Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Mwita Mwikwabe Waitara (95 total)

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, ninaomba niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa shida ya ulinzi iliyopo Dimani inafanana sana na Jimbo la Ukonga, nina Kata 13, sina kituo kikubwa cha Polisi, na ni eneo la pembezoni ikiwepo Msitu wa Kazimzumbwi, lakini hata kituo cha Sitakishari ambacho kinahudumia Jimbo la Segerea na Ukonga hakuna gari, sasa nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri, atatujengea Kituo cha Polisi Ukonga au apeleke gari Segerea Sitakishari ili ihudumie wakati mipango mingine inaendelea?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwasilishe, ahsanteni.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani ule umuhimu wa magari ambayo nimekuwa nikiuzungumza umeongezeka uzito wake, sasa niweke tu wazi kwamba katika yale magari ambayo tumeyapata, magari mengi ni kwa ajili ya doria, operation na matumizi ya kawaida ya polisi. Hayo magari yanayoitwa ya washawasha sidhani hata 24 sujui kama yanafika.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Waitara nadhani utakubaliana na mimi na Wabunge wengine kwamba, Jeshi la polisi linahitaji magari zaidi, ikiwemo katika Kituo chako ulichozungumza, mimi naomba hili nilichukue tuone tutalifanyia kazi vipi.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa Mnada wa Magena katika Mji wa Tarime unafanana na mnada ambao unaitwa Mnada wa Kimataifa wa Pugu lakini ukifika hakuna mazingira yoyote ya kimataifa ambayo unaweza ukaonyesha. Ng’ombe wote wanaofugwa mikoani mimi katika Jimbo la Ukonga kule Pugu ndiyo nawapokea na nawalisha watu wa Dar es Salaam. Naomba nijue, ni lini sasa Wizara hii itahakikisha jina la Mnada wa Kimataifa wa Pugu linasadifu na mazingira ya Pugu kwa maana ya malambo, umeme na huduma zingine? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mnada wa Magena ni Mnada wa Mpakani wakati Mnada wa Pugu ni Mnada wa Upili, kuna tofauti kubwa. Hata hivyo, naungana naye kukiri kwamba kuna changomoto nyingi ambazo zimejitokeza katika uendeshaji wa Mnada wa Pugu. Bado kuna fursa kubwa ya kuufanya mnada ule uwe na hadhi nzuri zaidi kuliko ilivyo sasa. Nimhakikishie tu kwamba tayari hatua zinachukuliwa ili kuboresha huduma katika Mnada wa Pugu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mwenyewe baada ya kupata uteuzi wa Mheshimiwa Rais, nilikwenda kutembelea Mnada wa Pugu na kuangalia hali ilivyo na tayari tumetoa maelekezo hatua mahsusi zichukuliwe ili kuboresha huduma pale ikiwa ni pamoja na huduma za maji na kuimarisha utaratibu wa kukusanya mapato. Kwa sasa karibuni Mnada wa Pugu utakuwa unatuma mfumo wa kukusanya mapato wa kielektroniki. Hata Mheshimiwa Waziri mwenyewe ameshatembelea Pugu. Kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba baada ya muda Mnada wa Pugu utaendeshwa katika hali ambayo ni nzuri zaidi ili kuweza kuchangia katika pato la Taifa.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nadhani kuna shida ya mawasiliano, wakati nilipoletewa nifanye marekebisho niliandika ni kifungu namba 20 na nikazungushia na sheria ninayo.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, naomba niseme tu kwamba nasikitika sana kwa majibu niliyopewa. Haya majibu, nimeuliza kuhusiana na mitaala utamsikiliza katika majibu Mheshimiwa Naibu Waziri hakugusa kabisa mitaala. Nimeuliza juu ya maswali ya kuchagua ya masomo ya hesabu, hakugusia. Nimeuliza kipengele cha tatu cha Waziri kutoa maelekezo, Sheria inasema The Minister may give the Council directions of a general or specific character and the Council shall give effect to every such direction, hakuna kushauriana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nitaomba niulize maswali mawili ya nyongeza wakati anajiandaa kunipa majibu sahihi kwenye swali hili.
Swali la kwanza, kwa nini Waziri wanang‟ang‟ania na kipengele cha kutunga mambo yao wao yaani kusema leo watu watumie GPA au watumie division, yaani leo waseme tufanye sayansi, hesabu na physics pamoja, biology na kemia. Haya wanakubali yawepo lakini hii ya ushauri na wataalam hawataki kwa nini naomba tujibu?
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, kwa nini Wizara hii inakataa kushirikisha Wataalam katika maamuzi ya kupima wanafunzi wetu, atueleza hapa wale watoto ambao walipimwa kwa kiwango cha kutumia GPA na wakapewa vyeti, sasa hivi Waziri ametoa tamko lake hapa anasema sasa ni division, hivi vyeti anavi-compromise namna gani katika elimu? Naomba atusaidie mambo hayo.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa amelalamika kwamba hatujazungumzia masuala ya kuchagua majibu ya hesabu na mambo mengine. Kimsingi najibu kadri ya swali lilivyowekwa, kule uliweka utangulizi lakini swali lako ulisema kwa nini kifungu hiki kisiondolewe na ndicho nilichokujibu.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo kimsingi lazima ieleweke Mheshimiwa Waziri hafanyi maamuzi kwa kukurupuka bila kupata taarifa mbalimbali zinazomwezesha kufanya maamuzi hayo. Hata hivyo si kwamba kila jambo linalofanyika kwenye Wizara linakuwa limetangazwa, lakini hatua mbalimbali zinakuwa zimechukuliwa, ikizingatiwa kwamba Wizara hii inazingatia sana masuala ya kitaalam.
Mheshimiwa Spika, katika maswali ya kuchagua majibu ya hesabu, siku za nyuma wanafunzi walikuwa hivyo hivyo wanachagua, lakini walikuwa na sehemu ya kufanyia kazi halafu wanachagua. Hata sasa hivi wanapewa karatasi wanazofanyia kazi, lakini wanachagua kwa ku-shade kwa misingi kwamba kwa siku za nyuma kwa sababu walikuwa wanasahihisha karatasi kwa mikono, sasa hivi inasahihisha mashine, ndiyo maana baada ya kuchagua lile jibu lake sahihi anakwenda ku-shade na kuweka ili mashine iweze kusahihisha.
Hiyo imepunguza kazi iliyokuwa inatakiwa kufanyika na watu 3000, sasa inafanyika na watu 300. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali lingine Mheshimiwa amezungumzia kwamba kwa nini tumeking‟ang‟ania hicho kifungu. Siyo suala la kuking‟ang‟ania, kifungu hiki kikitumika vibaya ndipo kina kasoro, lakini kama kinatumika vizuri kinaharakisha utendaji na maamuzi ya Wizara.
Kwa hiyo, nasimamia katika sura hiyo kusema kwamba, Waziri aliyeaminiwa na Serikali kutekeleza majukumu yake ipasavyo, naamini atakitumia kifungu hiki inavyostahili. Hata hivyo, baada ya kubadilisha GPA kuweka katika division, kimsingi hakuna athari zilizopatikana kwa sababu bado kuna uwiano katika hizo alama na wanafunzi hawa bado wanaendelea kupata haki zao kama kawaida.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kunipa fursa niulize swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa shida ya Nanyumbu na maeneo yaliyotajwa ni sawa na shida iliyopo Jimbo la Ukonga Dar es Salaam, ningependa kujua kauli ya Serikali kwamba barabara ya kuoka Banana – Kitunda – Kivule – Msongola ambayo imeahidiwa takribani ni awamu ya tatu, kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami, pamoja na Majimbo yote Mkoa wa Dar es Salaam ikizingatiwa kwamba Wabunge wengi humu ndani wanakaa Dar es Salaam na Majimbo yao yana hali mbaya sana ya barabara hasa wakati wa mvua.
Ni lini barabara hiyo itakamilika? Nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, barabara ya Banana – Kitunda – Kivule na kuendelea ni kati ya barabara ambazo zipo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 hadi 2020 kama ilivyo barabara ya Kongwa – Mbande ambayo Serikali imedhamiria kuijenga kwa kiwango cha lami katika kipindi hiki cha miaka mitano.
Mheshimiwa Spika, ninamhakikishia Mheshimiwa Mwita Waitara barabara hii kama sehemu ya ring roads za Dar es Salaam na kama ilivyoahidiwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi, tutaijenga kwa kiwango cha lami kama tulivyoahidi. Suala la lini, naomba sana katika masuala ya ujenzi wa barabara ni miradi mikubwa siyo rahisi sana kutoa tarehe.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naitwa Waitara, jina hili inabidi ulifahamu, jina rahisi kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, ameandika mwenyewe hapa kwamba gharama za upimaji ni shilingi 300,000 lakini mimi niliwaita hawa wahusika nikataka wanipimie eneo langu ambalo halifiki ekari mbili, wakafanya tathmini na wakaniambia natakiwa nilipe shilingi milioni tano, kwa hiyo nikapiga mahesabu wananchi wangu ambao wananizunguka pale Kivule na maeneo mengine wanawezaje kumudu hizo gharama kubwa za kupimiwa maeneo yao?
Kwa hiyo naomba kwanza anisaidie, gharama nilizopewa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ni milioni tano kwa eneo langu chini ya ekari mbili, yeye anasema hekta moja ni shilingi 300,000, na nini kauli yake sasa kwa maana ya maelekezo nchi nzima juu ya hili la upimaji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika maelezo yake Mheshimiwa Naibu Waziri anasema kwamba mimi nimeuliza swali langu ni hatua gani za dharura kwa sasa kwa sababu migogoro mingi ya ardhi iliyopo nchi nzima ni kwa sababu maeneo hayo kwa sehemu kubwa hayajapimwa na ikiwemo Dar es Salaam na watu wanasogeza mawe, kunakuwa na ugomvi mkubwa na kuna kesi nyingi katika mabaraza ya ardhi. Sasa nikataka mkakati wa dharura.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri anasema wana mpango wa kusogeza huduma, sasa naomba anisaidie, huu mpango walionao kuna bajeti yoyote ambayo imetengwa? Kwa sababu wakisema halmashauri inunue vifaa hivi ambavyo yeye mwenyewe amesema ni gharama, kama Waziri anakiri kwamba gharama ya vifaa vya upimaji wa ardhi ni kubwa Halmashauri ambayo haina fedha na imeomba fedha kutoka kwenye Bunge hili na Serikali hawajapeleka mpaka leo, hali ni mbaya, wao Serikali kwa maana ya hii Wizara wanasaidia nini katika mpango wa dharura kwa sasa ili huduma hizi ziweze kupatikana katika maeneo husika? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ameuliza maswali mawili, jambo la kwanza amesema, nimetaja kwamba gharama za upimaji ni 300,000 kwa hekta. Naomba niseme hizo ndizo gharama sahihi ambazo tulipitisha hapa kwenye kikao baada ya kupunguzwa ile awali iliyokuwa shilingi 800,000 na Bunge hili lilipitisha baada ya Mheshimiwa Waziri kuleta katika bajeti yake na kuomba ipunguzwe. Sasa kama Manispaa inatozo lingine tofauti na wewe ni mmojawapo katika Manispaa hiyo, ni vizuri pia kujua kwa sababu officially tunachojua na kiko katika maandishi ni shilingi 300,000 lakini kama Halmashauri huwa wana mipango yao kule kutegemeana na Baraza lenyewe la Madiwani wameridhia nini katika lile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwasababu kuna mambo mengine ambayo yanafanyika ndani ya Halmashauri kutegemeana na mamlaka walizonazo, lakini katika rate offial zilizoko ni shilingi 300,000 kwa hekta moja na ni shilingi 300,000 hiyo hiyo kwa kiwanja kimoja. Sasa pengine itabidi tuwasiliane kuweza kujua kwanini wanatoza shilingi milioni tano kwasababu zipi za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ameongelea habari ya harakati zipi za dharura ambazo tunazifanya ili kupunguza hilo na ni bajeti gani imetengwa. Naomba niseme; bajeti tuliyopitisha hapa Wizara ilileta bajeti ya shilingi bilioni nane kwa ajili ya kununua vifaa hivyo na tayari mchakato wa kununua umeshaanza na kwa sababu uko chini ya Benki ya Dunia ambao ndio wafadhili, mchakato ndani ya Wizara tumeshamaliza, tunachosubiri tu ni ile no objection kutoka Benki ya Dunia, wakishapitisha sisi hatuna tatizo kwasababu tayari ipo na tulisema itakwenda katika kanda zote nane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, harakati za dharura ambazo tunafanya sisi ndiyo katika hizo lakini bado tulishasema kuna makampuni zaidi ya 58 ambayo yapo na Halmashauri inaweza kuyatumia, Wizara imesharidhia yafanye kazi hiyo ili kuondokana na tatizo hili. Kama Wizara tunafanya kazi ya urasimishaji katika maeneo ambayo hayako vizuri, kwahiyo hilo naweza kujibu kuwa ndizo hasa harakati zetu tunazofanya kuhakikisha tatizo hilo linaondoka.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa nafasi ili kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shida ya maji katika Jimbo la Ludewa inafanana sana na shida ya maji katika Jimbo la Ukonga. Ukitembelea kata za Kivule, Msongola, Chanika, Buyuni, Zingiziwa, Pugu, Pugu Station, Ukonga, Gongo la Mboto na Kipunguni. Kata hizi zote hazina maji kabisa na hasa maji ambayo yanasimamiwa na Serikali ambayo ni maji safi na salama.
Sasa nilikuwa naomba kuuliza, kwa sababu nimezungumza mara nyingi Bungeni hapa kuuliza shida ya maji Dar es Salaam na hasa Jimbo la Ukonga ni nini kauli ya Serikali na hasa Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana kwamba baada ya Bunge hili tuongozane kwenda Ukonga akashuhudie watu wa Ukonga wanavyokunywa maji machafu na hasa kwenye shule, zahanati na vituo vya afya?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Jimbo la Ukonga lina changamoto ya upatikanaji wa maji. Lakini tunayo mipango ambayo inayoendelea katika Mpango wa Utekelezaji wa Programu Phase II ipo miradi ambayo Jimbo la Ukonga wametengewa fedha. Lakini katika mpango wa muda mrefu, maeneo ya Ukonga, Mkaranga na maeneo ya Kigamboni, maji yatapatikana kutoka chanzo cha Mpera na Kimbiji. Ambapo sasa utekelezaji wake tumeanza kuchimba visima karibu visima 20 vinakamilika. Baada ya hapo tunajenga miundombinu ambayo tutapeleka maeneo hayo ya Ukonga na kutakuwa hakuna tatizo kubwa na nikuahidi kwamba katika kipindi cha miaka hii minne ambayo imebakia katika Seriali ya Awamu ya Tano, tutahakikisha kwamba Ukonga inakuwa na maji ya kutosha.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa nafasi niulize swali moja dogo la nyongeza. Ni kweli kwamba eneo hili ni eneo muhimu sana katika utendaji wa Halmashauri zetu na ndiyo maana kumekuwa na Wakuu wa Idara wenye taaluma mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nimuulize Mheshimiwa Waziri anisaidie kitendo cha uteuzi wa Wakurugenzi kutoka nje ya wale Wakuu wa Idara na wakati mwingine watu ambao hawana taaluma kabisa ya kuendesha Halmashauri kuteuliwa kuwa Wakurugenzi katika maeneo haya na hata Waandishi wa Habari na maeneo mengine waliteuliwa ikaonekana kwamba ni form four na wakawa disqualified wakaondoka katika maeneo hayo na wengine wakaogopa kwenda kwenye maeneo waliyoteuliwa ……
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri haoni kwamba kitendo hicho cha kutoteuliwa wale Wakuu wa Idara kama sehemu ya promotion ni kuwavunja moyo katika utendaji wao wa kila siku?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nafurahi kwamba yeye mwenyewe amesema ni promotion na hili ni suala la uteuzi. Teuzi hata siku moja haziombwi, mwenye mamlaka ndiye anayeamua amteue nani. Vilevile, kwa mujibu wa Ibara ya 36, Mheshimiwa Rais anayo mamlaka ya kumteua mtu yeyote ambaye anaona anafaa. Kwa hiyo, ni sahihi kabisa na naamini Mheshimiwa Rais ametenda haki kwa kufuata taratibu.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Ni kweli kwamba kuna changamoto nyingi kwa watumishi wa umma, ni pungufu kwa uwezo mdogo wa Serikali kuajiri na wengine wametumbuliwa katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nijue ni nini kauli ya Waziri wa Utumishi kwa watumishi wale ambao wanashushwa vyeo, wanadhalilishwa na kutukanwa na viongozi, hasa Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa na ukizingatia matokeo ya form four yametoka, wameanza kutumbuliwa. Sasa nini kauli ya Serikali kuwatia moyo waliopo kazini na kuwatia moyo ambao watapata ajira, ili wajue wataenda mahali salama wakafanye kazi nzuri kutumikia Watanzania?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kupata majibu.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa niseme tu kwamba masuala mazima ya nidhamu, ajira pamoja na upandishwaji wa vyeo na kushushwa vyeo yanaongozwa na kanuni, sheria na taratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoweza kusema tu ni kwamba, kama kuna ambaye anaona kanuni hazikufuatwa, basi tuweze kupata taarifa ili tuweze kufuatilia. Lakini tumekuwa tukitoa miongozo mbalimbali kwa viongozi wa kisiasa pamoja na watendaji kuhakikisha kwamba, wanazingatia Sheria ya Utumishi wa Umma, wanazingatia Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma, pamoja na Kanuni za Utumishi wa Umma. Kwa hiyo, nipende tu kusema kwamba kama kuna mtumishi ambaye naona yeye hakutendewa haki basi asisite kuwasilisha malalamiko yake.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri sana yaliyotolewa na Waziri Mheshimiwa Kairuki, napenda niongezee tu kwenye swali lililoulizwa na Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, kumekuwa na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kutokana na watumishi wazembe. Na mtambue kwamba katika Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi tulisema kwamba kwa watumishi wazembe hatutakubali kuendelea nao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichukue nafasi hii kusema kwamba Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wamegawiwa maeneo yao ya utawala na wanasimamia masuala yote, lakini wanasimamia yote kwa mujibu wa sheria. Haiwezekani unapewa pesa ya basket fund, wewe ni DMO halafu huzitumii na watu wanakosa huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanya utafiti katika mikoa minne, ziko hela nyingi kwenye Halmashauri hazitumiki, wanataka kuzifanyia nini? Mnasema tusichukue hatua, haiwezekani. Haiwezekani unapewa shule una walimu zaidi ya 15 pamoja na changamoto zilizopo ambazo ni haki yao kuzidai, lakini si sababu ya wao kutokutimiza wajibu wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema tu kwamba Wakuu wa Mikoa wanayo haki ya kisheria kuchukua hatua kwa mtumishi yeyote awe ni Mkuu wa Shule, kwa mfano uteuzi wa Mkuu wa Shule unateuliwa na RAS ambaye ndio Katibu Mkuu wa Mkoa. Kwa hiyo, Mkuu wa Mkoa akichukua ile hatua, nimekuwa nikiulizwa na Wabunge wengi hapa kwamba mbona wanaingilia mambo mengine. Jamani, mkumbuke mlikuwa mnasema watumishi wetu ni wazembe. Ngonjeni kidogo tubanane ili twende kwenye ufanisi na Watanzania wanangojea hayo mabadiliko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwasihi tu Waheshimiwa Wabunge, tushirikiane. Wenzetu nao wale ni binadamu katika namna moja au nyingine wanaweza wakafanya makosa, tuwasiliane, turekebishane, ndio maana ya administration and leadership. Si kwamba wao hawakosei, wanaweza wakakosea kwa namna moja ama nyingine, lakini na mazingira yale tuyaangalie, lakini huku nikitambua kwamba watumishi nao wana haki yao, lakini na wao pia watekeleze majukumu tuliyowapa.

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nilitaka kuongezea tu kwenye jibu linalohusu mkakati wetu wa kupeleka huduma za upasuaji kwenye vituo vya afya nchini wakati hakuna watumishi wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekwishakutoa maelekezo kama Serikali kwa Makatibu Tawala wote wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kufanya redistribution ya watumishi ndani ya maeneo yao, kuwatoa kwenye maeneo ambapo wapo wengi na kuwapeleka kwenye vituo hivyo ambavyo tunataka vitoe huduma za upasuaji. Huu ni mkakati wa muda tukisubiri mkakati wa kudumu.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shida ya barabara ya Jimbo la Mtera inafanana sana na shida ya barabara ya Jimbo la Ukonga. Barabara ya kutoka Banana - Kitunda - Kivule - Msongora ni barabara ambayo imeahidiwa kwa miaka ishiri ambapo Mheshimiwa Rais wa sasa alikuwa Waziri kwenye eneo hilo aliahidi na haikutekelezwa, miaka kumi ya Mheshimiwa Kikwete iliahidiwa haikutekelezwa. Kwenye bajeti ya mwaka jana ilionyesha kuwa TANROADS wanasaida kujenga angalau kilometa 3.2.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapozungumza hapa walishaenda wakafanya survey wakapata na mkandarasi yupo anasubiri. Shida iliyopo ni kwamba fedha hazipo na ieleweke tu kwamba barabara hii ndiyo inayohudumia Kata ya Kitunda, Kata ya Mzinga, Kata ya Kivule, Kata ya Msongora na mojawapo ya shida ya barabara hii imeleta madhara makubwa kwa sababu shule zilizoongoza kwa kufanya vibaya, shule ya msingi Kitonga ipo eneo hili na shida mojawapo ya watoto wale kufeli ni kwamba wanatoka mjini kati, wanaenda kule hakuna usafiri wanatembea kwa miguu, kwa hiyo wanatega shule na wamefeli ndiyo maana wakaomba walimu wasiadhibiwe kwa sababu hii.
Sasa naomba nimuulize Mhesimiwa Naibu Waziri ni lini baabara hii itaweza kutengenezwa kwa kiwango cha lami au hata changarawe ili magari yatoke Banana mpaka Msongora – Kitonga, walimu na watumishi wengine, wanafunzi waende shuleni kwa uhakika kupunguza shida iliyopo sasa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO:Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waitara anafahamu kwamba tatizo hili aliliwasilisha kwangu vilevile kupitia kwa Afisa Elimu Sekondari ambaye naye alilalamika sana kuhusiana na kufeli shule zake, kuwa za mwisho katika Mkoa wa Dar es Salaam; na alisema kwamba mchango mmojawapo ni matatizo ya hii barabara na wanafunzi wanapangiwa kule mbali kwa sababu shule za karibu huwa zinajaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimuhakikishie, Serikali imelichukua hili, tutalishughulikia ili turekebishe haya. Naomba unipe fursa niwasiliane na TANROADS Mkoa wa Pwani nipate taarifa zao za karibuni maana yake nilishawaambia kuhusu hili tatizo baada ya kupata hiyo taarifa kutoka kwa Afisa Elimu wa Sekondari wa Wilaya ya Ilala, na baada ya kujua sasa alifanya nini baada ya malalamiko yale nitakuja nikuambie hatua ipi tunaichukua.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Tunaunga mkono juhudi ambayo inafanyika ya kuboresha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam. Lakini kuna malalamiko ya muda mrefu ya wananchi wa Kata ya Kipawa, Ukonga - Kipunguni, Kigiragira kule Buyuni, wanadai fidia Serikali mpaka leo na
wameshindwa kufanya shughuli za kimaendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kujua ni lini
mgogoro huo utamalizwa na Serikali ili uwanja ukamilike na wananchi wakaendelea kuwa na amani na kuishi maisha ambayo na wenyewe wanapaswa kuishi kama binadamu wa kawaida hapa Tanzania? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA
MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tena kumthibitishia Mheshimiwa Waitara pamoja na jirani yake Mheshimiwa Bonnah Kaluwa, Mbunge wa Segerea kwamba kazi mlioifanya, mtakumbuka mimi ndio Mbunge wa Segerea alinileta kukutana na wale wananchi wa Kipunguni, kuhusiana na suala hili. Niwaombe kwamba tulidhamiria suala hili tutalimaliza katika miaka hii mitano. Mnafahamu baadhi ya maeneo tumeshaanza kulipa fidia, Mheshimiwa Bonnah
Kaluwa unalifahamu hilo na umelifuatilia kwa kasi sana na ninakuhakikishia pamoja na Mheshimiwa Waitara kwamba wananchi wale watalipwa fidia katika miaka hii mitano. Kuna matatizo ambayo yapo katika suala hili la fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunashughulikia matatizo yaliyoingiliwa katika suala hili la fidia, kuna wajanja wachache walitumia fursa wakatumia fedha vibaya na tumepelekea PCCB wanafanya kazi, tutakapopata taarifa PCCB tutakuja kulimaliza hili suala la fidia katika wale ambao wamebakia kulipa.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri ambaye ni mwalimu wangu nampongeza sana kwa majibu mazuri. Kama hawatamharibu, ataenda vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba yeye mwenyewe kama mzazi na kama mwalimu umri wa mtoto wa kiume kuoa miaka 14 hakubaliani nao na umri wa mtoto wa kike kuolewa hakubaliani nao. Sasa Serikali kwa mujibu wa Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, maana yake anataka kuniambia Serikali inataka watoto wadogo waendelee kuolewa. Kwa hiyo, watoto wa kike wasipate haki yao ya kucheza na kupata elimu na kuwa viongozi wa umma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hukumu ilikuwa ni miezi sita na imeshapita na rufaa haijakatwa. Sasa naomba niulize swali, kwa nini Mheshimiwa Waziri sasa asilete Muswada Bungeni ili amri hiyo ya Mahakama ya Rufaa itekelezwe ili kuwapa haki watoto wadogo wa kike na kiume wapate haki ya kusoma na kuwa viongozi wa Taifa hili?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wale wote ambao wamesoma Legal Anthropology wataelewa kwamba mambo ya mila, desturi, imani ya dini na itikadi hayataki haraka, yanataka muafaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo yoyote na bahati mbaya, aah, kwenye Kiswahili hakuna bahati mbaya. Kuna umuhimu sasa wa vyuo vyetu kufundisha Legal Anthropology. Huwezi kubadili mila, desturi, imani ya dini na itikadi kwa kutumia sheria peke yake tu, utakuwa unajidanganya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natoka katika utamaduni ambao umekuwa na mila siyo nzuri ya ukeketaji. Sheria ipo, imezuia, lakini kwa sababu bado ni suala la imani na itikadi kwa watu, leo wamelihamishia kwa watoto wachanga. Sasa nazungumza kama Profesa wa Sheria, ni hatari. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Waitara Chacha, rafiki yangu mkubwa, anajua kabisa kuna mila na desturi za anakotoka leo, mimi siafikiani nazo, lakini zinahitaji elimu, zinahitaji uelewa. Ni vigumu sana mtu anayetoka nje ya eneo hilo kuelewa kwamba mapenzi ni pamoja na kipigo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namsihi Mheshimiwa Waitara, tukae nje, tukutane. Namsihi na nimesema hivi kwa masihara haya kwa sababu ni mtu tumeshibana, hawezi kunichukulia tofauti. Tutalijadili, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutalijadili, ahsante
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Barabara ya kutoka Kitunda - Kivule -Msongola ninapozungumza sasa hivi haipitiki kabisa nauli imepanda kutoka shilingi 500/= mpaka shilingi 1,000/=; walimu na wanafunzi ambao wanasoma shule ya Mvuti, Mbondole, Kitonga wanatembea kwa miguu kwa umbali wa zaidi ya kilometa 11.
Ningeomba kujua ni hatua gani kwasasa Mheshimiwa Waziri unaweza akachukua kuwasaidia wananchi wale na hasa watumishi wa umma ili waweze kuendelea kupata huduma muhimu katika eneo hilo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nafurahi sana hawa Wabunge wawili wanafanyakazi pamoja ikiwa ni pamoja na Mbunge Bonnah Kaluwa, Mbunge wa Segerea. Alishalileta hilo na kwa taarifa yako TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na TANROADS Taifa hivi tunavyoongea wanalishughulikia hilo kwa namna ambayo lililetwa kwetu na Mheshimiwa Bonnah Kaluwa. (Makofi)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba nimuulize swali dogo Mheshimiwa Naibu Waziri, kwanza nampongeza sana kwa kazi nzuri ambayo anafanya…
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Ukonga, Kata za Msongola, Buyuni, Zingiziwa, Majohe, Pugu, Pugu Station na Chanika hazina umeme na Mheshimiwa Naibu Waziri anafahamu. Kwa sababu kuna mkanganyiko kule Dar es Salaam kwamba ni mjini siyo vijijini, je, REA inaenda maeneo hayo au haiendi? Ahsante sana.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa, yako maeneo yako mjini, lakini kwa Mheshimiwa Mbunge wa Ukonga tumeshakaa naye. Maeneo anayoyataja ya Majohe, Chanika, Zingiziwa mpaka kwenye gereza lako kijijini kule, yale ni maeneo ya vijijini yatapatiwa umeme kupitia Mradi wa REA na tumeshaanza. Hata hivyo shule yake aliyosema Mheshimiwa ya Bombambili tumeshaifanyia kazi na yeye ni shahidi. Kwa hiyo, maeneo hayo yatapelekewa umeme kwa kupitia mradi wa REA.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu yaliyo chini ya kiwango ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji naomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza kwa niaba ya Mheshimiwa Saed Kubenea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza liliuliza kwamba mpaka sasa kasi ya kufufua viwanda imefikia wapi?Kwa hiyo, kwa majibu hayo inahitaji tujue kwamba Waziri yuko tayari kukiri kwamba kiwanda hiki hana mpango wa kukifufua kwa maelezo aliyotoa hapa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, mpaka sasa anaamini kwamba kauli mbiu ya Serikali ni kuinua viwanda au kuua viwanda? Ahsante.
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya Serikali iliyofanyika imeandikwa kwenye jibu langu ni kufanya utafiti; na mwaka jana nilipewa shilingi milioni 150 kwa ajili kufanya utafiti na umakamilika kwa hiyo kazi niliyopewa nimemaliza. Kazi ya Serikali ni kujenga viwanda na viwanda vitaendeshwa na Sekta binafsi, mwaka unaokuja 2017/2018 nimeomba pesa shilingi milioni 70 tu nitangaze tender sekta binafsi ifanye kazi.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kwanza naomba niseme tu kwamba nashukuru kwa ushirikiano ambao naupata kutoka pale TANESCO, Gongolamboto, Kisarawe na Mheshimiwa Naibu Waziri nikimpigia simu anapokea, siyo kama wengine walivyosema hapa.
Mheshimiwa Spika, pia naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Jimbo la Ukonga lina shida kubwa ya umeme, lakini pia kuna shida nyingine zimeongezeka, Ukonga kuna wajasiriamali wadogo wenye viwanda vidogo vya kusaga unga wa sembe na dona, lakini pia na chakula cha kuku; umeme unakatika sana katika eneo hilo. Kwa hiyo, naomba kama kuna utaratibu wa dharura, ufanyike ili kuzuia hiyo kero kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, eneo la Kitonga Sekondari, Mvuti Sekondari, Mbondole Sekondari, Bombambili Shule ya Msingi na Shule ya Msingi Nzasa II kuna visima vya maji havifanyi kazi kwa sababu kuna shida kubwa ya umeme katika eneo hilo.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza akawa na mkakati mahususi wa kuondoa kero katika maeneo haya ambayo ni maeneo muhimu kwa walimu, wanafunzi na jamii inayozunguka eneo hili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa na mimi namshukuru Mheshimiwa Mbunge anavyofuatilia masuala ya wananchi wake wa Ukonga. Niseme tu, katika swali la kwanza kuhusu kukatika kwa umeme; katika maeneo ya Kisarawe hivi sasa tulikuwa tunajenga miundombinu ya kusafirisha umeme kutoka Gongolamboto na Kipawa ili wananchi wengi wafikiwe na umeme unaojitosheleza. Ujenzi wa utaratibu huo unaendelea na unakamilika mwezi wa Oktoba tarehe 22.
Mheshimiwa Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Waitara kwamba mara baada ya kukamilika, tatizo la kukatika kwa umeme kwa maeneo ya Kisarawe, Gongolamboto, Mvuti pamoja na Chanika yatakwisha mara moja.
Mheshimiwa Spika, katika Jimbo la Ukonga yapo maeneo ambayo yanapata umeme kutoka eneo la Kisarawe na kwa maana hiyo yanahesabika kama yapo vijijini. Maeneo hayo ni pamoja na kama ambayo ametaja Mheshimiwa Waitara, ni Kitonga lakini yapo maeneo ya Namanga, Bombambili pamoja na Uwanja wa Nyani, yote hayo yanapata umeme kutoka Kisarawe. Kwa maana hiyo, visima vilivyopo katika maeneo hayo, yataunganishwa sasa na umeme wa Mradi wa REA ambao unakuja sasa ili wananchi waweze kupata maji kwa urahisi.
Mheshimiwa Spika, niseme tu kwa niaba ya wananchi wote kwamba Mradi wa REA Awamu ya Tatu, pamoja na kupeleka umeme kwenye vitongoji na vijiji, utaunganisha pia miundombinu ya maji kote nchini.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Waitara maeneo ya Kitonga, Uwanja wa Nyani, Msongole, Mvuti na Vijiji vingine ambavyo vina visima vitaunganishwa na mradi huu wa REA.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kuna mgogoro wa Hifadhi ya Kazimzumbwi kati ya Ukonga na Kisarawe na nimshukuru Mheshimiwa wa Maliasili na Waziri wa Ardhi na Mheshimiwa Waziri Mkuu tulishakutana tukafanya mazungumzo na kulikuwa na kesi Mahakamani ambayo imekwisha. Sasa wataalam wale wa Maliasili wameenda Kazimzumbwi, wamevunja nyumba za watu, wanapiga watu, wanaharibu mali za watu katika eneo hilo. Swali langu, hawa Waheshimiwa Mawaziri wawili, wapo tayari twende pale Kazimzumbwi au hapahapa Dodoma nipo tayari kuwaita wale wahusika tukae pamoja tukubaliane kumaliza mgogoro ule ili usilete maafa katika aneo lile? Ni hilo tu.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, swali lake linafanana na maswali yaliyoulizwa na muuliza swali la msingi hapo awali, ni changamoto za utekelezaji wa usimamizi wa maeneo yaliyohifadhiwa kwamba wananchi wamekuwa wakilalamika juu ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali zinazohakikishia Serikali kwamba tunasimamia maeneo yaliyohifadhiwa.
Mheshimiwa Spika, changamoto moja inayojitokeza hapa ni kwamba, kwa sababu suala hili linahusisha pande mbili; upande mmoja ni Serikali ambayo inasimamia sheria, kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu yako masuala ambayo ni lazima yatekelezwe ili kuhakikisha kwamba uhifadhi unafanikiwa lakini upande wa pili ni wananchi ambao kwa maoni yao wanadhani katika kutekeleza shughuli mbalimbali za usimamizi wa hizo hifadhi upo utekelezaji ambao una kasoro kwa sababu unaleta athari kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, sasa hapa haiwezekani kupata uhalisia, ukweli na uhakika bila kwenda kwenye uhalisia wenyewe. Kwa hiyo, nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwa sababu ameuliza Mawaziri hao wanaweza kuongozana naye kwenda kuona hali ilivyo huko au wale wananchi labda kupitia viongozi wao kama wanaweza kupata fursa ya kuja Dodoma na kuweza kuonana na Waziri mwenye dhamana na Msaidizi wake wanaosimamia Maliasili.
Mheshimiwa Spika, labda niseme tu kwa kifupi kwamba hii ya pili itakuwa ni nyepesi zaidi kwa sababu ahadi zetu za kufika kwenye maeneo mbalimbali ambayo yana changamoto zinazohusiana na maliasili na utalii zinakuwa ni nyingi na muda unakuwa hautoshi. Kwa hiyo, kama hili la pili Mheshimiwa Mbunge anaweza kulitekeleza kwa urahisi zaidi ni jepesi zaidi. Hebu tupate viongozi kutoka huko, waje hapa na kile ambacho wanaona kwamba ni sahihi kwa upande wao halafu tutakuja hapa kuzungumza masuala haya kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu kwa sababu suala hili la Kazimzumbwi limeshawekwa vizuri kwa mujibu wa sheria lakini kama zipo changamoto basi ni utaratibu tu wa Serikali sikivu kuweza kusikiliza wananchi wanasema nini.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge hebu fanya utaratibu wa kuweza kupata viongozi wanaotoka kwenye maeneo haya wakija hapa basi mimi na Mheshimiwa Waziri tutaweza kuona namna bora zaidi ya kuweza kuwasikiliza halafu tutaweza kuona namna ya kuweza kushughulikia matatizo yao kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Jimbo la Ukonga lina kata 13 na kata zote zina bodaboda karibu vijiwe zaidi ya kumi kila kata moja. Ukonga tumechangishana fedha tukajenga Kituo cha Polisi kule Chanika na kingine kinataka kujengwa pale Kata ya Kivule, lakini kwa hali ilivyo sasa, wananchi wa Ukonga na hasa bodaboda nikiwaambia wachangie fedha hawatachangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyozungumza usiku wa kuamkia leo, wanakuja askari zaidi ya 20 wana bodaboda, walikuwa wanakuja na gari wanaificha, halafu wanapiga watu mpaka na marungu, wana-search kwenye wallet, kwenye pochi kila mahali wanaomba fedha. Sasa wanaenda wanakusanya bodaboda zile wanaomba shilingi 10,000 kwa lazima, kama huna zinapakiwa kwenye gari zinapelekwa central.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natakiwa nijue, ili kuleta mahusiano mazuri kati ya vijana wa bodaboda na polisi, Waziri anatoa kauli gani kuhusiana na jambo hili? Hata haya mambo ya mauaji kama watu wana uhasama hawatoi taarifa. Wanawakimbia kwa sababu ukikamatwa na polisi wala hakuulizi leseni, wala hakuelekezi, kama huna pesa unatembea. Naomba Waziri atoe kauli hapa kusaidia vijana wa bodaboda Mkoa wa Dar es Salaam na hasa Jimbo la Ukonga. Ahsante Mwenyekiti.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba maelekezo ya Wizara tuliyotoa ni kwamba kuwa na bodaboda sio kosa na tumeelekeza watu wanaofanya makosa ndiyo wakamatwe. Kuwa tu na bodaboda haitoshi kuwa kosa kwa sababu hilo ni jambo ambalo lipo kisheria. Kwa maana hiyo nimepokea tu hiyo ya nyongeza aliyoisema ambayo yenyewe imekaa kituhuma zaidi nitalifanyia kazi, kama kweli lipo tutachukua hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini maelekezo yetu tumesema kama vijana wamekosea wafikishwe kwenye mkono wa sheria lakini kama hawajakosea waachwe wafanye kazi zao za kujitafutia maisha kwa uhuru na usalama na wala wasikimbie. Nilielekeza nikasema kuna wakati mwingine hata wanaweza wakawamata kwa bahati mbaya na ikafika mpaka vituoni, niliwaambia wasione aibu kumuachia yule ambaye walimkamata kimakosa ambaye alikuwa hausiki.
Nilisema hata wamuombe radhi kwamba wewe si tuliyekuwa tunakutafuta nenda kaendelee na shughuli lakini isiwe kosa kwamba yeyote ambaye ameshakamatwa akifika kituoni basi inakuwa kazi kutoka, tuwatendee haki kufuatana na kosa kama amefanya ama hajafanya.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Spika, huu ni mgogoro wa eneo ambalo limetathminiwa tangu mwaka 1997, huu ni mwaka 2017 miaka ishirini baadae.
Swali la kwanza, ni kwa nini Serikali inakataa kufanya tathmini upya katika maeneo haya hasa ukizingatia hali ya maisha ya sasa, kwamba hawa watu hata wakilipwa fidia leo hawawezi kufanya chochote kulingana na ugumu wa maisha ulivyo, kwa nini Serikali haipo tayari kufanya tathmini ya fidia ili walipwe kulingana na hali halisi ya maisha ya sasa?
Swali la pili, mgogoro huu pia umeathiri wananchi waliohamishwa kutoka Kipunguni ‘A’ kwenda Kipunguni ‘B’ Jimbo la Ukonga, Kipawa wakapelekwa Kata ya Buyuni Ukonga. Tunapozungumza hawa watu hawajalipwa fedha na walihamishwa kutoka Kipawa Kipunguni wakapelekwa Mbuyuni ambako hawakupewa tena maeneo. Sasa kuna mgogoro kati ya wananchi waliotoka Kipawa Kipunguni na wakazi wenyeji wa kule Buyuni.
Mheshimiwa Waziri yupo tayari baada ya Bunge hili au hata weekend yoyote tuambatane twende akawasikilize wananchi wenyewe awaone wanavyolalamika na kulia aone kama kuna sababu ya msingi sana ya kuchukua hatua mapema kwa kulipa fidia na kuondoa mgogoro uliopo katika eneo hilo. Nakushukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, sasa tumedhamiria kulipa fidia yote katika mwaka huu wa fedha unaoanza mwezi Julai, kwa sababu tumedhamiria tukisema tuanze kufanya uthamini upya itatuchelewesha kwa sababu kazi ya fidia nayo ni kazi ya muda mrefu.
Mheshimiwa Spika, ninawaomba sana ndugu zangu tulimalize hili suala na kwa kweli kwa namna fidia tulivyolipa ni kama tumekuja kulipa mara tatu zaidi ya ile thamani iliyokadiriwa mwanzo kwa sababu ya hiyo interest na interest ni kwa mujibu wa sheria, sehemu zote mbili kulipa kwa kufuata interest ya kila mwaka ama kuamua kufanya fidia upya zote ni njia sahihi na zote zinafuata sheria za nchi yetu.
Ninakuomba tulipe fidia kwa kufuata interest ambayo imekadiriwa kuanzia mwaka huo walipofanyiwa tathmini, najua Serikali tutaingia hasara kwa sababu tutalipa zaidi kuliko kama tungeweza kufanya evaluation upya, lakini Serikali imekubali ili tusipoteze muda tena tulimalize hilo once and for all.
Pili, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge niko tayari baada ya kumaliza Bunge hili tupange twende tukalishughulikie suala hilo huko. (Makofi)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mimi ni mwalimu wa hesabu na chemistry, nimesahihisha majibu ya Serikali na Mheshimiwa Naibu Waziri amepata 5% kati ya 100% ya majibu. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maelezo yake Mheshimiwa Naibu Waziri, ambaye ni rafiki yangu sana, ameandika kimoja tu cha ukweli kwamba mradi huu wa Kipunguni B umekamilika, mengine yote ni ya uongo.
Mheshimiwa Waziri, inaonekana ninaposema Jimbo la Ukonga lina shida ya maji hujui, upo tayari kutafuta taarifa sahihi ya miradi ya maji Jimbo la Ukonga uniletee kabla Bunge hili halijaisha? Hilo ni swali la kwanza.
Swali la pili, kipengele (b) hukujibu kabisa. Mimi nimeuliza kuchimba bwawa katika Mnada wa Pugu ambao ni Mnada wa Kimataifa, Dar es Salaam, hakuna mnada mwingine tofauti na huu, haukugusa kabisa. Umezungumza habari ya Kipera ambao ni mradi wa tangu mwaka 2016, uliandikwa kwenye Bajeti ya Maji na mwaka huu umeandikwa, haujaanza kutekelezwa. Nimeuliza bwawa la maji, hujajibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali la pili, upo tayari sasa nikuitie akina mama wote wa Ukonga pale ambao wanapata shida na hasa pale ambapo wanakwenda kujifungua hakuna maji zahanati kule Yongwe, Chanika, Msongola, Buyuni na Kivule ili uende Ukonga uzungumze nao wakueleze shida ambazo wanazipata wakienda kujifungua, wanaambiwa njoo na maji ambapo ndoo inauzwa shilingi 500? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa amesema kwamba taarifa niliyotoa siyo sahihi na amezungumzia suala la bwawa la Pugu.
Mheshimiwa Mbunge ni kwamba Serikali imefanya juhudi kubwa sana kupeleka maji katika Jiji la Dar es Salaam na miradi miwili mikubwa imekamilika ambayo inatoa kiwango kikubwa sana cha maji. Mradi wa tatu ambao utahusika na visima vile vya Mpera nao unakamilika mwezi Juni na utakuwa na lita zaidi ya milioni 260. Kazi iliyobaki ni kuyasambaza na tayari maeneo mengi ikiwemo na Kipunguni tayari mabomba yameshaanza kufika kule ikiwa ni pamoja na kuchimba visima. Siyo maeneo yote lakini tunaendelea. Matarajio yetu baada ya kupata fedha za kusambaza maji, maeneo yote yatapata huduma ya majisafi na salama, hilo nakuhakikishia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ameuliza kama niko tayari kuongea na wananchi? Nimhakikishie kwamba niko tayari, wakati wowote nitakwenda kutoa majibu kwa wananchi bila wasiwasi wowote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia amezungumzia suala la bwawa, ni kweli Mheshimiwa Mbunge swali hilo nimeliona, lakini wewe kwanza nikwambie umelelewa na CCM. Umechanganya maswali. Swali moja limekwenda Wizara ya Maji na Umwagiliaji lakini swali lingine lilikuwa ni swali la Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Eneo la Pugu, soko lile linahudumiwa na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, swali hilo lilitakiwa lielekezwe huko, bahati mbaya lilikua ni namba moja. Kama namba zingekuwa mbili ningelipeleka kule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa sababu kama ameuliza kama swali la nyongeza, nitajibu kama Serikali. Ni kwamba tayari Wizara husika imechimba kisima kirefu, kisima kile kinatoa lita 1,500 kwa saa na tenki kubwa limejengwa ambalo lina ujazo wa lita 10,000. Kisima hicho hakijaanza kutumika kwa sababu kwa sasa mvua inayonyesha ni nyingi, kwa hiyo, mifugo inapata maji ya mvua. Lakini pia baada ya huu mradi mkubwa wa kutoka Mpera na Kimbiji kukamilika, tenki lililojengwa pale Pugu na Wizara husika litapata maji hayo ili kuhakikisha kwamba mifugo inapata maji na hakutakuwa na wasiwasi wa aina yoyote Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kata ya Pugu, Jimbo la Ukonga kuna Mnada wa Kimataifa wa Pugu, nimuombe Mheshimiwa Waziri kama yupo tayari tumpeleke katika eneo hili akutane na wafanyabiashara wa eneo hili ili wamueleze kero kubwa ziliyopo zikiwemo za ukosefu wa malisho na bwawa la maji na vyoo na mnada huu unaitwa wa kimataifa ambao kimsingi ndio unalisha Mkoa wa Dar es Salaam.
Mheshimiwa Waziri, upo tayari kwenda Pugu ukutane na watu hawa wakueleze kero zao kiundani zaidi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, niko tayari kwenda Pugu kukutana na wafugaji hawa na wauzaji.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naomba niulize swali dogo la nyongeza.
Hivi karibuni Naibu Waziri wa Elimu ametoa kauli akisema watoto wakitaka kuolewa wawe na cheti cha kumaliza form four, wakati huo huo Serikali ilisema wale wanafunzi ambao wanapata ujauzito wakiwa shuleni wasiendelee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ningependa nipate
kauli ya Serikali katika mkanganyiko huu, nini hasa ni kauli ya Serikali sahihi. Vipi wanafunzi ambao wanapata mimba wakiwa shuleni na hawaendelei kwa mfumo wa shule, lakini na kauli ya Waziri ya kusema anayetaka kuolewa awe na cheti cha form four? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS – TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI) -MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa majibu sahihi kwa Mheshimiwa Waitara pamoja na Watanzania wote waliopata mkanganyiko kuhusu kauli hiyo ni kwamba, nilisema Sera Mpya ya Elimu ya mwaka 2014 huko tunakoelekea inabadilisha mfumo wa sasa wa elimu kwenda kwenye mfumo mpya ambao utahitaji mtoto aanze chekechea mwaka mmoja, asome shule ya msingi miaka sita, shule ya sekondari miaka minne na hii itakuwa ni lazima kwa yeyote atakayeanza darasa la kwanza hadi amalize form four. Kwa hiyo, nikasema kwamba tutakapofika wakati huo, kithibitisho muhimu kwamba huyu mtoto sasa amemaliza form four ni school leaving certificate, wakati huo siyo leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ndugu yangu Mheshimiwa Waitara huo ni ufafanuzi sahihi kabisa wa sera mpya. Sasa hivi tunaandaa utaratibu na maandalizi ikiwepo pamoja na miundombinu ili tuweze hatimae kuitekeleza hiyo sera muda utakapofika. Kwa hiyo, usiwe na mkanganyiko ndugu yangu Waitara. (Makofi)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza nifanye marekebisho kidogo kwenye majibu, hili Daraja la Mongolandege lipo kwenye Mto Msimbazi sio Mto Mzinga, lakini vilevile kwa majibu haya, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa sababu Serikali inakiri kwamba mvua ilinyesha ikaleta madhara makubwa na Daraja la Mongolandege na Mto Nyebulu unatenga maeneo mawili tofauti kwenye huduma za jamii yaani upande mmoja ndiyo kuna shule ya sekondari, msingi, afya na huduma zote za kijamii na upande mwingine wananchi wanakaa pale. Katika hali hiyo mvua ikinyesha huwa ni kisiwa, wanafunzi hawaendi shule mpaka mvua iishe.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujua ni kwa nini Serikali isijitahidi mwaka huu wa fedha ifanye usanifu na fedha itengwe kwa ajili ya kazi hii? Maana kwenye majibu yake anasema wataangalia na baadaye bajeti itengwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa sababu eneo hili ni muhimu na wananchi wanapata shida, tunaweza kupata huduma ya dharura ya daraja la muda katika maeneo yote mawili ili huduma ziendelee hasa wakati wa mvua tunapoelekea mwezi Aprili? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, uwezekano wa kuweza kutenga fedha kipindi hiki ambacho bajeti tayari imeshapitishwa na Bunge lako Tukufu jambo hili litakuwa na ukakasi mkubwa sana. Tutakubaliana na Mheshimiwa Waitara kwamba ili daraja hili liweze kujengwa kwa kina lazima usanifu ufanyike ili isije ikatokea kama yale yaliyotokea mwanzo.
Mheshimiwa Naibu Spika, namuomba Mheshimiwa Mbunge avute subira na leo nilikuwa nafanya mawasiliano na TARURA, kwa kuanzia kwa ajili ya usanifu itatengwa jumla ya shilingi milioni 100 na ujenzi kwa ajili ya kuanza, tutatenga jumla ya shilingi milioni 300. Kwa hiyo, asipate shida, naomba nimhakikishie kwamba jambo hili liko kwenye mikono salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, juu ya suala la daraja la dharura. Ni wazo jema, ni vizuri tukajua wapi tunaweza tukalipata daraja la muda, lakini baada ya kwenda site kutazama uhalisia wa jambo lenyewe likoje. Kwa sababu huwezi ukasema daraja la muda linafananaje bila kwenda site kujua uhalisia ukoje. Nashukuru.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa tunapozungumza Hospitali ya Amana imepelekwa katika Wizara ya Afya na kwa maana hiyo Manispaa ya Ilala haina Hospitali ya Wilaya. Bahati nzuri katika Jimbo la Ukonga, Kata ya Kivule kuna eneo la ekari 45, Manispaa ya Ilala imeshaanza kuweka msingi.
Je, ili kupata huduma ya afya katika Manispaa ya Ilala kwa kuwa na Hospitali ya Wilaya, nini kauli ya Serikali katika jambo hili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Hospitali ya Amana imechukuliwa na hivyo kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge hawana hospitali. Pia ni ukweli usiopingika kwamba jana nilipata fursa ya kuteta na Mheshimiwa Mbunge akaniambia katika own source yao walikuwa wametenga shilingi bilioni moja kwa ajili la kuanza ujenzi wa hospitali yao. Kwa hiyo, ninachowaomba, zile jitihada ambazo walishazianzisha za kuanza kujenga hospitali ya kwao ya Wilaya zisisimame, ni lazima zitiwe msukumo tuhakikishe kwamba wananchi wetu wanapata maeneo mengi ya kujitibia. Nikitoka hapa nitafanya kila jitihada niwasiliane na Mkurugenzi ili nimuelekeze hicho kiasi cha pesa ambacho kimetengwa kifanye kazi iliyokusudiwa.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri wa Maji kwamba Bunge lililopita niliwaomba kwamba Kata ya Msongola ina matawi tisa na ina maji kwenye visima vitatu katika mitaa mitatu tu. Kata ya Zingiziwa, Chanika, Buyuni na Pugu, hazina maji. Mvua ikinyesha ndiyo wananchi wanachota maji yale wanatumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali, ni kwa nini Mawaziri hawa wamekataa kuja Ukonga kuongea, hata kuwapelekea akina mama wenye shida ya maji pale na wanakaa Dar es Salaam?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyolieleza Bunge, kwa upande wa Jiji la Dar es Salaam na Miji ya Kibaha tayari tumeshakamilisha miradi miwili na tuna maji ya kutosha zaidi ya lita milioni 510 ambayo ni maji toshelevu. Kinachoendelea sasa hivi, tulikuwa tunahitaji dola milioni 100 ili tuweze kukamilisha usambazaji katika eneo lote la Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani na awali tulipata dola milioni 32 mradi ambao sasa utakamilika tarehe 15 Februari, 2018 lakini tumepata tena dola milioni 45 kutoka Benki ya Dunia. Tunarajia kutangaza tenda mwezi huu wa pili; tunaendelea, itakuwa imebaki fedha kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mpaka maeneo yote ya Zingiziwa unayoyazungumza tutahakikisha kwamba maji yanafika.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mgogoro wa misitu na wananchi wa Jimbo la Ukonga Kata ya Vingiziwa, Chanika, Buyuni na Pugu tangu mwaka 1998, mgogoro huu Mheshimiwa Waziri Mkuu anaufahamu, wameshaunda timu huko nyuma.
Ninaomba nipate kauli ya Serikali leo; mgogoro huu unafikia lini mwisho ili wananchi wale wajue kwamba wanaendelea kuishi kwa kufanya maendeleo au wanaondoka na wanakwenda wapi? Naomba nipate majibu hayo.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kumekuwepo na mgogoro wa muda mrefu katika msitu ule na mimi mwenyewe katika kipindi cha hivi karibuni nimetoka kule nimetembelea mipaka ile na kuangalia, lakini naomba nilitaarifu Bunge lako tukufu kwamba hatua zilichukuliwa na Serikali katika kuwaondoa wananchi wote waliokuwa wamevamia katika yale maeneo na mipaka rasmi imechorwa pamoja na kuweka barabara pembezoni ya mpaka. Kwa hiyo, wananchi wale wote ambao wako ndani wameshaondolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini yapo maeneo machache ambayo yamebaki ambayo sasa Mheshimiwa Waitara alisema kwamba bado inabidi tukae nao chini na mimi nakubali kwamba baada ya Bunge hili leo hii ntaomba tukutane ili tukae pamoja ili tuweze kutoa tamko la mwisho juu ya wale watu ambao wako katika haya maeneo yaliyobaki.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu yaliyo chini ya kiwango ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji naomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza kwa niaba ya Mheshimiwa Saed Kubenea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza liliuliza kwamba mpaka sasa kasi ya kufufua viwanda imefikia wapi? Kwa hiyo, kwa majibu hayo inahitaji tujue kwamba Waziri yuko tayari kukiri kwamba kiwanda hiki hana mpango wa kukifufua kwa maelezo aliyotoa hapa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, mpaka sasa anaamini kwamba kauli mbiu ya Serikali ni kuinua viwanda au kuua viwanda? Ahsante.
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya Serikali iliyofanyika imeandikwa kwenye jibu langu ni kufanya utafiti; na mwaka jana nilipewa shilingi milioni 150 kwa ajili kufanya utafiti na umakamilika kwa hiyo kazi niliyopewa nimemaliza. Kazi ya Serikali ni kujenga viwanda na viwanda vitaendeshwa na Sekta binafsi, mwaka unaokuja 2017/2018 nimeomba pesa shilingi milioni 70 tu nitangaze tender sekta binafsi ifanye kazi.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, naomba niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, mitihani ya kidato cha nne tunajua inatumika kwa lugha gani lakini kuna mitihani ya darasa la saba ambapo mitihani hii inatungwa maswali ya kuchagua yote. Sasa nilikuwa naomba niiulize Serikali ni lini mtaanza kutunga mitihani ambayo si ya kuchagua, hasa katika masomo ya hesabu ili watoto wetu wapimwe uelewa badala ya kuchagua na wengine wanabahatisha kufaulu kwenda sekondari? Swali langu ni hilo.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kumekuwa na mtazamo wa wadau tofauti tofauti katika maswali ya kuchagua hasa katika mitihani ya hisabati. Serikali nasi pia tumekuwa tunaliangalia hilo japo katika utafiti uliofanyika ilionesha kwamba kuchagua peke yake hakumwezeshi mtu kufaulu isipokuwa lazima kwanza awe ana msingi wa kujua swali analolifanyia uchaguzi.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kwa siku za nyuma hasa kipindi chetu sisi, ni kwamba hata kama unakuwa na mtihani wa kuchagua ilikuwa bado unakuwa na sehemu ya kufanyia kazi ambayo na yenyewe inakuwa ni sehemu ya kuiangalia. Kwa hiyo, tutaona namna gani tuweze kufanya hivyo ili yule anayekuwa amechagua tuweze pia kupata uthibitisho isiwe tu kwamba swali la mwisho ndio jibu la kuliangalia, lakini ni suala ambalo linafanyiwa kazi. (Makofi)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Ukonga kwa sasa lina wakazi wanaokaribia 700 na tuna Mahakama ya Mwanzo moja tu pale ya Ukonga na kulikuwa na mpango mwaka jana kujenga Mahakama nyingine mpya ya Mwanzo kule Chanika. Kwa hiyo, ningependa kujua kupitia Mheshimiwa Naibu Waziri kama mpango huo wa kujenga Mahakama nyingine mpya pale ili kupunguza msongamano mkubwa kule Ukonga ukoje? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wa Serikali wa mwaka 2017/2018; 2018/2019; 2019/2020 ni kuendelea kuongeza Mahakama nyingi za Mwanzo na Wilaya ili wananchi wengi waweze kupata huduma kwa wakati. Katika Mahakama ambazo zimeorodheshwa, pia Mahakama ambayo ni katika jimbo la Mheshimiwa Waitara ni kati ya Mahakama ambazo zilikuwa zimeainishwa katika wakati ujao wa fedha ili kuona namna ya kuweza kulishughulikia suala hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwa sababu hivi sasa chini ya Wizara ya Katiba na Sheria utaratibu ulioanzishwa sasa hivi ni ujenzi wa Mahakama kwa kutumia teknolojia rahisi sana ya moladi ambayo imerahisisha sana kujenga Mahakama nyingi kwa wakati mfupi.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge anaweza pia, kuwasiliana na mimi ili kuangalia katika orodha ya ujenzi wa Mahakama zile, Mahakama zake za Ukonga zimepangiwa mwaka gani wa fedha.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kata ya Msongola, Chanika, Zingiziwa, Buyuni na Pugu hazina maji; na kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri wa Maji alisema kuwa Mradi wa Kimbiji na Mpera ukikamilika ndio utaleta maji Ukonga. Ningeomba nijue mpaka sasa mradi huu umefikia katika hatua gani? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana na nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa namna anavyowapigania wananchi; lakini kubwa sisi tulifanya ziara katika Mkoa wa Dar es Salaam na nimefika hadi katika maeneo yake. Jitihada kubwa ambayo Serikali inaifanya mpaka sasa ni kuchimba visima 20 kwa maeneo ya Kimbiji na Mpera katika kuhakikisha wanapeleka maji maeneo yale. Hata hivyo kikubwa sasa hivi katika utekelezaji wa mradi ule lazima tusambaze kwa kutegemea na fedha. Kwa hiyo, tupo katika jitihada ya kutafuta fedha ili tuweze kutekeleza mradi ule na kuweza kuondoa tatizo la maji katika maeneo ya Ukonga. (Makofi)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru pamoja na majibu ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, lakini naomba niwashukuru sana Serikali ya Korea, Serikali ya Tanzania na Manispaa ya Ilala ambayo inaongozwa na UKAWA na wananchi wa Kata ya Chanika kwa kutoa ushirikiano wa kupata hospitali kubwa ya mama na mtoto katika eneo hilo. Nashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwenye majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri anaonesha kwamba fedha kutoka Serikali Kuu ni shilingi bilioni moja, lakini kwenye bajeti ya TAMISEMI ambayo tumeshapitisha katika Bunge letu Tukufu ilionesha shilingi bilioni 1.5. Napenda nijue hii ni nyingine imeongezeka au ni ile ya shilingi bilioni 1.5 ambayo sasa imeshuka tena imekuwa one billion?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa kuna changamoto kubwa katika eneo hili na Mheshimiwa Waziri anakubali kwamba kuna mpango wa kujenga hospitali hii; je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kutembelea eneo hili aone kwanza eneo lipo vizuri, wananchi wametoa ushirikiano wa ekari 45 twende tufanye ziara ili waweke msukumo kwa kujengwa kwa haraka na kwa uhakika ili huduma ya afya iweze kupatikana katika eneo hili ambayo itahudumia Jimbo la Ukonga, Mkuranga na eneo la Kisarawe? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waitara anauliza kwamba katika orodha ya Hospitali za Wilaya 67 ambazo zinajengwa, kwa hesabu yake anaona ilikuwa inaonesha kwamba Hospitali ya Kivule imetengewa shilingi bilioni 1.5, lakini taarifa nilizonazo ni kwamba imetengwa shilingi bilioni moja kutoka Serikali Kuu, lakini ukiunganisha na shilingi bilioni mbili ambayo ni mapato ya ndani ya Manispaa, maana yake wao wanakuwa na shilingi bilioni tatu. Kwa ramani ambazo zinatolewa kwa ajili ya awamu ya kwanza ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya ni shilingi bilioni 1.5. Kwa hiyo, wao wako mara mbili yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie kwamba lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba hospitali zinajengwa za kisasa, lakini kwa kutumia utaratibu wa Force Account.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kiasi hicho ni cha kutosha tukisimamia tukahakikisha kwamba kila shilingi ambayo inatoka inaenda kufanya kazi iliyokusudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la pili juu ya kwenda kutembelea maeneo hayo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba nina mpango wa kwenda kutembelea eneo ambalo kinapanuliwa Kituo cha Afya cha Buguruni, Kinyerezi na maeneo mengine yote ili na mimi nijiridhishe tuwe katika page moja tunapoongea na Mheshimiwa Mbunge.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Pamoja na majibu ya Serikali ningependa niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; pamoja na maelezo haya bado Walimu hao wameendelea kuchangishwa michango na kwa sababu wanaowachangisha ni mabosi wao ikiwemo michango ya mwenge na Mwalimu asipokubali kuchanga michango anawajibishwa kule kwa sababu Waziri hayupo. Je, ni hatua gani zinachukuliwa kwa wakubwa wa Walimu hawa kwa maana ya Wakuu wa Idara za Elimu, Maafisa Elimu kama wataendelea kuwachangisha michango ya lazima kinyume na maelekezo ya Serikali? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, kwa jibu hilo la Mheshimiwa Waziri ni wazi tunafahamu kwamba kuna waraka ulitembezwa ambao unatoa maelekezo, lakini baada ya maelekezo ya Mheshimiwa Rais ilizuka sintofahamu na wananchi walikuwa wamechanga vyakula katika mashule mbalimbali wakaanza kugawana, kuna miradi ya kuchangia madawati, madarasa na kuta mbalimbali wakaanza kukataa. Je, ni hatua gani za dharura kwa Serikali ili kutoa maelekezo kwa wananchi na wadau mbalimbali wa elimu warudi kama zamani washirikiane Walimu na walezi wa shule hizi ili shughuli za maendeleo ziendelee kuwepo kwa maana ya kuondoa kero za elimu katika maeneo mbalimbali? (Makofi). Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, baadhi ya michango halali kwa mfano michango ya Mwenge inatakiwa ichangishwe kupitia Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya na sio vinginevyo. Hii michango haitakiwi kupitia kwenye Kamati za Shule wala mikutano ya wazazi katika shule, hiyo hairuhusiwi. Kwa hiyo, Kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ndiyo inayoratibu masuala yote yanayohusu Mwenge michango ikiwepo michango ya mwenge.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili kuhusu sintofahamu ya michango iliyosababisha baadhi ya watu kwenda kudai michango ambayo walikuwa wamechanga hapo awali. Napenda nisisitize msimamo wa Serikali kwamba ilikuwa ni makosa hapo mwanzo tulivyokuwa tunachangisha kwa kuwahusisha Walimu kuwaondoa darasani wanafunzi kwa sababu tu wazazi wao labda kwa sababu ya umaskini wao hawakuwa wamechanga. Hilo lilikuwa ni kosa kwa sababu mtoto yule aliyekuwa anatolewa darasani hakuwa na kosa lolote.
Mheshimiwa Spika, maelekezo ya Mheshimiwa Rais yanasimama pale pale, isipokuwa utaratibu ambao sasa hivi tumeupitisha katika kutekeleza ule Waraka Na.5 wa Elimu kuhusu michango ni kwamba michango yote sasa itaratibiwa na Serikali za Vijiji na Kata chini ya usimamizi wa Mkurugenzi wa Halmashauri.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali ya Kijiji, Halmashauri ya Kijiji ikikutana ikapendekeza, wanapeleka kwenye Mkutano Mkuu wa Kijiji, wakikubaliana wanapeleka maamuzi yao kwenye Kamati ya Maendeleo ya Kata ambayo ikipitisha inapeleka kwa Mkurugenzi, Mkurugenzi anatoa idhini ya mchango ule kuchangwa. Mchango ukishachangwa ukikamilika taarifa inatolewa kwa Mkurugenzi ili hatua zaidi za utekelezaji ziendelee. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, ninayo maswali mawili ya nyongeza kwa niaba ya Mheshimiwa Lucy Magereli. Swali la kwanza, wakati wa Bajeti ya Wizara ya Maji, Kamati ya Kisekta na Waheshimiwa Wabunge walipendekeza kwamba tuongeze Sh.50 katika mafuta ili kupata fedha ya kupeleka maji vijijini na mijini ili kumaliza tatizo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni je, kwa maelezo ya majibu ya Wizara hii, na mradi umeanza tangu mwaka 2013 ulipaswa kuisha mwaka 2016, huu ni mwaka 2018; si kwamba kuna upungufu wa fedha ndiyo maana mradi huu unasuasua? Kwa hiyo ningeomba nipate kauli ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa mjadala wa Wizara ya Maji, ukurasa wa 56, mradi huu wa visima virefu wa Kimbiji na Mpera vinahusu pia Jimbo la Ukonga Kata ya Msongola, Chanika, Buyuni, Pugu, Kitunda na Ukonga. Sasa ningeomba nipate kauli ya Serikali hapa wamesema watu wa Kigamboni kuna mradi mbadala wa kupeleka maji katika eneo hilo. Nini kauli ya Serikali kuwasaidia watu wa Ukonga Kata ambazo nimezitaja, mradi wa dharura ili waweze kupata maji safi na salama? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kumpongeza Naibu Waziri kwa majibu mazuri kabisa. Nami pia niseme kwamba nimeshukuru Mheshimiwa Rais ametoa maelekezo moja kwa moja kwamba, sasa Wizara ya Maji ni eyes on, hands on kwenye halmashauri. Baada ya kauli hiyo kabla ya tarehe 30, nitafanya kikao kikubwa na Wahandisi wa Maji wote katika halmashauri ili tupeane mwelekeo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nichukue nafasi hii kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge. Kwanza kabisa kuhusu Visima vya Kipimbi na Mpera, tumefanya kazi kubwa sana, nampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Ndugulile, tumekuwa naye na tulikutana na Benki ya Maendeleo ya Ufaransa ambao wamekubali kwamba watatusaidia fedha kwa ajili ya kuweka miundombinu ya maji Wilaya ya Temeke pamoja na Kigamboni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi Serikali inaendelea na mazungumzo. Kwa hiyo, suala la fedha halina shida tena ni utaratibu tu, baada ya kusaini financial agreement mambo yote yatakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna shida yoyote kwamba mradi umechelewa kwa sababu hii Sh.50, hapana, kwa sababu hii Sh.50 kwanza inaelekezwa moja kwa moja vijijini. Hii ni miradi mikubwa ambayo inatekelezwa kwa fedha kutoka Central Government.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, tushakamilisha mazungumzo na Serikali ya Ufaransa na tukapata hiyo fedha, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, hii ni Serikali ya Chama cha Mapinduzi, itahakikisha kwamba maeneo yote ya Dar es Salaam yanapata maji safi na salama pamoja na kata alizozisema, pamoja na hata kwa Mheshimiwa Zungu kule Ilala, tunahakikisha kwamba tunakamilisha ili wananchi waweze kupata maji safi na salama sambamba na kuondoa majitaka.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Ni kweli kwamba kuna tatizo kubwa sana la ajira katika nchi hii hasa kwa vijana na vijana wengi wamejiajiri kupitia njia ya bodaboda na nyingi wamekopeshwa kwa mikataba mbalimbali na watu wenye fedha zao. Ukizunguka katika vituo vya polisi nchi hii, hata hapa Dodoma, bodaboda zimejaa kila mahali.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri anakiri kwamba fine ni kubwa kweli kweli, kwa hiyo, kuna kesi nyingi za vijana hawa na wenye bodaboda zao wanawadai fedha. Ni nini kauli ya Serikali na hasa Mheshimiwa Waziri, kuondoa bodaboda katika vituo vya polisi, kwa maana ya kupunguza gharama, ili vijana hawa waendelee kujiajiri na wapunguze kesi ambazo wameshtakiwa na watu wenye bodaboda zao ambao wamefunga nao mikataba? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, sikumpata vizuri babu yangu, Mheshimiwa Mwita, Wanyiramba tulishaondoka siku nyingi Mara, kwa hiyo, lafudhi kidogo imenishinda.
Mheshimiwa Spika, lakini ambacho tunafanya, moja, tunatoa elimu kuweza kuhakikisha kwamba wanafuata taratibu, kwa sababu kwa kweli maisha ya vijana wetu wengi sana yanakatika kutokana na wao kutokuzingatia taratibu za kujifunza maana bodaboda ni vyombo vya moto kama vyombo vingine na vimekuwa vikisababisha sana ajali. Kwa hiyo, tumeweka mkazo sana kwenye kutoa elimu lakini hata wao tumewaelekeza sana kuhakikisha kwamba nao wanaliongelea jambo hili kama moja ya jambo la hatari ambalo linasababisha madhara haya.
Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu kupunguza mishtuko hiyo pamoja na bodaboda nyingi kwenye vituo vya polisi, hilo tumeelekeza moja kwenye hili la upande wa fine, lakini la pili tumeelekeza hata kiutawala tu kwamba, kuwe na utaratibu wa kuwaandikisha na kuwaruhusu wawe na hivyo vifaa vyao ili waweze kulipa baada ya muda ambao wataweza kupewa. Nchi nyingine ambazo zimeendelea taratibu zote za mambo ya fine za usalama barabarani wanafanya kuandikisha na kumpa muda mtu aliyekutwa na kosa wa kufanya malipo hayo punde atakapokuwa ameshaanza kufanya kazi na hicho chombo chake.
Mheshimiwa Spika, utaratibu ambao umekuwa unatumika muda huu ni wa kushikilia bodaboda hiyo na kusema mpaka atakapokuwa amelipa ndipo atakapewa. Tumeelekeza tu zile bodaboda ambazo zinatakiwa kutumika kama sehemu ya ushahidi, kwa mfano, kwenye makosa makubwa kama ya madawa ya kulevya, mambo ya uhalifu wa kutumia silaha, hivyo ndivyo ambavyo tunaweza tukashikilia kwa sababu makosa yake kwa kweli haturuhusu yaendelee kufanyika kwa kutumia bodaboda hizo.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba niwashukuru sana Jeshi la Polisi la Zimamoto. Juzi walipata ajali ya moto katika Kata ya Zingiziwa na ukaunguza maduka zaidi ya 15 lakini kwa mara ya kwanza Zimamoto waliwahi mapema wakasaidia kuzima moto ule pamoja na kwamba mdhara yalikuwa makubwa lakini walisaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki kituo kimejengwa kwa nguvu za wananchi pamoja na wadau mbalimbali na Naibu Waziri anafahamu kwamba hii sehemu ndiyo mpakani mwa Mkuranga, unaenda Mkuranga, Kisarawe, mapori ya Dondwe na kama alivyosema vingine vyote ni Police Post. Kwa hiyo, naomba hii hoja ya kutafuta gari, kabla ya kuleta hili swali hapa Bungeni nimewasiliana na mapolisi, wanapata shida na eneo ni kubwa, Ukonga sasa ina watu zaidi ya 900,000. Kwa hiyo, kwa kweli tunahitaji gari kwani hilo gari lililopo linafanya kazi ya OCS na ikitokea dharura wanakuwa stranded wanakimbiza watu na pikipiki jambo ambalo ni hatari. Eneo hili Benki ya CRDB imefungwa kwa sababu ya kiusalama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningeomba hii hoja ya kutafuta gari ipewe uzito, gari liende pale liwe stagnant kwamba kuna gari ambalo viongozi wanalitumia na gari la doria kwa maana ya ku-control Ukonga yote. Kwa hiyo, ningeomba hilo lizingatiwe. Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza…
Haya la pili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Kata ya Kivule tunalo eneo tayari la kituo cha polisi, kama ambavyo Chanika wamejenga wananchi tumechangia, ningeomba commitment ya Waziri au Jeshi la Polisi, ni lini tutaenda kufanya harambee eneo lile kwa sababu tayari wananchi wameweka msingi eneo hili. Bunge lililopita Waziri aliahidi hajaja, kwa hiyo, leo naomba kauli yake.
Lini twende Kivule, tuchangishe fedha tujenge kituo kingine ili tupunguze uhalifu katika eneo lile? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya ya Mheshimiwa Waitara, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimepokea pongezi zake kwa niaba ya Jeshi la Zimamoto kuhusiana na kazi nzuri ambayo inaendelea kufanywa. Hii inathibitisha juu ya kuimarika kwa huduma za vyombo hivi vilivyo chini ya Wizara ya Mambo ya Nchi ikiwemo Jeshi la Zimamoto katika kutekeleza majukumu yake na kuwapatia huduma wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la kwanza, kama ambavyo nimejibu katika swali langu la msingi kwamba tutaangalia uwezekano huo. Kama unavyofahamu kwamba tuna changamoto za magari maeneo mengi nchini, kwa hiyo, tutaangalia vile vigezo na kulingana na idadi ya magari ambayo tutapokea ndipo tutaamua eneo hili linapaswa lipelekewe gari sasa hivi ama baadaye. Hata hivyo, tunatambua umuhimu wa kupeleka gari katika eneo hilo na maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ni kuhusu lini tutafanya harambee. Kwanza nimpongeze Mbunge kwa jinsi ambavyo ameweza kuhamasisha kuhusiana na hili suala la harambee, mimi nimwambie tuko tayari hata sasa hivi. Kwa hiyo, baada tu ya Bunge hili Tukufu tukae tuweze kupanga ratiba ya kuweza kufanya hiyo kazi. Tunathamini sana jitihada za Wabunge na wadau mbalimbali katika kusaidia kukabiliana na changamoto za vituo vya polisi nchini na hili jambo tutaliunga mkono.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Mimi ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Mstaafu, Mtaa wa Kivule. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kitendo cha Serikali kutokutoa maelekezo mahsusi ya Wenyeviti wa Mitaa kulipwa posho inapelekea mzigo huu kupelekwa kwa wananchi ndiyo matokeo ya zile barua ambazo zinalipiwa, wananchi wanatwishwa mzigo huu. Kwa hiyo, ningeomba nijue, kwa kuwa Serikali imechukua vyanzo mbalimbali vya mapato kutoka Halmashauri na Halmashauri haipeleki fedha hizo kulipa Wenyeviti wa Mitaa na wanafanya kazi kubwa masaa 24.
Mheshimiwa Spika, ni kwa nini isiwekwe sheria moja kwa moja ili wadai kama haki? Kwa sababu sasa hivi ni posho kwa hiyo hawana uhalali wowote ule, Halmashauri inaamua ilipe ama asilipe. Ni kwa nini Serikali isiwajali watu ambao ni wengi sana katika nchi hii, wanafanya kazi kubwa sana ya miradi, ulinzi na usalama, usafi na ku-impose sheria mbalimbali walipwe pesa ya kisheria badala ya hii ambayo ni hiari? Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) : Mheshimiwa Spika, kama anavyosema ni kweli Wenyeviti wa Serikali za Vijiji, Vitongoji na Mitaa wanafanya kazi kubwa na nyingi na kweli mzigo ni mkubwa sana kwa upande wao. Sisi kama Wabunge na Serikali tunawategemea sana katika kazi zetu za kila siku. Ili kazi zetu na za Serikali ziende lazima wale wafanye kazi.
Mheshimiwa Spika, sasa mapendekezo ambayo anayatoa na kuhusisha kwamba Serikali imechukua vyanzo vingi vya mapato kwenye Halmashauri, mimi nataka nimhakikishie kwanza kwamba vyanzo ambavyo vimechukuliwa siyo vingi…
Mheshimiwa Spika, vyanzo vingi bado vipo katika Halmashauri na ndiyo maana tumewaambia kwamba wafanye mapitio. Wakishafanya mapitio Halmashauri ambayo itakuwa na changamoto za ziada basi wataleta taarifa TAMISEMI na tutaweza kuifanyia kazi.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kauli ambayo Wakurugenzi walielezwa kwamba wamepewa ajira, wamepewa magari na wanalipwa mshahara na Mheshimiwa Rais, ole wake Mkurugenzi ambaye atamtangaza mpinzani. Kauli hii imeleta sintofahamu, kutojiamini na hofu katika chaguzi mbalimbali. Nini kauli ya Serikali sasa juu ya kauli hii ya tishio la uchaguzi ulio huru na haki? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ndugu yangu Mheshimiwa Waitara hajalieleza Bunge hili kwamba kauli hiyo imetoka lini? Alisema nani? Katika shughuli gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mzee wa zamani, nilifundishwa kwamba government moves on paper. Kwa hiyo, huwezi ukaja Bungeni hapa ukasema fulani alisema hivi na hivi na hivi. Kwa kifupi tu nataka nimjibu ndugu yangu Mheshimiwa Waitara kwamba Wakurugenzi tumewafundisha na tumewafanyisha semina wafanye kazi kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni zilizopo.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa Serikali inatoa elimu ya bure kwa ngazi ya shule ya msingi na kwa kuwa wanafunzi walewale ambao wametoka shule ya msingi wanaenaenda sekondari kwa maana ya Form I - Form IV na wanafunzi haohao wanafaulu kwenda high school. Kwa sababu hao watoto walikuwa na mazoea ya kutokulipa ada, sasa wanahangaika mitaani kwa kukosa ada ya kwenda Form V. Je, nini kauli ya Serikali kuwasaidia watoto hawa ambao walipata msaada kutoka shule ya msingi wamefanikiwa kwenda sekondari na sasa wamefaulu kwenda high school na hawana uwezo wa kulipa ada? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwita Waitara, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba maoni kama hayo tumekuwa tukiyapata Serikalini siyo kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge peke yao bali hata kutoka kwa wananchi na NGOs mbalimbali. Hata hivyo niseme kwamba Ilani ya Uchaguzi ya CCM imeelekeza kwamba Serikali iandae utaratibu wa kutoa elimu msingi bila malipo ambayo ni kuanzia shule ya msingi mpaka Form IV. Kadri uwezo wa Serikali utakavyokuwa unavyoendelea kuwa mzuri zaidi inawezekana tukachukua ile Form V na VI na mambo yakiwa mazuri zaidi, Serikali ikavyojizatiti ikawa stable zaidi inawezekana tukatoa elimu bure mpaka chuo kikuu.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Ninayo barabara ya Kitunda – Kivule – Msongola, mkandarasi yupo site kwa zaidi ya miezi 10 sasa na barabara hii inahudumia kata tano na magari yanakwama hata wakati wa jua kali. Ningeomba nipate kauli ya Waziri kwa nini mkandarasi asilipwe fedha ili aendelee na kazi kuondoa kero kwa wananchi wa Jimbo la Ukonga? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waitara anatambua barabara hii tumezungumza mara nyingi na hata tulikuwa na utaratibu wa kutembelea maeneo haya na wakati wa mvua kwa kweli eneo hili limeharibika sana na nilikuwa nimeelekeza kwamba sasa mkandarasi alipwe pamoja na juhudi kubwa za kulipa wakandarasi sehemu zote nchini lakini alipwe ili barabara hii iendelee kutengenezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitaendelea kufuatilia kuhakikisha kwamba mkandarasi anapata fedha na binafsi nimeongea na mkandarasi ili ajiandae kwamba atakapolipwa tu mara moja aingie kazini ili sehemu hii korofi iweze kurekebishwa. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kitunda, Mvute, Mbondole, Nzasa na Iyongwa kote huko kuna sekondari. Maeneo yote haya ambayo nimeyataja hayana umeme. Naomba nijue ni lini maeneo haya ya umma yenye zahanati, shule na wananchi watapelekewa umeme wa uhakika? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Waitara. Mimi kwanza ni mpiga kura wake katika Jimbo lake, naelewa sana maeneo yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti ni kweli kabisa maeneo ya Mbondole na maeneo mengi sana ya Chanika hayana umeme, lakini maeneo yote 27 yameingia kwenye Mpango mahususi wa Peri-Urban ambao utekelezaji wake umeshaanza. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge utekelezaji huu unaanza mwezi Julai na utakamilika mwezi Machi mwakani. Kwa hiyo, ni matarajio yetu ndani ya miezi mitano vijiji vyote vitakuwa vimeshapata umeme maeneo ya Mbondole.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza naomba nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri alifanya ziara katika Jimbo la Ukonga na tukafanya mikutano mpaka saa moja usiku, namshukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa tu nijue kwamba Jimbo la Ukonga lina shida kubwa ya umeme ambayo Mheshimiwa Waziri na Naibu wake wanafahamu. ningependa nijue katika hii mipango ya REA ambayo inaendelea Ukonga nao wategemee nini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa. Na mimi naomba nimpongeze Mbunge Mheshimiwa Waitara ni kweli tulifanya mikutano zaidi ya sita katika Jimbo lake na nimthibitishie baada ya mikutano ile kwa mwaka wa fedha unaokuja 2018/ 2019 Serikali inakuja na mpango wa Peri-urban kwa maeneo ya Mkoa wa Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani na kisha itaendelea Peri-Urban II. Ahsante.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru sana. Naomba nimuulize swali dogo Mheshimiwa Naibu Waziri. Barabara ya Kitunda – Kivule - Msongora mkandarasi yupo site kwa zaidi ya mwaka mzima sasa, lakini hajatekeleza kazi ile hata zaidi ya asilimia 20, amechimbachimba na kuiharibu. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kwenda Kivule ili akaangalie usumbufu ambao wananchi wanapata na kulazimisha ujenzi ufanyike haraka ili watu wapate barabara ya kupita?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niko tayari na inawezekana kesho pia…
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kwanza kabisa ya kuuliza swali katika Bunge hili Tukufu.
Mheshimiwa Spika, nawashukuru sana wana-CCM wote popote walipo kwa kunikaribisha Chama cha Mapinduzi. Nawashukuru wananchi wa Ukonga kuendelea kuniamini, pia namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini kwa kuchukua baadhi ya maeneo ya Jimbo la Ukonga kuingiza kwenye umeme wa peri-urban; eneo la Mbondole, Kitonga, Chanika, Kibanguro, Viwege, Zingiziwa na Buyuni, Mgeule na Mgeule Juu vimeingizwa kwenye peri-urban. Sasa ningependa nijue, ni lini sasa maeneo hayo muhimu katika Jimbo la Ukonga kwa kuwaheshimu watu waliounga mkono juhudu za CCM watapata umeme haraka iwezekanavyo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwita, Mbunge wa Jimbo la Ukonga kupitia Chama Cha Mapinduzi na nimpongeze sana kwa kushinda kwa kishindo katika uchaguzi huo. Kwanza ameishukuru Wizara yetu kwa namna ambavyo tumeingiza maeneo ya Jimbo lake la Ukonga kwenye mradi wa peri-urban.
Mheshimiwa Spika, lakini Mheshimiwa Mwita Waitara atakubaliana na mimi tulifanya ziara katika maeneo hayo katika maeneo mbalimbali ambayo ndiyo imekuwa kivutio cha kuipigia kura Chama cha Mapinduzi katika uchaguzi uliopita. Sasa kazi imeanza ya kupeleka umeme katika maeneo hayo kupitia TANESCO na kwa kupitia mradi wa peri-urban tuko katika hatua za kumpata mkandarasi na hivi karibuni kazi ambazo zimesalia katika maeneo mbalimbali zitakamilika. Hata baada ya Bunge hili pamoja na Mheshimiwa Mbunge tutawasha umeme katika maeneo ya Zingiziwa, Buyuni na Mbondole kutokana na kazi nzuri inayofanywa na Shirika la Umeme la TANESCO. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba nikiri kwamba Wizara ya Maji imetutendea haki Tarime angalau hali ya maji imeboreshwa. Nisipompongeza Mheshimiwa Waziri Aweso na Naibu wake itakuwa sijawatendea haki. Pamoja na kazi nzuri ambayo imefanyika naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza ni kwamba pale Sirari kuna mradi wa maji ambao tathmini ilifanyika ya kwanza ilikuwa shilingi 1,200,000,000, lakini tukarudia tathmini tukapata shilingi 534,000,000, sasa mradi unaendelea vizuri, imebaki shilingi 70,000,000 tu ili mradi ukamilike. Naomba nijue ni lini Serikali itapeleka fedha hizo pale mradi ukamilike Sirari ambapo ina wapigakura zaidi ya 17,000 ambao ndio ushindi wangu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ningependa tu nijue kwamba ni lini sasa huu Mradi wa Ziwa Victoria utaanza kwa sababu hili ni swali muhimu sana kwa Mbunge wa Tarime Vijijini, Sirari, Nyamongo na Nyamwaga lini mwaka wa fedha huu, mwaka wa fedha ujao au upi, ni lini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwita Mwikwabe Waitara, Mbunge wa Tarime Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nipende kupokea shukrani kwa namna ambavyo tunaendelea na kazi mbalimbali kwenye miradi mingi kote nchini lakini hususan kwenye Jimbo la Tarime Vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu ambao bado tu milioni 60 upo kwenye mchakato na mgao ujao kwa maana ya mwezi huu wa tano tutahakikisha tunawaletea hii milioni 60 ili mradi ukamilike, lengo ni kuona maji yanatoka bombani na tunawatua akinamama ndoo kichwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, miji 28 tunatarajia kuanza kutekeleza hivi karibuni, tayari kile kipingamizi ambacho kilikaa kwa muda mrefu kimekwisha. Kipekee nipende kumpongeza na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais mama Samia Suluhu Hassan kwa sababu ameingilia kati na sasa hivi tunakwenda vizuri, ni mfupa wa muda mrefu, lakini mama Samia ameweza kuutafuna, tunakwenda kuanza kazi katika miji 28.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba nimwulize Mheshimiwa Naibu Waziri: Ni lini Wizara ya Elimu itasaidia kwa dharura ujenzi Kituo cha VETA kule Nyamwaga, Nyamungo, kwa sababu fedha zimeshatengwa tangu mwaka 2021 mpaka sasa hivi imekaa inasubiri tu usaidizi wa Wizara yake? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu katika swali langu la msingi kwamba ujenzi wa Vyuo vya VETA katika Wilaya 63 tunatarajia kuanza mara tu fedha zitakapopatikana na miongoni mwa maeneo yatakayofikiwa ni pamoja na wilaya yake. Kwa hiyo, nimwondoe wasiwasi, ujenzi huo utaanza mara tu fedha hizo zitakapopatikana. Nashukuru sana.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Maeneo yote hayo mawili ya Sirari na Nyamongo ni ahadi za Viongozi Wakuu wa Serikali, sasa nimuombe Mheshimiwa Waziri kama yupo tayari majibu haya haya tuyapeleke pale Sirari na Nyamongo akayaseme mwenyewe? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, nipo tayari tuongozane na Mheshimiwa Mbunge na bahati nzuri wiki mbili zilizopita tulikuwa Tarime Vijijini tumefanya ziara pamoja na niko tayari turejee tena Tarime kwenda Sirari na Nyamongo.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwenye Tarafa yangu ya Ingo yenye kata kumi na Ichuku kata tano, Inano kata tano hakuna josho hata moja katika eneo hilo. Nini mpango wa Serikali?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, namuomba Mheshimiwa Waitara aainishe mahitaji yake, ashirikiane na Mkurugenzi wake Mtendaji alete Wizarani tutamhudumia kwa jambo hili katika Bajeti ya Mwaka 2023/2024 ambayo tunaielekea sasa. Ahsante.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro wa Hifadhi ya Serengeti na Kata za Nyanungu, Goroma na Kuhihancha, ni mgogoro wa muda mrefu na mipaka iliwekwa mwaka 68 bila kushirikisha wananchi. Naomba nijue Wizara ya Maliasili; ni lini sasa itaenda katika kata hizo ikae na wananchi pamoja bila kutumia mzinga na bunduki wasikilize wajadiliane kumaliza mgogoro katika eneo hilo. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Waitara, Mbunge wa Tarime, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna changamoto kubwa katika Jimbo la Mheshimiwa Waitara; na hivi karibuni tu askari wetu ameuwawa kwa kupigwa mshale. Hili kwa kweli sisi kama Serikali tunasikitika sana wananchi wanapojichukulia mamlaka ya kudhuru wahifadhi ambao wanalinda rasilimali zetu sisi kwa faida yao wenyewe. Hili naomba niliseme hadharani kwamba wale askari wako kwa ajili ya kulinda rasilimali za Taifa na si vinginevyo. Kwa hiyo tunaomba tuheshimu mipaka, tuheshimu hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapomuua askari hauwezi kuibadilisha ile ramani. Askari atakufa lakini ramani itaendelea kuwepo; ni mpaka pale Serikali itakaporudi kuutatua huu mgogoro. Kwa hiyo tunaomba wananchi wasijichukulie sheria mkononi, hilo ni la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala la pili, nataka nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, tunaenda wenyewe kwenda kutatua ana kwa ana na wananchi na kuwatahadharisha kwamba kuendelea kuua askari wataishia jela, kwa sababu lazima sheria ichukue mkondo wake. (Makofi)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nina maswali mawili ya nyongeza. Wananchi wa maeneo yote ambayo yanazunguka mgodi wa Barrick North Mara hawajui kwamba ardhi ndiyo ya kwao kilichopo chini siyo cha kwao.

Je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kwenda kufanya mkutano katika eneo lile ili kutoa elimu hii kwa wananchi ili wajue kwamba hawahusiki na dhahabu iliyoko chini ya ardhi ile?(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, pamoja na manung’uniko makubwa sana ya eneo hilo ni nili wananchi wa eneo la Nyamichele, Murwambe, Nyabichune na Kiwanja watalipwa fidia yao? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Waitara, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwenda kwenye eneo, yaani uwandani Wizara tuko tayari kwenda na tutawasiliana nae kwa ajili ya kupanga utaratibu wa jinsi ya kufika kule kwake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu fidia ya maeneo aliyoyataja nitawasiliana nae kujua viwango vya hatua zilizofikiwa hadi sasa. Ahsante.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafsi.

Mheshimiwa Spika, ninataka kujua kwamba, kwenye vijiji vyetu kuna watu ambao walipaswa kuwa na sifa kupata huduma ya TASAF na viongozi wengi wa vitongoji na vijiji wameweka watu ambao hawana sifa. Nini mpango wa Serikali kufanya auditing kuhakikisha kwamba watu wote ambao wanapaswa kuingizwa kwenye mfumo wanaingizwa na wale ambao hawapaswi kupata hiyo huduma watolewe katika huduma hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza katika swali lililoulizwa na Mheshimiwa Sekiboko, naomba kurudia tena mbele yako na kulieleza Bunge lako na Watanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, mfumo wa utambuzi wa wanufaika wa TASAF ni mfumo shirikishi ambao unaanzia kwenye ngazi za vijiji vyetu, kwa hiyo ninachotegemea kutoka kwa wananchi ambao watashiriki mkutano wa utambuzi ni kuweza kuwatambua watu wote wanaotakiwa kushiriki katika mfumo huo.

Mheshimiwa Spika, nataka nitoe taarifa ndogo, tumewahi kufanya ziara katika baadhi ya Wilaya, tumekwenda pale tukakutana na kituko cha mwaka. Watu wanakataa watu walioingizwa kwenye mfumo wa TASAF ndiyo haya ambayo Mheshimiwa Waitara anayasema. Nataka nirudie tena mfumo huu ni mfumo shirikishi na nitoe wito kwa wananchi wote katika maeneo yote, mnapoitwa katika mikutano ya TASAF hebu jaribuni kushiriki ili kuondoa ubabaishaji wa baadhi ya watu ambao wanachomeka ndugu zao na watu wasio na sifa katika mfumo huu na kudhulumu wale watu wenye sifa, wanaostahili kuingia katika mfumo wa TASAF. (Makofi)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kati ya mwezi wa nne mpaka mwezi wa tano kuna mauaji yamefanyika katika Mji wa Sirali wameua mtu pale Kubiterere Mwema wameua mtu katika Kata ya Pemba, wamepiga risasi pale Kiru kwenye kata yangu, na juzi walimuua daktari katika Kituo cha Afya cha Kilende Nyamungo. Kuna kata nane watu wanapigwa risasi hadharani, na hali hiyo haijafuatiliwa. Ningeomba nijue kauli ya Serikali wanachukua hatua gani za dharura ili kurejesha amani katika Jimbo la Tarime na hasa Mji wa Sirali ambao ni mji wa mpakani na biashara kwa kweli imekuwa hali siyo nzuri sana.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Waitara, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza jambo la kwanza na la muhimu ambalo ningependa Watanzania ambao wanatusikiliza hapa walifahamu ni kwamba hali ya usalama katika nchi yetu ni imara. Matukio ambayo yoyote yanayotokezea katika nchi yetu ya uhalifu wa aina yoyote unaofanywa na mtu yoyote hakuna hata tukio moja ambalo linatokea na polisi ama vyombo vya usalama visifanikiwe kulidhibiti.

Kwa hiyo, mauaji ya aina yoyote ambayo yamekuwa yakitokezea nchini aidha hatua zimeshachukuliwa ama zinaendelea kuchukuliwa. Wako ambao waliohusika wameshapelekwa katika vyombo vya sheria wako ambao uchunguzi unaendelea kufanyika. Na hata suala la jimbo lake, kwa sababu ametoa takwimu, sasa sina hakika kwa aina yake ya kusema ni nani na kwa hiyo siwezi nikamjibu hapa kumwambia tukio hili liko katika hatua gani. Nimhakikishie tu kwamba hakuna sehemu yoyote katika nchi hii ikiwemo katika jimbo la Mheshimiwa Waitara ambapo kutatokea uhalifu wa aina yoyote na vyombo vyetu vya usalama vikiwemo jeshi la polisi vishindwe kuchukua hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe Mheshimiwa Mbunge, kama ana jambo mahsusi katika jimbo lako ambalo unahisi mpaka sasa hivi hajaridhishwa na hatua iliyochukuliwa naomba, kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maswali unipatie taarifa hizo ili tuweze kuzifanyia kazi.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Katika ajira mpya ambazo zinaendelea sasa, Serikali ina mpango gani kupeleka walimu katika shule mpya sita; Shule ya Sekondari Kimusi, Nyagisya, Barata, Inchugu na Nyanungu pamoja na Kubiterere ili watoto wetu waweze kusoma, na shule hizi zimejengwa na nguvu ya wananchi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI):
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ajira mpya hizi ambazo Serikali imetoa, tutaangalia maeneo yenye upungufu ikiwemo shule hizi za Kimusi, Nyagisya, Nyamongo, zilizopo kule Tarime na Mkoa mzima wa Mara kwa ujumla.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kupeleka fedha, kiasi cha shilingi bilioni 138 kutoa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Rorya na Tarime. Nini kauli ya Serikali juu ya maji hayo kwenda katika Kata ya Komaswa, Manga, Nyamongo, Sirari, Pemba, Mbugi na Nyamwaga? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Marwa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa Ziwa Victoria wa kupeleka maji Rorya na Tarime, tayari usanifu unaendelea na Mheshimiwa Mbunge tumezungumza hapa juzi na nimekupa Katibu wangu amefanya kazi nzuri na wewe. Tutahakikisha mradi huu tunakuja kuutekeleza kwa wakati. (Makofi)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nimshukuru Mheshimiwa Rais ametupa fedha za x–ray mashine 150,000,000 katika Kata ya Sirari ambayo inahudumia Bumera, Mwema, Susuni Sirari, Kanyange, Itiryo, Mbuguni, Pemba na Ganyange.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kujua x–ray mashine ipo pale hakuna ukaguzi wa mataalam wa mionzi na hakuna mtaalam, hawa wananchi wanapata shida. Nini kauli ya Serikali katika jambo hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hii x–ray iliyopo Kata ya Sirari pale, tuna timu ambayo ni ya Ofisi ya Rais - TAMISEMI inayozunguka nchini kote kutoa mafunzo kwa wataalam wetu wa afya namna ya kutumia vifaa hivi vya kisasa. Sasa nitumie nafasi hii mbele ya Bunge lako tukufu kuelekeza timu ile iweze kufika Mkoani Mara na kufika Sirari kwa ajili ya kutoa mafunzo ili x–ray hii mashine iweze kuanza kutumika mara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara ya mwisho timu hii ilikuwa Mkoa wa Simiyu, kwa hiyo siyo mbali kutoka Mkoa wa Simiyu na kuweza kufika Sirari kwa ajili ya kutoa mafunzo haya ili wananchi waweze kupata huduma.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwa niaba ya watu wa Tarime naomba niishukuru sana Serikali kwa kutenga fedha ya kujenga VETA kule Tarime Vijijini, hasa Nyamongo, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; napenda kujua kimetengwa kiasi gani cha fedha angalau chuo kianze kufanya kazi kwa hatua ya mwanzo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; nini kauli ya Serikali kwa wananchi pale ambao wengi ni wachimbaji wadogo wadogo, wavuvi karibu na Ziwa Victoria, lakini pia na wakulima wa mazao mbalimbali na Tarime pia mazao yanastawi. Nini matarajio ya wananchi hasa vijana kwa uwepo wa Chuo cha VETA katika eneo langu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Waitara, Mbunge wa Tarime Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni azma ya Serikali kujenga vyuo hivi katika kila wilaya kama nilivyoeleza awali. Katika awamu ya kwanza hii ya mwaka 2022/2023 Serikali imetenga bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo hivyo. Tafsiri yake ni nini, katika kila chuo katika awamu ya kwanza tunapeleka bilioni moja na milioni 400 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa majengo tisa ya awamu ya kwanza. Majengo haya tisa ya awamu ya kwanza yatakapokuwa yamekamilika, vyuo hivi bila shaka vitaanza kufanya kazi ya kutoa huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wetu ni nini? Katika awamu ya pili vilevile tutatenga tena fedha kwa ajili ya kukamilisha majengo mengine tisa. Jumla kuu ya bajeti yote ili chuo kiweze kukamilika ni jumla ya bilioni tatu na milioni mia tano. Kwa hiyo, nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge, Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan imeweza kutenga katika mwaka huu, lakini vilevile katika mwaka ujao tunakwenda kukamilisha ujenzi huu ambapo vyuo hivi vyote vitakapokamilika ni zaidi ya bilioni 200 tunatarajia kutumia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa pili, upande wa mafunzo yatakayotolewa, tunafanya mapitio sasa hivi ya mitaala ile ya utoaji wa mafunzo ya ufundi wa VETA na hasa hasa tutazingatia zile shughuli za kiuchumi zinazofanyika katika maeneo husika. Kwa hiyo, nimwondoe wasiwasi kwenye maeneo ya kilimo kutakuwa na mitaala ya kilimo, kwenye maeneo ya madini kutakuwa na mitaala ya shughuli za madini, kwenye maeneo ya uvuvi, tutakwenda hivyo angalau ku-customize kulingana na shughuli za kiuchumi za eneo husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, napenda kujua ni lini Serikali itajenga daraja la kuunganisha Kata ya Matongo na Kata ya Kibasuka, Nyarwana ili kusaidia mawasiliano wakati wa mvua? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kumwelekeza Meneja wa TARURA wa Mkoa wa Mara, lakini pia Wilaya ya Tarime kwenda kufanya tathmini ya gharama zinazohitajika katika ujenzi wa daraja hili la Matongo linalounganisha upande wa pili, ili sasa Serikali ifanye tathmini kuona kama liko ndani ya uwezo wa bajeti ya kila mwaka au linahitaji special bajeti ili tuweze kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo, ahsante. (Makofi)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nina mwaka wa nane hapa Bungeni, sijawahi kuona mjadala wowote wa kupandisha posho za Madiwani, Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji. Napenda Mheshimiwa Waziri atueleze, ni lini mara ya mwisho Serikali ilipitia…

SPIKA: Mheshimiwa, hujawahi kuona nini? Samahani.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, sijawahi kuona mpango wa Serikali kupandisha posho za viongozi hawa. Napenda kujua, ni lini mara ya mwisho Serikali ilipitia posho za Madiwani, Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Serikali kwa kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Mama Samia amepeleka fedha nyingi sana vijijini na zinahitaji umakini wa usimamizi ili miradi iweze kukamilishwa kiukamilifu.

Je, kwa mwaka wa fedha ujao 2024/2025 Serikali ipo tayari kuongeza posho ya Madiwani, Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa ili kupunguza kelele za viongozi hawa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, kwanza namuhakikishia Mheshimiwa Mbunge, kwamba katika Bunge la Bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023, Ofisi ya Rais - TAMISEMI katika mjadala ambao Waheshimiwa Wabunge waliujadili kwa kina sana, ilikuwa ni uwezekano wa kuongeza posho za Waheshimiwa Madiwani, Wenyeviti, na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Spika, Bunge hili limeshajadili sana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI tulipokea, nimhakikishie kwamb lini posho hizi zilipandishwa, posho za Waheshimiwa Madiwani zilipandishwa. Nitakwenda kuona exactly ni lini lakini nafahamu kwamba zilipandishwa kutoka zilipokuwa, kidogo lakini sasa angalau ziko na hali nzuri.

Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba zinahitajika kuongezeka zaidi ili ziweze kukidhi mahitaji na safari ni hatua. Serikali inaendelea kulitazama na kuona uwezekano huo wa kupandisha posho za Waheshimiwa Madiwani.

Mheshimiwa Spika, pili, katika mwaka ujao wa fedha, kama tutaongeza posho hizo au vinginevyo. Tumelichukua, Serikali itafanya tathmini na kuona uwezekano huo na itatoa taarifa rasmi kama linawezekana ama tunahitaji kuijengea uwezo ili kuweza kuongeza posho hizo, ahsante sana.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwenye Jimbo langu eneo la Mgodi wa Barrick North Mara, Serikali ilipeleka Mthamini Mkuu wa Serikali ikafanye evaluation eneo la kiwanja na Mkomalela North tangu mwaka jana. Mwaka huu wanasema hawana mpango wa kutoa hilo eneo.

Je, nini kauli ya Serikali kwa wananchi wale katika maeneo ya kiwanja na Mkomalela?

SPIKA: Swali hilo nadhani limeshawahi kujibiwa na Wizara ya Madini ama sio swali hilo. Mheshimiwa Waitara ni swali hilo hilo au sio.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, ule mgogoro upo huu wamezua mwingine juzi tena hili ni jipya. Ni jipya kabisa.

SPIKA: Ambaye hana mpango wa kuchukua ni nani? Mgodi.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, yaani Mgodi ili ulipe fidia Wizara ya Ardhi inatuma Mtathmini anafanya tathmini walifanya hivyo na wakatoa notice kuzuia wanainchi wasiendeleze maeneo yale kwa sababu mgodi unachukua. Baada ya mwaka mmoja. Juzi madiwani na wenyeviti wa vijiji wakaitwa eneo hilo wakaambiwa sasa mgodi hauna mpango wa kutwaa hilo eneo, shida inabaki hapo.

SPIKA: Nataka kuelewa ni swali hilo hilo ambalo limewahi kujibiwa na Madini kwa sababu Serikali ni moja asije huyu wa ardhi hapa akajibu tofauti na wale wa madini halafu tukatekeleza mgogoro mwingine. Wewe niambie ni swali hilo hilo ambalo umeshawahi kuuliza kwa Wizara ya Madini au hapana.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, ni swali jipya kama hana majibu anaweza akajipanga. Mimi nitali...

SPIKA: Hapana, yeye sijampa nafasi ya kujibu bado nataka tuelewani mimi na wewe kwanza ili nijue nimpe nafasi yupi maana Serikali ni moja. Swali ni hilo hilo au ni tofauti.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, ni swali jipya, ahsante.

SPIKA: Kuhusu jambo hilo hilo.

MHE. MWITA M. WAITARA: Ndio, jambo hilo hilo.

SPIKA: Swali jipya kuhusu jambo hilo hilo.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, ndio.

SPIKA: Watu wa Madini, Waziri.
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, swali alilozungumza Mheshimiwa Waitara na hata tulivyojibu wakati ule, tulikuwa tunazungumzia eneo la Mrwambe na Nyamichune. Maeneo ambayo yalifanyiwa uthamini baadae mgodi ukaonesha kwamba hauyahitaji ukawarudishia wananchi. Sasa kwa sababu wananchi walikuwa wamesubiri kwa muda na kwa mujibu wa Sheria ikabidi walipwe kitu kinachoitwa fedha ya usumbufu au excrasher. Kwa hiyo, mwezi wa sita huu mgodi umeshakubali kulipa hizo fedha na Mheshimiwa Waitara tulishazungumza. Namuomba tu avumilie kidogo kwa sababu mwezi wa sita ndio huu tumeuanza watalipwa wakamilishe.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Mimi ni Mbunge wa Tarime Vijijini, pale Nyamwata, Kerende, Nyangoto ni vijijini kabisa. Maeneo haya yote wananchi wanalipa umeme kwa gharama kubwa. Kwa hiyo, Jimbo limegawanywa kuna watu wanalipia umeme kwa bei ya chini ya shilingi 27,000 na wengine bei kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nijue ni lini mchakato huu wa kurudisha bei ya shilingi 27,000 ya umeme kwa watu wa vijijini inarudishwa ili watu wapate umeme sawa? Huu mchahakto umechukua muda mrefu.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwikwabe Waitara, kwamba ni kweli tumebaini yapo maeneo mengi ambapo tulipofanya tathmini awali tumeyaacha, wale wataalam wameelekezwa warudi tena ili wakifanya iwe ni once and for all. Kwa hiyo, wanapita kwenye maeneo yetu, kazi ni kubwa inahitaji weledi na utulivu mkubwa ili tuweze kuwahudumia wananchi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waitara na Waheshimiwa Wabunge mtuvumilie kidogo tulikamilihse hili kwa usahihi na ufasaha kabisa. Tutakapokuja kuleta mbele yenu liwe ni tatizo ambalo tumelikamilishwa tuende kwenye hatua nyingine. (Makofi)

MHE. MWITA W. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii barabara inaunganisha Wilaya ya Tarime na Wilaya ya Serengeti na ndiyo barabara ya kwanza ya lami katika Jimbo la Tarime Vijijini. Tunampongeza Mheshimiwa Rais kupeleka fedha hapa kujenga barabara hii. Lakini kwa majibu ya Serikali barabara hii imefika asilimia 15, na tumeambiwa Tarehe 24 Mwezi wa Januari Mwaka kesho tunakabidhiwa barabara ya lami. Lakini mkandarasi alipeleka certificate Serikalini Oktoba 2022 akidai milioni 874, hajalipwa. Akapeleka certificate ya pili Machi 2023 akidai milioni 841, hajalipwa. Certificate ya tatu ni Mwezi wa tatu mwaka huu ambayo ni bilioni 1.6.

Je, ni lini, Serikali italipa fedha hizi ili tupate barabara ile Januari mwakani kutengeneza kura za Chama Cha Mapinduzi katika jimbo langu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Barabara hii ina center ya Mogabiri, center ya Nyamwigora, center ya Kimakolele, center ya Nyarero, center ya Kiwanja, center ya Gena na kule Nyamongo;

Je, maeneo haya tutawekewa taa za barabarani? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na swali la pili la Mheshimiwa Mbunge swali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tulivyosema katika barabara hii ya Tarime – Nyamwaga – Nyamongo hadi Mugumu, tumeainisha maeneo sita ambayo yatawekwa taa. Yale maeneo yote, vijiji vyote vile vikubwa, maeneo sita yatawekewa taa na Mheshimiwa Mbunge pengine baada ya hapa anaweza kuja nimwoneshe vijiji ambavyo vitawekewa taa katika hiyo barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ujenzi unaoendelea, mkandarasi bado yupo site anaendelea kujenga na tuna hakika changamoto iliyokuwepo kubwa ya barabara hii ni mvua kubwa inayoendelea kunyesha. Sasa Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba, kasi ya ujenzi itaendelea na hasa kwa kuwa Serikali sasa tumeshajipanga kuhakikisha kwamba, changamoto zilizokuwepo za malipo yote tunakamilisha na mkandarasi ataendelea na ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kipande kilichobaki tunategemea ikiwezekana kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha tutakuwa tumesaini mkataba kwa ajili ya barabara nzima hiyo ya Tarime – Nyamwaga hadi Mugumu. Ahsante. (Makofi)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ningependa kujua ni lini barabara ya kiusalama kutoka Susuni – Mwema - Sirari – Mriba – Nyamongo itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami mara tu tutakapokuwa tumekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Msimu uliopita wananchi wa Wilaya ya Tarime walipata shida sana kupata mbolea. Walikaa mpaka wiki tatu pale Tarime waking’ang’ania mbolea: Naomba nipate kauli ya Serikali kwamba msimu ujao wa kilimo watu wa Tarime watapata ile shida au itakuwa imeisha? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika msimu uliopita tulikuwa tuna changamoto ya upatikanaji wa mbolea kwa wakati, lakini Serikali imechukua hatua. Tumeshamwelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA na timu yake nzima kuhakikisha kwamba wanaongeza vituo vya mawakala wa uuzaji wa mbolea sambamba na kutumia vyama vya ushirika kama sehemu ya usambazaji wa mbolea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa kuliko yote, nataka niwaondoe hofu Waheshimiwa Wabunge kwamba mbolea itaanza kuingia nchini mapema mwezi Julai ili wakulima waanze kuinunua mapema kujiandaa na msimu unaokuja.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Watu wa Tarime wanamshukuru sana Mheshimiwa Rais, Mama wa Taifa, kwa kutoa fedha ya kujenga lami kilometa 25. Sasa naomba nijue: Lini kipande cha kitoka Kwinogo – Nyamongo hadi Serengeti Mugumu kitaanza kujengwa kwa kiwango cha lami? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, tulishaongea na Mheshimiwa Mbunge, na kweli kipande hicho tutakijenga kwa kiwango cha lami. Tayari mkandarasi alishapatikana, taratibu za manunuzi zimeshapatikana. Tunachofanya sasa katika maandalizi ni kutafuta siku ya kusaini kipande kilichobaki cha kutoka Nyamwaga hadi Mugumu - Serengeti kwa kiwango cha lami.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Pamoja na majibu ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba alienda Bikonge na Nyamuhonda; wananchi wa Jimbo zima walienda kwake wakitaka kujua ni lini wataweka pale kituo kwa sababu kitasaidia kuokoa fedha za Serikali na kufanya biashara mpaka watu wa Serengeti watanufaika hapa. Kwa hiyo niliomba nijue ni lini kituo hicho kitajengwa kama ambavyo Mheshimiwa Waziri wa Fedha aliahidi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ninapozungumza hapa Kanda ya Ziwa yote Shinyanga, Simiyu, Mwanza, Geita, Mara biashara ya mazao imesimama kwa sababu Sirari kuna vurugu kubwa kwa zuio ambalo limetolewa na Mheshimiwa Waziri kwa Niaba ya Serikali. Watu wa Sirari na kanda ya ziwa wangependa kujua ni lini zuio hili litaondolewa kwa sababu wakati wanatoa tamko la kuzuia tayari wafanyabiashara wa mazao walikuwa na mazao kwenye maghala yao, hawafanyi biashara; na ulikuwa ukipeleka mazao Kenya unaleta bidhaa nyingine kutoka Kenya. Kanda imesimama biashara haifanyiki;

Je, ni nini kauli ya Serikali katika jambo hili?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwita kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba nimpongeze sana kwa namna anavyofatilia kituo hiki kidogo cha forodha pale mpakani. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kituo hiki mara tu upatikanaji wa fedha utakapopatikana basi kituo hiki kitajengwa, asiwe na hofu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili naomba tulipokee kwa sababu limechanganya Wizara tofauti, Wizara ya Kilimo, Biashara na Fedha. Naomba tulipokee tukakae kama kamati tutakutana na wewe Mheshimiwa Mbunge tuone namna gani tutatatua changomoto.

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa majibu ya ziada katika swali alilouliza Mheshimiwa Waitara. Mimi na yeye tumeshaongea zaidi ya mara moja mara mbili, naomba nirejee na Watanzania wanielewe. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haijazuia watu kufanya biashara ya mazao na kuuza mazao nje ya nchi. Serikali ilichokizuia ni watu kufanya biashara bila kufuata utaratibu wa Kisheria. Haiwezekani mtu unanunua mahindi Songea unapakia kwenye malori huna business license ya aina yoyote, hata business name kusajili ambayo ni huduma inayotolewa. Huna tin number, huna tax clearance, huna export permit, huna phytosanitary halafu unataka nchi ikuruhusu kwenda kuuza nje mazao hayo. Malipo hayaonekani katika mfumo rasmi wa fedha, hatuzipati data katika export statement zetu za nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maelekezo ya Mheshimiwa Rais yako wazi, Mtanzania yeyote anayetaka kufanya biashara ya mazao kwa ajili ya kuuza nje ama kuuza ndani ya nchi akate leseni ya biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipitie kwenye Bunge lako Tukufu kuwaambia wafanyabiashara wa mazao, nendeni kwenye halmashauri kateni leseni za biashara, nendeni TRA chukueni Tin Certificate ili muingie kwenye mfumo rasmi na formalization ya biashara ya mazao ya kilimo. Hatuwezi kuendelea katika mfumo huu unao endelea. Na nia ya Serikali ni kurasimisha shughuli za kilimo na shughuli za biashara za mazao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana mtu yupo tayari apigwe penalty ya shilingi laki nane au milioni moja kwa sababu hana leseni avuke upande wa pili. Wiki iliyopita tumeruhusu malori Sirari, wiki hii tumeruhusu zaidi ya malori 506 na wote wamelipa faini ya shilingi milioni moja. Hatuwezi kuruhusu mfumo huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Wafanyabiashara, mazao ya kilimo yatauzwa popote, nendeni mkajirasimishe muwe na business license, muwe mna TIN, mna tax clearance. This is how we formalize economy. (Makofi)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba niulize Wizara, kwa nini katika jimbo zima hakuna josho la kuogeshea wanyama?

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwita Mwikwabe Waitara, Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mikakati ambayo tunayo katika mwaka wa fedha unaokuja, 2023/2024, Halmashauri ya Tarime ni miongoni mwa halmashauri ambazo zitapata majosho katika yale majosho ambayo tuliyatangaza katika fedha ambazo tuliziweka katika mpango, shilingi bilioni 5.7.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kule kwenye Jimbo la Tarime Vijijini eneo la Nyamungo na Nyamwaga wananchi wangu wamekwenda kulipia nguzo za umeme wa REA badala ya kulipia shilingi 27,000 wamedaiwa shilingi 515,000 kwa nguzo moja.

Naomba nipate kauli ya Serikali kwamba bei imebaki shilingi 27,000 ile ambayo tulikubaliana kwa wananchi wetu au kuna mabadiliko mengine sasa ya gharama ya umeme wa REA? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwita Waitara kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, bei za umeme za maeneo ya vijijini ni shilingi 27,000 bila kujali habari ya nguzo au transfoma au nini; kwa vijijini ni shilingi 27,000. Maeneo ya mijini ndiyo yamerudia kwenye zile bei ambazo tayari Serikali inaweka ruzuku ili ziweze kuwa za chini kidogo ili wananchi waweze kuzikimu, lakini kwa vijijini ni shilingi 27,000.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwamba mpaka wa Sirari ni mkubwa sana kutoka Sirari mpaka kule Nyanungu ambako ukimtaka mwananchi atoke aje apishe Sirari pale alipe kodi ya Serikali ni ngumu kidogo. Kwa nini kusiwe na kituo kidogo cha Forodha pale Witembe Itirio ili wananchi walipe mapato halali ya Serikali badala ya kufanya magendo kugombana na polisi? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, nimpongeze babu yangu Mheshimiwa Mwita kwa kuleta swali hilo. Nilishapokea swali la aina hiyo pia kutoka kule Kakonko kwa ndugu yangu Aloyce, niunganishe tu kwamba baada ya Bunge wale Waheshimiwa Wabunge ambao kwenye maeneo yao wangehitaji kuwa na mpaka mpya nizungukie mimi pamoja na Naibu wangu ama wataalam wetu ili tujiridhishe na zile sifa ambazo zinatakiwa kwa ajili ya kuanzisha mpaka mpya wa Tanzania na nchi jirani kwa upande wa ofisi ya Mamlaka ya Mapato ili tuweze kuwarahisishia wananchi wanapotaka kupata huduma ya Mamlaka ya Mapato.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba nimuulize swali la nyongeza Mheshimiwa Waziri kwamba kule Tarime eneo la Rorya, Sirari, Nyasicha, Muliva, Itilio, Nyanungu. Eneo hilo kuna malalamiko ya wananchi mengi kwamba wale maaskari wanatembea na marungu kwenye magari kwa hiyo, watu wakikamatwa wanapigwa sana. Nilitaka niulize utaratibu wa sheria umebadilika au huu ni mtindo wa kule Tarime ndio tu upo kwa sababu ni kanda maalum? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Waitara Mbunge wa Tarime Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, si mpango wa wizara wala Jesho la Polisi kutembea na marungu kwenye magari kwa ajili ya kupiga wananchi wake. Lakini nafahamu kwamba kuna wakati Askari wanalazimika kukamata wahalifu na wahalifu wanapofanya upinzani nguvu inayotakiwa kutumika ni ile tu inayoshabihiana na nguvu pinzani lakini si marungu kwa ajili ya kupopoa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru; nina vijiji 27, vitongoji zaidi ya 300 katika Jimbo la Tarime Vijijini vikiwepo Magoma, Kitenga, Masurura, Gibaso, Nyabitocho, Kebweye, Korotambe, Kegonga, Mosege, Kihongera na Soroneta. Wananchi hawa waliahidiwa kwamba mwaka jana mwezi Desemba umeme ungeweza kuwaka mpaka sasa haujawaka. Mheshimiwa Naibu Waziri ana kauli gani katika maeneo haya ya kupata umeme? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Waitara kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi yetu ya kupeleka umeme vijijini Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili inaendelea katika vijiji vyote nchini ambavyo havikuwa vimefikiwa na miundombinu ya umeme na tunatarajia kuanza Desemba tutaanza kukamilisha miradi hii, na upelekaji wa umeme katika vijiji na vitongoji upo katika hatua mbalimbali.

Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Waitara kwamba vijiji hivyo viko katika taratibu za kupelekewa umeme na kufikia Desemba tunaamini tutakuwa tumekamilisha mradi wa kupeleka umeme kwenye vijiji hivi.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwamba mpaka wa Sirari ni mkubwa sana kutoka Sirari mpaka kule Nyanungu ambako ukimtaka mwananchi atoke aje apishe Sirari pale alipe kodi ya Serikali ni ngumu kidogo. Kwa nini kusiwe na kituo kidogo cha Forodha pale Witembe Itirio ili wananchi walipe mapato halali ya Serikali badala ya kufanya magendo kugombana na polisi? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, nimpongeze babu yangu Mheshimiwa Mwita kwa kuleta swali hilo. Nilishapokea swali la aina hiyo pia kutoka kule Kakonko kwa ndugu yangu Aloyce, niunganishe tu kwamba baada ya Bunge wale Waheshimiwa Wabunge ambao kwenye maeneo yao wangehitaji kuwa na mpaka mpya nizungukie mimi pamoja na Naibu wangu ama wataalam wetu ili tujiridhishe na zile sifa ambazo zinatakiwa kwa ajili ya kuanzisha mpaka mpya wa Tanzania na nchi jirani kwa upande wa ofisi ya Mamlaka ya Mapato ili tuweze kuwarahisishia wananchi wanapotaka kupata huduma ya Mamlaka ya Mapato.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza ni kwamba, wakati wa bajeti tarehe 26 Machi, 2022 kwenye Kamati ya TAMISEMI, waliahidi wataalam kwamba watapeleka fedha hizi tarehe 30 Machi. Leo Waziri anasema tarehe 30 Mwezi Juni, maana yake miezi mitatu baadaye. Kama hii kauli ya mwanzo iliahidi Kamati ya Fedha, fedha haijaenda mpaka leo tunavyozungumza, tarehe 30 Juni, fedha itaenda kweli?

Swali la kwanza, fedha hiyo inaenda lini Ili iweze kujenga kituo cha afya pale? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; hapo Hospitali ya Mwaga ilikuwa ni zahanati kama kituo cha afya, sasa ni Hospitali ya Halmashauri mpya, hakuna mgao wa dawa pale, lakini hizi huduma ninazozizungumza wodi ya akinamama haijakamilika, wodi ya watoto haijakamilika, wodi ya wanaume haijakamilika, pharmacy haijakamilika, fedha ipo milioni 78 kwenye mgodi wa North Mara, Mheshimiwa Waziri wa Madini aliagiza kwamba ndani ya siku 14 fedha iende haijaenda, Waziri wa TAMISEMI aliagiza fedha haijaenda...

SPIKA: Mheshimiwa Mwita Waitara, ngoja kwanza. Jibu la msingi la Waziri, wewe kwa hilo swali lako la pili unalotaka kuuliza ni kwamba, hili jibu lake la msingi halitoi uhalisi wa kilichoko huko ndiyo unachojaribu kusema? Simama.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, ni kweli.

SPIKA: Kwa hiyo, hakuna hizo wodi mbili zilizokamilika.

MHE. MWITA M. WAITARA: Hazijakamilika.

SPIKA: Basi hilo swali lako la nyongeza la kwanza nitampa nafasi Mheshimiwa Waziri alijibu, hilo la pili unalosema hayo majibu hayako halisi Mheshimiwa Naibu Waziri atakapomaliza kujibu maswali hapa, nitampa nafasi aende akalifuatilie aniletee majibu hapa.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Waitara, Mbunge wa Jimbo wa Tarime Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Halmashauri ya Tarime Vijijini walitakiwa kupeleka milioni 100 lakini hawakupeleka milioni 100 katika kata hii kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kituo cha afya tarehe 30 Machi na jana nimewasiliana na Mkurugenzi na Katibu Tawala wa Mkoa na watapeleka ndani ya mwezi huu kwa sababu walikuwa hawajapata makusanyo ya kutosha kupeleka fedha hiyo kwa mujibu wa vipaumbele ambavyo vilikuwa vimewekwa. Ahsante sana.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri swali kwamba tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ambayo ameifanya jana kwa miji 28 kupata mradi wa maji na kwa kweli kwa nchi nzima kuna mabadiliko makubwa sana ya maji hata Tarime kuna mabadiliko makubwa sana.

Sasa nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba nilikuuliza swali hapo ukasema Tarime itapata maji katika miji ile 28, lakini kwenye hii list ya jana Tarime haimo; nini kauli ya Serikali juu ya watu wa Tarime ili waweze kusubiri maji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Waitara kama ifuatavyo: -

Tarime imo Rorya, Tarime ipo kwenye mradi wa miji 28; vuta subira wakati wa utekelezaji utakapoanza utashuhudia kwamba Tarime imo. (Makofi)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kulingana na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, anaonesha kwamba wananchi wanapaswa kuchangia ujenzi wa zahanati hadi kwenye maboma, lakini wapo watu ambao wamekuwa wakipita kwenye majimbo yetu wakiwaambia wananchi wasichangie ujenzi wa zahanati na maboma mengine ya elimu: Je, nini hatua ya Serikali dhidi ya hao ambao wanapotosha wananchi wasishiriki mendeleo yao? (Makofi
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Utaratibu wa ujenzi wa maboma ya zahanati kwa mpango wa maendeleo ya afya msingi upo kwa mujibu wa mwongozo wa 2007. Ni maamuzi ya Serikali kwamba wananchi wanashiriki kwa sehemu na Serikali inahitimisha. Kama wapo watu ambao wanapita katika maeneo yetu na kupingana na maelekezo ya Serikali basi naomba Serikali kwa maana ya Wakurugenzi, Wakuu wa Wilaya na Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa wawatambue watu hao ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao, ahsante. (Makofi
MHE. MWITA. M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Mwaka jana Serikali ilitoa maelekezo kwenye Majimbo yetu na Mikoa yetu na wakapeleka masharti wapendekeze maeneo ambayo wanataka kuongeza vitongoji, vijiji na Kata. Kwa hiyo, Kata mbalimbali zilikaa na kutumaini kwamba watapewa maeneo hayo waliyoomba.

Kwa sasa, nini kauli ya Serikali juu ya maelekezo ambayo waliyatoa katika maeneo yetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Waitara. Ni kama kwenye majibu yangu ya msingi kwamba kwa sasa, Serikali imeweka kipaumbele katika kuhakikisha yale maeneo mapya ya kiutawala yaliyopo yanapata miundombinu ambayo ni stahiki kwa maeneo yale.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni tumeona Halmashauri nyingi zimekwenda katika maeneo yao ya kiutawala na Serikali imepeleka fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu ikiwemo ofisi za Halmashauri, ofisi za Wakuu wa Wilaya kwenye Wilaya mpya na kadhalika. Kwa hiyo, mpaka pale ambapo Serikali itakapokuwa imekamilisha ujenzi wa miundombinu ya msingi katika maeneo yaliyopo sasa ndipo itaendelea na mchakato wa kuongeza maeneo mengine.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Wananchi wa Tarime na Serengeti wamekongwa mioyo na Mheshimiwa Rais Mama Samia kuwaunganisha kwa barabara ya lami. Kipande cha Tarime – Nyamwanga kimeanza. Mheshimiwa Naibu Waziri lini mkandarasi atakuwa site kujenga barabara kwa kiwango cha lami kutoka Kunyagu – Nyamongo kwenda Serengeti – Mugumu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwamba anatambua kwamba Mheshimiwa Rais ameamua kuiunganisha Tarime na Serengeti kwa kiwango cha lami. Taratibu zote zimeshakamilika za kuanza ujenzi kipande hicho. Kwa hiyo nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge mara baada ya Bunge hili na nina uhakika mvua itakapokuwa imekatika mkandarasi ataanza kukijenga hicho kipande ambacho kimebaki.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kupata nafasi. Tumepata barabara ya kutoka Tarime Mjini mpaka pale Mugumu, Serengeti, hasa maeneo ya Nyamongo, lakini barabara imesimama ujenzi wake kwa muda mrefu sasa kwa sababu, yule mkandarasi anadai shilingi bilioni 6.8 mpaka leo. Je, ni lini mkandarasi huyu atalipwa fedha ili ujenzi ukamilike kwa wakati na watu wetu waendelee kupata huduma? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, taarifa nilizonazo, nitaongea na Mheshimiwa Mbunge ni kwamba, tuna lot mbili, lot ya kwanza ni Mugabiri kwenda Serengeti na kipande kile ambacho ni cha pili, nilichoambiwa ni kwamba, yupo kwenye mobilization na anaendelea kuandaa camp kwa ajili ya kujenga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tumekuwa na changamoto kubwa, barabara nyingi zimesimama kwa sababu ya hali ya hewa ambayo inazuia wakandarasi kuendelea na kazi za ujenzi wa barabara, lakini nitaomba nionane na Mheshimiwa Mbunge, tuone kama kuna changamoto nyingine zaidi ya hii. Ahsante. (Makofi)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, Mradi wa Maji katika Kata ya Nyakonga, Magoto na Mradi wa Maji Itiryo ni mradi wa mserereko, lakini hauna chujio wala dawa. Kwa hiyo, wakati wa mvua, maji ni machafu. Ni lini watapeleka chujio katika maeneo hayo ili maji yawe safi na salama kwa wananchi wangu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ni dhamira ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi kuhakikisha kwamba inafikisha maji safi na salama. Kwa hiyo, kwa sababu ya changamoto hiyo, Serikali inalichukulia hatua moja kwa moja na tutakwenda kuona kwamba eneo ambalo Mheshimiwa Mbunge ameliongelea lina changamoto ipi ili wataalamu wetu waweze kuchukua hatua stahiki, ahsante, (Makofi)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Katika Jimbo la Tarime Vijijini maeneo ya Vijiji vya Nyangoto, Kerende, Mjini Kati, Nyabichune na Nyamwaga wananchi wangu wanalipia umeme shilingi 320,000 kinyume na sera ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nini kauli ya Serikali wananchi wapate umeme kwa bei nafuu ambayo imeelekezwa vijijini? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye maeneo haya ambayo ameyataja Mheshimiwa Mbunge, tutayapitia kuona kama yapo kwenye yale maeneo 1,570 ambayo tumeshayaainisha na kama hayapo tutayafanyia tathmini kuweza kuona kama na yenyewe yanaweza kuingia katika mpango huo ili wananchi waweze kupata huduma ya kuunganisha umeme kwa shilingi 27,000. Ahsante. (Makofi)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nataka nijue je, ni sahihi kituo cha afya kuwa na wodi moja inayolaza mama, baba, watoto na hata watu waliofanyiwa operation?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, utaratibu wa ujenzi wa vituo vya afya upo kwa mujibu wa mwongozo wa ujenzi wa miundombinu hiyo, lakini pia kwa mujibu wa Sera ya Afya. Vituo hivi vinajengwa wodi ya wanawake, wodi ya wanaume, wodi ya watoto lakini pia wodi ya wazazi, majengo ya upasuaji na majengo mengine. Kwa hiyo, siyo sahihi kwamba tunaweza tukawa tuna wodi moja ambayo inatumika na watoto, wanaume na wanawake jambo hilo halikubaliki. Kwa kweli nina uhakika kama kuna sehemu inafanya hivyo, tutachukua hatua kwa haraka, kwa sababu ni suala ambalo halipo katika utaratibu wetu.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, Naibu Waziri alienda Nyamuhonda, Mwema na Itiryo hakuna mawasiliano kabisa na watu wanasikiliza redio na Tv ya Kenya. Ni lini minara itawekwa katika maeneo hayo ili tupate mawasiliano ya Tanzania? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, UCSAF inaendelea kufanya tathmini maeneo mbalimbali hasa haya ya mipakani. Mheshimiwa Waitara naomba nikuahidi maeneo haya yote uliyotaja nayo tutayafikia ili waweze kupata huduma ya minara kutoka Tanzania.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, eneo hili Mheshimiwa Michael Kembaki, ameuliza mara kadhaa huku Bungeni, amemchukua Mheshimiwa Diwani wa Kata husika yeye mwenyewe wamekaa kikao cha wilaya na mkoa wakakubalina eneo hilo lisirudishwe kwa wananchi, lakini lirudishwe kwa jamii ile nalipangiwe matumizi ya kijamii, tuna uhaba mkubwa wa ardhi. Je, yamkini inaonekana Wizara ya Mambo ya Ndani ndio kikwazo na ndio wanazuia huo mpango usitekelezwe. Nataka nijue sababu ya Wizara kukataa ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kule Tarime Vijijini eneo la Mwema na Kata ya Regicheri, eneo lingine wamechukua wakawapa JKT wanalima, halafu lingine wamezuia zaidi ya mwaka mzima hakuna shughuli inafanyika pale. Je, huu utaratibu wa kutwaa maeneo ya watu wa Tarime na kuyahodhi na watu wanakuwa na shida ya kilimo utaisha lini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Waitara, kwa niaba ya Mheshimiwa Kembaki, naomba kujibu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la mlima huu kurudishwa kwa jamii badala ya kusimamiwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, nimeeleza msingi wa uamuzi ule ilikuwa moja, ni kuhifadhi mlima ule, lakini pili ni kuzuia uharamu wa mazao yaliyokuwa yanalimwa kwenye eneo lile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama Mbunge alikuja sasa sijui alikutana na nani waliopatana, lakini kwa msimamo wa Wizara na kwa msimamo wa Kamati ya Usalama ya Wilaya eneo lile lipo nchi ya uangalizi wa Magereza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la pili, la Mheshimiwa Waitara, naona ni kama amechomekea Mambo ya Ndani, kama ni JKT basi ni la Wizara ya Ulinzi, nimshauri aandae swali la msingi ili liweze kujibiwa ipasavyo na Wizara yenye dhamana na ulinzi, ahsante. (Makofi)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza; swali la kwanza, kwa kuwa Serikali ilipeleka mwongozo kwenye kata zetu na kwenye majimbo na viongozi kwenye maeneo mbalimbali wakajadili na kupendekeza maeneo mapya ya kiutawala na kama haya ndiyo majibu ya Serikali.

Je, Serikali ipo tayari kupeleka mwongozo wa kufuta ule ambao walipeleka kwamba tutapendekeza maeneo ili kupunguza usumbufu na maswali kwa Waheshimiwa Wabunge?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuna ahadi kwenye jimbo langu pale mamlaka ya mji maeneo mawili, Sirari na Nyamongo, kwa msimamo wa Serikali huo.

Je, ni nini kauli ambayo sasa watu wa Tarime wataambiwa juu ya ahadi za viongozi wakuu ambazo zilitolewa tangu mwaka 2011 mpaka leo? Ahsante.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, swali la pili anaweza akarejea sijalisikia vizuri.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, ahsante, ni hivi kule katika Jimbo la Tarime Vijijini eneo la Sirari na Nyamongo Waheshimiwa Mawaziri Wakuu kuanzia Mzee Pinda na Waziri Mkuu wa sasa, Mheshimiwa Kassim Majaliwa waliahidi kutoa Mamlaka ya Mji katika maeneo hayo.

Kwa majibu ya Serikali, lini sasa watu wa Sirari na Nyamongo wategemee kupata mamlaka za miji katika maeneo hayo?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ni kweli Serikali ilipeleka mwongozo wa namna ambavyo vikao vya kisheria vinatakiwa kukaa kwa ajili ya kuanzisha mamlaka mpya katika maeneo yetu. Mwongozo huo ni halali mpaka sasa kwa sababu Serikali haijafuta dhamira ya kuongeza maeneo hayo. Michakato inaendelea kama kawaida, inawasilishwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI na muda utakapofika kwa ajili ya kutenga maeneo mapya kazi itakayofanyika na Ofisi ya Rais, TAMISEMI ni kupitia maombi ambayo tayari yamekwisha kuwasilishwa na mamlaka mbalimbali kote nchini.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hatuna sababu ya kufuta mwongozo kwa sababu zoezi ni endelevu, linaendelea lakini muda ukifika tutakuwa tuna kazi tu ya kupitia yale maombi yamekwisha kuletwa.

Mheshimiwa Spika, lakini pili kuhusiana na uanzishwaji wa mamlaka ya mji ni utaratibu ule ule kwamba baada ya kukamilisha miundombinu katika mamlaka zilizopo tutakwenda sasa kuanzisha mamlaka nyingine na wakati huo tutalifanyia kazi suala hilo ambalo ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ahsante.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri Mheshimiwa Waziri alienda Sirari. Ilianza mwanzoni kwamba, nilitaka anieleze utaratibu wa kupata bidhaa moja kwa moja kutoka Kenya na Tanzania. Kwa sababu wale wachuuzi wa kawaida hawaruhusiwi kupitisha bidhaa pale na Jumamosi gari ya TRA ilimfukuza kijana akiwa na bidhaa ya plastiki ikampiga ikamwingiza kwenye mtaro na ninavyozungumza ndugu zake wameshazika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa anachozungumza hapa ni habari ya mikonge ambayo niliuliza mwaka jana. Bidhaa kutoka Kenya, sasa hivi kule Sirari mbolea ya Tanzania ni ghali kuliko ya Kenya; hakuna utaratibu hata wa kawaida kwa wakulima. Mabati yanatoka Kenya, ya Tanzania ni ghali. Sasa nataka nipate majibu kwamba ni lini Mheshimiwa Waziri ataweka utaratibu wa kawaida? Mtu wa kawaida bati 10 au tano, cement, mafuta ya kula, sukari wanapataje kutoka Kenya kuliko wale ambao wananunua kwa bulk procurement? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria bidhaa yeyote inayotoka nje ya nchi hata kama ni kalamu moja inapaswa kufuata utaratibu. Kwa hiyo anachokisema Mheshimiwa Mbunge anasemea kwamba kama mtu wa kawaida akiwa na bati 15 au 20. Kwa mujibu wa utaratibu, bidhaa yoyote inayotoka nje inatakiwa ifuate utaratibu wa kuvuka mpaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunachoweza tu kufanya sasa hivi tunaongea na wenzetu wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuangalia si tu kwa mpaka wa mikonge na maeneo mengine kuangalia utaratibu wa kuwarahisishia wananchi ambao wanatoka maeneo ya mbali zaidi na hicho ndiyo ambacho tunafanyia tathimini. Kwa sababu yako maeneo yale nilishamsikia ndugu yangu wa Ngorongoro, nimemsikia ndugu yangu wa Kakonko na mipaka mingine mingi Waheshimiwa Wabunge mmekuwa mkiongelea. Kwa hiyo tunatafuta jawabu la moja kwa moja kwa wananchi ambao wako mbali sana na mpaka na bidhaa walizobeba siyo nyingi, lakini kwa Sheria ilivyo sasa hivi bidhaa yoyote inatakiwa ipite mpaka ulio rasmi na iweze kuwa cleared na customs.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwa hoja za Waheshimiwa Wabunge tunaendelea kushauriana na wenzetu Ofisi ya Rais, TAMISEMI ambao coverage yao iko kubwa kuliko ofisi zetu za forodha ili tuweze kuona namna ambavyo tunaweza tukawarahisishia wananchi wa mipakani. (Makofi)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wa TAMISEMI alifanya ziara katika Jimbo la Tarime Vijiji, Makao Makuu ya Halmashauri Nyamwaga na aliahidi ujenzi wa kilometa mbili pale Makao Makuu, ninapenda kujua kama ile ahadi bado ipo au imeyeyuka? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nipokee alichokisema Mheshimiwa Mbunge na baada ya kipindi hiki cha maswali na majibu tutafanya ufuatiliaji ili kujua imefikia hatua gani, utekelezaji wa ujenzi wa hizi kilometa mbili zilizoahidiwa na Mheshimiwa Waziri.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Barabara ya kutoka Mogabiri – Nyamongo – Serengeti, Mkandarasi ametoa vifaa site na anaidai Serikali shilingi bilioni 7.8. Barabara hii inahudumia Wilaya ya Tarime na Wilaya ya Serengeti. Mheshimiwa Waziri, nini kauli ya Serikali juu ya ujenzi wa barabara hii kuendelea ili kutoa matumaini kwa watu wa Tarime?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Waitara, amekuwa akiifuatilia barabara hii kwa ukaribu sana na habari iliyo njema ni kwamba, zile advance payment tulizozipata, barabara hii pia ni miongoni mwa hizo barabara. Kwa hiyo, nampongeza Mheshimiwa Waitara kwa ufuatiliaji.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nilitaka nimwulize Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba je, wapo tayari kutoa hadharani vigezo wanavyotumia kwa vijana kupata ajira ili kuondoa usumbufu wa vijana wanaoomba ajira, kusumbua Wabunge wakidhani kwamba ukituma message kwa Mbunge atakuombea ajira ili wajue kwamba ajira inatolewa kwa haki na mtu atakayeomba ana sifa atapata nafasi hiyo, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Ni wazi kwamba kupitia Sekretarieti ya Ajira, vigezo vyote viko wazi na kwa namna ambavyo tunafanya usaili, matokeo yanatoka wazi na wale ambao wanatokea kukosa wanapewa sababu. Hata hivyo, tumetoa fursa ya kwamba yule ambaye anadhani hakutendewa haki, amepewa fursa ya kukata rufaa. Kwa hiyo, vigezo vyote viko wazi na kila Mtanzania yuko wazi kuomba kwa kadri ya nafasi anayotaka, nashukuru. (Makofi)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Nyarukoba ya Kijiji cha Msege umeme ulifika Makao Makuu ya Kijiji lakini katika eneo hilo kuna wachimbaji wadogo ambao wako tayari kutoa fedha zao wapelekewe umeme ili kupunguza gharama ya uzalishaji wa dhahabu. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kwenda kuwasikiliza wachimbaji wale kwa gharama zao ili wapate umeme wafanye kazi ya uchimbaji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake. Katika Kata hii ya Nyarukoba tayari nilishamwelekeza Meneja wa TANESCO, Mkoa wa Mara afanyie kazi na tayari wameshaanza kupeleka umeme kwenye hilo eneo. Niwahakikishie wachimbaji hawa wadogo tutawafikishia umeme kwa ajili ya kuboresha shughuli zao za kiuchumi. Ahsante.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria unatakiwa kuhudumia Jimbo la Rorya, Tarime Mjini – Vijijini, pale Sirari ujenzi wa tenki umesimama kabisa.
NAIBU SPIKA: Mwezi wa Kumi na Mbili, ahsante. (Kicheko/Makofi)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; hii Kata ya Susuni, Kijiji cha Kiongera ndiyo eneo ambalo Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI alitoa fomu humu ndani Wabunge wote tukajaza kuomba vituo vya afya. Nikaenda kwenye kata hii nikafanya mkutano wa hadhara nikawaahidi kwamba sasa Serikali inajenga kituo cha afya hapa. Sasa nataka nijue kwamba kwa majibu haya huo mpango haupo kabisa, tukawaambie kwamba hicho kituo hakijengwi au kutakuwa na majibu mengine katika swali hili hili? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri anasema kwamba mwaka wa fedha ujao 2025/2026 halmashauri itapeleka milioni 150 katika eneo hili. Lakini anasema wataboresha jengo la kufulia, jengo la OPD na wodi, jengo la kufulia linachukuwa mpaka milioni 187, OPD milioni 180 mpaka 187, wodi ni milioni 250. Je, Serikali wapo tayari kumwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Tarime DC kupitia mapato ya ndani apeleke fedha zote hizi ili kituo cha afya kijengwe Kiongera kwa sababu katika eneo hilo hakuna huduma ya afya na amesema mwenyewe kata ina vijiji vitano…

SPIKA: Mheshimiwa umeshauliza swali.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nimeshauliza eeh?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, ni kweli baada ya Serikali kuweka dhamira ya kujenga vituo vya afya kwenye kila Jimbo Mheshimiwa Mbunge alileta mapendekezo ya Kata hii ya Susuni na sisi kama Serikali tayari tumeshaiweka kwenye orodha ya kata ambazo zitapata fedha kwa ajili ya kujenga kituo hiki cha afya. Kwa hiyo, kwanza mpango wa kujenga kituo cha afya hiki kupitia kituo cha afya kila jimbo upo pale pale. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi kwamba Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kwenda kutekeleza miradi hiyo.

Mheshimiwa Spika, pili, ni kweli kwamba kituo cha afya kinahitaji majengo mengi zaidi na shilingi milioni 150 haitatosha kukamilisha majengo yote, lakini safari ni hatua tumeanza na majengo haya, tunaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kwenda kukamilisha majengo mengine.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumsisitiza pia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Tarime Vijijini kwamba kadri mapato ya ndani yanapopatikana tunaweza kuongeza fedha kutoka milioni 150 na kupeleka fedha zaidi kwa ajili ya ukamilishaji wa kituo hiki. Ahsante.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa fursa, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, Serikali kwa ujumla wakawa tayari kuleta takwimu za wanafunzi walioolewa, waliopata mimba ili tujue ukubwa wa tatizo tujaribu kutafuta mipango mizuri ya kuzuia shida hii? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Waitara kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu hizi zipo na kama nilivyoeleza hapo mwanzoni kwamba mpaka kufika Machi, 2024 zaidi ya wanafunzi 22,000 waliweza kurejea shuleni kwa wale ambao walipata ujauzito kwa namna moja au nyingne. Hata hivyo, Mheshimiwa Waitara wewe unafahamu umeshawahi kuhudumu kwenye Serikali. Tuna takwimu zile ambazo tunazichukua za kila mwaka katika shule zetu zote. Kwa hiyo, tuna takwimu ya kila mwanafunzi mahali alipo na kama amekatiza masomo kwa namna moja au nyingine. Kwa hiyo, tupo tayari kuziwasilisha takwimu hizo kwa kadiri zitakavyohitajika.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Tulipata wakandarasi kwenye majimbo yetu na hasa pale Tarime Vijijini na vitongoji zaidi ya 300 havina umeme. Walienda wakapima kupitia Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji wakaweka beacon. Sasa ni lini mradi huu wa umeme utaanza kutekelezwa katika jimbo la Tarime Vijijini ili watu wangu watoke kwenye giza nene? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa swali la Mheshimiwa Mbunge. Tayari tumeanza utekelezaji wa kupeleka umeme kwenye vitongoji. Tumeanza na vitongoji 15 ambavyo yeye mwenyewe Mheshimiwa Mbunge alituonyesha kwa list yake na kuanzia mwezi Desemba mwaka huu tuna mradi mwingine wa vitongoji 4,000. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, katika mradi unaofuata tutaendelea kupunguza vitongoji katika jimbo lake ili kuhakikisha vitongoji hivyo ambavyo havina umeme vinapelekewa umeme na wananchi wananufaika, ahsante.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la wachimbaji wadogo Nywarwana, Kata ya Kibasuka, Serikali inachukua kodi katika maeneo yale, lakini hakuna choo wala barabara ya kupita. Nini mwongozo wa Mheshimiwa Naibu Waziri katika eneo lile ili wachukue kodi halali, lakini pia watoe huduma za kijamii katika eneo lile kwani lina watu wengi sana na wanachafua mazingira? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu nimwombe ndugu yangu Mheshimiwa Waitara kwamba nikitoka kujibu maswali hapa tukutane ili niweze kujua changamoto hiyo imesababishwa na nini, kwa sababu haiwezekani tozo zichukuliwe halafu huduma muhimu kwa wananchi zisitolewe, kwa hiyo, hilo nitalifuatilia baada ya hapa. Ahsante. (Makofi)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi, naomba nitumie nafasi hii kutoa pole kwa kijana wangu aliyepata ajali katika Waitara Cup kule Sirari na namshukuru Mungu kwamba wahuni wote na shetani wameshindwa na Mungu ameshinda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali mawili ya nyongeza kwa Serikali; swali la kwanza. Serikali ipo tayari kuleta takwimu za maboma ya nyumba za walimu msingi na sekondari nchi nzima kwenye majimbo yote ambayo wananchi wameweka nguvu zao kuyajenga na yameishia kwenye lenta na kuonyesha mkakati namna ambayo watakamilisha maboma hayo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Halmashauri yangu ya Tarime DC ina mapato makubwa. Serikali ipo tayari kutoa maelekeza mahususi kukamilisha maboma yote ambayo wananchi wangu wamechangia nguvukazi ili wapate nguvu kuendelea kuchangia maboma mengine baada ya kukamilisha yale ambayo wameshiriki kuyajenga? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake haya yenye tija. Kuhusiana na swali lake la kwanza, Serikali tayari imeshafanya tathmini ya kubaini ni maboma mangapi kwenye sekta ya elimu pamoja na sekta ya afya ambayo yamejengwa kwa nguvu za wananchi na tayari tathmini imekamilika na Serikali inafanya taratibu za kuhakikisha fedha inapatikana ili kuweza kuunga mkono jitihada zile za wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali la takwimu Mheshimiwa Mbunge tunaweza tukawasiliana nikakupatia lakini tayari Serikali ilishafanya tathmini kubaini idadi ya mabama na kiasi gani cha fedha kinahitajika kwa ajili ya kukamilisha maboma hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la pili; Halmashauri anayotoka yeye anasema ina mapato makubwa na kwamba tayari kuna maboma ambayo wananchi walianza kuyajenga. Nitumie nafasi hii kuendelea kusisitiza kwamba pale kunapokuwa na juhudi za wananchi Halmashauri na Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa zinakuwa na uwezo na ni lazima ziweze kutenga fedha na kuzingatia vipaumbele kuweza kuunga mkono jitihada za kuendeleza miundombinu na hasa hii muhimu ya elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba nichukue nafasi hii kuendelea kumkumbusha Mkurugenzi wa Halmashauri kutoka anapotokea Mheshimiwa Mbunge ili waweze kutenga fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya kuendelea kuendeleza miundombinu hii muhimu katika sekta ya elimu.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, eneo hili Mheshimiwa Michael Kembaki, ameuliza mara kadhaa huku Bungeni, amemchukua Mheshimiwa Diwani wa Kata husika yeye mwenyewe wamekaa kikao cha wilaya na mkoa wakakubalina eneo hilo lisirudishwe kwa wananchi, lakini lirudishwe kwa jamii ile nalipangiwe matumizi ya kijamii, tuna uhaba mkubwa wa ardhi. Je, yamkini inaonekana Wizara ya Mambo ya Ndani ndio kikwazo na ndio wanazuia huo mpango usitekelezwe. Nataka nijue sababu ya Wizara kukataa ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kule Tarime Vijijini eneo la Mwema na Kata ya Regicheri, eneo lingine wamechukua wakawapa JKT wanalima, halafu lingine wamezuia zaidi ya mwaka mzima hakuna shughuli inafanyika pale. Je, huu utaratibu wa kutwaa maeneo ya watu wa Tarime na kuyahodhi na watu wanakuwa na shida ya kilimo utaisha lini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Waitara, kwa niaba ya Mheshimiwa Kembaki, naomba kujibu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la mlima huu kurudishwa kwa jamii badala ya kusimamiwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, nimeeleza msingi wa uamuzi ule ilikuwa moja, ni kuhifadhi mlima ule, lakini pili ni kuzuia uharamu wa mazao yaliyokuwa yanalimwa kwenye eneo lile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama Mbunge alikuja sasa sijui alikutana na nani waliopatana, lakini kwa msimamo wa Wizara na kwa msimamo wa Kamati ya Usalama ya Wilaya eneo lile lipo nchi ya uangalizi wa Magereza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la pili, la Mheshimiwa Waitara, naona ni kama amechomekea Mambo ya Ndani, kama ni JKT basi ni la Wizara ya Ulinzi, nimshauri aandae swali la msingi ili liweze kujibiwa ipasavyo na Wizara yenye dhamana na ulinzi, ahsante. (Makofi)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutupatia barabara ya kutoka Tarime Mjini – Nyamongo yenye kilometa 25. Mheshimiwa Naibu Waziri amefika, barabara hii ilikuwa iishe kwa kiwango cha lami Januari, 2024 sasa wameomba ongezeko la muda mpaka Desemba mwaka huu, 2024 wanadai fedha shilingi bilioni 6.8. Shughuli zimesimama kabisa, hakuna kazi ya ujenzi ambayo inaendelea. Je, nini kauli ya Serikali ili barabara ikamilike wananchi wa Tarime Vijijini wapate huduma? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ni kweli barabara nyingi zilikuwa zimesimama. Moja, siyo tu kwa sababu ya kutokulipwa, kwa sababu Wakandarasi hawa bilioni sita, haiwezi kumfanya asimame, lakini sehemu kubwa tulikuwa tumesimama kwa sababu ya mvua nyingi inayonyesha na hasa maeneo ambako anatoka Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Wakandarasi wote waliokuwa wamesitisha shughuli kwa sababu ya mvua ama shughuli nyingine, moja ni kwamba Serikali inapeleka fedha warudi kwenye maeneo ili waweze kukamilisha barabara kama walivyoomba zile extension kwamba kufika Desemba awe amekamilisha kipande hicho cha barabara, ahsante. (Makofi)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Serikali iliahidi kujenga kilometa mbili za lami kwa kila makao makuu ya halmashauri mpya na Mheshimiwa Bashungwa akiwa Waziri wa TAMISEMI aliwaahidi Wananchi wa Nyamwaga barabara ya kilometa mbili kwa kiwango cha lami...

SPIKA: Swali.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujua ni lini ahadi hiyo ya Mheshimiwa Waziri itatekelezwa katika Mji wa Nyamwaga? Ahsante
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha kwamba inaboresha miundombinu na hasa kwenye barabara zetu hizi za wilaya. Nimhakikishie Serikali itahakikisha inatafuta pesa kuhakikisha inajenga barabara aliyoitaja.
SPIKA: Mheshimiwa Boniphace Nyangidu Butondo, Mbunge wa Kishapu, sasa aulize swali lake.