Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Bupe Nelson Mwakang'ata (1 total)

MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itaanza kuweka mita za maji ambazo unalipia kabla ya matumizi kama ilivyo kwenye LUKU ili kuepusha malalamiko ya wananchi ya kubambikiwa bili za maji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Bupe, kwa kuendelea kuwa mdau mkubwa sana katika sekta yetu ya maji na kwa kuendelea kuwa msemaji wa akina mama kutoka katika mkoa wake. Haya kwanza ni maelekezo ya Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan na sisi tumeshayachukua na tayari tumeshaanza kutekeleza agizo la Mheshimiwa Rais. Vilevile naomba niseme kitu kimoja kwamba jambo ambalo sisi tunaenda kulifanya, tunaenda kwenye smart prepaid water meter ambayo ni tofauti kidogo na LUKU. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaponunua LUKU unamtumia mtu token anaingiza, sisi tunataka kwamba mtu akiwa Dar es Salaam maji yake yameisha Dodoma ana uwezo wa kununua maji yake ndani ya sekunde 20 tayari kule valve inakuwa imeshaachia imeshasoma na kuanza kutoa maji, hakuna haja ya kupitia njia nyingi nyingi kuhakikisha kwamba unatuma kwa mtu halafu anaingiza LUKU, hapana, sisi tunaenda kwenye smart prepaid water meter kuhakikisha kwamba itapunguza changamoto kwa wananchi kubambikiwa kama ambavyo Mheshimiwa amesema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine itasaidia upotevu wa maji ambayo imekuwa ni changamoto kubwa sana, Serikali kuzalisha maji kwa gharama kubwa, lakini mengine yanapotea bila ya kuwa na sababu. Tatu, itasaidia kwa wananchi wenyewe kujua matumizi halisi ya familia zao na kuji-regulate wao wenyewe kuhakikisha kwamba hatuendi kwenye upotevu wa maji ambayo yalikuwa yanapotea bila ya kuwa na sababu za msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali imeshajipanga tayari na tayari hivi tunavyoongea Mheshimiwa Waziri yupo China na ameenda kutembelea viwanda ambavyo vinazalisha smart prepaid water meter na atakaporejea tunaamini kwamba tutakuwa na jibu na muarobaini wa tatizo ambalo limekuwa likitusumbua katika Sekta ya Maji.