Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Questions to the Prime Minister from Hon. Pascal Yohana Haonga (3 total)

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Suala la kuongeza mishahara kwa watumishi wa umma siyo suala la utashi wa mtu bali ni suala la kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma, Na.8 ya mwaka 2002 pamoja na Kanuni zake za 2003. Ni lini sasa Serikali itaacha kukiuka sheria hii kwa kutopandisha mishahara kwa watumishi wa umma na ituambie rasmi ni lini itapandisha mishahara kwa watumishi wa umma?

SPIKA: Hiyo sheria inasomekaje?

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, ni Sheria ya Utumishi wa Na.8 ya mwaka 2002 ambayo inaeleza kupandisha mishahara pamoja na stahiki mbalimbali za watumishi wa umma.

SPIKA: Si ungetusomea basi hiyo sheria inavyosema. Siyo kila mtu ana nakala hata Mheshimiwa Waziri Mkuu hana nakala, hawezi kukariri sheria zote. (Makofi)

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, swali kwa ufupi linahusu kupandisha mishahara watumishi wa umma, ndiyo logic sasa ya swali hili. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Haonga, Mbunge wa Mbozi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza Serikali hajakiuka sheria unayoitaja, kama inasema hivyo, kwa kutolipa nyongeza ya mishahara. Serikali lazima iwe na mipango na mipango ile iliyonayo Serikali lazima imnufaishe mtumishi au yeyote ambaye anapata stahiki hiyo. Nia ya Serikali kwa watumishi ni njema bado ya kuhakikisha kwamba wanapata mishahara na stahiki zao na wanalipwa madeni yanayozalishwa kutokana na utendaji kazi wao. Hiyo ndiyo nia njema ya Serikali na tunatekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kwenye eneo la mishahara hili Watanzania wote na wafanyakazi mnajua kwamba nchi hii tulikuwa na idadi kubwa ya wafanyakazi na wengine hawakuwa wafanyakazi kwa mujibu wa orodha na wote walikuwa wanalipwa mishahara na posho mbalimbali. Kwa hiyo, ili kutambua nani anastahili kupata mshahara kiasi gani na kwa wakati gani Serikali ilianza na mazoezi makubwa mawili. Moja, tulianza kwanza kuwatambua watumishi halali na hewa. Baada ya kuwa tumekamilisha zoezi hili baadaye tulikuja kutambua watumishi wenye vyeti stahiki vya kufanya kazi hiyo kwa mujibu wa Kanuni za Utumishi wa Umma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuwa mazoezi yote yamekamilika huku pia tukiendelea kulipa na madeni ya watumishi ambao tumewatambua pia Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameunda Tume ya Mishahara Mishahara na Motisha. Baada ya kuwa tumemaliza kutambua watumishi stahiki sasa Tume ile inafanya mapitio ya kada zote za utumishi wa umma na viwango vya mishahara yao ili kutambua stahiki ya mshahara huo na kada hiyo baada ya kugundua kwamba ziko tofauti kubwa za watu wenye weledi wa aina moja, wamesoma chuo kikuu kimoja, lakini wanapata ajira kwenye sekta mbili mmoja anapata milioni 20 mwingine milioni 5, jambo hili kwenye utumishi halina tija. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nia ya Mheshimiwa Rais kuunda ile Tume ni kufanya tathimini nzuri ya kutambua weledi wa kazi lakini pia itahusisha na uwajibikaji mahali pa kazi na tija inayopatikana mahali pa kazi ili alipwe mshahara unaostahili. Kwa hiyo, jambo hili inawezekana limechukua muda katika kuhakikisha kwamba tunafikia hatua hiyo, inawezekana Mheshimiwa Mbunge ukasema kwamba Serikali haijatimiza Jukumu lake lakini nataka nikuhakikishie kwamba kwa taratibu hizi tunalenga kuhakikisha kila matumishi anapata mshahara kulingana na weledi wa kazi yake au daraja lake ili kuondoa tofauti ambazo zipo za kiwango cha mishahara ambazo zinapatikana kwenye maeneo haya watu wakiwa na weledi wa aina moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tutakapokamilisha kazi hii, kwa bahati nzuri ile Tume tayari imeshawasilisha taarifa Serikali na Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma inaendelea kuipitia, wakati wowote tunaweza kupata taarifa za matokeo ya Tume ile. Kwa hiyo, niwahakikishie watumishi wote nchini kwanza muendelee kuwa watulivu, mbili muendelee kuiamini Serikali yetu na tatu Serikali inayo nia njema ya dhati kabisa kuhakikisha kwamba watumishi wote wanapata haki zao stahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa bahati nzuri sana Mheshimiwa Rais wetu amekutana na viongozi wa vyama vya wafanyakazi, ameeleza vizuri haya na viongozi wamepata nafasi ya kueleza changamoto zilizopo kwenye sekta ya umma na Serikali tumechukua hizo changamoto zote na tunazifanyia kazi. Kwa bahati nzuri mjadala wetu na vyama vya wafanyakazi unaendelea vizuri. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge ambaye pia umewazungumzia wafanyakazi uendelee kuwa na imani na Serikali, utaratibu wetu ni mzuri na unalenga hasa kuleta tija kwa mfanyakazi ili aweze kufanya kazi yake vizuri. Kwa hiyo, wakati wowote kazi itakapokamilika tutatoa taarifa kwa wafanyakazi. Ahsante sana.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Suala la vitambulisho kwa wajasiriamali wadogo wadogo imekuwa ni kero kubwa sana katika maeneo mbalimbali nchini na limekuwa ni kero kubwa zaidi kwa wajasiriamali wale wanaouza mboga mboga kama mchicha, nyanya, tembere, maandazi na vitumbua. Kibaya zaidi, maeneo mengine hata wale wanaotoka shambani, amechuma mchicha wake, anaambiwa naye ni Mjasiriamali aweze kutoa shilingi 20,000/= apewe kitambulisho.

Mheshimiwa Spika, suala hili kwa mtazamo wangu mimi naona kama vile halijatafsiriwa vizuri kule chini hasa wale wanaolitekeleza kwa sababu maeneo mengine pia hata wapiga debe na walimu maeneo mengine wanaambiwa kwamba ni wajasiriamali waweze kulipia vitambulisho vya shilingi 20,000/=.

Mheshimiwa Waziri Mkuu sasa swali langu: Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka hili jambo lingeweza kusitishwa kwanza ili tuweze kufanya tathmini na kupanga vizuri kwamba hasa ni watu gani ambao wamelengwa na wenye mitaji ya namna gani? Kwa sababu kuna wengine wana mitaji ya shilingi 1,000/= wengine shilingi 2,000/=, lakini wanaambiwa walipe shilingi 20,000/= kwa ajili ya vitambulisho vya ujasiriamali?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwalimu Haonga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali imeweka utaratibu mzuri sana wa kuwafanya wajasiriamali wadogo kuweza kuchangia pato la Taifa; na Mheshimiwa Rais alibuni njia nzuri ambayo inawatambulisha hawa wajasiriamali. Hata hivyo, wajasiriamali hawa tumewaweka kwenye madaraja yao. Wako wale wadogo, wako wafanyabiashara wa kati na wale wajasiriamali wakubwa.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais aliwalenga Serikali imewalenga hawa wadogo ambao kipato chao kutokana na kazi wanayoifanya hakizidi zaidi ya shilingi milioni nne kwa mwaka ili nao wapate nafasi ya kuweza kuchangia pato la Taifa lakini kuwaondolea usumbufu kwenye maeneo wanayofanya biashara kwa kutozwa kodi kila siku ambayo pia na yenyewe inasaidia kupunguza mapato wanayopata kwa mwaka.

Mheshimiwa Spika, sasa vitambulisho vile vilipotolewa kwa Wakuu wa Wilaya, tambua kwamba kuna maeneo mengine utekelezaji wake siyo mzuri, kwa sababu wako wengine wanalazimisha watu badala ya kuwaelimisha namna ya kupata vitambulisho hivyo. Yako maeneo wanapewa hata wale wajasiriamali wakubwa wenye pato la zaidi ya shilingi milioni nne, linawafanya na wao wanashindwa kuchangia kulingana na biashara wanazozifanya kwa sababu wao kwa category yao wanachangia TRA moja kwa moja, lakini wale wadogo hupitia vile vitambulisho.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, maelekezo ambayo tumeyatoa tena baada ya kuwa tumepata malalamiko kutoka kwenu Waheshimiwa Wabunge, ni kwamba Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa watumie muda wao kuelimisha nani anapaswa kuwa na kitambulisho badala ya kutumia wakati mwingine nguvu au kwenda kulazimisha au kuwapa wajasiriamali wakubwa wenye mapato zaidi ya shilingi milioni nne na kuondoa maana ya uwepo wa vitambulisho? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kupitia Mheshimiwa Mbunge Serikali tumeipokea hiyo. Tunaendelea kutoa maelekezo kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya watumie nafasi hiyo kuelimisha zaidi kuliko kulazimisha, ni nani wanatakiwa wapate kitambulisho hicho ili kuwaondolea usumbufu wa kuwa wanatozwa fedha tena shilingi 200/=, shilingi 500/= kila siku anapoendelea kufanya biashara yake ya mchicha, maandazi, wale wanaokimbiza mahindi vituo vya mabasi.

Mheshimiwa Spika, watu wa namna hii ndio ambao Mheshimiwa Rais aliwalenga ili nao waone uchangiaji wa uchumi, pato la nchi ni sehemu yao lakini pia waendelee kufanya biashara yao bila kusumbuliwa ndani ya mwaka kwenye Halmashauri zao. Kwa hiyo, niseme tu, tumeipokea tena hiyo na tutaifanyia kazi zaidi ili kuleta utendaji ulio sahihi na wajasiriamali waweze kujitoa kuchangia kwenye nchi yao.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

SPIKA: Mheshimiwa Waziri Mkuu katika swali lake amesema pia kwamba walimu wanalazimishwa wapewe vitambulisho vya wajasiriamali. Sijui hilo nalo unasemaje Mheshimiwa Waziri Mkuu?

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Sawasawa, hilo limetokea Jimboni kwangu.

WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la swali la Mhehsimiwa Mwalimu Haonga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, inawezekana pia uko utekelezaji usio sahihi. Mwalimu kama Mwalimu ni miongoni mwa watu wenye pato la zaidi ya shilingi milioni nne kwa mwaka. Kwa hiyo, mwalimu anapofanya biashara, ile biashara anayoifanya kama yenyewe haimfikishi kwenye pato hilo, Mkuu wa Wilaya ambaye yuko kwenye eneo hilo, anajua mwenedno wa pato la huyo mtu ambaye yuko pale.

Mheshimiwa Spika, sasa suala la mwalimu na mfanyakazi mwingine, muhimu zaidi ni ile biashara anayoifanya, lakini pia namna ambavyo anaweza pia akachangia pato kupitia biashara hii anayoifanya ambayo uzalishaji wake haifikii kiwango hicho cha shilingi milioni nne kwa mwaka.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Waziri Mkuu, uchaguzi wa Serikali za Mitaa, mchakato wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa Mwaka 2019 uligubikwa na dosari nyingi sana, ikiwemo wagombea kutoka vyama vya upinzani kunyimwa fomu, ofisi kufungwa kwa muda wote, hivyo kusababisha baadhi ya wagombea, hasa wa upinzani kushindwa kupata fursa kuweza kugombea.

Mheshimiwa Spika, je, Serikali haioni kwamba ni vema uchaguzi wa wa Serikali za Mitaa uweze kurudiwa sambamba na Uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Haonga, Mbunge wa Mbozi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, chaguzi hizi zote zinasheria zake na kanuni zake; na hata kanuni za Serikali za Mitaa vyama vyote vya siasa vilishirikishwa katika kutengeneza kanuni zao. Moja kati ya kanuni hizo ni pale ambapo inatoa fursa kwa yeyote ambaye hajaridhika huko anakogombea, kwamba anaweza kukata rufaa, na atakapoona rufaa hiyo kwenye ngazi inayofuata haikutendeka haki aende mahakamani. Kwa hiyo kulichukuwa hili kwa ujumla ujumla si sahihi sana kwasababu kila mmoja alipo alikuwa na mamlaka yake inayoratibu na anayo fursa ya kwenda kwenye mamlaka kukatia rufaa pale ambapo hajaridhika na utekelezaji wa jambo hilo. Vyama vyote vilishiriki kwenye hii kanuni ya kukata rufaa, kwa hiyo ni wajibu wa huyo mgombea kwenye eneo hilo kwenda kukata rufaa.

Mheshimiwa Spika, na kama kulikuwa na dosari kama ambavyo nimeeleza bado zilikuwa zinaweza kuelezwa huko huko kwenye ngazi hiyo, kwa hiyo, huna sababu ya kutengua uchaguzi wote wakati mgombea mwenye malalamiko ana fursa huko huko aliko kwa kukata rufaa na hatimaye hukumu itachukuliwa. (Makofi)