Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Cecil David Mwambe (4 total)

MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:-

(a) Je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha wanafunzi hawarudishwi shule kwa sababu ya michango ya mlinzi, madawati na chaki?

(b) Je, Serikali ina mpango wa kuanzisha Chuo cha Ufundi (VETA) kwenye Jimbo la Ndanda?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Ndanda, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza Sera ya Elimu bila malipo, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi imetoa Waraka wa Elimu Na. 6 wa mwaka 2015 unaofafanua majukumu ya kila mdau katika utekelezaji wa elimu msingi bila malipo.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza utekelezaji wa utoaji wa elimu msingi bila malipo ambapo jumla ya shilingi bilioni 15.71 zimepelekwa katika Shule za Msingi na Sekondari za Umma kwa mwezi Disemba, 2015. Fedha hizi ni kwa ajili ya ruzuku ya uendeshaji shule, fidia ya ada kwa shule za sekondari za bweni na Kutwa na chakula kwa wanafunzi wa bweni.

Mheshimiwa Spika, Walimu Wakuu na Wakuu wa Shule wamepewa Mwongozo wa matumizi ya fedha hizo ambazo zitatumika kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia, zikiwemo chaki, gharama za ulinzi, mitihani na chakula. Aidha, Serikali kupitia Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji itahakikisha inatenga fedha kila mwaka kwa ajili ya ununuzi wa madawati. Sambamba na hilo, wananchi na wadau wengine wa elimu wataendelea kusaidia kuchangia katika upatikanaji wa madawati kwa kadiri watakavyoona inafaa.

Mheshimiwa Spika, kwa maelezo hayo, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba hakuna Mkuu wa Shule au Mwalimu Mkuu yeyote ambaye atamrudisha mwanafunzi nyumbani kwa kutolipa michango ya mlinzi, madawati na chaki kwa sababu, majukumu hayo ni ya Serikali. (Makofi)

Serikali ina dhamira ya kuendelea kuboresha utekelezaji wa mpango huu kadiri ya tafiti zitakavyoonesha, pamoja na maoni ya wadau mbalimbali yakiwemo ya ninyi Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Spika, Serikali ina mpango wa kujenga Chuo cha Ufundi Stadi katika Wilaya zote zisizo na Vyuo vya Ufundi Stadi vya Serikali au visivyo vya Serikali. Wakati utafiti wa kubaini Wilaya zisizo na Chuo unafanyika, Wilaya ya Masasi ilikuwa na Vyuo viwili vya ufundi stadi kikiwemo Chuo cha Ufundi Stadi Ndanda, chenye uwezo wa kudahili wanafunzi 180 na Lupaso chenye uwezo wa kudahili wanafunzi 38, vinavyomilikiwa na madhehebu ya dini. Kwa kuzingatia kigezo hicho, Jimbo la Ndanda ambalo lipo katika Wilaya ya Masasi, haipo katika mpango huu.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo katika kutekeleza azma hii ya kila Wilaya kuwa na Chuo cha Ufundi Stadi, Serikali imeviwezesha Vyuo 25 vya Maendeleo ya Wananchi vilivyopo katika Wilaya mbalimbali ili kutoa mafunzo ya ufundi stadi kikiwemo Chuo cha Maendeleo cha Wananchi Masasi kwa kuwajengea uwezo Walimu, kuboresha miundombinu na ununuzi wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia. Utekelezaji wa utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi katika chuo hicho ulianza mwaka 2012/2013. Napenda kumshauri Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Jimbo la Ndanda kutumia Vyuo hivyo vilivyopo Wilayani Masasi ili kupata mafunzo ya ufundi stadi.
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga wodi ya wazazi (maternal ward) kwenye Kituo cha Afya Chiwale kwa kuwa wazazi hujifungulia kwenye chumba kilichomo ndani ya jengo ambalo pia hutumika kulaza wagonjwa wa kiume na kike?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMESEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Ndanda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Kituo cha Afya Chiwale hakina wodi ya wazazi na hali hiyo niliishuhudia mwenyewe nilipofanya ziara kituoni hapo mnamo tarehe 9 Januari, 2016 ili kujionea hali ya utoaji wa huduma kituoni hapo. Katika bajeti ya mwaka 2015/2016, Halmashauri imetenga shilingi milioni 80 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa wodi ya wazazi katika Kituo cha Afya, Chiwale. Kati ya fedha hizo, shilingi milioni 20 zinatokana na mapato ya ndani ya Halmashauri na shilingi milioni 60 ni ruzuku kutoka Serikali Kuu ambazo bado hazijapelekwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuharakisha utekelezaji wa mpango huo, Halmashauri imeshauriwa kutumia fursa ya Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa (NHIF) ili kupata mkopo utakaowezesha kujenga jengo kila maabara na wodi ya kisasa ya wazazi kutokana na ukosefu wa miundombinu hiyo muhimu katika kituo hicho.
MHE. DAVID E. SILINDE (K.n.y. MHE. CECIL D. MWAMBE) aliuliza:-
Barabara ya Masasi – Nachingwea imekuwa na matatizo kwa muda mrefu ya kupitika kwa shida:-
Je, barabara hiyo itajengwa lini kwa kiwango cha
lami ili kufanya wananchi wa Jimbo la Ndanda waondoe imani kuwa wametengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Ndanda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Masasi – Nachingwea hadi Nanganga yenye urefu wa kilometa 91 kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, mradi huu umeombewa fedha za jumla ya sh. 3,515,394,000/= kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya barabara ya Masasi – Nachingwea yenye urefu wa kilometa 45 imekuwa ikifanyiwa matengenezo ya kawaida na matengenezo ya muda maalum kila mwaka na inapitika vizuri katika kipindi cha mwaka mzima. Serikali itaendelea kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali barabara hiyo ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka wakati barabara hii inaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami.
MHE. CECIL DAVID MWAMBE aliuliza:-
Wananchi wa Jimbo la Ndanda hawako tayari kabisa kuona mfumo wa uuzaji korosho wa stakabadhi ghalani ukiendelea.
Je, Serikali chini ya kauli mbiu “Hapa Kazi Tu” ipo tayari kuondoa kabisa mfumo huo ambao ni kandamizi na hauendani na gharama za uzalishaji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabla sijajibu lazima niseme kwamba kama Mheshimiwa Cecil Mwambe asingerekebisha swali ningeshangaa sana kama swali la aina hiyo lingetoka kwake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe Mbunge wa Ndanda kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa Stakabadhi za Maghala ni utaratibu ulioanzishwa kisheria wa namna ya uuzaji wa mazao kwenye maghala kwa wakulima kukusanyia mazao yao kupitia chama chake cha misingi na mazao hayo kupelekwa katika ghala kuu ambapo ubora wa zao huhakikiwa kulingana na Sheria ya Maghala na mkulima kupewa stakabadhi ambayo hutumika kama dhamana ikiwa mkulima atahitaji mkopo wakati akisubiri mazao yake kuuzwa sokoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo huu una mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na wakulima kupata uhakika wa soko, kupanda kwa bei ya zao la korosho ambapo wakulima waliuza korosho zao kwa bei ya ushindani sokoni kwa wastani wa shilingi 2,500 kwa kilo na bei ya juu kufikia hadi shilingi 4,000 kwa kilo katika msimu huu wa 2016/2017. Aidha, mfumo huu pia umewezesha kuongezeka kwa uzalishaji wa zao la korosho ambapo uzalishaji uliongezeka kutoka tani 155,244.64 katika msimu wa 2015/2016 hadi kufikia tani 264,887.52 kwa msimu wa 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, faida nyingine ya mfumo huu ni kwamba wakulima wa korosho kwa sasa wanapata bei za juu kutokana na wakulima kupata bei sokoni kwa utaratibu wa kuvumbua (pride discovery).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ajili hiyo, Serikali haiko tayari kwa sasa kuondoa mfumo wa Stakabadhi Ghalani katika uuzaji wa zao la korosho nchini kutokana na mafanikio hayo, badala yake Serikali itaendelea kusimamia na kuboresha mfumo huu na kuwahamasisha wakulima kuongeza uzalishaji wa korosho zenye ubora ili kujiongezea kipato chao na nchi kwa ujumla.