Contributions by Hon. Bupe Nelson Mwakang'ata (19 total)
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu na kuwashukuru wanawake wa Mkoa wa Rukwa kwa kuniwezesha kuwawakilisha Bungeni, Mwenyezi Mungu awabariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa ushindi mkubwa alioupata na kuanza kazi mara moja ya utekelezaji wa ilani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Waziri wa Fedha kwa kuwasilisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa utakaokuwa dira ya utekelezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze sasa kuchangia na kuishauri Serikali sikivu ya Chama cha Mapinduzi kwamba, mpango huu ungetoa kipaumbele cha kwanza cha maji safi na salama hivyo kutokana na shida kubwa wanayoipata wanawake wa Mkoa wa Rukwa kufuatia maji kwa mwendo mrefu wakati huo shughuli za kilimo zinawasubiri, kulea watoto kunawasubiria, hata akinababa wanawasubiri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake wa Mkoa wa Rukwa wanapata shida sana ya maji, imepelekea kwamba na wananachi wengine wameamua kuchimba visima vya kienyeji ambavyo vimepelekea kuleta matatizo ya watoto kutumbukia kwenye visima hivyo na vijana wengine wawili kufariki kwa sababu ya kutumbukia kwenye hivyo visima.
Mheshimiwa Injinia Stella Manyanya yupo hapa ni shahidi, naishukuru kwanza Serikali ya Chama cha Mapinduzi ilileta mradi wa bilioni 30, lakini huo mradi hakuna maji mpaka sasa hivi. Naomba niishauri Serikali ya Chama cha Mapinduzi huo mradi uishe mara moja ili tatizo la maji liweze kuisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niingie kwenye suala la kilimo, ili kwenda kuwa Tanzania ya viwanda lazima wakulima waangalie sana katika kuwapatia zana za kilimo na pembejeo. Suala la pembejeo ni muhimu sana kwa sababu wakulima wanapata pembejeo na mbolea kwa kuchelewa. Ili tuweze kwenda na wakati kwa Tanzania ya Viwanda lazima wakulima wapate pembejeo kwa wakati na mbolea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la uwezeshaji, kama ilani ya Chama cha Mapinduzi inavyoeleza kwamba itawawezesha wanawake na vijana kwa kutoa milioni hamsini kwa kila kijiji, Mpango huu ni mzuri naomba sasa Serikali itekeleze.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Awali ya yote namshukuru sana Mwenyezi Mungu kutujaalia uzima. Pia naomba niwashukuru wananchi wa Mkoa wa Rukwa kwa kuniamini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa umahiri wake wa kazi, uwajibikaji na kuiletea heshima Serikali. Nimpongeze pia Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa kwa kuchaguliwa kwake na uchapakazi wake. Niwapongeze Mawaziri wote na Manaibu wote kwa uchapakazi wao mzuri, hakika tunayo majembe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono hoja wakati nikitaka ufafanuzi wa hoja zifuatazo; Mkoa wa Rukwa uliiunga mkono Serikali hii kwa kukipatia Chama cha Mapinduzi kura nyingi sana za kishindo, sasa nipe nikupe. Je, uwanja wa ndege wa Sumbawanga utaanza kujengwa lini? Wananchi wanapata shida sana kutokana na umbali, hasa wanaposafiri kwenda Dar es Salaam ambako huduma nyingi za Serikali hutolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wananchi wa Sumbawanga, wenyeji wa Bagwe, wanaoishi pembezoni mwa uwanja walifanyiwa tathimini ya nyumba zao muda mrefu kwamba watalipwa na nyumba zao zikawekwa alama ya “X” kwa muda mrefu. Mpaka sasa hawajalipwa na wanakosa huduma muhimu za kibenki na huduma nyingine mbalimbali, je, watalipwa lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ningependa kuishukuru Serikali kwa kutambua umuhimu wa Barabara ya Sumbawanga - Mpanda - Nyakanazi yenye urefu wa kilometa 346.6 kwani barabara hii ni kiungo muhimu cha mawasiliano. Lakini kuna barabara ya Kibaoni - Muze - Mtowisa - Ilemba - Kilyamatundu kilometa 200 ijengwe kwa kiwango cha lami kwani ukanda huu wa Bonde la Ufa ndiko mazao mengi yanatoka huko kama ngano, asali, mpunga, samaki, ufuta na mazao mengine. Kwa hiyo, ni vema ikajengwa kwa kiwango cha lami na madaraja yajengwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo barabara ambazo zinasimamiwa na Halmashauri ambazo hawawezi kuzihudumia kutokana na fedha wanazozipata, ikiwemo Kalambazite - Ilemba ambapo hii barabara iliomba ibadilishwe iwe ya TANROADS kwa sababu inakidhi viwango na nyingine ni barabara ya Miangaluna - Chombe, Mtowisa - Kristo Mfalme, Mawenzusi - Msia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sijajua Serikali inafikiria nini juu ya mgogoro wa shamba la Efatha ambao ni wa muda mrefu. Wananchi wanapata shida hata kupitisha barabara, matokeo yake wananchi wameendelea kuwa maskini kwa kushindwa kuwasomesha watoto. Naomba Serikali yako sikivu iwarudishie shamba hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nichukue fursa pekee kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano ambayo ni ya Hapa Kazi Tu, chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwa uamuzi wa kununua ndege zetu. Hii itatujengea heshima kubwa na tutaendelea kumuunga mkono Rais wetu kwa jitihada zake za kutumbua majipu na kukusanya kodi kwa wingi na hususani Mkoa wa Rukwa. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Awali ya yote, namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima. Pia nawashukuru wananchi wa Mkoa wa Rukwa kwa kuniona mimi niweze kuwawakilisha katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza pia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa umahiri wake, kwa uchapakazi wake, hatimaye kuirudishia heshima Serikali yetu. Naomba pia niwapongeze Mawaziri wote na Manaibu kwa uchapakazi wao mzuri. Hakika kweli tuna majembe na Mungu awabariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono hoja nikitaka ufafanuzi wa hoja zifuatazo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Rukwa uliiunga mkono Serikali hii kwa kukipatia Chama cha Mapinduzi kura nyingi sana za kishindo. Sasa nipe nikupe!
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Mkoa wa Rukwa wanapata shida sana hasa kwenye suala la ardhi. Suala la ardhi limekuwa ni shida upande wa shamba la Efatha. Imekuwa ni kizungumkuti kwa shamba la Efatha kwa sababu mpaka sasa hivi hatujajua Serikali ina mpango gani na wananchi wanaolizunguka lile shamba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanapata shida sana, wamekuwa maskini, hawawezi kusomesha watoto wao kwa sababu tu ya hili shamba limechukuliwa na mtu mmoja ambaye anaitwa Efatha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefikia wapi juu ya mgogoro huu? Huu mgogoro umekuwa wa siku nyingi sana, Wabunge wa Mkoa wa Rukwa wote wamelipigia kelele sana hili suala, lakini mpaka sasa hivi halijapata ufumbuzi wowote. Je, Serikali ina mpango gani na hili shamba? Kuna tatizo gani kulikomboa hili shamba kuwarudishia wananchi? Naiomba sana Serikali yangu sikivu ya Chama cha Mapinduzi chini ya Mheshimiwa Lukuvi, hili shamba lirudi kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee pia wananchi wanaoishi uwanja wa ndege wa Sumbawanga Rukwa. Wale wananchi walifanyiwa tathmini za nyumba zao na ziliwekewa X muda mrefu, zaidi ya miaka saba. Wananchi hawa hawana urafiki tena na mabenki, wanashindwa kufanya shughuli zao za msingi kwa sababu tu hizi nyumba ziliwekewa X, wanashindwa kuzipangisha. Naomba sana Serikali iwaangalie kwa jicho la huruma hawa wananchi wa Vijiji vya Bangwe, Izia wanaozunguka uwaja ule wa ndege. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee pia hizi nyumba za National Housing. Kabla Serikali haijaanza kujenga, inatakiwa ifanye utafiti kwanza kuangalia vipato vya wananchi ili ipange bei kulingana na vipato vya wananchi. Wananchi hawawezi kuzinunua zile nyumba kwa sababu vipato vyao ni vidogo. Kwa hiyo, naomba sana Serikali iliangalie suala hili. Nawapongeza sana kwa kujenga zile nyumba, lakini zile nyumba gharama yake ni kubwa sana kiasi kwamba wananchi hawawezi kuzinunua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa haya machache, naomba Serikali iyafanyie kazi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika hotuba hii ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima, lakini pia nichukue nafasi hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na naomba nichukue dakika moja kumuombea katika kazi anazozifanya naanza kwa kusema Baba katika jina la Yesu, damu ya Yesu imfunike Dkt. John Pombe Magufuli, imfunike Majaliwa, imfunike Jenista Mhagama, ifunike Mawaziri wote, ifunike Serikali ya Tanzania ninakushukuru Baba wa Mbinguni kwa sababu Serikali ya Tanzania inafanya kazi kwa jinsi watu wanavyoitaka wote tuseme Amen.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze sasa kwa kuchangia katika Wizara ya Elimu. Mkoa wa Rukwa hauna Chuo cha VETA. Chuo cha VETA kimezungumziwa muda mrefu sana lakini mpaka sasa hivi hakuna kinachoendelea nataka kujua tatizo ni nini? Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuleta majibu hapa atuambie kuna tatizo gani kuanzisha chuo cha VETA katika Mkoa wa Rukwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee maabara, Serikali ya John Pombe Magufuli ilianzisha kujenga maabara katika shule za sekondari na ilikuwa na nia nzuir lakini mpaka sasa hivi maabara nyingi hazijaisha tatizo ni nini watoto wanaotaka kusoma chemistry, science wanashindwa kupata elimu nzuri, ninaomba Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi safari hii kwenye bajeti hii iweke fungu la maabara ziishe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la walimu, tangu zoezi hili la kuwabadilisha walimu wa sekondari waende wakafundishe kwenye shule za msingi limeleta shida kidogo kwa sababu shule za sekondari sasa zimepungukiwa na walimu. Nilikuwa naomba Serikali ifanye haraka kuwaajiri walimu ili shule za sekondari sasa ziweze kukidhi mahitaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la ukubwa wa Mkoa wa Rukwa, Mkoa wa Rukwa una majimbo matano, lakini kuna majimbo mawili ni makubwa sana nataka niongelee Jimbo la Kwela, jimbo la Mheshimiwa Malocha, jimbo lile lina kata 27 limejigawa Ufipa wa Juu na Ufipa wa Chini. Ufipa wa Juu una kata 14 na Ufipa wa Chini una kata 13. Mheshimiwa Malocha amekuwa akifanya kazi ngumu sana na kubwa, lile jimbo ni kubwa sana na ameliongelea muda mrefu kwamba tunaomba basi ligawanywe kwa sababu wananchi wanashindwa kupata huduma kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mweyekiti, ukianza Ufipa wa Chini ukizungukia Ufipa wa Chini kabla haujamaliza unapandisha Ufipa wa Juu unakuwa umeishiwa mpaka mafuta. Ufipa wa Juu wanaanza kulalamika kwamba Mbunge hatufikii sisi hapa watu wa Ufipa wa Juu ni kwa sababu lile jimbo limekuwa kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni sawa na jimbo la Mheshimiwa Kandege na lenyewe lina kata 27 nilikuwa naomba kwa sababu hili linatuletea shida sana hata kwenye upande wa kisiasa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika Wizara hii ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uzima, hatimaye kuwawakilisha wananchi hapa Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kuwapongeza Mawaziri wote kwa uchapakazi wao mzuri na uwajibikaji. Hakika hawa Mawaziri hawajakaa maofisini kama tunavyojua Maofisa wanavyokaa maofisini kusubiri changamoto. Wamekuwa wakizunguka Mikoa kwa Mikoa, Majimbo kwa Majimbo kuhakikisha wanajua changamoto za wananchi. Mheshimiwa Rais hakukosea kuwateua, hakika Mungu awasaidie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kumpongeza Waziri wa Kilimo na Naibu Waziri wake kwa kazi nzuri wanazozifanya. Pamoja na changamoto wanazozipata za hali ya hewa, lakini wamekuwa wakichapa kazi kuhakikisha wanaendeleza Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi ya pekee kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa uchapakazi wake mzuri, kwa uwajibikaji, hatimaye kuliletea Taifa nidhamu. Rais huyu amekuwa akifanya kazi usiku na mchana japokuwa kuna watu wamekuwa wakimbeza wakisema Rais huyu ni wa ajabu, siyo kweli!
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais huyu ametenda maajabu ambayo hawakuyategemea. Rais huyu kwa muda mfupi tu ameweza kufanya mambo makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ameweza kuhakikisha kwamba watoto wanasoma bure, pili, ametengeneza barabara zote, sasa hivi zinapitika kwa kiwango cha lami, tatu, ameweza kununua ndege, mmeziona, mmeshuhudia na nyingine bado zinakuja, Rais huyu amefanya mambo mengi sana. Amerekebisha mambo mengi sana! Ni mtambo wa kurekebisha tabia za mafisadi! Mungu amjalie huko aliko, nasi tupo nyuma yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze sasa kwenye suala la pembejeo. Mkoa wa Rukwa umekuwa ni mkoa ambao unalima mazao mengi yanayokubali. Mkoa huu umekuwa ulikilisha mikoa mingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali yangu sikivu ya Chama cha Mapinduzi iangalie mikoa hii ambayo mvua ni za uhakika ipeleke pembejeo kwa wakati. Huu mpango ambao umeanza kutumia mawakala, naomba mawakala wapeleke pembejeo kwa wakati hatimaye wananchi wa mikoa hii wapate kulima kilimo kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la Benki ya Kilimo. Benki hii tunaisikia Dar es Salaam na Arusha. Nilikuwa naiomba Serikali, kwa sababu kuna mikoa ambayo mvua ni za uhakika na kilimo ni cha uhakika, ipelekwe benki hii ianzishe mabenki mikoa yote, ikiwezekana wilaya zote, wakulima waweze kukopa pesa za kulima na kukopa matrekta, itasaidia sana kuongeza kiwango cha kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la Soko la Samaki la Kimataifa. Mkoa wa Rukwa, Wilaya ya Kalambo lilianzishwa Soko la Samaki la Kimataifa, lakini mpaka sasa hivi soko hili linaonekana kama limetelekezwa. Kule Kalambo Ziwani kunapatikana samaki wengi sana ambao ni migebuka, sangara na samaki wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo inaonekana kwamba kwa sababu ya kukosa lile soko, kwamba halifanyi kazi, wanakuja Wakongo na Wazambia wanavua samaki mle tani na tani, wanapeleka huko. Serikali na Halmashauri zinashindwa kupata mapato na wananchi pia hawapati mapato, hilo soko haliwasaidii. Naomba Serikali ilifufue hilo Soko la Samaki la Kimataifa ili wananchi waweze kufaidiaka na Serikali pia iweze kufaidika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia bajeti hii muhimu.
Awali ya yote namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika bajeti hii muhimu. Pia naomba nimpongeze Waziri Mheshimiwa Dkt. Mpango na Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Kijaji kwa kazi nzuri wanazozifanya pamoja na Makatibu Wakuu wote wa Wizara hii nawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee naomba nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anazozifanya na nina salamu zake nyingi sana kutoka Mkoa wa Rukwa. Wanawake wa Mkoa wa Rukwa wanampongeza sana Mheshimiwa Rais, wanasema sehemu zingine wamezoea kumuandalia Rais ng’ombe, kuku na ndama lakini wanawake wa Mkoa wa Rukwa wamenituma wanasema hivi wa kazi nzuri alizozifanya Dkt. Pombe Magufuli, wamemwandalia mgolole, watambeba na mbeleko ya mgolole. Watambeba mgongoni kwa kazi nzuri anazozifanya, Mungu ambariki huko aliko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze kwenye maji. Wanawake wa Mkoa wa Rukwa hawana maji, karibu asilimia 20 wana maji, ukienda vijijini wanawake wanapata shida sana ya maji lakini Wilaya ya Sumbawanga Mjini ninaishukuru Serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli imesimamisha matenki, maji watapata ya uhakika. Ninaishauri kule vijijini wanawake wanapata shida, maji yaende kule, ile shilingi 40 ya mafuta naungana na bajeti kwamba iende kwenye maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niingie kwenye suala la barabara. Mkoa wa Rukwa ni Mkoa ambao unalima mazao na yanakubali, una mvua za uhakika, lakini barabara ya Wilaya ambapo mazao yanatoka mengi, barabara inayotoka Kibaoni inapita Muze, Mtowisa na inaishia Mlowo ile barabara ni muhimu sana, imejengwa kwa kiwango cha kokoto, lakini bado madaraja yake ni shida. Kutokana na umuhimu wa barabara hii, ningeomba bajeti ya safari hii iweke kiwango cha lami kwa sababu ufuta, mpunga, ulezi na matunda yanatoka kule, ninaomba kwa bajeti hii ikumbuke hiyo barabara ijengwe kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze kwenye suala la elimu. Mkoa wa Rukwa hauna Chuo cha VETA, vijana wanapata shida sana. Suala la VETA limeongelewa muda mrefu sana na naipongeza Serikali katika bajeti yake imeongea kwamba itajenga Chuo cha VETA, ninaomba iipe kipaumbele Mkoa wa Rukwa kujenga hicho chuo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna chuo kingine ambacho amejenga mwanamke/mama ambaye hajasoma lakini amediriki kujenga Chuo cha Wauguzi, amejenga Chuo cha Ualimu na Chuo cha Kilimo, lakini Chuo cha Wauguzi kimefungwa bila sababu za msingi. Naomba Dkt. Mpango atakapokuja kutoa majumuisho hapa anieleze hicho chuo ni kwa nini kimefungwa? Chuo ambacho ni cha mwanamke ambaye hajawahi kwenda shule, ameamua kuanzisha chuo, kwa nini kifungwe bila sababu za msingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze kwenye suala la afya Mkoa wa Rukwa karibu Wilaya zake zote hazina Hospitali ya Wilaya. Ninaipongeza Serikali kwamba pale Mkoa wa Rukwa, Sumbawanga Mjini ile hospitali iliyokuwa ya Mkoa imepandishwa kuwa ya rufaa lakini hakuna Hospitali ya Wilaya. Wanawake na watoto wanapata shida sana wanapotaka kujifungua, wanaambiwa kwamba mkaanzie kwenye vituo vya afya na vituo vya afya kule wanaambiwa hatuna bajeti za mtoto na mama kujifungua bure. Ninaomba bajeti hii ikawasaidie kujenga Hospitali ya Wilaya ya Sumbawanga Mjini, Nkasi na Kalambo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia katika Wizara hii ya Ujenzi. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima, nasi kuweza kuchangia katika Wizara hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anazozifanya. Mwenye macho haambiwi tazama; na mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni. Mheshimiwa Dkt. Magufuli Mungu yupo pamoja nawe, pamoja na Serikali yako, pigeni kazi. Watanzania wote wako nyuma yenu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeze pia Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Profesa Mbarawa pamoja na Naibu Mawaziri wake wote wawili kwa kazi kubwa wanazozifanya. Hakika Wizara hii wanaitendea haki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze sasa kwenye suala la Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga. Kwanza kabisa naishukuru sana Serikali kwa kutenga fedha. Nimeona katika ukurasa wa 154 zimetengwa fedha karibu shilingi bilioni 12 kwa ajili ya Uwanja wa Sumbawanga wa Mkoa wa Rukwa. Pamoja na shukrani hizi, bado nina hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanaouzunguka uwanja, wananchi wa Mkoa wa Rukwa walifanyiwa tathmini ya muda mrefu. Tumepiga kelele sana; Mheshimiwa Aeshi, Mbunge wa Jimbo la Sumbawanga Mjini amepiga kelele sana hapa, lakini bado wananchi wale hawajalipwa. Bajeti ya mwaka 2017 pesa zilitengwa, lakini wananchi hawakulipwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo yote Serikali inayofanya, naomba sana katika fedha hizi zilizotengwa kipaumbele kiwe kuwalipa kwanza wale wananchi. Wanatia huruma sana wale wananchi. Wengine wamekufa wameacha watoto yatima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nyumba zile hawawezi tena kuchukulia mikopo, zimebaki tu zimewekwa X. Katika hii fedha iliyotengwa, pamoja na kwamba Serikali inakwenda kujenga uwanja, lakini ichukue kipaumbele kwanza cha kuwalipa wale wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali yangu na Mheshimiwa Waziri kwa kununua ndege. Ni kazi kubwa sana waliyofanya Serikali, lakini pamoja na ununuzi wa ndege naipongeza sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi. Tunaomba Mkoa wa Rukwa hizi Bombardier nasi tupate angalau route kwa wiki hata mara moja, Bombardier ishuke pale Rukwa, wananchi wafurahie matunda ya Rais wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze sasa kwenye suala la barabara. Naipongeza sana Wizara, inafanya mambo mengi makubwa, lakini bado barabara ya kutoka Sumbawanga Mjini kwenda Kala. Ile barabara imekatika kabisa, yaani wananchi sasa hivi magari yakifika pale kwenye daraja wanapeana zamu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado barabara ya kutoka Katongolo kwenda Namansi, imekatika; barabara ya kutoka Marongwa kwenda Kasura Junction imekatika; na barabara ya kutoka Nkana – Kala imekatika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Rukwa Jimbo la Nkasi Kusini kwa Mheshimiwa Mipata hali ni mbaya sana. Mheshimiwa Mipata amekuwa akihangaika sana kutafuta hata pesa za dharura, lakini imeshindikana. Tunaomba watuangalie, watoe hata pesa za dharura ili kutengeneza hizi barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara zimekatika kabisa.
T A A R I F A . . .
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeipokea kwa mikono miwili, tena namshukuru sana kwa kunisaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi barabara yaani tuna hali mbaya sana. Ninavyosema hivi, Mheshimiwa Mipata ameomba pesa ya dharura mpaka sasa hivi bado hajapata majibu. Wananchi kule wanampigia simu, wanapiga simu kwa Wabunge wote lakini hakuna majibu. Tunaomba sana angalau TARURA au Wizara itoe pesa za dharura ili barabara hizi na haya madaraja yajengwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze sasa kwenye mtandao. Wilaya ya Nkasi tunashukuru Serikali ilituletea mtandao katika Kata ya Wampembe, lakini bado Kata za Kala, Sintari, Ninde, wananchi wanapanda kwenye mti, hasa wanawake usipovaa bukta sasa unapandaje kwenye mti ili ukaongee na simu? Wanakwenda kwenye milima, vichuguu kwenda kuongea na simu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Wizara hii iliangalie hili suala watuletee mtandao kwenye hizi Kata. Wanawake tunashindwa sasa kupanda kwenye ile miti maana miti mingine ni mirefu, mtandao unapatikana juu kabisa. Kwa hiyo, suala hili lichukuliwe kwa umuhimu wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee barabara za hapa Dodoma. Sisi tunaokaa Area D, barabara zinazotoka kwenye yale maghorofa wanayokaa Wabunge zimeharibika sana kiasi kwamba wakati mwingine tunaweza tukapata ajali hapa hapa mjini. Tunapita hii njia ya kwenda Morogoro tunakatisha kwenye vichochoro mpaka tukafike kule Area D Sengia unakuwa umepata shida sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba wangetufungulia japo kwa muda tuwe tunakatisha pale kwenye uwanja ule wa ndege ambao wamefunga, sisi Wabunge tuwe tunapita kwa muda kwa sababu tunavyopita kwenye vichochoro tunaweza tukakabwa. Vile vichochoro tunapita kwenye nyumba za watu, kwenye milango. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia zile nyumba za TBA zimechoka, TBA hawazifanyii ukarabati. Sisi tunaoishi kwenye zile nyumba tunapata shida. TBA waje watufanyie ukarabati zile nyumba, tunalipa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni hayo, nashukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu. Kwanza kabisa, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uzima na tunaweza kusimama katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri wa Wizara hii, Mheshimiwa Ummy Mwalimu na Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile kwa kazi kubwa wanazozifanya. Hakika wanaitendea haki Wizara hii. Mheshimiwa Ummy, kwa kweli umetupa heshima wanawake wenzio, Mwenyezi Mungu aendelee kukupigania na kukuinua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze pia Katibu Wakuu, Naibu Katibu Mkuu na Madaktari wote Tanzania nzima kuanzia Taifa na wale wa wilayani na mikoani. Kwa kweli madaktari wanafanya kazi nzuri na kubwa. Mwenyezi Mungu aendelee kuwatia nguvu na kuwabariki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee, nampongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa na nzuri anazozifanya. Ndani ya kipindi kifupi ameweza kufanya mambo makubwa; nikianza la kwanza, ameweza kuboresha upatikanaji wa madawa hospitalini; pia ameweza kukarabati vituo vya afya takribani 325; na amefanikiwa kutoa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali za mikoa mipya. Kazi nyingi sana amezifanya Mheshimiwa Rais, nikianza kuziorodhesha hapa nina dakika saba zitaisha. Kwa kweli anastahili pongezi. Mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siwezi nikaitendea haki roho yangu bila kumwombea Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli. Naanza kwa kusema Baba katika Jina la Yesu, mbariki sana Mheshimiwa Dkt. Magufuli, mbariki Mheshimiwa Waziri Mkuu, mbariki Mheshimiwa Ummy Mwalimu, wabariki Mawaziri wote akiwemo Mheshimiwa Jenista Mhagama, wabariki Mawaziri wote na Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Tanzania. Mwenyezi Mungu kibariki Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nasema wote tuseme Amen. (Makofi)
WABUNGE FULANI: Amen! (Makofi/Kicheko)
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, niingie sasa kwenye hoja za msingi. Nianze kwa kuomba. Jimbo la Nkasi Kusini lipo umbali mrefu sana kutoka Makao Makuu ya Wilaya. Wanawake wanaotoka Kata za Kara, Ninde na Nkandase wanapata shida sana wanapopata ujauzito.
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi juzi mwanamke mmoja amefia njiani wakati anakwenda hospitali kujifungua. Namwomba mdogo wangu Mheshimiwa Ummy Mwalimu atufikirie sana Jimbo la Nkasi Kusini kutuletea ambulance. Wanawake wale wakipata ambulance tutakuwa tumeokoa maisha ya akina mama wengi katika Tanzania hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa niipongeze Serikali kwa kutujengea Hospitali za Wilaya. Katika Mkoa wa Rukwa wilaya zote zimepata Hospitali za Wilaya, lakini bado Wilaya moja ya Sumbawanga Mjini haijapatiwa Hospitali ya Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia bajeti iliyopita ilipanga kujenga Hospitali ya Rufaa katika Mkoa wa Rukwa ambapo ilipanga kujenga katika Kijiji cha Milanzi, lakini mpaka sasa hivi hatujaona ujenzi ukianza Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Rukwa. Pia hospitali iliyopo ya mkoa majengo yake yamechakaa, jengo la mortuary limechakaa, halina hadhi ya mkoa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tulikuwa tunaomba Mheshimiwa Waziri aliangalie hili, ile hospitali ya rufaa ianze kujengwa, itasaidia sana kuepusha msongamano katika hospitali iliyopo ya mkoa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee sasa Wilaya ya Nkasi, kuna vituo vya afya vimeanza kujengwa, wananchi wanajenga kwa nguvu zao.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Bupe Mwakang’ata muda wako umeisha, lakini kwa maombi uliyopiga, nakuongeza dakika mbili. (Makofi)
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nakushukuru sana, Mungu akubariki sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Akasu, Kate, Ninde na King’ombe wameanza kujenga maboma ya vituo vya afya. Naomba Mheshimiwa Waziri atuongezee nguvu, awape moyo wale wananchi wanaojenga wapate support ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpongeze Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Mjini, kaka yangu Jacob Ntalitinginya ameweza kuwakopesha wanawake vikundi karibia 99 ambapo walikuwa wanasubiri kwamba labda Benki ya Wanawake ingejengwa Mkoa wa Rukwa lakini haijajengwa. Yeye ameweza kuwakopesha wanawake, pia ameweza kukusanya mapato karibia asilimia 110. Kwa hiyo, nampongeza sana Jacob Ntalitinginya, Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, dakika mbili zimeisha na nilikuwa na hoja nyingi lakini naomba kwa haya tu, niongelee sana suala la ambulance kwa wanawake katika Jimbo la Nkasi Kusini kwa Mheshimiwa Mipata.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika hoja hii muhimu ya Wizara ya TAMISEMI Ofisi ya Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujaalia uzima na afya tumeweza kuendelea kushiriki kujadili hoja zetu muhimu katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumpongeza Rais wetu, Jemedari wetu tingatinga, burudoza namba moja yetu si mwingine tena bali ni namba moja yetu Dkt John Pombe Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia kumpongeza Waziri Mkuu niwapongeze Mawaziri wote, niwapongeze Naibu Mawaziri wote, niwapongeze Makatibu Wakuu wote, niipongeze Serikali yote kwa ujumla kwa kazi kubwa na nzuri walizofanya ndani ya kipindi cha miaka minne kazi zenye weledi kazi zinazoonekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuzisoma kazi zilizofanywa na Serikali yetu sikivu Serikali ya Chama cha Mapinduzi ndani ya miaka minne imeweza kuleta elimu bure bila malipo kuanzia shule ya msingi na sekondari watoto wanasoma bure na ndiyo maana watoto wengi wameweza kujitokeza kwenda shule kwa sababu kabla ya hapo watoto walikuwa wanabaki nyumbani wazazi walikuwa wanashindwa kulipa hiyo elfu 10, elfu 40, elfu 50. Lakini baada ya kuleta elimu bila ada watoto wamekuwa ni wengi wamejitokeza kwa wingi, naipongeza sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndani ya miaka minne na ushee imeweza kuboresha upatikanaji wa madawa mahospitalini, ndani ya kipindi cha miaka minne imeweza kukarabati na kujenga vituo vya afya takriban 433 si kazi ndogo hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza sana Serikali ya Chama Cha Mapinduzi imefanya kazi kubwa sana kwa watanzania imeweza kuleta mikopo kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu imeweza kununua ndege takriban nane na zingine zinaendelea kuja tuseme nini mbele ya macho ya Mungu? Mungu atupe nini atupe kidonda bado watu wanasema hawaoni kilichofanyika bado watu wanasema hiyo elimu bure haina maana kwa kweli Mwenyezi Mungu anawaona. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza sana Serikali yangu ya Chama Cha Mapinduzi kwa kazi kubwa lakini nikupongeze wewe pamoja na Mheshimiwa Spika kwa kazi kubwa ya kuliendesha Bunge hili kwa utulivu mpaka tunaenda kumaliza kipindi chetu cha miaka mitano nakupongezeni sana wewe pamoja na Spika wetu wa Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizi ninaenda sasa kwenye hoja zangu za msingi nianze na TARURA. TARURA imefanya kazi nzuri sana TARURA imefanya kazi nzuri sana lakini kutokana na changamoto ya mvua nyingi za mwaka huu barabara nyingi zimeweza kuharibika na madaraja mengi yameweza kuharibika kwa hiyo, naiomba Serikali iweze kuongeza zile 30% iweze kuwa 50 na TANROADS pia iweze kupewa fungu la kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bado barabara nataka niiongelee barabara ya kutoka Tunduma kwenda Sumbawanga. Barabara ile ina mabonde ni barabara nzuri sana lakini ina bumps nyingi sana kiasi kwamba wanaume wanaoendesha magari kwenye barabara ile na wanawake viuno vyao sasa hivi wanaumwa. Barabara ile imezidi sana zile bumps ni kilo mita zaidi 280, 300 lakini ma-bumps yamekuwa mengi matuta ni makubwa yamekuwa karibu karibu kiasi kwamba mabasi yanayokwenda kule yanaharibika yanayobeba abiria yanaharibika hata magari madogo madogo na yenyewe kila wakati yanaharibika kutokana na matuta makubwa yaliyokithiri kwenye ile barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri alipokuja Mheshimiwa Rais kwenye Mkoa wa Rukwa alitamka mbele ya mkutano wa hadhara kwamba matuta yatapunguzwa sasa ninaomba atakapokuja kuhitimisha atuambie ni lini matuta hayo yatapunguzwa hata kama siyo kuyamaliza yote basi yapunguzwe yanaharibu sana magari lakini binadamu pia wanarushwa sana wanaposafiri kwenye ile barabara wanaumwa ninavyosema hivyo ukiwapima wanaume wanaosafiri safiri kwenda kule viuno vyao haviko salama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee tena suala la ukubwa wa Jimbo ukumbwa wa Majimbo. Mkoa wa Rukwa umebarikiwa sana kuwa na Majimbo makubwa Jimbo la Kwela maarufu kama Sumbawanga DC ni kubwa sana tunamshukuru Mheshimiwa Rais alipokuja alirudisha halmashauri ikapelekwa kwenye mji mdogo wa Laela tunamshukuru. Lakini bado kuna changamoto kubwa lile Jimbo limegawanyika katika sehemu mbili Ufipa wa Juu na Ufipa wa Chini, lile Jimbo lina kata 28 sasa Ufipa wa chini huku sasa hivi madaraja yamebomoka na Mwenyezi Mungu aliligawa automatically lile Jimbo aliligawa katika sehemu mbili upande wa chini, ziwani kuna kata 14 na upande wa juu kuna kata 13 kwa hiyo, wananchi wanapata tabu sana kufuata huduma wanapata shida kufuata huduma huku juu ambako halmashauri imepelekwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tulikuwa tunaomba na kule wapelekewe mamlaka ili waweze kujitegemea kwasababu kipindi hiki wakati wa mvua hakuna mawasiliano kabisa madaraja yamebomoka hakuna kabisa watu wanapata tabu kwenda kufuata huduma ufipa wa juu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana suala hili ni kilio kikubwa sana cha wananchi wa Jimbo la Kwela, wanaomba mamlaka igawanywe aidha Jimbo ligawanyike katika sehemu mbili na wenyewe huku chini wapate mamlaka na huku juu iendelee mamlaka kama Mheshimiwa Rais alivyotupelekea halmashauri yetu pale mji mdogo wa Laela.
NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa kengele ya pili imeshagonga.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana naunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Mpango uliopo mbele yetu. Kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima. Pia nawashukuru wanawake wa Mkoa wa Rukwa kwa kunichagua tena kwa kura nyingi sana za kishindo, nawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kukushukuru wewe na ofisi yako na Wabunge wenzangu wote kwa ujumla wao kwa kunisaidia nilipopata matatizo ya kufiwa na kaka yangu hapa Dodoma, lakini Wabunge hawakuniacha, waliweza kunisaidia mpaka kwenda kuhifadhi mwili huko kwenye nyumba yake ya milele. Nawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niingie sasa kwenye mchango wangu. Nachukua nafasi hii kuipongeza sana Serikali kwa kazi kubwa ambayo imefanya. Imeweza kufanya miradi mingi mikubwa ndani ya kipindi cha miaka mitano. Kwa kweli kazi inaonekana, kwanza kabisa imeweza kumtua mama ndoo kichwani kwa asilimia 90, pia imeweza kutengeneza barabara, umeme, mambo ya afya, sisi wanawake mpaka sasa hivi tumepata heshima kubwa sana, tunajifungulia sehemu nzuri. Kwa hiyo, Serikali imefanya mambo mengi mazuri na makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, palipo na mambo mazuri na makubwa hazikosekani changamoto. Mkoa wangu wa Rukwa unakabiliwa na changamoto kubwa sana kwenye Sekta ya Kilimo. Mkoa wa Rukwa ni miongoni mwa mikoa minne ambayo inazalisha kwa wingi sana chakula cha aina nyingi, lakini wakulima wamesahaulika sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wa Mkoa wa Rukwa wanalima, lakini changamoto kubwa ni masoko. Naomba Serikali yangu Tukufu ya Chama Cha Mapinduzi, iwakumbuke sana wakulima hawa hasa wa mikoa minne ile ambayo inazalisha sana chakula kwa wingi. Kwanza kabisa, kuwatambua wakulima wadogo, wa kati na wakubwa, Serikali iweze kuwatambua na mahali wanapolima. Ikiwatambua, uwezekano wa kuwasaidia kuwapa mikopo itakuwa ni rahisi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia iwaletee wakulima Maafisa Ugani, kwani Maafisa hawa ni changamoto kwenye maeneo yetu. Mimi mwenyewe ni mkulima, lakini sijawahi kumwona Afisa Ugani akinitembelea hata siku moja kwenye shamba langu. Kwa hiyo, wakulima wanajilimia wanavyojua wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile Serikali kama Rais wetu alivyosema kwamba tunakwenda kwenye Tanzania ya Viwanda; tukianzisha viwanda vingi vya pembejeo, nadhani pembejeo pia zitashuka bei na wakulima watapata pembejeo kwa bei nafuu. Naiomba Serikali ijikite sana katika kuanzisha viwanda vya pembejeo ili wakulima nao wapate nafuu ya kupata pembejeo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine naomba kwenye mikoa ambayo inalima sana kwa mfano Rukwa, zingeanzishwa Benki za Kilimo ili wakulima waweze kujikopea wenyewe kwenye hizo benki, walime kilimo chenye tija. Hivi sasa wanahangaika sana, kwa sababu pembejeo zenyewe ni bei kubwa, kwa hiyo, utakuta wanapata shida sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni masoko. Naomba ile taasisiya NFRA ingeweza kuongezwa fedha. Ile inasaidia sana kwa sababu wakulima wakiuza mazao NFRA at least wanapata soko kidogo. Hata hivyo kwa mwaka 2020 kwa mfano kwa Mkoa wa Rukwa tuliambiwa NFRA watanunua milioni 50, matokeo yake walinunua tani 5,000 tu, kwa hiyo ikawa ni changamoto kubwa sana. Mpaka sasa hivi wananchi wale wanapata tabu sana, mahindiyako ndani, hawajauza hata kidogo. Kwa hiyo, naomba Serikali kupitia Wizara ijikite kuongeza fedha kwenye taasisi ile ya NFRA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Madini
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara hii ya Madini. Kwanza kabisa nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima, sisi sote tukawepo hapa Bungeni tukijadili mambo muhimu.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote nichukue nafasi hii kutambua mchango wa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, lakini nimpongeze Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu, Mama Samia Suluhu kwa kazi kubwa, lakini pia kwa Hotuba yake nzuri iliyowafuta machozi Watanzania kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii pia kumpongeza Waziri kijana Mheshimiwa Doto Biteko na Naibu wake, kwa kweli wameitendea haki wizara hii, wameituliza kiasi kikubwa wameweza kuongeza mapato kwenye wizara hii, kwa kweli mnafanya vizuri mheshimiwa Doto Biteko endelea na moyo huo Mwenyezi Mungu aendelee kukupigania. Mnyonge mnyongeni haki yake mpeni Mheshimiwa Doto Biteko amefanya vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Sasa niingie kwenye hoja zangu za msingi kwasababu ya muda. Mkoa wetu wa Rukwa kuna utajiri mkubwa sana, utajiri wa helium. Helium gas inapatikana Rukwa, ipo kwa wingi sana, lakini Serikali haijawa serious sana kwenye jambo hili. Natoa ushauri, kwamba Serikali ihakikishe kwamba sasa inatafuta wawekezaji wakubwa ambao wanajiamini na wako serious kwenye jambo hili. Kwa sababu utajiri tunao mkubwa sana wa hiyo helium ni utajiri kwa Taifa lakini utajiri kwa Mkoa wa Rukwa kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kupata wawekezaji hao, tutaomba sisi kama wawakilishi wa Mkoa wa Rukwa tuweze kupata taarifa kwasababu sasa hivi tumesikia kuna wawekezaji ambao wamepatikana lakini hakuna taarifa ambazo tunazijua, tunazisikia sikia tu tunaomba Serikali sasa iwe inakuwa wazi. Kwanza kabisa iweze kuweka sheria ambayo itawabana wawekezaji wetu waweze kuwasaidia wananchi wa eneo husika. Wawekezaji wakipata fursa kama hizo wamekuwa wakisaidia vitu vidogo vidogo hasa utakuta amesaidia shule, amesaidia zahanati lakini utakuta mradi wenyewe ambao anaoupata pale ni mradi wa fedha nyingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilikuwa naiomba Serikali iangalie hawa wawekezaji wawe wanasaidia wananchi wa eneo husika kwa kiasi kukubwa sana kulingana na mapato yao ya mradi husika. kwa mfano kama hao wawekezaji watakaokuja kuwekeza kwenye helium tunaomba sana wawaangalie sana wale watu, wananchi wanaokaa kwenye maeneo husika kuwasaidia kwa kuwapa aidha, hizo shule lakini shule za maana, sio inajengwa shule tu ili mradi shule imejengwa lakini shule haina ubora wowote. Lakini pia Serikali iweze kuwapa elimu, elimu wananchi wa eneo husika faida za mradi lakini pia na hasara za mradi huo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia kwenye Mkoa wetu wa Rukwa, kwasababu kuna miradi mikubwa kama hiyo tunaomba basi Serikali ikumbuke kuujenga ule uwanja wa Ndege yaani miundombinu ikae vizuri. Lakini pia barabara, barabara ni changamoto kubwa sana kwenda kufika miradi kama hiyo kwa mfano; mradi huo uko kwenye Ziwa Rukwa. Kule upande wa Ziwa Rukwa barabara ni mbaya sana, sasa tulikuwa tunaomba Serikali iangalie sana miundombinu ya Mkoa wa Rukwa ikiwemo uwanja wa Ndege lakini pia ikiwemo barabara ambazo zinakwenda kwenye mradi huo.
Mheshimiwa Spika, nihame kwenye eneo hilo sasa, niongelee sasa upande wa dhahabu. Kama nilivyompongeza waziri kwamba amefanya vizuri tunaomba sasa kama alivyotoa tamko mama yetu Rais wetu Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan kwamba yale maeneo ya hifadhi waachiwe wananchi waendelee kuchimba lakini kujipatia kipato kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika ni muhimu sana, Waziri Doto Biteko alifanyie kazi haraka iwezekanavyo suala hili ili sasa waraka utoke wananchi waweze kufaidika na maeneo hayo kwa kupata waraka maana toka alivyotoa tamko hilo mama, wananchi wamekuwa wakiingia kwenye maeneo hayo sasa watumishi wa wizara husika au watumishi wa idara husika wamekuwa wakiwapa adhabu kubwa sana wananchi wanaoingia kwenye hifadhi kujipatia kipato. Kwa hiyo, nilikuwa naishauri sana Serikali ifanye haraka sana kutoa waraka kwenye haya maeneo ya hifadhi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Lakini lingine ni hawa watu wa TRA wana wa-harass sana wachimbaji wadogo wadogo. Mchimbaji akionekana tayari ana vitu vya kuchimbia basi wana mkadiria mapato kwa wingi bila kujali kwamba amepata dhahabu kiasi gani au bila kujali kwamba kiasi alichopeleka pale kwenda kupima kinafanana na hizo tozo ambazo wamamtoa.
Suala lingine ni ucheleweshaji wa leseni, leseni za wachimbaji zinachelewa sana utakuta mchimbaji ameomba sehemu ya kuchimba lakini kupata leseni imekuwa ni changamoto. Lakini hilo pia suala hilo Mheshimiwa Waziri aliangalie sana leseni ziwe zinawahi kutoka mchimbaji mdogo akiomba leseni basi apatiwe kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, suala lingine nilikuwa naomba wale wachimbaji wakubwa ambao wana maeneo makubwa
SPIKA: Malizia Mheshimiwa Bupe Mwakang’ata.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Spika, ambao wana maeneo makubwa, kwa kumalizia. Yale maeneo ambayo hawayatumii wawagawie wachimbaji wadogo wadogo kwasababu mchimbaji mkubwa ana eneo kubwa halitumii. Lakini mchimbaji mdogo anahangaika pa kuchimba wakati maeneo yamekaa bure. (Makofi)
SPIKA: Ahsante sana.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Wawe wanachukua wanawagawia wachimbaji wadogo wadogo. Ahsante sana, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara hii ya Miundombinu. Kwanza kabisa, nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa kibali cha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia kumpongeza Waziri na Manaibu wake wawili kwa uchapakazi wao mzuri wa kuhakikisha kwamba barabara zetu zinaunganika karibia Tanzania nzima. Hongereni sana kwa kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bila kupoteza muda naomba niingie sasa kwenye hoja zangu za msingi. Hoja yangu ya kwanza ni kwamba pamoja na kazi nzuri ambayo Serikali inafanya kwenye miundombinu lakini kuna changamoto ya wakandarasi. Wakandarasi wanalalamika sana wanapokuwa wamefanya kazi wanacheleweshewa sana malipo yao lakini pia wakifanya kazi kabla hata hawajalipwa wanakatwa pesa zao kwenye akaunti zao na kufungiwa bila utaratibu. Kwa kweli hilo Wizara iliangalie kwa makini na ilifanyie kazi. Wakandarasi wetu ni wazalendo na ni Watanzania na wamefanya kazi nzuri ya kuhakikisha kwamba barabara zetu ni nzuri pamoja na changamoto ya mvua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni Uwanja wa Ndege wa Mkoa wa Rukwa, Sumbawanga Mjini. Uwanja huu wa ndege umezungumziwa muda mrefu sana, zaidi ya miaka minne tunapitisha bajeti ya Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga lakini hakuna kinachoendelea. Tunaishukuru Serikali mwaka juzi iliweza kuwalipa wananchi waliokuwa wanauzunguka uwanja ule wa zamani mdogo lakini baada ya hapo kumekuwa kimya kabisa, hakuna kinachoendelea na wakati Mkoa wa Rukwa una fursa nyingi ikiwemo na utalii wa aina mbalimbali; Kalambo Falls, mbuga za wanyama na madini ya kutosha. Pia kuna wafanyabisahara wakubwa ambao wangeweza kutumia usafiri wa ndege kuja Dar-es- Salaam na kurudi Dodoma na kwenda Sumbawanga. Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind up hapo atueleze Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga Mjini utajengwa lini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni barabara. Kuna barabara moja ambayo ni uchumi kabisa wa Mikoa ya Rukwa, Katavi, Songwe na Mbeya. Barabara hiyo inatoka Kibaoni – Maji Moto - Muze - Iremba – Kilyamatundu - Mloo. Barabara hii nayo imezungumziwa muda mrefu sana, Serikali imekuwa ikitengeneza vipande, utakuta imetengenezwa daraja baada ya muda linaacha mto Serikali inarudi tena kutengeneza. Nachoweza kuishauri Serikali, barabara hii muarobaini wake ni kuweka lami. Barabara hii imepita kwenye Bonde la Rukwa ambapo mazao mengi yanalimwa kule. Mpunga, ufuta na mazao ya kila aina yanastawi kwenye Bonde hilo la Rukwa. Kwa hiyo, tunaiomba barabara hii ijengwe kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bila kupoteza muda niongelee tena suala la bandari. Mkoa wa Rukwa tumekuwa na bandari kama tatu lakini hazifanyi kazi yoyote. Serikali imewekeza pesa za kutosha kwenye bandari hizo lakini mpaka sasa hivi hakuna bandari hata moja inayofanya kazi. Kwa maana hiyo, naishauri Serikali iweke nguvu kwenye bandari hizi ikiwemo Bandari ya Kipili na Bandari ya Kabwe; bandari zile Serikali imeweka pesa nyingi kwa hiyo, irudi kwenda kuzifanyia kazi ziweze kufanya kazi na kuingiza pato la Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maneno haya mafupi, naomba Serikali iwakumbuke wakandarasi kwa kuwalipa pesa zao kwa wakati. Ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika bajeti hii muhimu. Kwanza kabisa namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima na afya Wabunge wote tuliopo humu ndani ya Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nimpongeze Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu kwa kazi nzuri. Bajeti aliyotuletea kwa kweli, imekidhi viwango, imegusa sehemu zote na matatizo yote ya Watanzania kwa kweli, imeweza kugusa kila nyanja. Tunakushukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Waziri na Naibu wake kaka yangu Mheshimiwa Masauni kwa kazi nzuri na bajeti nzuri waliyotuletea. Kwa kweli, bajeti imekidhi viwango. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuwapongeza kwa suala zima la kuwajali bodaboda. Bodaboda kwa kweli lilikuwa ni tatizo kubwa sana, tulikuwa na vijana wetu ambao walikuwa wanavuta bangi, wanajiunga kwenye makundi mbalimbali ambayo sio ya kimaadili, lakini sasa hivi bodaboda wameweza kujiajiri wenyewe. Shida yao ilikuwa ni changamoto hizo za barabarani, za kukamatwa hovyohovyo bila mpangilio. Tunashukuru sana Serikali imeweza kuwajali kwa kuwapunguzia fine kutoka shilingi 30,000 mpaka shilingi 10,000. Hata hivyo, Serikali isiishie hapo tu iendelee kuwalinda hawa bodaboda maana unaweza ukampunguzia bodaboda kwamba, asilipe shilingi 30,000 lakini akaweza kukamatwa mara tano, mara tatu, ikarudi palepale shilingi 30,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali ikimkamata bodaboda kosa moja, basi kosa hilo liendelee mpaka siku nzima iishe. Sio leo asubuhi unamkamata, mchana unamkamata, jioni unamkamata, kwa hiyo, ile shilingi 30,000 itakuwa tena imerudi palepale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningeweza kuishauri Serikali kwamba, hawa bodaboda wangeanzishiwa mafunzo. Bodaboda wengi wanajifunza wenyewe huko mtaani, anajifunza siku tatu, baada ya hapo anaingia barabarani. Hajajifunza kokote, hajajua sheria anaingia barabarani. Naiomba Serikali sasa kwa sababu imewatambua bodaboda na imewapunguzia adhabu basi iwaandalie tena na mafunzo kwa ajili ya kuzijua sheria za barabarani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze tena Serikali kwa kuwakumbuka Madiwani. Madiwani kwa kweli wamekuwa wakifanya kazi kubwa sana huko waliko, lakini naishukuru Serikali imeweza kuwakumbuka. Naiomba Serikali pamoja na kwamba, imewakumbuka kuwalipa posho zao kupitia Serikali Kuu, pia iwakumbuke kwa kuwaongezea posho, lakini pia kwa kuwakopesha angalau hata usafiri wa kuwafikia Watanzania popote pale walipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niipongeze Serikali kwa kuwakumbuka watumishi kuwapandisha madaraja. Hiki kilikuwa ni kilio kikubwa sana kwa watumishi Watanzania, hasa Walimu. Walimu walikuwa kwa muda mrefu hawajapandishwa madaraja na wale waliopandishwa madaraja walikuwa hawajalipwa na wala walikuwa hawapatiwi hata semina zozote za kuongezewa ujuzi, lakini kwa utaratibu huu wa Serikali kuwapandisha madaraja kwa kweli, wamefuta kilio cha Watanzania, wamewaongezea tija Walimu watakwenda klufanya kazi vizuri na watumishi wote kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze pia Serikali kwa kutenga bajeti ya maji. Kwa kweli bajeti hii imekwenda kukidhi matatizo ya wananchi, kwa sababu ukimkumbuka mama kumtua ndoo kichwani, basi unakuwa umelikumbuka Taifa lote kwa ujumla, kwa sababu, hakuna kama mama. Sisi wanawake tulikuwa tunapata tabu sana wakati wa kutafuta maji, tulikuwa tunakwenda mwendo mrefu sana, ndoa zetu zilikuwa ziko hatarini, ndoa zetu zilikuwa zinavunjika, lakini bajeti hii inakwenda kutibu ugonjwa huu. Tunaishukuru sana Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizi, sasa niingie kwenye hoja zangu za msingi. Nilihudhuria semina moja ya takwimu, Mkoa wa Rukwa uliongelewa kwamba, ndio wa kwanza kwa umaskini. Nilijiuliza kwamba, Mkoa wa Rukwa unakuwaje maskini wakati sisi Mkoa wa Rukwa tuunaweza kulisha hata Tanzania nzima kwa kilimo tunacholima Wanarukwa, lakini inakuwaje tunaambiwa sisi ndio wa kwanza kwa umaskini? Nikajiuliza ni kwa nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipata jibu kwamba, ni kwa sababu ya miundombinu hafifu, barabara zetu hazijakaa vizuri, hasa barabara inayotoka Mkoa wa Songwe, Tunduma kuelekea Sumbawanga Mjini. Barabara ile imejengwa kwa kiwango cha lami vizuri kabisa, lakini tatizo la barabara ile ni matuta. Barabara ile ina kilometa 300, lakini matuta makubwa sana; matuta ni takribani 270, matuta hayo yametuletea matatizo makubwa sana hasa kwa wanaume wengi wanaoendesha magari Mkoa wa Rukwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukipita mara tatu ile barabara kiuno chako kinakosa ushirikiano. Ukiwapima wanaume wanaoendesha magari Mkoa wa Rukwa na hasa wale wanaosafiri mwendo mrefu, mabasi na magari madogo, ukiwapima viuno havina ushirikiano kabisa. Tunaomba sana Serikali katika bajeti hii angalau itupunguzie yale matuta, matuta ni makubwa sana. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata sisi wanawake tunaposafiri ukiwa mjamzito, ujauzito huwezi kufika Mbeya, unaharibika ndani ya gari. Tunaomba barabara hii ipunguzwe matuta yale, matuta yamekuwa ni mengi sana, yamezidi hata kilometa za barabara. Kilometa ni 300 matuta 270 na matuta ni makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, Mkoa wa Rukwa wanasema ni maskini, lakini sisi tuna bandari, bandari ziko tatu; tuna Maziwa mawili, kuna Ziwa Tanganyika halafu na Ziwa Rukwa. Ziwa Tanganyika tuna bandari tatu, bandari hizo hazijaanza kufanya kazi mpaka sasa, naomba katika bajeti hii bandari zile zikifunguliwa tutapata usafiri wa kuvuka kwenda nchi za nje kama Kongo, Zambia, tutasafirisha mazao yetu ambayo yanakosa soko. Kwa mfano mahindi, pale Kongo mahindi wanahitaji sana, lakini tukiwa na bandari inafanya kazi, basi tutaweza kupata soko ambalo linaweza kukidhi mahitaji ya Wanarukwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni uwanja wa ndege. Uwanja wa ndege wa Mkoa wa Rukwa umezungumziwa muda mrefu, lakini naiomba Serikali kwenye bajeti hii basi angalau iikumbuke mikoa hii ambayo inaitwa maskini iikumbuke kwa kujenga miundombinu kama uwanja wa ndege, kufungua hizo barabara, nadhani na sisi tutawafikia wenzetu ambao wamefikia kiwango cha juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru sana kwa kunipa nafasi iliniweze kuchangia katika hoja hii muhimu ya Waziri Mkuu. Kwanza kabisa nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima na kutupa kibali cha kuweza kusimama katika Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Waziri Mkuu kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya, lakini kipekee nimpongeze sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama yetu Samia Suluhu kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya. Kwa kweli Mwenyezi Mungu aendelee kumpa afya na kibali ili kuwatumikia Watanzania vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuipongeza nakuishukuru Serikali kwa mambo mazuri ambayo wameendelea kufanya. Sisi wanawake tunashukuru sana kwa kitendo cha kutujali kwa kutupa asilimia 10 ya wanawake, watu wenye ulemavu na vijana, kwa kweli tunashukuru sana, hiyo asilimia 10 imefaidisha sana, ikiwemo na sisi wanawake wa Mkoa wa Rukwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuipongeza Serikali tumeona madarasa mazuri kabisa ya kisasa, watoto wetu wanasoma bure, tunaishukuru sana Serikali. Haikuishia hapo tu tumezunguka kukagua miradi ya maendeleo miradi, inakwenda vizuri, miradi mikubwa na midogo inaendelea, kwa kweli kazi ni nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuipongeza Serikali na kuishukuru kwa suala zima la hotuba ya Rais aliyohutubia siku ya tarehe 4 Aprili, ambayo iligusa moja kwa moja kwenye suala zima la kilimo. Tunajua kilimo ndio ilikuwa ndio kilio kikubwa sana kwa wananchi wa Tanzania, lakini ile hotuba inakwenda kuwafungua wakulima kuwapa ahueni, inakwenda kuwafanya walime kilimo cha kisasa, lakini chini ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo ambaye kaka yetu tunamwamini sana, kwa hiyo tunaishiwa hoja za kusema kwa sababu tayari ameonyesha mwelekeo wa kwenda kumsaidia mkulima. Ahsante sana Serikali, tunamtia moyo Mheshimiwa Waziri kwenye suala zima la kilimo, akaze buti tuko nyuma yake, aendelee kuwa ngangari, ahsante sana Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizi sasa niinge kwenye changamoto za Mkoa wangu wa Rukwa. Nianze kwenye changamoto ambayo inawasibu sana wana Rukwa kiasi kwamba wamenituma nije niseme mbele ya Waziri Mkuu. Kwa kweli tunashukuru sana Serikali imeweza kutujengea stendi mpya ya kisasa ambayo iko mbali kidogo na Mji wa Sumbawanga Mjini. Pamoja na mafanikio hayo kutujengea stendi mpya, stendi hiyo imekuwa na machungu ndani yake kwa sababu wananchi wa Mkoa wa Rukwa wanapata mateso makubwa sana pale ambapo Serikali imepiga marufuku wananchi wale kupanda magari wakiwa Mjini Sumbawanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, magari yamepigwa marufuku kushusha au kupandisha pale Mjini Sumbawanga. Kwa hiyo adha hii imewafanywa wananchi wa Mkoa wa Rukwa hasa Sumbawanga Mjini wanapata mateso makubwa sana. Tunaomba Serikali pamoja na kwamba imejenga stendi mpya ya nzuri mpya ya kisasa hiyo stendi iko mbali na Sumbawanga Mjini, kwa hiyo tunaomba zitumike stendi zote mbili wananchi wapandie stendi ya zamani ambayo iko mjini, lakini pia wapandie na ile stendi mpya, zitumike stendi zote mbili, kuliko sasa hivi wananchi wanapata adha kubwa sana wanatumia usafiri kutoka pale mjini kwenda kufuata stendi ambayo iko mbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kule unakuta wananchi wanaamka asubuhi saa 10 kufuata stendi iliko mbali, ni gharama kubwa, lakini pia magari yanayotoka mikoani au wilayani yanaishia huko nje ya mji, kwa hiyo inakuwa ni adha kubwa sana. Tunaomba leo hii ningechangia kwenye wizara husika ningeweza kushika shilingi ya Waziri mhusika wa hiyo, lakini kwa vile nimechangia kwenye Hotuba ya Waziri Mkuu namheshimu sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu amekuwa akifanya kazi nzuri kazi kubwa kwa hiyo siwezi kushika shilingi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Naomba atakapokuja kuhitimisha hoja yake hili suala la kutumia stendi zote mbili, basi atoe neno moja tu ili wananchi wa Mkoa wa Rukwa na wananchi wanaoishi Sumbawanga Mjini waweze kupona roho zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kwenye changamoto za Mkoa wangu wa Rukwa. Tuna changamoto ya maji, lakini naishauri Serikali, suluhisho kubwa la tatizo la maji katika Mkoa wa Rukwa, tunaomba tuna chanzo ambacho kinaweza kuwa ni suluhisho la kudumu, chanzo cha kutoa maji kwenye Ziwa Tanganyika na kuleta kwenye Wilaya zote za Mkoa wa Rukwa. Hiki ni chanzo ambacho hakiwezi kuleta tena shida, tunaomba kama ikiwezekana, basi Serikali iweze kutoa maji Ziwa Tanganyika na kuleta kwenye Mkoa wa Rukwa kwa ujumla na mikoa mingine ya pembezoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto nyingine, tunaomba barabara narudia tena, nimewahi kuleta hoja hii hapa barabara ya kutoka Tunduma mpaka Sumbawanga Mjini. Barabara ile nilisema ina matuta mengi makubwa sana, matuta yale yaliweza kusababisha viuno vya wanaume wa Mkoa wa Rukwa kutokufanya kazi ipasavyo, sasa naleta tena hoja hii naomba sana, Serikali inapata ugumu gani wa kutoa yale matuta? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana yale matuta yanatuletea matatizo makubwa sana, hata kwenye magari yanaharibika, ile barabara tunaitegemea kwa uchumi wa Mkoa wa Rukwa, matuta yamekuwa ni kitu ambacho kinatuletea matatizo. Rais hayati aliyekuwepo…
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
T A A R I F A
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa tu Mheshimiwa anayezungumza hivi sasa hoja ya matuta na viuno wanaume wa Mpanda wamethibitisha wanalalamika sana humu ndani ya hili jingo. Nakushukuru sana. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Bupe, taarifa hiyo?
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea taarifa tena kwa mikono miwili. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameona tunavyopata tabu sana wanaume wa Mkoa wa Rukwa, kwa kweli ni shida nyumba nyingi zinavunjika chanzo ni matuta, matuta ni makubwa sana hata hayati Dkt. Magufuli alimwambia Waziri wakati ule alikuwa Waziri wa Mambo ya Uchukuzi, alimwambia matuta yale nakupa mwezi mmoja yatoke, lakini haikutosha hata Katibu wa Chama Cha Mapinduzi alipofanya ziara kuja Mkoa wa Rukwa alipata tabu mgongo siku hiyo hakulala. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, akawaa anawapa wiki mbili watoe hayo matuta, lakini mpaka leo hii imekuwa ni kimya. Tunaomba basi Serikali iweze kulitilia maanani suala hili matuta yale yaweze kuondolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, naomba kuhusiana na barabara inayotoka Kibaoni kwa Waziri Mkuu Mstaafu Mheshimiwa Pinda inayopita Muze, Kilemba, Kiriyamatundu inakuja kutokea...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika hoja iliopo mbele yetu hoja ya TAMISEMI. Kwanza kabisa nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima lakini pia nichukue nafasi hii kumpongeza Dada yangu Kairuki na Manaibu wake wawili mapacha kwa kazi nzuri wanazozifanya hakika nimejionea. Mheshimiwa Kairuki hata ukipiga simu saa nane usiku anapokea. Anapokea anakusikiliza lakini pia hata Manaibu wake wawili wanapokea simu wanakusikiliza wanakutatulia changamoto, hongera sana, huo ndio uwajibikaji na utumishi ulio wa kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kumsahau Mkuu wangu wa Mkoa Queen Sendiga, naye nampongeza sana anaisimamia ilani vizuri katika Mkoa wetu wa Rukwa. Kipekee nimpongeze sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anazozifanya. Wanawake na wananchi wa Mkoa wa Rukwa wamenipa salamu tunamshukuru sana, tumeweza kupokea miradi; miradi ya madarasa, miradi ya maji, miradi ya barabara, miradi mingi fedha nyingi sana tumezipokea katika Mkoa wetu wa Rukwa. Hongera sana Rais wetu, chapa kazi tuko pamoja na wewe, 2025 kitaeleweka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kuwapongeza Simba. Wamembamiza mtu jana, wamembamiza vibao viwili. Hongera sana Simba Sports Club. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niingie sasa kwenye hoja zangu za msingi. Mkoa wangu wa Rukwa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa kuna taarifa.
TAARIFA
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kuniona. Naomba kumpa taarifa mchangiaji kwamba wananchi hawakututuma huku ndani kuja kuongea ushindi ushindi wa michezo. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Bupe naomba uipokee hiyo taarifa, uipokee hiyo taarifa.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namsamehe ngoja niendelee asinipotezee muda.
MWENYEKITI: Uipokee hiyo taarifa.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sipokei. Niingie kwenye suala la 10% ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu…
MWENYEKITI: Taarifa inatoka wapi? Haya taarifa Mheshimiwa.
TAARIFA
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mchangiaji kwamba miongoni mwa mambo ambayo Mheshimiwa Rais anayaunga mkono ni pamoja na mambo ya michezo. Kwa hiyo kilichofanyika jana ni jambo ambalo linaendeleza hamasa kubwa ya Mheshimiwa Rais na Simba wameitekeleza kwa vitendo. Naomba kutoa taarifa. (Makofi)
MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, hiyo taarifa ya mwisho kuhusu suala la michezo. (Makofi)
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepokea kwa mikono miwili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niingie sasa kwenye mambo yangu ya msingi nianze kuongelea suala la 10% ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Nimshukuru sana Rais na Serikali yetu. Kwa kweli jambo hili la 10% ni zuri sana na limefanya hamasa kubwa sana kwenye jamii yetu, lakini nimesikia juzi Mheshimiwa amesema kunakuwa na ubadhirifu wa fedha ambazo zinapotea bila sababu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi fedha kama zinapotea tusiwahukumu wanawake wale wanaokopa. Wale wanawake wanaokopa na vijana wanarudisha kwa uaminifu mkubwa sana. Wanacheza VICOBA wanarudisha. Hizi fedha kama zinapotea inawezekana kuna vikundi hewa ambavyo vinapoteza hizo fedha kwa asilimia kubwa. Naomba tuliangalie vizuri. Hii fedha ibakie kwanza halmashauri, wanawake wakihamishiwa mikopo hii kwenye mabenki wengi wao watashindwa kwenda kukopa kwa sababu ya dhamana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, 10% hii inasaidia sana makundi haya na sisi kama Mkoa wa Rukwa tunasubiri sana hii utaratibu ulioanza wa kilimo tunasubiri tunajua kwamba 10% hii itasaidia sana wanawake wengi wanalima Mkoa wa Rukwa kwa hiyo 10% hii, 4% na 2% itawasaidia sana makundi haya kwa ajili ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ya pili. Nichukue nafasi hii pia kumpongeza Rais kwa kutangaza ajira 21,200. Ajira ni nzuri, nyingi sana na tunamshukuru sana Rais kwa kujali watoto wake ambao wamesoma lakini wanaishi mitaani hawana kazi. Ushauri wangu, hizi nafasi 21,200 zigawanywe kwenye mikoa husika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi nafasi ni Rais na Serikali yetu inatangaza kila mwaka. Mwaka uliopita ilitangaza ajira 6,000 lakini wengine mikoa mingine hatukuona kama kuna vijana wetu ambao wamepata hizi ajira. Ushauri wangu, hizi ajira zigawanywe kwenye mikoa tugawanye kwa uwiano bila kupendelea ili vijana wa mikoa yote waweze kufaidika na hizi ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Bupe ahsante sana, muda umekwisha.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nashukuru na mimi kwa kunipa nafasi. Nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, pia nitumie nafasi hii kumpongeza sana Kaka yangu, Mheshimiwa Bashe, na Naibu wake Mheshimiwa Mavunde na Wataalam wote wa Wizara ya Kilimo, kwa kazi nzuri wanazozifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya. Waswahili wanasema mzigo mzito mpe Mnyamwezi, lakini mzigo mzito usimpe Mnyamwezi, mzigo mzito mpe mwanamke, anaweza kuubeba mzigo wa aina yoyote na akaufikisha ukiwa salama. Kwa hiyo, Mama yetu Samia Suluhu Hassan anaubeba mzigo mzito na umekuwa mwepesi na anaupiga mwingi, mpaka 2030 mwanamke anajikubali, anajiweza. Hongera sana Rais wetu Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite sasa kwenye hoja zangu ambazo nimeziandaa. Nianze na BBT (Building a Better Tomorrow, block farms). Nitumie nafasi hii kumpongeza sana Kaka yangu, Mheshimiwa Bashe kwa ubunifu mkubwa sana amebuni mbinu hii ambayo imeweza kuajiri vijana wengi wakiwemo wa kike na wa kiume. Mheshimiwa Bashe amebuni mtindo huu, lakini usiishie tu kwa vijana. Huu utaratibu umelenga vijana wa kike na wa kiume. Mimi ninamshauri kwamba utaratibu huu uwahusishe pia wanawake, wanaweza pia kulima. Wanawake ni wakulima wakubwa, kwa hiyo ukimuwezesha mwanamke umeliwezesha Taifa zima kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu lingine kuhusiana na hii BBT, ninaomba kwa sababu tayari utaratibu umeanza Dodoma lakini bado kuna Mikoa mingine ambayo inalima kwa uhakika, ninashauri huwezi ukamtoa kijana Mkoa wa Rukwa akaja kulima Dodoma. Kwa nini hizi block farms zisianzshwe na Mikoa mingine ikiwemo Rukwa, Ruvuma, Mbeya, Katavi na Kigoma. Huko ukiweza kuanzisha hizi block farms utaweza kupata vijana wengi ambao watajiajiri na wanawake kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niingie kwenye suala zima la Benki ya Kilimo. Benki hii imezungumziwa muda mrefu lakini hatuioni. Tunasikia tu benki iko Dar es Salaam, Da es Salaam ndiyo kuna mashamba? Mashamba yako mikoani? Kwa nini benki hii isiweze kuanzishwa mikoani, ikaandikwa kabisa Benki ya Kilimo, siyo mnasema kwamba eti wakulima waende kukopa kwenye mabenki mengine ambayo Benki ya Kilimo itakuwa ndani yake. Tunaomba Benki ya Kilimo ianzishwe hata kama itakuwa kwenye baadhi ya Mikoa lakini iwepo kwenye Mikoa ambayo inalima chakula kwa wingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niingie kwenye suala zima la mbolea. Tunaishukuru sana Serikali imeweza kuingiza pesa nyingi sana kwenye mbolea. Hapo katikati kuna kidudumtu, hawa mawakala wanachakachua, unakuta kwamba mbolea unafikiri ni urea kumbe humo ndani imechanganywa na uchafu. Wizara naomba ijipange kuhakikisha kwamba wakulima wanapata mbolea kwa wakati, mbolea ambayo ni original isiyochakachuliwa. Mimi naomba Mheshimiwa Bashe utakapokuja ku-wind up hapo atueleze amejipangaje kuhakikisha suala hili unalidhibiti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mbegu bora. Wananchi wa Mkoa wa Rukwa tunapata mbegu nyingi zinatoka nchi za nje. Kwa mfano, tunatoa mbegu Zambia, sasa huwezi ukawa na uhakika mbegu imetoka Zambia huwezi kujua humo ndani wamechanganya na vitu gani. Tunaomba Serikali ianzishe mashamba ya kulima mbegu bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Mazao Mchanganyiko. Hii taasisi ni nzuri sana kwa sababu ni soko la uhakika ambalo liko ndani ya nchi. Ninaiomba Serikali iongeze mtaji kwenye Bodi ya Mazao Mchanganyiko. Pamoja na kwamba shirika hili linajiendesha kibiashara, lakini bado halijawa na uwezo wa kununua mazao mengi. Naomba Serikali iwaongezee pesa Bodi ya Mazao Mchanganyiko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii pia kumpongeza Mkurugenzi wa Bodi ya Mazao Mchanganyiko, Kaka yangu Maige, anafanya kazi nzuri. Hapo ni kuongeza mtaji tu ili Bodi hii iweze kujiendesha vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu bima ya wakulima. Nasikia tu kwamba kuna bima ya wakulima lakini hatuoni kinachoendelea imeishia wapi? Tunajua wakati mwingine kunakuwa na mabadiliko ya nchi, huwezi kujua kunaweza ikatokea mvua isinyeshe, ukame ukawepo, wadudu wakatokea, lakini bima ya wakulima ikiwepo itasaidia sana wakulima waweze kujiendesha na kukabiliana na changamoto hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni Maafisa Ugani. Kwanza ninaishukuru sana Serikali, imeweza kutoa pikipiki takribani zaidi ya 7,000 zimekwenda kwa Maafisa Ugani lakini hatuwaoni Maafisa Ugani hawa wanachakarika kwenda kuwasaidia wakulima. Wakulima wanajitegemea wenyewe, wanalima pasipo utaalam wakati tayari pikipiki zimetolewa. Tatizo ni nini? Kama tatizo ni mafuta, tunaomba Serikali iweze kuwawekea hawa Maafisa Ugani mafuta ya kwenda kufanya ziara huko kwa wakulima ili wakulima waweze kulima kilimo kilicho bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na mimi kwa kunipa nafasi ili nichangie katika Wizara hii muhimu, Wizara ya Kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri kaka yangu Bashe na Naibu wake; lakini pia niwapongeze Makatibu Wakuu wote watatu kwa kazi nzuri wanayoifanya. Kipekee nimpongeze Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Mama Samia Suluhu kwa kazi nzuri na kwa kuijali Wizara ya Kilimo kwa kuongeza takribani shilingi bilioni 751. Hiki si kitu kidogo, hongera sana Mama yetu, kazi unaipiga na unaupiga mwingi Mama yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niingie sasa kwenye hoja zangu. Kwa sababu ya muda niongelee suala la pembejeo. Mkoa wa Rukwa maisha yetu sisi ni kilimo lakini pia mbolea ndiyo kila kitu. Hata hivyo, changamoto iliyopo mbolea imepanda bei kubwa sana. Waheshimiwa Wabunge wengi wameongelea kuhusu mbolea. Mbolea ndiyo habari ya mjini, mbolea ndiyo imeshika maisha ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Bashe akiweza kutatua changamoto ya mbolea kwa bajeti iliyopangwa hii kwa kweli maisha ya Watanzania na kilio cha Watanzania na machozi ya Watanzania yatafutika.
Mheshiimwa Naibu Spika, Mkoa wetu wa Rukwa unalima mazao mengi sana ikiwemo mahindi, maharage, ufuta, miwa na mazao mengine mbalimbali yanalimwa Mkoa wa Rukwa. Hata hivyo changamoto kubwa ni hilo suala la bei ya mbolea. Tunaomba Serikali iweke ruzuku. Hili si ombi, ni lazima Serikali iangalie suala zima la kuweka ruzuku kwenye pembejeo hasa kwenye mbolea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niingie sasa kwenye suala zima la kilimo cha miwa Mkoa wa Rukwa. Mkoa wa Rukwa pamoja na kulima mazao mengine yote tunalima pia miwa. Tunaomba Serikali ifanye utafiti iweze kujenga kiwanda cha kuchakata miwa, tutaweza kupata sukari ambayo imekuwa nayo ni tatizo kubwa sana katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee pia suala la matrekta. Wizara hii kupitia taasisi yake ya NBC iliweza kukopesha matrekta kwa Watanzania, lakini matrekta haya yamekuwa ni kichomi, adhabu, matrekta ni mabovu, matrekta uki-test mitambo tu ukiwa shambani trekta linabongonyoka, trekta linakuwa kama muhogo, ukilishika kidogo mara kichwa kule, mara kiwiliwili huko, matrekta hayaeleweki.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali ikayachukuwe matrekta kwa wananchi, matrekta yale imekuwa ni kichomi, matrekta yale yanawatesa wananchi wanawekwa ndani kila siku. Kama unaweza kuona hata Wabunge humu walikopa yale matrekta yani yale matrekta yamekuwa ni kichomi, ikiwezekana Serikali iweze ikayabeba ikayarudisha huko walikoyatoa, kuliko adhabu hii wanayopata wananchi, wanawekwa ndani wanalipa kila siku, lakini matrekta ni mabovu hayaeleweki.
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee tena suala lingine, niingie kwenye suala la benki. Benki ya Kilimo haijatunufaisha hasa sisi wa Mkoa wa Rukwa. Benki ya Kilimo tunaisikia tu iko Dar es Salaam na Dodoma, lakini kwenye mikoa hii ambayo inalima sana mazao hakuna hiyo benki. Sasa maana yake ni nini benki inaitwa Benki ya Wakulima, kwa wakulima hakuna benki hiyo, basi naomba Serikali iweze kupeleka benki kwenye mikoa ambayo inalima sana mazao, kwa mfano, Rukwa ipelekwe kabisa iandikwe Benki ya Kilimo kama zilivyoandikwa benki zingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, benki nyingine zinaandikwa Benki ya NBC, NMB zinaeleweka, lakini Benki ya Kilimo hatujaona, kwa hiyo Serikali ijitathimini sana kupitia Benki hii ya kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee tena suala lingine…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante kwa mchango mzuri.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika hoja yetu iliyopo mbele yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uzima lakini nichukue nafasi hii kumpongeza Amiri Jeshi Mkuu, Rais wetu, Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kuviendeleza vyombo vyetu vya ulinzi na usalama. Nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri kwa kuweza kuiongoza vizuri Wizara hii nyeti ya Ulinzi na Usalama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze pia Katibu Mkuu Kaka yangu Mnyeti kwa kazi nzuri, lakini pia niendelee kuvipongeza vyombo vyetu...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa tamka jina vizuri la Katibu Mkuu.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, Kaka yangu Mnyepe, Katibu Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kupongeza vyombo vyetu vya Ulinzi kwa ujumla Jeshi letu la ulinzi linafanya kazi nzuri sana, mipaka yetu yote ipo imara, Watanzania wote tunaamani na bahati nzuri mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, tumeweza kutembelea nchi za wenzetu ambazo wana migogoro kwa kweli wanashinda, sisi Watanzania tunaamani kwa sababu Jeshi letu la Ulinzi lipo imara na linafanyakazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu muda wote wanawake ni kubeba mizigo, hekaheka, lakini sisi Watanzania tunalala usingizi, tunafanya mambo yetu kwa uhuru na amani kwa sababu vyombo vyetu vya ulinzi vipo imara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze CDF - Mkuu wa Majeshi, nimpongeze Mnadhimu Mkuu kaka yangu Othman, niwapongeze maofisa wote na wakuu wote wa Kamandi wanafanya kazi nzuri sana katika nchi yetu hii, nchi yetu tunaamani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niingie sasa kwenye suala la JKT; nimpongeze sana pia kaka yangu Meja Jenerali Rajabu Mabele, anafanya kazi nzuri sana, vijana wetu wote sasa hivi kimbilio lao wanatamani sana waingie JKT. JKT inafanya kazi nzuri sana tukiimarisha sana JKT itafanya vizuri kwa sababu vijana wetu wengi watapunguza mambo ya ushoga, wakienda kujiunga na JKT watakuwa imara na nchi yetu itakuwa na vijana imara wanaoweza kujitegemea hata pasipo kuajiriwa. Kwa hiyo nipongeze sana jeshi letu la JKT linafanya kazi nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nichukue nafasi hii kupongeza Shirika letu la Mzinga na nimpongeze pia Brigedia Hamis, amefanya kazi nzuri sana ya ugudunzi wa bomu baridi la kufukuza tembo, lakini pia kufukizia wanyama wakali. Wote hapa Wabunge tulikuwa na kilio cha tembo, tembo walikuwa wanaleta maafa mazito katika nchi yetu, lakini shirika hili wameweza kugundua silaha baridi ya kuweza kuwafukuza tembo hawa bila kuwaua, hongera sana Mzinga.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nilikuwa natamani sana Mzinga hao wanafanya shughuli zao za kujipatia kipato katika shirika lao, lakini hawalipwi, naomba taasisi zile za umma ambazo zimefanya kazi na Shirika la Mzinga, wanaodaiwa waweze kuwalipa Shirika la Mzinga. Nimeona kuna deni hapa takribani shilingi bilioni 1.9 ambazo hawajalipwa watu wa Mzinga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba hizi taasisi ziweze kuwalipa haraka sana, hawa watu wanafanya kazi nzuri hawalali kwa ajili yetu kwa nini tuwacheleweshee pesa zao. Mheshimiwa Waziri utakapokuja hapo...
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
TAARIFA
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumwongezea taarifa mzungumzaji anayezungumza kwa sasa kwamba Shirika la Mzinga kwa kweli ni shirika ambalo linafanya kazi nzuri sana, kwa kugundua bomu hilo la machozi baridi tunaomba lisambazwe nchi nzima, halmashauri zote zinunue ambazo zinasumburiwa na tembo ili mambo yaweze kwenda vizuri. Tunawashukuru sana kwa uvumbuzi wao, ahsante. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Ahsante. Mheshimiwa Bupe muda wako umekwisha.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, naunga mkono hoja...
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nachukua nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia kwenye bajeti hii muhimu iliyoko mbele yetu, Bajeti ya Kilimo ya 2024/2025. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uzima na kuweza kuchangia katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kazi yake ni njema na nzuri hasa kwenye suala zima la kilimo. Mama amefanya mapinduzi makubwa sana. Tukiangalia 80% ya Watanzania ni wakulima. Mama amefikiria, ameweza kuweka ruzuku kwenye suala zima la pembejeo za kilimo. Hongera sana Mama, umeupiga mwingi, tumpe mama maua yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii pia kumpongeza kaka yangu Mheshimiwa Bashe na Naibu wake, kaka yangu Mheshimiwa Silinde kwa kazi nzuri na ubunifu mkubwa kwenye sekta hii ya kilimo. Hongereni sana, nami namwomba Mwenyezi Mungu aendelee kumpa kibali mama na aendelee kuwapa nafasi ili muweze kuwatumikia Watanzania kama mlivyowatumikia kwenye suala zima la sekta ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Katibu Mkuu na Wakurugenzi Watendaji wote wa Taasisi za Wizara ya Kilimo, tukianza na TFC, NFRA, CPB, ASA, Kahawa, Korosho, Tumbaku, TOSCI na Tume ya Umwagiliaji. Kwa pamoja wameweza kufanya kazi nzuri na ndiyo maana Wizara ya Kilimo na sekta ya kilimo sasa hivi imekuwa ni nzuri sana na ni kimbilio la Watanzania. Wakulima wengi zamani walikuwa wanaonekana ni maskini, lakini kwa sasa mkulima ni tajiri na tunakwenda kupata mabilionea kwenye sekta ya kilimo. Yote hii inatokana na uongozi mzuri kuanzia kwa Rais, Waziri na Watendaji wote wa sekta hii, hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naingia kwenye hoja yangu ya msingi, kwanza ni suala la BBT. Nimesoma ukurasa wa 10, kwanza kabisa naipongeza Wizara, nampongeza Waziri kwa mawazo mazuri ya kuleta wazo hili la BBT, ni wazo zuri sana. Mwanzoni watu walibeza, lakini hili wazo linakwenda kumkomboa Mtanzania, hasa vijana, wanawake na Watanzania kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusoma hapa, nimeona mpango wa program ya BBT umelenga kwenye mikoa ya Dodoma, Kigoma, Mbeya, Singida, Pwani, Tanga, Njombe na Kagera, lakini sijaona Mkoa wa Rukwa. Mkoa wa Rukwa ni miongoni mwa mikoa ambayo inalima sana na inaweza kulisha Tanzania nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe mwenyewe na Mheshimiwa Waziri ni mashahidi kwamba Mkoa wa Rukwa tunalima sana, lakini kwenye suala la BBT, hapa sijaona jina la Mkoa wa Rukwa. Naomba sana Mkoa wa Rukwa tuna vijana wengi wakulima wanaoweza kulima vizuri, lakini hawana pa kulima. Tunaomba hii BBT na Mkoa wa Rukwa pia tuwemo kwenye mikoa hii ambayo mmeitaja hapa. Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapo naomba arekebishe na Rukwa iwemo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naingia kwenye suala la pembejeo. Naipongeza sana Serikali kwamba katika Mkoa wangu wa Rukwa tumepata pembejeo za kutosha, pembejeo zenye ruzuku. Wakulima wanamshukuru sana Rais na Mhesimiwa Waziri kwa kuwa tumeona na tumeshuhudia tumepata pembejeo na mbolea ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua unapomaliza msimu, msimu mwingine unaanza. Basi mwaka huu mbolea ziwahi kufika na kwa kiwango cha kutosha. Mbolea inapokuja kwa mfano, kwa mwaka huu mbolea ya CAN imekuja nyingi, lakini mbolea ya UREA imekuja kidogo. Muda wa kuweka mbolea ya UREA ulipofika ikawa kidogo, kwa hiyo, tunaomba msimu huu mbolea zote zije kwa kiwango sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mtovu wa shukrani nisipompongeza Mkurugenzi wa Taasisi ya TFC, kaka yangu Samwel Mshote na Watendaji wote wa TFC, wamefanya kazi nzuri. Pia wameweza kuleta mbolea na pembejeo kwa wingi katika Mkoa wa Rukwa. Mkoa wetu wa Rukwa tunakwenda kuvuna mahindi kwa wingi na changamoto yetu itakuwa ni soko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Wizara izingatie sana, mmehamasisha wakulima wameweza kulima kwa wingi, sasa tatizo litakuja kwenye suala zima la soko, nasi mnajua kabisa tumepakana na nchi jirani ambazo tayari zina majanga ya njaa. Tunaomba mtakapojiridhisha kwamba sasa NFRA imenunua mahindi ya kutosha, basi mtupe kibali cha kufungua zizi, ili tuweze kuuza kwenye nchi jirani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la NFRA. NFRA pia wamefanya kazi nzuri sana, wamenunua mazao yetu kwa wingi, lakini changamoto ilikuwa ni kidogo tu, marekebisho kwenye suala zima la mizani. Mizani ilikuwa ni changamoto kubwa sana. Kwa hiyo, tunaomba safari hii mrekebishe mizani iweze kutenda haki, mkulima atakapokwenda pale amepima kilo zake 100 kutoka huko nyumbani kwake, lakini akifika pale akipima, kilo tano au kumi zinapungua. Kwa hiyo, muweze kurekebisha suala zima la mizani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, niongelee suala la mbegu. Tumeshuhudia kabisa wakulima wengi wanapenda sana mbegu za wenzetu wa Zambia, sijajua za kwetu tatizo ni nini? Ninachoomba ni kwamba, mfanye utafiti ili mbegu zetu ziweze kuingia kwenye ushindani wa masoko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee pia suala la kuleta mbolea. Mbolea isiishie tu wilayani, iende mpaka vijijini, lakini pia mbolea hiyo iweze kuuzwa kwenye viroba vya kilo tano tano, kilo 50 na kilo 25 kwa sababu, kwenye Mikoa na wilaya zetu kuna wakulima wadogo na wakubwa ambao wana uwezo wa kununua kilo tano wanunue kilo tano, wenye uwezo wa kununua kilo 25, wanunue kilo 25. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, niongelee suala la ushuru. Suala la ushuru limekuwa ni changamoto huko, kwa sababu mkulima anapotoa mahindi yake shambani, tayari wataalamu wanafika pale kumtoza ushuru. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Bupe, muda wako umeisha.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)