wizarani tutaweza kupima kuona ikiwa sababu hizo za kukabidhi kimondo hicho kwa Halmashauri linaweza likafanya eneo hilo likafanyika utalii kwa namna bora zaid na kwa tija zaidi kuliko ilivyo sasa.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Ningependa kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa kuna taasisi nyingi za Serikali ambazo zinafanya kazi zinazofanana na hii inasababisha kwamba bado gharama ziendelee kubaki kuwa kubwa. Serikali ina mpango gani wa kupitia upya taasisi zake zote ili kuhakikisha kwamba zile zinazofanana zinaunganishwa, kusudi kuweza kupunguza matumizi zaidi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa niseme tu kwamba, kama alisikiliza vizuri jibu langu la msingi, hiyo ndiyo azma na mwelekeo wa Serikali. Hata hivyo, nimpongeze na kumshukuru sana, kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia masuala mazima ya utumishi wa umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie kwamba tayari Katibu Mkuu Kiongozi, kupitia Ofisi ya Rais, alishatoa maelekezo kwa Wakuu wote wa Taasisi za Umma na tayari Taasisi zote, Wizara zote zimekwishawasilisha mapendekezo katika Ofisi ya Rais, kuhusiana miundo na mgawanyo wa majukumu ambayo wao wangeipendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunachokifanya hivi sasa tayari Ofisi ya Rais tumeishaunda timu ya wataalam na wameanza kupitia ili kuangalia endapo majukumu yaliyopo kwa taasisi fulani fulani, kama yanaweza kuhalalisha uwepo wake. Lakini vile vile kuangalia ni majukumu gani, nitolee tu mfano ziko Wizara unakuta zimeunganishwa Wizara mbili, Wizara moja ilikuwa tayari ina kitengo chake cha mawasiliano, ina kitengo chake cha mambo ya teknohama, lakini na Wizara nyingine vile vile, ilikuwa na kitengo kama hicho na idara zingine zinazofanana na mambo haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni dhahiri kabisa kwamba ni lazima itabidi kufanyia mapitio idara moja tu ndiyo iwepo. Vile vile watumishi hao wengine itabidi waangaliwe sasa ni wapi watapelekwa, katika sehemu zingine ili waweze kuleta tija zaidi na kupunguza gharama kwa Serikali.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini naomba niulize maswali madogo ya nyongeza. Kwa kuwa mfumo wa ugatuaji wa madaraka ulikuwa na lengo la kuwapa madaraka wananchi kuweza kuwa na maamuzi yao na kutekeleza masuala yao yanayohusiana kufuatana na mazingira yaliyopo; na kwa kuwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wamekuwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu hayo katika maeneo husika: Je, Serikali haioni haja ya kuupitia upya huu mfumo ili Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya ndio wabaki badala ya kuwa na Wenyeviti wa Halmashauri za Miji, Halmashauri za Wilaya pamoja na Wenyeviti wa Halmashauri za Majiji ambao kidogo wamekuwa wakiongeza gharama kwenye Serikali?
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili; kwa kuwa Ofisi za Wakuu wa Wilaya sasa hivi zimekuwa zikikabiliwa na upungufu mkubwa sana wa mapato na kwa sababu Serikali kuu imekuwa haina fedha za kutosha kuweza kuzipatia hizo Wilaya. Je, Serikali haioni haja kwamba Wakuu wa Wilaya sasa iwe ni sehemu ya kutegemea mapato yanayotokana na hizo Halmashauri ili waweze kuendesha majukumu yao na kusimamia sera vizuri katika maeneo husika?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimeelezea pale awali maeneo haya mawili; nafasi za Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kwa mujibu wa Katiba, Ibara ya 61 na ile ya Serikali za Mitaa Ibara ya 145 na 146.
Mheshimiwa Naibu Spika, wazo la Mheshimiwa Mbunge ni kwamba ikiwezekana basi hizi nafasi nyingine zitolewe. Kutokana na Katiba hiyo sasa zimekwenda kutungwa sheria. Kuna Sura namba 287 na 288, ambapo 287 inaelekeza katika Halmashauri, kuonyesha structure, jinsi gani kama Mwenyekiti wa Halmashauri, Diwani na kiongozi wa ngazi ya Kijiji anayechaguliwa ndiyo maana ya ile dhana kubwa ya D by D kushusha madaraka kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukisema uondoe hilo, maana yake umetoa dhana ya D by D. Kwa hiyo, maana yake ni Katiba sasa imetupeleka katika utengenezaji wa sheria ambapo leo hii kijiji kinahakikisha kina Mwenyekiti wake wa Kijiji na Mwenyekiti wake wa Vitongoji, wanafanya maamuzi katika maeneo haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya, jukumu lao kubwa ni kusimamia utaratibu na kanuni kuhakikisha kwamba unaendelea kama ilivyo. Kwa hiyo, kitendo cha kuondoa kimojawapo, maana yake, kwanza utakuwa umevunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini Sheria za Bunge ambazo zimewekwa humu kwa mujibu wa sheria itakuwa inaonekana hatuko sawasawa. Naamini kwamba mfumo tuliokuwa nao hivi sasa uko sawasawa. Kama kutakuwa na mawazo mengine, basi tutaendelea kuboresha kwa kadri siku zinavyoendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala hili la Wakuu wa Wilaya kwamba hawana mapato na mapato yao ikiwezekana yanayotoka kwenye Halmashauri ndiyo yangeweza kuwasaidia kufanya kazi zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo kubwa ni kwamba, tunajua Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa wakati mwingine wanakuwa na changamoto kubwa sana kwenye OC. Jukumu letu kubwa sisi kama Ofisi ya Rais ni kuhakikisha tunaziwezesha ofisi hizi. Kitendo cha mfano, hata hatukipendi sana, saa nyingine kitendo cha Mkuu wa Wilaya kwenda kuomba kwa Mkurugenzi kupewa pesa ya mafuta, mwisho wa siku anashindwa hata kuisimamia Halmashauri husika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili ni jukumu la Serikali Kuu na sisi tutajitahidi, ndiyo maana tunasema kwamba tufanye collection ya mapato. Serikali Kuu inavyopata fedha za kutosha zitasaidia ku-facilitate kazi zake kwa Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa ziweze kufanya kazi vizuri.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Jafo, nataka niongezee majibu hayo katika swali lililoulizwa na Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Vwava kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, amesema yeye angependekeza kwamba hawa Wenyeviti wa Halmashauri waondoke na badala yake, kazi zile kwa sababu zinafanywa kwa pamoja katika dhana ya ugatuaji wa madaraka kwenye Halmashauri, basi Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya hawa wachukue nafasi ile. Nataka tu niseme kwamba kusema ukweli hapa itakuwa imekiuka dhana ya checks and balances kwa sababu Wenyeviti ni Wawakilishi wa wananchi na wao ndiyo political figures kwenye maeneo yale, kwa maana ya uwakilishi wa wananchi per se.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya ni Wawakilishi wa Serikali Kuu. Kazi yao, pamoja na kazi nyingine ni kuziangalia hizi Halmashauri kama zinafuata sera, sheria za nchi, kanuni, taratibu na maagizo mbalimbali ya Serikali Kuu, pale chini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wanamwangalia nani? Wanamwangalia huyu Mwakilishi wa wananchi ambaye yuko pale na wataalam wake hawa kuanzia Mkurugenzi na wataalam wengine kama wanafanya vizuri. Ndiyo maana tunasema, hakuna mwingiliano kwa sababu mwingiliano ni pale ambapo Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya anaingilia jambo ambalo linakwenda vizuri. Huo ni mwingiliano; lakini anapofanya intervention ya jambo linalokwenda vibaya ili sheria izingatiwe, hii inaruhusiwa kwa sababu ndiyo kazi yake iliyomweka pale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka niongezee majibu haya na niwahakikishie kwamba mfumo wetu sisi Watanzania wa ugatuaji wa madaraka ni mfumo mzuri ambao nchi nyingi za Kiafrika zinakuja kujifunza hapa kwa sababu ni mfumo uliokaa vizuri na unasababisha amani na utulivu katika nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani tuendelee nao huu hadi hapo baadaye ingawa tunakubali kwamba huwa kuna reforms zimekuwa zikifanyika kuanzia mwaka 1982, mwaka 1992, mwaka 1998, lakini ipo haja ya kuendelea kuboresha lakini siyo katika eneo hili la checks and balances. Tutaharibu system nzima ilivyokaa.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ningependa kuuliza swali dogo tu la nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri. Kwa kuwa hapo nyuma, shule nyingi zilikuwa zinategemea sana michango ya wazazi ili iwasaidie katika kuweza kutoa mafunzo hasa katika zile fani ambazo hazikuwa na Walimu wa kutosha. Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza fungu maalum kwa ajili ya wale Walimu ambao watakuwa wanatoa mafunzo hasa ya masaa ya ziada baada ya ule muda wa kazi kukamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwamba tutafanyaje katika kuongeza fungu maalum kwa ajili ya Walimu?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tunaanza, maana tumepata mahali pa kuanzia. Kama nilivyosema kwamba mgawanyiko wa fedha unapelekwa katika jinsi gani kugharamia elimu hii na naamini kama nilivyosema kwamba kila jambo lina changamoto yake. Jambo hili limekuwa na mafanikio makubwa sana na ndiyo maana kwa kadri tunavyoenda tunafanya tathmini vile vile ili kuangalia na changamoto zilizojitokeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, basi tutaangalia jinsi gani tutafanya, lakini lengo kubwa ni kuweza kuwaajiri Walimu ili waweze kutatua tatizo la upungufu wa Walimu hasa Walimu wa sayansi katika maeneo yetu.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2007/2008 Serikali kupitia Ofisi ya Rais - Utumishi ilikipa Chuo cha Utumishi wa Umma kikishirikiana na chuo kimoja cha Macintosh cha Canada kuandaa framework ya kuwandaa viongozi ambayo ilijulikana kama Leadership Competence Framework. Na katika framework hiyo ilikuja na sifa 24 yaani leadership competencies 24. Sasa, je, ni lini Serikali itakuwa tayari sasa kuziingiza hizo competencies katika mafunzo ambayo tayari yameandaliwa na Serikali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa katika utaratibu wa majeshi yetu kuna utaratibu kwamba mtu hawezi kupata cheo chochote mpaka kwanza apate mafunzo fulani. Sasa kwa kuwa Serikali imesema inaandaa utaratibu wa kozi ambazo zitakuwa ni lazima kwa watumishi wa umma waandamizi. Je, ni lini sasa tamko la Serikali hizo kozi zitaanza ili watumishi hawa wawe wanafundishwa na wanaandaliwa ili wawe mahiri kabla hawajapata uteuzi wa madaraka ya aina yoyote?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Hasunga, alikuwa ni mtumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma kwa hiyo, anaifahamu sekta hii vizuri sana na anakifahamu chuo vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la kwanza kwamba ni lini sasa Serikali itakuwa tayari kuingiza zile sifa 24 za uongozi katika mafunzo yake; nisema tu kwamba sasa tunaandaa utaratibu katika hayo mafunzo ya lazima, utakapokamilika na zile sifa zote 24 katika leadership competence zitaweza kuingizwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili, ni lini sasa katika mafunzo ya in-service, kabla watu hawajapandishwa cheo yataweza kuwekewa utaratibu, nipende tu kusema kwamba pamoja na haya tumeandaa pia, utaratibu wa kuwa na assessment centre ambao tutaweza kuweka kuwa na pool ya watu mbalimbali ambao wana-managerial positions ambazo wakati wowote wanaweza wakateuliwa. Watakuwa tested, lakini pamoja na hayo pia, kutakuwa na yale mafunzo ya lazima ambayo niliyaeleza awali yatakapokamilika basi wataweza kupatiwa na tutakuwa hatuwezi kupandisha cheo mtu kabla hajapata mafunzo hayo.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, mazingira ya swali hili yanafanana kabisa na mazingira ya wakulima wa Wilaya ya Mbozi na hasa katika Jimbo la Vwawa. Kwa kuwa, moja ya gharama kubwa ambazo wakulima wa kahawa wanazipata ni pamoja na kusafirisha kahawa yao kupeleka kwenye mnada kule Kilimanjaro. Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba Mnada wa Mloo unafunguliwa ili kupunguza ushuru na tozo mbalimbali ambazo zinawakabili wakulima wa zao la kahawa wa Wilaya ya Mbozi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba mnada mkubwa wa zao la kahawa upo Moshi. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika jitihada za Serikali za kuboresha mazingira ya zao la kahawa suala la minada na mahali panapofanyika ni moja kati ya masuala tunayofanyia kazi. Kwa hiyo, avute subira, nina hakika muda sio mrefu tutakuwa na suluhisho katika hili.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Kwa kuwa takwimu za mwaka 2016 zinaonyesha kwamba Watanzania ambao ni zaidi ya miaka 15 na ambao hawazidi miaka 54 wako takribani milioni 25 na kuendelea; na kwa kuwa asilimia 22.4 ni kubwa sana, maana yake ni kwamba karibu takribani watu 5,813,066 hawajui kusoma na kuandika.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kurudisha sasa vituo vya kufundishia kama ilivyokuwa zamani katika kila kijiji, kwa sababu tatizo hili ni kubwa sana na hasa katika Jimbo la Vwawa na maeneo mengine nchini?
Swali la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri umesema kwamba mmeziagiza Halimashauri kutenga fedha ili wahakikishe kwamba huo mfumo wa KKK unatekelezwa.
Je, mmeweka mkakati gani wa kuhakikisha kwamba kutakuwa na uwajibikaji na ufuatiliaji wa utekelezaji wa agizo hili?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namshukuru Mheshimiwa Hasunga kwa kuridhika na majibu yetu ya awali, pia kwa majibu yanayofuata ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi ni kwamba kila mahali kwenye taasisi ya elimu, iwe ni shule ya msingi, iwe ni sekondari, iwe ni chuo ni kituo halali cha watu wasiojua kusoma na kuandika kuweza kupata elimu au mahali pa kujifunza.
Vilevile Wizara baada ya kutembea na kuona kwamba eneo hilo bado lina uhitaji mkubwa, tumeshaweka mikakati ya kuona kwamba elimu ya watu wazima inapewa kipaumbele na kuona kwamba wananchi wetu wa Tanzania tupungue ikiwezekana angalau tufikie asilimia tano mwaka 2025.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na ufuatiliaji katika Halmashauri ili kuhakikisha kwamba wanatimiza wajibu wao, niwaombe tu Waheshimiwa Wabunge kwa kuwa sisi sote ni Madiwani kwenye Halmashauri zetu, basi tuone umuhimu wa kutenga fedha kwa ajili ya shughuli hiyo ya kuhakikisha wenzetu wote wanajua kusoma, kuandika na kuhesabu.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata hii nafasi. Kwa kuwa Mheshimiwa waziri amesema kwamba wana mpango wa kupeleka vitendea kazi na magari katika Ofisi za Ukaguzi wa Elimu, lakini kwa muda mrefu kumekuwa na matatizo makubwa ya ukosefu wa fedha za uendeshaji, unaweza ukapeleka magari kama hakuna fedha za uendeshaji bado hawataweza kufanya kazi; na kwa kwa muda mrefu wakaguzi wamekuwa wakifanya ukaguzi katika shule ambazo ziko jirani tu kwa sababu ya ukosefu wa fedha. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapelekea OC ofisi hizo zote za kanda ili ziweze kufanya kazi yao sawasawa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimesema awali ni kwamba kimsingi Wizara imedhamiria kuboresha eneo hili la ukaguzi. Suala la OC limekuwa likiimarishwa kila wakati na ndio maana tunataka kuangalia mfumo mzima, hata ikiwezekana mafungu yao ya upatikanaji wa OC yaende moja kwa moja bila kupitia katika ngazi nyingine.
Vilevile ukaguzi tunaotaka kuuzingatia si tu ule wa kuangalia masomo peke yake, mpaka miundombinu, shule iko wapi? Inafundisha vipi na imesajiliwa katika sura ipi? Kwa hiyo, tunataka kwenda kwenye ukaguzi kwa njia ambazo ni pana zaidi ili kuwezesha kuona kwamba mambo ambayo tunaagiza kupitia sera zetu na miongozo yanatekelezwa pia katika shule zetu za Serikali.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya walimu wamekuwa wakijiendeleza wao wenyewe katika vyuo mbalimbali na kupata vyeti lakini kwa muda mrefu Serikali imekuwa ikivikataa vyeti hivyo, imekuwa haivitambui. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuvitambua hivyo vyeti ili waweze kupandishwa madaraja zaidi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kujiendeleza ni kujiendeleza tu aidha Serikali imekusomesha ama umejiendeleza mwenyewe kinachotakiwa ni kujiendeleza. Ndiyo maana katika jibu la msingi mwanzo nimesema mtu akijiendeleza maana yake ana-submit cheti chake, kinapitiwa na kuhakikiwa na Afisa Utumishi mtu huyo anastahili kupanda daraja na kuwekwa katika nafasi yake anayostahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama kuna kesi kama hiyo, maana wakati mwingine hatuwezi tukajibu kesi hapa zote kwa ujumla, inawezekana kuna case by case, kama likiwa hilo basi tunaomba tujulishane hiyo kesi imejitokeza wapi tuweze kuifanyia kazi. Mtu yeyote aliyesoma provided kwamba amesoma na ana cheti halali jambo hilo halina mashaka la kuwekwa katika muundo anaostahili. (Makofi)
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali na hatua ambazo zimechukua katika kudhibiti matumizi ya fedha za umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya eneo ambalo limekuwa na matatizo makubwa katika taasisi za umma ni eneo linalohusu ununuzi wa vipuri na matengenezo ya magari pamoja na mafuta.
Swali la kwanza, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba wafanyakazi wote walioko katika Menejimenti za Mashirika hayo wanakopeshwa magari badala ya kutumia magari ya Serikali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ndiye mwenye wajibu wa kukagua hesabu zote za Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Taasisi za Umma, lakini kwa muda mrefu tumeona kwamba hesabu za taasisi za umma, Mkaguzi Mkuu amekuwa akizipatia sekta binafsi zimekuwa zikikagua kwa niaba yake, lakini sekta hizo binafsi zimekuwa ziki-charge fedha kubwa sana ya ukaguzi. Je, ili kupunguza matumizi Serikali ina mpango gani wa kuimarisha ofisi ya CAG ili iweze kufanya kazi hiyo sawa sawa badala ya kutumia sekta binafsi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ununuzi wa vipuri na matengenezo na watumishi kukopeshwa magari, tunapokea wazo lake zuri na tutalifanyia kazi kuona ni jinsi gani utekelezaji wake ili kuona tunapunguza matumizi haya kama alivyosema kwenye magari. Tusisahau pia ni taratibu na kanuni za utumishi ndizo ambazo zinaelekeza haya yote ambayo yanatendwa na Serikali yetu, pale ambapo itaonekana inafaa tofauti na uamuzi uliopo sasa, basi Serikali yetu haitasita kufanya hivyo ili kupunguza matumizi yasiyo ya lazima kama ambavyo Serikali imekusudia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuimarisha ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, napenda kuliambia Bunge lako Tukufu Serikali yetu inatambua umuhimu wa ofisi hii ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na imekuwa ikiimarisha kila mwaka hatua kwa hatua kuhusu wafanyakazi kupewa ujuzi lakini pia kuhusu na bajeti yake. Sote ni mashahidi tumeona juzi tumepitisha bajeti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na imeongezeka kama Bunge lako Tukufu ambavyo ilipendekeza, ni imani yangu ofisi hii itakagua ofisi zetu na taasisi zote za umma pale ambapo inaonekana inafaa.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Mazingira ya swali hili yanafanana kabisa na hali halisi iliyopo katika Jimbo la Vwawa hasa katika Wilaya ya Mbozi. Kwa kuwa, Wilaya ya Mbozi inajishughulisha sana na kilimo na niwazalishaji wakubwa. Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha Tawi la Benki ya Kilimo ili liweze kutoa mikopo kwa wakulima hawa wa Wilaya ya Mbozi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo tumekuwa tukisema hapa, Benki ya Kilimo sasa inaelekea kufungua Ofisi za Kanda na ofisi mojawapo ya Kanda itakayofunguliwa katika Mkoa wa Mbeya, ambapo najua ni karibu kabisa na Wilaya ya Mbozi. Ni imani yangu wananchi wetu na wakulima wetu wa Wilaya ya Mbozi watapata faida za kupata mikopo nafuu kutoka katika benki hii.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona.

Kwa kuwa katika Jimbo la Vwawa kuna Kituo cha Afya ambacho kimejengwa kwenye Tarafa ya Iyula ambacho kimekamilika karibu miaka miwili iliyopita, lakini mpaka sasa hivi hakina watumishi wa kutosha na hakina vifaa.

Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba watumishi wa kutosha wanapelekwa na vifaa vya kuweza kuwasaidia kutoa huduma mbalimbali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Japhet Hasunga, Mbunge wa Jimbo la Vwawa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba sote tunafahamu kazi kubwa sana iliyofanywa na Serikali yetu katika kuboresha miundombinu ya huduma za afya kwa kujenga vituo vya afya takribani 487 ndani ya miaka mitano iliyopita, lakini harakati hizo za ujenzi zinaendelea katika maeneo mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba katika maeneo mbalimbali bado tuna changamoto ya idadi ya watumishi wanaohitajika kuanza kutoa huduma, lakini pia tuna changamoto ya vifaa tiba, na ndiyo maana katika mpango wetu wa vituo vya afya katika mwaka wa fedha ujao tunatarajia kuomba takribani shilingi bilioni 22.5 kwa ajili kwanza ya kuhakikisha vituo vyote na hospitali za halmashauri zilizojengwa zinapata vifaa tiba kwa kushirikiana na mapato ya ndani ya halmashauri. Lakini pili, mpango upo wa kwenda kuwaajiri watumishi kwa ajili ya kuwapeleka katika vituo hivyo.

Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Hasunga na Waheshimiwa Wabunge wote wenye hoja kama hiyo, kwamba Serikali ina takwimu za kutosha za mahitaji ya vifaa tiba katika vituo vyetu vya afya, za mahitaji ya watumishi katika vituo hivyo vya afya na itakwenda kuajiri watumishi kwa kadri ya upatikanaji wa fedha lakini pia tutakwenda kupeleka vifaa tiba. Kwa hiyo, Mheshimiwa Hasunga nikuhakikishe kwamba kituo hicho cha afya kipo kwenye mpango na tutahakikisha kinaanza kutoa huduma bora kwa wananchi.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, mazingira ya swali Arusha yanahusika kabisa na Mkoa mpya wa Songwe, yanafanana vizuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa katika Mkoa wa Songwe, kuna eneo ambalo lilikuwa limetengwa la Mbimba TaCRI kwa ajili ya ujenzi wa stendi ya Mkoa. Kwa kuwa michoro tayari ilishakamilika kwa muda mrefu karibu zaidi ya miaka sasa mitatu. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba stendi kubwa ya Mkoa wa Songwe inaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Japhet Hasunga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wa Songwe tunahitaji kujenga Stendi ya Kisasa ya Mabasi. Katika majibu yangu ya msingi, nimeeleza kwamba tunatarajia kujenga stendi katika maeneo haya yote ambayo tayari yamekwishatambuliwa na sasa tunaendelea kufanya mazungumzo na Benki ya Dunia ili kupata fedha kwa ajili ya kuwezesha sasa ujenzi wa maeneo haya ya miradi ya kimkakati kuanza. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Hasunga kwamba katika miradi hiyo inayokuja, mara mazungumzo yatakapokamilika na fedha hizo kupatikana basi tutaweka kipambele pia katika kuwezesha Kituo cha Mabasi cha Mkoa wa Songwe kuanza kujengwa.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, natoa shukrani kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Ushirika, ushirika ni kwa wana ushirika wenyewe lakini sasa hivi hali ilivyo ushirika umekuwa ukiwalazimisha watu ambao sio wanachama kwenda kuuza mazao yao kupitia kwenye Vyama vya Ushirika. Serikali ina mpango gani wa kuwaruhusu kampuni binafsi na wafanyabiashara kwenda kununua moja kwa moja kwa wakulima siyo kupitia kwenye ushirika? Hilo ni swali la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa sasa hivi hili ni moja ya mazao ya kimkakati na limekuwa likishuka uzalishaji; kwa mfano takwimu za Mkoa wa Songwe limeshuka, ni upi mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba wanawakopesha wakulima fedha ili waweze kununua pembejeo kama mbolea na dawa na CPU ili kusudi waweze kuongeza uzalishaji na ubora wa kahawa hapa nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hasunga, mwalimu wangu kama ifuatavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini haturuhusu wafanyabiashara kwenda kwa mkulima mmoja mmoja na Mheshimiwa Mbunge na yeye anafahamu, utafiti na experience imeonyesha kwamba mfumo wa kuwaruhusu wafanyabiashara kwenda kwa mkulima mmoja mmoja hasa wa zao la kahawa umepelekea wakulima wengi hasa kwa upande wa Kagera kupata bei ndogo kwani walikuwa wanauza kahawa yao katika mfumo ambao sio halali kwa shilingi 500 au shilingi 700, mpaka wengine kukopeshwa na mashamba yao kunyang’anywa. Kwa hiyo, mfumo wa ushirika umesaidia kumfanya mkulima wa kahawa kuwa na bargaining power.

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo changamoto katika ushirika ambazo hata Mheshimiwa Mbunge anazifahamu na ambazo zinapelekea mapendekezo ya kufanya mabadiliko ya sheria ambapo tunachukua hatua. Mpaka sasa tunaamini kwamba mfumo wa ushirika ndiyo njia sahihi ambayo itamsaidia mkulima mdogo mdogo kuwa na collective bargaining power ambayo itamsaidia kuweza kupata haki yake. Kwa nini wasikopeshwe?

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inawagawia miche bure, lakini ili wakopeshwe lazima wawe na vehicles. Wakulima wa pamba ni mashahidi mfumo wa ushirika ndiyo njia pekee itakayowafanya wakulima waweze kukopeshwa. Tumefanya majaribio, tumeona kwenye zao la pamba mwaka huu wakulima wa pamba wamekopeshwa kupitia ushirika zaidi ya shilingi bilioni 37, wamepatiwa input bila collateral yoyote. Kwa hiyo, kama zipo changamoto specific kwa eneo moja tujadiliane tuweze kuzitatua lakini ku- abandon mfumo ambao umetusaidia kuwapatia wakulima bei nzuri. Tunaamini kwamba wafanyabiashara wanaweza kununua kahawa katika Vyama vya Msingi kwa makubaliano yanayoonesha bei na volume bila kuwaruhusu kwenda kwa mnunuzi mmoja mmoja.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi. Ningependa kujua ni lini Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe iliyopo Vwawa Ilembo itakamilika kwa sababu ilikuwa ianze kufanya kazi mwaka 2020? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anakumbuka yeye alikuja akanieleza suala hilo na nilikwenda kwenye ile hospitali. Ninachotaka kumwambia jengo la OPD na maabara limeshakwisha lakini sasa jengo ambalo liko kwenye level ya msingi linajengwa ni jengo la wazazi ambalo nalo linaendelea na Waziri Mkuu alikuwa amepanga ziara ya kwenda kuzindua hayo majengo mawili.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwenye bilioni 80 iko kwenye bajeti ya kuweka vifaa kwenye hilo jengo la wagonjwa wa nje. Kwa hiyo, mara tu baada ya Bunge hili ratiba ile ya Waziri Mkuu ya kwenda kulizindua itakamilika na kazi itaanza kwenye hospitali wakati majengo mengine yanaendelea kuingizwa kwenye bajeti. (Makofi)
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri ambayo yanatoa matumaini kwamba hospitali hii sasa itaanza kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, ili hospitali iweze kuanza kufanyakazi inahitaji matayarisho ya kuwa na vifaa tiba vya kutosha ikiwemo ultrasound, x-ray na vinginevyo vyote.

Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba inapofika Julai vifaa tiba vitakuwa vimeshapatikana ili wananchi wa mkoa huu waweze kupata huduma?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa ujenzi wa majengo haya mawili ambayo ameyasema umechukua muda mrefu sana kutokana na mfumo uliokuwa unatumika wa force account ambao haukuleta tija sana kwa sababu ya usimamizi hafifu.

Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba majengo yaliyobaki sasa wanatumia mkandarasi badala ya force account ili yakamilike kwa viwango vinavyokubalika?
WAZIRI WA AFYA MAENDELEO YA JAMII JINSIA WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Japhet Hasunga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusu upatikanaji wa vifaa tiba hivi ikiwemo x-ray, ultrasound na vingine vyote kwa ajili ya kuhakikisha kwamba huduma zinaanza Julai napenda kumhakikishia kwamba tayari tulishapewa fedha MSD inaendelea na manunuzi na ufuatiliaji unafanyika na x-ray itakayokuja na ultrasound tumelenga kuelekeza kwenye hizi hospitali kubwa ambazo tayari zimeshakamilika kwa ajili ya kuanza huduma.

Mheshimiwa Spika, aidha kwa sababu swali lingine la pili la nyongeza ni kuhusu mfumo huu wa force account kuchukua muda mrefu ni kwa sababu gani tusihamie kwenye utaratibu wa mkandarasi. Naomba kulichukua hili nikaangalie na kabla ya Bunge hili kwisha nitafika pale mimi mwenyewe nikaone uhalisia wa kasi jinsi unavyoendelea sasa hivi kwa ajili ya kufanya maamuzi hayo ambayo ameyapendekeza, ahsante.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri ambayo yanatoa matumaini kwamba hospitali hii sasa itaanza kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, ili hospitali iweze kuanza kufanyakazi inahitaji matayarisho ya kuwa na vifaa tiba vya kutosha ikiwemo ultrasound, x-ray na vinginevyo vyote.

Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba inapofika Julai vifaa tiba vitakuwa vimeshapatikana ili wananchi wa mkoa huu waweze kupata huduma?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa ujenzi wa majengo haya mawili ambayo ameyasema umechukua muda mrefu sana kutokana na mfumo uliokuwa unatumika wa force account ambao haukuleta tija sana kwa sababu ya usimamizi hafifu.

Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba majengo yaliyobaki sasa wanatumia mkandarasi badala ya force account ili yakamilike kwa viwango vinavyokubalika?
WAZIRI WA AFYA MAENDELEO YA JAMII JINSIA WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Japhet Hasunga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusu upatikanaji wa vifaa tiba hivi ikiwemo x-ray, ultrasound na vingine vyote kwa ajili ya kuhakikisha kwamba huduma zinaanza Julai napenda kumhakikishia kwamba tayari tulishapewa fedha MSD inaendelea na manunuzi na ufuatiliaji unafanyika na x-ray itakayokuja na ultrasound tumelenga kuelekeza kwenye hizi hospitali kubwa ambazo tayari zimeshakamilika kwa ajili ya kuanza huduma.

Mheshimiwa Spika, aidha kwa sababu swali lingine la pili la nyongeza ni kuhusu mfumo huu wa force account kuchukua muda mrefu ni kwa sababu gani tusihamie kwenye utaratibu wa mkandarasi. Naomba kulichukua hili nikaangalie na kabla ya Bunge hili kwisha nitafika pale mimi mwenyewe nikaone uhalisia wa kasi jinsi unavyoendelea sasa hivi kwa ajili ya kufanya maamuzi hayo ambayo ameyapendekeza, ahsante.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuuliza Mamlaka ya Mji wa Vwawa inahudumia Mkoa wa Songwe. Je, ni lini Serikali itaupandisha hadhi Mamlaka ya Mji wa Vwawa kuwa Halmashauri ya Mji.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Hasunga, Mbunge wa Vwawa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru sana kwa kunisaidia kujibu. Kikubwa ni kwamba kwanza na mimi mwenyewe nina interest kwa sababu natokea katika Mkoa huo huo wa Songwe na ninaufahamu vizuri Mji Mdogo wa Vwawa ambao unahudumia kwa sasa Makao Makuu ya Mkoa wetu wa Songwe.

Kwa hiyo, kikubwa mimi na wewe pamoja na Mkuu wa Mkoa wetu ambaye anatusikia sasa hivi nafikiri tuanzishe tu mchakato mapema halafu ikishafika katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI ninaamini tuki-meet vigezo vyote basi tutafanya hilo ambalo Mheshimiwa Mbunge ameliomba, ahsante.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, kwanza nashukuru sana kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri na jitihada za Serikali ambazo imefanya. Nashukuru kwa mpango wa muda mrefu, lakini mpango wa muda mrefu utachukua muda mrefu, sasa kwa mpango wa muda mfupi pale kwenye Mto Mantengu pale Vwawa; iwapo mnaweza kufunga pump mbili zenye uwezo wa kusukuma maji tunaweza tukapunguza upungufu wa maji katika Mji wa Vwawa kwa kiwango kikubwa.

Sasa je, ni lini Serikali itakuwa na mpango wa kufunga pump mbili kubwa za kuweza kusukuma maji katika katika Mto Mantengu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Rais wa Awamu ya Tano alipotembelea Mji wa Vwawa mwaka 2019 alitoa shilingi milioni 100 na ndio zikaenda kuchimba visima vitatu katika eneo la Ilolo, Old Vwawa na Naihanda. Lakini visima hivyo vilitelekezwa mpaka leo bado havijafunga miundombinu.

Sasa je, Mheshimiwa Waziri utakuwa tayari kuambatana na mimi baada ya kipindi hiki cha Bunge ili twende tukaangalie hali halisi na tutatue changamoto ya muda mrefu ya wananchi wa Mji wa Vwawa? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ukimuona mtu mzima analia ujue kuna jambo. Sasa nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge maji hayana mbadala na kwa kuwa tukiweka ama tukifunga pump mbili wananchi wako wanakwenda kupata maji toshelevu, nikuombe baada ya saa Saba tukutane tutoe fedha kuhakikisha kwamba pump zile zinapatikana na wananchi wako wanapata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili, nipo tayari kuongozana na wewe Mheshimiwa Mbunge kuhakikisha kwamba tunakwenda kukulindia jimbo lako la Vwawa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, kwanza nashukuru sana kwa majibu ya Serikali. Naomba nitumie nafasi hii kuishukuru sana Serikali kwa kutenga shilingi bilioni
1.3 kwa ajili ya mradi huu ambao ni wa muda mrefu. Naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza: -

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa katika awamu ya kwanza inahusu vijiji vitano; na kwa kuwa maji haya yanatoka katika Kijiji cha Lukululu ambao ndio wanalinda hata vyanzo vya maji, lakini hawapo katika awamu ya kwanza; na kwa kuwa maji yanapotoka Kijiji cha Lukululu yanakuja Mlangali yanakwenda Shaji na Mahenje, lakini Kijiji cha Shaji ambacho kiko katikati hakiko katika mpango huu wa kwanza: -

Je, atakuwa tayari kubadilisha huu mpango ili hivi vijiji viwili, cha Lukululu ambako maji yanatoka na kile cha Shaji viwepo katika awamu ya kwanza? Hilo ni swali la kwanza.

Swali la pili: Kwa kuwa Mbewe umeitaja na imeandikwa kwenye maeneo mawili; kwenye mpango awamu ya kwanza na awamu ya pili; sasa kuna kijiji ambacho kimesahaulika kilitakiwa kiingie katika vile vijiji kumi vya awamu ya pili, ambacho ni Ihoa: -

Je, Serikali itakuwa tayari sasa kukiingiza hicho kijiji ili nacho kiwemo katika orodha ya vijiji vitakavyopata maji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hasunga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa Vijiji hivi vya Lukululu na Shaji sifa yake tu namna ambavyo ipo inafaa kuingia kwenye awamu ya kwanza, hivyo hatutakariri namna ambavyo tuliweka. Kwanza, Sera ya Maji inatutaka kijiji kile ambacho chanzo kipo kiwe mnufaika namba moja, hivyo tutazingatia hilo kama Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na maji kufika Ihoa, hii nayo nimeipokea. Kwa kuwa nia njema, dhamira safi ya Mheshimiwa Rais ni kuona kwamba maeneo yote yanafikiwa na huduma ya maji safi na salama, tutafikisha maji Ihoa pia. (Makofi)
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri; kwa kuwa katika eneo la TaCRI pale Mbimba Vwawa lilitengwa kwa ajili ya kujenga stendi kubwa ya Mkoa wa Songwe. Je, ni lini stendi hiyo itaanza kujengwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Japhet Hasunga, Mbunge wa Mbozi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba baada ya stendi ya mkoa kukosekana katika Mkoa wa Songwe ulifanyika mpango wa kuandaa eneo kwa ajili ya ujenzi wa Stendi ya kisasa ya Mabasi ya Mkoa wa Songwe katika eneo ambalo Mheshimiwa Mbunge amelitaja. Nimhakikishie kwamba lengo la Serikali bado liko vile vile na mipango inafanyika ya tathmini ya mahitaji ya fedha na kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga stendi ile. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mpango bado upo na taratibu za kutafuta fedha zinaendelea ili tuanze ujenzi. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa hii nafasi.

Je, ni lini Serikali itaanza kujenga Kituo cha Afya cha Kata ya Msiha na Kata ya Hiyanda?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Japhet Hasunga Mbunge wa Jimbo la Vwawa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeshatoa maelekezo kwa Halmashauri zetu zote kuweka vipaumbele vyao vya ujenzi wa vituo vya afya katika tarafa na kata za kimkakati. Kwa hivyo kama hizi ni kata za kimkakati, nimhakikishie Mheshimiwa Hasunga, kwamba Serikali kupitia mapato ya ndani lakini kupitia fedha ya Serikali Kuu tutaendelea kuweka hatua za ujenzi ili vituo viweze kukamilika. Ahsante.
MHE. JOSEPHAT N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa, eneo la Mlowo mpaka Vwawa kumekuwa na msongamano mkubwa sana wa magari na hasa malori ya mizigo yanayopitia pale Tunduma na kuelekea huku sehemu mbalimbali, na barabara hii ambayo tunaisema ya kuanzia Mahenje, Ndolezi, Hasamba inaweza ikangezewa upembuzi yakinifu katika eneo la Ilyika, kwenda kule Kilima Mpimbi mpaka hadi pale Iboya na ikawa ni bypass.

Je, Serikali iko tayari sasa kuongeza hicho kipande kilichobaki kwa ajili ya kufanya usanifu wa kina na kuhakikisha kwamba inakuwa ni bypass? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali pili, kwa kuwa sasa wanajenga hizo mita 800 mpaka hadi pale karibu na hospitali ya Mkoa wa Songwe.

Je, Serikali itakuwa tayari katika mwaka ujao wa bajeti huu ambao tunaujadili kutenga tena kiasi fulani cha fedha kwa ajili ya kujenga kutoka pale kwenda Hasamba mpaka Ndolezi kwenye kimondo ili kusudi watalii mbalimbali waweze kufika katika eneo la Kimondo?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hasunga, Mbunge wa Vwawa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba barabara ya kutoka Mlowo hadi Tunduma kumekuwa na msongamano mkubwa wa magari. Kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, tunafanya usanifu kuanzia Mahenje, Hasamba hadi Vwawa, sasa swali alilolitoa la kutoka Mahenje Vwawa na kufanya bypass hadi Iboya ni barabara ambayo kimsingi kwa sasa haiku chini ya TANROAD lakini wazo hilo kwa maana ya kupunguza msongamano kupita Wilaya ya Vwawa, Serikali imelichukua na italiangalia namna ya kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara aliyoisema ya kuendeleza ni utaratibu wa kuendelea na ndiyo maana tumesema tutakwenda kwa awamu. Kwa hiyo, tunauhakika kwamba katika bajeti inayokuja, baada ya kukamilisha hizo mita 800 tutaendelea na lengo ikiwa ni kukamilisha barabara zima ambayo sasa tunafanyia usanifu. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu ya Serikali. Ninayo maswali mawili ya nyongeza: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa katika Bajeti ya mwaka huu Serikali ya Awamu ya Sita imeongeza fedha hadi kufikia takribani shilingi bilioni 954; ni kwa nini Serikali haikuweka kipaumbele cha ujenzi wa soko hili katika hizo fedha?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Mkoa wa Songwe ni moja ya mikoa ya kimkakati, ambayo inapakana na nchi mbalimbali jirani na ambao unaongoza katika uzalishaji wa chakula, ni mkoa wa tatu kwa uzalishaji wa chakula.

Je, ni upi mkakati wa Serikali wa kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa soko hili muhimu kwa wananchi wa mkoa huo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Vwawa, kwa pamoja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tunampongeza Mbunge kwa kazi kubwa aliyoifanya kuhakikisha kwamba eneo lile linapatikana kutokea TACRI. Pili, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tunatambua umuhimu wa Mkoa wa Songwe katika kilimo cha nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hili tutalipa kipaumbele katika bajeti inayokuja ili basi wananchi wa Mkoa wa Songwe na hasa wakulima wa mazao mbalimbali waweze kupata fursa hii ya kuwa na kituo cha mazao; na kwa sababu pia Songwe inaungana na nchi nyingine, itakuwa ni fursa ya kipekee kwa wananchi wetu kupata masoko ya uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba tunalipa kipaumbele na ataona katika bajeti inayokuja.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naomba kuuliza Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba inakamilisha uwanja wa ndege wa Songwe kwa kuweka vifaa vya kupoozea mazao yaani cold rooms ili kusudi wananchi wa Wilaya ya Mbozi na mikoa ya Nyanda za Juu Kusini waweze kuhakikisha kwamba wanasafirisha maparachichi na matunda mengine?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hasunga, Mbunge wa Vwawa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, uwanja wa ndege wa Songwe sasa hivi tuko kwenye kukamilisha kuufanya kuwa kati ya viwanja vikubwa vya Tanzania vya ndege ambapo kutakuwa na uwezo wa kupokea ndege zote kubwa zinazoruka katika Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, na hatua ya pili ni kujenga storage facility zikiwepo na hizo za kutunza vifaa ambavyo ni baridi kwa ajili ya kusafirisha nje na ndio maana Serikali ina mpango tayari wa kununua ndege ya kusafirisha mizigo. Kitu cha kufanya ni kujenga hizo storage facility ikiwepo Mkoa wa Mbeya, ahsante.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, ahsante.

Mheshimiwa Spika, naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri katika Kata ya Nanyara pale Songwe pana kituo cha afya ambacho kimejengwa takribani zaidi ya miaka minne sasa na hakina wafanyakazi kabisa wa kutosha.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba inapeleka wafanyakazi katika kituo hicho cha afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Japhet Hasunga Mbunge wa Vwawa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kituo hiki cha Nanyara ambacho kimekamilika zaidi ya miaka Minne iliyopita kina watumishi wachache, nimhakikishie kwamba mpango ni kuhakikisha tunapeleka watumishi ambao angalau watakidhi mahitaji ya kituo cha afya na hivyo tutahakikisha tunapeleka watumishi katika kituo hiki ili waweze kutoa huduma bora za afya. Ahsante. (Makofi)
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, katika Kata ya Isalalo kwenda kwenye Kata ya Ikunga, kuna mto mkubwa wa Nkana.

Je, Serikali ina mpango gani ili kuwafanya wananchi wa Isalalo waweze kuvuka kwenda Kata ya Ipunga kwenye Kijiji cha Ipanzya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Hasunga, Mbunge wa Jimbo la Vwawa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri eneo ambalo amelianisha Mheshimiwa Mbunge ninalifahamu na bahati nzuri niko huko huko katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeshawaagiza watu wa TARURA Mkoa wa Songwe waende wakafanye tathmini katika eneo hilo ili watupe tathmini ili tutafute fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja katika eneo hilo.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Katika Kata ya Msia pana bwawa dogo ambalo lipo katika Kijiji cha Msia. Bwawa hili linaweza kutumika sana katika kilimo cha umwagiliaji hasa katika mashamba ya kahawa. Na kwa muda mrefu limekuwepo kwenye bajeti lakini Serikali haijaweza kutekeleza. Ni lini Serikali itaanza kutekeleza lile bwawa ili liweze kutumika katika kilimo cha umwagiliaji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hasunga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha ya kwamba ifikapo mwaka 2025 tumekuwa na eneo la umwagiliaji la hekta milioni moja na laki mbili yakiwa ni maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, ya kwamba katika kufikia azma hiyo ni lazima pia tutekeleze miradi mingi kadri iwezekanavyo ili wananchi wengi waweze kunufaika. Nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba bwawa alilolisema tutaelekeza wataalamu katika bwawa la pili pia kulipitia ili waje watushauri vizuri namna ya utekelezaji wake lakini ni jambo ambalo ndani ya wizara tunaona kwamba ni jambo muhimu na hivi sasa changamoto kubwa ni upatikanaji wa mabwawa yenye uhakika wa maji. Kama bwawa lipo tayari ni njia rahisi zaidi ya kuanza utekelezaji wa mradi. Nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge tutalisimamia hilo na mradi utatekelezeka.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, je, ni lini barabara ya Ihanda-Ipunga hadi Chinji itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Hasunga, Mbunge wa Jimbo la Vwawa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilishawaelekeza mameneja wa TARURA katika wilaya zetu kuhakikisha wanatenga vipaumbele vya barabara ambazo zinahitaji kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo naomba nimwelekeze Meneja wa TARURA wa Wilaya hii ya Mbozi kuhakikisha kwamba wanaleta maombi hayo kama ni kipaumbele ili Serikali iweze kufanya tathmini na kuona uwezekano wa kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi huo, ahsante.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwanza naishukuru Serikali kwa kuanza kumpata mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo lakini kwa kuwa kuna baadhi ya maeneo ambayo barabara hiyo imewafuata wananchi. Je, Serikali inampango gani kuhakikisha kwamba wananchi hao wanapewa fidia stahiki?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa barabara hiyo ina urefu wa kilometa 79 na bado haijakamilika upembuzi yakinifu, Serikali inamkakati gani wa kuhakikisha kwamba inakamilisha upembuzi yakinifu kwa kilometa zote zilizobaki?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Vwawa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Wananchi wa Jimbo la Vwawa kwamba tayari jedwali baada ya kuhakikiwa la malipo ya fidia kwa wale ambao barabara imefuata liko hazina kwa ajili ya uhakiki na hatua inayofuata sasa ni kwenda kufanya disclosure, yaani kuwaonyesha kila mtu atalipwa nini kwa maeneo ambayo bado. Kwa hiyo, naomba niwahakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi kwamba suala hili linaendelea na watalipwa hiyo fidia yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kukamilisha upembuzi na usanifu tuko kwenye hatua za mwisho kabisa kukamilisha usanifu ambapo ni hiyo Barabara ya Idiwili lakini Mahenge – Hasamba hadi Ileje.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, ahsante.

Mheshimiwa Spika, nil in Daraja la Isararo – Ipanzya litajengwa, ambayo imekuwa ni ahadi ya muda mrefu sana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika,
naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hassunga, la ahadi ya kujenga madaraja haya ambayo ameyataja: -

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimekuwa nikimjibu Mheshimiwa Shangai hapa; maelekezo yalitoka kwa mameneja wote wa TARURA wa mikoa na wote wa Wilaya kuhakikisha barabara hizi ambazo pia ni ahadi za viongozi lakini, lakini ambazo ni kipaumbele katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu yatengewe fedha. nitakaa na Mheshimiwa Mbunge kuweza kuangalia katika ahadi hizi na barabara hii kama imetengewa fedha.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa kwa muda mrefu nimekuwa nikifwatilia juu ya ujenzi wa soko la mazao pale Vwawa;

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba lile soko linajengwa kama ambavyo imekuwa ikiahidi kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Jimbo la Vwawa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri Mheshimiwa Hasunga tunatokea katika mkoa mmoja na anatambua kabisa Soko la Vwawa liko katika Mradi wa TACTIC Tier III kwa hiyo, utekelezaji wa mradi utakapoanza ambapo mimi na yeye tuko katika kundi moja, maana yake na yeye atapatiwa hiyo huduma. Ahsante sana.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nashukuru sana kwa Serikali kutoa hizo fedha ambazo zimetumika katika hilo eneo.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kipande cha Idunda – Soga kuelekea katika eneo la Mbeya Vijijini, Serikali imelima tu lakini haikuweza kuweka changarawe na kujenga kidaraja kidogo katika lile eneo. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba inakamilisha hilo eneo ili liwe linapitika wakati wote wa mwaka?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa ili wananchi wa Idunda, Ipyana waweze kusafiri hadi Iyula hadi kuelekea Makao Makuu ya Jimbo la Vwawa ni lazima kipande cha Iyula – Hatete – Mbewe kikamilike ambacho mpaka sasa hivi bado hakijakamilika.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba inakamilisha kipande hicho ili kuwasaidia wananchi hao waweze kusafiri kiurahisi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, nikijibu swali lake la kwanza la kipande cha Idunda – Soga ili kiweze kujengwa kuwa changarawe na kuna daraja ambalo Mheshimiwa Hasunga amelitaja lina changamoto. Katika mwaka wa fedha 2020/2021 TARURA katika Wilaya ya Songwe, Halmashauri ya Songwe DC ilikuwa imetengewa shilingi milioni 650 tu, lakini katika mwaka wa fedha 2021/2022 na huu tunaokwenda wametengewa zaidi ya shilingi bilioni 2.8 kwa ajili ya utekelezaji wa barabara. Hivyo basi, nichukue nafasi hii kumuelekeza Meneja wa TARURA wa Mkoa wa Songwe kuhakikisha wanafika kwenye barabara hii na kuona changamoto ambayo ipo ili waweze kutengeneza daraja hili ambalo amelitaja Mheshimiwa Hasunga la kuunganisha wananchi kati ya Songwe na Mbeya.

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili la wananchi wa Igana kupita barabara ya Iyula - Katete na Mbewe. Nirejee tena yale maelekezo ambayo nilikuwa nimeyatoa kwenye swali lake la kwanza, Meneja wa TARURA wa Mkoa wa Songwe anapotembelea barabara hii ya Idunda – Soga ahakikishe anaangalia nini kimekwamisha barabara hii ambayo nimetoka kuitaja hivi sasa na kuweka mikakati ya kuweka changarawe na kuimalizia.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza naishukuru Serikali kwa kutenga fedha na kukamilisha hilo jengo.

Je, ni kwa kiwango gani jengo hili limekuwa jumuifu kwa maana ya kuwa na Mahakama ya Mwanzo, Mahakama ya Wilaya na Mahakama ya Mkoa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kwa kuwa kuna msongamano mkubwa sana katika Gereza la Ilembo pale Vwawa: Je, ni kwa kiwango gani jengo hili sasa litasaidia kuhakikisha kwamba kesi nyingi ambazo zimesongamana katika Mahakama zitaweza kwisha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Naomba kujibu maswali mawili sasa ya Mheshimiwa Japhet, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza anataka kufahamu kama hili jengo litakuwa linajumuisha na Mahakama nyingine. Nimwarifu kwamba, katika mpango wetu wa Mahakama, miongoni mwa mikoa ambayo tunajenga majengo ambayo yatajumuisha Mahakama zote, ni pamoja na Mkoa wake. Kwa hiyo, hili limezingatiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, anataka kufahamu kama sasa kesi zitakwenda kwa kasi. Ni dhahiri kwamba kesi zitakwenda kwa kasi kwa sababu jengo hili baada ya kukamilika, efficiency ya Waheshimiwa Mahakimu wetu itaongezeka. (Makofi)
MHE. JAPEHT N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Barabara ya Vwawa – London – Iganduka hadi Msiya hivi sasa haipitiki kabisa; Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba barabara hiyo inawekwa lami ili iweze kupitika wakati wote?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali la Mheshimiwa Hasunga la Barabara zake hizi za Vwawa kuwekewa lami. Nitakaa naye Mheshimiwa Hasunga kuona ni kiasi gani kimetengwa katika mwaka wa fedha 2023/2024 katika jimbo lake kule ili tuweze kuhakikisha kwamba upatikanaji wa fedha huu unakuwa wa haraka na hizi ziweze kuanza kujengwa mara moja na kama hazijatengewa fedha basi tutahakikisha na Mheshimiwa Hasunga tutakaa naye kuona zinatengewa fedha katika mwaka wa fedha wa 2024/2025.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa kuwa katika msimu wa mwaka jana ambao unaishia sasa hivi baadhi ya wakulima wa zao la kahawa wanavidai Vyama vya Ushirika vingi tu ambavyo bado havijawalipa. Lipi tamko la Serikali kuhusiana na madai hayo ya wakulima?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, biashara ya mazao ni biashara kama biashara nyingine yoyote. Vyama vya Ushirika vyote ambavyo havijafanya malipo kwa wakulima vinapaswa kufanya malipo kwa wakulima kwa wakati ili kumsaidia mkulima huyu aendelee na shughuli zake za kilimo, hivyo natumia jukwaa hili la Bunge lako tukufu kuwataka wale wote ambao hawajafanya malipo kwa wakulima wafanye mara moja ili kuwaruhusu wakulima kuendelea na msimu unaokuja wa kilimo.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa katika Jimbo la Vwawa kuna vijiji 31 ambavyo bado havina umeme, na kwa kuwa mkandarasi sasa hivi karibu mwaka mmoja umekatika hakuna kijiji hata kimoja ambacho kimepata umeme.

Je, Serikali inatuhakikishiaje kwamba kufikia Desemba vijiji vyote hivyo vitakuwa vimewashwa umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Japhet Hasunga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, taratibu za kupeleka umeme wa REA na miradi mingine mikubwa uko katika awamu tofauti tofauti na kwa harakaharaka tunayo awamu ya kumpata mkandarasi na tukishasaini mkataba anakwenda site kufanya physical verification, anakwenda kukagua maeneo na kuona uhalisia wake, lakini tunarudi mezani yeye pamoja na TANESCO na REA kuangalia na kukubaliana scope ya kazi yenyewe ambayo inatakiwa ifanyike halafu anakwenda kwenye hatua ya tatu ya kuagiza vifaa na hatua ya nne ni ya kwenda site na kuanza kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, ninaamini kabisa kwa Mheshimiwa Japhet Hasunga mojawapo au mbili au tatu ya hatua hizo zinaendelea, na tunatarajia ifikapo Desemba muda wa kufanya kazi kwa miezi hii sita, saba iliyobakia tutakabana na wakandarasi kuhakikisha kwamba tunafikisha huduma hii ya umeme kwenye maeneo yote kwa sababu tayari vifaa vimeshanunuliwa na surveys zilishafanyika na sasa wako site wanaendelea kufanya kazi, kwa hiyo kazi zitakamilika. (Makofi)
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, Mji wa Vwawa una Mamlaka Ndogo ya Mji wa Vwawa na Mkoa wa Songwe kwa muda mrefu umekuwa hauna Manispaa.

Je, ni lini Serikali utaupandisha hadhi Mji wa Vwawa ili iwe Manispaa kwa ajili ya kuhudumia Mkoa mpya wa Songwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Japhet Hasunga, Mbunge wa Jimbo la Vwawa kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Spika, bahati nzuri Mheshimiwa Mbunge anayezungumza anajua kabisa katika eneo alilolitaja na mimi mwenyewe nina interest nalo kwa sababu ni mkoa wangu. Ni moja ya mjadala ambao tumekuwa tukijadili katika vikao vya RCC. Kwa hiyo, ambacho tulishauri Mkoa wa Songwe ni kwamba wafuate zile taratibu ambazo zimeianishwa kuleta maombi, halafu yatapelekwa kwa mamlaka, wakati huo sasa hivi mamlaka imejikita zaidi kwenye kuboresha. Kwa hiyo, tufuate taratibu na baada ya taratibu kukamilika basi tutashauri mamlaka kuona namna bora ya kulitekeleza hili. Ahsante.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; kwa kuwa katika halmashauri kwanza Serikali imetoa mafunzo kwa maafisa 210 ambao ni wachache sana ukilinganisha na halmashauri zilizopo hapa nchini mikoa iliyopo; na kwa kuwa uandaaji wa hesabu unahitaji ujuzi na maarifa maalum ambayo yanatakiwa yatolewe na wafanyakazi wengi wamekuwa hawana maarifa hayo.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba Wahasibu pamoja na Wakaguzi wa Ndani wanapatiwa mafunzo wanayostahili katika utayarishaji wa hesabu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Japhet Hasunga, Mbunge wa Jimbo la Vwawa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana tumejibu hawa tumetoa mafunzo kwa maafisa 210 sasa hivi tumeongeza fedha katika bajeti yetu, kuhakikisha tunawafikia watu wote wa vitengo, wahasibu pamoja na wakaguzi wa ndani ili kuhakikisha kwamba sasa wanafanya kazi ambayo imekusudiwa. Kwa hiyo, fedha zimeongezeka na mwakani tutafanya hivyo kwa watu wote wa idara hiyo.

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwa kuwa wananchi wa Kata ya Ihanda na Msia, wametenga maeneo na wametayarisha matofali na mawe kwa ajili ya vituo vya afya.

Je, upi mkakati wa Serikali katika kuwaunga wananchi hao kuhakikisha vituo vya afya hivyo vinajengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKAO NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hasunga Mbunge wa Jimbo la Vwawa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeweka mpango, kwa mwaka ujao wa fedha wa kukamilisha vituo vya afya, zahanati na hospitali za halmashauri, lakini kununua vifaa tiba kwa ajili ya kuhakikisha vituo vile vinaanza kutoa huduma na baada ya hapo sasa tuaendelea na ukamilishaji wa vituo vya afya, vikiwemo vituo vya afya vya Jimbo la Vwawa.

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, katika Kata ya Ihanda kuna Kijiji cha Shilanga na Seketu ambazo zina maboma ya zahanati ambayo yamekaa muda mrefu sana. Upi mkakati wa Serikali wa kuhakikisha maboma hayo yanakamilika ili wananchi waweze kupata huduma za afya katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Japhet Hasunga, Mbunge wa Jimbo la Vwawa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwapongeze wananchi wa Jimbo la Vwawa kwa kutoa nguvu zao na kujenga maboma ya zahanati, lakini nimuhakikishie kwamba Serikali hii ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kipindi cha mwaka mmoja zaidi ya maboma 900 ya zahanati yaliyoanza ujenzi kwa nguvu za wananchi yamekamilishwa na zoezi hili ni endelevu. Katika mwaka ujao wa fedha tuna maboma 300 ya zahanati kwa ajili ya ukamilishaji. Kwa hiyo tutahakikisha pia katika ukamilishaji huo maboma haya ya Jimbo la Vwawa pia tunayapa fedha kwa ajili ya kuanza kukamilisha kwa awamu. Ahsante.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwanza naomba nishukuru kwa majibu mazuri ya Serikali.

Kwa kuwa mahitaji ya Chuo cha VETA ni ya muda mrefu sana katika Jimbo la Vwawa na katika Mkoa wa Songwe, ni lini zabuni za ujenzi wa chuo hicho zitatangazwa ili kuhakikisha kwamba kwa kweli chuo hicho kinakamilika katika mwaka huo wa fedha?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa vijana wengi wa Jimbo la Vwawa na Mkoa wa Songwe wamekuwa wanahitaji sana hiki chuo na inaweza ikachukua muda mrefu sana kukimalisha kukijenga.

Je, Serikali itakuwa tayari kutumia majengo mbadala kutoa mafunzo hayo kwa vijana ambao wanahitaji mafunzo hayo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Japhet Hasunga, Mbunge wa Vwawa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye ujenzi tunakuwa na taratibu au models tofauti tofauti sana za ujenzi. Tuna model hii ya sasa hivi ambayo Serikali tunaitumia ya force account, lakini tuna model ile ya zamani ya kutumia wakandarasi. Kwa hiyo kwamba ni lini Serikali itatangaza zabuni itategemea na model ambayo tutakayotumia na mara nyingi sana kwa ujenzi wa vyuo vyetu vya VETA huwa tunatumia force account. Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge mara tu Mwaka wa Fedha ujao utakapoanza mwezi Julai, taratibu za ujenzi zitaanza kwa sababu sasa hivi tunaandaa zile tittle kwa ajili ya kumilikisha lile eneo kwenye Wizara ya Elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini eneo la pili amezungumza utayari wa kutumia majengo. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge baada ya Bunge hili tukufu tuweze kufanya ziara na timu yetu ya wataalam. Twende tukafanye tathmini ya hayo majengo anayoyazungumza ambayo tunaweza tukayatumia katika kipindi hiki kifupi wakati tunaendelea na ujenzi. Tutakapofanya tathmini hiyo na tukajiridhisha kwamba majengo hayo yanajitosheleza katika utoaji wa huduma hii, basi tunaweza tukafanya hivyo. Nakushukuru sana.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, je, upi mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba watumishi wanapelekwa katika Kituo cha Afya cha Songwe katika Kata ya Nanyara ambacho kina upungufu mkubwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, mkakati wa Serikali, kwanza tumeainisha maeneo yenye upungufu mkubwa wa watumishi na ajira zinazofuata tutahakikisha kituo hiki kinapatiwa watumishi wa sekta ya afya, ahsante.

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, je, ni lini Serikali itaanza kujenga kwa kiwango cha lami Barabara ya kutoka Vwawa – London - Msiya hadi Isarawe, ambayo ni ahadi ya Serikali kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, tutaanza kutekeleza ahadi hii kadri ya upatikanaji wa fedha, lakini tutakaa tena na Mheshimiwa Mbunge, kuweza kuona ni namna gani tutaratibu hili kupitia Mameneja wetu wa mikoa na hasa Meneja wa Mkoa wa Songwe kuona tunaanzaje kutekeleza ahadi hii ya Serikali.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa pale Vwawa eneo Isangu kuna maghala yalikuwa yanajengwa na Serikali ambayo yametelekezwa; na tangu mwaka 2020 mkandarasi aliondoka akaacha ule mradi.

Je, ni upi mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba maghala yale ambayo ni ya kisasa kwa maana ya vihenge yanatekelezwa ili yaweze kuchangia katika uchumi wa taifa letu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mpango wa Serikali kwa Maghala ya Vwawa na maeneo mengine yakiwemo yale ya Songea ni kwamba tulishawapa kazi NFRA kufanya tathmini halisi ya gharama ya maghala yote nchini, kuhakikisha tunayamaliza katika mwaka wa fedha unaokuja kwa kutumia fedha zetu za ndani. Huo ndiyo mpango wetu, kwa sababu lengo la Serikali ni kuongeza uhifadhi wa chakula kutoka tani laki 3 za sasa walao mpaka mwakani tuende kwenye tani laki saba na mwaka 2030 tufikie tani milioni tatu. Kwa hiyo mpango tulionao wa muda mfupi ni kuyamaliza yote kwa fedha za ndani.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa wananchi wamejitolea kwa kiwango kikubwa sana katika ujenzi wa maboma haya na waliahidiwa kwamba Serikali itakamilisha na maboma hayo ni mengi sana, je, Serikali haioni umuhimu wa kutenga bajeti maalum ili kukamilisha majengo hayo kuwaunga mkono wananchi hawa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa katika maeneo mengi sasa hivi Serikali imekuwa ikipeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mapya, ni kwa nini Serikali isipeleke fedha kukamilisha haya madarasa ambayo yameshaanzishwa na wananchi badala ya kuanza madarasa mapya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hasunga, la kwanza kwa nini isitengwe bajeti maalum kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma haya?

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi, Serikali imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali na wananchi wenyewe katika kuhakikisha kwamba maboma yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi nchini kote yanakamilishwa. Hivi sasa Serikali hii ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ipo katika mchakato wa kutafuta fedha kwa ajili ya kwenda kuunga mkono jitihada za wananchi nchini kote waliojenga maboma yao ikiwemo kule jimboni kwa Mheshimiwa Hasunga ambapo kuna maboma zaidi ya elfu moja na mia tano kwa ajili ya kwenda kuyakamilisha.

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili; kwa nini hizi fedha zinazokwenda sasa kwenye kujenga madarasa, kwenye kujenga shule mpya zisiende kwa ajili ya kumalizia yale maboma?

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikijenga shule na madarasa kupitia miradi mbalimbali, ambayo ni vigezo vya miradi ile kuhakikisha kwamba inajenga madarasa mapya inajenga shule mpya na kupimwa kulingana na matokeo yale yanayotokana na ujenzi ili tuweze kupata fedha nyingine nyingi zaidi kwa ajili ya kujenga shule nyingine nyingi na madarasa mengine mengi.

Mheshimiwa Spika, nirejee katika majibu yangu ya swali lake la nyongeza la kwanza, Serikali hii ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ipo katika mchakato wa kutafuta fedha kwa ajili ya kuunga mkono jitihada za wananchi nchini kote waliojenga maboma ya madarasa. Vilevile kuna fedha ile ya maendeleo ambayo Halmashauri inatakiwa kutenga na ndiyo kazi yake hii, Wakurugenzi kuhakikisha kwamba wanaunga mkono jitihada za wananchi kwa kutumia fedha ile ya maendeleo kwenye halmashauri zao.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, je, lini Serikali itaanza kuwaunga mkono wananchi wa Kata ya Msia katika ujenzi wa kituo chao cha afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za wananchi katika ujenzi wa vituo vya afya kwa kutoa fedha kutoka Serikali Kuu, pia kutoa fedha kutoka mapato ya ndani. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kumkumbusha na kumsisitiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Vwawa, Mbozi kwa ajili ya kuanza kutenga fedha za mapato ya ndani wakati Serikali Kuu ikitafuta fedha kwa ajili ya kuunga mkono, ahsante.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Ahsante sana. Kuna treni ya TAZARA ambayo inatoka Dar es Salaam mpaka Tunduma. Je, upi mpango wa Serikali wa kuhakikisha kwamba inaipanua treni hiyo ili iwe ya mwendokasi na iweze kukidhi mahitaji ya nchi yetu kwa Nyanda za Juu Kusini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Japhet Hasunga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba reli yetu ya TAZARA inaongozwa na nchi mbili kati ya Tanzania na Zambia. Kumekuwepo na changamoto nyingi katika uendeshaji wa reli hii, lakini habari njema ni kwamba ndani ya mwezi huu ifikapo tarehe 30 ya mwezi huu Mawaziri wa pande zote mbili kutoka Tanzania na Zambia watakutana. Lakini pili, tunataka tubadilishe Sheria. Hivi sasa Sheria inayotumika ni Sheria ya tangu ilivyoanzishwa TAZARA. Sasa sisi upande wa Tanzania tukitaka tuwekeze tunashindwa kwa sababu ile Sheria imetubana. Tayari maandiko au maandalizi ya Sheria hii imeshapitishwa. Kwa hiyo tunasubiri sasa kikao hicho cha Mawaziri watakapokaa halafu hizo Sheria zije ndani ya Bunge la Tanzania za upenda wa Zambia ili tuweze kuhuisha hii reli. Ahsante. (Makofi)
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naishukuru Serikali kwa majibu hayo mazuri ambayo imeyatoa, lakini ningependa kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka huu wa fedha 2023/2024 fedha hizi zilikuwa zimetengwa, hasa ningependa kujua nini kimetokea chuo hicho kimeshindwa kuanza kujengwa kwa mwaka huu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, ni aina gani ya mafunzo na katika ngazi gani chuo hiki tarajiwa kinategemea kuyatoa? (Makofi)
WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Hasunga kwa kuwa mfuatiliaji mzuri wa ujenzi wa Chuo cha Afya Vwawa, lakini kubwa maswali yake mawili pia la kwanza, kipi kimetokea fedha zilizotengwa 2023/2024 hazijafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni kuchelewa kwa kulipwa kwa fidia na hivyo tumeshindwa kuanza ujenzi kwa sababu fidia ilichelewa kulipwa, lakini jambo la pili Mheshimiwa Hasunga ni kwa sababu bado chuo hakijapata hatimiliki na hili nikuombe sana Mheshimiwa Hasunga ukatusaidie pamoja na mamlaka nyingine za Serikali mkoani Songwe na hususani Vwawa kuweza kupata hati ili tuweze sasa kuanza ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni muhimu sana kwa sababu tunatumia fedha pia za World Bank...

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, tupunguze sauti tafadhali.

WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya sharti ambalo Benki ya Dunia imetupa ni kutokuanza ujenzi hadi tuwe na hati ya eneo husika kwa ajili ya kujenga chuo. Kwa hiyo naomba sana utusaidie katika eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lako la pili kozi gani au level gani ya mafunzo ya afya itatolewa, itakuwa ni ngazi ya cheti (certificate) pamoja na diploma. kwa hiyo tutaendelea kufanya kozi ya uuguzi lakini pia tutaongeza na kozi nyingine ambazo ni muhimu katika utoaji wa huduma za afya ikiwemo wataalamu wa maabara. (Makofi)
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itamaliza mgogoro uliopo katika Kitongoji cha Isela, Kijiji cha Ndolezi na eneo la Kimondo kati ya wananchi na Ngorongoro?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye swali lililopita, utatuzi wa migogoro ni mchakato naomba tutoe fursa kwa Serikali iweze kushughulikia migogoro hii ili iweze kumalizika.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kuna upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi, hesabu na biashara ambayo ni 172 katika shule za sekondari mpya; na kwa kuwa katika shule za msingi kuna upungufu wa walimu 693.

Je, zipi hatua za Serikali za muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu wa kukabiliana na changamoto hii ya upungufu wa walimu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa katika maeneo mengi kuna walimu wengi ambao wamehitimu na bado hawana ajira, upi mkakati wa Serikali wa kuwatumia hao walimu kwa muda mfupi ili waweze kusaidia katika kupunguza changamoto ya upungufu wa walimu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, ni kweli katika shule zetu kote nchini zikiwemo shule hizi za Jimbo la Vwawa kuna upungufu wa walimu wa sayansi, hisabati lakini na masomo mengine kama masomo ya biashara, lakini Waheshimiwa Wabunge ni mashuhuda kwamba Serikali hii ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeajiri walimu kwa wingi kwa makumi elfu katika kipindi cha miaka hii mitatu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama ambavyo walimu wameendelea kuajiriwa na kupelekwa katika shule hizo Serikali itaendelea kuajiri kadri kibali cha ajira kinavyojitokeza na kipaumbele cha ajira hizi huwa ni walimu wa sayansi, walimu wa hisabati na masomo mengine yenye upungufu mkubwa zaidi. Kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge zoezi hilo linaendelea na tutahakikisha kwamba walimu wanafika kupunguza upungufu wa walimu katika shule hizo.

Mheshimiwa Spika, lakini pili, Serikali ilishatoa mwongozo wa namna ambavyo halmashauri zinaweza kutumia mapato ya ndani kuingia mikataba na walimu ambao wamehitimu wako katika maeneo yao kwa ajili ya kufundisha. Sisi sote tumeshuhudia kote nchini shule nyingi zina walimu ambao wameajiriwa kwa mikataba na wanaendelea kufundisha wakisubiri ajira za kudumu. Nitumie nafasi hii kusisitiza na kuhamasisha Wakurugenzi wahakikishe wanatumia fursa hii vizuri, ahsante
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa kuwa vipaumbele vya Kitaifa ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu, je, upi mkakati wa Serikali wa kuwa na mdahalo mkubwa wa Kitaifa ambao utajadili vipaumbele vitakavyotumika kwa muda wa miaka 50 ijayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Hasunga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kweli kabisa tuna vipaumbele kama Taifa na lazima tushirikishe wananchi au wadau wote katika kuandaa mkakati huo kwa maana ya kuandaa Dira ya Maendeleo ya Taifa letu. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tumekwishaanza, kupitia ile Tume ya Mipango ambayo iko chini ya Ofisi ya Mheshimiwa Rais wetu tumekwishaanza kufanya hizo taratibu na tayari midahalo imekwishaanza.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi tumetoa njia mbalimbali za kuingiza maoni kwa Watanzania kuleta kwenye Tume ya Mipango. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tunamkaribisha katika midahalo hiyo aweze kushiriki pamoja na Wabunge wote ili kutoa mawazo na maoni yao kuelekea Dira ya Taifa ya mwaka 2050.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, ni lini barabara ya kutoka Vwawa – Londoni - Msiya hadi Isarawo itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami ambayo imekuwa ni ahadi ya muda mrefu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayoifanya ya uwakilishi kwa wananchi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba dhamira ya Serikali ni kuhakikisha inafikia barabara nyingi iwezekanavyo, kupanua mtandao wa barabara hizi za Wilaya ziwe zina hadhi nzuri na ziweze kupitika katika kipindi cha mwaka mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali itaendelea kuhakikisha inatenga fedha kila mwaka na barabara hii ipo kwenye mpango, hivyo nimhakikishie kwamba barabara hii itajengwa. (Makofi)
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naishukuru Serikali kwa majibu hayo mazuri ambayo imeyatoa, lakini ningependa kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka huu wa fedha 2023/2024 fedha hizi zilikuwa zimetengwa, hasa ningependa kujua nini kimetokea chuo hicho kimeshindwa kuanza kujengwa kwa mwaka huu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, ni aina gani ya mafunzo na katika ngazi gani chuo hiki tarajiwa kinategemea kuyatoa? (Makofi)
WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Hasunga kwa kuwa mfuatiliaji mzuri wa ujenzi wa Chuo cha Afya Vwawa, lakini kubwa maswali yake mawili pia la kwanza, kipi kimetokea fedha zilizotengwa 2023/2024 hazijafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni kuchelewa kwa kulipwa kwa fidia na hivyo tumeshindwa kuanza ujenzi kwa sababu fidia ilichelewa kulipwa, lakini jambo la pili Mheshimiwa Hasunga ni kwa sababu bado chuo hakijapata hatimiliki na hili nikuombe sana Mheshimiwa Hasunga ukatusaidie pamoja na mamlaka nyingine za Serikali mkoani Songwe na hususani Vwawa kuweza kupata hati ili tuweze sasa kuanza ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni muhimu sana kwa sababu tunatumia fedha pia za World Bank...

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, tupunguze sauti tafadhali.

WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya sharti ambalo Benki ya Dunia imetupa ni kutokuanza ujenzi hadi tuwe na hati ya eneo husika kwa ajili ya kujenga chuo. Kwa hiyo naomba sana utusaidie katika eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lako la pili kozi gani au level gani ya mafunzo ya afya itatolewa, itakuwa ni ngazi ya cheti (certificate) pamoja na diploma. kwa hiyo tutaendelea kufanya kozi ya uuguzi lakini pia tutaongeza na kozi nyingine ambazo ni muhimu katika utoaji wa huduma za afya ikiwemo wataalamu wa maabara. (Makofi)
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, je, ni upi mkakati wa Serikali wa kujenga kituo cha afya katika Tarafa ya Vwawa, Eneo la Ihanda ambacho kitatumika pamoja na Ipunga na Ukwile? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kwamba maeneo yote ya kimkakati ambayo yanakidhi vigezo vya kuwa na vituo cha afya, yanajengewa vituo hivyo vya afya kwa awamu. Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge, ikiwa vigezo vinatimia, tutahakikisha tunatenga fedha, tunajenga kituo cha afya ili wananchi wapate huduma bora za afya, ahsante.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa stendi ya mkoa katika Mji wa Vwawa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Hasunga na Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Songwe mara nyingi wameulizia kuhusiana na ujenzi wa stendi ya Mkoa wa Songwe na Serikali siku zote tumewahakikishia kwamba, ni kipaumbele cha Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe tu, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, mipango ya Serikali bado inaendelea na tunahakikisha kwamba tutapata fedha kwa ajili ya ujenzi wa Stendi ya Mkoa wa Songwe. (Makofi)