Primary Questions from Hon. Mwita Mwikwabe Waitara (23 total)
MHE. SUSAN A. J. LYIMO (K.n.y. MHE. MWITA M. WAITARA) aliuliza:-
Zahanati ya Kitunda inahudumia wananchi wa Kata za Kitunda, Kivule, Kipunguni, Msongola na baadhi ya wananchi toka Chamazi na Tambani katika Mkoa wa Pwani.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuifanya zahanati hiyo kuwa Kituo cha Afya ili kiweze kumudu mahitaji makubwa ya wananchi wa maeneo yaliyotajwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Mwikabe Waitara, Mbunge wa Ukonga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Zahanati ya Kitunda iliyopo Kata ya Kitunda haina eneo la kutosha kukidhi ongezeko la miundombinu inayohitajika kuwa kituo cha afya jambo ambalo litalazimu Serikali kuwaondoa wananchi na kulipa fidia. Ili kuboresha huduma za afya katika Kata ya Kitunda, Kivule, Kipunguni na Msongola na maeneo jirani, Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imeanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya katika Kata ya Kivule.
Katika bajeti ya mwaka 2015/2016 zimetengwa shilingi milioni 900 na tayari ujenzi uko katika hatua ya msingi. Vilevile katika bajeti ya mwaka 2016/2017 zimetengwa shilingi bilioni moja ili kuendelea na ujenzi.
Mheshimiwa Spika, sambamba na ujenzi wa hospitali, Serikali imepanga kujenga zahanati mpya na kuimarisha zilizopo. Kutokana na juhudi za kufanikisha jambo hilo muhimu Serikali imepanga kutumia shilingi milioni 600 katika mwaka wa fedha 2015/2016 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ya Lubakaya, Mbondole na Luhanga pamoja na nyumba za watumishi zilizopo katika Kata ya Msongola.
Aidha, kwa mwaka wa fedha 2016/2017 zimetengwa jumla ya shilingi milioni 659.13 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati na nyumba za watumishi katika Kata mpya ya Mzinga na Kipunguni B katika Kata ya Kipunguni.
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza:-
Kumekuwa na utaratibu mbovu na Mawaziri wa Elimu kuingilia shughuli za mitaala kwa kubadilisha mitaala, mfumo wa madaraja na hata aina ya mitihani hasa kuweka maswali ya kuchagua katika somo la hisabati:-
Je, ni lini Serikali italeta marekebisho ya Sheria ya NECTA ili Bunge libadili Sheria ya Baraza kifungu cha 30 ili kuondoa nguvu ya Waziri ya kutoa maelezo bila kuhoji na hata bila kushirikisha wataalam wa elimu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Mwikabe Waitara, Mbunge wa Jimbo la Ukonga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Baraza la Mitihani Tanzania haina kifungu cha 30 kama alivyouliza Mheshimiwa Mbunge. Hata hivyo, Wizara inaona kuwa maudhui ya swali hili yanapatikana katika kifungu cha 20 cha Sheria ya Baraza la Mitihani Tanzania. Kifungu hiki kinampa mamlaka Waziri mwenye dhamana ya Elimu kufanya maamuzi kwa niaba ya Serikali pale inapolazimika kufanya hivyo kwa kuzingatia mahitaji ya jamii kulingana na wakati, mazingira halisi na matokeo ya tafiti mbalimbali kutoka kwa wataalam pamoja na maoni ya wadau wa elimu. Kwa kuzingatia matakwa ya sheria hii, Baraza la Mitihani Tanzania hutakiwa kuyatekeleza maamuzi hayo.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali haina mpango wa kukifanyia marekebisho kifungu cha 20 cha Sheria ya Baraza la Mitihani Tanzania kwa kuwa kinamwezesha Mheshimiwa Waziri kufanya marekebisho mbalimbali kutokana na mahitaji ya jamii yanayojitokeza kwa wakati husika.
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza:-
Suala la Mpango Miji ni jema na mtu aliyepimiwa ardhi na kupata hati ya eneo lake huweza kutumia hati hiyo kukopa kirahisi lakini gharama za kupima ardhi ni kubwa sana kiasi kwamba wananchi walio wengi wanashindwa kupima maeneo yao.
Je, Serikali ina mpango gani wa dharura wa kupunguza gharama za upimaji ardhi ili wananchi wengi zaidi waweze kupima maeneo yao na kuyaongezea thamani?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali namba 12 la Mheshimiwa Mwita Mwikabe Waitara, Mbunge wa Ukonga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, upimaji wa ardhi hapa nchini unafanywa na Wapima wa Ardhi wa Serikali walioajiriwa na Serikali na Wapima Binafsi walioajiriwa na Bodi ya Wapima Ardhi na kupewa leseni za biashara ya upimaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Serikali, gharama za upimaji rasmi kwa sasa ni shilingi 300,000 kwa hekta ya shamba moja na kiwanja kimoja. Gharama hizi zilipunguzwa na kuridhiwa na Bunge lako Tukufu kwa mwaka wa fedha 2015/2016 ambapo kabla ya hapo zilikuwa shilingi 800,000 kwa hekta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama kubwa za upimaji zinatokana na sababu zifuatazo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, Halmashauri nyingi hazijajengewa uwezo wa wataalam na vifaa na jukumu la kuajiri wataalam na kununua vifaa ni la Halmashauri yenyewe hivyo upungufu wa vifaa pamoja na wataalam ni mkubwa kwa nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya pili ni kwamba gharama za vifaa vya upimaji ni kubwa sana na upatikanaji wa seti moja ya kawaida ya upimaji kwa kutumia darubini ni shilingi milioni 18 kwa seti moja na GPS ni shilingi milioni 48. Ukubwa huu wa gharama na vifaa husababisha wapima wengi kutokuwa na uwezo wa kununua vifaa na hivyo kutegemea kukodi kwa gharama kubwa hivyo kufanya pia upimaji kuwa ghali ili kuweza kurejesha gharama za vifaa kwa sababu ni vya kukodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na ongezeko la gharama za upimaji nchini, Serikali ina mpango wa kusogeza huduma zote zinazotolewa Wizarani kwenda kwenye kanda. Hatua hii itawezesha kanda hizo kujengewa uwezo na hivyo kuchangia kupunguza gharama. Katika kuzijengea uwezo, Serikali inategemea kununua vifaa vya upimaji katika mradi wa World Bank na kuvigawa katika kanda zake ambavyo vitasaidia Halmashauri katika kanda husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nitoe rai kwa Halmashauri zote nchini kutenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya upimaji pamoja na kuajiri wataalam wa kutosha katika kada hii ya upimaji na wengine wa sekta ya ardhi ili kuondokana na gharama kubwa za kukodisha vifaa hivyo kutoka katika taasisi binafsi.
MHE. CECIL D. MWAMBE (K.n.y. MHE. MWITA M. WAITARA) aliuliza:-
Baadhi ya wakazi wa Ukonga wanafuga kuku wa mayai na wengine wanatengeneza chakula cha mifugo, shughuli zinazowainulia kipato na kuweza kupata mahitaji muhimu ya kimaisha, lakini shughuli zao zimeathiriwa na watu wanaoingiza mayai toka nje ya nchi:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuzuia uingizaji wa mayai toka nje kwa sababu unaharibu soko la ndani la bidhaa hiyo?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kusimamia malighafi ili chakula cha mifugo kiendane na bei ya mayai na kuku?
(c) Je, Serikali ipo tayari kusimamia wananchi walipwe fidia kutoka kwa wawekezaji wanaoingiza vifaranga wasio na chanjo toka nje ambao wengi wao hufa na kusababisha hasara kwa wananchi wafugaji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Mwikwabe Waitara, Mbunge wa Ukonga, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwaka 2006, Serikali iliweka katazo la kuingiza kuku na mazao yake nchini ili kudhibiti Ugonjwa hatari wa Mafua ya Ndege. Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Na. 17 ya Mwaka 2003 na Kanuni zake za Mwaka 2007 na 2010 zinatumika kudhibiti na kukagua uingizwaji katika maeneo ya mpakani, bandari na viwanja vya ndege. Hakuna mwekezaji yeyote anayeruhusiwa kupewa kibali cha kuingiza vifaranga au mayai nchini kwa ajili ya biashara na katika kusimamia hili kuanzia mwaka 2013 hadi 2017, vifaranga 67,500 vilivyoingizwa nchini kinyume na sheria viliteketezwa.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inasimamia ubora wa malighafi za kusindika vyakula vya mifugo kupitia Sheria ya Maeneo ya Nyanda za Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Wanyama Na. 13 ya Mwaka 2010. Changamoto katika kusindika vyakula hivyo ni gharama kubwa ya viinilishe vya protini kutokana na matumizi ya maharage aina ya soya. Maharage haya huagizwa kutoka nje ya nchi hususan Zambia na India. Wizara inaendelea kuhamasisha uzalishaji wa soya hapa nchini katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, wapo wawekezaji wachache ambao hupewa vibali maalum vya kuingiza nchini mayai au vifaranga wa kuku wazazi (parent stock) tu. Ukaguzi kwa ajili ya kudhibiti uingizaji wa vifaranga na mayai unaendelea na hatua kali zinachukuliwa kwa yeyote atakayekamatwa kwa kukiuka utaratibu.
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza:-
Jimbo la Ukonga lina shida kubwa ya umeme katika Kata zifuatazo; Kata ya Chanika (Ngwale, Nguvu Mpya, Virobo, Kidugalo, Yongwe, Lukooni, Vikongoro na Tungini); Kata ya Zingiziwa (Zogoali, Zingiziwa, Ngasa, Ngobedi, Somelo na Gogo, Lubakaya na Kimwani); Kata ya Majohe (KIvule na Viwege); Kata ya Buyuni (Zavala, Buyuni, Mgeule Juu, Nyeburu, Mgeule Chini, Kigezi, Kigezi Chini na Taliani); Kata ya Pugu Station (Bangulo, Pugu Station na Kichangani); Msongola (Yangeyange, Mbondole, Kidle, Mkera, Sangara, Kiboga, Uwanja wa Nyani, Kitonga, Mvuleni na Mvuti) na Kata ya Kivule (Bombambili). Maeneo hayo yote yanahudumiwa na Wilaya ya Kisarawe kama maeneo ya vijijini. Je, ni lini maeneo hayo yatapata umeme wa REA?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swai la Mheshimiwa Mwita Mwikwabe Waitara, Mbunge wa Ukonga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, maeneo ya Kidole, Bangulo, Kitonga, Mvuti na baadhi ya maeneo mengine pamoja na Msongole yalipatiwa umeme kupitia Mradi wa REA Awamu ya Pili uliokamilika mwezi Disemba, 2016. Kazi ya kupeleka umeme katika maeneo hayo ilijumuisha pia vijiji vilivyokuwa vinatoka katika Wilaya ya Kisarawe ambapo pamoja na mambo mengine vimefungiwa transfoma 55 za kVA 50, kVA 100 na kVA 200; ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 pia umejengwa kwa urefu wa kilometa 187.22 lakini njia ya msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 239.7 pamoja na kuwaunganishia umeme wateja 1,083. Gharama ya mradi huu ni shilingi bilioni 5.3.
Mheshimiwa Spika, mitaa mingine iliyobaki ya Kata za Chanika, Zingiziwa, Majohe, Buyuni, Pugu Station pamoja na Msongola, zitapatiwa umeme kupitia Mradi wa Urban Electrification chini ya ufadhili wa Maendeleo wa Benki ya Dunia.
Mheshimiwa Spika, kazi hizi zinajumuisha ujenzi wa njia ya msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 66.3, msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 336.7 pamoja na ufungaji wa transfoma 73 za kVA 200 na kVA 100. Gharama ya mradi huu ni shilingi bilioni 10.73 na utaunganishia wateja 7,083.
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza:-
Jimbo la Ukonga lina shida kubwa ya maji.
(a) Je, ni lini Serikali itakamilisha miradi ya maji ya Kata za Chanika, Kipunguni na Majohe ili wananchi wa Kata hizo na maeneo ya jirani wapate maji ya uhakika?
(b) Je, ni lini Serikali itachimba bwawa kubwa katika Mnada wa Kimataifa wa Pugu ili ng’ombe wanaouzwa hapo wapate maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Mwikwabe Waitara, Mbunge wa Jimbo la Ukonga, lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kukamilisha miradi ya maji katika Kata za Chanika, Kipunguni na Majohe. Miradi mingi imekamilika na inahudumia wananchi na mingine ipo katika hatua za mwisho za ujenzi. Miradi iliyokamilika ni pamoja na Kipunguni B, Kwa Mkolemba, Chanika Shuleni, Majohe, Nyang’andu na Msongola. Miradi inayoendelea kujengwa ni bomba mbili za Kipunguni B, ambao unatekelezwa na Manispaa ya Ilala. Aidha, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maji kulingana na upatikanaji wa fedha ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imepanga kuleta maji katika maeneo ya Pugu kutoka katika mradi mkubwa wa visima virefu vilivyopo Mpera katika Wilaya ya Mkuranga. Kazi ya uchimbaji wa visima hivi inaendelea na matarajio ni kukamilisha uchimbaji mwaka huu wa fedha na baada ya hapo Serikali itatekeleza mradi wa ujenzi wa mabomba ya kusafirisha maji hayo hadi Pugu na kuyasambaza maeneo yote ya Pugu, Chanika, Ukonga, Gongolamboto, Kinyerezi, Kitunda, Kipawa, Yombo na maeneo ya barabara ya Nyerere kuanzia Pugu hadi TAZARA.
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza:-
Katika Mtaa wa Mongolandege, Kata ya Ukonga, kuna daraja la Mongolandege ambalo huunganisha Jimbo la Ukonga na Jimbo la Segerea. Aidha, daraja la Mto Nyebulu huunganisha Kata ya Buyuni na Kata ya Chanika Magengeni.
Je, ni lini Serikali itajenga madaraja hayo muhimu ili kurahisisha huduma za kijamii katika maeneo yaliyotajwa?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Mwikabe Waitara, Mbunge wa Ukonga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, daraja la Mongolandege linatakiwa kujengwa katika Bonde la Mto Mzinga ambalo awali palijengwa makalavati kwa nguvu za wananchi. Kalavati hizo zilishindwa kufanya kazi kwa ufanisi baada ya mkondo wa mto kupanuka.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, mwaka 2012, Manispaa ya Ilala ilijenga box culvert ili kuwezesha eneo hilo kupitika. Hata hivyo, mvua zilizonyesha kwa wingi katika kipindi hicho zilileta madhara makubwa ambapo bonde hilo lilitanuka na kalavati hiyo kusombwa na maji na kusababisha kukosekana mawasiliano katika eneo hilo. Daraja la Nyebulu linatakiwa kujengwa katika Mto Vikorongo na litakuwa na wastani wa upana wa mita 30.
Mheshimiwa Naibu Spika, TARURA katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilala itatenga fedha katika mpango wa matengenezo ya barabara na madaraja kwa mwaka wa fedha 2018/2019 za kufanyia usanifu wa kina kwa ajili ya madaraja yote mawili. Aidha, baada ya usanifu huo kukamilika, gharama halisi za ujenzi wa madaraja hayo zitafahamika na kutengwa kwenye bajeti.
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza:-
Hospitali ya Amana imepelekwa Wizarani, hivyo Wilaya ya Ilala kwa sasa haina Hospitali ya Wilaya.
Je, Serikali ina mpango gani wa kumalizia Hospitali ya Kivule itumike kama Hospitali ya Wilaya ya Ilala?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Mwikwabe Waitara, Mbunge wa Ukonga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imeandaa mikakati mbalimbali kuhakikisha kuwa inapata Hospitali ya Wilaya ikiwa ni pamoja na kutenga fedha jumla ya shilingi bilioni tatu katika mwaka wa fedha 2018/2019 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Kivule. Kati ya hizo shilingi 2,000,000,000 ni mapato ya ndani ya Halmashauri na shilingi 1,000,000,000 ni ruzuku ya Serikali Kuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na ujenzi wa Hospitali ya Kivule, Serikali inaendelea na ujenzi wa Vituo vya Afya vya Mzinga, Kinyerezi na upanuzi wa Kituo cha Afya Buguruni. Lengo la kuimarisha vituo hivyo ni kupunguza msongamano katika Hospitali ya Wilaya na kuimarisha utoaji wa huduma za afya katika ngazi za msingi.
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kukipatia Kituo cha Chanika gari la patrol?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Mwikabe Waitara, Mbunge wa Ukonga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kipolisi ya Ukonga ipo katika Mkoa wa Kipolisi Ilala na Kituo Kikuu ni Kituo cha Polisi Stakishari ambacho kinasaidiwa na vituo vingine vidogo kama vile Pugu, Chanika, Msongola, Gongolamboto, Mazizini, Karakata, Kinyerezi, Tembo Mgwaza na Kitunda. Vituo hivi vyote huhudumiwa kwa magari saba toka katika Kituo cha Stakishari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha katika Kituo cha Polisi cha Chanika lipo gari Na. PT 1889 Toyota Land Cruiser Pickup, ndilo hutumika kufanya doria katika eneo hilo likisaidiwa na magari mengine toka katika Kituo cha Stakishari, kwani kituo hiki ni kikubwa ukilinganisha na vituo vingine vilivyotajwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Jeshi la Polisi litaangalia uwezekano wa kuongeza gari katika Kituo cha Polisi Chanika na kuzingatia vigezo kama vile hali ya uhalifu, idadi ya watu, sababu za kiutawala na kijiografia kwa kulinganisha na maeneo mengine yenye mahitaji kama haya.
MHE. LUCY S. MAGERELI (K.n.y. MHE. MWITA M. WAITARA) aliuliza:-
Jimbo la Ukonga katika Kata za Msongola, Chanika, Zingiziwa, Buyuni na Pugu kuna shida kubwa sana ya maji.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa muda mrefu wa kuondoa kero ya maji katika kata hizo?
(b) Je, ni lini miradi viporo vya maji na visima vyenye pampu mbovu vitafanyiwa matengenezo ili kupunguza kero ya maji Ukonga?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Mwikabe Waitara Mbunge wa Jimbo la Ukonga lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango wa muda mrefu wa kuondoa kero ya maji katika Jiji la Dar es Salam na viunga vyake kwa kutumia maji ya visima virefu 20 vilivyochimbwa katika Manispaa ya Kigamboni eneo la Kimbiji na Mpera vyenye uwezo wa kutoa kiasi cha maji cha mita za ujazo 350 mpaka 700 kila kimoja. Kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha na kusambaza maji katika maeneo hayo. Kukamilika kwa mradi huu kutaondoa kero ya maji katika Jiji la Dar es Salam na viunga vyake zikiwemo Kata za Msongola, Chanika, Zingiziwa Buyuni na Pugu. Mradi huu unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2018/2019.
b) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Awamu ya Pili ya Utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP II) Serikali imeweka kipaumbele cha kukamilisha miradi viporo kabla ya kuanza miradi mingine mipya. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imepanga kukamilisha miradi viporo na kukarabati visima vyenye pampu mbovu kwa kutumia fedha za Mpango wa Malipo kwa Matokeo (Payment by Result). Mpaka sasa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imekarabati na kumalizia ujenzi wa miradi viporo sita ya maji katika Jimbo la Ukonga kwenye Kata za Msongola, Pugu, Mzinga na Pugu Stesheni.
MHE. JAFARI W. CHEGE K.n.y. MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itawawezesha wananchi wa Jimbo la Tarime Vijijini, Tarime Mjini na Rorya kupata bidhaa kutoka nchi jirani ya Kenya?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Mwikwabe Waitara, Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ni miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na inatekeleza makubaliano ya hatua ya pili ya ushirikiano ya Soko la Pamoja ambapo wafanyabiashara kutoka nchi wanachama wameruhusiwa kusafirisha bidhaa kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa katika nchi husika. Hivyo, kutokana na mazingira hayo, Serikali haijaweka zuio lolote la bidhaa kutoka nchi jirani ya Kenya kuingia Tanzania. Nakushukuru sana.
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza: -
Je, ni lini maji kutoka Ziwa Victoria yatafika katika Mji wa Tarime, Sirari, Nyamwaga na Nyamongo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Mwikwabe Waitara, Mbunge wa Tarime Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, jukumu la Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama na yenye kutosheleza. Katika mipango ya muda mfupi ya kupunguza kero ya uhaba wa maji katika Wilaya ya Tarime, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imekamilisha Miradi ya Maji ya Sirari na Nyamwaga na inaendelea kutekeleza Miradi ya Nyangoto (Nyamongo), Sabasaba na Gimenya (Mjini Tarime). Miradi hiyo inatarajia kukamilika mwezi Juni, 2022 ambapo hali ya huduma ya maji katika Mji wa Tarime itaimarika kutoka asilimia 45 hadi asilimia 56 na maeneo mengine ya Wilaya ya Tarime kutoka asilimia 70 hadi asilimia 75.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango wa muda mrefu, Wilaya ya Tarime itanufaika na Mradi wa Kuboresha Huduma ya Maji katika Miji 28 ambapo chanzo cha maji cha Ziwa Victoria kitatumika. Kupitia Mradi huo Miji ya Tarime, Sirari, Nyamwaga na Nyamongo na maeneo mengine ya Wilaya ya Tarime yatanufaika na lengo la asilimia 85 vijijini na 95 mijini litafanikiwa ifikapo mwaka 2025.
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza: -
Je, ni lini Kata za Sirari na Nyamongo zitapandishwa hadhi na kuwa Mamlaka za Miji Midogo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Mwikwabe Waitara Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka kufikia mwezi Januari, 2023, nchi yetu ina jumla ya Halmashauri za Miji 21 na Mamlaka za Miji Midogo 71.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa mwongozo wa uanzishaji wa mamlaka za Serikali za Mitaa wa mwaka 2014, utaratibu wa kuomba kuanzisha Mamlaka za Miji Midogo huanza na mikutano ya kujadili. Mikutano hiyo hufanywa katika ngazi ya vijiji, kisha Kamati ya ushauri ya Wilaya (DCC), Kamati ya ushauri ya Mkoa (RCC) na kuwasilishwa Ofisi ya Rais - TAMISEMI.
Mheshimiwa Naibu Spika, kusudio la kuanzisha Mamlaka za Miji Midogo katika Kata za Sirari na Nyamongo mchakato wake uliishia kwenye Kamati ya Ushauri ya Wilaya kwa kikao kilichofanyika mwaka wa fedha 2011/2012. Hivyo, Halmashauri inashauriwa kutimiza matakwa ya mwongozo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, mpango wa Serikali kwa sasa ni kukamilisha kwanza miundombinu kwa mamlaka zilizopo kabla ya kuanzisha mamlaka mpya. Ahsante.
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaboresha bei ya ardhi inayotwaliwa na Migodi ili iendane na thamani ya ardhi ya eneo husika?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Mwikwabe Waitara, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, bei ya soko la ardhi huandaliwa kwa kuzingatia Kifungu Na. 70 cha Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini ya mwaka 2016 pamoja na Kanuni Na. 53 ya Kanuni za Uthamini na Usajili wa Wathamini za mwaka 2018. Kanuni hiyo imeelekeza bei ya soko la ardhi kuzingatia visababishi vinavyoathiri bei ya soko la ardhi kati ya eneo moja na jingine na namna ya kufanya tafiti kwa kukusanya taarifa za soko la ardhi katika maeneo mbalimbali. Aidha, Kifungu cha (2) cha Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999 kimetafsiri kuwa petroli na aina zote za madini yanayopatikana chini ya ardhi siyo sehemu ya ardhi bali ni mali ya umma na hivyo umiliki wa ardhi hutolewa tofauti na leseni ya uchimbaji wa madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na umuhimu wa kuhuisha viwango vya thamani ya ardhi na mali ili viendane na wakati, viwango vya bei ya soko la ardhi vimeboreshwa kwa kuzingatia sheria na kanuni za ardhi. Ahsante.
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza: -
Je, lini Wananchi wa Komarera, Nyamichele na Murwambe katika maeneo ya Mgodi wa Barrick North Mara watalipwa fidia?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI K.n.y. WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Madini naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Mwikwabe Waitara Mbunge wa Tarime Vijijini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mgodi wa Barrick North Mara ulionesha nia ya kutaka kuchukua baadhi ya maeneo ya Vijiji vya Komarera, Nyamichele na Murwambe ambavyo ni sehemu ya vijiji vinavyozunguka mgodi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Baada ya wananchi wa vijiji hivyo kupata taarifa ya maeneo yao kuhitajiwa na mgodi wa Barrick North Mara, walianza kuongeza majengo haraka haraka maarufu kama Tegesha. Hali hiyo ilipelekea mgodi huo kuachana na maeneo hayo kwani hayaathiri uendeshaji wa shughuli zao za kila siku, ahsante.
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga Chuo cha VETA Nyamongo Wilayani Tarime?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita, Mwikwabe Waitara, Mbunge wa Tarime Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni azma ya Serikali kujenga Chuo cha Ufundi Stadi katika kila mkoa na wilaya nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/23, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kujenga Vyuo vya Ufundi Stadi katika Wilaya 64 ambazo zilikuwa hazijajengewa vyuo hivyo. Tayari Serikali imeshakamilisha kuandaa michoro na upatikanaji wa maeneo kwa ajili ya ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya ya Tarime eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi ni katika Kijiji cha Nyabichune, Kitongoji cha Komoware, Kata ya Matongo. Aidha, pamoja na kiasi cha shilingi milioni 45 kilichotolewa awali kwa ajili ya shughuli za maandalizi, tayari Serikali imetuma kiasi cha shilingi milioni 228 kwa kila Chuo kwa ajili ya kuanza ujenzi wa miundombinu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza: -
Je, lini Serikali itaongeza posho za Waheshimiwa Madiwani na Wenyeviti wa Vijiji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Mwikwabe Waitara, Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kazi kubwa inayofanywa na Waheshimiwa Madiwani na Wenyeviti wa Vijiji katika kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi. Kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka za Serikali za Mitaa Sura ya 290, kila halmashauri inatakiwa kuweka utaratibu wa kuwalipa posho, Waheshimiwa Madiwani na Wenyeviti wa Mitaa na Vijiji kutoka katika vyanzo vya mapato ya ndani ya halmashauri.
Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto za mapato kwenye halmashauri nyingi nchini, Serikali ilianza kutenga bajeti katika mwaka wa fedha 2021/2022 kwa ajili ya kulipa posho za Waheshimiwa Madiwani pamoja na Wenyeviti wa vijiji.
Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 22.5 kwa ajili ya kulipa posho za Waheshimiwa Madiwani na Wenyeviti wa vijiji katika halmashauri 168.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuzijengea uwezo Mamlaka za Serikali za Mitaa ili ziweze kubuni na kuimarisha vyanzo vya mapato pamoja na kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha kwa kutumia mifumo ya kieletroniki ya kukusanya na kutumia fedha katika kutekeleza miradi ya maendeleo pamoja na matumizi mengineyo ili kuongeza uwezo wa malipo kwa viongozi.
MHE. MWITA W. WAITARA aliuliza: -
Je, lini ujenzi wa barabara ya Tarime – Mugumu utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Mwikwabe Waitara, Mbunge wa Tarime Vijijini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza ujenzi wa Barabara ya Tarime – Mugumu kilomita 87.14 kwa kiwango cha lami kwa awamu. Ujenzi kwa kiwango cha lami awamu ya kwanza sehemu ya Mogabiri – Nyamongo kilomita 25 unaendelea na utekelezaji wake umefikia asilimia 15. Aidha, Serikali ipo katika hatua za mwisho za manunuzi za kumpata Mkandaraasi atakayetekeleza ujenzi wa sehemu ya pili ya kutoka Tarime Mjini – Mogabiri na Nyamongo hadi Mugumu zenye jumla ya kilometa 62.14.
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaweka Kituo kidogo cha Forodha katika Kata ya Itiryo – Bikonge Tarime Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Mwikwabe Waitara, Mbunge wa Tarime Vijijini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania imeanza utekelezaji wa Mpango wa Miaka Mitano (2022/2023 – 2026/2027) wa ujenzi wa nyumba za wafanyakazi na ofisi katika maeneo yote yaliyobainishwa kupitia utafiti wa mwaka 2021/2022 kuhusu mahitaji ya ofisi za TRA nchini. Mpango huo umejumuisha Mkoa wa Mara na utekelezaji umeanza katika ujenzi wa nyumba mbili za wafanyakazi na usanifu wa ujenzi wa Ofisi ya Forodha mpakani Kilongwe – Rorya. Aidha, usanifu wa ujenzi wa majengo ya nyumba za watumishi mpakani Sirari umekamilika na ujenzi utaanza mapema baada ya kumpata mzabuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji katika vituo vingine vya Mkoa wa Mara utaanza kadri ya upatikanaji wa fedha, ikiwa ni pamoja na Kogaja, Borega, Kirumi na Itiryo – Bikonge.
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza: -
Je, ni lini Kata ya Kwihancha itapata Kituo cha Afya na ni lini huduma za afya zitaimarishwa katika Hospitali ya Nyamwaga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Mwikwabe Waitara, Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali katika mwaka wa fedha 2021/2022, imetenga Shilingi Milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la Wagonjwa wa Nje (OPD) na Maabara katika kituo cha afya. Fedha hiyo itapelekwa kabla ya tarehe 30 Juni, 2022. Aidha katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga shilingi Milioni 400 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa kituo hicho.
Mheshimiwa Spika, huduma za afya katika Hospitali ya Nyamwaga zinaendelea kuimarika ambapo Serikali katika mwaka wa fedha 2021/2022, imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa hospitali hiyo. Ujenzi wa wodi mbili za wanaume na wanawake umekamilika na ujenzi wa majengo ya maabara, wodi ya watoto na jengo la kuhifadhia dawa upo katika hatua za umaliziaji. Aidha, huduma zinaendelea kutolewa ikiwemo huduma za uzazi na upasuaji.
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza:-
Je, lini Serikali itatangaza maeneo mapya ya kiutawala?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Mwikwabe Waitara, Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, uanzishaji wa maeneo mapya ya utawala huzingatia Sheria ya Serikali za Mitaa Mamlaka za Wilaya, Sura 287 na Sheria ya Mamlaka za Miji, Sura 288 pamoja na Mwongozo wa Uanzishwaji wa Maeneo ya Utawala wa mwaka 2014.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali imetoa kipaumbele katika kuboresha na kukamilisha miundombinu kwenye maeneo ya kiutawala yaliyopo ili yaweze kutoa huduma kwa ufanisi zaidi na baadaye kuendelea na maeneo mengine kwa kufuata taratibu na vigezo vilivyoainishwa, ahsante.
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaweka kituo kidogo cha forodha katika Kata ya Itiryo/Bikonge pamoja na kuweka utaratibu mzuri wa kupata bidhaa kutoka Kenya?
WAZIRI WA FEDHA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo cha forodha Kata ya Itiryo/Bikonge ni miongoni mwa vituo tarajiwa vya forodha vitakavyofanyiwa tathmini na Mamlaka ya Mapato Tanzania katika mwaka 2024/2025. Tathmini itafanyika kwa kuzingatia vigezo mahsusi ikiwemo uwiano wa gharama za ukusanyaji wa mapato na kiwango cha kodi kinachotarajiwa kukusanywa katika kituo hicho. Endapo kituo hicho kitakidhi vigezo, mchakato wa uanzishwaji utaanza kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kuwaelekeza wafanyabiashara wanaotumia mpaka wa Tanzania na Kenya uliopo Kata ya Itiryo/Bikonge, kuendelea kutumia vituo rasmi vya forodha vya karibu ikiwemo Kituo cha Forodha cha Sirari ili kurahisisha zoezi la ulipaji kodi na ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza:-
Je, lini Serikali itajenga Kituo cha Afya Kata ya Susuni, Jimbo la Tarime Vijijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): alijibu:-
Mheshimiwa Spika, Kata ya Susuni iliyopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ina jumla ya Vijiji vitano (5) vya Matamankwe, Kiongera, Keroti, Kikomili na Nyabilongo. Kati ya vijiji hivyo, Vijiji viwili vya Matamankwe na Kiongera vina zahanati.
Mheshimiwa Spika, Serikali imepanga kuipandisha hadhi Zahanati ya Kiongera kuwa Kituo cha Afya, ambapo katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali imepeleka fedha shilingi milioni 207 kwenye zahanati ya Kiongera kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wazazi lenye huduma ya upasuaji wa dharura na jengo la maabara.
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2025/2026, Serikali kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri itatenga shilingi milioni 150 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa miundombinu iliyosalia ikiwa ni pamoja na ujenzi wa jengo la kufulia, jengo la kuhudumia wagonjwa wa nje (OPD) na jengo la wodi ya kulaza wagonjwa, ahsante.