Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Dr. Mary Machuche Mwanjelwa (96 total)

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake haya mazuri, majibu yenye kutia moyo, majibu ambayo yanaonyesha dhamira ya kweli ya Serikali katika kuondokana na dhana hii ya upungufu mkubwa wa chakula, hasa katika mikoa kame, mikoa ya katikati.
Mheshimiwa Spika, majibu yake haya yameonyesha kwamba wanakopesha vyama vya akiba na mikopo kama SACCOS. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anasemaje juu ya wananchi wa Jimbo langu ambao wengi wao hawajajiunga na SACCOS, wataweza kupatiwa mikopo hii ya matrekta?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Serikali imeanza kuonesha nia na wanawekeza katika kuunganisha matrekta hapa nchini, ikiwemo pale TAMCO Kibaha.
Je, katika kuwahi msimu huu wa kilimo anaweza akatutengea matrekta hata matano tu ambayo tuko tayari kuyalipia kwa awamu ya kwanza katika Jimbo la Manyoni Magharibi, Halmashauri ya Itigi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba niseme kwamba katika majibu yangu ya msingi nikianzia na lile swali lake la pili nimejibu kwamba wananchi wanaweza wakajiunga katika vikundi ili waweze kukopeshwa kupitia katika Mfuko wa SACCOS. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini vilevile nikija katika swali lake la kwanza, ameuliza kama wananchi wanaweza wakakopeshwa mmojammoja. Na mimi naomba nimwambie kabisa Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Manyoni Magharibi kwamba Wizara ya Kilimo imefanya utaratibu kupitia Mfuko wake wa Taifa wa Pembejeo na Kilimo, kwamba tunaruhusu mkulima yeyote mmojammoja kuweza kukopa jinsi anavyotaka.
Mheshimiwa Spika, kubwa la msingi aweze kwenda kwenye halmashauri zetu kule atakutana na maafisa wa kilimo na mkurugenzi, atajaza fomu atapeleka katika mfuko wetu wa pembejeo akiwa na proforma invoice yake na sisi kupitia mfuko huo tuko tayari hata kutoa mifuko kwa wakulima na mikopo kwa wakulima wadogo wadogo. Ahsante. (Makofi)
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa furda hii niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri Dkt. Mary Mwanjelwa Dada yangu niipongeze Serikali katika majibu haya.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa katika jibu lake la msingi amekiri kwamba Serikali ina vituo ama vyuo 14 kwa ajili ya kilimo hapa nchini, lakini chuo/kituo hiki kilianza kujengwa tangu 2009 na kilikabidhiwa kwa halmashauri na halmashauri imeshindwa kukiendeleza. Je, hauoni kuna umuhimu sasa kupitia Wizara yako muweze kuchukua jukumu hili ili chuo hiki kiweze kukamilika maana ni zaidi ya miaka nane hadi sasa?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, pamoja na kwamba kuna vyuo hivyo 14, tumekuwa tukitoa wataalam na watafiti mbalimbali na wanakuwa wanazalisha kwa tija; lakini changamoto kubwa iliyopo ni kwamba anapokwenda kufanya kazi ama kwenye field changamoto kubwa ni kwamba masoko ya mazao wanayozalisha yanakuwa hayapo. Wizara imejipangaje, ni mechanism gani itatumika kutafutia masoko kwa bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini hasa hasa katika kilimo ukizingatia kwamba mahindi sasa hivi yameshuka bei, viazi mviringo vimeshuka bei, choroko zimeshuka bei na mazao mbalimbali? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, katika swali lake la (a) amezungumzia kwamba kituo hiki kimechukua miaka nane; na mimi ni kweli ninakiri kwamba kituo hiki kimechukua miaka nane. Hata hivyo kwenye majibu yangu ya msingi nilishaeleza kwamba kituo hiki kilikabidhiwa kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe.
Mheshimiwa Spika, sisi kama Wizara; na kwa sababu masomo yanayofundishwa pale yanahusiana na kilimo; ningependa niwasiliane na Mheshimiwa Mbunge ili tuweze kuangalia ni taratibu gani ambazo zinatakiwa kufuatwa, na ikiwezekana kwenye bajeti ya msimu wa fedha ujao basi tuweze kukiingiza. Vilevile niko radhi kwenda kutembelea kituo hiki ili niweze kujithibitishia kitu amcaho kiko mahali pale.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la (b) Mheshimiwa Mbunge amzungumzia kwamba kuna wataalam wengi ambao wanasoma katika vyo vyetu hivi vya mafunzo. Ni kweli na mimi naomba niendelee kusisitiza na kwamba sisi kama Wizara tunasisitiza sana kuwa na uzalishaji wa tija. Kwa hiyo nini kifanyike sasa? Ni kwamba tunaendelea kuwahamasisha wakulima wote kujiunga katika vikundi vya SACCOS kwa sabbau wataendelea kupata mikopo ambayo itakuwa na riba nafuu na vile vile waweze kujiajiri wenyewe binafsi. Ahsante
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu kwa kujibu maswali kwa ufasaha sana na natambua kazi nzuri inayofanywa na Waziri wa Kilimo akimsaidia katika kuhakikisha kwamba tunaboresha soko la korosho, nataka niulize maswali mawili ya nyongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, msimu wa ununuzi wa korosho umeshaanza, na katika Wilaya ya Msasi kuna uhaba mkubwa sana wa magunia kiasi cha kupelekea wananchi wote kuchanganyikiwa kutokana na kutopata magunia ambayo yanawawezesha wao kwenda kuuza korosho zao katika maghala.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anawambia nini wananchi wa Wilaya ya Msasi ambao hivi sasa hawajui la kufanya baada ya Serikali kushindwa kuwapelekea magunia?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, wakulima wa Wilaya ya Masasi katika msimu wa mwaka 2015/2016 hawajalipwa kiasi cha shilingi bilioni moja na milioni mia sita. Katika msimu wa 2016/2017 hawajalipwa kiasi cha shilingi bilioni moja, na katika msimu huu wa sasa tayari minada mitatu imefanyika lakini kumekuwa na kusua sua kwa kuwalipa wakulima. Je, Serikali inatoa tamko gani juu ya madeni makubwa haya yaliyopo kwa wakulima wa Wilaya ya Masasi?
Je, pia Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuandamana na mimi kwenda Masasi pamoja na Mbunge wa Msasi kwenda kushuhudia tatizo la magunia lakini pia kuangalia mnada?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba kukiri kabisa kwamba nimkweli kumekuwa na uhaba wa magunia kwa wakulima wa korosho katika Mikoa ya Lindi na Mtwara hususani katika Wilaya ya Masasi.
Mheshimiwa Spika, lakini kuchelewa huko naomba niliambie Bunge lako Tukufu, ni kwamba kumetokana na mkandarasi aliyekuwepo kuchelewa kufikisha magunia haya kwa wakati. Nimemuagiza Mrajisi wa Vyama vya Ushirika ambaye ndiye muhusika kwamba mkandarasi huyu awe amepewa seven days awe ameshakabidhi magunia haya pamoja na kamba kwa wakulima hawa wa korosho, failure to do that basi zabuni yake ivunjwe mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile naomba nitoe habari njema kwa wakulima wote wa korosho hususani katika Mikoa ya Lindi na Mtwara kwamba meli itawasili katika Bandari ya Mtwara kesho kutwa Jumapili tarehe 12/11/2017, magunia milioni moja pamoja na kamba yatafika mahali pale. Vilevile na mimi katika swali la Mheshimiwa Mbunge niko radhi kwenda huko Mtwara na nategemea kwenda wiki ijayo kuhakikisha na kujiridhisha kabisa kama magunia haya na yameshafika kule site.
Mheshimiwa Spika, vilevile ni kwamba vyama vile vya msingi vya ushirika ambavyo viko kule, vilikuwa vimefanya uzembe katika kugawa magunia haya kiholela; na mimi namuagiza Mrajisi wa Vyama vya Ushirika ambaye ndiye anayehusika na vyama hivi kwamba avunje bodi zote za msingi za vyama hivyo vya ushirika. Mimi nitafuatilia kwa ukaribu ili kuhakiksha kabisa kwamba hili jambo limefanikiwa na linatendeka kwa haki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la (b) kuhusu wale wote ambao wamefanya ubadhirifu katika kuhakikisha kwamba zao la korosho haliendi jinsi vile ambavyo inapaswa. Ninatoa rai kwa vyombo vya dola vyote, wale wote waliosababisha ubadhirifu huu katika zao hili la korosho wahakikishe vyombo vya dola kwamba wanawakamata, wanawapeleka mahakamni na hatua kali sana za kisheria zinachukuliwa na sisi kama Wizara kwa sababu huyu ni mtoto wetu tutafuatilia kwa karibu. Ahsante.
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, jambo mojawapo linaloyumbisha uzalishaji wa kahawa hususan Mbinga, ni kutokuwa na bei ya uhakika mwaka hadi mwaka. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuanzisha mfuko wa kuimarisha bei ya mazao hususan kahawa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuambatana na mimi baada ya mkutano huu, ili akajionee mwenyewe ni jinsi gani utekelezaji na uzambazaji wa miche mipya ya kahawa unavyofanyika na Kituo cha TaCRI - Ugano, kama ilivyojibiwa kwenye swali la msingi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge wa jimbo hilo kwa ajinsi ambavyo anafuatilia kwa ukaribu sana katika zao zima hili la kahawa katika Jimbo lake. Lakini nikija katika swali lake la (a) ni kwamba, sisi kama Wizara kupitia Bodi ya Kahawa tunatoa bei elekezi kwa wakulima wale wadogowadogo wote kwa maana ya kwamba, farm gate market kwamba wawe wanapata bei elekezi kupitia njia ya mtandao wa simu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile tumegundua kwamba, njia hii ya mtandao wa simu iko more effective ukilinganisha na ile minada mingine, lakini hii tunaifanya kila wiki. Lingine naomba nitoe rai hata kwa wakulima wale wadogowadogo wote katika mashamba kwamba, wanapaswa wazingatie sana ubora wa zao hili la kahawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine vilevile kule Moshi ambako tunafanya mnada, huu mnada kule Moshi hatuwezi tukafanya kwa bei elekezi kwa sababu, mnada wa kule unategemea sana soko la dunia na kwa maana hiyo, soko la dunia inategemea na wakati wa ile market price iliyoko wakati huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho naomba nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba niko tayari kuongozananae kwenda kujithibitishia zao la kahawa. Ahsante.
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi, kwanza niipongeze Serikali kwa mwaka wa fedha tuliopo kwa kuweza kupunguza hizo tozo 10 ambazo sasa zinaweza kusaidia kwa kiasi fulani wakulima wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hizi tozo zilizopunguzwa tozo tano zinahusiana na makampuni ambayo hayaja washawishi katika kuboresha bei ya ununuzi wa tumbaku, na tukizingatia kwamba wanaendelea kushusha kiwango cha kununua toka tani 60,000 mpaka tani 55,000 na imepelekea wakulima wanazalisha zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kutokana na tumbaku ya ziada ambayo ilizalishwa na ikapelekea Serikali kuwa na maongezi na makampuni bei ya dola 1.25 kwa grade ya juu. Lakini kwa sasa hivi tunavyozungumza wananunua tumbaku hiyo mpaka senti 64 kwa kilo. Sasa Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba wakulima wa tumbaku wanafaidika katika suala la bei kuliko na matatizo ambayo yametokea mwaka jana na tumbaku imekuwa sasa hivi inanunuliwa kwenye grade ambayo iko ya chini kwa kukaa muda mrefu kupata unyevu nyevu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Swali la pili, Chama cha Wakulima wa Tumbaku Mkoa wa Katavi (RATCO) kutokana na masawazisho ya bei ya pembejeo ilipelekea kuwa na madeni ya zaidi kudai vyama vingine/mikoa mingine zaidi ya dola 400,000 na ambazo kuna vyama vingine vimekufa na vingine bado viko hai.
Sasa Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wakulima wa tumbaku wa Mkoa wa Katavi ili waweze kulipwa madeni yao kutokana na masawazisho ya bei ya pembejeo ambayo ilitokana na usafirishaji wa hizo pembejeo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwanza ninamshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mawili ya nyongeza na ninaomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbogo kwa jinsi ambavyo amekuwa akifuatilia sana katika zao zima hili la tumbaku na jinsi wakulima wanavyopata shida katika eneo lake la Katavi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maswali yake ya (a) na (b) naomba nijibu; la kwanza naomba niseme tu kwamba kwa upande wa wakulima wa tumbaku zao la tumbaku, kunakuwa na makubaliano ya bei za kuzalisha kila mwaka, kwa mfano sasa hivi tuko katika mwaka wa 2018 unakuta kwamba tangu Septemba, 2017 wakulima hao walikuwa wameshajadiliana ni bei gani watazalisha kwa kiwango gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa mfano mwaka huu, tayari tutakapokuwa tunazalisha lile zao la tumbaku, tumeshajua ni shilingi ngapi wale wakulima watanunua. Lakini nikija katika swali lake la bei, kuhusu bei ya zao la tumbaku kwa maana amezungumzia dola 1.25.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe rai kwa wakulima wote wa tumbaku kwamba kwanza wazalishe tumbaku kwa kiwango cha ubora, lakini vilevile ninaomba ntoe siku saba kwa Mrajisi wangu kutokana na lile deni ambalo anasema wananchi wakulima wa Katavi wamekuwa wakiwadai kutokana na mambo ya WETCO hawajalipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema yale siyo madeni, wakulima wa tumbaku wana tabia ya kufidiana na kuchangiana katika zao la tumbaku bila kujali eneo, bila kujali umbali, bila kujali bei. Lakini kwa sababu ya Mheshimiwa Mbunge ameli-raise hili na mimi ninampa Mrajisi siku saba awe ameshashughulikia kuhakikisha kwamba wananchi wa Katavi wanapata haki yao ya malipo yao.
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mwaka jana Serikali ilipunguza tozo 17 kutoka kwenye zao la kahawa. Lakini kwa bahati mbaya sana tozo 17 hizi hazimgusi mkulima wa zao la kahawa moja kwa moja na hivyo haijamletea mkulima unafuu hata kidogo.
Je, Serikali sasa iko tayari kupitia upya tozo zile ambazo zitamgusa mkulima moja kwa moja ambazo ni kero na iweze kuzipunguza? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu langu la msingi nimezungumzia kwamba Serikali imepunguza au imetoa tozo 80 zaidi ya tozo 139 katika msimu huu wa fedha wa bajeti ya mwaka 2017/2018 zao la kahawa likiwemo. Sisi kama Serikali tunasema zao la kahawa na lenyewe ni mojawapo ya mazao mkakati ya biashara kwa nchi yetu na tumezingatia sana kuhakikisha kwamba tunaendelea kupunguza tozo katika zao la kahawa. Ahsante.
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza nawapongeza Wizara kwa juhudi zao za kuwasaidia wakulima wetu. Pamoja na majibu yaliyojitosheleza suala langu, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wananchi wamehamasika sana kulima kilimo cha pamba, nauliza Serikali ni kwa nini haioni umuhimu wa kuanzisha soko huria la uzalishaji wa mbegu bora ili kumrahisishia na kumpa unafuu mkulima wa pamba na kuachia kampuni moja tu ya Quton ambayo inazalisha mbegu hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kutokana na majibu ya Serikali, pamba imehamasika sana na kwa wastani tani 600,000 itazalishwa na itakuwa sokoni. Je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha pamba yote iliyozalishwa inanunuliwa ili kuwaondolea usumbufu wakulima wa pamba?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru naomba nichukue fursa hii kwanza kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge Khadija Aboud kwa maswali yake mawili ya nyongeza na vilevile kuwa makini katika kufuatilia kilimo ambacho ni mojawapo ya zao la mikakati kilimo cha zao la pamba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maswali yake ya msingi (a)na (b) swali la (a) amezungumzia kuhusu Kampuni ya Quton ambayo ndio imekuwa iki-dominate katika kufanya biashara hii ya pamba.
Naomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba ni kweli Kampuni hii ya Quton ilikuwa imeshinda tender, lakini katika kushinda tender yenyewe ilikuwa inafanya tu ...ginnery na kwa maana ya kwamba ilikuwa inafanya mbegu zile za kunyonyoa tu halafu inapeleka kwa ginners. Sasa baada ya Serikali kuona mapungufu hayo ikawa imefuta ile tender na ikaamua kuweka soko huria kwa ginners ili wao waweze kuwa wanafanya biashara moja kwa moja na wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo naomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge pamoja na wakulima wote wa zao la pamba ambalo ni zao la kimkakati kwamba kuanzia sasa hivi zao la pamba litakuwa linafanyika katika soko huria bila kujali kwamba ni nani anafanya hiyo biashara. (Makofi)
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, katika kuitikia wito wa Serikali wananchi wa mikoa ya Mwanza, Simiyu katika majimbo mbalimbali ikiwemo na Jimbo la Bariadi, Misungwi, Sumve pamba imelimwa kwa wingi sana.
Swali langu Mheshimiwa Waziri, endapo wanunuzi wa pamba watashindwa kuinunua pamba yote kwa sababu pamba imelimwa kwa wingi sana msimu huu. Je, Serikali imejipangaje kuwanusuru wakulima hawa ambao wameitikia wito wa Serikali wa kulima Pamba kwa wingi?
MHE. NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali naomba niwaambie wakulima wote wa zao la pamba kwamba tulishakutana na wadau wote wanaolima zao la pamba. Tulishakutana pia na mabenki yote kuhakikisha kwamba pia yale mabenki yanatoa mikopo kwa wafanyabiasha ili waweze pia kutoa mbegu na ukizingatia pia kwamba katika kile Kitalu cha Igunga ambacho kinatoa mbegu bora kabisa ile ya UKM 08 kwamba wakulima wanapata mbegu kwa wingi na vilevile wakulima hao na wafanyabiashara wanapata mikopo kutoka benki ili kuweza kuhakikisha kwamba zao la pamba linazalishwa kwa ufanisi na kwa ubora, ahsante.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba nimuulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Moja, kwa kuwa tunafahamu kwamba soko la kahawa bei yake imekuwa ikipanda na kushuka, Serikali haioni sasa umuhimu wa kuanzisha ruzuku maalum kwa ajili ya wakulima wa kahawa ili hata soko linapoporomka mkulima asipate maumivu sana kwenye upande wa mauzo? (Makofi)
Pili, tunaamini kwamba Vyama vyetu vya Ushirika vinayo nafasi kubwa sana ya kuhakikisha wakulima wan chi hii wananufaika. Ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha Vyama vya Ushirika vinaimarika na kuwa msaada kwa wakulima? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuhusu ruzuku katika bei ya mazao. Naomba niseme kwamba bei ya ruzuku kwa upande wa Serikali, sisi tunatoa mazao yote katika standardization na vilevile tutaangalia siku zijazo kuhusu Vyama vya Ushirika kama vinafanya vizuri basi tutaoa hiyo standardization na ruzuku katika vyama na mazao yote yanayohusika.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake (b) ni kuhusu Vyama vya Ushirika. Serikali tumejipanga kuhakikisha kwamba tunafanya total transformation, vilevile operations katika Vyama vya Ushirika. Ni kweli vingi havifanyi vizuri na tumeangalia kabisa vingine hata havifanyiwi mahesabu lakini kama Serikali, kama nilivyosema tumefanya total transformation kuhakikisha kwamba Vyama vya Ushirika vitakuwa vinafanyiwa mahesabu, vitakuwa vinafanyiwa ukaguzi ili tuweze kupata bei nzuri na mazao bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wote naomba niwataarifu kwamba hivi majuzi mwezi uliopita Tume ya Vyama vya Ushirika imeundwa na tayari imeshaanza kazi. Nashukuru. (Makofi)
MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa na mimi nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, naomba niulize swali dogo tu la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja kati ya matatizo yaliyosababisha wakulima wapate shida sana na zao la kahawa kuporomoka ni utendaji mbovu wa hivyo Vyama vya Msingi na Vyama vya Ushirika. Mwaka huu tunakwenda kwa mara ya kwanza kwa kuwa na Chama Kikuu cha Ushirika na Mkoa ambacho kitanunua kahawa kwa niaba ya wakulima.
Je, Serikali imejiandaa vipi kuwaandaa Watendaji Wakuu wa Vyama vya Msingi kwa sababu tumebakiwa na muda mchache na uwezo wao unaweza ukawa ni mdogo huko nyuma walishatuletea hasara, kwa mfano, Mbinga, hoteli ya Mbiku, ma-godown, viwanja na majengo yote yako kwa Msajili wa Hazina….
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi ambavyo amekuwa akifuatilia sana katika suala zima la Vyama vya Ushirika hususan katika Jimbo lake la huko Mbinga.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Jimbo la Mbinga na lenyewe limekuwa likilima sana zao hili la biashara la kimkakati la kahawa na ni kweli naomba nikiri kwamba vyama vingine vya ushirika vimekuwa havifanyi vizuri. Lakini kama nilivyomjibu Mheshimiwa Mbunge Stanslaus Mabula, katika maswali yake mawili ya nyongeza ni kwamba Serikali imejipanga sawasawa kufanya total transformation katika suala zima la Vyama vya Ushirika na tumejipanga kuingia kwa miguu miwili. Tutakuwa tunafanya mafunzo ya mahesabu na vilevile kuhakikisha kwamba ukaguzi utakuwa unafanyika kwa kina ili tuweze kupata mazao bora ambayo pia yatakuwa yanatupatia bei nzuri. (Makofi)
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nami nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la Kigoma Kaskazini linafanana kabisa na tatizo la wananchi wa Mkoa wa Simiyu kwa wakulima wa pamba. Katika Mkoa wa Simiyu kumezuka wadudu waharibifu wanaoharibu zao la pamba na mahindi na hitaji la dawa za wakulima hawa ni sawa na chupa milioni moja na laki nne, lakini mpaka sasa wakulima hawa wamepatiwa chupa 350 tu ni sawa na asilimia 25. (Makofi)
Je, Serikali ina mpango gani wa haraka kuwasaidia wakulima hawa ili kuhakikisha kwamba mazao hayo hayaharibiki? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Serikali naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Gimbi Masaba kwa swali lake la kuhusu pamba pamoja na wakulima wa zao la pamba na Waheshimiwa Wabunge wote ambao wanatoka katika Mikoa inayolima pamba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa habari njema naomba niseme tu kwamba Serikali tumejipanga kuhakikisha kwamba zao la pamba ambalo mdudu wa kweleakwelea pamba mbegu zake zinaharibika. Serikali imeshatoa shilingi bilioni tatu tayari kuhakikisha kwamba mpango huu wa dharura na tatizo hili la dharura linafanyiwa kazi na vilevile shirika la FAO limeshatupatia US dollar milioni 250 kwa ajili ya kutatua tatizo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba niwahakikishie kabisa wakulima wa pamba kwamba tatizo hili litatatuliwa hivi karibuni. Ahsante. (Makofi)
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kulitendea haki swali langu maana yake ni swali la muda mrefu miaka mitatu, lakini hizo fedha tumeshazipokea na tumezisahau.
Hata hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza; swali la kwanza, Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa kuwa NFRA walipewa eneo la kujenga godown au kiwanda katika Halmashauri ya Mji wa Babati kwa ajili ya kuchakata mahindi yetu kuongezea thamani, pamoja na kuwapa kiwanja hicho au eneo hilo zaidi ya heka sita mpaka leo mwaka wa tatu NFRA hawajafika kujenga godown kiwanda hicho. Naomba nifahamu ni lini NFRA watafika katika Halmashauri ya Mji wa Babati kujenga kiwanda hicho?
Swali la pili, kwa kuwa wananchi wetu wengi katika Mkoa wa Manyara na katika Halmashauri ya Mji wa Babati msimu huu wa kilimo cha mahindi hawajapata pembejeo za kilimo, hawajapata mbegu na mbolea, wamelazimika kupanda mahindi ya mwaka jana waliyovuna mashambani, mbegu hawajapatiwa. Mbegu zilizopo zinauzwa kwa bei ya juu kilo mbili shilingi 12,000.
Naomba nipate kauli ya Serikali ni kwanini hampunguzi bei ya mbegu za mahindi ili wananchi wetu waweze kupanda mbegu hizo badala ya kuwaachia sasa wanapanda mahindi ya mwaka jana? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote pia na mimi naomba nimpongeze kwa dhati kabisa Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi ambavyo kama alivyosema amekuwa akifuatilia jambo hili tangu miaka mitatu iliyopita. Vilevile naomba nichukue fursa hii kuwapongeza wananchi wote wa Jimbo la Babati Mjini kwa jinsi ambavyo wanafuatilia na kuzingatia umuhimu wa kilimo na vilevile kuweza kutoa ardhi kwa ajili ya kujenga mradi huu wa maghala.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu hiyo ninaomba nitamke hapa mbele ya Bunge lako Tukufu kwamba mradi huu tayari umeshakamilika na ninamuagiza Mtendaji Mkuu wa NFRA kuanza kazi mara moja ifikapo mwisho wa mwezi wa tatu. Huu mradi unagharimu milioni 8000. Kwa hiyo, Mtendaji Mkuu wa NFRA hili ni agizo, mwezi wa tatu mwishoni mradi huu uanze kazi mara moja kwa ajili ya kuongeza thamani ili wananchi hawa wa Babati waweze kupata ajira na thamani ya mazao yao pia iweze kuongezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili, Mheshimiwa Mbunge ameuliza suala zima la mbegu. Katika suala zima la mbegu, sisi kama Serikali mbegu huwa zinakusanywa na makampuni binafsi na ndiyo maana unakuta bei inakuwa ni kubwa, lakini kupitia Wakala wetu wa Taifa wa Mbegu tumeanzisha mpango mahsusi wa kuhakikisha kwamba tutakuwa tunazalisha mbegu ambayo inaitwa hybrid kwa ajili ya kuboresha ili iweze kuwa na bei pungufu.
Vilevile tunashirikiana na makampuni binafsi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wakulima wetu wanapata mbegu bora na kwa bei nafuu.
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Swali langu la nyongeza lilikuwa ni hilo aliloliongelea Mheshimiwa Ryoba, labda swali (b), kutokana na hizo posho kusuasua na wananchi wanakuwa hawazipati kwa muda, ni lini sasa Serikali itakaa na wale wananchi ili kuongea nao au kuwapa uhakika wa kuwapa hizo fidia kwa muda?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali moja dogo la nyongeza la Mheshimiwa mdogo wangu Agnes Marwa na wifi yangu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza sisi Wizara ya Kilimo kama nilivyosema kwenye jibu langu lile la nyongeza, ni kwamba hatuwezi tukafanya Wizara ya Kilimo peke yetu sisi kama Wizara ya Kilimo kwa sababu inawahusu wakulima kwa sababu hii inahusisha Wizara tatu; Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo ningependa kuwaasa Maafisa Kilimo wetu, Maafisa Ugani wetu kule kwenye halmashauri wajaribu ku-review zile posho na viwango vya posho ambavyo huwa wanavifanyia tathmini kwa wakulima wetu kabla hawajapeleka Wizara ya Maliasili na Utalii ili wakulima hawa waweze kupata haki zao stahiki. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuongezea majibu kwa yale Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo ameyajibu vizuri sana. Basi katika hili suala ambalo nimelisema Wizara ya Maliasili na Utalii sasa hivi inafanya mapitio ya zile kanuni zetu za kifuta jasho za mwaka 2011 ambazo ndizo zinaongoza namna ya kutoa kifuta jasho, si fidia kama inavyosomeka, ni kifuta jasho kwa wale wananchi ambao wameathirika. Kwa hiyo, baada ya hizi taratibu kukamilika basi mambo yatakuwa yamekwenda vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusu hili suala lake kwamba ni lini watalipwa, kama nilivyosema katika jibu langu la kwanza kwamba tarehe 29 na tarehe 30 mwezi uliopita maafisa wetu wameshakwenda kufanya tathmini. Baada ya tathmini hiyo kukamilika basi taratibu za kuwalipa hao wote walioathirika zitafanyika mara moja.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na mimi niulize maswali ya nyongeza, lakini kabla sijafanya hivyo, kwa ruhusa yako, kwanza naomba nichukue nafasi kwa niaba ya wananchi wa Urambo kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa kupitia Ofisi yake ya Rais, Manejimenti ya Utumishi kwa kauli aliyoitoa hivi karibuni, Mheshimiwa George Mkuchika, Waziri Mhusika, ya kuwarudisha kazini Watendaji wa Vijiji na Madereva waliokuwa wameachishwa kazi kutokana na elimu yao ya darasa la saba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuwarudisha kazini na kuamrisha walipwe mishahara yao yote ambayo wameikosa katika kipindi walichokuwa wamesimamishwa ni ishara na ushahidi tosha kwamba Serikali inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi ni sikivu. Tunaiomba Serikali yetu iendelee kuwasikiliza wanyonge na kuwatengenezea yale ambayo wanaona hayakwenda sawa. Ahsante sana Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyotoa lakini pia kuishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na Waziri Mkuu mwenyewe kwa kuunda Bodi ya Tumbaku mpya ambayo imeanza kazi vizuri. Ombi langu tu kwa Serikali ni kuiwezesha kwa kuipa vifaa zaidi kama komputa na kadhalika, lakini pia ateuliwe Mwenyekiti ambaye naamini atakuwa ana uzoefu na zao la tumbaku.
Mheshimiwa Spika, sasa naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa muda mrefu Serikali imekuwa ikiombwa na wakulima wa tumbaku kutafuta wanunuzi zaidi wa tumbaku ili walime tumbaku zaidi lakini pia ilete ushindani wa bei ili mkulima wa tumbaku anufaike na zao lake, nataka kujua suala hili limefikia wapi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Serikali haiwezi kuagiza mbolea kwa wingi hasa NPK ili mbolea hiyo iwafikie wakulima mapema kuliko kama ilivyokuwa kipindi kilichopita? Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwanza, naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mama yangu Mwalimu Margaret Simwanza Sitta kwa jinsi ambavyo amekuwa akifuatilia suala hili la zao la tumbaku kule Tabora na Tanzania nzima kwa muda mrefu kuhakikisha kwamba zao hili linakuwa na tija. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikija katika maswali yake mawili ya nyongeza ni kweli kabisa Bodi ya Tumbaku haina Bodi ya Wakurugenzi lakini imezinduliwa Disemba, 2017 na sasa hivi tunakaimu Mwenyekiti, ni miezi mitatu tu tangu imezinduliwa. Kwa hiyo, tunaamini kabisa Mheshimiwa Rais akiridhia kuteua Mwenyekiti basi na Bodi hii itaongeza tija katika utendaji wake wa kazi.
Mheshimiwa Spika, nikija kwenye swali lake hilohilo la nyongeza kuhusu ku-monopolize hii biashara ya tumbaku ni kwamba kama Serikali sasa hivi tuna makampuni manne tu ambayo yananunua tumbaku lakini tuko kwenye majadiliano na Zimbabwe, Misri, China na Vietnam. Vilevile Serikali ya Indonesia kupitia Kampuni ya Star International wao wameshakubali pia kununua tumbaku yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Spika, nikija katika swali lake la pili kuhusu ununuzi wa mbolea kwa pamoja, sisi kama Serikali tuna mbolea ya DAP pamoja na UREA ambayo yenyewe ndiyo iko katika mfumo ule wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja, NPK haiko katika mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, naomba niliarifu Bunge lako Tukufu na Mheshimiwa Mbunge kwamba mbolea hii ya NPK ambayo inatumika sana katika zao la tumbaku pia tunalichukua suala lake tutalifanyia kazi na hasa ukizingatia kwamba mbolea ya NPK mwaka jana ilitumika tu asilimia 21 ukilinganisha na ile ya UREA ambayo ilitumika asilimia 46. Kwa hiyo, wazo lako Mheshimiwa Mbunge ni zuri tunalipokea ili kuhakikisha kwamba mbolea inafika kwa wakulima kwa msimu. Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. DKT. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Mheshimiwa Naibu Waziri kwanza nikupongeze kwa sababu ulipopata tu Unaibu Waziri ulikuja Masasi na ukatembelea wakulima wa korosho. Kwa hiyo, changamoto za wakulima wa korosho unazifahamu. Nina maswali mawili yanyongeza.
Swali la kwanza; kwa kuwa hadi sasa wakulima wa korosho waliouza korosho zao katika msimu uliopita wanadai fedha zao takribani zaidi ya shilingi milioni 90 katika Jimbo langu tu la Masasi kwa hiyo fedha hizo ni zaidi ya shilingi milioni 90. Je, ni lini Serikali itahakikisha wakulima hawa wamelipwa fedha zao?
Swali la pili, lini Serikali sasa itaingiza sulphur ambayo itauzwa kwa wakulima kwa sababu tunafahamu wakulima wananunua sulphur kwa mwaka huu. Sasa lini Serikali itaingiza sulphur hiyo na kuisambaza kwa bei nafuu kwa wakulima wetu, kwa sababu kwa sasa begi moja ya sulphur imefika shilingi 70,000 mpaka shilingi 80,000? Ahsante sana.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwanza ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa umahiri wake wa jinsi anavyofuatilia wakulima wa zao la korosho katika Mkoa wa Lindi na Mtwara hususan katika Jimbo lake la Masasi na ninaomba kwa maana hiyo nijibu maswali yake yenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nikianza na lile la (a) ni kweli wakulima wa zao la korosho wanadai Serikali na naomba niseme tu kwamba Mkoa mzima wa Lindi na Mtwara ikiwemo Masasi wakulima wanadai zaidi ya shilingi bilioni 5.770 Serikali naomba niseme tu kwamba katika Mkoa wa Lindi wataanza kulipwa mwezi huu mwishoni na vilevile katika Mkoa wa Mtwara watalipwa mwezi ujao mwishoni.
Mheshimiwa Spika, nikija katika swali lake la (b) kuhusu suala zima la pembejeo, ni kweli kabisa tunaelewa kwamba kumekuwa na changamoto kubwa sana ya pembejeo katika zao zima la korosho na ninaomba nilitaarifu Bunge lako tukufu kwamba kwa upande wa sulphur habari njema ni kwamba Serikali tumeagiza tani 35,000 na lita 520 za viwatilifu na tunategemea mwezi huu Aprili awamu ya kwanza itafika na awamu ya pili itafika mwezi ujao mwishoni.
Mheshimiwa Spika, ninaomba niliarifu Bunge lako Tukufu kwamba pembejeo hizi kuanzia sasa zitanunuliwa kwa bei ambayo kwa upande wa sulphur haijazidi shilingi 40,000; vilevile kwa upande wa vile viwatilifu haitazidi shilingi 30,000; kwa maana hiyo ni habari njema haitakuwa shilingi 70,000 au 80,000 kama Mheshimia Dkt. Chuachua alivyosema bali itakuwa shilingi 40,000. Ahsante. (Makofi)
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri. Ninayo maswali madogo mawili ya nyongeza mafupi sana.
Kwa kuwa Serikali imetoa takwimu za mikopo inavyotolewa, lakini uhalisia wenyewe mikopo imekuwa haiwafikii wananchi wa vijijini ikiwemo Mkalama na Wilaya ya Dodoma ambako wanalima sana alizeti.
Je, Serikali iko tayari kuzielekeza benki hizo kwenda kwenye maeneo hayo mahsusi ili kununua zao la alizeti na vitunguu.
Swali la pili, swali la pili, je, Waziri yuko tayari kufuatana na mimi kwenda kuona wakulima wa vitunguu ambao sasa wanavuna ili aweze kutoa maelekezo ya upatikanaji wa mbegu bora na pembejeo kwa haraka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, nikianza na lile swali lake la nyongeza la (b) kwanza niko tayari kuongozana na Mheshimiwa Mbunge kwenda katika Jimbo lake la Iramba Mashariki ili kujionea hilo.
Vilevile ni kwamba Serikali sasa hivi tunaimarisha tafiti zetu kuhakikisha kwamba tunapata mbegu ambazo zitakuwa bora na za uhakika na za bei nafuu tukishirikiana na wakala wetu wa mbolea.
Mheshimiwa Spika, pia tuko katika awamu ya mwisho ya kufanya tafiti ya mbegu tatu za alizeti na zenyewe hizo tafiti hatua ya mwisho tunategemea mwakani tutaanza kutumia.
Mheshimiwa Spika, nikija kwenye swali lake la (a) ni kwamba lengo la Benki ya Kilimo ni kuhakikisha kabisa kwamba Wilaya zote za Tanzania wanapata mikopo kupitia Benki hii ya Kilimo na kama nilivyosema kwa kujibu katika swali langu la msingi Benki ya Kilimo riba yake ni asilimia nane mpaka 14 kitu ambacho ni masharti nafuu. Vilevile unalipa kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Spika, pia Benki ya Kilimo tumeigawa au imegawa kwa Kanda Nane na Mkalama iko katika Mkoa wa Singida na Mkoa wa Singida uko katika Kanda ya Kati kwa maana hiyo na yenyewe iko katika huo mpangilio.
Mheshimiwa Spika na vile vile Benki ya Kilimo ni kwamba inawafuata wakulima kule waliko. Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru. (Makofi)
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri wa Fedha, napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, kwa kuwa Mkoa wa Ruvuma ni miongoni wa mikoa ambayo ni food basket nchini Tanzania, je, Serikali inachukua hatua gani za makusudi za kuweka benki hii kila mkoa badala ya kuweka benki hii kikanda? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika,swali la pili, ili kuboresha uchumi wa viwanda tunaoutarajia ambao kimsingi malighafi zinatokana na kilimo asilimia 75. Je, Serikali ipo tayari kuongeza ruzuku ya mbolea ili mbolea iuzwe Sh.10,000 kwa kila mfuko wa kilo 50 badala ya mfuko ambao unauzwa sasa Sh.60,000 mpaka Sh.65,000? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kunipa nafasi ili niweze kufafanua swali la Mheshimiwa Mbunge, Jacqueline Msongozi wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Ruvuma, hususan katika kile kipengele chake cha (b) kuhusu ruzuku katika suala zima la mbolea.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Wizara ya Kilimo, kama alivyosema Mheshimiwa Waziri wangu siku chache zilizopita ni kwamba tupo katika mkakati na mpango maalum katika Bunge hili la bajeti kuhakikisha kwamba ule mfumo wa ununuzi wa mbolea ya pamoja, tutawaletea semina Waheshimiwa Wabunge wote ili waweze kujua nini maana ya bei elekezi ya mbolea ili waweze kuwa na uelewa mpana nini maana ya kutoka kule kwenye ruzuku na sasa hivi tupo katika mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, lakini wakulima wa pamba katika mikoa ambayo inahusika kulima pamba kama vile Mikoa ya Shinyanga, Simiyu na kwingineko bado ni wakulima wadogowadogo. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wakulima hawa wanakuwa wakulima wakubwa ili kuleta tija katika zao hili la pamba ambalo ni zao la kibiashara linalotegemewa hapa nchini Tanzania ili kuongeza Pato la Taifa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri Mkuu alifika Mkoa wa Mwanza na kufanya kikao na wadau wa pamba na kuwaahidi kwamba atarudi tena mwezi Mei ili kuweza kupanga bei ya pamba kwa msimu huu ambao unakuja; naomba kuiuliza Wizara, je, ni kwa nini isione kwamba waweze kupandisha bei ya pamba kutoka Sh.1,200 kwa msimu uliopita hadi Sh.2,000 kwa msimu ambao unakuja kwa sababu zao hili la pamba ndiyo dhahabu ya Mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu na mikoa mingineyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba kuchukua fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge, mdogo wangu Mheshimiwa Kiteto Koshuma kwa maswali yake mawili mazuri ya nyongeza na vilevile kwa jinsi ambavyo anafuatilia zao hili la kimkakati Tanzania, zao la pamba.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na swali lake la kwanza; ni kweli kwamba uzalishaji wa pamba ulikuwa ukishuka na kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, Serikali tumejipanga kwamba sasa hivi tutakuwa na mfumo bora wa uzalishaji wa zao la pamba kwa maana ya uzalishaji wa mbegu ile niliyoisema kwenye jibu langu la msingi, UKM08 na vilevile tuweze kuzalisha pamba zaidi kwa kuzingatia kwamba kitakuwa ni kilimo chakisasa na ni mfumo bora wa mbegu hii ambayo tumeianzisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye swali lake la pili, naomba niseme kabisa kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu amekuwa ni champion kabisa katika zao hili la pamba na mpaka sasa hivi ameshafanya mikutano na wadau mbalimbali kuhusu zao la pamba; mikutano zaidi ya sitana leo hii pia tunakutana na wadau wengine wa pamba, jana pia Mheshimiwa Waziri Mkuu alifanya tena mkutano mwingine na ginners wote wa pamba.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie mdogo wangu, Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali tumejipanga safari hii kuhakikisha kabisa kwamba zao la pamba litakuwa pia ni zao bora na litaendelea katika uzalishaji, ukizingatia tumeshaanzisha hii mbegu nyingine mpya niliyoisema ya UKM08.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tarehe 26, mwezi huu wa Nne, wadau wote wa pamba tutakusanyika kwa ajili ya kuangalia indicative price ya zao la pamba itakuwa ni shilingi ngapi. Kwa maana hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge mwezi huu kabla ya mwisho wa mwezi tutakuwa tumeshajua bei ya zao la pamba itakuwa ni shilingi ngapi.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mheshimiwa Naibu Waziri amejibu swali lake vizuri na linatia faida kwa wananchi. Lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maelezo yake amelezea kwamba Serikali itasimamia uuzaji wa mazao ya wakulima kwa njia ya mnada ili kuweka ushindani. Sasa mimi nataka kumuuliza hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, kwa nini Serikali isiweke masoko huria ili mkulima aweze kuuza mazao yake popote atakapo kwa kujiridhisha na bei itakayokuwepo kwa faida yake? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumejitokeza mtindo baadhi ya wakulima kuuza mazao yao bado yakiwa yangali shambani ili kukidhi matakwa ya haja yake wakati inapomkumba na yeye fedha hana.
Je, Serikali itachukua hatua gani ili kusitisha tabia hiyo ambayo inamnyonya mkulima anapouza mazao yake shambani, na kwamba anatajirika ambaye yule anayekwenda kununua mazao shambani na akavuna mazao yale na kwamba wakati mkulima anapata hasara kwa pesa anayopata ni ndogo na mazao yake yote yameshamilikiwa na mtu mwingine? Ningeomba tamko la Serikali linasemaje. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kwenye swali lake la kwanza amezungumzia Serikali kama tunaweza tukaruhusu mazao haya kuuzwa katika soko huria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye jibu langu la msingi nimesema kabisa kwamba Serikali imejipanga kuwa na mfumo rasmi wa uuzaji kupitia ile TMX kwa maana ya kwamba tutakuwa na soko huria lakini kupitia mfumo rasmi wa uuzaji kupitia chombo hiko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali naomba nitoe rai na onyo kwa wanunuzi kwa wakulima wote ni marufuku kuuza mazao yakiwa bado kondeni/shambani, wote watakaopatikana na hilo jambo watachukuliwa hatua stahiki za kisheria, ahsante. (Makofi)
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Katika msimu huu wa kilimo…
Mhesimiwa Mwenyekiti, nakushukuru katika msimu huu wa kilimo tumeshuhudia wakulima wa zao la mahindi mazao yao yameshambuliwa na viwavi jeshi aina ya fall army worms na viwavi jeshi hao bado ni tatizo. Nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba viwavi jeshi hao wanatokomezwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tumejipanga na sasa hivi ninapozungumza Shirika la WFP wameshatoa dola 250,000 na Serikali pia imeweza kutoa pesa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba viwavi jeshi vinatokomezwa katika msimu huu wa kilimo, nashukuru.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana Serikali kupitia Bodi ya Korosho waliingia mkataba na baadhi ya wakulima kuzalisha mbegu za korosho na miche hii hawa wakulima wakaisambaza lakini mpaka sasa tunavyoongea wakulima hawa hawajalipwa na hii ni baada ya Bodi ya Korosho kuchukua kazi iliyokuwa inafanywa na Mfuko wa Pembejeo ambao walikuwa wakizalisha watu wanalipwa kwa wakati.
Sasa ni lini Serikali itaisimamia Bodi ya Korosho kuhakikisha inawalipa hawa wazalishaji wa mbegu za korosho waliofanya kazi ya kizalendo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kweli Serikali tunaelewa kwamba zao la korosho ni mojawapo ya zao la kimkakati na ni kweli kabisa kwamba kuna wakulima hawa ambao wanaidai Bodi ya Korosho. Hata hivyo Serikali tumejipanga kwamba pesa hizi zinafuatiliwa na wakati wa bajeti Mheshimiwa Nape ataelewa majibu haya ya uhakika na ya kweli tunaweza kumpatia, ahsante. (Makofi)
MHE. MWANNE J. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2017 wakulima wa tumbaku wa Mkoa wa Tabora walisumbuliwa sana katika suala la ununuzi wa bei ya tumbaku. Je, Serikali imejipangaje kuhusu suala la ununuzi wa tumbaku kwa bei nzuri ili isijirudie kama ilivyokuwa mwaka 2007?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa hivi kwa upande wa zao la tumbaku tuna wanunuzi wakuu wanne. Hata hivyo kama Serikali tumejipanga kutafuta masoko mengine nje ya nchi, tumeweza kuongea na nchi ya Vietnam, China na Singapore; na naomba niwaeleze Waheshimiwa Wabunge na Bunge lako tukufu kwamba mpaka sasa hivi nchi ya Singapore tumeweza kufanikiwa na watanunua tani 1,000 kwa msimu huu. (Makofi)
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Katika majibu ya msingi ya Serikali imeeleza kwamba tani 62,000 za mahindi zilinunuliwa mwaka 2016/2017 na tani 26,000 zilinunuliwa mwaka 2017/2018. Unaona kwamba kiwango kinapungua badala ya kuongezeka wakati uzalishaji umeongezeka maradufu na wakulima wanaozesha mazao kwenye maghala. Ni zipi sababu zinafanya kiwango hiki kishuke? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, jinsi alivyozungumza ni kweli imekuwa ikishuka, mazao yetu yamekuwa yakishuka, lakini naomba niseme tu kwa kipindi cha mwaka wa fedha uliopita bajeti ilikuwa ndogo na tunategemea mwaka huu bajeti itaongezeka na hivyo tatizo zima hilo litakuwa limeshakamilika, ahsante. (Makofi)
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Singida pia tumehamasika sana kulima pamba na katika Jimbo langu la Singida Kaskazini pamba imelimwa kwa ekari 1,300 na tulipata pembejeo kutoka Serikalini ikiwemo dawa. Dawa hii ambayo tuliitumia kulingana na maelekezo ya wataalam; pamoja na Bodi ya Pamba kuja kupiga kwenye pamba lakini pamba hiyo imepukutisha majani na hivi sasa ninavyozungumza wananchi wa Kata za Ilongero, Ughandi, Mtonge, Kinyeto, Muhunga na Msange wanashindwa kabisa kupata mazao katika pamba ambayo wamelima katika msimu huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa kuuliza Serikali inatoa kauli gani kuhusiana na hasara hii ambayo wananchi wameipata?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nichukue fursa hii kuwapa pole sana wananchi wa jimbo lake kutokana na tatizo lililojitokeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kama alivyosema ni kwamba sisi kama Serikali tutatuma wataalam wetu kwenda kwenye jimbo lake kwanza kuthibitisha kama tatizo hilo limetokea, na kama ni kweli limetokea basi ninaagiza Bodi ya Pamba, na sisi tuna mfuko wetu kwenye Bodi ya Pamba kwamba maeneo yote ambayo yamelimwa pamba tutatoa vile viuatilifu kwa bure isipokuwa mbegu wataendelea kununua. Ahsante.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, bila kuathiri wajibu wa Serikali wa kuratibu, ni kwa nini kusiwe na soko huria la mbolea kwa sababu haipatikani kwa wakati?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, wakati watu wanaongezeka, ardhi hususan inayofaa kwa kilimo haiongezeki. Nini mkakati wa Serikali wa kuja na mkakati mpya wa kuratibu kilimo chenye tija katika eneo dogo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu ameuliza swali ambalo pia linaendana na Wabunge wote hususan wale wanaotoka katika majimbo ya mijini, naye ni Mbunge wa mjini, hususan kuhusu kwamba watu wanaongezeka lakini ardhi haiongezeki.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nilieleze Bunge lako tukufu kwamba sisi kama Serikali tumejipanga kuongeza uzalishaji na teknolojia ya hali ya juu. Vilevile lengo letu kubwa ni kuhakikisha kwamba wakulima hawa siyo tu kwamba wanalima kilimo cha kujikimu lakini vilevile kiwe ni kilimo cha kibiashara. Naasa kila Halmashauri zote nchini ziweze kuwa na zile green houses. Kilimo kile kinalimwa katika sehemu ndogo lakini uzalishaji wake unakuwa ni mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza ni kwamba soko huria Serikali kazi yetu ni kuratibu, ku-control na ku-regualte, kwa maana hiyo, kwenye mbolea soko huria lipo, isipokuwa katika zile mbolea za DAP pamoja na Urea kwa maana ya kupandia na kukuzia, hiyo sisi kama Serikali kama tulivyosema ni kwamba Jumapili tutatoa semina kwa Waheshimiwa Wabunge ili waweze kuwa na uelewa mpana na wa pamoja kuhusu nini maana ya bei elekezi. Vilevile mbolea kuanzia sasa ziweze kufika kwa wakati na ziweze kuenea kwenye maeneo yote ya vijiji ili iwe kama soda na sukari. Ahsante.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa Mkoa wa Katavi unazalisha mazao ya kilimo ya biashara na chakula, nini mkakati wa Serikali wa kuwasaidia wakulima hawa ambao wamejitolea, wanafanya kazi kwa bidii lakini tatizo kubwa ni ukosefu wa masoko kwa mazao wanayozalisha? Nataka kupata…
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mazao ya chakula na mazao yale ya kimkakati ya biashara sisi tumesema kama Serikali hatufanyi biashara, kazi yetu ni ku-regulate na ku-control. Isipokuwa kama Serikali, sisi kuanzia sasa tunatoa vibali ili wakulima wote wawe na uhuru wa kuweza kuuza bidhaa zao zote au mazao yao yote nje ya nchi lakini kwa kuhakikisha kwamba pia kama Serikali tuna chakula cha kutosha ndani ya nchi.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Naipongeza Serikali kwa jitihada zake kuhakikisha inaboresha zao la kahawa.
Mheshimiwa Spika, kwenye zao la kahawa kulikuwa na kodi nyingi na Serikali imejitahidi kuondoa kodi 17, lakini hizi kodi hazimnufaishi mkulima moja kwa moja zinawalenga wafanyabiasha. Je, Serikali imejipanga vipi kuondoa hizi kodi ambazo zinamgusa moja kwa moja mkulima ili aweze kupata bei nzuri ya kahawa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, mara nyingi mkulima anapoanza kulima, kupalilia mpaka kuvuna hasaidiwi kitu chochote, mwisho anaanza kukatwa kodi na mambo mengine. Je, Serikali imejipanga vipi kumsaidia huyu mkulima ili iweke miundombinu mizuri kuanzia anapolima akiwa shambani mpaka kwenye mnada? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bilakwate, Mbunge Kyerwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza, naomba nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi ambavyo anafuatilia kwa ukaribu sana zao hili la kahawa ambalo linalimwa pia kwa wingi katika Jimbo lake lile la Kyerwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikija kwenye maswali yake mawili ya nyongeza, katika swali lake la kwanza, ni kweli kwamba Serikali tumeliona hili na ndiyo maana tumeanzisha ule utaratibu wa kuuza kahawa mnadani moja kwa moja kupitia Vyama vyetu vya Ushirika. Vilevile Serikali tumepunguza tozo ya mauzo ya mazao kupitia cess au farm gate price kutoka asilimia 5 hadi asilimia 3.
Mheshimiwa Spika, swali lake lile la pili ni kwamba zao la kahawa linategemea sana na muonjo ule wa kahawa. Kwa maana hiyo, katika kuweka ubora wa miundombinu pia na ubora wa zao lenyewe, ni kwamba kulekule shambani wakulima wanapaswa kutumia zile CPU kwa ajili ya kuchakata zile kahawa kwa sababu kahawa mbichi hairuhusiwi, hivyo iweze kuanikwa na kusafishwa vizuri, kabla haijapelekwa kukobolewa kule kwenye curing.
Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwanza nampongeza kwa kazi nzuri ambazo anazifanya kwa ufuatiliaji wake. Hata hivyo, zao hili la mkonge Serikali haijalipa umuhimu unaostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais alifuta hati za mashamba mbalimbali Mkoani Tanga na katika zile hati, Halmashauri zetu zimeshatenga maeneo maalum ya kutafuta wawekezaji. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri tushirikiane kupata wawekezaji wa kuaminika ili kuweza kuja kuwekeza kwenye hili zao la mkonge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali mawili. La kwanza, tulikuwa tunahitaji sana Mkutano wa Wadau wa Mkonge ambao unajumuisha Wabunge ili tuweze kujadili kwa undani zao hili la mkonge na kuona namna gani tunaweza kulifufua. Sasa Wizara iko tayari kuitisha mkutano huo mapema ili tuweze kujadili suala hilo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, Kampuni ya Katani Limited iliingia mkataba na wakulima wa mkonge mbalimbali katika Mkoa wa Tanga na mkataba huo umekuwa unalalamikiwa sana na wadau hawa (outgrowers) ambao wanalima mkonge. Wizara ina mpango gani, pamoja na kuboresha mkataba huo, kumilikisha wale wakulima wadogo wadogo ardhi ambazo wamepewa na Katani Limited? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Balozi Adadi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nami naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Balozi, amekuwa akifuatilia juu ya zao hili la mkonge hata pale ofisini kwangu amekuja mara kwa mara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali la kwanza, ni kweli tumegundua kabisa kwamba mikataba hii ya wale wakulima wadogo wa mkonge haiwanufaishi wao. Nasi kama Serikali tumejipanga kuhakikisha kwamba kabla ya mwezi huu tutaitisha kikao kikubwa sana cha wadau kwa maana ya kwamba wale wakulima wadogo (outgrowers) kupitia chama chao kile cha SISO, Bodi ya Mkonge pia Mamlaka ile ya Katani Limited pamoja na Msajili wa Hazina na Wabunge wote wa Mkoa wa Tanga ili tuweze kujadiliana na kukubaliana kwa pamoja na mwisho wa siku mkulima aweze kunufaika na tuweze kuwa na win-win situation.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye swali lake la pili ni kwamba sisi kama Serikali tumeshaanza kufanya ile mapping na survey katika hatua za awali na namwomba Mheshimiwa Mbunge awasiliane pia na Halmashauri. Nitoe rai kwa Halmashauri husika iwasilishe na ihakikishe inashiriki katika zoezi zima la kuwamilikisha wakulima hawa kwa njia zote ili waweze kupata haki yao. Ahsante.
MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Spika, kwanza ahsante sana kwa kunialika kwenda kuona ngoma, niko tayari kwenda huko. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kwanza kumpongeza Naibu Waziri wa Kilimo kwa majibu yake mazuri aliyonijibu. Hivi sasa maeneo mengi yameonekana kuwa na ugonjwa wa mbegu hii UKM08. Je, Serikali inatoa tamko gani kwa wakulima wa zao la pamba kwa maeneo ambayo yanaathirika na ugonjwa huu Fusarium hasa ikizingatia kwamba viuatilifu vinavyokuja havifikii viwango na kusababisha mashamba mengi kuharibika?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri ameelezea kwamba kuna mkakati mzuri kwa mwaka 2016/2017 ekari moja imeweza kuzalisha kilo 300 lakini kwa mwaka 2016/2017 wastani ambao tumeweza kukusanya kwa nchi nzima kwa maana kwa mikoa 17 na wilaya 56 ni takribani kilo milioni 120. Kwa hiyo, atakubaliana nami kwamba zao la pamba linazidi kuporomoka. Ukigawanya kwa wastani katika zao zima kwa nchi nzima ni Mkoa mmoja tu wa Simiyu wenye kuzalisha kilo 70,000 na mikoa 16 ndiyo unaigawanya. Kwa hiyo, kama Wizara iko shughuli ya kufanya kuhakikisha zao hili linaongezeka kwa uzalishaji. Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, awali kabisa, naomba nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa sababu amekuwa akifuatilia sana juu ya zao zima la pamba na hasa ukizingatia na yeye pia ni mfanyabiashara wa zao hili la pamba.
Mheshimiwa Spika, nikija kwenye maswali yake mawili madogo ya nyongeza kwa ufupi kabisa na kwa pamoja ni kwamba zao la pamba kama zao la pamba na mbegu, sisi kwenye zao la pamba zile mbegu huwa inachukua muda mrefu sana na ukizingatia kwamba mbegu hizo tunazosema utafiti unafanyika muda mrefu muda wa karibu sana na kwa haraka ambao unaweza ukafanyika ni ile miaka mitano. Kwa maana hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote wajue kabisa kwamba suala zima la utafiti huwa linachukua muda mrefu na muda mfupi ambao unaweza ukafanyika ni kipindi cha miaka mitano.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake lile la pili la nyongeza kwamba kwa nini kilimo hiki cha zao la pamba kimeporomoka, ni kweli kwamba wakulima walikuwa hawafuati zile kanuni bora za kilimo cha pamba. Nichuke fursa hii kumpongeza na kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu amekuwa ni champion, amekuwa akihamasisha na akiwaeleza hata Wakuu wa Mikoa juu ya ufuatiliaji wa zao zima la pamba.
Mheshimiwa Spika, vilevile amemuagiza hata Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI kuboresha suala zima la ugani. Pia kama Serikali tumejipanga kuhakikisha kwamba katika msimu wa 2018/2019, tutaboresha zao la pamba kutoka hiyo tani 300,000 kwa ekari hadi tani 600,000 kwa kuzingatia hayo maelezo ambayo nimesema ili wakulima wote nchini waweze kuhakikisha kwamba wanafuata kanuni bora za kilimo cha pamba. Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza naomba nimpongeze Naibu Waziri wa Kilimo kwa majibu mazuri na kihakika kama Wizara wanaonesha wanalitambua suala hili vizuri. Kwa hilo, nawapongeza sana kwa majibu haya.
Mheshimiwa Spika, kuanzia 2011 - 2018 ni miaka saba sasa, hawa wakulima 435 wanaodai zaidi ya milioni 150 au Dola 74,000 bado wanadai. Kwa kuwa Bodi ya Kahawa ilifanya makosa kumlipa mtu mwingine na Mheshimiwa Waziri amekiri kwenye majibu yako kwamba iko kwa Mwanasheria, wakulima hawa wanataabika na hii ni Serikali ya wakulima, ni lini fedha hizo zitapatikana na Mwanasheria ataweza kuliharakisha suala hili?
Mheshimiwa Spika, la pili kwa kuwa hii inatokana na matatizo ya soko hili la kahawa, ni mkakati gani uliopo wa bei na masoko ya kahawa kwa wakulima wetu? Wananchi wanataka kusikia. Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nichukue fursa hii nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi ambavyo amekuwa akifuatilia sana suala zima la zao hili la kahawa katika jimbo lake. Kwenye maswali yake madogo mawili ya nyongeza, mimi nimejibu kwenye majibu yangu ya msingi kwamba hili suala liko Mahakamani na jambo linapokuwa Mahakamani, sisi kama Serikali tunaviachia vyombo vya sheria viweze kuchukua mkondo wake na ukizingatia pia Mwanasheria Mkuu ndiyo in charge katika suala zima hili.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili la nyongeza, ni kwamba, kama Serikali hata zao la kahawa tumejipanga na tumesema tunafufua, tunaimarisha Vyama vya Ushirika kuhakikisha kwamba wakulima wetu wa Kitanzania hawaonewi na wanakuwa na strong bargaining power kupitia Vyama vya Ushirika ili bei zao ziwe nzuri na mazao yaweze kuwa bora. Nashukuru.
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru mimi nina swali dogo la nyongeza. Tarafa ya Herujuu huko Kasulu tunalima Kahawa nyingi na hasa Kata ya Herujuu, Kata ya Muhunga na Kata ya Muganza lakini eneo hilo halina Chama cha Ushirika na Chama cha Ushirika kiko Buhigwe kilometa 45. Ni kwa nini Mheshimiwa Waziri asitoe ruhusa sasa wakulima hawa wakauza kwa watu binafsi?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, hatuwezi kuwaruhusu kuuza kwa watu binafsi kwa sababu tutakuwa tume-distort mfumo tunaojaribu kuujenga. Tunajaribu kujenga mfumo hapa ambao tukiruhusu hicho anachokisema tutakuwa tumeuvuruga tena wenyewe wakati tunajaribu kutengeneza.
Mheshimiwa Spika, mimi binafsi Jimboni kwangu tunalima kahawa, lakini wale wakulima wa kwangu tumewaunganisha na vyama vingine ambavyo vina uwezo wa kufika sokoni na sisi tunaendelea tu kumshauri Mheshimiwa Nsanzugwanko kufanya namna hiyo. Jambo muhimu hapa ni kuangalia uwezekano wa wao wenyewe kuwa na AMCOS yao; na AMCOS zinaruhusiwa kufikisha Kahawa kwenye soko kule Moshi.
MHE. JAMAL KASSIM ALI: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kumpongeza Naibu Waziri kwa kazi kubwa anayoifanya. Pamoja na majibu mazuri aliyotoa nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa vile Sera ya Serikali yetu ni kwenda kwenye uchumi wa viwanda na viwanda vingi vimekuwa na uhaba wa malighafi ambazo zinatokana na bidhaa za mazao na kupelekea viwanda vyetu kuagiza malighafi kutoka nchi za nje, je, Serikali ina mkakati gani kupitia benki hii sasa kuanza kukopesha wakulima wakubwa ambao wataongeza uzalishaji wa malighafi ambazo zitaenda kulisha viwanda vyetu?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, benki hii imekabiliwa na uhaba wa mtaji, ilianzishwa kwa mtaji wa shilingi bilioni 60 lakini lengo lake lilikuwa kufikia mtaji wa shilingi bilioni 80. Je, nini commitment ya Serikali kuhakikisha kwamba mtaji wa benki hii utaongezeka ili kusaidia kuongeza idadi ya wakopeshaji lakini pia kuongeza single borrow limit kama ambavyo maelekezo ya BOT yameelekeza?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Jamal, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nieleweke kwamba Benki yetu ya Kilimo ni benki ya kisera tofauti na zile benki zingine za kibiashara. Benki hii ya Kilimo ambayo ni ya kisera ilikuwa imeundwa kwa makusudi maalum kwa ajili ya kusaidia wakulima wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake hili kuhusu wakulima wakubwa, ni kweli hawa Niche Farmers kwa maana ya wakulima wakubwa sera na sheria yetu ni katika kuhakikisha kwamba na wenyewe wanafanya na wakulima wadogo kwa maana ya outgrowers ili kuweza kuongeza ule mnyororo wa thamani katika mazao yetu ya kilimo. Katika Benki yetu ya Kilimo ni kwamba wenyewe tunaposema ni benki ya kisera ni kwa sababu riba yao ni ndogo zaidi kutoka asilimia 8 hadi asilimia 12 kulingana na wakati ule ambao wao wenyewe wanaomba kama ni muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu ambao unafika miaka 15.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili kuhusu mkakati pamoja na mtaji, kama nilivyosema hii ni benki ya kisera kwa maana hiyo Serikali imewekeza asilimia 100 katika benki hii ili kuhakikisha kwamba inawakomboa wakulima. Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu limeshapatiwa majibu, lilikuwa linafanana na swali la Mheshimiwa Lwakatare.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri sana ya Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, naomba nitoe ufafanuzi mdogo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na maswali ambayo yameulizwa sisi kwenye Wizara ya Kilimo tuna mpango mkakati wa kuendeleza kilimo ambao pia ulikuwa umezinduliwa juzi na Mheshimiwa Rais. Na suala la vijana pia limezungumzwa na hili jambo lipo, kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba tunatakiwa tuwe na vitalu nyumba kwenye kila Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile ni kwamba kama Wizara ya Kilimo tuna mfuko wetu ule wa pembejeo ambao unatoa mikopo kwa riba asilimia saba hadi nane ili kumuwezesha mkulima aweze kunufaika. Vilevile niwaombe Waheshimiwa Wabunge wote kupitia halmashauri zao waweze ku-endorse kule kwenye halmashauri ili mfuko wetu wa pembejeo uweze kutoa hii mikopo ya bure kabisa ambayo ni asilimia saba hadi nane; huo ulikuwa ni ufafanuzi. Nashukuru. (Makofi)
MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Swali la kwanza, kwa kuwa Serikali inatambua kwamba zao hili la mchikichi nchi yetu iliipatia nchi ya Malaysia miaka ya 70 na limekuwa likifanya vizuri sana kwenye nchi hiyo na kukuza uchumi. Kwa kuwa zao hili linazalisha bidhaa zaidi ya 10, naweza nikataja tu chache kwa kifupi sana, linatumika kuzalisha mafuta ya mawese lakini pia mafuta ya mise kutokana na mbegu iliyoko ndani. Pia zao hili majani yake yanasaidia kuezekwa katika mapaa yetu ya nyumba, lakini pia linasaidia katika utengenezaji …
Wa sabuni za magadi ambazo hata Wabunge wako katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wamekuwa wakizitumia na mazao mengine kutokana na muda naomba nisiyataje. Kwa nini sasa Serikali haioni ni wakati muafaka wa kutengeneza Bodi maalumu ambayo itashughulika na mchikichi na kutotegemea Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kwa sababu Bodi hiyo inaendeshwa kwa kusuasua? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, haiwezekani zao la mchikichi kwa kiwango kikubwa lilimwe katika Mkoa wa Kigoma na mikoa jirani, lakini Kituo cha Utafiti kikawekwa Mikocheni Dar es Salaam na Tabora. Kwa nini sasa wasifungue ofisi ya utafiti katika Mkoa wa Kigoma ili wakulima wetu wa michikichi waweze kwenda kufanya consultation na kupata ushauri mbalimbali katika mkoa wao? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimjibu ndugu yangu Mheshimiwa Sabreena Sungura maswali yake mawili, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge anayetoka Kigoma kwa kufuatilia zao zima hili la mchikichi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye maswali yake, swali la kwanza, kila zao linataka liwe na Bodi yake, kwa maana hiyo gharama zake zinakuwa kubwa sana. Naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba Bodi yetu ya Mazao ya Nafaka Mchanganyiko si kwamba inasuasua, tunawashukuru sana Wabunge juzi wamepitisha bajeti yetu ya Wizara ya Kilimo na sasa hivi tumejipanga kuhakikisha kwamba Bodi yetu ya Mazao Mchanganyiko inafanya kazi kwa kuboresha zaidi ili hili zao letu la mchikichi ambalo linasimamiwa na Bodi ya Mazao Mchanganyiko liweze kufanya vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye swali lake la pili kwamba kwa nini Mkoa ule wa Kigoma usiweze kuwa na Kituo cha Utafiti. Ni kwamba hivi vituo vyetu vya utafiti hususan katika zao la michikichi vimewekwa kikanda. Kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi kwamba katika Mkoa wa Tabora, pale Tumbi tafiti zetu zinafanyika mahali pale. Kwa maana hiyo, hata kile Kituo cha Mikocheni kinafanya tissue culture. Naomba niseme kwamba Mkoa wa Tabora uko katika Kanda ya Magharibi ambapo Mkoa wa Kigoma upo chini yake. Ahsante.
MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Faida zote zinazopatikana katika michikichi zinapatikana pia katika zao la minazi. Je, Serikali ina mikakati gani ya kufufua zao la minazi ambalo linalimwa zaidi katika Mikoa ya Ukanda wa Pwani?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimjibu Mheshimiwa Dau swali lake moja dogo la nyongeza kuhusu minazi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunaelewa kwamba minazi nayo ni zao muhimu sana kwa kilimo katika nchi hii. Kama nilivyosema ni kwamba kupitia Bodi yetu ya Mazao Mchanganyiko ambayo Bunge lako Tukufu limepitisha bajeti hapa, minazi nayo ipo chini ya Bodi yetu ya Mazao na Nafaka Mchanganyiko. Kama Serikali tuko tayari kuhakikisha kwamba tunaimarisha zao la minazi ili nalo liweze kuwa ni zao la kibiashara na chakula kama kiungo. Ahsante.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itakubaliana nami kwamba uanzishwaji wa Vituo vya Utafiti wa Mazao ya Kilimo, vilianzishwa vingi kwa kanda na lengo lilikuwa zuri, lakini utendaji wa vituo hivyo umeanza kusuasua hivi karibuni kwa sababu ya kutokupata fedha za kutosha za kusimamia shughuli zake. Mfano mzuri ni Kituo cha Utafiti wa Mazao ya Korosho pale Naliendele. Ni lini Serikali sasa itapeleka fedha za kutosha ili vituo hivi vianze kufanya kazi kama vilivyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa mkwe wangu Nape Nnauye, Mbunge wa Jimbo la Mtama, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Vituo vingi vya Utafiti vya Wizara yetu ya Kilimo, vinasuasua lakini kama tunavyoelewa kwamba vituo hivi na sisi kama Wizara tumewaambia pia wajiongeze zaidi hata wao, si tu kutegemea pesa ya Serikali kwa sababu vituo vyetu vya utafiti vinaweza pia vikaandika proposal kwa ajili ya kuweza kupata fedha pia kutoka kwa wafadhili mbalimbali ili viweze kufanya kazi yake vile inavyotakiwa. Ahsante.
MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Zao la mawese ambalo ndiyo mchikichi linazalisha vilevile petroli na mafuta ya kula. Nchi ya Malaysia ambayo imechukua mbegu hii Tanzania ina mafanikio makubwa sana ya zao hili. Je, Serikali namna ilivyofanya sasa kupeleka zao la korosho kila mkoa, kwa nini kusiwe na affirmative action ya kupanda michikichi siyo chini ya milioni 30 ili Serikali i-benefit na zao hili ambalo ni zuri kwa uchumi wa nchi hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zungu, Mbunge wa Ilala, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimjibu tu kwamba sisi kama Serikali tumejipanga kuhakikisha zao hili la mchikichi ambalo linatoa mafuta ya mawese linafanikiwa kwa kasi. Kama Wizara ya Kilimo tuna programu yetu ya Supporting Indian Trade and Investment in Africa (SITA), kuhakikisha kabisa zao hili la mchikichi nalo linatiliwa mkazo na liweze kufanya vizuri. Ahsante.
MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Februari, 2017, Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Kigoma RCC ilipitisha mkakati wa kuendeleza zao la michikichi. Mpaka leo toka barua imepelekwa Wizara ya Kilimo hata kujibu kwamba imepokea barua ile kutoka Mkoa wa Kigoma haijajibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu yote yanayotolewa hapa kuhusiana na tissue culture Mikocheni, utafiti pale Tabora si ya kweli kwa sababu Kigoma ndiyo imepeleka mbegu Mikocheni na wala si Serikali. Je, Serikali haitaki kututhibitishia kwamba imeshikwa na wafanyabiashara wanaoagiza mawese ghafi kutoka Indonesia na Malaysia na ndiyo maana haitaki hata kujibu barua ya Mkoa wa Kigoma ya kuendeleza zao la michikichi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja dogo la nyongeza la kaka yangu Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake ni zuri na kwa sababu Serikali hii ya Awamu ya Tano ni ya Hapa Kazi tu basi ningemwomba sana, sana, sana Mheshimiwa Mbunge kaka yangu kwa heshima na taadhima atuletee nakala ya hiyo barua sisi tuko tayari kuifuatilia na kuhakikisha kwamba tunaifanyia kazi.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuulizwa maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tulitegemea kwamba baada ya kuanzisha Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ingekuwa Mkombozi wa mazao mengine ambayo hayana bodi, lakini kuna changamoto ya fedha kwenye bodi hii.
Je, Serikali ina mpango gani wa kutenga fedha nyingi za kutosha ili Bodi ya Nafaka na Mazao iweze kununua mazao mengine pamoja na mbaazi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa soko la India limeonesha kulegalega na kwenye zao la korosho tulipoachana na soko la India tumeona kuna mafanikio baada ya kuja Waturuki na Wavietinam; Serikali ina mpango gani wa kuingia kwenye masoko mengine ili kuacha utegemezi wa soko la India?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge RAS Mstaafu na kaka yangu Mheshimiwa Chikota maswali yake madogo mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, kama Serikali ni kwamba tumeielekeza na kusisimamia Bodi yetu ya Mazao Mchanganyiko kwamba kuanzia sasa wajikite zaidi katika kufanya biashara ile ya kilimo cha ushindani. Tayari tumeshaanza kufanya mazungumzo na NSSF na mazungumzo hayo yamefanikiwa na tayari tumeshapata shilingi bilioni 3.6 kwa ajili ya kununua mashine zile kwa ajili ya viwanda vya mahindi na alizeti kwa maana ya mashine mbili na tayari zimeshafika bandarini.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili la nyongeza, ni kwamba ni vyema sisi kama Serikali; naomba niwaase Halmashauri zote nchini kwamba tutoe elimu kwa wakulima wetu kuweza kufanya kilimo cha kibiashara (commercial farming) kwa sababu unapokuwa kwenye commercial farming, utaweza kujua ulime kilimo cha aina gani? Mazao gani? Kwa bei gani? Utauza wapi? Kwa maana hiyo, hakutakuwa na hasara yoyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba niwaeleze Waheshimiwa Wabunge kwamba mbaazi ni chakula kama vyakula vingine, tena ina protini zaidi kuliko maharage na inaongeza damu mwilini kuliko maharage. Vilevile nawaomba hata wale wanaofanya vyakula vya mifugo, ni kwamba hizi mbaazi zetu pia zinatumika vizuri sana katika vyakula vya mifugo kama ilivyokuwa soya. Ahsante. (Makofi)
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, napongeza majibu mazuri ya dada yangu Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa, mchapa kazi na ninaona kabisa anakwenda kuchukua Jimbo la mtu huko Mbeya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza; kwanza kabisa Rufiji tunatambua jitihada anazofanya Mheshimiwa Rais za ujenzi wa bwawa la Stiegler’s Gorge kama ambavyo amelisema Mheshimiwa Naibu Waziri na kwamba tunatambua Serikali inapelekea zaidi ya shilingi trilioni mbili kwenye mradi huu na kuifanya Rufiji kuwa moto moto kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu wa Stiegler’s Gorge una zaidi ya ekari 150,000 ambazo zimetengwa kwa ajili ya kilimo. Swali langu kwa Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo: Je, Serikali inawaandaaje Warufiji sasa ili kuweza kupokea fursa hizi za eneo hili la kilimo zaidi ya ekari 150,000 katika kuweka miradi mbalimbali ikiwemo na ule mradi wa kiwanda kikubwa cha sukari kule Rufiji? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, Watanzania wa Rufiji kwa asilimia 90 wanategemea kilimo na RUBADA ilikuwa katika Kata ya Mkongo pale Rufiji; na hii ndiyo kata iliyoathirika sana kwa wafugaji kuingiza mifugo yao eneo la wakulima; je, Serikali inajipangaje kuwasaidia wakulima hususan katika vijiji vya Mbunju, Ruwe pamoja na Mkongo Kusini ambao wameathirika sana kwa mazao yao kuliwa na wafugaji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwanza kipekee kabisa naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji kwa dhati kabisa kwa maana yeye alikuwa ni sehemu mojawapo ya watu ambao walishatueleza na wakatuambia kabisa kwamba mradi huu wa RUBADA ni non-starter na yeye alikuwa ni sehemu kama Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Sheria, kuleta na kupendekeza kwamba mradi huu wa RUBADA haufanyi kazi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya utangulizi huo, sasa naomba naiende moja kwa moja kumjibu maswali yake madogo sana ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba sisi kama Serikali katika Bonde hili la Rufiji ni hekta 1,350 kwa ajili ya mradi wa Stiegler’s Gorge. Naomba niseme kwamba eneo la hekta 300,000 limetengwa kwa ajili ya kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hizo hekta 300,000 zilizotengwa kwa ajili ya kilimo, ni kwa ajili ya irrigation scheme. Kwa maana hiyo, naomba nimhakikishie kwamba wananchi wa Rufiji na maeneo mengine yote watanufaika kwenye kilimo kupitia mradi huu ambao unaitwa irrigation scheme.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine lile la (b) ni kuhusu suala zima la migogoro aliyoizungumzia kuhusu ardhi. Ni kwamba Serikali tumejipanga na mpaka sasa hivi sheria inaandaliwa; tunaangalia suala zima la migogoro hii ya ardhi na maandalizi tayari yameshafanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge avute subira, Serikali inaandaa suala zima la ardhi kwa sababu tumegundua kwamba kuna migogoro mingi sana kati ya wakulima na wafugaji. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali ambayo nimeyaelewa yameeleweka nina maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, utafiti ni muhimu kwa ajili ya maendeleo ya kilimo lakini nao ustawi wa wananchi kwa kujipatia kipato nayo ni muhimu. Kwa kuwa wananchi hawa wana eneo dogo la kulima na nyuma ya kitongoji hicho ni hifadhi. Je, Serikali haioni umuhimu wa angalau kugawa pori hili ambalo ni zaidi ya heka mia tano, kugawa kidogo kuwapatia wananchi waweze kulima?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri anafahamu sana kitongoji hicho na hiyo kata anaifahamu kwani wapiga kura wake wako huko. Je, yuko tayari kuongozana na mimi kwenda kwenye kitongoji hicho kwenda kuwaelimisha wananchi hao kwamba utafiti ni bora?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze sana, kwa sababu ni Mbunge ambaye anajitoa kwa dhati katika lile Jimbo lake la Chunya kuhakikisha kwamba wakulima wote hususani wa zao la tumbaku na hata hiki kituo kidogo cha utafiti wanatendewa haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, naomba niseme tu kwamba, kile kituo chetu cha utafiti pale Mtanila ni kweli kuna wapiga kura wangu wako pale na mimi nakifahamu na nimefika lakini kinachukua eneo la hekari mia tano na ni hekari tatu tu zinatumika tu kwa ajili ya kituo hicho kwa sababu vituo vya utafiti huwa vinachukua eneo kubwa sana. Kwa maana hiyo nimtake kabisa Mheshimiwa Mzee wangu Kilasile Mwambalaswa kwamba eneo hilo linatumika kwa ajili ya utafiti na ndio maana hata Kituo chetu kile cha Uyole kinatumia eneo hilo katika suala zima la mazao ya mahindi na maharage pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la nyongeza la pili niko tayari kufika Chunya na baada ya Bunge lako Tukufu nitafanya ziara ya kwenda huko. Ahsante.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuuliza swali la nyongeza; kwa kuwa Vituo vya Utafiti wa Kilimo kama Uyole kama alivyoeleza Mheshimiwa kwenye jibu lake vina umuhimu wa pekee katika kuendeleza mazao yote. Ni lini basi Serikali itafikiria kuja katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa ambako sisi maeneo sio tatizo, wakajenga kituo cha kushughulikia zao la pamba kama ilivyo Uyole na Naliendele kwenye zao la korosho?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Igunga sisi tuna kituo kidogo cha Mbegu na ardhi yao ni nzuri lakini kama Serikali tunajipanga kuhakikisha kwamba tunapanua suala zima la vituo vyetu vya utafiti na hata ukizingatia kwamba sasa hivi tumehakikisha kwamba tuna Taasisi yetu ya TARI ambayo itakuwa inajitegemea kwa masuala yote ya utafiti kwa ajili ya kuboresha na kuweza kuandika maandiko mbalimbali ili waweze kupata pesa nyingi zaidi kutoka kwa wahisani mbalimbali katika kuhakikisha suala zima la utafiti linatendewa ubora na haki inayostahili. Ahsante.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Ahsante, kwa kuwa jibu la msingi la Mheshimiwa Naibu Waziri, suala la tafiti katika vyuo hivi ni kutokana na ucheleweshwaji wa pesa za maendeleo na ndio maana ardhi inabaki kubwa kwa muda mrefu bila kutumika. Je, Serikali imejipanga vipi katika bajeti hii kupeleka pesa katika Wizara hii hasa eneo la Uyole kwenye hicho Kijiji cha Nkena, lakini na Uyole Mbeya Mjini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye majibu yangu ya msingi nimejibu, lakini vilevile wakati najibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Kafumu kuhusu Igunga nimesema hapa kwamba sisi kama Wizara ya Kilimo tumeboresha kuhakikisha kwamba ile directorate yetu ya utafiti sasa hivi itakuwa ni taasisi inayojitegemea kwa maana ya TARI. Pia nimetoa maagizo kwamba TARI ama vituo vyetu vya utafiti vyote visitegemee tu pesa za Serikali, lakini pia vijiongeze kuhakikisha vinaandika maandiko (proposals) ili waweze kupata pesa za ziada kwa ajili ya kuhakikisha tafiti zetu zinaboreshwa na zinatendewa haki. Ahsante.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri sana ya mdogo wangu Mheshimiwa Waziri Dkt. na pamoja na kunikaribisha Ofisini kwake na kulijadili suala hili nina maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, kwa vile kituo hiki kina mfanyakazi mmoja tu. Huyu mfanyakazi mmoja atafundisha wanyama yeye, atatengeneza zana za kilimo yeye na hili ndio ninalosema suala la mzigo mzito kumpa Mnyamwezi hebu tuache, mzigo mzito wapunguze wabebe wenye mzigo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali haioni umuhimu wa kuongeza wataalam kituoni pale ili waweze kufundisha na kutengeneza vifaa vingi au zana za kilimo kwa ajli ya wanyamakazi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je Serikali ina mpango gani sasa wa kupeleka mitambo mipya baada ya kupata umeme ili waweze kutengeneza zana za kilimo kwa ajili ya wakulima wangu jimboni kaskazini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu amekuwa akifuatilia suala hili kwa kipindi kirefu na pia ameweza kufika hata ofisini kwetu kwa ajili tu ya wananchi wake wa kule Upuge pale Tabora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nikija katika maswali madogo mawili ya nyongeza ni kweli kabisa kwamba kituo hiki cha Upuge kina mtaalam mmoja, lakini kama Serikali kama Wizara ya Kilimo tulishatoa vituo vyote hivi vya zana za kilimo kwenye halmashauri zote nchini. Kwa maana hiyo nihase halmashauri zote nchini kuhakikisha kwamba zinatilia mkazo vituo vya zana vya kilimo ili viweze kufanya kazi kwa ufanisi.
Mhesimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine katika swali lake la pili la nyongeza, ni kweli kulikuwa hakuna umeme na kwa sababu umeme umeshapatikana, Wizara yangu nitatuma wataalam kwenda pale Upuge kufanya assessment kabla ya mwezi wa Nane, kwa sababu kuna mashine zingine pale hazijawahi kutumika kama ile ya vipuri vile vya kuchongea. Nakushukuru.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Suala la wakulima limekuwa ni tatizo kubwa, kilio hawana mbolea, hawana pembejeo, hawana mbegu kwa wakati, lakini hata hiki kituo cha kilimo ambacho kinawasaidia wakulima kupata unafuu katika kilimo chao kimekuwa nacho ni tatizo. Je, Mheshimiwa Waziri hebu atuambie hasa ni upi mkakati wa Serikali? Nami naipongeza Serikali kwa kuweka kituo hiki hapa Tabora, ni upi mkakati wa Serikali sasa? Wa kuwapunguzia watoto wangu hawa Wanyamwezi na Wasukuma ugumu wa kilimo cha kutumia zana duni?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala zima la wanyamakazi kwa mfano kule Nyanda za Juu Kusini, kilimo la maksai kimeimarika sana. Ni kweli upande wa huku Mikoa ya Magharibi hakijaimarika, lakini kwenye jibu langu la msingi nilisema kabisa kwamba, Wizara ya Kilimo kupitia TARI, tumeanzisha TARI ili kuhakikisha kabisa kwamba tunaimarisha na kuboresha vituo vyetu vyote vile vya utafiti pamoja na vya zana za kilimo ambavyo vinasimamiwa na halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge, kaka yangu Mheshimiwa Yussuf mpango mkakati wa Serikali upo imara, hususan Serikali hii ya Awamu ya Tano na ndio maana tumesema tuwe na TARI kuboresha na kuimarisha vituo vyetu vyote vya utafiti na nimesisitiza waandike proposals wasitegemee tu kabisa pesa ya Serikali au fungu la Serikali, wajiongeze. Nakushukuru.
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuongeza swali dogo la nyongeza. Kwanza napenda nimpongeze Naibu Waziri wa majibu yake mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumbaku kwa Mkoa wa Tabora na mikoa mingine inayolima tumbaku, tumbaku ni maisha, tumbaku ni uchumi, lakini tumbaku ni maisha yetu. Napenda kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo. Kwa kuwa kasi ya upandaji wa miti haiendani sambamba na upandaji na tunaona kabisa zoezi hili limefeli, nataka niulize Serikali, ina mpango gani kwa sasa kuzihakikishia hizi AMCOS ambazo zina jukumu la upandaji wa miti ili ziweze kutimiza Sheria ya Namba 24 ya mwaka 2001, ambayo inaitaka kila AMCOS kabla ya kusajiliwa iwe na shamba la miti ambayo itawatosha idadi ya wakulima wake kwa mwaka mzima?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, napenda kufahamu; kwa kuwa Bodi ya Tumbaku ndiyo yenye jukumu la kusimamia na kuratibu shughuli zote za tumbaku ikiwa ni sambamba na uhifadhi wa mazingira inashindwa kutekeleza majukumu yake kutokana na changamoto mbalimbali, je, Serikali ina mpango gani wa kuiwezesha hii Bodi ya Tumbaku kuondokana na changamoto za magari, nyumba na ofisi za wafanyakazi ili iweze kufanya kazi kwa uhakika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, naomba nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge ambaye ninaamini kabisa na yeye ni mkulima wa zao la tumbaku kule Tabora na amekuwa akilima hiyo tumbaku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika maswali yake mawili ya nyongeza, kuhusu suala AMCOS na wakulima ni kwamba sisi kwenye ile Tobacco Industrial Act. No. 24 ya Mwaka 2001 wakulima wetu wote pamoja na hizo AMCOS na mambo mengine ambayo yanaelezea katika Sheria hiyo Namba 24 ya Mwaka 2001, ni kuhakikisha kwamba, wakulima wote pamoja na hizo AMCOS wanaposajiliwa kuhakikisha kwamba mashamba yao yanaendana na miti isiyopungua 250. Vile vile kuhakikisha kabisa kwamba wanatumia yale mabani ya kisasa na si yale mabani ya zamani ambayo yalikuwa yanatumia magogo kama ilivyokuwa kule mwanzo. Hii yote ni katika kuhakikisha kwamba, tunatunza na kulinda hifadhi ya mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili la nyongeza, kuhusu Bodi yetu ya Tumbaku; ni kweli sisi kama Serikali tunahakikisha kabisa kwamba tunaimarisha na tunaboresha hizi bodi zetu zote. Naomba niziase bodi zetu zote kwamba zifanye kazi kwa umahiri na kwa ubunifu zaidi, na vile vile waweze kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha kwamba wanatumia zile fursa mbalimbali za kilimo zilizopo katika kuboresha mazao yao, ahsante.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru sana na mimi niulize swali moja dogo la nyongeza kuhusu suala la tumbaku. Tumbaku ndiyo siasa na ndio uchumi wa Mkoa wetu wa Tabora. Tatizo kubwa ni masoko, mwaka jana hapa mpaka tukapewa majina ya wazee wa tumbaku na akinamama wa tumbaku, sisi Wabunge wa Tabora. Swali, je, Serikali imefanya nini ili kutafuta masoko mengine ya tumbaku ili sisi tuuze tumbaku yetu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii hata yeye Mheshimiwa Mbunge pia kumpongeza; kama alivyosema kwamba ni kweli tumbaku ni maisha kwa wananchi wote wa Mkoa wa Tabora na maeneo yote yanayolima tumbaku. Hata hivyo, kama Serikali tumejipanga. Sasa hivi tuna kampuni nne na tayari tumeshaanza kufanya mazungumzo na tumeongea na nchi ya Vietnam nao pia wamekubali kununua tumbaku yetu. Katika msimu huu wameahidi kabisa kwamba watanunua tani 1000 za tumbaku. Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa kuboresha mazingira ya kilimo ni pamoja na upatikanaji wa mbegu bora au miche bora ya zao husika, na kwa kuwa wazalishaji wa miche ya korosho imechukua muda mrefu sana kulipwa pesa zao na wengi wao walikuwa wamekopa fedha kwenye vyombo vya fedha. Je, Serikali pamoja na kuwalipa malipo yao ya stahiki, wako tayari sasa kuwalipa fidia ya ziada kutokana na hasara iliyotokana na mikopo waliyochukua kwenye vyombo vya fedha?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli anachoouliza, tumeshafanya uhakiki wa miche milioni kumi na tatu mpaka sasa hivi. Naomba niliambie Bunge lako Tukufu, pesa ya kuwalipa wananchi hawa ipo tayari, lakini suala la fidia halipo. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa alizeti inayolimwa Mkoani Singida ni alizeti bora Afrika Mashariki na Kati. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha wakulima wa alizeti Mkoani Singida, kulima kilimo chenye tija kwa kuwapa pembejeo, mikopo yenye gharama nafuu pamoja na elimu ili waweze kulima kilimo bora?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kilimo cha alizeti kinalimwa sana katika Mkoa wa Singida na sisi kama Serikali, tunahamasisha na tunahimiza kuwa na kilimo cha kibiashara na vile vile kuwa na kilimo kinachozingatia kanuni, kwa maana ya kilimo kilicho bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nihamasishe halmashauri zote nchini na wale Maafisa Ugani wetu wote kuhakikisha kwamba wanatoa na wenyewe elimu kwa umma, wasikae tu ofisini, kazi yao iko mashambani, kuhakikisha wanakwenda kwa wakulima, wanatoa elimu ili wakulima waweze kuwa na kilimo bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kama Serikali tumejipanga kwamba hili zao la alizeti ambalo nalo ni zao la kibiashara na linasaidia sana katika kuleta mafuta ili kupunguza tatizo la kuagiza mafuta zaidi kutoka nje, tumejipanga katika mwaka huu wa fedha kuhakikisha kwamba litazingatiwa na litakuwa ni Kilimo Bora na cha kisasa. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Ulimaji wa tumbaku ni uhai kwa wananchi wa Urambo na Mkoa wa Tabora kwa ujumla; na wamekuwa wakiwa na changamoto kubwa sana ya upatikanaji wa pembejeo kwa wakati na bei isiyoeleweka. Je, Serikali inasemaje kuhusu kufika kwa pembejeo kwa wakati na ununuzi wa tumbaku kwa utaratibu wa bulk procurement ili bei ya tumbaku isibadilike badilike hovyo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tumbaku ni maisha, kama nilivyokuwa nimesema, hususani katika Mikoa ile inayolima tumbaku ikiwemo na Tabora. Katika swali lake linalohusu pembejeo, ni kweli tumbaku na ile mbolea ya NPK ambayo inatumika sana katika suala zima la zao la tumbaku, sisi tumeviagiza Vyama vyetu vyote vile vya Msingi vya Ushirika kuhakikisha kwamba wanafanya jitihada kwa sababu wao wenyewe ndiyo wakulima ili mbolea na pembejeo hizi zifike kwa wakati kwa msimu unaotakiwa kwa sababu unaeleweka ili wao wenyewe kwa sababu ndio wanaolima, basi ule usumbufu usiweze tena kutokea. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa kilimo cha mbogamboga na matunda hukubali kuzalishwa sana katika Ukanda wa Kaskazini na Nyanda za Juu Kusini; je, ni nini mkakati wa Serikali katika kuimarisha kilimo hiki.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nichukue fursa hii kuwapongeza wakulima wote nchini ambao wamegundua umuhimu wa kilimo hiki ambacho tunaita tasnia ya horticulture. Sisi kama Serikali ni kweli tumeona kuna umuhimu sana wa tasnia ya horticulture, ndiyo maana hata pale katika Wizara yetu ya Kilimo sasa hivi tumeamua kuweka mtu ambaye atakuwa anashughulikia tu masuala ya horticulture, kwa maana ya focal person.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tunasisitiza kwamba tasnia hii ya horticulture iendelee kuwa ni kilimo cha kibiashara. Kwa sababu licha ya kwamba ni afya katika mwili vile vile kinaliingizia Taifa pato kubwa sana. Pia niziase tena halmashauri zote nchini kuhakikisha kwamba wanakuwa na kitalu nyumba kwenye kila halmashauri na kuweza kufanyika hayo mavitalu nyumba kama shamba darasa. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Changamoto zilizoko kwenye zao la tumbaku ni nyingi sana na kwa Mkoa wa Katavi Wilaya ya Mpanda Kampuni ya TLTC iliiandikia barua Bodi ya Tumbaku kwamba ina kusudio la kuacha kununua tumbaku katika Wilaya ya Mpanda. Je, nini kauli ya Serikali kuhusiana na suala hili kwa sababu mpaka sasa wakulima hawana uhakika wa kuuza tumbaku yao kwa msimu ujao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika zao la tumbaku mara nyingi wakulima wote wa tumbaku wanalima kilimo cha mkataba. Kampuni hizi ambazo zinaingia mikataba na wakulima wale kawaida ile mikataba huwa wanasaini kabla ya msimu kuanza. Niitake Kampuni ya TLTC kuhakikisha kwamba pamoja na wale wananchi wa Jimbo la Mheshimiwa Mbunge ule mkataba wao kama unasema alitakiwa kununua kiwango hiki cha tumbaku, basi mkataba ule lazima uheshimiwe na lazima wanunue kiwango kile kinachotakiwa. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa kunipa nafasi. Zao la tumbaku linategemea sana kununuliwa kwake kuwa na wateuzi wa zao hilo, kwa maana ya ma-classifier; Serikali ina mpango gani wa kuongeza classifier ili waweze kuliteua zao hilo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipokuwa najibu swali la Mheshimiwa Mbunge Almas Maige nilisema kama Serikali tumejipanga kutafuta Classifiers wengine, na nikasema zaidi kwamba mpaka sasa hivi tumeongea na nchi kama ya Vietnum na wameshaji-commit kwamba katika msimu huu watanunua tani 1,000 za tumbaku. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Serikali imekuwa ikijichanganya kuhusu suala la kilimo na matumizi ya tumbaku, kwa sababu Serikali kupitia Wizara ya Afya imeridhia Sera ya Umoja wa Mataifa ya kupiga vita matumizi ya tumbaku; lakini Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inahamasisha kilimo cha tumbaku. Sasa nataka kujua kauli ya Serikali, ni upi hasa msimamo wetu kuhusu kilimo na matumizi ya tumbaku hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, alichoongea Mheshimiwa Mbunge ni kweli, kwamba katika Shirika letu lile la WHO wanapiga vita tumbaku na hususani katika masuala mazima yale ya afya lakini vile vile na mazingira na suala zima la child labour. Naomba nichukue fursa hii kipekee kabisa kusema kwamba nicotine yetu sisi kwenye tumbaku ni ndogo. Hata hivyo, niase wakulima wote nchini, kwamba wasitegemee tu zao la tumbaku vile vile kuna mazao mengine mbadala ambayo na yenyewe wanapaswa wawe wanazingatia na kuyalima pia. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kujibu swali langu vizuri. Swali la kwanza, kama Waziri alivyoeleza ni kwamba mfumo umebadilika lakini kama ilivyo kule Hanang bei bado haijashuka na madhumuni ya kuwa na mfumo huu wa sasa ni kushusha bei. Nataka kujua kwa nini bei haijashuka mpaka sasa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, mfumo wa sasa unapaswa kuwafikia wakulima wote badala ya ule wa ruzuku kufikia watu wachache peke yake. Hata hivyo, nataka kujua kwamba huu ununuzi wa pamoja wa mbolea kama kweli umewanufaisha watu kama wanavyotarajia na kama Serikali inavyotaka na kama sivyo watuambie ni msimu upi mfumo huo wa sasa utanufaisha wakulima wote kuliko ilivyokuwa pale awali?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze sana kwa jinsi ambavyo amekuwa akishugghulikia suala zima la mbolea na mfumo wa pamoja na ukizingatia yeye alikuwa ni Mwenyekiti wa Kamati yetu ya Kilimo, Mifugo na Maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye maswali yake mawili ya nyongeza ni kwamba ni kweli bei haijashuka kwa sababu mfumo huu tumeuanza sasa hivi na matokeo yake mazuri tutayaona kuanzia msimu ujao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika lile swali lake la pili ni kwamba mbolea yetu ambayo tunasema ina bei elekezi ya Serikali tunapaswa tuwaambie wananchi wote wasubiri msimu unaotakiwa ili iuzwe kwa pamoja lakini vilevile hata wale wazabuni wetu tunataka wawe wanafanya order kwa wingi kwa pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba nitoe ushauri, hata wale wafanyabiashara kwenye yale maghala yao wajenge kwa wingi ili maghala yale kulekule katika halmashauri wawe wanazalisha ili huu msimu unapofika basi wananchi na wakulima wetu waweze kupata mbolea zile kwa wakati na kwa pamoja inavyotakiwa.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Wakulima wa zao la chai, hasa wakulima wadogowadogo wamekuwa wakinunua pembejeo kwa bei ya juu sana. Ni lini Serikali itatoa mbolea ya ruzuku, kwa maana ya pembejeo ya ruzuku kwa wakulima hawa wadogo kama ilivyo kwenye mazao mengine ya korosho na pamba, ili waweze kupata faida kutokana na kilimo hiki cha chai? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba niwaambie kwa faida ya Waheshimiwa Wabunge wote, msimu huu tumeamua kwamba hakutakuwa na bei yoyote ya ruzuku kwenye mbolea. Ndiyo maana hata kwenye sulphur ambayo ilikuwa inatolewa kwa ruzuku, safari hii tumeamua kwamba na yenyewe iwe inauzwa.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Uti wa mgongo wa nchi hii uko kwenye kilimo. Tunategemea kilimo ili tuweze kupata maendeleo kwenye nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza swali. Shinyanga na Kahama tunaongoza kwa kilimo cha mpunga na mahindi. Mpaka sasa ninapoongea ruzuku imepungua kwa zaidi ya 50%. Nini mpango wa Serikali kuongeza ruzuku ili tuweze ku-improve kwenye kilimo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza amezungumzia kwenye zao la mpunga na mahindi na juu ya kuongeza ruzuku. Nilipokuwa najibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hongoli nimesema kabisa kwamba hatutakuwa na ruzuku kwa mwaka huu kwa sababu mazao yote yawe ya kimkakati, yawe yale ya nafaka, wote watakuwa wananunua isipokuwa kwa bei elekezi.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Chama cha Msingi cha Imalamakoye AMCOS kimesababishia hasara kubwa wakulima wa tumbaku katika Wilaya ya Urambo ya zaidi ya Dola 19,500 sawa na Shilingi za Kitanzania milioni 40 na zaidi na hivyo kusababisha kushindwa kununua pembejeo kwa ajili ya kilimo chao cha tumbaku. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wakulima hawa ili Chama hiki cha Imalamakoye kiweze kuwalipa pesa zao waweze kupata pembejeo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nichukue fursa hii pia na yeye kumpongeza kwa jinsi anavyofuatilia suala zima hili la tumbaku. Ni kweli kwamba hii AMCOS ya Imalamakoye ambayo ameisema imekuwa ina matatizo, kumekuwa na ubadhirifu katika na mpaka sasa hivi tunapozungumza ni kwamba Mwenyekiti wa Bodi ameshashtakiwa na kesi hii iko Polisi, uchunguzi unaendelea kufanyika. Mara itakapobainika basi hatua kali sana za kisheria zitachukuliwa.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Msimu uliopita mbolea na mbegu Mkoa wa Rukwa hazikufika kwa wakati na hazikuwa na impact yoyote. Je, msimu unaokuja atatuhakikishia kwamba mbolea na mbegu zitafika kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye jibu langu la msingi la Mheshimiwa Dkt. Nagu, nilijibu kabisa kwamba Serikali imeshajipanga kuhakikisha kwenye msimu ujao mbolea inafika kwa wakati.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mkoa wa Singida unazalisha kwa wingi mazao ya biashara na chakula kama vitunguu, mahindi, alizeti na viazi vitamu. Tatizo kubwa lililopo kwa wakulima wetu ni bei kubwa ya pembejeo pamoja na zilizopo sokoni kukosa ubora. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha pembejeo zinapatikana kwa bei zilizokuwa nzuri lakini zina ubora wa kutosha? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza pembejeo zinanunuliwa lakini sisi kama Wizara ya Kilimo tuna Mfuko wetu ule wa Pembejeo ambao tunatoa mikopo yake kwa asilimia saba au nane kwa masharti nafuu. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru sana…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza naipongeze Serikali kwa jitihada ambazo walizifanya na kutoa ushirikiano kwangu na kuwawezesha wakulima hawa waweze kulima zao hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la msingi, kwa kuwa wakulima wamelima pamba kwenye maeneo ya Wilaya ya Mpanda Tanganyika na wamelima kupitia mfumo usiokuwa na ushirika, je, hawaoni sasa ni wakati muafaka kwa wakulima hawa ambao wamelima zao hili waruhusiwe kununuliwa zao lao kupitia makampuni binafsi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Halmashari za Manispaa ya Mpanda na Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika watanufaika vipi na zao hilo hasa kupitia cess ambayo Halmashauri wanatakiwa waipate? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwanza naomba nichukue fursa hii kumpongeza kabisa Mheshimiwa Kakoso kwa sababu amekuwa ni champion kwa uanzishwaji wa zao la pamba katika Mkoa wa Katavi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye maswali yake mawili ya nyongeza; la kwanza ni kuhusu mazao yale ya cess. Naomba nitoe rai kwa Halmashauri zote nchini, ushuru wa mazao wanatakiwa wajipange na kufanya mikakati thabiti kuhakikisha kwamba mazao ndiyo yanayoingizia Hamlashauri mapato. Kwa hiyo, natoa rai kwa Halmashauri zote nchini zihakikishe kwamba zinatilia mkazo katika ushuru wa mazao ambao ni ule tunaita cess.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naomba nitoe rai kwamba wakulima wote nchini wajiunge kwenye AMCOS (Vyama vya Msingi vya Ushirika) na ndivyo ambavyo sisi kama Serikali sasa hivi tunaimarisha katika kuleta mapinduzi ya vyama vya ushirika. Nashukuru.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nilikuwa naomba kumwuliza Mheshimiwa Waziri, je, anajua kwamba mpaka sasa Bodi ya Pamba haijatoa leseni kwa wanunuzi wa pamba na sababu ni nini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumjibu Mheshimiwa Ndassa kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo swali lake moja dogo la nyongeza kuhusu Bodi ya Pamba kutotoa leseni mpaka sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba sasa hivi tuko kwenye mchakato wa kuhakikisha kwamba Bodi ya Pamba inatolewa leseni na haitazidi mwezi ujao leseni itakuwa imetolewa. Ahsante.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Je, Mheshimiwa Waziri anafahamu kwamba Vyama vya Ushirika vimeshakufa muda mrefu na kwamba sasa wakulima wanalazimishwa wauze pamba kupitia Vyama vya Ushirika. Je, nini tamko la Serikali kuwasaidia wakulima wa pamba?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kama nilivyosema ni kwamba tumeamua kufanya total transformation kwenye Vyama vya Ushirika ili tuweze kuimarisha na kuboresha. Kwa maana hiyo, Serikali tumejipanga kuhakikisha kwamba wakulima wote kupitia Vyama vya Ushirika tutakuwa tunahakikisha wanapouza mazao yao wanalipwa pesa zao pale pale bila kungoja kupitia kule Benki. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia na mimi nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Songwe au Wilaya ya Songwe kwa ujumla hatuna zao la biashara zaidi ya zao la Pamba ambalo tulikuwa tunalima mwaka 1995 wakati sisi tunasoma mpaka leo. Wananchi wa Songwe hawana zao la biashara kabisa.
Sasa naiuliza Serikali, je, toka mwaka huo wanafanya utafiti wa huyo mdudu mwekundu lakini maeneo haya ya Tanganyika kama alivyosema Mheshimiwa Kakoso na Katavi yote ni Ukanda ule ule wa kwangu Mbeya, Songwe na alikotokea Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itaruhusu sasa Bonde la Songwe tuweze kulima pamba kama ambavyo leo ametoa kibali kwa Wilaya ya Tanganyika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye jibu langu la msingi nimesema Mkoa wa Katavi Serikali tumeruhusu baada ya utafiti wa kina kufanyika kwamba zao la pamba liweze kulimwa kwenye Mkoa wa Katavi. Kwenye jibu langu la msingi nilisema, maeneo yale yanayopakana na Mkoa wa Katavi ikiwemo kwenye Jimbo la Mheshimiwa Mulugo kule Songwe, ni kwamba utafiti unaonyesha kwamba bado funza mwekundu yupo katika eneo lile la Mheshimiwa Mbunge.
Kwa hiyo, naomba atoe subira kwa Serikali ili utafiti wa kina ufanyike kwamba funza mwekundu ameshaondoka katika eneo hilo. Ahsante.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wilaya ya Nkasi hatuna kabisa zao la biashara, na kwa kuwa Wilaya ya Tanganyika inapakana na Wilaya ya Nkasi, naiomba Serikali, je, iko tayari kwenda kufanya utafiti ili wananchi wa Wilaya ya Nkasi wapate kuruhusiwa kulima zao la pamba? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye jibu la swali la nyongeza la Mheshimiwa Mulugo na katika swali la nyongeza la Mheshimiwa Mipata, hayo maeneo yote yanapakana na Jimbo la Mpanda pamoja na lile la Katavi. Kama nilivyosema ni suala la utafiti katika Wizara yetu ya Kilimo ili tujiridhishe kwamba funza mwekundu bado yuko kwenye maeneo hayo au ameshaondoka? Kwa hiyo, tunaomba muda tumalize kufanya utafiti wa kina na wa haraka ili tuweze kuwapatia majibu ya msingi na ya uhakika. Ahsante.
MHE. JACQULINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitishwa sana na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jambo kubwa hili la Mawakala wa Pembejeo. Pamoja na majibu hayo, naomba niulize swali moja dogo la nyongeza lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
• Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokuwalipa Mawakala kwa wakati kwa kisingizio cha uhakiki kwa kipindi cha miaka minne ambapo Mawakala hao wamekuwa wakiishi kwa shida, wamekuwa wakifilisiwa mali zao na wengine wamekuwa wakipoteza maisha, naomba sasa commitment ya Serikali, ni lini Serikali itawalipa mawakala hao?
• Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inachelewesha malipo ya mawakala kwa zaidi ya miaka mitatu na thamani ya fedha kwa huduma waliyotoa haitalingana na thamani hiyo endapo wangelipwa kwa wakati. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwalipa mawakala hawa fedha zao ikiwa ni pamoja na riba ya asilimia tano?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaelewa concern ya Mheshimiwa Mbunge, ninaamini pia na Wabunge wengi na hata katika bajeti yetu ya Wizara ya Kilimo alitoa na machozi, nampa pole katika hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufupi kabisa ni kwamba Serikali ya Awamu ya Tano ina nia njema na intention yake siyo kwamba haitaki kuwalipa mawakala hawa wa pembejeo, lakini kwenye jibu langu la msingi kama nilivyosema ni kwamba uhakiki unaendelea na uhakiki huu ni wa kina; na mara utakapofanyika sisi kama Serikali tutatoa taarifa na vilevile kama Wizara ya Kilimo wale wahusika wote ambao walikuwa chini yetu watumishi wa Serikali, tumeshawafukuza kazi.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa korosho ambazo zimegundulika kuwa zimechanganywa na mawe zilipitia Bandari ya Dar es Salaam na tatizo hilo halipo katika Bandari ya Mtwara: Kwa nini Serikali isitoe kauli kwamba kwa korosho za Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma ni marufuku kupitishwa katika Bandari ya Dar es Salaam?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, huu uchunguzi unaonekana umechukua muda mrefu sana na swali langu niliuliza walioruhusu, ni rahisi sana kukamata walioruhusu korosho hizo ziende kwa sababu kulikuwa na uwezekano kabisa kuzigundua kabla hazijasafirishwa kwenda nje ya nchi. Kwa nini Serikali inasita kuwataja waliohusika ili iwe fundisho kwa wengine katika msimu ujao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza uhalifu hauna destination lakini sisi Kama Serikali hilo tumelipokea, tutalifanyia tathmini na tuangalie jinsi gani Bandari ya Mtwara inaweza ikatumika pia badala ya ile ya Dar es Salaam ingawa pia hao watu wabeba mizigo hata meli unakuta wakati mwingine anataka apeleke mzigo mahali ambapo pia anaweza akarudi na mzigo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili, Serikali sisi sio kwamba tunapata kigugumizi. Tume ya kitaalam ilimaliza kazi yake na tumeshawasilisha hili jambo kwenye vyombo vya dola, inafanyia kazi na mara tu ule uchunguzi wa kina na wa uhakika utakapofanyika wote waliohusika watatajwa na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao. Ahsante.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Baada ya tasnia ya korosho mwaka 2017 kufanya vizuri sana msimu uliopita, mwaka huu kumekuwa na matatizo ya mgogoro katika Mkoa wa Lindi kati ya Chama cha Ushirika cha Runali na Bodi ya Korosho. Jambo hili limefanya mpaka sasa hivi sulphur iwe bado haijafika katika Mkoa wa Lindi jambo ambapo limefanya sasa hivi mfuko mmoja wa sulphur kufika shilingi 70,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali itoe tamko, ni lini mtatuletea sulphur ili kupunguza bei ya sulphur ambayo imepanda baada ya kuwa na mgogoro kati ya Runali na Bodi ya Korosho?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna tatizo la kuchelewa kwa sulphur, lakini kutokana na swali lake alilouliza, mpaka sasa hivi ni kwamba Chama kile cha Runali kimeshaagiza tani 128 za sulphur, zimeshafika na zimeshasambazwa. Vilevile kwa faida ya wengine hata TANECU wameshaagiza tani 1,100 na tayari zimeshasambazwa na zinauzwa kwa shilingi 32,000. Nashukuru.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba mkulima mdogo wa korosho hawezi kufanya hujuma hizi na hujuma hizi zinafanywa na makampuni makubwa na msimu wa korosho unatarajia kuanza mwezi wa tisa.
Kwa nini Serikali inakuwa na kigugumizi cha kuwataja makampuni hayo ili msimu ujao wasiingie katika soko la korosho? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati najibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dada Hawa Ghasia, nimesema kwamba Serikali hatuoni na hatujapata kigugumizi chochote, ni kwamba tayari tume ya wataalam tumeshawasilisha ile taarifa ya uchunguzi kwenye vyombo vya dola, vinalifanyia kazi na mara tu ule uchunguzi wa uhakiki utakapofanyika na wa kina basi wote watatajwa na hatua kali za kisheria dhidi yao zitachukuliwa. Ahsante.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nashukuru kwa majibu ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa Bunge lako limechaguliwa na wananchi na wananchi hao ndio wanachama wa Vyama vya Ushirika wa Mazao wa Kuweka na Kukopa, kwa nini Serikali inaona mashaka kuleta taarifa za COASCO hapa Bungeni ili zichambuliwe na kujadiliwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kama kikwazo ni Sheria ya Ushirika aliyoitaja Mheshimiwa Waziri, nataka kuuliza, ni lini sasa Serikali itaileta sheria hiyo hapa Bungeni ili ifanyiwe marekebisho na hivyo kutoa nafasi ya kujadili hesabu hizi za ushirika za wananchi wetu na ukizingatia Serikali sasa hivi inaweka nguvu nyingi kuufufua ushirika? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naomba nimjibu Mheshimiwa Ndaki Mashimba maswali yake mawili madogo ya nyongeza kwa pamoja na kwa ufupi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi ambavyo amekuwa akifuatilia sana masuala yote ya vyama vya ushirika na amekuwa ni mfuatiliaji mzuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya msingi, kama Serikali tuko katika kufanya mapinduzi ya vyama vya ushirika kwenye kuboresha, kufufua na kuimarisha. Kwa maana hiyo, sote tuelewe kabisa kwamba kila zao lina msimu wake katika kulima na kwa maana hiyo hata katika ukaguzi wa mahesabu unatofautiana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo sisi kama Serikali hatupati kigugumizi jambo lake tumelipokea. Kama nilivyosema katika lile jibu langu la msingi, kwenye ile Sheria Na. 6 ya mwaka 2013, kifungu cha (4)(1)(b), tutalichukua jambo hili na tutalifanyia kazi ili tuweze kuleta Bungeni kwa ajili ya kurekebisha hiyo sheria ndogo ili mfumo mzima wa vyama vya ushirika na ile dhana nzima ya kuimarisha, kufufua na kuboresha vyama vya ushirika iweze kutiliwa mkazo. Nakushukuru.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJABU: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri na yenye kutia moyo ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza:-
Mheshimiwa Spika, la kwanza, tunashukuru sana kwa kutengewa fedha hizo kwa sababu majengo ya chuo hicho yako kwenye hali mbaya sana. Hata hivyo, suala la kutengewa fedha na suala la kupelekewa fedha ni vitu viwili tofauti. Ningependa kujua, fedha hizo zilizotengwa kwa ajili ya Chuo cha Mlingano zitapelekwa lini ili kazi hiyo iweze kuanza?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili linahusiana na suala la mbegu ambazo zinafanyiwa tafiti katika Chuo hicho cha Mlingano na mbegu ya zao la chai. Atakumbuka Mheshimiwa Naibu Waziri, mwanzoni mwa mwaka huu tulikwenda na wadau, Makampuni ya Chai ya Amani kwenye ofisi yake pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Chai.
Mheshimiwa Spika, suala kubwa ambalo lilitujia huko lilikuwa ni waruhusiwe kuweza ku-blend chai hiyo hapa hapa nchini, ku-pack chai hiyo hapa nchini; na badala ya kwenda kuuza kwenye mnada chai hiyo kule Mombasa. Sasa alielekeza mambo fulani fulani yafanyike na yameshafanyika na naambiwa mambo hayo yako kwenye Wizara na bado hawajayatolea uamuzi. Ni vizuri sasa hivi akaliambia Bunge hili na wananchi wa Muheza kwamba uamuzi huo ni vipi, kwa sababu tunataka kuweka kiwanda…
…kwa hiyo, nataka kujua uamuzi wa Serikali ni nini?
Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA): Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba nimpongeze sana; ni kweli alifika ofisini kwangu kuulizia swali lake la pili, juu ya kiwanda kile cha East Usangara ambapo wao wanafanya usindikaji na walikuwa wanataka kufanya blending.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake hili la (b) ni kwamba, sisi kama Serikali tulikuwa na policy mwaka 2006 kwamba wale wasindikaji wote wa chai wawe wanaomba separate registration wanapotaka kufanya blending. Katika kuepuka ukiritimba ni kwamba Bodi ya Wakurugenzi imeshakaa kuhakikisha kwamba tunawatendea haki wafanyabiashara wote na kuboresha zao la chai ili sasa yule ambaye anasindika aweze pia kupata na kufanya blending ama packaging kama anataka. Jambo hili tumeshaanza kulifanyia kazi ndani ya wiki mbili litakuwa limeshakamilika.
Mheshimiwa Spika, lakini nikija katika swali lake lile la kwanza, ni kwamba sasa hivi vyuo hivi vya kilimo ambavyo nimezungumzia, Chuo cha Mlingano chenyewe kimetengewa Sh.570,000,000 kwa sababu ile bilioni nne ni katika vyuo vyote nchini; na hizi Sh.570,000,000 mwezi ujao wa Desemba zitakuwa tayari zimeshafika ndani ya chuo.
Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri sana ya Naibu Waziri, pamoja na kazi nzuri inayofanywa na TASAF, naomba niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa katika Mpango mzima wa TASAF, moja ya kazi kubwa ni kuzisaidia kaya maskini angalau zipate mlo. Hata hivyo, kuna watu ambao walisahaulika hasa wenye ulemavu, sehemu nyingi walikuwa wameachwa. Je, katika huo Mpango ujao, Serikali itakuwa tayari kuzingatia watu wenye ulemavu wote wakiwepo wa Kilolo na sehemu nyingine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja dogo la nyongeza la kaka yangu Mheshimiwa Venance Mwamoto, Mbunge wa Jimbo la Kilolo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza katika kutambua kaya maskini, naomba niliambie Bunge lako Tukufu kwamba tunazingatia vitu vingi wakiwemo na walemavu wenye watoto na wasio na watoto; wazee wenye watoto na wasio na watoto wakiwemo hata na watoto wenyewe ambao pia wote hao tunawapa category ya kwamba ni kaya maskini sana. Kwa hiyo, naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge kaka yangu wa Jimbo la Kilolo kwamba walemavu wako katika kundi ambalo tunasema ni kundi la kaya maskini na wenyewe wataangaliwa na kuhudumiwa. Ahsante sana.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Vitongoji vingi katika Jimbo la Lushoto havijafikiwa na Mpango wa TASAF wa kunusuru kaya maskini nchini. Je, ni lini TASAF itavifikia vitongoji hivyo katika Mpango wake wa Kunusuru Kaya Maskini nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii kujibu swali moja dogo la nyongeza la Mheshimiwa Shekilindi, Mbunge wa Jimbo la Lushoto, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwamba Awamu ya Pili ya Mpango na Mradi huu wa TASAF tunaanza kuutekeleza Juni, 2019. Nimezungumza hapa kwamba tulikuwa tumebakiza asilimia 30 ya kuhudumia zile kaya maskini sana. Pia nimesema tumeboresha madodoso na tutayafanya kielektroniki na tutahakiki ili kupunguza zile kaya hewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimwambie Mheshimiwa Shekilindi kwamba zile asilimia 30 ambazo nimezisema hapa kwamba zimebaki basi na Jimbo la Lushoto litakuwa mojawapo pamoja na majimbo yote na Watanzania wote ambao wanaishi katika kaya maskini wote tutawafikia. Halmashauri zile 185, vijiji, shehia na mitaa zaidi ya 15,000 vyote tutavifikia. Ahsante.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Pia nichukue fursa hii kumpa pongezi sana kwa namna anavyowajibika tangu amepata nafasi hii, anamsaidia vizuri Mheshimiwa Mkuchika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina swali moja la nyongeza, kwa kutambua kwamba Awamu ya Pili itakapoanza mwezi Juni, 2019 na Wilaya ya Bagamoyo ina majimbo mawili, Chalinze na Bagamoyo, haitoweza kuzifikia kaya zote maskini katika Wilaya ya Bagamoyo kwani ni zaidi ya vijiji na mitaa hii 110. Je, nini tamko la Serikali kuhusu kaya maskini zile ambazo zitakuwa zimeachwa wakati Awamu ya Pili inaanza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa kwa jinsi ambavyo amekuwa akifuatilia kwa ukaribu sana wananchi wa Jimbo lake la Bagamoyo hususani wale ambao wanaishi katika kaya maskini sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilieleze Bunge Tukufu kwamba Mpango wetu huu au Mradi wetu huu wa TASAF unahudumia na umezingatia sana Muungano kwa maana unahudumia Tanzania Bara na Tanzania Visiwani. Kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi mpaka dakika hii katika Jimbo la Bagamoyo au Wilaya ya Bagamoyo tumeshafikia zaidi ya vijiji 66 awamu ya kwanza na vijiji 44 vitafikiwa katika awamu ya pili hivyo kufanya jumla ya vijiji 110.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema tena kwenye jibu langu la awali kwamba mpaka dakika hii tumeshafikisha asilimia 70 kwa kaya maskini zote nchini tumebakiza asilimia 30. Naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge, Waheshimiwa Wabunge wote na Watanzania wote kwamba katika Sehemu ya Pili ya Mpango wetu ule wa TASAF tumehakikisha kwamba tunauboresha zaidi kwa kutumia njia za kielektroniki kwa maana ya GPS ili kuweza kuboresha yale madodoso ili kuhakikisha kwamba tunaepuka zile kaya hewa. Vilevile tutafanya uhakiki kuhakikisha kwamba yale madodoso ambayo tumeyaboresha kweli yanafikiwa katika kaya zile maskini ili kila Mtanzania ambaye anaitwa yuko kwenye kaya masikini aweze kunufaika na mradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, naomba niliambie Bunge lako Tukufu kwamba katika asilimia 30 iliyobaki kwa mpango na mradi wetu wa TASAF tutahudumia kaya maskini zote Tanzania na tutarudia tena kuhudumia zile kaya zingine za mpango wa kwanza ambazo zilikuwa ni asilimia 70. Kwa hiyo, naomba Watanzania wote wafahamu kwamba tumeboresha Mpango huu na kuanzisha mfumo wa kielektroniki ili tuweze kuhakikisha tunafikia malengo na wale wote wanaoitwa wako kwenye kaya maskini waweze kunufaika. Ahsante.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa niko kwenye Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa na ndiyo tunayekagua miradi hii; na kwa kuwa tulishatoa maelekezo kwa Serikali kwamba wale wote walioandikishwa na kupata msaada wa TASAF na siyo kaya maskini wafutwe kwenye orodha lakini mpaka sasa bado wanapata zile fedha. Je, sasa Serikali imeshawafuta wale ambao wana uwezo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja dogo la nyongeza la mzee wangu Mheshimiwa Lubeleje, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama yeye mwenyewe alivyosema ni Mjumbe wa Kamati yetu inayosimamia Utawala pamoja na Serikali za Mitaa na sisi kama Serikali mara nyingi huwa tunazingatia sana ushauri wa Kamati. Naomba nilieleze Bunge lako Tukufu kwamba ni kweli siku za nyuma kulikuwa na makosa ambayo sisi kama Serikali tumeshayarekebisha na ndiyo maana nimesema sasa tunaendelea kuboresha mfumo na tutaanza kutumia mfumo wa kielektroniki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. JANETH M. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imefanya mabadiliko makubwa ya kiutendaji kwa watumishi wa umma na ambayo yana mwelekeo wa kuifikisha Tanzania kwenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025. Je, Serikali imejipanga vipi kikanuni kuwa na mfumo endelevu na madhubuti wa uwajibikaji na uwajibishaji kwa awamu zote za utawala zinazofuata?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali haioni umuhimu wa kuajiri vijana waliopo kwenye private sector na wale wanaoshi nchi za nje (Diaspora) kwa kuwashirikisha pamoja ili tuweze kupata chachu ya maendeleo kwa kutumia ujuzi mbalimbali walionao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mbunge wa Kuteuliwa ambaye pia ni wifi yangu Mheshimiwa Janeth Masaburi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ameulizia kuhusu mfumo. Naomba nimueleze Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kwamba sisi kama Serikali sasa hivi tumejipanga kuboresha mfumo mzuri zaidi tofauti na ule tuliokuwa nao ambao tulikuwa tunatumia LAWSON version 9 ambapo sasa hivi tuna mfumo mpya wa utumishi pamoja na mishahara. Mfumo huu unatengenezwa na vijana wetu wa Kitazania na wazalendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo huu wa utumishi na mishahara wenyewe utakuwa na uwezo mkubwa sana wa capture taasisi zote za umma nchini tofauti na ule ambao tunautumia sasa na ndiyo maana kumekuwa na malalamiko mengi. Mfumo huo tunategemea uanze rasmi Juni, 2019 ambao utahusisha taasisi zote za umma na utaboresha hata mifumo mengine ya utendaji kazi wa mtumishi wa umma mfano OPRAS. Kwa maana hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali tumejipanga na mfumo huu ambao utakuwa mpya na uwezo mkubwa utaweza kuhakikisha unapata taarifa za kila mtumishi wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili amezungumzia juu ya kuajiri watumishi ambao watatoka katika taasisi binafsi. Naomba nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba sisi kama Serikali kwa wale wote ambao wanaomba ajira kwa mara ya kwanza hatuna restriction yoyote wala hatubagui na huwa tunatoa matangazo ya kazi na sasa hivi tumejiongeza zaidi tunatumia online kwa maana ya Ajira Portal. Kwa hiyo, mtu yeyote ambaye anataka kuomba kazi Serikalini anakaribishwa mradi sifa, vigezo na mienendo yake na michakato inayotakiwa itafanyika. Ahsante.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mimi niko Kamati ya Utawala, Mheshimiwa
Mzee Mkuchika na Waziri na Naibu Waziri wanafanya kazi na sisi vizuri nawapongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuuliza ni kweli kwamba sasa hivi katika nchi yetu wako watumishi ambao hawatoi maamuzi kwa kisingizio maagizo kutoka juu, tumekuja hapa kwa kazi maalum, ushirikiano hafifu katika Idara mbalimbali na siku za karibuni tumesikia hata vipigo vinatokea maofisini na kadhalika. Pamoja na kazi nzuri ya Mheshimiwa Mzee Mkuchika, Waziri na Naibu wake hivi Serikali inafanya vetting kama zamani ili kupata watumishi wanaofaa au mnachukua tu kwa sababu ya ukabila, ya undugu, ya kulipana hisani kwa sababu watu kama hawa wanaaibisha Taifa hili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja dogo la nyongeza la shemeji yangu Mheshimiwa Selasini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, naomba niseme tu kwamba Ofisi yangu ndiyo inayoshughulikia pia suala la maadili ya watumishi na viongozi na tumejipanga na linaendelea kufanyika vizuri. Kama tunavyoelewa sasa hivi kwamba utendaji kazi na maadili Serikalini yameongezeka kwa kiwango kikubwa. Ofisi yangu haijasita, bado tunaendelea kulipigania kuhakikisha kwamba wale wote wanaotumia madaraka yao vibaya wanachukuliwa hatua kwa vitendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la vetting, naomba nilieleze Bunge lako Tukufu kwamba vetting ipo na inaendelea. Ndiyo maana katika majibu yangu nilipokuwa namjibu Mheshimiwa Masaburi nilisema wananchi wote wanaruhusiwa kuomba kazi lakini utaratibu na mchakato maalum huwa unafanyika. Kwa maana hiyo, nazungumzia hili katika kusisitiza kwamba watumishi wote wa umma wanapaswa kuhakikisha wanatii, wanafuata na wanaheshimu miiko yote ya utumishi wa umma. Ahsante.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, napenda kuongezea majibu ya swali la ndugu yangu Mheshimiwa Selasini, Mbunge wa Rombo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya CCM inaajiri watumishi wa umma kwa sifa zilizotangazwa. Hatuajiri kuangalia mkoa, wala ukabila, wala dini, sisi Chama chetu kwenye mambo hayo ya ukabila na dini tumehama huko; sisi tunashughulika na Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine aligusia kwamba wako watu wana kigugumizi kufanya maamuzi. Nataka nimhakikishie Serikali hii ya Awamu ya Tano inafanya maamuzi kwa wakati (promptly). Ametoa mfano, ingawa hakutaka kusema, nadhani amerudi nyumbani kwake Moshi kule, watu wamepigana ni kweli, waliohusika tayari tumewachukulia hatua, mmoja hayupo kazini na mwingine anachunguzwa. Hiyo inaonesha namna ni gani Serikali ya CCM inachukua hatua kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, amezungumza suala la vetting; huo ni utaratibu wa Serikali. Huwezi ukamteua mtu kufanya kazi ya umma hasa nafasi ya uongozi bila kumfanyia vetting lakini wanaofanya vetting ni binadamu. Leo Mheshimiwa Selasini anaweza akawa Mbunge mzuri sana siku nyingine akateleza. Sasa husemi kwamba kwa kuwa alikuwa mzuri siku za nyuma aendelee tu. Ndiyo maana mnasikia tunafanya mabadiliko na tunatengua uteuzi. Kwa hiyo, nimhakikishie ndugu yangu Mheshimiwa Selasini tuko pamoja. Nilidhani mwishoni utasema napenda nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali ya CCM kwa hatua mlizochukua Mkoa wa Kilimanjaro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Waziri, amenijibu vizuri na ametoa faida kwa Watanzania katika kuona Serikali imeishupalia rushwa ili iwe mfano kwa wengine. Nina maswali mawili madogo ambayo ningetaka pia anipatie ufafanuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mtoa rushwa na mpokea rushwa ni tendo la siri kubwa ingawa wote kisheria wana. Je, ni jambo lipi na wanalithibitishaje? Kitu kinachofanyika kwa siri wanawezaje kukijua wakati kitendo hiki hakifaywi hadharani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, rushwa ziko za aina mbalimbali, mojawapo ni rushwa ya ngono na hii pia imejificha, kuitambua siyo rahisi, inataka mbinu kubwa: Je, atawasaidia vipi vijana wetu kubaini mbinu hii ya rushwa ya ngono ili kabla ya tatizo hili halijawafika wakaweza kuliabini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa
Mwenyekiti, awali ya yote naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana kwa jinsi ambavyo amekuwa ni sehemu ya wapambanaji katika mapambano haya dhidi ya rushwa. La kwanza, anazungumzia suala la kukamatwa kwa hawa wala rushwa na anasema kabisa tuna uhakika gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niliambie Bunge lako Tukufu kwamba katika ile Sheria Na. 11 ya mwaka 2007 ina makosa 24, lakini katika kile kifungu cha 15 kinazungumzia suala la hongo, nasi kama TAKUKURU tutamkamata mtu kama tukiwa na ushahidi katika suala zima la kile kitendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine linategemea na circumstantial evidence, inategemea na mazingira; nasi sote humu ndani ni wanasiasa. Kwa hiyo, mfano katika ile Sheria ya Uchaguzi, mambo mengi huwa yanatokea na sote humu ndani tunaelewa. Kwa hiyo, hilo ni swali la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili kuhusu ngono ya rushwa, naomba niseme kwamba hili limekuwa ni tatizo, kubwa ngono ya rushwa iko katika kifungu Na. 25. Ninapomjibu swali lake Mheshimiwa Mbunge, hata ninyi Wabunge humu ndani mnafuatiliwa kwa sababu ni kosa na huwa linatokea hata mashuleni, vyuoni, maofisini, unakuta wanawake wananyanyaswa kutokana na tatizo hili la ngono ya rushwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sisi kama TAKUKURU…

MWENYEKITI: Waheshimiwa mmeelewa, endelea.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba, tuna wataalam wa kutosha kugundua kwamba, hii ni ngono ya rushwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru. (Makofi)
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na maelezo mazuri ya Naibu Waziri, napenda niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, swali langu la (b) linauliza ni kesi ngapi DPP amezuia majalada hayo ya watuhumiwa, ndiyo msingi wa swali. Kwa maoni yangu swali hilo naomba lijibiwe sasa kwa sababu halikujibiwa katika maelezo yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, Halmashauri ya Mji wa Kasulu tuliibiwa fedha takribani shilingi bilioni 5.9 ingawa baadaye nasikia uhakiki ulibainisha kwamba takribani shilingi bilioni 2 zilikuwa zimeibiwa. Washtakiwa wale walisimamishwa kazi, wakahojiwa na TAKUKURU lakini cha ajabu ni kwamba watuhumiwa hawa hawajafikishwa Mahakamani eti kwa sababu DPP hajatoa kibali. Ni kitu gani hicho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa kaka yangu Nsanzugwanko, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, naomba nimpongeze sana kwa jinsi ambavyo anafuatilia sana masuala ya watumishi wa Jimbo lake la Kasulu ambao wanategemewa kutoa huduma kwa wapiga kura wake ambao pia ni wapiga kura wake. Jambo la kwanza, kwenye majibu yangu ya msingi hapa nimesema DPP ni Ofisi inayojitegemea na ipo kwa mujibu wa Katiba. Kwa maana hiyo, siyo kwanza amezuia isipokuwa majalada haya yamechelewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili, Kasulu siyo kwamba kulikuwa na ubadhirifu wa shilingi bilioni
5.9 bali ni ubadhirifu wa shilingi bilioni 1.6 na kulikuwa na kesi 12. Katika kesi hizo 12 aliyekuwa DT wa Halmashauri hiyo ya Kasulu anahusika kwenye hiyo kesi moja lakini kesi sita zenyewe zilifutwa kwa sababu zilikosa ushahidi na kesi tano zinasuasua kwa sababu kuna mashahidi wengine wanaogopa kutoa vielelezo. Kwa hiyo, naomba niliarifu Bunge lako Tukufu na kuwaasa Watanzania wote kwamba wawe na kiu ya kutoa ushirikiano na Taasisi yetu ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kwa sababu rushwa ni adui wa haki. Nakushukuru.

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongezee kidogo maelezo kwa kuelezea mamlaka ya DPP kwa mujibu wa Katiba ambapo ni Ibara ya 59B(2) ambayo inampa Mkurugenzi wa Mashtaka uwezo wa kufungua, kuendesha na kusimamia mashtaka yote nchini. Kwa hiyo, ana mamlaka ya kufungua au kuendesha lakini kama haendeshi anasimamia mashtaka yote yanayohusu makosa ya jinai nchini. Hata Ibara ndogo ya (3) inaeleza vizuri kwamba mamlaka hayo anaweza kuyatekeleza yeye mwenyewe au mtu mwingine kwa maelekezo yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la DPP ama anazuia au hazuii ma-file kwenda kwenye mashtaka, Mheshimiwa DPP hazuii bali anatoa kibali au hatoi kibali. Pia hafanyi hivihivi, anachopaswa kufanya DPP kwa sababu yeye siyo Mamlaka ya Uchunguzi bali ni mamlaka ya mashtaka, kwa hiyo ni lazima apime ushahidi ulioletwa kutoka kwenye Mamlaka ya Uchunguzi kama unajitosheleza kuweza kufungua mashtaka. Kama anaona kwamba ushahidi ulioletwa kutoka kwenye mamlaka ya uchunguzi haujitoshelezi kufungua mashtaka hatatoa kibali cha kufungua mashtaka, mpaka pale atakapojiridhisha kwamba ushahidi unajitosheleza. Ahsante.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijamuuliza maswali ya nyongeza, nichukue fursa hii kumpongeza Naibu Waziri wa Utawala Bora na Utumishi japokuwa ni muda mfupi tu tangu apewe dhamana ya kusimamia nafasi hiyo utendaji wake unaonekana na kasi yake nafikiri ni sehemu ya kasi anayohitaji Rais wa nchi kuona katika utendaji wa Mawaziri wetu. Hongera sana mama, nakuomba uendelee kukaza buti umsaidie Rais kazi aliyokupa dhamana ya kuifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hilo, swali langu la kwanza, kwa kuwa katika Wilaya ya Longido lenye jumla ya vijiji 49, kuna vijiji 22 ambavyo mpaka sasa hivi havina Watendaji wa Kijiji walioajiriwa, wako wanaokaimu tena wengine wamekaimu kwa miaka mingi. Ni lini sasa Serikali inakwenda kuipatia Halmashauri ya Wilaya ya Longido kibali cha kuajiri Watendaji hao ili kuziba pengo lililopo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, naomba kupata majibu kwamba kwa kuwa katika baadhi ya zahanati tulizonazo katika Wilaya yangu ya Longido na vituo vya afya na kuna vingine viko mbioni kukamilishwa kama kile cha Kimokorwa, Engarenaibo na kadhalika ambavyo vinajengwa kwa nguvu za wananchi na naamini Serikali mwaka huu watatupatia bajeti ya kuvimalizia. Pia Hospitali ya Wilaya ambayo nayo imeanza kujengwa na inakwenda kasi na hata Siha nimeona Hospitali ya Wilaya ambayo imejengwa jumba la ghorofa linakalibia kukamilika.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba watumishi watapatikana ili facility hizi ziweze kutoa huduma shahiki kwa Watanzania? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza yote kwa pamoja ya Mheshimiwa Mbunge Kiruswa wa Longido, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru sana kwa pongezi, nazipokea, aendelee tu kuniombea kwa Mungu ili nisiwaangushe Watanzania wote na Mheshimiwa Rais mwenyewe. Pia na yeye binafsi nimpongeze kwa kazi nzuri ambayo anaifanya kwenye Jimbo lake la Longido hususani katika kufuatilia huduma zinazotolewa na watumishi wa umma kwa wapiga kura wake wa Jimbo la Longido.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu tu kwa ufupi na kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nafasi zote za kukaimu; kwanza kukaimu ni nafasi ya muda, wala siyo ya kuthibitishwa. Naomba niwaeleze Watanzania wote kwa faida ya wengine, kwa sababu kuna wengine huwa wanafikiri kwamba ukipewa nafasi ya kukaimu, basi ndiyo leeway yako ya kuthibitishwa, hapana. Kukaimu unakaimu kwa muda na mara nyingi watu wengi wamekuwa wakikaimu kwa muda mrefu kwa sababu watu wamekuwa wakikaimishwa kienyeji bila kufuata utaratibu. Utaratibu ni kwamba unapotaka kumkaimisha kiongozi yeyote yule ambaye ameshafikia katika ile level ambayo tunaita superlative substansive post (nafasi ya uongozi) basi unatakiwa kupata kibali kutoka utumishi. Utumishi wakupatie kibali.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile mwaka 2018 mwezi Septemba, Serikali yetu imetoa waraka kwamba nafasi zote zile za kukaimu zisizidi miezi sita. Unapotaka yule Afisa aendelee kukaimu, basi unatakiwa utoe sababu nyingine wewe kama Mwajiri kwa nini unataka aendelee kukaimu? Hiyo yote ni katika lengo la kuboresha ili viongozi wetu wasiwe wanakaimu kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, kwenye jibu langu la msingi nimesema katika Jimbo lake la Longido tumetoa vibali na nafasi za ajira 177. Katika hizo 177, 65 zinakwenda katika Sekta ya Afya, 69 zinakwenda katika Sekta ya Elimu na zinazobaki nyingine zote zinakwenda katika kada nyingine mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika zile kada nyingine ambazo ni za kimuundo, zenyewe hazihitaji kukaimishwa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge mwaka huu wa Fedha 2018/2019, hizi nafasi 177 tutakuwa tumeshazijaza katika Wilaya ya Longido hususan Jimbo lako.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora naomba nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri, Mwanjelwa kwa majibu mazuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongeze jibu kwenye swali linalohusiana na Watendaji wa Serikali za Mitaa. Hii hoja ya Mheshimiwa Mbunge wa Longido ni kweli, lakini naomba niseme tu kwamba kupata Watendaji kwenye ngazi za Halmashauri na huu ni mwaka wa bajeti kwenye Bunge hili Tukufu, tunatarajia Wakurugenzi ambao ndio waajiri wa watu hawa, Watendaji wa Vijiji, Watendaji wa Mitaa watakuwa wameingiza kwenye bajeti zao ili tupitishe na waweze kupata ajira. Kwa hiyo, Wakurugenzi wanapaswa kujua upungufu wa maeneo yao ya kiutendaji, kama wakiwasiliana na Ofisi ya TAMISEMI kwamba hawa watu wanafanya kazi kubwa sana waweze kusaidiwa utendaji katika ngazi ya chini. Ahsante.
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri, mkwe wangu, kwa majibu mazuri aliyoweza kunipatia, lakini (a) kwa kuwa Serikali imekiri kwamba kati ya watumishi 15,000 walioondolewa waligundua kwamba watumishi 4,160 waliondolewa kimakosa. Hawa ni wale waliopata nafasi ya kuja Dodoma, Utumishi na kwenda Dar es Salaam kwenye Tume. Wale ambao hawakuwa na uwezo, tafsiri yake ni kwamba wamebaki huko.

Sasa swali; ni lini sasa Serikali itaunda tume ambayo angalau itakwenda kila Halmashauri au Mkoani pale iwaite wale wote waliokumbwa na mkasa huu wa kupoteza ajira waje ili vyeti vyao viweze kuhakikiwa ili wale ambao hawakupata nafasi ya kuja waweze kurudi kazini?

Swali la pili; tunatambua kwamba wako watumishi ambao wamekaa au wametumikia nchi hii katika kipindi kirefu na wengine walibakiza tu mwaka mmoja wastaafu na kwa bahati mbaya wamekumbwa na huo mkasa; Serikali ina mpango gani angalau hata kuwapa kifuta machozi ili waende wakaanze maisha yao huko waliko kuliko kuwaacha kama ilivyowaacha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia sana suala la watumishi wa Umma, hususan wale ambao walikuwa wameandika taarifa zisizokuwa na ukweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza kujibu swali lake la kwanza; kwanza kabisa naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge na kwa faida ya Watanzania wengine na Watumishi wa Umma wote kwamba Serikali ilishafanya zoezi la ufuatiliaji kwa zaidi ya asilimia 95 na hilo zoezi limeshakamilika. Wale watumishi wote ambao waliandika taarifa zao siyo sahihi katika personal records au kwenye OPRAS, naomba niliambie Bunge lako Tukufu kwamba kama walidanganya watakosa stahiki zao zote kwa sababu Kanuni ya Utumishi wa Umma, kile kifungu D.12 kinasema mtumishi yeyote ambaye anaandika taarifa za uongo hataruhusiwa kuwa Mtumishi wa Umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali pia ilitoa msamaha hadi tarehe 31 Desemba, 2017, kwamba wale wote ambao walikuwa wamejiendeleza, basi walete taaifa zao kwenye Ofisi yetu ya Utumishi maana ilishatoa msamaha ili taarifa zao ziweze kuingia na waweze kurudi kazini. Kwa hiyo, zaidi ya watumishi 500 wamesharejeshwa na wale ambao walijiendeleza baada ya muda huo basi waweze kutuletea vyetu vyao tuweze kuhakiki na waweze kurudi kazini. Ahsante.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Naomba kuuliza kuhusu watumishi waliochishwa kazi kwenye hili zoezi wenye vyeti vya Darasa la Saba wakaenda chuo; kwa mfano kuna waliokwenda Chuo cha Simanjiro cha Mifugo wakapata vyeti, waka- perform vizuri wakaenda kusoma Diploma ya Udaktari wa Mifugo katika chuo cha Serikali kule Tengeru, lakini baada ya zoezi kupita walipogundulika tu kwamba hawana cheti cha form four – lakini hawajadanganya – wakaachishwa kazi.

Je, Serikali inaweza kutoa tamko gani kuhusu hawa ambao wanaona kwamba wameonewa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza lazima tukumbuke kwamba tarehe 20 Mei, 2004, baada ya hapo wale wote ambao walikuwa wametoa taarifa zisizo sahihi tulitoa msamaha hadi tarehe 31 Desemba, 2017 kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi na wale wote waliojiendeleza, kwa mfano katika masuala ya recategorization.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme, Serikali tunasisitiza, tunathamini, tunaheshimu recategorization kwa wale wote wanaojiendeleza kimasomo. Nimesema kwamba hadi hiyo tarehe 31 Desemba, 2017 kama walijiendeleza na vyeti vyao viko sahihi, watuletee Utumishi tutahakiki watarejeshwa kazini. Ahsante.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali moja tu la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wako maredeva ambao waliondolewa katika mfumo wa Serikali kwamba wamemaliza Darasa la Saba, kwa hiyo hawastahili kuwa madereva. Naomba kuiuliza Serikali, ni kigezo kipi ambacho kilitumika kuona kwamba dereva wa Darasa la Saba anaweza kuendesha gari vibaya kuliko yule wa Darasa la 12?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba niliambie Bunge lako Tukufu kwamba Serikali pia inawajali hata hao madereva wa Darasa la Saba. Naomba niliambie Bunge lako Tukufu kwamba madereva wote wale wa Darasa la Saba ambao walikuwa wamebainika kwamba vyeti vyao viko safi na taarifa zao ziko safi na waliandika ukweli, wapo kazini na wanaendelea na kazi kama kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Suala la kupandishwa madaraja linaambatana na ongezeko la mishahara. Serikali hii ya Awamu ya Tano imekuwa haipandishi watu madaraja kwa wakati, mtu anakaa mpaka miaka sita, saba, hajapandishwa madaraja. Nataka tu kujua Serikali iko tayari kuwalipa wale watu arrears zao kwa ile miaka ambayo hawakupandishwa madaraja kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, Mheshimiwa Waziri amesema wafanyakazi wafanye kazi kwa bidii. Hivi kweli anafikiri unaweza kumkamua ng’ombe maziwa kama humpi chakula cha kutosha? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Tunza Malapo, Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba kipekee nimpongeze sana kwa jinsi ambavyo anafuatilia masuala yote ya watumishi wa umma nchini. Hata hivyo, naomba niseme kwamba, katika upandishwaji wa madaraja tuna madaraja ya aina tatu, kuna kupandishwa kwa madaraja kwa maana ya salary increase, kuna annual increment na kuna salary promotion, lakini katika suala la upandishwaji wa madaraja Serikali ilitoa tamko hapa wiki tatu zilizopita kwamba, kuanzia Mei Mosi mwaka huu (2019) Serikali inatarajia kupandisha madaraja, vyeo, watumishi zaidi ya 193,000. Hilo zoezi limeshaanza, lakini vilevile mwaka 2017/ 2018 Serikali ilishalipa annual increment zaidi ya bilioni 72.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile naomba niseme kabisa kwamba, Walimu walishalipwa zaidi ya bilioni 37, lakini kada nyingine za utumishi wa umma walishalipwa zaidi ya bilioni 35, lakini malimbikizo ya mishahara zaidi ya bilioni 75 zimelipwa. Isitoshe tu, lakini zaidi ya wastaafu waliokuwa wanaidai Serikali wameshalipwa zaidi ya bilioni tisa na hawa wastaafu ni zaidi ya 1,800.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili ni kwamba, Serikali inawajali sana watumishi. Sio lazima iwe katika nyongeza tu ya mshahara, lakini vilevile tukumbuke kwamba, Serikali ndio guarantor, watumishi wanapotaka kujenga nyumba, watumishi wanapotaka kufanya mikopo, kuna bima za afya zote hizo ni sehemu ya motisha. Kwa hiyo, naomba niseme kabisa Serikali inawajali watumishi katika njia mbalimbali na hata katika kupanda madaraja hiyo imeshaanza kutekelezwa. Ahsante.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na nampongeza dada yangu Mheshimiwa Mary Mwanjelwa kwa majibu mazuri yaliyokwenda shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina swali la nyongeza. Kwa kuwa, Serikali iliwafukuza watumishi ambao walighushi vyeti au hawakuwa na vyeti vya kidato cha nne na kati ya hao watumishi ambao walifukuzwa ni kwamba, walikopa katika benki zetu na mpaka sasa hawajui hatima yao na wengine wamekufa na wengine wamekimbia nyumbani kwa sababu, benki zinawafuata mpaka nyumbani. Nataka kujua kwa sababu, wakati wanachukua Serikali ndio ilikuwa guarantor wao. Sasa je, nini Kauli ya Serikali kwa benki ambazo zinawasumbua hawa watumishi na hawana jinsi ya kuweza kurudisha hizo fedha? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la mdogo wangu, Mheshimiwa Amina Mollel, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa Serikali Mei, 2016 ilienda kwenye zoezi la kusitisha upandishwaji wa madaraja na vilevile kusimamia hilo zoezi zima la vyeti feki, lakini sio vyeti feki tu hata watumishi hewa. Tukumbuke kabisa kwamba, wakati najibu hapa swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Tunza Malapo nimesema Serikali inakwenda mbali zaidi katika kuwajali watumishi kwenye motisha hata katika kuwapatia guarantor mbalimbali ikiwemo na mikopo ya benki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tukumbuke watumishi hawa walikuwa ni halali, walikuwa ni watumishi halali na ndio maana Serikali inakuwa ni guarantor. Sasa kama wewe tayari umeshafukuzwa na hiyo tunasema ni crime kwa maana hiyo, sisi tunazingatia tu kwa yule mtumishi ambaye ni halali, Serikali itamjali, Serikali itakuwa ni guarantor pamoja na mambo mengine ya motisha. Ahsante.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nina swali moja dogo la nyongeza. Annual increment ipo kisheria, kutowapatia wafanyakazi annual increment kunasababisha wakati atakapostaafu kupungua, kupunjwa kwa mafao yao sambamba na kupungua kwa pension zao za uzeeni na wanasema kwamba, hii awamu ya kuwasaidia wanyonge na maskini.

Je, hawaoni sasa kuendelea kutowapatia annual increment wafanyakazi hawa wanaendelea kuwapunja, kuwadhulumu wanyonge hawa na lini Serikali wataacha tabia hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Masoud, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudie tena kujibu kile nilichojibu kwamba, suala la annual increment mwaka 2017/2018, Serikali imeshalipa annual increment kwa watumishi wote wa umma bila kujali kada zozote. Pia nimesema imelipa zaidi ya bilioni 72, lakini sio kwamba, Serikali inawapunja ni sehemu ya mtumishi wa umma kupata motisha; tena nilitegemea kaka yangu hata angeshukuru kwamba, Serikali inawajali watumishi na ndio maana imeweza kuongeza hiyo mishahara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme jibu langu nilishalijibu, Serikali inawajali watumishi na ndio maana mwaka 2017/2018 imelipa zaidi ya bilioni 72. Ahsante.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi kuuliza maswali ya nyongeza kwa niaba ya Mheshimiwa Eng. Makani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, nimpongeze Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana na Naibu wake kwa utendaji mzuri wa kazi. Pamoja na majibu hayo naomba maswali madogo ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, ni lini Serikali itashughulikia changamoto katika kaya za vijiji kwenye Tarafa za Nakapanya, Matemanga, Nampungu na Mlingoti? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni lini Serikali itapitia upya utaratibu wake na kuhakikisha kwamba wanufaika wanakuwa ni wale wenye kaya maskini na siyo wale wenye uwezo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba nimjibu maswali madogo mawili ya nyongeza wifi yangu Mheshimiwa Jacqueline Msongozi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kama mwanamke naomba nimpongeze kwa sababu walengwa wengi ambao ni wanufaika wa kaya maskini ni wanawake kwa sababu wameonyesha uaminifu mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika swali kuhusu Tarafa za Napakanya, Matemanga, Nampungu na Mlingoti, naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba sasa hivi TASAF tumekuwa katika Awamu ya Tatu na mwezi ujao Oktoba tunategemea kuzindua rasmi sehemu ile ya pili ambapo tumemaliza sehemu ya kwanza. Hizi Tarafa zote nne ambazo amezisema basi walengwa wote wale ambao hawajafikiwa watafikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali la pili, naomba niseme kwamba Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Mpango huu wa Kunusuru Kaya Maskini tumejipanga kuboresha zaidi kuhakikisha kwamba walengwa wote ambao tulikuwa tunawawezesha na sasa hivi wameweza kusimama wenyewe, tutakuwa na mpango mkakati kuhakikisha kwamba wamefuzu tunaita graduation ili sasa waweze ku- phaseout ili tuweze kusaidia wale wengine ambao hawajiwezi kwa sababu wasiojiweza, maskini sana, wazee, walemavu wapo kila siku basi tuendelee kuwahudumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, tumeboresha mfumo kuhakikisha kwamba kuanzia sasa hivi tutakwenda kielektroniki ili kuondokana na suala zima la kaya hewa. Niwatake Wabunge wote na Watanzania wote kuhakikisha kwamba wanaendelea kuunga mkono juhudi hizi za Serikali ya Awamu ya Tano kuhakikisha kwamba walengwa wote wanaotokana na kaya maskini ndiyo hao wanaostahili kupewa misaada yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa Mpango huu wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) umefanikiwa kwa kiwango kikubwa na umenufaisha nchi na sisi Wabunge tukiwa wamojawapo. Je, Serikali itakuwa sasa tayari kutoa takwimu ni Wilaya, Mkoa na Kijiji gani mpango huu umefanyika vizuri ili iwe mfano kwa Wilaya au Mikoa mingine ambayo imeshindwa kufanya vizuri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja dogo la nyongeza la Mheshimiwa kaka yangu Mheshimiwa Mwamoto, kama ifauatvyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango mzima huu wa TASAF, takwimu zipo na muda wowote anapozihitaji tutampatia kwa sababu ni zoezi endelevu. Sisi kama TASAF tumejipanga kuonyesha kwamba sasa hivi tutakuwa tunaonyesha zaidi multiply effect ya walengwa wote na mpango mzima mpaka leo hii tumetumia shilingi ngapi ili kuonyesha kwamba impact yake inaonekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba niulize swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Kamati yetu ya Utawala na Serikali za Mitaa tulipotembelea Mikoa ya Mwanza, Mara na Simiyu, tulikuta madaftari mengi wameorodheshwa watu ambao siyo walengwa, ni vijana ambao ni matajiri, wana mali na nyumba nzuri. Tulikwishatoa ushauri kwenye Wizara hii hawa vijana wote waondolewe. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, orodha ile mlihakiki na kuondoa majina hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba nimjibu swali dogo la nyongeza Mzee wangu Mheshimiwa Lubeleje, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli siku za nyuma kulikuwa na walengwa wengine ambao wana uwezo lakini walikuwa kwenye mpango. Serikali ya Awamu ya Tano hilo tumelidhibiti na hao wote tuliwaondoa. Ndiyo maana pia katika jibu langu la nyongeza nimesema katika sehemu yetu hii ya pili tunakwenda kielektroniki kudhibiti wale wote ambao wanasema wanatokana na kaya maskini lakini kumbe ni kaya maskini hewa. Hilo tumelidhibiti na tumeboresha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Pamoja namajibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri na ninampongeza kwa kazi nzuri, nilikuwa na maswali madogo mawili.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa katika miradi ya TASAF Awamu ya I na TASAF Awamu ya II, ulikowepo pia utekelezaji wa miradi ya miundombinu kama ujenzi wa barabara, ujenzi wa madarasa, miundombinu ya maji, utoaji wa fedha kwa ajili ya VIKOBA na miradi mingine mbalimbali, zikiwemo zahanati. Lakini baadaye katika TASAF three, TASAF Awamu ya II miradi hiyo kwa kiwango kikubwa iliondolewa, ama ilikuwepo kwa kiasi kidogo au haikuwepo kabisa.

Sasa je, katika huu mpango wa awamu ya pili wa TASAF inayofuata sasa miradi hii itahusika katika utekelezaji katika vijiji vyetua mbapo ilikuwa imetoa faida kubwa sana katika sekta mbalimbali? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili, kwa kuwa Awamu hii ya III ya ugawaji wa fedha kwa walengwa walikuwa wanakwenda kugawa fedha moja kwa moja kwa walengwa kwa maana hizi kaya maskini, lakini ilijitokeza pia uwepo wa kaya hewa, jambo ambalo lilisababisha fedha hizi za Serikali kwenda mahali ambapo kwa watu hawakuwa waaminifu na hivyo kutokufikia malengo yaliyokusudiwa.

Je, katika awamu hii ya pili ya ugawaji wa mradi huu wa fedha za TASAF Serikali imejipangaje kuhakikisha kwamba hakutokei tena walengwa hewa ili fedha hizi ambazo zimepangwa na Serikali kupelekwa huko ziweze kupelekwa huko ziweze kufanya kazi iliyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza na yeye ninampongeza akiwa mmoja wapo wa watu ma-champion mahiri katika kufuatilia walengwa wetu wa kaya maskini kupitia mpango wetu wa TASAF.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge kabisa kwamba, mpango wa kunusuru kaya maskini, ni kweli awamu ya kwanza ulihusisha sana miundombinu, na ninaomba niliambie Bunge lako Tukufu kwamba, katika awamu yetu hii ya tatu kipindi cha kwanza, ambacho kinaisha mwezi huu na kipindi cha pili ambacho kinaanza mwezi ujao wa 12 mwaka 2019, tutaendelea na mpango wa miundombinu lakini tutajikita zaidi katika public works, kwa maana ya kwamba, zile ajira kwa muda, kwa wale walengwa ambao wanatokana na kaya maskini sana ili waweze kufanya kazi, waweze kupata ujira na ajira katika kuwawezesha maisha yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, anasema Serikali tumejipangaje katika awamu ya tatu, Awamu ya II niliambie Bunge lako Tukufu kwamba tumejipanga, Serikali ya awamu ya tano, kuhakikisha kwamba walengwa wote kuanzia sasa hivi tutakuwa tunawaendea kwa kutumia njia za kidijitali kwa maana ya GPS, tutakuwa tunapiga picha kwenye kaya husika, lakini tayari tumeshafanya pilot project areas katika Mtwara DC, katika Halmashauri ya Nanyamba, lakini hata kule Siha na changamoto tulizozipata kule, ndizo ambazo zitatufanya tuboreshe katika maeneo mengine ambayo tutafika katika sehemu yetu hii ya pili inayoanza mwezi ujao.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile naomba niliambie Bunge lako Tukufu kwamba pia tutakuwa tunawalipa walengwa kwa njia za kielektroniki, vilevile VIKOBA na tayari tumeshaweka mpango mkakati mwingine, kuhakikisha kwamba tutakuwa na wale wanaofuzu, kwa maana ya graduation, tutakuwa tunawapatia mafunzo na tunawaunganisha na taasisi za kifedha na hii yote ili kuweza kuwa na multiply effects. Ahsante.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa wanufaika wengi wa TASAF ni wazee wasiojiweza na wanatoka katika maeneo ya pembezoni na inapofikia siku ya kupokea mafao, huwa wanafika pale katika maeneo ya vijiji kwa kutumia usafiri na usafiri huo wanalipia zile fedha za mafao. Je, Serikali haioni umefikia wakati wa kubaini wazee hawa wasiojiweza na kuweza kuwapelekea zile fedha katika maeneo yao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, hapa wakati najibu maswali yangu ya msingi na ya nyongeza ya Mheshimiwa Badwel nimesema, mkakati mmoja wapo wa Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha tunaboresha, kwamba tutakuwa tunawalipa walengwa wote kwa njia za kielektroniki kwa maana ya kwamba tumegundua kwamba walengwa wengine walikuwa wanakatwa fedha zao bila ridhaa yao na wengine walikuwa wanadhurumiwa, ndiyo maana katika kuboresha, tumeamua kwamba tutakuwa tunawalipa kwa njia ya kielektroniki. Ahsante.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, kumekuwa na utaratibu mbovu kwa baadhi ya viongozi wanaogawa fedha hizi, wakitumia itikadi za kisiasa, ikiwepo ukiwa mwanachama wa chama fulani, unaweza ukapewa fedha hizo, lakini ukiwa mwanachama wa chama kingine hupewi fedha hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba Serikali itoe tamko fedha hizi wanaotakiwa kupewa ni watu wa aina gani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli haina ubaguzi. Ni Serikali ya Watanzania wote. Naomba niliambie Bunge lako Tukufu kwamba pesa hizi zinazotokana na Mpango wetu wa TASAF ni kwa walengwa wote wanaotokana na zile kaya masikini sana na hakuna ubaguzi wowote. Nitoe rai na agizo kwamba yeyote atakayeleta ubaguzi katika kuhakikisha kwamba walengwa wanaotokana na mpango huu wa kunusuru kaya masikini wanasaidiwa, watoe taarifa na watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, swali langu la msingi nilisema wahitimu wa vyuo vikuu waliokidhi Vigezo, sikusema waliohitimu tu ndiyo wote wanastahili kuajiriwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Serikali, kila mwaka takribani Wahitimu laki nane, kwa mwaka, na wanaoajiriwa ni elfu arobaini peke yake, kwa hiyo laki saba na sitini wanabaki mtaani. Ningependa kujua Serikali ina Mkakati gani wa ziada, kwa sababu Mkakati uliopo umeshindwa kukidhi vigezo vya kuweza kuwaajiri vijana wengi ambao wamehitimu? Ni Mkakati gani wa ziada ambao Serikali inao kwa ajili ya kuwasaidia Vijana hawa ambao wengi wako mtaani?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Kumekuwa na vikwazo mbalimbali kwa hawa wahitimu wanapokuwa wanaomba kazi, na kikwazo namba moja, ni kikwazo ambacho wanawaambia kwamba wawe na uzoefu, na wakiamini wametoka chuoni. Ningependa kujua, Serikali haioni ni kuna Mkakati ambao unahitajika wa ziada sana, kuwa na programu maalum ya kuwa andaa Vijana hawa kabla ya hawajakwenda kazini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, naomba niseme kabisa kwamba kila Mtanzania ana haki ya kuomba ajira kwenye Utumishi wa Umma. Lakini vilevile, tuangalie kwamba ajira za Serikalini huzingatia sana scheme of service, huzingatia sana ikama, na bajeti iliyopangwa kwa wakati huo, na vilevile kutegemea na vipaumbele vya Taifa wakati huo. Niwahase wahitimu wote nchini waendelee kuomba ajira kupitia sekretarieti yetu ya ajira ambayo tumeboresha sasa hivi inapitia ajira portal kupitia njia ya mtandao.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba niliambie Bunge lako Tukufu pia kwamba mwaka ule wa fedha 2018/ 2019 Serikali iliweza kuajiri ajira mbadala na ajira mpya zaidi ya elfu arobaini na moja na laki na sita na Kada ya Walimu ilikuwa elfu nne na mia tano. Lakini kwa mwaka huu wa fedha naomba niliambie Bunge lako Tukufu kabisa kwamba Serikali inatarajia kuajiri zaidi ya ajira elfu arobaini na nne na laki na nane, lakini kana kwamba hiyo haitoshi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niliambie Bunge lako Tukufu kwamba Serikali ya Awamu ya Tano pia imejipanga tumeanzisha Sera ya local content ili private sector zote nchini ziweze kuajiri Watanzania na nichukue fursa hii kuwapongeza sana Mkoa wa Pwani kwa sababu wao wamezingatia sana Sera ya Viwanda na Uchumi na wameweza kuajiri zaidi ya Watanzania elfu hamsini, iwe ni in direct iwe ni direct na naomba nitoe Rai, Mikoa mingine pia iweze kuiga mfano wa Mkoa wa Pwani ambao wanaufanya mpaka sasa hivi, ili Watanzania wengi pia waweze kupata ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili, la Mheshimiwa Mbunge Khenani anazungumzia Mikakati ya Serikali ambayo mingine nimeitaja, amezungumzia kuhusu uzoefu na naomba niseme katika Sera yetu mpya ya Utumishi 2004 Serikali imesema kabisa kwamba ajira mpya hazitazingatia uzoefu, uzoefu unakuja kwa wale ambao tayari wako kazini. Ahsante.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini nirudi kwenye swali la nyongeza la pili la Mheshimiwa Aida Khenani na hasa eneo lile ambalo vijana wengi wa Kitanzania wamekuwa wakipata shida sana ya kigezo cha uzoefu, katika kutafuta ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na vijana, kweli limekuwa ni tatizo, Ofisi ya Waziri Mkuu inasimamia masuala ya Ustawi wa Vijana, na baada ya kugundua kwamba vijana wengi wamekosa sifa za kuajiriwa kwa sababu ya kigezo cha uzoefu, Ofisi ya Waziri ya Mkuu, iliamua kutengeneza mwongozo mpya, wa internship ili kuhakikisha vijana wanapomaliza masomo yao, waweze kupata maeneo ya kupata uzoefu kwenye private sector na maeneo mbalimbali, na zinapotoka nafasi za ajira kigezo cha uzoefu kiwe tena siyo kikwazo kwa ajili ya ajira zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa program hiyo sasa imekwisha kuanza, na Ofisi ya Waziri Mkuu imeshasimamia makundi ya kutosha ya vijana na kuwapeleka kwenye maeneo mbalimbali kwa ajili ya internship programme tayari kwa kuwafanya wawe na uzoefu wa kuajiriwa. (Makofi)
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Serikali, bado malipo ya mishahara na makato kwa watu ambao sio Watumishi wa Umma bado yanaendelea kulipwa kulingana na hoja za Mkaguzi CAG. Kwa mfano 2017/2018 shilingi milioni 207.3 zililipwa. Je, ni kwa nini Wizara ya Fedha inachelewa kukamata yaani ku-hold makato yaliyolipwa kwa Taasisi mbalimbali na kusimamisha makato ya mishahara kwa kiwango sawa na watumishi wasiostahili kulipwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; je, Serikali inachukua baada ya muda gani kuweza kuhuisha taarifa za watumishi ili waweze kushughulikiwa haraka kwa kuondolewa katika Mfumo wa Malipo ya Mishahara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba nami nijibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Leah Komanya kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kama Serikali tulifanya HR Audit kwa Watumishi wote wa Umma wakiwepo na hawa wa TAMISEMI zaidi ya 197,000 mwaka ule wa 2016, lakini watumishi wote wale wanaoacha kazi, waliofukuzwa kazi, waliofariki, hawasalii kabisa kwenye Payroll ya Serikali. Naomba niliambie Bunge lako Tukufu na Watanzania wote kwamba kama Serikali sasa hivi tumeboresha Mfumo wa Utumishi na Mishahara kiasi cha kwamba hatutatumia tena ile Lawson Version 9 ambayo tulikuwa tunatumia, tuna Mfumo wetu wenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, taarifa zozote zinazotoka kwa waajiri wote, kama ziko sahihi zinatolewa siku hiyo hiyo ikiwepo pamoja na malipo ya madai yote. Kwa hiyo, nawataka waajiri wote nchini kuhakikisha kwamba wanatuletea taarifa ambazo ni sahihi na kwa wakati na kutokana na mfumo wetu huu mpya ambao tunauanza mwezi ujao, basi taarifa za watumishi wote zitatolewa siku hiyo hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. (Makofi)
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Swali la kwanza, Serikali imekiri kwamba matukio ya kujifungua watoto njiti au mtoto zaidi ya mmoja hayakuwa makubwa hapo awali ila tunaongea kujifungua watoto njiti na mtoto zaidi ya mmoja ni matukio ambayo yamezidi kuongezeka.

Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kutengeneza kanuni ya kuongeza siku kwa familia ambayo inapata hususan watoto njiti au watoto zaidi ya mmoja kwa sababu changamoto yake ni kubwa badala ya kuacha ilivyo leo inakuwa kama amnesty ya kupewa hiyo nafasi ya kulea hao watoto? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa wanaume ni kiungo muhimu katika familia na hasa familia inavyopitia changamoto ya kupata watoto njiti au watoto zaidi ya mmoja. Serikali haioni umuhimu pia wa kubadilisha kanuni ya kumruhusu mwanaume kukaa nyumbani kusaidiana na familia kwa si chini ya zaidi ya wiki mbili mpaka tatu ukizingatia kwamba hiyo likizo inatolewa mara moja kwa miaka mitatu ili akaisaidie familia pia? Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya mdogo wangu Mheshimiwa Anatropia, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza sana kwa kuona umuhimu wa maternity na paternity kwa watumishi wa Umma. Hata hivyo, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi ni kwamba katika kile kifungu cha Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma cha 12(3) kama Serikali tumeongezea siku 14 zaidi kwa wale wamama wote wazazi ambao wanajifungua watoto ya wawili.

Mheshimiwa Spika, hii ni kuonesha umuhimu kwa mama mzazi kwa sababu sote humu ndani ni wanawake na wanaume, tumezaliwa tumelelewa na wanawake na tunajua kabisa huyu mama mzazi anapojifungua anakuwa na complications nyingi lakini vilevile ndiyo anayenyonyesha watoto hata afya ya yule mama inahitaji kuimarika. Ndiyo maana kwa msingi huo tumeweza kuongeza siku 14 zaidi kwa mama mzazi huyu ambaye atajifungua watoto zaidi ya wawili.

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili kuhusu paternity; vilevile nimeshajibu kwenye jibu langu la msingi kwamba katika kifungu kile cha 13 cha Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma baba mzazi na yeye anatambuliwa kuwa ni baba wa mtoto na ndiyo maana tumetoa kile kifungu kisheria kabisa kwamba angalau siku tano maana siku tano zile za mwanzoni mama akijifungua ndiyo kipindi hatarishi ambacho mama naye anamuhitaji baba awepo nyumbani.

Mheshimiwa Spika, vilevile huyu baba endapo mazingira kutokana na ile familia hayaruhusu, basi anaweza akaomba kibali kutoka kwa Katibu Mkuu Utumishi kupitia kwa mwajiri wake. Ahsante.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Kanuni za Utumishi wa Umma hazikuainisha waziwazi mtumishi mwanamke anayezaa watoto zaidi ya wawili ama mtoto njiti anaongezewaje siku; na kwa kuwa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini imetoa fursa ya kuingia mikataba ya hali bora mahali pa kazi, je, Serikali haioni umefika sasa wakati kwa kutumia hii fursa ya kutengeneza ama ya kuingia mikataba ya hali bora ya kazi kwa watumishi wanawake wanaopata watoto zaidi ya wawili ama kwa mwanamke anayezaa mtoto njiti? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali moja dogo la nyongeza la Mheshimiwa mdogo wangu Mheshimiwa Hawa Mchafu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, wakati najibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge Anatropia nimesema kwamba Serikali inatambua na inajali wanawake wote ambao wanajifungua watoto zaidi ya wawili na ndiyo maana kama Serikali tumeweza kuongezea zile siku 14 ili kwa pamoja ziweze kuwa siku 98 kwa sababu likizo ya uzazi ni siku 84. Kwa maana hiyo wale wote wanaojifungua watoto njiti au watoto zaidi ya wawili tumewaongezea siku 14. Hii iko kisheria ili kuthibitisha na kuhakikisha kwamba huyu mama mzazi anastahili kupewa haki yake.

Mheshimiwa Spika, hili jambo naomba niwaambie Wabunge wote kwamba liko kisheria na tumeongeza hizo siku 14 zaidi kwa ajili ya akina mama wote wanaojifungua mtoto zaidi ya mmoja. Ahsante.