Primary Questions from Hon. Esther Lukago Midimu (22 total)
MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza:-
Wilaya ya Itilima ni moja kati ya Wilaya mpya zilizoanzishwa hivi karibuni ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi:-
Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kuwezesha kujenga ofisi na nyumba za watumishi katika Makao Makuu ya Wilaya ya Itilima eneo la Itilima?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORAalijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa ujenzi wa nyumba za watumishi na viongozi katika Wilaya mpya ya Itilima umeshaanza na uko katika hatua ya ujenzi wa nguzo za jamvi. Fedha zilizopokelewa kwa kazi hiyo ni shilingi milioni 100 kati ya shilingi 500 zilizotengwa mwaka 2014/2015. Katika bajeti ya mwaka 2016/2017 zimetengwa tena shilingi milioni 500 ili kuendelea na ujenzi wa nyumba na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Itilima imesaini Mkataba na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa ajili ya ujenzi wa nyumba saba za watumishi kwa gharama ya shilingi milioni 450 na fedha hizo zipo. Kati ya fedha hizo, shilingi milioni 47 zimetumika kuwalipia fidia wananchi waliohamishwa kupisha ujenzi huo. Vilevile katika bajeti ya mwaka 2016/2017 zimetengwa shilingi milioni 500 ili kuendelea na ujenzi wa nyumba na ofisi ya Halmashauri.
MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza:-
Vijana wengi wa Mkoa wa Simiyu hawana ajira kutokana na ukosefu wa viwanda mkoani humo na Serikali ilitunga Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda vya kusindika mwaka 1996-2020 itakayosimamia maendeleo ya kusindika mazao ya kilimo ili kuongeza thamani ya mazao:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga viwanda vya kusindika mazao katika Mkoa wa Simiyu?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya vipaumbele vya Serikali hadi mwaka 2020 ni kuhimiza wawekezaji kujenga viwanda vinavyotumia malighafi za ndani hususan kwenye Sekta ya Kilimo na Maliasili, viwanda vinavyozingatia fursa za kijiografia, viwanda vinavyotoa ajira kwa wingi na vile vinavyochochea ujenzi wa viwanda vingine. Kwa sasa Serikali inaendelea kuhamasisha uwekezaji katika maeneo hayo. Aidha, Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi ili kuvutia sekta binafsi kuwekeza katika ujenzi wa viwanda kwa kuzingatia vipaumbele tajwa ikiwa ni pamoja na maeneo ambayo malighafi ya kutosha inapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maelezo hayo napenda kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kuwa, tushirikiane kubaini fursa za uwekezaji katika viwanda, tuhamasishe wawekezaji na tuweke mazingira mazuri kwa wawekezaji popote nchini ikiwemo Mkoani Simiyu. Uwekezaji tunaoulenga hasa ngazi za vijiji mpaka wilayani ni ujenzi wa viwanda vidogo sana, viwanda vidogo na viwanda vya kati. Hili ndilo tabaka la viwanda linalotoa ajira kwa wingi, lakini tabaka linaloweza kusambaa kwa urahisi toka mijini mpaka vijijini. Mafanikio ya jukumu hili yanahitaji ushirikiano mkubwa kuanzia ngazi ya vijiji mpaka mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu kupitia Kurugenzi ya Viwanda na Biashara ndogo pamoja na Taasisi za SIDO, TANTRADE, TBS na EPZA tuko tayari kushirikiana na mamlaka za Mkoa wa Simiyu ili kuhamasisha na kuwezesha ujenzi wa viwanda watakavyobaini na vile vilivyoahidiwa na viongozi wakuu wa Taifa hili.
MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza:-
Wanawake katika Mkoa wa Simiyu wamehamasika sana kujiunga kwenye vikundi ili kukusanya nguvu za kiuchumi kwa lengo la kujiendeleza kiuchumi zaidi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia wanawake hawa mafunzo ya kimtaji ili waweze kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa ufanisi zaidi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikiwawezesha kiuchumi wanawake kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake ambao kila Halmashauri inatakiwa kutenga asilimia tano ya mapato yake ya ndani. Katika mwaka wa fedha 2015/2016, Mkoa wa Simiyu ulitoa mikopo kwa wanawake na vijana yenye thamani ya shilingi milioni 116.5 ambapo kati ya hizo wanawake walikopeshwa shilingi milioni 75.7 kwa vikundi vipatavyo 74. Kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Mkoa wa Simiyu umetenga shilingi milioni 978.08 kwa ajili ya vijana na wanawake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri zote zimeelekezwa kulipa madeni ya fedha ambazo hazikupelekwa kwenye Mifuko ya Vijana na Wanawake kwa mwaka wa fedha 2015/2016. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kushirikiana na Hazina iliweka kigezo kwa kila Halmashauri kuonesha fedha zilizotengwa kwa ajili ya vijana na wanawake kabla ya kupitisha bajeti yake na Halmashauri zote zimetenga fedha hizo jumla ya shilingi bilioni 56.8.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mafunzo, Halmashauri kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii zimeendelea kutoa elimu ya masuala ya biashara na ujasiriamali kwa vikundi vya wanawake na vijana kabla na baada ya kupata mikopo ili kuhakikisha kwamba mikopo inayotolewa inatumika na kusimamiwa ipasavyo. Katika utekelezaji wa jukumu hili, Serikali inashirikiana na sekta binafsi zikiwemo asasi za kiraia.
MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza:-
Wilaya ya Maswa ni moja ya Wilaya kongwe hapa nchini, lakini haina kituo cha Polisi cha Wilaya:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kituo cha Polisi cha Wilaya.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayo Wilaya 162 na kati ya hizo tumefanikiwa kujenga vituo vya Polisi katika Wilaya 97. Serikali ina mpango wa kujenga vituo vya Polisi katika Wilaya 65 zilizosalia kutegemeana na upatikanaji wa fedha. Hata hivyo, tumepata jengo ambalo litafanywa kuwa kituo cha Polisi cha Wilaya wakati tukisubiri utekelezaji wa mpango wa ujenzi wa vituo vya Polisi nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Mbunge avute subira hadi hapo hali ya fedha itakapokuwa nzuri tutakamilisha ujenzi wa vituo vya Polisi katika Wilaya zilizosalia Maswa ikiwa miongoni mwao.
MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza:-
Kumekuwa na tatizo kubwa sana la ukosefu wa maji safi na salama katika Mkoa wa Simiyu pamoja na Wilaya zake ambao ni Bariadi, Itilima, Busega, Maswa na Meatu:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia maji wananchi wa Mkoa wa Simiyu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshaanza utekelezaji wa mradi wa majisafi kutoka Ziwa Victoria katika Mkoa wa Simiyu kwa miji mikuu ya Wilaya za Bariadi, Maswa, Meatu, Itilima, Busega na vijiji 253 vilivyopo umbali wa kilometa 12 kandokando ya bomba kuu. Tayari Mtaalam Mshauri anakamilisha upembuzi yakinifu, usanifu na uandaaji wa makabrasha ya zabuni. Gharama za utekelezaji wa mradi mzima zinakadiriwa kuwa kiasi cha Euro milioni 313. Mradi huu utawanufaisha wakazi wapatao 834,204 na unatarajiwa kutekelezwa katika awamu mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu ya kwanza itahusisha kufikisha maji katika Wilaya ya Bariadi, Itilima na Busega pamoja na vijiji vilivyopo kando kando ya bomba kuu ambapo Benki ya Maendeleo ya Ujerumani imeahidi kutoa Euro milioni 25 na tayari mkataba wa fedha (financial agreement) umesainiwa. Fedha zingine kiasi cha Euro milioni 80 zitatolewa na Global Climate Fund na ujenzi wa mradi huu unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2017/2018 na utachukua miaka miwili hadi kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu ya pili ya mradi itafikisha maji katika Wilaya za Meatu, Mji wa Mwanhuzi na Maswa kwa gharama ya Euro milioni 208. Fedha hizi pia zinatarajiwa kutoka katika Global Climate Fund.
MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza:-
Mkoa wa Simiyu hauna Chuo cha Ufundi (VETA):-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Chuo cha VETA katika Mkoa wa Simiyu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa kujenga vyuo 43 vya ufundi stadi ngazi ya Wilaya kwa awamu. Kipaumbele ni zile Wilaya zisizo na chuo chochote cha ufundi stadi na ambazo maeneo yake yana miradi mikubwa ya Kitaifa kwa manufaa ya Watanzania. Lengo ni kuongeza fursa za kuwapatia ujuzi vijana zaidi ya milioni moja ambao humaliza elimu ya msingi na sekondari na kuingia katika soko la ajira kila mwaka bila ujuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi sasa Chuo cha Ufundi Stadi Makete kimekamilika na kuanza kutoa mafunzo na vyuo sita vya Wilaya za Namtumbo, Kilindi, Chunya, Chato, Nyasa na Ukerewe vipo katika hatua mbalimbali za maandalizi ya ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vyuo vipya ngazi ya Mkoa katika Mikoa ya Manyara, Pwani, Lindi, Kipawa ICT na Chuo cha Hoteli na Utalii Arusha vimejengwa. Aidha, hatua mbalimbali za maandalizi ya ujenzi wa vyuo ngazi ya Mkoa vya Njombe, Geita, Rukwa, Simiyu na Kagera zinaendelea.
Serikali itaendelea kutenga bajeti ya maendeleo kila mwaka pamoja na kutafuta wafadhili wa ndani na nje ili kuwezesha kujenga vyuo vingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Chuo cha VETA Mkoa wa Simiyu kwa mkopo wa fedha za Benki ya Maendeleo ya Afrika upo katika hatua za maandalizi. Mshauri Elekezi wa kusanifu majengo na kusimamia ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Mkoa wa Simiyu amekamilisha kazi ya kuandaa michoro, makadirio ya ujenzi na makabrasha ya zabuni mwezi Oktoba, 2017. Hatua zinazofuata ni kutangaza zabuni na kumpata mjenzi mwezi huu wa Novemba na kuanza ujenzi wa chuo mwezi Februari, 2018. (Makofi)
MHE. MASHIMBA M. NDAKI (K.n.y MHE. ESTHER L. MIDIMU) aliuliza:-
Barabara za Vijiji katika Wilaya ya Maswa ni mbovu kiasi kwamba sehemu nyingi za maeneo ya vijijini hayapitiki.
Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka fedha za kutosha za Mfuko wa Barabara ili barabara hizo zifanyiwe matengenezo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Maswa inao mtandao wa barabara wenye jumla ya kilometa 1,055. Kwa mwaka wa fedha 2017/2018, Halmashauri hiyo imetengewa shilingi bilioni 1.4 kutoka katika Mfuko wa Barabara kwa ajili ya kufanya matengenezo ya kawaida kilometa 203.5, matengenezo ya sehemu korofi kilometa 54, matengenezo ya muda maalum kilometa 32, kujenga madaraja manne, Makalvati yenye urefu wa mita 28 na mtandao wa kupitisha maji ya mvua yenye mifereji ya mita 400.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutafuta fedha ili kuimarisha mtandao wa barabara za Halmashauri hapa nchini.
MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza:-
Wilaya ya Itilima na Busega ni Wilaya mpya na hazina Hospitali za Wilaya.
Je, ni lini Serikali itajenga Hospitali za Wilaya kwenye Wilaya hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri za Wilaya ya Itilima na Busega zilianzishwa mwaka 2015 na zina idadi ya watu 346,170 kwa Itilima na 224,527 kwa Busega. Ni kweli kwamba Halmashauri hizi bado hazina Hospitali za Wilaya na wananchi wanapata huduma kupitia zahanati 45 na vituo vya afya saba ambapo kati ya hivyo zahanati 27 na vituo vya afya vitatu vipo Halmashauri ya Wilaya ya Itilima na zahanati 18 na vituo vya afya vinne vipo Halmashauri ya Wilaya ya Busega.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia mpango wa maboresho na uimarishaji wa huduma za afya kwa kushirikiana na wadau (Canada na UNFPA), Serikali imepeleka kiasi cha shilingi bilioni 1.215 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya vituo vya afya. Kati ya fedha hizo, shilingi milioni 525 ni kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu katika Kituo cha Afya Ikilindo kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Itilima na shilingi milioni 450 ni kwa ajili ya Kituo cha Afya Nasa katika Halmashauri ya Wilaya Busega. Shilingi milioni 240 ni kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya zahanati nane ambapo kila zahanati imepatiwa shilingi milioni 30; zahanati hizo ni Gaswa, Mahembe, Migato na Nangale zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Itilima na Badugu, Nayamikoma, Ngasamo na Kikoleni zilizopo Halmashauri ya Wilaya za Busega.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri za Wilaya ya Itilima na Busega zimetengewa shilingi bilioni 1.5 kila moja kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali za Wilaya.
MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza:-
Mradi wa maji toka Ziwa Victoria utapeleka maji kwenye Wilaya za Busega, Bariadi na Itilima kwa awamu ya kwanza.
Je, kwa nini Serikali isipeleke maji hayo Makao Makuu ya Wilaya zote za Mkoa wa Simiyu katika awamu ya kwanza ili kutatua shida ya maji inayojitokeza mara kwa mara katika miji hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mradi huu umepangwa kutekelezwa kwa awamu mbili kutokana na upatikanaji wa fedha. Fedha kwa ajili ya utekelezaji wa awamu ya kwanza kwa ajili ya miji ya Wilaya ya Busega, Bariadi, Itilima pamoja na vijiji 170 zimepatikana. Awamu hiyo itagharimu kiasi ya Euro milioni 105 ambapo Benki ya KfW ya ujerumani itatoa Euro milioni 25 na Green Climate Fund itatoa Euro milioni 80.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa awamu ya pili utahusisha miji ya Mwanhuzi na Maswa pamoja na vijiji vipatavyo 83. Kwa sasa Serikali inaendelea na majadiliano na Green Climate Fund kwa ajili ya kupata fedha kiasi ya Euro milioni 208 kwa ajili ya utekelezaji awamu hii.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa awamu ya pili unatarajiwa kuanza baada ya kukamilisha taratibu za upatikanaji wa fedha. Serikali itaendelea na juhudi za kuhakikisha fedha kwa ajili ya utekelezaji awamu hii zinapatikana mapema ili kuwezesha wananchi wa Mkoa wa Simiyu kupata huduma ya maji kama ilivyotarajiwa.
MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itakamilisha ununuzi wa Vifaa Tiba ikiwemo vya upasuaji katika Kituo cha Afya cha Mwabayanda Wilayani Maswa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Kituo cha Afya Mwabayanda kilipatiwa shilingi milioni 400 kwa ajili ya upanuzi kwa kuwa awali ilikuwa ni zahanati. Ujenzi na ukarabati wa Kituo cha Afya Mwabayanda umekamilika na kituo kimeanza kutoa huduma za dharura za upasuaji kwa akina mama wajawazito kuanzia mwezi Oktoba 2020 baada ya kupatiwa vifaa tiba kutoka kwenye vituo vingine vilivyopo katika Mkoa wa Simiyu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2020/2021, Serikali imetoa shilingi bilioni 26 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika vituo vya afya vilivyojengwa awamu ya kwanza na ya pili na vifaa vya shilingi bilioni 15 tayari vimeshapokelewa na taratibu za kupeleka vifaa vya shilingi bilioni 11 zinaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya cha Mwabayanda kilijengwa katika awamu ya nne; na hivyo vituo vyote vya afya vilivyojengwa awamu ya tatu na ya nne vitatengewa fedha ya ununuzi wa vifaa tiba katika bajeti ya mwaka 2021/2022. Aidha, naishauri Halmashauri ya Wilaya ya Maswa kupitia mapato yake ya ndani itoe kipaumbele cha ununuzi wa vifaa tiba kwa awamu ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi wakati Serikali ikiendelea kutafuta fedha za ununuzi wa vifaa tiba.
MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza: -
Ununuzi wa zao la pamba utaanza mwezi Mei au Julai: -
Je, Serikali inatarajia kuwalipa wakulima watakaouza pamba kwa utaratibu gani kabla ya kuanza kwa ununuzi wa zao hilo ifikapo Mwezi Mei – Julai, 2021?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu wakulima wa pamba wamekuwa wakilipwa fedha za mauzo ya pamba kwa utaratibu wa fedha taslimu kwa maana ya hard cash kupitia Vyama vya Ushirika. Hata hivyo, mfumo huo umekuwa ukisababisha changamoto kwa wakulima ikiwemo wizi na ubadhirifu uliokuwa ukifanywa na baadhi ya viongozi wa AMCOS kwa kutoroka na fedha za wakulima hasa katika msimu ambao ipo changamoto ya uuzaji wa ununuzi mfano msimu wa 2019/2020. Katika kutatua changamoto hizo, Serikali katika msimu wa 2020/2021, imeratibu kwa majaribio mfumo wa kulipa wakulima kupitia akaunti za benki na simu za mkononi (mobile money).
Mheshimiwa Spika, mfumo huo umeleta mafanikio ambapo baadhi ya benki ikiwemo CRDB, NMB, Azania na NBC zimewezesha wakulima kufungua akaunti za Benki bila malipo na baadhi ya akaunti za wakulima kufutiwa tozo ikiwemo tozo za withdraw. Aidha, pamoja na mafanikio hayo, kumekuwepo na changamoto katika matumizi ya mfumo huo kutokana na kukosekana kwa matawi ya benki katika baadhi ya maeneo yaliyo karibu na wakulima. Taarifa za Benki na majina ya wakulima kutofautiana na hivyo kuchangia kukwamisha malipo ya wakulima kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, katika kutafuta suluhu ya changamoto hizo msimu wa 2021/2022 fedha za wakulima zitalipwa katika kaunti za AMCOS, kwa maeneo ambayo hayana changamoto za ukosefu wa ukaribu wa matawi ya benki. Aidha, Serikali itaruhusu kutumia mifumo yote ya malipo ikiwemo mfumo wa malipo wa fedha taslim hususan pale ambapo mazingira hayaruhusu kufanya malipo kupitia benki na mitandao ya simu. Aidha, mfumo wa malipo ya fedha taslim utasimamiwa na AMCOS na mnunuzi ili kudhibiti ubadhilifu wowote unaoweza kujitokeza hususan pale ambapo malipo yanapokuwa zaidi ya shilingi 10,000.
MHE. LUHAGA J. MPINA K.n.y. MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza: -
Mwaka 2018 Mkoa wa Simiyu ulitenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa Kiwanda cha Kuzalisha Vifaa Tiba vitokanavyo na malighafi ya pamba na utaratibu wa kuanza ujenzi umeshakamilika, lakini kibali cha ujenzi toka Serikali kuu kimechukua muda mrefu.
Je, ni lini Serikali itatoa kibali kuruhusu ujenzi kuanza?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Midimu, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia mifuko ya WCF na NHIF ilipanga kujenga kiwanda cha kuzalisha vifaa tiba vinavyotumia malighafi ya pamba chenye thamani ya shilingi bilioni 59.4. Wakati wa upembuzi yakinifu wa awali ilionekana kutumia miundombinu tuliyonayo, kiwanda hicho kinaweza kujengwa kwa shilingi bilioni 8.4 na kuokoa shilingi bilioni 51.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tathmini ya mwisho inamalizika mwishoni mwa mwezi wa pili ili kukutanisha mifuko husika na Serikali ya Mkoa wa Simiyu kupeana mwelekeo.
MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza: -
Je, ni lini ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Simiyu utaanza baada ya kukamilika zoezi la uthamini wa eneo la Uwanja utakapojengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Kiwanja cha Ndege cha Simiyu kilifanyiwa Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina kwa ufadhili wa Benki ya Dunia mwaka 2017 kupitia Mradi wa
Transport Sector Support Project (TSSP).
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali imekamilisha uthamini kwa maeneo na mali zitakazoathiriwa na utekelezaji wa mradi na kuandaa jedwali la uthamini ambalo tayari limeidhinishwa na Mthamini Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kuendelea na taratibu za malipo.
Mheshimiwa Spika, mara baada ya taratibu za kulipa fidia kukamilika, mipango ya ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Simiyu itaanza kulingana na upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. LEAH J. KOMANYA K.n.y. MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga Hospitali ya Wilaya katika Halmashauri ya Wilaya ya Meatu kwa kuwa hospitali iliyopo ina hadhi ya kituo cha afya na haikidhi mahitaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Meatu ilianza kutoa huduma kwa ngazi ya Kituo cha Afya. Aidha, mwaka 1989 ilipandishwa hadhi na kuwa Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Spika, Hospitali hii ni miongoni mwa hospitali kongwe 50 ambazo katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga fedha shilingi bilioni 16.5 ili kufanya ukarabati wa hospitali 19.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali itatenga fedha za ukarabati wa hospitali 31 zilizobakia ikiwemo Hospitali ya Wilaya ya Meatu, ahsante.
MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza vyanzo vya mitaji kwa akina Mama wajasiriamali mbali ya fedha zinazotolewa na Halmashauri?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, napenda kujibu Swali la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikiwawezesha kimtaji akina mama kupitia Mifuko ya Uwezeshaji inayoratibiwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Serikali ilianzisha Mifuko hii ili kuwasaidia wananchi wake hasa makundi maalum kwa lengo la kupunguza changamoto ya upatikanaji wa mitaji yenye masharti nafuu.
Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali ilianzisha Benki ya Wanawake Tanzania na ili kuboresha huduma shughuli za Benki hiyo zilihamishiwa katika Benki ya Tanzania Postal Bank sasa hivi inaitwa Tanzania Commercial Bank. Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2020/2021 Benki hiyo kupitia dirisha la wanawake imeendelea kutoa mikopo kwa wanawake, ambapo kiasi cha Shilingi Bilioni 22.3 kimetolewa kwa wanawake 6,327. Nakushukuru.
MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kurudia ujenzi wa Barabara ya Mwigumbi – Maswa ambayo imejengwa chini ya kiwango na imeshaharibika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, mkandarasi alianza kazi za kurudia ujenzi wa maeneo yote ambayo yalionekana hayakidhi viwango vya ujenzi kwa gharama zake mwenyewe mnamo tarehe 10 Juni, 2021. Kazi za marudio ziko katika hatua za mwisho ambapo zimefikia asilimia 98 na zinatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Mei, 2023.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga Daraja la Mto Duma Bariadi Mkoani Simiyu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Mto Duma ni mto mkubwa unaoanzia Kata za Gibishi kupitia Kata ya Matongo, Mwaubingi na Gilya. Mto huu ni wa msimu ambao hujaa kipindi cha Mvua kutokea Mbuga ya hifadhi ya Serengeti kuelekea Ziwa Victoria na hukauka kipindi cha kiangazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kukidhi haja ya kuwa na mawasiliano kwa Wananchi wanaotenganishwa na mto huu, jumla ya madaraja mawili yanahitajika ambapo hadi sasa ni daraja moja limejengwa katika barabara ya Igegu – Matongo - Gibishi. Kwa upande wa barabara ya Gasuma – Gilya, Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 50 katika mwaka wa fedha 2023/2024 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa daraja ili kujua gharama halisi za ujenzi wake.
MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza:-
Je, lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya mradi wa maji Sumve, Malya na Malampaka baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza utekelezaji wa miradi ya maji Sumve, Malya na Malampaka kupitia chanzo cha maji cha Ziwa Victoria. Mji wa Sumve utapata maji kupitia mradi wa maji Ukirugulu – Usagala – Kolomije hadi Sumve. Mkandarasi yupo eneo la mradi anaendelea na kazi. Aidha, Miji ya Malya na Malampaka itapata maji kupitia mradi wa maji wa Hungumalwa na Mkandarasi ameajiriwa mwezi Mei, 2023.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo, na Serikali itaendelea kutenga fedha kila mwaka hadi kukamilika kwa miradi hiyo.
MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itakamilisha kuweka umeme katika vijiji 138 vilivyobaki vya Mkoa wa Simiyu?
WAZIRI WA NISHATI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Simiyu una jumla ya vijiji 471; kati ya vijiji hivyo, vijiji 269 tayari vina umeme na vijiji 202 bado havijafikiwa na huduma ya umeme. Vijiji vyote ambavyo havijafikiwa na umeme katika Mkoa wa Simiyu vitapatiwa umeme kupitia Mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili unaotekelezwa na wakandarasi wawili yaani M/S Sengerema Engineering Group Ltd na M/S Steg International Services. Aidha, hadi sasa jumla ya vijiji 40 kati ya 202 tayari vimeshawashiwa umeme. Mradi huu unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2022.
MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza:-
Je, lini Serikali itajenga Kituo cha Afya katika Kata za Luguru na Sawida Wilayani Itilima?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na ujenzi wa vituo vya afya katika kata za kimkakati zenye idadi kubwa ya watu na umbali mrefu kutoka kituo cha karibu cha huduma.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 hadi Septemba 2023, jumla ya vituo vya afya 348 vimejengwa nchini kote. Kazi ya ujenzi huu ni endelevu hivyo tathmini ya vigezo kwa Kata za Luguru na Sawida itafanyika na kuingizwa kwenye mipango ya ujenzi, ahsante.
MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza: -
Je, lini Serikali itajenga uzio katika Hospitali ya Mkoa wa Simiyu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni mbili kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa wodi za kulaza wagonjwa wa ndani pamoja na ujenzi wa uzio katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. LUCY J. SABU K.n.y. MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza:-
Je, lini Serikali itajenga Wodi za Kulaza Wagonjwa katika Kituo cha Afya Zagayu Wilayani Itilima?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa kituo cha afya hufanyika kwa awamu, ambapo awamu ya kwanza inahusisha majengo ya OPD, maabara, upasuaji wa dharura, wodi ya wazazi, upasuaji, jengo la kufulia na kichomea taka; na awamu ya pili inahusisha ujenzi wa wodi za kulaza wagonjwa. Hivyo, Kituo cha Afya Zagayu kitatengewa bajeti ya ujenzi wa wodi katika awamu ya pili ya ujenzi, ahsante.