Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Capt. (Mst). George Huruma Mkuchika (5 total)

MHE. CAPT. MST. GEORGE H. MKUCHIKA aliuliza:-
Mradi wa Maji wa Makonde ulijengwa mapema miaka ya 1950 kwa lengo la kuondoa kero ya maji katika uwanda wa Makonde wenye Wilaya za Newala, Tandahimba na sasa Mtwara Vijijini; lakini mradi huu mitambo yake imechakaa na watumiaji wameongezeka ambapo upatikanaji wa maji kwa Wilaya ya Newala ni 31% tu.
Je, Serikali inalifahamu tatizo hilo na inachukua hatua gani kutatua tatizo hili?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Huruma Mkuchika, Mbunge wa Newala Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua tatizo la upatikanaji wa maji katika maeneo mengi hapa nchini likiwemo eneo linalohudumiwa na Mradi wa Maji ya Kitaifa wa Makonde.
Mheshimiwa Spika, katika mpango wa muda mfupi mwaka 2015/2016 Serikali kwa kushirikiana na shirika la DFID kutoka Uingereza ilikamilisha ukarabati wa visima virefu sita eneo la Mitema na kufunga pampu katika visima hivyo. Kukamilika kwa kazi hizo kumeongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 7.4 hadi lita milioni 14.8 kwa siku, hivyo kuongeza huduma ya maji katika baadhi ya maeneo yanayohudumiwa na Mradi wa Makonde.
Mheshimiwa Spika, katika mpango wa muda mrefu, Serikali kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji ilifanya upembuzi yakinifu na usanifu wa Mradi wa Kitaifa wa Makonde na kugundua kuwa chanzo cha Mitema katika Bonde la Mambi kina maji ya kutosha ya kuweza kuhudumia wananchi wa maeneo mbalimbali ya Wilaya za Nanyamba, Tandahimba pamoja na Newala.
Mheshimiwa Spika, kupitia mkopo wa masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 500 kutoka Serikali ya India, Mradi wa Makonde umetengewa dola za Marekani milioni 87.41 kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa mradi huo. Aidha, wakati mradi mkubwa ukisubiriwa Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni mbili katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Mradi wa Kitaifa wa Makonde.
MHE. CAPT. GEORGE H. MKUCHIKA aliuliza:-
Mji wa Newala tangu utawala wa kikoloni ulikuwa na Uwanja wa Ndege mdogo uliowezesha kutua ndege ndogo. Uwanja huo kwa sasa umejengwa nyumba za kuishi. Kwa vile Mji wa Newala unapanuka sana na una hadhi ya Halmashauri ya Mji na Uongozi wa Wilaya umetenga eneo la kujenga uwanja mpya wa ndege:-
Je, Serikali imefikia hatua gani katika maandalizi ya kujenga Uwanja Mpya wa Ndege katika Halmashauri ya Mji wa Newala?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Huruma Mkuchika, Mbunge wa Newala Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilikifunga Kiwanja cha Ndege cha Newala mwaka 1998 kutokana na uwepo wa mazingira yasiyo salama ya uendeshaji wa ndege, uliosababishwa na makazi ya watu kusonga katika maeneo yanayozunguka kiwanja hicho. Aidha, ukatizaji wa watu kiwanjani na mmomonyoko wa ardhi uliopo eneo la kiwanja ulionekana kuhatarisha usalama wa ndege na watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya Halmashauri ya Mji wa Newala kutenga eneo jipya kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja kipya cha ndege, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, ilipeleka wataalamu wake kukagua eneo hilo na ikaonekana kukidhi vigezo vya kiwanja cha ndege kulingana na viwango vya Kimataifa vinavyotolewa na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO Standards).
Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia kukamilika kwa ukaguzi huo, utaratibu unaofuata ni kwa Halmashauri husika kutekeleza jukumu lao muhimu ambalo ni kukamilisha upimaji na uthamini wa mali zilizomo ndani ya eneo hilo. Hadi sasa hatua hizo za kulitwaa eneo husika hazijafanyika. Hivyo, kupitia Bunge lako Tukufu, Wizara yangu inawataka Halmashauri ya Mji wa Newala kukamilisha hatua za utwaaji wa eneo hilo na kulikabidhi kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege ili waweze kuanza hatua ya upembuzi na usanifu wa Kiwanja Kipya cha Ndege cha Newala.
MHE. KAPT. (MST.) GEORGE H. MKUCHIKA Aliuliza:-
Serikali iliwaahidi wananchi wa Mikoa ya Mtwara na Lindi umeme wa uhakika na wa kutosha baada ya kugundulika kwa gesi na baada ya neema ya muda mfupi hivi sasa kuna tatizo kubwa la kukatika kwa umeme mara kwa mara katika Mikoa hiyo ikiwemo na Wilaya ya Newala.
Je, tatizo ni nini na Serikali inachukua hatua gani kumaliza kabisa tatizo hili?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kepteni Mstaafu George Huruma Mkuchika, Mbunge wa Newala Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya kukatika kwa umeme mara kwa mara katika maeneo ya Mikoa ya Lindi na Mtwara inatokana na ubovu wa jenereta moja kati ya tisa katika kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia kilichoko Mtwara chenye jumla ya MW 18 ambayo imepungua hadi MW 16. Tatizo lingine ni uchakavu na urefu wa njia inayosambaza umeme wa msongo wa kilovoti 33 kutoka Mtwara kuelekea Wilaya za Mtwara – Tandahimba – Newala – Masasi – Nanyumbu- Nachingwea hadi Ruangwa ambao ni umbali wa kilometa 206.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua zinazochukuliwa na Serikali ili kuondoa tatizo hilo ni pamoja na kufanya ukarabati wa mtambo ulioharibika ili kurudisha uwezo wa kituo katika kuzalisha hali yake ya kawaida MW 18. Kazi hii inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Mei, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango mwingine ni kuongeza mitambo mingine sita yenye uwezo wa kuzalisha umeme wa jumla ya MW 12 kila moja itakayofikisha MW 30 ambao unatosheleza kwa mahitaji ya mikoa hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuboresha hali ya upatikanaji endelevu wa umeme katika Mikoa hiyo, TANESCO inajenga njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 132 yenye urefu wa kilometa 80 kutoka Mtwara hadi Mnazi Mmoja, Lindi. Kazi hiyo inajumuisha pia ujenzi wa vituo vya kupoza umeme msongo wa kilovoti 132/33 na transfoma za MVA 20 kwa ajili ya kusambaza umeme wa njia tano. Mradi huu unakamilika mwishoni mwa mwezi Mei, mwaka huu na gharama za mradi huu ni shilingi bilioni 16.
MHE. KAPT. GEORGE H. MKUCHIKA aliuliza:-
Sheria ya Jeshi la Kujenga Taifa ya Mwaka 1964 (The National Service Act. 1964) imeweka ulazima wa Vijana Watanzania wanaomaliza kidato cha sita kujiunga na mafunzo ya Jeshi la kujenga Taifa kwa mujibu wa Sheria.
(a) Je, katika miaka mitatu iliyopita ni vijana wangapi waliomaliza kidato cha sita kila mwaka na kati yao wangapi walijiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa?
(b) Je, waliojiunga ni asilimia ngapi wa waliotakiwa kujiunga?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa George Huruma Mkuchika, Mbunge wa Newala Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Sheria ya Jeshi la Kujenga Taifa ya mwaka 1964 imeweka ulazima wa vijana wa Tanzania wanaomaliza kidato cha sita kujiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa Sheria. Hata hivyo, mwaka 1994 Serikali iliyasitisha kwa muda mafunzo hayo na kuyarejesha mwaka 2013 na yameendelea kutolewa hadi sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu za vijana waliohitimu kidato cha sita na kuhudhuria mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa Sheria ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2014, vijana waliomaliza kidato cha sita ni 41,968, kati yao waliojiunga na mafunzo ya Jeshi la kujenga Taifa ni 31,692, ambayo ni sawa na asilimia 75.5.
Mwaka 2015, vijana waliomaliza kidato cha sita ni 40,753, kati yao waliojiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa ni 19,990, ambao ni sawa na asilimia 48.8.
Mwaka 2016, vijana waliomaliza kidato cha sita ni 63,623, kati yao waliojiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa ni 14,747, ambao ni sawa na asilimia 23.2.
Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zilizopo zinaonesha kupungua kwa idadi ya vijana wanaojiunga na mafunzo hayo muhimu ya Jeshi la Kujenga Taifa. Hali hii imesababishwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kugongana kwa tarehe za kuanza mafunzo ya vijana kwa mujibu wa Sheria na kufunguliwa kwa vyuo mbalimbali hapa nchini ambapo mihula ya mafunzo huanza.
Hali hii imewafanya vijana wengi walioteuliwa kujiunga na vyuo kukosa nafasi za kujiunga na mafunzo ya JKT kwa mujibu wa Sheria. Changamoto nyingine ni uhaba wa miundombinu, rasilimali watu na fedha. Hata hivyo Serikali inaendelea na juhudi za kupata suluhu ya changamoto zilizopo.
MHE. GEORGE H. MKUCHIKA aliuliza:-
Serikali ya Awamu ya Kwanza ilijenga viwanda vikubwa viwili vya kubangua Korosho kwa lengo la kuongeza thamani ya korosho, kupanua ajira na kukuza uchumi. Viwanda hivi vilibinafsishwa na mpaka sasa ni kiwanda kimoja tu kinachofanya kazi kwa robo ya uwezo wake na kingine hakifanyi kazi kabisa:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha viwanda hivyo vinafufuliwa na kufanya kazi?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa George Huruma Mkuchika, Mbunge wa Newala Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kuanzia mwaka 1992, Serikali ilitekeleza Sera ya Ubinafsishaji na kurekebisha mfumo wa uendeshaji wa Mashirika ya Umma vikiwemo viwanda. Katika kutekeleza sera hiyo, jumla ya viwanda 10 vya kubangua korosho nchini vikiwemo viwanda viwili vilivyoko Wilaya ya Newala (Newala I na Newala II) vilibinafsishwa.
Mheshimiwa Spika, lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa viwanda vyote vilivyobinafsishwa vinabangua korosho ili tupate ajira, tuongeze thamani na kuuza bidhaa yenye chapa ya Tanzania (brand) hatua itakayotupatia pato kubwa katika Shilingi za Kitanzania na fedha za kigeni. Zaidi ya uwepo wa viwanda, tunataka kuongeza wigo wa walipa kodi.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2005 Serikali iliuza asilimia 100 za hisa za kiwanda cha Newala I kwa kampuni ya M/S Agro Focus Limited kwa bei ya shilingi milioni 75 ambayo walilipa.
Mheshimiwa Spika, mwekezaji alifanya uwekezaji mkubwa ambao ulifanya kazi na kuzalisha mpaka mwaka 2013 alipofunga kiwanda. Chini ya operation inayosimamiwa na Wizara ya Viwanda na Wizara ya Fedha ambapo lengo lake ni kuhakikisha viwanda vinafanya kazi ili kupata manufaa yaliyobinafsishwa hapo juu, kiwanda cha Newala I kimehusika.
Mheshimiwa Spika, chini ya zoezi hili, mmiliki wa kiwanda amelipa deni la benki ambayo ni moja ya sababu zilizosababisha kiwanda kufungwa. Atafunga mitambo mipya na ataongeza mtaji katika shughuli za ubanguaji na biashara ya korosho.
Mheshimiwa Spika, Kiwanda cha Newala II chenye uwezo wa kubangua tani 3,500 kwa mwaka, kilibinafsishwa kwa kampuni ya Micronix Systems Limited kwa shilingi milioni 75 kwa mwaka 2004. Mwekezaji alifanya ukarabati kwa kuongeza mashine mpya, vyumba vya kukaushia korosho na jenereta la kuendesha kiwanda.
Mheshimiwa Spika, kutokana na ukarabati huo unaoendelea ubanguaji wa korosho umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka. Takwimu zinaonesha kuwa, mwaka 2013 walibangua tani 1,500; mwaka 2014 tani 1,800; mwaka 2015 tani 2,500; mwaka 2016 tani 3,000; na mwaka huu tunategemea abangue tani 3,500.