Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Stanslaus Shingoma Mabula (5 total)

MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:-
Je, Serikali haioni umuhimu wa kumaliza ujenzi wa nyumba za kambi ya Polisi Mabatini zilizoanza kujengwa tangu mwaka 2012 na sasa zinazidi kuwa magofu ili zisaidie hizo familia chache zipatazo 13?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing‟oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli nyumba za kambi ya Polisi Mabatini zilianza kujengwa mwaka 2012. Kutokana na ufinyu wa bajeti nyumba hizo hazikuweza kukamilika kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imetenga fedha katika mwaka wa Fedha 2016/2017 ili kukamilisha ujenzi wa nyumba hizo.
MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:-
Jimbo la Nyamagana ni jimbo pekee lililochangia mradi wa ujenzi wa nyasi bandia kupitia TFF shilingi 160,000,000.
Je, ni lini Serikali itawasisitiza TFF kuhakikisha kuwa uwanja huu unakamilika kwa wakati na kuendeleza malengo yaliyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing‟oma Mabula, Mbunge wa Nyamangana kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, uboreshaji wa uwanja wa Nyamagana wa kuweka nyasi bandia ulianza mwaka 2014 ukiwa na thamani ya dola za Kimarekani 737,886 sawa na shilingi za Kitanzania 1,193,161,662. Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA) lilitoa msaada kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) kiasi cha dola za Kimarekani 618,946 sawa na shilingi za Kitanzania 1,000,835,682 na Halmashauri ya Nyamangana ilichangia dola za Kimarekani 118,943 sawa na shilingi za Kitanzania 192,330,831.
Mheshimiwa Naibu Spika, nyasi hizo bandia zimegharimu tozo kiasi cha dola za Kimarekani 100,121.93, sawa na shilingi za Kitanzania 220,268,400 ikujumuisha import duty na VAT. TFF kama msimamizi wa mpira wa miguu kwa niaba ya Halmashauri ya Nyamangana na Serikali, wameshughulikia mchakato wa kutoa msamaha wa tozo hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nyasi bandi tayari zimewasili Dar es Salaam tangu tarehe 17 Aprili, 2016. Baadhi ya vifaa tayari vimeshafika katika Uwanja wa Nyamagana na mkandarasi amekwishaanza kazi ya ukarabati wa uwanja huo. TFF sasa wako katika mchakato wa kumalizia kusafirisha vifaa vilivyobaki.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na ukweli kwamba ukarabati wa uwanja wa Nyamagana kuufanya uwe wa nyasi bandia unahitaji umakini mkubwa ili uwe mzuri, imara na wenye hadhi ya Kimataifa ni lazima mkandarasi ahakikishe kuwa ubora wa viwango vinazingatiwa. Kwa vile mpango wa ukarabati huo ulitakiwa ukamilike mwishoni mwa mwezi huu, natoa wito kwa mkadarasi huyo kuhakikisha kwamba ukarabati huo unakamilika haraka iwezekanavyo ili uweze kutumika.
MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:-
Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu aliahidi ujenzi wa barabara ya lami kutoka Igoma – Kishiri – Kanindo kupitia Kata za Lwanhima na Bulongwa.
Je, ni lini ujenzi wa barabara hiyo utaanza kutekelezwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Igoma – Kishiri – Kanindo ina urefu wa kilometa 15 ikiwa ni mzunguko kupitia Kata za Igoma, Lwanhima na Buhongwa katika Jiji la Mwanza. Ili kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais, Serikali imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali katika bajeti ijayo ya mwaka 2017/2018 ikiwa ni hatua muhimu katika kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua hiyo itawezesha Serikali kujua gharama za mradi na kutenga bajeti kwa ajili ya kuanza ujenzi. Napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa ahadi hii ya Mheshimiwa Rais itatekelezwa kama ilivyoahidiwa.
MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:-
Fedha zinazotengwa na Halmashauri kutokana na mapato ya ndani; asilimia 10 ya fedha hizo zinatakiwa kwenda kwa vijana na wanawake na zinatakiwa ziwafikie walengwa kila mwaka bila kukosa.
Je, Serikali iko tayari kutoa agizo la msisitizo kwa Halmashauri zote nchini kutenga fedha hizo na wala wasichukulie kama ni hisani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Halmashauri zote zinatakiwa kutekeleza agizo la kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya Mfuko wa Vijana na Wanawake. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 Halmashauri zilitengewa jumla ya shilingi bilioni 56.8 ambapo hadi Machi, 2017 kiasi kilichopelekwa kwenye mifuko kilikuwa ni shilingi bilioni 16.05. Halmashauri ya Jiji la Mwanza pekee imeshapeleka shilingi milioni 147.0.
Mheshimiwa Spika, natoa wito kwa Halmashauri zote nchini kuanza kutenga maeneo rafiki ya kufanyia biashara kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo wadogo, kupeleka fedha kwenye mifuko na kusimamia marejesho ili ziweze kunufaisha makundi mengine. Utekelezaji wa maagizo haya ya Serikali ni kipimo cha utendaji kwa Wakurugenzi wote nchini na kushindwa kutekeleza, sio vyema kabisa. Aidha, hatua zitachukuliwa kwa kuzingatia taratibu zilizopo.
STANSLAUS S. MABULA aliuliza:-
Rais wa Awamu ya Nne alipofanya ziara katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana mwaka 2014 aliahidi kupatia x-ray.
Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo ya Rais hasa ikizingatiwa kuwa hospitali hiyo kwa sasa haina kifaa hata kimoja katika kitengo cha mionzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli ahadi hiyo ilitolewa na Mheshimiwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne mwaka 2014 wakati wa ufunguzi wa jengo la upasuaji katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana. Katika mwaka wa fedha 2017/ 2018, Serikali imetenga jumla ya shilingi 133,136,000 kwa ajili ya kununua mashine ya x-ray mpya ikiwa ni utekelezaji wa ahadi hiy iliyotolewa na Mheshimiwa Rais inayolenga kuboresha huduma za afya kwa wananchi.