Contributions by Hon. Mansoor Shanif Jamal (9 total)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MANSOOR S. HIRAN: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja ambayo ipo mbele yetu. Naomba nichukue nafasi hii kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Kwimba kwa kunichagua awamu ya pili na nawaahidi sitawaangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri wa Fedha na Mipango kwa bajeti nzuri ambayo ameileta ya trilioni 29 na nusu; ambapo amepanga asilimia 40 itatumika kwenye miradi ya maendeleo. Nampongeza sana kwa hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitachangia kwenye maeneo matatu. La kwanza, nitachangia kwenye mchango wa Msajili wa Hazina kwa bajeti kuu. Kwenye kitabu cha volume one, kwa bajeti ya mwaka wa kesho amepangiwa atachangia trilioni 1.3. Msajili wa Hazina anasimamia Mashirika ya Umma na Taasisi mbalimbali ambazo zina makusanyo ya zaidi ya trilioni 10 kwa mwaka. Sasa kama mashirika haya umma yanakusanya zaidi ya trilioni kumi kwa mwaka, kutoa mchango wa trilioni 1.3 ni kidogo sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningeshauri Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango aangalie upya hili suala jinsi ya kutoza na kukusanya fedha nyingi zaidi kutoka kwenye taasisi zilizo chini ya Msajili wa Hazina ili Msajili wa Hazina aweze kuchangia trilioni tatu au zaidi, kwenye mfuko wa bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwenye kitabu hiki cha Volume one tunacho hapa, ni kwamba bajeti ya mwaka huu wa 2015/2016, Airtel walichangia Shilingi bilioni moja lakini mwaka ujao Airtel hawatachangia chochote, sasa sijui ni makosa au kuna suala lingine, tunaomba Waziri aweze kutufafanulia hilo, kuna tatizo gani pale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine; Tanzania Breweries mwaka huu wa bajeti wamechangia bilioni 5.7, lakini mwaka ujao hawachangii chochote, sasa sijui TBL hawatachanga, labda kuna makosa hapa, tungeweza kuelewa kuna tatizo gani pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukifika kwenye suala la Mashirika ya Umma; naomba niseme Shirika moja la Umma la Tanzania Ports Authority. Kwenye taarifa ya Msajili wa Hazina anasema mwaka huu, Mamlaka ya Bandari Tanzania haijachangia chochote wakati taarifa ya Mamlaka ya Bandari iliyoko kwa Msajili inasema mwaka huu wamechangia bilioni 150. Huyo huyo Msajili anasema hawajachangia chochote, huku bandari inasema wamechangia bilioni 150. Sasa ni muhimu tupate ufafanuzi, kwamba hizo fedha zimechangiwa zimekwenda wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, mwaka huu huu tena Msajili wa Hazina amesema Mamlaka ya Bandari Tanzania haitachangia chochote.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme masuala machache kuhusu bandari. Bandari hii, Tanzania Port Authority wana bajeti yao ambayo ipo mbele yangu hapa waliyoipeleka kwa Mhazini wa Serikali. Wanaonesha mapato na matumizi, naomba ku-declare interest mimi ni mjumbe kwenye Kamati ya Miundombinu. Mamlaka hii ya Bandari, mwaka jana, 2014 walipeleka shilingi bilioni 105 wakawela kwenye fixed deposit bank, wanasema ni pesa za ziada wanazitunza pale, huku hawachangii chochote. Mwaka wa jana wamepeleka bilioni 99 zimekwenda kwenye fixed deposit zinatunzwa pale wanakula riba, jumla ya Mamlaka ya Bandari Tanzania ina jumla ya bilioni 440, ziko kwenye mabenki hawana kazi nazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa huku kwenye bajeti hizo fedha hazionekani, kwenye bajeti waliopeleka hawaoneshi kama kuna fedha ziko benki. Naomba Waziri wa Fedha afuatilie hili suala, kwamba huku hazionekani hizo fedha ziko wapi? Sasa hili ni Shirika moja nimelisema hapa, tuna Mashirika mengi sana, tunaomba CAG afanye kazi ya ziada, azikague tuangalie fedha ngapi ziko kwenye mabenki ambazo hazioneshwi kwenye ripoti. (Mkofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ningependa kulichangia hapa ni Deni la Taifa. Kila mwaka deni la Taifa linakua, lakini taarifa tuliyoipata kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa 16 ni paragraph moja tu.
Ningeomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha atupe taarifa ambayo ni pana, ya kina ili tujue kwamba fedha za madeni ambazo tunazitenga kila mwaka kwenye bajeti zinatumika vipi?
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka ujao tumetenga trilioni nane kwa ajili ya madeni, mwaka jana pia tulitenga matrilioni ya fedha. Ni muhimu tupate taarifa ya hizo trilioni za fedha ambazo tunazipanga kwenye bajeti zinatumika vipi kwenye kulipa madeni ya nje na ndani, kwa sababu makandarasi na wazabuni wengi sana wa ndani wanalalamika hawajapata fedha. Ni muhimu tujue fedha zinatumika vipi?
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Waziri, baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuanza kazi, ndani ya miezi mitano wamelipa wakandarasi wa barabara bilioni 698. Naomba walipe na wakandarasi wanaojenga miundombinu ya maji. Naomba maji pia yapewe kipaumbele, wapeleke fedha kwenye maji, wakandarasi wanalalamika sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Jimbo langu mradi mmoja wa maji umekaa unasubiri milioni 500, mabomba yamenunuliwa ya plastiki yapo juu yanasubiri kutandazwa chini, yanaoza yanapigwa jua lakini mkandarasi hajalipwa ili amalize huo mradi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la Deni la Taifa naomba Mheshimiwa Waziri atupe taarifa za kina zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ningependa kulisemea hapa ni Kituo cha Biashara na Huduma Kurasini. Mheshimiwa Serukamba asubuhi alilisemea vizuri, naomba niongeze machache tu. La kwanza huu mradi hauelekweki unakwenda kwendaje. Mwaka juzi mwaka 2014 wakati nilipokuwa mjumbe kwenye Kamati ya Bajeti tulienda kwenye ziara pale kwenye mradi tukaenda kuangalia pale Kurasini hatukuelewa. Tuliomba tupate taarifa ya mkataba ambao wamefunga na yule mbia lakini haujapatikana mpaka leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Waziri wa Viwanda na Biashara aliangalie hili suala kwa undani zaidi, kwa sababu sisi Tanzania hatutaki Mchina aje kufanya biashara hapa ya kuuza vitu kwenye maduka. Hiyo kazi tunaweza kuifanya sisi Kariakoo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hii miradi inaonekana kuna tatizo sisi tumeshawekeza bilioni 100 kwenye fidia, sasa huyo atakapokuja kuwekeza pale lazima sisi kama Serikali tuwe na share kwenye kampuni hiyo, hatuwezi kuwekeza halafu tukamwachia yeye akafanya peke yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili kwa taarifa niliyoipata 2014 wakasema wana mpango wa kuleta vifaa kutoka China na kuanza kuuza Afrika Mashariki na kati. Sasa wale watu wanataka kuanzisha shughuli kama ya Dubai. Unapokwenda Dubai unakutana na dragon mart Dubai pale watu wengi wanaifahamu. Wachina wanakaa sehemu moja wanauza vifaa vyao vyote pale, sasa lile suala sisi hapa Tanzania hatulitaki wale wakija hapa Kariakoo itafungwa na wakija hapa watatumaliza kabisa biashara itakuwa hovyo. Kwa hiyo, naomba hili suala liangaliwe upya. Kwanza huyu mwekezaji bado hajaleta chochote hapa kwa hiyo hatujachelewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine walisema wanataka kuwekeza kwenye viwanda. Ushauri wangu kama wanataka kuwekeza kwenye viwanda basi wawekeze kwenye viwanda ambavyo sisi hapa nchini hatuna, wasije wakatuwekea viwanda vya biskuti wakati tunavyo wenyewe viwanda vyetu. Waweke viwanda ambavyo sisi Tanzania tuna shida navyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MANSOOR S. HIRAN: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu. Kwanza kabisa, naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema ili niweze kusimama mbele yako.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia kuwashukuru wananchi wa Kwimba kwa kunipa ushirikiano mzuri ili niweze kutimiza wajibu wangu wa kuwatumikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri wa Fedha, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara ya Fedha kwa bajeti nzuri sana ambayo wamependekeza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu ya kusema bajeti hii ni nzuri ni kwa sababu mimi kwa mara ya kwanza kwenye historia ya bajeti yetu nimekutana na bajeti ambayo haijapandisha kodi kwenye mafuta ya dizeli na petroli. Ni busara nzuri sana ambayo Mheshimiwa Waziri ametumia kuhakikisha kwamba mafuta hayapandi bei. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema hivyo kwa sababu unapotaka kupata uchumi wa viwanda unatakiwa uhakikishe nishati ya mafuta ni bei nafuu. Nampongeza kwa hilo na kama tukienda hivi Mheshimiwa Waziri nina uhakika uchumi wa viwanda ataweza kuufikia vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwenye historia ya nchi yetu kwa mara ya kwanza mwaka huu tumekutana na riba za benki kushushwa. Riba za kukopa zimeshuka, hiyo ni mara ya kwanza imetokea kwenye historia. Pia ameweza kupambana na inflation ambayo iko tarakimu moja, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri ambayo anafanya yeye na Wizara yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze kwenye mchango wa bajeti iliyowasilishwa. Naomba nijielekeze kwenye hotuba ukurasa wa 46, paragraph ya kwanza. Naipongeza Wizara kwa kuleta mapendekezo ya kupunguza Corporate Tax kwenye viwanda vipya vya dawa za binadamu na ngozi. Nachoomba kwa Mheshimiwa Waziri asibague, viwanda vyote vinavyotengeneza dawa za binadamu na ngozi ambavyo vipo na ambavyo zitakuja vyote azipe incentive ya corporate tax asilimia 20. Atakapowabagua, wale wenye viwanda sasa hivi watashindwa kushindana na viwanda vipya ambavyo vitafika. Kwa hiyo, ni vizuri kuwe na Corporate Tax ambayo inafanana kwa wote. Pia nashauri Waziri asiishie kwenye dawa za binadamu, naomba pia viwanda vya dawa za mifugo na kilimo vihusishwe kwenye hili punguzo la Corporate Tax. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu nyingine nayopenda kuelekeza mchango wangu ni kwenye ukurasa wa 51, paragraph 12 ambayo inazungumzia Ushuru wa Bidhaa kwenye sigara zisizo na kichungi. Naomba ni-declare interest kuwa mimi ni mdau. Nimesoma hotuba vizuri, amesema kwamba sigara ambazo zinatengenezwa kwa tumbaku inayozalishwa hapa Tanzania kwa asilimia 75 na zaidi ambazo hazitumii kichungi atazichaji Excise Duty ya Sh.12,447 na zile nyingine ambazo zinatumia kichungi atazichaji Sh.29,425.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi sikuelewa sababu ya kuweka tofauti hiyo kwa sababu kwanza kabisa mtu anayevuta sigara ambayo haina kichungi anapata madhara makubwa zaidi kuliko yule anayevuta sigara ambayo ina kichungi. Kwa hiyo, mimi nashauri ingekuwa opposite; kwamba zile za Sh.12,000 angeziwekea Sh.29,000 ili watu wavute sigara ambayo ina kichungi kwa sababu ile ambayo haina kichungi maana yake anaivuta tumbaku moja kwa moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo ukienda sokoni sigara ambayo ina kichungi au haina kichungi zote zinauzwa kwa Sh.100 mpaka Sh.150 kwa sigara moja. Ukichukua hizi sigara ambazo hazina kichungi zinazotozwa Sh.12,447, sigara hiyo inatakiwa iuzwe kwa Sh.60 mpaka Sh.65 kwenye soko, lakini sasa hivi inauzwa kwa Sh.100 kwa sababu sisi hatuna coins za Sh.20 na Sh.30. Kwa hiyo, alichotaka Waziri ni kupunguza bei ya sigara ili mwananchi wa kawaida apate faida ya kupata sigara ya bei nafuu, hiyo faida haipo, anayefaidika ni mwenye kiwanda, mwananchi analipa ileile Sh.100. Kwa hiyo, kuna karibu Sh.40 ambayo inapotea kama kodi kwa sababu ya kutokuchaji hiyo bei. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Waziri aende kuangalia suala hili kwa undani zaidi. Asilimia 70 ya Watanzania wanavuta sigara bila kichungi. Ni vizuri ku-discourage suala hilo na ku-encourage watu waende kwenye ile yenye kichungi ili angalau madhara yapungue.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu nyingine ambayo napenda kupeleka mchango wangu ni ukurasa wa 52, paragraph 48 inayohusiana na stempu za kodi za kielektroniki. Mimi napongeza Wizara kwa maamuzi haya mazuri sana, naunga mkono maamuzi haya mia kwa mia. Shida yangu ni moja tu, ni gharama ya hiyo huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo gharama ya kununua stempu moja ya kuweka kwenye boksi la sigara unanunua kwa Sh.13. Naomba nirudie ili Mheshimiwa Waziri anisikie vizuri, leo gharama ya kununua stempu ya sigara kwenye boksi unalipa Sh.13, huyu SCIPA ambaye mmemteua kuwa ndiye atakayetoa huduma hii ataitoa kwa Sh.29.75, mara tatu ya bei ya sasa hivi ambayo tunalipa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mimi sielewi hiyo hesabu imefikaje mpaka mmekubaliana na hii Sh.29.75 wakati sasa hivi tunalipa Sh.13. Ningetegemea tungepata hiyo huduma kwa bei nafuu zaidi kwa sababu ni electronic tax stamps si tena karatasi, maana yake gharama zingepungua zaidi kuliko kupanda, ningetegemea ingekuwa Sh.10 au Sh.5. Kwa hiyo, ningependa hili suala mliangalie kwa undani zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwa hesabu ya haraka haraka, mwekezaji anawekeza shilingi bilioni 44, ana mkataba wa miaka mitano, kwenye taarifa ya Kamati ya Bajeti imesema kwamba kwa mwaka atakuwa anafanya biashara ya bilioni 66. Kwa hiyo, kwa miaka mitano mtu amewekeza bilioni 44 anachukua bilioni 330 kwa nchi yetu, kweli hesabu ya wapi ndugu zangu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri pia Ofisi ya Attorney General iangalie mkataba huu kwa sababu taarifa nilizonazo ni kwamba huu mkataba alishapata huyu bwana mwaka 2016 lakini ulikuwa na matatizo ndiyo maana ulikuwa umechelewa kutoka sasa hivi ndiyo umetoka. Kwa hiyo, naomba Serikali iangalie upya hili suala kwani ni zito.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabla sijamaliza nichukue nafasi hii pia kumpongeza Commissioner General wa TRA kwa kazi nzuri wanayofanya yeye na timu yake maana bila makusanyo tusingeongea mambo ya bajeti hapa. Kwa hiyo, naomba nichukue nafasi hii pia kuwapongeza TRA na Wizara ya Fedha kwa kazi nzuri ambazo wanafanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. MANSOOR S. HIRAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru umenipa nafasi na mimi nichangie hoja iliyo mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema niweze kusimama mbele yako kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Kwimba kuzungumza kuhusiana na suala la maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la maji naomba niseme mambo matatu. La kwanza, kuna Mradi wa Shirima; ulianza mwaka 2013, mwaka jana ulipofanya ziara kwenye Jimbo la Kwimba nilienda na wewe tulikupeleka mpaka kwenye mradi huo wa Shirima, Kata ya kukibizi, ulitoa ahadi kwamba mradi ule utakamilika ndani ya miezi mitatu. Mheshimiwa Waziri mradi bado haujakamilika, nashukuru mkandarasi huyo mkataba wake ulikuwa ume-expire, tarehe 28.03.2019 Serikali imekataa ku-extend mkataba huo na imekabidhi ule mradi kwa MWAUWASA ili waweze kuumalizia. Naomba Mheshimiwa Waziri uwaambie MWAUWASA waumalize mradi huo mapema sana kwa sababu wananchi wana shida sana ya maji kwenye Kata hii ya Kikubizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kulizungumzia ni kwamba kuna maombi ya mradi wa tenki la kutunza maji Ngudu. Wilaya ya Ngudu ni Makao Makuu ya Wilaya ya Kwimba lakini tuna matatizo ya maji, wakati KASHWASA wanapofanya matengenezo kwenye tenki ya Mhalo wananchi wa Ngudu wanakosa maji. Tumepeleka maombi Wizara ya Maji kupata tenki ya lita milioni tatu. Mheshimiwa Waziri maombi yako kwenye Wizara yako naomba utusaidie ili wananchi waweze kupata maji ya uhakika Wilayani Kwimba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine kuna mradi wa tenki ya Kizida. Tunaomba pesa kutoka Mfuko wa PBR na maombi yameenda siku nyingi yako Wizarani yanasubiri majibu. Tunaomba mradi huo ukamilike kwa sababu ukikamilika Vijiji vya Shikangama, Shilembo, Nguliku, Mwamakelemo, Ilula, Kibitilwa, Mwamapalala vyote vitapata maji. Naomba Mheshimiwa Waziri usikie kilio chetu cha maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba Wilaya ya Kwimba ni Wilaya ambayo tabianchi imetuathiri sana, hatuna ziwa wala mito ambayo ina maji ya kudumu tunatemegea visima…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. MANSOOR S. HIRAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. MANSOOR S. HIRAN: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kazi nzuri ambayo anafanya na wasaidizi wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kushukuru kwa kutuletea ambulance mpya kwa ajili ya Kituo cha Mwamashimba.
Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Kwimba ambayo iko Ngudu ina changamoto nyingi; hatuna mashine ya kufua nguo, x-ray ni ya zamani sana inaharibika mara kwa mara, ni analogue, tunaomba digital, duka la dawa la MSD, tunaomba watufungulie pale kwenye hospitali yetu ili wananchi wapate dawa kwa bei nafuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Daktari wa Macho walituletea lakini sehemu ya kufanyia kazi hakuna, hatuna chumba cha huduma ya macho, tuna jengo, lakini halijakamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri watoto wetu wanaokwenda shule za msingi na sekondari wengi wana magonjwa yafuatayo; pumu, sikosell, kisukari. Watoto wengi wanapata shida shuleni lakini Mwalimu hana uwezo wa kuwasaidia kwa sababu hatujawawezesha. Nashauri Mheshimiwa Waziri awapatie emergency kit kwenye shule zote za msingi na sekondari na Walimu wafundishwe jinsi ya kutoa first aid kwa mtoto ili wakati anapelekwa hospitali awe amepata huduma ya kwanza ili maisha yake yapone.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Hungumarwa unakua kwa kasi kubwa sana, tunaomba watujengee kituo cha afya kwani zahanati zinaelemewa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Nishati
MHE. MANSOOR S. HIRAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru umenipa nafasi hii ili na mimi nichangie hoja ambayo iko mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema nisimame mbele ya Bunge lako Tukufu kuwawakilisha wananchi wa Jimbo la Kwimba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa bajeti nzuri ambayo ameiwasilisha hapa Bungeni. Mimi nitajielekeza kwenye masuala ya REA III. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa mpango kabambe wa kupeleka umeme vijijini. Mheshimiwa Waziri, amezindua miradi mingi sana vijijini. Wilaya ya Kwimba tarehe 13 Julai, 2017 alizindua mradi wa umeme vijijini, jana ndiyo kijiji cha kwanza kimewasha umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu unasuasua sana, miezi nane kijiji kimoja ndiyo kimepata umeme. Tukifuatilia kwa mkandarasi anasema Serikali bado haijasaini mkataba wa kufungua LC, mara Hazina hajasaini mkataba. Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Mheshimiwa Waziri wa Fedha, tunawaomba mtusaidie, fedha za umeme za REA III ni ring- fenced tunaomba zifike kunakotakiwa ili miradi hii ya REA III isichelewe.
Mheshimiwa MWenyekiti, pamoja na hayo, wakati wa uzinduzi wa mradi huu tulifanya maboresho, kuna vijiji vingi na taasisi mbalimbali za Serikali na za kidini zilikuwa zimerukwa wakati wa REA II. Tulikaa na Mhandisi Msofe, mkandarasi na wawakilishi wa TANESCO tukaboresha hiyo orodha, Mheshimiwa Waziri naomba mtusaidie hiyo orodha iliyoboreshwa tupatiwe ili tuweze kuiwasilisha kwa wananchi wetu ambao wanasubiri umeme huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya mwaka huu ambayo inaendelea tuna shilingi bilioni 469, bajeti ya mwaka kesho ambayo tunataka kupitisha hapa tunapitisha shilingi bilioni 375, tunapunguza shilingi bilioni 94 kwenye bajeti ya Nishati. Mimi naomba Serikali isipunguze bajeti ya REA ibaki pale pale au iongezewe zaidi kwa sababu REA ndiyo mkombozi wa wananchi kwa maendeleo. Viwanda vitapatikana kama REA imefika vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine niende kwenye hotuba ukurasa namba 93 ambapo ameongelea kuhusu Single Receiving Terminal, naomba ni-declare interest mimi ni mdau, naelewa hili suala vizuri. Hotuba hii ni tofauti na uhalisia uliopo. Wiki mbili zilizopita, TPA waliita kikao ambacho wadau wote tuliitwa mara ya kwanza, tulikuwa tunasikia fununu kwamba suala hili linakuja lakini kiliitwa kikao wiki mbili zilizopita. Kwenye kikao hicho TIPER ndiyo walifanya presentation kwamba wao ndiyo wapo tayari kupokea mafuta ya Single Receiving Terminal, wakatoa changamoto zilizopo na maandalizi yanayofanyika, lakini kwenye hotuba Mheshimiwa Waziri amesema kwamba hiyo shughuli itafanywa na TPA (Tanzania Ports Authority). Sasa ningeomba ufafanuzi kwa Mheshimiwa Waziri kwa sababu hiyo ni tofauti na uhalisia uliopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ningependa kusema kwamba katika miaka hii miwili na nusu ya kazi ya Mheshimiwa Waziri nimeona ni Waziri mzuri sana lakini nguvu nyingi ameelekeza kwenye nishati ya umeme, kwenye mafuta amewaachia wasaidizi wamsaidie. Mimi ningeshauri Waziri akae na wadau ambao wanamchangia pesa kwa ajili ya kupeleka kwenye miradi ya REA. Ni muhimu kukaa na wadau, wadau wanaunga mkono hoja hii ya Single Receiving Terminal lakini wanasema kuna ukakasi kidogo jinsi mambo yanavyoenda huko kwani hayaendi sawasawa. Kwa hiyo, naomba na kushauri Waziri akae na wadau, awasikilize, asitume watu, suala hili ni zito sana ni suala la uchumi wa nchi, ni muhimu akae na wadau awasikilize, kuna mambo mengine labda haletewi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningeshauri hata Kamati ya Nishati na Madini ikae na wadau, iwasikilize. Wadau wako tayari kukaa na Kamati ili waeleze changamoto zilizopo na tunawezaje kutoka kwenye hizo changamoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo napenda kuliongelea kwenye suala hilo ni kwamba Mheshimiwa Waziri kasema tunaanza biashara hiyo ya Single Receiving Terminal kwa sababu tuna ubia na TIPER kwa asilimia 50. Mimi nakubaliana kwamba kuna ubia lakini ni vizuri sana kwa sababu kuna gharama ambazo zinahusika kwenye kutoa hiyo huduma, TIPER hawatoi huduma bure, kuna gharama kubwa sana ambazo zipo ambazo hajazitaja kwenye hotuba yake, mimi nitaziweka mezani hapa ili Waziri azielewe na awaulize hizo gharama kama zipo ni lazima zishindaniwe, lazima ieleweke wamefikia vipi hiyo gharama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mafuta yanayoingia ndani ya nchi leo asubuhi Mheshimiwa Waziri kasema kwa mwezi tunapokea karibu takriban milioni 450 ya mafuta. Kwa mwezi ukipokea milioni 450 ya mafuta kwa gharama waliyopanga kwenye kabrasha ya TIPER ambayo ninayo hapa wanasema watatoza dola 2.35 kwa siku 10. Kwa hiyo, haya mafuta yote yakipita kwa TIPER takriban utakuwa unalipa kwa mwezi bilioni mbili na milioni mia nane na lazima ulipe ili mafuta yapite pale na hiyo ni kwa siku 10. Mafuta hayo yakikaa zaidi ya siku 10, kuna mkataba ambao Serikali haijahusishwa ambao unaingiza sasa gharama inakuwa shilingi 30 kwa lita moja. Kwa hiyo, ukisema ndani ya milioni 450, kama nusu ya mafuta hayo yamebaki pale kwa siku 11 au 12, utakuwa unalipa karibu bilioni saba zingine kwa mwezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachoomba kwa Mheshimiwa Waziri, huyo mbia wake ni mfanyabiashara, anafanya biashara ya mafuta, ana-supply mafuta kwenye tender, sasa anapewa nafasi ya kusimamia mafuta katikati na kuingiza ndani ya nchi na kusambaza pia anapewa kazi hiyo yeye na huku chini pia tunashindana naye kwenye biashara. Mheshimwa Waziri, huyo mtu utashindana naye vipi kwenye biashara? Wengine wote sisi tutashindwa kufanya biashara hiyo kwa sababu huyo mtu mmoja ana-advantage ya kushinda kwenye tenda, anasimamia katikati pale na huku chini pia yumo, unampa undue advantage. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri ashirikishe hata Fair Competition Commission ili waangalie kama utaratibu huu unaendana na sheria zetu. Ningeshauri pia Attorney General atusaidie suala hili na aliangalie kwa undani zaidi. Mheshimiwa Waziri ana sifa nzuri sana kwa kazi anazofanya lakini hii inatukumbusha mwaka 2005 wakati nchi ilikuwa ina giza, Serikali ikaagiza kwamba tunataka tupate umeme kwa haraka sana, Wizara ya Nishati ikaenda, ikaleta kampuni ya mfukoni inaitwa Richmond, wakaingia mikataba mibovu, imetugharimu mpaka leo, tunarudi huko tulikotoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkataba huu haueleweki umepita vipi kwa sababu wakati wamefanya presentation tukasema tunaomba kujua makubaliano kati ya Serikali na TIPER, hakuna makubaliano. Tukaomba makubaliano kati ya TPA na TIPER, hakuna makubaliano. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, ningeomba hili suala aliangalie kwa ndani sana, nampenda sana na pia Serikali ya Awamu ya Tano haipendi kabisa ihusishwe na mambo ya ufisadi, rushwa na mambo ya hovyo hovyo. Kwa hiyo, ningeshauri Mheshimiwa Waziri, aliangalie hili suala kwa ndani, tusimharibie Rais wetu sifa zake nzuri ambazo anazo za kupambana na ufisadi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nalopenda kulisema hapa, kwenye hotuba Mheshimiwa Waziri amezungumzia ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta safi, kwenye ukurasa wa 87. Naomba ni-declare interest, mwaka 2014, Wizara ya Nishati na Madini mliletewa andiko, mwekezaji kampuni ya Kitanzania, Petroleum Logistics Tanzania Limited akasema atajenga bomba kutoka Dar es Salaam mpaka Zambia, gharama iliwekwa pale, akafanya presentation, Wizara ikamuita Katibu Mkuu kutoka Zambia akafika hapa, mwekezaji akafanya presentation mbele ya Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Maji ya Zambia na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati alikuwepo, wataalam walikuwepo na taasisi mbalimbali zilikuwepo. Wamechukua huo mradi, wameugeuza kuwa mradi wa Serikali, sasa wanasema Serikali inaanza mchakato wa kutengeneza mradi. Hiyo kampuni ya Kitanzania, haikuomba mkopo wa Serikali wala haikuomba guarantee yoyote ilisema itafanya kwa gharama zake. Naomba Mheshimiwa Waziri aliangalie hilo pia anasema anaanza mchakato wakati mchakato uko tayari kwenye ofisi zake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MANSOOR S. HIRAN: Mheshimiwa Spika, nakushukuru umenipa nafasi na mimi nisimame leo Bungeni hapa nizungumze. Kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kunipa afya niweze kusimama kwenye Bunge hili Tukufu kuzungumza kuhusu hoja ambayo iko mbele yetu.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri ya bajeti aliyowasilisha leo asubuhi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kabla sijaanza kutoa mchango wangu, naomba nipongeze Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri sana ambayo inaifanya. Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu imesema mambo mengi sana, naomba nipongeze mambo machache. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, naomba nipongeze Serikali kwa maamuzi ya kujenga reli ya kisasa ambayo ni ya historia, kwa Afrika nzima itakuwa ni reli ya kwanza ambayo inatumia umeme. Pili, ni Surrender Bridge ambalo ni kero kubwa kwa wananchi kwa sababu ya msongamano wa magari. Kwa kweli hilo daraja pia litapunguza msongamano wa magari. Mambo mengi sana yamefanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, tuna mradi wa Stigler’s Gorge na sera ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala ambalo nitalichangia hapa ni ajira. Nchi yetu tuna changamoto kubwa sana ya ajira. Jimboni kwangu hata nchi nzima tuna changamoto ya ajira ni za aina mbili. Jimboni kwangu Wilaya ya Kwimba changamoto ya ajira ni kwanza ya wale vijana wanaomaliza form four ambao wanashindwa kuendelea na masomo kwa sababu hakufaulu kwenye mtihani wake au hana uwezo wa kuendelea na masomo. Changamoto nyingine ni wale ambao wamepata digrii, wamesoma mpaka chuo lakini hawana ajira. Kwa hiyo, kuna aina mbili ya vijana ambao hawana ajira.
Mheshimiwa Spika, changamoto ya ajira ni kubwa sana, natambua Serikali ina mipango mingi kupunguza kero ya ajira lakini kero ya ajira Jimbo la Kwimba ni kubwa sana. Mara nyingi utaona ajira zinatangazwa kwenye Mikoa na Miji mikubwa, vijana wa Jimbo la Kwimba hawana uwezo wa kufuta ajira hizo kwenye Miji mikubwa wanabaki pale pale, wanadumaa hawana pa kwenda.
Mheshimiwa Spika, nashauri Serikali ingefanya utaratibu wa kuwa na mpango mkakati wa kusaidia vijana vijijini ambao hawana uwezo wa kwenda mijini kutafuta ajira. Tuwe na mpango mkakati ambapo kuna mambo mawili, nashauri Serikali itusaidie Jimbo la Kwimba. La kwanza, tuna maombi ya miaka mingi sana tujengewe Chuo cha VETA. Vijana wengi ambao wanafeli masomo na kurudi nyumbani hawana pa kwenda kusoma wangeenda kwenye Chuo cha VETA, wangepata ufundi na wangejiongezea ujuzi wakajiajiri wenyewe wakasaidia familia zao. Hiyo ni kero kwa wananchi wa Jimbo la Kwimba ya miaka mingi sana. Eneo lipo, tunaomba Serikali itufikirie itujengee VETA itapunguza kero ya ajira kwenye Wilaya ya Kwimba.
Mheshimiwa Spika, pili, tuna utaratibu wa kutoa asilimia 10 kutoka Halmashauri kwa ajili ya vijana, akina mama na walemavu hizo fedha hazitoshi hasa kwa sisi Wilaya Kwimba kwa sababu mapato ya Halmashauri yetu si kubwa sana. Ukiangalia Mkoa wa Dar es Salaam wana mapato ya shilingi bilioni ya 12 kwa vikundi vya akina mama, vijana na walemavu, sisi Wilaya ya Kwimba hatufiki hata shilingi milioni
300. Ukiangalia ukubwa wa Wilaya ya Kwimba ambayo ina majimbo mawili vijana ni wengi sana wanatafuta mitaji lakini mitaji ambayo inatoka Halmashauri haitoshi.
Mheshimiwa Spika, naomba Serikali itafute mikakati mingine ya kutafuta mitaji ya kusaidia vijana ambao wako vijijini kupata mikopo ili waweze kufanya biashara. Kusubiri fedha za Halmashauri ni ndogo sana, hazitoshelezi mahitaji ya wananchi au vijana wa Jimbo la Kwimba.
Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo napenda kulizungumzia ni changamoto ya maji. Jimbo la Kwimba tuna matatizo mengi sana ya maji. Mheshimiwa Waziri Mkuu mwaka jana alifanya ziara kwenye Jimbo la Kwimba, aliagiza Serikali ya Wilaya na Mkoa kwamba kuna Mradi wa Maji wa Kijiji cha Shilima ambao unategemea kupeleka maji kwenye vijiji takribani 14, kata takribani tatu kwamba ukamilike ndani ya miezi mitatu lakini mpaka sasa maagizo ya Mheshimiwa Waziri bado hayajatekelezwa. Kwa unyenyekevu mkubwa Watendaji wananisikia, maagizo ya Waziri Mkuu hayajatekelezwa, naomba angalau wafuatilie ili yatekelezwe.
Mheshimiwa Spika, kwenye masuala ya afya, nashukuru Serikali kwenye Kituo chetu cha Afya cha Mwambashimba tumeletewa shilingi milioni 400, tumeongeza majengo matano, sasa hivi tutakuwa na Ultrasound na majengo ya mama na watoto. Naomba nichukue nafasi kuishukuru sana Serikali kwa mradi huu wa kuboresha kituo cha afya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho naomba Serikali kwenye Wilaya ya Kwimba, Makao Makuu yetu ambayo ni Ngudu tuna Hospitali yetu ya Wilaya ambayo ilianzishwa kama Kituo cha Afya lakini tunakitumia kama Hospitali ya Wilaya tuna changamoto ya X-ray. Tuna X-ray ambayo ni ya zamani sana ambayo inatumia gharama kubwa sana na kila mara inaharibika na ni analog, tunaomba tupate X-ray ya kisasa ili tuweze kutoa huduma nzuri kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Spika, pia Hospitali yetu hiyo ya Wilaya hata mashine ya kufua nguo haina, tuna watumishi wanafua mashuka kwa kutumia mikono. Sasa kwenye Hospitali ya Wilaya mnaosha shuka kwa kutumia mikono kwa kweli sidhani kama inaweza kuwa ni salama.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. MANSOOR S. HIRAN: Mheshimiwa Mheshimiwa, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami nichangie hoja ambayo iko mbele yetu. Kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa pumzi nami nipate nafasi ya kusimama hapa na kuzungumza ndani ya Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara ya Afya kwa kazi nzuri ambayo wanafanya. Naomba kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kutupatia ambulace ambayo ilikuwa ni shida kubwa kwenye Kituo chetu cha Afya cha Mwamashimba. Ilikuwa ni ahadi yangu wakati wa kampeni na nashukuru sana amenisaidia ambulance mpya, ambayo nimetimiza ahadi ya wananchi wangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Kwimba Makao Makuu yetu ni Wilaya ya Ngudu Mjini. Ngudu Mjini tuna Kituo cha Afya ambacho tunakitumia kama Hospitali ya Wilaya. Kituo cha Afya hiki kina changamoto nyingi. Naomba niseme baadhi ya changamoto ambazo tunazo. Kwanza, hatuna mashine ya kufua nguo. Hospitali ile ni kubwa, inatoa huduma kwa wagonjwa wengi, kuna magonjwa ya kuambukiza, unakuta shuka zile zote zinaoshwa na binadamu ambaye anaweza akapata magonjwa, anapata shida sana kuosha hizo shuka. Kwa hiyo, namwoamba sana Mheshimiwa Waziri mashine ya kufulia nguo ili Hospitali yetu iweze kutoa huduma inayostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine tuliyonayo ni kwamba kuna extra machine ambayo ni analogy, tuliletewa zaidi ya miaka 15, tuna X-Ray machine ya zamani sana ambayo kwa kweli inaharibika mara kwa mara. Tunaomba sana tuletewe X-Ray machine ya digital kwa sababu huduma ya X-Ray machine ni kubwa sana kwa sababu ile ina Majimbo mawili, tuna changamoto ya wagonjwa wengi sana na X-Ray inapatikana pale Wilaya ya Ngudu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ningependa kusema tatizo tulilonalo kwenye Hospitali yetu ya Wilaya ni kwamba tuliletewa Daktari wa macho, miaka miwili yuko pale, lakini hana vifaa vya kufanya kazi, hana chumba cha kufanyia kazi. Kwa hiyo, amekaa pale, anaangalia, anatoa huduma pale huku amekaa nje. Naiomba Wizara itutengenezee chumba, itupe vifaa ili huyo Daktari atoe huduma ya macho kwa wananchi wa Wilaya ya Kwimba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine tunaomba tupate pharmacy ya duka la MSD la dawa. Dawa ni shida, zinapatikana mitaani kwa bei kubwa sana, naomba MSD wafungue duka la dawa kwenye Hospitali yetu ya Wilaya angalau wananchi wapate huduma ya kununua dawa kwa bei nafuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ningependa kusema ni kwamba sisi mji wetu wa Hungumarwa unakuwa kwa kasi kubwa sana, tuna Zahanati pale ambayo inatoa huduma sawa na Kituo cha Afya. Tunaomba sana tujengewe Kituo cha Afya kwenye Kata yetu ya Hongumarwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine napenda kusema ambacho kinanipa shida sana, Mheshimiwa Waziri anisikie kwa usikivu kidogo ni kwamba watoto wetu shuleni wanapata shida. Wengi wanapoteza maisha yao kwa sababu wanaugua. Kuna magongwa matatu ambayo watoto wanapata mara kwa mara; ugonwa wa pumu, Sickle cell na Kisukari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwa Wizara, tungeweza kupata First Aid Kit ambazo tungezipeleka kwenye shule zetu zote za msingi na sekondari na pia walimu tukawafundisha ili waweze kutoa First Aid. Mara nyingi tunakuta unapoteza watoto kwa sababu shuleni wanapougua mwalimu anachofanya ni kumpeleka mtoto nyumbani badala ya kumpa First Aid na kumpeleka Hospitalini, anampeleka nyumbani unakuta mtoto anapoteza maisha yake, kitu ambacho tungeweza kuepusha, mtoto akapata First Aid shuleni ili akifika hospitalini anakuwa ameshapata First Aid.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina mengi ya kusema, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusiana na Umiliki wa Maliasili wa Mwaka 2017.
MHE. MANSOOR S. HIRAN: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru umenipa nafasi ili na mimi nichangie hoja hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa busara na ujasiri wake wa kuleta Muswada huu wa Marekebisho ya Masharti Hasi yanayohusu maliasili ya nchi. Naomba pia nimuombee Mwenyezi Mungu ampe afya njema na maisha marefu Rais wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina mambo mengi lakini muda hautoshi lakini naomba nishauri mambo yafuatayo kwa Serikali yangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, hapa tunajadili masuala ya wawekezaji, sisi tuna wawekezaji wa aina mbili kwenye Miswada hii tunayoijadili. Kuna wawekezaji wa zamani ambao tuna mikataba mibovu na tuna wawekezaji wapya. Mimi ningependa kushauri kwa Serikali yetu kwamba wale ambao wana mikataba mibovu wana zaidi ya miaka 20, walipofika kuwekeza ndani ya nchi yetu walikuja na business plan yao ambayo ilikuwa inasema ndani ya miaka mingapi watakuwa wamesharudisha faida yao. Sasa hivi kwa taarifa nilizonazo wale wote tena sio wawekezaji, wameshapata faida zao maradufu sasa hivi wale watu ni waendeshaji tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachotakiwa kufanyika sasa hivi ni Serikali ichukue migodi yote ambayo ina zaidi ya miaka 20 kwa sababu business plan zao zimesha-expire na wameshapata faida zao, sasa hivi wale watakuwa ni waendeshaji tu. Serikali tunatakiwa tuwe na asilimia zaidi ya 75 kwenye hiyo migodi ambayo ina zaidi ya miaka 20. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri mwingine ni kwamba migodi mipya tusiwe chini ya asilimia 50 na zaidi. Nakubaliana na Mheshimiwa Zitto aliyosema kwamba wale wawe waendeshaji tu, wasijekuwa ndiyo wawekezaji, wawe waendeshaji wa migodi ambayo inaendelea ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuishauri Serikali Serikali yangu kwamba tuna misamaha ya Kodi ya Forodha na VAT kwa wawekezaji. Naomba hilo suala nalo lifutwe kusiwe na misamaha yoyote. Misamaha yote iende kwenye Kodi ya Mapato, misamaha ya Kodi ya Forodha ifutwe, sisi tunataka fedha za kuendesha bajeti yetu, hatuwezi kusubiri mpaka mwekezaji apate faida ndiyo sisi tuanze kupata fedha. Tunataka fedha siku ya kwanza akija atupe fedha ili sisi tutoe huduma za jamii za maji, barabara na afya kwa wananchi wetu, kwa hiyo, hakuna misamaha. Tufute misamaha yote hata kwenye mafuta tufute misamaha yote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri amesema kwamba watafungua akaunti yao ya biashara hapa nchini. Sio akaunti tu, napenda pia madini yanayotoka hapa yasipelekwe kwenye maeneo yao,
yauzwe kutoka Tanzania. Madini ya Tanzania mpaka leo hayatoki the invoice, yanatoka madini peke yake. Ningeshauri dhahabu itoke na invoice iende kwa mnunuaji tujue kodi ya mapato tunayopoteza. Sasa hivi madini yote yanatoka hapa yanaenda Afrika Kusini huko ndiyo wanakouza tunapoteza mapato mengi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa madini yetu yatoke na invoice na ningeshauri pesa zote zile zirudi ndani ya nchi yetu, kama Mheshimiwa Waziri amesema kwamba wafungue akaunti. Mimi ningependa isiwe akaunti ya kuongeza earnings pia akaunti ya kulipa madeni yote ya mgodi yalipwe kutoka Tanzania. Wakifanya manunuzi wanunue kutoka Tanzania. Mimi ningependa hilo lifanyike. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine la mwisho ambalo napenda kushauri kwa Serikali, tumesema by laws zitatengenezwa na Waziri. Mimi napenda tusimuachie Waziri peke yake mwenye dhamana kwa kazi hiyo, baada ya by laws kutengenezwa na Mheshimiwa Waziri ningeshauri hizo by laws zipitishwe katika cabinet au na Bunge ili tusirudi huko tunakotoka leo. Tusimuachie Waziri akatengeneza by laws peke yake lazima tushirikishe cabinet au Bunge kuhakikisha kwamba ziko sawasawa otherwise tutakuwa tunarudi palepale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za Nchi wa Mwaka 2017.
MHE. MANSOOR S. HIRAN: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru umenipa nafasi ili na mimi nichangie hoja hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa busara na ujasiri wake wa kuleta Muswada huu wa Marekebisho ya Masharti Hasi yanayohusu maliasili ya nchi. Naomba pia nimuombee Mwenyezi Mungu ampe afya njema na maisha marefu Rais wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina mambo mengi lakini muda hautoshi lakini naomba nishauri mambo yafuatayo kwa Serikali yangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, hapa tunajadili masuala ya wawekezaji, sisi tuna wawekezaji wa aina mbili kwenye Miswada hii tunayoijadili. Kuna wawekezaji wa zamani ambao tuna mikataba mibovu na tuna wawekezaji wapya. Mimi ningependa kushauri kwa Serikali yetu kwamba wale ambao wana mikataba mibovu wana zaidi ya miaka 20, walipofika kuwekeza ndani ya nchi yetu walikuja na business plan yao ambayo ilikuwa inasema ndani ya miaka mingapi watakuwa wamesharudisha faida yao. Sasa hivi kwa taarifa nilizonazo wale wote tena sio wawekezaji, wameshapata faida zao maradufu sasa hivi wale watu ni waendeshaji tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachotakiwa kufanyika sasa hivi ni Serikali ichukue migodi yote ambayo ina zaidi ya miaka 20 kwa sababu business plan zao zimesha-expire na wameshapata faida zao, sasa hivi wale watakuwa ni waendeshaji tu. Serikali tunatakiwa tuwe na asilimia zaidi ya 75 kwenye hiyo migodi ambayo ina zaidi ya miaka 20. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri mwingine ni kwamba migodi mipya tusiwe chini ya asilimia 50 na zaidi. Nakubaliana na Mheshimiwa Zitto aliyosema kwamba wale wawe waendeshaji tu, wasijekuwa ndiyo wawekezaji, wawe waendeshaji wa migodi ambayo inaendelea ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuishauri Serikali Serikali yangu kwamba tuna misamaha ya Kodi ya Forodha na VAT kwa wawekezaji. Naomba hilo suala nalo lifutwe kusiwe na misamaha yoyote. Misamaha yote iende kwenye Kodi ya Mapato, misamaha ya Kodi ya Forodha ifutwe, sisi tunataka fedha za kuendesha bajeti yetu, hatuwezi kusubiri mpaka mwekezaji apate faida ndiyo sisi tuanze kupata fedha. Tunataka fedha siku ya kwanza akija atupe fedha ili sisi tutoe huduma za jamii za maji, barabara na afya kwa wananchi wetu, kwa hiyo, hakuna misamaha. Tufute misamaha yote hata kwenye mafuta tufute misamaha yote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri amesema kwamba watafungua akaunti yao ya biashara hapa nchini. Sio akaunti tu, napenda pia madini yanayotoka hapa yasipelekwe kwenye maeneo yao,
yauzwe kutoka Tanzania. Madini ya Tanzania mpaka leo hayatoki the invoice, yanatoka madini peke yake. Ningeshauri dhahabu itoke na invoice iende kwa mnunuaji tujue kodi ya mapato tunayopoteza. Sasa hivi madini yote yanatoka hapa yanaenda Afrika Kusini huko ndiyo wanakouza tunapoteza mapato mengi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa madini yetu yatoke na invoice na ningeshauri pesa zote zile zirudi ndani ya nchi yetu, kama Mheshimiwa Waziri amesema kwamba wafungue akaunti. Mimi ningependa isiwe akaunti ya kuongeza earnings pia akaunti ya kulipa madeni yote ya mgodi yalipwe kutoka Tanzania. Wakifanya manunuzi wanunue kutoka Tanzania. Mimi ningependa hilo lifanyike. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine la mwisho ambalo napenda kushauri kwa Serikali, tumesema by laws zitatengenezwa na Waziri. Mimi napenda tusimuachie Waziri peke yake mwenye dhamana kwa kazi hiyo, baada ya by laws kutengenezwa na Mheshimiwa Waziri ningeshauri hizo by laws zipitishwe katika cabinet au na Bunge ili tusirudi huko tunakotoka leo. Tusimuachie Waziri akatengeneza by laws peke yake lazima tushirikishe cabinet au Bunge kuhakikisha kwamba ziko sawasawa otherwise tutakuwa tunarudi palepale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja.