Contributions by Hon. Ahmed Mabukhut Shabiby (31 total)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naunga mkono hoja kwa hotuba hii ya 2016. Kwa vile Hotuba ya Waziri mpya na Awamu mpya ya Tano, lakini uhalisia Wizara hii. Umuhimu wa Wizara hii kwa miaka mingi sasa imekuwa haina msaada kwa wakulima hasa wa Mkoa wa Morogoro na zaidi Wilaya ya Gairo. Wilaya ya Gairo ni moja ya Wilaya zinazolima sana nchini pamoja na kuwa haipo kitakwimu na umaarufu cha ajabu Wilaya hii haipati ruzuku za pembejeo na ikipata zinakuja nje ya muda wa kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, mwaka huu mbegu imekuja mwezi wa Kwanza katikati, wakati kilimo cha Gairo mbegu inatakiwa mwezi Novemba. Gairo ina Tarafa mbili, Tarafa ya Gairo na Nongwe, Tarafa ya Nongwe yote ina maji ya kutosha, mito ya kudumu mingi, lakini hakuna mpango wowote wa kuendeleza kilimo cha umwagiliaji katika maeneo haya pamoja na Halmashauri ya Gairo kuomba pesa, lakini imekuwa haipewi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tuna nia ya kuondoa nchi katika matatizo ya chakula na mazao ya biashara, wataalam wa Wizara wajiongeze na kujua kila sehemu inayofaa kwa kilimo. Siyo kunakili kila siku kuwa maeneo fulani ndiyo wanafaa au yanafaa kwa kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukija upande wa mifugo Wilaya hii ina mifugo mingi lakini kuna uhaba wa mabwawa ya maji kwa ajili ya mifugo, hasa katika Vijiji vya Kitaita, Ngayaki, Chogoali, Misingisi, Mkalama, Meshugi, Ndogomi, Kumbulu, Chilama. Tunaomba sana huduma hii ya mabwawa ichukuliwe kwa jicho la huruma na haraka, kwani wafugaji hawa wanapata tabu sana kwenda zaidi ya kilomita kumi hadi kumi na tano kwa ajili ya maji na mara nyingine wasipate maji ya kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, nategemea mtashughulikia suala hili.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa pongezi za dhati kwa Wizara hii na kwa viongozi wake wote. Natambua Wizara hii ni kiungo muhimu kati ya wafanyabiashara na Serikali. Bila Wizara hii kufanya kazi kwa umakini na uweledi, basi ndoto ya Serikali yetu ya kuwa na viwanda itakuwa ndoto isiyotimia. Kwa sababu kumekuwa na kila aina ya matamko na sheria za ovyoovyo za kuua biashara ndani ya nchi hii hasa kutoka katika mamlaka zilizopo kama EWURA, TBS, NEMC, SUMATRA na zinginezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, ili mtu apate leseni ya NEMC ya Petrol Station, kwanza lazima apate consultant ambaye amepitishwa na NEMC na baada ya hapo asajili mradi, consultant pekee analipwa shilingi millioni saba (Sh.7,000,000/=) na kusajili mradi napo fedha. Ukimaliza consultant, ili watu wa NEMC waje kukagua ripoti ya consultant nao unalipa gharama zao za kuja site.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo wakiridhika kukupa leseni, unalipa shilingi milioni kumi (Sh.10,000,000/=) na baada ya hapo utaendelea kulipa ada ya kila mwaka shilingi laki tatu (Sh.300,000/=). Utakuta inagharimu zaidi ya shilingi milioni ishirini na tano kupata Leseni ya NEMC kwa kituo kimoja na bila kujali kipo kijijini au mjini. Je, kwa faida ya Sh.90 kwa lita kuna biashara hapo, bado gharama za kodi, upungufu wa mafuta, mishahara na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii nimetoa mfano kwa kituo cha mafuta lakini ndiyo hivyo hivyo kwa hoteli au viwanda ukitaka kupata leseni ya NEMC. Kwa mfano huu mdogo, Wizara hii inachukua hatua gani kuhakikisha mamlaka zilizopo zinafanya kazi zake kwa ufanisi na siyo kuwa wakusanya faini na watoza kodi au Wizara hii ni jina tu? Kwa nini chochote kinachofanywa na mamlaka kuhusu biashara ndani ya nchi hii kisihusishe Wizara kwanza kabla ya sheria na kanuni zao?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba majibu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kwanza ya kuchangia. Kwanza nimpongeze dada yetu, Waziri wa Afya pamoja na msaidizi wake, Ndugu yetu Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla kwa kuwakilisha hotuba yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita katika sehemu chache tu na za muhimu sana kwa watu wetu wa vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na huu Mfuko wa Afya ya Vijijini (CHF). CHF ukiiangalia sana muundo wake na jinsi ilivyoanzishwa iko ki-theory sana. Ukiiangalia utajua labda huu mfuko ni ukombozi wa wananchi wanaoishi vijijini. Lengo lake kwa wanachama wake ni kuchangia ili kupata huduma za dawa pamoja na vifaa vinavyohusiana na tiba.
Ukiangalia kiundani katika practical hakuna kitu kama hicho. Utakuta vituo vya afya au zahanati zinachangia Mfuko huu wa CHF, zile pesa zinakwenda CHF makao makuu, badala ya watu kuletewa dawa hawaletewi dawa, utakuta wanaletewa condom au vitu vingine tu havina hata msingi, hata chanjo za watoto vijijini zinashindikana. Mimi sioni huu mfuko wa CHF maana yake nini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiangalia katika muundo wake kwa kweli una maana kubwa sana. Mwanachama wa CHF akienda kwenye kituo cha afya au kwenye zahanati kitu atakachoambulia kupata pale ni kipimo tu kama akiambiwa ana malaria hicho kipimo kidogo basi ameshamaliza, zaidi ya hapo dawa nenda kanunue, hakuna dawa. Sielewi mpango huu wa CHF una faida gani!
Mimi nitoe ushauri kama huu mpango wa CHF umeshindikana kwa nini msiunganishe hii mifuko ili mfuko wa bima uwe mmoja? Nina maana kwamba CHF na NHIF uwe mfuko mmoja, kuna faida gani ya kuwa na mifuko mingi ambayo haina faida yoyote? Hilo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kuhusu madaktari, kwa mwaka wanahitimu zaidi ya madaktari 1,000 lakini wanaoajiriwa hawazidi 300. Halafu tunakwenda vijijini na kwenye vituo vya afya tunawaambia watu wachangie kujenga vituo vya afya na zahanati. Kwa mfano, pale Gairo kuna zahanati zaidi ya sita zimeshajengwa, vituo vya afya viwili mpaka leo havina Muuguzi wala Daktari sasa maana yake nini? Tukija hapa tuna kazi ya kuambiwa tu tuwashawishi wananchi. Mimi kama Mbunge kwa kweli sasa hivi nimechoka simshawishi mtu hata mmoja ajiunge CHF, namwambia kwanza achana nayo nenda na hela yako cash, haina maana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba dada yangu aliangalie sana hili kwa sababu ni Waziri mgeni uwe makini sana na suala hili. Tunapozungumzia habari za afya za watu basi Madaktari muwape ajira na mhakikishe kwamba wanafika Wilayani. Kwa mfano, Wilaya ya Gairo mpaka sasa hivi haina Madaktari kabisa na Wauguzi. Mwaka huu mmetupangia Wauguzi wanne Wilaya nzima na hao Matabibu watano Wilaya nzima kwa kweli haina maana ya aina yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu nataka kufahamu, hii Wizara ya Afya iko tu kazi yake kutengeneza sera au iko kwenye majukumu? Maana mimi naona iko kwenye kutengeneza sera kwa sababu yenyewe inapohudumia inahudumia mwisho Hospitali za Rufaa tu, lakini ukija huku kwenye Hospitali za Wilaya utakuta ziko chini ya Halmashauri. Ukiuliza ambulance, utaambiwa ambulance kwani ninyi hamna mapato? Sasa hizi Halmashauri zinatakusanya wapi mapato ya kutosha wakati ambulance moja ni zaidi ya shilingi milioni 150 au 200! Hizi Halmashauri zitawezaje kupata vitu vyote hivi, zihudumie elimu, maji, majengo yao na ambulance? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kufahamu maana inaonekana hii Wizara ingekuwa Bodi tu ingekuwa hamna tena Wizara ya Afya iwekwe Bodi fulani tu basi kwa sababu ukiangalia huduma zake zote ziko chini ya TAMISEMI. TAMISEMI ndiyo imebebeshwa kila aina ya mzigo. Ukiangalia TAMISEMI siyo imebebeshwa mizigo tu imebebeshwa hata majitu mabomu mabomu yale yote yasiyojua kazi yote yako TAMISEMI, sasa kuna huduma gani hapo itakayofanyika ya ukweli? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nazungumza kile kitu cha ukweli, ndiyo ukweli huo. Huduma za afya ni mbovu na utakuta Halmashauri za Wilaya kama kituo cha afya kiko mjini manesi pamoja na upungufu kama wako watano au sita, utakuta wanne wako kwenye kituo cha mjini, kule kijijini utakuta wakati mwingine kama kuna Daktari mmoja ndiyo huyo mpaka anazalisha akina mama, tunawadhalilisha akina mama. Sasa mimi sielewi, kama iko kisera, mimi nataka kujua kisera tu kwa sababu ukija kwenye TAMISEMI ndiyo ina mambo yote ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia pale Gairo, namshukuru sana Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii alizungumza kwamba unaweza ukatoka hapa unaenda Morogoro ukapata accident, sasa ukiangalia katikati ya Tumbi ya Morogoro hapa ni Gairo, kilomita 131 kutoka Dodoma na kilomita 131 kwenda Morogoro, kila siku tunapiga kelele pawepo na madaktari na ambulance lakini mpaka leo hakuna. Mimi nashangaa hapa mkitoa mifano mnatolea Kanda ya Ziwa tu sijui wapi hakuna madaktari mbona hamtolei mfano Gairo, Gairo Madaktari hawapo na ndiyo barabara kuu hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee MSD. Naomba pesa zao wanazodai walipwe zaidi ya shilingi bilioni 130, wapewe hela zao ili watoe huduma safi. Ule mpango wa MSD kuweka maduka ya dawa kwenye Hospitali ya Rufaa isiwe hivyo, waweke maduka yao mpaka Hospitali za Wilaya. Kinachotakiwa kufanyika pale wao wapewe nafasi tu lakini waweke maduka yao. Wanaopenda huduma za afya siyo kwamba wako mijini tu, wako vijijini na Wilayani basi angalau wapewe nafasi kwenye Hospitali ya Wilaya ili nao waweke maduka ili wananchi nao wa sehemu za vijijini na kwenye Halmashauri wapate huduma za MSD. Naona kila atakayezungumza au kwenye vyombo vya habari utasikia MSD imeweka duka Muhimbili sasa hivi ina mpango wa kuweka Morogoro, ina mpango wa kuweka wapi, huku Wilayani vipi au MSD haiko Kitaifa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaki kugongewa kengele ya pili nafikiri kwa haya machache nimeeleweka, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa namshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake ambayo imegusa kila sekta na kila kona ya nchi yetu. Vile vile namshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na wasaidizi wake kwa kuwezesha vijana zaidi ya 1,000 kupata ajira katika Kiwanda cha Nguo cha Morogoro wakiwepo vijana wa Wilaya yangu. Nawashukuru kwa hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo nitaanza na pombe ya viroba. Najua wengi watashangaa, watasema huyu jamaa Muislam; na najua wale watu wanaopenda kuweka maneno kwenye midomo ya watu wengine, wataweka maneno mengi. Siyo kwamba naunga mkono watu wanywe viroba, napinga na viroba visiwepo kwa sababu vinaathiri hali za watu na hata sasa hivi watu wananenepa baada ya viroba kuacha kuwepo mitaani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nashauri kitu kimoja; kwa sababu katika bajeti ya mwaka 2016 wakati tunaweka kodi katika vinywaji na katika bajeti yetu na mapato yetu, hata viroba navyo tulivihesabu na vilikuwepo kihalali.
Mheshimiwa Spika, ni kweli pombe hii inadhuru watu, lakini naomba au nashauri kwa wakati mwingine utaratibu utakaotumika kuzuia vitu kama hivi, basi uchukuliwe kwa umakini sana. Waanze kuzuia kwenye production ili huku zinakouzwa, basi ziishe.
Mheshimiwa Spika, mimi ni mfanyabiashara sikuingia hapa kama nachunga ng’ombe wala kama mkulima au nani, nimeingia kama mfanyabiashara.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni lazima nizungumze habari ya biashara na kama sisi Wabunge wa vyama vyote hapa tusipozungumza wenyewe basi tujue biashara kwenye nchi hii itakufa. Kwa sababu mtu amenunua mali ya shilingi bilioni moja, shilingi milioni 300 halafu amenunua kisheria, ana risiti zote za TRA na amelipa kodi leo unakuja unamwambia kuanzia sasa hivi hii mali ni haramu. Tayari ameshaingia kwenye matatizo amekopa katika mabenki huko na biashara yake imeshafungwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba mnielewe vizuri, siungi mkono unywaji wa viroba lakini utaratibu uliotumika naomba usirudiwe tena. Kwa sababu leo anaweza akaja mtu hapa akasema tena kitu kingine kikaleta madhara. Kwa hiyo, tuangalie utaratibu mzuri wa kufanya mambo haya. Hilo la
kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la pili, wewe mwenyewe Spika ni shahidi kwa sababu kati ya watu wanaoathirika na jambo hili ni mimi na wewe. Wakulima wetu ambao wanalima katika upande wa Wilaya ya Kiteto wamekuwa wananyanyaswa kupita kiasi hasa na vyombo vya dola ambavyo viko pale wilayani na mkoani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika Mbuga ya Murtangos wanasema ile ni hifadhi. Hawawazuii watu kulima wakati wanakwenda kulima, wanangoja mahindi yameshafika labda mwezi mmoja, wanakuja ng’ombe wanachungia mule wakienda wale wakulima kushtaki na wao wanawekwa
ndani. Mpaka sasa hivi ninavyozungumza wapo watu wa Pandambili ambayo ni wilaya yako na wapo watu wa Gairo wapo ndani mpaka sasa hivi na wale Wamasai ambao wanachungia kwenye ile mbuga wapo nje, hao jamii ya kifugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama mnataka kuzuia, hatukatai kuzuia, kwa nini msizuie wakati wanalima mnakuja kuzuia wakati mahindi yameshakuwa makubwa? Kama hiyo ni hifadhi, hifadhi gani ambayo ng’ombe wanachungwa lakini wakulima hawaruhusiwi, hiyo ni hifadhi ya aina gani?
Naomba viongozi wetu na Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu ambaye ni mtiifu na msikivu akienda pale asisikilize masuala ya wilayani wala mkoani, aangalie tu yeye mwenyewe atume watu wake wachunguze atapata jibu ambalo lipo sahihi. Akitaka na majina nitampa ya wakulima wetu ambapo zaidi ya heka 3,000 watu wamechungia na wako nje halafu tunasema zaidi ya asilimia 80 ya wananchi ni wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata hizi pesa, watu wanasema tu, pesa zimepotea, hamko kwenye mzunguko wa kibiashara, ukiujua vizuri mzunguko wa kibiashara pesa imepotea kwa sababu wakulima wa mwaka jana hawajapata mazao. Hawa wakulima wadogowadogo wangeweza kuvuna
mwaka jana kila mtu hapa angefanya biashara na mzunguko wa pesa ungekuwa mkubwa. Tunasema tu aah Magufuli kazuia pesa, Magufuli kafanya nini, Serikali imezuia pesa, wakulima hawakuvuna mwaka jana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi ni mfanyabiashara sasa hivi nina zaidi ya miaka 25, najua mwaka wowote mkulima mdogo anayelima heka mbili au tatu akipata mazao atakwenda kwa fundi cherehani atanunua sare, atakwenda kwa huyu atanunua maji, atakwenda kwa huyu atanunua
hiki, ndiyo mzunguko. Yule naye biashara yake ikitoka atapanda basi, ataenda Dar es Salaam, kwa hiyo kila mtu atafanya biashara. Wakulima hawa wasipopata pesa ina maana mzunguko haupo, kila kitu kitakuwa kibaya tu, tutalalamika tu. Hata ukiachiwa hizo pesa za benki, unasema
mkopo hakuna, hata ukiachiwa, security zenyewe unazo? Maana yake mabenki siyo rafiki wa mtu maskini, huo ndio ukweli.
Mheshimiwa Spika, kuna jambo lingine la matrekta. Tunashukuru matrekta 1,860 yale ya SUMA JKT yamekuja na waliwakopesha wananchi kwa kulipa asilimia 30. Hata kwangu Gairo pale nimepata matatizo makubwa sana maana niliambiwa Mbunge weka dhamana, nimeweka
dhamana nyingine badala ya kuandika jina la niliyemkopea limeandikwa jina Ahmed Shabiby ndiyo kakopa. Sawa watu wangu nawajua najua tu yatalipwa lakini wakati SUMA JKT anapewa auze matrekta hajui hata sheria za kuuza, kwanza na yeye mwenyewe akatafuta tena dalali mwingine ndio amuuzie. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, halafu baada ya hapo haya matrekta hata ukilipa hupewi kadi wala halina namba, kwa hiyo, linatembea tu kama mkokoteni wa ng’ombe. Tafuteni watu wote wenye matrekta haya, waliopewa kadi hawazidi 300. Mkulima akiomba kadi anaambiwa hebu soma engine number, wewe angalia namba yoyote bandika, sasa anabandika namba ipi, atakataje insurance? Kwa hiyo, matrekta yale hayana namba sasa sijui ni utaratibu gani. Halafu leo tena mnakwenda mnakamata, mnafanya kuangalia rangi, lile la bluu wanakimbiza wanakamata
yamejaa pale, hii ni dhuluma? Mkulima anataka umpe kadi yake akumalizie deni humpi, kwa sababu ameshaambiwa na wenzake waliomaliza madeni kwamba hatupati kadi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa matrekta yote ya Manyara, Tabora na Tanzania nzima kwa ujumla yamekamatwa halafu watu tunasifia tunasema hawa wameshindwa kulipa madeni, wameshindwa nini, jamani tusiwaangushe hawa wakulima wetu tuwaombee tena yaje matrekta mengine wakope, tuangalie kosa liko wapi. Naomba Waziri anayehusika aende akachunguze kama SUMA JKT wanazo registration cards za haya matrekta. Hakuna namba, hata insurance atakataje? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine ni maji. Leo maji nimeamua kuzungumzia chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Toka mwaka 2007, Gairo imepewa Sh.6,600,000,000, lakini kilichofanyika wamekwenda kuchimba visima vile vya maji tisa vinatoa maji lakini yale maji hata akinywa ndege anatapika. Haijawahi kutokea. Wamekwenda kupima kwa Mkemia hayafai. Nimewapa ushauri wa kila aina hawajafuata ule ushauri, sasa miaka 10 na mimi Mbunge nakwenda hiki kipindi cha tatu, kwa hiyo, hata wale wananchi wangu kwa sababu wengine hawana uelewa wanasema Mbunge amekula pesa alipewa yeye hela za mradi kafanyia biashara zake sasa maji hakuna. Nimewaambia basi huu
mradi kama mmefeli hizi pesa zilizobakia kuna chanzo cha maji kiko pale karibu tu, kilometa kama 25, nunueni basi mabomba tupate maji ya mserereko lakini imekuwa hadithi. Ukiongea hapa unajibiwa hiki lakini hakuna linalofanyika. Tunakwenda kwenye uchaguzi hiyo miaka ijayo, pesa zipo lakini hazitumiki, ndiyo maana leo nimeamua kumwachia Mheshimiwa Waziri Mkuu alifuatilie suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu niende naye Gairo, hapa na Gairo saa moja tu, aende akashuhudie matenki yamejengwa, mitandao ya matenki ipo lakini kuvuta tu maji kupeleka pale sasa hivi mwaka wa kumi hakuna kinachofanyika. Ndiyo na pesa ipo. Kila siku ukiwaambia kaleteni maji ya mserereko hakuna kinachofanyika. Wamekuja watu ambao wameletwa na Wizara ya Maji wamechora ramani wamefanya kila kitu lakini bado hatupati maji. Kila nikiongea na Mheshimiwa Waziri anasema subiri kidogo safari hii tayari wewe maji umepata, sasa maji nimepata yako wapi, haya maji nitasema mpaka lini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama unavyojua Jimbo la Gairo watu wanalima sana, wanapata sana mazao lakini tatizo maji yake chini ya ardhi yako mbali na hasa pale Gairo Mjini huwezi kupata maji matamu hata ufanye nini, utapata tu haya maji ya chumvi. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu safari hii angalau aje Gairo pale kwa sababu yeye kidogo wakimwona na akifahamu maendeleo ya pale ya miaka kumi na asilimia iliyofikiwa mpaka sasa hivi kwa kuona kwa macho itasaidia. Ndiyo maana leo hili suala la maji nimeona naweza nikakosa nafasi kwenye Wizara ya Maji nimuachie Waziri Mkuu ili siku nyingine mwakani kama hakuna maji mimi nitachangia tena Wizara hii hii nimuulize Waziri Mkuu imekuwa vipi. Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuwa mmoja wa wachangiaji. Kwanza niunge hoja mkono na niishukuru Wizara hii na niwashukuru Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na wote wanaohusika kwenye Wizara hii. Labda na mimi sana sana ni kutoa ushauri na ushauri wangu utajikita katika sehemu za biashara hasa katika wafanyabiashara wa kati na wa chini na hii katika ushauri tu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanza nitaanza na mashine za EFD kwa sababu tupo kwenye Wizara hii ya Bajeti na Fedha. Hizi mashine za EFD lazima zitafutiwe mikakati katika hawa wafanyabiashara wadogo na hata wale wakubwa ambao wanatumia mashine za EFD. Mashine za EFD sasa zimekuwa kero sasa sijafahamu ni makampuni yaliyopewa hii tender za ku-supply kwa sababu utakuta mtu ana duka dogo lakini ile mashine kila siku ni mbovu na sasa imekuwa ni mataji kwa wale watu wenye mashine, utakuta sasa unatakiwa ubadilishe mashine leta hela nyingine, uiboreshe lete pesa nyingine. Sasa hii imekuwa tatizo kwa wafanyabiashara kwa hiyo zingaliwe upya. Hawa-supply au model ya hizi mashine zinazotumika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kitu kingine ni kwenye biashara ya transportation na hasa malori, mimi sina malori. Lakini nafikiri uchunguzi haujafanyika kwa kina kwamba sasa hivi tunazidi kupoteza Watanzania wote ambao wanafanyabishara ya transportation ya malori. Mheshimiwa Rais pamoja na sisi Wabunge tulijitahidi sana wakati ule wa VAT na ile single customer ili bandari yetu ifanye kazi, lakini sasa hivi bandari yetu inafanya vizuri sana, custom pale wanafanya vizuri sana, lakini transportation yote wanafaidika watu wa nje Burundi, Zambia na Rwanda.
Mheshimiwa Spika, watu hawalifahamu lakini sasa hivi magari yote ya Watanzania yanasajiliwa Zambia, Rwanda Burundi na Uganda. Ukitaka kufanya uchunguzi huo kaa barabarani zikipita gari za transit nne; tatu au mbili zina namba ya Rwanda, Burundi au Uganda au Zambia na kwa ushahidi zipo gari zinakuja mpya gari 100/gari 50 zinaenda Zambia zinasajiliwa lakini za Watanzania zinakuwa namba ya kule, kwa hiyo, kodi yote inalipiwa nchi za nje. Na ukitaka kujua kwa akili nyepesi ukiangalia gari za Rwanda, Rwanda wanatumia left hand drive utaona gari ina right hand drive unajua hii gari ya Mtanzania.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo gari zote za transit sasa hivi zinahamia nchi jirani, tatizo ni nini? Lazima hapa tujiulize hapa kuna shida gani. Nilikuwa naomba watu wa TRA hasa ndugu yangu aliyepewa ukamishna sasa hivi kwa sababu najua ni msikivu, ajaribu kukaa na hawa wafanyabiashara angalie kuna shida gani hadi watu sasa wanahama kupeleka kodi kwenye nchi zingine na nilikuwa nashauri sehemu kama hii ni lazima waweke limit kwa mfano kama income tax, najua ukiweka kwenye mambo ya transportation iwe mabasi iwe malori kwamba kodi yetu tukipiga mahesabu kwa jumla ya transportation zote zilizopo Tanzania idadi ya magari labda tunapata kiasi fulani, lakini tuwekea limit kila gari iwe inalipa kiasi hiki najua kabisa mtapata zaidi ya mara kumi ya kodi ya sasa hivi. Kwa sababu wafanyabiashara watanzania ukitaka wafanye hesabu saa nyingine hata tunalaumu TRA, lakini wafanya mahesabu wenyewe wa Tanzania nao ni fake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, unaweza ukawa mfanyabiashara unafanyiwa mahesabu unampekea consultant wa mahesabu anakufanyia mahesabu anaonesha unadaiwa wewe sasa TRA atafanya nini? Wakati huo unayemuamini kwenye mahesabu yeye ndio aliyekufanyia mahesabu anaonesha unadaiwa wewe sasa TRA atakwambia hudaiwi? Kwa hiyo, lazima tuangalie hizi biashara watu wanazozifanya wengi ni watu wa kawaida na watu wa kati. Kwa hiyo, lazima tuangalie namna gani yakuwasaidia na namna gani Serikali itakusanya kodi yake bila kupunguza kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitakuja kwenye EFD za kwenye mafuta, hizi ni wizi mtupu kwenye petrol station na wewe nafikiri ni sahidi kwa sababu unafanya hii biashara, hizi ni za wizi na ninajua kabisa Dkt. Mpango, Ndugu Kichere...
MHE. RICHARD M. NDASSA: Kichere hayupo.
MHE. AHMED M. SHABIBY: ... Ndugu Kidata na wote walikuja hawakushiriki katika mchakato wa kuleta hizi EFD walikuta ule mchakato upo, hatuwezi kuwalaumu hao watu.
Mheshimiwa Spika, lakini unanunua lile dubwasha kwa dola 3,000 mpaka 5,000; unalifunga kwenye petrol station kwa mwaka unalipa shilingi 1,200,000 kwa ajili ya yule fundi. Halafu mkoa mzima kuna fundi mmoja, halafu ikiharibika unatoa ripoti TRA kwamba mashine imeharibika, unaendelea kuuza, ile mashine haifanyi kazi, kesho na kesho kutwa anakuja fundi anakwambia kadi imekufa, anachukua shilingi 300,000 kwenye kila pump, yale makaratasi yanayotumika pale ni ya mamilioni kila siku halafu haina faida yoyote kwa sababu EWURA wanatoa bei, tuna chombo cha Serikali kinaitwa EWURA kinajua kabisa mfanyabiashara wa rejareja kwenye kila lita anapata kiasi gani.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano mtu anaendesha Kituo cha Engen au Total au Oryx au Gapco au nani anajulikana kabisa kwa lita anapata shilingi 72. Huyo mwendeshaji wa kituo na mafuta yote yanatoka depot. Kwa nini msichukue huko mkate kwenye ile profit ya huyo muuzaji kwa nini msikate pesa yenu huko? Mkatie huko Dar es Salaam kama hii ni shilingi 72 tunachukua tunakata shilingi 15 kwa lita, kusanyeni huko. Kwa sababu mnapotaka kukusanya mafuta yakuja kwa muuzaji wa retail, sasa hivi Wilaya zote kuna boda boda na kuna nini na kuna watu wanauza kwenye mapipa na wanashindwa kudhibitiwa, mtu wanamshushia kutoka kwenye tenki la gari, ana mapipa yake 20 chumba cha 4,500 yanaenda moja kwa moja kwenye mapipa.
Mheshimiwa Spika, mtu ana malori yake, anashusha gereji, haipitii kwenye petrol station, sasa hiyo EFD inafanya nini? Kwa sababu mtu anaamua kuiba anavyotaka yeye, sasa hiyo EFD inafanya nini? Leo mimi nina mabasi, naamua kushusha gereji kwangu na EFD gereji? Kwa hiyo nimechukua mafuta lakini hayakupita kwenye EFD nataka kumuuzia mtu anaenda kuuza kwenye mapipa natoa kwenye gari direct moja kwa moja mpaka kwenye mapipa, kuna EFD? Napeleka shambani kuna EFD? Kwa hiyo kateni huko angalieni kwamba katika vituo vyote tunapata milioni ngapi na tukikata hapa huku basi hatupotezi wala hatupunguzi yale mapato tunayopata.
SPIKA: Mheshimiwa Waziri wa Fedha ukilichukua hilo utapata hela nyingi sana, hizi EFD machine yaani ni kupoteza muda tu kabisa kabisa. Endelea Mheshimiwa Shabiby. (Makofi)
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, ndio cha msingi.
SPIKA: Kata kule kule Dar es Salaam upate hela yako.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, juzi nimekwenda Kiteto unakuta fundi anaambiwa amemuita fundi ana wiki tatu hajafika kutengeneza mashine za EFD wakati kuna njia rahisi kabisa za kukusanya mapato. Halafu sisi tunawashauri na tunasikia kwa wafanyabiashara wenzetu ili Serikali ipate fedha, basi tunaomba muwe wasikivu hata kwenye haya magari wangeamua tunasema labda kila gani fulani linakwenda transit tunachukua kodi yetu milioni mbili au tatu kwa mwaka wewe shauri yako.
Mheshimiwa Spika, sasa utakuta mtu akiwa ana gari nne hafanyi hesabu, analipa labda milioni moja, mwenye gari tano kwenda mbele anafanya hesabu analipa milioni tatu. Mtu akifikia uwezo wa kununua gari huyo ana uwezo wa kulipa kodi. Kuna haja gani ya kumwambia asifanye hesabu au kama mtu anafanya hesabu afanye lakini pawe na bei inayoeleweka kwamba gari hii mtaondoa hata vyanzo vingine sababu ya kutoa rushwa si kukamata. Hata uweke wakamataji wawe wa wangapi utakamata wote? Sababu ya utoa rushwa ni kutoa vyanzo vya rushwa, kwamba nini kinasababisha hapa ndio unatoa rushwa. Kwamba hiki kinasabaisha rushwa tukiweke mazingira kitakuwa hakina rushwa, hiki kina sababisha kero hii tukiondoa kitakuwa hakina kero, lakini tusitegemee TAKUKURU, TAKUKURU atakamata watu wangapi? Hii kitu haiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, haya kuna ile watu hapa mwaka jana ilifutwa ilikuwa milioni tatu sijawahi kufanya hiyo. Wala kwa mimi siipendi kuweka jina langu kwenye gari, lakini kuna watu wanapenda kuweka majina kwenye magari, unakuta mtu anaandika King Musukuma, nitolee mfano Musukuma gari yake imeandikwa King Musukuma alikuwa nalipa shilingi milioni tatu lakini wakaja wakapandisha, sasa mwingine haweki lile jina la kwenye plate namba kwa sababu labda ni starehe. Mwingine ana kama akina dada hapa Wabunge na wadada wengine walioko mtaani gari zao wanazitumia vizuri ana TZB hataki hiyo gari ionekane ni TZB anaamua kuandika jina lake pale ili afute ile namba gari isijulikane kama ni gari zamani au gari mpya. Kwa sababu gari yake bado ni nzuri. Wewe unaenda unaweka kodi kubwa, sasa hata nikiangalia sasa hivi kama mapato yapo pale pale lakini waliosajili ni wachache, eeh, tuweke bei ndogo watu wawe wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna yale bango yalikuwa kwenye malori hatuna sisi viwanda, lakini mabango ya kwenye viwanda hata sasa hivi ukiangalia unasema malori ya bakhresa yako wapi mbona hayapo, malori ya fulani yapo wapi mbona hayapo, sio kwamba hayapo yale mabango yalikuwekewa sijui milioni nne kwa mwaka ukiandika kwenye lori tu kwamba hii bidhaa fulani inauzwa unalipia milioni nne/ milioni ngapi sasa mwishowe watu wameamua kufuta tu wamebakiza magori mawili/matatu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, weka pesa kidogo upate mapato mengi. Kuna hii...
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Nimekuongeze dakika kidogo endelea Mheshimiwa Shabiby. (Makofi)
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Kwa hiyo, utakuta tunachotakiwa sisi kufanya tusizungumze sawa tunasema kwamba kuna biashara zimefungwa labda 1,000 zimefunguliwa biashara 14,000. Lakini biashara zilizofunguliwa 14,000 na zilizofungwa zipo sawa? Inawezekana biashara wamefungua 14,000, 12,000 lakini biashara za briefcase, mtu akenda BRELA kasajili, kaenda TRA kachukua clearance, kaenda Halmashauri kachukua leseni, kafungua biashara, lakini hata duka lenyewe hana. Ukingalia biashara zinazofungwa na zinazofunguliwa na kero nyingine haijatajwa kwenye bajeti hii watu tumeng’ang’ania kero za TRA, lakini kuna watu wengine wana kero kuliko hiyo TRA.
T A A R I F A
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Taarifa Mheshimiwa Susan.
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante naomba nimpe taarifa mzungumzaji Mbunge Mheshimiwa Shabiby kwamba anasema kwamba biashara za kuandika bango na hii imepoteza hela nyingi sana katika nchi yetu kwa mfano mtu ana salon yake akiandika bango ama hoteli wanam-charge hela nyingi, matokeo yake watu wanafuta. Kwa hiyo biashara nyingi hata sasa hata hoteli, maduka, salon wote wameondoa mabango kwa hiyo TRA wanapoteza hela nyingi sana. Bora wapunguze bei ili hawa watu waendelee kuweka bango katika biashara zao. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Shabiby ilikuwa ni taarifa kwako tu.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, naipokea kwa sababu ni taarifa ya kujenga na tupo pamoja. (Makofi)
Kwa hiyo sisi tunaishauri TRA na nina uhakika kabisa hata watu wanapoizungumzia habari ya TRA lazima tuseme ukweli. Ukiangalia huko juu kwa Makamishna huko hakuna matatizo kabisa, huku chini na ndio maana Rais alisema. Hapa Dodoma mlikuwa mnashuhudia wenyewe mtu anakwenda anafunga duka anasema hapa kazi tu. Kumbe ana roho mbaya, huyo anakuwa ana roho mbaya na Rais Magufuli tu wala hana kitu kingine, hapa kazi tu tumetumwa, wanasema.
Mheshimiwa Spika, lakini sasa hivi bahati nzuri tunashukuru kuna Meneja wa TRA amekuja mpya hapa Dodoma ameondoa hilo tatizo, kwa hiyo, mimi ushauri wangu ni huo. (Makofi)
SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Shabiby.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana naunga mkono hoja ahsante. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili nami kuwa mmoja wa wachangiaji katika hotuba yetu ya leo ya mipango. Katika kuchangia nitajikita kwenye vile vitu ambavyo vinaleta impact ya haraka. Mipango ya haraka ambayo pesa yake inapatikana kwa haraka ambayo italiingizia Taifa faida kwa haraka. Nitachangia vitu viwili, nitachangia utalii na kilimo, nikipata nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika hotuba ya leo inaonekana kabisa wazi kwamba, sekta ya utalii ni ya pili kwa uchangiaji kwa Taifa kwa sababu, inachangia asilimia 17.5, lakini ukiangalia katika mpango wake wa miaka mitano katika hotuba unasema kwamba, itakua hadi kufika asilimia 28. Sasa ukiangalia katika sekta hii ambayo kuna nchi zinaishi kwa kutegemea utalii peke yake kwa mfano, nchi nyingi sana zinategemea utalii hata hapo ukichukua hiyo Seychelles waliyokuwa wanaitajataja hapo, ukiangalia hata Ufaransa asilimia nayo inategemea utalii kama watu hawafahamu, Misri, Thailand, Morocco. Sasa nchi kama Tanzania ambayo uwekezaji wake katika utalii hauna gharama kwa sababu vitu vingi tayari ni vya asili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika vivutio, Tanzania ni nchi ya pili ukitoa Brazil, lakini hakuna mkakati wowote wa kutangaza utalii kwenye hii nchi na hakuna mkakati wowote wa kuonesha kwamba, utalii unaweza ukachangia zaidi ya asilimia 80 ya mapato ya nchi hii.
MWENYEKITI: Chief Whip, wakati Mheshimiwa Shabiby anazungumzia jinsi ambavyo sekta ya utalii ni muhimu kiasi hicho, humu kwenye ukumbi hamna cha Waziri wa Utalii wala Naibu wake, wana yao tu. Endelea Mheshimiwa Shabiby.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Sasa ukiangalia nini tunakwama? Tunakwama sana kwenye advertise, kwenye utangazaji. Hatutangazi kabisa utalii kwenye hii nchi wala hakuna mpango wa kutangaza. Kwa hiyo, ushauri wangu kwenye hizi Balozi zetu lazima pawepo na wale commercial attaches lazima wawepo. Tunaita muambata wa kibiashara kwa sababu, ukiweka muambata wa kibiashara kwenye kila ubalozi utakuwa unatangaza utalii, unatangaza uwekezaji, unatangaza na biashara nyingine kwa hiyo, tunakuwa na watu wa diplomasia ya uchumi ndani ya zile balozi kwa hiyo, tunakuwa tunaangalia nchi. Kwa mfano, nchi kama America tunahitaji watalii, basi tunampeleka muambata yule ambaye yeye anakuwa ni mtaalamu wa kutangaza utalii. Tunaangalia nchi fulani tuna mawasiliano nayo labda kwa ajili ya kilimo, tunampeleka muambata wa kiuchumi ambaye anahusika na kilimo, kwa hiyo, tunakuwa tunafanya hivyo. Hiyo itasaidia kuutangaza utalii wetu vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia leo hii mbuga ya Serengeti ni mbuga bora duniani, lakini haifahamiki kama Masai Mara ya Kenya. Sasa hapo unaweza ukajiuliza ni kitu gani kwa sababu, watalii wengi wanaokwenda Kenya wanakuja kwa ajili ya kuangalia Masai Mara ndio baadaye waje Serengeti au waje Kilimanjaro. Hata Kilimanjaro inatangazika sana Kenya kuliko Tanzania kwa hiyo, tunachezea na hapa ndio mahali ambapo pana pesa kabisa nyingi. Mimi huwa sitaki kutoa ile mipango ambayo itafanyika huko ya maneno maneno, hapana, huu ni mpango ambao uko wazi na hii ni hot cake kabisa, haina shida kwenye hii pesa ya utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia leo Brazil kwa nini imekuwa ya kwanza duniani, ni kwa ajili ya utalii wa bahari. Sisi huku tuna utalii wa asili, lakini leo bahari kama pale Kigamboni, bahari mali kabisa, beach zake ni safi, leo yamejaa magereji, yamejaa maviwanda, yaani hata mpango wa kutumia ardhi haueleweki. Mimi Mbunge niko muda mrefu, hata hivi kusimama basi, maana saa nyingine mnaongea tu halafu vitu havitekelezeki. Sasa Mheshimiwa Waziri lazima aangalie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu watu wanalalamika kuhusu habari ya utalii sijui asilimia 10 hiyo iliyoongezwa kwenye utalii. Lazima vitu vingine watu wawe wazalendo, kumleta mtalii mmoja haya makampuni ya binafsi yanachukua dola 5,000, kwa hiyo, wewe kuongezewa dola 10 tu unapiga kelele utalii Tanzania utakufa, utakufa kwa msingi gani? Hauwezi kufa utalii kwa ajili ya dola 10, haiwezekani kitu kama hicho. Cha msingi tu ni kuutangaza utalii watalii waje wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi lingine katika utalii, lazima tuwe na regulations, private regulations, katika kama zilivyokuwa sekta nyingine. Leo ukija huku kwenye sekta labda ya Mawasiliano kuna TCRA, ukienda labda huku Uchukuzi kuna hawa wengine hawa sijui LATRA, ukienda kwenye Nishati kuna EWURA. Huku nako lazima kutengenezwe regulation ya private ili iangalie na kudhibiti maslahi pamoja na kuchukua hao wadau nao kuangalia watafanyaje, ili utalii uendelee kukua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye masuala ya kilimo; hii lazima watu mkubali, tunapanga vitu vingi sana, lakini bahati nzuri unanifahamu vizuri ni mkulima, mfugaji, mfanyabiashara, vyote nafanya. Nchi hii tusidanganywe na mambo mengi sana, kama tutadharau kilimo, kilimo tumebadilisha slogan za kila aina; kilimo ni uhai, kilimo sijui ni uti wa mgongo, sijui nguvu kazi, sijui kilimo kwanza, sasa hivi kilimo cha biashara, lakini mafanikio hakuna. Hata Mheshimiwa Bashe wakati anajibu mpango huu, mpango huu, mpango huu, wakati hela hazipo na hautekelezeki. Hii ni hadithi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tajiri namba moja wa Tanzania kwanza ni mkulima anayelima kuanzia nusu eka mpaka eka 50. Hii yote mnazungumza tu hela zimebanwa, sijui hela mtaani hakuna, kwa nini hamshangai mwezi wa Januari, Februari na Machi wakati mkulima yuko shamba ndio hela hamna ninyi? Si mjiulize? Ukiingia mwezi wa Januari, Februari na Machi, hakuna anayepanda basi, hakuna anayeingia dukani, hakuna anayenunua chochote na huko mabenki nako pesa hakuna, hakuna kila sehemu, lakini kuna mkakati gani? Kuna mpango gani wa kumnyanyua huyu mtu? Hakuna mpango wowote wa kumnyanyua huyu mtu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza Habari ya irrigation. Irrigation ya Tanzania tunaangalia tu mito kwa nini hatuangalii na nchi kavu kama Dodoma na sehemu nyingine? Tunatafuta dola, lakini tunapoteza dola kila siku ya Mungu kununua ngano. Tunapoteza dola kila siku ya Mungu, hizo alizeti tunasema viwanda, alizeti inayolimwa Tanzania inatosha kwa miezi mitatu tu alizeti imeisha, kwa hiyo, viwanda vinasimama. Ngano, kwa miaka hiyo ya Awamu ya Kwanza, Basutu, wale wanaotoka Arusha, mashamba ya Basutu yalikuwa yanalisha nchi nzima ya Tanzania ngano, leo hata eka moja ya ngano hailimwi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya Saudi Arabia hakuna mvua. Mvua inanyesha baada ya miaka mitano, inanyesha mvua mara moja, lakini wanalima ngano tani laki saba kwa mwaka. Mwaka jana kuja mwaka huu 2019/2020 wamelima tani laki saba. Hapa Tanzania kuna bahati ya mvua mpaka tunaichukia, eka mbili hakuna, halafu tunazungumza kitu gani? Halafu tunachukua hiyo hiyo pesa tunayoitafuta, dola, tunaenda kununua ngano ambayo tunaweza tukalima tukajilisha. Tunaenda kununua mafuta ya kula ambayo tunaweza kuleta hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango ya irrigation tusidanganyane wala tusipakane mafuta hapa, Wizara ya Fedha haitoi pesa kwenye Wizara ya Kilimo, wala tusitake kupambana, haitoi pesa kabisa. Hayo mambo ya irrigation ni maneno tu. Labda Wabunge wageni, kama hamjui, hizi hela zinazopangwa zote ukija kuangalia zimetoka robo au hata robo isifike. Sasa mipango ya Wizara itaenda vipi? Nawashangaa tunang’ang’ania tu TARURA, TARURA, kama kilimo hakuna, TARURA watabeaba nini huko kwenye mabarabara hayo? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda cha mwisho, nashauri. kodi ya mafuta inayotolewa…
MWENYEKITI: Wabunge wageni mnawaona Wabunge wenyeji wanavyochambua hoja? (Makofi/Kicheko)
Endelea Mheshimiwa malizia.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashangaa kitu kimoja, hii habari ya TARURA; watu wanazungumza tunatoa mazao yetu, yepi? Kama sio kupita sisi Wabunge kwenye barabara, wale wazee wameshazoea wanataka hela tu. Mwananchi akiwa na hela hata ukimpitisha shimoni hapa mradi kichwa kionekane yeye anaona barabara si ziko kama lami tu. Kinachotakiwa hapa ni kuwajengea mazingira wao kupata pesa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe ushauri, kwenye barabara hizi tunachangia shilingi 263 kutoka kwenye mafuta, kila lita moja na kwenye umeme tunachangia shilingi 50 kila lita; nashauri, mimi nina vituo vya mafuta na mafuta yanapanda na kushuka, kwa nini pale tusiongeze shilingi 37 iwe shilingi 300 iende kwenye kilimo ili iweze kuchukua hili eneo? Kwa sababu, kama kuna mtu mwingine na mimi mwenyewe nina mabasi na malori silalamiki kupandishwa mafuta, sasa nione mtu alalamike humu. Ipandishwe shilingi 37 iende kwenye kilimo, tunachangia tu EWURA, sijui nani TARURA, TARURA wenyewe hawa ni wezi tu mimi nawashangaa mnapiga kelele, barabara wanapata hela hawatengenezi lolote. Huku kuwatoa sasa hivi hawahusiki kwa Madiwani, wamekuwa Mungu mtu, nashangaa Wabunge hamzungumzi hapa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana TARURA sasa hivi Madiwani ndio wana mikakati ya barabara zile. Diwani ndio anayesema barabara ya kimkakati ni barabara fulani kutoka pale kwenda pale, lakini leo TARURA wamekuwa wao Mameneja wa Wilaya, Mameneja wa Mikoa wamekuwa kama Mungu mtu kwa sababu, hawawajibiki kwa Madiwani. Wabaki kwenye management, lakini lazima mipango yao irudi kulekule kwa Madiwani. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii kwa kuwa mmoja wa wachangiaji katika hoja ya Waziri Mkuu, lakini leo mimi nitachangia kwa upole sana na kwa ushauri tu angalau kidogo.
Mheshimiwa Spika, labda watu wengi hawajazungumzia au Wabunge wengi wapya lakini hawajaiona athari ya TARURA na RUWASA kwenye Wilaya zetu.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia muundo wa uliounda RUWASA na TARURA mimi sina shida nao sana na wala sina matatizo na Mameneja wangu wa Mkoa, mimi natoka Mkoa wa Morogoro wala wa Wilaya ya Gairo, wapo vizuri kabisa. Lakini ukiuangalia ule muundo unapishana kabisa na Katiba, Ibara ya 145 na 146 iliyoweka mamlaka kwa umma katika kuamua mambo yao katika Sheria za Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia leo wakati inaundwa TARURA ilikuwa kama technical agency, lakini sasa hivi yenyewe ndio imekuwa na mamlaka ya kila kitu. Utakuta Meneja wa TARURA wa Wilaya hawajibiki kwa chochote katika Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tatizo linapokuja sasa, kwa hiyo, Diwani amechaguliwa na wananchi kama mwakilishi kwneye Kata yake, na yeye naye ana maswali ya kuulizwa habari ya RUWASA kuhusu maji na ana maswali ya kuulizwa kuhusu barabara za TARURA, lakini anakuwa hana majibu ya aina yoyote. Na watu wa TARURA kwa mamlaka waliyopewa wao wanaamua barabara watengeneza ipi bila kushirikisha Baraza la Madiwani wala Mbunge na ukiona Mbunge kashirikishwa basi ujue hiyo ni hisani tu, umekaa naye vizuri Meneja wako, mnashirikiana, lakini akija Meneja kichaa na wewe ataamua kupeleka barabara kwa hawara wake na ya kwako ya kimkakati isipelekwe. (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, ipo sehemu hata kwa Mheshimiwa Kakunda pale Meneja wa TARURA kapeleka barabara guest kwake.
Mheshimiwa Spika, nilizungumza nyuma kidogo lakini sikupata nafasi ya kuichambua zaidi. Mama Samia juzi amesema kabisa sasa TARURA mtashirikiana na TAMISEMI, lazima sasa TARURA na RUWASA wa maji kwenye menejimenti zao sina shaka nazo, fedha zao wanavyokaa nazo na technical zao sina shaka nao, waendelee hivyo hivyo, lakini mipango mikakati yote ya bajeti ianzie kwenye Halmashauri za Wilaya. Barabara za kutengeneza zitoke pale kwenye Baraza la Madiwani, visima vya maji au maji yanatoka na kwenda wapi na kwenda wapi yaanzie kwenye Baraza la Madiwani, wao wawe watekelezaji, watoa fedha na mambo mengien yote. Lakini utakuta bajeti wanapanga, wanarudishiwa, hawasemi zimekuja shilingi ngapi, wanaanza wao, wewe una barabara ya kimkakati huku ina watu 10,000 wao wanaenda kutengeneza barabara ya watu 500.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hili jambo tusipoliangalia kwa kweli hawa TARURA na RUWASA wanakuwa sasa ni Mungu mtu kwenye Halmashauri, na ukiangalia na jiulize huyu Mkurugenzi wa Maendeleo sasa anafanya kazi gani kama anashindwa kumdhibiti Meneja wa TARURA au Meneja wa RUWASA Mkurugenzi wa Maendeleo wa Wilaya ni ni sasa, si mkitoe tu hicho cheo na mtupe sisi Wabunge tuwe Wabunge na Wakurugenzi wa Maendeleo.
SPIKA: Kwanza nikuongezee Mheshimiwa Shabiby, hao Mameneja wa TARURA na RUWASA wana mshahara kuliko huyo Mkurugenzi wa Maendeleo, yalivyo mambo ya ajabu.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Sawa kabisa na nalifahamu hilo.
SPIKA: Kamkurugenzi tu ka-TARURA yaani, tayari.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu aliangalie hili, hawa watu warudi na wawajibike, hivi leo TARURA anatengeneza barabara, RUWASA anatengeneza maji, halafu Diwani kupitia Baraza la Madiwani haruhusiwi kwenda kukagua, yaani anatengeneza yeye, anakagua yeye na yeye ndio kaamua, sasa Diwani anafanya kazi gani, Diwani leo kabakia na madarasa na zahanati. Sasa Diwani ana kazi gani na Mkurugenzi wa Maendeleo ana kazi gani kama anashindwa kumdhibiti TARURA na RUWASA? Tunaomba lirudi hili suala, menejimenti na fedha zibaki kwao kama mnasema Madiwani wanafuja fedha, lakini lazima wawajibike pale na akifanya vibaya baada ya ukaguzi wa Madiwani; Madiwani wawe na amri ya kusema huyu hafai. Nataka niseme na sisi Wabunge tukiwa kule kwenye Wilaya zetu na sisi ni Madiwani.
Mheshimiwa Spika, cha pili tunatafuta hela kila siku za TARURA, lakini wewe ni shahidi na Waziri Mkuu ni shahidi, aliyekuwa zamani Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kabla hajawa Waziri Madini Mheshimiwa Doto Biteko ni shahidi. EWURA kila lita moja ya mafuta tunayoweka wanachukua shilingi 17 mpaka 16 kila lita moja ya Mtanzania, hata jenereta ukiweka wanachukua fedha, kisingizio wanasema tunaweka vinasaba kwenye mafuta. Vinasaba kwenye mafuta zimeleta mzozo, wewe umevunja Kamati ya Nishati na Madini, na walikuja hata kwako wakusomeshe ukawafukuza. Ndio mjue kule kuna wezi, kuna baadhi ya Wabunge hapa walikuwa wanakula rushwa nje, nje, tena mkinikera nitataja, ila basi acha leo ninyamaze, kwa sababu ya kutetea huu wizi. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, sasa leo mkataba kwa yule mwekezaji kwa mwezi anachukua zaidi ya shilingi bilioni tano, ambapo kila mwezi tungejenga hospitali moja.
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
T A A R I F A
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Spika, nadhani allegation aliyotoa kwamba Bunge limekula rushwa ni allegation kubwa, mimi ningeomba tu kama wapo waliokula rushwa wawataje ili wengine tubaki na heshima zetu. (Kicheko)
SPIKA: Hilo nalikataa. Mheshimiwa Shabiby endelea. (Kicheko)
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, hiyo nimetoa onyo, sasa hivi wapya hamjala. (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, lazima tuliangalie, tunao TBS ambao ndio kazi yao, kwa nini wasipewe hii tender na TBS wanachukua fedha kutoka sehemu tofauti. Hii fedha shilingi 17 tuipeleke TARURA ili TARURA wafanye kazi vizuri zaidi. Profesa Muhongo pamoja na kuchambuliwa na Mheshimiwa Musukuma hapa lakini alishawaita, wakati ule ulitoa amri kwamba wafanyabiashara tukutane na Profesa Muhongo, EWURA walishindwa kujibu. Kwa sababu waliitwa watu wa TRA, watu wa TRA wakasema sisi tunadhibiti mafuta yetu, tunajitosheleza kwa asilimia 100. Kwa sababu kama gari ya transit inaenda Rwanda au Burundi tunaweka king’amuzi, tunaiona gari kila kona mpaka inafika.
Mheshimiwa Spika, nakumbuka mimi wakati ule EWURA inaanzishwa ilikuwa watu wasichanganye mafuta ya taa na dizeli na mafuta ya taa na petroli ndio lilikuwa lengo. Mimi ndio nilikuwa Mbunge pekee niliyeongea miaka mitatu hapa mpaka mafuta ya taa yakapanda bei, niliyechakachua nikashinda wao wakahama, wakaona ulaji huku umeisha, wakahamia sasa tunadhibiti transit na mafuta ya kawaida, ilimradi tu ulaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na yule jamaa anachukua five to seven billion per month. Huyo agent/mkandarasi aliyepewa kuweka hiyo.
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
T A A R I F A
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, huyu GFI anachukua shilingi 14 kwa lita, halafu kuna tozo zingine zote zilizopo pale sasa hivi zinafika shilingi 90; fedha inayotumika kwa siku kwa lita milioni 12 zinazouzwa ni shilingi bilioni moja na elfu themanini kila siku ya Mungu, kwa mwezi ni shilingi bilioni 32.4.
Mheshimiwa Shabiby endelea, tunapigwa vya kutosha. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Shabiby.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa yake ni nzuri sana.
Sasa hizo fedha zote zikichukuliwa na kupelekwa TARURA hatujapata mtaji? Na tukiongeza....
SPIKA: Yaani ni kutumbukiza tu hicho kinasaba tu hivi halafu ndiyo mabilioni yote hayo?
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, ndiyo.
SPIKA: Na taasisi ya Serikali hiyo TBS hawezi kuwa unanyunyiza hiyo? Endelea Mheshimiwa.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, nataka nikuambie kwanza mimi namiliki vituo vya mafuta.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Waziri afadhali, Mheshimiwa Kalemani.
T A A R I F A
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge lakini pia nimpongeze kwa hoja hii na tumeshatoa taarifa katika Kamati yetu kuwa ile kampuni inayofanya vinasaba tumeshasitisha mkataba wake na wala haifanyi kazi hiyo. (Makofi)
Kwa hiyo yale maeneo mengine nadhani yanaweza kuendelea kujadiliwa lakini la vinasaba tumeshasitisha na nimetoa maelekezo kuwa kazi hiyo ifanywe na Taasisi ya Serikali ya TBS. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa taarifa hiyo.
SPIKA: Mheshimiwa Waziri ahsante sana, tungekuwa na taarifa hiyo mapema ingetuokolea muda. Tunakushukuru sana na tunaishukuru sana Serikali.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, ahsante. Taarifa yake siipokei kwa sababu bado ipo na huyu niliyekaa naye hapa ana kampuni ya mafuta na leo wameweka. Sasa umesitisha mkataba huku unaendelea? Kwa naomba ukasitishwe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi nililalamika kipindi fulani hapa Bungeni wakaniandika kwenye gazeti, walikuwa wahonga mpaka baadhi ya magazeti, wakaandika Mbunge wa Gairo ni mwizi wa mafuta tunamdhibiti wakaja hawakuweka vinasaba kwenye mafuta yangu na mimi nikawafanyia timing gari sikushusha nikaenda kuchongea kwa Waziri Mkuu, ndio wakakimbia, Waziri Mkuu akanambia andika na nikaandika, kwa hiyo wizi wote unafahamika.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunaomba hawa watoke kwa sababu wameshakula fedha ya nchi siku nyingi, huyu Mheshimiwa Doto aitwe hapa alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ambaye sasa ni Waziri wa Madini alikuja kutishwa na mtu mkubwa kwa sababu wakati akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Madini alishikilia kidedea, akaja kutishwa mtu wa juu kabisa, akaambiwa wewe dogo tunakupoteza sisi ukiendelea kufuatilia hii kitu. (Makofi/ Kicheko)
Mheshimiwa Waziri nimekaa na wewe zaidi ya mara tatu lakini kila nikikueleza nilikuwa naona hunielewi, sasa nikaona napoteza muda wangu, kila nikimwelewesha. Hivi wewe unawekewa kitu, kwa mfano mimi nakodisha gari ya Mheshimiwa Shangazi, Mheshimiwa Shangazi anamtuma dereva wake aende depot anapakia mafuta ya Shabiby halafu dereva anawekewa mkojo wa punda anaambiwa hii ndio kinasaba hata haujui, halafu wewe unakuja kupima kwangu mimi, hapo uhalali upo wapi? Halafu hainekani kwenye rangi, wala haionekani kwenye chochote, wote ni upigaji tu, shilingi bilioni saba, bilioni sita na mpaka bilioni 30 alizosema Mheshimiwa Mbunge pale.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, Kuhusu Utaratibu.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Utaratibu umeshaisha. Nimeshamaliza. (Makofi/Kicheko)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuwa miongoni mwa wachangiaji wa hotuba hii ya TAMISEMI. Kwanza kabisa, niwapongeze Mawaziri wote wawili katika Ofisi hii ya Rais (TAMISEMI) na nasema bado mapema kabisa naunga mkono hoja hii isipokuwa tu kuna sehemu nataka nitoe ushauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ukurasa wa 16 tumeona kwamba sasa hivi Halmashauri zetu zote zinataka zitumie mfumo wa kielektroniki kwa ajili ya udhibiti na ukusanyaji wa mapato, jambo jema sana. Pia tumesikia hotuba mbalimbali za Mheshimiwa Waziri Mkuu ambazo zinahitaji sana msaada wa kutoka katika Wizara hii. Tunajua Serikali ina nia nzuri sana na ndiyo maana inaanzisha maeneo mapya kama vile mikoa na wilaya. Hata tunaposema kwamba hotuba ya Waziri Mkuu inahitaji msaada mkubwa kutoka TAMISEMI, kwa mfano ile kusema kwamba tutafuta Halmashauri zile ambazo hazikusanyi mapato yanayotakiwa, naiomba Wizara ya TAMISEMI imsaidie Waziri Mkuu, kwanza ianze kufuta wafanyakazi wabovu kwenye hizi Halmashauri za Wilaya kabla ya kufuta Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukianza kufuta Halmashauri kabla ya kufuta wafanyakazi wabovu mtakuwa hamjatutendea haki. Wafanyakazi kwenye Halmashauri ni wabovu, wamechoka hasa ukichukua kwa mfano Halmshauri yangu ya Gairo, kuanzia Mkurugenzi, Afisa Mipango, Mweka Hazina wote hakuna kitu. Sasa kwa kweli utategemea Diwani au Mbunge atatoa ushauri gani wa kitaalam ili hiyo Halmashauri iwe na mapato? Cha msingi kwanza tuangalie hawa watendaji wetu, watendaji ni wabovu, lazima tukubaliane.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata nikisoma kwenye hiki kitabu cha Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kusema kwamba kuna Halmashauri zingine zina hati nzuri, zingine hati kidogo za mashaka, zingine hati chafu, ukiangalia ukweli Halmashauri zote zina hati chafu tu. Huo ndiyo ukweli. Ndugu yangu Mheshimiwa Simbachawene nakujua uhodari wako, naomba uziangalie kwa umakini sana Halmashauri, ndiyo kwenye mchwa, wanapewa pesa nyingi na Serikali na zote zinaishia huko.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tujaribu kuziangalia hizi Halmashauri mpya kwa jicho la huruma, tumeanzisha Halmashauri nyingi sana. Nitoe mfano wa Halmashauri yangu ya Gairo toka ianzishwe mpaka sasa hivi haina hata gari. Wakati tuko Halmashauri mama ya Wilaya ya Kilosa tunagawana pale, tumepewa magari sita na mpaka sasa hivi linalotembea ni moja tu na lenyewe ukipanda kilometa saba unasukuma kilometa saba. Kwa hiyo, Mkurugenzi hana gari, kituo cha afya hakina ambulance, hebu mtufikirie, mtuonee huruma hizi Halmashauri mpya, tupeni vitendea kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika ukurasa wa 32 wa hotuba ya Mheshimiwa Simbachawene amezungumzia kuhusu habari ya Hospitali za Wilaya, hapa nchini Hospitali za Wilaya ziko 84 tu, wilaya 97 zinatumia hospitali za taasisi za umma au za dini. Kwa mfano, kama pale Gairo, Wilaya ya Gairo inategemewa na wilaya nyingi za pembeni kwa mfano Kiteto, Kilindi, Kongwa na Mvomero wote wanategemea sana pale Gairo lakini Gairo pana kituo cha afya na toka tuanzishiwe wilaya ile hatujapata fungu la aina yoyote la kujenga Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Gairo tuna kituo cha afya ambacho kinatoa huduma za hospitali pamoja na operesheni pamoja na vitu vingine lakini hatuna ambulance na Gairo ni kama Tumbi pale maana ni katikati ya Morogoro na Dodoma. Sasa mnataka mpaka kiongozi aje avunjike miguu pale ndiyo muone umuhimu wa Gairo kwamba panatakiwa ambulance? Tunaomba tupate ambulance na tupewe fungu la kijenga Hospitali ya Wilaya ya Gairo. Tumeshaomba sasa hivi ni zaidi ya miaka miwili, huu wa tatu, hatujapata. Tunaomba sana mtufikirie kwa hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwenye upande wa barabara, sasa hivi kila Mbunge anataka barabara yake ihame kutoka TAMISEMI ipandishwe hadhi iende TANROADS. Ilitakiwa TAMISEMI mjiulize ni kwa nini Wabunge hawataki barabara zao ziwe TAMISEMI au ziwe chini ya Halmashauri? Utakuta kilometa tano inayotengenezwa na TANROADS na kilometa tano inayotengenezwa na Halmashauri ni vitu viwili tofauti na ndiyo maana Wabunge wote hawataki barabara sasa hivi ziwe chini ya Halmashauri. Kuna maombi zaidi ya 3,400 ya kupandisha daraja barabara ili ziwe chini ya Barabara za Mikoa kwa sababu huku kwenye Halmshauri ndiyo kwenye mchwa wa kula pesa zote za barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata mgao wa pesa ukiangalia utakuta Wilaya kama ya Gairo na bahati nzuri Mheshimiwa Waziri anaifahamu vizuri sana Wilaya ya Gairo, anafahamu kuanzia Gairo mpaka Nongwe, anaijua vizuri sana milima yake ile ilivyo inazidi hata milima ya Lushoto. Mwaka jana tumeomba shilingi bilioni 1.5 tunakwenda kuwekewa shilingi milioni 400 na katika hizo mpaka sasa hivi imefika shilingi milioni 22. Sasa hata huyo mama aliyeko hapa TAMISEMI, anayeangalia hizi barabara za Wilaya sijui mmemuweka tu akae, hatembei au hajui mazingira ya hizi wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nashauri itengenezwe agency ambayo itakuwa ina mamlaka ya kuzisimamia barabara za TAMISEMI na kuangalia ubora wake ili Wabunge tusiwe tunaomba barabara nyingi ziwe chini ya TANROADS. Pawe na kitu ambacho kinasimamia ufanisi wa barabara vinginevyo tunakuwa tunaacha watu wanakula hela tu. Utakuta barabara ya TANROADS ina shilingi milioni 200, ya Halmashauri ina shilingi milioni 300 lakini ya TANROADS ina kiwango cha juu na hao hao Ma-engineer bado wapo, usimamizi mbovu, lazima kitengenezwe chombo ambacho kitasimamia hizi barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwenye bajeti hii, nikisoma katika hiki kitabu, Ofisi ya TAMISEMI, fedha za 2016/2017, ukienda kwenye kilimo hapa utakuta Wilaya ya Ilala imetengewa shilingi milioni 100, Wilaya ya Kinondoni shilingi milioni 148, Wilaya ya Temeke shilingi milioni 113, halafu ukija hapa Wilaya ya Gairo shilingi milioni 15, ina maana Temeke wanalima sana kuliko Gairo? Kinondoni, Ilala wanalima sana kuliko Gairo, haiwezekani! Angalia, ukisoma humu utakuta miji mikuu imewekewa hela nyingi sana za kilimo kuliko zile wilaya. Sasa nafikiri haya mambo tujaribu kuyaangalia hayako sawasawa kabisa. Hivi hapa kuna sehemu inalima viazi kuliko Gairo katika nchi hii, kuna sehemu inalima mahindi mazuri kuliko Gairo, acha mahindi ya wapi sijui huko hayakoboleki hayo. Kwa hiyo, naomba hili liangaliwe kwa umakini zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia Wizara yetu ya Ujenzi na Uchukuzi kwanza kabisa nianze kwa kusema kama sitopata haya majibu sahihi sitounga mkono hoja. La kwanza ni kuhusu barabara yangu ya Jimbo la Gairo ambayo inakwenda Jimbo la ndugu yangu Omari Kigua Kilindi. Ile barabara imekuwa na maslahi mapana kati ya Wilaya ya Kilindi, Gairo pamoja na Handeni na ni barabara nyepesi sana hata ya kutoka Dodoma kwenda Tanga, lakini ina kata nyingi sana za upande wa Gairo ziko ng’ambo ile ambayo inakaribiana na Wilaya ya Kilindi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ina madaraja ya Chakwale na daraja la Nguyani viongozi wote wa Wizara ya Ujenzi mmefika pale Waziri kafika, Naibu Waziri kafika, Katibu Mkuu kafika mara mbili mbili, lakini hakuna matumaini ya aina yeyote na mwaka jana yameondoa magari zaidi ya tisa na imeleta vifo zaidi ya nane, lakini barabara hii siioni kwenye huu mpango kila siku upembuzi yakinifu sasa huu sijui mpaka lini utakwisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninataka Mheshimiwa akija aniletee majibu ambayo ni sahihi, na kuna barabara ya kumalizia pale Gairo Mjini inayokwenda mpaka pale Halmashauri pamepakia kama kilometa 120 ya lami na sehemu nyingine ya kwenda kuunganisha na barabara kuu zimebakia kama mita 800 na ilipitishwa kwenye bajeti miaka minne lakini mpaka leo haijaguswa nataka na hiyo nayo nipate majibu ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ni mfanyabiashara na nimfanyabiashara nyingi lakini mojawapo ni ya usafirishaji wa abiria leo nilikuwa nipo hapa na ndugu yangu Kiswaga hapa alishalizungumza kidogo hili suala baada ya kuja watu wa Kanda Ziwa na sehemu nyingine kutaka kuanzisha mgomo kama mliusikia kipindi cha nyuma kama miezi mitatu nyuma wa mabasi walitaka kugoma lakini migomo mingine wasije wakagoma wafanyabiashara wa mabasi alafu wakaonekana kwamba ni maadui wa Serikali, si kweli kuna mifumo ambayo imeanzishwa na Serikali na hizi mamlaka
ambazo zimepewa kwenye Serikali ya wizi na ya ajabu kabisa ambayo haitekelezeki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano kwenye mabasi sheria inayoleta la LATRA sasa hivi unatakiwa ununue kwanza possy kile kimashine kile cha kuuzia kile, kila basi kile kimashine ni shilingi 1,000,000 mpaka shilingi 800,000 na kwenye ofisi zote kwa hiyo kama una mabasi 50 uwe na vile 50 na kama una ofisi 50 uwe na vile 50 kama huna kuna vendor anakukopesha unamlipa percent angalia wizi huo, halafu ukitaka kuuza kama una basi la abiria 57 unataka kumuuzia Mheshimiwa Kiswaga hapa tiketi kwanza ile mashine unahesabu abiria 57 labda 1,140,000 unaingiza kwenye ile mashine kwanza pesa, pesa yako wewe sio ya abiria, unakijaza kwanza fedha ya basi zima alafu ndio uanze kuuza hasa huoni kama ni kituko hicho? Halafu yaani bado ninadaiwa basi alafu tena kama nina mabasi 50 nitafute Milioni 57 za mtaji kila siku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, halafu ukishauza tiketi fedha haiji kwako inapita kwanza database inapita TTCL, inapita.... halafu wao ndio wanakupelekea benki, yaani fedha yangu, gari yangu halafu wewe unishikie fedha inatokea wapi hiyo. Hiyo biashara ya wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, haya ukienda benki ile statement unapewa nauli 5,000, 10,000 lundo namna hii kwa hiyo, ukizubaa kuangalia utakuta haijaingia wiki fedha, nilimwambia Naibu Waziri kaenda Tanga akashuhudia kuna mtu milioni 23 haijaingia, mwenyewe millioni saba hazijaingia kuna wengine milioni 10 hazijaingia, sasa kwa hiyo na hauna dashboard ya kuangalia kila siku kwa hiyo kila siku uwe una re-statement kwanza biashara gani duniani? Nafanya vitu ninauza halafu fedha yangu sipati, hela yangu Serikali ndio ukaniwekee wewe benki?
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeshindwa kuweka hii jamani muangalie mifumo hii halafu mnasema leo wawekezaji wawepo, mwekezaji gani atakayefanya biasahra ya kipuuzi kama hii hapa, haiwezekani hata siku moja biashara ya namna hii! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nisingelisema hili alafu mimi ninafanya biashara ya mabasi na watu wote wa mabasi wanajua …ya mabasi ningekuwa mnafi hiki kitu hakiwezekani tunajua sisi EFD machine peke yake mnataka leteni EFD mashine watu watumie EFD mashine huwezi ukawa na duka eti unapiga thamani ya mali za duka milioni 300 halafu unaingiza kwenye mashine ndio uanze kuuza duka inawezekana wapi? Halafu hapa katikati kuna ma-vendor wanakukata two percent haiwezekani huu utapeli ni utapeli wa hali ya juu sana, na wafanyabiashara siku ile walimvisia sana Mheshimiwa Hayati Dkt. Magufuli pale Ubungo wakati anafungua stendi lakini bahati mbaya walikosa nafasi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, walipiga kelele mzee mzee lakini hajawaona lakini kwakweli ilikuwa hatari kubwa sana hii, hii biashara haiwezekani kwa hiyo, wafanyabiashara wa mabasi hawawezi.
Mheshimiwa Naib Spika, kingine Waziri wa Uchukuzi…
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kiswaga Taarifa.
T A A R I F A
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa taarifa mzungumzaji kwamba wenye mabasi wakati mwingine basi linaweza kuharibika njiani abiria anatakiwa arudishiwe fedha, na fedha zipo kwa vendor atafanyaje huyu mfanyabiashara wa basi? (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Shabiby.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa ninaipokea kwa mikono miwili. Kwa hiyo, nilikuwa ninaomba haya mambo yafanyiwe kazi watu wasije wakagoma halafu baadaye watu wakaanza kulaumu kingine, lakini na Waziri ulichukulie vizuri kwa sababu wakati linapitishwa wewe ulikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi kwa hiyo uwe nalo makini na nilipokuuliza ukasema ulikuwa haujui kama lipo hivi na bahati nzuri kulikuwa na Waheshimiwa wengine Wabunge na hata Mheshimiwa Katibu Mkuu wetu wa zamani mstaafu alilikemea sana hili akiwa Katibu wa CCM lakini lilishindikana wakasema huyo mwanasiasa tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kingine stendi zinajengwa kweli za Serikali na zinatumia gharama nyingi ninazungumza hili kwa sababu Naibu Waziri wa Uchukuzi yupo hapa. Stendi ya Dodoma mwanafunzi anasoma chuo au shule anakuwa na nauli wakati mwingine hata mnamsaidia shilingi 20,000 mnaenda kumshusha nanenane halipii chochote halipi fedha ya mapato ya aina yoyote ya kuingia stendi lakini unamlazimisha ashuke akodishe bodaboda au taxi hilo lipo Dodoma lipo Songea, lipo Iringa.
Mheshimiwa Naibu Spika, stendi ya Iringa kilometa 21 kutoka pale stendi wanaposhushwa abiria mpaka mjini na Halmashauri ile Manispaa haiingizi faida yeyote ila tu wanawaambia shule tu hapa basi liende tupu, basi linaenda huko huko mjini lakini haliruhusiwi kwenda na abiri ili umtese abiri ilimradi tu ashuke. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nilichogundua…
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa!
NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge ukiwa unazungumza taarifa ukishasema mara moja unasimama ili nijue uko wapi, ukishasema taarifa unasimama kimya halafu nikishakuona…
MBUNGE FULANI: Tatizo huyo mrefu sana.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Vita Kawawa.
T A A R I F A
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa taarifa mzungumzaji kwamba sio Dodoma peke yake hata Ruvuma ni Kilometa 25 Songea kituo cha mabasi kilipo na mpaka Makao Makuu ya Mji wa Songea ahsante.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Shabiby unaipokea taarifa hiyo.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, ndio hiyo nilikuwa ninaitaka, kwa hiyo Waziri wetu wa Ujenzi na Naibu wako hebu angalieni mnawatesa abiria kama mimi mwenye basi nimeamua kumchukua huyu abiria kumpeleka mpaka anapotaka wewe kinakuuma nini wewe ambaye huna hata basi nini kinakuuma? Na haupati fedha ya aina yeyote labda angekuwa anaingia ungesema unachukue ile shilingi 300 lakini anashuka ila tu unataka kwamba bodaboda sijui taxi wao unawaangalia wapo pale 60 lakini unatesa watu maskini wengine tumewapa mle lifti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ninataka nizungumzie bandari, bandari ya Dar es Salaam mambo mengi yamezungumzwa lakini ninataka niwaambie haitafanyakazi vizuri tusipoangalia hata siku moja, hapa maneno roho ya kuviziana vyeo, chuki ndizo zilizojaa kuna ule mfumo unaitwa TANCIS upo slow sana bandarini, upo slow sana kwa hiyo ubadilishwe au urekebishwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine, mimi hapa niliongea Bungeni, tulibishana sana wakati ule na akina Mheshimiwa Mwakyembe na wengine hadi tukafanikiwa kuipeleka ile bandari ya pale Vigwaza, inaitwa Bandari ya Kwala (Dry Port).
Nafikiri mimi ndio nilikuwa mtu wa kwanza kuzungumza baadaye nikawa nimeungana na Mheshimiwa Hawa Mchafu. Bahati nzuri bandari ile mpaka sasa hivi imeshajengwa, imebakia vitu vidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, TPA, bandari wamenunua vichwa vya treni viwili kwa ajili ya kutoa mizigo yote makontena yote kutoka bandarini yaje na ile reli ya kwenda Arusha, waje washushe Kwala, pale Vigwaza na ile bandari iko tayari, bado kumalizia tu ili malori yote yasiingie kule Dar es Salaam na ili foleni yote ya bandari hii isiwepo. Cha ajabu hii nchi mpaka leo, nendeni mkaangalie jamani, sisi watu wa Kamati ya Miundombinu tumeenda pale, ile bandari imekwisha, TPA wameshanunua treni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kutoka pale bandarini treni inaweza kwa mara moja ikabeba kontena 60, 70 na zikiwa treni tatu au nne; na Kadogosa nimemwuliza, anasema yeye anazo treni, anaweza akaweka hata nne au tano pale. Kwa hiyo, kwa siku tunaweza tukatoa kontena zaidi ya 1000 bandarini kuja pale Kwala ili malori yasiende kule mjini. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Muda umeisha!
NAIBU SPIKA: Muda umeisha Mheshimiwa.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Dah, nilikuwa nataka niseme ya ndege. Haya, basi ahsante sana. Ila siungi hoja mkono mpaka nipate majibu ya kutosha. Bandari ya Kwala nataka nijue inaanza lini kazi; na barabara zangu. Pia ndege za Dodoma - Mwanza bado hamna hapa. (Kicheko/Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa kabla sijasahau, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Naunga mkono kwa sababu yale ambayo niliyazungumza sana siku za nyuma ambayo yalikuwa hayafanyiwi kazi, namshukuru mama yetu pamoja na Waziri wake wa Fedha kwa kuyashughulikia. Kwa mfano, mimi sio mpenzi wa kuweka majina kwenye magari, lakini mlipoweka shilingi milioni 10 mlikuwa mnapoteza sana mapato kwa plate number za binafsi. Tulitoa ushauri, tunashukuru safari hii mmeufanyia kazi. Mabango yote ya matangazo iwe ya kwenye magari, iwe kwenye maduka na hili nalo mmelifanyia kazi. Kwa hiyo, nakuunga mkono Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa kazi nzuri uliyoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lazima nizungumze, kwenye hii Wabunge wengi walizungumzia habari ya pesa kuongezwa kwenye mafuta kwa ajili ya kwenda TARURA. Mimi ni msafirishaji wa mizigo na abiria. Shilingi 100 haiwezi ikaleta madhara ya kuongeza nauli wala kuongeza kitu chochote.
Nimejaribu kuongea na wamiliki wa vyombo mbalimbali vya usafiri hasa TABOA nao wakaniahidi kabisa, wakasema hilo ni jambo zuri sana kwa sababu hiyo pesa inapelekwa sehemu ambayo ni muhimu, sehemu ya TARURA. Kwa sababu huwezi ukaikwepa ile shilingi 100/=. Utakwepa shilingi 100/= lakini ile gari ikitembea kwenye njia mbovu itavunja vitu zaidi ya ile shilingi 100/=. Kwa hiyo, utakwepa shilingi 100/= lakini gari inaweza ikavunja vitu mara 20 ya ile shilingi 100/=. Kwa hiyo, barabara zikiwa safi, gharama nyingi sana zitapungua. Nataka nikuhakikishie kwamba hii haitaongeza gharama ya aina yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilishawahi kusema hapa katika Bunge hili kwamba Wachina hawakupata maendeleo hivi hivi kama mnavyofikiria. Miaka ya nyuma kidogo tu hapo walikuwa sawasawa na Watanzania, lakini wale hata walipokuwa wanaamua kuvaa suti, siku moja wote wanavaa chew and lie zote za rangi moja. Ilikuwa agizo la nchi yao. Wakiamua kuvaa suti moja wiki, ni wote. Masharti hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni lazima tufunge mkanda. Hili narudia, wewe unalikumbuka. Kama tunataka kweli maendeleo kwenye hii nchi, ni lazima kufunga mkanda, siyo kuzungumza. Maana Wabunge wote sisi kazi yetu ni kuishauri Serikali. Kuna watu wengine wanaitwa wachambuzi wako huko nje; na kuna watu wengine wanatoa mawazo. Sasa unatoa mawazo, mbadala wake nini? Unazungumza kodi hii, wananchi hapa watateseka, nini na nini; na nchi inataka pesa. Nini unaleta mbadala wake? Kama hutaki kodi hii iende kwenye simu, iende kwenye mafuta, mbadala wake unaochangia ni upi? Ukilalamikia kitu, lazima ulete na mbadala. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, utakuta kuna mchambuzi hajawahi kufanya kitu cha aina yoyote. Mtu anachambua hapa, anasema wananchi kwenye simu watapata shida; wakati hajasoma hata hiyo yenyewe inazungumza nini? Imeshasema, kuanzia shilingi 10 mpaka shilingi 200. Mimi na- recharge kwenye simu yangu shilingi 50,000 sasa nikikatwa shilingi 200 kuna ubaya gani? Mtu anaweka shilingi 2,000, shilingi 1,000 anakatwa shilingi 10, kuna ubaya gani kuchangia maendeleo ya nchi yake? Hata hivyo, watu hawaelewi, wanapotosha. Utakuta kwenye vyombo vingine vinaandika tu, yaani hata haelewi, shilingi 200, kila siku shilingi 200/=. Kama kitu huelewi, acha kuzungumza. Kama unataka kupinga, lete mbadala wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ndani ya bajeti hii nakumbuka mama ameahidi kule Mwanza siku ya Mei Mosi kwamba mwakani ataongeza mshahara. Hatuna walimu, tunalalamikia walimu; tunalalamikia maji kama Mheshimiwa Mbunge pale alizungumza vizuri sana; tunalalamikia vitu vingi; na bajeti hii tunatakiwa tupate shilingi trilioni 36 kwa ajili ya kuleta hivyo vitu. Sasa kama huna mbadala wa kuleta hiyo pesa, wewe unalaumu tu, sasa tufanyaje? Nchi isimame! Haiwezekani! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hii bajeti ni nzuri sana, wala haina shida ya aina yoyote. Hata ile kuweka kodi ya viwanja ni vizuri, tena hata baadaye tuje tuangalie na kodi ya ardhi, ije iingie huku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme tu, TRA wanafanya kazi nzuri sana. Namjua Kidata, ni mlokole na ni mtu mzuri sana pamoja na Makamishna wake, lakini huku chini kuna matatu; na siyo tena kwa mameneja wa mikoa. Hawa watu wengine tu wako TRA lakini wamesumbua sumbua na nafikiri sasa hivi kidogo kumetulia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lililopo, TRA kulazimishwa kutumia na vyombo vingine ambao hawana utaalam wa kodi; unamshauri TRA akachukue TAKUKURU, TAKUKURU anaelewa nini kuhusu mambo ya kodi? Unamchukua TRA unamshauri, unamwambia atakula rushwa, yuko na watu wengine wa vyombo vya usalama, wanajua nini katika masuala ya kukusanya kodi? Kodi ni elimu na ndiyo maana kuna Chuo cha Kodi. Unapoleta mtu mwingine kwa wafanyabiashara, kwanza sura yake peke yake inatisha. Unaweza ukamuua yule mfanyabishara hata kabla ya kukusanya kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuangalie hii. Mambo ya task force ambazo hazina mpango ni za kutisha. Mfanyabishara na TRA wanatakiwa wawe pamoja kueleza kwa lugha nzuri, mtu atalipa kodi. Kwa wafanyabishara nao, Mheshimiwa Waziri nimeona ulianza kuzungumza pale kwamba sasa hivi watu kwenye account wasiingiliwe, wasikamatiwe vitu vyao, lakini kuna mfanyabiashara mwingine anaenda TRA, anapigwa kodi shilingi milioni 200, anapeleka mahesabu yake, inakuja kodi labda mpaka shilingi milioni 80, anapewa miezi sita ya kulipa, anaomba mwenyewe au mwaka, lakini unaisha mwaka hajalipa hata shilingi 100/=. Sasa unategemea hiyo pesa itapatikana vipi? Kwa style gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, huwezi kubembeleza mtu ambaye amekubali mwenyewe, kasaini mwenyewe halafu kodi yake mwenyewe halipi. Halafu unasema asichukuliwe kitu wala asikamatiwe mali au asichukuliwe hela yake benki. Hivyo vitu viwili tofauti. Lazima hilo tuliweke sana Mheshimiwa, usije ukaanza kuwa mpole mpole sana ukataka kufurahisha watu kwenye sheria. Sheria ing’ate huku na huku, pande zote mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme na Serikali nayo isiwe na fitina na wananchi wake. Sekta Binafsi ndiyo Sekta ambayo inaajiri watu wengi. Sasa kama ninyi Serikali mnataka kufanya kila kitu, basi sameheni na kodi. Punguzeni kodi. Maana sasa hivi ukitaka, ukienda sijui matangazo; vyombo vya binafsi havipewi matangazo. Wanapewa vyombo vya Serikali, halafu vyombo vya Serikalini hatusomi, maana wanajisifia wenyewe kwa wenyewe tu. (Makofi/ Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, utakuta matangazo. Halmashauri inaweza ikatoa tangazo inataka Mkandarasi kwenye magazeti sita, hajapatikana Mkandarasi, lakini ikienda kutolewa kwenye gazeti binafsi au kwenye media yoyote binafsi, tayari utakuta Wakandarasi 80 au 40. Kwa hiyo, mnakula hela zetu za Halmashauri bila sababu kwa kutulazimisha taasisi zetu za Serikali zifanye matangazo kwenye sekta binafsi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukija kwenye Wakandarasi, mnataka nini? Kwa mfano, pale kwangu Gairo hakuna Engineer wa Wilaya. Kuna technicians. Unamwambia ajenge hospitali ya wilaya, ikibomoka! Ooh, tunatumia force account, hatuna wataalam. Pelekeni basi kwanza wataalam. Yote hiyo ni Mkandarasi asipate pesa wakati anaajiri watu wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwa hawa wenzangu kama akina Mheshimiwa Vita Kawawa wenye kumbi nakadhalika; aah, hatutaki kumbi, tunataka sisi tufanyie maofisini. Ofisi zote za Serikali sasa hivi zinanukia chapati tu kwa sababu ya haya mambo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, jamani sasa kama ninyi mnataka kodi kwa watu binafsi na ndiyo wanaajiri watu wengi, lakini hamtaki wapewe kazi, sasa watafanya kazi gani? Ukienda kule bandarini, kuna TASAC, hawataki wale clearing and forwarding wafanye kazi; anaingilia sheria hata siyo zake. Iliundwa ifanye kazi ya sheria, mizigo ya Serikali shehena za dawa na vitu vingine, lakini sasa wanaingia wanataka wafanye kazi wao. Sasa watu watafanya kazi gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tuangalie na hizi kazi. Ujenzi ni JKT, halafu mafundi wenyewe ni hawa hawa. TEMESA wanataka kazi za Serikali. Kwa mfano, Gairo, generator imeungua, nimeenda kwa fundi anataka shilingi 700,000/=, wamekuja TEMESA wanataka shilingi 4,000,000/= halafu fundi ni yule yule niliyekubaliana naye mimi shilingi 700,000/=. Sasa Serikali sehemu nyingine mnapigwa kwa ajili ya kukunja roho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri nataka nikwambie kwenye mambo ya VAT ya maduka na sehemu nyingine. Utakuta hapa pana mtu amesajiliwa VAT, kuna mtu hajasajiliwa VAT. Kwa hiyo, akinunua huyu biashara kwa sabbau hana VAT anauza kitu shilingi 10,000, duka la pili anauza shilingi 11,800 maana yake ameshaweka ile shilingi 1,800. Sasa ni nani atakwenda kununua kwa huyu aliyezidisha bei kwa shilingi 1,800?
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu wanayonunua hii ni moja labda kule kwenye kiwanda, lakini kwa sababu huyu amesajiliwa VAT atauza shilingi 11,800 na kwa sababu huyu hana usajili wa VAT, anauza kwenye duka hilo hilo kwa shilingi 10,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, jaribu kutafuta kwa hawa wanaoleta vitu kwa jumla kwenye viwanda; kama VAT, basi waangalie technique yake wanafanyaje kiutaalamu? Kwamba VAT ipigwe kule kule, ikija huku watu wote wameshalipa VAT. Uangalie tu utafanyaje asilimia zile kwamba hii akiuza ile VAT ya kwanza itatoka kiwandani na ya pili itakuwaje ili ilipishwe kule kule moja kwa moja? Ikija huku kila mtu na kila kitu kiwe kwa VAT ili competition ya maduka iwe iko sawa. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii, lakini kabla sijaongea masuala yangu ya bei za mafuta, kwanza nataka nitoe kabisa tahadhari kwa Mawaziri wa Wizara ya Maji kwamba nitachangia kwenye Wizara yake kuhusu habari ya mpango wa maji yale ya kutoka Changongwe kwenda Kata ya Lubeho, Kata ya Msingisi, Kata ya Gairo, Kata ya Kibedia na Kata ya Chakwale. Kwa hiyo najua bajeti iwekwe mapema. Vile vile kwenye TAMISEMI, Mheshimiwa Waziri Mkuu ni shahidi, Mheshimiwa Rais alipita pale Gairo na tulimwambia ile shida yetu ya kuhusu ule mfereji ambao unazuia mafuriko pale Gairo, lakini mpaka leo hatujawekewa bajeti kwa ajili ya ule mfereji ya kuzuia maji pale Gairo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, nataka niseme tu kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri wanafanya kazi nzuri na tunataka wafanye kazi bila woga ili waweze kumsaidia Mheshimiwa Rais. Nia ya Mheshimiwa Rais ni nzuri na tunaona kwenye majimbo yetu mambo yanavyokwenda, mimi ni Mbunge wa kipindi kirefu kidogo, lakini naona fedha zinazokwenda kwenye majimbo. Tunashuhudia barabara, tunashuhudia minara ya simu, tunashuhudia hospitali, tunashuhudia kila tu, ila nao wasibaki kusema tu mama kaupiga mwingi, huyu mama nilivyomsoma soma mimi hataki sifa sana, anataka kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mama kaupiga mwingi iendane na ufanyaji kazi wenu Mawaziri na kumsaidia kazi, wasije wakajidanganya kwamba mama anaupiga mwingi kwamba mwenzenu anapenda sifa sana mimi nilivyomsoma soma huyu sifa hataki, anataka kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kusema Watanzania kila kinachofanyika kama kuna wizi sehemu unakuja au wizi unafanyika, Watanzania wa sasa hivi wana akili wanajua kwamba hapa pana wizi umefanyika au wizi unakuja. Pakiwa na chochote kinachopitishwa kikiwa cha deal Watanzania wanajua kabisa, hili hapa ni dea,l si hawa Watanzania wa sasa hivi ni wale Watanzania wa zamani. Hapa niliongea miaka minne nili-spend sana kuongea habari ya mafuta, lakini imebidi tena na leo niongee, lakini miaka minne akina Ole-Sendeka ni mashahidi hawa, nilikuwa nazungumzia habari ya mafuta ya taa kufanywa malighafi kuchanganywa na diesel na petrol, akina mama Kilango wote walikuwepo hapa, miaka minne ndiyo Serikali imekuja kuchukua hatua za kuweka kodi kwenye mafuta ya taa.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo mmeshuhudia wenyewe robo ya yale mafuta ya taa yaliyokuwa yanatumika hayatumiki, Serikali imepata mapato mengi imefanya vitu vingi sana. Hili suala tumechangia sana kwamba itakuja kuleta athari kubwa sana za kupanda kwa bei ya mafuta. Ule mpango wa bulk procurement wakati unakuja. Kuwa na vita Urusi na Ukraine kwa Tanzania ni fursa na kwa nchi zingine ni fursa ya kupata mafuta kwa bei rahisi, lakini kwetu sisi sasa imekuwa ni moto. Tulishasema na narudia kusema kipindi kile imekuja kampuni ya Li lance ya tajiri mmoja wa India anaitwa Ambani mwaka 2007 ilipokuja hapa Reliance iliponunua GAPCO na GAPWAY kwa ajili ya kuendesha biashara ya mafuta.
Mheshimiwa Naibu Spika, Reliance ndiyo wenye refine kubwa sana duniani kipindi kile ndiyo ya kwanza hata hao Urusi hata Saudi Arabia hawana. Wao wana meli zao walipokuja hapa wakati wameanza kuleta mafuta, mafuta yalishuka zaidi ya shilingi 400 au 500 kwa lita kwa makampuni mengine yote walikuwa hawapati nafasi ya kuuza mafuta. Haya makampuni makubwa ya kizungu yanashirikiana na baadhi ya Wabunge wengine wapo upande wetu na mwingine alikuwa kiongozi kabisa wa chama fulani kule upinzani naye alikuwemo. Wakapiga deal kule, wale wajamaa wakawaambia bwana hebu sasa tunafanyaje huyu Reliance anashusha bei, na nini wakawaambia nyie hebu anzisheni mgomo hapo, msiuze mafuta hata siku mbili jifanyeni bei ndogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema vile vituo vilivyogoma kidogo wakaja huku, twendeni kule kwenye depots, sijui twendeni wapi, mbwebwe tu, kumbe wenzetu kuna ulaji. Baadaye tukaleta hoja maalum tujadili. Baada ya kujadili tukasema hakuna mtu binafsi kuleta mafuta, tununue kwa bulk procurement, matokeo yake ni nini? Ukishanunua mafuta kwa pamoja, sasa nani maana wote mnanunua bei hii halafu wote mnaleta mnapangiwa bei hii, sasa atakayeshusha nani, wote mnakuwa na bei moja, hakuna tena ushindani wa mafuta. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yule bwana akaamua kuuza kabisa, akawauzia TOTAL ile GAPCO na GAPWAY, maana yeye alitegemea ataleta mafuta yake atauza kwa ushindani kama alivyokuwa anafanya atashusha bei, lakini mnamwambia sasa bwana tunaenda kununua wote kwa pamoja, sasa ushindani uko wapi? Hebu kumbukeni angalieni kuanzia ile miaka ile kuna makampuni mpaka ya Watanzania World Oil ni ya Mtanzania, mtu wa Kigoma; hawa akina Vedasto Manyinyi huyu Mbunge wa hapa wa Musoma hawa nao walikuwa na kampuni yao; wako akina Barongo, watu wa Bukoba huko walikuwa na makampuni yao, watu kibao walikuwa na makampuni yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi ninavyokwambia kule deep sea kuna meli zinauza robo ya bei ya dunia yanatoka huko Urusi mengine yanatoka nchi zilizowekewa vikwanzo yako pale yanauza robo ya bei ya dunia, ukimruhusu mfanyabiashara wa binafsi yeye kazi yake anachokwenda pale ship to ship anachukua mafuta, meli kwa meli anapakia mzigo anakuja, ninyi watu wa huku wa EWURA, watu sijui wa Serikali, watu wa TBS, kazi yenu ilikuwa panga bei bwana, mafuta haya kwa bei ya dunia yasizidi hapa na TBS kiwango chetu tunataka hiki, yanatimiza kiwango basi, kwisha lakini unataka tu kupanga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naangalieni kwenye hiyo bulk procurement, watu wanakula pesa siyo mchezo, nchi hii inatumia lita milioni mia nne kwa mwezi. Sasa fanya tu wale kwenye ile Kamati wanachosema kwamba fulani nikupe tender ya kwenda kununua wakiweka dola tano tano wana shilingi ngapi? Hata dola mbili mbili wana bei gani? Tunachokizungumza hatukizungumzi kwa kukisia, lakini ukiongea sana hapa ukishika mishiko ya watu unasikia huyu Shabiby atakuwa mwizi wa mafuta huyu yaani nyie mnajuaga wizi wizi tu. Wakati wezi wako huko huko, ndiyo majambazi halafu wanatengeneza na nataka niseme kwamba kila kitu sasa hivi ni deal na kuna watu wachache ambao kazi yao ni kupanga deal kwenye hii nchi, sisi huku tunapelekeshwa tu, tunapitisha sheria kumbe sheria hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii mkiruhusu kampuni binafsi ziagize mafuta na kama mtu anaona kuna unafuu kama mnavyodai bulk procurement nayo iwepo, kama ataona kuna nafuu aende huko, kama ataona hamna nafuu alete yeye, Serikali kazi yake iwe kuangalia tu kiwango inachokitaka na bei inayotakiwa, lakini vitu vingine wanatunga tu utasikia ukileta mafuta mtu mmoja mmoja yatakuwa yanakwepa ushuru, meli zote zinashusha kwenye mita, zinashushia wapi? Hii kazi waachieni TRA, TRA ya nchi hii inafanya kazi nzuri, waaminini TRA lakini wao wanawapa kazi TRA wanakula deal. Sasa hivi tukiangalia toka ile bulk procurement mpaka sasa hivi ile mita imekufa mara ngapi? Imekufa mara nyingi kuliko wakati wanaleta watu binafsi ile mita ya bandarini. Naombeni sana turuhusu hayo bei ya mafuta itashuka kuliko tulivyotegemea na wala tusidanganyane na tusiwadanganye watu na watu wengine hata waliopo huko nje wasiwadanganye kwamba Serikali inaweza ikatoa kodi ya kwenye mafuta, ukitoa kodi nchini, hii mishahara haipo wala hakuna madawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunategemea hiyo kodi ya petrol tusidanganyane eti kodi sijui elfu moja na ngapi? Kodi yetu ndiyo inayotulisha sisi Serikali wala tusiwadanganye watu kama tunaweza kutoa kodi, kodi hatuwezi kutoa tunachotakiwa kufanya ni kupata mafuta kwa bei rahisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine, dakika yangu moja imepotea kwa ajili ya makofi, naomba uilinde. Serikali imeleta matrekta yale matrekta yapo pale Kibaha yanaitwa Alice sijui Ursus yanaitwa nini? Serikali imewaletea wakulima kuja kuwaua, imeleta matrekta mabovu mimi sijawahi kuona toka nizaliwe, mimi ni mkulima nina trekta zaidi ya ishirini sijawahi kuona trekta inakatika katikati kichwa kinaenda peke yake matairi ya nyuma yanabaki peke yake. Haya matrekta yote ni mabovu, leo wamewatia watu umaskini hawa, huko yalikonunuliwa wapo wapi wale watu, hawajatoa guarantee? Yale matrekta leo wanasumbua wakulima wetu wanawadai wanataka kuwanyang’anya matrekta wao walikuwa hawana guarantee na yule aliyeagiza yale matrekta naye ashtakiwe, huwezi kuleta trekta kwanza ina jina la mama linaitwa Alice, halafu inakuja inasumbua, nenda unakuta dereva yupo mbele matairi yamebaki nyuma, kiuno kimekatika karibu matrekta yote hamna hata moja mikoa yote Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, halafu leo hii wanaandikiwa barua usipolipa tutakunyang’anya trekta. Mtu unamdai milioni 20, ukimnyang’anya trekta unaenda kulipiga mnada kwa milioni mbili kwa hiyo hapa pana kila aina ya njia ya wizi. Serikali iangalie namna ya kuwasaidia kuyatengeneza yale matrekta na wawasaidie namna ya kuwaongeza muda ili waweze kulipa yale madeni wanayodai. Vilevile wachunguze haya matrekta nani kaleta na yana mkataba gani na yana guarantee gani, maana yake trekta haiwezi kuwa na guarantee ya mwaka mmoja kama lori au kama basi au kama gari ndogo, linatakiwa liwe na muda mrefu. Kwa hiyo…
NAIBU SPIKA: Ahsante.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Kwa hiyo naomba wayafuatilie hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, ahsante, nashukuru kunipa nafasi na mimi kuwa mmojawapo wa wachangiaji katika hotuba hii ya Wizara ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Ndugu yangu Mheshimiwa Waziri wetu Profesa Sospeter Muhongo pamoja na Naibu wake. Pamoja na kuwa ni mgeni lakini tunaona ana nia njema katika Wizara hii na Taifa hili. Vilevile nimpongeze Katibu Mkuu wa Wizara hii pamoja na wote katika Wizara ya Nishati na Madini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitaanza na REA, cha kwanza nitapingana kidogo kuunga mkono juu ya hoja ya ndugu yangu Mheshimiwa Ally Mohamed Keissy, kwamba REA wanafanya vizuri kwa sababu moja. REA katika mipango yao ya kugawa umeme vijijini wana upendeleo, hili liko wazi, kwa wale Wabunge waliopita, Bunge lililopita wameona, katika ile miradi ya awamu ya pili. Kuna baadhi ya wilaya na majimbo yana vijiji mpaka sitini; kwa mfano Majimbo ya Karagwe na Bunda.
Mheshimiwa Spika, ukija Jimbo la Gairo lina vijiji vinne na havijawaka umeme hata kimoja. Karagwe kuna vijiji 110, ukija Bahi kuna vijiji viwili, hapa Dodoma hakijawaka hata kimoja, sasa nataka kujua, hawa REA wanafuata vigezo gani? Wanataka sisi Wabunge tukashinde ofisini pale kwa Meneja au kwa ndugu yangu yule Msofe tuanze kuomba umeme, tusifanye kazi nyingine? Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri ameliona hili ndiyo maana safari hii hata vijiji hajavitaja humu kwa sababu nafikiri nia yake labda ni kwenda kugawa keki hii kwa kila mwananchi na kila Wilaya au kila Jimbo wapate sawa, wasirudie yale. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwaka jana wameandika Gairo vijiji 27 ndani ya kitabu cha Wizara, nimekwenda kule na Waziri aliyepita, Mheshimiwa Charles John Mwijage, nimekwenda na Mheshimiwa Simbachawene, hawaelewi, wala watu wa REA hawajui wakati wapo Wizara ya Nishati wanaishia vijiji vinne. Kwa kweli mwaka huu ndio utakuwa wa mwisho wangu kuunga mkono hii habari ya REA.
Mheshimiwa Spika, REA hawana maana kabisa katika ugawaji wa umeme vijijini. Hata kama pesa hawapewi basi tupewe hata maneno kwamba utawekewa kijiji hiki, kijiji hiki, tubaki tunadai, sasa hata pa kudai hakuna. REA ni tatizo kubwa na ninyi Wabunge wageni mtaliona tatizo hilo, bado hamjaliona. Mwaka huu nasubiri kwa sababu nimeangalia sana kwenye hotuba ya Waziri hivi vijiji sijaviona humu mwaka huu tumetajiwa tu idadi ya pesa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kitu kingine, mimi ni mfanyabiashara na katika biashara zangu nafanya biashara nyingi mojawapo ikiwa ya mafuta. Na-declare interest na humu ndani kuna watu wengi kuna Walimu, wakulima, wafugaji, kila mtu ana fani yake. Kwa hiyo nisipozungumzia habari ya biashara ya mafuta wakati najua na na-declare interest nitakuwa sijajitendea haki. Kwa wale waliopita Bunge lililopita wanajua kabisa vituko vya EWURA, wanavifahamu, na ndiyo maana hata Mbunge, Mheshimiwa David Silinde nafikiri alikuwa anataka kuizungumzia lakini muda ulikwisha.
Mheshimiwa Spika, kwanza lazima tukumbuke hata neno chakachua aliyelileta Bungeni na Tanzania nzima ni mimi hapa wakati nazungumzia habari ya kuchakachua mafuta ya taa, diesel na petrol ndiyo hilo likaingia chakachua matokeo, sijui chakachua kitu gani, chakachua kitu gani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, EWURA ilianzishwa wakati ule mafuta ya taa yalikuwa hayana kodi, petroli na diesel zilikuwa na kodi ziliyazidi mafuta ya taa karibu shilingi mia sita. Kwa hiyo, wafanyabiashara wengi wakawa wanachukua mafuta ya taa wanayafanya malighafi wanachanganya na diesel au na petroli kwa ajili ya kujipatia kipato. Tukaanzisha mfumo wa kuweka vinasaba kwenye mafuta ili mtu akichanganya mafuta ya taa na petroli au na diesel anaona kwamba amechanganya na mafuta ya taa.
Mheshimiwa Spika, baadaye EWURA walishindwa kabisa kuondoa ule uchakachuaji kwa vinasaba vyao kwa ajili ya rushwa iliyoko EWURA. Kwa hiyo, Bunge hili likaamua kupandisha mafuta ya taa kwa kuweka kodi kwa sababu EWURA walishindwa kufanya kazi yao. Lakini cha ajabu EWURA wakahamia sasa wakawa wanaendelea kuweka vinasaba kwenye petroli na diesel. Sasa wakija kwenye petrol station wanakwambia vinasaba vimepungua, kwa hiyo, umeshusha mafuta yanakwenda mgodini au yanakwenda transit. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini vinasaba wanawekaje? ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge nataka niwaeleze. Mtu yuko Dodoma ananunua mafuta anapiga simu BP, nataka kununua mafuta, BP anamwambia bei yangu hii, anamwambia nimekubali, anamwambia weka hela Dodoma kwenye benki nitaziona kwa internet hapa Dar es Salaam. Unaweka hela Dodoma benki mtu wa BP anakwambia lete gari, nampigia simu nikiwa Dodoma Transporter peleka gari yangu BP kanipakilie mafuta.
Mheshimiwa Spika, Transporter anamtuma dereva wake nenda kapakie mafuta labda ya Shabiby BP, dereva akifika pale yuko mtu aliyepewa tenda na EWURA wanaitwa GFI, mtu wa GFI anakuja anamwambia dereva, wakati huo dereva hana elimu yoyote wala hajui vinasaba au anawekewa mkojo wa punda au anawekewa juice, anaambiwa umeona hii hivi ndiyo vinasaba hivi usinuse, nakuwekea hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kumbuka vile vinasaba havibadilishi mafuta rangi wala nini, unaletewa Dodoma. Siku ya pili anakuja mtu na gari la EWURA na havionekani kwa macho ameshaambiwa na yule mwenzie kwamba kule nilikoweka nimeweka kidogo nenda kapime. Anakuja anapima kwako, kwanza anakwambia kabisa nipe milioni tatu kama hutaki napima, usipotoa hiyo pesa na sisi Wabunge wabishi kutoa rushwa anapima, anakwambia vinasaba vipo lakini vimepungua kidogo wakati huvioni kwa macho, hujahusishwa kwenye kuviweka, wala havikuhusu; sasa huu ni wizi.
Mheshimiwa Spika, nikwambie kwa Tanzania kwa mwezi inaingiza meter tones laki mbili na elfu hamsini, sawasawa na lita mia tatu na vinasaba mtu wa mwisho anayeweka mwenye gari anachajiwa shilingi kumi na mbili na senti themanini na nane, kila lita moja unayoweka wewe mafuta. Kwa mwezi yule aliyepewa tenda analipwa bilioni tatu na milioni mia nane, kwa mwaka bilioni arobaini na sita, umenielewa.
Mheshimiwa Spika, hii kampuni ya GFI imepewa tenda bila kutangazwa kwenye magazeti na mpaka leo tenda hiyo inaendelea. Tafuteni GFI imepewa wapi hiyo tenda, haijawahi kutangazwa na imepewa tenda mpaka leo hii. Tusizungumze hapa tunasema sijui hii kampuni ya nani, hii kampuni ni ya wao wenyewe na ukimchukua leo Kalamagozi wa EWURA na yule Kaguo utaona anavyojieleza, wanajieleza kuliko hata waandishi wa habari. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baadhi ya magazeti hayawezi kuandika EWURA vibaya, baadhi yao, yanayopewa matangazo, kwa sababu ukiandika vibaya tangazo hupewi. Ukiandika vibaya habari ya EWURA, hupati tangazo. Hivi leo bilioni arobaini na sita hii ukiigawanya hata kama tununue madawati tu tunapata madawati laki saba.
Mheshimiwa Spika, siungi mkono hoja hii mpaka nipate jibu sahihi la hawa watu wa EWURA. Ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuwa mmoja wa wachangiaji. Kabla sijaingia kwenye mpango zaidi, niseme tu kwamba, lengo la nchi yote au mipango ya nchi yote ni kukuza uchumi wa nchi yake. Kwa hiyo masuala yote ya Mpango wa Maendeleo lazima yaendane na mipango ya muda mrefu. Wabunge wengi wameongea lakini bila mpango wa muda mrefu nchi yetu tutakuwa tunapiga marktime muda wote. Maana yake tutakuwa tunajenga na kubomoa. Nitoe mfano mmoja, ukiangalia wataalam wetu, ikiwezekana saa nyingine hawa wataalam wa mipango mirefu kama Watanzania wenzetu wanashindwa, basi tungetafuta hata consultant kutoka nchi za nje waje kutusaidia ili tusipate hasara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuna mipango ile ya muda mrefu ya kuona mbali, tunaangalia hapa, kesho tunabomoa, tunajenga hapa, keshokutwa tukipata kipya tunabomoa kile tulichogharamia tunajenga kipya. Kwa mfano, wewe angalia barabara hata zile za pale Morogoro Road yaani mipango hata haijafika miaka 15 au 16 tayari imekuja mwendokasi, barabara nyembamba inang’ang’anizwa hiyo hiyo ili mradi tu daladala hizi za mwendokasi zipite.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija Sam Nujoma barabara haina hata miaka 10 limekuja lile daraja lile flyover, kuna madaraja pale yale mawili makubwa yalikuwa pale upande wa external nayo yamevunjwa tayari yaani tunapata gharama, tunavunja na kujenga. Sasa ukiangalia ni kwa kuwa hatuna mipango ya muda mrefu, yaani kwamba ujue kwamba mji huu utakuwa hivi, barabara hii itakuwa hivi, eneo hili litakuwa hivi. Kila siku tunajenga, tunapata hasara. Kwa hiyo tunatumia kodi za wananchi kwa kuvunja na kujenga upya kwa muda mfupi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija hapa Dodoma peke yake tunajua kabisa ndani ya miaka mitano nyuma kwamba kuna airport ya Msalato inakuja, lakini leo hapa tumeongeza runway tumelipa yale majumba, wakati tunajua kabisa tunajenga kule. Kwa hiyo tumeifanya Dodoma leo tumeigawanya katikati. Kwa nini hizo pesa tulizolipa wale runway ile tuliyojenga na zile fidia zile ingetosha kujenga kiwanja kidogo kama kile ili watu watue. Leo kule kwenye Uwanja wa Msalato kuna Marais watashuka pale, viongozi watashuka pale, uwanja mkubwa. Sasa palikuwa na haja gani ya kupoteza pesa wakati kuna mpango mwingine unakuja? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hawa watu wa mipango kwenye nchi hii ni shida, hawana mipango ya kuangalia mbele. Sasa hivi ukiangalia Bandari Kavu, tumepiga kelele bandari kavu imepelekwa pale Kwala pale Vigwaza, Bandari kila siku ya Mungu inafunguliwa kesho, inafunguliwa kesho, sasa hivi tayari imeishakuwa nayo ya kizamani, maana yake reli ya standard gauge itafika hapa Dodoma, kwa hiyo itakuwa nayo haina thamani standard gauge itafika pale Morogoro, sasa una haja gani tena kwenda kufuata mzigo Kwala badala ya kuweka Bandari Kavu Morogoro kwa ajili ya watu wa Kongo, watu wa Malawi na Dodoma ni kwa ajili ya watu wa Uganda na sehemu nyingine kwa kuanzia, kwani hatuna mipango ile endelevu? Hiyo Kwala imeishakula mabilioni ya pesa na aina kazi yeyote tena ya msingi kama itafunguliwa hii standard gauge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia barabara sasa hivi katika bajeti hii inayokuja lazima tukubali kwamba sasa hivi kwenye barabara lazima tutumie PPP. Mheshimiwa Waziri wa Fedha, ufanye kila aina uwezavyo leo hii accident nyingi zinauwa mpaka Viongozi wengi hapa Maprofesa, Madaktari, kwa mfano yule wa SUA. Kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro ile barabara ni foleni si ya kawaida, kutoka Morogoro mpaka hapa panaitwa Makunganya foleni si ya kawaida, kutoka hapa Dodoma Mjini kwenda mpaka pale Ihumwa foleni si ya kawaida. Hivyo leo, au ninyi kwa sababu wengine mnapitapita humu kwenye vinanii nanii humo hatuonani huku vizuri, tuangalieni sisi tunaokaaa foleni! Ndiyo maana hata saa nyingine kila mtu anajiwekea king’ora na vile vitaa, mnasema ahaaa! anayeruhusiwa hapa ni kuanzia Waziri Mkuu, watu kila mtu anaweka ili apige mkwara apite, kwa sababu barabara hazipitiki, kwa hiyo tutumie mpango wa PPP. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kila Mbunge hapa akipiga kelele mnampa kilometa tano, yule mwingine karuka sarakasi, pamoja na sarakasi kapewa kilometa ishirini mpaka barabara ije ifike kwake ni miaka kumi. Sasa hatuwezi kumaliza barabara zote. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda pale panaitwa nini; Mlima Nyoka pale Mbeya kila siku accident lakini ukiziangalia zote zinasababishwa na barabara, pale panatakiwa four-way, six-way akija huyu Waziri wa Ujenzi, anasema tunao mpango, lakini ukiangalia ule mpango wa muda mrefu hatuwezi kujenga wenyewe, Dunia nzima inajenga kwa PPP na kama PPP hatupati? Basi kopeni, kukopa siyo dhambi. Mimi mtu anaponiambia kama mnasema wenyewe deni himilivu kopeni! Kama Inyala pale kila siku watu wanakufa kopeni, hapa Dar-es- Salaam-Morogoro na siyo hapo sehemu nyingi hata huko Mwanza barabara nyingi hazipitiki. Kopeni halafu wekeni mpango wa road tall nyinyi Serikali wenyewe badala ya kutumia PPP mtakuwa mnachukua road tall, mtu anataka kupita pale atapita kwa road tall mtarudisha ile mikopo siyo shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini unapokopa kitu unapokopa kitu, maana yake mimi sitaki kuwa mnafikimnafiki wananchi huko nje.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyeki, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Shabiby, taarifa.
T A A R I F A
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa Kaka yangu Mheshimiwa Shabiby, kwamba hata hizo kilometa 25 nilizopigia sarakasi bado hazijatangazwa mpaka sasa. (Kicheko/Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Shabiby, endelea.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo taarifa naipokea na nilijua kwa sababu nafanya research na nipo Kamati ya Miundombinu. Ni kweli. Bila PPP huwezi kupata Mheshimiwa Mbunge.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Shabiby, subiri. Waziri wa Fedha na Mipango.
T A A R I F A
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge aliyemaliza kuongea ni mtani wangu, lakini Mheshimiwa anaechangia, anachangia vizuri lakini nilitaka niweke kumbukumbu sawa kwamba moja naunga mkono mchango wake, anachangia vizuri Mheshimiwa Shabiby.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nitoe taarifa kwamba Serikali tayari imeishatoa tangazo la kazi la kupata watu wa kufanyakazi na wameandika barua kuonyesha nia, kwa utaratibu huu anaousema wa PPP tutajenga barabara inayotokea Kibaha mpaka Morogoro njia za kutosha kama za majuu kule. Pia kwa utaratibu ule ule kutokea Igawa mpaka Tunduma na Mbunge wa kutoka Songwe naye alisema hilo. Hii ni tayari ipo kwenye hatua ya taratibu za kimanunuzi, watu wameishaonesha nia kwa hiyo taratibu zinaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hii barabara ndefu anayosema pamoja na kupiga sarakasi siyo kwamba hajapewa, nayo pia zabuni zilishatangazwa na shortlisting imeishafanyika. Barabara ndefu kwenye historia inayoanzia Mbulu inakwenda mpaka Maswa kupitia Sibiti imeishatangazwa, barabara inayotoka Ifakara mpaka Lumecha kule na yenyewe imeshatangazwa kwa utaratibu uleule. Barabara inayotoka Handeni mpaka Singida na yenyewe imeshatangazwa, barabara inayotoka Arusha mpaka Kongwa imeishatangazwa, ile barabara ya kule Mtwango pamoja na Nachingwea inaunga mpaka inatokea somewhere Masasi inapita Wilaya tatu hizo zimeishatangazwa na shortlisting zimeishafanyika, zenye urefu wa zaidi ya kilometa 2,500 kwa utaratibu wa EPC+F. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile na kwa hapa Dodoma tayari tulishaweka Jiwe la Msingi na ujenzi unaendelea wa ile by-pass ambayo ni zaidi ya kilometa
100 na ninaamini pia na yenyewe itatoa suluhisho hilo. Tukiishamaliza hii PPP ya kwanza na tunaleta Sheria Bunge linalokuja kurekebisha ile Sheria ili iweze kuweka urahisi wa kutekelezeka kwa sababu hilo ni dirisha ambalo tunaamini litapunguza Deni la Taifa pia litatoa space kwenye Bajeti ya Serikali ili Serikali iweze kutoa zaidi huduma za jamii ikiwepo Mikopo ya Elimu ya Juu. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, hujazungumzia barabara za Dar-es-Salaam, tunaendelea Mheshimiwa Shabiby.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumza dakika tatu naomba msimamishe muda. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sijakataa, lakini nipo Kamati ya Bunge ya Miundombinu, hizo barabara alizozitaja zote tuna kilometa 25, kilometa 30, kilometa ngapi… za kuanzia, hata mkiangalia ile ya Kiteto kwani imepitishwa leo? Si ina miaka kama mitatu, minne? Ndiyo maana nimesema Serikali yeyote duniani haiwezi ikamaliza barabara kwa kupitia pesa zake. Ukienda nchi yeyote iliyoendelea unakuta kuna barabara zinalipiwa road tall kwahiyo tumieni PPP na mkishindwa kopeni pesa halafu zile barabara mzifanye za road tall ili hela ikusanywe kwa road tall ili Wabunge wote watapata hiyo pesa. Kwa sababu hao wanaonesha nia wanaonesha nia siku nyingi lakini hawapati majibu, maana yake mimi nipo kwenye Kamati ya Miundombinu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme huko nje mitaani watu wengi wanaamini kwamba Serikali ya Awamu ya Tano iliacha pesa kwenye Serikali hii. Kwamba ilikusanya pesa mpaka zingine zimebaki, zipo na watu wanaamini kwamba miradi yote ilikuwa inafanya kama reli, kama Bwala la Mwalimu Nyerere bila mkopo pamoja na madaraja. Hata hivyo nataka niseme hakuna ukweli, kwamba hizo reli tunazojenga ni mkopo, hilo bwawa tunalojenga ni mkopo na watu lazima wafahamu kwamba hiyo Serikali ya Awamu Tano ilikopa kiasi kikubwa cha pesa. Hata tunapokuja hapa Serikali ya Awamu ya Sita, inapoanza kuingia kigugumizi wakitishwa kidogo mkopa sana hawakopi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali wakiambiwa tu ninyi mna kazi ya kukopa toka muingie mnakopa na wao kweli wanaingiwa woga hawakopi kweli. Nataka niseme hii reli waliyoipeleka mpaka Mwanza bila kukopa kufika Kigoma ni sawasawa na mtu umechukua mkopo, umejenga jumba linatakiwa likurudishie pesa hujalifanyia finishing, sasa utarudishaje hiyo pesa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo ni lazima wakope, wafikishe hii reli Kigoma, lazima wakope, wafikishe hii reli Kalimwa hadi Kalema, bila hivyo hii Reli ya Mwanza bila kushirikisha nchi ya Uganda na nchi ya South Sudan reli ya Mwanza itakuwa haina faida yeyote katika Serikali hata tone, kwa sababu utakwenda Mwanza treni utarudi na nini? Hakuna chochote. Lazima ukienda Mwanza unaporudi upate mzigo wa kwenda South Sudan, upate mzigo wa kwenda Uganda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii reli ya Kigoma ndiyo ambayo italipa zaidi kwa sababu leo hii pale wanayo machimbo ya nickel ambayo kila siku itakuwa inasafiri kutoka Burundi kuja Dar e Salaam. Leo hii Kalemi kuna Shaba nyingi sana inatoka kule inakuja Tanzania lakini inashindwa kwa ajili usafiri wa reli haupo na Serikali imetoa bilioni 48 kwa ajili ya kujenga ile bandari lakini bandari imekaa haina faida yeyote ile kwa sababu ya ukosefu wa reli.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho nataka nizungumzie ni kuhusu mazingira. Mazingira nchi hii tunakazi ya kuzungumza tu. Maji, tuchukue maji ya bahari tuchuje, mara tuchimbe mabwawa, hivyo mlishawahi kujiuliza Wabunge huko yanakotoka maji kuna mtu alienda kupanda mti hata mmoja? Tuna kazi ya kusema tu tabianchi.
Mimi kwangu pale Gairo kule Tarafa ya Nongwe kuna Mito Minne, Mto Msowelo, Mto Ludewa, Mto Mvumi, Mto Mkondoa ambayo inaenda Dakawa, inaenda Mto Wami. Ukienda kule mpaka Mbunge ufanye kuhemea uweke watu wawafukuze watu wasikate miti. Vyanzo vya maji vinakufa lakini hakuna Mamlaka yeyote inayoweza kupanda hiyo miti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunalalmika tabianchi, ukiangalia ukienda kwenye Wizara ya Maji wanamabonde, kuna Bonde Wami, Ruvu, kuna Bonde siijui la Kanda gani, ukija huku Mazingira wanatoa hela mpaka zawadi Million 50, lakini mtu anaepewa hizo zawadi za Million 50 na Mazingira wamepanda miti kwenye nyumba za gorofa mbele mijini, kule kwenye vyanzo vya mito hakuna! Ukienda TFS wapo, wanasimamia misitu. Basi waungane hawa kati ya maliasili, mazingira na hawa watu wa maji na hizi pesa wanazopewapewa za kupanda miti itafutwe Taasisi moja isimamie vyanzo vyote vya maji hapa Tanzania, zaidi ya hivyo tunapiga kelele! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunapiga kelele Mto Ruvu, lakini Mto Ruvu chanzo chake ni kule Morogoro Kusini, nenda kaangalie kila kona kuna ng’ombe! Ng’ombe peke yake wamemaliza ile miti yote, wamekula kila kitu, wamekata kila kitu, ukienda si ng’ombe tu wakulima wamefanya mashamba mpaka ile mbuga ilikuwa inaitwa Gode yote, sasa maji yatatoka wapi? Mnatafuta vyanzo vingine wakati mlivyonavyo tunashindwa kuvitunza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba sana hawa Maliasili, Wizara ya Maji na Wizara ya Mazingira wakae pamoja waangalie kama nikumkabidhi TFS wamkabidhi TFS kwa sababu sasa hivi yeye ana Jeshi atunze ile misitu na apange ile miti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni barabara ile ya kutoka Gairo kwenda Kilindi ya lami ambayo inaenda kukutanika na ile barabara ya kutoka Handeni mpaka Tanga kwenda mpaka Minjingu, ile Barabara ina ahadi ya Marais watatu, Rais Kikwete, Rais Magufuli lakini mpaka leo haijawekwa kwenye mpango naomba ikae kwenye huo mpango, kwa sababu ni barabara nyepesi kabisa. Ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami kuwa mmoja wa wachangiaji kwenye hotuba ya Wizara ya Fedha. Kwanza nitaanza kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha, maana kwenye ukweli lazima tuseme ukweli. Mimi huwa sipongezaji sehemu ambazo naona zina matatizo, lakini kama sehemu ni ya ukweli, tutapongeza sehemu ya ukweli na tutasema ukweli. Nitampongeza kwenye kufuta misamaha ya maduka ya majeshi. Hapa nampongeza. Kwa nini nasema nampongeza?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wale ambao hawajatembelea haya maduka au hawajawahi kupitia haya maduka, wanaweza wakaona wamefanya kosa kubwa sana, lakini kama ulishawahi kwenda kwenye haya maduka ukajionea kinachofanyika pale, utagundua alichokifanya ni sahihi kabisa. Niwapeni mfano mmoja tu, hapa Dodoma kuna duka la Magereza, liko hapa Magereza na hata sasa hivi ukienda liko wazi muda wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia wanunuzi wa vile vitu, mtu yeyote pale ananunua kwa msamaha wa kodi na kibaya zaidi viwango vya vile vitu ni vibovu vilivyopindukia. Unaweza ukaenda ukapata kitu cha Sumsung, labda TV ya Sumsung lakini ukiingalia ile inafanya kazi miezi sita, imekufa. Kwa hiyo, siyo kuwasaidia wanajeshi au siyo kuwasaidia watu askari wetu, hapo ni kuwaumiza na kuzidi kuwalia fedha zao kwa kutumia exemption. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hilo, niko tofauti kidogo na baadhi ya wenzangu kwa sababu naona kwamba hilo ni tatizo, liwekewe utaratibu mzuri ambao utawanufaisha hawa askari wetu, nao wataridhika, ndiyo cha msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa 64 anazungumzia kodi za magari na pikipiki. Mimi ni mfanyabiashara wa magari lakini leo sizungumzii habari yangu, nitazungumzia habari ya Watanzania. Amezungumzia usajili, sasa hapa hatujaelewa ni ule usajili wa mara moja, ukishasajili gari hulipii tena au ndiyo road licence?
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ni road licence, ukiangalia hapa kwenye pikipiki sh. 95,000/= kwa mwaka, hii ni pesa nyingi mno kwa mtu wa bodaboda. Kwa gari ni sh. 250,000/=, hiyo siyo shida. Kwa nini usiweke utaratibu mwingine? Ubadilishe utaratibu! Utaratibu huu ndiyo ule ambao ulileta matatizo miaka ya nyuma; na Bunge la nyuma watu walilalamika sana. Mabunge ya miaka iliyopita, TRA haiwezi ikaanza kufukuzana na watu wa bodaboda, hawana askari wa kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa Polisi wetu hawatoshi kufukuzana na watu wa bodaboda kisa hawajalipa hiyo sh. 95,000/=. Ibadilisheni system yake, iwekeni angalau katozo kadogo kwenye mafuta ili msiwe mnapata usumbufu wa kufukuzana na hawa watu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, pikipiki moja ikitumia lita saba tu kwa siku, kwa mwezi ina lita 210 kwa mwaka ina lita 2,520; kwa hiyo, ukimwekea shilingi kumi, atalipa 25,200/=. Ukienda kwenye magari kwa mfano, malori yanayokwenda nje na yanayotembea mikoani, kwa safari moja tu au tuseme kwa mwezi, weka kima cha chini, litatumia lita 4,800 pamoja hata na mabasi, kwa kima cha chini kabisa kwa mwezi. Ukiangalia kwa mwaka litatumia lita 57,600/=; ukiweka kwa shilingi kumi tu utakusanya sh. 576,000/=.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pamoja na kuwa bodaboda atakuwa amelipa kiasi kidogo cha pesa, lakini hawa wengine huku watakuwa wamefidia ile gharama na kufikia lengo la Serikali, kuliko kwenda kusukumana na hawa wafanyabiashara wadogo wadogo kufukuzana nao.
Nakumbuka mwaka juzi 2014 kilichotokea Morogoro, kutaka kuuana watu wa TRA na hawa watu wa bodaboda kwa ajili ya hayo mambo ya kufukuzana na watu wa bodaboda. Kamua ng‟ombe wako huku unamlisha majani, unamkamua polepole kuliko kwenda kufukuzana fukuzana huko. Wekeni tozo hii ya sh. 10/= tu kwenye mafuta imalize haya matatizo yote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine, sasa hivi hakuna asiyejua nchi hii ukame wa pesa ulioko mitaani. Kuna ukame mbaya sana wa pesa huko mitaani, nani asiyefahamu? Kama mfanyabiashara mkubwa leo hii ataweza kwenda kukopa Standard Bank, City Bank, Stanbic, lakini je, hao walipa kodi mnaowatarajia kuwaongeza, watakopa wapi? Watakopa NMB, watakopa CRDB, watakopa NBC, watakopa TIB na ukiangalia hizi Benki zina asilimia ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii wanachukua pesa zote; pesa za bandari, Mashirika ya Umma, wanazipeleka zote BOT; mzunguko wa pesa utatoka wapi ili hao watu wadogo wakope? Ni sawasawa na binadamu unaitoa damu yote unaipeleka kwenye kichwa ikae huko huko isizunguke, haiwezekani hiyo! Huo ndiyo ukweli wenyewe. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama mnaona mabenki yanafaidika, basi wapeni hizo pesa at least kwa interest, nao muwapangie interest kiasi cha kuwakopesha wafanyabiashara wadogo wadogo, lakini ukichukua pesa ukizipeleka BOT ambapo haina mzunguko wa aina yoyote kifedha, BOT Gairo haipo, BOT haipo Ngara, BOT haipo Sengerema, haipo Kaliua wala Kasulu, wanaenda kukusanya pesa zote wanaziweka. Wafanyabiashara nao wakiamua kukusanya pesa zao waweke kwenye madebe, kutakuwa na pesa nchi hii? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, lazima tuangalie, wakizizuia pesa sehemu moja kama BOT, wanazuia mzunguko wa pesa kwenye hili Taifa, maana yake itafikia sasa wafanyabiashara nao watachukua pesa nao wataweka kwenye debe lake hapeleki Benki. Wa bajaji naye ataweka kwake, sasa mzunguko utatoka wapi? Hao watu wanaokopa shilingi milioni mbili, shilingi milioni 10, watakopa wapi? Maana mfanyabiashara mkubwa ataenda kwenye mabenki ya nje, atapata pesa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tujiangalie, kama tunaona mabenki yanafaidika, basi hizi pesa tuziwekee mpango mwingine angalau hata tuwape hawa mabenki kwa interest lakini siyo kuzizuia sehemu moja hizi pesa. Tukizuia huo mzunguko, pesa itakuwa shida nchi hii, nakwambieni ukweli kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hili suala la mafuta, nashukuru kwamba kuongeza mafuta kwenye mafuta ya nje ni jambo jema kwa asilimia 10, lakini aangalie na viwanda vya ndani toeni kodi ya VAT kwenye viwanda vya alizeti vya ndani ya nchi na viwanda vingine vya mafuta. Kwa sababu mpaka sasa hivi ukiona mafuta ya nje yako sh. 50,000/=, ujue ya alizeti itatofautiana sh. 2,000/= tu bei yake, kwa sababu bado kuna kodi. Kwa hiyo, bado hujamsaidia mkulima hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi wakulima wadogo wadogo wote wana viwanda vyao vidogo vidogo; lakini katika vile viwanda vimetofautiana; yuko yule ambaye hajafikisha kodi ya shilingi milioni 100 ambaye haingii moja kwa moja kwenye VAT, anasaga alizeti na yuko yule wa kwenye shilingi milioni 20, 30 anasaga alizeti hiyo hiyo lakini hana VAT.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sasa usawa uko wapi? Usawa haupo. Ili upate usawa, viwanda vya ndani vyote vitolewe hiyo kadi ya VAT. Mimi sina kiwanda, lakini ukweli ndiyo huo; ili pale tuweze kupata hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, halafu kwenye ngano pale, mmezungumzia ngano kutoka asilimia 35 kuja asilimia 10. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi kuwa mmoja wa wachangiaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitaanza kwa upande wa TANESCO na ninataka niseme kwamba Mheshimiwa Waziri kwa upande huu pamoja na Naibu wako Bunge lililopita mliongea vitu vizuri sana kuhusu mipango yenu ya kusambaza umeme kwenye nchi hii na sehemu mojawapo uliyoigusa ilikuwa ni katika eneo la Jimbo la Gairo na maeneo ya Mpwapwa, Kongwa na sehemu nyingine ambayo tunatumia line moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mheshimiwa Waziri anakumbuka nilishakwenda kumlalamikia mara nyingi maeneo ya Gairo umeme unakuwa unakatikakatika sana na mojawapo ya sababu ni nguzo kuanguka hizi za miti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa bahati nzuri sasa hivi tunaona mnabadilisha mnaweka nguzo za zege, lakini hizi nguzo nazo naomba kwa ushauri wangu mjaribu kuziangalia. Hizi nguzo za zege ni fupi kuliko nguzo za umeme zile za miti hata mkiziangalia barabarani unaona ni vifupi vifupi na katika maeneo haya ya kuja Dodoma maeneo haya mpaka kule Gairo watu wengi wanajenga. Kwa hiyo, sasa mtawapa watu usumbufu wenye vile viwanja, otherwise mtaanza tena kuwaambia nunua nguzo ndefu ili labda kama kuna magari yanapita au nini kwa ajili yasiguse. Kwa hiyo, tunaomba muwe makini kwenye nguzo mzidishe kidogo urefu wa nguzo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naomba uharakishaji wa kile kituo cha kupooza umeme, kwa ajili ya kupata umeme wa kuanzisha viwanda katika maeneo hayo niliyoyataja kwa sababu sasa hivi huwezi ukaanzisha pale kiwanda cha mafuta wala kiwanda cha sembe kwa ajili umeme ni mdogo na bahati nzuri Gairo tuna bahati moja, katika Wilaya ya Gairo tunatumia umeme wa aina mbili; tunatumia umeme wa Bwawa la Kidatu na tunatumia umeme wa Bwawa la Mtera. Kwa hiyo, tunatumia umeme pote, pale pana switch kwa hiyo umeme wa Dodoma ukikatika tunawasha wa Morogoro lakini uwezo nao wa umeme ni shida.
Kwa hiyo, tunaomba na kile kituo cha Morogoro-Msamvu toka ile transfoma kubwa iungue hamjaweza kuweka tena transfoma kubwa. Tunajua mna mipango, lakini tunaomba ile mipango mharakishe kwa sababu mipango ya transfoma ile ndio itaweza kuweka umeme mkubwa Morogoro Mjini, Mvomero, Kilosa, Morogoro Vijijini pamoja na Gairo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna matatizo yanajitokeza bahati nzuri nawashukuru REA pamoja na TANESCO kwamba vijiji vyote vya Gairo vimo kwenye programu ya umeme na vimeshapata umeme, kasoro vijiji vya Tarafa ya Nungwe ambayo kuna milima mikubwa sana kama ya Lushoto. Sasa pale wakandarasi wa REA wameweka umeme karibu vijiji vyote, lakini kuna kisehemu ambako wako TFS, kuna misitu kama mita 400 au mita 300. Sasa wale hawataki kuachia ule msitu ili zile nyaya zipite wanadai shilingi milioni 400. Sasa mimi nashangaa Serikali kwa Serikali mnadaiana fedha ili wananchi wapate huduma, wakati wananchi wangu wamekubali kutoa mashamba yao na maeneo yao bure kupeleka huo umeme na hata hao wenyewe watu wa TFS watafaidika na huo umeme kwa sababu mashamba yao ya miti yale yatapata mashine sasa za kutumia umeme badala ya majenereta na dizeli kwa hiyo tunaomba hilo ulishughulikie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ahadi ya Waziri aliyepita Mheshimiwa Kalemani ya gari pale Gairo baada ya kuona yale maeneo ya mlimani na alisema pale pale na aliongea na Mkurugenzi aliyepita kwamba iende pale gari, zilikuwa gari mbili TANESCO moja iende Gairo lakini sasa sijajua je, haya matamshi ya Mawaziri akiondoka linakuwa la kwake binafsi au linakuwa la Kiserikali na Wizara? Naomba ile gari ya Gairo ya TANESCO ifike, tuliongea na wewe, tulimtafuta Mkurugenzi wa TANESCO lakini hatukumpata, naomba ile gari iliyoahidiwa kwa sababu ilikuwepo, tunaiomba ile gari yetu iwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni masuala ya bili za umeme. Bili za umeme ni shida sana, yaani kwa mfano nianze na watumiaji wadogo, yaani mtumiaji mdogo akiwa anaweka umeme wa shilingi 20,000 siku akijiroga tu labda awe na LUKU tu lakini kwa mfano kama ana mita siku akirogwa akiweka umeme wa shilingi 50,000 hata akifunga nyumba wale watakuja na umeme wa shilingi 50,000. Kwa hiyo, nikuambie Mheshimiwa Waziri TANESCO na Wizara yako usione watu wengi sana wamechomoka chomoka humu kwenye Uwaziri hata Mheshimiwa Muhongo, akina Mheshimiwa Kalemani, akina nani na nani sio kwamba walikuwa hawafai, walikuwa wanafaa, lakini watendaji wengi kwenye TANESCO ni matatizo. Kwa hiyo, unaliendesha halmashauri maana yake TANESCO na Wizara yako ni kama halmashauri fulani ya Wilaya hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mazingira mabovu mabovu ni mengi sana humo ndani, kwa hiyo wanafanya timing/kupanga na mimi nimekurushia bili mbili, wewe pamoja na Naibu wako. Kuna sehemu unatumia umeme kuna kitu kinaitwa KVA ile KVA ni nini? Mbona haieleweki maana yake unakuja mtu unaambiwa hapa umeme per unit, labda kwenye wale wanaotumia umeme mkubwa sasa wa viwanda na nini kama alivyosema Mheshimiwa Muhongo kwamba hamuwezi kuendelea bila kuwa na umeme mkubwa na wa bei rahisi. Lakini unapewa unit unaambiwa unit zako ulizotumia ni hizi bei yake ni shilingi milioni sita, halafu unaambiwa kuwa KVA shilingi milioni tatu halafu plus VAT. Sasa ukiangalia hii KVA hujui unaipata wapi, wala haisomeki mahali popote KVA ni kitu gani haijulikani ukiwauliza unaambiwa, unajua umeme ukizima ukiwaka unavyokuja kuwasha mitambo yako pale ndio hii KVA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa huo unawaka kila siku unawaka tu, kwa hiyo kila mwezi na nilikurushia kwa mfano moja kwa jengo moja la Morogoro na lingine la Dodoma; la Dodoma matumizi makubwa KVA shilingi milioni mbili katika shilingi milioni 10 KVA shilingi milioni mbili, jengo lingine la Morogoro matumizi shilingi milioni sita KVA shilingi milioni tatu. Sasa hii yaani tunaonekana kama ni aina fulani ya ujanja ujanja ambao hauna sababu yoyote ya msingi.
Kwa hiyo, hili neno KVA kama mnataka KVA iwepo basi bora muongeze tu bei kwenye unit na mtu anasoma, halafu hamumletei mtu zile mita zenu mnayofunga kubwa mtu hana access ya kusoma. Kwa hiyo, mpaka wewe umletee bili unavyotaka wewe, kwa hiyo unaweka unavyoandika wewe, sasa mteja anapata wapi mahali pa kuangalia pale? Kwa hiyo, hapo tunaomba sana mshughulike na hili suala. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nimeshazungumza sana masuala ya mafuta kuna sehemu umeyatekeleza tunakuunga mkono kwa hilo na tunajua wewe hujui chochote kwenye hii Wizara mgeni, lakini nataka nikuambie wewe ni mgeni, Katibu Mkuu ni mgeni Naibu Katibu Mkuu ni mgeni na Naibu wako Waziri ni mgeni. Nilishawahi kujaribu kuongea na wewe siku moja na ulishuhudia kitu nilichokuambia ukakishuhudia mwenyewe na ukakiamini.
Sasa nataka nikuambie haya mambo ya mafuta tunavyochangia najua mnahangaika sana watu wako kutujibu jibu hata kwenye ma-tv na nini, kama yule mmoja Kamishna wa Mafuta anahangaika anasema waliongea Wabunge na sisi mkitujibu na sisi tunajibia hapa, umeona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema hawa Wabunge mafuta yakija na mmehangaika sana, wameita hata semina juzi za Kamati tatu tu kuja kuwaweka sawa pale Hazina, lakini nataka nikuambieni sisi hatuchangii wala hatuchukii mtu, sisi tunachangia kwa sababu tunapenda nchi yetu na tunavyovichangia tunajua, unaweza ukawa profesa wa biashara lakini hujawahi kufanya biashara, unaongea kwa maneno. Unaweza ukawa profesa wa kilimo, lakini huna hata heka moja, kwa hiyo hujui hiyo biashara. Mtu anakuambia nikiagiza mafuta kwa kila mtu nchi italeta mafuta machafu, nchi itapata sijui upungufu wa mafuta toka enzi ya Nyerere, kaja Mwinyi, kaja Mkapa, kaja Kikwete mpaka mwishoni, tuonesheni nchi hii ilipata upungufu lini na ilikuwa inatumia system hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilikuwa inatumia system hiyo lini ilipata upungufu? Hakuna kitu kama hicho na mimi najua kabisa Mheshimiwa Waziri, wewe hujui lolote na ndio maana nilikuambia ukitaka ufanye vizuri hata hawa EWURA safisha kitengo cha…
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Shabiby.
T A A R I F A
MHE: TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumpa taarifa msemaji Mheshimiwa Shabiby kwamba TPDC toka mwaka 1970 inafanya biashara ya mafuta mpaka mwaka 2002, nchi hii ilikuwa haijapata kukosekana kwa mafuta na ilifanya kazi ya kutafuta petroli na TPDC ikafanya kazi ya kuuza mafuta na bei zikawa nzuri katika nchi hii ahsante endelea. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Shabiby, unaipokea taarifa?
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa yoyote inayokuja mimi napokea. (Kicheko)
Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wangu na Katibu, hebu jaribuni kuangalia juzi nilikuonesha kitu kimoja tu na nikakuambia twende tukapige simu huko uangalie bei za mafuta ni hizi? Kwa hiyo, sisi hatujasema hatutaki bulk procurement, tumesema iwepo lakini ipate ushindani na wawepo na watu binafsi, hakuna mtu amekataa bulk procurement isiwepo iwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hebu ingieni basi hata angalau angalieni kwenye gesi mlitaka muweke bulk procurement wale watu wa gesi wamekataa, leo gesi katika Afrika, Tanzania ni nchi ya kwanza yenye bei rahisi kuliko nchi yoyote ya Afrika, hamjiulizi swali na iko chini ya Nishati? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hao wataalam wanaokupakupa utaalam wewe ni utaalam wa maneno na wa masilahi, mimi narudia kusema hayo maneno. Kuwa mwenyewe na msiweke mtu wa kati. Mnaposema kwamba haya makampuni 28 yameomba kuomba kuleta mafuta, lakini tumechagua sita sasa sisi tunakuwa na uhakika gani si sita yale yale mnayoyapenda? Ninyi mruhusuni kila mtu alete na ile bulk procurement iwepo hiyo ndio ukweli, halafu nilitaka ujiulize swali moja tu na Wabunge wote mjiulize, angalieni toka wakati wa bulk procurement ilipoanza petrol station sasa hivi zinaota kuliko shule za kata. Sasa hapo mjiulize na kuna vitu vingine mimi nataka nikuambie ukweli mimi nitakupa kwa maandishi, sitaki nikupe ushahidi wa maneno maneno ninayoongea hapa, nitakupa kwa maandishi. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua wako wengine wamepata shilingi 2,000/shilingi 3,000 hapa hao tuachane nao, kuna watu duniani hawapo na mbinguni hawajafika wanaelea katikati tu umeona bwana. (Kicheko)
Mimi nataka nikupe kwa document, sitaki kuongea kwa mdomo nitakupa kwa document na ninashukuru kwamba umekubali ukaniambia kwamba nikuletee utafanyia kazi. Mimi naomba uliangalie, je, kweli kuna ukweli na hata Mbunge anayetaka naye aje nimueleweshe halafu aone tunavyotandikwa, ahsante sana. (Makofi/Kicheko)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na mimi kuwa mmoja wa wachangiaji katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziiri pamoja na timu yake yote katika Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, cha pili ni kuhusu barabara zangu za jimbo la Gairo ambayo ni ahadi ya aliyekuwa Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, ambayo aliitoa tarehe 26 Juni, 2014 tarehe 26. Kwanza ni shukuru, maana usiposhukuru na kidogo basi ujue wewe shukrani huna tu hata ukienda mbinguni huko ni hivyo. Ukiangalia hata kwenye youtube ukiandika tu Magufuli Gairo au Magufuli aitwa jembe Gairo utaona hotuba yake inakuja pale. Alitoa ahadi ya barabara ya kutoka Gairo kwenda Chakwale kwenda Kilindi kwa kiwango cha lami. Alitoa ahadi ya kuweka Mji wa Gairo kilometa 5 za lami Gairo Mjini. Alitoa ahadi ya Gairo - Nongwe kilometa 76 kuchukuliwa au kukasimiwa na TANROADS. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nasema hivyo kwanza na mpongeza Mheshimiwa Rais, na ninamshukuru Mheshimiwa Rais na ninamshukuru Waziri wa ujenzi kwamba; nikiangalia katika hotuba ya kitabu cha Waziri wa Ujenzi ukurasa wa 339 naiona barabara ya Nongwe imetengewa zaidi ya milioni 900 na kwa bahati nzuri mkandarasi wa kuweka lami Gairo Mjini tayari yupo kazini pale na anaendelea kazi ya kuweka zile kilometa tatu za lami.
Nilikuwa namuomba Mheshimiwa Waziri, kwamba katika ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kilomita 5 zimebakia kilometa mbili, na wakati Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi anatupa ahadi ya unjezi wa kilometa tano alikuwa anaelewa matatizo yaliyopo pale. Kwa hiyo, tumepewa kilometa tatu lakini tunaomba hizi kilometa mbili zimaliziwe haraka, kwa sababu mwaka huu sijaziona kwenye bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ukiacha hizi kilometa tatu peke yake ni sawa sawa na mtu kumvalisha koti la suti halafu chini umemvalisha kaptula. Kwa hiyo naomba tumalize hizi kilometa mbili. Vilevile nikiangalia ile barabara ya kutoka Gairo kwenda Kilindi kwa ndugu yangu Kigua, ambayo ingesaidia hata watu wanaotoka Iringa kupitia Dodoma, Zambia wapi kwenda bandari ya Tanga kwa sababu pale ni karibu sana kutoka Gairo mpaka Kilindi ni kilometa 100 tu nayo haimo kwenye bajeti. Kwa hiyo na washauri na najua hii Wizara ni sikivu mtaweka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, cha zaidi ambacho nilitaka kukiongea kwa leo ni kuhusu habari ya mashirika ya umma. Watu wengi wamepongeza sana mashirika yote ya umma ambayo yako chini ya Wizara hii ya Ujenzi. Wizara hii ya Ujenzi ni moyo wa nchi, Wizara hii ina taasisi 37, na moja ya hizo Taasisi kubwa nizitaje chache kuna TTCL, Posta, Bandari, ATC, TRA, hizo nikutajie tano ambazo zote ni kubwa kabisa. Nataka niseme kwamba namshukuru Mheshimiwa Rais, nimpongeze pamoja na Mheshimiwa Wazari na Mheshimiwa Naibu Waziri na Makatibu wa Wizara hii wote kwa kupata Bodi ambazo zinaongozwa na watu ambao wana weledi, wajumbe wenye weledi na ma-CEO. Ukichukua taasisi zote nilizozitaja ma-CEO ni vijana na ni wazuri kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, wasiwasi wangu uko wapi? Haya mashirika ambayo yako kwenye hii Wizara ukiangalia sana ya natakiwa yaendee kibiashara. Shirika la Reli lazima liende kibiashara, TTCL lazima iende kibiashara, ATCL lazima iende kibiashara, Posta lazima iendee kibiashara, bandari lazima iendee kibiashara hata Mheshimiwa Rais wakati ananua ndege alijua kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika hakuna watu wanafiki kama baadhi ya sisi Wabunge. Miaka ya juma tunapiga kelele tunafananishwa na Rwanda. Rwanda wana ndege sisi hata kimoja hichi kibovu bovu, leo ndege zimekuja mnaanza kusema ndege sio kipaumbele cha kwanza. Mimi nasema vyote ni vipaumbele, lakini viongozwe kwa mujibu wa sheria za kibiashara, hicho ndio cha msingi. Kwa mfano, unaunda
Bodi, zina madaktari, zina maprofesa zina wajumbe safi halafu baadaye tena hapo hapo yanatoka maagizo, matamko kutoka huku ya naingilia kwenye ile Bodi. Sasa kuna faida gani ya kuweka Bodi mpya? Acheni watu wafanye kwa kutumia utaalamu wao. Kama mmeweka Bodi basi acheni Bodi pamoja na ma-CEO wao na Menejimenti zifanye kazi yake; lakini kutakuwa na faida gani ya kuweka bodi mpya halafu mnaziingilia ingilia? Hii ni biashara jamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni wapeni mfano mmoja hili shirika letu la TTCL; hili ni shirika ambalo lingekuwa linachangia uchumi wa Taifa. Tuchukue mfano wa shirika la simu la Ethopia, kwa mwaka wanatengeneza dola bilioni 3.3, ukitoa kodi wanabaki na dola bilioni 1.5. Kwenye mfuko wa Serikali wanachangia karibu dola milioni 300, hiyo ni sawa sawa na bilioni zaidi ya 700 za Tanzania. Sasa haya sio tunawategemea TRA lazima tuwe na mashirika ambayo yataingiza hela kwenye Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia uwekezaji wa TTCL, ili ifike Tanzania nzima itachukua zaidi ya miaka, na ikimaliza kufika huko vijijini na sehemu nyingine hawa Vodacom na kampuni zingine kama Tigo, watakuwa tayari wana mitandao mipya. Wakati huko huko Serikali tena ina asilimia 40 kwenye Shirika la Airtel, kama Wabunge hawafahamu. Asilimia 40 ya Airtel ni hela ya Serikali ya Tanzania, lakini toka hizo asilimia 40 ziwekwe kwenye Airtel kila siku Airtel wanapata hasara hawaleti faida hata shilingi moja kwenye Serikali. Sasa kwa nini hizo hisa za kwo 60 zilizobakia tusizinunue ziwe za Serikali (TTCL) halafu tutakuwa tayari tumeshajigawanya, tumeshachukua mitambo ya Airtel tunakuwa tayari tuko Tanzania nzima na tunaingia kwenye compentintion? Kuliko kuacha asilimia 40 wakati ilie asilimia 40 kila siku hawapati faida. Kwa hiyo, hela ya Serikali imekaa tu Airtel. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukija kwenye shirika la ndege; uwekezaji wa ndege si mchezo. Ukiwa bilionea ukitaka kuwa milionea ingia kwenye biashara ya ndege. Inataka lazima muwe na mtaji na lazima uweke mtaji.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, ila hilo shirika linatakiwa lipewe hela lijiendeshe, TTCL.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa nimshukuru Waziri wa Fedha na Naibu wake na wataalam wote, na waliomshauri kutengeneza bajeti hii. Washauri wote wamefanya vizuri sana; kazi yetu sisi kama Wabunge ni kushauri, na ninajua kabisa wao ni wasikivu, watasikia zile sehemu ambazo tunashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza kwanza kidogo tu kuhusu masuala ya magari. Umezungumzia magari kwamba sasa income tax yake itakuwa ni 3,500,000 pamoja na mabasi makubwa, lakini najua umezungumza kwenye yale magari makubwa hujaenda kwenye yale magari madogo. Kwa hiyo ninaomba muweke mchanganuo vizuri wasije wakachanganya tu gari kubwa na dogo likawa na kodi moja. Lakini na hiyo nayo tunaomba angalau ipungue, kwa sababu 3,500,000 ni kubwa, angalau ingekuja 2,500,000 au hata 3,000,000.
Halafu ya mafuta kuchukua ile faida ya mwenye kituo cha rejareja shilingi 20 katika faida yake ya shilingi 100 ikumbukwe kwamba kuna wengine wana faida ya shilingi 70, kwa hiyo ukishamchukulia tena shilingi 20, ni sawa, hiyo itaondoa milolongo mingi, lakini sasa iwe ndiyo inafaa lakini iwe imekwisha, siyo tena baadaye mnaanza tena hesabu, kunakuwa tena kuna usumbufu ambao si wa kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie kingine, kuhusu magari. Katika bajeti yako umezungumza kwamba sasa hivi watumishi wa Serikali mtawakopesha magari, lakini sasa hapa hujaliweka sawa au tunaomba ukija uliweke sawa; unawakopesha magari, magari yale ukishawakopesha yanakuwa ni ya kwao, na gari likishakuwa mtu ya kwake huwezi tena ukampangia kwamba hili gari sasa hivi labda mtu Mkurugenzi wa Dodoma ukamwambia nenda kijiji fulani. Kitakachotokea ni kwamba watakuwa wanayachunga sana magari yao, kwa hiyo na zile safari za kiserikali au za kwenda kutembelea wananchi zitapungua, huo ndio ukweli. Kwa sababu hawatayatumia kama wanavyoyatumia magari mengine kwa sababu watakuwa wanayaonea huruma na watapunguza safari. Au kuna mpango, je, mtakuwa mnawalipa? maana gari nimeshaikopa, ni yangu, sasa una nilazimisha tena niende nikafanyie kazi nyingine ambayo si yangu. Hiyo nayo tunataka ufafanuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ushauri wangu ni kwamba kwenye magari mimi nilikuwa nafikiri tu Serikali mjaribu kudhibiti na mjaribu kutoa miongozo. Nakumbuka kuna Mbunge mmoja Musukuma, aliwahi kulalamika kuhusu Mkurugenzi wake kanunua VX V8. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge; lakini ni kweli hamna mwongozo wa Serikali kuonesha kwamba hapa Wakurugenzi labda wa wilaya, Wakurugenzi wa halmashauri si watumie tu Land cruiser tu na double cabin? Wekeni miongozo kama hii; yaani pawe level ya watu kutumia magari ya V8.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi Serikali mnataka mwende na fashion, leo hii kuna watu tayari hapa wana LC300 hizi new model Land cruiser za milioni 500, zipo. Sasa muwe mnaangalia; kama Serikali mnataka kwenda na fashion ninyi ndio mnaleta hasara kwenye hii nchi; muangalie. Kuna watu kama Mawaziri, Rais Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na watu wengine sawa wakitumia magari kama hayo; lakini kuna sehemu zingine huku muwapangie magari gani ya kutumia, double cabin, watumie labda level nyingine, watumie gari hizi prado ndogo, wengine watumie hata crown kama sisi Wabunge; mbona sisi hela mnazotupa ni za crown?
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba hela anayopewa Mbunge anapewa hela ya kununua crown mpya, lakini huko nje watu wanajua Wabunge wanakopeshwa ma-V8. Ukimuona Mbunge ana V8 ujue hela kaongeza ya kwake mwenyewe, ndio ukweli huo. Piga hesabu, hela unayompa Mbunge haifiki milioni 100, ananunua gari gani mpya kama siyo crown new model? Ndio ukweli. Sasa huko Serikalini mjibane. Sisi hatuna TEMESA Mbunge unatengeneza gari mwenyewe kila kitu mwenyewe, hupeleki TEMESA. Mtu wa Serikali anapeleka TEMESA anapeleka wapi na bado unataka kumpa gari la gharama; ndiyo maana mnaibiwa. Nataka nikuambie Mheshimiwa Waziri, wewe ni msikivu, fanya uchunguzi, hata hii kampuni ya Toyota spare zingine zinazouzwa siyo original; na mimi nilimwambia Mheshimiwa Mbarawa kwenye kamati ya Miundombinu; kwamba hata spare siyo original; fanyeni uchunguzi ninazo huku. Kwa hiyo mnapigwa sehemu nyingi sana.
MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa
T A A R I F A
MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango mzuri wa Mheshimiwa anayechangia katika kubana matumizi ya Serikali lakini cha ajabu kwenye sensa wameleta mwongozo wa kununua Rover Four kwa milioni 129 ilhali tofauti na Land cruiser ni milioni mbili naomba nichangie tu hivyo.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ahmed Shabiby unaipokea hiyo taarifa?
MHE. AHMED M. SHABIBY: Naipokea kwa mikono miwili. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri tunajua kabisa wewe na watu wako wote ambao mko mnapanga hiki kitu, mnalitakia Taifa hili mambo mazuri; tunaomba muangalie, wekeni mwongozo wa magari namna ya kufanya, au kama mna mpango wa kuwakopesha basi mtatuletea tutaujua vizuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine amezungumzia habari ya interest. Tunaona kwenye kila hotuba za kila kiongozi anazungumza interest ni kubwa kwenye benki. Benki zijitahidi kupunguza interest; lakini sielewi. Yaani ni vipi mnakuwa mnafumba macho? Hivyo fedha zote za Serikali, na nyinyi Serikali ndio wenye mtaji mkubwa, zote mnapeleka BOT? Kwa mfano kuna fedha za bandari, TANAPA, TANESCO na za mashirika mengi tu; na hata haya mashirika ya mifuko wa jamii sasa hivi mmeachia kidogo, lakini nusu ziko BOT nusu ziko huku. Kuna baadhi ya taasisi zina hela zao ziko kule BOT zaidi ya miaka mitano hazizalishi wala hazifanyi chochote. Kama mnadhibiti hizi fedha lakini mjue kabisa kwamba fedha yoyote inayokwenda kwenye benki za nje ni Commercial Bank peke yake, ndizo zinasambaza fedha kwa watu, na ndivyo fedha zinakuwa nyingi kwa wananchi wa kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunalalamika fedha hamna lakini fedha mmeziweka wenyewe kule halafu hapo hapo tena mnakuja tena mnakopa kwenye benki hizo hizo, lakini fedha mnaziweka kwenu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano mkichukua hela zenu zile mnazoweka BOT ambazo hazizai ukiweka kwenye benki za biashara hata kama unazitumia kila siku, unatoa na kuingiza lakini unapata asilimia 3.5. Ukiziweka fixed account unaweza ukapata asilimia sita mpaka saba; kwa hiyo wewe utamkopesha mtu kwa asilimia kumi au tisa, zile benki za biashara zitayakopesha kwa asilimia tisa au kumi. Lakini leo wenye pesa nyingi mnazikumbatia; sasa hivi mnatisha hata wafanyabiashara. Kama ninyi watu wa Serikali hamuamini hizi benki, mna wasi wasi nazo na hata sisi sasa itabidi tutengeneze makabati nyumbani tuwe tunaficha hela zetu, na huo ndiyo ukweli. Yaani lazima mbadilishe hii sera yenu, kwamba kwenda kuweka mabilioni na fedha zote hazikai kwenye mzunguko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu wajiangalie, kwenye treasury bond kuna watu wanaweka pesa wanapata asilimia 15, sasa nani atakayefanya kazi? Sasa hivi mmeshusha mmeweka asilimia 12, mnamwambia mtu aweke miaka 25 mpaka miaka 20 mtampa asilimia 12.5, tena mmeshusha juzi, lakini ziko mlikuwa mnawapa mpaka 15%. Sasa mtu akishaweka hela pale zinakaa kule mtu anakula interest, ana haja ya kuzungusha hiyo fedha? Na ninyi mnawaambia benki washushe, watashushaje hiyo interest kwetu haiwezekani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano mlivyo wafanyakazi, wafanyakazi leo mnatumia Benki ya CRDB na NMB. Ile payroll mnatayarisha Wizara ya Fedha, check list Utumishi. Mnapeleka fedha kule wana-charge service charge, si mbaya ni ki-benki. Lakini angalia mfanyakazi wa umma, huku CRDB ana 13% imeshushwa juzi huku NMB sijui 15%; na hawezi ku-negotiate kwenye kupata mkopo. Lakini mfanyakazi wa mtu binafsi atakwenda benki atafanya negotiations, kwamba tunatakiwa hapa tufanye hivi hivi itakuja hata 12% hata 11%. Sasa, ili kuwasaidia watumishi wetu bora Wizara ya Utumishi ingekuwa inaweka tu kama tender. Kwamba, jamani watumishi wetu mwaka huu wanataka kukopa, benki zijitokeze zilete interest yake, na atakayeonekana ana interest ndogo ndiye aruhusiwe kukopesha watumishi wa umma lakini msiwabane…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Shabiby
MHE. AHMED M. SHABIBY:… nilikuwa bado naendelea; basi ahsante, naunga hoja mkono.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuwa mmoja wa wachangiaji katika hotuba hii iliyopo mbele yetu. Leo nilikuwa sitaki kuchangia habari za haya mambo ya Road License lakini imenibidi nichangie kidogo tu ili tuelewane vizuri tu siyo labda kwa kushindana au nini ila kueleweshana tu.
Mheshimiwa Spika, nafikiri kama Waziri wa Fedha angefuata yale mawazo yetu ambayo tulikuwa tunampa siku tano za nyuma basi ina maana kwamba angepandisha Sh.140/= kwenye bei ya mafuta, asingepandisha Sh.40/=. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, hii ni kwa sababu Wabunge wengi tuliokuwa tunachangia humu, mimi sikupata nafasi lakini wengi walikuwa wanasema kwamba, Sh.50/= weka kwenye maji, Sh.50/= weka REA na Road License weka kwenye mafuta. Sasa leo kwa busara zake tu akaamua kuweka Sh.40/= tu peke yake ile Sh.100 akaiacha lakini bado na hii nayo tunamgeuka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Ndugu yangu hapa Mheshimiwa Kamala yeye ni Mwalimu, ameeleza vizuri sana na mimi sasa ni Mwalimu wa huko mtaani nitawaeleza kidogo. Kwa hesabu tu nyepesi, niwape hesabu nyepesi tu, Road License gari lenye CC2500 ilikuwa inalipiwa Sh.200,000/= kwa mwaka. Sasa tuchukue mfano tu mwenye gari hiyo, maana yake tuangalie kwanza hawa watu wa kawaida, kila siku akijaza lita 10 ya mafuta kwa mwezi atajaza lita 300. Akijaza lita 300 ukiweka mara ile Sh.40/= kwa mwezi analipa Sh.12,000/=, ukiweka ile Sh.12,000/= kwa mwaka analipa Sh.144,000/=. Kwa hiyo, hata hiyo Sh.200,000/= bado hajafika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niwapeni mfano mmoja, tunaposema kwamba usafiri utapanda sijui kilimo kitapanda, Mungu ananisaidia mimi ni mkulima na msafirishaji, lazima ku-declare interest, bei ya EWURA ya mwezi huu tuliomaliza nao ilishusha dizeli kwa Sh.81/= na petroli kwa Sh.30/=, kwa mwezi huu wa Tano tuliomaliza. Mwezi huu bei iliyotangazwa juzi, dizeli imepanda Sh.43/= na petroli imepanda Sh.25/=. Kwa hiyo, hata ukiweka na hii Sh.40/= hatujafika bei ya mwezi wa Nne na bado hizo nauli zipo pale pale. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna mtu jana alizungumza, nataka nizungumze kweli, bei ya mabasi iliyotolewa na SUMATRA imetolewa miaka mitano iliyopita lakini mpaka leo hakuna basi limefikisha ile bei waliyopangiwa na SUMATRA, hakuna. Dar es Salaam – Arusha ni Sh.33,000/= lakini watu wanaenda kwa Sh.25,000/=; Dodoma – Dar es Salaam ni Sh.24,000/= watu wanaenda kwa Sh.17,000/= mpaka Sh.20,000/=. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka niseme hii kodi, hata Wabunge wengine wapo upande wa CCM na wengine wapo upande mwingine, walikuwa wanasema iingie kwenye maji, tumetoa Road License na gharama za Road License zilikuwemo kwa wasafirishaji hata msingepandisha mafuta walikuwa wanalipa Road License, kwa hiyo gharama ilikuwa ipo pale pale tu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, gharama hii ya Road License ibaki kama Road License kwenye mipango yake ya Serikali. Kama kuna mpango mwingine wa kupandisha maji basi tuweke tena Sh.50/= nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tusiingize hii huko kwamba tuitoe kwenye mipango yake ya Serikali, sijui ifanye hiki na kile kwa sababu hata usipopandisha mafuta, ukiacha Road License si ni pesa msafirishaji ataingiza tu ile.
Mheshimiwa Spika, nataka nizungumze tu ili watu walielewe hili suala vizuri, hii ni nchi yetu. Kule China watu walikuwa wanavaa chunlai siyo kwamba walikuwa wanapenda, leo wanavaa bluu watu wote kesho kijani, walikuwa wanafunga mikanda ili wafike mahali wanapohitaji. Kwa hiyo, twendeni tufunge mikanda tufike mahali tunapotaka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kitu kingine huyu Ndugu yangu Mheshimiwa Mpango leo nampa shikamoo. Mara ya kwanza humu tulikuwa tunakujadilijadili, tukaona huyu jamaa mpole sana kwa sauti lakini mbona kama haelewielewi, hataki ushauri.
Mheshimiwa Spika, lakini sasa hivi kwenye Bunge hili tumegundua kwamba katika watu wanaopenda ushauri Mheshimiwa Mpango naye mmojawapo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka niseme kwa nini nimempa shikamoo. Ukiangalia taarifa ukurasa wa 54…
TAARIFA....
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Taarifa yake naipokea kwa sababu ni rafiki yangu huyu najua ananichangamsha tu, hakuna hata matatizo lakini najua nilishamwambia kwamba ni mkulima na mfugaji, ni rafiki yangu Waitara hakuna matatizo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, kwa nini nilikuwa nasema Mheshimiwa Mpango shikamoo, amerudi pale pale kwenye vile viwanda vya Mwalimu Nyerere. Hii ni kwa sababu ukiangalia ukurasa wa 54, kipengele cha tatu, amezungumzia kupunguza ushuru wa vile viwanda vitakavyoletwa kwa ajili ya kuunganisha matrekta, boti na magari. Ametoa ushuru huu wa Corporate Income Tax kutoka asilimia 30 mpaka 10. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini nataka nitoe ushauri, mpaka leo hakuna mtu aliyefikia rekodi ya mzee wetu Mwalimu Nyerere. Wakati ameanzisha kile Kiwanda cha TAMCO pale Kibaha cha kuunganisha magari ya Scania, pamoja na kuwaambia wawekezaji waje lakini aliwapa masharti ya kununua bidhaa zinazotengenezwa Tanzania ili kuunganisha yale magari.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, rejeta zote zilizokuwa zinatumika kwenye magari yote yaliyokuwa yanaunganishwa Tanzania zilikuwa zinatoka kwenye Kiwanda cha Serikali kinaitwa Afro Cooling, betri zote zilikuwa zinatoka kwenye Kiwanda cha Serikali kinaitwa YUWASA, wiring zote zilizokuwa zinafanyika kwenye magari zilikuwa zinatoka East African Cable, matairi yote yalikuwa yanatoka General Tyre, spring zote zilikuwa zinatoka Tasia Spring na muffler zote zilikuwa zinatoka Tanzania kwenye kiwanda cha Serikali. Sasa hapo ndiyo unaongeza ajira kwa sababu bila kufufua viwanda kama General Tyre, Afro Cooling na viwanda vyote nilivyovitaja na vingine viko vingi tu bado kuna tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ulikuwa ukiangalia ile gari ilikuwa inatengenezwa na Watanzania kwa asilimia zaidi ya 18. Kwa hiyo, ile gari ili ifanyiwe assemble hapa hivi viwanda vingine vyote vilikuwa vinafanya kazi na vinatoa ajira nyingi sana kwa Watanzania. Kwa hiyo, naomba kwenye huu ukurasa wa 54 hapa basi aweke hayo masharti ya kwamba mwekezaji yeyote atakayekuja kuunganisha magari hapa Tanzania basi lazima atumie bidhaa za Tanzania. Namwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha ajitahidi juu chini ahakikishe hivi viwanda vinafufuka kama General Tyre, Afro Cooling… (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hivyo namwomba Mheshiiwa Waziri afufue hivi viwanda ili hii dhana yake iende vizuri.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Kwanza, nianze kumpongeza Mheshimiwa Mawaziri wote wawili pamoja na Naibu Mawaziri wao na Katibu Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka kujikita kwenye Jimbo langu na hasa kwenye Kituo cha Afya cha Gairo kwa sababu Gairo ni Wilaya lakini bado haina hospitali ya Wilaya. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri baada ya kufika Gairo na kuona kwamba kile kituo cha afya kina umuhimu sana na kiko katikati ya barabara ya Morogoro Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo kile kinapokea majeruhi wengi sana na wagonjwa wengi kutoka Wilaya ya Kongwa ambayo imepakana nayo, Wilaya ya Kilindi pamoja na Wilaya ya Kiteto. Kituo kile kimekuwa ndiyo sehemu yao ya hospitali yao ya rufaa pamoja na kuwa ni kituo cha afya. Namshukuru pia kwa kutupa pesa milioni 400 kwa ajili ya kujenga majengo ya operesheni na mambo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo moja cha ajabu sijui huku TAMISEMI kwa hawa Wakurugenzi wa hizi Idara nini wanafikiria, nini wanafanya na wanaangalia kwa vigezo gani kugawa watumishi kwenye wilaya, bado sipati jibu, leo nimeheshimu tu, lakini siku nyingine kwa kweli hatutoelewana hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Mheshimiwa Waziri anajitahidi, lakini Wilaya ya Gairo kituo hicho cha afya na Wilaya nzima wametuletea mwezi wa Novemba mwaka jana Wauguzi Wasaidizi watatu, wakati upungufu ni zaidi ya Wauguzi 70. Wametuletea Matabibu wametuambia ni Matabibu baada ya kuwachunguza kumbe ni Matabibu Wasaidizi, tumewarudisha huko watubadilishie mpaka leo hakuna kibali cha kubadilisha ili waajiriwe. Kwa hiyo, ina maana hatukupata mtumishi yoyote kwenye kituo cha afya cha Gairo na Wilaya nzima ya Gairo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mpango wa kufungua vituo vya afya vitano, lakini hatuna Matabibu wala hatuna Wauguzi. Ukija kwa wale Madaktari pale ni sehemu ya barabarani nimesema ile ndiyo ‘Tumbi’ ya Dodoma - Morogoro kwa sababu mtu yoyote akipata matatizo na ukiangalia hata idadi ukisoma ya accident nyingi zinazotokea katika maeneo yale, Madaktari wenyewe operesheni na Madaktari wengine tunahitaji zaidi ya wanne au watano lakini hatujapata hata mmoja. Sasa sielewi ni nini kinachofanyika hapa kwenye hizi Idara zenu za TAMISEMI. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija hata watumishi katika Halmashauri ya Gairo; ukienda uhasibu hakuna watumishi wa daraja la pili, halafu leo tukipata hati chafu watatufungia hiyo Halmashauri kama alivyozungumza Waziri Mkuu? Haiwezekani kwa sababu watumishi Wahasibu hawapo! Utumishi kwenyewe hamna kitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru dada yangu hapa Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu ametupatia gari la wagonjwa, Wilaya ile haina kabisa magari ya wagonjwa. Bahati mbaya ina Tarafa nyingine kutoka Gairo ni kilometa 100 inaitwa Tarafa ya Nongwe, hii Tarafa milima yake ni kuliko milima ya Lushoto, nako wanahitaji gari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo gari lililoletwa na Wizara ya Afya nalo halina Madereva. Halmashauri imeomba kuajiri Madereva watano lakini kutoka Wizara ya Utumishi hakuna kibali mpaka leo. Kwa hiyo sasa mnataka hiyo gari aendeshe Mbunge? Matatizo tupu! Naomba sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu shule za Msingi wale wengine wenye vyeti feki wameondoka wengi na mwaka huu wanastaafu Walimu 50 na sasa hivi pana upungufu wa Walimu zaidi ya 270. Kwa hiyo, shule za msingi utakuta kuna shule sasa hivi ina Walimu wawili ama Mwalimu mmoja. Sasa ndugu zangu wa TAMISEMI sielewi ni vigezo gani wanavyotumia kutafuta hawa watumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine, wakati tunatoka Wilaya ya Kilosa kugawanya kuwa Wilaya mbili tuliangalia ukubwa wa eneo Wilaya ya Kilosa ilikuwa na Tarafa saba, tukakubaliana kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kwamba ianzishwe Wilaya ya Gairo kuwa na Tarafa tatu, Tarafa ya Nongwe, Tarafa ya Gairo na Tarafa ya Magole.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikatokea baada ya ile Wilaya kuanzishwa uchaguzi wa 2010 ulishafanyika, kwa hiyo Mheshimiwa Rais aliyepita akasema sasa itabidi kwa sababu huku wamechagua Mbunge na huku nako wameshachagua Mbunge kwa hiyo NEC wametuambia baada ya zoezi hili likishapita wakati wa uchaguzi 2015, ile Tarafa ya Magole irudi Wilaya ya Gairo kama ilivyoamuliwa hapo mwanzo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, 2015 ile Tarafa haijarudishwa, kwa hiyo utashangaa wa pale Gairo ukitoka kilometa sita unakuta tena kijiji kipo Wilaya ya Kilosa, Berega yote, Kiegeya yote hata pale wanakouza viazi kwa mbele pako Wilaya ya Kilosa, kwa hiyo wanawatesa wananchi bila sababu. Wale Wapinzani sasa wameingia na majungu wanasema kwamba Mbunge wa Gairo hawapendi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna lingine liko kwenye Utumishi; hili lazima tulizungumze wazi mimi ni Mbunge wa CCM na nimepitia kwenye ngazi nyingi nimekuwa Kamanda, nimekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, nimekuwa Mbunge miaka mingi sana kwenye hiki Chama. Sasa hivi kuna watu kwenye ofisi za Serikali huku kwenye utumishi wanatafuta mbinu ya kujifanya watu wanafanya kazi zao lakini kuichafua Chama cha Mapinduzi na kuchafua Viongozi wa Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Kijana yule Abdul Nondo ana umaarufu gani mpaka wamwite kwa kutumia vyombo vya habari, hawawezi kufanya investigation, wafanye investigation, wamwandikie barua anaitwa, lakini hapo ni kutaka kuichafua tu wanataka kuichafua Serikali ya CCM kwamba aambiwe yule kuna mbinu ya aina yoyote anatafutiwa, ana umaarufu gani mpaka yule mtu wa Immigration aende akakae anaanza anataka cheti cha bibi, cheti cha mjomba, cheti cha babu mpaka aandike kwenye vyombo vya habari? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawapa watu umaarufu wakati kesi iko Mahakamani mtu anapatikana, kuna watu wengine watatumia ile kusema mmeona sasa, Serikali ya CCM ikimtaka mtu inaanza kumwambia siyo raia, wakati siyo kweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kwenye utumishi waambieni watu wenu, televisheni kila mtu anaipenda, lakini uwe na mambo ya maana ndiyo uende ukajiangalie kwenye televisheni. Sasa itakuwa basi kila mtu akitaka kitu anatoa taarifa kwenye televisheni au kwenye mitandao siyo sawa! Wanachafua Serikali yetu wakati hakuna mtu mwenye habari na mtu mdogo kama yule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kwenye utumishi tuangalie haya masuala, mnayaona ya kawaida lakini kuwapa watu maneno na mambo mengine ya kuongea au watu kufikiria au kuwasababisha watu wajue kwamba Serikali inamtafuta yule kijana, wakati Serikali nina uhakika kabisa haina mpango na mtu mdogo kama yule kwa sababu hana madhara yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ndiyo yangu, ahsanteni sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kuwa mmoja wa wachangiaji katika Wizara yetu hii nyeti ya Wizara ya Maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikisimama mara nyingi sana kuchangia Wizara hii Wizara ya Maji. Pale Gairo pana mradi wa maji sasa hivi una muda mrefu, lakini kila nikisimama au kila Wizara ikileta bajeti ule mradi uko asilimia tu 84 na mwaka unaofuata unashuka unakuwa asilimia 75. Kwa hiyo, sasa sielewi mwaka mwingine unapanda bado haujaisha mwaka mwingine unashuka. Kwa leo sitaongelea sana huu mradi ila nitatoa ushauri kwa sababu nimeona kwenye gazeti la Mwananchi la tarehe 3 kwamba sasa hivi anatafutwa mzabuni wa kuweza ku-supply pump pamoja na mashine ya kuchuja chumvi ambayo ina uwezo wa kuchuja zaidi ya lita nafikiri kulingana na matenki zaidi ya mita milioni moja au zaidi kwa siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara kwa mpango huo nimeona kwenye gazeti la juzi hapa la terehe tatu, naomba iwe kweli kwa sababu huu mradi kwanza utakuwa ni mradi wa mfano kwa sehemu zingine za nchi yetu, kukuta maji mengi chini ya ardhi ni suala lingine na
kukuta maji salama ni suala lingine, unaweza ukachimba maji lakini ukakuta yana chumvi na ukienda kupima hayafai kwa matumizi ya binadamu. Kwa hiyo, siyo kila sehemu yenye maji mengi kwamba ni baraka unaweza ukakuta maji lakini yana chumvi ambayo hayafai kwa matumizi ya binadamu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi ule wa Gairo itakuwa ni mwanga kwa Wziara na sehemu zingine zote ambazo zina maji chini lakini hayafai kwa matumizi ya binadamu, nafiki ni mradi wa kwanza Tanzania ambao maji yatachunjwa sasa na kuwa maji salama na wananchi kutumia, naomba utekelezaji. Kwa sababu ule mradi ni wa muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tofauti na Wabunge wengine waliotangulia, siwezi nikasema Wizara ya Fedha haijaleta pesa haijaleta nini, tayari ule mradi wa shilingi 6,666,000,000 mkandarasi amechukua zaidi ya asilimia 80 ya pesa ameshachukua tayari, lakini haujakamilia sasa mimi siwezi kulaumu, siwezi kusema hapa pesa iko wapi haiwezekani! Hata huyo Waziri wa Fedha kama amezuia pesa bora azuie tu, kama asilimia 80 imechukuliwa na bado utekelezaji wake hata hauna dalili sasa hizo pesa zinakwenda wapi!
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wangu hapa amejitahidi sana pale Gairo na nushukuru tumemuomba aje pale Gairo na anakuja na nafikiri atakuja kwa ajili ya miradi ile ya maji kuja kuangalia. Atakuja Mvomero, atakwenda Gairo anaangalia miradi kwa sababu pesa tayari Kilosa, Mvomero, Turiani, Gairo, lakini kasi iko wapi ndugu zangu? Ingekuwa pesa haijatoka mngesema kweli hapa pesa haijatoka kuna matatizo, labda Wizara fulani haijaleta pesa hizo pesa zipo, maji yako wapi, tumekaa sasa hivi pale unajua kuna watu wengine duniani hawapo, mbinguni hawapo hawaelewi wanajua labda Mbunge huwa anapewa hela anaweka mfukoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu kabisa wanasimama pale wanakuambia Mbunge huyu wa Gairo amekula pesa zetu za maji, wanajua labda Wabunge tunapewa pesa kwa hiyo sisi ndiyo tunatoa toa pesa kwenye miradi. Wabunge hatupewi pesa, pesa ziko kwenu na ninyi ndiyo mnahudumia hizo au kama mmeshindwa mtu ukweli basi fedha zetu tuwe na account zetu za Mfuko wa Jimbo halafu tuweke watu muangalie nchi nzima kama haina maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, usimamizi wa maji wa mradi huu maji hakuna, lakini ukiangalia hapa kwenye bajeti utaona usimamizi tu wa maji Gairo, Mvomero, Turiani na Kilosa ni shilingi milioni 490, usimamizi tu! Sasa si ulaji huu?(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu namuomba Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Katibu Mkuu wamekuja pale, huu mradi wa Gairo utakuwa na gharama kubwa sana kwa wananchi. Nawakumbusha kwamba mradi huu wakati wa Waziri Maghembe alishasema ukiwa na gharama kubwa Serikali/Wizara italipia yenyewe gharama zile za pale siyo wananchi maana tuwekane sawa kabisa, muangalie kwenye Hansard. Ukiwa na gharama Wizara kama alivyosema Waziri aliyetangulia kwamba ninyi ndiyo mtakaowalipia gharama hizo wananchi wa Gairo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumewapa plan nyingi, tumewapeleka kwenye vyanzo vya Mserereko lakini kila watalaam wenu wakifika unasikia ooh! maji haya hayatoshi. Hivi maji haya ndiyo Mto Mkondoa yanasumbua watu kila siku yanaleta mafuriko pale Kilosa halafu unasema hayatoshi kusambaza Gairo? Tumewapeleka kwenye chanzo cha Mto Mkondoa unapotoka Gairo kila siku mafuriko pale Kilosa, Mto Ludewa, Mto Mvumi yote inatoka Gairo pale juu, kwa hiyo hata macho na sisi hatuoni kwa macho? siyo watalaam wa maji lakini hata kwa macho hatuoni?
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya tumeomba pesa mtupe kile chanzo tunachotumia sasa hivi cha mserereko kina bomba za nchi tatu, tupeni bomba za plastic tu ambazo hazifiki hata shilingi bilioni moja tutoe pale kwenye chanzo cha Mserereko tulete pale. Mwaka jana mmetoa milioni 312 hazijatumika popote. Mnaweka tu hapa, litatumika bomba la chuma yaani mnapiga plan za ulaji ulaji, pesa ipo lakini plan za ulaji tu! Mwaka huu tena ukiangalia kuna shilingi milioni 300 eti hizi kufunga mita Mijini, kwanini msikusanye ile shilingi milioni 300 ya mwaka jana haijatumika na hii shilingi milioni 300 ongezeni hapo.
Waheshimiwa Wabunge, hatufuatilii tu mkiangalia, lakini kwenye Wilaya pesa za maji zinakuja nyingi, miradi ya utapeli mingi. Mimi mtu akiniambia hela haziji labda Wabunge wenyewe tu hatufuatilii tu, lakini ukifuatilia kwa makini, mimi pale Gairo naangalia pale na kwa Ndugu yangu Mheshimiwa Saddiq na sehemu nyingine nyingi tu hata Mheshimiwa Mabula nimeongea nao hapa, kuna miradi mingi! Hata ya kwenye Halmashauri mnatoa hela, lakini Wizara hamsimamii siyo tuende mpaka TAMISEMI ile si mambo ya maji? Wizara ninyi mmetoa labda Gairo maji, kwa mfano pale Chakwale na Kibedi kuna mradi wa karibia shilingi milioni 500 lakini maji mpaka leo hayatoki na wakandarasi wameshakabidhi. Ukifungua yale maji mabomba yote yanapasuka, kwa hiyo mnataka sisi kama anavyokuja Mheshimiwa Magufuli hata haya mambo ya maji tukamlalamikie Rais? Sasa hawa wataalam wamewekwa kwa ajili ya nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani, halafu mnajua kabisa Mji kama Gairo ni mji mkavu kama Dodoma, kwenye kutenga pesa mnatufananisha sisi na sehemu ambayo watu wakichimba hata na mkono kama panya hapa wanapata maji, huu utalaam unatoka wapi? Muwe mnaangalia, lazima muwe na usawa kwamba sehemu zingine maji hayapatikani kirahisi. Kwa hiyo Ndugu zangu tunaombeni sana... (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Leo nitachangia kiasi tu. Kwanza nianze na ile shangwe ya akinamama kwa kuondolewa kodi ya taulo za kike. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa kutoa kodi hii, lakini bado tuna wasiwasi na sio wasiwasi kwamba bei itakuwa ipo pale pale. Kwa sababu ametoa kodi kwa nia nzuri, lakini cha msingi lazima aangalie aweke na bei, kwamba itauzwa bei gani? kwa sababu ukitoa kodi yule mwenye duka hawezi akajua hiyo kwamba imetolewa kodi wala haitofahamika na hivyo yeye atauza bei ile ile; kwa hiyo manufaa kwa wananchi hayatakuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunaomba aangalie namna ya kurekebisha, kwamba waweke na kiwango cha bei, kwamba hii itauzwa kiasi fulani ili wale wenye maduka wasiweze kujipatia faida hii ya ushuru ambao umetolewa na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha pili, nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwenye Viwanda, kwa kweli ameonesha nia nzuri sana ya kuweza kunyanyua viwanda vya nchi hii; na wale watu ambao kweli wana nia ya kuanzisha viwanda huu ndio wakati wao. Nasema hivi kwa sababu bajeti hii imeonesha kabisa na ipo wazi kabisa, kwamba kama unaweza kuanzisha viwanda anzisha na Serikali inakuunga mkono.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano kwenye mafuta, ameongeza ushuru kwenye crude oil na viwanda vya Tanzania vya ndani ya nchi kama mawese ametoa ushuru. Ila tunamshauri, hata kwenye mashudu nayo hajayaekezea vizuri, nayo atoe ushuru wake ule wa ongezeko la thamani (VAT).
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huu nataka niwaambie wafanyabiashara, wakati huu wa Serikali ya Awamu ya Tano ndio wakati wa kufanya biashara. Kwa sababu bado watu wanadanganyana danganyana hali mbaya, TRA inafilisi, sijui nini, huku na benki nazo ndio zimeshusha Interest. Sasa huu ndio wakati wa kukopa, hela zimejaa, wakati watu wanaogopa sasa ndio wakati watu kukopa na kufanya biashara, ukichelewa hapa ndio biashara imekwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa cha msingi tu, nataka nitoe ushauri na nataka niseme ukweli; kwamba hapa inaonekana kabisa Mawaziri wetu wanafanya kazi lakini ushirikiano haupo, ni zero. Kwa sababu unataka kuanzisha viwanda vya mafuta lakini ushirikiano wa Waziri wa Viwanda na Waziri wa Kilimo uko wapi? Maana unapiga kelele uanzishe kiwanda cha mafuta ya alizeti wakati kwa wakulima hamna lolote wala hakuna support ya aina yoyote ili wazalishe alizeti kwa wingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unaanzisha kiwanda, kwa mfano kama hapa Dodoma ukiweka kiwanda inatakiwa kiwe kimoja tu na hata hivyo hakitoshi kwa sababu alizeti yote hii ya Dodoma inakwenda Singida. Kwa hiyo hata ukianzisha kiwanda kingine hawatoweza kupata alizeti za kutosha. Mbegu ya alizeti inayotumika Tanzania inatoa 22 percent ya mafuta wakati South Africa kuna mbegu inatoa 60 percent. Nataka kusema hapa Mawaziri hapa maneno mengi, ushirikiano hakuna, vitendo hakuna; huu ndio ukweli na lazima tuambiane ukweli; tusipoambiana ukweli hapa, tukianza kuogopana, tutasalimiana, tutakunywa chai lakini ukweli ndio huo; wengine ndio maana sasa wanafikia hamna sifa wanaenda kupima samaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunafanya tu, ukiangalia ile video inakuangalia hamna kitu. Nataka nimtafute Mheshimiwa Rais kwa wakati wangu, ntamwambia mzee hawakusaidii hawa pangua tena, si dhambi kupangua pangua Mawaziri mara nne, mara tano. Waangalie, maana Mawaziri ukiangalia kwenye nchi hii wanaofanya kazi kwa moyo kabisa hawazidi watano. Wengine nao wamekuwa walalamikaji kama sisi Wabunge, tukikutana humu, aaa’ nchi hii’, mimi naogopa’, yaani hawahawa ndio wanaichafua, halafu mnapiga kelele; hawa ndio wanaomchafua Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bora hata upate adui mpinzani wa chama kuliko mpinzani wa ndani ya Serikali, mbaya zaidi kwa sababu humjui. Kwa hiyo, naomba Wizara hii, Mheshimiwa Dkt. Mpango ana shida sana, ana shida sana kutokana na Mawaziri wengine kutokupa support, huo ndio ukweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine nilisikia kina tajwatajwa hapa, mimi nafanya biashara, kwa hiyo nitakiongelea kila siku kama nitaona kinaenda tofauti. Kuna Mbunge mmoja hapa nilikaa naye hataki yeye TIPER itumike, anataka mafuta yakija yaingie moja kwa moja kwenye madepo ya kampuni binafsi, hicho kitu hakiwezekani. TIPER imejengwa tangu enzi ya Mwalimu Nyerere kwa ajili ya kudhibiti kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mfumo unaotumika sasa hivi ndio mfumo sahihi, wakati ule hizi kampuni nyingi hazikuwepo. Ili Serikali ijue mapato yake lazima mafuta yote yaende sehemu moja, yakitoka kwenye meli moja kwa moja yaende TIPER. Wakati huo ndivyo ilivyokuwa, hizi kampuni nyingine zote; Oryx, Gapco, zote hazikuwepo hizi. Puma zilikuwa hazipo, Oilcom, nani, hawakuwepo hawa. Kwa hiyo wakati ule yakienda TIPER ndio yanaenda Esso,Agip na Shell. Sasa hivi anakuja mtu anasema hiyo italeta leakage, sijui na nini. Yakifika pale TIPER, wewe kama una lita milioni tano utasubiri Milioni tano zako utapata zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikwambie kwa nini wanafanya hivi? Wanafanya hivi kwa sababu kampuni chache hizi zinapanga hata bei, kwamba hawa sasa tuwagonge hivi. Sasa hivi vikampuni vya Watanzania vidogo vidogo hivi ndivyo vinavyoshusha, vinasababisha na wao washuke. Kwa hiyo nia yao ni kuuza kampuni ndogo ndogo ili wabaki wao; na kila mtu akiweka mafuta kwao wanachukua karibu kwa metric tons wanachukua dola ishirini. Kwa hiyo wanajua yakienda kule wao watakosa...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Kwanza niwashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu pamoja na wakuu wote wanaoongoza taasisi kwenye Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda tu mimi nianze na barabara ya Gairo – Iyogwe ambayo inakwenda mpaka Mkoa wa Tanga kwenye Wilaya ya Kilindi pale kwa ndugu yangu Mheshimiwa Kigua. Nafikiri hii barabara Mheshimiwa Waziri amefika muda si mrefu kama miezi miwili iliyopita na Mheshimiwa Naibu Waziri naye amefika kwenye barabara hii kama miezi mitatu iliyopita na kwa bahati nzuri wakati unafika Mheshimiwa Waziri ulishuhudia pale magari yakiwa yamekwama watu hata kwa miguu wanashindwa kupita, ulijionea kwa macho. Kwa bahati nzuri ukaongea na Eng. Mfugale ukaahidi kwamba patakuwa na madaraja ya temporary angalau barabara hii ipitike lakini katika kitabu changu cha bajeti hapa sijaona matengenezo ya barabara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ikumbukwe kwamba iko katika ahadi ya Rais ya kuwekwa lami kwa sababu inaunganisha Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Tanga kupitia Wilaya ya Gairo na Wilaya ya Kilindi na ni barabara muhimu sana na wote mnaifahamu. Hata katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi pale Gairo tarehe 26 Juni, 2014 aliitaja sana barabara hii, mpaka leo iko Youtube humu bado sijajua ni kwa nini haipo lakini nafikiri ataangalia namna ya kufanya ili iweze kupitika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ile barabara ya Gairo Mjini ambayo toka mwaka jana ilipewa shilingi bilioni 1.5, mwaka jana ilitolewa shilingi milioni 500 mkandarasi amejenga madaraja lakini mwaka huu mmetoa hela chache kabisa shilingi milioni 120. Kwa hiyo, nina wasiwasi kama kuna mkandarasi atakayekubali kuanza kutengeneza barabara ile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichotokea ile barabara pale Gairo Mjini haipitiki tena ya kutoka pale njiapanda ya hospitali mpaka Magoeka kwa sababu TARURA tena hawamo na TANROADS nao hawaishughulikii, sasa haipitiki. Kwa hiyo, naomba hii barabara ya Gairo Mjini iweze kupangiwa pesa ya kutosha ili iweze kushughulikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ile barabara ya Gairo – Nongwe. Ukiangalia katika bajeti ya mwaka huu imepangiwa vihela hela vingi vingi sana vidogo vidogo. Kweli lazima nishukuru, mara nyingi imekuwa inapangiwa pesa lakini hakuna hata mara moja imeshawahi kuwekewa changarawe. Kila mwaka tunaitengeneza na mvua za mwanzo tu imeharibika. Pesa zinazopangwa hata nikiangalia hapa ni nyingi zinatosha hata changarawe lakini haijawahi kuwekewa changarawe hata mwaka mmoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri mliangalie hili la barabara ya Gairo – Nongwe kwa sababu pesa mnazozipangia ni nyingi lakini hakuna sehemu iliyowekewa changarawe. Kwa hiyo, hata manyunyu kidogo haipitiki na ile barabara imekaa kama ya Lushoto, unavyoona milima ya Lushoto au zaidi ya milima ya Lushoto ndiyo inakopita barabara hii ya Gairo – Nongwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia minara ya simu, nilikuwa nataka ndugu zangu Mheshimiwa Waziri na Naibu wako Mheshimiwa Nditiye muangalie sana. Minara ya kijiji cha Masenege na Idibo ipo siku nyingi na ni ahadi ya siku nyingi na hata katika vitabu vyenu kila siku ipo. Mnara katika Kata hii ya Idibo, Makao Makuu ya Kata mpaka leo hauna hata dalili ya kujengwa. Tukiweka minara hii ya Gairo pale Idibo, Masenge na Chogoa katika Kata ya Chogoa tutakuwa tumemaliza kabisa shida katika wilaya ya Gairo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho nataka nikizungumzie ni habari ya bandari. Lazima niseme ukweli au nikiri Bandari ya Dar es Salaam kwa sasa hivi inafanya vizuri sana, wizi wote uliokuwa pale katika Bandari ya Dar es Salaam sasa hivi haupo. Mmoja ambaye alikuwa hatumii Bandari ya Dar es Salaam ni mimi hapa lakini sasa hivi nina mwaka wa tatu natumia Bandari ya Dar es Salaam na huwa naweka mpaka mitego, naweka vitu loose nione kama vitaibiwa lakini iko vizuri sana. Haina wizi na ina speed ya hali ya juu sana na ndiyo maana mnaona sasa hivi inaleta changamoto ya malori. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na uzuri wa bandari hii sasa hivi kumekuwa na malori ambayo yamepita kiasi kwenye barabara zetu. Tulizungumza sana na mimi bahati nzuri ni mjumbe wa Kamati kwa muda mrefu katika hii Kamati ya Miundombinu kwamba tuanzishe dry port ya pale Vigwaza ili haya malori yote yawe yanaishia pale. Ukifika pale mzigo wote wa bandari uwe unachukuliwa na ile reli ambayo sasa hivi hata haifanyi kazi ya kwenda Tanga na Arusha, mizigo iletwe mpaka pale Vigwaza, malori yote yaishie pale Vigwaza yasiende mjini. Tumelizungumza sana suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba muangalie malori yamezidi, sasa hivi foleni ya Dar es Salaam sio ya kawaida. Pamoja na kuwa tunatengeneza reli ya standard gauge kuja Dodoma lakini suala hili hata tukitengeneza dry port hapa Ihumwa itasaidia tu mikoa ya Kanda ya Ziwa pamoja na Burundi, Rwanda na Uganda. Hata hivyo, bado ile bandari kavu (dry port) ya pale Vigwaza itasaidia sehemu zote za Malawi, Congo, Zambia na sehemu nyingine na cha zaidi ni kuondoa msongamano ambao upo sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa TPA walishatoa mpaka pesa zaidi ya USD 2,000,000 kwa ajili ya kutengeneza kichwa cha treni na tulikiona pale Morogoro kwa ajili ya kufanya kazi kama hizi. Je, kile kichwa cha treni kiko wapi? Kwa sababu ukiangalia dry port za Dar es Salaam zinavyochaji usafiri ule tu wa kutoka pale bandarini kwenda kwenye dry port pale Mandela Road au sehemu nyingine ni pesa nyingi kuliko hata kukodisha hiyo treni kutoka mjini mpaka pale Vigwaza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana mjitahidi kuhakikisha kwamba ile dry port inaisha. Sisi tulienda kuikagua na ilishaanza kujengwa, tunaomba haraka sana ifanye kazi na malori yote yaishie Vigwaza ili kuondokana na foleni. Maana sasa yanasababisha vifo, mara utasikia kontena limeangukia hiace na limeua watu, mara limefanya nini, tunaombeni sana mtusaidie kwa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, mimi si Mbunge wa Wilaya ya Mpwapwa, lakini kwa usafiri nafanya biashara na ndiyo nilikoanzia kwenda katika biashara yangu ya mabasi, kwenda Mpwapwa, Dar es Salaam, jamani huyu mzee Mheshimiwa Lubeleje mtamuua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka na miaka analalamikia habari ya barabara ya Mpwapwa kuja Kongwa, kipande kile kidogo cha lami, kila siku mzee mpaka sasa hivi mzee meno yameng’oka bado anaongea lakini hamtaki kumsikiliza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naombeni sana, kwa uwezo wako Mheshimiwa Mfugale, barabara ya Mpwapwa ni barabara muhimu sana, kulinganisha na barabara zingine za wilaya zingine. Tunaomba jamani kwenye bajeti hii nimeangalia na mzee wangu, lakini hatujaiona hii, na imo katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015/2020. Lakini haina dalili yoyote mpaka leo. Tunaomba sana hii barabara ya Mpwapwa, nayo iwemo kwenye mpango huo na ninajua Mheshimiwa Waziri ni Engineer na bahati nzuri na wewe Mpwapwa huwa unakwenda mara nyingi, kwa hiyo, nayo mtaishughulikia, ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, Naunga mkono hoja, asilimia 100. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kwanza ya kuwa mwongeaji kwa siku ya leo kwenye hii Wizara ya Viwanda na Biashara. Kwanza nataka niseme tu kwamba, humu ndani Wabunge tumeingia kila mtu ana fani yake, wako wakulima, wako wafugaji, wako Walimu, tuko wafanyabiashara, wako Wanasheria. Kwa hiyo, kila mtu anaijua sekta yake vizuri, pamoja na kuwa wapo wengine wanajua kila sehemu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme, Wizara ya Viwanda na Biashara, kama inavyoitwa, Waziri wa Wizara hii anachotakiwa ni kuhakikisha kwamba anatengeneza biashara inakwenda vizuri kwenye nchi yetu ya Tanzania, asiwe ni mmoja wa sehemu ya kubomoa biashara kwenye nchi hii. Kwa nini nasema hivyo? Inaonekana kabisa wazi Wizara hii ya Viwanda na Biashara haielewi chochote kuhusu biashara kwenye hii nchi. Kabisa, hili ni suala la wazi, kwenye ukweli lazima tuseme ukweli, na ndiyo maana sasa hivi Rais wetu anapata tabu sana, kila anapokwenda anaelezea mambo, anakuwa yeye ndiye Waziri, yeye ndiye Rais. Kwa kweli, Rais mwishowe atapasuka kichwa, watu aliowaweka hawamsaidii! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwenye ukweli huwa sipindishi maneno, ukweli ni ukweli tu. Hivi, mimi nauliza Wizara ya Biashara, leo hii ukiangalia kodi kila Wizara inaanzisha kodi kuhakikisha kwamba inakomesha biashara au inakomoa biashara, kila Wizara. Leo hii ukienda kwenye Wizara ya Kazi, Vijana na Ajira, unakuta kuna WCF, hawa wanaambiwa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, wao wana chaji zao kibao. Ukienda kuna OSHA, (Usalama wa Mahala pa Kazi), wao wana kodi zao nyingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupe mfano mmoja tu wa hawa OSHA, mimi nafanya biashara zote, ya mafuta nafanya na biashara zingine. Nitolee mfano kwenye biashara ya mafuta, wanachukua kodi kwa mwaka laki tano, OSHA. Mwaka huu wanataka milioni tatu na laki tano, kwenye kituo cha kijijini. Kituo cha mjini mpaka milioni sita, kwa mwaka, ada. Sasa imekuwa kila mtu anakusanya fedha na anaona sifa, kwamba akimkomesha, akimfungia mfanyabiashara, yeye anaona sifa! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka niulize, hapo hapo kuna WCF, wako hivyo hivyo. Ukija Halmashauri kuna service levy, anachukua kwenye mauzo, siyo kwenye faida, kwenye mauzo, 0.3%. Sasa ukiangalia kwenye viduka vidogo, nendeni hapa Dodoma tu, viduka vyote vidogovidogo hivi, mtu anaanzisha kiduka chenyewe kina thamani ya milioni tatu, nne, anapigwa mpaka laki tatu, laki nne, hiyo service levy, halafu sasa Waziri wa Viwanda na Biashara yupo. Sasa yeye biashara yake ni ipi, ni kuua biashara au kukuza biashara? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndiyo ukweli, nini biashara ambayo anaitetea, maana yake anatakiwa atetee wafanyabiashara wawe wengi, aingilie kila sehemu ambapo anaona wafanyabishara wanaonewa. Ndiyo maana ya biashara, lakini sasa kila mtu amekuwa sasa mchukua kodi, ukija vipimo, anakwenda dukani mtu wa vipimo, ameshapima ule mzani wa dukani, kagonga na label yake, kila kitu, kwenye duka dogodogo tu linauza mchele na nini, kesho anakuja tena, anasema mbona huu mzani wako unapunja, wakati yeye ndiye kagonga ule muhuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nijue, ndugu yangu, Mheshimiwa Kakunda, maana ya kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara maana yake lazima ahakikishe kwamba anakuza biashara, si kuua biashara. Kwa hiyo, inatakiwa kila sehemu ambako mfanyabiashara anaonewa, yeye aingilie, kutetea, lakini wamejielekeza sana kwenye viwanda, viwanda, viwanda, sawa, kuna kiwanda cha General Tyre, kilikuwa namba moja katika East and Central Africa kwa ajili ya kutengeneza matairi bora. Wote hakuna mtu ambaye hajapenda tyre la General Tyre, mpaka leo hiki kiwanda kipya hakifufuki! Kiwanda cha Serikali, leo hii tunashindwa na firestone ya Kenya, inaingiza mpato makubwa sana kwenye Serikali ya Kenya, lakini sisi General Tyre, tumeingia tu tunapiga siasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi siyo Mbunge wa kushangilia, kwenye ukweli nitasema ukweli kutetea maslahi ya nchi yangu. General tyre ni muhimu, mimi siwezi kukaa hapa nasema tu haya tu Mheshimiwa Waziri, umeanzisha kiwanda fulani, umeanzisha kiwanda fulani wakati viwanda havipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Yuasa, Yuasa mpaka Uingereza walikuwa wananunua betri za Yuasa, kiwanda cha Serikali, kimebinafsishwa, mpaka leo, wameangalia kinafanya kazi gani! Kuna viwanda vingapi vilibinafsishwa nchi hii, vinafanya kazi gani, watu wamevikalia tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vimekaliwa tu, kwa hiyo, naomba…
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimweleze ndugu yangu, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, asimamie Wizara yake ya Viwanda na Biashara na hasa upande wa biashara, ahakikishe kwamba biashara anaisimamia katika Wizara zote….
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa muhimu.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Sasa wewe naona, ungekaa kwanza kidogo, unanichanganya.
MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, samahani, taarifa!
MWENYEKITI: Mheshimiwa Shabiby naomba uendelee.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ahsante. Kwa hiyo, ninachoomba, kwamba hatua zichukuliwe, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara aangalie biashara, kila Wizara sasa hivi, wanasema TRA tu, TRA kweli inachukua kodi yake, lakini kuna kodi zingine kubwa kuliko za TRA, tozo zimekuwa nyingi sana sana kuliko hata hizo za TRA. Kwa hiyo, naomba sana waangalie sana na Waziri afanye vikao na wadau ili apate hayo matatizo, siyo kila siku tunamwona tu naangalia tiles, anaangalia mbolea, ajaribu kukaa na wadau wamwambie, wampe changamoto hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya mimi kuwa mmoja wa wachangiaji lakini mimi leo nitachangia tofauti na watu wengi kidogo. Mimi nataka nizungumzie habari ya watumishi wa nchi hii hata sisi Wabunge ni watumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ukweli tuzungumze ukweli bila ya kupepesa pepesa, hii ndiyo tutakuwa tunaisadia hii nchi, lakini kama kwenye ukweli tunaweka woga au kutozungumza ukweli wakati ukweli tunauona haifai. Sawa sawa na mtu unakaa na Rais hapa na Waziri Mkuu na Naibu Spika na Spika wanakuambia angalia yule farasi anapendeza kweli wakati wewe machoni kwako unaona yule ni punda, unatakiwa umwambie hapana huyu siyo farasi Mheshimiwa umekosea ni punda, lakini kwa ajili ya woga unasema aah! farasi mzuri kweli kwa ajili woga wako, hii hapana! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu Nyerere alishawahi kusema maendeleo ya nchi yaendane na maendeleo ya watu, huwezi kufanya maendeleo ya nchi bila ya maendeleo ya watu. Leo tupo kwenye mpango wa bajeti, Mheshimiwa Waziri wa Fedha fanya maarifa yako ya aina yoyote 2022, ujue vyanzo utapata wapi sijui wapi lakini hakikisha mishahara ya watumishi inapanda wala tusidandanganyane. Nchi hii imekuwa na hali mbaya watu wamezungumza maneno mengi sana, hela zimebanwa, hela hazipo, lakini mimi katika utafiti wangu nilichokuja kugundua bila ya watumishi kupandishiwa mishahara hali itazidi kuwa mbaya kwa watu wote, kuanzia hao machinga, makulima na watu wengine wote watakuwa na hali mbaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wengi ambao wakipewa pesa na inaweza ikasambaa kwa wananchi ni watumishi peke yake, huo ni ukweli wala tusidanganyane! Leo watumishi miaka sita, saba hawajaongezewa mishahara mnategemea hela hiyo itakuwepo mtaani wakati vitu vimepanfa bei lakini mishahara ipo pale pale? Haiwezekani! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo mnaongeza vi-percent viwili, vitatu, hakikisheni Serikali mnakuja na mpango muangalie mapato mtapata wapi, tumewaambia mapema mhakikishe watumishi wanaongezewa asilimia kubwa ya kutosha ili waweze kukidhi, watumishi ndiyo watumiaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtumishi akitoka hapa anaenda Dar es Salaam njia nzima atanunua, akitoka hapa atanunua karanga, akifika Gairo atanunua viazi, akifika Dumila atanunua mahindi, akifika Mikese mpaka aje afike nyumbani laki moja kishapoteza, hawa ndiyo wanaosambaza pesa, ukienda hata sehemu za starehe ni watumishi ndiyo wanasambaza pesa! Watumishi wakiongezewa pesa mjue kila kitu kwenye hii nchi kitakaa vizuri na pesa itaonekana, hii lawama ya kwamba pesa haipo mifukoni mwa watu, tusidanganyane eti Wakandarasi hawajalipwa, Mkandarasi nikiwa mimi Shabiby ukinilipa hiyo hela yangu ya kuchezea nitagawagawa kwa kila mtu, nina wafanyakazi kumi hadi kumi na tano, watumishi wapo wangapi? Halafu tuangalie kodi ya nchi hii asilimia kubwa inalipwa na nani kati ya wafanyabiashara na watumishi, wanaolipa asilimia kubwa ni watumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hii naomba sana kwenye bajeti yako, Mheshimiwa Waziri wa Fedha tunajua Mama yetu aliahidi lakini tumekupa mapema ili uangalie na vyanzo vyako utakavyovipata mishahara ipande asilimia ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la Machinga alichozungumzia Ndugu yangu Mheshimiwa Musukuma, naungana na Serikali katika mipango ya kuweka mji vizuri sana, kweli mji unapendeza vizuri lakini tukumbuke hawa machinga nao wakiwekewa mazingira mazuri wanaweza wakaleta mapato makubwa sana kwenye hii nchi, ni mazingira tu! Hivi leo mimi najiuliza hii Serikali hawa watu wataalam wetu wa Serikali wanapokwenda Vyuo Vikuu huwa wanaenda kule kujifundisha kumwagilia maua kwenye bustani au utaalam? Maana yake hata huelewi mtu ana akili timamu unaenda kupeleka majengo ya machinga kule Ilala ndani Shaurimoyo, kuna kibarabara kimoja hata mahali pa kufika hakieleweki, hamna stendi ya daladala unampeleka mtu kule, nani anaweza kufanya biashara?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuiga nchi nyingine zilizoendelea? Dunia nzima tuangalie hata tuende pale Nairobi, majengo yote yaliyopo mijini ni ya Serikali, tukitoka hapo majengo yote ya National Housing yalikuwa ya Msajili wa Majumba haya yote ya kwetu, ukiangalia yale majengo makubwa ukichukua kodi wanayochukua Serikali lile jengo zima labda utachukua milioni Mbili au Milioni Tatu, lakini ukiyavunja yale majengo ya mjini hapa kama pale mtaa wa Congo, Msimbazi mpaka kule anakozungumza ndugu yangu hapa Musukuma, ukivunja yale majengo yale ya Serikali ujenge Malls tena Shopping Malls za ghorofa hazina gharama kwa sababu Malls zipo waziwazi halafu waingize watu.
MBUNGE FULANI: Au jangwani.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, au jangwani kokote pale, ndani lakini katikati ya Miji siyo ukampangie mtu huko katikati ya miji, hivyo mtaingiza machinga wangapi? kwa hiyo ni lazima kuwe na mipango tuchukue haya majengo ya Serikali tufanye kama Guangzhou - China, tufanye kama Dubai, tufanye kama nchi zingine, tuvunje yale majengo ya Serikali. Serikali ni yetu, Serikali ndiyo yenye machinga, Serikali ndiyo yenye watu wake, tuwajengee kwenye Miji katikati siyo kuziba barabara hapa, eti umchukue machinga ukamuweke sijui wapi huko hakuna hata stendi ya daladala nani atakaekwenda kununua? Unajua kuna vitu vingine tuzungumze ukweli siyo Mkurugenzi anapanga tu hapa ndiyo penyewe nimewajengea choo, sasa mtu anataka choo ataenda kuomba tu akibanwa huko hata porini ataenda, watu wanataka kupata huduma na wanaotaka kutoa huduma nao wanataka nao kufata watoa huduma na wapate faida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ushauri wangu ni kuhakikisha pale Msimbazi hebu angalieni majengo yale yote ni ya Serikali National Housing, ukienda kule mjini kote ni majengo ya Serikali, hivyo kweli wanaambulia tu kupata milioni mbili, tatu watu wamekaa kule majumba yenyewe kupiga rangi wanashindwa, vunja yale weka Malls, weka ghorofa mbili, tatu, nne tena haina gharama kabisa, halafu machinga wakae mle, hapa msimbazi watakuwepo machinga, hapa sijui Lumumba watakuwepo machinga, hata katikati ya mjini kule karibu na hii station yetu ya railway tunayoijenga watakuwepo wamachinga, watu wata-enjoy, lakini hii kufukuzana halafu mpango hamna! Mimi nimeamua kutoa mpango kabisa ili kuelekeza mpango uweje sitaki kulalamika.(Makofi)
MBUNGE FULANI: Na mishahara ya Wabunge!
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mwingine hapa anasema mishahara ya Wabunge, hiyo utasema kesho hamna wasiwasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukweli ndiyo huo. Lingine, kabla dakika zangu hazijaisha, kweli watu wanajitangaza tu tunatoa mikopo kwa wakulima, kuna Mheshimiwa alizungumza hapa nafikiri, Mheshimiwa Almasi alizungumza kwamba zinajitoa benki na Mheshimiwa Waziri unaangalia na wewe tunakuamini sana na tunajua utalifanyia kazi. Hizi zote zinakopesha matajiri…
MWENYEKITI: Muda wako umekwisha Mheshimiwa Shabiby…
MHE. AHMED M. SHABIBY: Ah?
MWENYEKITI: Muda wako umekwisha.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nipe dakika moja tu nimalizie.
MWENYEKITI: Muda wako umekwisha!
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, haya, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, asante kwa kunipa nafasi na mimi kuwa mmoja wa wachangiaji katika hizi Kamati zetu tatu. Mimi leo nitachangia sehemu mbili tu; sehemu za kilimo na sehemu ya mifugo kwa sababu hizi zote, hawa maafisa ugani, nani wako kwenye TAMINSEMI.
Mheshimiwa Naibu Spika, labda tu niseme, nataka niwaambie ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge. Tunazungumza sana habari ya mfumuko wa bei. Mfumuko wa bei kwa sasahivi ni lazima uwepo; na kwa nini upo? Ni kwa sababu miaka hii miwili, mitatu ya nyuma kwanza kidogo palikuwa na shida ya mvua na vilevile vyakula vilikuwa bei ya chini. Kwa hiyo mkulima hakuweza kupata pesa ya kulima eka nyingi anavyohitaji. Mkulima atalima eka nyingi anazohitaji, akiwa na eka 100 ili alime zote lazima alichokivuna kiendane sambamba, ili auze, kiendane sambamba na eka anazoweza kulima mwakani. Akipata kidogo badala ya kulima 100 zile alizonazo atalima 20. Kwa hiyo automatically mazao yatakuwa machache na bei itakuwa kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mkulima akipata bei kubwa, kama ya mwaka huu, na mnaona wenyewe, kwa mfano Jimboni kwangu Gairo na majimbo mengine yote, wamelima takriban mashamba yote, hata mkipita njiani mnaona watu wamelima mashamba yote. Kwa hiyo, mavuno yatakuwa mengi na bei automatically itashuka. Lakini hapa habari ya kusema kwamba kuna mfumuko wa bei, lima na wewe, kama alivyosema Mheshimiwa Katani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani ukalalamikia mfumuko wa bei, nasikiasikia hata huko nje. Unasikia maharage yamepanda bei, yule pale Mheshimiwa Mwijage amelima shamba la maharage, safari hii amepata maharage ndiyo maana anachekacheka tu, kapata hela nzuri, miaka yote anapata hasara. Kwa hiyo, lazima tusichanganye mambo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkulima, kama alivyosema Mheshimiwa Katani, mkulima tumuache auze anavyotaka yeye kwa sababu yeye ndiye amelima, tusimpangie. Na Serikali nayo tusiilaumu sana kwa sababu Serikali nayo hailimi, ila tumshauri tu Mheshimiwa Waziri atoe chakula kama alichosema kwenye Halmashauri na aangalie watu wa kuwapa. Apeleke tu pale sokoni, asimpe dalali kwa sababu dalali naye ataminya baadaye naye atauza bei kubwa. Kwa hiyo wangalie namna ya kutoa kile chakula ili kishuke bei. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama kweli tuumize watu asilimia 70 wakulima wa nchi hii kwa sababu tu ya kutetea watu asilimia 30, halafu hawa asilimia 70 tunaowaumiza ni kwa ajili ya jasho lao, haiwezekani kitu kama hiki. Na mimi ninataka kama kuna Mbunge yeyote anataka mkulima hapa ashushe bei ya mahindi hebu tusimame hapa, Wabunge wangapi wanataka wakulima washushe wasimame hapa tuwaone hapa? Muone hapa kama mtapata kura hata mbili majimboni huko. Ndio ukweli huo, tusiingilie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi ninamshangaa Mheshimiwa Bashe ana maneno mengi tu, aah ngoja, mimi hapa, wakulima, wambie ukweli kwamba hatuwezi tukaingilia masuala ya mkulima, muacheni mkulima auze anavyotaka. Na ninawahakikishia kwa mwaka huu kwa bei hii mtaona kuanzia mwezi wa saba, wa sita, vyakula vitashuka mpaka mtashangaa. Hilo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili. Hawa wafugaji nao sasa wamekuwa wanasumbuliwa yani, wamekuwa sasa kama hawaishi kwenye maeneo ya nchi yao. Mimi nilishangaa nilijua labda Waziri wa Mifugo atakuja na mpango wa kupima maeneo ya ufugaji akazanie huko, yeye anakazania heleni. Maana ng’ombe nao sasahivi wamekuwa masharobaro, wanatakiwa wavae heleni. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, halafu hizo heleni zimejaribiwa pale, nimeona Pandambili, zimejaribiwa Katavi. Mimi napenda sana kufanya research; nimezichukua, hata sasahivi nina heleni nne pale, lakini ukizi-track; nimewapa mpaka watu wa IT; hazioneshi ng’ombe kama yuko Dodoma. Maana ukichukua heleni si ni lazima ng’ombe aonekane yuko Dodoma? Hazioneshi.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
NAIBU SPIKA: Taarifa.
T A A R I F A
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nilikuwa nataka kumpa taarifa mzungumzaji kwamba, yaani wanaokazania heleni wanataka ziishe ndani ya mwaka mmoja, wakati vitambulisho vya taifa vinatakiwa viishe miaka 11 havijaisha. Yaani vitambulisho vya taifa havijaisha ila heleni ziishe. (Makofi/Kicheko)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Shabiby.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, naikubali taarifa. Imekaa vizuri. Haiwezekani kitu kama hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mimi nina wasiwasi, jamani, huyu Mama yetu, Mheshimiwa Rais, mambo kama haya hajui; lakini ninataka niseme ana kazi ya ziada upigaji an chi hii uko waziwazi. Sisi wengine tunajua na bahati nzuri tunawajua mpaka hao wenye hizo tenda, tunawafahamu. Kama kweli kule Katavi walikofanyia majaribio watuambie ng’ombe wangapi waliokufa? Ng’ombe wangapi ambao waliwaona wamechepuka wameingia labda kwenye hifadhi au kwenye nini, kama wanayo hiyo taarifa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii wazungu ulaya wanatumia, lakini wanajua kila kitu. Hapa Kenya hawatumii, Uganda hawatumii, South Sudan hawatumii, eeh, hapa tunataka sisi tunaanzisha vitu ambavyo havina mfano? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii ng’ombe mlianza na chapa, chapa imekuja imeshindikana. Mmekuja kengele, kengele imekuja imeshindakana. Sasa mmekuja na heleni, heleni ikishindikana mtataka wavae shanga za kiuno; eeh! ndiyo maana yake hiyo. Ikitoka hapo mtataka wavae vikuku vya miguu; maana yake sasa tunawavisha ng’ombe hawa. Mimi nasema, kwa suala kama hili msiichafue hii Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutoweka mipango. Kama mipango ni mizuri mna harakanayo ya nini? (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, halafu Mheshimiwa fanyeni uchunguzi…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Sekunde 30.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, fanyeni uchunguzi. Yule mwenye tenda hiyo wale wanaotaka kuzigawa ndio wanakaa na hawa watu wa Wizara ya Mifugo wanaongea, waklimaliza kuongea ndipo wanaenda kuwashauri wale wafugaji. Haya ni mateso makubwa sana, mimi sikubaliani kabisa na hii heleni. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kuwa mmoja wa wachangiaji kwenye Wizara yetu ya TAMISEMI. Mimi leo nitachangia vitu vichache tu; lakini kwanza kabla sijachangia naunga mkono hoja ya TAMISEMI. Si kwamba naunga mkono hoja ya TAMISEMI kwamba wanafanya vizuri, hapana isipokuwa naona wageni. Kwa hiyo kwa hili safari hii tunaunga mkono hoja kwa sababu tunajua kuna dada yetu Kairuki, kuna akina Deo na mwenzetu Dugange huwa ni wazuri wanapokea simu zetu wa Wabunge. Kwa hiyo na mkiona makofi haya msivimbe kichwa halafu muache kupokea tena. Kwa hiyo tunaunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ila tunaka kusema, kwamba mmekabidhiwa gari bovu, ambapo hili gari ni la tani 30 lakini lina injini ya bodaboda, huo ndio ukweli, tusitake kila kitu tunasifu. Kwa hiyo dada yangu hapa pana kazi ya ziada na pana kazi ya ziada kuanzia kwako TAMISEMI kwa watumishi wa TAMISEMI. Nimeona Wabunge hapa waliochangia, hawa wawili kabla yangu nimeona wamezungumza kwa uchungu hata yale niliyotaka kuzungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu mgao wa watumishi hasa walimu, watumishi wa hospitali ukiangalia mara nyingi ukiona jimbo la Waziri utaona lina mgao mkubwa, jimbo la Mbunge lina mgao mdogo. Hiki kitu kiko wazi; na juzi niliongea na wewe na ndiyo maana leo nimekuwa mpole, na nilikuonesha mfano nikakutajia mahali fulani, na mimi huwa naongea kitu kwa uchunguzi. Utakuta, kwa mfano vituo vya afya; sisi Gairo kuna Kata ya Chanjare, iko umbali wa kilometa 90 mpaka kufika Gairo Mjini. Tumeomba kituo cha afya, Naibu wako hapo Dkt. Dugange hapo anafahamu, amenisaidia sana, lakini kile kituo hakijapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikamwonesha sehemu vituo vya afya vimejengwa kuna watu hata 2,000 hawafiki kuna kituo cha afya. Mwenyekiti wako wa Kamati, Mheshimiwa Londo anajua. Sasa, hivi kweli, mama,Mheshimiwa Rais, anatoa vituo vya afya kwa ajili ya kusaidia wananchi wake; hivi vituo mvifanye viwe vya mkakati. Muangalie, si lazima iwe kila kata inapata kituo cha afya lakini at least muangalie kwamba hapa pana kata labda tatu kimkakati kwamba wapi tuweke kituo cha afya ambapo watu wana shida. Sasa ninyi wenyewe kwa wenyewe huko mnagawana tu vituo. Waheshimiwa Wabunge nachosema ni kweli, wengine tumepata kimoja, viwili lakini kuna watu wamepata vinne, kumi, sita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naombeni sana jamani, dada yangu naomba sana uwe makini na hilo. Kama Kata yetu ya Chanjari sisi ni lazima tupate kituo cha afya hata kama havimo kwenye mpango mkakati, mkatafute hela mtuletee kituo cha afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye watumishi walimu hivyo hivyo ukiona mtu anapelekwa Sumbawanga, anapelekwa wapi, ujue anapelekwa tayari hapo TAMISEMI wameshamwajiri halafu wao ndio wanaandika vimemo huyo mpe uhamisho, msaidie arudi huku. Utakuja kukuta ile wilaya imepelekewa walimu 50 baadaye unakuja kukuta ina walimu 24, wale wote wametoka. Safari hii kwenye mgao huu mimi kwenye shule za msingi nina uhaba wa walimu takriban 800, huwezi ukaja ukanipa walimu 100 ukaniambia eti tunapunguza polepole wakati mijini wamejaa huko, wachumba, wote mmewaweka kwenye miji huko, hii haitowezekana. Mtupe, na muhakikishe kabisa wakija hawatoki sio mnawaleta halafu mnaandika vimemo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninavyo vimemo nitakuletea apewe mkurugenzi huyo. Fanyeni uchunguzi huko mnakosema kwamba walimu wanahamishwa, wanahamishwa kutoka TAMISEMI. Wale mabosi huko wanaandika tu vimemo basi wanaondoka. Kwa hiyo wanajiajiri kwa undugu halafu wanawatoa ndugu zao wanawapeleka sehemu nzuri hawataki wakae vijijini.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wamelalamika sana hapa kuhusu habari ya wale walimu wanaojitolea…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Shabiby subiri kidogo kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mbunge wa Nyang’hwale.
T A A R I F A
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka nimpe taarifa mchangiaji, ameizungumzia ile Kata ya Chanjale. Mimi nimefanya ziara kutembelea maeneo yale, ukweli kuna shida kubwa na mimi namuunga mkono namwongezea Mheshimiwa Waziri alifikirie hilo la kuweka Kituo cha Afya Chanjale. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Shabiby unapokea taarifa.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ndiyo nilikuwa nahitaji hii, nimeipokea. Ni ukweli na ndiyo maana saa nyingine hata mnasema kwamba aah! kuna chuki kati ya Wabunge hivyo inakuwaje kama ukienda sehemu zingine uko utakuta kuna kituo cha afya cha ghorofa halafu kwako cha mabati ya kienyeji, utampendaje hapo? Kwa hiyo kwenye ajira hizi ajira ya afya hivyo hivyo; sehemu kama Gairo tuna upungufu wa watu karibia 200 na kitu, lakini ukiangalia hawaji. Safari hii kwa kweli tunao, na kama vipi tuje tuazimie humu Wabunge, tuazimia hapa watu wafukuzwe kazi na Spika naye kama hataki naye tunamuazimia sisi si ndio tuliomchagua? Ndiyo maana yake. Sasa sisi hapa bosi wetu ni Spika na Rais, kwa hiyo kama tunaye humu watu wanatufanyia vituko huko majimboni tuna kazi ya kulalamikalalamika humu tunajifichaficha, haiwezekani kitu kama hicho. Tuje tuazimie tu Spika alete hapa, TAMISEMI pale huyu, huyu, huyu hatakiwi sisi ndio tunasimamia Serikali na Spika naye akituletea siasa zake tunamwambia naye kaa pembeni na wewe tunakuazimia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwenye vituo vya afya na walimu tunaomba kabisa wafanyakazi hao tuwapate.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TARURA kwa kweli inafanya kazi nzuri sana lazima tuseme ukweli. Hata Mkurugenzi wa TARURA huyu CEO wao ni mtu mzuri sana, lazima tuseme ukweli, pale wanapofanya watu ukweli huwa tunasema vitu vya ukweli. Mama Rais wetu ametupa ile mia mia za barabara, kweli tunaona zinafanya kazi, lakini bado hazitoshi na sijaona watu wanatafuta hata ile vyanzo huko Serikalini hawatafuti vyanzo. TARURA lazima itafute vyanzo siyo lazima iwe mafuta. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna service levy, hivyo ukiichukua service levy ile ni kodi ya nini? Hujui! Unaambiwa kodi ya huduma, ukiangalia mfanyabiashara analipa yeye; kuzoa uchafu, zimamoto, sijui nini, kila kitu analipa halafu kuna service levy, halafu service levy wanakwenda wanajenga majumba, majumba tu eti kitega uchumi, kitega uchumi kipi? Hapa Dodoma wamejengajenga magorofa yale, sasa hivi wanalala panya na watu wawili, watatu, kitega uchumi, kwa nini wasichukue hizi hela za service levy basi angalau iwe na maana ziende TARURA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndiyo ukweli. Hii service levy Waheshimiwa Wabunge wazifanyie uchunguzi, haya mashirika yote yanayohusika na TAMISEMI angalia hata yale majengo waliyojenga kwa mfano haya ya Shirika la LAPF, si wamejenga majengo, majengo kama ile Millennium Tower na mengine, mwende mkaangalie kama wamerudisha robo ya pesa ya gharama iliyotumika, mimi najiuzulu Bunge hapa. Kila siku baada ya miaka fulani wanatoa bilioni nne au tano ukarabati, wakati hata bilioni mbili halijaleta yaani kuna pesa, Mheshimiwa Waziri, Dada yetu uwe makini. Halafu kuna vitu vingine...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa unga mkono hoja, kengele ya pili imegonga.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ya kwanza.
MWENYEKITI: Haya tunaendelea na uchangiaji hii ni kengele ya pili kiti ndivyo kinavyoelekeza Mheshimiwa Shabiby.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, haya ahsante. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Nimekuwa mmoja wa wachangiaji lakini kwenye mchango wangu sitokita sana kunukuu maprofesa au watu wengine. Nitakwenda sana kuongea kwenye lugha nyepesi ambayo watanzania au Wabunge wenzangu wataielewa. Leo michango yangu ni miwili tu. Mchango wa kujiunga kwa viwanda hivyo viwili pamoja na kiwanda cha pale kibaha cha kuunganisha magari.
Mheshimiwa Spika, kwanza nitaanza na kile kiwanda cha kuunganisha magari FAO pale Kibaha. Nataka niwape maangalizo Mawaziri wetu na hasa Waziri wa Viwanda kwa sababu wewe ndio mhusika wa viwanda, lakini vilevile na Waziri wa Fedha kwa sababu katika nchi hii tunakusanya kodi mpaka kwa watu wa chini ndio maana kuna tozo kuna nini kuna nini kwa sababu hatuna mapato kwenye hii nchi ili tuajiri wafanyakazi tufanye nini yani lazima tupate mapato. Lakini unavyoona kuna kitu kinaanzishwa hakina msingi wa aina yoyote halafu tena kuna kodi inatolewa pale bila manufaa yoyote.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano kile kiwanda cha kuunganisha magari cha assembly pale Kibaha. Kile sio kiwanda cha assembly kile kiwanda cha kuchukua gari ambalo limefunguliwa kutoka China pale wanakuja kuliunganisha yaani sawasawa na gari lako unalichukua hapa Dodoma unalifungua fungua unaliweka kwenye boksi halafu unalipeleka Dar es Salaam unalichukua engine unalibandika unachukua cabin unabandika mnasema assembly, hiyo sio assembly. Halafu baada ya hapo unamwambia kwamba yule atakaye mwenye magari mengine akileta kutoka China analipa VAT ila lile linaloungwa ungwa pale halipi VAT kwa hiyo, ni kuikosesha Serikali mapato bila sababu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, maana ya assembly za Mwalimu Nyerere mpaka zimekuja kwa kina Mwinyi mpaka wakina Mkapa maana yake ni nini? Maana ya assembly gari inatengenezwa Tanzania kwa 21% ni malighafi kutoka Tanzania kwa mfano, wakati ule TAMCO imeanzishwa ilikuwa inaunganisha magari ya Scania.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, wale Afro Cooling kiwanda cha Tanzania nacho kimeajiri wafanyakazi wengi, kilikuwa kinatoa rejetor zote made in Tanzania. AFRI cable walikuwa wanatoa wire zote zinaunganishwa wire za Tanzania Yuasa zilikuwa betri za Tanzania. Kiwanda cha Tanzania mali yake inaunganisha pale, Tasia walikuwa wanatengeneza spring ndio wanaenda spring za Tanzania zinatumika, Mangula walikuwa wantengeneza letras zote zinakwenda pale zinatumika. Hawa Coast sterio walikuwa wanatengeneza ngazi na vitu vingine kwa hiyo ukiangalia 21%. General Tyle walikuwa wanatengeneza matairi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ukichukua maana ya kuongeza ajira kwa ajili ya assembly unaunganisha na hivyo viwanda vyote. Leo kwenye magari haya hakuna mali yoyote ya Tanzania inayohusika pale. Halafu mnasema tunaongeza ajira Tanzania, wale wafanyakazi wako 100 tu pale, ajira ipi? lakini ukosefu tunayokosa kwenye VAT mabilioni ya pesa. Hii utapeli wa aina huu haiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, maana yake na sisi wafanyabiashara wa mabasi tunataka na sisi, maana yake basi moja ushuru peke yake ukiuliza Tanzania ni 100,000,000 wakati lori ni 30,000,000 sasa wa mabsi nae akija kwa hiyo Serikali mtakusanya wapi pesa? Tuachane na hii Habari ya viwanda vya utapeli tapeli huu na Mheshimiwa nilishaongea nae hata kwa mdomo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kingine ni hiki kiwanda cha nilikuwa sitaki kuongea lakini nimeona ndugu yangu Mnzava amenitaja pale na mimi acha niseme. Hiki kiwanda kuungana kiwanda cha Twiga Cement na Tanga Cement sioni shida, hivi shida iko wapi? Mwenye mali mwenyewe wa Tanga cement ana 68.8% hawa mashirika yetu haya ya Mifuko ya Jamiii yana hisa 32.2% anayetaka kujitoa ni yule mwenye 68% anataka kuuza share yake mtu anataka kuuza share yake tatizo liko wapi? Hakuna shida, ukisema hivyo kwamba huyu mtaleta competition kuna viwanda 11 nchi hii na cha Tanga sasa hivi ni cha nne kwa uzalishaji wala sio cha pili kama mnavyosema, kuna viwanda 11 vya cement. Hivyo TBL ameshika soko la nchi hii asilimia ngapi? Yapombe, si Kashika Zaidi ya 90%, ukija Bakhresa asilimia ngapi za unga? Zaidi ya asilimia 80%, ukija Mtibwa Sugar, Mtibwa Sugar ndio mwenye kiwanda cha Kagera Sugar sio mtu mmoja? Kwa hiyo kama…
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Shabiby kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mnzava.
TAARIFA
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa mzungumzaji sekta ya saruji ni moja kati ya non regulated sectors kwenye nchi yetu, na kwa sababu hiyo kanuni za ushindani kusimamiwa ni jambo muhimu kuliko kitu kingine chochote kile, nakushukuru. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Shabiby unaipokea taarifa hiyo?
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, naipokea kwa mikono miwili. Isipokuwa ninachozungumzia tusiwe tuna hiyo mambo kama hayo, tunachotakiwa sisi kuangalia je, Tanga Cement ana clinker nyingi Zaidi ya kuvuna miaka 100 pale kwake? Twiga cement hana clinker nyingi. Kinachotakiwa ni kusimamia kwamba hiki kiwanda kitafanya kazi? Wafanyakazi wale hawatakosa ajira? Sasa ni kazi ya Serikali muwe na mikataba ya aina ile, kiwanda kifanye kazi na wasije Twiga wakanunua wakachukua ile clinker wakaihamisha. Hicho ndio cha msingi lakini cha msingi kusema FCC, f ni nini sasa imekuja kwenye hii cement, nataka niiulize hii Serikali kwamba haina mpango maalumu wa kupanga bei?
Mheshimiwa Spika, Lazima uwe na wataalamu, waangalie je uzalishaji wa Tanzania una cost bei gani? Niwapeni mfano nchi kama Oman au Kenya tu, nchi mbili tu, cement ya aina yoyote inayozalishwa kuna wataalamu wetu tuna Maprofesa tuna manini huko Vyuo Vikuu wako wasomi wataalamu wanaangalia ina-cost bei gani? wakiweka na kodi bei gani? Wanaweka na bei ya kuuza ni hii hasa kama hii nchi kila mtu akizalisha kitu anauza anavyotaka basi itakuwa ni balaa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tusiogope kwa hilo tusiseme eti mtu kwamba mimi hapa nina mali yangu nataka kuuza eti unaniambia eti peleka kwenye mashindano, mashindano yapi hayo? Kitu changu haya, kwa mfano nimeamua kuhujumu? Sipeleki lakini taarifa ya uzalishaji umepumzika. (Kicheko)
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Shabiby kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Getere.
TAARIFA
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nataka kumpa mzungumzaji mzuri tu, Mheshimiwa Shabiby rafiki yangu mkubwa kwamba kiwanda cha Tanga Cement ni moja ya viwanda vinavyothaminiwa katika Uhuru wa Tanzania na kiwanda kilichobinafsishwa mwaka 1966 ni kiwanda cha wananchi na ni kiwanda cha Serikali kwa masharti ya kubinafsisha sio cha mtu binafsi.
SPIKA: Mheshimiwa Shabiby, unaipokea taarifa hiyo?
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, taarifa naiopokea lakini naona haelewi. (Kicheko)
Mheshimiwa Spika kwa sababu kama mnataka hivyo nyumba za Serikali zote zilikuwa nyumba za Uhuru ziko hapa? si zimeuzwa? Viwanda vyote vya Nyerere vilikuwepo hapa, si vimeuzwa? Sasa mkitaka, zimeuzwa nyumba mpaka kwenye makao ya Polisi, utakuta nyumba ya Polisi ipo kwenye eneo la Polisi kauziwa RPC sasa mkitaka namna hiyo hiyo msizungumze vitu hivi. Sisi twende tuzungumze kile kitu cha kweli, hizi ni biashara tunazungumzia mambo ya biashara hatuzungumzi Habari ya sijui ilikuwa hivo ilikuwa hivo, tuzungumzie biashara. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, nawasihi ndugu zangu tusijiingize huko kwenye mambo ambayo hatuyajui tuwachie wawekezaji wawe huru sisi tuwabane tuweke vitu vya regulation kwa ajili ya kuwabana kwenye bei na vitu vingine, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza nawapongeza Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Wakuu wote wa vyombo vya usalama kwa kazi nzuri wanazofanya, lakini nami leo nina michango yangu tu midogo midogo. Nitaanza na Uhamiaji. Pale Gairo mlisema tuwatafutie kiwanja kwa ajili ya kujenga ofisi. Kiwanja kipo, tunasubiri ofisi ije uhamiaji. Mwakani nikija, nakuja kivingine, naomba hiyo ijengwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni masuala ya Zimamoto. Nataka kujua tu, hivi ninyi Mawaziri mnavyopewa hivyo vyeo, mnakuwa waoga, mnakuwa kama sisi tu huku hatuongei na kwenye Mabaraza ya Mawaziri, mnakuwa wenzetu au mnakuwa vipi? Mimi unajua sielewi kabisa! Hili suala la Zimamoto liko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Ukijenga jengo, yako majengo yanatoa mpaka Shilingi milioni 40, Shilingi 30, Shilingi milioni tano, wanalipia Zimamoto hata jengo hujaanza kujenga. Kwenye magari, kuna kodi ya Zimamoto, lakini ukiangalia kwenye miji yetu, magari ya Zimamoto hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nikupe mfano wa Dodoma, Makao Makuu ya Nchi ina majengo mapya mengi, majengo marefu mengi, ukienda kuangalia pale vigari vya zimamoto vile, hata moto ukiwasha na nyasi havizimi. Tatizo ni liko wapi kwenye upande wa Zimamoto? Ukienda kule Mtumba kuna majengo ya Serikali. Hata kama yale majengo yamewekewa vifaa vya Zimamoto, lakini yako wapi magari ya Zimamoto? Hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Dar es Salaam, ukienda kule Tegeta, wapi, hakuna. Sana sana utayakuta magari ya watu binafsi. Kuna shida gani na fedha ziko nyingi za zaidi ya kununua magari ya Tanzania nzima? Mfano, pale Gairo, amekuja Mheshimiwa Rais, ameongea na wananchi pale, amesema Gairo ijengwe Mahakama, imeshajengwa. Gairo yajengwe madaraja, yamo kwenye bajeti; Gairo ijengwe mfereji wa kuzuia mafuriko, imeshajengwa; Gairo iletwe gari la Zimamoto kwa sababu ni katikati ya Dodoma na Morogoro kwa ajili ya accidents zinazotokea pale barabarani, lakini mpaka leo hata mpango hamna. Mmeleta watu wa Zimamoto zaidi ya sita. Sasa mnataka wazime na mikono?
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake mtuambie basi, mtupe course wenyewe tu, hamna haja ya kuweka watu wa Zimamoto pale. Kama watu wa Zimamoto wako sita, wanapewa mshahara, lakini hakuna chombo chochote cha kufanyia kazi. Hilo ni agizo la Rais. Mheshimiwa Waziri, nataka ukija uwe na majibu ya kutosha, kwa sababu wakati ule alikuwa Waziri, Mheshimiwa Simbachawene. Sasa sifahamu kila akija Waziri mpya na mambo yanabadilika? Nilikuwa naliomba sana hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la accidents zinazotokea hasa kwenye magari yetu, mabasi. Mimi ni msafirishaji wa zaidi ya miaka 27 sasa, nafanya hiyo kazi. Kuna vitu vingine hamtaki kushirikisha wadau. Mkiita wadau, mnaita wapiga debe, wale wadau wahusika kabisa hamtuiti tuwapeni ushauri. Toka enzi ya Hayati Mwalimu Nyerere, akaja Mheshimiwa Mwinyi, akaja Hayati Mkapa, mpaka leo, ukienda LATRA kuchukua leseni ya usafirishaji; kwa mfano, kama unatoka Dar es Salaam kuja Dodoma unapewa na kitu kinaitwa time table kwamba gari itatoka Dar es Salaam saa ngapi, itafika Chalinze saa ngapi, itafika Morogoro saa ngapi, itafika Gairo saa ngapi, na itafika Dodoma saa ngapi? Zile time table zinawekwa kulingana na speed ambayo unatembea, unawekewa na kituo, ukiingia dakika tano, utoke, yaani kila kitu inaeleza kwamba gari inatakiwa ifike saa ngapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadaye mkaleta speed governor, zimefanya kazi, zikafeli kwa sababu madereva wanazichezea, wanaweka switch, hazina kazi yoyote. Zimefeli speed governor. Sasa hivi mmeleta VTS. Nayo kuna kipindi inafanya vizuri, kuna kipindi nayo inachezewa. Sasa tena nimekusikia Waziri tena unarudisha tena speed governor ambayo ilifeli mwanzoni. Msifanye mchezo jamani. Nani atanunua kila siku? Eti mtu una gari 60 ukanunue speed governor shilingi 1,800,000 kwa magari 60 ambayo ilishafeli na unajua kabisa dereva ataichezea. Kwa nini msiweke utaratibu wa kufuata time table?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mweke speed 95. Haya magari ya sasa hivi siyo speed 80 na hata ukiangalia Sheria ya Traffic, speed 80 haiko kisheria. Inasema iwapo TANROADS kama wataweka kibao cha speed 100 ndiyo hizo hizo, lakini sisi tumeweka kichwani kwamba ni speed 80. Wekeni speed 95. Magari ya sasa hivi hayatumii breki tu, yanatumia na umeme ambapo ni kitu kinaitwa retarder kuwa kama breki. Wekeni speed 95, fuateni time table, gari ikitoka Dar es Salaam, Chalinze imewahi weka pembeni gari, piga faini. Inakuja mpaka Morogoro, gari imewahi, piga faini, weka gari pembeni isiondoke. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kipindi hapa niliona mabasi yamekamatwa pale Same. Askari wa Same walikuwa wanafanya kazi vizuri sana, lakini kuna baadhi hata ya Wabunge hapa wakaanza kupiga kelele, wananchi wanateseka. Siyo wanateseka, Polisi wafanye kazi yao bila kufuata watu wa siasa. Gari imewahi, time table inapokuonesha, weka pembeni piga faini. Dereva baadaye atapigwa na abiria, akionekana anawahi wahi tu, mwishowe abiria watambadilikia. Watampiga. Hiyo ndiyo kumaliza accidents. Sasa kama tuna Polisi kila kona na wanashindwa kuangalia time table na time table za kila gari wanazo, haiwezekani kitu kama hicho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni masuala ya kikotoo. Kwenye Jeshi la Polisi, tunapata taabu, tunawaona ndugu zetu, jamaa zetu, wako kama pale Gairo, wako sehemu nyingine. Kikokotoo wanachotumia cha mafao ni kikokotoo cha watumishi wa Umma. Kwa nini wasitumie kikokotoo kama wanachotumia JWTZ au TISS? Leo Askari anamaliza kazi yake, amefanya kazi miaka 30 anakwenda anakuwa masikini wa kutupwa, anakufa hata kabla ya siku zake. Hiyo lazima tufanye haki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata uhamisho. Utakuta kwenye uhamisho miaka 10 mnahamisha Askari hapa, mnapeleka pale, miaka 10 hamjawalipa. Wako wanaodai mpaka Shilingi milioni 100, wako wanaodai mpaka Shilingi milioni 80. Kwa hiyo, kwenye Wizara mnazidi kuongeza mzigo. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Shabiby, taarifa kutoka kwa Esther Matiko.
TAARIFA
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka nimpe tu taarifa, licha ya kwamba wanapewa kwa kama watumishi wengine na siyo kama JWTZ, lakini pia hata hayo mafao yao kwa maana ya michango wanacheleweshewa kupeleka. Wakistaafu wanaenda kufuatilia mafao yao wanaambiwa, hawawezi kupewa mafao mpaka watoe riba. Yaani wakatwe wenyewe ile adhabu ambayo wanatakiwa walipie waajiri wao ambao ni Serikali, wanalipa wao wenyewe. Kwa hiyo, unakuta Askari hawa wengine mpaka wanafariki hawajapewa mafao yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka nimpe tu hiyo taarifa iwe kwenye kumbukumbu yake.
MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Shabiby, taarifa hiyo unaipokea?
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo nilikuwa naitaka hiyo. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hawa Askari saa nyingine mnasema wanakula rushwa, hata mimi ningekuwa Polisi ningekula, kwa style hii. Ndiyo ukweli huo. Lazima mafao yao jamani wapate. Unajua kuna vitu vingi sana tunachangia tu, tunachukia, lakini tunaangalia kuanzia mishahara yao? Tunaangalia kuanzia maslahi yao? (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. AHMED M. SHABIBY: Hiyo ni kengele ya mwisho Mheshimiwa?
MHE. AHMED M. SHABIBY: Ni kengele ya pili?
MWENYEKITI: Ndiyo.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Dah, haya bwana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga hoja mkono. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia. Mimi nitachangia masuala ya Bandari yetu ya Dar es Salaam lakini si kwamba nitachangia kwa sababu labda kuna sintofahamu fulani lakini nitachangia yale ambayo hata kama kusingekuwa na uwekezaji lakini haya ningeyasema kwa sababu nilishasema kwamba nitasema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza nataka niseme tu na nitoe rai kwa Waheshimiwa Mawaziri wetu, kwamba haya yanayozungumzwa na wananchi kuhusu kuboresha mkataba wa utekelezaji huu unao kuja ni lazima yazingaitiwe. Lazima tuzingatie mkataba wa utekelezaji, tusiyapuuze maoni ya wananchi kwa sababu si kila mwananchi anayechangia basi anakuwa mpinzani wa Serikali, Hapana. Wako watu wazalendo ambao wanachangia kwa manufaa ya nchi. Kwa hiyo tuchukue mawazo yao mazuri yaingie kwenye hiyo mikataba ya utekelezaji, tusiwaone kwamba ni watu ambao labda wanapinga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema, kwenye uwekezaji kwenye bandari ndugu zangu ni kitu cha msingi sana. Kwa nini nasema hivyo? Mimi niko kwenye Kamati ya Miundombinu sasa hivi nafikiri karibia ni kipindi cha nne. Kamati ya Miundombinu tumetembelea bandarini pale zaidi ya mara tano sita. Ukisikiliza bandari kwa watu na yale mapato unayoambiwa kwamba yanakusanywa tofauti na faida wanayoileta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwape mfano tu; kwa mfano mapato ya 2021/2022 ilikuwa ni shilingi trilioni 1,144 (shilingi trilioni 1.14). Matumizi ni shilingi bilioni 805, faida ni shilingi bilioni 339. Kwa hiyo ukiangalia matumizi ni asilimia 73 faida ni asilimia 27 hilo ni tatizo. Kwa nini nasema ni tatizo? Faida ni ndogo matumizi ni makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiangalia hata kwenye ushushaji wa mizigo; ushushaji wa mizigo 2019/2020 tumeshusha tani milioni 17.2; 2020/2021 milioni 17.6; 2021/2022 milioni 20. Sasa nia yangu ya kuzungumza ni kama reli ya standard gauge tunayoijenga ina uwezo wa kubeba tani milioni 25 peke yake ambayo imezidi uwezo wa bandari, hapo bado reli ya kati tunaifanyia ukarabati, bado reli ya TAZARA tunaifanyia ukarabati, bado kuna malori ya nchi nzima maana yake itabidi yasimame.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama reli hii moja tu ya standard gauge ikichukua tani milioni 25 wakati bandari uwezo wake ni milioni 20 ina maana hakuna reli hata moja itakayofanya kazi. Sasa athari yake ni nini? Athari inakuja moja; kwenye malori tunaona kama yanaharibu barabara, yanaleta matatizo lakini ndio yenye mchango mkubwa na yenye ajira nyingi kuliko sehemu yoyote kwenye hii nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lori moja likitoka hapa kwenda Rwanda au Burundi linatumia lita 2,000 za mafuta, kodi ya Serikali kila lita inachukua shilingi 1,200, kwenye 1,200 ina maana Lori likienda hapa na Burundi katika lita 2,000 ina maana kodi inachukuliwa milioni mbili na laki nne kwenye trip moja ya Lori. Kwa hiyo lori likienda mara nne Burundi kwa Mwezi ina maana ni 8,800,000. Na ukiangalia mfuko wa barabara, nimeona hapa Wabunge wengi mnasema hapa barabara ndizo zinafungua uchumi. Barabara zinatengenezwa na magari kwa sababu zinatengenezwa na kodi ya mafuta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kama bandari yetu isipofanya vizuri, tunasema tu reli ikija barabara zitapona na mfuko gani utakaotoa fedha ya kutengeneza barabara kama malori hayatapata mzigo? Cha msingi ni kuhakikisha kwamba bandari inafanya kazi ya ziada kuhakikisha kwamba treni zinafanya kazi na malori nayo yanapata mzigo wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ukisema usimamishe malori ina maana umeshapoteza ajira zaidi ya milioni moja, kwa sababu tayari malori yapo zaidi ya laki moja kwa hiyo kila lori moja lina Tingo, lina dereva na mafundi. Ukija malori yanakopita kuna guest houses kuna, mama ntilie kuna kila aina. Ina maana miji yote ya pembezoni isiyopitiwa na reli nayo itakuwa ndiyo biashara yao imekufa. Kwa hiyo cha msingi tuzingatie kuweka mikataba yetu vizuri lakini lazima tuweke uwekezaji, bila uwekezaji haitawezekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine katika kupitia bandari, tutabadilisha Ma-MD wa bandari lakini hakuna kitu. Nataka niwaambie nchi hii wazalendo ni wachache, wapigaji ni wengi. Pale pale bandarini utakuta mashine za kushusha unaambiwa zimekufa ilhali haizijafa halafu kuna watu wenye tender ya kuleta Spear wanaingia na kagari, wakitoka unaambiwa tumetengeneza milioni 500, kumbe ile mashine haijafa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu kuna kingine ambacho tulikigundua hata zile Meli ambazo zinapaki kule nje, hata Mheshimiwa Waziri Mkuu juzi mmesema amesema kwamba demurrage charge ni dola 25,000 lakini zipo Meli ambazo zinalipwa demurrage charge mpaka dola 35,000 ambazo ni takriban milioni 95, ile kupaki tu. Kwa hiyo wakiharibu hivi vifaa wanafanya mpango na hawa watu wa bandarini, wakiharibu vile vifaa zile meli kule zinatengeneza faida huku zimesimama kwa sababu wanalipwa charge ya milioni 95, ya milioni 58 mpaka 60 huku meli imesimama, kwa hiyo uwekezaji kwenye bandari ni muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na Watanzania tusiogope uwekezaji, 2014 walikuja hapa Qatar kuja kuwekeza kwenye ndege, tukaona aaa, amekwenda sasa hivi Rwanda Air. Rwanda Air asilimia 51 ni ya Qatar, sasa hivi anajenga uwanja pale iwe hub; kwa hiyo maana yake Watanzania, Wakenya, watu wa Afrika Mashariki na Kati tukitaka kusafiri kwenda Ulaya, kwenda wapi twende tena tukapandie Rwanda. Kwa hiyo tusiogope, kama uwekezaji Serikali ilishashindwa, imeshindwa, tuache wawekezaji lakini wawekezaji wenye mikataba mizuri yenye manufaa na nchi wawepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni masuala ya viwanda hivi vya nguo. Muda umeisha au niendelee mzee kidogo…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Endelea Mheshimiwa.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vya nguo vya Tanzania.
MWENYEKITI: Mheshimiwa, tumia sekunde 30 kumalizia muda wako, nyongeza hiyo.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, hii nilikuwa nataka nizungumzie vitenge sasa hii habari ya sekunde thelathini haiwezi kutosha, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuwa mmoja wa wachangiaji katika Wizara yetu ya Mambo ya Nje. Kwanza ifahamike kwamba tunapochangia hatuchangii kwamba tunaipinga Serikali au mambo mazuri yanayofanywa na Serikali, kazi ya Mbunge ni kuishauri Serikali, hiyo ndiyo kazi ya Mbunge. Sasa Serikali walichukue au wasilichukue ni juu yao (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunataka tusema tu kwamba mimi naunga mkono hoja hii, lakini tunataka tumshauri mama yetu na Waziri wetu, labda kwanza nianze na hili tu ambazo ameliacha mama la uraia pacha. Uraia pacha ni muhimu kwa nchi yote hata kama kuna kuja hilo neno la hadhi maalum au chochote na tunaposema uraia pacha yule mtanzania atakayepata hiyo passport labda atakuwa na passport mbili, sisi hatuna haja kama mimi sina haja mimi nataka passport ya Tanzania tu inanitosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wengi waliokuwa kule ughaibuni ni wale watu ambao wameenda kutafuta maisha hawajaenda kule kutalii, watu lazima wafahamu hicho kitu, ebu tuzungumze je, hawa wanafunzi wanaomaliza vyuo vikuu au hao watu wanaomaliza shule hapa Tanzania kuna kazi za kuwapa? Hakuna kitu kama hicho, watu wanakwenda kule kutafuta maisha tuchuke kama nchi ya Philipines, Philipines leo inajengeka lakini inapata fedha nyingi sana kutoka kwa hao watu wake ambao wapo nje. Kwa hiyo mpango wowote na Wizara ya Mambo ya Nje haijawahi kufanya Semina ituambie je, kuna shida gani kwenye uraia pacha. (Makofi)
Mheshiimiwa Naibu Spika, kuna shida gani kwenye usalama, kuna shida gani kwenye hiki, hatujawahi kufanyiwa semina sisi Wabunge. Kwa hiyo Mbunge akisimama akizungumzia kitu kama hicho haki yetu lazima tukizungumze kitu kama hicho, lakini uraia pacha kwa watu waliokaa kule, waliopo kule sizungumzii kwa waliopo ndani ya nchi, uangaliwe utaratibu wa aina yoyote hawa watu wapewe uraia pacha kwa sababu wanamaliza hata fedha za Tanzania bila kujua. Mimi nina mtoto labda yupo Marekani au Uingereza raia wakule halafu nimeuza shamba unafiriki mimi simtumii fedha hizo na yeye akapata urithi, kwa hiyo fedha si inakwenda huko nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tuangalie nilitaka kuzungumza kwa kifupi tu kwamba Serikali ijaribu kujipanga vizuri iweke utaratibu kama kwenye vyombo vya usalama, kama kwenye siasa ijue vyote lakini kuwapa uraia ni kitu cha msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la kwangu kubwa la leo Mheshimiwa Waziri amezungumzia habari ya diplomasia pamoja na biashara na kwamba ametuambia anatengeneza sera inayokuja, lakini nataka niseme hii nchi hii sasa hivi Mama yetu Rais yupo katika mpango wa kufungua nchi, lakini ukiangalia sisi tunafungua tu Mawaziri lazima muwe makini sana, sisi tunafungua wapi kuja kufanya biashara Tanzania, lakini hatufungui wafanyabiashara wa Tanzania waende kufanya biashara nchi nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wewe ni shahidi na nafiriki pale Kariakoo ipo chini ya Jimbo lako, hivyo leo Wachina wanauza hadi vikombe vya plastiki, wanauza karanga, huko ndiko kufungua nchi? Halafu Watanzania tunakatazwa kwenda China, sasa hivi nchi zote mimi sio mfanyabiashara wa kutoka China, sifanyi biashara yoyote kutoka china zaidi ya kuagiza magari naagiza kwa IDC likija baya nawarudishia basi, lakini wapo watu wanaofanya retail, wanaofanya wholesale hizi kweli ni biashara ya kidiplomasia kweli za kufanya wachina kwenye hii nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Waziri wetu wa Mambo ya Nje pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara lazima waangalie hili suala Watanzania leo Wachina wanakuja kama shamba la bibi kila siku wanaingia, lakini Mtanzania hauruhusiwi kwenda China, unaambia uagize kwa whatsApp bidhaa, kwa hiyo aliyekuwa na bidhaa anaweza akaagiza anayetaka kwenda kuanza biashara au anayetaka kupeleka vitu China akauze China haiwezekani kitu kama hicho kwa sababu unajua hivi ni vituko, nchi zote Europe kweli China ni rafiki yetu, lakini angalia wa Europe, angalia India, angalia Dubai, angalia Marekani ukiwa una chanjo unaingia hiyo nchi bila kufanywa chochote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini China mpaka leo uchanje usichanje hakuna kitu, ndege yetu ya Tanzania imejaribu kwenda mara ya kwanza wakaambiwa kuna watu wana corona, mara ya pili kuna watu wana corona Wachina wenyewe hao hao ndege msileta, lakini KLM inaruhusiwa inakwenda kutoka hapa hadi China dola 14,000, kutoka China kuja hapa dola 7,000 na ndege ya Tanzania imezuiliwa na kila Ijumaa ndege ya Tanzania inakwenda China, lakini inakwenda tu kuchukua mzigo hairuhusiwi kupakia hata mtu mmoja. Sasa huu urafiki au diplomasia ipi! Hebu tuulizane hapa swali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wao wa China kuja Tanzania wanakuja kwa wingi basi hata wangeturuhusu ndege yetu iwapakie wao tu kwa dola 14,000 maana tukipakia watu 40 ndege imelipa, lakini hata hiyo ndege hawataki kupanda wanaenda kupanda KLM sasa hivi naona Ethiopia imeruhusiwa na Kenya Airways nayo imeruhusiwa diplomasia hii ya kibiashara lazima iwe fair wao wafaidike na sisi tufaidike, hiyo ndio diplomasia na lazima pawe na sheria na utaratibu kuhusu mambo ya biashara ya nchi za nje hizo sio biashara ndogo ndogo anazofanya Mtanzania anakwenda kufanya mtu wa nje haiwezekani hicho kitu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo Kariakoo mtu akichukua kontena moja mbili za vitu china ujue ni mara yake moja, mara ya pili mchina anakuja kufungua duka Tanzania, yaani ukionekana tu unafanya biashara pale ya vitu vitu hivi ukileta siku ya pili wanaleta wao. Sasa Watanzania wataendelea kuwa wachuuzi siku zote haiwezekani, mimi ushauri wangu kwa mama yetu aangalie…(Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
NAIBU SPIKA: Taarifa.
T A A R I F A
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, nilitaka kumpa taarifa mchangiaji kwamba Watanzania wengi tunafanya biashara na China na hata kukubali kuchanja chanjo za corona tulitegemea nchi zitafunguka kwenye sehemu zetu za biashara kama China na nchi nyingine zimechanjwa madawa kama ya kwetu kutoka Marekani na sehemu nyingine wanaruhusiwa kuingia Marekani, lakini sisi tuliochanjwa za China, sisi tuliochanjwa hizo dawa tunaonekana bado hatujapona.
Kwa hiyo nilitaka kukupa Taarifa Mheshimiwa kwamba tulichanjwa ili tukubali masharti ili tukubali kuingia China kwa sababu ndio mji wa kibiashara kwa Tanzania.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Shabiby.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakubali taarifa yake, ipo vizuri kabisa.
Kwa hiyo la mwisho nataka kumshauri mama yetu akae na hawa kama wanataka na wao wawe wanaingia huku na sisi waturuhusu na sisi watu wetu waingie kule, kama hawataki na sisi tuwe hatuna imani na chanjo zao sio wao wanafanya biashara na nataka nikwambie wanatumia akili sana mwishoni biashara zote za Tanzania, sisi tutakuwa tutabaki tu kuuza mahindi na maharage, watafanya wao, wao Wachina, watu wa Europe kama anavyosema Mheshimiwa Musukuma wanaruhusiwa kuingia lakini watu wa Afrika hawaruhusiwi kuingia. Kwa hiyo tusipoamka tutakuwa tunawafanyia wao biashara, ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuwa mmoja wa wachangiaji kwenye bajeti kuu. Mimi nitanyoosha maelezo, sitosifu sana kwa sababu sitoki Singida. Tutazungumza yale ambayo yana ukweli. Ili Waziri wa Fedha na Waziri wa Uwekezaji muonekane mnafanya kazi ni lazima kazi yenu ionekane kwa wananchi. Kwa hiyo, siyo kwa sababu tuko CCM pekee humu basi tunasifiana sifiana tu hata kama vitu haviendi vizuri. Kama vitu vinakwenda vizuri tusifiane ndio ubinadamu na kama vitu vinakwenda vibaya tutaambiana ukweli. Kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu penda sana watu wanaokwambia ukweli kama sisi hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka leo nijikite kwanza kwenye barabara. Mheshimiwa Dkt. Mwigulu naomba unisikilize vizuri sana. Mimi niko kwenye Kamati ya Miundombinu, kwenye Kamati ya Miundombinu barabara ambazo zimechoka Tanzania kongwe ni 71 ambazo muda wake umekwisha na sasa hivi ziko hoi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukichukua mfano tu Barabara ya Shinyanga - Mwanza, Lindi – Dar es Salaam, Njombe – Songea, Morogoro – Dodoma. Pia, chukua barabara za mijini na nyingi nyingi tu, barabara ziko hoi tu. Ukiangalia bajeti ambayo mmeipangia Wizara ya Ujenzi ni shilingi1,700,000,000,000 lakini madeni ni shilingi 1,200,000,000,000. Kwa hiyo, ina maana wao watabakia na shilingi bilioni 500, shilingi bilioni 500 itafanya kazi gani? Hamna chochote tunachotengeneza kwenye hizi barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutawalaumu hawa TARURA na TANROADS wao wanafanya kazi nzuri, na ni lazima tuwashukuru hawa ma-MD wa TARURA na TANROADS wanafanya kazi nzuri. Mheshimiwa Waziri, mimi hapa kama hii ndiyo bajeti na kama bajeti ya Ujenzi, bajeti ya TARURA hazitaongezewa pesa za barabara, mimi ndiyo nitakuwa wa kwanza kupinga bajeti. Chukua yale maoni tuliyokupa kutoka Kamati ya Miundombinu ya kuongeza vyanzo vya uhakika vya barabara, huo ndiyo ukweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sitaki kuzungungumzia habari ya sukari, sijui ya nani na nani kwa sababu ukichimba kote, hawa na hawa tukiongea hapa itakuwa balaa, bora tunyamaze lakini tujikite kwenye hizi barabara zetu. Mheshimiwa tafuta vyanzo vya uhakika, chukua ushauri wetu wa Kamati ya Miundombinu agalau tupate shilingi trilioni 2.2 kwenye TANROADS na tupate shilingi bilioni kama 400 kwenye TARURA ili Wabunge tukienda kule tuonekane tumefanya kazi ndugu zangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine mwaka 2022 ulisema Serikali inatumia zaidi ya shilingi bilioni 500 kwa ajili ya kuagiza magari ya Serikali Tanzania lakini bado najiuliza swali moja, hii Serikali ni tajiri sana au kuna shida gani? Umekuja ukalalamika na ukaleta mpango kwamba sasa hivi kwa kuondoa gharama hizo kila mtumishi atanunua gari lake ili alionee uchungu atalimiliki. Mwaka huu sijalisikia, sasa inaonekana na sijajua imekuja mpya au ile imeshindikana au vipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha msingi mimi najiuliza hivi twende Halmashauri zote za Serikali za Mitaa, Manispaa zote, majiji yote na twende Serikalini kwenye Wizara zote haya magari mabovu mpaka yanaoza na mengine hayauziwi na yakiuzwa, wanajiuzia wenyewe. Hivi hii nchi ina utajiri wa kiasi gani kwamba haipigi mnada yale magari? Nani alishawahi kusikia hapa kwamba kuna gari la Serikali linauzwa kwenye minada? Haijawahi kutokea. Kwa hiyo, magari yote mnajiuzia wenyewe tena kwa tender. Unakuta gari ambalo lingepigwa mnada kwa shilingi milioni 70, shilingi milioni 80 utakuta limenunuliwa kwa milioni tano, milioni sita. Halafu tunazungumzia habari ya kwenda kuwaminya watu wadogo wadogo hawa huku chini wakati huku kuna pesa nyingine zimelala lala tu, hicho kitu hakiwezekani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, twendeni pale kwangu Gairo tu nina magari saba, ukienda hapa kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma huwa napitapita magari yako kibao. Ukienda manispaa zote yanauzwa vipi? Yanatakiwa yauzwe kwa mnada, tunaomba usimamie vitu kama hivyo. Mimi ukitekeleza hivyo na ukinijibu hivyo nitaunga mkono hoja yako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni habari ya hii pesa. Hizi taasisi zenu za Serikali mnakwenda mpaka huko mnazisifu kwamba fulani wameweka gawio bilioni tatu, Bandari wameleta shilingi bilioni nne, EWURA shilingi bilioni tatu halafu mnashangilia kweli sasa hivi taasisi zetu… Haya National Housing bilioni ngapi wakati ina madeni kibao? Sijui nani ana bilioni ngapi. Sasa mimi najiuliza swali hivi sasa hivi kila taasisi imekuwa TRA? Yaani sasa hivi hatuna TRA. Pamoja na kuwa Serikali inategemea TRA kukusanya kodi na kufanya maendeleo ya nchi lakini sasa hivi kila taasisi ya Serikali ikianzishwa inakuwa TRA. Ikianzisgwa sijui EWURA inakuwa TRA, ikianzishwa LATRA inakuwa TRA, ikianzishwa Bandari inakuwa TRA, OSHA nayo TRA yaani kila mtu anakuwa TRA. Ukienda kule TANAPA nayo imekuwa TRA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa nafikiri ule mpango wa awamu ya tano ulikuwa siyo mbaya wa kuchukua zile pesa zote halafu wao waandike bajeti kwamba sisi ni taasisi fulani bajeti yetu ya mwaka ni hii. Ninyi BOT mnachotakiwa kufanya ni kuwafungulia akaunti tu iwe single treasury account. Wafungue single treasury account ili pesa zote wanazokusanya ziingie kwenye akaunti kuu ya Serikali halafu wao wanakuwa na bajeti na ninyi msiwache kuwapelekea. Halafu zinazobaki kwa mwaka ndiyo gawio. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ikibaki labda kwenye taasisi fulani imekusanya shilingi bilioni 100 lakini bajeti yao ilikuwa ni shilingi bilioni 50 maana yake pale tayari kuna shilingi bilioni 50 zetu. Sasa mnawaachia wao wanapanga, wanatengeneza, wanatunga na wanatandika (wanazila) zile pesa halafu zikija huku mnashangilia vihela vidogovidogo. Mnapewa vihela vidogo, aah, hii taasisi inajiendesha na ina gawio shilingi bilioni tatu. Hivi kweli bilioni tatu kwenye taasisi zinazokusanya pesa namna hii, halafu tunakuja hapa tunakuwa washangiliaji. Mimi siwezi kuwa mtu wa kushangilia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndiyo ukweli na ukiona Wabunge wametulia namna hii ujue wanasikiliza kwa makini, hii inawangia, ndiyo ukweli. Kwa hiyo, nilikuwa nakuomba Mheshimiwa na nakuona hata unavyopata taabu. Juzi hapa nilikuona unapata taabu sana ya kutafuta pesa lakini kuna baadhi ya taasisi zako zilikuwa zinakupinga, hiyo mimi ninaijua lakini ukiwa Waziri wa Fedha unatakiwa uwe ngangari. Kama umeshindwa kuwa ngangari unatakiwa uachie nafasi ili hata mimi nije nikae hapo. Mheshimiwa Waziri uwe ngangari, unafanya kazi nzuri lakini kuwa ngangarti kwenye hivi vitu. kila mtu akitaka achukue pesa na Mheshimiwa Waziri hapo ukitaka kuwa mzuri kwa kila taasisi hiyo kazi haiwezekani. Nchi imefikia mahali sasa hivi na lazima tuseme ukweli, wapigaji wamekuwa wengi. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wapigaji ni wengi na wengine utasikia tu Mama anaupiga mwingi. Siyo anaupiga mwingi kwamba anamsifia kwenye moyo, hapana anaupiga mwingi yeye anaiba hela. Anatandika pesa halafu akija huku anajifanya anasifia. Hata wewe Waziri wa Fedha na taasisi yako ya Mamlaka ya TRA nyie ndio mnaopata taabu. Ninyi lazima mkusanye kodi, mzilete kwenye mishahara, lazima ninyi huku ndiyo mzipeleke kwenye maendeleo wakati ukiangalia kuna taasisi nyingine mkizichanganya zinakusanya nusu ya TRA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi leo sitaki kuongea mambo mengi. Nafikiri amenielewa na ndiyo maana ameweka mikono hivi najua hapo amenielewa. Ahsante sana kwa kunielewa naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)