Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Katani Ahmadi Katani (11 total)

MHE. KATANI A. KATANI: Naitwa Katani Ahmad Katani, Mbunge wa Jimbo la Tandahimba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Wilaya ya Tandahimba ina vyanzo vingi vya maji ukiwepo Mto Ruvuma na Mahuta lakini bado wananchi wake wanapata tatizo kubwa la maji.
Je, Wizara ina utaratibu gani wa kuhakikisha inaleta mashine ikafunga pale watu wake wakapata maji ya kutosha?
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli pale Tandahimba kuna mto na ni kweli wana changamoto ya maji. Kama nilivyosema pale mwanzo kila jambo lazima tuwe na mchakato wa upatikanaji wa fedha.
Kwa suala hili katika kikao chetu cha juzi tulifanya maamuzi tukasema lazima Wizara ya Maji na TAMISEMI utendaji wetu wa kazi uwe wa karibu sana. Katika haya nini cha kufanya?
Mheshimiwa Naibu Spika, tumesema kila Halmashauri kwanza angalau itenge bajeti ya kuanza kushughulikia yale mambo ya awali mfano kufanya upembuzi yakinifu sehemu ambayo chanzo cha maji kinaweza kupatikana. Hali kadhalika katika mchakato wa bajeti, naomba nizielekeze Halmashauri zote zihakikishe katika bajeti zao ajenda ya maji ni ya msingi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba ajenda kubwa ya Serikali ni kuhakikisha inatatua tatizo la maji kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Katani hili ulilolizungumzia Serikali imesikia na inalichukua na lengo kubwa la Mheshimiwa Rais wetu amesema ni lazima tuhakikishe tunamtua ndoo mama, suala hili tutakwenda kulifanyia kazi.
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Spika, msimu kwa Korosho unapofika kwenye minada yetu kumekuwa na ubora wa Korosho. Korosho ile ile yenye ubora wa outturn 52 ya Tandahimba, nut-count ya 180 ya Tandahimba, moisture ya 8 ya Tandahimba, inakuwa na bei tofauti na Korosho ya Newala, lakini kila kitu kiko sawa. Je, Serikali inatuambia nini? Kuna nini kati kati yake kinachofanya bei hizi ziwe tofauti wakati ni Korosho zile zile zinazotoka Tandahimba kwenda Newala?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, bahati nzuri Mheshimiwa Katani anafahamu changamoto zilizopo na michezo iliyoko. Nataka tu nimwahidi kwamba, michezo iliyoko na ambayo imekuwepo kwa muda mrefu katika ukanda huo, safari hii tunaenda kuimaliza na tumeanza hatua ya kwanza kwa kuwa na transparency system, Mheshimiwa Waziri Mkuu ametusaidia sana kwamba minada badala ya kulaza gudulia kesho, kesho kutwa halafu bei ndiyo ifunguliwe, utaratibu huo umeondoka kwa mwaka huu wa kwanza. Mwaka huu tumefanya transparency kwa mara ya kwanza minada hadharani inafunguliwa kwa uwazi.

Mheshimiwa Spika, vile vile tumejifunza jambo jipya. Nataka nimuhakikishie, mbinu za kivita hazitangazwi hadharani, lakini tutalimaliza Mwenyezi Mungu akitujaalia msimu ujao.
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Spika, Kata ya Michenjele ambayo iko mpakani na Msumbiji nako kuna tatizo kubwa la usikivu wa mawasiliano ya simu hakuna hata mnara wa aina moja ambao unapatikana kule Michenjele: -

Je ni lini Serikali itapeleka huduma hii kwenye maeneo yale ya mpakani?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Katani kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kata ya Michenjele ipo katika vijiji ambavyo vimeshafanyiwa tathmini kwa ajili ya Awamu ya Sita ya mipakani na border and special zone. Lakini kata hizi ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitaja kwa mfano Kata ya Mihambwe tayari kuna mtoa huduma wa airtel ambao anaendelea na utekelezaji wa ujenzi wa minara.

Mheshimiwa Spika, lakini pia Kata ya Mdimba kama ambavyo nilijibu katika swali langu la msingi kuna mtoa huduma tayari ambaye ni tigo ambaye anaendelea na utekelezaji lakini pia kina Kata ya Chaume ambapo tayari kuna mtoa huduma ambaye anaendelea na ujenzi wa mnara katika maeneo hayo. Ahsante.
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu ya Serikali nadhani haielewi Swali langu la Msingi. Chikongo tunaposema upande wa pili wa Msumbiji, wenzetu tayari wanacho kituo cha uhamiaji, upande wa Tanzania ndio hatuna kituo cha uhamiaji: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali languni kwamba, ni lini Serikali itapeleka kituo cha uhamiaji upande huu wa Tanzania? Si suala la mashauriano na Msumbiji kwa sababu, Msumbiji wao tayari wanacho kituo cha uhamiaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili. Je, wenzetu wa Msumbiji tunapopeleka bidhaa kule wana custom pale, wana shughuli zote pale. Upande wa Tanzania wananchi wetu wakileta bidhaa wanapata shida kwa sababu hawana custom hapo, TRA hawapo pale. Tupe kauli ya Serikali, ni lini mtajenga kituo cha uhamiaji pale na kupeleka huduma nyingine zote za msingi ili Watanzania wapate huduma kwa urahisi pale?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Katani, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niruhusu nimpongeze sana Mheshimiwa Katani kwa kazi nzuri anayoifanya; na ndiyo maana wananchi wa Tandahimba walimuamini na kumpa nafasi ya kuwawakilisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme kwa ujumla wake kwamba lengo la Serikali ni kudhibiti maeneo yote ya mipaka yetu, ikiwemo uingiaji wa wageni na utokaji pia wa wananchi wetu. Pia kudhibiti mapato kupitia TRA, yako pia masuala ya afya pamoja na masuala ya usalama kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kuhusu maswali yake yote mawili kwa ujumla. Ni kwamba niwatoe hofu tu wananchi wa Tandahimba, tunaona uko umuhimu. Kituo cha uhamiaji ambacho tunacho kiko makao makuu ya wilaya, ni mbali kidogo na sehemu ambapo wananchi wanavuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Katani, kwamba suala hili tumelichukua. Nitumie nafasi hii tu kumuelekeza Kamishna wa Uhamiaji atume wataalam pale. Kwa sababu wananchi kama wanagonga passport zao ng’ambo wanapoingia; ni muhimu wananchi pia wa Tanzania waweze kupata huduma vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, suala hili nalielekeza tu lifanyiwe kazi mara moja na sisi tutaendelea kusimamia kama Serikali kuona wananchi hawapati shida na tunapata manufaa makubwa sana kutoka kwa nchi za majirani kupitia biashara na mambo mengine ambayo yanahusiana na mambo ya mipakani. Ahsante sana.
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Spika, Vijiji vya Kata ya Mkundi, Nanyanga pamoja na Mchichira, Wizara ilileta mitambo ya kuchimba maji na maji yakapatikana lakini mpaka leo wananchi wale hawajaanza kuyatumia maji yale. Je, ni upi mpango wa Serikali kuhakikisha inaleta vitu ili wananchi waweze kutumia maji.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Katani Katani kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuchimba kisima ni hatua moja, baada ya hapo tunakuja sasa kwenye usambazaji. Hivi punde tutajitahidi kuhakikisha visima hivi vilivyochimbwa siyo tu kwenye eneo lako hata pale Mtwara mjini tuna visima tulishachimba na sasa tunaelekea sasa kwenye utekelezaji wa usambazaji Mheshimiwa Mbunge.
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Spika, kutoka Mpwiti, Mkonjoano kuelekea Tandahimba ni barabara ambayo upembuzi yakinifu imeshafanywa zaidi ya miaka minne.

Je, ni lini barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Katani Katani Mbunge wa Tandahimba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaji ninataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kuwa usanifu ulishakamilika Serikali inajipanga kutafuta fedha ili iweze kuijenga kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, azma Serikali ni kuijenga na tuna uhakika itajengwa fedha itakapopatikana. Ahsante.
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali: -

Kata za Mahuta na Mkwedu hazina shule ya sekondari kabisa; je, Serikali inaweza ikatupa fedha kwa ajili ya kujenga sekondari hizo kwa sababu tayari wananchi wameshaanza kujenga maeneo yale?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, kata hizi alizozitaja Mheshimiwa Katani hapa Serikali tayari iko mbioni kupeleka shilingi milioni 470 kwenye halmashauri 184 nchi nzima kwa ajili ya ujenzi wa shule nyingine za sekondari katika kata zile ambazo bado hazijapata shule hizi za sekondari. (Makofi)
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Serikali imefanya uchambuzi yakinifu wa Barabara kutoka Mtama – Mkwiti - Ng’unja – Litehu mpaka Tandahimba miaka mitatu nyuma. Je, lini Serikali itajenga barabara hii kwa kiwango cha lami?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa barabara hii ina kipande korofi cha kutoka Ng’unja kuja Mkwiti. Je, Serikali iko tayari kutenga fedha ya dharura kwa ajili ya kuweka lami kipande kile?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Katani, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye upande wa swali la kwanza, ujenzi utaanza lini. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Katani kwa namna ambavyo amefuatilia mpaka Serikali tukafikia hatua ya kukamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Mara fedha zitakapopatikana ujenzi wa barabara hii utaanza mara moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusu kipande korofi toka Ng’unja kwenda Mkwiti, Mheshimiwa Mbunge ameomba fedha za dharura. Natumia nafasi hii kuwaelekeza Mameneja wa TANROADS Mikoa yote kuangalia maeneo kama haya, maeneo korofi na kuyabainisha na kufanya assessment na kuleta Wizarani ili tunapokuwa tunaandaa bajeti, maeneo haya kama aliyoyasema Mheshimiwa Katani tuweze kuyaweka kwenye kipaumbele. (Makofi)
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Luagara kwenda Liponde kilometa 1.5 ilishafanyiwa feasibility study na watu wa TARURA na walishaweka kwenye bajeti miaka miwili nyuma, ni lini sasa Serikali itakwenda kuweka lami kipande kile?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu barabara hii tayari imeshafanyiwa usanifu na tayari ipo kwenye bajeti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tutafuatilia kwa karibu hata baada ya kutoka kwenye maswali hapa tutakaa tutafuatilia kwa karibu ili tuhakikishe kwamba mwaka huu kwa sababu fedha tayari imeishatengwa ili iweze kujengwa barabara hii.
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, vile viwanda ambavyo viliuzwa na Serikali kwa dhamira ya kuendeleza ubanguaji na walionunua viwanda hawakufanya ubanguaji na badala yake wamefanya maghala.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuvirejesha viwanda vile kwa sababu havijafanyiwa kazi iliyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwanza nishukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo kuhusiana na uongezaji thamani kwenye sekta hii ya korosho. Kimsingi ni kweli viwanda vingi ambavyo vilikuwa vimebinafsishwa wakati ule ambavyo viko kwenye sekta ya korosho, walionunua wengi/waliobinafsishiwa hawakuviendeleza na moja ya anachokisema Mheshimiwa Katani ni kweli na tumeshasema tayari Serikali imeshaanza mchakato wa kuvirejesha viwanda vyote ambavyo viliuzwa au vilibinafsishwa na havifanyi kazi na walionunua hawajaviendeleza. Kwa hiyo, naomba tu watupatie nafasi tukamilishe mchakato huu ili tuvirejeshe Serikalini na kuwatafutia wawekezaji wengine.
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Luagara kwenda Liponde kilometa 1.5 ilishafanyiwa feasibility study na watu wa TARURA na walishaweka kwenye bajeti miaka miwili nyuma, ni lini sasa Serikali itakwenda kuweka lami kipande kile?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu barabara hii tayari imeshafanyiwa usanifu na tayari ipo kwenye bajeti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tutafuatilia kwa karibu hata baada ya kutoka kwenye maswali hapa tutakaa tutafuatilia kwa karibu ili tuhakikishe kwamba mwaka huu kwa sababu fedha tayari imeishatengwa ili iweze kujengwa barabara hii.