Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Abdallah Dadi Chikota (67 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pia naomba nichukue nafasi hii kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kujiunga katika Bunge hili na nimshukuru zaidi Mwenyezi Mungu kwa sababu amerahisisha safari yangu ya kutoka kwenye Utumishi wa Umma na kuingia kwenye Ubunge kwa sababu nilipita bila kupingwa, kwa hiyo Ubunge wangu ulianza tangu tarehe 21 Agosti, 2015 wale wenzetu wa upande mwingine hawakurudisha form. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nichukue nafasi hii sasa, kumpongeza Waziri wa Mipango Dkt. Philip Mpango, na Watumishi wenzake, ambao wametuletea mapendekezo ya Mpango na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ambao wote tunauona unafaa, unatoa matumaini mapya na ni kweli Tanzania yenye viwanda inawezekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu, utajikita kwenye maeneo ya vipaumbele. Eneo la kwanza ni lile la kutangaza Mtwara kuwa eneo la uwekezaji, naomba niishauri Serikali, unapozungumzia Uchumi wa Gesi, huwezi kutofautisha Mtwara na Lindi. Kwa hiyo, naomba vilevile Lindi uangaliwe uwezekano na yenyewe kuwekwa kama eneo maalum la uwekezaji, kwa sababu unapozungumzia uchumi wa gesi na mafuta unazungumzia Mtwara na Lindi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nikizungumzia Mtwara ambapo kumetangazwa eneo la uwekezaji kuna changamoto nyingi sana ambazo naomba tupeleke rasilimali za kutosha ili eneo hili litumike ipasavyo. Kwanza kuna ujenzi wa bandari, fedha za kutosha zipelekwe kwa ajili ya upanuzi wa bandari yetu ya Mtwara.
Pili, kama walivyosema wachangiaji waliyopita kuna suala la uwanja wetu wa Ndege wa Mtwara ukabarati umefanyika miaka ya nyuma sana, uwanja huo sasa hivi wa Mtwara hauna taa na hivyo Ndege haziwezi kutua au kuruka usiku, sasa eneo gani la uwekezaji ambao unaweka masharti kwamba Mwekezaji afike mchana tu usiku hawezi kuingia, kwa hiyo turekebishe kasoro hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, kuna ujenzi wa reli ya Mtwara Bamba bay na mchepuko wake ule wa kwenda Liganga na Mchuchuma. Reli hii imesemwa tangu siku nyingi sasa muda umefika tutekeleze, kwa hiyo naomba Serikali yetu sikivu ya awamu ya tano ihakikishe kwamba inatenga fedha za kutosha ili Mradi huu sasa uanze. Ni aibu kwa sababu Mwekezaji wa Kiwanda cha Dangote analeta sasa malighafi ya mkaa toka nchi za nje wakati tuna mkaa wa kutosha toka Mchuchuma ni vizuri reli hii ijengwe ikamilike ili Dangote aanze kutumia rasilimali za humu humu nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna suala la hospitali ya Rufaa ya Kanda ya kusini. Wawekezaji watapenda kujihakikisha masuala ya uhakika wa afya zao. Kwa hiyo, naomba ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Kanda yetu ya Kusini nashukuru ujenzi umeishaanza na kama alivyojibu Naibu Waziri wakati ule wakati anajibu swali la nyongeza alisema kwamba jengo la wagonjwa wa nje linakaribia kukamilika, tunaomba fedha za kutosha zitengwe ili hospitali hiyo Rufaa ikamilike mapema ili isiwe kikwazo kwa Wawekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ili Mji wetu wa Mtwara uweze kuwa kivutio cha Wawekezaji tunaomba barabara ambazo zinaunganisha Wilaya za Mkoa wa Mtwara nazo zijengwe kwa hadhi ya lami, kuna barabara maalum barabara ya uchumi, barabara ya korosho, Mtwara, Nanyamba, Tandahimba, Newala Masasi. Barabara hii inasafirisha asilimia themanini (80%) ya korosho ya Tanzania. Kwa hiyo Barabara hii ni muhimu na lazima zitengwe fedha za kutosha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili utajikita kwenye zao la korosho. Hapa nitazungumzia changamoto zilizopo kwenye Mifuko yetu miwili kwanza kuna Mfuko wa Kuendeleza Zao la Korosho, Mfuko huu unapewa fedha nyingi sana, takribani bilioni 30 kwa mwaka, lakini matumizi ya fedha hizi hayana matokeo yaliyokusudiwa kwa wananchi. Kwa hiyo, naomba tathmini ifanywe, uchunguzi ufanywe na kama kuna kasoro ambazo ziko wazi, basi hatua za mara moja na za makusudi zichukuliwe ili fedha nyingi ambazo zinapekekwa huku, zionekane katika upatikanaji wa pembejeo, pembejeo zipatikane za kutosha, kwa wakati na za bei nafuu na sivyo ilivyo sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu kwamba eneo la uchunguzi ukifika Mtwara ni pamoja na Mfuko huu, umeniambia kwamba una ziara karibuni ya kuja Mtwara. Tembelea Mfuko huu, upate maelezo ya kutosha kwa Watalaam, kwa Management, lakini hata na wanufaika, Wakulima na wale wauzaji wa pembejeo za korosho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili ni kuhusu Bodi ya Korosho, ukisoma ile Sheria ambayo imeanzisha Bodi ya Korosho wana majukumu mengi sana, lakini ile Bodi ya Korosho ufanyakazi wake bado hauna matokeo makubwa tunayotarajia kwa Mkoa wetu wa Mtwara. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mwigulu Waziri wa Kilimo hebu fuatilia kwa ukaribu, utendaji wa Bodi hii na ikiwezekana marekebisho makubwa yafanywe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka nizungumzie suala la umeme vijijini. Mtwara ndiko kwenye Kiwanda cha Uchakataji wa Gesi Madimba na kile Kiwanda cha Msimbati. Hata hivyo, umeme vijijini bado haujawanufaisha vizuri wakazi wa Mkoa huo, kwa hiyo, naomba idadi ya Vijiji iongezwe na sioni kwa nini Serikali isitangaze kwamba tuwe na universal coverage kwa Mkoa wa Mtwara kwamba vijiji vyote vya Mkoa wa Mtwara vipitiwe na mradi huu wa umeme vijijini, kwa sababu wao ndiyo wazalishaji wa ile gesi ambayo ipo Madimba na kule Msimbati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, katika Jimbo langu la Nanyamba nina Vijiji 87, lakini viijiji ambavyo sasa hivi kuna umeme wa uhakika ni vijiji vitatu tu, sasa hapo Wananchi hawatuelewi. Gesi ipo kama kilometa 30 kutoka Nanyamba lakini Vijiji vitatu tu vyenye umeme hatueleweki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa mwisho niende kwenye uboreshaji wa sekta ya Elimu. Kwanza nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa jitihada ambazo inafanya ya kutoa elimu bure. Kwa kweli manufaa yake yanaonekana kwa wananchi wale ambao wanabeza ni kawaida yao kubeza, lakini mwananchi wa kawaida anajua kabisa nini ya maana ya Elimu bure, lakini ningeomba sana Serikali yangu ya Awamu ya Tano sasa hivi tujikite kwenye process teaching and learning process tusijikite kwenye output mambo ya division, GPA hayamsaidii mtoto anapotoka shuleni, tujikite maarifa na ujuzi anaoupata mtoto akiwa darasani.
Tuhakikishe vitabu vinapatikana vya kutosha, Walimu wanalipwa vizuri ili wawe na moral ya kufanya kazi, vilevile Walimu hawa wanajengewa nyumba za kutosha, lakini pia zana za kufundishia zinapatikana za kutosha na maabara zinakamilika na kutumika ipasavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili kuna Kitengo cha Udhibiti wa Ubora wa Elimu, Wakaguzi wa shule. Hiki kitengo hakifanyi kazi yake ipasavyo, vilevile hawapewi rasilimali za kutosha, kule nyuma kulikuwa na mawazo kwamba kitengo hiki nacho kipelekwe TAMISEMI. Kukawa na mawazo kwamba hawawezi kumkagua Mkurugenzi, lakini sikubaliani na hoja hiyo, kwa sababu kwenye Halmashauri kuna Mkaguzi wa ndani bado anamkagua Mkurugenzi na anapeleka ripoti kwake. Kwa hiyo, naomba ili kitengo hiki kiwe fanisi basi wathibiti wa ubora wa shule nao wapelekwe TAMISEMI.
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umemalizika.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanazofanya. Wenye macho wanaziona, endeleeni, tuko pamoja, tunawaunga mkono.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu utajikita katika maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wa Kuendeleza zao la Korosho (CDTF) unapokea fedha nyingi za Export Levy na sh. 10/= kwa kilo zinazochangwa na wakulima. Hata hivyo, Mfuko huu hauna uwazi na sehemu kubwa ya fedha zinatumika kwenye Administrative Expenses badala ya kuendeleza zao la korosho.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Waziri afuatilie matumizi ya fedha za Mfuko huu na kuhakikisha kuwa, kuwe na Menejimenti na Bodi ambayo ni “vibrant” na “aggressive.”
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali sasa iwe na mpango unaotekelezeka wa kubangua korosho na kuacha kuiuza korosho ghafi. Pia Serikali iwe na mkakati wa kuhamasisha ubanguaji mdogo kwa kutumia vikundi vya vijana na akinamama na Viwanda vya zamani vya Korosho vifufuliwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Mtwara una uzalishaji mkubwa wa zao la muhogo. Wakulima wengi wanaacha kulima kwa kukata tamaa ya kukosekana kwa soko la uhakika. Naomba Serikali iweke wazi kuhusu soko la muhogo. Kuna tetesi kuwa China wapo tayari kununua muhogo huu, naomba kauli ya Serikali kuhusu suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Mtwara unafaa kwa kilimo cha pamba, lakini Serikali iliweka zuio kwa kuhofia ugonjwa ambao ungeenea katika maeneo mengi. Je, itaondoa lini zuio hili ili hata Mtwara iendelee na mipango yake ya kuendeleza zao la pamba?
Mheshimiwa Naibu Spika, nawasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kumpongeza Waziri, Mheshimiwa Profesa Ndalichako na Naibu wake Mheshimiwa Stella Manyanya kwa kazi nzuri zinazofanywa. Nawapongeza pia kwa kushirikiana na watendaji, wameandaa taarifa ambayo inaleta matumaini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kuwa aspect ya quantity tumefanikiwa sana na sasa tujielekeze kwenye aspect ya quality. Serikali iwekeze kwenye kuboresha namna tendo la kujifunza na ujifunzaji linavyotaka kwa kuangalia upya idadi ya wanafunzi kwa elimu ya msingi kwani wanafunzi 45 ni wengi ibadilike iwe 35; Walimu wapewe motisha ili waongeze morali; vifaa na vitabu vya kufundishia vipatikane na kuongeza idadi ya Walimu wanaopata mafunzo kazini kwa kutumia vituo vya walimu vilivyopo TRCS.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kitengo cha Udhibiti wa Ubora wa Shule (Wakaguzi wa Shule). Kitengo hiki kipewe fedha za kutosha ili waweze kukagua shule nyingi. Wadhibiti ubora wapewe mafunzo ya mara kwa mara na nyenzo za kufanyia kazi. Vilevile idadi ya shule zimeongezeka muundo wa Wadhibiti Ubora wa Elimu urekebishwe badala ya kuwa kwenye kanda wawepo kimkoa na kuwe na mawasiliano na Katibu Tawala wa Mkoa (RAS).
NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT)
172
Mheshimiwa Mwenyekiti, ada elekezi. Nashauri Serikali ijielekeze kwenye hoja za wananchi wengi, tuboreshe shule zetu na wananchi wataacha kupeleka watoto shule binafsi. Hali hiyo ikifikiwa wamiliki wa shule watapunguza ada kwa kufuata nguvu ya soko. Serikali ijikite katika kuboresha elimu katika ngazi zote na si vinginevyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hoja ya Wizara hii ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Nitaanza kuchangia kwa kuzungumzia hoja ya Bandari ya Mtwara na kama walivyosema wenzangu waliopita kwenye masuala ya Kitaifa, basi itikadi tuweke pembeni. Umuhimu wa bandari ya Mtwara umeelezewa vizuri sana na hotuba ya Kambi ya Upinzani ukurasa wa 26; zimetajwa sababu 12, lakini na wewe Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa 84 umeelezea umuhimu wa Bandari ya Mtwara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa masikitiko makubwa naomba ninukuu kauli za utatanishi ambazo zipo kwenye hotuba hii. Naomba kunukuu, ukurasa wa 84 unasema kwamba, “Bunge lako lilitaarifiwa juu ya kukamilika kwa majadiliano baina ya Mamlaka ya Bandari na mkandarasi wa mradi wa kupanua Bandari ya Mtwara kwa kujenga ghati mpya nne kwa utaratibu wa sanifu, jenga na gharamia,” mwisho wa kunukuu. Lakini hapo chini kuna sentensi ambayo ni ya utatanishi inasema; “napenda kuliarifu tena Bunge lako tukufu kuwa, majadiliano hayo sasa hayakufanikiwa”; kule juu tuliambiwa yamekamilika, sasa tunaambiwa kwamba hayakufanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajikaanga sisi wenyewe, uwekezaji tukiwekeza kwenye Bandari ya Mtwara, hatuisaidii Mtwara tu tunaisaidia Tanzania, sasa hivi wakati wa msimu wa korosho meli ya Dangote ikiingia Bandari ya Mtwara, basi korosho haziwezi kusafirishwa kwa sababu Bandari ya Mtwara inakuwa haina uwezo wa kuudumia meli nyingi. Na tuliaminishwa kwamba, ghati nne zinajengwa na tarehe 26 Februari, 2016 Mheshimiwa Waziri Mkuu alitembelea bandari hii akaulizia kwamba, mkandarasi anaendelaje? Maana nasikia kwamba anazungushwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, alijibiwa kwamba anaendelea vizuri na hakuna tatizo, lakini leo hii tunaambiwa kwamba majadiliano hayakufanikiwa.
Mimi niungane na waliosema kwamba TPA kuna matatizo, Mamlaka ya Bandari kuna matatizo. Kwa hiyo, naomba Waziri utakapokuja kufanya majumuisho utuambie nini kilijiri, nini kilitokea, kwa sababu, kampuni hii ni kampuni kubwa, ni kampuni ya Hyundai ya Japan, haiwezi kuacha mradi huu kwa sababu nyepesi tu ambayo imetajwa hapa. Maana sababu yenyewe imeelezwa kwamba mkandarasi kwa sasa hawezi kugharamia mradi badala yake aikutanishe mamlaka na benki itakayotoa mkopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kampuni ya Hyundai haiwezi kufanya jambo hili inawezekana kuna uzembe ulifanyika na mtu fulani. Kwa hiyo, naomba Waziri utakapokuja utuambie nini kilijiri mpaka mradi huu mkubwa ukaahirishwa tena kwa dakika za mwisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi niungane na wenzangu kuzungumzia kwamba, uwekezaji kwa Kanda ya Kusini haufanywi kwa kiasi kinachotakiwa; nimezungumzia Bandari ya Mtwara, lakini unapozungumzia eneo maalum la uwekezaji tunazungumzia Mtwara na Lindi, lakini hata Bandari ya Lindi…
MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara kwa matayarisho ya hotuba nzuri yenye kutoa mwelekeo wa kutafakari kwa mabadiliko ya kweli kwa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri yafuatayo:-
(i) Kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya kukarabati ofisi zetu za Ubalozi. Baadhi ya ofisi zetu hazijakarabatiwa kwa muda mrefu.
(ii) Pia kuwe na uratibu mzuri wa wanafunzi wanaofanya mafunzo mbalimbali katika nchi mbalimbali ili Balozi zetu ziweze kutoa maelezo ya kina pindi wanafunzi hao wanapopatwa na madhila/matatizo wakiwa huko.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nianze mchango wangu kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi nzuri wanazozifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nichukue nafasi hii niwapongeze Mawaziri wote. Wahenga wanasema nyota njema huonekana asubuhi, mmeanza vizuri, msikate tamaa, songeni mbele, tuko pamoja. Pia nichukue nafasi hii kuwapongeza Mawaziri ambao wametoa hoja hii leo, Mheshimiwa Simbachawene, Mheshimiwa Kairuki na Mheshimiwa Jafo, hongereni sana. Kabla sijaendelea na mchango wangu niseme kwamba naunga mkono hoja zote mbili kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa na maeneo yafuatayo katika mchango wangu. Kwanza nianze na maeneo mapya ya utawala. Hata kama Mheshimiwa Simbachawene wakati anajibu swali moja alituambia kwamba Waheshimiwa Wabunge tuwe wapole kuhusu maeneo mapya ya utawala, sisi Waheshimiwa Wabunge tutaendelea kuomba kwa sababu maeneo mengine tumeahidi na maeneo mengine kuna umuhimu huo wa kuanzisha maeneo mapya ya utawala. Hii haifuti jukumu la Serikali kufanya maandalizi ya kutosha, hapa suala ni Serikali kufanya maandalizi ya kutosha kabla ya kuanza kutangaza maeneo hayo ya utawala. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwangu tuna Halmashauri ya Mji wa Nanyamba, imeanzishwa hivi karibuni, ni miongoni mwa Halmashauri ambazo kama walivyosema Wabunge wengine hakukuwa na maandalizi ya kutosha ili Halmashauri hiyo ianze. Mkurugenzi na watendaji wake wamejibanza tu kwenye ofisi ambayo zamani ilikuwa ya Mtendaji wa Kata. Kwenye bajeti ya mwaka 2015/2016, hii ambayo inaendelea, zilitengwa fedha shilingi milioni 800 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi mpya ya Mkurugenzi lakini hadi tarehe ya leo hata shilingi haijapokelewa kwa hiyo ujenzi huo haujaanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile si suala tu la miundombinu kuna suala la wafanyakazi. Kwenye Halamshauri ya Mji wa Nanyamba tuna upungufu wa watumishi 456 lakini tuna idara na vitengo sita ambavyo havina Wakuu wa Idara na kitengo kimojawapo ni Idara ya Maji ambayo ni muhimu na jimboni kwangu kuna tatizo la maji lakini idara hiyo inaongozwa na pump attendant. Sasa hebu fikiria tunapotengeneza mpango wetu wa kuivusha Nanyamba ipate maji kwa asilimia 85 mpago huo utasimamiwa na nani kama hiyo idara kwa sasa hivi inaongozwa na pump attendant? Kwa hiyo, naomba yale ambayo yanawezekana yafanywe haraka. Najua kuna tatizo la kibajeti kuhusu ujenzi wa ofisi ya utawala lakini hili la watumishi inawezekana kabisa kuwahamisha watumishi kutoka maeneo mengine na kupelekwa Halmashauri ya Mji wa Nanyamba.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili, Halmashauri hizi mpya huwa hazijaunganishwa katika mifumo iliyopo. Kuna mfumo wa EPICAR ambao upo kwenye Halmashauri zetu, Halmashauri ya Nanyamba bado haujasimikwa lakini kuna mfumo wa LAWSON ambao nao vilevile katika Halmshauri yetu ya Nanyamba bado haujasimikwa. Kwa hiyo, naomba sana ofisi ya TAMISEMI ishughulikie changamoto hizi ili Halmashauri ya Nanyamba iweze kwenda kama inavyokusudiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu nyingine ni kuhusu uboreshaji wa huduma za jamii na hapa nitajikita sana katika huduma ya afya. Kama nilivyosema Halmashauri yangu ya Mji wa Nanyamba ni mpya ina changamoto nyingi na naomba TAMISEMI i-take note na iangalie jinsi ya kushughulikia huduma hizi katika bajeti ya 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Halmashauri hii haina Hospitali ya Wilaya lakini pili hakuna kituo hata kimoja cha afya. Kati ya vijiji 87 tuna zahanati 24 tu kwa hiyo utaona changamoto kubwa tuliyonayo katika utoaji wa huduma za kijamii. Nafikiri TAMISEMI itatuunga mkono kwa sababu kwenye bajeti yetu kwenye own source tumetenga fedha kidogo kwa ajili ya uanzishwaji wa ujenzi wa vituo vya afya na ulipaji wa fidia eneo la ujenzi wa Hospitali ya Wilaya. Ni matarajio yangu kwamba TAMISEMI itatuunga mkono ili kutatua changamoto hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu mwingine utajikita kwenye uendeshaji wa Halmashauri za Wilaya. Sikuona kwenye kitabu alichowasilisha Waziri suala la kuwajengea uwezo Waheshimiwa Madiwani. Madiwani wetu wana majukumu mazito ya kuzisimamia Halmashauri lakini Madiwani hawa wanahitaji kujengewa uwezo. Sijaona kwenye kitabu cha Waziri, kwa hiyo, naomba sana TAMISEMI ilichukulie suala hili kwa uzito unaohitajika ili Madiwani wetu wajengewe uwezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa umuhimu wa kipekee Wenyeviti na Mameya hawa wanasimamia uendeshaji wa shughuli za kila za Halmashauri. Kwa hiyo, wanahitaji taaluma mbalimbali kwa mfano uendeshaji vikao na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo. Tunacho chuo chetu cha Serikali za Mitaa Hombolo tunaweza tukakitumia kwa ajili ya kutoa mafunzo hayo kwa Waheshimiwa Madiwani.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile imefika wakati tujiulize kwenye Kanuni zetu za Kudumu za Uundaji wa Halmashauri, je, hizi kanuni zetu ambazo tumejiwekea hasa kuhusu uendeshaji wa vikao vya Halmashauri vikao hivyo vinakuwa na tija? Tufikirie kwenye Halmashauri kuna sekta zote maji, elimu, afya na kila kitu lakini Baraza la Madiwani wanafanya kazi kwa muda wa siku mbili, siku ya kwanza wanapokea taarifa toka kwenye kata, siku ya pili wanaendesha hilo Baraza wanazungumzia maji, elimu, afya na mambo mengine kwa muda wa saa nne tena Diwani mwingine yupo kwenye kikao anapigiwa simu kwamba gari ya kijiji inaondoka kwa hiyo anaomba aondoke mapema ili akawahi hiyo gari ya kijijini kwao. Muda umefika sasa hivi tufikirie kuendesha Halmashauri zetu kwa session kama tunavyofanya session za Bunge hata kama siyo muda mrefu, lakini wachukue siku tatu au nne waweze kujadili kwa kina maendeleo ya Halmashauri yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni la maji katika Jimbo langu. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Maji Engineer Kamwele kwa sababu nilimwambia tatizo langu na akafanya ziara amejionea. Kwa kweli Jimbo la Nanyamba kuna shida ya maji, ni takribani asilimia 35 tu ya wakazi wake wanapata maji ya uhakika. Sasa maji ni maendeleo, ni vigumu kuzungumzia maendeleo wakati huna maji kwa sababu akina mama wengi wanahangaika kutafuta maji badala ya kushughulika na shughuli za maendeleo lakini vilevile magonjwa mengi yanasababishwa na kutopatikana kwa maji safi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana kwenye bajeti hii upatikane ufumbuzi. Ufumbuzi wenyewe upo kwa sababu tatizo la maji Nanyamba ni miundombinu lakini tunavyo vyanzo vya uhakika kuna Mto Ruvuma, kuna mradi wa muda mrefu wa maji wa Makonde lakini tuna Bwawa la Kitele na miradi 18 ambayo ilifadhiliwa na AMREF ambayo ikikarabatiwa inaweza kupunguza kiwango cha watu wengi wanaokosa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie mchango wangu kuzungumzia kuhusu sekta ya elimu. Niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuja na Sera ya Elimu Bure na hii imeongeza udahili katika taasisi zetu za elimu ya msingi, sekondari na vyuo lakini bado kuna changamoto. Kuna changamoto kuhusu miundombinu, madarasa na nyumba za Walimu kwa sababu mpango wa MMES na MMEM ulijenga miundombinu lakini sasa hivi kuna ongezeko la wanafunzi na walimu. Kwa hiyo, inahitajika tutenge fedha za kutosha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu na madarasa mapya, lakini kuna madarasa ya MMEM na MMES ambayo tulijenga mwaka 2002 sasa yanahitaji ukarabati mkubwa lazima fedha za kutosha zitengwe kwa ajili ya ukarabati huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba sana TAMISEMI na Wizara ya Elimu zijikite katika kufuatilia kile kinachofanyika darasani ili walimu wapewe motisha na vilevile tusiangalie matokeo…
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, umeme wa REA katika Jimbo langu lenye vijiji 87 na mitaa tisa mradi wa REA II umehusisha vijiji vitatu tu. Hii inakuwa ngumu kujibu maswali ya wananchi. Nashauri kuwa phase III ihusishe vijiji vyote kama Mheshimiwa Waziri alivyoahidi wakati nimempelekea hoja hii kwa mapendekezo ya vijiji vitakavyohusika kwenye REA phase III vijiji au mitaa ifuatayo haijawekwa.
Mitaa ya Nanyamba Mjini, Natoto, Chitondela, Chikwaya, Mibabo, Vijiji Miule, Mtimbwilimbwi, Shaba, Mbambakofi, Hinju Mtiniko, Maili, Maranje, Ngorongoro, Misufini, Kiromba, Kiyanga, Mayembe Juu, Mayembe Chini na Mchanje.
Mradi wa REA Mtwara Manispaa eneo la Ufukoni, Mbaye na Mji mwema ambao phase II ulitakiwa kukamilika mwezi Juni unasuasua, hivyo usimamiwe ili ukamilike kwa wakati.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwapongeza Waziri na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii kwa kazi nzuri wazozifanya. Aidha, nawapongeza watendaji wa Wizara hii kwa maandalizi mazuri ya bajeti. Pamoja na pongezi hizi nashauri yafuatayo:-
(i) Wakati umefika wa kuboresha utalii kwa Mikoa ya Kusini (Mtwara na Lindi) kwa kuwekeza fedha za kutosha kwenye miundombinu itakayowezesha watalii kufika maeneo hayo.
(ii) Mbuga za wanyama na hifadhi zingine zitangazwe kwa uwiano sawa badala ya kutangaza zile za Arusha na Mara.
(iii) Wilayani Newala kuna Shimo la Mungu na lina maajabu ya aina yake. Naomba Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri waende wakajionee ili waweze kuchukua hatua ya kuweza kukiendeleza kivutio hiki.
(iv) Mto Ruvuma una pwani yenye kilometa 156 ambazo zinafaa kwa ufugaji wa mamba kwa ajili ya vivutio, tutumie beach hii ipasavyo.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Na mimi nianze kwa kuunga mkono hoja zote mbili ile ya Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji na ile ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utajielekeza kwenye masuala mawili, suala la kwanza ni la korosho. Nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu na Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Dkt. Tizeba na Naibu wake Mheshimiwa Ole-Nasha kwa hatua walizochukua kwa tasnia ya korosho katika msimu huu wa korosho. Kuna mambo matano muhimu wametufanyia sisi wakulima wa korosho. Kwanza, walikuja Mtwara kushughulikia wezi waliohusika na ubadhirifu wa msimu wa mwaka 2014/2015 na walianza na Wilaya ya Masasi kukawa na changamoto kwamba hawakupewa support lakini hawakukata tamaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili baada ya kupata malalamiko yetu, Mheshimiwa Tizeba na timu yake waliamua kumuondoa Mrajisi wa Vyama vya Ushirika. Kiongozi huyu alikuwa ana viongozi wa AMCOS ambao walihusika na wizi na ubadhirifu wa msimu uliopita. Kwa hiyo, kwa ujasiri wake aliweza kumuondoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Wizara hii katika kipindi kifupi cha msimu baada ya kuonekana kuna dosari ilithubutu kuvunja Bodi ya Korosho na kuisuka upya. Bodi hiyo mpya imeanza kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa na matunda yake tumeona msimu huu kwamba korosho imeuzwa hadi shilingi 4,000 kwa kilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, si hivyo tu baada ya kuona mabilioni mengi ya fedha yanapelekwa kwenye Mfuko wa Kuendeleza Zao la Korosho na hakuna kinachofanyika, Wizara hii chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Tizeba waliamua kusitisha shughuli zote za mfuko ule na shughuli zake zote kufanywa na Bodi ya Korosho. Hii sasa itasaidia kujipanga upya na kutekeleza majukumu ambayo kimsingi kwa muda wa miaka mingi walikuwa wanapata fedha nyingi lakini hawatekelezi chochote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini si hivyo tu, Wizara sasa imethubutu kuendesha mchakato wa kuhakikisha kiuatilifu muhimu au pembejeo muhimu kwenye zao la korosho sulphur dust kuagizwa moja kwa moja viwandani badala ya kuchukua kwa mawakala. Huu ni ujasiri mkubwa, kuna maneno mengi yamesemwa kwamba Waziri ana-interest na makampuni fulani lakini mti wenye matunda lazima upigwe mawe na kwenye vita ya mawe ya usiku ukiona mtu analalamika basi amegongwa jiwe. Kwa hiyo, hawa wanaolalamika kuna kitu walikuwa wanakipata kwenye mfumo wa ubadhirifu wa ununuzi wa hizo pembejeo, Mheshimiwa Waziri endelea na sisi wana Mtwara tunakuombea usiku na mchana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Wizara ina kazi kubwa tatu sasa hivi. Kazi ya kwanza wasimamie ujenzi wa viwanda vya korosho kwa sababu huu Mfuko wa Kuendeleza Zao la Korosho unapata zaidi ya shilingi bilioni 36 au 37 za export levy kwenye zao la korosho, lakini kwa miaka mingi hakuna kilichofanywa. Kwa hiyo, matarajio yangu sasa baada ya kazi hii kusimamiwa na Bodi ya Korosho tunaona sasa ujenzi wa viwanda vya korosho unaanza mkoani Mtwara na fedha ipo kwenye mfuko huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili kuna kiporo ambacho kimebaki. Tulikuwa tunasubiri taarifa ya ukaguzi ya COASCO. COASCO amekuja na taarifa kwamba msimu wa mwaka 2014/2015 kuna fedha zaidi ya shilingi bilioni sita hazikufika kwa wakulima. Taarifa ya TAKUKURU inaonyesha shilingi bilioni 30, taarifa ya Bodi ilionyesha shilingi bilioni 16; lakini juzi COASCO wamewasilisha taarifa kwamba kuna fedha shilingi bilioni sita zilitakiwa ziende kwa wakulima wa korosho lakini hazikwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni matarajio yangu sasa Wizara itaendelea na moto ule ule isimamie haki ya wakulima ili waliohusika na ubadhirifu huu hata kama mkubwa wa ngazi yoyote awajibishwe ili fedha hizi ziende kwa wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna AMCOS 34 kwenye taarifa ile ya COASCO inasema hazikukaguliwa, kwamba hakuna kitu kilichoandikwa kwa msimu mzima. Uzembe huu hapa unalindwa na Maafisa Ushirika. Kwa hiyo, ni matarajio yangu kwamba Mheshimiwa Waziri chini ya usimamizi wako na Mrajisi mpya aliyeteuliwa …
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA:Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nami niungane na Wabunge wenzangu kuwapongeza Mawaziri wa Wizara hii, Mheshimiwa Lukuvi na Naibu Waziri Mheshimiwa Mabula kwa kazi nzuri wanazozifanya na kwa kweli wanastahili pongezi, tunawapongeza sana. Pia nimpongeze Ndugu yangu Katibu Mkuu Dkt. Yamungu Kayandabila na Naibu Katibu Mkuu Dkt. Kusiluka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunashuhudia mabadiliko makubwa sana kwenye Wizara hii. Zamani tulikuwa na urasimu mkubwa sana wa kutoa huduma. Ukifika pale Wizarani sasa hivi unaona kabisa mabadiliko ambayo yamefanywa. Kwanza kuna sehemu imeandaliwa kwa ajili ya watu kupewa huduma na eneo lile sehemu kubwa tatizo la mteja linashughulikiwa kidigitali, kwa hiyo tunapongeza sana Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tunaona jinsi Wizara hii inavyozingatia ugatuaji. Wamepunguza shughuli nyingi makao makuu wamepeleka kwenye ngazi ya kanda na ugatuaji kwenye ngazi ya kanda si wa madaraka tu wamepeleka na fedha na rasilimali watu, kwa hiyo nawapongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kwenye Wizara hii sasa tunaona jitihada ambazo zinafanywa kuziwezesha Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Mheshimiwa Waziri amesema nini atakifanya kuziwezesha mamlaka ya Serikali za Mitaa waweze kuandaa hati wao wenyewe. Mheshimiwa Waziri tunampongeza na tunamwombea kwamba awe na nguvu zaidi na hekima ili aweze kutuletea mazuri zaidi ya hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo nina mchango ufuatao mwingine. Kwanza kuhusu suala la usimamizi wa ardhi na huduma za upangaji miji na vijiji. Suala hili ni mtambuka na suala hili ni muhimu. Pamoja na mazuri yote yanayofanywa katika ngazi ya Wizara bila kuwa na watendaji wa kutosha katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa haya mazuri yote ambayo yamekuwa yameandaliwa na Wizara kule chini hayataonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto kubwa ya watumishi wa sekta hii kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Kama nilivyosema suala hili mtambuka na Mamlaka ya Serikali za Mitaa ina nafasi kubwa sana katika utekelezaji wa yale ambayo yamepangwa Wizarani. Ili shughuli ya ardhi ishughulikiwe vizuri kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa ina vitengo vitano, lazima kuwe na mthamini (valuer), lazima kuwe na mpima (surveyor), lazima kuwe na afisa ardhi vile vile kunahitajika mrasimu ramani na town planner. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya watumishi katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa ni ya kutisha. Kwenye jimbo langu la Nanyamba kwenye hao wote walioorodheshwa hapa hawapo. Kuna surveyor msaidizi tu ndiye anayeendesha ile idara. Sasa utakuta yote yanayoamuliwa na baraza huyu mtu peke yake hawezi kutekeleza na mwezi Agosti anastaafu. Kwa hiyo, akistaafu mwezi Agosti ile ofisi tunafunga kabisa. Kwa hiyo nashauri, huko nyuma Serikali iliona tatizo la wahasibu kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Wizara ya Fedha ikaomba kibali cha jumla ikaajiri wahasibu wengi ikapeleka kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa, kila Mamlaka ya Serikali za Mitaa ilipelekewa wahasibu watano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba Wizara ya Ardhi iombe kibali cha jumla cha kuajiri watumishi watakaopelekwa kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa ili kibali hiki kikipatikana waajiriwe vijana ili wapelekwe kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Vijana wasomi wapo mitaani, kwa hiyo naomba Mheshimiwa Waziri aombe kibali cha jumla ili watumishi wapatikane, ili haya mazuri ambayo anayafanya kwenye ngazi ya Wizara yakafanywe kule kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Tusipofanya hivi itakuwa kule juu mnafanya vizuri lakini huku chini kuna malalamiko mengi na kama anavyoona kwamba gharama za watu binafsi au kampuni binafsi (private sector) bado ni za juu na wananchi wetu bado hawawezi kuwatumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili unahusu urejeshaji wa fedha za kodi ya matumizi ya ardhi (retention) kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya LAAC, hoja hii imesimama kwa muda mrefu sana. Nina taarifa hapa ya CAG ya 2015/2016, CAG anasema vizuri kabisa kwamba asilimia 80 ya makusanyo ya kodi ya matumizi ya ardhi hayakurudishwa kwa halmashauri husika shilingi bilioni 6.7. Taarifa ya CAG inasema hivyo, na CAG ali-test kwenye halmashauri 71 akakuta biloni 6.7 hazijarejeshwa. Je, kwenye halmashauri zilizokaguliwa 171 kuna shilingi ngapi ambazo hazijarejeshwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba Mheshimiwa Waziri afanye jitihadi za makusudi kwa sababu ukiangalia ile Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa ya Mwaka 1982 inasema miongoni mwa vyanzo vya mapato vya halmashauri ni pamoja na kodi hii hapa. Vile vile kuna waraka ulitolewa na TAMISEMI kuhusu hiyo asilimia 30.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kama kuna maelekezo mapya, kama hizi fedha hazitolewi basi waraka utolewe ili kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa wasiweke kama vyanzo vya mapato. Kwa sababu sasa hivi kuna maelezo mengi, ukiuliza unaambiwa kwamba Wizara haipewi fedha kutoka Hazina, lakini pili kuna maelezo mengine yalitoka katikati pale kwamba Mamlaka ya Serikali za Mitaa haziwezi kupewa mpaka ilete mpango wa matumizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inashangaza kwa sababu Mamlaka ya Serikali za Mitaa wakati inapoandaa bajeti kuna kitu kinaitwa Medium Term Expenditure Frame Work (MTEF) inaonyesha activities zote ambazo zitafanywa na council kwa mwaka husika na fedha ambazo zitahusika. Kwa hiyo, sioni sababu ya kuwaambia Mamlaka ya Serikali za Mitaa walete tena mpango wa matumizi wakati kuna MTEF wa halmashauri husika. Kwa hiyo naomba hizi fedha wapewe ili waweze kutekeleza majukumu yao ambayo yapo kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la CDA. Nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa maamuzi mazito aliyoyafanya ya kuivunja CDA, lakini pia kufutwa kwa hati miliki ya CDA na kupeleka majukumu yake kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo awali nikiwa mtumishi niliwahi kufanya kazi Manispaa ya Dodoma na Mheshimiwa Waziri wakati huo alikuwa Mkuu wa Mkoa wangu, aliona jinsi ambavyo CDA ilikuwa inaendeshwa kwa ubabe, ilikuwa inatengeneza kero. Tulikuwa tunatafuta eneo la kujenga sekondari lakini kuna siku alituita Mheshimiwa Lukuvi ofisini kwake tukakaa masaa matano, CDA hawataki kutoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto wa Dodoma sasa hivi wanahangaika wanakwenda shule ya Mnadani, Shule ya Lukundo, ile Shule ya Sechelela mbali kabisa na nje ya Dodoma. Kata ya Kilimani hii hapa Uzunguni ikaamuliwa kwamba shule ya sekondari ya kata ijengwe Ntyuka watoto wale wanaumia kila siku kupanda ule mlima lakini kwa ubabe wa CDA kwamba hawawezi kutoa lile eneo na maeneo ambayo sisi tuliona kama Manispaa kwamba ijengwe sekondari wamepewa watu wengine tu wamejenga mahoteli na shughuli zingine. Kwa hiyo, namshukuru Mheshimiwa Rais kwa uamuzi wake wa kuivunja CDA na nashauri sasa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma ichukue majukumu hayo mazito na iyatekeleze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nina ushauri wa aina mbili kwa Wizara. Kwanza wale watumishi wa CDA wote wasirundikwe Manispaa, watakuwa na subortage kwa Mkurugenzi wa Manispaa ili aonekane kwamba hafai.

Naomba watumishi wale wasambazwe kwenye Mamlaka zingine za Serikali za Mitaa na cream iletwe Dodoma ili waweze kuchapa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini na sasa hivi Mamlaka ya Manispaa ya Dodoma iwezeshwe kutekeleza yale majukumu kwa sababu tukiwalaumu tu kwamba hawawezi wale kwa muda mrefu hawajafanya shughuli za ardhi, shughuli hizi walikuwa wanafanya CDA, kuna madeni, kuna viwanja ambavyo hawajapewa wenyewe waliolipia. Kwa hiyo shughuli hii sasa itafanywa na Manispaa. Kwa hiyo lazima tuwape muda manispaa waweze kuchukua majukumu hayo; tuwawezeshe, tusiwalaumu mapema ili waweze kutekeleza majukumu haya mazito kwa urahisi na hatimaye tuweze kuendeleza makao makuu ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kuunga mkono hoja na nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi lakini pia nianze kwa kuwapongeza Mawaziri wote wawili kwa hotuba nzuri ambayo wamewasilisha nikianza na kaka yangu Mheshimiwa Mkuchika vilevile na Mheshimiwa Jafo na timu yake wakiwepo na Naibu Waziri Mheshimiwa Kakunda na Mheshimiwa Kandege, hongereni sana kwa kazi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niwapongeze Watendaji Wakuu, kuna Dkt. Ndumbaro wa Utumishi lakini pia Kaka yetu Injinia Iyombe wa TAMISEMI; Dkt. Chaula pia na kaka yangu Nzunda, Naibu Makatibu Wakuu wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, hongereni sana kwa kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza kwa pongezi kwa sababu asiyeshukuru kwa moja hata akipewa tano hatashukuru. Niishukuru TAMISEMI kwa uratibu mzuri wa ujenzi wa vituo vya afya na hospitali za wilaya. Wote mtakuwa mashahidi katika hotuba zilizopita tulikuwa tunauliza Ilani ya Chama cha Mapinduzi inasema kila kijiji kutakuwa na zahanati, kila kata kutakuwa na kituo cha afya, lakini mtekelezaji ni nani? Wizara ya Afya hawakuwa na mpango na TAMISEMI hawakuwa na mpango. Leo ukienda ukurasa wa 25 utaona mpango wa ujenzi wa vituo vya afya, hongereni sana TAMISEMI. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna vituo 208 ambavyo vinajengwa na vinakarabatiwa na mwezi Aprili vitajengwa vingine 25. Haya ni mapinduzi makubwa na wasikate tamaa kwa wale ambao wanawabeza kwamba watachukua sijui miaka mia tano kukamilisha nchi nzima, hiyo siyo sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mipango ya maendeleo tunapanga kulingana na rasilimali zilizopo, mwaka huu wameweka fedha ya vituo 208, mwakani unaweza kuweka fedha ya vituo 1,000. Kwa hiyo, siyo sahihi kwamba kwa idadi ya vituo vya afya vilivyopo nchini tutakarabati kwa muda mrefu inategemea na upatikanaji wa rasilimali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanya hivi hata elimu ya msingi, PEDP tukajenga madarasa, SEDP tukajenga madarasa na tukajenga maabara. Kwa hiyo, wasikate tamaa waendeleze kuweka mipango mizuri, watafute fedha kwa wafadhili ili tuongeze kasi. Tunatarajia bajeti ya mwakani tutaona ukarabati na ujenzi wa vituo zaidi ya 1,000 ili wale wanaowabeza wakose cha kusema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru kaka yangu Mheshimiwa Jafo, Mheshimiwa Kandege na Mheshimiwa Kakunda wote mmefika Jimbo la Nanyamba na waliona hali halisi. Walipofika kulikuwa hakuna kituo hata kimoja cha afya na tukawaambia mikakati yetu kwamba hatusubiri fedha za Serikali, tunaanza kwa fedha zetu za korosho. Wakati tumeanza ujenzi wa OPD pale Dinyecha, namshukuru sana Mheshimiwa kaka yangu Jafo kwa sababu ametupa fedha shilingi bilioni moja na milioni mia nne kwa ajili ya ukarabati wa vituo vitatu vya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kwa sababu tuliona kwamba hakuna kituo cha kukarabati tukaanza na ujenzi, tumesimamia vizuri na yale majengo ambayo walisema tujenge tumeongeza mengine. Mheshimiwa Kakunda atakuwa shahidi pale Dinyecha walituambia tujenge wodi ya akinamama sisi tumejenga wodi mbili, tumejenga wodi ya akinamama na wodi ya jumla lakini tumejenga na OPD kwa fedha za korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, pamoja na fedha za TAMISEMI lakini na sisi kwenye mipango yetu tumeongeza fedha. Pale Majengo wametupa shilingi milioni mia nne na sisi tumeongeza shilingi milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa OPD. Nimshukuru vilevile ametupa ambulance, Mheshimiwa Jafo amefanya kitu kikubwa sana kwa mara ya kwanza ambulance imeingia Halmashauri ya Mji wa Nanyamba, tunamshukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, si hivyo tu Mheshimiwa Waziri amesoma Halmashauri ya Mji wa Nanyamba ni miongoni mwa halmashauri zitakazopata fedha za ujenzi wa hospitali ya wilaya. Kwa hiyo, namshukuru na nampongeza kwa sababu ameangalia mahitaji halisi ya halmashauri yetu na jinsi sisi wenyewe tunavyotumia rasilimali chache tulizonazo kuwekeza katika afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende sasa kwenye suala la Madiwani. Ukisoma Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Toleo la mwaka 1977, Ibara ya 145 na 146 inazungumzia kuanzishwa kwa majukumu ya Serikali za Mitaa. Madhumuni ya kuanzisha Serikali hizi ni kupeleka madaraka kwa wananchi na kuna Diwani ambaye ni mwakilishi wa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie sasa package ya Madiwani hawa. Madiwani hawa wana majukumu mengi, wana kazi nyingi lakini bado package yao hairidhishi. Madiwani wana malalamiko, wana matumaini makubwa sana na Mheshimiwa Jafo, awasikilize Madiwani hawa. Aunde Tume afanye tathmini ya majukumu ya Madiwani aangalie ukubwa wao wa kazi na si vibaya sasa kupitia posho zao na maslahi yao kwa sababu posho yao ambayo wanayo sasa hivi ina zaidi ya miaka sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tusiwajibu majibu mepesi mepesi kwamba uwe na kazi nyingine au uwe na shughuli nyingine ndiyo uombe udiwani, Diwani ana majukumu mengi, kumlipa shilingi laki tatu kwa mwezi na Diwani huyu unategemea asimamie miradi ya maendeleo, asimamie fedha za halmashauri lakini kwa mujibu wa sheria zetu Baraza la Madiwani ndiyo mamlaka ya nidhamu kwa watumishi wa halmashauri, kwa posho ya shilingi laki tatu uhukumu kesi ya Mkuu wa Idara ambaye ana mshahara wake ni shilingi milioni mbili ni rahisi kuwa corrupted.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutengeneze vizuri package ya Madiwani ili wafanye kazi kwa uaminifu, kwa uadilifu ili kusukuma maendeleo ya halmashauri zetu. Kama ninavyosema Mheshimiwa Jafo wana matarajio makubwa sana na yeye, awasikilize, atengeneze timu ikawasikilize, afanye tathmini tuje na kitu kipya kwa Madiwani wetu kama anavyofanya reform katika maeneo mengine pale TAMISEMI na mimi nina matarajio na Mheshimiwa Waziri na najua hatawaangusha Madiwani wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la tatu, kuna fedha zinaitwa payment for result ambazo zinakwenda kwenye mamlaka zetu za Serikali za Mitaa na zinakwenda kwenye sekta zote za elimu, afya nafikiri na maji. Fedha hizi TAMISEMI sijaona kwenye kitabu chao, nikawa najiuliza fedha hizi wanatoa TAMISEMI au Wizara ya Elimu. Kama zipo Wizara ya Elimu naomba nishauri fedha hizi ziende TAMISEMI ili Wizara ya Elimu ibaki na mambo ya sera tu. Hawa ambao wanakwenda field na TAMISEMI sasa hivi wana kitengo kizuri cha ufuatiliaji wa fedha kwenye Serikali za Mitaa na Mkoani, hizi fedha ziende kwao lakini vilevile zionekane kwenye vitabu. Wenzao wa Wizara ya Maji mwaka jana walionesha kabisa fedha za OC na fedha za P for R.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wao pia Wizara ya TAMISEMI na Wizara ya Elimu waige wanavyofanya Wizara ya Maji, inaonekana kabisa na zile key performance indicators zionekane kwamba halmashauri inapata fedha nyingi kwa sababu ipi. Wizara ya Maji walitengeneza vizuri kabisa na hata sasa hivi wameshatoa matokeo ya halmashauri na TAMISEMI waige kitu kama hicho ili tusije tukawa tuna hisia tu kwamba zimepelekwa nyingi Nanyamba kwa sababu Mheshimiwa Kandege na Chikota ni marafiki, hapana. Tupeleke kwa vigezo vilivyowekwa na vya wazi na halmashauri ziwe zimeshindanishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la TARURA. Nami niungane na wenzangu kuwapongeza TAMISEMI kwa kuanzisha TARURA na TARURA inafanya vizuri. Ningeomba Waheshimiwa Wabunge tuipe muda TARURA tusianze kuwalaumu, huwezi kumlaumu mtoto wa mwaka mmoja ukasema hawezi kutembea. TARURA imeanzishwa na imeanza kufanya kazi vizuri, tuipe muda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, TARURA wana changamoto ya rasilimali fedha, watumishi na usafiri. Kwa hiyo, Mheshimiwa Jafo natarajia kwa kipindi hiki atapunguza haya matatizo ambayo TARURA wanakabiliana nayo. Suala kubwa ambalo tunamwachia Mheshimiwa Jafo na hili ningependa kusikia kauli yake wakati wa kuhitimisha ni kile kilio chetu cha Wabunge kwamba mgao ubadilishwe, wa fedha za Road Fund ambazo zinakwenda TANROAD na hizi za TARURA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna majukumu mengi TARURA wanayo na network ya barabara za vijijini ambazo mwananchi wa kawaida, mpiga kura akiamka anakutana na barabara za TARURA halafu ndiyo anakwenda za TANROAD. Kwa hiyo mgao ubadilishwe…

(Hapa baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walikuwa wakiongea bila mpangilio)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja hii ambayo ipo mbele yetu; hoja ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Pia niungane na wenzangu kwa kumpongeza Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mheshimiwa Engineer Lwenge na Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Kamwelwe. Pia nawapongeza Watendaji; Engineer Mbogo na Naibu Katibu Mkuu, Engineer Kalobelwe. Sina mashaka na watu hawa, ni watendaji wazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanzia tu, katika Jimbo letu la Nanyamba tunamshukuru sana Naibu Waziri wa Maji kwa sababu ndiyo Naibu Waziri wa kwanza katika Awamu hii ya Tano kufika katika Halmashauri yetu mpya ya Nanyamba. Alifanya ziara, alitembelea lakini sina wasiwasi na Waziri mwenyewe kwa sababu na-declare interest, kabla sijaingia kwenye siasa nilikuwa Mkurugenzi huko nyuma, alishafika mpaka Newala na nikampeleka katika mradi wa maji wa Makonde. Kwa hiyo, hata hiki ninachokiongea, anafahamu maeneo hayo na miradi hiyo ninayoizungumzia hapa anaifahamu kwa undani wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia hoja yangu kuhusu suala la takwimu. Naomba sana niishauri Wizara kwamba tumefikia asilimia 72, lakini tuna changamoto kwamba hii asilimia 72 ni asilimia ya jumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto sasa ya kwenda case by case kwenye kata, kwenye wilaya na kwenye mikoa. Kuna tofauti kubwa sana! Katika Jimbo langu, upatikanaji wa maji vijijini sasa hivi ni asilimia 40. Jirani yangu Tandahimba kwa Mheshimiwa Katani ni asilimia 45; jirani yangu Mheshimiwa Mkuchika pale amesema pale vile vile ni asilimia 47. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wakati National average ni hiyo 72, kuna maeneo wako chini sana. Kwa hiyo, hata tunapo-design miradi yetu, tuangalie sasa kwamba hali ya upatikanaji wa maji katika kila kata, wilaya na mkoa ikoje, ndiyo hapo tutatenda haki na kutengeneza miradi ambayo itajibu kero za wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwakumbushe vile vile kwamba kwa kweli hakuna maendeleo bila maji. Pili, maji ni siasa kama walivyosema watu wengi. Asilimia kubwa ya akinamama wanatumia muda wao mwingi sana badala ya kushughulika na shughuli za maendeleo, wapo wanahangaika na maji. Kwa hiyo, tukipeleka maji vijijini, tutaokoa kundi kubwa la akinamama ambao wanahangaika na maji na watafanya shughuli za maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi magonjwa mengi ambayo yanaathiri watu wetu ni kwa sababu ya kutokupatikana kwa maji safi na salama. Tukipata maji safi na salama, basi tutakuwa tumezuia hizo gharama ambazo tunazitumia kwa ajili ya kutibu magonjwa hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nijielekeze kwenye mradi wa maji wa Makonde. Sitarudia yale ambayo yamesemwa na Mheshimiwa Mkuchika, lakini nisisitize tu kwamba, kwa Wizara sasa mchukue hatua, huu mradi ni mkubwa, wa siku nyingi na umechakaa. Pale Mitema ukifika kuna kazi inahitajika kufanywa. Hebu tuwekeze vya kutosha ili tumalize suala la maji Newala, Tandahimba na Nanyamba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachotakiwa kufanywa sasa hivi ni ukarabati mkubwa ambao unaendelea pale Mitema. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa jitihada zake kwamba kuna kazi inaendelea kule sasa hivi, lakini kuna kazi imebaki, lazima tubadilishe mabomba, umbali wa kilometa nane kutoka pale Mitema kwenda Nanda; na tukifanya hivyo tutakuwa tumeboresha upatikanaji wa maji Tandahimba.
Pili, wakati Mheshimiwa Naibu Waziri alipotembelea, tulikabidhi andiko letu ambalo silioni kwenye vitabu vyake hapa, lakini naamini kwamba ahadi ya Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri na ahadi ya Serikali, bado naendelea kuamini kwamba ataendelea kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi pale tulipendekeza na andiko limeshakabidhiwa kwa Mheshimiwa Naibu Waziri wa kutoa maji Kijiji cha Lyenje na kupeleka Nanyamba. Mradi huu utanufaisha kata tisa, vijiji 43 na wananchi takriban 24,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hawa ni watu wetu, wanahitaji maji na wana shida kubwa sana ya maji. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya sum up atuambie kwamba andiko lile sasa wana-accommodate vipi kwenye ukarabati mkubwa wa mradi wa Makonde ambao napongeza jitihada za Wizara yake kwa sababu bado anaendelea kufanya mazungumzo na Serikali ya India ili tupate fedha kwa ajili ya mradi huu mkubwa. Kwa hiyo, naomba na hili andiko letu sasa la kuchepusha maji Lyenje na kwenda Nanyamba, basi lifanyiwe kazi ili fedha zikipatikana miradi hiyo yote iweze kutekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie vile vile kuhusu mradi wa kutoa maji Mto Ruvuma kupeleka Manispaa ya Mtwara Mikindani. Naipongeza Serikali yangu ya Awamu ya Tano ya Chama cha Mapinduzi kwa jitihada ambazo imezifanya, kwa sababu mradi huu ukitekelezwa utakuwa umemaliza tatizo la maji Manispaa ya Mtwara. Kwa sababu kama iliyoelezwa kwenye kitabu, upatikaji wa maji sasa hivi ni lita milioni tisa lakini mradi huu ukikamilika, tutakuwa na uhakika wa lita milioni 120.
Kwa hiyo, mahitaji ya maji Dangote na viwanda vingine vyote ambavyo vitafunguliwa Manispaa ya Mtwara hatutakuwa na maji. Huku ndiko kutengeneza mazingira wezeshi kwa wawekezaji wetu. Kwa hiyo tukikamilisha mradi huu basi tutakuwa tumetengeneza hata mazingira mazuri ya uwekezaji katika Manispaa yetu ya Mtwara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushauri. Maji haya tunayatoa Mto Ruvuma kwenye Kijiji cha Maembe Chini ambako ni Jimbo langu. Mheshimiwa Waziri amesema vijiji 26 vitafaidika, lakini naomba tuongeze idadi ya vijiji. Tunaweza tukaongeza idadi ya vijiji kiasi kwamba Kata ya Kiromba, Kitaya, Mbembaleo, Chawi na Kiyanga wakafaidika na mradi huu; na hiki kinawezekana na nilijadiliana muda fulani na Naibu Waziri akasema watalifanyia kazi. Naomba sana walifanyie kazi ili wananchi hawa wafaidike na mradi huu mkubwa.
tukianzisha mamlaka bila kuwa na maji ya kutosha…
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu na ni-declare interest na mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), nikiwa kama Makamu Mwenyekiti wa Kamati.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kabla sijaanza kutoa michango yangu nilitaka tuweke record sawa na hasa kuhusu taarifa yetu. Kilichosisitizwa kwenye taarifa yetu ni mafunzo kwa Wakurugenzi wapya. Taarifa yetu imeweka wazi kabisa kwamba hatuna maswali, hatuhoji uteuzi wa watu mbalimbali kutoka kwenye kada mbalimbali kwenda kwenye Ukurugenzi lakini watu hawa sasa wanatakiwa wapate mafunzo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, alivyofanya Mheshimiwa Rais kuchukua breed nyingine kutoka nje kupeleka kwenye utumishi wa umma na hasa kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa ni kitu ambacho ni kizuri na kinaweza kuleta matunda ambayo tunayatarajia. Kuna watu ambao wametoka kwenye private sector wakaenda kwenye mashirika yetu, kwa mfano Mkurugenzi wa Shirika letu la Nyumba, Ndugu Mchechu, anafanya vizuri, lakini ametoka kwenye private sector.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wakurugenzi waliokuja mbele yetu wakati tunafanya mahojiano, wapo Wakurugenzi ambao wamefanya vizuri kabisa niwataje baadhi tu, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kiteto alifanya vizuri na alikuwa na miezi miwili tu ofisini; Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ileje, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Mkurugenzi wa Tandahimba, lakini na Mheshimiwa Heche pale atakuwa shahidi, Mkurugenzi wa Tarime na yeye ni kijana mdogo, lakini ni mchapakazi vizuri na alionesha uwezo mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii haikwepi jukumu la TAMISEMI kuwapeleka vyuoni hawa Wakurugenzi. Ukurugenzi ni kazi kubwa, kwenye council kuna idara na vitengo visivyopungua 15. Mkurugenzi huyu inabidi awe mganga, Mkurugenzi huyu ajue masuala ya elimu, Mkurugenzi huyu anatakiwa ajue masuala ya manunuzi, Mkurugenzi huyu anatakiwa ajue masuala ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni vema Wakurugenzi hawa pamoja na kubana matumizi, tuwaandalie programu maalum ili tuwapeleke kwenye Chuo chetu cha Hombolo wakapitishwe kwenye taratibu za kawaida tu. Kwanza waifahamu sheria ambayo imeanzisha Mamlaka ya Serikali za Mitaa, ile Sura ya 288, Sura ya 289, lakini na Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa Sura ya 290, ili zikawasaidie katika kutekeleza majukumu yao, hicho ni kitu cha msingi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna kitu hapa kimezungumzwa kuhusu mahusiano ya Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya. Kwenye mafunzo hayo wapitishwe kwenye Sheria ile ya Regional Administration Act ambayo wataona mahusiano kati ya Serikali Kuu na Serikali ya Mitaa. Kwa hiyo, naomba sana TAMISEMI pamoja na kubana matumizi mafunzo haya ni muhimu kwa Wakurugenzi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya pili ambayo napenda nichangie ni kuhusu udhaifu wa mfumo wa udhibiti wa ndani. Haya yote ambayo tumeyaongea hapa yangeweza kudhibitiwa kama tungekuwa na mifumo imara ya udhibiti wa ndani na hapa naomba niseme tu kwamba Ofisi ya Internal Auditor General ilifanya kazi sana miaka mitatu, minne iliyopita chini ya uongozi wa Ndugu Mtonga. Aliandaa mafunzo kwa Wakaguzi wa Ndani ili wakasimike mifumo ya udhibiti wa ndani kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niseme tu kwamba, mafunzo yale hayakuleta tija ambayo tulitarajia kwa sababu mafunzo yale yalilenga kwamba Wakaguzi wa Ndani wakirudi kwanza watengeneze kitu ambacho kinaitwa Risk Management Policy kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa, watengeneze Risk Framework, lakini vilevile watengeneze Risk Register ambazo watakuwa wanazi-update kila mwaka kuangalia ni maeneo gani yana vihatarishi katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa na haya yanaweza yakafanyika vizuri chini ya Internal Auditor.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nitofautiane na wale ambao wanasema kwamba Internal Auditor anatakiwa ahamishwe, hapana. Internal Auditor ni jicho la karibu la Mkurugenzi Mtendaji. Ndugu zangu mimi nilikuwa mtumishi wa umma nilifanya kazi hiyo ya Ukurugenzi, Mkurugenzi ambaye anataka aone matokeo katika council yake mtu wake wa karibu ni Internal Auditor. Kuna Idara 15 kwa hiyo, atamsaidia Mkurugenzi katika Idara zake 15, Risk Department ni hi hapa kwa hiyo, Internal Auditor ni mtu wa karibu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkurugenzi ambaye anataka matokeo atamuwezesha huyu Internal Auditor, atampa usafiri Internal Auditor kwa sababu hata Mkurugenzi akisafiri anajua kwamba kuna jicho lake la karibu ambalo ni Mkaguzi wa Ndani, lakini si vinginevyo kwa sababu watu wanafikiri kwamba kuwepo kwake huyu basi anaweza aka-collude na Mkurugenzi, hapana, Mkurugenzi ambaye anataka matokeo katika Halmashauri yake atamtumia vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba, TAMISEMI mlikuwa na utaratibu wa kuwezesha hivi vietengo, mlinunua magari, lakini magari yale yameenda kwenye Halmashauri chache. Kuna Mamlaka ya Serikali za Mitaa tumeongeza Halmashauri mpya, hawana yale magari hebu wezesheni kwenye zile Halmashauri mpya wapate magari kwenye vitengo hivi ili viweze kuwasaidia hawa Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala langu la pili ambalo nataka nichangie ni kuhusu udhaifu katika mikataba. Sehemu nyingine ambayo ina udhaifu katika Mamlaka yetu ya Serikali za Mitaa na CAG ameonesha wazi ni udhaifu wa kwanza uingiaji wa mikataba yenyewe katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa, lakini pili na usimamizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana ulifanyika ukaguzi na CAG ametuonesha kwenye taarifa yake kwamba kwenye mikataba ya kukusanya fedha, kwanza Halmashauri hazifanyi assessment ya vyanzo vya mapato, yaani wanaingia mikataba na Mawakala wa Kukusanya Mapato bila kuangalia chanzo hiki kitapata Shilingi ngapi, na Halmashauri inategemea takwimu kutoka kwa Wakala. Hiyo ni taarifa mbaya sana kwa sababu Wakala anatafuta faida lazima atadanganya kwa hiyo, ni vizuri Halmashauri zifanye assessment ya chanzo cha mapato kabla ya kuingia mkataba na Wakala.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapo kwenye Taarifa ya CAG inaonesha kabisa kwamba kwenye Halmashauri 76 kuna fedha bilioni 5.3 Mawakala hawakuwasilisha, waliingia mikataba, lakini kwa sababu ya usimamizi mbovu wa mikataba fedha hizo wameondoka nazo Mawakala, Halmashauri hawakuzipata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu nyingine ambayo nilitaka nichangie kwenye hiyo hiyo mikataba, mimi naona TAMISEMI sasa mikataba kama hii ambayo inaonekana kwamba Halmashauri sasa imezidiwa hebu tuingilie kati mapema. Kwa mfano mkataba ule wa Oysterbay Villa na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, mkataba ambao hauna tija. Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ina apartments 17 wamepewa, lakini hadi leo hawajapangisha na hawapati zile fedha. TAMISEMI mnatakiwa muingilie kati ili chanzo kile kisaidie kupata mapato ya Kinondoni kwa sababu, Kinondoni kama mmiliki amezuiliwa kuingia kwenye ule mradi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mkataba mwingine ambao tuliona kwamba nao una mashaka ambao wenzangu mmeshasema ni ule wa UDA ambapo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ilipeleka barua kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Sasa tunaomba ule ushauri ambao ameutoa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ufanyiwe kazi ili zile fedha ambazo ziko benki zaidi ya bilioni tano zitumike kwa maendeleo ya wananchi wa Jiji la Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine ni usimamizi wa matumizi ya fedha. Hapa naomba TAMISEMI ilivalie njuga suala hili kwa sababu Mamlaka ya Serikali za Mitaa imeonekana tena kuanza udhaifu wa kuanza hoja ambazo huko nyuma zilikuwa zimeshafutwa. Kuna hoja hapa kwenye taarifa ya mwaka 2014/2015 kwamba Halmashauri za Wilaya zimefanya malipo ya bilioni 10 na milioni 31 bila kuwa na viambatisho muhimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hizi hoja ni za kizembe, hizi hoja sasa tuna Mfumo wa EPICOR kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa, kwa nini hoja kama hizi ziendelee kuwepo? Kwa hiyo, naomba TAMISEMI muingilie kati ili uzembe kama huu usiendelee kutokea na watumishi ambao wanafanya uzembe huu wachukuliwe hatua mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile naomba sasa ule Mfumo wa EPICOR usimikwe katika halmashauri zote. Kuna halmashauri mpya ambazo mfumo wa EPICOR haujasimikwa bado. Kwa hiyo naomba TAMISEMI ihakikishe kwamba, inatenga fungu la kutosha, ili halmashauri zote sasa ziweze kufunga mifumo hii ya EPICOR ili na wao waweze kufanya hesabu zao kupitia mfumo huu badala ya kutumia mifumo ya kizamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie tu kuhusu uteuzi wa Wakuu wa Idara. Wakuu wa Idara kwa sheria iliyopo wanateuliwa na Mkurugenzi wa Halmashauri, lakini kuna mchakato, lazima waende kwenye vetting. Kwa hiyo, naomba mamlaka zinazohusika ziongeze uharaka katika mchakato huu, ili tusiwe na makaimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja na ninashukuru kwa kunipa nafasi.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Usimamizi wa Matumizi ya Fedha za Umma katika Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2017
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi kwa kuwa ni Mjumbe wa Kamati ya LAAC mchango wangu utajikita katika taarifa iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati yetu ya LAAC. Kwanza nianze kuipongeza TAMISEMI kwa hatua ambazo zinachukuliwa kwa sababu ukisoma hikhi kitabu cha taarifa ya CAG inaonekana kuna maboresha katika hati zinazopatikana. Hati za kuridhisha kwa councils ambazo zilikaguliwa mwaka jana 185, kuna ongezeko la halmashauri ambazo zimepata hati ambayo inaridhisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia takwimu utaona kwamba kwa taarifa ya mwaka 2015/2016 tulikuwa na councils 135 kati ya 171 ndio zilipata hati ya kuridhisha, lakini taarifa hii tunayoijadili kuna ongezeko, mwaka huu kuna halmashauri 165 zimepata hati ya kuridhisha kati ya halmashauri 185 ambazo ni sawa na 90%. Kwa hiyo, niwapongeze sana TAMISEMI kwa shughuli za ufuatiliaji ambazo zinafanywa na matokeo yake tunaanza kuyaona sasa hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, si hivyo tu halmashauri ambazo zinapata hati za mashaka nazo zinaanza kupungua, ukiacha halmashauri za Kigoma Ujiji ambayo imepata hati mbaya kwa miaka mitatu mfululizo, lakini katika maeneo mengine kuna maboresho ambayo yanaonekana. Kwa hiyo kwa sababu Waheshimiwa Wabunge ni Madiwani, nimshauri kaka yangu Mheshimiwa Zitto kwamba naye awe anahudhuria vikao vya Kamati ya Fedha ili inapojadiliwa ripoti ya CAG na yeye aweke inputs zake kwa sababu kupata hati isiyoridhisha kwa miaka mitatu mfululizo ni kitu kisicho cha kawaida na kinahitaji intervention za haraka ili Kigoma Ujiji iweze kupata hati safi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi hizi sasa nichukue nafasi hii kuishauri TAMISEMI, kama walivyosema wenzangu kwenye taarifa yetu tumesema matatizo yote ambayo yanatokea katika halmashauri zetu sababu kubwa ambayo inasabisha ni mifumo yetu ya ndani kutokuwa imara. Kwa hiyo mifumo wa udhibiti wa ndani inabidi iimarishwe. Tunapozungumzia mifumo ya udhibiti wa ndani tunaangalia Kitengo cha Ukaguzi, Kamati za Ukaguzi za Wilaya, matumizi ya TEHAMA katika ukaguaji au ufungaji wa hesabu, kuwepo kwa sera ya viashiria hatarishi na vilevile kuwa na fraud assessment. Kwa hiyo hayo yakizingatiwa, tutapunguza sana ubadhirifu ambao unatokea katika halmashauri zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma agizo la 12, Local Authority Financial Memorandum kuna agizo kabisa limetolewa pale kwamba, kila halmashauri lazima kuwe na Kitengo cha Ndani. Changamoto iliyopo kwenye Kitengo chetu cha Ukaguzi wa ndani ni kukosekana kwa rasilimali fedha na rasilimali watu. Kwa hiyo, nichukue nafasi hii kama walivyopendekeza kwenye Kamati yetu, TAMISEMI na kwa kushirikiana na Mkaguzi Mkuu ambaye yupo Wizara ya Fedha Internal Auditor General, basi waimarishe kitengo hiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, huko nyuma kulikuwa na jitihada za makusudi TAMISEMI walikuwa wanahangaika na vitendea kazi, lakini na Interanal Auditor General ambaye yupo Wizara ya Fedha na Mipango ambaye alikuwa anatoa mafunzo kwa Wakaguzi wa Ndani. Kwa hiyo tunaiomba Serikali sasa kurejesha yale mafunzo ili Wakaguzi wetu waweze kuwa na ujuzi wa kuweza kufanya kazi yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, si hivyo tu, ripoti hii inaonesha wazi kwamba kuna uchache, ikama inasema kila halmashauri kuwe na Wakaguzi wasiopungua wane, lakini halmashauri nyingi ambazo zilikuja ndani ya Kamati zina Mkaguzi wa Ndani mmoja au wawili. Kwa hiyo wanashindwa kutekeleza majukumu yao. Kama tulivyopendekeza kwenye ripoti yetu kwamba, Serikali ichukue jitihada za makusudi kuomba kibali cha jumla ili Wakaguzi wa Ndani waweze kuajiriwa na wasambazwe kwenye halmashauri kwa ajili ya kuimarisha Kitengo hiki cha Ukaguzi wa Ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la Kamati za Ukaguzi, ukisoma agizo la 13 la Local Authority Financial Memorandum, zinazitaka halmashauri kuwa na Kamati za Ukaguzi na Mwenyekiti atoke nje ya ile taasisi, lakini hapa kinachoendelea ni tofauti, halmashauri nyingi ambazo zimekuja kwenye mahojiano, Wakuu wa Idara au watendaji wa halmashauri ndio walikuwa Wenyeviti wa hizo Kamati, kinyume na mwongozo ambao umetolewa na Wizara na kinyume na agizo hili hapa. Kwa hiyo naomba TAMISEMI kusimamia kwa karibu ili halmashauri zote zipate Wenyeviti wa Kamati za Ukaguzi ambao wanatoka nje ya taasisi ili kuimarisha kamati kwa ajili ya kuweza kutimiza majukumu yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye udhibiti wa ndani kuna suala la TEHAMA; kumekuwa na mtindo sasa hivi mwezi wa Saba, mwezi wa Nane halmashauri zinasimama kila kitu, ukiuliza wanasema mfumo, Madiwani hawalipwi, vikao haviendelei, hakuna malipo yanayoendelea. Tulipofanya mahojiano na TAMISEMI, walisema hakuna kitu kama hicho, tatizo ni changamoto ya utalaam. Kwa hiyo naiomba Serikali kutoa mafunzo, kama tulivyopendekeza kwenye taarifa yetu, kwa wataalam ili kusiwe na kisingizio kwamba mwezi wa Saba na wa Nane hakuna kinachoendelea halmashauri kwa sababu ya kusingizia hiyo mifumo iliyopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni mafunzo kwa hawa Wakaguzi; inachekesha sana kwamba kuna mifumo mingi ambayo Serikali imeanzisha tuna EPICOR, Lawson kwa ajili ya mishahara, tuna ile ya kukusanya mapato (LGRCIS), lakini Mkaguzi wa Ndani hajapata mafunzo jinsi ya kuingia kwenye mifumo hii. Kwa hiyo, Mkaguzi wa Ndani anapokwenda kukagua anakumbana na changamoto ya matumizi ya mifumo hii. Hivyo, kama tulivyoshauri kwenye Kamati yetu Internal Auditor General ambaye ipo Wizara ya Fedha na Mipango na TAMISEMI wahakikishe kwamba Wakaguzi wetu wa Ndani wanapata mafunzo ya kutosha ili waweze ku-assess hii mifumo ambayo imeanzishwa kwenye halmashauri zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze TAMISEMi kwa kuanzisha kitengo cha ukaguzi na ufuatiliaji wa fedha katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Hiki ni kitengo muhimu sana na kitengo hiki kikiimarishwa kitasaidia sana kupunguza ubadhirifu au utekelezaji wa miradi usioridhisha katika halmashauri zetu. Tulipowahoji maafisa ambao wapo kwenye kitengo hiki kuna changamoto kubwa sana, kitengo kimeanzishwa lakini ni ombaomba, tunaomba Wizara ya Fedha na TAMISEMI ihakikishe kwenye bajeti inatenga fedha za kutosha ili kitengo hiki kiwezi kutekeleza majukumu yake. Ni kitengo kizuri ambacho kikiimarishwa kitazuia ubadhirifu ambao unatokea kwenye halmashauri zetu kabla CAG hajaingia.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kitengo hiki kina watumishi wachache lazima kiongezewe watumishi kitengo hiki ili kiweze kutekeleza majukumu yake na kitengo hiki pia kiwezeshwe kutumia mifumo iliyopo ya TAMISEMI iliyopo sasa hivi ili waweze ku-assess ku-information, sio lazima wakimbie kwenye halmashauri, wanaweza kuitisha taarifa zilizopo kwenye mifumo na wakajua kwamba kwenye halmashauri X kuna changamoto hii na baadaye wakaenda kufuatilia kule kule kwenye halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kitengo hiki kikiimarishwa kitasaidia na kitapunguza wazo ambalo watu wanalo, kuna watu wana wazo kwamba Internal Audit asiwe sehemu ya Mkurugenzi, sasa Internal Auditor akiwa nje ya Mkurugenzi inavuruga maana ya kuwepo Internal Auditor, Internal Auditor kile kitengo kimeungwa ili liwe jicho la Mkurugenzi au Afisa Masuuli. Internal Auditor akitolewa nje ya ofisi huyu atakuwa External Auditor mwingine, kwa hiyo tukiimarisha kitengo hiki itasaidia kutoa ishara kwa Mkurugenzi kwamba idara yako X kuna hali mbaya, kwa hiyo chukua hatua haraka. Kwa hiyo, napendekeza kitengo kiimarishwe na sio kuondolewa kwenye Ofisi ya Afisa Masuuli.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie mchango wangu kuhusu utekelezaji wa miradi kwenye Halmashauri zetu. Kuna changamoto nyingi sana katika kutekeleza miradi kwenye Halmashauri yetu. Changamoto ya kwanza, ni fedha kupelekwa pungufu. Fedha zinatengwa kwenye bajeti lakini hazipelekwi na hivyo mipango ya Halmashauri kushindwa kutekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba TAMISEMI kila wanapopata fedha wahakikishe kwamba wanapeleka kwenye mamlaka ya Serikali za Mitaa ili waweze kutekeleza miradi kwa wakati. Kuna wakati mwingine tunaambiwa Halmashauri hazina uwezo, kumbe tunapeleka fedha Mei, 30 halafu tunawaambia watekeleze mradi. Mradi huu hauwezi kutekelezeka kwa sababu procurement process yenyewe inachukua siku nyingi. Kwa hiyo, mpaka kumaliza mchakato wa manunuzi fedha zile zitakuwa bakaa kwenye mwaka unaofuata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto nyingine ni gharama za mradi kama ilivyoelezwa kwenye taarifa yetu pale Morogoro Manispaa tuliona mradi wa lami ambao ni wa kilomita 4.6 lakini unagharimu takribani shilingi bilioni 12. Sisi kwa hesabu zetu za haraka fedha zile zingeweza kujenga zaidi ya kilomita 10. Tulipouliza kwenye Halmashauri zingine viwango vinakuwa tofauti.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Kitengo cha Usimamizi wa Miradi kwenye Halmashauri kilichopo TAMISEMI lazima tuweke standard za miradi yetu, standard za utekelezaji katika mamlaka ya Serikali za Mitaa ili kutotoa mwanya kwa wale ambao wana nia mbaya ya kupiga fedha za Halmashauri wasiweze kufanya hivyo. Tunapokuwa na viwango tofauti na Halmashauri inajiamulia kwamba nitajenga barabara kilomita 1 kwa shilingi bilioni 3, mwingine anajenga kilomita 1 kwa shilingi bilioni 2, hapo lazima upotevu wa fedha utajitokeza. Kwa hiyo, naomba Kitengo cha Usimamizi wa Fedha TAMISEMI, Kitengo kinachosimamia miradi kihakikishe kinatoa standard ili miradi yetu tuweze kutekeleza kwa kile kiwango ambacho tumekikusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema mimi ni Mjumbe wa Kamati ya LAAC, naunga mkono taarifa ya Kamati yetu kwa asilimia 100 na nakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti,nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja iliyoko mbele yetu ambayo ni Wizara mbili, Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Kwanza nipende kuchukua nafasi hii kuwapongeza Mawaziri wa Wizara hizi mbili, Mheshimiwa Jafo na Mheshimiwa George Huruma Mkuchika hongereni sana. Pili, nichukue nafsi kuwapongeza Manaibu wa Wazara hiyo, Ofisi ya TAMISEMI kuna Mheshimiwa Waitara na Mheshimiwa Kandege, lakini Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kuna dada yetu Dkt. Mwanjelwa, hongereni sana kwa kazi mnazozifanya.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitaanza kupongeza kwa kazi nzuri ambazo TAMISEMI wamefanya na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ambazo ziko wazi kwa sababu si vyema kuanza kulaumu bila kupongeza, mnyonge mnyongeeni lakini haki yake mpeni. Kuna ujenzi mkubwa wa vituo vya afya 352 ambavyo vimesimamiwa vizuri na vingi vimeshakamilika na Mheshimiwa Rais wiki iliyopita alifanya uzinduzi Mkoani Mtwara katika kituo cha afya, Mbonde, Wilayani Masasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna ujenzi wa hospitali za Wilaya 67 ikiwemo na ya Jimbo langu la Nanyamba na kwenye vituo vya afya 352 Mheshimiwa Jafo na TAMISEMI nawapongeza sana kwa sababu katika Jimbo langu tulikuwa hatuna kituo hata kimoja lakini wametuona na tumepewa vituo vitatu na vimeshakamilika na vimeshaanza kutoa huduma, kilichobaki sasa tunasubiri mashine na vifaa vingine ili huduma ziweze kutolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, si hivyo tu kuna fedha zaidi bilioni 29 zimetolewa kwa ajili ya kukamilisha maboma. Kila siku tulikuwa tunaimba hapa kwamba kuna nguvu za wananchi zimetumika, lakini Serikali haijaunga mkono. Kwa hiyo naipongeza sana TAMISEMIkwa kuliona hili nakupeleka bilioni 29 na kunusuru hayo maboma 2,392 ambayo fedha hizo zimeenda katika Mikoa yote Tanzania Bara. Si hivyo tu kuna kimiradi ya TASAFna MKURABITA tumeona jinsi inavyotekelezwa katika maeneo yetu. Kwa hiyo nawapa hongera sana.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijatoa rai na ushauri kwa Wizara hizi nataka niweke record vizuri kuhusu mambo mawili ambayo wachangiaji waliopita wamezungumzia. Kwanza kuna mzungumzaji jana alisema maamuzi mabaya ya Serikali imepelekea Mheshimiwa Rais kusema kwamba kangomba hawana makosa. Mheshimiwa Rais kwenye ziara yake ya Mtwara hakusema hivyo, alichosema Mheshimiwa Rais ni kutoa msamaha kwa kangomba na hakusema kwamba kangomba siyo makosa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma Sheria iliyoanzisha Bodi ya Korosho, Sura 203, kifungu cha 4(1), kinatoa majukumu ya Bodi ya Korosho, jukumu la kwanza ni kuhakikisha linasimamia suala la soko la korosho, lakini la pili kutoa leseni kwa mnunuzi na muuzaji wa korosho, kangomba hana leseni. Kwa hiyo Mheshimiwa Rais hakusema hivyo, Mheshimiwa Rais ametoa msamaha na hiyo ni sifa ya viongozi ambao wanasikiliza watu wao, hongera sana Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, tusimwekee maneno Mheshimiwa Rais wetu, hakusema hivyo Mtwara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nataka tuweke rekodi sawa, kaka yangu hapa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha CUF Taifa, Mheshimiwa Maftaha amesema Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kazi yake ni kuwanyima wapinzani nafasi kwenye mikutano. Hiyo siyo sahihi, Mkuu wetu wa Mtwara anajua majukumu yake, ni mtu ambaye anafuata taratibu lakini sisi Wabunge kama viongozi tufahamu itifaki ya ugeni wa Rais. Siku ya ugeni wa Rais kuna itifaki zake na mgeni pale ni mmoja tu Mheshimiwa Rais. Tulikuwa na Mawaziri wengi hawakupewa nafasi ya kuongea.

T A A R I F A

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Tulikuwa na Wabunge wengi walipewa nafasi ya kuongea.

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Maftah taafifa.

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa Mheshimiwa Chikota namheshimu sana kwa yale ambayo anayozungumza kwa sababu alivyokuja Mheshimiwa Rais siku ya tarehe 2 tulipewa ratiba siku moja kabla ya ziara yake katika Jimbo langu la Mtwara Mjini ilikuwa ni pale Uwanja wa Ndege (Airport) na pale Naliendele na ratiba imepangwa, Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini ambaye ndiyo mimi ninayezungumza sikuwepo kwenye ratiba hiyo. Sasa asijaribu kupotosha Bunge, kile nilichokizungumza ni kitu sahihi kabisa kwamba Mkuu wa Mkoa anakiuka taratibu za utawala bora.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Abdallah Chikota.

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei taarifa hiyo, nilikuwa naendelea kusema kwamba siku ya pili, siku ya uzinduzi wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Mtwara - Newala - Masasi kilometa 50, Mheshimiwa Rais alimuita Mbunge wa Jimbo husika na Mheshimiwa Maftah hakuwepo na ndiyo maana Mheshimiwa Rais akasema Mbunge wa Viti Maalum, akampa nafasi Mheshimiwa Wambura. Kwa hiyo, angekuwepo siku ile angepewa nafasi ya kuongea.

T A A R I F A

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Taarifa.

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea na mchango wangu.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea na mchango wangu na kuweka record sawa.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Haya Mheshimiwa Bwege, taarifa.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge anayeongea sasa hivi asipotoshe. Mimi nilikuwepo katika msafara na Mheshimiwa Maftaha ni Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini na Mkutano wa kwanza ulifanyika Mtwara Mjini, Mheshimiwa Maftaha hakupewa nafasi lakini tulipofika pale…

MWENYEKITI: Sasa unachangia au taarifa? Si umeshasema taarifa tayari?

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Tulipofika katika Kiwanda cha Korosho akaitwa Mheshimiwa Hawa Ghasia akapewa nafasi akahutubia. Kwa hiyo, kuna ubaguzi mkubwa katika jambo hili, kwa taarifa yako. Mlipotambua Mheshimiwa Maftaha hakuwepo siku ya pili ndiyo mkamuita, kwa hiyo, ubaguzi…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Chikota.

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sipokei taarifa hiyo, Mheshimiwa mzungumzaji aliyepita sasa hivi hakuwepo siku ya pili alikimbilia Chuo cha Ualimu Kitangali kwa ajili ya ufunguzi wa Chuo cha Ualimu Kitangali, kwa hiyo, hajui kilichotokea pale Naliendele asilipotoshe Bunge.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: (Hapa hakutumia kipaza sauti)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Bwege, naomba unyamaze tu, endelea.

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea na mchango wangu na sasa nataka nitoe rai kwenye mambo matatu kuhusu Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Suala la kwanza ni kuhusu fedha za mchango wa Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake, Vijana na Walemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi fedha kwa sababu sasa hivi Wizara inaandaa Kanuni, naomba tuzingatie ushauri ambao tumepokea katika maeneo mbalimbali. Mimi kama Mjumbe wa Kamati ya LAAC tumepita maeneo mbalimbali, ushauri unaotolewa tusizingatie kutoa fedha hizi kwenye vikundi tu, tufikirie wazo la kutoa fedha hizi za mkopo kwa mtu mmoja mmoja, mlemavu mmoja, kijana ambaye ana mradi wake ambao unawezekana kupewa mkopo akiwa peke yake apewe na mwana mama ambaye ana mradi wake ambao ni viable kupewa mkopo siyo lazima awe kwenye vikundi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunaweza kwenda mbali tukajifunze Mkoa wa Shinyanga hasa Wilaya ya Kahama, wameamua kutenga eneo maalum kwa ajili ya vijana. Tunaweza kuchukua mfano ule tukapeleka kwenye mikoa mingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa pili ni kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao unakuja. Naomba Ofisi ya Rais, TAMISEMI itenge fedha za kutosha kwa ajili ya kugharamia uchaguzi huu. Tuna uzoefu kwenye chaguzi zilizopita zinatengwa fedha ndogo na kuwaambia Halmashauri wachangie kiasi kinachobaki. Halmashauri zetu uwezo wake tunaufahamu, kwa hiyo, tusiwape mzigo, tutenge fedha za kutosha ili uchaguzi huu uende kama ulivyopangwa, tukamilishe bila ya kuwa na dosari zozote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa tatu ni kuhusu TARURA. Kama walivyosema Wajumbe waliopita; TARURA kwa kipindi kifupi imeonyesha mafanikio makubwa sana, imefanya kazi nzuri sana lakini ina changamoto mbili. Changamoto ya kwanza bado fedha wanazopewa ni chache lakini changamoto ya pili ni watumishi. Walipewa watumishi wachache kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa na kutengeneza pengo la uhaba wa Wahandisi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kwa hiyo, nashauri Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kushirikiana na Ofisi ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma watoe kibali maalum ili TARURA waweze kupata wafanyakazi wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu mwingine ni kuhusu Ofisi ya Rais, TAMISEMI; kuna changamoto ya Wakuu wa Idara wengi kuwa makaimu na hii naomba mshirikiane na kaka yangu Mheshimiwa George Huruma Mkuchika, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa sababu malalamiko mengi ambayo wanatoa Wakurugenzi kwamba suala la upekuzi kwa wale watarajiwa linachukua muda mrefu sana. Kwa hiyo, hili suala la upekuzi kama walivyosema Wajumbe wengine tuliwekee mkakati ili upekuzi ufanyike kwa muda mfupi na wale wenye sifa waweze kuteuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Niungane na wenzangu kukupa pongezi kwa jinsi unavyoendelea kusimama imara na kuliongoza vizuri Bunge letu Tukufu. Sisi tupo pamoja na wewe na kwenye wengi kuna Mungu na kwenye Bunge hili sisi ndiyo wengi. Kwa hiyo, kaza buti na tunakutabiria kuna mambo mengine makubwa yatakujia mbele yako. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nichukue nafasi hii vilevile nimpongeze Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mpango na Naibu Waziri wa Fedha kwa kuja na bajeti ambayo kwa kweli inaonyesha kuna matumaini kwetu sisi Watanzania. Kwa mara ya kwanza tumeona kwamba bajeti yetu ya maendeleo ni asilimia 40, haya ni maendeleo makubwa lakini tumeona jinsi gani bajeti hii inavyopunguza kero za wananchi. Mimi natoka Jimbo ambalo ni la wakulima wakubwa sana wa korosho, kuna tozo tano pale zimeondolewa, hongera sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nipongeze kwa ujasiri wa kutenga fedha nyingi kwenda Wizara ya Afya, karibu shilingi trilioni moja na bilioni mia tisa ambazo zitasaidia vilevile kulipa deni la MSD. Tunapolipa deni la MSD tuna uhakika sasa zahanati zetu, vituo vya afya, hospitali za wilaya na hospitali za rufaa za mikoa kutakuwa na dawa, wagonjwa wetu wakienda hospitali hawatarudi na cheti tu, watarudi na dawa. Kwa hiyo, naipongeza sana Serikali yangu ya Awamu ya Tano ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nianze kuchangia hili suala la tozo tano. Kama nilivyosema, niendelee kuipongeza Serikali yangu ya Awamu ya Tano kwa sababu hii ilikuwa ahadi ya Mheshimiwa Rais wakati anaomba kura. Alisema kwenye korosho kuna kodi nyingi na akiingia Ikulu atapunguza na mwaka wake wa kwanza ameanza na hizi tozo tano na hiki kitabu kinasema kwamba hii ni awamu ya kwanza, kazi inaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishauri sasa, Serikali au Wizara ya Kilimo itoe mwongozo, sasa hivi kuna hofu na kuna maneno mengine kwamba kuondolewa kwa tozo hizi kutaathiri mfumo wa stakabadhi ghalani. Kwa hiyo, naomba sasa Wizara ya Kilimo itoe mwongozo kupeleka kule chini kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, mikoani na kwenye Vyama Vikuu vya Ushirika kwamba utaratibu gani utafuatwa kuhusu masuala ya usafirishaji wa korosho na minada ili tuwaondolee hofu wale ambao wanaanza kueneza maneno mengine kwamba kwa kuondosha tozo basi mfumo wetu wa stakabadhi ghalani utakuwa ni kifo chake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nitoe rai kwa wale wenzetu ambao wapo kwenye mfumo huu, mabadiliko yoyote yale lazima yalete hofu. Kwa hiyo, naomba sana wale ambao wanahusika na mfumo huu wa ununuzi wa korosho wajikite kuangalia the way forward na siyo kujadili kwamba tozo hii kwa nini itoke au isitoke, tuangalie mbele sasa baada ya kutolewa hizi tozo nini kifuate ili kuboresha uendeshaji wa mfumo wetu wa stakabadhi ghalani.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala langu la pili ni kuhusu CAG kuongezewa fedha. Bajeti ambayo amepewa CAG ni shilingi bilioni 44.6, hiki kiasi cha fedha hakitoshi. Ukiangalia kwenye fedha hizo kuna shilingi bilioni 12 ambazo ni za maendeleo lakini vilevile CAG ana deni ambalo amevuka nalo la shilingi bilioni nne kwa hiyo ukitoa kwenye hesabu hiyo bado fedha zake zinazidi kupungua. Hata hivyo, kwa maneno yake mwenyewe CAG wakati tunafanya discussion kule Dar es Salaam alisema kwa fedha hii sasa atashindwa kukagua Halmashauri 94. Sasa hebu piga hesabu, tuna Halmashauri 181, kama atashindwa kufanya ukaguzi kwenye Halmashauri 94, ina maana karibu nusu ya kazi yake hataikamilisha. Kama Halmashauri 94 hazitakaguliwa unajua ni athari gani ambayo itapatikana kwa sababu fedha zetu nyingi tunazipeleka kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna ahadi ambayo ilitolewa kwamba ataongezewa fedha kwenye mid-year review pengine Desemba. Kwa CAG kupewa fedha Desemba yeye haimsaidii kiutendaji kwa sababu kwenye ukaguzi kuna phases tatu na zinakamilika kabla ya Desemba. Januari mpaka Machi kwa CAG ni muda wa kuandika ripoti, kwa hiyo additional yoyote ya fedha mwezi Januari kwake haimsaidii kwenye ukaguzi. Kwa hiyo, naomba sana tusimpe fedha wakati wa kuandika ripoti, tumuongezee sasa ili CAG aweze ku-cover maeneo yake. Kwa sababu punguzo hili la fedha, kwanza hata scope ya ukaguzi itaathirika lakini hata ubora. Kama unavyofahamu kwamba chombo chetu hiki sasa kilishapata hadhi ya Kimataifa. CAG sasa anakagua taasisi za Umoja wa Mataifa, kwa hiyo, tusimshushe nguvu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende tena upande wa property tax ambayo sasa tumesema kwamba itakusanywa na TRA badala ya Mamlaka za Serikali za Mitaa. Niwakumbushe tu Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwamba huko nyuma kulikuwa na policy paper ya Local Government Reform ilitolewa mwaka 1998, ina maeneo manne, mimi kwa sababu ya muda sitaki kuyataja mengine, lakini eneo kubwa ambalo ilitakiwa tutekeleze ni financial decentralization, lazima Mamlaka za Serikali za Mitaa tuzipe uwezo wa kifedha. Dawa ya mtu ambaye hana uwezo wa kukusanya siyo kumnyang‟anya, nilitarajia kwamba tungekuja na mbinu za kuziongezea uwezo Mamlaka za Serikali za Mitaa kukusanya lakini kusema hawana uwezo tupeleke TRA hiyo kwa kweli siyo solution. Tufanye kwa mwaka huu kwa sababu tumeshaamua hivyo lakini naomba sana Serikali yangu Tukufu tuangalie jinsi ya kuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa ili ziweze kukusanya fedha za kutosha, zikikusanya fedha za kutosha basi wataweza kutoa huduma ambazo tunazitarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tuwe na wazo la kuzipa Mamlaka za Serikali za Mitaa vyanzo ambavyo ni vya uhakika. Vyanzo vilivyobaki kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa havina uhakika na mapato yake ni ya kusuasua. Kwa hiyo, tuangalie kwenye suala la ugatuaji wa madaraka siyo kupeleka mamlaka tu kule, tupeleke na fedha. Hii inanikumbusha wazo la Mheshimiwa Oliver ambaye alisisitiza sana umuhimu wa kuwa na semina ya ugatuaji, semina ya D by D kwa Waheshimiwa Wabunge na Waheshimiwa Mawaziri kwa sababu sasa hivi inaonekana kwamba tunataka kurudi nyuma tulikotoka.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie hoja iliyo mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuwapongeza viongozi wa Wizara hii, Mheshimiwa Waziri Mheshimiwa Hasunga, Manaibu wake Mheshimiwa Bashungwa na Mheshimiwa Mgumba; kwa kweli wote tumejionea ni jinsi gani wanavyohangaika kusukuma sekta ya kilimo. Wamekuwa wakihangaika usiku na mchana kuhakikisha yale mazao yetu ya kimkakati yanapata ufumbuzi wa changamoto zilizopo, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu unajikita katika maeneo matatu; kwanza zao la korosho, umwagiliaji na sekta ya ushirika. Nikianza na korosho, nichukue nafasi hii kipekee kumpongeza Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa maamuzi ya kijasiri ambayo aliyafanya mwaka jana kwa kuamua kununua korosho baada ya soko la korosho kuanza kuyumba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, anayeitakia mema sekta hii ya korosho hawezi kubeza juhudi zilizofanywa mwaka jana. Sekta ya Korosho inahitaji fedha nyingi na ndiyo maana hata baada ya kufanya maamuzi yale aliamua kuvunja Bodi ya Korosho na kuagiza Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko isimamie zoezi lile. Nichukue nafasi hii kuipongeza Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kwa kazi ambayo waliifanya lakini pia na Benki ya Maendeleo ya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwapongeze Wakuu wa Mikoa kwa mikoa ambayo inalima korosho, kwa changamoto ya mwaka jana walisimama kidete kuhakikisha kwamba wakulima wanapata haki yao na kusimamia mazoezi mbalimbali yaliyokuwa yanaendelea likiwemo na zoezi lile la uhakiki ambalo Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa walishirikiana kuhakikisha kwamba wakulima ambao ni wakulima wa korosho kweli ndiyo wanaolipwa fedha za korosho na siyo wengineyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee niipongeze Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji, ilifanya ziara kwenye mikoa ya kusini na kusaidia kuisimamia Serikali kufanya malipo haraka kwa wakulima wa korosho ambao bado walikuwa wanadai fedha zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizi bado kuna changamoto. Sasa hivi bado kuna wakulima ambao bado wanadai fedha zao takribani bilioni 100. Mimi naamini kwa sababu Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo mahsusi alipokuwa kwenye ziara ya mikoa ya kusini, naamini kwamba Wizara ya Fedha na Wizara ya Kilimo wataweka mikakati ya kutekeleza agizo hili ili wakulima hawa waweze kulipwa pesa zao kabla ya msimu mpya haujaanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, nishauri mambo yafuatayo kuhusu zao la korosho. Kwanza tunapomaliza msimu huu, kwa sababu kuna watu bado wanadai, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo kama ulivyohamia wakati ule tunaanza kununua, hebu tengeneza timu ya wataalam na watu waadilifu kwa sababu wewe mwenyewe ulishuhudia kwamba katikati pale wakati wa uhakiki kuna vijana wako hawakuwa waaminifu; na nikupongeze kwamba ulichukua ulichukua hatua za makusudi mapema ili kuzuia zile dalili za rushwa ambazo zilitaka kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili tumalize msimu vizuri, unda timu ndogo izunguke kila wilaya kusikiliza manung’uniko ya wakulima. Kuna wakulima bado wana manung’uniko, kuna mkulima alipeleka kilo 500 amelipwa kilo 300, akienda kwa viongozi wa AMCOS anaambiwa kwamba mwaka huu sisi hatukusimamia. Kwa hiyo, timu yako itasaidia ku-clear doubts za wakulima kabla ya msimu mpya haujaanza, nakuomba sana ufanye hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili; kuna changamoto zingine, kuna maeneo, mimi kesi yangu naifahamu kuna Mwenge AMCOS kuna akaunti za wakulima 200 zimefungwa, wanatupiana lawama kwamba amefunga fulani. Kwa hiyo, timu yako kama hiyo itatoa suluhisho kwa matatizo madogo madogo ambayo yamebaki katika sekta hii ili tuanze msimu mpya na mambo mapya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri pia kuhusu suala la ubanguaji. Changamoto nyingine tunazipata kwenye zao la korosho kwa sababu bado tunapeleka nje korosho ghafi.

Wenzetu wa Msumbiji wamekaza kamba kuhusu ubanguaji na wanafanya vizuri. Ni muda umefika sasa hivi tujikite katika ubanguaji. Tuna viwanda 12 vya awali vile ambavyo vilijengwa bado havifanyi kazi na wanunuzi wengine wamefanya maghala, kwa hiyo wanyang’anywe. Hata hivyo kuna wawekezaji wapya wameanza kujitokeza sasa hivi kutaka kujenga viwanda vipya vya ubanguaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali yangu sikivu kwanza iweke vivutio kwa wawekezaji hawa lakini pili ipunguze kodi kwa mitambo na mashine mpya wanazoingiza ili gharama za uwekezaji zisiwe kubwa; tukifanya hivyo korosho yetu nyingi tutabangua. Kwanza tutaongeza ajira na tuta-add value kwenye korosho zetu na hivyo mkulima atapata fedha ambayo itaongeza kipato chao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye tasnia ya korosho kuna mambo mengi na bado tasnia ya korosho inahitaji usimamizi mkubwa. Kwa hiyo nikuombe Waziri wa Kilimo mwaka jana kwa sababu ya uzembe wao ambao walifanya Bodi ya Korosho ilivunjwa, niombe sasa kwamba muda umefika tuunde hiyo Bodi ya Korosho ili isimamie tasnia yetu ya korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ilifanya jukumu lile kwa wakati ule kwa dharura iliyojitokeza lakini sasa hivi utafute watu waadilifu, na Tanzania wapo waaminifu, ili waanze kusimamia sekta hii ya korosho ambayo takwimu zipo wazi kwamba inaingiza fedha nyingi katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye ushirika. Ushirika kama alivyosema mzungumzaji aliyepita, Mheshimiwa Jitu Soni, tulitarajia kwamba ingekuwa mkombozi kwa mkulima kwa ni ukweli usiopingika kwa Tanzania ushirika bado unamuumiza mkulima, watumishi wa ushirika hawasaidii wakulima. Kwenye zao la korosho ukifuatilia ubadhilifu mwingi unafanywa watumishi wa ushirika wamo ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi katika sekta hii ya ushirika sijui kwa nini; ukienda kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa watumishi wa ushirika na ardhi zamani utakuta wamejitenga pembeni, siku hizi Mheshimiwa Lukuvi amefanya mabadiliko makubwa sana, watumishi wa ardhi wanafuatiliwa. Mheshimiwa Hasunga muda umefika sasa, wafuatilie watumishi wa ushirika, fanya mabadiliko makubwa, wahamishe. Haiwezekani Afisa Ushirika ameanza kusimamia korosho tangu akianza kazi mpaka anastaafu. Mpeleke kwenye pamba akasimamie tasnia ya pamba na pareto atakuwa active, lakini Afisa Ushirika amezaliwa kwenye korosho mpaka anastaafu yupo kwenye korosho hata tija yake na ufanisi utakuwa umepungua. Fanya maamuzi magumu wa Mtwara peleka Musoma akasimamie pamba na wa Musoma peleka Songea akasimamie kahawa na hivyo wataongeza tija lakini watakutana na mazingira mapya ya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nikushauri sana Mheshimiwa Hasungam pamoja na mambo ambayo yanatakiwa ufumue, fumua ushirika, ushirika bado kuna uozo haumsaidii mkulima, ni mzigo kwa mkulima. Mheshimiwa Hasunga tunakuamini na uwezo huo unao; na ulivyoingia tu kwa sababu umeapa tu ukaenda kusimamia korosho, Inshallah utafanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la umwagiliaji. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hatua alizochukua juzi kwa kuwasimamisha wale viongozi wa Tume ya Umwagiliaji. Mheshimiwa Hasunga unga mkono pale alipoishia Mheshimiwa Waziri Mkuu, bado kwenye ngazi ya kanda nako kuna madudu vitu, nenda kafumue kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya Umwagiliaji kama ingekuwa inafanya kazi yake vizuri tusingehangaika sasa hivi kutafuta chakula kutoka maeneo mengine. Sisi Mtwara tuna Ruvuma Basin, Kitere, Rufiji Kusini lakini hayatumiki ipasavyo. Haiwezekani mradi wa mwaka mmoja lakini watu wa tume wanauandaa kwa miaka mitatu na watu wa tume kwa sababu tuna organization structure ambayo ni ya kizamani, wapo kwenye kanda. Kanda ya Kusini ashughulikie Mtwara, Lindi na Ruvuma, hawezi kuwa na ufanisi. Hii tume ivunjwe sasa hivi wawepo kwenye mikoa, yule wa mkoa awajibike kwa RAS na wawepo watendaji kwenye Wilaya wawajibike kwa wakurugenzi; lakini sasa hivi wapo wapo tu, wakiwa kwenye kanda hawajibiki kwa RAS yeyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Chikota kwa mchango wako.

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami nitoe mchango wangu kuhusu hoja iliyo mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niungane na wenzangu kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Dkt. Mpango na Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wengine wa Wizara ya Fedha na Mipango kwa kazi nzuri ambayo wameifanya, na hata wakaja na documents hizi mbili ambazo sasa hivi tunazijadili; ile ya mwongozo wa uandaaji wa bajeti ya Serikali, lakini vilevile na mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo 2020/2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli ukisoma document hii unaona kabisa kuna uwiano na kile ambacho tumekitekeleza mwaka 2018 na ume-take into consideration ile miradi ambayo so far haijakamilika. Kwa hiyo, ni mpango ambao unaendeleza kile ambacho tumeshakianza. Ukiangalia vipaumbele vyetu bado ni vilevile. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa kazi nzuri ambayo wameifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tunawajibika kikanuni na kisheria kuchangia, basi nina mchango katika maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza ni la kilimo, ule ukurasa wa 65. Ukurasa ule unazungumzia ujenzi wa maghala ili kuhifadhi nafaka. Mheshimiwa Ninashauri kwamba, ni wazo zuri kuwa na maghala ya kutosha kwa ajili ya hifadhi ya mazao yetu, hususan mazao ya biashara; korosho, pamba na kadhalika, lakini hili eneo tungetumia vizuri litakuwa eneo ambalo litaongeza uwezo katika Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ambazo zinalima zao la korosho tungeweza kuwapa kazi hii na ikawa chanzo kikubwa cha mapato. Sasa hivi maghala ya watu binafsi tunalipa zaidi ya shilingi 38/= kwa kilo. Sasa kama kwa kazi hii tutawapa fedha na Halmashauri nyingi za Mikoa ya Mtwara na Lindi wameshaandika maandiko yao, wamepeleka TAMISEMI na Wizara ya Fedha na Mipango ili wajenge maghala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, council ambayo inavuna kwa mfano tani 30,000 za korosho wanaweza kupata mpaka shilingi milioni 900 au shilingi bilioni moja kwa mwaka. Kwa hiyo, tukitoa fedha hizi kwa Halmashauri wakajenga maghala ya Halmashauri itakuwa chanzo kizuri cha mapato na hivyo tutaongeza uwezo wa Halmashauri zetu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. Mpango nakuomba sana kwamba hili ni wazo zuri lakini kazi hii tutoe kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa ili tuongeze mapato kwenye Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maghala haya yatatumika muda wote. Kwa maeneo ambayo tunalima korosho utahifadhi korosho, lakini vilevile muda wa msimu wa kusambaza pembejeo yatatumika kuhifadhi pembejeo. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, ile mipango ambayo imeandaliwa na Halmashauri ambazo zinalima korosho, ni muda mwafaka wa kufikiria tuwape fedha ili fedha hizi zizunguke katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na hivyo kuongeza mapato katika Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili kwenye kilimo ni kuhusu muuzaji wa mazao yetu. Napenda sana sehemu hii ya mapendekezo ya mpango yaeleze wazi kwamba mazao ya biashara sasa ni muda mwafaka tutumie TMX. Sheria tulishapitisha mwaka 2015, lakini kuna kusuasua. Kwa mfano, msimu huu wa korosho tuliambiwa kwamba TMX ingeanza kutumika lakini ghafla tukaambiwa kwamba kuna elimu kwa wakulima haikutolewa na ukiangalia sana kuna uwoga tu ambao siyo wa lazima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuchukue nafasi hii sasa tutoe elimu kwa wadau wote wa mazao ya biashara ili Sheria yetu ya Commodity Exchange ambayo tuliipitisha mwaka 2015 ianze kufanya kazi. Nina uhakika kwamba kuna uwezekano mazao mengi ya biashara tukapata bei ya juu tukianza kutumia TMX. Ni taasisi ya Umma, nashangaa kwa nini tunakuwa na wasiwasi kutumia taasisi hii. Ukiangalia sana ni mfumo ule ule wa stakabadhi ghalani, isipokuwa ni advanced stage tu, kwamba unakuwa na maghala na unakuwa na huo mnada kama tunavyofanya sasa hivi kwenye mazao mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri sana kwamba siyo kitu cha kutia uwoga, wadau wote wahusika wapewe elimu ya kutosha ili mazao yale ya kimkakati; korosho, kahawa, tumbaku, tuanze kutumia taasisi yetu ambayo tulishapitisha sheria yake mwaka 2015 na kuna watumishi wapo pale bado wapo idle.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu mwingine kwenye kilimo, Mapendekezo ya Mpango yameelezea vizuri kabisa kwamba kuna kujenga mazingira rafiki katika uwekezaji katika kilimo na bima ya mazao. Hiki ni kitu muhimu sana, lakini bado mazingira ya uwezeshaji kwa wakulima wetu siyo rafiki, mikopo kwa wakulima siyo rafiki, haipatikani kwa wakati, wakulima wanapewa masharti mengine ambayo wanashindwa kutekeleza. Unapomwambia mkulima wa mbaazi au wa korosho kwamba alete andiko la mradi, unamfukuza moja kwa moja, kesho hatakuja tena. Kwa hiyo, tutafute taasisi ambazo zitatoa mikopo rahisi kwa wakulima wetu ili waweze kuongeza uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mikopo hii ina riba kubwa ambapo mkulima mdogo hawezi kuilipa na haipatikani kwa wakati. Ukiniuliza mimi mkulima wa korosho kwamba unatakiwa upate mkopo mwezi wa ngapi ili ukusaidie katika kuzalisha korosho, nitakwamba mwezi Aprili, lakini mikopo ya aina hii inapatikana mwezi Oktoba wakati msimu au korosho zimeshaanza kuuzwa sokoni. Kwa hiyo, haimsaidii mkulima. Kwa hiyo, naomba tuangalie taasisi zilizopo jinsi ya kusaidia mikopo kwa wakulima wetu na kiwango cha riba kiwe kidogo na iwe rafiki na ipatikane kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la kufunganisha uchumi na maendeleo ya watu. Ukisoma ukurasa wa 68 umezungumzia suala la elimu, nami niunge mkono kwa sababu kuna mapendekezo mazuri yametolewa pale kwenye elimu ya msingi, sekondari na vyuo vikuu, lakini tunasahau watumishi wetu; in-service training haipo na hakuna kitu muhimu kwa watumishi wetu kama in-service training. Kwa hiyo in-service training isisitizwe kwenye Mapendekezo ya Mpango wetu kwamba ni kitu muhimu ili watumishi wetu wapate maarifa na ujuzi mpya ili waweze kufanya kazi vizuri. Vilevile nilisahau, kuwe motisha kwa wafanyakazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la miundombinu, nalo napenda kushauri. Imeelezewa vizuri kabisa; ujenzi wa madaraja mipakani, ujenzi wa barabara kuunganisha mikoa, lakini changamoto iliyopo sasa hivi ni barabara za vijijini. Mpango unaelezea vizuri kwamba kujenga na kukarabati barabara zenye kufungua fursa; fursa nyingi sasa hivi zipo vijijini, lakini changamoto kubwa sasa hivi ni barabara za vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeanzisha TARURA lakini TARURA haina fedha, haina uwezo wa kufanya kazi, hakuna Wahandisi. Kwa hiyo, inaomba sasa ile formula ya kugawa fedha za Mfuko wa Barabara iangaliwe upya ili fedha za kutosha zipeleke TARURA ili iweze kutimiza majukumu yake. TARURA ndiyo wanajenga barabara za vijijini, tunatoa mazao vijijini na kupeleka sokoni. Kwa hiyo, mgao wa road fund uangaliwe vyema ili TARURA wapate fedha za kutosha ambazo zitasaidia katika ujenzi wa barabara za vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ujenzi wa barabara za mipakani, Mheshimiwa Waziri alifika Kilambo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji na aliahidi kutoa gari, nimpongeze na kumshukuru kwamba kwa taarifa tulizonazo gari imeshafika Mtwara lakini bado dereva hajapatikana. Kama Waziri ameshakula ng’ombe mzima sidhani atashindwa kumalizia mkia. Naomba Katibu Mkuu wako afanye mpango dereva apatikane ili Kituo cha Kilambo kipate usafiri ili waweze kukusanya vizuri mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya pili pale Kilambo lazima tujenge daraja la kudumu kati ya Tanzania na Msumbuji. Tulijenga Mtambaswala lakini Mheshimiwa Waziri kama alivyoona pale watu wengi kutoka Msumbiji wanatumia kivuko cha Kilambo. Ukitoka Kilambo mpaka Mji wa Palma - Msumbiji ni kama saa mbili wakati ukitoka kule Mtambaswala ni zaidi ya saa tano. Kwa hiyo, watu wengi wanapenda kutumia kivuko cha Kilambo na kwa sababu kwenye biashara hatuwezi kulazimisha watu na mizigo mingi inapita pale, tujenge daraja, tujenge kituo kingine cha forodha ili tukusanye fedha za kutosha kwa ajili ya kuongeza mapato ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na huo ndiyo mchango wangu, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie hoja iliyopo mezani kwetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ambayo anaifanya, niwapongeze wasaidizi wake; Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango na Waziri Mkuu wetu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, kwa kazi nzuri ambayo anaifanya. Na tumeona jinsi anavyoshughulika kwenye sekta mbalimbali; kilimo, elimu, madini na shughuli zingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nitumie nafasi hii kumpongeza Waziri wa Fedha na Mipango, kaka yangu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba na Naibu wake, Mheshimiwa Eng. Masauni, kwa kazi nzuri wanayoifanya. Watu hawa wamedhihirisha wazi kwamba ni wasikivu, na ni watu ambao wanafikika na wanapokea ushauri ambao wanapewa.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile niwapongeze watendaji wa Wizara hii, Katibu Mkuu na Naibu Makatibu Wakuu. Lakini vilevile kipekee, nimpongeze Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na Wajumbe kwa kuja na ushauri na maoni ambayo yatasaidia katika uboreshaji wa bajeti yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze mchango wangu kwa kujielekeza kwenye usimamizi, ufuatiliaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kwanza nianze kuipongeza Wizara kwa kasi kubwa ya kupeleka fedha kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa. Hii imejidhihirisha wazi kwa sababu zimepelekwa fedha, milioni 500, kwa ajili ya TARURA. Lakini vilevile kuna ongezeko kubwa la fedha ambazo zitakwenda baadaye kwenye TARURA. Kuna fedha za ukarabati na fedha za maboma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu ni kwamba hizi fedha sasa ni nyingi, na kusimamia miradi hii kutoka Dodoma hatuwezi kufanikiwa. Ushauri wangu ni kwamba tuimarishe sekretarieti za mikoa. Nimpongeze dada yangu, Mheshimiwa Ummy, kwa wazo la kuimarisha sekretarieti za mikoa. Ni wazi kwamba tukiimarisha sekretarieti za mikoa watafanya ufuatiliaji kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa na miradi yetu itatekelezwa kwa uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, na ikiwezekana marekebisho ya sheria yafanywe; ile Sheria yetu ya Tawala za Mikoa (Regional Administration Act) Na. 19 ya mwaka 1997, sheria zile za Serikali za Mitaa na Sheria ya Utumishi. Kwa sababu kwa sasa hivi Katibu Tawala wa Mkoa ni mamlaka ya nidhamu kwa watendaji waliopo kwenye regional secretariat, anapokwenda kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa hawezi kumgusa mtendaji yeyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaweza tukarekebisha sheria hizo ili kuhakikisha tuna usimamizi imara katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na hivyo kusababisha usimamizi imara katika miradi yetu ya maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu wa pili unahusu mradi wa Liganga na Mchuchuma. Nitumie nafasi hii kumpongeza Rais kwa maelekezo yake aliyotoa hivi karibuni akiwa ziarani Mwanza. Rais ameelekeza mambo makubwa mawili; kwanza kupunguza urasimu, na pili, kuondoa vikwazo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na ninaomba ninukuu; “Tumeimba toka nikiwa Waziri, mpaka leo nimefika hapa nilipo Mchuchuma na Liganga haijatoa matunda.” (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namshukuru Mheshimiwa Rais kwa maelekezo haya. Mradi huu ni mkubwa na ni kichocheo cha maendeleo kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na mikoa ya kusini. Mradi huu ukitekelezwa utaongeza kasi ya mahitaji ya ujenzi wa reli kwa kiwango cha SGR kutoka Mtwara kwenda Mbambabay. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hivyo tu, ile dhana sasa ya Mtwara Corridoe itaonekana. Na utaongeza matumizi ya Bandari ya Mtwara; hapa imeonekana kwamba Bandari ya Mtwara sasa hivi matumizi yake ni machache, lakini Bandari ya Mtwara umefanyika uwekezaji mkubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, una bilioni 157 zimewekezwa pale; una mitambo ya kisasa; vilevile sasa hivi inaweza kuhudumia metric tons milioni moja, lakini mizigo pale ni michache. Mradi wa Liganga na Mchuchuma ukianza kutekelezwa basi Bandari yetu ya Mtwara itatumika ipasavyo na hivyo kuongeza uchumi wa wana Mtwara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kodi ya VAT na ushuru wa bidhaa wa vifungashio na mashine za kufungashia korosho na karanga. Sekta ya ubanguaji wa korosho bado ni changa, inahitaji kuendelezwa. Na kuna changamoto nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tunabangua asilimia 20 tu ya korosho ambayo tunazalisha, tunauza korosho ghafi asilimia 80. Maana yake ni nini; tunapeleka ajira kwa wenzetu. Kama tukibangua korosho kwa asilimia kubwa ina maana tunazalisha ajira, lakini tunaongeza thamani ya korosho yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa pamoja na kushushwa kodi katika maeneo mbalimbali, kuna sehemu ndugu yangu, Waziri wa Fedha, naomba uiangalie tena. Kuna mashine za kufungashia korosho ambayo ni HS Code 8422300; kuna vifungashio SH Code 3923210; hivi mmevisahau na matokeo yake wabanguaji wadogo wanapata vifungashio kwa shilingi 3,000 mpaka 3,500. Tukitoa VAT kuna uwezekano kabisa wabanguaji wadogo watanunua vifungashio hivi kwa shilingi 600. Na hivyo itaongeza uwezo wetu wa kubangua kwa makundi ya vijana na akina mama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba sana kwamba VAT iondolewe katika maeneo hayo ili kukuza sekta yetu ya ubanguaji na hatimaye tuuze nje korosho zilizobanguliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la export levy kwenye korosho. Ni matarajio yangu kwamba wakati wa majumuisho Waziri wa Fedha na Mipango atakuja kutuambia kwamba nini kitafanyika katika export levy. Na hapa lengo kubwa ni kuchukua sehemu ya export levy kwenye korosho tupeleke kwenye sekta ya korosho. Tutoe motisha kwa wabanguaji, lakini vilevile itafute pembejeo kwa wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo haya maeneo mawili; incentive kwa wabanguaji na upatikanaji wa pembejeo za kutosha, utasaidia kusukuma au kuendeleza sekta ya korosho ambayo sasa hivi kwa miaka minne uzalishaji unaendelea kupungua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema pale awali, vilevile ubanguaji wetu tunabangua asilimia 20 tu ya kile ambacho tunazalisha. Kwa hiyo namuomba Waziri wa Fedha wakati anafanya majumuisho aliangalie hili na atueleze waziwazi kwamba sehemu ya export levy itapelekwa kwenye sekta ya korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu yangu ya mwisho ni suala na Madiwani na Udiwani. Mheshimiwa Waziri wa Fedha amezungumza vizuri kabisa, kwamba Madiwani ni Wabunge katika kata zetu. Madiwani wanafanya kazi nyingi, wana changamoto nyingi na wanafanya kazi zetu nyingi wakati sisi Wabunge hatupo majimboni.

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Serikali kwa kuamua kulipa posho kutoka Hazina. Lakini bado kuna kazi ya kufanya hebu tukiangalie kile anachokipata Diwani. Kama kweli ni Mbunge wa kata tumuongezee maslahi yake, tuongeze posho yake ili aweze kutekeleza majukumu yake vizuri, ili aweze kufanya kazi yake vizuri. Asiwe ombaomba kwa wakuu wa idara, asiwe mnyonge kwa mkurugenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kukiwa na Madiwani dhaifu kutakuwa na halmashauri dhaifu, tukiwa na Madiwani imara tutakuwa na halmashauri imara. Kwa hiyo, naomba, uamuzi wa kupia posho zao kutoka Hazina ni mzuri lakini twende mbele zaidi tuangalie kile kinachotoka Hazina ni shilingi ngapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Madiwani wengi baada ya kuingia kwenye Udiwani wamepata mikopo kama tulivyofanya sisi Wabunge. Kwa hiyo, Madiwani sasa hivi wanapata kitu kidogo sana. naomba turekebishe ili na wao ukifika mwisho wa mwezi wawe na appetite ya kuangalia kwamba nini kilichopo kwenye akaunti zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukifanya hivyo tutawahamasisha Madiwani, watakuwa madhubuti, wataweza kuwa na ujasiri wa kuwahoji watendaji na kumsimamia mkurugenzi. Lakini tukiwa na Madiwani ambao vipato vyao ni vidogo, hawana kipato cha kutosha, watakuwa dhaifu na hivyo wao watakuwa kazi yao ni kuitikia kile ambacho kimewasilishwa na wakurugenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi kuchangia taarifa hizi za Kamati mbili, Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa na ile ya Katiba na Sheria. Mchango wangu utajikita katika maeneo manne, eneo la kwanza linahusu utekelezaji wa miradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyooneshwa kwenye taarifa zote mbili kwamba, utekelezaji wa miradi bado sio wa kuridhisha kwa sababu fedha kutoka Hazina hazipelekwi kwa wakati. Hii ina madhara sana kwa sababu, mamlaka za Serikali za Mitaa kwenye ngazi ya Wizara inapopanga mpango mpya wa bajeti wakati fedha zile za mwaka uliopita hazijapelekwa kwa wakati huwa wanakuwa katika kigugumizi kwamba, nini kifanyike katika mwaka uliopita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipobadilisha budget circle tulikuwa na matarajio sasa kwamba, kwenye quarter ya kwanza au ya pili, fedha za maendeleo zingetolewa, budget circle imebadilishwa, mambo ni yaleyale, fedha hazitolewi kwa wakati. Sasa hivi Mamlaka za Serikali za Mitaa zinaandaa bajeti, lakini hawajapata fedha nyingi za maendeleo! Kwa hiyo, wanaishia katika kugombana tu kwamba, watekeleze ipi? Ile bajeti ya mwaka jana iwe kama bakaa kwamba ni miradi ambayo haikutekelezwa ili watenge fedha nyingine mwaka huu au wa-assume kwamba fedha zitaletwa ili watekeleze hiyo miradi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zinapochelewa hata hili tatizo ambalo limebainishwa kwenye Kamati ya Sheria kwamba Ofisi ya Makamu wa Rais inatengenezwa chini ya kiwango ni kwa sababu ya fedha kutolewa kidogo kidogo, kwa hiyo, hata Mkandarasi hawezi kutekeleza mradi kama ilivyopangwa kwenye mpango wa awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili utahusu huu mradi wa TASAF, hakuna anayepinga mradi huu. Mradi huu kwa kweli umenusuru kaya maskini na umeleta mchango mkubwa sana katika kuboresha maisha ya kaya maskini katika nchi yetu, vilevile umewezesha sasa kaya maskini kupata huduma za kiafya, kielimu, ambapo bila mradi huu hawa wananchi wasingepata huduma hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto mbili ambazo nimeziona katika utekelezaji wa mradi huu. Kwanza lile zoezi la kuwatoa wanufaika ambao hawana sifa. Wale wanufaika walichaguliwa kwa kupitia mchakato ambao ulihusisha watu wengi sana na baadaye wakaanza kupata ule msaada, lakini lilipokuja zoezi sasa la kuwatoa hawa watu wameondolewa na wanaambiwa sasa hivi kwamba, warejeshe fedha zote ambazo wamelipwa chini ya mpango huu, wengine hawana uwezo kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi katika Jimbo langu, Kijiji cha Namisangi kuna wananchi ambao wakisikia mlio wa gari tu wanakimbia kwa sababu wamepewa barua na Mkurugenzi warejeshe zaidi ya sh. 400,000 na hawana uwezo wa kurejesha. Kwa hiyo, naomba Wizara husika sasa imchukulie hatua yule Mratibu ambaye kwa uzembe wake alipeleka fedha kwa watu ambao sio wahusika, lakini isiwe hawa wananchi ambao sasa wanapata taabu ya kulala porini wanaogopa kukamatwa kwa sababu ya fedha ambazo walikuwa wananufaika wakati ule mchakato ulipoendeshwa kwa taratibu ambazo zilifuatwa wakati huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kuna changamoto katika uratibu wa mradi huu kwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa mipya. Kwenye Halmashauri mpya unaambiwa kwamba, wanufaika wataendelea kupata huduma kutoka kwenye Wilaya Mama, kwa hiyo, inakuwa ngumu sana Mkurugenzi wa Wilaya Mpya kufuatilia zoezi hili kwa sababu, bado Mratibu anatumika wa ile Wilaya Mama. Nafikiri wakati umefika sasa kwa Wizara husika ione kwamba, eneo la utawala likianzishwa basi na taratibu za Wilaya ile kunufaika na mradi huu ziendelee kama ilivyo Wizara nyingine, hili suala la kwamba, waendelee kuratibiwa kutoka kwenye Halmashauri Mama inaleta urasimu na inakuwa ni vigumu katika kusimamia mradi huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu yangu ya tatu ni kuhusu Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC). Imeoneshwa hapa na Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa kwamba kuna kusuasua kuanzishwa kwa Tume hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha sana kwa sababu, baada ya kupitisha Sheria hii tuliona kwamba, ni mkombozi kwa Mwalimu, lakini bado kuna kusuasua. Sasa wakati sheria hii ilipoanzishwa watu walitoa maoni yao kwamba, tusibadilishe jina, hii Tume ipewe nyenzo. Tunakokwenda sasa hivi inalekea hii Tume haitapewa nyenzo, kwa hiyo, inakuwa tumebadilisha jina tu, lakini utaratibu ni ule ule. Ni kama tulivyofanya kwenye sekta ya elimu, Ofisi ya Mkaguzi wa Shule tukabadilisha kwamba, Mdhibiti wa Ubora wa Elimu, lakini tumebadilisha jina tu rasilimali bado ni chache na Wakaguzi bado wanapata shida na hawawezi kuzifikia shule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipotenga fedha za kutosha kwa ajili ya kuanzisha Tume ya Utumishi wa Walimu tutakuwa tunawadai Walimu wawajibike wakati haki zao hatujawapa. Tunakimbilia kuwavua vyeo, sijui kuwateremsha madaraja, wakati vitu vyao vya msingi hatuwatekelezei! Hebu niiombe Serikali yangu itenge fedha za kutosha ili tuanzishe hii Tume ya Utumishi wa Walimu, Walimu wapate stahiki zao, Walimu wapate motisha, Walimu wawe na chombo kimoja cha kuwatetea halafu baadaye tuwabane katika uwajibikaji. Haiwezekani tuwabebeshe mzigo mkubwa, lakini inapokuja kuzungumzia maslahi ya Walimu sisi tunarudi nyuma. Kwa hiyo, lazima tuhakikishe kwamba, Walimu hiki chombo kinaanzishwa haraka na kinatengewa fedha za kutosha ili kiweze kutatua kero za Walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie suala la utawala bora. Yamesemwa mengi sana kuhusu madaraka ya Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa. Hili suala ni two way traffic, kuna watendaji ambao ni wabovu, naomba Waheshimiwa Wabunge tunapochangia tusiwalee wale watendaji wabovu. Kuna watendaji ambao wapo kwenye mamlaka ya Serikali za Mitaa ni nusu miungu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna DMO mmoja katika Halmashauri fulani akipata fedha za Busket Fund anaangalia zile semina tu za kuhamasisha sijui kutoa mabusha, kufanya nini, lakini dokezo la kununua dawa, amepata fedha migao miwili ya Busket Fund, hajanunua dawa, lakini zile za posho za kwao wameshatumia tayari! Kwa hiyo, wananchi wanapata shida kwa sababu ya uzembe wa mtu mmoja, anapochukuliwa hatua tusione kwamba ni matumizi mabaya ya sheria, hapana ni two way traffic!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande mwingine wale Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa wasitumie vibaya ile sheria iliyoanzisha Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Sura Na. 97 ya mwaka 2002 inatoa maelekezo, iko wazi kabisa. Inatoa maelekezo nini kifanyike mtu anapokamatwa kwa masaa 48 lakini Wakuu wengi wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa, hawaitumii. Hata Wakurugenzi kwa sababu kuna ishara sasa hata Wakurugenzi wanataka kuingia huko kwamba kuna maeneo mengine hakuna maelewano kati ya Mameya na Wakurugenzi. Kwa hiyo, tutengeneze mafunzo sasa kwa Wakurugenzi, Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja iliyopo Mezani kwetu ambayo ni Bajeti Kuu ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nianze kwa kumpongeza Rais wetu kwa kazi nzuri ambayo anaifanya, na kwa maelekezo ambayo ameyatoa wakati wa uandaaji wa bajeti hii na kuja na bajeti ambayo inajibu hoja za wananchi wetu. Nampongeza sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nimpongeze kaka yangu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, kwa kazi nzuri anayoifanya; pamoja na kaka yangu, Mheshimiwa Hamad Hassan Chande, kwa kazi nzuri ambayo anaifanya; pamoja na Katibu Mkuu na Mlipaji Mkuu wa Serikali na watendaji wa Wizara ya Fedha na Mipango kwa kazi nzuri ambayo wanaendelea kuifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza mchango wangu katika sekta ya korosho. Na nianze kwa kuipongeza Serikali kwa mambo matatu ambayo yamefanyika hivi karibuni; kwanza, usambazaji wa pembejeo bure kwa wakulima wa korosho. Kwa hilo naipongeza Serikali yangu. La pili, kwa kuondoa ushuru wa forodha kwa vifungashio; hii itarahisisha, kwanza kwa wabanguaji na katika ufungashaji wa korosho, kwa hiyo mwaka huu hatutakuwa na changamoto ya vifungashio.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, nipongeze kitu kikubwa ambacho kimefanyika; suala la kurejesha asilimia 50 ya export levy kwenda kwenye korosho tena. Mtakumbuka mwaka 2017/2018 hiki kitu kiliondolewa na sasa hivi kimerejeshwa, hongereni sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mimi kwenye export levy nina mambo ya kushauri. Kwanza, hiyo export levy hapo awali ilikuwa asilimia 65, ilikuwa inachukuliwa na mfuko kuendeleza zao la korosho na 35 inachukuliwa na Mfuko Mkuu wa Serikali. Sasa hivi imekuwa 50 kwa 50, asilimia 50 inakwenda kwenye Mfuko wa Kuendeleza Kilimo (ADF) na asilimia 50 inakwenda kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Naomba nishauri kwamba fedha hizi ziende Bodi ya Korosho zikaendeleze korosho.

Mheshimiwa Naibu Spika, korosho inahitaji gharama kubwa; unahitajika utafiti, zinahitajika pembejeo, kunahitajika maafisa ugani, kunahitajika maelekezo kwa wakulima, tuna mpango wa mtu wa block farming kwenye korosho. Kwa hiyo fedha hizi zisibaki kapu kuu, fedha hizi zibaki Bodi ya Korosho ili zikaendeleze zao la korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na kama kuna mahitaji ya kiasi cha fedha hizi kupelekwa ADF, basi turudi kwenye formula ya awali, twende 65 ili 15 iende ADF, 50 iende Bodi ya Korosho. Huo ndiyo ushauri wangu na kwa Serikali yangu sikivu naona hili litafanyiwa kazi kwa manufaa ya kuendeleza zao letu la korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi inasema itakapofika mwaka 2025 uzalishaji wa korosho uwe tumezalisha kwa tani 700,000. Mwaka huu tuna tani 240,000, kwa hiyo tuna kazi kubwa ya kufanya. Tukiwekeza fedha nyingi kwenye korosho, basi malengo haya yatafanikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili kuhusu korosho ni suala la viwanda 12, vile vya ubanguaji wa korosho. Naishauri Serikali kuchukua maamuzi magumu. Wale wanunuzi wa vile viwanda hawana mpango wa kuvifufua tena, vile viwanda walipewa kwa bei ya chini sana, si zaidi ya milioni 55, na wao wanavigeuza kuwa maghala sasa hivi. Kwa sababu wameshapata faida nyingi, sasa ni muda mwafaka wa kufanya maamuzi magumu ili viwanda vile virejeshwe Serikalimi zipewe taasisi zetu; wanaweza kupewa Bodi ya Korosho, Halmashauri au vyama vikuu vya ushirika, tuna TANECU na MAMCU Mtwara, wanaweza kuviendesha hivi viwanda ili ubanguaji wa korosho uweze kufanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu Msumbuji wanatuzidi sasa hivi kwenye ubanguaji, sisi bado kiwango chetu cha ubanguaji ni kidogo sana; na korosho iliyobanguliwa thamani yake ni kubwa sana kwenye Soko la Dunia. Kwa hiyo naomba tufanye maamuzi magumu, viwanda hivi virejeshwe. Na wale wanunuzi hawana mpango wa kuviendeleza, wanafanya ma-godauni, na hawana mpango wa kubangua korosho.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu mwingine ni kuhusu nafasi ya kitengo cha wakaguzi wa ndani. Kwenye hotuba ya Waziri amesema vizuri kwamba tunataka kurejesha udhibiti wa fedha za umma na nidhamu ya fedha za Umma. Na amesema atafanya maboresho makubwa sana kwenye nafasi ya Internal Auditor General, na anasema atampa vote maalum, na amesema atamuongezea watumishi na vitendeakazi; hili ni suala la kupongeza sana. Kwa sababu tukiimarisha ukaguzi wa ndani tutafanya udhibiti wa fedha katika taasisi zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hapa ninashauri mambo yafuatayo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, siyo suala tu la kuongeza rasilimali fedha, tupate wakaguzi wa ndani waadilifu. Tusipofanya hivyo, ripoti ya ukaguzi inakuwa ni biashara. Mkaguzi anakwenda kukagua pale, hoja kwake ni biashara. Anamwonesha Mkuu wa Idara au Mkuu wa Kitengo kwamba kuna hoja hii kwako, unatoa ngapi ili tuifute? Kwa hiyo, lazima tuwe na wakaguzi wa ndani ambao wana maadili ya kutosha, uzalendo na weledi wa kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hivyo tu, Mheshimiwa Waziri amesema kwamba taarifa za ukaguzi wa ndani ziwe shared na viongozi wa juu ili kutoa udhibiti. Kwa mfano, umesema taarifa za halmashauri apewe Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya. Hapo nashauri zisiishie kwa Mkuu wa Wilaya, kwa sababu Mkuu wa Wilaya anashiriki kwenye mabaraza ya Madiwani na kila baada ya miezi mitatu, taarifa ya internal auditor inapelekwa pale. Naomba taarifa hizi zipelekwe kwenye RS, kule Mkuu wa Mkoa na RAS watapanga mechanism ya ufuatiliaji. Vilevile zile za RS ziende kwa Katibu Mkuu TAMISEMI, zisiishie kwa RC. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu ya tatu ni kuhusu matumizi ya bandari zetu. Tunafanya vizuri sana kwenye Bandari ya Dar es Salaam, lakini Bandari ya Tanga na Mtwara bado hatujafanya ipasavyo. Hatujafanya ipasavyo kwa sababu tumefanya uwekezaji mkubwa sana kwenye Bandari ya Tanga na Bandari ya Mtwara, lakini return yake bado ni ndogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Balozi wa Tanzania nchini Malawi, ndugu yangu Polepole ameanza vizuri. Wakati anawasilisha hati zake, amesisitiza nchi ya Msumbiji kutumia Bandari ya Mtwara na ushoroba wa Mtwara, na hii ndiyo dhana ya Mtwara Development Corridor. Kwa hiyo, naomba mabalozi wengine wa Southern Sudan wahakikishe kwamba bandari yetu ya Tanga inatumika ipasavyo. Congo DRC, Zambia watumie bandari ya Mtwara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie sasa kwa kuishukuru Serikali yangu kwa shughuli ambazo zimefanyika wiki mbili zilizopita. Kwanza, kuna kusaini mkataba wa makubaliano ya awali ya LNG. Hiki ni kitu ambacho kilikuwa kimelala kwa muda mrefu. Namshukuru na ninampongeza Mheshimiwa Rais kwa kufufua mazungumzo haya na sasa yanaenda vizuri. Ushauri wangu kwa Serikali ni kwamba, muda ni huu sasa wa kuwaelekeza wananchi wa Mikoa ya Mtwara na Lindi kutumia fursa kwa uwekezaji huu mkubwa wa zaidi ya Shilingi trilioni 70 ili mradi utakapoanza, basi nao wasiwe watu wa kushangaa, nao washiriki katika fursa hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nampongeza Mheshimiwa Rais, alitoa maelekezo maalum siku ya kusaini ule mkataba. Alisema kwanza lazima kuwe na uwekezaji maalum au kuwe na maboresho maalum maeneo ya mradi kwa maana ya Mtwara na Lindi kwa maana ya upatikanaji wa huduma za jamii. Maelekezo ambayo tumepewa pale ni kwamba kwa ajira zisizo rasmi na rasmi kutakuwa na wafanyakazi zaidi 10,000 kwenye project hii ya LNG. Haitakiwi Lindi iwe kama ilivyo sasa hivi, haitakiwi Mtwara iwe kama ilivyo sasa hivi. Kuwe na upatikanaji wa maji ya kutosha, umeme wa uhakika na matibabu ya uhakika ili hata wageni watakapofika, basi waweze kupata huduma hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tulikuwa na utiaji saini wa miji 28 ikiwepo na mradi wetu mkongwe wa Makonde. Naomba sasa hao watekelezaji wa mradi waje katika mradi ili ujenzi mradi uanze kujengwa katika maeneo yetu ili kuhakikisha upatikanaji wa maji katika Halmashauri ya Newala, Mtwara na Nanyamba.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi naungana na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayofanya katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni Mheshimiwa Rais alifanya ziara Mkoani Mtwara na ametufanyia kazi kubwa sana, mojawapo ikiwa ni kutatua changamoto ambayo ilikuwa inakabili Kiwanda cha Dangote. Hapa jana kuna mchangiaji mmoja alitoa maelezo ambayo pengine
alichokifanya Rais kule Mtwara hakukielewa, anasema Dangote amepewa eneo la mgodi kwa ajili ya kuchimba makaa na maamuzi yale yatakuwa na athari kama tutakavyofanya mchanga kutoka kwenye migodi ya almasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichofanyika Mtwara ni tofauti na hicho alichokisema mchangiaji kwa sababu Mheshimiwa Rais ametatua changamoto mbili kuu ambazo Kiwanda cha Dangote kilikuwa kinakabiliwa nayo. Changamoto ya kwanza ilikuwa ni upatikanaji wa Makaa na alisema tunaamua hapa hapa. Mheshimiwa Muhongo na Mawaziri wengine walikuwepo na walipewa siku saba kwamba taratibu zote zifuatwe ili achimbe mkaa mwenyewe na kodi zote stahili alipe ili apeleke kwenye kiwanda chake cha Mtwara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu cha pili, Mheshimiwa Rais alitatua tatizo la muda mrefu ambalo ni upatikanaji wa gesi asilia kutoka Madimba. Tulikuwa tunalalamika hapa kwamba wawekezaji wakubwa hawasikilizwi, kwa hiyo, Mheshimiwa Rais akatoa maamuzi pale kwamba TPDC impe
umeme Dangote bila kupitia kwa mtu mwingine wa pili. Kwa hiyo, maamuzi yale ni ya kumpongeza sana Mheshimiwa Rais na siyo ya kumkatisha tamaa kwamba alichofanya siyo sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwa niaba ya Wabunge wa Mtwara na kwa niaba ya wananchi wa Mtwara tunamshukuru sana Rais wetu kwa maamuzi mazito aliyoyafanya katika ziara yake Mkoani Mtwara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nichangie hoja nyingine ukurasa wa 23 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hatua alizochukua katika kusimamia zao la korosho. Wananchi wa Mtwara na wananchi wa Kusini wanakupongeza kwa kile ulichokifanya mwaka huu. Kwanza hukusita kuvunja bodi pale uzembe ulipotokea, lakini pili, ulichukua hatua ya kusimamisha uendeshaji wa Mfuko wa
Pembejeo na kazi hiyo sasa ikapelekwa kwenye Bodi ya Korosho na kusimamia kwa karibu kwa yale yanayoendelea katika tasnia ya korosho katika msimu wote. Hata pale zilipopotea tani 2,000 kwenye lile ghala la Masasi, ulichukua hatua za haraka na wale watuhumiwa sasa hivi
wamefikishwa kwenye vyombo vya sheria. Tunakupongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada hizo, bado kwenye mfumo wetu wa Stakabadhi Ghalani kuna changamoto ambazo kwa usimamizi wako Mheshimiwa Waziri Mkuu na Waziri wa Kilimo nafikiri msimu huu mtazirekebisha ili bei ya korosho izidi kupaa, na sisi Wana-
Mtwara tunategemea bei ya korosho mwaka huu itafika kilo shilingi 5,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto zilizopo ni pamoja na wakulima kucheleweshewa malipo na hii ni kwa sababu vyombo vingi havikujiandaa na ununuzi wa msimu wa mwaka huu na ule utaratibu wa mwaka huu. Tumeona pale ghala ya Benki Kuu ilikuwa inaingia Mtwara kila baada
ya siku moja. Kwa hiyo, nafikiri kwa sababu sasa hivi Tawi la Benki Kuu limezinduliwa Mtwara, yale ambayo yalikuwa yanatokea mwaka huu kwamba kila baada ya siku moja zinapelekwa fedha Mtwara, nafikiri msimu ujao hayatajitokeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kuna changamoto ya usafirishaji. Tumeona pale zikitokea kauli mbili; Watendaji wa Bandari wanasema Bandari ya Mtwara inaweza kusafirisha korosho lakini Mkoa wa Lindi wanasema kwamba Mtwara hawana uwezo wa kupeleka korosho zote, kwa hiyo, tusafirishe kwa barabara. Yote kwa yote, kuna changamoto pale zimejitokeza. Kwa hiyo, ni matarajio yangu kwamba Mamlaka ya Bandari, Wizara husika na Wizara ya Kilimo wataishughulikia hii changamoto ili mwakani korosho zote zisafirishwe kwa Bandari yetu ya Mtwara kwa sababu korosho zinaposafirishwa kwa Bandari ya Mtwara, tunawapa vijana wetu ajira, lakini vilevile tunadhibiti ununuzi wa korosho holela ule ambao unajulikana kwa jina la kangomba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo tunatakiwa tulifanye katika mfumo wetu wa Stakabadhi Ghalani, tuongeze uwazi. Sasa hivi kuna malalamiko kwa wakulima kwamba mkulima anauza korosho yake kwenye mnada wa pili, lakini amelipwa kwa bei ya mnada wa tano. Kwa hiyo, nafikiri hili Wizara ya kilimo italifanyia kazi. Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, katika mfumo huu wa Stakabadhi Ghalani, kuna tozo moja. Kwanza tumshukuru na tumpongeze Mhesimiwa Waziri Mkuu, mwaka 2016 kwa usimamizi wake walifanikiwa kuondoa tozo tano kwenye zao la korosho. Kwa hiyo, kuna tozo moja ambayo inalalamikiwa sana na wakulima, tozo ya uchangiaji wa gunia. Ni matarajio yangu kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya kilimo na wadau watalishughulikia suala hili ili gunia zinunuliwe na Bodi ya Korosho au Mfuko wa Kuendeleza Zao la Korosho ili wakulima wasichajiwe ile fedha ya kuchangia ununuzi wa gunia kila kilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende ukurasa wa 36 ambao unahusu elimu na mimi nakubaliana kauli ya Waziri Mkuu kwamba uchumi wa viwanda lazima unahitaji rasilimali watu yenye weledi, lakini rasilimali watu yenye weledi inapatikana kukiwa na mfumo bora wa elimu. Lazima hapa
tukubaliane kwamba tunapozungumzia mfumo bora wa elimu au tunapozungumzia elimu bora, hatuwezi kusahau mahitaji na kero za walimu. Kwa hiyo, naomba sana Serikali yangu ya Awamu ya Tano ijikite katika kuondoa changamoto zinazowakabili Walimu. Walimu bado wana malalamiko kwamba wana madai, bado hatujaandaa incetive package kwa Walimu wapewe motisha; lakini Walimu vile vile wanahitaji mafunzo kazini. Kwa hiyo, naomba Serikali chini ya Mheshimiwa Profesa Ndalichako na Mheshimiwa Simbachawene, basi walishughulikie hili suala la matatizo ya walimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie mchango wangu kuhusu suala la maji. Kwanza naipongeza Wizara ya Maji kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya na katika Jimbo langu kuna harakati ambazo zinaonekana, za kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maji kutoka asilimia 40 kwenda kwenye malengo yetu ya kufika asilimia 85, lakini bado kuna changamoto nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya kwanza kuna ule mradi ambao tunatarajia kupata mkopo kutoka Benki ya India, miradi 17 ambapo ni pamoja na mradi wa Muheza, ule mradi wa Makonde. Kwa kweli ni muda mrefu sasa hivi tunataka mradi huu uanze kutekelezwa. Kila siku
mnasema kwamba tunamalizia financial agreement, lakini sasa hivi natarajia Wizara ya Maji itaongeza speed ili mradi huu uanze kutekelezwa. Mradi huu ukianza kutekelezwa kwa miradi ile 17, tuna uhakika kwamba asilimia ya watu wetu ambao wanapata maji vijijini itaongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, kwa sisi Wana- Mtwara kuna mradi wa kutoa maji Mto Ruvuma na kupeleka Manispaa ya Mtwara. Mradi huu ni tegemeo kwetu na utaongeza upatikanaji wa maji katika Jimbo langu la Nanyamba. Kwa hiyo, naomba pia na utekelezaji wa mradi huu usimamiwe kwa karibu na fedha zipatikane ili utekelezaji wake uanze mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na yale yote ambayo yapo katika kitabu cha Waziri Mkuu yakitekelezwa, tuna uhakika kwamba nchi yetu tunakwenda kule ambako tunatarajia. Ahsante sana.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri katika Wizara hii. Pamoja na pongezi hizo nina mchango katika maeneo yafuatayo:-
Hifadhi ya Mazingira ya Bahari; ni wazi kuwa jitihada zetu za kuzuia uvuvi haramu ambao huharibu mazingira ya bahari na kuathiri maisha ya viumbe baharini bado hatujafanikiwa vya kutosha. Bado kuna matukio mengi ya uvuvi haramu ambayo yamekuwa yakitokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na sababu nyingine zinazochochea uvuvi huu ni kukosa nyenzo za kisasa za kuvua kwenye bahari kuu. Huko awali tulikuwa na mradi wa MACEMP ambao ulikuwa unasaidia kukabiliana na changamoto hizi. Katika mradi huu wakazi wa pwani waliwezeshwa kutegemea shughuli nyingine na kupunguza utegemezi wa bahari. Kwa kuwa bado wananchi wa pwani wanaendelea kukumbana na changamoto hizi ni vema Mradi huu ukaendelea hata kwa kutumia fedha zetu za ndani baada ya kukamilika kwa muda wa mradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mto Ruvuma; tabia ya kubadilika uelekeo wa Mto Ruvuma na matawi yake usiachwe bila kuwa na stadi ya kutosha. Naomba Serikali ichukue hatua za makusudi ili kudhibiti madhara yanayoweza kujitokeza hapo baadaye. ‘stadi’ hiyo ifanywe tangu unakoanzia na unakoingia Mto Ruvuma.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara kwa jinsi inavyotekeleza vema Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Nampongeza Waziri na Naibu Waziri kwa utekelezaji wa majukumu yao. Pamoja na hayo nachangia yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali kwa kutenga fedha za ujenzi wa gati mita 300 shilingi bilioni 87, pia ujenzi wa gati la mafuta Shangani. Aidha, ukarabati wa gati Na. 3 tunaomba fedha hizo zitolewe kwa wakati ili miradi hiyo itekelezwe kwa muda uliopangwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami Mtwara- Newala- Masasi kipande cha kilomita 50, Mtwara- Mnivate, Mkataba wa kazi hii ni miaka miwili na thamani yake ni zaidi ya bilioni 90. Kwa fedha zilizotengwa bajeti ya mwaka jana na mwaka huu fedha zilizotengwa ni takribani shilingi bilioni 29, hivyo kama Mkandarasi atafanya kazi kwa nguvu zote na kasi kubwa hakutakuwa na fedha za kumwezesha. Naomba angalizo hili lifanyiwe kazi ili barabara hiyo ijengwe kwa muda uliopangwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mawasiliano ya simu. Katika Jimbo la Nanyamba kuna Kata nyingi ambazo hakuna mawasiliano ya simu. Baadhi ya Kata hizo ni Njengwa, Nitekela, Nyundo, Hinju, Mnima, Kiromba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliuliza swali Bungeni kuhusu lini Kata hizo zitapewa mawasiliano ya simu, nikajibiwa kuwa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) utagharamia ujenzi wa minara katika maeneo hayo. Naomba tena kupitia Mfuko huu kuharakisha ujenzi wa minara katika maeneo hayo ili kuwe na mawasiliano ya simu za mkononi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanayoifanya. Aidha, pongezi za kipekee ziwaendee kwa namna wanavyosimamia tasnia ya korosho tangu waingie Wizarani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utajikita katika maeneo yafuatayo, kwanza ni pembejeo za korosho. Naipongeza Serikali kwa uamuzi wake wa kutoa pembejeo za ruzuku kwa asilimia 100. Matarajio yangu ni kuwa pembejeo hizi zitakuwa motisha kwa wakulima wa korosho na hivyo kuongeza uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kama ilivyokuwa inafanyika huko nyuma pembejeo hizi hazitoshelezi mahitaji ya pembejeo kwa wakulima wa korosho. Wakulima watalazimika kununua zingine kwa bei ya soko ili kukidhi mahitaji yao. Kiasi hiki nacho kisiachwe hivi kuwe na utaratibu wa manunuzi kama itakavyofanywa kwenye mbolea. Tusipofanya hivyo mkulima atapata pembejeo kiasi ya ruzuku na nyingi kununua kwa bei ya juu, hivyo atailaumu Serikali kwa utaratibu huu badala ya kupongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utendaji kazi wa Maafisa Ushirika. Kumekuwa na malalamiko mengi juu ya utendaji kazi wa Maafisa Ushirika hususan katika tasnia ya korosho. Maafisa hawa baadhi yao hushirikiana na viongozi wasio waadilifu wa vyama vya ushirika ili kufanya ubadhirifu kwa fedha za wakulima. Naishauri Serikali kupitia Tume ya Ushirika na Wizara kufuatilia utendaji kazi wa Maafisa hawa ili wale ambao siyo waadilifu wachukuliwe hatua ya kinidhamu kusafisha uozo uliopo katika kada hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo cha mihogo. Mikoa ya Mtwara na Lindi, inazalisha kiasi kikubwa cha mihogo lakini wakulima wanakata tamaa kwa sababu ya bei ndogo ya zao hili sokoni. Naishauri Serikali kutumia fursa iliyopatikana hivi karibuni ya kuingiza muhogo wetu nchini China kwa kusimamia vizuri taratibu za soko la zao hili ili mkulima apate bei ya juu itakayomshawishi kuzalisha zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dosari zilizojitokeza katika mfumo wa stakabadhi ghalani kwa msimu 2016/2017; msimu wa mwaka huu, 2016/2017 kulikuwa na mafanikio makubwa ya marekebisho ya mfumo huu. Hata hivyo, kuna dosari zifuatazo:-

(i) Kuchelewa malipo kwa wakulima na hivyo kuleta manung’uniko yasiyo ya lazima;

(ii) Wakulima kulipwa fedha tofauti na bei iliyouzwa kwenye mnada, kama korosho zilizouzwa kwa kilogramu Sh.3,800, wakulima wanalipwa Sh.3,400 bila maelezo yoyote; na

(iii) Wanunuzi kupanga bei hivyo bei mnadani kushuka siku hadi siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali ifanyie kazi dosari hizi ili kuimarisha mfumo wa stakabadhi ghalani.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza uongozi wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya. Pongezi ziende kwa Waziri wa Maji Mheshimiwa Injinia Gerson Lwenge, Naibu Waziri Mheshimiwa Injinia Isack Kamwelwe, Katibu Mkuu Profesa Kitila Mkumbo na Naibu Katibu Mkuu Injinia Emmanuel Kalobelo.

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo yangu ya uchangiaji ni kama ifuatavyo:-

Kwanza ni Wizara kupewa fedha za kutosha. Takwimu za mwaka jana zinaonyesha Wizara ilitengewe fedha za maendeleo shilingi bilioni 915.2, hadi Machi zimetolewa shilingi bilioni 181.2 sawa na asilimia 19.8. Hakuna miujiza kuwezesha Wizara hii kupata asilimia 80.2 zilizobaki. Tunasisitiza Hazina kutoa fedha kwa wakati kwa Wizara hii. Mwaka huu fedha za maendeleo zimetengwa shilingi bilioni 623.6, fedha ambazo ni pungufu ikilinganishwa na mwaka jana. Kufidia pengo hili nakubaliana na wazo la kuongeze tozo kutoka shilingi 50 hadi shilingi 100 kwa lita ya diesel na petrol.

Pili, miradi ya maji 17 ya AMREF. Kwa niaba ya wananchi wa Nanyamba napenda kutoa shukrani zetu za dhati kwa kutoa fedha za kukarabati miradi ya maji iliyokuwa imejengwa kwa ufadhili wa AMREF, ukarabati unaendelea na Halmashauri Mji ilipokea shilingi milioni 400 ya awali. Ni matarajio yetu kuwa kiasi kilichobaki kitatoka mapema ili mkandarasi aweze kulipwa kwa wakati.

Tatu, ni kuhusu mradi wa maji wa Makonde. Mradi huu unahitaji ukarabati mkubwa, tunashakuru Serikali kwa kutenga fedha shilingi milioni 87.41 mkopo kutoka India. Ukurasa wa 62 wa kitabu cha bajeti imeelezwa utekelezaji unaanza mwaka huu lakini ukurasa 173 imeandikwa mradi wa Makonde upo Phase III. Hii maana yake nini? Wakati ukihitimisha Waziri atoe ufafanuzi kwa nini kuna maelezo ya kuwekwa Phase III mradi wa Makonde utapewa fedha baada ya kukamilika utekelezaji wa Phase I and II? Ufafanuzi unahitajika kuhusu utata huu unaotolewa na baadhi ya watendaji wa Wizara.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha nakumbusha Wizara kuhusu utekelezaji wa mradi wa maji kutoka Makonde na kupeleka kata vijiji 23 vya Halmashauri ya Mji Nanyamba. Andiko la awali limeshawasilishwa na usanifu wa mradi unaendelea.

Nne, mradi wa maji kutoka Mto Ruvuma hadi Manispaa ya Mtwara Mikindani; mradi huu unatoa maji kijiji cha Mayembe chini kilichopo Halmashauri Mji ya Nanyamba na matarajio ni vijiji vyote vya jirani wapate maji, Mheshimiwa Naibu Waziri alifika hapa na kuahidi vijiji vya Mayemba Juu, Chawi na Kiromba, vijiji vilivyotajwa 26 ni vichache sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, nashauri Wizara iangalie uwezekano wa usanifu mradi mwingine wa kutoa maji Mto Ruvuma na kupeleka vijiji vya Halmashauri ya Mji Nanyamba. Kata za Kiromba, Kiyanga, Mtiririko, Mbembako na Kitaya wanaweza kupata maji kutoka Mto Ruvuma.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza viongozi wa Wizara kwa kazi nzuri wanayoifanya; Mheshimiwa Profesa Joyce Ndalichako (Mb) Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na Naibu Waziri Mheshimiwa William T. Ole Nasha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utajikita katika maeneo manne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kuhusu ubora wa walimu na mabadiliko ya mitaala; ubora wa walimu umeelezwa na wachangiaji wengi kuwa umeshuka; maelezo haya si sahihi, wengi wanazungumzia matokeo ya shule ya private kama kigezo cha kushuka kwa elimu kwa shule za umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri changamoto zilizopo ambazo wengi wanahusisha na kushuka kwa elimu zifanyiwe kazi. Changamoto hizo ni upungufu wa miundombinu ya shule za vijijini, mafunzo kazini kwa walimu na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna madai ya kubadilika mara kwa mara kwa mtaala jambo ambalo si sahihi, wakati wa majumuisho Mheshimiwa Waziri atoe ufafanuzi tangu tupate Uhuru mtaala umebadilishwa mara ngapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu wa sekondari kuhamia msingi, naipongeza Wizara kwa uamuzi huu kwani walimu wamepelekwa shule za msingi ambako kulikuwa na uhaba mkubwa wa walimu. Walimu hawa wamepata mafunzo ya kuweza kuwapa ujuzi na maarifa hata watoto na si kama wanavyodai wajumbe wengine kuwa walimu wa sekondari hawawezi kufundisha; si ya kweli. Vyuo vingi siku hizi wanawapeleka walimu tarajiwa wa diploma na degree kwenye mazoezi ya kufundisha (BTP) kutumia shule za msingi za jirani na chuo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Wasimamizi Ubora wa Elimu; Idara hii inakabiliwa na changamto ya rasilimali fedha na vitendea kazi, ili kuweza kukagua shule zote na kutoa ushauri uliotarajiwa katika kuboresha elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ofisi hii haina fedha za kutosha kwa ajili ya matengenezo ya magari yao. Nashauri Wizara kutenga fedha nyingi na kuwezesha Wizara hii kutekeleza majukumu yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri nyingi zinapoanzishwa basi na Wadhibiti Ubora wa Elimu wapelekwe. Halmashauri ya Mji wa Nanyamba haina Wadhibiti Ubora wa Elimu hivyo ukaguzi wa shule inategemea wale wa Mtwara DC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vyuo vikuu vya binafsi, vyuo hivi vina changamoto nyingi ikiwemo uhaba wa wahadhiri, majengo na mazingira yasiyo rafiki ya kufundishia na kujifunzia. Serikali iongeze ufuatiliaji katika vyuo hivi ili vile visivyokuwa na sifa au vinavyoshindwa kutimiza vigezo vifungwe.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi niungane na Waheshimiwa Wabunge ambao wametangulia kusema kuunga mkono na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa hatua anazochukua katika ulinzi wa rasilimali zetu. Kazi anayoifanya ni kubwa, kazi hii inahitaji uthubutu mkubwa na kazi hii ni ya kizalendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunachotakiwa kukifanya wote kwa umoja wetu tunaomba tumuunge mkono Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya. (Makofi)



Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili kama anvyoomba yeye mwenyewe, tuendelee kumuombea katika sala zetu ili aweze kuendelea kutekeleza majukumu yake na hatimaye ahamie kwenye sekta ndogo zingine hata sekta za gesi, utalii na maeneo mengine ambapo kunahitaji usimamizi madhubuti ili kuweza kuleta tija katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili niungane na wenzangu kumpongeza Waziri kwa kazi nzuri aliyoifanya, Mheshimiwa Dkt. Mpango na Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji na wataalam wa Wizara hii wakiongozwa na Ndugu Dotto na Gavana wa Benki Kuu Profesa Ndullu. Tunaona kabisa waziwazi kwamba utaalam wao na weledi wao unasaidia sasa kuja na sera za kifedha ambazo zinasaidia katika uchumi wa nchi yetu. Kama takwimu zinavyoonesha kwamba uchumi wa nchi yetu unaendelea kupanda na kuimarika kwa asilimia saba kila mwaka, kwa hiyo tunakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, udhibiti wa mfumuko wa bei tumeona kwamba muda mrefu mfumuko wa bei bado uko kwenye digit moja. Siyo hivyo tu, pamoja na takwimu zinazotolewa kwamba kuna biashara zinaendelea kufungwa lakini kwenye kitabu cha Waziri hapa imeonesha wazi kwamba kuna biashara mpya zaidi ya laki 224,000 zimefunguliwa. Vilevile kitabu kimeonesha takwimu kwamba sasa pato la kila Mtanzania yaani per capita income imeongezeka kutoka milioni 1.9 mpaka milioni 2.1. Kwa kweli wanastahili hongera, bila usimamizi wa Waziri na watendaji wakuu haya yote yasingetokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nikupongeze vilevile kwa kuja na kitabu chako ambacho kimejibu hoja nyingi za wananchi na za Wabunge. Utakumbuka mwaka jana hapa uliambiwa kwamba wewe huna jimbo na una mpiga kura mmoja, lakini maneno hayo mwaka huu yote tumeyafuta, kwa hiyo, tunakupongeza sana kwa usikivu wako na kwa kweli Wabunge tunakupongeza kwa sababu mimi kila nikiangalia ukurasa, naona unajibu hoja ya Mbunge au unajibu kero za wananchi. (Makofi)



Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo naomba nitoe mchango wangu kuhusu mambo matatu, suala la kwanza ni hii ukurasa wa 48 umezungumzia hatua za mapato na hapa umezungumzia kuwatambua rasmi wafanyabiasha wadogo wadogo wasio rasmi na wanaofanya biashara katika maeneo yasiyo rasmi, mama lishe, wauza mitumba, wauza mazao ya kilimo wadogo wadogo, mboga mboga na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki ni kitendo kibubwa sana kwa sababu mara nyingi kundi hili lilionekana kwamba halina msaada na halina nafasi katika uchumi wa nchi yetu. Kwa hiyo, tendo la kuwatambua na kuwasajili hii inaonekana wazi kwamba hawa sasa ni wadau wa maendeleo ya nchi yetu. Nishauri sasa kwamba kinachotakiwa kufanya sasa hivi ni kwamba Mamlaka ya Serikali za Mitaa basi zishirikiane na watu hawa yaani mipango ya kuwatambua na kuwatafutia maeneo iwe shirikishi tusiwe na ule utaribu kila siku tunawafukuza watambuliwe, wawekwe kwenye maeneo rasmi na tusahau ile miradi ya zamani, nafikiri wote tuna historia ya mradi ule wa Machinga Complex na lile soko la Mchikichini nini kinaendelea ni kwa sababu hatukuwashirikisha. (Makofi)

Kwa hiyo, kwa tendo hili ambalo sasa hivi tunaenda kuwatambua tuwasajili hii itasaidia sasa kuwapa maeneo ambayo yatakuwa karibu na wateja wao na maeneo yao ya biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa pili sehemu ya pili ni ile suala kupunguza Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye vyakula vya mifugo, lakini vilevile ni kupunguza Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa mayai ya kutotoa vifaranga hii itaongeza ajira kwa vijana wetu, kwasababu kuna vikundi vingi vya kinamama na vijana wanashughulika na ufugaji kwahiyo tukifanya hivi tutaongeza ajira kwa vijana wetu. Tunachotakiwa kutoa ushauri kwa mambo mawili kwamba tupunguze kodi ya madawa ya mifugo, lakini pili vikundi hivi vya vijana na kinamama sasa iweze kupewa mkopo ili waweze kufuga vizuri. (Makofi)



Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya tatu naenda kwenye sekta ya kilimo. Sekta ya kilimo nako kuna unafuu umepatikana kwa kupunza tozo mbalimbali kwa wakulima. Lakini kwa kipekee niishukuru Serikali kwa uamauzi wao kwa kuamua kugawa pembejeo za kilimo bure kwa wakulima wa korosho nawapongeza sana, lakini kwenye korosho bado tunatakiwa twende mbele zaidi tujikite katika ubanguaji wa korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakosa fedha nyingi sana tuna viwanda vya kubangua korosho 12; lakini kwenye mpango wetu tunazungumzia viwanda viwili tu. Kuna viwanda vingine kumi hebu tuviwekee mkakati ili tupate fedha nyingi lakini vilevile tutaongeza ajira kwa wananchi wetu, na wenzetu wa Msumbiji wana-practice policy, korosho nyingi za Msumbiji zinabanguliwa kwa nini sisi Tanzania tusibangue, kwa hiyo naomba sasa tujikite katika ubanguaji wa korosho ili tuache kuuza korosho ghafi nchi za nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu mwingine ni utekelezaji wa miradi. Inaonekana miradi yetu inachukua muda mrefu sana kwenye utekelezaji kuna mradi huu wa miradi 17 ambayo inagusa Muheza, mradi wa Makonde, kuna mradi wa Njombe, miradi hii inatakiwa kuanza kutekeleza…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na niungane na Wabunge wenzangu kwa kuwapongeza Mawaziri wa Wizara hii Mheshimiwa Waziri Mpango na Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Manaibu Katibu Wakuu, Wakurugenzi pamoja na Kamshina wa Bajeti kwa kazi nzuri wanayoifanya Wizarani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utaanza na Benki ya Maendeleo ya Kilimo na kama nilivyochangia wakati wa uchangiaji wa Wizara ya Kilimo ningeomba sasa benki hii ijikite kwenye mazao ya biashara. Kwanza benki hii ina tatizo la mtaji; kwa hiyo nashauri Serikali sasa iongeze mtaji wa benki hii vilevile bado matawi ni machache, nilishauri kwamba miongoni mwa maeneo ambayo yanatakiwa benki hii sasa ipeleke nguvu zake ni Kanda ya Kusini ambapo kuna uzalishaji mkubwa wa zao la korosho na kama mnavyofahamu zao la korosho mwaka huu ni zao ambalo linaongeza kwa kutuletea fedha za kigeni. Limeingiza zaidi ya dola milioni 700 kwa hiyo ni zao ambalo siyo la kubeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba benki hii sasa ijikite katika kutoa mikopo ya muda mfupi ili wakulima wetu wa korosho waweze kuwa na uwezo wa kununua pembejeo. Mkulima wa korosho anahangaika na shamba lake wakati wa palizi lakini unapofika wakati wa pembejeo anahitaji kupewa msaada. Kwa hiyo, naomba benki hii sasa ifungue matawi Kanda ya Kusini ili itoe mikopo kwa wakulima wa korosho na isijikite tu kwenye mazao ya chakula, kwa sababu ukiangalia kwenye kitabu cha Waziri ambacho amewasilisha kwenye mnyororo wa thamani. Mazao ambayo yameorodheshwa pale ni mazao ya chakula kuna mahindi, mpunga kwa hiyo tunaomba twende sasa kwenye zao la korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia namba ya wakulima ambayo wamefaidika na benki hii ni wachache. Kwenye taarifa ya Waziri inaonesha kwamba ni wakulima 2,575, sasa hebu angalia nchi takriban asilimia 75 ya wananchi wanategemea kilimo, kwa kundi hili dogo ambalo limepata msaada ni kiasi kidogo sana. Kwa hiyo naomba Mheshimiwa Waziri tuwe na mkakati kwanza tuongeze matawi tuongeze mtaji, lakini tuongeze na idadi ya wananchi ambao watafaidika na benki hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili, utahusika na taasisi ambazo ziko chini ya Wizara hii. Nizungumzie taasisi hiyo ya Uhasibu na nitajikita kwenye taasisi ya Uhasibu kwenye tawi la Mtwara. Taasisi hii ni nyeti na inatoa taaluma ambayo ni muhimu kwa sasa lakini mazingira ya kujifunzia na kujifundishia hasa kwa tawi la Mtwara hayaridhishi, hivyo naomba Wizara itenge fedha za kutosha ili ukarabati mkubwa ufanywe kwenye taasisi hii na hasa tawi la Mtwara ambapo vyumba vya madarasa havitoshi, hawana hosteli za kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto ambao wako pale wanahangaika kupanga mitaani na wanafunzi hususan wa kike si vema sana kwa sababu pale wanatoa certificate. Wengine wamemaliza Form Four juzi tu hawawezi kukaa nje ya familia yao, kwa hiyo wanafunzi wale wanaangaika. Ni vema kukawa na hosteli kubwa inayochukua wanafunzi wengi ili watoto wote ambao watapata udahili pale wakae katika mazingira ya Chuo cha Uhasibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa tatu nitajikita kwenye usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za umma, hapa kwenye kitabu chake Mheshimiwa Waziri amesema kwamba atajikita katika kuimarisha Kamati za Ukaguzi kwenye taasisi mbalimbali, lakini nimsihi sio Kamati za Ukaguzi tu, hebu atuelekeze katika kuimarisha vitengo vya ukaguzi wa ndani hasa kwenye mamlaka ya Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiimarisha vitengo vya ukaguzi wa ndani kwenye mamlaka ya Serikali za Mitaa, tutakuwa tumeokoa mambo mengi sana kwa sababu Mkaguzi wa Ndani ndiyo jicho la kwanza la Afisa Masuuli kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa, hivyo naomba tujikite katika kuimarisha Kamati za Ukaguzi lakini ofisi ya wakaguzi wa ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia hali ilivyo sasa hivi kwa kweli inasikitisha, utakuta kwenye Halmashauri nyingine mkaguzi wa ndani ni mmoja hana gari, hana vifaa vya kufanyia kazi, kwa hiyo hawezi kufanya kazi yake vizuri, akitaka kwenda kukagua usambazaji wa madawa na utoaji wa huduma katika zahanati anamwomba msaada DMO, sasa yule mkaguliwa ndiyo anampa posho, anampa gari, hata nguvu ya kukagua pale inapungua. Kwa hiyo, naomba Wizara sasa ijikite licha ya kuangalia tu Kamati za Ukaguzi tuangalie na kitengo hicho ambacho ni muhimu na nyeti katika kudhibiti matumizi ya fedha zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hiyo tu katika suala la Usimamizi wa Fedha za Serikali tuingalie kwa jicho la pekee Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Mwaka jana tuliona alivyofanya kazi nzuri, alikagua taasisi nyingi lakini fedha hakupewa kwa wakati. Kwa hiyo ilibidi aji-stress, naomba CAG apewe fedha za kutosha lakini siyo za kutosha tu, bali kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukaguzi una misimu yake, ukimpa CAG fedha kuanzia Januari hazimsaidii sana, kwa sababu wakati ule na timu yake wanajifungia mahali kwa ajili ya report writing. Tujitahidi kutoa fedha za kutosha kama ilivyo kwenye bajeti yake kwa kipindi cha Julai hadi Novemba, tukifanya hivyo tutakuwa tumemsaidia CAG na atafanya kazi yake kwa ufanisi na atakuwa amekwenda kuangalia fedha zetu ambazo tumepeleka katika miradi yetu ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu mwingine utajikita kwenye uhakiki na ulipaji wa madeni ya Watumishi wa Umma na Wazabuni. Kama walivyosema wenzangu kwamba tuongeze kasi ya uhakiki wa haya madeni. Kwenye taarifa pale imeonekana kwamba tumeshaanza kulipa madeni ya wazabuni, kwenye deni la trilioni tatu tumelipa milioni 796. Ningeomba Serikali yangu isiwe chanzo cha kuua mitaji ya wafanyabiashara wadogo, tulipe madeni kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tulipe madeni ya Watumishi kwa wakati ili kuongeza morali kwa watumishi. Watumishi wakilipwa stahili zao morali inaongezeka, lakini madeni kwa watumishi yasipolipwa kwa wakati kwanza yanafifisha ari kwa watumishi na hivyo mtumishi anakwenda kazini wakati hana ari ya kufanya kazi. Kwa hiyo, naomba kwenye trilioni tatu kwa sababu tumeana kulipa milioni 796 basi tujitahidi ili tulipe deni hili ili wazabuni waweze kutoa huduma lakini na watumishi waweze kufanya kazi ili tuliyoitarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa mwisho unahusu mfuko wa huduma ndogo za fedha (microfinance) na hii ni taasisi muhimu sana. Nchi za wenzetu wanawapa kipaumbele sana SMEs, kwa hiyo na sisi hizi taasisi za microfinance hebu tuzipatie fedha za kutosha na tupunguze mifuko. Kwenye Mfuko wa Uwezeshaji tumeambiwa kuna mifuko 19, sasa ile mifuko ni mingi sana. Tupunguze tuwe na mifuko miwili au mitatu ambayo itatoa huduma ambayo inajulikana na wananchi watakuwa na taarifa za kutosha. Kwa hiyo, itakuwa wanapohitaji mikopo midogo midogo au uwezeshwaji wanakwenda kwenye taasisi hizo na kuhudumiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kuunga mkono hoja na nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kutoa mchango wangu kuhusu Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa mwaka wa fedha 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nitaanza na mchango wangu kipengele cha mazingira wezeshi kwa uendeshaji wa biashara na uwekezaji na hasa sehemu ya miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi kubwa inayoifanya katika ujenzi wa barabara katika nchi yetu. Pia kipekee nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali kwa kuanza barabara ambayo Wabunge wa Mtwara tulikuwa tunaipigia kelele, ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Mtwara – Nanyamba – Tandahimba – Newala hadi Masasi; barabara yenye urefu wa kilometa 210. Sasa hivi mkandarasi yuko site anaanza ujenzi wa kilometa 50 kwa kiwango cha lami kutoka Mtwara hadi Nnivata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni matarajio yetu Wanamtwara kwamba mpango ujao sasa utaonesha maendelezo ya ujenzi wa barabara hii. Tunatarajia sasa tuone kipande kingine cha kilometa 50 kutoka Nnivata kuendelea hadi Newala na hatimaye tukamilishe kilometa 210.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ni muhimu sana kwa uchumi wa korosho. Tunapozungumzia korosho Tanzania tunazungumzia Wilaya ya Nanyamba, Tandahimba, Newala na Masasi. Takribani asilimia 60 za korosho ya nchi hii inazalishwa katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa wazo la kuanzisha Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA). Wazo hili ni jema, na wazo hili litaharakisha ujenzi wa barabara ambazo zinamgusa mkulima, zile feeder roads. Hapa ninaomba niishauri Serikali yangu, kwanza niwapongeze TARURA kwamba wameanza vizuri sana. Kuna Mtendaji Mkuu yupo na Wakurugenzi wake wanaanza kuchakarika kwa kasi kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtandao wa barabara za TARURA ni takriban kilometa 108,000. Mtandao huo ni mkubwa na tukiendelea na formula ile ya zamani wa kwenye Road Fund yaani TANROADS wanachukua share kubwa kuliko hii TARURA, sabini kwa thelathini, TARURA watashindwa mara moja.

Kwa hiyo ninaomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha utakapokuja na mpango wa maendeleo wa mwaka 2018/ 2019 utueleze TARURA sasa itapata asilimia ngapi ya fedha za Road Fund na TANROADS watapa asilimia ngapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ningependekeza, kwa sababu mtandao wa barabara wa TARURA ni mkubwa, kama nilivyosema ni takriban kilometa 108,000 tufanye nusu kwa nusu; yaani 50 iende TANROADS na 50 iende TARURA ili ikajenge barabara ambazo mkulima wan chi hii anatumia kila siku akiwa na baiskeli, bodaboda akibeba mazao yake na kupeleka shambani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili unahusu matumizi ya gesi. Wasemaji wengi sana wamechangia kuhusu gesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado nchi yetu imejaaliwa kuwa na reserve kubwa ya gesi, lakini kama walivyosema wachangiaji wengi hatujatumia hii fursa vizuri. Matumizi yake bado ni ya kusuasua. Mwekezaji aliyopo Mnazi bay (MNP) ana uwezo wa kuzalisha au kutupa cubic feet milioni 136 kwa siku ili zitumike pale Madimba na Mtwara lakini kwa siku tunatumia cubic feet milioni 40 tu, kwa hiyo utaona ni kiasi gani yule mwekezajia anazalisha lakini hakitumiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba sana Serikali yangu kuongeza kasi ya matumizi ya gesi; mtumiaji mmojawapo ni kiwanda cha Dangote. Hadi leo pamoja na maamuzi ambayo alitoa Mheshimwia Rais akiwa pale Mtwara, kwenye ziara kwamba Dangote apewe gesi hadi leo kiwanda cha Dangote hakujapewa gesi. Kuna urasimu usio wa lazima, hebu tupunguze urasimu tumpe Dangote hiyo gesi na kiwanda cha Dangote kikipata gesi hata bei ya saruji anasema itashuka mpaka shilingi 8,000 kwa mfuko, na hii itawasaidia Watanzania wetu. Kwa hiyo, naomba Serikali yangu iongeze kasi ya kutataua changamoto ambazo zinakwanza Dangote kupewa gesi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ukisoma Mpango wa Maendeleo wa mwaka jana ulisema kuna mradi wa kujenga miundombinu ya kusambaza gesi majumbani kwa mikoa ya Mtwara na Lindi, mradi huu hadi leo haujaanza. Naiomba Serikali yangu itoe pesa kwa TPDC ili mradi huu uanze. Mradi huu ukianza basi matumizi ya gesi yataongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti. kuna mradi mkubwa wa kuchakata gesi na kuwa kimiminika ule wa Lindi, Mradi wa LNG. Mradi huu kila siku tunaambiwa kwamba tupo kwenye maandalizi ya eneo la mradi. Maelezo haya sasa tumeyachoka ni ya muda mrefu tunaomba sasa tuwe na lugha nyingine. Ni mradi mkubwa na naomba Serikali iongeze kasi ya kukubaliana na hawa wafadhili ili mradi huu uanze. Mradi huu ukianza utatoa fursa nyingi za ajira kwa vijana wetu wa Mtwara na Lindi na vile vile tutaongeza matumizi ya gesi ambapo sasa bado gezi ipo ya kutosha lakini matumizi yake bado ni ya kususua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu maji; hakuna Tanzania ya viwanda bila maji ya kutosha. Tangu mwaka juzi tukiwa Bungeni hapa tumeambiwa kuhusu miradi 17 ya maji ambayo itapata ufadhili kutoka Benki ya India. Miradi hii itanufaisha miradi ya Makonde, Muheza, Njombe na Zanzibar. Hadi leo hii tunaambiwa bado kusainiwa financial agreement… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi, nami niungane na wenzangu kuwapongeza Wenyeviti na Wajumbe wa Kamati hizi mbili kwa kazi nzuri walioifanya wale wa PAC na wale wa LAAC. Pia nichukue nafasi hii vilevile nimpongeze CAG kwa kazi nzuri anayoifanya, kwa sababu Kamati hizi mbili zinategemea na taarifa ambazo zinawasilishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Kwa kazi nzuri hizi amewezesha Kamati hii kufanya kazi yake kwa umakini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niipongeze Serikali kwa kuwezesha Ofisi ya CAG kwa sababu kwa mwaka huu wa Fedha CAG ameripoti kwamba amepewa fedha kwa kadiri alivyohitaji na ndiyo maana amewezesha kufanya ukaguzi wake kwa wakati na kaleta taarifa kwa wakati. Kwa hiyo, naipongeza Serikali kwa kusikiliza kilio cha Ofisi ya CAG.

Mheshimiwa Mwenyekiti, michango yangu itajikita sana sana kwenye taarifa ya ya Hesabu za Serikali za Mitaa LAAC. Nianze na lile la ukaimu wa Wakuu wa Idara, nami niungane na Wajumbe waliosema kwamba imefika hatua sasa Serikali ichukue hatua mapema na kama ni sababu ya mchakato mrefu basi irahisishwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yetu ya LAAC tulipoenda Korogwe, tumekuta kwenye Wakuu wa Idara 16 kuna proper Wakuu wa Idara watano tu; 11 ni Makaimu. Kwa hiyo utaangalia ni jinsi gani Ofisi hii au Halmashauri hii ya Korogwe haitaweza kutekeleza majukumu yake kwa umakini kwa sababu kuna Makaimu wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kaimu anapokaa ofisini kwanza anakosa kujiamini, anakosa ubunifu kwa sababu muda wote anafikiri kwamba Mkuu wa Idara anaingia. Kwa hiyo, naomba Serikali iharakishe na ili kuisaidia Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe naomba Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI ichukue hatua za haraka. Kwa sababu kwenye Wakuu wa Idara 16 kuna Proper Head of Departments watano hapo kuna athari kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ninaomba kuliongelea ni suala la Kitengo cha Wakaguzi wa Ndani. Kitengo hiki ni muhimu sana na Kitengo hiki ni msaada mkubwa sana kwa Maafisa Masuuli. Hata hivyo, kama taarifa yetu inavyoonesha kwamba Kitengo hiki kuna upungufu wa rasilimali watu na upungufu wa rasilimali fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kama tulivyopendekeza kwenye taarifa ya mwaka jana, mwaka huu tumerudia kuwe na mkakati maalum wa kuongeza Watumishi katika Kitengo hiki cha Ukaguzi wa Ndani kwa sababu Halmashauri nyingi ambazo zinakuja mbele ya Kamati kuna Mkaguzi mmoja au wawili na wakati Ikama inatakiwa kila Halmashauri iwe na Wakaguzi wa Ndani watano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba jitihada za makusudi zifanywe ili kuongeza Wakaguzi wa Ndani ili kurahisisha Wakurugenzi kufanya kazi zao kwa umakini. Hili ni jicho la karibu sana kwa Mkurugenzi au Afisa Masuuli kuonesha ni nini kinafanyika katika Taasisi. Kwa hiyo, kuwe na jitihada za makusudi za kuajiri Wakaguzi wa Ndani ili Kitengo hiki kiweze kufanya kazi yake kwa umakini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kwanza niipongeze Serikali kwa kuanzisha miradi mingi ya maendeleo na kama tulivyopitisha kwenye bajeti kwamba fedha nyingi zimeenda kwenye miradi ya maendeleo. Hata hivyo, hapa kuna changamoto mbili; changamoto ya kwanza kama tulivyosema fedha nyingi hazipelekwi kwa wakati, lakini fedha zinazopelekwa kuna maelekezo mengine ambayo yanachelewesha utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa wazo kwamba TBA na na SUMA JKT wapewe kazi, lakini miradi mingi ambayo imekaguliwa hivi karibuni imeonesha Taasisi hizi mbili zimeshindwa kutekeleza ile miradi ambayo imepewa kwenye halmashauri nyingi. Kwenye Halmashauri mpya TBA na SUMA JKT walipewa kujenga majengo ya Ofisi za Wakurugenzi, lakini ukaguzi ambao unafanywa sasa hivi wa kutembelea miradi hii bado TBA na SUMA JKT wameshindwa kuitekeleza miradi hii kwa wakati, wamepewa fedha lakini inaelekea wameelemewa na miradi mingi. Kwa hiyo, naomba Serikali iangalie upya uamuzi huu ili kuharakisha utekelezaji wa miradi katika mamlaka ya Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza sana Ofisi ya Rais, TAMISEMI juzi juzi walienda kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara wamechukua uamuzi wa haraka wa kuvunja Mkataba na TBA. Kwa hiyo, naiomba Ofisi ya Rais, TAMISEMI itembelee miradi mingine hasa ya ujenzi wa Ofisi za Wakurugenzi katika Halmashauri mpya 17. Ujenzi bado ni wakusuasua na bado hakuna kasi ambayo inaonesha kwamba miradi hii itakamilika kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua wakifika kule watajionea wenyewe na inawezekana ikachukuliwa hatua kama ilivyochukuliwa kwa mradi ule wa Musoma, ambao Naibu Waziri Mheshimiwa Kandege aliamua kuvunja Mkataba kwa niaba ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Kwa hiyo nakupongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, nichangie kuhusu miradi ya maji kama ulivyosema katika taarifa yetu kuna utekelezaji wa kusuasua katika miradi ya maji na hapa kuna changamoto kubwa sana. Changamoto kubwa iliyopo, kuna utofauti sana wa utekelezaji wa miradi kati ya halmashauri na halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulienda Mkoa wa Tanga tukakuta Halmashauri ya Korogwe kuna changamoto kubwa sana ya utekelezaji wa miradi ya maji, inaanzia kwenye usanifu. Kuna miradi mingine wananchi wamekataa kutoa maji kwa sababu kwenye chanzo pale cha maji wananchi hawapewi water point. Mradi unatoa maji Kijiji X wananchi wa Kijiji X hawapewi maji wanapeleka Kijiji Y, wanachi wa eneo husika wanasema haiwezekani. Sasa huu ni udhaifu wakati wa usanifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tumeona miradi inachelewa kutekelezwa, mradi mmoja ulikuwa unatekelezwa kwa milioni 900, lakini kwa sababu ya kuchelewesha sasa hivi gharama yake ni bilioni nne, kwa hiyo, hizo ni hasara kwa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili hata huo usimamizi wa miradi yenyewe ya maji ni changamoto kubwa. Tulienda kwenye mradi mmoja ambapo limetengenezwa hozi ya kunyweshea mifugo wakifika ng’ombe au mbuzi hawawezi kunywa maji na Mhandisi wa Maji yupo na Mhandisi wa Ujenzi yupo lakini wameshindwa kushirikisha wananchi wakatengeneza hozi ambayo ingetumika katika mazingira yale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo miradi ya maji ina changamoto kubwa sana katika mamlaka ya Serikali za Mitaa na ndiyo maana ndiyo maana Kamati yetu tukaja na wazo basi uundwe Kamati maalum ya kufuatilia miradi hii ili tujue chanzo na sababu yake ni nini. Pengine tutoe mapendekezo ambayo yataisaidia Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maji. Kwa hiyo, naomba Wabunge tuungane katika wazo hili ili Mheshimiwa Spika aunde Kamati Teule ifanye shughuli hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa hoja ya ucheleweshaji wa fedha za maendeleo. Kama nilivyosema kuna miradi mingi fedha zinakwenda kwa kusuasua na zinapofika kunakuwa na maelekezo tofauti lakini mbaya zaidi kwamba fedha hizi sasa zingine zinaletwa mwezi Juni, mwezi ambao kwa taratibu za manunuzi huwezi kufanya chochote. Kwa hiyo, naomba Hazina waharakishe utoaji wa fedha hizi ili mamlaka za Serikali za Mitaa zisiwe na bakaa na kusababisha hoja nyingi za ukaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hoja iliyopo mezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze tu kwa kuwapongeza viongozi na watendaji wa Wizara hii, tukianza na Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mheshimiwa Engineer Kamwelwe kwa kazi yake nzuri anayoifanya, vilevile Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mheshimiwa Aweso, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo na Naibu Katibu Mkuu, Engineer Kalobelo, hongereni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi mnazozifanya tunaziona na jinsi mnavyohangaika kurekebisha sekta ya maji na mna nia njema ya kumtua mama ndoo lakini changamoto kubwa ambayo mnakabiliwa nayo ni ukosefu wa fedha, lakini kwa fedha chache zilizopo matokeo tunayaona, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tukabiliane na tatizo hili la fedha ambazo Wizara hii muhimu na nyeti na ambayo inamgusa kila mwanafamilia asubuhi anapoamka basi niungane na wazo ambalo limetolewa na Kamati na wazo ambalo limetolewa na baadhi ya Wabunge, kwamba sasa ni muda muafaka wa kuhakikisha kwamba ile tozo ambayo mwaka jana tuliahirisha kwamba tusiongeze shilingi 50, mwaka huu tuongeze ili tupate fedha za kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ni ushahidi ulio wazi, kama Kamati ilivyosema vizuri kwamba fedha ambayo ina uhakika ni fedha ya Mfuko wa Maji, kwa hiyo tuongeze tozo kwenye Mfuko wa Maji ili tupate fedha za kuwezesha kutekeleza miradi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna maendeleo bila maumivu. Kwa hiyo tuongeze shilingi 50 kwenye maji, tutaumia kwenye mafuta lakini kwenye utekelezaji wa miradi ya maji matokeo yataonekana, hivyo na mimi naunga mkono kwamba tuongeze hiyo tozo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili utajikita kwenye miradi ambayo inafadhiliwa na fedha kutoka nje. Inawezekana Wizara inatoa taarifa hizi mapema sana kwa sababu miradi inachukua muda mrefu. Katika Mkoa wetu tuna mradi wa maji wa Makonde na tulishaambiwa kwamba kuna fedha, dola milioni 87 kutoka mkopo wa India na ni zile fedha za miradi 17.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizi hata viongozi wetu wa kitaifa nakumbuka mwaka juzi, Mheshimiwa Makamu wa Rais alifanya mkutano mkubwa pale Tandahimba na akawaambia wananchi wa Tandahimba kwamba tatizo la Mradi wa Makonde sasa limefika mwisho tumepata fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu wa Makonde unahusisha Halmashauri nne ambazo ni Halmashauri ya Newala, Halmashauri ya Mji Newala, Halmashauri ya Tandahimba na Halmashauri ya Mji wa Nanyamba. Kwamasikitiko makubwa Kaka yangu Mheshimiwa Mkuchika amekuwa akielezea mara kwa mara kwamba mradi huu ulijengwa wakati wa mkoloni, unahitaji ukarabati mkubwa, lakini kwa masikitiko makubwa fedha hizi hadi leo hazijapatikana na ukiangalia ule ukurasa wa 72 utakuta bado majadiliano yanaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niiombe Serikali yangu sikivu kwamba sasa mharakishe haya majadiliano. Hiyo finanicial agreement isainiwe ili hii miradi 17 sasa ianze kutekelezwa. Kwa sababu ukiangalia kitabu cha mwaka 2016/2017 maelezo yapo, 2017/018 maelezo yapo na sasa hivi 2018/2019 maelezo ni hayohayo. Kwa hiyo, naiomba Wizara ya Fedha iharakishe hayo mazungumzo sasa..

T A A R I F A . . .

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa yake, lakini Serikali ipo hata kama Waziri wa Fedha hayupo, Serikali ipo kwa hiyo message itafika kwa Waziri wa Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Mtwara tuna mradi mwingine ambao mzungumzaji aliyetoa taarifa naye unamgusa vilevile, mradi wa kutoa maji Mto Ruvuma na kupeleka Manispaa ya Mtwara. Mradi hii vilevile ni wa mkopo kutoka Exim Bank ya China, lakini huu mwaka wa tatu sasa fedha hizo hazijapatikana na mradi haujatekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba hii miradi ambayo inachangiwa na wahisani tuweke kwenye taarifa zetu pale tunapokuwa na uhakika kwamba fedha sasa ziko tayari, la sivyo mnatupa kazi wanasiasa, tunapokwenda kule tunaulizwa na wananchi. Kwa sababu taarifa hizi sasa wananchi wanazo, kwamba kuna fedha za utekelezaji wa mradi kutoka Mto Ruvuma kupeleka Manispaa ya Mtwara. Mheshimiwa Waziri wa Maji wewe unaufahamu mradi huu vizuri, ulishatembelea kule na umezunguka maeneo yote na unaona shida ya maji ya Vijiji vya Chawi, Maembechini na maeneo mengine ya Kitae, kwa hiyo nafikiri hili litafanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utekelezaji wa miradi ya maji; kama nilivyosema, Wizara inafanya kazi vizuri sana, mmerekebisha upelekaji wa fedha, mmerekebisha hata mgao wa fedha. Ukiangalia hiki kitabu ukurasa wa 114 kila Halmashauri imeweka kiasi ambacho watapata ila changamoto iliyopo hamuweki fedha za usanifu wa miradi. Mradi hauwezi ukafikia hatua ya kutangazwa bila kusanifiwa, fedha hizo hamuweki. Hivyo, inailazimu Halmashauri ikope kwenye vyanzo vingine mradi usanifiwe, utangazwe hiyo tender document itoke ndiyo baadae mkandarasi akipatikana a-raise certificate Wizara ndiyo mnaanza kulipa. Kwa hiyo, naomba hapo Wizara hebu mrekebishe, muweke fedha kidogo kwa council ili waweze kufanya hizo kazi za awali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango Mradi wa Maji wa Mitema – Lienje – Nanyamba. Kwanza nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali yangu ya Awamu ya Tano na kipekee nimshukuru Mheshimiwa Waziri wa Maji kwa sababu ulifika Mitema, naona umetenga shilingi milioni 600, nakushukuru na kukupongeza sana, lakini andiko la awali la mradi huu gharama ya mradi huu ni shilingi bilioni kumi na moja (11)).

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipokea hii shilingi milioni 600 kwamba tutaanza na utekelezaji wa mradi lakini Mheshimiwa Waziri hebu katika bajeti ijayo basi muweke fedha za kutosha ili mradi uweze kutekelezwa kwa wakati lakini pia kwa eneo kubwa la mradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu ni mkubwa sana utahusisha takribani kata tisa, vijiji 35 na wewe eneo hili umelitembelea na ni muhimu kwa Mkoa wa Mtwara, kwa hiyo nakuomba kwenye bajeti ijayo basi tutenge fedha za kutosha ili mradi huu wa Mitema – Lienje – Nanyamba uweze kutekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie vilevile kuhusu wazo la kuanzisha Wakala wa Maji Vijijini. Hili ni suala zuri na ni suala ambalo kila mtu anaunga mkono, lakini tuwe na tahadhari wakati wa kuanzisha, kwamba tujiandae. Wakati wa Wizara ya TAMISEMI tulikuwa tukiilaumu TARURA hapa kwa sababu tumeanzisha TARURA bila kuwa na maandalizi ya kutosha kwa hiyo Wakala wa Maji Vijijini hebu tuwe na fedha ya kutosha ili watekeleze miradi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie hoja iliyopo mezani kwetu. Nianze kwa kuwapongeza viongozi wa Wizara hii; Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Makatibu Wakuu kwa kazi nzuri ambayo wameifanya hadi wakaja na Kitabu cha Bajeti. Mchango wangu utajikita kwenye Sekta ya Kilimo na itajikita sana kwenye zao la korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge aliyemaliza kuongea sasa hivi, amezungumzia Export Levy na Mheshimiwa Bundala muda fulani alizungumzia Export Levy. Nami nitaendeleza hapo hapo, kwamba kwa miaka mitatu mfululizo, tumeona Serikali ikiufanya uwekezaji mkubwa sana kwenye zao la korosho, kwa hili naipongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilianza kutoa tozo ikaweka matumizi sahihi ya fedha ya Serikali kwenye Mfuko wa Zao la Korosho na Bodi ya Korosho na hata kufikia hatua ya kuvunja Bodi ya Korosho. Mwisho ikatolewa incentive kwa wakulima, mwaka 2017 zikatolewa pembejeo ambazo wakulima walipewa bure. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji huo ulifanya uzalishaji wa korosho uwe double. Kwa sababu uzalishaji wa korosho nchini, mwaka 2015/2016 ilikuwa tani 155,000. Mwaka 2017 ilikuwa tani 315,000, kwa uwekezaji mdogo tu huo. Nasikitika sana kwamba kinachoendelea mwaka huu ni kudhoofisha Sekta ya Korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulianza majadiliano na Mheshimiwa Waziri wa Fedha atakumbuka, tulienda ofisini kwake kama Wabunge wa Mkoa wa Mtwara na Lindi wanaozalisha zao la korosho, kuhusu upatikanaji wa fedha za pembejeo. Alitujibu vizuri tu kwamba kuna kasoro kwenye ile sheria, kwa sababu Sheria ya Korosho ilisema fedha hizi zitatumiwa baada ya kutengenezwa kanuni. Mheshimiwa Waziri wa Kilimo alitengeneza kanuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake sasa, tunaona ukurasa wa 69 kwamba Serikali inadhamiria kwamba ile Sheria ya Tasnia ya Korosho ambayo ilikuwa inakusanya korosho, asilimia 35 zinakwenda kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali na asilimia 65 zinakwenda kwenye uendelezaji wa zao la korosho. Sasa inakusudiwa kufutwa na nimechungulia kwenye Finance Bill ipo, inafutwa ili fedha zote ziingie kwenye Mfuko Mkuu. Hapa tunaua korosho. Hapo wanafanya siasa ya Mikoa ya Mtwara na Lindi iwe ngumu. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, kwa hili tuungane. Kwa taarifa ya Kituo cha Utafiti Naliendele sasa hivi, wamejikita kwenye Mikoa 17. Kwa hiyo, wale wenzangu wa Chunya, Singida na Tabora, fedha hii ikiondoka hawatawaona wataalam wa Naliendele wanakwenda kwao kwa ajili kuliendeleza zao la korosho. Kwa hiyo, tuungane ili fedha hizi zirejeshwe, Kituo cha Utafiti Naliendele kifanye kazi yake, nao wazalishaji wapya wa korosho wapate hayo matunda ambayo yameonekana kwenye zao la korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwenye hili kuna changamoto nyingi sana, kwa sababu madhara yake, kama nilivyosema kwanza, sasa hivi hakuna kinachoendelea kwenye sulphur. Inasikitisha sana, mwaka 2017 Serikali ilileta tani 28,000 hazikutosha, lakini mwaka huu tuliambiwa kwamba zimetolewa shilingi bilioni 10 kupelekwa TFC ili waagize pembejeo ya sulphur, hakuna hata kilo 50 ambayo imeeingia sasa hivi nchini. Shilingi milioni kumi hizi zimekuwa dana dana. Kwa hiyo, mwaka huu wakulima wamechanganyikiwa kuhusu sulphur. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, fedha hizi zingetumika kulipa vikundi vidogo vidogo vya wazalishaji wa miche ya mikorosho. Kwa bahati mbaya sana wakulima hawa au vikundi hivi walishazalisha hiyo miche, miche imeshachukuliwa kwa wakulima, hawajapewa hata shilingi. Kwa hiyo, Mbunge ukionekana kule unazunguka zunguka wanakwambia Mbunge fedha zetu tulizotumia kuzalisha miche ya mikorosho bado hazijatolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shughuli ambayo itaenda kuua kabisa tasnia ya korosho ni kwamba asilimia ya fedha hizi zilikuwa zinakwenda Kituo cha Utafiti Naliendele kwa ajili ya utafiti wa zao la korosho. Kule hali ni mbaya. Tulikutana na wataalam wanasema kule hakuna kinachoendelea. Madhara ya kwanza ni upungufu wa mbegu za korosho. Mbegu za korosho lilikuwa jukumu la Kituo cha Utafiti Naliendele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapoondoa fedha hizi na wao wamesimamisha uzalishaji wa mbegu za korosho. Kwa sababu kuna mikoa mipya 17 ambayo imeingia kwenye uzalishaji wa korosho, mahitaji yao wao ni tani 165 za korosho. Kwa hiyo, mwaka huu hizo hazitaingia kwenye tasnia ya korosho. Madhara ya pili ni kwamba watashindwa kuendeleza kilimo cha korosho kwenye maeneo mapya. Kama nilivyosema, Chunya, Kyela, Singida na Tabora, walishaanza uzalishaji. Kwa hiyo, wale hawatawaona tena wataalam kutoka Naliendele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, masikitiko yetu makubwa ni kupotea kwa ajira. Kituo cha Utafiti Naliendele kilikuwa kinatumia sehemu ya fedha hizi kwa ajili ya ajira ya watumishi wa pale, takriban watumishi 77 watapoteza ajira na kituo kile sasa hivi kuna ajira za kudumu watumishi wawili tu, madereva. Kwa hiyo, fedha hii inapokosekana, Kituo cha Utafiti cha Naliendele kitapoteza watumishi 77 na kitabaki na madereva wawili tu. Hebu angalia tasnia ya korosho inavyoteketea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Dkt. Mpango asiingie kwenye kumbukumbu mbaya kuua zao la korosho katika nchi yetu. Hebu naomba tutafakari hili turejeshe. Naelewa kwamba lengo lake ni kufanya matumizi mazuri ya fedha hizi, tusimamie, kama udhaifu ni Watendaji wa Bodi ya Korosho, tuwawajibishe, lakini siyo kuchukua fedha shilingi bilioni 211 ambazo zingeingia katika kuendeleza zao la korosho na kuzipeleka kwenye Mfuko Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ya pili ni kuhusu produce cess, ushuru ambao Halmashauri au mamlaka ya Serikali za Mitaa zinatakiwa kulipwa. Sheria inasema kwamba wapewe 3% ya farm gate price. Kumekuwa na upotoshwaji wa sheria hii unaofanywa na Wizara ya Kilimo na Bodi ya Korosho. Wanachaji 3% kwa bei dira, siyo sahihi. Kwa 3% inatakiwa iwe bei ya mnadani, ndiyo ushuru ambao unatakiwa uende Halmashauri na mlipaji sio mkulima, ni mnunuzi wa korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tufanye marekebisho hayo, tusimamie vizuri. Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba imefika mpaka Mahakamani. Kwanza ilienda kuomba ushauri Ofisi ya AG Mtwara. Ofisi ya AG Mtwara ikajibu vizuri kabisa kwamba definition ya Farm Gate Price ni bei ya mnadani na siyo bei dira. Kwa hiyo, naomba hii wakati wa kufanya majumuisho, Mheshimiwa Waziri na hususan Waziri wa Kilimo, aiagize Bodi ya Korosho kwa sababu kila msimu huwa anatoa mwongozo; aiagize Bodi ya Korosho msimu ujao watoze ushuru wa Halmashauri kwa bei na mnadani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi fedha zinazoenda kwenye Halmashauri siyo sadaka, zinatumika kwa ajili ya Maendeleo ya Halmashauri zetu. Halmashauri zetu vyanzo vingi tumewanyang’anya. Wamebaki na produce cess tu. Sasa walipwe kile wanachostahili na siyo 3% ya bei dira, iwe 3% ya bei ya mnada. Hii inawezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile Mheshimiwa Waziri wa Kilimo aiagize Bodi ya Korosho isi-charge hii 3% kwa mkulima, sheria iko wazi kabisa. Anayelipa produce cess ni mnunuzi (buyer). Mkulima akifika sokoni, hatakiwi kuchajiwa hiyo produce cess, anayetakiwa kulipa ni mnunuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu na Naibu Waziri Mheshimiwa Injinia Masauni kwa kazi nzuri wanazofanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utajikita katika maeneo matatu. Kwanza ni kuongeza askari Kituo cha Polisi Nanyamba. Kituo cha Polisi Nanyamba kilijengwa miaka mingi kuhudumia wakazi wa Nanyamba kama tarafa. Mwaka 2015 ilianzishwa Halmashauri ya Mji Nanyamba na Jimbo la Nanyamba. Kituo hicho sasa kimechakaa na idadi ya askari ni wachache. Naomba idadi ya askari iongezwe, kituo kipya kijengwe na wapewe na usafiri ili waweze kukabiliana na changamoto zinazojitokeza kwa kuwa kuna ongezeko kubwa la watu na uhalifu na wahalifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ni ujenzi wa nyumba za askari. Kuna upungufu mkubwa wa nyumba za askari katika Mkoa wa Mtwara na katika Halmashauri ya Mji Nanyamba. Katika Halmashauri ya Mji Nanyamba hakuna nyumba ya askari na kuna kituo cha polisi. Naomba mgao wa nyumba mpya kwa Mkoa wa Mtwara na Jimbo la Nanyamba kwa ajili ya askari wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, ni changamoto za ulinzi na usalama kwa maeneo ya mpakani. Kuna changamoto ya usalama kwa maeneo tunayopakana na nchi jirani ya Msumbiji. Naomba askari wa Nanyamba wawezeshwe vitendea kazi ili waweze kufanya patrol maeneo ya Kifaya ambako kuna mwingiliano na wenzetu wa Msumbiji.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, naipongeza Wizara kwa kazi nzuri inayofanya katika kutekeleza majukumu yake, ikiongozwa na Waziri, Mheshimiwa Kangi Lugola na Naibu wake Mheshimiwa Mhandisi Hamadi Masauni.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu utahusu maeneo matatu. Kwanza ni nyenzo za kufanyia kazi. Kuna changomoto kubwa ya vitendea kazi kwa Majeshi yetu ya Polisi, Magereza na lile la Zima Moto. Naomba Serikali kuangalia kwa karibu suala hili kwani imefika mahali ikitokea dharura, Polisi wanategemea msaada wa vyombo vya usafiri kutoka kwa watu binafsi kwa kutokuwa na gari au gari kukosa matengenezo. Si ajabu kuona Magereza nao wanaomba kusaidiwa usafiri kutoka kwa watu binafsi ili kwenda kusaga chakula cha wafungwa. Nashauri majeshi haya yapewe fedha za kutosha kugharamia vitendea kazi, ununuzi wa mafuta, posho za askari na stahili zao zingine pamoja na sare zao.

Mheshimiwa Spika, pili, Kituo cha Polisi Nanyamba. Kituo hiki kilijengwa kama Police Post kuhudumia Tarafa ya Nanyamba miaka ya nyuma. Kwa sasa Nanyamba ni Halmashauri ya Mji na Jimbo na idadi ya watu imeongezeka na matukio ni mengi. Naomba yafuatayo yafanywe: Kituo hiki kiboreshwe ili kukidhi haja ya kuhudumia eneo husika; idadi ya askari waongezwe; na wapewe usafiri wa magari na pikipiki.

Mheshimiwa Spika, tatu, magari ya Zimamoto ni ya muda mrefu, machache na hayatoshelezi. Nashauri zitengwe fedha za kununua magari zitakazopelekwa kila Halmashauri hata kwa kununua awamu kwa awamu.

Mheshimiwa Spika, nawasilisha, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza viongozi wa Wizara hii ikiongozwa na Waziri Mheshimiwa Profesa Ndalichako, Naibu Waziri Mheshimiwa Ole-Nasha na Katibu Mkuu Dkt. Akwilapo. Nawapongeza kwa kazi nzuri wanayoifanya na mabadiliko chanya yanaonekana kwenye sekta hii ya elimu. Mchango wangu utajikita kwenye maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kitengo cha Udhibiti Ubora wa Elimu (Ukaguzi wa Shule), kitengo hiki kipewe rasilimali za kutosha ili kitekeleze majukumu yake, wapewe rasilimali fedha na watumishi. Kitengo hiki kibadilishwe muundo, badala ya kuwa na ofisi ya kanda sasa zifunguliwe kwenye mkoa. Ofisi za kanda ziliweza kudumu wakati idadi ya shule za sekondari ni chache, kwa sasa idadi imeongezeka na hawawezi kukagua shule zilizopo kwenye kanda husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Matumizi ya TRC (Teachers Resource Centre), huko nyuma tulikuwa na program ya DBSPE (District Based Support to Primary Education) na kulikuwa na mtando wa TRC ambazo zilitumika kutoa mafunzo kazini kwa Walimu wetu. Naomba vituo hivi vitumike kama lengo lake lilivyokuwa hapo awali. Vitengewe fedha za kutosha ili viweze kuendesha semina za Walimu katika maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taasisi ya Elimu iachwe ifanye kazi zake za awali za kutunza mtaala, shughuli ya ufundi wa vitabu na uhakiki wa machapisho yatakayotumika kwenye mfumo wa elimu ipewe chombo kingine na sekta binafsi iachiwe kwenye uchapishaji.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami nichangie mapendekezo ya mpango yaliyo mbele yetu. Pia nami niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wa Wizara hii kwa kuteletea mpango ambao unaonekana kabisa kwamba ni mwendelezo wa utekelezaji wa mpango wetu wa miaka mitano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita sehemu mbili, ya kwanza itakuwa ni kilimo. Kuna watu ambao wanabeza kwamba hatuwekezi vya kutosha katika kilimo lakini ukiangalia ukurasa wa 29 wa kitabu cha Waziri tunaona kabisa kwamba sekta hii mwaka jana ilipanda kwa asilimia 7.1, hongera sana. Kuna uwekezaji ambao unafanya kwenye sekta hii ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nimpongeze Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa kwa kazi kubwa anayoifanya kwenye mazao ya kimkakati. Tumeona anahangaika na kawaha, chai, mchikichi vile vile amehangaika na tumbaku na pamba kwa kiasi kikubwa sana. Nampongeza kwa sababu jitihada zake kwa kiasi kikubwa zimechangia ongezeko hili la sekta ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma sasa takwimu utakuta zao la korosho ndilo lililochangia zaidi kwenye mafanikio hayo. Kwenye zao la korosho kwa miaka mitatu mfululizo kuna ongezeko la uzalishaji. Mwaka 2015/2016 tulikuwa na tani 155; mwaka 2016/2017 tani 265; na mwaka 2017/2018 kuna tani 315,000. Hili ni ongezeko kubwa na linatokana na uwekezaji mkubwa ambao ulifanywa kwenye zao hili la korosho. Rai yangu kwa Serikali, korosho bado inahitaji uwekezaji mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, bado Serikali ina mambo ya kufanya ili kuhakikisha uzalishaji wa korosho unaendelea kuongezeka kama takwimu zinavyoonesha. Kwanza lazima tuwe na mipango sahihi ya kupatikana kwa pembejeo. Tusiachie wafanyabiashara binafsi walete pembejeo ambazo hatuna uhakika na ubora wake na wanawauzia wakulima wetu kwa bei ya juu. Kwa hiyo, Serikali bado kuna kitu inahitajika kufanya ili kuhakikisha zao letu la korosho halishuki kwa uzalishaji kama tunavyoona kwenye takwimu za miaka hiyo mitatu iliyopita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye korosho kuna changamoto mwaka huu. Takwimu zinaonesha hadi sasa kwa Mkoa wa Mtwara tu Chama Kikuu cha Ushirika cha Tandahimba na Newala (TANECU) wana tani 30,000 na Chama cha Ushirika cha Mtwara, Nanyumbu na Masasi (MAMCU) kuna tani takribani 30,000 zimekusanywa lakini hadi sasa ni tani 2,200 zimenunuliwa. Hapa kuna changamoto ya soko la Dunia lakini vilevile mwaka huu kuna syndicate ya wanunuzi wa korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali yangu, hawa wanunuzi wamewasilisha barua kuhusu punguzo la kile ambacho Mheshimiwa Rais na nimpongeze anavyosimamia ununuzi wa korosho mwaka huu, kwa sababu amekuwa akifuatilia siku hadi siku nini kinaendelea kwenye soko la korosho. Kwa hiyo, naishaiuri Serikali yangu ifanye mashauriano na hawa wafanyabiashara, kama kweli madai yao ni ya msingi basi itafutwe mbinu ya kufidia ile Sh.200 ambayo wanaomba wapunguziwe ili waende sokoni wakanunue korosho. Kama madai yao si sahihi basi lile pendekezo au wazo la Mheshimiwa Rais, kwamba korosho zitanunuliwa na Serikali yetu, muda umefika sasa Serikali itoe tamko ili korosho zikanunuliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu tuna wiki tatu tu ambazo sisi tuna nafasi ya kuuza korosho ikishafika mwezi Desemba korosho za nchi nyingine zinakuwa tayari na wanunuzi wataenda maeneo mengine. Kwa kuwa Serikali yangu ni sikivu haya watayafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuondoke hapa nini kifanyike? Tuwekeze kwenye ubanguaji. Siku za nyuma tulifanya kazi kubwa sana ya kuwekeza kwenye viwanda, tuna viwanda 12 vya ubanguaji wa korosho. Viwanda hivi umefika wakati sasa tufanye maamuzi magumu. Wale wanunuzi walionunua viwanda hivyo ambao hawafanyi kazi ya ubanguaji wanyang’anywe viwanda hivyo. Kuna Kiwanda Mtwara, Newala, Masasi, Nachingwea, Mtama, Likombe, Lindi, Kibaha, Tanita I, Tanita II, Newala II na Tunduru. Viwanda hivi havifanyi kazi ya kubangua korosho, kuna viwanda vingine sasa hivi vinatumika ma-go-down.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Serikali ifanye maamuzi magumu. Wale ambao wamevichukua viwanda hivi na kuvifanya ma-go-down, hawabangui korosho wanyang’anywe ili wapewe wawekezaji wapya ambao wameonyesha nia ya kubangua korosho yetu hapa hapa nchini. Kwa kufanya hivyo, tutaondokana na tatizo la kupeleka korosho ghafi India ambako kwa njia moja au nyingine wafanyabiashara wa nchi hii huwa wana kawaida ya kupanga bei na hivyo kumdhoofisha mkulima wa zao la korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mpango huu vilevile naomba nichangie kuhusu eneo maalum la uwekezaji na hasa eneo la Mtwara. Nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa inayofanya katika upanuzi wa Bandari wa Mtwara. Tumeona kuna uwekezaji mkubwa sasa hivi umefanyika kwenye Bandari ya Mtwara na sasa hivi meli za mafuta zimeshaanza kutia nanga na hivyo kurahisisha upatikanaji wa mafuta Kanda ya Kusini Mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma na hata nchi za jirani Malawi na Msumbiji. Vilevile tunaona kuna ukarabati mkubwa ambao umeanza kwa uwanja wa ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili eneo hili la Mtwara liwe rahisi kuwekeza kuna kazi mbili zimebaki sasa hivi. Kwanza kuna suala la barabara yetu ya uchumi, barabara ya Mtwara- Nanyamba-Tandahimba-Newala-Masasi, km 210. Barabara ile matengenezo yameanza kwa km.50. Tunaomba sasa mpango ujao zitengwe fedha za ujenzi wa barabara kuanzia Mnivata-Newala-Masasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna barabara nyingine muhimu sana, barabara ya ulinzi ambayo ipo Kusini mwa Tanzania na inaunganisha Wilaya zote na pembeni mwa Mto Ruvuma. Barabara hii haitengewi fedha za kutosha. Tunaomba katika mpango ujao zitengwe fedha za kutosha kwa ajili ya matengenezo makubwa ya barabara yetu ya ulinzi kwa ajili kuimarisha ulinzi wa nchi yetu. Kama mnavyofahamu kwamba kule wenzetu Msumbiji kuna nyakati kunakuwa na changamoto za ulinzi, kwa hiyo, barabara yetu iwe inapitika muda wote na vijana wetu wa ulinzi na usalama waweze kuitumia kwa ajili ya kulinda nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu mwingine utajikita kwenye suala la kufungamanisha uchumi na maendeleo ya watu. Kuhusu elimu na ujuzi, hapa lazima tuwekeze vya kutosha. Mpango ujao unatakiwa utenge fedha za kutosha kwa ajili ya sekta ya elimu. Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Msingi ambao ulitekelezwa kuanzia mwaka 2002 kulikuwa na ujenzi mkubwa wa madarasa pamoja na nyumba za walimu, lakini madarasa yale yanahitaji ukarabati mkubwa sana. Wote mtakuwa mashahidi zilitengwa fedha takribani shilingi milioni tatu na laki moja kwa ajili ya ujenzi wa chumba cha darasa kwa miaka hiyo. Ujenzi uliofanyika kwa wakati ule muda wa kukarabati majengo hayo sasa umeshafika. Naomba mpango ujao utakaowasilishwa zitengwe fedha za kutosha kwa ajili ya kukarabati miundombinu ya elimu ya msingi kama vile vyumba vya madarasa, nyumba za walimu na ujenzi wa matundu ya vyoo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini si hivyo tu, bado kuna suala la motisha kwa walimu. Walimu wetu wanahitaji motisha na kupata mafunzo kazini. Ni mwaka wa tatu sasa mishahara ya walimu na watumishi wengine bado haijaongezwa.

Mimi ninawasemea walimu kwa sababu ni kundi kubwa na ni asilimia 60 ya watumishi wa umma wa nchi hii. Watumishi hawa wakikata tamaa basi kazi zote ambazo tunawekeza katika maeneo mengine hazitakuwa na maana. Kwa hiyo, naomba katika bajeti ijayo tutenge fedha za kuongeza mishahara ya walimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie hotuba iliyo mbele yetu, hotuba ya Wizara ya Maji, hoja ambayo ni muhimu na ni nyeti kwa Watanzania wote.

Mheshimiwa Spika, nianze kuwapongeza viongozi wa Wizara hii; nianze kumpongeza Waziri wa Maji, Mheshimiwa Prof. Mbarawa; nimpongeze Naibu wake, Mheshimiwa Aweso; nimpongeze Katibu Mkuu, Prof. Kitila Mkumbo na Naibu Katibu Mkuu Eng. Kalobelo; wakurugenzi wa Wizara pamoja na watendaji wa maji katika ngazi mbalimbali, Mamlaka ya Serikali za Mitaa pamoja na mikoa. Kwa kweli wanafanya kazi kubwa na kazi wanazozifanya zinaonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri ulikuja kukagua mradi wetu wa Chawi, ulifanya kazi kubwa ulizunguka mpaka Nanyamba, Mheshimiwa Aweso ulitatua changamoto kubwa ya mradi ambao ulikuwa unatekelezwa Nanyamba, unasimamiwa na Mtwara Vijijini, baada ya kikao chako kifupi ulitoa suluhisho la changamoto ile.

Mheshimiwa Spika, niwashukuru kwa miaka miwili mfululizo mlikuwa mnatenga fedha za kutosha kwa ajili ya miradi ya maji ya Halmashauri ya Mji wa Nanyamba, nawashukuru sana. Lakini kipekee niwashukuru hivi karibuni mmetoa kibali kwa ajili ya ujenzi wa visima kumi. Kwa hiyo. nichukue nafasi hii Mheshimiwa Waziri nikushukuru kwa jinsi unavyotoa jicho la kipekee kwa Halmashauri ya Mji wa Nanyamba.

Mheshimiwa Spika, nichangie sasa kuhusu Mradi wa Maji wa Makonde; mradi huu ni wa siku nyingi na upo katika ile miji 28, na mradi huu katika eneo letu utahudumia Mamlaka za Serikali za Mitaa zisizopungua nne na majimbo kama matano. Mradi huu ni wa siku nyingi na unahitaji kujengwa upya. Sasa Mheshimiwa Waziri nikukumbushe tu kwamba tulishawasilisha andiko Wizarani kwako na ulipofika pale Chawi uliahidi kwamba hakuna Mtanzania atakayekosa maji kwa sababu ya gharama.

Mheshimiwa Spika, mradi huu ni wa siku nyingi na unahitajika kujengwa upya. Sasa Mheshimiwa Waziri nikukumbushe tu kwamba tulishawasilisha andiko Wizarani kwako na ulipofika pale Chawi, uliahidi kwamba hakuna Mtanzania atakayekosa maji kwa sababu ya gharama. Nanyamba andiko letu ni kutoa maji Mitema na kupeleka Halmashauri ya Mji wa Nanyamba, mradi ambao unahusisha kata tisa, mitaa tisa na vijiji 34. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watendaji waliniahidi kwamba tutaingiza kwenye utekelezaji wa fedha za mkopo wa Serikali ya India hata kama hawajatoa maandishi kwa Mkurugenzi wetu, lakini kauli ya Waziri, kauli ya Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu tunaiamini. Rai yangu kwa Mheshimiwa Waziri ni kwamba Serikali inafanya kazi kwa maandishi. Naomba mtoe andiko mumpelekee Meneja wa Mradi wa Makonde ili wakati wa utekelezaji asione kwamba ni annex aone kwamba ni component muhimu katika mradi huo.

Mheshimiwa Spika, mradi huu kama nilivyosema unahusisha vijiji 34 na mitaa tisa; kwangu wananchi wanaopata maji ni asilimia 45, lakini mradi huu ukitekelezwa, tutafikia asilimia 85. Kwa hiyo, naomba component hii ya kutoa maji Mitema kupeleka Nanyamba isisahauliwe na aandikiwe barua Meneja wa Mradi ili wakati wa utekelezaji basi isiwe annex iwe ni sehemu ya mradi wa Makonde. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichangie mradi wa maji wa kutoa Mto Ruvuma na kupeleka Mtwara Manispaa. Wachangiaji waliopita wamezungumzia mradi huu lakini naamini kwa sababu chanzo cha maji kipo Jimboni kwangu Mahembe Chini, naomba sasa mradi huu utekelezwe, ni mradi wa muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, suala lingine, kuna kauli mbili Wizarani, kuna kauli ya kutekeleza mradi huu, lakini kuna maneno ya chini chini kwamba mradi huu siyo viable kwa hiyo, hautatekelezeka. Kwa hiyo, naomba wawe wazi tuambiwe kama mradi unatekelezwa au autekelezwi. Wananchi wa Mtwara wanataka maji whether wanatoa Ziwa Victoria kupeleka Mtwara au Mto Ruvuma, tunachotaka ni maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama mradi unatekelezwa tuambiwe kwamba mradi unatekelezwa; na kama kuna mabadiliko ambayo yameonekana kwamba kwa Wizara kutekeleza mradi huu kuna gharama ambazo siyo za lazima, basi mtuambie. Wanachohitaji wananchi wa Mtwara, Nanyamba na sehemu ya Mtwara Vijijini ambapo linapita bomba hili, wajulishwe ili na wao waweze kufahamu na pia ili miradi inayotayarishwa na Mamlaka ya Serikali ya za Mitaa iweze kujumuisha maeneo haya ambayo hapo awali tuliacha kwa sababu kuna mradi mkubwa wa kutoa maji Mahembe Chini, yaani Mto Ruvuma na kupeleka Manispaa ya Mtwara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 106 wa kitabu cha Mheshimiwa Waziri unazungumzia changamoto za utekelezaji wa miradi ya maji. Hapa changamoto ya kwanza amesema upatikanaji mdogo wa fedha za kutekeleza miradi. Naungana na wale wanaosema tuongeze shilingi 50/= ili tupate fedha za kutosha za kutekeleza miradi yetu ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna haja ya kuwa na wasiwasi. Professor amesema kwenye kitabu chake kwamba kuna changamoto ya fedha na isije tukawalaumu baadaye kwamba Mheshimiwa Prof. Mbarawa alishindwa, kumbe siyo kwamba alishindwa, hakuwezeshwa, hakupewa fedha za kutosha. Kwa hiyo, tuwape fedha za kutosha ili Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji waweze kutekeleza miradi ya maji kama walivyojipangia. Tusipofanya hivyo, tutawalaumu kwa makosa ambayo siyo ya kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia hapa Mheshimiwa Waziri ameweka wazi kwamba fedha za maendeleo hadi Aprili amepata asilimia silimia 53, fedha za uhakika ni za Mfuko wa Maji, wenye kufanya maamuzi ni sisi. Mheshimiwa Chenge amesema vizuri kwamba kuna Azimio la Bunge. Kwa hiyo, tuliunge mkono Azimio la Bunge, Wizara hii ipate fedha ili itekeleze miradi ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye Ilani ya Chama chetu cha Mapinduzi inasema tutatekeleza miradi ya maji kwa asilimia 85 ifikapo 2020. Bila kuwaongezea fedha tutakuwa na maswali magumu sana mwakani. Hii ni Mei sasa hivi, 2020 siyo mbali. Tuwape fedha ili wakatekeleze miradi ya maji ili 2020 tusipate kazi ya kuzungumza maneno marefu majukwaani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchango wangu wa mwisho unahusu mabadiliko ambayo tumeyafanya hivi karibuni kuhusu sheria Na. 5 ya 2019 kuhusu Huduma ya Maji na Usafi wa Mazingira. tunaazisha RUWASA, ushauri wangu kwa Wizara, hebu tufanye matayarisho ya kutosha ili chombo hiki kipya tunachokianzisha kianze kwa ufanisi.

Mheshimiwa Spika, Mamlaka za Serikali za Mitaa zina hadhi tofauti. Tumeona pale tulipoanzisha TARURA, tuliwaambia kwamba Mhandisi wa Maji aende kule na gari yake. Ukitamka hivyo, Meneja wa RUWASA wa Nanyamba hatakuwa na gari, kwa sababu so far Nanyamba haina gari ya maji. Kwa hiyo, ukisema atumie gari ambayo alikuwa anatumia Halmashauri, Meneja yule ameanza kazi kwa kufeli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba matayarisho ya kutosha yafanywe ili RUWASA atakapoanza, Meneja wa RUWASA wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa awe na rasilimali za kutosha. Kwanza apate ofisi, awe na rasilimali za kutosha, awe na vitendea kazi na aanze kwa kujiamini na siyo kuwa omba omba wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, rai yangu kwa Wizara, tufanye maandalizi ya kutosha. Sheria tumeitunga vizuri, lakini tusipofanya maandalizi ya kutosha tutaanza kuilaumu RUWASA wakati hatujawapa rasilimali za kutosha.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kuwapongeza Viongozi wa Wizara hii, Waziri Mheshimiwa Ummy Mwalimu na Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile kwa kazi nzuri wanayofanya ya kusimamia Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu utajikita katika maeneo matatu. Kwanza, Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini inayojengwa Mtwara. Ujenzi wa Hospitali hii umeanza muda mrefu na sasa umesimama. Mheshimiwa Waziri alipotembelea ujenzi huu mwaka juzi aliahidi kuwa ni bora jengo lililopo likakamilika na baadhi ya Idara zikaanza kufanya kazi. Nashauri ujenzi uendelezwe kwenye eneo hili na hospitali ifunguliwe kwa kuanza na idara ambazo zinaweza kutumia jengo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mtwara (Ligula). Hospitali hii inahitaji ukarabati mkubwa wa majengo yake na ina idadi chache ya watumishi kwa maana ya madaktari na wauguzi. Hatua zichukuliwe ili kukabiliana na changamoto hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, dawa za magonjwa yasiyoambukiza (kisukari na shinikizo la juu la damu). Kuna ongezeko kubwa la wagonjwa wa magonjwa hayo na kwa kuwa wagonjwa hao hutumia dawa muda mrefu na bei zake ni za juu, nashauri Serikali iangalie kwa karibu tatizo hili kwa kufanya yafuatayo:-

(i) Kuwa na programu za kutoa elimu kwa jamii ili kupunguza watu wanaoambukizwa;

(ii) Kuhakikisha kuwa dawa zinapatikana kwa bei nafuu hadi ngazi za chini; na

(iii) Kliniki za binafsi zidhibitiwe kwa kuwa zinatoa huduma kwa bei ya juu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kuwapongeza viongozi wa Wizara hii. Mheshimiwa Kakunda Waziri wa viwanda na Biashara na Naibu wake Mheshimiwa Engineer Stella Manyanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu utahusu maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni tozo ya usafirishaji kwa wafanyabishara. Kuna malalamiko ya wafanyabiashara kuwa na tozo nyingi na taasisi nyingi za udhibiti. SUMATRA, Zimamoto, TFDA, OSHA, TRA, Mamlaka ya Serikali za Mitaa, WCF na zinazofanana na hizo. Tozo zifuatazo; Corporate Tax, Service Levy, OSHA, TFDA, TBS, tozo ya ukaguzi wa Zimamoto, nashauri kuwe na kituo kimoja cha ulipaji tozo hizo na taasisi zipunguzwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri viwanda vya korosho vilivyobinafsishwa vifufufuliwe na vifanye kazi ya kubangua korosho. Wanunuzi wengine wanafanya maghala, nashauri wanyang’anywe. Tuwe na mkakati mahsusi wa muda mfupi wa kuuza nje korosho zilizobanguliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, SIDO ni taasisi ambayo inaweza kuwakomboa wakulima na wajasiriamali wengine katika kutoa teknolojia mpya katika uzalishaji. Naomba taasisi hii ipewe fedha za kutosha ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi. Pia maonyesho ya SIDO yaboreshwe na teknolojia zinazotumika ziwe za kisasa. Aidha, kuwe na utaratibu wa kuwasilisha teknojia hiyo kwa wakulima au wajasiriamali wa vijijini.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, nawapongeza viongozi kwa kazi nzuri wanazofanya. Mheshimiwa Waziri Dkt. Medrad Kalemani na Naibu Waziri Mheshimiwa Mgalu, hongereni sana. Mchango wangu utajikita katika maeneo matatu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, vijiji vilivyo kwenye line kubwa Mtwara-Nanyamba Newala, vijiji takribani nane vipo chini ya line hii. Nimpongeze Waziri kwa maagizo yake ambayo aliyatoa hivi karibuni akiwa Mtwara kuwa vijiji hivyo vipewe umeme. Nashauri TANESCO Mtwara wawezeshwe ili waweze kutekeleza maelekezo hayo.

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya Majengo; kituo hiki kipo Kata ya Njengwa na hakuna umeme. Namshukuru Waziri kwa kuelekeza TANESCO Mtwara kuwa waanze mpango wa kuleta umeme katika kituo hiki. Nashauri msisitizo utolewe ili kiweze kupata umeme ili kiweze kutoa huduma zilizokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, mradi wa kusambaza gesi majumbani; mradi huu ni muhimu na naomba fedha zitengwe za kutosha ili idadi ya nyumba/kaya zitakazopewa gesi ziongezeke katka Miji ya Mtwara, Lindi na Dar es Salaam. Pia na maeneo mengine na wilaya zake na si Makao Makuu ya Mikoa tu.

Mheshimiwa Spika, kukosekana kwa umeme katika baadhi ya Mitaa-Nanyamba Mjini; naomba Mitaa ya Madina, Namkuku na Kilimanjaro iliyopo Nanyamba Mjini iwekewe umeme.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri. Pia na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayoifanya pamoja na hotuba nzuri.

Mheshimiwa Spika, naomba nichangie katika maeneo matatu; kwanza Finance Bill ijayo ilete na mabadiliko ya matumizi ya fedha za export levy kwenye zao la korosho ili zitumike pia kuendeleza sekta ya korosho.

Pili, miradi ya gesi asilia na LNG ianze kutekelezwa ili kuinua uchumi wa watu wa Lindi na Mtwara na Watanzania kwa ujumla. Mazungumzo yanayoendelea yaharakishwe na utekelezaji uanze.

Mheshimiwa Spika, Kitengo cha Maafa kishughulikie maombi ya Wabunge wa Nanyamba na Tandahimba na barua ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara yanayohusu wananchi wa vijiji vilivyovamiwa na kikundi cha maharamia kutoka Msumbiji wapewe msaada wa kibinadamu. Vijiji hivyo ni Kitaya, Kilimahewa (Nanyamba) na Kilimahewa (Tandahimba).
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2019
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA - MAKAMU MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI YA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushuru kwa kunipa nafasi ya kuhitimisha hoja yangu. Wabunge waliochangia hoja yetu ni Wabunge 14, na kiujumla hoja zao zilikuwa zinalenga katika kutoa msisitizo wa yale ambayo kamati iliwasilisha kama mapendekezo ili baadaye yalidhiwe kuwa maazimio ya Bunge. Kwa muhtasari nitapita hiyo michango yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya kwanza ilikuwa malipo kwa Waheshimiwa Madiwani. Na hii imechwangiwa na Mheshimiwa Lubeleje, Mheshimiwa Msuha na Mheshimiwa Sikudhani Chikambo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Mheshimiwa Jafo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI ametoa ufafanuzi jinsi gani ametoa maagizo kwa mamlaka ya Serikali za Mitaa. Lakini Kamati inaendelea kusisitiza kwamba pamoja na maagizo hayo TAMISEMI iendelee kufuatilia ili Waheshimiwa Madiwani walipe kabla ya mabaraza ya kuvunja hayo mabaraza yao. Kwa hiyo, naomba sana TAMISEMI mfuatilie ili ifikapo Juni Waheshimiwa Madiwani hawa wawe wameshalipwa stahili zao zote, posho za mwezi na posho za vikao vyao.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya pili ambayo wachangiaji wengi wamechangia na imechangiwa vizuri na Mheshimiwa Msuha ni hoja ya dosari katika kanuni ambayo imetolewa na hivi karibu na Ofisi ya Rais TAMISEMI ambayo inasimamia uendeshaji wa mfuko wa wanawake, vijana na walemavu. Hapa kuna changamoto zimeshaanza kujitokeza kwanza kipindi cha kuanza malipo uundaji wa vikundi. Lakini je, mamlaka ya serikali za mitaa zitachangia fedha hizi 10% kwa muda gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kuna mamlaka za Serikali za Mitaa zina uwezo mkubwa, kwa mfano juzi tulikuwa Jiji la Dodoma wao wanatenga takribani bilioni 6 kila mwaka. Je watachangia bilioni 6 kila mwaka kwa muda gani? Kwa hiyo, nafikiri Wizara yenye zamana itafanya marekebisha kuhusu kanuni hii kwa sababu ya hii sio Quran au Bible wanaweza kurekebisha kulinga na mapato ya halmashauri husika. Kuna halmashauri zina kipato kikubwa na kuna halmashauri ambazo uwezo wao ni mdogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia kuhusu mashine hizi ya kieletroniki kwa ajili ya kuchangia mapato POS Mheshimiwa Chatanda, Mheshimiwa Msuha, Mheshimiwa Komanya na Mheshimiwa Wambura wamechangia kuhusu hili. Na wameelezea changamoto ambazo zimejitokeza kuhusu PoS ambazo zimenunuliwa huko nyuma kwanza zilikuwa zinachezewa lakini zimenunuliwa kwa bei ya juu. Nichukue nafasi hii kuipongeza Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa tendo la hivi karibu la kutoa bure mashine hizi 7,200 kwa mamlaka ya Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunawaomba sasa TAMISEMI wafuatilie matumizi ya POS hizi na kutatua changamoto ambazo zitajitokeza. Naomba Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi iimarishe mitandao katika mamlaka ya Serikali za Mitaa zilizopo pembezoni ili basi mashine hizi ziweze kutumika kwa ufanisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala lingine ambao Wabunge wengi wamelichangia suala la Forces Account. Wachangiaji wote wamekubaiana na maoni ya kamati kwamba Force Account imeonyesha mafanikio makubwa sana tunajenga vituo vya afya, hospitali za wilaya kwa gharama nafuu na kwa ubora ambao ukubalika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ambayo hata sisi kwenye kamati yetu tumeisisiza kwamba kuna upungufu wa wataalam wa ujenzi (waandisi). Kwa hiyo, kama huko nyuma ilivyofanya ajira maalum kwa wahasibu basi kwa kuwa ma-engineer wengi wamehamia TARURA naomba Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Utumishi watoe kibali cha ajira maalum kwa ajili ya watumishi hawa wa kitengo cha ujenzi ili miradi hii isimamiwe ipasavyo. Lakini kwa ujumla force account ni mkombozi kwa fedha za umma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya tano ambayo Wabunge wengi wamechangia ni kuhusu miradi ya kimkakati, na kipekee nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais na Wizara wa Fedha na Mipango kwa ubunifu huu mkubwa kwa kuzianzishia mamlaka ya Serikali za Mitaa miradi ya kimkakati. Miradi hii ikikamilika itapunguza utegemezi wa halmashauri kwa Serikali Kuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, ushauri wa kamati kama tulivyotoa kwenye Kamati yetu, kwanza Ofisi ya Rais, TAMISEMI miradi hii inakaribia kukamika sasa hivi, tumetembelea Soko la Job Ndugai hapa Dodoma, tumetembelea Dodoma Bus Terminal. Lakini kuna soko kubwa linajengwa pale Morogoro, miradi hii sasa naomba Ofisi ya Rais, TAMISEMI iweke utaratibu maalum wa kuikabidhi kwenye Serikali za Mitaa na namna yakuziendesha ili ilete tija. Tumeambiwa hapa soko la Ndugai na ile Dodoma Bus Terminal miradi hii ikikamilika itakusanya bilioni 18 kwa mwaka. Huu ni ukombozi mkubwa kwa mamlaka ya Serikali za Mitaa na itapunguza utegemezi kwa Serikali Kuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ombi letu la pili kwenye kamati tumezungumzia suala la viwango kwa sababu suala hili la kimkakati fedha zimetoka hazina kama ruzuku. Basi tuhakikishe viwango tutakavyoviweka vya tozo viwe rafiki kwa wananchi wetu tusiweke viwango vikubwa na miradi hii ikakimbiwa na wafanyabiashara. Tujifunze lile funzo ambalo limetokea soko la Mwanjelwa kule Mbeya wameweka viwango vikubwa na wafanyabisha wadogo wamekimbilia lile soko. Ni matarajio yetu Ofisi ya Rais, TAMISEMI itasimamia vizuri na miradi hii ya kimkakati ikawa na manufaa kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema wachagiaji wote hakuna aliyepinga hoja ya kamati, walikuwa walikuwa-qualify au wanasisitiza kile ambacho kamati imekifanya. Kwa hiyo, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa jinsi anavyosimamia Mamlaka ya Serikali za Mitaa na jinsi alivyoongeza usimamizi wa fedha za umma na jinsi anavyoelekeza matumizi ya fedha za Umma kwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Ni matarajio yetu kwamba speed hii itaendelea na mwenye macho haambiwi tazama kuna mabadiliko makubwa sana kwenye mamlaka ya Serikali za Mitaa sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo sasa nikushukuru wewe kwa jinsi ulivyoendesha mjadala wa Kamati yetu. Niombe sasa maapendekezo yetu tisa ya kamati ambayo tumewasilisha naomba sasa yawe maazimio ya Bunge lako tukufu yote tisa tuliyowasilisha yapitishwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye ametuwezesha kukutana katika Bunge hili la Kumi na Mbili, lakini kipekee nikishukuru Chama changu cha Mapinduzi na wananchi wa Jimbo la Nanyamba kwa imani yao kwa kunirejesha tena kwa mara ya pili, nawashukuruni sana. Na niwaahidi Wana Nanyamba kwamba nina nguvu na nitaendelea kuwatumikia kwa nguvu zangu zote ili kuhakikisha changamoto za Nanyamba tunapata ufumbuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hotuba ya Mheshimiwa Rais ina mambo mengi na imetoa maelekezo mengi katika sekta mbalimbali na mimi nitajikita katika sekta mbili, ya kilimo na miundombinu na nianze na sekta ya kilimo. Hotuba imeelezea vizuri kwamba kilimo chetu sasa kinataka kuwa cha kibiashara, lakini Mheshimiwa Rais ametoa ahadi ya upatikanaji wa pembejeo na viuatilifu kwa wakulima tena kwa wakati sahihi na kwa bei nafuu.

Mheshimiwa Spika, sisi Wana-Mtwara zao kuu la uchumi ni zao la korosho. Niiombe Serikali sasa kuwe na mkakati maalum wa kuhakikisha pembejeo ambazo zinatumika kwenye zao la korosho zinapatikana kwa wakati na kwa bei nafuu, lakini sio hivyo tu tuhakikishe kwamba zao la korosho tunapanua soko lake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna minada ambayo inaendelea, lakini tuna TMX, TMX sasa hivi wanashiriki wanunuzi wale wale ambao wanaingia minadani. Hebu TMX iwezeshwe ili tuwapate wanunuzi wakubwa kutoka Vietnam, China na maeneo mengine wasi-bid wale wanunuzi ambao tunawaona kwenye minada. Tuwe na tofauti kwenye TMX tuwaone wale wanunuzi wakubwa na huku kwenye minada tuone wale wa kawaida ambao tunakuwanao. (Makofi)

Vilevile niombe Serikali sasa ielekeze kwenye kuwawezesha wabanguaji wadogo tuongeze thamani korosho badala ya kuuza korosho ghafi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu miundombinu, naomba niipongeze TARURA kwa kazi nzuri ambayo imeifanya na ambayo inaendelea kuifanya, lakini kama walivyosema Wabunge wenzangu kuna changamoto ya kibajeti. Naomba Serikali itafute chanzo kingine cha fedha ili kuiongezea fedha TARURA ili iendelee kufanya kazi nzuri ambayo inaendelea kuzifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini si hivyo tu, miundombinu kwa upande wetu wa Kusini tuna barabara yetu ya Ulinzi inatoka Mtwara mpaka Newala, Tunduru hadi Songea. Nivipongeze vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri ambayo vinaifanya katika mpaka huu wetu wa Kusini, mpaka wa Mto Ruvuma, lakini kwa changamoto ya usalama kwa nchi za jirani sasa barabara hii naomba ijengwe kwa kiwango cha lami kutoka Mtwara kwenda Newala, Tunduru mpaka Mbinga na maeneo ya Songea. Barabara hii ni muhimu na ni muhimu kwa ulinzi na usalama wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu miundombinu vilevile kuna changamoto ya Bandari yetu ya Mtwara. Naibu Waziri hapa asubuhi amejibu kwamba kuna uwekezaji wa bilioni 157 zimepelekwa pale na kuna changamoto ya meli kwenda Mtwara, lakini sababu kubwa ni kwa sababu ya zao moja tu la korosho. Mimi naomba Serikali itoe kiwango maalum cha tozo kwa meli zinazoingia Mtwara ili kuvutia wamiliki wa meli wapeleke meli nyingi kwa wakati huu kwa sababu ukiifanya Bandari ya Dar es Salaam na Mtwara kuwa na rate sawa watu hawawezi kupeleka meli Bandari yetu ya Mtwara. Kwa hiyo, naomba sana kuwe na kiwango maalum ili kuwavutia wasafirishaji walete meli Mtwara.

Mheshimiwa Spika, nimalizie na changamoto ya maji. Niiombe Serikali sasa kwamba kwa changamoto ya maji kwa maeneo ya Mtwara tutumie maji ya Mto Ruvuma kujenga miradi mikubwa ya maji.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Abdallah Chikota.

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, nampongeza Rais kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika majimbo yetu. Nampongeza Waziri na Naibu Mawaziri wake kwa kazi nzuri wanazofanya. Mchango wangu utajielekeza katika maeneo manne; kwanza ni utekelezaji wa mradi wa TACTIC uongezwe kasi katika makundi yote matatu ya mradi; na pili, Serikali ije na sheria ya ugatuaji (decentralization) ili kuwa na mipaka ya kisheria kuhusu majukumu ya Serikali za Mitaa na Serikali Kuu.

Tatu, Halmshauri ya Mji wa Nanyamba ina upungufu mkubwa wa watumishi, mahitaji ni watumishi 744 na waliopo ni 133 sawa na asilimia 19. Naomba kuwe na mpango wa haraka kupunguza upungufu huo; na nne, walimu wanaojitolea wapewe kipaumbele wakati wa kuajiri walimu wapya.
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nitoe mchango wangu kuhusu hoja ambazo zipo Mezani. Kabla sijaanza kuchangia, nitumie nafasi hii, kwa moyo wa dhati, kuipongeza Serikali yangu ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri ambayo imeifanya katika utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa nchi yetu. Kwa kweli kazi kubwa imefanyika, miradi mingi imetengenezwa, mingi tumeiona katika maeneo yetu. Changamoto iliyopo kwa pale ambapo haikutekelezwa ndiyo taratibu za mipango. Imeingizwa kwenye Mpango huu wa Tatu ili itafutiwe fedha iendelee kutekelezwa. Kwa hiyo naipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu unajikita katika maeneo mawili. Sehemu ya kwanza ni sehemu ya kilimo na hapa nitashauri namna gani ya kupata fedha ili tuendelee kutengeneza miradi mingine na itahusu kuongeza thamani kwenye mazao ya biashara na hususan zao la korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ubanguaji ndiyo njia pekee ya kuhakikisha kwamba korosho yetu inapata bei nzuri kwenye soko la dunia. Kubangua korosho ni mkakati ambao tulishauanza hapo nyuma. Lengo la kuweka export levy ilikuwa ni kuwazuia wanunuzi wasisafirishe korosho ghafi, lakini mpango huo naona kama una dosari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwezo wetu wa kubangua korosho kwa viwanda tulivyonavyo ni kama tani 70,000 na sasa hivi tunazalisha mpaka tani 220,000. Kwa hiyo korosho nyingi tunaziuza zikiwa ghafi. Nashauri kwamba tukose fedha kidogo leo ili tupate fedha nyingi baadaye na hii itawezekana kwa kufanya nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tuondoe tozo na kodi zilizopo wakati wa uingizaji wa mashine za kubangua korosho. Wawekezaji wanalalamika kwamba kodi ni kubwa kwa hiyo tuondoe hizo kodi ili mashine nyingi ziweze kuingizwa. Pili, nashauri, tuweke vivutio maalum kwa wawekezaji wapya wa viwanda vya korosho. Ushauri wangu wa tatu, tuondoe kodi na tozo kwenye vifungashio. Wale ambao wana viwanda sasa hivi wanalalamika kwamba vifungashio vina kodi kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya hivyo faida yake hapa ni nini? Faida ya kwanza ni kwamba tutapunguza gharama za uwekezaji, kwa hiyo tutapata wawekezaji wengi; Pili, tutawapata wawekezaji wa ndani badala ya kuwategemea wawekezaji wa nje tu; na tatu, tutapata wawekezaji au wabanguaji wadogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda kidogo cha korosho unaweza ukatumia mtaji wa milioni 60. Kwa hiyo kwa sababu sasa hivi korosho inalimwa na zaidi ya mikoa 12, tunaweza tukatumia halmashauri zetu badala ya kutoa zile fedha za Mfuko wa Vijana kwa vijana mmoja mmoja, tunaweza tukaamua waanzishe viwanda vidogo vidogo vya kubangua korosho. Hapo tutaongeza ajira kwa vijana wetu, tutaongeza ajira kwa wanawake na utakuta thamani ya fedha ile tutakuwa tunaiona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wa Vietnam na India wanatumia sana korosho yetu kuongeza ajira kwao. Mipango hii wakiisikia wenzetu watakuwa na hofu sana kwa sababu korosho ghafi hazitakwenda kwao. Kwa hiyo muda ni sasa tuwekeze katika ubanguaji ili tuongeze ajira. Naona kabisa tukiwekeza kwenye korosho hizi ajira milioni nane ambazo tumeahidi kwenye Ilani ya chama chetu karibu robo yake zitatoka kwenye viwanda vya kubangua korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ya pili, niungane na Mheshimiwa Hokororo kuhusu Mradi wa Makaa ya Mawe Mchuchuma na ule wa Chuma Liganga. Ukiangalia Mipango yetu yote mitatu ile inaendelea kutajwa. Wakati umefika sasa tuweke fedha za kutosha ili miradi hii iende kutekelezwa. Mradi huu unakwenda sambamba na ujenzi wa reli kutoka Mtwara – Mbambabay na ile pacha ya Mchuchuma na Liganga. Tuwekeze katika miradi hii sasa ili tuweze kupata fedha za kutosha. Tukiwekeza kwenye reli hii ya Kusini basi Bandari ya Mtwara itatumika ipasavyo na siyo kama malalamiko yaliyopo sasa hivi kwamba inategemea zao la korosho, tutasafirisha tumbaku kutoka kwa wenzetu Songea lakini Malawi, Zambia na DRC Kongo wanatumia bandari yetu na hivyo tutapata kodi nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, naipongeza Wizara kwa kazi nzuri mnayoifanya. Wizara ina viongozi wasikivu katika kusikiliza hoja za Wabunge kuanzia ngazi ya Wizara, Mikoa na Wilaya.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu utajikita katika maeneo mawili; kwanza ni kuhusu Mradi wa Makonde. Tunaipongeza Wizara ya Maji kwa kuanza kutekeleza mradi huu ambao unanufaisha wakazi wa Halmashauri za Nanyamba; Newala na Tandahimba. Mradi huu kwa usanifu wa sasa unaonekana inaishia kwenye baadhi ya maeneo tu na kusema kuwa sehemu zingine itakuwa Phase II. Tunaomba kazi hiyo ifanywe kwenye Phase I ukizingatia kuwa Wilaya nufaika na mradi huu upatikanaji wa maji upo chini ya asilimia 50.

Pili ni kuhusu mradi wa kutoa maji Mto Ruvuma na kupeleka Mtwara Manispaa, mradi huu ni wa muda mrefu na bado haujaanza kutekelezwa. Mradi huu utanufaisha Halmashauri ya Nanyamba, Mtwara na Manispaa ya Mtwara, mradi huu sasa utengewe fedha ili uanze kutekelezwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie hoja iliyoko mezani kwetu. Nami nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa mawasilisho ya hotuba yake; pili, nimpongeze Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri aliyoianza, lakini na ahadi yake ya kuyaenzi maono ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitajielekeza katika Sekta ya Kilimo na nitaanza na kuchangia kuhusu zao la Korosho. Tangu mwaka 2004 - 2017 tumeshuhudia ongezeko la uzalishaji wa Korosho na hii ilitokana na uwekezaji mkubwa ambao Serikali iliweka kwenye zao la Korosho. Kwa sababu mwaka 2004 tulikuwa na tani 72,000 na mwaka 2017 tulifikisha tani 313,000 za Korosho. Kwa hiyo, kulikuwa na uwekezaji mkubwa na ndiyo maana tukafanikiwa kwa kiasi hicho. Kuanzia mwaka 2018 kuna kushuka kwa uzalishaji wa Korosho na hii ni kwa sababu tulipunguza fedha katika Sekta ya Korosho. Nachukua nafasi hii sasa kuipongeza Wizara ya Kilimo, hususan Waziri na ndugu yangu Mheshimiwa Bashe kwa jitihada ambazo wanazichukua sasa hivi kuhakikisha pembejeo za uhakika zinapatikana kwa wakulima ili uzalishaji uanze kuongezeka. Hongereni sana Wizara ya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, nizungumzie kuhusu Soko la Korosho. Ukurasa wa 30 wa Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ameweka kinagaubaga kwamba ushirika utaendelezwa na vile vile mauzo kwa mazao ya kimkakati utaendelea kuwa chini ya minada chini ya mfumo wa Stakabadhi Ghalani. Naiomba Wizara kurekebisha dosari chache zilizopo. Mfumo huu umeleta mafanikio makubwa sana kwenye zao la Korosho, naomba tuulinde ili wakulima wetu wanufaike na Korosho ambazo wanazalisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, hilo suala la TMX kwa sasa hivi kwa sababu tumeona kuna upungufu ambao umeanza kujitokeza, ni kama alivyowasilisha Mheshimiwa Waziri Mkuu hapa, litumike katika kutafuta masoko ya nje, lakini soko la ndani tuendelee na mfumo wetu wa Stakabadhi Ghalani, kwa sababu TMX imeonekana bado ina changamoto ambazo hazijapatiwa ufumbuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nijielekeze kwenye suala la miundombinu. Ukurasa wa 30 unaelezea vile vile suala la miundombinu, nami nijielekeze katika matumizi ya Bandari yetu ya Mtwara. Kuna uwekezaji mkubwa sana umefanywa katika Bandari ya Mtwara, zaidi ya shlingi bilioni 57 zimewekwa pale; na sasa hivi Bandari yetu ya Mtwara ina uwezo wa kupokea tani milioni moja. Naomba ule mradi wa kujenga reli kutoka Mtwara Mbambabay sasa uanze kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mradi wa Mchuchuma na Liganga sasa uanze ili bandari hii iweze kutumika ipasavyo. Sasa hivi tunasema Bandari ya Mtwara haitumiki kwa sababu Mradi wa Mchuchuma na Liganga bado hatujautekeleza, lakini tukiutekeleza mradi huu Bandari yetu ya Mtwara itakuwa effective. Kwa hiyo, muda umefika sasa, tutekeleze Mradi wa Mchuchuma na Liganga na pia tujenge reli kutoka Mtwara kwenda Mbambabay. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la maji. Juzi hapa niliuliza swali kuhusu Wizara au Serikali imejipangaje kutumia maji ya Mto Ruvuma kwa ajili ya kutatua changamoto za maji zilizopo katika Mikoa ya Mtwara? Kama tumeweza kuthubutu kutekeleza kutoa maji kutoka Ziwa Victoria mpaka sasa tunafikisha mpaka Nzega, ni matarajio yangu sasa tutaanza kutumia maji ya Mto Ruvuma ili kujenga miradi mikubwa kwa ajili ya Mtwara Mjini, Lindi, Masasi, Tunduru hadi Songea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni muda muafaka sasa wa kuhakikisha kwamba, maji haya ya Mto Ruvuma yanatumika kutatua changamoto za maji iliyopo katika miji yetu ya Kusini ili kuhakikisha tunatekeleza Ilani ya Chama chetu ambayo inasema ifikapo 2025, basi vijijini tuwe tumepeleka maji kwa asilimia 85. Kwa Mkoa wetu wa Mtwara hali bado ni tete kwa sababu tumefikisha asilimia 60 tu. Tutazipata asilimia 25 zilizobaki tukianza kutumia maji ya Mto Ruvuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Wizara ya Maji kwa sababu wameshatuhakikishia kwamba Bajeti ya mwaka huu wataanza kutumia maji ya Mto Ruvuma, kwa ajili ya kutatua changamoto za maji katika Mkoa wa Mtwara na maeneo ya jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa suala la mabadiliko katika Sekta ya Elimu. Kuna mjadala mkubwa unaendelea sasa hivi kuhusu elimu yetu. Naiomba Wizara ya Elimu ikubali hicho kilio cha Watanzania. Kwa kweli elimu yetu sasa hivi inahitaji mabadiliko makubwa. Kuanzia elimu ya awali, msingi, sekondari na vyuo vikuu. Hakuna mtu ambaye anabisha sasa hivi, kwa sababu falsafa yetu ya elimu ni Elimu ya Kujitegemea.

Mheshimiwa Naibu Spika, huko zamani ilikuwa mtoto wa Shule ya Msingi akimaliza anaweza kutumia maarifa yale kuishi katika mazingira yake. Sasa hivi tumebadilisha Elimu yetu ya Msingi inamwandaa mtoto kuingia sekondari. Tumepotoka, tufanye kila kiwango cha elimu kuwa kinajitosheleza. Elimu ya msingi ijitosheleze, Elimu ya Sekondari ijitosheleze na Elimu ya Chuo Kikuu iwe kamili, ijitosheleze. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukifanya hivyo, hakutakuwa na malalamiko kwamba graduates wetu wakifika mitaani, wakifika mahali pa kazi, wanapwaya, hawatakuwa na maarifa ambayo yanasaidia katika kuzalisha katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie hoja iliyopo Mezani. Niungane na wenzangu waliopita kuchangia kuwapongeza viongozi wa Wizara hii tukianza na Waziri wa Elimu, mwalimu wangu, Mheshimiwa Profesa Ndalichako; Naibu wake, Mheshimiwa QS Omari Kipanga; na Katibu Mkuu, kaka yangu, Dkt. Akwilapo; na wasaidizi wake kwa jinsi wanavyochapa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiangalia hotuba hii unajua kabisa imeandaliwa na walimu, ina maelezo machache na takwimu nyingi na inajieleza wazi nini kimefanywa ndani ya mwaka mmoja na miaka mitano iliyopita.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile hotuba hii imekuja na majibu ya kilio cha Watanzania kuhusu sekta ya elimu. Ukisoma ukurasa wa 69 utakuta dhamira ya Wizara kwamba sasa inakusudia kufanya mapitio makubwa, siyo mtaala tu, wataanza kupitia Sera ya Elimu ya Mwaka 2014. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu, tusianze kudai mtaala, tuanze na mabadiliko ya sera. Tukibadilisha sera na vitu vingine vitabadilika. Kwa hiyo, hongereni sana Wizara ya Elimu, mmesema mtabadilisha sera, mnapitia Sera ya Elimu ya 2014 lakini siyo hivyo tu, mtapitia na Sheria yetu ya Elimu, ile Sheria Na. 25 ya Mwaka 1978 pamoja na mabadiliko ambayo yamefanywa. Hapo kwa kweli mnakuja vizuri, kwa sababu lazima tufanye mabadiliko ya jumla na siyo vipande vipande.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muda wa miaka mitano tumeona Wizara hii ikifanya kazi kubwa ya ukarabati katika miundombinu ya shule. Mkoani Mtwara tumeshuhudia, siyo ukarabati wa Chuo cha Elimu Kitangali, ni ujenzi mpya kwa sababu majengo yote yamewekwa chini na tukaanza na ujenzi mpya, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitachangia maeneo matatu. Sehemu ya kwanza, pamoja na mambo mazuri ambayo yamefanywa, nami nitilie mkazo kwenye mabadiliko haya ya mtaala. Ni kweli kwamba sasa hivi kilio kikubwa cha wanajamii ni kwamba wahitimu katika mfumo wetu wa elimu wanashindwa kukidhi haja ya mahitaji ya kule wanakokwenda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sasa hii dhamira ya mabadiliko ya mtaala yafanywe kiukweli kwa sababu hayo ndiyo mahitaji ya sasa. Ukiangalia sababu za kubadilika kwa mitaala, mojawapo ni mahitaji ya kwenye jamii, ambayo ni haya yanayojitokeza sasa hivi. Kwa hiyo, tufanye mabadiliko ya kweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba wakati shughuli hii itakapofanyika basi tuwe na ushirikishaji mkubwa wa makundi yote. Tuanze kuwashirikisha wanajamii, tushirikishe walimu kama watekelezaji wa mtaala, wanafunzi wenyewe washirikishwe, siyo hivyo tu, na taasisi mbalimbali ambazo zinahusika na masuala ya elimu, nao washirikishwe. Hili suala la mabadiliko ya mtaala lisiwe suala la watu wa Wizara ya Elimu tu, iwe ni jamii kwa upana wake na taasisi mbalimbali. Siyo hivyo tu, na wadau mbalimbali ambao wanahusika kwenye sekta ya elimu nao washirikishwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukishabadilisha mtaala, siyo kwamba tumefanikiwa, kuna kazi kubwa sana inabidi ifanyike. Tuna kawaida ya kubadilisha mtaala bila kuangalia tunakwendaje katika kuutekeleza huo mtaala. Kwa hiyo, tukishabadilisha ule mtaala mpya tuandae mazingira ya vyuo vyetu na shule zetu kutekeleza mtaala mpya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwanafunzi au mwanachuo akishaenda kwenye hivyo vyuo vyetu, akute kuna facilities za kutosha kujifunza maarifa mapya ambayo yapo kwenye mtaala mpya. Tukiacha hata shule au taasisi zetu kama ilivyo, tutakuwa na mtaala mpya ambao utashindwa kutekelezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile tunahitaji maandalizi makubwa ya walimu na wakufunzi wetu ili waweze kutekeleza mtaala mpya, kwa sababu hawa ndio watakaokwenda kuutekeleza mtaala. Wasipoandaliwa, kuna kawaida ya kufanya mabadiliko ya mtaala tukaishia kwenye watu wa Wizara au kazi ya kanda tu, tufike mpaka kwa mwalimu wa darasa naye ashirikishwe aweze kutekeleza mtaala mpya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie mchango wangu wa pili kuhusu muundo mpya wa Wizara ya Elimu, hususan nafasi ya Kamishna wa Elimu. Ukisoma Sera ya Elimu na Sheria ya Elimu, Kamishna wa Elimu ana majukumu mazito sana, lakini kwa muundo wa Wizara ya Elimu uliopo, kamishna unampa kusimamia maeneo mawili tu; Elimu ya Msingi kwa maana ya primary na secondary na elimu maalum. Kamishna wa Elimu hagusi elimu ya juu na elimu ya ufundi. Hapa kuna changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamishna wa Ardhi anasimamia ardhi yote, hasimamii ardhi ya mjini tu na kuacha vijijini; na Kamishna wa Kodi anasimamia kodi zote. Kwa nini Kamishna wa Elimu, asimamie elimu ya msingi tu na elimu maalum; elimu ya vyuo vikuu hashughulikii na elimu ya ufundi hashughulikii? Tumpe mamlaka Kamishna wetu wa Elimu. Kama hoja ni sifa, kitu ambacho sioni kama ni sifa, kwa sababu Kamishna wa sasa wa Elimu ni Doctor, ana sifa na ninamfahamu, ni mcha Mungu, ni mwadilifu na mchapa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ili kamishna wetu awe na majukumu kama yanavyotajwa kwenye Sera ya Elimu na Sheria ya Elimu, asimamie sekta zote; ahusike kwenye elimu ya msingi, elimu ya sekondari, elimu ya juu na elimu ya ufundi. Haiwezekani kama mtaaluma mkuu akajifunga katika maeneo machache tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Wizara ya Elimu na Wizara ya Utumishi mlishughulikie hili, turudishe muundo wa zamani ambapo Kamishna wa Elimu, kwa tafsiri nyingine Chief Education Officer basi awe Msimamizi Mkuu wa Sekta ya Elimu na siyo ilivyo sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie hoja iliyopo mezani kwetu. Niungane na wenzangu kuwapongeza viongozi wa Wizara hii tukianza na Mheshimiwa Waziri Aweso na Naibu wake kwa kweli mnafanya kazi na mna kipaji cha kipekee cha kusikiliza watu na hiyo ndiyo sifa kubwa ambayo mnayo. Mnatenga muda kusikiliza watu badala ya ninyi kusema ili watu wawasikilize. Kwa hiyo, endeleeni na moyo kama huo ili mpate kushauriwa na ninyi muweza kuyatekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile, nimpongeze Katibu Mkuu, Engineer Sanga lakini kipekee nimpongeze Mtendaji Mkuu wa RUWASA, Engineer Kivegalo. Ni watendaji wachache sana ambao wakifanya ziara wanatenga muda wa kukutana na wanasiasa. Engineer Kivegalo alivyofanya ziara Mkoani Mtwara alitenga muda wa kukutana na Wabunge wote wa Mkoa wa Mtwara. Watendaji wengi wana kawaida ya kusema wanasiasa wana nini hao lakini huyu alitembelea miradi, akawasiliza watendaji, jioni akatenga muda kwamba nimewasikiliza watendaji sasa nataka niwasikilize ninyi wawakilishi wa wananchi. Hongera sana Engineer na endelea na tabia kama hiyo utafanikiwa, naona future yako ni kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niungane na Wabunge wenzangu wa Mtwara waliochangia kuhusu suala la maji Mkoani Mtwara. Kwa kweli suala la maji Mkoani Mtwara ni tete na hata kikao cha Kamati ya Ushauri cha Mkoa kilichopita agenda ya maji iliwekwa pembeni kwamba tuwe na kikao maalum kwa ajili ya kuzungumzia maji Mkoa wa Mtwara. Mheshimiwa Aweso nakupongeza kwa sababu tulivyofika hapa tulikutana, tukafanya kikao cha Wabunge wa Mtwara ukatusikiliza na wewe umeanza kuyafanyia kazi. Ndio maana nikakwambia kwamba una sifa ya kusikiliza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maombi yetu makubwa yalikuwa mawili na nikushukuru kwa yote umeshayafanyia kazi. Cha kwanza, tulikwambia kwamba Mradi wa Maji wa Makonde ambao kwa bahati mbaya uliondolewa kwenye Mradi wa Vijiji 28 umeurudisha tena kwenye orodha ile, tunakupongeza sana. Mradi wa Makonde unahudumia karibu asilimia 40 ya Mkoa wa Mtwara, unahudumia halmashauri nne, Newala Mjini, Newala Vijijini, Tandahimba na Nanyamba. Kwa hiyo, mradi huu ukitekelezwa ipasavyo tutakuwa tumepunguza tatizo la maji katika Mkoa wetu wa Mtwara. Nikuombe usikilize ushauri wetu kwamba mradi wa maji wa Makonde chanzo kikubwa cha Mitema kuna maji mengi sana. Kwa hiyo, tutumie chanzo cha Mitema kupeleka maji Tandahimba na Nanyamba mtakuwa mmetatua changamoto ya maji kwa kiasi kikubwa katika Mkoa wetu wa Mtwara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi letu la pili kwenye kikao kile tulikwambia muda umefika sasa tutumie maji ya Mto Ruvuma. Mimi Jimbo langu la Nanyamba, Mheshimiwa Katani amesema kwake ni kilometa nane tu mimi ni zero distance, kwa sababu wananchi wangu wakati ule walikuwa wanalala Tanzania wanafanya kazi Msumbiji wanavuka kwa miguu Mto Ruvuma, kabla ya matatizo yale ya Msumbiji hayajaanza.

Mheshimiwa Spika, kile chanzo cha maji cha mradi wa kupelekeza maji Manispaa ya Mtwara kipo Nanyamba na maji yapo ya kutosha. Nimeona hapa tumetenga fedha kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu kuyatoa maji Maembe Chini kwenda Nanyamba kama nilivyoshauri siku ile. Hongera sana uendelee kusikiliza hivyo, mradi huu unagusa vijiji 74 na Kata zaidi ya 13 ambazo ni za Nanyamba, Mtwara Vijijini na inawezekana mradi huu ukavuka ukaingia Jimbo la Mtama kwa sababu tumepakana. Kwa hiyo, mradi huo ukitekelezwa utatatua changamoto nyingi sana si za Nanyamba tu na maeneo mengi ya jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama walivyosema wenzangu kwamba muda umefika sasa kuanza utekelezaji wa mradi huu wa kutoa maji Mto Ruvuma na kupeleka Mtwara Manispaa. Nimeona shilingi bilioni sita zimetengwa maana siku za nyuma ilikuwa mradi huu unazungumzia tutatoa fidia, tutafanya upembuzi yakinifu lakini leo nikupongeze Waziri kwamba umeanza kuweka fedha. Naomba wakati wa utoaji wa fedha basi hizi fedha zitolewe ili mradi huu mkubwa uanze kutekelezwa na Manispaa ya Mtwara tuwe na maji ya uhakika kiasi kwamba hata wawekezaji wakija wajue wanawekeza Mtwara ambayo ina maji na umeme wa uhakika ambao sasa hivi upo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Mji wa Nanyamba imesajiliwa kama Halmashauri ya Mji na kwa Sheria ya Maji tuna uwezo wa kuwa na mamlaka yetu. Sasa hivi tunahudumiwa na Mamlaka ya Maji ya Mtwara (MTUWASA) katika kipindi hiki cha mpito.

Kwa hiyo, naomba na hili sasa Mheshimiwa Waziri alifanyie kazi, sisi tuna hadhi ya kuwa na mamlaka ya kwetu na hakuna sababu ya kuitumia ile Mamlaka ya MTUWASA. Ni muda umefika sasa kufanya taratibu zinazotakiwa ili na sisi tuwe na Mamlaka ya Maji ya Mji wa Nanyamba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu wa mwisho ni kuhusu RUWASA. RUWASA ni mtoto mchanga anafanya kazi vizuri lakini kama walivyosema Wabunge wengine ana changamoto hebu tuiwezeshe RUWASA. Tuiwezeshe kwa vitendea kazi na rasilimali watu. Wilaya nyingine zina halmashauri zaidi ya moja, kwa mfano mimi Meneja wangu wa RUWASA anashughulikia Mtwara Vijijini na Nanyamba, lakini ana watendaji wachache. Naomba tuongeze watumishi ili mamlaka hii ambayo imeanza kufanya kazi vizuri iendelee kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na ahsante kwa kunisikiliza. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia mjadala huu ambao upo mbele yetu.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuwapongeza viongozi wa Wizara hii, Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu wa Wizara hii, Wakurugenzi wa Mashirika pamoja na Watendaji Wakuu wa Mashirika yaliyo chini ya Wizara hii. Kwa kweli mmeandaa hotuba safi ambayo inaanza kujibu baadhi ya changamoto ambazo zipo kwenye sekta yetu ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuchangia kuhusiana na sekta ya korosho. Korosho ni zao pekee ambalo kwa sasa tuna-export levy na export levy ipo Tanzania mpaka Ivory Coast wazalishaji wakubwa wa korosho duniani. Wenzetu wanatumia export levy siyo kama chanjo cha mapato kwanza ni katika kuhamasisha ubanguaji wa ndani na kutoa vivutio kwa wale wanaobangua korosho. Vilevile policy hii inatumika hadi Msumbiji kwamba wale ambao wanabangua korosho ndani wanapewa vivutio.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano Ivory Coast wanatumia kama senti sitini kwa kila mzalishaji wa ndani anayebangua korosho, uki-convert kwa fedha yetu ni kama ni Sh.1,500. Fedha hii inasaidia watu wengi kujiingiza kwenye sekta ya ubanguaji na hivyo viwanda vya ndani vinafanya kazi na hivyo kutoa ajira nyingi. Kwa hiyo, sisi tuliweka export levy na tukafanya hivyohivyo tukapeleka asilimia 65 ya export levy kwenye Mfuko wa Kuendeleza zao la Korosho. Sitaki nikukumbushe kilichotokea maana unajua kabisa kwenye Sheria ya Fedha, 2018 tulitoa ile asilimia 65 ambayo ilikuwa inaenda kwenye Mfuko kuendeleza zao la korosho tukapeleka kwenye mfuko mkuu na tangu hapo sekta ya korosho ikaachwa bila kuwa na ugharamiaji mkubwa.

Mheshimiwa Spika, sekta ya korosho inahitaji fedha nyingi sana na sasa hivi tunahesabu mikoa 17 ambayo inalima korosho, kwa hiyo lazima tuwe na mpango wa kugharamia sekta hii ya korosho. Niungane na wenzangu ambao wanasema kwamba kwanza export levy itumike katika kuendeleza sekta ya korosho, tutoe motisha kwa wabanguaji wa wetu ndani.

Mheshimiwa Spika, niliuliza swali wiki iliyopita tunawapa motisha ipi wabanguaji wa ndani? Kwenye minada ya awali wakulima hawapeleki korosho kwa sababu bei ni ya chini, tukiwapa motisha kwa kutumia fedha hizi wanunuzi au wakulima watakubali kupeleka korosho kwenye minada ya awali na viwanda vyetu vitapata korosho za kutosha na hivyo kutoa ajira kwa wanawake na vijana wengi.

Mheshimiwa Spika, lakini si hivyo tu na mimi nichangie kwenye hoja ya pembejeo za msimu wa mwaka huu. Kwanza nianze kuipongeza Wizara kwa kazi kubwa ambayo wameifanya kwanza kuja na mfumo wa kuagiza pembejeo nyingi kwa wakati mmoja. Tunavyoongea sasa hivi kuna tani 21,000 za sulphur zimeshaigia nchini, hili ni ongezeko kubwa sana lakini tuna viuatilifu vya maji kama lita 1,300,000 hatujawahi kuagiza sulphur na viuatilifu vya maji kwa kiasi kikubwa kama hiki. Kwa hiyo, naipongeza Wizara kwa hatua hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, changamoto iliyopo ni ugharamiaji, tunagharamiaje pembejeo hizi. Naungana na wenzangu kusema kwamba lile wazo la kumtaka kila atakayeuza korosho gulioni Sh.110, hizo ni fedha nyingi sana kwa sababu mkulima huyu tayari ameshakatwa Sh.50 kwa ajili ya Naliendele na Bodi ya Korosho, ameshakatwa fedha za export levy kwa sababu ile export levy mnunuzi anapokuja kwetu anapunguza bei ili aweze kulipa export levy, kwa hiyo, ile export levy anaibeba mkulima, sasa tukimchangisha tena Sh.110 anakuwa na mzigo mkubwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niungane na wenzangu waliokwishachangia kusema kwamba zitafutwe hizi shilingi bilioni 55 mpaka 60 tupeleke ili sulphur hiyo igawanywe kwa wakulima. Utafiti umeonesha wazi kwamba mwaka ambao sulphur na viuatilifu vya maji vimegawanywa kwa wingi na uzalishaji unaongezeka. Mwaka 2017/2018 ambapo tulifikisha tani 520,000 ndiyo mwaka ambao tuligawa bure sulphur kwa wakulima. Kwa hiyo, tukitoa sulphur hii tutafikisha lengo letu la kufikisha tani 280,000, tusipofanya hivyo basi uzalishaji utaendelea kuporomoka kama unavyoporomoka kila mwaka.

Mheshimiwa Spika, vilevile nichangie kuhusu Bodi yetu ya Korosho. Kama nilivyosema kwamba fedha za export levy zipelekwe kwenye uendelezaji wa zao la korosho, kwa hiyo Mfuko wa Kuendeleza zao la Korosho lazima urejeshwe ili kuhakikisha fedha hizi zinatumika ipasavyo. Pia ili fedha hizi zitumike vizuri kwenye Mfuko lazima uwe na Bodi imara, kilichopo sasa hivi kwenye sekta ya korosho ni kizungumkuti kwa sababu Bodi haijaundwa kwa miaka mitatu sasa, lakini hata Mtendaji aliyeko ni Kaimu na ile Bodi ni dudu lizito lazima tupate Mtendaji ambaye yuko imara na muda wote atakuwa anashughulikia korosho na pengine hata mzigo uliopo Wizarani utapungua kwa sababu mambo mengine watafanya kwenye ngazi ya Bodi ya Korosho.

Mheshimiwa Spika, Mfuko ule ulikuwa muhimu sana kwa sababu ulitoa fedha kwenye utafiti, wagani katika halmashauri yetu lakini kwa ajili ya usimamizi kwenye halmashauri, uligharamia ubanguaji mpaka usambazaji wa miche. Ile miche ambayo imefika Kongwa na Manyoni ni kwa sababu ya Mfuko huu lakini tukaridhika mapema kwamba korosho ina fedha za kutosha tukaziondoa zile fedha. Zile fedha tungeziacha kulekule sasa hivi tungekuwa tunahesabu tumeshazalisha tani 500,000 lakini tukazinyofoa mapema kabla ya muda wake. Turejeshe ule Mfuko ili hata mikoa mingine ambayo inalima korosho sasa hivi inufaike na sekta hii, tusipofanya hivyo itakuwa maumivu.

Mheshimiwa Spika, nichangie kuhusu ushirika. Watu wengi waliochangia kuhusu ushirika siyo kwenye korosho tu, kwenye pamba, mahindi mpaka maparachichi watu wanalalamika, kuna changamoto kwenye ushirika. Mwaka jana nilichangia hivi hivi kwamba hebu tuangalie kilichoko kwenye ushirika tatizo ni nini? Ni Sheria ya Ushirika, Tume au Ofisi ya Mrajisi wa Ushirika? Litafutwa tatizo liko wapi? Sasa hivi Wizara inataka kufanya marekebisho ya sheria, inawezekana hata tukibadilisha sheria matatizo yatabaki vilevile. Tuangalie mfumo wa uendeshaji wa ushirika, mfumo wa kitaasisi wa ushirika na uwezeshaji wa ushirika, kuna changamoto kule. Haiwezekani Sheria ya Ushirika inasema kwamba mtendaji kwenye AMCOS kiwango chake cha elimu kisipungue kidato cha nne lakini anachukuliwa mtu ambaye hana kiwango hicho, Afisa Ushirika na Mrajisi wapo, hakuna hatua inayochukuliwa, fedha zikipotea tunaanza kulalamika. Kwa hiyo, ushirika uchunguzwe na yafanyike mabadiliko makubwa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Viwanda Na Bishara
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niungane na wenzangu kwa kukupongeza kuteuliwa tena kuwa mwenyekiti na hatuna mashaka na wewe, tunaomba Mwenyezi Mungu akupe afya njema na hekima ili uendelee ku-chair katika kiti chako hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia nimpongeza Mheshimiwa Waziri Profesa Kitila Mkumbo kwa kazi nzuri anayoifanya pamoja na Naibu wake, lakini pia na watendaji wa Wizara wakiongozwa na Katibu Mkuu Dotto James pamoja na Wakurugenzi wa taasisi mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mchango wangu utaanza na kujikita na jinsi tunavyoshughulikia matatizo ya wawekezaji na kipekee nichukue nafasi hii kukushukuru na kukupongeza Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo jinsi ulivyoshughulikia mgogoro wa kiwanda cha Dangote, hongera sana. Umechukua hatua za haraka, umefika site, ndugu zangu Dangote ni taasisi kubwa, isingefaa kwa kipindi kirefu iendelee kuachwa vilevile mgogoro unaendelea wakati Dangote ni taasisi kubwa, wakati mgogoro ule unaendelea hapa Tanzania, delegation ya Benki ya Dunia ilitoka Washington kwenda kuonana na Dangote kule Nigeria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwetu huku tuone jinsi ukubwa wa taasisi ya Dangote. Kwa hiyo anapopatwa na tatizo naomba tulikimbilie kama ulivyofanya Mheshimiwa Waziri na uendelee kusikiliza matatizo ya kiwanda kile, kwa sababu kiwanda kile kuna ajira rasmi kwa Watanzania zaidi ya 500. Lakini kuna ajira zisizo rasmi zaidi ya 2,000, lakini kuna fleet ya magari pale zaidi ya 1,000. Sasa fanya lori moja lina wafanyakazi wawili ina maana kuna ajira 2,000 pale zipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini si hivyo tu, kwamba kwa sisi Wana Mtwara kuna vijana wetu wengi, kuna akina mama, wanapata ajira pale na wanapata mkate wao wa kila siku kutoka katika kiwanda cha Dangote. Mheshimiwa Waziri, pale bado kiwandani kuna changamoto nyingi na naomba utenge muda mkawasikilize. Mimi nitazitaja chache tu, changamoto ya kwanza ni bei ambayo TPDC wanaiuzia Dangote ile gesi asilia. Lakini vilevile kuna changamoto ya meli kwa sababu wana mpango wa kusafirisha saruji sasa kwa kutumia Bandari yetu ya Mtwara, kwa hiyo, tuwasikilize kwa hilo, lakini kuna gharama za bandarini nazo tuziangalie vilevile ni kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Tume ya Madini sasa hivi imekuja na hoja nyingine kwamba wana-categorize Kiwanda cha Dangote kama mining company na kutaka kodi nyingi walipe. Kwa hiyo, nalo Mheshimiwa Waziri ukalifanyie kazi. (Makofi)

Suala la pili, ni kuhusu soko la korosho, Mheshimiwa Waziri naipongeza Serikali kwa jinsi inavyochukulia kwa unyeti suala la korosho, lakini naomba iongeze nguvu zaidi. Itafute masoko mapya ya korosho. Tusiende na India kila mwaka, twende na masoko mapya na yapo mengi Vietnam, Japan na maeneo mengine.

Kwa hiyo, naomba sana kwamba tutumie taasisi yetu ya TMX ili kuhakikisha tunawapata wanunuzi wapya wa korosho, lakini vilevile tuhakikishe sasa kwamba korosho ambazo zinatoka mipakani kwa mfano kule kwetu mpaka wa Msumbuji Jimbo la Cabo Delgado wanaleta korosho zao Tanzania. Lakini mwaka juzi ilitokea sintofahamu tukazuia korosho zile zisiiingie kwamba ni chafu. Korosho za Jimbo la Cabo Delgado zina ubora kama korosho za Mtwara. Kama kahawa yetu inaingia Uganda kwa nini tusiruhusu korosho za Msumbiji ziingie kwetu.

Kwa hiyo, naomba zile korosho za Msumbiji ziingie ili ziongeze uzalishaji wetu kwa sababu Kaskazini mwa Msumbuji yanayoendelea mnayafahamu na wenzetu kule hakuna soko rasmi kama lilivyo sisi la korosho kwetu. Mheshimiwa Waziri ruhusu korosho kutoka Msumbiji ziingie nchini bila ya kuwa na vikwazo vyovyote kwa sababu wafanya biashara wetu wadogo wanafanya biashara hiyo lakini wakulima wa Msumbiji wanaingiza korosho kusiwe na vikwazo ambavyo sivyo vya lazima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili, niungane na wenzangu kuzungumzia Mradi wa Mchuchuma na Liganga. Ni mradi wa muda mrefu, basi sasa hivi utekelezwe na ukitekelezwa mradi huu tunatimiza ile dhana ya Mtwara corridor. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Chikota.

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie hoja iliyoko Mezani. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa uamuzi wake wa dhati wa kuongeza Bajeti ya Kilimo kutoka Shilingi bilioni 294 mpaka Shilingi bilioni 751. Haya ni mapinduzi makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee niwapongeze viongozi wa Wizara hii; Mheshimiwa Bashe na Mheshimiwa Mavunde pamoja na Katibu Mkuu na timu yake kwa kazi nzuri ambayo wanaendelea kuifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu unajikita kwenye zao la korosho na nianze na soko la korosho na bei ya korosho. Naomba Wizara iimarishe Kitengo cha Masoko katika Wizara hii lakini pili, na Bodi ya Korosho ili korosho yetu ipate bei nzuri sokoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachoendelea sasa hivi kwenye Mnada wa Korosho, tunapata bei nzuri kwenye mnada wa kwanza na minada yote inayofuata korosho bei inashuka. Hatujui kushuka huku ni kwa kupanga au ni kwa sababu soko limeshuka. Tukiwa na taarifa za kutosha kwenye soko, basi itasaidia kupata taarifa za uhakika na kuimarisha bei yetu ya korosho na kudhibiti uuzaji wa korosho katika minada.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu ya pili ni kuhusu ubanguaji wa zao la korosho. Tuna mkakati wa kubangua zao la korosho. Tulikuwa na viwanda vyetu 12 hapo nyuma mpaka sasa hivi havifanyi kazi na vingine vimegeuzwa kuwa magodauni. Mheshimiwa Bashe wewe ni bingwa wa kuthubutu, chukua angalau viwanda vitatu vianze kubangua korosho na hilo unaliweza ili tuanze kubangua korosho badala ya kupeleka korosho ghafi huko nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la tatu ni kuhusu pembejeo. Naipongeza sana Wizara kwa kutoa pembejeo bure kwa wakulima na nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa mwaka wa pili kutoa pembejeo bure kwa wakulima wa korosho. Naomba udhibiti ufanywe ili pembejeo hizi zifike kwa wakulima husika na siyo mikononi mwa walanguzi. Pili, pembejeo hizi sasa wasambazaji watoe mafunzo kwa wakulima kama ilivyofanya Kampuni moja ya BEZ naipongesa sana. Imetoa mafunzo kwa wakulima ili kupunguza dosari za utumiaji wa dawa hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala langu lingine ni kuhusu Export Levy. Mheshimiwa Waziri utakuja na Muswada hapo wa Export Levy ili fedha isiwe chanzo cha mapato kwa Serikali. Export Levy irudi kwa mkulima ili iongeze uzalishaji, ili tufufue viwanda vyetu vya korosho, ili iimarishe utafiti, ili ile fedha ambayo anachangia mkulima sasa hivi Shilingi 25/= kwa ajili ya TARI Naliendele asikatwe mkulima, ichukuliwe kwenye Export Levy. Export Levy itasaidia kutoa uhamasishaji kwa wabanguaji wa korosho. Kwa hiyo, naomba kwenye Muswada wa Fedha ujao, basi utuletee ili Export Levy irudi na asilimia 65 iende kwenye zao la korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja iliyopo mezani kwetu. Nianze kwa kuunga hoja mkono, lakini nitajikita katika maeneo matatu. Eneo la kwanza ni lile ambalo ameishia dada yangu Mheshimiwa Husna, ni kuhusu upungufu wa watumishi katika sekta hizi mbili ambazo Kamati yetu inahusika, idara ya elimu na idara ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna upungufu mkubwa sana wa watumishi katika kada hizi mbili. Waheshimiwa Wabunge humu wakitaka watoe takwimu wataonesha wazi kwamba, kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa au kwenye Majimbo kuna changamoto kubwa ya upungufu wa idadi ya Walimu na watumishi katika sekta ya afya. Kazi kubwa ambayo imefanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan na ujenzi wa madarasa zaidi ya 15,000 na hostels 50 na vituo vya afya impact yake haitaonekena vizuri sana upungufu huu ukiendelea. Kwa hiyo, naomba Serikali sasa ichukue hatua za makusudi kuhakikisha kwamba, kibali maalum kinatolewa kwa ajili ya ajira ya Walimu na ajira ya watumishi wa sekta ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nyuma kulikuwa na upungufu wa Wahasibu katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Serikali ikafumba macho ikatoa ajira ya Wahasibu watano kila halmashauri. Naiomba Serikali yangu sikivu ifanye hivyo, itoe kibali maalum kwa ajili ya watumishi wa sekta ya afya na watumishi wa sekta ya elimu

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye taarifa yetu tumezungumzia vilevile kuhusu Chuo Cha Ualimu Mtwara. Wakati tunatekeleza Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari mwaka 2005 hadi 2009 kulikuwa na mapendekezo, ili kuongeza idadi ya Walimu wa sayansi vyuo vitatu vibadilishwe kuwa vyuo vikuu vishiriki; Chuo Cha Ualimu Mtwara, Chuo Cha Ualimu Dar-es-Salaam na Chuo Cha Ualimu Mkwawa. Vyuo viwili hivi vimeshabadilishwa kuwa vyuo vikuu vishiriki, Chuo Cha Ualimu Dar es Salaam ni DUCE sasa hivi na Chuo Cha Mkwawa kimeshabadilishwa kuwa MUSE, ni chuo kikuu kishiriki cha Mkwawa, bado Chuo Cha Ualimu Mtwara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Ualimu Mtwara kina facilities zote; kuna eneo la kutosha kwa ajili ya upanuzi, kuna bwalo la kutosha, madarasa ya kutosha na majengo ya utawala na vyumba vya mihadhara vya kuanzia vipo tayari. Kwa hiyo, naomba Serikali itekeleze ile azma yake ya kukibadilisha Chuo cha ualimu Mtwara kuwa Chuo Kikuu Kishiriki cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Facilities zote kama nilivyosema zipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye elimu kuna kitu kinaitwa skill over effect; tukijenga Chuo Kikuu Kishiriki Mtwara Wana-Mtwara wengi watahamasika kusoma kutoma elimu ya Chuo Kikuu kwa sababu wataona Chuo Kikuu kipo jirani yao. Kwa hiyo, naomba azma hiyo itekelezwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine, wakati tunafanya mahojiano na Wizara hizi mbili za kisekta; elimu na afya, kuna kuingiliana kwa majukumu kati ya TAMISEMI na Wizara za kisekta; elimu na afya. Hata juzi tulifanya kikao cha kuwakutanisha TAMISEMI na Wizara ya Elimu. Hata kama tunafahamu kwamba kuna collective responsibility, siyo vizuri mtumishi au mtumishi wa Wizara fulani kusema Wizara fulani inamwingilia, lakini ukienda kwenye utekelezaji, tunaona kuna changamoto ya kuingiliana, yaani Wizara za kisekta na TAMISEMI wanaingiliana. Hili liko wazi tu kwamba ile (D by D) ugatuaji bado haujaeleweka vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watumishi wa Serikali bado dhana ya ugatuaji hawajaielewa, lakini mpaka kuna baadhi ya viongozi vile vile dhana ya ugatuaji bado haijaeleweka. Udhaifu mwingine ni kwamba hakuna sheria ambayo inalinda ugatuaji. Ugatuaji unaongozwa na policy paper ya mwaka 1998. Kwa hiyo, naomba vitu viwili kama tulivyoshauri kwenye kamati yetu; kwanza, elimu ya ugatuaji itolewe kwa watendaji na viongozi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, muda sasa umefika wa kuhakikisha kwamba Serikali inaleta sheria ya kusimamia huu ugatuaji ili kusiwe na kuingiliana kati ya Wizara na TAMISEMI. Tukifanya hivyo, tutarahisisha utekelezaji wa majukumu katika ngazi ya chini. Huko chini kuna kuingiliana sana kati ya TAMISEMI na Wizara nyingine za kisekta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)

MWENYEKITI: Umeunga mkono hoja Mheshimiwa?

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilishaunga mkono hoja mwanzoni. Kwa hiyo naunga mkono hoja kwa mara ya pili sasa hivi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja iliyopo mezani kwetu na mimi niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya maana ndiye Waziri ambaye ana dhamana ya Wizara hii kwa sababu ni Ofisi ya Rais – TAMISEMI, niwapongeze Mheshimiwa Bashungwa na timu yake Naibu Mawaziri wote, Katibu Mkuu na Naibu Makatibu Wakuu na watendaji wote wa TAMISEMI kwa kazi nzuri wanayoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu utaanzia pale alipoishia Mheshimiwa Jerry Silaa, Meya Mstaafu wa Ilala yeye amezungumzia kwenye ngazi za vijiji na Mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa ngazi ya Halmashauri. Mimi nitazungumzia kwenye Sekretarieti ya Mkoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma Sheria ya Tawala za Mikoa Sura Namba 97 lakini na policy paper ya ugatuaji ile decentralization ya mwaka 1998 utakuta majukumu ya Region Secretariat ni pamoja na kuzishauri Mamlaka za Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile kuzisimamia mamlaka za Serikali za mitaa na kutengeneza mazingira wezeshi ili Mamlaka ya Serikali za Mitaa ziweze kutimiza wajibu wake, tulitegemea kwenye Region Secretariat kuwa na maafisa waandamizi na wabobezi ili wakienda kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa wakashauri, lakini changamoto iliyopo sasa hivi Sekretarieti za Mikoa hazina wataalam hao, unakuta mtaalam anayekwenda kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa kushauri ni junior kuliko aliyeko kwenye Halmashauri, kwa hiyo hata ushauri wake hauwezi kusikilizwa na hata cha kushauri hana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, muda umefika sasa na Mheshimiwa Bashungwa tuna matarajio makubwa sana na wewe, hebu tufanye mapitio ya Sheria yetu hii ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1997, lakini tufanye re-structuring kwenye RS je, muundo wa sasa wa RS unakidhi mahitaji ya sasa kusimamia Mamlaka za Serikali za Mitaa? Tumeona hapa juzi Mheshimiwa Aweso ameenda mahali fulani anauliza nionesheni bwana la shilingi milioni 600 na watu wa Mkoa wapo na wao wanashangaa kama tungekuwa na strong RS yale yasingetokea Mawaziri msingekimbia kimbia kungekuwa na kazi kubwa zinafanywa na Sekretarieti ya Mkoa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba tufanya mabadiliko, naomba tuziwezeshe tuwe na wataalam mahiri natuwape rasilimali fedha ili ziweze kutekeleza majukumu yake na Mawaziri mtatulia kufanya maamuzi ya kimsingi na sio kwenda kukagua vitu ambavyo Sekretarieti ya Mkoa wangeweza kutekeleza mambo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu wa pili, unahusu miradi ya kimkakati; nakupongeza Waziri umesema kwamba umeunda timu ya kuzishauri na kuziwezesha Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuandika maandiko ya miradi, lakini Mheshimiwa Waziri nikuombe tu kwamba kuna changamoto ya kuchelewesha maandiko katika ofisi yako, maandiko yamekaa muda mrefu sana na kule kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuna wataalam wa kuandika hayo maandiko, wachumi miongoni mwa course ambazo wanazofanya vyuo vikuu ni project writeup, sasa nashangaa kwamba wachumi hawa wame-graduate vyuoni lakini hawawezi kuandika andiko la mradi tu kujenga ghala kwenye Mamlaka ya Serikali ya Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, muharakishe kupitia hayo maandiko ili fedha zitolewe umesema hapa mwaka jana fedha zilizotumika ni asilimia 32 tu ya fedha zilizotolewa, ina maana kwamba maandiko hayapitishwi kwa wakati, na maandiko mengine Mheshimiwa Waziri yanahitaji maamuzi ya muda mchache tu, nikupe mfano kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa Mkoa wa Lindi na Mtwana tunapolima korosho wengi wameomba kujenga maghala ya kuhifadhi korosho, mamlaka hizi zingepewa fedha wangeweza ku-back even kurejesha hivi fedha kwa muda mfupi sana kwa sababu kwa sasa hivi kwa mjengepo wa bei kilo moja ya korosho zinapoingia ghalani inalipwa shilingi 38. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri za Mkoa wa Mtwara mwaka huu zimezalisha tani 178 kwa bei hii kuna ina maana kuna takribani shilingi bilioni tano ingepatikana hawa hata wakiruhusiwa kwenda kukopa kwenye mabenki ya kibiashara uwezekano wa kuridisha ni mkubwa sana kwa kipindi kifupi, hivi andiko kama hili linakaa miaka mitatu linasubiri nini, na ni fedha ipo wazi kwa sababu kila msimu wa korosho yanahitajika maghala kila msimu wa korosho wapo wanunuzi wanakuja wanahitaji haya maghala kila msimu wa korosho kunahitajika maghala ya kuweka pembejeo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye stakabadhi ghalani kunahitajika maghala, sasa maandiko kama hayo yanakaa miaka mitatu yanasubiri nini? Mheshimiwa Waziri ebu fast track vitu kama hivyo tupunguze Mamlaka ya Serikali za Mitaa kutegemea utegemezi kutoka Serikali Kuu. Hapa tungeruhusu Halmashauri hizi kujenga maghala takribani kila Halmashauri ingekuwa na uhakika kupata shilingi 500,000,000 kila mwaka, sasa hii ingesaidia kufanya vitu vingi sana. Hebu naomba Mheshimiwa Bashungwa fanya maamuzi watu wajenge maghala na fedha hizi ziweze kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ninalotaka kuchangia ni kuhusu mradi wa TACTIC; huu mradi nampongeza Waziri kwamba mmeongeza kasi ya mazungumzo ili uanze kutekelezwa na mimi kipekee nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuingiza Halmashauri ya Mji wa Nanyamba katika mradi huu, tupo kwenye miji 45 na tunausubiri sana kwa hamu. Mheshimiwa Waziri nikuombe kwamba tusifanya makosa yaliyopita huko nyuma miradi hii tujenge kulingana na mahitaji ya sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Rais ameelekeza kwamba masoko yafuate watu na sio watu wafuate masoko. Tuna miradi mingi pale Mtwara Mjini kwa kaka yangu Mheshimiwa Mtenga limejengwa soko pale Chuno la fedha nyingi, lakini kukawa na mgogoro kati ya wafanyabiashara kwenda kuhamia kwenye lile soko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye maeneo mapya tusiruhusu vitu kama hivyo nafahamu huu mradi unachangamoto ya fidia ni bora tutafute fedha mahali tufidie kwenye masoko yaliyopo sasa hivi tujenge ili tuboreshe hapo ili kusiwe na kujenga miradi ambayo haina manufaa. Tukijenga masoko ambapo watu wapo tuna uhakika wa kurudisha hizi fedha. Kwa hiyo pamoja na kuona kwamba kuna miradi hii wafadhili haina fidia basi Mheshimiwa Waziri tafuta chanzo kingine ili tulipe fidia, tujenga miradi maeneo ambayo kuna watu na hasa mradi wa soko na mradi wa vituo vya mabasi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichangie suala la uhaba wa walimu; kama walivyosema wenzangu kuna changamoto kubwa ya upungufu wa walimu na hapa Mheshimiwa Waziri nimeona umekokotoa upungufu kwa kutumia ratio ya mwalimu mmoja wanafunzi 60 sijui kama ratio hii imebadilika siku hizi lakini mimi ninavyofahamu ratio ili mwalimu aweze kufundisha vizuri kwa kiwango chetu tulijiwekea kwamba darasa la class size darasa moja watoto 45 na mwalimu hivyo hivyo ahudumie watoto 40, hilo darasa la watoto 60 ni wengi sana darasa la wanafunzi 60 halifundishiki. (Makofi)

Kwa hiyo tumeona hapa kwenye takwimu kwamba tunaupungufu mdogo lakini kwa sababu tumetumia ratio kubwa tukirudi kwenye ratio yetu ya zamani kuna uhaba mkubwa wa walimu hili halikwepeki lazima tutoe kibali maalum kwa walimu ili waboreshe elimu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja na ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie hoja iliyopo mezani. Nami nianze kwa kumpongeza dada yangu Mheshimiwa Ummy Mwalimu kwa kazi nzuri anayoifanya; pili, kwa Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Mollel kwa kazi nzuri ambayo anaifanya. Mawaziri hao kwa kweli ni wasikivu na ni miongoni mwa Mawaziri ambao wanapokea simu hadi saa 8:00 za usiku, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee nampongeza Katibu Mkuu wa Wizara hii, Mheshimiwa Prof. Makubi, Naibu Katibu Mkuu Dkt. Shekilage na Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Sichwale. Watendaji hawa wanafanya kazi vizuri na tunaona muda mwingi wanahangaika kutatua kero katika sekta yetu ya afya. Hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika mjadala wa leo, watu wengi wanachangia sana kwenye suala la dawa na utumishi kwa sababu ndiyo maeneo makuu ambayo yatasaidia kuboresha sekta yetu ya afya. Nami nitatumia muda huu kujikita kuhusu suala la upatikanaji wa dawa.

Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeze Waziri, kwenye kitabu chake ukurasa wa 44 amekuja na takwimu za uhalisia. Huko nyuma tulikuwa tunapewa takwimu ambazo siyo za uhalisia kwamba kuna upatikanaji wa dawa asilimia 90, au asilimia 80. Nampongeza Waziri na hata kwenye kamati yetu alikuja akasema takwimu nyingine za dawa siyo sahihi. Hapa katika ukurasa wa 44 ameonesha uhalisia kwamba kwenye MSD upatikanaji wa dawa ni asilimia 51, hakutaka kuficha. Nakupongeza sana Waziri, na unachokifanya Mwenyezi Mungu atakulipa. Badala ya kuwadanyanya Watanzania unaamua kusema ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa maagizo yake aliyotoa kuhusu MSD na kipekee nimpongeze Waziri Mkuu kwa kazi kubwa aliyoifanya MSD. Nakuomba dada yangu sasa Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Rais ameshatekeleza kwa upande wake, kuna kazi sasa ambazo Waziri, Katibu Mkuu na Mtendaji Mkuu lazima mzifanye. Mafanikio ya taasisi hayaletwi na management peke yake, kuna wafanyakazi wa kati na wafanyakazi wa chini. MSD ifumuliwe ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wafanyakazi wa kati wanaweza kumkwamisha CEO wa taasisi. Madereva wanaweza kumkwamisha mpaka CEO wa taasisi. MSD wanasambaza dawa, tukiwa na timu ya madereva ambao wanataka kufanya sabotage, wanaweza kumwambia Afisa Utumishi kwamba, mimi ni CEO wa nane hapa kwenye taasisi, hamnibabaishi, na akashindwa kupeleka dawa kwa wakati. Kwa hiyo, overhaul ya MSD isiwe kwa CEO na bodi tu, twende mpaka kwa madereva, watumishi wa kati na watumishi wengine ili MSD sasa tuipe muda iweze kutekeleza majukumu yake.

Mheshimiwa Spika, suala lingine, kuna upotevu wa dawa. Hili nalo lazima lidhibitiwe. Sehemu kubwa kuna mgongo ambao watu wanajificha kwamba kuna suala la msamaha. Hili nalo liangaliwe. Hii fedha ya dawa ambayo tunasema kwamba inaingia kwenye msamaha: Je, ni kweli zimeenda kwenye msamaha? Kwa sababu tulitarajia kwamba fedha tunazopeleka kwenye dawa iwe revolving fund, tunapeleka kila mwaka, na kule dawa hazitolewi bure, zinauzwa. Kwa hiyo, lazima zile fedha zizunguke. Otherwise kila mwaka tutakuwa tunapeleka fedha na matokeo hatuyaoni. Kwa hiyo, lazima tufuatilie zile fedha ambazo zinapatikana kwenye vituo vyetu vya kutolea huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni kuhusu bajeti ya MSD. Lazima hawa tuwaongeze fedha. Baada ya kufanya overhaul tuwaongeze fedha sasa. Pia tumefanya mabadiliko kuhusu Sheria ya MSD kwamba sasa wanaruhusiwa hata kujenga viwanda kutengeneza dawa. Wana mradi wao pale Keko na wana kiwanda chao pale Keko Pharmaceutical, tuwaongezee mtaji ili waweze kuzalisha dawa zenye ubora ili tuweze hata kuuza nchi majirani. Kwa hiyo, naomba tuwaongezee mtaji ili waweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala langu la pili ni kuhusu upungufu wa watumishi. Mheshimiwa Waziri amesema kinagaubaga kabisa katika ukurasa ule wa 75 kwamba watumishi waliopo kwenye sekta ya afya ni asilimia 47 ya mahitaji yao na asilimia 55 ni upungufu. Kwa hiyo, hapo utaona wazi kwamba lazima tuwe na jitihada za makusudi za kuajiri watumishi wa afya ili kupunguza hii nafasi iliyopo. Ndiyo maana kila Mbunge hapa akisimama anazungumzia upungufu wa watumishi wa sekta ya afya. Kwa hiyo, naomba kibali maalum kitolewe ili kupunguza changamoto hiyo. changamoto hii ni kubwa sana tunapokwenda kwenye maeneo ya vijijini. Kwa mfano kwenye Jimbo langu mimi la Nanyamba tuna upungufu wa asilimia 79. Mahitaji ya watumishi wa sekta ya afya ni 425, waliopo ni 106 tu. Kwa hiyo, utaona hapo tuna upungufu wa asilimia 79. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba tutoe kibali maalum, kwa sababu kuna vituo vingine vya afya kama Kiromba na Majengo, hakuna madaktari, ni wauguzi tu wanaendesha vile vituo. Sasa hii ina madhara makubwa sana. Tutoe kibali maalum, watumishi waajiriwe ili wakatoe huduma kule ambako tumeshafanya uwekezaji mkubwa kwa kujenga vituo vya afya, hospitali za Halmashauri na zahanati zetu.

Mheshimiwa Spika, nimalizie mchango wangu kuhusu suala la hospitali yetu ya Kanda ya Kusini Mtwara. Naipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutoa fedha nyingi za kumalizia ujenzi kwa phase one hospitali yetu ya kanda ya Kusini inayojengwa pale Mikindani, Mtwara, tunawashukuru sana. Isipokuwa sasa hivi tuna changamoto ya watumishi kama nilivyosema hapo awali. Ilipofunguliwa ile hospitali ya kanda walitolewa watumishi kutoka katika maeneo mbalimbali wakapelekwa pale watumishi 42. Sasa hivi idara inayofanya kazi ni moja tu ya OPD. Naomba Mheshimiwa Ummy na timu yako muongeze idadi ya watumishi ili mtumishi akienda kwenye hospitali ya rufaa apate zile huduma za kibingwa ambazo anazitarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza naipongeza Serikali kwa kutenga fedha, Shilingi bilioni saba kwa ajili ya kununua, vifaa muhimu; CT-Scan na MRI. Naomba sasa vifaa hivyo msambazaji avilete kwa wakati ili tuweze kutoa huduma iliyokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kuipongeza Wizara hii na ninaunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ambayo ipo Mezani pako ambayo ni hoja ya Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nami nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya kwa Watanzania ambayo ni kazi tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayoifanya, lakini kwa kutuletea hotuba ambayo ina matumaini kwa Watanzania. Amegusa kila sekta. Pia tunamwona Waziri Mkuu jinsi anavyohangaika kuisimamia Serikali, tunamwona anavyosimamia miradi mbalimbali ya Serikali, na anavyofanya ziara kufuatilia maagizo ya viongozi wengine. Kwa hiyo, tunampongeza sana Waziri Mkuu kwa kazi tukufu anayoifanya. Tunamwombea kwa Mwenyezi Mungu ampe afya njema, aendelee kuwatumikia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza pia Mheshimiwa Jenista Mhagama na Mheshimiwa Profesa Ndalichako kwa kazi nzuri anayoifanya, pamoja na Naibu Waziri. Kipekee nawapongeza kwa jinsi walivyoratibu shughuli za Mwenge katika Mkoa wetu wa Mtwara. Wametoa usaidizi wa kutosha na shughuli zilifana. Nachukua nafasi hii kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mheshimiwa Kanali Abbas kwa jinsi alivyosimamia zoezi hili, na uzinduzi ulifanyika kwa kufana sana. Nampongeza yeye pamoja na Kamati mbalimbali ambazo zimehusika katika shughuli ile ya Mbio za Mwenge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utaanza kujikita kwenye Hotuba ya Waziri Mkuu, Ukurasa wa 30 ambao unazungumzia kwamba, Serikali itaendelea kuratibu upatikanaji wa pembejeo, viuatilifu na mbegu. Kipekee naipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kazi kubwa ambayo inaifanya katika kuwekeza katika tasnia ya korosho. Tumeona kwa muda wa miaka mitatu mfululizo Serikali ikitoa pembejeo bure kwa wakulima wa korosho. Tunaendelea kuishukuru Serikali na mwaka huu kuna mikataba yenye thamani ya shilingi bilioni 340 ambayo imetolewa. Nina matumaini pembejeo hizi zitafika kwa wakati na wakulima wa korosho watanufaika na pembejeo hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushauri ufuatao: Pamoja na uwekezaji huu ambao umefanywa kwenye tasnia ya korosho, bado kuna anguko la uzalishaji wa korosho katika nchi yetu. Msimu wa mwaka 2017/2018 Tanzania tulifikisha tani 320,000, lakini kwa masikitiko makubwa msimu huu uliopita uzalishaji umepungua hadi tani 160,000 pamoja na uwekezaji mkubwa uliofanywa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiuliza Bodi ya Korosho, hawana majibu ya uhakika, ukiuliza TARI Naliendele, hawana majibu ya kutosheleza. Napendekeza iundwe tume huru ya kufuatilia nini kimeikumba tasnia ya korosho mpaka kukawa na anguko kubwa kiasi hiki? Kwa sababu haiwezekani mikoa ya uzalishaji wa zao la korosho imeongezeka, Serikali inawekeza vya kutosha, lakini tumetoka kwenye tani 340,000 hadi tani 120,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi ndogo tu, Ivory Coast, kila mwaka wanaongeza zaidi ya tani 100,000 na mwaka huu wamefikisha tani 1,000,000. Malengo ya Bodi ya Korosho mwaka huu ilikuwa ni kufikisha tani 400,000, lakini tumeishia kupata tani 160,000. Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi inasema tutakapofika msimu wa 2025 tufikishe tani 700,000. Kwa anguko hili tuna kazi kubwa sana ya kufanya ili kufikia malengo ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba uunde tume huru ili kuchunguza nini kimejiri? Ninapendekeza tupate wataalamu kutoka nje; kuna wataalam kutoka SUA; tusiendelee kuwatumia wale wale wa TARI na wa Bodi ya Korosho kwa sababu watatuletea majibu yale yale ambayo tumeyazoea. Tupate timu mpya, ikiwezekana twende hata nchi nyingine tuchukue wajumbe, kwa mfano, Ivory Coast ambao wamezalisha vizuri. Msumbiji wanafanya vizuri, tuchukue uzoefu kutoka huko, kwa sababu, tukileta TARI au watu wa Bodi ya Korosho watatupa majibu yaleyale ambayo kila mwaka bado uzalishaji unapungua.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza hadidu za rejea ya tume hiyo vile vile iangalie mfumo wetu wa uagizaji na udhibiti wa pembejeo. Kuna malalamiko kwamba pembejeo ambazo zinaingia kwenye tasnia ya korosho hazina ubora unaotakiwa. Kwa hiyo, Tume hii tutaipa na kazi hiyo, waangalie; je, hizi pembejeo ambazo zinaingia kwenye tasnia ya korosho zina ubora unaotakiwa? Zinatoa matokeo ambayo tunayatarajia? Kwa sababu haiwezekani tukaambiwa kuna mabadiliko ya tabia ya nchi wakati Mtwara na Msumbiji tunapakana na Mto Ruvuma; Msumbiji wanafanya vizuri, lakini Mtwara haifanyi vizuri. Kuna kitu ambacho hakiko vizuri katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili utajikita katika kuifungua Mtwara. Naipongeza Serikali kwa kazi kubwa sana ambayo imeifanya katika kuufungua Mkoa wetu wa Mtwara. Kuna uwekezaji mkubwa kwenye Bandari yetu ya Mtwara, kuna uwekezaji mkubwa katika kiwanja cha ndege na maboresho katika barabara, lakini kuna kazi ambayo ninatakiwa ifanyike ili Mtwara yetu iweze kufunguliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara ya Mnivata – Newala – Tandahimba mpaka Mbamba Bay, kipande cha kilometa 160. Tumekuwa tukibadilisha tarehe ya kuanza utekelezaji. Tulikutana na Katibu Mkuu akatuambia Machi tutaanza utekelezaji, lakini jana tumesikia jibu hapa kwamba ni mpaka Juni. Changamoto ni nini? Hii barabara ianze kujengwa. Barabara hii ni kiunganishi kizuri na kitakamilisha Mtwara Corridor ambayo itafungua mikoa ya Mtwara, Ruvuma, Njombe mpaka Mbamba Bay. Kwa hiyo, naomba huo mchakato wa ununuzi uendeshwe haraka, ili barabara hii iweze kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara ya Masasi – Nachingwea, ni ya muda mrefu, kwa nini haitengewi fedha za kutosha ikajengwa? Vilevile kuna suala ambalo ukichukua vitabu vya bajeti miaka mitano, tutakuwa tunazungumzia reli kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay na Tawi la Mchuchuma na Liganga. Kila mwaka tunataja, lakini utekelezaji haupo. Naomba Serikali yangu sikivu tuanze kuutekelea huu mradi. Mradi huu kama nilivyosema, utaifungua mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Njombe na hivyo tutafungua ushoroba wa kusini.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Chikota kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kuchauka.

T A A R I F A

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwongezee taarifa Mheshimiwa anayeongea. Ametaja Mtwara Corridor; kwa ufahamu wangu, naona Mtwara Corridor imeshakufa. Kwa sababu, Mtwara Corridor ilitegemewa kuifungua, kama route aliyoisema; lakini kwa miaka saba niliyokaa Bunge hili sijawahi kuona mradi wa barabara Mtwara wala barabara Lindi, zaidi ya barabara iliyotajwa Mnivata, kila mwaka inatajwa, na hii barabara ya Nachingwea – Masasi. Hakuna barabara yoyote Mkoa wa Lindi iliyotekelezwa kwa muda wa miaka saba yote niliyokaa hapa. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Chikota, taarifa unaipokea?

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea. Niongezee kwamba, ile barabara inaitwa barabara ya Masasi – Nachingwea mpaka Liwale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna mradi wa maji kutoka Mto Ruvuma kupeleka maji Mtwara Manispaa. Mradi huu ni mkubwa na mradi huu una mwaka wa saba sasa. Kwenye kitabu cha Wizara kunabadilika maneno tu, tunatafuta fedha, tunafanya usanifu, tunafanya mazungumzo. Mradi huu ni muhimu sana kwa Manispaa ya Mtwara. Mradi huu siyo kwa Manispaa ya Mtwara tu, utanufaisha Wilaya ya Mtwara, lakini vilevile na Halmashauri ya Mji wa Nanyamba kwa sababu, chanzo cha maji kipo Maembechini; lakini wananchi wamesitisha kufanya shughuli zao za maendeleo kwa kupisha mradi huu. Fidia haijalipwa bado, lakini vilevile hakuna kinachoendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba mradi huu ambao ni muhimu kwa upatikanaji wa maji kwa uwekezaji wa Mji wa Mtwara, kwa sababu, hata Kiwanda cha Dangote kina mahitaji makubwa sana ya maji. Mradi huu ukitekelezwa, basi hata na Kiwanda cha Dangote kitapata maji ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mradi huu utekelezwe na ninaunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami nichangie hoja ya Wizara ya kilimo ambayo iko mezani kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuwapongeza Mawaziri, Bashe na Mheshimiwa Mavunde, kwa kazi nzuri ambayo wanyoifanya. Ni Mawaziri wachapakazi, wabunifu na ni wasikivu na wanafikika kwa urahisi. Kipekee nimpongeze na nimshukuru Mheshimiwa Rais, kwa maono yake na jinsi anavyopeleka fedha nyingi kwa sekta hii ya Kilimo na amepelekea sasa hivi bajeti yetu kuongezeka mpaka hiyo bilioni 970. Tunakupongeza sana Mheshimiwa Rais na ni matarajio ya wakulima sasa kwamba sekta hii sasa italeta manufaa ambayo sisi Wabunge kila mwaka tulikuwa tunalilia kwamba bajeti ya sekta ya kilimo iongezeke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda nitajikita kwenye uchangiaji ukurasa wa 169. Ukurasa wa 169 wa bajeti umezungumzia suala la kuongeza thamani. Nitazungumzia uongezaji wa thamani wa zao la Korosho, na kwenye korosho wenzangu waliotangulia kuchangia wamezungumzia changamoto. Kwenye Korosho kuna changamoto nyingi na zimekwisha tajwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye korosho kuna changamoto ya kupungua kwa uzalishaji, tumeona kwa kipindi cha miaka mitatu sasa hivi uzalishaji unapungua mwaka hadi mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye korosho kuna bei ndogo kwa mkulima ambayo haina tija, ambayo sasa hivi kwa muda wa miaka miwili kwenye minada yetu mkulima hapati bei ambayo inatija kwake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye korosho tumeshuhudia utitiri wa makato na tozo ambayo hatimaye inapunguza bei kwa mkulima. Pia, kwenye korosho ni zao pekee ambalo lina export levy. Hili nazungumzia kwa sababu export levy baadae inapunguza bei kwa mkulima, sio kwamba inalipwa tu na mfanyabiashara lakini anayeumia baadae ni mkulima anapokwenda sokoni kwamba bei yake inapunguzwa .

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Wizara kwa kuja na mwarobaini, inasema kwamba zimetengwa fedha bilioni 10 ili Bodi ya Korosho ipelekwe kwenye private sector kwa ajili ya kujenga kiwanda cha kubangua korosho. Huu ni mpango mzuri na suluhisho la kuuza korosho ghafi. Kwa sababu tukiendelea kuuza korosho ghafi wakuilima wetu hawafaidiki lakini tukiuza korosho karanga tutapata bei nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikupongeze Mheshimiwa Bashe, kwa wazo lako sasa la kuingia kwenye ubanguaji. Lakini tamko hili Mheshimiwa Bashe, nikushauri kwamba hii ni vita ya kibiashara. Kwa sababu kuna nchi duniani hawapendi Tanzania wauze Korosho karanga, wanataka kila mwaka wauze korosho ghafi kwa sababu ni ajira kwa wananchi wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanachukua korosho yetu na kupeleka nchini kwao na wanatengeneza ajira. Kwa hiyo, hili tamko ambalo umelitoa na kwenye mkutano wetu wa wadau wa korosho ulisema msimu wa 2025/2026 utakuwa ni mwisho wa kupeleka korosho ghafi, ina maana korosho yote itabangulia hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nakuomba sasa tuwe na maadalizi ya kutosha. Tusipokuwa na maandalizi ya kutosha tutavurugwa, kwa sababu kama nilivyosema kuna nchi ambazo hawako tayari kuwekeza Tanzania kwa ajili ya kubangua korosho. Wanataka kila mwaka tupeleke korosho ghafi kwa sababu inatoa ajira kwao. Kwa hiyo, wao kwa gharama yoyote hawako tayari kuona Tanzania sasa inaanza ubanguaji. Kwa hiyo, tufanye vetting wakati wa kuwapata watu hao watakaoingia kwenye private sector wawe na nia ya kuwekeza na kubangua Tanzania. Kwa sababu tuna uzoefu wa viwanda 12 vya zamani, tulifungua viwanda 12 lakini baada ya muda mfupi vikafungwa. Haya vile viwanda vilibinafsishwa mpaka leo viwanda vile havifanyi kazi ni magodauni tu. Kwa hiyo, lazima tuwafanyie vetting ambao tutakuwa nao katika uwekezaji, la sivyo kutakuwa na changamoto kama ilivyokuwa zamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile, hawa wawekezaji lazima tuwape motisha. Tupunguze kodi ya mitambo wakati wanapoingia ili kupunguza gharama ya uwekezaji. Tukifanya hivi tutapata wawekezaji ambao ni serious, watakuwa na mtaji mkubwa na wataingia kwenye ubanguaji serious.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Mheshimiwa Waziri, nikushauri kwamba wakati hao wawekezaji wanaendelea na shughuli zao za uwekezaji basi tuwe na forum za kuasikiliza ili pale wanapopata changamoto waweze kusikilizwa. Kwa mfano; sasa hivi kuna changmoto ya upatikanaji wa kosrosho kwa wabanguaji wa ndani, tuna mfumo wa soko la awali ambao unalalamikiwa, ni vizuri Waziri ukakaa na hao wenye viwamda ukatafuta mfumo ambao hautashusha bei kwenye minada, mfumo ambao hautapunguza bei kwa mkulima ili na wao wapate korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niingie kwenye suala la umwailiaji. Nimeona hapa umesema kwamba umeingia mikataba 22 kwa ajili ya kuanza umwagiliaji katika mabonde mbalimbali, hili ni wazo zuri. Kipekee kuna Bonde la Ruvuma Basin, ambalo linaanza Songea, Namtumbo, Tunduru, Masasi, Mtwara. Bonde hili bado hatujalitumia ipasavyo, lina kilometer square 60,000. Kwa hiyo, naomba yule mkandarasi ambae amepewa kazi ya kufanya usanifu aanze songea mpaka Kilambo – Mtwara Vijijini. Tukifanya hivyo tutatoka na Mradi ambao utasaidia Ruvuma Basin. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu gani? Mto Ruvuma una changamoto na ukiangalia jiografia ya Mto Ruvuma kwamba mto uko kwa chini na maeneo ya umwagiliaji yapo kwa juu. Ni lazima tuje na designing ya kujenga mabwawa mengi ili yatumike wakati wa umwagiliaji. Kwa hiyo, usanifu lazima ufanywe kutoka Songea kama nilivyosema hadi Wilaya ya Mtwara ili maeneo yote haya yafaidike na mradi huu. Tukitumia vizuri bonde hili tutaweza kunufaisha uzalishaji wa mazao ya mpunga lakini na mbogamboga na kuweza kuwasaidia wananchi wetu ambao sasa hivi wana utegemezi wa zao moja moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Songea wanategemea mahindi lakini Mtwara watu wengi wanategemea korosho. Lakini tukifanya upembuzi yakinifu na bonde hili likatumika ipasavyo basi tutawanufaisha watu wetu. Kuna maeneo ya Lipeleng’enye na kule Chikwedu kwa Mzee wangu Mkuchika, kuna changamoto ya mafuriko, lazima tujenge ukuta wa kutosha ili kuhakikisha sasa maji ya Mto Ruvuma hayawezi kuathiri mashamba ya hao wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye maazimio ya mkutano wetu wa wadau tulikubalina kwamba tuunde tume ya ufuatiliaji kwenye korosho nafikiri tutafanya kazi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya katika sekta hii ya nishati, kipekee nikupongeze Waziri wa Nishati, Kaka yangu Mheshimiwa Makamba hongera sana kwa kweli unachapa kazi. Ninakupongeza Wakili Msomi Naibu Waziri, ni msikivu, unafikika na unapokea simu muda wote, niwapongeze Watendaji nikianza na Mtendaji Mkuu Engineer Mramba ambaye ni Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu Ndugu yangu Athumani Mbuttuka kwa kweli mnachapa kazi na kazi inaonekana katika Wizara hii, hongereni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ina changamoto kubwa sana lakini jana Mheshimiwa Waziri Mkuu amesema maneno ya faraja wakati anakagua ile wiki ya nishati pale kwenye mabanda. Amesema acha wao waseme Wizara chapeni kazi. Mheshimiwa Makamba chapa kazi. Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere kulikuwa na maneno mengi sana, lakini umesema kwenye mawasilisho yako hapa tumefikia asilimia 87 sasa hivi, bado kumi na tatu tu hongera sana. Tunao mradi wa REA, mradi mkubwa na Afrika kwa sasa hivi tunaongoza coverage ni vijiji asilimia 82, tumebakiwa na asilimia 18 hongereni sana, chapeni kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nijielekeze kwenye mradi wa LNG. Ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kama wenzangu walivyosema mradi huu ulienda kwa kasi sana huko nyuma, baadae miaka saba mradi huu ulisinzia lakini kwa upendo wake Dkt. Samia Suluhu Hassan akaagiza majadiliano yaanze tena kwa kasi. Ninakupongeza Mheshimiwa Waziri Makamba kwa kusimamia hayo majadiliano na ku-fast track majadiliano na tuliona ulitualika Wabunge wa Mtwara na Lindi pale Ikulu wakati kuna signing ceremony ya makubaliano ya awali, lakini kwenye taarifa yako umesema makubaliano, majadiliano mmeshahitimisha mna-draft mkataba, hongereni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama walivyosema wachangiaji waliopita wenzetu wa Jimbo la Cabo Delgado Msumbiji wakati tunasinzia na mazungumzo wao walianza kwa kasi mwaka 2019, hivi karibuni nafikiri watakamilisha, lakini kwa jitihada zako nafikiri kutangulia siyo kufika ili mradi sisi tumetoka nyuma lakini kwa kasi kubwa tutafanikiwa, kwa hiyo endelea hapo na tunakuombea kila la kheri hatua iliyobaki ikamilike ili wananchi wa Mtwara na Lindi kama walivyosema wenzangu na Watanzania kwa ujumla wanufaike na mradi huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nina ushauri kuhusu mradi wa LNG. Wakati mradi huu ulipoanza Serikali na wale wawekezaji waliunda Kamati mbili kubwa. Kamati ya kwanza ilikuwa kwa ajili ya upatikanaji wa ardhi (Land acquisition) na Kamati ya pili ilikuwa ni kuihusisha jamii kwenye mradi (community engagement) na Kamati hizi zilifanya kazi zake kwa kushirikiana na wananchi wa maeneo husika ya mradi kule Likong’o – Lindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ardhi limekwishakamilika kama ulivyosema nikupongeze Mheshimiwa Hamida kwa kufuatilia na sasa wananchi wake wengi wamepata fidia. Suala la kuishirikisha jamii naomba Waziri Kamati hii iendelee, kuna mambo mengi ya kufanya kwenye jamii. Vijana, wanawake, wazee na makundi ya kijamii ni lazima yajulishwe hatua zinazoendelea katika mradi huu, waelezwe fursa zilizopo, waeleze jinsi watakavyonufaika na mradi huu na mipango ya Serikali kuwa – engage wao katika mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri umesema vizuri kwamba unajenga chuo kikubwa pale Lindi lakini huko nyuma tulikuwa tunawapeleka vijana wapate elimu ya kati katika Chuo cha VETA Mtwara na VETA Lindi ili wapate ujuzi na maarifa ambayo mradi ukianza wataweza kuajiriwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, si hivyo tu Kamati hii ina kazi ya kuwaelimisha jamii jinsi ya kuishi na mradi. Miradi hii Kwa wenzetu ambao wametangulia kuna changamoto nyingi, wanaweza kuja watu wakaichonganisha jamii na Serikali yao, tujifunze yaliyotokea Nigeria kuhusu Boko haramu, lakini Jimbo la Cabo Delgado Msumbiji kuna maharamia ambao wanahujumu mradi, wamekwenda kule wakashawishi vijana kwamba Serikali inafanya mradi huu lakini ninyi hamtanufaika wakaanza kufanya zile vurugu. Kwa hiyo, sisi tuwatayarishe vijana wetu, wananchi wetu kuishi na mradi kama sehemu ya jamii ili yale yanayotokea kule Cabo Delgado Msumbiji na Boko Haram kule Nigeria yasitokee nchini kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku ya kusaini makubaliano ya awali pale Ikulu, Mheshimiwa Rais alitoa maagizo makubwa sana kwa Mheshimiwa Waziri alisema “wananchi wa maeneo husika ya mradi wasiishi kama walivyo sasa hivi” tunatarajia kwamba mradi ukianza Lindi haitakuwa kama ilivyo leo tunatarajia sasa Uwanja wa Ndege wa Lindi sasa ujengwe ili wawekezaji watumie uwanja ule wa Lindi. Tunatarajia sasa barabara za Lindi na Mtwara zitaimarishwa kwa sababu tuna kundi la watu zaidi ya 10,000 kwa ajili ya ajira rasmi na zisizo rasmi, watu hao ni wengi lazima tupanue huduma za afya huduma za elimu na huduma za kijamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuntarajia sasa hivi kwamba hata upatikanaji wa maji, wananchi wa Lindi wasitegemee mradi wa Ng’apa tu, tuwe na miradi mingine ili kuhakikisha wageni watakapokuja kusiwe na changamoto ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili utahusu changamoto za umeme Mkoani Mtwara kama walivyosema wenzangu. Mheshimiwa Waziri ninakupongeza kwa usikivu wako tulifanya kikao juzi na sina haja ya kurudia mambo tuliyokubaliana, ninakuomba sasa kayatekeleze yale, nikupongeze kwa sababu nimepata taarifa timu yako sasa iko Mtwara, kwa hiyo, yale tuliyokubaliana kwanza yale ya muda mfupi kwambab utapeleka sasa turbine kutoka Dar es salaam ili iende Mtwara ikazalishe megawatt 20 basi kazi hiyo ifanyike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, furaha kwetu wana Mtwara umesema kwenye hotuba yako kwamba ule mradi mkubwa wa megawatt 300 wa eneo la Naumbu pale Mtwara utaanza kutekelezwa tunakushukuru sana. Tunaomba mazungumzo na Serikali ya Japan yaendelezwe kama ulivyosema kwamba wameahidi kutoa fedha yaharakishwe, fedha zipatikane mradi ujengwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi ule umesema utajenga line ya kilometa 208 kutoka pale Mtwara hadi Somanga Fungu hapo unatudhihirishia kwamba sasa umeme wa uhakika kwa Mikoa yetu ya Mtwara na Lindi utakuwa unapatikana. Si hivyo tu, umetuthibitishia sasa kwamba ile kazi ambayo inafanywa kutoka Songea hadi Tunduru – Masasi kuiunganisha Mtwara kwenye gridi ya Taifa, basi fedha zimepatikana ili kazi iendelee kutoka Masasi hadi Mahumbika - Lindi. Ukifikisha gridi ya Taifa pale Mahumbika tuna uhakika sasa Lindi na Mtwara tutakuwa na umeme wa uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkurugenzi wa TANESCO nawaombeni sasa yale ambayo tumekubaliana basi mtembee katika matamshi yenu na sisi tuna imani na ninyi na tutaendelea kuwapa support na pale tutakapohitaji kuwakumbusha tutawakumbusheni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwishoni usambazaji wa….

MWENYEKITI: Mheshimiwa Chikota, muda wako umeisha, malizia sekunde thelathini.

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la langu la tatu ni usambazaji wa gesi asilia majumbani. Tumeona hapo taarifa ambayo imeandikwa kwamba Mtwara hadi sasa kuna nyumba 420 tu, Lindi kuna nyumba 209, naomba fedha zitengwe kasi iongezwe ili wananchi wa Mtwara na Lindi wanaufaike na gesi asilia pia tupunguze matumizi ya kuni majumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga hoja mkono. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ambayo ipo mezani kwetu.

Mheshimiwa Spika, nianze kuwapongeza wenyeviti wa Kamati zetu hizi tatu za PAC, LAAC na PIC kwa taarifa zao nzuri ambazo wamewasilisha, lakini pia niwapongeze Wajumbe kwa uchambuzi ambao wameufanya kuhusu Ripoti ya CAG. Nichukue nafasi hii kumpongeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kwa kutupa taarifa ambazo ni za bayana ya nini kinachoendelea katika Wizara zetu, Serikali za Mitaa na Idara ambazo zinajitegemea, ni ripoti ambayo haina mashaka na uzalendo wa CAG tunaufahamu, kwa hiyo hongera sana Ofisi ya CAG.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda mimi nitajikita sana kwenye Taarifa ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na niendelee kuipongeza taarifa hii kwamba ni taarifa ambayo imeandaliwa vizuri. Imeonesha madhaifu mengi kwenye makusanyo ya mapato ya ndani, imeonesha udhaifu katika udhibiti wa ndani, imeonesha udhaifu katika mfumo wa usimamizi, lakini imeonesha udhaifu wa Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani ambacho kingekuwa imara kingekuwa kinawasaidia Mamlaka za Serikali za Mitaa, lakini pia imeonesha udhaifu wa Sekretarieti za Mikoa katika kusimamia Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, taarifa hii iko vizuri na sipendi kwenda kwenye takwimu kwa sababu ukisoma taarifa yao kila kurasa wametoa maelezo na takwimu za fedha ambazo zimepotea na hasara ambayo Serikali imeipata.

Mheshimiwa Spika, ningejielekeza kwenye nini tukifanye na hasa kwenye ku…, kwa sababu ukiiangalia hii taarifa kuna mambo kama matatu hivi; kwanza kuna suala la sheria zinazoongoza Mamlaka za Serikali za Mitaa, kuna miongozo yetu, lakini kuna muundo. Mimi nitajikita hapo ili pengine tuweze kurekebisha kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia kwenye sheria zetu ambazo zinaongoza Mamlaka za Serikali za Mitaa zimetungwa muda mrefu sana, ni muda sasa wa kufanya mapitio au tujiulize je, zinafaa kuendelea hadi sasa? Kuna mjumbe mmoja pale kaka yangu Mheshimiwa Mwambe amesema kwamba sisi ni sehemu ya Madiwani na tunahusika na ubadhirifu unaotokea. Ndugu zangu kwa mifumo iliyopo sasa hivi na miongozo iliyopo sasa hivi hata Madiwani wenyewe hawafahamu kinachoendelea kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi nani anamsaidia Diwani kuifahamu Taarifa ya CAG, nani anamsaidia Diwani kujua final account za halmashauri? Menejimenti inaamua nini ipeleke kwenye Baraza na nini isipeleke, lakini je, hivi kweli inawezekana taarifa za sekta kama kumi hivi Madiwani wakutane siku moja tu kwenye Baraza wazungumzie elimu, wazungumzie afya, wazungumzie maji na wazungumzie nini. Hii mifumo kwa kweli sasa hivi haituwezeshi.

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile ukisoma ile Sheria ya Tawala za Mikoa, Katibu Tawala wa Mkoa siyo mamlaka ya nidhamu kwa watumishi wa halmashauri, yeye ni mamlaka ya nidhamu kwa watumishi wa RS. RAS akienda kwenye Halmashauri pale hata kama atapiga kelele Wakuu wa Idara wataulizana kwani huyu mmemjazia mafuta aondoke zake, kwa sababu hawezi kufanya chochote. Atapiga kelele zake atafanya hivi, anaondoka zake. Mamlaka ya nidhamu ya RAS ni kwa watumishi wa RS tu, lakini wale wa Mamlaka za Serikali za Mitaa siyo wa kwake.
Mheshimiwa Spika, vilevile kuna suala hili la ugatuaji, tuna Sera yetu ya Ugatuaji ya mwaka 1998; je, hiyo ni valid mpaka sasa hivi? Kuna malalamiko yapo kwamba TAMISEMI sasa kumekuwa congested.

Mheshimiwa Spika, kuna malalamiko yapo sasa hivi kwamba kwa mfano Katibu Mkuu Uvuvi akitaka kuandika barua kupeleka kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa ni mpaka ipitie kwa Katibu Mkuu, TAMISEMI. Ina maana kwamba tuna Chief Secretary mwingine sasa mdogo, kwamba hatuwezi kupeleka taarifa huko mpaka zipitie TAMISEMI, lakini je, kuna coordination gani kati ya TAMISEMI na hizi Wizara za kisekta?

Mheshimiwa Spika, naomba kwa sababu Mheshimiwa Rais amekuja na 4R hii R ya reform lazima tufanye reform kubwa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa. Tufanye reform kwenye Regional Secretariat, RC, RAS wawe na nguvu kwenye usimamizi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa. Ikibaki hivi hivi tutaendelea kama business as usual na ndiyo maana Mawaziri mnapata shida sana, viongozi wetu wa Kitaifa wanapata shida sana, wanapofika mikoani wanashughulikia isuue ambazo zingefanywa na ma-DC na ma-RC. Naomba tufanye mabadiliko ya hizi sheria. Hizi sheria siyo bible siyo msahafu, tuzibadilishe sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile naomba sasa kwenye mabadiliko haya tuangalie nafasi za Wakurugenzi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa, isiwe mtu akiteuliwa basi ndiyo huyo Mkurugenzi, Wakurugenzi hawa tuwape mikataba sasa na kuwe na KPI za kuwapima, akimaliza muda wake kama ha-perform basi aondoke, lakini Mkurugenzi akishateuliwa anaona ameula, Akiharibu Kiteto anakuja Nanyamba, akitoka Nanyamba anakwenda Nanyumbu anabadilisha badilisha tu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo lazima ifike mahali sasa tena mimi Mheshimiwa Mchengerwa nakutegemea sana. Wewe ulipoingia TAMISEMI tuna matumaini makubwa sana. Ni mtu wa kuthubutu, hebu kafukunyue hivi vitu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mamlaka za Serikali za Mitaa sheria nyingine zimetungwa wakati wa Baba wa Taifa tuzibadilishe sasa hivi. Mchengerwa unaweza na timu yako, kafanye mabadiliko ili tuwe na strong RS. Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala, akifika kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa haonekani kuwa ni mtu ambaye anaweza kuchukua hatua, lakini anafika pale anapiga maneno kwamba hizo ni kawaida zao. Ni kama mnavyowaambia Mawaziri mmeapa mkienda kwenye Wizara, watumishi wanasema kwamba huyu ni Waziri wa nane mimi huyu, mwenzake alikuja hapa na ukali huu huu, lakini alitulia. Kwa hiyo, twendeni tukafanye hayo mabadiliko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile tuangalie nafasi za wenye viti na mayor wa Halmashauri. Hivi kwa mtindo wa sasa hawa kweli wana uwezo wa kusimamia Mamlaka za Serikali za Mitaa? Nani anamsaidia Mwenyekiti wa Halmashauri kuifahamu vizuri Halmashauri yake kwa sababu Mkurugenzi anamficha taarifa muhimu Mwenyekiti wa Halmashauri ili asimsumbue kwenye vikao, anapata wapi zile taarifa? Anapata wapi usaidizi na anakwenda siku mbili tu kwa wiki? Tena siku nyingine anaambiwa leo hakuna gari tutakutumia posho yako huko huko ulipo anasema sawa, basi hafiki Halmashauri. Kwa hiyo, naomba tufanye mabadiliko kama hayo.

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, vilevile…

SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja nakushukuru sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudia Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie hoja iliyo mezani kwetu. Kwanza, niwapongeze Waheshimiwa Mawaziri wote wawili, Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo na Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, kwa kuja na hotuba nzuri ambazo zimetupa mwelekeo wa kule tuendako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nimpongeza Mheshimiwa Rais kwa miongozo ambayo ameitoa kwa Wizara hizi na kuepelekea kuletwa kwa hotuba hiyo ambayo tunajadili sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utajikita katika maeneo mawili. Nianze na Sekta ya Gesi Asilia. Naipongeza Wizara ya Nishati kwa kazi nzuri ambayo inaifanya, lakini nina ushauri katika mambo matatu. Kwanza ni kuhusu mradi wa LNG, nimesoma kwenye mapendekezo ya mpango, kuna mikataba imeshaanza kusainiwa. Ni jambo zuri lakini wamekwenda mbali, kwamba kuna kampuni ya TPDC Likong’o LNG Company Limited imeanzishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba, shughuli hizi za LNG zifanyike kwenye eneo husika. Likong’o ni mtaa au ni kijiji katika Manispaa ya Lindi. Siyo busara sasa shughuli hizi zikaendelea kufanyika Dar es Salaam na Arusha, wakati eneo la mradi lipo. Kwa hiyo, naomba sasa Shughuli za LNG zihamie katika eneo husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la pili ni kuhusu Ujenzi wa Vituo vya CNG. Wote ni mashahidi sasa bei za mafuta duniani hazitabiriki. Sasa hivi kuna mpango mkubwa au kuna uhamasishaji wa watu tutumie gesi asilia katika vyombo vya usafiri lakini vituo hivi ni vichache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali sasa, kwanza naipongeza TPDC kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya kwenye suala hili na EWURA. Sasa naomba Serikali itoe vivutio maalum kwa watu ambao wanataka kujenga vituo hivi ili viongezeke. Kwa sababu kwa sasa nafikiri tunavyo vinne tu. Kuna makampuni zaidi ya 30 wameomba, tuwe na special incentive ili hata kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma kuwe na vituo vya CNG, kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza kuwe na Vituo vya CNG na maeneo mengine. Tutoe punguzo maalum, tutoe vivutio ili sasa wawekezaji wajikite katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la tatu ni usambazaji wa gesi viwandani na majumbani. Naipongeza TPDC kwa kazi ambayo wanaifanya vizuri, lakini TPDC hawapewi fungu la kutosha. Naomba mpango ujielekeze kwamba utatoa fedha za kutosha ili usambazaji huu sasa uende kwenye mikoa yote. Isiwe Mtwara, Lindi na Dar es Salaam tu, gesi asilia sasa iende kwenye mikoa yote. Niipongeze Wizara ya Nishati, imesaini mkataba jana wa kupeleka hii gesi kwenda Uganda, sasa ielekee Uganda lakini na mikoa ambayo bomba hili litapita inufaike na mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili ni kuhusu suala la elimu. Naipongeza Serikali kwamba imeidhinisha matumizi ya Sera Mpya ya Elimu ya 2014. Sera hii ya elimu ya 2014, kama mtakumbuka ilizinduliwa huko nyuma na imekaa miaka nane kabla ya utekelezaji wake kwa sababu ya kukosa funding. Naomba sasa Serikali ijielekeze katika ugharamiaji wa hii sera mpya ya elimu ambayo inakuja na mambo mengi sana ambayo yatabadilisha uendeshaji na usimamizi wa elimu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia mwakani tunaanza kutekeleza mtaala mpya kwa wanafunzi wa darasa la tatu. Kwa maana hiyo, Mtihani wa Darasa Saba mwaka 2027 hautakuwepo. Kutakuwa na kitu kinaitwa National Assessment, lakini kwa sasa hivi kwa takwimu zilizopo kila inapofanika mtihani, wanafunzi takribani asilimia 25 hawaendelei na kidato cha kwanza. Tutakapofanya National Assessment ina maana wanafunzi wote wataingia kidato cha kwanza kwa hiyo, kuna mahitaji mapya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuchukulie mfano wa watahiniwa mwaka huu, tulikuwa na watahiniwa 1,397,370. Sasa asilimia 25 ambao kwa matokeo ya kawaida ya mtihani ni kama watoto 350,000 hivi hawataingia kidato cha kwanza. Tutakapoanza utekelezaji wa sera mpya, hawa 350,000 wataingia kidato cha kwanza. Tutahitaji madarasa mapya, walimu wapya na tutahitaji matundu ya vyoo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa wanafunzi hao 350,000 tunahitaji madarasa ya ziada 8,733, siyo mapya, ni ya ziada ukiacha haya yaliyopo sasa hivi. Tutahitaji matundu ya vyoo 17,497. Kwa hiyo, lazima mpango wetu ujikite katika education financing, tutapata wapi fedha za kugharamia huu mfumo mpya wa elimu, elimu isigharamiwe kama kawaida. Tukifanya kama tunavyotenga bajeti ya kawaida hatutaweza kujenga shule mpya za ufundi ambazo zinatakiwa. Kwa sababu kwa maelekezo ya mtaala wetu mpya, tutakuwa na mikondo miwili; ule mkondo wa kawaida wa taaluma na mkondo wa amali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkondo wa taaluma na mkondo amali ina maana kwamba sasa huku kwenye amali ni kitu kipya. Tutahitaji walimu wapya wa michezo, wa ufundi na walimu wapya wa sanaa. Hao walimu wanahitaji ajira, yaani itatakiwa ajira mpya ili waingie katika mfumo huu. Sasa pasipokuwa na fedha za kutosha hatutaweza kutekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile wanahitaji maabara ambazo zimesheheni, siyo maabara ambazo kuna Bunsen burner na test tube. Inabidi tuwe na maabara ambazo mwanafunzi akiingia ajue kweli ameingia maabara. Kwa hiyo, hilo linahitaji uwekezaji, siyo hivyo tu, tunahitaji in service training kwa walimu. Hao Walimu sasa tunawaambia kwamba mtoto akiingia darasa la kwanza anafika form four. Hao waliopo kazini lazima tuwe na mafunzo kazini, tuwawezeshe kwenye mbinu mpya, tuwape maarifa mapya na tuwape ujuzi mpya. Tukigharamia kama tunavyofanya sasa hivi hatutaweza kutekeleza mtaala huo mpya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nianze kwa kumpongeza Waziri wa Fedha kwa hotuba yake. Nimpongeze pia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kwa hotuba yake. Vilevile niwapongeze kwa utendaji wao wa kazi; Waziri wa Fedha pamoja na Naibu wake na Waziri wa Mipango pamoja na Naibu wake pia na Watendaji Wakuu wa Wizara hizi mbili kwa kazi nzuri ambazo wamezifanya kwa maandalizi mazuri ya hotuba na ndiyo maana wameleta kitu ambacho kinajadiliwa kwa nguvu zote, kwa sababu kitu ambacho kina matumaini kwa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu utaenda kwenye hotuba hizi zote mbili, nikianza na Hotuba ya Hali ya Uchumi ambayo imewasilishwa na Profesa. Mpango wa Maendeleo umezungumzia ule mradi wa kimkakati, Mradi wa LNG na mimi nichukue nafasi hii kipekee kumpongeza Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa nguvu kubwa anayoiweka kuhakikisha kwamba Mradi wa LNG unatekelezwa, hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu ambao utahusisha vitalu vitatu, kitalu namba moja, mbili na nne ambavyo vipo kwenye kina kirefu utakuwa na manufaa makubwa sana kwa nchi yetu. Kwa hotuba yake Mheshimiwa Waziri amesema kazi ambazo zimepangwa kufanyika katika mwaka huu wa fedha ni kukamilisha majadiliano ya mradi ya mkataba kati ya nchi yetu na wawekezaji. Hivyo, tutakaribia kupata Host Government Agreement (HGA), vilevile mkataba wa ugawaji wa mapato. Kazi nyingine ambayo ameifanya ni kuelimisha wananchi umuhimu na manufaa ya mradi huu, vilevile utoaji wa elimu kuhusu fursa na huduma kwa bidhaa za ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wataalamu wa masuala ya gesi wanasema tuna vyanzo vitano vya mapato mradi huu ukitekelezwa. Chanzo cha kwanza kikubwa ni faida yenyewe ya gesi. Chanzo cha pili tutapata kodi ya mapato, chanzo cha tatu tutapata mrabaha, vilevile tutakuwa na Tozo ya LNG (LNG fee) lakini kwa kwetu Tanzania kwa sababu mradi huu unatekeleza kwa ubia na Shirika letu la TPDC basi ule ushiriki wa TPDC kuna mapato tutayapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hapa tuna vyanzo vitano vya uhakika katika mradi huu. Kwa hiyo niipongeze Wizara kwa shughuli zile ambazo zimepangwa, ushauri wangu ni kwamba shughuli hizi zifanyike kwa weledi kwa sababu hili suala sasa la kuelimisha jamii kuhusu manufaa ya mradi huu lazima tulifanye kwa umakini. Awamu ya kwanza kuna dosari ambazo tulizifanya, tuliwaaminisha Wananchi wa Mtwara na Lindi kwamba itakuwa Singapore na itakuwa Dubai kwa hiyo, wataacha kilimo cha korosho watategemea uchumi wa gesi. Kitu ambacho kilikuwa ni makosa makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba timu ya wataalamu ambao wanaandaa community engagement na communication strategy wahakikishe wanatumia wanasiasa. Wanatumia wawakilishi wakaelezee nini kitafanyika kwa mradi ule? Na si kuwaambia kwamba jamani Mradi wa LNG ukianza basi Lindi itakuwa Singapore kwa hiyo korosho mtaacha kulima hamtalima mpunga hamtalima vitu vingine. Makosa yale tuliyafanya na tusirudie tena kwa sababu awamu za kwanza za hamasa tulitoa matamko kama hayo ambayo sisi kama wanasiasa sasa hivi tunaulizwa maswali mengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba wakati wa uelimishaji, timu ya wataalamu ichanganyike na timu ya wawakilishi na wananchi, Waheshimiwa Madiwani, Waheshimiwa Wabunge kwa maana ya wanasiasa ili waende wakafanye kazi hiyo ya kuelezea kwamba nini kitafanyika mradi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nafahamu kwamba tuna Kamati ya Majadiliano ambayo ina watu mahiri sana. Tuna usimamizi mzuri wa Wizara yetu, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati anafanya kazi kubwa sana kuhakikisha kwamba majadiliano yanakamilika. Tuna timu ya wataalamu wabobezi ambao wanashauri timu ya majadiliano lakini kama alivyosema Mheshimiwa Profesa Muhongo jana majadiliano haya yamechukua muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wanauliza sasa kinachojadiliwa ni kitu gani? Tutoke tuwaambie wananchi tumefikia hatua gani? Mazungumzo yamechukua muda mrefu sana. Mazungumzo yenyewe yanafanyika Arusha, Lindi hawajui na Mtwara kwenye kitalu hawajui. Kwa hiyo naomba muda wa majadiliano upunguzwe. Hapo awali sisi tulikuwa mbele ya Msumbiji kwenye utekelezaji wa mradi huu lakini kwa sababu ya muda mrefu sasa hivi Msumbiji wapo mbele zaidi yetu sisi. Kwa hiyo, naomba muda wa majadiliano upunguzwe, vilevile tuhakikishe kwamba kile ambacho tutaendelea kukipata tunakipata katika mradi wetu wa gesi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la manufaa na huduma za bidhaa ambazo zitakuwa supplied na watu wetu wa ndani na hapa nakuomba Waziri uratibu jinsi shughuli zitakavyofanyika. Ukiangalia ule uchumi wa gesi na shughuli itakayofanyika pale wakati wa ujenzi wa mradi tutakuwa na watu wengi sana, lakini baada ya ujenzi kukamilika watu watapungua. Kwa hiyo lazima tuwa-engage Watu wa Lindi na Mtwara ni muda tunafikiri wao wanaweza kunufaika zaidi wakati wa ujenzi wa mradi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile vitu vinavyotakiwa pale vinahitaji mtaji mkubwa sana lakini kuna vitu wakazi wa Mtwara na Lindi wanaweza ku-supply: nyanya, kunde na mbogamboga. Ndiyo muda sasa Waziri wa Kilimo kupitia mradi wetu wa irrigation (umwagiliaji) kuwekeza kwenye mabonde sasa yalipo Mtwara na Lindi. Tuna Bonde la Kinyope, kuna Ngongowele kule Kilwa na Nachingwea kuna miradi ya umwagiliaji, pia kuna Ndanda kuna mradi wa umwagiliaji. Miradi hiyo sasa ipelekewe fedha ili mradi utakapoanza wananchi wa Liwale wa Ndanda, Nanyamba na Newala waweze ku-supply kwenye mradi. Hapo tutakuwa tumewasaidia wananchi wa maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ushauri wangu mwingine ni kwamba sasa Wizara zingine sasa zitekeleze majukumu yao. Tunajenga mradi mkubwa pale Lindi lakini Mji wa Lindi hauna kiwanja cha ndege, Mji wa Lindi kiwanja chake ni cha vumbi, hivyo hizo gharama za mradi zitakuwa kubwa kwa sababu wawekezaji watakuwa wanaishi Dar es Salaam wanashukia Mtwara wanakwenda na asubuhi wanarudi. Ni muda mwafaka sasa wa kutekeleza mradi wetu wa ujenzi wa Uwanja wa Lindi, muda ni huu ili mradi ule ukikamilika basi utaendana na mradi wetu mkubwa ambao tunaujenga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ni muda sasa mwafaka wa kukamilisha Ujenzi wa Bandari ya Lindi ambayo vilevile itatoa huduma wakati mradi huu unatekelezwa. Pia, ni muda mwafaka sasa wa ujenzi wa Barabara ya Mtwara – Mingoyo mpaka Masasi, barabara ambayo ni sehemu ya barabara muhimu sana kwa Mikoa ya Lindi na Mtwara. Ni muda mwafaka sasa wa kuimarisha hospitali yetu ya Kanda ya Kusini ili chochote kikitokea basi kundi kubwa ambalo litakuwepo pale lipate huduma kwenye hospitali zetu za rufaa zilizopo Mtwara na Lindi, vilevile hospitali yetu ya rufaa ya kanda yetu ya kusini iliyopo pale Mitengo – Mtwara (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni muda mwafaka wa kuhakikisha kwamba huduma zote za msingi, huduma zote za kibingwa zinapatikana katika hospitali yetu ile ya kanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu wa pili ni kuhusu Hotuba ya Wizara ya Fedha ni kuhusu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante, kengele ya pili hiyo…

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, nakushukuru sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Nne na Mkutano wa Kumi na Tano, pamoja na Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Mbili na Mkutano wa Kumi na Tatu
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Ninampongeza Mwenyekiti kwa uwasilishaji wa taarifa yetu vizuri. Pia, ninaungana na wenzangu kuipongeza Serikali kwa jinsi inavyosimamia maagizo ambayo yanatolewa na Wizara. Kipekee naipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, ya Mheshimiwa Lukuvi, kwa kazi ambayo wanaifanya. Wamekuwa wakiratibu vizuri Wizara na taasisi mbalimbali kuja kwenye Kamati ili kujibu zile dosari au hoja ambazo zimeibuliwa na Kamati.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kipekee naipongeza Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kwa kazi nzuri ambayo wamekuwa wakiifanya. Kama alivyosema mchangiaji aliyepita, Makamu Mwenyekiti, kwamba huko nyuma kulikuwa na dosari kubwa sana, hivyo, nami mchango wangu utajikita kwenye Sheria Ndogo ambazo zinatungwa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, huko nyuma tulikuwa na changamoto kubwa sana, lakini kwa maboresho waliyofanya kwenye regional secretariat na kile Kitengo cha Huduma za Kisheria pale TAMISEMI na kule kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa unaona sasa kwamba kuna maboresho mazuri ambayo yanaonekana katika utunzi wa sheria ndogo na hivyo kupunguza dosari na madhara wakati wa utekelezaji wa sheria yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri kama inavyofahamika kwamba sheria zetu ndogo zinaanza kutumika kabla hazijaja Bungeni. Kwa hiyo, zikiboreshwa kule zinapunguza madhara kwa wananchi kwa sababu mwananchi wa kawaida anapoamka ofisi ya kwanza kwenda kupeleka malalamiko yake ni kwa Mkurugenzi wa Halmashauri au Mkurugenzi wa Jiji au Mkurugenzi wa Manispaa. Kwa hiyo, naipongeza TAMISEMI kwa kusimamia vizuri kitengo hicho na ni matarajio yangu kwamba wataendelea kukiboresha ili kiendelee kutoa huduma inavyotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu utajikita kwenye dosari ambazo zimeonekana kwa sheria ndogo ambazo hazina uhalisia. Mjumbe aliyemaliza kusema ametaja baadhi na mimi nitarejea kwenye Tangazo la Serikali Na. 220 na 217 ambazo ni sheria ndogo ambazo zilitungwa na Mtwara Manispaa. Kwa kweli kuna sheria nyingine ambazo zinatungwa zinakuwa kama adha kwa wananchi na hii tuliiomba hata TAMISEMI sheria kama hizo waweze kuziondoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sheria mojawapo, Mtwara Manispaa wameanzisha ushuru kwa ajili ya wapaa magamba ya samaki. Kwa kweli ushuru huu utakuwa ni adha kwa wananchi ambao wanafanya shughuli hiyo. Ukiangalia sana wanaofanya shughuli hiyo ni watu ambao hawana uwezo kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, halafu vilevile unapokusanya ushuru angalia kwamba tunatarajia kukusanya nini. Unakusanya shilingi 200; kwa sababu hata ukipiga hesabu ile roll ya karatasi ya kutolea EFD machine unapokusanya shilingi 200, nafikiri ile karatasi yenyewe ya risiti ina gharama kubwa kuliko kinachokusanywa. Pia, akina mama, vijana na wazee wanaoshughulika na upaaji wa samaki wanapata kipato kidogo mno. Sidhani kama halmashauri sasa zimefikia hatua hii ya kukosa vyanzo vingine, tuanze kukimbizana na wapaa samaki. Kwa hiyo, naomba ushuru kama huo ambao utakuwa adha kwa wananchi na ambao hauna uhalisia, basi tuuondoe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine nataka nichangie ni kwamba, kuna sheria ndogo ambayo imeanzishwa na Halmashauri ya Mtwara vilevile na Mufindi, kuhusu muda wa kukusanya ushuru. Muda wa kukusanya ushuru wameweka kuanzia saa 12.00 asubuhi mpaka 2.00 usiku.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa hivi hakuna uhalisia, kwa sababu sasa hivi kuna mabasi na kuna malori yanatembea usiku na mchana. Kwa hiyo, tusipokusanya ushuru huu, si kwamba haukusanywi, watumishi ambao siyo waaminifu wanaweza kutumia loophole hii wakachukua yale mapato badala ya kuyaingiza halmashauri, yakaingia kwenye mifuko yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mazingira ya sasa hakuna sababu ya kuweka kigezo kama hicho, kwamba ushuru wa halmashauri ukusanywe kuanzia 12.00 asubuhi mpaka saa 2.00 usiku. Ni matarajio yangu kwamba wanaweza kukusanya kwa muda wote. Sheria za utumishi wa umma zinasema mtumishi afanye masaa manane unaweza kuwa na shift ili ushuru huu ukakusanywa kwa manufaa ya halmashauri na si kama ilivyo sasa; kwamba inaweza kukusanywa usiku na watumishi ambao si waaminifu na ikaingia kwenye mifuko yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, huo ndio uliokuwa mchango wangu. Ninakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niungane na wenzangu kwanza kumpongeza Mheshimiwa Waziri Jerry Silaa kwa kazi kubwa ambayo anaifanya, hongera sana. Pili, nampongeza Mtendaji Mkuu wa Wizara hii Injinia Sanga kwa kazi kubwa ambayo anaifanya. Vilevile nawapongeza Wakurugenzi na Watendaji wengine katika Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa uteuzi ambao ameufanya. Wale ambao tunamwelewa Mheshimiwa Jerry Silaa, hatukushangaa kwa haya ambayo anayafanya. Mheshimiwa Jerry Silaa amekuwa Mayor wa Jiji la Dar es Salaam, na mengi ambayo yanafanyika leo Jijini Dar es Salaam ni mipango mizuri na mikubwa ambayo Mheshimiwa Jerry Silaa aliifanya, ambaye alishika umeya akiwa Mayor kijana kwa Afrika Mashariki. Kwa hiyo, ubunifu wake na ujasiri wake. Tunaona ujasiri wake kwa sababu hatukujua sisi kama kuna mapapa sita wa tasnia ya ardhi, lakini amewaleta hadharani. Amemchomoa papa mmoja baada ya papa mwingine. Vilevile na uzalendo wake, kwa sababu mengine angeyamaliza gizani tu lakini akaamua kuleta hadharani kwa manufaa ya nchi yetu. Si hivyo tu, na uthubutu, kwa sababu hivi vitu vinahitaji moyo wa uthubutu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, mimi nawapa moyo kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya. Macho ya Watanzania yanawaangalia na kila siku wanaombewa. Ndiyo maana kama alivyosema msemaji mmoja kwamba hata viongozi wa dini wanawaombea. Wameokoa mali za misikiti, wameokoa mali za makanisa, wameokoa mali za wanyonge na wanasimamia haki. Hongera sana na Mwenyezi Mungu atawalipa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa kwanza utahusu ikama ya watumishi wa sekta ya ardhi. Kazi hii nzuri ambayo inafanywa huku juu na Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Kamishna na watu wengine, matunda yake yanaonekana kwa uchache sana huku chini kwa sababu ya upungufu mkubwa wa watumishi wa sekta ya ardhi katika maeneo yetu. Nimepitia baadhi ya taarifa, ikama ya watumishi katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa kwenye kitengo cha ardhi ilitakiwa kuwe na watumishi wasiopungua watano. Kuwe na Afisa Ardhi, Afisa Mipango Miji, Mpima na Mthamini wa Majengo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Waheshimiwa Wabunge wote watakuwa mashahidi, katika maeneo yetu ni nadra sana kupata ikama kama hii. Kwenye Halmashauri yangu ya Mji wa Nanyamba tuna mtumishi mmoja tu kwenye kitengo hiki. Sasa migogoro inaanzia hapo, kwa sababu yeye hawezi akawa Afisa Ardhi wakati huo huo awe Afisa Mipango Miji, halafu achukue tape aende kuwa mpima na baadaye awe mthaminishaji. Kwa hiyo, naomba, ili kazi nzuri ambayo inayofanywa kule juu na Waziri na Naibu wake na watendaji wengine kule juu katika maeneo yetu ya upangaji, kwa mfano, kwenye mamlaka ya Serikali za Mitaa, basi Wizara hii ipewe kibali maalum ili watumishi wa kada ya ardhi waweze kuajiriwa na kupunguza hili tatizo lililopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi sasa ifanye msawazo. Pamoja na uhaba mkubwa uliopo kuna maeneo mengine watumishi wa ardhi wamelundikana, wako wengi, na ndiyo maana sehemu nyingine ina wachache, kwa hiyo, ni muda muafaka sasa waangalie staffing level katika mikoa yetu, katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa ili tuhakikishe kwamba na maeneo mengine tunapata watumishi wa kutosha ili mipango mizuri ambayo imetajwa, iliyowasilishwa na Waziri wetu, iweze kutekelezwa kwa umahiri na kwa ufanisi unaotarajiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili unahusu hii programu ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi. Ni mpango mzuri na ni mradi mzuri ambao unatekelezwa katika maeneo yetu. Hata hivyo, tumeona hapa kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri pamoja na Kamati, kwamba bado kuna halmashauri hawajarejesha fedha ambazo walikopeshwa. Fedha zilizopelekwa ni shilingi bilioni 50 lakini hadi sasa zimekusanya shilingi bilioni 23.7.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni mkopo ambao hauna riba, ni kama revolving fund. Zile halmashauri ambazo zimefanya vizuri tunawapongeza; na wameorodheshwa kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri, lakini zile halmashauri ambazo hawajarejesha, naomba TAMISEMI wasiwaachie Wizara ya Ardhi tu, washirikiane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri wa TAMISEMI kwa sababu alitoa tamko kwamba hadi tarehe 30 Juni hizi halmashauri ambazo hazijarejesha, basi wawe wamesharejesha, la sivyo, hatua nyingine zitachukuliwa. Kwa hiyo, naomba TAMISEMI na Wizara ya Ardhi watembee kwenye hili agizo lao ili wale ambao ikifika tarehe 30 Juni watakuwa bado hawajarejesha hizi fedha zikatwe moja kwa moja kutoka kwenye ruzuku zao ambazo wanapewa ili halmashauri nyingine waweze kukopeshwa na waweze kutumia katika mipango yao ya kuendeleza ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu mwingine unahusu mpango wa matumizi bora ya ardhi. Kwenye taarifa ya Waziri hapa amesema vizuri kwamba tuna vijiji 12,316 lakini vilivyopimwa ni vijiji 4,011, na kazi iliyobaki ni kwenye vijiji 8,305. Hapa nilikuwa natafuta fedha za kufanya kazi hii. Kwenye hii bajeti fedha hatuioni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naiomba Serikali, kama alivyosema mchangiaji aliyepita, tutafute fedha kwa ajili ya shughuli hii muhimu na nyeti. Fedha hii tukiipeleka Wizara ya Ardhi tunaipeleka mara moja. Uzuri tukishapima vijiji vyote 8,305 vilivyobaki hatutarejea tena kama madarasa au nyumba za walimu, kwamba baadaye zitachakaa na tutakarabati. Tukishatoka na mpango wetu wa matumizi bora ya ardhi, utakuwa huo unatumika kwa miaka hiyo yote, tutakuwa tunafanya maboresho madogo tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hiyo fedha ambayo inatakiwa takribani shilingi bilioni 125, naomba Serikali itafute mahali popote pale tuipe Wizara ya Ardhi ili kazi nzuri ambayo inafanywa na Waziri huyu mbunifu, Waziri mchapakazi, Waziri ambaye ana maono mapana, Waziri ambaye ana uthubutu, basi aweze kukamilisha kipindi hiki na aandike historia kwamba wakati wa uwaziri wake alikamilisha vijiji vyote 8,305 vilivyobaki. Hili linawezekana. Kama tumefanya hivyo kwenye Wizara nyingine, basi na Wizara hii ambayo ni nyeti, Wizara ya Ardhi, tutafute fedha ambazo zitakwenda kuleta matunda ambayo kwanza tutapunguza migogoro iliyopo sasa hivi kati ya wakulima na wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji vyetu tukipangilia vizuri na tukitengeneza mpango wa matumizi sahihi ya ardhi vijijini, hii migogoro ambayo ipo sasa hivi itapungua. Siyo hivyo tu, itakuwa rahisi wawekezaji watakapokuja tayari tutakuwa tumetenga maeneo mahususi kwa ajili ya uwekezaji na hivyo wawekezaji watapatra ardhi kwa kipindi kifupi na badala ya muda wanaoutumia sasa hivi kiutafuta ardhi kwa ajili ya uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Serikali hii kwa sababu ni Serikali sikivu na kwa kuwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameamua kuisimamia ipasavyo sekta hii ya ardhi, nina matumaini makubwa kwamba kama mwaka huu itakosekana, basi tuiweke kwenye mipango yetu ili mwakani fedha hizi zipatikane. Insha’Allah kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu Waziri Silaa bado ataendelea kuwepo kwenye Wizara hii, akamilishe kazi yake na kwa ubunifu wake basi atakuwa ameandika kitabu kizuri kwamba alipokuwa Waziri wa Ardhi amekamilisha upangaji wa vijiji vyote 12,516 vya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wa Mwaka 2016
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nachukua nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi, lakini nichukue nafasi hii kuungana na wenzangu kuipongeza Serikali kwa kuja na miswada hii miwili na mchango wangu utajikita katika muswada huu wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara Mkemia Mkuu wa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema naipongeza Serikali kwa kuleta muswada huu kwa wakati kwa sababu, Ilani ya Chama cha Mapinduzi inanadi kuwa na Tanzania ya viwanda na Tanzania ya Viwanda ina maana kwamba Maabara hii ya Mkemia Mkuu wa Serikali sasa itakuwa na majukumu mengi, lakini vilevile kutakuwa na biashara nyingi ya kemikali, kwa hiyo, kuletwa kwa muswada huu kutaifanya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kufanya kazi yake kwa ufanisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizitaje faida chache tu ambazo nimeziona baada ya kupitia muswada huu; faida ya kwanza kwamba sheria ambayo itawekwa sasa itabainisha waziwazi majukumu ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kama tulivyoona kwamba maabara hii huko nyuma ilikuwa ina-operate chini ya sheria kumi, lakini sasa kwa kuwa na sheria moja basi na ufanisi utaongezeka kwa sababu sasa majukumu ya Maabara hii ya Mkemia Mkuu wa serikali yamebainishwa kama ilivyo kwenye clause ile ya 8(1) yanatajwa majukumu ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, si hiyo tu, lakini sheria hii itampa nguvu sasa ya kisheria Mkemia Mkuu wa Serikali kukusanya vielelezo na sampuli pale majanga na malalamiko yanapotokea na hii huko nyuma alikuwa anafanya kwa discretion yake, lakini sasa kwa sababu itamlazimu kisheria basi hii itamwezesha kufanya kazi yake kwa ufanisi Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile sheria hii itawezesha kudhibiti taarifa za uchunguzi wa kimaabara, ili zisitolewe na vyombo au watu wasiohusika kwa sababu, tumeona hapa jinsi utoaji wa taarifa za uchunguzi wa kimaabara zitakavyodhibitiwa na sio kama kiholela ilivyokuwa inafanyika huko nyuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sheria hii ukisoma kile kifungu cha 3 unaona kabisa kwamba, sasa imeongeza uwajibikaji kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa sababu akiteuliwa hatakuwa wa kudumu, atafanya kazi hii kwa muda wa miaka mitano na kama performance yake itaonekana kwamba anaweza kuendelea atateuliwa tena, lakini kama hata-perform hataendelea. Sio kama ilivyo sasa kwamba mtu akipata uteuzi basi hiyo nafasi itakuwa ni ya kudumu. Kwa hiyo, hii itaongeza uwajibikaji na itamfanya Mkemia Mkuu wa Serikali a-perform na atembee na malengo yake ili baada ya miaka mitano apimwe kulingana na malengo yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile sheria hii inaiwezesha Serikali sasa kusimamia Maabara za Uchunguzi wa Kemia kwa sababu, sasa kutakuwa na usajili. Lakini sio usajili tu kwamba sheria hii sasa inampa Mamlaka Mkemia Mkuu wa Serikali kufuta zile maabara ambazo haziendeshwi kwa kufuata vile viwango ambavyo vimewekwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, si hivyo tu kwamba, sheria inasema sasa kwamba, kutakuwa na kanzi data ya vinasaba vya binadamu. Hii kama walivyosema wenzangu, itasaidia kupunguza malumbano katika familia kwamba mtoto ametokea mweupe unasema kwamba, aah, mimi ni Mmakonde au Mmwera, kwa nini huyu ametokea mweupe? Ile kanzi data itasema kweli kwamba, huyu mtoto wako ni wa kwako hata kama wewe ni Mmwera au ni kabila lingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na faida hizo nyingi ambazo nimezitaja sasa, naomba na mimi nitoe dosari ambazo nafikiri Mheshimiwa Waziri inabidi tuzifanyie kazi; kwanza, wakati wa kutengeneza kanuni au wakati tutakapofanya marekebisho. Kwanza niungane na wenzangu ambao wamezungumzia ile clause 7(2) kuhusu composition ya Bodi ya Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, Bodi hii ukiiangalia kuna wawakilishi wengi sana kutoka Wizara mbalimbali. Kuna Jeshi la Polisi, Afisa Sheria, Mwakilishi kutoka Utumishi wa Umma. Nafikiri sasa tuwaamini watumishi wetu, nimekuwa naangalia huyu mwakilishi kutoka Idara ya Utumishi wa Umma, anatafuta nini hapa?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu hapa nafikiri tulilenga kwamba watumishi wakifanya makosa. Tusiwatege watumishi kwamba wanaenda kufanya makosa. Tuwe na positive thinking kwamba watu wetu watatenda kama yale waliyopangiwa na yupo Afisa Sheria hapa anaweza kushawihi yale masuala ya kinidhamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naona huyu mwakilishi kutoka Idara Kuu ya Utumishi hana nafasi katika bodi hii, bodi hii ya kitaalam, tuwaache wataalam wafanye kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ningependekeza hapa tumuweke mwakilishi kutoka sekta binafsi. Kuna watu wanafanya biashara hii ya kemikali, lakini kuna watu wana-run maabara binafsi, kwa hiyo, tuteuwe wawakilishi kutoka kule na tutapata inputs ambazo zitasaidia katika kuendesha bodi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu nyingine ambayo ninashauri kwamba tuangalie kwa kina zaidi kwa sababu naona kama ni dosari ni ile clause 16(4) ambayo inasema, mamlaka haitawajibika na mabadiliko yoyote ya muonekano au mabadiliko ya sampuli yanayoweza kujitokeza wakati na baada ya uchunguzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, huku ni kukwepa uwajibikaji, lakini pili hii inalinda watumishi wazembe na watumishi ambao sio waadilifu. Tumeona mara nyingi sampuli zikibadilishwa kwa hiyo, hapa napendekeza tufanye mabadiliko ili watu wawajibike kwa yale yatakayotokea, lakini tukiweka clause hii ina maana tunalinda uzembe, lakini vilevile tunafifisha uwajibikaji katika taasisi yetu hii mpya ambayo tutaianzisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile naona kuna dosari katika ile clause 15(2), majukumu na mamlaka ya wachunguzi. Hapa inasema kwamba kuchukua kitu chochote au mali iliyotumika katika kutenda makosa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili neno kitu chochote, kwa kweli, hapa tuwe waangalifu sana kwa sababu tumeona mara nyingi kwamba mtu anaenda kufanya assignment fulani akachukua vitu vingine ambavyo havihusiki. Kwa hiyo, tutape proper definition ya kitu chochote au tutakapoandaa kanuni tuwe na angalizo hili kwamba kitu chochote isiwe kitu chochote, kiwe specific kwa yale mambo ambayo yanahusika na lile tukio ambalo limetokea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie mchango wangu kwa kutoa ushauri kwamba kama ilivyosemwa na wenzangu pale nyuma kwamba sheria hii inayotarajiwa kutungwa ni nzuri, lakini inaweza kuchelewa kuanza kutumika kwa sababu tu ya Waziri mwenye dhamana kuchelewa kutayarisha kanuni. Kwa hiyo, nakuomba sana, najua dada yangu Mheshimiwa Ummy ni mchapakazi na ni baada ya muda mfupi kwamba, utakuja na kanuni. Kwa hiyo, nakuomba sana kwamba hii utembee nayo, timu imetimia hapo nakuona Mheshimiwa Ummy, Mheshimiwai Dkt. Kigwangalla, wote mna-fit katika nafasi zenu. Baada ya muda mchache tuone kanuni zimetoka na sheria hii ikisainiwa basi tuone inafanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu wa pili ni kuhusu tutakapotayarisha kanuni tusi-underrate zile maabara nyingine ambazo zipo, kuna forentsic lab zile ambazo ziko polisi, yaani, tusitengeneze kanuni zikaonekana kwamba hii Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa sababu tumesema itakuwa final, tuka-underrate hizi nyingine. Kuna maabara ambazo zinashughulika na specific issues kama hii ya polisi, hii tuipe hadhi yake na matokeo yake bado yaendelee kuthaminiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na ninaunga mkono hoja. Ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari za Mwaka 2016
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Muswada huu uliopo mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Waziri, kaka yangu Mheshimiwa Nape na Naibu Waziri Mheshimiwa Wambura kwa jitihada zao ambazo zimewezesha leo kuwasilisha Muswada huu ambao umechukua takriban miaka 20, bado unasuasua tu. Kwa hiyo, nawapa pongezi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nichukue nafasi hii pia kuwapongeza watendaji wa Wizara ambao kwa njia moja au nyingine wameshiriki katika maandalizi ya Muswada huu. Kipekee nimshukuru na nimpongeze Mwenyekiti wa Kamati ambayo amechambua Muswada huu. Kulikuwa na maneno mengi kwamba Serukamba sasa amekuwa upande wa Serikali lakini alisimama imara kuhakikisha kwamba kazi ya Kamati inatekelezwa na hatimaye kuja na maoni na mapendekezo ambayo yatasaidia sisi Wabunge kupitisha Muswada huu. Kwa hiyo, nakupongeza sana Mwenyekiti wa Kamati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hofu nyingi sana na maneno ya upotoshwaji ambayo yalienea mitaani. Kuna watu walikuwa wanasema kwamba ukikutwa na kipande cha gazeti tu ambacho kina habari za uchochezi basi wewe umetenda kosa kitu ambacho Muswada hausemi hivyo. Watu wengine walikuwa wanaeneza kwamba Muswada huu haufafanui maana ya mwandishi wa habari kinyume na maelezo ya Muswada.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona kabisa kuna ufafanuzi kwamba nani mwandishi wa habari na nini kitafanyika ili mwandishi wa habari aweze kuthibitishwa. Vilevile kuna upotoshwaji ambao ulienezwa kwamba TV zote kuna muda zitaambiwa kwamba zitangaze habari za Serikali ukiupitia Muswada huu mpaka mwisho kitu kama hicho hakipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uandishi wa habari sasa unataka kuwa taaluma kama ilivyo taaluma nyingine, kwa hiyo, lazima uwekewe professional code of conduct. Profession zote zimewekewa standards kwa nini uandishi wa habari uachwe hivi hivi? Ukiangalia kifungu cha 10 cha Muswada huu kinaeleza wazi kabisa kwamba nini kinaanzishwa kwamba kutaundwa Bodi ya Ithibati. Hizi bodi kama walivyosema waliotangulia siyo kitu kipya, profession zote ualimu, uhandisi, udaktari, kuna kitu kama hicho na hata kada kama hizo kuna register na ndio maana wanasema kutakuwa na orodha ya wanahabari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye profession ya ualimu kwa sababu mimi ni Mwalimu licha ya kuhitimu kwenye vyuo vyako unaandikisha na unapewa namba, wale Walimu wenzangu wanafahamu kuna TSD namba, unaorodheshwa na unapewa namba, kila Mwalimu ana namba yake. Kwa hiyo, ndiyo kama orodha hii itatumika kwa wanahabari kwamba lazima tuwe na orodha ya wanahabari. Kwa hiyo, sio kitu cha kusema kwamba wanahabari wananyanyaswa, wanahabari sasa wanathaminiwa kwa sababu watakuwa na orodha yao ambayo itatambuliwa kisheria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 18 kinaeleza wazi majukumu ya bodi na ukisoma kifungu kidogo cha kwanza unaona kabisa kwamba sasa waandishi wa habari sio kila mtu atakuwa mwandishi wa habari. Anasema mtu hataruhusiwa kufanya kazi ya uandishi wa habari isipokuwa kama mtu huyo amethibitishwa na sheria hii. Kwa hiyo, siyo kila mtu akiamka asubuhi atakuwa mwandishi wa habari na hii itasaidia sana kujua kwamba nani mwandishi wa habari na nani amerukia gari ya uandishi wa habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge tuupitishe Muswada huu ili hata sisi tutakapofanya shughuli zetu tujue kwamba tunaofanya nao kazi ni waandishi wa habari, kuna wengine wanachafua hii profession ya uandishi wa habari kwa sababu wao sio wanataaluma ya uandishi wa habari lakini wameingia tu kwenye uandishi wa habari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile wanasema kwamba atakuwa amethibitishwa na imeelezwa wazi tu kwamba atakuwa amethibitishwa na bodi na kwa utaratibu ambao utaainishwa na kanuni. Sasa kuna watu wanalalamika kwamba Waziri ana mamlaka makubwa sana, hakuna sheria ambayo haimpi Waziri mwenye dhamana ya hiyo sekta kuandaa kanuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hapo lazima Waziri aandae kanuni ambayo itasaidia kuandikisha hao waandishi wa habari. Hayo sio madaraka makubwa ya Waziri ni kuhakikisha kwamba ana dhamana katika sekta hiyo na anasimamia vizuri kwa sababu tusiseme tu kwamba hapa Mheshimiwa Nape atakuwa Mhariri Mkuu hapana, ni Waziri mwenye dhamana leo yupo Mheshimiwa Nape kesho atakuja mwingine kwa hiyo tusi-personalize hiki kitu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu Muswada unatekeleza matakwa ya Sera yetu ya Habari ya mwaka 2003 ambayo inatamka wazi kabisa na inaitaka Serikali kuanzisha chombo huru kitakachosimamia masuala ya habari. Huu mwaka 2016 miaka takriban 13 sera imetamka hivyo na sisi bado hatujaunda, sheria hii sasa inaunda Baraza la Habari. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwamba mfupa ambao umeshindikana huko nyuma ameweza sasa kutekeleza sera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana kuna watu walisema waandishi wa habari ni passion lakini hayo maneno siku za nyuma yalisemwa na watu wengine kwamba ualimu ni wito na Walimu sasa hivi wanakataa wanasema ni profession kama zilivyo profession nyingine. Uandishi wa habari ni profession na kila profession kuna profession code of conduct, kwa hiyo, tuache uandishi wa habari kuwa profession. Unakuwa na profession code of conduct halafu ndiyo inafuata passion lakini huwezi ukaanza na passion ukasema kusiwe na profession code of conduct. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uki-check ukurasa wa 14 wa hotuba hii ya Kambi ya Upinzani inasema Serikali imeamua sasa kuja na aina ya waandishi wa habari ambayo inawataka. Jamani ku-define kwamba mwandishi wa habari awe na sifa hizi sio matakwa ya Serikali ni wakati wa sasa hatuwezi kuwa na watu ambao hawajawa defined kwamba mwandishi wa habari awe na sifa gani ya elimu na hiyo ni standard za kidunia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, si kweli kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi inataka kuleta waandishi wa habari ambao inawataka, ni matakwa ya mabadiliko ya dunia lazima tuseme kwamba mwandishi wa habari minimum qualification ya elimu iwe kiasi gani. Kwa hiyo, hapa tuna-set standard na hiyo siyo ya CCM ni suala la wakati wa sasa na mabadiliko ya kidunia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme tu naunga mkono hoja na Mheshimiwa Waziri nikushauri tu kwamba sheria hii ambayo tutaipitisha muda siyo mrefu basi usichukue muda mrefu kutoa kanuni zake ili iweze kutekelezwa kwa urahisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja.
The Finance Bill, 2022
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kunipa nafasi ya kuchangia Muswada huu wa Fedha.

Mheshimiwa Spika, mimi nitajielekeza sehemu ya tano ambayo inazungumzia mabadiliko atakayofanya kwenye sheria ya tasnia ya korosho.

Mheshimiwa Spika, nataka nikurejeshe kule nyuma ambapo kabla hatujafanya mabadiliko ya 2017/2018 sehemu hii tulikuwa na sheria ambayo ilikuwa inatamka wazi kwamba fedha ambazo zitakusanywa kwenye export levy asilimia 65 ilikuwa inakwenda kwa ajili ya kuendeleza zao la korosho na asilimia 35 ilikuwa inakwenda Mfuko Mkuu wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza niipongeze Serikali kwa uamuzi huu wa kurejesha hii asilimia 50 kwa sababu ilikuwa ishaondolewa kabisa. Lakini nipongeze kwa hatua iliyofikiwa sasa hivi ambayo sasa tuna asilimia 50 inaenda Wizarani kwa ajili ya kuendeleza zao la korosho kupitia Mfuko wa ADF na asilimia 50 itakwenda kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu ni huu, kwamba zao la korosho linahitaji uwekezaji mkubwa sana. Utafiti ambao umefanywa na TARI - Naliendele unaelezea wazi kwamba kukiwa na ongezeko la matumizi ya pembejeo basi uzalishaji unaongezeka na mfano halisi ni msimu wa mwaka 2017/2018 ambapo Serikali ilithubutu kutoa tani 23,000 za Sulphur na tulifikisha tani 314,000, kiwango ambacho hatujawahi kufikia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulivyoondoa hizi fedha za export levy uzalishaji uliporomoka kwa miaka mitatu. Lakini kwa mapenzi mema ya Mama, Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alivyotoa pembejeo mwaka jana za korosho bure, mwaka jana uzalishaji uliongezeka kwa tani 40,000 na ndiyo maana tumefikia tani 240,000. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sehemu hii mimi naishauri Serikali kwamba, cha kwanza hizi fedha zisemwe kabisa categorically, kwamba zinakwenda Wizarani kwa ajili ya ununuzi wa pembejeo na shughuli zingine zinazohusiana na zao la korosho. Kama nilivyosema korosho inahitaji pembejeo, korosho inahitaji utafiti, korosho inahitaji kujiwekea malengo kwamba sasa tuingie kwenye ubanguaji. Kuna wabanguajia wadogo ambao wanahitaji kusaidiwa. Lakini korosho inahitaji usimamizi, Maafisa Ugani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Bashe alitoa pikipiki na vifaa vya kufanyia kazi kwa Maafisa Ugani. Sasa, tukipeleka hizi fedha za export levy kiasi kidogo basi wale Wagani wanaoshughulikia zao la korosho watafanya kazi kwa umakini zaidi na kwa ufanisi mkubwa zaidi.

Mheshimiwa Spika, korosho sasa hivi inazalishwa kwenye mikoa 17, na ndiyo maana tunaomba sasa kwamba hii asilimia 50 ieleze waziwazi kwamba inakwenda Wizara ya Kilimo lakini itaenda kwa shughuli za kilimo. Vilevile, kwa sababu kuna mfuko mpya huu wa kuendeleza kilimo (ADF), tunapendekeza sasa asilimia 15 nyingine itoke kwenye export levy ikapeleke kwenye mfuko huu mama ambao kama tulivyosema kwamba tunakusudia kwenda mapinduzi ya kilimo. Kwa hiyo, hapa mapendekezo ambayo ninaishauri Serikali ni kwamba turudi kwenye kiwango kilekile cha zamani asilimia 65, asilimia 60 iende kwenye korosho kwa maana pembejeo, utafiti na mambo mengine. Asilimia 15 iende kwa ajili ya Mfuko wa Kuendeleza Kilimo (ADF).

SPIKA: Mheshimiwa Chikota hebu tusaidie kidogo, kwa sababu ndiyo tuko tunaangalia hapa na hayo marekebisho yaliyopendekezwa. Hii export levy ni nani anayelipa? Ni mkulima au ni yule anayepeleka korosho nje? Nani anayelipa export levy?

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, export levy analipa mnunuzi lakini…

SPIKA: Ngoja ngoja, analipa mnunuzi wa korosho siyo mkulima?

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, mnunuzi wa korosho siyo mkulima.

SPIKA: Hiyo ni ngazi ya kwanza. Umesema hapo kwamba Mheshimiwa Rais mwaka jana alitoa Sulphur bure.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, ndiyo.

SPIKA: Hizo fedha zilitokana na export levy au hapana?

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, hapana hizo fedha ni kwa uamuzi wake tu kwamba anataka kutoa…

SPIKA: Ahaa hazikutokana na export levy?

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, haikutokana na export levy.

SPIKA: Haya ahsante.

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, sasa nataka nitoe ufafanuzi hapo kwamba pamoja na kwamba anatoa mnunuzi, lakini mnunuzi anapokwenda sokoni anajua kwamba baadae atatoa kiasi kwa ajili ya export levy kwa hiyo, hata ile fedha ya sokoni anapunguza. Kwa hiyo, utakuta anayeathirika zaidi pale ni mkulima.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa sababu hiyo ninashauri, kwamba ukiwekeza fedha kwenye pembejeo basi uzalishaji utaongezeka na Serikali itapata fedha zaidi. Kwa hiyo, naomba hii asilimia 50 tuipeleke kwenye korosho, asilimia 15 tupeleke kwenye Mfuko wa Kuendeleza Kilimo (ADF) kwa hiyo, itakuwa jumla 65 na Mfuko Mkuu wa Serikali iende asilimia 35.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)