Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dr. Haji Hussein Mponda (6 total)

MHE. DKT. HADJI H. MPONDA aliuliza:-
Mwaka 2012 Serikali kwa kushirikiana na kampuni ya China, Railway Bureau 15 Group Corporation, waliingia mkataba wa miaka miwili wa ujenzi wa Daraja la Kilombero na barabara zake za maingiliano kwa gharama ya Sh.53.2 bilioni lakini mpaka sasa ujenzi huo bado haujakamilika:-
(a) Je, ni kiasi gani cha fedha kimetengwa na kutolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo tangu mkataba huo uanze?
(b) Je, ni lini daraja hilo litakamilika na kuanza kutumika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Hadji Hussein Mponda, Mbunge wa Malinyi, jirani yangu, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwaka wa fedha 2010/2011 hadi mwaka huu wa fedha 2015/2016, Serikali imekwishatenga jumla ya shilingi bilioni 25.59913 kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Kilombero na gharama za Mhandisi Msimamizi anayesimamia ujenzi wa daraja hilo ni shilingi bilioni 2.75 bila ya Kodi ya Ongezeko la Thamani.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu ulipangwa kukamilika tarehe 20 Januari, 2015. Hata hivyo, haukuweza kukamilika katika muda uliopangwa kutokana na ufinyu wa fedha uliosababisha kuchelewa kulipwa kwa madai ya malipo ya mkandarasi kwa kazi zilizofanyika. Kutokana na tatizo hilo, mkandarasi alikosa mtiririko mzuri wa fedha za kufanya kazi na hivyo kupunguza kasi ya utekelezaji wa mradi.
Hata hivyo, hadi Februari, 2016 Serikali imeweza kulipa madeni yote ya mkandarasi aliyokuwa anadai. Aidha, Serikali itaendelea kumlipa mkandarasi kulingana na kazi atakazozifanya. Kwa sasa kazi ya ujenzi wa daraja imesimama kutokana na Bonde la Mto kilombero kujaa maji. Kazi ya ujenzi wa daraja itaanza mara maji yatakapopungua katika Bonde la Mto Kilombero.
MHE. OMARY T. MGUMBA (K.n.y. MHE. DKT. HADJI H. MPONDA) aliuliza:-
Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini iliahidi kupeleka huduma za umeme katika Hospitali ya Lugala ambayo ni hospitali pekee na tegemezi katika Wilaya nzima ya Malinyi. Katika kutekeleza agizo hili, Oktoba, 2014, TANESCO Mkoa wa Morogoro ilitengewa fedha kwa kuanza ujenzi huo wa 33KV, HT line ya kilometa 3.5 na kuunganisha umeme katika hospitali hiyo na Kijiji cha Lugala lakini hadi leo agizo hilo halijatekelezwa:-
(a) Je, sababu gani zilifanya mradi huo usitekelezeke licha ya kutengewa fedha?
(b) Je, ni lini hospitali hiyo muhimu kwa wakazi wa Wilaya ya Malinyi itapatiwa huduma ya umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Hadji Hussein Mponda, Mbunge wa Malinyi, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa kupeleka umeme katika Hospitali ya Lugala, Wilayani Malinyi haukuweza kutekelezwa kwa sababu fedha iliyotarajiwa kutengwa kutoka kwenye bajeti ya TANESCO ya mwaka 2014/2015 haikutengwa kutokana na ufinyu wa bajeti ya TANESCO. Hata hivyo, Hospitali hiyo pamoja na Kijiji cha Lugala vitapatiwa umeme mwaka huu kupitia bajeti ya TANESCO. Kazi hii itajumuisha sasa ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa tatu, ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa tano pamoja na ufungaji wa transfoma mbili za kVA 100 na kVA 200.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na utekelezaji huo, kazi nyingine itakayofanyika ni kuwaunganishia umeme wateja wapatao 116 katika maeneo hayo. Kazi hii inatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Juni, 2016 na itakamilika mwezi Julai, 2016 kwa gharama ya shilingi milioni 329.27.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA aliuliza:-
Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Mitambo wameahidi kuhamishia kivuko cha MV Kilombero II kwenda katika kivuko cha Kikove katika Mto Kilombero Juu (Mnyera) baada ya kukamilika kwa ujenzi wa daraja la Kilombero.
Je, ni lini matayarisho ya uhamisho wa Kivuko hicho yataanza rasmi kwa kuwa ujenzi huo wa daraja la Kilombero unatarajia kukamilika hivi karibuni?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Hadji Hussein Mponda, Mbunge wa Malinyi, kama ifuatavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), imeanza maandalizi ya kuhamisha vivuko vya MV Kilombero I na MV Kilombero II kuvipeleka eneo la Kikove katika Mto Kilombero kwenye barabara inayounganisha Mlimba na Malinyi. Wakala wa Barabara kwa kushirikiana na Wakala wa Ufundi na Umeme umefanya ukaguzi wa barabara ya Mlimba hadi Malinyi ili kubaini mahitaji ya miundombinu itakayowezesha kivuko hicho kufanya kazi katika eneo hilo la Kikove. Miundombinu hiyo ni pamoja na maegesho na barabara unganishi katika kila upande wa mto.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Serikali ni kuhamisha vivuko vilivyopo eneo la Ifakara kwenda eneo la Kikove katika barabara ya Mlimba – Malinyi mara tu baada ya mradi wa ujenzi wa daraja la Mto Kilombero na barabara za maingilio kukamilika. Hivi sasa ujenzi wa daraja la Mto Kilombero umekamilika na Mkandarasi anakamilisha ujenzi wa barabara za maingilio ili daraja lianze kutumika.
MHE. OMARY T. MGUMBA (K.n.y. MHE. DKT. HADJI H. MPONDA) aliuliza:-
Vijiji vya Ngoheranga na Tanga katika miradi ya maji inayofadhiliwa na Benki ya Dunia (Phase II World Bank Project), vimepangiwa kufanyiwa upembuzi yakinifu, usanifu wa kina, uchimbaji wa visima na ujenzi wa miundombinu ya maji; zoezi hili limeishia tu kwa uchimbaji wa visima virefu nane na mradi kusitishwa.
(a) Je, ni lini Serikali itakamilisha utekelezaji wa miundombinu ya usambazaji wa maji ya bomba kama ilivyo katika vijiji vingine vinavyofadhiliwa na Benki ya Dunia?
(b) Je, ni lini Serikali itapelekea maji katika vijiji vilivyosahaulika vya Mtimbira, Majiji, Kiswago na Ihowanja?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali Mheshimiwa Dkt. Hussein Mponda, Mbunge wa Malinyi, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vya Ngoheranga na Tanga ni kati ya vijiji kumi ambavyo vilifanyiwa usanifu mwaka 2008 na mwaka 2010 vilichimbwa visima vitatu ili vitumike kwa ajili ya usambazaji wa maji ya bomba. Kati ya visima hivyo visima viwili vilikosa maji kabisa na kitongoji kimoja cha Mkanga kilipata maji kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2015 wataalam wa Halmashauri ya Wilaya kwa kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge walishauri vichimbwe visima virefu na kufungwa pampu za mkono kwa kila kitongoji ikiwa ni mbadala wa maji ya bomba. Ushauri huu ulizingatiwa na visima 13 vilichimbwa ambapo visima vinane vilipata maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itakamilisha uwekaji wa miundombinu ya usambazaji wa maji ya bomba katika visima vinane vilivyopata maji kupitia Awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji ambayo imeanza kutekelezwa mwezi Julai, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, vijiji vya Mtimbira, Majiji, Kiswago na Ihowanja havijasahaulika kwani Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya maji katika vijiji hivyo kupitia Awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji. Halmashauri inaendelea kukamilisha taratibu za utekelezaji wa miradi katika vijiji hivyo ili wananchi waweze kunufaika na huduma ya maji.
MHE. DKT. HAJI H. MPONDA aliuliza:-
Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo (SAGCOT) imekamilisha ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji, Itete ambapo imehusisha ujenzi wa miundombinu ya banio na mfereji mkuu wa kilometa 6.6, lakini katika kipindi kifupi cha matumizi ya skimu hii mfereji huo mkubwa umeshaanza kuharibika kutokana na kiwango duni cha ujenzi:-
(a) Je, ni lini Serikali itamalizia ujenzi wa mfereji mkuu na mifereji ya kati, ili kuendeleza kilimo katika hekta 7,000 zilizobaki katika skimu hiyo?
(b) Je, ni lini Serikali itafanya ukarabati wa mfereji mkuu uliobomoka katika kipindi hiki cha uangalizi?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Hadji Hussein Mponda, Mbunge wa Jimbo la Malinyi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa mradi wa umwagiliaji katika Skimu ya Itete ulianza mwezi Mei, 2013 na kukamilika mwezi Oktoba, 2015.
Mheshimiwa Naibu Spika, upanuzi wa mradi huu unategemea kwa kiwango kikubwa kiasi cha maji katika Mto Mchilipa, kwani usanifu wa awali ulibainisha hekta 1,000 ambazo ndizo zilizoendelezwa. Ili kuweza kuendeleza miundombinu ya umwagiliaji katika eneo lililobaki Serikali inajipanga kufanya upembuzi yakinifu kuona kama kuna uwezekano wa kujenga bwawa ili kutunza maji ya mvua ya Mto Mchilipa, ambayo yatatumika katika kuendeleza eneo lililobaki.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ndogo iliyobomoka ya mfereji, Wizara yangu kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Kanda ya Morogoro imeshafanya mawasiliano na Mkandarasi aliyejenga skimu hiyo na amekubali kufanya marekebisho katika sehemu hiyo katika kipindi cha uangalizi.
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA aliuliza:-
Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) iliingia mkataba wa utafiti wa uchimbaji wa gesi na mafuta na Kampuni ya Mafuta ya Swala (SOGTP). Katika utekelezaji wa mpango huo wamegundua kuwepo kwa wingi mafuta ya petroli na gesi katika vijiji vya Kipenyo na Mtimbira Wilayani Malinyi katika Mkoa wa Morogoro.
(a) Je, ni lini uchimbaji wa visima na uvunaji wa mafuta utaanza rasmi katika maeneo hayo?
(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwatayarishia wananchi wa maeneo hayo ili kuondoa migogoro inayoweza kujitokeza baina yao na Serikali kama vile gesi ya Mtwara?
WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Hadji Hussein Mponda, Mbunge wa Malinyi, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti wa mafuta katika kitalu cha Kilosa – Kilombero unafanywa na Kampuni ya Swala Oil Gas Tanzania ulianza mwezi Februari, 2012. Utafiti huo ulianza baada ya kusainiwa kwa Mkataba wautafutaji kati ya Serikali kupitia TPDC na Swala mwezi Februari, 2012.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo ambalo limeainishwa kwa ajili ya uchimbaji wa kisima hicho lipo katika Kijiji cha Ipera Asilia katika Hifadhi Tengefu ya Bonde la Kilombero.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kisima hicho kinatarajiwa kuanza kuchimbwa mwezi Septemba, 2018 kutegemea matokeo ya utafiti huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TPDC imekuwa ikitoa elimu kwa wananchi wa maeneo kunakofanyika utafiti huo. Tarehe 06 hadi 17 Februari, 2017 TPDC kwa kushirikiana na Kampuni ya Swala ilitoa elimu ya masuala ya gesi na mafuta katika maeneo ya Halmashauri ya Mji huo ikiwa Mji Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na Wilaya za Kilombero pamoja na Malinyi. Aidha, wananchi wa Kata ya Mtimbira, Njiwa pamoja na Kitete katika maeneo vijiji vya Mtimbira, Kipenyo, Ipera Asilia na Warama pia walipata elimu ya hifadhi ya mazingira pamoja na manufaa ya mradi huo.