Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Capt. (Mst). George Huruma Mkuchika (12 total)

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. CAPT. GEORGE H. MKUCHIKA - MWENYEKITI KAMATI YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi tena. Sitamaliza hiyo robo saa kwa sababu Kamati yangu wamechangia watu watatu; hapakuwa na maneno mengi sana. Nadhani hiyo ni kuonesha alama wanazoipa Kamati, nadhani zaidi ya asilimia 90 hawakuwa na mambo ya kusema. Mheshimiwa Mwenyekiti, Wajumbe wawili wamechangia humu ndani, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete na Mheshimiwa Dkt. Semesi. Mheshimiwa Juma Othman Hija alichangia kwa maandishi. Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshukuru Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, yeye ametoa rai kwamba kila Mbunge ajiheshimu mwenyewe kwanza. Sisi tunakubaliana naye na ndiyo msimamo wa Kamati yangu kwamba kama hapa ndani kila mmoja atajiheshimu, nafikiri hata kazi ya Kamati hii itakuwa rahisi sana. (Makofi) Mheshimiwa Dkt. Semesi amependekeza Kamati iwe na Wajumbe 50 kwa 50. Nataka nimweleze kwamba Kamati hizi hapa ndani zinaundwa kulingana na uwiano wa Wabunge kwenye Vyama. Kamati zote zilizomo humu ndani kile Chama ambacho kina Wabunge wengi ndicho kina Wajumbe wengi. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Kamati zote zinategemea hiyo. Ukichambua hizi Kamati, ni yale yale ninayoyakemea kwamba kwa utaratibu wa humu ndani, kama mmoja anaongea, wewe unanyamaza. Nadhani ndiyo mnaona umuhimu wa Kamati yangu, kwamba wako watu ambao lazima tushughulike nao ili hapa ndani pawe shwari. (Kicheko/Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukitoka hapa, nenda kachambue Kamati yote, in reality, ratio iko 7:3 nenda Kamati zote. Kwa hiyo, siyo kwamba hii Kamati ya Maadili isan exception, hapana. Ndivyo ilivyo kwa muundo wa Kamati zote. La mwisho, niseme tu kwamba anayeunda hizi Kamati, sio Wajumbe wa Kamati, ni Mheshimiwa Spika. Mheshimiwa Mwenyekiti, watatu, ndugu yangu hapa, Mheshimiwa Juma Abdallah Juma, yeye amechangia kwa maandishi, anaipongeza kazi ya Kamati na anapendekeza kanuni ziangaliwe upya ili kuwabana wanaofanya fujo ndani ya Bunge. Ninachotaka kusema ni kwamba, Kamati ya Kanuni ndiyo inayotengeneza kanuni, sisi tunafanya kazi kwa kutumia kanuni zilizotengenezwa na Kamati ya Kanuni na kupitishwa na Bunge Zima. Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nimalizie tu kusema kwamba sisi kama Kamati ya Maadili, tunatoa rai na kama tulivyosema pale mwanzo, hapa ndani kuna maendeleo makubwa sana. Ukilinganisha vurugu zilizokuwepo mwanzoni wakati Bunge linaanza na tulivyo leo, yapo mabadiliko makubwa. Kwa mtu yeyote ambaye akili yake haina matatizo, anaelewa kwamba tumepiga hatua. Yule ambaye hataki kuelewa, mwache aendelee kutokutaka kuelewa kwa sababu ndiyo watu wengine walivyo, lakini hali ya hapa katika Bunge nadhani kwamba tumeanza kwenda vizuri. Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nimalizie... Mheshimiwa Mwenyekiti, si ndiyo haya haya ninayokemea? Mimi si ndiyo nimepewa nafasi hapa kusema? Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimalizie kwa kusema hivi, tukiwa hapa ndani, naomba tuendelee kuheshimiana, kuvumiliana, kuzingatia kanuni, kuheshimu kiti na nimalizie kusema tu kwamba ukizomea wakati mwingine wanasema, haujajenga hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka leo tuondoke wote na msemo huu ambao katufundisha Baba yetu Mwalimu Nyerere. Alitufundisha hivi, argue, don’t shout. Tuondoke na spirit hiyo, Baba yetu katufundisha, “argue don’t shout.” Kama mwenzio anaongea, kapewa nafasi, nawe ghafla bin vup, unabonyeza unasema „nini wewe?” “Mambo gani hayo?” You are shouting. Argue, don’t shout. Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba Bunge lako Tukufu likubali kuipokea taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge pamoja na mapendekezo yake ili yakubaliwe na kupitishwa na kuwa maazimio ya Bunge. Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hasa maeneo yanayohusu Wizara yangu ya Utumishi na Utawala Bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuipongeza Kamati ambayo tumefanya nayo kazi, Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa, imetuongoza vizuri miaka miwili hii. Mwenzangu aliyenitangulia wameshirikiana naye vizuri na mimi nilipofika nimepata ushirikiano katika miezi hii minne ambayo nimefanya nao kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kushukuru kwa pongezi zilizotolewa na Kamati kwa vyombo vitatu vinavyofanya kazi katika Wizara yangu, kwa maana ya TASAF, MKURABITA na Mfuko wa Rais wa Kujitegemea. Kamati inakubali kwamba wanafanya kazi nzuri, wanaomba tu ikiwezekana wawezeshwe ili waweze kufanya kazi nzuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme kwa upande wa TASAF, kwamba tupo TASAF Awamu ya Tatu, utekelezaji tumefikia walengwa asilimia 70, bado walengwa asilimia 30. Tunafanya utafiti sasa kujiandaa kwa utekelezaji Awamu ya Pili ya TASAF ya Tatu na lengo la Serikali ni kuwafikia walengwa wote ili Watanzania wote wanaohitaji msaada wapate kusaidiwa na Mfuko wa TASAF. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lilikuwepo swali hapa kuhusu ajira ya wataalam, ilizungumzwa wataalam katika afya, lakini kwa sababu Bunge hili hushughulika na ajira kwa watumishi wote, ningependa kusema yafuatayo kuhusu ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua kuwa zoezi la uhakiki wa watumishi limeleta upungufu wa watumishi wa kada mbalimbali ikiwemo watumishi wa kada ya ualimu na afya, Serikali imetoa vibali vya kuajiri watumishi 15,000. Hao 15,000 tumekwishwa waajiri katika hao 4,000 wako afya, 4,000 wako elimu na hasa elimu ya sekondari kwa walimu wa sayansi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshatoa ikama iliyoidhinishwa kwa mwaka 2017/2018 ambapo jumla nafasi zilizokubaliwa 52,436 wanatarajiwa kuajiri, tulikuwa tunaziba pengo la wale ambao wametolewa kwa ajili ya vyeti fake, sasa tunataka kuingia katika mchakato wa ajira zile 52,000 ambazo zilikwishaidhinishwa na Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nataka niseme, nimesikia hapa ndani na baadhi yao wameniandikia vikaratasi, kwamba zipo Halmashauri zahanati imefungwa au kituo cha afya kimefungwa kwa kukosa muhudumu.

Mimi naomba endapo kuna mtu yeyote, Mbunge au mwananchi yeyote anayenisikia ambako katika Halmashauri yake zahanati imesimama kwa kukosa muhudumu nipewe taarifa, tutamuajiri mara moja ili huduma za afya ziweze kuendelea. Maeneo mengine tunaweza tukasubiri, lakini kwa afya ya binadamu hatuwezi tukaendelea kusubiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, limegusiwa hapa suala la utawala bora na mimi ni Waziri wa Utawala Bora. Nisingelipenda kubishana sana, lakini nataka niseme hivi, utawala bora maana yake nini? Utawala bora maana yake ni watu kuishi katika jamii kwa kufuatana kwa sheria na taratibu walizokubaliana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Tanzania sheria na taratibu walizokubaliana zinatoka hapa katika Bunge, kwa hiyo mtu anayekwenda kinyume na yanatoka hapa katika Bunge huyo anakwenda kinyume na Utawala Bora na anapaswa ashughulikiwe kwa sababu anakwenda kinyume na sheria za nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nataka niseme, magazeti ya leo kama mmesoma Daily News wameandika, gazeti la Habari Leo wameandika, kiswahili wameandika lile la kiswahili Tanzania yang’ara katika utawala bora, tumeambiwa katika nchi za Afrika Mashariki, Tanzania ni ya kwanza; Rwanda wanatushinda katika fighting corruption wao wa kwanza, sisi wa pili, lakini ile utawala bora ikiunganishwa, akina Mpango mnasema uchumi shirikishi, Tanzania ni ya kwanza katika Jumuiya ya Afrika ya Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maneno hayo yanaungwa mkono na TWAWEZA, maneno hayo yanaungwa mkono na Transparent International, maneno hayo yanaungwa mkono na REPOA, maneno hayo yanaungwa na World Economic Forum. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi naomba yale mambo yetu mengine si vizuri tukalumbana. Mimi sikuona mahala, nimefatilia na bahati kipindi hicho pia nilikuwa Waziri wa Utawala Bora, sikuona mahala aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arumeru katiwa hatiani na Mahakama ya nchi hii. Kwa hiyo, unavyosimama hapa ukasema kapewa promotion mtu ambaye ametenda kosa hili, hili, hili nchi hii chombo peke yake chenye mamlaka ya kutafasiri sheria ni Mahakama, hakuna mahala yule mtu ametiwa hatiani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengine ambayo yamezungumzwa hapa ni kuhusu bomoa bomoa. Siwezi kujibu yote, lakini nataka niseme tunataka kutengeneza reli standard gauge, tunataka kupeleka barabara iwafikie watu, nyumba yako ipo barabarani tuiache? Mimi nasema Serikali hii haina double standard, nyumba za watu binafsi zilizoko barabarani zimevunjwa, sasa hivi jengo la TANESCO mali ya Serikali linavunjwa. Linavunjwa kwa nini, kwa sababu liko barabarani. Hii Serikali haina double standard. Habari …
(Makofi)

T A A R I F A . . .

AZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa
Mwenyekiti, kwa jinsi nilivyobobea katika siasa sikusudii kubishana naye, nakusudia niendelee tu kujenga hoja niliyokuwa naijenga. Yeye hakai Arumeru, mambo ya Arumeru hayajui. Mwenyekiti Mao Tse Tung anasema no research, no right to speak, anajua hao Madiwani wameingiaje? Hivi mimi inanihusu nini hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka nimalizie katika hilo suala la utawala bora. Mmegusia katika habari ya kufungia magazeti, nataka niseme hivi, katika utawala wa nchi hii hakuna vacuum, Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 ilikuwa inampa Waziri kufungia magazeti, baadae tumebadilisha Sheria katika vyombo vya habari kuna committee inayoitwa Content Committee, wale wanafuatilia kama gazeti au redio au luninga imekwenda kinyume wanamshauri Waziri Kamati (Content Committee) wanamshauri Waziri kwamba hawa hapa wamekwenda kinyume na sheria za nchi, Waziri anachukua sheria, hatukurupuki tu hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ile Sheria ya Vyombo vya Habari tulikuja tukairekebisha, tukaipitisha hapa. Kwa hiyo mimi nataka niseme kwamba suala la good governance (utawala bora) ni kuishi kwa kuzingatia sheria za nchi ambazo tumekubaliana katika jamii. Inawezekana wewe ulitaka sheria iwe hivi, iwe hivi, bado hujawa na majority ya kutunga sheria, fuata wale walio wengi walivyotunga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, palikuwapo na hoja kwamba watu wanakaimu muda mrefu bila kudhibitishwa. Nataka kusema kwamba ulitolewa mwongozo unaosema kwamba kabla hujamkaimisha, kabla hujamfukuza, wasiliana na Utumishi, Utumishi watambue kule kukaimu kwako ili utakapokuwa unaomba kwamba yule adhibitishwe liwe lisiwe jambo jipya kwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine watu wanakaimishwa bila Utumishi kuhusishwa, watu wengine wanafukuzwa hata bila Utumishi kupewa taarifa. Tunaomba tu kwamba taratibu tu zifuatwe na taratibu zikifuatwa sisi tukiletewa majina hata kama ni upekuzi tunasimamia na zoezi linaenda kwa jinsi ambavyo limekusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dada yangu pale Mollel kauliza maswali mawili ya msingi sana. Tunawafanyaje darasa la saba wale? Tunafanyaje wale ambao tumewafukuza kwa sababu ya vyeti fake? Niseme lile la vyeti fake na hilo la watu wa darasa la saba; Serikali imekaa na TUCTA (Chama Huru cha Wafanyakazi), ni mambo ambayo tumezungumza, tunaendelea kuzungumza nao, tumepeana muda ili jambo hili tuweze kulimaliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nataka niseme lile la vyeti fake, Serikali ilishasema kwamba kama mtu wakati wa kutafuta ajira alipeleka vyeti fake na yeye akaingia mkataba na Serikali maana yake mkataba wake ule ni null and void. Maana mwajiri alimtaka apelike cheti ambacho ni sahihi, cheti ni halali. Yule ambaye aliyepeleka cheti fake maana yake mkataba nao ni fake. Swali linakuja je, unamu-award mtu ambaye ana cheti fake?

Mheshimiwa Mwenyekiti, TUCTA wameiomba Serikali na Serikali imeshasema, kama ni kuwashitaki wale wangeshtakiwa na TAKUKURU, wangeweza kushtakiwa na Kanuni za Utumishi, Serikali imetoa msamaha. TUCTA wametuomba kwamba tunaomba Serikali iwe na jicho la huruma kwa hawa watu wa darasa la saba, kwa hawa watu wa vyeti fake na Serikali inalifanyia kazi jambo hilo, muda utakapofika Serikali itatangaza uamuzi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sijui nimebakiwa na dakika ngapi, maana yake mambo yapo mengi ambayo yalikuwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru, naounga mkono hoja ya Kamati tunazozijadili, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. CAPT. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa
Mwenyekiti, barabara ya Newala -Kitangari – Mtama inahudumiwa na TANROADs. Hii barabara inaunganisha Mkoa wa Mtwara na Lindi, lakini ni barabara ya vumbi. Wananchi wa Newala wanaomba barabara hii ijengwe kwa kiwango cha lami, maana pia ndiyo njia kuu wanayotumia watu wa Newala kwenda Dare es Salaam na Dodoma. Tunashukuru kwa jitihada za Serikali maana sehemu korofi kama za Kitangari na mlima Kinolombedo zimejengwa kwa kiwango cha lami. Ni vizuri kuongeza kilomita zilizojengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu Uwanja mpya wa Ndege wa Newala. Baada ya eneo la Uwanja wa Ndege wa zamani kupima viwanja, Uongozi wa Wilaya umetenga eneo jipya la Uwanja wa Ndege. Wataalam wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege walitembelea Newala na kuelekeza ukubwa unaohitajika na mwelekeo wa Uwanja. Nilipouliza swali Bungeni, Mheshimiwa Waziri alinijibu kuwa Serikali italipa fidia eneo la uwanja, wakati inafanya mipango ya Ujenzi. Wananchi wa Newala wanaomba Serikali ilipe fidia eneo la Uwanja wa Ndege ambalo halina mazao mengi ya kudumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami toka Newala Mjini kuelekea Masasi palitengenezwa mfereji wa kutolea maji barabarani. Mfereji huu umeleta uharibifu mkubwa kwa kutengeneza korongo kubwa zinazotishia usalama wa nyumba za wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika katika Kijiji cha Mkunya, korongo kubwa lililosababishwa na mvua linahatarisha usalama wa nyumba za wananchi. Alipotembelea Wilaya ya Newala, Mheshimiwa Waziri Mbarawa alikagua eneo la korongo la Newala Mjini, akaahidi kutafuta fedha za kujenga makorongo hayo vizuri. Wananchi wa Newala tunakumbusha ahadi ya Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. KEPT. MST. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nipate kuchangia kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Newala Mjini. Mimi nataka kutangulia kusema naunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nataka nichukue nafasi hii kuwapongeza vijana wangu wa Young Africans Sports Club kwa kuchukua ubingwa wa nchi hii kwa mara ya tatu, kama nilivyowaagiza vijana, nataka mje Dodoma, mcheze mpira hapa Dodoma lakini mje na kikombe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nataka pia niwapongeze vijana wetu wa Serengeti Boys kwa kazi nzuri waliyoifanya jana kuifunga Angola. Nataka niwashukuru Watanzania wote waliochangia Serengeti Boys kufika mpaka pale na mimi nina imani watafika mbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni mkulima wa korosho, kwa hiyo nitazungumza masuala ya korosho. Kwanza, nataka nichukue nafasi hii kuwapongeza sana wakulima wote wa korosho katika nchi hii kwa sababu mwaka huu zao…

T A A R I F A . . .

MHE. KEPT. MST. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa hiyo nimeipokea na ninawaagiza vijana wa Yanga wakashinde mechi iliyobaki ya Mbao ili mjadala wa mezani usituhusu kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nimesema nawapongeza wakulima wa korosho nchi nzima, mwaka huu limekuwa zao la kwanza kwa kuingiza mapato mengi katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, leo mimi nina furaha sana, hakuna mjadala wa Wizara ya Kilimo ninaouchangia kwa raha kama leo kuliko mwaka wa jana. Kuna sehemu moja tu sijaridhika na nitawaambia, lakini nataka nianze kuipongeza Serikali kwa kutufanyia yafuatayo wakulima wa korosho. Kwanza Bodi imeundwa upya, juzi tulikuwa na mkutano wa wadau, ulikuwa mzuri, nawapongeza, hatujawahi kuwa na mkutano wa wadau mzuri kama wa mwaka huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nataka nikupongeze ndugu yangu Waziri kwa kuvunja ule uongozi wa Mfuko wa Uendelezaji wa Zao la Korosho, pale palikuwa pananuka rushwa. Watu waling’ang’ania pale, kila mwaka ni hao hao, ukitaka uwabadili haiwezekani, walikuwa wanafanyaje, wanajua wao. Na tumeona matunda sasa kwamba ule mfuko umekuja kwenye bodi mwaka huu, nitaeleza baadaye matunda yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuipongeza tena Serikali, juzi mmetutangazia, na ninataka wakulima wote wa korosho Mtwara, Mkinga, Pwani, Lindi mjue kwamba Serikali yenu juzi imetutangazia mwaka huu tutagaiwa sulphur bure, hiyo ndiyo neema ya Serikali ya Awamu ya Tano, tutagawiwa magunia bure, Mungu akupe nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nataka kuchukua nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kuondoa kero, mimi sitaki kurudia, lakini nataka kutaja zinazonihusu mimi mtu wa korosho. Kero ya unyaufu, mtunza ghala, task force, usafirishaji, ushuru wa chama kikuu; ninaiomba tu Serikali mkishafuta haya mhakikishe kwamba mikoani kule inatekelezwa kama mlivyoagiza. Kwa sababu msimu wa mwaka jana kuna mikoa ilipindisha baadhi ya maagizo ambayo mliyatoa, watu kule wakatozwa unyaufu, wakatozwa task force. Mheshimiwa Waziri, mimi naomba maagizo yatekelezwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nichukue nafasi hii kupongeza sana Mfumo wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani. Sisi kule Mtwara, Lindi, tunasema Mfumo wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani ndiyo mkombozi wetu. Tumepata bei nzuri ya korosho mwaka huu, kubwa sana. Na hii imetokana na ushindani, siku zote wananunua India peke yake, mwaka huu wamekuja Vietnam, ushindani ule ndio umetufanya tupate bei nzuri. Wapo watu wanasema wao ndio wameongeza bei ya korosho, kama wewe umeongeza bei ya korosho, je, nani ameongeza Lindi, nani ameongeza Mkinga?

Mheshimiwa Naibu Spika, korosho mwaka huu tumepata bei nzuri kwa sababu ya ushindani katika mtindo wetu wa stakabadhi ya mazao ghalani kwa sababu ya ujio wa watu wa Vietnam.

Mheshimiwa Naibu Spika, mkitaka kujua Watanzania kwamba kweli mwaka huu tumenufaika na korosho, mwaka jana wakulima wa korosho tuligawana shilingi bilioni 203 tu basi, lakini msimu huu uliomalizika tumegawana bilioni mia nane na tisa, kutoka shilingi bilioni 203 mpaka shilingi bilioni 809, hii ni hatua kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nihame hapo niende kwenye ushirika; hapa ndipo niliposema, nimesema na kusema. Mheshimiwa Waziri ushirika una misingi yake, Rochdale Principles za Cooperative Unions. Rochdale Principles za Cooperative Unions zimekuwa ndizo zinazofuatwa na International Cooperative Alliance. Moja inasema democracy ndani ya vyama, Serikali ihakikishe kwenye ushirika kuna democracy. Sisi kule Mtwara tuna chama kinaitwa TANECU, kina vyama 55 Newala na 124 Tandahimba, jumla vyama 179, hawawezi kusimamia hawa, kama ingekuwa kompyuta unasema computer overload, ndivyo ilivyo TANECU, Newala, uongozi unashindwa kwenda chama kwa chama.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumepeleka miaka mitatu iliyopita, wameomba vyama Newala kwa muhtasari, Tandahimba kwa muhtasari, tunaomba mkutano mkuu union tugawe chama hiki, Mrajisi akaandika barua akasema gaweni, Mrajisi aliyekuwepo amehudhuria mikutano yote, agizo lake la kusema gaweni halikujadiliwa hata siku moja. Naomba Serikali kwa madaraka ya Mrajisi gaweni TANECU kwa sababu ndiyo matakwa ya watu wa Tandahimba na Newala. Mwaka jana, mwaka huu Council ya Newala, Council za Tandahimba wameomba kugawa TANECU ili pawe na ufanisi. Ndugu yangu Mheshimiwa Waziri, mimi na wewe tunapatana kweli, tunakosana katika hili moja tu basi, hili ukilimaliza basi! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi nilitaka kusema hayo, lakini neema ya hela iliyoingia mwaka huu Mtwara imesababisha watu wengine kujitokeza uhodari wa wizi hasa kule Masasi, wizi mkubwa kwenye vyama vya msingi, mmekagua mmekuta shilingi bilioni tatu zimeliwa mmewabana wamerudisha, sasa bado shilingi bilioni 1.4 hazijarudi. Mimi naiomba Serikali, viongozi na watendaji walioshirikiana na vyama vya ushirika kutuibia hela yetu ya korosho wote washughulikiwe na vyombo vya dola, wote, msibague, msishughulike na vingozi wa vyama vya msingi peke yake, tazameni nani alishirikiana nao na yeye aende akasimame mahakamani. Hapo ndipo watu wa Mtwara na Lindi tutafurahi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nataka niseme ushirika wa TANECU umeandikishwa kama ushirika wa mazao, lakini wananunua korosho peke yake. Naomba Waziri, Vyama vya Ushirika vinunue na mazao mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kwa ushirika, nasema moja ya misingi ya ushirika niliyosema (Rochdale Principles) inasema corporate social responsibility, chama kikitengeneza faida kirudishe kiasi cha hela ile kwenye jamii, watengeneze barabara, wasaidie shule, wasaidie hospitali, vitanda vya wagonjwa; TANECU tangu imetengenezwa faida miaka nenda rudi, tumewasema, juzi ndiyo wameanza kutoa mifuko kumi ya saruji kwa ajili ya sekondari. Hivi hela inayotengenezwa TANECU unatoa mifuko kumi, si aibu? Mbona mifuko kumi mimi naweza kuitoa hata ukiniamsha usingizini? Kwa hiyo, wasimamieni, waulizeni kuhusu corporate social responsibility wanafanya nini.

Sasa mimi nataka kurukia kwenye suala la mihogo. Mimi nimeshukuru Serikali yetu imesaini mkataba na China, sisi Mtwara ndio wakulima wakubwa wa mihogo, mwaka 1974 nchi hii ilipata njaa, wakati National Milling inanunua mihogo tumelisha mikao kumi, mihogo iliyokuwa imenunuliwa na National Milling Mtwara.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mtwara tuko tayari kupeleka mihogo China, Mheshimiwa Waziri tuambie lini inahitajika, tumeacha kulima mihogo kibiashara (commercially) tunalima tu ya kula sisi wenyewe, tumefurahi kusikia neema hiyo ya China.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwisho, naona kengele kama inapiga, sisi kule pia tunalima soya, soya ile imesimama kwa sababu haina soko.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwisho, naomba ndugu yangu simamia vile viwanda viwili vya korosho Newala vifufuliwe, wale watu walionunua, kimoja kinafanya kazi kwa robo na kingine hakifanyi kazi kabisa. Ahadi ya Rais alipokuja Newala ilikuwa kwamba viwanda hivi tutavifufua ili wananchi wa Newala wapate ajira…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. KEPT. MST. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Nampongeza sana mdogo wangu Waziri, ameanza vizuri aendelee vizuri pamoja na Naibu wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama kueleza hoja moja tu, baadhi ya watu mmezungumza juu ya utendaji kazi wa Idara ya Usalama wa Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme kama ifuatavyo, ukijua kazi inayofanywa na Idara ya Usalama wa Taifa yale mliyoyazungumza humu ndani msingeyazungumza, ninayo sheria hapa ya Usalama wa Taifa ya mwaka 1996 nataka nikusomeeni kwa mujibu iliyopitishwa na Bunge, nataka nikusomeeni kazi za Idara ya Usalama wa Taifa, ukizisikiliza hayo yote mliyoyasema hayahusiani na Idara, fulani kapotea police case, fulani kaumizwa police case, haihusiani na Idara ya Usalama wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kifupi kazi ya Idara ya Usalama nchi yoyote ni kutafuta habari na kuishauri Serikali.

Nasema imeandikwa kiingereza Mimi nitasema kwa Kiswahili kwa sababu ili Watanzania wanaosikia waliopo hapa wote tupate uelewa mmoja kifupi ninachotaka kusema hoja mlizozitoa kuhusu Idara hazihusiani na Idara, hoja mlizozitoa kuhusu Idara haishauri Serikali mambo ya uchumi, haifanyi nini, haifanyi nini hamna ushahidi, katika nchi zote duniani Idara ya Usalama inatafuta habari nakuishauri Serikali yake kimya kimya (Makofi).

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana hakuna nchi utasikia msemaji wa Idara ya Usalama wa Taifa kasema hili, kasema hili, hakuna kitu kama hicho, kwa hiyo unaposema Serikali hawakuishauri unao ushahidi?

Sasa Sheria inasema hivi; “Subject to the control of the Minister the functions of the service shall be” shughuli zimewekwa nne;

(a) to obtain, correlate, and evaluate intelligence relevant to security (kukusanya habari, kutafuta habari na kuzifanyia tathimini) wanapofanya hayo hawayafanyi kwenye mkutano wa hadhara.

(b) To cooperate as far as practicable and necessary with such other organs of state (kushirikiana na vyombo vingine vya Idara zinazoshughulikia na usalama wa nchi), mna ushahidi hawana ushirikiania nao.

La tatu, linasema; to advise Ministers, where the Director-General is satisfied that it is necessary to do so (kuwashauri Mawaziri, kuishauri Serikali).

La nne, inasema to inform the President, and any other person or authority which the Minister may so direct, of any new area of potential espionage, sabotage, terrorism or subversion. Haya yote haya mambo ya kuhujumu uchumi ya nini, nini yanafanywa kimya kimya hakuna nchi inaita mkutano wa hadhara na kusema jamani tumevamiwa, hakuna nchi inaita mkutano wa hadhara na kusema tumefanya hivi, tumefanya hivi ninaomba Waheshimiwa Wabunge...

Mdogo wangu Zitto nakuheshimu sana, nimepewa mimi nafasi ya kuongea, ulipewa nafasi ya kuongea, hivi kwa nini mna-disturb wenzenu wakisema.

Sasa kwa sababu ya dakika tano nataka nifunge pia kwa haya maneno yamo ndani ya sheria inasema hivi; “It shall not be a function of the service (haitakuwa shughuli ya Idara ya TISS) (a) to enforce measures for security; mambo ya mabavu mabavu kushika, kumkamata huyu haitakuwa kazi yake. (Makofi)

(b) Inasema; to institute..., sikilizeni nikupeni darasa.(Makofi)

(b) Inasema haitakuwa shughuli ya Idara to institute surveillance of any person or category of persons by reason only of his or their involvement in lawful protest, haitakuwa kazi ya Idara ya Usalama wa Taifa kumchunga chunga mtu, kumfuata fuata imo ndani ya sheria. (Makofi).

Kwa hiyo, kifupi ninachotaka kusema ndugu zangu, tukitaka kusema mambo mazuri yanafanywa na Idara hii mashahidi ninyi mimi nataka kutoa mfano, palikuwa na kilio mahala palikuwa kuna msiba, watu waliofiwa wamenuna, wakataka kumpiga kiongozi wa chama, wakamwambia wewe ndiye umesababisha mtu wetu afe, alitoroshwa na watu wa Idara ya Usalama nini hamjui? (Makofi/Kicheko)

Kwa hiyo, tatizo mkiambiwa yale mnayoyajua yanayowauma mnapiga kelele.

Mheshimiwa Naibu Spika, Nakushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. KEPT. MST. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Mtwara haujafanya vizuri mitihani ya darasa la saba hata kidato cha pili. Moja kati ya sababu zilizotufikisha hapo ni uhaba wa walimu, Mkoa una upungufu wa walimu kwa asilimia 40. Baadhi ya shule za msingi zina walimu watatu wakati madarasa ni saba.

Je, watafundishaje? Tunaomba Wizara inapoajiri walimu izingatie kuwa Mkoa wa Mtwara una upungufu mkubwa hivyo wapewe walimu wengi ili walingane na mikoa mingine.

Suala la pili ni vuguvugu la kufuta ujinga wa kutojua kusoma na kuandika limepungua sana. Waratibu wa Elimu Kata zamani walikuwa wasaidizi wa EWW. Idadi ya wananchi wasiojua kusoma na kuandika inaongezeka mwaka hadi mwaka, Wizara ifufue na iweke mkakati wa kufufua EWW. Waratibu wa Elimu Kata hawana kazi nyingi wapewe jukumu la kusimamia EWW kama ilivyokuwa hapo zamani.

Tatu, hali ya taaluma katika shule za msingi na sekondari hairidhishi na hii inasababishwa na shule zetu kutokaguliwa, wakaguzi hawatoshi na hawana usafiri. Serikali iongeze idadi ya wakaguzi na wapewe usafiri wa uhakika ili waweze kukagua shule zao zote. Naunga mkono suala la kuifanya Idara ya Ukaguzi kuwa Wakala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Dokta John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua anazochukua kukabiliana na Upotevu wa Mapato ya Serikali katika Sekta ya Madini
MHE. CAPT. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa tena nafasi. Mimi leo nimefarijika sana katika Bunge hili. Watu wote waliochangia upande wa CCM na upande mwingine hakuna aliyesema Rais kakosea. Hakuna aliyesema Rais kakosea, mwingine anasema hapana tunashangilia mapema mpira, tusubiri mwishoni. Mimi ninavyofahamu mpira unashezwa dakika 90, filimbi ikipigwa tu mwenye timu yake anashangilia hangoji dakika ya mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema kwa kifupi sana, ndugu yangu pale Mheshimiwa King ameunga mkono hoja tunashukuru, Mheshimiwa Mchengerwa ameunga mkono hoja tunashukuru, ndugu yangu Mheshimiwa Mtolea pale ndiyo yule kasema kwa nini tunapongezana bado safari ni ndefu (encouragement), watu wote wa Tanzania wanajua kwamba Rais anafanya kazi ngumu ili aendelee kuifanya ile kazi nzuri anahitaji kutiwa moyo, ndiyo hiki tunachokifanya hapa. Hata hivyo, nampongeza ndugu yangu Mheshimiwa Mtolea, wala hajasema Rais kakosea kuunda wala hajasema, ndiyo nilichompenda hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia anasema tuongeze nguvu za kuzuia dhahabu. Kwa upande mwingine ukilinganisha lugha yake hiyo ni kama vile yupo pamoja na Rais, hivi wenzangu mnaonaje? (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu Mheshimiwa Hasunga ameunga mkono hoja, lakini hili suala la mikataba mimi nilisikiliza juzi Rais wakati anapoongea, alisema yale mambo ya kisheria, pale ambapo mikataba haikukaa sawa, pale ambapo sheria haikukaa vizuri, Serikali itatuletea hapa Bungeni ili tuipitie na kurekebisha. Sasa naomba usitie unga kupika ugali kabla maji hayajachemka. Ukitia mapema utapata uji badala ya ugali. Tusubiri muda ukifika hiyo kazi tutaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu yangu Mheshimiwa Kangi Lugola ameunga mkono, ndugu yangu Mheshimiwa Tundu Lissu pale alikuwa anacheka maana yeye pamoja na lugha yote ya ukali, hakuna Mheshimiwa Tundu Lissu aliposema napinga Rais kuunda Tume, mmemsikia anasema hivyo? Tuko naye pamoja katika hili. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua Bunge moja hapa aliwahi kuja Spika wa Bunge la Kenya anaitwa Ole Kaparo, akasema kwamba, katika nchi zingine vipo vyama vinaitwa Chama Pinga. Chama Pinga maana yake yeye hata ukimwambia mbili jumlisha mbili jawabu nne atakwambia hapana tano. Sasa sifikiri kama ndugu yangu Mheshimiwa Tundu Lissu amefika huko kwenye hatua ya kusema mbili jumlisha mbili saba. Kwa hiyo, nasema nimemsikiliza sana ndugu yangu Mheshimiwa Lissu yeye ni mzalendo na jana kwa mfano hata wenzetu upande wa Upinzani walisema,. tulikuwa tukipiga kelele hamkutusikia, hamkutusikia, sasa tumekusikieni leo, si mseme basi Alhamdulillah mmetusikia. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lile la kuwasifu Marais waliotangulia nadhani Mkuu wa Shughuli za Serikali Bungeni kasema, sisi ni Bunge la mwaka 2015-2020 tunashughulika na mambo yaliyomo ndani ya kipindi chetu. Wale Marais waliotangulia walianza Magufuli anaendeleza pale walipoachia wenzake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, kama nilivyosema sitaki kupoteza muda, hili Azimio limepokelewa vizuri, pande zote mbili wamelipamba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. KAPT. (MST). GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, upatikanaji wa maji mradi wa maji Makonde hauridhishi. Tunapata maji ya bomba chini ya asilimia 30 ambayo ni kidogo sana ukilinganisha kitaifa. Moja, booster station ya kati ya Mkunya na Makote ilijengwa tangu 2006 lakini haijakamilika na haijakabidhiwa, kwa nini hawaifanyii kazi? Serikali ieleze mradi huu utakamilika na kukabidhiwa lini.

Mheshimiwa Naibu Spika, mbili, mabomba na mitambo ya Mradi wa Maji Makonde yamechakaa. Chanzo cha Mkunya kinatakiwa kuwa na pump tatu lakini iko moja tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, chanzo cha Mitema kinahitaji pump sita ila ziko mbili tu. Mradi uliagizwa kutangaza tenda ya kubadilisha mabomba kwa shilingi bilioni mbili, mkandarasi alipatikana lakini fedha hazikutumwa. Serikali inunue kwanza pump na iharakishe upatikanaji wa mkopo kutoka India, ulioahidiwa, ili mradi uweze kukarabatiwa na kuongeza upatikanaji wa maji. Msimu wa mvua kwetu umekwisha wasio na visima hawawezi tena kukinga maji ya mvua.

Mheshimiwa Naibu Spika, skimu ya umwagiliaji ya Chikwedu – Chipamanda. Tumeelezwa mkataba bado kwa sababu taratibu za manunuzi zimechelewa Ofisi ya Mkurugenzi wa Wilaya. Hili halikubaliki, halmashauri isimamiwe skimu iweze kukamilishwa tuweze kuendeleza kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nne, Wilaya ya Newala ilikuwa na mradi mdogo wa maji – Luchemo. Mradi huu ulikumbwa na mafuriko mwaka 1990 hivyo ukafa. Wizara haijachukua hatua za kuufufua. Nashauri mradi huu ujengwe upya maana wananchi waliokuwa wanategemea mradi huo sasa hawapati maji safi ya bomba.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. CAPT. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nianze kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kusema na kwa sababu katika Bunge hili ni mara yangu ya kwanza kuzungumza. Nataka niwashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Newala Mjini kwa kunirejesha tena katika jengo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo mengi ya kusema kabla sijaenda mbali. Nikiwa ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa Klabu ya Yanga nataka kuipongeza klabu yangu ya Yanga kwa kuchukua ubingwa. Vijana wetu tunawapongeza, mmefanya yale tuliyowatuma mfanye, tunataka mfanye hivyo na nchi za nje pia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo mimi nataka nichukue nafasi hii kuwapongeza maraisi waliotokana na Chama changu kwa kushinda uchaguzi. Tupo awamu ya tano ya maraisi, na faraja niliyonayo kwamba wote waliopokezana vijiti wametoka Chama cha Mapinduzi.
Nampongeza Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa kushinda, nampongeza Mheshimiwa Makamu wa Rais, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, naipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais, Mabaraza ya Mawaziri yote ya Muungano na lile la Baraza la Mapinduzi Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuna kazi moja tu ya kutekeleza Ilani ya Uchaguzi, pamoja na Waheshimiwa Mawaziri chapeni kazi. Ukimsikia mtu anakuambia mnakwenda kasi muulize nilipoapishwa niliambiwa niende speed gani? Kwa hiyo, mimi nataka kupongeza sana. Lakini wanasema mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. (Makofi)
Ndugu zangu uongozi wa nchi ni kupokezana. Kabla ya Magufuli tulikuwa na Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, kafanya mambo mengi nchi hii. Mimi nataka niwape mfano ambao ni my personal experience.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimaliza shule form four mwaka1967 wengi mlikuwa hamjazaliwa. Shule inaitwa St. Joseph College Chidya, nikapelekwa kwenda Ilboru, kwa sababu ya matatizo ya mawasiliano ya Mtwara na Arusha mimi nilikuwa natembea wiki nzima kwa gari katika barabara ya vumbi kutoka Newala, Nachingwea, Tunduru, Songea, Njombe, Iringa, Morogoro nikifika Chalinze napanda basi kwenda Arusha; wiki nzima niko njiani, hatukuwa na barabara ya lami. Akaja Mzee Mwinyi akatuanzishia daraja, Mzee Mkapa akatujengea daraja, Jakaya akatuwekea lami. Leo unatoka Newala kwa gari saa nane mchana na saa mbili jioni upo Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amefanya kazi nzuri, ametuwekea sekondari kila kata, amejenga barabara za lami nchi hii, kama ilikuwa ni kushindana ndiye anayeongoza kwa kujenga barabara za lami nyingi kuliko waliomtangulia. Kigoma mlikuwa mnalalamika tupo gizani, ameondoa tatizo la umeme, amewawekea daraja mto Malagarasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwanza tunampongeza Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, ameiongoza nchi salama miaka kumi amemaliza, kijiti amemkabidhi Mheshimiwa John Pombe Magufuli, sasa sikilizeni kazi ya Magufuli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya miezi sita tu vijana wanasoma bure toka fstandard one mpaka form four, ndani ya miezi tu. Ndani ya miezi sita amesema ile Mahakama ya Ufisadi mliyokuwa mnaidai tarehe 01 mwezi Julai inaanza. Miezi sita bado…
(Hapa baadhi Wabunge walizungumza bila kutumia vipaza sauti)
Mtu mzima naongea mambo ya kuzomea zomea wakati hujaruhusiwa, mtu mzima anaongea. Mimi nilidhani mnawafanyia vijana wenzenu hata mimi size ya mzee wenu? (Makofi)
MKUCHIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani hii disturbance iliyotokea utaniongezea muda. (Makofi/Kicheko)
Kwa hiyo nasema nchi ipo salama. Ametoka Rais wa CCM amemkabidhi kijiti Rais wa CCM, ilani ya uchaguzi iliyokuwa inatekelezwa sasa Mheshimiwa John Pombe Magufuli amechukua pale alipoacha Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, ndiyo maana nchi ipo shwari, haijashikwa na watu wababaishaji, imeshikwa na watu makini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa baada ya kusema hayo niseme mengine. Kwanza nataka niombe sana Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli ana nia nzuri na nchi hii, Mawaziri wake wana nia nzuri na nchi hii, hebu tuwape ushirikiano ili Tanzania pawe mahala pazuri pa kuishi. Mbona kila nchi nje huko wanatupongeza? Wanawashangaeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa baada ya kusema hayo nataka kwenda kwenye barabara. Nataka niishukuru Serikali yangu ya CCM Serikali sikivu, watu wa Mtwara tumeomba barabara ya lami kutoka Mtwara – Tandahimba – Newala – Masasi. Hotuba ya Waziri inasema bajeti ya mwaka huu kuanzia tarehe 1 Julai, 2016 barabara inajengwa. Naomba watu wa Tandahimba, Newala, Masasi, Mtwara, kazi mliyotutuma tumeifanya majibu ya Serikali ndio hayo, barabara itajengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili barabara ya mkoa. Mheshimiwa Waziri Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Mtwara tumeomba barabara ya mkoa kutoka Newala – Nyambe – Ndanda ichukuliwe na mkoa kwa sababu, watu wa Tandahimba na Newala Hospitali yetu ya Rufaa ni Ndanda. Tunaomba ombi hilo lichukuliwe barabara iwe ya mkoa ili iweze kutengenezwa vizuri kwa sababu, Halmashauri zetu uwezo umekuwa mdogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Newala tulikuwa na uwanja wa ndege ambao umetumika sana wakati wa vita vya Msumbiji. Bahati mbaya nyumba zimejengwa karibu sana mpaka uwanja wa ndege ule umefutwa, lakini Halmashauri imeomba ipewe barua rasmi ya kuufuta uwanja wa ndege wa Newala, hilo jambo halijafanyika, tunaomba lifanyike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, Wilaya tumetafuta eneo la kuweka uwanja wa ndege, Waziri uliwatuma wataalam kuja kuona, wametuambia shughuli gani tufanye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba suala la ujenzi wa uwanja wa ndege Newala, utakapokuwa unajibu, watu waliozoea kuwa na uwanja wa ndege tangu enzi ya mkoloni sasa inapokuwa hatuna uwanja wa ndege tumerudi nyuma. Tutapenda kusikia kauli ya Serikali kuhusu lini mnaanza kujenga uwanja wa ndege wa Newala, lakini kwa hatua za awali tunaomba wale watu wafidiwe eneo lile mlichukue. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Newala tuko mpakani na Mto Ruvuma; nimeona hapa hotuba kivuko hapa, kivuko hapa, sisi tuna mawasiliano ya karibu sana na Msumbiji. Kuna daraja kule la Umoja, kuna daraja la Kilambo, lakini Tandahimba na Newala pale tuna vivuko vingi na nafikiri ndio tunaingiliana zaidi na watu wa Msumbiji kwa sababu ya kupakana, kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri, Wizara iangalie uwezekano wa kutuwekea kivuko katika Mto Ruvuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, iko barabara inaitwa barabara ya Ulinzi, hii ni barabara inatoka Mtwara inaambaa ambaa kandokando ya Mto Ruvuma mpaka Tunduru mpaka mkoa wa Ruvuma. Barabara hii haijatengenezwa miaka yote na Serikali kuu, muda mrefu mmeaicha kuitengeneza, tunapata tabu kusomba korosho kwa sababu ya hali ya barabara na korosho za Mtwara nyingi zinatoka katika bonde la Ruvuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, nilikuletea barua, bado uko mgeni Wizarani kwamba, vijiji vya bonde la Ruvuma Wilaya yangu ya Newala, hawana mawasiliano ya simu. Walikuwa wanatumia simu za Msumbiji ambazo dakika moja tu shilingi 1,000, lakini haraka haraka ulituma watu wako, watu wa Halotel wakaja, bonde la Ruvuma leo Halotel ni Halotel kweli kweli. Tatizo lile la watu wa Newala, watu wa Tandahimba kutumia simu za Msumbiji umetuondolea tuko ndani ya Halotel ndani ya nchi yetu. Mheshimiwa Waziri, mimi nataka nikushukuru sana kwa uharaka wako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, nakushukuru, lakini kwa kumalizia uwanja wa ndege wa Mtwara uwe uwanja wa Kimataifa wa Mtwara. Ninakushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. KAPT. MST. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Napenda nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kuteuliwa kuongoza Wizara hii, lakini nataka nikupe pole kwa kazi ngumu iliyoko mbele yako, kati ya wewe na wapiga kura wangu, wanaotegemea Mradi wa Maji Makonde, ambao upatikanaji wa maji badala ya kupanda umeporomoka. Tunapata maji asilimia 30 ukilinganisha na vijiji vingine au Wilaya zingine ambako wameshafika asilimia 65 vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea Waziri hoja yangu ni kwamba wala hatutaki Tandahimba, Newala Mtwara kunakofika huu mradi, hatutaki hela za kuendesha mradi, tunataka hela za kukarabati mradi ili kuongeza uzalishaji wa maji. Mchango wa wananchi wanaotegemea mradi huu kwa Serikali kila mwezi ni mdogo sana, kwa sababu maji mnayotuuzia ni kidogo sana, hatuna tatizo la kuchangia maji kwa sababu tangu tulivyoaanza Makonde Water Corperation tulikuwa tunanunua maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ujumbe wangu siyo kupitisha mafungu ya kuwezesha uendeshaji wa Mradi wa Maji Makonde, hoja leo hapa utakapokuwa unamalizia kesho kutwa, ueleze nini Wizara yako inafanya kuongeza uzalishaji maji kwa Mradi wa Maji Makonde. Mheshimiwa Waziri wewe umefika kule lakini nataka kukuomba, Naibu Waziri alikuja juzi wakati mvua inanyesha, watu wa Tandahimba, Newala ni hodari kwa kuvuna maji, kila nyumba ya bati utakayoiona tunachimba kisima, tunavuna maji ya mvua, mimi naishi kijiji kwangu, sina maji ya bomba katika nyumba yangu, nina visima viwili, napata maji ya shower na ya kunywa kwa sababu tunachimba visima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa Tandahimba na Newala kama wangelitegemea tu maji ya bomba ya Serikali hali yetu ya maisha ingekuwa ngumu sana. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri ninachoomba hapa siyo utueleze unafanya nini katika administration uendeshaji wa Mradi wa Maji Makonde, aaah aah! Utakapokuwa una- wind up utoe maelezo nini Wizara yako inafanya kuongeza uzalishaji wa maji katika Mradi wa Maji Makonde. Hiyo ndiyo hoja yangu, umri huu siyo wa kutoa shilingi, lakini kama hutatufikisha huko, kuna vijana wengine humu ndani wanategemea mradi huo huo mimi nitakaa pembeni huku nawapigia kwa chini chini (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Maji Makonde, Tatizo la maji Newala, Tandahimba ni kubwa kwa sababu ya jiografia, ile inaitwa Makonde plateau, niliposoma jiografia niliambiwa a plateau is arised flat peace of land. Plateau ni kitu gani, ni eneo ambalo limeinuka, na juu kuko flat ndivyo ilivyo uwanda wa Makonde ukija kwetu Tandahimba na Newala, ukienda Masasi, Mto Ruvuma, Lindi, Mtwara unateremka, ndiyo maana katika eneo la kwetu hatuna agenda visima vifupi haipo. The water table is so below unaweza ukachimba hata maili ngapi sijui, siku hizi mnatumia kilometa, unaweza ukachimba sijui kilomita ngapi hujapata maji, hatuna visima vifupi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia hapa the oldest scheme ya maji ambayo inaendeshwa na Taifa ni Mradi wa Maji Makonde, lakini naona tumepewa shilingi bilioni mbili. Shilingi bilioni mbili upeleke maji Tandahimba yaende mpaka Mtwara, mradi mwingine wa Kitaifa three hundred thirty thousand Euro, mradi mwingine twenty thousand billion, mradi mwingine three point; Mradi wa Maji Makonde shilingi bilioni mbili, Waziri naomba hili jambo ulitazame.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo sitaki kwenda katika historia, watu wa Newala - Tandahimba baada ya kuona shida zetu za maji ni kubwa, enzi ya mkoloni 1953 tulianzisha kampuni iliyokuwa inaitwa Makonde Water Corporation, kwa wazee waliokuwepo hisa ilikuwa shilingi 20 kampuni ikaenda kukopa hela Uingereza ikaanzisha Mradi wa Maji Makonde na mwaka 1954 mradi ukafunguliwa kwa sababu palikuwa na cost sharing kila mwaka tulikuwa tunapeleka maji vijiji vipya, maji yakawa yanapatikana bila matitizo every domestic point.
Baada ya mradi kuchukuliwa na Serikali kusema sasa hapana, tuachieni tunaendesha sisi tumerudi nyuma. Nimekaa Bungeni hii term ya tatu, nilipoingia upatikanaji wa maji Newala ulikuwa 22 percent miaka yangu kumi ya kufurukuta pamoja na uzito niliokuwa nao tumeongeza asilimia nane tu. Kama miaka kumi asilimia nane mpaka tufike hiyo asilimia 65 itatuchukua miaka mingapi? (Makofi)
Mheshimiwa Waziri ninachotaka kusema Mradi wa Maji Makonde una matatizo makubwa yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo hayo ni pamoja na uchakavu wa mitambo, mabomba yale enzi ya mkoloni hayakuwa plastic yalikuwa ni ya chuma yameoza yametoboka kwa hiyo maji yanayopotea njiani ni mengi. Hatuna pampu za kutosha, wataalam hawatoshi, vituo vichache vya kugawia maji, kwa ujumla uzalishaji mdogo wa maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri utakapokuwa unajibu narudia tena ueleze mwaka huu Serikali inafanya nini kuongeza uzalishaji wa maji Makonde, nakuomba uje kiangazi, Waziri wako alikuja wakati wa masika hakuona shida ya watu, wakati wa masika ndoo moja ya maji shilingi 1,000!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi mingine ndugu yangu pale Mheshimiwa Bwanausi ameelezea, mradi wa maji Chiwambo ulikuwa unafika mpaka Newala hauji tena, Mradi wa Maji wa Luchemo tulipata mafuriko mwaka 1990 mashine zile zikasombwa na maji tangu 1990 mpaka leo hakuna replacement. Mheshimiwa Waziri naomba sana fufueni Mradi wa Luchemo tuunganisheni watu wa Newala na Mradi wa Chiwambo kwa ndugu yangu Mheshimiwa Bwanausi na ninashukuru ameuzungumzia hapa, naomba sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kwamba tunapata taabu Viongozi, mradi wa maji wa Kitangari – Mitema, Mji mdogo wa Kitangari upo kilomita tatu kutoka pale, hawapati maji. Maji yale ya Mitema yanasukumwa yanafika mpaka Tandahimba, hapa kwenye source ya maji hawapati maji.
Mimi mnanipa taabu sana maana inabidi niwabembeleze wapiga kura wangu, wanataka wapige shoka maji yale ili tukose wote, nawaambia hapana subirini Serikali inachukua hatua, sasa mwisho nitaitwa muongo, hivi umri huu na mvi hizi niitwe muongo Mheshimiwa Waziri unafurahi? Hivyo, tuaomba tatizo la maji la Mji Mdogo wa Kitangari lishughulikiwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo tatizo sugu ambalo watumishi wa maji Newala hawataki kusikia. Tumepitisha maazimio kwenye Halmashauri, marufuku kupeleka maji katika visima vya watu binafsi, palekeni maji katika domestic point za public pale ambapo kila mmoja anapata maji. Maafisa wako wanachofanya wanapeleka maji katika nyumba za watu binafsi, wanawajazia maji baadae wale wanawauzia wananchi maji ndoo shilingi elfu moja, ukiwaambia kwa nini hampeleki katika domestic point ambayo watu wote tunapata pale hawana majibu! Jawabu nini corruption. Hebu Waziri tamka kesho kutwa utakapo wind up na uwaagize watumishi wa maji Newala kwamba….
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja nakutakia kila la kheri mdogo wangu unijibu vizuri kesho kutwa. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE.KAPT.MST. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwakunipa nafasi, nitangulie kusema kwamba, naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kupongeza sana kazi nzuri inayofanywa na majeshi yetu. Kazi nzuri inayofanywa na askari waliopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, bila wao hapa Tanzania pasingekalika, wanafanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe pole kwa ndugu zangu wa Rufiji, Kibiti, wajukuu zangu kwa mikasa wanayopata, wanauawa bila sababu, lakini kama mlivyosikia Jeshi la Polisi liko pamoja na ninyi jambo hili la muda litazimwa na majeshi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitoe pole kwandugu wanaohusika na msiba wa jana kule Arusha, niseme jambo moja, mchangiaji mwenzetu mmoja hapa asubuhi alisema kwamba itakuwa vizuri kama kila Mbunge akaonja jela, ili kuweza kujua mambo ya kule ndani. Nataka nimjibu kwamba Wabunge wa Tanzania ni waadilifu sana, tunajitahidi kila tunavyoweza ili tusiende jela na kwa sababu tulimpata mtu kaenda jela katusimulia, imetosha. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nijikite katika Jeshi la Zimamoto. Kwamba, Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Jeshi la Zimamoto kama Jeshi bado ni change, ilikuwa ni Idara chini ya Jeshi la Polisi lakini baada ya kufanywa kuwa Jeshi la Zimamoto na Ukoaji, Wizara mnatakiwa mlilee Jeshi la Zimamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema hivi kwa sababu gani mimi ni Mjumbe ya Kamati ya Ulinzi na Usalama. Nilipotembea Majeshi ya Zimamoto tumegundua matatizo mengi. Kwa mfano, iko Tume ya Majeshi inayopandisha vyeo, kuajiri ni Tume ya Majeshi, Magereza wamo, Polisi wamo, bado hamjawaweka Zimamoto. Sasa kama hawamo kwenye Tume watapandaje vyeo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kule Zimamoto ukimwondoa Thobias Andengenya ambaye ni Kamishna Jenerali wanaomsaidia wote acting,hizo bado tangu lilipoanza Jeshi pale mpaka leo wana act? Hii inawezekana kwa sababu Tume ya kuwapandisha haipo. Natoa kutoa rai watu wale hatua ichukuliwe haraka, tuwe na Makamishna siyo acting. (Makofi)

Suala lingine kuonesha kwamba sisi Wajumbe tuna mashaka kwamba pengine Waziri jicho haliangalii sana Jeshi hilo, asubuhi umetueleza hapa majengo mapya ya Polisi, Uhamiaji, Magereza, tukawa tunasubiri Zimamoto kimya, hata hela kumalizia Zimamoto ambayo tayari wameanza kujenga kule Dar es Salaam, kimya! Niishie hapo.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nizungumzie juu ya magereza. Leo bajeti ya magereza ni kubwa kwa sababu Magereza hawajitoshelezi kwa chakula. Tumetembelea kambi za magereza nyingi tu. Tumekwenda Songwe tumeona ardhi nzuri, eneo nzuri la kulima, walituambia tunaomba Waheshimiwa Wabunge iambieni Serikali itupe matrekta, itupe vifaa vya kilimo, tuna uwezo wa kulima na kugawa chakula kwa magereza mengine, badala ya kuomba hapa Mheshimiwa Waziri hela ya magereza ya chakula omba matrekta wale watu wako tayari kujilisha wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni maeneo ya utawala. Leo Wilaya mpya zote zina matatizo ya kiutawala, kwa sababu hawana magereza hawana vituo vya polisi, hawana mahakama. Kwa hiyo, kuna kazi kubwa sana inafanywa na magereza kubeba askari kutoka Wilaya mpya kuwapeleka Wilaya mama watuhumiwa kwenda kusikiliza kesi, gharama ile ya mafuta ni kubwa. Ushauri wangu ni kwamba maeneo mapya ya utawala yanapoanza izingatiwe kwanza magereza, kituo cha polisi, mahakama ni sehemu ya utawala. Mkuu wa Wilaya hawezi kukamilika kama hana kituo cha polisi, kama hana magereza, kama hana mahakama…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE.KAPT. MST. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nilidhani dakika zangu ni kumi kumbe tano. Naunga mkono hoja kwa kuombatu kwamba Uhamiaji wajenge kituo cha uhamiaji kule Newala na mmalizie kituo cha polisi ambacho mnasema kimefika asilimia 85.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji
MHE. KEPT. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nikushukuru kwa kunipa nafasi hii kuweza kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Napenda kuchukua nafasi hii kwanza kumpongeza Rais wetu John Pombe Magufuli anavyoiendesha nchi hii. Wapo ndugu zetu walikuwa wanapiga kelele za ufisadi, ufisadi, amewafungulia Mahakama ya Ufisadi. Wale waliokuwa wanasema kwamba huyu fulani fisadi wamewachukua, tuleteeni kwenye Mahakama ya Ufisadi tuwashughulikie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua nafasi hii kuunga mkono hoja ya Wizara ya Maji. Nataka niwakumbushe Wabunge wenzangu Kanuni zetu zinasema Kamati Ndogo ya Bunge ya Kudumu inapofanya kazi ni sawasawa na Spika amekaa anaendesha Bunge. Bajeti tuliyoletewa hapa imefanyiwa kazi na wenzetu wa Kamati inayohusika na suala la maji. Kwa hiyo, unapokuja hapa tu ghafla bin vuu ukasema tufumue, turudishe, tufanyeje, mbona mnawadharau Wajumbe wenzetu wa Kamati waliofanya kazi hii?

Mimi naungana na wenzangu wanaosema tutafute namna ya kuboresha Mfuko wa Maji, yale mawazo yanakaribishwa, lakini wewe unasema tufumue, tuikatae, darasa hilo sisi wanafunzi tunalikataa, darasa la kukataa bajeti sisi tunalikataa, bajeti hii itapita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nataka nianze kwa kuwapongeza wapigakura wangu wa Jimbo la Newala. Kule kwetu Newala tuna ustaarabu wa kuvuna maji ya mvua, kila nyumba ya bati utakayoona ina kisima kimechimbwa na kwa sababu kule kwetu water table iko very low tunachimba mpaka futi 14, tunajenga kwa zege, tunajenga kwa tofali, tunakinga maji ya mvua ya kutosha familiaile mwaka mzima. Ndiyo maana hali ya maji Newala unafuu upo kidogo, si kwa sababu ya maji ya bomba ya Serikali, hapana, tunakinga maji ya mvua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tusingekinga maji ya mvua hali yetu ingekuwa mbaya sana. Nataka nitoe mfano na hili mimi nataka niiseme Serikali yangu, mnapofanya vizuri nawapongeza, mnapoharibu nawasema. Hivi mradi wa maji wa Makonde kwa muda wa miezi miwili mmewakatia umeme, watu wa Newala tupate wapi maji ya bomba ya kunywa?

Nimeambiwa umeme juzi umerudi, naomba jambo hili lisirudiwe tena. Mheshimiwa Rais aliposema kata umeme amewahimiza Maafisa wa Serikali mnaotakiwa kulipa maana yake mlipe kwa wakati siyo mnazembea kulipa halafu wanakwenda kuadhibiwa wananchi ambao kila mwezi mkiwapelekea ankara wanalipa. (Makofi)

MHE. KEPT. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, upande wa pili ule hata ukawaelimishe namna gani, huyo anayeongea…
Mheshimiwa Naibu Spika, huyo anayeongea alituhamasisha humu tuikatae bajeti, mimi sikukubaliana naye lakini nilikaa kimya, ndiyo ustaarabu wa humu ndani. Ndiyo maana tunawaambia nchi hii CCM itatawala ninyi mtabaki tu kama mnyama fulani anaona mkono wa binadamu unatembea anasema unadondoka kesho, unadondoka kesho, ndiyo mlivyo, tunakamata Serikali kesho, kesho, kama mwendo wenu ni huo hampati kushika nchi hii. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nataka wale ambao hamuifahamu Newala, Waziri anaifahamu, Naibu Waziri anaifahamu, sisi tunaishi mahali kunaitwa Makonde Plateau. Wale wanaokumbuka geography Makonde Plateau definition yake wanasema a raised flat piece of land (kipande cha ardhi kilichonyanyuka), ukiwa kwenye plateau maana yake umekaa kwenye meza, ndivyo ilivyo Newala na Tandahimba. Tuko juu kwa hiyo water table iko chini sana, hakuna mahali tunapoweza kuchimba tukapata maji na ndiyo maana tunategemea sana maji ya bomba na ndiyo maana kwenye miaka ya 1950 watu wa Newala wenyewe tukaanzisha Kampuni inaitwa Makonde Water Corporation, tukakopa hela Uingereza tukaanzisha mradi wa maji Makonde, tukawa tunauza maji, tunatengeneza pesa, watu wanapata maji ya kunywa. Serikali baada ya uhuru ikatuhurumia, ikauchukua ule mradi ikaufanya mradi wa maji wa kitaifa. Nakuomba ndugu yangu Wenje, aah nakuombandugu yangu Lwenge… (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu Wabunge ni yale yale ya kutokujua, mimi nilidhani upande wa pili wanaelewa kwamba ulimi hauna mfupa kumbe hawajui. Mimi nimewasamehe maana tumefundishwa, baba uwasamehe maana hawajui watendalo, mimi nimewasamehe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kampuni ile ya Makondeko ilichukuliwa na Serikali, ukafanywa ndiyo mradi mkubwa wa kitaifa. Mheshimiwa Naibu Waziri, mradi wetu ule wa kitaifa unasuasua kwa sababu upatikanaji wa maji siyo mzuri, miundombinu imechakaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu upande wa Wizara yale mambo ambayo nilitaka kuyamalizia nitawaandikia, mimi naunga mkono hoja.