Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Pascal Yohana Haonga (20 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nichangie ukurasa ule wa nane na wa 17 wa hotuba ya Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa ule wa nane hotuba ya Mhesimiwa Rais imegusa suala la walimu pamoja na malalamiko yao kwamba wana malalamiko. Ni kweli kabisa kwamba suala hili ni suala ambalo lipo. Walimu wana malalamiko kwamba hawana nyumba, lakini pia imefika mahali wana madai ya muda mrefu sana. Mheshimiwa Naibu Spika, kama Serikali ya awamu ya tano ambayo ina slogan ya Hapa Kazi Tu; kama kweli itakwenda kujenga nyumba za walimu, italipa madeni sugu ya walimu ya muda mrefu sana, nadhani nchi hii kweli itakwenda, kwa sababu awamu zote zilizopita wote hawakuona umuhimu wa kuwalipa walimu madeni na kuwajengea nyumba bora. Kwa hiyo, nadhani Serikali hii ikifanya hivyo mambo yatakwenda vizuri kabisa. Mheshimiwa Naibu Spika, natoa mfano mdogo. Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi hivi ninavyozungumza inaonekana kwamba walimu waliosimamia mtihani wa kidato wa cha nne mwaka 2014 hawajalipwa fedha zao; na sio walimu tu lakini pia na Watumishi mbalimbali wa Halmashauri wakiwepo askari na madereva. Kwa hiyo, naomba katika haya maneno aliyoyazungumza Mheshimiwa Rais muweze pia kuliangalia hili. Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani kabisa kwamba Serikali yoyote ambayo iko makini inafika mahali deni la mwaka wa jana halijalipwa, lakini leo sina uhakika sana kama sisi Wabunge kuna Mbunge ambaye anaweza akawa anadai deni la mwaka wa jana au mwaka wa juzi. Inawezekana walimu wamesahaulika sana katika Taifa hili, ndiyo maana tunafikia hali kama hii. Mheshimiwa Naibu Spika, naomba walimu wakumbukwe na deni hili lilipwe kwa kweli;
walimu wa Halmashauri ya Mbozi na walimu wengine wowote wanaoidai Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nichangie ukurasa ule wa 17. Wakulima imefika mahali wana malalamiko makubwa sana. Mheshimiwa Rais alipokuwa akilihutubia Bunge, alisema atawasaidia wakulima, ataondoa ushuru wa kwenye mazao. Kwa mfano, Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi tunalima sana kahawa, wakulima wana shida kubwa sana, wanatozwa ushuru wa kahawa 5%, ambayo ni sawasawa na shilingi 175/= kwa kilo moja; lakini pia wanatozwa ushuru wa Bodi ya Kahawa; ushuru wa utafiti; wakulima wamebebeshwa mzigo mkubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali hii ya awamu ya tano iweze kuliangalia hili. alichokuwa anakizungumza Mheshimiwa Rais naomba akifanyie kazi kweli kweli na isiwe maneno tu. Ninaamini kabisa kwamba Mungu atambariki na atakwenda kuwasaidia wakulima wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, imekuwa ni mzigo, inafika mahali mkulima wa kahawa licha ya kwamba anatozwa ushuru huo ambao nimesema ni 5%, pamoja na matatizo mengine lakini mkulima huyu wa kahawa na mazao mengine ameshindwa kutafutiwa somo zuri na mwisho wa
siku inaonekana kwamba anauza kwa bei ndogo sana. Kwa mfano, msimu uliopita wakulima wa Kahawa wameuza kahawa yao kwa bei ndogo sana. Naomba Serikali iangalie suala hili maana bila kuwasaidia wakulima kwa kweli tutakuwa tunarudi nyuma, maana tunajua kabisa kwamba kilimo kinachangia zaidi ya asilimia 70 ya pato la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia niweze kuzungumza kwa ufupi sana ukurasa wa nne wa hotuba ya Rais. Alizungumzia suala la siku ya uchaguzi kwamba ilikuwa na utulivu na amani. Naomba nizungumze tu kwamba katika hili nadhani Rais wetu atakuwa kidogo aliteleza.
Siku ya uchaguzi tarehe 25 Oktoba, 2015 ilikuwa na amani na utulivu; hayo maneno sijajua vizuri kwamba labda alikosea au aliteleza.
Ni kwamba kuna maeneo mengi sana vurugu zilifanyika, kuna watu walipigwa, watu waliwekwa ndani, watu wamebambikiziwa kesi, watu hadi leo wengine wamekimbia maeneo yao, halafu Rais anasema eti siku hiyo ilikuwa ya amani na utulivu. Mimi nadhani kuna watu
labda walimpotosha Mheshimiwa Rais kwenye hili, nami naomba tu Mheshimiwa Rais inabidi kidogo afuatilie hili vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano natoa mfano mdogo wa Jimboni kwangu Mbozi.
Jimbo la Mbozi uchaguzi siku ya Jumapili, tarehe 25 Oktoba, 2015 watu waliwekwa ndani wakiwa wanadai matokeo. Wamefunguliwa kesi hadi leo! Wengine wameshakimbia, hivi ninavyozungumza hawapo kwenye Jimbo langu. Mheshimiwa Rais anakuja anasema kwamba
Uchaguzi ulikuwa wa amani na huru.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu kwamba siku nyingine Serikali tujipange vizuri. Kunapokuwa na uchaguzi tujaribu kutumia Jeshi la Polisi vizuri na yule aliyeshinda kihalali atangazwe haraka sana. Kwa sababu mambo yote haya yanajitokeza pale mtu ameshinda wanashindwa kutangaza matokeo mapema, inafika mahali watu wanadai matokeo wanaanza kupigwa, wanapelekwa ndani, wanafunguliwa kesi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili kwa kweli linasikitisha sana na machafuko mengi tu yametokea katika sehemu mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mwingine mdogo tu naweza nikatoa. Hata ndugu zetu kule Zanzibar hali kwa kweli haiko shwari kabisa hadi hivi ninavyozungumza. Hali haiko shwari! Hili limejitokeza! Mwenyekiti wa ZEC amekaa peke yake anatangaza kwamba tunarudia uchaguzi
wakati huo unaona kabisa kwamba hawajakubaliana na Tume.
Mheshimiwa Naibu Spika, imefika mahali na ushahidi upo, tutajaribu kuuwasilisha kama utahitajika kwa muda ambao tutapangiwa, Makamu Mwenyekiti wa ZEC alikamatwa akawekwa ndani.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Haonga naomba umalize!
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Kwa hiyo, hali haikuwa nzuri, hapakuwa na utulivu wowote ule. Naomba tunapoelekea huko siku za usoni kweli kabisa tuishauri Serikali isimamie uchaguzi vizuri, aliyeshinda awe ameshinda na mambo yaweze kwenda vizuri kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nichangie suala lingine. Kwenye kilimo kuna suala dogo nilikuwa nimelisahau, kuhusu mfumo wa vocha ambao Serikali inautumia kuweza kuwapa wakulima. Mfumo wa vocha kusema ukweli siyo mzuri kabisa. Vocha hizi zinawanufaisha wale watendaji wachache, Watendaji wa Vijiji, Watendaji wa Kata na watu wachache, mara nyingi sana wanazigawa kwa kufuata itikadi ya Vyama vya Siasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hizi vocha za pembejeo zinazotolewa kuna mtu akiwa chama fulani cha upinzani vocha hizi hazimhusu, hata kama ni mnufaika, hapewi. Vocha hizi zinawanufaisha watu wachache sana. Natoa mfano mdogo tu, Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, msimu wa kilimo huu uliokwisha vocha zilikuja 13,000 kwa Wilaya nzima ya Mbozi. Wilaya ina wakazi zaidi ya 500,000 vocha zimekuja 13,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani kwamba mfumo huu siyo mzuri kabisa, ni mfumo wa ubaguzi, hauwezi kuwasaidia wakulima wetu. Nasema kabisa kwamba kuna namna ambayo inatakiwa tuifanye ili kubadilisha mfumo huu wa kugawa vocha hizi za kilimo. Kama kuna
uwezekano Serikali itafute utaratibu mzuri kwamba mbolea inapoingizwa nchini, kama Serikali inaweza ikatoa ruzuku moja kwa moja kwa ile mbolea inapoingizwa nchi nzima, inapouzwa basi iwe imeshalipiwa ruzuku na kila kitu, angalau sasa ionekane ni ya ruzuku nchi nzima, hata kama ni pesa kiasi kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama mfuko wa mbolea leo unauzwa shilingi 70,000/=. Labda mfuko wa mbolea Dar es Salaam hapo unauzwa shilingi 70,000/=. Kama Serikali inaweza ikaweka pesa yake ya ruzuku kidogo pale, ikalipa kwa mfano hata 40% au 50%, maana yake
shilingi 70,000/= inaweza ikashuka hadi kufikia shilingi 35,000/=hadi shilingi 40,000/=. Hiyo ni nchi nzima, maana yake watu wa Mbozi wanunue kwa bei hiyo, lakini pia watu wa Kigoma wanunue kwa bei hiyo kuliko mfumo wa sasa ambao unawanufaisha wafanyabiashara
wachache, lakini pia ni mfumo wa kibaguzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba suala hili tuliangalie sana kwa sababu Tanzania bila kilimo haiwezekani, ninaamini Kilimo kinachangia asilimia kubwa sana katika pato la Taifa.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Haonga, muda wako umekwisha.
MHE. PASCHAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kidogo.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Haonga muda wako umekwisha tafadhali! Mheshimiwa Haji Khatib Kai! Mheshimiwa Abdallah Mtolea.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nisahihishe kidogo jina langu naitwa Mwalimu Pascal Yohana Haonga, Mbunge wa Mbozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie na mimi kwenye Wizara hii ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na ninaomba nianze kwa kusema kwamba kwa muda mrefu sana wakulima Watanzania wamesahaulika sana. Takwimu zilizoonyeshwa hapa kwenye hotuba hii, wote nadhani tumesoma, tumeona kwamba sekta ya kilimo imeendelea kushuka mwaka hadi mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona kwa mfano mwaka 2015 tumeambiwa kwamba kilimo kilikua kwa asilimi 3.1, lakini mwaka 2014 tunaambiwa kilikua kwa asilimia 3.4. Ikumbukwe kwamba siku za nyuma huko mwaka 2009, kilimo kimeshawahi kukua kwa asilimia hadi 5.1. Hivyo ni dhahiri kwamba wakulima wamesahaulika, japokuwa sasa Sekta hii ya Kilimo inaajiri Watanzania walio wengi, lakini wamesahaulika sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaambiwa kwamba uzalishaji wa mazao ya nafaka, hivyo hivyo umeendelea kushuka mwaka hadi mwaka kama tulivyoambiwa kwamba mwaka 2015 mazao ya nafaka uzalishaji ulikuwa tani milioni 9.8, lakini hivyo hivyo tunaambiwa kwamba mwaka 2015 umeendelea kushuka.
Kwa hiyo, naomba niseme tu kwamba wakulima wamesahaulika na zaidi kwa nini tumefikia mahali hapa? Tumefikia hapa kwa sababu Serikali haijachukua hatua ambazo zinaweza kuwasadia wakulima wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Serikali imeshindwa kuwapunguzia wakulima wetu mbolea, wananunua mbole kwa bei kubwa sana na imefika mahali mkulima mwingine anaamua kuahirisha kulima kwa sababu mbolea ipo juu sana. Hali hii ikiendelea, wakulima ambao ndio wengi zaidi katika Taifa hili, siku moja wataungana na kusema sasa basi, inatosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua Waziri wa Kilimo yuko hapa Mheshimiwa Mwigulu Nchemba na Naibu wake, naomba wakumbuke kwamba wako waliowatangulia mbele akiwepo ndugu yangu Mheshimiwa Wassira, lakini yuko aliyekuwepo Naibu Waziri Mheshimiwa Godfrey Zambi na mwingine Mheshimiwa Chiza; leo hawapo kwenye Bunge hili kwa sababu ya ugumu wa kilimo katika Taifa hili.
Mheshimiwa Waziri, kama hamtakuwa makini katika suala hili, kama hamtakuwa tayari kuwasaidia wakulima wa Tanzania, kupunguza bei ya mbolea, kutafuta masoko kwa wakulima wetu ni dhahiri kwamba hali itakuwa ni mbaya kweli kweli, na ninyi nadhani mpaka mwaka 2020, mnaweza mkafuata nyao za akina Mheshimiwa Wassira, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba nchi ndogo kama ya Malawi, imefika mahali inauza mbolea kwa bei ndogo sana; inauza mbegu kwa bei ndogo sana kwa wakulima wake, lakini mbolea hiyo inapita kwenye Bandari ya Dar es Salaam. Ingekuwa ni jambo la busara sana kwenda kuiga kwa wenzetu wanafanya nini hadi mbolea yao wanauza kwa bei ndogo wakati wanaipitisha kwenye bandari yetu, wanatoa na ushuru wa bandari, leo wao wanauza kwa bei ndogo. Nadhani suala hili tungeweza kufanya utafiti tujue ni kwa nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashangaa sana, ninaambiwa kwamba mwaka 2014 pesa kwenye mbolea zilitengwa shilingi bilioni 96, tukaambiwa mwaka 2015 zilitengwa shilingi bilioni 78 kwa ajili ya mbolea, lakini mwaka huu pesa zilizotengwa kwenye mbolea tunaambiwa ni shilingi bilioni 20.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna hii hatuwezi kusonga mbele! Hali ni mbaya kweli kweli na ni dhahiri Serikali hii haitaweza kwa kweli kuwasaidia wakulima na haina nia njema na wakulima wetu. Huyu Rais wetu anayesema kwamba mniombee Watanzania, ajue kwamba wengi wao ni wakulima. Sidhani kama wanaweza wakamwombea kama hatawasaidia kwenda kupunguza kodi katika mbolea na kuongeza fedha katika Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosikitika kingine ni kwamba tunaambiwa wenzetu zao lao la korosho wamepunguza ushuru; ushuru wa Chama Kikuu cha Ushirika, lakini kuna ushuru wa usafirishaji, ushuru wa mnyaufu, ushuru wa Bodi ya Korosho, ushuru wa Mrajisi wa Vyama vya Ushirika; kwenye korosho wamepunguza ushuru huu na tozo hizi.
Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kwenye majumuisho atuambie na sisi wakulima wa kahawa kama mna mkakati wa kupunguza ushuru kwenye kahawa. Kwa sababu kumekuwa na mzigo mzito sana, imefika mahali mkulima wa kahawa anatozwa ushuru wa Bodi ya Kahawa, ushuru wa utafiti (TACRI) kule mkulima analipia, wakati Serikali ingeweza kabisa kuwasaidia wakulima hawa. Vile vile kwenye Halmashauri, wakulima wa Kahawa pia wanatozwa ushuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kabisa Mheshimiwa Waziri atakapokuja kwenye majumuisho, atawatangazia neema wakulima wa kahawa nchi nzima kwamba tumeamua tupunguze ushuru kwenye mazao haya, maana huu utakuwa ni ubaguzi wa hali ya juu sana kama utapunguza kwenye korosho halafu kwenye kahawa ukaacha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumze suala linguine. Wakulima wa kahawa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wanaomba Serikali ianzishe mnada kuliko ilivyo leo ambapo wanapeleka kahawa yao Moshi ambapo kuna mnada, wakati asilimia 90 ya kahawa inayouzwa kwenye mnada wa Moshi, inazalishwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo wakulima hawa wamenituma, wanaomba tuwe na mnada wa kahawa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, watu wa Ruvuma na Mkoa mpya wa Songwe ikiwezekana waje Mbeya wauze kahawa yao pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nakumbusha tu kwamba Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, hili ni eneo la muhimu sana. Siku hizi tuna uwanja wa ndege pale Songwe. Kwa hiyo, mazingira yanaruhusu kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kabisa Mheshimiwa Waziri atakapokuja kwenye majumuisho atatuambia kwamba suala hili atakubaliana na wakulima wa kahawa wa Kanda za Juu Kusini kuweza kuanzisha mnada wa kahawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la NFRA kutenga fedha za kununua mazao ya nafaka. Msimu uliopita wakulima wetu wamekopwa mahnidi na wengi hadi sasa walilipwa nusu imefika mahali hawawezi tena kununua mahindi, wamekosa mtaji kwa sababu Serikali kwa jitihada za makusudi kabisa imeamua kuwafilisi wajasiriamali.
Msimu huu tunapokwenda kununua mahindi, naomba Serikali isiwakope wananchi. Ikiwezekana itenge fedha kabisa ya kwa ajili ya kwenda kununua mahindi ya wananchi bila kuwakopa. Wakiendelea kuwakopa wananchi ambao ni maskini na wengi wao pesa wanakopa benki, tunawalipa nusu nusu, hatutafika na mwisho wa siku tutakuwa hatuwasaidii wakulima wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ni la msingi zaidi japokuwa wengine wameshaligusia sana, ni mfumo wa kugawa voucher. Mfumo wa usambazaji wa voucher siyo rafiki kwa wakulima wetu. Imefika mahali watu wanagawa voucher wanaangalia, huyu ni ndugu yangu, huyu ni shemeji yangu, huyu ni nani! Leo Wenyeviti wa Vijiji, Madiwani wamekosana na wananchi kwa sababu pia nao wanaambiwa kwamba mnapendelea na mnabagua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mfumo huu wa voucher ikiwezekana tuufute kabisa na badala yake mbolea iweze kupunguzwa bei, tupunguze ushuru kwenye mbolea na baada ya hapo mbolea ipatikane nchi nzima kwa bei nafuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kabisa tukifanya hivi wakulima wetu itafika mahali watafarijika na wataendelea vizuri kabisa, watalima, tutapata mazao ya biashara na chakula; lakini mambo yatakwenda vizuri kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia naomba niseme kwamba leo tuko mahali hapa, lakini nasikitika sana, kuna watu ambao bado hawajalipwa fedha zao za mahindi waliyopima.
Naomba kwa sababu Waziri yuko mahali hapa, ikiwezekana aonane na Mbunge wa Jimbo la Mbozi ili nimwambie ni akina nani hawajalipwa mahindi yao na ni kwanini Serikali inakopa wananchi mahindi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini inafika mahali inawadhulumu na wengine masikini? Hatuwezi kukubali kabisa! Tumesema kwamba sasa inatosha, lakini tukiendelea na utaratibu huu tutakuwa tunawaumiza wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nami sasa niweze kuchangia Wizara hii muhimu ambayo kwa kweli na mimi naomba ku-declare interest kwamba mimi pia ni Mwalimu kama ambavyo wengine wame-declare interest. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunajadili bajeti ya Wizara ya Elimu, wanafunzi ambao wako Vyuo vya Elimu ya Juu, tangu wamefungua chuo hawajapata mkopo; na hili ni jambo la kusikitisha sana. Imefika mahali wanafunzi wetu wanacheleweshewa mikopo na mikopo ambayo mwisho wa siku watakuja kuirejesha, lakini wanapokuwa sasa wanadai hizo fedha, tunaenda kuwapiga mabomu, tunawapelekea Polisi jambo ambalo linasikitisha sana. Kiukweli kabisa kama mikopo inakuwa inacheleweshwa, nadhani mtu wa kwanza kupigwa bomu inatakiwa awe Waziri wa Elimu na Watendaji wake lakini siyo wanafunzi wetu. Tunawaonea sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba japokuwa pia wenzangu amegusia sana kwenye suala hili la Bodi ya Mikopo, naomba nami niguse baadhi ya vitu pia. Kuna kitu fulani kinaitwa Quality Assurance Fee kwenye elimu ya juu. Mwanafunzi anaambiwa alipie shilingi 20,000/= kwa ajili ya kudhibiti ubora wa elimu. Kimsingi jukumu hili la kudhibiti ubora wa elimu ambalo linafanywa na TCU ni jukumu la Serikali. Hivyo, kumbebesha mwanachuo mzigo, ni suala ambalo kwa kweli haliruhusiwi hata kidogo! Kwasababu TCU ni sehemu ya majukumu, inakuwaje tunakwenda kumbebesha mzigo mwanafunzi masikini? Kwa kweli hali hii inasikitisha sana na sidhani kama inatakiwa tuendelee kuivumilia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri, pamoja na sifa ambazo amepewa mimi sitaki kumsifia, kwasababu siwezi kumsifia mtu wakati ni majukumu yake. Naomba suala hili ukaliangalie sana Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nizungumzie suala linguine, kwenye elimu ya juu. Leo wanafunzi hakuna mawasiliano kati ya Wizara ya Ulinzi pamoja na Wizara ya Elimu. Wametangaza kwamba wanafunzi waliomaliza Form Six waende JKT kuanzia tarehe 1 mwezi wa Sita hadi tarehe 6 walipoti JKT. Wakati wowote kuanzia sasa wanafunzi watahitajika kuomba mkopo waliomaliza Form Six. Tafsili yake ni nini? Tafsiri yake ni kwamba wanafunzi wanaoenda JKT wengi wanakosa fursa ya kuomba mkopo. Mwaka 2015 wanafunzi 80 waliokwenda JKT walikosa mkopo Chuo Kikuu cha Dar es salaam peke yake sehemu ya Mlimani. Kwenda JKT imekuwa dhambi leo hii? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba suala hili Mheshimiwa Waziri aliangalie sana, kuwe na utaratibu maalum; kabla hawajaenda JKT, waombe mkopo mapema ili wanapomaliza pale waende chuo tayari wakiwa wameshaomba mkopo. Kama tatizo ndiyo hilo, mwisho wa siku watu watasema kwamba JKT hatuendi kwasababu tukitoka JKT tutakosa mkopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine ambalo limekuwa ni tatizo kubwa sana. Hakuna mawasiliano kati ya TCU na Bodi ya Mikopo. Kwanini nasema hakuna mawasiliano? Leo ukisoma kitabu cha TCU kinakuonesha kozi ambazo ukienda kusoma utapata mkopo (priority course), lakini wakati huo huo anapoomba mwanafunzi kozi hizo kwenda kusoma Bodi ya Mikopo inasema kwamba hizi kozi siyo za mkopo. Hakuna mawasiliano kati ya Bodi ya Mikopo pamoja na TCU. Alishaongea Mheshimiwa Godbless Lema kwamba hii nchi imekuwa kama ghetto, hamna utaratibu, nami nadiriki kusema kwamba nchi hii ni kweli hakuna utaratibu! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme maneno makali, tunaendesha nchi utafikiri ile nchi ya kijuha, kwasababu kama Bodi ya Mikopo ni chombo cha Serikali, TCU ni chombo cha Serikali hawa wanakwambia hii kozi inakopesheka, ukienda kule wanakwambia hii kozi haina mkopo. Maana yake ni nini? Mheshimiwa Waziri, naomba ukaliangalie hili. Kama Taifa tunaaibika sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninaomba nizungumze suala linguine. Leo kuna changamoto nyingi sana katika elimu ya juu. Ukienda katika hostel za wanafunzi wetu; kwa mfano pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tu sehemu ya Mlimani, wanafunzi ambao hostel inaweza ku-accommodate ni wanafunzi 6,500, lakini idadi ya wanafunzi ni 18,000. Wanafunzi wengi wanabebana, wanalala wawili kwenye kitanda kimoja. Hali ambayo ni mbaya sana! Leo hii kama kuna fedha inatakiwa zipelekwe basi zinatakiwa zipelekwe kwenye elimu ya juu za kutosha. Kama Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli alipeleka pesa kwa Mahakimu akasema hakuna pesa, kesho kutwa kapeleka; baada ya siku mbili akapeleka, leo mnaonaje kupeleka pesa elimu ya juu? Pesa zipo. Tatizo la nchi hii siyo pesa, tatizo la nchi hii ni uongozi mbovu ambao nadhani kwa muda mrefu sana tumekuwa tukilia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nizungumze suala lingine kuhusu mfumo wa uandaaji wa vitabu vya kufundishia na kujifunzia. Leo kutokana na elimu yetu jinsi ilivyo, kila mtu anapanga la kwake. Akilala Mheshimiwa Waziri anaamka asubuhi anasema, leo tunachanganya Physics na Chemistry, wanafunzi wanaanza kusoma. Kesho mwingine anarudi anasema hapana ulikosea. Hii hali ni kwasababu ya kukosa uongozi bora. Tatizo ni Uongozi katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongezee, leo tunataka elimu yetu iwe bora, kuna tatizo la kutowalipa Walimu wetu wanaoidai Serikali. Nataka nitoe mfano mdogo tu. Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Walimu wanainaidai Serikali zaidi ya shilingi milioni 800 na kitu, hawajalipwa. Watoto wetu watafaulu vipi kwa namna kama hii ambapo Walimu waliokata tamaa wanaidai Serikali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Momba wanaidai Serikali zaidi ya shilingi milioni 600. Walimu hawajalipwa hizo fedha! Ileje Walimu wanaidai Serikali zaidi ya shilingi milioni 400, hawajalipwa. Unataka watoto wafaulu vipi? Suala hili halihitaji kufunga kwa maombi wala kupiga ramli, tatizo ni Serikali! Walimu wengi wameshakata tamaa. Suala hili lisiposhughulikiwa kwa kweli tutaendelea kulia na vilio vyetu havitaisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongezee, kuna Walimu wamesimamia mtihani a Kidato cha Nne mwaka 2015 hawajalipwa fedha zao, karibu shilingi milioni 118 Halmashauri ya Mbozi; leo ni nani Mbunge hapa, ni nani Waziri hapa ambaye posho yake ya mwaka 2015 hajaichukua? Posho yake ya mwaka 2014 hajaichukua! Mshahara wake wa mwezi uliopita hajachukua? Ni nani Waziri hapa au Mbunge? Tuwaonee huruma Walimu! Walimu hawa waliokata tamaa mwisho wa siku wakianza kuandamana, msije mkaanza kutafuta mchawi ni nani. Mchawi ni Serikali ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu hawa walipwe fedha hizo na wasipolipwa fedha hizo kwasababu sisi ni Wawakilishi wao, nimechangia hata mara ya kwanza nilizungumzia suala hili; tuataenda kukaa nao, ikiwezekana tuingie barabarani. Muwe tayari kutupiga na mabomu! Sawasawa! Kwasababu hatuwezi kuvumilia Walimu wetu wanateseka! Hata mimi pia ni Mwalimu, nina uchungu sana! Naomba kama kweli tunawapenda Walimu wetu, tukalipe fedha hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vivyo hivyo, bado kuna suala la makazi bora ya Walimu, ni tatizo! Ameongea mwenzangu pale kwamba ametokea mahali, kwa mfano wanasema hii ni TAMISEMI, hii ni wapi; lakini makazi bora kwa Walimu ni tatizo. Kuna shule moja ambayo nilikuwa nafundisha kabla sijawa Mbunge, shule hiyo ina nyumba moja tu ya mwalimu. Walimu wanalala nane kwenye nyumba moja. Unaweka kitanda, unaweka godoro chini, this is shameful! Kwa kweli suala hili ni aibu sana, Serikali hii lazima ifike mahali iangalie sana kwenye suala la elimu, ahsante.
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Yohana. Tunaendelea na..
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, naomba nisiunge mkono hoja na nimshukuru sana Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa kazi nzuri ambayo anaendelea kuichapa; tunamuunga mkono, Mungu ibariki UKAWA. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, nchi hii ina matunda mengi kama vile maembe, mananasi, machungwa, zabibu na mengineyo, Serikali haina sababu ya kuagiza juice na wine nje ya nchi kwa kuwa uwezekano wa kuanzisha viwanda vya juice na wine hapa nchini ni mkubwa, kuagiza juice nje ya nchi ni upotevu wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mafuta ya kupikia ambayo ni ya pili kuingizwa nchini yakitangulia mafuta ya magari, Serikali ipige marufuku uingizaji wa mafuta ya kupikia kwa kuwa mazao ya kutengenezea mafuta kama vile karanga, alizeti na mawese vinapatikana hapa nchini. Alizeti inalimwa katika Mikoa ya Singida, Iringa, Mbeya, Rukwa, pamoja na Mikoa mingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vivyo hivyo, uagizaji wa toothpick ungepigwa marufuku kwa kuwa tuna miti mingi inayoweza kutengenezea toothpick. Serikali ikizingatia haya yote tutaokoa fedha nyingi sana, lakini pia tutatengeneza ajira kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nawasilisha kwa Waziri wa Nishati na Madini vijiji ambavyo havipo kabisa kwenye mpango wa umeme wa REA Jimbo la Mbozi. Vijiji hivi ni pamoja na:-
Ikonga, Maninga, Iporoto, Twinzi, Halambo, Shasya, Mbuga, Rungwa, Hamwelo, Insani, Itentula, Mboji, Iyenga, Nsega, Ileya, Igaya, Magamba, Mtunduru, Naulongo, Iwalanje, Nambala, Mbulu, Myovizi, Ivufula, Isenzanya na Manyara.
Mheshimiwa Naibu Spika, niaba ya wananchi wa Mbozi naomba Mheshimiwa Waziri awasaidie ili waingizwe katika REA phase III.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia makaa ya mawe yanayochimbwa Kijiji cha Magamba na Kampuni ya Wagamba Coal Company katika Jimbo la Mbozi kuna changamoto zinajitokeza. Kampuni hii haijawahi kulipa service levy katika Halmashauri ya Mbozi tangu uchimbaji wa makaa ya mawe uanzishwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kampuni hii iagizwe kulipa service levy katika Halmashauri ya Mbozi ili kuchochea maendeleo. Pia kampuni hii ielekezwe kutengeneza barabara ya kutoka Magamba-Isansa-Shiwinga-Mlowo katika Jimbo la Mbozi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwekezaji anayemiliki shamba kubwa Kijiji cha Senzaya amewakosesha wananchi maeneo ya kulima. Eneo analomiliki ni kubwa na ameshindwa kuliendeleza kwa miaka mingi sana. Naomba Mheshimiwa Waziri aingilie kati ili wananchi waweze kurejeshewa eneo la kulima. Jambo baya zaidi ni kwamba sehemu ya eneo hilo lilichukuliwa kinyemela bila kufuata taratibu/sheria za umiliki wa ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia shamba kubwa na NAFCO - Magamba zaidi ekari 12,000 limechukuliwa hivyo wananchi hawana maeneo ya kulima. Ni vyema Serikali ikarejesha sehemu ya shamba hilo ili kuwasaidia wananchi wa maeneo yanayozunguka mashamba hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mashamba yote mawili (Isenzanya na NAFCO) yapo Wilaya ya Mbozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti naomba kuwasilisha.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kilimo halijapewa kipaumbele, limezungumzwa kidogo sana katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/2018. Ni vema kilimo kikapewa kipaumbele ili pia kufikia nchi yenye viwanda tunayoiota. Karne ya 18 na 19 mwanzoni, nchi ya Uingereza ilifanya mapinduzi makubwa sana ya kilimo (Agrarian Revolution) na ndiyo matokeo ya viwanda vya Uingereza vilivyopo hadi leo. Vivyo hivyo nchi za China na India zote zilifanya mapinduzi ya kilimo (Agricultural Revolution) na hatimaye zikafikia hatua ya kuwa na viwanda ambavyo vipo hadi leo. Hivyo hakuna nchi yoyote duniani inayoweza kufikia mapinduzi ya viwanda bila kuboresha kilimo.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba na mimi nichangie Kamati hii ya Kilimo, Mifugo na Maji na ninaomba ku-declare interest kwamba mimi ni mjumbe wa Kamati hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kusema kwamba kwa bahati mbaya sana tunadhani kwamba tunaweza kuwasaidia Watanzania angalau kuondokana na umaskini kupitia kilimo; jambo ambalo kwa kusema ule ukweli kwa haya yanayofanyika imekuwa ni vigumu sana na sidhani kama kweli tupo serious. Unaona leo kwenye ruzuku ya pembejeo za kilimo wamepeleka bilioni 20 kwenye bajeti, na bilioni 20 yenyewe hii, hizi fedha bado inaonekana hali ni mbaya na hizi fedha bilioni 20 haziwezi kuwatosha wakulima wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti tulishapendekeza siku za nyuma kwamba ikiwezekana huu mfumo wa kuweka ruzuku kwenye pembejeo za kilimo, Serikali iachane nao kabisa kwa sababu hauwasaidii wakulima wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukitaka kumsaidia mkulima ni mara mia ukapunguza kodi kwenye mbolea, kwa sababu kinachopandisha bei ya mbolea tunajua kabisa ni kodi; hii kodi ambayo ipo kwenye mbolea. Bahati nzuri hata Waziri amewahi kuzungumza kwamba kwenye mbolea kule kuna tatizo moja, kuna kitu kinaitwa udalali. Tukitaka kuwasaidia wakulima twendeni tukapunguze kodi kwenye mbolea na kwenye pembejeo nyingine ili wakulima wetu waipate dukani kwa bei ndogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ajabu sana leo nchi kama Malawi inatumia Bandari ya Dar es Salaam na inapofikisha mbolea nchini kwake bei ni ndogo sana mfuko hata shilingi elfu 20 haufiki; unapokwenda Zambia vivyo hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wetu tumewachezea vya kutosha na Mheshimiwa Waziri, naomba niwe muwazi kabisa, msema mkweli ni mpenzi wa Mungu, tutakapokuwa tunaenda kwenye Bunge la Bajeti kabisa kama mchezo tunaoenda nao ndio huu, nitashika Shilingi ya Mheshimiwa Waziri na nitaomba huko mbele ikiwezekana uweze kuachia Wizara hiyo kwa sababu naona kama ina changamoto nyingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema ule ukweli kabisa hali jinsi ilivyo hata kwa wafugaji wetu; leo mifugo inakufa. Ukimuuliza Waziri hapa ndugu yangu mifugo iliyokufa; karibu nchi nzima mifugo inakufa kwa sababu ya ukame; hata takwimu hana. Hajui mifugo mingapi, ng’ombe wangapi wamekufa na mbuzi wangapi wamekufa. Sasa kwa hali kama hii, huu ni uzembe na udhaifu mkubwa sana kwa Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wamekuwa wakijipendekeza wanazungumza na uongo hadi wanadanganya wanasema kwamba njaa hakuna kwa sababu Mtukufu Rais amesema njaa hakuna na wao wanafuata hivyo hivyo. Kwa hiyo, inapofika mahali Rais akisema hii ni nyekundu si nyeupe, Waziri nae anasema hii ni nyekundu kwa sababu Rais kazungumza, huko sio kuwasaidia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwe muwazi kabisa nchi nyingine, kwa mfano nchi kama Kenya mifugo ikifa Serikali inaamua kwenda kufidia, inawapa wananchi angalau mifugo kidogo kwa ajili ya kufidia kidogo wananchi wasiingie hasara. Sasa nashauri ikiwezekana na sisi Serikali yetu tuweze kuiga kwa majirani wa zetu hapa Kenya na nchi nyingine tuweze kuiga mfumo wanaoutumia. Mifugo inapokufa angalau tuweze kuwafidia kidogo wafugaji wetu, maana leo katika Taifa letu mifugo imekufa hatujui sasa ukame huu ukiendelea itakuwaje, maeneo mengine; hali ni mbaya zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanya ziara maeneo mbalimbali, Kamati yetu tumekwenda Simanjiro na Kiteto, hali ni mbaya kweli kweli tunakutana na mifugo mingi, mizoga ng’ombe wamekufa njiani. Leo Serikali yetu kama haitachukua hatua za kuwafidia wale wafugaji hakika hali itakuwa ni mbaya zaidi kuliko wakati mwingine wowote ule katika Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme; kusema ule ukweli kabisa yapo maeneo mengine mengi tu ambayo bado Wizara hii ina matatizo. Alikuwa anaongea Mwigulu Nchemba hapa akiwa Waziri. Kuna matumaini fulani fulani hivi ambayo kidogo alitaka kuonesha. Anasema mbolea itapatikana madukani kama coca cola; Mheshimiwa Waziri amewasiliana na Mwigulu hiyo mbolea kama coca cola madukani ime… (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti na mimi naomba nichangie, lakini naomba nianze kwa kusema kwamba taarifa hii ya Kamati, vitu vingi wamezungumza kusema ule ukweli kabisa vitu ambavyo ni vya ukweli japo kuna baadhi ya vitu naona kwamba kidogo kuna shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika taarifa hii ukurasa wa nane, wamegusia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu na Waziri wa Elimu yuko hapa. Miongoni mwa vitu ambavyo Mheshimiwa Waziri vitakuja kukuondoa siku za hivi karibuni nadhani ni Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu. Mheshimiwa Waziri kusema ule ukweli kabisa ameshawahi kuzungumza na ndugu yangu Heche hapa Bungeni, ulipokuwa Baraza la mitihani pale ulikuwa na heshima kubwa sana Mheshimiwa Waziri lakini leo umeletwa kuwa Waziri wa Elimu kwa kweli to be honestly heshima yako imeshuka sana kutokana na yale ambayo yanaendelea katika Taifa hili hasa kwenye elimu yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wale watoto wetu ambao walikuwa wanadahiliwa siku za nyuma kwa mfano mwaka 2014/2015 walidahiliwa wanafunzi 58,000 na TCU; lakini waliopata mikopo ni zaidi ya 40,000 zaidi ya nusu ya wanafunzi walipata mikopo. 2016/2017, wamedahiliwa wanafunzi 58,000 waliopata mkopo ni wanafunzi 20,000. Ukiangalia Awamu ya Nne walifanya vizuri zaidi katika suala hili la kutoa mikopo kwenye elimu ya juu lakini Awamu ya Tano ime-prove failure kabisa na Mheshimiwa Ndalichako hili unatakiwa ujipime, ujitathmini uone kama unatosha kuendelea kuiongoza Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema ule ukweli wako wanafunzi ambao walikuwa wanaendelea na masomo, wameshakopeshwa, yupo mwaka wa pili, mwaka wa tatu leo unasema kwamba hana sifa, unamuondoa kwenye mkopo. Sijajua vizuri kama hizi ni akili au ni matope lakini najua kabisa kwamba ni Serikali ambayo haipo makini kabisa katika kuhakikisha kwamba wanaboresha elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema ukweli kabisa kwenye hii mikopo wapo wanafunzi ambao wanadai haki baada ya kuona mikopo imecheleweshwa, wanapokuwa wanadai haki wanafunzi hawa wanafukuzwa chuo, wanaonekana kwamba ni wakorofi, hawafai kuendelea kusoma. Kuna mwanafunzi mmoja anaitwa Alphonce Lusako, huyu kijana amefukuzwa chuo mwaka 2011 kwa sababu alikuwa anadai fedha za wale ambao wamecheleweshewa mkopo mwaka 2011, kijana huyu amerudishwa chuoni mwaka jana 2016, lakini mwaka huu 2017 amefukuzwa tena kwa sababu ya kudai haki ya wanafunzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri leo ulitakiwa uwe wa kwanza kuondolewa kwenye nafasi yako kuliko kusimamisha wanafunzi wanaodai mkopo, chanzo cha kudai mkopo ni kwa sababu ninyi mnachelewesha, mikopo yenyewe haitoshi, wanapokuwa wanadai haki mnawafukuza badala ya kwamba Serikali iweze kuwajibika.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Elimu ya Juu kwa kweli hapa lazima iondoke na watu, kama Taifa tuweze kujitathmini upya tuangalie ni akina nani wanaweza wakaongoza. Naomba niseme tu kwamba yapo mambo mengi na madudu mengi sana kwenye Bodi ya Elimu ya Juu wamezungumza wengi sitaki nirudie sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala lingine japokuwa kuna mmoja amesema suala hili la TAMISEMI ni kweli kabisa. Kuna mambo ya TAMISEMI na kuna mambo mengine ya Wizara ya Elimu, lakini mambo haya ni kama mapacha yanaenda pamoja. Leo watoto wetu wanafeli kwa sababu walimu walishakata tamaa. Leo walimu wanaidai Serikali fedha nyingi sana. Serikali inawaambia walimu kwamba asiyetaka kazi aache. Ni kweli walimu wengi leo wameacha kazi wamebaki na utumishi. Kilichotufikisha leo hapa ni kwa sababu ya walimu kukata tamaa na ndiyo maana mmoja ametoa takwimu hapa shule za binafsi zinafanya vizuri kwa sababu kule hakuna madai. Shule zetu za Serikali, hizi za umma zinafanya hovyo kwa sababu walimu wetu tunawakatisha tamaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukiangalia kwa mfano Mkoa wa Songwe madai zaidi ya shilingi bilioni mbili hayajalipwa kwa walimu wetu, Wilaya ya Momba, Wilaya ya Mbozi na Wilaya ya Ileje, shilingi bilioni mbili hawajalipwa. Waziri ninaomba katika hili tafadhali muweze kuliangalia muone kama mnaenda sawasawa.
MWENYEKITI: Ahsante, Mheshimiwa Haonga muda wako umeisha.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni kuhusu TBC..
Mheshimiwa Mwenyekiti, TBC tunailipia kodi zetu lakini inatangaza habari za Chama cha Mapinduzi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kuchangia hii hotuba ya Waziri Mkuu. Awali ya yote niweze kwanza kumpongeza Rais mpya wa TLS ndugu yangu Mheshimiwa Tundu Antipas Lissu kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi sana. Kwa hiyo, pongezi sana japokuwa mchakato huu ndugu yangu Mwakyembe alitaka kuingilia, bahati mbaya akawa amelemewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza hayo naomba sasa niweze kujikita kwenye hotuba ya Waziri Mkuu na naomba nianze na suala moja la wakulima wa zao la kahawa. Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati yupo kule kusini alifanya mambo mazuri sana kwenye suala la watu wa korosho akapunguza tozo kwenye korosho na mambo mengi sana, lakini kiukweli kabisa amewasahau wakulima wa zao la kahawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa Mbozi pamoja na Mkoa wa Songwe na Mikoa yote ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wanaolima kahawa wana maeneo mengine wanasema kwamba kama Waziri Mkuu hatapunguza tozo na kodi kwenye zao la kahawa maana yake Waziri Mkuu
atakuwa ameonesha upendeleo wa hali ya juu sana na atakuwa amefanya ubaguzi ambao kwa kweli hatutegemei kuuona. Wao pia wanasema kwamba amefanya hivyo kwa sababu kule ni nyumbani kwao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wakulima wa zao la kahawa wanasema kwamba wanategemea kusikia atakapokuwa anahitimisha na hapa nimepokea meseji kama 200 hivi kutoka Jimboni kwangu; wanategemea kusikia anapunguza kodi na tozo mbalimbali kwenye zao la kahawa.
Zipo tozo nyingi sana; kuna ushuru Bodi ya Kahawa, iko tozo kwenye TaCRI na iko tozo kwenye Halmashauri kule asilimia 0.5.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo wanaomba tafadhali suala hili Mheshimiwa Waziri Mkuu aweze kulichukulia kwa umakini sana maana kule kwake nadhani ameshamaliza sijui ndio alikuwa anatengeneza mazingira lakini kwa kusema ule ukweli kwenye mazao mengine kama kahawa nahitaji kuona anapunguza tozo na kodi mbalimbali kwenye zao la kahawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kwetu Mbozi kahawa ndio dhahabu yetu; kahawa ndio kila kitu, mtoto anapokwenda shule lazima unaangalia kwenye kahawa na mtoto anapotaka kuoa unaangalia kwenye shamba la kahawa, kila kitu kahawa. Kwa hiyo, tafadhali suala hili ajaribu kuliangalia Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu wakulima wetu wa kahawa sasa wamefika mahali wamekata tamaa na wameanza kung’oa miche ya kahawa kwa sababu bei kwanza ni ndogo na hizo tozo na kodi zimekuwa nyingi hivyo wanategemea atatoa majibu mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu kama hatozungumza lolote kuhusu kahawa mimi na Wabunge wengine tunaotoka kwenye Majimbo na maeneo wanayolima kahawa tutahamasishana kuwaleta wote hapa Dodoma ili waje kupewa majibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naomba kuzungumzia kidogo suala la maafa amegusa kwenye ukurasa wa 48. Suala la maafa tunajua ndugu zetu wa pale Bukoba tetemeko lilitokea wakapata matatizo makubwa sana. Cha kusikitisha Rais wa nchi hii amechukua muda mrefu
kwenda pale kuwafariji wananchi wale. Kibaya zaidi zipo fedha ambazo zilichangwa bilioni sita kutoka EU na lakini ziko pesa ambazo tulikatwa hapa Bungeni kwa ajili ya ndugu zetu wa Bukoba, hizi pesa zimeliwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatujui hatujaambiwa hadi leo lakini inaonekana fedha hizi zimepigwa. Tulifanya mechi pale Dar es Salaam uwanja wa Taifa; Wabunge tumecheza mechi hadi miguu imeuma, tumepata zaidi ya milioni mia mbili na kitu pesa hizi zinaonekana kama mmeshazipiga. Sasa hatujui kwa nini watu wanapata matatizo badala ya Serikali kuchukua fedha zile kuwasaidia, mnaamua kuzitumia kinyume na matarajio, kinyume na ile kazi ambayo tulikuwa tunategemea zifanye. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunategemea kabisa kwamba pale wananchi wanapopata matatizo, Rais wa nchi, Serikali iweze kutoa lugha nzuri. Leo kama Rais wa nchi anasema mimi sikuleta tetemeko, hatutawasaidia chakula ina maana kwamba Taifa hili tumekosa Rais. Nadhani suala
hili tujaribu kuliangalia sana. Naomba niwe muwazi kabisa kwamba Rais wetu lugha anazozitoa watu wanapopata matatizo…
KUHUSU UTARATIBU.....
MHE.PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme tu kwamba, mara ya kwanza ulisema kuwa hutatoa taarifa yoyote ila nasikitika umetoa taarifa kwa huyo bwana. Labda inawezekana ilikuwa kasoro kwa Simbachawene tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo nililokuwa nalizungumza hapa ni kwamba watu wanapopata matatizo wananchi wakipata maafa, Serikali inatakiwa ikae karibu na wananchi. Sasa kama Serikali fedha zinachangwa inafika mahali fedha zile zinatumika kinyume ni lazima tuhoji, lazima
tuulize. Sasa leo hii tusipouliza unategemea nani atauliza suala hili sisi ndio tunaowakilisha wananchi; tumekaa hapa huu ni mkutano wa hadhara wa wananchi nchi nzima hawawezi kukusanyika wote hapa.
TAARIFA....
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba uweze kulinda muda wangu na najua bado nina dakika kama saba hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niende kuzungumzia suala lingine, suala ambalo Waziri Mkuu amelizungumzia kwenye ukurasa ule wa 11 kuhusu kufanya siasa za kutuunganisha badala ya kufanya siasa za kutugawa. Naomba sitanukuu sana kile alichokisoma pale Waziri Mkuu,
naomba niseme tu kwamba nchi yetu ilipofikia siasa za kuwagawa Watanzania zimeasisiwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siasa hizi zimeasisiwa juzijuzi hapa kwenye vyombo vya habari, imeripotiwa tu Mwenyekiti wa CCM Taifa anasema kwamba Wabunge wa Chama cha Mapinduzi ni marufuku kwenda kumwona Mbunge mwenzao Mheshimiwa Godbless Lema aliyekuwa amewekwa ndani. Siasa hizi za kutugawa Watanzania…
TAARIFA....
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ulinde muda wangu na naomba niseme kwamba ninachochangia hapa sichangii kitu ambacho hakipo, nachangia Hotuba ya Waziri Mkuu ukurasa wa 11.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wale ambao labda hawajasoma hotuba hii vizuri wangepata muda waweze kusoma vizuri, hapa kwenye ukurasa wa 11 amezungumza vizuri sana Waziri Mkuu, kwamba tufanye siasa za kutuunganisha badala ya kufanya siasa za kutugawa na
nilichokizungumza mimi, siku ambayo Mwenyekiti wa CCM Taifa amewaasa baadhi ya Wabunge wasiende kumtembelea Mbunge mwenzao vyombo vya habari vilitangaza, magazeti yaliandika, Kituo cha Utangazaji cha TBC kilitangaza, ITV walitangaza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sasa nashangaa sana, labda inawezekana kuna wengine ambao inawezekana hawafuatilii vyombo vya habari, labda hawajasoma na Hotuba ya Waziri Mkuu. Kwa hiyo, naomba tafadhali usiingie kwenye mtego, hii Hotuba ya Waziri Mkuu naichangia vizuri sana, hii ninayo hapa, ni ukurasa ule wa 11. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naomba nizungumze; wapo ndugu zetu wengi ambao walifukuzwa siku za hivi karibuni Msumbiji, Mheshimiwa Waziri Mkuu nadhani anakumbuka na Wabunge wote mnakumbuka kwenye Bunge hili. Wale Watanzania wamefukuzwa Msumbiji wamepelekwa mpakani pale wengine wamepoteza maisha, wengine wamebakwa. Rais wa nchi, naomba niseme tu kwamba kiongozi mkuu wa nchi, maana yake mmesema tusimtajetaje, sijajua tatizo ni nini, anasema kwamba walikwenda kwa njia za panya warudi kwa njia za panya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunategemea viongozi wetu, watu wetu wanapopata matatizo tuwe wa kwanza kwenda kuwasaidia, tuwe wa kwanza kwenda kuwatia moyo. Watanzania wengi wanaoondoka nchini hawaendi nchi za huko mbali kwa ajili ya kwenda kutalii, wanatafuta
maisha, wanatafuta fursa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkuu wa mkoa alipojaribu kupeleka hata gari lile la jeshi kwenda kuwabeba wale watu alikatazwa akaambiwa kwamba usiwabebe, waache kama walivyo, walikwenda kwa njia za panya warudi kwa njia za panya. Suala hili kwa kweli linasikitisha sana na kwa jinsi hali ilivyo kwenye nchi yetu kama tutaendelea kwenda hivi, mimi naamini kabisa kwamba tutakuwa hatuwatendei haki Watanzania ambao wametuchagua sisi Wabunge na ambao wamemchagua Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na ambao wametuchagua sisi wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba tu kwamba ifike mahali sisi viongozi ambao ndio tumaini la Watanzania tufanye kazi ya kuwawakilisha wananchi wetu vizuri na tufanye kazi ya kuwatetea, tufanye kazi ya kuwasemea, lakini inapofika mahali unasema kwamba
sikuwatuma mimi kwa kweli hatuwatendei haki hata kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumze suala lingine ambalo linapatikana ukurasa ule wa 21 wa Hotuba ya Waziri Mkuu kuhusu ziada ya chakula ambayo ameizungumza kwenye hotuba hii. Mheshimiwa Waziri Mkuu anafahamu yeye na Wabunge wote wanafahamu kwamba
takribani halmashauri 55 zina tatizo la njaa japokuwa sasa hatujaambiwa, hatujaletewa taarifa rasmi Bungeni kwamba kwa sasa tumefikia wapi, lakini taarifa iliyokuwepo siku za nyuma ni kwamba halmashauri 55 zina njaa. Imefika mahali tunaambiwa kwamba chakula hakitapelekwa, sasa watu waliotuchagua leo tu…
MWENYEKITI: Nakuongeza dakika moja!
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, dakika zangu nadhani umenipunja kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nataka nizungumze tu kwamba sasa tuulize, wakati Watanzania wanapata njaa kipindi cha Nyerere alikipata wapi chakula cha kuwapelekea, wakati Watanzania wamepata njaa kipindi cha Mkapa, kipindi cha Mwinyi, kipindi cha Kikwete, chakula kilitoka wapi na hii Serikali leo kwa nini inashindwa kuwapelekea Watanzania chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hili la njaa halina baunsa, mtu yeyote anaweza akapata njaa kutokana na kwamba inaweza kuwa mvua labda haijanyesha, kumetokea ukame, kumetokea matatizo mbalimbali, sasa leo Serikali inasema kwamba sisi hatutapeleka chakula kwenye maeneo ya njaa, hii ni fedheha kubwa sana kwa Taifa letu na nina… (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na umuhimu wa barabara ya kutoka Mlowo (Mbezi) kwenda Kamsamba (Momba) kuelekea Kilyamatundu (Kwela) hadi Kasansa na hatimaye Kibaoni (Katavi). Ni vyema Serikali itengeneze barabara hii kwa kiwango cha lami. Mosi, hii barabara inaunganisha Mikoa mitatu ya Songwe, Rukwa na Katavi na kwa kuwa ni Sera ya Serikali kutengeneza kwa kiwango cha lami barabara zinazounganisha mikoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wananchi wanaoishi maeneo yanayopitiwa na njia hii wanalima mazao ya kahawa, mpunga, mahindi, ufuta, alizeti, mtama, maharage na mazao mengineyo. Naishauri Serikali itengeneze barabara hii kwa kiwango cha lami ili wananchi waweze kusafirisha mazao yao kupeleka sokoni kirahisi. Soko kuu la mazao katika ukanda huu linapatikana Mlowo – Mbozi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na barabara hiyo hapo juu, pia kuna barabara ya kutoka Mji Mdogo wa Mlowo, Wilaya ya Mbozi kupitia Vijiji vya Shiwinga – Isansa - Magamba na kuelekea Kata ya Magamba, Wilaya ya Songwe. Hii barabara ni ya muhimu kwa sababu inaunganisha Halmashauri ya Mbozi na Songwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mazao mbalimbali kama vile kahawa, mahindi, maharage, alizeti, ufuta na mengineyo yatasafirishwa kirahisi. Pia makaa ya mawe yanayochimbwa Kijiji cha Magamba yatasafirishwa kirahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hongera na utekelezaji wa majukumu ya Wizara. Ili kuwasaidia Watanzania walio wengi wanaosumbuliwa na magonjwa makubwa, mfano magonjwa ya moyo, ni vema Serikali iwekeze sana kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete inayoshughulika na magonjwa ya moyo. Vifaa vyote vinavyotakiwa kwa ajili ya matibabu ya moyo vinunuliwe kwani kuwa na Madaktari Bingwa peke yake bila vitendea kazi haitasaidia. Kwa kuboresha Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Serikali itaokoa fedha nyingi sana ambazo zingetumika kuwatibu wagonjwa wetu nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo iwe na mikakati kabambe ya kuimarisha michezo ili kuibua vipaji vya wanasoka nchini. Academics za mpira zianzishwe katika maeneo mbalimbali nchini kwa ushirikiano wa Serikali na wadau mbalimbali wa soka. Vijana wakijifunza mpira katika academy zitakazoanzishwa watajifunza soka na michezo mingine wakiwa bado wadogo. Kujifunza soka ukiwa mdogo unapata uzoefu wa kutosha na hivyo kuna uwezekano wa kucheza soka la kulipwa baadaye. Hivi ndivyo nchi nyingi zenye mafanikio makubwa ya soka duniani zinavyofanya.

Mheshimiwa Spika, pia Shirika la Utangazaji la TBC lizingatie weledi katika ufanyaji kazi. Mfano, kuna muda Shirika hili linajisahau na kutangaza habari za Serikali na Chama cha Mapinduzi na kupuuza habari za Vyama vya Upinzani. Kwa kuwa Shirika hili linaendeshwa kwa kodi za Watanzania wote hivyo ni jambo jema Shirika hili likaacha ubaguzi katika kutoa na kutangaza habari.

Mheshimiwa Spika, uhuru wa vyombo vya habari Tanzania umeendelea kupotea siku hadi siku. Yapo baadhi ya matukio ya hivi karibuni yamethibitisha kupotea kwa uhuru wa vyombo vya habari mfano; kuvamiwa kwa studio za clouds TV na Radio siku za hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Tukio hilo limeishusha sana nchi yetu katika utekelezaji wa uhuru wa vyombo vya habari, pia limeichafua sana nchi yetu duniani kote. Serikali ichukue hatua thabiti katika kushughulikia suala hili.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Maliasili na Utalii idhibiti mauaji ya tembo ambao wapo mbioni kupotea kabisa. Tembo wameendelea kuuawa mwaka hadi mwaka hivyo tutapoteza watalii wengi kutokana na suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Wizara ya Maliasili na Utalii iwazuie askari wake kuwapiga risasi na kuwaua wananchi wanaoingia maeneo ya hifadhi. Kuwaua wananchi ni kosa kubwa sana, ni bora hatua kali zichukuliwe kwa askari hawa watovu wa nidhamu. Naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kupata fursa ya kuchangia Wizara hii. Nitachangia maeneo makuu mawili, nitaanza na madai ya walimu lakini pia nitazungumzia Bodi ya Mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na suala la madai ya Walimu. Mwaka 2016 Walimu zaidi ya 80,000 wamepandishwa madaraja lakini wanaidai Serikali zaidi ya shilingi bilioni 200, fedha hizi hadi leo hazijalipwa. Tunajua kabisa kwamba haya madai ambayo ni shilingi bilioni 200 ni
fedha ambazo Serikali ingekuwa makini na inawajali Walimu ingekuwa imeshalipa. Leo tutaanza kutafuta mchawi ni nani, kwa nini watoto wetu wanafeli wakati tunajua kabisa kwamba Walimu wetu wana madai makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali iweze kulipa madeni haya kwa sababu Walimu wetu wengi wanakata tamaa sana. Walimu wakiendelea kukata tamaa matokeo tutayaona muda si mrefu na tusianze kutafuta mchawi ni nani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu fedha za Walimu wa maeneo mbalimbali nchini waliosimamia mitihani ya kidato cha nne mwaka 2015. Mheshimiwa Naibu Waziri nimewahi kumwona na kuwambia Wilaya ya Mbozi Walimu wanadai Serikali zaidi shilingi milioni 170, walisimamia mitihani ya kidato cha nne, 2015 akasema atashughulikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika kusema kwamba Walimu hao hadi leo hii hawajalipwa hizo fedha za kusimamia mtihani wa kidato cha nne mwaka 2015. Naomba niulize, ni nani Mbunge humu au Waziri hapa ndani ambaye anaidai fedha Serikali za mwaka 2015 ambazo hajalipwa hadi leo hii? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kwa masikitiko makubwa kabisa wale Walimu wanasema kwamba wameshakata tamaa. Ukisikia Mwalimu anazungumza kwamba amekata tamaa, hili jambo kwa kweli madhara yake ni makubwa sana na haya mambo yatasababisha watoto wetu wafeli. Mheshimiwa Waziri naomba tafadhali Bunge litakapokuwa limeahirishwa mwezi Juni achukue angalau muda akaonane na wale Walimu wa Mbozi. Walimu hawa wanadai Serikali zaidi ya shilingi milioni 170 walisimamia mitihani hawajalipwa fedha zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya madai ni vizuri wakayalipa kwa sababu Walimu wetu kuendelea kudai nadhani sio afya na haitaleta picha nzuri katika matokeo yanayokuja. Kama wanataka kusubiri majuto tutayapata ila majuto ni mjukuu. Namwomba Mheshimiwa Waziri chonde- chonde katika hili afike Mbozi akawasikilize Walimu wanaoidai Serikali fedha hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu Bodi ya Mikopo. Bodi ya Mikopo leo hii inafanya mambo ya ajabu sana Mheshimiwa Waziri na kama inawezekana ivunjwe. Maana kinachotokea wale watoto yatima ambao hawana baba wala mama wananyimwa mikopo. Mheshimiwa Waziri nimemwona juzi, nimemletea mwanafunzi ambaye baba na mama yake amekufa na nimempelekea na Death Certificates za wazazi wote wawili hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu mwanafunzi alinyimwa mkopo na yuko CBE mwaka wa kwanza. Mwanafunzi huyu niliyempelekea hivyo viambatanisho vyote alishawahi kuomba apatiwe mkopo kwa sababu hiyo na hadi ame- appeal bado amenyimwa. Tunao watu wa aina hii wengi sana katika Taifa hili ambao wamepoteza wazazi na wamenyimwa mikopo. Kama huwezi ukampa yatima mkopo unampa nani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunazo taarifa kwamba watoto wa Mawaziri ndio hao wanaonufaika na mikopo ya elimu ya juu wanapewa 100%. Mheshimiwa Waziri, kwa kweli suala hili tafadhali naomba mlichukulie kwa umakini sana, kuwanyima watoto wa maskini mikopo hii ni hatari sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine mikopo hii ukiangalia wako wengine waliosoma…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kabla sijaanza kuchangia Wizara hii, naomba niungane na mchangiaji mmoja aliyetangulia, anaitwa Profesa Jay. Mheshimiwa Waziri naomba nimpe ushauri kidogo, kabla sijaendelea kuchangia, anapokuja kwenye Majimbo yetua jaribu kutushirikisha Wabunge wenye Majimbo.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwambia hili kwa sababu mimi huwa sitaki nikae na kinyongo na huwa sitaki tufanye kazi kwa kinyongo na Waziri wangu. Alikuja Jimboni kwangu, ameenda kufanya mkutano na wananchi, anawaambia wananchi Mbunge wenu yuko wapi? Ameanza kuruka sarakasi kama za Bungeni? Mheshimiwa Waziri hii haifai hata kidogo na kwa wananchi wangu hii siyo haki hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri amefanya hivi pia kule kwa Profesa Jay na Majimbo mengine. Alikuja Mheshimiwa Mwigulu Nchemba Jimboni kwangu, ameniandikia message, amenipigia simu nimempa ushirikiano mzuri. Kwa hiyo, naomba wakati mwingine ajaribu kuwa na ushirikiano na mahusiano mazuri na Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kwamba ukuaji wa Sekta ya Kilimo umeendelea kushuka mwaka hadi mwaka. Ukuaji wa Sekta ya Kilimo, tunaambiwa kwamba ni asilimia 1.7 kwa takwimu za NBS na hii unakuja kuona sasa hata bajeti ambayo imetengwa kuanzia mwaka 2010/2011 tuliona asilimia 7.8 ambayo ndiyo ilikuwa bajeti kubwa kwa mara ya mwisho. Tumekuja kuona mwaka 2011/2012, ikawa asilimia 6.9 mwaka jana, 2016/2017 ni asilimia 4.9.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kuwasaidia wakulima wa Tanzania kwa kuendelea kutenga bajeti ya kilimo kidogo kiasi hiki. Naomba niseme tu kwamba Maputo Declaration walipendekeza kwamba angalau nchi wanachama wa AU wajaribu angalau kutenga asilimia 10 kwenye bajeti za kilimo. Hii Maputo Declaration kwa Tanzania tutakuja kuitekeleza lini? Kwa hiyo, naomba niseme kwamba ili kuwasaidia Watanzania hebu tujaribu kutenga bajeti ya kutosha. Kwa mazingira haya, hatuwezi kupata viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, jana nimemwona ndugu yangu hapo Waziri wa Viwanda amebeba makabrasha mengi sana, lakini kwa bajeti hii ya kilimo, kwa kweli naamini kabisa hata Waziri wa Viwanda asitegemee kuwa na viwanda kwa sababu hawezi kuwa na viwanda bila kuboresha kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, historia inatuonesha duniani popote pale, walifanya mapinduzi kwenye kilimo. Tunajua ile Agrarian Revolution iliyofanyika kule Britain, tunajua Agrarian Revolution iliyofanyika kule Marekani, tunajua Indian Green Revolution, tunajua ile China Green Revolution ndipo tukaona sasa wenzetu viwanda vinakuja. Viwanda ni matokeo ya kuboresha kilimo na kupeleka fedha nyingi na kuhakikisha kwamba wakulima mambo yao yanakwenda vizuri kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano viwanda vya nguo, wanategemea pamba; bila kuwekeza kwenye pamba hatuwezi kuwa na viwanda. Bila kuwekeza kwenye mbegu kwa mfano kama alizeti na ufuta hatuwezi kuwa na viwanda vya mafuta. Kwa hiyo, niseme tu kwamba Mheshimiwa Waziri naomba tafadhali, ajaribu kushauri. Najua tu tatizo la viongozi wetu walio wengi hasa Mawaziri mnamwogopa Bwana mkubwa. Hii ndiyo shida kubwa! Mwambieni ukweli, msiogope! Ukweli ndiyo utakaokuweka huru. Kwa bajeti hii, hatuwezi kufika popote na mwakani tutarudi kuja kupiga kelele tena hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo ambalo Mheshimiwa Waziri amezungumza kwenye hotuba yake kuhusu suala la bulk procurement ya mbolea. Siyo jambo baya, lakini naomba tungekuwa tuna-focus zaidi kwenda kujenga viwanda vya mbolea nchini kote.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukijenga viwanda kwa mfano ukajenga Kiwanda cha Mbolea kanda ya Nyanda za Juu Kusini ambao ni wazalishaji wakubwa sana, ukijenga kiwanda kwa mfano Kanda ya Kaskazini, ukajenga Kiwanda cha Mbolea Kanda ya Magharibi, Kanda ya Kati, Mheshimiwa Waziri mbolea itashuka bei. Kwa sababu tunajua kabisa, kwa mfano, hili suala la saruji, leo kidogo bei ni nafuu kwa sababu viwanda vya saruji viko vingi. Watafanya biashara ya ushindani na mwisho wa siku mbolea itashuka bei. Kwa hiyo bulk procurement ni jambo moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, hili la kujenga viwanda. Tungeendelea kabisa kufikiria hili zaidi kuliko tukawa na hizi kuzibaziba tu angalau kwa muda mfupi, haliwezi kutusaidia sana. Kwa hiyo, naomba niseme tu kwamba alikuja hapa Mfalme wa Morocco, Mohamed wa Sita, tukamwomba atujengee uwanja wa mpira Dodoma. Nadhani wanapokuja watu wetu, kama hawa wadau wa maendeleo, tungekuwa tunawaomba wawekeze kwenye viwanda vya mbolea. Wakiwekeza kwenye viwanda vya mbolea, wakulima wetu watanufaika. Mbolea itashuka bei.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nchi yetu zaidi ya miaka 50 baada ya uhuru tunamwomba mtu uwanja wa mpira badala ya kumwomba viwanda vya mbolea! Mheshimiwa Waziri kwa kweli mimi hili naona siyo sahihi kabisa. Naona leo tumeomba viwanja vya mpira, kesho tutaomba jezi, kesho kutwa tutaomba mipira. Hili jambo halitatufikisha popote pale. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niweze kuzungumzia jambo lingine kwenye bei ya zao la kahawa. Zao la kahawa limeendelea kushuka bei miaka yote. Wenzetu wa korosho mmerekebisha mambo vizuri kabisa kule, leo korosho wananufaika kweli kule Kusini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kahawa imeendelea kushuka bei mwaka hadi mwaka. Ndugu zetu wa jirani tu hapa wa Kenya wanauza kahawa bei nzuri, Uganda wanauza kwa bei nzuri, Tanzania ni nani aliyeturoga? Tatizo liko wapi, Tanzania kahawa yetu tunauza kwa bei ndogo? Leo wakulima wangu Mbozi kule wameamua kuanza kung’oa miche ya kahawa kwa sababu wameona hailipi. Wanaamua walime mazao mengine kwa sababu ya bei ndogo ya kahawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuwasaidie wakulima hawa wa Kahawa, tupandishe bei na ikiwezekana kabisa tuweze kuangalia namna gani ya kuweza kupandisha bei. Kwa nini tusiende kujifunza kwa majirani zetu? Mbona Kenya siyo mbali, hata kwa pikipiki unafika hapa jirani Kenya! Mbona Uganda siyo mbali, kwa nini tusiende kuwauliza ninyi mnauzaje kahawa yenu kwa bei nzuri? Kwa nini Tanzania sisi hatuuzi kahawa yetu kwa bei nzuri?

Mheshimiwa Waziri kwenda kujifunza kwa ndugu yako siyo dhambi hata kidogo! Naomba sasa tukajifunze tuangalie wenzetu, kwa nini wanauza kahawa yao kwa bei nzuri, tuone sisi tuliteleza wapi, tuweze kuwasaidia wakulima wa kahawa, zao ambalo linaelekea kwenda kufa siku za hivi karibuni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, naomba nizungumzie suala la kuanzisha Mnada wa Kahawa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini. Leo nchi nzima, Watanzania wanaolima kahawa wanaenda Moshi kwenye Mnada wa Kahawa. Tukianzisha Mnada wa Kahawa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, kwa mfano, tukaweka Kiwanda cha Kahawa pale Songwe au tukaweka Mbeya, wakulima wetu wataenda kushiriki moja kwa moja kwenye Mnada wa Kahawa pale. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, Vijiji vya Jimbo la Mbozi vinakabiliwa na tatizo kubwa sana la maji. Baadhi ya Vijiji hivyo ni Iyenga, Ilea, Itumpi, Magamba, Mtunduru, Utambalila, Maninga, Mahenje na vijiji vinginevyo. Hivyo katika miradi ya maji vijijini ni vizuri Serikali ikavikumbuka na vijiji hivi vya Jimbo la Mbozi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mji Mdogo wa Mlowo wenye idadi ya watu wasiopungua 60,000 unakabiliwa na tatizo sugu na la muda mrefu sana la maji. Bajeti ya mwaka uliopita 2016/2017, Mji Mdogo wa Mlowo ulitenga fedha kwa ajili ya maji. Kwa bahati mbaya na masikitiko makubwa sana, hadi sasa hakuna shughuli yoyote inayoendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atatue tatizo la maji Mji Mdogo wa Mlowo kwani wananchi wanateseka sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, vipo vyanzo vingi vya maji Wilaya ya Mbozi mfano, Mto Lukululu, Mto Mkama na mito mingine. Ni vyema Serikali ijikite kuwapatia maji wananchi wa Mbozi kutoka katika vyanzo hivi. Pia maji ya ardhini hayapo mbali, maeneo mengi yanapatikana mita 75 kuelekea ardhini.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo, wa Mwaka 2016
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nami niweze kuchangia juu ya Miswada hii miwili ambayo wenzangu tayari wameshaanza kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo. Nimesoma Muswada huo nimeupitia vizuri, lakini tatizo ninaloliona ni kwamba sijaona eneo ambalo ni specific kabisa linalohusu namna ya upatikanaji wa fedha za kwenye hii taasisi ya utafiti ambayo tunakwenda kuipitisha. Tatizo hili tusipoweza kujadiliana kwa makini sisi kwa pamoja leo kwamba fedha zinapatikana wapi, tutarudi kwenye kutelekeza hizi Taasisi za utafiti ambazo nyingi tumeshazianza tayari na nyingine nyingi tulishazitelekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, wapo hawa jamaa tunawaita TaCRI, hawa wanaofanya utafiti wa zao la kahawa. Tunafahamu kabisa na Mheshimiwa Waziri anajua kabisa hili kwamba waliokuwa wanafadhili TaCRI ni European Union ambao hadi sasa hajawahi kupeleka fedha, tunajua kwa nini hajapeleka fedha kwa sababu tunajua European Union iko miradi mbalimbali ambayo walikuwa wanaendesha, lakini baada ya kutokea mgogoro wa kisiasa kule Zanzibar wameamua kujiondoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, leo bado tunaona kuna wadau wengine, kwa mfano mkulima wa kahawa alikuwa anakatwa karibu asilimia 0.75 anapouza kahawa yake ili aweze kuichangia TaCRI, lakini leo tutakwenda kuwabebesha wakulima wetu mzigo mzito sana tusipokuwa makini namna ya kuweza kupata fedha za kugharamia utafiti huu. Tunajua kabisa kwamba wakulima wetu kila tunapoanzisha utafiti wa aina yoyote ile tunaangalia wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii ni sawa na mzazi unakwenda kuzaa watoto halafu unapanga gharama kwamba bajeti ya chai atakunywa kwa jirani, chakula atakula kwa mtu fulani. Kwa hiyo, tusipokuwa makini tutatelekeza hata hii Taasisi ya Utafiti wa Kilimo. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind up labda kesho hiyo, naomba atuambie hizi fedha zinatoka wapi na nimepitia sijaona ni maeneo gani wanapata hizi fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu huyu Mkurugenzi Mkuu wa Utafiti, wanasema awe na ujuzi uliothibitika na uzoefu usiopungua miaka 10 katika masuala ya sayansi na utafiti wa kilimo. Ukisoma ukurasa wa 41 na 42. Huyu Mkurugenzi unayeniambia kwamba awe na uzoefu usiopungua miaka 10, hili litakuwa kama ni eneo ambalo watu wetu wenye uwezo mzuri tutawanyima nafasi kama hizi. Leo unaweka miaka 10 uzoefu, kwa hali ya kawaida miaka 10 ni mingi sana, kama amezaa mtoto maana yake yuko darasa la nne au la tano. Sasa hii nadhani tungepunguza kidogo hapa, kwa nia njema, siyo kwa nia mbaya, angalau tuweke hata miaka mitatu, siyo dhambi, tuweke miaka mitatu, naamini tutapata watu wazuri kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hii ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo naomba niondoke kidogo niingie kwenye huu Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania. Amezungumza Mbunge mwenzangu aliyekaa, kuna tatizo moja ambalo linaonekana lazima tulijadili mapema kwa mfano suala la utafiti wa masoko ya samaki ili kuongeza pato la wavuvi na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima hapa tujaribu pia kuzingatia haya, tueleze vizuri kwamba utafiti huu utasaidiaje kutafuta masoko kwa sababu shida katika Taifa letu ni kwamba tunao samaki wa kutosha na mazao mengine ya baharini, tatizo kubwa ni masoko na nadhani kwa sababu sheria hii tunakwenda kuipitisha, naamini kabisa hili suala la masoko pia tulizingatie tuweze kuangalia ni namna gani tutatafuta masoko kwa ajili ya samaki wetu na mazao mengine ya baharini, tutakuwa tumeongeza pato la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyojua baadhi ya nchi duniani zinazotegemea zao la samaki kuendesha uchumi wa nchi zao, kwa mfano, zipo nchi kama Mauritius, nchi kama Seychelles, nchi kama Phillipines, Norway, Australia na nchi nyingine nyingi ambazo zinategemea samaki kwa ajili ya kuendesha uchumi wa nchi zao. Sasa na sisi hapa lazima tuangalie tunafanyaje kwenye huu utafiti, tunaingiza wapi angalau eneo la kuweza kutafuta masoko kwa ajili ya samaki wetu na mazao mengine ya baharini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo dagaa wengi sana wanavuliwa kwa mfano Ziwa Victoria wanapelekwa Congo, lakini hatujui nchi inapata shilingi ngapi, kwa sababu soko kubwa la samaki na dagaa tunajua kabisa ni Congo. Sasa leo tunapeleka kule, wenzetu wanapeleka kuchakata viwandani, wanatoa ajira lakini sisi Taifa hatunufaiki na chochote na kama ni kunufaika basi itakuwa ni kidogo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine naomba nizungumzie ni kwenye suala la udhaifu wa sheria za utafiti. Kumekuwa na tatizo kwa muda mrefu sana, leo wanakuja wageni katika Taifa letu, kwa mfano mdogo walipokuja wale jamaa wa China wamevua samaki kwa muda wa wiki tatu wamepata samaki wengi sana. Wale samaki wamepatikana wengi, lakini wale jamaa walikuja kwa njia za ujanja ujanja, sasa sijui kama walikuja kufanya utafiti au walikuja kufanya uhuni wale samaki jina maarufu samaki wa Magufuli nadhani mnakumbuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa kwa sababu ama kwa kukosa sheria ambazo haziwabani vizuri watu wa namna hii tukajikuta kwamba wale watu wamevua samaki wengi kwa muda wa wiki tatu wamepata samaki wengi na mwisho wa siku tukawakamata tukachukua na ile meli tuka- seeze lakini bahati mbaya sana ile kesi walitushinda Mahakamani, hadi leo hii tumeingia hasara kama Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mambo yote hayo naomba tu tujaribu kuangalia tuweke sheria ambazo zitawabana wale watu wanaokuja kufanya utafiti kutoka nje ya nchi, zitakazowabana wale wezi wanaotuibia samaki wetu. Tunaamini kabisa kwamba tukiwabana samaki tunao wa kutosha, tutauza nje ya nchi tutatengeneza ajira kwa watu wetu, lakini tukikaa kimya na sheria tusipoziweka vizuri itakuwa ni business as usual, tutaibiwa sana na tutaendelea kulalamika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme tu kwamba suala hili tujaribu kuliangalia kama Taifa kwa pamoja. Kwa mfano hizi tafiti tunazozianzisha zote kwa maana ya hizi sheria, hii Miswada tunayoipitia, yote miwili inafika mahali kama alivyoongea Mbunge mwenzangu, tumepitisha sheria, ukiangalia unaona kama nzuri kwenye maandishi lakini hizi tafiti zinaishia kwenye makaratasi, haziwasaidii wananchi wetu, hatuzifikishi kule chini ili watu wetu waweze kujua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa mfano leo bado kama tunazo hizi sheria za utafiti ambazo tumeshazipitia siku nyingi, bado kwenye mazao mbalimbali hapa nchini tumeona kuna ugonjwa wa mihogo, kuna ugonjwa wa kahawa. Kwa mfano, kwenye kahawa kuna ugonjwa fulani unaitwa CBD (Coffee Berry Disease) leo ukimuuliza hata Mheshimiwa Waziri anajua kwamba hadi leo ukiuliza ugonjwa huu wa Coffee Berry Disease, hadi leo hauna dawa zaidi ya kusema kwamba unatakiwa uzuie. Sasa tujue je, hizi taasisi za utafiti ambazo tunazo, tumezianzisha zimetusaidia kwa kiwango gani na tunapoenda kuanzisha nyingine zitatusaidia kwa kiwango gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwamba mwisho wa siku tutaishia kuanzisha hizi taasisi za utafiti, hazitatusaidia lakini tukiwa makini naamini kabisa kwamba zitatusaidia. Shida kubwa katika Taifa hili, ameongea Mbunge mwenzangu, ni kwenye suala la implementation. Tumekuwa na Taasisi nyingi, tumekuwa na tafiti nyingi, tumezipaki kwenye makabati, tumezipaki huko hatuzifanyii kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba kwa pamoja bila kujali itikadi ya Vyama vyetu, tunapokwenda kujadili haya mambo yakafanye kazi kwa wananchi wote kule chini. Taifa lolote lile duniani ambalo halifanyi tafiti, Taifa hili limekufa na mwisho wa siku haliwezi kuwasaidia wananchi wake. Kwa hiyo, naomba kwa nia njema hizi tafiti ziwafikie wananchi wetu na ziweze kuwanufaisha, hatutaki ziishie kwenye makabrasha kama ilivyokuwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kuna Sheria hii ya Uvuvi ambayo ilianzishwa siku za nyuma huko, tujue je, upungufu ambao yalikuwepo siku za nyuma, je tunaweza kuyarekebisha kiasi gani kwa kuanzisha sheria nyingine hii ya uvuvi. Kama kuna upungufu ulikuwepo, tumekwenda kuanzisha sheria nyingine tafsiri yake ni kwamba hii sheria pia itaishia kwenye makabrasha humu, tutaiacha hapa na mwisho wa siku tutakuja miaka mingine mbele kuanzisha sheria nyingine.
MWENYEKITI: Ahsante.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2017.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Naomba niseme tu kwamba kuna usemi unaosema if we fail to plan then we plan to fail.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo ambalo kwa kweli limeendelea kupigiwa kelele sana siyo tu kwamba ni Wabunge wa upande fulani, bali hata wadau ambao mmewaona tangu wamekuja ile siku ya kwanza wamepigia kelele sana kuhusu suala hili la muda mdogo kwenye hili jambo la muhimu sana katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kabisa kwamba hili jambo la Hati za Dharura ambalo hata miaka ya nyuma pia limewahi kulalamikiwa kwa muda mrefu sana na limekuja kuleta madhara, hasara zake ni kubwa mno kuliko faida ambazo tutaweza kuzipata. Kwa mfano, leo hii tungeweza tukasema kwamba tutafute case study nchi gani ambazo zimefanikiwa katika mikataba ya madini tungeenda kufanya, labda katika nchi kama Ghana, ziko nchi mbali mbali South Africa, Botswana na nchi nyingine tungetumia muda mrefu, tutume watu wetu kule waweze kuangalia namna gani nchi hizi zimeweza kunufaika hili suala halikuwa suala la muda mfupi, halikuwa ni suala la dakika mbili wala dakika tatu kama ambavyo tunakimbia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi Profesa Luoga alisema kwamba tumepewa siku Sita tu, tungekuwa tumepewa Mwezi hata mmoja, yaani walipewa siku sita kuandaa Miswada hii, wangepewa mwezi mmoja wangefanya vizuri sana, huyu ni Profesa Luoga. Alizungumza maneno haya alipokuwa anajaribu kutoa ufafanuzi kuhusu Miswada hii ambayo imeletwa. Kwa hiyo, naomba suala hili la kuharakisha mambo haya utafikiri nchi iko kwenye vita, utafikiri ni vita ya Iddi Amini na Tanzania, utafikiri ni sijui ni vita ya nini.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tafadhali tujaribu kuangalia, tunazungumzia maisha ya watoto wa watoto wetu, tunazungumzia miaka 100 ijayo, miaka 200 ijayo, hatuwezi tukajadili suala la mustakabali wa Taifa letu ndani ya siku mbili, tatu tu. Leo unasema kuna wachangiaji nane na wengine wanagawana dakika mbili mbili, halafu huku wako watatu tunajadili suala kubwa kama hili. Naamini mwakani hili suala linaweza kurudi tena, kama siyo mwakani basi miaka ya hivi karibuni. Kwa hiyo, naomba tu mambo ya muhimu kama haya tujaribu angalau kuweka muda wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ziko changamoto nyingi sana za madini, kwa mfano Sheria ya Madini ya 1998 ilitamka kwamba mwenye miliki ya madini na fedha yote itokanayo na mauzo ya madini ni mwenye leseni ya kuchimba madini. Mambo yote haya unaweza ukaona kwamba changamoto zote hizi pamoja na nyingine za kutorosha madini yetu, pamoja na mrabaha kidogo yote haya tungekuwa tumepata muda mwingi wa kutosha zaidi, naamini tunaweza kuyashughulikia vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, hili suala amezungumza na mwenzangu na wengine wameongea juzi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumiliki madini kwa niaba ya Watanzania wote, amezungumza jana Mheshimiwa Lema, wamezungumza na wengine suala hili naona tu kwamba kuna sehemu tumeteleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha naamini yeye ni msomi mzuri sana, naamini kabisa kama mnakumbuka wakati wa Tume ya Warioba ile ya Katiba, Mheshimiwa Waziri yeye mwenyewe ni miongoni mwa watu waliosema kwamba Rais apunguziwe majukumu, Rais apunguziwe madaraka, Mheshimiwa Waziri leo anasema Rais amiliki madini yote ya nchi hii kwa niaba ya Watanzania wote, wakati naamini kabisa kwamba ni miongoni mwa watu waliotoa ushauri tumpunguzie Rais mamlaka kama hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la ardhi inatosha, lakini ya madini tuangalie utaratibu mwingine, naamini yeye ni msomi, ni mtaalam mzuri, lakini kwenye hili Mheshimiwa Waziri

ameteleza kabisa. Najua kabisa Mheshimiwa Waziri alipokuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amefanya mambo mazuri mengi tu, lakini baada ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria naona kuna vitu vinaanza kupungua.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi mle ndani Mheshimiwa Waziri anatuambia kwamba stupid, anatukana Wabunge stupid, lakini naamini kabisa mambo yote haya tukijaribu kwenda mbele yanaweza kidogo yakawa yanapunguza hata ile sifa yake nzuri tunayoijua akiwa Mwalimu wetu. Yeye ni Mwalimu wangu mimi nimesoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, tunamjua uwezo wake, kwa hiyo naomba tu ajaribu kuisaidia Serikali….

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2017.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nami niweze kuchangia Muswada huu. Awali ya yote naomba niseme kwamba kumetokea sintofahamu tangu siku ya kupitisha bajeti hadi leo, jana nimesikia baadhi ya Manaibu Waziri wakiwa wanajibu maswali ya Wabunge wanasema kwamba “wewe unauliza swali na wewe, au unahitaji mradi fulani kwako? Kwa sababu ulikataa kupitisha bajeti hatutakuletea.” (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lile onyo ambalo ulilitoa nadhani unavyoahirisha Bunge mchana nadhani pia ungewapelekea baadhi ya Manaibu Waziri pia maana inawahusu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kupeleka maendeleo kwenye Jimbo fulani hivi sio hisani. Kupeleka maendeleo kwenye Jimbo ni lazima, kodi zinalipwa wananchi wa Majimbo husika wanalipa kodi lazima wapelekewe huduma. Mwananchi anapokuwa ananunua sabuni, anapokuwa ananunua nguo, anapokuwa ananua bidhaa mbalimbali analipa kodi. Anapolipa kodi anategemea kodi hiyo iweze kurudi kutengeneza barabara, kodi hiyo iweze kuleta dawa hospitali, kodi hiyo iweze kufanya shughuli mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba ili mambo haya yaweze kwenda vizuri ili siku nyingine basi hizi kura tatu hii kura ya ndiyo, hapana na abstain ondoeni zote basi ibaki ya ndiyo ili muweze kwenda vizuri kama mnadhani kwamba itasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, upotoshaji huu tukiuruhusu ukaendelea, naamini kwamba kama alivyoongea Mheshimiwa Silinde tutakuwa tunaligawa Taifa, hatuwezi kufika popote pale tutaligawa Taifa hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba baada ya kuzungumza hayo wako baadhi ya Mawaziri au Manaibu Waziri kwa mfano, yuko ndugu yangu hapa Naibu Waziri kutoka kule Katavi, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji unapotoka hapa unaenda Katavi lazima upitie kwangu pale Mlowo, kama utapitia Mlowo pale kwangu maana yake mkisema kama hayo yanayozungumzwa kwamba hayatafanywa kwenye Majimbo yetu, maana yake na wewe Naibu Waziri tukuzuie usipite pale kwa sababu hiyo barabara hawatumii wa Mbozi tu, wanatumia hata ninyi Mawaziri mnapopita maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee marekebisho katika…

T A A R I F A ...

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa ya ndugu yangu hapa naipokea kwa mikono yote kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sidhani kama amewatuma hao watu kuzungumza hayo maneno kwamba hawatapeleka bajeti huko, kwa sababu alichaguliwa na wananchi wa maeneo mbalimbali, hata kama kuna maeneo mengine kura hazikutosha, lakini walimchagua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuzungumza hayo, naomba niende sasa katika maeneo mengine kuhusu marekebisho katika Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Sura 290.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushuru wa mabango na kodi ya majengo kuchukuliwa na Serikali Kuu huku ni kwenda kuziua Halmashauri zetu. Tunaenda leo kukusanya ushuru wa majengo, tunaenda kukusanya ushuru wa mabango, leo Halmashauri zetu zitakufa kwa sababu hivi ndivyo vyanzo vya mapato kwenye Halmashauri zetu hapa nchini. Sasa kama leo tunakusanya ushuru huu Serikali Kuu inaenda kuhodhi, Halmashauri zetu kwa kweli zitakuwa katika hali mbaya sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, atakapokuwa anahitimisha Waziri wa Fedha naomba haya mambo ujaribu kuyaangalia, leo tupo hapa ndani wako wachache ambao wao wenyewe jambo likizungumzwa hata kama ni baya kwa wananchi wanapiga makofi, kesho litakapokuwa limeharibika hao hao wanakuruka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba tafadhali akili za kuambiwa changanya na za kwako, kama ni wataalam wako walikupotosha tafadhali katika hili jaribu kurekebisha, kwa sababu leo huwezi ukaenda kupora vile vyanzo vya mapato kwenye Halmashauri zetu, kwa sababu ndivyo tunavyovitegemea huko.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine naomba pia nizungumzie suala la kuwatambua wafanyabiashara wadogo, kuna jambo moja mmelizungumza hapa na kuna mtu mmoja hapa alikuwa anasema hapana, eti Machinga hawatalipa kodi, mnapotosha. Naomba hii hotuba ya Waziri msome ukurasa ule wa 47 inawezekana kuna wengine hawasomi . Ukurasa ule wa 47 unasema naomba nisome kidogo kwamba:

“Hatua za mapato na maboresho ya mfumo wa kodi, ada na tozo mbalimbali, hatua za kisera na kiutawala.”

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa pale kwenye hatua za kisera na kiutawala wameweka baadhi ya mambo pale kwa mfano jambo mojawapo ni kwamba kukusanya kodi kwa kutumia machine zetu (electronic machine) lakini ukisoma kipengele cha nne kinasema kwamba:

“Kuwatambua rasmi wafanyabiashara wadogo wadogo wasio rasmi na wanaofanyia biashara katika maeneo yasiyo rasmi.”

Mfano, Mama Lishe, wauzaji mitumba wadogo, wauza mazao ya kilimo wadogo kama mbogamboga, ndizi, matunda na na kadhalika, kwa kuwapatia vitambulisho maalum kwa kazi wanazozifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hapa tunazungumza haya mambo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapohitimisha aweze kulitolea maelezo vizuri, huu ni uwongo mchana kweupe, mnataka hawa wafanyabiashara mkishawatambua ili muweze kuanza kuwatoza kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka Mbunge mmoja wa Mwanza alikuwa analalamika, anasema kwamba Machinga wanafukuzwa na Rais akaagiza kwamba Machinga wasionewe popote pale wala wasifukuzwe, leo mnasema Machinga wasifukuzwe, mnataka muanze kuwatoza kodi. Hii ni aibu kubwa sana kwa Taifa letu ambalo lina rasilimali za kila aina, Taifa ambalo lina madini, lina Tanzanite, lina dhahabu, lina gesi, lina kila kitu, kwenda kukimbizana na ushuru wa Mama Lishe…..

T A A R I F A ...

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, huyu bwana nadhani inawezekana kabisa kwamba hayuko makini na taarifa yake naomba sasa rasmi niikate kwa sababu kuna vitu ambavyo nadhani havielewi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachokizungumza hapa ni kwamba, unapoenda kuwatoza wa machinga kodi, unapoenda kuwatoza mama lishe kodi, leo tuna madini; dhahabu, Tanzanite na juzi mmesema kuna trilioni 108, mnataka kudai hizo ndiyo sasa ziongezwe kwenye bajeti hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme badala ya kuwatoza hawa Mama Lishe, kuwatoza hawa wauza mboga mboga na matunda nendeni mkawatoze wale wanaochimba madini katika nchi yetu, wanaotorosha madini, nendeni mkawatoze wawekezaji wakubwa kwenye vitalu vya uwindaji, nendeni mkawatoze wale wakubwa ambao wamewekeza kwenye miradi mikubwa mikubwa. Naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, kama Chama cha Mapinduzi kimechoka kutawala nchi hii na mnataka 2020 muambulie zero, nendeni kwenye hili ambalo mnataka kulianzisha hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakuhakikishia kabisa Mheshimiwa Waziri kwa sababu najua na wewe pia inawezekana ni mgombea mwenzangu kwa sababu nimesikia juzi unawapongeza wananchi wa Jimbo la Buhigwe, unasema unawashukuru wananchi wa Buhigwe wakati wewe ulichaguliwa na Rais, wale wananchi unakutana nao maeneo gani mpaka unaenda kuwapongeza? Kwa hiyo, inawezekana ukawa ni mgombea na wewe kama ulivyokuwa wagombea wengine, sikukatazi wewe nenda, lakini wale wananchi kule utakachokutana nacho utakutana na wamachinga hao hao ambao umewatoza kodi, utakutana na mama lishe, utakutana na wauza mboga mboga, ndiyo wapiga kura wetu kule.

Naomba kwenye hili kama Serikali haitachukua hatua Mheshimiwa Waziri imekula kwako, hii na nina amini kabisa usifanye mchezo Jimbo si mchezo, na nina amini lakini Obama yupo makini sidhani kama ataruhusu hali hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye jambo lingine, yuko Mbunge mwenzetu humu ndani amezungumza jambo, amesema mimi nilidhani kumbe hizi kodi zitakusanywa kwenye Majiji, sijui kwenye Miji, kwenye Halmashauri haihusiki, amedanganya na kama hajadanganya basi hakuelewa vizuri, kwa sababu..

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)