Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. Jasmine Tiisekwa Bunga (3 total)

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi katika Bunge lako hili Tukufu. Kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama na kuongea, nilikuwa naendelea ku-observe majadiliano yanavyokwenda.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu na kumpongeza sana Mheshimiwa wetu Rais kwa jinsi anavyopambana katika kuondoa umaskini, kupambana na rushwa, mafisadi na kadhalika ili kuona kwamba sasa nchi yetu itafikia mahali ambapo ile keki itagawanywa mpaka kule kwa wanyonge. Pia nichukue nafasi hii kumpongeza mama yetu Mheshimiwa Samia kuwa mwanamke wa kwanza kuongoza Taifa hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kazi tunaiona, nawapongeza Mawaziri wote kazi zetu tunaziona na mnatosha lakini pia kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge kwa kurudi mjengoni na wengine mara yetu ya kwanza kama hivi. Niwapongeze wapiga kura wangu wa Mkoa wa Morogoro pamoja na wanawake UWT Taifa kwa kuniamini kuweza kuwawakilisha bila kusahau support ninayoipata kutoka kwa familia yangu ikiongozwa na mume wangu mpendwa Profesa Tisekwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, napenda sasa niweze kuchangia hii bajeti. Nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha pamoja na timu yake yote akiwemo Mheshimiwa mdogo wangu Dkt. Ashatu Kijaji, nafahamu uwajibikaji wake na weledi wake, kwa hiyo nawapongeza sana. Bajeti hii inaleta matumaini hasa kwa kutenga asilimia 40 kupeleka kwenye masuala ya miradi ya maendeleo, hongereni sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naungana na wajumbe wote ambao wamejadili suala hili hasa kwa kuwapongeza jinsi walivyopanga mikakati ya kuweza kukusanya kodi na kuongeza wigo wa kodi, nawapongeza sana. Pia nashauri sasa tuangalie zile kero ambazo zinaambatana na kodi na tozo za aina fulani ambazo wananchi bado wanazilalamikia kama Serikali muweze kuangalia kwa undani na kwa macho mawili ili kuondoa misuguano ambayo inaweza ikatokea kati ya Serikali na wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nichangie kwa kusema kwamba sasa hivi Watanzania sera yetu ya maendeleo tunaelekea kwenye uchumi wa viwanda baadaye kufikia uchumi wa kati. Viwanda peke yake bila ya kuwa-empower wananchi wake hasa wananchi waishio vijijini haviwezi vikawa endelevu. Kwa nini nasema hivyo? Ni lazima tuweze ku-empower maendeleo vijijini na kwa wananchi wa vijijini kwa sababu asilimia 75 ya wananchi wako vijijini, rasilimali nyingi za Taifa zipo kijijini, nguvu kazi ipo vijijini lakini umaskini uliokithiri upo vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kuna sababu zote za msingi kuhakikisha miradi hii ya maendeleo ambayo imeelekezwa vijijini zile fedha ambazo zimepangwa basi fedha hizi zote zipelekwe ili kuendeleza vijiji vyetu. Tukifanya hivyo tunaweza sasa kuwa-empower hawa wananchi wetu na kuweza kuwa na purchasing power kwa sababu ukiwa na kiwanda parameter mojawapo lazima ku-create soko la ndani na la nje. Kama watu wako ni maskini ina maana hivi viwanda sustainability yake kidogo inaweza ikawa kwenye question mark. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuangalie suala la usawa wa kijinsia. Miradi ambayo imeelekezwa kule vijijini au mijini ile yote ambayo imelenga kupunguza matatizo ya wanawake (reproduction roles zao) mfano maji, afya, elimu na kadhalika ipewe fedha kama ilivyokuwa imepangwa. Kama tunavyoona 51% ya population ya Tanzania ni wanawake, ukiwaacha watumie saa tabi au sita kwenda kuchota maji, kuhangaika kwenda kwenye kituo cha afya hawataweza kushiriki katika uzalishaji. Kwa hiyo, huyu mwanamke ili aweze kuwa productive kwa sababu wako wengi na waweze kujikwamua kiuchumi tufikie ile fifty fifty mwaka 2030, lazima hawa wanawake wapunguziwe ile mizigo ya reproduction roles. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda nizungumzie suala la shilingi milioni 50. Hii shilingi milioni ya kila mtaa naona kwamba imeelekezwa sana kwa wajasiriamali na SACCOS. Mimi naona hii approach tunayoitumia siyo sahihi sana kwa sababu tunasahau hili kundi la maskini wa kipato cha chini watakuwa hawana msaada.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini Sh. 5,000 inaweza ika-transform maisha ya huyu maskini ambaye hana kitu. Kwa sababu kule kijijini huyu mtu maskini wa kipato cha chini ambao wanaishi under poverty line kwa mfano anaweza akawa na nguvu, yupo physically fit, ana ardhi lakini hana jembe, hana mbegu. Kwa hiyo, huyu mtu ukamkopesha Sh. 5,000 akanunua mbegu, akanunua jembe that means next season tayari umeshamwezesha lakini sasa tukijikita kwenye wajasiriamali tukawasahau hawa, hatutafika mbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine nasema sasa ili kupunguza milolongo ya kodi na tozo kwa wananchi wetu tutumie rasilimali zetu kwa mfano utalii, madini na kadhalika. Sisi kule Morogoro (Kisaki) tuna hot spring eneo kubwa, kilometers and kilometers lakini halitumiwi. Kwa mfano, ukienda Swaziland walikuwa na ka-spot kamoja ka hot spring wamejenga pale hoteli, swimming pool, hela zinatengenezwa. Sisi kwetu ukienda kwenye zile hot spring unakuta vibanda vya waganga wa kienyeji vimejazana pale. Kwa hiyo, tutumie rasilimali zetu ili tuweze kupunguza hizi tozo ambazo mara nyingi ni kero kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Kitengo cha Monitoring and Evaluation lazima kipewe kipaumbele kwa sababu on desk work mtu anakuja anatengeneza mikakati bila research, tathmini, hatutafika mbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nizungumzie upande wa environment. Sikubaliani na kusema mifuko ya plastic sijui microns 50 sijui nini, nashauri ipigwe marufuku, inailetea hasara Taifa letu. Mafuriko haya mengi ukiangalia ni kwa sababu ya mifuko ya plastic. Huyu mzalishaji mwenye kiwanda anapata super profit lakini Serikali inapata super loss kwa sababu kila mwaka lazima itengeneze miundombinu ya barabara, umeme na kadhalika. Kwa hiyo, mimi naona hapana, ikatazwe kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwisho napenda nimalizie kwa kusema kwamba, mimi nashangaa sana, Waheshimiwa Wabunge, wachumi, wasomi na kadhalika kazi yao kusimama kwenye media na kubeza Serikali. Hii bajeti tunayoipitisha ni ya Serikali lakini kila Mtanzania lazima awe na bajeti yake ku-top up kwenye bajeti ya Serikali. Mimi nashangaa kwa mfano ukienda Bangladesh, Profesa Yunus alichukua dola zake 27 kwa kila mwanamke wale waliokuwa wanatengeneza furniture mpaka ikazaa Grameen Bank ambayo na yenyewe ikazaa na vingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii Profesa mzima aliyebobea anaenda eti kwenye media kuanza kulaumu Serikali, wewe Mbunge unasimama unalaumu Serikali eti mpaka nipewe nafasi ya kwenda Ikulu, wewe role yako ni nini kama Mbunge, kwa sababu wewe ni kiongozi! Wewe role yako ni nini kama Profesa kwa sababu wewe ni kiongozi, wewe role yako ni nini kama mwananchi wa kawaida kwa sababu sasa hivi mpaka Mheshimiwa Rais aende akawafanyie watu usafi kwenye kaya zao, inakuja hiyo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi nasema bajeti ya Serikali lazima iwe supported na sisi wananchi kwa umoja wetu. Watu hapa ni mabilionea badala ya kuweka hela benki chukueni hizo pesa wagawieni kama alivyofanya huyu Profesa Yunus wa Bangladesh kwa riba nafuu. Kwa sababu bajeti ya Serikali hata siku moja haiwezi kutosheleza kuleta maendeleo ya nchi yetu, ni sisi. Vita dhidi ya umaskini ni vita na kila mwananchi lazima awe askari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nasema, naomba bajeti hii fedha zipatikane ili kuweza kuleta maendeleo. Naunga mkono hoja, ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Mapendekezo ya Mpango huu unaoendelea. Kwanza kabisa, napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha pamoja na timu yake yote kwa kutuletea huu mpango mapema zaidi ili tuweze kuufanyia kazi, uboreshwe na baadaye tuweze ku-achieve yale ambayo tunatarajia kuyafanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kumpongeza sana Mheshimiwa wetu Rais wa Awamu hii ya Tano kwa nia njema kabisa ya kutaka kuleta maendeleo ya nchi hii hasa ukiangalia kwamba anataka keki ya Taifa igawanywe kuanzia kwa mwenye kipato cha chini mpaka mwenye kipato cha juu. Kwa hiyo, jitihada nyingi sana anazifanya na tukizingatia kwamba yeye ndiyo mara yake ya kwanza kushika uongozi ni lazima kutatokea changamoto za hapa na pale. Kwa mfano, anapambana na ufisadi, rushwa, wafanyakazi hewa, matumizi mabaya ya Serikali na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachotokea sasa hivi kwa mtazamo wangu, watu wanalaumu wanaona kwamba it is a government failure, kwangu mimi sioni kwamba Serikali imeshindwa, ni muda mchache, hapa tupo kwenye transitional period, kwamba kuna reforms nyingi zinafanyika ili tuweze ku-achieve haya ambayo Mheshimiwa Rais wetu anayataka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika change ya aina yoyote huwa kuna early adapters, slow adapters na late adapters kwamba wapo wale wanaokubali mabadiliko haraka sana na wapo ambao tayari wanampongeza Mheshimiwa Rais, hawa ni wale wanyonge ambao haki zao hazitolewi. Hata hivyo, wapo wale ambao wanakubali taratibu tunawaita slow adapters, hawa wanaangalia kwanza mazingira wajiweke sawa, lakini kuna wale late ambapo yeye anasubiri kwanza mambo yafanikiwe ndiyo aende.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kinachotokea kutokana na change, wale wanaolaumu inawezekana ni katika kundi la wale watu ambao ni mafisadi, wala rushwa ndio wanamkwamisha Mheshimiwa Rais wetu. Kwa hiyo, hawa kwa vyovyote hawawezi kukubali hizi reforms ambazo zimepangwa ili tuweze ku-achieve kwamba sasa keki ya Taifa wafaidi wananchi kuanzia wa kipato cha chini mpaka kipato cha juu. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi anayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu ni kwamba sasa tumpe support kwa sababu kila utawala mpya lazima utakuwa na changamoto zake. Yeye ni mara yake ya kwanza. Tukianza hata kihistoria Mwalimu Nyerere wakati amepokea utawala kutoka kwa wakoloni alipambana sana kwenye ujamaa na wapo watu ambao walikuwa ving’ang’anizi ndiyo wakatuletea hata huu ujinga ujinga wa structural adjustment ambayo hailingani. Kwa hiyo, alipambana na watu wengine walikataa kwa sababu ya maslahi yao, tuliwaona kina Kambona walikimbilia nje, ndiyo hiyo hiyo ambayo inatokea sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija upande wa Mheshimiwa Mstaafu Rais Mwinyi, watu walimuita ruksa lakini kutokana na mazingira aliyoyakuta wakati ule, bidhaa hamna akafungulia. Kwa hiyo, ni kama vile tunavyosema kila zama na kitabu chake. Pia ukiangalia wakati wa Mheshimiwa Mkapa watu waliita ukata lakini mwaka wa kwanza aliyumba baadaye mambo yakaenda, vizuri sasa hivi tunamkumbuka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija upande huu wa Mheshimiwa Rais wetu aliyestaafu juzi, Rais Kikwete, wengi wakasema labda mpole lakini alifanya mambo makubwa lakini mwanzoni alivyoanza watu wakaona haendi. Sasa na hii Awamu ya Tano, hizi reforms jamani nani anayetaka ufisadi uendelee au rushwa iendelee, wafanyakazi hewa, tunapoteza fedha bure, ndiyo hiki kinachofanyika. Kwa hiyo, tumpe support Mheshimiwa Rais wetu afanye kazi na sisi Watanzania ndiyo tunaotakiwa tumuunge mkono badala ya kumbeza na kuibeza Serikali. Nafikiri hii siyo vizuri kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande sasa wa mpango, naomba nichangie kuhusu viwanda. Sera ya viwanda ni nzuri lakini tuangalie, je, Tanzania sasa hivi tunataka viwanda vya aina ngani? Kwa sababu sasa hivi tukumbuke tuko kwenye utandawazi, ni free market, tusije tukatengeneza kiwanda ambacho tunategemea labda soko la ndani tuko karibu milioni 50 labda consumers ni milioni 20, kwa hiyo soko la ndani halitoshelezi. Tufanye utafiti na soko la nje, siyo kwamba viwanda ili mradi viwanda. Nia ya viwanda ni kuajiri watu wengi mbali ya production, kwa hiyo, tuhakikishe tunaanzisha viwanda vile ambavyo vitawalenga hawa watu wetu wa chini waweze kupata ajira hasa vijana wetu wanaomaliza vyuo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kuna hili suala la kodi na tozo nyingi. Niungane na wenzangu, jamani sasa wasi-take advantage ya Serikali kukusanya kodi, kufanya mauzauza huko kuiharibia Serikali na ndiyo kinachofanyika sasa hivi. Kwa hiyo, tunaomba sana Waziri aliangalie suala hili, zile kodi na tozo ambazo ni kero kwa wananchi ziondolewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ukienda kwenye mabenki kwa mfano CRDB, jamani ukitaka statement ya karatasi moja ni Sh.11,000/= hivi kweli! Ile si ni ku-print out tu kwa nini wasitoze hela kidogo lakini sasa watu wanatengeneza business. Sasa hivi ukitumia ile mashine ya CRDB labda umeenda kununua kitu wanakata asilimia tano ya value ya kile kitu ulichonunua. Kama ni shilingi milioni tatu asilimia tano ya milioni tatu inakatwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni wizi kwa sababu wewe ni mteja wao lazima wakupe hizo fursa, wachukue hata elfu moja kama vile unavyochukua kwenye ATM, kwa hiyo hizi ni kero. Hata parking fee hizi za magari jamani kwa siku mtu akipaki Sh.1,000x30 ni Sh. 30,000, Sh. 30,000x12 ni Sh. 360,000 hiyo ni mbali na tax nyingine ambazo tunalipa. Kwa hiyo, kodi kama hizi ziangaliwe either zitolewe au zipunguzwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ni emphasize kwenye maendeleo vijijini, hii ni area yangu maendeleo vijijini. Huwezi ukawa na uchumi wa kati bila ya kuwa-empower hawa watu wa vijijini. Kwa hiyo, naomba miradi ya maendeleo ile iliyoachwa 2014/2015, 2015/2016 ipewe kipaumbele ili ile continuity ya kuleta maendeleo na ile Tanzanian vision iweze kuwa achieved. Tukiiruka ile tukaanza na hii mipya hatutaweza kufika kule, programu zetu zitakwama. Kwa hiyo, ni-emphasis tuangalie vitu ambavyo ni mahitaji ya msingi vijijini kama vile maji, elimu, barabara na masoko kwa ajili ya mazao yao. Tuki-promote hivi naamini kabisa huu uchumi wa viwanda na kipato cha kati utafanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme pia kitu kingine, tusi-undermine human capital, ili tuweze kupata maendeleo lazima tuwekeze kwenye capacity building. Kwa hiyo, hizi semina za ndani na nje ni lazima hawa washiriki kwa sababu kwa dunia hii ya utandawazi ya sasa hivi kuna new technologies, new skills, new approaches concept ili tuweze kuingia kwenye hili soko la dunia na sisi tuweze ku-compete. Otherwise tukiangalia tu miradi tukasahau kwenye human capital itakuwa ni shida sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kweli naipongeza Serikali, napongeza Mapendekezo ya huu Mpango ambao umeletwa ili tuyafanyie kazi, tuboreshe badala ya kubeza na kudharau, hapana, huu ni mwanzo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Fedha azingatie haya maoni ambayo wachangiaji mbalimbali wanatoa, yale ambayo tunaona kweli yanafaa ili kuboresha huu mpango na hatimaye nchi yetu iweze kufikia maendeleo endelevu ifikapo 2030.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. JASMINE T. BUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii. Pamoja na kwamba dakika ni tano lakini mimi kama Mjumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii sitaacha kuipongeza Serikali yangu pamoja na Mheshimiwa Waziri kwa juhudi kubwa walizozifanya kwa muda mfupi katika kuboresha huduma ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli tumejionea, ukiangalia pale Ocean Road akina mama wengi wanafariki kwa sababu ya cancer lakini kumeboreshwa kwa hali ya juu. Sasa hivi kusubiri mionzi sio miezi mitatu ni wiki sita na tunaelekea wiki mbili, huduma ya dawa kutoka asilimia nne mpaka asilimia 60 bado vifaa vya kupima pamoja na PET Scan ambayo itapunguzia gharama Serikali lakini pia kuokoa maisha ya Watanzania hususan wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri atusaidie Mkoa wetu wa Morogoro, ni mkubwa sana tuna Wilaya nane, lakini Hospitali za Wilaya ni chache sana. Kwa hiyo, ili kupunguza vifo vya akina mama inabidi kwa kweli uliangalie suala hili ingawa kwako inakupa shida sasa inabidi uende TAMISEMI ndiyo maana tulisema kama inawezekana Waziri wa Afya ashuke mpaka chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nijikite kwenye Idara ya Maendeleo ya Jamii. Idara hii inachukuliwa kama kitu ambacho hakina umuhimu na mpaka kuna viongozi wa kitaifa wakisimama wanasema hawa walioajiriwa hawaoni kazi yao, lakini wanasahau kwamba Idara ya Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii ndio engine ya maendeleo katika nchi yetu. (Makofi)

Sasa hivi Tanzania wananchi hawaelewi, hamna mtu wa kuwaunganisha wananchi na Serikali yao, utakuta wanaunganishwa na wanaharakati. Mwanaharakati hata siku moja haisaidii Serikali, kazi yake ni kukosoa lakini hawa Community Development Officer na Social Workers ndio kiini na ndio hasa engine ya maendeleo. Kwa hiyo, tunaomba hii fedha sasa iliyotolewa itolewe yote muende kufufua sekta hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, watu wanafikiri kwamba uchumi unaletwa na wanauchumi na sayansi asilia, siyo kweli. Baada ya industrial revolution watu walipata social problem nyingi, wana-commit suicide, wanatumia dawa za kulevya, family breakdown, watoto wa mitaani, maadili, sisi tunabaki kupiga makelele lakini kazi kubwa ni hii ya Idara ya Maendeleo ya Jamii. Tukiweza kuiboresha wao ndio wanaotafuta solutions kwamba wafanye nini katika jamii yao. Utakuta sasa hivi hata barabara ikiharibika wanasubiri Serikali, kujenga vyoo wanasubiri Serikali kwa sababu hakuna mtu wa kuwaongoza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana, sana Idara hii ya Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii ipewe kipaumbele. Ikiwezekana sasa tuboreshe vyuo vyetu kama cha Tengeru, kule kumechakaa, hakuna training, watu hawana new skills, tunategemea maendeleo yatatoka wapi? Tusione kwamba maendeleo ni kitu kingine hapana, tuanzie hapa chini. Kwa hiyo, naomba sana Serikali yangu Tukufu iweze kuangalia suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba sasa niongelee suala la UKIMWI. Wale watu wanaoishi na VVU tunaomba halmashauri iwasaidie wapate CHF ili waweze kupata septrin wanaumia sana kule, hakuna dawa na vitu vingine. Kwa hiyo, ombi lao kubwa dawa hizi za septrin ziweze kupatikana ingawa ni sehemu ya Halmashauri, lakini sasa ndiyo bado tunarudi kwenye changamoto ileile kwamba Wizara ya Afya kama itaishia kwenye sera haiwezi kuangalia utekelezaji wa sera zake mpaka huku chini bado tutaendelea kupata matatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana.