Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Bernadeta Kasabago Mushashu (3 total)

MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka nenda, miaka rudi tofauti na kada nyingine za watumishi, kero imekuwa madeni ya walimu, madeni ya walimu. Leo hii mnatuambia kwamba madeni ya walimu yamefikia takribani shilingi bilioni 34 plus. Walimu hawa wanaidai Serikali wengine kama matibabu, likizo, kwa miaka zaidi ya mmoja hadi miwili. Walimu waliopandishwa mishahara miezi 12 iliyopita hadi leo hawajalipwa huo mshahara wanausikia harufu tu. Walimu wengine wamestaafu zaidi ya miezi sita hawajapata mafao yao.
Ningependa kujua kwa kuwa sasa hivi Serikali mnasema mmeshahakiki ni lini, na mnipe tarehe na mwezi hawa walimu watakuwa wamelipwa haya madeni kwa sababu wamechoka kila siku madeni ya walimu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuna walimu waliosimamia mitihani mwaka 2015. Leo hii tunazungumza mwaka 2017, kwa nini hadi leo hawajalipwa na ni lini Serikali itakuwa imewalipa hiyo stahili yao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema awali, kwanza tuweke kumbukumbu vizuri. Katika kada ambayo Serikali katika njia moja ua nyingine imekuwa ikishiriki vizuri sana katika ulipaji wa madeni ni kada ya walimu. Ukiangalia miaka mitatu mfululizo, trend ya malipo ya madeni ya walimu ambayo tulikuwa tumezungumza hapa katika Bunge kila wakati, kwa kweli Serikali inajitahidi sana. Na ndio maana katika kipindi cha sasa hata ukiangalia katika mwezi wa 11 uliopita huu kuna baadhi ya madeni ya walimu especially katika baadhi ya Wilaya, Halmashauri, kwa mfano kuna Temeke na Halmashauri zingine kulikuwa na outstanding deni karibuni ya shilingi bilioni moja nayo ililipwa vilevile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio maana katika ulipaji wa madeni mapya mengine; ndio maana Serikali ilikuwa inafanya zoezi zima la uhakiki. Na bahati nzuri, ofisi yetu ya TAMISEMI pamoja na Ofisi ya Hazina ndio ilishiriki, na jambo hili sasa hivi limekamilika. Na ndio maana nimesema hapa siwezi kutoa deadline ni lini, deni hilo litalipwa lakini kwa sababu mchakato wa uhakika umekamilika, hili deni la shilingi bilioni 26 ninaamini sasa hazina si muda mrefu mchakato wa malipo utaanza kuanza.
Naomba Mheshimiwa Mbunge, najua uko makini katika hili lakini amini Serikali yako kwa vile zoezi la uhakiki ambalo lilikuwa ni changamoto limekamilika basi walimu hawa si muda mrefu wataweza kulipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala zima la deni la kusimamia mitihani na ndio maana nilisema deni hili lilikuwa ni miongoni mwa madeni haya ambayo yaliyohakikiwa ambayo takribani ilikuwa ni shilingi bilioni sita.
Naomba tuondoe hofu walimu wangu katika mchakato wa sasa walimu hawa wote wataendelea kulipwa ili mradi kila mtu haki yake iweze kulipwa, na Serikali haitosita kuhakikisha inawahudumia vyema walimu wake kwa sababu italeta tija kubwa sana katika sekta ya elimu.
MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU: Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na mikakati mizuri na mingi ya Serikali, lakini bei ya kahawa ya mkulima Mkoani Kagera bado ni Sh.1,000 kitu ambacho kinamuumiza mkulima. Kwa kuwa soko la kahawa linategemea soko la dunia, linategemea mauzo nje ya nchi, mahali ambapo mkulima wa kawaida au Vyama vyetu vya Ushirika hivi vya Msingi hawana uwezo wa kuyafikia hayo masoko. Pia kwa kuwa msimu unaofuata wa kahawa unaanza hivi keshokutwa mwezi wa Tano, ili makosa yasijirudie mkulima akaendelea kulipwa 1,000, je, Taasisi za Serikali ambazo zinahusika na utafutaji wa masoko wana mipango gani ya kwenda kule nje ya nchi wakawatafutia Watanzania masoko ikiwezekana wakaingia na mikataba na nchi hizo ili Watanzania wauze kahawa zao na waweze kupata bei nzuri? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwenye baadhi ya super market huko China imeonekana kahawa ambayo inaonekana imetoka Uganda imekaangwa tu haijasindikwa zaidi ya hapo na ikawekwa kwenye kifungashio kizuri, robo kilo inauzwa kwa dola 40 ambayo ni zaidi ya Tanzanian Shillings 88,000 wakati sisi mkulima anapata 1,000 kwa kilo. Je, Wizara zinazohusika kama Wizara ya Kilimo, Wizara ya Viwanda na Biashara, wanawaandaaje Watanzania kwa maana ya wakulima na wafanya biashara wasindike kahawa badala tu ya wakulima kuuza zile zilizo ghafi kusudi Mtanzania aweze kupata bei nzuri na hasa hasa mkulima kutoka Mkoa wa Kagera?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata nafasi hii. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mushashu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza anataka kujua mikakati iliyopo kwa ajili ya kuongeza bei ya mkulima kutoka Sh.1,000 wanayolipwa sasa mpaka ile ambayo itaridhisha na kukidhi gharama za uzalishaji. Kwanza kwa niaba ya Serikali, Wizara ya Kilimo, baada ya kuona changamoto hiyo ya zao la kahawa, bei yake na mazao mengine, tumeanzisha Kitengo cha Utafiti wa Biashara na Masoko ambacho kimeanza kazi tangu tarehe Mosi Julai, 2018. Lengo la kitengo hiki ni kuratibu na kufuatilia mwenendo wa masoko duniani na kutoa taarifa sahihi kwa wakulima wetu wakishirikiana na wenzetu wa Wizara ya Viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa pili tunashirikiana kwa karibu sana na Balozi zetu zilizokuwa nje. Hapa nichukue nafasi kumpongeza sana Balozi wetu wa China, Ndugu Kairuki kwa kazi kubwa anayoifanya na ameweza kutupatia soko jipya la kahawa nchini China lakini pia na Mabalozi wa nchi nyingine kama za Japan, Ujerumani, wote hawa wamekuja na mikakati mizuri na kupanua soko la kahawa yetu inayotoka hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili anataka kujua kwamba mikakati ya kuongeza thamani ya mazao yetu ikiwemo kahawa ili kahawa hii badala ya kuuzwa ghafi tuweze kuiuza wakati imechakatwa. Kwanza niendelee kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa muono huu, lakini nataka nimwambie kwamba Serikali tulishaanza muda mrefu mipango hii na ndiyo maana siyo kwa zao tu la kahawa, hata korosho umeona mwaka huu tumeanza kubangua na mwakani Insha Allah tutabangua zaidi ya asilimia 50 kwenda juu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali lake la msingi la kahawa; pia tulishaanza kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vyetu na kiwanda kimojawapo cha Amir Hamza kimeshaanza kuchakata kahawa ya Mkoani Kagera kwa ajili ya kuiuza kahawa iliyokuwa imeshachakatwa badala ya kuuza kahawa ghafi. Pia kwa wakulima hawa tunaendelea kuwasisitiza wajiunge kwenye vikundi vyao vya ushirika ili Serikali tuweze kuwasaidia kwa ukaribu kwenye umoja wao kuongeza mitaji na kununua mashine ndogo ndogo za kuchakata mazao yao, kuuza mazao ya kahawa iliyosagwa badala ya kuuza kahawa ghafi.
MHE. BERNADETHA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Bukoba Sekondari ina umri wa miaka 80, Rugambwa Sekondari ina umri wa miaka 55 lakini pamoja na uzee shule zote zilipitiwa na tetemeko na Bukoba Sekondari ikaja vilevile ikaezuliwa na kimbunga. Kwa niaba ya Mkoa wa Kagera na wanafunzi wanaosoma katika shule hizo, naipongeza sana Serikali kwa kutoa Sh.1,481,000,000 kwa ajili ya kukarabati Bukoba Sekondari na kuahidi kukarabati Rugambwa mwaka huu kuanzia mwezi huu wa Aprili. Kwa kuwa Rugambwa wakati wa tetemeko nyumba za walimu na zenyewe zilianguka na nyingine zikaathirika sana, hadi leo Mkuu wa Shule hana mahali pa kuishi, je, Serikali ina mpango gani wa kuwajengea nyumba za kuishi walimu wa Shule ya Sekondari Rugambwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, shule zote mbili, Bukoba Sekondari na Rugambwa zinahitaji kumbi za mikutano. Bukoba Sekondari haina ukumbi kabisa, Rugambwa ukumbi wake ni mdogo sana unachukua watoto 300 wakati wako wanafunzi karibu 700/800. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwajengea kumbi za mikutano ili wanafunzi wapate mahali pa kufanyia mitihani na kufanyia mikutano?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba kwa dhati kabisa na kwa furaha kubwa nipokee shukrani na pongezi za Mheshimiwa Mbunge kwa kazi ambayo Serikali imefanya katika shule zake. Lazima niseme kwamba Mheshimiwa Mushashu ni moja kati ya Wabunge makini sana katika Sekta ya Elimu na tumeendelea kufarijika na uzoefu wake mkubwa kama Mwalimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maswali yake, kwanza kuhusiana na nyumba za Walimu katika Shule ya Rugambwa, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunavyozungumza tayari Serikali inafikiria kujenga nyumba nane za Walimu katika shule ya Rugambwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na kumbi za mikutano katika shule zote mbili, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia ikiwa ni pamoja na miundombinu katika shule zake kadiri uwezo wa fedha utakavyoruhusu.