Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Catherine Valentine Magige (7 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza kabisa naomba niwashukuru akinamama wa Mkoa wa Arusha kwa kuniamini na kunipa kura kwa ajili ya kuwawakilisha Bungeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hotuba nzuri aliyoileta wakati wa ufunguzi wa Bunge la Kumi na Moja. Hotuba hiyo iligusa maeneo mengi katika nchi yetu. Vilevile ilitupa mwelekeo na
dira ya Serikali ya Awama ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze moja kwa moja katika mchango wangu, nimefarijika sana Mheshimiwa Rais aliposema kuwa Tanzania itakuwa nchi ya viwanda. Katika Mkoa wangu wa Arusha, miaka ya 1970 na 1980 kulikuwa na viwanda vingi sana vya Serikali
pamoja na watu binafsi kama vile Kiwanda cha Tanelec, Kiwanda cha Biskuti na cha Matairi cha General Tyre. Viwanda hivi vyote kwa sasa hivi havifanyi kazi, hali iliyopelekea madhara makubwa sana kwa wakazi wa Arusha na maeneo jirani na Mkoa wetu wa Arusha.
Mheshimwa Naibu Spika, Kiwanda cha Matairi cha General Tyre kilikuwa kiwanda kikubwa sana cha kuzalisha matairi Afrika Mashariki. Kiwanda hiki kilikuwa kimeajiri watu zaidi ya 400, kiwanda hiki kilikuwa kinaingiza mapato shilingi bilioni 100 kila mwaka na takwimu hizi ni kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2008. Kiwanda hiki kilifikia stage kikawa kinaajiri watu hadi milioni moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1971, Kiwanda cha General Tyre kilikuwa kiwanda namba moja Afrika Mashariki kwa kuzalisha matairi 1,200 kwa siku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama kipindi hicho kiliweza kuzalisha matairi 1,200 kwa siku, sasa hivi tunashindwa kitu gani? Kwa sasa hivi soko la matairi lipo kubwa sana, kwa sababu tukianza kukitumia Kiwanda cha Matairi cha General Tyre, tutaanza na Serikali na taasisi zake zote kununua matairi ya General Tyre pamoja na mashirika ya Umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile soko la matairi bado kubwa sana, watu wengi sasa hivi wanatumia magari, magari yote hayo yanahitaji matairi. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali ikianzishe upya Kiwanda cha General Tyre ili kiendelee kuleta mapato katika nchi yetu.
Kiwanda cha General Tyre kimepunguza ajira kwa vijana wa Arusha, wananchi wa Arusha, vijana wa Arusha, wanahitaji ajira, ajira hii itapatikanaje? Itapatikana kwa kurudisha viwanda vyetu ambavyo vilikuwa havipo tena. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Arusha hawaamini kama Serikali imeshindwa kufungua kiwanda kile. Wananchi wa Arusha tunaamini kuna hujuma za baadhi ya wafanyabiashara ambao wana-import matairi kutoka nje kwa ajili ya faida zao wenyewe hali ambayo inapelekea sisi kukosa uwezo wa kufungua kiwanda kile cha General Tyre.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa taarifa nyingi za kipolisi zinaonyesha ajali nyingi zinatokea kutokana na matairi yasiyokuwa na ubora ambayo tunayaagiza kutoka nje.
Tumekuwa tunapoteza ndugu zetu katika ajali kwa sababu ya matairi. Sasa naona ni wakati muafaka kwa Serikali kukifungua upya Kiwanda cha Matairi cha Arusha (General Tyre) ili tuweze kutumia matairi yale ambayo yana ubora. (Makofi)
Naomba niende moja kwa moja katika suala la maji. Tatizo la maji limekuwa kubwa sana kabla ya uhuru na baada ya uhuru. Kina mama wa Mkoa wa Arusha wamechoka kuhangaika na tatizo la maji. Kuna maji Ngorongoro, Monduli na Longido. Wamenituma niombe
Serikali yao, wanamwamini Mheshimiwa Magufuli, wanaimani kubwa na Serikali ya Mapinduzi.
Tunaomba sana kina mama hawa wa Arusha wasahau shida hii ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mradi wa maji wa West Kilimanjaro. Serikali ikitusaidia kuanzisha mradi ule vijiji kadhaa vitapata maji. Mradi ule tunaomba upelekwe mpaka Longido ambapo vijijini vya njiani kama Tingatinga, Singa, Kerenyai, Engiraret, Orbebe, Orpesi, Ranchi
mpaka Longido navyo vipate maji. Vilevile Monduli, Monduli kulikuwa na mabwawa matatu na yenyewe yamepasuka. Wananchi wa Monduli wanakunywa maji ya mabwawani pamoja na mifugo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana Serikali iangalie suala hili la tatizo la maji katika Mkoa wa Arusha. Naomba sana Waziri wa Maji unisaidie sana kutatua tatizo hili. Nakuamini najua ndiyo maana Mheshimiwa Rais wetu tunayemuamini akakuchagua, tunaomba utusaidie.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na migogoro ya wakulima na wafugaji. Kila siku wananchi wamekuwa wakiuwawa, mifugo imekuwa ikiuwawa lakini migogoro hii imekuwa haishi, nenda rudi migogoro hii inaendelea na wananchi wanazidi kuisha kwa ajili ya kufa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini sana wateuzi wa Rais, namwamini sana Mheshimiwa Lukuvi. Mheshimiwa Lukuvi nakuomba baada ya Bunge hili uje Mkoa wa Arusha kuna matatizo mengi ya ardhi, kuna tatizo la ardhi Loliondo, wananchi wamekuwa wakipata shida
hawajielewi, hatujui Serikali inataka nini, hatujui wanavijiji wanataka nini, hatujui wafugaji wanataka nini? Tunaomba sana Serikali iliangalie suala hili. Wananchi wamekuwa wanachomewa nyumba zao, mifugo yao inauliwa lakini sasa hivi Awamu ya Tano, tuna imani kubwa sana na Serikali na ukizingatia hotuba ya Rais wetu imeeleza kila kitu, tunaimani hawatatuangusha watatusaidia sana. (Makofi)
Naomba niongelee pia suala zima la Polisi. Polisi tumekuwa tukiwalaumu sana lakini vilevile Polisi wanaishi katika mazingira magumu sana. Nikitolea mfano Arusha Mjini kuna zile nyumba za Fire, ukipita pale ni aibu. Nyumba za Polisi ni chafu sana, ni nyumba ndogo na mnajua familia zetu za Kiafrika tunavyoishi. Polisi wale wanaishi katika mazingira ya shida sana na hata kwa kupita tu kwa mbali nyumba ni chafu sana. Tunaomba sana Serikali iangalie jinsi gani ya kuwasaidia Polisi katika suala zima la nyumba.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mabadiliko ya tabia nchi limekuwa linasababisha matatizo makubwa sana ya malisho ya mifugo pamoja na maji. Nakumbuka mwaka 2007 kulikuwa na ukame. Wilaya za Monduli, Longido, Ngorongoro, wafugaji walikosa malisho, mifugo
yao ilikuwa inakufa na wenyewe wakawa wanaishi kwa kuhamahama. Tunajua wafugaji wanaishi kwa kuhamahama siyo kwa kupenda bali kutokana na mazingira wanayokuwepo, unakuta mifugo yao haipati maji, haipati huduma kwa hiyo, inabidi wahame. Mheshimiwa
Waziri wa Ardhi, tunaomba sana mliangalie wafugaji wa Mkoa wa Arusha kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana hotuba ya Rais imegusa mambo mengi sana. Nashangaa sana watu wanapokaa na kuikejeli hotuba ya Rais. Mmeona hata juzi Mheshimiwa Magufuli amefika Arusha wananchi walivyomlaki kwa furaha. Mbunge mwenzangu wa Arusha pale awe makini sana, kwa kauli alizozitoa hapa wananchi wa Arusha wanaweza wakampiga mawe na kumzomea kwa sababu wamemkubali Magufuli na Serikali ya Chama cha CCM.
Nilitegemea Mbunge mwenzangu atasimama na kumsifu Mheshimiwa Rais Magufuli na kusifu wananchi wa Tanzania pamoja na wananchi wa Mkoa wa Arusha kwa kumpa kura za kutosha Rais Magufuli. Naomba sana tukubali, upinzani siyo kupinga kila kitu. (Makofi)
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kutoa mchango wangu. Kwanza kabisa, naomba nielekeze mchango wangu kushukuru Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi chini ya Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuanza kutimiza ahadi zake ambazo aliahidi kipindi cha kampeni. Aliahidi shilingi milioni 50 kila kijiji, tumeona zimeanza kwenda, tunashukuru sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Shilingi milioni 50 hizi za kila kijiji tumeona wanawapa Baraza la Wawekezaji, ni mpango mzuri sana. Hata hivyo, tunaomba Baraza la Wawekezaji wahakikishe wamepita kata hadi kata ili fedha hizi zifike kwa walengwa.
T A A R I F A....
Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa yake kwanza naikataa.
Fuatilia vizuri, naona Magufuli anawapa moto na hiyo ni bado. Arusha tumeshachukua kata, tumeshaanza kuchukua mitaa…
Tulieni, tulieni. Mheshimiwa Naibu Spika, ulinde muda wangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana jembe Rais Magufuli, Rais wa wanyonge, Rais wa maskini, sasa hivi maskini wote wanaimba Chama cha Mapinduzi kwa sababu ya Rais Magufuli. Hongera sana Rais wetu na Arusha tutarudisha Majimbo kwa hii kasi ya Magufuli.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee kutoa mchango wangu, tunaomba sana hizi shilingi milioni 50 za kila kijiji, Wabunge wa maeneo husika hasa wa Chama cha Mapinduzi tushirikishwe ili tujue zinapoenda na vilevile sisi ndiyo ambao tunajua watu ambao wanahitaji fedha hizi. Tunaomba zile asilimia tano ambazo zilikuwa kwenye Halmashauri kwa ajili ya akinamama na vijana ziendelee kuwepo, siyo shilingi milioni 50 itoke zile zisiwepo, ziendelee kuwepo kama sheria inavyosema.
Mheshimiwa Spika, naomba nijielekeze katika suala zima la elimu. Tumeona Serikali ya Chama cha Mapinduzi imesema elimu bure. Mpango huu umesaidia sana watoto wa maskini sasa hivi wanapata elimu. Watoto wengi wa maskini walikuwa wanachukuliwa wakiwa wadogo kwenda kufanya kazi za ndani, lakini sasa hivi tunaona Serikali ya Chama cha Mapinduzi imeleta usawa kwa watoto wetu na imeleta usawa kwa maskini na matajiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili ni zuri sana ingawa lina changamoto chache. Tumeona baadhi ya shule za kutwa wazazi wanaendelea kutoa fedha kwa ajili ya chakula. Tunaomba sana Serikali yetu sikivu chini ya Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Magufuli irekebishe suala hili ili watoto waweze kupata mlo shuleni wazazi wasiendelee kutoa michango.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nije katika suala zima la madawati. Naipongeza sana TAMISEMI kwa jinsi inavyoshughulikia suala la madawati. Katika Mkoa wangu wa Arusha kulikuwa na tatizo la madawati 24,304 lakini uongozi wa Mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya za Mkoa wa Arusha wamejitahidi mpaka sasa hivi wameshakusanya madawati zaidi ya 18,000. Tatizo la madawati lililobaki kwa sasa hivi kwa shule za msingi ni kama madawati 6,000. Naomba sana tuendelee kusaidiana katika suala hili hata kwa mikoa mingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende katika suala zima la afya. Naomba Serikali ilitoe suala la afya TAMISEMI ili Wizara hii ijitegemee waweze kughulikia matatizo ya wananchi kiundani zaidi. Naomba niendelee kwa kumpongeza Mkuu wangu wa Mkoa wa Arusha kwa jitihada ambazo amekuwa akizionesha katika suala zima la afya. Kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameweza kukarabati Kituo cha Afya cha Ngarenaro, Hospitali yetu kubwa ya Mount Meru wamefungua duka la dawa pale la MSD na limeshaanza kufanya kazi, Hospitali ya Kaloleni wameikarabati na sasa hivi ninavyoongea wanaendelea na Hospitali ya Levorosi, nawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba Serikali iuangalie sana Mkoa wangu wa Arusha, Wilaya ya Ngorongoro hasa Hospitali ya Loliondo inayoitwa Waso. Hospitali ile imekuwa ikipokea wagonjwa wengi sana na akinamama wajawazito, lakini kwa sababu eneo lile ni la wafugaji akinamama wamekuwa wakiacha wagonjwa wao kwenda kuwatafutia chakula nyumbani wakati mwingine wanakwenda umbali wa kilometa mpaka tatu. Naiomba Serikali katika bajeti yake ya Hospitali ya Loliondo ya Waso watuwekee chakula ili wagonjwa wawe wanapata chakula pale pale na wawe na matumaini makubwa na Serikali yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hili suala la ugonjwa wa endometriosis ambapo tumemwona mwanamitindo maarufu kama Millen Magese amejitokeza hadharani na kukubali kuwa anaumwa endometriosis. Ugonjwa huu ni mbaya sana kwa watoto wetu wa kike na wanawake kwa ujumla kwani unapelekea utasa. Mwanamitindo huyo amejitokeza na anapita mpaka kwenye shule kuelezea kuhusu ugonjwa huu, ni ugonjwa ambao unaweza ukamkuta ndugu yako, dada yako au watoto wetu. Tunaomba sana Serikali ielezee kiundani kuhusiana na ugonjwa huu, athari zake na vilevile watoto wetu wa kike wapate matibabu ya ugonjwa huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Ummy na Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla na Makamu wetu wa Rais, mwanamama Mheshimiwa Samia, tumeona wamemuunga mkono mwanamitindo huyu kwa ajili ya kuelimisha jamii nzima ya Watanzania hususani watoto wa kike ili waelewe tatizo hili na jinsi ya kujikinga maana wakijikubali kama mwanamitindo huyo nadhani watakuwa free kueleza tatizo lao na kutibu ugonjwa huu ambao unapelekea utasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Ilani yetu ya Uchaguzi tuliahidi bima ya afya kwa kila mwananchi. Tunaomba sana Serikali ilete Muswada huu Bungeni mapema ili tuweze kuupitisha, wananchi wetu waweze kupata huduma ya afya kupitia Serikali yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sana Serikali iangalie upya suala zima la ugonjwa wa kisukari. Ugonjwa wa kisukari hasa huu wa kurithi, tumeona watoto wadogo wanapata sukari na zimekuwa zikiwatesa sana. Wananchi waelimishwe watajikinga vipi na kisukari, tumeona hata watu wazima, wanaume wanaachwa mpaka na wake zao kwa sababu ya ugonjwa huu wa sukari.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali i-take serious ugonjwa huu, kwa kweli wananchi wanapata shida, akinamama wanapata shida kwa sababu wanaume zao wanakuwa na ugonjwa wa sukari. Tunaomba sana Serikali iangalie kwa makini ugonjwa huu na kuelimisha watu jinsi ya kujikinga na itawasaidia vipi kaka zetu na baba zetu katika suala zima la ugonjwa huu wa kisukari.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba safari hii fedha za miradi ya maendeleo ziende kama ilivyokusudiwa. Tumeona katika sekta ya afya hususani kwenye vituo vya afya na maeneo mengi fedha za maendeleo hazifiki kama zilivyokusudiwa na hivyo kuzorotesha shughuli za maendeleo. Tunaomba sana Serikali ifikishe fedha za maendeleo kama ilivyopangwa kwa sababu tumekuwa tunapata matatizo mengi lakini fedha haziendi kama ambavyo zimekusudiwa. Tunaomba Serikali ihakikishe inafikisha fedha hizi kama ilivyopangwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaendelea kumshukuru Rais wetu John Pombe Magufuli kwa jitihada zake za kutumbua majipu, tunamuunga mkono aendelee na kazi hiyo ya kutumbua majipu. Tunaona wananchi wanamkubali, tumeanza kuirudisha Arusha kidogo kidogo, mitaa Arusha tumepata, yote hii ni kutokana na kwamba wananchi wanakubali utendaji wa Rais wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwenye macho haambiwi tazama, lakini ndiyo hivyo Serikali ya CCM iko juu na tukiendelea hivyo tutarudisha majimbo yetu yote na watu wa Arusha siku hizi hata nguo za kijani tunavaa na tunashangiliwa tunaambiwa Hapa Kazi Tu. Tunaomba waendelee kuboresha hospitali zetu ili Chama chetu cha Mapinduzi ambacho ni cha ukweli, kinatekeleza ahadi, kinawajali maskini na ambacho mafisadi walikikimbia wenyewe walivyoona moto wake kiendelee kukubaliwa na wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu katika uchumi wa nchi yetu. Naomba nijielekeze moja kwa moja kwenye mchango wangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Hifadhi la Taifa (TANAPA) ni miongoni mwa mashirika ya umma yanayotuingizia pesa nyingi sana katika nchi yetu. Utalii katika nchi yetu unachangia 18% ya GDP ya Taifa. Jambo la ajabu na la kusikitisha sana, miaka zaidi ya mitatu TANAPA haina Bodi ya Wakurugenzi. Maamuzi muhimu yamekuwa yakitolewa na viongozi wa Wizara akiwemo Waziri na Makatibu Wakuu walioondoka na hata wa sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, miaka kadhaa kulitokea mvutano juu ya ada zinazotakiwa kulipwa na wenye mahoteli maarufu kama concession fee, walishtakiana wakapelekana Mahakama Kuu na TANAPA walishinda kesi ile lakini mpaka sasa hivi hakuna kinachoendelea kwa sababu hakuna Bodi ambayo ndiyo ilitakiwa wapange jinsi gani ada hizi zitatozwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tunapoteza mapato mengi sana kutokana na kukosa hizi fee za kwenye mahoteli. Kwa mwaka TANAPA inapoteza shilingi bilioni 10 kwa kukosa fees hizi. Shilingi bilioni 10 siyo pesa ndogo, ni pesa nyingi sana. Tunaona Rais wetu anavyohangaika kutafuta pesa, anabana matumizi, shilingi bilioni 10 hizi zingeweza kupeleka maji Arusha, Karatu, Longido, Ngorongoro na zingeweza kusaidia watoto wa maskini wakakaa kwenye madawati. Sijui ni kwa nini mpaka sasa hivi pesa hizi hazijaanza kukusanywa na ni kwa nini Bodi ya TANAPA mpaka sasa hivi haijaundwa. Waziri atakapokuja ku-wind up naomba aniambie ni lini Bodi ya TANAPA itaundwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA Ndugu Allan Kijazi kwa sababu amekuwa akimsaidia Rais kusaidia maskini. Tumeona juzi wamemkabidhi Mheshimiwa Makamu wa Rais shilingi bilioni moja kwa ajili ya madawati kwa mikoa 16, tunamshukuru sana kwa hilo. Nimeona nikitaja TANAPA bila kumtaja Ndugu Allan Kijazi nitakuwa sijaitendea haki hotuba yangu, nampongeza sana, naomba aendelee hivyo hivyo kum-support Rais wetu kuwa sasa ni kazi tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba moja kwa moja niende katika suala zima la ujangili. Ujangili umeshamiri sana, wanyamapori wamekuwa wakiuawa, tembo wapo hatarini kutoweka licha ya Serikali pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kufanya jitihada za kutatua tatizo hili. Majangili wana silaha kali sana hasa katika mapori yetu kama Ugala, Loliondo na mapori mengine mengi. Mbaya zaidi sheria haziruhusu walinzi wa makampuni ya vitalu vya uwindaji na YWMA kutumia silaha.
Mheshimiwa Naibu Spika, naona sasa hivi ni wakati muafaka wa kuleta sheria ili walinzi wa haya makampuni waruhusiwe kutumia silaha kwenye hifadhi zetu ili washirikiane na walinzi wa wanyamapori na wa TANAPA, majangili wamekuwa wakitamba sana kwenye hifadhi zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba iwekwe adhabu kali sana kwa ajii ya majangili siyo kuwa watozwe fine tu hapana, majangili wana pesa nyingi, fine kwao ni kitu kidogo. Tumeona Serikali ya Kenya wameweka sheria atakayekutwa kwenye hifadhi bila kibali anapigwa risasi sisi hata kama hatuwezi kufanya hivyo, lakini ni wakati muafaka wa Serikali kuleta sheria hapa Bungeni ikiwezekana majangili wafungwe kifungo cha maisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia inasemekana kuwa baadhi ya Wabunge ni majangili, wamekuwa wanajihusisha na biashara hii ya ujangili.
Nina imani hakuna ambaye yupo juu ya sheria. Hata gazeti la Jamhuri la leo limeandika Mbunge jangili. Huyo Mbunge jangili ni nani, ni Munde Tambwe, Catherine Magiga au Ally Keissy, tunataka tufahamu. Vyombo vya usalama, vyombo vya sheria vipo wafuatiliwe ijulikane Mbunge jangili ni nani. Hakuna mtu ambaye yuko juu ya sheria na akikutwa kiongozi ambaye ni jangili kama Mbunge jangili ,naomba mfano uanze kuoneshwa kwake. Siyo tunalaumu tu watu wengine wakati majangili tuko nao humu humu ndani, tunataka kuwafahamu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi majuzi gazeti ya Jamhuri liliandika makala ikaonesha jinsi vibanda vinavyokusanya mapato ya watalii kwenye mapori ya Loliondo na Longido, vibanda vile vilikuwa vinasikitisha sana, ni vibanda vya miti tu. Kweli watalii wanatuletea dola wanakuta watu wamekaa kwenye vile vibanda wanapokea mapato tuko serious na utalii wetu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua Wizara haihusiki zinazohusika ni Halmashauri ya Longido na ya Monduli lakini mtalii anapokuja hazitambui zile Halmashauri bali Wizara ya Maliasili, naomba tuwe serious kwa hili. Tunataka kupokea dola za watalii, tunapokea kwenye vibanda, vibanda vya ajabu, ni aibu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, moja kwa moja naomba nielekeze mchango wangu katika misitu. Misitu inamalizwa, biashara za mkaa zimeshamiri sababu kubwa wakisema bei ya gesi au nishati mbadala ni kubwa. Naomba suala hili la mkaa ingawa kwa Wizara ni suala mtambuka lakini bado kuna ukweli misitu yetu ambayo iko chini ya Maliasili watu wanakata mikaa wanaimaliza.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali iliangalie sana suala hili la kukata misitu na iwachukulie hatua ambao wanauza mikaa, maana wanakata miti bila vibali na sasa hivi tumeona magari yanasafirisha mkaa usiku kwenye ma-container. Naweza nikatolea mfano pale kwa Msuguli kuna watu wanakaa pale kwa ajili ya kukagua hizi lumbesa za mazao sasa huoni kama ni wakati muafaka watu wa misitu nao wakawepo pale kwa ajili ya kuhakikisha kuwa miti yetu haikatwi ovyo na kukwepa kodi kupitia misitu? Tunaomba sana Serikali iangalie suala hili zima la mkaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona hapa watu wanaongelea kuhusu ndege, mimi akinamama wa Arusha hawaniulizi kuhusu ndege, wanauliza kuhusu maji na mitaji. Kwa hiyo, naomba tujielekeze sana kuona haya masuala ambayo ni muhimu kwa ajili ya wananchi wetu, siyo tunajiangalia sisi tu maana wale wapiga kura kule hata ndege hawapandi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba TANAPA iendelee kuwasaidia vijana na akinamama kwa kuwapa mitaji. Kuna akinamama na vijana wengi ambao wanafanya biashara ya utalii hasa katika Mkoa wangu wa Arusha iwasaidie kuwapa semina wapate elimu ya ujasiriamali ili waweze kutumia vizuri fursa hii ya utalii. Vilevile wawatafutie masoko, kuna akinamama wanauza shanga na vinyago kwa watalii watusaidie akinamama hao wapate soko ili waweze kujitosheleza na mahitaji yao mbalimbali kama ya kusomesha watoto wao na waweze kufanya biashara za kiutalii na wanufaike na utalii wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja ila naomba tu Waziri atakaponijibu aniambie ni lini ataunda Bodi ya TANAPA, la sivyo nitatoa shilingi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) ni miongoni mwa mashirika ya umma yenye kulisaidia Taifa kupata fedha nyingi za kigeni. Utalii nchini mwetu unachangia asilimia 18 ya GDP na sasa kiasi hiki kinaweza kuongezeka zaidi. Jambo la ajabu, TANAPA kwa miaka zaidi ya mitatu sasa haina Bodi ya Wakurugenzi. Mambo yote yamekuwa yakiamriwa na viongozi wa Wizara yaani Waziri na Katibu Wakuu waliopita na waliopo sasa. Hii ni hatari kwa shirika kama hili lenye fedha nyingi zinazohitaji utaratibu wa Bodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujangili unashamiri, idadi ya wanyamapori ni kubwa mno. Tembo wako hatarini kutoweka licha ya juhudi za Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama katika kukabiliana na hali hiyo. Majangili wana silaha hasa katika mapori kama ya Ugalla, Moyowosi, Loliondo na mengine mengi. Mbaya zaidi sheria haziruhusu walinzi wa kampuni zenye vitalu vya uwindaji katika mapori ya akiba na WMA kuwa na silaha. Hali hiyo imesababisha majangili watambe. Kwa nini Mheshimiwa Waziri asilete sheria Bungeni ili walinzi hao wapewe silaha na kwa hiyo, wasaidiane na wale wa TANAPA na wa wanyamapori kukabiliana na ujangili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, adhabu kwa majangili zisiwe faini, bali ziwe hukumu za kifungo cha maisha. Kenya wana sheria kali zinazosaidia sana kulinda wanyamapori wao. Kwa mfano, wao mtu akipatikana ndani ya hifadhi kinyume cha sheria, wanampiga risasi. Sisi tunaweza tusiwe na adhabu ya aina hiyo, lakini wakati umefika kwa Serikali kuleta hapa Bungeni mabadiliko ya sheria ili majangili wajue tumedhamiria kukomesha vitendo vyao. Serikali isiwe na kigugumizi cha kuwashughulikia viongozi wanaotajwa kuwa ni washiriki wakuu wa ujangili. Yapo maneno kuwa hata miongoni mwetu Waheshimiwa Wabunge kuna majangili. Kama kweli wapo, ni vizuri sheria zikatekelezwa badala ya kuendelea kuwaaminisha wananchi kwa maneno tu kuwa kuna Waheshimiwa Wabunge majangili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka kadhaa iliyopita kulitokea mvutano kuhusu ada wanazopaswa kulipa watu wenye hoteli (concessions fee). TANAPA walifungua kesi katika Mahakama Kuu na kushinda kesi hiyo. Ikaamuliwa wenye hoteli walipe, lakini utekelezaji wake ulipaswa uanze kwa Bodi kukaa na kupanga viwango vya ada hiyo. Sasa miaka zaidi ya mitano uamuzi huo haujatekelezwa na haujatekelezwa kwa sababu hakuna Bodi. Kwa kutoweka ada hizo, TANAPA wanapoteza wastani wa shilingi bilioni 10 kwa mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ahakikishe anamshawishi Mheshimiwa Rais mapema iwezekanavyo ili Bodi ya TANAPA iundwe; na kwa kufanya hivyo, iweke viwango vya ada na utekelezaji uanze mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mifugo katika mapori ya akiba, mapori tengefu, WMA na Hifadhi za Taifa ni mingi sana. Mapori kama Maswa, Moyowosi, Kijeleshi, Ugalla yanaelekea kufa. Pori tengefu la Loliondo limevamiwa na malaki ya mifugo kutoka nchi jarani (Kenya). Loliondo ni kama imekufa. Shughuli za kibinadamu zikiwamo za kilimo ni kubwa mno. Wanyamapori wamekimbia, Loliondo hii ni buffer zone ya Serengeti na eneo ambalo ni mazalia ya nyumbu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mifugo imekuwa mingi sana kiasi cha kufikia hatua sasa ya kuona hatari siyo ujangili tu, ila mifugo katika mapori ya hifadhi. Pamoja na umhimu wa mifugo katika nchi yetu, Serikali isisite kutekeleza Operesheni Ondoa Mifugo ambayo imepangwa kuanza tarehe 15 Juni, 2016. Bila kufanya hivyo rasilimali wanyamapori itatoweka katika nchi yetu na hii itakuwa aibu kubwa kwa kizazi kijacho na ulimwengu kwa jumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu tuweke kando siasa na tujikite kwenye uhifadhi. Faida za uhifadhi ni kubwa; kwa mfano, nyati mmoja anayewindwa anaiingizia Serikali zaidi ya shilingi milioni tatu. Simba mmoja anaingiza zaidi ya shilingi milioni 10. Kwa hiyo, tusiifanye mifugo ikawa mbadala wa wanyamapori kwa sababu faida yake ni kwa wachache wenye kuimiliki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni Gazeti la Jamhuri lilitoa makala ikionesha vibanda vibovu kabisa vya kukusanya mapato kutoka kwa watalii katika maeneo ya Oldonyo Lengai na Engaruka. Ile ni aibu kubwa kwa sababu vibanda vyenyewe vimeshikiliwa na nguzo za miti visianguke. Hata watalii watatushangaa kuona dola zinakusanywa kwao na watu walio kwenye vibanda vibovu. Ingawa vibanda hivyo vipo chini ya Halmashauri za Longido na Monduli, bado Wizara ya Maliasili na Utalii inapaswa kuitazama aibu hii na kuiondoa kwa sababu watalii hawazijui Halmashauri hizo, isipokuwa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara ya mkaa inashamiri sana. Misitu inamalizwa na sababu inayotolewa ni kuwa bei ya gesi au nishati mbadala ni kubwa. Ingawa suala hili la mkaa ni mtambuka Kiwizara, bado ukweli unabaki kuwa mkaa mwingi unatolewa katika mapori yanayohifadhiwa kisheria chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Mbaya zaidi, hata huo mkaa unaouzwa watu wengi hawalipi ushuru. Malori ambayo kisheria hayaruhusiwi kusafirisha mkaa, leo yanasafirisha hadi kwenye makontena nyakati za usiku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri pale Dar es Salaam watumishi wa Wizara wakae kwenye maegesho pale kwa Msuguri ili kuyakamata malori yote yanayopakia na kusafirisha mkaa bila vibali wala kulipa ushuru. Watumishi wa Wakala wa Vipimo wapo hapo sasa wakidhibiti upakiaji wa lumbesa kwa mazao kutoka mikoani. Sioni kwa nini Wakala wa Misitu nao wasikae hapo kwa Msuguri ili kuyadhibiti malori haya yanayotumika kutenda makosa haya ya uhifadhi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kazi kubwa inazofanya dhidi ya kukwamua kiuchumi wananchi wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuongelea suala zima la afya hasa katika Mkoa wangu wa Arusha katika Wilaya ya Longido, wananchi walio mpakani mwa nchi jirani ya Kenya maeneo ya Namanga wamekuwa wakivuka mpaka na kwenda kutibiwa nchi jirani ya Kenya. Jambo hili limekuwa kero sana kwa wananchi wa Wilaya ya Longido. Tunaomba Serikali iwasaidie wananchi wa Longido kuwajengea hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Arumeru Magharibi ni jimbo kubwa sana hali inayopelekea wananchi wengi kutofikiwa na huduma muhimu. Naomba Serikali iangalie upya jinsi ya kugawa jimbo hili ili wananchi wengi waweze kufikiwa na huduma muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jimbo hili kumekuwa na migogoro ya ardhi mara kwa mara na migogoro hii inapelekea wananchi kuishi bila amani. Kuna baadhi ya wawekezaji wamejilimbikizia ardhi kubwa na wanatumia tofauti na ilivyokusudiwa. Wananchi wana shida ya ardhi
huku wawekezaji wamejilimbikizia ardhi kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo hili la Arumeru Magharibi kuna tatizo kubwa la akinamama ambao wamekuwa wakitembea mwendo mrefu kutafuta maji. Naiomba Serikali iangalie kwa ukaribu changamoto nyingi zilizomo katika jimbo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jimbo hili lina changamoto kubwa ya barabara, barabara zake ni mbovu. Naiomba Serikali iliangalie hili ilki wananchi wake wafaidike na Serikali yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Mchango wangu nitauelekeza moja kwa moja katika Shirika letu la Ndege la ATCL. Katika vipindi viwili vya 2016/2017 na mwaka 2017/2018, tumeona imetengwa karibu shilingi trioni moja kwa ajili ya ATCL ambapo kwa kila kipindi itakuwa shilingi bilioni
500. Uwekezaji huu ni mkubwa mno na unahitaji umakini wa hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ili ATCL ipate faida, ni lazima twende sambamba na uwekezaji katika mambo makuu mawili. Jambo la kwanza ni uwekezaji wa ndege kama hivi tunavyofanya sasa hivi; jambo la pili ni kuwekeza katika uendeshaji wa ATCL, yaani mtaji wa kazi na rasilimali watu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa ndege, naomba nimpongeze sana Mhshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutuletea ndege za kisasa na ametuhakikishia ni salama kabisa. Itakapofika mwaka 2020 kama siyo 2019 zitakuwa ndege saba. Nampongeza sana Rais wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wasiwasi mkubwa unakuja kwenye uwekezaji katika uendeshaji wa ATCL. Tumezoea tukinunua tu ndege tunaacha, tunajua tayari tumeshanunua ndege bila kuwekeza. Tunategemea kupata faida, lakini hatuwezi kupata faida tu bila kuiwezesha ATCL iweze kuendesha biashara ya ndege. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sote tunajua kuwa ATCL ilibaki jina tu, haikuwa inafanya vizuri, ndege zake zilikuwa hazieleweki, lakini sasa Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kaanza kuturudishia ATCL mpya. Vilevile haikuwa na rasilimali watu na mtaji; naongelea kwa upande wa kujiendesha. Kwa hiyo, lazima tuisaidie ATCL kujiendesha ili iwe kibiashara zaidi. Tunajua ATCL ilikuwa ni jina tu au Kampuni isiyokuwa na rasilimali watu wala chochote; tunajua kwa sasa hivi ATCL kitu ambacho inahitaji ni working capital na siyo startup cost. Ni wazi kwamba bila kuiwezesha ATCL haitaweza kujiendesha yewenye na haitaweza kujiendesha kibiashara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, uwekezaji uliofanywa na Serikali ni mkubwa mno, lazima uambatane na uwekezaji wa kuiendesha ATCL ili iweze kutoa huduma nzuri. Tumeanza kuona mabadiliko ya ATCL, tumeona safari hazikatishwi, tumeona inaenda vizuri sana. Vilevile naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutuletea Mtendaji anayeweza hii nafasi, ana uzoefu. Ni muda mfupi sana naweza nikasema ametuonyesha wonders. Naomba sana tum-support Mtendaji huyu Ledislaus Matindi kwa kazi kubwa anayofanya, ana uzoefu na anajua changamoto za ATCL. Lazima tuunge juhudi za Serikali mkono na tuwe wazalendo kwa nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona Mheshimiwa Rais ameteua Bodi nzuri; lazima tuhakikishe Bodi na Menejimenti wamejikita zaidi kuisaidia ATCL ijiendeshwe kibiashara na siyo kukaa tu kusema kuwa ni Shirika la Serikali. Hatuna wasiwasi na matumizi ya fedha kwa sababu ya uongozi uliopo sasa hivi tunauamini, tunajua hata tukiwawezesha mapato yataenda vizuri, fedha zitatumika kama zilivyokusudiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tujifunze kwa wenzetu ambao waliweza kuendelea kama Shirika la Ndege la Ethiopia. Serikali yao iliwawezesha Ethiopia na waliendelea vizuri, ilivumilia na walijipanga vizuri. Walianza mambo yao ya ndege mwaka 1945, lakini walikuja kupata faida 1990 walikuwa wavumilivu, waliwekeza katika mishahara, matangazo na hadi sasa hivi inajiendesha kibiashara. Tusitegemee ATCL itaanza tu, tayari tupate faida asilimia 100, hapana. Lazima kama sisi Serikali kuiwezesha ili iweze kujiendesha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mafanikio ya Ethiopia yalikuwa na uvumilivu, mkakati na nidhamu. Uvumilivu ulisaidia sana mpaka kufika 1990 ukiangalia ukiangalia kuanzia mwaka 1945, ni kipindi kirefu sana, kwa hiyo, kilihitaji uvumilivu. Nasi tukifanya hivyo, Serikali ikiwawezesha ATCL nina uhakika kabisa tutafika na tutaweza kuendelea vizuri na ATCL. Kwa hiyo, naomba Tanzania tui-support ATCL. Mpaka sasa hivi tumeona inaenda vizuri, ni muda mchache sana lakini imefanya vizuri na wote tumekubali.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tuonyeshe uzalendo kwenye ndege zetu. Tumeona kuna ndege ndogo ambazo zinafanya safari kwenye miji mikubwa, kwenye barabara kuu ambazo zingeweza kufanya ndege zetu. Naomba pia Serikali iliangalie hili tumetumia kodi za wananchi. Ndege ndogo zinaweza kupewa trip nyingine kwenda sehemu ambazo hizi ndege zetu za ATCL haziwezi zikafika. Zenyewe zikaenda zikawaachia njia ATCL.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tumeona kuna tabia moja kuwa ndege inapokuwa na nguvu kuna baadhi ya ndege zinakuja zinawakwamisha, zinaua kabisa. Tumeona ndege tayari ambazo tayari zilikuwa zinafanya vizuri zimekufa, lakini tusikubali hili kwa ndege zetu ambazo zimenunuliwa kwa kodi ya wananchi. Tumeona ATCL inaweza ikaenda Mwanza labda kwa kiasi fulani lakini ndege nyingine ikaenda ikashusha kabisa. Hao ndio wauaji wakuu wa soko letu, Watanzania tusikubali, tuwe wazalendo wa nchi yetu. Mheshimiwa Waziri naomba uje unijibu wakati unajibu hili la ndege nyingine kuja kutuharibia biashara huku tukijua tunatumia kodi za wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tusipokuwa makini tunaweza tukajikuta ATCL inakufa, tukaishia kwenye madeni yasiyolipika. Kwa hiyo, tuunge mkono juhudi za Mheshimiwa Rais na nia yake nzuri ya kufufua Shirika letu la ndege ili lije kufanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie na uwanja wangu wa Ndege wa Arusha Airport. Kiwanja cha Ndege cha Arusha Airport, njia ya kurukia ni fupi, hali inayopelekea ndege za kati na kubwa kushindwa kutua, ikiwemo ATCL, inashindwa kuruka. Kwa hiyo, inabidi wakatize trip za kwenda Arusha. Ukizingatia Arusha ni Jiji lenye biashara, Jiji la utalii, ni kitovu cha utalii ambapo tungeweza kuiingizia Serikali mapato mengi sana kutokana na utalii. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wakati ananijibu, naomba aniambie ana mpango gani na Kiwanja cha Ndege cha Kisongo cha Arusha ili nasi wana-Arusha tuweze kupata hizo ndege tuweze kuiingizia Serikali mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, naomba Waziri aniambie ameandaa kiasi gani cha uwekezaji kama mtaji na rasilimali watu kuwekeza kwa ajili ya ATCL iweze kujiendesha yenyewe kibiashara? Siyo kuwekeza tu kwenye ndege tukasahau kuwa inahitaji na yenyewe kujiwekeza? Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.

Kwanza kabisa naomba sana niipongeze Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi chini ya Rais John Pombe Magufuli kwa kuendelea kutimiza Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi kuwa tunajenga Tanzania ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuwa nikiongea kila siku hapa kuhusu Kiwanda cha General Tyre cha Arusha nimeona kimetengewa pesa ili kianze, lakini ninachoomba je, tumejipangaje kuhusu viwanda vingine vinavyotengeneza matairi hasa vya nje? Je, Kiwanda cha General Tyre tumejipangaje ili kifanye biashara vizuri? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nilikuwa naomba reli ya Tanga – Arusha mpaka Moshi. Reli hii itasaidia sana katika usafirishaji wa matairi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Arusha kuna viwanda vingi tu, kuna Kiwanda cha Lodhia Plastic. Kiwanda hiki kimeajiri Watanzania 700; ni kiwanda cha mabomba na ma-sim tank. Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuja tulitembelea kiwanda hiki, ni kiwanda chenye ubora wa hali ya juu na aliagiza baadhi ya ofisi zetu za Serikali zitumie kiwanda hiki, lakini ma-engineer wa Serikali wamekuwa wakikwamisha kiwanda hiki. Wamekuwa wakiagiza mabomba nje ya Arusha, wamekuwa wakiagiza mabomba Dar es Salaam ambapo kwanza ni gharama kubwa sana, wamekuwa wakiagiza wakandarasi wanunue mabomba kwenye viwanda fulani, sijui kuna nini (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hizo figisu figisu hizo nahisi kuna rushwa. Tumekuwa tunakwamisha Watanzania ambao wanajitokeza kuendeleza viwanda vyao kutimiza kauli ya Rais wetu Tanzania yenye viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri aangalie hili, Mheshimiwa Waziri Mkuu alishatoa amri sijui kama kuna amri nyingine zaidi ya Waziri Mkuu. Tujue hawa ma-engineer wa Serikali ni kitu gani hasa wanapata mpaka wanatoa amri kwa makandarasi ili waende wakachukue mabomba kutoka kwenye viwanda vya nje ya Arusha, kwa sababu kwanza ni gharama. Tunasema tunabana matumizi matumizi gani tunabana kama ni hivi? Tunahujumu na tunamhujumu Rais wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Arusha tuna Kiwanda cha Gypsum kinaitwa Saint Gabain Lodhia Gypsum. Kiwanda hiki kinatumia makaa ya mawe wanatoa Kiwira, mpaka wafike Arusha wanatumia dola 120 mpaka 130. Kiwanda hiki kimekuwa kinatozwa pesa nyingi tofauti na viwanda vingine. Wamekuwa wananunua makaa ya mawe dola 65 mpaka 70; huku viwanda vingine vimekuwa vinatoa dola 35.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamwomba Waziri aangalie sana, tunazidi kukwamisha jitihada za Rais wetu za kuwainua Watanzania. Pia kiwanda hiki kimeajiri Watanzania 450. Hiki cha plastic tayari Watanzania 250 wameshapunguzwa kwa ajili ya hawa watu ambao wanatuhujumu. Ninaomba sana kwa kweli Mheshimiwa Waziri mimi nitashika shilingi nisipopata jibu la kiwanda hiki cha plastic, nisipopata jibu kiwanda hiki ambacho kinatumia Makaa ya Mawe ya Kiwira. Naomba Mheshimiwa Waziri uje na majibu yanayoeleweka ama sivyo sitakuelewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri Mkuu alikuja tulitembelea Kiwanda kimoja cha Hans Paul. Yule ni Mtanzania ana kiwanda, anachukua magari Anaya-design yanakuwa magari ya kubebea taka. Magari yake anauza shilingi milioni 200 mpaka 220. Mheshimiwa Waziri Mkuu mwenyewe aliona alishaanga sana hakutegemea kama watanzania wanaweza wakawa na ujuzi kama huo. Ni magari mazuri na yana ubora wa hali ya juu. Ningeshauri baadhi ya Halmashauri zetu zitembelee zione kuliko uangize magari kwa bei zaidi ya shilingi milioni 500 huku tunaweza tukapata magari yenye ubora wa juu hapa hapa nchini kwa shilingi milioni 220. Naomba sana tulinde viwanda vya ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, Arusha tulikuwa na kiwanda kikubwa sana cha dawa kimefungwa mpaka leo na kimefungwa na Tanzania tuna uhaba wa dawa. Kwa nini kisifunguliwe hata kisaidie hata Kanda ya Kaskazini yote?

Naomba sana Mheshimiwa Waziri uje kunijibu na hili kiwanda cha dawa cha Arusha kimefungwa mpaka leo. Naomba sana kiwanda hiki kifunguliwe Serikali ijipange ifungue kiwanda hiki. Tunayosema Tanzania yenye viwanda haitakuwa yenye viwanda bila kutekeleza haya ninayokuambia Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua kuna watu ambao walipewa viwanda vilivyokuwa vya Serikali, lakini viwanda vile wameng’oa mashine, viwanda vingi tu havitumiki tena. Tunaomba viwanda hivi mkiweza mvirudishe Serikalini ili vifanye kazi, Watanzania waweze kupata ajira tuweze kutumia na sisi bidhaa zetu. Watu wengi walipwa viwanda lakini wamefanya ma-godown.

Mheshimiwa Naibu Spika, Arusha tunajua ni mkoa ambao unaongoza sana kwa mifugo, ni Mkoa ambao una wafugaji wengi sana. Tunaomba na sisi mtuwekee angalu kiwanda cha ngozi ili tuweze kutumia mifugo yetu na itufaidishe tuweze kutengeza viatu. Ngozi inatengeza vitu vingi sana tunaombasana mtuangalie Arusha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na malalamiko makubwa sana kwa wafanyabiashara, wanakata tamaa wanashindwa kuendelea, tunakwamisha jitihada za Watanzania. Kuna process ndefu sana katika kupata vibali cha kuanzisha biashara. Wanapitia sehemu nyingi sana mpaka wanakata tamaa. Tunaomba sana Mheshimiwa Waziri wasaidie Watanzania wengi, hiki ni kilio cha watu wengi sana. Tunakuomba Mheshimiwa Waziri narudia tena.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakuomba sana mimi leo kweli nitashika shilingi Mheshimiwa Waziri asiponijibu kuhusu Kiwanda cha Plastiki cha Lodhia. Vilevile nilikuwa naomba washirikiane na Waziri wa Maji hata idara zetu za maji mfano kama AUWSA watumie watu ambao wako kwenye mikoa yao maana viwanda ni vizuri, kuna hujuma hapa; na hawa ma-engineer wa Manispaa wa mikoa yetu nilitaka nifahamu wenyewe wana nguvu gani kuliko Mheshimiwa Waziri Mkuu? Kama Mheshimiwa Waziri Mkuu anatoa amri hawaitekelezi wanatuma mabomba wakachukue mabomba Dar es Salaam inawezekana kweli? Wanapatanini? Kwanza gharama ni kubwa; tunasema Serikali yetu tunabana matumizi naomba tusimuangushe Mheshimiwa Rais ana nia nzuri na Watanzania ana nia nzuri na nchi yetu, ana nia nzuri na chama chake ambacho ndiyo anatekeleza Ilani yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, sina mengi, naunga mkono hoja, lakini Mheshimiwa Waziri nitashika shilingi leo.