Primary Questions from Hon. Bupe Nelson Mwakang'ata (33 total)
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-
Kituo cha Afya cha Kirando katika Wilaya ya Nkasi kinatoa huduma kwa vijiji zaidi ya ishirini katika mwambao wa Ziwa Tanganyika na katika kituo hicho wodi za watoto na akina mama zimekuwa ni ndogo sana ikilinganishwa na idadi ya watoto na akina mama wanaohudumiwa katika kituo hicho.
Je, ni lini Serikali itajenga wodi hizo ili kuondoa kero kwa akina mama na watoto wanaohudumiwa katika kituo hicho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang‟ata, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha wodi ya akina mama na watoto katika kituo cha afya cha Kirando, tathmini ya awali imefanyika na kubaini kuwa zinahitajika shilingi milioni 250 ili kukamilisha ujenzi huo. Baada ya kukamilika kwa tathmini hiyo Serikali itaweka katika mpango na bajeti wa Halmashauri ili kuanza ujenzi wa wodi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na umbali wa kituo hicho kutoka Makao Makuu, Serikali imepeleka gari la wagonjwa ili kuboresha huduma za Rufaa kwa akina mama na watoto. Aidha, katika bajeti ya mwaka 2016/2017, Halmashauri imeweka kipaumbele katika ujenzi wa Kituo cha Afya Kata ya Kabwe ili kiweze kuhudumia wananchi wa Korongwe na Kabwe ambao wanahudumiwa na kituo cha afya cha Kirando.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-
Asilimia kumi ya bajeti ya Halmashauri nchini hutengwa kwa ajili ya mikopo ya vijana na wanawake.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kusimamia fedha hizo zitolewe kwa kila Halmashauri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang‟ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tulivyojibu hoja hii mara kadhaa hapa Bungeni, Serikali imejipanga kuhakikisha asilimia kumi ya fedha za vijana na wanawake zinatengwa na zinapelekwa kwa njia ya mikopo. Usimamizi wa suala hili uliwekewa mkazo katika mwongozo wa bajeti ya mwaka 2016/2017 ambapo Halmashauri zote zimetenga shilingi bilioni 56.8 kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na Wanawake kutokana na mapato ya ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa Serikali ni kuimarisha makusanyo ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa kutumia mfumo wa kielektroniki ili kuhakikisha fedha hizo zinatengwa na kupelekwa kwa vijana na wanawake. Maamuzi ya kutenga fedha hizi ni kadri ya makusanyo kila robo mwaka yanafanywa na Halmashauri kupitia Kamati ya Fedha na Mipango na Baraza la Madiwani.
Hivyo, naomba kutoa wito kwenu Waheshimiwa Wabunge wote tushirikiane katika kusimamia suala hili ambalo liko kwenye Halmashauri zetu ili kila tunapofanya maamuzi ya kugawa rasilimali fedha kutokana na mapato ya ndani, tuweke kipaumbele katika kutenga fedha hizo.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-
Serikali ilipanga kujenga na kupanua Uwanja wa Ndege wa
Sumbawanga Mjini.
Je, ni lini ujenzi huo utakamilika pamoja na kuwalipa fidia wananchi
wanaozunguka uwanja huo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang‟ata,
Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepanga kujenga Kiwanja cha Ndege
cha Sumbawanga kwa kiwango cha lami pamoja na jengo jipya la abiria
(Terminal Building). Kiwanja hiki ni miongoni mwa viwanja vinne ambavyo
vitajengwa kwa fedha za mkopo kutoka Benki ya Rasilimali ya Ulaya (European
Investment Bank). Viwanja vingine vitakavyojengwa kwa mkopo kutoka
European Investment Bank katika kundi hili ni Viwanja vya Shinyanga, Kigoma na
Tabora.
Mheshimiwa Naibu Spika, zabuni kwa ajili ya kumpata mkandarasi
zilitangazwa mwezi Agosti, 2016 na kufunguliwa mwezi Oktoba, 2016 ambapo
Mkataba na Mkandarasi wa kujenga kiwanja hiki utasainiwa baada ya kupata
idhini (no objection) kuhusu taarifa ya uchambuzi wa zabuni ambayo watu wa
EIB (European Investiment Bank) tunatarajia kuipata. Aidha, napenda
kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa zoezi la uhakiki wa mali za wananchi
ambao wataathirika na mradi huo lipo katika hatua za mwisho.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-
Serikali inatambua uwepo wa Wenyeviti wa Vitongoji na Vijiji ambao wanatekeleza majukumu yao moja kwa moja
na wananchi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwalipa posho viongozi hao kama inavyofanya kwa Madiwani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia kila Halmashauri imeweka utaratibu wa kuwalipa posho Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji na Mitaa kutoka katika vyanzo vya mapato vya ndani ya Halmashauri. Katika makusanyo ya mapato kupitia vyanzo vya ndani kila Halmashauri hupeleka asilimia 20 kwenye vijiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgawanyo wa fedha hizo ni kwamba 3% hutumika kwa ajili ya maendeleo na 17% hutumika kwa ajili ya utawala ikiwemo kuwalipa posho za Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji na Mitaa. Viwango vya kulipa posho hizo hutofautiana kati ya Halmashauri moja na nyingine kulingana na makusanyo ya mapato ya ndani katika vyanzo vilivyopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuimarisha usimamizi na upatikanaji wa fedha hizo, Ofisi ya Rais, TAMISEMI imependekeza kulifanya suala la asilimia 20 kuwa la kisheria katika marekebisho ya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290. Maandalizi ya sheria hii yako katika hatua za mwisho na Muswada huo utawasilishwa na kujadiliwa hapa Bungeni.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-
Lengo la Serikali ni kuwainua kiuchumi wananchi maskini vijijini hasa wanawake ambao hawana dhamana ya kuweka benki ili waweze kupata mikopo kwa sababu nyumba nyingi za vijijini hazina Hatimiliki ambazo zingeweza kutumika kama dhamana benki.
Je, Serikali inawasaidiaje wananchi na hasa wanawake kwa kuzungumza na benki ili zikubali kukpokea Hatimiliki za kimila kama dhamana ya mikopo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, utoaji wa Hatimiliki za kimila ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria ya Vijiji Namba 5 ya mwaka 1999 na kanuni zake. Utoaji wa hati za Hakimiliki ya kimila ulianza mwaka 2004 Wilayani Mbozi na baadae uliendelea katika Wilaya zingine ambapo hadi sasa takribani hati za Hakimiliki za kimila 400,761 zimekwishatolewa kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa kifungu cha 18(1) cha Sheria ya Vijiji Namba 5 ya mwaka 1999, hati za Hakimiliki za kimila zina hadhi sawa kisheria na hati inayotolewa na Kamishna wa Ardhi. Hadi sasa hati za Hakimiliki za kimila zimewezesha wananchi kupata mikopo yenye thamani ya takribani shilingi bilioni 59 kutoka taasisi mbalimbali za fedha ikiwemo NMB, CRDB, TADB, Stanbic Bank, Meru Community Bank, Agricultural Trust Fund Bank, SIDO, NSSF na Mfuko wa Pembejeo katika Wilaya ya Mbozi, Iringa, Babati, Bariadi, Arumeru, Mbarali, Manyoni, Kilombero, Bagamoyo, Mbinga na Tandahimba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, baadhi ya taasisi za fedha zimekuwa hazikubali kupokea hati za Hakimiliki ya kimila kama dhamana kwa wananchi kupata mikopo. Sababu ambazo zimekua zikitolewa na taasisi hizo ni pamoja na baadhi ya maeneo kutokuwa na thamani au ardhi husika kutoendelezwa; vikwazo katika kuuza dhamana pale mkopaji anaposhindwa kurejesha mkopo kutokana na sharti la kutaka ardhi iuzwe kwa mkazi wa kijiji husika na baadhi ya wamiliki wa ardhi kutokuwa na sifa za kukopesheka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto hizo, Wizara yangu kupitia marekebisho ya Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995 yanayoendelea inaangalia uwezekano wa kuondoa vikwazo vinavyozuia uuzaji wa dhamana pale mkopaji anaposhindwa kurejesha mkopo pamoja kuzungumza na taasisi za fedha kuwa hati ya Hakimiliki ya kimila ina hadhi sawakisheria na hati inayotolewa na Kamishna wa Ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, wananchi hawana budi kuyaendeleza maeneo yao hususani yale yaliyopatiwa hati za Hakimiliki za kimila ili kuyaongezea thamani na hivyo kuzishawishi taasisi za fedha kuyakubali maeneo hayo kama dhamana ya mikopo.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-
Halmashauri za Wilaya ya Nkasi na Sumbawanga Mjini hazina Hospitali ya Wilaya; wanawake na watoto wanapata shida ya matibabu wakati wa kujifungua na huduma za watoto.
Je, ni lini Serikali itajenga Hospitali katika Wilaya hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Rukwa umeanza taratibu za ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa katika eneo la Milanzi. Hospitali ya Mkoa inayotumika sasa itabaki kuwa Hospitali ya Manispaa ya Sumbawanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa wananchi wa Manispaa ya Sumbawanga wanapata huduma za afya katika Hospitali Teule ya Dkt. Atman inayomilikiwa na Kanisa ambayo imeingia mkataba na Serikali wa utoaji huduma za afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi imetenga eneo lenye ukubwa wa ekari zaidi ya 100 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya. Taratibu za kulipa fidia wananchi waliopisha ujenzi huo zinakamilishwa. Kwa sasa wagonjwa wanapata huduma katika Hospitali Teule iliyopo pamoja na vituo vya afya na zahanati. Serikali itajitahidi kutafuta fedha na kushirikiana na wananchi wa Nkasi ili kufanikisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-
Serikali ilipanga kujenga na kupanua Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga Mjini:-
Je, ni lini ujenzi huo utakamilika pamoja na kuwalipa fidia wananchi wanaozunguka uwanja huo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa ukarabati wa uwanja wa ndege wa Sumbawanga upo kwenye hatua ya manunuzi. Mkataba wa usimamizi wa kazi ya ujenzi ulitiwa saini baina ya Serikali na kampuni ya SMEC kutoka Australia mwezi Oktoba, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Mwezi Juni, 2017 Serikali ilitiliana saini mkataba wa ujenzi wa ukarabati wa uwanja huo na Kampuni ya Sino-Shine Overseas Construction and Investment East Africa Limited kutoka Nchini China. Utekelezaji wa mradi huo utakapoanza unategemewa kukamilika ndani ya miezi 18. Kazi ya ujenzi wa uwanja huo zitaanza mara baada ya Serikali kukamilisha taratibu za malipo ya fidia kwa wananchi wanaostahili kulipwa ili waondoke kupisha ujenzi wa uwanja.
Mheshimiwa Naibu Spika, maandalizi ya ulipaji wa fidia kwa wananchi watakaoathirika na mradi huo yapo katika hatua ya uhakiki wa mwisho kabla ya ulipaji wa fidia kuanza.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia vikundi vya wanawake waliopo katika Mkoa wa Rukwa katika suala la mikopo na kuwapatia elimu ya ujasiriamali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, vikundi vya wanawake vinawezeshwa kupitia mfuko wa wanawake unaotokana na asilimia tano ya mapato ya ndani ya Halmashauri. Sambasamba na hilo Serikali inawahimiza Maafisa Maendeleo ya Jamii kuendelea kutoa elimu ya ujasiliamali kwa vikundi vya wanawake ili kuwajengea uwezo, kuibua miradi yenye tija itakayosaidia kupata kipato na kurejesha mkopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2016/2017 vikundi vya wanawake 55 vyenye wanachama 698 vimepatiwa mikopo ya shilingi milioni 56.87 kati ya shilingi bilioni 6.5 zilizokusanywa kutokana na mapato ya ndani katika Mkoa wa Rukwa.
Vilevile katika mwaka wa fedha 2017/2018 vikundi 33 vya wanawake vimepatiwa mikopo yenye jumla ya shilingi milioni 118 kati ya shilingi bilioni 4.2 ya makusanyo ya mapato ya ndani hadi machi, 2017 sawa na asilimia 2.78.
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia kutoa maelekezo kwa Halmashauri kuimarisha makusanyo kwa kutumia mifumo ya kielektroniki iliyowekwa katika Halmashauri zote 185 na kuhakikisha kwamba fedha zinapelekwa kwenye mfuko kila zinapokusanywa.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-
Wanawake ni nguzo muhimu katika kukuza uchumi na kusimamia nchi yetu na kwamba ukimwezesha mwanamke umeiwezesha familia na Taifa kwa ujumla.
Je, ni lini Serikali itafikiria kuboresha huduma za kibenki zitakazoweza kuwahudumia akina mama walio mikoa ya pembezoni?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua mchango wa mwanamke katika familia na Taifa kwa ujumla. Kwa kutambua hilo, Halmashauri zote nchini zinatakiwa kutenga asilimia 10 ya mapato yao kwa ajili ya mikopo ya wanawake na vijana. Suala hili lipo kisera na ni maamuzi ya Serikali katika kuhakikisha kuwa wanawake wanawezeshwa na kujengewa uwezo kiuchumi. Aidha, Serikali itaendelea kuibua programu wezeshi kwa wanawake kwa kadri itakavyoona inafaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na juhudi za kisera za Serikali za kuwawezesha wanawake kiuchumi, jukumu la msingi la Serikali ni kuweka mazingira wezeshi ili watu binafsi, taasisi za umma na binafsi ziweze kuwekeza katika miradi mbalimbali ya kuzalisha mali pamoja na huduma zikiwemo huduma za kibenki. Badala ya Serikali kujiingiza moja kwa moja kusambaza huduma za kibenki hapa nchini, Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji, upatikanaji wa maji, umeme, mawasiliano na usalama wa watu na mali ili kuvutia wawekezaji kusambaza huduma za kibenki katika maeneo mbalimbali hapa nchini yakiwemo maeneo ya pembezoni mwa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo ya kuboresha mazingira ya kufanya biashara, hususan sera, miundombinu na usalama yamevutia wawekezaji binafsi wa ndani na nje kuwekeza hapa nchini na hivyo kuimarisha huduma jumuishi za kifedha kwa njia ya simbanking, wakala wa benki, mobile money, NGO’s, SACCOS na benki za kijamii. Jitihada hizi zimesaidia kuongeza matumizi ya huduma rasmi za fedha kutoka asilimia 58 mwaka 2013 hadi asilimia 65 mwaka 2017. Aidha, matumizi ya huduma zisizo rasmi za fedha zimepungua kutoka asilimia 16 mwaka 2013 hadi asilimia saba mwaka 2017. Hivyo basi, ni wajibu wetu kuendelea kuwashawishi wawekezaji binafsi kusogeza huduma za fedha karibu na wananchi badala ya kuitegemea Serikali.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA (K.n.y. MHE. BUPE MWAKANG’ATA) aliuliza:-
Vijana wengi wamejiajiri katika shughuli mbalimbali ikiwemo waendesha bodaboda, lakini waendesha bodaboda hao wamekuwa wakisumbuliwa sana na askari wa barabarani kwa kutozwa faini ambazo muda mwingine hazina maana na hivyo kuwakatisha tamaa.
Je, Serikali inachukua hatua gani ili kudhibiti vijana hawa wasinyanyaswe?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua mchango mkubwa wa biashara ya pikipiki kwa huduma ya usafiri kwa jamii ambapo vijana wengi wamepata ajira hivyo kukuza kipato chao. Umuhimu mkubwa wa usafiri huu hauwaondolei wahusika wa usafiri huu wajibu wa kuzingatia Sheria na Kanuni za Usalama Barabarani ili kuufanya usafiri huu kuwa salama kwa watumiaji.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba Jeshi la Polisi litaendelea kuwachukulia hatua wale wote ambao wanakiuka Sheria na Kanuni za usalama barabarani, ni rai yangu kwa wale wote ambao wanahisi kuonewa ama kunyanyaswa wakati wakitumia usafiri huu kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ama Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
MHE. ALLY K. MOHAMED (K.n.y. MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA) aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itamaliza mgogoro wa shamba la Efatha Mkoani Rukwa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kumekuwa na mgogoro wa muda mrefu wa matumizi ya Shamba Na. 48/1 la Malonje kati ya mmiliki ambaye ni Mdhamini wa Efatha na wananchi wa vijiji vinavyozunguka shamba hili, hususan Vijiji vya Songambele, Sikaungu na Msanda Muungano. Madai ya wananchi hao ni kuwa sehemu ya shamba hili imeingia ndani ya vijiji vyao.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapo awali Shamba la Malonje lilikuwa likimilikiwa na Wizara ya Maji na Maendeleo ya Mifugo likiwa halina upimaji ambapo lilipimwa mwaka 1997 likiwa na ukubwa wa hekta 15,000. Mwaka 2007 shamba hili liligawanywa ambapo hekta 10,000 ziliuzwa kwa wamiliki ambao ni Efatha Ministry na hekta 5,000 zilizobaki zilipimwa vitalu na kugawiwa wafugaji. Mwaka 2010 baada ya kupokea malalamiko na kuyafanyia kazi, ilibainika kuwa upimaji wa vijiji uliofanyika umeingiliana na mipaka ya shamba husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga na Mkoa wa Rukwa, imefanya jitihada mbalimbali za kumaliza mgogoro huo. Baada ya jitihada hizo kutozaa matunda, tarehe 7 Novemba, 2017 nilikutana na Mwenyekiti wa Bodi ya Huduma ya Efatha na baadhi ya Watendaji wake kwa lengo la kukubaliana namna bora ya kumaliza mgogoro huu ili kuboresha mahusiano ya ujirani mwema kati ya mmiliki na wananchi wa vijiji vinavyozunguka shamba hilo. Wizara yangu ilipendekeza kwamba Efatha iridhie kuachia sehemu ya ardhi ya shamba yenye ukubwa wa ekari 8,392.9 na kuigawa kwa wananchi wa vijiji husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya Bodi ya Wadhamini kukaa, waliridhia kutoa ekari 3,000 kwa Vijiji vya Songambele, Sikaungu na Msanda Muungano kwa maana ya kila kijiji kigawiwe ekari 1,000. Hata hivyo, Kijiji cha Sikaungu kimekataa kupokea ekari hizo kwa kuwa wao wanataka kiasi cha ardhi kama ilivyoonekana kwenye vyeti vyao vya ardhi ya kijiji.
Aidha, majadiliano bado yanaendelea kati ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Efatha na Serikali ya Kijiji cha Sikaungu. Baada ya majadiliano hayo kukamilika, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Halmashauri itasimamia upimaji wa ardhi hiyo.
MHE. BUPE N. MWAKANG‟ATA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga visima virefu vya maji katika Wilaya ya Nkasi ili kutatua changamoto ya maji iliyopo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang‟ata Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua tatizo la maji lililopo katika Wilaya ya Nkasi Serikali katika mwaka wa fedha 2019/2020 imepanga kuchimba visima virefu 9 katika maeneo ya Masolo, Katogolo, Mpata, Mienge, Itindi, Kacheche, Lyele, Mbwendi na Kakoma. Kiasi cha shilingi milioni 315 kimetengwa katika bajeti ya mwaka 2019/2020 kwa ajili ya kazi hiyo. Hadi kufikia mwezi Disemba 2019, Visima 7 vimechimbwa katika vijiji vya Masolo, Katogolo, Mpata, Mienge, Kanazi na Ipanda na kiasi cha shilingi milioni 220 kimetumika katika upimaji na uchimbaji wa visima hivyo ambavyo vitatumika kama vyanzo vya maji katika vijiji husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wa muda mrefu wa kutatua tatizo la maji katika Wilaya ya Nkasi, katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imepanga kutumia zaidi ya bilioni 1.3 kwa kupitia Programu ya PforR kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji katika Wilaya ya Nkasi. Wizara imeshatuma fedha hizo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji 6 Wilayani Nkasi ambapo miradi yote hiyo itatekelezwa kwa mfumo wa wataalam wa ndani (Force Account).
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-
Mkoa wa Rukwa una wilaya nne na hakuna Hospitali ya Wilaya:-
Je, ni lini Serikali itajenga Hospitali za Wilaya katika wilaya hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali imeupatia Mkoa wa Rukwa kiasi cha shilingi bilioni 4.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Halmashauri za Sumbawanga, Nkasi na Kalambo ambapo kila Halmashauri imepatiwa kiasi cha shilingi bilioni 1.5. Vilevile katika mwaka wa fedha 2019/2020, Mkoa wa Rukwa umetengewa kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa hospitali za Halmashauri za Sumbawanga, Nkasi na Kalambo, ambapo kila Halmashauri itapewa kiasi cha shilingi milioni 500. Aidha, kiasi cha shilingi milioni 500 kimetengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa hospitali katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-
Je, ni lini Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa itaanza kujengwa?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Rukwa unao Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sumbawanga inayotoa huduma za rufaa kwa halmashauri nne za mkoa huo hadi sasa. Hata hivyo hospitali hiyo inayo changamoto ya ufinyu wa nafasi kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mipya ya kutolea huduma za afya ili kukidhi mahitaji ya wananchi. Kutokana na changamoto hiyo Ofisi ya Mkoa wa Rukwa imeshapata eneo jipya la ukubwa wa hekari 100 lililopo Milanzi ndani ya Manispaa ya Sumbawanga litakalotumika kwa ajili ya ujenzi wa hospitali mpya ya rufaa ya mkoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi huu utaanza baada ya kumalizika ujenzi wa hospitali za rufaa katika mikoa mipya ya Katavi, Songwe, Njombe, Simiyu na Geita.
MHE. JACQEULINE N. MSONGOZI (K.n.y MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA) Aliuliza: -
Je, ni lini ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga Mjini utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga ni miongoni mwa viwanja vya ndege vinne (4) ambavyo ni Kigoma, Tabora, Sumbawanga na Shinyanga vinavyotarajiwa kujengwa na kukarabatiwa kwa ufadhili wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European Investment Bank – EIB).
Mheshimiwa Naibu Spika, taratibu za makubaliano ya mkataba wa miradi hiyo baina ya Serikali (kupitia Wizara ya Fedha na Mipango) na Mfadhili (Benki ya Uwekezaji ya Ulaya – EIB) tayari zimekamilika na idhini (No Objection) ya kuanza utekelezaji wa miradi yote minne (4) imetolewa na Mfadhili wa miradi husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa Mkandarasi (M/ s Sino Shine Overseas Construction & Investment East Africa Limited) na Mshauri Elekezi (SMEC International PTY Limited) ikishirikiana na Kampuni ya SMEC International Tanzania Limited) kwa ajili ya kutekeleza kazi hii, wamepatikana. Hivyo hivi sasa, Serikali iko katika hatua za awali za kuanza utekelezaji wa mradi huu.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-
Je, ni lini barabara ya kutoka Kilando – Katete – Kazovu – Korongwe katika Wilaya ya Nkasi itakamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa Rukwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Barabaraya Kirando – Korongwe ina urefu wa kilomita 35. Matengenezo ya barabara hii yalianza mwaka wa fedha 2017/2018 kwa kuanza na usanifu wa barabara yote ya kilomita 35 na usanifu wa daraja moja la mita 40 la Mto Kavunja; Usanifu wa madaraja mawili yenye urefu wa mita 12.6 kila moja.
Aidha, katika mwaka wa fedha 2016/2017, TARURA ilifungua Barabara ya Kirando – Kazovu yenye urefu wa kilomita 22 iliyotengenezwa kwa gharama ya shilingi milioni
108.37. Katika mwaka wa fedha 2021/2022, kiasi cha shilingi milioni 11.4 zitatengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara yenye urefu wa kilomita 11.4.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2018/ 2019, Serikali ilianza ujenzi wa daraja la Mto Kavunja lenye urefu wa mita 40 kwa gharama ya Shilingi bilioni 1.76 na shilingi milioni 954.70 zimeshapokelewa na ujenzi unaendelea ambapo daraja hili linatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2021. Vilevile, katika mwaka wa fedha 2021/2022, daraja hili litatengewa kiasi cha shilingi milioni 500.
Aidha, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara na madaraja yaliyobaki kwenye Barabara ya Kirando – Korongwe kulingana na upatikanaji wa fedha ili kuondoa changamoto ya usafiri kwa wananchi wa Kazovu, Kitete na Korongwe katika Wilaya ya Nkasi.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-
Je, ni lini Mradi mkubwa wa Maji wa Kabwe katika Wilaya ya Nkasi utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakangata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji Kabwe una miundombinu yote kwa ajili ya kutoa huduma ya maji. Miundombinu hiyo ni matanki matatu yenye ujazo wa lita 50,000, lita 10,000 na lita 135,000, vituo vya kuchotea maji 29, nyumba ya pampu ya kusukuma maji na mabomba ya kilometa 10.9. Changamoto iliyojitokeza kwenye mradi huu ni uwezo wa nishati ya umemejua kushindwa kusukuma maji ipasavyo kwenda kwenye matanki hayo, hivyo, kusababisha huduma ya maji kusimama kwa wananchi hususan kipindi cha usiku.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha huduma ya maji kwa wananchi wa Kabwe inapatikana muda wote, Serikali imeamua kubadili mfumo wa umemejua kwa kufunga umeme toka kwenye gridi kupitia REA na kazi hiyo inatarajiwa kukamilika kabla ya mwishoni mwa mwezi Juni, 2021.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza: -
Je, ni lini Barabara ya kutoka Kibaoni – Kasansa – Muze – Ilemba – Kilyamatundu hadi Mlowo itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakangáta, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Kibaoni hadi Mlowo ni barabara ya mkoa yenye jumla ya urefu wa kilomita 363 na inaunganisha mikoa ya Katavi, Rukwa na Songwe. Barabara hii inapita katika bonde la Ziwa Rukwa ambalo ni maarufu kwa uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara pamoja na uvuvi na hivyo kuwa kichocheo kikubwa cha kiuchumi katika mikoa ya Rukwa, Katavi na Songwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, Serikali ilianza mipango ya kuijenga kwa kuanza na ujenzi wa Daraja la Momba ambalo lilikuwa kikwazo kikubwa cha mawasiliano kati ya mikoa hii mitatu ya Rukwa, Katavi na Songwe ambao umekamilika. Ili kukamilisha ujenzi wa barabara yote kwa kiwango cha lami kuanzia Kibaoni hadi Mlowo ambayo ni kilomita 363, Serikali ipo katika hatua ya awali ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ambapo kazi inaendelea kwa sehemu ya Kibaoni – Majimoto yenye urefu wa kilomita 27 iliyopo mkoani Katavi na sehemu ya Muze – Kilyamatundu yenye urefu wa kilomita 141 iliyopo Mkoa wa Rukwa. Kwa upande wa Mkoa wa Songwe, kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa sehemu ya Mlowo – Kamsamba yenye urefu wa kilomita 130.1 imekamilika na Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, Serikali itaanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami kulingana na upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara ya kutoka Kalambo Falls hadi barabara kuu inayokwenda Matai yenye urefu wa kilometa17?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa ukarabati wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 17 kwa kiwango cha Changarawe unaendelea ambapo kwa mwaka wa fedha 2020/2021, Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa Halmashauri ya Wilaya Kalambo kwa kushirikana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kwa maana ya TFS ulitumia kiasi cha shilingi milioni 139.72 kukarabati sehemu ya barabara hiyo kipande chenye urefu wa Kilometa 10.
Mheshimiwa Spika, vile vile kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Halmashauri ya Wilaya Kalambo umetenga kiasi cha shilingi milioni 84.5 kwa ajili ya matengenezo ya muda maalum kwa maana Periodic Maintenance kipande chenye urefu wa kilometa 4 na Mkandarasi amekwisha patikana na yupo eneo la mradi akiendelea na kazi.
Mheshimiwa Spika, hali ya barabara hii kwa sasa inaridhisha kwani inapitika katika kipindi chote cha mwaka. Aidha, kutokana na umuhimu wa barabara hii, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya matengenezo yake kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza kiwango cha mkopo wa 10% kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali ilianzisha utaratibu wa kutoa mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili kusaidia makundi haya kuendasha shughuli zao za ujasiriamali na kujiongezea kipato.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali haijaweka mpango wa kuongeza asilimia ya mikopo hiyo. Aidha, tathmini ya kina inafanyika ili kubaini mafanikio na changamoto zilizopo ili hatua stahiki zichukuliwe katika kuboresha mikopo hiyo.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka Madaktari Bingwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziriwa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa hadi sasa ina jumla ya Madaktari Bingwa watano wa fani za afya kama ifuatavyo; mama na uzazi wawili, magonjwa ya watoto wawili pamoja na madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani (physician) mmoja. Katika kuongeza idadi ya madaktari bingwa, Wizara imepeleka kusoma jumla ya madaktari watano kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa, ambao ni madaktari wawili wanasomea upasuaji, daktari mmoja anaesomea upasuaji wa mifupa, daktari mmoja anasomea magonjwa ya dharula na daktari mmoja anaesomea kinywa, sikio na koo, ahsante.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango wa kukamilisha ujenzi wa uwanja wa Ndege wa Sumbawanga Mjini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga ni miongoni mwa miradi ya Ujenzi na Upanuzi wa Viwanja vya Ndege Vinne (4) ambavyo ni Kigoma, Tabora, Sumbawanga na Shinyanga inayotarajiwa kutekelezwa kwa Ufadhili wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European Investment Bank - EIB).
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa, matakwa ya kimkataba kati ya Serikali na EIB yamekamilishwa na mfadhili tayari ameshatoa fedha kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa miradi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mradi huu ulichelewa kuanza kwa wakati, kwa sasa taratibu za kimkataba kati ya Serikali na Mkandarasi zinaendelea. Aidha, Mkandarasi amewasilisha maombi ya kufanyika kwa marekebisho ya Mkataba wa awali. Hivyo, marekebisho haya yameshafanyika na kuwasilishwa kwa Mfadhili (EIB) kwa ajili ya kupata idhini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa, Serikali imejipanga kuanza utekelezaji wa mradi huu kabla ya mwaka wa fedha 2021/2022 haujaisha endapo idhini itatolewa na mfadhili kwa wakati.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga josho katika Kata ya Miula Wilayani Nkasi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI aljibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Wizara ilipeleka kiasi cha shilingi milioni 108 kwa ajili ya ujenzi wa majosho sita katika Hamashauri ya Nkasi katika Vijiji vya Kipande, Katani, Chala, Mikukwe, Chalatila na Sintali. Majosho hayo yapo katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea kuwasiliana na Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi ili kukamilisha ujenzi wa majosho hayo na kutoa fursa kwa Serikali kutenga fedha zaidi kwa ajili ya ujenzi wa majosho mengine Nkasi Kusini ikiwemo Kata ya Miula. Aidha, Serikali inaendelea kuhamasisha wafugaji kuchangia ujenzi wa miundombinu ya mifugo ikiwemo majosho katika maeneo yao. Ahsante.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kufungua vituo vingi zaidi vya kuuza gesi asilia?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiachana na usambazaji wa gesi asilia kwa kutumia bomba la kusafirisha gesi Mtwara, Lindi, Pwani na Dar es Salaam, kuna vituo vitatu vya kugandamiza na kuuza gesi asilia nchini (Compressed Natural Gas (CNG) Stations) ambapo Dar es Salaam viko viwili (2) na Mtwara kipo kimoja (1). Vituo viwili vinamilikiwa na wawekezaji binafsi na kimoja ni ubia wa Serikali na Sekta Binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2022/2023, Serikali imempata Mkandarasi wa ujenzi wa vituo vitatu (3) vya (CNG) na kazi hiyo itaanza kabla ya mwaka huu wa fedha kwisha. Vilevile, kituo kimoja (1) kitajengwa na mwekezaji binafsi (Dangote) eneo la Mkuranga, Pwani. Aidha, Serikali imeshatoa idhini kwa kampuni binafsi 20 kujenga vituo vya kujaza gesi katika magari. Kampuni hizo zipo katika hatua mbalimbali za kupata vibali vya ujenzi.
Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine, Serikali imepanga kujenga vituo vya CNG katika Bohari Kuu za Serikali za Dar es Salaam na Dodoma ili kuwezesha magari ya Serikali na watu binafsi yanayoendelea kuunganishwa na mfumo wa kutumia gesi asilia kuweza kupata nishati hiyo. Taratibu za utekelezaji wa mradi huu zinakamilishwa Serikalini ili utekelezaji uanze mara moja.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itapeleka wapimaji wa miamba ya madini katika Mikoa ya Rukwa na Songwe?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imekwishafanya utafiti wa miamba katika Mikoa ya Rukwa na Songwe na kuchora ramani za miamba katika kipimo cha skeli ya 1:100,000 ambazo hutumika kuonesha uhusiano wa miamba na madini. Ramani hizi za miamba zinapatikana GST na ndizo kwa sasa hutumika kuvutia uwekezaji katika sekta ya madini kwa maeneo hayo. Ahsante sana.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-
Je, lini Serikali itaviendeleza viwanda vya nyama na samaki Mkoani Rukwa?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, uendelezaji wa sekta ya viwanda ikiwemo viwanda vya nyama na samaki katika Mkoa wa Rukwa na mikoa mingine nchini ni endelevu. Serikali inaendelea na juhudi za kuhamasisha uwekezaji wa viwanda vipya na uendelezaji wa viwanda vilivyopo katika sekta ya mifugo na uvuvi hususani viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo na uvuvi.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto ya upatikanaji wa malighafi ya mazao ya mifugo na uvuvi inayovikabili viwanda vya nyama na samaki katika Mkoa wa Rukwa na mikoa mingine nchini. Kwa sasa Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeweka nguvu kubwa katika unenepeshaji wa mifugo pamoja na ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba, kutenga na kuboresha maeneo ya ukusanyaji samaki (collection centers) pamoja na minada ya mifugo ili kukidhi haja ya upatikanaji endelevu wa malighafi bora ya viwanda vya nyama na samaki nchini ikiwemo katika Mkoa wa Rukwa.
Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali inaendelea na juhudi za kukabiliana na tatizo la utoroshaji wa mazao ya samaki na mifugo kwenda nchi za jirani bila kufuata taratibu ili kukidhi mahitaji ya malighafi katika viwanda vyetu vya ndani. Hivyo, nitoe rai kwa wavuvi na wafugaji kuviuzia malighafi viwanda vyetu vya ndani ili viweze kukidhi mahitaji yake, nakushukuru.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kupunguza gharama za matibabu kwa akina mama wanapokwenda Kliniki Sumbawanga?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Sera ya Afya ya mwaka 2007 kifungu Na. 5(3) na (4)(c) kinaelekeza kuwa huduma za afya ya uzazi ikiwemo kuhudhuria kliniki, wakati wa uchungu, wakati wa kujifungua, na baada ya kujifungua pamoja na uzazi wa mpango zitakuwa zikitolewa bila malipo.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa wito kwa watumishi katika vituo vya kutolea huduma za afya kutowatoza gharama za uzazi wanawake wote wanaofika vituoni kupata huduma ya afya ya uzazi.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA atauliza: -
Je, ni lini mradi wa maji Kata za Kaengeza na Kanda Sumbawanga Vijijini itakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Kaengesa ina vijiji vinne ambapo katika mwaka 2022/2023, Serikali inaendelea kutekeleza mradi wa maji Mkunda Group utakaohudumia vijiji vya Mkunda, Kaengesa A na Kaengesa B. Mradi huo unatarajia kukamilika mwezi Septemba, 2023 na wananchi Kijiji cha Mkunda wameanza kupata huduma ya maji. Kwa Kijiji cha Itela, Serikali itafanya usanifu na kujenga mradi wa maji katika mwaka wa fedha 2023/2024.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Kata ya Kanda yenye vijiji vinne, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali inaendelea kutekeleza mradi wa maji utakaohudumia vijiji vya Lula na Chitete. Vijiji vinavyobaki vya Lyapona A na Lyapona B usanifu utafanyika katika mwaka wa fedha 2023/2024 na miradi kujengwa.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza: -
Je, ni lini Mradi wa Maji wa Ikozi uliopo Sumbawanga Vijijini utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imeendelea na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Bwawa la Ikozi unaohudumia Viijiji vya Ikozi, Kazwila, Chituo na Tentula vya Kata ya Ikozi, Wilaya ya Sumbawanga Vijijini. Mradi huo unahusisha ujenzi wa bwawa, ulazaji wa bomba kuu umbali wa kilometa 1.2, nyumba ya mtambo, ununuzi na ufungaji wa pump za kusukuma maji na ujenzi wa mfumo wa kusafisha na kutibu maji. Utekelezaji wa mradi utakamilika katika mwaka wa fedha 2022/2023.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza: -
Je, lini Serikali itamaliza Mgogoro wa Shamba la Gereza la Mollo – Rukwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miaka ya nyuma kabla ya mwaka 2018 kulikuwepo na mgogoro wa mipaka ya ardhi kati ya gereza la kilimo Mollo na vijiji vya Msanda, Muungano, Malonje, Songambele na Sikaungu vinavyopakana na gereza hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kikao cha Tarehe 24 mwezi Novemba 2023 kilichowahusisha Mheshimiwa Jerry William Silaa, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na wataalamu wa ardhi kilimaliza mgogoro uliyokuwepo kati ya Gereza la Mollo na vijiji husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kumaliza mgogoro huu ilikubalika na pande zote kwamba Jeshi la Magereza libakie na eneo lenye ukubwa wa ekari 8,989.4 na vijiji vibakie nae neo lenye ukubwa wa ekari 1,800. Baada ya makubaliano hayo Jeshi la Magereza lilipima na kubainisha mipaka ya eneo lake huku vijiji pia vikitambua maeneo yao. Hivyo kwa sasa hakuna mgogoro tena baina ya Gereza la Mollo na vijiji vinavyopakana nalo. Ahsante. (Makofi)
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itakamilisha mradi wa maji uliopo Mpasa, King’ombe, Kata ya Kala, Wilayani Nkasi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekamilisha Miradi ya Maji ya Mpasa na King’ombe, Wilayani Nkansi, Mkoa wa Rukwa na inatoa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi. Kwa sasa skimu hizo zinasimamiwa na chombo cha Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO) cha Chipiruka kwa ajili ya uendeshaji na matengenezo. Skimu hizo zinahudumia jumla ya watu 11,267 waishio kwenye vijiji vitatu vya King’ombe, Mpasa pamoja na Mlambo kupitia vituo 42 vya kuchotea maji, ahsante.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza:-
Je, kuna mpango gani wa kukamilisha mradi wa maji kutoka Ziwa Tanganyika na kusambaza katika Mkoa wa Rukwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum Rukwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha huduma ya maji safi na usafi wa mazingira inaimarika katika Mkoa wa Rukwa, Serikali imekamilisha upembuzi yakinifu wa awali wa kutumia chanzo cha Ziwa Tanganyika ambacho ni cha uhakika. Hadi sasa, taratibu za manunuzi za kumpata mtaalam mshauri wa usanifu wa kina wa kutoa maji Ziwa Tanganyika na kuyapeleka katika Mikoa ya Rukwa, Katavi mpaka Kigoma zimeanza na zitakamilika katika mwaka 2024/2025.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA aliuliza: -
Je, lini Serikali itamalizia ujenzi wa Vituo vya Polisi vilivyoanza kujengwa Mkoani Rukwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Rukwa una Vituo vya Polisi vya Kata vinavyojengwa kwa kutumia nguvu za wananchi, ambavyo ni Kate, Kambo, Milepa, Ilemba na Kirando. Tathmini kwa ajili ya kumalizia ujenzi imefanyika na kiasi cha fedha shilingi 311,000,000/= kinahitajika.
Mheshimiwa Spika, ili kuunga mkono jitihada za wananchi, Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI, imeviingiza vituo hivyo kwenye mpango wa kumaliza ujenzi wa maboma 77 ya Vituo vya Polisi vya Kata kuanzia mwaka wa fedha wa Bajeti ya Serikali 2024/2025.