Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mwita Mwikwabe Waitara (12 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Naomba nimshukuru sana Mungu, ameniwezesha kupitia wananchi wa Jimbo la Ukonga kuingia kwenye jengo hili na naomba nitoe mchango wangu. Naomba Waheshimiwa Mawaziri wanisikilize vizuri kwa sababu Wabunge hawa wa CCM hawatawasaidia sana kwenye utendaji wa kazi, kwa hiyo, ni muhimu sana. Wanasifia yote, halafu wanalalamika mwanzo mwisho, kwa hiyo mimi utaratibu huo siupendi. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kaulimbiu ya Serikali hii ni Hapa Kazi Tu maana yake inaonesha hawa watu walikuwa wazembe muda wote tangu mwaka 1961. Wazembe tu ndio maana nasema wamezinduka sasa, eti hapa kazi. Kwa hiyo, mnapokuwa mnapendekeza kauli hizi ni muhimu mkachunguza kama zina mwitikio chanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, Serikali inatumbua majipu, maana yake kuna wagonjwa wengi na ugonjwa huu umesababishwa na wenyewe CCM. Halafu Serikali ya CCM waoga sana. Ndio maana kuna polisi huku, wamezunguka jengo la Bunge, wanajaza askari humu ndani watu waogope kutoa hoja, maana yake ni waoga kweli kweli. Wangekuwa sio waoga wangetulia tushughulikiane kwa hoja na kwa vyovyote itakavyokuwa. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine waongo, Serikali hii inawaambia watu utawala bora, tena utawala wa kisheria, lakini ukiangalia kauli hii na yote yametajwa kwenye mapendekezo, mmetaja, nilikuwa nasoma hapa.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mmesema utawala bora, mimi naenda kwenye hoja. Hamjasoma vizuri, utawala bora. Naamini kikwazo cha maendeleo ya Tanzania ni CCM wenyewe.
Kwa hiyo, tukipanga mipango tukajadiliana, siku CCM ikitoka madarakani, nchi hii itapata maendeleo makubwa sana. Kwa hiyo, nawaambia Watanzania wajipange kuiondoa CCM madarakani ili wapate maendeleo kwa sababu shida ni CCM, mipango hakuna shida, rasilimali zipo, wataalam wapo, ardhi ipo, kila kitu kipo, shida ni hao wenyewe tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo yangu mawili ya msingi. Moja ni elimu. Nashangaa sana Waziri, kaka yangu Simbachawene wakati anachangia, akawa anakataa tusiseme elimu ya bure haipo. Jambo la kawaida kabisa, kwamba unalipa ada ya shilingi 20,000/= kwa shule za kutwa na shilingi 70,000/= shule za boarding, gharama zingine wazazi wanaingia halafu unasema eti elimu hii ni ya bure, lugha ya kawaida ya Kiswahili tu. Wekeni lugha hii ili msiwachanganye wananchi, elimu ni ya kuchangia, Watanzania wajue na wajue majukumu yao, wafanye kazi ya kusomesha watoto wao, kwamba Serikali ilichofanya imepunguza gharama, very simple ili watu waelewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu mnapowaambia watu elimu ni bure, akienda pale anadaiwa mahindi, apeleke maharage, halafu michango mbalimbali, wanaambiwa walipie mlinzi, semeni ili jambo lieleweke vizuri, kwani siyo dhambi. Hapa hakuna elimu ya bure, ni elimu ya kuchangia na Watanzania wajue. Kwa hiyo, nadhani ni muhimu sana hili jambo likawekwa wazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika hizi shule, kwa mfano, nina madai hapa ya waraka uliotolewa ili wale walimu, wanasema Waraka kwa Watumishi wa Serikali Namba 3 wa mwaka 2014 kuhusu mishahara na posho ya madaraka kwa viongozi wa elimu. Hawa ni wakuu wa shule za sekondari na msingi na vyuo. Maana yake mpaka leo hawa watu wanadai, wametengewa tu shilingi 250,000/-, kwa hiyo maana yake hawa hawawezi kuwa na moyo wa kuendeleza elimu vizuri kama wenyewe wana madai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani Mkuu wa Chuo analalamika, Mwalimu Mkuu analalamika, na wazazi wanalalamika, wanafunzi wanalalamika, kwa hiyo mkitaka mambo yaende sawa, nilimsikia Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini amesema, yeye hataenda kwenye mpango wa tatu wa REA, mpaka makando kando ya mpango wa kwanza…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri hii kauli ikifanyika itasaidia sana. Miradi yote ambayo Wabunge wanataja hapa, barabara ambazo zilipangwa, kama ile ya kutoka Kitunda kwenda Msongora, tangu wakati Mheshimiwa Magufuli akiwa Waziri awamu ya kwanza, awamu ya pili mpaka leo Rais, ni wimbo. Mvua ikinyesha watu hawawezi kwenda mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda hivyo katika miradi mbalimbali ya maji kule Chanika, Msongora, Kidole, Mgeule, ikakamilika, maana yake watu wale ukizungumza habari ya maendeleo na uchumi wa kati watakuelewa. Kwa hiyo, mambo haya ni muhimu sana mkayakamilisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja ya msingi sana ambayo mambo haya hamjayafanyia kazi na nimwombe Mheshimiwa Waziri anisaidie. Kwa mfano, kwenye upande wa elimu, Mawaziri, kila mtu anaibuka na jambo lake katika nchi hii. Tuliwahi kuwa na Mungai akaja hapa na unified science, mimi bahati nzuri ni mwalimu wa hesabu na kemia, akachanganya masomo watoto wakaogopa sana masomo ya sayansi, kwa hiyo watu wakarudi nyuma sana, Waziri akawa na mamlaka hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeenda hapa, akawepo Kawambwa, akaibuka na GPA na nampongeza Mheshimiwa Waziri Profesa Ndalichako amefuta ile, namuunga mkono, turudi kwenye division. Kwenye Sheria za Baraza la Mitihani, kifungu namba 20, kinasema, The Minister may give the Council directions of a general or specific character and the Council shall give effect to every direction. Kumbe hiki kifungu ndiyo kifungu ambacho Waziri anaibuka asubuhi, anaenda anatoa maelekezo Baraza la Mitihani, wanaambiwa sasa hivi ni GPA, ni Division, hiki kifungu kiondolewe. Hata kama Waziri ana mamlaka ashauriane na wataalam wenzake, ili mambo haya yasiwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake mnawayumbisha Watanzania, watoto hawa mnawayumbsha, mara division, yaani mnachofanya nyie ni kwamba kuna golikipa yupo mlangoni pale, anachofanya ameshindwa kiutaalam, kimpira, anaamua aongeze tu ukubwa wa goli, ili ionekane kwamba wamefunga. Hiyo maana yake ni failure, haiwezekani! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mpango wa elimu hapa, hatuna vile vitu vya kitaalam kwa mfano Teachers’ Profession Board, haipo, Quality Assurance Board, haipo. Kama ambavyo kuna Wanasheria wana Chama cha Wanasheria, Walimu wana chama ambacho kinaelekea kuwa chama cha kisiasa siku hizi. Sasa hawa watu lazima wawezeshwe ili waweze kusimamia, lakini ni muhimu sana mkaangalia mambo ya maslahi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi unaleta mpango wa kipato cha kati unazungumza habari ya viwanda, halafu shuleni hata matundu ya choo hamna, hivi kweli hayo ni maendeleo? Yaani uzungumze upate mainjinia wakaendeshe viwanda, matundu ya choo tu ni shida. Yaani madawati ni shida, mnazungumza vitu vikubwa, vidogo tu vimeshindikana hapa. Wewe unazungumza habari hii wakati hata choo hakipo shuleni. Sasa hivi watoto wameandikishwa katika shule hizi, kuna shule ina watoto 617, ina madarasa mawili ya darasa la kwanza. Sasa huu uchumi wa kati nataka nione miujiza, hapa kazi tu na jipu, tuone mambo yatakavyokuwa. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya mwisho, utawala bora. Zamani niliwahi kumuunga mkono Mheshimiwa Nape, wakati nilipokuwa kule chama cha zamani, lakini nikagundua Mheshimiwa Nchimbi aliwahi kufuta kanuni ili Nape asigombee Uenyekiti, naona alikuwa sahihi.
Huyu jamaa amekuja hapa, anaondoa hoja, unawaambia watu utawala bora, wana haki ya kupata taarifa kwa mujibu wa Ibara ya 18, Waziri anakaa chumbani, tumelalamika jana yake, kesho yake amekuja hapa akatuambia kuna utafiti wa Uingereza, yaani unawezaje Waziri kujifunza kuzuia taarifa, usijifunze demokrasia ya Uingereza, miundombinu na vitu vingine vikubwa, wewe ukajifunza kuzuia taarifa tu. Unatuambia, kuna utawala bora hapa? Yaani, unazuia Watanzania wasijue tunazungumza kitu gani humu kwenye hili Bunge. Halafu Waziri Mkuu na Mawaziri, wengine ni wataalam na wasomi, wanaunga mkono na kupiga makofi. Ndiyo maana nikawaambia Waheshimiwa Mawaziri, Wabunge wa CCM hawawezi kuwasaidia sana. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo mambo kwa kweli ni muhimu mkayatafakari upya. Haiwezekani mkazuia taarifa ya kile kinachoendelea, unatuambia suala la muda wa kazi, sasa, hivi asubuhi na jioni, upi ni muda wa kazi mzuri? Kwa hiyo, asubuhi mnaonesha, jioni mnazima. Yaani jioni saa tisa na nusu, ndiyo muda sasa umekwisha, halafu asubuhi mnaonesha. Unarekodi masaa saba, halafu mna-edit mnatoa kwa saa moja, mnatoa mnayotaka wenyewe muone.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Zanzibar itakuwa hoja yangu ya mwisho. Mimi najua na CCM wanajua kwamba Zanzibar uchaguzi ulikwenda vizuri na Maalim Seif alishinda. Huo ndio ukweli, hata kama hamtaki. Dunia inajua, Afrika inajua, Tanzania inajua, CCM mnajua na Taifa hili mnajua na Mwenyekiti unajua. Uchaguzi wa Zanzibar ulikwisha. Kwa hiyo, mnachofanya ni magumashi na sisi kama watoto wa Tanzania hii hatuwezi kuunga mkono mambo haya. Nchi hii ni ya demokrasia kila mtu ana haki ya kuongoza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tukienda kwenye uchaguzi watu wakapiga kura, hakuna malalamiko, aliyeshinda apewe haki yake, ndiyo mpango mzuri wa maendeleo utakavyokwenda. Twende kwa amani kwa kuheshimiana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, sijaunga mkono hoja mpaka kwanza Mpango wa Maendeleo uje, ndio nitaunga mkono hoja. Ahsanteni sana. (Makofi)
TAARIFA
MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa.
MBUNGE FULANI: Mwenyekiti, kuhusu utaratibu, kanuni ya 63, ile ile inayotumika. Mimi ninao ushahidi ya kwamba...
MBUNGE FULANI: Kanuni ya 63 ngapi?
MBUNGE FULANI: Kanuni ya 63(3)
MBUNGE FULANI: Mbunge mwingine yeyote anaweza kusimama mahali pake na kutamka kuhusu utaratibu na baada ya kuruhusiwa na Spika kudai kwamba, imetosha. Mbunge aliyezungumza kuhusiana na kwamba Maalim Seif ameshinda, amesema uongo.
WABUNGE FULANI: Kweli!
MBUNGE FULANI: Kwa mujibu, nathibitisha sasa, Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, kifungu cha 42 kutoka (i) mpaka (v) kinazungumzia Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar pekee ndiyo yenye mamlaka ya kumtangaza na kujumuisha kura za ushindi.
(Hapa baadhi ya Wabunge walimzomea Mzungumzaji)
MBUNGE FULANI: Kama Mheshimiwa Mbunge amezungumza, maelezo hayo, kama ameeleza maelezo hayo, kwamba uchaguzi wa Zanzibar ulikuwa una mshindi, naomba atoe uthibitisho.
WABUNGE FULANI: Aaaa, hakuna.
MHE. MWITA M. WAITARA: Kuhusu utaratibu Mwenyekiti.
MBUNGE FULANI: Aah, atoe.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Waitara, unaipokea hiyo taarifa?
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikuhakikishie na Kamati hii kwamba sipokei na yeye yupo humu baada ya uchaguzi wa Zanzibar, uchaguzi ulikuwa na karatasi tano, kwa nini wamehesabu moja ni halali nyingine zote nne sio halali?
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ili na mimi nichangie, lakini kabla sijachangia naipongeza Ofisi ya Bunge kupitia Katibu wa Bunge kwa kitendo cha kuiwezesha Ofisi ya Mbunge wa Ukonga kuwa na fenicha. Kwanza ameonesha uzalendo kwa kuwa fenicha zenyewe zinatengezwa pale Ukonga kwenye Jimbo langu, vilevile kwa kutengeneza mahusiano akaanzia kwangu, hivyo nawapongeza sana waendelee na moyo huo. Nawashukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, sitaunga hoja kama CCM, kwa sababu wanaunga mapema halafu asilimia 95.5 wanalalamika! Huu mtindo haupaswi kuwa entertained kwenye Bunge, mimi nitaenda tofauti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshauri Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana, taarifa ya Upinzani Bungeni imempa maswali wala asiyabeze ni mambo ya msingi kweli, kwa rekodi tu nataka nikumbushe mambo machache ambayo nataka ayazingatie kama atapenda, maana yake anaweza akakaidi tu.
Kwa mfano, nchi hii inataka kuwa nchi ya viwanda, lakini Watanzania wanataka kuhakikishiwa na Serikali hii, mimi siiti Serikali Tukufu sasa Mungu atakuwa nani! Wanasema hivi viwanda vilikuwepo……
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MBUNGE FULANI: Hiyo kengele ni ya mtu mwingine wewe endelea tu.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mwongozo wako hivi vitu vinachanganya hapa.
MWENYEKITI: Endelea.
MHE. MWITA M. WAITARA: Naomba unilinde, hizi kengele na kelele uzuie kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa inaonesha kwamba viwanda viliuzwa, sasa wakati tunaenda kuleta huu Mpango ambao ni mzuri sana kwa Watanzania, lazima Watanzania wahakikishiwe tukianzisha havitauzwa tena, kutolewa bure au kugawanywa kama shamba la bibi? Hilo ni jambo la msingi kabla ya kwenda kwenye mpango wenyewe, hatuwezi kuweka hela mahali ambapo anaweza akaja mtu mwingine hapa, hapa Mheshimiwa Magufuli amekuja na habari ya viwanda, anaweza akaja mwingine na ajenda zake akaanza kuvigawa tena bure, unakuta nchi inapiga marktime. Sheria inasema nini juu ya hayo mambo ambayo yamefanyika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumelalamika sana, watu waligawana viwanda, waliovunja utaratibu hawajashughulikiwa, hawajawajibishwa, hakuna mtu yupo Mahakamani, tunaleta mpango mwingine! Sasa nadhani hili jambo ni muhimu sana likazingatiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, kwenye ukurasa wa tatu, napitia ile taarifa ya Upinzani, wamesema fedha zilizotolewa ni asilimia 26, ni muhimu Waziri akatuonesha kama mipango iliyopangwa ilikamilika kwa asilimia 26 kwa eneo hili, hivi hizi zilizobaki asilimia takriban 74 amekuja na miujiza gani tena mingine mipya ambayo itawasaidia ili iweze kuwa sustainable, ni muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi yote iliyopangwa haikuzidi nusu tangu imeanza kuzungumza Serikali hii mpya ya CCM sababu haya ni majina tu, alikuwepo Mheshimiwa Nyerere, amekuja Mheshimiwa Mwinyi amekuja Mheshimiwa Kikwete, sasa ni Mheshimiwa Magufuli. Sasa haya ni majina tu lakini Serikali ya Chama kilekile asilimia 60 ya mipango ya maendeleo haijawahi kufikiwa nchi hii .
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nadhani mambo haya yangetusaidia kwa mfano, yametajwa hapa mambo ya msingi kabisa kwamba Deni la Taifa limeongezeka, nimejaribu kugawa hapa hizi trillion 41536.6 ni kama takriban 923,000 kwa kila Mtanzania hata aliyezaliwa leo, ambazo kama Taifa tunadaiwa katika nchi hii. Sasa nataka kujua, deni likiwa kubwa namna hii athari yake kiuchumi ikoje na watu wategemee nini? Maana tunadaiwa hapa tulipo kila mtu sh. 923,000 kwa mahesabu yaliyotajwa hapa, sasa nikasema haya mambo ni muhimu sana kuyazingatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye rasimu ya Mheshimiwa Warioba haya mambo yangeweza kujibiwa, sasa mkachakachua Waheshimiwa ndugu zangu CCM mkaleta mambo yenu, figisu figisu nyingi, mkapindisha haya mambo. Ile rasimu ilikuwa inaelekeza ili Taifa likope, ili hiyo hoja ije Bunge lijadili, liruhusu ili tuelezwe unakopa, haya maswali ambayo Mheshimiwa Silinde kwa niaba yetu, anauliza, uliweka dhamana ya nini, mlifanyia kitu gani, mipango ikoje, nani alikopa, vitu vya namna hiyo vingeweza kujibiwa sasa ile rasimu mmeichakachua, sisi Katiba hatuna, haya mambo yangeweza kujibiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nirudi kwenye hoja hizi ambazo zimezungumzwa. Miundombinu; tumezungumza hapa, mimi nilipo ni karibu na uwanja wa ndege, nitaomba Waziri mwenye dhamana na eneo hili anisaidie, uwanja wa ndege unajengwa terminal III, lakini taarifa ambazo ninazo phase one walikuwa na mkataba, phase two wanaendelea hawana mkataba eneo lile, lakini unazungumza kutengeneza miundombinu, tuimarishe uwanja wa ndege, lakini wako wananchi pale Kipawa walihamishwa kutoka pale wakapelekwa Kata ya Buyuni na Chanika, kuna ugomvi mkubwa wananchi wale hawajawahi kulipwa mpaka leo. Serikali imechukua watu imewahamisha kutoka eneo la Kipawa ikawapeleka Buyuni wakaenda kuwakabidhi maeneo ya watu, hakuna fidia. Kwa hiyo, aliyekabidhiwa eneo hawezi kujenga kwa sababu mwenye eneo hajalipwa, hivyo kuna mgogoro mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tunapoandaa mipango hii tusitengeneze matatizo kwa wananchi. Unawekeza eneo, unaweka watu pale wanafanya biashara zao lakini wananchi wako wanaishia kulia na kulalamika watu wana makabrasha mezani yamejaa, kesi nyingi na hawajui wazipeleke sehemu gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mwenyekiti Lukuvi amelipokea hili, nadhani na yeye kama ataendelea hivi atakuwa mzuri, angalau amesikiliza, ametoa taarifa ameleta ramani ya maeneo yale angalau uweze kuonesha maeneo ya wazi na maendeleo yaweze kwenda vizuri. Sasa hilo ni kwenye uwanja wa ndege, lakini kuna Mheshimiwa mmoja hapa amezungumza habari ya Dar es Salaam kwamba hakuna wakulima, siyo kweli! Zile hela zije.
Mimi ni Mbunge wa Jimbo la Ukonga nawakilisha Kata ya Kivule, Kata ya Kitunda, kata ya Mzinga, Msongola, Uwanja wa Nyani, Ukwende, Zingiziwa kuna maeneo watu wana mashamba makubwa wanalima mihogo na hata Wabunge wote mnaokaa Dar es Salaam mboga nyingi zinatoka Jimbo la Ukonga ziko safi kabisa. Kwa hiyo kuboresha huduma hii siyo dhambi watu wasibeze hapa, kama mtu anaomba huduma kwenye Jimbo lake asibeze Majimbo ya watu wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la umeme. Ni kweli kwamba tunahitaji viwanda lakini Dar es Salaam pale maeneo mengi ni giza. Nimshukuru Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana anachukua hatua lakini kama hata Dar es Salalam ambako hawa Wawekezaji wanapita watu wetu ni giza, umeme ni wa kusuasua mpaka leo tunapozungumza, yaani kuna watu wanakaa pale kama wanakaa kijijini halafu unazungumza habari ya viwanda, umeme wa kawaida wa majumbani hautoshelezi, viwanda itakuwaje? Yaani umeme wa kawaida tu haujitoshelezi viwanda inakuwaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini huwezi kuwa na viwanda, huna umeme, mazao ya kilimo na mifugo. Kuna watu wamekataa tamaa, wamezungumza wenzangu wa Mtwara, hata kule Tarime ukienda watu wa kahawa, wananchi wamefyeka mashamba, wengine wanaenda kulima zile bangi ambazo mmesikia watu wamesema na mirungi, wameweka tumbaku haina kiwanda, hamna usaidizi sasa lazima mje na mbinu Mheshimiwa Waziri ya kuonesha watu waliokata tamaa kulima mazao ya biashara kwamba soko lipo na bei itakuwa ni nzuri na makato na manyanyaso mengi ambayo yapo yataondolewa, maeneo yale hata ile kahawa na mahindi, wapo watu ma-settler wachache ambao ndiyo wanamiliki soko pale. Wanapanga bei, pembejeo zile zikienda kwenye Halmashauri wanagawana, kwa hiyo, kuna ulanguzi wa hali ya juu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, makandokando haya yangeweza kurekebishwa, angalau Watanzania mnapozungumza habari ya viwanda, watu wanakwenda njia imenyooka, vizingiti vimeondoka, ubaguzi pale hakuna, mambo ya namna hiyo yangetakiwa yafanyike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mbunge wa Ukonga, Ukonga kuna viwanda vya chakula cha kuku, lakini mayai yanapatikana na kuku wa nyama wa kisasa, lakini kule hakuna kiwanda cha kutotoa vifaranga rasmi. Vifaranga vingi vinatoka nje ya nchi na baadhi ya material inatoka nje ya nchi. Sasa wananchi wale wanachukua vifaranga wanawekeza, mtu amedunduliza, mama lishe, kijana wa boda boda pamoja na kupata shida mjini hapa, kukamatwa kamatwa sana, lakini akipata kidogo anawekeza kuku wake 200, 500, wakikua baada ya miezi miwili, mitatu, minne kuku wote wanakufa, ukienda kuulizia unaambiwa kwamba shida ilikuwa ni kiwandani vifaranga vilikuwa na shida ambavyo hatuna viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani mambo kama haya pamoja na kwamba tunawekeza tuone ubora wa mali ambayo inaletwa ili watu wetu wasiingizwe kwenye umaskini ambao kwa kweli tunajitengenezea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Dar es Salaam kwenye biashara kuna habari inaitwa DECI na Malingumu, kwamba watu walikuwa wanapanda pesa. Nimesikia Watanzania wote hapa na Wabunge mnafahamu, yaani pesa ikawa miujiza ya Mungu kwamba pesa unaweza ukapanda ikaota kama uyoga, ikazaa mara mbili, tatu na watu wakavuna na Mawaziri wa Serikali hii ya CCM walishiriki zoezi hili na wakataja maeneo kesi ikaenda Mahakamani. Mpaka leo wananchi wale wanasubiri malipo wamekuwa maskini, wameuziwa nyumba zao. Kwa kweli mnapozungumzia Mpango Mheshimiwa Waziri ungejua hali iliyoko hiyo ungeenda sijui kujifungia wapi kama ni Mungu akutembelee upate miujiza uje na mipango ambayo inatekelezeka. Hizi ni kero ambazo zinaumiza wananchi wale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Afya; sasa mmetangaza kwamba kuna, kwa mfano, mimi kule Ukonga, jana nimejibiwa swali langu na Mheshimiwa nimesikitika majibu, Jimbo la Ukonga na Segerea tunategemea hospitali ya Amana. Tumesema tujenge pale hospitali, Halmashauri imetenga kwa mwaka bilioni moja au milioni 900, hiyo hospitali itagharimu zaidi ya bilioni 600 kwa mpango uliopo, maana Waziri alisoma alichofanya hapa na ndicho mmefanya kuzuia TBC isioneshe na TV zingine watu wasione, watu wa Ukonga walikuwa wanalia. Waziri ametuma mtu hapa ameenda akachukua ame-copy na ku-paste ambacho tulipitisha Manispaa ya Ilala hakuongeza kutoka Serikali Kuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ina maana kwa mpango ule ile hospitali itajengwa kwa miaka 26, nimewaambia ile Wilaya kama mpango wenyewe ni ule, ile fedha tuifanyie reallocation, utajenga magofu fedha itapotea haiwezi kusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unakuwa na viwanda, watumishi wetu hawa ni maskini hawana afya, unafanyaje? Mkienda kwenye viwanda vyenyewe, malipo pale pale Gongo la Mboto kuna Kiwanda cha Namela, mwenye kiwanda anawalipa watu wale sh. 4,000/= ambayo imetajwa hapa ndiyo posho ya kufanya kazi. Katika hali ya kawaida Mheshimiwa Waziri, wewe ni mtaalam wa mambo ya finance, hivi sh. 4,000/= Dar es Salaam utaishi kweli? Ndiyo mpango uliopo na Sheria imesema l50,000/= kwenye viwanda. Kwa hiyo, kuna mianya mnatoa wale wawekezaji wakija kwa nia njema tunawapa support, wamechukua ardhi yetu, nguvu kazi ya kwetu, tuna wataalam wanalipwa kidogo sana, lakini mwisho wa siku watatunyonya kweli kweli, sasa mikakati kama hii na mambo haya yangetakiwa yapangiliwe vizuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, reli litakuwa jambo langu la mwisho. Reli inayozungumzwa hapa tunahitaji pale Ukonga, huduma ya TAZARA na reli ya Kati kwa maana ya kusafirisha kupunguza misongamano, sasa hili jambo likifanyika itatusaidia.
Nimeona kwenye Mpango imeonekana, sasa shida ni kwamba na kwa ujumla haya makaratasi ukisoma uko chumbani unafurahi kweli kweli, nendeni mahali sasa myaondoe yaende kwenye vitendo ndiyo mahitaji! Shida ya nchi hii siyo mipango, shida ni kwamba mlichokiandika kiwe transformed kwenye actions, watu waone actions zote zimefanyika, barabara za lami zimetajwa, Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Rais ametaja barabara ya Kitunda – Kivule - Msongola mara nne zote akiwa Bungeni hapa sasa imetajwa tena akiwa Rais nataka nishuhudie kama Rais atakuwa mwongo tena, maana yake kama alikuwa ananyimwa hela kugawiwa sasa hivi anagawa mwenyewe, anatumbua majipu na anafanya reallocation nataka tushuhudie mambo haya, ni matarajio ya Wabunge wengi kwamba mipango mliyoileta hapa inatekelezeka.
Halafu Wabunge wa CCM muache kupiga makofi sana huku, mnaunga mkono mwanzo halafu mnalalamika mwanzo mwisho hivi utawala bora unakujaje? Hivi ninyi Viongozi, Mheshimiwa Waziri, Waheshimiwa mnazima TV, mpango mzuri, maneno mengi na majibu mazuri ya Upinzani ya Mheshimwa Silinde hayajaonwa na Watanzania, hoja zetu hazisikilizwi, tuko hapa gizani kama wachawi humu ndani. Watu wamenywea humu ndani, humu ndani hamtaki watu waone kwa nini? Hivi ninyi nani amewaroga! Nani amewaroga? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, dunia hii ya sasa hivi Serikali inakaa kabisa inafunga Vyombo vya Habari, mlisema TV yenu ni gharama siyo? Hizi za watu binafsi zinawahusu nini? Mmeombwa hela? Haki ya Mungu nimesikitika sana, yaani watu wazima, Mawaziri kabisa mnakubali kwenda kuwazuia Watanzania, Ibara ya ndani ya Katiba ya nchi mnaivunja hivi ya haki ya kupata taarifa. Gharama mmesema ni bilioni…! hiyo TBC fungeni ni chombo chenu cha uenezi, endeleeni na mambo yenu, watu binafsi waruhusiwe humu ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii nchi imekuwa giza tunaongea hapa yaani mwende mchuje, mrekodi muweke mnayotaka ninyi halafu mtuletee tufurahie, halafu mnatuambia habari ya elimu hapa, mnatuambia mambo ya TEHAMA, humu mmeweka mambo ya TEHAMA, sasa TEHAMA maana yake nini? TEHAMA maana yake ni eti watu wafanye kazi, yaani mchukue viboko muwapige watu ambao hawaendi shamba sasa, kawatandike watu ambao hawaendi shambani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna mtu amemwajiri mtu mzembe anaangalia TV ofisini kwake amfukuze kazi.
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. MWITA M. WAITARA: Nataka nipate majibu.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
eze hotuba nzuri ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani kwenye idara hii ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nishukuru kwa kupata nafasi hii nichangie. Nikupongeze sana wewe binafsi, kulikuwa na maneno sana, sasa najaribu kulinganisha maneno yale juu yako na uongozi wako, wewe ni Mwenyekiti smart kweli kweli, hongera sana Mheshimiwa. Nitakuomba kwa umri wako na uzoefu umsaidia Naibu Spika asiharibu hili Bunge, kwa kweli nasema haya ni muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana Mheshimiwa maana msema ukweli ni mpenzi wa Mungu kama unafanya vizuri tukupongeze, ukifanya vibaya tunakusema lakini sitarajii kwamba wewe utafanya vibaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni Wizara ya Viwanda na Biashara na nina hoja hapa ambazo ningeomba Mheshimiwa Waziri mhusika asikilize. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Waziri kwamba hoja za msingi sehemu kubwa ya hoja hizo zinatoka Upinzani naomba utusikilize vizuri, yale mambo mengine wayapuuze. Kwa sababu kwa mfano mtu akikusikiliza vizuri Mheshimiwa Waziri na akatafakari na mimi nimekusikiliza hapa mara kadhaa nikaenda nikakaa, nikarudi hapa nikaona maneno yako yale kama utaweza kuyatekeleza utakuwa ni Waziri wa kwanza ndani ya CCM kufanya kazi kubwa sana na mimi nakutakia kila la kheri. Siyo kwa sababu ni mtani wangu umekula senene hapana, lakini unavyozungumza nitaomba hayo mazungumzo ya-reflect actions pamoja kwamba kuna kazi kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atusaidie, CBE ipo chini ya Wizara yake na Mheshimiwa Waziri wa Elimu asikilize hapa. Nimepata taarifa kwamba CBE pale kuna majipu, ninazo document hapa ambazo Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana anazo, Mheshimiwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anazo tena ni Profesa, Mheshimiwa Mwenyekiti wa Bodi ambaye ni Profesa wangu wakati nikiwa Chuo Kikuu Dar es Salaam nikiwa Rais wa Chuo kile alikuwa anaendesha Baraza la Chuo nikiwepo, Mheshimiwa Profesa Luhanga na wadau wengine. Wameleta malalamiko wanadai kwamba katika kile chuo, Mkuu wa Chuo pamoja na Mkurugenzi wa Fedha, chini ya Idara yako na hii sasa inaweza ikapunguza maneno yako haya nikatafsiri tofauti, kwamba kuna Mkurugenzi wa Fedha amekusanya zaidi ya shilingi milioni 400 bila kutoa stakabadhi anatoa risiti za karatasi zile baadaye hazionekani, vielelezo hivi hapa vipo, hii ni Idara yako na ulipopata taarifa hapa, wale watu ambao wameleta document hapa wakapigiwa simu wanatishiwa kwa nini wameleta taarifa kwako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hizi tuhuma Katibu Mkuu alipoandikiwa, yaani shilingi milioni 400 zimekusanywa, CBE pale kuna campus nne, nazungumzia Dar es Salaam wamekusanya fedha zaidi shilingi milioni 400 kwa utaratibu ambao kimsingi ni kinyume na utaratibu. Wanasema kuna wanafunzi ambao hawalipi ada wakiongea na Mkurugenzi wa Fedha wanamkatia kidogo anaenda anafuta zile kumbukumbu, wale wataalam wa fedha wanasema bad debtors kwa maana ya kupoteza ushahidi, pia haya ni malalamiko ambayo yapo kule. Kwa maelezo yao inaonesha kwamba Mkuu wa Chuo anaelekeza alama 50 ziongezwe kwa wanafunzi ambao wamefeli ambao yeye ana maslahi nao. Hii inaingia kwenye standard ya elimu na hivi vyuo vimekuwa na malalamiko muda mrefu kwamba wanafanya kazi pale kuonesha urembo CBE almost zote wanashiriki sana haya mambo yako.
Kwa hiyo, ina maana hapa inahusu vilevile na Waziri wa Elimu atambue kwamba ni suala la Wizara ya Biashara lakini pia kuna jambo hilo linazungumzwa. Kuna Mkaguzi wa Nje alipelekwa pale alikuwa hired na chuo, akaahidiwa kupewa shilingi milioni 13 akakubali kufanya forgery kwenye ukaguzi wake, aka-abuse profession lakini badaye akapewa shilingi milioni 3.5 sasa hivi analalamika mtaani kwamba amedhulumiwa, huyu naye ni jipu. Nilipoleta malalamiko kwamba kile chuo kichunguzwe, Mkuu wa Chuo kwa kuzungumza na Mkurugenzi wake wakazunguka hilo zoezi halijafanyika kufanya ukaguzi wa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, CBE ya Mwanza na yenyewe ina malalamiko, kuna mtu pale anaitwa Rose yupo Gerezani Segerea tangu mwaka 2011 lakini kapandishwa mshahara analipwa mshahara. Sasa unatafuta wafanyakazi hewa kumbe wapo, document hizi zipo, Waziri anazo, Katibu Mkuu anayo, Bodi inajua na Mkuu wa Chuo anafahamu. Sasa haya mambo Mheshimiwa Mwijage yatapunguza kasi na maneno yako yanaweza yakatia wasiwasi katika mazungumzo. Vielelezo hapa vipo mpaka risiti, mpaka bank statement hizi hapa zimetolewa. Kwa hiyo, ni muhimu sana haya mambo unapopanga uyaangalie, haya makandokando tunaposema wala siyo kuzomea huu ni ukweli mambo yapo, yafanyieni kazi haya, nendeni mkapeleke special audit, CAG akague hivi vyuo alete taarifa, hilo ni la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, mimi ni Mbunge wa Jimbo la Ukonga. Kule Ukonga tunayo shida ya sehemu ya kupata vifaranga, vingi vinatoka nje ya Jimbo na vingine hata nje ya nchi. Wananchi wengi wanafuga kuku, akina mama, vijana wa bodaboda, wauza maandazi wamekopa VICOBA wanafanya biashara ile kwa maana ya kujikimu. Mtu analisha almost miezi miwili, mitatu kwa gharama kubwa vinakufa vyote na hakuna fidia. Unakuja kutafuta unaambiwa eti havikuchanjwa, nani alipaswa kuchanja, nani ana-control standard, bidhaa inatoka wapi, kiwanda kinalipaje, hayo mambo yote wananchi wangu wanapata shida sana. Kwa hiyo, nitaomba unapokuja hapa pia ni muhimu tukapata majibu hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunajua kwamba kulikuwa na mpango hapa unazungumzia habari ya biashara lakini Serikali hii ya chama changu cha zamani na mimi huwa nazungumza nawashangaa ambao wanapiga humu. Mimi nilikuwa kada wa hicho chama yalinishinda nikabwaga manyanga, lakini niko vizuri kweli kweli. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa namwambia Mheshimiwa Nape kama wakiruhusu kuongea pumba sisi tunaweza kutengeneza pumba tukaitumia vizuri kuliko mtu anayeokota pumba. Kwa hiyo, ni muhimu sana tukazungumza mambo serious. Kule kuna kitu kinaitwa DECI na MALINGUMU, fedha zinapandwa, Serikali ilisajili watu wakawa wanalipa kodi, wakafungua na ofisi, hili jambo na lenyewe mpaka leo wananchi wangu wamepata shida. Watu wa Dar es Salaam wamedhulumiwa fedha kesi imeenda Mahakamani inaendelea au haiendelei haijulikani. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ulivyozungumzia wafanyabiashara wadogo wasaidie hawa watu, hii DECI na MALINGUMU uje na majibu nani alisajili na Mawaziri wastaafu walihusika na fedha zilikusanywa zikaenda Hazina mpaka leo hawajarudishiwa mitaji yao, hawajalipwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo ndiyo maana tukasema viwanda vilikufa watu wakauziana, leo mnakiri wenyewe na mnajua kwamba viwanda vingi vimekuwa scraper. Sasa watu hawa watengenezee matumaini waone hali sasa ni nzuri, makandokando yameondoka, viwanda vikianzishwa vitaendelea kudumu, vitazalisha, watapata ajira, ni muhimu sana kujua hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimeenda kwenye kiwanda cha Mbagala kule, kuna kiwanda pale Ukonga cha Nguo kinaitwa Namel, hivi viwanda mmepitisha mshahara wa wafanyakazi maskini wetu wale wanalipwa shilingi laki moja kwa mwezi, nataka utuambie hivi unavyoanzisha sasa na vyenyewe mshahara shilingi laki moja inasaidia kitu gani. Wanafanya overtime wanalipwa shilingi elfu mbili, hawana gumboot, hakuna usalama mle ndani, wanafanya kazi zaidi ya masaa ya kazi, mikataba hawapewi, kwa hiyo ina maana watu wanaonewa. Kwa hiyo, viwanda vinaweza vikaja mkafurahi kupata kodi, hii milolongo ambayo hamjarekibisha wananchi wakaendelea kuumia na hiyo ni shida tutaomba pia uoneshe kama kuna mazingira rafiki ambayo yametengenezwa ili watu wetu waweze kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, chakula cha kuku Dar es Salaam ni shida sana, bei ni kubwa, kilikuwa kinauzwa shilingi 36,000 kimepanda mpaka shilingi 60,000. Nimejaribu kuuliza wananiambia mahindi, pamba na alizeti zinapelekwa nje bila kuwa processed na wafanyabiashara wakubwa wanaificha kwa hiyo inavyorudi bei inakuwa ni kubwa sana, hatuwezi ku-control.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeuliza kwa mfano dawa zikoje, zile dawa za chanjo za kuku hata ng‟ombe nyingi hazina TBS, nendeni pale Ukonga mkague maduka yale hakuna TBS, hawalipii, kwa hiyo bei wanajipangia wenyewe. Kuna biashara holela na hili linaweza kuhatarisha maisha yetu kwa sababu tunakula mayai ya kuku hawa kumbe yako below standard tunapata magonjwa mengine ya kutisha. Kwa hiyo, Mheshimiwa naomba utusaidie pia katika hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nataka unisaidie ni kuhusu mifuko ile ya kijamii. Kumekuwa na malalamiko hapa kwamba wafanyakazi wale michango yao haipelekwi kwenye mifuko hii ya jamii. Sasa lazima uweke mazingira rafiki kwamba hili nalo ikitokea unafanyaje…
MHE. MWITA M. WAITARA: Dah, ahsante sana, siungi mkono hoja, ila nawasilisha.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kupata fursa hii ili niweze kutoa maoni yangu. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Joseph Mbilinyi Msemaji wa Kambi ya Upinzani, juu ya habari lakini niwapongeze sana pia wale ambao walishirikiana nao kuandaa mambo mazito namna hiyo, nafikiri Mheshimiwa Nape atakuwa amesikiliza hiyo misumari na ataifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nachangia kwenye Wizara ya mtu ambaye ninamfahamu vizuri na imetangazwa hapa kwamba ni shemeji yangu kwa sababu mke wake anatwa Rhobi na Mheshimiwa Nape hatukukutana barabarani, ni kweli kwamba ni shemeji yangu sasa nitaomba Dada yangu Rhobi ninapochangia kwenye hotuba ya mume wake Mheshimiwa Waziri kwa sababu tupo kazini na tumeshachukua mahari, biashara ya ushemeji itakaa pembeni kidogo, hapa kazi tu, kwa hiyo tunaenda na kauli mbiu ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilisema nitakuwa mkweli sana, nimejaribu kutafakari kitu gani nichangie kwenye hotuba hii nikapanga haya yafuatayo niyaseme.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza Mheshimiwa Nape akiwa Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi aliwaita wenzake ni mizigo akiwepo Mheshimiwa Profesa Maghembe, Mawaziri wenzake wale aliowaita, kwa hiyo nilipoona amepewa Wizara ya Habari nikatarajia kwamba ataruhusu mijadala ya wazi ili tumuone kwamba yeye hatakuwa mzigo lakini anaweza kwa lumbesa ili tumjadili na wananchi wamuone. (Makofi)
Sasa hilo amelizuia kwa hiyo tunashindwa kumpima yeye na wenzake nani mzigo zaidi, nani lumbesa hilo na lenyewe kidogo linaleta shida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili Mheshimiwa Nape atakumbuka kwamba wakati nilipokuwa nimeminywa sana kutoa maoni yangu kama kijana msomi kutoka Chuo cha Dar es Salaam, nikapingana na viongozi wa CCM nilipofikiria kuhama CCM Mheshimiwa Nape nilimshirikisha akiwa na Mheshimiwa Kubenea, tulienda kule Kitunda nikamwambia hawa watu ndugu zako, hawa viongozi wa CCM hawa wamenikwaza kwa sababu wamezuia uhuru wa kuzungumza, kutumia akili zangu kitaaluma kama mwalimu tena mwalimu wa Hesabu na Kemia. Kwa hiyo nikamwambia mimi nahama akaniambia safari njema.
Kwa hiyo, anajua wakati nahama Mheshimiwa Nape alikuwa anafahamu. Kwa sababu msimamo ule ule ambao tulitofautiana kule na wenzake yeye ameurejea tena, kwamba hatuwezi kuwa na uhuru wa kutoa maoni hapa na yeye ndiyo msemaji. Nimepitia taarifa yake hapa ameeleza vizuri kwamba yeye ndiyo anasimamia vizuri Wizara hii na kusema akifanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi mojawapo ambayo Mheshimiwa Waziri anasimamia moja, alikiri hapa kwamba hiki kinachoendelea hapa Bungeni cha waandishi wa habari wa TBC kufanya kazi hapa Bungeni alikiri kwamba ni kweli wametoka TBC maana yake kwenye Bunge hili hao wanaozuia taarifa na ku-censor tunachozungumza Mheshimiwa Nape ana mkono wake, kwa hiyo hawezi kukataa na alikiri kwamba hawa watu wapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimefuatilia mara tatu usiku, mara ya kwanza niliamka saa 7.42 usiku na juzi ile nikakuta ndiyo TBC inaonyesha taarifa ambayo imerekodiwa. Siku iliyofuata niliamka saa 8.15 usiku nikakuta tena wanaonesha, juzi nimeamka saa 9.40 usiku maana yake saa kumi kasoro dakika ishirini nikakuta ndiyo wanaonesha taarifa, nikaenda mpaka saa kumi ilikuwa inaendelea. Usiku wa kuamkia leo niliamka saa 7. 17 usiku nikakuta wanaonesha ile taarifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni nini! Mheshimiwa Nape ni muongo na huenda naye vilevile ni jipu humu ndani, anapaswa kutumbuliwa, kwa sababu Mheshimiwa Nape amedanganya hili Bunge. Alipokuja kutoa tamko la Serikali alisema kwamba hoja mojawapo muhimu ni kwa nini taarifa isirushwe na TBC ni gharama. Akaeleza wametafuta muda mzuri wa kuonesha ufanisi wa watu waangalie taarifa ya habari lakini waende kazini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama mwalimu, kama mtu mzima, kama mzalendo nikajaribu kufanya assessment ya kawaida kwamba kama unaonyesha kipindi cha Bunge saa kumi kasoro dakika ishirini na unataka kwa watu wa Dar es Salaam kwa mfano kule Ukonga, Msongola, Mbondole, Kibanda cha Maiti kule au Uwanja wa Nyani atoke ili awahi mjini kati ni lazima aamke saa kumi na moja, maana yake baada ya kumaliza kuangalia taarifa ya habari ambayo imeanza saa tano au saa nne ataoga saa kumi na moja anaanza safari huyu mtu lazima asinzie. Nikajiuliza hapa kuna kuna ufanisi! Hapa kuna ufanisi wa kazi? Nikalijua jibu hapana siyo kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, ninyi viongozi wa Bunge hili mmebariki hicho kitu kifanyike, ninyi mnakubali tuzunfumze hapa, mtu akiongea hapa leo, kuna miongozo imetolewa watu wathibitishe tunataka uongo wa Mheshimiwa Nape athibitishe kabla ya kuhitimisha hoja yake hapa, kwa nini amedanganya Bunge, kwa nini amedanganya Watanzania! Hoja ambazo wametoa siyo za kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mmemwambia Mheshimiwa Kubenea athibitishe mambo aliyozungumza, sasa ufanisi wa kazi unaoonekana hapa ni nini! Haya mambo lazima tuyajadili. Mimi ningekuwa na uwezo hii hotuba isingejadiliwa kwa sababu hili jambo tungekuwa na watu ambao hili Bunge siyo CCM wengi, hii Serikali tungeiangusha leo, tungepiga vote of no confidence. Kwa sababu jambo hili siyo jambo la Waitara, siyo jambo la UKAWA, siyo jambo la CHADEMA au la CCM ni jambo la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yupo Mwanasheria hapa na wapo wataalam mbalimbali wamebobea. Ukisoma Ibara ya 18 ni haki ya Watanzania, tukisema mmevunja Katiba mnakataa kwa nini? Mnataka tusemeje sasa? Kama kweli mna nia njema ya kufanya kazi Serikali hii hapa kazi tu tena kwa mara ya kwanza tumepata Rais ambaye ni mwanasayansi, mwalimu, mtaalam maana yake masomo yangu na Magufuli sawa sawa, kwa sababau yeye ameongezeka cheo amekuwa Rais, mimi Mbunge! (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tunafanana. Ameongeza degree ya pili ni mwalimu wa Hesabu na Kemia, ndiyo Rais wa kwanza wa Tanzania msomi, mwanasayansi, mwalimu. Walimu hatuongopi challenges, tutasema chochote ili mradi kuna fact. Kama kuna kazi inafanyika kwa nini mnaficha, kwa hiyo hilo jambo kwa kweli nimeumia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine kitendo cha Mheshimiwa Nape kuja hapa jana wametangaza anasema kuna Diamond ataburudisha sijui wapi, kutakuwa na mwanamuziki King Kiki jioni ya leo maana yake ni rushwa, hiyo ni rushwa! (Makofi)
Kwanza mnaposema mnabana matumizi mnaondoa starehe. Huyu King Kiki na wenzake gharama za nani zimemleta hapa, anapiga pale nani analipia hizo gharama? Wabunge wote ambao wataenda kwenye hiyo miziki ili kuunga mkono habari ya Mheshimiwa Nape maana yake mtakuwa mmekula rushwa na wote mlaaniwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ninataka mnisaidie, Mheshimiwa Nape amezungumza, mimi nimesikia story, amezungumza habari ya ngoma na nini, nimeangalia kwenye matumizi. Tulimuita Mheshimiwa Naibu Waziri Mheshimiwa Anastazia Wambura, alikuja Dada yangu kwenye Kamati ya UKIMWI na masuala ya dawa ya kulevya. Ikaonyesha kwamba hawakutenga fedha kwa ajili ya michezo kwa maana ile UMISHUMTA, UMISETA hawakutenga fedha na wanasema hawana mpango huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimepitia hapa wanapozungumza, wamezungumza habari ya Samatta, hawa ni watu ambao wamejikuza wenyewe kama kuku wa kienyeji, mkakuta wamefanikiwa mnawapongeza sana, mnawapa sifa kubwa. Wapi mpango wa Serikali ya kuendeleza vijana, wapi mpango wa kuendeleza michezo shuleni? Kuna vipaji vinakufa pale! Hapa nimeona kwenye vote 6002 Youth Development Program ni zero zero tu! Nimeona kwenye vote 6004 kwenye Sports Youth Development, hakuna fedha ambayo imetengwa pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, wenyewe wanasema fedha ambazo zinatengwa na Kamati imezungumza ukweli hakuna kilichopelekwa sasa unazungumza habari gani hapa? Kwa hiyo sisi tukae hapa Bunge kila mwaka bajeti ikija, King Kiki, Diamond biashara inaisha si ndiyo? Hiyo biashara mtafanya wenyewe watu wa CCM sisi hatufanyi biashara hiyo bwana.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nataka mnisaidie hapa iwe very clear. Wako Wabunge wa CCM humu ambao wanapiga makofi sana, wanafikiri hii hoja ya habari ni ya kwetu. Mimi nitaomba leo Watanzania wajue wale ambao wanapiga makofi kwamba tv isioneshwe waonekane halafu muwe tayari twende kwenye Majimbo tukawaambie kwamba hiyo ndiyo biashara mnayoifanya humu ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunawaambia Rais amehasisha vizuri anawaambia Watanzania kila ukinunua kitu ulipe kodi, kama umelipa kodi upewe risiti, kama hujapewa udai. Hizo fedha zilizokusanywa hapa ndipo mahala pake kwa kuzipanga matumizi yake, hamtaki waone! Wananchi walipwe kodi, lakini mipango wasione! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa mmepunguza bajeti, leo tumejadili hapa bajeti ya Afya imepunguzwa kwa shilingi bilioni 18. Mimi naomba wako wataalam pale, yupo ndugu yangu Ayoub Ryoba amepewa TBC, hii TBC ambayo Mheshimiwa Nape amezungumza alifanya kazi nzuri amesema sehemu kubwa ilikuwa inaisemea Serikali, lakini taarifa rasmi ni kwamba TBC ilifanya kazi ya CCM katika Uchaguzi Mkuu uliopita hiyo ndiyo bottom line.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mimi siungi mkono.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naunga mkono hotuba ya Kiongozi wa Upinzani Bungeni; naunga mkono pia hotuba mbili za Utumishi na mambo ya TAMISEMI kwa Wasemaji wa Upinzani Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo kadhaa hapa ya kuzungumza. Kuna hoja hapa ya ndugu yangu, Mheshimiwa Angellah Kairuki aliyowasilisha, ya Utawala Bora; ndiyo nataka nianze nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utawala bora ambao unazungumziwa ni muhimu tungeanzia hata humu ndani kwenye Bunge hili kama kweli kuna utawala bora. Bunge limengolewa meno, limekuwa butu kweli kweli!
Bunge limekuwa kibogoyo! Bunge limekuwa na watu waoga kweli kweli! Wabunge hawana uhuru wa kuzungumza na kutoa maoni yao! Hili Bunge ni aina ya Mabunge ambayo hayajawahi kutokea, labda hii ndio kazi tu! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya masuala ya UKIMWI na Dawa za Kulevya. Nimesikiliza Wabunge wa CCM wengi waliopangwa kwenye Kamati ile. Inaonekana walipangwa na Mheshimiwa Spika kwa maelekezo na naambiwa kwamba kikao kilikaa, wale wengi ambao walikuwa wanamuunga mkono Mheshimiwa Lowassa walitupwa kwenye Kamati yangu na mimi naipenda sana, kama sehemu ya kuwaadhibisha. Maana yake hiyo kazi Spika aliifanya kwa maelekezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Naibu Spika mwenyewe ningependa awe hapa. Jana alimwita Mheshimiwa Mbunge mwenzetu hapa bwege. Akamwambia aache ubwege! Yaani bwege asionyeshe ubwege!
Kwenye kikao cha Bunge jana! Ilizungumzwa, wala siongei uongo. Hapa nitaongea mambo ya ukweli tupu. Alisema Mheshimiwa Bwege, naomba uache ubwege. Sasa wataalam wa Kiswalihi wanaweza wakasaidia.
KUHUSU UTARATIBU......
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuelewa na nitazingatia ushauri wako. Kwa hiyo, maneno yote yale yameondolewa eeh! Mnapenda sana hiyo eeh!
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba muda wangu ulindwe.
Hoja yangu tu ni kwamba, Bunge hili Waheshimiwa Wabunge hawana uhuru, wanapigiwa pigiwa simu, haijalishi nani amepiga lakini wanapigiwa na watu wa ngazi ya juu kwa kuwatishatisha ili wasiwe na uhuru wa kutoa maoni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye taarifa mbalimbali za ukaguzi inaonyesha kwamba hata Ikulu yenyewe kunakuwa na rushwa. Taarifa mbalimbali zipo, wala hili huwezi kupinga. Sasa kama Mheshimiwa Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kwamba Ikulu ni mahali patakatifu, kama kuna chembe chembe za rushwa kwa nyakati mbalimbali, sasa huo utawala bora utawaelezaje watu wa kawaida kama kule jikoni kwenyewe chakula kinaibiwa, watu wananyofoa minofu jikoni...
Tutafanyaje katika mazingira hayo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ulizikataa, nakushukuru sana.
MHE. MWITA M.WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nashauri pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kaka yangu, sisi watu wa kule kwetu huwa hatuogopi kusema ukweli. Namshauri Mwanasheri Mkuu wa Serikali, asiwe anatoa tafsiri za sheria za ki-CCM atoe tafsiri za kisheria za sheria in profession. Namshauri sana maana yake nimevumilia imebidi niseme tu hadharani kwamba ni muhimu Mwanasheria aseme sheria za kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, hapa kuna mambo yanaelezwa, sisi tulichosema ni kushauri kwamba katika mambo kadhaa yaliyofanyika, Mheshimiwa Rais hajafuata utaratibu kwa maana ya kutumia mamlaka yake vibaya, kwa maana ya kufanya reallocation ya fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ushauri na sheria hizi zipo, utakuja na tafsiri nyingi sana kwa maana ya kuficha mambo, lakini ukweli unabaki pale pale. Naomba nitaje kwa mfano, Katiba ya Nchi Ibara 18(a), (b) na (c) kinaeleza uhuru wa kupata habari; tena unasema hata nje ya mipaka ya nchi. Hili jambo huhitaji kupata mkalimani, inaeleweka tu, kwamba Watanzania wamenyimwa fursa ya kupata taarifa ya Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapanga wananchi hawa walipe kodi, tunawashawishi namna gani? Hawa jamaa wa CCM wameenda wamekaa kwenye mkutano wao, wanaaminisha watu kwamba ooh, watu wa Upinzani tutaonekana. Hii siyo hoja! Ni hoja ya kitoto kabisa! Hoja hapa ni kwamba ni kwa nini kama kweli mnafanya kazi vizuri, wananchi wasiwe na uwezo wa kujadili na kuona tunachokiona? Nawa…
MWENYEKITI: Ahsante, muda wako… Aalah! (Kicheko)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kengele ya kwanza. Nakushukuru! Naona sasa unaanza kunitania! Aisee! (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Hoja nyingine, ukisoma Ibara ya Katiba ya 135, mambo yale ya Hazina inaeleza, Katiba ya Ibara ya 146(1) inaeleza, vitu vingi vimezungumzwa.
Niende kwenye hoja ya TAMISEMI; kuna jambo la bodaboda hapa; hawa vijana na hasa Dar es Salaam. Sasa hivi kuna uhalifu mkubwa, vijana wetu walishawishika, wengine wamechukua mikopo, wanajikopeshea fedha zao kwa watu binafsi na wengine VICOBAvile wanapata fedha ya kujiendeshea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na mitindo wa kusumbuliwa sana Dar es Salaam pale! Kuna watu wameitwa Askari wa Jiji, nadhani wale tutawashughulikia kwa sababu Jiji la Dar es Salaam tunaongoza sisi, nami ndio Mwenyekiti wa Mkoa, naelekeza sasa, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, hili jambo alifanyie haraka mapema sana. Hawa vijana wanapata shida kule Dar es Salaam, wanakamatwa hovyo, wanasumbuliwa! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ameenda kuteua hawa Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa, Ma-RAS waliostaafu Majenerali. Sasa hawa vijana ambao wanahitaji hapa ajira, si angewapa kazi hao vijana! Humu ndani kuna Wabunge wana vyeo viwili viwili; yaani mtu ni Mbunge halafu ni DC, halafu ajira ni shida! Hivi huyu mwenye vyeo viwili ana nini? Ana pembe kichwani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wanyang’anywe vyeo, tugawane kilichopo. Mtu amefanya kazi, amestaafu, anapewa kazi nyingine tena, halafu mnataka ufanisi! Watu wameshachoka, wanasinzia ofisini mnawapa kazi nyingine. Hii kitu kwa kweli vijana hawa msiwanyanyase na utaratibu uwekwe sawa sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye bajeti ya Manispaa ya Ilala tumekadiria kukusanya shilingi bilioni 85 ikiwepo kodi ya majengo na mabango lakini shilingi bilioni 28; Shilingi bilioni 18 majengo na Shilingi bilioni kumi ni mabango. Maana yake huu mpango, kwenye hotuba ya Waziri wa TAMISEMI inaeleza kwamba Halmashauri itasimamia, kwenye Mpango wa Waziri wa Fedha inaonyesha vinginevyo. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind-up hapa aeleze kipi ni kipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Manispaa ya Ilala ilifanyiwa ukaguzi mwaka 2011/2012 - 2012/2013 lakini na hii ya leo nimeisoma, Manispaa ile inaonekana ni miongoni mwa hati isiyoridhisha. Sasa haya mambo, walikaguliwa watu 2011, Mkaguzi Mkuu alikagua, akaleta taarifa; lakini ninavyozungumza hapa, tuna vitengo na idara zaidi ya 18 lakini viongozi wale watano tu ndio wamethibitishwa, wengine wote wanakaimu. Nimejaribu kuhesabu hapa, karibu 13! Sasa katika mazingira hayo, tunafanyaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, siungi mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwapongeza viongozi wote wa Wizara ya Nishati na Madini kwa:-
(i) Kupunguza urasimu wa wateja na kutembelea wahitaji wa umeme;
(ii) Kusambaza nguzo kwa sehemu kubwa; na
(iii) Kutenga 94% bajeti ya maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja juu ya mradi wa Kinyerezi II. Mradi huu unagusa mitaa 40 lakini hadi sasa ni mitaa nane tu imefanyiwa tathmini na mitatu tu ndiyo wamepewa cheque ambazo hadi sasa hakuna pesa kwa wananchi. Fidia kwa wananchi hawa imechukua zaidi ya miaka mitano (5) sasa na hivyo hata malipo yake hayatakuwa halisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mitaa inapewa pesa za kulinda mabomba ya gesi. Naomba pesa za ulinzi ziangaliwe upya ili kuboresha malipo haya kwa mazingira ya sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, umeme wa Kinyerezi II unapitia Kata za Kivule, Kipunguni, Gongo la Mboto, Majohe na Kinyerezi. Hata hivyo, Jimbo la Ukonga lina ukosefu wa umeme katika Kata za Pugu, Buyuni, Chanika, Msongola na Zingiziwa. Naomba Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini pamoja na kupeleka umeme mijini na vijijini, ni muhimu kipaumbele kiwe kwenye maeneo ya shule, vituo vya polisi, zahanati na visima vya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Ukonga lina changamoto ya kuhudumiwa na sehemu mbili yaani Kituo cha Gongo la Mboto na Kisarawe. Suala hili linasumbua wananchi, naomba uwekwe utaratibu wa kupunguza hiyo kero.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana aangalie kwenye migodi hasa huduma za jamii kwa wanaozunguka mgodi na mrahaba wa 0.3% namna unavyokokotolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwapongeza Wizara ya Ardhi ikiongozwa na Waziri Mheshimiwa William Lukuvi kwa kuonyesha nia ya kutatua migogoro ya ardhi kwa kushirikisha wadau wa ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumshukuru Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri wa Ardhi na Waziri wa Maliasili kwa kuonyesha uongozi na nia ya kumaliza mgogoro wa ardhi katika msitu wa Kazimzumbwi uliopo katika Kata za Chanika, Zingizwa, Buyuni na sehemu ya Pugu ambao umedumu tangu mwaka 1994 kutokana na kupunguza mipaka mwaka 1954.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu kumaliza mgogoro wa Bonde Msimbazi hasa maeneo ya Kinondoni, Segerea na Ukonga ambapo nyumba za wananchi zimewekwa alama ya “X” na zingine kubomolewa, huko ni kuwarudisha nyuma wananchi wa nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu Mheshimiwa Waziri kumaliza mgogoro wa Kipawa Kipunguni, eneo la Uwanja wa Ndege. Pia mgogoro wa ardhi kati ya watu wa kutoka Kipawa na Kipunguni waliopelekwa Kinyerezi Pugu na Buyuni katika Jimbo la Ukonga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kulinda maeneo ya umma kama vile shule, zahanati, masoko na polisi; ni muhimu upimaji na kulinda maeneo ya huduma za jamii liwe shirikishi kwa viongozi wa mtaa, kata, Wabunge na wananchi ili kuondoa mianya ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama za upimaji ni kubwa sana kiasi kwamba wananchi wengi wanashindwa hivyo kuishi bila kupima maeneo yao. Ni vema Wizara ikaangalia namna ya kupunguza kero hizo ili wananchi walio wengi au wote wapime ardhi yao ili kujipatia manufaa ikiwemo uwezekano wa kukopesheka katika vyombo vya fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara ya Ardhi iongeze kasi ya kuondoa migogoro ya ardhi na hasa maeneo ya maliasili ili watu wetu waishi kwa amani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwapongeza Wizara ya Ardhi walau kwa kuweka mipango shirikishi na kuanza kumaliza baadhi ya migogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nianze kwenye kitabu hiki cha Mpango, ukurasa wa saba ambapo anasema, mwenendo wa uchumi unaashiria kuendelea kuimarika kwa uchumi na utoaji wa huduma za jamii unaboreka. Ndiyo maana kukawa na hoja kwamba ingelazimika tukapata tathmini ya kipindi kilichopita kwa muda huu tulionao ili tuweze kujua mwelekeo. Hii kauli inachanganya sana wananchi wa kawaida na hata mimi mwenyewe. Ukiangalia hali halisi ya kiuchumi ilivyo, ukitembelea maduka mitaani, wafanyabiashara mbalimbali wanalalamika na hata sisi wenyewe Wabunge tunalalamika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana imeelezwa kwamba imefikia hatua hata kwenye Kamati za Bunge unapewa maji moja ndogo kuanzia asubuhi mpaka jioni. Pia ukipewa chakula kimepangwa unasimamiwa usije ukazidisha vipande vitatu ni viwili tu, maana yake inawezekana ukizidisha utashikwa mkono. Hiyo maana yake inaashiria hali ya kiuchumi ni ngumu lakini kwenye vitabu wataalam wetu Mheshimiwa Dkt. Mpango na wenzake wanasema hali inaimarika na huduma za kijamii zinaboreshwa. Kwa hiyo, naomba hata atakapokuja kuhitimisha hoja ambayo mimi siungi mkono, basi atueleze angalau kinaga ubaga na kwa lugha ambayo tutaweza kuelewa anamaanisha kitu gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niunge mkono hotuba nzuri sana ambayo imetolewa na Kambi ya Upinzani Bungeni. Niseme Waziri yeyote makini tukitoa hotuba hapa ni muhimu akapitia kile tunachokisema kwa sababu takwimu ambazo zinatolewa na sisi upande wa Upinzani hatuzipiki sisi bali zinatoka kwenye nyaraka mbalimbali Serikalini humohumo. Kwa hiyo, tunapotoa hotuba hapa siyo kuibeza na mimi ningekuwa ninyi ningekuwa mjanja sana kwa sababu mngekuwa mkisema naenda kuyafanyia kazi ili next time mkose hoja. Badala yake mnaweza kukaa hapa miaka mitano mnaambiwa mambo yaleyale ukirudi unatoa siasa, unapiga story, unapiga porojo, miaka inaenda na huboreshi. Kwa hiyo, kimsingi unakuwa hufanyi lolote lile. Hoja ikitolewa iangalie na kama ina ukweli ifanyie kazi na kwa kufanya hivyo utakuwa unalisaidia Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kupitia hiki kitabu, mimi nitajikita kwenye kitabu hiki kilichoandikwa, ukurasa wa 66 – 67, Waziri mwenye dhamana amezungumzia utawala bora na utawala wa sheria, lakini nilipoangalia utawala bora alioandika hapa alikuwa anaandika kuboresha majengo na kuongeza polisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyoelewa utawala bora angeeleza hapa kwamba mpango wa Serikali ni pia kuheshimiana katika maeneo yetu ya kazi. Kwa sababu kwa utawala huu ambao mnauita utawala wa Awamu ya Tano na mnakwepa kusema utawala wa Chama cha Mapinduzi mnataka watu waamini kwamba miaka inatofautisha matendo yenu, ndiyo maana mnahimiza sana utawala wa Awamu ya Tano, sema Serikali ya Chama cha Mapinduzi, Watanzania wajue ni ileile hakuna jipya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika hali ya sasa ambayo unataka kuboresha elimu lakini Mwalimu huyu ambaye anadai na hapa katika kuboresha elimu sikuona unaboresha namna gani, wapo Walimu ambao wanadai madai yao tangu mwaka 2012 mpaka leo. Ili uboreshe elimu lazima Walimu walipwe madai yao, wapandishwe vyeo, walipwe likizo na malimbikizo yao ili migogoro iishe. Huwezi kuboresha elimu kwa maana ya majengo wakati Walimu wanadai na Walimu haohao Wakurugenzi ambao mnawateua makada wa CCM wanawaambia wapige deki mbele ya wanafunzi halafu unasema unataka kuboresha elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unazungumzia utawala bora mahali ambapo Mkuu wa Mkoa wa Simiyu anaagiza eti kuanzia leo Walimu wote nimewashusha vyeo, huo ndiyo utawala bora kweli? Sasa hapa hamzungumzi, mnazungumza habari ya kujenga majengo, haya mambo lazima tuzungumze ukweli. Sasa mnapotuandikia, sisi siyo wajinga, tunaweza kusoma mnachoandika na kuchanganua, lazima mtueleze utawala bora maana yake ni nini? Sasa hivi hali iliyofikia watu hawaheshimiani yaani unakuta Rais ameagiza kwamba Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya watumie ile Sheria ya saa 48, kwa hiyo, Mbunge kwenye eneo lake, Diwani kwenye eneo lake, Mwenyekiti wa Halmashauri au Mstahiki Meya anaweza akaambiwa kamata weka ndani, unasema huu ndiyo utawala bora halafu unataka upewe ushirikiano katika eneo hilo. Kwa hiyo, nashauri wahusika wa haya mambo lazima waangalie vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile kuhusu utawala wa sheria, sasa hivi kinachotawala Tanzania wala siyo sheria ni amri mbalimbali, sheria wala haifuatwi. Bahati nzuri Waziri wa Utawala Bora ndiyo alikuwa mpiga kura kule Kinondoni kwenye uchaguzi wa Meya, walikuwepo hawa. Katika hali ya kawaida inawezekanaje unafanya uchaguzi ambapo unajua idadi ya UKAWA ni nyingi kuliko Chama cha Mapinduzi na Naibu Spika ambaye ni mwanasheria tena alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amehusika kuchakachua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria inasema wateule wa Rais hawatazidi watatu katika Halmashauri lakini mlichokifanya mlipeleka watu wanne pale Kinondoni. Sheria inasema ni lazima mahudhurio yaandikwe, akidi ni mbili ya tatu (2/3), haikutimia hakuna mahudhurio. Watu wa CCM mlikuwa 18, tena viongozi mmekaa pale mkapiga kura mkajiapisha halafu unaandika makaratasi hapa utawala bora wa kitu gani, unamdanganya nani hapa? Huu ndiyo utawala bora kweli, huu ndiyo utawala wa sheria? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, viongozi wasomi, Mawaziri, Maprofesa, Wanasheria, Naibu Spika na wenzenu, Mawaziri wazima hata aibu hawana, tena Waziri wa Elimu ambapo Waziri wa Elimu alikuja kupiga kura Ilala. Mimi ni Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Mheshimiwa Profesa Ndalichako mama yangu na mtani wangu ambaye namheshimu sana alikuwepo ameletwa kujiandikisha kupiga kura Ilala halafu tena akakubali kubebwa mzobemzobe anashinikizwa kuja kupiga tena kura Kinondoni, wewe unafanya kitu gani kweli? Hata aibu hamuoni?
Aibu sana kwa Chama cha Mapinduzi, chama kongwe, ndiyo maana mnaitwa chama kizee.
Hata busara na hekima inapotea. Sasa hapa utawala bora mnaozungumzia ni kitu gani? Tangu mmeanza kufanya uhuni katika nchi hii mimi kwa kweli nimekuwa confused.
Ndiyo maana mnachofanya hata hapa kwenye elimu ni maigizo, tumegundua mtaji wenu katika nchi hii ni ujinga.
Ndiyo maana mnavuruga elimu makusudi. Rais amewaambia Watanzania yeye hatakubali mtoto wa maskini asiende chuo kikuu atawakopesha, Waziri anasema ataangalia bajeti ilivyo sasa nani mwenye kauli?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza habari ya afya hapa, Makamu wa Rais anasema dawa hakuna Waziri anasema dawa zipo tele na jana Naibu Waziri amethibitisha, akasema tumwonyeshe, tumemwambia tumpelekee nyumbani kwake akakataa. Sasa haya mambo ukisoma kwa kweli, mimi vitabu vyenu huwa navisoma sana, nipo tayari nisilale usiku lakini navisoma sana, lakini mnatuchanganya sana, kwa nini msiandike ukweli? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, akija hapa Waziri wa Viwanda atapiga ngonjera zake utamwona huyu ndiyo mwanaume ametoka Bukoba wengine hawapo kabisa. Akiimba hapa ngonjera zake utashangaa, sasa nenda kwenye hali halisi, yote haya hamna. Anafukuzwa na Kamati yake kwamba mzee umeandika makabrasha mengi, pesa hakuna, Kamati ya Viwanda inasema hujafanya lolote, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda acha kuimbia watu ngonjera. General tyre mpaka leo haijaanza, watu wanataka kuona mnaleta tena story zilezile. Kwa kweli hii habari inatusumbua sana. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme kuhusu hii habari ya mifugo, Wabunge wengi wanakaa Jimbo la Ukonga na Dar es Salaam kwa ujumla, hata kama mtu hakai ana kibanda pale lakini Dar es Salaam hakuna machinjio ya kisasa. Kuna machinjio ndogo kweli kweli pale Vingunguti na yale mazizi ni ya mtu binafsi siyo ya Serikali. Pale Zingiziwa kuna ekari zaidi ya 120, kama mkiweka mifugo pale na kuna mnada wa Kimataifa wa Pugu ambao kimsingi na wenyewe ni jina, ni mnada lakini ni kijiwe cha ng‟ombe, hakuna maji, hakuna chochote pale, ukiboreshwa utasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar es Salaam ndiyo kuna Mawaziri, ndiyo ipo Ikulu lakini hakuna nyama safi, watu wanaweza kuchinjia vichochoroni wakauza mitaani, sijui kwa nini hampangi haya na maeneo yapo, hapa sikuona chochote kwamba mnaboreshaje suala hili. Dar es Salaam kuna watu wengi na wageni pia lakini suala hili haliwekewi mipango. Mbona mmesema tupande miti ili Jiji lipendeze Wazungu wafurahi, tengenezeni basi na mazingira mazuri ya kuchinjia nyama kwa afya zao. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme habari ya maji. Watu mikoani wanalia, lakini nawaambia hata Dar es Salaam kule Jimbo la Ukonga katika kata 13 ni kata moja au mbili zinaweza zikawa na uhakika wa maji na visima vingi zaidi ya asilimia 90 ni watu wamechimba wenyewe. Mheshimiwa Dkt. Mpango anakaa Zingiziwa pale Nzasa, yeye ni mpiga kura wangu kule, tupange siku moja aende Zingiziwa aone wale watoto na wazazi wa pale maji ambayo wanakunywa, Dar es Salaam acha kule kwao Kigoma, Dar es Salaam, maana anavyoandika hivi vitu twende kwa ushahidi aende aone, hajaandika chochote hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, afya; Jimbo la Ukonga lina wapiga kura zaidi ya laki sita na kata 13. Watu wote wale kutoka Zingiziwa, Chanika, Msongola, Mvuti, Uwanja wa Nyani wanakuja Amana. Tuna eneo kubwa ekari 45 kwa ajili ya kujenga hospitali na tangu mwaka jana niliwaambia kwamba ile hospitali ikijengwa itasaidia mpaka na Kisarawe mpaka Mkuranga. Halmashauri ina uwezo wa kutenga shilingi milioni moja kwa mwaka na gharama yake ni shilingi milioni 26 maana yake Halmashauri ikiachiwa ijenge itatumia miaka 26 watu wanasubiri huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda anapopanga zahanati, kituo cha afya na hospitali ataje majina ili Mbunge ajue zamu hii ni ya Msigwa, zamu ijayo itaenda labda Kwimba na sehemu nyingine, tuwatajie, asiweke kwenye bracket hapa. Aseme anataka kujenga hospitali ipi, zahanati ipi ili tujue kama siyo zamu yangu nisubiri mwaka ujao na akiandika atekeleze, aache kutuimbia ngonjera hapa. Mlishatuambia tutaisoma namba, tutaisoma wote pamoja, bahati nzuri hatuisomi wenyewe na nyie mnaisoma sana. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Shirika la Ndege amelizungumzia, nataka nihoji hapa, tuna taarifa kwamba Chato kwa Mheshimiwa Magufuli pale nyumbani kwao Chato unajengwa uwanja wa ndege, mbona kwenye mipango hapa hiyo hela haipo? Bajeti iliyopita haikutajwa na hii hapa haijatajwa lakini unajengwa uwanja wa ndege kule Chato. Tunaomba tujue hiyo bajeti ya kujenga uwanja huo iko wapi mbona hapa kwenye mipango hamuutaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu mtuambie, hivi Chato kujenga uwanja wa ndege, sawa kweli wale ni watani na wakwe zangu, hivi kule Chato mtafanya biashara gani, projection ni nini pale? Yaani mnataka mjenge uwanja wa ndege ili Mheshimiwa Magufuli akitaka kupumzika aende na ndege nyumbani kwao? Kujenga uwanja wa ndege ni lazima kuangalia economic zone kwamba biashara itafanyika kwa sababu population ni kubwa na vitu vya namna hiyo. Haya hata hapa hamuonyeshi, sasa hiyo siyo siri tunajua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile kumekuwa na malalamiko ya ndege mlizonunua, mimi siyo mtaalam, ndege zenyewe ni Bombardier?
Wanasema mikataba duniani mnalipa kwa advance nyie mmeenda kulipa kwa bei ya jumla. Mmechukua hela zote mkaenda kununua ndege kwa mbwembwe, eti mnazindua kununua ndege, hivi kweli nyie mnaumwa, unazindua kununua ndege? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, karne ya 21, Serikali ya Chama cha Mapinduzi zaidi ya miaka 50, umri wa mtu mzima yaani miaka ya chama chenu inanizidi mimi Waitara, Mbunge wa Ukonga hebu niangalie halafu mnasherehekea kununua ndege. Muangalieni mwenzenu Kagame, ndege ya kwanza aliyonunua na mambo anayofanya. Ameleta ndege ambayo inaendesha kwa mitambo, shabash, nyie mnapiga makofi hapa! Wabunge wanasimama hapa hoja ambazo hazina maana eti anaunga mkono ili asisahau maana wamezeeka halafu wanalalamika, mambo gani haya bwana? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme. Mimi ni Mbunge wa Ukonga, ukienda Kata ya Msongola, robo tatu ya kata hakuna umeme. Kivule ina mitaa minne, mitaa miwili ndiyo ina umeme. Ukienda Zingiziwa kuna mitaa nane ni mtaa mmoja tu wa Mheshimiwa Waziri wa Fedha ndiyo kuna umeme. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Chanika kuna mitaa nane, miwili ndiyo ina umeme. Ukienda Pugu kuna mitaa mitano, mitatu ndiyo ina umeme miwili haina umeme. Ni Dar es Salaam hiyo sikutaja majimbo mengine ya Kigamboni na kadhalika na mnasema ule ndiyo mji ambao una population kubwa, ndiyo mji wa kibiashara, ndiyo Rais yuko pale lakini umeme ni shida. Kule mnatoa matamko kushughulikia watu kwenye vikao, kupindishapindisha na kuiba kura za Kinondoni, mnatangaza Meya hewa, mmeleta Meya hewa pale wakati nyie mnatafuta wafanyakazi hewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu Waziri anayehusika ashughulikie suala hili ili umeme isiwe wimbo Dar es Salaam. Watu wanakaa Dar es Salaam kwa maana ya majina lakini akimwambia mtu amtembelee anamzungusha mjini anamkimbia kwa sababu akienda nyumbani kwake hatafanana na mbwembwe alizokuwa anasema. Kwa hiyo, tunahitaji suala hilo lishughulikiwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Waitara muda wako umeisha tafadhali naomba tu ukae.
Haya basi siungi mkono hoja mimi.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza niseme tu kwamba mimi ni Mjumbe wa Kamati hii ya Utawala na Serikali za Mitaa, kwa hiyo naunga mkono maoni yote ambayo yamewasilishwa na Kamati yangu hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipata fursa ya kushiriki Kamati kwenye ziara na kuangalia miradi na kwenye mawasilisho mbalimbali ambayo yalifanyika kwenye Kamati yetu, yapo maeneo muhimu ambayo nataka kuchangia hapa. Jambo la kwanza; tulizungumza hii Kamati inahusika na mambo ya utawala na tukaangalia eneo la kero kwa wananchi, rushwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, rushwa imekuwa ni kubwa ingawa upande wa Serikali ukizungumza nao watakwambia rushwa imepungua kwelikweli, si kweli. Jambo hili limechagizwa sana na kauli ya Mheshimiwa Rais kwamba maaskari wanaruhusiwa kuchukua rushwa ndogondogo, 5,000 hela ya sabuni na kubrashia viatu. Bahati mbaya sana kwa sababu ya hofu na woga uliopo hakuna mtu ambaye alienda front kumshauri ama kubadilisha ile kauli na imekuwa ni kero kwa wananchi na hasa vijana wa bodaboda ambao wanajitafutia maisha katika jua kali, wanaombwa sana hizi fedha mnaita ndogondogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni maoni yangu kwamba ni muhimu upande wa Serikali wakaliangalia jambo hili upya na ni muhimu kuangalia pia kauli za viongozi wetu na hasa Mheshimiwa Rais. Haiwezekani kiongozi ambaye ameapa kuitii Katiba ya nchi na sheria na kanuni anasimama hadharani bila hofu wala woga anasema askari wakipewa sh. 5,000 ya kiwi ya viatu ni sawasawa kabisa na anasema ni hela ya kiwi, lakini hili jambo limekuwa ni kero kwa wananchi wetu ambao kimsingi maisha ni magumu na kipato ni kidogo na unapokosa sh. 5,000 inaweza kupelekea hata kung‟oa matairi na mambo mengine chungu nzima ambayo yanafanyika, hilo ni eneo la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo tuliliona ni eneo la TASAF. Mimi ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, kwa hiyo nafahamu vizuri namna ambavyo watu wetu wamepata msaada mkubwa kupitia fedha hizi na ni mpango mzuri pamoja na kwamba zipo changamoto mbalimbali ambazo inabidi zifanyiwe kazi kwa maana ya kuboresha ili hii fedha iendelee kupatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia wapo wananchi wengi sana ambao hawana uwezo na michakato haikuwapitia, wakazikosa. Kwa hiyo, niishauri Serikali, ni muhimu yale maeneo ambayo watu walikuwa wanakidhi vigezo, wana uwezo mdogo na hawakupata zile fedha, basi maeneo hayo yaangaliwe upya ili watu hao waweze kupata msaada wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni yangu ni kwamba ni muhimu hizi fedha pamoja na kuwapa watu wetu ili kuwasaidia wapo wachache, kama tulipokwenda Zanzibar, Pemba na Unguja ikaonekana baadhi ya maeneo ya Tanzania Bara yamefanya hivyo, wale wazazi wanapewa zile fedha wanatumia wanabakisha kidogo wanaweka miradi midogomidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri tuwekeze kwenye miradi midogo midogo kwa sababu mpango huu sio mpango wa miaka yote, maisha yao yote, kama wakijifunza ku-save kidogo wanatumia na wakaanzisha miradi midogomidogo hata akili zao zinachangamka katika kujipangia mapato na matumizi yao. Kwa hiyo tungependekeza jambo hili muhimu likachukuliwa kwa uzito. Wawezeshwe fedha lakini pia waelekezwe namna ya kuwekeza kwenye miradi midogo midogo ili iwasaidie huko baadaye. Hata kama fungu hili likiondolewa watakuwa wamejipanga vizuri juu ya namna ya kupata huduma kwa sababu lengo ni kuwasaidia hapa walipo na waweze kujiinua kimaisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli wamepata msaada, wengine wamesomesha watoto, wengine wamejenga hata vibanda hata kama ni vibovu lakini imesaidia kwa kweli. Kwa hiyo, ile kauli ambayo inaonekana kwamba kuna taarifa huu mpango haujasaidia; leo wale wazazi ambao hawana uwezo, watu wetu wale, badala ya kwenda kupanga foleni kwa Diwani au kwa Mbunge kuomba hela ndogondogo wanakwenda kupanga foleni kwa Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo cha muhimu hapa fedha ni muhimu, ni kuboresha mazingira ambayo yana changamoto mbalimbali na uwazi uwepo, wale wahusika wapewe, hilo ndilo jambo la msingi sana. Mtu ambaye anashauri kwamba hii fedha iondolewe, kwa kweli huyu mtu ni wa kulaani sana, hawatakii mema watu wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la watumishi hewa. Ni kweli kwamba Serikali imechukua hatua ya kuangalia watumishi hewa, lakini jambo hili linachukua muda mrefu sana. Wapo watu ambao maslahi yao yamezuiliwa kwa sababu ya hoja ya watumishi hewa na hasa ajira mpya kwa vijana wetu. Sasa ni muhimu jambo hili kuwe na deadline, kwamba mnafanya kwa muda wa mwezi mmoja, miwili, mitatu au minne, jambo limalizike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu watumishi hewa; kwanza watu wanataka kujua nani ni mtumishi hewa ajulikane na hawa ndio wanaotakiwa wawajibishwe; wale waliopokea fedha na wale viongozi ambao ni wa Utumishi waliotengeneza miundombinu ya kupata watumishi hewa, wasiwawajibishe watumishi wasiokuwemo. Kwa sababu kama kuna fedha inalipwa kutoka kwenye akaunti, wale wakubwa wawajibishwe. Hata hivyo, jambo hili liishe ili watu wetu wapate ajira na waweze kutumikia Watanzania kwa ubora zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la utawala bora. Leo asubuhi nilisikitika sana Mheshimiwa Simbachawene. Kwanza anajua hapa karibuni umetengenezwa mgogoro mkubwa sana Serikali za Mitaa. Lilizuka jambo la mihuri hapa mpaka wenyeviti wenzangu wa mitaa wakafikia hatua ya kuandamana, kuunda Kamati mbalimbali na kuanza kufanya zile kazi. Sasa hapa ni muhimu tukajua, zipo kazi za Wenyeviti wa Mitaa, zielekezwe vizuri. Mtendaji anapoajiriwa anajua kazi zake na Wenyeviti wa Mitaa waelekezwe. Sasa kutujumlisha kwamba wote tunapiga maeneo ya umma si kweli, mimi ni Mwenyekiti wa Mtaa, sina kesi ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni muhimu maelekezo yaende kwamba kama kuna Mwenyekiti ambaye kwa kweli ametumia nafasi yake vibaya huyo awajibishwe. Wale ambao wamepewa, kwa mfano Mheshimiwa Waziri ukiulizwa tangu uchaguzi umefanyika mwaka 2014 ni mpango gani mmefanya kutoa semina kwa Wenyeviti wa Mitaa, Madiwani na hata watendaji? Mtu amekuja hapa Hombolo kapata mafunzo yake, kapata ajira akifanya makosa sio fault yake ni fault ya Wizara, kwa hiyo naomba Wizara itimize wajibu wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, nimesikitika sana leo asubuhi, sisi tunasema Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa wanajiita Marais; wewe umeunga mkono hiyo hoja kama ni kweli eti kwa sababu madaraka yanashuka kutoka kwa Mheshimiwa Rais, kwa hiyo nchi hii kila mtu ni Mheshimiwa Rais! Sisi tulichouliza ni kwamba, Wakuu wa Wilaya wanahujumu mpaka Waheshimiwa Wabunge, hatuheshimiani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam amefanya ziara Dar es Salaam pale Ukonga, kwa heshima nimetoka nyumbani kwangu nimekwenda kwenye eneo lile, nikakuta, Mkuu wa Mkoa anatukana watumishi kwamba ninyi ni mizigo, ninyi ni misumari. Mwanamke, yule mama wa Kinondoni, ninyi wanawake mnasema hapa wanawake wapewe fursa wafanye kazi! Afisa Utumishi wa Kinondoni Makonda anamwambia wewe ni mzigo, hivi nani amekuweka hapa! Toka hapa potea pale mbele!
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkuu wa Mkoa, kwenye public, kwenye mkutano wa hadhara, yule mama ameshindwa hata kutembea miguu imekuwa mizito, hayo ndiyo mambo tunayokataa hapa. Mkuu wa Mkoa yupo kwenye mkutano eneo la mgogoro, limeunda Kamati pale, Diwani amefanya kazi yake, Afisa Utumishi amekwenda, Afisa Mipango ya Maendeleo wa eneo lile, Mkuu wa Mkoa anakuja pale kwa sababu ana polisi anamwambia Diwani apate fursa ya kutoa taarifa, mimi hata kusalimia alinizuia, akasema hiki kikao ni cha Mkuu wa Mkoa, halafu tuheshimiane namna gani? Hayo ndiyo mambo ya msingi ya kuzungumza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani shule zinafelisha; mwaka jana Mkuu wa Mkoa wa Simiyu ameagiza mkoa mzima, eti wakuu wa shule amewatumbua, halafu mnataka matokeo yawe mazuri yataanzia wapi, hatuheshimiani kwenye kazi. Kwa nini Mkuu wa Mkoa asione kuna shida? Tumesoma ile sheria vizuri, kama kuna shida, kama kuna mkuu ninayempongeza sana ni Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, nilimwona kwenye TV, naomba mumpigie makofi basi hata huyu amefanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu amekwenda anajadili matokeo ya form four, ameita watumishi kwenye idara husika, anasema tulifanya kikao tukasema atakayezembea eneo lake atawajibishwa, anasema naomba idara husika ya elimu iwajibishe wahusika, simple. Kwa hiyo, ukishasema hivyo watafanya utafiti, watafanya enquiry fulani, itakuja taarifa anayehusika na mambo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, haya mambo ndiyo tunataka yafanyike. Hatutaki watu wazembe ila hatutaki watu waonewe tunataka mtu akiwajibishwa; na Waziri ni Mwanasheria wa eneo hili, wote wawili, Waziri wa Utumishi na Waziri wa TAMISEMI na nawaheshimu sana ndugu zangu, lakini tunataka utaratibu tu. Hivi Mkuu wa Mkoa kweli ni rais kwenye mkoa wake! Ni rais kwenye wilaya yake! Kwa hiyo kuna vitu ambavyo mnadanganya watu hapa, naomba tuheshimu hiki chombo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachosema sisi ni kwamba hatupingi kila kitu, yapo mambo yanafanyika mazuri tunaunga mkono. Tunapiga kelele sana kwa mambo mabaya, kukatisha watu tamaa na matumizi mabaya ya madaraka. Hivi inawezekana Mheshimiwa DC amekwenda kwenye mkutano, anamwambia Diwani kamata weka ndani halafu tupige makofi? Ni kiongozi mwenzake halafu anataka ampe ushirikiano, hizo taarifa anazipataje na hao ni watu ambao kwa kweli wameletwa kwenye maeneo yale na kuna mtu amepigiwa kura na watu wake, kwa hiyo mnajenga chuki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Nkamia amesema hapa leo asubuhi, kwamba inawezekanaje DC anatukana wananchi halafu huyu anasema eti ndiyo Rais wa eneo lile…
MWENYEKITI: Ahsante.
Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa Mwaka 2016
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mimi sijaku-miss ila nimefurahi wewe angalau kupata fursa ya kuongoza Bunge baada ya muda kidogo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo yamezungumzwa hapa, wapo Wabunge wanasema Tanzania kupitisha sheria hii itakuwa nchi ya 67 kwa dunia na wengine wakasema ni nchi ya tano Afrika na story nyingi sana za mataifa mengine. Nikawa najiuliza tu kwamba hivi tunahitaji sheria nzuri au tunahitaji idadi ya nchi ambazo zimetunga sheria mbovu yaani tunataka tuige kitu gani hapa, ina add value gani kwenye sheria hii? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Sheria amenisaidia jambo muhimu sana ambalo lilikuwa kwenye mchakato wa Katiba Mpya. Alipoanza Ibara ya 2 anasema, sheria hii itatumika Tanzania Bara. Huyu ametukumbusha kwamba kumbe bado tunahitaji Serikali tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Waziri wa Sheria amekaa maana ni Ofisi ya Wanasheria wa nchi hii wamekaa wakaona hii sheria itumike Tanzania Bara peke yake na Bunge hili lina Wabunge kutoka Zanzibar wanawakilisha maslahi ya Zanzibar na kumbe tulikuwa na hoja ya akina Jaji Warioba ya Serikali tatu, mimi nadhani hiki kipengele kimewaumbua kweli kweli. Unajua njia ya muongo huwa ni fupi, mmetusaidia.
Kwa hiyo, Watanzania wajue na dunia inajua kwamba tunalazimika kuwa na Serikali tatu kwa sababu hata nyie wenyewe hamuitambui Zanzibar ila wakati wa kuchakachua matokeo mnafanyaga kwamba ni kwenu ila kwenye sheria mbalimbali wala hamhusiki.
TAARIFA...
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza sipokei taarifa za design hiyo, mimi napeleka wapi hizi? Hili ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunazungumza mambo ya Tanzania ya wote, hili siyo Baraza la Wawakilishi. Kwa hiyo, naomba niendelee, hawa watu wana copy na ku-paste lazima tuwape habari zao. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mapendekezo yangu baada ya kupitia muswada huu vizuri, nimeusomasoma sana, kama Waziri angekuwa ana nia njema sina shida na jina lililotajwa kwamba ni kupata taarifa ambayo of course inatumika interchangeably mara taarifa, mara habari maana na hiyo pia inabidi uweke very clear unamaanisha kitu gani hapa. Ndiyo maana watu wakahoji leo asubuhi jina likabadilika ghafla kwa hiyo ikazungumzwa kitu kingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukizungumzia taarifa na ukasoma ile Ibara ya 18 maana yake jambo lote hili lina expire, halina maana. Kwa sababu mmesema kwamba mnataka kuwasaidia wananchi wapate taarifa lakini umeweka masharti mengi kweli kweli na adhabu mbalimbali ambazo taarifa ikitoka zinatumika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, leo nilikuwa nasoma Gazeti la Habari Leo linaandika sana habari zenu hili, ukurasa wa pili, nasoma kidogo kwa ruhusa yako, anasema, watoa taarifa fake za uhalifu kutupwa jela, faini ya shilingi milioni tatu au mwaka mmoja au vyote kwa pamoja. Sheria ya Kuwalinda Watoa Taarifa za Uhalifu na Mashahidi ya mwaka 2017, huyu ni mwandishi wa habari ameandika wa gazeti la leo, hivi sheria hii ipo kweli? Kwa hiyo, huyu naye anatakiwa afungwe miaka kumi si ndiyo maana katoa taarifa ambayo sio sahihi. Si ndiyo maana yake? (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mwandishi ukimuuliza amekosea kidogo tu kwamba hii sheria haipo, alikuwa anamaanisha kitu kingine lakini kalamu ikateleza na kwenye printing hakusoma vizuri ikatoka. Sasa adhabu imeshatolewa kwenye sheria ambayo mnazungumza leo. Nilikuwa nawaonesha haya mnayozungumza hapa yanawahusu na ninyi wenyewe pia huenda hata huyu mwandishi ni mtoto wa kada wa CCM halafu ndiyo anawajibishwa na wewe unapiga makofi hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ni muhimu sana awasaidie Watanzania na mimi pia sielewi, hii Ibara ya 6 yote ilipaswa iondoke kama ambavyo Kambi ya Upinzani ilipendekeza kama kweli nia ni kusaidia watu wapate taarifa mbalimbali zinazohusu maisha yao ya kila siku kwa mujibu wa Ibara ya 18. Kwa mfano, unazungumziaje habari ya mtu anamiliki biashara yake nikitoa taarifa eti ataathirika, mliongea naye lini, yaani wewe una share kwenye hiyo kampuni? Kwa nini usipokee taarifa yangu halafu uifanyie utafiti, kwa sababu kuna zile sheria za defamation na Waziri anafahamu, kama taarifa inatolewa ambayo inamhusu mtu itatumika hiyo lakini siyo kunihukumu mimi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge lazima wajue ilivyo mpaka sasa hivi watu wengi ambao wamewajibishwa ni wale wakuu wa taasisi. Hawa Maafisa wa Habari watakuwa wanateuliwa na wakuu wa taasisi. Hivi Mkuu wa NIDA yuko wapi, naona wanasema anasota mahakamani si ndiyo? Hiyo ilikuwa NIDA maana yake huyo ndiyo bosi wa NIDA, anamteua Afisa Habari ambaye kabla hajatoa habari inabidi aende kwake aka-confirm atampa atoe taarifa za kuficha madhambi yake halafu huyu unaenda kumuuliza asipokupa taarifa. Kwa hiyo, kama kuna mfanyakazi mwingine kwenye Idara ile akinipa taarifa waandishi wakiitoa nje Watanzania wakajua hawa ndiyo wanatakiwa kuwajibishwa ila huyu ambaye ametoa taarifa ya uongo hatakiwi kuwajibishwa. Ndiyo maana mnaambiwa hayo mnayozungumza humu ni mambo ambayo mnatengeneza mazingira ya kujificha kwenye mgongo wa nyuma, lakini ukweli wa mambo ni kwamba mnaficha ukweli. Hilo ndiyo lengo la sheria hii ambayo mmeileta hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Ibara ya 6(5), hapa imezungumzwa miaka thelathini, kwanza Waziri hapa ametaja kijiji, bahati nzuri mimi ni Mbunge wa Ukonga inawezekana wajanja wajanja ni wengi pale kuna mwingiliano mkubwa sasa, mimi nipo Tarime nyumbani, kule Kegonga, Masanga, kutoka Nyanungu aje Tarime Mjini ili akamuone Afisa Habari wa Manispaa inabidi kwanza awe na nauli ya shilingi 15,000 kwenda na shilingi 15,000 kurudi yaani akitaka taarifa ya Serikali ni mpaka awe na shilingi 30,000. Halafu hawezi kufika akarudi siku hiyo hiyo, mvua kwa mfano imenyesha itabidi alale mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, anayetaka taarifa hapa inabidi kwanza awe na nauli ya kwenda na kurudi, apate hela ya kulala gesti, apate hela ya chakula, kwa hiyo, lazima uwe na bajeti ya kutafuta taarifa ya Serikali. Hivi mnadhani Waziri hii kweli ni haki? Hiki kitu kinachofanyika hakikubaliki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu mnasema taarifa ikiombwa huyu atazungukazunguka siku thelathini. Ikitokea sikupata taarifa, maana anaweza akaamua kunipa au asinipe halafu aende kwa bosi wake, bosi wake anaweza akahamisha akasema hili halinihusu na ndiyo tabia yao, apeleke kwa mtu mwingine tena, sheria hapa inasema utaanza upya tena. Imagine umechukua siku 30 wakikusikiliza ndiyo wanakujibu siku ya mwisho ndiyo wanakujibu siku ya mwisho kwamba hii taarifa haiko kwangu nenda kwa Waziri Mwakyembe. Anakaa nayo tena siku nyingine zile ishirini na tisa anahamisha anasema kwamba hili jambo liko kwa Mheshimiwa Maghembe angalia mchezo unaofanyika hapa na hiyo ipo all over.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ile Ibara ya 6 ametoa adhabu miaka 15 na isiyozidi 20. Niliona mapendekezo ya Sheria ya Dawa za Kulevya wametoa adhabu mpaka ya miaka mitano, hivi kweli Bunge hili, ndiyo maana huwa sisemi Tukufu ila tuseme kwa sababu imeandikwa, Bunge hili kweli hivi mtu anayeuza dawa za kulevya, anaharibu vijana wa Tanzania, anaharibu nguvukazi ya Watanzania ni sawa na mtu ambaye amepotosha taarifa tu au kwa sababu hakupewa taarifa na mhusika katika Idara husika, inaweza kuwa sawasawa kweli? Hebu tuwe makini katika mambo haya tunayoleta kama viongozi na watu wazima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye Ibara ya 12, nilitaka nijue, kama nimeenda kwenye Idara fulani, nikaomba taarifa, wakanipa taarifa ambayo naona ni ya uongo, kuna mtumishi mle ndani akanipa taarifa sahihi, kwa sababu tu mimi ninayo ya kweli ambayo nimetoa kwenye source halisi kwa watu ambao wako jikoni, lakini nimepewa iliyopotoshwa hapa napewa adhabu kwa taarifa hizi. Kwa nini sheria isiseme unaweza ukapewa taarifa mahali popote ila ikichunguzwa ikaonekana kwamba kweli haina ukweli huyu mhusika ndiyo ashughulikiwe lakini hapa inabana kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 10 ameelezea namna ya kupata taarifa, hajaruhusu kupiga simu ambayo ni njia rahisi kwamba mtu kama hana nauli, anataka taarifa akapiga simu, anajieleza, anajitambulisha, anahojiwa apate taarifa. Hapa mmeorodhesha kwamba unaweza ukaandika barua, njia ya elektroniki lakini simu hazipo. Maana yake ni lazima mtu asafiri akapate taarifa, kwa hiyo mnaingiza watu kwenye gharama ya kutafuta taarifa hizi katika maeneo ambayo ni mbali na wanapokaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kulizungumzia ni Ibara ya 21, kinasema:-
“Mmiliki wa taarifa ambaye maombi ya kupata taarifa yatatumwa kwake anaweza kutoza ada iliyowekwa kwa ajili ya kutoa taarifa hiyo.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, unaona sasa? Kwa hiyo, sasa mnaanza kufanya biashara ya kuuza habari, mnaanza kuwauzia wananchi taarifa, ndiyo mmesema hapa kwenye Ibara ya 21 na huyu atakuwa na discretion ya kupanga ada awadai kiasi gani kwamba mwananchi anahitaji taarifa fulani inabidi alipie kiasi hicho. Kwa hiyo, kama huna hiyo ada iliyowekwa na mwenye chombo chake ambaye ana taarifa hiyo ina maana hiyo taarifa hautapata na biashara yako itakuwa imeishia hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo nilitaka niseme la jumla, hii sheria kwa namna mlivyoileta ukiisoma vizuri maelezo ya Waziri mdomoni anamaanisha kitu kingine, alichokiandika ni kitu kingine. Kwa sababu ni Mwanasheria anajua akiandika hivyo watu wa kawaida hawatajua.
Waheshimiwa Wabunge hiki kinacholetwa kimsingi kinaenda kuumiza watu wetu na sisi wenyewe tukiwa miongoni mwao. Wakati Mheshimiwa Bashe anazungumza hapa watu wa CCM wamekaa kimya kama wamelowa, hawasemi ili baadaye wampeleke kwenye vikao vyao wakamtishe sio, hawakumpigia makofi. Hata hivyo, ukweli ni kwamba hii habari ya kutoa taarifa mbalimbali, hili Bunge lilikuwa linajadili habari ya Lugumi, Lugumi ilianza kwenye vyombo vya habari hakuna afisa aliyetoa taarifa, hiyo habari mmeizugazuga hapa imeisha. Mambo ya IPTL ni waandishi wa habari waliibua mijadala mbalimbali, Balozi Ole alikuwa Italia mpaka anashtakiwa ni waandishi wa habari waliandika habari za kiuchunguzi. Yako mambo mengi ambayo yameibuliwa na vyanzo ambavyo sio rasmi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ningewashauri kama kweli mna nia njema mngekubali taarifa ipatikane kwa mujibu wa Ibara ya 18, mtu yeyote anaweza atakayetoa taarifa ahojiwe, iwe verified halafu kama kuna mtu ambaye atakuwa amekiuka misingi ya utaratibu katoa taarifa ya uongo, zipo sheria zile za forgery, defamation na mambo mengine yasaidie. Hilo ndiyo lingekuwa jambo la msingi sana lakini unaleta sheria ambayo inataka kuwatisha kwanza watu yaani hapa itakuwa ukitaka taarifa unaulizwa nani amekuambia, upelelezi haujakamilika, wewe siyo mhusika, nani amekupa mamlaka maana yake tunajenga nchi ya uoga. Waziri wa Sheria wewe umri wako siyo mkubwa sana siyo kwamba utaendelea kuwa Waziri kila siku, angalia wenzako wapo mtaani, wengine wameenda lupango, hizi sheria ambazo unaleta hapa kwa kweli lazima mziangalie mara mbili mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, lakini siungi mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wa Mwaka 2016
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, naomba nianze tu na hii ya Chemistry Professional Act maelezo ya jumla tu kwamba nimejaribu kuusoma huu muswada nia ni njema ya Serikali na mimi ni mwana chemist pia.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama alivyosema Mheshimiwa Susan Lyimo hapa ukiangalia ile composition ya namna ya kuwapata hawa wanataaluma ni kama huu muswada hautoi uhuru wa wao wenyewe kupatikana. Nadhani Mheshimiwa Waziri ambacho ungefanya ilitakiwa hao watu iwekwe utaratibu ambao wanakutana na wanachaguana halafu Wizara iwe ni kusimamia na kuondoa kero mbalimbali, ku-facilitate utendaji wao ingekuwa jambo jema sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na hata mimi ningependa nipate maelezo sikuona sababu ya kuingiza polisi katika eneo hilo kwa sababu hawa watu kimsingi au kumpa Waziri mamlaka makubwa sana kuwadhibiti kwa sababu wao ni wataalamu kama umeingia kwenye maabara kuna jambo linazungumzwa ni professional yaani huwezi kuingiza siasa katika eneo lile. Kwa hiyo, sioni kuna sababu yoyote ya msingi ya kuwa na hofu kwamba lazima wabanwe sana waminywe mamlaka yao na lengo ni jema kwamba tuwe na watu hawa na Bodi yao na Baraza lao ambalo wanaweza kufanya maamuzi yao kitaalamu halafu Serikali inayachukua inayafanyia kazi mwisho wa siku hawa watu kazi wanayofanya itakuja Serikalini tu. Kwa hiyo, nadhani muangalie utaratibu wa kuwapa uhuru wakufanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nije sasa kwenye hii ya Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali. Kwanza nilisikitika sana, katika mawasilisho ya Kamati ile wanaonyesha kwamba hawakukutana na wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alitaja kama nakumbuka vizuri hawakukutana. Lakini wataalam kutoka SUA hawakuwepo na wataalam kutoka Muhimbili, sasa kwa kadri ninavyofahamu hivi ni vyuo vikubwa na vya muda mrefu na vina wataalam wa waliobobea hata vinavyoanzishwa wanakuwepo na wataalam kutoka maeneo haya na ninyi wenyewe mnafahamu kama Naibu Spika na wataalam wengine mnafahamu hili.
Sasa ningeomba nielezwe aliandika kupewa maandishi kutoka Mlimani uje kusoma unless huyu mtu ametuma mtu ambaye ni professional afanye interpretation alimaanisha kitu gani kwa hiyo ina maana Kamati haikupa fursa ya kukutana wataalam wenyewe ipendekeze.
Mheshimiwa Naibu Spika, na ninaamini kwamba ilipotengenezwa huu muswada mpaka unakuja hawakuwa tena wameshirikishwa, sasa kwa kweli ni jambo ambalo sikuona kama ni sawa sawa yaani huwezi kuwa unazungumza habari ya Ofisi ya Mkemia Mkuu na Mamlaka yake na Bodi unaunda halafu Muhimbili ambao unapozungumza haya mambo biologist na nini ndio wataalamu wetu pale.
Kwa hiyo, nadhani mngesaidia maelezo mwanzoni mtusaidie kama kulikuwa na shida gani yaaani wali-divert, hawakutoa ushirikiano au ilikuwaje.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya nne, kifungu kidogo cha (4) anasema; “bila kujali masharti yaliyotangulia katika kifungu hiki, Mwanasheria Mkuu wa Serikali atakuwa na haki ya kuingilia kati katika kesi au shauri lolote lililofunguliwa dhidi ya mamalaka.”
Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake huyu anakwenda kwenye government interest ya kuwa-defend. Lakini ningetaka hapa niliposoma hapa tafsiri ya Kiswahili kwenye Kiingereza pale inaeleweka vizuri lakini hapa ilivyowekwa ni kana kwamba anaingilia kusimamia shitaka ambalo dhidi ya mamlaka lakini anaweza kaathiri upande mwingine usipate haki vizuri, kwa hiyo, naomba lugha hapa ieleweke. Kwamba huyu anaweza akingilia kwa maslahi ya Serikali na maslahi ya mamalaka hii, lakini vilevile bila kuathiri au kuminya haki ya upande mwingine katika zile pande mbili zinazokuwa zinasigana. Kwa hiyo, ni muhimu sana nimeona hiyo lugha haijakaa sawasawa Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya tano, (section 5) ile mamalaka itakuwa maabara ya rufaa na matokeo yake ya uchunguzi itakuwa ni ya mwisho kuhusiana na masuala yanayohusu uchunguzi wa kimaabara.
Sasa kwenye kipengele (a) itafanya shughuli za kitafiti, uchunguzi na kimaabara na kuishauri Serikali na taasisi nyingine kuhusu masuala yanayohusu uchunguzi wa sumu, kibaiolojia, vinasaba na dawa za kulevya. Sasa hapa hoja yangu ilikuwa ni kwamba kwanza niipongeze Serikali kwa sababu tulipokutana mimi ni Mjumbe wa Kamati ya UKIMWI na Dawa za Kulevya, kwa hiyo, ninapoona maeneo ya madawa ya kulevya nina interest nayo. Lakini hii tulipokutana na Mkemia Mkuu mojawapo ya mapungufu ya utendaji ilikuwa ni haya mamlaka ya kukamata, kuchunguza na kushitaki.
Kwa hiyo, nadhani hili neno lote kwa pamoja nikupongeze kwamba angalau umei-capture hii hoja ambayo tulipokutana na Ofisi ya Mkemia Mkuu walitoa hiyo kwa hiyo hilo nashukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kipengele cha 7 kina shida pale, hii sehemu kwa mfano ndio inatoa composition hivi sasa ya Wajumbe wa Mamlaka hii kwenye Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali. Wametajwa hapa kwanza (c) anasema mwakilishi kutoka taasisi za elimu ya juu au utafiti wenye utaalamu katika masuala yafuatayo....
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hii nilikuwa nashauri, ametaja hapa pathologia, kemia na madini. Hapa mimi naona kulikuwa na sehemu mbili muhimu sana, ningedhani katika composition ya member hawa ni muhimu kuwe na mtu ambaye ni professional chemist ili a-deal moja kwa moja na mambo ya kemia na nini, lakini pia kuwe na biologist katika eneo hili.
Kwa hiyo, ningependekeza kwamba, hapa ni muhimu hawa watu wawili wawepo bila kusema either of these two, angalau wawili hawa kwa sababu, kama ni chemist mambo anayojua ni tofauti na biologist na Dkt. anafahamu. Kwa hiyo, nadhani mngesaidia ile ili at least kama hoja inaingia pale kila mtu yupo kwenye reli yake ambayo ni professional na itakuwa haina shida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine kuna hii hoja ya (e) hapa sikuona imetajwa kwamba, kuna watu ambao ni ma-chemist, lakini hawapo Serikalini ni binafsi. Sasa na yenyewe hapa hii hoja haijawa captured hapa. Hata vyuo binafsi, kule kwenye professionals ndio mmetaja, lakini hapa kwenye hawa Wajumbe hamkutaja kama kuna uwakilishi wa taasisi binafsi, kama kuna uwakilishi wa vyuo binafsi, kama kuna watu kwa mfano TBS maana wenyewe ndio wanapima viwango na nini, kwa mfano kuna Wizara ya Kilimo hapa. Sasa nadhani hayo mambo ni muhimu mkayaangalia kwa maana hiyo, sasa hii namba haipaswi kuwa fixed kama ilivyo sasa inabidi iwe iwe ziada kulingana na maeneo ambayo na mimi naona ni muhimu sana mkayazingatia.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia, kuna tafsiri ya Kiswahili hapa ni tofauti kule. Nilipoona kwamba, mwakilishi wa Wizara haikuwa imetaja Wizara gani, lakini kule kwenye ile sehemu ya Kiingereza imetaja Minister responsible for Health kwa hiyo, nadhani hapo pia katika maeneo ya nyongeza hiyo (b) inabidi useme ni mwakilishi wa Wizara ipi. Haukuwa umetaja.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pale kwenye hiyo hiyo 7(5) muda wa kuwa madarakani Wajumbe, mwenendo wa Bodi pamoja na masuala mengine yanayohusiana na Bodi yatakuwa kama yalivyoainishwa kwenye jedwali. Kwenye jedwali nimesoma ile sehemu ya miaka mitatu, sasa mimi nikawa nashauri kwa nini isiwe miaka mitano kwa sababu, hawa watu ukiwa na muda mfupi sana wa kufanya kazi ina maana unaweza ukawa umeanza labda ndio una-take off halafu muda unaisha. Kwa hiyo, mtu mwingine anakuja tena mpaka uchukue mazoea ya nini, unaanza upya; nikaona kwamba, ingependeza kama ungempa miaka mitano anakuwa angalao na muda wakutosha ku-perform. Hata kama atateuliwa term ya pili mtu aki-serve miaka 10 inakuwa ni rahisi kupima mabadiliko yake na kazi ambayo imefanyika na watu hao kwa wakati huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu nyingine ambayo nimeiona ni kifungu cha 10. Kwenye kifungu cha 10 pale hasa (a) atakuwepo Mkemia Mkuu wa Serikali atakayeteuliwa na Rais. Sasa (a) anasema angalau na sifa ya Shahada ya Uzamili ya Kemia au na taaluma zingine, sasa ukishasema ni Mkemia Mkuu wa Serikali maana yake unatakiwa uwe ni Mkemia yaani hutakiwi kuwa na taaluma nyingine. Kwa hiyo, ningeshauri kama wanamaanisha Mkemia huyu mtu lazima awe professional chemist, lakini wanaposema awe na level nyingine maana yake nini sasa? Maana yake hapo unatoa room kwamba unaweza kuletewa mtu mwingine yoyote halafu ukasema huyu ni Mkemia Mkuu kumbe sio mwana-chemistry. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani mtakuwa hamjatendea hata hilo jina lenyewe wala huhitaji Mheshimiwa Waziri na mwenzako kuzunguka, yani huyu mtu awe professional chemist. Labda uongeze kwamba, awe m-chemist angalau na taaluma nyingine inayofanana na hiyo, hiyo itakuwa imeenda vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye kifungu cha 3 kuna sehemu hapo unazungumza tu kwamba, awe ni Mtumishi wa Serikali.
Sisi tunapendekeza na mimi, kama walivyosema wenzangu wa upande wa Upinzani, ni muhimu tusiwe na limitation hata kama mtamteua huyu mnayemtaka wa Serikalini, lakini kwenye sheria ionekane kwamba mtu yeyote ambaye anaweza kuwa mkemia ili mradi anakidhi hizi sifa atateuliwa. Sasa kama ni Mtumishi wa Serikali, kama ni private sector, kama taasisi yoyote, lakini angalau kusiwe na ubaguzi, huyu awe ni mtu Mtanzania ambaye ana sifa za kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye kipengele cha 16ambacho kinahusu usimamizi, sasa pale imezungumzwa na wenzetu na Kambi Rasmi ya Upinzani hapa, inaweza kuwa hapa inasema hii nia njema, ile habari ya nia njema ile ina shida, yaani maana yake kwamba kwa mfano mabadiliko yakitokea hawa watu hawahusiki, lakini kama mtu amekula deal amepiga hela mahali anaweza aka-delay tu halafu akasema mimi nilifanya hiki kitu kwa nia njema kumbe ni makusudi na kuna kitu anakificha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya 17(3) pale (a) kulipa faini isiyopungua shilingi 5,000,000 au kifungo kisichopungua mwaka mmoja au vyote kwa pamoja iwapo mkosaji ni mtu binafsi; hapo maana yake una-deal na mtu ambaye ni tofauti na, ingiza hapo na hata kama ni mtumishi, hata kama ni Afisa wa Serikali anafanya kazi lakini amefanya hili kosa hii adhabu iende pande zote. Kama ni mtu wa kawaida amefanya kosa awajibishwe kama ni mtumishi wa Serikali awajibishwe pia, maana yake utawatisha watasimamia utaratibu wa kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu cha 26. Hii naona nimeifuta kwa sababu, niliangalia 11 haikuwa sehemu ya rufaa, lakini 26 ime-capture ya kwamba kama kuna maamuzi yametoka na mtu hajaridhika basi anaweza akakata rufaa kwa Waziri au kwenye Bodi na kwa Waziri na kuendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niseme mambo ya jumla pamoja na ile sehemu ya 45 ambayo wenzangu wamesema ile nia njema. Sisi tungeshauri hii habari ya nia njema kuwa na mipaka, ukiiacha hivi ilivyo watu watafanya makosa kwa kusingizia kwamba unajua niliamua haya maamuzi kwa sababu ya nia njema, kumbe yeye alikuwa na mambo yake tu. Sasa mambo ya jumla ni kwamba ningedhani, nimesoma sana huu muswada ambao kimsingi nauunga mkono, lakini inaonekana sehemu kubwa yaani ni kupimapima tu DNA na nini, yaani haioneshwi kwamba watafanya hata utafiti, watafanya hata uchambuzi kama ufumbuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano hapa Tanzania gongo inapatikana na gongo watu wanakunywa na ipo, sasa hawa kwa nini wasisaidie kwenda hata kuboresha vitu vya namna hiyo? Yaani haiwezi kwenda kuzuia uvumbuzi, kama mtu anaweza kutengeneza gongo hawa wakaboreshe ili isiweze kudhuru, kama ilivyo konyagi na vinywaji vingine, watapata kipato na watakuwa wamechangia katika ufumbuzi wa kisayansi. Mimi nilikuwa nashauri hilo liangaliwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile naamini kwamba hii miswada yote miwili itasaidia. Kwa mfano, wapo akinamama na akinadada ambao wanajichubua na nini kwa hiyo, na hili lenyewe litasaidia kudhibiti hivi vipodozi vya design mbalimbali na matumizi yake, hata wanaume kama wapo, mimi si miongoni mwao. Lakini hiyo ni muhimu kwamba ikaangaliwa hata kwa mfano dawa mbalimbali; yaani hii inatakiwa kitu kikubwa ambacho ambacho tutakuwa tunapata products mbalimbali za kisayansi katika eneo hili. Kwa wale wanamaabara, lakini pia na hii Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata vilevile utafiti, kwa mfano kuna mbolea zipo hapa zinaharibu ardhi yetu, hazizalishi vizuri. Hao pia watasimamia kudhibiti vitu vya namna hiyo na matokeo yake tutakuwa na heshima kubwa kwa sababu tutakuwa tumepanua. Kwa namna ilivyo hapa ni kama tunasubiri tu uende upime kama DNA, ukague kama labda kuna sumu, kuna poison na nini, lakini niwapongeze kwa mara nyingine kwamba angalau changamoto ambayo Mkemia Mkuu alikuwa anasema ya kwamba wanashindwa kufanya kazi kwa sababu ya ukosefu wa fedha; sasa angalao hapo kutakuwa na vote itakuja kwenye Bunge litapitisha, kutakuwa na bajeti ambayo itakuwa allocataed, hili jambo zuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia pale walituambia mitambo ni mibovu, lakini kwa sababu, shida ilikuwa ni pesa. Sasa with this maana yake anaweza akanunua mitambo na iwe ya kisasa, lakini pia, kama atafungua kwa mfano kwenye Kanda mbalimbali, sikuona mahali popote kama kutakuwa na Kanda, walikuwa wanadai unaweza ukaona dawa zimekamatwa kwa mfano Tabora halafu inabidi zije hapa Dar es Salaam; sasa inategemea expire date ikoje na hiyo bajeti haikuwepo, hii shughuli ikachelewa. Sasa kwa muswada huu ina maana uta-facilitate kazi iweze kufanyika vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mkemia alisema kwa mfano, kulikuwa na shida ya upungufu wa watumishi, sasa kwa hili maana yake ni lazima kuajiri, kwa hiyo, kutakuwa na uwezekano mkubwa sana wa kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili la DNA kwanza gharama ilionekana ni kubwa sana, kwanza ilikuwa ni moja mashine au mbili halafu gharama ni kubwa, lakini sasa kama wana bajeti watafanya hii kazi, kutakuwa na mashine kila eneo nah ii habari kwamba 60% angalau ya watoto hawajulikani baba na mama wanatofautiana, lakini wote ni wazazi nah ii itasaidia kidogo, ili kila mtu ajue mtoto wake ni yupi na aweze kumhuduamia vizuri na kweli hata itapunguza ugomvi katika familia zetu. Maana sasa kama mtoto hafanani fanani hivi unajihisihisi, hata kutoa matumizi kidogo inakuwa ngumu. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo naomba niwasilishe. Ahsanteni sana.
Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo, wa Mwaka 2016
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Utafiti wowote, ukitaja tu neno utafiti kwa lugha ya kawaida mtu anategemea kwamba ni kazi ambayo inafanyika kujibu baadhi ya matatizo au kuleta mafanikio au kuboresha. Kwa namna yoyote ile lazima kuwe na kitu kinafanya utafiti ufanyike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia tu uanzishwaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo na sitaenda sehemu nyingine ile. Pamoja na kwamba nimepata marekebisho ya Serikali, lakini nina shida ya mwanzoni kabisa hapo anapozungumzia hii section ya kwanza tu, mwanzoni walikuwa wamesema kwamba sheria hii itatumika Tanzania, lakini baadaye wameandika kwenye Ibara ya kwanza wanasema ni Tanzania Bara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanzoni walikuwa hawajasema inatumika wapi ndiyo wamefanya marekebisho kwenye schedule of amendment ambayo ninayo hapa wakasema itafanya kazi Tanzania Bara. Ukisoma Katiba ya Tanzania Nyongeza ya Kwanza katika mambo ya Muungano neno la 18 inaonesha kwamba utafiti ni jambo la Muungano. Ikishakuwa jambo la Muungano sasa vinginevyo Waziri aje anieleze au alieleze Bunge na Watanzania waelewe wanapozungumza hili jambo ni miongoni mwa mambo ya Muungano halafu baadaye unaleta sheria ambayo inasema itatumika Tanzania Bara, unataka kuniambia kwamba ni kauli ya Waziri alichokiandika hapa ndiyo inafanya kazi au ni Katiba ndiyo inafanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wakati gani neno utafiti linakuwa jambo la Muungano na ni wakati gani neno hili linakuwa siyo la Muungano. Tukisema ni jambo la Muungano maana yake inabidi uende kwenye Katiba Ibara 98 ambayo inaeleza namna ambavyo sheria hii inapaswa kupitishwa. Sasa kama ni jambo la Muungano kwenye Ibara ya 98 ya Katiba ya nchi inaeleza kwamba jambo hili litapitishwa kwa 2/3 ya Wabunge wa Tanzania Zanzibar na kwa 2/3 ya Bunge hili la Tanzania kama hivi tulivyo humu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mambo haya yameshafanyika maana yake vinginevyo maelezo yaletwe kwa nini inageuzwa hapa, kama wenzetu wa Zanzibar waliwahi kujadili jambo hili kama ambavyo imefanyika katika maeneo mengine kwenye Ibara hizi basi ni muhimu. Vinginevyo huu Muswada maana yake utakuwa haujatimiza vigezo ilibidi uahirishwe ili Katiba ifuatwe na uletwe hapa pia. Sasa nitategemea kwamba kabla ya kwenda mbele haya mambo inabidi yatolewe ufafanuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwenye huu Muswada wa Sheria ukisoma hapa sijajua Waziri anamaanisha nini, nimejaribu kuangalia hivi nini malengo yake! nimesoma mwanzo mpaka mwisho haya mapendekezo ya Muswada wa Sheria hii inaonesha kwamba bado mambo ya msingi hayatajibiwa. Kwa mfano, wakulima wa kawaida wa Tanzania hata kama ni wa mahindi, korosho wanatarajia ukitaja tu, kwamba sasa Tanzania inakuwa na Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo yaani waone sasa shida ya mbegu mbovu haitakuwepo, hilo jibu kama Watanzania kupata sijaliona hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wale watumia mbolea wanataka waone kwamba taasisi hii ikiwa imeimarika sasa itasaidia kuboresha kwamba mbolea itakayotumika haitaharibu ardhi yao, yaani kuchujuka kwa muda fulani baada ya kutumia mbolea zetu za kawaida, hayo majibu inabidi yawepo. Sheria inabidi pia itaje kwamba hivi uchumi wa Tanzania economic growth itakuwaje kama kuna taasisi ambazo zita-control mambo hayo, mambo ya msingi mimi sikuyaona hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalishaji, (productivity) kwamba hii sheria inawezaje kusaidia Watanzania kuboresha mazao yao wazalishe kwa faida na walime kilimo cha kisasa hayo mambo hapa sikuyaona. Kilimo cha kisasa kwamba angalau ipendekeze kusimamia mambo gani kufanya watu wasilime kutegemea mvua ya kawaida baada ya utafiti wa tasnia ya kilimo hii watu watalima kwa kutumia mvua ya kawaida au umwagiliaji au nini, hayo mambo yote ya msingi hapa hayajajibiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine tulitegemea malengo ya sheria hii lazima yaoneshe kwamba contributional agriculture research kuleta kilimo cha kisasa itasaidia nini hii taasisi. Mambo haya ni mambo ya kawaida kabisa kwamba angalau katika malengo ya sheria Mtanzania wa kawaida bila kuwa Mtaalam, bila kuwa Mbunge, mkulima wa kawaida huko aliko awe na matumaini na atamani kwamba sheria ikipitishwa moja kwa moja ananufaika bila kumuuliza Waziri, bila kumuuliza Mbunge, kwa maneno tu ya mazungumzo humu ndani, mambo hayo sikuyaona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile sheria hii itawasaidia nini wakulima wa Tanzania kwa kuanzishwa kwa mambo ya soko (market economy) inawajibika vipi kutafuta soko la wakulima wetu, hilo pia katika mazingira hayo sikuona chochote hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile usalama wa mbegu zetu na mazao wamesema wenzangum wamelalamika kwamba nchi hii kumekuwa watu wanalima mazao kwa sababu hatusindiki mazao yetu yanaharibika, thamani yake inashuka, haya mambo yote yalipaswa yawepo maana yake inapendekezwa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya Tanzania, sasa haya mambo yote ya usalama sikuyaona mahali popote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cost effectiveness sijaona teknolojia itasaidia vipi kwenye teknolojia ya kisasa wakulima walime; teknolojia gani itumike ku-control bei yake na vitu vingine vya namna hiyo, hayo mambo yote sijayaona. Mamlaka ya Taasisi ya Utafiti itakuwaje coordinating ata-oversee namna gani au atatoa guidance namna gani katika taasisi zingine za utafiti wa mambo ya kilimo hilo sikuliona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilivyozungumza hapa sikuona mahali ambapo inaonesha kwamba kuna mambo ya ku-control mbegu kama nilivyosema. Wenzetu kama Waganda wana taasisi wanayo National Crop Resource Research Institution. Hapa tunazungumza lakini ukiangalia kwa namna yeyote ile inabidi ihusiane na mambo ya mifugo hivi kwa sababu huwezi kuzungumza habari ya kilimo bila kuzungumza habari ya mifugo, maana yake ndiyo chakula chao, hivi vitu vinategemeana sana. Leo kuna ugomvi katika maeneo mbalimbali sasa utasaidiaje katika mazingira hayo. Hayo mambo mengine nimeona nizungumze.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo pili ambalo nataka nilizungumze hapa sijaliona kwenye haya mapendekezo usalama wa chakula chetu nimesema, lakini vilevile hii sheria lazima ionyeshe kwamba taasisi itasaidia kupunguza umaskini wa Watanzania uliokithiri, tumeona mashahidi hapa juzi kama hii taasisi ikiwepo je, wale watu ambao wanalima nyanya hapa Kilosa hivi halafu ngombe wanakula, hivi hii itasaidia nini katika mambo hayo. Walime mazao gani kwa wakati gani na soko likoje na hao wana-link, maana yake kwenye sheria hapo wameonesha tu kwamba anaweza mtu akafanya utafiti kutoka nje, lakini hawaoneshi kwamba tunaweza tukafanya utafiti Tanzania tukaunganisha na sehemu nyingine tukaboresha kilimo chetu kiwe cha kisasa. Hiyo na yenyewe haipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria inasema tu kwamba wanaweza wakaruhusu mtu ambaye siyo Mtanzania akaja akafanya utafiti na akishafanya utafiti; je, wenzetu mbona hamsemi sheria itaruhusu hawa na wenyewe wafanye utafiti mahali popote, waende wakope teknolojia ya kisasa waboreshe kilimo chetu ili tuweze kushindana na nchi zingine, hilo jambo pia silioni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile sheria haisemi hapa kuna adhabu nyingi sana zimeoneshwa, kwa mfano haioneshi kwamba hii sheria itaifanya Taasisi ya Kilimo iwe ni kitu shirikishi, haioneshi kwamba kama kutakuwa na transparency, haioneshi kwamba mwananchi wa kawaida, mkulima wa kawaida kama ana malalamiko!
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnajua mbolea zinaletwa hapa wenzetu wakulima wa pamba wamesema, wanapewa mbegu za pamba zinaharibu ardhi yao, zingine hata hazioti, hiyo transparency, uwezo wa mkulima wa kawaida kuhoji na kupata taarifa kwenye taasisi ya utafiti wa kilimo nakulalamika, hapa vilevile sioni jambo hilo. Integrity ya hii italindwa namna gani, accountability ya hawa watu wote wanaohusika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshangaa sana nchi hii ina Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, chuo ambacho ni chuo kikongwe katika Afrika Mashariki na Kati, lakini hii sheria inaletwa hapa ya kuunda Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ambayo haigusi au haitaji kabisa kwamba SUA ina mchango wowote, nimeshangaa sana! Maana yake wanataka kutuambia hawa wataalam wetu ambao wapo siku zote hamtambui mchango wao, najua hawa ndiyo benki yetu ya mawazo, hawa wana uzoefu wa muda mrefu sana, wangeweza kutushauri namna ya kwenda mbele, mambo gani yamekosewa na hawa ndiyo tumewapa task hiyo kwa muda mrefu na Wakufunzi wengi nchi hii wametoka pale. Mambo haya ningeomba nimshauri Mheshimiwa Waziri mnapoleta sheria kama hizi, haya mnazungumzia maisha ya wakulima wa Tanzania, wafanyabiashara na watu mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine wamependekeza maneno mengi, sikuona wanasema hawa kama watafanya utafiti kwenye taasisi ya kilimo, kilimo ni chakula, hawaoneshi kwamba watashirikiana namna gani hata na hii Mamlaka ya Chakula Tanzania, hawatajwi katika hii sheria mahali popote, nimesoma sikuona. Sasa mambo kama haya nadhani na wengine watakaofuata hata hiyo Miswada inayofuata ya kesho ule wa Fisheries, ni lazima mkileta Muswada hapa hata kama mmeandika Kiswahili/Kingereza mwananchi wa kawaida aweze kuona, hivi ananufaika namna gani bila kuhoji bila kuuliza, kukusikiliza tu ataona kwamba hii kitu kweli ni ukombozi.
MWENYEKITI: Ahsante.