MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwanza niseme tu kwamba majibu ya Mheshimiwa Waziri Mkuu yamenishtua; amesema fedha inatolewa mara moja kwa mwaka na wengine wanasema ni mara mbili kwa mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka tu nijue, mimi ni Mbunge wa Jimbo la Ukonga; niliposoma sheria inasema unapogawanya zile fedha inabidi kuangalia population na mazingira ya Jimbo. Kwa mfano, Jimbo la Ukonga na Jimbo la Segerea, mwenzangu anapokea shilingi milioni 33, mimi napokea shilingi milioni 16. Ni kama mara mbili yangu, lakini wananchi wa Segerea ni karibu 600,000; mimi watu wa Jimbo langu tumezidiana kama watu 50,000 hivi.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu upo tayari kusimamia Serikali yako ili kuangalia hali halisi ya majimbo yetu yalivyo. Mtu mwenye mazingira magumu ya Jimbo lake apate fedha nyingi zaidi kwa sababu hata mahitaji ya miundombinu ni mingi zaidi kuliko Majimbo mengine? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kumejitokeza matatizo kidogo kwenye Halmashauri zenye Jimbo zaidi ya moja na hasa Majimbo yale ambayo yameanzishwa kipindi hiki cha karibuni. Jukumu la Serikali kupitia Wizara husika ni kuendelea kufanya sensa kabla hatujaanza kuzipeleka fedha ya kutambua idadi ya wananchi walioko kwenye Jimbo husika baada ya kuwa Halmashauri yote kuwa ina Majimbo zaidi ya moja; tuweze kujua kila Jimbo lina wananchi wangapi ili sasa tunapopeleka fedha, tupeleke tukiwa tuna maelekezo hasa kwenye Halmashauri zenye Majimbo zaidi ya moja, kwamba kila Jimbo sasa lipate mgao kiasi gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mwita niseme, tatizo lililoko Ukonga na eneo la Segerea litakwisha kwa sababu kazi hiyo inafanyika ndani ya Wizara kabla hatujaanza kupelekka fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaamini kama Jimbo lako lina idadi kubwa ndilo ambalo litapata fedha nyingi kulinganisha na Jimbo lingine ambalo lina idadi ndogo ya wananchi ili sasa kila Mbunge kwenye eneo lake aweze kupanga mipango ya maendeleo kwa fedha ambayo imekuja inayolingana na idadi ya wakazi kwenye eneo hilo.