Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Bernadeta Kasabago Mushashu (5 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri pamoja na Mheshimiwa Jenista Mhagama na Mheshimiwa Antony Mavunde kwa kazi nzuri wanayofanya katika shughuli zao za kumsaidia Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Magufuli pamoja na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa kwa kazi nzuri mnayofanya. Ni mwaka mmoja tu tangu mmeingia madarakani lakini mambo mnayofanya ni mazuri sana, uchumi wa nchi hii umeendelea kuwa mzuri hadi sasa hivi viashiria vyote vya uchumi vinaonekana kwamba tunafanya vizuri sana kwenye uchumi. Pato la Taifa limeendelea kukua hadi sasa hivi linaendelea kukua kwa asilimia saba na mmeweza kuu-contain mfumuko wa bei ukaendelea kukaa kwenye tarakimu moja. Vilevile ni furaha ilioje niliposikia kwamba Tanzania iko kati ya nchi sita the best in Africa ambao uchumi wao unakuwa kwa kiasi
kikubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo mengi ya kujivunia, tumeambiwa TRA sasa hivi makusanyo yameongezeka kutoka kwenye shilingi bilioni 850 mpaka kwenye shilingi trilioni 1.2 ndiyo maana mmeweza kuyafanya mambo makubwa kama kununua ndege. Anayependa apende, asiyetaka
asitake lakini makubwa yanafanyika ndani ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Mmeweza kuwa mnapeleka shilingi bilioni 18.77 kwenye shule kwa ajili ya elimu bure kila mwezi, hongereni sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba yake Mheshimiwa Waziri Mkuu amezungumzia kwamba mabenki yako salama, mitaji na ukwasi upo wa kutosha. Hapa nina wasiwasi kidogo kwa sababu tukienda kule chini, tukienda mijini na vijijini tunaona kwamba mabenki ya biashara
yamepunguza kutoa mikopo. Tunahamasisha wajasiriamali wengi wajitokeze wafanye shughuli mbalimbali, wafanye shughuli za kilimo, biashara ndogo ndogo, tunahamasisha wananchi waanzishe viwanda vidogo na vikubwa, hivi kama mabenki hayatoi mikopo hawa mitaji watapata wapi? Niombe Mheshimiwa Waziri Mkuu atusaidie ili Serikali sasa iweke mpango wa makusudi wa kuziwezesha hizi benki ili zianze kutoa mikopo kama walivyokuwa wanatoa kwa ajili ya wajasiriamali wadogo wadogo waliopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitajikita kwenye suala la kahawa. Kahawa ni zao la muhimu sana katika nchi yetu ya Tanzania, lakini lina umuhimu wa pekee kwa sababu tunaliuza nje linatuletea fedha za kigeni. Bei ya kahawa imeendelea kuwa chini kiasi ambacho inakatisha tamaa na ukilinganisha bei ya kahawa ya Tanzania na nchi jirani ya Uganda unakuta bei ya kahawa ya Uganda iko juu pamoja na kwamba nchi hizi zimepakana, ndiyo kitu kinachoshawishi watu wauze kahawa ya magendo kuitoa Tanzania kuipeleka Uganda. Bei ya kahawa kuwa chini ni kwa sababu bei ya kahawa ya Tanzania imegubikwa na tozo nyingi, ada nyingi, kodi nyingi. Wataalam wanasema hizi kodi na tozo zinafikia hadi 26. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano, kuna kodi na tozo za zimamoto, OSHA, land rent, crop cess pamoja na kwamba sheria inasema crop cess inaweza kuwa kati ya asilimia tatu mpaka tano, sisi halmashauri zinatoza maximum, five percent. Kuna income tax, cooperate tax, VAT kwenye inputs zote zinazoingaia kwenye kahawa, research cess, Coffee Development Fund ambapo hela zinakatwa kwenye kila kilo, lakini sijawahi kuona huu mfuko unakwenda kumuendeleza au kuendeleza kilimo cha kahawa. Kuna labour charge, service levy, property tax, coffee bags duties, coffee industry licence et cetera mpaka zinafika 26.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tozo hizi ziko kwenye ngazi mbalimbali za uzalishaji pamoja na pale wanapouza nje. Ukienda pale mkulima anapouza kahawa kwenye chama cha msingi, kwenye chama kikuu cha ushirika, kule kwenye mnada Moshi ambapo wana-export kahawa kote kuna tozo kila mahali, lakini mzigo mzima anaubeba mkulima. Tozo hizi ndiyo zinasababisha bei ya kahawa inakuwa chini sana. Kwa msimu huu Mheshimiwa Waziri Mkuu, bei ya kahawa kwa Mkoa wa Kagera ni shilingi1,300, mtu anatunza ule mbuni kwa miezi tisa anapalilia, anakatia na kadhalika lakini anakuja kuishia kupata kati ya shilingi 1,100 na shilingi 1,300.
Mheshimiwa Mwenyekti, tukijilinganisha na nchi jirani ambazo ni washindani wetu katika hili zao la kahawa kama Ethiopia wao wanakata 0.04% kama exchange rate sale price, Uganda wanakatwa 1% export levy, Kenya wanakata 3% tu kwa ajili ya cess, lakini Tanzania tuna different cess’s, licence fees, taxes na tozo mbalimbali zinazofikia zaidi ya 26 na kuifanya hiyo bei iwe chini sana na kuwafanya wakulima wa
kahawa wakate tamaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu amefanya mambo mazuri sana kwenye korosho, tumemuona. Ameweza kuifanya bei ya korosho ikapanda kutoka kwenye kilo moja shilingi 1,200 mpaka shilingi 3,800. Tumuombe chondechonde, mimi kama mwakilishi wa wakulima wa Mkoa wa Kagera na nyuma yangu wakiwa Wabunge wote wa Mkoa wa Kagera, tunamuomba hebu aangalie kwenye hili zao la kahawa, watu wamelia ni kilio cha siku nyingi. Hebu aangalie tunatoa ada, tozo na fees gani ili kumwezesha huyu mkulima na yeye mwenyewe aweze kufaidi jasho lake aweze kupata bei ya juu ili angalau kilo moja isiteremke chini ya shilingi 3,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati namalizia, unakumbuka kwamba watu wa Mkoa wa Kagera na Mwanza wanafanya biashara na Uganda kwa kupitia Ziwa Victoria. Meli ya Mv Bukoba ilizama, Victoria imezeeka inakarabatiwa kila kukicha lakini wafanyabiashara wanapata matatizo kwa sababu ili waweze kupeleka mazao yale ina… (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye hoja hii. Kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii pamoja na Kamati nzima na Kamati ya UKIMWI kwa kazi nzuri waliyofanya ya kuchambua taarifa za utekelezaji wa Wizara mbalimbali na kuweza kuyaleta mapendekezo mbalimbali. Nasema hongera sana, nami naunga mkono hoja mapendekezo yaliyoletwa mbele ya Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na afya, napenda kuchukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri kwa utendaji mzuri sana, wamefanya mambo makubwa sana kwenye upande wa afya. Wote tumeshuhudia operations kubwa sana zinazofanywa kwenye Hospitali ya Mifupa ya MOI, wote tumeshuhudia operation za kileo zinazofanyika kwenye Hospitali ya Moyo ya Jakaya Kikwete, wote tumeshuhudia hata upandikizaji wa figo sasa hivi unaweza kufanyika Tanzania na watu wanatoka nchi za jirani kuja Tanzania kupatiwa huduma hizo. Kwa hiyo, nasema hongera sana kwa kazi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na ugonjwa wa cancer. Ugonjwa wa cancer ni ugonjwa wa ambao umesambaa sana, sasa hivi watu wengi wanaugua ugonjwa wa huu. Kuna cancer ya damu, ubongo, tezi dume, mlango wa kizazi, cancer matiti; kwa hiyo, cancer ziko za aina nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili mtu aweze kugundulika kabisa ana cancer, iwe confirmed, anapaswa afanyiwe vipimo vingi ikiwemo na CT-Scan. Unakuta gharama ya vipimo hivyo hasa kwenye Hospitali ya Bugando ambayo kwa Mkoa wa Kagera tunatumia hiyo, unakuta vipimo vina- cost kati ya shilingi 500,000 mpaka shilingi 600,000 kuweza kugundua kama huyu ana cancer kweli au hapana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda sasa kwenye matibabu labda amewekewa chemo, dose moja ni kati ya shilingi 600,000 mpaka shilingi 700,000. Je, hawa Watanzania tunaowajua na uwezo wao mdogo waliokuwa nao, ni wangapi wanaweza ku-afford kulipa hizo hela zote kusudi wagonjwa wao waweze kupata matibabu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza kwa Serikali yangu sikivu na Mheshimiwa Waziri kwamba kwa ugonjwa huu wa cancer na kwa wingi na ukubwa wa tatizo lilivyojitokeza, Serikali ingeweka ruzuku kwenye dawa za ugonjwa wa cancer kusudi dawa hizi ziendelee kutolewa bure katika hospitali zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuwa Wizara imefanya kazi nzuri sana kwenye Hospitali za Rufaa kama Muhimbili na nyingine zote, nilikuwa naomba sasa concentration iende kwenye Hospitali za Mikoa, Hospitali za Wilaya, Vituo vya Afya pamoja na Zahanati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia Mkoa wa Kagera; ukienda mkoa wa Kagera utakuta karibu Wilaya zote hazina Hospitali za Wilaya, sana sana tunadandia kwenye hospitali zile za mission.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na Wilaya ya Kyerwa. Wote tunajua kwamba Wilaya Kyerwa ni mpya, hawana kabisa Hospitali ya Wilaya, wanatumia pale Isingiro pamoja na Nkwenda ambapo sana sana zile ni sawasawa na zahanati. Nilikuwa naomba Serikali iwasaidie kwa kuwa ni Wilaya mpya hii, iweze kupata Hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda pale Manispaa ya Bukoba, tangu mwaka 2013 wanajenga Hospitali ya Wilaya. Wameshindwa kwa sababu huu ni mradi mkubwa, kwa bajeti za Halmashauri hawawezi kuukamilisha. Nilikuwa naomba Serikali isaidie kukamilisha Hospitali ya Wilaya ya Manispaa ya Bukoba ikiwemo vilevile na Hospitali ya Wilaya ya Muleba. Hospitali ya Wilaya ya Muleba wananchi walijitahidi, wamejenga majengo mazuri, ila haijakamilika. Sasa hivi MSD wanapatumia pale, wakiondoka yataendelea kuwa magofu na zile juhudi za wananchi zitaharibika bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali itusaidie, kwa kuwa hii ni miradi mikubwa na najua siyo kwa Kagera peke yake, kuna maeneo mengine waendelee kutusaidia kuweza kukamilisha hii miradi kusudi huduma ziweze kutolewa kama ilivyokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tunajua kwamba katika Mkoa wa Kagera tulipata tetemeko la ardhi. Tulipata athari nyingi, watu walifariki, taasisi mbalimbali ziliathiriwa na nyumba za watu zimeanguka na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia Kituo cha Afya ambacho kiko katika Wilaya ya Misenyi kinaitwa Kabyaile. Hiki kituo kimejengwa kwa nguvu ya Kamati ya Maafa ambayo ni michango ya wananchi na ya Serikali, ni kituo kizuri sana kimejengwa, hata Rais alishapelekwa kukikagua kile kituo. Pamoja na majengo mazuri, kuna theatre lakini hakuna vifaa, kuna mortuary lakini hakuna mafriji na kuna laundry lakini hakuna vifaa vya kusafishia. Naomba Serikali itusaidie kuweka hivyo vifaa kusudi Kituo cha Afya cha Kabyaile kilicho Ishozi, Misenyi kiweze kuanza kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie Hospitali ya Mkoa wa Kagera ambayo inaitwa Bukoba Government Regional Referral Hospital. Hii ndiyo kimbilio la mkoa mzima. Wilaya zote tunategemea hii hospitali, lakini haina wataalamu, ina Madaktari Bingwa wanne tu ambao ni wa meno, wa watoto pamoja na wa macho. Wanne kati ya Madaktari Bingwa kama 24 wanaotakiwa. Ukienda kwa wauguzi, hao ndio kabisa. Kwa hiyo, tulikuwa tunaomba Serikali kwa hospitali hii ipatiwe wataalamu kusudi iweze kufanya kazi. Hatuna surgeon, hatuna daktari wa mifupa. Wote mnajua accidents za boda boda ni kila siku. Sasa bila kuwa na hawa Madaktari Bingwa inakuwa ni shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hiyo hospitali, kuna wodi ya wazazi ambayo ni ndogo sana. Ina vitanda sita tu na hii ni Referral Hospital ya Mkoa, havitoshi na hakuna theatre. Mwanamke akitoka kule, ana uchungu, akaletwa pale kwenye Regional Hospital, akakuta ile multpurpose theatre ambayo na yenyewe ni ndogo, kuna mtu anafanyiwa operation, inabidi huyu mama amcheleweshe. Kwa hiyo, inabidi huyu mama afe kwa sababu amekuta ile theatre inatumika. Tulikuwa tunaomba basi, katika Hospitali ya Mkoa ijengwe labour ward kubwa ikiwa na theatre yake ili tuweze kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tukumbuke kwamba Mkoa wa Kagera hatuna mahali pa kukimbilia; ukienda huku ni Uganda, ukienda huku ni Rwanda; ukienda huku ni Burundi; sana sana umkimbize mgonjwa kumpeleka Bugando ambayo iko something like kilometa 500 kutoka Mkoa wa Kagera. Ukitaka kutembea kwa meli ni masaa kama manane mpaka 10 au ukizunguka lile ziwa. Tulikuwa tunaomba ile hospitali ipewe ambulance, kwanza na Mheshimiwa Waziri Mkuu alishakuja akaahidi pale kwamba atatoa ambulance. Namuomba Mheshimiwa Waziri Ummy, hilo alichukue kwamba Hospitali ya Government Regional Hospital waweze kupata ambulance kwa sababu ni mbali sana na Bugando waweze kufanya hizo kazi zinazotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza sana Wizara ya Elimu kwa kazi nzuri mnayofanya. Nawapongeza kwa uamuzi wenu wa kuweza kukarabati zile shule kongwe. Wote hapa tumesoma zile shule za zamani, shule kongwe karibu
100. Pia naomba Mheshimiwa Waziri aikumbuke na shule yangu, mimi nilikuwa Mkuu wa Shule pale, lakini ni shule ambayo inasomesha wanafunzi wengi wasichana, Shule ya Rugambwa Sekondari na yenyewe imeanza tangu mwaka 1965 inahitaji ukarabati mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumza juu ya matamko ya Waziri wa Elimu. Mheshimiwa Waziri hivi juzi ametamka kwamba watoto ambao watashindwa kufikia ile alama ya ushindi au pass mark wasikariri madarasa. Sasa hapa mimi nazungumza kama mwalimu. Huyu mwanafunzi asipokariri darasa au huyu mtoto aliyeshindwa kufikia alama ya ufaulu, kwa mfano akapata sifuri kati 100, akapata 10 kati 100, akapata 20 kati ya 100 tunamwambia apande tu darasa, tunakuwa tunamsaidia huyu mtoto au tunamlemaza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke kwamba watoto wengine hawataki kusoma. Tukumbuke kuna mahali ambapo walimu hawataki kufanya kazi. Sasa kwa nini huyu mtoto badala ya kumpitisha tu akafika form four akapata division zero, akikariri anakuwaje? Mbona hata humu ndani kuna wengi walikariri na wala hawakuathirika? Napendekeza kwamba watoto wawe wa private au wa government, yeyote ambaye atashindwa kufikia alama ya ufaulu akariri darasa tusije tena tukaanza kukimbizana kuangalia namna ya kufuta zero. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu shule za private. Kabla mzazi hajampeleka mtoto private anatafuta mwisho anapata shule moja, anaangalia ile shule ina vigezo gani? Wanataka nini? Discipline ikoje? Ufaulu ukoje? Karo ikoje? Mzazi mwenyewe anachagua kwamba anataka kumpeleka kwenye shule fulani ambapo wengine wanatoza karo kubwa, lakini mzazi anaamua anamtafutia mtoto elimu bora, anampeleka kwenye ile shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba Serikali kama inawezekana, hizi shule za private wangeziacha na alama zao za ufaulu kwa kuwa wazazi hawalazimishwi na wala wanafunzi hawalazimishwi kwenda kwenye hizo shule. Wazazi wanawapeleka kabisa kwa mapenzi yao, wawaache kusudi waweze kuwapeleka kwenye hizo shule na pass mark iendelee kuwa zile zile kama shule watakazokwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu leo tunajivunia, naona Wizara tunatangaza kwamba baada ya mtihani wa form four, kati ya shule kumi za kwanza au bora zilizofanya vizuri unakuta most of them ni za private ambao walikuwa wameweka viwango vya ufaulu. Kwa hiyo, nilikuwa naomba nishauri kama Mwalimu kwamba shule za private waziache ziweze kuweka ufaulu wao na hii itasaidaia kuboresha elimu katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Wanataaluma wa Kemia wa Mwaka 2016
MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri wa Wizara ya Afya kwa kuleta muswada huu. Muswada huu ni muhimu sana kwa sababu wote tunajua umuhimu wa kemia katika maendeleo lakini vilevile teknolojia imepanuka sana kwa hiyo kuna changamoto nyingi zinazotokana na upanuzi huo therefore huu muswada umekuja kwa muda muafaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, umuhimu wa muswada huu ni mkubwa, hii Ofisi ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa ipo siku nyingi, lakini hawakuwa na sheria yao wenyewe, walikuwa wanatumia sheria za hapa na pale kukiwa na tatizo la mambo ya mazingira basi wanatumia Sheria ya Mazingira lakini kwa kutunga sheria hii sasa tutakuwa tumemuwezesha huyu Mkemia Mkuu wa Serikali kuwa na sheria yake moja ambayo itaweza kuongeza ufanisi (principal legislation). Sheria hii ikishatungwa itaifanya maabara hii kuwa ya mwisho na ya rufaa. Hii itampa nafasi mtu ambaye hajaridhika na matokeo ambayo yametoka labda kwenye hizi maabara ndogo ndogo aweze kupata mahali ambapo anaweza akakata rufaa na akaweza kusikilizwa, kwenye maabara kama za TBS, TFDA basi kama mtu atakuwa hajaridhika huko anaweza kukata rufaa kwenye hiyo maabara. Hivyo basi, kifungu cha nne (4) kwenye Muswada huu kieleze wazi majukumu ya Mkemia Mkuu wa Serikali kusudi sasa kusiendelee kuwa na migongano ambayo ilikuwepo kati ya majukumu ya hii maabara pamoja na maabara zile ndogo ndogo zinazoshughulika na hayo mambo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kifungu cha 10 kinazungumzia uteuzi wa Mkemia Mkuu na kinamtaka huyu atakayeteuliwa awe na shahada ya uzamili ya kemia au taaluma nyingine zinazofanana na hizo. Hata hivyo, tukumbuke sasa hivi vipo vyuo vingi, wengine degree tunapata tu kwenye internet, wengine tunapewa tu, ili kuondoa matatizo ambayo yanaweza kujitokeza tukakuta ameteuliwa mtu ambaye hana sifa zinazotakiwa hicho kipengele kiseme kwamba hiyo shahada ya uzamili iwe imetoka kwenye chuo kinachotambuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kifungu cha 16(4) kinachozungumzia usimamizi wa sampuli zinazopelekwa kwenye maabara kwa ajili ya uchunguzi, kinataka maabara isiwajibike kwa mabadiliko au muonekano wa sampuli utakaojitokeza wakati wa uchunguzi au hata baada ya uchunguzi.
Ndugu zangu, mkumbuke kwamba hii maabara itakuwa inapima kemikali, sumu, vinasaba, dawa za kulevya na sampuli za kesi za jinai, kwa hiyo, lazima tuwe waangalifu. Ikitokea mtendaji ambaye syo mwaminifu hiki kifungu cha 16(4) kinaweza kikatumika vibaya, ukakuta mtu unapeleka sampuli ukihisi kwamba ni sumu iende kupimwa ikapimwa lakini ukaambiwa kwamba hii haikuwa sumu ilikuwa ni chumvi au ukapeleka bhangi unakwenda kuangalia unakuta imeshakuwa mchicha. Kwa hiyo, napendekeza kwamba hicho kifungu kielezwe vizuri kusudi hao watu ambao siyo waaminifu wasiweze kukitumia vibaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, siku hizi wanaume wengi wanawapa wanawake mimba, lakini wanawakana watoto. Wengine wanawapa mimba wanafunzi, wanawatelekeza, watoto wa watu wanaishia kufukuzwa shule na kwa sababu hawawezi kupata kazi kwa hiyo watakuwa hawana kipato, wataendelea kuwa maskini na watoto wao wataendelea kuwa maskini. Pia wote tunaona ukatili kwa watoto unaongezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna takwimu zimetolewa juzi juzi na Dawati la Jinsia na Watoto katika Jeshi la Polisi ambapo wamebaini kwamba kwa mwaka huu tu tangu mwezi Januari mpaka Julai, watoto 2,571 wamebakwa. Je, wamebakwa na nani? Unaweza ukakuta hata mtu mwingine unaishi naye humo ndani ndiye mbakaji, lakini hujui. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuwabaini wanaume wanaowakana watoto, wanawapa mimba wanawake lakini wanaogopa majukumu wanawakana watoto, kuwabaini wanaowapa wanafunzi mimba na kuwabaini hao wanaobaka watoto na kuwalawiti, Maabara hii ya Mkemia Mkuu wa Serikali inaweza ikatumika au itatumika kupima DNA ambayo itakuwa ni kipimo sahihi kuonesha ni nani amefanya tukio hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ili watendaji wasije wakashawishiwa kwa rushwa kubwa au ndogo, napendekeza adhabu iongezeke ambayo iko kwenye kifungu cha 53. Adhabu kwenye kifungu hiki iongezeke ili isomeke kwamba fine isiwe chini ya shilingi milioni tano na kifungo kisiwe chini ya miezi kumi na mbili kusudi mtu aweze kupewa adhabu kubwa kufuatana na kosa atakalokuwa amelifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ipendekeze kwamba sheria hizi zikishapita basi kanuni zitungwe haraka sana kusudi hizi sheria ziweze kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa sijajitendea haki na nitakuwa sijawatendea haki wana Kagera, mimi kama Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Kagera ambaye ni mwakilishi bila ya kulizungumzia hili ambalo limetokea Mkoani Kagera.
Mheshimiwa Naibu Spika, naanza kwa kuwapa pole wenzangu wote ambao wako kule walioathirika kwa matatizo makubwa waliyoyapata ambayo yametokana na tetemeko la ardhi. Najua imetokea Kanda ya Ziwa lakini Mkoa wa Kagera umeathirika vibaya sana na hasa hasa Bukoba Mjini. Leo hii tumeambiwa watu 17 wameshafariki, tumesikia katika taarifa mbalimbali na kwamba watu zaidi ya 252 wamejeruhiwa, nyumba zaidi ya 840 zimeanguka, nyumba zaidi 1,264 zimepata nyufa kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nikuhakikishie ukifika pale Bukoba Mjini utakuta karibu nyumba zote zina nyufa, Bukoba Vijijini nyumba nyingi zina nyufa, Misenyi, Muleba na kadhalika lakini vifaa vya ndani vimeharibika kwa kweli ni tatizo kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana na kumpongeza Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuona umuhimu wa tatizo hili na akaamua kuahirisha ziara yake ili aweze kulishughulikia akiwa hapa hapa. Namshukuru Waziri Mkuu, Mheshimiwa Majaliwa kwa upendo wake, kwa kuwajali watu na uharaka alioutumia kufika Bukoba kwenye site akaweza kuwafariji watu lakini akashiriki vilevile kwenye hatua za awali za mazishi. Niwapongeze viongozi wa Mkoa ambao wako kule kule, kuna Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi, Mstahiki Meya wa Manispaa, Madiwani, Kamati za Maafa wote hawalali sasa hivi kila mtu anahangaika afanye nini. Nimshukuru Waziri, Mheshimiwa Jenista Mhagama ambaye yuko huko kwa sasa wanapanga mipango na kuangalia wanasaidiaje. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwashukuru na Wabunge wa CCM na Wabunge wa Upinzani ambao wamekwenda kule…
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba Serikali iongeze nguvu ya kuweza kupeleka vitu haraka kwa sababu watu wanalala nje na mvua zimeanza.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari za Mwaka 2016
MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia muswada huu.
Kwanza kabisa, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Nape, Mheshimiwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Anastazia Wambura, kwa kuleta muswada huu mbele ya Bunge hili, muswada ambao umesubiriwa kwa muda mrefu sana. Naipongeza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Peter Serukamba kwa kuweza kujadili na kurekebisha muswada huu kwa kiasi kikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, historia ya muswada huu ni ndefu sana, ina zaidi ya miaka 20. Tumeelezwa hapa, kwa mara ya kwanza muswada huu uliletwa Bungeni mwaka 1993, lakini wanahabari wakalalamika kwamba walikuwa hawajashirikishwa vya kutosha na kwamba muswada huu ulikuwa unabana uhuru wa habari, kwa hiyo, ukaondolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, muswada huu ukaendelea kurekebishwa, ilipofika Machi, 2015 ukaletwa tena Bungeni, wanahabari wakalalamika kwamba hawajashirikishwa tena, lakini vilevile wakawa wanahoji, kwa nini umeletwa chini ya hati ya dharura, muswada ukaondolewa tena. Serikali ikaendelea kuurekebisha huu muswada, ilipofika mwaka huu mwezi wa nane, ikatangaza kwenye Gazeti la Serikali na ilipofika tarehe 16 Septemba, muswada huu ukasomwa mara ya kwanza humu Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mwezi mmoja, wadau wa habari wakaitwa mbele ya Kamati ili watoe maoni yao, wakasema hawana maoni kwa sababu muda umekuwa mfupi. Kamati ikawapa muda wa siku kumi zaidi. Baada ya siku kumi wengine wakaleta maoni lakini wengine wakaendelea kusema kwamba muda ulikuwa hautoshi wanataka mpaka Februari, 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii kwa kweli mimi ilinishangaza sana kwa sababu, huu muswada umesubiriwa zaidi ya miaka 20 na hao hao wanahabari. Wanahabari wameendelea kulalamika kwamba Sheria ya Magazeti inawatesa, wamepata nafasi, muswada wenyewe wenzangu una kurasa 28 tu, mtu ambaye una interest na huu muswada utashindwaje kusoma kurasa 28 katika karibu siku 43 walizopewa ukajadili na ukaweza kutoa maoni?
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo wale wale waliosema hawana maoni, wakawa wanaonekana kila siku kwenye vyombo vya habari, wanatoa maoni juu ya huu muswada kifungu kwa kifungu. Kwa sababu hii Kamati ilikuwa sikuvu, tukaendelea kuyasikiliza hata yaliyokuwa kwenye vyombo vya habari, na kwa kiwango kikubwa yote yameingizwa kwenye huu muswada ambao upo mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende sasa kwenye vifungu. Ukiangalia kifungu cha 7(1)(b)(iv), hiki kinaonekana bado kina ukakasi kwa sababu kinazungumzia wajibu na haki ya vyombo vya habari kwamba kutangaza na kuchapisha habari au muswada ambao ni muhimu kwa Taifa kwa kadri Serikali itakavyoelekeza.
Ndugu zangu, hapa Serikali inachosema ni kwamba ikitokea kwa mfano dharura, leo hii kimekuja kimbunga kama vimbunga tunavyoona huko Amerika, inatakiwa watu wa Dar es Salaam centre pale waondolewe na kupelekwa Kibaha, au ikitokea vita mahali popote hapa Tanzania, wanategemea kwamba vyombo vyote vya habari vitakuwa vinatangaza juu ya hiyo vita; kisije kikatokea chombo cha habari wakati huo kikaendelea na programu zake za kawaida na wengine wanatangaza burudani. Kwa wakati huo watatakiwa kutangaza kitu hicho muhimu ambacho ni kwa ajili ya maslahi ya Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 7(3) kinaipa ukuu hii sheria ambayo tunaitunga sasa. Ikitokea mgongano kati ya sheria hii na sheria yoyote ile, basi hii sheria ndiyo itatumika kuamulia huo mgongano. Mimi hiki nakiona kama ni kitu kizuri kwa sababu sheria ambayo inaweza kumtetea au kutetea chombo cha habari ni hii hapa. Kwa hiyo, naona ni vizuri kiendelee kuwemo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia vifungu vya 9, 17, 10, 50(4); Kifungu cha 9 kabla ya kurekebishwa kilikuwa kinampa Mkurugenzi wa Habari uwezo wa kukataa maombi ya kutoa leseni kwa yeyote ambaye hajatimiza vigezo au kufuta leseni kama mwenye leseni atakuwa hakuzingatia masharti.
Kifungu cha 17(1) kilikuwa kinatamka kwamba Waziri ndio mamlaka ya mwisho ya nidhamu, lakini kwa sasa kifungu cha 10 kinampa uwezo mhusika ambaye hajaridhika kwenda kukata rufaa mahakamani na akasikilizwa. Kwa hiyo, wale ambao wanajadili, tusipotoshe umma, hivyo vipengele vingine vilishafutwa au vilishaondolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 56 kilimpa Mkurugenzi wa Habari au Afisa Polisi kutwaa kifaa kwa sababu kama angekuwa anaona kwamba chombo cha habari kinaendeshwa kinyume na sheria.
Kifungu cha 50(4) kilikuwa kinaruhusu mashine ya kupiga chapa iliyotumika kuchapa taarifa ya uchochezi kuchukuliwa au kuzuiliwa na Afisa wa Polisi kabla ya hata kusikilizwa. Hayo mambo yote yamefutwa tusiwadanganye Watanzania, hayapo tena kwenye muswada huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii inaanzisha utaratibu, sheria hii imeweka mchakato, sheria imeweka hata na Kamati ya Malalamiko. Hivyo ukiangalia hata 56(2), wale waliokuwa wanaogopa kwamba Waziri ana mamlaka kubwa, anaweza kuamka asubuhi akafungia chombo chochote au gazeti lolote analolitaka, hayo hayapo kwa mujibu wa sheria hii tunayotunga, yote yameondolewa; kila mtu atapewa haki na mahakama. Kama hujaridhika na uamuzi wa Waziri unaweza kwenda ukakata rufaa kwenye mahakama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 18 cha Muswada huu, kinaanzisha Bodi ya Ithibati ya Wanahabari na vilevile kifungu cha 23 kinaanzisha Baraza Huru la Wanahabari. Hii sasa maana yake ni nini? ni kwamba sasa tunakwenda kuifanya tasnia hii kuwa taaluma kamili. Sasa tunakwenda kuijengea taaluma hii heshima, tunakwenda kupunguza makanjanja ambao walikuwa wanaharibu tasnia hii kwa kuandika habari ambazo ziko substandard tukiweza kuweka Bodi pamoja na Baraza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha 18 kinazungumzia juu ya ithibati ya wanahabari; mtu hataruhusiwa kufanya kazi ya habari kama hatakuwa amethibitishwa na utaratibu unaowekwa na sheria hii. Nimewasikiliza waliokuwa wanaongea na nimewashangaa sana. Wanataka kutuambia kwamba katika karne hii na baada ya sayansi na teknolojia iliyokuwa mpaka kiwango hiki, mtu yeyote anayejua kufunga kidonda, tumuite daktari; mtu yeyote yule ambaye amekwenda kwenye semina ya wiki moja, akirudi kwa sababu ilikuwa inahusu sheria awe mwanasheria; na mtu yeyote anayejua kushika kalamu na karatasi akaandika aitwe mwanahabari, haiwezekani. Hii Bodi ya Ithibati lazima iwepo na wanahabari wenyewe ndiyo kitu wanachokitaka, wanataka iwe taaluma, iheshimike ili na viwango vya mishahara yao viweze kufahamika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine wanapotosha, wanadanganya watu kwamba kuna kiwango cha elimu, kwamba mtu ambaye hana degree hawezi kuitwa mwanahabari. Hakuna mahali popote kwenye muswada huu yalipoandikwa hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii imetambua kwamba sasa tutakuwa na Bodi ya Ithibati, tutakuwa na Baraza Huru la Wanahabari; yote hii itakuwa na wanahabari ambao wamebobea. Watakaa chini, wataweka vigezo vya nani awe mwanahabari. Hivi vigezo vitawekwa kwenye kanuni kwa sababu ukiweka kwenye sheria, vikitakiwa kubadilishwa ni rahisi kubadilisha kanuni kuliko kubadilisha sheria.
Kwa hiyo, hivi vigezo vitawekwa kwenye kanuni. Hivyo jamani msiwadanganye watu, waache tuwaboreshee wawe na tasnia nzuri ambayo itakuwa inaheshimika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 11 kinazungumzia juu ya muundo wa bodi, hakijazingatia jinsia. Napendekeza waweke kifungu kidogo kimoja cha kuweza kuzingatia jinsia. Hebu angalia Wanahabari wote Waandamizi, karibu wote ni wanaume. Kwa hiyo, hiki kipengele kikiachwa hivi hivi unaweza ukakuta Bodi nzima ina watu wa jinsi moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, muswada huu ni mzuri, utaifanya tasnia hii kuheshimika, itakuwa ya kitaaluma, lakini kwa kupewa ithibati, kitawafanya wamiliki wa vyombo vya habari waweze kuwalipa wanahabari mshahara unaostahili na vilevile wataweza kuwakatia bima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, tumwombe Mheshimiwa Waziri baada ya sheria hii kuwa imesainiwa aharakishe kuandaa kanuni ili sheria hii ianze kutumika mara moja kwa sababu imesubiriwa kwa zaidi ya miaka 20.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma wa Mwaka 2017
MHE. BENARDETHA MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu pamoja na Wakurugenzi Wakuu wa mifuko kwa kuandaa na kutuletea huu muswada. Naipongeza sana Serikali, nimeangalia huu muswada waliotugawia leo asubuhi, naona wamezingatia maoni ya wadau pamoja na marekebisho makubwa yaliyofanywa na Kamati. Ahsanteni sana Serikali kwa kuwa wasikivu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, muswada huu unalenga kuunganisha hii mifuko yote mitano tukabakia na mifuko miwili, mmoja wa Umma na mwingine wa binafsi kwa lengo la kuboresha mafao ya wafanyakazi. Kwa hiyo, ni kitu kizuri, nakiunga mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Ibara ya 18 ya muswada huu inayozungumzia michango kwamba mwajiri atachangia asilimia 15 ya mshahara na mwajiriwa atachangia asilimia tano; lakini ukiangalia 18(b) hii imempa Waziri mamlaka ya kuweza kubadilisha viwango kadri atakavyoona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikitokea tukawa na Waziri wakati fulani ambaye hajali wafanyakazi, unaweza ukakuta huyu Waziri ameamua kupanga kwamba contribution ya mfanyakazi iende mpaka asilimia 30. Hii inaweza ikawa shida, kwa sababu kwenye mshahara huo huo labda ukute alikuwa ni mwanafunzi anakatwa Bodi ya Mikopo, anakwata PAYE, anakatwa na vitu vingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nafurahi kwamba sasa hivi kwenye kipengele hicho wamebadilisha wakasema kwamba mpaka ifanywe actuarial valuation. Sasa nataka nimuulize Mheshimiwa Waziri kwamba hiyo actuarial valuation inafanywa kwenye mfuko au inafanywa kwa mfanyakazi aonekane ana nguvu kiasi gani ya kuweza kuchangia? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 20 inazungumzia juu ya michango isiyowasilishwa. Hali ilivyo sasa hivi ni kwamba unakuta wastaafu wengi wanapostaafu, wanalipwa mafao kidogo sana kwa sababu michango ilikatwa kutoka kwenye mishahara yao, lakini haikuwasilishwa kwenye mifuko. Katika kipengele cha 20 kimeainisha kwamba huyu mtu sasa awe michango yake imeshawasilishwa kwenye mifuko au haijawasilishwa, mfuko utatakiwa umlipe mafao yake yote na ule mfuko wenyewe ndiyo uendelee kudaiana na mwajiri Hiki ni kitu kizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nilikuwa napendekeza ilivyoandikwa pale kwenye kipengele cha 20 kinachosema; “Where the Director General is satisfied that an employee’s contribution has been deducted from his earnings, but the employer has failed to remit the contribution together with the paid employer’s contributions to the fund, he shall treat the unremitted contributions as wholly or partially paid to the purpose...” Nilikuwa napendekeza neno “partially” liondoke pale, linaleta ukakasi kusudi tuhakikishe kwamba huyu mwajiriwa atalipwa mafao yake yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 29 inazungumzia mafao atakayopata mwanachama; ni mafao saba. Naipongeza Serikali kwa sababu wameweka mafao ya yule ambaye atakuwa amestaafu, lakini vile vile kuna namna ambapo huyu hajafikia umri wa kustaafu, atafaidika. Napenda kuuliza kwamba kuna invalidity benefits ambayo inahusu watu wenye ulemavu. Ni kitu gani kitalipwa na hii mifuko ya hifadhi ya jamii na kitu gani kitalipwa na Workers Compensation Fund?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kitu kinaitwa unemployment benefit, nawashukuru sana kwa kuliweka hili fao. Kwa mara ya kwanza katika Tanzania tutakuwa sasa tumetoa faraja kwa mtu aliyepoteza ajira. Pia naomba Mheshimiwa Waziri atufafanulie zaidi, ni kitu gani huyu mtu anategemewa kupata kwenye unemployment benefit?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 56 inazungumzia juu ya msamaha wa kodi kwenye mafao. Hii ibara imekaa vizuri kwa sababu huyu mtu amehangaika, sasa amefikia kustaafu, ukute na ile pension yake ya kila mwezi au ile gratuity anayoipata ikatwe kodi. Kwa hiyo, kipengele hiki kimesomeka kwamba huyu mtu hatakatwa kodi. Kwa hiyo, naipongeza Serikali kwa kufanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ila ningependa kuona, inaweza ikatokea wakatunga Sheria za Kodi ambazo zinalazimisha sasa kwamba ile pension ambayo iko kwenye sheria hii iende kukatwa kodi. Napenda kuona kwenye muswada huu au sheria hii waweke kipengele kinacholinda pension ya mfanyakazi kwamba hata zikitungwa sheria nyingine za kodi zisilazimishe pension ya mfanyakazi kukatwa kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, msingi wa muswada huu ni mapendekezo ya wafanyakazi na mategemeo ya wafanyakazi ni kwamba mifuko hii iunganishwe; gharama za uendeshaji zipungue, kusudi wao waweze kupata mafao makubwa zaidi. Sasa bahati mbaya kikokotoo kweli hakipo kwenye huu muswada na Mheshimiwa Waziri anasema watakiweka kwenye kanuni. Napendekeza kanuni zikishatungwa zipelekwe mbele ya Kamati itakayokuwa inahusika hizi… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)