Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Esther Lukago Midimu (65 total)

MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba nimuulize swali dogo tu la nyongeza. Kwa kuwa, watumishi wetu hawa inawalazimu kuishi Wilaya nyingine ya Bariadi ambapo kuna umbali wa Kilometa 100 kwenda na kurudi kila siku.
Je, Serikali haioni kuna umuhimu wa kuharakisha makazi haya ili watumishi hawa waishi katika maeneo husika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali inaona hilo, ndiyo maana hata Halmashauri yenyewe ya Itilima katika mkataba wao waliosaini na National Housing, bahati mbaya mkataba ule ulikuwa haujahusisha Ofisi ya Rais -TAMISEMI wala Ofisi ya Mkuu wa Mkoa pale katika Ofisi ya RAS na ndiyo maana Ofisi ya Rais - TAMISEMI iliona kwamba licha ya mapungufu yaliyokuwepo lakini ofisi iweze kutoa kile kibali kwa mkataba ule. Hivi sasa Ofisi ya Rais - TAMISEMI imeshatoa kibali, na kwa sababu fedha tayari ninazo na kibali kimeshapatikana, imani yangu ni kwamba ujenzi kupitia Shirika la Nyumba utakamilika haraka iwezekanavyo ili kuondoa kero ya watumishi ambao wanapata taabu kutoka katika Halmashauri moja kwenda Halmashauri nyingine.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwanza kabisa nimshukuru Waziri kwa majibu yake mazuri sana. Kwa kuwa vijana ni nguvu kazi ya Taifa, je, Serikali haioni umuhimu wa kuanzisha viwanda vidogo vidogo na kuwawezesha vijana wa Mkoa wa Simiyu, wajasiriamali mitaji ya uhakika na kuwatafutia masoko nje ya nchi, ambapo itapunguza ukosefu wa ajira?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu swali la Mheshimiwa Mbunge limekuwa mahususi naomba nitoe maelekezo yafuatayo:
Mheshimiwa Mwenyekiti, awasiliane na Meneja wa SIDO wa Mkoa wa Simiyu, atambue kikundi cha Vijana ambao wanatabia ya ujasiriamali, wataelekezwa biashara ya kufanya na katika mkopo wa NDF unaokuja watatengewa fedha kusudi tuwalee na kusudi mje mnipime kwa mwaka mmoja ujao.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwanza kabisa namshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya kuridhisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Kituo cha Polisi cha Maswa ni cha muda, kiko kwenye hifadhi ya barabara ambapo kinaweza kikabomolewa wakati wowote ili kupisha ujenzi wa barabara; je, ni lini Serikali itajenga kituo cha kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa vile tatizo lililoko Wilaya ya Maswa liko sawa kabisa na tatizo lililoko Wilaya ya Itilima, hakuna kituo cha Polisi cha Wilaya; je, ni lini Serikali itajenga kituo cha Polisi cha Wilaya ya Itilima?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Esther alitaka kujua ni lini Serikali itajenga kituo cha Polisi Itilima pamoja na Kituo cha Kudumu Maswa. Naomba nimjulishe Mheshimiwa Esther kwamba kama nilivyojibu katika swali langu la msingi ni kwamba tunatambua upungufu wa vituo 65 nchi nzima katika Wilaya 65 ikiwemo Maswa na Itilima. Kwa hiyo, pale ambapo tutafanikiwa kupata fedha za ujenzi huu tutatoa kipaumbele katika maeneo hayo kama ilivyo maeneo mengine ya Wilaya zilizobakia 65 ambazo hazina vituo vya Polisi mpaka sasa hivi.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwanza kabisa, namshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri yanayotia moyo. Kwa kuwa mradi wa maji wa Ziwa Victoria utachukua muda mrefu ili kuwezesha Wilaya zote za Mkoa wa Simiyu kupata maji, je, Serikali ina mpango gani wa dharura wa kuwapatia maji ya uhakika wananchi wa Mkoa wa Simiyu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Mji wa Maswa sasa hivi una matatizo makubwa ya maji, wanakunywa maji machafu na kuna mradi wa chujio ambao ni wa muda mrefu. Je, ni lini Serikali itakamilisha ili wananchi wa Maswa wapate maji safi na salama? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza amesema kwa sababu mradi huu utachukua muda mrefu, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha sasa wananchi wanapata huduma ya maji? Kupitia mpango wa uendelezaji wa hii sekta ya maji, tayari tumeshatekeleza miradi mbalimbali katika Mkoa wa Simiyu na kuna maeneo ambayo kwa mfano, Nyangili, Mwamanyili, Bukapile, Bulima, Lamadi, Lukugu, Manara, kuna ambayo imekamilika na mingine inaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia juzi tumepitisha bajeti na katika Mkoa wa Simiyu tumeweka shilingi bilioni tisa ili Halmashauri ziendelee kutekeleza miradi ya maji kuhakikisha kwamba wakati tunasubiri ule mradi mkubwa, lakini wananchi wanaendelea kupata huduma ya maji. Vilevile Bariadi kuna huu mradi wa visima vya Misri tumechimba visima pale na nimeenda mwenyewe Simiyu maji yanapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Maswa, ni kweli ukiangalia ule mradi hata utakapoanza eneo la mwisho utakwenda Maswa. Kutokana na hilo, hata jana tulikuwa na kikao, tayari tumeagiza KASHWASA washirikiane na Halmashauri ya Maswa ili tuweze kuona uwezekano wa kutoa maji kutoka bomba lile pale Shinyanga kupeleka maji kwa muda pale Maswa wakati tunasubiri mradi mkubwa. (Makofi)
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwanza kabisa niipongeze Serikali kwa mpango wake wa kujenga chuo kila Mkoa. Kwa kuwa vijana wengi Mkoa wa Simiyu hawana kazi na ukosefu wa ajira unasababisha vijana wengi kujiingiza kwenye vitendo vya uhalifu. Namwomba Naibu Waziri anihakikishie, ni lini sasa huo ujenzi utaanza Mkoani Simiyu ili vijana wajifunze ujuzi waweze kujiajiri wenyewe waondokane na umaskini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, kwamba kwa namna tulivyopangilia tutajitahidi tusitoke nje ya mipango yetu, ujenzi unatakiwa uanze Februari mwaka kesho.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi hicho wakati tunasubiri chuo kikamilike, tunaendelea kuwasihi vijana wa Simiyu na wengine wa Tanzania waendelee kuachana na uhalifu kwa sababu inawezekana isiwe tiba ya changamoto iliyopo.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwanza kabisa namshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa wanawake wa Mkoa wa Simiyu ni wajasiriamali wazuri sana. Je, ni lini Serikali itaanzisha Benki ya Maendeleo ya Wanawake ili wanawake wa Mkoa wa Simiyu waweze kujikomboa na kujinufaisha na benki hiyo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa ahadi ya Mheshimiwa Rais ni kupeleka kila kijiji na kila mtaa shilingi milioni 50 ili kuwawezesha wanawake na vijana. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweza kusimamia pesa hizo na kuhakikisha kwamba zimewafikia walengwa, zisije zikaishia mikononi mwa watu wachache, wajanja kama mapesa ya JK? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kumbukumbu ya Wabunge yote wakati Waziri wa Afya ambaye anahusika na mambo ya maendeleo ya jamii ambapo Benki hii ya Wanawake iko katika dhamana yake, nakumbuka katika bajeti ya mwaka huu alizungumza wazi kwamba suala la ufunguaji wa matawi ya benki hii utafanyika kwa kadri rasilimali fedha inavyopatikana. Imani yangu ni kwamba kauli ile ya Mheshimiwa Waziri itaendelea kusimamiwa na katika Ukanda ule wa Ziwa benki hii itafunguliwa lengo kubwa likiwa ni kufikisha huduma kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la shilingi milioni 50, ni kweli, sisi tunafahamu kwamba katika mchakato wa bajeti ya mwaka huu zile fedha zilitengwa na naamini Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo inahusika na kusimamia jambo hili inapanga utaratibu mzuri na ndiyo maana wakati Mheshimiwa Waziri Mkuu anapita maeneo mbalimbali alikuwa akitoa maelekezo kwamba watu waache kuunda vikundi vya kitapeli ambapo mwisho wa siku fedha zile zitakuja kupotea. Imani yetu ni kwamba katika kipindi tutashirikiana vizuri wananchi wote na Serikali ili tusifanye makosa yale yaliyojitokeza katika kipindi cha nyuma katika fedha zile za mamilioni ya JK, sasa tunasema hatutarudia tena utaratibu ule wa mwanzo.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwanza kabisa, namshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri yaliyojitosheleza. Pia naishukuru Serikali yangu kwa kutenga hizo shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya za Itilima na Busega. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize swali la nyongeza; kwa kuwa Hospitali ya Mkoa wa Simiyu jengo la OPD lipo tayari na maelezo ya mkandarasi ambaye ni TBA amesema jengo hilo litakabidhiwa tarehe 28 Mei, 2018 kwa Katibu Tawala wa Mkoa. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kuweza kutujengea wodi ya wazazi, watoto, wanawake na wanaume ili hospitali hiyo ianze kazi haraka? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Hospitali Teule ya Mkoa haina kabisa gari la kubebea wagonjwa kupeleka Hospitali ya Rufaa Bugando, gari lililopo wanatumia hardtop almaarufu chai maharage; je, ni lini Serikali itatuletea gari la kubebea wagonjwa kupeleka katika Hospitali ya Rufaa. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya Wizara ya Afya ambayo tumeipitisha hivi karibuni, Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 30 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Rufaa za Mikao ya Katavi, Njombe, Simiyu, Songwe na Mara. Kwa hiyo, Hospitali ya Simiyu ni sehemu ya hospitali ambazo zitaendelezwa kujengwa katika mwaka huu wa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba ya hilo, Serikali imeagiza ambulances na zitakapofika Mkoa wa Simiyu utakuwa ni mmoja ya mkoa ambao tutaufikiria kupata ambulance. (Makofi)
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Kwanza kabisa nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri ya kujitosheleza. Naipongeza sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa mradi wa maji wa Wilaya ya Busega, je, mradi huo utaanza lini ili kukidhi mahitaji ya wana Busega?

Swali la pili kwa vile Mkoa wa Simiyu una changamoto kubwa sana ya maji. Je, Naibu Waziri uko tayari kuongozana na mimi baada ya Bunge ukajionee mwenyewe changamoto ya maji ilivyo Mkoa wa Simiyu ili uweze kutatua tatizo hili?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza awali ya yote nimpongeze mama yangu Mheshimiwa Esther Midimu ni miongoni mwa wa mama majasiri na shupavu katika kuhakikisha wanapigania haki za akinamama wakiwemo wamama wa Simiyu.

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri Bunge langu halina wamama hili Bunge lina Waheshimiwa tu.

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge, jasiri na mpambanaji katika kuhakikisha anapigania haki za akinamama wakiwemo akinamama wa Simiyu. Nataka nimuhakikishie sisi kama Wizara ya Maji tunatambua kabisa maji ni uhai hatupo tayari kupoteza uhai wana Simiyu tunatarajia mnamo mwezi wa nane mradi huo utaanza na mkandarasi atakuwa site. Lakini suala la kuongozana na mimi kwa kuwa anafanya kazi nzuri nipo tayari kuongozana naye Mheshimiwa Mbunge. Ahsante.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza kabisa naipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kutupatia pesa shilingi bilioni 5.4 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya ya Bariadi, Bariadi DC, Itilima na Busega. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize swali la nyongeza; kwa kuwa tuna upungufu mkubwa wa watumishi katika hospitali zetu hizo za Wilaya nilizozitaja, je, ni lini Serikali itatuletea watumishi wa kutosha hasa madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya ujenzi wa miundombinu ya hospitali, vituo vya afya na zahanati, Serikali imeweka mkakati ambao tayari umeanza kutekelezwa wa kuajiri watumishi wa kada za afya kuanzia madaktari na wauguzi na ajira hizi zinatolewa kwa awamu. Lengo la ajira hizi ni kwenda kuhakikisha majengo yote yaliyojengwa yanatoa huduma bora za afya kama ilivyotarajiwa.

Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hilo ni kipaumbele cha Serikali na itaendelea kuajiri wataalam wa afya kadri ya upatikanaji wa fedha ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi katika Halmashauri za Mkoa wa Simiyu na nchini kote.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniruhusu niulize swali la nyongeza pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwanza, naomba niipongeze Serikali kwa kuongeza bajeti ya madawa na vifaa tiba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Kituo cha Afya cha Mwabayanda jengo la kuhifadhi maiti liko tayari lakini halina friji, je, ni lini Serikali itapeleka friji ya kuhifadhia maiti? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa hospitali na vituo vya afya vya Mkoa wa Simiyu tuna upungufu wa madawa; je, Serikali imejipangaje kutupelekea madawa za kutosha kwenye hospitali na vituo vyetu vya afya? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napokea pongezi zake kwa Serikali kwamba imetenga fedha kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na shilingi bilioni 30 mwaka 2015 mpaka takribani shilingi bilioni 270, karibu mara tisa ndani ya miaka hii mitano. Hiyo ni dalili kwamba Serikali inathamini na imedhamiria kuhakikisha inaboresha upatikanaji wa dawa, vitendanishi na vifaa tiba katika vituo vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu jengo la mortuary kukamilika na kuhitaji jokofu, naomba nimueleze Mheshimiwa Mbunge Esther Lukago Midimu kwamba Serikali inapeleka fedha kwa ajili ya kukamilisha miundombinu ya huduma kama ambavyo tulifanya katika Kituo hiki cha Mwabayanda. Pia tumeelekeza watendaji katika Mamlaka za Serikali za Mitaa baada ya Serikali kupeleka fedha katika vituo hivyo na kukamilisha miundombinu, ni wajibu wao pia kupeleka sehemu ya fedha za maendeleo, ile asilimia 40 au 60 kwa ajili ya kununua baadhi ya vifaa tiba ili kuboresha huduma katika jamii zao. Kwa hiyo, ni muhimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Maswa aone namna bora pia ya kutenga fedha za kununua jokofu kwa ajili ya chumba cha kuhifadhia maiti katika jengo lile la Kituo cha Afya cha Mwabayanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na upungufu wa dawa; Serikali imeendelea kuboresha sana upatikanaji wa dawa katika vituo vyetu kutoka asilimia 65 mwaka 2015 mpaka takribani asilimia 90-94 katika mwaka huu wa fedha. Lengo la Serikali, kwanza ni kuendelea kuboresha upatikanaji wa dawa kwa kuboresha makusanyo ya fedha za uchangiaji wa huduma za afya katika vituo vyetu. Pili ni kuendelea kupeleka fedha Bohari Kuu ya Dawa ili kuendelea kupata dawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kuboresha upatikanaji wa dawa kwenye vituo vya afya katika Mkoa wa Simiyu na nchini kote.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naipongeza Serikali kwa kutoa pembejeo bure na mbegu bure za pamba. Imeleta motisha kwa wakulima. Hongera sana Mheshimiwa Bashe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niulize maswali ya nyongeza mawili. Kwa kuwa, mwaka jana AMCOS imechelewesha sana malipo ya wakulima na mpaka sasa…

SPIKA: Waheshimiwa, naomba sauti zenu mzipunguze tumsikilize Mbunge.

MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, niulize maswali mawili sasa. Kwa kuwa AMCOS, mwaka jana imechelewesha sana malipo ya wakulima na mpaka sasa kuna baadhi ya wakulima wanadai. Serikali haioni sasa umuhimu wa kuwarudisha wakulima kwenye soko huria ili wauze pamba walipwe cash? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali ikiwaruhusu wanunuzi ma- dealers kuingia sokoni moja kwa moja hiyo itasaidia wakulima kwenda kuuza pamba na kulipwa cash halafu itawasaidia vijana wengi kupata ajira kwa vile kuna ukosefu wa ajira. Je, ni nini tamko la Serikali kuhusu kuingia kwenye mfumo wa manunuzi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwanza mfumo wa ushirika ni takwa la Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Hii ni ahadi ambayo wananchi walikichagua Chama Cha Mapinduzi kuhakikisha kwamba tunajenga ushirika. Hili ni jambo la kwanza. Jambo la pili, ushirika ndiyo njia sahihi ya wakulima wadogo wadogo kufanya aggregation na kwa kutumia ushirika kama alivyosema kwamba tumegawa dawa bure, tumegawa pembejeo bure, tumetumia ushirika kufanya namna hiyo. Kwa hiyo, ziko changamoto kama alizosema Mheshimiwa Mbunge. Utafiti umeonesha kwamba kwenye Sekta ya Kilimo ambayo wakulima wake ni wadogo wadogo, tunapoondoa mfumo wa ushirika hasa katika haya mazao makubwa, mara nyingi wakulima hudhulumiwa na wanunuzi. Kwa hiyo, tutatatua changamoto zilizopo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu AMCOS ambazo hazijalipa wakulima kama wapo tuletewe majina tuchukue hatua. Hili ni jambo la kwanza na kutokumlipa mkulima ni uhujumu uchumi, wako ambao tumeshawafunga. Kuhusu namna gani tunalipa, tumekaa kikao cha wadau wa pamba, tumekubaliana na nitumie Bunge lako kuagiza mambo yafuatayo kwa kuwa msimu wa pamba tunaanza sasa hivi.

Mheshimiwa Spika, wanunuzi wanaruhusiwa kupeleka ma-cashier wao katika vyama vya msingi na waende na fedha wawalipe moja kwa moja wakulima pale pale kwenye chama cha msingi mahali ambapo hakuna mfumo wa kulipia benki. Hili la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, chama cha msingi ushuru wake utalipwa kupitia benki na wala hautaenda cash kwenye chama cha msingi. Lakini tunaruhusu mifumo yote mitatu. Mnunuzi anaruhusiwa kupeleka walipaji wake kwenye chama cha msingi. Kama chama cha msingi A, kuna makampuni matano, makampuni matano yapeleke ma- cashier wao pale pale ili mkulima anapofikisha pamba yake alipwe cash aondoke na fedha yake na pamba isiondoke kwenye cham acha msingi bila mkulima kupewa fedha yake.

Mheshimiwa Spika, hatuwezi kuua mfumo wa ushirika katika hatua hii. Hili ni takwa la kikatiba na tuna sheria ya ushirika. Kama tuna nia ya kuufuta ushirika katika nchi iletwe sheria na Bunge hili hili likiifuta sisi wizara tutaufuta ushirika bila matatizo yoyote. (Makofi)
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mradi wa chujio wa Maswa, Kata ya Zanzui, umeshakamilika na mradi ule unategemewa kusambaza maji katika vijiji kumi, Maswa Mashariki vijiji vitano na Maswa Magharibi vijiji vitano.

Ni lini sasa maji yale yatasambazwa ili wananchi wa Maswa na akinamama wa Maswa wapumzike na adha ya maji? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, kwa kweli anatosha mpaka chenji inabaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa namna nyingine ambayo nataka kusema wananchi wa Maswa changamoto kubwa sana lilikuwa ni chujio kwamba wanapata maji, lakini sio safi na salama na yenye ubora. Kwa hiyo, tumepata fedha, chujio lile tumelikamilisha kazi iliyobaki na ninatoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa pale na tumekwishamthibitisha, kipimo chake cha kwanza ni kuhakikisha maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyaeleza kuhakikisha wanapata huduma ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Wizara tutampatia fedha kuhakikisha kwamba anatimiza majukumu yake na wananchi wanapata huduma ya maji. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.

Kwa kuwa barabara ya kutoka Bariadi - Itirima - Mwandoya mpaka Isibiti Iguguno ni kilometa 289 na iko kwenye Ilani. Je, ni lini Serikali itaanza kuijenga kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Esther Midimu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara anayoisema inatoka Mwandoya junction kwenda Mwandoya ni barabara ambayo ilikuwa bado haijafanyiwa usanifu wala upembuzi yakinifu.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha huu barabara hii imepangwa kufanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili iwe sasa tayari kujengwa kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.

Kwa kuwa barabara ya Mwigumbi Maswa imejengwa chini ya kiwango na imeanza kubomoka bomoka. Je, ni lini Serikali itarudia ujenzi huo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther, Mbunge kama Mheshimiwa Naibu Spika, ni kawaida barabara zikishajengwa baada ya muda hasa muda wake unapokuwa umekwisha zinachakaa na hivyo kufanyiwa mategenezo kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hiyo itaingizwa kwenye mpango wa ujenzi mara tu fedha itakapopatikana hasa katika awamu tunazoziendea, kwa sababu ni taratibu kwamba tunafanya tathmini kuangalia gharama halafu barabara hiyo itafanyiwa rehabilitation kubwa. Ahsante.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii niweze kuuliza swali la nyongeza. Mkoa wa Simiyu una vijiji 470 na vijiji vilivyopata umeme ni 332 vimeshapata umeme vijiji vilivyobaki ni 138.

Je, ni lini Serikali itakamilisha kupeleka umeme katika vijiji vilivyobaki. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Midimu, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Simiyu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tulivyosema ni kweli kwamba kuna maeneo bado hayajapata umeme katika vijiji takribani kama 1,500 nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba hivyo vijiji 132 ambavyo bado havijapata umeme kwa Mkoa wa Simiyu na vyenyewe vitapelekewa umeme kabla ya mwezi Desemba 2022 kwa sababu tayari mkandarasi tumempata na tunaamini amesharipoti site yupo katika hatua za kwanza za kufanya survey kuhakiki kwamba vijiji vimechukuliwa na baada ya hapo kazi itafanyika kwa muda uliopangwa na kukamilisha umeme kufikia Desemba 2022. (Makofi)
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa barabara ya kutoka Korandoto kuelekea Meatu iko kwenye Ilani: Je, ni lini itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Midimu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja ya Kolandoto ambayo inapita Sibiti kwenda Karatu – Haydom – Mbulu, barabara hii ni ndefu na tuko kwenye mpango wa kuanza kuijenga kipande cha Mbulu kuja Haydom kilomita 50. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge na kipande cha Sibiti tayari daraja limeshajengwa na tutategemea katika bajeti ya mwaka huu na ambayo tunaendelea nayo kuwa na barabara za maingilio zisizopungua kilomita 20 pande zote mbili. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tumeshaanza kutekeleza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Hospitali ya Mkoa wa Simiyu haina wodi za kulaza wagonjwa, wodi ya wanaume, wanawake na watoto; je, ni lini Serikali itajenga wodi hizo?
WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Esther Midimu kwa swali lake la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwenye bajeti yetu ya 2022/2023 tumetenga fedha kwa ajili ya kuongeza wodi za kulaza wagonjwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu na baada ya Bunge mimi mwenyewe nitakwenda Simiyu pamoja na Mheshimiwa Esther Midimu ili kuhakikisha kwamba ujenzi unaanza haraka iwezekanavyo. (Makofi)
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuuliza swali la nyongeza. Serikali ina mpango gani kujenga uwanja wa michezo Mkoa wa Simiyu unaoendana na hadhi ya Mkoa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa nafasi. Naomba nijibu swali la Mheshimiwa Midimu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye mikoa yetu tuna ma-RAS ambao ni wenyeviti wa michezo, lakini kwenye wilaya zetu tuna ma-DAS ambao ni wenyeviti wa michezo, lakini tuna Wakurugenzi wetu tuna Maafisa Michezo kama ambavyo nimejibu kwenye majibu yangu ya msingi kwamba ni jukumu sasa Serikali za Mitaa wakatenga bajeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili jambo linapaswa lianze haraka ili wananchi ambao wana vipaji vyao viendelee kuibuliwa kwa kucheza katika viwanja ambavyo ni vizuri. Kwa hiyo, nitoe rai kwa Mkoa wa Simiyu kutenga fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi huo. (Makofi)
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa kuna upungufu mkubwa wa nyumba za walimu katika shule za msingi na sekondari Mkoa wa Simiyu.

Je, ni lini Serikali itajenga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, tunafahamu kwamba Mkoa wa Simiyu lakini pia Mikoa yote kote nchini bado kuna changamoto ya upungufu wa nyumba za watumishi wa sekta ya afya, sekta ya elimu pia sekta na idara nyingine. Mpango wa Serikali tumeendelea kujenga nyumba za watumishi lakini safari ni hatua tunakwenda kwa awamu. Tumeendelea kujenga, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kutumia mapato ya ndani ya Halmashauri hizo, Serikali imeelekeza kuhakikisha wanaanza kutenga fedha kwa ajili ya kujenga nyumba hizo, pia Serikali Kuu itaendelea kujenga kwa awamu. Ahsante. (Makofi)
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itakarabati Bwawa la Nyangokorwa lililoko Wilaya ya Bariadi ili liweze kutumika katika kilimo cha umwagiliaji?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Midimu na Wabunge wote wa Mkoa wa Simiyu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara sasa hivi inachokifanya ni kuangalia namna gani tunaweza kutumia resource ya maji inayotoka katika Ziwa Victoria na kwa kuwa kuna Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria, unayoyatoa maji Ziwa Victoria kuyaleta Mkoa wa Simiyu, sasa hivi tutashirikiana na wenzetu wa Wizara ya Maji, ili tuweze ku-tap yale maji yanayotoka Ziwa Victoria ili kuweza ku-develop skimu katika Mkoa wa Simiyu.

Mheshimiwa Spika, changamoto iliyopo Simiyu, ni maeneo yenye ukame na Wilaya zote za Simiyu zina ukame na zinapata mvua za muda mfupi. Kwa hiyo, njia ya kudumu ni ya kuyatumia maji ya Ziwa Victoria kwa ajili ya kutengeneza miradi ya umwagiliaji katika Mkoa wa Simiyu.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mkoa wa Simiyu upo kwenye ilani na eneo tayari limeshatengwa,

Je ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Uwanja wa Ndege Mkoa wa Simiyu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Simiyu, kama, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Uwanja wa Simiyu unatakiwa Kujengwa na mwaka huu tumetenga fedha kwa ajili ya kufanyia usanifu. Ahsante
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa majibu yanaendelea kutolewa haya haya kila tukiuliza swali; je, nini kauli ya Serikali kuhusu lini uwanja huu utaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba Serikali imeshakwenda hatua kubwa mbele, tayari tumeshathamini na tayari maandalizi ya malipo ya watakaopisha mradi huu yako yanafanyiwa kazi na tumeahidi kama Serikali kwamba baada ya kukamilisha suala hilo, ujenzi wa Uwanja wa Simiyu utaanza. Ahsante.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kutoa pesa za ujenzi wa VETA ya Mkoa wa Simiyu na mpaka sasa ujenzi unaendelea. Kwa kuwa sSera ya Serikali ni ujenzi wa VETA kila Wilaya; ni lini sasa Serikali itajenga VETA katika Wilaya ya Simiyu ambayo haina VETA?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Esther Midimu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni azma ya Serikali kujenga vyuo hivi katika Wilaya ambazo hazina vyuo na hivi sasa tuko katika mkakati au mchakato wa kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa VETA hizi. Mara tu pesa zitakapopatikana tutahakikisha kwamba, tunaanza ujenzi mara moja. Nakushukuru sana.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa vile Serikali inasema itawarudishia ng’ombe wao je, itakaporudisha itawalipa na fidia?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Midimu Mbunge wa Simiyu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba nifafanue hapa nimesema hapa kwamba tunapokamata mifugo kesi zao tunazipeleka Mahakamani hukumu inakuwa kati ya Hakimu na sisi tunasimama pale kama mashahidi tu ambao tunaonyesha vielelezo. Kwa hiyo suala la kwamba tutarejesha mifugo ni pale ambapo Serikali itajiridhisha kwamba hawa wahalifu watakaoingiza mifugo yao kwenye hifadhi wanastahili kurejeshewa hiyo mifugo na tunapopeleka kesi Mahakamani tunakabidhi vielelezo vyote, kwa hiyo sisi hatukai na mifugo. Ahsante.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa kituo cha Polisi Wilaya ya Itilima tayari umeshaanza na jengo limesimama, na Mheshimiwa Waziri kipindi kile alikuwa Naibu Waziri wa Fedha alikuja kutembelea, Waziri wa Mambo ya Ndani alikuja kutembelea.

Je, ni lini Serikali itatoa pesa za kumalizia ujenzi huo? Na Mheshimiwa Waziri nikuombe uje utembelee katika Wilaya yetu ya Itilima. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Midimu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua juhudi za wananchi wa Itilima pamoja na Mbunge wao Mheshimiwa Njalu Silanga katika kufuatilia ujenzi wa kituo hiki. Na kuhusu ombi lake, kwamba nitembelee Itilima, niko tayari kutembelea Itilima ili kuweka msukumo wa kupata fedha kutoka tunzo na tozo ili ukamilishaji wa kituo hiki uweze kufanyika.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Kata ya Nyaruhande, Shigala, Wilaya ya Busega hazina minara ya mawasiliano, je, ni lini Serikali itajenga minara ya mawasiliano katika kata hizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Midimu, Mbunge wa Mkoa wa Simiyu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Nyarukande tayari imeingizwa katika utekelezwaji wa miradi 763. Kwa hiyo tuombe tu kwamba utaratibu utakapofika katika maeneo hayo, basi wananchi waandaliwe kwa ajili ya kutoa maeno kwa ajili ya ujenzi wa minara hiyo. Ahsante sana.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.

Kwa kuwa, kuna upungufu mkubwa wa nyumba za Walimu katika Mkoa wa Simiyu kwenye shule za sekondari.

Je, ni lini Serikali itajenga nyumba hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Esther Midimu Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu katika swali la msingi ni kwamba, moja ya mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kwamba tunatafuta fedha ili tuendelee kujenga nyumba, hususan katika yale mazingira magumu huo ndiyo mkakati wetu.

Mheshimiwa Spika, hata katika bajeti ambayo tutakwenda kuipitisha kuna fedha tumetenga kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu katika maeneo yale ambayo ni magumu. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutaendelea kupeleka fedha kwa kadri ya mahitaji na tutagawanya kwa nchi nzima ili kuhakikisha tunaleta usawa kwenye hilo.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.

Kwa kuwa, ujenzi wa uwanja wa ndege wa Mkoa wa Simiyu upo kwenye Ilani na eneo tayari limeshajengwa.

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa ndege katika Mkoa wa Simiyu?
NAIBU WAZIRI UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Midimu Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyomjibu Mheshimiwa Shangazi, nimetaja kiwanja cha Simiyu kwamba ni kati ya viwanja ambavyo vipo katika bajeti ambayo tunaenda kwenye mpango wa kuanza kivijenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.

Kwa kuwa, kuna upungufu mkubwa wa watumishi katika hospitali zetu Wilaya ya Itilima na Wilaya ya Busega. Je, ni lini Serikali italeta watumishi wa kutosha katika Wilaya hizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Midimu Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Itilima na Busega ni moja ya Halmashauri zenye upungufu wa watumishi lakini zitapewa kipaumbele kwenye ajira hizi ambazo zimekwishatangazwa. Ahsante.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwanza kabisa nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kufuta riba kwa mkopo wa asilimia 10 kwa wanawake.

Mheshimiwa Spika, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa wanawake wengi ni waaminifu sana katika masuala ya kurudisha mikopo, Je Serikali ina mpango gani wa kuongeza muda wa marejesho? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili kwa kuwa mahitaji ya mikopo ni mengi kwa wanawake, vijana na walemavu. Je, Serikali au Wizara ina mpango gani wa kuongeza asilimia 15, asilimia Saba wakopeshwe wanawake, asilimia Tano wakopeshwe vijana, asilimia Tatu watu wenye ulemavu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Esther Midimu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Esther Midimu kwa kufuatilia kwa makini sana kuhusiana na maendeleo ya wanawake na hasa kushiriki katika shughuli za kiuchumi kupitia ujasiriamali.

Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali kama nilivyosema kwa kuanzisha mifuko pia kwa kuweka mfuko maalum ambapo kuna Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake, pia mfuko wa asilimia 10 zinazotengwa katika Halmashauri lakini pia kupitia taasisi za fedha nyingine zinazolenga kuhudumia makundi mbalimbali yakiwemo wanawake.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaendelea kuongeza fedha kwa namna tofauti tofauti ili kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika kuongeza uchumi wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu hitaji la pili nipende kumshukuru Mheshimiwa Esther kwamba ametoa mawazo ya kuona namna gani Serikali itaongeza asilimia kutoka zile asilimia 10 zinazotengwa katika Halmashauri kwenda asilimia 15. Nadhani hili ni suala zuri tunalichukua ili kulifanyia kazi pamoja na wenzetu wa TAMISEMI. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.

Kwa kuwa wananchi wa Kata ya Isanga na Guduwe Wilaya ya Bariadi wana shida sana ya maji, muda mwingi wakina mama wanaupoteza kutafuta maji kuliko kufanya kazi za maendeleo. Ni lini Serikali itachimba visima virefu katika kata hizo?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli kwanza kilio cha Wanabariadi kwa maana ya Mkoa wa Simiyu kimesikika na tumepata fedha kama nilivyoeleza zaidi ya shilingi bilioni 400 katika kuhakikisha tunaenda kutekeleza mradi mkubwa. Tumefanya jitihada kubwa za kuchimba visima eneo la Mkoa wa Simiyu, lakini imekuwa ni changamoto. Kwa hiyo, solution pekee kwa ajili ya kutatua tatizo la maji Bariadi na Mkoa wa Simiyu ni kuhakikisha tunayatoa maji ya Ziwa Victoria katika kuhakikisha Wanasimiyu na Wanabariadi wanapata maji safi na salama.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Maswa ni wilaya kongwe, lakini mpaka sasa haina Kituo cha Polisi.

Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi Wilaya ya Maswa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Midimu, Mbunge Viti Maalum, Mkoa wa Simiyu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tunatambua kwamba Maswa ni wilaya kongwe katika Mkoa wa Simiyu lakini inacho kituo cha polisi ambacho ni chakavu na kwa kweli ni majengo ya kuazima. Tutawasiliana na uongozi wa mkoa ili kupata eneo, hatimaye kuweka mipango ya ujenzi wa vituo vya polisi kwenye maeneo ambayo hayana ikiwemo Wilaya ya Maswa. Nashukuru.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itachimba visima vya maji katika Kata ya Mwabazuru, Budekwa na Busiriri Wilaya ya Maswa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nipende kumpongeza sana Mheshimiwa Esther, amekuwa akifuatilia hivi visima.

Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kuhakikisha maeneo haya yanayohitaji huduma ya maji kupitia visima yanafikiwa, hivyo hata Wilaya ya Magu nayo ni miongoni mwa wilaya ambazo tunakwenda kuzifikia. Mwaka ujao wa fedha tuna visima vya kutosha tulivyovitenga katika bajeti yetu, hivyo tutahakikisha kwamba Magu nao wanapata.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa barabara ya kutoka Bariadi – Itilima – Meatu – Sibiti mpaka Singida iko kwenye ilani. Je, ni lini Serikali itaanza kujenga kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii barabara ni sehemu ya Barabara ambayo ni ya kutoka Maswa – Sibiti Kwenda Haidong ambayo ipo kwenye mpango wa EPC+F na nimekwisha itolea maelezo mengi kwamba tayari taratibu zinaendelea na sasa tayari upande wa Wizara ya Ujenzi tumemaliza sasa tumekwishapeleka kwa wenzetu Wizara ya Fedha kuweza kupitia mapendekezo yetu. Ahsante.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Kata za Kijirishi na Nyaruhande, Wilaya ya Busega, kuna changamoto sana ya mawasiliano ya simu.

Je, ni lini Serikali itajenga minara ya simu katika kata hizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Midimu, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Simiyu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, eneo ambalo amelitaja Mheshimiwa Esther Midimu ni katika vijiji 2,116 ambavyo tayari vimeshafanyiwa tathmini. Hivyo, Serikali iko katika mchakato wa kutafuta fedha ili kuhakikisha kwamba tunafikisha mawasiliano katika maeneo hayo. Ahsante.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Maswa ni wilaya Kongwe katika Mkoa wa Simiyu, lakini haina Kituo cha Polisi kabisa. Ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi katika Wilaya ya Maswa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa
Spika, tunatambua uwepo wa baadhi ya wilaya kongwe kama ilivyo Maswa ambazo hazina Kituo cha Polisi. Mara kadhaa tumetoa ahadi hapa, naomba nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba katika bajeti zetu zinazofuata tutaangalia uwezekano wa kutenga fedha kwa ajili ya kuanza wa ujenzi wa Kituo cha Polisi ngazi ya wilaya katika Wilaya ya Maswa, nashukuru.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itawapa vitambulisho machifu wetu ili kuweza kuwatambua kwamba ni machifu wa nchi hii?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali za kuhakikisha tunawekeza nguvu nyingi kuhakikisha utamaduni wetu haupotei. Na miongoni mwa mambo ambayo yanafanyika ni kutambua uwepo wa machifu wetu. Na hilo limefanywa hata na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukaa kikao na machifu mbalimbali – siyo mara moja – na kuwatambua kwenye masuala mbalimbali ya sherehe za Kitaifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, machifu bado wanatambulika na Serikali, lakini juhudi mbalimbali bado zinaendelea kufanyika ili kuhakikisha kutambulika kwao kunafahamika Kitaifa na kimataifa. Ahsante. (Makofi)
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza: -

Je, ni kwa kiasi gani Serikali imejiridhisha kuwa marekebisho hayo yamekidhi viwango?

Swali la pili; kwa kuwa barabara ya Kolandoto – Meatu mpaka Kateshi iko kwenye ilani, je, ni lini Serikali itaijenga kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejiridhisha kwanza kwa kumsimamia zaidi mkandarasi na kuhakikisha kwamba kila hatua anayoifanya mhandisi mshauri pamoja na mkandarasi kupewa majukumu ya kuhakikisha kwamba anakwenda kufanya kazi kwa kiwango kinachotakiwa. Hata hivyo, atakapokuwa amekamilisha kazi hii itahakikiwa na wataalam kuhakikisha kwamba vigezo vyote vya barabara kwa maana ya jinsi ilivyosanifiwa ndivyo ilivyorekebishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili; barabara aliyoitaja ya kuanzia Kolandoto – Meatu kwenda Katesh ni sehemu ya barabara ndefu ambayo ipo kwenye mpango pia wa EPC+F. Ahsante.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakusukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itajenga hosteli katika Shule ya Sekondari ya Nasa?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu kama ifiatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa shule ambazo ziko katika mpango wa Serikali kuongezewa hosteli ni pamoja na shule ya Sekondari Ngaza ambayo Mheshimiwa Mbunge ameianisha hapo, ahsante.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Namshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Nimuulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa daraja la Mto Tungu ni muhimu sana Wilaya ya Maswa, inaunganisha Maswa na Kishapu.

a) Je, ni lini Serikali itatenga pesa za kujenga daraja hilo?

b) Je, ni lini Serikali itajenga Daraja la Sandai, Wilaya ya Itilima kwenda Hospitali ya Wilaya ya Nkolo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kipaumbele cha Serikali kupia TARURA kuhakikisha kwamba barabara zote zinazounga wilaya na wilaya zinapata huduma bora ya barabara, na barabara hii ambayo Mto Tungu umepita inayounganisha Wilaya ya Kishapu na Maswa nayo itatengewa fedha kwa ajili ya kuweza kujenga daraja hii ili iweze kupitika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu swali lake la pili la barabara ya Saadaye-Nkolo, hii barabara inaelekea katika hospitali kama sikosei nimeshawahi kupita maeneo hayo, na ni kipaumbele cha Serikali kuhakikisha kwamba barabara hii inatengenezwa vilevile ili wananchi waweze kuapata huduma ya afya katika hospitali ya mission iliyokuwepo kule. Kwa hiyo tutatenga fedha kuhakikisha kwamba barabara hii inatengenezwa.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa kuna upungufu mkubwa wa walimu katika Shule za Msingi na Sekondari katika Mkoa wa Simiyu: Je, ni lini Serikali itatuletea walimu wa kutosha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyokuwa nimeshasema kwenye majibu yangu ya msingi, Serikali imetangaza ajira 13,390 na kipaumbele pale watakapokuwa wanapangiwa shule walimu hawa, ni kwa mikoa ile yenye upungufu mkubwa, ukiwemo Mkoa wa Simiyu.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa, Shule ya Mwanhale, Kata ya Mkula, Wilaya ya Busega, majengo yake yamechakaa sana. Je, ni lini Serikali itakarabati majengo hayo?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itakarabati shule hizi chakavu zilizokuwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Busega kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kituo cha Afya Kiloleni Wilaya ya Busega hakina wodi za kulaza wagonjwa, wodi ya wanaume, wanawake na watoto. Je, ni lini Serikali itajenga wodi hizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Midimu, Mbunge wa viti maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kituo cha Afya cha Kiloleni katika Halmashauri ya Busega hakina wodi za kulaza wagonjwa. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, kwamba vituo hivi vya afya vinajengwa kwa awamu. Tunaanza na awamu ya kwanza ya majengo ya OPD, Maabara lakini pia majengo ya mama na mtoto na majengo ya upasuaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua zinazofuata ni kukamilisha kujenga mawodi na miundombinu mingine. Kwa hiyo, ni mhakikishie Mheshimiwa Mbunge, muda huo utakapofika tutahakikisha pia tunatafuta fedha kwa ajili ya kituo hiki cha afya cha Kiloleni, ahsante. (Makofi)
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Skimu ya Bukangilija na Masela ni lini itaanza kujengwa Wilaya ya Maswa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, skimu zote ambazo ziko kwenye mpango na bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 na pia hata hizo mpya ambazo tunaendelea kuzipata zitawekwa kwenye mipango ya bajeti na hivyo zitajengwa kwa kadri ambavyo tumepangia kwenye mipango yetu ya Serikali pamoja na skimu aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge, nayo pia itaweza kufanyiwa kazi kadri ambavyo Serikali itakuwa imejipanga, nakushukuru sana.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itajenga nyumba za Askari Wilaya ya Itilima, Mkoa wa Simiyu?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo umesema ni kweli Serikali inajua umuhimu wa kuwa na vituo hivi vya Polisi, kwa hiyo, katika bajeti zake tutaendelea kutenga fedha ili kuhakikisha maeneo haya yote yanajengewa vituo vya Polisi, kadri ya muda utakavyohitajika. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itafikisha Mkongo wa Taifa Mkoa wa Simiyu?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Midimu, Mbunge wa Mkoa wa Simiyu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa katika mikoa 26 ya Tanzania Bara ni Mkoa wa Simiyu pekee ambao haukuwa umeunganishwa na Mkongo wa Taifa lakini Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametafuta fedha zimeshapatikana na tayari Mradi wa Ujenzi wa Mkongo wa Taifa kutoka Shinyanga kupita Bariadi kuelekea Bunda umeshaanza.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuweza kuuliza swali la nyongeza.

Kwa kuwa kuna upungufu mkubwa wa walimu katika shule za msingi na sekondari Mkoa wa Simiyu hasa walimu wa sayansi; je, ni lini Serikali itapeleka walimu wa kutosha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Simiyu ni miongoni mwa mikoa 11 ambayo Ofisi ya Rais - TAMISEMI iliiainisha ikiwa ni mikoa yenye upungufu mkubwa zaidi wa watumishi wa sekta ya elimu, lakini pia wa sekta ya afya. Kila ajira zinapotokea, mikoa hii inapewa kipaumbele cha hali ya juu zaidi kuliko mikoa mingine ambayo ina nafuu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama ambavyo ajira mbili zilizopita walivyopata watumishi wengi Mkoa wa Simiyu, tutaendelea kupeleka watumishi wengi ili waweze kupunguza pengo la watumishi katika vituo lakini na shule zetu, ahsante.

MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.

Kwanza kabisa ninamshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Naomba uniruhusu nimshukuru Mheshimiwa Rais wangu ametupatia fedha shilingi bilioni 440 kwa ajili ya mradi wa Ziwa Victoria kuleta Simiyu na Wilaya zake Busega, Bariadi, Itilima, Maswa na Meatu, mkataba tumesaini juzi tarehe 27 mwezi wa Tano. Ahsante sana Mama yangu.

Mheshimiwa Spika, swali dogo, kwa kuwa Mkoa wa Simiyu ni Mkoa wa wafugaji; je, napenda kujua mradi huu utahudumia na upande wa mifugo pia? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Esther Midimu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, namshukuru kwa kutambua jitihada za Mheshimiwa Rais na tutaendelea kuunga jitihada zake kwa kuhakikisha tunasimamia vema fedha zote ambazo anazielekeza kwenye miradi hii mikubwa. Kuhusiana na mifugo wakati Mheshimiwa Waziri akisaini mradi huu mkubwa alioshukuru Mheshimiwa Mbunge Esther, tayari tumetenga malambo sita kwa ajili ya mifugo, hivyo mifugo pia itanufaika. (Makofi)
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Kituo cha Afya Kiloleni Wilaya ya Busega hakina wodi za kulaza wagonjwa kabisa. Je, lini Serikali itajenga wodi hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa ujenzi wa wodi ni katika vipaumbele vya Serikali hii ya Awamu ya Sita ya Daktari Samia Suluhu Hassan, ujenzi wa wodi za kulaza wagonjwa, ujenzi wa vyumba vya upasuaji, ujenzi wa mochwari na kadhalika katika vituo vya afya na tutaangalia ni namna gani katika kituo cha afya alichokijata Mheshimiwa Midimu kinaweza kipata fedha kwa ajili ya ujenzi wa wodi hizi kule Wilayani Busega.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Kituo cha Afya Sangamwalugesha Wilaya ya Maswa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaanza ujenzi wa vituo hivi vya afya ambavyo amevitaja Mheshimiwa Mbunge Wilayani Maswa kadiri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Je, Serikali ina mpango gani kutuongezea visima virefu Mkoa wa Simiyu tukiwa tunasubiri mradi wa Ziwa Victoria?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nampongeza Mheshimiwa Esther Midimu kwa kweli naye pia ni mfatiliaji mzuri lakini nikupongeze kwa sababu ulishiriki katika usainishaji wa mradi ule mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria lakini masuala haya ya uchimbaji wa visima pia yatakwenda sambamba na maji kuvutwa kutoka Ziwa Victoria na visima hivi vyote mwaka ujao wa fedha tutajitahidi maeneo mengi kuyafikia.

MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza;

Je, ni lini Serikali itajenga kituo cha Afya Kata ya Sawida wilaya ya Itilima?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, Serikali itajenga kituo hicho cha afya baada ya kufanya tathimini ya kuona uhitaji ulioko pale lakini vile vile kadri ya upatikanaji wa fedha; na tutatenga katika bajeti za miaka ya fedha inayofuata.

MHE ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.

Kituo cha Afya cha Ngw’angw’ali na Ngulyati Wilaya ya Bariadi kina upungufu wa vifaa tiba; je, ni lini Serikali itapeleka vifaa tiba vya kutosha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, kuhusu upelekaji wa vifaa tiba Bariadi kama nilivyotoka kusema hapa awali, Serikali katika mwaka wa fedha 2023/2024 imetenga kiasi cha shilingi bilioni 112 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kote nchini na katika hivyo tutahakikisha yale maeneo yenye uhitaji mkubwa yanapata vifaa tiba hivi ikiwemo kule Bariadi alikokutaja Mheshimiwa Midimu.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mikoa tisa iliyokabiliwa na ukame, Mkoa wa Simiyu ni mmoja wapo, je, Serikali ina mpango gani kupeleka gesi asilia?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, gesi asilia inaweza kupelekwa kwa njia ya mabomba au kwa kugandamizwa na kuwekwa kwenye magari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa tuko katika Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Mtwara na Lindi, lakini mipango iliyopo Serikalini ni kusogea sasa kuja katika Mikoa ya Bara kwa ndani zaidi kwa njia zote hizo, kwa maana ya kuwekeza katika kuleta kwa malori na treni au kuleta kwa bomba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wa Simiyu na maeneo ya Mkoa wa Mwanza ambapo kuna watumiaji wengi wanahitaji gesi kwenye viwanda, mipango ya Serikali ni kuendelea kupanua wigo wa upelekaji wa gesi katika maeneo hayo. Mkoa wa Simiyu nao pia utafikiwa pale ambapo uwezeshaji utakuwa umekamilika.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Ni lini Serikali itasambaza umeme katika vijiji 202 vya Mkoa wa Simiyu vilivyobaki ili viweze kupatiwa umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Midimu Mbunge wa Mkoa wa Simiyu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwamba tayari REA III Round II inaendelea katika maeneo yote ya Tanzania katika maeneo ya vijiji ambavyo havikuwa na umeme na tunaamini kufikia Desemba tutakuwa tumekamilisha kwenye baadhi ya maeneo na wengine wataendelea kukamilisha kwa mujibu wa ratiba walizokuwanazo. Kwa hiyo, umeme katika eneo lake utaendelea kupelekwa na kuwafikia wananchi.
MHE. ESTHER L. MIDUMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Itilima ni Wilaya mpya haina jengo la Mahakama.

Je, ni lini Serikali itajenga jengo hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Kwimba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Kwimba ni Wilaya mpya na katika maelezo yangu ya utangulizi nimeeleza uhalisia wa mpango kazi ambao tunakwenda nao. Mimi nitapenda tu kuwasiliana nae baada ya kipindi hiki leo hii ili nimpe kalenda ya ujenzi utakavyoanza katika eneo lake la Kwimba. Ingawa katika mazingira ya kawaida Kwimba ipo katika mpango wa 2021/2022 program ambayo nina uhakika kabisa Kwimba kuna jengo linaendelea.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itaboresha usambazaji wa mabomba ya maji katika Kata ya Bariadi, Mtaa wa Kidinda, Majengo Viwandani?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, usambazaji wa maji katika mji wa Bariadi kwenye maeneo aliyoyataja ni moja ya maeneo ambayo tumeyapa jicho la kipekee kuhakikisha tunakwenda kuyafikia lengo ni kumtua mwanamama ndoo kichwani na kusambaza maji safi na salama.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa sera ya Serikali ni kuwa na VETA kila wilaya. Je, ni lini Serikali itajenga Chuo cha VETA Wilaya ya Maswa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Midimu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyokwishaeleza kwenye majibu ya swali la msingi, kwamba Sera yetu kama Serikali ni kuhakikisha kwamba tunakuwa na Chuo cha VETA katika kila wilaya nchini ikiwemo na Wilaya ya Maswa. Namwomba tu Mheshimiwa Mbunge awe na subira katika hiki ambacho Serikali tunaendelea kutafuta fedha na tunaamini katika mwaka ujao wa fedha tutaweza kuzifikia baadhi ya wilaya lakini tutaipa kipaumbele vilevile Wilaya ya Maswa; kuhakikisha kwamba miongoni mwa vile vyuo vichache ambavyo vitapata fedha basi tuweze kutekeleza mradi huo katika Wilaya ya Maswa. Nashukuru sana.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza; kwanza kabisa nampongeza Waziri kwa majibu mazuri sana.

Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali kwa kutenga zaidi ya shilingi bilioni 66 kwa ajili ya kujenga kituo cha kupoza umeme katika Mkoa wa Simiyu na shilingi bilioni 55 tayari zinatoka mwaka huu. Je, ni lini ujenzi huo utaanza?

Swali la pili, chanzo cha maji kinachohudumia Hospitali ya Mkoa wa Simiyu kinatumia umeme wa jua siku jua halipo maji hamna hospitalini. Je, ni lini Serikali itapeleka umeme wa TANESCO pale kwenye kituo cha afya?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Esther Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka ujao wa fedha ni kweli zimetengwa shilingi bilioni 65 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kupoza umeme Bariadi, lakini pia na line ya kutoka Ibadakuli, Shinyanga mpaka Bariadi na ujenzi huu utaanza mara moja baada ya mwaka wa fedha kuanza.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kituo cha kupeleka maji katika Hospitali ya Mkoa wa Simiyu ambacho kinaendeshwa na solar, katika mwaka ujao wa fedha tumetenga shilingi milioni 150 ili kupeleka umeme katika kile chanzo cha maji ili kiendeshwe na umeme badala ya solar, hivyo kutoa maji ya uhakika katika Hospitali ya Mkoa wa Simiyu.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais alipopita Lamadi Wilaya ya Busega aliahidi ujenzi wa stendi, je, ni lini utaanza ujenzi huo?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Midimu, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahadi za viongozi wetu ni maelekezo kwa Wizara na mimi nimhakikishie kwamba tumeshapokea maelekezo hayo tunachofanya sasa tunatafuta fedha, lakini tunafanya usanifu kwa ajili ya kutafuta fedha, lakini tunafanya usanifu kwa ajili ya kuanza kujenga stendi ya mabasi ya Busega baada ya kupata fedha kwa ajili ya shughuli hiyo. Ahsante sana.
MHE. ESTHER L. MIDUMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Itilima ni Wilaya mpya haina jengo la Mahakama.

Je, ni lini Serikali itajenga jengo hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Kwimba kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Kwimba ni Wilaya mpya na katika maelezo yangu ya utangulizi nimeeleza uhalisia wa mpango kazi ambao tunakwenda nao. Mimi nitapenda tu kuwasiliana nae baada ya kipindi hiki leo hii ili nimpe kalenda ya ujenzi utakavyoanza katika eneo lake la Kwimba. Ingawa katika mazingira ya kawaida Kwimba ipo katika mpango wa 2021/2022 program ambayo nina uhakika kabisa Kwimba kuna jengo linaendelea.

MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwanza kabisa nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri.

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kujenga Vituo vya Afya na Hospitali za Wilaya tena nzuri za kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kata ya Luguru ni kata yenye idadi ya watu wengi, kituo cha afya kikijengwa Kata ya Luguru kitahudumia Kata ya Sawida na Kata ya Kinamweli. Je, Serikali ina mpango gani wa kuharakisha ujenzi wa kituo cha afya Kata Luguru?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; vituo vya afya vya Mkoa wa Simiyu na hospitali za wilaya tuna upungufu wa vifaa tiba na Watumishi.

Je, ni lini Serikali itatuletea vifaa tiba vya kutosha na watumishi wa kutosha? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, kwamba tayari Serikali ilishamwelekeza Katibu Tawala wa Mkoa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu pia na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Itilima kuwasilisha maombi ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Luguru ili tuweze kuandaa fedha kwa ajili ya kwenda kuanza ujenzi katika kituo hicho cha afya.

Mheshimiwa Spika, pili, Serikali imeendelea kupeleka vifaa tiba pia imeendelea kuajiri watumishi wa sekta ya afya na kuwapeleka katika Halmashauri zetu kote na Halmashauri ya Wilaya ya Itilima ni moja ya Halmashauri ambazo tayari zimepelekewa zaidi ya shilingi bilioni moja ya fedha kwa ajili ya vifaa tiba. Pia imeshapelekewa Watumishi wa Sekta ya Afya na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kila mara ambapo fedha itapatikana itaendelea kupelekwa kwa ajili ya vifaa tiba, lakini pia Watumishi wataendelea kupelekwa Itilima, ahsante.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Hospitali wa Mkoa wa Simiyu haina uzio kabisa na hospitali ikikosa uzio ni hatari sana;

Je, ni lini Serikali itajenga uzio katika Hospitali ya Mkoa wa Simiyu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, nimepokea ombi lake la uhitaji wa uzio; lakini nimuombe Mheshimiwa Mbunge, kwa sababu kwanza, Hospitali hiyo ya Simiyu ni mpya na iko bado kwenye ujenzi, Tukamalizie kwanza majengo ya kimkakati ambayo bado yanahitajika kujengwa kwenye eneo hili. Tukimaliza tutaelekea kwenye eneo la uzio kama ambavyo yeye Mheshimiwa Mbunge ameshauri, ahsnate sana.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuuliza swali la nyongeza. Mabwawa mawili, Bwawa la Luguru na Bwawa la Mwamapalala, Wilaya ya Itilima, Mkoa wa Simiyu yana hali mbaya, yamejaa tope: Je, ni lini Serikali itafanya ukarabati wa mabwawa hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mabwawa haya aliyoyataja niseme tu kwamba, tuko kwenye utaratibu wa kuona kama tutaweza kuendelea kuyatumia tuje tuweze kuyakarabati. Pia kwa Mkoa wa Simiyu tuna mradi mkubwa sana ambao unakwenda kutatua changamoto ya maji katika maeneo haya mengi. Kwa hiyo, huenda tusikarabati, lakini tukautumia mradi ule wa mabadiliko ya tabianchi kuhakikisha maeneo haya aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge tunayapelekea maji safi na salama. (Makofi)
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Hospitali ya Mkoa wa Simiyu muda mrefu hatuna gari la kukusanya damu salama; je, ni lini Serikali itatununulia gari la kukusanya damu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, magari katika hospitali za rufaa za mikoa yanaratibiwa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, lakini kwa kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Afya. Kwa hiyo, kwa sababu hospitali hii iko chini ya Wizara ya Afya tutawasiliana na Wizara ya Afya ili tuone uwezekano wa kupata gari hilo kwa ajili ya huduma za damu. Ahsante.