Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Maftaha Abdallah Nachuma (25 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia katika Mpango huu wa Maendeleo wa mwaka mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kuzungumza lolote, naomba kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kuwa Mbunge …
MWENYEKITI: Nataka tu Jimbo Mheshimiwa.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mtwara Mjini.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru kwa kunibariki kuwa Mbunge wao. Pili, naomba niwashukuru wananchi wangu wa Mtwara Mjini kwa kuniamini na nawaambia waendelee kuniamini nitawawakilisha vyema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kuchangia hoja, naomba niliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Mtwara Mjini kumetokea maafa, mvua imenyesha, kuna mafuriko na jana nilitoa taarifa hii kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba Waziri husika ashughulikie suala hili, kuna nyumba zaidi ya 500 zimeharibika. Nachukua fursa hii pia kuwapa pole wananchi wote walioathirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kuchangia kama ifuatavyo. Mpango huu umezungumzia suala zima la viwanda na Mheshimiwa Waziri wakati anatoa hoja alisema kuna utaratibu wa kuhakikisha inatawanya viwanda kila eneo la nchi. Pia alisema kuna maeneo ni special investment zone kwa maana kwamba ni ukanda maalumu wa uwekezaji na akataja Mtwara, Bagamoyo na maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Mtwara Mjini kuna Kiwanda cha Dangote. Kiwanda hiki kina wafanyakazi wengi lakini kwa masikitiko makubwa kabisa mle ndani kuna kampuni tatu za Wahindi na Wachina, kuna AYOK, UCC na CYNOMA. Naomba nimpe taarifa Waziri husika kwamba kampuni hizi zilizopo mle ndani zinanyanyasa wafanyakazi. Sijui ni utaratibu gani huu wa kwamba tunajenga viwanda badala ya kuwanufaisha Watanzania vinawanyanyasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine katika Kiwanda hiki cha Dangote, lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba inaondoa umaskini kwa wananchi wa maeneo husika. Kwa kiasi kikubwa kiwanda hiki kinaajiri watu lakini wenyeji wa Mtwara wengi hawapati nafasi. Mimi kama Mbunge nimejaribu kutembelea kiwanda hiki zaidi ya mara mbili kwenda kuzungumza na Maafisa Masuuli lakini kuna manyanyaso makubwa ya wafanyakazi mle ndani. Mishahara inatoka kiasi kikubwa lakini wale vibarua na wafanyakazi wanapewa pesa ndogo sana. Nimuombe Waziri husika atembelee Kiwanda cha Dangote - Mtwara kuona manyanyaso yanayofanywa na Wahindi pamoja na Wachina lakini manyanyaso yanayofanywa kwa wananchi wa Mtwara Mjini, Mtwara Vijijini na maeneo ya Kusini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia suala zima la bandari. Katika hoja hii limeelezwa suala zima la kuboresha bandari, lakini Bandari ya Mtwara imetajwa tu kwamba kuna mpango na mkakati wa kujenga magati. Mimi kama Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini nimetembelea Bandari ile ya Mtwara. Pale kuna gati moja limechukuliwa na watu wa gesi wanaitwa BG, lakini ile gati kwa muda mrefu zile meli za BG hazipo. Sasa hivi tumebakiwa na gati mbili tu ambapo tunataka tusafirishe korosho lakini ile gati iko empty na wanasema kwamba pale meli nyingine yoyote hairuhusiwi kutia nanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba katika mpango huu wa kuendeleza bandari wahakikishe Bandari ya Mtwara ambayo ina kina kirefu Afrika Mashariki na Kati, wala haihitaji kutumia gharama kubwa kama ilivyo ujenzi wa Bandari mpya ya Bagamoyo, Wizara husika irekebishe Bandari ya Mtwara na ijenge yale magati manne. Sambamba na hilo ihakikishe inamwezesha yule mwekezaji ambaye ameomba eneo, Mheshimiwa Aliko Dangote kuweza kumaliza mchakato wake ili tuweze kuongeza magati kwa ajili ya Bandari ile ya Mtwara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nazungumzie suala zima la miundombinu. Kule Mtwara tuna barabara inaitwa barabara ya Ulinzi, ni miaka mingi barabara hii haizungumziwi kabisa. Naomba Wizara husika ihakishe inashughulikia barabara ya kutoka Mtwara Mjini – Kitaya - Newala na maeneo mengine kwani ni barabara ya Ulinzi ambapo mwaka 1972, mashujaa wetu au wanajeshi wetu walikuwa wanaitumia barabara ile kulinda mipaka ya Tanzania Ukanda huu wa Kusini lakini imesahaulika kabisa. Kwa hiyo, naomba Mpango huu uhakikishe barabara hii ya Ulinzi inajengwa kwa kiwango cha lami, inapita Kitaya - Mahulunga na maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine naomba barabara hii ambayo ni kitovu kikubwa cha uchumi wa korosho inayoanzia Mtwara Mjini kuelekea Majimbo yote ya Mkoa wa Mtwara kwa maana ya Mtwara Vijijini, Nanyamba, Newala, Tandahimba hadi Masasi iwekwe kwenye Mpango ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami. Mimi kabla sijazaliwa naisikia barabara hii inazungumziwa kila siku. Mheshimiwa Nandonde alishawahi kuzungumza kwa miaka mingi sana katika Bunge hili lakini mpaka leo bado barabara hii inasahaulika, kwa hiyo, tunaomba iwekwe kwenye Mpango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala zima la utalii. Pale Mtwara Mikindani kuna magofu ya kihistoria lakini Serikali imeyaacha na haina mkakati wowote wa kuhakikisha kwamba tunatangaza vivutio vile ili viweze kutoa ajira na kuingiza kipato kwa Serikali hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Maeneo yale ya Mikindani kuna vivutio kuliko hata maeneo mengine ya Tanzania, naomba Serikali ianze kuyatangaza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa kusema mambo machache. Ilizungumzwa hapa kwamba amani na utulivu ndiyo chachu ya maendeleo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ndiyo chachu itakayowavutia wawekezaji kuja kuwekeza Tanzania. Kila mmoja ni shahidi, hata Waheshimiwa wazee wetu wa Chama cha Mapinduzi wanafahamu kabisa tarehe 25 Oktoba, 2015 kule Zanzibar chama kilichoshinda ni Chama cha Wananchi - CUF lakini Tume ya Uchaguzi na yule aliyeshindwa hawakutaka kumtangaza aliyeshinda. Kwa hiyo, niombe tu mshindi wa Zanzibar atangazwe ili nchi yetu iendelee kuwa na amani na utulivu na ili wawekezaji waweze kuja kuwekeza Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema kwamba usafirishaji wa reli ni muhimu sana. Kama ilivyokuwa kwenye reli ya kati na kule Kusini pia kuna reli, lakini kwenye Mpango huu sijaona sehemu yoyote iliyoandikwa kwamba reli hii ya kutoka Mtwara – Liganga - Mchuchuma itajengwa lini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la usafiri wa ndege, niungane na wenzangu kusema kwamba ATC ina ndege moja tu tena ni ya kukodi, tuna ubia na wale watu wa South Africa. Naomba ndege ziongezwe kwa sababu ni za Serikali lakini pili gharama yake ni nafuu sana. Nilienda kuulizia tiketi ya ndege kutoka Dar es Salaam kwenda Mtwara...
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru sana. (Makofi)
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. ABDALLAH N. MAFTAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia mpango huu kwa niaba ya wananchi wa Mtwara Mjini. Nianze tu moja kwa moja kuangazia huu Mpango kwa sababu Mpango kwa kiasi kikubwa unaonesha namna gani nchi yetu sasa hivi inaingia katika uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la msingi sana ambalo sijaliona katika Mpango huu, ni usimamizi wa hivyo viwanda. Kwa masikitiko makubwa kabisa, hivi sasa tuna baadhi ya viwanda ambavyo vimejengwa katika nchi yetu na wawekezaji mbalimbali kutoka nje ya nchi. Kwa mfano, ukija pale Mtwara Vijijini kuna Kiwanda kinaitwa Kiwanda cha Dangote, lakini ukiangalia katika kiwanda hiki unaweza kuona kuna changamoto nyingi sana ambazo Serikali imeshindwa kuzisimamia na kuzitatua, lakini tunaleta Mpango ambao unasema kwamba Tanzania itaondoa umaskini kupitia Sekta hii ya Viwanda wakati hivyo viwanda vichache tunashindwa kuvisimamia na kuleta tija kwa wananchi wetu ili kuondoa umaskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa sana, niliweza kuzungumza suala hili katika mwelekeo wa Mpango kwamba Kiwanda cha Dangote kilichopo Mtwara kimeajiri Watanzania ambao wanatoka sehemu mbalimbali ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini kuna Makampuni mle matatu ambayo ni ya kigeni yanayosimamia uendeshaji. Ipo Kampuni ya Kichina, kuna Kampuni kutoka India na Kampuni nyingine kutoka kule Nigeria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi kampuni zilizopo katika Kiwanda hiki cha Dangote zinanyanyasa kwa kiasi kikubwa sana wananchi wa Tanzania. Sasa swali langu katika Mpango huu ni kwamba, kama tumetengeneza utaratibu wa kuhakikisha kwamba viwanda vinatatua changamoto za umaskini wakati tunashindwa kusimamia viwanda hivi; na pale nilizungumza katika mwelekeo wa Mpango huu kwamba malipo ya mishahara ya wafanyakazi wa Tanzania ambao ni wazalendo ni midogo na hata hiyo midogo yenyewe wanapunjwa. Badala ya kulipwa Sh. 12,000/= kwa siku ambazo zinaandikwa kwenye makaratasi, wanapewa Sh. 7,000/=.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nilizungumza katika mwelekeo wa Mpango hapa Bungeni lakini mpaka leo hii tunapotaka kupitisha huu Mpango, bado marekebisho hayajafanyika katika Kiwanda cha Dangote. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara aunde Tume Maalum iweze kutembelea Kiwanda hiki cha Dangote kwa sababu kinanyanyasa Watanzania walioajiriwa pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumze suala zima la bandari. Kwa mujibu wa mwelekeo wa Mpango huu, umesema tutaboresha uchumi wa nchi kwa kujenga bandari mbalimbali na Mheshimiwa Profesa Maji Marefu kazungumza hapa kwamba, bandari siku zote tunaangalia Bandari ya Dar es Salaam na sasa hivi tunaenda kujenga Bandari mpya ya Bagamoyo wakati Mwenyezi Mungu ametubariki, Mtwara tuna bandari ambayo ina kina kirefu Afrika Mashariki na Kati, Bandari ambayo Mwenyezi Mungu ametujaalia wala haihitaji kuchimba, lakini tunaenda kujenga bandari mpya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nashangaa, wakati Serikali hii ina mpango wa kuhakikisha kwamba inabana matumizi, lakini tunaenda kujenga bandari mpya ambayo itatumia Dola za Marekani bilioni karibu 22.5, wakati Bandari ya Mtwara ambayo Mwenyezi Mungu ametubariki ilikuwa ni kuboresha tu kidogo na iweze kutumika kuinua uchumi wa nchi hii. Sasa mipango hii, ni kweli lengo letu ni kuhakikisha kwamba tunaondoka hapa tulipo ili kuwa na maendeleo ya nchi hii wakati tunatumia pesa bila mpango ambao kimsingi unastahiki?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu, kama kweli tunahitaji kuboresha uchumi wa nchi hii, tuboreshe Bandari za Mtwara, tuboreshe Mtwara Corridor, tuboreshe Tanga na maeneo mengine. Tusifikirie tu Dar es Salaam, Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala zima la elimu. Sasa hivi tunasema kwamba Serikali imeweka sera ya kutoa elimu bure, lakini kwa masikitiko makubwa kabisa, ukitembelea mashuleni huko, hii sera ya elimu bure imekuja kudumaza usimamizi wa elimu. Tunaangalia fedha za uendeshaji wa hizi shule, kwa mfano, Shule za Msingi; nilitembelea baadhi ya shule kama tano, sita pale Mtwara Mjini katika Jimbo langu, ukipitia fedha zilizoingia shuleni kwa miezi hii mitatu, ni jambo la kusikitisha sana. Kwa mwezi Sh. 27,000/= pesa za maendeleo halafu tunasema kwamba tunahitaji kuinua elimu kwa Sera ya Elimu Bure. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba kwa namna ya kipekee kabisa, Serikali iweke utaratibu wa kupeleka fedha mashuleni kama kweli tunahitaji kusimamia elimu na elimu ndiyo chachu ya maendeleo katika dira ya nchi yoyote duniani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kwa kifupi kilimo na uvuvi. Mpango huu umeelekeza kwamba tutainua kilimo kwa kuboresha mazao ya biashara na mazao ya chakula kwa wakulima, lakini nikizungumzia kwa mfano suala zima la zao la korosho Tanzania, tuna Bodi ya Korosho Tanzania, Bodi ambayo inasimamia Sekta hii ya Korosho Tanzania, lakini kwa masikitiko makubwa kabisa, hawana mkakati hata mmoja kuhakikisha kwamba huyu mkulima anayelima zao la korosho anapewa pesa ambazo zinastahiki pale anapouza mazao yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha ajabu kabisa, ukiangalia katika uuzaji wa mazao haya, zao la korosho kwa mfano, mkulima amewekewa tozo nyingi sana, mpaka tozo ya gunia ambalo Mhindi anakuja kusafirishia korosho kutoka Tanzania kwenda India anabebeshwa mkulima, halafu tunasema tunahitaji kuinua kilimo wakati mpaka leo tunavyozungumza bado bei ya korosho iko chini sana. Korosho inauzwa Sh. 1,800/= hadi Sh. 2,000/=. Ni jambo la kusikitisha kwamba Serikali inashindwa kumtafutia mkulima masoko ya zao la korosho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, korosho ni zao ambalo mwaka 2015 na mwaka 2014 limeingiza pesa nyingi Serikalini. Ukiondoa tumbaku, zao linalofuata ni korosho, lakini tunashindwa kuweka mikakati ya uhakikisha kwamba tunainua zao hili na mkulima anaweza kunufaika na kilimo hiki cha korosho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, Mungu ametubariki Tanzania tuna Bahari ya Hindi kuanzia kule Mtwara mpaka Tanga, lakini cha ajabu ni kwamba Serikali katika Mpango huu sijaona kwamba imeweka utaratibu kuona inaboresha namna gani Wavuvi wetu wa Tanzania ili waweze kununuliwa vifaa, kupewa vifaa vya kisasa vya uvuvi ili waweze kuwa na uvuvi wenye tija na mwisho wa siku waweze kuondokana na umaskini. Leo tunakuja tunasema tunataka kuboresha kilimo na uvuvi wakati mipango yetu haioneshi namna gani tunaweza kuondoa umaskini kupitia Sekta hii ya Uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wazungu wanasema kwamba Tanzania Mungu ametubariki na hasa upande huu wa Kusini, tunasema ni vision sea, ni bahari ambayo ina samaki kedekede huko chini lakini Serikali haina mpango wowote wa kuinua Sekta hii ya Uvuvi ili Watanzania tuweze kuondokana na umaskini. Tunapiga danadana tu! Ooh, tutajenga Chuo cha Mikindani, wakati hatuna utaratibu, hatujaweka mkakati wowote wa kuhakikisha kwamba tunanunua maboti na vifaa vya uvuvi ili tuweze kuwasaidia wavuvi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kidogo suala zima la maendeleo. Maendeleo yoyote yanategemea amani na utulivu wa nchi, lakini kwa masikitiko makubwa kabisa, kwa mfano ukija Mtwara Mjini tangu mwaka 2013, 2014 mpaka leo hii 2015, Serikali iliweza kuchukua ardhi ya wananchi, maeneo ya Tanga na maeneo ya Mji mwema. Nimezungumza hili jana hapa kwenye briefing na hii ni mara yangu ya tatu nazungumza; Mtwara kuna mgogoro mkubwa sana wa ardhi. Wananchi wamenyang‟anywa ardhi zao na Serikali wakasema kwamba wataenda kulipa fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu mwaka 2013 mpaka leo hii, hakuna senti yoyote iliyotolewa na Serikali. Cha ajabu Serikali ukiiuliza, inasema tutafanya, tutafanya. Wananchi hawana sehemu za kulima, halafu tunakuja na Mpango wa kusema kwamba eti tunataka kuondoa umaskini Tanzania, wakati wananchi wananyang‟anywa ardhi na hawapewi fidia zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu, kwa sababu Waziri wa Ardhi, Mheshimiwa Lukuvi yupo hapa, atembelee Mtwara, akaangalie changamoto za ardhi ambazo zinaelekea sasa kuleta mpasuko wa Kitaifa na mtengamano wa Kitaifa kwa sababu wananchi wanasema tutafika wakati tumechoka na mwelekeo huu utakuwa hauna maana, Mheshimiwa Mwenyekiti, suala zima la amani na utulivu ni jambo la msingi sana. Kama tunahitaji kweli kuhakikisha tunaleta tija katika Taifa hili, umaskini unaondoka, ni lazima tuvutie uwekezaji. Huwezi kuvutia uwekezaji kama hakuna amani na utulivu. Issue ya Zanzibar nayo ni ya msingi sana, siyo issue ya kubeza. Tunahitaji kukaa pamoja ili kujadiliana namna gani tunaweza kuleta amani na utulivu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma Mikataba ya Tanzania, kwa mfano Mikataba ya Uwekezaji, mingi haina tija katika Taifa hili. Kwa mfano, kuna Mkataba wa Mlimani City, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kiliingia mkataba na Mwekezaji kutoka Botswana, Mkataba ambao kimsingi Serikali ya Tanzania inakusanya kwa mwaka asilimia 10% tu ya mapato yanayopatikana pale, wakati kuna mamilioni mengi ya pesa yanakwenda kwa Mwekezaji. Kwa hiyo, tunahitaji sasa kama Taifa tuingie kwenye Mikataba na huu Mpango uoneshe ni namna gani Bunge linaweza kupitisha Mikataba yote ya Tanzania ili tuweze kuwa na uwekezaji wenye tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze angalau kwa kifupi suala zima la afya. Afya ni jambo la msingi sana. Hatuwezi kusema kwamba tunahitaji maendeleo kama Watanzania wengi wanakufa kwa sababu ya afya. Ukija Mikoa ya Kusini, nilizungumza hili wakati wa kikao cha pili kwamba Kanda zote Tanzania tayari zimekamilika kuwa na Hospitali za Rufaa. Kanda ya Kusini mpaka hivi sasa, ujenzi wa Hospitali hii, jengo moja tu, unasuasua ambalo Mheshimiwa Waziri hapa alizungumza kwenye Bunge lako Tukufu kwamba iko katika hatua za umaliziaji ujenzi wa OPD, lakini mpaka hivi sasa ujenzi huo unasuasua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Hospitali ya Mkoa ya Mtwara hakuna X-Ray, Hospitali ya Wilaya hakuna X-Ray, halafu leo tunasema tunataka kuondoa umaskini, tunapitisha Mpango huu. Naomba kwa namna ya kipekee kabisa, kama kweli tunahitaji kuondoa umaskini Tanzania, ni lazima tujali afya za Watanzania, ni lazima tuboreshe afya za Watanzania, tuhakikishe kwamba vifaa tiba vinapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo, naomba nikushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia hoja iliyopo Mezani leo hii ya Viwanda, Uwekezaji na Biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaanza kusema lolote, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunibariki kuwa na afya njema. Kwa kuwa katika kuchangia Wizara hizi, hii ni mara yangu ya kwanza nitumie fursa hii pia kuwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Mtwara Mjini na niwaeleze kwamba naendelea kupambana vizuri na nitawawakilisha vyema kwa kipindi chote cha miaka mitano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hotuba hii ambayo imetolewa na Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara, nianze tu kwa kusema kwamba mkakati wa Wizara hii wa kuhakikisha kwamba nchi ya Tanzania inakuwa ni nchi yenye uchumi wa viwanda kupitia bajeti yake hii, kimkakati ni jambo zuri sana. Wenzetu nchi nyingi duniani, ukisoma historia, nchi za Ulaya ziliweza kuendelea kwa kiasi kikubwa kupitia sekta hii ya viwanda. Tangu karne ya 15 kule nchi zote za Ulaya ziliweza kufanya mapinduzi ya viwanda na kuweza kuondoa umaskini na hata kuitawala dunia kwa kutegemea sekta hii ya viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu ya Tanzania, baada ya uhuru, Mwalimu Julis K. Nyerere alijitahidi kwa kiasi kikubwa sana, aliweza kuanzisha viwanda vingi sana. Wakati huo ikumbukwe kwamba tulikuwa katika mfumo wa ujamaa na kujitegemea, uchumi wetu ulitegemea kwa kiasi kikubwa sekta hii ya viwanda, lakini kwa bahati mbaya kabisa, Serikali ya Chama cha Mapinduzi mwaka 1995-1996 iliweza kuingia katika mfumo wa uwekezaji, mfumo ambao haukufuata kanuni, sheria na taratibu za kiuwekezaji na hatimaye zaidi ya viwanda 446 viliweza kuuawa kwa kupewa wawekezaji ambao hawana sifa ya kuwekeza Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumze tu angalau kwa kifupi sababu zilizopelekea kuuawa kwa viwanda ikiwa ni kwamba tuliwapa wawekezaji ambao they were not credible buyers katika nchi yetu ya Tanzania, walikuwa hawana uwezo na ujuzi. Jambo lingine lilikuwa ni mazingira yenyewe ambayo tuliyatengeneza hayakuwa rafiki kwa kuweza kuuza viwanda vyetu. Mwisho wa siku leo hii tunasema tunahitaji kufufua uchumi wa viwanda, wakati hatuna utaratibu, hatuna mkakati wowote ili Taifa kama Taifa liweze kuwekeza katika sekta hii ya viwanda kwa kuwapata wawekezaji ambao tunasema ni credible buyers. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wa Viwanda, Uwekezaji na Biashara amewasilisha bajeti yake hapa lakini nimepitia hii bajeti takribani kitabu chote hiki sijaona hata sehemu moja ambapo ameeleza ni utaratibu gani ambao utatumika katika kuhakikisha kwamba uwekezaji wa ndani ya nchi unakuwa ni uwekezaji wenye tija. Ameeleza tu kwamba tutahakikisha kwamba wawekezaji wa ndani na viwanda vidogo wanapewa kipaumbele lakini sijaona utaratibu wowote ambao wameuweka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, nizungumzie suala zima hili la mashirika ya umma na hasa mashirika ya hifadhi za jamii. Kuna mashirika ambayo yana mkakati wa kuwekeza ndani ya nchi lakini katika uwekezaji wao wanatumia mamilioni ya fedha kinyume na utaratibu. Wizara kama Wizara sijaona mkakati wowote ambao wameueleza ni namna gani watadhibiti mashirika haya kutumia fedha za umma hovyo hovyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, Shirika la GEPF wakati tunapitia mpango wao ule wa uwekezaji katika Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma unaweza ukashangaa kuona kwamba wameweka mkakati wamenunua viwanja kwa mfano kule Mtwara wamenunua square meter moja kwa shilingi laki moja na elfu arobaini na nne na something, ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kiwanja hiki sijui wamenunua mbinguni au wamenunua wapi, ni uwekezaji ambao hauna tija. Nazungumzia suala hili la uwekezaji kwamba lazima kama Wizara wahakikishe kwamba wanaweka mechanism iliyokuwa bora kabisa ili waweze kuhimiza uwekezaji wenye tija na Taifa letu liweze kuwa na manufaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia pia kuna kiwanja kimenunuliwa Mwanza ambapo GEPF wanaenda kujenga shopping mall lakini ukiangalia square meter moja wamenunua shilingi laki moja na elfu kumi na tano kana kwamba hicho kiwanja kina dhahabu. Hapa nazungumzia suala zima la uwekezaji wenye tija kwa sababu Wizara hii kazi yake ni kuhakikisha kwamba inachochea Watanzania na mashirika ya ndani ya nchi yaweze kuwekeza uwekezaji wenye tija na siyo uwekezaji wa kifisadi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kidogo suala zima la viwanda. Waziri hapa kazungumzia kwa kiasi kikubwa sana na alikuwa anaruka sana wakati anazungumzia kwamba sasa hivi Taifa letu litajenga viwanda vya kutosha na nchi yetu itaondokana na umaskini kupitia sekta hii ya viwanda. Nizungumza hapa wakati ule tunachangia Mpango wa Serikali kwamba viwanda hivi lazima viwekewe utaratibu maalum wa kuhakikisha kwamba Watanzania walioajiriwa wanafanya kazi kwa tija ili waweze kuondokana na umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiangalia Kiwanda cha Dangote, nimekuwa nikilia sana kwenye Bunge lako hili, ambacho kipo Mtwara Mjini pale, kile kiwanda kimewekezwa na wawekezaji kutoka nje, mwekezaji kutoka Nigeria anaitwa Aliko Dangote, lakini mashirika yaliyopo mle ndani ambayo yanaajiri Watanzania ambao ndio leo hii tunawazungumzia hapa kwamba waondokane na umaskini kile kiwanda kinanyanyasa kwa kiasi kikubwa Watanzania waliopo mle ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia hata namna ya upataji wa kazi, wananchi wa Mikoa ya Kusini wa Mtwara na Lindi ili wapate kazi mle ndani lazima watoe rushwa kuanzia shilingi laki tatu na elfu hamsini. Nilizungumza hapa na nilimwomba Mheshimiwa Waziri ahakikishe kwamba anaunda Tume Maalum ije Mtwara ifanye ukaguzi wa haya ninayozungumza na mwisho wa siku waweze kuwachukulia hatua wale watu, lakini kama Waziri anarukaruka na kusema kwamba tunawekeza katika viwanda wakati hivyo viwanda vichache vilivyopo, watu wananyanyaswa, wanapewa mshahara mdogo, wanapewa shilingi elfu sita kwa siku badala ya shilingi elfu kumi na mbili halafu tunasema kwamba tunataka tuondoe umaskini kupitia viwanda! Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri ahakikishe kwamba anatembelea kiwanda hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la ajabu kabisa kwa wananchi wa Mikoa ya Kusini, hiki Kiwanda cha Dangote kimeanza kuzalisha cement, cement inazalishwa kwa wingi sana. Cha ajabu ni kwamba, bei ya cement Mtwara na Lindi ambako ndiko cement yenyewe inatoka ni shilingi elfu kumi na tatu na mia tano ukija Dar es Salaam, cement ile ile inayotoka Mtwara mpaka Dar es Salaam kilomita zaidi ya mia tano inauzwa shilingi elfu kumi na mbili, huku sio kuwadharau wananchi wa Kusini?
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tunazungumza sana kwamba, tumenyanyasika sana Wanakusini lakini tukizungumza mnatupiga mabomu, mnatuletea Wanajeshi. Haiwezekani na haikubaliki hata kidogo na wala haingii akilini kwa watu wenye akili, kiwanda kiko Mtwara, halafu kinazalisha cement, pale pale Mtwara shilingi elfu kumi na tatu na mia tano, ikisafirishwa kwenda Dar es Salaam na maeneo mengine shilingi elfu kumi na mbili na mia tano, huku ni kuwadharau wananchi wa Kusini na wananchi wa Kusini tunasema tutachoka hivi sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumze kidogo suala zima la Viwanda vya Korosho. Viwanda vya Korosho kwa mfano pale Mtwara, kulikuwa na kiwanda kidogo kinaitwa Kiwanda cha OLAM, lakini kwa usimamizi mbovu wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi kile kiwanda kimeachwa kinahamishwa badala ya kutengeneza mazingira rafiki, hiki kiwanda niseme tu kwamba kilikuwa kinaajri takribani akinamama 6,000 ambao walikuwa wanabangua korosho, lakini hakikutengenezewa mazingira rafiki, kikafanyiwa hujuma, mwisho wa siku yule mwekezaji amekihamisha hiki kiwanda na kukipeleka Mozambique. Halafu tunasema kwamba tunataka tuweke mazingira rafiki!
Mheshimiwa Naibu Spika, kila mmoja anafahamu kwamba kama kweli Serikali ingekuwa makini ikajikita katika kuwekeza na kufungua viwanda vidogo vidogo vya korosho, tunaamini kabisa umaskini ungeweza kuondoka katika Mikoa yetu hii ya Kusini na Tanzania kiujumla. Tunasema tu kwenye makaratasi, mikakati yetu haioneshi kwamba kweli tuna nia ya dhati ya kuhakikisha tunajenga viwanda hivi ili tuweze kuwakomboa wananchi wetu ambao ni maskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana, kama kweli tunahitaji kufufua viwanda ili viweze kuleta tija kwa Watanzania, tujenge Viwanda vya Korosho. Korosho yenyewe, kama unavyojua kwamba, kila kitu kinachotoka kwenye korosho ni thamani. Maganda yenyewe ni thamani, mafuta ni thamani, korosho zenyewe ni thamani! Tuhakikishe kwamba tunayenga viwanda vya korosho maeneo ya Kusini na Tanzania kiujumla ili tuweze kuondokana na umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimalizie kwa kusema kwa mfano tuna madini ya Tanzanite, nilikuwa nafanya utafiti mdogo tu, nilikuwa naingia kwenye maduka kuangalia ni madini gani sasa hivi yana thamani. Ukiingia dukani ukakuta Tanzanite unaona ni miongoni mwa madini ambayo yana thamani kuliko madini mengine sasa hivi. Nashauri tujenge viwanda vya kufanya processing.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru sana kwa
kunipa nafasi hii niweze kuchangia taarifa hizi mbili za Kamati ya Nishati na Kamati ya
Miundombinu. Lakini kabla ya yote naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye
ameendelea kunipa afya njema na leo hii nimesimama hapa katika upande huu nikiwa peke
yangu kabisa na afya njema kuwawakilisha wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini ambao
wamenituma nije nieleze haya ambayo nakusudia kuyaeleza hivi sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze Wenyeviti wote wa Kamati zote mbili kwa
mawasilisho yao mazuri kabisa. Niungane na wenzangu kutoa vipengele kadhaa ambavyo
wameweza kuvionesha katika taarifa zao zote mbili.
Nianze na Wizara hii ama taarifa hii ya Miundombinu, moja kwa moja sehemu moja
wamezungumza kwamba, Serikali imeweka ama imeanza mkakati wa kupanua viwanja vya
ndege na mimi ni-declare interest ni Mjumbe wa Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma,
tuliweza kutembelea pale Dar es Salaam, Terminal III kuangalia upanuzi wa ule uwanja.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo ambalo naweza kulizungumza kwamba, tulipata
maelezo pale kwa yule mkandarasi kuna suala hili ambalo Mwenyekiti wa Kamati kaeleza
kwamba ucheleweshwaji wa kupewa pesa ili waweze kuendelea na ule ujenzi na ule ujenzi
uweze kukamilika kwa wakati. Hili suala kwa kweli, Serikali inatakiwa iliangalie kwa jicho la
kipekee kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka hivi sasa tunavyozungumza ni kwamba ujenzi wa
utanuzi ule unasuasua kwa sababu yule mkandarasi hajamaliziwa pesa zake. Kwa hiyo, tulikuwa
tunaomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hoja atueleze kwa nini anachelewesha
kumpa mkandarasi pesa ili utanuzi wa ile Terminal III uweze kwisha kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nizungumzie utanuzi huu uendane sambamba na
utanuzi wa viwanja vile tunaita viwanja vya kanda, kwa mfano Kanda ya Kusini kiwanja kikuu
kiko Mtwara Mjini na pale Mtwara Mjini tulizungumza wakati wa bajeti mwaka uliopita kwamba
ule uwanja hauna taa, ule uwanja unatakiwa utanuliwe! Ule uwanja safari moja tulishindwa
kutua pale tukalazimika kurudi Dar es Salaam kwa sababu ya ukosefu wa taa na taa zilikuwepo
huko miaka ya nyuma, lakini ziliweza kuondolewa hatujui zilipelekwa wapi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaomba sana Mheshimiwa Waziri
atakapohitimisha hoja hii atueleze ya kwamba mkakati upoje wa kutanua ule uwanja wa
Mtwara ikiwemo sambamba na kuweka taa za ule uwanja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine nizungumzie suala hili la utanuzi wa bandari,
wenzangu wamezungumza sana hapa kwamba kuna mkakati huu kwa mujibu wa Kamati wa
kutanua Bandari za Mtwara na Tanga. Lakini katika utanuzi wa bandari hizi, Mtwara haikutajwa
kinaga ubaga kama ilivyotajwa bandari zingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Waziri atakavyokuja
kuhitimisha hoja atueleze kwa sababu mwaka jana tulipitisha bajeti hapa kwamba kuna utanuzi
wa gati moja Mtwara Mjini ambapo Bandari ya Mtwara tunasema ni bandari yenye kina kirefu
kuliko bandari zote Afrika Mashariki na kati lakini bado nimezungumza na Meneja wa ile bandari
pale Mtwara anasema bado mkataba ule haujasainiwa; pesa zilitengwa sasa tunataka kujua
kwamba tatizo ni nini mpaka leo hawajasaini ule mkataba wa kutanua gati la Mtwara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nizungumze suala hili la meli ambalo limetajwa katika
Kamati kwamba inaipongeza Serikali kununua meli na wanataka kukarabati meli za Ziwa
Victoria lakini niombe kwamba isiwe tu katika Ziwa Victoria; tuna Bahari ya Hindi kwa mfano
Mtwara miaka ya nyuma tulikuwa tunasafiri kwa usafiri wa meli kwa kiasi kikubwa na niseme tu
kwamba sasa hivi pale kuna kiwanda ambacho kinazalisha cement kwa kiasi kikubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Dangote anasafirisha anasafirisha cement yake kwa
barabara na barabara inaharibika sana wakati Mtwara tuna bandari yenye kina kirefu
angeweza kununua meli mzigo wake ukawa unapitia katika Bandari ya Mtwara kuelekea Dar es Salaam na kwingineko duniani. Lakini tunaacha hatuboreshi, hatununui meli kwa ajili ya
usafirishaji wa mizigo kwa kupitia Bandari ya Mtwara - Dar es Salaam na kipindi kile tulikuwa
tunaafiri kutoka Mtwara mpaka Zanzibar kwa kupitia Bahari ya Hindi; sasa hivi haya mambo
hayapo kabisa na wala hayatajwi kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe sana kwamba Serikali ihakikishe ya kwamba
inavyoboresha ununuzi wa meli katika Ziwa Victoria wahakikishe na Bahari ya Hindi pia kuwe na
ununuzi wa hizi meli, lakini hata kule Ziwa Victoria, ukienda kule Ziwa Tanganyika pia kule
Kigoma wana shida sana ya usafiri wa meli kuelekea nchi zile za jirani. Nilikuwa naomba kuwe
na uunganishaji wa aina hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala hili la barabara ambalo Kamati imezungumza kwa
kiasi kikubwa kwamba kuna ucheleweshwaji wa pesa za ujenzi wa barabara na niseme tu hata
barabara ile ya kutoka Mtwara Mjini kwenda Mivata ambayo inaunganisha Wilaya zote za
Mtwara Mjini na Mheshimiwa Ghasia juzi aliuliza swali hapa ndani kwamba mkataba ule
unasubiri nini kusainiwa? Na ukimuuliza Meneja wa TANROADS anasema tayari umesainiwa lakini
Waziri anasema bado haujasainiwa kuna mambo wanayashughulikia; sasa sijui imekwama wapi
kusaini ujenzi ule wa kilometa 50 kutoka Mtwara Mjini mpaka Mivata; tunaomba tupate taarifa
kutoka kwa Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nije katika nishati na madini; hivi sasa ninavyozungumza
Mtwara na Lindi takribani miezi zaidi ya mitatu hivi sasa umeme unakatika sana; kila sekunde
umeme unakata. Tunashukuru sana Serikali kwamba imeweza kutanua wigo wa umeme kutoka
Mtwara Mjini kuelekea Lindi na Wilaya zake zote. Sasa tunashangaa kwamba utanuzi huu
hauendani sambamba na kuhakikisha kwamba nishati ile inapatikana na ufanisi. Mtwara Mjini,
Lindi na Wilaya zake zote umeme unakatika sana, tunaomba maelezo ya kina kutoka kwa
Mheshimiwa Waziri hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nizungumze kidogo ambalo Kamati pia imegusia suala la
madini Tanzanite One. Hili suala mimi nikiwa chuoni mwaka 2008 alitembelea Rais wa Afrika
Kusini wakati ule Mheshimiwa Thabo Mbeki alikuwa na article yake aliandika inaitwa “African
Renaissance” yaani kwamba Waafrika tunatakiwa tufufuke tena upya na alikuwa ametueleza
sana kwamba watanzania nyie sisi tuna madini haya ya Tanzanite ambayo yanapatikana
Tanzania tu; dunia nzima wanategemea Tanzania lakini wanufaikaji wa kwanza ni Wamarekani,
wanufaika namba mbili ni Wahindi, watatu ni Waafrika Kusini, wanne ni Wakenya na watano ni
sisi wenyewe Watanzania; yaani sisi wenyewe ni wa mwisho. Alitueleza haya Mheshimiwa Rais
Thabo Mbeki pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Nkurumah Hall. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tangu mwaka 2008 yule ametufungua masikio lakini
mpaka leo bado tuaambiwa kwamba kampuni ama taasisi hii ya madini ya Serikali (STAMICO)
inajiendesha kihasara; tunashangaa hasara hizi zinatoka wapi? Wakati madini tunayo yamejaa
kweli kweli na haya yapo Tanzania tu hata tungeamua wenyewe kuuza bei yoyote tunayohitaji.
Kwa nini tusiende kujifunza kwa wenzetu ambao wameendelea kupitia sekta hii ya madini kwa
mfano Botswana kanchi kidogo tu, tunashindwa nini na Wizara ipo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nieleze kwamba hii STAMICO kampuni ama taasisi hii ya
madini imeshindwa kufanya kazi zake, wakati tunahoji kwenye Kamati ya PIC juzi tu hapa
hawana hata mtaji, wanadaiwa kwelikweli wakati tuna madini yamejaa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana kama Serikali imeshindwa kuziwezesha hizi
taasisi zake ikiwemo STAMICO basi ni vyema ingeifuta kwamba kusiwe na hii taasisi kwasababu
tunaendelea kutumia resources nyingi za Kiserikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimalizie suala hili la kusambaza gesi ambalo Kamati
imezungumza pia kwamba kuna ucheleweshwaji wa kusambaza gesi ambayo tulipitisha
kwenye bajeti hapa katika Bunge lako hili Tukufu lakini nieleze na niombe sana kwamba
usambazaji huu uanzie kule inakotoka gesi Mtwara na Lindi ili iweze kutunufaisha sisi na
baadaye kunufaisha Watanzania wote kama ilivyokuwa kwenye korosho. Ahsante sana kwa
kunipa nafasi hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ABDALLAH N. MAFTAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii nami niweze kuchangia mjadala huu jioni hii ya leo inayohusu Wizara ya Elimu. Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kunipa afya njema na leo hii niweze kuchangia Wizara hii ipasavyo. Niseme tu kwamba ninayezungumza hapa pia ni Mwalimu, lakini bahati nzuri nimekuwa kwenye sekta hii ya elimu kama Mkuu wa Shuke kwa miaka mitano, kwa hiyo, nitakachozungumza hapa naomba kitiliwe maanani sana na Waheshimiwa Mawaziri wote wanaonisikiliza; Waziri wa TAMISEMI na Waziri wa Elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kauli ya Mwalimu Nyerere mwaka 1968 kwenye kitabu chake cha Education and Self Reliance, naomba nimnukuu, alisema hivi: “an antithesis of education is a kind of learning that enables an individual a learner to attain skills and knowledge and use that skill and knowledge to liberate himself and society in which he or she lives by participating in doing developmental actions.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni Mwalimu Nyerere mwaka 1968 alizungumza maneno haya, akiwa na maana ya kwamba, kinyume kabisa na mambo mengine yote, elimu ni jambo la msingi sana; na yule aliyeenda shule, lazima miaka yake yote anayosoma darasani aweze ku-acqure skills, ujuzi na knowledge ile lakini aweze kuitumia ile knowledge kujikomboa mwenyewe lakini kuikomboa jamii inayimzunguka kwa maana ya kwamba kulikomboa Taifa hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza haya kwa masikitiko makubwa sana. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikileta danadana katika suala hili la elimu kwa miaka mingi sana. Kila Waziri anayeingia anakuja na mitaala yake, anabadilisha system ya elimu; kila Waziri anayekuja anakuja kutunga Sera za Elimu. Mwisho wa siku Taifa kama Taifa hatuna sera, hatuna mtaala mmoja; kila siku tunayumba na hatuwezi kufikia malengo haya ambayo Mwalimu Nyerere aliyazungumza ya kwamba lengo la elimu ni kumfanya aliyesoma aweze kujikomboa mwenyewe na kuikomboa jamii yake inayomzunguka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawezi kuikomboa wala kujikomboa mwenyewe kwasababu elimu yenyewe anayoipata kwasababu inakuwa haina dira, haina mwelekeo kwa maana kwamba hapati elimu ile tunasema quality education, elimu bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nalizungumza hili kwasababu leo hii tunavyozungumza kuna Wizara mbili, zote zinashughulikia elimu. Ipo Wizara ya TAMISEMI na ipo Wizara ya Elimu. Cha ajabu kabisa, nimesikia hapa baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wakizungumza wakisema hiki usizungumze kwenye Wizara hii ya leo kwasababu hili lipo ndani ya TAMISEMI, wakati sisi Wabunge tunafahamu ya kuwa wakati Waziri Mkuu alivyowasilisha kwa kiasi kikubwa hatuweza kujadili mambo ya elimu. Kwa hiyo, leo ni siku yetu kama Wabunge tuweze kuwaeleza Waheshimiwa Mawaziri wote wawili kwasababu nchi hii, mitaala yake na mfumo wake unayumbayumba katika elimu, lazima tuwaeleze. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika hili kwa mtazamo wangu na kwa uelewa wangu na kama Mwalimu mzoefu, siwezi kutofautisha kati ya Wizara ya Elimu ya Waziri Mheshimiwa Ndalichako na Wizara ya TAMISEMI inayoshughulikia elimu. Wote ni kitu kimoja!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala hili la elimu; ili tuweze kuwa na elimu bora ni lazima tuanze katika ngazi zote za elimu. Leo hatuwezi kuzungumzia suala zima la vocational training; elimu ya ufundi ambayo Mheshimiwa Profesa Ndalichako anaishughulikia na elimu ya juu kama hatujaweka misingi imara kuanzia pre-primary education. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kuwa na wanafunzi wazuri ambao wakifundishwa vocational skills katika vyuo mbalimbali vya VETA Tanzania, ambao wataweza kufundishwa elimu ya juu, lazima wawe wamefundishwa vizuri kuanzia chekechea. Kwa hiyo, Serikali lazima ihakikishe kwamba inawekeza Elimu ya Msingi kuanzia pre-primary school education. Nazungumza haya kwasababu tumezungumza sana kuhusu elimu ya juu kana kwamba hii elimu ya juu inaanzia elimu ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2015 na mwaka 2014 nilikuwa nimefanya utafiti mmoja nikiwa Mwalimu; Mwenyekiti wa Wakuu wa Shule Wilaya ya Lindi, nilipewa paper ya ku-present mbele ya Mheshimiwa Kassim Majaliwa inayohusu matokeo makubwa katika elimu. Katika conclusion yangu niliweza kuzungumza baada ya utafiti wangu nilioufanya kwamba huwezi kuzungumia matokeo makubwa katika elimu and then ukaweka neno sasa hivi, kitu ambacho hakiwezekani kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwasababu elimu kama elimu ni mchakato ambao ni endelevu. Mwanafunzi anatakiwa afundishwe kwa muda wa miaka miwili au miaka mitatu elimu ya awali. Afundishwe vizuri! Afundishwe vizuri elimu ya msingi lakini akifika sekondari afundishwe vizuri, ndiyo mwanafunzi huyu atakuwa na uwezo wa kufundishwa elimu ya ufundi kwa kufundishwa masomo ya Form Five na Six na masomo ya degree yake, ataweza kufanya vizuri na ataweza kuwa mwanafunzi ambaye atajikomboa yeye mwenyewe na kuikomboa jamii yake inayomzunguka, lakini siyo danadana na mzaha tunaoufanya leo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwakuwa hili haliwezi kuepukika kama nilivyoeleza hatuwezi kufanya separation kati ya Elimu ya Msingi, Sekondari na Elimu ya Vyuo. Naomba nizungumzie suala zima ambalo Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumza, kuhusu elimu bure. Wizara kama Wizara imetoa Waraka Na. 6 na hapa Mheshimiwa Waziri amezungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ule waraka kuna maelekezo Waheshimiwa Wabunge naomba myasikilize ambayo yanaeleza, nami hapa waraka wenyewe ninao hapa, huu hapa Waraka Na. 6. Imeelezwa mle ndani kwamba katika mgawanyo wa pesa zinazopelekwa shuleni inatakiwa zitumike katika muktadha ufuatao: Matumizi ya kwanza ni matumizi ya jumla ya ofisi. Hapa tunamaanisha vitambulisho, shajara, maandalio, ulinzi, umeme, maji na fedha za kujikimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine (b), kuna suala zima la uendeshaji wa taaluma, kuna suala zima la mitihani endelezi, kuna suala zima la madawa baridi ya binadamu, mahitaji ya wasichana na kadhalika na matengenezo madogo madogo. Sasa jambo la kusikitisha, ukija katika utekelezaji wa hiyo sera, nilikuwa nafanya utafiti tu kwenye shule zangu kule Jimbo la Mtwara Mjini, ni jambo la ajabu sana. Shule imepelekewa shilingi 27,000/= halafu inaambiwa ifanye mgawanyo huo wote.
MHE. ABDALLAH N. MAFTAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, siungi mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia makadirio haya ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenijalia kuwa na afya njema na leo hii naweza kuchangia bajeti hii ipasavyo na siyo matusi kama wanavyofanya wachangiaji wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza moja kwa moja na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa…
Taarifa...
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeipokea taarifa, wasubiri, wasikilize kwa sababu sichomi sindano nazungumza maneno tu ya kawaida. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati niko mwaka wa kwanza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nilikuwa napitia kitabu kimoja kimeandikwa na Ishumi na Nyirenda cha saikolojia. Kuna kipengele kimoja amekieleza kwa kiasi kikubwa sana, kwamba philosophy is the study of fundamental
questions. Wakati anaeleza Mheshimiwa huyu Ishumi na Nyirenda akaliweka neno moja kwamba falsafa maana yake wewe unayesoma lazima uweze kujiuliza swali kwamba hiki unachoelezwa maana yake ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, lazima uweke swali, why, kwamba umeelezwa nenda Bungeni, kamtukane Mheshimiwa Sakaya, Mheshimiwa Profesa Lipumba, Mheshimiwa Maftaha na Msajili wa Vyama vya Siasa halafu unabeba kama mbuzi, umebeba kama mzigo kwenye gunia unakuja Bungeni na wewe unakuja kutukana. Hii ni kukosa weledi na kukosa ufahamu wa kielimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi kama nimesoma shule nimeelimishwa, siwezi kufanya haya. Kila unalotumwa na mtu kwamba kalifanye hili, lazima nijiulize kwa nini eti unanituma niende nikamtukane Mwenyekiti wa Chama Taifa, siwezi kufanya haya kwa sababu nina uelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna suala hapa limepotoshwa kwa kiasi kikubwa sana. Waheshimiwa Wabunge hapa wamekuwa wakizungumza na hawapo wamekimbia nje, kwamba eti Msajili wa Vyama vya Siasa amemrudisha Mwenyekiti wa Chama Taifa, Profesa Ibarahim Lipumba kuwa Mwenyekiti wa Chama, hili naomba nikanushe na Watanzania na Bunge hili liweze kufahamu sio kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chama cha Wananchi CUF mwaka jana 2016 mwezi Agosti, tarehe 21, tulikuwa na Mkutano Mkuu wa Chama Taifa. Naomba nizungumze haya ili Watanzania waweze kufahamu kwamba ni nini kinaendelea ndani ya Chama cha Wananchi CUF badala ya kumbebesha mzigo Msajili wa Vyama vya Siasa. Tarehe 21 Agosti 2016 tulipofanya Mkutano Mkuu Chama cha Wananchi CUF kulikuwa na mambo ambayo hayakufanywa sawasawa na Katibu wa Chama kwa makusudi kabisa eti kwa sababu hamuhitaji Profesa Lipumba kuwa Mwenyekiti wa Chama wakati Katiba ya Chama cha Wananchi CUF, Ibara ya 117(1)(2) kinaonesha kabisa kwamba Mwenyekiti wa Chama
cha Wananchi CUF ni Profesa Ibrahim Haruna Lipumba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwa katika mkutano wetu wa ndani ya chama tuliweza kuona mambo ambayo kimsingi siyo mambo ambayo yanaweza yakafanywa na kiongozi mkubwa kama Katibu Mkuu wetu wa Chama cha Wananchi CUF. Mambo yaliyotokea, kwa sababu
tunazungumza suala la utawala bora hapa na utawala bora pamoja na vyama viendeshe taratibu zao sawasawa. Naipongeza Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kusimamia vyama vyetu vya siasa sawasawa kwa sababu watu wanatumia kama SACCOS zao binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulivyoingia kwenye ukumbi wa mkutano upande wa Katibu Mkuu wa Chama, Maalim Seif Shariff Hamad alileta wajumbe 116 kutoka Zanzibar kinyume na taratibu za Katiba ya CUF eti waje kupiga kura ya hapana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa miongoni mwa watu waliouliza maswali ndani ya ukumbi ule, nikahoji kwamba hawa wajumbe 116 ambao wameongezwa kutoka upande wa Zanzibar wapo kwa mujibu wa Katiba na kama wameongezwa mbona upande wa Bara hawapo? Majibu yalikuwa ni kwamba hao wameongezwa ni wajumbe maalum. Tukamuuliza wajumbe maalum mbona huku Bara haukuwateua wajumbe maalum, wakawa hawana majibu wakasema tutawafukuzeni chama, hivi vyama lazima viangaliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kusema kwamba eti Msajili kazi yake ni kusajili tu vyama vya siasa na baadaye kuvifuta, Sheria Na. 5 ya mwaka 1992 ilivyoanzisha vyama vya siasa inampa mamlaka Msajili wa Vyama vya Siasa kusajili pamoja na kuvilea. Naomba niulize swali, hivi unavyosema kuvilea maana yake ni nini, ni kwamba kumchukua mtoto kumweka pale na wewe ukatembea zako, si lazima umwangalie mwenendo wake na takwimu zake ziko vipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Wajumbe wa Mkutano Mkuu Taifa wa Chama cha Wananchi CUF tarehe 21, Agosti, 2016 tulivyoona kwamba yanafanyika mambo ambayo ni kinyume na taratibu za uendeshaji wa vikao vyote duniani tukasema kwamba hatuwezi kukubaliana na haya. Wajumbe asilimia 99 kutoka upande wa Tanzania Bara tulikuwa tunataka marekebisho na utaratibu uendeshwe sawasawa likiwemo suala la kuondolewa wajumbe 116 walioletwa kinyume na taratibu za Katiba ya CUF. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulivyomueleza Mheshimiwa Katibu akasema hapana hatutakubaliana na hilo. Pia tukamhoji kwamba kuna watu wameongezwa tunaambiwa wanatoka vyama vingine wameongezwa kama wajumbe waje kupiga kura humu ndani tunaomba tufanye uhakiki wa kila wilaya, akakataa akasema hatufanyi uhakiki, mimi ndio Katibu Mkuu, mimi ndiyo mwenye chama. Sisi tulichofanya tukasema hatuwezi kuendelea na mjadala huu mpaka haya yarekebishwe, kama Wajumbe wa Mkutano Mkuu Taifa tuna uhalali wa kuyarekebisha haya. Wakaenda juu wakaleta vyombo vya habari wakasema kwamba tunakwenda kulazimisha kupiga kura wakati wajumbe zaidi ya 400 tulikataa kwamba tusipige kura kwa sababu hoja ya Kujiuzulu kwa Mwenyekiti ni lazima sisi Wajumbe wa Mkutano Mkuu tukubali sasa Mheshimiwa umejaza wajumbe kutoka Zanzibar ambao sio halali ili kuongeza namba, hatuwezi kukubaliana na hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mengi sana, wakaingia wakaita vyombo vya habari wakasema Mkutano Mkuu umeridhia kujiuzulu kwake kitu ambacho siyo sahihi kabisa. Sisi ndani ya ukumbi tukasajili majina yetu, zaidi ya 324 tukaenda kwa Msajili wa Vyama vya Siasa tukilalamika
kwamba taratibu za uendeshaji wa vikao vya Chama hiki cha Siasa cha CUF zimekiukwa kwa makusudi, tunaomba utupe tafsiri. Msajili wa Vyama vya Siasa alituita sisi wote, upande wa walalamikaji sisi Wajumbe wa Mkutano Mkuu zaidi ya 320, upande wa Katibu Mkuu, tukaitwa tukakaa wote tukawa tumepewa miongozo zaidi ya mara nne, mara tano na mwisho wa siku Msajili wa Vyama vya Siasa akatoa mwongozo kwamba kwa mujibu wa Katiba ya CUF Profesa Ibrahim Lipumba ndio Mwenyekiti halali wa Chama cha Wananchi CUF Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nazungumza haya kwa sababu yameelezwa sana, kuna upotoshwaji unaofanywa kwa makusudi eti kwa sababu ya kuwahadaa Watanzania kwa sababu ya kutafuta huruma kupitia Bunge hili wanakuja wanasema uongo eti kwa sababu wametumwa na mtu mmoja. Chama ni taasisi, chama sio mtu mmoja, chama ni uamuzi wa wanachama ndugu zangu na tunasema tutasimamia hili mpaka mwisho wetu na Profesa Lipumba ndiyo Mwenyekiti halali wa Chama cha Wananchi CUF. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala hapa limezungumzwa kwamba Msajili wa Vyama vya Siasa eti ametoa ruzuku akishirikiana na wahuni wake. Naomba nizungumze tu kwamba ruzuku ya Chama cha Wananchi CUF imeletwa kwa mujibu wa Sheria ya Ruzuku za Vyama vya Siasa na hivi ninavyozungumza baada ya ruzuku kuletwa kwenye chama, Mheshimiwa Mwenyekiti na Kamati Tendaji Taifa, hata mimi ni mjumbe pia, ni Mkurugenzi wa Mambo ya Nje ya Chama cha Wananchi CUF, tulikaa tukapeleka ruzuku wilayani. Tulivyopeleka ruzuku Wilayani ili ziweze
kujenga chama na kulipia posho, Mheshimiwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF akaandika barua kwa Meneja wa Benki Kuu kwamba afungie ruzuku akaunti za wilaya ambazo hata yeye hana mamlaka nazo na tunashangaa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Ofisi ya Waziri Mkuu ilishughulikie hili suala kwamba kwa nini Meneja wa NMB Tanzania ameandikia barua akaunti zote za wilaya za Chama cha Wananchi CUF ambazo wao ndiyo wamefungua akaunti, hazikufunguliwa na Katibu Mkuu Maalim Seif Shariff Hamad lakini hivi ninavyozungumza zimefungiwa na zile pesa hazifanyi kazi ya chama, ziko kwenye akaunti za NMB Tanzania nzima. Tunaomba sana huyu Meneja wa NMB Taifa achukuliwe hatua kwa nini anaingilia akaunti za Chama cha Wananchi CUF ngazi ya wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka nizungumze ni suala hili la viwanda ambalo limeelezwa kwa kiasi kikubwa sana. Miaka ya karibuni Serikali iliweza kupitisha sera kwamba ajira zote hivi sasa ziweze kusimamiwa na wamiliki wa viwanda na taasisi husika. Hata hivyo, pale Mtwara katika kiwanda cha… (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na niseme tu kwamba naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia mwelekeo huu wa mpango asubuhi hii ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kuchangia mwelekeo huu wa mpango, naomba Nimshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu-Wataala ambaye ameendelea kunijalia afya njema leo hii, lakini pia niweze kumshukuru Mwenyekiti wa chama changu, Chama cha Wananchi (CUF), full-bright Profesa Ibrahim Haruna Lipumba, kwa kuendelea kushirikiana vizuri kutetea maslahi ya Watanzania na hasa katika rasilimali zetu za madini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niweze kuzungumza kidogo kwamba sisi Chama cha Wananchi (CUF) ilani zetu zote za uchaguzi kuanzia mwaka 1995, mwaka 2000, mpaka mwaka 2010 tulikuwa tunazunguka Tanzania nzima kuwaeleza Watanzania ya kwamba rasilimali za madini ya nchi hii zinatumiwa kwa kiasi kikubwa na wageni wa nje na sisi wenyewe kila shilingi 100 tunapata shilingi tatu tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii nizungumze katika Bunge lako hili kwa namna ya kipekee kabisa niweze kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu huyu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba anasimamia Ilani ya Chama cha Wananchi (CUF), anasimamia itikaChama cha Wananchi (CUF), Sera ya Utajirisho kwamba madini yetu yaweze kuwanufaisha Watanzania na sisi lazima tuunge mkono kama chama imara cha siasa, CUF - Chama cha Wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kuchangia mwelekeo huu wa mpango kwa kusema ya kwamba viwanda kwa kiasi kikubwa sana, nilikuwa nasikiliza hotuba zote mbili, hotuba ya Mheshimiwa Waziri na hotuba ya Kamati ambazo zimezungumzia suala zima la viwanda, na tumekuwa tunazungumza sana kwamba sehemu hii ya viwanda ni sehemu muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilishawahi kusema katika Bunge hili wakati nachangia mpango mwaka wa jana na mwaka wa juzi, kwamba nchi nyingi duniani ziliweza kuendelea kupitia sekta ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, karne ya 15, ukisoma historia, sisi tuliosoma historia tunaambiwa ya kwamba nchi zote za Ulaya ziliweza kufanya mapinduzi ya viwanda na hatimaye wakaweza kuwa matajiri mpaka leo hii tunasema wao ndio wanaotusaidia sisi nchi za ulimwengu wa tatu. Kwa hiyo, kwa umuhimu wake hili suala ni suala nyeti sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la ajabu, tulikuwa tumezungumza wakati wa bajeti hapa kwamba wapo wawekezaji wengi wanaohitaji kuwekeza Tanzania. Kule Mtwara kuna wawekezaji wa Kijerumani na Kamati hapa imeeleza ambao wanataka kujenga viwanda vya mbolea, pale Mtwara Msangamkuu. Kule Kilwa pia kuna mwekezaji ameamua kuwekeza kwa kujenga kiwanda cha mbolea, lakini bado Serikali tunaona inasuasua kuwapa rasilimali ya gesi wale wawekezaji ili waweze kujenga vile viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini viwanda vikijengwa pale Mtwara Msangamkuu wananchi wengi wa Mtwara watapata ajira, wananchi wa Kilwa kule kikiwepo kiwanda watapata ajira na umaskini utaweza kuondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana katika mwelekeo huu wa mpango kwamba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hotuba yake atueleze kwa nini mpaka leo wale wawekezaji wanaotaka kuwekeza viwanda vya mbolea pale Msangamkuu, Mtwara Vijijini ambapo ni karibu kabisa yaani ni pua na mdomo katika Jimbo langu la Mtwara Mjini, lakini pia kule Kilwa bado mpaka leo Serikali inasuasua kuwapa wale wawekezaji gesi waweze kujenga viwanda vya mbolea ili kuweza kuondokana na umaskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuzungumzia suala la umeme REA. Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mpango, amezungumza hapa kwa kiasi kikubwa kwamba umeme unaotumika mikoa ya kusini unatoka Mtwara Mjini, viwanda vya kusindika ile mitambo vimejengwa Mtwara Mjini, lakini jambo la ajabu nimekuwa ninazungumza sana, kwenye Mabunge yako yote nimekuwa nazungumza hili; kwamba pale Mtwara Mjini kwenyewe ambapo ndipo mitambo yote ya kusindika umeme ipo, bado kuna maeneo mengi haujapelekwa mtandao wa umeme ikiwemo kule Mbawala Chini, Naulongo, Mkunjanguo na maeneo mengine ambamo pia tulisema kwamba mule mnapita kitu kinachoitwa mkuza wa gesi, lile bomba la gesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tumelia sana kwa muda mrefu katika Bunge hili na Mheshimiwa Waziri akiwa anaahidi kwamba atapeleka umeme kule kote. Sasa ni jambo la ajabu sana kwamba kila mwaka tuwe tunarudia na kurudia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaomba katika Mpango huu ambao unaandaliwa, hili suala la kuhakikisha ya kwamba umeme wa REA unasambazwa basi usambazwe kwenye maeneo yote kwa sababu wananchi wa maeneo yale ambapo ni vijiji ambavyo viko mjini lakini bado tunaita ni vijiji kwa sababu vinahitaji kupita umeme wa REA uweze kwenda kule; Tunaomba Serikali ihakikishe ya kwamba inapeleka na sio kila mwaka kupiga dana dana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vipo vijiji vingi pia kule Mtwara na Lindi, bado, na wakandarasi wenyewe waliopewa ukiwauliza wanatuambiwa huko sisi hatuna bajeti, bajeti yetu sisi ni kutoka kijiji hiki tunaingia vijiji vya Tandahimba, Newala na wapi, lakini bado tunahitaji wananchi wale waweze kupelekewa umeme. Ili tuweze kuondokana na umaskini lazima kila kijiji, hata kama kipo mjini, basi umeme uweze kufika. Tunaomba sana hili Mheshimiwa Waziri aje atueleze mpango huu wa maendeleo ameliwekaje mwaka huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninataka nilizungumze hapa ni suala la kilimo. Katika Mkutano wa Bunge wa bajeti, wakati tunapitisha Bajeti ya Wizara ya Kilimo nilizungumzia suala zima la korosho. Kulikuwa na suala la mboleo, nilieleza wakati ule na nilimnukuu mtaalam mmoja anaitwa Kunz, mwaka 1988/1989 katika kitabu chake cha Managerial, alisema kwamba failure to plan is planning to fail, kwamba ukifeli kupanga maana yake unapanga kufeli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilizungumza suala la mbolea, kwamba walisema kwamba watagawa mbolea bure kwa wakulima wetu wa korosho lakini halikupangwa lile; na hapa leo kwenye mwelekeo huu wa Mpango bado sijaona pia kama limepangwa. Kilichotokea wakulima wamelanguliwa mbolea badala ya kuuziwa shilingi 20,000 wakanunua mbolea mfuko mmoja shilingi 100,000, 150,000 wengine mpaka shilingi 200,000 baadhi ya maeneo, ni kwa sababu Serikali ilishindwa kupanga sawasawa suala hili la kugawa mbolea bure kwa wakulima wa korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na korosho ndilo zao ambalo linaingiza pesa nyingi Serikalini kuliko zao lolote. Linaanza zao la korosho then inakuja tumbaku. Kwa hiyo, ninaomba kwamba mpango wetu wa safari hii upange sawa sawa, kwamba ni kiasi gani cha mbolea kitapelekwa kwa wakulima wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la ajabu katika korosho pia, nilikuwa napitia taarifa za masoko ya dunia; bei ya korosho soko la dunia, kilo moja ni dola 29. Ukijumuisha, ukigawa kwa pesa yetu ya Kitanzania ni sawa sawa na almost kama shilingi 49,000; shilingi 50,000 hivi kwa kilo moja, katika soko la dunia. Kama Bandari ya Mtwara itatumika sawa sawa, ukisafirisha korosho kutoka Bandari ya Mtwara mpaka soko la dunia, bei ya korosho haizidi kilo moja shilingi 2,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba sana, pamoja na kwamba tunajigamba, na tunashukuru kwa kweli kwamba Serikali imejitahidi kuongeza bei ya korosho kwa wakulima, hivi sasa ni shilingi 3,800 mpaka 3,850, lakini bado mkulima angeweza kupata bei kubwa zaidi ya hii kutokana na umuhimu na unyeti wa zao la korosho duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana Serikali ihakikishe inatafuta wanunuzi wa korosho ili korosho yetu hii iweze kuingiza pesa nyingi zaidi ya hizi ambazo tunazipata Hazina, lakini kwa wananchi wetu waweze kuondokana na umasikini, hasa maeneo ya Mtwara na Lindi pamoja na Pwani na maeneo mengine wanayolima korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la ajabu sana nilikuwa napitia taarifa pia za kimtandao kwamba hata katika zile nchi ambazo zinalima korosho duniani, Tanzania haipo. Afrika kuna Côte d’Ivoire, imewekwa Afrika Kusini, imewekwa Thailand na nchi nyingine, Tanzania sisi tunajulikana kwamba hatulimi korosho wakati wanunuzi waliopo Thailand, wanunuzi waliopo India wanakuja kununua korosho Tanzania. Hili linapoteza pia thamani na pato zaidi. Kwa sababu hawa wanunuzi wa kule nchi za nje wanakwenda kununua kule kwenye nchi ambazo zimewekwa kwenye taarifa mbalimbali za kidunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba hili mlizingatie, ni jambo la muhimu sana ambalo ninaomba kuchangia katika huu Mpango ni sekta ya utalii nchini. Ninaomba kuzungumzia suala zima la sekta ya utalii nchini…

T A A R I F A

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei taarifa kwa sababu kadandia gari kwa mbele. Nilichozungumza ni kwamba katika orodha ya nchi zinazouza korosho duniani Tanzania haipo, ndiyo taarifa iliyopo pale. Sasa yeye anazungumza yawezekana kwamba hajasoma sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kwa sababu kanipotezea muda bure tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninaomba kuchangia katika huu mwelekeo wa mpango ni sekta ya utalii nchini. Sekta hii ya utalii nchini ni sekta muhimu sana na taarifa ambayo tulipewa hapa Bungeni, tulielezwa ya kwamba Tanzania ina vivutio vingi sana, ukiondoa Brazili inayofuata ni Tanzania. Hata hivyo nikapitia mpango wa Wizara ya Maliasili na Utalii, kuna pesa ambazo wameziweka zinaitwa pesa za REGROW, wamekopa Benki ya Dunia kwa ajili ya kuendeleza sekta ya utalii kule Nyanda za Juu Kusini. Sasa ninaomba sana zile pesa dola milioni moja ambazo zimekopwa Benki ya Dunia kwa ajili ya kuendeleza utalii Nyanda za Juu Kusini basi zifike kule Kusini pia ili sekta hii ya utalii iweze kutangazwa sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na katika hili, pale Mtwara Mjini tuna eneo la Mikindani. Mikindani kuna majengo ya kale sana. Sasa nimeangalia taarifa hapa sijaona mpango uliowekwa sawasawa juu ya sekta ya mambokale katika utalii kwamba Serikali imejipangaje kutangaza mambokale ili iweze kuwaingizia pesa Serikali ya Tanzania, lakini wananchi kwa ujumla kwa kupata ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mikindani kuna majengo na vivutio vingine vingi vya kale, lakini vivutio vile vimeachwa kwa wazungu, watu wanaoitwa Trade Aid ndio wanaokarabati, ndio wanaotangaza na kukusanya pesa wakati Serikali hii ina shida ya pesa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba sana kwamba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha mpango sekta hii ya utalii iangalie sekta ya mambo kale na hasa hasa utalii katika maeneo haya ya Mikoa ya Kusini ya Mtwara na Lindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninataka kulizungumza ni suala hili la miundombinu. Tunaishukuru Serikali kwa kiasi kikubwa imekuwa ikijenga miundombinu, imekuwa ikijenga barabara lakini pia imeweza kuleta pesa za kutosha pale Mtwara Mjini na linajengwa gati linajengwa la mita 300.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana, sambamba na upanuzi wa Bandari uliopo Mtwara Mjini hivi sasa tunaomba swala la reli hili ambalo imekuwa Serikali imekuwa ikizungumza kila mwaka, kila siku, reli ya Kusini, ili Mtwara corridor iweze kufunguka, iweze kufungua uchumi wa ukanda ule wa Kusini lazima hili suala la kujenga reli kutoka bandari ya Mtwara kwenda Mchuchuma na Liganga kule kwenye makaa ya mawe iweze kuwekwa kwenye bajeti ya mwaka huu, pesa ziweze kutengwa ili sasa uchumi wa Kusini na Watanzania uweze kusheheni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, reli hii ilikuwepo miaka ya nyuma lakini iliondolewa, sijui iliondolewa kwa sababu gani. Sasa tunaomba sana, kwa sababu kuna mkakati unaitwa Mtwara corridor wa kufungua Kusini mwa Tanzania ili Tanzania yetu sasa iweze kweli kuwa ni Tanzania ya uchumi. Bandari yetu inavyojengwa kama reli ikijengwa mizigo ikiletwa pale tunaamini ya kwamba bandari itaingiza pesa nyingi na bajeti yetu itakuwa haisuisui tena kwa sababu ya makusanyo. Tusiangalie sana Bandari ya Dar es Salaam, tutanue Kusini, tutanue Mtwara corridor kama tulivyokuwa tunaahaidi siku zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, naomba nizungumze suala zima la ardhi. Wakati tunapitia bajeti hapa, Mheshimiwa Waziri wa Ardhi alizungumzia mipango mikakati, na tunashukuru kwa kweli pale Mtwara Mjini tumezindua mpango kabambe wa ardhi. Hata hivyo kuna mambo ambayo yalizungumzwa na kuahaidiwa katika Bunge lako hili Tukufu, suala la kulipa fidia kwa maeneo ambayo Serikali ilichukua. Kwa mfano, Mtwara Mjini eneo la Mji Mwema, Serikali ilihaidi kwamba mpaka mwezi wa nane mwaka huu itakuwa tayari imelipa fidia. Jambo la ajabu wanaleta taarifa kwamba Serikali imeshindwa kuwalipa wale watu wa Mji Mwema wakati wale watu wamechukuliwa ardhi tangu mwaka 2013, ni jambo la ajabu sana. Tunazungumza ndani ya Bunge, tunapanga ndani ya Bunge wananchi wanasikia halafu baadaye Serikali inasema haina pesa kupitia UTT, UTT wameghairi kulipa. Ni jambo la ajabu kwa kuwa tunazungumza, tunapitisha kwenye bajeti lakini utekelezaji wa haya mambo ya msingi unakuwa hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri atakavyokuja atueleze kwamba mkakati upoje kuhusiana na sekta hii ya ardhi ambayo bado ina changamoto nyingi; Tanzania pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia bajeti hii ya Nishati na Madini. Kabla sijaanza kutoa salamu za Wanamtwara na maagizo ya Wanamtwara kwa Wizara hii, naomba kwanza nitoe masikitiko yangu kwa kiasi kikubwa sana. Mheshimiwa Waziri hapa wakati anawasilisha hotuba yake kazungumzia mambo mengi yanayohusu gesi, mambo mengi yanayohusu petroli na mambo mengi yanayohusu mafuta ambayo ndiyo chachu ya uchumi wetu wa sasa hivi hapa nchini Tanzania.
Mheshimiwa Spika, masikitiko yangu, nilikuwa napitia gazeti leo hii, gazeiti la The Citizen, CAG ameeleza masikitiko yake makubwa kabisa na naomba ninukuu, halafu nimuulize Mheshimiwa Waziri swali langu. Amesema hivi:
“It was unfortunate that NAOT does not have a single expert in auditing accounts related to oil and gas despite trillions of cubic feet of fossil fuel reserves having been discovered in Tanzania”.
Mheshimiwa Spika, gazeti la leo, kwamba anasikitika na anaeleza, analiambia Taifa hili kwamba pamoja na umuhimu wa gesi na mafuta tuliokuwa nayo na wingi wake wote, lakini hana mamlaka ya kwenda kukagua, sasa sijui tatizo ni nini? Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kutoa majibu atueleze kwa nini account zile zinazotokana na visima vya mafuta na gesi havikaguliwi na CAG.
Mheshimiwa Spika, naomba nianze kuzungumzia suala zima hili la umeme vijijini. Ile Mikoa ya Kusini tuna bomba la gesi na kwa bahati nzuri Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini alizungumza katika mihadhara yake mingi sana kwamba Wanamtwara na Lindi watakuwa wananufaika na gesi kupitia mle lilimopita bomba la gesi kupitia Sekta ya Umeme.
Mheshimiwa Spika, mpaka hivi sasa ninavyozungumza ule unaitwa mkuza wa bomba la gesi ambalo Serikali imekuwa inaahidi kupitia miradi yake ya REA Awamu ya Kwanza, REA Awamu ya pili, mpaka hivi sasa tunakwenda kwenye REA Awamu ya tatu bado vijiji vile vyote havijapata umeme huu pamoja na ahadi nyingi na majigambo makubwa ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri ya kwamba, ni lini sasa atahakikisha kwamba maeneo yote yanayopita bomba la gesi, mkuza wa gesi, anatekeleza ahadi yake ya kupeleka umeme? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna suala hili la wananchi wa mikoa ya kusini kunufaika na gesi. Hata hivyo, nitoe masikitiko yangu makubwa sana, kwamba tumekuwa tunazungumza sana, tumekuwa tukiahidi sana, tukieleza sana, kuliko kutekeleza.
Mheshimiwa Spika, nilikuwa napitia mpango wa TPDC wakati tuko kwenye Kamati, lakini juzi taarifa yao tumekuwa tunapitia. Kuna mkakati ambao Serikali wameweka wa kuhakikisha kwamba gesi inayotoka mikoa ya kusini, Mtwara na Lindi inafika Dar es Salaam, baadaye itapelekwa mikoa mingine ya kaskazini kwa mfano Tanga, Mwanza na maeneo mengine. Katika mkakati ule pia wameeleza kwamba hii gesi itakuwa inapelekwa kwa ajili ya matumizi ya majumbani kuanzia Dar es Salaam, lakini cha ajabu ukipitia taarifa ile ya TPDC mikoa ya kusini, Mtwara na Lindi haipo.
Mheshimiwa Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri atakapokuja na majibu yake atueleze wananchi wa Mtwara na Lindi mkakati ukoje. Kwa sababu niliuliza swali hili wakati tunasikiliza taarifa ya Kamati ya Nishati na Madini tulivyowaita kwenye Kamati yetu hii ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma na wakasema kwamba watakwenda kulishughulikia. Naomba majibu ya Mheshimiwa Waziri kwamba asije akawa anazungumza tu wakati kwenye maandishi kule hakuna na Wanamtwara na Wanalindi pia wanasubiri majibu stahiki kutoka kwa Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Spika, nizungumzie pia suala zima ambalo Mheshimiwa Silinde ameligusia hapa, la kuwapa wawekezaji ambao wapo mikoa hii ya kusini nishati hii ya gesi waweze kutumia kama nishati. Leo hii tuna kiwanda ambacho kilitarajiwa kujengwa Mtwara maeneo ya Msangamkuu, ni kwa miaka minne hivi sasa yule mwekezaji anaomba apewe gesi ili aweze kujenga kiwanda cha saruji, mpaka leo tunavyozungumza ni danadana tu kwenye Wizara hii ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Spika, niombe sana Mheshimiwa Waziri ahakikishe kwamba wawekezaji hawa ambao wana nia ya kuwekeza Mikoa ya Kusini wanapewa nishati hii ya gesi ili waweze kuondoa umaskini ambao wananchi wa mikoa hii ya kusini umekuwa unatutawala kwa muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kama hiyo haitoshi, Mheshimiwa Silinde kazungumza, mwekezaji Aliko Dangote, kwa muda mrefu sana amekuwa akiomba gesi ili aweze kuitumia kama nishati. Mheshimiwa Silinde kazungumza kwamba ananunua makaa ya mawe kutoka Msumbiji, sio Msumbiji Mheshimiwa Silinde, ananunua makaa ya mawe kutoka South Africa. Meli inakuja Mtwara ku-gati kutoka South Africa ambayo mwekezaji huyu Aliko Dangote anatumia kama nishati wakati Mtwara tuna gesi iko kedekede, cubic meter za kutosha, kwa nini asipewe hizi gesi sambamba na kwamba yuko tayari kuuziwa, lakini Wizara mpaka leo inaleta danadana? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwaka 2012, wananchi wa Mtwara na Lindi waliandamana kwa kiasi kikubwa sana wakidai manufaa ya gesi, kwamba kwa namna gani hii gesi itaanza kuwanufaisha wananchi wa mikoa ile. Na madai yetu yale yalipotoshwa sana, watu walifikia wakati, wengine viongozi kabisa wa Kitaifa wakiwabeza wananchi wa kusini kwamba wao wanahitaji kutumia gesi peke yao. Madai yetu yalikuwa ni kwamba gesi inayotoka mikoa hii, kwa sababu inaanzia pale, kwanza tunufaike kwa kupata mrabaha. Nimepitia na nimesikiliza hotuba ya Mheshimiwa Waziri, wakati anawasilisha sijaona hata sehemu moja na sijamsikia anasema kwamba mrabaha kiasi gani utabakizwa Mtwara na mikoa ile ya kusini ya Mtwara na Lindi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini cha ajabu kabisa kule kwenyewe inakotoka hii gesi, Msimbati, hata barabara ya kufika Msimbati ni kizungumkuti. Kwa nini Wizara na Serikali isitenge bajeti ya kujenga angalau barabara ile kiwango cha lami kutoka Mtwara Mjini mpaka kule Msimbati? Wananchi wa kusini wakidai haki hizi mnawapiga mabomu, mnatuletea Wanajeshi na kwamba sisi hatuipendi Serikali. Tunachosema ni kwamba, Serikali ihakikishe kwamba manufaa yanayotokana na gesi hii na sisi wananchi wa kusini tuweze kunufaika nayo.
Mheshimiwa Spika, upotoshwaji unaofanywa wa kwamba tunataka tuitumie gesi peke yetu si kweli. Nazungumza haya kwa sababu tuna ushahidi wa kutosha sana, tuna ushahidi wa kutosha. Sisi wote ni mashahidi, kwa kiasi kikubwa Korosho inazalishwa Mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani, lakini korosho ile kwa taarifa za mwaka jana na miaka mingi mfululizo limekuwa ni zao ambalo linaingizia Taifa pesa nyingi sana. Mwaka jana, 2014/2015 limekuwa ni zao la pili, lakini zile pesa zinazokusanywa na mapato ya korosho zote zinapelekwa Hazina zinanufaisha Watanzania wote.
Mheshimiwa Spika, tunachosema Wanakusini, tunachosema Wanamtwara na Lindi ni kwamba tunufaike na fursa za ajira na isiwe Serikali na Wizara inaondoa fursa hizi. Kwa sababu unapomnyima mwekezaji huyu kutumia gesi, kwa mfano, Aliko Dangote akiagiza makaa yake ya mawe kutoka South Africa anakodi meli, gharama zinakuwa ni kubwa, mwisho wa siku simenti inakuwa bei mbaya. Tunaomba sana wananchi wa Mtwara na Lindi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini jambo la ajabu sana, Serikali hii imekuwa ni sharp sana katika kuondoa rasilimali za kimaendeleo Mikoa ya Kusini kuliko kupeleka kwingine. Nimekuwa nazungumza hili kwa muda mrefu sana. Bomba la gesi limejengwa kwa miezi 18 tu. Kwa miezi 18 pesa zilizotumika zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni mia mbili kama na hamsini na tano, lakini tunavyosema kwamba, tunahitaji maendeleo yaletwe kusini yanachukua muda mrefu sana. Suala la kufanya negotiation ya mkataba tu kwamba huyu mwekezaji wa Kiwanda cha Mbolea Mtwara, Dangote na yeye mwekezaji wa simenti inachukua muda mrefu, kwa nini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, siungi mkono hoja mpaka haya maswali yangu yaweze kupatiwa majibu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MAFTAH A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nguvu, uzima na afya njema ili niweze kuchangia hotuba ya Waziri wa Nishati na Madini kwa maandishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka Waziri wa Nishati na Madini afahamu kuwa mwaka 2012 Mtwara na viunga vyake kulitokea vuguvugu la gesi na wananchi wakidai haki ya ajira kupitia sekta hii muhimu, lakini kwa makusudi kabisa Serikali ilitumia nguvu kubwa kuwapiga wana Mtwara na hata kuwaua kwa risasi akiwemo mama mjamzito eneo la Mkanaled. Wapo waliovunjwa viungo vya miili yao na wapo waliochomewa nyumba moto na wapo waliopoteza mali na rasilimali ambako kulifanywa na vyombo vya dola.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali baadaye iliunda tume ya kuchunguza athari za vurugu hizo ambayo iliongozwa na Chara Mwijage, lakini cha ajabu mpaka leo hawajaleta mrejesho na wananchi pamoja na askari kadhaa pia wameathirika sana. Je, ni lini Serikali italipa athari hizi kama ilivyoahidi?
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa kutumia gesi majumbani ambao utaanza Dar es Salaam, Mwanza, Tanga na maeneo mengine, tayari mchakato wake umekamilika maeneo hayo isipokuwa Lindi na Mtwara ambako gesi yenyewe inatoka, wanasema watafanya upembuzi yakinifu. Ni jambo la ajabu sana Bomba la gesi limejengwa kwa miezi 18 tu limekamilika ila kuleta maendeleo Kusini Serikali inaleta kigugumizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri aseme ni tarehe ngapi huo upembuzi umefanyika maana mimi ni Mbunge wa Jimbo sina taarifa yoyote Mtwara? Je, ni lini gesi itasambazwa majumbani Mtwara na Lindi na ni kwa nini Waziri asianze Mtwara na Lindi ambako gesi inatoka na ipo karibu?
Mheshimiwa Naibu Spika, Mtwara mjini kuna mitaa mingi sana kama vile Chipuputa, Kihoro, Komoro, Mbawala Chini, Lwelu, Dimbuzi, Kata ya Mtawanya, Likombe, Mitengo na Naliendele maeneo mengi nguzo za umeme hazijafika.
Mheshimiwa Naibu Spika, umeme unatoka Mtwara mjini ambapo kuna plant ya kufua umeme, Makao Makuu ya TANESCO Mkoa umeme hakuna. Wananchi wanauziwa nguzo kwa pesa nyingi ambayo hawana uwezo kutokana na hali ngumu kiuchumi kwa kuwa fursa za ajira hakuna.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Wizara kwa niaba ya wananchi wa Mtwara, kupeleka nguzo kata zote za Mtwara mjini na wasiwape wananchi mzigo wa kulipia nguzo kwa kuwa wanatakiwa kunufaika na rasilimali ya gesi ikizingatiwa ndiyo waangalizi wa miradi yote ya gesi ambayo ni muhimu kwa Taifa hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia pesa ya kuunganisha umeme hii iliyosemwa imepunguzwa hadi 99,000, bado ni nyingi, wananchi wengi hali zao ni mbaya kiuchumi, hivyo wanashindwa kumudu gharama hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba gharama hii ya 99,000 iondolewe kwa wananchi wa Mtwara na Lindi kwa kuwa rasilimali hii muhimu inalindwa na wananchi hawa, hivyo ni vyema wakalipa gharama za umeme na siyo kupewa mzigo mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, bomba la gesi liko nje sana, mimi kama Mbunge nimekuwa nawaasa wananchi walinde rasilimali hii muhimu kila siku, hivyo Wizara ihakikishe inafunika Bomba hili na hasa maeneo yaliyoathirika na mvua. Nimeeleza hili kwenye Kamati (TPDC) na leo naiomba Wizara bomba lipo nje sana Mtwara.
Mheshimiwa Naibu Spika, Msimbati inakotoka gesi yenyewe Serikali inashindwa kujenga barabara ya lami ya kutoka mjini. Ni jambo la ajabu sana hakuna kituo cha afya, maana ni kata kwa mujibu wa maeneo ya kiutawala, kwa nini Serikali isijenge kituo cha afya? Jengeni tafadhali.
Sambamba na hilo, Mtwara nzima hakuna hata shule moja au hospitali ambayo imejengwa kwa rasilimali hii inayotoka mkoani humo. Hivi naomba kuuliza, wananchi wa Mtwara wakidai haki hii ni dhambi?
Mheshimiwa Naibu Spika, namsihi sana Waziri katika hotuba yake kueleza asilimia 94 ni maendeleo, basi aiangalie Mtwara kwa namna ya kipekee kabisa ili malalamiko yaweze kwisha na Watanzania wanufaike na rasilimali hii muhimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mrabaha ni muhimu sana kwa wana Mtwara, mwekezaji wa kiwanda cha Mbolea anaomba gesi kwa kununua Msanga Mkuu apewe ili wana Mtwara wapate ajira, Dangote apewe gesi maana anaagiza makaa ya mawe Afrika Kusini. Pia Wizara ijenge shule ya gesi Mtwara ili kuondoa malalamiko.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuendelea kunipa uzima na afya njema, na leo naomba nichangie hoja hii ya maliasili na utalii kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Mikindani upo Manispaa ya Mtwara Mikindani ambalo ni jimbo langu. Mji huu ni mji wa asili ambao una magofu na vivutio vingi vya utalii ikiwemo Old Boma ambayo ilijengwa na Mjerumani kama ngome yake kuu ya ulinzi karne ya 19. Cha ajabu, mji huu umesahaulika, umeachwa na jambo la ajabu kabisa yanatangazwa maeneo ambayo hayana vivutio kama Mikindani. Namuomba Waziri aje na majibu juu ya kuutangaza mji huu kuwa ni mji wa kitalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtwara kuna fukwe nyingi nzuri sana ambazo kama Serikali ikitangaza watalii wengi wanaweza kuja Mtwara na hatimaye Taifa hili kupata kipato kikubwa kupitia sekta hii. Nimeuliza swali la utalii Mtwara tangu kipindi cha Kikao cha Kwanza katika Bunge lako hili mpaka leo sijapata majibu. Namtaka Waziri akija anieleze, yupo tayari hivi sasa kutangaza fukwe za Mtwara sambamba na kuzitambua katika Wizara yake kuwa kitovu kikuu cha utalii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Msimbati, Mnazibay kuna fukwe ambayo haipo duniani na kuna maua ambayo hayapo na hayaoti popote duniani isipokuwa Mnazibay tu. Nimuombe Waziri aje Mtwara nifuatane naye kama Mbunge, na asije kimya kimya ili nimuoneshe vivutio hivi vya utalii Mtwara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Lindi eneo la Mipingo, Kata ya Nangaru alichukuliwa mjusi na Wajerumani ambaye mabaki yake yapo Ujerumani. Tangu mwaka 1907 mpaka leo Wajerumani wanapata pesa nyingi kupitia mjusi huyu
mkubwa kuliko mijusi yote duniani. Serikali hii ya CCM ni lini itaenda kumrudisha mjusi huyu na kumleta Tanzania ili tunufaike na pesa za utalii?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyenzi Mungu, kwa kunijaalia uzima na afya njema na leo naomba kuchangia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa maandishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengi ya Mtwara Mjini hayapapimwa. Katika kikao cha kwanza Bunge lako hili la Kumi na Moja nimeuliza maswali juu ya upimaji na urasimishaji wa ardhi Mtwara Mjini ambalo mpaka sasa halijajibiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri atakapokuja kujumuisha hoja yake aje na majibu stahiki, ni lini maeneo mengi ya Mtwara Mjini yatapimwa na kurasimishwa? Swali hili ni muhimu sana kwa kuwa mtu akimiliki kipande chake cha ardhi kisheria anaweza kukopa benki kwa kutumia dhamana ile na kuweza kumsaidia kujikwamua kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtwara Mjini kuna migogoro ya ardhi mingi sana. Nashangaa Mheshimiwa Waziri ameweka/ametaja mgogoro mmoja tu ambao ni wa Libya. Siyo kweli kwamba Mtwara Mjini kuna mgogoro huu tu. Ipo mingi sana ambayo Serikali inakwepa kwa makusudi kabisa kupitia Maafisa wake wa Ardhi Mtwara Mjini wakiongozwa na Afisa Mipango Miji. Kuna eneo la Mji Mwema na Tangla, maeneo ambayo yalikuwa ya wananchi Serikali, imechukua tangu mwaka 2013 mpaka leo Serikali haijalipa fidia kwa wananchi wale. Wananchi hawana sehemu ya kulima na wengine wamebomolewa makazi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo tathmini iliyofanyika kila squire meter moja walilipia shilingi 250 tu. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri kwa nini Serikali hii inawadhulumu na kuwanyanyasa wananchi wa Mtwara?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua kwa kuwa ni miaka mitatu sasa tangu wananchi wamenyang‟anywa maeneo yao na hawajapewa fidia, je, Serikali ipo tayari kulipa fidia ya miaka mitatu ili ilingane na thamani ya ardhi ya sasa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wananchi wameibiwa katika tathmini iliyofanywa na watendaji wa Halmashauri na kupewa shilingi 250 - 450 kwa square meter moja, Serikali ipo tayari hivi sasa kufuta bei hii na kufanya tathmini upya kwa maeneo hayo ya Mji Mwema na Libya?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mgogoro huu ni mkubwa sana Mtwara Mjini na wananchi wamemwelezea mpaka Waziri Mkuu na kuahidi kuutatua, Mheshimiwa Waziri Lukuvi lini atakuja Mtwara Mjini ajionee mwenyewe kuliko kutegemea taarifa za uongo za Maafisa Ardhi ambao ndio wahusika wakuu wa utapeli huu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Plot Na. 99 ya Mzee Mayunga ekari 15 ambazo amenunua tangu miaka ya 1980 na amekuwa akilipia kila mwaka, leo Maafisa Ardhi wameshirikiana kuficha file la huyu mzee na wamemwambia kiwanja hicho hakitambuliki ili wauze eneo hilo kwa mtu mwingine. Plot hii Na. 99 anayonyang‟anywa ili wauze na wamethubutu mpaka kuficha file la mzee huyu ambalo lilikuwa Halmashauri, hii ni dhuluma ya hali ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba Mheshimiwa Waziri Lukuvi ahakikishe anamrudishia mzee huyu plot yake Na. 99 ambayo wameitisha watendaji wa Halmashauri na Mkoa wa Mtwara. Watendaji wa Ardhi Mtwara Mjini ni majipu makubwa yaliyoiva, tafadhali uje Mtwara kuyatumbua au mnasubiri mpaka watu waandamane na Mheshimiwa Rais aje kutumbua?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna msemo unaosemwa sana Mtwara kuwa kutokana na sakata la gesi Mtwara, viongozi wengi wamenunua viwanja kupitia hawa Maafisa wa Ardhi. Naomba sana msipokuja kuwatumbua watu hawa, usemi huu tutauamini sana kwamba mnawalinda kwa kuwa mnawatumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nyumba zinazoitwa za bei nafuu siyo kweli kwani bei yake ni ya juu sana. Mwalimu mwenye mshahara wa shilingi 100,000 kwa mwezi kama basic salary hawezi kununua nyumba hizi kwa shilingi milioni 40, shilingi milioni 50 na kuendelea, mnasema ni za bei nafuu? Hapana, hizi ni nyumba za wale wale wenye fedha nyingi ambazo sitaki kutumia jina maarufu sana lililopita mtaani kuwa ni nyumba za mafisadi. NHC iwezeshwe kujenga nyumba za bei nafuu.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujua katika mwelekeo wa Mpango huu, juu ya hoja ambayo tulijadili sana mwaka jana wakati wa Mpango wa Serikali 2016/2017, nayo ni kuhusu Mahakama ya Mafisadi. Suala hili limekuwa kimya nashangaa kwa nini wakati mafisadi wapo, wengine wamestaafu, ni kwa nini kwenye mwelekeo wa Mpango huu wa 2017 suala hili la Mahakama ya Mafisadi halipo?
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nataka kujua juu ya mwelekeo wa Mpango huu kuhusu ujenzi na ukarabati wa Mahakama Tanzania na hasa katika Jimbo langu la Mtwara Mjini Mahakama ni chakavu sana na hazikidhi haja. Je, ni lini suala hili litatatuliwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda vya korosho ni muhimu sana katika kuinua uchumi wa nchi hii hasa Mikoa ya Kusini. Naomba kujua ni lini Serikali itafufua Viwanda vya Korosho, Mikoa ya Kusini ili kuinua uchumi kwa kuongeza thamani ya korosho na bei?
Mheshimiwa Naibu Spika, mikataba ya gesi na mafuta ni muhimu sana kuletwa Bungeni ili ijadiliwe kabla ya kuingia kwenye mikataba hii. Kwa muda mrefu mikataba imekuwa haina tija kwa Taifa hili na mapendekezo ya Mpango huu suala hili halipo, naomba majibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la ardhi ni muhimu sana maana kumekuwa na migogoro mingi ya ardhi hapa nchini. Kwa mfano, kumekuwa na utaratibu wa Serikali kuchukua ardhi kwa wananchi na kukaa muda mrefu bila kulipa fidia kwa mfano Mtwara Mjini tangu mwaka 2012 mpaka leo UTT ilipima viwanja Mji Mwema ambako ni mashamba ya wananchi hawajalipwa. Hili ni jambo la hatari sana, naomba majibu tafadhali.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia elimu ndiyo msingi wa maendeleo wa nchi yoyote ile duniani. Sera ya Elimu bure iangaliwe upya ili shule ziweze kujiendesha. Shule zinapata OC ya Sh. 27,000/= tu kwa mwezi itaweza kuendesha ofisi na shule kweli? Ni jambo la ajabu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, mikopo ya elimu ya juu iangaliwe upya ili kila Mtanzania mwenye sifa ya kusoma elimu ya juu apate mkopo kama Mheshimiwa Rais alivyoahidi. Kunyima mikopo watoto maskini kama ilivyo kwa mwaka huu ni jambo hatari sana kwa mustakabali wa Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana miundombinu ya barabara kama vile reli kutoka Mtwara Mjini hadi Mchuchuma na Liganga kwenye chuma na makaa ya mawe iwekwe kwenye Mpango wa mwaka 2017/2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, utanuzi wa Bandari ya Mtwara ufanyike kwa haraka ili kuinua uchumi wa nchi yetu. Bandari hii haihitaji gharama sana kwa kuwa ni natural harbour, Serikali itenge fedha haraka kwa ajili ya utanuzi wa bandari hii. Sijaona suala hili kwenye mapendekezo ya Mpango huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo barabara ya Mtwara - Newala imetengewa fedha lakini mpaka sasa hata robo kilomita haijatengenezwa, ni jambo la ajabu sana. Naomba barabara hii ianze kujengwa tafadhali.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika mwelekeo wa mpango huu wa mwaka 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na suala hili la mashirika ya umma, Mama Lulida alikuwa kazungumza hapa siku ya jana akieleza kwa masikitiko makubwa sana. Alikuwa amezungumza kwamba baadhi ya mashirika ambayo takribani tuko nayo Tanzania kwa kiasi kikubwa mashirika ya umma yanaendeshwa kihasara. Yapo mashirika mpaka hivi sasa ninavyozungumza, miradi na mali walizokuwa nazo takribani na madeni yote madeni waliyokuwa nayo inazidi mali walizokuwa nazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa mfano Shirika la Mbolea Tanzania (TFC), wakati tunapitia mpango wao katika Kamati ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma, unaweza ukashangaa sana kwamba deni walilokuwa nalo ni takribani shilingi bilioni 66. Lakini madeni, mali waliyokuwa nayo, mali nzima ukiuza majengo na kila kitu wana mali zenye thamani ya shilingi bilioni 23.8. Kwa hiyo, unaweza ukaona ni jambo la ajabu sana kwamba haya mashirika yamefilisika, Serikali, Waziri wa Fedha na Mipango, sijaona wakati napitia taarifa yake hapa na mwelekeo wa mpango hajaeleza kinaga ubaga kwamba kuna mkakati gani wa kuhakikisha kwamba anafufua mashirika haya ya umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tumeona hapa na Wabunge wengi wamezungumza kwa kiasi kikubwa sana kwamba Serikali imekuwa ikikopa kwenye mashirika haya, mashirika ya fedha na mashirika ya umma ya ndani ya nchi. Tuhakikishe kwamba tunaweka mikakati kabambe ili haya mashirika yaweze kufufuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia uendeshaji wa haya mashirika, yanaendeshwa kinyume na taratibu za kimaadili. Kwa mfano, mwaka jana tuliweza kuzungumza katika mpango hapa kwamba yapo baadhi ya mashirika yanatumia madaraka yao vibaya. Kwa mfano, Shirika la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kiliweza kuingia mkataba na mwekezaji kotoka Botswana, mkataba ambao haunufaishi Serikali. Lakini jabo la ajabu tuliweza kuzungumza katika mpango tukaongea kwenye bajeti hapa, lakini kwenye mpango aliokuja nao Mheshimiwa Mpango hapa hakuna mwelekeo wowote kwamba kuna nini kitafanyika ili kuhakikisha ya kwamba haya mashirika ambayo yanawekeza kinyume na taratibu na sera za uwekezaji Tanzania na kwamba hayaingizi kipato katika Serikali yetu yanachukuliwa hatua stahiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ukisoma mkataba wa Mlimani City ambao Mbotswana aliingia kwa kiasi kikubwa yule jamaa anakusanya pesa nyingi sana. Lakini jambo la ajabu Serikali inakusanya asilimia 10 tu ya mapato yote na hakuna uhakiki wowote ambao unafanyika wa kuhakikisha kwamba kile anachokusanya kinafanyiwa mahesabu sawasawa ili ile asilimia 10 ama anapata zaidi ya ile asilimia 10 anayotoa Serikali ya Tanzania iweze kunufaika. Ni kwa sababu mipango yetu haioneshi namna gani tunaweza kuweka mazingira ya kiuwekezaji ambayo hawa wawekezaji kutoka nje wanaweza kuliingizia Taifa hili pato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia suala zima ambalo niliweza kuzungumza katika mpango uliopita, kwamba mashirika haya kwa mfano PSPF, wamekuwa wakiwekeza kwenye viwanja kwa kiasi kikubwa sana na wakati wananunua hivi viwanja wananunua square meter moja kwa pesa nyingi sana kinyume kabisa na bei halisi na halali katika nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, niliweza kueleza hapa, na leo naomba nilizungumze tena, Shirika la PSPF waliweza kununua kiwanja Mjini Mwanza square meter moja walinunua shilingi 250,000, ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lakini ukija kule Mtwara pia, wamenunua square meter moja shilingi155,000, maeneo ambayo bei hiyo haijafika, ni kwa sababu mashirika haya yanawekeza kiufisadi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana katika mpango huu tuhakikishe ya kwamba haya mashirika yanapitiwa upya na waweze kuja na mpango kabambe ambao utaweza kuinua uchumi wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze pia suala zima la PPP (sekta binafsi). Tumeweza kuzungumza kwa muda mrefu katika Bunge hili kwamba hawa wawekezaji kutoka nje ya nchi ndio ambao wanategemewa sana na Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi, ambao tunawategemea wajenge viwanda na vile viwanda viweze kutoa ajira. Lakini cha ajabu mazingira mpaka leo tunavyozungumza sio rafiki kwao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilizungumza hapa wakati wa mpango uliopita na nikazungumza wakati wa bajeti pia, kwamba tunao wawekezaji wamejenga viwanda, kwa mfano mwekezaji huyu Aliko Dangote kule kiwanda cha saruji Mtwara, lakini mpaka leo huyu mwekezaji ananyimwa kupewa gesi ambayo anaweza kuitumia kama nishati ili sasa bei ya saruji iweze kushuka na saruji iweze kuzalishwa kwa wingi Tanzania na watu wengi waweze kujenga, ni jambo la ajabu sana. Tunaomba sana hawa wawekezaji wapewe gesi, mwekezaji huyu wa saruji apewe gesi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kuna mwekezaji wa mbolea ambayo ni kwa muda mrefu hivi sasa, tuliongea wakati wa mpango, wakati wa bajeti pia tulizungumza, ambaye anaomba apewe gesi aweze kujenga kiwanda cha mbolea Msangamkuu pale Mtwara Vijijini. Mpaka leo yule mwekezaji hajapewa hiyo gesi. Tunaomba Waziri Mpango atakapokuja kuhitimisha atupe maelezo kwamba mpango ukoje wa mwakani wa kuhakikisha kwamba hawa watu, hawa wawekezaji wanapewa hii gesi ili iweze kunufaisha katika sekta hii ya viwanda na kweli iweze kuinua uchumi wa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nizungumze suala zima la miundombinu ambalo tumezungumza kwa kiasi kikubwa sana, lakini sijaona mkazo katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mpango hapa wakati anazungumza. Tulizungumza sana kwamba uchumi wowote hauwezi kuimarika popote duniani kama miundombinu ni hafifu. Tunayo miundombinu ya barabara ambayo imesimama hivi sasa na tuliweza kuzungumza, kwa mfano barabara kadhaa za hapa nchini kama ile barabara ya Ulinzi kule Mtwara ambayo sijaona kwenye mwelekeo wa mpango wapi imewekwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliweza kuzungumza pia reli ya kutoka Mtwara kuelekea Liganga na Mchuchuma ambayo Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumza. Kwa hiyo, niombe sana kwamba kama kweli tunahitaji kufufua uchumi tuhakikishe kwamba tunajenga miundombinu imara ili kweli Watanzania waweze kuondokana na umaskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa sababu ya muda.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na pia nitoe shukrani zangu za dhati kwa Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kusaini ujenzi wa gati moja la Bandari ya Mtwara ambayo ndiyo chachu ya uchumi Kanda yote ya Kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Mtwara Corridor inategemea kwa kiasi kikubwa ujenzi huu wa bandari ulioanza kwa kusafisha maeneo ya ujenzi huo. Ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri ni kwamba, ahakikishe mara tu baada ya kumalizika ujenzi huo, basi magati mengine yawekwe kwenye orodha ya kujengwa ambayo ni matatu. Gati moja halitoshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwamba utanuzi wa bandari uendane na ujenzi wa reli ya Kusini ambayo itaanzia Mtwara – Liganga – Mchuchuma – Mbamba Bay na nchi nyingine za Kusini mwa Afrika. Ujenzi wa reli hii utasaidia sana kufungua uchumi na Bandari yetu ya Mtwara itapata mizigo ya kutosha, hivyo kuliingizia Taifa pato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mitandao ya simu kwa baadhi ya maeneo ya Mtwara Mjini haipo. Mfano, Mbawala Chini, Mkangala, Naulongo, Namayanga, Dimbuzi; maeneo haya network hakuna kabisa na yapo Mtwara Mjini. Sambamba na hilo, Mtwara Mjini hakuna network ya TBC kabisa. Hii inafanya Wanamtwara wakose huduma ya taarifa mbalimbali hivyo kuwa nyuma ya wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Ulinzi; mwaka 2016 tuliongea sana juu ya umuhimu wa barabara hii ambayo inaanzia Mtwara Mjini mpaka Ruvuma. Tunaomba iwekwe kwenye bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Viwanja vya Ndege ambavyo havimilikiwi na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, naomba kujua, kwa nini Serikali imeruhusu hili? Haioni kama ni hatari kwa Taifa letu na uchumi? Naomba Wizara itoe tamko juu ya hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna eneo ambalo hivi sasa Jijini Dar es Salaam ambalo lina msongamano mkubwa kama Mbagala hasa njia panda ya Charambe. Hapa kuna ulazima wa kujenga flyover haraka sana. Naomba bajeti ieleze, ujenzi wake utaanza lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Kilwa Road hasa eneo la Somanga - Nangurukuru imeharibika sana na ina mashimo na mabonde makubwa na sioni ujenzi au ukarabati kabambe unafanyika hasa eneo hili. Tunaomba majibu ya Waziri ili nayo ianze kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya uchumi imesainiwa kwa kilomita 50. Tunaomba Mkandarasi asimamiwe kama alivyosema Mheshimiwa Rais alipokuja Mtwara Machi, 2017 na kusema kuwa Mkandarasi hayuko sharp, tunaomba asimamiwe barabara hii ijengwe haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa sasa kuna utanuzi wa bandari unaanza, tunaomba Wanamtwara Kusini tupatiwe usafiri wa meli hasa kwa ajili ya mizigo, kwa kuwa barabara inaharibika kwa cement kupitia barabara ya lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Uwanja wa Ndege wa Mtwara ni mbovu, hauna taa za kuongozea ndege; ndege hazitui usiku na inaleta usumbufu sana sambamba na kudumaza uchumi. Naomba bajeti hii ianze kukarabati na kuweka taa katika bajeti hii.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Afya kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Mtwara ya Mkoa haina X-Ray na iliyopo ni mbovu. Naomba kuuliza, kwa nini hospitali hii ya Mkoa wa Mtwara haipelekewi X-Ray ya uhakika wakati kila mwaka tunaongea hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali inayotumika kama ya Wilaya inaitwa Hospitali ya Likombe iliyopo Mtwara Mjini, kwa nini haina X-Ray mpaka leo? Bajeti ya mwaka 2016/ 2017 Mheshimiwa Waziri alisema hospital hizi za Mtwara Mjini zitapelekewa X-Ray, mpaka leo bado. Kwa nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Waheshimiwa Wabunge wamepewa Ambulance: kwa nini Mtwara Mjini Wizara haijatuletea Ambulance hizo? Naomba Wizara itueleze Wanamtwara Mjini, juu ya Ambulance kwa ajili ya Tarafa ya Mikindani na Tarafa ya Mjini ili kuondoa kero na adha kubwa wanayopata wagonjwa wa Mtwara Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wodi ni chache katika Hospitali ya Likombe ambayo ndiyo Hospitali ya Wilaya, Mtwara Mjini. Naomba kujua, ni lini wodi zitaongezwa, nyumba za Madaktari na Wauguzi wa Hospitali ya Likombe?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mazingira ya Wodi za Hospitali ya Mkoa (Ligula) siyo nzuri kabisa, naomba hospitali ipakwe rangi, vyoo vitengenezwe na huduma ya maji katika Hospitali ya Ligula yarekebishwe haraka iwezekanavyo, maana hali ya vyoo ni mbaya sana katika hospitali hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye taarifa ya Waziri katika kitabu chake kinaonesha Mtwara Mjini dawa zinapatikana kwa asilimia 92% kitu ambacho ukienda Hospitali ya Ligula ya Mkoa na Wilaya hali ni tofauti kabisa. Wagonjwa wanaambiwa baada ya siku mbili tu dawa zimekwisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ufafanuzi, kwa nini tunaambiwa dawa zinapatikana kwa asilimia kubwa, lakini hospitali dawa hakuna na zikiwepo zinakwisha kwa siku mbili tu?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Spika, michezo na hasa mpira wa miguu ni mchezo unaotoa ajira ya pesa nyingi kwa wiki au mwezi. Wapo wachezaji wengi duniani kutoka Afrika ambao wanalipwa mabilioni ya fedha kwa wiki mfano Samweli Eto wa Cameron na Didie Drogba wa Ivory Coast. Wizara ihakikishe inainua michezo kwa kuanzisha timu za vijana kila wilaya ili kutengeneza vipaji ambavyo vitaweza kupata ajira ya kucheza mpira wa kitaaluma ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, Viwanja wa Michezo; ili michezo ikue lazima kuwe na viwanja vizuri vyenye ubora.

Mheshimiwa Spika, Viwanja vya Michezo vya Kikanda; viwanja hivi ni muhimu kujengwa ili kuwe na uwiano katika nchi. Kanda ya Kusini ikiwa na uwanja pale Mtwara itachochea wananchi kupenda michezo na kuinua uchumi wa vijana na Watanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, michezo mashuleni ndio chachu ya kuinua vipaji vya Watanzania. UMISETA na UMITASHUMTA iwekezwe ipasavyo. Wizara itenge pesa zipelekwe mashuleni badala ya kuwabebesha mzigo huu TAMISEMI peke yake na hata TAMISEMI hawapati pesa mashuleni kwa ajili ya michezo badala yake wanabebeshwa mizigo Wakuu wa Shule na Walimu Wakuu mzigo ambao hawajatengewa bajeti yake.

Mheshimiwa Spika, ili timu ya shule iende katika kituo cha tarafa au cha wilaya kilichotengwa kwa ajili ya michezo kuna gharama kubwa mfano chakula na gharama za wasimamizi. Wizara itenge pesa za UMISETA na UMITASHUMTA ili iweze kufanyika effectively maana kinachofanyika hivi sasa ni kuondoa lawama tu na sio effective kwa sababu haifanyiki kwa siku zinazotakiwa kwa kukwepa gharama.

Mheshimiwa Spika, Wizara iweke siku maalum ya maonyesho ya ngoma za asili ambayo itafanyika kikata, wilaya, mkoa na kitaifa hii itasaidia kufufua utamaduni wetu nchini na pia kujitangaza kwa mataifa na baadaye kuingiza pato la Taifa kupitia utamaduni wetu.

Mheshimiwa Spika, Mtwara na Lindi hakuna frequency za TBC (television) na zinapatikana kwa taabu sana. Naomba Wizara iweke mawimbi ya Television hizi Mtwara (TBC1 na TBC2). Mimi tangu TBC2 imewekwa binafsi sijawahi kuiona na wala sijui inafananaje. Katika maeneo yote imefungwa isipokuwa Mtwara na Lindi tu.

Mheshimiwa Spika, si kweli, kwamba waandishi wanavamiwa nchini, isipokuwa waandishi wa habari wanapokuwa kazini wanaweza kupata ajali kama mfanyakazi yeyote yule na sio kama inavyodaiwa na baadhi ya Wabunge kwamba waandishi wanavamiwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu na Kiti chako, napenda kuchangia Wizara hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kuhusu Mji wa Mikindani. Mji huu ni wa kale wenye majengo mengi na historia kubwa ya asili tangu wakati wa miaka 200 BC. Mji huu umeachwa na historia hii ya pekee nchini inatoweka bila sababu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ni kuhusu Trade Aid. Kuna taasisi ya Kiingereza inaitwa Trade Aid ambayo ni charity group inayofanya kazi ya kuangalia baadhi ya majengo kwa maslahi yao binafsi na sio Taifa kama Taifa. Kampuni hii ya Kiingereza wanakarabati baadhi tu ya majengo na kutangaza nje ya nchi, kwa bahati mbaya kila kinachokusanywa ni chao kwa kigezo kuwa wanasaidia jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kusaidia jamii ni jambo jema, lakini Serikali lazima ikarabati majengo ya kale ya Mikindani sambamba na kujenga kituo cha watalii Mtwara ili kuvutia watalii kufika Mtwara Mjini eneo la Mikindani. Ukikarabati majengo haya na kujenga vivutio vingi ni wazi kwamba vijana wetu watapata ajira kwa kuhudumia wageni mbalimbali na hivyo kuondoa umaskini Mtwara Mjini na Tanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu ni kuhusu ukarabati wa jengo la miaka 100. Kuna jengo ambalo linasemwa limekarabatiwa lakini jengo hili kubwa na muhimu halijakarabatiwa bali limezibwa milango tu. Wito wangu kwa Serikali, Waziri aje Mtwara – Mikindani kujionea hali; jengo hili muhimu likarabatiwe na Serikali siyo kuiachia Trade Aid na Mikindani Tourist Center ijengwe Mtwara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, utalii wa Kituo cha Mikutano Arusha (AICC). AICC Arusha ni nguzo muhimu ya watalii wanaokuja kwa ajili ya mikutano nchini. Kupitia kituo hiki cha AICC, Serikali inakusanya pesa nyingi sana bahati mbaya pesa hizi zinarudishwa kwa Mkurugenzi wa AICC na kufanya ukarabati ambao hauko sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, AICC wamekarabati Ukumbi wa Simba kwa shilingi bilioni 3.5 lakini wamejenga majengo marefu yenye ghorofa sita kwa shilingi 1.8. Ukarabati wa Ukumbi wa Simba umetumia pesa vibaya kuliko kujenga jengo kubwa jipya. Wito wangu CAG aende akakague ukarabati huu wa AICC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema haya kwa sababu sheria iliyoanzisha Shirika hili la AICC ni kuendeleza ujenzi wa kumbi nyingine za mikutano nchini. Kama ukarabati tu unazidi ujenzi, sidhani kama tunaweza kujitanua katika utalii wa mikutano. Naomba CAG akakague ukarabati wa AICC Ukumbi wa Simba. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia dakika hizo tano ulizonipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwamba ili tuweze kuwa na wanafunzi ambao wanafundishika vizuri level zote za elimu, iwe sekondari kwa maana ya kwamba O-level na A-level lakini Vyuo vya Ufundi, Universities ni lazima tuanze na uwekezaji katika elimu, pale tunasema Pre–Primary Education yaani Elimu ya Msingi na Elimu ya Chekechea kabisa kule chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanafunzi yeyote ambaye amefundishwa vizuri, akiwa chekechea, elimu ya awali, mtoto huyu atakuwa na uwezo mzuri wa kuweza kufundishika vizuri atakapokuwa Shule ya Msingi. Akifundishwa vizuri shule ya msingi, atafundishika vizuri sekondari, elimu ya kidato cha nne lakini pia kidato cha tano na kidato cha sita, hata anapofika level ya elimu ya juu, kwa maana ya Chuo Kikuu, atafundishika vizuri na mwisho wa siku tutaweza kuwa na wasomi wazuri katika nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashangaa sana kwa kuona kwamba sasa hivi katika nchi yetu kuna mkanganyiko wa usimamizi wa elimu. Tuna Wizara ya Elimu, tuna Wizara ya TAMISEMI, mimi nashangaa sana na nazungumza haya nikiwa Mwalimu, lakini pia nikiwa Msimamizi wa Elimu, kwamba tunavyoangalia Wizara ya Elimu, kwamba imepewa kusimamia miongozo, ni jambo la ajabu sana. Tunataka Wizara ya Elimu isimamie elimu, tunataka Wizara ya Elimu isimamie miundombinu ya elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ninavyozungumza, ukija Mtwara Mjini pale kwa mfano, tuna Shule ya Msingi Mbae, ina madarasa mawili; haina vyoo, lakini ina wanafunzi zaidi ya 630 halafu leo hii tunasema kwamba eti wanafunzi Mtwara na Lindi hawafanyi vizuri katika mitihani yao. Hatufanyi vizuri kwa sababu hatuna miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine Mikoa ya Mtwara na Lindi hatufanyi vizuri katika elimu kwa sababu pia Walimu hawatoshi. Shule za Msingi, Shule za Sekondari hatuna Walimu wa kutosha. Tunaomba Wizara itusaidie hili. Mkoa mzima wa Mtwara tuna upungufu wa Walimu, hawatoshi, watuletee Walimu tuweze kufanya vizuri kama ilivyo katika mikoa mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa dakika zangu ni chache, naomba nizungumze suala hili ambalo Serikali ya Awamu ya Nne ililianzisha. Mimi nilikuwa Msimamizi wa elimu wakati huo, nilikuwa Mkuu wa Shule, Mchinga Sekondari kwa miaka mitano. Tulipewa miongozo ya kusimamia elimu kupitia BRN, lakini tangu mwaka 2016 hatuoni kuna nini? Kwa nini huu mpango unaoitwa BRN (Big Result Now) ambao Serikali iliiga kutoka nchi ya Malaysia. Ule mpango ulikuwa ni mzuri kwa sababu ule mpango ulikuwa unaleta usimamizi katika elimu kwamba Mwalimu anapofanya vizuri, anapofundisha vizuri, mwisho wa siku anakuja kupewa motivation kupitia Wizara ya Elimu na TAMISEMI, lakini sasa hivi BRN haitajwi kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwamba kama kweli tunahitaji matokeo mazuri katika elimu, turudishe huu mpango wa BRN katika elimu, ulikuwa unasaidia sana kuchochea Walimu kuweza kufanya kazi, Walimu kuweza kufundisha kwa sababu walikuwa wanapewa motisha pale ambapo wanafaulisha vizuri masomo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili la kuboresha elimu linaendana sambamba na kuboresha maabara. Kulikuwa na mpango wa kujenga maabara, nami kipindi kile nikiwa Mkuu wa Shule, tuliweza kujenga maabara nyingi sana, lakini mpaka leo tunavyozungumza zile maabara hazina vifaa, hazina kemikali, hazina Walimu wa sayansi ambao watakuja kufundisha yale masomo ya sayansi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama kweli tunahitaji kuipeleka elimu yetu mbele, lazima Wizara ya Elimu iliangalie suala hili la maabara tupeleke kemikali mashuleni. Jambo la umuhimu zaidi ni usimamizi wa elimu kwa Wakuu wa Shule. Wakuu wa Shule ndiyo nyenzo pekee ambapo tukiwatumia ipasavyo, hawa Walimu wanaweza kusimamia elimu yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango huu wa elimu bure hivi sasa hasa katika Shule za Mikoa ya Lindi na Mtwara, hakuna michango inayokusanywa, hakuna pesa za ulinzi wala taaluma na hizi shule maeneo mengi ziko vijijini, ziko maeneo ya vijiji na Halmashauri zenyewe…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu na Kiti chako, napenda kuchangia Wizara hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, korosho wakulima hawajalipwa; kutokana na taarifa za TAKUKURU mwaka 2015/ 2016 wakulima wa Mkoa wa Mtwara wa zao la korosho hawajalipwa bilioni thelathini na vyama vya msingi. Hali hii imekuwa inawavunja nguvu sana wakulima kwa kuwa Serikali ilijigamba kwa kiasi kikubwa kuwa Mfumo wa Stakabadhi Ghalani unamsaidia mkulima. Hata hivyo, pamoja na wizi wote huu kwa wakulima wanyonge, hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa kwa wahusika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Malipo ya Korosho 2016 Mtwara Mkindani; Mtwara Mjini kuna AMCOS mbili, moja ya Naliendele na nyingine ya Mikindani. Wananchi wameniambia wamepeleka korosho zao kwenye vyama hivi vya msingi lakini cha ajabu;

(a) Baadhi yao mpaka sasa hawajalipwa.

(b) Kuna minada mine ambayo ilifanyika mfululizo lakini vyama hivi vimelipwa minada ya tatu na nne (ya mwisho na kuacha ya kwanza ambayo ilikuwa na bei kubwa).

(c) Korosho kuuza kwenye mnada Sh.4,000/= lakini wananchi wamelipwa Sh.3,100/= (elfu tatu na mia moja) tu au chini ya hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wakulima hawa walipwe pesa zao haraka iwezekanavyo na wahusika wote wachukuliwe hatua stahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Pembejeo ya Salfa (sulfur). Naomba sana Serikali inunue pembejeo na kugawa bure kama ilivyoahidi. Kuna wakulima ambao wanahitaji salfa ya maji ambayo wanadai ni nzuri kuliko ya unga, hivyo, wasikilizwe wakulima hawa juu ya salfa hii ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Uvuvi Mtwara. Mtwara kuna Bahari ya Hindi yenye samaki wengi sana. Naomba Wizara ijenge viwanda vya samaki kama ilivyo Mwanza. Viwanda vya samaki vikijengwa itasaidia watu wetu kupata ajira na kuondokana na umaskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Zana za Kisasa za Uvuvi; Wizara hii kazi zake ni pamoja na kuhakikisha inawasaidia Watanzania wavuvi waweze kuvua uvuvi wa kisasa. Naomba Wizara itenge pesa ya kutosha ili kununua zana za uvuvi, mfano boti za kisasa na mashine za boti hasa kwa wavuvi wa Mikindani, Misete na Kianga ambako wanavua uvuvi ambao hauna tija kwa sababu hawana vifaa vya kisasa. Serikali itenge pesa za kutosha kwa ajili hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Cooperate Social Responsibility. Wizara kwa mwaka 2016/2017 imekusanya pesa nyingi sana za mapato ya korosho, lakini jambo la ajabu hivi vyama vya msingi havina mchango wowote kwenye kusaidia jamii. Hakuna shule hata moja kupitia fedha nyingi zinazokusanywa katika korosho, Bodi ipo, vyama vya ushirika vipo wanakusanya pesa nyingi sana, kwa nini hawasaidii katika elimu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara itoe miongozo ili pesa za korosho Kusini zitumike kuinua kiwango cha elimu Kusini. Serikali inakusanya pesa nyingi kwenye korosho kuliko zao lolote lile nchini, vyama vya ushirika vya korosho viwe vinasaidia elimu kwa lazima Mtwara.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia Wizara hii. Kabla ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kuendelea kunipa afya njema, lakini kwa namna ya pekee kabisa, nashukuru kiti chako kwa kuendelea kutenda haki hasa katika upande wetu huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mtaalam mmoja anaitwa Kunzi mwaka 1988/1989 aliandika kitabu chake cha Managerial and Planning ambacho aliweza kueleza kwamba “failure to plan is planning to fail,” yaani siku zote wewe ukishindwa kupanga jambo maana yake ni kwamba unapanga kufeli. Alizungumza Kunzi maneno haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma kitabu hiki cha hotuba hapa, kwa kiasi kikubwa naomba niishukuru Wizara hii kwamba imeweza kuondoa tozo nyingi sana katika zao ambalo kwa kiasi kikubwa linalimwa Mikoa ya Mtwara na Lindi; zao la korosho. Tozo nyingi sana zimeondolewa. Tunashukuru sana Wizara hii kwa sababu kupitia kuondoka ama kuondolewa kwa hizo tozo, hivi sasa bei ya korosho iko juu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru pia Wizara hii kwa kuhamasisha wanunuzi wengine kwamba mwaka wa 2016/2017 wanunuzi wa korosho waliweza kuongezeka. Miaka yote tulikuwa na Wahindi tu, lakini mwaka 2016 tumeweza kuona Vietnam na watu kutoka Uturuki wamekuja kununua korosho Mikoa hii ya Mtwara na Lindi na Tanzania kiujumla; na bei sasa imekuwa kubwa kwa sababu kuna ushindani huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo yote, naomba nizungumzie changamoto kadhaa ambazo zipo katika zao hili la korosho hasa mwaka 2016 kwa maana kwamba msimu wa mwaka 2016/2017.

Mheshimiwa Naibu Spika, wapo wakulima wameweza kutueleza Wawakilishi wao, sisi Wabunge; kwa mfano, pale kwangu Mtwara Mjini tuna AMCOS mbili; kuna AMCOS ya Mikindani na kuna AMCOS ya Naliendele. Hivi Vyama vya Msingi vimechukua korosho za wakulima lakini kwa bahati mbaya wameweza kuchukua hizo korosho kupitia minada. Imefanyika, minada zaidi ya minne; mnada wa kwanza mpaka wa nne.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la ajabu sana, la kushangaza ambalo naomba Mheshimiwa Waziri akija atuletee majibu ya kina kwa wananchi hawa, kwamba hizi AMCOS zimeweza kulipa minada miwili ya mwisho, yaani mnada wa tatu na mnada wa nne na wakaacha mnada wa kwanza na wa pili, ambao bei zake zilikuwa ni kubwa kuliko hii minada miwili ya mwisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba akija Mheshimiwa Waziri atupe taarifa, kwa nini hawa wanunuzi wa korosho kupitia hivi vyama vya msingi? Wameruka bei zile kubwa ambazo zilikuwa ni Shi.4,000/= na ilitangazwa kupitia vyombo vya habari kwamba korosho sasa mwaka huu zimepanda, zinauzwa Sh.4,000/= kwa kilo, lakini hawakulipa bei hiyo ya Sh.4,000/= wakaja kulipa minada ya mwisho ambayo imekuja kununuliwa na Wahindi kwa bei ya Sh.3,700/= na Sh.3,600/=.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa anipe maelezo ya kina katika hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo naishukuru Wizara hii, imeelezwa hapa kwamba mwaka huu 2017/2018 kutatolewa pembejeo za sulphur bure kwa wakulima wa Korosho. Nimesoma kitabu chote hiki mpaka kwenye bajeti yenyewe ambayo ni shilingi bilioni 266, sijaona hata eneo moja hilo ambapo wameweza kueleza kwamba pesa hiyo ya kununua sulphur ambayo itaenda kugawiwa bure kwa wakulima wa korosho, imekuwa indicated kwenye hiki Kitabu cha bajeti. Sasa isije ikawa tunazungumza tu lakini kwenye bajeti humu hakuna.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili suala la kugawa pembejeo bure, ni suala kubwa sana kwa sababu wakulima wa korosho ni wengi; na kama likifanikiwa hili kwa kweli Wizara hii itakuwa imefanya jambo kubwa sana. Kwa hiyo, naomba maelezo ya kina, hizi pesa zimewekwa katika fungu gani? Kama hazijawekwa zinapatikana sehemu gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala hili la Taasisi ya TFC, Taasisi hii ya kushughulikia pembejeo na mbolea Tanzania. Ni Taasisi ambayo wakati tunapitia kwenye Kamati yetu ya PIC ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, tuliweza kupitia documents zake. Ni Taasisi mfu, yaani wanapewa ruzuku kila mwaka, wanapewa pesa nyingi na Serikali, lakini wana madeni kweli kweli! Hawana hata kiwanda kimoja cha kuzalisha mbolea Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashangaa sana, kwa nini tunaendelea kuienzi na kuilea TFC? Kwa nini isifutwe? Naomba Mheshimiwa Waziri aje atueleze, kwa nini hili Shirika linaendeshwa kihasara? Halileti tija kwa Taifa letu, halisaidii wakulima lakini bado tunaendelea kulilea. Naomba maelezo ya kina kutoka kwa Mheshimiwa Waziri wa Kilimo na Mifugo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumze pia suala hili la uvuvi. Tunashukuru hivi sasa pale Mtwara Mjini kuna jengo lile ambalo inasemekana kwamba litakuwa ni Chuo cha Uvuvi. Ni muda mrefu hivi sasa, lile jengo limejengwa, hakuna vifaa, hatuoni mkakati wowote wa kuhakikisha kwamba kile chuo kweli kinaanza, wanafunzi wanaanza kusoma pale. Mwaka 2016, tuliongea kwenye bajeti hapa, walieleza katika bajeti yao pia kwamba hiki Chuo kitaanza. Sasa naomba kujua hiki Chuo cha Uvuvi Mikindani pale kitaanza lini?

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, maeneo yale ya Kusini mwa Tanzania lakini maeneo yale ya Magharibi kule, tuna bahari hii ambayo ni bahari ya Hindi ambayo ina samaki wengi sana. Nilieleza hapa mwaka 2016 kwamba Waingereza wanasema maeneo yale ya Kusini yanaitwa, tunasema it is just virgin sea; yaani ni bahari bikira ambayo ina samaki ambao hawajawahi kuvuliwa tangu tupate uhuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujua kwamba Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba inanunua vifaa vya uvuvi kwa wavuvi wa maeneo haya ya Kusini? Pia hata kule Ziwa Tanganyika kuna samaki wa kila aina; kule Kigoma ukienda kuna samaki wa kila aina, lakini hawana vifaa vya kisasa vya uvuvi. Naomba Wizara itueleze kwamba mkakati wao wa kusaidia wavuvi ukoje katika kuwasaidia kununua zana za kisasa za uvuvi?

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusema kwamba wakati tupo katika RCC pale Mtwara tuliweza kupewa taarifa na TAKUKURU kwamba mwaka 2015/2016 wakulima wa Kkrosho wa maeneo ya Mtwara wanadai vyama vya msingi shilingi bilioni 30. Yaani vyama vya msingi vimechukua korosho kwa wakulima, wameenda kuuza, lakini hawajawapa pesa wananchi wale. Shilingi bilioni 30 hazijalipwa, kwa taarifa ya TAKUKURU.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Kiti chako kiamrishe hii Wizara ipeleke TAKUKURU waende kukagua kwenye Vyama hivi vya Msingi kwa sababu wanawaibiwa wakulima sana. Tulivyohoji, tulivyowauliza, wakatuambia siyo shilingi bilioni 30 ni shilingi bilioni 11, lakini taarifa zinasema
na chombo cha uhakika kabisa, TAKUKURU kwamba wakulima wameibiwa shilingi bilioni 30. Tunaomba CAG aende akakague Vyama hivi vya Msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho, kuna taarifa ambazo siyo rasmi sana, lakini zinazungumzwa na wafanyabiashara wa korosho. Naomba Mheshimiwa Waziri hapa akija atupe majibu kwamba mwaka 2016 kulikuwa na fraudulent iliyofanyika bandari ya Mtwara ili iweze kuzuiwa kusafirisha Korosho kupitia bandari ya Mtwara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na wajanja inasemekana ndani ya Wizara yake ambao walikuwa wanaweka vingingi; na inasemekana kwamba ilikuwa kusafirisha korosho kutoka Mtwara tani moja kuelekea Soko la Dunia, ilikuwa ni dola karibu 14,000; lakini kutoa mzigo kutoka bandari ya Dar es Salaam ilikuwa ni dola 400.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba tupate ufafanuzi, kama hilo ni kweli kwa nini iwe hivyo? Lengo ni nini? Kuzuia bandari ya Mtwara isiweze kusafirisha korosho au tatizo ni nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atuletee majibu ya kina atakapokuja kuhitimisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haya, naomba kushukuru sana kwa kunipa nafasi. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze tu kwamba, Mtume Muhammad Karne ya sita alishawahi kusema kwamba “Manla-yashkurunnasa la-yashkurullah” yaani yule ambae hawezi kumshukuru binadamu mwenzake basi hata Mwenyezi Mungu kwa neema alizompa hawezi kumshukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti naomba nichukue fursa hii kukushukuru wewe na kiti chako, lakini kwa namna ya kipekee kabisa kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuja Mtwara kuzindua mradi mkubwa wa utanuzi wa Bandari ya Mtwara Mjini, ninamshukuru sana na nimuombee tu Mwenyezi Mungu aendelee kutusainia mikataba mingine magati yale matatu yaliyobaki yaendelee kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikichangia moja kwa moja kwenye Wizara hii ya maji, mwaka jana niliuliza swali hapa namba 197 ambalo niliulizia suala zima la ujenzo wa maji kutoka Mto Ruvuma kuja Manispaa ya Mtwara. Majibu ya Mheshimiwa Waziri, alieleza Bunge lako hili Tukufu kwamba kwa sasa Serikali inaendelea na majadiliano na Serikali ya China kwa ajili ya kupata mkopo nafuu wa utekelezaji wa mradi huo. Ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2016/2017 na kazi zitakazofanyika ni pamoja ujenzi wa chanzo, mtambo wa kutibu maji, bomba kuu la kupeleka maji Mtwara Mikindani pamoja na kujenga matenki lakini pia na usambazaji wa maji hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nikiangalia katika kitabu hiki, Mheshimiwa Waziri amepanga vizuri sana, ameweka na ameeleza kwamba mradi huu bado mpaka leo haujapata pesa wakati mwaka jana walitueleza kwamba mradi huu wa kutoa maji Mto Ruvuma na kusambaza maji Mtwara Mjini ungeweza kuanza katika bajeti iliyopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba atueleze Mheshimiwa waziri kwamba tunavyoelezwa hapa ndani ya Bunge hili na kwenye Hansard inaeleza kwamba pesa zimetengwa, lakini huu mradi mpaka leo naambiwa majibu yale yale ya mwaka jana mabyo alitueleza, aje na majibu ambayo kimsingi yatawaridhisha wananchi wa Mtwara Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nieleze tu kwamba baadhi ya maeneo ya Mtwara Mjini na hasa kata ya Ufukoni na kata ya Mitengo maji hatuna kabisa na mimi kama Mbunge niliweza kutenga pesa zangu baada ya kuona kwamba huu mradi ni mradi wa muda mrefu na utachukua muda mrefu kuweza kuanza, lakini pia kumalizika, nikapeleka pesa zangu milioni 10 kwa ajili ya kichimba kisima pale. Hata hivyo niliweza kuomba Idara ya Maji, kuna gari pale wanalo la Wizara ambalo linafanya utafiti na kuchimba maji lakini pesa alizonieleza ni pesa nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwambiwa kwamba tutashirikiana na Mbunge tuweze kuchimba kisima maeneo ya Comoro ambako utafiti tayari nilishatoa pesa yangu ya mfukoni tukafanya utafiti, lakini mpaka leo wananinyima gari la kwenda kuchimba kisima pale ili wananchi waweze kupata maji ni jambo la ajabu sana. Nilikuwa namuomba Mheshimiwa Waziri aliangalie hili, atusaidie gari kwa sababu huu mradi bado haueleweki kwa sababu kila siku tunapewa dana dana kwamba watu wa Benki ya China hawajatoa pesa; kila nikiuliza naambiwa watu wa Benki ya China hawajatoa pesa na wananchi kule wanapiga simu sana na wanadai sana maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, mle ambamo tathmini imeweza kufanyika kutoka Kitaya, Jimbo la Nanyamba mpaka Mtwara Vijijini, vijiji vile 26 wote wanahitaji fidia lakini mpaka leo, miaka zaidi ya mitatu hivi sasa wale wananchi wamechukuliwa maeneo yao na fidia hawajalipwa, wanasumbua kweli kweli Wabunge wote wa Mtwata Mjini na Mtwara Vijijini wanatusmbua sana. Kwa hiyo, nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri anisaidie hilo, atupatie gari tuweze kuchimba kata hizi ambazo Mtwara mjini hatuna maji, nitasaidia na mimi Mbunge ili tuweze kuondoa tatizo hli la maji. Pia nizungumzie…………..

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru, muda wenyewe ndiyo hivyo tena, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. MAFTAH A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, nashukuru ofisi na kiti chako kwa kuendelea kutenda haki juu ya mijadala ya Bunge. Katika Wizara hii ya Maji na Umwagiliaji naomba kuchangia mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji Mtwara Mjini umekwama kwa nini? Ni muda mrefu hivi sasa Mtwara Manispaa haina maji ya kutosha na Serikali ilianzisha mradi wa kutoa maji Mto Ruvuma hadi Mtwara Mjini ili kuondoa tatizo la maji. Bajeti ya 2016/2017 Mheshimiwa Waziri alisema tayari fedha zimetengwa, usanifu umekamilika na taratibu za kutafuta mkandarasi zinafanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kushangaza ni kwamba mpaka leo ukiuliza unapata majibu ya Mheshimiwa Waziri kuwa hakuna pesa na pesa zilitarajiwa kutoka Exim Bank ya China. Kwa nini tunadanganya umma wakati pesa hakuna? Kwa nini tumechukua maeneo ya wananchi kwa miaka mitatu hivi sasa bila kuwalipa fidia juu ya mradi huu? Kwa nini mpaka leo Serikali haina majibu ya kina juu ya suala hili?

Mheshimiwa Naibu Spika, kila siku wananchi ambao maeneo yao yamechukuliwa wanapiga simu na wanasema wamechoka, Serikali haioni kama wananchi huwa wamechukuliwa maeneo yao na kuwazuia kufanya shughuli za kimaendeleo kama vile kilimo na hatimaye kuwadumaza wananchi wa Mtwara? Mradi huu unapelekea wananchi wa Mtwara waone kuwa wanaonewa kwa kutowalipa fidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Miradi ya Maji Nchini; Mheshimiwa Waziri kwenye kitabu chake cha bajeti ametaja miradi mingi itakayotekelezwa kupitia bajeti hii lakini cha ajabu mradi wa kutoa maji Mto Ruvuma/Mtwara haupo kwenye orodha hii, huku ni kututenga wana Mtwara.

Mheshimiwa Naibu Spika, Maji Mbagala. Mkoa wa Dar es Salaam upande wote wa Mbagala ambako kuna watu wengi kuliko maeneo yote hakuna mtandao wa DUWASA/ DAWASCO, hali hii haikubaliki. Watu wa Mbagala wanahitaji maji safi na salama. Jambo la ajabu kuna bore holes Kimbiji ambako ni karibu na Mbagala lakini mtandao hakuna.

Mheshimiwa Naibu Spika, majadiliano na China (Exim) yanaendelea mpaka lini? Mheshimiwa Waziri anasema ili mradi wa Mtwara uanze majadiliano yanaendelea, kila mwaka anatoa kauli hii. Naomba kuuliza majadiliano haya yatakwisha lini? Kuendelea huku hakuna mwisho ili tuwapatie maji safi na salama kutoka Mto Ruvuma? Sisi Waheshimiwa Wabunge wa Mtwara Mjini na Nanyamba tumeongelea sana suala hili na Serikali haitoi majibu ya kina badala yake inasema tu fedha hakuna. Haya ni majibu rahisi wakati wananchi wamezuiwa maeneo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Pesa Ndogo Zilizotengwa kwa ajili ya Mtwara Manispaa. Kutokana na mradi wa kuleta maji kutoka Mto Ruvuma kukwama mwaka 2015/2016 na 2016/2017, nilitarajia mwaka huu wa fedha Wizara ingetenga fedha kwa ajili ya mradi huu. Hata hivyo nasoma bajeti ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 147 pesa zilizotengwa hazihusishi fidia na gharama za mradi huu mkubwa, bado Wizara haioneshi kama Wanamtwara wana umuhimu wa kupata maji safi na salama.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia. Kwanza kabisa naomba nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhanah Wataala ambaye ameendelea kunijalia afya njema na leo hii niweze kuzungumza machache niliyokuwa nayo, pili nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi asubuhi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema kwamba wakati nachangia bajeti ya Wizara ya Maji, nilizungumza hapa kwamba Mtume Mohammed alisema Karne ya Sita kwamba Man laa yashkur nnasa,laa yashkur Allah, kwamba mtu yeyote ambaye hashukuru binadamu wenzake kwa wema wanaofanya basi hata Mwenyezi Mungu kwa neema alizompa hawezi kumshukuru pia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee kabisa naomba nikiwa kama mzalendo wa Taifa hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kitendo kikubwa alichokifanya jana, kwa maamuzi magumu aliyoyafanya jana, kuhakikisha kwamba wale wanaotorosha madini yetu kwenda nje ya nchi wanachukuliwa hatua kwa kunyang’anywa yale madini. Tunampongeza kweli na ni kitendo cha kishujaa kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nieleze tu kwamba nchi hii kama hatuchukui maamuzi magumu tutaendelea kuwa maskini mpaka kiama. Wenzetu walioendelea duniani kupitia sekta hii ya madini, nchi ndogo kama Botswana ni kwa sababu wanachukua maamuzi magumu. Nimwombee Mwenyezi Mungu aendelee kumpa afya njema Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania achukue maamuzi magumu zaidi, Tanzania tuondokane na umaskini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata mimi ninayezungumza hapa kama siyo kufanya maamuzi magumu nisingekuwa Mbunge leo hii, mimi nilikuwa Mwalimu, nikaandika barua kuomba likizo isiyokuwa na malipo ili niweze kugombea Jimbo la Mtwara Mjini, lakini kulikuwa na ujanja ujanja ulifanyika wakaninyima ruhusa nikamua kuacha kazi masaa 24 ili niweze kugombea Ubunge na leo hii nazungumza ni Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Jimbo la Mtwara Mjini ni kwa sababu ya maamuzi magumu. Kwa hiyo, hii nchi kama tunahitaji maendeleo lazima tuwe na Viongozi wanaochukua maamuzi magumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kwa namna ya kipekee kabisa, niishukuru Wizara hii ya Ardhi, siku kadhaa zilizopita nilikuwa Mtwara nikiwa na Mheshimiwa Waziri hapa tulienda kuzindua mpango kabambe ambao unaitwa master plan kwa mara ya kwanza tangia Serikali hii ya Awamu ya Tano mpango wa kwanza kuzindua ni mpango wa master plan wa Mtwara Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kufanya kazi kubwa sana na wananchi wa Mtwara sasa kwa sababu hii master plan ambayo tumeizindua juzi ndiyo mwarobaini ya migogoro yote ya ardhi pale Manispaa ya Mtwara Mikindani. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na namshukuru sana, Mungu ambariki aendelee kutatua migogoro mingine ambayo ipo katika maeneo mbalimbali ya nchi hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, wakati nafanya kampeni 2015 niliweza kuzungumza mambo mengi sana yanayohusu ardhi, kwa sababu Mtwara Mjini kulikuwa na changamoto nyingi sana za ardhi. Miongoni mwa mambo mengi ambayo nilikuwa nayahutubia na wananchi wangu wakanituma nije kueleza katika Bunge hili, ilikuwa ni suala la urasimishaji wa ardhi. Mheshimiwa Waziri hapa wakati anazungumza kwamba maeneo kadhaa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivi sasa urasimishaji unaendelea ikiwemo Jimbo la Mtwara Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara hii na namshukuru Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kwa kubariki Mtwara Mjini, lakini pia kutuletea Wataalam ambao tunashirikiana nao katika suala hili la urasimishaji wa ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wito wangu kwa Madiwani wa Jimbo la Mtwara Mjini, wahamasishe wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini ili zoezi hili liweze kukamilika kwa wakati. Kwa namna ya kipekee kabisa nawashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Mtwara Mjini kwa kuendelea kuwa na imani na Mbunge wao na nawaambia kwamba naendelea kupambana, nitawatetea kipindi chote cha miaka yote iliyobaki na Mtwara Mjini sasa ni Mtwara kuchele kweli kweli, siyo kama kauli za kubeza za miaka ya nyuma kulivyokuwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shukrani hizo za dhati kabisa naomba nizungumze suala moja ambalo hivi sasa pale Mtwara Mjini, nimwombe Mheshimiwa Waziri atusaidie katika hili. Mtwara Mjini kuna eneo linaitwa Mangowela, sasa hivi wamebatiza jina panaitwa Libya, hili eneo lilikuwa linamilikiwa na Wazee Nane wa Mji wa Mtwara, na hapa nina majina yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niyasome haya mbele ya Bunge lako hili Tukufu, wamiliki wa eneo hili ni Mzee Mohammed Saidi Mussa, Mussa Ismail Selemani, Ndugu Karama Akidi Ismail, Ndugu Abdallah Mfaume Mkulima, Ndugu Fatu Mchimwamba, Ndugu Abubakari Zarali Mohammed, Ndugu Musa Saidi na Ndugu Ashiraf Makuti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wazee hawa ni wazee ambao wamezaliwa miaka 1920 huko nyuma, walikuwa wanamiliki eneo hili la Mangowela, lakini hivi sasa linaitwa eneo la Libya, lakini jambo la ajabu sana ambalo lilifanyika miaka ya 2000 wameamka asubuhi wakakuta beacon zimewekwa, walivyoulizwa hizi beacon zilizowekwa katika eno hili la Libya ni za nini, wanaambiwa kuwa hili eneo limeuzwa na wamiliki wa eneo hili. Wakashangaa sana, kwamba wamiliki wa eneo hili ni watu wa aina gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, huu mgogoro ni mgogoro ambao ni mkubwa sana hivi sasa Mtwara, naipongeza Wizara hii kwamba jana niliuliza swali hapa juu ya mgogoro wa Mji Mwema na kwamba tayari wameshamaliza na fidia ile inaenda kulipwa mwisho wa mwezi huu, tunashukuru sana kwa hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri mgogoro huu wa Mji wa Libya, naomba sana wananchi hawa wamekuja Ofisini kwangu zaidi ya mara nne, wametembea maeneo yote kudai haki yao, lakini mpaka leo wanaambiwa lile eneo limeuzwa na wao wameuzwa bila wao kuelezwa. Hata hao waliouza wanasema kwamba walipewa na watu fulani, lakini hakuna documents zozote kwamba lile eneo lilikuwa ni la kwao, wamiliki wa eneo hili la Libya ni hawa wazee ambao nimewasoma hapa, kwa hiyo tunaomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja atusaidie katika hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuzungumza Mbunge mmoja kaongea hapa kuhusu shirika la NHC (Shirika la Nyumba Tanzania), kwa kweli linafanya kazi kubwa sana ya kuhakikisha wanaboresha makazi ya Watanzania, wanajenga majumba maeneo mengi, lakini nyumba hizi ambazo zinajengwa kwamba eti ni nyumba za maskini, kimsingi siyo nyumba za maskini. Mfano tu hata nikiwa Mwalimu pale Lindi, mwaka 2007, kuna nyumba zilijengwa pale Lindi, lakini zile nyumba mimi nilienda kuomba kama Mwalimu, Mwalimu ambaye nilikuwa nachukua mshahara 940,000 wakati ule, nikaambiwa kwamba zile nyumba wewe kama Mwalimu huwezi kuzinunua ni nyumba ambazo zinaanzia Sh.50,000,000/= na Sh.60,000,000/= huko na kuendelea. Sasa hizi kweli ni nyumba za bei nafuu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba Waziri ahakikishe kwamba hii NHC kweli ijenge nyumba za bei nafuu ili Watanzania wengi maskini waweze kupata hizi nyumba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze pia suala hili la kucheleweshwa hati, Mheshimiwa Waziri ana mpango mzuri sana hapa, kazungumza vizuri sana, kwamba ametoa maagizo kwa Taasisi zote, kwa Halamshauri zote, wahakikishe kwamba tunaenda kama Wabunge kukagua Masjala za Halmashari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe atoe agizo lingine kwamba ucheleweshaji wa hizi Hati unafanywa na Watendaji wa Halmashauri na watu wa ardhi wa Halmashauri na wale ambao wataendelea kukiuka agizo lako Mheshimiwa Waziri, basi hawa watu aweke hatua za kuchukuliwa mara moja ili sasa tatizo hili la kuchelewesha Hati Tanzania liweze kwisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu na kiti chako, napenda kuchangia Wizara hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara hii inahusisha pia uwekezaji ambao kwa kiasi kikubwa uwekezaji bado haujapewa kipaumbele. Kwa kiasi kikubwa hotuba ya Waziri Mheshimiwa Mwijage imejikita katika kuzungumzia viwanda ambavyo kwa kiasi kikubwa ni mbwembwe kuliko uhalisia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Taasisi zote za Umma zenye mitaji ya umma ilitakiwa tuelezwe, kwa kuwa taasisi hizi, mfano Mifuko ya Hifadhi yote inajikita katika uwekezaji. Kwa kiasi kikubwa uwekezaji huu hauna tija. Nilitegemea hotuba ya Mheshimiwa Waziri ieleze juu ya uwekezaji butu unaofanywa na Mifuko ya Hifadhi za Jamii pamoja na Taasisi za Serikali kama vile Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, ununuzi wa viwanja bei ni za juu, hifadhi za Jamii kama LAPF wamenunua Kiwanja Mwanza Square metre moja kwa Sh.255,000/= kitu ambacho siyo kweli. Kuna harufu ya matumizi mabaya ya Ofisi. Mtwara wamenunua kiwanja eneo la Rahaleo Square metre moja ni Sh.155,000/= eneo ambalo mimi nalijua. Niliwaambia haya, wakasema valuer ameruhusu. Valuers wanacheza deal na wahusika. Tunataka uwekezaji wenye tija kama Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimeingia mkataba wa miaka 50 na mwekezaji kutoka Botswana. Huu mkataba unampa mamlaka ya kukusanya kila anachokipata na kuipa Serikali asilimia 10% tu. Hali hii haikubaliki. Kibaya zaidi, anajenga vibanda na anakusanya billions of money. Hivi baada ya miaka 50 vibanda vile vitakuwa na thamani kweli?

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri apitie uwekezaji unaofanywa na Taasisi za Umma sio kuwaza viwanda vya watu ambao yawezekana wasije kabisa kujenga. Hivi vilivyopo vifanyiwe uhakiki wa kina.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumuuliza Waziri, Mheshimiwa Mwijage, Kiwanda cha Mbolea Mtwara kina tatizo gani? Kwa nini hakijengwi wakati mwekezaji yupo tayari? Kwa nini hawawezeshwi kujenga kiwanda hicho? Kwa nini hawampi rasilimali anazotaka ili ajenge kiwanda Mtwara? Kila kitu kipo mpaka kwenye eneo, kigugumizi cha nini au Mheshimiwa Waziri hataki maendeleo ya Mtwara?

Mheshimiwa Naibu Spika, Mtwara Mjini kulikuwa na Viwanda vingi vya Korosho, vyote sasa hivi havipo. Baya zaidi kilikuwepo kiwanda cha OLAM, mwekezaji aliwekeza Mtwara Mjini na kiwanda hiki kilikuwa kinaajiri wananchi wengi sana, lakini Serikali ilimwekea mazingira mabaya ya kodi; huyu mwekezaji, amehamisha kiwanda na kukipeleka Msumbiji. Kwani kuna nini wawekezaji wa Mtwara hamwataki wawekeze Mtwara? Au Wizara inataka Mheshimiwa Rais aje tena Mtwara atamke aliyotamka tarehe 4 Machi, 2017? Naomba wawekezaji wenye nia ya kuwekeza Mtwara wapewe mazingira rafiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu third party katika ajira, UCC Dangote Mtwara; kuna usumbufu mkubwa kiwanda cha Dangote kwa kuwa kuna mtu kati anaitwa UCC ndio anayesimamia na kuajiri watu, baadaye anampa mahindi na mahindi anampeleka Dangote. Hawa watu wakati wanapokonya haki za waajiriwa kiwandani, wananyanyasika sana, wafanyakazi hawana utaratibu, wanadhulumiwa haki zao wakidai mwajiri anasema hawamhusu na anamwambia UCC wafanyakazi kadhaa hawatakiwi na wanafukuzwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuuliza, Serikali ilitoa waraka mwaka 2014 wa kuzuia mtu kati kutoa ajira ya mawakala, umefikia wapi?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumshukuru Mwenyezi Mungu na kiti chako na katika Wizara hii ya fedha naomba kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kodi ya Majengo (Property Tax), naomba sana irudishwe kwenye mamlaka ya mwanzo ambayo ni Halmashauri ili ziweze kukusanya ipasavyo. Tangu Serikali Kuu ichukue kodi hii ya majengo, Halmashauri zimekosa mapato na kodi hii haikusanywi tena. Serikali Kuu irudishe kodi hii Halmashauri kwa maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti iliyopita, kuna fedha nyingi sana hazijapelekwa Halmashauri ili miradi mingi iende kama ilivyopangwa. Ucheleweshaji wa fedha za maendeleo kama ilivyopangwa ni kurudisha nyuma kasi ya maendeleo nchini. Naomba suala hili liangaliwe ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kitendo cha Serikali kukopa ndani ya nchi na hasa mashirika ya Hifadhi za Jamii kama vile PSPF, LAPF, NSSF na nyingine, kunaleta ushindani na wananchi wa kawaida ambao huweka fedha zao huko kwa wakati maalum hivyo wanapotaka kujitoa huwekewa vigingi vingi kwa kuwa mifuko hii inakosa fedha. Pia Serikali inachukua muda mrefu sana kulipa madeni ya mifuko ya Hifadhi ya Jamii, hivyo mifuko hii hudumaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali ni kwamba, kwa kuwa inakopesheka nje ya nchi, basi ifanye hivyo ili mzunguko wa fedha ndani ya nchi kupitia mifuko hii ya Hifadhi za Jamii na mabenki yetu ziendelee kutoa mikopo kwa wananchi wa kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mabenki hutoa riba kubwa sana kwa wananchi wanaowakopesha. Wananchi hawa hushindwa kulipa mikopo hiyo na hatimaye kufilisiwa mali zao na vitu vyao vya ndani, hivyo kuwafanya kuwa maskini zaidi badala ya kuwainua kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbunge kila mwezi analipa fedha nyingi sana ya VAT na kodi ya mapato kupitia mshahara wake kila mwezi. Kitu cha ajabu, Wizara imeweka kodi nyingine kwenye kiinua mgongo kilicholipiwa kodi kabla hakijawekwa kutunzwa. Hali hii ni mbaya sana na siyo ya kuvumilika kuweka kodi juu ya kodi kwenye gratuity ya Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Mashirika ya Umma yakaguliwe na CAG kwani matumizi yao, mfano kuna taasisi ya AICC iliyopo Arusha ambayo kazi yake kubwa ni kujenga Vituo vya Mikutano kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha Sheria ya Taasisi hii ya AICC. Bahati mbaya badala ya kufanya kazi yao, wanatumia shilingi bilioni 3.5 kwa kukarabati ukumbi wa Simba na huku wakijenga nyumba kubwa yenye ghorofa sita kwa shilingi bilioni 1.8 tu. Haiwezekani ukarabati uzidi majengo makubwa. CAG akague Arusha AICC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vema Wizara ikaweka katika bajeti zake shilingi milioni 50 za kila Kijiji ambazo ziliwekwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Kwa nini haziwekwi kwenye bajeti?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nashauri fedha za Mfuko wa Jimbo ziongezwe Mtwara Mjini, watu ni wengi, hazitoshi.