Supplementary Questions from Hon. Abdulaziz Mohamed Abood (10 total)
MHE. ABDUL-AZIZ M. ABOOD: Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili mafupi ya nyongeza. Kwa kuwa Serikali ina mpango wa kusambaza mabomba maeneo ambayo hayana mabomba ya maji, nataka kujua muda gani ambao Serikali itasambaza mabomba hayo?
Swali la pili, kuna baadhi ya maeneo Morogoro Mjini hawapati maji karibu miezi miwili, lakini cha kushangaza wanapelekewa bili za kulipa maji, je, ni lini Serikali itaondoa kero hiyo ambayo imekuwa kama dhuluma kwa wananchi wa Jimbo la Morogoro Mjini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ni muda gani tutakamilisha kuweka mtandao wa mabomba ya kusambaza maji ili yaweze kufika maeneo yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge Abood aangalie katika kitabu cha bajeti, tumetenga zaidi ya shilingi bilioni nne kwa mwaka wa fedha unaokuja wa 2016/2017 kwa ajili ya kuendelea na kazi ya kuweka mabomba ya mtandao katika Jimbo lake la Morogoro Mjini. Kwa hiyo ni muda gani, kwa sababu utekelezaji una mchakato wake, mchakato wa bajeti tayari umekamilika fedha Serikali imetenga. Kwa hiyo, tutaendelea na usanifu, tutaendelea na kutangaza tenda na baada ya kutangaza tenda kumpata mkandarasi ndiyo program kamili lini tutatekeleza mradi kwa miezi mingapi itapatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu tatizo la bili za maji. Nashukuru kwamba nimepata hii taarifa, Mheshimiwa Mbunge hili suala tutalifuatilia kuona inakuwaje kwamba mtu analetewa bili za maji wakati maji hatumii?
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili nililikuta pia katika Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara nilipokwenda kule. Suala hili wakati mwingine linakuwa na udanganyifu. Kuna connection ambazo hazijatambuliwa na mamlaka, mtu anaiba maji, sasa wakimtambua wanakwenda kumpiga bili analalamika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo mengi ambayo yanajitokeza katika hili suala la bili, lakini pia kuna uzembe vile vile hata ndani ya watendaji wetu kwa upande wa mamlaka. Kwa hiyo, nimwombe tu Mheshimiwa Abood tushirikiane. Nitatoa taarifa kwa Mamlaka ya Mji wa Morogoro ili waweze kuliangalia hili na tutampatia majibu.
MHE. ABDUL-AZIZ M. ABOOD: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; Morogoro inaelekea kuwa Jiji, je, Serikali ina mikakati gani ya kumaliza maeneo yote ya Mji wa Morogoro kuwa na umeme?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuna maeneo ambayo umeme umeshafika, wananchi wameshalipia kuunganishiwa umeme, lakini majibu wanayopewa ni kuwa nguzo hakuna. Je, Serikali itaondoa lini kero hiyo ya nguzo katika Mji wa Morogoro ili wananchi waweze kupata umeme, maeneo waliyokwishapata umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali kupeleka umeme ni kama ambavyo nimeeleza, ipo miradi ya REA, lakini pamoja na REA bado TANESCO wana bajeti zake za kupeleka umeme. Katika Mkoa wa Morogoro, hasa Morogoro Mjini, mkakati uliopo wa kwanza kabisa, Serikali imetenga shilingi milioni 106 kwa mwaka huu ambayo itapeleka umeme kwenye vijiji vya Mheshimiwa Abood ikiwemo Kihonda, Mafisa pamoja na maeneo mengine kama kule Kanisani ambako ameeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengine ambayo Mheshimiwa Mbunge hajayataja pamoja na eneo lake lile ambalo amesema eneo la Bomba la Zambia. Kile Kijiji cha Bomba la Zambia ambacho kipo mbali sana kitapelekewa umeme mwaka huu. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Abood kwamba Serikali ina mkakati madhubuti wa kupeleka umeme kwenye vijiji vyake vyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili kuhusiana na nguzo, ni kweli kabisa yako maeneo Morogoro Mjini wananchi wamelipia, lakini hawajawahi kuunganishiwa umeme. Utaratibu unafanyika sasa na nimhakikishie Mheshimiwa Abood hivi sasa tunapoongea hapa wananchi wake wa Lokole Juu pamoja na Lukobe Kanisani wanaunganishiwa umeme kwa sababu wameshalipia na nguzo zimeshakuja na vijiji vinne ambavyo amevitaja pamoja na Kauzeni na maeneo mengine wataendelea kuunganishiwa umeme mara baada ya nguzo kuingia mwezi ujao.
MHE. ABDULAZIZ M. ABOOD: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Spika, tatizo la Urambo linafanana na tatizo la Morogoro Mjini, wananchi wa Morogoro Mjini wanategemea maji Bwawa la Mindu. Vyanzo vingi vinavyomwaga maji katika bwawa la Mindu vimekauka. Kuna Mto Mgeta kilomita 60 kutoka Bwawa la Mindu.
Je, Serikali haiwezi ikaanzisha mradi wa maji kutoka Mto Mgeta ili kuweza kujaza Bwawa la Mindu na wananchi wa Morogoro wakaondokana na kero ya maji?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, tutaangalia mapendekezo yake. Kwa sasa hivi tumeanzisha Awamu ya Pili ya Programu ya Maji katika nchi nzima.
Kwa hiyo, tutaangalia vyanzo vya maji vilivyopo na vingine vipya ili kuhakishisha kwamba azma ya kupeleka maji kwa wananchi wote inatekelezeka. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge ushauri wako tutauzingatia.
MHE. ABDUL-AZIZ M. ABOOD: Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza;
Swali la kwanza, zahanati ya Mafiga inahudumia kina mama wengi lakini haina madawa kwa ajili ya akina mama na pia haina ultra sound machine ya akina mama.
Je, lini Serikali itaipatia zahanati ya Mafiga vifaa hivi?
Swali la pili, hospitali ya Mkoa wa Morogoro ambayo ipo njia panda ya barabara ya Morogoro inayokwenda Mikoa mingine yote ya Bara na ajali nyingi zinatokea, lakini haina mashine ya X-Ray, mashine iliyopo sasa hivi haifanyi kazi vizuri.
Je, Serikali haioni kama kuna uharaka wa kuipatia hospitali ya Mkoa wa Morogoro mashine ya X-Ray?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika maeneo yangu ambayo nimetembelea ni Morogoro, na jambo ambalo nimeshuhudia pale ni kwamba kama Mheshimiwa Mbunge pale kwa kweli kwa kutumia, licha ya ushawishi wakati mwingine anatumia resources zake mwenyewe kwa ajili ya wananchi wake. Naomba nikuhakikishe kwamba katika hii zahanati ya Mafiga uliyoisema ambayo changamoto kubwa ni madawa pamoja na vifaa tiba especially ultra sound na nimesema katika maelezo yangu ya awali. Katika research tuliyofanya haraka haraka vitu vingine vingekuwa vinaweze kupatikana kwa ukaribu sana lakini tatizo kubwa tulilokuwa nalo mwanzo ni kutokana na ile management ya fedha zilizokuwa zinapatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia idadi ya wanaofika katika zahanati ya Mafiga pale lakini collection ilikuwa ni changamoto kubwa sana. Ndiyo maana tulitoa maelekezo ya kutosha licha ya kufanya juhudi zingine za upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, changamoto kubwa ni kwamba tukienda kukusanya mapato yetu vizuri ambayo katika njia moja au nyingine unakuta kwamba baada ya kutumia mifumo ya electronic, collection imeenda zaidi ya asilimia 800. Watu waliokuwa wanakusanya shilingi laki moja leo wanakusanya shilingi milioni moja, unaona kwamba jinsi gani pesa hizi zikikusanywa vizuri zitaenda kusaidia katika suala zima la madawa na vifaa tiba.
Kwa hiyo Mheshimiwa Abood naomba nikuambie ninakuhakikishia kabisa kwamba katika zahanati ya Mafiga mimi na wewe kwa sababu tumeshaahidi kwamba tutaenda Morogoro, hii ni sehemu ya kwanza kwenda kubaini kuwa tatizo la msingi ni nini, na tutafanyaje kuondoa tatizo la madawa, kwa sababu mwanzo watu hata mwongozo walikuwa hawaufuati, pesa hata zikikusanywa haziendi katika madawa na vifaa tiba, isipokuwa watu wanagawanya kwa per diem na vikao vingine visivyokuwa na maana yoyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo nimhakikishie Mheshimiwa Abood kwamba, hapa tutafanya ukatabati mkubwa ili utendaji wa zahanati hii na nyinginezo zinafanya kazi vizuri kwa ajili ya wananchi wa Morogoro.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la hospitali ya Morogoro ni kweli na mimi nikuambie kwamba miongoni mwa field practical zangu wakati nilipokuwa Chuo Kikuu mwaka 1998, nilifanya research zangu pale na field practical nilifanyia pale Morogoro, naifahamu vizuri hospitali ya Mkoa wa Morogoro. Ni kweli inapokea wagonjwa wengi sana na wakati mwingine hata ajali zikitokea watu wengi ni sehemu ya kimbilio, wanaotoka Iringa, Dodoma na sehemu mbalimbali pale ni kimbilio. Tunajua X-Ray machine ipo lakini haifanyi kazi vuziri, tuna mpango mpana sasa hivi wa Serikali hasa kwa ajili ya hospitali zetu za Mikoa na hospitali zetu za Kanda. Mpango huo sasa kwa Serikali ya Tanzania kwa kushirikana na Serikali ya Uholanzi tutahakikisha kwamba tunapeleka vifaa tiba katika hospitali zetu za Kanda na hospitali za Mkoa. Ninaamini na hospitali yetu ya Mkoa wa Morogoro tutaipa kipaumbele kutokana na strategic area yake ya kijiografia, lazima tuipe nguvu wananchi wa Morogoro waweze kupata huduma, ili wanufaike na huduma njema ya Serikali yao ya Awamu ya Tano ambayo inafanya kazi kwa maslahi ya Watanzania.
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI, kuhusu suala la uhaba wa dawa katika vituo vyetu vya afya, ningependa kuwafahamisha Waheshimiwa Wabunge kwamba tunapitia upya vigezo vya kugawa fedha za dawa. Kwa sababu kwa kweli tumeona hakuna uwazi, unakuta kituo kingine kina wananchi wengi lakini mgao wa dawa fedha ya dawa ni ndogo. Kwa hiyo, nataka kuwathibitishia Waheshimiwa Wabunge tunaangalia upya vigezo kama ni hospitali ya Mkoa wanatakiwa kupata shilingi ngapi na taarifa hizi tutazitoa kwa kila Mbunge ajue kituo chake cha afya kinapata shilingi ngapi, hospitali yake ya Wilaya inapata shilingi ngapi na hospitali ya Mkoa inapata shilingi ngapi. Kwa hiyo, tunataka kuwa wawazi zaidi katika mgao wa fedha za dawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. ABDUL-AZIZ M. ABOOD: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, ni lini Serikali itasaini mkataba huu wa Euro milioni 70 maana toka mwaka 2017 tunaambia itasaini. Sasa tunataka kujua ni lini Serikali itasaini mkataba huu ili wananchi wa Morogoro wapate maji? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Morogoro Mjini kuna mgao wa maji, mwananchi anaweza akakaa miezi mitatu hajapata maji lakini cha ajabu analetewa bili ya maji mwisho wa mwezi ili aweze kulipa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa namna ya kipekee anavyowapigania wananchi wake, ni namna gani jinsi anavyowapenda. Mimi nataka niwahakikishie wananchi wa Morogoro hawakukosea kumpata Mbunge huyu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kubwa mimi kama Naibu Waziri nilifika Morogoro na niliona hali ya upatikanaji wa maji katika Mji ule wa Morogoro na namna gani wananchi wanavyolalamika kuhusu suala zima la maji. Anataka kujua ni lini sasa tutakaposaini mkataba ule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa miradi ya maji unategemeana hasa katika suala zima la fedha na suala la fedha lazima lifuate taratibu zake. Sasa nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa maji hayana mbadala, si kama wali ukikosa wali utakula makande au ugali kuna haja ya haraka kuwapatia wananchi wake maji na sisi kama Wizara ya Maji tutafanya jambo hilo haraka ili wananchi wake waweze kupata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala zima la bili nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kutokana na changamoto hiyo Waziri wangu aliitisha kikao cha Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Maji nchini katika kuhakikisha wanajadili changamoto hii ya maji na akawapa maelekezo. Nataka niwaagize tena Wakurugenzi wote. Maagizo ambayo ametoa Waziri kuhusu suala zima la kutokuwabambikia wananchi bei lazima watoe bei ambazo zimeidhinisa na EWURA na yale maelekezo ambayo yanahusu suala zima la bei wafanye kama walivyoelekezwa.
Mheshimwia Mwenyekiti, kama kuna Mkurugenzi atakayekaidi atakavyoenda ndivyo sivyo atuharibie sisi kazi tutamharibia yeye kabla ya sisi kutuharibia. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ABDUL-AZIZ M. ABOOD: Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro ipo katikati ya barabara za Iringa, Mbeya, Dodoma na ajali nyingi zinatokea lakini mpaka leo kuna matatizo ya X-ray machine. Je, ni lini Serikali itaipatia uwezo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro X-ray machine kwa sababu ajali nyingi huwa zinatokea katika barabara hizi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro ni moja kati ya hospitali 10 ambazo tutazipatia mashine ya X-ray. Tunatarajia ifikapo mwezi Juni mwaka huu mashine hii itapatikana.
MHE. ABDUL-AZIZ M. ABOOD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa, wananchi wa Kauzeni na Luhungo walihamia pale mwaka 1969 wakati wa Vijiji vya Ujamaa na wakapewa maeneo ambayo yalipimwa mwaka 1970 ikawekwa mipaka kati ya shirika na wananchi;
Je, kwa nini Serikali isitumie mipaka hiyo ya mwaka 1970 ili wananchi wakapata haki yao na mashamba yao yakawa katika eneo lao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, si swali lakini ningemwomba Mheshimiwa Waziri angekuja katika maeneo haya akaangalia yeye mwenyewe na kuweza kukutana na wananchi akapata ukweli ulivyo katika meneo haya. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba upimaji wa awali umefanyika mwaka 1970 na baada ya pale kutokana na migogoro hii ya kuingiliana kati ya maeneo ya Jeshi na Wananchi, mwaka 2002 ulifanyika upimaji mpya ambao ulikuwa na lengo la kuondoa wananchi waliokuwa ndani ya mipaka ya Jeshi kwa hivyo wakaachwa nje, sasa inaonekana baada ya pale mgogoro umeendelea. Nataka nimkubalie na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba niko tayari kwenda katika eneo hilo pamoja na wataalam wangu ili tukazungumze na wananchi na kutafuta ufumbuzi wa kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee tu kusema kwa ufupi kwamba, matatizo ya mipaka kati ya maeneo ya Jeshi na wananchi yako sehemu nyingi sana. Naomba niwaarifu tu Waheshimiwa Wabunge kwamba nimetengeneza utaratibu maalum wa kupita katika maeneo hayo ili mimi na wataalam wangu tuthibitishe mipaka hiyo na kuhakikisha kwamba tunaondoa hii mogogoro ambayo imeendelea kwa siku nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu hapa kwamba kuna mgogoro ambao nimeupata kutoka kwa Mheshimiwa Mwakyembe kwenye Kata za Bondeni, Ipiyana na Kajunjumele katika Wilaya ya Kyela, nimhakikishie pia kwamba katika utaratibu nitakaopanga wa kuzunguka katika maeneo haya nitafika na pale nizungumze na wananchi ili hatimaye tuondoe matatizo yanayowakabili wananchi katika maeneo hayo. (Makofi)
MHE. ABDUL-AZIZ M. ABOOD: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza nilitaka kujua mradi wa maji wa Kihonda na Mkundi ambao unaunganisha Mitaa ya Yespa, Kilimanjaro umeshaanza; tunataka kujua ni lini utakamika kwa sababu umechukua muda mrefu mpaka sasa haujakamilika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, Mradi wa Maji wa AFD ambao utagharimu Euro milioni 70 Morogoro kama unavyojua kuna kero kubwa za maji; sasa nilitaka kujua ni lini utasainiwa ili uanze kazi uwakombe wananchi wa Morogoro Mjini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji nimpongeze Mheshimiwa Abood ni miongoni mwa Wabunge ambao wachapakazi na amekuwa ni mfuatiliaji mkubwa sana hususan changamoto zinazohusina na wananchi wake, lakini kubwa ambacho ninachotaka kusema pamoja na changamoto zipo jitihada ambazo sisi kama Serikali tunazozifanya katika Mkoa ule kwa maana ya Morogoro Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mradi wa Kilimanyari Yespa mradi takribani milioni 715 ambazo tunatekeleza nimwagize Meneja kwa maana Mkurugenzi wa MORUWASA kuhakikisha mradi ule unakamilika kwa mujibu wa mkataba ili wananchi wale waweze kupata huduma ya maji. Na mimi nataka nimhakikishie Mheshimiwa Abood baada ya Bunge nitafika eneo lile kujionea utekelezaji wa mradi ule. Lakini kikubwa kuhusu la huu mradi huu mkubwa kwa maana kuondoa tatizo la maji Morogoro wa Euro milioni 70 ninachotaka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge ukiona giza linatanda ujue kuna kucha.
Mheshimiwa Abood jana sisi tumefungua tender document kwa maana ya kuwapata wataalam wa ushauri ili kuhakikisha mradi ule unaweza kuanza na wananchi wako wanapata maji. Ahsante sana.
MHE. ABDUL-AZIZ M. ABOOD: Mheshimiwa Spika, Morogoro ina barabara mbili kuu zinazounganisha nchi za SADC na Afrika Mashariki. Morogoro ilitenga hekari 500 kwa ajili ya bandari kavu, je Serikali ina mpango gani wa kujenga Bandari Kavu katika Mji wa Morogoro?
NAIBU WAZIRI UCHUKUZI (MHE. FREDY A. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Abdul-Aziz, Mbunge wa Morogoro kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli Morogoro pia tuna eneo kwa ajili ya ujenzi wa Bandari Kavu na kwa kuwa reli yetu SGR itaanza kazi hivi karibuni na katika mwaka wa fedha ujao nimwombe Mheshimiwa Mbunge apitishe bajeti yetu ya Wizara ya Ujenzi kwa kuwa ni miongoni mwa Bandari Kavu zitakazojengwa katika mwaka wa 2023/2024. Ahsante.
MHE. ABDUL-AZIZ M. ABOOD: Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Rufaa ya Manispaa ya Mkoa wa Morogoro inazidiwa na wagonjwa. Ni lini Serikali itamalizia ujenzi wa Hospitali ya Manispaa ya Morogoro ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kumwelekeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro kwamba ifikapo Ijumaa, ndani ya wiki hii, atuletea taarifa tuone wamefikia hatua gani katika ujenzi wa Hospitali ya Manispaa ya Morogoro, wamekwama eneo gani na gharama kiasi gani inahitajika, ili tukubaliane kwa pamoja na kuhakikisha kwamba, tunakwamua mkwamo huo na hospitali hiyo ikamilike kwa wakati, ahsante.