Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Bupe Nelson Mwakang'ata (57 total)

MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, kwa kuwa tatizo hili limeikumba pia hospitali ya Namanyele - Nkasi Kusini na kwa bahati nzuri Serikali imejenga majengo ya wodi. Je, ni lini sasa Serikali itakabidhi na kufungua majengo haya?
Swali la pili, azma ya Serikali ni kuwa kila kata kuwa na kituo cha afya na kila kijiji kuwa na zahanati, je, ni lini vijiji hivi vinavyotegemea hospitali ya Kirando vitapatiwa zahanati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipende kushukuru kama facilities zimekamilika, sasa bado kuweza kufunguliwa nadhani kikubwa zaidi tutawasiliana na uongozi wa mkoa kuangalia utaratibu tukishirikiana na wenzetu wa Wizara ya Afya, vifaa hivyo vikishakamilika basi hospitali hiyo iweze kufunguliwa. Hilo ni jambo ambalo tunasema kama Serikali tunalichukua kwa ajili ya kwenda kulifanyia kazi ili wananchi waweze kupata huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ajenda ya pili ni jinsi mchakato wa ujenzi wa vituo vya afya ya zahanati ni kweli sasa hivi tuna karibuni ya kata 3390, lakini vituo vya afya tulivyonavyo ni vituo 484 maana yake tuna gap kubwa sana ya kufanya. Ndiyo maana leo hii Waziri wa Afya ata-table bajeti yake hapa ikionyesha mikakati mipana kwa ajili ya kufikia maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukijua wazi kwamba katika hao wenzetu wa eneo hili wanachagamoto kubwa sana na nikifanya rejea ya Mheshimiwa Keissy hapa alishasema mara nyingi sana. Hiki hasa kituo chako cha Kirando na yeye alikuwa akiomba ikiwezekana iwe Hospitali ya Wilaya kwa mtazamo wake. Lakini alikuwa akifanya hivi ni kwa sababu wenzetu wa kule wa pembezoni wakati mwingine wanapata wagonjwa wengine mpaka kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo Serikali naomba tuseme wazi kwamba tutashirikiana vya kutosha na mimi naomba nikiri kwamba katika maeneo yangu ya mchakato wa kuanza kutembelea nina mpango baada ya Bunge hili la Bajeti kutembelea katika mkoa huu ili kuangalia changamoto zinazowakabili ili kwa pamoja tuweze kuzitatua tukiwa katika ground pale tuone ni lipi linalowakabili wananchi wetu.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, kwa kuwa asilimia kumi iliyopo sasa hivi imepitwa na wakati, na wanawake na vijana wanakuwa kwenye makundi ya watu watano, watano, wanagawana hiyo asilimia 10 wanagawana shilingi laki moja, pesa ambayo haiwezi kukidhi matakwa ya mahitaji yao. Je, serikali ina mpango gani wa kuongeza asilimia kumi iliyoko sasa hivi? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa asilimia kumi iliyoko sasa hivi haitoki kwa wakati na wakati mwingine inasubiri matukio muhimu kama vile Mwenge. Je, ni lini Serikali itafanya sasa asilimia hii itoke kwa wakati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Bupe, kwa sababu nimeona akiguswa sana na kinamama na vijana katika maeneo yake. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge hiyo ni credit kwako, kwa sababu naona unawatumikia wananchi wako wa Mkoa wa Rukwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema awali asilimia kumi ni mgao katika mapato ya ndani, na asilimia kumi hii inatofautiana kutoka Halmashauri moja na kwenda Halmashauri nyingine. Kwa mfano, Halmashauri ambayo collection yake kwa mwezi ni shilingi milioni 200, unapozungumzia asilimia kumi maana yake unazungumzia shilingi milioni 20. Lakini tujue kwamba kiwamba kiwango hiki ni (own source) mapato ya ndani ya Halmashauri, na katika yale mapato ya ndani kuna mgawanyiko wa aina mbalimbali kutoka mapato ya ndani, kuna mingine kutoka miradi ya maendeleo, kuna vitu mbalimbali. Kwa hiyo, hii asilimia kumi kiundani ni asilimia yenye kutosha kabisa katika mchakato wa own source, kwa sababu ile pesa ya ndani bado kuna mahitaji mengine ya miradi ya maendeleo inatakiwa ifanyike katika Halmashauri.
Kwa hiyo, hii asilimia kumi siyo ndogo, isipokuwa lengo kubwa ni kila Halmashauri iweze kujipanga ikusanye mapato ya kutosha kutoka katika vyanzo vya ndani. Kuna Halmashauri zingine kwa mwezi wanakusanya shilingi milioni 500, asilimia kumi ni shilingi milioni 50; ni imani yangu kubwa kama kila Halmashauri imejipanga vizuri wanapofanya collection zao mfano hata shilingi milioni100, asilimia kumi yake ni shilingi milioni kumi, wakiamua kuzigawa zile vizuri, wakipanga mpango mkakati vizuri, zitawasaidia kina mama na vijana katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo letu kubwa lilikuwa pesa tulizozipanga katika own source ten percent ilikuwa haiendi kwa akina mama na vijana, na ndiyo maana katika Kikao cha Bunge kilichopita nilisema kwamba kipindi kilichopita own source peke yake ambazo hazikupelekwa kwa kina mama na vijana zaidi ya shilingi bilioni 39; maana yake ni kwamba Madiwani na sisi tulivyokuwa katika Kamati ya Fedha hatukutimiza wajibu…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, tafadhali naomba ufupishe majibu, tafadhali! (Makofi/Kicheko)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka angalau kidogo tuelezane hili, suala la asilimia kumi halitoki, nilikuwa nakuja asilimia kumi kutoka maana yake ni maamuzi ya wenyewe Wabunge na Madiwani, ndiyo tunakaa katika Kamati ya Fedha tunapanga kwamba asilimia kumi zitoke. Ina maana sisi tukishindwa kutimiza wajibu wetu, zitakuwa bado haziwafikii vijana, kwa sababu ten percent inafanywa katika Kamati ya Fedha ya Halmashauri husika.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja
na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali
la kwanza; kwa kuwa, wananchi wale walifanyiwa tathmini ya nyumba zao
muda mrefu na kwa kuwa, pesa inapanda thamani kila kukicha. Je, Serikali ipo
tayari kuwafanyia tathmini upya na kuwalipa kwa wakati?
Swali la pili; kwa kuwa, wananchi hawa wamepoteza imani na matumaini
ya kulipwa fidia zao kwa wakati na kwa kuwa, jitihada za Mbunge wa Jimbo
Mheshimiwa Aeshi Hilaly, amekuwa akifanya juhudi muda mrefu. Je, Mheshimiwa
Waizri yupo tayari kuongozana nami mpaka kwa wananchi ili akajionee
mwenyewe nyumba zinavyobomoka? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa
Naibu Spika, kama ambavyo nilieleza katika jibu la swali la msingi kwamba hivi
tunavyoongea suala la uhakiki wa mali za wananchi ambao wataathirika na
mradi huu lipo katika hatua za mwisho. Kwa maana hiyo, taarifa kamili ya nani
na nini watalipwa inatarajiwa kupatikana hivi karibuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kwenda kujionea madhara ambayo
wananchi wale waliosimamishwa muda mrefu kuendeleza nyumba zao,
naomba sana uwasiliane na Mheshimiwa Aeshi ili Mheshimiwa Aeshi aniruhusu
niongozane naye. Kwa sababu, nina uhakika Mheshimiwa Bupe Mwakang‟ata
na Mheshimiwa Aeshi wanafanya kazi moja ya kuwatetea wana Sumbawanga,
nimhakikishie tu kwamba nitakuwa tayari kuongozana na yeye akiwa na
Mheshimiwa Aeshi.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Pamoja
na majibu mazuri ya Serikali, sote tunajua kazi za Wenyeviti, wamekuwa wanafanya kazi nzuri sana katika mitaa na vijiji vyetu, lakini hakuna hata siku moja wamelipwa posho.
Nataka Serikali iniambie leo ni lini itapanga kiwango cha kuwalipa Wenyeviti hawa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Wenyeviti hawa wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira
magumu sana, wakati huo hawa ndio wasimamizi namba moja wa usalama katika vijiji na vitongoji vyetu, wanatatua migogoro kila siku, watoto wa mitaani wakipotea, wanapelekwa kwenye Wenyeviti, tukigombana usiku break ya kwanza kwa Wenyeviti, sote tunajua kazi za Wenyeviti.
Je, Serikali ipo tayari kuwapa hata usafiri angalau baiskeli za kuwasaidia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kweli kama anavyosema Mheshimiwa Bupe, Wenyeviti wetu wanafanya kazi kubwa sana katika vijiji, hili jambo halipingiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema lini? Naomba nizungumze wazi, kwa sababu tulikuwa na changamoto
kubwa hapa nyuma, hata ukija kuangalia Halmashauri zetu, hata kupeleka zile fedha, Halmashauri nyingine ilikuwa
inaonekana kama ni hisani. Ndiyo maana sasa hivi tunafanya haya marekebisho na muswada huu utaingia Bungeni wakati wowote. Hivi sasa umeshaiva na wadau wameshiriki vya kutosha. Katika Sura ya 290 kifungu cha 54 kinafanyiwa marekebisho na Waziri mwenye dhamana sasa atapewa utaratibu wa kuweka kama misingi ya kisheria, kuzielekeza Halmashauri sasa kupeleka zile fedha. Mwisho wa siku ni kwamba aidha, Halmshauri wataweza kupata hasa Wenyeviti wetu wa vijiji ambao tunatambua kwamba wanafanya kazi kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la usafiri, ni kweli kama nilivyosema ni kwamba utakuta sehemu nyingine
Mwenyekiti wa Kijiji anatoka kitongoji kimoja anakwenda kitongoji kingine, changamoto yake ni kubwa. Vilevile kwa sababu kama tutaweka utaratibu mzuri wa kisheria na hata ukiangalia sheria, sehemu inayozungumza mambo ya expenditure pale, inazungumza kama kuna matumizi ya fedha nyingine zinazoweza kutumika kwa maslahi mapana ya kujenga eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utaratibu huo tukishafanikiwa vizuri, basi tutatoa maelekezo ya kutosha kuona jinsi gani tutafanya, tutaangalia na rasilimali fedha zilizopatikana angalau kama itawezekana baadhi ya vipando hasa baiskeli, lakini maelekezo hayo yatakuja baada ya kurekebisha sheria yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge jambo, lako ni la msingi na Serikali tunalifanyia kazi kama nilivyozungumza.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mojawapo ya shida inayowapata wanawake ni mitaji na Serikali imeweka pesa nyingi sana kwenye mabenki ili wakope, lakini wanapotaka kwenda kukopa kwenye mabenki wanaambiwa wapeleke hati, wanapokwenda kutafuta hati kwenye Ofisi za Ardhi wanahangaishwa sana; wanaambiwa wapeleke vitu vingi sana na wanaambiwa milolongo ya mambo mpaka wanaamua kuacha, zaidi ya mwaka mtu anafuatilia hati. Ni lini sasa Serikali itaweka gharama halisi za kupata hati?(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Benki ya Wanawake ipo Dar es Salaam tu, ni lini sasa Serikali itaamua kufungua matawi mengine katika mikoa mingine ili wanawake wapate huduma hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna usumbufu katika kupata hati na hasa hizi Hakimiliki za kimila ambazo tunazizungumzia kwasababu shughuli yote inafanyika katika maeneo husika na katika vijiji husika. Kwa hiyo, mimi niseme pale ambapo Halmashauri yoyote inaonekana kwamba ni kikwazo katika kuwapatia wananchi hati za Hakimiliki za kimila tuwasiliane kwa sababu lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba mwananchi wa Kijijini tunamuwezesha kuweza kupata hati yake ya Hakimiliki ya kimila.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kwasababu ndio sehemu pekee ambayo inaweza kumkomboa na mpaka sasa kama nilivyosema hati 400,761 zimeshatoka ni kwasababu tu ya ushirikiano wa karibu sana na wenyewe baada ya kuwa tumewaelimisha kwamba hati zile zinakwenda kuwakomboa katika shughuli za kimaendeleo. Kwa hiyo, pale wanapokwama naomba tuwasiliane ili tushughulikie.

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru; naomba kujibu swali la pili la nyongeza la Mheshimiwa Bupe Mwakang’ata na ninaomba majibu yangu yaende kwa wanawake wote wa Tanzania kwamba Benki ya Wanawake ilianzishwa kwa malengo ya kuwahudumia, lakini kwa sasa ina changamoto kubwa za kimtaji na tutafungua matawi mikoani pindi ambapo uwezo wetu wa kimtaji wa Benki ya Wanawake utakavyoimarika. Ila kwa sasa tulichokifanya ni kuhakikisha tunafungua vituo vya kuwahudumia na kuwawezesha wanawake kwenye mikoa zaidi ya 18 nchini ili kuwapa elimu ya ujasiriamali lakini pia mikopo midogo midogo isiyo na dhamana ambapo wanawake wanadhaminiana wao kwa wao. (Makofi)
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini maswali mawili ya nyongeza ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Sera ya Afya inasema itajenga zahanati kila kijiji na pia itajenga vituo vya afya kila kata na pia itajenga Hospitali za Wilaya kila wilaya. Je, ni lini sera hii itatekelezwa kikamilifu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa afya ni kipaumbele cha mwanadamu hasa kwa mama na mtoto, je, Serikali haioni umuhimu wa kuupa kipaumbele Mkoa wa Rukwa kwa kuwa hauna Hospitali ya Wilaya hata moja? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli sera yetu inatueleza hivyo na ndiyo maana ukiangalia mchakato wa Serikali kwa kushirikiana na ninyi Waheshimiwa Wabunge, wananchi na wadau mbalimbali mnaona ni jinsi gani tunajitahidi kwa kadri iwezekanavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli naomba nitoe pongezi zangu za dhati, katika maeneo mbalimbali nilikopita nimekuta Wabunge wengi sana na wengine wakitumia Mfuko wa Jimbo na kuungana nguvu na wananchi katika suala zima la ujenzi wa zahanati na vituo vya afya. Nilishawahi kuzungumza hapa siku za nyuma kwamba katika bajeti ya mwaka 2017/2018 tumetenga shilingi bilioni 251 lakini katika hizo shilingi bilioni 68 ni kwa ajili ya ku-top up shughuli hizo za ujenzi wa zahanati huko tunakokwenda kumalizia haya maboma.
Kwa hiyo, mpango wa Serikali ni kuhakikisha kwamba tunafanya kila liwezekanalo sera hii iweze kutekelezwa. Najua kila jambo lina time frame, katika miaka hii mitano mtaona mabadiliko makubwa sana katika sekta ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mahsusi katika Mkoa wa Rukwa, ni kweli kuna changamoto kubwa sana ndiyo maana Serikali tukaona katika Halmashauri zake kutokana na changamoto lazima tuboreshe kwanza vituo vya afya vilivyopo. Leo hii kwa kaka yangu Mheshimiwa Ally Keissy kule Nkasi amepigia kelele sana Kituo chake cha Kirando, tumefanya utaratibu tunaenda kujenga theatre na majengo mengine. Ukienda pale Sumbawanga DC halikadhalika kuna suala la ujenzi wa Kituo cha Afya cha Mirepa lakini hilo tutafanya kwa kadri iwezekanavyo na ndiyo maana katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo hivi sasa tumepeleka karibia shilingi milioni 340 kwa ajili ya zoezi la ujenzi wa Hospitali ya Wilaya.
Kwa hiyo, ni jukumu la Serikali kuhakikisha Mkoa wa Rukwa nao uweze kujengewa miundombinu ili wananchi wa kule waweze kupata huduma nzuri za afya.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa wananchi hawa walifanyiwa tathmini ya muda mrefu mpaka sasa hawajalipwa, nataka kujua, je, ni lini Serikali sasa itawalipa wananchi hawa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa wananchi hawa walifanyiwa tathmini muda mrefu ya nyumba zao na wameshindwa kuziendeleza na kufanya maendeleo. Je, Serikali iko tayari kuwaongezea tathmini ya fidia ili walipwe kiasi kikubwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia maendeleo mbalimbali kwa wananchi wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu kwamba hivi karibuni Mheshimiwa Waziri alitembelea eneo hili walizungumza na alipata pia taarifa kwamba muda siyo mrefu, wakati wowote wananchi watalipwa hizi fidia. Kwa hiyo, nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge avute subira wakati wa hatua za kukamilisha ili tuweze kuwalipa wananchi wale na ujenzi uweze kuanza basi avute tu subira na wananchi wa Sumbawanga nawashukuru kwa uvumilivu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kulipa kwa ziada inategemea na sheria yenyewe na utaratibu wenyewe. Kwa hiyo, nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge labda kama kuna suala la ulazima basi tuzungumze tuone kwamba je, wanastahili kulipwa ziada kutokana na kuchelewa au iko katika hali gani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza kwa kuwa wanawake wengi wamehamasika sana kuanzisha VICOBA na wengine wameanzisha vikundi mbalimbali kwa lengo la kujikwamua kimaisha lakini wamekuwa wakiangaishwa sana kwa kupata hiyo asilimia 10; sasa ni lini Serikali itaweka mazingira mazuri ili hata kama hiyo asilimia 10 ipo lakini wawekewe mazingira mazuri ya kupata mikopo kwenye mabenki?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kwa kuwa asilimia 10 ya wanawake, walemavu na vijana inachelewa sana kuwafikia walengwa; sasa basi kwa nini Serikali isipunguze masharti ya kukopa kwenye mabenki ili wanawake waweze kukopa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba ukilinganisha masharti yaliyopo katika upatikanaji wa hii asilimia tano ambayo imekusudiwa kwenda kwa wanawake na vijana masharti yake ni rahisi sana ukilinganisha na masharti ambayo yanatolewa na taasisi za fedha kama mabenki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachoomba kumekuwa na dhana potofu kama vile fedha hizi zinatolewa kama vile ni pesa ambayo haitakiwi kurejeshwa, ni wajibu wetu kuhakikisha kwamba tunasimamia ili pesa hizi zinazotolewa ziweze kurejeshwa na wengine waweze kukopeshwa, vizuri tukawa na mfumo ambao ni rasmi ili kuhakikisha kila shilingi ambayo inatolewa inarudi ili wakinamama wengine waweze kukopeshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili angependa masharti ya benki yakapunguzwa ili wakina mama waweze kuna access ya kwenda kukopa kwenye taasisi hizi za fedha. Hili ambalo lipo ndani yuwezo wetu kama ofisi ya Rais TAMISEMI ni kuhusiana na asilimia tano kama ambavyo swali lake la msingi lipo ni vizuri kwanza tuhakikishe kwamba fedha hizi ambazo zinakusanywa asilimia tano inatengwa na zile zinazotengwa zinakopwa ikionekana kwamba kuna gap ya uhitaji hapo ndio twende kwenye taasisi zingine za fedha.

NAIBU WAZIRI VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sambasamba na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, TAMISEMI ni kwamba katika mwezi huu wa tatu Mheshimiwa Rais alikaa na wadau mbalimbali wenye masuala ya kibiashara na viwanda katika moja ya jambo ambalo alizungumza ni kuwashauri watu wa mabenki kuweza kupunguza riba na kuweka masharti ambayo yatawasaidia zaidi wafanyabiashara. (Makofi)
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Swali la kwanza, kwa kuwa gharama za maisha zimepanda na asilimia 10 ni sawa na milioni moja, sasa je, Serikali haioni umuhimu wa kuongeza kutoka asilimia 10 kwenda asilimia 50? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa Benki ya Wanawake iko Dar es Salaam tu, wanawake wa mikoa ya pembezoni wanaisikia tu hiyo benki. Je, ni lini Serikali sasa itafungua Tawi la Benki ya Wanawake Mkoa wa Rukwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, swai lake la kwanza kuhusu kuongeza asilimia 10 hadi 50, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, Serikali yetu inatambua mchango wa wanawake katika kujenga uchumi wa Taifa letu. Hili ni pendekezo, tunalichukua kama Serikali. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kufuatia kuwatambua wanawake kwenye uchumi wa Taifa letu, ndiyo maana tulipopitisha bajeti ya TAMISEMI tuliondoa riba ambayo ilikuwa inachajiwa katika hii asilimia 10 ya mikopo waliyokuwa wanakopeshwa wanawake, hii ikiwa ni hatua ya kwanza kuhakikisha kuwa akina mama na vijana wanaendelea kupata mitaji inayopatikana na bila kurejesha kwa gharama nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, napenda kumwambia Mheshimiwa Bupe na Bunge lako tukufu kwamba Benki ya Wanawake Tanzania ilikumbwa na changamoto na sasa Serikali inaisimamia vizuri na tunatengeneza mfumo mzuri wa kuweza kufanya iweze kusimama. Moja ya mikakati ya kuiwezesha kusimama ni kupata mtaji wa kutosha, ndiyo maana kwa sasa kuna mapendekezo, wanafanya kazi kwa karibu na Benki yetu ya TPB na itakapoimarika ni nia ya Serikali kuona kwamba Benki ya Wanawake inaendelea kuwafikia wanawake kule walipo.
MHE. BUPE N. MWAKANG‟ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nichukue nafasi hii kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Kiongozi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Kwa kazi kubwa ya kuweza kumtua mama ndoo kichwani. Serikali hii imewaza kutuliza hata ndoa za wanawake wa Tanzania, wameweza kutulia kwa sababu maji yanapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizi sasa naomba niulize maswali mawili ya nyongeza;

(i) Wilaya ya Nkasi ina takribani ya vijiji 35 wanaoishi pembezoni mwa Ziwa Tanganyika, na wanatumia maji ya ziwa Tanganyika ambayo yanawasababishia kupata magonjwa mbalimbali ikiwemo kipindupindu na magonjwa ya kuhara. Sasa ni lini sasa Serikali itawajengea visima virefu ambavyo vitawasababisha wapate maji salama?

(ii) Wilaya ya Nkasi imegawanyika katika sehemu mbili, Nkasi Kusini na Nkasi Kaskazini. Naishuruku Serikali imeweza kujenga visima 9 ambavyo sasa hivi vinaendelea kujengwa, lakini bado Nkasi Kusini ambavyo havijajengwa visima takribani 7 ambavyo tuliomba kijiji cha Masolo, Kijiji cha Milindikwa, Malongwe, Sintali, Nkana na vijiji vingine bado havijachimbiwa visima.

Je, nili sasa Serikali itachimba visima hivyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge amekuwa mpiganaji mkubwa hususani kwa kina mama wa Mkoa wake wa Rukwa. Lakini nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge sisi kama Wizara ya Maji hatuta kuwa kikwazo kwa Mkoa wa Rukwa na Nkasi katika kuhakisisha wanapata maji. Ziara ya Mheshimiwa Waziri katika Jimbo la Nkasi kwa Mheshimiwa Kessy alilia sana pale Mheshimiwa Mbunge na tumetoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa katika mji wa Kilando pamoja na Namanyele zaidi ya milioni tano kwa ajili ya miradi ile mikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumepata fedha za PforF zaidi ya bilioni nne kwa Mkoa wa Rukwa, tumepeleka bilioni 1.3 katika Wilaya ya Nkasi katika kuhakikisha tunakwenda kutatua tatizo la maji. Naomba Waheshimiwa Wabunge waende kusimamia miradi ile katika kuhakikisha wakinamama wanaendelea kutua na ndoo kichwani na ndoa zao zinaendelea kuimarika. Ahsante sana.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niulize swali la nyongeza. Shida iliyopo Mwanza ni sawa na shida iliyopo Mkoani Rukwa, Wilaya Sumbawanga Vijijini Kata ya Kaengesa katika vijiji vya Mkunda, Kaengesa B, Kaengesa A na Italima na vijiji vyote vya wilaya Sumbawanga vijiji.

Ni lini sasa Wizara itapeleka maji katika vijiji hivyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji napenda nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wake, lakini kubwa ambacho ninachotaka kusema jukumu la wananchi kupata maji ni jukumu letu sisi Wizara ya Maji na nilishasema si mara moja si mara mbili, sisi ni Wizara maji si Wizara ya ukame tumepata fedha ambazo tumetengewa zaidi ya shilingi bilioni 301 na uwanzaishaji huu wa wakala wa maji vijiji kwa maana ya RUWASA tumejipanga miradi mingi katika kuhakikisha tunaitekeleza kutumia wataalamu wetu wandani, nimhakikishie Mheshimiwa Bupe sisi kama Wizara ya maji vijiji ambavyo ameainisha tunajipanga kuhakikisha tunavitatua ili wananchi wake waweze kupata huduma maji. Ahsante sana.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa, nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa ambayo imeifanya katika Mkoa wa Rukwa kutujengea Hospitali za Wilaya. Wakati nauliza swali hili tulikuwa hatujajengewa hospitali hata moja lakini ndani ya kipindi kifupi hospitali na vituo vya afya zimejengwa. Kwa hiyo, naipongeza Wizara na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, hakika kazi ameifanya, Mwenyezi Mungu ambariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo, sasa naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, ni lini sasa hospitali hizi zitaanza kufanya kazi na kuletewa vifaa tiba ikiwemo X-ray, MRI na vifaa tiba vingine?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali sasa ina mpango gani wa kutuletea madaktari bingwa, manesi na wafanyakazi wa kada nyingine zote katika hospitali hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Serikali tunazipokea pongezi ambazo zinatoka kwa Mbunge na naamini na Wabunge wote wanatoa pongezi hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza anataka kujua ni lini sasa hospitali hizo ambazo zimejengwa zitafunguliwa ili zianze kutoa huduma kama zilivyokusudiwa. Naomba nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wengine, ni azma ya Serikali na ndiyo maana tulianza na majengo 7 yakamilike na yakishakamilika yaanze kutoa huduma wakati tunaongezea fedha zingine kwa sababu ili hospitali za wilaya zikamilike yanahitajika majengo yasiyopungua 22. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pale ambapo majengo yakishakuwa tayari, vifaa vikipelekwa tutapeleka watumishi ili wananchi wapunguziwe adha ya kutembea umbali mrefu kwa ajili ya kufata huduma za afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na ujenzi, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba wanakuwepo watumishi wa kutosha. Ndiyo maana tunaenda kuajiri hao 550, ni njia ya kuanza kupeleka wengine sio kwamba 550 ndiyo mwisho, hapana, tutaajiri na wengine kwa kadri bajeti itakavyoruhusu. (Makofi)
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza naipongeza Serikali kwa kutujengea hospitali za wilaya tatu katika Mkoa wa Rukwa, lakini katika hizo wilaya tatu bado wilaya moja ya Sumbawanga mjini haijapatiwa hospitali ya wilaya. Je, ni lini sasa itajengewa hospitali ya wilaya?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni lini Serikali sasa itapeleka fedha za ukarabati hospitali hii ya mkoa ambayo inatumika kwa sasa?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Bupe Mwakangata kwa kazi nzuri ambayo anafanya katika kufuatilia upatikanaji wa huduma za afya katika Mkoa wa Rukwa hasa huduma ya afya ya mama na mtoto naamini wanawake wa Mkoa wa Rukwa wamemuona na wameiona kazi yake nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ni lini tutajenga hospitali ya wilaya katika wilaya moja ambayo haijapata hospitali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI kama alivyoeleza tumeanza hospitali 67 mwaka huu katika bajeti ziko hospitali 28 kwa hiyo, tuombe tu uvumilivu kwa wananchi ambao hawajapata hospitali moja ya wilaya, Serikali ya Awamu ya Tano ni Serikali ya vitendo ni Serikali ya kutekeleza kwa hiyo tutajenga hospitali.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba nitoe angalizo kwa sababu pia tunataka kujenga hospitali mpya ya Mkoa wa Rukwa. Kwa hiyo, ningeomba subira tukimaliza ujenzi wa mikoa mitano mipya kutekeleza ilani hii ya uchaguzi 2015/2020. Kwa hiyo, ile hospitali ya mkoa sasa tutaikabidhi kwa hospitali ya manispaa ya Sumbawanga kama tulivyofanya kwa Shinyanga na Singida ndio tutafanya hivyo, tukimaliza hospitali mpya hizi zilizokuwa zinatumika za mikao zitakabidhiwa katika manispaa. Sasa ni lini tutapeleka fedha ya ukarabati tumepata fedha takribani shilingi bilioni 14 kutoka mfuko wa Dunia wa kupambana na UKIMWI, TB na Malaria kwa hiyo tutapeleka Mkoa wa Rukwa kwa ajili ya kuboresha huduma za magonjwa ya dharura na ajali pia kuboresha huduma za ICU wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum pamoja na huduma za mama na mtoto.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza kabisa naipongeza Serikali kwa kutenga kiasi cha shilingi bilioni 1.7 kwa ajili ya barabara hiyo, lakini barabara hiyo imechukua muda mrefu sana, zaidi ya miaka mitano haijatengenezwa kabisa na madaraja yote yamekatika kabisa. Wananchi wa Kata ya Isaba, Kazovu, Bumanda, Korongwe, Katete wanapata tabu sana wakati wanapotaka kwenda kupata huduma za afya katika Kata ya Kirando. Swali la kwanza; nataka kujua, ni sababu zipi zimesababisha kusimama kwa ujenzi wa barabara hii?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuongozana nami mguu kwa mguu kwenda kuona tatizo lililopo katika wilaya hiyo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza tunakiri kabisa kwamba sababu kubwa ya kuchelewa ama kutokukamilika kwa wakati kwa barabara hii kwa muda mrefu ni kutokana na kuwa na bajeti finyu. Hivyo tumeendelea kufanya matengenezo ya kawaida kwa kipindi hiki cha miaka hii ambayo Mheshimiwa Mbunge alikuwa anaieleza. Hata hivyo, tunaahidi mbele ya Bunge lako Tukufu kwamba Serikali bado itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya barabara hii kwa ajili ya kuwasaidia wananchi katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, kwa sababu ya kazi nzuri anayoifanya Mheshimiwa Mbunge ya kuwapigania wananchi wa maeneo ya Nkasi pamoja na Mkoa mzima wa Rukwa na najua kila siku amekuwa akitukumbushia katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwenye barabara hizi, nimuahidi kabisa mara baada ya Bunge hili nitaongozana naye tukawasikilize wananchi na kupatia ufumbuzi barabara hizo. (Makofi)
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwanza kabisa naishukuru Serikali imeweza kuingiza kiasi cha shilingi bilioni 1.3 kwenye mradi huu. Mradi huu ulifanya kazi miezi mitatu tu na watu wakaihujumu ile miundombinu kwa kuiba vifaa kama solar, betri na pampu. Sasa swali langu linakuja, ni lini sasa Serikali itarudisha vifaa hivi ili wananchi waweze kuendelea kupata maji? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa wezi wapo wanajulikana kabisa kwenye Kata ile, Serikali ina mpango gani sasa wa kuwachukulia hatua kazi za kinidhamu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bupe Mwakang’ata, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake namba moja lini vifaa vile vitarudishiwa pale kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi na kadiri ambavyo tumekuwa tukiongea naye kuhusu suala hili na nimpongeze kwa namna ambavyo amekuwa mfuatiliaji mzuri. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hili hatutazingatia zaidi kwenye vile vifaa vya solar, tutazingatia kuleta umeme kwa kupitia REA ili tuwe na umeme wa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na wale wezi kuchukuliwa hatua, kwanza niombe ushirikiano Zaidi, tuendelee kuwasiliana, hawa wezi Mbunge akiwa kama mwakilishi wa akinamama wa eneo lile, aende akaripoti polisi, lakini tumekuwa tukimsikia mara nyingi Mheshimiwa Waziri wetu kwamba mwisho wa kuchezea miradi ya maji ni sasa. Kama una mambo ya kutaka kuchezea, kachezee kitambi chako. Kwa hiyo, tutaendelea kuhakikisha kwamba miradi ya maji mwisho kuchezewa. (Makofi)
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyogeza. Kwanza kabisa nipende kuipongeza na kuishukuru Serikali kwa kutujengea hilo daraja liligharimu zaidi ya karibu bilioni 17. Tunashukuru sana. lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; Serikali sasa ina mpango gani wa kutujengea hata basi kuitengeneza hiyo barabara hata kwa kiwango cha changarawe ili wananchi waweze kupita katika barabara hiyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili ninaomba sasa commitment ya Serikali, kwa sababu barabara hiyo ni muhimu sana kwa uchumi wa Mikoa ya Rukwa, Katavi na Songwe. Ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi wa barabara hiyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bupe Mwakang’ata Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Rukwa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ni kweli kwa mwaka jana na mwaka huu ilikuwa imeharibika sana. Nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, hivi ninavyoongea madaraja yote yameshajengwa, bado madaraja mawili ambayo mkandarasi anakamilisha. Kwa sasa barabara hii inapitika vizuri kwa kiwango cha changarawe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili la Mheshimiwa Mbunge, kwamba ni lini tutaanza ujenzi; kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi. Barabara hii tunatambua umuhimu wake ndiyo maana tayari tumeshakamilisha usanifu wa kina kwenye kilomita zote, na bado kilomita 27 ambazo wako tayari wanafanyia usanifu ili barabara yote ikamilike kwa usanifu na baada ya hapo ndipo ujenzi kwa kiwango cha lami utaanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kwa niaba ya Wizara nimshukuru kwamba ameipongeza Serikali kwa kujenga Daraja la Mto Momba ambalo lilikuwa ni kikwazo kikubwa. Hiyo ndiyo adhma ya Serikali; na sasa mizigo yote kutoka Rukwa inapita daraja la Momba kwenye Mlowo. Ahsante.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Spika, ahsante nashukuru sana, kwanza naipongeza Serikali kwa kazi inayoondelea, lakini pia nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa maporomoko haya ya Kalambo Falls ni kivutio kikubwa sana kwa Mkoa wa Rukwa, sasa Serikali ina mpango gani wa kujenga lami kwa sababu wawekezaji na watalii wanapenda sana vitu vizuri kama lami, vitu vizuri kama umeme. Sasa Serikali ina mpango gani wa kutengeneza miundombinu kwenye maporomoko hayo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Rukwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba hili alilolileta Mheshimiwa Mbunge ni ombi kwa sababu ya umuhimu mkubwa wa maeneo haya ya maporomoko ya Kalambo Falls. Kwa hiyo na sisi tuseme tu kwamba tumelipokea tutafanya tathimini na tutaangalia mfuko wetu jinsi ulivyo kama fedha itapatikana basi tutailekeza Ofisi ya Rais kupitia TARURA Kalambo waweze kwenda kujenga huko. Lakini kwa sasa tutakwenda kufanya tathimini halafu tuone jinsi tutakavyopata fedha kwa ajili ya ujenzi wa lami katika eneo hilo. Ahsante sana.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Spika, ahsante, ninashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza ni, kwa sababu wanawake au makundi haya kwa sasa hivi yanapata mkopo kwa kiwango kidogo sana kiasi kwamba mkopo huo hauwasaidii.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza kiwango hicho kutoka milioni mbili na laki tano kwa kila kundi mpaka milioni kumi ili waweze kufanya vizuri kwenye biashara zao?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Serikali sasa ina mpango gani wa kuwajengea mafunzo na uwezo kabla makundi haya hayajapewa mkopo?

Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, makundi haya ambayo ni ya wajasiriamali wanawake, vijana na watu wenye ulemavu yanakopesha asilimia 10, kwa maana ya 4:4:2, lakini kiwango cha ukopeshaji hakijaainishwa, inategemea aina ya shughuli ya ujasiriamali, si kila kikundi kinakopesha milioni mbili na laki tano. Kila kikundi kinakopeshwa kuliangana na uhitaji wa biashara yao, lakini pia uwezo wa kurejesha fedha zile baada ya kukopeshwa.

Mheshimiwa Spika, na Serikali imetoa tamko kwamba tunahitaji kuona vikundi vya wajasiriamali wanakopeshwa fedha zenye kiwango ambacho kinaleta tija ya kuwawezesha kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine badala ya kutoa fedha kidogokidogo ambazo kwanza haziwawezeshi kiuchumi, lakini pili inakuwa ni changamoto kuzirejeshwa. Kwa hiyo, maelekezo haya yametolewa, na Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ameelekeza na sisi Ofisi ya Rais TAMISEMI tunalitekeleza.

Mheshimiwa Spika, na nichukue nafasi hii kutoa maelekezo kwa halmashauri zote kuhakikisha kwamba wanatoa fedha yenye tija badala ya kutoa fedha kidogo kidogo kwa vikundi vya wajasirimali.

Mheshimiwa Spika, mpango wa mafunzo umewekwa vizuri. Maafisa Maendeleo ya Jamii katika hamashauri zetu wanawajibika kwanza kuwajengea uwezo kwa maana ya mafunzo pamoja na kuwatembelea na kuhakikisha kwamba wanafanya biashara zao, na zoezi hili ni endelevu. Ahsante.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Nakumbushia barabara ya kutoka Kibaoni – Mfinga inapita Mto Wisa inakuja kutokea Mloo, barabara hii ni muhimu sana kwa Mkoa wa Rukwa.

Je, ni lini itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba nikubaliane na Mheshimiwa Bupe Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Rukwa kwamba barabara aliyoitaja inaunganisha Mkoa wa Mbeya na Rukwa hadi Katavi, ni barabara ambayo tayari upande mwingine imeshakamilika usanifu lakini bado tunaendelea kukamilisha usanifu wa kina kwa kipande kingine tayari tumeshaanza kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kituo cha Polisi cha Sumbawanga Mjini ni cha toka enzi za mkoloni.

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa kituo hicho? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza Mheshimiwa Mbunge kwamba vituo vyote ambavyo ni chakavu, wakati fulani tuliwahi kusema hapa Bungeni vimefanyiwa tathmini na kinachosubiriwa ni upatikanaji wa fedha tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipaumbele kikubwa tulikielekeza kwenye maeneo ambayo hayakuwa na vituo vya Polisi kabisa, ndiyo maana ukarabati kidogo tumekuwa tukienda taratibu ili kuhakikisha wale ambao hawana huduma za usalama wa raia kabisa angalau waweze kupata. Ninakuahidi Mheshimiwa Mbunge tunajua eneo unalolitaja linakaribia kupakana na mpakani na kuna matukio mengi ya uhalifu. Kwa hiyo tutahakikisha kwamba katika mipango yetu ya ukarabati jicho linaelekezwa kwenye kituo hicho ili kiweze kufanyiwa ukarabati. (Makofi)
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali lakini bado nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; wakati huwa tunasubiri madaktari waliokwenda kusoma lakini pia bado ile hospitali ni chakavu, na miundombinu yake imechoka; na wakati huo tuna eneo ambalo lilipimea na limefanyiwa usanifu.

Je, ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili wakati huwa tuna changamoto za madaktari inalazimika wagonjwa kuwasafirisha kuwapeleka rufaa ya Mbeya.

Je, ni lini Serikali itaongeza magari kwenye hospitali ya Rufaa Mkoa wa Rukwa ikiwemo na ambulance? ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge Bupe Mwakang’ata kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza la kwamba wameshatenga eneo na kwamba ni lini Serikali itaanza ujenzi kwenye eneo jipya ambalo hospitali ya mkoa inataka kujengwa. Kwenye bajeti kwa mwaka huu imetengwa Bilioni tatu kwa ajili ya kuanza ujenzi wa hospitali hiyo, pamoja na Shilingi milioni mia tisa kwa ajili ya kufanya ukarabati kwenye eneo lile ambalo sasa hivi bado majengo yake ni chakavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ni kwamba sasa hivi wagonjwa wanapekekwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, kwa maana ya rufaa wanapokuwa wanashida. Umeona idadi ya madaktari bingwa waliopo kwenye hospitali yako ya Mkoa. Maana yake ni nini, wanaopeleka rufaa Mbeya ni wale ambao wanahitaji kutibia kwenye hospitali ya level ya Kanda. Lakini tanategemea kwa idadi hii ya madaktari tulionao ambao sasa hivi katika hao watano waliopo shuleni watatu watamaliza mwezi ya kumi mwakani. Maana yake ni kwamba tutaongeza idadi ya madaktari bingwa na hata rufaa nayo itapungua, ili ifikie kwamba wale wanaohitajika kanda ndio waende lakini wa level ya mkoa ibadi pale pale mkoani. Ahsante.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Spika, ahsante nashukuru kwa kunipa nafasi.

Ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya kutoka Namanyere - Kilando mpaka Kipili kwa kiwango cha lami? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bupe Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Rukwa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara ya Namanyere hadi Kipili ambayo inaenda bandarini ni barabara muhimu na barabara hii iko kwenye usanifu, kwa hiyo baada ya kukamilisha usanifu wa kina Serikali itatafuta fedha ili ianze kuijenga kwa kiwango cha lami. Ahsante. (Makofi)
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Mkoa wa Rukwa, Wilaya ya Sumbawanga Mjini, Kata ya Malangali, TANESCO waliweka kipooza umeme kwenye Kata hiyo.

Je, ni lini sasa Serikali itawalipa wananchi wa kule fidia? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bupe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ninaomba nikimaliza maswali nikapate eneo maalum, eneo ni eneo gani na fidia ni fidia gani ili niweze kulishughulikia na kujua kwa nini halijafanyiwa kazi kama changamoto hiyo bado ipo.
MHE. BUPE N. MWAKANG’TA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali.

Je, ni lini uwanja wa ndege wa Sumbawanga Mjini utaanza kujengwa? Nataka commitement ya Serikali.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Mwakang’ta, Mbunge wa Rukwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika jibu langu la msingi nililotoa, jibu hili linafanana kabisa na swali la Mheshimiwa Bupe. Tuna viwanja vinne ambavyo ni Kigoma, Sumbawanga, Tabora na Shinyanga, ambavyo vyote vinafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Ulaya. Pia, huyu mfadhili ameshatoa fedha na muda wowote uwanja huu, kama nilivosema wa Kigoma, nao utaanza kujengwa ikiwa ni pamoja na Uwanja wa Tabora na Shinyanga. Ahsante.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama hapa kwa mara ya saba kulalamikia uwanja wa Sumbawanga Mjini, leo nataka commitment ya Serikali, ni lini kazi ya ujenzi wa uwanja wa Sumbawanga Mjini utaanza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali sasa ina mpango gani wa kuweka basi hata route ya kutoka Songwe moja kwa moja mpaka Dodoma wakati huo inaendelea kujipanga kwa ujenzi wa Sumbawanga Mjini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Rukwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, ilitakiwa kiwanja hiki kianze kujengwa mwaka wa fedha wa 2017/2018, lakini kutokana na changamoto ambayo ilikuwepo EIB hawakutoa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mbunge amenisikiliza tayari EIB wameshatoa Dola Milioni 12 kwa ajili ya kuanza viwanja hivi vinne. Lakini kwa kuwa usanifu ulifanyika zamani, Mkandarasi ameomba mkataba huo urudiwe kwa sababu ya gharama, na kwa sababu gharama zitabadilika lazima tuwasiliane na mtoa fedha ili aweze kutoa no objection.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu langu nimesema kama atatoa kwa sababu Mkandarasi yupo basi itaanza kujengwa kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu route ya Songwe hadi Dodoma, tumelichukua lakini pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Shirika letu la Ndege la ATCL inayafanyia kazi masuala yote haya ya usafiri kuona namna ya kuunganisha kati ya Dodoma - Mwanza, Dodoma- Kilimanjaro, Dodoma – Mbeya, lakini hii itategemea na wao watakavyofanya study kuona kama wakifanya hivyo kwao biashara itakuwa ni nzuri. Kwa hiyo, wapo wanaendelea kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza kabisa niipongeze Serikali kwa kutuletea pesa katika miradi hiyo aliyoitaja, Mradi wa Chala, Kate, Mtuchi, Kandasi na sehemu zingine zote. Hata hivyo miradi hiyo ni kama imetelekezwa. Wananchi wanalalamika hakuna kwa kupeleka ng’ombe kwenda kuogelea. Swali la kwanza; je, ni lini Serikali itaweka mkakati madhubuti wa kusimamia miradi hii iweze kutekelezeka?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Wilaya ya Sumbawanga DC ina mifugo mingi. Je, ni lini Serikali itajenga mabwawa ya kutosha kwa ajili ya mifugo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ni mkakati gani wa Serikali juu ya kuhakikisha kwamba tunakuwa na umadhubuti kwenye usimamizi wa miradi hii? Tumejaribu kuona namna wa kurekebisha mfumo wetu na mfumo ambao tutakwenda nao katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 ni wa kupeleka fedha hizi moja kwa moja kwenye maeneo ya wanufaika, kwenye vijiji ili waweze kusimamia miradi hii ambayo itakwenda kuwanufaisha wananchi wao wenyewe moja kwa moja. Ambapo kwa sasa tunatumia mbinu ya kwamba miradi inalipwa na Wizara ingawa inasimamiwa na Halmashauri za Wilaya. Kwa hiyo tunaamini kwamba baada ya kuboresha mfumo huu sasa hakutakuwa na uzubaifu tena wa miradi yetu.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, ni lini tutapeleka miradi mipya ya mabwawa kwa kuwa kuna ng’ombe wengi kule Nkasi? Naomba Mheshimiwa Bupe atupatie haya maeneo ili tuangalie katika bajeti hii ya mwaka huu kama tunaweza pia kupeleka miradi hii katika Jimbo la kule Nkasi.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Serikali ina mpango gani wa kuwarudishia mashamba wananchi waliodhulimiwa na taasisi ya EFATHA Kijiji cha Moro, Msandamungano na Mpwapwa, vilivyopo Wilaya ya Sumbawanga Vijijini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bupe Mwakang’ata, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua mgogoro uliopo baina ya vijiji hivo vilivyotajwa na Shirika la Efatha Ministry ambapo katika kuhangaika nalo, tunatambua kwamba zipo kesi zinazoendelea na nyingine ambazo zimeshaamuliwa. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakapokuwa tunafanya ziara ya Nyanda za Juu Kusini, tutafika na eneo la Rukwa ili kuzungumza na wananchi na kutatua mgogoro uliopo.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Hospitali ya Rufaa Mkoani Rukwa kwa sababu tayari uwanja ulishapatikana na ufundi sanifu ulishafanyiwa. Je, ni lini Serikali sasa itaanza ujenzi wa hospitali hiyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namwelewa anachosema na usanifu ni kweli umefanyika kama Mheshimiwa Mbunge anavyosema. Kwanza nimpongeze kwamba anafatilia masuala mazima ya afya ya hopsitali yao ya mkoa. Kwa mwaka huu zimetengwa bilioni 5.5 kwa ajili ya hospitali anayosema na usanifu anaouzungumzia unaenda kufanyika.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Spika, asante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Hospitali ya Rufaa Mkoani Rukwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bupe
Mwakang’ata Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali kupitia Wizara ya Afya ni kuhakikisha mikoa yetu yote inakuwa na hospitali za rufaa za mikoa za kisasa na zenye vifaa tiba. Ninafahamu Hospitali ya Mkoa wa Rukwa ni ya siku nyingi, hivyo, Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirkiana na Wizara ya Afya tutaona mpango wa kuhakikisha inajengwa hospitali au kukarabatiwa ili iweze kuwa na sifa ambazo zinafanana na hospitali ya rufaa ya mkoa. Ahante.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.

Ni lini Serikali itapeleka umeme katika Kijiji cha Malangali kilichopo Wilaya ya Sumbawanga Mjini, ambacho waliambiwa wananchi wanaokaa pale watalipwa fidia halafu watapelekewa umeme. Sasa ni lini Serikali itapeleka umeme katika Kijiji hicho? Ahsante.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bupe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya Bunge la Bajeti nitatembelea Mkoa wa Rukwa na nitafika eneo hilo ili kupata taarifa ya kina lakini na kutoa uhakika kwa wananchi kuhusu lini mradi wa umeme katika Kijiji hicho utakamilika.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Ni lini sasa Serikali italigawa Jimbo la Sumbawanga Vijijini ambalo hata Mwenyezi Mungu aliligawa kati kati, Ufipa wa Chini kata 13 na Ufipa wa Juu kata 14. Sasa ni lini Serikali italigawa jimbo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA
MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bupe Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Rukwa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nilijibu katika swali la msingi, ni kwamba wafuate tu utaratibu na sisi tutazingatia endapo hizo halmashauri zimetimiza vigezo vyao, na baada ya hapo maana yake sisi tutapeleka katika mamlaka husika kwa ajili ya maamuzi. Kwa hiyo, kikubwa tu waanze mchakato halafu mamlaka husika italiangalia hilo. Ahsante.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; Serikali sasa ina mpango gani wa kuendelea kujenga vituo hivyo vya kuuza gesi asilia katika mikoa ya mingi Tanzania hususani Mkoa wa Rukwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Serikali sasa imejipangaje kupunguza bei ya vifaa vinavyotumika kurekebishia mfumo wa magari kwenye mafuta na kwenye kit ya kujazia gesi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bupe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kwenye jibu la msingi kama nilivyosema Serikali imejipanga vipi kuongeza Vituo vya Kujaza (CNG), tayari vibali kwa wakandarasi na wawekezaji 20 vimetolewa kwa ajili ya kwenda katika maeneo mbalimbali kuweza kuongeza wigo wa eneo hili. Tunaendelea kuvutia wawekezaji mbalimbali waje kuwekeza katika eneo hili la gesi asili ambalo litakuwa linatumika katika maeneo mbalimbali. Kwa hiyo michakato hiyo inaendelea na Serikali katika mwaka huu wa fedha itajenga hivyo vituo vyetu viwili ambao tunaamini kabla ya mwaka huu wa fedha kwisha vitaanza utekelezaji wake maeneo ya Mlimani City na maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali la pili, Serikali inafanya nini kuhakikisha bei ya hizi zinazoitwa conversion kits zinapungua. Mojawapo ya kitu tunachokifanya tunahamasisha watu wengi wanaoweza kuja katika biashara hii ya kutengeneza conversion kits waje, biashara ikisha kuwa na watu wengi wanaoshiriki automatically ushawishi utakuwa ni mkubwa na gharama tunatarajia zitapungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile pia tumewaza namna ambayo tunaweza tukashirikiana na wenzetu wa Wizara

nyingine za Kisekta, Wizara ya Fedha na wengine kuona namna ya kuweka fedha au punguzo la kodi kwenye vifaa hivi kwa watalam watakavyoshauri ili tuone namna ambavyo tunaweza tukapunguza gharama za hizi conversion kits ili kuweza kuvutia watu wengi zaidi kuweza kuingia katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo la mwisho, tayari vituo vinavyouza gesi vimeweka utaratibu wa kukopesha wale wanaokuwa na haya magari wanaotaka kufanya conversion kit wanawakopesha na wanakuwa wanalipa kidogo kidogo kwa sharti la kwenda kuchukua gesi katika kituo chake hizo zote ni mbinu katika kuhakikisha kwamba gharama zinapungua na watumiaji wanaweza kupatikana kwa wingi.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya kutoka Mlowo – Kilyamatundu – Ilemba – Mtowisa hadi Majimoto kwa kiwango cha lami? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bupe Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Rukwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara ya kipande cha Mloo hadi Kamsamba imewekwa kwenye mapendekezo ya bajeti. Pia ilikuwa ni ahadi ya Waziri Mkuu, aliaagiza, lakini upande wa Kilyamatundu hadi Muze tumeshaanza barabara hiyo kutoka Ntendwa hadi Muze kwenda Kilyamatundu. Kwa hiyo, barabara hiyo tumeshaianza na ni matumaini yetu kwamba tutaendelea kuikamilisha. Ni barabara ndefu yenye kilometa zisizopungua 300, ahsante.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza: -

Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali itajenga barabara ya kutoka Lyazumbi inayounganisha Mkoa wa Rukwa na Katavi kupitia Mbuga ya Wanyama Katavi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, barabara hii ni barabara kuu, lakini kabla ya kuijenga hiyo barabara, ndiyo maana tumeamua kuijenga kwanza barabara ya Kizi – Kibaoni, Kibaoni kwenda Stalike. Kwa sababu hizo barabara zitakuwa zinakwenda parallel, baada ya kukamilisha, ndiyo sasa tutahamia pia kwenye hiyo barabara ambayo inapita katikati ya mbuga, ahsante.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza kabisa nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali lakini pamoja na hivyo nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, kwa kuwa Serikali tayari ina taarifa za miamba yenye madini katika Mkoa wa Rukwa na Songwe. Je, ni lini sasa itatoa taarifa na kusambaza kwa wananchi ili wananchi hawa waweze kuomba leseni kwa ajili ya uchimbaji? (Makofi)

Swali la pili, ni nini sasa mpango wa Serikali kwa kuwapa mitaji wachimbaji wadogo wakiwemo wanawake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, taarifa za kijiolojia za maeneo yenye madini nchini hutolewa na GST kupitia chapisho la kitabu cha madini yapatikanayo Tanzania ambacho toleo la mwisho lilitolewa mwaka 2019. Kutokana na tafiti zilizoendelea kuna aina nyingi za madini zimeendelea kugundulika na hivyo toleo la tano limekamilika, tuko kwenye hatua za kuandaa uzinduzi wa kitabu kipya cha madini hayo na siku ya uzinduzi wa hicho kitabu tutawaalika Wabunge wote na wadau mbalimbali wa madini waweze kupata nakala ya vitabu hivyo ili taarifa hizi ziweze kuwafikia walengwa katika maeneo ya Wilaya zote za nchi yetu.

Swali lake la pili kuhusu mpango wa kuwapatia wachimbaji wadogo mitaji ulikwishawekwa kupitia maelewano na mabenki ya ndani, kwamba watoe mikopo kwa wachimbaji wadogo waliokidhi vigezo na tayari mabenki ya ndani yameshatoa zaidi ya shilingi bilioni 145 kwa wachimbaji wadogo wenye leseni, ahsante sana.
MHE BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Swali la kwanza; Kata ya Mpui, Ikozi na Lusaka hayana kabisa minara ya simu. Ni lini sasa Serikali itajenga minara ya simu kwenye kata hizo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; minara iliyopo Kata ya Milepa, Zimba, Mfinga na Lusaka minara hiyo haina kabisa internet. Ni lini sasa Serikali itaweza kuweka internet kwenye minara hiyo hili wananchi wasiweze tena kupanda kwenye miti kutafuta internet? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kuhusu kata ya Mpui pamoja na Ikoze Serikali iko katika utaratibu wa kufanya tathimini na tathimini hiyo itakapokamilika Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kufikisha huduma ya mawasiliano katika kata hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili maeneo ya Milepa pamoja na Zimba ni azima ya Serikali kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya kuhakikisha kwamba tunapanua wigo wa matumizi ya internet kutoka asilimia 45 mpaka 80 Serikali imeshaanza na minara 488 katika awamu ya kwanza na katika awamu ya pili tutajumuisha Kata ya Milepa na Zimba ili wananchi wa maeneo hayo wapata huduma ya internet, ahsante.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ni lini Serikali itajenga barabara ya kutoka Chombe – Igonda – Kaoze mpaka Ilemba? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bupe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii aliyoitamka kadri Serikali itakavyopata fedha, tutakwenda kuitekeleza barabara hii.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Je, ni lini Serikali itajenga barabara ya kutoka Kaoze- Chombe kwenda Igonda iliyopo Sumbawanga Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE.ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii bado hatujaiingiza kwenye mpango wa kuijenga kwa mwaka huu. Lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kabla ya kuanza kuijenga tutatafuta fedha kwa ajili ya kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika bajeti inayokuja, siyo kwa bajeti hii; kwamba hatukuipangia fedha kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Mkoa wa Rukwa, Wilaya ya Kalambo, Tarafa ya Mwimbi kuna mito mingi sana ya kutosha: Je, Serikali ina mpango gani wa kuendeleza kilimo cha umwagiliaji katika tarafa hiyo? Ahsante (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA (K.n.y. WAZIRI WA KILIMO): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Azma ya Serikali ni kutumia vyanzo vyote vya maji vilivyopo, ikiwemo mito ambayo ni muhimu sana kwa ajili ya kuhakikisha skimu za umwagiliaji zinafanya kazi. Kwa hiyo, katika maeneo ambayo tutaendelea pia kuyafanyia kazi ni mito hiyo iliyopo katika Jimbo la Kalambo ili kuhakikisha nayo inatumika kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji katika eneo husika ambalo Mheshimiwa Mbunge amelitaja, nakushukuru sana.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali. Ni lini Serikali itapunguza tozo ya shilingi 7,000 ambayo wavuvi wanatozwa wanapoingia kuvua samaki mle ndani ya Ziwa Rukwa? Ni lini sasa Serikali itakuja kupunguza tozo hiyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) K.n.y WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la lini Serikali itapunguza tozo, kwanza ni kupata uhakika wa aina ya tozo na kiwango kinachotozwa kwenye maeneo hayo. Kwa hiyo, naomba suala hili nilichukue kwa sababu linahusiana zaidi na takwimu ili kuweza kupata uhakika kwanza wa tozo zinazotozwa, na pili, kuweza kuona utaratibu wa kisera pamoja na kanuni na sheria zinasemaje katika eneo hilo na hatua ya tatu itakuwa ni kuleta mapendekezo ya kuona unafuu utapatikanaje kwa wavuvi wetu ili waweze kupata faida zaidi, ahsante. (Makofi)
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Spika, ahsante, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Mkoa wa Rukwa ukepakana na maziwa mawili likiwemo Ziwa Tanganyika na Ziwa Rukwa. Serikali ina mpango gani wa kuanzisha uvuvi wa vizimba katika maziwa hayo, ili kupata malighafi ya samaki kwa wingi?

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili; nilitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kukiendeleza Kiwanda cha SAAFI kilichopo Mkoa wa Rukwa ambacho kilianzishwa na Hayati Chrisant Mzindakaya? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, kwanza nimshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kutambua umuhimu wa ufugaji wa samaki kwa njia ya kisasa, kwa maana ya vizimba katika Maziwa ya Rukwa na Tanganyika.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi tayari imeshaanza zoezi hilo. Tumeanza katika Mkoa wa Mwanza kwa maana ya Ziwa Victoria, tayari tunafuga kupitia vizimba. Kwa hiyo, nitoe wito kwa wataalamu wetu waweze kutembelea kwenye maziwa haya kwa kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge, ili waweze kuanzisha ufugaji wa samaki kupitia vizimba katika Ziwa Rukwa na Ziwa Tanganyika na ninakuomba Mheshimiwa Mbunge uweze pia, kushirkiana nasi ili uweze kuwa kinara katika ufugaji huu wa kisasa wa samaki.

Mheshimiwa Spika, pili; kuhusiana na kiwanda hiki cha Sumbawanga Agricultural and Animal Food Industries Limited kwa maana ya SAAFI, changamoto kubwa ilikuwa ni fedha na uendeshaji wa kiwanda hiki ambacho ni kiwanda cha kisasa sana hapa nchini. Serikali tayari imeshaanza kupitia Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIDB), kutafuta mwekezaji mpya baada ya changamoto zilizokuwepo kwa mwekezaji yule wa mwanzo.

Kwa hiyo, tumeshatangaza tayari kupitia gazeti mwezi wa Agosti, kupata mwekezaji mpya ili aweze kuingia ubia na waliopo ili kuhakikisha kiwanda hiki kinafufuliwa, nakushukuru.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza: -

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, ninapenda kujua;

Je, ni kwa nini sasa sera hii haitekelezeki kikamilifu, kwa sababu wanawake wajawazito na watoto chini ya miaka mitano bado wanalipishwa kwenye suala zima la afya?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; wazee zaidi ya miaka 60 bado pia wanatozwa pesa wanapokwenda kutibiwa;

Je, kwa nini sera hii haitekelezeki?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo anashirikiana na Waheshimiwa Wabunge wa mkoa wake kufuatilia masuala muhimu ya afya katika mkoa wake.

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza, ni kwa nini sera hii haitekelezwi kwa asilimia 100 kama ilivyozungumzika. Ni kama maeneo mengine, wote tunajua kuna kipindi tulipitia kwenye shida ya upungufu wa dawa, kwa hiyo kunapokuwa na upungufu wa dawa na vifaa tiba basi linaathirika eneo hili kama yanavyoathirika maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, lakini pia unakumbuka hapa wakati wa bajeti yetu mlizungumzia suala la mtaji kwa MSD. Sasa maana yake MSD ikishapata mtaji badala ya kutegemea fedha kutoka kwenye vituo, basi sasa ule mnyororo wa upatikanaji wa dawa hautakatika tena kama ambavyo umekuwa ukikatika, na sasa tutaweza kuhakikisha kwamba sasa dawa zitakuwa zinapatikana wakati wote na vifaa tiba vinapatikana wakati wote, na akina mama wanaweza kupata huduma kama ambavyo inatajwa na sera. Tumeshaainisha, Mheshimiwa Waziri ameunda tume imeonesha kwamba tunahitaji bilioni 167 kuweza kuhudumia wananchi katika eneo hili.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu wazee linafanana na hili lingine. Kwanza niseme tu kwamba tumeagiza kila kituo cha afya, kila zahanati, kila hospitali kuwepo na dirisha la wazee. Na tunawaomba wenzetu wakuu wa wilaya na wakurugenzi wasimamie eneo hili la akina mama na eneo la wazee kuhakikisha hili takwa la kisera linatekelezwa ipasavyo, ahsante. (Makofi)
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Nilitaka kujua ni lini Serikali itamaliza mgogoro wa shamba la EFATHA ambalo unavikumba vijiji vya Msanda, Muungano, Kaungu, Sandulula, Malonje, Ulinzi na Mawenzusi. Ni lini sasa mgogoro huu utaisha wananchi wanapata tabu sana sana hawana pa kulima. Tunaomba Serikali imalize mgogoro huu. Ni lini sasa Serikali itamaliza mgogoro huu? Ahsante.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza Waheshimiwa Wabunge ni wape angalizo. Vyanzo vingi vya migogoro ni matumizi ya nguvu yasiyozingatia utaratibu. Tunapotoa shamba kwa mwekezaji, mwananchi mwingine yeyote haruhusiwi kwenda kulivamia lile shamba bila kuzingatia taratibu. Kama unaona kabisa kwamba zile taratibu za umiliki wa yule mmiliki zimekiukwa fuata taratibu tulishatoa maelekezo. Halmashauri zianzishe ule mchakato wa kumjadili huyu muhusika wa shamba hilo ambaye amelitelekeza.

Mheshimiwa Spika, wananchi kuanza kuvamia maeneo haya kwa kweli sio kitu cha busara sana. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge sisi ni viongozi wote tushirikiane kwenye hili kuwaelimisha wananchi juu ya taratibu zinazoweza zikafatwa ili kupata kile ambacho tunakihitaji kwa matumizi yetu.

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri anataka kujua mgogoro utamalizwa lini maana yake mgogoro upo wewe umeelezea kuzalishwa kwa mgogoro sasa kwa kuwa mgogoro tayari upo utakwisha lini ndio swali la Mbunge.(Makofi)

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kusema maelezo haya tayari tumekwishaanza na tumeunda timu ya ufatiliaji ili makundi ya pande mbili zote yakutane ili kuona uwekezekano wa kulimaliza hili tatizo.

Mheshimiwa Spika, kama mninavyosema vyanzo vikubwa vya migogoro hii ni matumizi ya nguvu zisizozingatia taratibu.

SPIKA: Hilo umeshaeleweka, hoja ni kwamba mgogoro ukisha kuwepo lazima umalizwe, lazima umalizwe. Ukishakuwepo mgogoro umeshatengenezwa lazima umalizwe sasa aliyepelekea huko. Naona Waziri amesimama.

Mheshimiwa Waziri.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa fursa kwa ajili ya kujibu suala hili na nimshukuru pia Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri.

Mheshimiwa Spika, mgogoro huu wa EFATHA na wananchi wa Sumbawanga kama alivyosema. Mgogoro huu ni wa siku nyingi na mgogoro ulisha wahi kufika mahakamani lakini ulitokana pia na mgawanyo wa maeneo katika lile eneo ambapo mwekezaji alipewa. Mwekezaji alifata taratibu zote katika kupewa yale maeneo. Changamoto inapokuja ni kwamba kadri mahitaji ya wananchi yanavyozidi kuwa makubwa basi wanaona kama vile mwekezaji pengine amekiuka taratibu katika kupewa, lakini taratibu zote zifuatwa.

Mheshimiwa Spika, naomba niwahakikishie wananchi wa Jimbo la Sumbawanga ambako ndiko kuna mgogoro huo, nitakwenda mwenyewe kule kwa ajili ya kuzungumza nao ili tuweze kuumaliza kwa sababu umekuwa ni wa muda mrefu. Tutapanga na Mbunge kwenda kuumaliza mgogoro huo. (Makofi)
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Je, ni lini Serikali itapeleka Walimu wa kike katika shule ya msingi iliyoko Nkasi inaitwa Shule ya Itete na Shule ya Kala?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, katika ajira hizi mpya 13,130 ambazo Serikali imetoa katika mwaka huu wa fedha tutaangalia na kuweka kipaumbele katika shule hizi alizozitaja za Itete na Kala kule Wilayani Nkasi.

MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, nilitaka kujua ni lini sasa Serikali itapeleka fedha kwenye mradi uliochukua muda mrefu mradi wa Inkana Isarye ulioko Nkasi Kusini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili, nilitaka kujua ni lini sasa Serikali itakamilisha mradi wa kutoa maji katika Ziwa Tanganyika na kusambaza Mkoa wa Rukwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote nipende kumpongeza Mheshimiwa Bupe Mwakang’ata Mbunge wa Viti Maalum kwa ufatiliaji wake mzuri na nipende kuhakikishia malipo ya mradi huu ambao umechukua muda mrefu ni mmoja wa vipaumbele vya Wizara kuhakikisha miradi yote inakamilika. Lengo la kupata maji bombani linatimia kwa sababu tunahitaji kuona tunapunguza umbali mrefu wananchi wa kutembea, vilevile kusambaza maji kutoka Ziwa Tanganyika ni moja ya vipaumbele vya Wizara. Mheshimiwa Bupe hili nalo pia Wizara tunalipa uzito na tutahakikisha maeneo yote ya Nkasi Kusini na Kaskazini kote tuweze kuyafikia na miradi iweze kukamilika.
MHE. BUPE N. MWAKANGA’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwanza kabisa nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kumaliza mgogoro wa uwanda wa game reserve Mkoani Rukwa lakini nina swali dogo la nyongeza. Je, ni lini sasa Serikali itapunguza tozo za token ambazo wananchi wanalipa wanapoingia kuvuna na kutoka? Ni lini Serikali itapunguza hizo tozo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru kwa sababu mgogoro huu umeisha. Kwenye suala la token sasa tutaenda uwandani kuangalia ni jinsi gani tukae na wadau ili tuone bei ambayo ni nzuri zaidi kwa wao na kwetu sisi twende sambamba na mahitaji ya wananchi, ahsante.

MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini barabara ya Chombe – Kaoze – Igonda mpaka Ilemba itajengwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bupe Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, Rukwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu cha kwanza ni kuifanyia usanifu wa kina hiyo barabara halafu baada ya hapo Serikali itajua gharama halisi ya kuijenga hiyo barabara na ndiyo sasa tutaiingiza kwenye mpango wa kuijenga kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itamalizia Hospitali ya Wilaya Sumbawanga Mjini inayoitwa Isyofu, ambayo bado wodi hazijaisha. Ni lini sasa Serikali itapeleka fedha ili wodi zijengwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Bupe Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Rukwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli hospitali ya Sumbawanga Mjini nilifika mimi mwenyewe pale na nilijionea adha ambayo inaendelea pale na najua bado haijakamilika. Commitment ya Serikali ni kuhakikisha kwamba tunatafuta fedha ili tuongezee na kuikamilisha ile hospitali kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Afya katika Kata ya Miula Jimbo la Nkasi Kusini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeshaweka mkakati wa kuainisha maeneo ya kujenga vituo vya afya, ikiwemo katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, kwa hivyo, kadri ya upatikanaji wa fedha katika bajeti inayofuata tutahakikisha tunatenga fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vituo vya afya katika maeneo hayo. Ahsante.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Kituo cha Polisi cha Sumbawanga Mjini Mkoani Rukwa ni cha toka enzi za mkoloni, ni kidogo hakina hewa. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Rukwa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tunatambua wilaya za zamani ikiwemo Wilaya ya Sumbawanga ina Vituo vya Polisi ambavyo moja vimejengwa muda mrefu baadhi vimeanza kuwa chakavu lakini vingine havikidhi haja ya viwango vya Vituo vya Polisi vinavyotakiwa kuwepo sasa hivi ngazi ya Wilaya. Kwa hiyo, ninachukua dhima kumuahidi Mbunge kwamba katika kazi tunayoifanya ya kuimarisha maeneo ambayo hayana kabisa vituo, jambo jingine ni kukarabati na kuboresha vituo vya kizamani ili kuweza kukidhi mahitaji ya sasa. Kwa hiyo, Sumbawanga itakuwa ni eneo litakalozingatiwa.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Ni lini Serikali itapasua na kumalizia barabara inayotoka Mtowisa, Ngongo mpaka Kristo Mfalme Sumbawanga DC? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY KASEKENYA MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bupe Mwakang’ata Mbunge wa Viti Maalum Rukwa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara aliyoitaja pia ni ahadi ya viongozi wa kitaifa. Naomba nimwakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatafuta fedha ili kuweza kuipasua hii barabara inayoanzia Mtowisa kama ambavyo viongozi waliahidi kufanya hivyo, ahsante.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Afya katika Kata ya Miula Jimbo la Nkasi Kusini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeshaweka mkakati wa kuainisha maeneo ya kujenga vituo vya afya, ikiwemo katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, kwa hivyo, kadri ya upatikanaji wa fedha katika bajeti inayofuata tutahakikisha tunatenga fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vituo vya afya katika maeneo hayo. Ahsante.

MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Wananchi wa Mkoa wa Rukwa wanateseka sana kuhusiana na stendi, stendi iko mbali na stendi ya zamani iko mjini. Je, ni lini sasa Serikali itaruhusu wananchi wa Mkoa wa Rukwa watumie stendi zote mbili kama inavyotumia Mkoa wa Mbeya, wanashusha Uyole, wanashusha Nane Nane na wanashusha stendi ya zamani. Hivyo, ni lini sasa Serikali itaruhusu wananchi wa Rukwa watumie stendi ya zamani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bupe Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, maamuzi ya mkoa kwa maana ya Viongozi wa Mkoa; Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala na Menejimenti za Halmashauri zetu zote, nawaelekeza wakae wafanye tathmini kwamba kwa nini stendi ya zamani haitumiki na inatumika stendi mpya ambayo iko mbali na waone uwezekano wa kufanya maamuzi stendi ipi itumike au zitumike zote na watupe mrejesho Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Kwa hiyo, suala hilo litafanyiwa kazi na Serikali. Ahsante.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Kwanza kabisa tunapenda kuishukuru Serikali kwa kutujengea Chuo cha VETA Mkoa wa Rukwa, chuo cha kisasa, chuo kizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali langu ni lini sasa chuo hicho kitafunguliwa na wanafunzi waweze kupata mafunzo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kulikuwa na mikoa ambayo vyuo vya VETA vya mikoa bado havijakamilika, miongoni mwa mikoa hiyo ni pamoja na Mkoa wa Rukwa na mwingine ni Mkoa wa Njombe, Geita pamoja na Simiyu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ukamilishaji wa majengo yale sasa unakamilika. Katika fedha zile za Uviko-19 tulizopata mwaka uliopita tumeweza kupeleka pale zaidi ya bilioni nne kwa ajili ya ukamilishaji wa chuo kile na tunataraji ujenzi ule unaweza ukakamilika katika kipindi hiki kifupi cha mwezi huu wa Juni na mwezi wa Julai, ili basi ifikapo mwezi wa kumi au mwezi Januari mwakani mafunzo pale yaweze kuanza. Nakushukuru sana.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawilli ya nyongeza.

Swali la kwanza; Serikali ina mpango gani sasa wa kuwalipa fidia wananchi ambao walikuwa wanaishi katika eneo lile na walikuwa wanalima mashamba yao?

Swali la pili, shida iliyoko Ikozi ni sawa na shida iliyoko Mpui kata ambazo zinakaribiana, Serikali sasa ina mpango gani wa kukamilisha mradi ulioko Mpui pale ambao mradi upo lakini wananchi hawapati maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Bupe Mwakang’ata kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ina mpango gani wa kulipa fidia, tayari Serikali kupitia Wizara ya Maji kwa maeneo ambayo miradi inapita tumeshaanza malipo na mradi wa eneo hili pia watafikiwa hivi punde. Kata zinazokaribiana hiyo Kata ya Mkuyu na yenyewe pia kuna mradi, mradi huu sasa hivi tunaendelea kuufuatilia kwa karibu sana kuhakikisha dhima ya Serikali kumtua mama ndoo kichwani inakwenda kutekelezeka hata kwa wananchi watokao Mkuyu.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza ujenzi wa Hospitali ya Rufaa pale mkoani Rukwa kwa sababu tayari eneo limetengwa, lakini Serikali bado haijaanza ujenzi. Ni lini Serikali itaanza ujenzi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwenye bajeti ya mwaka huu imepangiwa kwa ajili ya kufanya ujenzi kwenye eneo ambalo amelitaja.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Kituo cha Polisi cha Sumbawanga Mjini Mkoani Rukwa ni cha toka enzi za mkoloni, ni kidogo hakina hewa. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Rukwa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunatambua wilaya za zamani ikiwemo Wilaya ya Sumbawanga ina Vituo vya Polisi ambavyo moja vimejengwa muda mrefu baadhi vimeanza kuwa chakavu lakini vingine havikidhi haja ya viwango vya Vituo vya Polisi vinavyotakiwa kuwepo sasa hivi ngazi ya Wilaya. Kwa hiyo, ninachukua dhima kumuahidi Mbunge kwamba katika kazi tunayoifanya ya kuimarisha maeneo ambayo hayana kabisa vituo, jambo jingine ni kukarabati na kuboresha vituo vya kizamani ili kuweza kukidhi mahitaji ya sasa. Kwa hiyo, Sumbawanga itakuwa ni eneo litakalozingatiwa.