Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Prosper Joseph Mbena (10 total)

MHE. PROSPER J. MBENA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Kwa kuwa tatizo hili ni kubwa sana nchini kwetu na kwa kuwa wahusika Wizarani wanaonekana kutolitambua vizuri ukubwa wake pamoja na kwamba watoto wa mitaani wanaonekana kila siku; je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kuanzisha register pale Wizarani kwake ambako itapokea majina ya wanaume pamoja na wanawake wachache ambao wanatelekeza watoto wao ili aweze kuwa na kumbukumbu nzuri? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri atakubali kupokea ushauri binafsi kutoka kwa wadau wanaokerwa na tatizo hili ili ushauri huo aweze kuutumia katika kuleta mapendekezo ya kurekebisha Sheria Namba 21 ya Watoto?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti naanza na la (b), Serikali iko tayari sana kupokea ushauri kutoka kwa mtu yeyote Yule.
Lakini (a) kwamba Serikali kuanzisha registers pale Wizarani namba nijibu kwamba Serikali kupitia Sheria ya Mtoto Namba 21 ya mwaka 2009 ambayo ilitungwa na Bunge lako Tukufu, kwenye kile kifungu cha 94 inatoa mamlaka kwa Halmashauri yaani Serikali za Mitaa kuwabaini watoto wote wa mitaani na kuwahudumia.
Kwa maana hiyo Waheshimiwa Wabunge tusikwepe jukumu hili kusimamia utekelezaji wa sheria hii kwenye Halmashauri zetu. Lakini kusema jambo hili litashughulikiwa centrally pale Wizarani wakati watoto wako kwenye Serikali za Mitaa ni kujaribu kuweka urasimu ambao hauhitajiki.
Hivyo Waheshimiwa Wabunge wote na Halmashauri zetu tukiwa kama viongozi wajumbe kwenye Halmashauri hizi, tuweke mikakati mahsusi ya kuwahudumia watoto hawa kule kule kwenye Halmashauri zetu.
MHE. PROSPER J. MBENA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa barabara inayozungumzwa hapa kujengwa kwa kiwango cha lami ni Bigwa - Kisaki na siyo Bigwa - Mvuha ambayo ni sehemu tu ya barabara hii; na kwa kuwa Serikali inazungumzia ufinyu wa bajeti pamoja na kupatikana kwa fedha ndipo ujenzi kamili wa barabara hiyo uanze:-
Je, Serikali ipo tayari kuruhusu ujumbe wa wananchi wa Morogoro Vijijini ukiongozwa na Wabunge wao wa Jimbo la Morogoro Kusini na Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki ili waweze kwenda kumwona Mkuu wa Nchi na kufikisha kilio chao na ikiwezekana waweze kujua kwa nini wafadhali wa MCC II ambao walipangiwa kuutekeleza mradi huu wameuacha na sasa unawaadhibu wananchi wa sehemu hiyo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa madaraja yaliyotajwa hapo hususan daraja la Ruvu, Mvuha pamoja na Dutuni yanahatarisha sana maisha ya wananchi wanaopita humo barabarani kwa kutumia madaraja hayo:-
Je, Serikali itafanya mara moja matengenezo ya haraka ya kuwawezesha wananchi kupita kwa usalama? Naomba kauli ya Serikali, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Prosper Joseph Mbena, aliyekuwa Msaidizi wa Rais wa Awamu ya Nne, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kumwona Mheshimiwa Rais, nadhani anafahamu utaratibu kwamba anahitaji kuwasiliana na Viongozi wa Mkoa na kadiri Mkoa utakavyoona kutokana na hoja zitakazoongelewa hilo linaweza kufanyika. Kikubwa ninachomweleza, niliyomjibu hapa ni dhamira ya dhati za Serikali. Kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, barabara hii ya kutoka Bigwa hadi Kisaki, tutaijenga kwa kiwango cha lami kama tulivyoahidi katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Kama ambavyo Viongozi wetu Wakuu wakati wa kampeni na wakati wa misafara mbalimbali wameahidi, tutaitekeleza katika kipindi hiki cha miaka mitano na tunaanzia na nusu yake kutoka Bigwa -Mvuha. Tayari ma-consultant wanafanya kazi tarehe 30 Juni wanakamilisha na baada ya hapo tutaanza kutafuta fedha kujenga hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa swali lake la pili, ni kama nilivyojibu katika swali la msingi kwamba TANROADS Morogoro wataendelea kuyaimarisha madaraja hayo na kuyafanyia matengenezo ili yaweze kupitika kwa usalama wa wananchi wa maeneo hayo.
MHE. PROSPER J. MBENA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na napenda kumpa taarifa kwamba tayari vikao hivyo vimeshafanyika na tayari mkataba kati ya Kanisa Katoliki pamoja na Halmashauri ya Wilaya Morogoro umeshakamilika na nitampatia nakala ya mkataba huo. Baada ya hatua hiyo kufikiwa. Je, Mheshimiwa Waziri sasa atashughulikia lini? Itachukua muda gani kushughulikia suala la kupatikana kwa watumishi pamoja na kada nyingine zinahitajiwa kwa hospitali hiyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu kama mchakato huu tayari umeshaanza, basi ina maana kwamba walikuwa mbele ya tukio zaidi. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni jukumu la Serikali sasa kwamba mara baada ya mchakato huo kukamilika, sasa ni kuangalia kipi kinachohitajika katika eneo lile hasa tukitoa kipaumbele katika suala zima la watumishi kama alivyozungumza. Kuhusu lini, naomba niseme ni katika kipindi kifupi kijacho. Kwa kuwa lengo letu kubwa ni kuhakikisha kwamba tunaongeza kada katika maeneo mbalimbali, basi Wilaya yake tutaipa kipaumbele hasa katika eneo hili ambapo nami nilifika kule katika Wilaya yake nikaona kwamba ni kweli, wananchi wanaotoka kule Mvuha mpaka kuja Morogoro Mjini ni kilomita nyingi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuna kila sababu ya kuiwezesha hospitali hii. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ni commitment ya Serikali kuwezesha kituo kile katika vifaa tiba na wataalam. Lengo kubwa ni kwamba wananchi wa eneo lile wapate huduma.
MHE. PROSPER J. MBENA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri, naomba kumuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwa kuwa fidia kamili kwa wale waliohusishwa na kuchukuliwa maeneo yao haijalipwa kama alivyozungumza Mheshimiwa Waziri kwamba kuna bakaa ya shilingi bilioni mbili ambayo wametenga kwa ajili ya kulipwa; na kwa kuwa, ninayo taarifa kwamba DAWASCO wameshapeleka mabango ili yawekwe kwenye maeneo yote ya sehemu hizo kuzuia wananchi wasifanye shughuli zozote za maendeleo, kwa maana kwamba tayari wameshakabidhiwa maeneo hayo.
Je, sasa Serikali iko tayari kusitisha uwekaji wa mabango hayo hadi wananchi watakapolipwa fidia yao kamili? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa maeneo ya Bwakila Chini, Kiganila na Magogoni katika kata hii ya Serembala imekumbwa na mafuriko makubwa sana na wananchi wako kwenye maji kwa wiki tatu sasa.
Je, Serikali itapeleka msaada wa chakula na madawa ya dharura? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa ni kweli tayari tumeshalipa zaidi ya shilingi bilioni saba katika hilo eneo na kilichojitokeza ni kwamba baada ya DAWASCO kulipa ile fedha yale maeneo kwa taarifa ambazo tulizipata wananchi walianza kuwauzia watu maeneo yale ambao hawajui kwamba maeneo yale yameshalipwa fidia. Baada ya taarifa hiyo kupatikana, Mkurugenzi wa Halmashauri yako Mheshimiwa Mbunge ndiye aliyeamua kuweka vibao ili kuweza kuwapa tahadhari wananchi kwamba lile eneo wasiuziwe kwa sababu lilishalipwa fidia vinginevyo tutapata matatizo zaidi katika Serikali. Kwa hiyo mabao yale niseme kwamba hayajawekwa na DAWASCO yamewekwa na Mkurugenzi wa Halmashauri yako.
Swala la mafuriko, kwanza nikupe pole kweli nami ninayo taarifa kwamba kuna baadhi ya vijiji ambavyo vimeingiliwa na maji, kwa vile taarifa hii uliyoitoa ya mafuriko na kuomba msaada Serikali imesikia na iko Idara husika inayohusika na jinsi ya kusaidia maeneo ya maafa basi nafikiri naomba ulifikishe huko ili liweze kushughulikiwa.
MHE. PROSPER J. MBENA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nashukuru majibu ya Serikali hasa kwa kubaini umuhimu wa kulirudisha hili Shirika la TAFICO kufanya uvuvi hasa kwenye bahari kuu, nadhani wamechukua ushauri wetu, naomba kuwapongeza. Nina swali moja tu la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa uvuvi ni sekta muhimu sana hasa katika sera hii ya Serikali ya uchumi wa viwanda: Je, ni lini Serikali itasaidia Jimbo la Morogoro Kusini kuleta wataalam wake kufanya utafiti kwenye mito mikubwa yenye utajiri mkubwa wa samaki na dagaa ili nao waweze kuchangia kwenye uchumi huo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ombi lake ni kwamba, Serikali iweze kupeleka wataalam Jimboni kwake wakafanye utafiti. Naomba nilichukue tukaliangalie ndani ya Wizara ili ikiwezekana wataalam waweze kwenda kule.
MHE. PROSPER J. MBENA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na rai aliyoitoa kwa wahusika. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa tatizo hili linaonekana kuongezeka nchini; je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba Hospitali Maalum ya wagonjwa wa akili nchini yaani hospitali ya Mirembe inawezeshwa kiutaalam na vifaa ili kuweza kukabili tatizo hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kuwahakikisha kwamba hospitali zote za Wilaya pamoja na za Mikoa zinapatiwa angalau Daktari mmoja ambaye ni mtaalam wa mambo ya akili ili kuweza kutoa huduma ya karibu kwa wananchi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuifanyia maboresho Hospitali ya Rufaa ya Mirembe. Hivi tunavyoongea tunakamilisha ukarabati ambao umetugharimu zaidi ya milioni 976 na itaongeza kupanua wigo sana kuiboresha hospitali yetu ili kutoa huduma nzuri na za ziada. Sambamba na hilo tumeendelea kuongeza Wataalam na kutoa mafunzo kwa wataalam walioko ili waweze kutoa huduma bora na zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili alitaka kujua, je, tuna mkakati gani wa kupeleka wataalam katika ngazi za mikoa na wilaya. Katika utaratibu wetu wa sasa ngazi ya rufaa katika masuala ya afya ya akili ni ngazi ya mikoa hili tunalifahamu na tuko katika mchakato wa kuhakikisha kwamba tunawajengea uwezo Madaktari ili tuweze kupata Madaktari Bingwa wa Afya ya Akili kuweza kutoa huduma hizo katika ngazi ya rufaa ya Mikoa.
MHE. PROSPER J. MBENA: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Pia nifanye marekebisho kidogo Mheshimiwa Waziri alipozungumzia Jimbo langu mimi ni Mbunge wa Morogoro Kusini siyo Morogoro Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa Serikali imekubali kufanya matengenezo ya mara kwa mara katika barabara ya Bigwa mpaka Kisaki ili iweze kupitika wakati wote; na kwa kuwa hivi sasa kuna tatizo kubwa katika sehemu ya Milengwelengwe katika Kata ya Mngazi, usafiri umekuwa mgumu barabara imeharibika. Je, Waziri yuko tayari kuagiza Mkandarasi pamoja na Meneja wa TANROAD Morogoro kwenda haraka eneo hilo na kufanya matengenezo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa nini Serikali isirahisishe matengenezo ya mara kwa mara katika barabara hii kwa kuruhusu kutengeneza vitengo vya matengenezo ya barabara katika Tarafa tatu ndani ya barabara hii ya Bigwa hadi Kisaki ili kurahisisha matengenezo ya barabara? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Mbena kwamba Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro anatakiwa aende haraka eneo la Ilengwelengwe kuhakikisha kwamba mawasiliano kati ya Kisaki na Morogoro Mjini yanapitika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili nimepokea ushauri wake, ngoja tupeleke kwa wataalam waangalie, wakachakate waone uwezekano wa kulitekeleza hilo. Nadhani anakumbuka kwamba zamani tulikuwa na vikosi vya PWD au tulikuwa tunajulikana zaidi PWD na baadaye tulivyoondoa na TANROADS ikaunda hiyo ofisi za Mikoa na ofisi za Mikoa zinafanya kazi zile zile ambazo PWD ilikuwa inafanya kazi zamani. Hata hivyo, kama nilivyosema ngoja nilichukue hilo wazo likachakatwe halafu tuone tutasonga mbele vipi.
MHE. PROSPER J. MBENA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Shirika la Chakula Duniani (FAO) ni moja kati ya wafadhili wa miradi hii ya kilimo kwenye nchi yetu na wanao mkataba maalum kwa wataalam wao wanaostaafu kuendelea kufanya kazi kati ya umri wa miaka 60 mpaka 70 na labda ni-declare interest tu kwamba mimi ni mstaafu, lakini nauliza swali hili kwa maslahi mapana ya nchi.
Je, kwa nini Serikali mpaka sasa haijasaini mkataba wa utumiaji wa wataalam (national experts) na Shirika la FAO wakati kuna nchi zaidi ya 67 wanachama wa FAO wameshasaini?
WAZIRI WA MADINI (K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI UMMA NA UTAWALA BORA):
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa kwa niaba ya Serikali nimpongeze kwa namna ambavyo amekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha utumishi wetu wa umma, lakini zaidi kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia maslahi na mustakabali wa wastaafu wetu. Nipende tu kumwambia Mheshimiwa Mbunge kwa takwimu za mwaka 1995 mwezi Machi, ndipo ambapo Tanzania ilikuwa bado haijaweza kusaini mkataba huu.
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwaka 1998 Tanzania ilikuwa imeshasaini na kwa sasa hivi tunayo Technical Cooperation among Developing Countries pamoja na Countries in Transition na ninaamini Serikali itaweza kunufaika, lakini pia na wataalam wetu katika sekta mbalimbali, lakini nimshukuru kwa kuleta hoja hii na tutaendelea pia, kufuatilia na mikataba mingine ya kimataifa ili watu wetu waweze kunufaika.
MHE. PROSPER J. MBENA: Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali kwa msaada huo katika sehemu hizo mbili zilizotajwa naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Je, ni lini Serikali itazisaidia Vituo vya Afya vya Mtamba pamoja na Kisaki ambavyo mchakato wake Serikali ulishaanza kushughulikia?

Je, ni lini Serikali itapeleka au itasaidia Hospitali Kuu ya Mkoa wa Morogoro mashine ya CT-Scan ili kuokoa maisha ya watu ambao yanapotea bure kwa ajili ya kukosa huduma ya mashine hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimetaja katika jibu la msingi Wilaya ya Morogoro Vijijini ambayo Mheshimiwa anatoka ni miongoni mwa Wilaya ambazo zimepata nafasi ya kujengewa Hospitali za Wilaya na tumeanza kupeleka shilingi bilioni 1.5 lakini ili ikamilike tunahitaji tunahitaji jumla ya shilingi bnilioni 7.5. Lakini mwenyewe anakiri kwamba tayari tumeanza kujenga Kituo cha Afya pale Duthumi, najua kabisa kiu ya Mheshimiwa Mbunge kwamba na maeneo mengine Vituo vya Afya vijengwe naomba nimuakikishie kwamba ni azima ya Serikali kwa kadri bajeti inavyoruhusu tumeanza na vituo 350 lakini azma kuhakikisha kwamba katika kata zetu zote kwa kadri bajeti itakavyo kuwa inaruhusu kama ambavyo tumeahidi kwenye ilani ya CCM tunaenda kutekeleza.

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa mwongozo wetu wa Wizara ya Afya huduma za CT-Scan zinapatikana kuanzia Hospitali za ngazi ya Rufaa za Kanda. Lakini baada ya kuwa tunafanya mapitio katika hii sera mpya tunajaribu kuangalia huduma sasa hivi katika nchi yetu zimekuwa sana na tumeona kwamba baadhi ya hospitali za mikoa ambazo ziko kimkakati. Lakini vilevile huduma hizi za CT-Scan zinahitaji utaalamu wa hali ya juu kuweza kuzitumia ambazo zingine huduma hizi hazipatikani katika Hospitali za Mikoa, Hospitali Wilaya na kushuka chini.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mkakati wetu sisi kama Serikali nikujaribu ku-identity mikoa ile ambayo ni ya kimkakati ikiwa ni pamoja na Morogoro kwa sababu kuna aya inapita pale ili huduma hizi ziweze kupatikana kwa lengo kuhakikisha kwamba tunazuia ajali baadhi ya Mikoa lakini hatutaweza kuzishusha huduma chini ya ngazi ya hospitali ya rufaa Mikoa kwa sasa.
MHE. PROSPER J. MBENA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri sana ya swali hili; na kwa kweli ni majibu sahihi. Napenda tu niulize maswali madogo ya nyongeza.

Swali la kwanza, yapo maeneo ambayo hayakutajwa hapa ambayo ni Dutumi Bwakila Chini, wana dhahabu na ruby; Konde wana dhahabu na gemstone, hiyo spinels; pia Singisa wana ruby ya kutosha. Sasa swali langu la msingi kwa maana ya yale yaliyojibiwa yajumuishwe na maeneo haya mapya ili sasa tuweze kupata uhalisi wa sehemu ambazo madini haya yanapatikana. Hili ni ombi tu.

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili. Je, Serikali ina utaratibu gani kuwasaidia hawa wachimbaji wadogo kifedha pamoja na vifaa kwa ajili ya kuboresha uchimbaji wao?

Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kuna maeneo ambayo hayajatajwa. Maeneo ambayo tumeyataja ni yale maeneo ambayo tumeona ni potential kwa uchimbaji. Vile vile nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba maeneo yote ya Morogoro tunayafahamu na tumetengeneza ile Quarter Degree Sheet ambayo inaonesha ramani zote za uwepo wa madini.

Mheshimiwa Spika, vile vile uwepo wa madini ni kitu kimoja, lakini madini yanayolipa automatically tu utaona kwamba wachimbaji wanaelekea katika maeneo yale. Ni kama vile inzi anavyofuata kidonda; wachimbaji wakishaona kuna potential maeneo ya uchimbaji, wenyewe unaona wameshasogea pale.

Mheshimiwa Spika, kwa uchambaji ule mkubwa inabidi utafiti wa kina ufanyike na pawe na ile hali ya kuonesha kwamba kuna madini ya kutosha na hata uwekezaji mkubwa unaweza ukawekezwa pale. Kwa wachimbaji wadogo wana uwezo wa kusogea na tuko tayari kuwasaidia kuendelea kuwapa taarifa za kijiolojia.

Mheshimiwa Spika, napenda tu kusema kuhusiana na kuwawezesha wachimbaji wadogo; Wizara imekuwa bado inasaidia kuwawezesha wachimbaji wadogo. Hapo nyumba tulikuwa katika huo mradi wa SMMRP, tulikuwa tunatoa ruzuku kwa wachimbaji wadogo, lakini ruzuku hiyo ilikuwa inatumika vibaya.

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa hivi tumesimamisha utoaji wa ruzuku hiyo, sasa tunaangalia namna bora ya kuwawezesha wachimbaji wadogo ambapo tukiwapa fedha zile, basi waweze kununua vifaa, wafanye tafiti mbalimbali na kuwawezesha kuchimba. hapo awali, walikuwa wanapewa hata wasiyokuwa na sifa, na kweli mpaka sasa tunafuatilia na kuhakikisha kwamba tunakwenda kuwasaidia wachimbaji wadogo tunapokuja na modality nzuri.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.