Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Cecil David Mwambe (21 total)

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, lakini ningependa kuuliza swali la nyongeza lenye sehemu (a) na (b).

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa tufahamu wazi kwamba Serikali sasa hivi imeamua kutoa elimu ya bure, lakini hata hivyo haikujipanga nayo. Naweza nikatoa ushahidi katika hili kwa sababu katika Jimbo la Ndanda kuna shule inaitwa Liloya, wamepelekewa pale shilingi 86,000/=. Hii ni shule yenye idadi ya wanafunzi 600, na hiyo ni sawasawa na shilingi 146/= kwa kila mwanafunzi kwa mwezi mmoja. (Makofi)

Je, Serikali haikuona kwamba jambo hili ingeliacha kwanza mpaka pale itakapokaa Bunge la Bajeti na kupitisha bajeti ambayo itakidhi mahitaji ya wakati badala ya kukurupuka kufanya jambo ambalo haijajipanganalo? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili la msingi niliuliza kwamba lini Serikali itakuwa tayari kupeleka ruzuku katika Chuo cha Ufundi Ndanda ili kiweze kudahili wanafunzi wengi zaidi kwa sababu kile ni Chuo kilicho bora kuliko vyuo vyote vya Serikali vinavyotoa elimu ya ufundi vilivyopo katika Mkoa wa Mtwara na Lindi? Naomba kuwasilisha maswali yangu.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, naomba nijibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Cecil Mwambe, Mbunge wa Ndanda kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali haijakurupuka. Haijakurupuka kwa sababu Serikali hii ndiyo inayoishi na wananchi na kufahamu matatizo yao. Ndiyo inayofahamu hali halisi ya mazingira tuliyonayo na ndiyo maana ikajiwekea mpango kupitia Ilani yake ya Uchaguzi wa CCM kwamba itatoa elimu bure kuanzia Chekechea mpaka kidato cha nne. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hali hiyo basi, kama ambavyo tumejionea katika mipango mingine tuliyokuwa tumeianza, ikiwemo na Mipango ya MMEM, Mipango ya MMES na mipango katika sekta nyingine, kila wakati tumekuwa tukianza na tunaboresha kadiri tunavyoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hali hiyo, kama ambavyo nimesema, kimsingi tunafahamu hata baadhi ya shule, tulipowaambia walete idadi ya wanafunzi pamoja na mahitaji kulingana na uhalisia, kuna wengine walileta sawa, kuna wengine hawakuleta vizuri. Pamoja na hayo, tumeshadhamiria kuona ni namna gani tunaendelea kufanya uchambuzi na kuboresha kadiri itakavyowezekana.

Hivyo tunasema kwamba katika majukumu yale yanayoihusu Serikali kwa sababu elimu inaendeshwa kwa ubia baina ya Serikali na wananchi; wazazi kwa ujumla, kwa hali hiyo, katika yale majukumu yote ambayo tumejipangia, tutahakikisha Serikali inatimiza wajibu wake. Huo ndiyo msimamo wa Serikali yangu. Katika swali la pili…
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Najibu swali la nyongeza la pili. Katika swali la nyongeza la pili la Mheshimiwa Cecil, kimsingi swali la mwanzo ulikuwa unahitaji ujenzi wa Chuo na sasa hivi umezungumzia juu ya utoaji wa ruzuku.

Kwa sasa hivi bado hatujafikiria kutoa ruzuku katika Chuo hicho ambacho kipo Ndanda. Hata hivyo, ni suala la kuangalia, kama kuna uwezekano na itaonekana lina faida kufanya hivyo, basi tutazidi kushauriana na kuona suala hilo linaweza likafanyika.

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Swali la Mheshimiwa Mdee linafanana kabisa na suala ambalo liko katika Jimbo la Ndanda hasa katika maeneo ya Lukuledi - Chikunja - Nachingwea. Barabara ile siku za karibuni itajengwa kwa kiwango cha lami lakini tunaomba kufahamu fidia ya watu wale itafanyika kwa njia gani na ni umbali gani toka katikati ya barabara mpaka mwisho wa hifadhi ya barabara? Watu wale wanahitaji kufahamu jambo hili, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge swali la nyongeza la kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyosema hiyo barabara hatujaanza kuijenga na tumeiwekea bajeti mwaka huu unaokuja wa 2016/2017. Nadhani unafahamu kwamba tunafuata ile Sheria ya 1967 ya Road Reserve ambayo sasa hivi tunaongelea kila upande kutokea katikati ya barabara wale wote ambao wako ndani ya mita 60 na wale ambao wako nje ya mita 60 wana haki tofauti. Wale ambao wako nje ya road reserve wana haki ya kulipwa fidia na wale ambao waliifuata barabara, nadhani kama sheria inavyosema na kama tulivyopitisha humu Bungeni hawana haki ya kulipwa fidia. Kwa hiyo, huo ndiyo umbali ambao umwekwa kisheria na ni sisi wenyewe tulipitisha humu ndani. Sisi kazi yetu ni kuisimamia tu, hapa kazi tu.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza. Nataka kufahamu pia kuhusiana na mgogoro wa wafanyakazi uliopo katika Hospitali ya Ndanda. Serikali iliahidi itaajiri wafanyakazi 85 na wale Wamisionari sasa hivi wameamua kupunguza wafanyakazi 59 kwa sababu Serikali haijatekeleza ahadi yake toka mwaka 2012 hali inayotishia kuifanya Hospitali ya Ndanda isiwe tena Hospitali ya Rufaa katika eneo la Kusini. Je, ni lini Serikali itakuwa tayari kutekeleza ahadi yake ya kupeleka pesa kwa ajili ya wafanyakazi wa Ndanda Hospitali?
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kufahamu pia ni lini Serikali italipa pesa za fidia katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi kwa vile katika vitu vilivyoharibika ni pamoja na gari la wagonjwa la hospitali ya Chiwale ili waweze kujinunulia wenyewe tena lile gari liweze kusaidia baada ya kujenga wodi ya akinamama katika eneo lile? Ahsante
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala la changamoto ya watumishi ni kwamba Serikali tumelichukua. Sasa hivi tuna mchakato wa kuajiri watumishi mbalimbali katika Halmashauri zetu na Wizara ya Afya ina-finalize stage hiyo. Nina imani kwamba siyo muda mrefu ndani ya mwezi huu wa Mei na Juni tutaenda kupunguza hii gape ya watumishi, lakini changamoto ya Ndanda tutakwenda kuifanyia kazi. Naomba nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakwenda kulifanyia kazi kwa karibu zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la ambulance zilizoungua, ni kweli na mimi mwenyewe nimefika pale. Pale kuna ambulance tatu zilichomwa moto na kwa njia moja au nyingine siyo kwamba Serikali ni ya kulaumiwa. Katika hili, naomba nitoe maelekezo kwa wananchi, inawezekana kwa jazba zetu tunaharibu vitu ambavyo vilikuwa kwa maslahi ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipindi kile pale Mtwara watu walienda kuchoma ambulance ambazo zinabeba akinamama na watoto. Fikiria mtu anachukua kibiriti na petrol anakwenda kuchoma ambulance tatu mpya, unategemea nini katika mazingira hayo? Kwa kweli ni jambo lenye kuhuzunisha na ndiyo maana nilipofika pale Masasi nilienda kutembelea maeneo yake, kwa kweli ni jambo la kuhuzunisha, lakini Ofisi ya Rais, TAMISEMI tutaangalia jinsi gani tutafanya kwa sababu mwisho wa siku ni wananchi na akinamama ndiyo wanaopata shida zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunalichukua hili kwa upana wake lakini kwa kweli kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumesikitika sana kwa sababu ile ni fursa ambapo wananchi walikuwa wanapata huduma kila siku. Naomba nitoe onyo kwa watu wote, tusichukue jazba zetu mbalimbali tukazielekeza katika vitu ambavyo vinawasaidia wana jamii kupata huduma bora katika maisha yao.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza kwa Wizara ya Nishati na Madini. Kwa vile Wilaya za Masasi, Nanyumbu na hasa Masasi Mjini, Kijiji cha Ndanda pamoja na Chikundi, kuna tatizo sana la umeme kukatika kila mara na umeme huu ndiyo ambao tunaambiwa sasa unapelekwa Liwale. Je, Mheshimiwa Waziri anawahakikishiaje wakazi wa Liwale kuwa na umeme wa uhakika, wasije wakapata matatizo ambayo wakazi wa Masasi wanayapata kila mara?
Swali la pili, tuliambiwa watakapoanza kutumia umeme wa gesi, basi hata gharama za kuunganisha, lakini pia na gharama za kuwafikia wale wakazi umeme toka siku ambazo wamelipia zitakuwa ni chache sana. Katika hali ya kushangaza kuna wakazi wa maeneo ya Nachingwea, pia Ndanda na hizo Wilaya nyingine nilizozitaja wanaweza kukaa hata miezi mitatu au minne bila kuunganishiwa umeme toka tarehe waliyolipa. Pia, kuna vijiji vingi ambavyo vinapitiwa na nguzo kuu za umeme zinazokwenda Liwale na Masasi Mjini; Unawaambiaje wakazi wa Masasi juu ya mambo haya mawili?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kuna changamoto za upatikanaji wa umeme hasa katika maeneo ya Masasi na Nanyumbu, siyo Masasi tu hata maeneo mengine ya Liwale pamoja na Nachingwea. Hata hivyo, juhudi zilizofanyika ni kubwa. Nimhakikishie Mheshimiwa Cecil Mwambe kwamba kazi inaendelea. Hata hivyo, kwenye Awamu ya Pili ya REA ni vijiji kwa Wilaya zote alizotaja 152 vimepatiwa umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kuna vijiji mia moja na kumi na moja (111) kwa Wilaya zote havijapata umeme. Mkakati uliopo kwa niaba ya wananchi wa maeneo ya Masasi, Nanyumbu, Nachingwea na maeneo ya karibu yatapelekewa umeme kwenye REA Awamu ya Tatu inayoanza mwezi Oktoba, Novemba hadi Disemba mwaka huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la uhakika wa umeme kwa wananchi wa Masasi nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na nakushukuru sana kwa sababu umekuwa ukifuatilia jambo hili. Suala la upatikanaji wa umeme kwa Wilaya za Masasi na maeneo ya jirani linafanyiwa kazi na kwa kweli litatatulika kwa muda mfupi sana kuanzia sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, gharama za umeme; kwanza kabisa nichukue nafasi hii kuwaeleza wananchi kwamba gharama za umeme kwa kweli zinashuka. Ni kweli kabisa baada ya kuanza kutumia gesi asilia gharama za umeme zimeshuka na kwa nchi nzima. Gharama za umeme kwa miradi ya REA ni sh. 27,000 na hiyo ni nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, gharama za kulipa umeme kwa wananchi wanaotumia gesi asilia, hasa kwa Mikoa ya Lindi na Mtwara na maeneo ya jirani, hata kwa kazi wanazounganishiwa na TANESCO ni za chini; badala ya sh. 177 kwa mikoa hiyo miwili ni sh. 99. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutaendelea kutumia gharama hizo kwa Mikoa ya Lindi, Mtwara pamoja na Wilaya nyingine za Masasi na Nanyumbu.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri wa Ujenzi. Nataka kufahamu kwa uhakika ni lini Serikali itasema waziwazi siku ambayo kazi ya ujenzi wa barabara ya Masasi, Nachingwea utaanza? Kwa sababu upembuzi yakinifu ulifanyika pale muda mrefu, wananchi wanakosa amani katika eneo lile kwa sababu nyumba zao nyingi zilichorwa „X‟ na hawajui lini zitavunjwa au waendelee na ujenzi katika eneo lile. Tuliona tija ya Serikali imetoa nguvu kubwa sana na sasa hivi wanakaribia kuanza ujenzi wa barabara inayokwenda Ruangwa kuanzia Nanganga. Tunataka tuone pia na upande wa Masasi Nachingwea na wenyewe ujenzi unaanza mara moja.
Kwa hiyo, tunaomba commitment ya Serikali watueleze, ni lini ujenzi wa hii barabara utaanza au kama siyo hivyo, basi wananchi wale waambiwe waendelee kuendeleza yale makazi yao kwa sababu wanaishi katika maisha duni, hawajui ni lini nyumba zao zitavunjwa kwa sababu ya uendelezaji wa barabara katika eneo hilo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Mwambe awaelimishe wananchi waliopo katika barabara hiyo kwamba wasijenge, kwa sababu Serikali ina dhamira ya dhati ya kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami. Mheshimiwa Mbunge anafahamu kwamba katika mwaka huu wa fedha kuna fedha zimetengwa kwa ajili hiyo. Suala la lini, naogopa sana kusema kwa sababu kuna process ya kufikia hiyo hatua. Naomba tukamilishe hiyo process, itakapokamilika tutamjulisha lini tunaanza.
nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tatizo Kyerwa linafanana moja kwa moja na tatizo lililopo katika Halmashauri ya Wilaya Masasi. Tatizo letu kubwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi ni masuala ya miundombinu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuna maji ya kutosha. Serikali iliahidi kutenga shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuleta miundombinu itakayofikisha maji katika Vijiji vya Mbemba, Mbaju, Maparagwe pamoja na Chikunja. Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kupeleka pesa angalau kidogo kidogo katika hii miradi ili iweze kutekelezwa mara moja?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka 2016/2017, kila Halmashauri imetengewa fedha kwa ajili ya kuendeleza miradi ambayo ilishakuwa imeanza. Hii ni pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Fedha hizo hatutapeleka moja kwa moja; tumeagiza kwamba walete certificate kwa sababu nyingi wameshakuwa na Wakandarasi. Walete certificate ili tuweze kuwalipa wale Wakandarasi waweze kuendelea na utekelezaji wa miradi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama Mheshimiwa Mbunge kuna Mkandarasi na kuna certificate ambayo haijalipwa, niletee ili tuweze kulipa, fedha zipo. Hatuwezi kupeleka fedha zikakae tu, tunataka fedha ziende na zifanye kazi.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi, kuna jambo moja nataka tuliweke kwenye rekodi lakini pia swali langu kwa Mheshimiwa Waziri; kwa sababu kwa muda mrefu Serikali ilikuwa ikitangaza kwamba gongo ni pombe haramu kama ambavyo umeona watu wengi swali hili wakiliuliza, lakini kuna pombe mbalimbali zinazotengenezwa kutokana na mazao.
Mheshimiwa Spika, kule kwetu kuna pombe inatengenezwa nipa ndiyo hiyo hiyo gongo inatokana na mabibo makavu lakini pia ni sehemu ya kuongezea wakulima kipato.
Je, Serikali haioni sasa kama hawataki wakulima wale wapike gongo kwa kutumia zile malighafi zao ambao ni sehemu ya korosho kwa nini sasa isinunue wakaenda kufanya hata chakula cha mifugo kwa nia ya kuwaongezea wakulima kipato?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, kama nilivyozungumza kwenye suala la Mheshimiwa Selasini, suala linalotukwamisha, na ndiyo maana watu wengine kwa kutokujua wanaichukia TFDA, hoja ni kwamba kinywaji kile kinatengenezwa vipi? Kinakuwa packed vipi? Na kinapimwa kuthibitisha huo ubora, na nimeshaahidi, na niwaeleze wataalam wangu watakao kwenda Mikoa ya Lindi kafuatilie kinywaji hicho.
Mheshimiwa Spika, lakini nikutake wewe Mheshimiwa Mbunge rafiki yangu Bwana Mwambe na wewe ni rafiki yangu na unajua. Njoo unieleze wazo hilo tutumie wawekezaji wa ndani hata wa nje tuweze kutengeneza kinywaji kizuri hicho tuweze kuuza Tanzania na masoko ya nje.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante kwa kunipa swali kwenye Wizara ya Afya. Suala linalotokea Hospitali ya Mnazi Mmoja ni sawasawa kabisa na masuala yanayotokea katika Hospitali ya Rufaa ya Ndanda, Mkoa wa Mtwara. Mheshimiwa Waziri atakubaliana na mimi alipotembelea alitoa ahadi ya wafanyakazi wasiopungua 85; hivi ninavyoongea sasa hivi hospitali ya Rufaa ya Ndanda inakaribia kukosa hadhi ya kuitwa Rufaa kwa sababu kuna Daktari Bingwa mmoja tu. Je, Wizara yake ina mpango gani wa kuwawezesha watu hawa ili waendelee kutoa huduma kwa sababu ni hospitali ambayo ina vifaa vingi lakini inakosa wataalam wa kuvitumia?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamba mpango tulionao ni kusubiri kibali kutoka kwa wenzetu wa utumishi kitoke, kitakapotoka tutaajiri Madaktari Bingwa kwa kiasi ambacho tutakuwa tumekasimiwa na kuwatawanya kwenye hospitali zote za Rufaa za Mikoa nchini ikiwemo Hospitali ya Ndanda.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nataka kufahamu kwamba kwa muda mrefu Serikali kupitia Mfuko wa Wakfu wa kuendeleza zao la korosho umekuwa ukiruhusu pesa kwa ajili ya kufanya tafiti mbalimbali kwenye kuongeza thamani ya mazao ya wakulima ikiwemo mabibo kwa ajili ya kupata juice ambayo inaonekana ina uwezo mara tano zaidi wa kupata vitamin c kuliko ilivyo kwenye machungwa. Pia mabaki ya korosho kavu ambayo ni kochoko na yenyewe kuna uwezekano mkubwa sana wa kuweza kupata gin. Baada ya tafiti hizi kukamilika ni muda mrefu sana umepita, je, Serikali iko tayari kuanzisha viwanda kwa ajili ya kutengeneza juice pamoja na gin ili kuweza kuongezea wakulima hawa kipato kwa sababu mabibo pamoja na kochoko sasa vitakuwa rasmi na vitaweza kununuliwa na Serikali?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nilijibu swali la Mheshimiwa Conchesta na naomba nirudie kwa maslahi ya Wabunge wote na Watanzania. Serikali kazi yake ni kuweka mazingira bora ya wawekezaji. Mheshimiwa Mbunge, nakuomba uje tukae wote kusudi hizo taarifa ulizonazo za fursa ya uwekezaji tuweze kuziweka pamoja kwenye andiko zuri, tutangaze ili tuweze kupata wabia wa kuweza kuwekeza kwenye kiwanda hicho. Hata hivyo, mwekezaji mzuri ni Mtanzania, ni mwananchi wa Jimbo lako, ni wewe mwenyewe Mheshimiwa Mbunge. Kwa hiyo na sisi tutafute rasilimali tuweze kujenga viwanda sisi wenyewe.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kimsingi swali langu linafanana na swali namba 107 linakwenda Wizara ya Kilimo. Kimsingi ninataka kufahamu, tukiwa tunaelekea kwenye uuzaji wa korosho msimu uliopita tumeshuhudia Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Mtwara (MAMKU) viongozi wake, watendaji wakuu wakishikiliwa kwa ajili ya uchunguzi kutokana na ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala hili pia limejitokeza katika vyama vikuu vya TANECU, Lindi Mwambao, Ilulu pamoja na Chama Kikuu cha Mkoa wa Pwani. Tumeona Mheshimiwa Waziri Mkuu akichukua hatua kwa viongozi hawa wa Chama Kikuu cha MAMCU sasa tunataka kufahamu kutoka kwa Waziri amejipangaje na yeye kuwachukulia hatua viongozi wa vyama vikuu nilivyovitaja kwa sababu ya kudhulumu na matumizi mabaya ya pesa za wakulima za korosho katika Mikoa ya Mtwara, Lindi pamoja na Pwani? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kama alivyosema katika msimu uliopita wa korosho kumekuwepo na changamoto nyingi sana kuhusu malipo kwa wakulima wa korosho na ndiyo maana Waziri Mkuu alichukua hatua ya kuhakikisha kwamba sheria inachukua mkondo wake kwa watu wa MAMCU, lakini vilevile mtunza ghala wa Chama cha Msingi cha Ushirika ambapo kosrosho ziliweza kupungua bei na tunavyozungumza tayari wahusika wamefunguliwa kesi ya kuhujumu uchumi na kesi inaendelea mahakamani, lakini vilevile tunawahakikishia wakulima wale ambao wamepata changamoto hiyo ya fedha zao kutolipwa kwa kiwango ambacho kilitarajiwa kwamba Chama cha Ushirika ambacho kilisababisha korosho zile ziweze kuingia kwenye sales catalogue wao watalazimika kurudisha ile tofauti ili mkulima asije akapata tatizo lolote. Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunafahamu kwamba changamoto iliyotokea Mtwara lakini vilevile Nanyumbu tunafahamu vilevile imetokea Mkoa wa Pwani kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Serikali inachunguza changamoto hizo, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kashafanya uchunguzi huo na tumepata repoti.Lakini vilevile Waziri Mkuu mwenyewe aliagiza ufanyike uchunguzi wa kina na repoti iko tayari Serikali inapitia taarifa zile ili wale wote ambao wamehusika wakiwemo viongozi na watumishi wa MAMCU, TANECU na vyma vingine vya ushirika kama KORECU ambao watakuwa wamehusika watachukuliwa hatua za kisheria. Cha maana zaidi, wakulima wale ambao hawakupata malipo stahiki kwa sababu ya vurugu au uzembe wa watumishi wa Vyama Vikuu au Vyama vya Msingi tunawahakikishia kwamba fedha zao zitalipwa.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kadri ya muuliza maswali, kipengele namba (c) kinasema je, Serikali ipo tayari kusimamia wananchi walipwe fidia kutoka kwa wawekezaji wanaoingiza vifaranga wasio na chanjo toka nchi za nje?
Kimsingi kwenye jibu lake haja-commit, hajasema kama Serikali sasa hivi iko tayari kuhakikisha wafugaji wale wanaopata hasara wanalipwa fidia yao, kwa hiyo tunaomba Serikali itoe neno kwenye hili. Pia itueleze kama hali ni hii basi izuie kabisa watu wasiingize vifaranga ambavyo havina chanjo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kutokana na kuongezeka kwa gharama za uzalishaji hasa wa chakula kama alivyosema yeye mwenyewe na tumeona gharama kubwa sana kwenye chakula cha mifugo. Kwa kipindi hiki ambapo kuna tatizo kubwa la chakula na njaa, Serikali haioni sasa umefika wakati iondoe angalau kodi fulani ili kuweza ku-compensate wakulima katika kupata chakula chenye bei nafuu na wananchi waweze kununua kuku kwa bei nafuu?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu fidia, kimsingi suala la fidia halitokei kwa sababu kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, kimsingi ni kinyume cha sheria na taratibu kuingiza kuku na mayai kutoka nje, kwa hiyo wale ambao
wanaingizwa kwa taratibu ambazo sio rasmi, wanaingizwa kwa utaratibu wa njia za panya. Kwa hiyo, kimsingi Serikali imeweka utaratibu kuhakikisha kwamba hairuhusu uingizwaji, hivyo kutokea na ndiyo maana tumesema tayari
katika kipindi cha miaka minne tumeteketeza vifaranga zaidi ya 67,000. Hata hivyo, tunachotaka kutoka kwa Mheshimiwa Mbunge ni kuonesha ushirikiano kama wanaweza wakatuonesha watu ambao wanaingiza vifaranga na mayai kinyume na taratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na gharama ya vyakula vya mifugo, hasa kuku, kama nilivyosema vilevile ni kweli kwamba kuna gharama kubwa sana katika kutengeneza vyakula vya kuku kwa sababu kiinilishe kinachotumika ni maharage ya soya ambayo hatuzalishi hapa nchini. Kwa hiyo, hatua ambazo tunazichukua ni
pamoja na kuhamasisha wananchi walime zao la soya.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kupitia hotuba ya bajeti ya Wizara yetu kwa ajili ya mwaka wa fedha unaokuja, Serikali imechukua hatua kadhaa kupunguza kodi na tozo za mazao na bidhaa mbalimbali ili basi vyakula vya kuku na mazao mengine viweze kupatikana kwa bei nafuu. Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba suala la kodi na tozo litashughulikiwa.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona na kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Swali la Mheshimiwa Masoud ambalo kwa masikitiko tu niseme Mheshimiwa Waziri hajalijibu kadri ya mahitaji ya watu wa Mtwara na Kusini kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali letu sisi ni kwamba kwa kipindi cha miaka 50 iliyopita Serikali ilikuwa haijatengeneza barabara inayounganisha Mtwara na Dar es Salaam. Baada ya utengenezaji wa barabara hii na mara Kiwanda cha Dangote kikafunguliwa ambacho kina magari zaidi ya 1,500 yanayosafirisha cement kutoka Mtwara na kuzileta Dar es Salaam.
Sasa tunataka kufahamu Serikali kwa nini isizuie usafirishaji wa cement kwa kutumia magari ambayo yanaleta uharibifu mkubwa sana kwenye barabara za Mtwara, Lindi kufika Dar es Salaam na badala yake wanawaaachia wasafirishaji wale wale wa magari. Kwa nini wasizuie na wakapa uwezo watu wa kuleta meli wakasafirisha cement hiyo mpaka Dar es Salaam kwa distributors?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO:
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyozungumza na Mheshimiwa Naibu Waziri alivyosema kwenye jibu lake la msingi, kwanza barabara ile imekuwa designed kuchukua mzigo mkubwa, hilo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili mzigo wote wa Dangote wa cement hauendi Dar es Salaam, unaenda sehemu mbalimbali za Tanzania na tatu, Serikali tunaendelea kufanya utaratibu na kampuni mbalimbali za meli kuhakikisha kwamba mzigo huo unakwenda kupitia vilevile upande wa baharini.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nilitaka nimueleze Mheshimiwa Waziri kwamba Mkoa wa Mtwara ndiko inakozalishwa gesi inayozalisha umeme wa Dar es Salaam ambako haukatiki kila mara, kiasi tumeanza kuamini gesi yetu haitunufaishi ni bora tungerudishiwa yale majenereta yaliyokuwa yanazalisha umeme Mtwara wakati huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la umeme la Mtwara linasababishwa na kuharibika kwa transfoma ya jenereta moja yake ambayo nafahamu mpaka sasa kuna mvutano mkubwa kati ya TANESCO pamoja na MANTRAC Tanzania Limited kwa ajili ya ku-supply ile transfoma kwa sababu ya madeni sugu ambayo TANESCO hawajalipa.
Mheshimiwa Waziri, naomba utueleze kinagaubaga ni lini matatizo ya TANESCO na MANTRAC yatakwisha ili kuwarejeshea wananchi wa Mtwara umeme wa uhakika? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mweyekiti, ni kweli kabisa liko tatizo la kuharibika kwa mashine moja Mtwara kiasi cha kushindwa kupeleka megawatt 18 kwa ujumla wake. Kwa sasa hivi ni kweli kabisa Mtwara wanapata megawatt chini ya 18, wanapata 16 na 15.6
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wa Mtwara na Lindi lakini hatua zilizochukuliwa ni kwamba hivi sasa ukarabati umeshaanza. Mgogoro uliokuwepo kati ya TANESCO na MANTRAC umekwisha na jenereta inatengenezwa, ni hatua ya kwanza. Hatua ya pili, Mtwara tunawaongezea mashine nyingine sita ambapo kila mashine itakuwa na megawatt mbili. Kwa hiyo, mtakuwa na megawatt nyingine za ziada 12 na jumla kuwa na megawatt 30. Kwa hiyo, sasa umeme wa Mtwara pamoja na Lindi maeneo ya jirani utakuwa ni wa uhakiki zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hili linashughulikiwa na baada ya Bunge hili Mheshimiwa Mbunge tutakwenda wote kukagua mashine hii ikiwa imeshakamilika na umeme unapatikana.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la Mheshimiwa Mhagama, matatizo yaliyoko Madaba yanafanana moja kwa moja na matatizo yaliyoko Jimbo la Ndanda. Kwenye bajeti ya mwaka jana Mheshimiwa Waziri utakumbuka zilitengwa fedha shilingi bilioni moja kwa ajili ya kupeleka MANAWASA ili kununua viunganishi pamoja na mabomba ambayo yangeweza kupeleka maji katika kata za Chikukwe, kijiji cha Maparagwe pamoja na kijiji cha Chikunja. Wananchi walikubali watajitolea nguvu zao, lakini mpaka sasa hivi mabomba yale hayajakwenda.
Je, unaweza kutueleza ni lini Serikali itapeleka pesa hiyo, wakati tumebakisha siku chache tu kumaliza mwaka wa bajeti? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kweli kabisa kwamba Serikali ilitenga shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuendeleza Mradi wa Mbwinji pale Masasi, kupitia Mamlaka ya MANAWASA. Juzi juzi hapa Mheshimiwa Mbunge tuliwasiliana, walileta andiko na andiko hilo tayari limesapitishwa ili MANAWASA waweze kusaini mkataba kwa ajili ya procurement ya hivyo vifaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari kwa maana ya Wizara imeshaidhinisha kwa hiyo, ni kazi ya Mkurugenzi wako sasa kusaini mkataba na mkandarasi yule ambaye mmempa kazi. Ile kazi ni ya kununua vifaa; vifaa vile ni kitu cha wiki mbili vitakuwa vimeshanunuliwa na mkishamaliza, kwa utaratibu wetu, mnaleta certificate tunatoa hela, mkandarasi analipwa. Kwa hiyo, kama MANAWASA watafanya haraka, hela hiyo lazima mtaipata katika huu mwaka wa fedha.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Swali lililoulizwa na Mheshimiwa Martin Mtonda kuhusu madai ya Mawakala wa Pembejeo Mbinga Vijijini linafanana kabisa na tatizo lililopo Wilaya ya Masasi Mkoa wa Mtwara na hasa Jimbo la Ndanda; kwamba katika msimu wa kilimo wa mwaka 2016 wakulima wa korosho na hapa Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri kwamba hasara nyingine huwa zinasababishwa na watumishi wa Serikali wasio waaminifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jambo hili pia limetokea Mtwara kwa wakulima wa korosho baada ya wamiliki wa maghala kwa kushirikiana na Watendaji wa Chama Kikuu cha Ushirika kuwaibia wakulima pesa zao na kesi zinaendelea kwenye Mahakama. Je, Serikali haioni sasa ni wakati wa kutoa pesa zilizopo kwenye Mfuko wa Wakfu na kufidia hasara hii waliyoipata wakulima wakati wao wanaendelea na wale watu waliopo Mahakamani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na uwezekano wa Serikali kulipa fedha ambazo kwa sasa zipo kwenye Mfuko wa Wakfu kwa ajili ya kufidia zile fidia, ingekuwa ni jambo jema, lakini kwa sababu suala lenyewe bado liko Mahakamani, ni vizuri tukasubiri tupate majibu, kwa sababu inawezekana kule Mahakamani, wale ambao tunafikiri wamesababisha hasara ikaja ikatokea uamuzi tofauti. Kimsingi tunataka kila mtu abebe mzigo wake ili kama wale watakuwa wamehusika kulingana na hukumu ya Mahakama, wenyewe watabeba jukumu la kurudisha fedha za wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachofanya sisi kama Serikali ni kuhakikisha kwamba matatizo kama haya hayatokei tena. Ndiyo maana tunavyozungumza, tayari Bodi za Vyama vya Ushirika zaidi ya 200 Mtwara na Lindi zimevunjwa, ni kwa sababu tunajaribu kuwalinda wakulima wasiendelee kuibiwa na watu wachache ambao sio waaminifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile hizo kesi ziko Mahakamani na Afisa yeyote wa Ushirika au wa Serikali ambaye atabainika kuhusika katika upotevu wa fedha za wakulima, naye vilevile atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuboresha ubora, ni swali ambalo liliulizwa awali ambalo linahusiana na hili. Sasa hivi Serikali ina mpango wa kuagiza mbolea kwa mkupuo (bulk procurement) na hii itasaidia sana sisi tuweze kuchagua mbolea ambayo tunahakikisha kwamba inakuwa na ubora. Kampuni yetu inayohusika na ubora wa mbolea itahakikisha kwamba mbolea yote inayoingia ni bora lakini vilevile hata kwa mbegu…
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, lakini kuna suala moja hajatoa ufafanuzi wa kina.
Mheshimiwa Spika, mwekezaji analalamika kwamba 6% za uzalishaji na gesi inayochukuliwa haitamfanya aweze kurejesha gharama za uwekezaji kwa kipindi cha miaka 25 kadri walivyokubaliana na Serikali; na Mheshimiwa hapa anasema kwamba kadri siku zinavyokwenda basi gesi nyingine itahitajika.
Mheshimiwa Spika, nataka kufahamu, ni lini Serikali itamhakikishia mwekezaji kwamba bomba hili litatumika kwa asilimia 100 ili aweze kurejesha gharama zake ndani ya miaka 25, ikizingatiwa kwamba sasa hivi yupo kwenye mwaka wa 11? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa niseme mradi ule ni wa Serikali kwa asilimia 100, hilo ni la kwanza kabisa. Kwa hiyo, unamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100. Hata hivyo, kama nilivyosema, mwaka gani tutaweza kupata gesi asilimia 100 inayozalishwa pale? Ni mradi ambao ni endelevu. Iko miradi mingine inajengwa Mtwara ambayo inaanza mwezi Machi mwakani ambayo tutaanza kuzalisha megawati 500 kwa Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niseme tu kwamba bado kuna muda wa kutosha, ifikapo mwaka 2020/2022 tuna matarajio kwamba gesi inayozalishwa katika Madimba tutaweza kuitumia kwenye miradi yetu ya umeme.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwa sababu miradi ni mingi, ifikapo mwaka 2022 matarajio kati ya asilimia 80 hadi 100 tutaanza kutumia gesi yote asilia.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nitakuwa nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba Serikali imejipanga kuhakikisha wanafikisha umeme pamoja na maji hasa zaidi kwenye shule pamoja na sehemu zingine za kutolea huduma za kijamii, lakini ningependa kwa uhakika kabisa aseme kwamba ni lini Serikali itatimiza suala hili kwa sababu ni muda mrefu wamekuwa wakiliongea kila mara bila kuwa na tarehe ya uhakika kwamba itakapofika wakati fulani tutakuwa kwa kweli tumetekeleza, bado shule nyingi pamoja na vituo vya afya vinakosa huduma ya umeme pamoja na maji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuna vijiji vingi sana, kama anavyosema kwamba Serikali imeazimia kupeleka umeme kwenye vijiji vyote zaidi ya 7,000, lakini ukipita Jimbo la Ndanda kwa mfano Vijiji vya Nangoo, Liputu, Ndolo pamoja na Mdenga vinapitiwa na umeme wa msongo wa megawati 33. Sasa Waziri angetusaidia kutueleza ni lini kwa hakika Serikali sasa wako tayari kushusha umeme ule kwa ajili ya matumizi ya watu wale walioko chini ya hizi waya ambazo kwao ni hatari kwa maisha?Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika maswali yake mawili ya nyongeza aliyouliza Mheshimiwa Cecil Mwambe, Mbunge wa Ndanda yeye mwenyewe ni shahidi anafahamu kwa sababu ameshiriki kupitisha bajeti hapa anajua mipango ya Serikali ilivyo. Sina shaka kwamba anatambua kwamba ahadi iliyoko kwenye Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano inaendelea kutekelezwa vizuri na tuna uhakika vijiji vyote nilivyovitaja kwenye jibu la msingi vitapata umeme pamoja na vitongoji vyake kama ambavyo Wizara ya Nishati imeahidi, na mikakati iko wazi na yeye mwenyewe Mheshimiwa Mbunge ni shahidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la maji, Mheshimiwa Waziri wa Maji ametoa ahadi hapa Bungeni kuhusu kutekeleza awamu ya pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji, na hii itaongezeka kasi zaidi pale ambapo tutaanza kutekeleza miradi ya maji vijijini kupitia ile Wakala wa Maji Vijijini ambao utafanya kazi sawasawa na REA inavyofanya kazi. Kwa hiyo, ndugu yangu Mwambe ondoa shaka katika swali lako la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, huu umeme ambao umepita kwenye vijiji alivyovitaja na msongo anaujua ameutaja, mimi kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati namuahidi kwamba mikakati ya Serikali itatekelezwa na wanavijiji aliowataja hao watapata umeme.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kwa kuuliza swali la nyongeza, linalohusiana na masuala ya madini kama ambavyo Mheshimiwa Hamida ameuliza hapo mwanzoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lililopo Ruangwa linafanana kabisa na tatizo lililopo Jimbo la Ndanda katika kijiji cha Chiwata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kijiji cha Chiwata sasa hivi kuna uwekezaji unaendelea kwa ajili ya madini ya graphite, lakini uwekezaji huu umekuwa ukufanyika kwa siri kubwa sana kiasi kwamba wananchi wa Chiwata hawafahamu nini kinaendelea na hawako tayari kuendelea kukaa kimya, wamenituma nimuulize Waziri.
Je, Serikali ipo tayari sasa kuleta mkataba ambao utatumika kwa ajili ya uchimbaji wa madini katika kijiji cha Chiwata ili kuondoa sintofahamu ambayo inaweza ikajitokeza miaka ya baadaye ya kuhitaji kufanya review na ku-cancel mikataba ile? Ninaomba commitment ya Serikali ni lini iko tayari kuleta mkataba ule ujadiliwe na Bunge ili ukatumike kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa Jimbo la Ndanda? Ahsante.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Mheshimiwa Mwambe nampongeza sana, tumekuwa tukishirikiana naye sana kwenye masuala ya wachimbaji wadogo mbali na masuala yake ya masuala ya nishati kwenye eneo lake. Kuhusiana na eneo analolitaja yuko mwekezaji ambaye sasa anajiandaa na kukamilisha utafiti, atakapokamilisha utafiti ndio aanze shughuli za uchimbaji, kwa hiyo hata hatua ya kuingia mkataba bado.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo nikuombe sana Mheshimiwa tukae, tujue kitu gani kinahitajika na itakapofikia wakati wa kuingia mikataba tukushirikishe, sasa ni lini mkataba tutauleta nadhani bado sana kuzungumza jambo hilo akamilishe utafiti, akishaanza uchimbaji akaingia mikataba tutajadiliana, kama kutakuwa na haja ya kuuleta basi tutaona ni utaratibu gani utumike ili Mheshimiwa Mbunge kuweza kuuona mkataba huo.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza na nitakuwa nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya changamoto zilizojitokeza kwenye msimu wa korosho mwaka wa jana ni pamoja na wizi uliofanyika katika maghala ya YURAP yaliyoko Masasi kwa kushirikisha wamiliki wa ghala lakini pamoja na viongozi wa mkoa walibariki jambo hili; na sasa hivi kuna kesi zinaendelea mahakamani kwa ajili ya kuweza kupata haki ya wakulima wale. Sasa tunataka kufahamu Serikali haioni haja ya kuwalipa wakulima pesa zao, kwa sababu walikuwa wanatoa michango kwenye mfuko wa kuendeleza zao la korosho wakati ninyi mnahangaika na wale wezi wenu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, sasa hivi tunaelekea kwenye msimu wa kilimo na wananchi wanaendelea kutayarisha mashamba yao kwa ajili ya msimu wa korosho ujao. Hata hivyo kumekuwa na sintofahamu kubwa sana kuhusiana na pembejeo baada ya Serikali kutangaza kwamba itapeleka pembejeo za bure. Sasa tunataka kufahamu, ni lini pembejeo zitawafikia kwa asilimia 100 ili waweze kutayarisha mashamba yao, kwa sababu wanategemea zinatolewa na Serikali tena kwa bure? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajibu maswali yake ningependa kusema kwamba zao la korosho ni moja kati ya mazao ambayo yamefanikiwa sana katika miaka ya karibuni. Mwaka huu korosho ndiyo imeongoza kwa kuiingizia nchi yetu fedha za kigeni kati ya mazao yote, imeipiku tumbaku. Vilevile katika msimu huu Serikali imefanikiwa kuwapatia wananchi wa mikoa inayolima korosho shilingi bilioni 800. Kwa hiyo, tunapozungumza korosho tunazungumza mafanikio makubwa sana ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kuhusu utaratibu wa Stakabadhi Ghalani tunaelekea sasa kwenye mazao mengine hususan Kahawa, lakini vilevile na mazao ya jamii ya mikunde.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maswali yake, ni kweli kwamba kuna mapungufu yametokea ikiwa ni pamoja na mapunjo ya fedha za wakulima. Kama mnavyofahamu, tayari kuna watumishi wa MAMCU wamepelekwa mahakamani na kufunguliwa mashtaka ya kuhujumu uchumi. Vilevile katika fedha ambazo zimepotea tayari Serikali imesha- recover shilingi bilioni 1.5 na hizo zitaenda kwa wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu pembejeo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tani 9,000 za sulfur tayari zimeishaingia nchini na sulfur hiyo inagaiwa bure na iko njiani kuelekea kwenye mikoa inayolima korosho ili wananchi waweze kugawiwa, nashukuru sana. (Makofi)
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Matatizo yaliyopo Uyui kwenye miradi inayosimamiwa na TASAF na TAMISEMI yanafanana kabisa na matatizo yaliyopo katika Jimbo la Ndanda hasa kwenye Kata ya Mwena.
Mheshimiwa Mwenyekit, kwenye hii TAMISEMI phase III ambayo imekuwa ikishirikisha wananchi. Kuna miradi pale ya mabomba ambayo Mheshimiwa Diwani kwa kushirikiana na watendaji wamekuwa hawatekelezi wajibu wao; kwa maana ya thamani ya pesa haionekani kwenye miradi. Sasa Mheshimiwa Waziri tunaomba atuleze badala ya kusubiri mpaka haya mambo yaharibike kabisa ndipo Wizara yake ikachukue hatua, je, hawaoni kuna haja ya kufuatilia utoaji na matumizi ya pesa ya TASAF katika maeneo mbalimbali kadiri siku zinavyokwenda?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme wazi kwamba jambo la kusimamia fedha (value for money) katika maeneo yetu naomba tulipe kipaumbele sana. Mheshimiwa Cecil nakumbuka tumetembelea mpaka kwenye bwawa lake pale chini. Kama fedha lakini usimamizi si mzuri na kama fedha imekwenda wengine wanatengeneza caucus kule kwa ajili ya kula ile fedha, jambo hilo halikubaliki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Waheshimiwa Wabunge kwa sababu wao ni Wajumbe wa Kamati ya Fedha, wasikubali kupitisha mradi wa aina yoyote katika site na Majimbo yao ambayo wanaona katika njia moja au nyingine, mradi huu baadhi ya watu wanahujumu kwa makusudi. Tukifanya hivi ndipo tutalinda fedha hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sasa naomba nitoe maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Masasi, kwamba aangalie kwanza nini kilichotokea katika mradi huo ambao tunasema kwamba lengo ni kuweza kuwasaidia wananchi halafu tupate taarifa. Nitaenda kufanya follow up ya haraka ili fedha zinapokwenda kule site lazima fedha zile ziweze kuleta matunda makubwa sana kwa manufaa ya wananchi.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza linalohusiana na masuala ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la maji lililopo Songea linafanana kabisa na tatizo lililopo Wilayani Masasi hasa katika Vijiji vya Lukuledi, Chikunja, Maparagwe, Liputu, Mlingura pamoja na Namajani. Maeneo haya yote yanahudumiwa na mradi wa maji wa MANAWASA kutokea mradi wa Mbwinji ambao unapeleka maji mpaka Nachingwea. Tunataka kufahamu sasa kwa sababu tatizo kubwa ni miundombinu ya kusambaza maji haya kwa watumiaji. Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi yake ya kupeleka pesa kwa ajili ya kununua vitendanifu kwa ajili ya kuunganisha maji katika maeneo niliyoyataja? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, wiki mbili zilizopita nilienda Masasi mpaka mradi wa Mbwinji, Mamlaka ya Maji MANAWASA Mkurugenzi wake ameomba milioni 500 na tunampatia ili akamilishe kuunganisha vijiji vilivyobaki ambavyo viko pembezoni mwa bomba linalotoa maji Mbwinji kupeleka Masasi Mjini, lakini pia kwenda Nachingwea pamoja na vijiji kadhaa vya Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, kwa hiyo kote tunapeleka maji.