Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Charles John Tizeba (6 total)

MHE. DKT. CHARLES J. TIZEBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sengerema hali haiko tofauti sana na Rufiji. Mahakama za Mwanzo tisa zilifungwa kwa sababu mbalimbali zaidi ya mwaka mmoja na nusu sasa. Je, upo utaratibu sasa katika Wizara yako unaoweza kuziwezesha Mahakama hizi kufunguliwa ili haki iweze kupatikana kirahisi kwa wananchi?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nina bahati kwamba, mwezi uliopita nilitembelea Jimbo la Sengerema na Buchosa. Kwa kweli hali ya miundombinu ya Mahakama hata mimi mwenyewe nimeona inahitaji kusaidiwa kwa jicho la pekee. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika Mpango wa Mahakama wa miaka mitano ambao ni mkubwa kupita mipango yote toka uhuru, hatuwezi kusahau kabisa miundombinu mibovu katika Jimbo la Buchosa na Sengerema hasa upande wa Mahakama za Mwanzo na Mahakama za Wilaya. Pia tutazingatia kwamba Wilaya ya Sengerema ina visiwa zaidi ya 28 kitu ambacho nilikiona ni kigumu sana kukiacha hivi hivi bila kuingilia kati kwa mpango maalum wa kuwasaidia.
MHE. DKT. CHARLES J. TIZEBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru pia kwa kuniona.
Suala la umeme katika vijiji vingi hapa nchini bado halijawekwa wazi kuhusiana na maeneo ya visiwa. Jimbo langu tu kwa mfano linavyo visiwa 25. Nisizungumzie Jimbo la Mheshimiwa Mwijage huko Gozba, Bumbire na maeneo mengine.
Sasa mimi ningependa tu Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini labda atuambie ni kwa namna gani Wizara au Serikali kwa ujumla imejipanga kufikisha umeme katika maeneo haya ambayo kimsingi si rahisi sana kufikisha umeme wa Gridi ya Taifa?
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli kwamba visiwa vyetu vinahitaji kupata umeme na cha kwanza vilivyopata umeme ni visiwa vya Zanzibar ambapo tumejenga cable chini ya bahari. Wao wana megawati 100 lakini mahitaji ya Zanzibar ni megawati 50, kwa hiyo wanayo 50 zaidi. Na Mheshimiwa Tizeba yeye mwenyewe anafahamu kisiwa cha kwanza kabisa katika Ziwa Victoria kupata umeme ni kisiwa chake ambacho kwa mara ya kwanza tumepitisha cable chini ya Ziwa Victoria, na tumemuomba Waziri Mkuu akazindue huo umeme kwa sababu ni wa kipekee kabisa. Na hivi sasa Kisiwa cha Ukara vilevile wamepatiwa umeme na ni mtu binafsi aliyewekeza umeme pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Wabunge wote ni kwamba hivi visiwa vingi vidogo vidogo hatutaweza kujenga cable kwa kila kisiwa, ila umeme watakaoupata ni umeme wa jua.
MHE. CHARLES J. TIZEBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona. Kwa kweli, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri ningependa tu kujua baada ya Halmashauri zetu kuleta haya maombi na ilikuwa katika matarajio yetu kwamba uharibifu huu usikutane na msimu mwingine wa mvua kwa sababu uharibifu utakuwa mkubwa zaidi na bajeti tuliyoipitisha inaweza ishindwe kukidhi hayo mahitaji. Sasa, labda ni lini tu Mheshimiwa Waziri watatuona kabla mvua hazijaanza tena hasa sisi tunaotoka kwenye maeneo ya misimu miwili ya mvua?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini naomba niseme kwamba hapa siwezi kusema kesho au keshokutwa, kwa sababu tunachofanya ni needs assessment. Tuna Halmashauri zipatazo 181, kila Halmashauri ina changamoto yake ya jinsi gani miundombinu ya barabara imeharibika. Kwa hiyo, wataalam wetu wanalifanyia assessment katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikopita maeneo mengine ni kweli huo uharibifu umekuwa wa kiwango kikubwa sana. Hivi sasa wananchi wengine wanashindwa hata kufika katika maeneo mbalimbali. Kwa hiyo, jukumu letu kubwa ni ku-fast truck hii process ili angalau kitakachopatikana kidogo tuweze kugawana ili wananchi waweze kupata huduma kwa kipindi hiki cha sasa.
MHE. DKT. CHARLES J. TIZEBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri yanakubaliana na ukweli kwamba viko vituo vingi vya afya vyenye vyumba vya upasuaji nchini lakini havifanyi kazi kwa sababu mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, Benjamin Mkapa Foundation wamejenga vituo vingi karibu 20 Mkoa wa Rukwa vyenye vyumba vya upasuaji na havifanyi kazi kwa sababu ya kukosa wataalam. Huko Buchosa kuna kituo cha Mwangika, planning international wamejenga hakina Wataalam wa usingizi. Sasa nimwombe tu Waziri, kwamba labda wanaweza kuchukua takwimu kutoka Halmashauri zote ili kabla ya Bunge hili kuahirishwa tujue ni vituo vingapi ambavyo vina theatres na bado hazifanyi kazi kwa sababu ya upungufu wa Wataalam hawa wa usingizi.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba ushauri wa Tizeba japokuwa tumeshakuwa na current data lakini tutazifanyia kazi bila shaka.
MHE.DKT. CHARLES J. TIZEBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwakunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Wavuvi katika Ziwa Victoria, moja ya mambo yanayowakwaza sana ni masoko ya uhakika ya mazao ya samaki. Sasa katika Jimbo la Buchosa tulikuwa na soko mojaambalo lilihudumia karibu wavuviwote wa Jimbo hilo na Wizara ililifunga kwa maelezo kwamba halikuwa linasimamiwa vizuri, lakini tuna uhakika, suala la usimamizi wa soko hilo ni jukumu la Serikali na kwa hiyo, ilipaswa yenyewe ndiyo iweke usimamizi mzuri ili wananchi waweze kuuza mazao yao. Sasa swali langu, ni lini tu Waziri atakwenda kufungua soko hili ili wananchi wasiendelee kuhangaika? Ahsantesana.
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nitakwenda mwezi huu, soko hilo tutalifungua.
MHE. DKT. CHARLES J. TIZEBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Huko katika Ziwa Victoria kutokana na mvua nyingi zinazonyesha msimu huu, magati mengi yamemezwa na maji katika hili pamoja na gati alilolisema Mheshimiwa Bukwimba lakini Gati la Kisiwani Maisome na Gati la kule Bugorora Ukerewe na yenyewe yamezama, wananchi wanaingia kwenye vivuko kwa kuvua nguo. Tunaomba Serikali itupe kauli kwamba itashughulikia vipi kwa haraka magati haya ili wananchi wasiendelee kupata aibu na usumbufu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimia Dkt. Charles Tizeba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tunatambua kwamba kutokana na mvua hizi zilizonyesha magati mengi yamepata changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoweza kupitika vizuri baada ya kuwa yamejaa maji. Tumeendelea kufanya utafiti wa kina kwa kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari. Tukumbuke tu kwamba magati mengi ambayo yapo nchini bado yanamilikiwa na Halmashauri.

Kwa hiyo lazima kuwepo vikao vingi vya kukubaliana namna ya kuyachukua magati yale na kuyaendesha, kwa sababu sheria ilikuwa haijapitishwa na kwa kuwa sasa sheria imepitishwa ni lazima sasa tunakwenda hatua kwa hatua kuhakikisha kwamba yale magati yote ambayo yako chini ya kiwango yaliyokuwa yanamilikiwa na Halmashauri sehemu mbalimbali nchini yanarekebishwa kwa kiwango ambacho kinakidhi standard za kuendeshwa na Mamlaka ya Bandari.

Kwa hiyo namwomba sana Mheshimiwa Dkt. Charles Tizeba atuvumilie kidogo, tunakwenda kufanya utafiti wa kina na kuyarekebisha magati yote nchi nzima yaweze kupitika kwa kiwango na yaweze kuhudumia wananchi.