Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula (11 total)

MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Spika, kwanza niruhusu nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa fursa ambayo nimeipata kuja kuuliza swali hapa. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa imani yake kubwa kwa kuniamini, nimefanya kazi na nimetua kijiti kwa Mheshimiwa Silaa na niko tayari kutoa ushirikiano wakati wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina swali la nyongeza. Kwanza natambua kwamba Serikali imeweka katika bejeti yake kuongeza chanzo kingine cha maji katika Jiji la Mwanza, hususan Manispaa ya Ilemela kutokana na changamoto kubwa ya maji katika mji ule: Je, ni lini utekelezaji wa mradi huo wa chanzo kipya cha maji utaanza kutekelezwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Angeline Mabula Mbunge wa Ilemela kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nipende kumpongeza kwa sababu suala hili amesha lileta mara kadhaa katika ofisi zetu na niseme tu jitihada zako zimesababisha Mheshimiwa Waziri Jumaa Hamidu Aweso kukuletea Mkurugenzi wa mamlaka mpya mwanamama, mchapakazi. Jitihada zako zimesababisha kuileta task force ya wataalam kuona kwamba Mwanza sasa inaenda kupata suluhu.

Mheshimiwa Spika, chanzo hiki kipya Mheshimiwa Dkt. Angeline Mabula naomba nikupe amani kwamba kadri wataalam wetu watakapo kamilisha kazi waliyopewa na Mheshimiwa Waziri Jumaa Hamidu Aweso, chanzo hiki mara moja kinakwenda kufanyiwa kazi ndani ya mwaka huu wa fedha.
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Spika, ningependa kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, wamejenga barabara ya kilometa 2.5 ya breweries kwa kiwango cha lami kwa kilometa 1.7 na kimebaki kipande kidogo cha mita 750. Je, ni lini watakamilisha ujenzi huo kwa maana sasa ujenzi umesimama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, nitakaa na Mheshimiwa Mabula kuona ni namna gani ambavyo Serikali inaweza ikaliratibu hili na kukamilisha kipande hiki cha barabara ambacho kimesalia kwa kuwasiliana na Meneja wa TARURA, Mkoa wa Mwanza na Meneja wa TARURA, Wilaya ya Ilemela kuona ni kiasi gani kinahitajika ili kuweza kukamilisha ahadi hiyo.
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Spika, naomba kumuuliza Naibu Waziri, kwanza kwa kuwashukuru namna ambavyo wanatatua kero ya maji katika Jiji la Mwanza hususani Wilaya ya Ilemela. Wamekuja na mkakati wa matokeo ya muda mfupi, wameanza kusambaza sim tank katika maeneo yenye changamoto.

SPIKA: Swali Mheshimiwa, mmesimama Wabunge wengi.

MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Spika, swali langu ni kwamba walishafanya survey katika maeneo ambyo wanaweza kuchimba visima kwa ajili ya ku-save maji hapo;

Je, ni lini visima vitajengwa katika Kata ya Kayenze Mtaa wa Lutongo ambako tayari feasibility study imeshafanyika na maji yalipatikana?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Angeline Mabula kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli tumeshafanya survey na baadhi ya maeneo katika vijiji hivyo alivyovitaja tumepata maji. Katika eneo la kata aliyoitaja tumepata maji kidogo lakini maji hayo tutahakikisha tutayatumia kujenga vichotea maji vichache ili wananchi wale waweze kupata huduma ya maji.
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ninashukuru kwa kunipa fursa na mimi niulize swali la nyongeza. Kwanza, ninashukuru kwa huduma tuliyoipata miundombinu katika Ziwa Victoria. Wilaya ya Ilemela asilimia 87 ni eneo la maji, na wanawake na vijana wengi wanashughulika na mazao ya samaki hususani dagaa lakini miundombinu yao ya kukausha samaki si mizuri hasa kwa afya ya binadamu. Ni lini Wizara itasaidia kuweka miundombinu kwa ajili ya kukausha samaki kwa wafanyabiashara hao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimesema kwamba Serikali imeshaanza na katika Ziwa Victoria tumeshaanza kuwasaidia Wavuvi namna ya kuvua zile samaki lakini pia kuhifadhi samaki. Hili wazo la Mheshimiwa Mbunge tumelichukua tutakwenda kulifanyia kazi kuwasidia Wavuvi wakanda ya ziwa. (Makofi)
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa nami niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Manispaa ya Ilemela katika kuunga mkono uwekezaji ilitenga eneo la ekari 52 katika eneo la Nyamungoro, eneo lenye miundombinu yote; maji, barabara na liko kwenye main road ya kwenda Musoma kwa ajili ya kuweka industrial park na tayari andiko lilishafika katika Ofisi za Serikali; ni lini mradi huu utatekelezwa ili tuongeze ajira na kukuza TEHAMA kwa watu wa Mwanza na ukizingatia ni ukanda wa maziwa makuu ni hub katika eneo hilo? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, maendeleo ya Industrial Park tunafanya pamoja na Wizara ya Viwanda, ipo chini ya EPZA. Nalifahamu hili eneo na nilishafika na tayari lipo katika Taasisi yetu ya EPZA wakilifanyia kazi, linaenda kwenye bodi na baada ya hapo tutalitolea maelekezo maalum kwamba ni lini hasa ratiba itatoka ya utekelezaji. Naamini katika mpango na bajeti ambao tutawasilisha kwenye Mkutano ujao, tutaeleza mpango maalum kuhusu Industrial Park ya Manispaa ambayo Mheshimiwa Angeline Mabula ameieleza.
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kinipa fursa na mimi kuuliza swali la nyongeza. Naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Nyamhongolo katika Manispaa ya Ilemela walitoa eneo la square meter 6,339 kwa ajili ya kujenga miundombinu ya kituo cha polisi zikiwemo nyumba 12 pamoja na kituo chenyewe. Tayari nyumba sita zimekamilika na askari wapo, nyumba sita hazijakamilika na kituo kimefikia asilimia 75 kwa nguvu za wananchi.

Je, ni lini Serikali sasa itakamilisha miundombinu hiyo ili kituo hicho cha polisi kiweze kuanza kazi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mabula, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza kwa namna ambavyo anavyofuatilia kwa karibu na kuhakikisha kwamba ujenzi wa kituo kicho unakamilishwa. Kwa kweli kwa maendeleo makubwa yaliyofanyika katika Wilaya ya Ilemela, hasa kwa kuwa kituo hiki kiko karibu na Kituo Kikuu cha Mabasi cha Nyamhongolo; ni kipaumbele chetu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Jeshi la Polisi kukipa fedha ili kiweze kukamilika. ninamwahidi Mheshimiwa, tutafuatilia maelekezo tuliyoyatoa ili ujenzi wa kituo hicho ukamilishwe, ahsante.
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa na mimi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Barabara ya Airport – Nyanguge yenye urefu wa kilometa 46 imekuwa ikiingia katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa vipindi viwili mfululizo na mwaka huu Serikali ilitangaza kujenga kilometa 10.

Je. Ni lini ujenzi huo sasa utaana ili kurahisisha by pass ya kwenda Serengeti kutoka Mwanza? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, habari njema kwa Mheshimiwa Mbunge tender ilishatangazwa ya kilometa hizo 10 zilizokuwa zimehaidiwa. Nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge mara tutakapokuwa tumekamilisha kazi za tender ujenzi utaanza kwa sababu tunatambua pia ndiyo barabara ambayo itapunguza foleni. Ni kama by pass ya Mji wa Mwanza kuelekea Simiyu na Mara kupitia Barabara ya Airport.
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Nyanguge – Airport yenye urefu wa kilometa 46, Serikali ilipanga kuijenga kwa kilometa 10 na tayari mkandarasi alipatikana. Je, ni lini mkandarasi huyu atakabidhiwa site ili aanze kazi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tumetangaza na Mkandarasi amepatikana, lakini kutokana na ukubwa wa barabara imehamishiwa, badala ya kusimamiwa na mkoa sasa itasimamiwa na TANROADS, Makao Makuu. Kwa hiyo, ni suala linalosubiri kumkabidhi mkandarasi hiyo site ili aanze kazi ya ujenzi. Ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Spika, wananchi waishio katika Visiwa vya Besi na Tefu hawana maji safi na salama kwa maana ya maji ya bomba. Ni lini Serikali itawapelekea maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Angelina Mabula, Mbunge wa Ilemela, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kisiwa cha Base ni moja ya visiwa vidogo vidogo ambavyo viko katika Ziwa Victoria, lakini Ofisi ya Bonde la Ziwa Victoria walifanya tathmini na kugundua kwamba hakuna maji ardhini. Tunachokifanya kwa sasa kupitia Mamlaka ya Maji Mwanza, MWAWASA wanaenda kuanzisha mradi mdogo ili waweze kuchakata maji kutoka Ziwa Victoria kwenda katika kisiwa hicho ambacho zaidi kinakaliwa na wavuvi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kushirikiana na Serikali kuhakikisha katika mwaka huu wa fedha 2024 tutaanza mradi huo na hatimaye wananchi wa kisiwa hicho watapata maji. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali iliweka minara katika maeneo ya visiwa base ambako kulikuwa hakuna mawasiliano, sasa hivi mawasiliano wanapata, changamoto waliyonayo hawana zile voucher za kukwangua na si wote waliozoea kununua kwa kutumia simu. Ni lini voucher hizo zitapatikana ili mawasiliano yao yawe mazuri? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza kuhusu vocha za kukwangua, naomba niseme nimelipokea nitalifikisha kwa watoa huduma lakini kama Serikali tunaendelea kutaka kuboresha kuondokana na hizi hard copies na kuingia kwenye voucher moja kwa moja kupitia mtandao.
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu hili sasa naliuliza kwa mara ya tatu na Serikali inaahidi, lakini hakuna kinachofanyika. Naomba nimwulize Mheshimiwa Waziri kwamba, wananchi wamefanya kila juhudi kuweza kujenga boma na limefikia kwenye lintel, lakini tayari kuna maboma sita pale kwa ajili ya Askari: Je, ni lini watakamilisha kazi hii ili kituo kile kianze kufanya kazi na tayari kuna nyumba sita ambazo zina Askari, lakini wanakwenda mbali na kituo hakijaanza kutumika?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nawapongeza wananchi wa Jimbo la Ilemela kwa kazi kubwa walioifanya ya ujenzi wa maboma kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kazi ambayo wananchi walishaianza, Serikali inaunga mkono na nitapata fursa ya kukaa na Mheshimiwa Mbunge baada ya kipindi hicho niweze kuzungumza naye kuona namna bora ya kumalizia maboma haya ambayo tayari wananchi wameshayajenga.