Supplementary Questions from Hon. Capt. (Mst). George Huruma Mkuchika (7 total)
MHE. CAPT. MST. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kuchukua nafasi hii kuishukuru Serikali kwa kutambua tatizo la maji Mradi wa Maji wa Makonde na kutenga fedha za kutosha kutokana na mkopo uliopatikana kutoka Serikali ya India. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, la kwanza; kitakachoondoa tatizo la maji Mradi wa Maji Makonde ni utekelezaji wa huu mradi mkubwa wa fedha ambazo tumepata mkopo kutoka India. Ningependa kumuuliza Mheshimiwa Waziri, ni lini utekelezaji utaanza wa huo mradi mkubwa?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, jirani na chanzo cha maji Mitema kama alivyosema Mheshimiwa Waziri ambako kuna maji ya kutosha, kuna mji mdogo wa Kitangari na watu wengi, pana Kituo cha Afya, Chuo cha Ualimu, sekondari mbili, watu wengi sana pale, soko kubwa lakini Mji ule ambao uko kama kilometa tatu tu kutoka chanzo cha maji hawapati maji. Maji yanafika Tandahimba, yanafika Mtwara Vijijini, pale kwenye chanzo cha maji hawapati maji. Je, Serikali inajua tatizo hili na kama inajua tatizo hili inawaahidi nini wananchi wa Mji Mdogo wa Kitangari?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ni lini utekelezaji wa huu Mradi wa Makonde kupitia mkopo wa masharti nafuu wa Serikali ya India utaanza.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusaini makubalianoya nchi mbili sasa hivi Serikali mbili zinaendelea na taratibu ili kuweza kufikia kusaini financial agreement, baada ya kusaini financial agreement kwa sababu tayari usanifu upo tutakuwa na muda mfupi sana ku review nyaraka za mradi wa Makonde na kutangaza tender na baadae utekeleji uweze kuanza. Kwa hiyo nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba haitachukua muda mrefu maana yake tatizo lilikuwa ni fedha na fedha zimepatikana kwa hiyo kilichobaki ni taratibu zingine ndogo ndogo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mji wa Kitangari ni kweli. Mji huu uko kilometa tatu na Mheshimiwa Mbunge wewe ni shahidi kwamba nilikuja pale na mpaka nikaja Mji wa Kitangari nikaongea na wananchi. Ni kweli kabisa kwamba maji yanatoka chanzo cha Mitema, bomba linapita Kitangari kwenda Tandahimba. Katika huu mradi mkubwa kwa sababu fedha ni nyingi Tutahakikisha kwamba bomba linatoka chanzo cha Mitema pale linakwenda moja kwa moja eneo la Kitangari.
Kwa hiyo, niwahakikishie wananchi wa Kitangari kwamba tatizo la maji walilokuwa nalo muda mrefu sasa kupitia mkopo huu tunalimaliza. (Makofi)
MHE. KAPT. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni taratibu dunia nzima katika mfumo wa vyama vingi Ilani ya Chama kilichoshinda uchaguzi ndiyo inayotekelezwa. Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba elimu hiyo au uelewa huo unawafikiwa viongozi wa vyama vyote vilivyosajiliwa katika nchi hii?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijajibu swali la Mheshimiwa Mkuchika, naomba nimpongeze sana kwa kushinda kesi yake ya uchaguzi na kuwabwaga wale wapinzani ambao walikuwa wanafikiri kwamba Mheshimiwa George Mkuchika hakushinda kihalali. Kwa hiyo, naomba nimpongeze sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Gerge Mkuchika ameomba kujua ni kwa kiasi gani Serikali itajitahidi kuhakikisha inatoa elimu na hasa kwa vyama ili viweze kutambua umuhimu wa kutii na kuamini kwamba Katiba inayotutawala inaelekeza ilani inayotekelezwa katika nchi ni Ilani ya chama kilichoshinda.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa kadri tunavyoendelea katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya Serikali, Serikali imeendelea kuwafahamisha Watanzania wote, vyama vya siasa vilikuwa vikipata elimu hiyo kabla ya uchaguzi na hata baada ya uchaguzi kwamba waendelee kuamini chama kilichoshinda ndicho kitakachotekeleza Ilani yake ya Uchaguzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie Bunge hili lako Tukufu kuendelea kuvikumbusha Vyama vyote vya Siasa vipitie Sheria ya Uchaguzi, vipite Katiba na vilevile viendelee kusikiliza na kupata maelekezo yanayotolewa na viongozi mbalimbali tukiendelea kusisitiza kwamba chama kilichoshinda, Chama cha Mapinduzi ndicho chenye Ilani ya Uchaguzi na Serikali itapanga mipango kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi na siyo vinginevyo.
MHE. CAPT. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kushukuru majibu mazuri ya Serikali, lakini pia napenda nishukuru ushirikiano tulioupata kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege; kama walivyosema, walifika Newala na wameelekeza kiwanja kikaeje na wametueleza ukubwa wa eneo linalohitajika. Nina maswali mawili ya nyongeza.
La kwanza, kwa kuwa taratibu za Kimataifa zinataka kabla hatujahamisha uwanja ule wa ndege, ule uwanja wa mwanzo ufutwe; na kwa kuwa Halmashauri imeandikiana sana na Wizara na viwanja vya ndege kutaka kufuta ule uwanja wa zamani, jambo ambalo halijafanyika mpaka sasa. Je, Serikali inaweza kutuhakikishia kwamba kazi ya kufuta ule uwanja itafanyika mara moja?
Swali la pili, kwa kuwa majibu ya Mheshimiwa Waziri ametupa majukumu Halmashauri ya Mji kufanya tathmini ili eneo lile liweze kutwaliwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, kazi ambayo tutakwenda kuisimamia mara baada ya kutoka hapo. Je, Halmashauri ya Mji ikishamaliza suala la tathmini na kwa kuwa viwanja vya ndege ni mali ya Serikali Kuu, siyo mali ya Halmashauri, Serikali itakuwa tayari kuwafidia wale wananchi wachache ambao walikuwa wanalima pale kwa kuzingatia kwamba gharama hazitakuwa kubwa kwa sababu pale hakuna mazao ya kudumu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu Mheshimiwa Huruma kwa jina lake ni mtu wa huruma…
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa George Huruma Mkuchika, ana kaka yake anaitwa Uchicheme Wala Uchimumunye; Ukimumunya Nchale Ukitema Nchale.” (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mkuchika kwamba uwanja huu ukishakamilisha suala la process ya kulitwaa tutafanya kama anavyopenda na kama wenzetu wa Halmashauri ya Newala wanavyopenda.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba, tena naomba sana masuala ya kuvamia viwanja vya ndege, ndugu zangu, vinginevyo tutakuwa tunaipa hasara Serikali. Naombeni sana viongozi wenzetu wa Halmashauri mbalimbali watunze viwanja vyetu vya ndege ili viweze kutusaidia katika shughuli za kitalii na usafiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la kwanza namhakikishia kwamba tutachukua hizo hatua na pengine nichukue fursa hii kuwaagiza Bodi ya TAA ichukue hatua za haraka kuhakikisha kwamba uwanja huu unafutwa kwa mujibu wa taratibu tulizojiwekea.
MHE. KAPT. (MST.) GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kushukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Napenda kuipongeza Serikali kwa kusambaza umeme (REA II) vijiji karibu Tarafa zote sita za Wilaya ya Newala. Hata hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, majibu ya Mheshimiwa
Naibu Waziri yanaonesha kwamba tatizo la umeme maeneo ya Mtwara Mjini, Lindi yataisha na tumeshuhudia juzi Rais ameweka jiwe la msingi, lakini upande mwingine Naibu Waziri
anakubali kwamba Wilaya za Tandahimba, Newala, Masasi, Nanyumbu, Nachingwea na Ruangwa hali ya upatikanaji wa umeme si nzuri na kule tatizo si kwamba umeme haupo tatizo
ni miundombinu. Nyaya zimekatika, ikinyesha mvua nguzo imeanguka, ni lini Serikali itachukua hatua madhubuti kuhakikisha kwamba kukatikakatika kwa umeme na kuanguka nguzo kuna malizwa mara moja ili Wilaya hizi nazo
zifaidi umeme kama wanavyofaidi Wilaya zingine?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili,
pamekuwepo na matamshi mengi upande wa Serikali juu ya gharama halisi za mwananchi wa kawaida kuingiza umeme katika nyumba yake. Nini kauli ya leo ya Serikali kwamba kijiji fulani kinataka kuingiza umeme pale Newala, yule mwananchi wa kawaida anatakiwa alipe shilingi ngapi kwa sababu matamko ya huko nyuma hayafanani na gharama halisi ambazo zimekuwa zikilipwa? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Mkuchika jinsi ambavyo anashughulikia maslahi ya umeme ya wananchi wa Newala Mjini, nampongeza sana. Lakini
pamoja na hayo, Mheshimiwa Mkuchika niseme tu maana hapa tutakaa tutajadiliana zaidi kwa sababu najua unafuatilia mambo yao sana na sisi kama Serikali tusingekuwa tayari kukuangusha, kwa hiyo, tunakuomba sana uendelee kutupa ushirikiano.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusiana na maswali yake mawili ya nyongeza; la kwanza kabisa, ni lini Serikali sasa itachukua hatua za kutatua tatizo la kukatikakatika kwa umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imechukua hatua zifuatazo katika maeneo hasaa ya Mtwara na Lindi na maeneo mengine. La kwanza kabisa, Serikali sasa inajenga miundombinu ya kusafirisha umeme, ule mkuwa kutoka Mtwara na kurekebisha miundombinu iliyoharibika hapa
ambayo tumesema ya urefu wa kilometa 2016. Njia za miundombinu kutoka Mtwara hadi Newala, Tandahimba na maeneo mengine ilikuwa ni ndefu sana, kwa hiyo, hatua ya kwanza Serikali inaanza kujenga transmission line ya umbali wa kilometa 80 ambayo itakamilika mwezi Mei mwaka huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hatua ya pili inajenga kituo cha kupoza umeme kitakachokuwa Mnazi Mmoja maeneo ya Lindi ambacho kitahudumia sana maeneo yote ya Newala, Tandahimba na maeneo mengine ili kupunguza
tatizo la kukatika kwa umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine ni
kwamba inarekebisha pia mashine ambazo zilikuwa mbovu kama nilivyoeleza na kununua nyingine mpya ili kufikia mahitaji halisi ambayo ni megawati 30 kwa wananchi wa Mtwara na Lindi na Wilaya zake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na gharama za umeme. Gharama za umeme kwa manufaa ya wananchi wote ningependa niseme ifuatavyo; kwa vijijni kupitia mradi kabambe wa REA gharama za umeme za kuunganisha kwa wananchi ni shilingi 27,000/= tu basi hakuna gharama nyingine. Ningependa lieleweke hili ili kusudi wananchi
wengine wasibambikiziwe bei. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sambamba na hilo, zipo gharama za kutandaza nyaya kwenye nyumba. Hizo ni gharama zinaotegemea na ukubwa wa nyumba lakini pia zinategemea na mkandarasi waliokumbana nae. Tunachofanya kudhibiti hilo ni kuhakikisha sasa wakandarasi wote wanaounganisha nyaya kwenye numba za wateja sharti la kwanza lazima waidhinishwe na TANESCO na majina yao yabandikwe katika Ofisi za TANESCO ili ikitokea ulaghai tuweze kuwafuatilia. Hizo ni gharama za vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini upo mpango
mwingine kwa wananchi wa kawaida ambao nyumba zao zina chumba kimoja hadi vinne. Tunawaptia chombo kinachoitwa UMETA yaani maana yake Umeme Tayari Ukikiweka. Gharama yake ni shilingi 36,000. Kwa hiyo, nataka kuweka wazi kuhusu gharama kijijini. Lakini gharama halisi kwa maeneo ya mijini kwa umbali usiozidi nguzo moja ni shilingi 177,000/= na kwa mijini ni shilingi 320,000/=.
Mheshimiwa Naibu Spika, haya ni mambo muhimu ningependa kuyafafanua, lakini pia mambo mengine inategemea sasa na mambo ambayo mteja pia anahitaji. Ahsante sana.
MHE. KAPT. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nasubiri ruhusa yako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake ambayo si mazuri sana kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi yetu. Hata hivyo, kabla sijauliza maswali yangu mawili ya nyongeza, nataka niwapongeze Waheshimiwa Wabunge vijana wa Bunge la 10 ambao kwa hiari yao walijiunga na mafunzo ya Jeshi la kujenga Taifa, walionesha kwamba kuongoza ni kuonesha njia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yangu ya nyongeza ni kama ifuatavyo:-
Kwa kuwa Baba wa Taifa alituandalia akafanya JKT kama ndiyo jando, mahali pa kuwafunda, kuwaandaa vizuri vijana wa Tanzania kimaadili, kiuzalendo na kiulinzi; na kwa kuwa sasa inaonekana vijana wengi hawaendi tumeporomoka kutoka asilimia 75 mpaka mwaka huu 23. Je, kwa kutokuwapeleka hawa vijana JKT, Serikali haioni kwamba inachangia kuwaunda vijana ambao hawana maadili, legelege, ambao hawana uzalendo katika nchi yao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa changamoto zilizoelezwa na Wizara nimezipitia zote ziko ndani ya uwezo wa Serikali. Je, Serikali inaweza kuliahidi Bunge hili kwamba itaunda kikosi maalum cha kupitia changamoto hizi, kuziondoa na kuhakikisha kwamba vijana wote wanakwenda Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa Sheria na kwamba hata kama ikibidi kuomba pesa walete maombi hapa Bungeni; kwa sababu Watanzania tuna uzoefu wa kushughulikia matatizo mbalimbali kaa UPE; na kama mwaka wa jana tulivyopeleka watoto wote kutoka darasa la kwanza mpaka form four wamekwenda bila malipo? Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba vijana ambao hawapati fursa ya kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa, kwa kweli hawawezi kuwa sawa kimaadili na kiuzalendo kama wale ambao wamepitia Jeshi la Kujenga Taifa. Hata hivyo, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi ni kwamba Serikali ina nia na dhamira kubwa ya kuhakikisha kwamba vijana wote wanaomaliza kidato cha sita wanajiunga na Jeshi la Kujenga Taifa, lakini tunakabiliwa na changamoto kama nilivyoziorodhesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli nakubaliana na Mheshimiwa Mkuchika, kwamba wakati umefika wa kuunda kikosi kazi cha kupitia changamoto zote hizi au tuseme kufanya mikutano na wadau wote kwa sababu moja ya tatizo kubwa ni mihula ya masomo. Wale wanaoanza Chuo Kikuu wanaanza mwezi Septemba jambo ambalo linasababisha tusiweze kuwachukua vijana hawa wote wengine wanakuwa wameshaanza masomo. Kwa maana hiyo ni kukaa pamoja kuangalia ni jinsi gani tunaweza tukafanya marekebisho ya mihula hii, aidha vyuo vikuu au muda ule wa kumaliza form six ili vijana wote waweze kupitia JKT angalau kwa miezi mitatua ambayo inatolewa sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine kubwa ni changamoto ya rasilimali fedha. Jambo hili limekuwa ni kikwazo kikubwa, tutaendelea kuomba bajeti mwaka hadi mwaka ili kuziondoa na wakati huo huo tunajipanga ili JKT liweze kujitegemea. Nadhani hiyo ndiyo njia nzuri zaidi ya kuhakikisha vijana wote wanapita huko.
MHE. KAPT. MST. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa huruma yako kuniruhusu niulize swali la nyongeza. Kwanza nataka niipongeze Serikali kwa kazi nzuri waliyofanya ya kujenga kwa kiwango cha lami katika maeneo korofi kama Mlima Kinombedo na Kitangari.
Mheshimiwa Naibu Spika, Lakini swali langu ni hili; kwa sababu ni sera ya Serikali kwamba mikoa iunganishwe kwa barabara za lami, barabara hii inaunganisha Mikoa ya Mtwara na Lindi, barabara hii inategemewa sana na wananchi wa Tandahimba, Newala na nchi ya Msumbiji wale wanaovuka. Nini kauli ya Serikali, tunajua kwamba sasa hivi inatafutwa fedha. Je, Serikali inaweza kutoa kauli hapa kwamba sasa kuanzia bajeti ijayo wataanza kutenga pesa za kufanya upembuzi yakinifu wakati fedha zinatafutwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa barabara hii inaunganisha Mikoa ya Mtwara na Lindi, kama ambavyo tuna barabara ya lami imeunganisha Mikoa ya Mtwara na Lindi kutokea Masasi na vilevile tumeunganisha barabara ya kutoka Mtwara yenyewe mpaka Lindi zote kwa barabara ya lami. Hii tunayoongelea ni kama barabara ya tatu na ina umuhimu wa pekee kutokana na mazingira, kama nilivyosema ya korosho.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie kwamba nia ya Serikali ya kuunganisha mikoa, iko katika maeneo ambayo hatuna barabara kabisa, lakini katika eneo hili kwa barabara hii nimhakikishie kwamba tutaendelea kuhakikisha inajengwa na mara tutakapopata fedha tutalishughulikia hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ingawa haipo katika ile sera yetu ya kuunganisha mikoa kwa sababu tunazo barabara mbili zinazounganisha mikoa hiyo miwili hii ni ya tatu, lakini nayo tutaitekeleza, sio kwamba hatutaitekeleza. Kubwa hasa linalovuta ni mazingira ya kiuchumi yaliyopo Newala, ndiyo yanayotuvuta, lazima hii barabara nayo ijengwe kwa lami. Kwa hiyo, mara tutakapopata fedha nikuhakikishie barabara tutaijenga.
MHE. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Spika, namshukuru Waziri kwa majibu aliyoyatoa. Majibu ambayo mimi na wananchi wa Newala wanaomsikiliza, yametukatisha tamaa kwa sababu swali la msingi halijajibiwa.
Mheshimiwa Spika, swali langu nimeuliza, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha viwanda hivi vinafanya kazi? Ndiyo swali la msingi, lakini majibu ya Mheshimiwa Waziri yanaeleza, mwekezaji atafanya hiki, atafanya hiki. Tangu miaka 14 huko nyuma; tumesubiri miaka 14, bado Serikali inaridhika na maelezo yake, atafanya hiki, atafanya hiki, atafanya hiki.
Mheshimiwa Spika, nataka nikwambieni Serikalini, hawa watu waliochukua viwanda vya Newala walivigeuza kuwa warehouse stores wakavikodisha. Hiyo shilingi milioni 75 waliyolipa imerudi siku nyingi.
Mheshimiwa Spika, sasa swali langu la kwanza, Mheshimiwa Waziri: kwa kuwa, huyu mtu ameshindwa kutekeleza mkataba baina yake na Serikali kwa zaidi ya miaka 10; na kwa kuwa kuna watu wengi waliokuja Newala kuomba wanunue kiwanda hiki. Je, sasa Serikali iko tayari kumnyang’anya kiwanda hiki na kuwauzia watu ambao wakipewa leo leo wanaanza kazi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kile Kiwanda cha Newala II ni kweli kinafanya kazi na tunamshukuru kwa hapo alipofika, lakini kiwanda kile nimekitembelea, kuna matatizo makubwa mawili; moja maslahi ya wale akinamama wanaobangua korosho pale; pili, hawana hata gloves, zile zana za kufanyia kazi ya kubangua korosho. Je, Serikali iko tayari kumtuma wiki hii Mkaguzi wa Viwanda aende Newala akakague mazingira wanayofanya kazi akinamama wa Newala wanaobangua korosho? (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Spika, nianze na swali la pili ambalo ni rahisi. Nachukua fursa hii kutoa maelekezo kwa Maofisa wa Serikali wanaohusika na usalama viwandani watembelee viwanda vyote, siyo vya korosho tu, ili wahakikishe kwamba mazingira ya kufanya kazi ni salama na kazi zile ni za staha, ndiyo maelekezo ya Serikali. Kwa hiyo, fanyeni kazi OSHA, wote mnaohusika, fanyeni kazi na mtoe ripoti watu wafanye kazi za staha.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, maagizo ya Serikali kupitia Mpango wa Miaka Mitano ni kwamba viwanda vyote lazima vifanye kazi. Katika operation ambayo nimeiandika humu, viwanda vyote viko chini yangu sasa. Kwa hiyo, tunahakikisha kila kiwanda kinafanya kazi. Watu wa Newala wanaotaka viwanda vya korosho, waende kwa Msajili wa Hazina kama ni kutaka viwanda.
Mheshimiwa Spika, niwahakikishie, mwaka huu viwanda vyote vinafanya kazi. Nimweleze Mheshimiwa, wamekuja watu wengi waliokuwa na viwanda kueleza kwa nini hawafanyi kazi na nimewapa maelekezo. Mnihurumie, mnipe miezi miwili nifanye kazi iliyoshindikana miaka 14.