Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Richard Mganga Ndassa (22 total)

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pia nishukuru kwa majibu ya utangulizi, lakini naomba tu kuiambia Serikali kwamba barabara hii ni muhimu sana kwa ajili ya uchumi pamoja na kijamii. Pia niseme barabara hii ni ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne na wakati barabara hii inaahidiwa na Rais wa Awamu ya Nne, Rais wa sasa Dkt. John Pombe Magufuli alikuwepo. Sasa hili suala la upembuzi yakinifu, ni lini hasa kwa sababu swali hapa la msingi, ni lini barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami kwa kuzingatia kwamba hii ni ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna nilivyomwelewa, anasisitiza tu kwamba hii kazi ya upembuzi yakinifu ikamilike haraka ili ahadi ya Marais wetu, Rais wa Awamu ya Nne na Rais wa Awamu ya Tano wakati alipokuwa Waziri wa Wizara ya Ujenzi itekelezwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchukua nafasi hii kumthibitishia kwamba Wizara yetu itatekeleza ahadi hiyo kikamilifu.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Ninaomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, kwa sababu hapa Tanzania tunayo mazao makuu ya biashara, ambayo yalikuwa yanajulikana katika kuongeza uchumi wa nchi yetu ambayo ni pamba, kahawa, korosho pamoja na katani.
Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba mazao haya ambayo yalikuwa yanatoa ajira kubwa, uchumi kwa nchi yetu, kwamba mazao haya sasa yanatafutiwa soko lenye uhakika hasa pamba ambayo zaidi ya Mikoa 14, Wilaya 42 zilikuwa zinategemea zao la pamba, Serikali ina mpango gani hasa? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Richard Ndassa, Mbunge wa Sumve kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana kwa kazi yake nzuri ya Ubunge aliyoifanya na Wabunge wengi wapya tuige kwake, maana yake Mheshimiwa Ndassa ameaminiwa na wananchi wake kwa muda mrefu kwa ajili ya kufanya kazi nzuri namna hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mpango mzuri sana wa kuendeleza mazao yote ya biashara, mpango wa kwanza ambao Serikali imeweka uzito mkubwa ni kuanzia kwenye ubora wa zao, kwa sababu ubora wa zao una uhusiano wa moja kwa moja na upatikanaji soko lake.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la pili ambalo Serikali imeweka mkazo mtasikia hata kwenye Mpango utakapowasilishwa na Dkt. Mpango muda siyo mrefu, imeweka mkazo kwenye kuongeza thamani ya mazao, kwa sababu na yenyewe ni hatua nzuri unapoenda kwenye kupata soko la zao husika na baada ya hapo tukishaongeza thamani kwa kupitia viwanda tutakuwa na uhakika wa kuweza kuuza mazao yanayotokana na mazao yetu ya biashara kwa bei ambayo itawaletea manufaa wanachi wetu na kuweza kuwafanikisha kuweza kuchochea watu wengi kujihusisha na uzalishaji wa mazao hayo kwa sababu yatakuwa na tija.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza naomba niipongeze sana Serikali kwa kazi nzuri sana inayofanya ya kusambaza umeme kupitia REA, REA I, REA II na REA III kwa sasa. Swali langu kwa sababu kuna vishoka wamejitokeza ambao wanaharibu sifa nzuri ya TANESCO, wanaojifanya kwenda kutandaza nyaya kwenye nyumba za watu lakini wanachukua pesa zao halafu hawa hawarudi tena kwa ajili ya kusambaza huo umeme. Je, Serikali inaweza ikawaagiza Mameneja wa Kanda, Mameneja wa Mikoa, Mameneja wa Wilaya ili kusudi waende wawabaini hao vishoka wasiwaibie wananchi hasa katika Jimbo la Sumve?
NAIBU WAZIRI NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa kati ya wahudumu wanaotoa huduma kwenye Shirika la Umeme kuna wafanyakazi wengine wala siyo wa TANESCO ni wafanyakazi bandia ambao wanaitwa vishoka. Pamoja na Wabunge mnaonisikiliza nichukue nafasi hii tu kuwatahadharisha kwamba wafanyakazi wa Mashirika ya Umeme Tanzania ni wafanyakazi ambao wanafanyakazi kwa maadili ya utumishi wa umma. Hata hivyo, tunatambua inawezekana wapo wachache kati yao ambao pia wanashirikiana na vishoka kuhujumu nguvu umeme ya TANESCO.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa hivi tumechukua hatua makusudi tumeanza kuwabaini wale Mameneja ambao wanashirikiana na vishoka tumeshaanza kuwa-identify na mpaka sasa kuna vishoka takribani 19 wamekamatwa na naomba sana nitamke hili na kuanzia sasa ofisi zetu zote za Kanda pamoja na Mikoa wale Makandarasi wanaohusika kuunganisha nyaya kwenye nyumba wanaorodheshwa kwenye ofisi zetu.
Kwa hivyo basi, kama kutakuwa na wakandarasi ambao hawapo kwenye orodha ya ofisi zetu hao ni vishoka na hawakubaliki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niongeze kwenye jibu hilo, hadi sasa Shirika la Umeme TANESCO limeshaanza kuchukua hatua kwa watumishi wake wasio waadilifu, hadi sasa watumishi 12 wamesimamishwa kazi kwa sababu ya kuhujumu miundombinu ya TANESCO pamoja na kushiriki kwenye kuwaunganishia umeme watu kwa njia ya vishoka.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nimwulize Mheshimiwa Waziri kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ahadi ya Serikali na Waziri mwenyewe humu Bungeni aliwaahidi Watanzania kwamba Miradi ya REA II itakamilika yote Juni, 2015; siyo mara moja wala mara mbili; ni sababu ipi iliyopelekea miradi hii kutokukamilika kama Mheshimiwa Waziri alivyosema? (Makofi)
La pili, kwa sababu huyu Mkandarasi mara kwa mara amekuwa akiwachangisha Watanzania shilingi 200,000/= au shilingi 300,000/= kwa kila nguzo ya umeme wale wanaohitaji; Serikali inatoa tamko gani ili kusudi wananchi hao wapate huduma hii kama ilivyotarajiwa? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli ni kwamba tulikusudia kwamba ikifika Juni, 2015 miradi iwe imekamilika, lakini tuwe na ukweli wa kiuchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Pato letu la Taifa ni karibu dola bilioni 53 na mwaka jana tulikuwa na uchaguzi, tulikuwa na Katiba, uchumi wetu hauna uzito wa kukabili vitu vikubwa kwa wakati mmoja. (Makofi)

WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, huo ni ukweli wa kifedha na kiuchumi. Kwa hiyo, ndiyo maana sasa Serikali imemaliza majukumu makubwa fedha zinaenda REA, kwa hiyo, miradi itakamilika kama ilivyopangwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile napenda kuongezea kwamba miradi ya REA na Miradi yote ya umeme, ndugu zangu Watanzania inahitaji fedha nyingine za kutoka nje. Kwa hiyo, sisi Wizara tumeanza kutafuta fedha kutoka nje. Kwa mfano, Tanzania ndiyo iliwakilisha Afrika kuweka hizi taratibu za umeme kwa kila raia wa sayari hii (Sustainable Energy for All 2030). Ni sisi ndiyo tuliwakilisha Bara la Afrika na tutahakikisha sisi ndiyo tutapata fedha nyingi kutoka huko na tumeishaanza kuzipokea. Kwa hiyo, miradi itaenda kwa kasi kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili la Chico, tumewaambia Wakandarasi kwamba endapo pataonekana kuna rushwa, adhabu kubwa kabisa ni kwamba huyo mkandarasi hatapata miradi mingine ya REA. Kwa hiyo, kama huyu mkandarasi anachangisha, ni kwamba na wiki ijayo tunafanya tathmini adhabu yake nyepesi sana ni kutopata mradi wowote wa REA kuanzia mwaka huu.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza naomba nisahishe jina langu hapa inasomeka Ngassa, siyo Ngassa ni Ndassa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na maelezo mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini naomba Serikali itambue kwamba suala la maji ni suala kila Mtanzania, kila mwananchi anahitaji maji na ndiyo maana unaona Wabunge wote wanasema kuhusu maji.
(a) Swali langu, kwa sababu Serikali katika mwaka 2000 na 2004 iliamua, maamuzi magumu yenye tija, kuyatoa maji ya Ziwa Victoria kuyapeleka Kahama, Shinyanga. Je, Serikali ina mpango gani mrefu wa kupeleka maji ya Ziwa Victoria katika Mikoa tisa ili maji hayo yawanufaishe Watanzania na mikoa hiyo ni Mwanza, Mara, Kagera, Simiyu, Singida na Dodoma. Serikali ina mpango gani kwa sababu mahitaji ya maji ni makubwa na maji ya Ziwa Victoria yapo hayana kazi nyingine. Je, Serikali ina mpango mkakati gani wa kuhakikisha kwamba maji yanafika katika maeneo hayo?
(b) Mheshimiwa Waziri wa Maji, wananchi wa Jimbo la Sumve katika Kata ya Nkalalo na Mabomba wanashida kubwa ya maji, naomba nikuombe pamoja na maelezo haya utembelee tuende ukajionee mwenyewe jinsi wananchi wa Tanzania wa Jimbo la Sumve wanavyopata taabu ya maji katika Jimbo langu.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimezungumza jana kwamba tumeleta mapendekezo ya mwongozo kwa kutengeneza mpango wa miaka 2016/2017 na nilisema katika sekta ya maji tumetoa ahadi kwamba katika miji yote ya Mikoa inayozungukiwa na Ziwa Victoria tutahakikisha tunachukua maji ya kutosha kuyafikisha kwenye maeneo husika kwa kiwango ambacho tumeshasema kwenye Ilani, kwamba Miji Mikuu ya Mikoa ipate asilimia 95 ikifika 2020 na ipate asilimia 100 ikifika 2025.
Kwa hiyo, naomba nilihakikishie Bunge hili kwamba azma hiyo ambayo pia Mheshimiwa Rais wetu ameahidi tutakwenda kufanya, tutaomba Waheshimiwa Wabunge muweze kutuunga mkono katika kupanua vyanzo vya upatikanaji wa fedha hasa kuongeza Mfuko wa Maji ili tuweze kutekeleza miradi yote hii ambayo kila Mbunge ameomba Serikali iweze kufanya, ahsante. (Makofi)
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na maelezo mazuri sana ya Mheshimiwa Waziri, lakini Serikali imekuwa ikiahidi kwamba itajenga Mahakama za Mwanzo kwa muda mrefu sana. Chikawe one aliahidi, akaja Chikawe two, mama Nagu, Kairuki, ahadi ni ile ile. Sasa ningependa kujua Mahakama ya Nyamikoma, Kata ya Iseni, Jimbo la Sumve Wilaya ya Kwimba itakuwa lini kwenye mpango wa kujengwa?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ni kweli, nakubaliana na mawazo ya Mheshimiwa Mbunge kwamba tangu Mheshimiwa mama Nagu, Chikawe na Asha-Rose Migiro tumekuwa tukizungumzia suala la ujenzi wa Mahakama za Mwanzo ikiwemo Mahakama ya Mwanzo ya Sumve.
Mheshimiwa Spika, nioneshe tu katika mwaka wa fedha 2012/2013, Mahakama ilipokea takribani asilimia 51 ya fedha kwa ajili ya maendeleo, mwaka 2013/2014 asilimia 18, mwaka 2014/2015 asilimia 7.5, mwaka 2015/2016 asilimia 100. Kwa hiyo, hoja ninayotaka kuijenga hapa chini ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli tutatekeleza mipango ya maendeleo kama tulivyoainisha katika program ya ujenzi wa Mahakama ikiwemo Mahakama za Mwanzo. Kwa hiyo, hili jambo linawezekana, nataka kumthibitishia Mheshimiwa Ndassa kwamba tutamaliza kuijenga Mahakama ya Mwanzo ya Sumve kama tulivyoahidi kabla ya mwaka wa bajeti wa 2016/2017 haujakamilika.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri, anajua kwamba Mradi Mkubwa wa Maji wa Ziwa Victoria unaanzia katika Kitongoji cha Ihelele, Kijiji cha Nyahumango. Cha kusikitisha Mheshimiwa Waziri, sina tatizo na maji kwenda Nzega, kwenda Kahama au sehemu nyingine, pale kwenye chanzo cha maji Ihelele penye matanki makubwa kuna kituo kimoja tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, hivi ungekuwa wewe ndiyo mwenye Jimbo hilo na una Waziri ungejisikiaje?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ningekuwa sijafanya ziara ningeshtuka sana, lakini kwa sababu sijawahi kwenda kwenye eneo hilo nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba nitaenda nikaone kwa nini vijiji ambavyo vinazungukwa na matenki makubwa ya maji havipati maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa ziara yangu Mkoa wa Mtwara, nilikwenda eneo la Mbwinji. Eneo la Mbwinji lina matanki makubwa sana ya maji ndiyo chanzo cha maji, kitu cha ajabu nilikuta wananchi wanaokaa lile eneo hawapati maji. Nilivyojaribu kuuliza ikaonekana kwamba maji pale yakishachotwa lazima yapelekwe Masasi kwenda kufanyiwa sasa utibabu, kuwekewa dawa ili yaweze kuwa safi kwa ajili ya matumizi ya binadamu, ndiyo baadaye sasa yaweze kusambazwa kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilipofika pale niliagiza na sasa hivi wananchi wa maeneo yale tayari wanapata maji. Sasa sielewi hilo eneo analozungumza Mheshimiwa Mbunge, linaweza likawa na tabia ya kufanana na hiyo kwamba, hapo ndipo wanapochota maji, wanaweka kwenye matenki halafu baadaye yanakwenda kwenye mtambo wa kutibu maji. Sasa, japo sijafika lakini naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hili suala nitalifuatilia na nitamjibu kabla hatujamaliza Bunge hili.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua kwamba itakuwa ni Serikali ya viwanda, je, Selikali ina mpango gani wa kuanza kufufua viwanda hivi ambavyo vilikufa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Kiwanda cha Chai cha Mponde kilichoko katika Wilaya ya Lushoto, Jimbo la Bumbuli, kimefungwa kwa takribani miaka mitatu sasa na mpaka sasa hakijaanza uzalishaji. Mara ya mwisho wakati Msajili wa Hazina anakuja pale alituambia kwamba zimeandaliwa shilingi bilioni nne kwa ajili ya kuanzisha shughuli za uzalishaji na kwenye randama ya Wizara ya Fedha na Wizara ya Viwanda na Biashara fedha hiyo hatujaiona. Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusu kufunguliwa kwa kiwanda hiki?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Shangazi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa Serikali imedhamiria kujenga viwanda na hasa kuanzia viwanda vidogo sana, viwanda vidogo, viwanda vya kati pamoja na viwanda vikubwa. Mikakati ambayo Serikali inaichukuwa kwa sasa ni pamoja na kutengeneza mazingira wezeshi ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu ili kuwawezesha Watanzania kuwekeza zaidi. Mkakati wa pili ni kufanya utafiti hasa kwa viwanda ambavyo vimedhoofika au vimekufa ili kuviweka katika mazingira mazuri ili kutafuta wawekezaji wengine kwa ajili ya kuviendeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na hayo, nimhakikishie Mheshimiwa Shangazi tu kwamba Serikali inafanya mikakati mingine ya ziada ikiwa ni pamoja na kutoa mikopo kama mnavyoona kwamba Serikali itatoa mikopo shilingi milioni 50 kila kijiji ili kuwawezesha Watanzania waweze kufanya pia biashara kuendesha viwanda vidogo vidogo. Pamoja na hayo, Serikali imeweka mazingira ya kisera na kisheria ili kuhakikisha kwamba sasa tasnia ya viwanda inaimarishwa zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusiana na Kiwanda cha Chai cha Lushoto, ni kweli kabisa kiwanda hiki kimedhoofu na siyo Lushoto tu, viwanda vingi vimekufa sehemu mbalimbali. Mkakati wa Serikali uliopo ni kuhakikisha kwamba inatafuta wawekezaji binafsi ili waweze kujadiliana na wenye kiwanda hicho ili wawekezaji hao waweze kukiimarisha Kiwanda cha Lushoto na kianze kufanya kazi kama kawaida.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri, Halmashauri zinatofautiana kimapato na Kituo cha Afya cha Nyambiti hakina gari, ni utaratibu gani sasa utumike ili kituo hiki kiweze kupata gari kwa sababu uwezo ni mdogo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, suala zima la upatikanaji wa gari katika vituo vya afya, tulipokuwa tunapitia mchakato wa bajeti yetu ya mwaka huu 2016/2017, tulikuwa tukifanya analysis ya halmashauri mbalimbali katika suala zima la sekta ya afya, kila halmashauri iliweka kipaumbele chake. Kuna wengine waliweka kipaumbele cha ujenzi wa miundombinu, kwa mfano kwa ndugu yangu pale zahanati aliyosema ya Chiwale, wametenga karibuni milioni 287 kwa ajili ya kituo kile cha afya. Wengine kipaumbele chao walichoweka ni ununuzi wa gari la wagonjwa. Kwa hiyo, vipaumbele hivi vinatofautiana kati ya zahanati na zahanati.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumjulisha Mheshimiwa Ndassa kwa sababu sijajua kipaumbele walichoweka katika eneo hili, sisi na wenzetu wa Wizara ya Afya tutaangalia katika bajeti ya mwaka huu tumegusa vipi katika eneo hilo. Mwisho wa siku ni kwamba, lazima kwa umoja wetu wote tuangalie jinsi gani tutafanya maeneo kama hayo ambayo wananchi wanapata shida waweze kupata fursa za kuwa na gari la wagonjwa ili mama akipata matatizo aweze kupelekwa hospitali ya karibu kupata huduma. Kwa hiyo, Mheshimiwa Ndassa naomba tulichukue hili tujadiliane kwa pamoja na kuangalia bajeti yenu ya halmashauri mlipanga vipi kama vipaumbele vyenu vya awali.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Mwanza hapo awali kulikuwa na zaidi vinu 15 vya kuchambulia pamba, kikiwepo na cha Nyambiti Ginnery, Ngasamo. Mheshimiwa Waziri kwa sababu nilishaongea na Mheshimiwa Waziri Marehemu Abdallah Kigoda, pia niliongea na Waziri aliyekuwepo wakati huo Mheshimiwa Mama Nagu; ni lini sasa angalau Nyambiti Ginnery iweze kutengeneza pamba nyuzi?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ndassa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pamba limekuwa na hoja kubwa kwenye bajeti yangu, majibu niliyotoa ni kwamba tarehe 02 Mei, nilizindua mkakati namna ya kuboresha pamba kusudi iendane na ujenzi wa uchumi wa viwanda. Ijumaa mikoa yote inayolima pamba, tunakutana Mwanza na mimi nitakuwepo niwapitishe kwenye mkakati na nitahakikisha kwamba Kiwanda cha Nyambiti kiweze kuingizwa katika mchakato wa kuchambua pamba na kutengeneza kiwanda ikiwezekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo siku ya Ijumaa shughuli nzima inafanyika Mwanza mimi nitakuwepo pale, tuchambue suala la pamba ili ule mkakati wangu wa nguo uweze kutekekezwa.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Tanzania tunayo makampuni binafsi mawili yanayotoa huduma za ndege kwa wasafiri hapa nchini, FastJet pamoja na Precision.
Mheshimiwa Spika, lakini ningependa kujua ni utaratibu gani wa gharama za nauli wanazotumia kupanga. Kwa sababu gharama ya kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza na kurudi inakaribia shilingi 800,000 vivyo hivyo gharama ya kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya inakaribia shilingi 800,000 sawasawa na nauli ya kutoka Dar es Salaam kwenda Dubai kwa ndege za Emirates. Nataka kujua, ni utaratibu gani unaotumika kupanga gharama za nauli kwa wasafiri hasa kwa Dar es Salaam, Mwanza pamoja na Mbeya, routes za ndani hizi ni nani anayepanga nauli hizi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, nauli za ndege kwa sasa zinapangwa na soko.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, kinachotokea taasisi yetu ya SUMATRA huwa inafanya kazi ya kuangalia kama hizo nauli ambazo hupangwa na soko na pengine soko haliko sawasawa inafanya utaratibu wa kurekebisha.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, kikubwa ambacho Serikali imeamua ni kufufua Shirika letu la ATCL liwe na ndege za kutosha ili tuweze kuondoa ukiritimba wa kampuni chache zinazotoa huduma za ndege kwa sasa, hatimaye bei ya soko iwe kweli bei ya soko. (Makofi)


SPIKA: Majibu ya nyongeza Mheshimiwa Waziri Profesa Mbarawa.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri zinapangwa na soko lakini Mamlaka ya TCA (Tanzania Civil Aviation) ndiyo inasimamia jambo hili. Kwa kulijua hili, Serikali inafanya kila linalowezekana tuweze kufufua Shirika la Air Tanzania na ambapo sasa tuna utaratibu wa kununua ndege mbili, Q400, wakati wowote zitaweza kufika hapa Tanzania kuhakikisha kwamba bei hiyo sasa tunaisimamia ipasavyo.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Katika maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba ruzuku ya pembejeo pia inapelekwa kwenye zao la pamba. Mheshimiwa Waziri unajua kwamba mpaka leo hakuna ruzuku yoyote inayopelekwa kwenye zao la pamba, kwenye mbolea pamoja na mbegu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia ruzuku katika zao la pamba linatolewa kwa utaratibu tofauti na ule unaotolewa katika mahindi na mpunga. Kwenye zao la pamba ruzuku inatolewa katika mbegu, kwa hiyo, niko tayari kuongea na Mheshimiwa Mbunge tujaribu kupitia yale ambayo yeye anayafahamu kuhusu hili lakini nimfahamishe tu kwamba kuna ruzuku inatolewa lakini ni katika utaratibu ambao ni tofauti kidogo. Kama nilivyosema mazao mengine kama kahawa, korosho vilevile ruzuku inatolewa lakini mara nyingi ni kwa kupitia mifuko maalum ambayo imeundwa kwa ajili ya mazao hayo. Lakini niko tayari kuongea naye tuangalie kuhusu hili.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri kwamba, nakumbuka ulifanya ziara mkoani Mwanza na ulizungumza na wadau wa pamba. Msimu wa pamba umeanza Jumatatu, bei elekezi tunaambiwa ni shilingi 1,000, lakini wapo wanunuzi wengine wanasema hawawezi kununua pamba kwa bei ya shilingi 1,000.
Je, nini msimamo wa Serikali kuhusu bei ya pamba, kwa sababu viwanda vyote hivyo Manonga, MWATEX, vinahitaji pamba ya kutosha; na ili wakulima wa zao la pamba waweze kulima zaidi lazima bei iwe nzuri, nini msimamo wa Serikali kuhusu bei ya pamba?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UFUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, sheria ya zao la pamba inataka bei elekezi itajwe na Bodi ya Pamba kwa kushauriana na wakulima, wanunuzi na wadau wengine wa zao lenyewe. Hiyo processes ilifanyika na hatimaye Bodi ya Pamba ikatangaza bei elekezi ya shilingi 1,000 kwa kilo moja pamba mbegu. Sasa wanunuzi wanayo hiari ya kupima wenyewe, kama hiyo bei wakinunua kwa bei hiyo elekezi au zaidi ya pale, watakuwa na faida katika biashara yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuarifu Mheshimiwa Mbunge, kwamba hadi hapa ninapozungumza makampuni nane, yamekwisha pewa license ya kununua pamba, na ununuzi wa pamba umeanza. Utaratibu wa msimu wa pamba ni mrefu kidogo, kwa hivyo kwa miaka ya nyuma msimu unapoanza kampuni hizi huwa zinaendelea kupata leseni na kuongezeka kadri msimu unavyokwenda mbele. Kwa hivyo, bei ya pamba ya sasa ni nzuri kwa wakulima, pia baada ya bodi kupitia vizuri ile mjengeko wenyewe wa bei, wana hakika pia itakuwa na manufaa hata kwa wanunuzi wa pamba.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nimwulize Mheshimiwa Waziri, kwa sababu Wakala wa Madini (TMAA) wanafanya kazi nzuri sana. Mwaka 2010 na mpaka mwaka 2015 waliweza kukamata madini yenye thamani ya Dola bilioni mbili, lakini pia kwa upande wa shilingi, jumla ya shilingi bilioni 64 zilikamatwa. Je, kwa utaratibu huo huo Serikali ina mpango gani wa kuzuia wachimbaji katika migodi hasa katika usafirishaji wa ule mchanga kwenda kupimwa nje?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli kabisa sasa hivi mchanga wote wa concentrate, yaani copper concentrate na hasa unaotoka kwenye mgodi mkubwa wa Bulyanhulu unasafirishwa kwenda ama China ama Japani. Sababu kubwa ya kufanya hivyo ni kwa sababu hapa viwanda vya kuchenjua dhahabu na kuachanisha madini, havijajengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia namwambie Mheshimiwa Ndassa, ni kweli kabisa uwekezaji huu unahitaji mitaji mikubwa; na siyo chini ya Dola 1,000 kuanzisha mradi wa kuchenjua madini hapa nchini. Hata hivyo, kama Serikali, tunatambua sana mchango wa TMAA mamlaka yetu. Kweli kabisa kwa kutumia TMAA imedhibiti asilimia kubwa sana ya upotevu wa madini ambao ulikuwa unatokea hapo nyuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimkumbushe tu Mheshimiwa Ndassa kwamba ni kweli, mwaka 2015, migodi mikubwa kama GGM ililipa shilingi milioni 117 kama dola kwa ajili ya royalty. Hii kutokana na kazi ya TMAA. Pia local levy iliyolipwa ni dola bilioni 4.7 za Marekani, hiyo ni kutokana na udhibiti wa TMAA.
Kwa hiyo, Serikali tunaendelea sasa kuangalia uwezekano wa kuhamasisha wawekezaji wakubwa kuanza sasa kujenga viwanda vya kuchenjua dhahabu hapa nchini. Hata hivyo, itachukua muda, bado Serikali tunalifanyia kazi. Hii ni kwa sababu inahitaji mitaji mikubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, wazo la Mheshimiwa Ndassa tumelichukua, tutalifanyia kazi kama ambavyo Mheshimiwa Ndassa tunashirikiana, tunakushukuru sana.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. TBC na Radio ya Taifa ndiyo visemeo vya Serikali. Je, wakati mnaboresha mitambo, Serikali ina utaratibu gani wa kuwapeleka wafanyakazi wa TBC na Radio ya Taifa kwenda nje kujifunza ili kusudi waendane na teknolojia ya sasa, kuwapeleka nje kwenda kusoma?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Ndassa kwa kazi nzuri anayofanya ya kutetea tasnia ya habari kwa sababu na yeye mwenyewe ana background ya habari. Pili TBC imekuwa na mipango mizuri ya kuwapeleka wafanyakazi wake kwenda kuongeza ujuzi wao nje ya nchi, lakini pia na kuwaalika Wataalam mbalimbali kuja hapa kwa ajili ya kuongeza ujuzi wao. Mfano mzuri, wenzetu wa China wamekuwa wakitusaidia sana, wafanyakazi wengi wanakwenda kujifunza. Hata hivi tunapoongea wako wafanyakazi ambao wanaongeza ujuzi wao China, lakini tunao Wachina ambao wako hapa kupitia ushirikiano wa TBC na Star Times, nao wanaongeza ujuzi wa watu wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaamini program hizi zitaendelea na tutaendelea kuziboresha mara kwa mara ili wafanyakazi wetu waendane na kasi ya mabadiliko ya teknolojia duniani.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, kwa sababu kazi ya ujenzi wa zahanati ni kazi nyingine, ujenzi wa vituo vya afya ni kazi nyingine, upelekaji wa tiba ni kazi nyingine. Je, Serikali kwa sababu inajua kwamba upo upungufu mkubwa sana wa wataalam katika ngazi zote, imejipanga namna gani kuhakikisha kwamba zahanati na vituo vyote vile vinakuwa na waganga wa kutosha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, juu ya mpango wa Serikali tumezungumza hapa. Ni kweli tunajenga structures hizi lakini lazima tupeleke vifaa tiba, dawa na wataalam. Hili tumelizungumza na mlikuwa mnajua tulikuwa na mchakato katika suala zima la ajira, lakini kutokana na changamoto ya watumishi hewa, maelekezo yametoka ya kumaliza kufanya analysis ya kuangalia watumishi hewa na baadaye tutaendelea na mchakato wa kupata ajira mpya na vijana wetu watapata kazi katika maeneo ya site.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamuomba Mheshimiwa Ndassa, tuwe na subira, jambo hili linakwenda vizuri, kwa sababu vijana wanaopakuliwa kutoka vyuoni, utaratibu wa Serikali utakapokaa vizuri sasa watapelekwa maeneo husika baada ya kupata ajira ili wakawapatie wananchi huduma ya afya.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Miji ya Sumve, Nyamatala, Malya, Nyambiti, Hungumarwa inakua kwa kasi sana. Mheshimiwa Waziri katika ziara yake aliyoifanya Kwimba nilimuomba vitendea kazi kama gari na vifaa vya kupimia. Nataka kujua ombi letu hilo limefikia wapi?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli nilitembelea kwenye Jimbo lake na hayo anayoyasema tuliyazungumza. Kikubwa ambacho nataka nimhakikishie, katika bajeti yetu ambayo imepitishwa na hata kwenye bajeti ya Wizara ya Fedha ambayo tunaendelea kuijadili, kuna fedha kiasi cha shilingi bilioni 8.8 zimetengwa kwa ajili ya kununua vifaa vya upimaji kwa sababu tatizo la upimaji ni tatizo kubwa katika nchi yetu na tunasema eneo lililopimiwa ni asilimia 15 tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pale ambapo tutakuwa tumefanikiwa kupata pesa hizo baada ya kuwa tumepitisha bajeti hii tunajua hizo shilingi bilioni 8.8 kwa ajili ya kununua vifaa vya upimaji ziko pale. Tukishapata, vifaa hivyo vitakwenda katika Kanda. Jimbo la Sumve liko kwenye Kanda ya Ziwa, kwa maana hiyo, eneo la Kanda wakipata vifaa hivyo basi upimaji katika maeneo ya Nyamatala na mengine aliyoyasema yatafanyiwa upimaji kwa wakati muda utakapofika.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mwaka 2013 Serikali ilitenga jumla ya shilingi bilioni 3.6 kwa ajili ya kuchimba visima vinane katika vijiji vinane, lakini hadi sasa shilingi milioni 184 tu zilizopelekwa.
Naiuliza Serikali ni lini sasa kwa sababu azma ya Serikali ilikuwa ni kuchimba visima vinane; ni lini sasa Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya visima hivyo?

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, ujasikia vizuri swali? Mheshimiwa Ndassa sehemu ya mwisho ya swali ni lini?
MHE. RICHARD M. NDASSA: Katika Jimbo la Sumve na Jimbo la Kwimba Serikali ilipanga kuchimba visima vinane katika vijiji vinane vya Isunga, Kadashi, Gumangubo, Shilima, Mande na Izimba A. Fedha zilizotengwa ni shilingi bilioni 3.6 lakini hadi juzi ni shilingi milioni 185 tu ndizo zilizopelekwa, kwa hiyo, miradi hii imekwama, ni lini sasa Serikali imepeleka fedha hizo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, tumeishaelekeza tayari, kwamba ukishapata bajeti, Halmashauri ikipata bajeti, kitu cha kwanza ni kufanya taratibu za manunuzi. Kuhakikisha kwamba mkandarasi anaanza kazi, na akishatekeleza kazi utuletee hati, ya madai ya mkandarasi tuweze kuipeleka kwa Waziri wa Fedha aweze kutupatia fedha.
Nina wasiwasi lakini tutashirikiana na Mheshimiwa Ndassa kuangalia ni kazi ipi imeishafanyika tangu kupeleka hiyo hela, inawezekana kwa sababu hata wakati wa ziara yangu niliona hiyo. Unakuta mtu ametengewa bajeti lakini hajafanya kazi yoyote, anasubiri kwamba kwanza aletewe hela, utaratibu huo kwa sasa hatunao. Ukishapata bajeti basi fanya taratibu za manunuzi na mkandarasi afanye kazi akifanya kazi ndio tutampatia hela.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, tarehe 11/10/2014 ilikuwa siku ya Jumamosi saa 5.32; Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne wakiwa na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano, walizindua daraja la Mto Simiyu kule Maligisu na kuahidi kwamba mita 50 kuingia kwenye daraja na mita 50 kutoka kwenye daraja itawekewa lami. sasa nataka kujua, je, ahadi hii ya Mheshimiwa Rais itatekelezwa lini?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Richard Ndassa ni Mwalimu wangu. Naomba nimhakikishie kama ambavyo nimekuwa nikiongea naye kabla kwamba maungio haya ya daraja la Mto Simiyu kama ambavyo Viongozi wetu waliahidi, tutahakikisha tunayatekeleza. Naomba tu aendelee kutukumbusha, kwa kadri hapa ninavyoongea, wahusika wote kuanzia TANROAD Mkoa wa Simiyu, pamoja na Makao Makuu, wananisikia. Tuhakikishe hili daraja pamoja na barabara yake ambayo iliahidiwa, tuifanyie kazi kama ambavyo viongozi wetu waliahidi.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri swali la nyongeza. REA Awamu ya II imebakiza siku 27, je, wameshafanya tathmini ya kutosha nchi nzima? Kama jibu ni ndiyo utekelezaji wake ni asilimia ngapi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nachagua swali la tathmini ya ujumla. Nimhakikishie Mheshimiwa Ndassa na nimshukuru tumeshirikiana, mpaka sasa tathmini tuliyofanya ukamilifu wa kazi ya REA Awamu ya II ni asilimia 91 ya kazi zote zilizokwishakamilika.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Wizara hii inashughulika na habari, utamaduni, sanaa na michezo. Kwa idhini
yako, naomba uniruhusu niulize swali la michezo. Timu yetu ya vijana under 17
imebahatika kwenda kwenye fainali itakayofanyika Gabon Aprili, ni mwezi
mmoja tu sasa umebaki. Je, Serikali pamoja na TFF tunajiandaa namna gani ili
timu yetu hii isiende kushiriki bali iende kushindana na kuleta ushindi katika nchi
yetu?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu
Spika, ni kweli kwamba Serengeti Boys wamefanya vizuri sana katika mchezo wa
mpira wa miguu katika nchi yetu na kuiletea heshima nchi yetu. Nichukue nafasi
hii kuwapongeza kwa moyo wao wa dhati ambapo wamejitahidi kupambana
na kwa kweli wanafanya vizuri. Kama Serikali, kwanza nilihakikishie Bunge lako
kwamba tumeshiriki kikamilifu kwa wao Serengeti Boys kufanikiwa kufika pale
walipofika ikiwemo kutafuta rasilimali kwa wadau. Niwashukuru sana wadau wa
sekta binafsi ambao wamekuwa wakijitolea kuhakikisha timu yetu hii inafanya
vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kwa kushirikiana na TFF tumejipanga
kwamba Serengeti Boys watakwenda kupiga kambi ya mwezi mzima kabla ya
kwenda kwenye fainali za mashindano haya. Serikali ikishirikiana na wadau wa
sekta binafsi, tutahakikisha zinapatikana rasilimali za kutosha kuhakikisha vijana
hawa wanapiga kambi yao, lakini pia wanakwenda kuchukua kombe na siyo
kushiriki. Kila tukiangalia uwezekano wa kushinda, ni mkubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe Waheshimiwa Wabunge na
Watanzania kwa pamoja tuungane pamoja kwa dua zetu na rasilimali zetu
kuhakikisha kwamba Serengeti Boys wanakwenda na wanarudi na ushindi hapa
nchini.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante sana, naomba nimuulize bwana Waziri; katika Wilaya ya Kwimba kuna vijiji kumi ambavyo vilipangiwa kupelekewa maji katika mradi wa vijiji kumi, zaidi ya miaka kumi leo,
naomba leo nijue katika hivi vijiji vya Kadashi, Isunga, Shirima na Mhande mkandarasi hayupo site mpaka leo na kwa sababu nilishafanya mawasiliano na Mheshimiwa Waziri wa Maji mwenyewe kwa muda mwingi, nataka leo anipe majibi kazi hii ya miradi hii ya maji katika Wilaya ya Sumve na Kwimba lini itakamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli anachokisema Mheshimiwa Mbunge haongopi na mimi naomba nikiri kwamba nimefika Jimboni kwake kule na miongoni mwa jambo katika taarifa ambayo niliyosomewa ni changamoto ya maji na hali kadhalika suala zima la vijiji kumi katika suala zima la mpango wa World Bank na ni kwa sababu nimesema hapa nyuma kwamba miradi hii ya maji maeneo mengi sana ilisimama na ilisimama kwa sababu hapa nyuma suala zima la kifedha lilikuwa siyo zuri zaidi, lakini
sasa hivi Serikali katika Mfuko wa Maji tumejipanga vizuri kuhakikisha miradi hii inatekelezeka. Lakini jambo lingine utakuta kuna changamoto ya mkandarasi, kwa hiyo kwa sababu taarifa zimeshakuja Serikalini na Waziri wa Maji taarifa hii anayo sasa kwa kina basi nadhani mpango mzuri utafanywa naamini jambo hili
litafanyika vizuri na miradi hii itakamilika na wananchi wa Jimbo lako watapata maji kwa sababu commitment ya Serikali hii kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji.